Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mbarouk Salim Ali (6 total)

MHE. MBAROUK SALIM ALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Lakini pamoja na majibu hayo nina maswali tena mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza katika awamu iliyopita kulikuwa na watu mashuhuri ambao walijilabu kwamba wanawajua watu ambao wanajishughulisha na biashara za dawa za kulevya. Je, Serikali inaonaje kuwaona watu hao au vingozi hao na kuwasihi ili wawapatie majina hayo ili Serikali ipate pa kuanzia? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, dawa za kulevya zinapiga vikali katika mishipa ya riyakh, na inaathiri sana nguvu za vijana ambao kwa kweli baada ya miaka 10, 15 nchi hii inaweza ikawa na mazezeta watupu. Sasa pamoja na Serikali kusema kwamba inabadilisha au ina muundo mpya wa mamlaka ya kudhibiti dawa za kulevya.
Je, Naibu Waziri anatuambiaje katika mamlaka hiyo mpya au katika mabadiliko hayo mapya kuna nini ambacho kinaweza kikakuhakikishia kwamba hali hii inapungua kwa kiasi kikubwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kwa kipengele cha kwanza kuhusiana na watu waliotoa taarifa kwamba wanawafahamu watu wanaojihusisha na dawa za kulevya, niseme tu kwamba Serikali iko tayari kushirikiana na mtu yeyote yule mwenye taraifa zinazohusu au zinaweza kupelekea kukamatwa kwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, japo sijalielewa vizuri niseme kwamba baada ya kupitishwa kwa sheria mpya ya mwaka 2015 kama nilivyoeleza awali Serikali itakuwa imepata nguvu katika maeneo yote ya kuchunguza kukamata na kuthibiti dawa za kulevya ikiwemo pia kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kwamba biashara ya dawa za kulevya inathibitiwa.
Mheshimiwa Spika, na jambo moja tu la uangalifu katika lugha hizi, watu wanaopata magonjwa ya akili kutokana na dawa za kulevya hatuwaiti mazezeta.
Mheshimiwa Spika, naomba Waheshimiwa Wabunge tuwe very sensitive katika lugha tunayotumia dhidi ya wagonjwa au watu wenye aina mojawapo au nyingine ya ulemavu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, inategemea na viwango, kuna wahanga au warahibu, kuna wagonjwa wa akili wa kawaida, lakini maneno kama mateja au mazezeta ni maneno ya unyanyapaa yaani stereo type. (Makofi).
MHE. MBAROUK SALIM ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri na mtiririko mkubwa wa mikakati na Kamati ambazo zimeundwa, lakini pia nina maswali mawili madogo tu ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, pamoja na mikakati na kamati nyingi ambazo zimeundwa, lakini uzoefu wa tetemeko la ardhi la Kagera na hili balaa la njaa linaloendelea sasa hivi nchini kote, inaonekana kwamba Serikali inapiga tikitaka jinsi ya kukabiliana na tatizo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujua, kwa sababu mikakati ni jambo moja, lakini pia na utayari. Sasa nataka kujua utayari wa Serikali juu ya kukabiliana na majanga kama hayo yanapotekea.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kuna tetesi kwamba kwenye miaka ya 1980 kuliwekwa vifaa katika baadhi ya maeneo ya hapa nchini ikiwemo Mbeya, nafikiri na Dodoma na Arusha. Nilitaka kujua uwepo wa vifaa hivyo, lakini pia na shughuli ambazo vinafanya kwa sasa? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mbarouk Salim Ali, swali lake la kwanza ameuliza utayari wa Serikali kukabiliana na majanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika majibu yangu ya msingi nimesema, imeundwa sheria makusudi kabisa kwa ajili ya kukabiliana na jambo hili, lakini ndani ya sheria imetengenezwa miongozo zaidi ya minne ambayo imetawanywa nchi nzima katika maeneo tofauti tofauti.
Lengo la hizi Kamati ni kwamba kupitia miongozo ile, kila maeneo na baada ya kuwa ilishafanyika assessment yako baadhi ya maeneo ambayo ni vulnerable, ambayo yako prone kwenye majanga, hasa hilo tetemeko la ardhi; na Mheshimiwa Mbunge kwa mujibu wa tafiti za kijiolojia zinasema, kwa mwaka mmoja duniani kote yanatokea matetemeko ya ardhi kuanzia 150 mpaka 1,500 ambayo yana nguvu za mtetemo kwa kipimo cha richter 4.5 mpaka 5.2.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika mazingira yetu haya na sisi tumeandaa utaratibu huo kupitia miongozo yetu ili kuwafanya watu wetu wawe tayari muda wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba kupitia Kitengo cha Maafa, utaratibu huu umewekwa na kutokana na experience mbalimbali sasa tunajiandaa kukiboresha kitengo hiki ili kiendane na hali ya sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili limeuliza kuhusu vifaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, masuala ya matetemeko ya ardhi yanasimamiwa chini ya Wakala wa Jiolojia Tanzania, ambayo ni GST. Ninavyozungumza hivi sasa, katika maeneo yale yote ambayo yako prone na suala hili la matetemeko, tayari tuna vituo tisa hivi sasa tunavyozungumza; katika Mkoa wa Dodoma, Geita, Singida, Kibaya, Kondoa, Mbeya na Mtwara na vituo hivi vinafanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba vituo hivi vipo na vinafanya kazi.
MHE. MBAROUK SALIM ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Kwanza nisikitike sana kwamba swali langu halikujibiwa na pamoja na kwamba Naibu Waziri amesema kwamba si kero, lakini Majaji wanasema ni kero. Kwa hiyo hizi ni kero za Muungano ambazo zinatambulika na kwa hiyo naomba na yeye atambue kwamba hizi ni kero za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niulize maswali yangu mawili ya nyongeza. Kulingana na makubaliano ya Muungano ambayo yaliasisiwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa pamoja na Baba wa Taifa wa Zanzibar Abeid Amani Karume ni kwamba miezi 12 tu iundwe tume ambayo itapanga mambo ya Muungano. Hata hivyo ni jambo la kusikitisha kwamba mpaka mwaka 1991 ndipo tume hiyo ikaundwa na Tume ya Jaji Nyalali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la kusikitisha, pamoja na kuundwa hiyo tume hakuna lolote lililofanyika mpaka hivi leo. Swali la kwanza, je, uko wapi huo uhalali wa Muungano?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili; hiyo Tume ya Jaji Nyalali iliainisha kero 40 za Muungano, lakini mpaka sasa Naibu Waziri anasema kwamba kuna kero 11 tu ambazo zimepatiwa ufumbuzi. Je, kuna nia safi kweli hapo ya Muungano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbarouk ni rafiki yangu wa karibu sana. Sasa anaposema kwamba swali lake halijajibiwa vizuri si kweli, naamini alikuwa ananitania kwa sababu swali lake ameuliza ni kero ngapi ambazo zimekwishatafutiwa ufumbuzi, tumemjibu kwa idadi hiyo ni kero 11. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge anavyokuja kimaswali na sisi kimajibu ndivyo tunavyokwenda kwake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Tume ya Jaji Nyalali, ni kweli kabisa kwamba Tume ya Jaji Nyalali iliweza kufanya kazi zake katika kuangalia masuala ambayo yanahusiana na Muungano na hasa masuala pia ya changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni suala ambalo si la kukimbizwa haraka haraka katika kutatua changamoto zake. Ndiyo maana baada ya Tume ile baadaye Kamati ya Pamoja ya pande zote mbili ya kutatua changamoto za Muungano iliweza kuundwa ambapo inahusisha Zanzibar na Tanzania Bara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali ya Muungano inayo nia na dhamira ya dhati kuhakikisha kwamba yale yote ambayo yaliweza kubainika yanafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwamba kero 40 na kwamba sasa zimetatuliwa kero 11 tu, kwamba Serikali ya Muungano haina dhamira ya dhati. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kero za Muungano pamoja na zile 40 ambazo zilibainika; kadri tunavyokwenda kila kukicha kuna baadhi ya changamoto zingine ambazo huwa zinajitokeza, sisi kama Serikali kadri ambavyo zinaibuka na kuongezeka na sisi tunaendelea kushughulika nazo na kuhakikisha kwamba tunazipunguza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa zilikuwa zimebaki kero 15 tu na katika kero 15, tayari 11 sasa zimepatiwa ufumbuzi na zilizobaki ni changamoto nne tu ambazo bado zinafanyiwa kazi yakiwemo masuala ya vyombo vya moto pamoja na haya masuala ambayo ni ya double taxation. Katika double taxation tayari tumeshafikia hatua ya turn fees kuhakikisha kwamba mifumo ya bara na kule visiwani na yenyewe inawekwa na inafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbarouk kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inashughulika na changamoto za Muungano na kuhakikisha kwamba zinakwenda vizuri pasipo kwenda kwa pupa au kwa uharaka. Hata dereva barabarani anawekewa alama za barabarani hapa uende 50, hapa uende 80; sasa kama yeye anataka katika kutatua hizi kero twende zaidi ya zile speed ambazo zinatupa usalama, basi chombo cha Muungano kinaweza kikapata ajali halafu Watanzania wakafa na wengine wakajeruhiwa. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri, ila nataka niweke record kidogo sahihi ili Mheshimiwa Mbunge awe na taarifa sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Jaji Nyalali haikuja na orodha ya kero 40 za Muungano. Ile namba 40 katika Tume ya Jaji Nyalali ni sheria ambazo zilipendekezwa zifanyiwe mabadiliko na baadhi nadhani zilichukuliwa katika mfumo wa Tume ya Marekebisho ya Sheria (Law Reform Commission) ambayo iliundwa na kuanza kuzifanyia mabadiliko ya sheria hizo 40, kwa hiyo hakukuwa na kero 40 zilizoainishwa na Tume ya Jaji Nyalali.
MHE. MBAROUK SALIM ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingi ambazo zina vivutio vya utalii utakuta miundombinu yake ni mibovu sana. Hii ndiyo sababu kubwa ambayo inasababisha wawekezaji warudi nyuma na washindwe kuwekeza katika maeneo ambayo yana vivutio na hivyo kushusha utalii.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba wanaboresha miundombinu katika maeneo hayo ya utalii? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kumekuwa na maeneo ya namna hiyo na bado kumekuwa na changamoto ya uwekezaji. Kazi kubwa tunayoifanya kama Serikali ni kuhakikisha kwamba tunaboresha kwanza mazingira ya uwekezaji na kuwahamasisha wawekezaji ili kusudi waweze kuwekeza katika maeneo yote hayo na yaweze kuchangia katika shughuli mbalimbali za utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme tu kwamba tutakaa na Mheshimiwa Mbunge ili tuone namna gani tunaweza tukafanya hiyo kazi ili kusudi wananchi wa eneo lile waweze kufaidika na matunda ya hiyo kazi.
MHE. MBAROUK SALIM ALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Pamoja na majibu hayo nina maswali mawili madogo tu ya nyongeza. Katika majibu yake ya msingi Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba wananchi wa Pemba pamoja na wananchi wetu wa Tanzania tayari wameshaunganishwa na soko hili la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika, bado niko kwa Pemba tu, nataka nijue kwamba hii Pemba imeunganishwa kinadharia au kivitendo kwa sababu karibu mwaka wa saba huu Viongozi Wakuu wa Afrika Mashariki walikubaliana kuijenga bandari ya Wete. Hizo ni jitihada na fedha kwa mujibu wa Naibu wa Wizara hii hii aliyepita ambaye kwa sasa hivi ni Naibu katibu Mkuu wa CCM Zanzibar alisema kwamba fedha tayari zilishakuwepo. Lakini mpaka leo hakuna lolote ambalo limefanyika nilitaka kujua ni nadhalia au ni vitendo.

Mheshimiwa Spika, hizo ni jitihada na fedha. Kwa mujibu wa Waziri wa Wiizara hii aliyepita ambaye sasa hivi ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, alisema kwamba fedha tayari zilishakuwepo, lakini mpaka leo hakuna lolote ambalo limefanyika. Nilitaka kujua, ni nadharia; ni vitendo?

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri katika jibu lake pia amewataka wananchi kwa ujumla watumie fursa zilizopo ili kulitumia soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Niseme tu kwamba kuna vikwazo vikubwa vya tozo nyingi pamoja na ushuru hasa katika uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa hizo:-

Je, ni lini Serikali nitaondoa tatizo hili hasa kwa wajasiliamali?

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote, namshukuru Mheshimiwa Mbarouk Salim Ali, Mbunge wa Wete kwa kuuliza maswali yake mawili ya nyongeza. Swali la kwanza amesema: Je, Pemba imeunganishwa kwa nadharia au kwa vitendo? Akitolea mfano ujenzi wa bandari kule Pemba.

Mheshimiwa Spika naomba kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kwamba Pemba imeunganishwa kwa vitendo kwa sababu Pemba ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jamhuri yote ya Muungano wa Tanzania imeunganishwa kwa vitendo kwa maana ya soko la pamoja, ambapo ndilo swali lake la msingi. Kwa maana ya mradi ya kimaendeleo ambayo ameisema, miradi hiyo inafanyika sehemu mbalimbali, sehemu zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuhusiana na Bandari ya Pemba tulishajibu ndani ya Bunge hili kwamba Serikali kwa kushirikiana na Afrika Mashariki inashughulikia mradi huo.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, anasema kuna vikwazo vikubwa vya tozo na ushuru. Maana ya soko la pamoja ni kwamba endapo bidhaa inakidhi vigezo vya uasili wa bidhaa (rules of origin), haipaswi kutolewa ushuru au tozo yoyote endapo inasafirishwa au kuuzwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Bidhaa ambazo hazikidhi vigezo kama niliongea kwenye jibu la msingi, ni kwamba zimetolewa nje ya Jumuiya Afrika Mashariki, lazima zilipe ushuru au common external tariff ambayo imewekwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. MBAROUK SALIM ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri, lakini mimi swali langu lilikuwa linajumuisha maliasili zote kwa ujumla ingawaje yeye amekwenda very specifically kwenye misitu, lakini hayo tuache.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, zoezi hili la ushirikishwaji wa jamii ni la muda mrefu kwa kweli, inasikitisha kwamba bado kuna malalamiko mengi ya migogoro na mambo mengine mengi. Nilitaka kujua ni kwa nini mpaka leo hii WMA’s nyingi hawapati gawio lao kwa wakati na kwa ukamilifu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, pamoja na miradi mingi ambayo inafanywa na Serikali katika jamii hizi ambazo zimezungukwa na maliasili hizi ni sawa lakini jamii hizi ni maskini wa kutupwa na miradi mingi imeelekea zaidi kwenye miradi ya kijamii. Je, Serikali haioni kwamba sasa kuna haja au ulazima wa kubadilisha mwelekeo na kuelekeza nguvu zao zaidi kwenye miradi ya kiuchumi na kuwapatia taaluma wananchi ili waweze kujikimu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbarouk Salim Ali, Mbunge wa Wete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anasema swali lake lilikuwa linauliza maliasili kwa ujumla na ili kumjibu swali hilo labda pengine ningehitaji nusu saa nzima kwa sababu kama unavyofahamu maliasili kwa ujumla almost asilimia 50 ya nchi hii iko kwenye maliasili. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge kama ana swali la nyongeza tunaweza tukawasiliana ili kuweka vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka kufahamu kwa nini WMA nyingi hazipati migao yake ya fedha kwa wakati na kwa kiwango cha thamani halisi. Naomba kwanza nitoe maelezo mazuri kwamba WMA ni jumuiya ambazo zinaanzishwa na vijiji kwa kutenga maeneo yao wanaanzisha jumuiya ambayo wanatafuta mwekezaji ambaye wanaingia naye mkataba kwa kutumia vikao mbalimbali wanakuwa na uongozi wao ambao unawajibika moja kwa moja kwenye kusimamia maslahi ya WMA. Hapa katikati tulirekebisha kanuni baada ya kuona tulikuwa na viongozi wengi ambao walikuwa wanapokwenda kwenye vikao hivi vya WMA wanazidiwa maarifa na wawekezaji tukarekebisha kanuni ili kuruhusu aina fulani ya elimu ili iweze kutumika lakini jumuiya ya WMA yenyewe imerudi na malalamiko kwamba inataka watu wote ili mradi anajua kusoma na kuandika waingie kwenye uongozi wa WMA. Kwa hiyo, hii ilikuwa ni changamoto lakini tumetoa maelekezo maalum kupitia Mkurugenzi wa Wanyamapori kuhakikisha kwamba inatoa msaada wa kitaalamu na kitaaluma katika usimamizi wa WMA ili iweze kupata maslahi yake kwa mujibu wa mkataba walioingia na mwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, jamii nyingi ambazo zinazunguka maeneo haya yenye maliasili ni maskini na kwa sababu Serikali labda imejielekeza zaidi katika miradi ya kijamii kama shule na kadhalika. Miradi yote inayofanywa na Mapori yetu ya Akiba na Hifadhi za Taifa na WMA ni miradi inayochaguliwa na vijiji vyenyewe. Vijiji vinakaa na kutenga miradi ya kipaumbele na vinapeleka muhtasari wa makubaliano haya kwenye mamlaka husika ya hifadhi, ndiyo inakwenda kujenga au kutoa msaada huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumeanza hivi karibuni sasa kuweka package ya kutoa elimu ya fursa mbalimbali ambazo zipo katika maeneo yanayopakana na hifadhi ili kuwaruhusu wananchi hawa kushiriki moja kwa moja kwenye mapato na biashara ya hifadhi na utalii yanayopakana na maeneo yao ya vijiji. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba tu nikushukuru kwamba maoni yako na ushauri wako tayari tumeanza kuufanyia kazi na tunashukuru kwa mtazamo huo na ndiyo mtazamo wa Wizara kuanzia sasa kuwashirikisha wananchi wote katika farsa ambazo zinapatikana katika maeneo yao.