Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Saada Salum Mkuya (15 total)

MHE. SAADA SALUM MKUYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa maelezo yake, lakini Mheshimiwa Waziri najua kwamba karafuu ya Zanzibar ndiyo Karafuu ambayo ni quality duniani kote. Je, Wizara ya Biashara na Viwanda ya Tanzania ina mkakati gani kushirikiana na Wizara ya Biashara na Viwanda ya Zanzibar kuhakikisha kwamba tunajenga kiwanda ambacho kita-absolve karafuu ya Zanzibar kwa ajili ya kutengeneza products, kusafirisha nje lakini vile vile kupatia vijana ajira kama ambavyo tunaelezwa na ndiyo mategemeo yetu?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu Zanzibar ilikuwa ni kwamba Makatibu Wakuu wa Wizara ya Viwanda Zanzibar na wale wa Tanzania kwa upande wa Bara wakutane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda nitoe maelekezo kwamba wanapokutana sasa, kwa sababu najua wananisikiliza; na suala la Karafuu na Kiwanda na lenyewe waliunganishe walete majibu hapa tuweze kupata suluhu ya kutengeneza Kiwanda Zanzibar. (Makofi)
MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; katika mikakati ambayo imeorodheshwa ni kazi gani hasa zimefanyika katika kituo cha Afya cha Jeshi kilichopo Welezo ambacho kinahudumia wananchi wengi na hali yake ni mbaya sana. Kwa hiyo, hii mikakati imeorodheshwa lakini katika mwaka 2016/2017 ni kazi gani hasa zimefanyika katika kituo kile.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; namwomba Mheshimiwa Waziri tukiondoka Dodoma tufuatane, mguu kwa mguu twende katika Jimbo la Welezo tukatembelee kituo hiki cha afya, kipo katika hali mbaya na kinahudumia wananchi wengi na wengi wanakitegemea. Kwa hivyo, akienda akiona utajua sasa ni jinsi gani anaweza kukisaidia. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika mikakati niliyoielezea kuna baadhi ambayo imeshaanza na kuna baadhi ambayo bado tunategemea itaanza siku za usoni. Lile la Bima ya Afya ambayo kwa kweli tunadhani ndio itakuwa mkombozi wa kuboresha huduma za afya, hilo bado halijaanza, tupo katika mchakato na ni matumaini yetu kwamba likianza fedha nyingi zitapatikana ili kuweza kuboresha vituo hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa yale yaliyoanza ni msaada uliotolewa na Serikali ya Marekani na Ujerumani. Tumeshafanya ukarabati na tumenunua vifaa, lakini tumeanza na ngazi za Hospitali za Rufaa za Jeshi. Kwa sababu hata kwenye Jeshi kuna vituo vya afya, hospitali na hospitali kuu. Kwa hivyo, kazi iliyofanyika kwa mfano katika Hospitali Kuu ya Lugalo, kazi zilizofanyika katika Ali Khamis Camp Pemba, kazi zilizofanyika Mwanza na kadhalika ni kubwa na tunajua kwamba kazi hii haijakamilika kwa sababu bado kuna vituo hatujavifikia ikiwemo hicho cha Welezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoweza kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba tutafika, tunakwenda kwa awamu ili na chenyewe tukiboreshe wananchi pamoja na Wanajeshi waweze kupata huduma nzuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kutembelea katika kituo hicho, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba nipo tayari, nitakapofanya ziara ya eneo la Unguja, basi moja ya kazi zangu itakuwa ni kufuatana naye kwenda kuangalia kituo hicho.
MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba mipango inaendelea kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kufungua Ubalozi. Hata hivyo, tunaomba tu awaambie Watanzania hii mipango imefikia hatua gani ili na wao wapate confidence kwamba Ubalozi huu utafunguliwa karibuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, kwa upande wa mashirikiano, Zanzibar inashirikiana kwa karibu sana na Cuba hasa katika nyanja ya afya na imekuwa ikipeleka wanafunzi mbalimbali kwa ajili ya masomo ya muda mfupi na mrefu. Je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba kuchelewa kufungua Balozi hii katika Mji wa Havana kunawapa maisha magumu wanafunzi wale kwa maana wanakuwa hawajui wanapopata matatizo wakimbilie wapi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa maswali mawili ya nyongeza ambayo yameulizwa na Mheshimiwa Saada Mkuya akitaka kujua hatua iliyofikiwa kwa sasa hivi. Naweza kumwambia tu utaratibu wa mwanzo huwa tunafanya kutafiti kutengeneza gharama za kuanzisha Balozi, uanzishwe wapi, watu wangapi wapelekwe, lakini mwisho kabisa ni lazima tuwe tumejiandaa kwamba tuna pesa ya kutosha na imewekwa kwenye bajeti ndipo hapo Ubalozi unaweza ukafunguliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa pia anajua kwamba tuna Balozi nyingine sita ambazo zimefunguliwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ambazo bado tunataka tuhakikishe kwamba tumekamilisha mambo yote yanayohusiana na staffing, gharama za nyumba na uendeshaji. Hatuwezi tu tukafungua kwa sababu tumesema, tukishakuwa tumejiandaa tutaweza kusema ni lini. Hata hivyo, utaratibu wa kuangalia aina ya watu watakaopelekwa na gharama za uendeshaji zimekwishakamilika, tunasubiria kwanza zile ambazo zimepangwa zikamilike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la pili tunatambua kwamba mahusiano baina ya Tanzania na Cuba ni mazuri na Zanzibar kama yeye anavyojua kwamba ni sehemu pia ya Tanzania. Nataka kumhakikishia kwamba wale wanafunzi ambao wanasoma kule Cuba kwa kozi za muda mrefu na mfupi watakuwa wanaendelea kusimamiwa na Balozi yetu ya Canada maana ndiyo wanaosimamia wanafunzi au wafanyakazi wote wa Tanzania walioko Cuba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimwambie mahusiano hayo hayako mazuri tu kwa upande wa Zanzibar ni mazuri kwa Tanzania nzima. Kwa kumpa tu taarifa mwaka jana Manesi 16 pamoja na Madaktari kwa mkataba wa miaka miwili wa kutoka Cuba watakuwa wanafanya kazi katika Hospitali yetu ya Muhimbili na Waziri wa Afya yuko hapa anaweza kukiri hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna mahusiano mazuri kwenye suala la elimu, kuna Madaktari na Wataalam wa afya ambao wanatoa mihadhara katika vyuo vyetu vikuu. Kwa hiyo, nataka kumhakikishia kwamba wale wanafunzi ambao wamepelekwa kutoka Zanzibar wataendelea kuhudumiwa na Balozi yetu ya Canada.
MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwakatika jibu la msingi Mheshimiwa Naibu Waziri alisema kwamba hii Bodi ya Baraza la Mitihani ni suala la Muungano katika Katiba imo katika nyongeza. Sasa nataka tu kumuuliza, hivi kuna wawakilishi wangapi kutoka Zanzibar katika Bodi ya Baraza la Mitihani na kwamba kama tunaona idadi hiyo inakidhi matakwa na haja ya wanafunzi kutoka Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyofahamu ni kwamba shughuli zote zinazofanyika zinazohusu masuala ya Muungano yanashirikishwa kikamilifu kwa pande zote mbili kwa idadi ni ngapi, kwa mujibu wa taratibu za Kibunge nadhani sitaweza kumpa hiyo namba kwa sasa hivi. Ahsante.
MHE. SAADA SALUM MKUYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nakubaliana sana na Mheshimiwa Naibu Waziri alipozungumza hasa hapo alipomalizia kwamba baadhi yetu tunatumia tu huu mwanya wa kuwepo kwa changamoto za Muungano kupitisha masuala ambayo kweli siyo changamoto za Muungano. Hili linatokea kwa sababu ya uelewa mdogo wa Muungano wetu na historia za nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini hasa Serikali itaona umuhimu wa kuingiza mtaala maalum wa Muungano kama vile iipoona umuhimu wa kuingiza masuala ya mazingira, reproductive health na kadhalika ili kuepuka hizi dhana za kutokuelewa hasa kiini na msingi wa Muungano wetu? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze tena Naibu Waziri kwa majibu mazuri kwa maswali yaliyopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mtaala wetu wa sasa kuna somo la Uraia ambalo linagusa historia ya nchi yetu na masuala ya siasa ya nchi yetu. kwa hiyo, wazo la Mheshimiwa Mbunge la kuongeza na kupandisha hadhi na kuupa umuhimu Muungano wetu katika somo la Uraia tumelichukua na tutaongea na wenzetu wa Wizara ya Elimu tuone ni kwa namna gani tunapandisha na tunaongeza uzito wa masuala ya Muungano katika somo la Uraia. (Makofi)
MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake, hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa utaratibu huu uliopo hivi sasa na tendency tunayoiona, je, Serikali haioni inanyima fursa uwakilishi wa wanawake hapa Bungeni kutokana na ongezeko la Viti hususani kwa upande wa Chama cha Mapinduzi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa sababu mwongozo huu unatokana na sheria, sasa ni lini Serikali italeta mabadiliko haya ya sheria hapa Bungeni ili tuweze kurekebisha tuone kwamba idadi ya wanawake inaongezeka hapa Bungeni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Saada Mkuya, kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya awali, msingi wa mgawanyo wa Viti Maalum unatokana na Ibara ya 78(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kama ilivyo ada, pamekuwepo na marekebisho mbalimbali ya Katiba kutokana na mahitaji. Inapotokea haja ya kufanyika hivyo basi Serikali tutaona umuhimu wa kuona jambo hili kwa uzuri zaidi ili iweze kubadilishwa kuendana na mazingira ya wakati husika, lakini kwa hivi sasa msingi unabaki kuwa Ibara ya 78(1) ya Katiba ndiyo ambayo inatuongoza.
MHE. SAADA SALUM MKUYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana kwa kuniona na mimi nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri na ya ufasaha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba kwa upande wa Zanzibar majimbo mengi tulijikusanya na tukawa tumewalipia bima ya afya watu mbalimbali, lakini baadae Mfuko huu wa NHIF ukasitisha kile kifurushi. Na sasa hivi nadhani karibu miaka miwili tunaambiwa assessment inaendelea ili kuona kwamba tunapata alternative ya ile bima ya afya ambayo ilikuwa imesitishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mpaka lini au lini sasa hii assessment itakamilika ili tuje na mpango mpya tuweze kuwahudumia wananchi wetu katika majimbo yetu ambao wanahitaji hii huduma ya afya kupitia Bima ya Afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kulikuwa kuna utaratibu wa kutoa bima ya afya kupitia vikundi, lakini kusudio lile naomba labda nianze kutoa maelezo ya awali ili Waheshimiwa Wabunge nanyi mnielewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi tunapokuwa tunazungumzia suala la bima tunwataka watu wanaojiunga ni wale ambao hawana magonjwa pale wanapokuwa wanaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sawasawa unataka kukata bima wakati gari lako limepata ajali. Sasa baadhi ya watu kilichotokea ni kwamba kuna vikundi vilikuwa vinajikusanya ambavyo tayari wana magonjwa makubwa na ya muda mrefu wanatengeneza vikundi, wanalipa hela ndogo shilingi 70,000 halafu wanaenda sasa hospitalini wanapata huduma kubwa, kwa utaratibu huo tungeweza tukaufilisi mfuko.
Kwa hiyo, baada ya kubaini kwamba, kulikuwa na changamoto hiyo, tulisitisha hilo fao, ili kuweza kupitia taratibu nzuri za kutengeneza vile vikundi na vigezo vya kuzingatia kwa hiyo, bado hiyo kazi inaendelea kufanyika na tutakapokamilisha tutautangaza upya utaratibu mpya wa kujiunga na vikundi hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suluhu ya kudumu, sisi kama Serikali tuko katika hatua ya mwisho ya kuandaa muswada na utakapokamilika ndani ya Serikali tutauleta hapa Bungeni na mimi niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge mtuunge mkono katika muswada huo.
MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu yake ya msingi fursa ambazo amezionesha ni pamoja na mikopo lakini tunajua kiukweli wale ombaomba hawana asset yoyote na taasisi zetu za kifedha mara nyingi zinahitaji at least uwe na asset au uwe na jambo linguine.
Sasa Serikali haioni umuhimu wa kupanga mkakati maalum specifically kwa ajili ya hawa ombaomba ili waondokane na hii hali waliyokuwanayo rather than ku- generalise wapate mikopo ambayo sio rahisi kiukweli?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama alivyosema kwamba taasisi nyingi za kifedha zinadai collateral ili watu wapate mikopo, lakini kwenye utaratibu wetu wa Serikali kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ambayo tumeipitisha mwaka huu hapa Bungeni ni kwamba, mtu atapata mkopo kutokana na shughuli anayofanya. Ndiyo maana nimetoa wito kwamba watumie fursa ya ardhi yenye rutuba kuzalisha mali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama hawa ombaomba watapata elimu nzuri kupitia halmashauri zao, Maafisa Maendeleo ya Jamii watoe elimu hiyo, wakajiunga kwenye vikundi vya uzalishaji mali wanayo fursa ya kupata mikopo kupitia halmashauri, ile 10% ambapo 4% inakwenda kwa vijana 4% inaenda kwa wanawake na 2% inaenda kwa walemavu. Kwa hiyo, hiyo ni fursa mojawapo ambayo ni nzuri ya kupata mkopo bila kuwa na collateral au kuwa na asset yoyote. Jambo la muhimu sana ni Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii watumike kuelimisha wananchi ili watumie fursa zilizopo.
MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu. Kabla sijauliza maswali yangu mawili ya nyongeza, nilikuwa nimepata confusion kwa sababu Mheshimiwa Waziri anasema kwamba, mwongozo umetekelezwa kwa asilimia 82.7 kwa 18 ambayo inawezekana ikawa ni jambo nzuri sana. Vile vile anasema kuna changamoto, kwa hivyo hizi statement zenyewe zina-contradict.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, huu mchanganuo wa asilimia 82.7 kwa Tanzania Bara na asilimia 18.3 umetumia vigezo gani? Maana yake huu mchanganuo yaani success, hii rate umetumia vigezo gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, as far as I understand kwamba, ni karibuni tu hivi kumetolewa kumbushio kutoka Wizara inashughulika na Utumishi wa Umma kwamba baadhi ya Taasisi hazitekelezi agizo hilo. Kutokana na miongozo hii kutolewa bila kuwa na utaratibu wa kisheria, je, ni lini Serikali itakuwa inaandaa miongozo hii ikiambatana na utaratibu wa kisheria ili tuone kwamba hizi taasisi pamoja na mambo mengine zinatekeleza hii miongozo kwa mujibu wa sheria?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, NA MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Saada Mkuya Salum ambaye amekuwa akifuatilia sana masuala ya Muungano na hasa changamoto za Muungano. Ni Mheshimiwa Mbunge ambaye kwa akinamama tunasema ni mama wa nguvu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, majibu tuliyoyatoa hayana confusion, ni majibu ambayo yamenyooka kwa sababu mwongozo ule unazungumzia asilimia 21 Zanzibar na asilimia 79 Tanzania Bara. Sasa kilichokuja kutekelezwa ambapo kwa Zanzibar ni asilimia 18.3 halafu Bara ni asilimia 82.7 ambapo pengine yeye anadhani ule ndiyo mkanganyiko, tumetoa sababu Mheshimiwa Saada Mkuya, kwamba tumepata ugumu sana wa kujua Wazanzibar ambao wanaajiriwa kwenye Taasisi za Muungano kwa sababu wengi wanatumia anuani za Bara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, miaka miwili tulikuwa na zoezi la kuhakiki watumishi hewa na vyeti hewa. Kwa hiyo, Serikali haikuweza kuajiri, ndiyo maana hizi asilimia hazikwenda juu sana. Hata hivyo, nimpe mfano mmoja; Wizara ya Mambo ya Nje, katika ajira za mwaka wa fedha 2014/2015, waliajiri watumishi 28, lakini kati ya 28 watumishi saba (7) wote ni Wazanzibar na ukipiga asilimia ni asilimia 25 ambayo iko juu zaidi asilimia 21 kwenye mwongozo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili anasema baadhi ya Taasisi hazizingatii, hazitekelezi mwongozo huo na kwamba na ili utekelezaji uwe na nguvu kwa nini kusiwe na sheria. Wazo lake ni nzuri kwamba, pengine mwongozo unaweza usitekelezeke, lije suala la sheria. Nimhakikishie kama ziko taarifa ambazo Mheshimiwa Mbunge anaweza akatuletea ofisini kwamba Taasisi zifuatazo hazitekelezi bado Serikali tuna uwezo wa kuzitaka zitekeleze hata kama Sheria haijatungwa. Kwa hiyo mawazo yake ni mazuri. (Makofi)
MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante lakini nachuka fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake ambayo yametoa mchanganuo mzuri na unaleta matumaini na tunatarajia kwamba hizo changamoto zitatatuka karibuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwongozo huo haufuatwi katika mashirika ya Muungano, je, Serikali lini itatoa utaratibu huo wa mwongozo katika mashirika ya Muungano kuona na yenyewe yanafuata utaratibu huu katika ajira?

Swali langu la pili ni kwamba utaratibu huu umekuwa ukifuatwa kama ambavyo umeelezea, lakini bado umekumbwa na changamoto, kuna mfumo gani ambao unafuatwa ili kufanya assessment kuona kwamba huu utaratibu liowekwa unafuatwa katika taasisi zote za Muungano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Saada Mkuya, lakini pia na mimi nichukue fursa ya kumpongeza kwamba mara nyingi tumekuwa tukishirikiana kwa namna ambavyo tunaweza kutatua changamoto za Muungano, lakini kama nimeeleza kwenye majibu yangu ya swali la msingi kwamba tayari mashirika haya tumeyapa mwongozo na suala kubwa sasa ni ufuatiliaji kwa namna gani wanatekeleza mwongozo ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia suala la pili juu ya assessment, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira tunawajibika moja kwa moja kupata taarifa kutoka kwa wenzetu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu wa kufuatilia assessment huu tumeuweka vizuri na tumeweka bayana, tutakavyo kutana nitamuelekeza vizuri namna ambavyo tumetekeleza. Ahsante.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongezee katika majibu mazuri aliyotoa Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni jambo muhimu sana ambalo linatusaidia kuimarisha Muungano wetu. Lazima nikiri kwamba katika maeneo ambayo hatufanyi vizuri ni hili la uwiano wa watumishi katika Taasis za Muungano na Wizara za Muungano, lazima tukiri ukweli huo. Bahati nzuri maamuzi yalishatoka na sisi kama Ofisi ya Makamu wa Rais na kama Serikali katika kuhakiksha kwamba maamuzi hayo yanatekelezwa kwa haraka tumeshirikiana na wenzetu wa Ofisi ya Rais, Utumishi kuhakikisha kwamba wanafungua Ofisi Zanzibar na kuajiri na kutangaza na kufanya interviews kwa Zanzibar vilevile.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutampa jedwari la kuonesha kila taasisi ya Muungano iwe Benki Kuu iwe TCRA na watu ilionao, Wazanzibari na Wabara ili kuwe na uwazi na tusaidiane katika usukumaji wa jambo hili, hilo la pili.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa rai vilevile kwa vijana wa Zanzibar ambao wanaomba nafasi katika taasisi za Muungano kuandika address sahihi, kwa sababu msingi wa taarifa tunazopata ni anuani kwenye maombi. Kwa hiyo, wengine ni Wazanzibar lakini wanaandika anuani za Bara; kwa hiyo, hatupati taarifa sahihi kuhusu hasa idadi ya Wazanzibar na watu wa Bara katika nafasi hizi. Kwa hiyo, wito wangu ni kwamba ukiandika anuani sahihi inasaidia kupata takwimu sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingi Wazanzibar wapo wengi zaidi kuliko inavyoonekana kutokana kwamba walioomba kazi hiyo kutokea Bara na waliandika anwani za Bara.
MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mheshimiwa Waziri ameelezea jinsi gani vikosi vyetu vitashiriki katika kuhakikisha kwamba amani inakuwepo wakati wa uchaguzi. Changamoto inayoonekana ni kwamba kunakuwa na uchache wa muda wa kutoa elimu ya uchaguzi (voters education). Je, ni kwa kiasi gani wamejitayarisha kushirikiana na Tume ya Uchaguzi kuona kwamba hiyo voters education inatolewa kipindi kirefu zaidi kabla ya uchaguzi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Saada Mkuya Salum, Mbunge Welezo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie kwamba wakati wowote tutakuwa tayari kushirikiana na Tume za Uchaguzi pale ambapo watapanga ratiba zao vizuri. Naamini kabisa Tume hizi zimekuwa zikijifunza kulingana na changamoto zilizopita. Kwa hiyo, kama kulikuwa na mapungufu ya muda watarekebisha utaratibu huo na sisi tutakuwa tayari kushirikiana nao pale ambapo watapanga ratiba hizo.
MHE. DKT. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza na nashukuru sana majibu ya Serikali kwa swali langu hilo.

Mheshimiwa Spika, biashara ni nyenzo muhimu sana katika uchumi wa mtu binafsi, lakini vilevile uchumi wa Taifa kwa ujumla. Sasa ucheleweshaji wa kutatua changamoto kama hizi ambazo zinapitia katika mfumo ambapo kama Waziri alivyoeleza wa vikao na taratibu, unaathiri moja kwa moja maisha ya watu na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Je, ni lini Serikali itaangalia utaratibu mahsusi wa kutatua changamoto hizi za kibiashara hususan kwa biashara ambazo zinatoka Zanzibar zinakuja katika soko la Tanzania Bara kwa sababu hiyo ndio changamoto kubwa ambayo inajitokeza na sio otherwise? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili Zanzibar kwa sasa kuna Taasisi ya Viwango (Zanzibar Bureau of Standards - ZBS), lakini mara nyingi bidhaa ambazo zinapimwa na ZBS zikiingia katika soko la Tanzania Bara, wafanyabiashara wanalazimika biashara zile kupimwa tena na TBS.

Je, mfumo wa uthibitishaji wa bidhaa wa ZBS hauaminiki au hauko sambamba na mfumo huu wa TBS mpaka inafanya bidhaa ambazo zinakuja zilizopimwa na ZBS zinapimwa tena na TBS?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Saada Mkuya Salum, Mbunge wa Welezo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusiana ni lini kutakuwa na utaratibu au mfumo maalum. Kwanza niseme tu kwamba kama ambavyo nilieleza hapo awali mfumo upo kulingana na ngazi zetu za kimashirikiano na hasa kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo inashughulikia pia masuala ya Muungano. Kwa bahati mbaya katika maswali yake hajasema hasa bidhaa zipi, amesema kwa ujumla wake, ingekuwa ni bidhaa ipi pengine ingenisaidia zaidi kujua ni kitu gani hasa kishughulikiwe.

Mheshimiwa Spika, lakini niseme tu kwamba kama ambavyo hata juzi tumeshuhudia ni kwamba changamoto muhimu au jambo muhimu linalotakiwa wakati tunapohitaji kujadili juu ya changamoto zinazowakabili wafanyabiashara hao, ni vyema kuwa na umakini, lakini pia kuwa na maelezo ya kina yanayozungumzia hilo suala baada ya kulifanyia utafiti na tafakari ya kutosha. Kwa mfano katika kipindi cha nyuma nimejibu zaidi ya maswali manne yakizungumzia suala la sukari kuingia Tanzania Bara, lakini hivi karibuni tumeshuhudia kuona kwamba kumbe sukari hata inayozalishwa katika Kiwanda cha Mahonda ilikuwa hata haitoshelezi kwa upande wa Zanzibar endapo hakuna sukari nyingine itakayoagizwa kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni mambo ambayo wote inabidi tuyaangalie kwa pamoja. Vilevile Mheshimiwa Makamu wa Rais juzi amesisitiza juu ya umuhimu wa sisi kufanya kazi kwa pamoja kwa mashirikiano na bila kubaguana na hiyo ndio iwe spirit yetu katika kujenga umoja wetu na mashirikiano.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili TBS na ZBS, niseme tu kwamba kupitia hii blueprint katika mambo ambayo yataangaliwa ni pamoja na taasisi ambazo zimekuwa zikifanya kazi kwa pamoja za Kimuungano na hata za Kimataifa ili kuwapunguzia vikwazo wafanyabiashara wetu.

Kwa hiyo, naamini na hilo pia litashughulikiwa kuweza kuona ni jinsi gani mamlaka zetu zote mbili zinajengewa uwezo na kuwa na uelewa wa pamoja ili bidhaa ikikaguliwa upande mmoja isiwe lazima kukaguliwa upande wa pili.
MHE. SAADA SALUM MKUYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa fursa nikauliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Waziri tunajua ama ni ukweli kwamba mazingira hasa kwenye upande wa carbon and mission ni nchi ambazo zilizoendelea ndio zinazo- emit hii carbon na athari kubwa inatokea kwa nchi ambazo zinaendelea ikiwemo Tanzania. Lakini nchi hizo ambazo zinaharibu sana mazingira haya zimekuwa zinasita kutoa finance kwenye climate change. Labda Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipangaje kuhakikisha kwamba inapambana katika kukabiliana na matatizo haya ya climate change ikiwemo mitigation adaption? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri ni kweli kuna baadhi ya nchi kubwa duniani ambazo zimejitoa kwenye mkataba huu wa tabianchi kutokana na maslahi yao binafsi, lakini vilevile nchi zilizobakia zikiongozwa na Ufaransa na Qatar na nchi zingine wameanzisha mfuko wa one bilioni 100 Us dollars ambazo zitatumika kwa nchi zote ambazo zitahitaji pesa hizi kuboresha mazingira katika nchi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania hatuko nyuma tulishaanza mkakati wa kuziomba pesa hizi na program mbalimbali za kuhakikisha nchi yetu inafaidika na pesa hizi na kulinda mazingira. Programu ya kwanza ni kuhakikisha tunapanda miti Mlima Kilimanjaro zaidi ya miti bilioni moja ili kulinda barafu ambayo ipo katika nchi yetu. (Makofi)
MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na kazi nzuri ambazo zinafanywa na vikosi vyetu hivi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, kuna maeneo ambako kuna Kambi za Majeshi na kumekuwa kuna uwekezaji ambao unaendelea, hususan kumbi za disco, pamoja na mambo mengine ambayo yanafanana na hayo ambayo mara nyingine zinaleta athari za kiutamaduni na maadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inasemaje kuhusiana na kambi hizo ambazo zinakuwa zinapigwa disko katika maeneo ya wananchi na hivyo kuathiri utamaduni pamoja na maadili ya maeneo yanayohusika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya kumbi za starehe katika nchi yetu yapo kwa mujibu wa taratibu tulizojiwekea na siyo katika makambi ya Jeshi tu, ni maeneo mbalimbali. Hata kumbi ambazo zipo katika maeneo ya Kambi za Jeshi kwa ajili ya starehe zinatakiwa zifuate utaratibu ule ule ambao tumejiwekea wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sidhani kama ni sahihi kuonyesha kidole katika maeneo ya kambi ya Jeshi peke yake, imani yangu ni kwamba ukizingatia maadili na misingi ya Jeshi letu la Wananchi wa Tanzania, nadhani itakuwa ni sehemu ya mwisho kuonyeshwa kidole katika ukiukwaji wa sheria hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kama ana kesi mahususi ambayo anadhani inahitaji kufuatiliwa, namwomba Mheshimiwa Saada Mkuya atupatie taarifa ya eneo la kambi ambalo anazungumza ili tufuatilie na kuona hatua za kuchukua.
MHE. SAADA MKUYA SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naishukuru Serikali, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri kabisa hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, inaonekana kwamba utaratibu huu wa utoaji wa elimu hauko effective na ndiyo maana haya matukio yameendelea kwa kiasi hicho ambacho Mheshimiwa Waziri amekitaja.

Je, Serikali haioni kama kuna umuhimu wa kubadilisha utaratibu wa utoaji wa elimu kwa wananchi ili wasiendelee kuchukua sheria katika mikono yao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, inawezekana kabisa yanatokea haya mauaji kwa sababu wananchi wenyewe wanakuwa wanakosa imani na jeshi la polisi na kwamba pengine wale watuhumiwa wakipelekwa katika vituo vyetu vya polisi, kesho yake wanawaona wako mitaani. Kwa hivyo, Serikali ina mkakati gani wa kuliondoa hili miongoni mwa jamii ili kuona kwamba haki inatendeka kwa kila ambaye amefanya kosa na wale ambao hawajafanya makosa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Sasa nijibu maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo; kuhusiana na utaratibu ambao tunatumia nadhani siyo utaratibu mbaya, hata hivyo tunachukua mapendekezo yake kama ni changamoto ili tuangalie jinsi gani tunaweza tukfikia zaidi wananchi waweze kupata taarifa. Hata hivyo nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi kwa kiasi kikubwa wana imani na jeshi lao la polisi na kutokana na amani na utulivu na upungufu wa takwimu za uhalifu nchini ambao unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikiri kwamba kwa wale wananchi ambao wanakosa imani na baadhi ya askari polisi wachache ambao pengine wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kinyume na maadili, niwahakikishie wananchi kwamba wakati wote tunavyobaini askari wa aina hiyo tumekuwa tukichukua hatua stahiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo bahati njema ni kwamba askari hao ni wachache, walio wengi wanafanya kazi zao vizuri kwa uadilifu na ndiyo maana nchi yetu inaendelea kuwa salama mpaka sasa hivi.