Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Ally Yusuf Suleiman (6 total)

MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mheshimiwa Waziri amesema kwamba kama ziko dosari katika kukimbiza Mwenge basi zitarekebishwa. Mimi nachotaka kumwambia hakuna dosari, dosari ni huu Mwenge wenyewe. Kwa sababu kwanza unapoteza fedha nyingi kupita kiasi na wakati na kwa kule kwetu tunaamini kukimbiza Mwenge ni ibada. Kwa nini tuendelee kulazimishwa kuabudu moto?
Swali langu ni hilo kwa nini tulazimishwe kuabudu moto? Sisi tunaamini ni ibada ya moto hiyo.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimia Mwenyekiti, labda tu nianze kwa kumnukuu mwanafalsafa mmoja ambaye nilimsoma anasema, vipo vitu vingine vinahesabika lakini huwezi kuvihesabu. Unaweza ukawa na vitu vinavyohesabika lakini ukashindwa kuvihesabu na nataka nikuambie hata wewe unaweza kuwa na mtazamo ambao ni hasi kuhusu Mwenge wa Uhuru lakini utashindwa kutekeleza mtizamo huo wa kuufuta Mwenge wa Uhuru katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nakuambia hivi Mheshimiwa Mbunge, mwaka jana wakati tunahitimisha mbio za Mwenge Mkoani Simiyu, kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Simiyu, kwa kutumia Mwenge wa Uhuru Mkoa wa Simiyu umeweza kuzindua viwanda vitatu ambavyo vimeongeza maendeleo ya kiuchumi na vimeongeza ajira kwa Watanzania. Kwa hiyo, ukiangalia faida za Mwenge huu ni kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu tumezindua
mbio za Mwenge wa Uhuru Mkoani Katavi. Mkoa wa Katavi haukuwa na uwanja mkubwa wa michezo wa Mkoa. Nje ya bajeti ya maendeleo ya mkoa, Mkoa wa Katavi umeweza kuanza ujenzi mkubwa wa kiwanja cha mpira katika mkoa huo. Nimeeleza hapa miradi ya kujitegemea ambayo imebuniwa na wananchi ambayo imeongeza chachu ya maendeleo na uchumi wa wananchi katika Tanzania nzima. Mwenge wa Uhuru utadumu, utaendelea kusimama kama tunu ya nchi yetu ya Tanzania.
MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ajali za baharini zimekuwa nyingi sana siku hizi na kadhalika majanga ya baharini (disasters) naiuliza Serikali: Je, imejipangaje kwa kujenga vituo karibu na bahari na pia kutumia sayansi ya kileo, yaani kutumia kama drowns ili kuweza kubaini haraka sehemu zilizofikwa na mabalaa na kuweza kutoa huduma ya mwanzo haraka sana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimthibitishie pia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua umuhimu wa kuimarisha usalama katika maeneo ya bahari hasa pale ajali zinapotokea. Ndiyo maana kwa kulitambua hilo, Serikali imeamua kuunda kikosi kazi cha coast guard ambapo Jeshi la Polisi ni taasisi mojawapo ambayo imo katika kikasi hicho. Kwa pamoja na mambo mengine, kikosi hicho kinaangalia masuala yote yanayohusu uokoaji pale majanga yanapotokea ikiwemo upatikanaji wa vifaa vya kisasa kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amezungumza.
MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, ikiwa Serikali inayaamini haya majibu waliyonipa, swali la kwanza, je, haioni kwamba kuwahamisha Masheikh ambao mnawatuhumu kwa ugaidi kutoka Zanzibar kuja kushitakiwa Bara, ni kuinyang’anya Mahakama ya Zanzibar mamlaka yake? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ukisoma Tanzania Law Reports ya mwaka 1998, ukurasa wa 48 inayohusu kesi ya Maalim Seif Shariff Hamad akipingana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inasema wazi kwamba iwapo mtu atafanya kosa Zanzibar kwanza anapaswa kushtakiwa Zanzibar, pili anapaswa kushtakiwa na Mahakama ya Zanzibar. Swali linakuja hapa ni sheria ipi iliyotumika kuwahamisha Mashekhe kutoka Zanzibar ambao ni Wazanzibar kuja kushtakiwa katika Mahakama za Bara? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, sipingani na muuliza swali kwenye upande wa vipengele vya kisheria lakini naomba tu nimwambie kwamba kuna makosa ambayo specifically siyo ya kijiografia. Kwa mfano, kama watu watafanya makosa ya kung’oa michikichi Kigoma hilo unaweza ukalitaja kama ni kosa la Kigoma. Kama watu watang’oa mikarafuu Pemba unaweza ukasema kwamba hilo ni kosa lililofanyika Pemba na ni karafuu ya Pemba, lakini yanapofanyika makosa ambayo ni ya nchi nzima, Mtanzania ama raia yeyote awe wa Tanzania ama nje ya Tanzania atachukuliwa na taratibu za kufuata haki/sheria zitafanyika pale ambapo mamlaka inayochukua hatua hizo inaona ndipo panapofaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, haya ambayo muuliza swali ameuliza yanaendelea kubakia kwa maeneo na makosa ambayo yamefanyika na ni mahsusi katika eneo husika na hicho ndicho kinachofanyika. Hatua zote zitaendelea kujulikana kadiri hatua zinavyochukuliwa na upelelezi unavyofanyika. (Makofi)
MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Mheshimiwa Naibu wa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Katika jawabu la msingi la Mheshimiwa Waziri amesema Jeshi la Polisi limepewa mamlaka kisheria kutuhumu, kukamata, kuhoji na kuweka watuhumiwa mahabusu kwa muda ulioruhusiwa kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, wako watu wengi ambao wanawekwa mahabusu ya polisi kwa zaidi ya siku 15, akiwemo mwanafunzi Abdul Nondo, ambao wanawekwa mahabusu ya polisi kwa zaidi ya siku 15 bila ya kupelekwa mahakamani. Nataka nijue ni sheria gani ambayo inatumika au inatumiwa na polisi kuwaweka watu mahabusu ya polisi kwa muda huo mrefu bila ya kuwapeleka mahakamani? Nataka kujua sheria ni sheria gani. Swali la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ni hatua gani ambayo Mheshimiwa Waziri ataichukua iwapo tutamletea orodha ya watu ambao wamebambikiziwa kesi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama nilivyosema jeshi la polisi linafanya kazi kwa mujibu wa sheria na katika ufanyaji kazi wake kuna hatua mbalimbali za kuchukua ikiwemo kufanya upelelezi, kufanya mahojiano na baadaye mambo yote yale yakikamilika hatua nyingine ndipo huwa zinafuatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa jambo la usalama ni kipaumbele, usalama wa mtuhumiwa lakini na usalama wa raia wengine wanaosalia, Jeshi la Polisi hutumia wajibu wake lililopewa wa kulinda usalama wa raia kuweza kuhakikisha kwamba linatimiza majukumu yake na huku watu wakiwa salama pamoja na mali zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu jambo la pili, kwa kuwa ni suala la takwimu nitamwomba Mheshimiwa Mbunge niweze kuwasiliana naye kuweza kumpa masuala yale ya takwimu na yeye kama ana orodha kuweza kubadilishana orodha hizo. Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana jambo la kwanza nataka nimwambie Mheshimiwa Naibu Waziri nimerekebisha waliodhurumiwa katika haki za Binadamu. Na ningeweza kujibu sana lakini sio wakati wake. Maswali yangu mawili, kituo cha haki za binadamu LHRC Tanzania huwa kinaweka wazi matukio yote makubwa ambayo yanayotokea nchini yakiwemo utekwaji, uteswaji, upoteaji, upigwaji risasi, kuonyesha bastola hadharani….

MWENYEKITI: Uliza swali sasa.

MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Ubambikizwaji…

MWENYEKITI: Uliza swali sasa

MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Ripoti za Serikali hazibebi mambo mazito kama haya.

Swali la pili, nataka kujua ni challenge zipi ambazo serikali inazipata inapokwenda kutoa ripoti zake katika vikao vya kimataifa huku kukiwepo na ripoti mbadala za ndani zinazo kinzana na ripoti za Serikali?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, ni kweli Legal Human Right Center mara nyingi hutoa ripoti yenyewe inavyoona kuwa mambo ya haki za binadamu yamekuwa yakiendelea nchini, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sheria zetu zina ruhusu na inatoa uhuru wa maoni sio Legal Human Right Center hata watu binafsi mashirika mengine sio ya kiserikali kwa hiyo wanaongea mengi. Lakini katiba na sheria zetu zimetambua hasa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwamba ndio imepewa jukumu la kikatiba la kuhakikisha kwamba haki za binadamu zina heshimiwa na ndio imepewa fursa ya kusikiliza malalamiko mbalimbali. kwa hiyo, yoyote yule mwenye malalamiko na manunguniko kuhusiana na uvunjifu wa haki za binadamu pamoja na ufunjivu wa taratibu za utawala bora waweze upeleka kwenye Tume kama inavyotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ni changamoto gani tunapata huko tunapoenda nje kuhusiana na haki ya haki za binadamu, naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba changamoto kubwa kuliko zote ni uposhwaji mkubwa sana unaofanywa na sio tu taasisi mbalimbali lakini vilevile mtu mmoja mmoja ikiwa na baadhi na wanasiasa. Lakini kama anavyofahamu hivi karibuni Serikali imeamua kuchukua hatua kuhakikisha kwamba kila upotoshwaji unaotolewa unajibiwa pale unapotolewa kwa sababu mara nyingi ni kwa ajili ya kuchafua sifa njema ya Taifa letu.
MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Mheshimiwa Spika, moja ya kesi ambayo inavuta hisia ya watu wengi ni kesi ya Mashehe wa Uamsho kutoka Zanzibar ambayo ilianza awamu iliyopita na kurithiwa na awamu hii. Sasa ni zaidi ya miaka saba na hata kuanza bado:-

(a) Je, ni sababu gani iliyosababisha ucheleweshaji huu mkubwa wa uoaji haki?

(b) Je, ni muda gani kesi iliyokosa ushahidi inatakiwa kufutwa?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, kesi anayoiuliza Mheshimiwa Mbunge bado ipo Mahakamani na hivyo kwa mujibu wa Kanuni za kudumu za Bunge, suala lolote ambalo lipo Mahakamani haliwezi kujadiliwa Bungeni. Ni vyema tukasubiri vyombo husika vikafanya kazi yake na kutoa maamuzi.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, zipo sababu zinazoweza kusababisha ucheleweshaji wa kukamilika upelelezi wa kesi ya jinai, nazo zinaweza kutokana na sababu zifuatazo:-

(i) Asili na namna kosa lilivyotendeka na wahusika wanaotuhumiwa kutenda kosa hilo iwapo wametenda kosa hilo wakiwa maeneo mbalimbali kwa maana ya kuwa hawakai eneo moja na wana mtandao mkubwa ndani na nje ya nchi.

(ii) Aina ya kosa husika, mathalani kesi yenye viashiria vya ugaidi, utakatishaji fedha, uhujumu uchumi, rushwa na kadhalika. Watu wanaofanya makosa ya aina hii wana mtandao mkubwa ndani na nje ya nchi.

(iii) Upelelezi kuhitaji upatikanaji wa taarifa, nyaraka na mashahidi nje na ndani ya nchi. Katika mazingira hayo upelelezi wake huchukua muda mrefu kukusanya ushahidi huo.

(iv) Mheshimiwa Spika, kesi ambayo haina ushahidi haiwezi kufikishwa Mahakamani. Hata hivyo, kutokana na uzito wa kosa la kesi iliyo katika hatua za upelelezi, kesi hiyo inaweza kukaa muda mrefu katika hatua hiyo kabla ya kuamua vinginevyo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwepo changamoto za ukusanyaji wa ushahidi ndani na nje ya nchi wa kesi hii, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa sasa hivi taratibu za upelelezi wa kesi hii zinahitimishwa na hivi karibuni hatua za kusikilizwa kwa kesi hii zitaanza.