Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Juma Kombo Hamad (12 total)

MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza. Imekuwa ni jambo la kawaida kwa Serikali kuwaacha wananchi mpaka wamejenga na baadaye Serikali utakuta inachukuwa hatua sasa ya kubomoa nyumba za wananchi ambao tayari wamekaa pale kwa muda mrefu.
Je, haionekani kwamba sasa inaweza kupelekea matatizo kwa wananchi na kushindwa kujiweza na kujimudu kutafuta makazi mengine? (Makofi)
Swali la pili; je, ni lini sasa Serikali itasimamia Mipango Miji yake kama sheria inavyotaka kama ambavyo amekuwa akizungumza Mheshimiwa Waziri ili kuondoa tatizo hili?
Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza naomba kujibu kwamba, siyo kweli kwamba tunawaacha wananchi wanaendelea na kazi za kujenga bila kuwazuia. Tatizo lililoko ni katika Halmashauri zetu ambazo mara nyingi katika kutoa katazo mtu anapokuwa amekiuka wanaweka pengine alama ya X, lakini wakati huo huo pia wanaendelea na shughuli za maeneo mengine pasipo kufuatilia kwa karibu.
Mheshimiwa Spika, kwa hatua hiyo, Wizara kama Wizara, sasa hivi imechukua hatua na tumeanza na Mkoa wa Dar es Salaam. Tunapeleka usimamizi kwa viongozi wa maeneo hayo na ndiyo maana tumetoa pengine Ramani kwa Wenyeviti wa Mitaa ili aweze kutambua maeneo yake na mpango uliopo katika yale maeneo ili kuweza kujua lipi ni eneo la wazi, lipi ni eneo ambalo halitakiwi kujengwa?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuna imani kwamba kama watatoa ushirikiano watakuwa ni sehemu ya usimamizi na hapatakuwa na mwananchi yeyote ambaye atakuwa amejenga kinyume cha sheria kwa sababu usimamizi tayari utakuwa chini ya viongozi wa maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, swali la pili nadhani limejibiwa pamoja na la kwanza kwamba ni lini tutafanya hivyo? Tayari hatua tumeshazianza. Natoa rai tu kwa sasa kupitia Bunge hili kwamba, tuombe Halmashauri zetu, kwa sababu maeneo mengi ambayo watu wanajenga kiholela; wapo wanaoona, wapo ambao wanakaa kimya na hawafuatilii.
Tuombe tu sasa kwamba popote pale ambapo mtu atajenga kinyume na utaratibu, halafu na uongozi wa pale upo unamwona mpaka anamaliza, atakapovunjiwa nyumba yake, kiongozi husika wa eneo lile atawajibishwa ikiwa ni pamoja na kulipa fidia kwa yule ambaye amekiuka taratibu na yeye akiwa anashuhudia.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Spika, ni kawaida kwa Wizara hii ya Mambo ya Ndani kila siku kuja na jawabu lilelile. Swali langu la mwanzo ni kukosekana kwa boti ya doria katika Kisiwa cha Pemba na mazingira ya jiografia yalivyo ya Kisiwa cha Pemba ni hatari kwa mazingira yela yalivyo; je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba kuwakosesha wanamaji hawa wa boti ya doria ni kuhatarisha mazingira ya amani kwa nchi yetu hii ya Tanzania?
Swali la pili, kimsingi Wizara ya Mambo ya Ndani imekuwa ikitenga bajeti ya lita kadhaa za mafuta yasiyopungua 1200 kila mwezi je, Mheshimiwa Waziri anaweza kutueleza mafuta haya yanatumikaje ukizingatia kwamba ndani ya Kisiwa cha Pemba hakuna boti ya doria kwa Kikosi cha Wanamaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi kwamba wakati jitihada za kupeleka boti Pemba pale uwezo utakapopatikana linaendelea kwa sasa hivi tunafanya kazi kwa mashirikiano mazuri na vikosi vingine mbalimbali kama vile vikosi vya SMZ ambavyo wana boti za doria zinazokidhi mahitaji kwa kipindi hiki kutoa huduma maeneo ya Pemba ikiwemo Jimbo la Wingwi.
Mheshimiwa Spika, lakini kuhusiana na mafuta kimsingi ni kwamba fedha kwa ajili ya matumizi ya mafuta ya Jeshi la polisi kiujumla hazitoshi kwa hiyo, ningedhani kwamba Mheshimiwa Mbunge badala ya kuhoji matumizi angehoji uwezekano wa kuongeza kwa sababu hata zilizopo hazikidhi mahitaji ya huduma katika matumizi ya Jeshi la Polisi.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba kwa ruhusa yako sasa niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika siku za karibuni kupitia Vyombo vya Habari tulimuona Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akitoa maagizo kwa Waziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kikatiba, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, je, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana Mamlaka Kikatiba kutoa maagizo kwa Waziri kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika level ya Jumuiya ya Afrika Mashariki tunashuhudia Mawaziri wakizungumzia masuala mbalimbali ambayo hayahusu Muungano, yakiwemo masuala ya kilimo, masuala ya biashara na shughuli nyingine. Je, Mheshimiwa Waziri anataka kudhihirisha sasa au anataka kutuambia kwamba, Tanzania Bara itaendelea kula kwa niaba ya Zanzibar hadi lini? Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema amesoma katika magazeti na magazeti siyo njia au sababu ya kueleza mambo hayo, ndio. Yeyote anayetumia magazeti hajui mamlaka na nafasi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maagizo ya Serikali yanatolewa kwa nyaraka, kwa barua. Sijawahi kupokea maagizo kwa gazeti au sms, napokea maagizo kwa barua au waraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayo mamlaka yote ya mambo yote yanayohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama nchi huru. Kwa hiyo, katika mambo yote yanayohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mkuu wa nchi ni mmoja tu, ni Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Yeye peke yake ndiye Amiri Jeshi, hakuna mtu mwingine yeyote wa kuyaamuru Majeshi ya Tanzania isipokuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa sababu yeye peke yake ndiye Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu na Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wa Zanzibar ni Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwenye heshima na hadhi ya Urais kwa mambo yote yasiyokuwa ya Muungano yanayoihusu Zanzibar, lakini pia ni Mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nafasi yake hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia usawa wa wabia wa Muungano katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atatoka Tanzania Bara, Makamu atatoka Tanzania Zanzibar na ikiwa Rais atatoka Tanzania Zanzibar Makamu atatoka Tanzania Bara. Huo ndio usawa uliowekwa ndani ya Katiba na Ibara iko wazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo basi, anayeiwakilisha nchi hii katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mambo yote ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muungano wetu ni wa aina yake ya kipekee na mara nyingi umewafanya watu wasielewe, ndiyo maana katika mambo yote duniani inayoonekana ni Jamhuri ya Muungano, lakini ndani ya Tanzania yenyewe kuna pande mbili, Tanzania Bara ambayo mambo yake yanasimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Tanzania Zanzibar ambayo mambo yake yanasimamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Ndio maana nchi hii ina Katiba mbili, Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Katiba ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. (Makofi)
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba sasa nimuulize Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, ni miaka 20 sasa toka pale ambapo Zanzibar ilitakiwa ijiondoe kwenye Jumuiya hii ya OIC. Zanzibar ilijiunga na Jumuiya ya OIC kwa maslahi ya kiuchumi na si siasa wala siyo dini kama vile wengine walitafsiri katika kipindi hicho. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, je, sasa kwa sababu Tanzania kwa miaka 20 imeshindwa kujiunga kama ilivyoahidi ipo tayari kutoa ruhusa kwamba Zanzibar ina haki ya kujiunga na taasisi hii? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Waziri ametaja miradi mingi na ameenda mbali lakini nataka kuona tu kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Tanzania, anionyeshe kwa Ibara kwamba Zanzibar ina nafasi hii ndani ya Jumuiya za Kimataifa lakini yeye kazungumza masuala mengine ambapo na mimi nitaelekeza nguvu zangu huko huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kataja miradi hapa, miradi hii kwa bahati mbaya au nzuri yote imetekelezwa upande mmoja wa Kisiwa cha Unguja, si vibaya yote ni Zanzibar, lakini katika ahadi ambayo imekuwa ikiwekwa kila bajeti ni upanuzi wa uwanja wa ndege wa Pemba pamoja na bandari ya Mkoani Pemba. Naomba Mheshimiwa Waziri anieleze ni lini sasa bandari hii na huu uwanja wa ndege kupitia Jumuiya hizi za Kimataifa utakelezwa na itapanuliwa kama walivyoahidi? Mheshimiwa Spika, nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, anasema kwamba kwa miaka 20 Zanzibar imejiondoa katika kujiunga na ile Jumuiya ya Kiislam na kwamba sisi kama Tanzania iko tayari kuiruhusu Zanzibara kujiunga na taasisi hiyo? Jibu langu nasema bado liko vilevile kama lilivyojadiliwa katika Bunge hili katika siku za nyuma na maamuzi yaliyofanyika siku za nyuma kwamba kama ni faida bado Tanzania ikiwemo Zanzibar inaweza ikafaidika tu kwa mahusiano yaliko baina yetu na nchi ambazo ni wanachama katika Jumuiya hiyo hiyo ya Kiislam.
Mheshimiwa Spika, kama anavyojua kwenye Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania suala la dini tumesema kwamba si suala ambalo tunataka tulijadili au kujihusisha na kuweza kuweka utenganishi kati ya sehemu ya nchi na nchi nyingine. Kwa hiyo, bado msimamo uko pale pale kwamba sisi kama Tanzania hatujakubaliana kwamba Zanzibar ijiunge na taasisi hiyo. Hata hivyo, faida za taasisi hiyo bado tunaweza kufaidika nazo kwa kufanya mikataba baina sisi kama Tanzania au upande wa Zanzibar kushirikiana na nchi hiyo kwa kufanya bilaterals. (Makofi)
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri katika jibu la msingi amesema kwamba jumla ya Walimu 3,655 walipoteza kazi baada ya uhakiki na kugundulika na vyeti feki. Nataka kujua tu katika mwaka 2016/2017 na 2017/2018 Serikali kama ilipoteza Walimu hawa; je, hadi sasa imeajiri Walimu wangapi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya zoezi hilo kukamilika Serikali katika miaka hii miwili 2016/2017 na 2017/2018 imeajiri jumla ya Walimu 6,495. Kati ya hao Walimu wa shule za sekondari wa masomo ya sayansi na hisabati ni 3,728 na Walimu wa shule za msingi ni 2,767. Idadi hiyo ni zaidi ya walioachishwa kazi ni kwa sababu ya kuwa na vyeti vya kughushi.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. pamoja na jibu la Mheshimiwa Waziri lakini zipo tafiti kadhaa na nyingi ambazo kimsingi zinaonesha kwamba bado kuna madhara makubwa ya watu kuumwa na kichwa na hata kupoteza kumbukumbu kutokana na mionzi inayotokana na minara hii ya simu.
Je, Serikali haioni kwamba kuna haja hasa ya kufanya tafiti za kina zaidi ili kubaini kwamba madhara haya yapo na namna gani Serikali itatumia njia ili kuyaondoa madhara hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, minara hii imejengwa na imo ndani ya Halmashauri, sasa kimsingi kuna malalamiko makubwa kwa wananchi ambao wamo ndani ya Halmashauri hizo ambazo minara hii imejengwa kwamba hawafaidiki na uwepo wa minara hii ingawa minara hii ipo kibiashara. Je, Serikali haioni kwamba kuna haja sasa kuandaa utaratibu maalum ili kuona kwamba wananchi na Halmashauri ambazo minara hii ipo zinafaidika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI UCHUKUZI NA MAWASIALIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa tafiti zilizofanyika na Umoja wa Mawasiliano Duniani (ITU) kama nilivyoeleza katika majibu yangu ya msingi siyo kwamba madhara hakuna kabisa, madhara yapo na hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa na makampuni ya simu kwa kuzungushia uzio eneo ambalo wamefunga mnara. Katika kufanya hivyo tunaamini kwa ule upungufu madhara wa mara 1,000 kwa kila mita moja kutoka kwenye mnara hakuna mtu anayeweza kudhurika. Hayo madhara mengine yanayotokana na mtu kuumwa kichwa ni yale ambayo siyo ajabu inawezekana hayatokani na matatizo ya mnara kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili ni kweli kwamba kumekuwa na changamoto ya wale ambao minara imefungwa kwenye maeneo yao na kutopata chochote kutokana na hilo na hilo limekuwa likishughulikiwa. Tumekuwa tukipata changamoto kama Wizara kwamba tunapowapa kazi wale watoa huduma labda Tigo, Vodacom, Airtel na kadhalika wanakwenda kwanza kuongea na wananchi kule vijijini. Kwa hiyo, wakishaongea nao wananunua maeneo yao kwa hiyo mwananchi wa kijijini kwanza anakuwa anapokea rent, lakini kunakuwa na tozo ya Halmashauri ambayo huwa inatoa kutokana na vikao walivyokaa Madiwani husika.
Kwa hiyo, hilo linakuwa ni gumu sana sisi kama Serikali kuendelea kuliingilia lakini nimuahidi Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge kwamba tunaendelea kulifuatilia kuhakikisha kwamba Serikali kupitia Halmashauri inapata tozo ambazo ni stahiki. (Makofi)
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante. Zanzibar ni Kisiwa kidogo chenye wakazi wachache sana, wakazi wa Zanzibar ni kati ya 1,000,000 mpaka 1,500,000 na kutokana na hali hiyo Zanzibar inategemea soko la bidhaa kutoka nje. Maana yake Zanzibar inategemea soko la bidhaa zinazotoka nje kusafirishwa nchi jirani au baadhi ya nchi nyingine ili kutafuta soko na ndiyo maana Zanzibar imejiandalia mfumo wake mahsusi ili kufanikisha wafanyabiashara kutoka nchi nyingine ikiwemo Tanzania Bara wafike Zanzibar wachukue bidhaa zinazotoka nje kwa ajili ya kwenda kufanya biashara sehemu nyingine.
Mheshimiwa Spika, sasa Serikali haioni kwamba kuilazimisha Zanzibar kufata mfumo wa TANCIS ndiyo maana ya kuua soko la bidhaa kutoka nje kwa pale Visiwa vya Zanzibar? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Waziri kasema haiwezekani kuunda Tume, Bunge haliwezi kuunda Tume. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, Je, Serikali kupitia Wizara ya Fedha ipo tayari kuunda Kamati Ndogo wakiwemo Wabunge, Maafisa wa TRA na yeye mwenyewe kwenda Zanzibar kukutana na wadau, wafanyabiashara wa Zanzibar hususan Taasisi ya Wafanyabishara Zanzibar ili kuangalia ukubwa wa tatizo hili na kulitafutia ufumbuzi? Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi ni kwamba hiki kinachotokea ni kuhakikisha kunakuwa na ushindani katika soko la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ndiyo maana bidhaa zinazouzwa kutoka Zanzibar zilizotoka nje kuja Tanzania Bara lazima zifanyiwe uthamini ili kuhakikisha wafanyabiashara wanaotumia Bandari za Serikali ya Jamhuri ya Tanzania Bara wanapata ushindani ulio sawia.
Mheshimiwa Spika, amesema kwamba wafanyabiashara kutoka nchi nyingine. Kumekuwa na tatizo la wafanyabiashara kutoka nchi nyingine kwenda kununua bidhaa Zanzibar na kuja kuzi-dump katika soko la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ndiyo maana kwa sababu bidhaa zile hazijazalishwa Zanzibar lazima zinapoingia Tanzania Bara ziweze kulipa kodi husika ili ushindani huo uweze kuwepo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, napenda kumwambia Mheshimiwa Kombo kwamba nimesema kwenye jibu langu la msingi Serikali zetu mbili, Serikali ya Zanzibar pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinalifanyia kazi tatizo hili na tuna uhakika kwamba changamoto hii itafika mwisho, kwa sababu majadiliano yamefika sehemu nzuri na tuna imani kubwa kwamba changamoto hii itafika mwisho sasa.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mara kadhaa maafisa mbalimbali ambao wanatumia magari ambayo yamekuwa na namba za Zanzibar wamekuwa wakikumbana na vikwazo vya TRA pamoja na Polisi kwamba, namba hizo ni namba za kigeni wakati anapotembea Tanzania Bara. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, je, yupo tayari sasa kutenga muda mahususi kuwapa taaluma Polisi pamoja na TRA kuona kwamba, Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kuambatana na sisi au na mimi kwenda kuangalia namna Maafisa wa TRA wanavyofanya kazi pale bandarini kwamba, unapokuja tu na kilo tano za sukari kutoka Zanzibar au Tv ya nchi 21 unatakiwa ulipe kodi? Je, hili yupo tayari kwenda kulishuhudia Bandari ya Zanzibar ili kutoa mwongozo na taaluma kwa ajili ya shughuli hizo za kibiashara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS – MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbarouk, kwa niaba yake Mheshimiwa Juma ameuliza vizuri sana:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza niko tayari kwa yote mawili, lakini kwa ufafanuzi zaidi hili la vyombo vya moto kwa sababu, bado lipo tayari kwenye majadiliano na vikao vinaendelea, nadhani baada ya hivyo vikao sasa nitakuwa tayari kwa ajili ya kutoa hiyo elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, niko tayari kuambatana na wewe na Wabunge wengine ambao wanatoka Zanzibar kwenda kushiriki kwa pamoja kuhakikisha kwamba, eneo hili tunalifanyia ufumbuzi. Ahsante sana.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, ni ukweli usiopingika kwamba yapo matukio ambayo yalitikisa sana ya aina hii Tanzania. Matukio haya ni pamoja na kitendo cha jaribio la mauaji ya Mheshimiwa Tundu Lissu, kutekwa kwa Mohamed Dewji, kutekwa, kupigwa na hatimaye kuuawa kwa Mheshimiwa Ali Juma Suleiman pale Unguja, matukio ya Kilwa na matukio ya kutekwa vijana saba pale Mkoa wa Kaskazini Pemba, Jimbo la Mtambwe. Je, Serikali inatuambia kwamba pamoja na matukio haya makubwa na mazito na ya kutisha, ndiyo ni mtu mmoja tu hadi sasa ambaye amekamatwa na kuchukuliwa hatua?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, naomba kutaka kufahamu, je, Serikali ipo tayari sasa kuunda Tume ili kuchunguza matukio haya ili kuyabainisha na kuwabainisha wanaohusika na matukio haya ili kuchukuliwa hatua za kisheria?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Juma Kombo Hamad, Mbunge wa Wingwi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ametaja matukio mbalimbali ambayo yametokea kwa wakati tofauti. Nataka tu nimthibitishie kwamba matukio haya kila moja Jeshi la Polisi liliyachukulia kwa uzito unaostahili na yapo katika hatua mbalimbali za upelelezi, yako ambayo upelelezi wake umeshakamilika na yameshawasilishwa kwa DPP, mengine yamepiga hatua hata zaidi ya hapo. Kwa hiyo, kuyazungumzia kwa pamoja matukio ambayo ni tofauti na yana mazingira tofauti inakuwa ni changamoto. Hata hivyo, nimthibitishie kwamba, kwa sababu suala la upepelezi mchakato, ni imani yetu kwamba matukio haya yataweza kufikia katika hatua nzuri na hatimaye haki itaweza kupatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na hoja yake ya kuundwa Tume, sijui sijaelewa anazungumzia Tume ya aina gani lakini nataka nimthibitishie tu kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pale ambapo imekuwa ikipokea malalamiko mbalimbali ambayo yanapelekwa katika vyombo vyetu vya usalama ikiwemo Jeshi la Polisi, tumekuwa na utaratibu wa kuunda Tume. Kuna Tume mbalimbali tumekuwa tukiunda na zimekuwa zikifanya kazi vizuri, kwa hiyo, si jambo geni.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Spika, ahsante. Serikali kwa muda mrefu imekuwa ikitegemea fedha kutoka kwa wafadhili katika kuhudumia waathirika wa gonjwa la UKIMWI fedha ambazo upatikanaji wake umekuwa na changamoto kubwa. Nilitaka kujua tu, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba sasa inatenga fedha za ndani katika kuhudumia kundi hili la wagonjwa wa UKIMWI? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali imekuwa inashirikiana na wadau katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI na wadau wakubwa ni pamoja na Global Fund na PEPFA.

Mheshimiwa Spika, katika kuliona hilo na kwa lengo la kuhakikisha kwamba hizi huduma za matibabu au huduma afua za VVU kwa waathirika zinakuwa endelevu, Serikali imeanzisha Mfuko wa Masuala ya UKIMWI ambao unaitwa AIDS Trust Fund ambapo Serikali inaweka fedha pale, inachangia fedha zake kwa lengo la kuhakikisha kwamba baadhi ya afua zinakuwa funded kwa kupitia mfuko huo.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Kabla sijauliza maswali mawili ya nyongeza, nione tu kwamba bahati mbaya sana Mheshimiwa Waziri hakujibu swali langu na badala yake ameenda kuzungumza vitu vingine. Nilichokiomba mimi ni kuona kwamba busara ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano inatumika na kuona suala la Bahari Kuu sasa Zanzibar wanalitekeleza kama Zanzibar kwa sababu ya kuendeleza uchumi wa Zanzibar hicho ndiyo ambacho kwamba nimekiuliza mimi. Bahati mbaya ameenda kujibu masuala ya sheria na vitu vingine. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza:

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar ni Visiwa na Bahari Kuu ni Sehemu ya rasilimali yake kubwa ambapo kama itawekezwa vizuri ina uwezo wa kuchangia kwa kiasi kikubwa kwa zaidi ya asilimia 50 kwenye uchumi wa Zanzibar na kwa sababu ni Visiwa ambavyo vimezungukwa na bahari. Je, ni mkakati gani wa Serikali kuisaidia sasa Zanzibar ili eneo hili la Bahari Kuu litumike vizuri na kukuza uchumi mahsusi hasa kwa upande wa Zanzibar?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naomba tu Mheshimiwa Waziri anijibu hii taasisi ambayo ipo kwanza ni taasisi gani na imesaidia kwa kiasi gani kuchochea uchumi hasi kwa upande wa Zanzibar toka kuanzishwa kwake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ningetaka kulijibu swali kama lilivyoulizwa ningeishia kusema tu Serikali haiko tayari kuondoa eneo hili la uvuvi wa Bahari Kuu kwa upande wa Zanzibar ikaachiwa kwa sababu ningekuwa nimejibu. Lakini nimeelezea msingi wake kwamba msingi wa hili ni wa Kimuungano zaidi kwa sababu kwenye sheria ile ya Kimataifa inatambulika kama ni sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika International Law.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi nini Zanzibar inanufaika? Kwa kweli, manufaa ni makubwa toka tulipobadilisha na kuleta hii sheria ambapo kwa sasa itaasisi katika mapato yanayopatikana katika uvuvi wa bahari ile exclusive economic zone basi asilimia 50 inayopatikana yale mapato yanaweka katika ile taasisi ya Kimuungano na makubaliano kwa sasa katika hatua ya mpito ni kwamba asilimia 50 inayobakia ndiyo itagawanywa kati ya Zanzibar asilimia 40 na Tanzania Bara asilimia 60.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi hapa hata ile sheria yenyewe ambayo ilipitishwa bado wenzetu wa Zanzibar Baraza la Wawakilishi hawajaiorodhesha. Kwa hiyo, kama wakiiorodhesha ndipo mnaweza tukaendelea tukatoka kwenye mpito tukaja kwenye mazungumzo halisi ya namna gani sasa hoja zingine kama hizi zinaweza zikaja. Kwa hiyo ni vizuri kwanza ikaorodheshwa halafu ndiyo tuendelee kuzungumza namna ya utekelezaji wa suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maelezo haya ninadhani rafiki yangu Kombo nimemjibu uzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD:Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, nina maswali mawili madogo sana ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa jibu la Mheshimiwa Naibu Waziri, ni kusema kwamba Serikali imeshindwa kuwapatia watanzania Vazi la Taifa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali namba mbili, nilitaka kujua tu, Serikali katika mchakato huu ambao kwa mujibu wa Mheshimiwa Naibu Waziri amesema ulianza mwaka 2011, ni muda mrefu kidogo na ni mchakato ambao ulichukua muda. Anaweza kutueleza ni fedha kiasi gani za Watanzania ambazo zilitumika katika mchakato huo ambao hadi sasa haukukamilika na ile ndoto ya Watanzania kuwapatia vazi la taifa sasa imepotea? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza amezungumza kwamba Serikali imeshindwa kukamilisha mchakato wa kupata Vazi la Taifa. Napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba Serikali haijashindwa na Serikali haijawahi kushindwa na jambo lolote, hususan Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, kitu ambacho tunakifanya, kama ambavyo nimejibu yangu ya msingi kwamba kwa sasa hivi tumeshaufufua upya huo mchakato na nikuhakikishie kwamba Mheshimiwa Mbunge kwamba mchakato huo, muda si mrefu utaenda kukamilika.

Kwa hiyo, nitumie fursa hii kuweza kutoa wito kwa Maafisa Utamaduni wote wa Mikoa yote ya Tanzania, lakini vilevile kwa Makatibu Tawala wote wa Mikoa ambao ndiyo tumewakabidhi hilo jukumu, ili Vazi la Taifa liweze kupatikana kuhakikisha kwamba wanasimamia huo mchakato uweze kukamilika kwa haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikija kwenye swali lake la pili, kwa sababu ametaka kujua kuhusiana na fedha ambazo zimetumika kuanzia mchakato ulipoanza mwaka 2011. Niseme kwamba kwa sababu ni suala la kitakwimu, naomba baada ya hapa Mheshimiwa Mbunge tuweze kuonana ili niweze kukupatia hiyo takwimu. Ahsante.