Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Muhammed Amour Muhammed (12 total)

MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED aliuliza:-
Kumekuwa na unyanyasaji mkubwa unaofanywa na JWTZ wa kuwanyang‟anya wavuvi samaki wao licha ya kwamba watu hao wanajitafutia kipato kupitia bahari kama Watanzania.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa unyanyasaji huo unaofanywa na Jeshi la Wananchi kwa wananchi wake?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa haijawahi kupokea tuhuma yoyote inayohusu unyanyasaji unaofanywa na askari wa JWTZ kwa wavuvi nchini. Aidha, kama tuhuma hizi zina ushahidi ni bora zikafikishwa sehemu husika ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua zinazostahili.
Mheshimiwa Spika, nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba, wanajeshi kama walivyo raia wote wanapaswa kuheshimu sheria za nchi na pale wanapokwenda kinyume huchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria na kanuni za jeshi.
MHE. RICHARD P. MBOGO (K.n.y. MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED) aliuliza:-
Kwa muda mrefu kumekuwepo na tatizo la wanafunzi wanaoingia vyuo vikuu kukosa mikopo na elimu ya juu ni suala la Muungano:-
Je, Serikali ya Muungano inaipatia SMZ kiasi gani cha fedha kwa mwaka kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi hao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu hutoa mikopo kwa kuzingatia kwamba muombaji ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, awe muhitaji aliyedahiliwa katika chuo cha elimu ya juu. Mikopo inayotolewa inatoa umuhimu wa kipekee kwa vipaumbele vya Taifa ambavyo ni Uhandisi wa Gesi na Mafuta, Sayansi za Afya, Ualimu, Ualimu wa Sayansi na Hisabati na Uhandisi wa Kilimo na Maji. Aidha, wanafunzi yatima na wale wenye ulemavu hupewa kipaumbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwepo kwa vyuo vya elimu ya juu Tanzania Bara na Visiwani. Aidha, Serikali inatambua kuwa fursa za kusoma elimu ya juu zinapatikana vyuo vyote vya elimu ya juu hapa nchini ambapo kumekuwepo na wanafunzi wa elimu ya juu wanaotoka Zanzibar na kusomea Tanzania Bara na wengine hutoka Tanzania Bara na kusomea vyuo vikuu vilivyoko Zanzibar. Hivyo basi, kupitia Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu Serikali inawatangazia wale wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu vyote nchini wanaohitaji mikopo kuomba mikopo bila kujali kama anatoka Tanzania Bara au Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba hakuna tengeo maalum la fedha kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ajili ya kugharamia mikopo ya elimu ya juu. Mikopo inatolewa kwa muombaji aliyekidhi vigezo na sifa za kitaaluma bila kujali anakotoka sehemu gani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, katika fomu ya kuwasilisha maombi ya mikopo hii hakuna mahali panapomtaka muombaji kutaja anakotoka sehemu gani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo Bodi inawatambua waombaji wote kuwa ni Watanzania.
MHE. ALLY SALEH ALLY (K.n.y. MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED) Aliuliza:-
Suala la usalama wa raia na mali zao ni moja ya dhamana ya Jeshi la Polisi nchini; ni muda sasa Zanzibar wananchi wamekuwa wakipigwa, kunyanyaswa na kunyang‟anywa mali zao kunakofanywa na vikosi vya SMZ.
Je, nini kauli ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuhusiana na matukio hayo huko Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa usalama wa raia na mali zao ndiyo dhamana kuu au kazi ya msingi ya Jeshi la Polisi nchini. Taarifa hizo hadi sasa hazijapata uthibitisho sahihi kutoka kwa wale ambao wanadai kutendewa vitendo hivyo, kwani hakuna taarifa yoyote iliyoripotiwa kwenye vituo vya polisi Visiwani Zanzibar kuhusiana na uhalifu huo. Kwa mujibu wa taratibu zilizopo ni kwamba mtu yeyote ambaye anafanyiwa kitendo chochote cha uhalifu anapaswa kutoa taarifa kwenye kituo cha polisi, ili hatua za kiuchunguzi na kiupelelezi zifanyike ili kubaini wahalifu ambao wamehusika na hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi bado inasisitiza kuwa haitambui uwepo wa vitendo hivyo na inatoa wito kwa wananchi wote ambao watafanyiwa au wamefanyiwa vitendo kama hivyo, watoe taarifa kwenye vituo vya polisi au kwa viongozi wa polisi waliopo Makao Makuu Zanzibar na Dar es Salaam ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi ya vitendo hivyo kwa watuhumiwa.
MHE. SALEH ALLY SALEH (K.n.y. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED) Aliuliza:- Kwa kipindi kirefu sasa kumekuwa na matendo ya dhahiri yanayoonesha kuvunjwa kwa haki za binadamu hapa nchini bila ya Serikali kuchukua hatua yoyote.
Je, Serikali haioni kwamba wananchi watakosa imani na Serikali yao?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya jukumu la msingi kwa Serikali ni kukuza, kulinda na kuhifadhi haki za binadamu na wajibu wao hapa nchini. Jukumu hilo ni la kikatiba ambapo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kama ilivyorekebishwa mara kwa mara na Katiba ya Zanzibar ya 1984 kama ilivyorekebishwa mara kwa mara pamoja na kuainisha haki za binadamu, imeipa Serikali wajibu wa kukuza, kulinda na kuhifadhi haki hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupitia Bunge lako Tukufu, nchi yetu imeridhia mikataba mbalimbali ya Kimataifa na kikanda ambayo inaweka misingi ya haki hizo na wajibu wa Serikali katika kuhakikisha nchi inaendeshwa kwa kufuata misingi ya haki za binadamu. Aidha, Bunge lako Tukufu kwa nyakati tofauti limetunga sheria mbalimbali zinazolinda na kukuza haki za binadamu pamoja na kutoa nafuu (remedy) kwa raia pale haki za binadamu zinapovunjwaaidha na Serikali au mtu binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa, zinadumishwa na zinastawishwa hapa nchini, Katiba imeipa Mahakama mamlaka ya kusikiliza na kuamua mashauri yanayohusu haki za binadamu na wajibu wao kama ulivyoainishwa katika Katiba. Aidha, Serikali imeunda taasisi mbalimbali zinazoshughulikia hifadhi ya haki za binadamu. Taasisi hizo ni pamoja na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Mabaraza mbalimbali kama yale ya Ardhi na Kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama pamoja na taasisi hizi zimekuwa zikichukua hatua pindi vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinapotokea na kuripotiwa au kufikishwa kwa maamuzi. Serikali kupitia vyombo vyake, imejidhatiti kuhakikisha kuwa kitendo chochote kinachovunja haki za binadamu kinachukulia hatua stahiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwasihi Waheshimiwa Wabunge tushirikiane na vyombo vyetu vilivyopewa mamlaka na dhamana ya kulinda haki pale tunapopata taarifa za vitendo vya uvunjwaji wa haki za binadamu vimefanyika au vinaweza kufanyika ili hatua stahikina za haraka za kisheria zichukuliwe.
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED aliuliza:-
Kwa kipindi kirefu sasa Bandari za Tanga na Mkokotoni zimekuwa zikitumika na kusababisha maafa makubwa kwa watumiaji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha usalama wa wasafiri hao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa wakazi wa maeneo ya Tanga, Visiwa vya Unguja na Pemba wanapata huduma bora na salama na hivyo kuwaepusha na usafiri wa vyombo vya majini visivyokidhi matakwa katika kubeba abiria na mizigo. Baadhi ya hatua hizo ni pamoja na:-
(a) Kuhakikisha kuwa vyombo hivyo ni salama kabla havijaanza kutoa huduma. Kwa sababu hiyo SUMATRA hufanya ukaguzi wa lazima (Statutory Inspection) wa vyombo kila baada ya mwaka ili kubaini kwamba vyombo hivyo vinaendelea kukidhi ubora na usalama wa kuelea majini. Aidha, SUMATRA hufanya kaguzi za kushtukiza ili kuhakikisha kuwa vyombo vya majini vinaendelea kuwa salama wakati wote.
(b) Kuweka na kutekeleza mikakati ya namna ya kudhibiti uibukaji na matumizi ya bandari bubu katika mwambao wa Pwani kwa kuwa vyombo vingi vinavyoanza safari zake katika bandari zisizo rasmi siyo rahisi kufuata masharti ya ubora na usalama wa kuelea majini. SUMATRA inashirikisha uongozi wa Serikali za Vijiji na Kata, vikundi vya kudhibiti uvuvi haramu na usimamizi wa mazingira ya mialo ambao husaidia kusimamia utaratibu wa uondokaji wa vyombo katika mialo ili kuhakikisha vyombo vinavyotumika vinatambulika na kuacha taarifa ya orodha ya abiria na mizigo.
(c) Kuhimiza sekta binafsi kuwekeza katika utoaji wa huduma za usafiri kwa kutumia meli za kisasa kati ya Tanga, Unguja na Pemba ili wananchi wapate huduma bora na za kutosha kupitia bandari rasmi hivyo kuondoa mazingira yanayolazimisha kutumia bandari bubu.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA (K.n.y MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED) aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo la kuvuja kwa mitihani ya Taifa hapa nchini hususani ile ya kidato cha nne (CSEE) hali inayoondoa ufanisi hasa ikizingatiwa matokeo yanayotoka yamejaa udanganyifu. Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeweza kudhibiti na kuondoa tatizo la kuvuja kwa mitihani ya kidato cha nne, ambapo kwa mara ya mwisho ilikuwa ni mwaka 2008 katika somo la hisabati pekee. Changamoto inayoendelea kujitokeza ni kwa baadhi ya watahiniwa kujihusisha na udanganyifu wakati mitihani inapofanyika kwa kuingia katika chumba cha mtihani na vitu visivyoruhusiwa kama vile notes na simu ya mkononi kwa ajili ya kufanya mawasiliano ndani ya chumba cha mtihani.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kujidhatiti na kuikabili changamoto ya udanganyifu katika mitihani kwa kuimarisha usimamizi na kutoa elimu kwa watahiniwa kuhusu madhara ya kufanya udanganyifu. Wizara imekuwa ikitoa adhabu ikiwa ni pamoja na kufutiwa matokeo ya mitihani pale inapothibitika kuwepo kwa udanganyifu huo. Mfano, watahiniwa waliofutiwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2011 ni 3,303, mwaka 2012 ni 789,
mwaka 2013 ni 272, mwaka 2014 ni 184, mwaka 2015 ni 87 na
mwaka 2016 ni 126.
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED aliuliza:-
(a) Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha inashirikisha sekta binafsi ili kufikia dhamira ya kuwa nchi ya viwanda na yenye uchumi wa kati?
(b) Je, Serikali haioni kwamba dhamira hiyo ya kuelekea nchi ya viwanda na uchumi wa kati ni ndoto tu na haiwezi kufikiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Mwenyekiti, dhima ya mpango wa pili wa miaka mitano ni kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. Katika mpango huo, imebainishwa wazi kuwa ni jukumu la sekta binafsi kujenga viwanda. Serikali inabaki na jukumu la kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na ufanyaji biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili Serikali iweze kutekeleza majukumu ya ujenzi wa viwanda kwa ufanisi, Serikali imetekeleza yafuatayo; kwanza, kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara kuhakikisha vikwazo vyote vinaondolewa.
Pili, kupitia Wizara na mamlaka husika kutenga maeneo ya kujenga viwanda kuanzia ngazi ya vijiji mpaka ngazi ya Taifa; tatu, kuweka miundombinu ya umeme, barabara, maji, mawasiliano na usafiri wa anga; nne, kupitia taasisi kama SIDO, TIRDO, TANTRADE na kutoa elimu na mwongozo wa kujenga viwanda na tano, kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika maeneo ya kipaumbele.
• Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Dira ya Taifa 2025 ni kuona nchi yetu inakuwa Taifa lenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Ili kutimiza dhamira hiyo, tunatekeleza Mipango ya Maendeleo mitatu ya miaka mitano mitano. Pia upo mkakati wa fungamanisho la maendeleo ya viwanda ukiongoza utekelezaji wa mipangi tajwa hapo juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini ya utekelezaji wa mipango mitatu ya maendeleo ambapo sasa tumefikia nusu, inaonesha dhahiri kuwa Taifa letu litafikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 likiongozwa na Sekta ya Viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati kuna hitaji kubwa la uwekezaji katika viwanda vinavyotegemea malighafi kutoka kwa wananchi, mpaka sasa maendeleo ni mazuri kwa viwanda vinavyozalisha biashara zinazotumika kwa wingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa uchumi wa viwanda ni jambo ambalo limeshaanza na kufikia uchumi wa kati mwaka 2025 ni jambo linalowezekana.
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED aliuliza:-
Kwa kipindi cha kirefu sasa nchi yetu imekuwa ikipeleka Askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) nje ya nchi ambako kuna vita vya wenyewe kwa wenyewe na kusababisha misiba mikubwa sana kwa Askari wetu:- Je, Serikali inasema nini kuhusiana na kadhia hiyo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania kama Mwanachama wa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Jumuiya za Kikanda kama East Africa Community na SADC na Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu inao wajibu wa kushiriki katika Ulinzi wa Amani katika nchi mbalimbali. Madhumuni ya kupeleka askari wetu huko ni kwenda kulinda amani na sio kushiriki kwenye mapigano. Kwa bahati mbaya sana, yapo matukio ya kushambuliwa kwa askari wetu yaliyofanywa na vikundi vya waasi yaliyopelekea kupoteza maisha ya baadhi ya askari wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Wananchi wa Tanzania limechukua hatua ya kutoa mafunzo ya kutosha kwa vikosi vyetu vinavyopewa jukumu hili, pamoja na kuwaongezea vifaa vya kisasa ili waweze kujilinda dhidi ya mashambulio ya vikundi vya waasi. Hivyo, mtazamo wa Serikali ni kuendelea kushiriki katika shughuli za Ulinzi wa Amani katika nchi mbalimbali ili kutimiza wajibu wetu Kimataifa na huku tukichukua kila tahadhari kuepusha maafa yaliyowahi kutokea.
MHE. HAMAD SALIM MAALIM - (K.n.y. MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED) aliuliza:-
Kwa kuwa huu ni wakati wa Sayansi na Teknolojia na vijana wetu wamekuwa wakizitafuta syllabus za Masomo mbalimbali madukani bila mafanikio:-
Je, Serikali haioni kuwa huu ni wakati muafaka wa kuziweka syllabus hizo mtandaoni?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhamed Amour Muhamed, Mbunge wa Bumbwini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inafanya kila jitihada kuhakikisha kuwa wadau wa elimu wanapata mahitaji yao ya Mitaala na Mihtasari kwa lengo la kufanikisha utoaji wa elimu nchini. Katika kuhakikisha hili, Wizara kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania, husambaza Mihtasari nchi nzima. Aidha, ili kukidhi mahitaji kwa wadau mbalimbali, Mihtasari imekuwa ikipatikana duka la TET na maduka ya vitabu nchini ambayo, wenye maduka ya vitabu huenda kununua kwenye duka la TET.
Mheshimiwa Spika, kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kupita TET, imeshaanza kuweka mihtasari kwenye mtandao wa Taasisi ya Elimu Tanzania ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa mihtasari hiyo. Baadhi ya mitaala na mihtasari ambayo tayari imewekwa kwenye mtandao wa Taasisi ya Elimu Tanzania ni Mitaala na Mihtasari ya Elimu ya awali, Msingi na Sekondari.
Mheshimiwa Spika, aidha, lengo la Wizara kwa sasa ni kuweka Mitaala na Mihtasari ya Masomo yote kwenye mtandao ili iwafikie walengwa kwa urahisi na kwa wakati. Wadau wote wa elimu wanashauriwa kutembelea Mtandao wa Taasisi ya Elimu Tanzania (http://www.tie.go.tz) ili waweze kuona na kupakua Mtaala na Mihtasari husika.
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED aliuliza:-

Suala la mafuta ni la Muungano na kumekuwepo na taratibu mbalimbali zinazofanywa ili kutafuta mafuta nchini:-

Je, ni taratibu zipi zilizopaswa kufanyika ili kuthibitisha kwamba mafuta yanapatikana katika eneo husika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kwa mujibu wa Katiba iliyopo, suala la utafutaji na uzalishaji mafuta ghafi ni suala la Muungano. Hata hivyo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mwaka 2015 kwa nia njema ya kuongeza ufanisi na tija katika shughuli za kutafuta na kuzalishaji mafuta ghafi, zilikubaliana kuwa kila upande usimamie shughuli hizo kwa kutumia sheria na taasisi zake. Serikali zetu za pande zote mbili za Muungano zimefanya hivyo katika masuala ya bandari na viwanja vya ndege, pamoja na kuwa masuala hayo ni ya Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuthibitisha mafuta yanapatikana katika eneo husika, taratibu zifuatazo hufanyika ikiwa ni pamoja na:

(a) Utafiti wa awali wa kukusanya sampuli za kijiolojia na kijiochemia;

(b) Kukusanya data za kijiofizikia (gravimetry na seismic);

(c) Kufanya tathmini (interpretation) ya data za kijiolojia na kijiofizikia;

(d) Kutambua maeneo ya mashapo (geological structures) katika miamba tabaka ambapo mafuta au gesi inaweza kukusanyika kufuatia matokeo ya tathmini ya data za kijiolojia na kijiofizikia; na

(e) Kuchimba visima vya utafiti (exploration wells) katika maeneo yalikotambulika mashapo ili kuthibitisha uwepo wa mafuta ghafi au gesi asilia.
MHE. MOHAMMED AMOUR MOHAMMED aliuliza:-

Idadi ya watu wenye ulemavu inakaribia asilimia kumi (10%) ya Watanzania na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kwa sababu mbalimbali.

Je, Serikali imejipanga vipi katika kuzisaidia na kuwezesha taasisi zinazoshughulikia watu wenye ulemavu nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WENYE ULEMAVU) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004 na Sheria Na.9 ya mwaka 2010 ya Watu Wenye Ulemavu, Serikali inayo majukumu yafuatayo katika kuhakikisha taasisi inayoshughulikia watu wenye ulemavu zinatoa huduma stahiki. Kwanza ni kuzijengea uwezo taasisi zinazoshughulikia watu wenye ulemavu kwa kuzipa mafunzo ya namna ya kuwahudumia watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, Taasisi hizo ni vyama vya watu wenye ulemavu ikiwemo Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Viungo, Chama cha Viziwi Tanzania, Chama cha Wasiona Tanzania, Chama cha Wenye Vichwa Vikubwa na Mgongo Wazi, Chama cha Viziwi Wasiona, Chama cha Watu Wenye Ugonjwa wa Akili, Chama cha Walioumia Uti wa Mgongo na Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Akili pamoja na Chama cha Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi.

Mheshimiwa Spika, pia tunatoa miongozo kwa jamii na sekta zote kuhusu Sera, Sheria, Kanuni na Mikataba ya Kimataifa inayohusu watu wenye ulemavu katika kuleta haki na usawa wao. Kuzitambua na kuzitembea na kuzipa ushauri wa kitaalam taasisi nilizozitaja hapo juu namna ya kuwahudumia watu wenye ulemavu kulingana na aina ya ulemavu na mahitaji yao. Vile vile kuziwezesha taasisi mbalimbali za watu wenye ulemavu, upatikanaji wa nyenzo za kujimudu kwa ajili ya kuwahudumia watu wenye ulemavu pale inapolazimu kufanya hivyo.
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED aliuliza:-

Matokeo ya mitihani ya Kidato cha Nne yamekuwa mabaya kwa kipindi kirefu sasa na hali haijapatiwa ufumbuzi wowote:-

(a) Je, nini tamko la Serikali kuhusiana na hali hiyo?

(b) Je, ni juhudi zipi za makusudi ambazo Serikali inakusudia kuchukua ili kupandisha hali ya ufaulu wa wanafunzi hao?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed Mbunge wa Bumbwini lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ufaulu wa wanafunzi katika mtihani wa kidato cha IV umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka ambapo katika mwaka 2018 watahiniwa waliofaulu ni asilimia 78.3 ikilinganishwa na asilimia 77.09 ya mwaka 2017, asilimia 70.35 ya maka 2016 na asilimia 67.91 ya mwaka 2015.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuongeza ufaulu katika ngazi mbalimbali za Elimu. Hatua hizo ni pamoja na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa kujenga na kufanya ukarabati mkubwa wa miundombinu katika shule ambapo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019, zaidi ya shilingi bilioni 93.8 zimetumika katika uboreshaji wa miundombinu ya shule 588 zikiwemo (Msingi 303 na Sekondari 285) yakiwemo madarasa 1,190, mabweni 222 na vyoo 2,141, mabwalo 76 na nyumba 99.

Mheshimiwa Spika, Aidha, Serikali imeendelea kusambaza vifaa vya kufundishia na kujifunzia vikiwemo, vifaa vya maabara katika shule na vifaa vya kielimu kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum. Vile vile katika kipindi cha mwaka 2017 hadi Aprili, 2019, Serikali imeajiri jumla ya walimu 17,884.

Mheshimiwa Spika, pia Serikali imeendelea kuimarisha Idara ya Udhibiti Ubora wa Shule ambapo imenunua na kusambaza magari 45 ya udhibiti ubora wa Shule na pikipiki 2,897 kwa ajili ya Maafisa Elimu Kata. Katika mwaka 2019/ 2020 Serikali inatarajia kujenga ofisi 100 za wadhibiti ubora wa shule na kuongeza idadi ya watumishi hao. Hivyo, Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuendelea kuimarisha ubora wa elimu nchini.