Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Medard Matogolo Kalemani (318 total)

MHE. LOLESIA J. M. BUKWIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza nianze kwa kutoa shukrani kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa sababu utekelezaji utaanza mara moja mwaka huu Julai, 2016. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kuna hizi huduma za jamii, shule za sekondari, zahanati, vituo vya afya ambavyo pia ni muhimu kuweza kupatiwa umeme. Napenda kujua sasa, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba pia vituo vya afya pamoja na zahanati na shule za sekondari zinapatiwa umeme huu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika Bunge lililopita, la Kumi, Serikali iliahidi kwamba ingehakikisha vile vijiji vyote ambavyo vinapitiwa na nguzo za umeme juu, zinapatiwa umeme, lakini mpaka sasa hakuna hatua zozote zinazoendelea kuhakikisha wanapatiwa umeme. Katika Jimbo la Busanda pia kuna vijiji ambavyo vimepitiwa na nguzo juu lakini hazina umeme. Napenda kujua:-
Je, Serikali ina mpango gani sasa kuhakikisha kwamba vijiji hivi ambavyo vikiwemo Kijiji cha Buziba, Bunekezi na Naruyeye vinapatiwa umeme ili wananchi waweze kunufaika na huduma ya umeme? (Makofi)
NAIBU WAZIRI NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kuna maeneo mengi ya ustawi kwa jamii ambayo pia yangepewa kipaumbele cha umeme kwenye mpango huu.
Niseme tu kwamba kwenye awamu ya kwanza na awamu ya pili ya (REA-Phase I na REA-Phase II), maeneo mengi sana ya Shule za Sekondari pamoja na hospitali yamepitishwa umeme. Hata hivyo kwenye REA-Phase III inayoanza mwezi Julai, naomba tu niungane na Mheshimiwa Bukwimba kwamba kama kuna shule za sekondari pamoja na vituo vya afya ambavyo havimo kwenye mpango huo na havikufanyiwa kazi kwenye awamu ya pili, naomba tufuatane naye baada ya Bunge lako ili tukabainishe maeneo hayo. Ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nijibu swali la pili la Mheshimiwa Lolesia Bukwimba, kuhusu vijiji vilivyopitiwa na nyaya za umeme lakini hazina umeme. Namhakikishiae Mheshimiwa Lolesia Bukwimba kwamba kwenye awamu inayokuja awamu REA-Phase III, kuna underground REA-Phase III. Maeneo ambayo yalipitiwa na nguzo za umeme lakini hayakupata umeme na yamo kwenye mpango wa umeme, yamekadiriwa kwenye nguzo za umeme under REA- Phase III, under REA Line, ambao pia ambapo itahusisha Vijiji vya Buziba, Bunekezi na maeneo ya jirani.
Mheshimiwa Spika, pia namwomba Mheshimiwa Bukwimba, kwa sababu tumeshirikiana naye sana kwenye masuala ya umeme kwenye Mkoa wa Geita, kama kuna vijiji vingine ambavyo havimo kwenye mpango huu, kadhalika baada ya Bunge hili, nionane naye ikiwezekana tukae sisi wawili tu, tujifungie, kuainisha maeneo hayo. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Kicheko)
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, niishukuru Serikali kwa mpango mzuri ambao sasa unatupa matumaini. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa, suala hili limechukua muda mrefu wa mradi huu wa REA na wa Songea na wa Makambako kwenda Songea ambao ulikuwa unaunganisha Kijiji cha Lyamkena na Kiumba. Je, ili kuwapa matumaini wananchi wangu kwa sababu suala hili kama nilivyosema limechukua muda mrefu, Waziri sasa atakuwa tayari baada ya kwisha Bunge tuende tukafanye mkutano atuambie kwamba alivyosema Machi mradi unaanza?
Swali la pili, kutoka ofisi ya TANESCO pale Makambako, kuna mita kama 400 hivi 500 kwenda kwenye Kijiji au Mtaa wa Kivavi na Mtaa wa Kibagange. Tunashukuru Serikali mlishatupa transfoma na nguzo zilianza kujengwa ni muda mrefu sasa zimesimama tumekwama nguzo za kumalizia na wire. Serikali itakuwa tayari sasa kutupa wire na nguzo ili tumalizie mradi huu wananchi waweze kufaidika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli Mheshimiwa nakubaliana na yeye na kwa ridhaa yako, baada ya Mkutano huu tutafuatana mimi na yeye kwenda kwenye maeneo yake kuhakikisha kwamba maeneo yake yanapata umeme uhakika.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, vijiji alivyovitaja kwa kweli vina urefu siyo mrefu sana kutoka umeme unapoishia na kwa kweli kuna transfoma ya zamani pamoja na nguzo zilizooza, kwa sasa tunafanya mabadiliko ya kubadilisha transfoma kwenye maeneo yake. Mabadiliko haya yatajumuisha pia vijiji vya Mheshimiwa Mbunge alivyouliza, kadhalika Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba katika ziara yangu kwenye swali lako la nyongeza la kwanza. Napenda niunganishe na vijiji vyako hivyo viwili nitavitembelea ili kuona kama hizo transfoma zilizopo zinafaa au hazifahi ili tufanye marekebisho.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza naomba niipongeze sana Serikali kwa kazi nzuri sana inayofanya ya kusambaza umeme kupitia REA, REA I, REA II na REA III kwa sasa. Swali langu kwa sababu kuna vishoka wamejitokeza ambao wanaharibu sifa nzuri ya TANESCO, wanaojifanya kwenda kutandaza nyaya kwenye nyumba za watu lakini wanachukua pesa zao halafu hawa hawarudi tena kwa ajili ya kusambaza huo umeme. Je, Serikali inaweza ikawaagiza Mameneja wa Kanda, Mameneja wa Mikoa, Mameneja wa Wilaya ili kusudi waende wawabaini hao vishoka wasiwaibie wananchi hasa katika Jimbo la Sumve?
NAIBU WAZIRI NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kati ya wahudumu wanaotoa huduma kwenye Shirika la Umeme kuna wafanyakazi wengine wala siyo wa TANESCO ni wafanyakazi bandia ambao wanaitwa vishoka. Pamoja na Wabunge mnaonisikiliza nichukue nafasi hii tu kuwatahadharisha kwamba wafanyakazi wa Mashirika ya Umeme Tanzania ni wafanyakazi ambao wanafanyakazi kwa maadili ya utumishi wa umma. Hata hivyo, tunatambua inawezekana wapo wachache kati yao ambao pia wanashirikiana na vishoka kuhujumu nguvu umeme ya TANESCO.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa hivi tumechukua hatua makusudi tumeanza kuwabaini wale Mameneja ambao wanashirikiana na vishoka tumeshaanza kuwa-identify na mpaka sasa kuna vishoka takribani 19 wamekamatwa na naomba sana nitamke hili na kuanzia sasa ofisi zetu zote za Kanda pamoja na Mikoa wale Makandarasi wanaohusika kuunganisha nyaya kwenye nyumba wanaorodheshwa kwenye ofisi zetu.
Kwa hivyo basi, kama kutakuwa na wakandarasi ambao hawapo kwenye orodha ya ofisi zetu hao ni vishoka na hawakubaliki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niongeze kwenye jibu hilo, hadi sasa Shirika la Umeme TANESCO limeshaanza kuchukua hatua kwa watumishi wake wasio waadilifu, hadi sasa watumishi 12 wamesimamishwa kazi kwa sababu ya kuhujumu miundombinu ya TANESCO pamoja na kushiriki kwenye kuwaunganishia umeme watu kwa njia ya vishoka.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri yenye kuakisi nia ya Wizara na Serikali kushirikiana nasi, nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la msingi, imeelezwa vizuri kabisa kwamba uvunjifu wa amani ni moja ya matokeo hasi ya kukosekana kwa fursa hizi za wananchi wa Mavota kushiriki kwenye uchumi uliowazunguka. Kwa sababu suala la uvunjifu wa amani si suala la kusuburi, ni la haraka, je, Serikali na Wizara iko tayari kutoa kauli inayothibitisha uharaka wao katika kuja kuzungumza na wananchi wa Mavota?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hatua ambazo Serikali imechukua kupitia Wizara yetu ni pamoja na kuhakikisha kwamba uchimbaji salama na makini unafanyika kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia umuhimu huo, ofisi yetu iko tayari kwenda kuzumgumza na wananchi kuwahakikishia amani zaidi kwenye shughuli za uchimbaji eneo la Mavota.
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pia nashukuru majibu ya Serikali na kuwapongeza Wizara hii kwa jinsi wanavyoshughulikia masuala haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wizara inatambua kwamba Magu bado vijiji 85 na 34 vitaingizwa kwenye mpango wa REA III, je, Wizara inaonaje kuviingiza vijiji vyote vilivyobaki kwenye mpango huu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa REA II inaendelea na miradi kule Magu na kwa sababu baadhi ya vijiiji mkandarasi ameondoa nguzo ambazo zilikuwa zinategemewa na wananchi na wananchi wengine hawajawekewa, je, Mheshimiwa Waziri anaweza kuambatana nami kwenda Jimboni kwangu kutembelea vijiji hivyo pamoja na Vijiji vya Mahaha, Nobola, Bungilya, Mwamabanza na Matale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakubaliana na Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine na naamini kila Mbunge angependa sana vijiji vyake vyote viingie kwenye REA III. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tunaendelea kufanya tathmini kama itaonekana ipo haja ya vijiji vyote kuingia basi vitaingia lakini kutegemeana na bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la pili la kuondoa nguzo kwenye maeneo mengine na kupeleka maeneo mengine, hili nimelichukua. Sambamba na hilo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi tuko tayari kutembelea maeneo yote yenye kero za umeme na kuhakikisha kwamba zinatoweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ridhaa yako niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge, usambazaji na upatikanaji wa umeme nchini ulianza mwaka 1908 enzi za ukoloni wa Mjerumani. Kwa hiyo, miundombinu mingi sana imeharibika kama transfoma na mingine, kwa hiyo, tunaendelea na ukarabati. Kwa hiyo, maeneo mengine ambayo Waheshimiwa Wabunge mtapenda tutembelee, tutaendelea kutembelea na tutaendelea kuboresha lengo ni kuhakikisha wananchi wote wanapata umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba lengo letu ni wananchi wote wapate umeme. Nimwombe sana Mheshimiwa Lukuvi kwa sababu anaimarisha nyumba za wananchi, sisi hatutajali kumwekea mtu umeme eti mpaka awe na nyumba nzuri, tutamtundikia umeme hata kwenye mkaratusi karibu na nyumba yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matatizo ya Jimbo la Kavuu yanafanana kabisa na matatizo ya Jimbo la Magu na hivi karibuni kupitia mpango wa REA wameweza kuweka umeme katika Kata yangu ya Usevya katika Jimbo la Kavuu. Hivi karibuni umeme umeanza kuwaka takribani wiki tatu baada ya REA kukamilisha ujenzi wake pale lakini mpaka sasa hivi wananchi hao hawana umeme ikiwemo pamoja na mimi. Je, kwa kuwa wananchi wale walikuwa na hamu na umeme huo ambao haupatikani, Serikali inasema nini kuhakikisha kuanzia sasa umeme unapatikana?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge kwamba yapo maeneo ambayo hayana umeme hadi sasa. Kwa ridhaa yako niombe kusema kwamba nitakaa na Mheshimiwa Mbunge ili tuyatambue kwa kina maeneo ambayo hayana umeme na tuyafanyie kazi ili wananchi wapate umeme.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimwia Spika, kwa kuwa Mkoa wa Kigoma pamoja na Wilaya zake zinaingiza gharama kubwa sana katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kutumia majenereta, zaidi ya bilioni 160 kwa mwezi, kwa nini Serikali pamoja na Wizara ya Nishati na Madini isifanye haraka mradi huu ili kuokoa pesa kwa Mkoa wa Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa shughuli za ugawaji wa umeme katika Mji wa Kigoma ni gharama kubwa na gharama alizozitaja Mheshimiwa Keissy kwa kweli ni kidogo siyo shilingi milioni 160 isipokuwa ni shilingi milioni 600 kila siku za mafuta tunatumia.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia uzito huo huo, ndiyo maana Serikali imesema itaanza ujenzi wa mradi huo wa Malagarasi ndani ya miezi sita kuanzia sasa, kuanzia mwezi Februari mwakani shughuli za ujenzi kwa ajili ya kuwapatia umeme wa uhakika wananchi wa Kigoma zitaanza. Kama nilivyosema shughuli hizi zitachukua miaka mitatu hivyo mwaka 2020 shughuli za ugawaji wa umeme katika Mji wa Kigoma zitakamilika na umeme utakuwa ni wa uhakika ambao haukatiki.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mchakato mzima wa uzalishaji umeme katika Mto Malagarasi umetumia vilevile fedha za Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC I). Ninataka nifahamu kwamba watu wa MCC wamekuwa wakipeleka fedha zao nyingi kwenye mradi wa umeme, na sasa hivi wamejitoa.
Je, sasa Serikali itupe commitment ya miradi yote ya umeme ambayo fedha zake zilikuwa za MCC, sasa Serikali itatumia vyanzo gani kuhakikisha kwamba miradi iliyopangwa inakamilika kwa wakati.
NAIBU WAZIRI NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba MCC wamejitoa kwenye mradi wa Awamu ya Pili, lakini kazi ya MCC iliyofanyika awamu ya kwanza ilifanyika vizuri, na pesa zote zilitumika. Sasa Serikali inafanyaje.
Mheshimiwa Spika, katika awamu ya mradi huu wa 2016/2017, nichukue mfano kwa Mto Malagarasi shilingi bilioni moja ilikuwa ni fedha za ndani, lakini dola za Marekani bilioni moja pamoja na zingine dola za Marekani bilioni tatu zitafadhiliwa na World Bank pamoja na Benki ya Dunia ya Maendeleo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na MCC kujitoa halijaharibika jambo. Ahsante sana.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini bado ulipaji wa fidia huu umeonekana kuwa ni kitendawili, kwa mara ya kwanza tuliambiwa kwamba fidia hizi zitalipwa tarehe 16 Februari, lakini sasa hivi Serikali inakuja na majibu mengine kwamba itaanza kulipa mwezi Juni. Sasa tunaomba kujua specific date ya fidia hiyo itakuwa ni lini?
Pili, kumekuwa na usumbufu mkubwa katika ulipaji wa hiyo fidia, je, kwa sababu muda utakuwa umeshapita fidia hii italipwa pamoja na fidia?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli fidia ilianza kulipwa tangu mwezi Februari mwaka huu.
Mheshimiwa Spika, lakini tutambue kwamba suala la ulipaji fidia ni suala endelevu, kadri tathmini inavyofanyika ndiyo fidia inavyoendelea kulipwa na ndiyo maana tunasema hata mwezi huu na mwezi ujao wataendelea kulipwa fidia. Suala kubwa Mheshimiwa Mbunge ni kwamba shughuli za ujenzi wa mradi huu zitaanza mapema tu baada ya fidia kukamilika.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kama wananchi watalipwa pia pamoja na nyongeza ya mapunjo ya awamu iliyopita.
Mheshimiwa Spika, taratibu za fidia kwa waathirika hufanyika wakati tathmini inapofanyika, kwa hiyo malipo ya fidia hulipwa kulingana na viwango wakati tathimini inafanywa na siyo vinginevyo.
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Spika, suala la ulipaji wa fidia Ludewa pia linafanana na sehemu ya Wilaya ya Geita ambapo wananchi wa mtaa wa Mgusu wanaishi katika eneo ambalo liko ndani ya beacon ya Geita Gold Mine na wananchi hawa wamekuwa wakiathirika na taka zenye sumu zinazomwagwa katika eneo lao.
Je, Serikali inaweka msukumo gani kwa Geita Gold Mine kuhakikisha kwamba inawalipa wananchi wa mtaa wa Mgusu fidia ili waweze kupisha eneo hilo na wasiathirike na taka katika hilo eneo la Geita? Asante.(
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa wananchi wa Mgusu wanaishi sehemu ya leseni ya utafiti wa GGM, lakini taratibu ya Sheria za Ardhi na Sheria za Madini zote hulingana. Kimsingi, mahali ambapo mgodi haulitumii eneo hilo wananchi wanaweza waka-co-exist na shughuli za mgodi, lakini mahali ambapo shughuli za mgodi zinafanyika, basi wananchi wanaoishi katika maeneo hayo hufanyiwa fidia na kupisha shughuli za ujenzi.
Mheshimiwa Spika, eneo la Mgusu linalozungumzwa, Mgodi wa GGM haujaanza kulitumia. Kwa sasa hivi wananchi wanaishi Mgusu na kimsingi Mgusu imeshakuwa ni mjini na GGM sasa hivi haioni sababu ya kulichukua. Ila itakapofika wakati wa kulichukua eneo hilo, Mheshimiwa Mbunge atawasiliana na sisi na taratibu za fidia za wananchi wa Mgusi zitafanyika.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, natambua umuhimu wa upembuzi yakinifu na kwamba unaendelea katika ujenzi wa uwanja wa Musoma. Je, ni lini ujenzi wa uwanja wa Musoma utaanza rasmi?
Pili, nimesikitika sana kwa majibu namba (c), nanukuu: “Ni vigumu sana suala hili kulitolea takwimu sahihi kwa kuwa linahitaji kufanyiwa utafiti.”
Mheshimiwa Spika, swali hili tangu nimelipeleka lina miezi mitatu. Je, jibu hili ndilo linaloendana na Hapa Kazi Tu? Ni lini swali hili litapatiwa majibu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI (K.n.y. WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO): Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kuanza kwa uwanja wa ndege, kama nilivyosema ni mara tu baada ya ukamilifu wa upembuzi yakinifu ambao ulitarajiwa kuanza mwezi Februari, 2017.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na takwimu za kina, ni kweli kabisa ili kupata ulinganifu wa hasara unazopata ndani na nje; na unapofanya takwimu za kisayansi, ni lazima uangalie mapato unayopata ndani na mapato unayopata ambayo unayakosa kwa kukosa ndege ambayo inasafiri Kimataifa.
Mheshimiwa Spika, hivyo unavyofanya ulinganisho siyo rahisi ukapata takwimu leo wakati unatakiwa ulinganishe na mataifa mengine pia yanapataje faida kwa matumizi ya ndege za aina hiyo hiyo.
MHE. ORAN M. NJENZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, kwanza napenda kumshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na vilevile kuipongeza Wizara hii kwa kazi nzuri inayoifanya kwa kusambaza umeme karibu vijiji vyote vya Tanzania hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuwapongeza Mainjinia wa TANESCO waliopo pale Mbeya akiwemo Engineer Maze na Engineer Kiduko pamoja na Engineer Mbalamwezi. Pamoja na hayo, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Wizara ina mpango gani wa kusambaza umeme pamoja na hii REA kwenye vitongoji vilivyobaki katika vijiji hivyo vilivyotajwa? (Makofi)
Swali la pili, kutokana na ongezeko la usambazaji wa umeme vijijini, inaelekea capacity ya watumishi wa TANESCO ikiwemo vifaa, haitoshelezi tena.
Je, Wizara ina mkakati wa kuhakikisha kuwa inaongeza capacity ya watumishi ili iendane pamoja na usambazaji wa umeme vijijini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na Mheshimiwa Mbunge, ni kweli kabisa, pamoja na mradi huu kabambe wa REA kuendelea kufanya kazi yake, lakini bado kuna miradi mingine itaendelea kwa ajili ya kukamilisha shughuli zinazoachwa na REA. Baadhi ya kazi zinazoendelea hapa sambamba na miradi ya REA ni pamoja na mradi wa Underline. Mradi wa Underline unaendelea kupita kukamilisha maeneo ambayo yanaachwa na TANESCO pamoja na REA.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusiana na uwezo na capacity pamoja na management, ni kweli kabisa, kama mnavyojua, TANESCO ni shirika la zamani, lakini tuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge pamoja Serikali ya Awamu ya Tano, ni kwamba tunapata uwezo wa kuongezewa nguvu. Kwa sasa hivi tunaongezewa nguvu Shirika letu la TANESCO kwa maana ya kulinunulia vifaa vya kutosha kama transfoma pamoja na generetors ambako tunatumia mafuta. Kwahiyo, Mheshimiwa Mbunge nimhakikishie kwamba Shirika la TANESCO pamoja na REA pamoja na miradi mingine, itaendelea kuimarishwa ili ifanye kazi zake vizuri.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Suala hili la Mbeya Vijijini linafanana sana na tatizo sugu la umeme katika Jimbo letu la Mikumi.
Swali langu ni kwamba, je, ni lini Serikali itapeleka umeme huu wa REA kwenye Kata za Tindiga, Mabwerebwere, Ulaya, Zombo, Muhenda, Uleling’ombe na Vidunda?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa hapa tulipofika REA Awamu ya Pili tunatarajia ikamilike mwezi Juni mwaka huu. Vijiji vyote ambavyo vitakuwa vimesalia bila ya kuwa na umeme pamoja na vijiji alivyovitaja Mheshimiwa Mbunge vya kwenye Wilaya pamoja na Jimbo la Mikumi, vyote tunatarajia tuvifikishie umeme kwenye REA Awamu ya Tatu. Kwahiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba vijiji vyake vyote vitapata umeme wa REA Awamu ya Tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge, kama tutakavyoleta bajeti yetu, tuna matumaini makubwa kwamba bajeti yetu ya kupeleka umeme vijijini itapitishwa na Waheshimiwa Wabunge na ikishapitishwa, kama tunavyosema siku zote, kwa sababu suala la umeme ni la kufa na kupona, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kupeleka umeme kwenye vijiji vyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka kwenye Awamu ya Tano ifikapo 2025 vijiji ambavyo vitakuwa havina umeme vitakuwa ni vya kutafuta. Kwahiyo, vijiji vyote vitapata umeme wa REA Awamu ya Tatu. Ahsante.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niulize swali moja dogo la nyongeza. Katika usambazaji wa umeme kwenye hii REA Phase II, Makao Makuu ya Wilaya ya Chemba, umeme ule umepelekwa kwenye nyumba ya Mkuu wa Wilaya tu. Pia katika vijiji vya Gwandi, Farko na Kwamtoro ambavyo vilikuwepo kwenye programu hii havijapelekewa hata nguzo. Mheshimiwa Waziri naomba anihakikishie hapa kwamba je, mpaka kufika Juni miradi hii itakuwa imekamilika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa baadhi ya maeneo ambayo yamepelekewa umeme tumepeleka kwenye vituo vikubwa hatujaanza kusambaza kwenye vijiji, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Nkamia kwamba ni kweli vijiji ambavyo vimesalia kwenye ile awamu ya pili sasa hivi kazi inayofanyika ni kuvihakiki ili tubaini ni vituo gani na vijiji gani havijapata umeme kwenye REA Awamu ya Pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, azma yetu ya kwanza ni kuhakikisha kwamba vijiji vyote vilivyokuwa kwenye scope ya REA Awamu ya Pili kwanza vinakamilika ifikapo Juni mwaka huu, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili kama itaoneka kwa dosari za kibinadamu vijiji vitasalia, vyote vitakavyokuwa vimebaki vitaingia kwenye REA Awamu ya Tatu pamoja na vijiji vya Mheshimiwa Nkamia.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Bukene, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa ziara ambayo aliifanya katika Jimbo hili hivi karibuni na vijiji vyote vilivyotajwa kwenye swali hili vya Mwangoye, Mambali na Mbutu, Mheshimiwa Naibu Waziri alivipitia na kutoa maelekezo maalum kwa TANESCO, REA na CHICCO…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Zedi, naomba uulize swali tafadhali.
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu ni kwamba kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi katika kijiji cha Mwangoye, Mambali na Mbutu, jambo ambalo limefanya wananchi wengi kufanya wiring na kuwa tayari na fedha ya kulipia, lakini kuna upungufu mkubwa wa nguzo na vifaa vya kuunganishia.
Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kutumia forum hii kutoa agizo au kauli maalum kwa watendaji wa REA, TANESCO na CHICCO kuhakikisha kwamba wananchi wote wa Mwangoye, Mambali na Mbutu ambao wameshajiandaa kupata umeme wanapatiwa nguzo na vifaa vya kuunganishiwa ili waweze kupata huduma muhimu ya nishati?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu niongeze maelezo kwenye shukrani alizotoa na mimi namshukuru sana Mheshimiwa Zedi kwa pongezi na shukrani za kuunga mkono. Nampongeza sana pamoja na wananchi wa Bukene. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye swali lake, kimsingi siyo swali lakini anataka wananchi wake wapate uhakika. Ni kweli kabisa nguzo zinaendelea kwenda Bukene katika vijiji vyote vitatu na katika mwezi ujao wananchi wapatao 50 watapatiwa umeme kwa sababu nguzo wameshapelekewa.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Naomba niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa amesema kwamba umeme umeunganishwa katika Gridi ya Taifa kule Hale; na kwa kuwa Korogwe imekuwa umeme unakatika mara kwa mara. Je, ni lini umeme utakoma kukatika ili kusudi wananchi wa Korogwe Mjini waweze kufanya shughuli zao za biashara pamoja na shughuli nyingine bila kuwa na kukatika kwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mary Chatanda kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa katika Mkoa mzima wa Tanga umeme unakuwa ukikatika mara kwa mara na suala la kukatika umeme mara kwa mara siyo kwa Mkoa wa Tanga peke yake, lakini sasa hivi tunachofanya, tunafanya marekebisho ya miundombinu yote katika Mikoa karibu yote. Kati ya mikoa yote, Mkoa wa Tanga tumeupa kipaumbele. Tunafanya marekebisho ya transfoma pamoja na chanzo cha umeme cha Hale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye bajeti hii inayokuja, tuombe sana Waheshimiwa Wabunge, tunadhani mtaipitisha; tumetenga pesa kwa ajili ya kurekebisha mitambo hiyo. Kwa hiyo, Mkoa wa Tanga na Korogwe mtapata umeme wa uhakika baada ya bajeti hii.
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishukuru kwa majibu mazuri ambayo yametolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini sambamba na hilo naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo kampuni ambayo ameitaja Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa muda huo wa miaka nane ambao wamekuwa wanafanya utafiti, wamekuwa wanatumia mashine, wamekuwa wanatumia magari ambayo yamekuwa yanaharibu barabara zinazounganisha, Nditi, Nero, Namakwia pamoja na Lionja.
Je, Mheshimiwa Waziri ananiambia nini kwa niaba ya wananchi wa Nachingwea juu ya fidia ya uharibifu mkubwa wa mazingira ambao unafanywa na kampuni hii? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni eneo la upatikanaji wa leseni. Wananchi walio wengi wanaozunguka Wilaya ya Nachingwea wana kipato cha chini na wanatamani kujinufaisha na rasilimali ambazo zinapatikana katika maeneo yao kama taarifa inavyojionesha, lakini upatikanaji wa leseni hizi umekuwa na mlolongo mkubwa.
Je, Wizara inaweka utaratibu gani rahisi ambao utawawezesha watu wa Nachingwea kujimilikisha na kupata leseni waweze kuchimba wao wenyewe badala ya kuwa vibarua? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya kwanza ameulizia kuhusu uharibifu wa barabara na miundombinu kutokana na shughuli za utafiti. Shughuli za utafutaji ziko za aina tatu. Shughuli ya kwanza kabisa ambayo hufanywa na mtafiti wa madini ni kufanya utafiti angani. Utafiti wa aina hii haugusi ardhi na hauhitaji fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, utafutaji wa pili ni ule ambao wanaweza wakatumia mimea pamoja na miamba kwa kugusa tu juu ya ardhi na wenyewe hauharibu mazingira, lakini utafiti wa tatu, ni ule ambao mtafiti anahitaji kufanya drilling. Anapofanya drilling sasa anaharibu miundombinu ya barabara na ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa utaratibu huo sasa, napenda kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba, taratibu za fidia kwanza kabisa, kama kuna miundombinu imeharibika kwa taratibu za utafiti na uchimbaji, Sheria ya Madini inatoa kifungu cha 96 kuhakikisha kwamba mwenye leseni ya utafutaji au ya uchimbaji wanakaa na mmiliki wa miundombinu kukubaliana aina ya uharibifu na viwango vya fidia. Ikishindikana fidia kwa taratibu za Sheria ya Madini ya mwaka 2010, basi Sheria za Ardhi za 1999 Namba 4 na Namba 5 ya 1999 Vijijini, hutumika kufanya fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nashauri sana wenye miundombinu hiyo wanaoshughulika na utafiti wakae na Kampuni hiyo wangalie uharibifu halafu waangalie namna gani ya kufidiwa barabara hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni upatikanaji wa leseni za utafiti na uchimbaji wa madini. Natumia nafasi hii kuwaambia tu kwamba taratibu zote za kumiliki leseni za uchimbaji na utafutaji mdogo; utafutaji na uchimbaji mkubwa; zote huzingatia Sheria ya Madini. Utaratibu uliopo, kwa Waingereza wanasema ni first come first served. Anayeomba mapema ndiye anayeanza kufikiriwa kupewa leseni.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wetu wa kutoa leseni ni ndani ya siku 14 tangu unapoomba na unaarifiwa. Ukishaarifiwa na wewe unajibu ndani ya siku 14. Pia mtoa leseni, Kamishna wa Madini kwenye ofisi zetu, anatoa leseni ndani ya siku nyingine 28.
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, nachukua nafasi hii kusema tu kwamba ni kweli kabisa upatikanaji wa leseni kwa utaratibu wa awali umekuwa ukitumika hivyo.
Hata hivyo, mwaka 2015 tumerekebisha Sheria ya Madini ya 2010, tumeingiza sasa kifungu cha waombaji kuomba leseni kwa kielektroniki, kwa kutumia mtandao. Kwa hiyo, unajaza fomu siku hiyo hiyo, unawasilisha fomu siku hiyo hiyo kwa njia ya mtandao na baada ya siku 28 unapata leseni. Kwa hiyo, nawaombe sana wachimbaji wa vijijini pia wanaweza wakatumia utaratibu huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine tumeboresha leseni kwa kuwegesha karibu na Ofisi za Madini kwenye Kanda zote. Sasa hivi karibu kila mkoa una ofisi tatu au nne za Madini. Kwa hiyo, nashauri basi, ili kupunguza mlolongo wa kuchelewa kupatikana kwa leseni, wananchi walio karibu na Ofisi zetu waende kwenye ofisi zetu ili waombe leseni na kuhudumiwa mapema iwezekanavyo.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nitambue jitihada ambazo zimefanywa na Waziri, Mheshimiwa Muhongo katika kujaribu ku-ssetle down issue hii na wananchi wa Tarime wanasubiria kwa hamu sana majibu yake kuhusu malipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, niulize maswali mawili ya nyongeza. Nataka Waziri atambue kwanza kwamba neno „mongo’ siyo neno la siku moja, ni neno la Kikurya lenye maana ya sehemu ya kutunza mali. Kwa hiyo, mgodi ule upo enzi na enzi na watu wa pale wametegemea maisha hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo Waziri anakuja na jibu hapa, siku moja nilimwambia awe anafanya research, anasema hakuna mkataba wowote ambao kijiji kinaingia na mgodi. Mimi nina mikataba ya Serikali ya Vijiji hivi, hii hapa ya mwaka 1995 ambayo mgodi uliingia na Serikali za Vijiji alivyovitaja hapo kwamba kwenye kila uchimbaji watakuwa wanatoa asilimia moja kama royalty kwenye Serikali za Vijiji. Hizi fedha zimesomesha watoto wetu pale, zimejenga shule na maisha ya vijiji vile wamekuwa wakifaidika na pesa hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tangu waanze kwenda underground wameacha kulipa royalty kwenye Serikali za Vijiji. Nataka Waziri atuambie ni lini mnauamuru mgodi huu uanze kulipa royalty, kwa sababu mnasema hauchimbi kwenye eneo la kijiji lakini pamoja na underground wako eneo la kijiji, hawako Singida wala hawako Mwanza, wako Tarime. Kwa hiyo, nataka majibu hayo atuambie ni lini wanaanza kulipa hiyo royality? Mkataba husika nitawapa hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Naibu Waziri wa Mazingira tangu mwezi wa Pili amekuja akachukua pale sample za maji na kwa wiki nzima hii pit ya Gokona imekuwa ikimwaga maji kwenye Mto Tigite ambapo watu wanalalamikia kwamba yana sumu na yanaathiri mali zao. Sasa nataka Waziri atoe kauli kuhusiana na hili kwamba pit ya Gokona sasa inamwaga maji kwenye Mto ule na yanaathiri maisha ya watu pale, mifugo na jamii nzima. Nataka atoe kauli kuhusiana na suala hilo ambalo linafanyika kwa wiki nzima sasa.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikubaliane na Mheshimwa Heche, kwamba neno mongo ni utajiri kule kwao na kuhila ni utajiri kule kwetu Usukumani, namshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijibu sasa kwa weledi sana swali lake la kwanza. Nimsahihishe kidogo Mheshimiwa Heche, mikataba iliyoingiwa kati ya vijiji saba pamoja na mgodi wa Acacia ni mkataba wa malipo ya royalty siyo mikataba ya uchimbaji. Hilo ni suala la msingi sana Mheshimiwa Heche na Waheshimiwa Wabunge kulielewa. Pamoja na hayo, nikubali tu kwamba ule mkataba ulioingiwa kati ya vijiji na mgodi ambapo kila kijiji kinalipwa royalty asilimia moja bado unaendelea na wataendelea kulipwa kwa mujibu wa mikataba ile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze kwenye swali lake la pili, inaonekana kwamba mtaalam wa NEMC ameenda kuangalia kwenye Mto Gokona na kuona kwamba kuna athari za mazingira. Serikali yetu ya Awamu ya Tano, Mheshimiwa Waziri wangu tarehe 22/2/2016 aliunda Kamati Maalum ya kufanya uchunguzi wa matatizo yote katika Mgodi wa North Mara. Katika Kamati ya watu 27 iliyoundwa Mheshimiwa Heche ametoa wawakilishi wake wanne. Kwanza, Mheshimiwa Heche tunakupongeza sana kwa kutuma wawakilishi wako wanne kwenye Kamati ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme tu kwamba Kamati iliyoundwa kwa ajili ya kuchunguza masuala yote ya Mgodi wa North Mara ikiwa ni pamoja na matatizo ya kimazingira ina ToR (Hadidu za Rejea) 27. Kati ya hizo, tano zinahusiana na matatizo ya athari ya mazingira kwenye Mto Gokona. Kwa hiyo, naamini kwamba taarifa itakapokuja na imeshakuja tunaifanyia kazi, utekelezaji wa mapendekezo ya Kamati hiyo yatatolewa na Mheshimiwa Heche atapewa maelekezo ya hatua za Serikali zilizochukuliwa.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kwamba itakuwa ni Serikali ya viwanda, je, Selikali ina mpango gani wa kuanza kufufua viwanda hivi ambavyo vilikufa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Kiwanda cha Chai cha Mponde kilichoko katika Wilaya ya Lushoto, Jimbo la Bumbuli, kimefungwa kwa takribani miaka mitatu sasa na mpaka sasa hakijaanza uzalishaji. Mara ya mwisho wakati Msajili wa Hazina anakuja pale alituambia kwamba zimeandaliwa shilingi bilioni nne kwa ajili ya kuanzisha shughuli za uzalishaji na kwenye randama ya Wizara ya Fedha na Wizara ya Viwanda na Biashara fedha hiyo hatujaiona. Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu kufunguliwa kwa kiwanda hiki?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Shangazi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Serikali imedhamiria kujenga viwanda na hasa kuanzia viwanda vidogo sana, viwanda vidogo, viwanda vya kati pamoja na viwanda vikubwa. Mikakati ambayo Serikali inaichukuwa kwa sasa ni pamoja na kutengeneza mazingira wezeshi ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ili kuwawezesha Watanzania kuwekeza zaidi. Mkakati wa pili ni kufanya utafiti hasa kwa viwanda ambavyo vimedhoofika au vimekufa ili kuviweka katika mazingira mazuri ili kutafuta wawekezaji wengine kwa ajili ya kuviendeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hayo, nimhakikishie Mheshimiwa Shangazi tu kwamba Serikali inafanya mikakati mingine ya ziada ikiwa ni pamoja na kutoa mikopo kama mnavyoona kwamba Serikali itatoa mikopo shilingi milioni 50 kila kijiji ili kuwawezesha Watanzania waweze kufanya pia biashara kuendesha viwanda vidogo vidogo. Pamoja na hayo, Serikali imeweka mazingira ya kisera na kisheria ili kuhakikisha kwamba sasa tasnia ya viwanda inaimarishwa zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusiana na Kiwanda cha Chai cha Lushoto, ni kweli kabisa kiwanda hiki kimedhoofu na siyo Lushoto tu, viwanda vingi vimekufa sehemu mbalimbali. Mkakati wa Serikali uliopo ni kuhakikisha kwamba inatafuta wawekezaji binafsi ili waweze kujadiliana na wenye kiwanda hicho ili wawekezaji hao waweze kukiimarisha Kiwanda cha Lushoto na kianze kufanya kazi kama kawaida.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa hivi karibuni kulikuwa wawekezaji kutoka China ambao walitarajia kufika Mkoa wa Tabora tarehe 22 na safari yao kuahirishwa Air Port baada ya kuwa na dosari ndogo ndogo za visa. Je, ni lini sasa wawezekezaji hao ambao wataanzia kusimamia na kuangalia maeneo ya Kiwanda cha Tumbaku pamoja na Manonga safari yao itakamilika?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, kwa kuwa Kiwanda cha Nyuzi kina historia ndefu na mpaka sasa hivi ninavyosema kiwanda hicho hakifanyi kazi na wameondoa mitambo yote ambayo ilikuwepo pale. Je, Serikali iko tayari kufuatilia mitambo hiyo ambayo imeng‟olewa pale?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Kiwanda cha Manonga kwamba kulikuwa na Wachina wanakuja, wameishia Air Port kwa sababu ya masuala ya Immigration na mambo mengine, ni lini sasa watakuja. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kuwasiliana nao ili kuona lini watakuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la pili kuhusiana na Kiwanda cha Nyuzi kwamba Serikali iko tayari kufuatilia sasa kuhakikisha kwamba kinafanya kazi. Nimhakikishie kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Serikali iko tayari kufuatilia na kuhakikisha kwamba kinafanya kazi.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nina swali moja dogo tu la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vilivyobinafsishwa ni kikwazo cha maenedeleo katika maeneo mengi. Katika hotuba ya Mheshimiwa alisema kuna viwanda 34 ambavyo vilibinafsishwa na Serikali ina mkakati wa kuweza kuvifufua. Pia kwenye majibu yako Mheshimiwa Naibu Waziri umesema kwamba mnapitia upya mikataba. Je, katika mikataba hiyo, mna mkakati gani wa ziada kuhakikisha kwamba mikataba ya Viwanda vya Korosho vya Lindi na Mtwara ambavyo vilibinafsishwa na hadi leo kuna tatizo kubwa la kupatikana kwa maendeleo katika mikoa hiyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati ya ziada ambayo Serikali inaifanya, cha kwanza kabisa, viwanda vingi vilikufa kwenye miaka ya 1990 na 1998. Jambo la pili, viwanda vingi vilikufa kwa sababu ya kukosekana kwa malighafi au kuwepo kwa malighafi lakini kupungua kwa soko.
Mheshimiwa Naibu Spika, cha tatu ni Sera ya Ubinafsishaji. Sasa mikakati ya kikatiba, kisheria na kimkataba, kwanza ni kutazama sasa hali halisi ya soko la dunia lakini hali halisi ya viwanda vingine na ku-review mikataba hiyo ya kiuwekezaji. Hatua ya pili, ni kutazama sera yetu sasa ya uchumi ambapo tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda na kutazama sasa mikataba yetu iwe namna gani ili kuvifufua viwanda hivyo.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, pamoja na kazi nzuri aliyofanya katika Jimbo la Rorya, naomba tu nimuulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile ahadi ya Serikali kupitia REA III itakamilisha mradi kabambe wa kuweka umeme katika Jimbo la Rorya kuanzia tarehe 1 Julai, 2016. Je, Waziri anawahakikishiaje wananchi wa Rorya kwamba katika REA III, vijiji vyote vilivyobakia kupata umeme vitapata umeme huo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa vile Mpango wa REA III uko mpaka Jimbo la Busega na kuna Kituo cha Afya cha Lukungu pale Lamadi hakina umeme na kimeshapatiwa tayari vifaa kutoka Shirika la AMREF. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kunihakikishia kwamba kupitia REA III Kituo hiki cha Afya cha Lukungu na chenyewe kitapata umeme huo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chegeni aliyeuliza kwa niaba ya Mheshimiwa Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa REA II tunatarajia itakamilisha kazi zake mwisho wa Juni, 2016. Nichukue nafasi hii, siyo kwa Jimbo la Rorya tu lakini na kwa Wabunge wengine, nimhakikishie Mbunge wa Rorya kwamba vijiji vyote ambavyo vilikuwa katika REA Awamu ya II ambavyo havitakamilishwa, pamoja na kwamba tunataka vikamilishwe, vitaingizwa katika REA Awamu ya III. Ni mpago wa Serikali kwamba vijiji vyote hapa nchini ambavyo havijapata umeme katika REA Awamu ya II vitapatiwa umeme katika REA Awamu ya III inayoanza Julai, 2016. Nirekebishe kidogo swali la Mheshimiwa, amesema tarehe 1 Julai siyo kukamilisha, tarehe 1 Julai sasa ndiyo tunaanza REA Awamu ya III itakayoendelea kwa miaka mitatu, minne hadi mitano, ile Awamu ya II ndiyo itakamilika Juni, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusiana na Jimbo la Busega kupatiwa umeme wa uhakika REA Awamu ya III, ni kweli viko vijiji vya Mheshimiwa Mbunge wa Busega, Mheshimiwa Dkt. Chegeni ambavyo vilikuwa viunganishwe umeme kwenye REA Awamu ya II lakini havijapata umeme ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Lukungu katika Mji wa Lamadi. Tunatambua eneo la Lamadi ni eneo la kibiashara kwenye Jimbo la Mheshimiwa wa Busega, eneo hilo litapatiwa umeme pamoja na vituo vingine na Kituo cha Afya cha Lukungu kitapatiwa umeme kwenye REA Awamu ya III.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nimuulize Naibu Waziri swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa huu umeme wa REA wananchi wengi hawajapata elimu ya kusaidiana na Serikali katika kutoa maeneo ya kuweka huu umeme wa REA. Je, Serikali mna mpango gani kuhakikisha mnakwenda kijijini kutoa hii elimu ili wananchi watoe maeneo haya ya kupitisha umeme wa REA?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa REA wanavyofanya kazi, elimu inayotolewa inatolewa kwa kiwango kidogo. Nichukue nafasi hii kutamka rasmi kwamba kuanzia tarehe 1 Julai, wafanyakazi wote wa REA pamoja na TANESCO watakuwa sasa wanawafuata wateja badala ya wao kufuatwa, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili tunawaelekeza sasa kutoa elimu sahihi kwa ajili ya taratibu za uunganishaji umeme pamoja na ada zinazotakiwa kulipwa. Kwa sasa wananchi wataelimishwa kwamba hawatakiwi kuweka mchango wowote kwenye maombi ya umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, wananchi wataeleweshwa kuhusu gharama za service levy kwamba zimeondolewa, kwamba huduma ya kuhudumiwa umeme sasa imeondolewa. Kwa hiyo, jitihada za Serikali za kuhakikisha kwamba wananchi wanapata elimu zitaendelea. Zilikuwa zikifanyika lakini sasa tutaongeza nguvu zaidi kwa kuwafanya watumishi wa TANESCO na REA kufanya kazi kibiashara kwa kuwafuata wateja na kuwapa elimu badala ya wao kufuatwa.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa wakandarasi wa REA wanalalamika hawajalipwa pesa mpaka juzi na hili linaweza kuathiri uanzaji wa Awamu ya III kwa sababu shughuli ya Awamu ya II haijakamilika, Serikali inatoa kauli gani?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, labda nipate ufafanuzi vizuri, tunataka tuwatambue wakandarasi wote wanaolalamika kwamba hawajalipwa pesa ili tujue wanalalamikia nini, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini inawezekana kukawa na malalamiko kwamba baadhi ya wakandarasi hawajalipwa pesa lakini kwa takwimu tulizonazo wakandarasi kwa mara ya mwisho, miezi miwili iliyopita tumewalipa pesa kwa ajili ya kuanza kazi. Inawezekana kuna baadhi ya wakandarasi nao wanaweka pia subcontractors, inawezekana wanaolalamika ni wale subcontractors. Napenda nimhakikishie kwamba suala hili tutalifanyia kazi. Nimelichukua, nitakaa na Mheshimiwa Mbunge tuone ni mkandarasi gani analalamika tuanze kulifanyia kazi mara moja.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Nishati ya umeme ni nishati muhimu sana hasa kwa maendeleo ya elimu. Hivi sasa sekondari zetu nyingi za kata, hasa kwa mikoa ya pembezoni kama Manyara na kwingineko hakuna umeme kabisa. Je, ni kwa nini usambazaji huu wa umeme vijijini unaofanywa na REA usilenge kwanza sekondari hizi za kata ambazo zina hali mbaya na ambazo zinahitaji kuboreshwa kielimu na kuboreshewa mazingira ya kusoma?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumebaini kwamba taasisi nyingi za jamii kwenye kuunganishiwa umeme zimekuwa zikisahaulika. Hata hivyo, niseme kipaumbele cha REA Awamu ya II, kipaumbele cha REA Awamu ya III itakayaoanza vinalenga sanasana kwa kuanzia kuzipatia umeme taasisi za jamii zikiwemo shule, zahanati na taasisi nyingine, hilo ni la kwanza. Niombe sana Wabunge tushirikiane sasa na wataalam wetu wa REA na TANESCO huko vijijini kuwaelekeza wanapoanza kazi waanze na taasisi za jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe tu kuwaambia Waheshimiwa Wabunge, vipaumbele kwa kawaida kabla ya matumizi ya nyumbani tunaanza na taasisi za jamii. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tutatembea na wewe kama ambavyo huwa unatembea siku zote, tutembee kwa karibu ikiwezekana siku nzima Mheshimiwa Mbunge, tuongelee hospitali yako ambayo haijapata umeme tuipelekee umeme kwa haraka iwezekanavyo. Naomba uvumilie tukitoka hapa, Mheshimiwa Naibu Spika naomba unipe fursa ya kukaa na Mheshimiwa Mbunge, tukitafakari namna ya kupeleka umeme kwenye maeneo aliyozungumzia.
MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa yapo mazungumzo yanayoendelea kwa ajili ya ujirani mwema kati ya mgodi na vijiji vinavyozunguka ikiwemo Kijiji cha Bugarama na kwa kuwa kijiji hiki kina shida ya maji na wana mpango wa kupata maji kupitia mgodi huu. Je, Serikali iko tayari kuratibu mazungumzao haya?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri kwamba Mgodi wa Bulyankulu umekuwa ukitoa pia huduma za jamii katika maeneo ya Ilogi, Kakora, Runguya na maeneo mengine lakini hivi karibuni mgodi umekuwa ukifanya mazungumzo na vijiji vya jirani na tumekuwa tukiendelea kuratibu shughuli za migodi pamoja na wananchi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko tayari, itaendelea kuratibu mazungumzo mpaka suluhisho la wananchi kunufaika na mgodi huo zipatikane kama kawaida.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Mkoa wa Mbeya umebarikiwa sana kuwa na madini pamoja na vyanzo mbalimbali vya umeme. Nataka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa mfano, kuna vyanzo vya umeme vya jotoardhi kule Busokelo lakini pamoja na Lake Ngozi, kuna makaa ya mawe, kuna maporomoko ya maji na vitu vingine katika sehemu nyingine mbalimbali. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini vyanzo hivi vitaanza kufanya kazi ili wananchi wa Mbeya na Tanzania kwa ujumla ipate umeme wa kutosha?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa, kati ya mikoa hapa nchini iliyojaliwa kwa kuwa na rasilimali za madini pamoja na maporomoko ya maji ni pamoja na Mkoa wa Mbeya na hasa Mbeya Vijijini. Nikubaliane naye, kwa sasa Wizara yetu inafanya utafiti na inakamilisha utafiti wa jotoardhi (geothermal) ambapo sasa tumegundua madini hayo yatakuwa na megawati 20 kwa kuanzia lakini baadaye tutakwenda hadi megawati 100, hiyo ni kwa jotoardhi. Bado tunafanya upembuzi yakinifu katika makaa ya mawe pamoja na maporomoko ya maji katika mito hiyo na hasa katika Mto Ngozi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hatua tunazochukua ni kukamilisha utafiti huo yakinifu na kadri itakavyowezekana tukipata fedha, shughuli ya kutekeleza miradi hiyo itaanza. Mradi wa geothermal unaanza kutekelezwa mwezi Julai, 2017.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda Waziri atuambie, kwa migodi kama ya Kiwira ambayo tayari inazalisha, je, tunapata kiasi gani kama Halmashauri?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nifanye masahisho kidogo, Mgodi wa Kiwira haujaanza kazi rasmi, uko katika kukamilisha detailed design na hatua za kumpata mkandarasi kwa ajili ya kuanza ujenzi. Hata hivyo, mgodi huo utakapoanza, Halmashauri zote zinazohusika zitanufaika na mambo yafuatayo. La kwanza, Halmashauri zitakuwa na uwezo wa kukusanya service levy ambayo ni asilimia 0.3. Kadhalika zitaweza kupata mrabaha ambao utaingia Serikali kuu. Pia, mradi wa Kiwira unakadiriwa kuajiri wafanyakazi zaidi ya 1,000 utakapoanza kufanya kazi. Kwa hiyo, wananchi wa Mbeya na Watanzania wengine wataendelea kunufaika na kupata ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, kadhalika mradi huo utakuwa sasa na kipengele kinachowalazimisha wakandarasi na wamiliki wa migodi kuanza kuwashirikisha Watanzania kwa kununua bidhaa zao pamoja na huduma za jamii ili huduma za jamii zianzie maeneo yanayozunguka mgodi huo. Kwa hiyo, napenda niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge Mradi wa Kiwira utakuwa na manufaa makubwa sana kwa Taifa lakini pia kwa wananchi wanaozunguka mgodi huo.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri swali dogo. Kwa sababu Mkalama kuna wachimbaji wadogo wadogo wa madini ya shaba, ni lini Wizara itawasaidia wachimbaji wadogowadogo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba eneo la Mkalama lina madini na siyo shaba tu, yapo madini ya shaba, madini ya ujenzi na madini mengine ya viwandani. Huduma ambazo zitatolewa na Serikali kwa wachimbaji wadogo ni kote nchini ikiwemo pia wachimbaji wadogowadogo wa Mkalama, ni kama ifuatavyo. Hatua ya kwanza kama tulivyosema kwenye bajeti yetu, Waheshimiwa Wabunge niwapongeze sana kwa sababu mmepitisha shilingi bilioni 6.68 kwa ajili ya ruzuku ya wachimbaji wadogo wadogo na ruzuku hiyo itatumika pia kwa wananchi wa Mkalama Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini manufaa mengine ambayo pia Serikali imejizatiti ni pamoja na kuyafanyia utafiti maeneo yote. Sasa hivi Wakala wa Jiolojia Tanzania anapita maeneo yote na kuyafanyia utafiti ili kubaini maeneo ambayo yanaweza kuchimbwa na wachimbaji wadogo kwa tija. Jambo lingine tunalofanya kama Serikali kusaidiwa wachimbaji wadogowadogo ni pamoja na kutoa elimu wezeshi na ushauri kwa ajili ya kuufanya uchimbaji mdogo uwe wa tija zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi tumesogeza sasa huduma zote za ugani huko wachimbaji wadogo waliko. Tumefungua ofisi za madini karibu kila mkoa ili kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata ushauri nasaha kwa masuala ya afya migodini pamoja na mazingira. Kwa hiyo, huduma za wafanyakazi, huduma za wachimbaji wadogo, zitaendelea kama kawaida na kama ambavyo nimeeleza.
MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ninaomba nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika REA Second Phase ambayo ilikuwa inaendelea ni robo tu ya vijiji vya Jimbo la Geita na Geita Mjini ambavyo vimepata umeme, vijiji kama Nyawilimilwa, Kagu, Senga, Bulela bado havijafikiwa; naomba kujua ananipa uhakika gani kwamba Vijiji hivi ambavyo bado havijapata umeme vitapata umeme kwenye Awamu ya Tatu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Mji wa Geita tumekuwa na tatizo la umeme kukatika katika kila siku kutokana na umeme mdogo ambao tunatoka Mwanza. Hata mji wenyewe wa Geita pale Mjini umeme unakuta upo lakini sehemu nyingine hauwaki. Ni lini Mheshimiwa Waziri atahakikisha Geita inapata umeme wa uhakika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza kuhusu kujumuisha vijiji vya Nyawilie na Bulila nimhakikishie kwamba vijiji hivyo vyote vitaingia kwenye REA Awamu ya Tatu inayoanza Julai mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kukatika katika kwa umeme nichukue fursa hii kuwataarifu kwamba ni kweli kabisa karibu nchi nzima siyo Geita tu umeme bado unakatika katika na suluhisho la kukatika kwa umeme kama tulivyosema miji ya Geita na maeneo ya Kanda ya Ziwa pamoja na maeneo mengine, itapata sasa umeme wenye kilovoti 400 unaotoka North West Grid unaotoka Mbeya unaopita Sumbawanga, unaopita Mpanda, unaokuja Kigoma unakwenda mpaka Nyakanazi na baadaye Geita na umeme huo utatoka Geita kwenda Bulyanhulu na utatoka Bulyanhulu kwenda maeneo ya Biharamulo. Umeme huu utakuwa na nguvu kubwa ya kilovolt 400 na unatembezwa kwa takribani ya kilometa 1148.
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu linafanana sana na swali la muuliza swali Mbunge wa Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua jitihada ambazo zilifanywa na Serikali hapo nyuma kwa baadhi ya maeneo na vijiji kupata umeme kupitia Wakala wa Umeme vijijini kwa maana ya REA, lakini pia tunatambua mapungufu makubwa ambayo yameonekana kwenye miradi hii. Vipo baadhi ya vijiji ambavyo wananchi walipitiwa, ramani ikapitishwa, Serikali ikawaagiza wakakata mazao yao, wakakata kahawa…
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Wakachimba mashimo na mashimo yakachimbwa na Serikali kupitia Wakandarasi waliopewa kazi kwa ajili ya kuwapa umeme, lakini badala yake Wakandarasi wameondoka watu hawajapata umeme, mashimo yamebaki, mazao yao yameanguka, ng‟ombe wanaanguka kwenye mashimo. Sasa ningetaka kauli ya Serikali kwamba ni kwa nini unamnawisha mtu unamuweka mezani halafu kama huwezi kumpa chakula, kwa hivyo ni lini wananchi hawa ambao tayari ramani zimeshapita kwao na mashimo yakachimbwa halafu yakaachwa na mazao yao yakakatwa, ni lini wanakwenda kufungiwa umeme? Vijiji hivyo ikiwa ni pamoja na Mulala, Kilinga pamoja na baadhi ya maeneo mengine?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kuna maeneo mengine mkandarasi ameendelea kuchimba mashimo na kuweka nguzo.
Sasa ni lini maeneo haya yatapatiwa umeme, jibu la uhakika kabisa ambapo Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tukiwaambia kwamba REA Awamu ya Tatu inakuja kusambaza umeme kwenye vijiji vyote, REA Awamu ya Tatu inaanza mwezi Julai baada ya bajeti yetu kupita mwaka huu. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge ni kuanzia mwezi Julai miezi inayofuata maeneo yenye mashimo yatapatiwa umeme kuanzia mwezi wa saba mwaka huu mara baada ya bajeti yetu kupita.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa dhumuni la REA Phase One ilikuwa ni kupekeka umeme kwenye kila makao makuu ya kata na kwa kuwa Kata ya Hemtoye, Mbaramo, Mbaru pamoja na kata ya Shagayu bado hazina umeme.
Je, ni lini Serikali itapelekea umeme katika maeneo hayo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda nisahihishe kidogo, siyo kweli kama Phase One ya REA ilikuwa inapeleka kata zote ni Kata chache. REA II pia ilichagua Mikoa na Kata na maeneo ya kati. Jibu la uhakika sasa kama alivyosema ni lini sasa atapewa, REA ya Awamu ya Tatu inayoanza mwezi wa saba ndiyo itakayopeleka umeme kwenye Vijiji vyote pamoja na vya Mheshimiwa Mbunge ambavyo havijapata umeme hadi sasa.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana.
Kwa kuwa, ni makosa ya uchapaji nashukuru amekiri kuwa Kata hii ya Qurus ipo na kwamba Kijiji hiki cha Gongali ndiko ofisi ya TANESCO ilipo. Sasa
kuna Vijiji ambavyo amevitaja hapa katika swali la msingi ambavyo vinaitwa Gendaa na Bashay;
Je, ni lini vitapata umeme?
Pia, kwa kuwa Wilaya hii ya Karatu ni pacha kabisa na jimbo la Mbulu Vijijini; Je, Vijiji vya Mbulu Vijiji ambavyo vinafanana kabisa kwa majina haya ya Gendaa ambavyo viko Mbulu Vijijini na Bashay ambavyo viko Mbulu Vijijini na Vijiji vingine vya Endara Gadati na Vijiji na Haidereri, Kantananati, Bashay, Yaeda Ampa lini vitapatiwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa katika Jimbo la Karatu ni vijiji vichache vimepata umeme. Lakini nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge anayeuliza swali kwa niaba ya Mheshimiwa Mbunge ambaye hayupo ni kwamba, vijiji vingi sana mbali na alivyovijata vya Qorong‟aida na vingine, ikiwemo na kijiji cha Changarawe kitapata umeme kule kwa Mheshimiwa wa Karatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengine kijiji cha Kambi ya Faru kitapata umeme kijiji cha Udongo Mwekundu kitapata umeme, pamoja na Vijiji vingine vya Rositeti vitapata umeme, hilo ni katika Jimbo la Karatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo lake Mheshimiwa Mbunge alivyouliza vijiji vya Mbulu ametaja Qorong‟aida, ametaja na vingine. Lakini kuna vijiji vingi ambavyo hajavitaja ni jumla ya vijiji 73 kwenye Jimbo la Mheshimiwa Mbunge havijapata umeme. Ninamshukuru sana anavyoendelea kuwahangaikia wananchi wa Mbulu, nimhakikishie tu ametaja vijiji vinne lakini bado kuna vijiji vingi ambavyo bado havijapata umeme kwenye Jimbo lako. Nikivitaja vitano tu kati ya vile 78 ambavyo havijapata ni pamoja na Masiedo haina umeme, Labei haina umeme, Mangandi haina umeme, vijiji vyote hivi vitapata umeme kwenye REA awamu ya tatu.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kutuhakikishia kuwa Karatu watapata umeme, maana Karatu ni katika Mkoa wangu. Vilevile katika Mkoa wa Arusha kuna maeneo mengi sana wana tatizo la umeme. Mfano wa Arumeru wananchi walitoa mashamba yao, wakachimba mashimo kwa ajili ya umeme wa REA, lakini mpaka sasa hivi wananchi wale wa Arumeru hawajapata umeme. Kuna malalamiko kuwa pesa zinazopangwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo hazifiki na hata zikifika hazifiki zote.
Je, Serikali itatatua vipi tatizo hilo la umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikubaliane na Mheshimiwa Katherine na nimpongeze sana, amehangaika sana hata kwenye ununuzi wa transformer tumeamua tununue hapa ndani kwa sababu ya juhudi zake, nakupongeza Mheshimiwa Catherine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kumuhakikishia tu wananchi wa Arusha watapata umeme, ni kweli kuna matatizo ya umeme Arumeru na kuna vijiji vingi sana kama vya Urojora pamoja na vingine havijapata umeme naelewa. Lakini kumhakikishia Mheshimiwa Magige kwenye Jimbo lote tumetenga bilioni 13.7 kwa ajili ya wananchi wa Arusha. Ili kuhakikisha kwamba, REA awamu III matatizo yote yanaisha. Sambamba na hilo yapo matatizo ya umeme hasa kwenye eneo la Arusha la kukatika katika kwa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu nilishazitaja lakini nidokeze tu, kwa sasa hivi Serikali kupitia TANESCO pamoja na wakandarasi tunaboresha sasa miundombinu ya umeme. Kuanzia leo, tumesema tatizo la low voltage tunakwenda kulikamilisha kwa sababu sasa tunasafirisha nguvu kubwa, tunasafirisha nguvu kubwa yenye kilovoti 400 kwa upande wa Arusha kutoka Dar es Salaam kupitia Chalinze kwenda Bagamoyo, kwenda Arusha mpaka Namanga, kilomita 664.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa upande ule tatizo la kukatika kwa umeme litakwisha kabisa, lakini juhudi nyingine pamoja tumeamua sasa kukatika kwa umeme kuna sababisha pia uharibifu wa transfomer na hii inasababisha wakati mwingine na utaratibu wa kununua transfomer kutoka nje. Sasa hivi kama mlivyokwisha kusikia tumetangaza na naendelea kusema tena, awamu inayokuja sasa na transfomer tutakuwa tumenunua hapa nchini kwa sababu TANALEC wana uwezo wa kutengeneza.
Mheshimiwa Naibu Spika, juhudi nyingine za kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme wakati mwingine ni matatizo ya nguzo. Sasa hivi TANESCO imeunda kampuni tanzu ambayo itakuwa inatengeneza concrete pole kwa ajili ya kutengeneza nguzo hizo hapa nchini. Hivyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi kwamba, sasa tatizo la umeme litakwisha mara moja.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona na kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Njombe Mjini halimo kwenye mpango wa REA limo kwenye mpango wa umeme unaoenda Songea, hiyo kazi hiyo haijaanza.
Je, ni lini kazi hiyo itaanza ili kusudi wananchi wa Njombe na wenyewe waweze kunufaika na umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa wananchi wa Njombe siyo kwamba hawatapata umeme wa REA wataendelea kupata umeme wa REA kama kawaida, lakini chanzo cha umeme kwa wananchi wa Njombe, Ludewa, Songea Mjini, Songea Vijijini, Namtumbo ni pamoja na ule umeme wa Makambako - Songea ambao ni wa Kilovoti 220.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kweli kwamba Mheshimiwa Mbunge, nakushukuru kwamba kwa sababu hujaona chini, watu nguzo wanaweka chini lakini kazi imeshaanza. Kazi za awali za upembuzi yakinifu zimekamilika na taratibu za Mkandarasi za kuanza kazi zimekamilika, kufikia Januari mwaka unaokuja kazi rasmi za kutifua na kuweka nguzo zitakuwa zimeshaanza kabisa.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza la nyongeza. Maeneo ya Kibiti, Ikwiriri, Bungu kumekuwa na tatizo la umeme kukatikakatika.
Je, lini Serikali itamaliza tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokwishakueleza kwenye jibu langu la msingi na maelezo mengine ya nyongeza. Ni kweli kuna maeneo mengi ambayo bado umeme unakatika katika na sababu za kukatika nimezieleza. Lakini niseme tu, taratibu za kukamilika kwa kukatikakatika pamoja na matatizo mengine ya umeme tutakapokamilisha kusambaza hizi nguvu kubwa za kilovolt 400 na kilovolt 220 ambapo kazi rasmi itakamilika 2018/2019, kwa hiyo kuanzia wakati huo, maeneo ya Kibiti, maeneo ya Ikwiriri na maeneo mengine ya kule chini, tatizo la kukatika katika kwa umeme litakwisha kabisa.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Ni kweli kwamba Serikali imeweza kujibu kwamba itawapa maeneo wachimbaji wadogo katika maeneo hayo, lakini imekuwa ni ahadi ya muda mrefu sana hasa katika eneo la Nyarugusu maeneo ya STAMICO, kila wakati Serikali imekuwa ikiahidi kwamba itawapatia maeneo na wananchi wanahitaji kujua kwamba ni lini sasa Serikali itawapatia maeneo haya ya wachimbaji wadogo hasa maeneo ya Nyarugusu? (Makofi)
Swali la pili, mwaka 2015 Serikali ilizindua mradi mkubwa sana wa wachimbaji wadogo pale Rwamgasa na tuliuzindua mradi huu kwa vigelele na shangwe, lakini sasa hakuna kinachoendelea mpaka sasa. Ni mradi wa World Bank! Napenda kujua, ni lini sasa mradi huu utaanza rasmi ili wachimbaji wadogo waweze kunufaika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Serikali imekuwa ikikusudia kuwatengea maeneo wananchi, hasa wa eneo la Mheshimiwa Bukwimba. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Bukwimba, amekuwa akifuatilia sana maeneo ya wachimbaji wadogo katika eneo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimkumbushe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, mwaka 2015 kwa juhudi zake ambazo aliomba wananchi wachimbiwe maeneo, walitengewa maeneo 95, eneo la Rwanyamgaza. Kadhalika, maeneo ya Kaseme, walitengewa maeneo 43.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba tu Mheshimiwa Bukwimba awahamasishe wananchi, kwa sababu kati ya maeneo 95 aliyotengewa, ni maeneo 25 tu kule Rwanyamgaza yanafanya kazi; na kati ya maeneo 43 kule Kaseme ni maeneo 17. Hata hivyo Mheshimiwa Bukwimba kwa juhudi zako bado tunakutengea maeneo mengine ambayo yanaachiwa wazi na wananchi hasa eneo la Buziba. Buckreef itaachia hekta 200, lakini bado Kampuni ya ARL itaachia hekta 100; bado Kampuni ya Bismak itaachia hekta 120, lakini na Ernest Masawe ataachia hekta 90, hiyo ni kwa ajili ya wananchi wako Mheshimiwa Bukwimba. Kwa hiyo, bado tunakutengea maeneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini sasa? Mwezi wa Kumi tunaanza kutenga maeneo rasmi. Hii ni kwa nchi nzima ikiwemo eneo la Igunga kule Iborogero, maeneo ya Kibao kwa Mfipa, maeneo ya kule Mkuranga kwa ajili ya Waziwazi lakini na maeneo mengine ya Busiri, pamoja na Londani Sambalu kule Singida kwa Waheshimiwa Wabunge. Kwa hiyo, bado tunaendelea kutenga maeneo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala lake la pili ni kwamba Kituo cha Kuchenjua Madini kwa ajili ya wachimbaji wadogo, kimechukua muda mrefu. Mheshimiwa Bukwimba nakupongeza sana, tuna kituo kimoja tu cha mfano cha kuchenjua madini hapa nchini na ndiyo kituo cha Rwamgasa ambao Mheshimiwa Bukwimba, mwaka 2015 na mwaka 2014 ulihangaika sana. Mheshimiwa Bukwimba nakupongeza sana, utakuwa ni Mbunge wa mfano kwa sababu ndiyo eneo tunalofungua Kituo cha Kuchenjua cha Mfano hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini kinakamilika sasa? Leo tumefungua tenda kwa ajili ya kumpata mjenzi na kazi ya kujenga itaanza mwezi Septemba mwaka huu na mradi ule utakamilika mwezi Mei mwakani. Gharama yake ni hela nyingi kidogo, ni Dola 800,000, tutazitenga ili kituo hiki kianze kufanya kazi. Pia nawapongeze mgodi wa GGM nao wanachangia Dola 200,000. Kwa hiyo, kituo hiki kitaanza kufanya kazi lakini mantiki ya kituo hiki kitasaidia sana wachimbaji wadogo kujua thamani sasa ya dhahabu wanayochimba hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawahamasisha wananchi wote ambako madini yanachimbwa sasa wote tupeleke kwenye eneo hili la Rwamgasa ambacho Mheshimiwa Bukwimba amekifungua ili wananchi wetu sasa wanufaike na rasilimali yetu ya dhahabu.
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Naitwa Ikupa Alex, samahani. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, wachimbaji hawa wadogo nchini ni muda mrefu sasa wamekuwa wakikumbwa na migogoro ya mara kwa mara na wachimbaji wakubwa hasa kule Mererani. Je, Serikali ina mpango ama mkakati gani wa kuhakikisha kwamba inatatua migogoro hii na kuhakikisha kwamba haijirudii tena?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa wachimbaji wadogo wadogo na siyo Mererani peke yake ni kote nchini, wamekuwa wakikumbwa na migogoro hasa kati yao na wawekezaji wakubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mererani, kwanza kabisa kuna migogoro ya aina mbili; iko migogoro ya wao kutoboza chini kwa chini kuingia kwenye mgodi wa Tanzanite One ambao ni mgodi mkubwa kwa ajili ya kuchukua kidogo Tanzanite. Huo mgogoro tunashughulika nao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia wachimbaji wa Mererani wana maeneo madogo, lakini hatua tuliyofikia sasa ni kuwatafutia maeneo wananchi wa Mererani ili wachimbe karibu na eneo la mgodi ule kwa sababu na kwenye kuna Tanzanite ya kutosha. Hiyo ni hatua ya pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya tatu, mgogoro ambao sana sana ni wa kiufanyakazi, ni mgogoro kati yao na waajiri wao. Mgogoro huu tunawasiliana kwa ukaribu sana na Wizara ya Kazi. Mwezi uliopita tulikaa kama Kamati na kusuluhisha mgogoro huo. Kwa sasa tunaamini kwamba wananchi wa Mererani kwa sababu watapata maeneo yao na taratibu za ajira zitazingatiwa. Kwa hiyo, matatizo sasa ya mgogoro kati yao na wachimbaji wakubwa zinakoma mara moja.
MHE. CONSTATINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Wakati wa kampeni tulihamasisha sana vijana kujiunga kwenye SACCOS ili baadaye waweze kupatiwa maeneo ya uchimbaji wa madini. Nataka kufahamu Mheshimiwa Naibu Waziri anawaahidi nini vijana waliolundikana kwenye maeneo ya Samina, Mgusu, Nyakabale kwamba watapata lini maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa wananchi wa Kasema, Wanela pamoja na eneo la Geita Mjini, lakini siyo Geita Mjini tu, Nyakabale na maeneo mengine wanahitaji maeneo. Namhakikishie Mheshimwia Constantine kwamba mwaka huu tumetenga hekta 12,000 na kati ya hizo, hekta 2,000 ni maeneo ya Geita kwa hiyo wananchi wa Nyakabale, wananchi wengine wa Mtakuja na wengine ambao walikosa mgao wa Geita watapata maeneo ya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, kwa Mkoa wa Geita, mwaka 2015 na mwaka 2014, kuna SACCOS sita zilizoundwa. SACCOS mojawapo ambayo haijapata eneo la uchimbaji, ni pamoja na wakeretwa wa SACCOS ambayo ilipata lesseni tano; lakini Tupendane SACCOS walipata ekari sita pamoja na Tunakuja SACCOS walipata ekari nane; Ujamaa SACCOS kwa sababu zote zinatoka Geita walipata ekari tisa, pamoja na Mapinduzi SACCOS Kwa hiyo, wananchi wote wa Geita tunaomba wajiunge na SACCOS ili kusudi tuendelee kuwagawia maeneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Constantine sana kwamba, ningependa sana waanze kuziunda SACCOS sasa hivi, kwa sababu utaratibu sasa wa kuwatengea maeneo unaanza mwezi wa Kumi mwaka huu. Kwa hiyo, tunaomba sana SACCOS zote na siyo kwa Geita tu, ziwe tayari ili kuanzia mwezi wa Kumi waanze kugawiwa pesa. Hata hivyo, tumewatengea ruzuku sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge walipitisha shilingi bilioni 6.68 kwa ajili ya ruzuku ya wachimbaji wadogo. Kwa hiyo, pamoja na kuundwa SACCOS, lakini pia tutawagawia ruzuku kwa ajili ya kuendeleza uchimbaji wao.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Mheshimiwa Rais alipokuja mwaka 2015 kwenye mikutano yake ya kampeni katika Jimbo la Nyang‟hwale, aliweza kuwaahidi wachimbaji wadogo wa Jimbo hilo kwamba eneo la Kasubuya litapimwa na kugawiwa wachimbaji wadogo wadogo. Je, Serikali inasemaje kwa hili kwa wachimbaji wadogo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kati ya maeneo 12 tuliyotenga kwenye Mkoa wa Geita pamoja na maeneo mengine ya Kahama ni pamoja na eneo la Kasubuya. Eneo la Kasubuya tumetenga hekta 4,098.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Hussein, wananchi wa Nyang‟hwale tayari wana eneo. Isipokuwa nawaomba sana, hata wakishindwa kupata maeneo pale Kasubuya, tunatenga maeneo mengine. Kule Chato kuna hekta 1,282. Kwa hiyo, wananchi wako bado wanaweza kwenda kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maeneo yale, maeneo ya kwa Mheshimiwa wa Mbunge wa Bukombe tuna hekta 682, wanaweza wakaenda kuchimba Bukombe. Kwa hiyo, tunaendelea kutenga maeneo ili wananchi wa Kasubuya na maeneo mengine wapate maeneo ya kutosha.
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nitakuwa na maswali mawili madogo ya nyongeza.
Moja, kwa vile Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza kwamba kila mteja katika kila ngazi anabeba gharama zake. Je, Naibu Waziri atakubaliana nami kwamba bei ambayo inatozwa Shirika la Umeme la Zanzibar yaani ZECO, ambaye ni mteja wa jumla (bulk purchaser) kwa unity moja ya KVA ambayo ni shilingi 16,550/= ambayo ni bei kubwa kuliko wale wateja wa reja reja wa ngazi ya kati na ngazi ya chini kuwa hii bei siyo stahiki kutozwa ZECO. Je, lini Serikali itaitaka EWURA sasa kufanya maboresho ya bei hii na kuitoza ZECO bei stahiki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Jamali kwa kutukumbusha kwamba gharama za umeme zinatakiwa zishuke. Nimhakikishie tu kwamba kuanzia mwezi wa Nne tulipofanya marekebisho ya bei watumiaji wakubwa kabisa wakiwemo ZECO tuliwapunguzia kwa asilimia 2.4, ilikuwa ni punguzo kubwa kweli kweli ukilinganisha na wateja wengine wadogo wadogo. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Jamal kwamba bei za gharama kama nilivyosema, zinategemea hasa mambo mawili:-
Jambo la kwanza ni vyanzo vya kuzalisha umeme. Vyanzo vinapokuwa vya bei nafuu na bei ya umeme inapungua. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Jamal kwamba ni kweli kabisa kwa unity moja kwa sasa kwa watumiaji wakubwa ni shilingi 16 na 55 unit, lakini zitaendelea kupungua kulingana na gharama ya uzalishaji wa umeme unavyoshuka. Kwa hiyo, Mheshimiwa Jamal nakuhakikishia tutaendelea kulifanyia kazi na EWURA bado wanaendelea na mchakato wa ku-review bei kulingana na gharama za umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ni lini sasa EWURA watafanya marekebisho hayo? Kwa sasa hivi tunazalisha umeme mwingi sana wa kutumia gesi na kwa kiasi kingine kikubwa kwa kutumia maji. Tumeeleza sana vyanzo vya gesi na jinsi ambavyo bei inaendelea kupungua. Kwa sasa hivi atupe muda tuendelee kuzalisha kwa vile ambavyo mmetupa bajeti, siyo muda mrefu, EWURA tena wataingia uwanjani kuanza ku-review bei. Kwa hiyo, Mheshimiwa Jamal nikuhakikishie kwamba bei itaendelea kuangaliwa wakati hadi wakati.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa Naibu Waziri. Kwa kuwa tatizo la umeme lililopo Zanzibar linafanana sana na tatizo la umeme lililopo Igunga, sasa kwa sababu Naibu Waziri anatambua vizuri sana: Je, nini kauli ya Serikali juu malipo ya fidia kwa Kata za Chabutwa, Simbo pamoja na Mwisi ili waweze hasa kujua watapata lini hiyo fidia yao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Niabu Spika, kwanza namshukuru Mheshimiwa Gulamali, jana na juzi tumehangaikia sana suala la fidia ya wananchi wako. Kama ambavyo tumelifikisha, kwanza nikupongeze. Sasa hivi mthamini wa ardhi wa Mkoa anapitia viwango vya fidia vya wananchi wa Manonga na hasa katika vijiji vya Chabutwa Simbo na maeneo ya jirani ambapo umetaja, ni kweli kabisa kuna wananchi 722 ambao hawajafidiwa na malipo hayo yako katika hatua za mwisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba jana wakati tunapitia, tulipoongea na Mkuu wa Mkoa wa Tabora nadhani alikwambia kwamba kabla ya mwezi ujao na miezi miwili ijayo wananchi wako watalipwa fidia. Kwa hiyo, nakuomba sana wafikishie taarifa waendelee kuwa na subira jambo la fidia yao linafanyiwa kazi.
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusiana na bei ya umeme bado Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) halijapunguza bei ya umeme kitu ambacho kinawanyima fursa wananchi wa Zanzibar kuweza kutumia nishati hii au rasilimali hii kwa ukubwa zaidi kuliko hali inavyokuweko sasa hivi. Kwa sababu wengine wanashindwa kuunga umeme kutokana na hali ya bei. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweza kukaa na ZECO ili kuona na kwamba na wao viwango vile vinaweza kupungua na kuwanufaisha wananchi wote kwa bei ya chini zaidi kama ilivyokuwa huku Tanzania Bara.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kule ZECO kama ambavyo mnajua, wanajua umeme wa jumla na kwa vile wananunua umeme wa jumla, siyo rahisi sana wakaona punguzo la bei ya umeme. Hata hivyo, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko tayari kukaa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na ZECO, TANESCO na EWURA ili kuona ni jinsi gani sasa gharama za umeme zinaweza kupitiwa upya. Nitoe tu angalizo, gharama za umeme zinazingatia sasa vyanzo vyetu pamoja na gharama nyingine za uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iko tayari, tutakaa pamoja na wewe pamoja na EWURA ili pia kuangalia upya bei za umeme huko Zanzibar.
MHE. JORAM ISMAEL HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuliza swali la nyongeza. Katika Jimbo la Lupembe, Kata ya Kidegembye tuna tatizo kubwa sana la umeme hasa tatizo la low voltage. Transformer iliyopo pale haiwezi kuzalisha umeme wa kutosha na hivyo kutoweza kusambaza umeme sehemu nyingi na wananchi wa pale hawawezi kufanya shughuli za kiuchumi kama vile welding na shughuli nyingine za kusaga nafaka. Je, ni nini kauli ya Serikali kutatua tatizo hili? Maana nimewaona watu wa TANESCO muda mrefu lakini mpaka leo hii tatizo hilo bado lipo.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kama mlivyoona katika maeneo mengi, sasa hivi bado tunaendelea na harakati ya kusafirisha umeme wa msongo mkubwa wa Kilovolt 400.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, Wizara yetu ina jumla ya miradi 42 sasa. Kati ya miradi 42, miradi 16 ni kwa ajili ya uzalishaji umeme wa gesi pamoja na usambazji wake; lakini miradi 11 ni kwa ajili ya miradi ya maji na kusambaza umeme wa maji. Miradi mingine minane ni kwa ajili ya vyanzo vingine na miradi saba ni rasmi kwa ajili ya usambazaji umeme mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukisema sana kwamba kuanzia sasa Wakandarasi wako site na kazi kubwa hasa maeneo ya Iringa, Njombe Dodoma, Sumbawanga na mengine, tunaanza sasa mradi wa kusafirisha umeme wa Kilovolt 400. Kazi ya mradi huu kuongeza nguvu kubwa ili umeme sasa usiwe unakatikakatika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa sasa hivi tunatumia umeme wa low voltage, lakini tutakapokamilisha miradi hii mwaka 2018/2019 low voltage sasa itakuwa imekwisha kwa sababu itakuwa na umeme mkubwa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge wa Njombe pamoja na maeneo ya Lupembe na mengine ni kuhakikishie kwamba taratibu wa umeme kukatika zinachangiwa pia sasa na low voltage lakini kwa sababu tuna umeme mkubwa gharama hizo pia zitashuka lakini na umeme utakuwa haukatiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, kama nilivyosema, maeneo mengine umeme unakatika siyo kwa sababu ya low voltage tu, ni kwa sababu ya miundombinu kuwa mibovu. Sehemu ya miundombinu ni pamoja na transformer.
Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge, mmepitisha Sheria ya Manunuzi na tumeshasema, kuanzia sasa transformer tutakuwa tunanunua hapa nchini kwa sababu shirika letu na kampuni yetu ya TANELEC sasa itakuwa na uwezo wa kutosha wa kutengeneza transformer na Serikali itanunua, kwa hiyo, matatizo ya transformer yatarekebika na kupunguza kabisa tatizo la kukatika kwa umeme.
MHE. ISSA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na ninashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Swali la kwanza, maeneo haya ambayo yanachimbwa madini yako mbali na makazi ya watu mfano Kimbiji na Chamazi, lakini Serikali imezuia. Je, umbali upi unaotakiwa kiasi kwamba mkafikia kufunga yale machimbo ya maeneo yale?
Swali la pili, madini haya sasa hivi yanatoka katika Mkoa wa Pwani hasa Wilaya ya Mkuranga. Je, kuna tathmini gani mmefanya kwamba machimbo haya sasa hivi hayataleta athari katika maeneo mliyoyapeleka?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa maeneo ya Kigamboni kwa sasa yana madini aina ya ujenzi na hasa ya changarawe pamoja na kokoto. Maeneo yanayochimbwa kwa Kigamboni hasa hasa ni maeneo ya Mjimwema pamoja na Kijisu. Hata hivyo, eneo alilotaja la Kimbiji pamoja na Chamazi ni kweli kabisa kuna wachimbaji wadogo wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba siyo kweli kwamba tumesimamisha au tumefunga eneo la Kigamboni. Tulipofunga ni eneo la Kunduchi ambapo sasa wachimbaji tena ambao walikuwa kidogo ni haramu wanachimba kuelekea upande wa barabara. Kwa hiyo, pale Kunduchi tulisimamisha tena miaka minne iliyopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimtahadharishe tu Mheshimiwa Mbunge kama nilivyosema, lakini namshukuru kwa kuwaulizia wananchi wa Kigamboni. Taratibu za Sheria ya Madini zinataka uache umbali wa mita 200 kutoka makazi, lakini kadhalika zinataka uache umbali wa mita 100 kutoka vyanzo vya ziwa au bahari kama ferry ya Kigamboni ilivyo na inataka uache umbali wa mita 100 kutoka umbali ambako sasa kiwanja cha ndege kitajengwa au city itajengwa. Sasa kwa Kigamboni kuna eneo kubwa ambalo limeainishwa kwa ajili ya satellite city. Eneo lile tumezingatia Sheria ya Madini kuacha umbali wa mita 100 usiopungua 100 hadi 200.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba taratibu sasa kule kigamboni tunatenga eneo rasmi la Mjimwema pamoja na maeneo ya Mkuranga aliyosema ya Visiwasiwa, pamoja na maeneo mengine ya kule Kibaha kwa Mathias na kwa Mfipa. Maeneo hayo tunayatenga kwa ajili ya wananchi wa Dar es Salaam ili wapate maeneo rasmi sasa ya kuchimba madini ya mchanga kwa ajili ya shughuli za ujenzi.
Kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Mbunge, tutakaa pamoja na utendaji wako ili tubainishe maeneo ambayo tutachimba kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa Kigamboni.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimwulize Mheshimiwa Waziri, kwa sababu Wakala wa Madini (TMAA) wanafanya kazi nzuri sana. Mwaka 2010 na mpaka mwaka 2015 waliweza kukamata madini yenye thamani ya Dola bilioni mbili, lakini pia kwa upande wa shilingi, jumla ya shilingi bilioni 64 zilikamatwa. Je, kwa utaratibu huo huo Serikali ina mpango gani wa kuzuia wachimbaji katika migodi hasa katika usafirishaji wa ule mchanga kwenda kupimwa nje?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kabisa sasa hivi mchanga wote wa concentrate, yaani copper concentrate na hasa unaotoka kwenye mgodi mkubwa wa Bulyanhulu unasafirishwa kwenda ama China ama Japani. Sababu kubwa ya kufanya hivyo ni kwa sababu hapa viwanda vya kuchenjua dhahabu na kuachanisha madini, havijajengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia namwambie Mheshimiwa Ndassa, ni kweli kabisa uwekezaji huu unahitaji mitaji mikubwa; na siyo chini ya Dola 1,000 kuanzisha mradi wa kuchenjua madini hapa nchini. Hata hivyo, kama Serikali, tunatambua sana mchango wa TMAA mamlaka yetu. Kweli kabisa kwa kutumia TMAA imedhibiti asilimia kubwa sana ya upotevu wa madini ambao ulikuwa unatokea hapo nyuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimkumbushe tu Mheshimiwa Ndassa kwamba ni kweli, mwaka 2015, migodi mikubwa kama GGM ililipa shilingi milioni 117 kama dola kwa ajili ya royalty. Hii kutokana na kazi ya TMAA. Pia local levy iliyolipwa ni dola bilioni 4.7 za Marekani, hiyo ni kutokana na udhibiti wa TMAA.
Kwa hiyo, Serikali tunaendelea sasa kuangalia uwezekano wa kuhamasisha wawekezaji wakubwa kuanza sasa kujenga viwanda vya kuchenjua dhahabu hapa nchini. Hata hivyo, itachukua muda, bado Serikali tunalifanyia kazi. Hii ni kwa sababu inahitaji mitaji mikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, wazo la Mheshimiwa Ndassa tumelichukua, tutalifanyia kazi kama ambavyo Mheshimiwa Ndassa tunashirikiana, tunakushukuru sana.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Nataka kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa mgodi mkuu uliokuwepo katika Mji wa Nzega wa Resolute ulishafungwa na kwenye ripoti ya TMAA inaonyesha Mwekezaji huyu aliondoka na fedha za Halmashauri ya Mji wa Nzega, ten billion shillings ambazo zilikuwa ni service levy: Je, kama Wizara, imefikia wapi kulifuatalia suala hili kuhakikisha haki hii ya wananchi wa Mji wa Nzega inarudi? ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Mheshimiwa Bashe nakushukuru sana. Kama unatukumbusha kwamba kampuni iliondoka na ten billion sasa umetupa taarifa, tutalifanyia kazi. Mimi na wewe pamoja na wataalamu na vyombo vingine tutashirikiana pamoja, tutalifanyia kazi ili pesa ziweze kurejea. Kwa hiyo, nakushukuru Mheshimiwa Bashe. Ahsante sana.
MHE. SHABANI O. SHELIKINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa suala la umeme wa REA ni suala la Kitaifa, je, ni lini Serikali itawapatia umeme wananchi wa Makanya, Ngwelo, Kwemashai, Gare na maeneo yote yaliyoba katika Jimbo la Lushoto?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya Makanya pamoja na Ngwelo ambayo yalizungumzwa na Mheshimiwa Mbunge ambayo kwa sasa hayajapata umeme, taratibu zinazofanyika sasa ni kukamilisha upatikanaji wa umeme kwenye maeneo ya REA Awamu ya Pili na maeneo aliyoyasema Mheshimiwa Mbunge, maeneo matatu kwa sasa yameshawekwa kwenye orodha ya maeneo ambayo yatapatiwa umeme kwenye REA Awamu ya Tatu inayoanza mwezi Julai mwaka huu.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri kuhusu mpango wa umeme vijijini. Mimi nina kata 15 lakini nina kata tatu ambazo zimepata umeme na ni vijiji vitatu vimepata umeme, je, Kata zifuatazo zitapata umeme katika mpango huu? Kata ya Bukwimba, Nyugwa, Busolwa, Shabaka, Nyijundu, Nyabulanda, Kafita, Kakola, Mwingilo, Kaboha, Nyabulanda na Izunya, je, serikali katika mpango wake wa mwaka huu tutapata umeme katika Jimbo la Nyang’hwale Kata zote hizo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa katika Jimbo la Nyang’hwale ni kata tatu tu ambazo zimepata umeme kwa mpango wa REA Awamu ya Pili, lakini REA Awamu ya Tatu pamoja na tathmini inayofanyika sasa katika REA Awamu ya Pili, vijiji vyote na kata zote zilizobaki za Nyang’hwale pamoja na vijiji alivyovitamka vimeingizwa kwenye mpango wa REA unaoendelea utakaonza mwezi Julai mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kadhalika kama nilivyosema bado TANESCO wanaendelea na kazi za kuunganisha umeme katika maeneo yote na maeneo ya Nyang’hwale ambayo hayatapitiwa yataingizwa kwenye mpango wa TANESCO ili vijiji vyote na kata zote za Nyang’hwale zipate umeme mwaka 2017/2018.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona.Ningependa kupata jibu, kwakuwa masuala ya madini hasa yale ambayo si ya kawaida yapo hata katika Mkoa wa Songwe; tuna migodi ya marumaru hususan Mbozi, Ileje, Chunya, yote haya bado hayajaendelezwa kwa kiasi ambacho yangeweza kuleta tija, je, Wizara ya Nishati na Madini itafanya lini utafiti wa kuja kutuletea na sisi uchimbaji wa migodi hii kwa sababu ina faida sana. Badala ya kuagiza tiles nje tungeweza kutumia za kwetu na ubora wake ni mzuri kuliko ule wa nje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile, je, mgodi wa Kiwira ambao uko Ileje na haujawahi kuifaidia Ileje utazinduliwa lini? Ahsante sana
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa katika Mkoa wa Mbeya pamoja na maeneo ya Songwe na Ileje kuna madini ya aina nyingi sana mbali na dhahabu. Na madini mengi yaliyoko katika maeneo yale ni madini ya viwandani. Kama nilivyosema kwenye swali langu la msingi, madini ya niobium yanapatikana kwenye Mkoa wa Mbeya na hasa kwenye maeneo ya Songwe karibu na Gereza la Songwe. Madini haya ya niobium ni adimu sana, na ni madini ya kwanza kupatikana kwa Tanzania na Afrika Mashariki. Kama nilivyosema madini haya yatatumika sana kwa shughuli za viwandani na hasa baadaye kwa kutengeneza computer, engine za ndege pamoja na rocket,, kwa hiyo ni madini ambayo yanapatikana sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti niongeze tu, kwamba sasa madini mengine yaliyoko pale utafiti unafanyika. Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) linaendelea na kufanya utafiti ili kubaini madini mengine ambayo yanapatikana kwenye maeneo ya Songwe, Mbeya Vijijini pamoja na Ileje ili na yenyewe yaweze kuchimbwa kwa faida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nije sasa kwenye mgodi wa Kiwira. Kama mnavyojua Mgodi wa Kiwira unatarajiwa kabisa kwa kuanza kuzalisha umeme, lakini kwa shughuli za uchimbaji wa Mgodi wa Kiwira sasa hivi kinachofanyika ni kukamilisha detail design na taratibu za kumpata mkandarasi. Na kwa utaratibu ambao kwenye bajeti yetu tutakayoisoma Alhamisi wiki hii tutawaeleza, taratibu za kuanza ujenzi huu zitaanza mwaka 2018 na mgodi huu utachukua takribani miaka 20 na kuendelea.
kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Katika Mpango wa REA kwamba itapeleka umeme vijijini, kuna vijiji vya Jimbo la Mufindi Kusini vyapata karibu 30 havijapata umeme, kuna nguzo zilipelekwa kule na baadaye zile nguzo zikaenda kuhamishwa na wananchi wana wasiwasi. Mheshimiwa Waziri naomba uwathibitishie wananchi kwamba kwenye mpango huu wa tatu wanaweza kupata huo umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa katika maeneo ya Mufindi kuna nguzo zilipelekwa na mashimo yakachimbwa, lakini kutokana na scope ya kazi ile ilionekana kwamba mashimo yalikuwa yamechimbwa maeneo ambayo siyo yenyewe. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tu, tumeshakaa na Mheshimiwa Mbunge, tumetathmini vijiji vyake vyote vya Mufindi Kusini na vyote alivyoviorodhesha vitaingia kwenye REA III na vitapatiwa umeme kwenye REA III inayoanza mwezi Julai mwaka huu.
MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la umeme hasa kwenye uunganishaji limekuwa ni tatizo kubwa hasa kwenye maeneo ya mita. Wananchi wengi na wateja wengi wamekuwa wakilalamika kwamba mita ambazo wanafungiwa zinaharibika baada ya muda mfupi. Ningependa kujua kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba je, analifahamu hili na kama analifahamu, hatua gani zitachukuliwa, ili kuhakikisha kwamba, utaratibu huu mbovu unasitishwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Jimbo la Kalenga limekuwa lina changamoto kubwa katika masuala haya ya umeme na nina vijiji kadhaa ambavyo mpaka dakika hii viko gizani na vinahitaji umeme. Kijiji cha Lupalama katika Kata ya Nzii, Kijiji cha Kipera, Kijiji cha Itagutwa, Kijiji cha Magunga na Lyamgungwe; ningependa kusikia commitment ya Mheshimiwa Waziri, je, ana utaratibu gani na mpango gani kuhakikisha kwamba, vijiji hivi vinapata umeme? Na kama je, yuko tayari kuungana na mimi kwenda moja kwa moja Kalenga ili kuweza kuwapa hamasa wananchi wangu? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, wakati REA wanapofunga umeme ni mara nyingi sana imekuwa ikitokea kwamba zile mita inaonekana kama hazina nguvu, tatizo siyo kwamba mita ni mbovu, tatizo tu ni kwamba umeme unaokuja ni wa low voltage.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge ni vizuri tukawaeleza baada ya REA kuunganisha umeme sasa, umeme tunaotumia ni wa low voltage ambao ni kilovolt 30 na mwingine 11 zaidi ni 132. Kuanzia Julai mwaka huu kuna mradi sasa wa kuongeza nguvu za umeme ambao ni kilovolt 400 utapita kwenye maeneo ambayo tuliyataja. Kilovolt 400 zitakapoingia na kuanza matatizo ya kukatika kwa umeme kwenye tatizo la mita yatakoma mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na vijiji alivyotaja Mheshimiwa Mgimwa, vijiji vitano vya Lupalama, Lupelo, Magunga na vingine ni kweli kabisa havijapata umeme na tulishavitembelea, kwa sasa tumezungumza na Mheshimiwa Mgimwa, kati ya vijiji vitakavyoanza kupatiwa umeme kwenye Jimbo lake tutaanza na hivi vijiji vitano ambavyo Mheshimiwa Mgimwa amevitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ameomba sana tupate fursa ya kutembelea kule mimi pamoja na Mheshimiwa Waziri tumekuwa tukitembelea sana maeneo ya Morogoro, hata hivyo, bado tumhakikishie baada ya Bunge lako Tukufu kuisha mimi na Mheshimiwa Mbunge bado tutakwenda kutembelea zaidi, hata akisema mara tano bado tutakwenda kuhakikisha wananchi wanapata umeme.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu linaelekea kwa Naibu Waziri. Katika mikoa ya Mtwara na Lindi tuna tatizo kubwa sana la usambazaji wa umeme kwa kuwa haikuwahi kupata Phase I ya REA wala fedha za MCC. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza akalithibitishia Bunge hili kwamba, katika awamu hii ya tatu ya REA vijiji vyote vitapewa umuhimu wa kupewa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, ni kweli kabisa Mtwara na Lindi yamekuwa ni maeneo ambayo kwa miaka mingi hayapati umeme, lakini baada ya ugunduzi wa gesi miaka miwili iliyopita, kati ya maeneo ambayo tuliyapa vipaumbele kuyapatia umeme wa gharama nafuu ni pamoja na Mtwara na Lindi. Hii ni kwa sababu tulianza sasa kutumia umeme wa gesi kwa mikoa yote hiyo miwili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie tu kwa mikoa hii miwili tuliwatengea kisima ambacho kwa ujumla wake kinapata megawatt 18 za umeme wa gesi. Kwa hiyo, watu wa Mtwara na Lindi wanaweza kupata umeme na tena wa gharama nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo kwenye REA Awamu ya Tatu inayokuja kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, tutahakikisha kwamba vijiji vyote vya Mtwara na Lindi ambavyo vimebaki kutopata umeme kwenye REA Awamu ya Kwanza kwa sababu haikuwepo na Awamu ya Pili ambayo imekwenda kwa kiwango kidogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahakikisha vijiji vyote vya Mtwara na Lindi ambavyo vimeingia kwenye mpango huu wa REA Awamu ya Tatu vitapata umeme wa uhakika.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa muda wa kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa umeme umefika Dongobesh miaka 11 iliyopita na haujawahi kwenda kijiji hata kimoja na pia miaka ya tisini umefika Haydom. Je, Serikali iko tayari sasa kusogeza umeme huo kutoka Kata hizo ambazo nimezisema kuelekea kwenye Kata ambazo amezitaja? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa tuna miradi ambayo ni ya maji, na inahitaji umeme na kwenye REA phase two, hatujawahi kupata mradi huo: Je, Serikali iko tayari kukubali sasa kuanza na Vijiji hivi vya Kata ya Hayderer, Getanyamba, Dinamu, Maretadu, Masieda, Laba na Dinamu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, Serikali iko tayari kusogeza umeme kwenye Vijiji alivyotaja Mheshimiwa Mbunge. Nikiri kwanza Vijiji ambavyo amevitaja kwa lugha yangu, naweza nisivitamke kwa usahihi, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hata Vijiji mbavyo amevitaja ambavyo havikuwa kwenye REA Awamu ya Pili, tunaviingiza kwenye REA Awamu ya Tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, pamoja na REA, Awamu ya Pili inayokamilika na REA, Awamu ya Tatu inayoanza, tutampelekea pia mradi mwingine wa kusambaza ma-transformer ili kuhakikisha Vijiji ambavyo viko karibu na Vijiji vilivyopewa umeme na vyenyewe vitapata umeme. Lengo ni kuvipatia Vijiji vyako vyote umeme kwenye REA, Awamu ya Tatu.
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri aliyonipatia, lakini naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ni kwamba amesema Mji wa Songea una uwezo wa kupata megawatt 4.7 na hivi sasa wana uwezo wakuzalisha megawatt 9.5. Lakini naomba niseme kwa masikitiko kwamba bado katika mji wa Songea kuna maeneo ambayo hayajafikishiwa kabisa umeme, maeneo kama Ndilima Litembo, Mletele, Lilambo B, Mwanamonga, Sinai, Mwenge Mshindo, Chandarua, Luhilaseko, Kuchile, Lizaboni katika eneo la London, Mang‟ua, Subira, Mtendewawa, Mkesho na kadhalika hayajafikishiwa umeme. Sasa naomba Mheshimiwa Naibu Waziri anithibitishie, je, maeneo haya ambayo umeme haujafikishwa ni lini Serikali itayafikishia umeme?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, lipo tatizo kubwa sana kwa Songea Mjini, la umeme kukatika mara kwa mara, na umeme unapokatika mara kwa mara unasababisha kuunguzwa kwa vifaa vya wananchi katika nyumba zao. Lakini la pili, inazuia kukua kwa shughuli za kiuchumi katika mji wa Songea. Je, Serikali ina mpango gani wa kukomesha tatizo la kukatika katika kwa umeme na lini litakuwa na utaratibu wa kuwalipa fidia wale wote wanaounguza vifaa vyao kwa sababu ya kukatika kwa umeme?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri anijibu maswali yangu.
NAIBU WAZIRI NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Gama na Waheshimiwa Wabunge, kama tulivyoeleza kwenye bajeti yetu na kama ambavyo kila mara ninaeleza, kwamba wananchi wa Songea, Ludewa, Njombe Mjini na Vijijini, utaratibu wa kuwapelekea umeme wa uhakika kutokana na usafirishaji wa umeme wa kilovoti 220 kwa umbali wa kilometa 250 ambao utaanza Januari mwaka huu unakuja, na kazi yake itakamilika mwezi Juni, 2018. Kwa hiyo, Mheshimiwa Gama nimhakikishie kwamba vijiji vya Mlima Litembo pamoja na Mwengemshindo na vingine vitapatiwa umeme kuanzia mwezi Juni 2018 na utakuwa ni umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali la pili la Mheshimiwa Gama, juu ya kukatika katika kwa umeme. Ni kweli kabisa na Waheshimiwa Wabunge kama mnavyojua, sasa hivi tunafanya kazi kubwa tatu. Kazi ya kwanza ni kuongeza nguvu ya umeme kutoka kilovoti 132 hadi kufikisha kilovoti 400. Lakini kwa Makambako – Songea tunaongeza umeme wa kilovoti 33 hadi kilovoti 220 ambao sasa utamaliza tatizo la kukatikakatika katika miji ya Songea, Njombe, Ludewa pamoja na maeneo ya jirani.
Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Gama, mara baada ya kuweka kilovoti 220 maeneo yote ya Jimbo la Songea Mjini, Ludewa, Njombe Mjini na Njombe Vijijini kukatikakatika kwa umeme kutakoma mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Gama kuhusiana na suala la fidia. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge, lakini pia nichukue nafasi hii kuwatangazia wananchi wote, kukatikakatika kwa umeme inawezekana kukachangia sana kuharibika kwa miundombinu ya nyumbani lakini pamoja na vifaa vinavyotumia umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hata hivyo matumizi sahihi ya umeme ni muhimu sana. Niwaombe sana wananchi na Waheshimiwa Wabunge, mara TANESCO na mashirika yanapokuwa yanakata umeme kwa ajili ya kufanya marekebisho tuwe tunapunguza au kuzima vyombo vyote vinavyotumia umeme ili umeme ukija sasa usisababishe uharibifu.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Gama kwamba kusababaishwa kwa uharibifu wa umeme kwenye vyombo vya ndani inawezekana kabisa ama uzembe wa matumizi, ama uzembe wa TANESCO. Mahala ambapo TANESCO itasababisha tutafanya utafiti, na tukiona kwamba kuungua kwa vyombo hivi kumesababisha na TANESCO tutafanya fidia kulingana na uharibifu uliotokea.
MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la usambazaji wa umeme lipo pia katika Wilaya ya Meatu. Wilaya ina vijiji 109 lakini ni vijiji 21 tu, sawa na asilimia 19 vilivyopatiwa umeme. Ni lini Serikali itavipatia umeme vijiji vilivyosalia?
NAIBU WAZIRI NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba katika maeneo aliyoyataja ni vijiji 21 tu vimepatiwa umeme, na ninadhani anazungumzia eneo la Meatu; na vijiji takribani 105 havijapata umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama nilivyosema kwamba ugawaji wa umeme unakwenda kwa awamu. Tumemaliza awamu ya pili ambayo imehusisha vijiji vingi sana, na awamu ya tatu inakwenda sasa kumalizia kwenye vijiji vyote vilivyobaki nchi nzima. Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, vijiji 100 vilivyobaki, pamoja na maeneo ya vitongoji ambavyo pia hajayataja nimhakikishie kwamba yote yatapata umeme kunzia mwaka 2017, 2018 hadi 2019.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Tatizo la uhaba wa umeme ni kubwa sana nchi nzima, na hili linatokana na gharama kubwa ya nguzo. Nilikuwa naomba kujua ni lini Serikali itachukua ushauri kwamba nguzo ziwe ni gharama za Serikali lakini zile gharama nyingine ziwe ni za watu binafsi kama ilivyokuwa kwenye masuala mazima ya simu, kwamba nguzo za simu zilikuwa bure, ni kwa nini Serikali isifanye utaratibu huo ili wananchi wengi waweze kupata umeme?
NAIBU WAZIRI NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kukatikatika kwa umeme pia kunachangiwa na uharibifu wa nguzo. Lakini nimueleze tu Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge kwamba kuanzia mwezi Januari mwaka huu TANESCO sasa inaanza kutengeneza nguzo zinazoitwa concrete pole, nguzo ambazo ni za concrete, ambazo zitakuwa haziozi. Nguzo hizo sasa zitahakikisha kwamba nguzo zitakuwa hazianguki na kukatikakatika kwa umeme kutakoma mara moja.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri niulize maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Singida mjini kwa asilimia kubwa ya wakazi wanajishungulisha na biashara za mazao hususani biashara ya vitunguu. Serikali ina mpango gani sasa wa kujenga Soko la Kimataifa la Vitunguu pale Misuna ambalo linawahusisha mpaka wenyeji wa nchi za Afrika Mashariki na Kati?
Swali la pili, kwa kuwa Serikali imeonyesha ina hisa nyingi kwenye Makampuni ya Umma, je Serikali ina mpango gani wa kuongeza hisa lakini pia hold share na kuongeza uzalishaji katika makampuni hayo? Ahsante.
HARA NA UWEKEZAJI): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Sima kwa anavyoshughulikia masuala ya masoko na viwanda hapo Singida, hakuna asiyejua kwamba Singida ni wakulima wa vitunguu na wakulima maarufu sana wa zao la alizeti. Serikali inachofanya pamoja na mambo mengine ni kuhakikisha kwamba sasa hivi inawasiliana na Halmashauri ya Singida ili kuona sasa zao la vitunguu linapewa kipaumbele na kuanzisha soko la kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, umuhimu wa Singida pamoja na mambo mengine hadi sasa kwa kilimo cha vitunguu pamoja na alizeti nadhani ni Mkoa unaongoza kwa Tanzania kwa sasa ukifuatiwa na Mkoa wa Iringa. Hivyo Serikali inaona kuna umuhimu kweli wa kuanzisha soko la Kimataifa kama ambavyo tumeanzisha masoko mengine mipakani kwa ajili ya kuimarisha mazao ambayo yanalimwa hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la Mheshimiwa Mbunge ni kuhusiana na hisa za Serikali. Ni kweli kabisa Serikali ina miliki hisa katika makampuni mengi sana. Kwa sasa hivi kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi Serikali ina hisa katika makampuni 61 na katika makampuni yale asilimia kubwa ya hisa za Serikali ni chini ya 50. Kama mnavyotambua tuna asilimia kwa sasa hivi kwa mfano Tanzania Oxygen tuna asilimia 9.59, ukienda Kilombero Sugar tuna asilimia 25, ukienda Tanelec tuna asilimia 30. Lakini hata ukienda kwenye makampuni mengine kama migodi Mwadui tuna asilimia 25.
Mheshimiwa Naibu Spika, upo mkakati wa kuongeza za Serikali katika mipango ya kimkakati, mipango ya kimakakati kwa mfano mathalani kwa sasa hivi viwanda vyetu vya nguo kama Urafiki Serikali ina asilimia 49. Serikali inajaribu kuangalia uwezekano wa kuongeza hisa zake ili iweze kuwa na maamuzi ya uzalishaji katika viwanda vile.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiongeza suala lingine kuhusu uongezaji wa hisa katika kuweka asilimia za Serikali, katika mipango na miradi na viwanda vya kimkakati kama viwanda vya chuma cha Liganga, kama viwanda vya Kiwira, Serikali inaona kuwa na asilimia nyingi ili iweze kuwa na uwekezaji yenyewe kama ambavyo inaweza kufanya kwa maendeleo ya wananchi wake.
MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru. Pamoja na majibu hayo, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, ni kwamba kwenye jibu lake la msingi la (b) anazungumzia malipo haya ya 2014, ni lini basi atatuambia pesa hizi zitalipwa ili Halmashauri ya Kaliua iweze kufanya shughuli zake kwa kutumia fedha hizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni la ujumla, kwamba miradi kama hii inafanywa katika sehemu nyingi za nchi, lakini mara nyingi pamoja na kufanya social na environmental impact assessment bado wananchi huachwa mpaka wakapata mateso ndipo Serikali ikaja kuwalipa baadaye. Je, Serikali inatuambia nini kwamba sasa watakuwa wanafanya malipo kabla ya athari kupatikana kwa wananchi? Atupe majibu ni lini. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa malipo ambayo yalitarajiwa kulipwa kwa kipindi hiki cha 2014 yangekuwa yameshafanyika hadi sasa, lakini hadi sasa hayajafanyika. Napenda nimpe uhakika Mheshimiwa Mbunge kwamba, TANROADS imeshafanya mahesabu na imeshamwandikia sasa mkandarasi kwa ajili ya kuanza malipo. Kwa sasa tumejipanga TANROADS pamoja na wenzetu, wataanza kulipwa kuanzia Agosti hadi Septemba mwaka huu kulingana na upatikanaji wa fedha
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili kuhusiana na malipo kufanyika mapema. Kwa mujibu wa Sheria ya Madini ni kwamba kabla ya shughuli za madini hazijaanza kufanyika, kazi inayotakiwa kufanyika kwanza ni kufanya tathmini na tathmini ikishafanyika na malipo yakakubalika na wadau wakakubaliana kuhusiana na malipo ya fidia, kawaida malipo huwa yanafanyika kabla ya shughuli kuanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiri tu kwamba kwa sababu wakati wanaanza uchimbaji wa kokoto wa kwenye barabara hii, tathmini zilichelewa kukamilika, kwa hiyo, malipo hayakuanza kufanyika mapema. Hata hivyo, kwa taratibu ambazo tunaanza kuanzia sasa, malipo yatakuwa yanafanyika kabla ya wananchi kuathirika. Kwa hiyo, malipo ya fidia yatakuwa yakianza kufanyika kabla ya shughuli za uchimbaji wa kokoto kuanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi hatuwezi kusema zitaanza lini kwa sababu walishaanza kuathirika na malipo hayajafanyika, lakini malipo yote ambayo hayajafanyika kwenye barabara hii, yatafanyika kati ya Septemba hadi Oktoba mwishoni mwa mwaka huu bila kuchelewa kwa ushirikiano wa wadau, TANROADS pamoja na Halmashauri ya Kijiji.
MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru sana. Kwa kuwa milipuko hii inaleta matatizo ya afya ya wananchi walioko karibu na sehemu ya mashimo hayo na kuacha mazingira yakiwa na mashimo. Je, ni lini Serikali itakuwa inahakikisha afya za watu hao zinakuwa sawa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikubaliane nae kwanza, kwamba, shughuli za madini hufanyika na kuacha madhara kiafya. Kuhusu ni lini, ni wakati wote shughuli za madini zinapofanyika tunatakiwa tuhakikishe kwamba afya za wananchi pamoja na wachimbaji zinabaki salama.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, je, Serikali ina mpango gani sasa wa kutoa elimu kwa wakati wa Mtwara na Lindi ili wapate uelewa juu ya mradi huu?
Lakini pili, waweze kujiandaa kutumia fursa zitakazopatikana baada ya ujenzi wa kiwanda hiki? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pili, maeneo ambayo yalianishwa na mradi huu ni mawili, eneo la kwanza ni kwa ajili ya ujenzi wa kile kiwanda cha LNG, eneo la pili ni industrial park kwa ajili ya viwanda vingine ambavyo vitajengwa hapo baadaye.
Sasa nataka nijue hatua iliyofikia katika kutwaa eneo hili ambalo litajegwa viwanda vingine yaani eneo la industrial park kwamba je, wananchi wameshafidiwa au bado hawajafidiwa hadi sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, mradi wa LNG ni mardi mkubwa sana, na nipende tu kusema kwa niaba yako na kwa niaba ya Wabunge; kati ya miradi mikubwa ambayo Serikali tumeitekeleza ni pamoja na mradi huu utakapo kamilika. Mradi huu kwa nchi za Afrika, Tanzania itakuwa ni nchi ya tatu katika kutekeleza.
Mheshimiwa Spika, lakini kujibu swali la msingi ambalo Mheshimiwa Chikota anataka kujua ni hatua gani imefikiwa katika kutoa elimu kwa wananchi; hatua tatu zimeshafanyika hadi sasa.
Mheshimiwa Spika, hatua ya kwanza ilikuwa ni kuwapa ufahamu na utambuzi wa manufaa ya mradi huu kwa viongozi wa Mikoa ya Lindi pamoja na Mtwara ambao vikao vimefanyika na kikao cha mwisho kilifanyika jana pamoja na juzi.
Mheshimiwa Spika, lakini hatua ya pili kulingana na hilo TPDC pamoja na wakandarasi na wazabuni waliopewa kazi hii wameshaanza kutoa elimu katika Vijiji vinavyoambaa katika mradi huu. Vijiji ambavyo vimeshatoa elimu hadi sasa ni pamoja na Kijiji cha Likong‟o ambapo mradi utachukuliwa, eneo la Kikwetu pamoja na Kijiji cha Mtomkavu. Hayo ni maeneo ambayo elimu wananchi wameshapewa kwa ajili ya umuhimu wa mradi huo.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili, kwamba ni maeneo gani yamechukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hiki. Kwa niaba ya wananchi ni vizuri niwatangazie kwamba eneo lililochukuliwa na mradi huu kimsingi ni eneo kubwa sana, ni jumla ya ekari 20,000 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa mradi huu, hata hivyo kwa awamu ya kwanza kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa LNG ni hekta 2,071 zitatumika.
Mheshimiwa Spika, na kwa niaba ya wananchi ni vizuri nikiwaeleza, mradi huu utakapokamilika utakuwa na manufaa mengi kwa sababu wawekezaji mbalimbali watatumia maeneo haya. Kwa mujibu wa swali la Mheshimiwa Chikota, nikushukuru sana Mheshimiwa Chikota kwa sababu mradi huu ni vizuri sana Watanzania tukauelewa. Tunapozungumza kujenga uchumi wa viwanda ni pamoja na viwanda vikubwa kama kiwanda hiki ambacho nimekieleza.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Kwa kuwa, Wakandarasi wengi wanaotumia bidhaa hizi hawafuati taratibu hizi ambazo zimeelezwa na Mheshimiwa Waziri, ama kununua mawe na bidhaa nyingine kwa watu wenye leseni, mara nyingine wamekuwa wao wenyewe wakiamua kuchukua hizo bidhaa katika maeneo yetu na bila kulipa mrabaha katika Halmashauri au bila kuwanufaisha wananchi katika maeneo yetu ambako bidhaa hizo zinatoka;
Je, Serikali iko tayari sasa kuangalia utaratibu mzuri ambao utanufaisha hizi Halmashauri zetu pamoja na wananchi husika katika maeneo husika ambayo bidhaa hizi zinapatikana?
Swali la pili, kwa kuwa wakati wa zoezi hili la uchukuaji bidhaa mbalimbali za ujenzi pia hutokea uharibifu wa mazingira katika maeneo yetu ikiwepo uchimbaji wa mashimo makubwa na kuacha hayo mashimo katika maeneo yetu, pia afya za wananchi zinaathrika kwa mavumbi na kadhalika;
Je, Serikali inachukua hatua gani madhubuti kuhakikisha kwamba inadhibiti suala la uharibifu wa mazingira pamoja na afya za wananchi katika maeneo husika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa wachimbaji wadogo hasa wanaojihusisha na uchimbaji wa madini ya ujenzi pamoja na viwandani kwa kiwango kikubwa sana hawalipi ada pamoja na malipo mengine Serikalini. Nichukue nafasi hii kuwataka rasmi wachimbaji wadogo wote popote walipo waanze sasa kufanya hivyo.
Hata hivyo, manufaa yanayoweza kupatikana kutokana na uchimbaji wa kokoto pamoja na mchanga ni pamoja na kutakiwa kama ambavyo sheria inawataka kulipa ushuru wa Halmashauri ambao ni asilimia 0.3, haya ni matakwa ya sheria, ni vizuri sana ninakushukuru Mheshimiwa Badwel, nichukue nafasi hii kuwahamasisha viongozi wa Halmashauri ili waanze kukusanya ushuru huo kutoka kwa wakandarasi wanaochimba kokoto pamoja na mchanga kote nchini. Kwa hiyo namshukuru sana Mheshimiwa Badwel kwa kuwakumbusha wananchi ili wachukue hatua hiyo, ninawaagiza pia wakandarasi wote waanze kufanya hivyo mara moja.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, athari za mazingira, kwanza nikubaliane na Mheshimiwa Badwel kwamba uchimbaji wowote wa madini jambo la kwanza kabisa wanalotakiwa kufanya ni juu ya kutokuharibu mazingira. Huwezi kuchimba madini bila kuharibu mazingira, lakini wana jukumu kwa mujibu wa Sheria za Mazingira na kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya 2010, wana wajibu wa kisheria wa kutunza mazingira.
Mheshimiwa Spika, hatua tunazochukua kwa wakandarasi na wamiliki wa leseni wasiotunza mazingira ni pamoja na kuwafutia leseni zao lakini pia kuwachukulia hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria hizo mbili.
Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Badwel pia natoa tamko rasmi, Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira huwa tunachukua hatua za kisheria kwa wale wasiotunza mazingira kwa mujibu wa sheria.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda niipongeze Serikali kupitia Mradi huu wa REA I, II na III. Kwa kuwa kuna Kata ya Badugu yenye vijiji vya Mwaniga, Manala, Badugu yenyewe na Busani mpaka leo wanaona nguzo za umeme zimepita tu, lakini hawajapewa transfoma. Je, Mheshimiwa Waziri ananihakikishia kwamba vijiji hivi vitapata umeme sasa kuanzia Julai?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa vijiji vya Nyakaboja vilivyoko kwenye njia kuu ya kwenda Musoma, Vijiji vya Mngasa, Kalago na Lukungu ambako kuna kituo cha afya mpaka leo hakuna umeme. Je, Mheshimiwa Waziri vilevile atanihakikisha kwamba vijijni hivi ambavyo vinatoa na huduma za Hospitali ya Lukungu pamoja na Hoteli ya Serenity na Speke Bay ambazo zinaingiza mapato kwa nchi hii, vitapatiwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Kata ya Badugu kupatiwa umeme, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba vijiji vyote vya Kata ya Badugu, kama anavyojua Mheshimiwa mwenyewe ni kwamba maeneo yote ya Nyamikoma, Nyakaboja, Nyakungula pamoja na yale yote ambayo yanaunganishwa Kata ya Badugu yatapatiwa umeme kwenye awamu hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, vijiji vya Kata ya Badugu ambavyo vimebaki ambavyo vinajumuisha maeneo ya Nyamanara, Nyamikoma, Nyazikungura pamoja na maeneo mengine ya Lamadi yatapatiwa umeme kwenye transfoma itakayofungwa kuanzia Julai, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu umeme kwa vijiji ambavyo vinaungainisha hospitali ya Lukungu pamoja na hoteli ya Serenity iliyopo Lamadi, nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Chegeni kwamba vijiji vyote vilivyobaki ambavyo ni vijiji 16 vitapatiwa umeme. Awamu ya kwanza ya REA kwenye Jimbo la Busega tulipeleka vijiji 22 na katika Awamu ya II ya REA kwenye Jimbo hilo hilo la Busega tumepeleka vijiji 18 na Awamu ya III ya REA kwenye Jimbo hilo hilo tunapeleka vijiji 19 vyote vilivyobaki. Vijiji hivyo ni pamoja na Ng‟wanangi, Ng‟wanale, Vijiji vya Lamadi vilivyobaki vyote vitawaka umeme kwenye Jimbo la Busega.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa changamoto za Jimbo la Busega zinafanana na zile za Jimbo langu la Bagamoyo, vijiji viwili, Kijiji cha Kongo na Kijiji cha Kondo ambavyo vilikuwa ndani ya mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya II ambapo mpaka hivi sasa havijaanza kuwekewa umeme. Naomba Mheshimiwa Waziri aniambie kuna mkakati gani wa kuwezesha vijiji hivi kuwekewa umeme kabla ya mwaka huu wa fedha kumalizika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa katika Jimbo la Mheshimiwa Kawambwa kuna vijiji 12 vimebaki ambavyo nataka tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba vijiji vyote 12 vilivyobaki tumeviingiza kwenye REA Awamu ya III.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji cha Kondo pamoja na maeneo ya jirani ambayo ameyataja ni maeneo ambayo yataanza kuwashiwa baada ya Julai. Mwezi wa Septemba na Oktoba kati ya vijiji ambavyo vitawashiwa umeme kwenye Jimbo la Bagamoyo ni pamoja na Kijiji cha Kondo ambacho amekitaja Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Kawambwa ameendelea kufuatilia sana mahitaji ya wananchi wa Bagamoyo kuhakikisha kwamba vijiji vyote na kwa vile viko karibu na Dar es Salaam vinapata umeme wa uhakika.
Nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Kawambwa umeme atakaoupata kwenye Vijiji vya Kondo na maeneo ya jirani utakuwa ni umeme ambao utaunganishwa na kilovoti 400 ambao utakuwa haukatiki mara kwa mara.
MHE. EMMANUEL P. JOHN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kutuona, kambi mbadala tuko wachache lakini tunajipanga kukuletea orodha yetu upange Baraza la Mawaziri vizuri hapo. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Waziri, lakini napenda kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Kiteto tuna Kata za Songambele, Magungu, Dongo, Raiseli na Sunya zenye jumla ya vijiji karibu 21. Vijiji hivi vyote vilipangiwa kwenye Awamu ya II ya REA. Napenda kuuliza, ni lini tutapatiwa umeme katika awamu hii ili maeneo hayo yaweze kuwa na umeme? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Papian, Mbunge wa Kiteto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, niruhusu tu nisahihishe kidogo alichosema Mheshimiwa Mbunge, vijiji vilivyobaki siyo 21, tunakuongezea, viko 22 Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, napenda sasa nijibu kwamba vijiji vyote ambavyo amevitaja vya Songambele, Dongo, Raiseli pamoja na Sunga vitapata umeme kwenye REA Awamu ya Tatu inayoanza mwezi Julai.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa nguzo nyingi za umeme katika nchi hii zinatoka Sao Hill huko kwetu Mafinga ambako pia kuna Kata ya Sao Hill yenye vijiji vya Sao Hill na Mtula. Je, Serikali iko tayari kuenzi Kijiji cha Sao Hill na maeneo jirani ambayo mpaka leo hakuna umeme kwa kufanya upendeleo maalum wa kupatiwa kwa kuwa huko ndiko zinakotoka nguzo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa eneo la Mafinga linazalisha nguzo nyingi hapa nchini. Wala hakuna haja ya kuwa na upendeleo kwa sababu vijiji vyake vyote vimo kwenye REA Awamu ya III. Eneo la Sao Hill alilosema liko REA Awamu ya Tatu lakini mpaka eneo la Isalanavu pia liko kwenye REA Awamu ya III. Kwa hiyo, maeneo yake yote yatapata umeme kwenye REA Awamu ya III.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili kama ifuatavyo:-
(a) Mpaka sasa Wizara imeweza kutoa leseni ngapi za utafiti wa madini katika Wilaya ya Kalambo?
(b) Kwa kuwa kuna taarifa kwamba kuna uwezekano mkubwa sana wa kupatikana mafuta hasa ndani ya Ziwa Tanganyika ambalo linafika mpaka Kalambo, je, Serikali imefanya jitihada gani za makusudi kuhakikisha kwamba utafiti huu unafanyika na kukamilika ili tuweze kupata mafuta ndani ya Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa kwa ujumla wake?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu leseni ngapi tumetoa, eneo la Kalambo bado linafanyiwa utafiti mkubwa sana na Wakala wa Jiolojia. Mpaka sasa leseni ambazo zimeshatolewa katika eneo la Kalambo ni tano tu ambapo leseni tatu za uchimbaji ambazo zimetolewa kwa Kampuni ya Agricultural Fast Limited na leseni mbili zimetolewa kwa kampuni ya binafsi ambayo inaitwa Shamze Ahmed Limited ambazo ni za madini ya dhahabu. Hata hivyo, bado eneo hili linafanyiwa utafiti na hadi sasa kuna waombaji wengine wameomba leseni nne za uchimbaji ambao ni pamoja na Mheshimiwa Antony Chilumba ambaye ameomba leseni za utafutaji wa madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la utafutaji wa mafuta, ni kweli kabisa eneo la Ziwa Victoria, Ziwa Natron, Eyasi na mengine mpaka Wembere bado TPDC na makampuni mengine wanafanya utafiti. Kwa eneo la Ziwa Tanganyika bado hawajagundua mafuta pamoja na gesi kwa ajili ya kufanyiwa utafiti wa kina. Bado TPDC na makampuni mengine wanafanya utafiti na wako katika hatua nzuri za kuweza kubainisha kama mafuta yanapatikana au la. Namuomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, TPDC wanaendelea na ukaguzi ili kuona kama bado kuna mafuta maeneo ya Ziwa Tanganyika.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Fedha, moja ya sababu ambazo zinasababisha shilingi yetu kushuka ni matumizi makubwa ya fedha za kigeni na katika bidhaa ambazo zinaagizwa ni makaa ya mawe. Ni kwa nini makaa ya mawe ya Tanzania hayatumiki tunaagiza makaa ya mawe kutoka South Africa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza anataka kujua kwa nini makaa ya mawe yaagizwe kutoka nje badala ya kutumika ya hapa nchini? Ni kweli kabisa, sasa hivi makaa ya mawe yanayopatikana yangeweza kupatikana kwa wingi sana pale Kiwira kwenye eneo la Kiwira lenyewe, lakini hata Kabulo. Kiwira ni kweli kabisa, kutokana na utafiti wa mwaka 2007 iko reserve ya tani milioni 30 na pale Kabulo ni tani milioni 50 lakini bado kuna maeneo mengi ya Mchuchuma na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ilizochukuwa Serikali sasa ni kuhakikisha kwamba wawekezaji wote wanapata makaa ya mawe kwa sababu yanajitosheleza. Hata hivyo, wako wawekezaji kama Dangote alikuwa anaagiza kutoka Afrika Kusini na maeneo mengine sasa hivi tumesitisha kutoa vibali vya kumruhusu kuingiza isipokuwa tunamlazimisha aanze kutumia makaa ya mawe ya hapa. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kusema Serikali itaanza sasa kuchukua hatua kuhakikisha makaa ya mawe yatakayopatikana hapa yananunuliwa hapahapa nchini.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Kumekuwa na taarifa zilizotapakaa katika mitandao ya kijamii zinazoeleza ugunduzi wa gesi aina ya helium. Je, Serikali inaweza kutueleza nini juu ya taarifa hizo, ni za kweli au ni za uongo?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba, utafiti umefanywa na vyuo ambavyo vinatambulika duniani kimojawapo ni Oxford na Durham na wamepiga mahesabu kutokana na utafiti wa Jiofizikia uliofanywa miaka ya 80 na 90 wakafikia kiwango cha gesi ya helium.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tofauti hapa ya hizi gesi, helium inapatikana kwenye kina kifupi lakini hii gesi nyingine methane inapatikana kwenye kina kirefu na duniani ambaye ana helium nyingi ni Marekani. Kwa hiyo, gesi kule Marekani inaanza kupungua ndiyo maana na sisi tunaitafuta kwa udi na uvumba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilichogundulika ni kutokana na mahesabu ya huko nyuma na kinachofuata kwa miezi michache inayokuja Helium One ikishirikiana na watalaam wengine watafanya drilling ya huko Ziwa Rukwa. Hapo ni upande wa Ziwa Rukwa ndiyo imepatikana kiasi hicho estimate ya kwanza 54.2 billion metric cubic feet. Hata hivyo, watachimba kule Lake Rukwa, wataenda Eyasi, wataenda Natron nadhani baada ya kama mwaka mmoja hivi tutajua kwamba tunaweza kuanza kuuza helium duniani. Kwa hiyo, hizo ni taarifa za uhakika zinatoka chuo cha uhakika cha Oxford.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Tunduru Kusini kama alivyozungumza, kuna kata 15 kati ya hizo ni vijiji vinne tu vya Kata ya Chiwana na Kata ya Mbesa ndivyo vimepata umeme. Je, kati ya kata hizi zifuatazo ni lini watapatiwa umeme wa REA, Kata za Mtina, Nalasi, Mchoteka, Malumba, Mbati, Ligoma, Namasakata, Mchesi, Lukumbule, Chiwana na Msechela?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kumekuwa na tabia ya mkandarasi anayejenga laini ya Mbesa kuwadai wananchi wetu Sh.200,000/- mpaka Sh.300,000/- kwa ajili ya kupelekewa nguzo na kuunganishiwa umeme katika nyumba zao. Je, ni hatua gani imechukuliwa ili mkandarasi huyu asiendelee na tabia hiyo kwani umeme huu ni haki yao wananchi kupewa bure kwa kulipa Sh.27,000/-? Ahsante
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikubaliane na Mheshimiwa Mpakate kwamba kwa kweli ni vijiji vinne tu ambavyo vimepata umeme kwenye jimbo lake lakini vijiji vingine vilivyosalia ambavyo jumla yake kwa kweli ni 67, vikiwemo Vijiji vya Semeni, Angalia, Jiungeni na vijiji vingine vya Mwenge vyote vitapata umeme kwenye REA Awamu ya III inayoanza mwezi Julai, 2016. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mpakate pamoja na wananchi wa Tunduru Kusini kwamba vijiji vyote vilivyosalia vitapata umeme kuanzia mwezi Julai 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusiana na gharama ya nguzo ambayo wananchi wanatozwa, napenda kutumia fursa hii kuwaomba sana Waheshimiwa Wabunge na kuwahakikishia wananchi kama ifuatavyo: Kwanza kabisa, katika Mradi wa REA mteja yeyote hatakiwi kutozwa gharama ya nguzo, si Sh.200,000/- wala Sh.300,000/-. Naomba niwahakikishie wananchi wa Tunduru Kusini na Watanzania wengine, gharama za nguzo kwenye miradi ya REA Serikali imeshagharamia, kwa hiyo, mwananchi hatakiwi kutozwa gharama yoyote ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, niendelee tu kusema kwamba kwenye miradi mingine ya TANESCO, gharama za nguzo ni kama ifuatavyo: Kwa mteja ambaye yuko umbali wa mita 30 -70, gharama yake ni Sh.177,000/- tu kwa vijijini na kwa mijini ni Sh.272,000/- tu. Kwa hiyo, napenda kutoa kabisa hili angalizo kwa wananchi, wasitozwe gharama zaidi ya hiyo kwa umbali ambao nimeutaja hata kwa miradi ya TANESCO.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nasi wananchi wa Mkuranga tumeomba miradi ya umeme katika baadhi ya vijiji vyetu zaidi ya 30, vikiwemo Vijiji vya Mlamleni, Lugwadu, Mkola, Kazole, Lukanga, Mwajasi, Vianzi, Malela na vinginevyo, je, miradi hii itakamilika katika muda gani ili wananchi wale waweze kujiandaa kupokea miradi hii ya umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimesema, kwa sasa hivi tunafanya uhakiki katika utekelezaji wa REA Awamu ya II na mradi kabambe wa REA Awamu ya III unaanza Julai, 2016 na kukamilika kwa mradi huu ni miaka mitatu hadi minne. Kwa hiyo, ifikapo mwaka 2018/2019, Watanzania wote ambao watakuwa kwenye miradi ya REA Awamu ya II vikiwemo Vijiji vya Rugumu, Rukola, Malela pamoja na maeneo mengine ya Mkuranga vitapatiwa umeme ndani ya kipindi hicho.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa sababu swali la msingi limeongelea kuhusiana na tatizo kubwa la umeme na Wilaya ya Kalambo ni miongoni mwa Wilaya chache ambazo zilikuwa na umeme sifuri, je, Mheshimiwa Waziri anatuambia nini wananchi wa Kalambo juu ya vijiji vile ambavyo havijapata umeme kupatiwa umeme kabla hatujaenda awamu ya III?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge wa Kalambo kwamba vijiji 24 vilivyobaki katika eneo la Kalambo ambavyo vilikuwa kwenye REA Awamu ya II vitakamilika ndani ya mwezi huu, siku 10 zilizobaki kwa mwezi wa Juni. Hata hivyo, vijiji ambavyo vimebaki ambavyo ni nje ya vijiji hivyo vitaendelea kupatiwa umeme katika Mradi wa REA unaokuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika bado TANESCO inaendelea kusambaza umeme kama kawaida. Kwa hiyo, vijiji ambavyo vitakuwa bado havijapitiwa umeme kwenye vitongoji vyake kwa umeme wa underline transformer ambao utakuwa unashusha umeme kwenye vijiji na vitongoji Mheshimiwa wa Kalambo bado vitapatiwa umeme. Tunataka kufikia 2025 vijiji vyote, kama nilivyokwisha kusema, vya Watanzania vitakuwa vimepatiwa umeme pamoja na vijiji vyote vya Jimbo la Kalambo.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa REA inapeleka umeme vijijini na wakandarasi ndiyo wanaosimamia uwekaji wa vifaa vya umeme kwenye vijiji, je, Serikali inaweza ikatuambia kuna tatizo gani katika Kijiji cha Zegero, Kata ya Kurui?
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna transformer imekaa pale zaidi ya miezi sita na wakati napita kwenye ziara nimeikuta pale toka 7 Aprili, je, Serikali inasema nini? Wananchi wanaiona ile transformer pale wana mategemeo ya kupata umeme lakini mpaka leo hii hawajapata umeme. Mbali ya hayo, transformer ile inaharibika kwa kunyeshewa na mvua bila kupata usimamizi na watoto kuichezea. Naomba majibu
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa sipendi kukataa, kama kuna transformer imeharibika na iko pale muda mrefu, Mheshimiwa Vulu naomba sana tukitoka hapa mimi na wewe tuongozane tukaone hiyo transformer na ikiwezekana ifanyiwe ukarabati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nichukue fursa hii kuwaambia Waheshimiwa Wabunge kwamba kuanzia sasa Serikali imekusudia ma-transformer yote yanayotengenezwa hapa nchini ndiyo yatakayokuwa yanatumika kwa ajili ya kuunganishia umeme wetu. TANESCO sasa haitaagiza transformer kutoka nje, itakuwa inanunua ma-transformer kutoka hapa nchini. Kampuni ya TANELEC sasa hivi ina uwezo wa kuzalisha transformer 883 kwa mwezi ambapo mahitaji ya TANESCO ni ma-transformer 80. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Vulu nikuombe sana, kama transformer bado ipo mimi na wewe tukitoka hapa tuongozane sambamba, tukae tujadiliane tufanye marekebisho ya transformer hiyo ili wananchi waendelee kupata umeme wa uhakika.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mimi naanza kutia mashaka kidogo kwenye miradi hii ya REA kwa sababu Waziri na Naibu Waziri wanasema mwezi wa sita ndiyo itakuwa mwisho wa REA Phase II lakini vijiji vyangu vya Jimbo la Bunda; Sanzati, Mikomahiro na Mihingo mpaka leo transformer iko moja kwenye Kijiji cha Sanzati na sioni kama kuna miradi inayoendelea pale, sioni kama kuna mafundi pale! Ni lini miradi hii itakwisha?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, tulishakaa na Mheshimiwa Mbunge na tukajadiliana kuhusu vijiji vyake vya Sanzati na vingine. Vijiji alivyotaja Mheshimiwa Mbunge hivi sasa tunapoongea kazi inaendelea. Isipokuwa katika maeneo anayoyataja Mheshimiwa Mbunge nadhani vile vijiji sita kazi ambayo imebakia sasa ni kushusha nyaya chini kabla hawajawasha. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Bunda Vijijini na Bunda Mjini kwa ujumla wake vijiji vyote ambavyo viko kwenye ile Awamu ya II kama ambavyo inatekelezwa itakamilika ndani ya mwezi huu wa Juni.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi kwa vijiji ambavyo itaonekana kazi haitakamilika ndani ya mwezi Juni, tunaendelea kuifanyia kazi kuviwasha katika mradi wa REA Awamu ya III unaoanza Julai, 2016. Kwa hiyo, vijiji vya Bunda vyote vitapata umeme ifikapo mwaka 2017 kama mnavyotarajia.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza kwa Wizara ya Nishati na Madini. Kwa vile Wilaya za Masasi, Nanyumbu na hasa Masasi Mjini, Kijiji cha Ndanda pamoja na Chikundi, kuna tatizo sana la umeme kukatika kila mara na umeme huu ndiyo ambao tunaambiwa sasa unapelekwa Liwale. Je, Mheshimiwa Waziri anawahakikishiaje wakazi wa Liwale kuwa na umeme wa uhakika, wasije wakapata matatizo ambayo wakazi wa Masasi wanayapata kila mara?
Swali la pili, tuliambiwa watakapoanza kutumia umeme wa gesi, basi hata gharama za kuunganisha, lakini pia na gharama za kuwafikia wale wakazi umeme toka siku ambazo wamelipia zitakuwa ni chache sana. Katika hali ya kushangaza kuna wakazi wa maeneo ya Nachingwea, pia Ndanda na hizo Wilaya nyingine nilizozitaja wanaweza kukaa hata miezi mitatu au minne bila kuunganishiwa umeme toka tarehe waliyolipa. Pia, kuna vijiji vingi ambavyo vinapitiwa na nguzo kuu za umeme zinazokwenda Liwale na Masasi Mjini; Unawaambiaje wakazi wa Masasi juu ya mambo haya mawili?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kuna changamoto za upatikanaji wa umeme hasa katika maeneo ya Masasi na Nanyumbu, siyo Masasi tu hata maeneo mengine ya Liwale pamoja na Nachingwea. Hata hivyo, juhudi zilizofanyika ni kubwa. Nimhakikishie Mheshimiwa Cecil Mwambe kwamba kazi inaendelea. Hata hivyo, kwenye Awamu ya Pili ya REA ni vijiji kwa Wilaya zote alizotaja 152 vimepatiwa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kuna vijiji mia moja na kumi na moja (111) kwa Wilaya zote havijapata umeme. Mkakati uliopo kwa niaba ya wananchi wa maeneo ya Masasi, Nanyumbu, Nachingwea na maeneo ya karibu yatapelekewa umeme kwenye REA Awamu ya Tatu inayoanza mwezi Oktoba, Novemba hadi Disemba mwaka huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la uhakika wa umeme kwa wananchi wa Masasi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na nakushukuru sana kwa sababu umekuwa ukifuatilia jambo hili. Suala la upatikanaji wa umeme kwa Wilaya za Masasi na maeneo ya jirani linafanyiwa kazi na kwa kweli litatatulika kwa muda mfupi sana kuanzia sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, gharama za umeme; kwanza kabisa nichukue nafasi hii kuwaeleza wananchi kwamba gharama za umeme kwa kweli zinashuka. Ni kweli kabisa baada ya kuanza kutumia gesi asilia gharama za umeme zimeshuka na kwa nchi nzima. Gharama za umeme kwa miradi ya REA ni sh. 27,000 na hiyo ni nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, gharama za kulipa umeme kwa wananchi wanaotumia gesi asilia, hasa kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara na maeneo ya jirani, hata kwa kazi wanazounganishiwa na TANESCO ni za chini; badala ya sh. 177 kwa mikoa hiyo miwili ni sh. 99. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kutumia gharama hizo kwa Mikoa ya Lindi, Mtwara pamoja na Wilaya nyingine za Masasi na Nanyumbu.
MHE. VEDASTO E. NGOMBALE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Katika jibu lake la msingi Mheshimiwa Waziri anasema kwamba, ndiyo kwanza wameanza ukarabati wa mitambo ile, nilifanya ziara mwezi wa Saba na nikakutana na Meneja na akanieleza kwamba, ukarabati umefanyika, lakini bado kuna tatizo kila inapofika saa tano ya usiku mashine zile hujizima na baada ya saa nane ndiyo huweza kuwaka tena. Nahitaji kufahamu ukweli ni upi, maelezo ya Mheshimiwa Waziri au yale aliyonipa Meneja wa kile kituo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; bado kuna tatizo kubwa na hasa la kiufundi. Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri anieleze kwamba, mkandarasi aliyetumika kufanya ukarabati ule ni yule aliyeelekezwa na mtengenezaji wa mashine au hawa wenzetu wa Magomeni? Mheshimiwa Naibu Waziri kama yuko tayari kufuatana nami kwenda kuangalia namna ya kutafuta suluhu ya tatizo lile? Ahsante.
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nitoe ufafanuzi mzuri wa matatizo ya umeme kule Kusini. Ukweli ni kwamba, umeme Mikoa ya Lindi na Mtwara una matatizo na matatizo ni ya kiufundi. Ilikuwa ni kampuni ya ARTMUS iliyopewa jukumu la kusambaza umeme huko, ilijenga miundombinu ya msongo mdogo wa kilovoti 33; ukizitoa Mtwara ziende mpaka Masasi, Nachingwea, ukweli ni kwamba umeme unakuwa na matatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kinachofanyika sasa hivi ambacho Mheshimiwa Naibu Waziri ameongea ni kweli kwamba, TANESCO inarekebisha hizo njia, zitajengwa sasa badala ya kilovoti 33 ni kilovoti 132 double circuit (njia mbili) za kuleta umeme mwingi zaidi. Kwa hiyo, hiyo kazi nadhani itakamilika mwisho wa mwaka huu, lakini nimemtuma mtu aende Mtwara kwa sababu, Mbunge wa Mtwara aliniuliza, nimemtuma Engineer aende alete jibu kabla ya Jumatano wiki ijayo. Kwa hiyo, jibu kamili mtalipata kama mradi unaendelea vizuri, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili kutatua hili tatizo, kama anavyosema Mheshimiwa, Somanga Fungu, lazima tukiri mitambo ya Somanga Fungu ina matatizo. Siyo Somanga Fungu tu ni kitu ambacho lazima tuwe wakweli tukifanyie kazi, kwa nini mitambo yetu inavyoanza kazi, ikifika miaka miwili tu inakuwa na hitilafu! Hicho kitu ni lazima tukifanyie kazi ni cha kitaalam; Somanga Fungu ilifungwa baada ya miaka miwili ikaleta matatizo. Ule wa Nyakato Mwanza umefungwa baada ya miaka miwili una matatizo! Mtambo wa Ubungo baada ya miaka miwili una matatizo, hivi ni vitu ambavyo lazima tuviongee kwa uwazi kuliko kuvificha, kuna tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Somanga Fungu ukweli ni kwamba, yule na nadhani Mbunge yuko makini sana alikuwa anauliza swali la kututega sisi; ukweli ni kwamba, aliyetengeneza ile mitambo na anayefanya repair sasa hivi ni watu tofauti, huo ukweli lazima tuukubali. Sasa tunachofanya ni kwamba, ukweli wamefanya rapair ya Somanga Fungu hatuna sababu ya kufunga safari kwenda kule kuthibitisha kwa sababu kazi yenyewe haijakamilika. Kwa hiyo, hakuna kujiridhisha, tunajua kazi haijakamilika, kwa hiyo tungoje ikamilike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la Somanga Fungu kulitatua na Mikoa ya Kusini ni kuingizwa kwenye gridi ya Taifa. Kwa hiyo, fedha zimepatikana na TANESCO wameanza kujenga miundombinu ya msongo mkubwa kutoka Somanga Fungu, kuunganisha na Kinyerezi, tunataka iwe ya kilovoti 400, walikuwa 200 nikasema hapana, tumezowea tunafanya vitu kidogo baada ya muda tena matatizo! Kwa hiyo, watapeleka kilovoti 400 kusudi ule umeme wa Somanga Fungu na wa Mtwara ukiingia Somanga Fungu unaweza kwenda Kinyerezi na nyie mkipata matatizo mnaweza mkapata umeme kutoka kwenye gridi ya Taifa.
Waheshimiwa Wabunge, hili tatizo linatatuliwa tulieni tu, halitachukua muda mrefu. (Makofi)
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina swali moja la nyongeza.
Ninaamini Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba zahanati karibu nane zimekwishapata umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Kwanza na ya Pili, lakini hazijaunganishwa.
Je, ni lini Wizara ina mpango wa kuunganisha umeme kwenye Zahanati hizo nane?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa hospitali alizotaja za Kibondo na Kasulu zote zimeunganishwa na umeme lakini hazijawashwa. Utaratibu wa kuwasha hospitali zote za Mkoa wa Kigoma na Mikoa mingine ya jirani zinafanyika mwezi wa 11 na 12 mwaka huu wa 2016.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Karema ni kituo ambacho kimekamilishwa ujenzi na Serikali lakini tatizo kituo hicho hakina umeme ili kiweze kufanya kazi. Je, ni lini Serikali itatoa fedha za kukamilisha kituo hicho ili kiweze kuwahudumia wananchi wa Tarafa ya Karema?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kakoso, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Jimbo la Mpanda hadi sasa linapata umeme kwa kutumia mafuta kitu ambacho ni gharama kubwa sana. Hata hivyo, tumeshakaa na Mheshimiwa Kakoso, tumeainisha vijiji vyote vya Mpanda na Katavi, vijiji vyote vya eneo lake pamoja na hospitali na maeneo mengine yatapata umeme kuanzia Julai, 2016.
MHE. VICKY P. KAMATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa wananchi wa Nyamalembo, Nyamasagata, Semina na sehemu zote ambazo hawa wawekezaji wa GGM wamechukua maeneo yao ningependa kufahamu ni nini manufaa ya moja kwa moja wanayoyapata wananchi hao ambao waliruhusu maeneo yao yanatumiwa na GGM?
Swali la pili, kwa kuwa Serikali imekuwa ikiahidi mara kwa mara kuwapatia maeneo ya uhakika na ya kudumu wachimbaji wadogo na kwa kuwa mpaka sasa bado haijawapatia wachimbaji hawa. Je, Serikali inapanga nini kutatua tatizo hilo, ukizingatia hivi karibuni mwezi wa saba ile PML ya STAMICO ina expire ni kwa nini Serikali isitoe tamko hili sasa hivi hapa kwamba mara baada ya hii PML ku-expire basi lile eneo litapewa wachimbaji wadogo wadogo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, manufaa ya wananchi wa Geita kulingana na mgodi huu ni kweli kabisa Watanzania wengi na wananchi wa Geita hasa wa maeneo yanayozunguka mgodi huu wamekuwa wakitarajia manufaa makubwa sana. Lakini hata hivyo mambo ambayo wananchi wa maeneo hayo wamenufaika ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mgodi ulipoanza mwaka 1999 wananchi wanaozunguka mgodi huo walifanyiwa fidia. Wananchi ambao waliofanyiwa fidia ni pamoja na maeneo ya Nyamalembo, wananchi wa Nyamalembo wapatao 346 walilipwa fidia jumla ya shilingi bilioni sita nukta nane, lakini wananchi wa Katoma ambao wanafikia karibu 732 walilipwa shilingi bilioni 2.7 kama fidia na wananchi wengine wa Nyakabale, Nyamatagata ambao wanafikia 700 walilipwa shilingi bilioni 732 hayo ni manufaa ambayo wananchi hao waliyapata.
Lakini hata hivyo, pamoja na manufaa hayo mgodi wa GGM umeendelea kutoa ushuru kwa wananchi wanaozunguka maeneo hayo ambayo ni service levy. Hadi sasa mgodi huo umeshatoa takribani shilingi bilioni 4.7 kama service levy lakini manufaa mengine wanayoyapata wananchi hawa ni pamoja na ajira. Mgodi wa GGM hivi sasa unaajiri Watanzania wanaofikia 1568 kama nilivyozungumza kwenye jibu langu la msingi wakati wa bajeti yetu. Lakini kadhalika bado mgodi GGM wananchi wanaozunguka maeneo ya Geita, Nyamatagata, Katoma, Nyakabale, pia wamezungumzia kujengewa hospitali, vituo vya afya pamoja na shule za msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, kuhusu kuwapatia maeneo hasa ya Mgodi wa Bacliff ambao sasa hivi unamilikiwa na STAMICO pamoja na wabia wenzake. Niseme tu nitumie nafasi hii nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge Kamata ameendelea kupambana sana kwa wananchi wa Geita na mimi nimuombe aendelee kupambana. Lakini nimhakikishie tu sasa hivi Serikali inakamilisha mazungumzo kupitia STAMICO pamoja na wabia wake ili kuona sasa ni eneo gani kampuni yetu ya STAMICO pamoja na wabia wake kwenye Mgodi wa Bacliff maeneo yapi wanaachi kwa ajili ya wananchi wa Geita. Hata hivyo Serikali inaendelea kuwategea maeneo mengine mbadala karibu na mgodi huo. Maeneo ambayo Serikali itayatenga kama ambavyo tunasema kila siku pamoja na maeneo ya Mgusu pamoja na maeneo mengine machache sana ya kule Nyakabale pamoja na Nyamalembo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tumeshatenga maeneo mengine kule Kasubuya, Mheshimiwa Mbunge Kamata unajua ulikwishakuja tukazungumza sana tumewatengea hekta 432; kule Kasubuya. Lakini kule Matabe tumewatengea hekta 568; kule Chato kule kwangu kule tumewatengea hekta 1258; lakini pia bado tunawatengea maeneo mengine hekta 232 maeneo ya Geita.
Kwa hiyo, nimuomba sana Mheshimiwa Vicky Kamata bado tuko na wewe naomba uje ukae tena tuendelee kukaa tupange kama ambavyo huwa tunapanga siku zote kwa niaba ya wananchi wa Geita, ahsante.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri napenda kusikia pia kauli ya Serikali kuhusu pia wachimbaji wadogo wa Biharamulo wakiwemo wa Busiri, Kalukwete, Mavota, Kalenge na wale Nyanchimba Wilaya Chato kwa sababu nao wanapenda kusikia kauli ya kutengewa hekta kadhaa 500, 600 kama ilivyofanyika kwenye maeneo ya Geita.
NAIBU WAZIRI NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimesema na nitumie nafasi hii nikushukuru sana rafiki yangu Mheshimiwa Mbunge wa Biharamulo kwa sababu ni jirani yangu, maeneo ya Biharamulo mwaka jana tumetenga hekta 1332 kwa Mheshimiwa Oscar, lakini Mheshimiwa Oscar bado tunakutengea eneo pale kwenye Mgodi wa Tulawaka, pale Mavota tunafanya mazungumzo. Tumeshakaa na wewe na Mbunge wa Bukombe tumeainisha mahektari kama hekta 2100 tuzitenge kwa ajili ya wananchi wako, lakini bado nikushukuru sana kwa sababu umependa pia nizungumzie kwangu kule Chato. Kule Chato Kampuni ya Wakawaka
imeachia eneo takribani ya hekta mbili ambako wananchi wako wa Biharamulo na wangu tutawagawia kwa utaratibu huo huo.
MHE. MBONI M. MHITA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuweza kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Jimbo la Handeni Vijiji kwenye Kata ya Kang‘ata eneo la Magambazi, kuna mgogoro kati ya wananchi na mwekezaji lakini kwa sasa mgogoro huo unasubiri maamuzi kutoka kwenye Wizara ya Nishati na Madini. Lakini wakati huo huo mgogoro huo umeweza kusimamisha shughuli nyingi ambazo kwa namna moja ama nyingine zingeweza kunufaisha wananchi wa Kata ya Kang‘ata na eneo la Magambazi. Je, ni lini Wizara itatoa maamuzi juu ya utatuzi wa mgogoro huu ili shughuli ziweze kuendelea? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli maeneo ya Handeni pamoja na maeneo mengi ya Kilindi kuna migogoro mingi sana kati ya wachimbaji wadogo, wananchi pamoja na wawekezaji kutoka nje. Lakini kwa jitihada ambazo tumechukua hasa kwa maeneo ya Handeni wiki iliyopita tulimtuma mkaguzi wa migodi kwenda kukagua migogoro iliyopo kati ya wananchi wa Magambazi pamoja na wawekezaji wanaochimba pale. Hivi sasa kampuni ambayo ilikuwa inachimba pale Kampuni ya Scanda ambayo pia ilifanya utafiti haijakamilisha kazi zake. Lakini nimhakikishie tu timu yetu ipo pale sasa na tukitoka hapa Mheshimiwa wa Handeni tukae tukubaliane tufuatilie timu imefikia hatua gani lakini tumeipa muda wa wiki mbili na wiki ijayo wataleta taarifa na taarifa hiyo tunahakikisha kwamba itatoa suluhisho na mgogoro wa wananchi wa Handeni pamoja na wachimbaji hao.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru naomba kumuuliza swali fupi Mheshimiwa Waziri pamoja na jitihada alizozifanya katika Mgodi wa Resolute, Nzega. Je, sasa Serikali iko tayari leseni iliyokuwa chini ya MRI iweze kugawia kwa wachimbaji wadogo wa Mwaishina ambayo maarufu kwa namba saba original katika mji wa Nzega?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lililokuwa likimilikiwa na kampuni maarufu sana ya uchimbaji iliyoanza hapa nchini Resolute lilimilikiwa sasa na Serikali kupitia Chuo chetu cha Madini (MRI). Ni kweli kabisa lengo kubwa la mgodi kumilikisha kwa Serikali ili ku-plan kutoa fursa kwa wanafunzi wa Tanzania ambao wanasoma masomo kwa nadharia waweze sasa kupata eneo kwa kufanya kwa vitendo ndiyo maana tunawagawia eneo lile. Lakini nikubaliane na hoja ya Mheshimiwa Bashe tumeshazungumza naye, tumeshaweka mikakati ili tuone ni eneo gani ambalo Serikali kupitia MRI hawalihitaji ili waweze kugawia wananchi wa Nzega lakini hata hivyo tumechukua hatua mbadala zaidi ya hapo. Mheshimiwa Bashe nikuhakikishie Kampuni ya Zari Exploration imeachia kilometa nyingine kumi karibu na eneo hilo ambao wananchi wako wa Nzega tutawagawia kwa utaratibu wa Serikali.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu mazuri yenye kuwaletea matumaini wananchi wa Hanang. Sasa naomba niulize maswali madogo mawili, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa kutambua kwamba, Wilaya ya Hanang ilisahauliwa katika Awamu ya kwanza na ya pili, sasa atakubaliana na mimi, na ninahakika atakubaliana na mimi kwamba, vijiji hivyo vya Hanang alivyovitaja sasa vitakuwa Awamu ya tatu viwe vya kwanza katika kupewa umeme katika Awamu hiyo ya tatu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; najua kwamba, awamu ya kwanza na ya pili ilipewa vijiji vichache mpaka sasa havijapata umeme. Je, Naibu Waziri atakubaliana na mimi kwamba, katika muda mfupi unaokuja vijiji hivyo vichache vipate umeme basi, ili viwape matumaini wananchi wa Hanang?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nirekebishe kidogo kwamba, katika Jimbo la Hanang kwa kweli, hatukupeleka vijiji vingi! Ni vijiji saba tu ambavyo tulivipatia umeme kwenye REA awamu ya pili, lakini niongezee kwa Mheshimiwa Mbunge kama alivyosema vijiji 19 ambavyo vilikusudiwa kupewa umeme kwenye REA awamu ya pili vyote vitakamilika ndani ya siku 20 zilizobaki. Kwa hiyo, awamu ya pili itakamilisha vijiji vyako Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu na vijiji vingine 44 ulivyoomba na vyenyewe vitapatiwa umeme kwenye REA awamu ya tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu vile Vijiji vya Kisambalang, Dang‟aida, Dawidu, Mwanga na Wandolendode, vyote vitapatiwa umeme katika awamu ya tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusiana na uhakika kwamba, je, muda uliobaki kweli kazi iliyobaki itakamilika?
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kufunga miundombinu mikubwa kwenye Jimbo la Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu imekamilika, kazi iliyokuwa imebaki sasa ni kusambaza transformer kama 10 ambazo tuliahidi. Bado transformer tano kukufungia Mheshimiwa Mary Nagu, mwezi ujao nadhani tutakamilisha transformer zote 10.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini baada ya kusema hayo, vile vijiji vingine 44 ambavyo umeviomba pamoja na shule za sekondari, vituo vya afya kwa bilioni 15.8 tulizokutengea nadhani tutakamilisha kazi yote Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, pesa ambazo mmetutengea kwa mwaka huu, bilioni 587 ambazo ni kwa ajili ya kuwasambazia umeme vijijini, zote tutazitumia kwa kazi hizo na vijiji vyote vilivyobaki vitapata umeme kwenye mradi kabambe wa REA awamu ya tatu unaoanza mwezi Julai mwaka huu.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi nzuri ambayo Wizara hii imefanya sasa naomba niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, kuna baadhi ya Vijiji vikiwemo Ng‟ang‟ange, Pomelini, Masege, Mwatasi, Kesamgagao, Masisilo, Ukumbi na vijiji vingine umeme tayari umeshafungwa na umefika, sasa tatizo ni kuwasha! Ni lini utawashwa ili wananchi sasa waendelee kuishi kwa matumaini na mategemeo makubwa kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, yeye suala lake ni kuwasha tu, lakini miundombinu yote ipo. Nimeshaongea na Meneja, wiki ijayo Jumanne atamwashia Mheshimiwa Mwamoto katika vijiji vyake vyote. Kwa hiyo, kwake umeme utawaka bila wasiwasi.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, je, Serikali ina mpango gani kupeleka umeme kwenye huduma zingine za jamii kama vile zahanati, Vituo vya Polisi na Ofisi za Serikali ya Kijiji katika Kijiji hicho cha Lugala?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sababu matatizo yaliyopo Malinyi yanafanana kabisa na matatizo yaliyoko katika Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, je, Serikali ina mpango gani kupeleka umeme katika Vijiji vya Luholole, Misala, Mmalazi, Kivuma, Ludewa na Amini kule kwenye Kata ya Kinole?
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali wa kupeleka umeme kwenye maeneo aliyoyataja hasa ya huduma za jamii uko pale pale. Kama nilivyosema mara nyingi kazi kubwa ya mradi wa REA awamu ya tatu, inakusudia kupeleka umeme kwa vipaumbele vya zahanati, shule za sekondari na shule za msingi lakini pamoja na taasisi nyingine za Serikali ikiwa ni pamoja na Magereza. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo yote ya vituo vya afya, zahanati, shule pamoja na taasisi nyingine yatapelekewa umeme wa uhakiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusiana na vijiji alivyovitaja, kama nilivyosema REA awamu ya tatu itapeleka umeme kwenye vijiji vyote ikiwa ni pamoja na vijiji vya Mheshimiwa Mbunge Omary kama alivyovitaja bila kubakiza kijiji chochote.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Mji wa Kigamboni au Wilaya mpya ya Kigamboni inakua kwa kasi sana. Umeme kwa wakazi wa Kigamboni unatoka katika Wilaya ya Ilala na ku-supply baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Ilala, Temeke, Mbagala yote, Mkuranga yote na Kigamboni yote. Je ni lini sasa Serikali itajenga kituo cha umeme katika Wilaya mpya ya Kigamboni ili kuendana na mahitaji ya sasa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Kigamboni ni mpya na kwa sasa unatumia umeme kutoka Ilala na umbali uliopo ni zaidi ya kilometa 50. Kwa nguvu iliyopo kwa sasa hivi, uwezo wa kupeleka umeme kwa Kigamboni hautoshi. Mpango wa Serikali utakapokuwa unasambaza umeme kwenye REA awamu ya tatu, utajenga pia kituo cha kupozea umeme kwenye Wilaya ya Kigamboni ili kuhakikishia upatikanaji wa umeme kwa wananchi wa Kigamboni.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa umeme ni kichocheo muhimu katika shughuli za kiuchumi. Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika Vijiji vya Langoni, Kikokwe pamoja na Kigulusimba Misufini ili kuhakikisha kwamba wananchi wa Pangani wanaenda kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kujiletea maendeleo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa hata sasa hivi bado Serikali inapeleka umeme kwenye vijiji vingi chini ya mradi wa REA awamu ya pili. Hata hivyo, kuna vijiji vingi havijapata umeme. Jimbo la Mheshimiwa la Pangani tunalifahamu, ni vijiji vichache sana vimepata umeme. Nimeshazungumza naye na nikamwambia alete orodha yake ya vijiji ambavyo havijapata umeme na ameshaniletea. Kwa hiyo, napenda kumwambia Mheshimiwa Mbunge wa Pangani vijiji vyake vyote alivyovitaja vitapata umeme kwenye REA awamu ya tatu.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Suala la umeme vijijini pamoja na ahadi nzuri za Serikali na kwenye bajeti hii ya 2016/2017, Serikali imeahidi vizuri sana na tunasema vijiji vyote vitapewa umeme. Kwenye shule za sekondari, shule za misingi, zahanati na sehemu nyingine za hospitali. Tunaomba Serikali itoe commitment kwamba katika mwaka huu wa fedha tuta-specialize hasa kwenye vituo vya afya na zahanati ili tusi-generalise kwamba tutapeleka kila sehemu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tumekuwa tukieleza, labda niwaombe Waheshimiwa Wabunge watupe ushirikiano kuhusu jambo hili. Wananchi na Waheshimiwa Wabunge wengi wamekuwa wakiomba sana kupelekewa umeme kwenye vijiji vyao badala ya huduma za afya na taasisi nyingine. Namshukuru sana Mheshimiwa Kigola lakini niseme tu mpango wa Serikali wa awamu ya tatu ya REA, unazingatia sana vipaumbele vya kuwapelekea umeme taasisi za jamii pamoja na kwamba tunawapelekea pia kwenye matumizi ya nyumbani. Kwa hiyo, mpango wetu unatekelezwa hivyo. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge ikibidi anilitee taasisi zake za umma kabla hatujatoka kwenye Bunge hili ili nimhakikishie kwamba tutaanza na hizo kabla ya kuwapelekea umeme kwenye nyumba zao.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa kumekuwa na matamshi yanayotofautiana kutoka Serikalini kuhusiana na maendeleo ya mgodi huu, tungependa sasa kupata tamko rasmi ambalo wananchi watalielewa kuhusiana na uendelezwaji wa mgodi huu. Mwaka jana mwishoni tuliambiwa kuwa tayari mwekezaji ameshapatikana na karibu ataanza kazi. Tukaja kuambiwa mwekezaji yule ameonekana hafai na anatafutwa mwingine. Sasa tunaambiwa wako kwenye hatua za mwisho za kumtambulisha mwekezaji. Napenda kupata tamko rasmi kuwa ni lini huyo mwekezaji atapatikana na wananchi wategemee kuanza kufaidika na mgodi huo lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa mgodi huu umetolewa leseni kwa miaka 25 na kwa muda mrefu sana huu mgodi umekaa bure. Je, huo muda wa leseni utaongezwa pindi atakapopatikana huyo mwekezaji au la sivyo mategemeo ni yapi mwekezaji huyo akija?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la kwamba mgodi umechukua muda mrefu bila kuanza kazi zake, ni kweli kabisa. Labda nitoe historia kidogo ni kwamba Mgodi huu wa Kiwira ulikuwa uanze tangu mwaka juzi lakini mkandarasi aliyepatikana kwa ajili ya ujenzi huo baada ya kufanya upekuzi rasmi (due diligence) hakuonekana kuwa na uwezo wa kifedha. Kutokana na msimamo wa Serikali, tuliona tusitishe badala ya kuingia hasara kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya pesa kupatikana sasa na kama mlivyoona tumepitisha shilingi bilioni mbili kwenye bajeti yetu na tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, tutaanza shughuli za awali ambazo zitahusisha pia ujenzi wa awamu ya kwanza pamoja na kuwalipa pia wakandarasi waliohusika katika feasibility study. Ujenzi kamili unatarajiwa kuanza Desemba 2017 au 2018 na utachukua miaka mingi kama inavyoonekana. Kwa hiyo, ujenzi wa mradi huu utaanza baada ya kumpata mkandarasi na matarajio makubwa mwaka 2018 utaanza kujengwa rasmi.

NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naona kwenye jibu langu nilijumlisha kwa harakaharaka. Labda nimweleze, ni kweli mgodi huu unachukua miaka 25 na miaka 25 ulikuwa ni uhai wa Mgodi wa Kiwira sawa na migodi mingine mikubwa hapa nchini. Sasa imechukua takribani miaka 11 wakati shughuli za upembuzi zinakamilika bila kuanza uzalishaji. Kwa utaratibu wa Sheria ya Madini Na. 14 ya 2010, kifungu cha 111, kama mwekezaji atagundua kwamba anahitaji kuongezewa muda anaweza pia kuongezewa uhai wa muda wa miaka 25 mingine mpaka atakapokamilisha shughuli za uchimbaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, uhai wa leseni, kama akiona reserve inatosha kuchimbwa na reserve iliyopo pale Kiwira ni tani milioni 30, kwa hiyo ni kweli kwamba tani milioni 30 inawezekana isichimbwe kwa ndani ya miaka 14 akahitaji muda mwingine mrefu. Akihitaji muda mwingine mrefu anaweza akaongezewa miaka mingine 25.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kule jimboni kwangu, Jimbo la Songwe na wilaya mpya, kuna kampuni moja inaitwa Sun Marie, walipata leseni mwaka jana mwezi Aprili kwa ajili ya kuanza uchimbaji wa makaa ya mawe Kata za Magamba na Namkukwe Jimboni Songwe, lakini mpaka sasa hawaonekani walipo. Walikuwa wanafanya utafiti wa kujenga barabara mpaka sasa hatujajua wako wapi, Halmashauri haiwajui, tunaomba msaada wa Serikali, hawa watu kwanza wako wapi na ni lini wataanza kazi za uchimbaji wa madini haya?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kampuni anayoitaja Mheshimiwa Mulugo ipo katika eneo lake na kwa sasa hivi imepewa miaka saba kwa ajili ya kukamilisha utafiti. Miaka mitatu iliyobaki ya utafiti ni matarajio kwamba watakamilisha na waanze kuchimba rasmi. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mulugo avute subira ni matarajio baada ya miaka mitatu watakamilisha feasibility study na wataanza uchimbaji. Kwa hiyo,
baada ya miaka mitatu Mheshimiwa Mulugo atawaona wanakuja huko na magreda kwa ajili ya kuanza uchimbaji kama feasibility itaonesha kuna madini hayo
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kule Songea kuna uchimbaji wa makaa ya mawe katika eneo Ngaka na uchimbaji wa makaa yale ya mawe unapita katika Mji wangu wa Songea. Kwa hiyo, pale Songea kuna uharibifu mkubwa sana wa mazingira kwa sababu yale magari yanayopita ni magari ya open body sio box body, matokeo yake ni kwamba mji unaharibika kimazingira lakini vilevile barabara zinaharibika. Nataka nijue Serikali ina mpango gani wa kuulipa fidia Mji wa Songea ili kukabiliana na majanga yanayotokana na usafirishaji wa makaa hayo ya mawe?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kama mnavyotambua, shughuli za uchimbaji wa madini zinaathiri mazingira kwa vyovyote vile hasa katika kusafirisha mitambo, kusafirisha madini lakini hata wakati wa uchimbaji. Nikubaliane na Mheshimiwa Gama kwamba kama kuna uharibifu wa mazingira kama ambavyo Sheria ya Madini inataja kwenye kifungu cha 65(1) (b) kwamba kama kutakuwa na uharibifu wa mazingira, Halmashauri inayohusika watakaa na mgodi kujadili uharibifu uliotokea kwa ajili ya kulipa fidia. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge akae na Halmashauri yake, kama itadhihirika kwamba kuna uharibifu wa barabara unaosababishwa na kampuni hii basi wakubaliane suala la fidia kwa mujibu wa Sheria ya Madini pamoja na Sheria ya Ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hayo, yapo majukumu mengine ya mgodi pamoja na Halmashauri. Nawashauri wakae wakubaliane juu ya tozo zinazoweza kutozwa kutokana na uharibifu wa mazingira. Hata hivyo, kabla ya mgodi kufungwa kwa kawaida kuna jambo linaitwa mine closure plan, hawa wamiliki wa leseni wana mine closure plan inayoonesha kwamba kama kuna uharibifu wa mazingira basi utafidiwa kulingana na uharibifu ulivyotokea.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza, wananchi wamekuwa wanalalamika sana kwamba vijiji ambavyo vimeshapatiwa umeme hadi sasa wanaopewa kipaumbele cha kuunganishiwa umeme ni wale tu wanaokaa kandokando ya barabara kuu. Je, ni lini wananchi wote ambao vijiji vyao vimeunganishiwa umeme watapatiwa umeme wanaohitaji?
Swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri aliahirisha mwezi uliopita safari yake ya kuja Sikonge kujionea matatizo. Je, ni lini sasa atapanga ziara yake kuwatembelea wananchi wa Sikonge?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa REA Awamu ya II inayoendelea ambayo itakamilika mwezi huu, mpango wake mahsusi ulikuwa ni kupeleka umeme kwenye vituo vya vijiji na siyo kusambaza kwenye vitongoji. Sambamba na hilo, kabla hatujaanza Mradi wa REA Awamu ya III, kuna mradi mwingine unaosambaza umeme kutoka kwenye vituo na center mbalimbali na kuwapelekea wananchi kwenye vitongoji vyao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi huu nimekuwa nikiusema, unaitwa Underline Distribution Transformer ambao unaanza Julai, 2016 na utakamilika ndani ya miezi 18. Mradi huu utasambaza umeme kwenye vitongoji vyote ambapo umeme wa msongo wa kilovoti 33 umepita.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge ni kweli tumekuwa tukiahidi kwamba tutapeleka umeme kwenye vitongoji. Nilimwomba Mheshimiwa Kakunda aniletee vitongoji vyake vyote, ameshaleta na namshukuru sana. Kwa hiyo, napenda kumwambia Mheshimiwa Kakunda vitongoji vyake ambavyo umeme umepita vitapatiwa umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ni lini tutatembelea, nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge, kwa ridhaa yako nadhani tukishamaliza Bunge hili, niongozane na Mheshimiwa Kakunda na niwahakikishie Wabunge wa karibu na Sikonge nitawatembelea wote mara baada ya Bunge hili la bajeti.
MHE. JOHN P. KADUTU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa vile Mradi huu wa REA katika Jimbo la Ulyankulu umekuwa ukisuasua na wakati mwingine unatia hofu kwa wananchi kwa sababu maeneo muhimu ya taasisi, zahanati na vituo vya afya mfano, kama Barabara ya Kumi pamoja na Shule ya Sekondari Mkindo na maeneo mengi tu yamekuwa yakirukwa. Serikali ituambie ni lini mradi huu utakamilika na umeme kuwashwa katika Jimbo la Ulyankulu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli umeme umekuwa ukirukaruka kama ambavyo wananchi wanasema na kama Mheshimiwa Mbunge anavyosema. Hata hivyo, kama nilivyokwishaeleza, maeneo yote ambayo yamekuwa yakirukwarukwa, siyo kwamba yalirukwa, kulikuwa na mpango madhubuti kwamba umeme mwingine utakuja chini kupita kwenye vitongoji vyote. Kwa hiyo, vitongoji vyote vya Mheshimiwa wa Ulyankulu vitapitiwa na umeme katika Awamu hii ya II.
Mheshimiwa Naibu Spika, Awamu ya II inakamilika mwezi Juni, 2016 kama ambavyo nimekuwa nikieleza na Awamu ya III inaanza mwezi Julai, 2016 na itakamilika baada ya miaka mitatu hadi minne. Kwa hiyo, vijiji vyote vya Ulyankulu vya Mheshimiwa Mbunge, ikiwa ni pamoja na eneo la Barabara ya Kumi, vituo vya afya, zahanati pamoja na shule zitapatiwa umeme chini ya mradi wa Underline Transformer na chini ya Mradi wa REA Awamu ya III unaoanza mwezi Julai, 2016.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililojitokeza katika Wilaya ya Sikonge kama alivyoeleza Mheshimiwa Kakunda ndivyo ilivyo katika Wilaya ya Urambo. Namshukuru Naibu Waziri alifika Urambo ila wananchi wa Urambo wanasikitika alifika lakini vijiji vingi hawajapata umeme. Je, ni kwa sababu ramani ilikosewa na yuko tayari kumtuma mhusika aende kuangalia tena kwa kuwa wananchi wengi hawakunufaika na umeme huo unaokamilika wa awamu ya pili? Hata hivyo, bado wanamkumbuka na wanaomba arudi tena, je, atarudi tena awaone?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile maswali ni mawili, nachagua swali la kwenda pamoja na Mheshimiwa Mbunge. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuhusu suala la kwenda wala sitatuma mtu, nitakwenda mwenyewe na nitakwenda na Mheshimiwa Mbunge.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri swali la nyongeza. REA Awamu ya II imebakiza siku 27, je, wameshafanya tathmini ya kutosha nchi nzima? Kama jibu ni ndiyo utekelezaji wake ni asilimia ngapi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nachagua swali la tathmini ya ujumla. Nimhakikishie Mheshimiwa Ndassa na nimshukuru tumeshirikiana, mpaka sasa tathmini tuliyofanya ukamilifu wa kazi ya REA Awamu ya II ni asilimia 91 ya kazi zote zilizokwishakamilika.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa MWenyekiti, pamoja na majibu hayo mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Jimbo langu la Mkuranga utafiti ulishafanyika na ikagundulika gesi asilia katika kijiji cha Kiparang‟anda na kisima kiko pale. Naomba sasa Serikali inieleze ina mpango gani wa kuhakikisha kisima kile cha gesi kilichopo pale Mkuranga kinatumika kwa manufaa ya Taifa letu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha gesi hii inatumika ipasavyo katika kuzalisha umeme wa uhakika ili kikidhi haja ya viwanda na makazi yanayokuwa kwa kasi katika Jimbo hili la Mkuranga? Ahsante
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa makampuni ya utafiti yamefanya utafiti wa mafuta na gesi katika maeneo mbalimbali hasa katika maeneo ya Pwani ikiwepo eneo la Kiparang‟anda. Nimhakikishie Mheshimiwa Ulega kwamba eneo la Kiparang‟anda bado linafanyiwa utafiti na kazi inayofanyika sasa ni kuthibitisha kama kweli gesi na mafuta vipo. Mara baada ya kuthibitika hatua itakayofuata ni appraisal kuangalia kibiashara kama mafuta hayo bado yanaweza kuchimbika. Hatua itakayofuata baada ya hatua hiyo ni eneo la kufanya uendelezaji yaani development na baada ya hapo sasa hatua inayofuata ni uchimbijaji wa mafuta. Kwa hiyo, nimshukuru sana Mheshimiwa Ulega, kazi inaendelea kufanyika na hatua zikifikia mwisho Mheshimiwa Ulega na wananchi wake watafahamishwa rasmi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusiana na manufaa ya gesi kutumika kwa ajili ya umeme. Ni kweli kabisa kwani kwa sasa asilimia kubwa ya umeme tunaotumia hapa nchini ni kutokana na gesi asilia. Ni vyema niwahakikishie wananchi pamoja Waheshimiwa Wabunge kwamba sasa hivi megawati 743 za umeme zinatokana gesi na ni kiasi kikubwa sana cha gesi. Kwa hiyo, wananchi wa Mkuranga na maeneo mengine ya Pwani na siyo Pwani tu Mtwara pamoja na Lindi hata maeneo mengine ya Ukanda wa Kaskazini tutaendelea kutumia umeme wa gesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Ulega vijiji vyake pamoja na vijiji vingine vya Rufiji, vijiji ambavyo ni 42 pamoja na 43 vya Mheshimiwa wa Rufiji pamoja na Kibiti vyote vitapata umeme kwa kutumia umeme wa gesi.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli anasema kwamba msema kweli ndiyo mpenzi wa Mungu na mimi naomba niulize maswali ya kiukweli ukweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la umeme Rufiji ni takribani mwaka mmoja sasa tunapata umeme kwa saa nne tu kwa siku. Hali hii imesababisha vijana wa pale Ikwiriri kufunga viwanda vyao vidogo vya furniture kwa kuwa umeme wakati mwingine unakuja usiku. Naomba kufahamu kauli ya Serikali waliyoitoa kwamba nchi hii hakuna mgawo wa umeme, je, Rufiji siyo sehemu ya Tanzania? Hilo ni moja.
Swali la pili, wananchi hawa wa Rufiji hawana barabara hata robo kilometa, hawana maji, hawana hospitali hata X-ray machine hawana japokuwa wilaya hii ni ya zamani sana. Mchango wa Rufiji kwa Pato la Taifa ni asilimia 19 kutokana na hifadhi ya Taifa pamoja na misitu. Naomba kufahamu kwa nini Serikali inawachonganisha wananchi wa Jimbo la Rufiji na Chama chao cha Mapinduzi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza sana Mheshimiwa Mchengerwa kwa maswali yake mazuri, lakini kwa jinsi anavyowawakilisha wananchi wa Rufiji. Mheshimiwa Mchengerwa hongera sana na wananchi wako nadhani watapata maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijielekeze kwenye maswali mazuri ya nyongeza ya Mheshimiwa Mchengerwa. Suala la kukatikakatika kwa umeme, maeneo yanayopatiwa umeme kutoka Somanga Funga ambao ni mtambo unaosambaza umeme maeneo ya Rufiji pamoja na Kilwa, ni kweli kabisa kuna tatizo hilo. Kama nilivyowaeleza juzi mtambo wetu wa Somanga Funga ulikuwa na matatizo. Mtambo huu una vituo vitatu na mashine tatu za kuzalisha umeme, lakini mashine zilikuwa na matatizo ya uchakavu jambo ambalo tunalifanyia kazi na Serikali imetenga shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ukarabati. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mchengerwa pamoja na wananchi wa Rufiji mtambo huo utarekebika na kukatika umeme kutaisha kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata ule mtambo wa tatu ambao pia ulikuwa na hitilafu tunafunga sasa mtambo mwingine kwa ajili ya kuboresha uzalishaji wa umeme kwenye Mji wa Rufiji ambao unagharimu shilingi bilioni mbili. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mchengerwa na wananchi wake watapata umeme wa uhakika hivi karibuni. Nimhakikishie vijiji vyake vyote vya Luwe, Ngarambe, Ngombani, Kilimani A na B na Mashariki vyote vitapata umeme. Kwa hiyo, wananchi watapata umeme wa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikiri kwamba Rufiji ni sehemu ya Tanzania kama vijiji vingine. Sasa nijibu swali la pili kwa nini Serikali inawachonganisha wananchi wa Rufiji na maeneo mengine, sidhani na sina uhakika Mheshimiwa Mchengerwa. Nikiri kwamba Serikali haiwachonganishi wananchi wa Rufiji na maeneo mengine. Japo swali lako linahusiana na masuala ya barabara, maji, umeme lakini kwa vile Serikali ni moja nimhakikishie kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haiwachonganishi wananchi na Rufiji na maeneo mengine. Ahsante sana.
MHE. WILLY Q. QAMBALO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo ya nyongeza pamoja na majibu yenye matumaini ya Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kisima hiki cha Karatu Mjini kimeombewa umeme sasa ni mwaka mmoja na nusu lakini bado haujaunganishwa na nikiangalia fedha zinazoongelewa kukamilisha kazi ile ni shilingi milioni 33, naona hizi ni fedha kidogo sana kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano Serikali ya Hapa Kazi Tu.
Mheshimiwa Waziri kwa nini Serikali isitafute fedha hizi shilingi milioni 33 ili kisima hiki kiweze kukamilika ili wananachi wapate huduma hii muhimu?
Swali la pili, Awamu ya Tatu ya REA inasubiriwa kwa hamu sana katika nchi yetu kwa sababu ni awamu ya kuiwasha karibu Tanzania yote. Hivi sasa tuko mwezi wa tatu ndani ya awamu hiyo; je, ni lini utekekezaji au ujenzi wa miundombinu ya umeme katika maeneo yetu utaanza ili wananchi wetu waweze kujiandaa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mji wa Karatu Mjini kweli ulikuwa upelekewe umeme tangu awamu iliyopita lakini Serikali kulingana na kutoa vipaumbele imetoa shilingi bilioni 33.81 kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, nimhakikishie tu kwamba hizo fedha zitatosha na isipotosha Serikali bado itatafakari namna ya kuongeza pesa kwa ajili ya kukamilisha mradi huo. Kwa sasa nina uhakika hizo fedha zinatosha na mji wa Karatu Mjini utapata umeme wa uhakika na visima vya maji vyote vitapata umeme kwa kutumia mitambo ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Qambalo tumekuwa tukishirikiana sana hata kwenye awamu ya Bunge lililopita. Vijiji alivyotaja ambavyo ni vijiji 21 ambavyo havijapata umeme, nimhakikishie Mheshimiwa Qambalo tumekupelekea umeme vijiji 27 bado vijiji 21 na kati ya vijiji 21 ambavyo bado vimebaki navitambua sana na nimeshafika eneo lile. Kijiji chako cha Endamarariek kitapata umeme, Kambi Faru vitapata umeme hata kule Mbuga Nyukundu itapata umeme kule Rhotia Mbulu kwenye kijiji chako Mheshimiwa Mbunge kitapata umeme pamoja na Mikocheni na Changarawe vyote vitapata umeme.
Kwa hiyo namhakikishia Mheshimiwa Mbunge vijiji vyake vyote ambavyo nimevitaja na ambavyo sijavitaja pia vitapata umeme na kwamba REA Awamu ya Tatu inaanza kuingia sasa site kuanzia mwezi wa Novemba na mwezi wa Disemba. Hivi sasa wakandarasi wameshapatikana wasimamizi wa kazi wameshapatikana, kazi iliyobaki sasa ni kuanza kutekeleza kwenye kipindi cha mwezi Novemba hadi Disemba. Nimhakikishie vijiji vyake vyote 27 hata kijiji chako Mheshimiwa kile Kijiji cha Kilimamoja kitapata umeme na Kilimatembo bado kitapata umeme. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Willy Qambalo pamoja na majibu yote hayo sijayaona makofi au umepiga ni mimi nilikuwa sioni. Tunaendelea Waheshimiwa Mheshimiwa Musukuma Joseph Kasheku Mbunge wa Geita, swali lake litaulizwa kwa niaba na Mheshimiwa Lolesia Bukwimba.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri lakini nina maswali mawili tu ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; katika upelekaji wa umeme vijijini, REA wanapeleka kwa kufuata barabara na kwenye centres, lakini unaweza ukaona kwamba kwenye shule za msingi, sekondari, vituo vya afya na zahanati kule umeme haupelekwi. Sasa Naibu Waziri naomba anihakikishie wananchi wa Jimbo la Mufindi Kusini kwenye maeneo haya niliyotaja kama watapewa umeme?
Mheshimiwa Mwenyekiti la pili, namuomba Naibu Waziri, kwa majibu haya aliyoeleza vizuri, kwa programu ya awamu ya tatu ambayo inaanza, je, utakuja lini Mufindi ukafanya mkutano angalau hata mmoja kuongea na wale wananchi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuwajulisha Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla kwamba mradi kabambe wa REA Awamu ya Tatu utapeleka umeme katika maeneo yote ya taasisi ikiwemo shule za msingi, sekondari, hospitali na katika taasisi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Kigola, jimbo lako la Mufindi Kusini, maeneo yote niliyoyataja ikiwemo pia katika vijiji vyako vya Mbaramaziwa, Tambarang‟ombe kwenda mpaka Tengereo mpaka kule Kilowelo vitapelekewa umeme kwenye taasisi nilizozitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu suala lake la pili, kwamba ni lini sasa tutatembelea katika maeneo yale? Nimhakikishie Mheshimiwa Kigola; kwanza kabisa nikupongeze umeshaanza kuchimba visima kwa ajili ya kuhitaji umeme. Napongeza sana kwenye Kitongoji chako cha Msumbiji umeshaanza kujenga, lakini pale Idambaravumo pia umeshaanza kujenga na pia unatarajia kupeleka umeme pale Kilowelo centre, na pia kwenye vijiji vyako vingi sana ikiwemo kama nilivyosema pale Kisaula tutakupelekea mashine ya umeme, lakini pia kwenye vijiji vyako vingine mbali na vijiji na Kitongoji cha Msumbiji na pale Changarawe kwa Mheshimiwa Kigola kwa vijiji vyako 47 vilivyobaki vyote vitapata umeme wa uhakika.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante. Kwa kuwa tatizo linalowakabili wananchi wa Mufindi Kusini linafanana sana na wananchi wa Jimbo la Nzega Mjini; nilitaka kusikia kauli ya Waziri, katika kata ya Migua, jimbo la Nzega Mjini, Kata za Mwanzoli, Mbogwe, maeneo ya Bulunde pamoja na Kashishi yote haya yalikuwa yapekelewe umeme kwa miradi ya MCC na miradi hii imefutwa. Je, Naibu Waziri anasema kauli gani kuwaambia wananchi wa jimbo la Nzega wa maeneo haya juu ya upatikanaji wa uhakika wa umeme katika maneo niliyoyataja? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nipende tu kusema wazi kwamba miradi yote iliyokuwa chini ya MCC ambayo haikuendelea sasa itapelekewa umeme kwa bajeti ambayo tumeipitisha kupitia mradi wa REA wa Awamu ya Tatu ikiwemo pamoja na vijiji kwa Mheshimiwa Bashe alivyovitaja kwenye jimbo lake. Lakini niseme tu, kijiji cha Kashishi tulishaanza kufanyia survey lakini pia vijiji vya Mbogwe na vingine vya karibu tulishaanza kuvifanyia survey na vyote vitapelekewa umeme kwenye kipindi hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Bunge lako mimi nitatembelea kwa Mheshimiwa Kigola mara tukimaliza Bunge, pia nitatembelea kwa Mheshimiwa Bashe na maeneo mengine kuhakikisha maeneo yote yanapata umeme.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ya matumaini kwa wananchi wa jimbo la Nyang‟hwale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika kijiji cha Busorwa pameshasimikwa nguzo, nyaya zimetandazwa na transfomer zimeshafungwa takribani zaidi ya miezi minane, kwa nini umeme kijiji cha Busorwa haujawashwa?
Na kwa kuwa kuna baadhi ya vijiji kama vile Izunya, Nyashilanga, Nyamikonze, Nyijundu nguzo na nyaya za umeme zimeshatandazwa lakini transfomer hazijafungwa. Ni lini trasfomer hizo zitafungwa ili umeme huo uweze kuwashwa na kuweza kuchochea maendeleo katika vijiji hivyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, Mheshimiwa Naibu Waziri nakuomba baada ya Bunge hili tuongozane pamoja mimi na wewe ukaone mradi huu unavyosuasua ili uweze kuleta changamoto ili mradi huu uweze kwenda haraka ili wananchi wa jimbo la Nyang‟hwale waweze kupata maendeleo kupitia umeme, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa katika Jimbo la Nyang‟hwale ni vijiji vitatu tu ambavyo vimeshaunganishiwa umeme, na nitoe masahihisho kidogo, Mheshimiwa na wala siyo vijiji 61, vijiji 62 mbavyo bado kwenye jimbo lako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kijiji cha Busorwa ambacho tayari kina transformer na tayari kina nyaya zimeshafungwa kulikuwa na shida ndogo tu ya vikombe ambavyo vilikuwa havijakamilika, na hivi leo vimekamilika kesho saa tisa mchana Mheshimiwa Hussein wanakuwashia umeme pale Busorwa na mtapata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ni lini vijiji alivyovitaja vitapata umeme. Ametaja vijiji vitatu lakini kuna vijiji 66 ambavyo vimepatiwa kwa nusu lakini vijiji 40 vikiwemo vijiji vya Busorwa kama ulivyotaja, Kakora, Kanegere, Nyamitongo, Nyabushishi, Nyaruzugwa, Nyaruyeye na Izuguna bado havijapatiwa umeme, kwa hiyo vyote tunavipelekea umeme kama ambavyo nimetaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuongeozana naye, kwa idhini yako kama ningepeta nafasi ningependa kwenda kushuhudia vijiji vitano ambavyo amevitaja vya Nyashilanga, Nyamikonze na Izunya ambavyo vitawashwa umeme Ijumaa ijayo. Lakini kwa ridhaa yako niombe kuongozana nawe Mheshimiwa Mbunge mara baada ya Bunge hili ili tukawashe umeme kwenye vijiji vyako kama ambavyo nimekusudia, ahsante sana.
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikiliza Waziri kwa majibu yake, amesema mwaka 2018 ndio mradi huo utakamilika, ni nini commitment ya Serikali kwa kuwa hadi kufikia mwaka 2018 na wananchi wanaihitaji nishati hii muhimu kwa ajili ya maendeleo. Je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuangalia njia mbadala kuweza kusaidia wananchi hawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa tatizo la nishati ya umeme katika Mkoa wa Katavi linafanana kabisa na matatizo ya umeme katika Mkoa wa Morogoro hasa katika Manispaa ya Morogoro katika Kata za Mindu, Kihonda na Mkundi ambapo wananchi hawa kwa muda mrefu hawana nishati ya umeme ingawa wanapitiwa na Gridi ya Taifa. Je, Serikali haioni kama kuna haja ya kuhakikisha wananchi hawa wanapata umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, commitment ya Serikali kwa Mkoa wa Katavi pamoja na Sumbawanga kwa kweli ni kubwa sana. Hadi sasa mbali na mradi huu wa kupeleka umeme wa kilovolti 400 hivi sasa Serikali imeanza kukarabati majenereta mawili yaliyokuwa na matatizo pale Mpanda. Yale majenereta yalikuwa na uwezo wa megawati 2.6 lakini yalikuwa yanatoa umeme wa megawati 2.3, ukarabati wa majenereta hayo umekamilika tarehe 5 mwezi huu kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa Mpanda pamoja na maeneo ya jirani umeme utapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hatua ya pili sasa hivi ujenzi umeanza kufunga jenereta mbili mpya ambazo pia zinatengenezwa, kama nilivyosema kwenye swali la msingi, kupitia mradi wa ORIO. Jenereta hizi zina uwezo wa kufua megawati 2.5 kwa ujumla wake kwa hiyo, Mji wa Mpanda pamoja na Sumbawanga sasa watakuwa na jumla ya megawati 5.1 ambapo matumizi yao kwa sasa hivi ni megawati 2.6. Kwa hiyo, vijiji vyote sasa vya Mchangani, Dilifu, Longililo, Mpakani, Gereza la Kakalankurukuru, pamoja na Kalamsenga vyote vitapata umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na vijiji vya Morogoro vikiwemo Mindu pamoja na Kihonda, vijiji hivi vinapelekewa umeme kupitia mradi kabambe wa REA Awamu ya Tatu unaoanza tarehe 15 Disemba, 2016. Na vijiji vyote vya Kihonda na maeneo ya jirani ikiwemo pamoja na Mindu vitapelekewa umeme wa uhakika mwaka huu.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa REA inafanya kazi nzuri sana na imesambaza umeme karibu nchi nzima na Mpwapwa kuna vijiji ambavyo havijapata umeme, kijiji cha Kibojani, Mgoma, Mzogole, Viberewele, Sazima, Mkanana, Igoji Kaskazini na Igoji Kusini pamoja na Iwondo.
Je, Mheshimiwa Waziri, utakuwa tayari kupeleka umeme katika vijiji hivi kwa sababu umeme ndio uchumi wetu na ndio maendeleo yetu katika nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa tuko tayari kupeleka umeme kwenye vijiji vyote vya Mheshimiwa Lubeleje. Mheshimiwa Lubeleje ni Mbunge mkongwe, nadhani kati ya Wabunge wote ambao tuko hapa Mheshimiwa Lubeleje ni wa zamani sana kwa hiyo, hatuwezi kumuangusha. Kwa hiyo, Mheshimiwa Lubeleje nikuhakikishie vijiji vyako vyote vya Lugoma na Kiwelewele vitapelekewa umeme kupitia REA Awamu ya Tatu.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nilikuwa naomba kumuuliza Naibu Waziri kwa kuwa REA wamejitahidi sana kusambaza umeme vijijini, lakini TANESCO hawaingilii kwenda kuanza kusambaza umeme kwenye maeneo mengine ambayo yameanzishwa hasa ya uzalishaji, mfano Kata ya Gumanga kuna kiwanda cha kusindika nyanya, umeme haujapelekwa Mkalama. Nilikuwa naomba kuuliza ni kwa nini TANESCO sasa wasiende kuanza kusambaza umeme? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji alivyotaja Mheshimiwa Mlata kwanza kabisa viko kwenye Mpango wa REA, lakini sambamba na Mpango wa REA bado TANESCO wanapeleka nguzo. Nimhakikishie tarehe 15 mwezi uliopita Mheshimiwa Mlata tulimpelekea nguzo 20 za umeme ambazo zitafungwa kuanzia tarehe 20 mwezi unaokuja. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mlata vijiji vyako vyote vya Manga pamoja na ulivyotaja Mkarama vitafungiwa umeme kupitia REA pamoja na TANESCO.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa kunipa nafasi hii. Namuuliza swali Naibu Waziri, alipokuja Mpanda alituhakikishia wananchi wanaoishi vijiji vya Kabungu, Mchakamchaka, Ifukutwa na Majalila ambako ni Makao Makuu ya Wilaya kwamba ataleta umeme ifikapo mwezi wa tisa. Je, ni lini Serikali itathibitisha kauli yake ambayo aliitoa yeye mwenyewe alipofika huko?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa nilitembelea maeneo mengi sana katika Jimbo la Mheshimiwa Kakoso na hasa kabla ya kutaja maeneo ya Majalila, Mheshimiwa Kakoso kwanza nikuhakikishie Gereza lako la Kakalankurukuru ambalo lina miaka 37 halina umeme litapatiwa umeme mwezi ujao kupitia Mradi wa REA unaoanza mwezi ujao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitembelea pia Kata ya Majalila ambako kuna mitambo na miradi ya maji. Nikuhakikishie Mheshimiwa Kakoso, mradi wa REA utakapoanza kufikia mwezi Januari hadi Februari mwaka unaokuja mradi wako wa Majalila utafungiwa jenereta za umeme, lakini pia jenereta ya umeme itaunganishwa na umeme ambao sasa unapitia mradi wa REA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kijiji cha Kabungu nilikitembelea pamoja na Mpanda Mji Mpya. Kwa hiyo, Mheshimiwa Kakoso nikuhakikishie, vijiji vyako vyote 32 vilivyobaki vitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA kuanzia Disemba na Januari mwaka unaokuja.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu ya kutia matumaini, naomba kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kiteto kwa sehemu kubwa inakaliwa na jamii ya wafugaji ambao shule haijawa kipaumbele sana, hasa kwa watoto wa kike. Kwa sehemu kubwa ukombozi mkubwa ni kuwa na shule za bweni ambako wasichana wanaweza wakabaki shuleni badala ya kurudi nyumbani kukwepa kuolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachosikitisha ni kwamba kuna baadhi ya sekondari za kata tena za muda mrefu zenye mabweni, kama sekondari ya Ndedo na Lesoit ambazo ni za bweni na zina wasichana wengi wa Kimasai, lakini inasikitisha kwamba hizo shule za kata hadi leo hazina umeme. Na sio hizo shule tu hata Kituo cha Afya cha Osteti ambacho kinasaidia sana huduma za afya kwa akina mama hakuna umeme.
Je, ni lini Naibu Waziri sasa atachukua jukumu la makusudi kutembelea Wilaya ya Kiteto, hasa maeneo haya niliyoyataja, ili kujionea mwenyewe jinsi ambavyo sekondari hizo hazina walimu na hata maabara tulizojenga hazitumiki kwa ajili ya kukosa umeme?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, naomba ku-declare interest kwamba nimetoa mikopo kwa takribani miaka 20 sasa katika Mkoa wangu wa Manyara. Uzoefu unaonyesha kwamba ufanisi mkubwa kwa kurejesha mikopo kwa wanawake na vijana ni katika vijiji vile vyenye umeme wa uhakika. Je, nini kauli ya Serikali kabla ya kutoa hizo shilingi milioni 50 katika maeneo haya ya wafugaji na mikoa ya pembezoni kuhakikisha kwamba vijiji hivyo vitakuwa na umeme kabla ya kusambaza hizo fedha?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Mradi wa REA Awamu ya Pili ulipokamilika maeneo mengi sana ya taasisi hayakupatiwa umeme. Nitoe rai tu kwamba, REA Awamu ya Tatu inayoanza sasa itaweka kipaumbele sana kupeleka umeme kwenye taasisi za umma ikiwemo shule, sekondari, pamoja na taasisi nyingine. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Umbulla kwamba, shule ya sekondari ambayo ameitaja Lesoit pamoja na shule ya Ndedo pamoja na Kituo cha Afya cha Osteti vitaanza kabisa kupelekewa umeme kwenye mradi wa REA Awamu ya Tatu unaoanza hivi karibuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nimpongeze tu Mheshimiwa Mbunge, amekuwa akifuatilia sana masuala haya, lakini nimhakikishie mbali na vituo vya afya kwa sababu viko vingi. Viko vituo vya afya katika eneo lake la Njiapanda ambako pia kuna kituo cha afya kitawekewa umeme, lakini kuna eneo la Songambele halijawekewa umeme pamoja na vituo vingi sana ikiwemo na vijiji vya katikati na vyenyewe vitapatiwa umeme katika REA Awamu ya Tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitapenda kutembelea, kwa ridhaa yako, mara baada ya Bunge tufuatane na Mheshimiwa Mbunge moja kwa moja ikwezekana tuanze kukaa hata kabla ya kuanza kutembelea maeneo yake.
Kuhusiana na vijiji ambavyo vitapewa mikopo au ruzuku ya shilingi milioni 50 kupata umeme. Tutaanza kuvipatia umeme, tutakaa na wenzetu wa TAMISEMI ili kusudi shilingi milioni 50 zisiende bure, ili waanze kutumia umeme mara watakapoanza kupata pesa hizo.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi, ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa Mradi wa REA Awamu ya Pili umeshapita baadhi ya maeneo tena ya barabarani katika Jimbo la Lushoto. Je, Serikali inaniahidi lini itapeleka umeme wa REA Awamu ya Tatu hasa katika Kata za Kilole, Kwekanga, Makanya, Ngwelo pamoja na maeneo mengine yaliyobaki?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kusema tu Mradi wa REA Awamu ya Tatu unapeleka umeme katika vijiji vyote, katika vitongoji vyote na katika taasisi zote za umma, lakini hata miji ambayo pia, iko isolated. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kijiji chake cha Kilole kitapelekewa umeme hata kijiji cha Makanya kitapelekewa umeme kwa sababu, ni mpango wa Serikali kupeleka umeme katika vijiji vyote kupitia REA Awamu ya Tatu.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kabla ya kuanza kwa Mradi wa REA III, kuna baadhi ya maeneo Miradi ya REA I na REA II bado haijakamilika ikiwemo katika baadhi ya maeneo ya Jimbo la Momba. Sasa tunataka assurance ya kukamilisha miradi kwanza ya REA I na REA II kabla ya hiyo REA III, lini itakamilika miradi hii, REA I na REA II? Ahsante Sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Silinde kwanza nakupongeza, Miradi ya Awamu ya Pili ya REA imeshakamilika na mahali ambapo Mradi wa REA ikitokea kwamba haukukamilika ni vijiji ambavyo sasa vitaanza kutekelezwa katika Miradi ya REA Awamu ya Tatu.
Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Silinde kama kuna kijiji specific ambacho hakijakamilika kupitia mradi wa pili, naomba tukae na tuanze kutekeleza hata kabla ya kuingia Mradi wa REA Awamu ya Tatu. Na vijiji vyote ambavyo havikukamilika kupitia miradi ya REA Awamu ya Pili, ambavyo havijakamilika, vitaanza kukamilika kwanza ndio tunaingia kwenye REA Awamu ya Tatu. Kwa hiyo, vijiji vyote Mheshimiwa Silinde katika Jimbo lako la Momba vitapatiwa umeme wa uhakika kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na nia na dhamira nzuri ya Serikali juu ya kuwasaidia wachimbaji wadogo wadogo lakini imeonekana kwamba masharti haya hayawasaidii hawa wachimbaji wadogo na tunajua kwamba sasa hivi wimbi kubwa la watu wanaokosa kazi ni vijana. Sasa, je, Serikali iko tayari kupunguza vigezo vile ili watu wengi waweze kunufaika na mpango huu?
Swali langu la pili, je, Naibu Waziri yupo tayari kuambatana nami kwenda Jimboni ili tuweze kuzungumza na wachimbaji wadogo ili wajue dhamira ya Serikali ya kuwasaidia hususan wachimbaji wadogo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Kigua kwa kutambua kwamba kulikuwa na vikwazo tulipoanza utaratibu huu. Tumepunguza vikwazo vya kuomba mikopo. Tulipoanza kutoa ruzuku mwaka 2013 ilikuwa siyo ruzuku, ilikuwa ni mikopo. Sasa Serikali imepunguza masharti ya mikopo na badala yake sasa inatoa ruzuku. Hilo ni jambo muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikwazo cha pili kilikuwa ni lazima wachimbaji wawe na Bankable statement inayoonyesha rasilimali ya madini iliyoko hapo chini. Sasa kulingana na uwezo mdogo wa wachimbaji wadogo, kigezo hicho kimeondolewa. Kwa hiyo, tunashukuru Mheshimiwa na vigezo vinaendelea kupungua ili Watanzania wengi wanufaike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niko tayari kutembelea kwenye Jimbo la Kilindi na hasa maeneo ya Tunguli. Ningependa nifike Tunguli lakini hata Kwa Manga mpaka kule kwenye Kijiji cha Kikunde na Mafulila ambako wanachimba wachimbaji wengi.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa mujibu wa jarida la The Citizen la tarehe 23, Oktoba mwaka huu, 2016, imeonyesha kwamba miongoni mwa mikopo iliyokopwa kutoka China mwaka 2015 ni pamoja na Dola za Kimarekani milioni 132 ambazo ni sawa na Shilingi bilioni 300 za Kitanzania kwa ajili ya mradi wa umeme wa upepo Singida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iwaeleze wananchi wa Singida fedha hizi zimekwenda wapi? Kwa sababu mpaka hivi sasa hakuna kinachoendelea, hakuna hata nguzo moja halafu tunaambiwa bado majadiliano yanaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa sababu mazingira kama haya ambapo mikopo inaombwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini fedha zinaelekezwa maeneo yasiyohusika. Ni lini Serikali itaona kuna umuhimu wa kumwagiza CAG akague mikopo inayoagizwa katika nchi hii? Kwa sababu katika deni la Taifa, inawezekana kuna ujanja ujanja unafanyika kwenye suala zima la mikopo. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa mradi wa upepo wa Singida ambao unazalisha Megawatt 100 hautokani na fedha za mkopo, ni wawekezaji binafsi, niweke wazi. Kadhalika, kuhusiana na masharti ya mikopo, ni Makampuni yenyewe yanakopa na kuja kuwekeza kwa ajili ya kufanya biashara na TANESCO inanunua umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la CAG, ni taratibu za Kiserikali. CAG ana utaratibu wa kukagua na Mashirika na ofisi za Serikali zina utaratibu wa kuwasilisha taarifa za kukaguliwa. Tutaendelea kupeleka taarifa kwa mujibu wa CAG ili hesabu zote zikaguliwe. Kwa hiyo, hakuna suala la kuficha kwenye ukaguzi; CAG ana ratiba ya kukagua na Serikali tuna wajibu wa kupeleka takwimu ili zikaguliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kupeleka takwimu zikaguliwe.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba kumuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza. Kwa kuwa kampuni ya Resolute imekuwa ikifanya utafiti kwa muda mrefu ni lini sasa Serikali itaitaka kampuni hii iweze kufungua mgodi kwa ajili ya manufaa ya Wilaya hii ya Mbogwe?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, yapo mazungumzo baina ya Serikali pamoja na kampuni yanayoendelea kuhakikisha kwamba kampuni hii inaachia eneo la Kanegere ili kusudi wananchi waweze kupata maeneo ya kuchimba dhahabu. Ni lini sasa Mheshimiwa Naibu Waziri atatembelea Mbogwe kuweza kuhakikisha kwamba jambo hili linaafikiwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Kampuni ya Resolute imekuwa ikifanya utafiti kwa muda mrefu na sasa hivi shughuli za utafiti kimsingi zimekamilika na hatua inayofata sasa ni kufungua mgodi. Kulingana sasa na taratibu za ufunguaji mgodi kampuni iko tayari kuanza kufungua mgodi miezi sita ijayo kutegemea sasa na bei ya soko la dhahabu pamoja na upembuzi yakinifu.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kutembelea eneo, kwanza kabisa nimshukuru Mheshimiwa Masele anavyowatafutia maeneo wachimbaji wadogo. Hivi sasa katika eneo la jimbo la Mbogwe, Wizara imeshatenga maeneo yanayoitwa Shenda Kaskazini ambayo yana ukubwa wa hekta 990.99 na eneo hilo litapatiwa leseni 100 kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa Mbogwe.
Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hatua hiyo bado Wizara pia imezungumza na mwekezaji na kupata eneo lingine la Kanegere namba mbili ambalo litakuwa na ukubwa wa hekta 177 ambazo pia zitapatikana leseni 18.
Lakini kadhalika eneo la Bukandwe ambalo Mheshimiwa amelizungumzia pia kampuni imeachia eneo la ukubwa wa hekta 300 ambapo pia zinapatikana leseni kama 10.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Masele nimshukuru sana kwamba, wachimbaji wake watapata maeneo mengi na nitatembelea huko mara baada ya Bunge hili kuahirishwa.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Spika, asante pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, mpango wa REA III una-cover mwaka 2016 mpaka 2019/2020. Serikali ina mpango gani kushirikisha Waheshimiwa Wabunge katika kupanga maeneo ya kupeleka umeme katika miaka hiyo husika kuzingatia kwa bajeti ya kila mwaka?
Mheshimiwa Spika, swali la pili Mkoa wa Ruvuma haujaunganishwa bado na umeme wa Gridi ya Taifa. Ni lini sasa mradi wa umeme wa Gridi ya Taifa kutoka Makambako kwenda Songea utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, nishukuru kabisa Mheshimiwa Mbunge ametukumbusha kwamba tuwaambie Waheshimiwa Wabunge. Kwanza kabisa niwaondoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge, mradi wa REA Awamu ya Tatu unaoanza sasa tunatumia utaratibu ufuatao:-
Mheshimiwa Spika, wakandarasi watakapokuwa wanaingia site kuanzia Disemba mwaka huu, hatua ya kwanza itakuwa ni kukutana na kukubaliana na Waheshimiwa Wabunge kabla hawajaanza kazi kwenye maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini nitoe tu angalizo lingine, kwamba tumeweka utaratibu sasa mahali ambako kuna Ofisi zetu za TANESCO tumeandaa kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali za Mitaa kuweka vituo rasmi ili wananchi wasiende kwenye Ofisi za TANESCO ila wafanyakazi wa TANESCO wakae kwenye vituo ambavyo Serikali za Mitaa zitakuwa zimetambua.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wabunge pamoja na Diwani watashirikishwa sana kabla ya utekelezaji wa mradi huu kuanza.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na mradi wa Makambako – Songea, mradi wa Makambako – Songea una sehemu tatu za utekelezaji. Sehemu ya kwanza ni ujenzi wa distribution line ambao inachukua urefu wa kilomita 900 kwa maeneo yote ya Mbinga, Songea na maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, mradi huu ulianza mwaka juzi na unakamilika mwakani mwezi Julai. Sehemu ya pili ni kujenga transmission line ambayo imeanza mwaka jana na hivyo itakamilika mwezi Septemba, 2018. Hatua ya tatu ni kujenga substations tatu, moja ikiwa Makambako, nyingine Songea na nyingine eneo la Madaba, kwa ujumla wake kazi zote zitakamilika mwezi Mei, 2018.
MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri na naamini kwamba haya yaliyozungumzwa yote yataenda kutekelezwa. Naomba kuongeza swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa, Vijiji vingi vya Jimbo langu ni vikubwa sana na kwa kuwa, umeme huu wa REA umekuwa ukifikishwa kwenye maeneo ya kati ya vijiji tu. Je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuusogeza umeme huu sasa kwenye vitongoji vilivyo mbali na maeneo ya kati ya vijiji ili wananchi hao katika vitongoji hivyo nao waweze kunufaika na umeme huu?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi, namshukuru sana Mheshimiwa Makanyaga kwanza kwa kuuliza swali hili.
Kwa kuwakumbusha tu, ni kweli kabisa kwa awamu ya II tumepeleka kwenye vituo, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Chilonwa kwamba awamu ya III inapeleka sasa kwenye vitongoji na kwenye vijiji vyote na kwenye mashine na kwenye taasisi za jamii ikiwemo shule. Nimhakikishie hata Kijiji chake Mheshimiwa Chilonwa cha Chalinze sasa kitapata umeme, Kijiji chake cha Kawawa kitapata umeme, Kijiji cha Malichela kitapata umeme, Kijiji cha Membe kitapata umeme, Kijiji cha Bwawani nacho kitapata umeme. Kwa hiyo, nimhakikishie kuwa vijiji vyote vitapata umeme.
MHE. LATHIFAH H. CHANDE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, mpango huu wa REA upo kwa ajili pia ya Mkoa wa Lindi hadi Lindi Vijijini, lakini mpaka sasa hivi maeneo mengi ya Mkoa wa Lindi bado hayana umeme. Je, ni vijiji vingapi katika Mkoa wa Lindi ambavyo vinatarajia kupewa umeme wa REA katika bajeti ya mwaka 2016/2017?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, Vijiji vinavyotarajiwa kuunganishwa umeme katika Mkoa wa Lindi kupitia REA Awamu ya III ni 117. Ahsante sana.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Katika Mkoa wa Dar es Salaam bado kuna maeneo mbalimbali katika Kata ya Mianzini maeneo ya Mponda Wilaya ya Temeke, Chamanzi, Tuangoma, Somangila, Kimbiji, Pemba Mnazi, Vijibweni, Chanika, Majohe na Pugu, vyote hivyo bado havijapata miradi ya umeme kusambazwa katika vijiji mbalimbali.
Je, Mheshimiwa Waziri, ni lini sasa Serikali itasambaza umeme pembezoni mwa vijiji hivi vya Mkoa wa Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa maeneo ya Dar es Salaam maeneo mengi hatujapeleka umeme na hasa Kigamboni. Awamu ya kwanza tunayofanya tunapanga kujenga sub-station Kigamboni kwa sababu population ya sasa ni kubwa. Kwa hiyo, vitongoji vyote vya Kigamboni vitapelekewa umeme kupitia Awamu ya II. Pia maeneo ya Chanika, maeneo ya Gongo la Mboto, maeneo ya Kinyamwezi, maeneo ya Buyuni na yenyewe yanapelekewa kwenye mpango huu wa REA unaoanza mwezi Desemba.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kwa niaba ya Mheshimiwa Mahmoud Mgimwa, Mbunge wa Mufindi Kaskazini kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kuna mradi wa densification na underline transformer. Mradi huu unafikisha umeme katika maeneo ambayo REA Awamu ya Pili ulifikisha katika baadhi ya Kata lakini siyo vijiji vyote.
Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusiana na maeneo ambayo Kata zile zimefikiwa na umeme lakini siyo vijiji vyote na chini ya mradi huo wa densification na underline transformer inaeleza kwamba unaweza kufikisha umeme ndani ya umbali wa kilometa 10, nini kauli ya Serikali kwa wananchi wa maeneo hayo?
Swali la pili, Mji wa Mafinga ni kati ya miji michache inayokua kwa kasi hapa nchini na ndiyo kitovu cha shughuli za uchumi za Wilaya ya Mufindi, lakini maeneo mengi hayajafikiwa na umeme kama vile Machinjio Mapya, Makalala, Ihongole, Mwongozo na Lumwago. Je, Serikali iko tayari kujenga sub-station ili kuwezesha wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa asilimia mia moja?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa mradi wa REA awamu ya tatu kimsingi una sehemu tatu. Sehemu ya kwanza ni kupeleka umeme katika maeneo yote ambapo kuna miundombinu ya awamu ya pili lakini component ya pili na kwa niaba ya Mheshimiwa Chumi na Waheshimiwa wananchi wa kule Mufindi pamoja na Mafinga ni kwamba awamu ya tatu itahusisha sasa kupeleka umeme kwenye vitongoji na vijiji vyote kupitia mradi aliosema densification.
Mradi wa densification unapeleka umeme kutoka kwenye miundombinu mikubwa kwenda kwenye vijiji na vitongoji. Nimhakikishie Mheshimiwa Chumi kwamba, vijiji vyake vyote vya Sao Hill vitapata umeme kupitia mradi huu, hata pale Changarawe atapata umeme. Isalavanu, Itubiravamu na Ibongoboni vyote vitapata umeme kupitia mradi huu. Nimhakikishie hata Kijiji chake cha Mkalala pamoja na Bubirayinga vitapata umeme kupitia mradi huu wa Itubiravamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili juu ya maeneo ya Mafinga. Ni kweli kabisa maeneo ya Mafinga sasa yana kazi kubwa. Mafinga sasa inapata umeme kutoka Iringa ambako ni kilometa 70, pia kutoka Mgololo kilometa 60, sasa ipo haja kwa kweli kujenga sub-station. Nimhakikishie tunajenga sub-station mwaka wa fedha unaokuja.
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja tu dogo la nyongeza. Katika mwaka huu wa fedha kuna baadhi ya vijiji katika Wilaya ya Chemba vimeorodheshwa kwamba vitapata umeme. Nataka Mheshimiwa Waziri na Serikali nzima hii inihakikishie mradi huu utaanza kutekelezwa lini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, miradi yote niliyotaja ya REA awamu ya tatu inaanza kutekelezwa tarehe 15 Desemba, mwaka huu na itakamilika 2019. Kwa hiyo, eneo la Chemba Mheshimiwa Nkamia nimhakikishie vijiji vyake vyote, shule zake zote, pamoja na vituo vya maji vitapatiwa umeme kuanzia mwezi niliotaja na kuishia 2019.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni ombi, baadhi ya vitongoji ndani ya Mji wangu wa Manyoni havijapata umeme mpaka sasa hivi ninavyozungumza, ukitembea usiku utakuta pale umeme unawaka, pale umeme hauwaki, karibu nusu ya Mji wa Manyoni upo gizani na tatizo kubwa ni gharama za nguzo kuwa kubwa.
Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali kwa bajeti ya kuanzia mwaka huu imtengee fedha Meneja wa TANESCO wa Wilaya ya Manyoni angalau aweze kununua nguzo na sisi tutaweza kuchangia gharama nyingine ndogo ndogo, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mkandarasi anayetekeleza Mradi wa REA II katika Tarafa ya Nkonko yenye vijiji 25 hajakamilisha mradi huu mpaka sasa hivi ambapo ilitakiwa aukamilishe Septemba, 2015. Pamoja na juhudi za Mbunge, Naibu na Waziri kufuatilia zimegonga mwamba, mkandarasi huyu anaonekana ni mzembe na mvivu. Wananchi wa Manyoni wamenituma, wanasema hawataki kumuona hata kwa sura yule mkandarasi, Kampuni ya Spencon.
Je, ni lini Serikali itatuletea mkandarasi mwingine kwa sababu yule hatumtaki tena, hatufai kabisa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mtuka kwa jinsi anavyofuatilia maslahi ya wananchi kwa upande wa umeme. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Manyoni Mashariki kwamba ni kweli kabisa vile vijiji ambavyo havijafikiwa na umeme, kulikuwa na shida ya nguzo kwa mkandarasi lakini nimhakikishie kwamba tumeanza kutekeleza Mradi wa REA III kuanzia tarehe 6 Januari, 2017. Nitumie nafasi hii kuwaarifu Waheshimiwa Wabunge wote pamoja na wananchi kwamba utekelezaji wa REA III umeanza tangu tarehe 6 Januari, 2017 na utaendelea kutekelezwa ndani ya miaka mitano ijayo.
Mheshimiwa Spika, tumeanza kutekeleza Mradi wa REA katika mikoa sita ikiwemo Mikoa ya Pwani, Tanga, Mara, Iringa, Arusha pamoja na Mbeya. Kadhalika tumeanza kutekeleza mradi huo katika mikoa mingine ambayo ilikuwa kwenye mikoa mama hapo awali ikiwemo Mkoa ya Songwe pamoja na Njombe.
Mheshimiwa Spika, sasa ili nijielekeze kwa swali la Mheshimiwa Mtuka, nimhakikishie vile vijiji 75 ambavyo havijapata umeme kikiwemo Kijiji chake cha Simbangulu, Makutupora, Mwembela na London vitapata umeme. Kwa hiyo, namhakikishie Mheshimiwa Mtuka kwamba vijiji vyake 75 vilivyobaki vitapata umeme bila mashaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusiana na mkandarasi Spencon, nichukue nafasi hii kusema rasmi kwamba yule mkandarasi amesimama kazi tangu mwezi Novemba. Ni kweli kati ya wakandarasi tuliokuwa nao hakufanya kazi kwa ufanisi na kama Serikali tumeshachukua hatua. Hatua ya kwanza tuliyochukua tumeshikilia mshahara wake wa mwezi Novemba. Hatua ya pili, tumepeleka shtaka rasmi kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili tumshtaki mahakamani na hatua ya tatu hatumpi kazi tena kwenye kandarasi zinazofuata. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hatua nyingine tuliyochukua ni kuanza majadiliano na kumpeleka mkandarasi Octopus katika Mkoa wa Singida ili ianze kutekeleza mradi huu mara moja. Kwa hiyo, wananchi wa Singida watapata umeme haraka iwezekanavyo.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, imeshajionesha kwamba katika machimbo mbalimbali ya madini, wananchi wanaozunguka maeneo hayo huwa wanaathirika sana na pia wanakuwa hawana shughuli ya kufanya katika ile migodi. Sasa kwa kuwa wananchi wa Mkoa wa Njombe ni wananchi wanaojituma sana kwenye kilimo, je, Serikali iko tayari sasa kuanza mchakato maalum wa kusaidia wananchi wanaozunguka maeneo yale hasa Jimbo la Ludewa na Njombe Mjini, waweze kuwa tayari kuzalisha bidhaa za chakula kitaalam, pindi migodi hii itakapoanza waweze kunufaika na soko litakalokuwepo pale migodini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa namshukuru Mheshimiwa Mwalongo kwa jinsi anavyofuatilia kwa ukaribu suala hili kwa manufaa ya wananchi wa Njombe.
Mheshimiwa Naibu Spika, juhudi za Serikali zinazochukuliwa kuhakikisha kwamba wananchi wananufaika hasa katika masuala ya local content kwa maana ya ushirikishwaji, Serikali imechukua hatua kadhaa; mojawapo ni pamoja na kuitaka kampuni itakayowekeza kutoa elimu pamoja na mikopo ili kuwawezesha wananchi hao kunufaika na rasilimali hiyo. Katika kazi hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na nimshukuru sana, vijiji vya Itoni pamoja na Nanundu ambayo ipo katika maeneo yale, vimeshapewa elimu kwa ajili ya ulimaji wa mboga mboga, lakini pia katika shughuli za kufuga kuku pamoja na kufuga nguruwe. Kwa hiyo, wananchi wataweza kufanya kazi kwa ajili ya kujiwekeza kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongeze tu kwamba Serikali kwa kushirikiana na kampuni, kampuni itaanza kutoa mikopo kwa ajili ya kuwawezesha wananchi wanaozunguka mgodi ule kufanya shughuli ndogo ndogo za kiuwekezaji ili pia sasa waanze kushiriki mara baada ya mradi kuanza kwenye shughuli za kibiashara na za kiuchumi katika maeneo yale. Inatoa elimu, lakini inatoa mikopo ya masharti nafuu ili wananchi waanze kufanya hivyo. Utaratibu huu ulianza tangu Oktoba, 2012 na unaendelea hadi sasa.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda tu kuzungumza hapo kwamba tarehe 19 mwezi wa nne liliulizwa swali kwenye Bunge lako Tukufu kuwa Mradi wa Chuma, Liganga na Makaa ya Mawe Mchuchuma, utaanza lini? Majibu ya Serikali yalikuwa kwamba kwanza fidia italipwa mwezi Juni, 2016 ambayo fidia hiyo haijalipwa mpaka leo na pili miradi hii kwamba itaanza mwezi Machi, 2017.
Je, mkanganyiko huo unatokana na nini na majibu hayo yote ambayo sasa hivi inaonekana hayajitoshelezi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa anavyosema Mheshimiwa Mbunge ni sahihi. Kwenye Bunge la mwezi Aprili tulisema kwamba mradi huu utaanza mapema ifikapo mwezi Machi. Hivi sasa bado tupo Januari, hivyo Mheshimiwa Mbunge nadhani avute subira.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kuhusu suala la fidia; fidia inayotarajiwa kufidiwa wananchi wale inafikia takribani shilingi bilioni 13.34, ni kiasi kikubwa. Kwa hiyo, kinachofanyika sasa ni kupitia tathmini halisi ya fidia hiyo, halafu baada ya zoezi hilo kukamilika, basi wananchi watalipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kama ambavyo nimeeleza kwenye jibu langu la msingi kwamba yapo masuala ya kimkataba ambayo Serikali pamoja na mwekezaji inayapitia, likiwemo suala la incentives kwa maana ya vivutio, mara baada ya kukamilika, basi mradi huu utaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni matarajio yetu zoezi hili likikamilika kabla ya mwezi Machi, basi kweli mradi huu utaanza mara moja.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya watu wa Tarime.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna utofauti wa uelewa wa wachimbaji wadogo kati ya uelewa walionao Serikali na uelewa tulionao sisi wananchi na tunaokaa maeneo ya migodi. Tunapozungumzia wachimbaji wadogo, hatuzungumzii watu wajanja wajanja wanaoweza kwenda mjini wakapata leseni, wakarudi wakajiita wachimbaji wadogo. Tunazungumzia watu waliopo kule kijijini ambao ndio wanachimba kwa kutumia majembe, sururu na nyenzo nyingine ambazo ni duni.
Sasa swali langu, kuna maeneo ambayo yalikuwepo na watu wanachimba pale na bahati mbaya watu wanatoka kule vijijini wanakwenda Dar es Salaam wanapewa leseni, Serikali haishirikishi hata Serikali za Vijiji, wanarudi wanaondoa wachimbaji wadogo, kama eneo moja linaitwa Tigite, bwana mmoja ameondoa zaidi ya watu 20 pale. Sasa nataka Naibu Waziri anijibu, ni lini Serikali itatenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo walioko kule vijijini, sio hawa wenye leseni wanaokwenda Dar es Salaam? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wakati Mgodi wa North Mara unaanza, ulitwaa eneo kwa maana ya ile leseni waliyopewa, walipewa eneo kubwa sana na kuna maeneo ambayo mpaka sasa hawayatumii na hawayafanyii kazi. Mojawapo ya eneo hilo ni Serengeti Crossing. Kwa nini Serikali isiuombe mgodi utoe lile eneo kwa wananchi kwa sababu mgodi haulitumii kabisa, ili wananchi wafanye kazi pale wajipatie kipato na waendeshe maisha yao?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Heche jinsi ambavyo ameendelea kutupa ushirikiano katika masuala mbalimbali ya migogoro ya wananchi wa Nyamongo. Nakupongeza sana Mheshimiwa Heche. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hayo, nijielekeze kwenye maswali yake ya nyongeza, ni lini Serikali itatenga maeneo katika maeneo mengine hasa katika eneo la Tigite ambalo amelitaja? Naomba tu mara baada ya kikao hiki nikutane na Mheshimiwa Heche atupatie maeneo kwa sababu Serikali bado inaendelea kuongea na mgodi ili ipate maeneo mengine kwa wachimbaji wadogo. Kwa hiyo, nitazungumza na Mheshimiwa Heche kuhusiana na hili ili eneo la Tigite alilotaja pia litengewe wananchi wa Nyamongo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili, kwanza tu nieleze kwamba Mheshimiwa Heche anavyosema kwamba North Mara imepewa maeneo makubwa, ni kweli, yapo maeneo ambayo Serikali inazungumza na mwekezaji ambayo ni makubwa na mgodi haujaanza kuyatumia. Tunafanya majadiliano, yakishakamilika, tutaongea na Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, kabla leseni hazijatoka, utaratibu tulioweka sasa ni pamoja na kushirikisha viongozi wa maeneo yale ili leseni itakapotoka waweze kutupa ushirikiano mkubwa. Kwa hiyo, eneo hili ambalo ni kubwa kwa wachimbaji wakubwa, tutazungumza na Mgodi wa North Mara, maeneo ambayo tutayapata Mheshimiwa Heche tutashirikiana na wewe ili wananchi waendelee kupelekewa maeneo zaidi.
MHE. TUNDU A. M. LISSU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naomba kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali la nyongeza linalofanana na swali ambalo ameuliza Mheshimiwa John Heche.
Mheshimiwa Naibu Spika, jimboni kwangu kuna eneo lina dhahabu na kampuni moja inaitwa Shanta Mining imeingia na kupewa eneo hilo tangu mwaka 2004. Leo ni miaka 13 haijaanza kuchimba madini, haijajenga mgodi na kwa taarifa za kitaalam ambazo nimeziangalia, hizo deposits za dhahabu siyo kubwa sana za kuweza kupewa kampuni ya kigeni. Namwomba Mheshimiwa Naibu Waziri alieleze Bunge lako kama Serikali ina mpango wa kulitwaa hilo eneo na kuwarudishia wananchi ili wachimbaji wadogo wadogo wenyeji wachimbe kwa sababu baada ya miaka 13 hawachimbi, hawa wawekezaji inaelekea hawana mpango au uwezo wa kuchimba dhahabu kwenye hili eneo la Mang‟oni.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, kwanza namshukuru Mheshimiwa Tundu. Nimekuwa nikiwasiliana naye mara kwa mara kuhusiana na kumpatia eneo. Niseme tu, ni kweli kabisa Kampuni ya Shanta Mining ilipewa leseni ya utafiti tangu mwaka 2004. Nieleze kidogo, muda wa kufanya utafiti kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya 2010, awali ya kwanza ni miaka minne, baada ya miaka minne anapewa tena miaka mitatu ya kuendelea na utafiti na hatimaye anamalizia miaka mitatu. Kwa hiyo, ni kweli kabisa shughuli za utafiti zinachukua muda mrefu. Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, baada ya kukamilisha utafiti, kampuni inatakiwa ianze shughuli za uchimbaji, hivi sasa kama ambavyo Mheshimiwa Tundu anasema haijaanza, matarajio ya mgodi ni kuanza shughuli za uchimbaji kati ya Juni, 2018. Kwa hiyo, baada ya shughuli za uchimbaji kuanza, basi maeneo mengine yata maeneo mengi yatashughulikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia yapo maeneo ambayo Kampuni ya Shanta Mining tunazungumza nayo. Hivi sasa tumezungumza na Kampuni ya Shanta Mining, inatarajia kuwa na maeneo ya hekta kama 200 ambayo inaweza ikawaachia wananchi wa Singida ili wachimbe kwa ajili ya uchimbaji mdogo kwa sababu yanaweza kuonekana siyo manufaa kwa kampuni hiyo. Baada ya taratibu hizo kukamilika, Mheshimiwa Tundu Lissu basi wananchi wako watawasiliana na Serikali tu na watapewa maeneo hayo.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa wananchi wa Geita walipewa magwangala fake, na kwa kuwa Sheria ya Leseni ya Uchimbaji Mkubwa inawataka wachimbaji wakubwa kila baada ya miaka mitano wamege baadhi ya eneo wawarudishie wachimbaji wadogo. Je, Wizara iko tayari sasa kulimega eneo la Nyamatagata na Samina kuwarudishia wananchi kuwafuta machozi kwa magwangala fake waliyopewa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa namshukuru Mheshimiwa Musukuma, katika jitihada ambazo ziliwasababisha wananchi wapewe magwangala ni pamoja na Mheshimiwa Mbunge. Kwa hiyo, tunakupongeza Mheshimiwa Musukuma. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitambue kwamba shughuli za utafiti na uchimbaji wa madini kwa kawaida kabisa, ni za kupata na kupotea. Sasa ni jambo la kawaida, mwekezaji anaweza akawekeza kwenye kuchimba na akakosa. Kama ambavyo ilikuwa kwenye magwangala, wananchi walitarajia pangekuwa na thamani, lakini bahati mbaya hapakuwa na thamani. Kwa hiyo, nilitaka tu kumwelewesha Mheshimiwa Musukuma na ninampongeza sana. Pia kwa wachimbaji wote, ni jambo la kawaida mchimbaji kuanza kuchimba na asipate madini ya thamani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba tu kusema, suala la Nyamatagata na Samina, ni kweli kabisa Serikali inazungumza na Mgodi wa GGM pamoja na wawekezaji wengine, hivi sasa tuko katika hatua nzuri. Mwaka 2016 Kampuni ya GGM ilirusha ndege kuangalia maeneo ambayo hayahitaji.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Musukuma nikuhakikishie kwamba mara baada ya taratibu hizi kukamilika, wananchi wa Nyamatagata na Samina, maeneo ambayo yataachiwa na mgodi, basi yatatengwa rasmi kwa ajili ya wananchi, lakini baada ya kukamilisha mazungumzo na mgodi.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Na mimi naomba kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa wananchi wa maeneo mengi ambayo wawekezaji wakubwa wamewekeza wameacha athari kubwa katika maeneo hayo na mojawapo ni Wilaya ya Nzega katika Mgodi wa Resolute, wananchi wameachiwa mashimo makubwa bila manufaa yoyote. Je, Serikali sasa iko tayari kumnyima mwekezaji Kampuni ya Resolute, certificate ya kumruhusu kuondoka nchini ambayo anatakiwa apewe mwezi wa sita kabla hajalipa deni ambalo anadaiwa la shilingi bilioni 10 na Halmashauri ya Mji wa Nzega?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Kampuni ya Resolute ilifunga mgodi wake miaka mitatu iliyopita. Katika utaratibu wa uchimbaji, mgodi unapoanza huwa kuna Mine Closure Plan. Kwa hiyo, wakati wanafunga mradi, kampuni ilitakiwa kutekeleza Mine Closure Plan, lakini sambamba na hilo, huwa inapewa certificate ya ku-close mgodi. Sasa Wizara ya Mazingira pamoja na NEMC wanalifanyia kazi suala hilo, watakapokamilisha taratibu Mheshimiwa Bashe utashirikishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la msingi ni kwamba je, ni kwa nini Serikali haioni sababu ya kuwanyima certificate? Ni jambo ambalo namwomba Mheshimiwa Bashe avute subira, watu wetu wa NEMC na Mazingira wanalifanyia kazi. Nitambue ushiriki wako Mheshimiwa Bashe kwa wananchi wa Nzega. Niseme tu sambamba na hilo, ili kuwawezesha wananchi wa Nzega wapate maeneo na kuondokana na athari, mara baada ya taratibu za mazingira kukamilika, maeneo ambayo yaliachwa na Resolute ambayo yako wazi, yatamilikishwa kwa wananchi wako ili waweze kupata shughuli za kufanya kazi.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kumrekebisha Mheshimiwa Naibu Waziri kidogo, mimi siyo Mbunge wa Viti Maalum Chakechake. Ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kusini Pemba ikiwemo Chakechake na Mkoani. Ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kama kawaida yake, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa ukataji wa miti kwa ajili ya kuchoma mkaa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania yanaleta uharibifu wa mazingira katika nchi yetu; na kwa kuwa gesi ipo lakini haifikishwi hasa kule vijijini ambako hiyo miti ndiyo inakatwa na kufanywa mikaa: Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasambazia wananchi gesi hasa za majumbani kwa ajili ya matumizi na waachane na tabia ya kukata miti na kutengeneza mkaa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa watu wengi wana hamu kubwa sana ya kutumia hii gesi hasa ya majumbani lakini wanaogopa, wanasikia kwamba gesi inaua; hawana elimu hiyo: Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kutoa elimu ya kuwaelimisha wananchi hasa vijijini na mijini ili kuweza kutumia gesi hiyo kwa manufaa ya wananchi wote hasa vijijini na mijini kwa ajili ya matumizi ya kupikia majumbani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Faida kwa jinsi anavyohangaika na kushughulika na kupambana na uharibifu wa mazingira hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati ambayo Serikali imechukua katika kuhakikisha kwamba uharibifu wa mazingira unapungua kwa kiasi kikubwa ni kuongezeka kwa matumizi ya gesi asilia hapa nchini. La kwanza, nimshukuru Mheshimiwa Mbunge, na hatua ya kwanza ambayo Serikali imeanza, TPDC imeanza sasa mradi wa kusambaza gesi majumbani na katika matumizi ya magari kwa ajili ya Dar es Salaam. Hatua ya kwanza imekamilisha usanifu ambao hivi karibuni utaanza utekelezaji wake na maeneo yatakayoanziwa ni pamoja na maeneo ya Mikocheni, Tabata na Sinza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, waharibifu wa kwanza kabisa wa mazingira hapa nchini ni wakazi wa Dar es Salaam. Dar es Salaam na wananchi kwa ujumla ni jumla ya magunia 45,000 yanaingia kwa siku kwa Jiji la Dar es Salaam. Sasa ili kupunguza athari hiyo, hatua ya kwanza ni kupunguza matumizi ya mkaa kwa wananchi wa Dar es Salaam kwa kutekeleza mradi huu.
Awamu ya pili itaenda katika maeneo ya Tabata, maeneo ya Ukonga kwa Mheshimiwa Waitara, lakini maeneo ya Kigamboni na maeneo mengine. Utaratibu huu utaenda sambamba na maeneo ya Lindi na Mtwara ambapo mradi huu pia utaanza mwezi Juni mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo utekelezaji huu wa kutumia gesi utaendelea katika Mikoa ya Morogoro na Dodoma ambayo inakuja kuwa Makao Makuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi kwamba matumizi ya gesi yatapunguza kwa kiasi kikubwa sana uharibifu wa mazingira. Huo ni mkakati wa kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa pili, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali imetenga pesa, jumla ya shilingi bilioni 6.5 kwenye bajeti ya mwaka huu ili gesi iweze kusambazwa katika maeneo mengi hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la elimu; ni kweli TPDC wameanza kutoa elimu japo siyo kwa kiwango kikubwa. Elimu ya kwanza ambayo imefanyika ni katika maeneo ya minada pamoja na maeneo ya maonyesho, lakini katika Mikoa ya Lindi na Mtwara TPDC imetoa elimu mashuleni, wameanza kutoa makongamano katika maeneo ya Mikoa ya Lindi na Mtwara, Mwanza, Arusha pamoja na Mkoa wa Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, harakati za kutoa elimu ili matumizi sahihi yaende sambamba na mahitaji, yanaendelea.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ningependa kuuliza maswali mawili. Kwanza ningependa kuipongeza Wizara hiyo kwa sababu Waziri wake Profesa Muhongo alifika kwenye baadhi ya kata za Jimbo la Muheza ambalo liko jirani na power station ya Hale na akasikiliza kilio cha Wana-Muheza kwenye Kata hizo za Kwafungo, Songa, Bwembwera na Makole. Mheshimwa Mwenyekiti, sasa swali langu la kwanza ni hili, REA Awamu ya Pili na ya Kwanza iliweka mkandarasi, na mkandarasi yule alikuwa hatimizi wajibu wake kwa wakati, kwa sababu alikuwa ana kazi nyingi sana. Sasa Serikali itawahakikishiaje wanamuheza kwamba REA hii Awamu ya Tatu itakapoanza mkandarasi ambaye atateuliwa atadhibitiwa na atafanya kazi hizo kwa wakati? (Makofi) Swali langu la pili, ni kwamba REA Awamu ya Pili na ya Kwanza ilipitisha nguzo kwenye baadhi ya vijiji na vitongoji lakini vitongoji na vijiji vile havikupata umeme. Sasa kwenye hii Awamu ya Tatu vijiji ambavyo vilipitiwa na nguzo tu bila kupata umeme, vitongoji na vijiji vile Serikali inasemaje kuhakikisha kwamba vijiji hivyo na vitongoji hivyo na vyenyewe vinapata umeme badala ya kuona nguzo tu zimepita mbele yao?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge Adadi Rajab anavyofatilia kwa kina sana kupatikana umeme katika katika Jimbo la Muheza. Nimpongeze sana tulipata orodha yako ya tarafa zako nne ikiwemo Tarafa ya Amani, Ngomeni, Bwembwera pamoja na Muheza yenyewe, kwa hiyo tunakupongeza sana. Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati ya kumaliza kazi kwa haraka, katika utekelezaji wa REA Awamu ya Tatu tumefanya maboresho katika usimamizi. Maboresho ya kwanza ni pamoja na kuweka msimamizi yaani supervisingengineer ambaye kazi yake ni kumsimamia mkandarasi ili amalize kazi haraka, hiyo ni kazi ya kwanza. Pili, tumeweka kila ofisi ya Wilaya kwa wasimamizi wa TANESCO, tumeteua Meneja Maalum atakayesimamia miradi ya REA yaani yeye akilala, akiamka anakumbuka REA, kwa hiyo tunaamini kwamba atamaliza kazi kwa haraka. Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ambalo ni muhimu sana kwa Waheshimiwa Wabunge ni kwamba tumeweka sasa kila mkandarasi akiingia site lazima kwanza amshirikishe Mheshimiwa Mbunge, kwa hiyo mtatusaidia sana kwenye usimamizi wa jambo hili. Kwa hiyo, Mheshimiwa Adadi Rajab tuna hakika kwamba itakwenda kwa kasi. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na vitongoji, kwanza kama nilivyompongeza, tunajua vitongoji vyake 137 Mheshimiwa Mbunge Adadi Rajab vingi havijapata umeme, kama ambavyo nilikueleza, tunajua vitongoji vyetu tumeweka densification, mradi wa densification unaenda kwenye vitongoji vyote nchi nzima. Hivi sasa ninavyoongea katika Mkoa wa Tanga mkandarasi ameshaingia. Kwa hiyo, nikuhakikishie vitongoji vyako vyote ambavyo Mheshimiwa Mbunge unavifatilia sana ikiwemo Kitongoji cha Mambo leo, Mbwembeza, Msongambele, Mto wa Mbuzi, Kwambambere pamoja na kwa Mpota na Maramba vyote vitapata umeme.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii adhimu ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Manyoni Magharibi kuna vijiji vya Mbugani, Agondi, Mabondeni, Kitopeni, Ipande, Muhanga, Damwelu, Kitalaka, Kaskazi Stesheni, Kintanura, Lungwa na Kalangali havina umeme. Je, Serikali inaweza kutoa tamko kwamba REA Awamu ya Tatu wananchi wa vijiji hivi watafikiwa na umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa, nakupongeza sana juzi uliniletea orodha ya vijiji vyako vyote, kwa hiyo vijiji vyako vyote Mheshimiwa Mbunge ulivyotaja katika Awamu ya Tatu vyote vitapitiwa na umeme, na nikuhakikishie kwamba kufikia mwezi Machi kama ambavyo tumeeleza, vijiji vyote kwa nchi nzima wakandarasi watakuwa site ikiwa ni pamoja na Jimbo lako la Manyoni Magharibi.
MHE. MAFTAH A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru niweze kuuliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kabisa kwamba Serikali iliweka mkakati wa kuhakikisha ya kwamba maeneo yote ambayo limepita bomba la gesi kitaalam wanaita mkuza wa gesi, kwamba vijiji vile na mitaa ile itakuwa imepatiwa umeme kupitia REA Awamu ya Kwanza, Pili na ya Tatu. Lakini mpaka sasa hivi ninavyozungumza maeneo mengi ya vijiji na vitongoji vya Mtwara Mjini na Lindi kwa mfano Dimbozi, Mbawala Chini, Mkunjanguo na Naulongo kule kote bado hakujapelekewa umeme. Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali ukoje kuhakikisha kwamba wanamaliza tatizo hili katika ule mkuza wa gesi kwamba wapate umeme wale wananchi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Maftaha kwamba tunapotekeleza Mradi wa REA Awamu ya Tatu, awali ya yote tunaanzia kwenye vijiji ambavyo viko kwenye mkuza wa bomba la gesi. Kwa hiyo, nikuhakishie Mheshimiwa Maftaha na niombe tu kwamba tutakapomaliza Bunge kama una fursa basi tutapanga siku tupitie kijiji hadi kijiji ili kuhakikisha wananchi wako wanapata umeme.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Singida Mjini imejaaliwa kuwa na rasilimali ya vyanzo vya umeme kwa maana ya upepo na jua na yako makampuni tayari yamekwishajitokeza kwa ajili ya kuzalisha umeme huo. Sasa na sisi wananchi wa Jimbo la Singida Mjini tumejitokeza kwa maana ya kutoa maeneo yetu kwa ajili ya uzalishaji. Serikali sasa ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba umeme huo unazalishwa ili Singida Mjini iweze kupata viwanda vya kutosha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Singida Mjini kunapita umeme wa kilovoti 40 kuelekea Shinyanga na Namanga na wananchi tayari wametoa maeneo yao kwa ajili ya kupisha mradi huo na wako ambao wameshalipwa fidia na wengine hawajalipwa fidia. Serikali inatoa tamko gani sasa kuhakikisha kwamba wananchi wote wanalipwa fidia kwa ajili ya kupisha umeme huo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa, Serikali ina mpango mahususi wa kuendeleza wawekezaji binafsi katika umeme mbadala hasa katika maeneo ya Singida ambako kuna umeme wa upepo. Hata hivyo, mkakati wa Serikali wa kwanza, Serikali imetenga kupitia mradi wake wa REA shilingi milioni 42 kwa ajili ya kuendeleza wawekezaji binafsi watakaofanya katika uzalishaji wa umeme pamoja na mambo ya miradi ya maji. Kwa hiyo, wananchi wa Singida watapata pesa hizi kupitia mradi wa REA ambapo watawezeshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mkakati mwingine badala ya kupitia mradi wake umeshafadhili sasa, nikizungumzia kwa nchi nzima miradi ya Lukonda kule Njombe pamoja na Ndoya kule Mbinga kama wajasiriamali wa Kitanzania ambao wanawezeshwa kupitia miradi ya Serikali, miradi ya REA. Kwa hiyo, miradi ya Serikali kupitia miradi ya REA kutoa mahususi kwa ajili ya kuendekeza wawekezaji. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Sima na kama kuna wawekezaji wengine kule Singida Mheshimiwa Sima basi walete wataalam wetu watashirikiana na watu wa REA ili waweze kushirikiana zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kuhusiana na mkakati wa Serikali kulipa fidia kwenye Mradi wa backbone wa kilovoti 400. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Sima alivyoshirikiana na Serikali mpaka wananchi takriban 200 wakalipwa fidia awamu ya kwanza. Awamu ya pili nimhakikishie Mheshimiwa Sima, hivi sasa vijiji vyake 13 ambavyo vinaingia kwenye mradi ule vitalipwa fidia jumla ya shilingi milioni 722.7, malipo yataanza mwezi Februari mwaka huu na yatakamilika mwezi Machi na nimhakikishie kwamba vijiji vyake vya Misuna ambavyo vilipitiwa na umeme pamoja na Mtipa pamoja na Kisaki pia vitalipwa fidia kwa utaratibu huo.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na pamoja na kazi nzuri ambayo Wizara hii inafanya, naomba niulize swali dogo tu la nyongeza. Niliwahi kuuliza hili swali kwamba kwa kuwa Wilaya ya Kilolo ndiyo wilaya pekee ambayo maji mengi yanayojaza Kihansi yanatoka kule ambayo ndiyo yanasaidia kupelekea kuleta umeme nchi hii. Je, Kilolo inanufaikaje sasa? Naomba kwa nafasi hii atueleze hapa wananchi wa Kilolo watanufaika vipi ili kuhakikisha wanapata umeme.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa eneo la Kilolo linatupatia maporomoko ya maji ambayo yanatusaidia sana kuingiza kwenye Gridi ya Taifa. Lakini wananchi wa Kilolo pamoja na hasa wananchi wa Kihesa Mgagao watanufaika sana na umeme huu na nitaje tu Mheshimiwa Mwamoto, hivi sasa katika Mkoa wa Iringa, REA Awamu ya Tatu imeshaingia na eneo mojawapo ambalo linapelekewa umeme ni pamoja na Kihesa Mgagao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi wa Kilolo wataendelea kunufaika na miradi ya umeme.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Jimbo la Tarime Mjini lina kata nane na kati ya kata nane, kata nne ziko pembezoni na hazina umeme kabisa na kata mbili zina umeme kwa asilimia chache. Ningependa kujua commitment ya Serikali ya kuhakikisha kwamba wananchi wa Jimbo la Tarime Mjini wanapata umeme kwa asilimia zaidi ya 90.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Esther, tumeshirikiana naye sana kwenye mradi wa REA Awamu ya Pili na ni kweli kuna kata nne na kata nyingine mbili ambazo hazijaguswa kabisa. Hata hivyo, nimhakikishie Mheshimiwa Esther kwamba Jimbo lako pamoja na Mkoa wa Mara tumeshaanza kutekeleza Mradi wa REA Awamu ya Tatu wa desification. Hapa ninapozungumza wiki ijayo mkandarasi ata-report kwake ili amwelekeze maeneo mahususi. Kwa hiyo, kata zake nne na zile tatu ambazo anazungumza Mheshimiwa Mbunge zitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Tatu unaoanza mwezi wa Tatu na kuendelea.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri akijibu swali mojawapo hapa Bungeni kuhusu mradi wa umeme wa upepo Singida alisema kwamba Serikali inakamilisha mkataba na taratibu za kusaini kati ya Kampuni ya Wind East-Africa na kwamba mwezi Februari mradi huo utaanza. Naomba atusaidie, je, maneno yale ni kweli au bado? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichowaeleza ni kweli kwanza, lakini cha pili nifafanue tu kwamba mradi wa REA unaokwenda kuendelea umeshaanza na mpaka tarehe 31 mwezi Machi, wakandarasi watakuwa wameshaingia mikoa yote kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa REA unaoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa upande wa umeme wa upepo kule Singida nimesema mradi wa Wind East-Africa pamoja na Geo Wind wanakamilisha taratibu za kimikataba na kufikia mwezi Juni ndiyo wataanza rasmi. Kwa wanaoanza Februari na mwezi Machi ni miradi ya REA na ile miradi ya upepo itaanza kuanzia mwezi Juni na kuendelea.
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Morogoro inaelekea kuwa Jiji, je, Serikali ina mikakati gani ya kumaliza maeneo yote ya Mji wa Morogoro kuwa na umeme?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna maeneo ambayo umeme umeshafika, wananchi wameshalipia kuunganishiwa umeme, lakini majibu wanayopewa ni kuwa nguzo hakuna. Je, Serikali itaondoa lini kero hiyo ya nguzo katika Mji wa Morogoro ili wananchi waweze kupata umeme, maeneo waliyokwishapata umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali kupeleka umeme ni kama ambavyo nimeeleza, ipo miradi ya REA, lakini pamoja na REA bado TANESCO wana bajeti zake za kupeleka umeme. Katika Mkoa wa Morogoro, hasa Morogoro Mjini, mkakati uliopo wa kwanza kabisa, Serikali imetenga shilingi milioni 106 kwa mwaka huu ambayo itapeleka umeme kwenye vijiji vya Mheshimiwa Abood ikiwemo Kihonda, Mafisa pamoja na maeneo mengine kama kule Kanisani ambako ameeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengine ambayo Mheshimiwa Mbunge hajayataja pamoja na eneo lake lile ambalo amesema eneo la Bomba la Zambia. Kile Kijiji cha Bomba la Zambia ambacho kipo mbali sana kitapelekewa umeme mwaka huu. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Abood kwamba Serikali ina mkakati madhubuti wa kupeleka umeme kwenye vijiji vyake vyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kuhusiana na nguzo, ni kweli kabisa yako maeneo Morogoro Mjini wananchi wamelipia, lakini hawajawahi kuunganishiwa umeme. Utaratibu unafanyika sasa na nimhakikishie Mheshimiwa Abood hivi sasa tunapoongea hapa wananchi wake wa Lokole Juu pamoja na Lukobe Kanisani wanaunganishiwa umeme kwa sababu wameshalipia na nguzo zimeshakuja na vijiji vinne ambavyo amevitaja pamoja na Kauzeni na maeneo mengine wataendelea kuunganishiwa umeme mara baada ya nguzo kuingia mwezi ujao.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Spika,
nashukuru kwa majibu mazuri na ufafanuzi wa swali langu la msingi umeeleweka lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, ni lini Serikali itapeleka umeme wa REA III katika Jimbo la Kwela? Nauliza hivyo kwa vile Ukanda wa Ziwa Rukwa haujaguswa kabisa karibu Kata 13 na Kata saba za Ukanda wa Juu na zenyewe hazijaguswa kabisa, jumla Kata 20 hazijaguswa hata kijiji kimoja.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni lini Serikali itamalizia kupeleka umeme katika REA III katika vijiji 68 ambavyo havijapelekewa umeme katika Kata za Mpwapwa, Jangwani, Mpuhi, Likozi, Kalambanzite, Lusaka, Lahela na Sandurula?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Malocha kwa jinsi anavyofuatilia masuala ya umeme kwa wananchi wa Jimbo lake. Mheshimiwa hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini ni lini Serikali itapeleka
umeme katika Kata zake 20 ambazo zimebaki, kwanza kabisa tunakubaliana na Mheshimiwa Malocha kati ya Kata 27 zilizopata umeme ni Kata mbili ziko katika Jimbo lake. Kwa hiyo, Kata 25 zilizobaki kama ambavyo ameeleza ikijumlishwa pia Kata zake za Kipeta, Kilangawani, Kigamadutu pamoja na Malegesya na shule za sekondari
alizozitaja zitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA ambao umeanza kutekelezwa nchi nzima mwezi huu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimpe uhakika
Mheshimiwa Malocha kwamba Kata zake zote 27 na zile mbili ambazo zimepata bado Vitongoji vyake navyo vitapelekewa umeme kuanzia mwezi huu hadi miaka minne ijayo. Kwa hiyo, tuna uhakika Kata zako 27 Mheshimiwa Malocha zitakuwa zimepata umeme wa kutosha.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na vijiji 68, ni kweli
kabisa vipo vijiji 68 katika Jimbo la Mheshimiwa lakini na vitongoji 237. Tunapopeleka umeme katika vijiji 68 katika Jimbo la Kwela tunapeleka pia katika vijiji 237 ambapo vitongoji vyake vyote havijapata umeme.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa
Malocha vitongoji vyake vyote ambavyo havijapata umeme vile vya Mpwapwa, Muze, Halula na Mwandui vyote vitapata umeme. Ahsante sana.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante, nishukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2013 wananchi wa Mtwara waliweza kuandamana kwa kiasi kikubwa sana Mtwara na Lindi wakidai namna gani kwamba rasilimali hii gesi inaweza kuwanufaisha na tunashukuru hivi sasa manufaa
hayo yanaanza kuonekana. Nilikuwa naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba ule mpango wa kuwapa wawekezaji ambao wana nia ya kuwekeza Mtwara gesi waweze kutengeneza ama wajenge viwanda vya mbolea umefikia wapi mpaka hivi sasa?
(b)Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba kujua, kulikuwa na mkakati na mwaka jana tulielezwa ndani ya Bunge hili kwamba kuna usambazaji wa gesi asilia kwenda majumbani kwa mana kwamba mikoa ya Dar es Salaam na maeneo mengine. Nilikuwa naomba kujua mkakati huu kwa Mkoa wa Mtwara na Lindi upoje kwa sababu tulipewa tu taarifa kwamba upembuzi yakinifu umeshaanza nataka kujua mimi kama Mbunge sina taarifa nao. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Maftaha kwa kweli kati ya Wabunge ambao wanahangaikia sana maslahi ya wananchi wake ni pamoja na Mheshimiwa Maftaha. Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusuaiana na maswali yake ya msingi kabisa, kwanza kabisa ujenzi wa kiwanda cha mbolea Mtwara; nataka tu nimwambie Mheshimiwa Maftaha pamoja na wananchi wa Mtwara na Lindi kwamba hatu ailiyofikiwa sasa hivi; kwanza kuna
Kampuni ya HELM kutoka Ujerumini imeshapata eneo kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanda cha mbolea na makadirio ya kukamilisha ujenzi huo ni mwaka 2020 lakini hata hivyo nimwambie tu hatua ambazo zinafanywa na Serikali. La kwanza kabisa; Serikali kupitia TPDC wanafanya majadiliano sasa ya kuelewana sasa bei ya kununua gesi kati ya TPDC pamoja na Kampuni ya HELM itakayojenga kiwanda hicho na kwa sasa wameshaonesha kutenga jumla ya dola za Kimarekani milioni 200 kwa kampuni hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini taratibu za kuuziana gesi wakishamaliza kujenga ujenzi huo 2020 wataweza kupewa gesi na mahitaji ya kiwanda hicho cha mbolea inafikia milioni 80 futi za ujazo mpaka 104; kwa hiyo matarajio yapo na wananchi wa Mtwara watanufaika na kiwanda
hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la pili; ni kweli kabisa tulitarajia sana tuanze usambazaji wa gesi majumbani katika mji wa Mtwara na Lindi na Dar es Salaam pia, lakini tumefikia hatua nzuri. Upembuzi yakinifu umekamilika, matarajio yameshapatikana na kwa sasa Mtwara na Lindi wanahitaji milioni tano za gesi hadi kumi futi za ujazo ambazo zinagharimu shilingi bilioni mbili, Kwa hiyo kuanzia Julai mwaka huu, Wananchi wa Mtwara, Lindi na Dar es Salaam wataanza sasa kupata gesi ya majumbani. Na Mheshimiwa Maftaha wale wananchi wako wale wa Mbawala chini pamoja na Mtajitambua wataanza kupata gesi asilia.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza kwenye swali la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Ziwa Tanganyika ni eneo ambalo kumefanyika utafiti wa gesi na mafuta hasa kwenye Tarafa ya Karema. Eneo hilo kuna uhakika wa kupatikana mafuta na gesi, je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Mkoa wa Katavi na ukanda mzima wa Ziwa
Tanganyika juu ya utafiti ambao umefanywa mpaka sasa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa utafiti umeshaanza kufanyika katika Ziwa Tanganyika ili kugundua gesi iliyopo na makampuni yaliyopita kufanya ni makampuni mawili ya Chuo Kikuu cha Ujerumani pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wanajiolojia wa Tanzania pamoja na TPDC.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachofanyika sasa ni
kuanza kufanya appraisal ili kujiridhisha na gesi iliyopatikana. Zipo dalili za kugundua lakini kinachofanyika sasa niappraisal na shughuli ya kukamilisha appraisal itafanyika mwezi Agosti
mwaka huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo baada ya Agosti mwaka huu Mheshimiwa Kakoso wananchi wanaozunguka Ziwa Tanganyika wataanza kupata gesi asilia katika maeneo hayo.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo; zipo hisia kwa wananchi wa Mkoa wa Mtwara kwamba Wizara ya Nishati na Madini haina nia ya dhati na kiwanda cha mbolea
cha Msanga Mkuu cha HELM ambacho amekielezea uwekezaji wake. Kwa sababu majadiliano yamechukua muda mrefu na ujenzi ambao ameusema utakamilika mwaka 2020 kuanza kwake ujenzi itategemea makubaliano ya bei ya kuuziana gesi.
Je, anatoa kauli gani juu ya hisia za wananchi wa
Mtwara kwamba kiwanda hcho hakitazamwi vizuri ndani ya Wizara yake hasa ukizingatia hata kwenye jibu lake la msingi hakukitaja kiwanda hicho?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Hawa Ghasia katika jibu langu la nyongeza nimeeleza mikakati ya Serikali ya kujenga kiwanda hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nimeeleza hatua ya majadiliano ya gesi kwa sasa nikupe taarifa Mheshimiwa Hawa Ghasia na mimi nakushukuru sana unavyohangaikia maendeleo ya wananchi wa Mtwara Vijijini, Kampuni ya
Helmo kutoka Ujerumani inapendekeza kwa sasa hivi ichukue gesi kwa dola 2.6 wakati ukifanya hivyo Mheshimiwa Hawa na wewe unajua makadirio ya gharama ya chini kabisa
katika standard price ulimwenguni kote na hapa kwetu ni dola 4.2.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Ghasia nikuhakikishie tu jitihada za makusudi zinafanyika kuhakikisha kwamba wananchi wa Mtwara wanapata gesi, lakini matumizi ya mbolea pia. Kwa hiyo, hatua tunayochukua majadiliano kati ya Kampuni ya HELM kwa kiwanda cha mbolea pamoja na Serikali yatakuwa yamekamilika na kiwanda cha mbolea kitaanza sasa kutekeza katika ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2020 waliosema ni makadirio yao ya kampuni kuwa wamesha-set taratibu zote na ujenzi wa kiwanda hicho kukamilika. lLakini jitihada za Serikali ziko pale pale. Ahsante sana.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Wilaya ya Liwale iko katika Mkoa wa Lindi na ndiyo Wilaya pekee ambayo bado mpaka leo hii inatumia umeme wa mafuta na mashine zile tumezitoa Rufiji, mashine zile zimechoka. Nini kauli ya Serikali kuipatia umeme wa gesi Wilaya ya Liwale ili tuweze kuwa na umeme wa uhakika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa katika umeme tunaotumia hapa nchini 50% ya umeme tunaotumia unatokana na rasilimali ya gesi.
Kwa hiyo, hata huko Liwale tunachofanya sasa hivi tunajenga miundombinu ya kusafirisha umeme kutoka Mtwara kuja Lindi utakaokwenda katika Wilaya za Liwale, Tandahimba, Nanyumbu pamoja na Masasi umbali wa kilometa 80 ili kupunguza umbali wa kilometa 206 zilizopo sasa. Lengo ni kuunganisha umeme wa gesi katika maeneo yote ya Mtwara na Lindi na maeneo ya jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mheshimiwa
Mbunge wa Liwale tunakuhakikishia kwamba kwa sasa hivi hata wananchi wa Liwale sasa wataanza kutumia umeme wa gesi.
MHE. KAPT. (MST.) GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kushukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Napenda kuipongeza Serikali kwa kusambaza umeme (REA II) vijiji karibu Tarafa zote sita za Wilaya ya Newala. Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya Mheshimiwa
Naibu Waziri yanaonesha kwamba tatizo la umeme maeneo ya Mtwara Mjini, Lindi yataisha na tumeshuhudia juzi Rais ameweka jiwe la msingi, lakini upande mwingine Naibu Waziri
anakubali kwamba Wilaya za Tandahimba, Newala, Masasi, Nanyumbu, Nachingwea na Ruangwa hali ya upatikanaji wa umeme si nzuri na kule tatizo si kwamba umeme haupo tatizo
ni miundombinu. Nyaya zimekatika, ikinyesha mvua nguzo imeanguka, ni lini Serikali itachukua hatua madhubuti kuhakikisha kwamba kukatikakatika kwa umeme na kuanguka nguzo kuna malizwa mara moja ili Wilaya hizi nazo
zifaidi umeme kama wanavyofaidi Wilaya zingine?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili,
pamekuwepo na matamshi mengi upande wa Serikali juu ya gharama halisi za mwananchi wa kawaida kuingiza umeme katika nyumba yake. Nini kauli ya leo ya Serikali kwamba kijiji fulani kinataka kuingiza umeme pale Newala, yule mwananchi wa kawaida anatakiwa alipe shilingi ngapi kwa sababu matamko ya huko nyuma hayafanani na gharama halisi ambazo zimekuwa zikilipwa? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Mkuchika jinsi ambavyo anashughulikia maslahi ya umeme ya wananchi wa Newala Mjini, nampongeza sana. Lakini
pamoja na hayo, Mheshimiwa Mkuchika niseme tu maana hapa tutakaa tutajadiliana zaidi kwa sababu najua unafuatilia mambo yao sana na sisi kama Serikali tusingekuwa tayari kukuangusha, kwa hiyo, tunakuomba sana uendelee kutupa ushirikiano.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na maswali yake mawili ya nyongeza; la kwanza kabisa, ni lini Serikali sasa itachukua hatua za kutatua tatizo la kukatikakatika kwa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imechukua hatua zifuatazo katika maeneo hasaa ya Mtwara na Lindi na maeneo mengine. La kwanza kabisa, Serikali sasa inajenga miundombinu ya kusafirisha umeme, ule mkuwa kutoka Mtwara na kurekebisha miundombinu iliyoharibika hapa
ambayo tumesema ya urefu wa kilometa 2016. Njia za miundombinu kutoka Mtwara hadi Newala, Tandahimba na maeneo mengine ilikuwa ni ndefu sana, kwa hiyo, hatua ya kwanza Serikali inaanza kujenga transmission line ya umbali wa kilometa 80 ambayo itakamilika mwezi Mei mwaka huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hatua ya pili inajenga kituo cha kupoza umeme kitakachokuwa Mnazi Mmoja maeneo ya Lindi ambacho kitahudumia sana maeneo yote ya Newala, Tandahimba na maeneo mengine ili kupunguza
tatizo la kukatika kwa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ni
kwamba inarekebisha pia mashine ambazo zilikuwa mbovu kama nilivyoeleza na kununua nyingine mpya ili kufikia mahitaji halisi ambayo ni megawati 30 kwa wananchi wa Mtwara na Lindi na Wilaya zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na gharama za umeme. Gharama za umeme kwa manufaa ya wananchi wote ningependa niseme ifuatavyo; kwa vijijni kupitia mradi kabambe wa REA gharama za umeme za kuunganisha kwa wananchi ni shilingi 27,000/= tu basi hakuna gharama nyingine. Ningependa lieleweke hili ili kusudi wananchi
wengine wasibambikiziwe bei. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo, zipo gharama za kutandaza nyaya kwenye nyumba. Hizo ni gharama zinaotegemea na ukubwa wa nyumba lakini pia zinategemea na mkandarasi waliokumbana nae. Tunachofanya kudhibiti hilo ni kuhakikisha sasa wakandarasi wote wanaounganisha nyaya kwenye numba za wateja sharti la kwanza lazima waidhinishwe na TANESCO na majina yao yabandikwe katika Ofisi za TANESCO ili ikitokea ulaghai tuweze kuwafuatilia. Hizo ni gharama za vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini upo mpango
mwingine kwa wananchi wa kawaida ambao nyumba zao zina chumba kimoja hadi vinne. Tunawaptia chombo kinachoitwa UMETA yaani maana yake Umeme Tayari Ukikiweka. Gharama yake ni shilingi 36,000. Kwa hiyo, nataka kuweka wazi kuhusu gharama kijijini. Lakini gharama halisi kwa maeneo ya mijini kwa umbali usiozidi nguzo moja ni shilingi 177,000/= na kwa mijini ni shilingi 320,000/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni mambo muhimu ningependa kuyafafanua, lakini pia mambo mengine inategemea sasa na mambo ambayo mteja pia anahitaji. Ahsante sana.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika,
nashukuru na mimi kunipa nafasi niulize nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali inafanya kazi nzuri ya kuwapelekea umeme wananchi katika nchi yetu; na kwa kuwa kipindi kilichopita Serikali kwenye Jimbo la Makambako hususan vijiji vya Ikwete, Nyamande, Manga, Utengule, Mlowa, Mahongole, Kitandililo na Kifumbe iliahidi kutuletea umeme katika Awamu ya Pili na mkandarasi ambaye tulikuwa tumepewa alikuwa ni LAC Export na mkandarasi huyu baadae Serikali kupitia Bunge hili walisema
wamemuondoa kwa sababu alikuwa hakidhi vigezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini sasa Serikali
itatupeleka katika vijiji hivi nilivyovitamka umeme Awamu hii ya Tatu ili wananchi hawa waweze kupata umeme kama ambavyo wanapata sehemu zingine? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nikubaliane na Mheshimiwa Sanga na nampongeza, kweli nilipomtembelea alinipa
ushirikiano mkubwa na inaonesha Mheshimiwa Sanga pamoja na kwamba wananchi wanakuoenda, lakini na sisi tunakupenda kwa kazi unayowafanyia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni kweli kabisa vijiji saba katika eneo la Makambako ikiwemo pamoja na vijiji alivyovitaja vya Ikwete pamoja na Kifumbe ilikuwa vipatiwe umeme kupitia mpango huo. Na kama utakumbuka Mheshimiwa Sanga, uko mradi unaojenga usafirishaji wa umeme kutoka Makambako kupitia Madaba hadi Songea
na ndiyo vijiji vilitakiwa vipatiwe umeme kutoka utaratibu ule.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata vijiji vyote vile, saba pamoja na vitongoji vyako vyote imeingia katika mpango wa REA ulioanza kutekelezwa katika maeneo ya Makambako pamoja na Njombe kuanzia tarehe 15 Januari,
2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuwamabia Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla kwamba utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Tatu umeanza rasmi tangu tarehe 15 Januari, 2017 na tunachofanya sasa na wananchi na Wabunge ni kuzindua Mkoa hadi Mkoa ili kuwakabidhi wakandarasi Waheshimiwa Wabunge mliko ili na ninyi wote mkitusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Deo Sanga tumeshazinfua tangu tarehe 15 Januari na wananchi wako wa vijiji hivyo saba pamoja na kijiji cha Kifumbe wataanza kupata umeme kupitia mradi huu wa REA wa Awamu ya Tatu.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la kukatika kwa umeme katika Mikoa ya Lindi na Mtwara halitofautiani na tatizo la kukatika kwa umeme katika Mkoa wa Kilimanjaro hasa Jimbo la Moshi Mjini. Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu kuhakikisha kwamba
wanatatua tatizo la ukatikaji wa umeme katika Jimbo la Moshi Mjini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa katika Mikoa ya Kilimanjaro, Dar es Salaam na Arusha kulikuwa na tatizo la mara kwa mara la umeme. Lakini uko mradi mmoja unaoitwa Trade Up unaotekeleza ukarabati wa miundombinu katika mikoa hiyo mitatu. Mheshimiwa Japhary nikuambie tarehe 22 Mei taratibu kabisa za kukamilisha ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika Mji wa Kilimanjaro utakamilika kupitia
mpango huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa hatua ya pili
tunajenga pia mradi wa kusafirisha umeme unaotoka Kinyerezi kwenda Tanga, unakwenda mpaka Namanga, lakini uko unaotoka hapa sasa kutoka SInginda kupita Manyara na kwenda mpaka Kilimanjaro wa kilovoti 400 ambao pia utaongeza nguvu ya umeme na kupunguza sasa
kukatika katika kwa umeme kwa sababu ya low voltage.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mheshimiwa
Japhary kuanzia mwezi Mei tunaweka kwamba kukatika umeme katika Mkoa wa Kilimanjaro utapungua kwa kiasi kikubwa.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Mkwajuni ambao ndiyo makao makuu ya Wilaya ya Songwe, kila wiki umeme upo siku tatu na umeme haupo siku nne mpaka hivi ninavyoongea, hata wiki iliyopita nilikuwa huko. Nini tatizo la
kukatika katika kwa umeme hasa ule unaotoka Mbeya Lwanjilo, Chunya, Makongolosi mpaka Mkwajuni. Tatizo ni nini kila mwaka maana huu ni mwaka wa nne sasa hatuna umeme wa uhakika pale Mkwajuni?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa maeneo mengi umeme tulionao haujitoshelezi ndiyo maana tunarekebisha na kuimaisha miundombinu ikiwemo Mkoa wa Mbeya pamoja na mikoa
ya jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua tuliyochukua kwa
sasa tunajenga mradi wa kusafirisha umeme wa KV 400 kutoka Mbeya kupita Sumbawanga kwenda Kigoma hadi Nyakanazi, lakini huo huo utakwenda mpaka Bulyanhulu na Geita umbali wa kilometa 1,108. Kwa hiyo, hatua hii itakapokamilika katika Mkoa wa Mbeya tatizo la umeme litapungua sana. Matarajio yetu, kufikia mwezi Julai, 2018 matayarisho, ujenzi pamoja na
uimarishaji wa njia za kuimarisha umeme katika Mkoa wa Mbeya utakuwa umekamilika. Kwa hiyo, kuanzia Julai mwakani kukatika kwa umeme katika Mkoa wa Mbeya kutapungua au kutakoma kabisa kwasababu ya kutekelezwa kwa mradi huu.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Kwa kuwa tatizo la kukatika katika kwa umeme lililopo Mtwara na Lindi linafanana kabisa na hali ilivyo katika Halmashauri ya Wilaya ya Temeke hasa katika Kata za Kurasini, Mtoni, Keko, Chang’ombe, Tandika Sandari, Buza na
maeneo yote ya Yombo ambapo kila siku ni lazima umeme ukatike na pale inapokuwa na hali ya mawingu au mvua basi umeme hukatika kwa muda mrefu zaidi. Sasa wananchi wa Temeke wangependa kusikia majibu ya Serikali, ni lini tatizo hili litakoma?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika kujibu swali la nyongeza katika Mkoa wa Kilimanjaro, mtekelezaji anayerekebisha mitambo pamoja na miundombinu katika maeneo ya Temeke, Kurasini, Kigamboni pamoja na Kiwalani
ni mradi mmoja. Lakini katika maeneo ya Temeke mwezi uliopita nilifatana na Mheshimiwa Mbunge wa Temeke, nimeenda kukagua mradi wa Temeke na Kurasini. Kinachofanyika sasa wanaimarisha na kuweka vikombe vipya kwa sababu maeneo ya Temeke, Kurasini yamezidiwa. Kwa hiyo, tunaongeza nguvu ya umeme ya kilovolti 220
kutoka 132, lakini kadhalika tunafupisha umbali wa nyaya uliokuwepo wa zaidi ya kilometa 57 ili ziwe chini ya kilometa 50 katika maeneo ya Temeke, Kurasini, Kigamboni pamoja
na Kiwalani.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa utaratibu wa
kukamilisha tarehe 27 Aprili, 2017 mradi utakamilika. Kwa hiyo, baada ya kukamilika kwa mradi huu maeneo ya Temeke, Kurasini, Kigamboni na maeneo ya jirani tatizo la umeme
litapungua sana kwa kiasi kikubwa.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nimshukuru Mheshimiwa
Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini katika jibu lake naomba nifanye marekebisho kidogo kwamba kwanza
haiwezekani watu wakalipwa halafu wakadai, kwa sababu wanaolipwa wanalipwa kwa coordinates na eneo
linajulikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa miaka 17 wananchi wa maeneo ya
Mizingamo, Ikumbiyaga, Compound pamoja na Mtakuja wako ndani ya eneo ambalo ni leseni ya mgodi, lakini
hawaruhusiwi kujenga, hawaruhusiwi kupima, hawaruhusiwi kuuza, lakini mgodi haujajiandaa kulitumia eneo hilo sasa wala kesho. Sasa ni nini hatima ya wananchi wa eneo hilo, kama mgodi sheria inasema utalipa tu fidia pale ambapo watataka kulitumia, lakini hawaruhusiwi kufanya chochote kwa miaka 17? Swali langu la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwa muda tofauti, Serikali kupitia Waziri wa Wizara husika, Naibu Waziri wa Mazingira, wamekuja na wameshuhudia aina ya uchimbaji wa madini wa Mgodi wa GGM ukiwa na madhara makubwa kwa wananchi wa Kata ya Kalangalala, Mjini Geita. Matokeo ya uchimbaji mbovu ni mipasuko ya nyumba inayotokana na mitetemo mikubwa, watu wengi wamezimia, lakini maji machafu yanatoka kwenye eneo la kuchimba na Mkurugenzi wa Mgodi aliyekuwepo ambaye alitaka kuleta suluhisho la migogoro hiyo, mgodi ulipoona anataka kuchukua hatua, ukamfukuza. Maagizo yote yaliyotolewa na Serikali hayajawahi kutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa Serikali itahakikisha mgodi unawalipa fidia wananchi ambao nyumba zao
zimepasuka kutokana na mitetemo ya uchimbaji wa dhahabu Geita?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza sana Mheshimiwa Kanyasu jinsi ambavyo anapambana na kuhangaikia maendeleo ya wananchi wa Geita Mjini. Hongera sana Mheshimiwa Kanyasu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la kwanza, ni kweli kabisa maeneo ya Compaund, Nyakabale,
Katoma pamoja na eneo lingine la Kagema, yako katika maeneo ya beacon. Kama ambavyo nilieleza kwenye jibu
langu la msingi, wananchi hawa ambao mgodi unahitaji eneo lile, tutakapolihitaji wakati wa uchimbaji, tutawalipa
fidia kwa wale ambao hawajalipwa fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa wako wananchi wachache ambao baada ya kulipwa fidia, pia walirejea katika maeneo yale. Kama haitoshi, mgodi ulilipa fidia ya umbali wa mita 570 badala ya mita 200 ili kuhakikisha
kwamba hakuna mwananchi ambaye anabaki bila fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Kanyasu kwamba suala hilo tumelipokea,
tutaendelea kulifanyia kazi. Kama kuna wananchi hawajafidiwa, basi itabidi wafidiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la pili, kuhusu mipasuko. Kwanza kabisa niendelee kumpongeza
Mheshimiwa Kanyasu na Wabunge wote wa Geita, wakiwemo Mheshimiwa Mbunge wa Busanda na
Waheshimiwa wengine, pamoja na Mheshimiwa dada yangu yule wa Chama cha Upinzani wa Mkoa, waliita Mkutano, nilifika kule mwenyewe nikaangalia taarifa ya kampuni.
Taarifa ya kampuni ya awali ilionesha kwamba mpasuko hausababishwi na kampuni. Tuliunda tume, ikaleta matokeo, ikaonesha baadhi ya maeneo kwa kweli yanasababishwa na mpasuko wa kampuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haitoshi, tuliunda tume nyingine kwenda kutathmini majengo yaliyoharibika.
Nimhakikishie Mheshimiwa Kanyasu, ilionekana nyumba takribani 890 zilisababishwa kwa kiasi fulani na mlipuko wa Mgodi wa GGM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mheshimiwa Kanyasu alitaka kujua ni lini sasa Serikali itatoa tamko? Tarehe
20 mwezi huu wa Aprili, timu ya wataalamu saba wakishirikiana na uongozi wa Wilaya pamoja na Jimbo lako
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mheshimiwa Mbunge na GGM watakwenda sasa kuangalia nyumba ngapi zinahitaji fidia ili fidia sasa itakapothibitika waweze kulipwa fidia wale ambao itaonekana kuwa halali.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Katika Jimbo langu la Bunda kuna vijiji vya Nyabuzume na Nyaburundu. Kuna wachimbaji wadogo wenye PL wa muda mrefu sana. Tatizo wale wachimbaji wanachimba, madini yanapatikana, lakini pale wanaambiwa kwamba wana leseni za utafiti. Serikali ya kijiji iliwaomba kutoa huduma za maendeleo katika maeneo hayo ya Nyabuzuma na Nyaburundu, hawataki kutoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua ni sheria ipi inawataka hawa wachimbaji ambao wanapata madini,
hawataki kusaidia vijiji hivyo vinavyohusika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa hakuna sheria inayowakataza
wachimbaji wadogo au wachimbaji wakubwa wasilipe levy au mapato yoyote yanayotokana na uchimbaji wao. Sheria ya Madini pamoja na Sheria ya Fedha inawataka walipe.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Getere kama kuna shida, wasiliana na sisi tukusaidie ili Halmashauri yako iweze kupata
fedha hizo.
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgodi wa Tanzanite uliopo Mkoa wa Manyara ni mgodi ambao unachukua idadi kubwa
ya vijana, lakini kumekuwa na vifo mfululizo miaka tisa sasa ambavyo havijawahi kufanyiwa utafiti wa kina ni kwa nini vifo hivi vinatokea.
Je, ni lini sasa Serikali itakaa na hawa wawekezaji wa vitalu husika ili kuanzisha utaratibu wa kifuta jasho kwa
familia zile ambazo zinapata maafa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa yapo madhara yanayotokana na uchimbaji, siyo katika mgodi wa Tanzanite One peke yake, hata katika migodi mingine. Sheria zinataka kama kuna mtu ameathirika na uchimbaji au na dhuluma yoyote, taratibu za kisheria lazima zifuatwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili tumelichukua kwa muda mrefu, tunashirikiana na Wizara ya Kazi pamoja na
Kitengo cha Maafa ili kutathmini ukubwa wa tatizo la namna hiyo ili hatua zifuatwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya pili, tumeunda timu inayojumuisha Wizara yetu, Wizara ya Kazi pamoja na
Halmashauri husika ili mwezi wa tano tuanze kuyatathmini madhara hayo. Baada ya tathmini itakapofanyika
Mheshimiwa Mbunge, tutakujulisha hatua kamili zitakazochukuliwa.
MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.
Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kunipa majibu yenye matumaini.
Mheshimiwa Spika, tatizo la kukatika kwa umeme limeleta madhara makubwa sana kwa wateja. Watu wamekuwa wakiunguliwa nyumba zao wengine vifaa ndani ya nyumba vikiungua kama friji, television na kadhalika. Tatizo
la hitilafu ya kukatikakatika kwa umeme na kuunguza vifaa vya wateja si tatizo la mteja, ni tatizo la TANESCO. Nataka kujua kutoka kwa Mheshimiwa Waziri ni lini sasa TANESCO itaanza kufidia wananchi kwa kuunguliwa na vitu kwa sababu siyo tatizo lao, kama ilivyo kwenye nchi za Ulaya ambako huwa wanafidia wananchi wakati matatizo yakitokea na kupata hitilafu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Sasa hivi tunakwenda katika Tanzania ya viwanda, na Mheshimiwa Waziri amesema Kilimanjaro tutakuwa na umeme wa uhakika. Nataka nijue na uwahakikishie wananchi wa Kilimanjaro, je, umeme huu utaweza kutosheleza kwa wafanyakazi na wafanyabiashara wa Mkoa wa Kilimanjaro ambao wanataka kuwekeza katika viwanda? Ahsante sana.
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza niongee tatizo la kukatikakatika umeme.
Waheshimiwa Wabunge njia nyingi za umeme nchini ni zile ambazo TANESCO ilianza nazo mwaka 1964. Hata mimi kwetu Musoma Mjini umeme ulikuja mwaka 1967, hata pale kwetu hazijabadilika. Sasa ni uamuzi wetu, tuamue kuwa na uvumilivu tuzime tutengeneze au tuendelee na matatizo uwe unawaka unakatikakatika. Kwa hiyo, nadhani jibu zuri ni kwamba tuvumilie miundombinu ni ya zamani na tunairekebisha, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala ambalo Mheshimiwa Mbunge amesema TANESCO ina taratibu za kutoa fidia ikiwa kama vyombo vimeharibika na kosa ni la umeme, kosa ambalo ni la TANESCO, wana taratibu zao unapeleka madai unajaza fomu wanafanya tathmini, huo utaratibu upo.
Sasa niongelee hili la kukatikakatika kwa ujumla lingine la umeme wa uhakika. Kilimanjaro kama alivyosema
Mheshimiwa Naibu Waziri ni kwamba inawekwa miundombinu mipya halafu Kilimanjaro na Arusha kuna sub
station tutakwenda kuifungua ya KIA ambayo ni mpya, umeme umeongezeka pale tumeweka substation. Lakini
isitoshe ni kwamba tunaongeza umeme wa msongo mkubwa. Hii Waheshimiwa Wabunge na Watanzania
wanaonisikiliza ni kwamba njia za kusafirishia umeme nchini zilikuwa za KV 220, sasa hivi tunaweka 440, ni karibu mara mbili.
Kwa hiyo, njia ya kutoka Iringa, Dodoma kwenda mpaka Shinyanga tayari, ndiyo maana siku hizi umeme
haukatikikatiki kwa sababu tuna umeme mwingine unasafirishwa humu, na uwezo wake unaweza ukachukua
mpaka MW 5000 kutoka Iringa kwenda Shinyanga. Kwa hiyo, inabidi tujaze mle umeme ni kama ambavyo unajaza maji zaidi kwenye bomba, kwa hiyo, umeme mwingi unakuja.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Kaskazini tunajenga transmission line mpaka kutoka Singida kwenda
Namanga ambayo nayo ni ya kilovolts 400; itachukua huo umeme. Juzi nilikuwa naongea na mkandarasi anataka
kujenga transmission line ya kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma.
Ndugu zangu wa pembeni mwa Ziwa Tanganyika, tunakamilisha majadiliano ya njia kubwa ya umeme kutoka
Iringa, Sumbawanga, Mpanda, Kigoma na Nyakanazi. Kuna ambayo imeshaanza kujengwa na Balozi anataka akaizindue ya kutoka Makambako kwenda Songea kusudi Songea iwe kwenye Gridi ya Taifa. Kwa hiyo, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote hii nchi ya viwanda itajengwa na Wizara ya Nishati na Madini, ndiyo yenye uwezo wa kuijenga msiwe na wasiwasi.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo nimeridhika nayo, bado nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa REA Awamu ya Kwanza, jimbo langu lilibahatika kupata umeme kwenye vijiji tano au sita na kwa kuwa mradi huu wa Awamu ya Kwanza haukuwa na kipengele cha kuweka umeme kwenye majengo ya huduma za jamii kama shule na vituo vya afya. Baada ya kuona hivyo ilibidi Mbunge nije hapa Bungeni nikope fedha kama shilingi milioni 150 ili nikalipe TANESCO waweke umeme kwenye sekondari saba; na kwa kuwa REA Awamu ya Pili nimepata vijiji vitano, lakini katika Kata ya Mtanila umeme haujaend kwenye Kituo cha Afya cha Mtanila. Swali langu sasa, je, hii REA Awamu ya Pili Mheshimiwa Naibu Waziri ananihakikishia majengo ya huduma za jamii kama vituo vya afya na shule yatapata umeme? La kwanza hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa amesema REA Awamu ya Tatu karibu itaanza; je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kwenda na mimi Chunya wakati wa ufunguzi wa mradi huo hasa hasa kuanzia Kata ya Ifumbo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze sana Mheshimiwa Mwambalaswa kwa kufuatilia mahitaji na maslahi ya wananchi wake katika Jimbo la Lupa na tunashirikiana naye kwa ukaribu sana hasa katika vijiji na kata ambazo zimebaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nikubali kwamba katika REA Awamu ya Kwanza na ya Pili hatukuchukua maeneo mengi sana na hii ni kwa nchi nzima, siyo katika jimbo la Mheshimiwa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mwambalaswa katika kata sita zilizobaki ambazo ameomba zipatiwe umeme ikiwemo Kata za Mtabila, Ifumbo, Itumbi, Kambikatoto pamoja na Matundasi A na B zote zitapelekewa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama alivyouliza, REA Awamu ya Tatu majukumu yake ya kimsingi pamoja na mambo mengine ni kusambaza umeme katika taasisi zote za umma kama hospitali, vituo vya afya, zahanati, shule, mitambo ya maji, makanisa, misikiti na sokoni.
Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mwambalaswa na nichukue nafasi hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wote kwenye Halmashauri zetu tuweze sasa kutenga walau pesa kwa ajili ya kuunganisha umeme kwenye taasisi zetu kwa sababu hili ni jukumu letu sote, na ndiyo maana wakandarasi tunapokwenda kuwakabidhi sasa tunawakabidhi Waheshimiwa Wabunge ili waweze kufuatilia utekelezaji wa miradi hii. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mwambalaswa nakuhakikishia kwamba vituo vya afya na taasisi nyingine zitapelekwa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili la kufuatana na Mheshimiwa Mwambalaswa, kwanza kabisa niko tayari lakini kabla sijafuatana nawe mkandarasi tumeshamtuma na tumeshazindua utekelezaji wa REA Awamu ya Tatu katika Mkoa wa Mbeya na Songwe. Sasa hivi mkandarasi yuko Ileje na tarehe 15 atafika kwako Mheshimiwa Mwambalaswa. Kwa hiyo, tuko pamoja na niko tayari kufauatana na wewe.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa Mbulu Vijijini katika REA Awamu ya Pili tumepata vijiji viwili tu na sasa Mbulu Vijijini hatuna sub-station tunapata umeme kutoka Katesh na Mheshimiwa Waziri anafahamu, amekuja, tunapata kutoka Babati na Mbulu Mjini. Je, mtatuhakikishiaje sasa katika awamu hii REA itafika maeneo yote ya kata na hasa katika vijiji vya mwanzo vya Mbulu Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa Mheshimiwa Flatei nakupongeza, mwaka jana mwezi Novemba tulitembea na wewe kwenye jimbo lako lote na ukanionesha vijiji vyako vyote 78 ambavyo havijapata umeme pamoja na vijiji vya karibu kabisa na Wilaya za jirani. Hata hivyo, natambua katika utekelezaji wa REA Awamu ya Tatu kazi zinazofanyika ni pamoja na kufunga transfoma. Kinachokosekana katika Jimbo lako Mheshimiwa Flatei ni ufungaji wa transfoma katika vijiji ambavyo umevitaja ikiwa ni pamoja na Katesh.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Flatei kazi ambayo itafanyika sasa ni kukupelekea umeme katika vijiji vyako 78 vilivyobaki pamoja na vitongoji 120 kama ambavyo umeomba. Kwa hiyo, niwahakikishie wananchi wa Mbulu Vijijini kwamba wote watafikiwa na umeme vijijini, vitongojini pamoja na kwenye taasisi zako za umma.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza kwenye Wizara ya Nishati na Madini. Wilaya ya Chemba ni miongoni mwa Wilaya mpya na upatikanaji wa huduma ya nishati kwa maana ya umeme ni kwa vijiji 60 tu kati ya vijiji 112. Nataka kufahamu ni lini sasa kwa REA Awamu ya Tatu itakwenda kukamilisha vijiji hivi 52 vilivyobaki ili Wilaya yetu na wananchi wale waweze kupata huduma hii ya umeme wa REA Awamu ya Tatu? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa katika Jimbo la Chemba tulipeleka umeme katika vijiji 62 na vikabaki vijiji 52; kwa hiyo viko 124. Niseme tu vijiji 52 vilivyobaki tumeshazindua katika maeneo ya Chemba na Wilaya zote, Mkoa wa Dodoma na tunaelekea katika Mikoa ya Singida na mingine. Upelekaji wa umeme katika REA Awamu ya Tatu umeanza tangu mwezi Machi na utakamilika kwa nchi nzima ikiwemo pamoja na Jimbo la Chemba mwaka 2020. Mradi huu unakwenda kwa awamu, baadhi ya vijiji na vitongoji vitakamilika mwezi Machi, 2019 na baadhi yake kwenye densification ni miezi 15 kuanzia sasa. Kwa hiyo, vijiji vyote 52 kati yake vijiji 12 vitapatiwa umeme 2019 na vilivyobaki vya Chemba mwaka 2020.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Swali la kwanza, katika Wilaya ya Kasulu katika kijiji cha Makere lakini pia katika Wilaya ya Kakonko wananchi wamekuwa wakipata kipato chao kwa kuchimba chokaa, lakini mara nyingi wamekuwa wakizuiliwa kufanya shughuli hiyo. Je, Wizara ya Madini na Wizara ya Maliasili iko tayari kukaa pamoja na wananchi hao ili kuweza kutatua tatizo hilo na kuwawezesha kuwa wachimbaji rasmi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha inatenga eneo la wachimbaji wadogo ili kuepusha migogoro inayoweza kutokea baadaye?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa
Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Genzabuke wakati tunatenga eneo la Kakonko mwaka 2002 alitupa ushirikiano mkubwa sana. Kwa hiyo, nakupongeza sana Mheshimiwa Genzabuke kwa kufuatilia maisha ya watu wa Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na maswali yake mawili, la kwanza alitaka kujua namna sisi pamoja na taasisi ya maliasili tunavyoshirikiana ili kuwawezesha wananchi hawa kupata maeneo na kufanya uchimbaji kwa ajili ya kuongeza pato lao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge, Sheria ya Madini ya mwaka 2010 katika kifungu cha 95 pamoja na Sheria ya Mazingira zinakubaliana kwamba mtu yeyote anaweza akamilikishwa leseni katika eneo lolote ikiwa ni pamoja na maeneo ya reserve na hifadhi kinachotakiwa ni kupata kibali cha maandishi. Tumekuwa tukifanya hivyo Mheshimiwa Genzabuke ndiyo maana katika eneo la Makere kuna leseni 15 za uchimbaji wa chokaa, lakini katika maeneo mengine ya Lugufu kuna leseni saba za uchimbaji ambayo pia yako kwenye hifadhi. Kwa hiyo, hilo halina shida, lakini kama ulivyosema tutaendelea kukaa na wenzetu ili wananchi wa Kasulu na maeneo ya jirani waendelee kunufaika na uchimbaji wa madini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na kutenga maeneo. Kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi na ambavyo nimesema katika swali langu la nyongeza la kwanza ni kwamba tunaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo nchi nzima. Kwa sasa tumeshatenga maeneo saba katika Mkoa wa Geita na katika Mkoa wa Kigoma katika eneo linaloitwa Kinyo na Janda tutatenga maeneo hayo kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa chokaa katika Wilaya ya Kasulu.
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa kuna baadhi ya maeneo nchini mfano Wilaya za Manyoni na Bahi imebainika kuwa kuna madini ya uranium na inasemekana kwamba madini haya yana thamani kubwa sana na yanahitajika maeneo mbalimbali nchini. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuchimba madini hayo ili wananchi wa maeneo yale pamoja na Serikali ifaidike? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilieleza Wakala wa Jiolojia wanafanya utafiti wa kubaini mbale, jiokemia, jiofizikia na jiolojia ili kujiridhisha kama maeneo fulani yana madini ya aina gani. Ni kweli kabisa katika maeneo ya Manyoni, Bahi pamoja na maeneo mengine ya Singida ikiwemo eneo la Sekenke, GST wamekuwa wakifanya utafiti. Sasa hivi wanakamilisha shughuli za utafiti kubaini kama hiyo uranium ambayo inaonekana inaweza ikatathminiwa ikachimbwa kwa kiwango gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika maeneo ya Bahi na maeneo mengine ya Manyoni pamoja na Sekenke yapo madini ya dhahabu na madini megine. Bado GST wanajiridhisha lakini mara baada ya kukamilisha maeneo haya yatatengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo ili waweze kuchimba sasa kwa uhakika. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge avute subira, zoezi la ukamilishaji wa utafiti la GST likamilike na linatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka huu.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali la kwanza, katika majibu ya Mheshimiwa Waziri amesema kuwa REA III imeanza Machi, 2017. Kwa kuwa wananchi katika vijiji hivyo vya Wangama, Ikuvilo, Tagamenda, Lupembelwasenga pamoja na Lyamgungwe ni wakulima na wanajihusisha na kilimo cha umwagiliaji na kuna wawekezaji ambao wameonesha nia ya kujenga viwanda na tunasema tunahitaji Tanzania ya viwanda lakini umeme haupo. Naomba commitment ya Serikali ni lini watapata umeme kwa sababu imekuwa ni muda mrefu kutopatiwa umeme katika maeneo hayo ili wanufaike na viwanda? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika kipengele
cha kwanza majibu ya Waziri ni tofauti kabisa na hali halisi ya eneo hilo la Malulumo kwa sababu mimi natokea eneo hilo na wanasema utekelezaji umefanyika kwa 90%. Je, Waziri yuko tayari kuongozana na mimi akaone huo utekelezaji wa 90% uliopo maeneo yale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na swali la pili, niko tayari kufuatana na Mheshimiwa Grace kwenda kwenye eneo lake ili kuangalia utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Tatu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Grace tukimaliza Bunge tu mguu mmoja mimi na wewe Iringa tukamalize kazi hiyo, lakini kwa ruhusa yako Mwenyekiti. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa vijiji vilivyobaki vitapatiwa umeme. Awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Grace na Wabunge wote wa Mkoa wa Iringa kwa jinsi ambavyo wanafuatilia utekelezaji wa miradi ya umeme. Niwahakikishie kwamba tarehe 21 Machi, 2017 tulizindua rasmi utekelezaji wa Mradi wa Umeme Awamu ya Tatu katika Mkoa wa Iringa na eneo la Iliwa kwa Mheshimiwa Mwamoto ndipo tulipofanyia uzinduzi kwa niaba ya mkoa.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwahakikishie kabisa Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Iringa pamoja na Mufindi, Kilolo, Njombe, tumeshawakabidhi wakandarasi wawili, NACROI na NAMIS na wameshaanza utekelezaji wa kazi hiyo. Kwa hiyo, kuanzia Machi tumeshaanza kutekeleza mradi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji ambavyo amevitaja Mheshimiwa Grace vya Wangama, Lupembelwasenga, Tagamenda na Mseke pamoja na vijiji vingine ambavyo amevitaja na kwa Mheshimiwa Mwamoto vitapatiwa umeme katika awamu hii ya mradi. Nimeenda kwa Mheshimiwa Mwamoto na Waheshimiwa Wabunge wengine, nimeenda Nang’uruwe, Kihesa Mgagao na huko tumeshawapelekea umeme. Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba utekelezaji wa mradi huu umeanza na utakamilika mwaka 2020/2021.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nilitaka nimueleze Mheshimiwa Waziri kwamba Mkoa wa Mtwara ndiko inakozalishwa gesi inayozalisha umeme wa Dar es Salaam ambako haukatiki kila mara, kiasi tumeanza kuamini gesi yetu haitunufaishi ni bora tungerudishiwa yale majenereta yaliyokuwa yanazalisha umeme Mtwara wakati huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la umeme la Mtwara linasababishwa na kuharibika kwa transfoma ya jenereta moja yake ambayo nafahamu mpaka sasa kuna mvutano mkubwa kati ya TANESCO pamoja na MANTRAC Tanzania Limited kwa ajili ya ku-supply ile transfoma kwa sababu ya madeni sugu ambayo TANESCO hawajalipa.
Mheshimiwa Waziri, naomba utueleze kinagaubaga ni lini matatizo ya TANESCO na MANTRAC yatakwisha ili kuwarejeshea wananchi wa Mtwara umeme wa uhakika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mweyekiti, ni kweli kabisa liko tatizo la kuharibika kwa mashine moja Mtwara kiasi cha kushindwa kupeleka megawatt 18 kwa ujumla wake. Kwa sasa hivi ni kweli kabisa Mtwara wanapata megawatt chini ya 18, wanapata 16 na 15.6
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wa Mtwara na Lindi lakini hatua zilizochukuliwa ni kwamba hivi sasa ukarabati umeshaanza. Mgogoro uliokuwepo kati ya TANESCO na MANTRAC umekwisha na jenereta inatengenezwa, ni hatua ya kwanza. Hatua ya pili, Mtwara tunawaongezea mashine nyingine sita ambapo kila mashine itakuwa na megawatt mbili. Kwa hiyo, mtakuwa na megawatt nyingine za ziada 12 na jumla kuwa na megawatt 30. Kwa hiyo, sasa umeme wa Mtwara pamoja na Lindi maeneo ya jirani utakuwa ni wa uhakiki zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili linashughulikiwa na baada ya Bunge hili Mheshimiwa Mbunge tutakwenda wote kukagua mashine hii ikiwa imeshakamilika na umeme unapatikana.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize swali moja la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa vijiji vya Makutupa, Mlembule, Tambi, Bolisazima na Mgoma tayari nyaya na nguzo zimeshawekwa bado transfoma. Sasa namuuliza Naibu Waziri, vijiji hivi vitapata lini transfoma ili waweze kuanza kupata huduma ya umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali moja la Mheshimiwa Lubeleje, Mbunge Mkongwe katika Bunge hili, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kulikuwa na transfoma mbili mbovu katika Jimbo lake na jana tulikuwa tunawasiliana na Meneja na amenihakikishia kwamba mwisho wa wiki hii transfoma mbili zitapatikana. Nimpongeze sana Mheshimiwa Lubeleje kwa niaba ya wananchi wake na nimwambie kwamba transfoma hizi mbili zitapatikana Ijumaa (kesho kutwa) mwezi huu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri anisaidie, kwanza napongeza kasi ya usambazaji wa umeme lakini kuna tatizo la nguzo kwenda chache.
Naomba aniambie katika kata ya Bumanga kwenye kiwanda cha akina mama cha kusindika mbogamboga, msitiki, kanisa na shule walikosa nguzo hivyo hamna umeme, ni lini mtapeleka nguzo hizo ili waweze kupata umeme? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile Mheshimiwa Mlata ameniambia kwamba kuna tatizo la nguzo, nitawasiliana na wataalam leo hii ikiwezekana mwisho wa wiki hii au wiki ijayo ziweze kupatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kusema kwamba kwa sasa nguzo, mashine na transfoma zinapatikana hapa nchini hatuagizi kutoka nje. Kwa hiyo, uhakika wa upatikanaji wa nguzo pamoja na vifaa vingine utakuwa ni rahisi zaidi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mlata tutafuatana lakini mwisho wa wiki hii au wiki ijayo nguzo zitapatikana.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2011 Serikali iliingia mkataba au ilikubaliana na Kampuni ya Total ya Ufaransa kwa ajili ya utafutaji wa mafuta katika Lake Tanganyika North Block baadae mazungumzo yakafa, mwaka 2014 Kampuni nyingine ya Ras Al Khaimah nayo pia ikawa imepewa zabuni ya utafutaji wa mafuta wa kitalu cha Kaskazini cha Lake Tanganyika, lakini mpaka sasa na kwenye majibu ya Mheshimiwa Waziri hakuna maelezo yoyote kuhusiana na hilo, kuna maelezo ya block ya Kusini peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015 TPDC ilifanya survey katika eneo lote la ziwa na katika majibu ya Waziri hakuna matokeo yoyote ya utafiti kama jinsi ambavyo Mheshimiwa Nsanzugwanko alikuwa anataka kupatiwa taarifa.
Swali la kwanza, Serikali inaeleza nini status ya sasa hivi ya utafutaji wa mafuta katika eneo la Kaskazini mwa Ziwa Tanganyika ambapo Waziri hujalitolea maelezo kabisa?
Swali la pili, nini status ya umeme wa maporomoko ya Mto Malagarasi ambao ni tegemeo kubwa sana la uzalishaji wa umeme katika Mkoa wa Kigoma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Zitto, nakumbuka tangu wakati wa uwekezaji katika Mto Malagarasi, wakati wa uwekezaji na ufadhili wa MCC alikuwa mbele sana kufuatilia umeme wa Kigoma, kwa hiyo nakupongeza sana kwa niaba ya wananchi wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana wananchi pia na Wabunge wa Kigoma wote Mheshimiwa Serukamba Mheshimiwa Nsanzugwanko kwa mshikamano wenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nijielekeze kwenye maswali mawili ya Mheshimiwa Zitto, status ya utafiti ikoje katika Ziwa Tanganyika. Kwanza kabisa pamoja na maswali ambayo yameulizwa na Mheshimiwa Zitto, kama alivyosema mwaka 2011 kampuni ya Total ilianza kufanya utafiti, lakini kulingana na gharama za uwekezaji ilishindwa na haikuendelea. Hata hivyo, taarifa zake zilitusaidia sana katika utafiti unaoendelea kwa sababu katika taarifa ambazo tulizipata, kampuni kwa kushirikiana na TPDC waliweza kuchora ramani za urefu wa kilometa 20,024 chini ya Ziwa Tanganyika ambazo zinatupa taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili walitathmini taarifa za utafiti za Total za miaka 80 iliyofanyiwa utafiti na makampuni ya nyuma, kwa hiyo, Kampuni ya Total iliacha lakini ilituachia taarifa Mheshimiwa Zitto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo status ikoje, ni kwamba baada ya utafiti huo TPDC mwaka 2014/2015 ilifanya geo-survey katika maeneo ya Ziwa Tanganyika na kwa kweli pesa kubwa sana zilitumika shilingi bilioni 6.96 kwa ajili ya utafiti huo na matokeo yake kwa kweli matarajio ya kupata mafuta katika Ziwa Tanganyika yapo. Hiyo ndiyo status Mheshimiwa Zitto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na mradi wa Malagarasi ni kati ya miradi muhimu sana katika ukanda wa Ziwa Tanganyika, maeneo ya Kigoma na maeneo ya jirani kwa sababu kwa sasa Mheshimiwa Zitto tumekamilisha upembuzi yakinifu na tumeshaanza majadiliano na wawekezaji pamoja na wafadhili wetu, tumepata fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika na mradi ule utagharimu dola milioni 149.5. Kwa hiyo, shughuli zitaanza mwezi wa saba mwakani na zitakamilika mwaka 2019/2020. (Makofi)
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri sana, lakini naipongeza Wizara hii kwa kuwa makini katika kufanya kazi katika sekta hii ya nishati na madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijauliza maswali
mawili ya nyongeza ningependa kuwapa pole wananchi wa Jimbo la Same Magharibi, hususan kata ya Hedaru ambao wamepoteza nyumba nyingi pamoja na mifugo na mazao kutokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia juzi.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu Subhuhana Wataallah, aweze kutupa mvua za kiasi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napenda kuuliza
maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Swali la kwanza, katika Mradi wa REA Awamu ya Pili, mkandarasi ambaye anaitwa SPENCON alishindwa kufanyakazi na kwa hiyo, vijiji vingi pamoja na vitongoji vingi vya Jimbo la Same Magharibi hususan vijiji 48, umeme haujakamilika kutokana na kwamba, mkandarasi huyo alishindwa kazi.
Je, REA Awamu ya Tatu, vijiji hivi ambavyo vilikosa umeme pamoja na vitongoji vyake, Serikali ina mkakati gani katika kuhakikisha kwamba, vitongoji vyote vinapata umeme na vijiji vyangu vyote vya Jimbo la Same Magharibi katika Awamu hii ya Tatu ya REA?
Swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari baada ya Bunge hili la Bajeti kuongozana na mimi kwenda katika Jimbo la Same Magharibi, ili akajionee mwenyewe vijiji na vitongoji ambavyo havina umeme katika Jimbo langu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, awali ya yote niungane na Mheshimiwa David kuwapa pole wananchi wake kwa tatizo walilopata.
Mheshimiwa Nibu Spika, kulingana na maswali yake mawili ni kweli kabisa katika utekelezaji wa REA Awamu ya Pili, Mikoa miwili ya Kilimanjaro na Singida haikukamilika ipasavyo na ni kweli kabisa mkandarasi SPENCON hakufanya kazi yake vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kutoa taarifa pia ya hatua za Serikali ambazo zilichukuliwa kutokana na kutofanya kazi vizuri kwa mkandarasi huyo.
Hatua ya kwanza tulichukua asilimia 10 ya mkataba wake ambayo ni retention kimkataba kabisa. Hatua ya pili, kazi hiyo sasa atapewa mkandarasi mwingine ili aikamilishe vizuri na wananchi wa Same waendelee kupata umeme. Lakini hatua ya tatu, tunaendelea sasa kuchukua hatua za kisheria, ili Wakandarasi wa namna hiyo sasa wapate fundisho waache kuwakosesha miundombinu wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David kwamba wananchi wa Same, vijiji vyako vyote 48 vitapata umeme. Naelewa viko vijiji vya milimani kwa Mheshimiwa Dkt. David kijiji cha Muhezi, Malaloni kule Malalo pamoja na kwa Hinka, vitapata umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, kadhalika naelewa vile vijiji 48 anavyosema Mheshimiwa, yapo maeneo kama kule Hedaru, yako maeneo kule ambako Mheshimiwa tumesema Chekereni, Mabilioni pamoja na Jificheni Mabilioni, pamoja na kijiji cha Njiro vyote vitapata umeme. Hivyo, ninakuhakikishia kwamba vijiji ambavyo havijapata umeme kwenye REA II, sasa vyote vitapata umeme. Siyo vijiji tu hata vitongoji vyake na taasisi za umma pamoja na maeneo mengine muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala lake la pili la kuongozana naye, kwanza kabisa niko tayari, ninaweza nikasema utakaponikaribisha utakuwa umechelewa,
ukichelewa sana utanikuta kwenye Jimbo lako, kwa hiyo, niko tayari kutembelea kwenye Jimbo lako.
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru majibu mazuri kutoka kwa Mheshimiwa Waziri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba mojawapo ya faida zilizomo katika mradi wa REA ambayo kawaida inaleta mvuto kwenye mradi huu ni pamoja na complementary au unafuu wa bei ambao wanapewa watu wanaosambaziwa umeme huo. Kwa mazoea ambayo yamezoeleka kwa umeme ambao unasambazwa na TANESCO ni kwamba bei za TANESCO zinakuwa kubwa kuliko zile bei au gharama za REA.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaomba Mheshimiwa Waziri anihakikishie kwamba hizi fedha zilizotengwa kwa ajili ya TANESCO na kwa maeneo ambayo ameyazungumza, ikiwemo na vijiji vya Ijuganyundo B ambavyo havina umeme kabisa, maeneo ya Makongo kule Kahororo na maeneo ya Chaya kule Busimbe, hizi gharama pia za TANESCO zitakuwa complimented au itakuwa ni gharama zilezile za TANESCO ambazo zimekuwa kubwa na watu wa maeneo haya ambao hawana uwezo wasiweze kupata umeme?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili,...
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaomba tu atajibu mojawapo atakaloliona linafaa kwenye…
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba baadhi ya vijiji ambavyo vinaonekana viko ndani ya mji vinapelekewa umeme kupitia Shirika la Umeme TANESCO na ni kweli kabisa bei ni tofuati, bei za TANESCO kwa wateja wa awali kabisa ni shilingi 177,000 na kwa upande wa REA ni shilingi 27,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Lwakatare kwa jinsi anavyofuatilia maslahi ya wananchi wa Bukoba Mjini, ni mdau mzuri, lakini tunamhakikishia kwamba tutafanya upembuzi kwa ukina kabisa tuangalie kama vijiji vina sifa ya kupelekewa umeme kwa mradi wa REA tutafanya hivyo, tutakaa naye pamoja ili ikibainika basi wapelekewe kwa utaratibu wa REA.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie pia Mheshimiwa Muganyizi Lwakatare kwamba vijiji vyote ambavyo amevitaja vikiwemo vya Kashai, Mafumbo Tweyambe, Turabirere, Kahororo pamoja na visiwa vyake vya Nyabisaka pamoja na Msira vitapata umeme kupitia Mradi wa REA. (Makofi)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mwezi mmoja uliopita Wizara ilikuwa inazindua umeme wa REA Awamu ya Tatu katika maeneo mbalimbali lakini baadaye wamesimama. Ni lini wanafanya uzinduzi huo katika Mkoa wa Geita na hasa Jimbo la Geita Mjini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ni kweli tulianza kuzindua mikoa kumi kwa Tanzania Bara na tulibakiza mikoa takribani 15. Nimhakikishie Mheshimiwa Kanyasu kwamba tumemaliza taratibu zote za kuwapata wakandarasi. Nitumie nafasi hii kwa heshima ya Bunge lako Tukufu kuwaambia Waheshimiwa Wabunge wote na wananchi kwa ujumla, kesho tarehe 18 Mei, saa 08.00 mchana hapa Mjini Dodoma, kupitia Ukumbi wa Mikutano wa Hazina, wakandarasi wote katika mikoa ya nchi nzima watakabidhiwa katika mikoa yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia niwakaribishe Waheshimiwa Wabunge watakaokuwa na nafasi ya kuhudhuria katika ukabidhiwaji wa mikataba hiyo na majukumu yale ili muweze kushiriki.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hayo tutakwenda kuwatambulisha wakandarasi wote mkoa kwa mkoa ili Waheshimiwa Wabunge muweze kufuatilia uwajibikaji wao na orodha pia mtakabidhiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nichukue nafasi hii pia kuwataka wakandarasi wote watakaokabidhiwa mikataba yao kesho, waende katika maeneo yao ya kazi na waanze sasa kutekeleza mradi wa REA kwa nchi nzima, kijiji kwa kijiji, kitongoji kwa kitongoji na bila kuruka kijiji wala tarafa.
Nichukue nafasi hii kuwaeleza Waheshimiwa Wabunge kama ambavyo umeme haubagui itikadi, umeme pia wa REA hautabagua aina ya nyumba, iwe nyumba ya tembe au vinginevyo, kila aina ya nyumba watapatiwa umeme kupitia mradi huu. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba nimuulize swali dogo Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza nampongeza sana kwa kazi nzuri ambayo anafanya…
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Ukonga, Kata za Msongola, Buyuni, Zingiziwa, Majohe, Pugu, Pugu Station na Chanika hazina umeme na Mheshimiwa Naibu Waziri anafahamu. Kwa sababu kuna mkanganyiko kule Dar es Salaam kwamba ni mjini siyo vijijini, je, REA inaenda maeneo hayo au haiendi? Ahsante sana.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa, yako maeneo yako mjini, lakini kwa Mheshimiwa Mbunge wa Ukonga tumeshakaa naye. Maeneo anayoyataja ya Majohe, Chanika, Zingiziwa mpaka kwenye gereza lako kijijini kule, yale ni maeneo ya vijijini yatapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA na tumeshaanza. Hata hivyo shule yake aliyosema Mheshimiwa ya Bombambili tumeshaifanyia kazi na yeye ni shahidi. Kwa hiyo, maeneo hayo yatapelekewa umeme kwa kupitia mradi wa REA.
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba umeme wa REA ni wa vijijini, lakini yako maeneo ya mjini ambayo yana maeneo mengi na makubwa ya vijijini. Nashukuru kwamba REA wameweza kutupatia umeme katika mitaa michache kama ya Nyabisare pamoja na kule Bukanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu, kwa kuwa, maeneo mengi ya taasisi yako kwenye hizo kata za pembezoni, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba REA wanaweza kutupatia umeme katika maeneo yote hayo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa yako maeneo, najua Tarime mko wawili na kuna Musoma na Tarime lakini ki-TANESCO ni Tarime, hakuna shida Mheshimiwa, nimeshakuona Mheshimiwa Esther Matiko.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kusema kwamba, ukweli yako maeneo ambayo yako pembezoni ingawaje yanasemeka yako mjini. Tumeshakaa na Mheshimiwa Manyinyi, yako maeneo na hasa kwa taasisi za umma, taasisi zote za umma zitapelekewa umeme kupitia mradi wa REA.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini viko vijiji ambavyo itabidi tuviangalie, vile vijiji ambavyo vinaonekana viko mjini vitapelekewa umeme kupitia miradi ya TANESCO lakini vile vya vijijini kama ambavyo amesema Nyabisare na vingine, tutachambua ili kuona ni vijiji gani vipelekewe kwa Mradi wa REA. Vijiji vyote vya Miradi ya REA tumeshakabidhiwa, kwa hiyo, kwa Mheshimiwa Mbunge ambaye anaona kuna sehemu kuna utata ni vema tukae ili isionekane kijiji fulani kinarukwa.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nina swali moja la nyongeza kufuatana na Wizara hii kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, REA ya Awamu ya Pili ilikuwa ina sehemu ambayo imepima lakini sehemu hizo mpaka leo hii bado hazijapata umeme. Mfano ni katika kata ya Magoma katika kijiji cha Makangala na Mwanahauya na Pemba na katika kata ya Kerenge katika vitongoji vya Ntakae, Mianzini, Kwaduli, Migombani, Mfunte na Kiangaangazi. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka kuhakikisha kwamba vijiji hivi na ile vya Kata mpya ya Mpale vinapata umeme kwa haraka?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Ngonyani kwa jinsi ambavyo anashughulikia maendeleo ya umeme kwa jimbo lake, hongera sana Mheshimiwa Ngonyani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuonesha tuna mkakati gani kwanza kabisa upatikanaji wa fedha ya mradi huu unakwenda vizuri na ni mkakati mzuri. Nimhakikishie Mheshimiwa Ngonyani vijiji vyake vitapata umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na kwamba ana wasiwasi na Kata ambazo ametaja za Magoma, Kelege pamoja na Mazizini lakini yako maeneo ya Foroforo pamoja na Majimoto Mheshimiwa Ngonyani atapata umeme kupitia mradi huu. (Makofi)
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la Korogwe Vijijini linafanana sana na Jiji la Mbeya ambalo linapanuka kwa kasi, jiji hili kwenye kata za pembezoni ambazo ni Tangano, Iduda, Itezi, Iganjo, Nsomwa, Sanga, Mwasekwa na Msalaga hazina kabisa umeme na ni kwa muda mrefu sana. Kata hizi mazingira yake yamekaa kwa mfumo wa REA na tunashukuru kwamba REA Awamu ya Tatu ilishazinduliwa katika Mkoa wa Mbeya. Swali langu ni kwamba Serikali ina mkakati gani wa kuvipatia umeme vijiji hivi ambavyo kwa TANESCO inaelekea imeshindikana?Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Mwanjelwa kwamba hata TANESCO bado inapeleka umeme katika maeneo mbalimbali kufuatana na bajeti zake. Tumeshakaa na Mheshimiwa Mbunge na ni kweli kabisa yako maeneo yenye utata kidogo kama eneo la Uyole.
Hata hivyo, vijiji anavyotaja vya Idunda, Kasilanda pamoja na vingine baadhi yake vipo kwenye miradi ya REA. Kwa hiyo, tutakaa na Mheshimiwa Mbunge tuone vijiji vinavyoingia mijini vitabaki TANESCO na vile ambavyo viko kwenye vijiji vitapelekewa umeme kupitia miradi ya REA.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Bagamoyo, vijiji vya Kondo na Kongo vilikuwa kwenye REA Awamu ya Pili lakini miradi hii haikutekelezwa na katika REA Awamu ya Tatu miradi ya vijiji hivi haimo. Nilishamsikia Mheshimiwa Naibu Waziri akitamka hapa Bungeni kwamba miradi yote ile ambayo haikutekelezwa kwenye Awamu ya Pili ndiyo itapata kipaumbele katika Awamu ya Tatu.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anawaambiaje wananchi wa vijiji vya Kongo na Kondo waliokwemo kwenye Awamu ya Pili lakini wamefutwa kwenye Awamu ya Tatu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nipende kusema viko vijiji kwa nchi mzima ambavyo havikutekelezwa katika scope ya REA Awamu ya Pili lakini vilikuwa ndani ya mradi. Vijiji vyote ambavyo vilikuwa chini ya REA Awamu ya Pili vitaendelea kutekelezwa katika Awamu ya Tatu ya REA.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Kawambwa kwamba vile vijiji vyake vya Kondo na Kongo na vingine, viko kama vijiji vinane hivi viko katika mradi wa REA Awamu ya Tatu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Kawambwa aamini tu kwamba vijiji hivyo vitapatiwa umeme katika mradi wa REA Awamu ya Tatu ambao umeshaanza na tayari katika Mkoa wake wa Pwani tumefanya uzinduzi.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Shukuru Kawambwa kama kuna shida tutakaa lakini tumhakikishie vijiji vyake vitapata umeme kupitia mradi wa REA.
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nilikuwa nimeanza kukata tamaa kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mji wa Geita tuna shida sana ya umeme na asilimia 70 ya vijiji vinavyozunguka Mji wa Geita viko katika giza. Ni lini Serikali itapeleka umeme katika kata za Nyanguku, Ihanamilo, Shiloleli, Bulela na Bugwagogo ili kuweza kusaidia katika huduma za jamii ambazo ziko katika maeneo hayo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli vipo vijiji ambavyo havijapata umeme kwa Mji wa Geita na ametaja vitatu lakini viko zaidi ya ishirini. Nimhakikishie Mheshimiwa Peneza vijiji ambavyo ametaja vya Nyanguku na vingine baadhi yake viko katika mradi REA lakini viko katika mradi wa TANESCO. Bahati nzuri sana nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Mkoa wa Geita na mikoa ya jirani iliyokuwa inapata umeme wa low voltage sasa tunakamilisha ujenzi wa mradi wa kusafirisha umeme mkubwa unaotoka Mbeya kwenda Sumbawanga mpaka Nyakanazi na baadaye utatoka Nyakanazi mpaka Bulyankulu na baadaye Geita. Kwa hiyo, wananchi watapata umeme wa kilovoti 400 lakini tutaanza na kilovoti 220.
Kwa hiyo, napenda nimjulishe Mheshimiwa Upendo Pendeza kwamba vijiji hivyo vitapata umeme kupitia miradi ya REA na baadhi yake vitaendelea kupata umeme kupitia miradi ya TANESCO.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa uzinduzi wa REA Awamu ya Tatu Mkoani Tanga, Naibu Waziri alikuja na mimi nilihudhuria. Tulipata orodha ya vijiji na Muheza tulipewa vijiji 44 kwenye REA Awamu ya Tatu. Baadaye orodha hiyo ilipunguzwa vijiji saba vikakosekana ambavyo ni Kwakopwe, Kibaoni, Magoda, Mbambara, Kitopeni, Masimbani na Msowero. Nataka kufahamu hatma ya vijiji hivyo kama vitarudishwa ili waweze kupata umeme kwa sababu wameshaanza kufanya matayarisho ya kuanza kufunga nyaya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa wakati tunazindua katika Mkoa wa Tanga na tulifanya uzinduzi katika maeneo ambayo ameyasema na katika utafiti ikaonekana viko vijiji saba au vinane hivi ambavyo vitaingia kwenye densification stage ya pili.
Mheshimiwa Adadi Rajab vijiji saba vitaendelea kupatiwa umeme, kilichofanyika densification inaanza kwanza kwa miezi kumi na tano. Baada ya miezi kumi na tano tutaendelea na miezi mingine kumi na mitano mpaka tukapofikia hatua ya kukamilisha vitongoji vyote.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Adadi Rajab vijiji vyake saba si kwamba vimeondolewa bali vimepelekwa mbele ili baada ya miezi kumi tano na vyenyewe vitaanza kupelekewa umeme kwa utaratibu huu wa REA. Kwa hiyo, Mheshimiwa Adadi awape faraja wananchi wake wa Muheza kwamba bado watapelekewa umeme kupitia mradi huu.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri sana ambayo imefanyika katika Jimbo la Mbogwe la kusambaza umeme maeneo mengi. Sasa naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, ni lini sasa Serikali itapeleka umeme katika Kata Nyasato, Bunigonzi na Vijiji vyote vya Jimbo la Mbogwe ambavyo bado havijapa huduma hii ya umeme?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni lini sasa mradi wa REA awamu ya tatu utaanza katika Mkoa wa Geita na Wilaya ya Mbogwe in particular? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Masele kwa sababu ameshughulikia sana masuala ya umeme katika jimbo lake ambapo kati ya vijiji 72, vijiji 44 vyote vimeshapatiwa umeme. Hongera sana Mheshimiwa Masele.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie vijiji vyote vilivyobaki, ameuliza suala la msingi sana ni lini sasa umeme utapelekwa katika Kata za Nyasato pamoja na Budigonzi. Nimhakikishie Mheshimiwa Masele kwa niaba ya wananchi wa Mbogwe, ni vijiji vyote 28 sasa tunavipelekea, Vijiji hivyo ni pamoja na Budigonzi, Buzigozigo, Mtakuja, Budura pamoja na maeneo mengine ya Kashenda na Nyashimba, yote yatapelekewa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini tunazindua Mkoa wa Geita? Nipende kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba tumeanza kuzindua utekelezaji wa mradi wa awamu ya tatu tangu tarehe 24 mwezi huu na tumeanza na Mkoa wa Manyara. Katika Mkoa wa Manyara tumefanya katika Jimbo la Babati na mengine. Tarehe saba na nane tunazindua katika Mkoa wa Kagera, tutakwenda katika Wilaya ya Karagwe. Tarehe 10 tutazindua katika Mkoa wa Geita Mheshimiwa Mbunge; na maeneo ya kuzindua ni maeneo ya Nyangh’wale pamoja na maeneo ya Mbogwe. Kwa hiyo niwahakikishie wananchi wa Mbogwe, wananchi wa Mkoa wa Geita na Wabunge wote wa Mkoa wa Geita basi tushirikiane wote tarehe 8 na 10 tutakapokuwa tunazindua katika Mkoa wa Geita.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nataka niulize Serikali kwa kuwa katika Mkoa wa Mbeya, REA III imezinduliwa tayari na mkandarasi yupo aliyeanzia Wilaya ya Rungwe. Sasa ni lini huyo mkandarasi atakwenda Wilaya ya Chunya ili akapeleke umeme kwenye Kata zilizobaki za Ifumbo, Kasanga, Nkunungu, Lwalaje, Kambi Katoto na Mafyeko?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Mheshimiwa Mwambalaswa nampongeza sana, hata tulipokwenda kule ni kwa sababu pia alishirikiana na sisi sana kwa hiyo hongera kwa kazi hiyo. Nimhakikishie kwa niaba ya wananchi wake; ni kweli kabisa katika Kijiji cha Ifumbwe pamoja na Kasanga bado hatujaenda; lakini tarehe 17 mwezi huu mkandarasi atakuwa kwenye Kijiji cha Kasanga katika jimbo lake. Kwa hiyo, katika maeneo mengine yataendelea kufanya kazi hiyo hiyo na niwaombe sana Wabunge wa Mkoa wa Mbeya tushirikiane kwa kazi hiyo kwa sababu mkandarasi tayari ameshaingia mkoani.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo la Mbogwe ni sawa na tatizo lililoko katika Mkoa wa Mara hasa Musoma Vijijini. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri atuhakikishie kwamba ni lini wananchi wa Musoma Vijijini watapata umeme wa REA?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa, tulipokwenda katika Mkoa wa Mara wakati tunazindua Mheshimiwa Mbunge alitupa support kubwa sana. Hongera sana pamoja na Wabunge wote wa Mkoa wa Mara; lakini ni lini sasa umeme vijiji hivyo vitapelekewa; tumeshaanza na kuja kufikia mwezi ujao wakandarasi watakuwa wameingia vijiji 42 katika Mkoa wa Mara na vijiji vilivyokuwa vimebaki vitakamilika sasa ifikapo mwaka 2020. Hata hivyo, si kwenye vijiji tu na vitongoji vyote Mheshimiwa Sokombi, Taasisi zote za Umma, Makanisa na Misikiti pamoja na visiwa ambavyo viko Mkoa wa Mara.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibnu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa, Serikali inaendelea kufanya kazi nzuri kupitia miradi ya REA, lakini nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba yako maeneo mengine kwenye miji na majiji bado yanazo sura za vijiji; kwa mfano kwenye Jimbo la Nyamagana iko mitaa inafanana kabisa bado na maeneo ya vijijini kama Fumagila, Rwanima, Isebanda, Kakebe na maeneo mengine kama Nyakagwe. Ni lini Serikali itakuwa na utaratibu wa kuhakikisha na maeneo haya yanapatiwa umeme wa REA ili yaweze kupata sawasawa na mengine? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mabula. Wakati ananiletea vijiji hivi tulipozungumza aliniletea vijiji vingine ambavyo vilikuwa kwenye hali ya kimtaa, lakini kisura vinaonekana kivijiji na tumeviingiza kwenye Mradi wa REA. Katika vijiji ambavyo ametaja hivi ambavyo inaonekana viko mjini, kwanza kabisa kuna mradi ambao unapeleka umeme kwenye miji yote nchi nzima na mradi huu unaitwa Urban Electrification na utapeleka katika miji na mitaa 314 kwa nchi nzima. Kwa hiyo, hata vijiji au mitaa ambayo iko mijini bado itapelekewa umeme kwa utaratibu huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tutakaa katika vijiji ambavyo amesema vya Fumagila pamoja na Kakene tuone hali itakavyokuwa. Nimwombe sana mara baada ya hapa tukutane na Mheshimiwa Mabula ili ikiwezekana vijiji hivi vipelekewe katika Mradi wa REA.
MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kutokana na mauaji yanayoendelea Wilayani Kibiti bado tunahitaji umeme. Je, Serikali ina mpango gani kupeleka umeme katika vijiji vilivyobakia?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze nilienda kwake na tulitembea sana mpaka kwenye Kijiji cha Jaribu Mpakani na tulipeleka umeme Jaribu Mpakani. Hata hivyo, Serikali imekusudia kuangaza umeme vijiji vyote nchi nzima. Napenda nitoe nafasi hiyo kwa sababu, Mheshimiwa Ungando tumeshirikiana sana, lakini niseme tu vijiji vyote vya Jimbo la Kibiti vitapelekewa umeme sasa kupitia Mradi wa REA; hadi kufikia mwaka 2021 vijiji vyake vyote vya Kibiti vitakuwa vimeshapata umeme. (Makofi)
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa, Mkoa wa Mtwara na Lindi ndiyo mikoa ambayo ina vijiji vingi sana ambavyo havijapatiwa umeme. Je, ni lini mikoa hii itapewa kipaumbele maalum ili vijiji vingi viweze kupata umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kabisa Mikoa ya Mtwara na Lindi maeneo mengi hayajafikiwa na miundombinu ya umeme. Nimhakikishie Mheshimiwa Bwanausi na namshukuru sana, alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini hapo nyuma, tumeshirikiana sana na amefanya kazi kubwa kwenye jimbo lake, naomba nimpongeze kwa hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tumeipa kipaumbele kikubwa sana mikoa hii miwili. Tarehe 15 hadi tarehe 18 tutakuwa tunafanya kazi ya kuzindua na kuelekeza Wataalam wetu wa TANESCO kupeleka umeme katika mikoa hii miwili, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; tunarekebisha miundombinu ya Mtwara. Hivi sasa tunajenga transmission line ya kutoka Mtwara umbali wa kilometa 80 na umeme wa KVA 132, ili umeme huo upelekwe Mtwara Mkoa mzima na maeneo mengine ya Lindi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Bwanausi Serikali imetumia hatua kubwa sana na imegharimu shilingi bilioni mia nane sabini na nane kufanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Bwanausi, lakini nampa uhakika kwamba, Serikali inaipa vipaumbele sana Mikoa ya Lindi na Mtwara na mwaka 2020 na 2021 vijiji vyote vya Mtwara na Lindi vitakuwa vimepata umeme.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwamba, kwa kuwa kule katika halmashauri ukiwaeleza jambo hili na wao wanatupia mpira kwenye Wizara, wakati Wananchi wa Maswa wanaendelea kupata tabu ya maji na katika Mradi wa Ziwa Viktoria wako phase two, ina maana watachelewa sana kupata maji. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari basi, angalau tushirikiane na ili tuweze kuchagua yale mabwawa muhimu zaidi kwa kutoa huduma kwa wananchi tuanze nayo hata kama ni machache? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe kwanza mfano; Mheshimiwa Bilakwate Halmashauri yake ya Karagwe tayari imeleta mapendekezo ya mabwawa sita na mabwawa hayo tunayafanyia kazi na tunazungumza kati ya halmashauri yake na Wizara ya Maji na Umwagiliaji ili tuweze kuona tunafanya nini kwa kushirikiana kwa sababu Serikali ni hiyo hiyo moja ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Nyongo, Halmashauri yake waanze kufanya kazi kwanza kidogo kule kwao, halafu wawasiliane na sisi tutaona suala la kufanya. Kwa bahati nzuri nimeshatembelea kwenye halmashauri yake na tukaona baadhi ya mabwawa. Basi halmashauri ianze kufanya kazi, Wizara haiwezi kuruka moja kwa moja kuja huko bila yeye mwenyewe. Mapendekezo haya aliyoyazungumza nafikiri wameyasikia, kwa hiyo, wayafanyie kazi, wawasiliane na sisi ili tuweze kufanya kazi.
MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima (Uganda) kuja Bandari ya Tanga nchini Tanzania ulitarajiwa kuanza mwezi Juni, 2017. Kwa kuwa pia majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ni kwamba Serikali itakuwa tayari kuwaandaa vijana wetu kupitia mitaala ya oil and gas kwenye Vyuo vya VETA mnamo mwaka 2018. Je, Serikali kwa kufanya hivi haioni ni sawa kabisa na kuweka rehani ajira ya kijana wa Kitanzania hususan vijana wanaotoka katika Mkoa wa Tanga?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mchakato wa uchimbaji, uchanjuaji na uchakataji wa zao la oil and gas Mikoani Lindi na Mtwara ulitarajia kuanza mwaka 2013, lakini hakuanza kutokana na sababu za ndani ya Serikali na kubwa ikiwa ni ukamilishwaji wa local content policy pamoja na msamaha wa kodi. Nini kauli ya Serikali kwa vijana wahitimu kwa nchi ya Tanzania hasa ukiangalia kwamba vijana wengi wanahangaika kutafuta kazi pasipokuwa na imani yoyote? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Mmasi, tumekuwa na yeye tangu mwaka 2013 katika jitihada za kufungua mafunzo kwa VETA kwa wanafunzi wa oil and gas. Kwa hiyo hongera sana Mheshimiwa Mmasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na maswali yake haya mawili, la kwanza, Serikali haioni kwamba ni muhimu sasa kuwapatia mafunzo hasa wanafunzi wa VETA kwa oil and gas. Ni kweli kabisa upo umuhimu na mwaka 2012/2013 kama nilivyosema, tulianza kutoa mafunzo hayo kwa ajili ya kuwafundisha vijana wetu wa VETA Lindi na Mtwara kwa ajili ya uchomeleaji, ufundi sanifu pamoja na theories za kawaida za utafiti wa kuchimba na kutafiti mafuta na gesi hapa nchini. Kwa hiyo, tunaona umuhimu Mheshimiwa Mmasi na tumeshafika hatua nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, matarajio ya mpango wa Serikali, kweli kabisa mwaka 2018 tunatarajia taratibu zote za taaluma ili kuingiza sasa mtaala katika Vyuo vya VETA kwa upande wa mafuta na gesi itafika sasa muda muafaka hasa kwa VETA ambavyo ni vyuo vipya ukiondoa vile vyuo ambavyo vimeshaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyowasiliana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, tumefika hatua nzuri, Serikali ya Norway pamoja na Serikali yetu itatenga shilingi milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha hatua hii. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mmasi, tutakapofika katika hatua hiyo tutashirikiana pamoja tuone namna ya kuwapatia vijana wetu mafunzo haya ambayo ni muhimu sana kwa ustawi wa nchi yetu.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa bomba hili la mafuta ghafi linaishia Bandari ya Tanga, je, Serikali imejipangaje kuona kuwa vijana wa Kitanzania hasa vijana wa Mkoa wa Tanga wanapata ajira hii katika soko la Kitanzania kupitia fursa hii ya uwekezaji?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimhakikishie Mheshimiwa Shekilindi, hili bomba la mafuta kutoka Hoima (Uganda) kuja Tanga (Tanzania) lina urefu mpana sana, lina jumla ya kilometa 1,443, lakini sehemu kubwa ya bomba hilo ambayo ni urefu wa kilometa 1,047 ni za hapa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, bomba hilo litapita karibu mikoa sita ya Kagera, Geita, Shinyanga, Dodoma hadi Tanga, kwa hiyo ni manufaa makubwa sana. Hivyo basi, ipo fursa kubwa sana kwa bomba hili kutoa ajira kubwa kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Shekilindi na wananchi wa Tanga kwamba ajira na fursa nyingi sana za kazi zitapatikana. Sambamba na hayo, tunawasiliana kwa karibu sana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ili kutoa fursa nzuri sasa kwa Watanzania kuwekeza kwa kutumia fursa hiyo ya bomba la Hoima hadi Bandari ya Tanga.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa ajira hizi zimekuwa zikitajwa kwa ujumla wake, je, ni lini Serikali itatengeneza mchanganuo ili kupata uwakilishi mzuri kwa pande zote mbili za Muungano?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ni lini, kinachofanyika sasa tupo katika hatua ya pili, hatua ya kwanza tumekamilisha utambuzi wa eneo ambapo bomba litapita. Hatua ya pili, tunakamilisha mazungumzo ili kuainisha maeneo na fursa muhimu kwa nchi zetu mbili lakini pia kwa nafasi za Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kwa masuala ya mafuta. Kwa sababu suala la ajira siyo la Muungano lakini fursa ziko palepale, utaratibu utakamilika baada ya majadiliano ndani ya mwaka huu lakini hatua ya pili itakuwa kuainisha fursa. Kwa hiyo, tutakapofikia hatua hiyo Mheshimiwa Mbunge tutawasiliana ili tuone namna ya kukamilisha na kuzinufaisha pande zote za Muungano.
MHE. PROF. NORMAN A. S. KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Naibu Waziri yanayoleta matumaini. Hata hivyo, nina maswali madogo ya nyongeza. Kwa kuwa mradi huu ulitegemewa kuzalisha umeme na wananchi wote wa Tanzania kunufaika, ni lini sasa Serikali itapeleka umeme kwenye vijiji 76 ambavyo havina umeme Wilaya ya Makete? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini Serikali itakamilisha upelekaji wa umeme kwenye vitongoji ambavyo havikupata umeme Awamu ya Kwanza ya REA? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Profesa anavyotupa ushirikiano katika jimbo lake na awali ya yote nimhakikishie vijiji vyake 76 vitapata umeme kwenye Awamu ya Tatu ya REA inayoanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa vijiji vilivyobaki vitapelekewa umeme, katika majibu yetu ya kila siku tumekuwa tukisema Mradi wa REA Awamu ya Tatu umeanza tangu mwezi Machi, 2017 na vijiji vyote vilivyosalia pamoja na vya Mheshimiwa Profesa King vya Makete pamoja na maeneo mengine vitapelekewa umeme kati ya mwaka huu wa 2017 hadi 2020. Kwa hiyo, Mheshimiwa Profesa, vijiji vyake vyote vitapata umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua sana Kata za Mang’oto, Lupende, Kambata na Mabacha pamoja na maeneo mengine ambayo anayataja yatapatiwa umeme katika awamu hii. Vilevile vitongoji na taasisi zake za umma vitapatiwa umeme na mradi huo ni mmoja umeshaanza, tumezindua kwa Mkoa wa Iringa na Njombe kwa Mheshimiwa Mbunge wa Kilolo na kwake wameshaanza, naambiwa wiki ijayo watafika kwa Mheshimiwa Profesa.
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitauliza maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya Mheshimiwa Susane Maselle, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, kutokana na majibu ya Naibu Waziri kuwa wachimbaji hawa wadogo walipata leseni, je, Serikali inatoa kauli gani juu ya Jeshi la Polisi lililotumia nguvu kupiga mabomu wachimbaji hao wadogo na kuwanyanyasa wenyewe na familia zao na kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia wanawake na watoto? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, je, Naibu Waziri yupo tayari kuongozana na Mheshimiwa Susane Maselle kwenda eneo hilo kuongea na wananchi hao kuhusu vitendo walivyofanyiwa na Jeshi la Polisi kuwa hawakufanyiwa kiusahihi kwa sababu walikuwa na leseni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na swali la pili, niko tayari kufuatana na Mheshimiwa Susane na kwa ridhaa yako kama itapendeza basi nitafuatana naye, nitembelee maeneo yale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na wachimbaji hao kupigwa mabomu pamoja na kufanyiwa harassment ni suala ambalo linatakiwa litazamwe kwa kina sana unaweza usiwe na jibu la moja kwa moja. Ninachoweza kusema ni kwamba pale inapotokea kunakuwa na vurugu katika maeneo ya uchimbaji kazi ya Jeshi la Polisi ni kutuliza ghasia ili kuhakikisha kwamba kunakuwa na amani na utulivu katika maeneo yale. Inawezekana ilifanyika katika hatua hiyo, lakini Mheshimiwa Mbunge tutakaa pamoja tuone ni hatua gani zilichukuliwa ili tushirikiane na wenzetu wa Mambo ya Ndani tuone nini cha kufanya zaidi.
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nataka niulize swali la nyongeza. Kwa wachimbaji wadogowadogo waliopo katika Mkoa wa Katavi hususan katika Machimbo ya Ibindi na Kapanda, vijana hawa wamekuwa na changamoto kubwa nyingi mno ikiwepo gharama kubwa ya kukata leseni za uchimbaji lakini pia gharama kubwa ya dawa za kusafishia dhahabu wanazopata na gharama za umeme pia ziko juu. Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha sasa inawasaidia hawa vijana kupunguziwa gharama hizi ambazo ni kero? Tamko la Serikali linasema nini ili kuwasaidia vijana kupata mikopo ili wajiendeleze kiuchumi na kupata kipato?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, ni kweli kabisa maeneo ya uchimbaji maarufu sana kwa maeneo ya Mpanda ni pamoja na Ibindi, Kapanda pamoja na Dilifu. Hata hivyo, nimtaarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba hatua ambazo Serikali imechukua, la kwanza kabisa ni kurasimisha maeneo hayo ambayo nimeyataja kuwa maeneo maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo na wapo wachimbaji wadogo wazuri sana kwenye eneo lako ikiwa ni pamoja na Mheshimiwa Kapufi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusu mkakati ambao tunafanya…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Niseme tu, tumetoa ruzuku mwaka juzi kwa wachimbaji wa Ibindi na Kapanda na bado tunawapatia elimu na uwezeshaji kwa ajili ya uchimbaji mzuri kwa wachimbaji hawa wadogo.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami naomba kumuuliza Naibu Waziri swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa kuna migodi ambayo inakuwa imeshafungwa na inakuwa si salama kwa wachimbaji wadogowadogo na hawa wachimbaji wadogowadogo wamekuwa wakikiuka sheria na kuvamia migodi hii na kuhatarisha maisha yao. Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha uvamizi huu wa wachimbaji wadogowadogo unakwisha na kuchukulia hatua za kisheria?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya 2010, hairuhusiwi kufanya uchimbaji wowote bila leseni na kwa hiyo uvamizi kwa hali ya kawaida hauruhusiwi. Hata hivyo, yapo mazingira ambapo wananchi wamekuwa wakivamia maeneo na hasa ambao wao wameanza kuchimba mapema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu na mkakati wa Serikali, kwanza ni kufanya mazungumzo na hao wachimbaji wadogo kuwaelewesha lakini hata wale wenye leseni ambao wameyashikilia bila kuyaendeleza nao kuzungumza nao. Tunachofanya sasa, maeneo ambayo yanachukuliwa na watafiti bila kuyaendeleza Serikali inayachukua na kuwagawia wachimbaji maalum wadogo kwa utaratibu wa kisheria ili kufanya uchimbaji huu uwe wa manufaa kwa wachimbaji wadogo pamoja na wachimbaji wakubwa.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali.
Kwa kuwa ukiangalia shule nyingi zilizoungua, chanzo kikuu huwa ni vibatari au mshumaa, hii ni kwa sababu ya kukosekana kwa umeme; kwa kuwa Serikali imeshatoa maelekezo kwamba kila sehemu yenye taasisi kama shule na sehemu nyingine muhimu umeme upite, lakini mpaka leo baadhi ya sehemu wamekosa haki hiyo ya kupelekewa umeme. Je, Serikali inasemaje?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tu kwamba shule zote katika Halmashauri zote kwa nchi nzima tumeshaanza sasa kuchukua stock taking kuona shule za msingi na sekondari ambazo zimekamilika ili zipelekewe umeme kupitia mradi wa REA ambao umeshaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge na nimhakikishie kwamba Halmashauri zote kwa kutumia nafasi hii, Wakurugenzi wote ambao hawajafanya hivyo niwaagize wafanye hivyo ili mradi utakapofika waweze kupitishiwa umeme haraka sana.
MHE. ABDALLAH H. ULEGA: Mheshimiwa Spika, asante sana, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jibu lake lenye kuleta matumaini ya kwamba siku moja na sisi watu wa Mkoa wa Pwani tunaweza tukapata madini ya dhahabu, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza ninependa kujua ni lini sasa Wizara itaanza kukitumia kisima cha gesi kilichopo katika eneo la kijiji cha Kiparang’anda ndani ya Wilaya ya Mkuranga ili kiweze kupata na kutuletea faida watu wa Mkuranga na Taifa letu kwa ujumla?
Swali la pili, ningeomba Naibu Waziri wa Nishati na Madini anieleze Wilaya ya Mkuranga tunachimba madini ya aina ya mchanga, madini ambayo kwa sasa Mkoa wa Dar es Salaam hayachimbwi yanachimbwa tu Mkuranga. Je, Wizara iko tayari kushirikiana na sisi watu wa Mkuranga kuboresha ushuru na tozo mbalimbali ili madini haya yaweze kuleta tija kwa watu wa Mkuranga?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Ulega, tumeshirikiana na wewe sana katika suala la mchanga na wananchi wa Jimbo lako najua wananufaika sana, kwa hiyo, hongera kwa hilo Mheshimiwa Ulega.
Mheshimiwa Spika, labda nianze na lini kwamba gesi asilia itaanza kutumika maeneo ya Kiparang’anda. Shughuli zinazofanyika sasa katika eneo la Kiparang’anda ni ukamilishaji wa utafiti wa madini ya gesi asilia na Kampuni ya Moran and Promi inakamilisha sasa, Mheshimiwa Ulega madini haya ya gesi asilia yataanza kutumika kwenye eneo lako baada ya utafiti kukamilika mwezi Agosti, 2018 na wananchi wa Mkuranga wana matumaini makubwa, kwa hiyo jitihada zinafanyika ili kuhakikisha kwamba gesi asilia inakamilika na mwakani yataanza kutumika maeneo ya Kiparang’anda na maeneo mengine ya Dar es Salaam pamoja na Pwani kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na madini ya mchanga, Mheshimiwa Ulega nikupongeze sana, eneo la Pwani kwa ujumla wake jumla ya hekta kama 182 zinatumika sana kwenye uchimbaji wa madini ya mchanga pamoja na kokoto. Kinachotakiwa wakandarasi wote na nitumie nafasi hii kuwataka wakandarasi wote kwa niaba yako Mheshimiwa mwenye Jimbo la Mkuranga waanze sasa kulipa tozo za Serikali za Mitaa kwa mujibu wa sheria ambayo ni 0.3%. Lakini pia waanze sasa kushiriki katika shughuli za maendeleo kwa sababu ni takwa la kisheria, lakini nitumie nafasi hii kuwaagiza Wakurugenzi wote nchi nzima sasa waanze kuyataka makampuni yanayochimba mchanga, kokoto kuanza sasa kutoa ushuru katika Serikali za Mitaa ili wananchi wa Mkuranga na Tanzania nzima wanufaike kwa ujumla wake.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo yanatupa matumaini wananchi wa Kigamboni hususani kwa changamoto ambayo inatukabili. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, katika mwaka
wa fedha 2017/2018 Wilaya ya Kigamboni haikupata miradi mipya na hii inatokana na kwamba miradi ya mwaka jana (2016/2017) haikutekelezwa kikamilifu. Changamoto moja ilikuwa ni hali ya upatikanaji wa vifaa kwa maana ya transfoma, nguzo ndogo pamoja nyaya. Je, Naibu Waziri anaweza akatuhakikishia kwamba katika mwaka huu wa fedha transfoma zaidi ya 30, nyaya kilometa zaidi ya 30 na nguzo takribani 1,000 ambazo tunazihitaji tunaweza tukazipata ili kutekeleza miradi hii?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Kigamboni iliingizwa katika REA Awamu ya Pili na kuna vijiji ambavyo vilirukwa. Je, utekelezaji wa REA Awamu ya Tatu kwa maeneo ambayo yalibaki unaanza lini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda nichukue nafasi hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge wa Kigamboni jinsi anavyofuatilia maendeleo ya wananchi wa Kigamboni.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kuhusiana na suala la vifaa, kwanza kabisa tukiri kwamba kulikuwa na shida ya upatikanaji wa nguzo, transfoma pamoja miundombinu ya TANESCO, lakini kuanzia mwezi Juni kwa niaba ya wananchi wa Kigamboni na Watanzania wengine wote, sasa nguzo zinapatikana hapa nchini na zinatosha kupeleka miundombinu katika maeneo yote. Nitoe tu tamko kwamba katika nchi nzima tulikuwa na wateja 29,000 ambao hawajaunganishiwa umeme wakati wameshalipia kuunganishiwa umeme, lakini wananchi hao wamepelekewa umeme bado wananchi 32 tu. Kigamboni eneo ambalo ni muhimu sana hadi sasa tumepeleka nguzo 2,100 na wateja waliobaki ni 30. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wananchi wako wa Kigamboni Mheshimiwa Ndugulile kule Mwanzo Mgumu tumeshawapelekea nguzo, Msongozi kwa Mpika Chai na Cheka tumeshapeleka nguzo. Kwa hiyo, wananchi wataendelea kuunganishiwa umeme kama kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na miradi mingine ya Jimbo la Kigamboni, ni kweli kabisa tulipeleka miradi ya REA katika vijiji viwili Kigamboni kwa sababu Kigamboni kimsingi ni mitaa kwa sababu ipo Jijini Dar es Salaam, lakini tulipeleka mradi wa REA Kisarawe II kwenye eneo la Cheka pamoja na Kimbiji. Tuna mradi mwingine ambao upo chini ya TANESCO na umeshaanza ambao utapeleka umeme kwenye vijiji vya Mheshimiwa Ndugulile. Vijiji ambavyo vitapelekewa umeme ni pamoja ni Changanyikeni, Gezaulole pamoja na maeneo yote ya Dege.
Sambamba na hilo, tumepeleka mradi mwingine, kule Kigamboni kulikuwa na transfoma moja yenye uwezo wa MW 5 tu, sasa tumeing’oa tumeweka yenye MW 100 ambayo itapeleka umeme kwenye vijiji vyote vya Kigamboni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimpe tu faraja mhesimiwa Mbunge wa Kigamboni kwamba matatizo ya umeme Kigamboni sasa yanaelekea kuisha. Utekelezaji wa REA umeshaanza tangu Juni, 2017 na utakamilika Machi, 2019.(Makofi)
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba na mimi nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, umeme wa REA unatarajiwa kuwa
ni tegemeo kubwa sana kwa wananchi, lakini pia kuinua uchumi kwa ajili ya viwanda vidogo vidogo, lakini Kaliua umeme wa REA umekuwa unakatika mara kwa mara, Mheshimiwa Waziri nimeshakuja kwako mara nyingi tu kuhusiana na suala hili. Kwa siku zaidi ya masaa nane, masaa manne unawaka, masaa nane hauwaki, kwa hiyo lile tegemeo halipo tena kwa wananchi wale. Mheshimiwa Waziri aliahidi kujenga substation pale Kaliua alivyotembelea mwaka 2015.
Naomba kujua sasa Serikali ina mpango mkakati gani kuhakikisha kwamba inajenga substation pale Kaliua ili umeme wa REA uweze kuwa na tija na kuinua uchumi wa wanachi wa Kaliua? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa, Mheshimiwa Sakaya nilipokuja kwako nilitembea na wewe sana na naomba niendelee kutembea na wewe nikija tena. Lakini pia … (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ni kweli alivyosema Mheshimiwa Mbunge, umeme unaosafiri kwenda Kaliua ni ule unaotoka Tabora - Urambo, - Kaliua hadi Uvinza, kwa hiyo, ni umbali mrefu sana. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Mbunge anavyosema, transfoma ya kusafirisha umeme iliyopo Tabora ndiyo inayohusika kusafirisha umeme katika Majimbo ya Kaliua, Urambo mpaka Uvinza, umbali wa kilometa 372. Mkakati madhubuti wa kumaliza tatizo hili la kukatika kwa umeme ni kuwa Serikali sasa inajenga substation katikati ya Kaliua pamoja na Urambo katika eneo la Gologolo.
Kwa hiyo, utaratibu umeanza na wakati utekelezaji
wa REA utakapoanza basi wananchi watapata umeme huo lakini katika jibu langu litakalofuata kwa swali la msingi nitaeleza kwa upana zaidi lakini nimpe uhakika Mheshimiwa Mbunge utaratibu fedha zimeshatengwa na survey imekamilika na ujenzi utaanza hivi karibuni.
MHE. DESTERY B. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na hasa niendelee kuanidka Kiswaga. Kwa kuwa swali langu linafanana kabisa na suala hili la Kigamboni, Wilaya ya Magu ambayo ni Jimbo lina vijiji 82, ni vijiji 29 tu vina umeme. Je, vijiji 53 ni lini vitapatiwa umeme ambavyo hata Mheshimiwa Dkt. Kalemani anavifahamu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimsahihishe kidogo Mheshimiwa Kiswaga, vijiji ambavyo havijapata umeme katika Jimbo la Magu siyo 53 vipo 56. Kwa hiyo, Mheshimiwa Kiswaga tutakupelekea umeme.
Mheshimiwa Spika, niseme tu utekelezaji wa REA Awamu ya Tatu umeshaanza na katika Wilaya yake, maeneo yote yameshafanyiwa survey na Mheshimiwa Mbunge tumeenda naye na tumetembelea maeneo hayo na nimhakikishie vile Vijiji vya Mahala, Igombe, Shishani, Nyasato, Kayera mpaka Mahala vitapatiwa umeme na utekelezaji huo umeshaanza. Nikupe tu uhakika kwamba survey itakamilika tarehe 10 mwezi huu na wakandarasi wataanza kazi rasmi. Kama nilivyosema tuliboresha kwa sababu vile vijiji vyako vitatu vimepelekewa nguzo moja moja kwa hiyo sisi tunahesabu kama vijiji vyote havijapata umeme, kwa hiyo, ni 56 katika Jimbo la Magu.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, awali ya yote nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jibu zuri pamoja na Serikali kwa ujumla kwa kukubali ombi letu la wananchi wa Urambo la kujenga kituo cha kupoza umeme (substation) Wilayani kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la nyongeza linasema, je, Serikali inaweza kuwahakikishia wananchi wa Urambo kwamba katika Awamu ya Tatu ya REA vijiji vyote vya Wilaya ya Urambo vitapata umeme? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kumpngeza Mheshimiwa Margaret Sitta kwa juhudi kubwa anazofanya kufuatilia maendeleo ya wananchi wa Urambo, hongera sana Mheshimiwa Sitta. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini niseme tu kwamba ni kweli
vijiji vyote 27 vilivyobaki katika Jimbo la Urambo vitapata umeme ikiwemo Yerayera, Igembesabo, Ifuta na vijiji vingine. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri atakumbuka kwamba walipokwenda kuzindua REA III kwa Mkoa wa Iringa, walifanya assumption kwamba ndiyo wamezindua na Mkoa wa Njombe, lakini hii mikoa ni mikoa miwili tofauti, inawezekana TANESCO mnaona kama ni Mkoa mmoja lakini hii ni Mikoa miwili tofauti. Je, ni lini mtakwenda kuzindua REA III kwa Mkoa wa Njombe specific kwa Mkoa wa Njombe badala ya kuunganisha Mkoa wa Njombe na Mkoa wa Iringa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; vipaumbele vya kusambaza umeme wa REA III katika maeneo mengi, katika vijiji vimefanyiwa ofisini na Watendaji wa TANESCO bila kushirikisha viongozi kwenye maeneo husika na hasa kwa Mkoa wa Lindi hasa katika Jimbo la Mtama. Yapo maeneo mengi ukiangalia vijiji vilivyowekwa, vipaumbele vyake nadhani vimezingatiwa zaidi ofisini bila kujali hali halisi ya mazingira. Je, ni lini hawa Watendaji wa TANESCO pamoja na Wakandarasi watakaa na viongozi kwenye maeneo husika ili wakubaliane vipaumbele wapi tuanzie na wapi tuishie wakati wa awamu mbalimbali zinazoendelea za kusambaza umeme kwenye maeneo yetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda sana kumpongeza Mheshimiwa Nape kwa jinsi ambavyo anatupa ushirikiano katika Jimbo lake la Mtama.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala la uzinduzi, tumefanya uzinduzi ambao kwa kweli katika miaka ya nyuma tulikuwa hatufanyi na mantiki kubwa ilikuwa ni kuwatambulisha Wakandarasi pia kuwajulisha viongozi pamoja na Waheshimiwa Wabunge ili waweze kushiriki ipasavyo kwenye zoezi zima. Kwa hiyo, nataka tu kusema kwamba, katika Jimbo la Mtama hata katika Mkoa wa Njombe, katika Mkoa wa Njombe kimsingi tulifanya uzinduzi Kesamgagao lakini kama ikibidi tutarudi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kazi yetu ni kuwafikishia umeme wananchi wa Njombe. Kwa hiyo, niseme tu kwamba wala halina shida, tutapanga siku na tutarejea ingawa Mkandarasi ameshafika site. Kwa hiyo, niwape faraja wananchi wa Njombe, tutaendelea kulifanyika kazi, watatualika tutakwenda pia kuwazindulia rasmi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na vipaumbele niseme tu, kazi ambayo Mkandarasi anatakiwa kuifanya na hili nitoe kama tangazo kwa Wakandarasi pamoja na TANESCO wanaowasimamia, utaratibu wa kwanza kwa Mkandarasi yeyote kabla hajaanza kazi anatakiwa kwanza awashirikishe Waheshimiwa Wabunge wa Majimbo husika na Viongozi wa maeneo hayo na kutofanya hivyo tutachukua hatua kali sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafanya hivyo kwa sababu tunataka kuepuka vijiji muhimu kurukwa, maeneo ya vipaumbele kurukwa, pamoja na taasisi za umma. Kwa hiyo, nitoe angalizo, nakushukuru Mheshimiwa Nape lakini nachukua nafasi hii kuwatangazia rasmi kuwatangazia rasmi Wakandarasi pamoja na TANESCO kuhakikisha wanawashirikisha Waheshimiwa Wabunge, Madiwani na Viongozi wa maeneo husika ili kuhakikisha kwamba hakuna maeneo, vijiji wala taasisi za umma zitakazorukwa. Hilo ni angalizo nashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Nape wakati wa uzinduzi wa Lindi ni kweli hakuwepo lakini vijiji vyako vya Rondo Mheshimiwa vitapata umeme, Nyangamara watapata umeme, Chiwerewere watapata umeme, kwa hiyo bado Mheshimiwa Nape wananchi wake wa Mtama awape uhakika huo.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwanza naomba niseme tu kwamba nashukuru kwa ushirikiano ambao naupata kutoka pale TANESCO, Gongolamboto, Kisarawe na Mheshimiwa Naibu Waziri nikimpigia simu anapokea, siyo kama wengine walivyosema hapa.
Mheshimiwa Spika, pia naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Jimbo la Ukonga lina shida kubwa ya umeme, lakini pia kuna shida nyingine zimeongezeka, Ukonga kuna wajasiriamali wadogo wenye viwanda vidogo vya kusaga unga wa sembe na dona, lakini pia na chakula cha kuku; umeme unakatika sana katika eneo hilo. Kwa hiyo, naomba kama kuna utaratibu wa dharura, ufanyike ili kuzuia hiyo kero kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, eneo la Kitonga Sekondari, Mvuti Sekondari, Mbondole Sekondari, Bombambili Shule ya Msingi na Shule ya Msingi Nzasa II kuna visima vya maji havifanyi kazi kwa sababu kuna shida kubwa ya umeme katika eneo hilo.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza akawa na mkakati mahususi wa kuondoa kero katika maeneo haya ambayo ni maeneo muhimu kwa walimu, wanafunzi na jamii inayozunguka eneo hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa na mimi namshukuru Mheshimiwa Mbunge anavyofuatilia masuala ya wananchi wake wa Ukonga. Niseme tu, katika swali la kwanza kuhusu kukatika kwa umeme; katika maeneo ya Kisarawe hivi sasa tulikuwa tunajenga miundombinu ya kusafirisha umeme kutoka Gongolamboto na Kipawa ili wananchi wengi wafikiwe na umeme unaojitosheleza. Ujenzi wa utaratibu huo unaendelea na unakamilika mwezi wa Oktoba tarehe 22.
Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Waitara kwamba mara baada ya kukamilika, tatizo la kukatika kwa umeme kwa maeneo ya Kisarawe, Gongolamboto, Mvuti pamoja na Chanika yatakwisha mara moja.
Mheshimiwa Spika, katika Jimbo la Ukonga yapo maeneo ambayo yanapata umeme kutoka eneo la Kisarawe na kwa maana hiyo yanahesabika kama yapo vijijini. Maeneo hayo ni pamoja na kama ambayo ametaja Mheshimiwa Waitara, ni Kitonga lakini yapo maeneo ya Namanga, Bombambili pamoja na Uwanja wa Nyani, yote hayo yanapata umeme kutoka Kisarawe. Kwa maana hiyo, visima vilivyopo katika maeneo hayo, yataunganishwa sasa na umeme wa Mradi wa REA ambao unakuja sasa ili wananchi waweze kupata maji kwa urahisi.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwa niaba ya wananchi wote kwamba Mradi wa REA Awamu ya Tatu, pamoja na kupeleka umeme kwenye vitongoji na vijiji, utaunganisha pia miundombinu ya maji kote nchini.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waitara maeneo ya Kitonga, Uwanja wa Nyani, Msongole, Mvuti na Vijiji vingine ambavyo vina visima vitaunganishwa na mradi huu wa REA.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kutokana na ripoti ya CAG mpaka sasa hivi inaonekana ni 6% tu ya gesi inatumika, inayosafirishwa na hilo bomba na uwekezaji huu ni wa pesa nyingi. Nataka kujua Serikali imejipanga vipi kuhakikisha uwekezaji huu unaleta tija kwa Taifa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa kuna utata mkubwa katika uwekezaji huu kujua gharama halisi: Je, Serikali ipo tayari kumtaka CAG afanye special audit katika uwekezaji huu? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza bomba la kusafirisha mafuta au gesi kwa sasa kutoka Madimba (Mtwara) hadi Dar es Salaam ndiyo bomba kubwa tulilonalo kwa upande wa gesi.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa sasa hivi gesi inayosafirishwa ni kati ya 6% hadi 10% ya uwezo wake na uwezo nimetaja ni milioni cubic feet 744. Sasa ni kwa nini? Bomba hilo lina upana wa inchi 36, ni kubwa; na mahitaji ya sasa ni megawati 668 tulizonazo kwa upande wa gesi, lakini miundombinu inayojengwa ndiyo mikakati sasa.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa tunajenga miradi miwili ya kusafirisha gesi Kinyerezi I na Kinyerezi II. Kinyerezi I tunafanya extension ya kuongeza megawati 185 ili katika Kinyerezi I pekee zifikie 335.
Mheshimiwa Spika, kadhalika tunajenga mradi mwingine katika Kinyerezi II ambao utaweza kutoa megawati 240. Sasa miradi hii miwili ikikamilika, mahitaji makubwa ya gesi yataongezeka. Kwa hiyo, itazidi 6% hadi 10% na tuna matarajio inaweza kufikia asilimia 20 hadi 30.
Mheshimiwa Spika, miundombinu inayojengwa kuhitaji gesi, bado ni mingi; tunahitaji umeme wa kutosha. Kwa sasa hivi umeme hautoshi. Ni matarajio yetu kwamba mara baada ya miradi mingine, tutakwenda Kinyerezi III utakaoanza mwaka 2018 utakaohitaji megawati 600. Kwa hiyo, mahitaji ya gesi bado yatakuwa ni makubwa.

Mheshimiwa Spika, lingine niseme mkakati mwingine, unapokuwa na gesi ya kutosha inakuruhusu kujenga miundombinu mingine kwa sababu una stock. Kwa hiyo, siyo hasara kuwa na gesi nyingi lakini kadhalika mikakati ya Serikali ni kuhakikisha kwamba hii gesi tunasafirisha kadri iwezekanavyo ili ichangie sana katika upatikanaji wa umeme. Mkakati wa Serikali ni kutumia gesi zaidi ili kuachana na mafuta ili kuwapunguzia mzigo wananchi, hilo ni katika ufafanuzi wa swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la ukaguzi, mahesabu ya Serikali hukaguliwa mara kwa mara, ni utaratibu wa kawaida. Kama ambavyo kila mwaka CAG hukagua, hata miradi hii ataendelea kuikagua.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme tu, suala la ukaguzi wa miradi ni endelevu, CAG ataendelea kukagua ili hali halisi iendelee kufahamika.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini kuna suala moja hajatoa ufafanuzi wa kina.
Mheshimiwa Spika, mwekezaji analalamika kwamba 6% za uzalishaji na gesi inayochukuliwa haitamfanya aweze kurejesha gharama za uwekezaji kwa kipindi cha miaka 25 kadri walivyokubaliana na Serikali; na Mheshimiwa hapa anasema kwamba kadri siku zinavyokwenda basi gesi nyingine itahitajika.
Mheshimiwa Spika, nataka kufahamu, ni lini Serikali itamhakikishia mwekezaji kwamba bomba hili litatumika kwa asilimia 100 ili aweze kurejesha gharama zake ndani ya miaka 25, ikizingatiwa kwamba sasa hivi yupo kwenye mwaka wa 11? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa niseme mradi ule ni wa Serikali kwa asilimia 100, hilo ni la kwanza kabisa. Kwa hiyo, unamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100. Hata hivyo, kama nilivyosema, mwaka gani tutaweza kupata gesi asilimia 100 inayozalishwa pale? Ni mradi ambao ni endelevu. Iko miradi mingine inajengwa Mtwara ambayo inaanza mwezi Machi mwakani ambayo tutaanza kuzalisha megawati 500 kwa Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba bado kuna muda wa kutosha, ifikapo mwaka 2020/2022 tuna matarajio kwamba gesi inayozalishwa katika Madimba tutaweza kuitumia kwenye miradi yetu ya umeme.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwa sababu miradi ni mingi, ifikapo mwaka 2022 matarajio kati ya asilimia 80 hadi 100 tutaanza kutumia gesi yote asilia.
MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yenye kutia moyo, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza; nilijulishwa na uongozi wa REA kwamba Vijiji vya Kongo na Kondo ambavyo havikutekelezewa miradi yake katika awamu ya pili vimeingizwa kwenye orodha ya miradi ya nyongeza kwenye REA-III ambayo imeombewa kibali kwa ajili ya utekelezaji. Sasa swali; je, lini kibali hicho kitaweza kutolewa ili miradi hiyo itekelezwe?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kufuatana na orodha ya miradi ya REA Awamu ya Tatu kwenye Jimbo la Bagamoyo, vijiji vingi katika Kata za Fukayosi, Makurunge, Mapinga, Kerege na Zinga havitopata umeme. Je, Serikali ina mkakati gani kuweza kuvipatia umeme vitongoji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Dkt. Kawambwa kwa juhudi zake anavyofuatilia mahitaji ya umeme kwa wananchi wa Bagamoyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyotaja, Vijiji vya Kondo, Kongo, Matimba pamoja na Fukayosi kimsingi vilishapata approval na viko kwenye REA awamu ya tatu hii inayoanza sasa hivi. Naomba nimhakikishie kwamba katika shule yake ya sekondari aliyojenga Fukayosi kwa wafadhili, tayari wiki ijayo wanafanya survey ili ianze kupelekewa umeme katika awamu hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vilivyobaki ambavyo amevitaja; Mapinga, Kerenge pamoja na maeneo ya Zinga ambavyo ni vijiji 22, navyo vitaanza kupelekewa umeme kuanzia mwezi Machi, 2019 na kufikia mwaka 2020 vyote vitakuwa vimeshapata umeme.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa matatizo yanayowakabili wananchi wa Bagamoyo yanafanana kabisa na ya Morogoro Kusini Mashariki. Kwenye mipango ya Serikali ya REA awamu ya tatu, Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki tumepata vijiji saba tu na kuacha vijiji 47 kati ya vijiji 64 ambavyo vyote havina umeme katika Kata za Tegetero, Kibuko, Tomondo, Maturi, Mkulazi na Seregeti. Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka umeme katika huu mradi wa REA awamu ya tatu, katika Kata hizo na vijiji vyake vyote?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge anavyosema. Kwanza nimpongeze, nilipokuja kuzindua Morogoro tulishirikiana na Mheshimiwa Omary na nilimwambia alete vijiji vyake tuviboreshe.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tumeshafanya mapitio siyo vijiji saba vinavyopelekewa umeme raundi ya kwanza bali ni vijiji 14. Hata hivyo, vile vijiji vingine 47 alivyotaja basi tutakaa tuvipitie, lakini vyote vitapatiwa umeme kwenye raundi inayofuata itakayoishia mwaka 2021.
MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Nabu Spika, nakushukuru na namshukuru Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa jitihada kubwa ya kusambaza umeme. Pamoja na hayo nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, toka mradi huu ulipoanza na wananchi kufanyiwa tathmini ni takribani miaka mitatu na wananchi hawa wameacha shughuli zao za maendeleo na hawana fedha kwa ajili ya kuanzisha shughuli nyingine ya maendeleo. Ni lini sasa Serikali itaanza kulipa fidia hii ili wananchi wajiandae kwa ajili ya kuwa na shughuli za maendeleo mbadala katika maeneo mengine?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; katika mradi wa umeme REA III, Vijiji vya Jimbo la Kibaha Mjini ikiwa ni pamoja na Mkombozi, Lumumba, Kalabaka, Saeni, Jonuga, Mbwawa, Miomboni, Madina, Mbwate, Visiga, Viziwaziwa, Mtakuja, Maili 35 na Kumba vimeondolewa katika utaratibu mzima wa REA III na katika kufuatilia kwangu hatujapata majibu ni utaratibu gani utatumika kuipatia Mitaa hii umeme kama ilivyokuwa imepangwa na wananchi wana mtafaruku mkubwa. Je, Serikali sasa ina mpango gani mbadala kuhakikisha mitaa hii yote inaendelea kupata umeme kama tunavyojua umeme ni uchumi na maendeleo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa Mheshimiwa Koka hongera sana katika kufuatilia masuala ya fidia. Mmefika hatua nzuri kwa sababu ya jitihada zako.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba katika maeneo yaliyofanyiwa tathmini kama nilivyoeleza kwenye swali langu na jibu langu la msingi kwamba taratibu zimeshakamilika na ni matarajio yetu mwisho wa Desemba na mwanzo wa Januari mwakani, malipo yatakuwa yameshaanza kutoka. Kwa hiyo, wananchi wa maeneo yale wategemee fidia katika kipindi hicho, lakini kama nilivyosema, taratibu za uhakiki zimeshakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili; nitumie nafasi hii kusema kwamba yako maeneo ambayo kwa kweli ni mitaa ingawa katika hali ya kawaida inaonekana kama vijiji. Maeneo haya ambayo yako mjini kwa sababu miradi ya REA inakwenda vijijini, uko mradi unaoitwa urban ratification ambao katika Wilaya ya Kibaha hasa Mjini na maeneo ya jirani yatapelekewa umeme kupitia mradi huu. Mheshimiwa Koka kwa bahati nzuri sana, katika maeneo ya Lumumba, Mtakuja na Viziwaziwa ziko transformer 11 zimetengwa kwa ajili yakupelekewa umeme katika maeneo hayo.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa watu wa Rufiji na sehemu nyingine ambapo gesi hiyo itapita ni watu ambao wanasubiria kwa hamu jambo hilo. Bado hawajapata elimu ya kutosha kujua umuhimu wa jambo hilo kwenye maeneo yao. Sasa Serikali itakuwa tayari kupita kutoa elimu ya kutosha, hasa mashuleni, ili wananchi kazi hiyo itakapoanza ya kupitisha gesi waone kwamba ile ni rasilimali yao?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa wananchi sasa walio wengi wanategemea gesi ikianza kutoka kwa wingi na tumepewa taarifa kwamba, kuna gesi ambayo inaweza ikatumika kwenye magari. Anatuambiaje Mheshimiwa tujue kwamba unafuu wa kutumia gesi ama petroli kutakuwa kuna tofauti kubwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mwamoto kwa kuuliza swali kwa niaba ya Mheshimiwa Mbunge wa Rufiji na Waheshimiwa Wabunge hawa wanafanya kazi nzuri sana kwenye majimbo yao. Ni matarajio yao kwamba wananchi wanawasikia vema.
Mheshimiwa Spika, elimu ambayo tumetoa mpaka sasa, nitoe tu taarifa kwa Mheshimiwa Mbunge wa Rufiji na Mheshimiwa Mwamoto, tumeshatoa elimu katika vijiji vya Mwaseni, vijiji vya Ngarambe, kijiji cha Korongo pamoja na Kotongo, lakini tunakwenda sasa kutoa mwezi wa 10 na wa 11 elimu katika maeneo ya Jaribu Magharibi na maeneo mbalimbali. Kwa hiyo, tutaendelea kutoa elimu kwa ajili ya manufaa ya miradi hii ili wananchi wa Rufiji nzima waweze kuipata kwa hiyo, tunaendelea na utaratibu wa elimu kama kawaida.
Mheshimiwa Spika, suala la pili kuhusiana na gesi kwenye magari, ni kweli kabisa ule mradi wa kutengeneza gesi kwa ajili ya matumizi ya kwenye magari na majumbani ulishaanza tangu mwaka 2016 na hivi sasa mwakani mradi huo utaendelea. Tulishaanza katika Vituo viwili vya DIT pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mpaka sasa magari 16 yameshaunganishwa kwa kutumia gesi badala ya petroli. Na unafuu wake ni kwamba, unapunguza asilimia 40 ya matumizi ya kawaida ya petroli unapotumia gesi.
Mheshimiwa Spika, mradi huu kwa niaba ya Watanzania wote, utaanza mwaka 2018 hadi 2020 kwa kwenda katika Mkoa wa Dar es Salaam, Mtwara pamoja na Lindi.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika,ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kuharibikaharibika kwa mara kwa mara kwa kinu cha gesi pale Kilwa na kutokana na uchakavu wa mitambo ile, hitajio la Wilaya za Kilwa, Lindi pamoja na Liwale, I mean Kilwa pamoja na Rufiji pamoja na Liwale kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa ni muhimu sana.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba Waziri atueleze hapa ni nini kinachelewesha wilaya hizi kuongizwa kwenye Gridi ya Taifa kwa sababu ya uchakavu wa mitambo ya Kilwa kunafanya umeme usiwe wa uhakika katika Wilaya hizi tatu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa maeneo ya Kilwa, Rufiji na maeneo ya Mkuranga hivi sasa hayapati umeme wa gridi na maeneo mengine ya karibu na pale, lakini hatua zinazofanyika sasa hivi tunajenga mradi wakusafirisha umeme kutoka Somangafungu ambao nimeutaja, lakini kutakuwa na Mradi wa Rufiji Stiegler’s Gorge ambao unaanza Disemba mwaka huu. Kwa hiyo, kinachochelewesha ni maandalizi ya ujenzi kabambe wa miradi mahususi ambayo itaunganisha wananchi wa maeneo yale na Gridi ya Taifa.
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Stiegler’s Gorge na huu niliosema ambao ni wa kusafirisha umeme wa kutoka Somangafungu kupita Kinyerezi mpaka Dar es Salaam ndio pia, utawapatia nguvu ya kutosha ya umeme na kuunganisha kwenye Gridi ya Taifa, maeneo yote ya Rufiji, Kilwa pamoja na Mkoa wa Mtwara pamoja na Lindi. Kwahiyo, wananchi wa mikoa hii miwili niwahakikishie kwamba, ifikapo mwaka 2019/2020 tayari watakuwa wameshaunganishwa na Grid ya Taifa.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimwia Naibu Waziri kwa majibu mazuri lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa kwa muda mrefu sana kuna baadhi ya sehemu kwa mfano ndani ya Jimbo la Busanda wana umeme, lakini katika Taasisi za Serikali na za Umma hazijaweza kufikiwa na umeme huo. Nikitoa mfano, Kituo cha Afya Bukoli, Kituo cha Afya Lwamgasa, Shule ya Sekondari ya Bukoli, Shule ya Sekondari Lwamgasa, Shule ya Sekondari Chigunga na kwenye Zahanati ya Chigunga umeme huu haujafika.
Je, Serikali inasemaje sasa kuhusu mpango wa kuhakikisha kwamba Taasisi zote za Umma pamoja na sehemu za kuabudia zinafikiwa na umeme wakati utekelezaji unapoendelea? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tumeona katika vyombo vya habari katika mikoa mbalimbali umeme ukizinduliwa ili Awamu ya Tatu ya REA iweze kuanza kufanya kazi lakini katika Mkoa wa Geita sijaona jambo hili likifanyika. (Makofi)
Je, ni lini sasa Serikali itazindua rasmi umeme wa REA Awamu ya Tatu katika Mkoa wa Geita ili wananchi waweza kuanza kuona utekelezaji wake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kumpa pole sana Mheshimiwa Bukwimba kwa wananchi wake wanne walioangukiwa na kifusi kwenye machimbo ya kule Nyamalimbe, pole sana Mheshimiwa Bukwimba kwa niaba ya wananchi wa Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyouliza Mheshimiwa Bukwimba, nianze kwanza kumpongeza anavyouatilia maendeleo ya umeme kwa wananchi wa Jimbo la Busanda. Hata hivyo, mradi kabambe wa REA Awamu ya Tatu, kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi unalenga kupeleka umeme katika vijiji vyote vilivyobaki lakini katika vitongoji vyote vilivyobaki na taasisi za umma. Nisisitize katika hili, Taasisi za Umma ninamaanisha vituo vya afya, shule, misikiti, masoko na kadhalika, haya yote yatafikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Bukwimba, vijiji vyake vya Nyaluyeya ambavyo vituo vya afya havina umeme sasa vitawekewa umeme. Kule Nyamalimbe vituo vya afya pamoja na shule vitawekewa umeme. Shule za Bukoli, shule za Kamena, Kaseme pamoja na vituo vya kwa Mheshimiwa Musukuma, kisiwa chake cha Izumachele tutaenda mpaka huko.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa wa Busanda kwamba vitongoji vyote ambavyo vina zahanati tutawekea zahanati umeme pamoja na shule. Umeme mwingine mbadala, kwenye taasisi za umma tutawawekea pia umeme wa solar. Hii ni kwa sababu ikitokea kuna hitilafu ya umeme basi umeme wa solar uweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ni lini sasa tunazindua, nitumie nafasi hii kusema kwamba ni kweli tumezindua mikoa kumi tu nchi nzima, tunaendelea kuzindua mikoa yote 15 iliyobaki ya Tanzania Bara, mkoa mmoja hadi mwingine na mahali pengine ikilazimika tutazindua kila wilaya ili wananchi waweze kujua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumueleza Mheshimiwa Lolesia Bukwimba kuanzia mwezi wa saba tutaanza uzinduzi, kwa hiyo, mwezi wa saba Mheshimiwa Bukwimba tufuatane ili tukazindue umeme wa REA Awamu ya Tatu katika Jimbo lako.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera kuna vijiji ambavyo vimewekwa katika mpango wa Rea Awamu wa Pili, vijiji kama Songambele, Kitwe, Mulongo lakini havikupatiwa umeme. Vijiji hivi hivi pia vimewekwa katika Mpango wa REA Awamu ya Tatu. Je, Serikali itahakikisha katika Mpango huu wa REA Awamu ya Tatu, vijiji hivi havitakosa umeme? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vya Kyerwa ambapo vimebakia 27 vitapelekewa umeme vijiji vyote na siyo tu vijiji ambavyo umetaja vya Mulongo pamoja na Songambele lakini viko vijiji na chuo vya ufundi pale Kyerwa na chenyewe tutakipelekewa umeme. Kwa hiyo vijiji vyote 27 vilivyobaki vitapelekewa umeme katika mradi wa REA Awamu ya Tatu.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Natambua katika Mkoa wa Mbeya tayari REA Awamu ya Tatu imeishazinduliwa, lakini kuna changamoto kubwa sana katika Wilaya ya Rungwe katika vijiji vya Lupoto, Katabe na Ibungu mpaka sasa hawajapata umeme na hatujajua ni lini watapata. Naomba majibu ya Serikali tuweze kujua ni lini Wilaya hizi zitapata umeme wa REA? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa Mheshimiwa Mbunge nakushukuru ulivyouliza, hapa tunapoongea katika kijiji cha Lugota wakandarasi wanaendelea na kazi, kwa hiyo wanaendelea kupata umeme, lakini vijiji vya jirani pia tutavitembelea ambavyo bado lakini vijiji vyote ulivyotaja kwenye eneo lako vitapata umeme wa REA na umeanza mwezi wa tatu na kwako wewe utakamilika mwakani mwezi wa saba.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ulitaka kupanua goli. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri aliyotoa kwa swali hili, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, katika eneo hili ambalo lina chokaa linaloitwa Bumuli maarufu Ngongogwa liko katika Hifadhi ya Moyowosi - Kigosi. Wafanyabiashara wanaotaka kuchimba hiyo chokaa wamekuwa wakikwamishwa na shughuli zinazofanyika katika hifadhi na Mamlaka ya Hifadhi kuwazuia kufanya shughuli hiyo. Je, Serikali inaweza ikatoa utaratibu mahsusi watakaofuata wananchi wa Kaknoko ili waweze kuchimba chokaa hiyo ambayo ni grade two? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo dhahabu ambayo imepatikana sehemu za Nyamwilonge na Nyakayenze na maeneo ya Ruhuli inayoendelea kuchimbwa na wachimbaji wadogo wadogo kwa kutumia zana hafifu. Je, Serikali iko tayari kutoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo wadogo katika maeneo hayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mheshimiwa Bilago lakini pia namshukuru kwa sababu anafuatilia sana maeneo ya wachimbaji katika maeneo yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imechukua hatua nyingi sana, lakini kulingana na Sheria ya Madini na Sheria ya Hifadhi ya Mazingira, kifungu cha 95 cha Sheria ya Madini kinatoa utaratibu na utaratibu unaotumika hivi sasa kuchimba madini katika maeneo mengine kwanza kabisa mtu anaruhusiwa kupata leseni lakini akishapata leseni ya uchimbaji anawaona watu wa maliasili ili apate kibali cha maandishi na huo ndiyo utaratibu unaotumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshatoa leseni 70 katika maeneo karibu na Hifadhi ya Moyowosi na hizo leseni wananchi wanachimba na kuna vikundi viwili vya ushirika ambapo wanafanya kazi hiyo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Bilago utaratibu upo lakini ni vizuri tukaa zaidi ili nikueleweshe ili wananchi wa Jimbo lako wanufaike zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la nyongeza la pili, maeneo ya Nyamwilonge na Nyakayenze pamoja na Makele na maeneo ya mbali, maeneo haya tumeshatoa leseni kwa sababu kuna uchimbaji mzuri wa dhahabu. Mwaka 2012 kuligunduliwa dhahabu na tukalitenga eneo hilo na hivi sasa kuna leseni 76 katika maeneo hayo. Nimuombe Mheshimiwa Bilago awahamasishe wananchi wa Jimbo lake ili eneo lililobaki tulilolitenga pia walitumie kwa manufaa ya maisha yao.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa chanzo kikubwa cha migogoro kati ya wananchi na wawekezaji wanaoenda kuwekeza kwenye sekta hii ya uchimbaji wa madini ni utaratibu unaotumika wa kumalizana na wawekezaji kitaifa na kutowashirikisha vizuri wale wa Wilayani na pale kijijini penyewe ambapo utafiti au uchimbaji unakwenda kufanyika na mfano mzuri ni katika Jimbo langu la Mtama, Kata ya Namangale kuna utafiti unafanyika wa graphite na Kampuni ya Nachi Resources lakini mgogoro uliopo ni kwamba wananchi wa eneo lile hawaelewi kinachoendelea na hivyo kubaki na malalamiko mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni lini Serikali itabadilisha huu utaratibu na kuwasaidia wananchi wangu wapate uelewa wa kinachoendelea ili waone ushiriki wao utakuwaje?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Nape tumekuwa tukishirikiana sana katika hili na wananchi wa Mtama nadhani ni mashahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii nisema utaratibu unaotumika ni kwamba mwekezaji yeyote anayepata leseni, hatua ya kwanza akishapata leseni ni kuonana na uongozi wa Halmashauri au uongozi unaohusika wa wilaya na kama hilo halifanyiki ni uvunjivu wa sheria na sisi tutalisimamia.
Lakini pia nichukue nafasi hii kusema kwamba tutapita katika maeneo ya kero, tumeshapanga utaratibu, kuanzia tarehe 02 Agosti, 2017 tunashughulikia matatizo hayo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Nape hata kwake tutafika. Ahsante sana.
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Isulamilomo, Jimbo la Nsimbo katika Mkoa wa Katavi kuna mwekezaji yuko pale, hana leseni na kuna vijana zaidi ya 4,000 hawana leseni, lakini mwekezaji huyu sijui anapata nguvu gani ya kuwazuia hawa wachimbaji wadogo wadogo zaidi ya 4,000 kuchimba lakini zaidi wanapigwa na wananyanyaswa kwenye huu mgodi mpya ulioko katika Jimbo la Nsimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nini tamko la Serikali sasa ili tujue nani ni halali kuchimba katika mgodi huu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninamshukuru kwa kutupa taarifa, lakini atusaidie zaidi mwekezaji huyu ni nani, utatusaidia sana Mheshimiwa Mbunge. Hebu tupatie huyo ni nani halafu tukafanyie kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu la msingi ni kwamba maeneo yote ambayo wawekezaji wameyashikilia bila kuyafanyia kazi Serikali sasa inayatwaa kwa mujibu wa sheria ili iwagawie wananchi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tutakaa pamoja tuone kero hiyo tuitatue kwa mujibu wa sheria, ikiwezekana kabisa tutachukua hatua za kisheria. (Makofi)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninaomba nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nilitaka kumtaarifu kwamba hiyo Blast Monitoring Committee ilivunjwa na haipo tena, na ninaomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, mgodi huu unaendelea na mfumo huu wa ku-blast ambapo kutokana na blasting hii watu wameendelea kupata madhara na tarehe 30 Machi watu nane walizimia, mama mmoja ambaye alikuwa ni mama lishe alizimia karibu siku tatu na kulazwa hospitali, lakini juhudi za Mkuu wa Wilaya za kuwataka watu wa mgodi kwanza walipie matibabu, lakini walipe gharama za mama lishe huyu ziligonga mwama baada ya watu wa mgodi kukataa.
Je, ni utaratibu gani utumike ili wanaoathirika kiafya waweze kulipwa fidia?
Swali la pili, kupitia Bunge na kupitia mikutano kadhaa Mheshimiwa Naibu Waziri na Nishati, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mazingira, Mheshimiwa Waziri wa Nishati aliyeondoka walitoa maagizo mengi ya kuhakikisha kwamba waathirika, wa milipuko hii wanalipwa fidia katika eneo la Katoma, lakini mpaka sasa tunapozungumza ni mwaka mmoja umepita. Je, ni lini ahadi hii ya Serikali itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Constantine anavyohangaika na matatizo ya wananchi hasa wa Katoma na Nyamalembo Compound na ninaamini wananchi wanaona juhudi zako Mheshimiwa Constantine.
Mgodi wa GGM kweli umekuwa ukifanya shughuli za ulipuaji na tarehe 30 mwezi Machi mwaka huu, ulifanya ulipuaji na kama alivyosema Mheshimiwa Constantine kuna mtu mmoja ambaye alipata madhara, kampuni tumeendelea kujadiliana nao na wanaangalia namna ya kufanya fidia. Kwa hiyo, Mheshimiwa Constantine huyo mwananchi pamoja na wananchi wengine watafidiwa fidia.
Mheshimiwa Spika, kuhusu ni lini, tuliunda timu kama ambavyo nimeeleza na kwa kweli tumetuma timu zaidi ya mara mbili na sasa hivi timu itakayokwenda sasa kutathmini yale wananchi wenye nyumba 890 ambao nyumba zao zimeathirika, tarehe 05 Juni watakwenda sasa kujadiliana pamoja na wenye nyumba zilizoathirika ili hatima yao ya kulipwa fidia iweze kufanyika. Kwa hiyo, Mheshimiwa Constantine wewe pamoja na uongozi wa Halmashauri pamoja na mgodi na timu itakayoundwa mtashirikishwa ili wananchi hao sasa waanze kulipwa fidia zao.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi niulize swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika awamu iliyotangulia Wilaya ya Kalambo ilipatia umeme vijiji vichache sana kutokana na scope ya kazi iliyokuwa imetolewa. Je, Serikali ipo tayari kuhakikisha kwamba vile vijiji ambavyo vilikuwa viwe kwenye REA Awamu ya Pili vinaanza kuwekewa umeme haraka iwezekanavyo, ikiwepo kijiji cha Mwazi ambacho tayari transfoma iko pale ni suala la kushusha umeme pamoja na kijiji cha Kazila? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri ni shuhuda, tulienda naye, akaenda kijiji cha Samazi na Ukanda wa Ziwa Tanganyika, miundombinu ya kule alikiri jinsi ambavyo iko haja kubwa ya kuhakikisha kwamba umeme unafika maeneo yale.
Je, yupo tayari kuhakikisha kwamba vijiji hivi vinapatiwa umeme haraka iwezekanavyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Kandege tumetembea naye kwenye Jimbo lake, hakika wananchi wa Jimbo lako Mheshimiwa wanafarijika sana.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na maswali yake mawili ya nyongeza, kweli katika Jimbo la Kalambo ni vijiji 12 tu vilipitiwa na vyenyewe tulipeleka kwenye vituo tu vya umeme, sasa nikuhakikishie Mheshimiwa Kandege, vijiji 89 vyote vilivyobaki, ikiwemo kijiji cha Jengeni, Nondo, Santa Maria, Legeza Mwendo na vingine vyote ninakuhakikishia kwamba vitapelekewa umeme sasa.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali la pili ninahakikisha vipi. Hatua ya kwanza kabisa tumempelekea mkandarasi, hivi sasa Mkandarasi Nakroi ameishaonana na Mheshimiwa Mbunge na ataanza sasa jitihada za kuendelea katika Jimbo lako la Kalambo. Nikuhakikishie kwamba ataanza na maeneo ambayo tayari kuna transfoma kazi iliyobaki sasa ni kuwasha na ataanza na kuwasha. Katika eneo la Santa Maria pamoja na kwamba msishindane na lenyewe itapelekwa transfoma ili umeme uanze kuwaka mara moja. (Makofi)
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kumuuliza swali Mheshimiwa Naibu Waziri.
Kwanza, kwa sababu Kampuni ya Resolute imeamua kuachia leseni zake tisa, je, Serikali itakuwa tayari sasa kuzigawa hizo sasa leseni kwa wachimbaji wadogo Wilayani Mbogwe ili waweze kunufaika na dhahabu iliyopo katika eneo hilo? (Makofi)
Swali la pili, dawa ya deni ni kulipa. Kampuni hii ya Resolute inadaiwa sasa shilingi bilioni 143 na Serikali. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba deni hili linalipwa kwa wakati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa Mheshimiwa Masele nakupongeza sana, najua juhudi zako na wananchi wako wanatambua jinsi unavyoshughulikia maslahi ya wananchi hasa wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni kweli kabisa tumejadiliana sana na kampuni hii, kampuni hii ina leseni 22 na maeneo mengi haiyafanyii kazi, kwa hiyo tumekubaliana na Kampuni hiyo sasa imeamua kuya-surrender maeneo tisa na maeneo hayo tunagawa sasa kwa wananchi wa Mbogwe, Mheshimiwa Mbunge ninakushauri sana sasa wananchi wako waanze kuunda vikundi ili sasa waweze kurasimishwa, mpango wa kuwagawia ifikapo mwezi wa Julai na Agosti, tutawamilikisha rasmi.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na deni, ni kweli kabisa dawa ya deni ni kulipa. Kampuni hii imekuwa ikidaiwa shilingi bilioni 143.007 na kwa sababu ilitaka kuhamisha umiliki wake sisi Serikali tulikataa mpaka deni litakapolipwa.
Mheshimiwa Spika, sasa hatua inayofanyika wamekubaliana na TRA na Kampuni imekubali kulipa, kwa hiyo kuja kufika mwezi wa Julai, kampuni imeahidi kulipa deni hilo. Baada ya kulipa sasa taratibu za umilikishaji zitaendelea rasmi.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nilitaka nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri au niombe tamko la Serikali, kwenye bajeti mwaka huu tulitaka Halmashauri zote ambazo ni class three ambazo zina madeni Serikali Kuu kupitia funds zinazokusanywa na EWURA zipelekwe Wizara ya Maji ili madeni hayo walipwe. Leo ni wiki ya pili Halmashauri ya Mji wa Nzega imezimiwa umeme na TANESCO kwa sababu ya madeni yaliyotokana na Serikali Kuu kutokupeleka fedha za utilities kwenye Halmashauri kwa miaka mingi.
Je Serikali iko tayari leo kuitaka TANESCO iweze kuruhusu watu wa Nzega waweze kupata maji?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Bashe. Tumetoa maelekezo na tumeshakaa na wadau wote kwamba taasisi zote muhimu za Serikali; afya, maji, usalama na maeneo mengi waje tukae tuweke utaratibu. Hatukati umeme kama tumeshaweka utaratibu, lakini tukishaweka utaratibu halafu utaratibu ukakiuka kwa kweli sisi tunakata umeme. Nichukue nafasi hii tutakaa na Mheshimiwa Bashe na Waheshimiwa wengine tuone namna gani ya kulifanya jambo hili ili wananchi waendelee kupata maji.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali katika kutatua tatizo la umeme kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara, baada ya mateso makubwa tuliyoyapata katika kipindi hiki cha miezi miwili/mitatu cha kukosa umeme kwa zaidi ya siku nne. Serikali inaambatanishaje juhudi hizo na ukarabati wa miundombinu hasa nguzo, kwenye yale maeneo ambayo nguzo zake ni mbovu. Kwa hiyo, hata wakikamilisha uzalishaji bado usambazaji wa umeme kwenye haya maeneo ambayo nguzo zake ni mbovu bado itakwama.
Sasa Serikali imejipangaje kuambatanisha juhudi hizo mnazoendelea nazo na ukarabati wa nguzo kwenye yale maeneo ambayo nguzo zimechoka?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Lakini niwape pole sana Waheshimiwa Wabunge wa Mikoa ya Mtwara na Lindi kwa kipindi ambacho Mheshimiwa Nape amezungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli zipo juhudi za makusudi ambazo sasa tunachukua kama Serikali, tuliporekebisha umeme katika Mkoa wa Mtwara tarehe 16 mwezi uliopita tuliacha feeder mbili ambazo matengenezo yake yanaendelea. Wananchi wa Mkoa wa Lindi kwa sasa wanapata umeme kutoka kwenye sub station ya Maumbika. Sasa sub station ya Maumbika marekebisho ya engine yake yanakamilika kesho. Kwa hiyo wananchi wa Mtwara, Lindi na maeneo mengine yategemee kupata umeme kuanzia kesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la nguzo kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amezungumza, tumeagiza nguzo mpya kutoka hapa nchini, tumeacha sasa kuleta nguzo kutoka nje ambazo zilikuwa zinakaa kwa muda mrefu mipakani. Nguzo zitakuwa mpya, kwa hiyo, niwahakikishie wananchi watapata nguzo na ukarabati utaendelea vizuri. (Makofi)
MHE. AISHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Tatizo lililopo Mtwara halina tofauti na tatizo lililopo katika Jimbo la Singida Kaskazini. Vijiji vingi vya Jimbo la Singida Kaskazini ambavyo vilikuwa katika Mpango wa REA II mpaka sasa havijapatiwa umeme. Vijiji hivyo ni Mrama, Madasenga, Mipilo, Meria, Mitula na Msange. Kwa kuwa sasa tunaelekea kwenye Tanzania ya Viwanda; je, ni lini sasa Serikali itavipatia vijiji hivyo umeme ukizugatia kwamba tupo katika Mpango wa REA III? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mkoa wa Singida mkandarasi ambaye alipewa kazi alikuwa na jukumu la kukamilisha masuala ya mikataba. Taratibu za mikataba amekamilisha juzi, siku ya Ijumaa, na hivyo ataanza kuingia site kuanzia Ijumaa wiki hii, kwa hiyo wananchi wa Singida na maeneo mengine watapata mkandarasi huyo.
Lakini cha pili Singida tunawapatia mkandarasi aliyeshindwa kukamilisha kazi katika REA II, Kampuni ya SPENCON iliondolewa kwa hiyo, tunawapa mkandarasi mwingine. Kwa hiyo, Mkoa wa Singida utapata wakandarasi wawili pamoja na mkandarasi wa REA III.
MHE. OMARY T. MGUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kama Serikali ilivyosema katika jibu lake la msingi kwamba kuna vijiji saba ambavyo umeniongeza kwa hiyo, je, nataka kuvijua vijiji hivi saba ni vipi na ni lini vitaanza kupatiwa umeme?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa, katika Kata ya Mkulazi kuna miradi miwili nya kielelezo inayofanyiwa kazi sasahivi na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli, Kiwanda cha Mkulazi cha Sukari pia na ujenzi wa Bwawa la Kidunda, je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka umeme katika kata hii yenye vijiji vinne na Kijiji cha Kwaba, ambavyo ni vijiji vya Kwaba, Kidunda pamoja na Usungura?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa Mheshimiwa Mgumba nakupongeza sana unavyoshughulikia masuala ya umeme katika Jimbo lako. Tulipokutana Morogoro ulituomba tukuongezee vijiji na tumekuongezea, lakini vijiji alivyotaka tumuongezee Mheshimiwa Mbunge pamoja na kwamba tumeshapeleka umeme katika vijiji vingine vikiwemo vijiji vya Mtego wa Simba pamoja na Kinonko, tunampelekea kwenye vijiji vingine ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameomba.
Mheshimiwa Naibu Spika, na vijiji ambavyo ameomba tumpelekee ni pamoja na Kibuko, Luhorole, Kizinga, Pangawe pamoja na Usungura. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikupe, kama vijiji ambavyo tumepeleka na vijiji vingine 40 tutakupelekea Mheshimiwa Mbunge, wala hakuna wasiwasi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la pili kwamba ipo miradi ya vielelezo katika maeneo ya Usungura, ni kweli kabisa. Maeneo yale kutajengwa viwana vya sukari, lakini kadhalika kuna bwawa la maj. Kwa hiyo, tumemuongezea mbali na vijiji vingine vile 11 nilivyotaja na wala sio saba, tunaviongezea vijiji vingine vitatu vikijumlisha na Bwawa la Kidunda, ili tupeleke umeme Kidunda, Usungura pamoja na Kwaba. Kwa hiyo, nimpe imani Mheshimiwa Mbunge kwamba vijiji vyote vya Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki vitapatiwa umeme kupitia mradi wa tatu wa REA. (Makofi)
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kupata fursa hii. Kama alivyouliza Mheshimiwa Mgumba, majimbo ya vijijini yana matatizo makubwa sana ya umeme hasa katika center za Kata ya Mpwayungu, Kata ya N’ninyi, Manzase na Makao Makuu ya Kata ya Muungano ambako hakuna umeme kabisa. Sasa je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika maeneo haya hususan katika Kata ya Muungano? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa katika Jimbo la Mtera tunapeleka umeme katika vijiji (a) Katika maeneo aliyoyataja kimsingi nimhakikishie Mheshimiwa Lusinde kwamba katika maeneo ya Manzese, Muungano, Mpwayungu pamoja na eneo ambalo hujalitaja linaitwa N’ninyi wanaanza Ijumaa inayokuja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nichukue nafasi hii kumueleza Mheshimiwa Mbunge. Nichukue nafasi hii kwa sababu Waheshimiwa wengi wamesimama, kuwaeleza rasmi Waheshimiwa Wabunge kwamba kuanzia tarehe 20 mwezi huu wakandarasi wote katika mikoa 21 tuliyosaini mikataba wanaanza kazi rasmi ya ujenzi wa mradi wa REA Awamu ya Tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mikoa miwili ya Katavi pamoja na Kigoma, taratibu tunazikalimisha wiki ijayo na mwanzoni mwa mwezi Desemba wanaanza ujenzi katika mikoa hiyo miwili. (Makofi)
MHE. HAWA S. MWAIFUGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Tatizo lililopo Morogoro Kusini Mashariki ni tatizo ambalo linafanana na Jimbo la Tabora Manispaa katika Kata 11 za vijijini ambapo mpaka sasa hazijaanza kupelekewa umeme wa REA III. Je, ni lini Serikali itaanza utaratibu huo? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwanza mkandarasi yupo Tabora na ameshakamilisha kazi ya survey na wiki iliyopita amekamilisha Igunga. Kwa hiyo, nimuambie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama nilivyosema tarehe 20 na bahati nzuri tunaanza kuwakagua ujenzi wa wakandarasi kuanzia Tabora na Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mkandarasi atakuwa site kuanzia tarehe 20 baada ya kumaliza Igunga na ataendelea na ujenzi wa vijiji vyote 16 katika Mkoa wa Tabora. (Makofi)
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo hili la Morogoro Kusini linafanana kabisa na Jimbo la Mtwara Mjini ambako umeme unatoka pale lakini bado kuna vijiji vingi kwa mfano Naulongo, Mkunjanguo, Namayanga na Mawala Chini kule kote mtandao wa umeme haujafika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nimemweleza Mheshimiwa Waziri mara nyingi sana, je, yupo tayari hivii sasa kutoa kauli ya mwisho kwamba ni lini mtandao wa umeme utapita kwenye vijiji hivi nilivyovitaja? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kama alivyosema, wiki mbili zilizopita nilikuwa Mtwara kushughulikia tatizo la umeme kukatika katika. Nilipita katika vijiji 16 na bahati nzuri vijiji vingine alivyosema Mheshimiwa Maftaha hivi leo mkandarasi yupo kule. Kwa hiyo, wakandarasi wameshaanza kazi Mheshimiwa Mbunge, asante sana. (Makofi)
MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na vilevile naishukuru Serikali kwa majibu mazuri na dhamira yao ya dhati kabisa kufanya mradi huo ukamilike. Nina maswali mawili madogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, uchimbaji wa kisima cha mradi huu,ulipangwa kufanyika mwaka 2016 na tafiti zilifanyika ikabainika kuna mafuta ya kutosha kupata mafuta ya kuendesha biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali kwa utaratibu ambao wameuwekeza ukiritimba umezidi mno umesababisha mpaka sasa hivi mkataba kati ya mwekezaji kampuni ya Swala ya Kitanzania na TPDC bado haujakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu ni lini sasa mtakamilisha mkataba huu ili mradi huo wa uchimbaji wa haya mafuta uanze kwa sababu haraka haraka tu pale itaajiri wananchi karibuni 500 kwa kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nakubali mmetoa elimu lakini mafundisho tuliyopata Mtwara mnaelekea huko huko, elimu mnayo toa mnafanya vi semina na mikutano, watu wachache sana wanahusishwa, eneo lengwa tarafa nzima ya Mtimbira lina wakazi karibu 75,000, hizo semina sijui mtaendeshaje nawashauri na baadaye nauliza swali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumieni media, tumieni vyombo vya habari ambavyo vitaweza kusambaza taarifa na habari haraka sana kuliko hizo semina mnazofanya. Katika maeneo yetu kuna redio za jamii mbili…
redio FM Ulanga, je, Serikali mpo tayari kutumia redio hizo za jamii ili kuelimisha jamii katika eneo hilo?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kabla ya kujibu maswali napenda nichukue nafasi hii nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Mponda anavyofuatilia utekelezwaji wa mradi huu. Mradi utakapoanza kutelezwa utaajiri watanzania takribani 200 hadi 300, Kwa hiyo, Mheshimiwa Mponda hongera sana kwa kufuatilia jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika swali lake la kwanza nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba mkataba ulishasainiwa tangu mwezi Februari, 2012 kwa hiyo, kilichobaki ni uekelezaji wa kufanya drilling kwa maana ya uchimbaji na ugunduzi wa mafuta, na katika eneo hilo Mheshimiwa Mponda mafuta yanayotarajiwa kuchimbwa katika eneo hilo yanafikia milioni 180 hadi milioni 200. Kwa hiyo, ni mtaji mkubwa na utakuwa na manufaa kwa wananchi wako na watanzania kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa uchimbaji utaanza, kama ambavyo nimeleeza kama ambavyo nimeleleza kwenye hilo la msingi kwamba kinachosubiriwa ni kupata kibali cha mazingira kutoka NEMC na wenzetu NEMC wanalifanyia kazi pamoja na Mamlaka ya TAWA yaani Hifadhi ya Mamlaka ya Wanyamapori, wametuhakikishia kwamba kuja kufika mwezi Julai vibali vimepatikana na mwezi Septemba uchimbaji utaanza rasmi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la pili kuhusiana na elimu, kwa kweli niwapongeze sana TPDC na Swala wametoa elimu katika mkoa mzima wa Morogoro sasa takribani ya watu 350 wamepewa elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumepeleka elimu pia katika vijiji vingi, ikiwemo kijiji cha Mheshimiwa Dkt. Mponda, Ipera, Kipenyo, Mtimbira lakini pamoja na maeneo ya Mnazini pamoja na vijiji vingine anavyovijua Mheshimiwa Mbunge na maeneo mengine ya Kijiji cha Kitete na kata zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, takribani ya wananchi 350 walipata elimu, lakini tutaendelea na kutoa elimu kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameshauri. Lakini kuhusu vyombo vya habari tumeshaanza kutumia TBC na nimechukua ushauri wake kwamba chombo cha FM media cha Ulanga nacho tutazingatia tutakipa kazi hiyo.
MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Moja; eneo la Karukwete lina wachimbaji wadogo na lipo jirani kabisa na Kijiji cha Busiri kinachazungumziwa kwenye swali la msingi. Waziri yupo tayari kulijumuisha kwenye mkakati wa kuwawezesha kielimu na uwezeshaji?
Swali la pili; naomba kujua orodha ya mambo ya kiuwezeshaji yatakayofanyika kwa wananchi wa Karukwete na Busiri na lini tutawenda kuzungumza nao kuwafahamisha? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mukasa kwamba eneo la Karukwete nalo litaongezwa kwenye maeneo ya kufikiriwa kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu langu la pili kwenye orodha ya huduma zitakazotolewa kwa msaada huu ni pamoja na kuwapatia ruzuku wachimbaji wadogo. Mwaka huu kwenye bajeti yetu mtaona tumetenga takribani shilingi milioni tisa za Tanzania pamoja na dola bilioni nne kwa ajili ya kuwawezesha wachimbaji wadogo. Pia tutaendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo ili waweze kuwa na uchimbaji wenye tija.
Pamoja na hayo bado Wizara yetu itatuma wataalam wa GST iyafanyie tathmini maeneo yote yatakayotengwa ili wachimbaji wawe na uhakika wa uchimbaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuongeza kwa manufaa ya wengine kwamba maeneo ambayo tutayatenga yapo mengi tunategemea kutenga eneo la Kasubwiya hekta 495, eneo la Nyaluyeye hekta 658, eneo la Matabe hekta 659 na maeneo mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tutaendelea kuwawezesha.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo kimsingi yana afya, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa mpango huo mzuri wa Serikali ili wachimbaji wadogo waweze kufikia hatua ya kupata mpango huo mzuri, ni lazima wawe na maeneo. Naibu Waziri anasema nini kwa maana ya kutenga maeneo kwa eneo hilo la Mpanda? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Swali la pili, nafahamu Wizara kwa ujumla wake imekuwa ikisaidia wachimbaji wadogo nchini. Je, ni utaratibu upi unaotumika kwa maana ya suala zima la utoaji ruzuku kwa wachimbaji hawa wadogo? Naliuliza hilo ili iwe faida kwa wachimbaji wote wadogo nchini? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nipate ridhaa yako nimshukuru sana Mheshimiwa Kapufi. Kwanza nampongeza kuwa mchimbaji mdogo kati ya wachimbaji wadogo maarufu hapa nchini. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Kapufi kama mdau mzuri na ni mchimbaji mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nampongeza sana Mheshimiwa Kapufi kwa kuwawakilisha vyema wananchi wa Mpanda. Mheshimiwa Kapufi nikuhakikishie kwamba wananchi wako ambao ni wachimbaji wadogo, kama ambavyo wewe unachimba nao watafikia kiwango chako cha uchimbaji kama unavyoendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba nijielekeze kwenye maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kapufi. Ni lini Serikali itawatengea maeneo wachimbaji wadogo?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa hivi Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) anafanya tathmini kwa mambo matatu; tathmini ya Kijiokemia, tathmini ya Kijiolojia na tathmini ya Kijiofizikia na mwezi wa saba tunaanza kuwatengea maeneo hayo. Zoezi la kuwatengea wananchi maeneo litakuwa ni endelevu; kuanzia mwezi wa saba na kuendelea tutafanya kazi ya kuwatengea maeneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa Serikali imetenga hekta 12,000 kwa ajili ya kuwatenga maeneo, kadhalika, imetenga shilingi milioni 640 kwa ajili ya Wakala wa Jiolojia kutathmini maeneo ambayo yatatengwa. Maeneo ambayo tutayatenga ni mengi sana ikiwa ni pamoja na Lindi, Geita, Sambaru – Singida, pamoja na Londoni. Maeneo mengine tutakayotenga kule Mpanda ni pamoja na eneo la Dirifu, Katuma, Society pamoja na eneo la Katasunga. Maeneo yote ya Mpanda Mheshimiwa Kapufi tutaendelea kuyatenga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la pili kuhusu utaratibu wa ruzuku, ni kweli kabisa mwaka 2015/2016, Serikali ilitenga shilingi bilioni 7.24 na mwaka huu kwa ridhaa ya Waheshimiwa Wabunge tumetenga shilingi bilioni 6.68, hii ni kwa ajili ya kuwagawia wananchi kama ruzuku.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongeze kidogo kuhusu hili. Utaratibu tunaotumia kwa sasa, kwanza kabisa leseni lazima ziwe za Watanzania peke yake kwa asilimia mia moja. Hilo la kwanza. Pili, leseni hizo lazima ziwe hai na zinafanyiwa kazi; na tatu, tunawahamasisha sana wananchi wajiunge kwenye vikundi ili ruzuku hii iwanufaishe Watanzania wengi. La nne, tumeongeza sasa badala ya kutenga dola 50,000 kwa msimu huu, tutatenga dola 100,000 kwa kila atakayekidhi vigezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningesema mengi sana kwenye eneo hili, lakini niwahamasishe Watanzania; Mheshimiwa Kapufi na Waheshimiwa Wabunge wengine ili waweze kunufaika na ruzuku hii.
MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza naomba ni-declare interest, na mimi ni mchimbaji mdogo japokuwa sijawahi kunufaika kutokana na mfumo mbovu wa Serikali. (Kicheko)
Tatizo lililoko Mpanda Mjini linafanana na lililoko katika Jimbo langu la Ulanga. Je, sasa Serikali haioni umuhimu wa kuwaelimisha na kuwawezesha wachimbaji wadogo wadogo wa Jimbo la Ulanga ili waweze kuyathaminisha madini haya wanayoyapata ili waweze kuyauza katika thamani halisi inayoendana na soko?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona umuhimu, hilo la kwanza. Tunaona umuhimu wananchi wako Mheshimiwa Mbunge kuendelea kuwaelimisha, lakini siyo kuwaelimisha tu, hata kuwapatia ruzuku wakikidhi vigezo. Napenda tu kusema katika Jimbo la Ulanga, maeneo ya Mvomero, maeneo ya Iringa, maeneo ya Singida, yote kwa pamoja tunaendelea kuyatathmini tuwatengee wananchi. Kwa hiyo, pamoja na kutoa elimu, tunawahamisha Waheshimiwa Wabunge wawahamishe wananchi washirikiane na Waheshimiwa Wabunge ili kunufaika na rasilimali hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi wa kwanza mwaka huu, Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini amekaa sana na wachimbaji wadogo Wawakilishi wao wa Katavi, Singida pamoja na kwa Mheshimiwa Mbunge wa Ulanga. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mlinga nakuhakikishia tutaendelea kusaidiana na wananchi wako kuwaelimisha waweze kunufaika na mapesa haya.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na kuitaja Singida, naomba atusaidie kwamba makampuni yale ambayo yanachukua leseni halafu wanakaa nayo muda mrefu bila kufanyia kazi na hivyo kuwafanya wachimbaji wadogo wasiende kufanya uchimbaji kwenye maeneo yenye madini kama Londoni, Sambaru, Muintiri, Sekenke pamoja na Mkalama. Ninaomba atoe tamko hapa kwa makampuni hayo na ni lini atatekeleza? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia sasa na kuanzia huko nyuma na tunaendelea kufanya hivyo. Naomba nichukue nafasi hii kutoa rai kwamba wachimbaji wote ambao hawayafanyii kazi maeneo yao, Serikali itayachukua na huo ni utaratibu wa kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Madini kifungu Na. 36(1), Sheria Namba 14 ya mwaka 2014 inakataza mwekezaji yeyote kushikilia maeneo bila kuyaendeleza. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mlata kwamba wananchi wa Sekenke, Sambaru, Londoni, Muintiri na wananchi wengine wote tunawapatia maeneo kutokana na wawekezaji ambao hawayaendelezi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili niwahakikishie na niwaombe sana Watanzania kwamba sasa tunatekeleza sheria. Maeneo yote ambayo yalikuwa hayafanyiwi kazi na wawekezaji na hasa wawekezaji wa nje, lakini hata wawekezaji wa ndani ambao walikuwa hawayaendelezi, sasa sheria inaanza kuchukua mkondo wake. Maeneo tutayachukua, tutayatumia kwa ajili ya wachimbaji wadogo waweze kupata maeneo ya uhakika kwa ajili ya kujipatia kipato.
Kwa hiyo, namshukuru Mheshimiwa Mlata, kama ambavyo siku zote anafanya; na Kampuni ya Ashanti Mining ambayo iko kwake, tunafanya mazungumzo nayo ili ikiwezekana na yenyewe iweze kuachia maeneo kwa ajili ya wananchi wa Singida.
MHE. LUCY S. MAGERELI: Nakushukuru sana Mheshimiwa Naibu Spika, kwa fursa niulize swali la nyongeza.
Changamoto ya umeme kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni bado ni kubwa sana pamoja na kwamba mwaka jana wakati wa bajeti, wakati Waziri akijibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ndungulile, alieleza bayana ya kwamba tatizo la msongo mdogo wa umeme eneo la Kigamboni litakuwa limekwisha mwaka jana mwezi Agosti, lakini hadi tunapozungumza leo bado changamoto ya umeme mdogo Kigamboni ni kubwa, lakini ukiachilia hilo umeme huo unakatika mara 15 kwa siku.
Je, Serikali ina maelezo gani kuhusu suala hili na kuchelewa kwa kutekelezwa kwa mradi huu wa kufunga transfoma kubwa yenye msongo wa kutosha kutupa huduma ya umeme eneo la Kigamboni?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Lucy kwa swali lake zuri na ni muhimu sana. Kupitia Bunge lako Tukufu, napenda nitoe taarifa ya Serikali kuhusiana na utekelezaji wa miradi ya umeme muhimu sana kwa wananchi wa maeneo ya Kigamboni.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa wananchi wa Kigamboni hivi sasa hawana umeme wa uhakika, lakini hatua madhubuti tunayofanya ni kujenga substation itakayowapelekea umeme sasa wananchi wa Kigamboni wote, mradi huu utakamilika mwezi tarehe 25 Mei tutakuwa tumeshawapelekea wananchi wa Kigamboni.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya haraka tunachofanya hivi sasa tunakamilisha utekelezaji wa mradi wa kabambe katika Jiji la Dar es Salaam kwa eneo la Mbagala. Mradi tunategemea kuuwasha kati ya tarehe 20 mwezi huu kuanzia tarehe 12 tutakuwa tumeshawasha na tarehe 20. Mradi huu utahudumia wananchi wa Mbagala, Kurasini, Kigamboni pamoja na maeneo mengine ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge, kazi hiyo inafanyika na wananchi wa Kigamboni watarajie kwamba umeme utapatikana kufikia mwisho wa mwezi huu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, shida iliyoko huko Njombe inafanana sana na iliyoko huko Kigoma. Mkoa wa Kigoma tuna mkandarasi ambaye ana mgogoro, sasa mgogoro huu umeendelea kati ya REA na Wizara ya Ujenzi. Tungependa kujua kwa Wilaya za Kigoma, Buhigwe, Uvinza na Kasulu, mgogoro kati ya mkandarasi na Wizara unamalizika lini ili mradi wa REA Awamu ya Tatu uweze kuanza? Nakushukuru.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mara nyingine tena ninapenda kumshukuru sana Mheshimiwa Nsanzugwanko anavyofatilia masuala ya umeme katika Mkoa wa Kigoma kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwa upande wa Mkoa wa Kigoma, Mkandarasi kwa ajili ya kutekeleza mradi wa REA Awamu ya Tatu mchakato umekuwa ukiendelea, lakini nitumie nafasi hii kusema kuwa, kweli wakandarasi walishtakiana, shitaka linaendelea mahakamani na kwa taratibu za Kisheria, jambo linapokuwa mahakamani huwezi kuliingilia kwa sababu ni muhimili mwingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninatoa taarifa tu kwamba Serikali imeshaanza kuwapelekea umeme wananchi wa Kigoma, wiki iliyopita tulizindua mradi wa utekelezaji wa umeme vijijini katika Wilaya ya Kibondo na tayari mkandarasi ameshawasha Kijiji cha Mabamba. Lakini katika Jimbo la Kakonko pia tumeshazindua, mkandarasi ameshawasha umeme katika Kijiji cha Katale na ataendelea Nyamtukuza. Niwape taarifa wananchi wa Kigoma kwamba mara baada ya taratibu za kimahakama kukamilika vijiji vyote 120 vilivyobaki vitapelekewa umeme.
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru.
Kumekuwa na tabia ya umeme kukatika katika Mkoa wa Lindi hususan maeneo ya Mchinga, Mvuleni na Kilolambwani kadri mvua inaponyesha, lakini siku mvua haikunyesha umeme huwa haukatiki.
Nataka kujua, kuna changamoto gani kwamba siku za mvua lazima umeme ukatike hata kama hatuoni nguzo iliyodondoka?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali moja zuri sana la Mheshimiwa Mbunge wa Lindi. Ni kweli, kwanza kabisa nitumie nafasi hii kuipongeza sana Serikali yetu, kulikuwa na matatizo makubwa sana ya umeme katika Mkoa wa Mtwara na Lindi miaka na miezi michache iliyopita. Lakini tangu mwezi Desemba, Serikali yetu imetenga fedha na imelipa fedha na tumekarabati mitambo yote iliyokuwa haifanyi kazi katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge na Mikoa ya Mtwara na Lindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kadhalika ni kweli mvua na umeme ni vitu viwili tofauti sana, mara zote kunapokuwa na mvua hasa ya muungurumo wa radi huwa inaingilia sana miundombinu ya umeme, hata inapokuwa mvua ya upepo mara nyingi nguzo zetu zinaanguka.
Mheshimiwa Naibu Spika, ingawa amesema mara zote kunapokuwa hakuna mvua umeme hauna shida, ili kuondokana na tatizo hilo sasa hivi tunaanza utaratibu wa kuleta nguzo za zege ambazo zitakuwa imara, wakati wa mvua zitakuwa hazidondoki. Kwa hiyo, tatizo hilo litakwisha mara moja, siyo kwa Lindi tu ni kwa nchi nzima.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu haya ambayo ameyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri wa Madini na Nishati, majibu ya jumla ambayo yanaelekeza katika maeneo yote ya uchimbaji wa madini, ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba katika Mkoa wetu wa Lindi tunayo madini mbalimbali lakini katika eneo hili la Wilaya ya Ruangwa tuna madini ya green gannet, green tomalin, dhahabu, safaya na graphite pamoja na madini mengine, lakini maeneo haya wachimbaji waliopo ni wachimbaji wadogo wadogo ambao wanatumia zana ambazo si bora, zana hafifu.
Ningependa kujua tunayo Sera na Sheria Mpya ya Madini ya kuwatengea maeneo wachimbaji hao wadogo wadogo, sera hii imewanufaisha vipi na Sheria mpya ya Madini wachimbaji wadogo wadogo wa maeneo hayo ya Wilaya ya Ruangwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la nyongeza ningependa kumuomba Mheshimiwa Waziri, yupo tayari sasa kuja katika Mkoa wetu wa Lindi maeneo ya Ruangwa kuja kuona maeneo ya machimbo haya ya madini na kuona changamaoto mbalimbali zinazowakumba wachimbaji hao wadogo wadogo na kuona namna gani Wizara yake inaweza kuwasaidia? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote sio tu nipo tayari kwenda Lindi isipokuwa nipo tayari kufuatana na Mheshimiwa Hamida twende pamoja mpaka Lindi. Kwa hiyo kwa ruhusa ya Kiti chako nipo tayari na ukitupa ruhusa hata kabla ya Bunge kumalizika nipo tayari Mheshimiwa Mbunge kwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Hamida Abdallah anavyoshughulikia masuala haya, tangu ameingia katika Bunge hili tumeshashirikiana naye sana na katika juhudi zake amefanikisha kutenga maeneo mawili muhimu sana katika Mkoa wa Lindi, eneo mojawapo ni Kitowelo pamoja na eneo la Maguja Nachingwea, kwa hiyo, Mheshimiwa hongera sana kwa kazi zako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Mkoa wa Lindi una madini mengi sana, baadhi ya madini yanayopatikana katika Mkoa wa Lindi kama alivyoyataja Mheshimiwa Mbunge ni pamoja green tomaline, safaya pamoja na madini load garden, lakini kuna dhahabu, kuna chumvi kuna madini mengi yanayoitwa ruby ambayo ni madini ya mfano sana katika nchi yetu. Kwa mkoa wa Lindi una utajiri wa madini mengi tu pamoja na chumvi. Nichukue nafasi hii kuwahamsisha sana Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Lindi na maeneo mengine ili kuhamasishe wachimbaji wadogo wakachimbe madini hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sera na sheria kweli kabisa zinataja kuwatengea maeneo wananchi nchi nzima. Katika Mkoa wa Lindi tumeshatenga maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetenga eneo la hekta 300 Kilwa Masoko kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya chumvi, tumetenga maeneo ya hekta 525 eneo la Kitowelo katika Wilaya ya Liwale na eneo la kilometa 7.2 katika eneo la Maguja Wilaya ya Nachingwea na tunakwenda sasa kutenga eneo lingine la hekta 825 katika eneo linaitwa Hoteli Tatu. Hivyo, Mheshimiwa Mbunge tunaendelea kutenga maeneo kama na sera ya madini inavyoelekeza.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kwa kuuliza swali la nyongeza, linalohusiana na masuala ya madini kama ambavyo Mheshimiwa Hamida ameuliza hapo mwanzoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo Ruangwa linafanana kabisa na tatizo lililopo Jimbo la Ndanda katika kijiji cha Chiwata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kijiji cha Chiwata sasa hivi kuna uwekezaji unaendelea kwa ajili ya madini ya graphite, lakini uwekezaji huu umekuwa ukufanyika kwa siri kubwa sana kiasi kwamba wananchi wa Chiwata hawafahamu nini kinaendelea na hawako tayari kuendelea kukaa kimya, wamenituma nimuulize Waziri.
Je, Serikali ipo tayari sasa kuleta mkataba ambao utatumika kwa ajili ya uchimbaji wa madini katika kijiji cha Chiwata ili kuondoa sintofahamu ambayo inaweza ikajitokeza miaka ya baadaye ya kuhitaji kufanya review na ku-cancel mikataba ile? Ninaomba commitment ya Serikali ni lini iko tayari kuleta mkataba ule ujadiliwe na Bunge ili ukatumike kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa Jimbo la Ndanda? Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Mwambe nampongeza sana, tumekuwa tukishirikiana naye sana kwenye masuala ya wachimbaji wadogo mbali na masuala yake ya masuala ya nishati kwenye eneo lake. Kuhusiana na eneo analolitaja yuko mwekezaji ambaye sasa anajiandaa na kukamilisha utafiti, atakapokamilisha utafiti ndio aanze shughuli za uchimbaji, kwa hiyo hata hatua ya kuingia mkataba bado.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nikuombe sana Mheshimiwa tukae, tujue kitu gani kinahitajika na itakapofikia wakati wa kuingia mikataba tukushirikishe, sasa ni lini mkataba tutauleta nadhani bado sana kuzungumza jambo hilo akamilishe utafiti, akishaanza uchimbaji akaingia mikataba tutajadiliana, kama kutakuwa na haja ya kuuleta basi tutaona ni utaratibu gani utumike ili Mheshimiwa Mbunge kuweza kuuona mkataba huo.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Ahsante Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuniona. Tatizo lililopo Ruangwa halina tofauti na tatizo lililopo Manyoni Magharibi, kwa kuwa sasa kuna Sera ya Madini inayotaka kuwapatia wachimbaji wadogo wadogo wa madini ruzuku.
Je, ni lini sasa Serikali itatoa ruzuku kwa wajasiriamali wachimbaji wa gypsum wa Wilaya ya Itigi ili kuongeza uzalishaji na hata kuanzisha viwanda? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nikupongeze Mheshimiwa Matembe, Mkoa wa Singida na hasa katika maeneo ya Itigi kuna maeneo mengi sana ambayo kuna madini ya dhahabu na katika maeneo hao kwa mwaka jana tumepatia ruzuku wachimbaji wadogo 32, lakini tunaendelea pia kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mbunge kushirikishe tu, tutakapofikia hatua sasa ya kugawa ruzuku nyingine awamu ya tatu ambayo ipo kwenye maandalizi tutakushirikisha na tunatarajia kuanzia mwakani taratibu zikikamilika tutaanza kukamilisha utaratibu mwingine wa kuwapatia ruzuku pamoja na mikopo. (Makofi)
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Ahsante Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kama ambavyo Naibu Waziri ameitambua Kitowelo kwamba atatenga kwa ajili ya wachimbaji wadogo.
Vilevile eneo hilo liko ndani ya kijiji cha Lilombe, lakini tangu uchimbaji huu mdogo umeanza kijiji kile cha Lilombe hakijawahi kunufaika kwa lolote na Halmashauri nzima ya Liwale haijawahi kunufaika kwa lolote, kwa sababu vibali vya uchimbaji vinatoka Kanda, halafu wale wakitoka kwenye Kanda wanaingia moja kwa moja vijijini wanaanza uchimbaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, nini kauli ya Serikali juu ya manufaa wanayoyapata vile vijiji ambavyo tayari machimbo hayo yapo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nakiri jambo ambalo anazungumza na tumezungumza naye kama miezi miwili iliyopita, nikaomba sana nimuagize Mheshimiwa Mkurugenzi wake na Watendaji wa Vijiji ili watumie fursa hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wachimbaji wote nchi nzima, wadogo na wakubwa wanatakiwa kutoa ushuru wa Halmashauri husika, wanatakiwa kuchangia maendeleo ya vijiji ambayo shughuli za uchimbaji zinafanyika. Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Mbunge ikiwezekana nitakafanya ziara huko tutaita mkutano chini ya Mkurugenzi wako, Watendaji wote wa Serikali ambao shughuli za migodi zinafanyika ili sasa Serikali za Vijiji vianze kunufaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu ni kwamba kila kijiji ambapo kuna mgodi wa aina yoyote mkubwa na mdogo lazima wachimbaji hao washiriki katika shughuli za maendeleo.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina masawali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgodi wa Kabanga Nickel una mda mrefu sana, kama nilivyouliza kwenye swali langu la msingi, tangu mwaka 1970 na wachimbaji walianza tangu mwaka 1973. Wananchi wa Ngara tulikuwa tukiona ndege za wazungu zikija na kuondoka wakidai kwamba wanapeleka sample na hawarudi tena, isije ikawa kama makinikia. Je, huu mgodi wa Kabanga Nickel utaanza lini rasmi ili wananchi wa Ngara na Serikali kwa ujumla tuweze kunufaika? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Sheria na mauziano ya Makampuni inataka mnunuzi na muuzaji kulipa kodi ya Serikali. Mgodi wa Kabanga Nickel umekwisha kubadilisha wamiliki zaidi ya wanne. Je, Serikali Kuu na Halmashauri Kuu ya Wilaya ya Ngara imenufaika vipi na huo umiliki wa kubadilisha wamiliki kila mara?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Semguruka kwa jinsi anavyofuatilia maslahi ya wananchi wa Mkoa wa Kagera pamoja na wananchi wa Ngara kwa ujumla wake. Nampongeza pia anavyoshirikiana na Waheshimiwa Wabunge wengine majirani wa Biharamulo, Ngara na wengine, hongera sana Mheshimiwa Semuguruka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na swali la kwanza. Ni kweli kabisa huu mradi umeanza tangu mwaka 2009, kwa kweli si miaka ya 1970 iliyopita. Hata hivyo niseme tu kwamba kazi inayofanyika sasa hivi ni kukamilisha upembuzi yakinifu, na natarajia kufungua mgodi mara tu baada ya bei ya nickel kuimarika. Hata hivyo tumempa muda wa mwaka asipofanya hivyo eneo hilo tutalichukua tutawamilikisha wawekezaji wengine wenye nia na uwezo wa kufanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, manufaa yatakayopatikana mgodi huo ukifunguliwa ni pamoja na kutoa ajira kwa wananchi wengi wa Bugarama na Kanyenyi, kadhalika watalipa mafao ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusiana na uhamishaji, Sheria za Kodi zinamtaka mmiliki yeyote akihamisha au kuuza hisa au leseni yake anatakiwa kulipa capital gain ya asilimia 10 na kwa upande wa Sheria ya Madini kifungu cha 9(1) cha mwaka 2010 kinataka mmiliki akianza kuhamisha analipa dola 3,000. Kwa hiyo, atakapofika hatua hiyo Mheshimiwa Semuguruka haya mafao ya Serikali yataingia. (Makofi)
MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira kule Mbeya umekuwa static kwa muda mrefu sana na Mgodi huu mimi naweza nikasema sasa wananchi wa Mkoa wa Mbeya na mikoa ya jirani tumekuwa yatima. Nini tamko la Serikali, nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana nae kwanza Mwanjelwa hongera sana. Hata mwaka jana amehangaika sana kuhakikisha kwamba mgodi huu unafanya kazi. Nimpe taarifa tu, mwaka 2017/2018 Shirika la STAMICO limeanza uchimbaji, na hivi sasa limeishachimba tani 500 ya makaa ya mawe na wataendelea na uchimbaji. Kadhalika kuna makampuni mawili yataingia ubia ili kuwezesha uchimbaji kuwa wa manufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mgodi wa Kiwira umeishaanza shughuli na kufika mwaka 2018/2019 tunatarajia tani 100,000 zitakuwa zimezalishwa katika mgodi ule. (Makofi)
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nashukuru. Katika milima ya Panda Hill Wilaya ya Mbeya kuna madini ya niobium ambayo yanatarajiwa kuchimbwa hivi karibuni. Je, Serikali imechukua hatua gani na tahadhari gani ili yasije yakatokea yale yaliyotokea kwenye Acacia na Barrick Gold Cooperation?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana, Mgodi wa Niobium hapa Tanzania ni mgodi pekee ambao unapatikana katika eneo la Songwe. Kinachofanyika sasa ni majadiliano kati ya Magereza ambako eneo la mgodi litachukua ili kuona kama kutakuwa na re-settlement na majadiliano kama yakikamilika.
Kwa hiyo, nimpe taarifa tu, taratibu zinazofanyika sasa ni majadiliano kati ya Kampuni pamoja na Magereza, taratibu zikishakamilika basi uwekezaji utaendelea.
MHE. TUNDU A. M. LISSU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusiana na huo mgodi unaopangwa kujengwa wa Kabanga Nickel, Serikali itapata asilimia ngapi kama mrahaba kwa mujibu wa Sheria za Tanzania? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Tundu Lissu, Mbunge mashuhuri kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimueleza Mheshimiwa Tundu Lissu; Mrabaha unaotozwa kwa sasa kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010 madini yote ya ujenzi ikiwa pamoja na madini ya chumu na iron ambayo ni nickel ni asilimia tatu, lakini madini mengine ya dhahabu ni asilimia nne na madini mengine ni asilimia moja, madini ya almasi ni asilimia tano. Kwa hiyo, asilimia tutakazopata kutoka kwenye mgodi ni pamoja na hiyo. (Makofi)
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu swali kwa ufupi lakini kama tunavyotegemea, ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri. Sasa naomba niulize maswali mawili madogo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ya Mji wa Katesh yanaendeshwa kwa umeme wa grid lakini bado gharama ni kubwa. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri anihakikishie kwamba atatuma wataalam kuona kwa nini gharama ile iko juu ili watu wa Katesh waweze kupata maji kwa sababu kwa sasa hivi wanapata mara katika wiki na ni hatari kwa mji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lingine dogo la pili ni kwamba; ninamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri huyu kwa kuona umuhimu wa vijiji kuwa na umeme ili wanapochimba visima waweze kusukuma maji kwa nguvu ya umeme. Hata hivyo Wilaya yetu ni moja ya Wilaya ambayo imepata vijiji vichache. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kunihakikishia kwamba vijiji vyetu vingi sasa vitapata umeme wa REA na kwamba Mkoa wa Manyara ataanzia na Wilaya ya Hanang? Ahsante.
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kuhusiana na kutuma wataalam wakaangalie kama bei ni halisi, Mheshimiwa Mary Nagu kwanza nakupongeza sana kesho wataalam watakwenda kwenye site wataangalia ili wajiridhishe kama ni sahihi, nitawaagiza waende washirikiane na watu wako walioko kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na vijiji ambavyo ameseme Mheshimiwa Mary Nagu, kwanza nakupongeza Mheshimiwa Mary Nagu, wakati wakati wa bajeti yetu ulitupatia vijiji vyako 44 ili tuvipelekee umeme. Sasa napenda kuwahakikishia wananchi wa Hanang kwamba vijiji vyako vyote 44 ulivyotupatia ikiwepo kijiji cha Gocho, kijiji cha Kaltaki, kijiji cha Gawindu pamoja na Kateto na vitengoji vyake vyote vitapata umeme Mheshimiwa Nagu.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza kabisa naomba nichukue fursa hii kuipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea kwa TANESCO hasa eneo la uzalishaji, lakini hasara ya Shirika la TANESCO imekuwa inaongezeka kwa kasi zaidi. Kati ya mwaka 2015 mpaka 2017 ambapo TANESCO wameongeza hasara ya shilingi bilioni 124 mpaka shilingi bilioni 346.
Swali langu, Serikali ina mkakati gani unaotekelezeka kuhakikisha inapunguza hasara hizi na hatimaye kupata faida? (Makofi)
Swali langu la pili, TANESCO itagawanywa lini ili kutofautisha uzalishaji na usambazaji wa umeme? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri katika swali hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba kwa muda mrefu Shirika letu limekuwa likijiendesha kwa hasara. Napenda kutoa taarifa tu katika Bunge lako kwamba hivi sasa Shirika la TANESCO limeanza kuongeza uzalishaji kuliko miaka iliyopita. Kipindi cha Julai mwaka 2017 hadi Machi mwaka huu, revenue ya TANESCO kwa wiki imeongezeka kutoka shilingi bilioni 29.1 mpaka shilingi bilioni 32.5. Kwa hiyo, ni maendelea mazuri ya Shirika letu katika hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu zilizochangia ni pamoja na kwanza kuzuia kuingiza vifaa kutoka nje, kitu kilichokuwa kinaligharimu shirika kwa kiwango kikubwa sana. Kitu cha pili ni kuwaunganisha wateja na LUKU kwa nchi nzima ambao ni mpango unaendelea na ni matumaini yetu Shirika litaendelea kuwaunganisha wateja na kupata mapato makubwa, na lingine ni kuondo kana na mafuta kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivyojibu.
Mheshimiwa mwenyekiti, swali la pili kwamba ni lini Shirika litagawanywa? Mantiki kubwa ya Shirika hili ni kulionyesha kwamba linafanya kazi kwa manufaa. Suala la kuligawa ni suala ambalo ni endelevu, ni suala ambalo tunatakiwa kulitafakari kwa kina sana kwa sababu kufanya hivyo ni lazima pia tuangalie madhara yake. Mantiki kubwa vile vile ni kwamba lazima Shirika lijiendeshe kifaida na liweze kumudu majukumu yake na kazi hizo zinaendelea.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini nimpongeze vilevile yeye mwenyewe kama Naibu Waziri na Waziri wake kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha kwamba wanawapatia wananchi umeme. Nina maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mradi huu unaonekana utakwenda hadi Arusha, na kwa kuwa tayari wananchi wa Kibaha wao wameshafanyiwa tathmini ya kuhakikisha kwamba wanapata hizi fedha ambazo zimetengwa. Je, hawa wananchi wengine ambao watapitiwa na umeme hadi Arusha ni lini sasa watafanyiwa tathmini hiyo ili nao waweze kulipwa fidia zao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Korogwe Mjini tunapata umeme ambao unawaka na kuzimika au unachezacheza, nini tatizo la umeme huo Korogwe Mjini? Naomba nipatiwe majibu. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ya msingi katika swali la Mheshimiwa Mbunge, nakupongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri. Lakini napenda sasa nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mary Pius Chatanda kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kabisa tathmini imefanyika katika awamu mbili, awamu ya kwanza imefanyika kutoka Kibaha na Chalinze na Chalinze hadi Segera na kadhalika imefanyika kutoka Segera hadi kwenda mpaka Arusha ambapo tathmini imepatikana. Kwa awamu ya kwanza shilingi bilioni 5.2 na lile eneo la pili mpaka Tanga shilingi bilioni 10.6. Kwa hiyo tathmini zote mbili zimeshafanyika na malipo yatafanyika kwa pamoja mara baada ya uhakiki kukamilika mapema iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na umeme kutokuwa imara katika maeneo ya Tanga na maeneo mengine, nipende tu kumpa taarifa Mheshimiwa Chatanda na kumshukuru sana kwa kuunga mkono juhudi za Serikali, kinachofanyika la kwanza ni kuhakikisha kwamba maeneo yote yanayopitiwa na miundombinu yanafanyiwa ukarabati. Tumeshaanza kusafisha njia kutoka Tanga katika maeneo yote ya Korogwe, Lushoto mpaka Muheza na mwisho wa mwezi huu itakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na maeneo ya pili ni kurekebisha nguzo pamoja na nyaya ambayo itakamilika mwezi huu wa Mei. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Chatanda baada ya mwezi Mei, hali ya umeme kwa Korogwe itaimarika sana. Ahsante sana.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naomba niulize maswli mawili madogo ya nyongeza na moja ni kwa sababu Serikali bado yako maeneo kwenye Jiji la Mwanza na hasa Wilaya ya Nyamagana kama Kata za Kishiri, Lwanima na Buhongwa bado hayajapata umeme wa uhakika.
Ni lini sasa Serikali kupitia Shirika la TANESCO itahakikisha maeneo hayo yanapata umeme wa kutosha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili Mji wa Mwanza bado unayo maeneo yenye taswira ya vijiji ikiwemo Jimbo la Ilemela. Ni nini mpango wa Serikali kupitisha umeme kwenye maeneo hayo hasa maeneo ambayo tayari yamebaki sambamba na Kata za Sangabuye, Bugogwa, Kahama na Shibula ili kuhakisha Mwanza yote inapata umeme wa uhakika? Ninakushukuru sana.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu ya swali la msingi, nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Mabula pia katika kufuatilia maeneo ya vijiji hivi 18.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa tulitenga fedha shilingi bilioni 8.7 kwa ajili ya kupeleka vijji tisa katika jimbo la Mheshimiwa Mbunge vipya, kupitia mradi wa TANESCO. Na nimwambie tu Mheshimiwa Mabula nimpongeze sana hivi sasa TANESCO wanapeleka umeme katika kijiji cha Lwanima na wakimaliza Lwanima wanakwenda Kanema, pamoja na Bukaga, Nyakwagwe watapeleka. Pia watapeleka mpaka Kigogo pamoja Isebanda na wakimaliza Isebanda Mheshimiwa wanakwenda pia kwenye kijiji cha Kigodo pamoja Nyangwi pamoja na mtaa wako wa Kagera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimpe uhakika Mheshimiwa Mabula kwamba hadi kufika mwezi Juni ambapo mradi unakamilika wananchi wote wa vijiji vyote vinane, umbali wa kilometa 9.2 utakuwa umefikishiwa umeme na Mwanza itakuwa inapata umeme wa uhakikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swala lake la pili, ni kweli yako maeneo ambayo yako mjini na visiwani na vijiji. Tuna mradi wa (Peri-urban) ambao Jiji la Mwanza katika maeneo ya Kishiri, Buhongwa Pamoja na Kata za Lwanima pia ziko kwenye mpango huo. Kwa hiyo, watapelekewa kupitia mradi wa (Peri-urban) lakini pamoja na mradi wa Densification utakaoanza Julai mwaka huu.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue nafasi hii nimpongeze Naibu Waziri pamoja na Waziri husika kwa kazi nzuri ambayo mnafanya ya kuhakikisha wananchi wanapata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri aliwahi kufika baadhi ya vijiji kikiwemo Kijiji cha Kihesa Mgagao na umeme tayari umeshafika. Naomba awaondoe wasiwasi wananchi wa sehemu umeme umefika hasa vitongoji kwamba umeme watapata au hawatapata?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Kata za Ukwega, Kising’a, Nyanzwa, Udekwa na Winome hawajapata umeme haujapimwa kabisa. Naomba niulize ni lini wataenda kupimiwa ili nao wawe na uhakika wa kuingia kwenye nchi mpya ya viwanda?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwa kweli mradi wa REA III unaendelea vizuri na umeshaanza katika mikoa yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwamoto, napenda kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mwamoto anavyofuatilia masuala ya umeme katika Jimbo lake la Kilolo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nilifika katika Jimbo la Mheshimiwa Mwamoto na kijiji cha Nghuruwe pamoja na Kihesa Mgagao kulikuwa na changamoto kubwa sana. Kijiji cha Nghuruwe kilishapata umeme na sasa wanaendelea kupeleka umeme katika Kijiji cha Kihesa Mgagao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mwamoto kabla ya mwezi huu kuisha vitongoji vyote vya Kijiji cha Kihesa Mgagao vitakuwa vimeshawashwa umeme. Kadhalika bado vitongoji vyake saba katika maeneo ya karibu na Kihesa Mgagao, navyo tutavitembelea wiki ijayo namhakikishia kwamba na vyenyewe vitapata umeme kabla ya mwisho wa mwezi ujao. Nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. JUMA S. NKAMIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali moja tu la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Chemba kwenye Kata za Kidoka, Jangalo na Msaada pamoja na maeneo ya vijiji vyake, kumekuwa na nyaya za umeme kwa muda mrefu lakini tatizo lililopo sasa ni kuwasha tu. Je, Serikali inanipa majibu gani ya uhakika kwamba ni lini maeneo haya yatapelekewa transfoma ili kuwasha umeme katika maeneo hayo?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Nkamia anavyofuatilia masuala ya umeme katika Jimbo lake la Chemba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpe taarifa Mheshimiwa Nkamia, nivyoongea hivi sasa transfoma tatu zinakwenda katika Kijiji cha Kidoka kwa ajili ya kuwasha umeme, lakini kesho pia wataendelea kupeleka nguzo pamoja na transfoma na nyaya katika Kijiji cha Msaada. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Jangalo, namwomba Mheshimiwa Mbunge tushirikiane baada ya vijiji hivi kuwashwa tutaendelea na Kijiji hicho. Wakati kazi hizo zinavyoendelea kule Kwa Mtoro nimhakikishie Mheshimwa Mbunge yapo magenge sita yanafanya kazi hivi sasa ili na yenyewe kabla ya mwisho wa mwezi wa kumi iweze kuwashiwa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Nkamia anavyoshirikiana na Serikali. Ahsante.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu pia niendelee kumpongeza Waziri Kalemani na Naibu pamoja na timu yake kwa kutuma wataalam kuja ku-survey katika Kata za Kwekanga, Mbwei, Migambo, Nguli, Lushoto, Magamba na Mlola.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, je, pamoja na ku-survey kata zote hizo pamoja na alilozitaja, ni lini sasa wananchi wangu watakuja kupimiwa hawa ili waweze kupata umeme kwani umeme ni huduma ambayo walikuwa wanaisubiri kwa muda mrefu sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mkandarasi aliyepewa kazi ya kujenga umeme katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto tokea mwaka jana mpaka leo hii amejenga kitongoji kimoja tu ambacho ni cha Magamba Mabughai. Hii inaonyesha uchelewaji mkubwa sana, je, Serikali haioni sasa kuwa kuna haja ya kubadilisha mkandarasi huyu kuweka mkandarasi mwingine ambaye anaendana na kasi ya hapa kazi tu?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Shekilindi anavyofuatilia masuala ya umeme katika Jimbo lake la Lushoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunakubali kupokea pongezi kwa kazi nzuri zinazofanywa na sehemu nyingine ya mkandarasi lakini zipo changamoto kweli kwa mkandarasi na nimeongea na Mheshimiwa Mbunge. Kwanza nilikuwa nimempa vijiji vinne tu kati ya vijiji kumi na mbili, nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwa niaba ya wananchi wa Lushoto tumemuongezea vijiji vingine vinane vipya ambavyo vimeshafanyiwa survey na mkandarasi anaanza kuvifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu lini vitapelekewa umeme, tunapoongea hapa mkandarasi ameshaweka magenge mawili, anaendelea na usambazaji wa nguzo pamoja na kufunga nyaya katika Kijiji cha Magamba pamoja na Mabughai. Kwa hiyo, ni matarajio yetu kwamba ndani ya mwezi huu wataviwasha vijiji hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la pilli la uwezo wa mkandarasi, ni kweli mkandarasi huyu alianza kwa kususasua lakini tumeshakaa naye na ameshaweka magenge kumi na mawili kwenye Jimbo la Mheshimiwa Mbunge ni matarajio yetu mbali ya kumbadilisha tutamsimamia, tutamshinikiza, tutahakikisha kwamba anafanya kazi na anakamilisha ndani ya wakati.
MHE. RASHID R. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Mimi naona wivu wenzangu wanapotoa pongezi kwamba maeneo yao umeme umeshapatikana, sasa mimi nina masikitiko makubwa kwamba bado katika Jimbo la Mlalo, Halmashauri hiyohiyo ya Lushoto, kata nne bado umeme haujawaka katika Kata za Mbalamo, Shagayu, Mbalu na Hemtoe. Barua ya kutoka REA kwenda kwa mkandarasi imetoka tangu mwaka jana. Nataka Mheshimiwa Waziri anipe commitment ni lini katika kata hizi na zenyewe umeme utawaka katika Jimbo la Mlalo, Halmashauri ya Lushoto?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Shangazi kwa maswali yake mazuri na kweli naungana na yeye kwamba kati ya maeneo ambayo mkandarasi alikuwa hajaanza kazi rasmi ni pamoja na Jimbo la Mheshimiwa Shangazi. Tunapoongea hapa na leo asubuhi tumeongea na Mheshimiwa Shangazi na mkandarasi ameshapeleka makundi manne, ni matarajio yetu atafanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimuahidi Mheshimiwa Shangazi kwa niaba ya wananchi wake, mimi baada ya Bunge hili kuisha Mheshimiwa Shangazi tutafuatana mimi na naye tutakwenda kusimamia mguu kwa mguu mpaka vijiji vyake vyote ambavyo havijapatiwa umeme sasa vitapatiwa umeme. Awape uhakika wananchi wake kwamba Serikali hii haina mchezo kwenye suala la umeme vijijini.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana kuniruhusu niulize hili la nyongeza, lakini kwanza nianze na shukurani kubwa sana, Mheshimiwa Waziri wa Nishati alikuja jimboni kwangu kuzindua REA III. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri kwa nini mkandarasi hajaanza kazi kwenye barabara ile ya kuja nyumbani kwangu, kijiji cha kwetu Kasenga, Majengo, Ikongolo, Kanyenye na Nzubuka?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Maige kwa swali lake la nyongeza. Kwanza nikubaliane na Mheshimiwa Maige, ameshafanya vijiji kumi na viwili kwenye jimbo lake lakini vijiji vya barabara ndiyo anaendelea navyo. Kwa hiyo, ni shauku ya Mheshimiwa Maige na wananchi kwamba vijiji vyote vingepatiwa umeme kwa siku moja. Nimhakikishie Mheshimiwa Maige kwamba hivi sasa anaendelea na Kijiji cha Lipogolo na kuna Kitongoji kinaitwa Kwa Muni ndipo anakosimika nguzo. Kwa hiyo, niungane na Mheshimiwa Mbunge kwamba ameshamaliza vijiji vya ndani sasa ameanza kufanya kazi katika vijiji vya kandokando mwa barabara. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Maige vijiji vyake kumi na moja vilivyobaki, vyote vitapelekewa umeme katika round hii ya kwanza.
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Tarehe 11 Julai, 2017, narudia tarehe 13 Julai, 2017 Mheshimiwa Waziri alikuja Nyamatala kuzindua umeme Kimkoa na uzinduzi ulifanyika katika Kijiji cha Nyamatala hadi leo ni kijiji kimoja tu ambacho kimeshawashwa umeme lakini kisingizio wanasema hakuna nyaya, nguzo na transfoma. Naomba majibu ya Serikali, hivi vijiji ambavyo vilikuwa vimepangwa kuwashwa umeme vitawashwa lini?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Ndassa na kwa kweli niseme tu katika Mkoa mzima wa Mwanza nitoe marekebisho kidogo ya hoja ya Mheshimiwa Ndasa, ni vijiji 21 tayari vimeshawashwa umeme siyo kijiji kimoja. Ni kweli kabisa katika jimbo lake Kijiji cha Nyamatala ambapo tulifanya uzinduzi tayari kimeshawashwa umeme na sasa wanaendelea na kijiji kinachofanya kwenda Sangabuye. Nikubaliane na Mheshimiwa Ndassa kwamba speed ya mkandarasi haikuwa nzuri, lakini tangu wiki iliyopita ameshaleta nguzo 500 katika jimbo lake ni matarajio yetu kwamba sasa speed itaongezeka. Nimwombe Mheshimiwa Ndassa tushikiriane atuletee maeneo yenye changamoto ili kazi iianze kutekelezwa haraka iwezekanavyo.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa wananchi wa Kata ya Maji Moto wameanza kuwekeza kuitikia kauli mbiu ya viwanda; na kwa kuwa hawana umeme wa uhakika; na kwa kuwa, REA Awamu ya Tatu, round ya kwanza haijulikani itaanza kutekelezwa lini katika Jimbo la Kavuu, je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kuharakisha hizi tafiti zao za geothermal kwa ajili ya kuwapatia wananchi wa Maji Moto umeme? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa vijiji vya Kibaoni, Usevya, Ilalangulu na Manga vimefikiwa na umeme unaotoka Sumbawanga, lakini kumekuwa na tatizo kubwa la kukatika kwa umeme katika maeneo hayo na kufanya wananchi katika Kata ya Kibaoni kupata hasara sana kutokana na kukatikakatika kwa umeme. Je, Serikali inawaeleza nini wananchi waliopata umeme huu ambao ni wa Kata ya Kibaoni kupata umeme wa uhakika ambao hauwatii hasara? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kushukuru maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kikwembe, lakini kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa katika Mkoa mzima wa Katavi na hasa Jimbo la Mheshimiwa Dkt. Kikwembe lina shida na kero za umeme. Katika maswali yake ya msingi mawili, la kwanza ni geothermal. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge, kati ya maeneo ambayo kwa kweli yanafanyiwa tafiti za kutosha katika upande wa geothermal ni pamoja na eneo la Maji Moto katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo 50 ambayo tunatarajia kuyafanyia upembuzi yakinifu kwa ajili ya kujua mashapo ya geothermal ni pamoja na Jimbo lake. Hivi sasa TGDC wanaendelea na kazi hiyo na mwaka huu tumetenga shilingi bilioni 20 kwa ajili ya kazi hiyo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Kikwembe nampongeza sana kwa hoja hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na umeme wa uhakika katika maeneo ya Mheshimiwa Mbunge, Katavi pamoja na Sumbawanga, Serikali imeanza utaratibu wa kujenga njia kuu ya kusafirisha umeme wa kilovoti 400. Katika maeneo ambayo tutayapatia kipaumbele sana ni pamoja na Jimbo la Kavuu ambapo maeneo ya Maji Moto ni maeneo ya kibiashara, kwa hiyo, njia kuu za kusafirisha umeme zitakamilika. na tumetenga shilingi bilioni 664 kwa ajili ya kazi hiyo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Kikwembe nampongeza sana, lakini Serikali inalifanyia kazi. Ni matarajio yetu kuanzia Januari miundombinu inaanza kujengwa.
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ujenzi wa miradi ya umeme awamu ya pili na awamu ya tatu bado utekelezaji wake hauendi kasi kama ilivyopangwa hasa katika Mkoa wa Rukwa, Jimbo la Kwela na tatizo kubwa ikiwa ni upatikanaji wa nguzo. Mkoa wa Rukwa unahitaji nguzo 13,000. Pamoja na jitihada zote, ni nguzo 350 tu zilizopatikana. Je, ni lini Serikali itatatua tatizo hilo ili miradi ya umeme iweze kutekelezwa haraka?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge na kweli nilitembelea eneo lake. Nimhakikishie tu kwamba kero ya nguzo kwa sasa kimsingi haipo. Mwanzoni mwa mwaka 2017 tulisitisha kuingiza nguzo kutoka nje ambapo ndiyo lilikuwa tatizo la Wizara kwa muda mrefu. Waagizaji wa nguzo walikuwa wanachukua miezi sita hadi nane kufikisha hapa nchini, hivi sasa nguzo zinapatikana. Mahitaji yetu ya nguzo kwa mwaka ni 200,800 wakati nguzo zinazopatikana kwa wazalishaji wa ndani ni nguzo 2,000,872. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge miradi hii itatekelezeka kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimetembelea Jimbo la Mheshimiwa Mbunge na nampongeza sana anavyohangaikia maendeleo ya wananchi wake. Ni kweli mkandarasi anasuasua na jana tumemwelekeza, hivi sasa anaendelea katika Kijiji cha Maendeleo ili kusudi aanze kuwapatia wananchi umeme. Kwa hiyo, tunampongeza sana Mheshimiwa Mbunge lakini suala la nguzo hivi sasa siyo kero kubwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kitunda, Mvute, Mbondole, Nzasa na Iyongwa kote huko kuna sekondari. Maeneo yote haya ambayo nimeyataja hayana umeme. Naomba nijue ni lini maeneo haya ya umma yenye zahanati, shule na wananchi watapelekewa umeme wa uhakika? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waitara. Mimi kwanza ni mpiga kura wake katika Jimbo lake, naelewa sana maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti ni kweli kabisa maeneo ya Mbondole na maeneo mengi sana ya Chanika hayana umeme, lakini maeneo yote 27 yameingia kwenye Mpango mahususi wa Peri-Urban ambao utekelezaji wake umeshaanza. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge utekelezaji huu unaanza mwezi Julai na utakamilika mwezi Machi mwakani. Kwa hiyo, ni matarajio yetu ndani ya miezi mitano vijiji vyote vitakuwa vimeshapata umeme maeneo ya Mbondole.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa nami niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme unaotokana na joto ardhi ama geothermal ni endelevu na sustainable ama renewable na Serikali ingeweza kutumia vyanzo vyote tungepata zaidi ya Megawati 5,000. Je, ni lini Serikali itaweza kukamilisha mradi wake ambao ilikuwa inaendelea kuufanya wa kuchoronga visima katika Ziwa Ngosi lililopo Wilayani Rungwe pamoja na Mto Mbaka uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali zuri. Kusema ukweli kati ya maeneo ambayo tunayafanyia upembuzi yakinifu kwa ajili ya kujua mashapo ya geothermal, yako zaidi ya 50. Tunachofanya sasa hivi, tunapitia marejeo ya takwimu sahihi katika Ziwa Ngosi ambao liko Mbozi, maeneo ya Katavi pamoja na Rukwa. Tathmini za awali zinaonesha kwamba mashapo yaliyopo ya geothermal yanaweza kutupa jumla ya Megawati 5,000 kwa wakati mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa tunakwenda hatua kwa hatua, tunataka kuanza Megawati 20 hadi Megawati 100. Kwa hiyo, ni matarajio yetu kwamba ndani ya miaka hii miwili tutakuwa tumeshapata mashapo sahihi ili tuanze sasa na Megawati 100 kwa ajili ya geothermal.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika Mradi wa REA III kuna Kitengo kimeanzishwa kinaitwa Peri-urban katika Halmashauri ambazo bado zina maeneo ya vijiji na vitongoji. Je, ni lini kitengo hiki kitaanza kufanya kazi katika Halmashauri zetu kwenye Kata za Kilare, Mzizima, Pongwe, Marungu na Maweni ili tuweze kupata huduma hii ya umeme wa REA III?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimeeleza katika ufafanuzi wangu uliotangulia, ni kweli tunatekeleza miradi miwili kwa mijini. Uko mradi wa urbanisation unaotekelezwa na TANESCO lakini uko mradi wa Peri-urban ambao unatekelezwa kimtindo wa REA, ingawa katika mitaa ya mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mheshimiwa Mbunge kule Tanga Mjini yako maeneo 17 ambayo tumeshaainisha ikiwemo na Izizima pamoja na Majani Mapana. Utekelezaji umeanza kufanyika, ndani ya miezi sita ni matarajio yetu utakamilika na maeneo yake yataanza kupata umeme kwa utaratibu wa Peri-urban.
MHE. DANIEL K. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwulize Mheshimkiwa Waziri, Mikoa ya Katavi na Kigoma, REA III haijaanza kwa sababu ya migogoro iliyoko Mahakamani, lakini taarifa tulizonazo ni kwamba ruling imeshatoka. Ni lini sasa mkandarasi ataanza kazi katika Mikoa ya Kigoma na Katavi?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Nzanzugwanko. Ni kweli kabisa Mikoa miwili ya Katavi na Kigoma ilikuwa na migogoro katika Mahakama zetu. Napenda kutoa taarifa mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba mgogoro huo kimsingi kwa upande wa Ujiji umetatuliwa, mgogoro uliobaki ni ile kesi ya kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe taarifa tu kwa upande wa Mkoa wa Kigoma, namshukuru sana Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ijumaa ametupa mwelekeo na sisi kuanzia Jumatano ijao, mkandarasi tunamkabidhi rasmi mkoa nzima wa Kigoma. Mkandarasi kwa upande wa Katavi tunakamilisha maandalizi ya manunuzi ili mwisho wa mwezi huu naye akabidhiwe. Ufikapo mwezi Julai, utekelezaji wa REA III kwa mikoa miwili ya Katavi na Kigoma utakuwa umeshaanza na tayari kukabidhiwa kwa wananchi.
MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Tarafa ya Ilongero iliyopo Wilaya ya Singida Vijijini ambayo iko kwenye bonde la ufa haijawahi kupata umeme tangu REA I na II na ya sasa imeanza kutekelezwa. Kuna Kituo cha Afya ambacho hawawezi kutoa huduma kwa sababu hakuna umeme. Je, ni lini sasa Serikali itawapatia umeme wananchi wale au Waziri aongozane tu nami twende kwenye Tarafa ile akashuhudie ili aweze kuwahimiza wakandarasi waweze kukamilisha umeme katika bonde lile? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mlata, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa natambua kwamba Kata ya Ilongero iko kwenye mpango wa upelekaji umeme katika awamu inayoendelea. Hivi sasa mkandarasi ameshakaribia maeneo yale, ametoka Marendi kwa Mheshimiwa Mwigulu na wiki ijayo atakwenda Ilongero ambapo kuna Kituo cha Afya. Kwa hiyo, nimpe uhakika Mheshimiwa Mlata kwamba atafika kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuongezana na Mheshimiwa Mlata, mimi sina wasiwasi, kama kawaida yangu nitaambatana na Mheshimiwa Mlata tukatatue kero za wananchi. Ahsante sana.
MHE. SEIF K.S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuipongeza Wizara hii ya Nishati ikiongozwa na Mheshimiwa Medard Kalemani pamoja na Mheshimiwa Subira Mgalu kwa kazi kubwa wanasozifanya kuhakikisha kwamba umeme unapatikana katika maeneo yenye shida ya umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu msingi ambalo nilitaka kujua kwa sababu tumeshaanza utelezaji wa uzambazaji wa umeme katika baadhi ya maeneo yaliyotajwa lakini tumeanza kwa kusuasua. Je, ni lini sasa kama Wizara; Mheshimiwa Waziri pamoja Mheshimiwa Naibu Waziri wataweza kuja kuona maendeleo ya mradi huu katika maeneo hayo yaliyotajwa kwa sababu uzambazaji wa umeme huo mwisho wake ni Juni, 2019? Ujio wao utasababisha msukumo kuwa mkubwa na kazi hii itafanyika kwa haraka zaidi. Je, ni lini wataweza kufika katika maeneo hayo tajwa? Ahsante.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nampongeza sana Mheshimiwa Gulamali kwa jinsi ambavyo anatupa ushirikiano katika kupeleka umeme kwenyeJimbo lake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa katika Jimbo la Gulamali mkandarasi yuko katika Kijiji cha Matinje ambacho pia ni cha wachimbaji wadogo wa madini. Nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge, wakandarasi watakapotoka Matinje wanakwenda Nsimbo na ili wafike Nsimbo ni lazima wapite Mwamala, Tambarale, Uswaya na Igoweko. Kwa hiyo, vijiji vyake ambavyo amevitaja kimsingi vitapata umeme kwa wakati mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ni lini tutakwenda tena, napenda kutumia nafasi hii kumwambia Mheshimiwa Gulamali kwamba mara baada ya Bunge tutatembelea maeneo yake kwa sababu tunataka tutembelee maeneo yote ya Mkoa wa Tabora. Mkoa wa Tabora unahitaji umeme wa nishati wa kutosha kwa sababu ni mkubwa. Kwa hiyo, tutakwenda Roya kwa Mheshimiwa Ntimizi, tutakwenda Mswaki pamoja na maeneo mengine ya Waheshimiwa Wabunge wa Tabora. Ahsante.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Wilaya ya Hanang ilipata vijiji vichache sana awamu ya kwanza ya REA na awamu ya pili. Hii awamu ya tatu Mheshimiwa Waziri ameniahidi atanipa vijiji vingi lakini vile tulivyokubaliana ameacha Gocho, Dumbeta, Gisambalang’ na Getasam. Mheshimiwa Waziri amesema atakwenda na mimi sasa anaahidi kila mmoja, sijui kama atapata nafasi ya kwenda na mama yake. Ahsante. (Kicheko)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ni kweli nilimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba nitakwenda Hanang, lakini kabla sijaenda Hanang tulimpa vijiji 47 vya kuanzia na tukamwongezea vijiji vingine 12, kwa hiyo, lazima tuvitembelee. Kati ya vijiji ambavyo tumeviongeza ni pamoja na Gocha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwahakikishie wananchi wa Hanang mbali tu na kuongozana na Mheshimiwa Mbunge lakini nitawatuma wakandarasi waanze kufanya kazi hizo ili wakati tunakwenda, tunakwenda kuwasha na wala siyo kukagua peke yake.
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli REA III ni vijiji 10 tu kati ya 42 ndivyo vimewekwa kwenye mpango. Je, ni lini Serikali itaongeza vijiji vingine katika REA III katika Halmashauri yetu ya Wilaya ya Monduli?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeze Mheshimiwa Mbunge. Tumekaa na Mheshimiwa Mbunge wiki iliyopita. Ni kweli kabisa tulipopitia katika Jimbo la Monduli tulikuta ni vijiji 10 tu ambavyo tumevipangia umeme. Baada ya kufanya mapitio kwa nchi nzima, tumeongeza vijiji 1,442 na vijiji 12 vya Mheshimiwa Mbunge wa Monduli vimo. Kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa wazo lake zuri lakini tumefanya mapitio na tumeongeza vijiji zaidi ya 1,542 kwa nchi mzima. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge maeneo yote ambayo tulikuwa tumeyaruka hivi sasa kwa kiasi kikubwa tumeyaingiza ili nao wapelekewe umeme kwa pamoja.
MHE. HASNA S.K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni timu ikiongozwa na Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kigoma walienda Tarafa ya Nguruka kukagua vijiji vyote vitakavyopatiwa umeme REA III lakini hadi leo hii tunavyoongea, mkandarasi alikuwa afike tarehe 2 Juni, 2018 hajakanyaga kwenye vijiji hivyo ambavyo vinatakiwa vipate umeme kwenye Tarafa yangu ya Nguruka. Je, ni lini sasa mkandarasi atafika na kuanza kazi kuingiza umeme kwenye vijiji vyangu vya Tarafa ya Nguruka?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati namjibu Mheshimiwa Nsanzugwanko nimesema, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge anavyofuatilia maeneo hayo. Jumatano ijayo mkandarasi kwa Mkoa wa Kigoma tunamkabidhi site nasi tutafuatilia utekelezaji wake. Nampongeza Mheshimiwa Mbunge wa Uvinza, eneo la Nguruka litakuwemo kwenye mpango huu pamoja na eneo la Ilagala na maeneo mengine. Kwa hiyo, Jumatano ijayo Mheshimiwa Mbunge wa Uvinza mkandarasi pia atafika na maeneo yake yataanza kupelekewa umeme kwa wakati mmoja.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Kata ya Lyamkena, Kijiji cha Kiumba Makatani Kilabuni, Mheshimiwa Waziri anajua, walichomeka nguzo na baadaye wakaziondoa. Ni lini mtawarudisha nguzo zile ili wananchi waendelee kupata umeme? Nataka kauli ya Serikali. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa nilifika Jimbo la Mheshimiwa Sanga na kwa kweli nilitembelea maeneo yale, eneo la Makatani, leo asubuhi kabla sijaja hapa wamepeleka nguzo nyingine 20. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wakandarasi wako site wanaendelea na kwa vile amenikumbusha pia kesho nitamwagiza Meneja akafuatilie utekelezaji wa maeneo hayo ambayo ameyataja.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Manispaa ya Mtwara Mikindani ina mitaa mingi ambazo nguzo za umeme hazijafika na nimekuwa nikiitaja hapa Bungeni kwa muda mrefu sana, kwa mfano, Kijiji cha Mbwala Chini, Mtaa wa Naulongo, Mkunja Nguo, Kata ya Magomeni, Kata ya Ufukoni na Kata ya Mitengo maeneo mengi hayana nguzo za umeme. Nilikuwa naomba kujua kwa sababu nimeongea kwa muda mrefu ndani ya Bunge hili, kwa nini Serikali haitaki kuwapatia wananchi hawa umeme? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Maftaha, lakini kusema kwamba Serikali haitaki, siyo kweli, ukweli ni kwamba Serikali inataka kuwapelekea umeme wananchi wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Mbunge, wiki iliyopita niliongea naye, Kijiji cha Mkunja Nguo tayari mkandarasi tumeshamtuma na ameshafanya survey. Maeneo mengine ya Mbwala Chini bado wanafanya survey. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge maeneo yote ya Mtwara Mjini ambayo ameyataja yatapelekewa umeme na mara baada ya Bunge hili tutakwenda kukagua. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge vijiji 12 na mitaa nane ya Mtwara Mjini tutaipelekea umeme kupitia mradi huo unaoendelea.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa mradi wa uzambazaji wa umeme REA III katika Jimbo la Lulindi ni wa kusuasua sana na mkandarasi hadi jana alikuwa hajafunguliwa LC. Je, Mheshimiwa Waziri anataka kuwaambia nini wananchi wa Jimbo la Lulindi ambao wanasubiri kwa hamu umeme huo?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Bwanausi anavyofuatilia maendeleo ya wananchi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tumeshafanya uzinduzi kwa Mheshimiwa Bwanausi na kijiji cha Kalipinde tayari kilishawashwa umeme na baada ya kutoka Kalipinde inakwenda kata inayofuata. Ni kweli kabisa mkandarasi hatua ya kwanza alianza kwa kusuasua kwa sababu kulikuwa na masuala ya kiutawala na kiusimamizi yaliyokuwa yanaendelea. Hivi sasa naipongeza Wizara ya Fedha imeshafungua LC, advance payments zimelipwa, ni matumaini yetu sasa mkandarasi atakwenda kwa speed. Nimhakikishie Mheshimiwa Bwanausi kwamba mara baada ya Bunge tutamfuatilia mkandarasi huyu ili awashe umeme vijiji vingi kwenye jimbo lako.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niulize swali la nyongeza. Kampuni ya East Africa Fossils Limited inakamilisha kazi ambayo iliachwa na Spencon ya kupeleka umeme awamu ya pili katika Tarafa ya Nkoko, Jimbo langu la Manyoni Mashariki. Kutokana na kasi kubwa ya kampuni hii kumekuwa na uhaba mkubwa sana wa nguzo za umeme. Mpaka navyozungumza hapa wameshachimbia mashimo karibu kilomita 10 nguzo hamna, kila wanapoulizwa wanasema Mufindi imezidiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini nguzo zitapelekwa katika kampuni hii ili tuweze kukamilisha suala la umeme katika Tarafa ya Nkoko?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampa pole kwa msiba alioupata hivi karibuni lakini tunafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa sana na Mheshimiwa Mtuka na ana kata nne ambazo hatujazigusa. Mkandarasi ameagiza nguzo 2,278 na amenipa taarifa kwamba kuanzia wiki ijayo nguzo zitaanza kwenda site. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mtuka kwamba maeneo yote ya kata zake 12 na hizi nne tulizoongeza yatapelekewa umeme kwa sababu sasa nguzo zinapatikana. (Makofi)
MHE. HASNA MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa kunipa swali la nyongeza. Kwenye Vijiji vyangu vya Mwakizega, Kabeba na Lilagala tangu Awamu ya II ya REA nguzo zimeshawekwa na taratibu zote zimekamilika. Mradi ule ulitakiwa uzinduliwe mwezi wa pili mwaka jana 2017 lakini kwa masikitiko yangu makubwa Mheshimiwa Waziri umeshakuja Kigoma umepita umeenda Kibondo, wananchi wanauliza maswali, tumewekewa nguzo na transfoma tuizone? Ni lini umeme wa Kata hizi mbili za Mwakizega na Ilagala utawashwa rasmi? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mheshimiwa Mwilima kweli nilitembea naye katika maeneo yake. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge huyu kwa sababu kwanza tulienda eneo la Nguruka lililokuwa na shida kubwa tukawasha umeme Nguruka tukiwa pamoja, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo hayo ambayo ameyataja eneo la Ilagala pamoja na Nguruka huyu mkandarasi wa REA Awamu ya Tatu anyekuja kufanya kazi ni kati ya maeneo ambayo ataanzia kuyafanyia kazi na kuyawashia umeme. Kwa hiyo, nimpe tu pongezi Mheshimiwa Mbunge kwamba avute subira wakati…
...mkandarasi tunampata katika mwezi huu kama ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza, tarehe 5 Mei ataanza kazi katika maeneo hayo na maeneo yatakayowashwa ni pamoja na Ilagala pamoja na Nguruka maeneo yaliyobaki. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira tutafanya kazi pamoja.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na ninaishukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara sasa hivi mkandarasi yupo Wilayani Chunya kwa kupeleka umeme REA III, anafanya upimaji katika Vijiji vya Ifumbo, Soweto, Mawelo na vinginevyo. Kuna Kijiji kinaitwa Itumbi katika Kata ya Matundasi, kijiji hiki Serikali kupitia Wizara inajenga kituo cha mafunzo kwa wachimbaji wadogo (center of excellence) lakini Kijiji hiki hakimo kwenye Awamu namba tatu ya kupeleka umeme. Je, Serikali haiwezi kukiangalia Kijiji hiki kwa jicho la pekee na kupeleka umeme katika awamu hii ya tatu?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge katika swali lake. Kwa kweli kituo cha Matundasi pamoja na Itumbi ni kati ya maeneo ambayo yapo kwenye center of excellence kwa upande wa madini na baada ya kufanya survey Mheshimiwa Mbunge, kijiji kipo kwenye mpango sasa kwa sababu ni maeneo ya vipaumbele kwenye miradi ya maendeleo, kwa hiyo, kipo kwenye mpango wa fedha wa mwaka huu. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mbulu Vijijini lina uhaba sana wa umeme na Mheshimiwa Waziri amefika. Sasa lini atakuja kuwasha umeme katika Jimbo la Mbulu Vijijini na anafahamu kwa sababu amefika na vijiji vingi havina umeme. Atutajie tu lini atafika Jimbo la Mbulu Vijijini kuwasha umeme? Ahsante.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, vijiji vya Mheshimiwa Mbunge vya Mbulu Vijijini na Mbulu Mjini vyote vipo kwenye mpango wa REA mwaka huu.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli wananchi wanahitaji umeme tena umeme wa uhakika lakini tumekuwa na tatizo la kukatika katika kwa umeme katika Mkoa mzima wa Dar es Salaam na hasa kule Temeke; na mwaka jana Mheshimiwa Naibu Waziri alituahidi hapa kwamba kufikia Disemba 2017 tatizo la kukatika kwa umeme litakuwa limekwisha, leo ni mwezi wa nne mvua zinanyesha na umeme unakatika sana Jijini Dar es Salaam. Serikali mnatuambia nini kuhusu tatizo la kukatika kwa umeme? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge. Kwanza napenda nitoe taarifa katika Bunge lako hili, katika maeneo ya Mbagala na Gongolamboto kulikuwa na kero kubwa sana ya kukatika kwa umeme, wiki mbili zilizopita tumejenga sub - station imekamilika na kwa hiyo Mbagala sasa nina amini wanapata umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hiyo, umeme huu wa Mbagala ambao ni wa gridi naishukuru sana Serikali yetu, tumeanza sasa kuunganisha umeme wa gridi kutoka Mbagala kwenda Ikwiriri kupitia Kibiti mpaka Somanga Fungu na umeme huu wa Mbagala ambao unatoka kwenye Gridi ya Taifa ndio tunaunganisha katika Mikoa yote ya Mtwara na Lindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuanzia mwezi uliopita nitoe taarifa katika Bunge lako kwamba hata Mikoa ya Mtwara na Lindi sasa itakuwa inapata umeme wa gridi badala ya umeme wa mashine inayotumia sasa. Hizo mashine zilizopo sasa zitatumika tu kama mashine za ziada. Kwa hiyo nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa sababu inanisaidia sasa kutoa taarifa kwa wananchi wa Mbagala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kukatika kwa umeme kunatokana na sababu nyingi, sio sababu ya kuwepo kwa umeme au miundombinu, wakati mwingine ni kasoro ndogo ndogo, tunakiri kabisa zipo changamoto za maeneo machache kukatika kwa umeme katika baadhi ya nyakati za mida. Tutashirikiana na Waheshimiwa Wabunge kutatua matatizo hayo. Tunachoomba tupate taarifa inapotokea itilafu ya namna hiyo, lakini nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa wananchi wa Mbagala kwa sasa wanaendelea kupata umeme wa uhakika zaidi. (Makofi)
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, nianze kwa kuishukuru hii Wizara ya Nishati chini ya Dkt. Kalemani pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Subira kwa kazi nzuri mnayofanya, hongereni sana. Ninaomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Manispaa ya Tabora kwa kuitamka inaonekana kama hata vile vijiji vinavyozunguka ni kama vipo karibu sana, lakini vijiji vingi vipo mbali na maeneo ya mjini. Huu mradi ambao unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa ajili ya kusambaza umeme unaonekana unasuasua maeneo mengi ya vijiji hivi ambavyo vimetajwa. Kama kuna uwezekano naomba Serikali iangalie uwezekano wa kuingiza vijiji hivyo kwenye mradi huu wa REA III ili viweze kupatiwa umeme haraka, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nilipata taarifa kwamba Mheshimiwa Waziri anaweza kufanya ziara Tabora wiki ijayo sehemu za Urambo, kwa kuwa Tumbi hii ninayoizungumzia ipo njiani, anapokuwa Mheshimiwa Waziri anaelekea Urambo lazima atapita Tumbi pale. Je, Waziri yupo tayari kusimama maeneo yale hata kwa dakika chache ili asikilize kero za wananchi pale zinazohusiana na hilo suala la usambazaji umeme?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Mwakasaka, kwanza hilo la pili nipo tayari kusimama, nitasimama na nitafanya kazi pale, Mheshimiwa Mbunge nakupongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na vijiji kweli kabisa Jimbo la Tabora kwanza lina kata 29 na kata 15 zipo mjini na kata 14 kimsingi zipo vijijini ingawa ni za Manispaa. Nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge kwa niaba ya wananchi wake zile kata 14 ambazo kimsingi zipo vijijini tumezipelekea kwenye miradi ya REA kwenye mpango wa Peri-Urban. Kwa hiyo, wananchi wake wataendelea kupata umeme kama kawaida. (Makofi)
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na nimpongeze pia Waziri mwenye dhamana kwa namna ambavyo waliweza kutembelea Jimbo langu la Busokelo na kufanya mikutano mingi na wananchi wale.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa mradi huu umechukua muda mrefu, ni zaidi ya miaka 21 sasa tangu upembuzi yakinifu ufanyike, je, Serikali haioni umuhimu wa kuharakisha mradi huu ili ifikapo 2022 uweze kukamilika badala ya mwaka ambao Mheshimiwa Waziri ameusema?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa umeme wa jotoardhi ni umeme endelevu kwa maana ya renewable na tumeona katika nchi yetu na tafiti zimeonyesha tunaweza kupata megawatts zaidi ya 5,000 kwa vyanzo vyote ambavyo vimeainishwa kwa nchi nzima ya Tanzania. Je, Serikali ina mpango gani wa kuviendeleza vyanzo hivyo ili Tanzania ifikapo 2025 iwe ni nchi ya uchumi wa kati?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake ya awali ambayo ametoa ufafanuzi mzuri sana katika mradi wa kuzalisha umeme wa jotoardhi. Sambamba na shukrani kwa Naibu Waziri wangu, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge Mwakibete kwa anavyofuatilia masuala ya rasilimali ya jotoardhi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, katika maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwakibete, la kwanza amesema imechukua muda mrefu kufanya utafiti kwa takribani miaka 21. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge lakini niwape taarifa Watanzania kwamba katika hatua za utekelezaji wa upembuzi yakinifu, mradi ambao umeenda kwa kasi katika miradi ya jotoardhi ni pamoja na mradi huu wa Ngozi ambao utatuzalishia MW 20.

Mheshimiwa Spika, kwa kawaida miradi ya jotoardhi, upembuzi yakinifu huchukua takribani miaka 25 - 40. Kwa hatua hii, ndiyo maana tunasema tumekwenda kwa kasi na tuna matumaini ya kukamilisha mapema mwaka uliotajwa wa 2023 tutapata MW 30.

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili, nchi yetu ina rasilimali nyingi sana na madini ya jotoardhi (geothermal) kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge. Rasilimali tuliyonayo inaweza kutuzalishia megawatt zaidi ya 5,000, ingawa kwa sasa tathmini zinavyoonyesha tunaweza tukaanza kuzalisha MW 200 kwa kuanzia ifikapo miaka mitano ijayo. Tutaanza na MW 30 ambayo itatoka kwenye eneo la Ngozi kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Spika, lakini nieleze tu kidogo, niwapongeze sana wananchi wa Mbozi na wananchi wengine wa maeneo yanayozunguka mradi huu kwa sababu wametupa ushirikiano mkubwa wa kufanya tathmini. Hivi sasa tunaendelea na kufanya tathmini ya maeneo mengine mengi nchini ikiwemo eneo la Majimoto kule Katavi ambayo nayo itatuzalishia megawatt za uhakika. Kwenye mradi wetu tutapata MW 5,000 miaka kumi au ishirini ijayo lakini itakuwa ni umeme wa uhakika ambao uta-stabilize sana upatikanaji wa umeme hapa nchini. Ahsanteni sana.
MHE. HUSSEIN M. BASHE: Mheshimiwa Spika, nashukuru na naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Pamoja na shukurani za dhati kwa niaba ya wananchi wa Nzega kwa kutatua tatizo la umeme katika chanzo cha maji katika Mji wa Nzega, Wizara ya Nishati nilitaka tu nipate kauli ya Waziri ama Naibu Waziri. Mradi wa REA Phase III katika Jimbo la Nzega unasuasua; mkandarasi ameonekana site mara moja alipokuwepo Waziri na kuweka nguzo. Hata hivyo mpaka sasa nguzo zile zimesimama vile vile na maeneo ambayo aliahidi kuwasha umeme mpaka leo hayajawashwa. Ni lini mradi huu utapata speed ambayo wananchi wa Jimbo la Nzega wanaitarajia?(Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Bashe anavyotupa ushirikiano kati ka kupeleka umeme kwenye Jimbo lake.
Mheshimiwa Spika, nitangulie tu kusema, kwa sasa Wakandarasi katika Jimbo la Nzega wanafanya kazi katika vijiji 11 na katika Jimbo la Mheshimiwa Bashe wanakamilisha kazi katika maeneo ya Migua karibu kabisa na Ziba katika Jimbo la Igunga. Kwa hiyo nimwambie tu Mheshimiwa Bashe kwamba vile vifaa vyote ambavyo vilikuwa vinasubiriwa kuja ikiwepo nyaya na transfoma vimeshafika tangu juzi; na sasa hivi katika Jimbo la Mheshimiwa Bashe kuna transifoma 12 zimewekwa juzi. kwa hiyo nimpe uhakika Mheshimiwa Bashe na wananchi wa Nzega kwamba kazi ya kupeleka umeme kwenye vijiji 32 katika Jimbo lake litakamilika kabla ya mwezi Julai mwaka ujao. (Makofi)
MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nina swali fupi sana la nyongeza kuhusu huu mradi wa Northwest Grid kutoka Mbeya – Tunduma mpaka Nyakanazi. Bunge hili tulishauri kwamba kwa sababu njia ni ndefu, takribani kilometa 2500, tulishauri kwamba angalau mkandarasi awe zaidi ya mmoja ili mmoja aweze kuanzia Kigoma kwenda Nyakanazi wakati mwingine anatoka Tunduma kuja Mpanda mpaka Kigoma. Maadam fedha zimepatikana sasa, je, ushauri huo umezingatiwa? Vinginevyo kitakachotokea ni kwamba itakuwa ni kazi ya muda mrefu kwa sababu njia ni ndefu sana. Ahsante sana.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, pia nimpongeze Mheshimiwa Nsanzugwanko kwa swali hili muhimu sana katika ukanda wa Kusini na hasa Magharibi mwa upande wa Kigoma, Katavi pamoja na Iringa.
Mheshimiwa Spika, kwanza katika mradi huu ni kweli kwamba tumepata fedha kutoka Benki ya Dunia jumla dola milioni 455 ambayo itatekeleza mradi wa kusafirisha umeme mkubwa wa kilovott 400 kutoka Iringa kupita Mbeya hadi Sumbawanga. Taratibu za kuanza mradi katika portion hii zimeshaanza, ujenzi rasmi utaanza mwezi Machi mwakani.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo wanashauri Waheshimiwa Wabunge, na yeye akiwemo, mradi huu ni mrefu sana, una umbali wa kilometa 2872 ambapo tumeugawa katika portion tatu. Kutoka Iringa, Sumbawanga hadi Tunduma ni portion moja ambayo tutaanza mwezi Machi na kuanzia Mei utaanza kuanzia Sumbawanga hadi Mpanda na kutoka Mpanda hadi Nyakanazi.
Mheshimiwa Spika, lakini mbali na mradi huo, tumeona wananchi wa Katavi na Kigoma watachelewa sana kupata umeme wa gridi tumeanza kujenga mradi mwingine wa kutoka Ipole, Sikonge kupeleka kilovott 132 Katavi ili kurahisisha wananchi wa maeneo ya katikati kupata umeme wa grid mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Spika, lakini vile vile mradi mwingine wa nne unaopeleka umeme wa grid katika Mkoa wa Kigoma ni pamoja na ule wa kutoka Tabora kupita Urambo hadi Kaliua umbali wa kilometa 370 nao uaanza kujengwa mwezi Februari mwaka ujao. Kwa hiyo ni matumaini yetu wananchi wa Katavi na Kigoma wataanza kupata umeme wa grid kuanzia mwezi Oktoba mwakani.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, pia nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Kwanza nitoe shukrani za dhati kwa ziara ya Mheshimiwa Waziri, alipokuja Jimboni kwangu nilimweleza shida ya umeme katika bwawa la maji na sasa tayari transforma imefungwa na umeme unawaka. Nashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina masikitiko kidogo, REA awamu ya kwanza, ya pili na ya tatu katika Jimbo la Igalula lenye vijiji takriban 98 ni vijiji sita tu ndivyo vimepata umeme katika Jimbo la Igalula; na katika vijiji hivyo sita ni baadhi tu ya maeneo ya vijiji ambavyo vimepata umeme maeneo mengine hayajapata umeme. Kwa mfano, katika Kata ya Igalula, yenye vijiji sita ni kijiji kimoja tu ndiyo kimepata umeme. Je, Serikali haioni usambazaji wa umeme katika Jimbo la Igalula unasuasua na hauridhishi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mheshimiwa Waziri alikuja kwenye ziara katika Jimbo la Igalula, alitembelea Kata ya Miswaki, Loya na Lutende. Alijionea hali ya uzalishaji mpunga mkubwa katika eneo lile na halmashauri ilivyowekeza mashine za kisasa za kukoboa mpunga katika eneo lile; akaahidi kupeleka umeme katika kata hizo tatu za Lutende, Loya na Miswaki. Je, ni lini zoezi hili litakamilika na wananchi wa kule waweze kupata umeme? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, kama ambavyo ameeleza kwenye kusoma majibu ya Mheshimiwa Mbunge. Pili, nimpongeze sana Mheshimwa Ntimizi anavyofuatilia maendeleo ya nishati katika Jimbo lake. Sambamba na hilo nipokee shukrani alizotupatia kwa kupeleka maji katika Kata yake ya Igalula na wananchi zaidi ya 1,000 wanapata maji kupitia mradi huo.
Mheshimiwa Spika, na sasa nijielekeze katika maswali yake mawili ya nyongeza. Swali la kwanza ni kuhusiana na vijiji vitano vya Igalula. Nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge, hivi mkandarasi sasa hivi yuko katika kijiji cha pili katika Kata ya Igalula na vijiji vyote vitano katika Kata ya Igalula vitapelekewa umeme kupitia mradi huu unaoendelea hivi sasa.
Mheshimiwa Spika, suala la pili; Mheshimiwa Mbunge ni kweli nilitembelea kata ya Lutende, Miswaki pamoja na Loya. Ni maeneo ambayo yana makazi mengi na yana uchumi mzuri. Nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge, Mradi huu wa kupeleka umeme katika kata hizo tatu tutautoa katika Jimbo la Manonga, Kata ya Simbo na mkandarasi ameshaanza kazi; ingawa kutoka Simbo kuelekea Lutende ni kilometa 20 lakini wakandarasi wameshaanza kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, kutoka Lutende kwenda Miswaki ni kilometa 27, kutoka Miswaki kwenda Rorya ni kilometa 13 na kuna jumla ya vijiji 14. Nimpe taarifa kwamba transfoma 17 zimeshapelekwa katika kata hizo tatu na wananchi wa kata hizo watapatiwa umeme ndani ya miezi sita ijayo. (Makofi)
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake, natambua kazi nzuri wanayoifanya. Ni kweli kabisa kwamba, Nguruka pale tulitoa ekari 30 kwa ajili ya ujenzi wa hiyo substation, lakini Meneja wa TANESCO alienda, hadi leo utekelezaji haujaonekana. Sambamba na hilo mwaka jana mwezi wa Nane mkandarasi alifanya survey katika Kata ya Nguruka, Kata ya Mtego wa Noti, Kata ya Itebula, Kata ya Mganza, Kata ya Sunuka, sambamba na vijiji ambavyo vilisahaulika kwenye Mradi wa REA awamu ya pili. Swali langu. Je, Wizara hii mnawaambia nini wananchi wa kata hizi, ni lini mkandarasi atapeleka materials ili sasa utekelezaji wa REA Awamu ya Tatu uweze kuanza rasmi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, natambua kwamba, kuna mazungumzo baina ya mwekezaji kutoka Marekani pamoja na Wizara ya Nishati kufua umeme kwenye Mto Ruwegere uliopo kwenye Kijiji cha Mgambazi, Kata ya Igalula. Sasa wananchi wa Kata ya Buhingu, Kata ya Herembe, Kata ya Sigunga na Kata ya Igalula yenyewe wanataka kusikia Kauli ya Serikali. Ni lini sasa mkandarasi huyu ataanza rasmi kutekeleza uzalishaji wa kufua umeme kwenye Mto Ruwegere, megawati tano? Nataka majibu ya Serikali.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa ufafanuzi wa swali la kwanza la Mheshimiwa Mbunge kwa vile ambavyo amelieleza. Napenda pia nimpongeze Mheshimiwa Mbunge jinsi ambavyo anafuatilia masuala ya nishati kwa wananchi wa Uvinza. Baada ya kusema hayo napenda sasa nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hasna Mwilima, Mbunge wa Maeneo ya Uvinza, Jimbo la Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kabisa mkandarasi alipata kazi dakika za mwisho ukilinganisha na mikoa mingine. Hata hivyo, napenda nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge na jinsi anavyofuatilia, hivi sasa mkandarasi ameshaanza ku-order materials na ataanza kupeleka materials kwenye eneo la Uvinza kuanzia tarehe 22 mwezi huu. Maeneo yatakayopelekewa ni pamoja na Kazuramimba, Ilagala, Kajeje kuelekea Sunuka, lakini pia maeneo ya Nguruka na katika maeneo mengine ya Uvinza ambayo hayajapelekewa nishati ya umeme. Maeneo yote 27 ya kwa Mheshimiwa Mbunge yatapelekewa umeme ndani ya miezi tisa ijayo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nimpe tu uhakika kwa wananchi wa Uvinza kwamba, mkandarasi amesha-mobilise material na kuanzia tarehe 22 mwezi huu ujenzi utaanza rasmi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la pili, ni kweli kulikuwa na mkandarasi aliyetarajia kufanya survey kwa ajili ya kuzalisha umeme megawati nane katika Mto Rwegere, lakini taarifa za awali baada ya kupewa kazi na baada ya kufanya tathmini za awali inaonesha Mto Rwegere unaweza kutupatia megawati tano kutokana na maporomoko ya maji ya Mto Rwegere.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kazi inayofanyika mara baada ya kuleta taarifa mkandarasi amefanya mapitio na wataalam wetu, ni matumaini yetu kwamba, mwezi ujao atatuletea taarifa za mwisho, ili kuona kama mradi huo utakuwa na tija na kuzalisha megawati tano. Kwa hiyo, nimpe pongezi Mheshimiwa Mbunge kwamba, hiyo kazi inatushirikisha sana, inaendelea vizuri na tunaweza tukapata megawati tano mbali na megawati 45 za Mto Malagarasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, samahani kidogo niongeze kwenye mradi muhimu sana kwa Kigoma, ujenzi wa transmission line kutoka Tabora kupita Urambo kwenda mpaka Nguruka hadi Kidahwe umeshaanza. Tunatarajia mkandarasi atakamilisha kazi Februari mwakani ili wananchi wa Kigoma waweze kupata umeme wa gridi nao kutoka umeme wa gridi unaotoka Tabora wa kilovoti 120. Nimeona nilifafanue kwa sababu, sasa hivi clearance ya major substation inafanyika Urambo na wiki inayokuja itafanyika Nguruka na Kidahwe wanamalizia mwezi ujao. Hiyo ni taarifa kwa ajili ya umeme wa wananchi wa Kigoma. Ahsante sana.
MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa line inayopeleka umeme Wilaya ya Mpwapwa inahudumia pia Wilaya za Chamwino, Kongwa, Gairo na Mpwapwa yenyewe na hivi karibuni line hiyo imeongezwa Tarafa ya Mwitikila, Mpwayungu na Nagulo. Kwa hiyo, line hii imekuwa overloaded na kusababisha kukatikakatika kwa umeme katika Mji wa Mpwapwa. Je, mko tayari kujenga line mpya ya umeme kuanzia Zuzu Main Station itakayopita Kikombo Station, Kiegea mpaka Mbande ambako mtajenga substation na pale ijengwe line moja kwa moja kuelekea Mpwapwa itakayojulikana kama Mpwapwa fider?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa vijiji vya Mima, Sazima, Igoji Mbili, Isalaza, Chamanda na Iwondo tayari vinapata huduma ya umeme lakini mkandarasi aliruka Kijiji cha Igoji Moja na tatizo la sasa ni transfoma. Je, uko tayari kupeleka transfoma katika Kijiji cha Igoji Moja ili wananchi wa pale waweze kupata huduma ya umeme?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Lubeleje kwa kufuatilia masuala ya nishati kwa wananchi wa Mpwapwa, hongera sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Lubeleje la kwanza, ni kweli umeme unaokwenda Mpwapwa unatoka Zuzu ambapo ni umbali wa kilomita 120 ni mbali sana. Mpango uliopo ni kwamba sasa hivi Serikali kupitia TANESCO tumeanza utekelezaji wa kujenga line mpya ya kutoka Zuzu kupita Kikombo ambapo ni kilomita takribani 42 na kutoka Kikomo mpaka Msalato kilomita 45 lakini kwenda Mpwapwa tutatoa sasa Kikombo kupita Kiegea kutoka Kiegea tunajenga substation Mbande na pale Mbande kwenda mpaka Mpwapwa itakuwa takribani kilomita 70. Kwa hiyo, wananchi wa Mpwapwa sasa wataanza kupata umeme kutoka Mbande ambao utakuwa ni mkubwa kuweza kuwahudumia wananchi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la pili, ni kweli tumepeleka umeme kwenye vijiji takribani 32 Mpwapwa lakini viko vijiji vya Mkanana, Mbande pamoja na maeneo aliyoyataja kama Igoji Moja au Igoji Kaskazini, nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge Igoji Kaskazini au Igoji Moja wakandarasi wameanza kazi tangu juzi na kufikia Jumapili ijayo watawasha umeme na watafunga transfoma nne za kilovoti 50 na kilomita zingine mbili wataweka na kufunga transfoma mbili za kilovoti 120 na wataunganisha wateja wa awali 78 wa phase one na wateja 9 wa phase three. Kwa hiyo, Igoji itakwenda kuwashwa umeme Jumapili ijayo. Nashukuru sana.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali na natambua jitihada kubwa sana zinazofanywa na Serikali katika kuongeza uzalishaji wa umeme lakini nina swali moja tu la nyongeza. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhamasisha na kuwezesha kisera uwekezaji wa miradi midogo midogo ya uzalishaji wa umeme hususan katika maeneo ambayo hayajafikiwa na gridi ya Taifa kama vile Mkoa wa Kigoma?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri katika swali la msingi la Mheshimiwa Katimba. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia wazalishaji wadogo wadogo katika nishati kwa upande wa maeneo ambayo hayana gridi ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, Serikali kama ambavyo tumeeleza katika jibu la msingi, pamoja na kuzalisha umeme mkubwa katika maeneo mbalimbali yenye gridi ya Taifa, bado Serikali inahamaisha sana uzalishaji wa umeme mdogo mdogo katika maeneo ambayo hayajafikiwa na gridi ya Taifa. Katika maeneo ya Kigoma mathalani; wazalishaji wadogo wameshajitokeza, Kampuni ya Nexgen Solar White imeanza kuzalisha megawatts tano ambazo sasa wanafanya majadiliano na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuingiza kwenye gridi ya Taifa. Kwa hiyo ni matumaini yetu maeneo mbalimbali ya Ujiji ambayo yameshafanyiwa utafiti kwenda mpaka Kaliua kuja mpaka Mkoa wa Tabora wazalishaji wataongezeka zaidi.

Mheshimiwa Spika, katika kuongeza maelezo ya upana zaidi kwenye suala la nyongeza la Mheshimiwa Katimba ni kwamba katika maeneo ya Mkoa wa Kigoma na Uvinza ambayo hayajapitiwa na umeme wa gridi ya Taifa, hivi sasa Serikali imeanza kujenga njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa gridi ya Taifa ili Mikoa ya Kigoma na Katavi nayo ifikiwe na gridi ya Taifa. Sasa hivi ujenzi unaanzia Tabora kupitia Jionee Mwenyewe-Juhudi-Nguruka mpaka Kidawe Mchini-Kigoma, kwa hiyo, hata wazalishaji wadogo wa umeme mdogo mdogo nao wataingizwa kwenye gridi ya Taifa.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Lindi na Mtwara ni Mikoa jirani sana. Katika majibu yake ya Msingi ya Mheshimiwa Naibu Waziri amesema gesi ya Mtwara itasambazwa majumbani katika Mkoa wa Mtwara, Pwani, pamoja na Dar es Salam, Lindi wameiruka. Sasa je, ni lini Lindi watasambaza gesi hii majumbani?
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kwamba ni kweli mpango wa kwanza unaanza na Mikoa mitatu ya Dar es Salaam pamoja na Mtwara na Lindi. Kwa sasa tumeanza kusambaza Dar es Salaam na tarehe 40 mwezi huu wataanza kujenga mabomba Mtwara na tarehe 30 mwezi Mei wataanza utaratibu wa kujenga mradi wa kusambaza gesi majumbani Lindi.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Meshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, lakini niipongeze Wizara ya Nishati, Waziri wake Mheshimiwa Dkt. Kalemani na Mheshimiwa Subira, Naibu Waziri na Watendaji wake wote kwa kasi ambayo wanaionesha sasa kwenye Jimbo la Bunda. Natambua kuna Vijiji vya Nyabuzume, Tiring’ati, Bigegu, Nyaburundu, Mihingo, Rakana, Manchimweru, Nyang’aranga, Sarakwa na Tingirima, wameweka nguzo za umeme. Swali langu la kwanza hapa, ni lini sasa umeme utawaka kwenye maeneo haya kwa sababu ninapouliza swali hili sasa hivi hapa kuna akinamama zaidi ya 100 wanataka kusikiliza wamechoka na mambo ya vibatari kwenye maeneo yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kuna maeneo ya Nyamatutu, Saba-Osanza, Mmagunga, Nyamakumbo, Sanzate, Nyansirori, Saloka-Guta, Nyamuswa A. Mheshimiwa Waziri rafiki yangu Dkt. Kalemani, kutoa transfoma nane kwenye maeneo ya taasisi kama vituo vya afya, shule za msingi, sekondari survey ilishafanywa na Serikali imetumia hela pale tangu 2016, ni lini sasa zile Taasisi zitapata umeme, kuweka transfoma nane shida iko wapi?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri alivyojibu majibu mazuri kwenye swali la Mheshimiwa Mbunge Getere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge Getere anavyofuatilia masuala ya umeme katika Jimbo la Bunda Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Getere, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza amependa kujua ni lini sasa vijiji vya Bunda ambavyo vinapelekewa umeme vitapata umeme. Kwanza nianze kusema hapa tunapoongea wakandarasi wako site na hivi sasa vijiji takriban 11 wameshavifanyia kazi. Leo na jana wakandarasi wako site, Derm Electric, wanafanya kazi katika Vijiji vya Mwanchimweru, Nyanharanga, Mahanga, Lakani pamoja na Tingirima ambapo vyote watawasha umeme katika wiki inayokuja. Katika Jimbo la Mheshimiwa Getere vimebaki vijiji vitano tu vya Sarakwa, Nyabuzume, Tingirigi pamoja na vijiji anavyovitaja vitatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala lake la pili ambalo ni la msingi kabisa, maeneo ya vijiji takribani 11 yana umeme na vitongoji vyake vina umeme shida ni shule za sekondari na zahanati ambazo hazijapata umeme. Nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge wakandarasi wameshaweka design, tuna mpango wa kuongeza umeme katika vitongoji unaoanza mwezi ujao. Kwa hiyo, maeneo yote ya Shule za Msingi za Nyamatutu, Saba Osama, Nyamakumbu, Maguga, Salokikwa pamoja na Musa na Makongolai A&B vitapelekewa umeme pamoja na taasisi zake.
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa kwa Mheshimiwa Getere. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu hata wapiga kura wa Mheshimiwa Getere wako hapa ndani leo wamesikia na wanausubiri huo umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia swali hilihilo niulize kwa Mkoa mzima wa Mara, kuna Wilaya ya Rorya ambako mimi nimezaliwa, Wilaya ya Msoma Vijijini pia nilikozaliwa lakini pia kuna shangazi zangu wa Wilaya ya Serengeti na Tarime. Swali langu sasa, ni lini Serikali itapeleka huduma za umeme wa REA katika huduma za shule, zahanati, vituo vya afya kwa maeneo mengine yote yaliyobaki ya Mkoa wa Mara?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Agness, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Mara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nampongeza Mheshimiwa Mbunge Agness anavyofuatilia masuala haya ya umeme katika taasisi za umma. Napenda kusema tu kwamba mkandarasi katika Mkoa wa Mara atapeleka umeme kwenye vijiji vyote 172 vya Mkoa wa Mara pamoja na vitongoji 318 na yuko site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini cha msingi kabisa, katika Wilaya ya Rorya ameshapeleka umeme kwenye vijiji 17 na shule za sekondari 18. Katika Wilaya ya Msoma Vijijini, mkandarasi anaendelea na kazi. Niseme kwamba vijiji vyote vitapelekewa umeme kuanzia sasa na kuendelea na mwezi Juni, 2020 miradi yote itakamilika.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililoko Bunda ni la Mkoa mzima. Tumeona ufunguzi wa REA Phase II na Phase III umefanyika lakini kilichofanywa na wakandarasi ni kwenda kumwaga nguzo tu. Naomba kujua ni lini vijiji vya Kabulabula, Bugoji, Mhoji, Komoge na Kabage vitapata umeme?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Sokombi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Kijiji cha Kabulabula kimeshapelekewa umeme isipokuwa vitongoji viwili kati ya vitongoji vinne. Niseme tu mahali ambapo wamemwaga nguzo siyo kwamba wamemwaga bali wameshakamilisha survey. Kijiji cha Kabulabula vitongoji vitatu vilivyobaki vitaanza kupelekewa umeme kuanzia mwezi Julai, 2019.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Katika Vijiji alivyovitaja kuwa vilipata umeme awamu ya kwanza na ya pili vya Azimio, Chiwana, Mkandu na Mbesa umeme ulipita barabarani ndani ya mita 100 kutoka barabara kuu ilikopita nguzo kubwa. Je, ni lini mradi wa kujazilizia mitaa iliyobaki katika Vijiji hivyo vya Azimio, Chwana, Mkandu na Kijiji cha Airport itaanza?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, mwaka 2017 nilipeleka maombi maalum kuongeza vijiji katika Mradi wa REA katika Vijiji vya Tuwemacho, Chemchem, Ligoma, Makoteni, Nasia, Semeni, Mtina, Angalia, Nalasi, Mchoteka, Kitani, Mkolola pamoja na Masakata. Nini kauli ya Serikali kuhusu uwekaji wa awamu ya tatu ya umeme katika Vijiji hivyo?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi la Mheshimiwa Mpakate, lakini vilevile nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mpakate jinsi anavyofuatilia umeme katika Jimbo lake.

Mheshimiwa Spika, ni kweli vijiji vingi tuliviweka kwenye round II ya awamu ya tatu inayoendelea, lakini baada ya kuona changamoto kubwa sana katika Jimbo la Tunduru Kusini tulifanya mapitio mapya na vijiji 13 tuliviingiza kwenye round inayoendelea. Kwa hiyo katika utaratibu tunaojenga line kwa sasa kutoka Tunduru Mjini mpaka Msingi umbali wa kilometa 20 tumechukua vijiji vingine 13 vikiwemo vijiji ambavyo anavisema vya Angalia, Semeni ambako Mheshimiwa Mbunge anatoka lakini mpaka Tuwemacho, Chemchem mpaka Chilundundu kwa vijiji vyote hivyo viko kwenye mpango. Pia Wakandarasi kupitia TANESCO sasa wanavifanyia kazi, kwa hiyo nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge pamoja na kumpongeza, vijiji 13 vya nyongeza tayari vimeshaanza kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu nyongeza ya vijiji vya ujazilizi; mradi umeshaanza na utekelezaji wa maeneo ya kujaziliza, maeneo ya vitongoji unaanza mwezi huu utachukua miezi 12, lakini maeneo ya Azimio pamoja na Mbesa ambako tayari umeme upo kwenye Vitongoji 17, tayari pia TANESCO wameanza kuvifanyia kazi.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuumuliza Mheshimiwa Waziri kwamba suala hili la nishati mbadala tuliaminishwa kwa ugunduzi ule wa gesi, basi wananchi wa vijiji wangefikishiwa ile gesi wakaachana kabisa na mambo ya kutumia mkaa ili kuweza sasa kutumia gesi ambayo inapatikana maeneo ya Mtwara. Hata hivyo, mpaka sasa hivi hata Mtwara kwenyewe matumizi ya gesi si makubwa kwa sababu ile miradi ni kama imekuwa abandoned, Serikali haiifanyii tena kazi. Sasa nataka kufahamu kutoka kwa Naibu Waziri, je, Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na masuala ya gesi iliyopo Mtwara?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimshuruku sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu ya maswali ya msingi ya Waheshimiwa Wabunge. Pia napenda niungane na Mbunge Mwambe kwa matumizi ya gesi kule Mtwara na nimpongeze kwa ufuatiliaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibu mwezi uliopita tumeanza kutekeleza rasmi, mwaka jana tulizindua usambazaji wa gesi Mtwara na katika maeneo 12 ambayo tunaanza nayo vifaa tayari vimepatikana na tarehe 30 mwezi huu ujenzi wa usambazaji gesi Mtwara unaanza. Tunaanza na vituo cha Chuo cha Ufundi pamoja na maeneo yote yanayokwenda mpaka gerezani na maeneo ya Mtwara Mikindani. Nitake tu kuwapa taarifa na uhakika wananchi wa Mtwara kwamba yataanza sasa mwezi huu tarehe 30 na yatachukua takribani miezi 15 ili wananchi wa Mtwara waweze kupata gesi kama ambavyo tumepanga.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi. Tatizo lililopo Kibiti pia lipo katika Jimbo la Lulindi na sisi hatujapitiwa na utaratibu huo wa kupewa umeme mbadala na kutumia gesi kwa ajili ya majumbani. Sasa nataka kumwomba Mheshimiwa Naibu Waziri atueleze maana sisi tunategemea umeme hali ya usambazaji umeme katika jimbo la Lulindi inasikitisha na iko katika kiwango cha chini sana. Je, nini kauli ya Serikali?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nijibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Bwanausi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika baadhi ya maeneo utekelezaji wa kandarasi umesuasua hasa mwanzoni lakini kwa upande wa Mheshimiwa Bwanausi yapo maeneo ambayo yalikuwa mbali sana na mtandao wa umeme, kwa hiyo, imechukua muda mrefu kwa wakandarasi kuyafikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Bwanausi kwa ushirikiano na Waheshimiwa Wabunge wa Mtwara pamoja na mkandarasi, sasa hivi mkandarasi mkandarasi anakamilisha shughuli za kusimika nguzo katika maeneo 22 ya Mheshimiwa Bwanausi. Ni matarajio yetu katika Jimbo la Bwanausi, maeoneo ya vijiji 22 yatawashwa kabla ya mwezi Septemba, 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba tunafanya kila namna kuhakikisha kwamba wakandarasi wanaongeza kasi. Tarehe 22, mimi mwenyewe nitakuwa Mtwara ili kuweka msukumo mkali kwa wakandarasi ili waweze kukamilisha kazi hizo kwa wakati.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri ametaja mkandarasi anayesimamia ujenzi kwenye hivyo vijiji, lakini amekuwa akifanya kazi hii kwa taratibu sana na analalamika kwamba hapewi pesa yake ya kukamilisha kazi zake kwa wakati. Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari kutueleza hivi viporo vya REA II vitakamilika lini specifically?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; matatizo yaliyopo Jimbo la Momba kwenye masuala haya ya umeme yanafanana moja kwa moja na shida pia zilizopo kwenye Jimbo la Ndanda, Wilaya ya Masasi, hasa zaidi kwenye Vijiji vya Mkwera, Mumburu, Chipite, Mdenga, Liputu, Ndoro pamoja na Mbaju pamoja na Kata za Msikisi na Mlingula. Vijiji hivyo nilivyovitaja vyote vinapitiwa na umeme mkubwa juu wa kilowati 33 lakini chini wanakokaa wananchi hakuna umeme. Je, ni lini Serikali kwa makusudi kabisa itatekeleza kazi hii ya kushusha umeme walau kwenye vile vijiji vinavyopitiwa na umeme mkubwa unaoelekea Masasi?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri katika swali la msingi, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Mwambe katika maswali yake mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, ni kweli yapo maeneo yaliyobaki katika utekelezaji wa REA II na maeneo yote yaliyobaki katika utekelezaji wa REA II yamechukuliwa na Mradi wa REA III unaoendelea sasa. Kwa maendeleo yote, hasa katika Jimbo la Mheshimiwa kama alivyotaja, eneo lote la kutoka Sumbawanga kwenda Tunduma kwenda mpaka Mpanda, yaliyobaki yote yamechukuliwa na Mradi wa REA III unaoendelea. Kwa hiyo nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge kwa niaba ya muuliza swali kwamba maeneo yote yaliyobaki yatachukuliwa na REA III inayoendelea kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la pili, ni kweli kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mwambe; maeneo ya Ndanda, hasa eneo la Liputi pamoja na Mbemba pamoja na Kitongoji cha Ndoro, yako chini ya line inayopita KVA 33, lakini kama ambavyo nimeshatoa utaratibu na Mheshimiwa Mbunge anafahamu, hivi sasa TANESCO wanapeleka umeme katika vitongoji vyote hivyo. Bahati nzuri sana Kitongoji cha Ndoro kiko nyuma ya Sekondari ya Ndanda ambayo tayari ina umeme. Kwa hiyo, maeneo haya yatafanyiwa kazi na yatakamilishwa ifikapo mwisho wa mwezi Juni, mwaka huu.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nami niulize swali dogo la nyongeza. Kuna kata iko pale inaitwa Kata ya Sirari, kata kubwa kabisa, ina wakazi zaidi ya 45,000, watu wana majumba mpaka ya milioni 200 pale; Kitongoji cha Nyamorege, Niroma, kuna maeneo ya Kimusi, tumezungumza na Waziri muda mrefu sana, watu wanahitaji umeme na wana uwezo wa kulipia. Ni lini hao watu watapata umeme kwenye hayo maeneo niliyoyataja kwa sababu watu wanahitaji umeme na wana nguvu za kulipa?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, ni kweli nilitembelea eneo hilo na kutoa maelekezo na nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa sababu anafahamu. Utekelezaji wa kupeleka umeme katika eneo hilo mpakani kabisa na Sirari umeshaanza na Kitongoji anachokisema cha Nyamorege ambacho kiko jirani sana na wilaya moja wapo ya mkoa wa kwanza kutoka Kenya tayari kuna umeme na wakandarasi kupitia kampuni yetu inayopeleka umeme vijijini kule Mara umeshaanza. Tarehe ya kumaliza kazi hiyo, nimwambie Mheshimiwa Mbunge ni tarehe 12 Juni, mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nimetoka kuongea na rafiki yangu, Mheshimiwa Dkt. Kalemani, hapa lakini nataka awatangazie wananchi wa Msalala. Halmashauri ya Msalala Makao Makuu yake yako Ntobo na wameshahamia, lakini shughuli zote inabidi zifanyikie mjini, kwenda kutoa photocopy, hata shughuli za kibenki au za kiuhasibu kwa sababu ya ukosefu wa umeme. Je, ni lini Serikali itapeleka umeme kwenye Kijiji cha Ntobo yalipo Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kwa dharura?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Maige, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli, ni kama takribani nusu saa tumemaliza kuongea na Mheshimiwa Mbunge. Kazi ya kupeleka umeme katika Kijiji cha Ntobo ambacho kiko kilometa nane kutoka umeme unapoishia inaanza Jumatatu ijayo na tayari leo wakandarasi wamekwenda ku-survey. Niwape taarifa wananchi wa Msalala, hasa wa Ntobo, kwamba kuanzia wiki ijayo kazi ya kupeleka umeme kwenye kijiji kizima na vitongoji vya Ntobo inaanza Jumatatu wiki ijayo.
MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Moja ya wilaya ambazo zilipata maeneo machache sana mwanzoni ni Wilaya ya Hanang na sasa bado changamoto ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri aliniahidi kwamba atatembelea Hanang, mimi nasubiri naomba awaambie wananchi wa Hanang ni lini atakwenda kule ili kuona changamoto zile na tushirikiane naye ili tuweze kuondoa hizo changamoto?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 2, mwezi ujao, baada ya bajeti yetu kumalizika tutafuatana mimi na Mheshimiwa Mbunge, twende kwenye jimbo lake.
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Athari ya moshi ni sawa na athari ya umeme unaopita juu ya nyumba za wananchi. Kuna mradi Mchikichini, Mtaa wa Ilala Kota eneo la Baghdad ambapo TANESCO walikubaliana na wananchi kupitisha umeme mkubwa sana juu ya nyumba zao lakini kwa kigezo cha kuwalipa fidia. Umeme umepita, umeme ulikuwa usiwashwe mpaka fidia ilipwe, lakini umeme umewashwa na fidia haijalipwa, watu wako chini ya umeme mkubwa na wanaathirika kiafya.

Mheshimiwa Spika, nilitaka tu kujua ni lini sasa Serikali au TANESCO itawalipa fidia wananchi hawa wa Mchikichini ambao wako hapo kwa zaidi ya miaka 50, huduma zote wanapata pale. Kuna kigezo kililetwa kuwa eneo lile ni hatarishi. Wananchi hawa wamekaa hapa miaka 50 wana huduma za maji, umeme na wanalipa bili zote na kikubwa kabisa inapokuja uchaguzi maboksi ya kura yanapelekwa maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali na TANESCO wawafikirie wananchi hawa ambao ni masikini, wawalipe fidia waondoke ili waondokane na athari ya kuathirika na umeme huu mkubwa katika nyumba zao. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Zungu kwa kuulizia na kufuatilia masuala ya fidia kwa wananchi Mchikichini. Ni kweli kabisa wananchi wa Mchikichini walipitiwa na umeme mkubwa katika Jiji la Dar es Salaam, Wilaya ya Ilala miaka sita ama saba iliyopita. Ni kweli katika eneo hilo bahati nzuri sana eneo hilo lilichukuliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Dar es Salaam lakini ni kweli wananchi hao wanatambulika na kwamba walikuwa wakidai fidia.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tunafanya majadiliano ya kina sana na Manispaa ya Ilala ili kuhakikisha kwamba wananchi ambao wanadai fidia ni wale ambao kweli waliathirika na fidia. Pili kwa sababu eneo hilo lilichukuliwa na Halmashauri ya Manispaa, tunafanya mazungumzo ili wananchi hao waendelee kupata haki yao kulingana na wanavyostahili.

Mheshimiwa Spika, la pili, nampongeza Mheshimiwa Zungu, wiki mbili zilizopita tumekaa na Mheshimiwa Zungu kupitia kwa Kamishna wetu wa Nishati na tumefanyia kazi kwa kina suala hili. Wananchi hao tunawasihi wawe watulivu wakati suala hili linafuatiliwa kati ya Wizara na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ili waweze kupatiwa haki yao ndani ya muda mfupi kadri inavyowezekana. (Makofi)
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja na juhudi nzuri za Serikali zilizofanywa pamoja na Kampuni hii ya Tanzania Oxygen Limited kuweza kuzuia baadhi ya wanyama watambaao pamoja na binadamu kwenda kwenye eneo hili la kisima ambacho mara nyingi miaka ya nyuma Wananchi na wanyama wengine walikufa kutokana na kuvuta gesi hii ya carbondioxide. Swali la kwanza; je, ni lini Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi ambao wanazunguka kisima hiki na kwa kuwa nguvu za asili za volcano bado zipo na volcano nii ni hai ili kuzuia madhara yatokanayo na kuvuta gesi hii ya carbondioxide?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa Serikali imeonesha nia njema kwa ajili ya kujenga viwanda hapa nchini lakini kumekuwa kuna changamoto kubwa kuingiza gesi hii ya carbondioxide ndani ya Nchi yetu ya Tanzania tukitambua kwamba carbondioxide gas inatumika katika mazingira ama kwenye vitu vingi ikiwemo vyakula pamoja na vinywaji ili visiharibike. Ni kwa kiwango gani Serikali itavutia zaidi wawekezaji kwenye maeneo mengine ambayo gesi hii ya carbondioxide bado haijaanza kuchimbwa.
WAZIRI NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu ya msingi ya suala la Mheshimiwa Mwakibete, lakini vilevile nimpongeze sana Mheshimiwa Mwakibete kwa kufuatilia masuala haya ya matumizi ya carbondioxide.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwanza ni lini Serikali itaendelea kutoa elimu; Kampuni ya Tanzania Oxygen kwanza imetenga takribani dola milioni tano kila mwaka kawa ajili ya kutoa elimu katika maeneo yao ya leseni. Kwa hiyo shughuli za kutoa elimu zinaendelea, lakini sambamba na hilo Serikali kwa kushirikiana na Tanzania oxygen zimeweka timu mahususi kwa ajili ya mpangokazi wa kutoa elimu kila mwezi katika maeneo hayo. Kwa hiyo shughuli za utoaji wa elimu ni endelevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la pili la kulinda soko la ndani; ni kweli, kwanza kuna nchi ambazo zinzalisha carbondioxide kama Tanzania, mathalani; DRC, Kenya na Nchi ya Msumbiji. Kwa Tanzania tunachofanya kwa sasa tumeunda timu mahususi kwa ajili ya kufanya tathmini ili kuangalia mahitaji ya ndani na uwezo tulionao ndani ya miezi mitatu, tukishajiridhisha kwamba uwezo wa ndani wa carbondioxide unatosha kuzalisha vinywaji kama soda pamoja na vinywaji vya bia, tutazuia kabisa carbondioxide kutoka nje badala yake tutumie viwanda vya ndani.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwanza tunaishukuru sana Serikali wananchi wa Mkoa wa Katavi kwa kutuletea mradi mkubwa sana huu ambao utatusaidia katika Mkoa wetu wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mradi huu wa Mkoa wa Katavi ni mradi wa mkakati, Mkoa wa Katavi tunataka kujenga bandari na vilevile tunataka standard gauge inafika katika Mkoa wetu wa Katavi. Na mradi huu unaenda kwa kusuasua sana ninavyoongea sasa hivi nilikuwa naongea na Meneja wa TANESCO wa Mkoa wangu wa Katavi mradi unaenda kwa kusuasua, tunaomba tupate majibu mazuri lini mradi huu utaanza na utaisha lini ili kwa manufaa ya wananchi wa Katavi kwa sababu tuna malengo ya kupata viwanda ndani ya Mkoa wa Katavi tumechelewa sana tunataka viwanda ili tuweze kufaidika na Serikali yetu ya Awamu ya Tano? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na vilevile swali langu la pili kwa kuwa Mkoa wa Katavi kuna vijiji vingi sana na umeme wa REA bado haujawafika, ni lini umeme wa REA utatufikia katika vijiji vyetu? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri katika eneo hili napenda pia nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia mradi huu mahususi wa North West Grid. Kwanza ni lini mradi utaanza mradi umeshaanza kupeleka Grid ya Taifa katka maeneo ya Katavi na kwa hatua ya kwanza tumeanza na utekelezaji wa kuutoa umeme wa Grid kutoka Mjini Tabora kama ilivyosoma katika swali la msingi kupitia Ipole, Inyonga na hatimaye Mpanda. Umbali wa takribani kilomita 381 na utekelezaji umeanza na tunatarajia mradi kukamilika kabla ya mwezi Mei mwakani, kwa hiyo wananchi wa Katavi watakuwa wameshapatiwa umeme wa Grid kabla ya mwezi Mei Mwakani huo ni Awamu ya I ya utekelezaji wa mradi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Awamu ya II, mradi utaanza kutekelezwa kuanzia mwakani mradi ambao unatokea kimsingi Iringa, Mbeya, Sumbawanga na baadaye kutoka Sumbawanga, Mpanda na hatimaye Kigoma umbali wa takribani kilomita 1384 kwa ujumla wake mpaka Nyakanazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika awamu hii eneo hili litaanzwa kutekelezwa kwa maana nyingine mwanzo mwa mwaka lakini utaisha mwaka 2022. Mradi huu ni muhimu sana kwa sababu unaunganisha kati yetu na nchi ya Zambia kwa umeme wa kilovoti 400 na umeme utakapopatikana maeneo ya Katavi wananchi wa Katavi wataweza sasa kufanya shughuli za kiuchumi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda. Kwa hiyo, nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwa niaba ya wananchi wa Katavi wavute subira mradi wakati unatekelezwa na utakamilika kama nilivyotaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali la pili kuhusu vijiji ambavyo havijapata umeme katika Mkoa mzima wa Katavi. Mkoa wa Katavi bado vijiji 132 havijapata umeme na vijiji vyote tumeviingiza kwenye mpango wa REA Awamu ya II unaoanza mwezi Februali hata hivyo vile vijiji ambavyo vinatekelezwa na mkandarasi kwa sasa vitakamilishwa vyote ifikapo mwezi Aprili mwaka huu 2020.
MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niipongeze Serikali kwa kusambaza umeme maeneo mengi katika nchi yetu lakini najua kipaumbele moja wapo cha Serikali ni kulenga zile Taasisi zenye kutoa huduma za jamii kama shule, zahanati nakadhalika. Shule ya sekondari ya Bama iliyoko Kata ya Nangwa Wilayani Hanang licha ya kuomba kwa muda mrefu hadi leo juhudi za kuomba huo umeme haujazaa matunda. Ni nini tatizo ambalo linasababisha sekondari hiyo isipate umeme hadi leo?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake la nyongeza Mheshimiwa Martha. Kwanza nimpongeze kwa sababu amefuatilia sana kuhusu shule hii, lakini nieleze tu shule hii ipo karibu sana na umeme takribani nusu ya kilomita na tumekuwa tukifuatilia sana halmashauri ile iweze kulipia ili umeme uweze kuingia kwenye hiyo shule ya sekondari. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nashukuru sana kwa kukumbushia hili lakini na mimi nitoe maelekezo wa Mkurugenzi wako na Mwenyekiti wa Halmashauri alipe gharama za kuunganishiwa umeme ili shule hiyo ipate umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kwa Waheshimiwa Wabunge kwa niaba ya Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri zote nchini wahakikishe wanatenga fedha mahususi kwa ajili ya kuingiza umeme kwenye Taasisi za Umma, hapa tuna maana shule, vituo vya afya, zahanati na Taasisi nyingine. Imekuwa ni changamoto kubwa sana tunapokwenda maeneo yale unakuta shule ipo karibu umeme lakini halmashauri haijalipia. Basi nitoe rai hiyo ili wafanye hivyo ziweze kuunganishiwa umeme na shule ambazo ziko mbali hata kama kijijini hatujapeleka umeme sisi tutapeleka umeme mahususi kwa ajili ya hizo shule za sekondari na vituo vya afya. (Makofi)
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Baada ya kusema hayo, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, misitu ni uhai na kama misitu ni uhai, kila mmoja wetu ana jukumu la kulinda misitu. Pamoja na jitihada nzuri za Serikali, ningependa kufahamu kwamba kumekuwepo na utaratibu wa kusafirisha magogo kwenda nje ya nchi; hii pia ni mojawapo ya chanzo cha uharibufu wa mazingira.

Mheshimiwa Spika, nataka kufahamu jitihada za Serikali katika kuhakikisha kwamba inalinda misitu yetu na misitu hii iendelee kutulinda na sisi Watanzania.

Mheshimiwa Spika, itakapofika mwaka 2022 tunafahamu kwamba bwawa la Mwalimu Nyerere la kuzalisha umeme litakamilika na ni dhahiri kwamba litapunguza gharama kubwa za umeme. Vile vile tukitumia gesi yetu itakuwa ni njia mojawapo pia ya kupunguza uharibifu wa mazingira.

Mheshimiwa Spika, nataka kufahamu mkakati wa Serikali katika kuhakikisha kwamba gesi tuliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu hapa nchini inafanya jitihada gani kuhakikisha kwamba wananchi wanaingia katika zoezi zima la kutumia gesi kuweza kulinda mazingira yetu? Nini jitihada za haraka za Serikali?

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri sana kwa mwuliza swali. Pia nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kufuatilia matumizi ya gesi katika mkakati wa kupunguza uharibifu wa mazingira.

Mheshimiwa Spika, ni kweli, kwanza mkaa unaoingia katika Jiji la Dar es Salaam kwa kila siku ni zaidi ya magunia 400,000 mpaka 500,000 na hiyo yote inahusisha ukataji wa miti na kuharibu mazingira. Vile vile kuni zinazotumika vijijini pamoja na mkaa ni zaidi ya wananchi zaidi ya asilimia 71. Sasa mkakati ulipo kwa sasa ni kuhakikisha kwamba gesi hii inatumika katika shughuli za majumbani ili kupunguza ukataji wa miti unaoharibu mazingira.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa kwa niaba ya Watanzania wanaosikiliza, zaidi ya wananchi 600 wameshaanza kutumia gesi na wiki iliyopita nimeunganisha gesi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa wafanyakazi 110 na cafeteria nne zimeanza kutumia gesi. Huu ni mkakati mzuri sana wa kupambana na mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongeze tu, awamu ya pili tunakwenda katika mikoa yote ya Tanzania Bara kwa kuanza kusafirisha mitungi iliyoshindiliwa na gesi na kujenga mabomba katika mikoa hiyo ili nako kuanza kusambaza katika vijiji vyote ikiwa ni harakati ya kupunguza uharibufu wa mazingira.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la kwanza la Mheshimiwa Amina Mollel. Kwanza naomba nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Amina Mollel ambaye ni Balozi wetu wa Utalii kwa kazi nzuri sana ambayo anaifanya. Mheshimiwa Amina Mollel alipata hati ya kutambuliwa kama Balozi wa Utalii wakati wa Maadhimisho ya Miaka 60 ya Ngorongoro na Serengeti na anafanya kazi nzuri sana yeye pamoja na wenzake. Nampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Amina Mollel ametaka kujua, kwa nini Serikali inaendelea kuruhusu usafirishaji wa magogo nje ya nchi wakati usafirishaji huu ni chanzo kikubwa sana cha uharibifu wa mazingira? Ni kweli kwamba hapo awali Serikali ilikuwa ikiruhusu usafirishaji wa magogo ya miti migumu nje ya nchi lakini kwa takribani miaka mitatu sasa, Wizara ilizuia usafirishaji wa magogo ambayo hayajaongezewa thamani kwenda nje ya nchi. Ni nia ya Wizara kuona kwamba mauzo yoyote ya mazao ya misitu nje ya nchi yanakuwa ni mauzo ya mazao yaliyoongezewa thamani. Kwa hiyo, jitihada hizo katika Wizara zinaendelea na sasa hivi tumefunga uuzaji wa magogo hayo na tutakapofungua tutatoa masharti na maelekezo ya namna ya kufanya biashara hiyo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, nimefurahishwa sana na majibu ya Serikali ambayo yanaonesha kwamba vijiji vingi vimepata umeme kwenye Wilaya ya Chunya, wilaya kongwe, na vijiji vilivyobaki vitapata umeme kwenye REA III inayoanza mwezi huu mpaka mwaka kesho.

Mheshimiwa Spika, nataka niweke tu rekodi sahihi kwamba katika Kata ya Sangambi, Kijiji cha Shoga – lakini sio shoga ya watu wa ughaibuni hapana, shoga ya Kitanzania ya urafiki – Kijiji cha Shoga; kwenye Kata ya Upendo Kijiji cha Nkwangu; Kata ya Nkung‟ungu Kijiji cha Nkung‟ungu, Majengo na Magunga; Kata ya Lualaje Kijiji cha Lualaje na Mwiji; Kata ya Matwiga Kijiji cha Mazimbo; Kata ya Mafieko Kijiji cha Mafieko na Biti Manyanga; Kata ya Kambikatoto Kijiji cha Kambikatoto na Sipa, je, vitapewa umeme kwenye REA Awamu ya III inayoanza mwezi huu? Ninafurahi sana na majibu ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, nina swala dogo tu la nyongeza, katika Vijiji vyote hivi ambayo vilibaki kuna Kijiji cha Itumbi ambapo Serikali inaweka central of excellence yaani inaweka shule ya kuwafundisha wachimbaji wadogo na kwenye Kijiji hicho kuna makarasha zaidi ya 100 ya wachmbaji wadogo.

Je, Serikali iaweza ikatumia umuhimu wa pekee kuweza kumpa huyu ukandarasi ana addition BOQ ili Kijiji hicho kipate umeme mapema kuliko Vijiji vingine? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli kabisa maeneo yote ya Jimbo lake yanaelekea kupata umeme kufikia mwezi Juni mwaka huu na hongera sana Mheshimiwa kwa kazi kubwa uliyofanya kwa niaba ya wana Jimbo.

Mheshimiwa Spika, katika Kijiji cha Itumbi ambapo central of excellence kwa wachimbaji wadogo itafanyika, mkakati wa Serikali umeshaanza, kwanza mbali na kupeleka Itumbi Mheshimiwa Mwambalaswa aliwaombea migodi ya wachimbaji takribani minne na hivi sasa mradi wa Matundasi ambao na wachimbaji wadogo wameshapata umeme migodi ya Makongorosi nayo imeshapata umeme na pia migodi ya wachimbaji kwa kuwa Sunshine nayo ilishapata umeme. Sasa kazi inayoendelea sasahivi nikupeleka umeme katika Kijiji cha Itumbi ambako kutakuwa na makarasha zaidi ya 128 na tumeshaandaa transfoma sita zenye uwezo wa kilovoti 115 kila mmoja na transfoma moja tutaifunga kwenye Kitongoji cha Matondo karibu kabisa na Itumbi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Kijiji cha Itumbi pamja na wachimbaji wadogo wenye makarasha na pamoja na maosheo watapata umeme tena mkubwa wa wachimbaji kuanzia mwezi Mei mwaka huu, ahsante sana.
MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa niulize swali moja la nyongeza. Matatizo ya Korogwe Mjini yanafanana sana na matatizo ya Wilaya ya Rungwe hususan Busokelo kwa kukatika katika umeme. Kwa siku umeme unaweza kukatika zaidi ya mara 10 na tatizo kubwa lililokuwepo ni kwamba, nguzo za umeme chini yake kuna miti.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru Wizara pamoja na Waziri kwa maana ya kuleta timu maalum kwenda ku-clear ama kukata hiyo miti, lakini bado tatizo kubwa limeendelea kuwepo. Ni mikakati gani Serikali iko nayo kuhakikisha kwamba wananchi wa Jimbo la Busokelo wanapata umeme masaa 24 kwa siku kuliko hivi ilivyo kwa sasa? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri katika swali la msingi, lakini hata la nyongeza kwa Mheshimiwa Chatanda; na niendelee kumpongeza Mheshimiwa Mwakibete kwa swali linalofafana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Shirika letu la umeme nchini na kwa niaba ya Serikali, napenda tu nisema mambo mawili kwamba ukarabati unaoendelea. Jambo la kwanza tumetenga kila Mkoa wa ki-TANESCO kwa nchi nzima takriban shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kufanya ukarabati mkubwa.

Kwa hiyo, wananchi katika maeneo yote ya mikoa yetu ambayo kuna kero ya kukatika kwa umeme, kwanza haukatiki kwa sababu ya hali ya umeme, isipokuwa tunakata kufanya matengenezo. Kwa hiyo, naomba nitoe taarifa hiyo kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, tumetoa muda mahususi wa miezi sita kukamilisha ukarabati wote kwa nchi nzima. Kwa hiyo, ni matumaini yetu Mheshimiwa Mwakibete katika eneo lake ambalo lilikuwa na kero kubwa sana ndani ya miezi sita ukarabati utakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, tumeleta transforma kubwa, tunabadilisha transformer kutoka ndogo kwenda kubwa, kwa sababu shughuli za uchumi za wananchi zinaongezeka. Kwa hiyo, tunaomba radhi kwa wananchi wote ambako ukarabati unaendelea. Tunaomba mtuvumilie tukamilishe kazi hiyo. Ahsante sana.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri lakini pamekuwa na malalamiko katika yale maeneo ambayo yameshapelekewa transfoma za Kilovolt 50. Je, tatizo hili kwa nini linajirudia tena? Kuna baadhi ya maeneo yametajwa kwamba katika transifoma 35, transifoma saba za KV 50 halafu kuna transifoma nyingine nne. Kwa nini tusipeleke zile ambazo ni za kuanzia KV 100?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili katika taarifa hii haikuainisha baadhi ya maeneo ambayo ndiyo hasa yaliyokusudiwa. Kwa mfano, kwenye Kata ya Kirare kina maeneo ya Mapojoni, Mtambuuni, Msakangoto, Kirombere lakini kwenye Kata ya Mzizima kuna maeneo ya Kihongwe, Rubawa, Mleni, kwenye kata ya Kiomoni kuna maeneo ya Pande Muheza, Pande Masaini, Pande Mpirani, Kata ya Marungu kuna Mkembe, Geza Ndani na Geza Barabarani; Pongwe kuna maeneo ya Pikinangwe; na Kata ya Maweni kuna Machembe, Mtakuja na Mwisho wa Shamba: Je, maeneo haya sasa hususan noyo yamo katika huu mradi na lini hasa yataanza kufanyiwa huu uwekezaji wa REA III? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli yako maeneo ambayo tulikuwa tukipeleka transfoma za KV 50 na nyingine 100 na 200 na kuendelea, lakini maeneo tunayopeleka KV 50 inategemea pia na uwekezaji na aina ya wateja. Ziko faida nyingi sana za kupeleka transfoma ndogo ndogo katika baadhi ya maeneo na hasa katika kukabiliana na uharibifu wa mitambo inapotokea dharura. Kunapokuwa na transfoma za 50 nyingi, kwa hiyo, kunapokuwa na dharura ya kuharibika transifoma moja, wateja wengine wanaendelea kupata umeme bila matatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hasara za kuwa na transifoma moja kubwa, ni kwamba ikishaharibika wateja wengi wanakosa umeme, lakini tumelichukua ombi la Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kusambaza transifoma za kila aina kukabiliana na hali hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili katika Jiji la Tanga tunayo maeneo 12 yatakayopelekewa umeme wa Perry Urban ikiwemo kama alivyotaja maeneo yake, lakini yako maeneo ya Chongoleani, Mabwakweni, Majani Mapana na maeneo mengine mpaka 12 na utekelezaji unaanza Julai mwakani na kukamilika mwezi Desemba, 2021. (Makofi)
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza kabisa naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri kabisa, lakini nina maswali mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Mkoa wa Kagera siyo vijiji peke yake ambavyo havijapata umeme wa REA. Kumekuwa na Taasisi kubwa kama shule na Vituo vya Afya ambavyo bado havijapata umeme wa REA na kupelekea kushindwa kutoa huduma zinazotakiwa kwa wakati. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha taasisi hizi zinapata umeme? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, wananchi wa Mkoa wa Kagera wamekuwa wakikumbwa na kadhia ya kulipishwa nguzo za umeme. Serikali au Wizara inazungumziaje kadhia hii inayowakuta wananchi wa Mkoa wa Kagera? Nakushukuru. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Halima Bulembo anapofuatilia masuala ya umeme katika Mkoa wa Kagera. Nampongeza sana na kweli kazi kubwa imeonekana kutokana na jitihada zake hasa kwa kupitia vijana. Hongera sana Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijielekeze katika masuala yake mawili ya nyongeza. Swali la kwanza anataka kujua kuhusiana na upelekaji wa umeme katika taasisi za Umma. Naomba nitoe maelekezo kwa Halmashauri zetu na Waheshimiwa Madiwani wanaonisikiliza. Ni kweli Serikali imekuwa ikipeleka umeme katika maeneo yote hasa vijijini lakini baadhi ya taasisi zimekuwa hazilipiwi na wamiliki wa taasisi hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sana wamiliki wanaohusika walipie gharama ya 27,000 ili taasisi zote zipelekewe umeme. Maelekezo na mwelekeo wa Serikali ni kuhakikisha taasisi zote zinapelekewa umeme. Nakupongeza Mheshimiwa Halima Bulembo kwa sababu katika Mkoa wa Kagera hadi sasa taasisi 897 zimepelekewa umeme na hii ni jitihada kubwa. Naomba maeneo mengine ambayo hayajapelekewa umeme, wanaohusika waendelee kulipia.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia taasisi tukiwa na maana ya shule, Vituo vya Afya, Zahanati, Misikiti, masoko na hata kama kungekuwa na maeneo madogo ya viwanda. Kwa hiyo, nitoe sana ombi kwa Waheshimiwa Wabunge kupitia kwa Madiwani na Wenyeviti wa Halmashauri tupeleke kwa kulipa shilingi 27,000/= katika Taasisi za Umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali la pili kuhusu kulipishwa nguzo; ni kweli zipo changamoto katika baadhi ya maeneo, yapo maeneo bado Wakandarasi na Mameneja wa TANESCO wanaendeleza kutoza nguzo wateja. Naomba nitoe tamko kali sana kupitia Bunge lako Tukufu kwamba ni marufuku kutoza nguzo kwa wateja wote; iwe Mkandarasi awe Meneja wa TANESCO, awe Injinia, awe Kibarua wake ni marufuku kulipiza mteja nguzo. Hii ni kwa sababu Serikali imegharamia kwa asilimia 100.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri na juhudi kubwa inayofanywa na Waziri wa Nishati ninayo maswali mawili ya nyongeza.

(i) Kwa vile katika mradi huu wa REA III uliokuwa na vijiji 18 katika Jimbo langu ni vijiji vinne tu ndiyo vimepata umeme mpaka sasa. Je, ni lini vijiji vyote 18 vitapata umeme?

(ii) Kwa kuwa Jimbo langu lote la Tabora Kaskazini lenye vijiji 82 ni vijiji saba tu ndiyo vimepata umeme. Napata wasiwasi kama kweli umeme utaenea karibu vijiji vyite 82. Je, Serikali inawahakikishia wananchi wa Jimbo la Tabora Kaskazini kwamba vijiji vyite 82 vitapata umeme?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi la Mheshimiwa Almas Maige, lakini zaidi nimpongeze sana Mheshimiwa Maige anavyofuatilia masuala ya umeme katika Jimbo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya mwaka 2015 Jimbo zima la Tabora Kaskazini halikuwa na kijiji chochote chenye umeme lakini kwa juhudi kubwa alizofanya Mheshimiwa Maige kufuatilia upatikanaji wa umeme hadi sasa tuna zaidi ya vijiji saba vina umeme. Kwa hiyo, nipende kumpongeza Mheshimiwa Maige lakini niwaombe wananchi wa Jimbo la Tabora Kaskazini wawe na imani na Serikali kwa sababu vijiji vyote 82 vitapelekewa umeme ifikapo mwezi Juni, 2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maswali yake mawili ya nyongeza kuhusiana na vijiji 18 ni lini vitapate umeme?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa mkandarasi anaendelea na vijiji vingine pamoja na kwamba ameshawasha vijiji saba alivyotaja Mheshimiwa Mbunge lakini tarehe 25 mwezi huu, mkandarasi atawasha vijiji vingine vine ikiwemo Kijiji cha Ibushi, Kagera ya Nsimbo, Majengo ambako Mheshimiwa Mbunge unatoka kwenye Kata ya Ikongolo pamoja na Mputi navyo vitawashwa umeme tarehe 25 mwezi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 15 mwezi ujao vijiji vingine vitawashwa umeme ikiwemo Kijiji cha Mkalya, Mpenge pamoja na Ngokoro. Kwa hiyo niwape taarifa wananchi ambavyo Mheshimiwa Mbunge anavyofanya kazi vijiji vyote vya Tabora Kaskazini vitapelekewa umeme ifikapo Juni mwaka 2020/2021.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ninakiri kutambua kazi kubwa inayofanywa na Wizara hii kuhakikisha kwamba maeneo mengi yanapata umeme na kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni dogo tu, kumekuwa na changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa nguzo kwa wateja wapya hasa kwenye Jimbo la Nyamagana, lakini pia ni lini sasa Serikali itahakikisha Nyamagana ambayo inajengeka kwa kasi kubwa sana kwenye maeneo yote kuanzia Kishiri, Fumagira, Rwanima, Bwigoma na Maina watapata umeme wa uhakika kabla hatujafika kwenye mwisho wa mwaka tuliokusudia? Nakushukuru sana.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Stanslaus Mabula, Mbunge wa Nyamagana kama ifuatavyo:-

Ni kweli, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nyamagana mwaka jana tulifanyakazi kubwa sana kuhakikisha wananchi wa mitaa yote ya Nyamagana wanapata umeme na hivi sasa tunavyoendelea kuzungumza vijiji na maeneo ya Kishiri, Fumagira, Buhongwa pamoja na Nyamagana yote kuna wakandarasi wanne wanaofanyakazi na nguzo zaidi ya 2000 zitaondoka tarehe 18 mwezi huu kwenda kufanyakazi Nyamagana. Niwaondoe wasiwasi wananchi na wakandarasi nguzo zipo za kutosha hapa Nchini kuliko hata mahitaji yetu. Kwa hiyo kazi zitafanyika na Nyamagana nzima itapata umeme. Ahsante sana.
MHE. ASHA MSHIMBA JECHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali ilielekeza TANESCO kwamba vijiji vyote ambavyo umeme umepita juu vipatiwe umeme. Miongoni mwa vijiji 74 ambapo kuna Vijiji vya Buyungi, Imenya, Itwangi na Nyambui, je, Serikali itavipatia umeme lini katika huu msimu wa 2019/ 2020? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Naibu Waziri aliahidi wananchi wa Nyambui atawapatia umeme. Je, ahadi hiyo itatekelezwa lini? Ahsante.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi lakini nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza swali kwa wananchi wa Shinyanga kwa niaba ya Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitoe taarifa Kijiji cha Itwangi kimewashwa umeme tangu juzi ingawaje swali wakati linajibiwa kilikuwa hakijawashwa umeme, kwa hiyo, kimeshawashwa umeme. Kwa hiyo, wananchi wa Itwangi sasa wanapata umeme kupitia Shirika la Umeme Nchini (TANESCO).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Buyubi pamoja na Minyami kitawashwa tarehe 17 mwezi huu wa Septemba. Kwa hiyo, wananchi wa maeneo hayo wategemee kuunganishiwa umeme katika maeneo hayo kwa wiki inayokuja. Ahsante.
MHE. DKT. TULIA ACKSON: Mheshimiwa Spika, nakushuru kwa fursa pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza Kata ya Lupepo haina umeme kabisa na hivyo shule ya Sekondari Lupepo haina huduma hiyo na pia zahanati ya Lupepo watu wanajifungulia gizani, ni lini kwenye Kata hii tutaletewa umeme wa REA? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Waziri alipokuja Jiji la Mbeya alitoa ahadi kwa Kata ya Usalaga na Kata ya Iduda kwamba wananchi wa maeneo haya watawekewa umeme kwa shilingi 27,000. Lakini kuna Kata zingine za Jiji la Mbeya ambazo pia hazina umeme na ningependa kusikia msimamo wa Serikali kuhusu bei ya umeme kwenye kata hizi, na kata hizi ni Kata ya Itende, Kata ya Iziwa, Kata ya Nsoho, Kata ya Iwambi, Kata ya Mwasanga, Kata ya Itezi, Kata ya Mwansekwa, Kata ya Nsalaga na Kata ya Idunda na Kata ya Itagala? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri katika swali la msingi la msingi la Mheshimiwa Naibu Spika kwa niaba ya Mheshimiwa Mbunge wa Rungwe.

Mheshimiwa Spika, napenda nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Naibu Spika kwa niaba ya Mheshimiwa Mbunge wa Rungwe kama ifuatavyo;-

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli kabisa katika shule ya sekondari katika Kata la Lupepo pamoja na kituo cha afya havijapatiwa umeme, lakini nilipotembelea Rungwe niliwaomba sana Mkurugenzi na Mwenyekiti wa Halmashauri waweze kulipia ili shule pamoja na zahanati zipelekewe umeme. Niombe tu Mkurugenzi wakandarasi wetu wako site na wamemfuatilia mpaka wiki iliyopita alipe ili shule ya sekondari na zahanati zote zipatiwe umeme ikiwezekano wiki ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili kweli nilitembelea Mbeya Mjini na maeneo mengine na katika maeneo ambayo nilitembelea nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Spika kwa niaba ya Mbunge na Wabunge wengine wa Mbeya kwa kufuatilia ipasavyo sana katika kupeleka umeme katika vijiji vya Mbeya Mjini.

Mheshimiwa Spika, nilipotembea Mbeya Mjini kwanza aliomba maeneo saba yapelekewe umeme ikiwemo eneo la Kitunda, Msalaga na maeneo mengine yote yameshapelekewa umeme nakupongeza Mheshimiwa Naibu Spika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini ameendelea kuomba maeneo mengine14 katika Jiji la Mbeya ili nayo yapelekewe umeme kwa shilingi 27,000, tumeanza kuyapelekea kuanzia mwezi huu Kata zote za Nsalaga mpaka Relini zitapelekewa umeme wa 27,000, nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Spika. (Makofi/ vigelegele)
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naomba pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni kwamba, mkandarasi wa Awamu hii ya III wa REA katika Mkoa wa Geita anaonekana anaenda anasuasua katika utekelezaji wake. Sasa ni nini hatua zinazochukuliwa na Serikali, ili kuhakikisha kwamba, maeneo ya utekelezaji wa mradi huu REA III unakamilika kwa mujibu wa ratiba?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika Wilaya ya Mbogwe kuna vijiji vilivyoachwa kwenye Awamu hii ya REA Phase III ikiwemo Kata Mpya ya Bonigonzi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba, vijiji vyote vya Wilaya ya Mbogwe vinapatiwa nishati hii ya umeme? Ahsante.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge Masele, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake ya mzingi:-

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Masele katika kuliza swali la msingi. Kwanza ni kweli Jimbo la Mbogwe lina vijiji 86 na kati ya vijiji hivyo ni vijiji 23 havijapata umeme, ikiwemo Kata Mpya ya Bonigonze. Lakini pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Masele na ufuatiliaji wake Kata Mpya ya Nyabunigonza ambayo inapitia Kijiji cha Lunguya kwenda Kijiji cha Chibutwe, umbali wa kilomate mbili na iko katikati imeshaanza kushushiwa umeme tangu jana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni matumaini yetu kwamba, kata nzima na vijiji vyake vitano itapelekewa umeme kuanzia mwezi huu hadi mwezi Septemba mwaka huu.

Nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge, nimefuatilia kazi hizi na kumpongeza sana kwenye wilaya yake itabakiza vijiji vitano ambavyo tunaanza kuvipelekea umeme kuanzia mwezi ujao na vitakamilika mwezi Disemba mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili ni lini mkandarasi, White City, atamaliza kazi katika Mkoa mzima wa Geita:-

Mheshimiwa Spika, kwanza mkandarasi huyu ameshafikia average ya asilimia 52 na muda wake wa kumaliza kazi kimsingi ni mwezi Juni mwakani, lakini tunamtaka amalize kazi mwezi Disemba mwaka huu, ilibaki kazi ndogondogo za kuunga wateja, hasa ambao watachelewa kulipa. Kwa hiyo, nimpe taarifa na kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza maendeleo ya mkandarasi katika Mkoa mzima wa Geita, lakini nimhakikishie kwamba, utakamilika ndani ya muda. (Makofi)
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Wizara ambayo yanatupa matumaini, nina maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa survey iliyofanyika Hemsambia ilifanyika kwa vitongoji viwili na kuacha vitongoji vingine vitano. Je, Waziri anatuthibitishia kwamba, kwa azma ile ya kuhakikisha kwamba, kila kijiji kinapofikiwa lazima kijiji chote kipate umeme; Je, vitongoji hivi vitajumuishwa kwenye kupatiwa umeme?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, wakati tunapeleka umeme kwenye Kata ya Bosha maeneo ya Vitongoji vya Miyongwe, Kwemsakazi, Kwashemwaondwa na Kibago B yalirukwa, lini maeneo haya yatapatiwa umeme?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi la Mheshimiwa Kitandula, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga na pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, katika maswali yake mawili ya nyongeza kwanza ni kweli, kwenye Kijiji cha Hemsambia tulifanya survey vitongoji viwili na tukabakiza vitongoji vitano ambavyo tayari wakandarasi tumeshaviingiza kwenye
marekebisho na yanafanyiwa kazi. Na hivi sasa Mheshimiwa Mbunge, pamoja na kupongeza, tulipokuwa katika jimbo lako wiki iliyopita tulitoa maelekezo na wakandarasi wameshaanza kuyafanyia kazi. Kwa hiyo, niwape taarifa tu Wananchi wa vitongoji vitano vya Kijiji cha Msambia kwamba, vitongoji vyote katika kijiji hicho vitafanyiwa kazi na vitakamilika mwezi Septemba mwaka huu.

Mheshimiwa Spika, katika swali la msingi la pili la Mheshimiwa Mbunge, ni kweli tunazo kata tano muhimu sana kwa Mheshimiwa Mbunge, lakini Kata ya Bosha yenye vijiji vinne vikiwemo Kijiji cha Kwashemhonda, pamoja na Kwesekazi, pamoja na Kibango vimeshaanza kufanyiwa kazi na Shirika la Umeme – TANESCO kwa sababu, sasa hivi bei ni ileile 27,000/=. Na jana tumewasiliana na Mheshimiwa Mbunge alikuwa kufuatilia na TANESCO pamoja na wataalamu wameshaingia site kuanzia leo. Kwa hiyo, ni matumaini yetu Mheshimiwa Mbunge na Wananchi wa Mkinga muwe na matumaini kwamba, Kata na Vijiji vyote vya Bosha vinakwenda kupatiwa umeme mwisho wa mwezi Disemba mwaka huu.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, Mji wa Tarime kwa hadhi ya kuwa mji ulitakiwa kuwa na umeme kwa zaidi ya asilimia 90, lakini maeneo yenye umeme ni chini ya asilimia 40. Na kwa sababu, Waziri wakati anajibu baadhi ya maswali hapa amehakikisha kwamba, na akatoa instructions kwamba, vituo vya afya, zahanati, shule kama sekondari vihakikishwe vinapewa umeme.

Mheshimiwa Spika, kwenye Jimbo langu Kata ya Nkende kuna kituo cha afya, kuna sekondari na kuna shule za msingi, lakini hazina umeme. Kata ya Kenyamanyori ina shule ya sejkondari, ina shule za msingi, ina kituo cha afya hakina umeme na Kata ya Kitale kuna Sekondari ya nkongole na Mogabili na vituo vya afya pale, zahanati hazina umeme, vilevile na Kata ya Nyandoto.

Mheshimiwa Spika, ningependa kujua sasa ni lini, na nimekuwa nikiuliza haya maswali, ni lini huu umeme wa REA utaweza kufika kwenye hayo maeneo ambayo hayana umeme kabisa, ili sasa hizo zahanati, vituo vya afya, sekondari na shule za msingi ziweze kupata umeme, pamoja na Wananchi? Ahsante.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza pamoja na kuwapongeza Wananchi wa Tarime kwa kupelekewa umeme katika vijiji vyote iko changamoto katika kata ambazo amezitaja, hasa Kata ya Nkende pamoja na Kenyamanyori na Kitale. Nimeshazungumza mpaka na Mkurugenzi alipie zahanati na shule zipelekewe umeme kwa sababu, vijiji na vitongoji vya maeneo hayo vina umeme. Kwa hiyo, nikupongeze Mheshimiwa kwa kufuatilia, lakini nikuombe uwasiliane na Mheshimiwa Mkurugenzi na Halmashauri ya Kijiji cha Nkende pamoja na Kijiji cha Kitale na Kenyamanyori waweze kulipia ili shule na zahanati zipelekewe umeme.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili, nyongeza ya hilo, nitapenda nitembelee mimi mwenyewe ili nikatoe maelekezo kwa wakurugenzi waweze kulipia. Mheshimiwa Esther hata akibaki nitakwenda mwenyewe ili kusudi maeneo hayo na zahanati ziweze kupatiwa umeme, ahsante sana. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Nyanghwale ina vijiji 62 na mpaka kufikia leo hii ni vijiji saba tu ambavyo vimeshawashwa umeme na vijiji 13 tayari nguzo zimeshasimama. Nimeongea na mkandarasi kwa nini hajawasha vile vijiji 12 akadai kwamba, kuna upungufu wa nyaya.

Je, Waziri anatuambia nini kuhusu upungufu huo wa nyaya?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza kwa taarifa hiyo nashukuru kuipokea, kwanza umenipa jukumu la kufuatilia, nikuhakikishie nitalifuatilia hilo.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusiana na upungufu wa nyaya naomba nitoe taarifa kupitia Bunge lako Tukufu na kwa Watanzania hivi sasa hapa nchini hatuna shida na nyaya wala nguzo wala mita, changamoto inaweza ikawa ni utaratibu wa wakandarasi wenyewe namna ya kuhifadhi hivyo vifaa.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii Mheshimiwa Mbunge nimfuatilie mkandarasi tumfuatilie tujue changamoto ni nini, lakini tunachomuagiza kupitia Bunge lako Tukufu, napenda nichukue nafasi hii kumuagiza Mkandarasi wa White City anayetekeleza Mradi wa REA katika Mkoa mzima wa Geita, ikiwemo na Nyanghwale, achukue hatua za kuhakikisha vifaa vyote vinapatikana site na kazi ikamilike ndani ya wakati.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza pamoja na majibu aliyonipa Mheshimiwa Naibu Waziri umeme mahali ambako umekwenda kama alivyosema kwenye majibu ya swali maeneo ya taasisi na visima vya maji vimerukwa. Swali la kwanza kata za Mahitadu, Masieda, Endage Chan, Heda Chini, Getiree, Bashai, Endamillai, Rolward, Endargati, Esheshi, lini zinapata umeme?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru pia umefika kwenye jimbo langu na Mheshimiwa Waziri amefika na iko ahadi ya vijiji 22 kupatiwa umeme mwaka huu. Na leo ni bajeti ya wizara yako je, Mheshimiwa Waziri vijiji hivi na ahadi hii vipo katika bajeti hii au nitegemee nini niwaambie wananchi wa Mbulu Vijijini?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri katika maswali ya msingi ya Mheshimiwa Mbunge. Nimpongeze sana Mheshimiwa Flatei Massay Mbunge wa Mbulu Vijijini alivyofuatilia masuala ya umeme vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli zipo kata sita ikiwemo Masieda, Yaendachini pia Endagi chan pamoja na Gorand, na Esheteshi pamoja na Bashi. Zipo umbali wa takribani kilometa 15 kutoka Ngoradi na kilometa 14 kutoka Mbulu Mjini. Lakini utaratibu tunaofanya sasa wananchi wa kata hizo TANESCO pamoja na REA wameshaanza kushirikiana na utekelezaji wa kupeleka umeme katika vijiji hivyo unaanza mwezi Julai mwaka huu na utakamilika Desemba mwaka huu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge wafikishie taarifa wananchi wa Mbulu Vijijini kwamba utekelezaji wa miradi hiyo katika kata hizo utafanyika kama kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili ahadi ni lini, taasisi pamoja na maeneo mengine tuwape uhakika. Mheshimiwa Mbunge anavyofuatilia masuala ya Mbulu Vijijini anavyo vijiji 76 na kati ya hivyo tayari vijiji 32 tumevipatia umeme, vijiji vinavyobaki nikupe taarifa na tathmini ya Serikali imekamilika vyote vitapelekewa umeme ifikapo mwezi Juni, 2021.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, pamoja na majibu ya matumaini ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, moja ya changamoto kubwainayochelewesha kukamilika kwa wakati kwa miradi yah ii ya REA ni tofauti ya size ya transfoma iliyopo kwenye mikataba ya kVA 33 na ukubwa na laini ambazo wanachukulia ule umeme. Jambo hili limesababisha kuchelewa kwa Miradi ya REA ya kukamika kwenye Jimbo la Korogwe Vijijini, kwenye vijiji vya Kulasi na vijiji vya Mswaha Majengo, nguzo zimesimama kwa zaidi ya miezi sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itatoa maelekezo kwa REA kuharakisha utatuzi wa changamoto hizi ili wananchi hawa waweze kupata umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika Jimbo la Korogwe Vijijini zipo kata tano ambazo vijiji vyake vyote katika kata hizo havijafikiwa na huduma ya umeme. Kata za Kizara, Foroforo, Kararani, Mpale na ya Mswaha. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, uko tayari kuwahakikishia wananchi wa kata hizi kuiwapa kipaumbele na kupata umeme kwenye mwaka wa fedha unaoanza Julai mwaka huu?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi la Mheshimiwa Mnzava, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Mnzava, pampja na kwamba si Mbunge wa muda mrefu, lakini kafanya mambo makubwa sana kwenye jimbo lake hata nilizotembelea. Baada ya kusema hayo basi napenda nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mnzava.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, ni kweli, katika Kijiji cha Kurasi Kibaoni pamoja na Mswaha Majengo, kuna transfoma zilifungwa za kVA 33, lakini tumeshamwelekeza mkandarasi kuanza kushusha kutoka kVA 33, kwenda kVA 11 kuanzia Jumamosi iliyopita. Kwa hiyo, vijiji viwili vya Kulasi pamoja na Mswaha vimeshaanza kupelekewa umeme na vitapata umeme mwisho wa wiki hii. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Mnzava katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kweli zipo kata tano ambazo zilikuwa hazijapata umeme katika Jimbo la Korogwe Vijijini na kati ya kata tano tayari kata moja ya Mswaha- Majengo imeshaanza kupelekewa umeme. Zimebaki kata nne ya Foroforo pamoja na Kirarani ambazo nazo zinaanza kupelekewa umeme kuanzia Julai mwaka huu na kufikia Juni, mwakani nafikiri zitakuwa zimepatiwa umeme. Nimpongeze sana Mheshimiwa Mzava, aendelee kutupa ushirikiano.

Mheshimiwa Naibu Spika, na nilipotembelea tarehe 22 kwa Mheshimiwa Mnzava, Kijiji cha Mkalekwa pamoja na Welei vilipelekewa umeme na nikaagiza Kijiji cha Kulasi nacho kiwashwe umeme. Kimeshawashwa umeme tangu tarehe 28 mwezi uliopita. Kwa hiyo, nashukuru sana Mheshimiwa Mnzava tuendelee kushirikiana. Ahsante sana.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, Serikali ilitoa maelekezo kwamba kwamba wananchi vijijini waunganishiwe umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 bila kujali kama ni kupita REA au TANESCO, lakini agizo hili bado halitekelezwi na wananchi maeneo mengi wanapata shida kwa kutakiwa kulipa gharama ileile ya zamani. (Makofi)

Je, nini kauli ya Serikali juu ya jambo hili? Nashukuru.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nijibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa
Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kuanzia tarehe moja Mei mwaka huu tumetoa maelekezo nchi nzima kwamba pamoja na kwamba katika baadhi ya maeneo ambako REA ilikuwa haijafika, kuunganishwa umeme ilikuwa ni tofauti na 27,000; lakini ili tuweze kushambulia, vijiji vyote vipelekewe umeme haraka iwezekavyo Serikali imetoa maelekezo kwamba vijijini umeme wataunganishiwa kwa 27,000 na si vinginevyo, iwe anapeleka TANESCO, iwe anapeleka REA, iwe anapeleka mkandarasi yeyote aliyepewa kazi na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niwape taarifa Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote nchini kote, hakuna mahala ambapo umeme utapelekwa tofauti na 27,000 ili mradi ni vijijini. Kwa hiyo, maagizo haya nimeyatoa na Serikali imeyatoa na tutaendelea kufuatilia hilo. Tupe ushirikiano Mheshimiwa Mbunge ikibidi tutatembelea jimbo lako ili tuwafafanulie vizuri wananchi. Hayo ndiyo maelekezo ya Serikali. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Waziri, utakumbuka siku za karibuni umefanya ziara kwenye Mkoa wa Mtwara na hasa Wilaya ya Masasi ili kuweza kuona athari zilizopo hasa zaidi kwenye vijiji vile ambavyo vinapitiwa na umeme mkubwa ukielekea Wilayani Masasi.

Sasa swali, toka umeondoka takribani ni wiki mbili sasa, unaweza kutueleza ni hatua gani na ni kazi gani inatakiwa kufanyika katika maeneo hayo?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nijibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mwambe kuwa ziko hatua tatu, la kwanza katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge, ingawaje nilifika jimboni uliniagiza tu haukuweza kuwepo, lakini tumekuwashia vijiji viwili.

Kwa hiyo, ni hatua ya kwanza imefanyika, lakini hatua ya pili tumeainisha maeneo yote ya Jimbo la Masasi ambapo umeme haukufika, wakandarasi wameshapewa maeneo hayo na mengine tumewapa TANESCO kwa sababu bei ni moja ili maeneo hayo yafanyiwe kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya tatu mkandarasi ameshapeleka nguzo na vitendea kazi maeneo yote ili kazi iweze kwenda kwa haraka zaidi. Hizo ndizo hatua tumechukua. (Makofi)
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa muda wa kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Mkoa wa Katavi unaongoza kwa vifo vya watoto wachanga. Takwimu tu za mwaka 2018 zinaonesha kwamba Mkoa wa Katavi ulipoteza watoto wachanga 581. Hii ilisababishwa na ukosefu wa vifaa bora wakati akina mama wakijifungua lakini hata vifaa hivyo vikiwepo kwenye vituo hivyo vya afya haviwezi kufanya kazi kwa sababu havina umeme. Je, Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini pamoja na WIzara ya Afya ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba vituo vile vya afya ambavyo havina umeme Mkoani Katavi vinapata umeme ili viweze kutumia vifaa vya kisasa kuokoa vifo vya mama na motto? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa wauguzi wengi Mkoani Katavi hawana mafunzo, Serikali kupitia Wizara ya Afya ina mkakati gani wa kutafuta wadau wa afya ya mama na mtoto ili tuweze kutokomeza vifo hivi Mkoani Katavi? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya katika majibu ya swali lake la msingi. Pia niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza swali kuhusu upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika Mkoa wa Katavi baadhi ya vijiji havijaanza kufikiwa na mkandarasi. Nimpe taarifa tu Mheshimiwa Mbunge maeneo yote ambayo ameyauliza Mheshimiwa Mbunge mkandarasi ameshaanza kwenda site. Katika Mkoa wa Katavi kuna vijiji 149 vitapelekewa umeme. Sasa hivi mkandarasi ameshawasha Mchakamchaka lakini anaendelea na Kaparara na katika vijiji vingine saba atawasha kuanzia wiki inayokuja. Kwa hiyo, wananchi wa Katavi wategemee kupata umeme katika maeneo yote. Kesho kutwa watawasha kwenye Mgodi wa Society kwa Mheshimiwa Kapufi. Kwa hiyo, mkandarasi yuko site vijiji vyote vitapatiwa umeme kwenye kipindi hiki cha Julai mpaka Desemba mwaka huu. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ambapo sehemu ya swali la kwanza ameshalijibu Mheshimiwa Waziri wa Nishati. Niendelee na kipengele kingine ambacho kilikuwa kimebaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge amesema kwamba idadi ya vifo vya watoto katika Mkoa wa Katavi ni vingi sana na hili ni kweli lakini halitokani na ukosefu wa huduma za afya kwa watoto wachanga. Mkoa wa Katavi una changamoto kubwa sana ya mimba za utotoni. Wastani wa Kitaifa sasa hivi tuna asilimia 27 ya watoto kati ya miaka 15 mpaka 19 aidha wana watoto au wana mimba. Katika mikoa ambayo inaongoza ndani ya nchi yetu ni pamoja na Katavi, umri wa kupata ujauzito bado ni mdogo sana na kwa kuwa bado hawajafikia ukomavu uliotosha, hili nalo linachangia sana katika vifo hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na masuala ya mafunzo, Serikali inaendelea kujipanga na imekuwa inaweka utaratibu wa mafunzo endelevu kwa watoa huduma wake wa afya katika ngazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafunzo kwa ajili ya huduma ya mama na motto. Katika Mkoa wa Katavi, Serikali imekuwa inashirikiana kwa karibu sana na wadau.
MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri na wananchi wa Kibaha Mjini wanaunga mkono jitihada za Serikali za maendeleo hususan katika sekta ya umeme.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo kama unavyoona ni takribani miaka sita sasa na leo ni mara ya nne nauliza swali hili hapa Bungeni. Naomba sasa Mheshimiwa Waziri atoe kauli thabiti kwamba malipo haya kwa wananchi wa Mnalugali, Boko, Sofu, Zegereni watalipwa lini fidia hii ili sasa na wenyewe waweze kushiriki na kufurahia miradi hii mikubwa ya umeme?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, miradi ya umeme katika Mji wa Kibaha na hususan peri-urban na densification imekuwa ikisuasua na haijakamilika. Miradi hii imepita pembezoni mwa wananchi wengi na wanalalamika kwamba hawakuweza kufikiwa na miradi hii. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha sasa miradi hii inakamilika na wananchi wanapata umeme ili kufaidi maendeleo na matunda ya nchi yao?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi la Mheshimiwa Koka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli usanifu wa mradi huo ulianza miaka mingi toka miaka mwaka 2015 na 2016 lakini baadaye tulipoanza kutekeleza mradi mkubwa wa Julius Nyerere mwaka 2018, tulifanya usanifu upya ili kuhakikisha kwamba mradi huu unakuwa ni mpana na endelevu. Mradi huu ambao unahusisha fidia ya wananchi wa Kibaha utahusisha pia fidia ya wananchi wa kutoka Kinyerezi, Kiluvya, Chalinze, Kibaha mpaka kufika Dodoma na unaelekea mpaka Singida.

Mheshimiwa Spika, taratibu kama ambavyo ameeleza Mheshimiwa Naibu Waziri, tumeanza kufanya matayarisho ya malipo na sasa tumetenga shilingi bilioni 21.56 kwa ajili ya kuwalipa wananchi wote. Wananchi wa Kibaha peke yake ambao wanafika 432 wenye jumla ya shilingi milioni 932 malipo yao yameshaanza kutayarishwa. Malipo hayo yanakwenda sambamba na ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme kutoka mradi mkuu wa Julius Nyerere utakaofua megawatt 2,115 kutoka Rufiji-Chalinze, Chalinze- Dar es Salaam (kilometa 115) na pia Chalinze-Dodoma, ambapo tumetenga jumla ya shilingi milioni 32.82. Kwa kuwa ujenzi wa mradi wa huu utaanza kabla ya mwezi Juni, ni matumaini yetu na kwa maandalizi mazuri ya watu wa Wizara ya Fedha tutaanza kuwalipa wananchi kabla ya mwezi Juni mwaka huu.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuhusiana na suala la peri- urban na densification, tumeanza programu ya kupeleka umeme kwenye maeneo yote ya ujazilizi. Maeneo ya kutoka Dar es Salaam mpaka hapa Dodoma takriban vitongoji 12,822, utekelezaji umeanza katika maeneo Dar es Salaam hadi Kibaha kwa vitongoji 272 ambapo vitongoji vya Mheshimiwa Koka vimo. Pia tunapeleka umeme kwenye peri- urban anayoizungumza Mheshimiwa Koka kwa maeneo yanayofanana na vijiji ya Kibaha ambayo siyo vijiji kwa kwa gharama ya shilingi 27,000 na utekelezaji umebaki mitaa 12 kati ya mitaa 128. Mradi huu unakamilika mwezi Mei, mwaka huu.

Napenda kumwambia Mheshimiwa Koka awape taarifa wananchi wa Kibaha kwamba peri-urban na densification katika eneo lao inakamilika mwezi Mei, mwaka huu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwa sababu amenihakikishia kwamba mradi unakamilika Machi mwaka huu, napenda sasa kupata kauli ya Serikali kwa sababu bado tuna vijiji takribani 25 pale Biharamulo ambavyo havina umeme, kwa hiyo, labda ningehakikishiwa na Serikali sasa kwamba wakazi wa Biharamulo wajipange kwa ajili ya kusambaziwa umeme kwa sababu jibu ilikuwa tuko low voltage ndio maana hatukusambaziwa umeme katika vijiji vingine. Kwa hiyo, labda nipate kauli ya Serikali kutuhakikishia kwamba vijiji vilivyobaki baada ya kukamilika mradi huu vitaweza kupata umeme pia? Ahsante sana.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, uniwie radhi sana ili niweze kusimama kwa ajili ya kuongeza majibu na nimesimama kwa sababu hivi karibuni nilitembelea Biharamulo.

Mheshimiwa Spika, Biharamulo wana vijiji takribani 79 na bado vijiji 27. Hivi karibuni pamoja na Mheshimiwa Mbunge nilitembelea vijiji hivyo, tumeshakamilisha matayarisho yote na si kwa Biharamulo peke yake.

Napenda nitoe taarifa mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba vijiji vyote ambavyo havijapata umeme 2,159 kati ya vijiji 12,268 tunaanza kuvipelekea umeme kuanzia tarehe 15 mwezi huu ndani ya miezi 18, nimeona nianze na taarifa hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa Biharamulo umeme ambao tunajenga ambao kwenye jibu la msingi umeelezwa wa kutoka Geita-Nyakanazi, Nyakanazi-Rusumo na Nyakanazi- Kigoma ni mwarobani kwa kuwapatia umeme wananchi wa Biharamulo na Mkoa wa Kagera na mikoa ya Geita pamoja na Kigoma. Mradi wenyewe peke yake kabla ya kupeleka umeme kwenye mpango wa REA utapeleka vijiji 32 na katika vijiji 32 vijiji saba ni vya Biharamulo, ikiwemo Nyakafundwa, Kalenge, Kasonta pamoja na Nyanyantakala, Mavota mpaka Nakahanyia vyote vitapelekewa umeme.
MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Wilaya ya Kasulu kuna mgao mkubwa sana wau meme. Yako maeneo hasa maeneo ya Makele, kila ikifika jioni lazima umeme ukatike na wananchi wanakosa huduma ya kuangalia tarifa ya habari, lakini na maeneo mengine mengi ya Wilaya ya Kasulu. Nataka kujua majibu ya Serikali nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba tena wa muda mfupi, kwamba unakomesha mgao huu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Mkoa wa Kigoma, REA awamu ya III imeanza kwanza kwa kuchelewa lakini pili maeneo mengi hayajafikiwa na mradi, lakini pia mradi huo unasuasua. Je, Waziri yupo tayari kutuma wataalam wake au yeye mwenyewe kuja Mkoa wa Kigoma hasa Kasulu Vijijini ili kuhakikisha kwamba anakutana na wakandarasi ili waweze ku-speed up utekelezaji wa mradi? Nashukuru sana.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri wangu, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Vuma, Mbunge wa Kasulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Vuma pamoja na Wabunge wengine wote kutoka Kigoma, kwa kazi kubwa walizofanya katika kufuatilia Mkoa wa Kigoma kupata Gridi ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kulikuwa na changamoto kubwa sana ya kiumeme katika Mkoa wa Kigoma na Mkoa wa Katavi, lakini kama ambavyo limejibiwa kwenye swali la msingi, Serikali imeanza kutekeleza mradi wa kupeleka umeme wa Gridi katika Mkoa wa Kigoma kutoka Tabora. Tumeanza kujenga toka mwaka jana mwezi Januari, kutokea Urambo, tunajenga sub-station na tumeshaanza kujenga na tumeshaanza kujenga sub-station ya pili tunajenga Nguruka na ujenzi unaendelea na sub-station ya tatu tunajenga Kidahwe Mjini Kigoma, nako ujenzi unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunajenga njia ya kusafirisha umeme mkubwa kilovoti 400 kutoka Kigoma na kusambaza maeneo yote ya Wilaya ya Kigoma ikiwemo, Kasulu, Kibondo, Kakonko na maeneo mengine na ujenzi umeshaanza. Naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Vuma, Mheshimiwa Profesa Ndalichako na Waheshimiwa Wabunge wengine wa Kigoma kwamba tunatarajia kukamilisha mwakani mwezi Desemba, shughuli zote na Gridi ya Taifa itakuwa imefika kwenye Mkoa wa Kigoma.

Pia kwa upande wa matumizi pia ya umeme Kigoma kwa sasa wanatumia mashine za mafuta ni vema nikawaambia Waheshimiwa Wabunge ili wajue, ingawa uendeshaji kwa kweli ni mkubwa na kwamba tunatambua mahitaji ya umeme, hatuna namna mbali na kuwalisha umeme kwa utaratibu huo kwa sasa.

Mheshimiwa Spika, mahitaji ya wananchi wa Kigoma kwa siku ni megawatt 5.2 pamoja na kwamba mashine tulizonazo pale ni megawatt 2.6 na tunazidisha mara nne zinafikisha kama megawatt 8 lakini kwa sababu ya njia kuwa ndefu na umeme unachotwa kwenye mafuta bado umeme ule unakuwa hauna nguvu. Ndio maana mnaona mara nyingi umeme unakatika sio mgao isipokuwa umeme unakatika kutokana na njia kuwa ndefu na source yake ni mafuta. Nimeona niliweke vizuri suala hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, maeneo ya REA yaliyobaki ni kweli katika Mkoa wa Kigoma na hasa Kasulu kwa Mheshimiwa Vuma, Mheshimiwa Vuma ana vijiji 61 na tumeshapeleka umeme kwenye vijijini 42 bado vijiji 19 na tulizindua pale Lusesa na Lusesa kazi inaendelea. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Vuma anavyofuatilia masuala haya na kwa sababu utekelezaji wa umeme katika vijiji vyote kama alivyoeleza Mheshimiwa Naibu Waziri unaanza tarehe 15 mwezi huu na tunarajia ndani ya miezi 18 kukamilisha vijiji vyote katika nchi yetu, vijiji vyote vya Mheshimiwa Vuma vitapata umeme mapema sana. Hata hapo Makere umeme unaokwenda kutoka pale mpaka mpakani mwa Rwanda na Burundi tutaunganisha na majirani zetu wa Rwanda na Burundi kupitia mradi wa Rusumo ili maeneo ya mipakani mwa Tanzania, Rwanda na Burundi nayo yapate umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi.

Kwa kuwa wananchi wa Jimbo la Kalenga hasa Vijiji vya Wangama, Lupembelwasenga pamoja na Welu kwa kutaja tu vichache tayari walishaunganisha umeme, walishalipia na walishafanya wiring lakini hawajawashiwa umeme mpaka sasa.

Je, Serikali inatoa kauli gani ili wananchi hao waweze kuwashiwa umeme wao? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri katika maswali ya nyongeza. Vilevile nawapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa kuuliza maswali ya msingi sana katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wateja wote ambao wameshafanya malipo na wanasubiri kuunganishiwa umeme pamoja na wateja wote ambao wameshafanyiwa survey, lakini wanasubiri kuunganishiwa umeme, tumetoa muda wa miezi mitatu wateja wote wawe wameshaunganishiwa umeme nchi nzima. Kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Mbunge wa Kalenga kwa kuuliza swali hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ili kuharakisha shughuli za kuwaunganishia umeme wateja nchi nzima, tumebadilisha mpango wa wataalam wetu kusubiri magari, badala yake TANESCO itawanunulia magari ma-surveyor wote na ma-technician ili wawahi kuwaunganishia umeme wananchi, ndani ya muda uliokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongeze kidogo kuhusiana na suala la maeneo ambayo ni ya mijini; kulingana na swali ninalojibu ambalo Naibu Waziri amejibu vizuri, lakini niongezee kidogo. Iko mitaa mingi ambayo iko karibu na miji na vijijini hasa katika maeneo ambayo ni ya Majiji na Manispaa, likiwemo Jiji la Mbeya, Iringa, Mwanza, Dodoma hapa, mradi wa peri-urban unaendelea na miradi yote katika mitaa 122 itapelekewa umeme ndani ya miezi sita ijayo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu yenye furaha kidogo kwa wananchi wangu.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kuna ajira nyingi sana zinasemwa kuwepo katika mradi huu, je, hawaoni kwamba wananchi wangu wa Kiteto hususan vijiji saba vile; Mwitikira, Ndorokoni, Dareta, Ovoponi, Kimana na Amei wakatengewa kabisa fursa za kibiashara na ajira za upendeleo kwa kuwa wao ndiyo wanabeba burden ya mradi huo kwa kilometa hizo 117?

Mheshimiwa Spika, swali lingine la pili dogo, je, Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuwa amesema Wizara itaendelea kuhamasisha wananchi wajitokeze kuchukua fursa hizi atakuwa tayari kuongozana na mimi tutembelee vijiji hivi saba ili tutumie wasaa huu kuendelea kuwaandaa wananchi wetu kwa fursa hizo, tena ikizingatiwa kwamba Mheshimiwa Rais, Mama Samia Hassan Suluhu jana amekwenda kwenye kutiwa saini sasa kwa mkataba huu na kwamba karibu sasa mradi unaanza? Nakushukuru.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nitoe shukrani kwa jibu zuri la Mheshimiwa Naibu Waziri katika swali la msingi la Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa taarifa ya jumla kwa wananchi wa Kiteto pamoja na maeneo mengine kwamba utekelezaji wa mradi huu unaanza mwezi huu Aprili, tulipanga tuanze mwezi Julai kama ambavyo tumeeleza kwenye jibu la msingi lakini tunaanza rasmi mwezi huu wa Aprili kwa muda wa miaka mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya wananchi wa Tanzania ni kweli mimi nilishiriki nikiwa na Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan utiaji saini utekelezaji wa mradi huu jana nchini Uganda. Mradi huu ni mkubwa utapita katika mikoa 8, wilaya 24, vijiji 127, vitongoji 502 vikiwemo vijiji na vitongoji vya Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi utatoa ajira kwa zaidi ya Watanzania 10,000 katika hatua za awali na hadi ajira za Watanzania 15,000 katika shughuli za ujenzi na shughuli za kawaida. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kuwaomba sana wananchi hasa katika maeneo ambapo mradi utapita wajitokeze kuchukua hizi fursa kwa sababu tumeziweka rasmi kwa ajili ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spili, swali la pili la kufuatana naye, tumepanga kuanzia Kyaka nchini Tanzania kule Kagera hadi Tanga Chongoleani, tutaanza kufanya ziara wilaya kwa wilaya, mkoa kwa mkoa ili kuhamasisha Watanzania kuchukua fursa hiyo. Kwa hiyo, tutafika na katika eneo lake na kutembelea vijiji hivyo saba ambavyo Mheshimiwa amevitaja.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini vilevile kwa commitment ambayo ameitoa kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe. Nataka nitoe tu ushauri kwamba katika kutekeleza mkakati huo, wasisahau taasisi muhimu, hususan shule za boarding, kwa sababu katika Mkoa wa Songwe, shule nyingi sana za boarding zinakabiliwa na changamoto ya kutokuwepo kwa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niulize swali langu moja la nyongeza. Utakubaliana nami kwamba upatikanaji wa umeme wa uhakika ni aspect muhimu sana katika kukuza uchumi wa eneo husika; nasi wananchi wa Mkoa wa Songwe tunakabiliwa na changamoto kubwa sana ya kukatika katika kwa umeme mara kwa mara; na hii imekuwa ni changamoto kubwa hususan katika ile miji mikubwa ya kibiashara kwa maana ya Miji ya Mlowo, Tunduma kule kwa Mheshimiwa David Silinde na Vwawa:- (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka kujua kwamba je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kwenda ama kutuma wataalam wake katika Mkoa wa Songwe ili kuweza kubaini changamoto hiyo na kuipatia ufumbuzi? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri katika swali la msingi la Mheshimiwa Shonza. Kwanza, ni kweli zipo taasisi nyingi ambazo kimsingi zinahitaji kupatiwa umeme, hasa huu wa Programu ya REA; na tumeainisha taasisi zote zikiwemo shule za msingi, sekondari na vituo vya afya, na tumetoa maelekezo kwa wakandarasi kuzingatia kipaumbele cha kupeleka umeme kwenye taasisi za Umma kama kipaumbele. Kwa hiyo, naomba nitoe msisitizo kwa wakandarasi kuzingatia hilo. Pili, nawaomba Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri kutenga fedha kidogo angalau kulipia kupelekea taasisi za Umma umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika swali la pili ambalo ni la uimara wa umeme katika Mkoa wa Songwe. Nampongeza sana Mheshimiwa Shonza na Wabunge wa Songwe kwa ujumla kwa kufuatilia masuala ya umeme katika mkoa wao. Ni kweli Mkoa wa Songwe unapata umeme kutoka Iyunga iliyoko Mbeya, na ni takribani kilometa 70 kutoka kwenye kituo cha kupoozea umeme.

Mheshimiwa Spika, tumechukua hatua mbili madhubuti, na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na wananchi wa Songwe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, hatua ya kwanza, tumejenga njia ya kusafirisha umeme kwa dharura kwa kuepusha kukatika kwa umeme katika Mkoa mzima wa Songwe kwa kujenga laini ya kilometa 70 kutoka Iyunga mpaka Mlowo; na tumeanza hivyo toka Januari na mradi unakamilika Mei mwaka 2021. Tumetenga shilingi bilioni 2.4 ambazo ni fedha za ndani.

Mheshimiwa Spika, maeneo yatakayopelekewa umeme ni Mlowo, Tunduma, Vwawa yenyewe pamoja na Momba; na tutagawa laini specific kwa kazi hiyo. Kwa hiyo, kuazia mwezi Mei mwaka huu, maeneo ya Songwe yatapata umeme wa uhakika. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Tatizo ambalo lipo katika Mkoa wa Songwe linafanana kabisa na tatizo ambalo liko katika Mkoa wa Dar es Salaam kwenye baadhi ya maeneo, na hasa katika Jimbo la Ukonga kwenye baadhi ya Mitaa ya Kata za Msongola, Chanika, Zingiziwa na Buyuni:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inasema nini kwa habari ya kuhakikisha kwamba Mkoa wa Dar es Salaam unapata umeme?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Dar es Salaam una mahitaji makubwa sana ya umeme, ingawa Dar es Salaam tuna jumla ya Megawati 572 zinazotumika kwa Dar es Salaam, lakini mahitaji yanaongezeka kila leo. Tumejenga dedicated line ya kutoka Kinyerezi kupita Gongo la Mboto kwenda mpaka Ukonga – Pugu mpaka Dondwe kule Chanika Zingiziwa kwa ajili ya kupelekea umeme wananchi wa huko.

Mheshimiwa Spika, tumewapatia mkandarasi wa peri-urban atakayepeleka umeme katika maeneo ya Bomba Mbili, Majohe, Mvuti, Songambele pamoja na Zingiziwa mpaka Kisasa, mpaka Magerezani kule Dondwe ndani. Kwa hiyo, wananchi wa Dar es Salaam watapata umeme, na ni ndani ya miezi sita utaratibu utakamilika na wananchi kupata umeme wa uhakika.
Je, ni lini wananchi wa Kata ya Ugalla watapatiwa umeme wa REA III?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, wananchi wa Kata ya Ugalla pamoja na vijiji tisa, wataanza kupatiwa umeme kuanzia mwezi Juni mwaka huu mpaka mwezi Mei mwaka ujao. (Makofi)
MHE. NOAH L.S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, kwanza jina langu naitwa Noah Lemburis Sabutu Mollel.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza kabisa, namshukuru Naibu Waziri kwa kurekebisha kwamba siyo milioni 314 badala yake ni bilioni 314 ndiyo inayodaiwa na Halmashauri Arusha DC.

SPIKA: Amerekebisha wapi.

MHE. NOAH L.S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, kwenye majibu ya maswali hayo iliandikwa milioni 314 badala ya bilioni 314.

SPIKA: Sasa wewe ndiyo unatutaarifu hilo Mheshimiwa, siyo walitakiwa waseme wao kama hivyo ndivyo? Endelea na swali lako lakini.

MHE. NOAH L.S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza maswali yangu mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa suala hili la ulipaji wa fidia ya umeme lilikuwa liende sambamba na usambazaji wa umeme kwenye Jimbo la Arumeru Magharibi na vijiji vyake hasa ukizingatia kwamba mkandarasi amechimba mashimo ameacha, ameweka nguzo ameacha ajaweka waya, ni lini sasa Serikali itamaliza tatizo hilo?

SPIKA: Tatizo gani?

MHE. NOAH L.S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, la kutokuwepo kwa umeme kwenye jimbo.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa sasa hali ni tete kwenye jimbo kuhusu masuala hayo mawili ya fidia na usambazaji wa umeme, Naibu Waziri yupo tayari tuweze kuongozana naye kwenda kuokoa jahazi ambapo hali ni tete kwenye jimbo?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwenye swali la msingi naomba niliweke vizuri hoja ya Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine ambao wanapitiwa na mradi wa kilovolt 400 wa kwenda Namanga. Ni kweli Serikali imetoa shilingi bilioni 52.67 katika maeneo yote ambako laini inapita. Lakini kila eneo ilipewa fidia yake kulingana na idadi ya watu waliofanyiwa tathmini kwa hiyo pesa hiyo inagawanywa katika maeneo yote ambako line imepita.

Mheshimiwa Spika, juzi nilikuwa Arusha na kati ya changamoto ambazo nilikutana nazo ni pamoja na hii, akiwepo na Mheshimiwa wa Longido, nilitoa maelekezo ya jumla kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, wananchi ambao hawajalipwa fidia kwa sasa ambao pesa zao zimeshapelekwa tayari kwa Wakurugenzi wao walipwe fidia hizo mara moja toka juzi. Ni kweli zinaweza zikawa zinatofautiana kiwango kwa kiwango kila wilaya lakini ya jumla ya fedha zake ni hizi. Lakini majibu ya jumla nishatoa juzi, kwa Mheshimiwa Mbunge wa Longido na wananchi walilidhika na Wakurugenzi walikubali na Wakuu wa Wilaya kuanza kulipa fidia hizo mara moja kutoka juzi ndani ya siku 10.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili kuhusiana na maeneo ambayo amezungumza ambayo ajapelekewa umeme nimetoa maelekezo na wakandarasi wote wako site na leo tunakutana nao, maeneo yote ambayo awajapatiwa umeme wakandarasi wameanza kazi toka Mwezi Machi na katika wilaya za Arusha wameanza wiki iliyopita na watapelekewa umeme ndani ya miezi 18 kutoka mwezi Machi hadi mwezi Mei. Ahsante sana.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa licha ya Kata ya Lukulaijo kuwa jirani na Kata ya Nkwenda ambayo ni mjini bado kuna vijiji viwili ambavyo havina umeme ambayo ni Kijiji cha Mgorogoro lakini na Kijiji cha Mkombozi, nataka nijue commitment ya Serikali kwa sababu vile vijiji havipo mbali; ni lini vitapelekewa umeme?
WAZIRI NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya katika maswali ya nyongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa Mheshimiwa Anatropia, vijiji vyote na mitaa yote ya mjini pamoja na maeneo ambayo ni Mgorogoro pamoja na Lukulaijo na maeneo mengine ambayo yamebaki tumesha-design mkandarasi wa peri-urban ambaye ataanza kupeleka umeme mwezi ujao, na ndani ya miezi tisa atakamilisha maeneo yote ya kwa Mheshimiwa Mbunge watakuwa wameshapekewa umeme. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Wilaya ya Tanganyika ni miongoni mwa Wilaya ambazo zilichelewa sana kupata umeme wa REA. Kwa bahati nzuri kwa sasa Serikali inatekeleza mradi huo. Kwenye Mradi wa REA phase II vipo vijiji vilisahaulika kuingizwa kwenye mradi. Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha vijiji vilivyosahaulika katika mradi wa phase II?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kakoso, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri katika swali la msingi na swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Mbogo. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Kakoso pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote wa Katavi pamoja na Mpanda wanavyofuatilia masuala ya umeme vijijini katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli yapo maeneo nchi nzima ambayo yalisahaulika na yalikuwa yanafikia takriban maeneo ama vijiji 610.

Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge pamoja na Mheshimiwa Kakoso vijiji vyote 610 ambavyo vilisahaulika tumefanya marejeo na vijiji vyote vimeingia kwenye mpango na vimekabidhiwa wakandarasi kwa ajili ya utekelezaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Kakoso kwa sababu ni kweli hata kata kubwa ya Mishamo pamoja na Mwese pamoja na Utamata vilisahaulika lakini vyote vimeingia kwenye mpango na wananchi wote watapata umeme kwa uhakika ndani ya miezi 18 kutoka sasa. (Makofi)
MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza, je, ni lini Serikali itaweza kutuongezea transformer nyingine kwenye Jimbo la Temeke kwani tuna mahitaji ya megawatt 117, lakini sasa hivi tunatumia megawatt 32. Je, tutapata lini transformer hii nyingine? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kilave, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Jimbo la Temeke pamoja na Mbagala na Mkuranga tumelazimika kuongeza vituo vitatu katika kila wilaya kwa ajili ya kuongeza transformer za megawatt 48 kila mahali, kwa hiyo Temeke, Mbagala pamoja na Mkuranga tunaongezea transformer ya megawatt 48 kila eneo. (Makofi)
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia swali dogo la nyongeza. Wilaya ya Shinyanga Mjini licha ya kuwepo kwa umeme wa kutosha kutoka kwenye gridi ya Taifa, lakini kumekuwa na tatizo kubwa sana la kukatikakatika kwa umeme. Je, Serikali ipo tayari sasa kuja na hasa Mheshimiwa Naibu Waziri, yupo tayari kuongozana na mimi kwenda kule Shinyanga Mjini kusikiliza wananchi jinsi wanavyoathirika kibiashara pamoja na kijamii?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mayenga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namruhusu Mheshimiwa Naibu Waziri kufuatana naye katika Jimbo lake kwa siku alizotaja. Hata hivyo, tatizo la kukatika kwa umeme katika Mkoa wa Shinyanga inatokana na matengenezo yanayofanyika kwa sasa katika line ya Segese ya umbali wa kilometa 12. Kwa hiyo mara nyingi tunataoa matangazo kurejesha hali ya umeme katika hali yake ya kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Shinyanga unapata umeme kutoka substation ya Ibadakuli yenye megawatt 182 ambapo mahitaji ya Mkoa wa Shinyanga ni Megawatt 123. Kwa hiyo umeme wa Mkoa wa Shinyanga unatosha, isipokuwa kwa sasa wananchi tunaomba radhi katika maeneo yote yanayopitiwa ikiwemo Ngokoro na maeneo mengine kwa sababu ya matengenezo ya line ya Segese. Ndani ya 14 matengenezo yatakamilika na umeme utarejea katika hali yake ya kawaida.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Njombe tunapitiwa na gridi inayotoka Makambako kwenda Songea, lakini bado tumekuwa na tatizo kubwa sana la ukatikaji wa umeme ambao sisi tunaamini pamoja na maelezo ambayo Waziri ameyatoa siku ya nyuma, tunaamini kutokana na grid stability, ni lini sasa suala la ukatikaji wa umeme usioisha wa Mkoa wa Njombe na Mji ya Njombe utafikia tamati? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwanyika, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli hasa katika eneo la Njombe pamoja na Ludewa umeme unakatika kwa kiasi kikubwa kwa sababu kuna matengenezo ya kufunga auto recloser ambayo inaimarika ndani ya siku 28. Pia katika maeneo ya Njombe na Ludewa ipo line ambayo tunaongezea, tumetenga shilingi bilioni 270 katika mikoa miwili na bilioni 100 kila mkoa kwa ajili ya shughuli za ukarabati wa mitambo na kuimarisha umeme katika Mkoa wa Makambako, Njombe pamoja na Ludewa. Kwa hiyo niwahakikishie wananchi wa Ludewa pamoja na Njombe kwamba ndani ya muda unaokuja ambao nimeutaja hali ya umeme itaimarika kwa kiasi kikubwa.
MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini ilitupa orodha ya makandarasi ambao wanafanya kazi katika wilaya zetu na majimbo yetu. Sasa, je, Serikali inaweza ikatupatia orodha ya awamu hii ya REA ya tatu, mzunguko wa pili, ni vijiji vipi na vitongoji vipi vitakavyofanyiwa kazi ili iwe rahisi kwa Waheshimiwa Wabunge kufuatilia na kutoa taarifa Serikalini?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vita Kawawa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipotoa yale mawasiliano ya mkandarasi na baadaye tukatoa mawasiliano ya Mbunge kwa Mkandarasi, tuliamini kwamba kwenye mawasiliano hayo masuala yote yanayohusiana na upelekaji wa umeme kwenye maeneo yetu yatafanyika. Aidha, sisi kama Wizara tuko tayari kuendelea kutoa ushirikiano na kutoa taarifa sahihi kabisa na kubwa kabisa za maeneo yapi yatakayofikiwa na umeme ili Waheshimiwa Wabunge sasa watuambie yale ambayo yanaonekana yamebaki kama Mheshimiwa Waziri alivyosema, vile vijiji 600 tayari tumevichukua ili sasa kwa wigo mpana tuweze kushirikiana pamoja kuhakikisha maeneo yote yanachukuliwa.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa majimbo ya mijini mitaa ndio kama vijiji. Swali, je, ni lini sasa Serikali itapeleka umeme kwenye mitaa yetu kwa mfano Jimbo la Iringa Mjini kata ya Isakalilo, Mtaa wa Kitasengwa Mkonga, Majengo Mapya; Kata ya Mkwawa, Mtaa wa Wahe na Hoho, Kata ya Igumbilo Mtaa wa Ulonge…

MWENYEKITI: Sio zote tena wewe taja moja tu.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia umeme katika mitaa. Sasa naomba nijibu swali lake la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumetenga mitaa 637 kwa nchi nzima ikiwemo mitaa kwa Mheshimiwa Jesca na mitaa yote itaanza kupelekewa umeme kuanzia mwezi Novemba mwaka huu ndani ya miezi 18. Tumetenga fedha hizo kwa awamu tunaanza na mitaa yote ambayo inafanana na hali ya kivijiji, lakini na mitaa mingine ambayo ipo katika majiji makubwa pamoja na manispaa kwa nchi nzima. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika awamu hii ya REA kila kijiji kimepewa kilomita moja, nataka nifahamu hizi kilomita moja zinaanza kuhesabiwa wapi, ndani ya kijiji au nje kwa sababu kuna vijiji vingine vimeachana kilomita tatu, kutoka kijiji kimoja mpaka kufika kingine? Ahsante.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwenisongole kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa katika swali la msingi na swali la nyongeza la Mheshimiwa Pallangyo. Vile vile nimpongeze Mheshimiwa Mwenisongole kuuliza swali la msingi ambalo kimsingi linawahusu Wabunge wote katika majimbo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumetoa utaratibu mkandarasi anapoingia katika kijiji angalau atumie umbali wa kilometa moja kusambaza umeme tofauti na ilivyokuwa huko zamani ambapo ilikuwa ni wateja wawili watatu wanne. Jambo la msingi hapa ni kwamba ile kilometa moja tunayoitaja ni ndani ya kijiji, sio kati ya kijiji kimoja na kingine, ndani ya kijiji akishafika. Hata hivyo, hao ni wateja wa awali, ataendelea kuunganisha wateja wengine kadri wateja wengine wanavyojitokeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, tusifungwe na kilometa moja, kilometa moja ni wateja wa kuanzia, badala ya kufunga transformer ukaiacha bila kuwa na mteja. Nimeona nitoe ufafanuzi wa jumla ili Waheshimiwa Wabunge wawe na imani na wateja wa kwanza wanaoanza na tuwaombe wananchi jirani na wateja wa kwanza wanaunganishwa waendelee kulipia umeme hili nao waendelee kuunganishiwa umeme. Ahsante sana.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na Kisiwa kikubwa cha Ukerewe kuwa kwenye matatizo ya umeme kwa takribani wiki tatu sasa, wananchi kwenye Visiwa vidogo vya Ilugwa na Ukara wamekuwa wananunua umeme, lakini hawapelekewi token. Je, nini kauli ya Serikali juu ya changamoto hii? Nashukuru sana.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Mkundi, Mbunge wa Ukerewe. Kesi ya wananchi wa Ukerewe inafanana sana na maeneo mengi ya visiwa, ambapo wakandarasi binafsi ambao wanapeleka umeme kwa wananchi wanaozalisha, kwanza wanauza umeme kwa bei kubwa tofauti na maelekezo ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, wameanza pia mchezo, wanapopeleka kwa bei ya Serikali hupeleka kwa kiwango kidogo. Naomba nitoe tamko mbele ya Mheshimiwa Mbunge wa Ukerewe na Waheshimiwa Wabunge, mara baada ya Bunge tutatembelea maeneo yote yenye kero ya namna hiyo na kutoa maelekezo kwa mameneja wetu kuwasimamia wakandarasi wa namna hiyo ili kupeleka umeme kwa bei elekekezi ya Serikali ya Sh.100 kwa unit na kuendelea kutoa umeme kwa wananchi kulingana na mikataba yao inavyowaelekeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitakwenda kwa Mheshimiwa Mkundi, Ukerewe. Pia nitatembelea Maisome na maeneo mengine ili kutoa maelekezo ya Serikali na namna ya kuyasimamia. Ahsante sana.
MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ni nini kauli ya Serikali kwenye Jimbo letu la Rungwe kuna vijiji 24 ambavyo vilikuwa kwenye REA II havijapatiwa umeme, lakini pia kwenye REA III, round ya pili vijiji tisa haviko kwenye orodha ya kupatiwa umeme katika hii REA III, round ya pili. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwantona, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza swali la maeneo ambayo yalisahaulika. Tumeshatoa maelekezo na taarifa kwa Waheshimiwa Wabunge, naomba tena nirudie tu. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Mbunge na kama kuna vijiji sita au tisa au vingapi ambavyo vilisahaulika tunaomba atuletee.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanya utaratibu baada ya wiki mbili zilizopita, kupitia maeneo yote ya nchi nzima katika vijiji vilivyosahaulika na viko vingi. Kwa Mheshimiwa Lukuvi vilisahaulika vijiji viwili na maeneo mengine, tumepata vijiji 610 na vyote tumeviingiza kwenye mpango wa kutekelezwa na tuna shilingi bilioni 150 na wakandarasi tayari wameshapewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niwape tu uhakikisho wananchi kupitia Bunge letu Tukufu kwamba kama kuna Mbunge yeyote, kijiji chake kimesahaulika tunaomba sana atuletee, Mradi wa REA III, round ya pili ni mradi wa kumbakumba wa vijiji vyote. Kwa hiyo niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge watuletee vijiji vyao vilivyosahaulika ili visisahaulike ili utekelezaji uende pamoja na maeneo yanayotekelezwa. Ahsante sana.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Swali langu pia lililenga hili ambalo limeulizwa na Mbunge wa Rungwe, lakini pia naomba basi niulize kwamba, kwa kuwa imekuwa ni tabia ya wakandarasi kuruka baadhi ya vitongoji, halafu wanapeleka sehemu ya mbele na vitongoji vingine ambavyo vimekatiwa miti yake havipewi. Je Serikali inasemaje kuhusu hili?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mlaghila kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge na tumeshaongea naye kuhusu vijiji na vitongoji vilivyorukwa. Naomba pia nitumie nafasi kupitia Bunge lako Tukufu kuwakumbusha tu wakandarasi na tumetoa maelekezo haya mara kwa mara, kwamba mradi wa vijiji ambavyo tunakwenda kuutekeleza sasa ambao pia una miradi ya vitongoji na mitaa, hauzingatii na hautarajii kuruka kitongoji chochote.

Kwa hiyo niwakumbushe wakandarasi kutoruka sio kitongoji tu kutoruka kijiji, kitongoji, kaya na nyumba, haitegemei ni aina gani ya nyumba. Nashukuru.