Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mbarouk Salim Ali (8 total)

MHE. MBAROUK SALUM ALI aliuliza:-
Pamoja na sheria kali ya udhibiti na usimamizi wa dawa za kulevya, bado biashara hiyo ni tatizo kubwa kwa Tanzania.
Je, nini mkakati mahususi wa Serikali wa kupambana na kadhia hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbarouk Salim Ali, Mbunge wa Wete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa dhamira ya dhati, inaendelea kuhakikisha kuwa inafanya udhibiti wa kutosha wa kupambana na kadhia ya dawa za kulevya nchini.
Mheshimiwa Spika, ili dhamira ya Serikali ya kudhibiti dawa za kulevya nchini itimie serikali kupitia Sheria Namba Tano ya mwaka 2015 imeanza kutekeleza maeneo yafuatayo ya kimkakati katika vita ya dawa za kulevya nchini:-
(i) Kukamilisha muundo mpya wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ili kuongeza nguvu ya kisheria ya kuchunguza, kupeleleza na kukamata watuhumiwa wa dawa za kulevya.
(ii) Kupunguza urasimu katika utendaji kwa kuwa na watendaji wa mamlaka wanaoshiriki moja kwa moja katika kutekeleza majukumu yao.
(iii) Kuharakisha kesi za dawa za kulevya kwa kuongeza nguvu katika maeneo ya uchunguzi, upelelezi na ukamataji.
(iv) Kuongeza nguvu katika huduma za matibabu na utengamao pamoja na kuzuia matumizi haramu ya dawa za kulevya, maabara na vifaa vya kuzalisha dawa za kulevya nchini.
Mheshimiwa Spika, nilihakikishie Bunge lako tukufu kwamba baada ya kuanza kutumika kwa Sheria Namba Tano ya mwaka 2015, shughuli za udhibiti wa dawa za kulevya nchini zitasimamiwa vyema na Serikali.
MHE. MBAROUK SALIM ALI aliuliza:-
Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizomo katika Bonde la Ufa pamoja na milima mikubwa; kutokana na hali hiyo, upo uwezekano mkubwa wa kutokea kwa matukio kama tetemeko la ardhi mara kwa mara kama ambavyo imeshaanza kutokea na kuleta athari kubwa kwa Taifa.
Je, Serikali ina mkakati gani iliyojiwekea wa kuzuia au kupunguza athari pale inapotokea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbarouk Salim Ali, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa nchi yetu kama zilivyo nchi nyingine imekuwa ikikumbwa na majanga mbalimbali ya asili na yale yanayosababishwa na shughuli za binadamu na kusababisha athari kubwa kwa Taifa letu. Miongoni mwa majanga hayo ni tetemeko la ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua uwezekano wa kutokea kwa majanga haya, imejiwekea mikakati mbalimbali ya kuzuia, kujiandaa, kukabili na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea. Aidha, kwa vile maafa ya asili kama vile tetemeko la ardhi ni vigumu kuyatabiri, Serikali kupitia Wakala wa Jiolojia imekuwa ikitoa elimu kwa umma juu ya kukabiliana nayo kwa lengo la kupunguza athari pindi yanapotokea.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia imeandaa Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ambayo imeainisha aina mbalimbali za maafa ikiwemo tetemeko la ardhi pamoja na jukumu la kila mdau katika kushughulikia masuala ya maafa. Vilevile Serikali imeandaa Mwongozo wa Taifa wa kukabiliana na maafa ambao unaelekeza taasisi ongozi wajibu wao katika kukabili maafa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mkakati kiongozi wa kudumu katika kuhakikisha kwamba suala la Menejimenti ya Maafa inatekelezwa, Serikali imetunga Sheria mpya ya Menejimenti ya Maafa Na. 7 ya mwaka 2015 ambayo pamoja na kusimamia mikakati ya kudumu ya kukabiliana na maafa, imeelekeza kuundwa kwa Kamati za Maafa katika ngazi mbalimbali. Moja kati ya wajibu wa Kamati hizi ni kuhakikisha zinafanya tathmini za kubaini maeneo ambayo yako katika hatari ya kukumbwa na maafa na zinaweka na kupendekeza mikakati ya kukabiliana nayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile suala la maafa ni mtambuka, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo (development partners), pamoja na Chuo Kikuu cha Ardhi, ilifanya tathmini ya kuainisha maeneo yenye viashiria vya uwezekano wa kukabiliwa na majanga mbalimbali (vulnerability assessment) ambayo ilifanyika nchi nzima. Baada ya kuona ukubwa wa tatizo hili, Serikali iliandaa Mpango wa Taifa wa kujiandaa na kukabiliana na maafa hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kusisitiza kuwa kila mmoja wetu achukue tahadhari kwa kusikiliza ushauri unaotolewa na watalaam wetu katika kukabiliana na maafa. Hii ni pamoja na kujenga nyumba katika maeneo yaliyopimwa na salama kwa kuishi, lakini vilevile kwa kuzingatia viwango sahihi vya ujenzi (building codes) kulingana na maeneo tunayojenga.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS (K.n.y MHE. MBAROUK SALIM
ALI) aliuliza:-
Moja ya jitihada za Serikali za kufufua Kiwanda cha General Tyre kilichopo Arusha ni pamoja na kuendeleza kilimo cha mpira katika mashamba yaliyoko Tanga na Morogoro ili kupata malighafi.
Je, mashamba hayo yana ukubwa gani na umri gani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbarouk Salim, Mbunge wa Wete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Matairi Arusha (General Tyre) bado hakijaweza kuanza kufanya kazi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uchakavu wa mitambo na teknolojia inayotumika kupitwa na wakati. Serikali imelenga kukifufua kiwanda hicho ambapo imefanya utafiti ili kubaini namna bora ya kukifufua. Taarifa ya awali imeeleza kuwa, mitambo iliyopo ibadilishwe na kuweka mipya inayotumia teknolojia ya kisasa. Vilevile kiwanda kipanuliwe ili kiweze kuzalisha matairi ya aina mbalimbali kwa wingi ili kuzalisha kwa faida na uendeshaji wake uwe chini ya sekta binafsi na Serikali iwe mbia kwa kwa hisa zinazolingana na rasilimali za kiwanda zilizopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kiwanda hicho na mashamba ya mpira hayana uhusiano wa karibu kwani hakitumii mpira unaozalishwa kwenye mashamba yetu. Hii ni kwa kuwa kinatumia malighafi iliyo katika mfumo wa majora wakati teknolojia ya kugema mpira inayotumika kwenye mashamba yetu inatoa malighafi iliyo katika mfumo wa vipande. Mpira unaozalishwa nchini unatumika katika viwanda vingine kama vile Ok Plastic, Bora Shoes na viwanda vingine vidogo vidogo lakini vilevile unauzwa nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, zao la mpira ni moja kati ya mazao ya biashara ambayo yamekuwa yakizalishwa nchini kwa muda mrefu katika mashamba yaliyopo Kalunga - Mang’ula katika Wilaya ya Kilombero Mkoa wa Morogoro na shamba la Kihuhwi lililopo Wilaya ya Muheza Mkoa wa Tanga ambayo yalianzishwa mwaka 1978. Shamba la Kihuhwi lina ukubwa wa hekta 790 na shamba la Kilunga Mang’ula lina ukubwa wa hekta 750. Mashamba ya mpira kwa upande wa Zanzibar yapo Machai na Mselem Unguja yenye hekta 637 na mashamba madogo saba yaliyopo Unguja na Pemba yenye ukubwa wa hekta 633.
Mheshimiwa Naibu Spika, mashamba haya, yaani ya Kilunga na Mang’ula yanazalisha utomvu kati ya tani 0.6 hadi 1.0 kwa hekta kwa mwaka kutokana na miti yake kuwa na umri mkubwa. Kitaalamu uzalishaji wa utomvu huwa kati ya tani 0.8 hadi 1.3 za utomvu kwa hekta kwa mwaka na kupungua kadri ya miti ya mipira inavyozidi miaka 35 tangu kupandwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mashamba ya Tanzania Bara uzalishaji umepungua kutoka kilo 183,420 mwaka 2009 hadi kilo 165,335 mwaka 2014. Kwa upande wa Zanzibar uzalishaji umeshuka kutoka kilo 4,229,226 mwaka 2008 hadi 2,249,021 mwaka 2011.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kuwa mashamba haya yamezeeka na hayapati matunzo ya kutosha ndiyo maana uzalishaji umeendelea kushuka. Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Taifa yaani NDC imeanza kuendeleza shamba la Mang’ula ambapo kiasi cha miche 212,500 imepandikizwa ili kuongeza uzalishaji wa utomvu. Aidha, Serikali inahamasisha wakulima na wawekezaji kuzalisha zao hili kwa kuwa soko lipo kwa viwanda vingine vya ndani na nje ya nchi.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN (K.n.y. MHE. MBAROUK SALIM ALI) aliuliza:-
Tanzania pamoja na kuwa na mifugo mingi bado kuna uhaba mkubwa wa maziwa.
Je, Tanzania ina ng’ombe na mbuzi wangapi wa maziwa?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbarouk Salim Ali, Mbunge wa Wete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nakubailiana kabisa na Mheshimiwa Mbunge kuwa Tanzania ina idadi kubwa ya mifugo lakini bado kuna upungufu wa maziwa ambapo takwimu za makadirio za mwaka 2016 zinaonyesha kuwa kuna jumla ya ng’ombe milioni 28.4, mbuzi milioni 16.7, kondoo milioni tano, nguruwe milioni 1.9, kuku wa asili milioni na kuku wa kisasa milioni 34.5. Aidha, katika kipindi hicho jumla ya lita bilioni 2.09 za maziwa zilizalishwa na unywaji wa maziwa kwa mtu kwa mwaka ulifikia lita 47, ikilinganishwa lita 200 zinazopendekezwa na Shirika la Chakula Dunian (FAO).
Mheshimiwa Spika, kati ya ng’ombe milioni 28.4, ng’ombe rasmi wa maziwa ni 782,995 tu sawa na asilimia tatu ya ng’ombe wote. Aidha, kati ya mbuzi milioni 16.7 ni mbuzi rasmi takribani 50,000 ndiyo wa maziwa ambao ni asilimia 0.3 ya mbuzi wote.
Mheshimiwa Spika, zipo jitihada mbalimbali ambazo zimechukuliwa na Serikali ili kukabiliana na upungufu wa maziwa hapa nchini. Jitihada hizo ni pamoja na kuimarisha mashamba ya kuzalisha mifugo ya Serikali (Livestock Multiplication Units) ili kuongeza idadi ya ng’ombe wenye uwezo wa kuzalisha maziwa kwa wingi.
Aidha, Serikali imeanzisha vituo vya uhimilishaji katika Kanda Sita hapa nchini ambazo ni Kanda ya Ziwa - Mwanza, Kanda ya Magharibi - Katavi, Kanda ya Kati - Dodoma, Kanda ya Mashariki - Kibaha, Kanda ya Kusini - Lindi, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini – Mbeya, kwa lengo la kutoa huduma ya uhimilishaji wa ng’ombe wa maziwa walioko kwenye maeneo hayo pamoja na ng’ombe wa asili ili kuzalisha idadi kubwa ya ng’ombe wa maziwa. Jitihada hizi zitawezesha idadi ya ng’ombe wa maziwa kufikia milioni 2.9 ifikapo mwaka 2021/2022 ambao pamoja na ng’ombe wa asili wataweza kuzalisha lita bilioni 3. 8 za maziwa.
Mheshimiwa Spika, pia Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo kuwekeza katika uzalishaji wa mitamba ya maziwa na mashamba ya ng’ombe wa maziwa kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa maziwa hapa nchini.
MHE. MBAROUK SALIM ALI aliuliza:-
Pamoja na jitihada za Serikali katika kutatua kero za Muungano bado kuna manung’uniko mengi kuhusiana na Muungano huu:-
Je, ni kero ngapi mpaka sasa zimeshapatiwa ufumbuzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, sasa napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbarouk Salim Ali, Mbunge wa Wete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijamjibu napenda nielezee kidogo maneno mawili ambayo kwenye Muungano yanachanganywa. Suala la kero na suala la changamoto. Sisi ambao tunashughulika na masuala ya Muungano, Muungano huwa una changamoto, huwa hauna kero. Kwa hiyo mara nyingi maswali yanayokuja Waheshimiwa Wabunge wanapenda kutumia neno kero, nawaomba tuwe tunatumia neno changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya kuwepo kwa changamoto chache za Muungano, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, Bunge lako Tukufu na Watanzania kwa ujumla kuwa Muungano wetu uko imara na changamoto ambazo zimekwishapatiwa ufumbuzi hadi sasa ni (11).
MHE. JUMA KOMBO HAMAD (K.n.y. MHE. MBAROUK SALIM ALI) aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa Watanzania hususan kizazi kipya, kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ili kutoa uelewa wa pamoja na dhamira njema za Muungano huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbarouk Salum Ali, Mbunge wa Wete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kwamba, karibu asilimia 80 ya kizazi cha sasa kimezaliwa baada ya Muungano na hivyo kuna haja ya kutoa elimu ya Muungano kwa wananchi wote, hususan vijana wa Kitanzania. Elimu hii ni muhimu kwa mustakabali wa Muungano kwani inaongeza ari ya uraia, uzalendo na kujenga undugu wa Kitaifa kati ya wananchi wa pande mbili za Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2018/2019, ofisi imetoa elimu ya Muungano kupitia vipindi vya redio na television, ili kuhakikisha makundi mbalimbali yanapata elimu ya Muungano, hususan vijana. Katika Mwaka wa Fedha 2017/ 2018, shughuli za elimu ya Muungano, hususan kwa vijana, zilitolewa kupitia kongamanko la vijana, hususan fursa zilizopo katika Muungano ambapo ilifanyika Zanzibar tarehe 22 Oktoba, 2017. Wanafunzi wa shule za msingi zilizopo Dodoma ilifanyika tarehe 18 Aprili, 2018 na Kongamano la Vyuo vya Elimu ya Juu vilivyopo Dodoma, itafanyika tarehe 21 Aprili, 2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, ofisi ilishiriki katika maonesho ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani iliyofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja kuanzia tarehe 31 hadi tarehe 6 Juni, 2018, ambapo wananchi walipata fursa za kujulishwa kuhusu masuala ya Muungano. Pamoja na kazi hizo, ofisi ilishiriki katika vipindi vya redio, television na magazeti katika kutoa elimu ya Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua faida zitakazopatikana kwa kutoa elimu ya Muungano, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, itaendelea kutoa vipaumbele katika Mwaka wa Fedha 2019/2020 na imetenga fedha kwa ajili ya kutoa elimu ya Muungano kwa vijana kupitia makongamano na warsha, ambayo yamelenga wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo vya elimu ya juu Tanzania Bara na Zanzibar.
MHE. MBAROUK SALIM ALI aliuliza:-

Pemba ni Kisiwa kinachozalisha viungo (spices) kwa wingi na wajasiriamali huzalisha bidhaa zinazotokana na viungo hivyo:-

Je, ni lini wakulima na wajasiriliamali wa Pemba wataunganishwa na soko la Afrika Mashariki ili waweze kufaidika na soko hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mhe. Mbarouk Salim Ali, Mbunge wa Wete kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, napenda kumtaarifu Mhe. Mbunge kuwa, wananchi wa Pemba na wa maeneo yote ya Tanzania wamekwisha unganishwa na soko la Afrika Mashariki kupitia Itifaki za Umoja wa Forodha na ya Soko la Pamoja la Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika, kwa mkulima au mjasiriamali yoyote kuweza kuuza bidhaa zake ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anapaswa kukidhi vigezo vya Afrika Mashariki vya kutambua uasili wa bidhaa (Rules of Origin). Nchi Wanachama zilikubaliana na kuweka vigezo vinavyoshabihiana kama bidhaa husika imezalishwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Vigezo hivyo vimejengwa katika misingi ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, bidhaa kuzalishwa ndani ya Jumuiya kwa kiwango cha asilimia mia moja mfano, bidhaa za kilimo, uvuvi, madini na kaadhalika; bidhaa kuzalishwa ndani ya Jumuiya kwa kutumia malighafi ya kutoka nje yenye thamani (ex-works price) ya kiwango kisichozidi asilimia 70 ya bei ya bidhaa hiyo bila kodi ikiwa kiwandani, mfano label za plastik, kuongeza ugumu wa kioo, utengenezaji wa nyaya za umeme na vifaa vingine vya umeme, utengenezaji wa pikipiki na baskeli n.k; bidhaa zinazozalishwa ndani kwa kutambua mchakato katika uzalishaji (process rule) kama vile uunganishaji wa magari na kusafisha mafuta ya petroli (refining); na bidhaa kubadilika utambuzi wa uasili kwa kubadilika umbo na matumizi kutokana na mchakato wa viwandani mfano malighafi ya plastiki kuchakatwa kuwa meza, viti, sahani n.k.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia misingi ambayo nimekwisha ielezea hapo juu, nichukue fursa hii kupitia Bunge lako Tukufu kuwashauri wananchi wa Pemba na Tanzania kwa ujumla kuzichangamkia fursa za kibiashara, ajira, uwekezaji n.k. zitokanazo na Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kujihakikishia maendeleo.

Mheshimiwa Spika, vilevile, kuwasihi wananchi kuzitambua taratibu za kufuata katika kuzitumia fursa za kibiashara zilizopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na kuwa na cheti cha Uasili wa Bidhaa (East African Communicate Certificate of Origin) na vibali/ nyaraka zinazobainisha kuwa bidhaa imezalishwa ndani ya Jumuiya kutoka mamlaka husika kutegemea na aina ya bidhaa mfanyabiashara anazotaka kuuza/kununua katika soko la Afrika Mashariki.
MHE. MBAROUK SALIM ALI aliuliza:-

Je, ni mafanikio gani yameweza kupatikana katika kushirikisha jamii katika jitihada za usimamizi wa maliasili nchini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbarouk Salim Ali, Mbunge wa Wete, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, dhana ya Ushirikishwaji wa Jamii katika Usimamizi wa Misitu nchini (Participatory Forest Management) inatekelezwa katika nyanja kuu mbili: Kuwashirikisha wananchi katika usimamizi wa misitu iliyopo kwenye ardhi ya vijiji (Community Based Forest Management) na kuwashirikisha wananchi katika kusimamia hifadhi ya misitu kwa ubia na Serikali (Joint Forest Management). Madhumuni ya dhana hii ni kuwapa fursa wananchi kushiriki katika usimamizi na uhifadhi endelevu wa rasilimali za misitu iliyopo katika maeneo yao hali wakiboresha maisha yao kupitia mapato mbalimbali yanayopatikana kutokana na misitu iliyopo katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu zinaonyesha jumla ya hekari milioni 7.7 zimehifadhiwa kupitia dhana hii ya ushirikishwaji wa jamii. Aidha, dhana hii imesaidia sana katika kupunguza matukio ya uharibifu wa misitu kama ukataji wa misitu hovyo, uchomaji wa mkaa holela na matukio ya moto yaliyokuwa yakifanyika katika misitu husika katika misitu ya hifadhi ya mazingira asilia (nature reserves). Ushirikishwaji huu umekuwa ni nyenzo muhimu ya kufanikisha ustawi wa misitu ambayo mingi kati ya hiyo ni misitu ya lindimaji (catchment forest).

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo faida mbalimbali ambazo jamii husika imefaidika kupitia dhana hii ikiwepo kupata msamaha wa mirahaba ya Serikali juu ya mazao ya misitu, kubakiza asilimia 100 ya mapato yatokanayo na mauzo ya mazao ya misitu japokuwa kodi zingine kama kodi ya mapato, Kodi ya Ongezeko la Thamani zimeendelea kulipwa, kubakiza tozo ya faini mbalimbali na utaifishaji wa mazao ya misitu na vifaa kutokana na uvunaji haramu katika misitu ya hifadhi ya kijiji. Aidha, sehemu ya fedha zinazopatikana zimetumika katika shughuli za maendeleo ya vijiji kama kujenga vyumba vya madarasa, zahanati, nyumba za watumishi, walimu na waganga, kutengeneza madawati na kuchimba visima. Vilevile sehemu nyingine ya fedha hiyo imeendelea kutumika katika shughuli za usimamizi wa misitu ikiwemo kununua vifaa vya walinzi wa misitu hiyo ikiwemo sare, buti, filimbi, baiskeli na kadhalika.