Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mussa Bakari Mbarouk (21 total)

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, jina langu naitwa Mussa Mbarouk, Mbunge wa Tanga Mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali ilianzisha mpango wa maji safi na salama vijijini katika mradi uliofadhiliwa na World Bank na mradi ule umekwama. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha katika Halmashauri ya Jiji la Tanga ili kuondoa kero ya maji katika Kata za Mabokweni, Chongoleani, Kilale na Marungu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali ilianzisha mradi wa vijiji 10 kupitia progamu ya Benki ya Dunia na mradi huo ungali unaendelea. Katika mradi huo tulikuwa na miradi 1,855 kama nilivyotoa taarifa ya awali kwamba katika miradi hiyo miradi 1,143 imekamilika na miradi 454 inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na tatizo la fedha ndiyo lililofanya hii miradi isikamilike kwa wakati lakini nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika eneo lako la Tanga kufuatia juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukusanya fedha, fedha zimeanza kutoka na nikupe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba wiki iliyopita tumeletewa shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kuendelea kulipa miradi hiyo mingi ambayo ilikuwa imesimama na siyo Tanga tu, ni karibu Mikoa yote miradi ilikuwa imesimama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nikuhakikishie kwamba Serikali inatoa fedha kuhakikisha miradi hiyo inakamilika ili katika progamu ya pili tuanze kuweka tena miradi mingine. (Makofi)
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mheshimiwa Naibu Spika, takribani mwezi sasa wakazi wa Jiji la Tanga wanapata maji kupitia mamlaka ya maji ambayo siyo safi na salama.
Je, Serikali ina taarifa kwamba wakazi wa Tanga wanaweza kupata maradhi ya milipuko kutokana na kutokunywa maji ambayo siyo safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mamlaka ambazo zinaongoza kutoa huduma ya maji iliyo bora ni pamoja na Mamlaka ya Maji ya Tanga na Mamlaka ya Maji ya Moshi. Sasa kama hilo limejitokeza basi Mheshimiwa Mbunge nikuahidi kwamba tutalifuatilia kuona ni nini kimejitokeza katika hilo. Kwa taarifa tulizonazo ni kwamba mamlaka zinazoongoza ni pamoja na Mamlaka ya Maji ya Moshi na Tanga. Kwa hiyo, nikuahidi kwamba tutalifuatilia kuona ni eneo gani ambalo lilipata hiyo shida ya maji kutokuwa salama.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na bandari iliyokuwepo Serikali ilipata uwezekezaji wa ujenzi wa bandari mpya ya Mwambani na kama sikosei ilikuwa ni Serikali ya Uganda na Serikali ya Kuwait. Swali la kwanza, kwa kuwa feasibility study pia ilikwishafanyika, je, ujenzi huu wa bandari mpya wa Mwambani nao umefikia hatua gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, zipo systems za
FIFO na LIFO method, First In First Out na Last In First Out, kwa nini naambiwa kwamba itaanza kujengwa bandari ya Bagamoyo katika siku za karibuni isianze kujengwa ile bandari ya Tanga? Nataka kujua hilo.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari ya Mwambani kama ilivyo bandari ya Bagamoyo tulikuwa tunatarajia ijengwe kwa njia ya PPP. Unapokwenda kwenye masuala ya PPP inategemea na yule aliyeonesha nia ya kujenga. Wapo watu wameonesha nia Bagamoyo na Tanga pia lakini tatizo lililotokea kwa Mwambani ni kwamba upembuzi yakinifu na usanifu wa kina uliofanyika ulionesha kwamba bandari ile haina faida. Sababu yake hawakufikiria mizigo ambayo italetwa na reli inatokea Musoma hadi Tanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa tumeanza kazi upya ya kuipitia hiyo taarifa ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili waunganishe na uwekezaji mpya uliojitokeza pale Tanga ili hatimaye bandari ile ya Mwambani ionekane ina faida kuijenga. Kwa hiyo, ni kweli kuna huo utaratibu wa FIFO na kadhalika lakini hatimaye kwa sababu unatumia PPP ni lazima ufuate wale wateja wako wanaotaka kuwekeza pale unaendana nao vipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa swali la pili, nalo nadhani nimelijibu wakati najibu hili kwa kirefu kwa sababu hoja ni ileile. Nakushuruku sana.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza niseme nashukuru kwa Serikali kutenga takribani shilingi bilioni nne kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Pangani. Je, ni lini kazi rasmi ya ujenzi wa barabara hiyo itaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba kumpongeza sana huyu Mheshimiwa Mbarouk kwa sababu anashirikiana vizuri na Wabunge wenzake wa Tanga katika kuhakikisha maendeleo katika maeneo yao yanafanikiwa bila kujali itikadi. Nikupongeze sana kwa sababu hatimaye ni wananchi wanaotuleta humu ndani na hatimaye ni wananchi watakaotuondoa tusipoangalia interest za wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikuhakikishie kama ambavyo nilijibu kwenye swali la msingi la Mheshimiwa Aweso ni kwamba mwaka huu wa fedha tumetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuanza maandalizi ya kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami. Ujenzi wa barabara una hatua, hii ndio hatua ya kwanza tunaianza mwaka huu wa fedha.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na Serikali kuondoa baadhi ya kodi katika sekta ya uvuvi na vilevile kujenga Soko la Kisasa la Samaki Pangani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuuliza Mheshimiwa Waziri, je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo cha Uvuvi katika Mkoa wa Tanga kama kile kilichopo Mwanza?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa chuo anachosema, Serikali itafikiria ombi lake kulingana na uwezo wa kibajeti lakini kwa sasa tunaendelea kuimarisha vyuo vilivyopo vya VETA ili kuweza kuendelea kutoa huduma hata wakati huko mbele tunafikiria kujenga vyuo vingine kadri uwezo utakavyoruhusu.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jiji letu la Tanga kuna upimaji unaoendelea katika eneo la Amboni kwa ajili ya kuongeza Kiwanda cha Saruji cha Sinoma cha Wachina. Katika maeneo yale kuna tatizo kubwa la kwamba, wananchi wenye mashamba yao wanaambiwa watalipwa fidia ya mazao ya muda mrefu tu na mazao ya muda mfupi kama mahindi, mihogo na mengineyo hayatalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali inalifahamu hilo na utaratibu huu ni utaratibu wa sheria gani inayotumika kulipa mazao ya muda mrefu, na pia pana maji koto au sulphur water pale katika eneo la Amboni ambayo ni kama tunu kwa mambo ya utalii.
Je, Serikali inafanya juhudi gani kuhakikisha ile sulphur bath itaendelea kuwepo ambayo iliendelezwa na Galanos lakini pia na wananchi wenye mzao mafupi nao watalipwa fidia yao?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili ni la Tanga. Walioamua kufanya haya ni Halmashauri ya Jiji la Tanga kwenye shamba hili. ningemuomba Mheshimiwa Mbunge kwa sababu kazi hii hata tathmini ya pale imesimamiwa na kufanywa na Wathamini waliopo kwenye Jiji la Tanga na upitishaji wa viwango huu ulikuwa shirikishi na maelekezo haya yametolewa pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba, unajua ni rahisi kufikiri kwamba Waziri akiwa hapa Dodoma anaweza akajua na akalitolea ufafanuzi kila jambo lakini jambo hili ni shirikishi limefanywa na Watendaji wenye Mamlaka ya Kisheria ya kutenda wa Jiji la Tanga kwahiyo kama halikufanyika vizuri, wale wananchi wanajua Bungeni hapa mwaka huu mmetunga Sheria ya Bodi ya Mfuko wa Fidia. Ninawaomba waisome, Waheshimiwa Wabunge muwasidie wananchi hawa wakate rufaa kwenye Bodi ya Mfuko wa Fidia ili iweze kufikiaria vinginevyo, lakini mimi kama aziri hapa siwezi kusimama nikatengua uamuzi halali uliofanywa na Halmashauri ya Jiji la Tanga. Hivyo, naomba wafuate hiyo sheria. (Makofi)
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kabla sijauliza swali langu la nyongeza kwanza niipongeze timu yangu ya Coastal Union ya Tanga ambayo imepanda daraja mwaka huu, lakini pia niwapongeze timu ya African Sports kwa kubakia katika ligi daraja la kwanza. Maswali yangu ya nyongeza ni kama ifuatavyo:- (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia ukarabati unaofanywa na ambao ulishawahi kufanywa uwanja wa ndege wa Tanga, katika eneo la Magomeni kuna nyumba zaidi ya 228 ambazo zilifanyiwa evaluation mwaka 2008 lakini mpaka leo hawajalipwa. Lakini pia kuna nyumba nyingine 802 ambazo nazo zinahitajiwa kuvunjwa ili kupanua uwanja ule wa ndege.
Sasa je, nataka kujua, Serikali ni lini itawalipa Wananchi wale fidia ili kuweza kufanya ukarabati huu mkubwa unaotakiwa kufanywa kufuatia ufadhili wa Benki ya Dunia?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili, kwa kuwa Jiji la Tanga sasa hivi route za ndege zimeongezeka na kuna shughuli nyingi za mipango ya kiuchumi amabzo zinafanyika. Je, ni lini Bombadier itaanza kwenda Tanga? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, nyumba zote ambazo zilifanyiwa evaluation kwa ajili ya malipo ya fidia, shughuli za fidia zinafanyika na evaluation imekwishafanyika na tunafahamu idadi ya pesa zinazodaiwa lakini tuko kwemnye uhakiki kupitia Wizara ya Fedha ya kulipa fidia hiyo, kwa hiyo, wakati Wizara ya Fedha itakapomaliza kupitia fidia hiyo, malipo yatafanyika kwa watu ambao wataathirika na upanuzi wa uwanja wa ndege huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, Bombadier itaanza lini safari za kwenda Tanga, kiutaratibu Bombadier wanafanya biashara pamoja na kutoa huduma kama mashirika mengine ya ndege kwa hiyo, hilo tutalichukua, tutawapelekea ATCL basi waje wafanye tathmini ya masuala ya soko, usalama na mambo mengine ambayo yanahusika kabla ya kupeleka ndege kufanya shughuli za safari za uwanja huo wa Tanga, ahsante.
MHE. BAKARI M. MUSSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Halmashauri ya Jiji la Tanga ni moja ya Halmashauri zilizobahatika kupata mradi wa vijiji 10 kila Halmashauri. Upande wa Kusini mradi wa maji umekamilika lakini upande wa Kaskazini hadi leo mradi haujakamilika kwa kuwa mzabuni anadai.
Je, ni lini Serikali itamlipa mzabuni ili akamilishe mradi wa maji na Wananchi waweze kupata maji safi na salama kwa vijiji vya Kiruku, Kibafuta, Bwagamoyo na Chongoleani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweka utaratibu Serikali inatoa fedha baada ya kuleta certificate na wewe kama Mbunge naomba usaidiane kusimamia huo mradi ili mkandarasi azalishe. Akileta certificate Mheshimiwa Mbunge dakika yoyote fedha tunayo na fedha kutoka Mfuko wa Maji na kwa bahati nzuri flow yake ni nzuri, akileta certificate tunalipa ili akamilishe huo mradi.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nishukuru kwa mradi wa maji wa vijiji kumi katika Jimbo langu, nimefanikiwa vijiji vitano na vitano nimeambiwa Mkandarasi yule apeleke certificate. Hata hivyo, kuna vile vijiji ambavyo havikupitiwa na mradi ule. Kwa mfano, Kijiji cha Pande Muheza, Mondura na Bagamoyo. Serikali ina mpango gani wa kuchimba visima virefu katika vile vijiji ambavyo havikupitiwa na mradi ule wa vijiji 10 katika kila Halmashauri?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea na Program ya Maendeleo ya Sekta ya Maji awamu ya pili ili tuhakikishe vijiji vyote ambavyo havikupitiwa tuvikamilishe. Pia tunatenga bajeti kila mwaka kupitia kwenye Halmashauri ya Mheshimiwa Mbunge na tayari tumeshatoa taarifa kwamba Halmashauri iwasiliane na Mamlaka yetu ya uchimbaji wa visima na atupe taarifa anapokwama ili tuweze kusimamia waende haraka vijiji vipate maji.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Tarehe 5 Agosti, 2017 wakati Rais alipokuja kuweka jiwe la msingi la bomba la mafuta pale Chongoleani-Tanga, tarehe 6 alizundua Kiwanda kipya cha Saruji cha Kilimanjaro na alinipa nafasi ya kuongea kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilimtaka Mheshimiwa Rais kupitia Serikali ya Awamu ya Tano kufanya categories za mizigo katika bandari zetu. Nataka kujua, mpango ule umeishia wapi kwa sababu Bandari ya Tanga sasa hivi inafanya kazi chini ya kiwango na hata vifaa vya kisasa vya kuteremsha makontena ya fourty feet hakuna, Waziri ananiambiaje?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, CHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mheshimiwa Mbunge ni mfuatiliaji mzuri nadhani atakuwa shahidi kwamba sasa hivi Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari imekwishaanza marekebisho na matayarisho ya kupanua Bandari ya Tanga. Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba Bandari ile ya Tanga inakwenda sambamba na wingi wa mizigo ambayo inategemewa kuanza kupatikana kupitia ujenzi wa bomba la mafuta la Hoima. Kwa hiyo, namwomba tu Mheshimiwa Mbunge asiwe na mashaka kuna utekelezaji wa upanuzi wa Bandari ya Tanga unaoendelea na wakandarasi wako pale wameshaanza kazi hiyo. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza kwa kuwa kuna tatizo kubwa la watoto kuzaliwa na vichwa vikubwa au vichwa kujaa maji. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kuniambia tatizo hili Serikali inalishughulikia vipi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Serikali inamudu kutoa dawa bure kwa wale watu wenye VVU au watu wenye TB; je, kwa nini isichukue jukumu la kuwatibu watoto hawa ambao wanaozaliwa na vichwa vikubwa ili kuondoa mateso yale ya maradhi ya vichwa vikubwa lakini pia kuondoa simanzi kwa wazazi. Kwa nini Serikali isichukue jukumu la kutoa huduma hiyo bure kwa magonjwa hao? Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, suala la watoto wenye vichwa vikubwa Serikali imechukua hatua gani. Jambo kubwa ambalo Wizara na Serikali inaendelea kulifanya ni kuhakikisha na kuendelea kuhimiza akinamama wajawazito kuhudhuria kliniki kama inavyoshauriwa na Daktari.
Mheshimiwa Spika, hii ni kwa sababu tatizo la watoto wenye vichwa vikubwa pamoja na mgongo wazi tunaweza kulitatua endapo mama ataweza pia kuongezewa dawa kwa mfano tunasema fefo dawa za folic acid ambapo nimeelekeza ziwepo katika vituo vyote vya kutolea huduma na nafurahi kusema kwamba sasa hivi ukienda kwenye zahanati ukienda kwenye kituo cha afya utakuta dawa zote za fefo zinapatikana.
Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Mbunge atusaidie kuhimiza wanawake kuhudhuria kliniki. Kwa mujibu wa takwimu ni asilimia 24 tu ya wanawake Tanzania wajawazito wanahudhuria kliniki ndani ya wiki 12 baada ya kujigundua wajawazito. Kwa hiyo pale ambapo kuna matatizo yanaweza yasionekane.
Mheshimiwa Spika, swali la pili ni suala la tunawasaidia vipi watoto wenye vichwa vikubwa na hili naomba nilibebe na Serikali ipo tayari kugharimia gharama zote za matibabu kwa watoto wote wenye vichwa vikubwa na tumeanza katika Taasisi yetu ya MOI tunafanya upasuaji bila malipo kwa watoto wote wenye vichwa vikubwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nitoe rai kwa wanawake wenzangu wasiwafiche watoto wenye vichwa vikubwa, bali waende katika vituo na hospitali za Serikali ili tuweze kuwasaidia na kuwapa huduma. Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru. (Makofi)
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nashukuru kwa mradi wa vijiji kumi katika kila Halmashauri, mradi wetu wa maji ule unakwenda vizuri.
Je, Serikali ina mpango gani katika vile vijiji ambavyo havitapitiwa na ule mradi wa vijiji kumi wa kuwachimbia visima virefu ili wananchi waweze kupata huduma ya maji safi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii nimjibu Mheshimiwa Mbunge wa Mkoa wangu wa Tanga, kaka yangu Mheshimiwa Mussa kwamba Wizara yetu ya maji kama nilivyoeleza, jukumu letu ni katika kuhakikisha tunawapatia wananchi maji mijini na vijijini na lengo la Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi ni kufikia asilimia 85 katika kuhakikisha vijijini wanapata maji. Sisi kama Wizara ya Maji tuna taasisi mbalimbali kwa maana ya DDCA katika kuhakikisha kwamba tunachimba visima hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mhandisi wa Maji katika Jimbo lake alete andiko, nasi kama Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo katika kuhakikisha tunawasaida wananchi wa Tanga. Ahsante.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ndiyo, maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, risiti ni supporting document katika masuala ya mahesabu. Sasa risiti zetu za EFD machines zina tabia ya kufutika maandishi baada ya muda mfupi, TRA tulipokutana nao katika Kamati yetu ya PAC walikiri kwanza kwamba karatasi wanazotumia ni dhaifu lakini wakasema kwamba watafanya marekebisho ya karatasi hizo ili zisifutike maandishi kwa muda mfupi. Mpaka leo, tarehe 10 Septemba, bado marekebisho hayo hayajafanyika.
Mheshimiwa Spika, nataka kujua sasa TRA tuipe muda gani ili iweze kufanya marekebisho ya karatasi hizi za risiti?
Pili, mwaka 2017 mwanzoni wafanyabiashara wa Mkoa wa Mbeya waligoma baada ya baadhi yao kwenda China na kubaini kwamba mashine zile gharama yake ni sawasawa na shilingi 90,000 ya Kitanzania kwa mujibu wa vyombo vya habari vilivyoripoti wakati ule. Sasa nataka kujua, je, hizi mashine bei yake halisi hasa na taarifa hizi zina ukweli kiasi gani?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza kuhusu karatasi zinazofutika, napenda kuliambia Bunge lako tukufu kwamba Serikali ilishatoa taarifa kwa wafanyabiashara wote kuhusu wapi pa kununua karatasi hizi kwa ajili ya kutoa risiti za mashine za EFD. Zipo karatasi fake, hatukatai, zipo sokoni, lakini tumewaelekeza wafanyabiashara wote waende kununua karatasi hizi kutoka kwa mawakala waliothibitishwa na kuidhinishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania ili kuepuka tatizo hili la karatasi kufutika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, anasema wawape muda mpaka lini, hatuhitaji kupewa muda kwa sababu tatizo hili tulishalishughulikia tayari kama Serikali.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili; nashukuru umenisaidia kumjibu kwamba gharama za mashine ndizo nilizozitaja hapa kulingana na aina ya mashine na aina ya biashara mfanyabiashara anayoifanya. Kwa hiyo, hizo nyingine za kwenye vyombo vya habari, hizo kama Serikali hatuzijui, tunazojua ni hizi nilizozisema, ndiyo kauli na taarifa sahihi kutoka Serikalini. (Makofi)
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nishukuru kwa kilio chetu watu wa Kanda ya Kaskazini…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa sisi watu wa Kanda ya Kaskazini kwa maana ya Mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimajaro, Manyara na Pwani, kilio chetu kusikilizwa na Serikali kwa ujenzi wa Daraja Jipya la Wami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na ujenzi wa daraja jipya, tatizo kubwa limekuwa ni magari aina ya semi kushindwa kupanda milima sababu ya mlima mkali uliopo pale. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuweka magari maalum ya kusaidia kuvuta haya magari ya semi pale ambapo yanashindwa kupanda milima kama ilivyo kwa njia ya Kasumulu Boarder karibu na Malawi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbarouk, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la magari kushindwa kupanda katika milima ni suala ambalo kwa upande wa Serikali tunaendelea kulitazama kwa sababu ya ukuaji wa teknolojia na magari yanayokuja sasa yamekuwa ya kisasa zaidi. Tunaliangalia kwa upana wake kwa sababu kwa records za ajali ambazo zimetokea hivi karibuni tunayo pia mashaka ya kuona namna gani magari haya yanakuja ya kisasa lakini pia madereva ambao wanaendesha magari haya waweze kupata elimu ili waweze kumudu kuyaendesha. Kwa hiyo, mara nyingi unaona technical faults zinazotokea inawezekana kuwa uko uwiano kati ya teknolojia mpya na elimu ambayo wanaipata madereva wetu. Kwa hiyo, tutaendelea kulifuatilia ili tuweze kutatua tatizo hili.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naamini kabisa kwamba Mheshimiwa Waziri kwa maneno yake ya mwisho amekubaliana na mimi kwamba vipo vyombo ambavyo vinatumia bandari bubu na havijafanyiwa usajili na wala havikaguliwi mzigo yake. Sasa kama wanavyosema watu nywele nyeupe ni sababu ya kuwa na busara zaidi. Sasa je, atakubaliana na mimi kwamba sasa Serikali ipo haja ya kuhakikisha hata hivi vyombo vinavyotumia bandari bubu sasa vinakuwa na vyombo/zana za uokoaji kama life jacket na vitu vingine? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la nyongeza la pili ni kwamba, kwa nini kuna bandari bubu ni kwa sababu kuna tozo na kodi za kuudhi kwa watu wanaotoka Zanzibar na maeneo mengine katika bandari zetu ndiyo maana wanatumia bandari bubu. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuondoa hizi kodi kama kwenye TV moja, redio moja au nguo chache kwa watu wanaotoka Zanzibar na Pemba wanaokuja maeneo ya Tanga. Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kama nilivyoeleza mwanzo, umuhimu wa kutumia bandari rasmi tunapata data na kuhakikisha uimara na utayari wa chombo husika kusafirisha abiria kwa usalama zaidi. Kama Serikali, hatuwezi kuruhusu bandari bubu zitumike.
Mheshimiwa Spika, suala la tozo nikijibu swali lake la pili, tozo zinazotozwa kwenye vyombo vya baharini na maziwa makuu siyo kubwa sana kiasi cha kuruhusu watu waendelee kutumia bandari bubu. Namwomba Mheshimiwa Mbunge akubaliane na Serikali kwamba tozo zinazotozwa na affordable kabisa na zinatumika na watu ambao wanataka kufanya kazi kwa uhakika na kwa usalama zaidi kwa ajili ya abiria wao.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika Mradi wa REA III kuna Kitengo kimeanzishwa kinaitwa Peri-urban katika Halmashauri ambazo bado zina maeneo ya vijiji na vitongoji. Je, ni lini kitengo hiki kitaanza kufanya kazi katika Halmashauri zetu kwenye Kata za Kilare, Mzizima, Pongwe, Marungu na Maweni ili tuweze kupata huduma hii ya umeme wa REA III?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimeeleza katika ufafanuzi wangu uliotangulia, ni kweli tunatekeleza miradi miwili kwa mijini. Uko mradi wa urbanisation unaotekelezwa na TANESCO lakini uko mradi wa Peri-urban ambao unatekelezwa kimtindo wa REA, ingawa katika mitaa ya mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mheshimiwa Mbunge kule Tanga Mjini yako maeneo 17 ambayo tumeshaainisha ikiwemo na Izizima pamoja na Majani Mapana. Utekelezaji umeanza kufanyika, ndani ya miezi sita ni matarajio yetu utakamilika na maeneo yake yataanza kupata umeme kwa utaratibu wa Peri-urban.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona, labda niseme tu kwamba Mradi wa Maji wa Vijiji Kumi kila Halmashauri kwa upande wetu wa Tanga mradi ule wa Tongoni, Marungu hauna matatizo, lakini mradi wa upande wa Kaskazini kwa maana ya Chongoleani, Kibafuta na Mabokweni kuna tatizo kidogo. Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba mradi ule umekuwa ukienda kwa kusuasua, je, ni lini Serikali itafanya utaratibu wa kuhakikisha kwamba mradi ule unawapatia maji wananchi wetu wa vijiji vile nilivyovitaja? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwa jukumu la Wizara ya Maji nikuhakikisha wananchi wanapata maji. Mheshimiwa Mbunge amesema Mradi ule wa Chongoleani umekuwa ukienda kwa kusuasua sisi kama Wizara ya Maji hatupo tayari kumuona mkandarasi anafanya kazi kwa kusuasua. Sasa tunamuagiza afanye kazi ili aweze kukamilisha na sisi kama Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo kumpatia fedha kuweza kukamilisha mradi huo. Lakini tukiona anaona hali yake inaendelea kusuasua tutamuondoa tutamuweka mkandarasi ambaye anaweza kukamilisha mradi kwa wakati na wananchi waweze kupata maji.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) wametupa upendeleo Jiji la Tanga kutaka kutujengea Uwanja wa kisasa, lakini cha kushangaza eneo lile halijazungushiwa uzio na watu wameshaanza kulivamia, sasa Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, je, ni lini harakati angalau za kuanza maandalizi na kujenga uzio katika lile eneo ili lisivamiwe utaanza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Jiji la Tanga ni eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya kujenga uwanja changamani wa michezo kwa fedha ambazo tunategemea zitatoka FIFA. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba as soon as fedha hizo zitakuwa zimefika, ujenzi wa uwanja huo utaanza. Kwa hiyo, nimtoe shaka kwamba, ujenzi utaanza mapema sana mara tu fedha zitakapokuwa zimefika. Ahsante.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu baada ya kupiga kelele hatimae kuna kila dalili za kujengwa barabara ya Pangani. Nataka kujua sasa je, wale wananchi ambao walielezwa kwamba wasiendeleze mashamba na majengo waliyoko pembezoni mwa barabara, ni lini wataanza kulipwa fidia zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI UJENZI (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejipanga vizuri kujenga barabara hii ya Tanga - Pangani kama Mheshimiwa Mbunge ulivyosema, lakini ni utaratibu wa Serikali ni kulipa fidia kwanza kabla ya ujenzi kuanza, kwa vile Mkandarasi ameshapatikana niwahakikishie tu wakazi wa maeneo haya ambao mradi utapita watalipwa fidia yao mara moja. (Makofi)
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri lakini pamekuwa na malalamiko katika yale maeneo ambayo yameshapelekewa transfoma za Kilovolt 50. Je, tatizo hili kwa nini linajirudia tena? Kuna baadhi ya maeneo yametajwa kwamba katika transifoma 35, transifoma saba za KV 50 halafu kuna transifoma nyingine nne. Kwa nini tusipeleke zile ambazo ni za kuanzia KV 100?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili katika taarifa hii haikuainisha baadhi ya maeneo ambayo ndiyo hasa yaliyokusudiwa. Kwa mfano, kwenye Kata ya Kirare kina maeneo ya Mapojoni, Mtambuuni, Msakangoto, Kirombere lakini kwenye Kata ya Mzizima kuna maeneo ya Kihongwe, Rubawa, Mleni, kwenye kata ya Kiomoni kuna maeneo ya Pande Muheza, Pande Masaini, Pande Mpirani, Kata ya Marungu kuna Mkembe, Geza Ndani na Geza Barabarani; Pongwe kuna maeneo ya Pikinangwe; na Kata ya Maweni kuna Machembe, Mtakuja na Mwisho wa Shamba: Je, maeneo haya sasa hususan noyo yamo katika huu mradi na lini hasa yataanza kufanyiwa huu uwekezaji wa REA III? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli yako maeneo ambayo tulikuwa tukipeleka transfoma za KV 50 na nyingine 100 na 200 na kuendelea, lakini maeneo tunayopeleka KV 50 inategemea pia na uwekezaji na aina ya wateja. Ziko faida nyingi sana za kupeleka transfoma ndogo ndogo katika baadhi ya maeneo na hasa katika kukabiliana na uharibifu wa mitambo inapotokea dharura. Kunapokuwa na transfoma za 50 nyingi, kwa hiyo, kunapokuwa na dharura ya kuharibika transifoma moja, wateja wengine wanaendelea kupata umeme bila matatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hasara za kuwa na transifoma moja kubwa, ni kwamba ikishaharibika wateja wengi wanakosa umeme, lakini tumelichukua ombi la Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kusambaza transifoma za kila aina kukabiliana na hali hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili katika Jiji la Tanga tunayo maeneo 12 yatakayopelekewa umeme wa Perry Urban ikiwemo kama alivyotaja maeneo yake, lakini yako maeneo ya Chongoleani, Mabwakweni, Majani Mapana na maeneo mengine mpaka 12 na utekelezaji unaanza Julai mwakani na kukamilika mwezi Desemba, 2021. (Makofi)
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini imekuwa ni kawaida ya Serikali kutupa matumaini halafu masuala haya yanachukua muda mrefu sana. Na ni ukweli usiofichika kwamba bandari hizi zinatumika na bidhaa zinazotoka Zanzibar mara nyingi zinapitia katika bandari hizi. Sasa ninataka kujua, je, kwa nini bidhaa hizi zinapopita kutoka Zanzibar zikipita katika bandari hizi zinatozwa ushuru mara ya pili?

Mheshimiwa Spika, lakini swali langu la pili, ni kusema kwamba kwa kutumia bandari hizi, kwa kuzirasimisha, tutakuwa tunaongeza mapato ya Serikali lakini pia ajira kwa watu wetu zitaongezeka lakini vilevile pia ajali zitapungua. Sasa ni lini ujenzi wa hiyo gati aliyosema Mheshimiwa Waziri na kujenga hivi vituo vya forodha utaanza rasmi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, kwenye majibu yangu ya msingi nimeeleza changamoto iliyopo kwenye bandari bubu na sisi kama Serikali tunaitambua changamoto iliyopo.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna majahazi huwa yanachukua bidhaa kutoka upande wa pili wa Jamhuri yetu kuleta upande wa Tanzania Bara, na Serikali kupitia Jeshi la Polisi wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana ya kuhakikisha kwamba biashara hiyo haifanyiki, na sina taarifa za moja kwa moja kwamba huwa wanatozwa ushuru kwa sababu wanatumia bandari bubu ambapo hatuna vituo vyetu vya forodha. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kuzidhibiti hizo bandari bubu na tunaendelea kuzidhibiti kuhakikisha kwamba hazileti bidhaa ambazo si rasmi.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la pili; nimekwishaeleza kwamba kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha tutakuwa tumeshapanga mikakati yote na mwaka ujao wa fedha tutaanza sasa kutengeneza magati kwa sababu ni bajeti kubwa inayotumika katika kutengeneza magati ya kurasimisha hizo bandari bubu.