Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Jumaa Hamidu Aweso (18 total)

Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Kwa namna ya kipekee nimpongeze sana sana Mheshimiwa wa Kamati yetu ya Mifugo pamoja na Maji Mheshimiwa Mahmoud Mgimwa pamoja na wajumbe wake wamekuwa wakifanya kazi kubwa na nzuri sana ya kutushauri sisi Wizara yetu ya Maji, wamekuwa msaada na wala hawakuwa kikwazo.

Mheshimiwa Spika, ninachotaka kuwahakikishia Watanzania na Waheshimiwa Wabunge, sisi kama viongozi wa Wizara ya Maji hatutokuwa kikwazo kwa Kamati yetu katika kuhakikisha tunaleta maendeleo makubwa sana katika sekta yetu ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesimama hapa kujibu hoja chache sana. Moja, kuhusu hoja ambayo imetolewa na Mheshimiwa Mbunge wa Mchinga kaka yangu Hamidu Bobali kuhusu suala zima la uvunaji wa maji ya mvua, kwamba lita zitakazozidi elfu 20 unatakiwa ulipie; nataka niweke sawa taarifa. Kwa mtu ambaye anavuna maji ya mvua lita zaidi ya elfu 20 hatakiwi kulipa chochote kama anatumia matumizi ya nyumbani. Hata kama ikitokea anatumia kwa matumizi mengine, ada yake ni shilingi laki moja tu lakini hii yote ni katika kuhakikisha tunalinda na kutunza vyanzo vyetu vya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya pili, imezungumzwa hapa na dada yangu ambaye ninamheshimu sana, Mheshimiwa Ester Bulaya, kuhusu suala zima la mradi wa maji wa Bunda. Nimeshtuka kidogo akiwa kama Mnadhimu kutoa taarifa ambazo binafsi zimenishtusha sana. Nikiri kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu alifika Bunda na akatoa agizo kutokana na athari ya baadhi ya miradi ya maji iliyokuwa ikisuasua na hata baadhi ya wataalam wetu, kwa maana ya kushirikiana kuhujumu miradi ya maji.

Mheshimiwa Spika, yule mkandarasi Nyakirang‟anyi alikamatwa na hatua ambazo tulizichukua sisi kama Wizara; tukasema mradi ule tunaukamilisha kwa kutumia wataalam wetu wa ndani. Fedha ambazo zilitakiwa kukamilisha mradi ule zilitakiwa kiasi cha shilingi milioni 375 lakini wataalam wetu wa ndani wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Musoma wamefanya kwa force account kwa shilingi milioni 200 na mradi umekamilika mwezi Desemba mwaka jana, Mheshimiwa nakupa taarifa hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mimi kama Naibu Waziri wa Maji nimeshafika na Waziri amekwishafika, na nipo tayari kwenda kuongozana na wewe Bunda kukuonesha kazi nzuri ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ilivyotekelezwa katika eneo lako la Bunda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo ninataka kusema, nataka nimjibu Mheshimiwa Mbunge kaka yangu Mheshimiwa Haonga. Wakati mwingine unapojenga hoja hebu jiridhishe basi kidogo kazi zilizofanywa. Amezungumza kwamba kazi ya miradi ya maji, sisi pale katika Jimbo lake tuna mradi wa milioni 550 tumeshalipa pesa zaidi ya milioni 500. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeshapeleka fedha ambazo tumepata kupitia fedha za P4R zaidi ya bilioni 119 ambazo zimetengwa kwa mikoa 17 na Halmashauri 86 ikiwemo Halmashauri ya Mbozi ya Mheshimiwa Haonga zaidi ya bilioni 1.3 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji.

Mheshimiwa Spika, kubwa Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kutekeleza miradi ya maji maeneo yote bila ya ubaguzi wowote. Sisi kama viongozi wa Wizara ya Maji hatulali, usiku na mchana katika kuhakikisha tunaisimamia na kuifuatilia miradi yetu ya maji ili wananchi waweze kupata huduma ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachotaka niwaambie wakandarasi na wataalam wa maji vipo vitu vya kuchezea, ukishiba unaweza kucheze kidevu ama tumbo lako, kwa maana ya kitambi; lakini kwa yeyote ambaye atakayetaka kuchezea miradi ya maji, sisi hatupo tayari tutashughulikiana ipasavyo katika kuhakikisha tunajenga nidhamu katika miradi yetu ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tangu Wizara ya Maji ianze kutekeleza miradi ya maji kwa kutumia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, tangu 2006 mpaka sasa tumeshatekeleza miradi 2,450. Hata hivyo Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli tangu aingie 2015 mpaka Desemba mwaka jana tumeshatekeleza miradi 1,423. Miradi 792 imekamilika na miradi 600 ipo katika hatua mbalimbali ya utekelezaji, na tumeshajipanga katika kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati ili azma ya Mheshimiwa Rais ya kumtua mwanamama ndoo kichwani, kwa maana ya asilimia 85 ya upatikanaji vijijini na asilimia 95 ya maji mijini.

Mheshimiwa Spika, tuna miradi mikubwa ambayo itaongeza hali ya upatikanaji wa maji. Leo ukienda Arusha mradi wa zaidi ya bilioni 520 unatekelezwa, ukienda Orkasmet pale zaidi ya bilioni 30 mradi unatekelezwa. Ukienda Longido zaidi ya bilioni 16 ya mradi umekamilika, Tabora, Igunga, Nzega zaidi ya bilioni 600 ule ni mradi wa standard gauge/Stierglers mfano katika kuhakikisha tatizo la maji na vijiji zaidi ya 102 vitaweza kupatiwa huduma hii ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge pia katika Miji 28 na …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana, malizia Mheshimiwa Waziri.

NAIBU WAZIRI WA MAJI: …ambapo tumepewa fedha zaidi ya dola milioni 500. Nataka niwape taarifa kwamba kibali tumeshapata vya Exim Bank, tunajipanga katika kuhakikisha tunatangaza tenda ile ili mkandarasi apatikane ili azma ya Mheshimiwa Rais kwa maana ya miji 28 miradi ile inatekelezwa na wananchi waweze kupata huduma ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, asante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nikupongeze wewe binafsi kwa ushirikiano mkubwa ambao umetupa katika kipindi chetu chote cha hotuba hii ya bajeti, ahsante sana, Mungu akubariki sana. Kwa namna ya kipekee utufikishie salaam kwa Mheshimiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mzee wetu Mheshimiwa Job Ndugai, tunamshukuru sana, amekuwa akitupa ushirikiano mkubwa sana sisi viongozi kuhakikisha kwamba tunatimiza wajibu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya kipekee namshukuru sana Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan; Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mzee wangu Mheshimwia Isidori Mpango; pamoja na Waziri wetu, Mheshimiwa Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa kwa ushirikiano mkubwa na maelekezo yao katika kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya maji safi salama na yenye kutosheleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe ahadi kwenye Bunge hili Tukufu, mimi Jumaa Aweso pamoja na timu yangu ya Wizara ya Maji akiwemo Naibu Waziri wa Maji, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na timu nzima ya Wizara yetu ya Maji hatutakuwa kikwazo kwa Watanzania kupata maji safi salama na yenye kutosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya kipekee, nitumie nafasi hii sana, sana, kulishukuru sana Bunge lako Tukufu; kiukweli michango ambayo imetolewa na Waheshimiwa Wabunge. Jana nilikuwa na Wahandisi wetu wa maji; kiukweli mawazo, hoja, maoni na ushauri ambao mmetupa sisi Wizara ya Maji Waheshimiwa Wabunge ni zaidi ya Wahandisi wetu wa Maji. Hongereni sana, Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nikiwa kama mwenye dhamana ya Wizara hii ya Maji, nimepata funzo kubwa na nitoe ahadi mbele yenu, tutafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa kuhakikisha Watanzania wanaenda kupata maji safi salama na yenye kutosheleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya kipekee nimpongeze Chief-Whip wetu, mama yangu Mheshimiwa Mhagama ahsante sana, Mungu akubariki sana. Sisi wengine kwenye hizi nafasi bado ni wageni. Tumetoka shule, tumekuwa Wabunge, tumekuwa Manaibu na leo ni Mawaziri, lakini umetupa ujasiri. Ahsante sana, Mungu akubariki sana dada yetu, nasi tutaendelea kujituma kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii tena kwa namna nyingine kulishukuru Bunge lako. Waheshimiwa Wabunge Zaidi ya 84 wameweza kuchangia katika bajeti yetu kwa kuzungumza. Pia tumepokea kwa maandishi mchango wa Mheshimiwa Mbunge Charles Mwijage. Itoshe kwamba hoja zote na maoni na ushauri, sisi kama Wizara ya Maji tumepokea na tutaenda kuyafanyia kazi yale ambayo Waheshimiwa Wabunge wametuelekeza katika Wizara yetu ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba Waheshimiwa Wabunge kutokana na uchache wa muda, nizijibu hoja za baadhi ya Kamati pamoja na Waheshimiwa Wabunge na kuwakikishia kwamba hoja nyingine zote tutazijibu kwa maandishi. Itoshe kusema, namshukuru sana Mheshimiwa Mwenyekiti wetu, Mheshimiwa Christine Ishengoma pamoja na Kamati yetu ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa namna ambavyo wamekuwa wakitupa ushirikiano sisi Wizara ya Maji katika kuhakikisha kwamba tunatimiza majukumu yetu. Ushauri wao mwingi ambao wametuelekeza juu ya kuanzishwa na kusimamia mpango mkakati wa kuhakikisha uvunaji wa maji ya mvua unakuwa endelevu kwa matumizi ya akiba, hasa na wakati wa kiangazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado wametuelekeza kutekeleza mpango wa ujenzi wa miundombinu wa maji taka katika miji na Makao Makuu ya Mikoa. Pia kuongeza kasi ya kutekeleza mipango na mikakati ya kuimarisha upatikanaji wa maji katika Jiji la Dodoma, itoshe tu kusema maoni ambayo mmetupa sisi tumeyapokea na tunayafanyia kazi katika kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya maji safi salama na yenye kutosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu hoja za Waheshimiwa Wabunge. Moja ya hoja ambayo imezungumzwa na Waheshimwa Wabunge wengi ni kuhusu suala zima la Ankara za maji. Naomba nizungumze hapa, ni haki ya mwananchi kupatiwa huduma ya maji, lakini mwananchi asisahau ana wajibu wa kulipia bili za maji. Sisi kama viongozi wa Wizara, jukumu letu ni kuhakikisha mwananchi hapewi bili bambikizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa kulizungumza, hata nami nilipopita maeneo mbalimbali nilizisikia hizo kelele. Nawapongeza katika hili kwa sababu anayelala na mgonjwa ndiye anayejua mihemo ya mgonjwa. Hongereni sana Waheshimiwa Wabunge kwa kujua changamoto za wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ambaye anaidhinisha bili ni Taasisi yetu ya EWURA. Baada ya kusikia hizi changamoto, tumetoa maelekezo mahususi kwa EWURA juu ya kufuatilia bili hizi bambikizi. Wameshaifanya hiyo kazi na ripoti hivi karibuni watanikabidhi. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, mamlaka yoyote ambayo imekwenda kinyume aidha kwa kuwabambikizia watu bili za maji, au kutoa bili ambazo hazijaidhinishwa na EWURA, tutazichukulia hatua hata wawe na mapembe marefu kiwango gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nitoe maoni na ushauri kwa wananchi, pamoja na changamoto hizo, lakini zipo changamoto ambazo tumeziona sisi kama Wizara. Unakuta wakati mwingine mwananchi anatumia maji, bili anayopata ni ya gharama kubwa. Leo mwananchi anapiga mswaki, bomba amelifungua zaidi ya dakika tano; leo unakuta mvua mvua inanyesha, lakini anatumia maji yaliyokuwa treated anamwagilia maua; leo anatumia maji ambayo yamekuwa treated kufyatulia matofali. Tunaomba sana EWURA pamoja na mamlaka zetu za maji kutoa elimu kwa wananchi ili kuhakikisha kwamba mwananchi anaweza kuyafahamu hayo ili kuhakikisha kwamba anapata matumizi sahihi ya maji na aweze kupata bili zilizokuwa sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hili la bili za maji, maelekezo ambayo tumeyatoa sasa hivi Wizara, mamlaka zetu zote za maji tumeanzisha mfumo mpya ambao unaitwa Unified bill system, kwamba wajiunge kuhakikisha tunakwenda kudhibiti ubambikizaji wa bili za maji. Hili ni sambamba na maelekezo ambayo tumeshayatoa; wasoma mita kuhakikisha kwamba hawawakadiriii wananchi mita za maji. Katika kusoma huko mita za maji lazima wawashirikishe wananchi wetu ili kuhakikisha kwamba wanalipa bili halisia.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa naomba niongeze, pamoja na suala zima la bili za maji, kumekuwa na tabia za mamlaka zetu za maji wakati mwingine kumkatia mwananchi maji kipindi cha sikukuu au kipindi cha week-end. Sisi kama Wizara ya Maji tumepiga marufuku; mamlaka zote za maji ni marufuku kumkatia maji mwananchi kipindi cha sikukuu ama kipindi cha week-end.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine katika kuhakikisha tunadhibiti bili hizo za maji, Waheshimiwa Wabunge sisi kama Wizara ya Maji tumetoa maelekezo mahususi kwa mamlaka zetu za maji zote nchini; ni marufuku kwa mwananchi yeyote wa Tanzania kuhakikisha kwamba wanamlipisha service charge. Tumeshaifuta. Ikitokea Mkurugenzi au mtu yeyote ambaye anataka kumbambikizia mwananchi kwa maana katika bili yake amemwekea service charge, tutashughulika naye ipasavyo ili kuhakikisha kwamba tunamwokoa mwananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Naibu Spika, linguine limezungumziwa suala la dira za malipo ya kabla, kwa maana ya prepaid meter. Itoshe tu kusema kizuri huigwa. Tumeona wenzetu wa Wizara ya Nishati kupitia TANESCO wamekua wakitumia meter za LUKU na sisi kama Wizara ya Maji tumetoa maelekezo mahususi kwa Mamlaka zetu za Maji kuhakikisha wanafunga prepaid meter na tumeshaanza na tumeona faida hiyo. Leo tulikuwa tukipata makusanyo milioni 23 pale bandari, baada ya kufunga Prepaid Meter DAWASA wanakusanya zaidi ya milioni 103, hayo ndiyo manufaa makubwa kwetu sisi. Kwa hiyo, maelekezo ambayo tumetoa ni kwamba Mamlaka zote za Maji ambazo ziko katika daraja A kuhakikisha kwamba wanafunga prepaid meter ili kuhakikisha kwamba tunaondokana na hizi changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa awamu hii tunayokwenda nayo, naomba nitoe maelekezo mahususi kwa Waheshimiwa Wabunge wote waweze kufungiwa prepaid meter ili kama kutakuwa na changamoto yoyote muweze kutupa maoni na ushauri tuweze kuyafanyia kazi wakati tunaelekea kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, imezungumzwa hapa changamoto ya gharama ya uunganishaji wa maji. Waheshimiwa Wabunge, sisi Wizara ya Maji jukumu letu ni kuhakikisha Mtanzania anapata maji, si maji tu ila ni kwa maana ya maji safi, salama na yenye kutosheleza lakini kwa gharama nafuu. Maelekezo ambayo ametupa Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha mwananchi anapatiwa maji bila ya gharama kubwa. Kwa hiyo sisi tumelipokea, tutakwenda kuliwekea utaratibu mzuri, lakini maelekezo ambayo tumewapa Mamlaka zetu za Maji kwa mwananchi ambaye anataka kuunganishwa maji kwa maana gharama inakuwa ni kubwa na yeye uwezo wake ni mdogo, maelekezo tuliyoyatoa wananchi hao walipe kwa awamu na zile gharama watalipia katika bili kama walivyokubaliana na Mamlaka zetu za Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine Waheshimiwa Wabunge wametoa maoni mengi, Kamati yetu wametoa maoni mengi, juu ya kutumia vyanzo toshelevu tulivyokuwa navyo. Waheshimiwa Wabunge nao wameelekeza mambo mengi kwa maana ya maziwa na mito tuliyokuwa nayo. Itoshe kusema tu, nchi yetu ya Tanzania Mwenyezi Mungu ameibariki sana. Ina rasilimali za maji toshelevu juu ya ardhi na chini ya ardhi takribani mita za ujazo bilioni 126. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mita za ujazo bilioni 105 ni maji yaliyokuwa juu ardhi na mita za ujazo bilioni 21 ni maji yaliyokuwa chini ya ardhi na mahitaji yote ya Tanzania ni bilioni 60 tu. Kwa hiyo hatuna sababu hata moja kuona wananchi wetu wanateseka juu ya suala nzima la maji. Kwa hiyo, wataalam wa Wizara yetu ya Maji, lazima tubadili mind set zetu katika kuhakikisha tunatumia rasilimali toshelevu na Watanzania wanaweza kupata huduma ya maji safi, salama na ya kutosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru sana maelekezo ya viongozi wetu, Mheshimiwa Makamu wa Rais pamoja na Waziri Mkuu sisi wasaidizi wao wametuelekeza namna ya kufanya uthubutu na tunaona namna viongozi wetu walivyofanya uthubutu mkubwa katika Taifa letu. Leo tunaona mambo ambayo yalikuwa hayawezekani, leo yanatekelezeka. Tunaona nchi yetu namna inavyojengwa Standard Gauge, kwa hiyo sisi kama Wizara ya Maji tumethubutu kwa kuanza ujenzi wa Standard Gauge kutoka Tabora, Igunga mpaka Nzega kwa kuyatoa maji kutoka Ziwa Victoria. Mradi ule umekamilika na Mheshimiwa Rais ametupa maelekezo mahususi maji yale yaliyofika Tabora tuyapeleke Kaliua, tuyapeleke Sikonge na mpaka Urambo kwa Mama Sitta ili kuhakikisha kwamba Watanzania wanaenda kunifaika na huduma hii ya maji safi, salama na ya kutosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kana kwamba haitoshi tunakwenda kuwatumia chanzo toshelevu cha Mto Ruvuma ili kuhakikisha wananchi wa Mtwara tunakwenda kutatua tatizo la maji pale Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukimwona mtu mzima analia ujuwe kuna jambo. Pamoja na Unaibu Spika wako lakini hukuacha kuja Wizara yetu ya maji kuomba tutumie Mto Kiwira ili wananchi wa Jimbo la Mbeya waweze kupata huduma ya maji. Nataka niwaambie wananchi wa Mbeya, sisi kama Wizara ya Maji si Wizara ya Ukame, tunakwenda kutumia Mto Kiwira ili kuhakikisha kwa wananchi wa Jiji la Mbeya tunakwenda kutatua tatizo la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala zima la miji 28. Kwanza nimshukuru Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan, maelekezo mahususi ambayo ametoa katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni dhahiri, dhamira yake, nia yake ni kuona Watanzania wanapata huduma maji na safi na salama. Ameona wanawake wenzake namna gani walivyokuwa wakinyanyasika, wakiteseka juu ya maji. Niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge mimi Juma Aweso pamoja leo ni Waziri wa Maji sikuwahi kuishi Masaki, nimetokea katika mazingira hayo ya maji ambayo akinamama walikuwa wanapata tabu. Nimemwona mama yangu mzazi wakati akimuacha baba yangu amelala badala ya kumpetipeti yeye anaenda kutafuta maji. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge mimi Juma Aweso uchungu wa mama ambao mnaupata naufahamu, tutafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya maji safi, salama na ya kutosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mahusiano mazuri ya nchi yetu na Rais wetu, tumepata fedha dola milioni 500 kwa ajili ya kuhakikisha Watanzania katika miji 28 wanakwenda kupata huduma ya maji safi, salama na ya kutosheleza. Hapa niwe muwazi zaidi, Wizara yetu ya Maji ilikua ikilalamikiwa sana, moja kutumia miradi kwa gharama kubwa. Utekelezaji wa miradi hii ya miji 28 financial agreement ilikuwa kwa ajili ya kutekeleza maji katika miji 16. Sisi kama viongozi wa Wizara ya Maji tukasema hapana, lazima tutazame design ya mradi huu juu ya utekelezaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuja kugundua kwamba, eneo ambalo leo linahitaji pampu tatu wanaweka pampu 11, tumezikata, tukasema ili hapana. Eneo ambalo wangeweza kuweka bomba la milimita 300 wanaweka milimita 900, tukasema hapana, fedha hizi ambazo zingeweza kutatua maeneo mengine tumezibana badala ya miji 16 tunakwenda kutekeleza miji 28. Waheshimiwa Wabunge tunaomba mtuamini katika kuhakikisha kwamba tunatekeleza miradi hiyo na Watanzania waweze kupata huduma ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tuko katika hatua ya mwisho na nataka niwaambie ukiona giza linatanda ujue kumekucha. Huu ni mradi wa muda mrefu sana, lakini sasa hivi tumeshakamilisha hatua za manunuzi, tuko katika utaratibu wa kupata kibali Exim, wakandarasi waende site, maelekezo mahususi ambayo nimeyatoa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na watendaji wote, signing ya wakandarasi zote zitafanyika katika majimbo yenu katika kuhakikisha wananchi wanaenda kufaidika na huu mradi wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wimbo mbaya haimbiwi mwana; sisi nikubali kama Waziri wa Maji, Wizara ya Maji ilichezewa sana na niwashukuru sana watangulizi wangu Mheshimiwa Kamwelwe, Profesa Kitila Mkumbo pamoja na Profesa Makame Mbarawa, tumefanya mageuzi makubwa sana katika Wizara yetu ya Maji. Tulikuwa tukifanya ziara, niliwahi kufika pale Njombe kuna Kijiji kinaitwa Ukarao, nipo na Mhandisi wa Maji unamuuliza kwa nini wananchi hapa hawapati maji? Anakwambia tatizo ni design, kama tatizo ni design mbona eneo la Njombe lina baridi, mbona wewe umeweka solar? Anasema Mheshimiwa nimeghafirika, naomba uniokoe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, achana na hilo, nilikwenda Mwakitolio, Shinyanga Vijijini, mradi wa bilioni 1.4, fedha imetolewa lakini wananchi hawapati maji, unamuuliza Mhandisi wa Maji, wewe hapa pesa imetolewa kwanini wananchi hawapati maji? Ananiambia Mheshimiwa Waziri naomba nikunong’oneze. Namwambia hapana kuninong’oneza, waambie wananchi kwa nini hawapati huduma ya maji, sijawahi kuona wananchi wachawi kama kijiji hiki, usiku mabomba yanapaa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, mageuzi ya Wizara yetu hatuwezi kuwa na Wahandisi wababaishaji wa namna hii, mageuzi tuliyofanya, Wahandisi 118 tumekwishaachana nao katika Wizara yetu ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, achana na hilo, moja ya vitu ambavyo vilikuwa vinaathiri Wizara ya Maji ni utitiri wa wakandarasi ambao hawana uwezo. Watu walikua wakipewa kazi kishemeji shemeji, kiujomba ujomba, zaidi ya makandarasi 59 tumeshaachana nao na majina yao tumeyapeleka katika Bodi ya Wakandarasi waweze kuchukuliwa hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo nataka kusema katika Wizara yetu ya Maji, ukicheka na nyenyere ambaye anakutambalia kwenye mapaja atakung’ata pabaya, mimi siko tayari kung’atwa. Tutawashughulikia makandarasi wote ambao watataka kuikwamisha Wizara yetu ya Maji ili kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata huduma ya maji safi salama na yenye kutosheleza. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wizara ya Maji pamoja na timu nzima hatutacheka na mkandarasi, sisi Wizara ya Maji hatutacheka na Mhandisi yeyote wa Maji, sisi tutacheka kwa kuona maji yanapatikana katika mabomba, huo ndiyo msimamo wetu. Kwa hiyo, nishawahi kusema kwamba vipo vya kuchezea, ukishiba chezea kidevu chako au kitambi si miradi ya maji, tutashughulikiana ipasavyo. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mageuzi hayo, tumefanya pilot kwa nini miradi ya maji itumie gharama kubwa. Tumeweza kutengeneza miradi 192 ambayo engineering estimation yake ilikuwa bilioni 207, lakini kutumia wataalam wetu wa ndani tumetekeleza kwa bilioni 163 na bilioni 44 tumeweza kuziokoa. (Makofi/ Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo ukienda Matamba Kinyika pale Njombe, mradi wa engineering estimation iliyoletwa ilikuwa bilioni 6.6, lakini sisi tukasema hapana, mradi huu tutatumia wataalam wetu wa ndani tuone, mradi hule vijiji tisa tumeukamilisha kwa bilioni 1.5, wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tuna mradi pale Sumbawanga Vijijini, Muze Group, mradi huu ni wa vijiji 10, lakini ulitakiwa kutekelezwa kwa bilioni 6.7, tukasema hapana, wataalam unapokuwa Mhandisi wa Maji kwa maana una taaluma ya kutengeza miradi ya maji, hii kazi mnaiweza na hamjashindwa ifanyeni. Sasa hivi vijiji 10 vimekamilika, wananchi wanapata huduma ya maji, bilioni 2 hazijaisha lakini wananchi wale wameanza kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo msimamo sisi Wizara tuliouweka, wakandarasi wababaishaji hawana nafasi, kwa hiyo hatuwezi kufanya kazi zote kwa force account, lakini tulichokifanya sisi kama Wizara ya Maji, tume- shortlist wakandarasi ambao wamefanya kazi nzuri katika Wizara ya Maji wale ndiyo tutakwenda nao kuwapa kazi kuhakikisha kwamba tunakwenda kutatua changamoto ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumekwenda mbali, tulikuwa tukifanya ziara katika wilaya na mikoa, unakuta wilaya moja tank design moja, lakini gharama tofauti. Tukasema hapana sisi tumeanzisha design manual, kesho Waziri Mkuu anakutana na Wahandisi wote wa Maji Nchini, atakwenda kuwakabidhi hizi ili kuhakikisha kwamba Wahandisi wa Maji wanakwenda kutekeleza miradi kwa kufuata designs hizi ili kuhakikisha kwamba Watanzania tunakwenda kuwatekelezea miradi bora, yenye uwezo mzuri na ambayo itadumu kwa muda mrefu kuhakikisha Watanzania wanapata huduma maji safi na salama na yenye kutosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ndugu zangu ni kuhusu suala nzima la ufuatialiaji wa miradi ya maji. Tulikuwa tukipita wakati mwingine Mhandisi au Technician anaweza akakwambia vituo vinatoa maji lakini havitoi, kumbe anashindwa kufuatilia kwa sababu ya changamoto ya usafiri. Kwa kipindi kifupi kwa mageuzi ambayo tumeyafanya, kesho Waziri Mkuu anakwenda kukabidhi pikipiki 145 ili kuhakikisha Technicians wetu hawakai ofisini na kuchezea computer, waende wakafie kwenye matanki ya maji kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na pikipiki hizo magari yanakuja hivi karibuni zaidi ya 22 ili kuhakikisha maeneo ambayo hayana vifaa hivi waweze kupatiwa ili waweze kupata huduma ya maji safi na salama. (Makofi/ Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine lililokuwa linatuathiri sisi kama Wizara ni muundo wa Wizara, leo Mhandisi tuna Wizara ya Maji lakini Mhandisi yuko TAMISEMI. Tumeona changamoto juu ya utumishi na hata kiutendaji katika kumchukulia hatua. Waheshimiwa Wabunge hili lilionekana Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kwa maana Wahandisi wa Maji wote waje chini ya Wizara yetu ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, achana na hilo, kwa dhamira ya dhati ya kuhakikisha kwamba tunakwenda kutatua tatizo la maji, tulileta hapa Muswada wa Sheria na Wabunge wakaupitisha juu ya uazishwaji wa Wakala Maji Vijijini. Sasa hivi ni mwaka mmoja RUWASA amezaliwa kama ndama, amezaliwa anakwenda, leo tumekutana na miradi kichefukichefu zaidi ya 177 ambayo tumei-list mpaka sasa hivi mwaka mmoja, zaidi miradi 85 tumeshaikwamua kupitia RUWASA. Mkakati wetu wa Wizara ya Maji kuhakikisha miradi yote ambayo haijakamilika kuhakikisha tunaikamilisha kwa wakati na Watanzania waweze kupata huduma maji safi, salama na yenye kutosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuwapatia maji ni vita, hatuwezi kukubali kuona kwamba hapa imeliwa milioni 100, hapa imeliwa 150, sisi ni viongozi na hii ni nchi yetu, maji ni uhai, maji hayana mbadala, maji si kama wali ukikosa wali utakula ugali ukikosa ugali utakula makande, ukikosa maji tu utapata maradhi. Kwa hiyo nii ni vita yetu sote na wala msiongope Waheshimiwa Wabunge, baba wa Taifa mwaka 1978 na 1979 wakati anakwenda kumtoa Nduli Iddi Amini alisema maneno yafuatayo: “Nia tunayo, uwezo tunao na sababu tunao”.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwezo wa kukabiliana na makandarasi wababaishaji tunao, kwa kushirikiana wote Waheshimiwa Wabunge. Niwaombe muwe mabalozi na maelekezo ambayo nimeyaelekeza Wahandisi wetu wa Maji hakuna siri, kama unatekeleza mradi Ludewa kwa nini usiwaeleze Baraza la Madiwani, kama unatekeleza mradi Ludewa kwa nini usimwambie Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kanuni na Sheria, zipo janjajanja zilizokuwa zinafanywa na Wahandisi wetu, baadhi unamwambia kwa nini ulete taarifa kwenye baraza? Anakwambia sasa hivi hatuwajibiki huko. Tumeianzisha RUWASA, hatujaanzisha RUWASA kwa maana taasisi iishi mbinguni, tumeanzisha kwa ajili ya kutatua matatizo ya watu, lazima washirikiane na viongozi katika maeneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nimekwishazungumza na Mheshimiwa Ummy dada yangu kuhakikisha kwamba tunashirikiana na Wizara ya TAMISEMI na Ofisi ya Mazingira kuhakikisha tunasimamia tunafuatilia kwa pamoja ili kuhakikisha kwamba Watanzania waishio vijijini wanapata huduma majisafi salama na yenye kutosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha kwamba tunaongeza nguvu mikoani na kukwamua miradi mingi kwa wakati na Watanzania waweze kupata huduma ya maji, tumeweza kuanzisha timu mikoani Water Rescue Team. Hapa tumeangalia kada tofauti tofauti ipo changamoto ya design, tumeweka wataalam wa design; kama kuna changamoto ya suala la manunuzi, kuna wataalam wa manunuzi; na kama suala la tafiti la maji, kuna mtu wa tafiti za maji. Kwa hiyo haya tumeyazingatia na tumeanza kutekeleza na tumeona miradi mbalimbali tunavyoikwamua kwa wakati na hii imetusaidia pia kubadili mind set za watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mind set za Wahandisi wetu wa Maji wakati fulani zilikua zinatuchelewesha. Kwa mfano, Serikali unaweza ukakuta imewekeza fedha nyingi Bukoba, Dar es Salaam, Mwanza na Tabora, lakini leo hata mtu akitaka kutengeneza mtandao wa mita kumi anakuja kuomba fedha katika Wizara, tumesema hapana. Leo tumeona DAWASA makusanyo yao walikuwa wakikusanya bilioni saba sasa hivi wanakusanya bilioni 13 na fedha zile wameweza kutekeleza miradi. Wameweza kutekeleza mradi wa bilioni 10 Kisarawe kwa kutumia pesa zao za ndani, wameweza kutekeleza mradi wa maji Kigamboni kwa bilioni 25 kupitia fedha zao za ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka niwaambie Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Maji ukibebwa na wewe basi hebu usijiachie, kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto maji. Kwa yeyote ambaye atashindwa, atatupisha ili kuhakikisha kwamba tunaenda kuwapatia Watanzania huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, limezungumzwa hapa suala la uvujaji wa maji. Si busara hata kidogo kuona Serikali imewekeza fedha nyingi katika miradi ya maji lakini unapita mtaani maji yanamwangika ili hali wananchi wengine hawana maji. Niliwahi kufanya ziara katika baadhi ya Mamlaka, unapewa taarifa, Mkurugenzi wa Maji anakwambia hapa upotevu wa maji ni asilimia 46. Mtu anapokwambia upotevu wa maji asilimia 46 lazima uhoji, mimi nategemea unaponiambia upotevu wa maji asilimia 46 nikipita mtaani niyaone mabwawa ya samaki au nione mafuriko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu ambacho nilichokigundua, kuna wizi mkubwa sana wa maji. Nilifanya ziara Morogoro pale, wamenipa taarifa lakini nikajiridhisha kulala, tumeenda kukikamata kiwanda kinaiba maji bila utaratibu wowote, tumebanana nao zaidi ya milioni 250 wamezilipa.
Kwa hiyo, nimeshawaita Wakurugenzi wa Mamlaka zetu za Maji na nimewapa maelezo mahususi; moja kudhibiti huu wizi na huu wizi wakati mwingine hata baadhi ya watumishi wetu wanashiriki. Kwa hiyo kikubwa hawa watu tutawachukulia hatua na hii ni vita yetu sote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni juu ya upashanaji wa habari, leo mwananchi anaweza akaona maji yanavuja, anatoa taarifa kwenye mamlaka husika hawa- respond, lakini mwananchi huyo huyo anajiunga bando anamtumia Waziri, Waziri ukitumia katika mamlaka hiyo hiyo, utaona wanapiga picha Mheshimiwa tumeenda hata kama usiku tumeshakwamua.

Mheshimiwa Naibu Spika, maelekezo ambayo tumewapa Wakurugenzi wa Mamlaka zetu za Maji utaratibu wa haraka ambao wanaufanya kama tunavyowatuma sisi viongozi, waende wakafanye pale mwananchi anapowapa taarifa, kwa sababu wananchi ndiyo mabosi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kulishukuru Bunge, lakini tumepata maoni mazuri sana. Ninachotaka kukisema, mvua katika nchi yetu ya Tanzania isiwe laana, iwe fursa, kwa maana ya kuhakikisha kwamba tunatengeneza miundombinu ambayo tunaweza tukavuna maji lakini tunaweza kujenga mabwawa yatakayoweza kutumika katika maeneo yenye ukame ambayo hayana maji, yaende kupatiwa huduma ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo niendelee kumpongeza sana Naibu wangu Waziri wa Maji ili ni jembe wembe amefanya kazi kubwa sana na namna anavyojituma, Waziri wako nitakupa ushirikiano mkubwa sana. Lakini kwa namna ya kipekee nimshukuru sana katibu wangu Mkuu Engineer Athony Sanga pamoja na Naibu Katibu Mkuu mama Engineer Sediki kamikimba katika kuhakikisha kwamba watanzania wanapata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tumejipanga leo Katibu Mkuu akiwa Ruvuma mimii nipo Songea yeye akiwa Ruvuma mimi zangu Mbeya Naibu Waziri akiwa Kilimanjaro Naibu Katibu Mkuu yupo zake Mtwara yote ni katika kuhakikisha tunasimamia na tunafuatailia miradi yetu ya maji na watanzani wanaweza kupata huduma maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Maendeleo ya sekta ya maji Waheshimiwa Wabunge yanaanza na mimi maendeleo ya sekta ya maji Waheshimiwa Wabunge yanaanza na wewe, maendeleo ya sekta ya maji yanaanza na sisi sote kwa kushikamana ahsante sana mungu awabariki sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi/Vigelegele)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda nimshukuru sana Mwenyezi Mungu, kwa sababu maandiko yanasema yapaswa kushukuru kwa kila jambo.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu. Kwa namna ya kipekee nimshukuru sana Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kuniamini kuwa kwenye dhamana ya Wizara hii ya Maji kuwapatia wananchi maji, kwa imani yangu ukiwapatia wananchi maji basi unapata baraka. Na nipo tayari kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge kuendelea kupata baraka hizi za kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee nikushukuru wewe binafsi kwa mijadala tangu mwanzo mwisho mmeusimamia mpaka leo tunafika katika suala zima la kuhitimisha; nimshukuru pia Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wote wa Bunge kwa namna walivyozisimamia shughuli zao katika Bunge mpaka leo hii tunakwenda katika hitimisho.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee nimshukuru sana Mwenyekiti wetu wa Kamati, Makamu pamoja na Wajumbe wote wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli Wizara yetu ya maji yawezekana kipindi hicho nyuma sikuwahi kuwa Mbunge lakini kuona Wizara inapongezwa, sijawahi kuona. Wizara ya Maji ilikuwa ni Wizara ya lawama, lakini leo hii Waheshimiwa Wabunge mnatupongeza; mmetutia moyo sana. Ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naninachotaka kukisema tu mbele ya Waheshimiwa Wabunge ni kwamba kama ni betri basi iko fully charged. Sisi viongozi wa Wizara ya Maji; mimi pamoja na Naibu wangu, Maryprisca Mahundi; Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Engineer Anthony Sanga; Naibu Katibu Mkuu, Nadhifa Kemikimba, na watumishi wote kwa maana ya wataalam wa Wizara ya Maji, tutafia kwenye matenki katika kukahikikisha Watanzania wanapata huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kumshukuru kwa dhati kabisa Mwenyekiti pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, kwa maoni na ushauri waliolenga kubadili mitazamo na fikra na kuboresha namna tutakavyofanya kazi Sekta ya Maji.

Mheshimiwa Spika, maeneo yaliyotolewa ushauri ni pamoja na upatikanaji wa fedha, uvunaji wa maji ya mvua, upatikanaji wa misamaha ya kodi, ujenzi wa miundombinu ya majitaka, matumizi ya maji kutoka katika vyanzo toshelevu kwa maana ya ziwa na mito, umuhimu wa matumizi ya dira za maji za malipo kabla ya matumizi, masuala ya takwimu pamoja na maji kwa ajili ya wananchi na mifugo yao katika maeneo yanayopitiwa na mabomba makuu. Nataka niseme tu yote tumeyachukua na tutayafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja yangu imechangiwa na jumla ya Waheshimiwa Wabunge zaidi ya 65, wamechangia kwa kuongea na kwa maandishi. Kwa dhati kabisa nitumie fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao ambayo kwa kiasi kikubwa inalenga kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu yetu ndani ya Wizara ya Maji na taasisi zake na sekta kwa ujumla. Itoshe tu kusema Waheshimiwa Wabunge kwa kuwa wachangiaji ni wengi sana nitaomba nijibu hoja kwa ujumla wake. Lakini kwa kweli nawashukuru sana na Mwenyezi Mungu awabariki sana Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza kwa ujumla, michango ilivyotolewa na Waheshimiwa Wabunge ni mingi na yote inalenga kuleta tija kwenye sekta yetu ya maji. Hata hivyo, michango kadhaa imerudiwa na Waheshimiwa Wabunge wengi na mingine imechangiwa kwa hisia kali. Kwa kuwa muda uliopo hautoshi kujibu hoja zote, moja baada ya nyingine, naomba nitumie fursa hii kujibu hoja chache kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hoja moja wapo ambayo imezungumza ni juu ya upotevu wa maji; ni aibu na hatuwezi kukubali kuona Serikali inawekeza fedha nyingi wananchi wapate huduma ya maji halafu zije taarifa kwamba kumekuwa na upotevu mkubwa sana wa maji.

Mheshimiwa Spika, na mimi kama Waziri wa Maji nilishawahi kufanya ziara katika baadhi ya mamlaka zetu za maji. Niliwahi kupata taarifa kwamba hapa kuna upotevu wa maji wa asilimia 40, nilihoji kama kuna upotevu wa maji wa asilimai 40 kwa akili yangu tu ya kawaida kwamba ninategemea kuona mabwawa ya Samaki mtaani.

Mheshimiwa Spika, kwa akili yangu ya kawaida nilitegemea nione chemichemi za mito. Asilimia 40 ya upotevu wa maji si jambo dogo Waheshimiwa Wabunge. Kwa bahati nikamwambia hebu nipitishe baadhi ya mitaa sasa nione maji yanayopotea; tumepita baadhi ya mitaa sikuona hiyo asilimia 40 ya maji inayopotea.

Mheshimiwa Spika, ukweli wa dhati kabisa ni kwamba maji tunayosema yanapotea asilimia kubwa au kwa kiwango kikubwa yanaibiwa. Baadhi ya viwanda wanaweza wakajiunganishia kinyemela pasipo kulipa halafu mamlaka ya maji inadai kwamba au inatoa taarifa kwamba maji yale yamepotea, lakini yule ni mteja ambaye ametumia maji lakini hahesabiki katika taarifa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hayo ni maelekezo ambayo tumetoa kwa baadhi ya mamlaka zetu za maji kuwajua wateja wao wakubwa na wadogo katika kuhakikisha wanadhibiti ili maji na malipo yaweze kupatikana na wananchi waweze kupata huduma ya maji safi na salama. Na vipo baadhi ya viwanda tulishawahi kukamata na tumeweza kuchukua hatua, lakini Waheshimiwa Wabunge hili jambo lazima tukubali kushirikiana. Serikali inawekeza fedha nyingi kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa namna nyingine sisi kama Wizara tumejipanga kutoa fedha na kukarabati maeneo ambayo yamekuwa na miundo mbinu chakavu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, mathalani, eneo la Mtwara pale mjini. Mahitaji ya Mji wa Mtwara ni lita milioni 15, uzalishaji wa vyanzo vyetu ni lita milioni 13, lakini changamoto ya pale Mtwara ni miundombinu chakavu tangu ukoloni. Kupitia bajeti hii tunatoa fedha kwa eneo la Mtwara kuhakikisha wanakwenda kutengeneza miundombinu ile na wananchi waendelee kupata huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kikubwa ni kwamba hili tumeliona na tutahakikisha kwamba kila mtumiaji anakua na dira bora ili kudhibiti upotevu huu wa maji na tuweze kuuweka katika asilimia ambayo inakubalika, asilimia 20. Sasa hivi kinchi tupo asilimia 36, lakini maelekezo ya Wizara ambayo tumewapa mamlaka zetu, na ndiyo kipimo, katika kuhakikisha kwamba lazima wasimame hapa na kwa kushirikiana na EWURA tunaendelea kudhibiti mamlaka zetu kuhakikisha kwamba tunakuwa katika hiki kiwango cha asilimia 20.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili lililozungumzwa ni tatizo la bei za maji mijini na vijijini; ni haki ya mwananchi kupatiwa huduma ya maji lakini mwananchi naye asisahau ana wajibu wa kulipia bili za maji. Ili gari liende lazima liwe na mafuta.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mwananchi kupatiwa huduma hii ya maji lazima atambue maji kutoka mtoni hayana miguu useme yatafika nyumbani lazima tuweke pampu na umeme ili kuhakikisha kwamba maji yale yanafika. Kwa maana hiyo, pale kutakuwa na gharama zinazohitajika.

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na wajibu wa mwananchi kulipia bili za maji, sisi kama Wizara ya Maji tunasema bili hizo zisiwe bambikizi. Haiwezekani mwananchi ametumia maji ya 15,000 unamwambia alipe 120,000; haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja, tumetoa maelekezo kwa wasomaji mita wetu kwamba lazima wawe waamini na waadilifu juu ya usomaji. Lakini tumekwenda mbali sisi kama Wizara ya Maji kwa maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge, sisi lazima tutumie teknolojia ya sasa kuhakikisha tunafanya mageuzi katika Wizara yetu ya maji.

Mheshimiwa Spika, tumeanzisha Unified Billing System. Kabla mteja hajasomewa mita zake au hajachajiwa bili anayotakiwa kulipa, anapokea message kwamba bwana fulani umetumia maji unit 30 unadaiwa kiasi fulani, thibitisha, anathibitisha mwisho wa siku tunaweza kum-charge bili ili aweze kulipa.

Mheshimiwa Spika, lazima tukubali kwamba sisi Wizara ya Maji si kisiwa, lazima tukubali kubadilika. Na kizuri huigwa. Tunaona wenzetu wa TANESCO wana mita za LUKU. Ni muda muafaka, na tumeshatoa maelekezo kwa Wizara. Na nimshukuru sana Katibu Mkuu wetu wa Wizara ya Maji, kaka yangu, Engineer Anthony Sanga, mimi nasema anatosha mpaka chenji inabaki, tumpigie makofi mengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi wadau mbalimbali wameshakuja, tunajifunza hizi mita kabla hatujaenda kumfungia mwananchi, zile changamoto ambazo tunaziona basi tuweze kuzitatua. Lakini eneo ambalo tunaweza kuondokana na changamoto ya bili za maji lazima tukubali mwarobaini wake ni prepaid meter, lazima twende katika katika uelekezo huo.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo naomba tusaidiane katika hili ili kuhakikisha kwamba tunafanya mageuzi katika Wizara yetu ya Maji.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo kama Waziri wa Maji nimejifunza, inakuwaje mwananchi Jijini Dar es Salaam unit ya maji analipa 1,600, lakini ukienda kijijini mwananchi anatumia maji ndoo ananunua kwa shilingi 50. Unaposema unit moja maana yake nini; unit moja maana yake ni lita 1,000. Lita 1,000 maana yake nini; lita 1,000 maana yake ndoo za lita 20, ziwe 50.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa mwananchi wa kijijini akinunua ndoo shilingi 50 maana yake ndoo 50 analipa shilingi 2,500 ilihali pale DAWASA Dar es Salaam mwananchi ananunua unit moja kwa shilingi 1,600 tena anapata nyumbani; hilo haliwezekani. Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, ametupa maelekezo Wizara ya Maji; wananchi watumie maji kwa bei rahisi na nafuu na wanufaike na matunda ya Serikali yao ya Awamu ya Sita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi Wizara ya Maji kupitia RUWASA tumetoa maelekezo mahususi kupitia bei zote za maji vijijini. Baada ya Bunge hili tutatoa bei elekezi kwa vijijini ili kuhakikisha wananufaika kwa kazi kubwa na maoni mazuri yanayotolewa na Waheshimiwa Wabunge wao hapa katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndugu zangu, nataka nizungumze jambo moja; lazima tukubali Rais wetu tangu ameingia ni mwaka mmoja tu. Hatuwezi kusema kwamba tumemaliza matatizo ya maji kabisa. Lakini tunachotaka kusema ni kwamba jitihada za muda mfupi ambazo amezifanya Rais wetu Mama Samia Suluhu si za kubeza hata kidogo, anatakiwa kuungwa mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi katika Wizara yetu ya Maji, haijawahi kutokea bajeti kutekelezwa kwa asilimia hata 80, leo tunaitekeleza bajeti asilimia 95; haijawahi kutokea. Yapo maandiko ya dini yanasema Waama “Bi-Neemat Rabbika Fahadithi”, zielezeeni neema za Mwenyezi Mungu kwa kushukuru; tumshukuru sana Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, actions speak louder than words, matendo yanaongea kuliko maneno. Leo tunaona Mheshimiwa Rais kwa mwaka mmoja kwa namna ya fedha hizo zilizotoka, achana na hilo tu la fedha, yeye kama Mama maelekezo ambayo ametupa sisi Wizara ya Maji, mimi ndio Waziri pekee ambaye niliwahi kusimamishwa katika Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, nakumbuka alisema Waziri wa Maji uko wapi nikasimama. Akasema yeye ni Mama na anatambua asilimia kubwa ya wanaoteseka ni akina mama Vijijini. Akina mama wanatembea umbali mrefu kwa kukosa maji kwa maana ya kutafuta maji, wengine wamepoteza ndoa zao. Hataki kusikia, hataki kuona akina mama wakiteseka juu ya tatizo la maji.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, nataka niwaambie baada ya maneno yale mimi sikuwahi kulala, lakini nilikaa na nikajitafakari na Waheshimiwa viongozi wenzangu kwa maana watendaji wote.

Mheshimiwa Spika, nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge, hakuna sikio lolote duniani lisilosikia vinywa vingi vikisema pamoja; tumewasikia.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Maji ilikuwa na changamoto nyingi sana lakini mpaka hapa tulipofika, tulipotoka ni mbali. Moja ya changamoto kubwa sana ambazo zilikuwa zinaiathiri Wizara yetu ya Maji ni miradi iliyojengwa chini ya kiwango ya vijiji 10. Ni miradi ambayo imejengwa matenki lakini haitoi maji.

Mheshimiwa Spika, kazi ya kwanza ambayo tumejipa – na tuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kuona haja ya kuanzishwa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA), hayo ni maoni yenu Waheshimiwa Wabunge. RUWASA ina miaka miwili hadi mitatu sasa tunakwenda, kama ndama, amezaliwa na kwenda. Ameikuta miradi 177. Kwa muda huu mfupi nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge miradi 127 tumekwishaikwamua katika kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kubwa tunaona nuru na mwendo wa Wizara yetu ya Maji, utekelezaji wa miradi ya maji unategemeana na fedha; Mheshimiwa Rais anatu- support. Tumezungumza hapa, Wizara ya Maji, kwa maana kama nchi, hatuna uhaba ama umasikini wa vyanzo vya maji, tuna maji juu ya ardhi zaidi ya mita za ujazo bilioni 105, maji chini ya ardhi ni mita za ujazo bilioni 21 kwa maana ya total ya bilioni 126; hatuna sababu ya kulalamika juu ya matatizo ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja ya changamoto zilizokuwa zinatuathiri sisi Wizara ya Maji ni vitendea kazi. Leo kwa Mheshimiwa Kuchauka, pale miaka yote watu wamefanya tafiti pamoja na tunatambua rasilimali za maji tulizokuwa nazo, ni mita za ujazo bilioni 21 lakini hatupati maji na tulishaaminishwa kwamba hapa maji hakuna. Lakini nashukuru sana wataalam wetu kwa mind set ambazo tunazigeuza, leo wamekwenda Liwale tumepata maji ya kutosha, na Mheshimiwa Mbunge ni shahidi, tunakwenda kupeleka fedha sasa kutatua tatizo la maji Liwale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nini maana yake; wakati mwingine tunashindwa kujua maji chini ya ardhi yapo au hayapo kwa sababu ya ukosefu wa vifaa vya kisasa. Uking’ang’ania vifaa vilivyopitwa na wakati utakuwa umepitwa na wakati. Samia Suluhu Hassan ndio suluhu ya matatizo ya maji hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ametupatia fedha, tunakwenda kununua mitambo 25 kwa ajili ya kuchimba visima. Na kila mkoa utakuwa na mtambo wake wa kuchimba; haijawahi kutokea, tumpigie makofi mengi sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, achana tu na mitambo, anatambua kwamba siyo maeneo yote ukichimba unaweza ukapata maji; siyo maeneo yote. Yapo maeneo ambayo tukichimba tunapoteza fedha za Serikali. Ametupatia fedha kwenda kununua seti tano kwa ajili ya kuchimba mabwawa, siyo tu kwa wananchi kupata maji, bali hadi mifugo yao nayo iweze kupata maji. Haya ni mageuzi makubwa sana kwa Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mitambo kwa ajili ya utafiti, zaidi ya minne, fedha ameshatupa. Ndani ya mwezi huu wa Sita tutapokea vifaa vile katika kuhakikisha watu wanakwenda kupata huduma ya majisafi na salama.

Mheshimiwa Spika, na ninataka niwaambie wakandarasi na wahandisi wetu wa maji – nilishazungumza kwenye bajeti – sisi viongozi wa Wizara ya Maji tutacheka kwa kuona maji bombani, lakini kwa mhandisi ama mkandarasi ambaye atatuchelewesha juu ya upatikanaji wa maji, ukicheka na nyani utavuna mabua, sisi hatupo tayari kucheka na mtu yeyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la miji 28. Tulikuwa na viporo ama miradi ambayo ilikuwepo tu kwenye makaratasi Waheshimiwa Wabunge. Suala la miji 28 lilikuwa likizungumzwa tu, halitekelezeki. Samia Suluhu Hassan ndiyo amekuja kuwa-unlock mradi huu wananchi wapate huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, amefanya mazungumzo na Viongozi Wakuu wa India, amemuita Balozi Ofisini kwake. Leo nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge, tumalize Bunge, Mheshimiwa Rais tumemuomba ashuhudie utiaji saini wa miradi hii kwenda kutekelezeka.

Mheshimiwa Spika, na narudia hapa; tusidanganyane, tunakwenda kutekeleza Mradi wa Maji HTM kwa maana Handeni, Korogwe, Muheza, Pangani; tunakwenda Kilwa Masoko, Nanyumbu, Ifakara, Chunya, Rujewa, Waking’ombe, Makambako, Njombe, Kiomboi, Singida, Manyoni, Chemba, Chamwino, Mugumu, Kasulu, Mpanda, Sikonge, Urambo, Kaliua, Kayanga, Geita, Chato, Mafinga, Makonde, Rorya, Tarime na Songea. Hizi ni jitihada kubwa zinazofanywa na Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, jana kaka yangu, Mheshimiwa Katani – hapa naona ameondoka – nataka nimueleze yafuatayo: -

Mheshimiwa Spika, sisi kama Wizara ya Maji maelekezo ambayo Mheshimiwa Rais ametupa hajatueleza kwamba sehemu fulani peleka maji, sehemu nyingine usipeleke. Ametupa maelekezo kuhakikisha asilimia 85 ya upatikanaji wa maji vijijini na asilimia 95 ya upatikanaji wa maji mjini.

Mheshimiwa Spika, tumetenga kiasi cha shilingi bilioni 29 kwenda kutekeleza miradi ya maji 44 katika Mkoa wa Mtwara. Lakini katika Jimbo la Mheshimiwa Katani tunakwenda kutekeleza mradi ambao unajumuisha zaidi ya vijiji 15 ambao unaoitwa Mradi wa Nanyuwila – Maundo. Mradi ambao utakwenda kutatua matatizo ya maji kwa Vijiji 15 vya Nakayaka, Mnyawa, Mchichira, Mkwajuni, Shangani, Pachani, Mnarani, Namahonga, Maundo, Chiumo, Chang’ombe, Kunanundu, Lukokoda, Ghanajuu na Ghanachini; hizi ni jitahada za Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tuna Mradi ambao tunauita wa Mkwiti ambao unakwenda kutatua shida ya maji katika vijiji 17, Kijiji kimoja sasa hivi cha Mangombya kimeshaanza kupata huduma ya maji. Mkandarasi yuko site anaendelea na ujenzi wa matenki matano ili kuhakikisha wananchi hawa wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumesikia maombi ya Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Mtwara juu ya ujenzi wa Mradi wa Makonde. Mimi binafsi Mheshimiwa Rais alinituma kwenda zangu Newala nimekwenda kujionea hali ya mradi ule.

Mheshimiwa Spika, mradi ule ni chakavu, mradi ule tangu Baba wa Taifa, mradi una umri mkuwa kuliko mimi Waziri wa Maji na hamna namna nyingine zaidi ya kujenga mradi mpya. Nataka nimpe taarifa baba yangu, Mheshimiwa Mkuchika, na Mheshimiwa Katani, waandae futi. Mheshimiwa Rais ametupa maelekezo na tumekwishapata mkandarasi, kilichobaki tunakwenda kusaini mradi wa zaidi ya bilioni moja kuhakikisha Wanamakonde, Tandahimba pamoja na Nanyamba wanakwenda kupata huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ipo miji tunasema kwamba imeachwa. Lakini pia moja ya hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezijenga ni kuhakikisha kwamba Serikali inatumia rasilimali toshelevu kwa ajili ya kutatua matatizo ya maji.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekwishaanza; ukienda Lindi pale Mjini tuna mradi wa bilioni 33 umekwishakamilika. Mradi ule wa bilioni 33 tumetoa bilioni tatu kwa ajili ya kupeleka maji Mitwero. Sasa hivi tumetoa bilioni 12 kwa ajili ya kupeleka maji Mchinga kwa mama yetu, Mheshimiwa Salma Kikwete. Hizo ni jitahada kubwa sana za Serikali.

Mheshimiwa Spika, leo hii ukaenda zako Musoma kwa dada yangu, Mheshimiwa Esther Matiko, Mkoa wa Mara, tuna mradi wa zaidi ya bilioni pale, tumeshaukamilisha. Lakini tumekuja na Mheshimiwa Rais katika Mradi wa Mugango – Kiabakari – Butiama, zaidi ya bilioni 70. Tumekwishautekeleza. Sasa hivi tumeshaukamilisha mradi pale Bunda Mjini zaidi ya bilioni 10; hivi Mheshimiwa Rais awape nini au awape donda mfukuze nzi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kikubwa sisi tunachotaka ni kumuunga mkono Rais wetu. Tumeona ameyatoa maji Ziwa Victoria tumeyaleta Tabora, tumeyapeleka Igunga, tumeyapeleka Nzega, zaidi ya bilioni 600, na vijiji 100 vinapata huduma ya maji safi na salama. Mradi ule sasa unakwenda Kaliua, unakwenda Sikonge hadi Urambo kwa Mheshimiwa Mama Sitta, katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, ukienda Arusha tuna mradi wa zaidi ya bilioni 520 hii; hii yote ni katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, ukienda zako pale Sumbawanga Mjini tuna mradi wa zaidi ya bilioni 35; hizi ni jitihada kubwa. Kwa hiyo kikubwa Waheshimiwa Wabunge tunakubaliana kwamba rasilimali toshelevu kwa maana ya maziwa na mito tuliyokuwa nayo, ikitumika itakwenda kutatua matatizo ya maji. Na mimi Waziri wa Maji naamini hilo kupitia Kamati yangu.

Mheshimiwa Spika, leo tunakwenda kutatua mradi mkubwa wa maji pale Mbeya kwa kutumia Mto Kiwira kwa maelekezo tu. Sisi Waheshimiwa Wabunge maelezo na maoni mliyotupa tumeyapata tutayafanyia kazi katika kuhakikisha watanzania wanapata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho; Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan lazima tumuunge mkono. Kama nilivyotangulia kusema awali, kuna mambo ambayo ni magumu kufanyika lakini Rais wetu ana uthubutu. Tumeona Dar es Salaam namna tulivyopitia kwenye changamoto ya crisis ya Mto Ruvu kukauka, leo tunakwenda kujenga Bwawa la Kidunda. Huu ni uthubutu wa hali kubwa sana, na tumpigie makofi sana Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)

Lakini tunaona eneo hili la Jiji la Dodoma tangu Serikali ihamie hapa kumekuwa na uhitaji mkubwa sana wa maji. Kwa muda mfupi Mheshimiwa Rais ameingia, kutokana na mahusiano yake mazuri, tumepata fedha kupitia African Development Bank, zaidi ya USD milioni 125 kwa ajili ya kwenda kuanza kujenga Bwawa lile la Farkwa; hizi ni jitihada kubwa sana. Bunge limeshauri kwa muda mrefu lakini utekelezaji wake ulikuwa wa kusuasua, leo tunakwenda kulitekeleza hili jambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuzungumza haya, ahsante sana na Waheshimiwa Wabunge Mwenyezi Mungu Awabariki sana. Naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema pamoja na ninyi sote na kuweza kuchangia bajeti ya Wizara yetu ya Maji. Waheshimiwa Wabunge, Mwenyezi Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu limeweza kujadili bajeti yetu ya Wizara ya Maji ya Mwaka 2023/2024 niliyoiwasilisha hapa Bungeni tarehe 10 Mei, 2023.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwako wewe binafasi kwa kazi kubwa na usimamizi mzuri katika Bunge lako hili Tukufu lakini kama kiongozi kijana yako mengi ambayo nimejifunza kutoka kwa Spika wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo moja ambalo nimejifunza kutoka kwako, kwamba hata uwe kiongozi na cheo kikubwa namna gani usisahau ulipotoka. Hata uwe na nyadhifa kubwa namna gani usiwasahau unaowaongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimepata dhamana ya kuwa Waziri wa Maji, niliwahi kufika pale Mbeya, pamoja na kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hujaacha hata siku moja kuwasemea wananchi wako katika Jiji la Mbeya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nikutie moyo, upo msemo unaosema” ukipigana vita ugenini nyumbani lazima kuwe na amani” pamoja na bajeti hii ambayo tunayopitisha, tunajua ombi ambalo ulilotupa kwetu sisi kama wizara, tunatekelea mradi wa bilioni 117 pale Mbeya na Advance payment tumekwishaitoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza Naibu Spika, pamoja na wenyeviti wote wa Kamati, kwa namna walivyoweza kusimamia bajeti yetu ya Wizara yetu ya Maji. Lakini kwa namna ya kipeke usione vyaelea ujue vimeundwa. Leo tunapongezwa Wizara yetu ya maji sio jambo jepesi sana. Mageuzi haya ambayo sisi kama viongozi wa Wizara ya Maji ambao tumeshirikiana na wenzangu haikuwa Rais. Kwa sababu tulipoyaleta katika Bunge lako Tukufu tulipata baraka zote. Hatuna cha kuwalipa Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo kabla sijaja kuhitimisha bajeti yetu, hivi mchana nilikuwa nimekaa na watendaji wetu wa wizara tulikuwa tunaangalia na kuweza kutoa commitment ya utekelezaji wa zile hoja ambazo zimetolewa na Waheshimia Wabunge. Moja wa mtendaji wetu alisimama na akasema Mheshimiwa Waziri, naomba utufikishie salamu kwa waheshimiwa wabunge. Pamoja na ukurugenzi wangu nimefanya kazi katika Wizara ya Maji leo inafika miaka 20. Wizara yetu hii ya Maji ilikuwa wizara ya kero na lawama tu. Kila tukija Bungeni hali ilikua ni tete sana. Leo Waheshimiwa Wabunge wanatupongeza, Waheshimiwa Wabunge, Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, funzo ambalo mmetupatia sisi kama viongozi na watendaji wa Wizara ya Maji, huna sababu ya kujitutumua wewe fanya kazi watu wanaona. Mmetutia moyo, mmetutupia nguvu kubwa sana. Commitment ambayo nimepewa na watendaji wetu wa Wizara ya Maji, kusema katika Bunge hili Tukufu na kumwambia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wanasema kama betri ambalo lilikuwa linachajiwa sasa liko full charge watafia site. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wametoa slogan katika kikao ambacho kilichokaliwa leo, wamesema slogan ya sasa ya Wizara ya Maji, itakuwa Die empty. Watatumia maarifa yao, watatumia nguvu zao kuhakikisha azma ya Rais wetu Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha maelekezo na target za Chama cha Mapinduzi kwamba itakapofika mwaka 2025, asilimia 85 ya upatikanaji wa maji vijijini na asilimia 95 ya upatikanaji wa maji Mjini tunakwenda kuitekeleza kwa dhati kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wamenituma niwaeleze waheshimiwa wabunge, pongezi ambazo mmezitoa wanadeni kubwa sana. Wanasema kwamba ukicheza ngoma lazima uangalie na jua. Maji ni pamoja na uhai, maji ni pamoja na huduma muhimu lakini maji ni siasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, michango yenu ambayo mmeieleza katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, utekelezaji wake maana yake ni kuhakikisha kwamba mnarudi. Kwa hiyo, sisi watendaji wa Wizara ya Maji, pamoja na kazi ya kupeleka maji lakini tuna kazi ya kulinda majimbo ya Waheshimiwa Wabunge katika kuhakikisha mnarudi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara yetu ya Maji kama nilivyoeleza hakuna hata mmoja asiyejua. Mheshimiwa Rais, aliwahi kuhutubia katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano tarehe 22 Aprili, alinisimamisha pale akatoa maelezo mahususi kwamba, yeye ni mama na hataki kusikia, hataki kuona wamama wa Taifa hili wanahangaika juu ya adha ya maji. Pia, akaenda mbali zaidi akaniambia, Waziri wa Maji, wewe unawaambia watendaji wako ukinizingua nitakuzingua.

Mheshimiwa Spika, hakuna siku ngumu katika maisha yangu kama siku ile. Niliweza kukaa na watendaji wangu kwa kina nikawauliza swali moja, je, hii kazi tunaiweza au hatuiwezi? Wameniambia hii kazi tunaiweza. Nataka niwambie pongezi hizi ambazo waheshimiwa mmezitoa, nataka nizirudishe kwa watendaji wote wa Wizara ya Maji. Waheshimiwa Wabunge, pongezi hizi zote ambazo mmezitoa naomba nizirudishe kwa Rais wangu Mpendwa, Samia Suluhu Hassan, ambae ameasisi kauli ya kumtua Mama ndoo kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja ya chanagamoto kubwa ya Wizara yetu ya Maji juu ya utekelezaji wa maji ni ufinyu wa bajeti. Ipo miradi ambayo sisi tumeikuta ambapo hata mimi sijawahi hata kumaliza chuo au sekondari. Kwa Mfano, ukienda Serengeti kulikuwa kuna mradi unaitwa Mugumu na kweli mgumu kweli kweli. Zimepita awamu zote mradi ule haujakamilika. Waziri ukija hapa kimbembe chake si mchezo. Mradi ule Mugumu umemalizwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna miradi ilikuwa ya kichefuchefu ambapo imejengwa unaweza ukawa kiongozi ukafika pale ukauzindua mradi, maji yanatoka leo ukiondoka unaondoka na maji yako. Wananchi wanateseka pesa zimetolewa, Mwakitolyo, Nyantukuza kule Nyang’wale lakini Mheshimiwa Rais alitupa maelekezo miradi ile ambayo ilikuwa ikiitwa kichefuchefiu ambayo tuliianisha 177, Waheshimiwa Wabunge mlipitisha mageuzi ya kuanzisha wakala wa maji vijijini RUWASA kwa ajili ya kwenda kutatua matatizo ya maji. Miradi 157 yote tumeikwamua watu wanapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara yetu ya Maji, ilikuwa inafanya sasa mageuzi. Nini? kwa maana ya designing manual, ipo miradi ilikuwa inajengwa kwa gharama kubwa sana. Kwa mfano, ukienda kwa Kaka yangu Festo, kuna miradi ambayo ilitakiwa kutekelezwa zaidi ya billioni sita, sisi tukasema hapana. Matamba - Kinyika, tulifika pale tukasema miradi hii haiwezi kutekelezwa hivi. Wewe unapokuwa Mhandisi wa Maji wewe umesomea maji. Badala ya kumpa mkandarasi hebu tuone uwezo wako, mradi ule umejengwa kwa bilioni mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda Shinyanga Vijijini mradi ambao unaitwa Muze Group ambao ulitaka kutekelezwa kwa zaidi ya bilioni tano tukasema hapana. Tunaposema mhandisi wa maji wewe umesomea maji unaweza kufanya hiyo kazi. Tumewapa ile kazi wameweza kutekeleza hata bilioni haijakamilika mradi umekwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Ukienda zako Babati mradi ambao unaitwa Singu Sibino, na Kamati ilifika imejionea, ulitakiwa kujengwa na mkandarasi kwa zaidi ya bilioni 20, tukasema hapana wataalamu mtafanya hii kazi. Wameifanya, na leo hata bilioni 12 haijakamilika na ule mradi unaenda kukamilika na watu wanapata maji.

Mheshimiwa Spika, nini maana yangu; niwashukuru sana viongozi wetu wakuu. Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja kutufungulia, nakumbuka pale Chuo Kikuu cha Mipango; Design Manual kwamba kila mhandisi wa maji katika Wizara ya Maji anapotaka ku-design lazima afuate design manual.

Mheshimiwa Spika, hatuweze kutekeleza miradi ya maji hapa Dodoma eneo moja lakini kila tenki saizi moja lakini gharama tofauti, haiwezekani. Tumeanzisha Chuo cha Maji kwa minajili ya kuwatumia wataalamu wasaidie sekta ya maji, mageuzi haya leo tunawapongeza ni kazi kubwa ambazo mmezifanya Waheshimiwa Wabunge, Mwenyezi Mungu atawabariki sana na mtakumbukwa katika historia ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukitaka kufika haraka nenda zako mwenyewe, lakini ukitaka kufika mbali nenda na wenzako. Nitumie nafasi hii kumshukuru sana Naibu Waziri Maryprisca Mahundi, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Katibu Mkuu wangu wa Wizara ya Maji Engineer Nadhifa Kemikimba - STK, mama wa sheria, taratibu na kanuni. Pia nitumie nafasi hii kumshukuru Naibu Katibu Mkuu wetu wa Wizara yetu ya Maji Engineer Cyprian Luhemeja, kwa muda mfupi na Menejimenti ya Wizara ya Maji na watendaji wote wa Wizara ya Maji Mwenyezi Mungu ndiye atakayewalipa; tutafanya kazi. Hii ni Wizara ya Maji si wizara ya ukame, tutafanya kila linalowezekana kuhakikisha Watanzania waishio mijini na vijijini wanapata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, ukimuona kobe juu ya mti amepandishwa, mara kwa mara nasema. Niishukuru Kamati yako kwa maoni, ushauri, maelekezo na maagizo mbalimbali. Leo tunaona faida yake jamii ipo tu, ukiishirikisha utafanikiwa, usipoishirikisha utakwama. Sisi kama Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo kwa kamati yetu, sisi Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote katika kuhakikisha tunatekeleza miradi yetu ya maji na iwe na matokeo chanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja yangu leo imechangiwa na jumla ya Waheshimiwa Wabunge 75, lakini Wabunge watatu akiwemo Mheshimiwa Mtaturu wamechangia kwa maandishi. Kwa muda mfupi ambao nimepewa haitakuwa rahisi kujibu kwa kina hoja zote zilizotolewa. Ningependa kuahidi mbele ya Bunge hili tukufu, kwamba hoja zote za Waheshimiwa Wabunge tutazijibu kwa maandishi na kuziwasilisha kuingizwa kwenye kumbukumbu za Bunge. Hivyo ninaomba nitumie muda huu mfupi niliopewa kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizotolewa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja, hoja ya Kamati za Kudumu za Maji na Mazingira, kukamulisha malipo ya wakandarasi, National Plan, National Water Grid, Non-Revenue water, mapitio ya Sera ya Taifa, Mradi wa Maji wa Tunduma, Mradi wa kukabiliana na mabaliko ya tabianchi Simiyu, vipi kuhusu utekelezaji wa mradi wa maji wa Ziwa Tanganyika, kwa maana ya Kigoma, Rukwa na Katavi, bili za maji na maunganisho ya gharama za maji.

Mheshimiwa Spika, labda nianze juu ya maji katika Jiji letu hili la Dodoma. Kabla Serikali haijahamia Dodoma mahitaji ya maji katika Jiji la Dodoma ilikuwa lita milioni 44, lakini kupitia mamlaka yetu ya maji DUWASA ilikuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 66. Tulikuwa na maji mengi kuliko mahitaji.

Mheshimiwa Spika, lakini baada ya Serikali kuhamia hapa Dodoma ongezeko kubwa la watu na mahitaji yameendana sambamba. Leo ukienda Dar es salaam maeneo mbalimbali unaona namna ujenzi unavyofanyika. Leo ukenda maeneo ya Singida maeneo ya Nara ujenzi unafanyika. Kwa hiyo baada ya kuongezeka kwa idadi ya watu tumefanya tathmini na tumeona mahitaji katika Jiji la Dodoma ni lita milioni 133 lakini uwezo wa mamlaka yetu kuzalisha ni lita milioni 68. Hapa kuna haja ya kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha Jiji hili la Dodoma linapata maji.

Mheshimiwa Spika, tuna mipango ya muda mfupi lakini tuna mipango ya muda mrefu. Mipango ya muda mfupi tumetumia wataalamu wetu wa rasilimali za maji. Tunatambua maji yaliyo chini ya ardhi ni mita za ujazo bilioni 21, tumewaambia wafanye kila linalowezeka watuoneshe wapi kuna mengi katika Jiji hili la Dodoma, kwa sababu chanzo cha maji tunachokitegemea peke yake ni cha Mzava.

Mheshimiwa Spika, niwapongeze sana wataalam wetu wa rasilimali za maji wamepata maji mengi Nzuguni na tumechimba visima vitano vyenye uwezo wa kuzalisha lita zaidi ya lita milioni saba, tunaziingiza kwenye mfumo ambapo zitaweza kuongeza maji kwa asilimia 11. Maji haya ambayo mradi wake tunauanzisha pale Nzuguni utaweza kuwanufaisha wananchi zaidi ya 75,000. Nini maana yake? Maeneo korofi ambayo yalikuwa na kero kubwa sana ya maji, Nzuguni yenyewe na maeneo ya Ilazo, Kisasa na Swaswa yatapata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Kunti amezungumza Mheshimiwa Mavunde anazungumzia Jiji la Dodoma, nataka niwambie mradi huu tunakwenda kuukamilisha mwezi wa nane ili kuweza kupunguza adha katika Jiji hili la Dodoma.

Mheshimiwa Spika, zipo jitihada kubwa ambazo tunazozifanya. Tunajua leo mvua badala ya kuwa fursa wakati mwingine imekuwa ikileta maafa. Tumeona mvua inanyeesha inapotea baharini, tunaona mvua inanyesha nyingine inapotelea kwenye mito lakini wananchi hawana maji. Mwelekeo wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni juu ya uvunaji wa maji, kwamba maji badala ya kuwa maafa sasa yawe fursa. Tumejielekeza juu ya ujenzi wa mabwawa, na huo ndio mwelekeo wa Kamati yetu. Kwamba kuwa na ujenzi wa mabwawa madogo makubwa na ya kimkakati ili kuhakikisha kwamba meneo haya kame ambayo hata ukichimba kisima hupati maji tunakwenda kuchimba mabwawa. Nataka niwahakikishie, Mheshimiwa Mbunge wa Kiteto, Mbunge wa Meatu na Mbunge wa Ngorongoro, kwamba tunakwenda kuchimba mabwawa. Mheshimiwa Rais ameshatupatia mitambo kwa ajili ya kuchimbia mabwawa.

Mheshimiwa Spika, yapo mabwawa ambayo yalikuwa yakisomeka tu kwenye documents, Bwawa la Kidunda na Bwawa la Farkwa; lakini dhamira njema na uthubutu wa Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan leo tunakwenda kuyatekeleza mabwawa haya, haijawahi kutokea Waheshimiwa Wabunge. Mlikuwa mkizungumza kwenye Bunge hili mnashauri kila mara mbona utekelezaji hautokei?

Mheshimiwa Spika, leo miradi mingi ambayo tulikuwa tukiitekeleza midogomidogo leo pale Dar es salaam tume- experience water crisis; baada ya pale tulijenga mradi wa bilioni zaidi ya 23 kwa fedha za ndani, ametoa Rais na mradi tumekamilisha. Amesema adha ile hataki aione tena. Mradi wa zaidi ya bilioni mia tatu naa ambao tulikuwa tukisubiri wafadhiri Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anasema tunaenda kuutekeleza kwa fedha za ndani. Amekwishatoa bilioni 49 na mkadaarasi yupo site, Mungu atupe nini ndugu zangu?

Mheshimiwa Spika, Bwawa la Farkwa ambalo tulikuwa tukilizungumza kila kukicha; leo nataka niwaambie tumezungumza na wenzangu hapa katika commitment ambazo tunazozifanya, kwamba kabla ya tarehe 30 mhandisi mshauri apatikatene kazi ya kuanza hilo bwawa ianze na mkandarasi apatikane ili mradi huu wa Bwawa la Farkwa uweze kutekelezwa kwa sababu fedha tumekwishapata na Mheshimiwa Rais ametupa, hatuna kisingizio.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, dhamira njema Rais wetu ya kumtua mwana mama ndoo kichwani hapa Dodoma inatamia.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wamezungumza, Kaka yangu Moni amezungumza, na Mheshimiwa Kunti, kwamba mradi huu wa Bwawa la Farkwa maji yanaelekezwa Dodoma vipi kuhusu Chemba? Nataka niwaambie, ukikaa na waridi lazima unukie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lengo la bwawa hili, pamoja na kuyapeleka maji Dodoma lakini wanufaika wa kwanza watakuwa Wana-Chemba. Mpango wetu ni kuhakikisha hadi Bahi tunayapeleka maji ili wananchi wa Bahi wapate maji. Pamoja na hilo Mheshimiwa Rais anatuelekeza kwamba tuna rasilimali toshelevu hivyo lazima tutumie Ziwa Victoria kuhakikisha kwamba tunaleta maji hapa ambapo pia atawasaidia wananchi wa Singida. Itoshe kusema kwamba Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ni suluhu ya matatizo ya Watanzania. Tumpigie makofi mengi sana Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, limezungumzwa hapa suala la pamoja na haya mageuzi ambayo tunayafanya, na mimi kuna baadhi ya mambo lazima nikubali. Yapo maeneo ambayo tunafanya vizuri lakini pia yapo maeneo ambayo hatufanyi vizuri. Msema kweli ni mpenzi wa Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Spika, tunasema kwamba vijijini tuna asilimia 77 lakini ukweli kuna baadhi ya maeneo ukienda, hata mimi Waziri wa Maji wakati mwingine napata unyonge. Ukienda Kilindi hali siyo nzuri, ukienda Ushetu kwa kaka yangu Chereheni hali siyo nzuri, ukienda Meatu hali siyo nzuri. Lakini nataka niwaambie, kwa muda mfupi ambao tumefanya, mpaka sasa tuna vijiji Tanzania takribani 12,318. Pamoja na jitihada zilifanywa na fedha zilizotolewa tumeweza kufikia vijiji zaidi ya 9,000 kwa muda mfupi. Sasa hivi tuna deni la vijiji zaidi ya 3,000.

Mheshimiwa Spika, nini maana yetu? Tunatambua tuna rasilimali za maji juu ardhi mita za ujazo bilioni 105 na pia tuna maji chini ya ardhi mita za ujazo bilioni 21. Nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge, sehemu ambapo tukichimba kisima tutapata maji tunakwenda kuchimba kisima kwa sababu magari tunayo. sehemu ambapo tunaona kabisa ukichimba kisima haupati maji tunakwenda kuchimba mabwawa kwa sababu vifaa tumekwishapewa. Nataka niwatie moyo Waheshimiwa Wabunge, ukiona giza nene ujue kumekucha, baada ya dhiki siyo dhiki bali baada ya dhiki ni faraja na faraja yetu ni Mheshimiwa Rais Samia Suluhu hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii kazi tunaiweza, tunaiweza sana na tutafanya kila linalowezekana kuhakikisha adhma ya Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ya kumtua mwana mama ndoo kichwani inatimia. Kwa hiyo Mheshimiwa wa Ushetu umezungumza hili suala, tumetuma wataalamu wanafanya tathmini. Acha wamalize kazi, tutahakikisha hatuwezi kufikisha maji maeneo mengine ilhali Ushetu wasipate maji. Tutaweka historia katika Jimbo la Ushetu.

Mheshimiwa Spika, amezungumza dada yangu hapa, Mheshimiwa Rehema wa Bulyanhulu na mama yangu Mama Sitta kuhusu Urambo, Kaliua na Sikonge. Ni kweli maeneo haya yana changamoto, na ndiyo maana nasema yapo baadhi ya maeneo hatukufanya vizuri. Sisi Waheshimiwa Wabunge tulikuwa na mradi hapa unaitwa miji 28. Mradi huu ni wa muda mrefu, ulikuwa ukizungumzwa tu Bungeni. Mheshimiwa Rais alipoingia muda mfupi ameweza ku-unlock mradi ule na tumeweza kusaini na makandarasi.

Mheshimiwa Spika, tukawa na changamoto ya msamaha wa kodi; na hapa nitumie dhati ya moyo nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Naibu Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha pamoja na Naibu Makatibu Wakuu wote na kamishna wa bajeti; wametutendea haki sisi Wizara ya Maji. Nataka niwaambie Mheshimiwa Rehema, Mheshimiwa Kakunda na Mheshimiwa Mama Sitta unyonge basi. (Makaofi)

Mheshimiwa Spika, msamahawa kodi kwa wakandasi wale ambao ni kwa ajili ya miji 28 umetoka na advance payment imekwishatolewa, kwa hiyo, hawana kisingizio, kazi yao ni kwenda kutekeleza mradi kwa sababu mradi ule fedha zake zote zipo. Na ninataka niweke commitment, nipo tayari kufanya ziara rasmi ili tukafanye mikutano Kaliua, Sikonge na Urambo ili kwenda kuwakabidhi wakandarasi kwa sababu advance payment wamekwishapewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge, tumezungumzia fedha zilizotolewa, na hata angalieni bajeti yetu ilivyonono kitabu kizima. Fedha hizi zinahitaji usimamizi na ufuatiliaji. Ndiyo maana nilizungumza kwamba ukiona hapa tunasema mradi umefanya vizuri ni kwa sababu umesimamiwa vizuri. Hii kazi peke yangu Waheshimiwa Wabunge sitaiweza, lazima tukubali kushirikiana. Ndiyo maana nilizungumza, ukisoma Ezra inasema; “Inuka hii shughuli inakuhusu na ukaitende kwa moyo mkuu.” Sisi wasaidizi wa Mheshimiwa Rais tupo pamoja na ninyi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miradi yetu hii tukienda kuisimamia vizuri matokeo yataonekana, na matokeo yakionekana nini maana yake, ukisoma Isaya 12:3 inasema; “Kwa shangwe mtachota maji katika visima vya wokovu.” Kwa hiyo niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge twende tukasimamie hili jambo ili liende vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, imezungumzwa kwamba tuna rasilimali toshelevu, kwa mfano maeneo ya Kigoma, Katavi na Rukwa. Mimi mwenyewe nimefika, nilipangiwa ziara na watendaji wangu, nilighairisha, nikasema hebu tusikie mawazo ya Waheshimiwa Wabunge. Kwa kweli nimeamini, wakati mwingine tutoe nafasi kwa Waheshimiwa Wabunge, ninyi ni consultancy wa ukweli, mnatoa mawazo kwa maslahi ya Watanzania na kwa ajili ya kumsaidia Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, nitawapa mfano mmoja; study za Wizara ya Maji zilikuwa zinasema maji Liwale hakuna, zinasema hivyo; mimi nikasema haiwezekani, tukaja kwa Mheshimiwa Mbunge. Kweli, study zinasema, lakini hebu ngoja twende. Tukaenda tena, leo tumechimba visima maji ni bwerere. Nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Liwale, tutaweka historia ambayo ilikuwa imekata tamaa kwa muda mrefu. Hii ni kazi kubwa na nzuri ya Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wa Kigoma Katavi na Rukwa wamezungumzia suala la Ziwa Tanganyika, na mimi mwenyewe nimekwenda kujiridhisha na Katibu Mkuu amekwenda kujiridhisha. Nimefika mpaka kwenye chanzo pale Kalema. Nikiri na kusema kwa dhati kabisa dada yangu Aida umezungumza na Waheshimiwa Wabunge wote mmezungumza, kwamba Ziwa Tanganyika ndilo suluhu ya changamoto ya maji katika mikoa ile. Niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge twendeni tukaweke historia ya pamoja. Leo hapa ninavyozungumza naisikia sauti ya Rais wangu juu ya moja ya maelekezo ambayo ametupatia akiwemo na kiongozi wetu katika Bunge, Mheshimiwa Waziri Mkuu, ni kwamba, mawaziri chukueni hatua; tunakwenda kuchukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatua tunayokwenda kuchukua ni kumwajiri mhandisi mshauri ili aweze kwenda kufanya usanifu juu ya ujenzi wa mradi huu. Suala la fedha tutakaa na Mheshimiwa Rais, kama maeneo mengine tulivyotekeleza Mheshimiwa Rais wetu atakwenda kutekeleza mradi huu na wananchi hawa waweze kupata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, imezungumzwa hapa, pamoja na mageuzi haya tunayoyafanya lakini sasa hivi tunakwenda kwenye mabadiliko ya tabia ya nchi, vipi kuhusu Sera ya Maji? Sera ya maji imeanzishwa 2002 leo 2023.

Mheshimiwa Spika, ni kweli Sera yetu imepitwa na wakati, na ndiyo maana hata katika vipaumbele ya Wizara tumesema lazima twende tukafanye mapitio ya Sera yetu. Kamati pia imelizungumzia hilo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kihenzile amezungumza, nadhani hili wala halihitaji mjadala. Maelekezo ya Mheshimiwa Spika wa Bunge pamoja na Bunge lako ni kuhakikisha kwamba twende tukaipitie hii Sera ili ije kuendana na mazingira ya sasa na kasi ambayo anaifanya Mheshimiwa Rais wetu ili kuhakikisha kwamba tunafanya mageuzi na kuleta matumaini makubwa kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni kuhusu suala la gridi ya maji ya taifa. Mwenyezi Mungu ameijalia nchi yetu. Ukienda Kanda ya Ziwa kuna Ziwa Victoria, ukienda mkoa wa Ruvuma kuna mto Ruvuma, ukienda Kigoma, Rukwa na Katavi kuna Ziwa Tanganyika. Pia ukienda Mbeya kuna Mto Kiwila, ukienda kila eneo; leo ukienda zako Mtwara, ukienda kusini kuna Mto Rufiji.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ametupa maelekezo, kwamba twende tukahakikishe; hii i ndiyo ajenda yake, na Waheshimiwa Wabunge hii kazi tumeshaianza. Leo hii ukienda zako Ziwa Victoria tunayachukua maji ya Ziwa Victoria tunakwenda kupeleka maji katika Jimbo la Rorya, tunayapeleka Tarime Mjini hadi Tarime Vijijini.

Mheshimiwa Spika, ukienda pale Musoma upo mradi wa bilioni 134, mradi mkubwa, tumejenga hadi tenki kubwa la Bahima. Ukienda Mgango Kiabakali na Butiama tuna mradi wa zaidi ya bilioni 70 kwa ajili ya kutumia Ziwa Victoria. Ukienda Mwanza, leo tumeona mahitaji katika Jiji la Mwanza ni lita milioni 154, mamlaka yetu ya maji ina uwezo wa kuzalisha lita milioni 90.

Mheshimiwa Spika, tuna mradi wa bilioni 69 wa Butimba sikulisaidia tu Jiji la Mwanza, maji yale yanakwenda mpaka Magu na yanakwenda mpaka Jimbo la Misungwi.

Mheshimiwa Spika, achana na hilo, leo hii tunazungumza mradi ambao tulikwishautekeleza ya kuyatoa maji kuyaleta Shinyanga, tumeyapeleka Tabora, tumeyapeleka Igunga, tumeyapeleka Nzega. Mheshimiwa Rais anatueleza kwamba sasa hivi tanayapeleka Igalula, lakini tunayapeleka Kaliua, tunayapeleka Sikonge na tunayapeleka mpaka Urambo kwa Mama Sitta, tumpigie makofi mengi sana Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, achana na hilo, leo imekuja hoja hapa ya Ziwa Tanganyika, hii ndio Gridi ya Taifa ambayo tunatakiwa kwenda kuifanya, tunakwenda kuweka historia hii. Nilizungumza hata Baba wa Taifa alivyokuwa anakwenda kupigana vita vya Idd Amini, alisema maneno machache tu kwamba, uwezo tunao, nia tunayo na sababu pia tunayo. Sababu ya kwenda kujenga mradi huu wa Ziwa Tanganyika kwa maeneo haya tunayo na Mheshimiwa Rais kazi hii alishaianza. Ukienda Kigoma Jimbo ambalo lina kata 19, amejenga mradi wa bilioni 42, zaidi ya kata 19 zimepata maji. Mradi ule tumeshaufanyia extension, tumepeleka mpaka Mwandiga, nini sasa kilichobaki? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi ule uongezewe kufanyiwa extension na huyu Mhandisi Mshauri aliyepatikana maeneo ya Rukwa na Katavi waende kupata huduma ya maji safi na salama. Leo tunakwenda kutumia Mradi wa Maji wa Mto Ruvuma, target yetu katika miji hii 28 tunaendea kuanza. Mkandarasi yuko site, tunayatoa maji ya Mto Ruvuma tunayapeleka katika Jimbo la Nanyumbu ambalo lilikuwa na shida kubwa sana ya maji, lakini maji yanayofika Nanyumbu tutayashusha mpaka Masasi ili kuhakikisha Jimbo la Masasi wanapata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, ukienda kwa Mheshimiwa Mkuchika, tuna mradi mkubwa wa Makonde. Mradi una umri mkubwa umekuwa chakavu kuliko mimi Waziri wa Maji, leo Rais ameshatupatia bilioni 84. Tunayatoa maji pale kwa Mheshimiwa Mkuchika Newala tunayapeleka Tandahimba kwa Mheshimiwa Katani, yanafika mpaka kwa Mheshimiwa Chikota. Huo ndio uelekeo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi ambao ulikuwa umekwama wa Same - Mwanga, ambao mradi wenye uwezo mkubwa wa uzalishaji mkubwa si kuwasaidia Wanamwanga na Same, mradi ule unafika hadi Tanga. Achana na hilo, tuna mradi wa zaidi ya bilioni 170, ambapo tunakwenda kuyachukua maji ya Mto Pangani. Mkandarasi yupo site maji yale yanaenda Korogwe, Muhenza mpaka Kilindi huko, lakini mpaka katika Jimbo la Pangani. Kwa hiyo, huo ndio uelekeo.

Mheshimiwa Spika, hata ukienda zako Mbeya, ulizungumza katika Bunge lililopita, pale tuna Mto Kiwira tukichukua Mto Kiwira, nitapeleka katika Jiji la Mbeya lakini katika maeneo mengine. Umeona kazi tuliyoifanya, safari moja huanzisha nyingine, safari tumeianza acha tuiendeleze.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wasisahau miradi hii mikubwa inahitaji fedha nyingi, lakini Rais wetu ameonyesha uthubutu. Nilivyokuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kulikuwa somo likuwa linaitwa haya mambo ya civics, civics, development studies. Tuliambiwa development is the progressive change from low level to higher level. Maendeleo ni mchakato na Rais wetu amekwishayaanza na maendeleo yanaonekana na namna Wabunge wanavyompongeza. Kikubwa tumpe ushirikiano, yale mambo ambayo tulikuwa tunaamini hayawezi kufanyika, leo yanafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Maendeleo katika Sekta ya Maji na Tanzania yanaanza na mimi. Maendeleo ya Taifa letu yanaanza na wewe, maendeleo ya Taifa letu yanaanza na sisi sote kwa kushikamana.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine lilizungumzwa na Mheshimiwa Shonza, Mheshimiwa Hasunga na Mheshimiwa Stella juu ya utekelezaji wa mradi katika Jimbo la Tunduma la kuyaleta maji Vwawa, Mloo. Tumeshakubaliana kabla ya Mwezi wa Saba mkandarasi atakuwa amepatikana, tunakwenda kuanza utekelezaji wa mradi wa maji katika kuhakikisha tunapeleka maji katika Eneo la Tunduma.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo tumelizungumza, hatuwezi tukawa na Wizara ambayo haina National Water Master Plan, haya ni maoni ya Kamati, haya ni maoni ya Waheshimiwa Wabunge, lakini pia sisi katika vipaumbele vyetu vya Wizara tumeliona hili. Tunalipokea acha twende tukalifanyie kazi juu ya utekelezaji wake.

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Simiyu, huu ni mradi mmoja wa miradi ambayo utekelezaji wake ulikua mgumu. Tulikuwa na miradi mitatu, Mradi wa Same - Mwanga, Mradi wa Miji 28 pamoja na Mradi huu wa Simiyu. Tuliwaita wafadhili KfW, tulikaa nao ofisini. Huu ni mradi wa muda mrefu sana na Serikali pale imeahidi, tutapoteza imani ya Serikali yetu, tunaomba twende juu ya utekelezaji. Waheshimiwa Wabunge wali mtamu sana kwa maini, lakini ukikaa sana unakuwa kiporo na kiporo kikaa sana kina chacha na mwisho wake kinaumiza tumbo. Wafadhili wale wametuelewa… (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri dakika mbili, malizia.

WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, wafadhili wale wametuelewa na nataka niwaambie Wabunge wa Mkoa wa Simiyu, naomba wa-note tarehe hii hapa, kwamba tarehe hii 30 Mei tunakwenda kusaini mradi ule ili kuhakikisha Wanasimiyu kwa maana ya Bariadi, Itilima wanaenda kupata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee niendelee kukushukuru na niendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais pamoja na Bunge lako tukufu pamoja na Kamati yote na Watendaji wote wa Wizara ya Maji, Wenyeviti wa Kamati bila kusahau familia yangu. Ninachotaka kusema sisi tutafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii lakini la pili nimshukuru sana Rais wangu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuniamini. Kwa kuniamini mimi maana yake ametuamini sisi vijana tuweze kumsaidia. Nataka nimuhakikishie Rais wangu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuniamini kwamba kama kijana naweza kumsaidia katika Wizara hii Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Rais wangu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuniamini kama kijana niweze kumsaidia katika Wizara hii ya Maji. Nataka nimuakinishe Rais wangu Dkt. John Pombe Magufuli kama kijana na kwa niaba ya vijana wengine wote na Waheshimiwa Wabunge sitokuwa kikwazo katika kuhakikisha Watanzania wanapata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia kumshukuru sana Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa ushirikiano wanaoutupa Wizara yetu ya Maji. Kwa namna ya kipekee nimshukuru mzee wangu Isack Kamwelwe kwa ushirikiano anaotupa sisi vijana katika wizara ile, nataka nimwambie waziri wangu ni Waziri jembe, na mimi kama kijana nitahakikisha namsaidia Waziri wangu katika kuhakikisha mipango mizuri inatekelezeka ili Watanzania wapate maji safi na salama na yenye kuwatosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Katibu wangu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara ya Maji. Tumejipanga na tuna nia ya dhati katika kuhakikisha tunaenda kumtua mwana mama ndoo kichwani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sikumshukuru mama yangu mzazi, leo nipo naye kwa mafundisho aliyonifundisha mimi pamoja na mzee wangu kufariki na shughuli zake ndogo ndogo za biashara ya mama ntilie, lakini kwa kuamua kunisomesha leo nimesimama hapa kama Naibu Waziri wa Maji na Mkemia. Mama yangu ahsante sana na Mwenyezi Mungu anasema unapaswa kushukuru kwa kila jambo, ahsanteni sana mwenyezi mungu awabariki sana. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda mchache niliokuwa nao naomba sasa nifafanue baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge kwa michango mizuri waliowasilisha katika Wizara yetu, ni michango yenye afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia maji ni rasilimali muhimu na maji hayana itikadi, hayana rangi, hayana dini na wala maji hayana mbadala, si kama wali ukikosa wali utakula ugali au utakula makande. Ukikosa maji tunaingia kwenye matatizo makubwa, hasa katika maradhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii sasa kujielekeza kujibu maswali na hoja za Waheshimiwa Wabunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ilielekezwa katika Wizara yetu ni kuhusu miradi 17 ya Serikali ya India. Nilivyoingia katika Bunge hili zilikuwa zinakuja hoja za miradi 17 mwili ulinisisimka, mwili ulinitetemeka, kwamba naenda kujibu nini; lakini Mheshimiwa Mpango leo nisimame kwa ujasiri umetuvisha nguo sisi Wizara ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi kumshukuru Rais wangu Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada kubwa sana alizozifanya. Sisi kama Wizara ya Maji tunachokisema fedha zile zitakazotoka kwa miradi 17 ya India tutazifatilia shilingi kwa shilingi kuhalikisha kwamba Watanzania wanapata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili hatutamuonea haya mtu kwa sababu wakati mwingine fedha za Serikali zinaliwa kwa sababu ya kuoneana haya au kupeana kazi kiujomba ujomba au kiushemeji shemeji. Kwenye hili hatutakuwa na haya na mkandarasi ambaye atapewa, hata awe mtoto wa kigogo. Kama yeye atakuwa mtoto wa kigogo anatekeleza mradi lakini hana uwezo tunamcharanga ili aweze kuwa kuni akawaahida, wananchi waweze kupata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine imezungumzwa na Mama yangu Anna Lupembe kuhusu mradi wa Ikolongo One pamoja na Ikolongo Two kwamba maji hayatoshelezi kwa kuwa miundombinu ni mibovu, hivyo maji hayawafikii wananchi kwa makanyagio na majengo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inafanya jitihada kubwa kuhakikisha Mji wa Mpanda unapata huduma ya uhakika ya maji kwa kutekeleza miradi mbalimbali. Kwanza kuna mradi wa Kanonge uliopangwa kujengwa kwa awamu mbili; awamu ya kwanza imekalimika na utekelezaji awamu ya pili unaendelea. Mradi huu ukikamilika utazalisha maji lita za ujazo 1,200,000 kwa siku. Aidha, ujenzi wa maji kutoka Ikolongo Two utaanza mwezi Julai, 2018. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumepokea hoja kutoka kwa dada yangu Esther Bulaya kuhusu DAWASCO kwamba ilishauliwa kununua kifaa cha kupunguza upotevu wa maji agizo hili halijatekelezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumjibu dada yangu Esther Bulaya kuwa vifaa vya kutambua uvujaji chini ya ardhi yaani liquid detector vipo. Vifaa hivyo vilinunuliwa wakati wa mradi wa kupunguza upotevu wa maji Jijini Dar es Salam.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine napenda kujibu hoja ya Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota kuhusu mradi wa Maji Makonde kwamba umechakaa na hivyo kuhitaji ukarabati mkubwa. Nataka nimwambie Mheshimiwa ndugu yangu Chikota ukiona giza linatanda ujue kunakucha. Pamoja na changamoto ambazo wamezipata wananchi wake lakini Mheshimiwa Mpango sasa ameshatupangia mambo yetu yapo vizuri, tunaenda kutekeleza mradi ule ili wananchi waweze kupata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine inahusu Mheshimiwa Mbunge Maftaha Abdallah Nachuma, amezungumzia mradi wa maji kutoka Mto Ruvuma hadi Mtwara Mjini unaopita vijiji 26 vya Mtwara Vijijini kwamba haujatekelezwa kwa miaka mitatu sasa na wananchi wameshachukuliwa maeneo yao lakini fidia haijalipwa. Nataka nimjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iliandaa mradi wa maji kutoka Mto Ruvuma hadi Mtwara Mjini na kupitia vijiji 26 vilivyopo Mtwara Vijijini. Tayari usanifu wa mradi umekamilika na taratibu za kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi zinaendelea ikiwemo kufanya majadiliano na Exim Bank ya China. Tathmini ya maeneo ya mradi yalishafanyika kwa ajili ya kulipa fidia, lakini wananchi bado hawajaondolewa katika maeneo yao. Kabla ya utekelezaji wa mradi huo kwanza waanchi watalipwa fidia zao. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge sisi kama Wizara hatutakuwa kikwazo katika
kuhakikisha wananchi wako wanalipwa fidia na mradi ule uweze kutekelezeka kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ni ya dada yangu Lucy Owenya, kuhusu ujenzi wa mradi wa maji katika Jimbo la Moshi Vijijini Kata ya Mbokomu kwamba umejengwa chini ya kiwango na kusababisha mradi huu usifanye kazi. Mradi huu ulikuwa chini ya Halmashauri ya Moshi Vijijini ambao uko chini ya TAMISEMI. Baada ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kupata malalamiko haya, imemuagiza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Moshi Mjini kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Moshi Vijijini kwenda kuangalia tatizo na kuandaa gharama za ukarabati wa chanzo hicho ambacho kitawezesha wananchi wa Kata ya Mbokomu kupata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine imetolewa na kaka yangu Mheshimiwa Ahmed Shabiby kuhusu mradi wa maji kwa mji wa Gairo kwamba ni muda mrefu ambapo mkandarasi amelipwa asilimia 80 lakini mradi huo hautoi maji. Ni kwei mradi wa maji Gairo umechukua muda mrefu kukamilika. Mradi ulianza kutekelezwa tangu tarehe 22 Agosti, 2010 na umetekelezwa kwa asilimia 87 ambapo hadi sasa mkandarasi amelipwa kiasi cha shilingi bilioni 3.844; dola za Kimarekani 1, 071,525 ambazo kwa ujumla ni sawa na asilimia
64 ya gharama za mradi mzima ambazo ni shilingi 5,315,612,551 na dola za Kimarekani 1,919,763.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi haujaanza kutoa maji kwa kuwa unahitaji kufungw amtambo wa kuchuja chumvi yaani reverse osmosis plant kwa kuwa visima vilivyochimbwa maji yake yalionekana kuwa na chumvi zaidi ya viwango vilivyokubalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuonekana mkandarasi ameshindwa kuagiza na kufunga mtambo huo kwa wakati, Serikali iliamua kumnyang’anya kipengele cha uagizaji na ufungaji wa mtambo wa kuchuja chumvi pamoja na pump. Tangazo la kumpata mzabuni kwa ajili ya kazi hizo lilitangazwa tarehe 3 Mei, 2018 ambapo ufunguzi wa zabuni unatarajiwa kufanyika tarehe 5 Juni, 2018. Mradi huu unategemewa kukamilika na kuanza kufanya kazi mwishoni mwa mwezi Novemba, 2018.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kujibu hoja ya Mheshimiwa Zainab Mndolwa Amir kuhusu kwamba Serikali itoe elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji mfano katika Milima uya Uluguru Morogoro. Ushauri wake umezingatiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia napenda kujibu hoja ya Mheshimiwa Mbunge wa Songea kuhusu suala la wananchi wake kuweza kulipwa fidia. Nataka nimhakikishie Mzee wangu Ndumbaro akae sasa mkao wa kula. Katika bajeti hii ya mwaka 2018/2019 tutawalipa wananchi wale fidia kiasi cha shilingi bilioni sita. Kwa hiyo, jukumu sasa la Mheshimiwa Mbunge kuwasimamia wananchi wale badala ya fedha zile kwenda kuoa, sasa wazitumie katika mipango ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu hoja ya Mheshimiwa Elibariki Emmanuel Kingu kwamba Bwawa la Kidunda lijengwe. Wizara ipo katika hatua za mwisho za mazungumzo na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili kupata fedha za utekelezaji wa mradi huu muhimu. Matarajio ni kufikia makubaliano haya ya mwezi Juni, 2018 ili zabuni za kumtafuta mkandarasi wa ujenzi ziweze kutangazwa mwezi Julai, 2018.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu hoja ya Mbunge wa Kasulu Mheshimiwa Daniel Nsanzugwanko kuhusu dola za Kimarekani milioni 500, kuna phase one, logic yake ni nini, kwa nini isiwe sambamba kwamba miradi yote ifanyike kwa wakati mmoja. Napenda kujibu hoja hii kwamba mradi wa miji 17 wa dola za Kimarekani kwa maana ya milioni 15 utatekelezwa kwa awamu mbili yaani phase one na phase two. Awamu ya kwanza itahusisha usanifu wa miradi katika miji yote 17 na awamu ya pili itahusisha ujenzi wa miradi husika hivyo mradi yote inategemewa kukamilika bada ya miaka minne.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu hoja ya Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Mrisho Kikwete kuhusu usimamizi wa mradi wa Chalinze uangaliwe kwa makini. Serikali imekuwa ikisimamia mradi wa Chalinze kwa makini kwa kuweka wahandisi maalum kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa kila siku. Hatua mbalimbali za kimkataba zimekuwa zikichukuliwa kwa mkandarasi kila aliposhindwa kutekeleza matakwa ya mkataba ikiwa ni pamoja na kutoa onyo na kumkata fedha. Hata hivyo, ilipofika tarehe 22 Februari, 2018 Serikali ililazimika kumsimamisha kazi mkandarasi kwa mujibu wa mkataba baada ya kusindwa kutekeleza makubaliano yaliyopo ndani ya mradi. Hivi sasa Serikali inashauriana na mfadhili wa Benki ya Exim ya India jinsi ya kumaliza kazi zilizobaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu hoja ya Mheshimiwa Mary Pius Chatanda wa Korogwe, kwanza anatoa shukrani kwa kupelekewa na Wizara kiasi cha shilingi milioni 500. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba shukrani zake tumezipokea na sisi kama Wizara tutaendelea kumpa ushirikiano ili wananchi wake wa Korogwe waweze kupata maji safi na itakapofika mwaka 2020 waende kumchagua kwa mara nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu hoja ya Mheshimiwa Hamidu Hassan Bobali, Mbunge wa Mchinga kuhusu kuchanganya kwa takwimu za maji. Mfano Dar es Salaam takwimu zinaonesha wakazi wengi wanapata maji lakini maji hayajafika.

Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu zilizotolewa ni za ujumla, wananchi wanapata maji ya uhakika ni wale walioko katika maeneo yanayopata maji kutoka Ruvu Juu na Ruvu Chini. Ni kweli kuna maeneo ambayo hayapati maji ya bomba kwa sababu yako mbali na mfumo wa Ruvu Juu na Ruvu Chini au mtandao wa bomba haupo. Maeneo haya ni pamoja na Mbagala, Kongowe, Kigamboni, Chamazi, Chanika, Msongola, Kitunda, Yombo Vituka, Pugu, Gongolamboto na Kinyerezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya 2018/2019 Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuongeza mtandao wa mabomba ili kufikisha maji kwa wananchi wengi zaidi. Pamoja na changamoto katika Wizara yetu ya Maji, Mwenyezi Mungu anasema; “Waama bii neemati rabikka fahadith” (zielezeeni neema za Mwenyezi Mungu kwa kushukuru). Nataka nimwambie kaka yangu Mnyika, moja ya hoja yake alikuwa akilalamika kuhusu eneo lake la Kibamba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwambie Mheshimiwa Mnyika, kazi kubwa sana imefanywa na Wizara hii ya Maji. Kulikuwa na kilio kikubwa sana Dar es Salaam lakini kumekuwa na utekelezaji wa kupanua Ruvu Juu na Ruvu Chini katika kuhakikisha wanaongeza lita kutoka lita 300 mpaka lita 504, Mwenyezi Mungu atupe nini? Atupe donda tufukuze nzi? Zipo changamoto lakini tunachotaka tunaomba ushirikiano ili zile kata zake sita sasa ambazo hazina maji twende kuwapatia maji na hii ni kazi nzuri yote inayofanywa na Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukizaa mtoto anafanya vizuri, jukumu lako ni kumuombea dua. Rais wetu anafanya vizuri Waheshimiwa Wabunge, jukumu letu ni kuhakikisha tunampa ushirikiano wa dhati na sisi wasaidizi wake tutafanya kila linalowezekana ili wananchi tuweze kuwapatia maji safi, salama na yenye kuwatosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu hoja ya Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, kaka yangu kuhusu upungufu wa wataalam katika sekta ya maji na hatua zinazochukuliwa na Wizara kukabiliana na upungufu huo. Ni kweli kuna upungufu wa wataalam katika sekta ya maji hapa nchini, hali ambayo imesababisha baadhi ya mamlaka za Serikali za Mitaa kushindwa kusimamia miradi yake. Wizara imechukua hatua zifuatazo:-

Moja katika mwaka 2017/2018 Wizara ilipata kibali cha kuajiri watumishi 154 wa sekta ya maji ambapo hadi mwezi Mei, 2018 wataalam 106 walipangiwa vituo vya kazi.

Kati ya wataalam hao 37 walipangiwa ofisi za mikoa na Halmashauri za Wilaya na 76 walipangiwa katika Bodi za Maji za Mabonde, Miradi ya Kitaifa na Mamlaka za Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa iliyopo kwenye eneo hili ni kwamba sekta inaendelea kukua, lakini pia kuna upungufu wa wataalam unaotokana na vifo, kustaafu, kuacha kazi na kufukuzwa kazi kutokana na sababu mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu hoja ya kaka yangu Mheshimiwa Dunstan Kitandula kuhusu Makao ya Wilaya ya Mkinga kwamba hakuna maji. Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa wananchi wote wanapata huduma bora ya majisafi na salama ikiwa ni pamoja na wananchi waishio katika Makao Makuu ya Wilaya…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Aweso, muda wako umekwisha. Dakika mbili malizia.

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie tena kuwaomba Waheshimiwa Wabunge, sisi kama Wizara ya Maji na nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wangu wa Maji nilivyoteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maji aliniambia nipite maeneo mbalimbali kuangalia hali na utekelezaji wa miradi ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na ninyi, hali ilikuwa hairidhishi. Ipo miradi ambayo imekamilika lakini haitoi maji, hakuna sababu ya kulalamika. Mheshimiwa Waziri amechukua hatua sasa ya kuunda RUWA ili twende kuisimamia ili wananchi waweze kupata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, sina maneno mengi sana. kikubwa tunachoomba Waheshimiwa Wabunge ni ushirikiano, na sisi kama viongozi wa Wizara, tutafanya kazi kwa moyo na michango yenu leo mliyoitoa imetupa ari na moyo katika kuhakikisha tunafanya kazi hizi ili wananchi wetu waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda nimshukuru sana Mwenyezi Mungu, lakini nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuwaletea maendeleo Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee nitumie nafasi hii kumpongeza Waziri wa Wizara hii pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya, wamekuwa wakizunguka maeneo mbalimbali ya nchi yetu katika kuhakikisha wanatatua changamoto mbalimbali zinazohusiana na wakulima. Pongezi za kipekee katika nia yao ya dhati kabisa kuondoa tozo zaidi ya 21 katika kuhakikisha zinawaondolea kero wananchi hawa wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kabisa nchi yetu asilimia kubwa ya Watanzania wanaishi vijijini na wanategemea kilimo na kilimo chenyewe ni cha kudra za Mwenyezi Mungu kwa maana ya mvua, lakini Wizara yetu imejipanga vizuri sana katika kuhakikisha na kujua namna ya kuweza kumtoa Mtanzania, lazima tuwekeze katika kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumebainisha eneo ambalo linafaa kwa kilimo cha umwagiliaji katika nchi yetu ni hekta milioni 29,000.4, lakini mpango wa Serikali mpaka itakapofika mwaka 2025 tuwe angalau tuna hekta milioni moja, na moja ya mipango ambayo tumeipanga tumeshafanya mapitio ya miradi yote kuona changamoto. Tumeona kuna miradi mingi ya umwagiliaji lakini haijakamilika, lakini bado uzalishaji wake unakuwa wa msimu mmoja. Tumeshajipanga, baadhi ya miradi ya umwagiliaji sasa hivi inafanya vizuri na imekuwa ikilima zaidi ya msimu mmoja, kama Mradi wa Lower Moshi, Madibila – Mbarali pamoja na Dakawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali kwa kutenga fedha zaidi ya shilingi bilioni 29 ambayo imewekeza katika suala zima la kilimo cha umwagiliaji. Nataka nilihakikishie Bunge lako Tukufu, sisi kama viongozi wa Wizara tutasimamia fedha hizi katika kuhakikisha tunajenga miundombinu ya maji ili hatimaye miradi hii ya umwagiliaji iweze kuwa na tija. Kwa sababu tunapozungumzia uchumi wa viwanda ni lazima tuwe na kilimo cha umwagiliaji kitakachoweza kutuzalishia mazao ya kutosha na yenye msimu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi kama Wizara tumejipanga vizuri, na tunaahidi kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kuhakikisha tunawekeza katika kilimo cha umwagiliaji ili mwishowe uchumi wa viwanda uweze kukamilika. Kubwa niwaombe san Waheshimiwa Wabunge tuipe ushirikiano wa dhati kabisa Wizara hii ya Kilimo kwa sababu watendaji wanafanya kazi nzuri sana, na sisi kama Wizara ya Maji tutawapa ushirikiano wa dhati katika kujenga na kuunda miundombinu hii ya umwagiliaji katika kuhakikisha azma ya Mheshimiwa Rais ya uchumi wa viwanda inatimilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine katika bajeti hii tumeona nia ya dhati kabisa ya Serikali kuhusu ujenzi wa Bwawa la Kidunda. Bwawa hili litatumika katika suala zima la maji, lakini pia tutakuwa na kilimo cha umwagiliaji. Hii ni nia njema kabisa ya Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli, katika uwekezaji wa kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza mtoa hoja, Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kazi nzuri anayoifanya. Pia nitumie nafasi hii kuwapongeza wasaidizi wake, Mheshimiwa Jenista pamoja na Mheshimiwa Angellah Kairuki pamoja na Naibu Mawaziri wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa sisi katika Wizara yetu, tuna mambo mawili, moja ubadhirifu wa fedha za miradi ya maji vijijini. Tukiri kabisa kulikuwa kuna changamoto kubwa sana hasa katika maeneo ya vijijini kuona fedha zinalipwa lakini mradi haujakamilika na hata ukikamilika unatoa maji leo, kesho hautoi. Sisi hiyo kama changamoto tumeiona na baada ya kubadili muundo kwa maana Wahandisi wa Maji wengi walikuwa hawawajibiki kwetu na kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini, tunawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kupitisha Muswada ule na Mheshimiwa Rais amekwisha usaini, tunaamini uanzishwaji wa Wakala wa Maji Vijijini tunaenda kuwa na muarobaini ambao utaenda kutatua tatizo la maji kabisa vijijini. Tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali kwa Wahandisi wa Maji pamoja na wakandarasi wababaishaji ambao wanatuchelewesha katika utekelezaji wa miradi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili ni kuhusu suala zima la ulipaji wa madeni ya wakandarasi. Utekelezaji wa miradi ya maji unategemeana na fedha. Tulikuwa na madeni takribani zaidi ya shilingi bilioni 88 tunayodaiwa na wakandarasi, lakini nitumie nafasi hii kuwashukuru sana Wizara ya Fedha kuliona hilo, wametupa takribani zaidi ya shilingi bilioni 44 ndani ya mwezi uliopita na wametupa commitment ndani ya mwezi huu watatupa tena shilingi bilioni 44. Kwa hiyo, tupo vizuri na tumejipanga katika kuhakikisha kwamba tunakamilisha miradi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Hussein, amezungumzia hoja ya mradi wake wa Nyang’wale, tumelipa zaidi ya Sh.1,705,000,000. Mwambie mkandarasi afanye kazi, hana uwezo, tutamuondoa katika kuhakikisha miradi ya maji inakamilika ili wananchi waweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto, yapo mafanikio makubwa sana. Sisi kama Wizara ya Maji ambayo siyo Wizara ya Ukame, ukienda Arusha zaidi ya mradi wa shilingi bilioni 520; mradi wa Same Mwanga zaidi ya Dola milioni 300; ukienda Longido zaidi ya bilioni 16 wananchi wanapata maji; tunatoa maji Zziwa Victoria na kuleta Tabora, Nzega na Igunga na hata Simiyu kwa Mheshimiwa Mbunge wa Bariadi kwako Mwenyekiti tunakupelekea maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumejipanga vizuri katika kuhakikisha kwamba hatutokuwa kikwazo sisi kama Wizara ya Maji kwa wananchi na Waheshimiwa Wabunge ili wananchi wetu waweze kupata maji safi salama na yenye kuwatosheleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza napenda nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na kuniwezesha kushiriki katika Bunge lako Tukufu. Kwa namna ya kipekee nimshukuru sana na nimpongeze Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu na Waziri Mkuu kwa ushirikiano mkubwa wanaotupa sisi Wizara ya Maji katika kuhakikisha tunatimiza majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee nimshukuru mke wangu mpenzi Kauthar Francis na mama yangu kwa malezi na matunzo wanayonipa, Waswahili wanasema, usione vyaelea ujue vimetunzwa. Kwa hiyo, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wifi yenu yupo vizuri na ndiyo maana nami nipo vizuri katika utendaji wangu wa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wangu Profesa Makame Mbarawa, huyu ni jembe wembe. Ukiachana na Uwaziri wake lakini amekuwa mlezi katika kuhakikisha maagizo na maelekezo anayotupa katika Wizara yetu ili yawe na tija na kuleta mabadiliko makubwa katika Sekta ya Maji. Mheshimiwa Waziri ahsante sana, Mungu akubariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee, sisi hatuwezi kufanya kazi peke yetu, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Katibu Mkuu Profesa Kitila Mkumbo, Naibu Katibu Mkuu Eng. Kalebelo, Wakurugenzi wote na watendaji wa Wizara ya Maji; tumekuwa tukifanya kazi kwa ushirikiano mkubwa sana. Pamoja na changamoto tunazopitia lakini bahari kubwa ndiyo inayovukwa, tutaivuka katika kuhakikisha tunawaletea maendeleo makubwa sana Watanzania katika sekta ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii sana kumpongeza Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa kazi nzuri, mapendekezo na ushauri wao lakini pia Waheshimiwa Wabunge wote na Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani kwa michango yao, tumeipokea na tutaifanyia kazi. Tumepata bahati ya kipekee kuona Wabunge kila aliyesimama ametoa mawazo, amezungumzia suala la maji na namna gani tunaweza kuboresha Wizara yetu katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji. Nataka niwahakikishie Wabunge sisi kama viongozi wa Wizara hatutokuwa kikwazo katika kuhakikisha Watanzania waishio mijini na vijijini wanapata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kujibu hoja; moja ya michango ya Waheshimiwa Wabunge ilikuwa ni suala zima la ubadhirifu wa fedha za miradi na usimamizi wa miradi ya maji. Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alivyoniteua nikiwa kama Naibu Waziri wa Maji tulipeana mikakati pamoja na watendaji wote, Katibu Mkuu na Waziri kwamba tupite maeneo yote ambayo tumepeleka fedha za miradi ya maji hususani maeneo ya vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa ushirikiano mkubwa ambao wametupa sisi viongozi wa Wizara ya Maji kubaini changamoto kwenye eneo la maji vijijini. Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakijua miradi ya maji kuliko hata Wahandisi wetu wa Maji, lakini wamekuwa wakitoa solutions za kutosha. Niseme tu itoshe kwamba Waheshimiwa Wabunge wametusaidia kuokoa miradi mingi ya maji katika eneo la vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifanya ziara Mbeya Vijijini kwa Mheshimiwa Oran Njeza, tulivyofika pale Mhandisi wa Maji alitupa taarifa ya miradi iliyotekelezwa katika miradi ya maji, lakini nami nikawa na taarifa yangu, baada ya kutupa taarifa nikamwambia nipeleke Mradi wa Galijembe ingawa hakutupa katika taarifa yake. Mhandisi yule wa Maji ananiambia Mheshimiwa Waziri kule eneo unapotaka twende kuna miinuko mikubwa utachoka, nikamwambia hapa sisi tumekuja kufanya kazi, tupeleke Mradi wa Galijembe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na mvutano mkubwa sana, tulivyofika katika eneo la Mradi ule wa Galijembe, mradi zaidi ya milioni 290 Mkandarasi amelipwa 260 hayupo site zaidi ya miaka mitatu. Unamuuliza Mhandisi wa Maji, mkandarasi yupo wapi, anasema Mheshimiwa huyu ni msumbufu huu mwaka wa tatu tukimwandika barua haji. Nikatoa agizo kwamba kesho lazima aje katika eneo la mradi. Kweli alivyokuja tukamuuliza mkandarasi nikiwa na Katibu Mkuu Profesa Kitila Mkumbo, unawezaje kulipwa fedha za miradi ya maji ilhali hujatekeleza? Mkandarasi ananiambia

Mheshimiwa Naibu Waziri tusipoteze muda, mimi nataka kikao chako kiwe kifupi, fedha tumelipwa lakini hizi fedha tulizopewa tumegawana na Mhandisi wako wa Maji; kama nalipwa certificate ya milioni 20, milioni 10 yangu na 10 yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukuishia hapo, nilikwenda Shinyanga Vijijini katika Mradi wa Mwakitolyo, zaidi ya 1.4 billion, fedha zote zimelipwa za mradi huu wa maji, lakini unafika pale katika eneo la mradi wa maji unakagua, unakuta maji hayajapanda hata katika tenki, unamuuliza Mhandisi wa Maji fedha zimekamilika zote mkandarasi amelipwa, kwa nini maji hayapandi? Ananiambia Mheshimiwa Naibu Waziri naomba nikunong’oneze; nikamwambia hapana toa taarifa kwa wananchi watuelewe. Ananiambia Mheshimiwa Naibu Waziri sijawahi kuona kijiji wachawi kama hawa, tumetandika mabomba usiku yanapaa kama bombardier; hatuwezi tukawa na Wahandisi wa Maji kama hawa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mambo ya ajabu, hii siyo stori, lakini kutokana na changamoto hizi tulizoziona, sisi kama Wizara ya Maji tukakumbuka maneno ambayo Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli pale Ikulu alituambia sisi kama viongozi wa Wizara ya Maji, anatupa Wizara ya Maji wananchi wa Tanzania waishio mijini na vijijini wapate maji safi na salama, tukishindwa kuifanya hiyo kazi atatutumbua. Sisi kama Viongozi wa Wizara ya Maji hatupo tayari kutumbuliwa, hawa wahandisi wa namna hii hawana nafasi katika Wizara yetu ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtatusamehe hawa wahandisi baada ya maelezo haya, tuliwabeba wazima wazima, mpaka hivi sasa wanaendelea na kesi mahakamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa la utekelezaji wa miradi ya maji ukiachana na fedha, wataalam wetu baadhi yao walikuwa siyo wazalendo. Sisi tulikaa na viongozi wa Wizara tukaona haja ya kuunda Kamati Maalum ya watu 10 ambayo inaongozwa na Profesa Mbwete, kukagua miradi yote ya vijijini na kuona changamoto yake ili tuje na mapendekezo ambayo tutaweza kutatua changamoto hii. Profesa Mbwete alifanya kazi hii kubwa, lakini akabaini kuna changamoto 17 ambazo zinatukabili sisi katika Sekta ya Maji Vijijini. Alikuja na mapendekezo 50 katika kuhakikisha sisi tunayatatua ili mwisho wa siku sekta hii ya eneo la vijijini liwe linafanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya mapendekezo ambayo amekuja nayo Profesa Mbwete ilikuwa kuanzishwa kwa Wakala wa Maji Vijijini na ndiyo maana sisi kama Wizara ya Maji tukaja katika Bunge lako Tukufu na tukawaomba Waheshimiwa Wabunge ili waweze kutupitishia Muswada ule ili wale Wahandisi wa Maji waje katika Wizara yetu ya Maji. Nataka niwaambie Wahandisi wa Maji nchini popote walipo, kuna Mheshimiwa Mbunge hapa alichangia katupa stori ya movie Fulani, akasema kwamba we will meet again, nataka niwaambie Wahandisi wa Maji we will meet again. Sisi tutakutana nao, lakini kwa kuwa wametupa rungu, sisi kama viongozi wa maji hatuna kisingizio kingine tena, tutawashughulikia katika kuhakikisha tunaleta nidhamu katika Wizara yetu ya Maji na tuweze kuleta matokeo chanya kabisa katika sekta yetu ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine cha msingi, pamoja na changamoto hizo zote ambazo tumezibaini, tumefanya kazi kubwa na kazi nzuri ya baadhi ya wataalam wetu. Leo ukienda kwa Mheshimiwa Mwakajoka pale Tunduma tuna mradi mkubwa na ndiyo maana Mheshimiwa Mwakajoka anakubali kazi tunayoifanya. Ukienda kwa Mheshimiwa Haonga kwake pale Mlowo, tuna mradi mkubwa tumeutekeleza na wananchi wake wanapata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ukienda Chunya na maeneo mengine yote miradi ambayo tumeianza, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Rais na Waheshimiwa Wabunge, hakuna single cent itakayopotea, sisi kama viongozi kwa kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge tutasimamia miradi hii ili iweze kuleta tija na maana kubwa kwa wananchi wetu. Maji hayana mbadala, maji siyo kama wali, ukikosa wali utakula ugali, ukikosa ugali utakula makande; ukikosa maji utapata maradhi. Sisi ni Wizara ya Maji siyo Wizara ya ukame, tutahakikisha Watanzania waishio mijini na vijini wanapata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo ililetwa na Waheshimiwa Wabunge ilikuwa suala zima la madai ya wakandarasi. Tunajua kabisa kwamba kulikuwa na kusuasua kukubwa sana wa baadhi ya miradi, kwamba wakandarasi wamefanya kazi lakini hawajalipwa. Nikiri tulikuwa na madai zaidi ya bilioni 88 ambayo tunadaiwa na wakandarasi, nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais pamoja na Wizara ya Fedha, mpaka ninavyozungumza tumeshapata zote bilioni 88 na tumeshawalipa wakandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wote ambao tumewalipa wakandarasi wao, certificates zipo na tutawapa orodha ya wale watu tuliowalipa. Sisi jukumu letu ni kusimamia na miradi iendelee kufanya kazi na sisi kama Viongozi wa Wizara ya Maji tunaomba bajeti yetu watupitishie ili twende tukasimamie fedha zile na zilete miradi mikubwa kabisa katika kutatua changamoto hii ya suala zima la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imeletwa na Waheshimiwa Wabunge ilikuwa manung’uniko ya suala zima la ulipaji wa vibali, kwa maana ya umilikaji wa visima, kwamba mtu amechimba kisima kwa fedha zake mwenyewe na pale kulikuwa na changamoto ya maji, lakini anatakiwa alipe kibali lakini alipe ada kila mwaka. Hii ni changamoto, sisi kama viongozi wa Wizara tumeiona, tunakwenda kubadilisha kanuni zetu na tunaziwasilisha kwa Waheshimiwa Wabunge ili tuondokane na changamoto hii katika kuhakikisha Watanzania hawapati tabu katika suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina maneno mengi sana, Mheshimiwa Profesa yupo hapa, atazungumza kwa kina. Sisi tunachotaka kusema Mheshimiwa Profesa anafanya kazi nzuri, sisi tutakupa ushirikiano wa dhati kabisa katika kuhakikisha tutatatua tatizo hili la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine iliyokuja, kuona kwamba kuna baadhi ya wananchi wanaishi katika vyanzo vya maji. Leo kuna Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa, lakini wananchi wa maeneo yale hawapati maji. Sisi kama Wizara tumeliona na tumeagiza tufanye usanifu unaendelea katika kuhakikisha tunabuni miradi ili wananchi wale wa pembezoni waweze kupata maji na kutumia rasilimali muhimu iliyokuwepo. Nataka nimhakikishie Mbunge wa Sumve, Mheshimiwa Mzee Ndassa ukisoma Tenzi za Rohoni zinasema unapotembea na kuzuru wengine naomba usinipite Mwokozi, hatutokupita pale Sumve katika kuhakikisha unapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hayo, naomba nimalizie kwa kuzungumza na kaka yangu Mheshimiwa Mbunge wa Kibamba, Mheshimiwa Mnyika. Miaka ya nyuma kabla mimi sijaja Bungeni nilikuwa mwanafunzi, alikuwa unajenga hoja kuhusu suala zima la uboreshaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam, hali ilikuwa mbaya sana Dar es Salaam. Kulikuwa na mabomba ya Mchina yalikuwa hayatoi maji, nilimfahamu kwa kusimamia hoja yake, namheshimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilifanya kazi kubwa sana, Quran inasema waamma biniimati rabbikka fahaddith, zielezeeni neema za Mwenyezi Mungu kwa kushukuru. Serikali imefanya kazi kubwa sana, leo eneo la Kibamba zaidi ya kilometa 360 tumezitandika katika kuhakikisha wananchi wa Kibamba wanapata maji. Leo hii ninavyozungumza wananchi wa Kibamba walikuwa wanapata maji kwa saa nane, lakini sasa hivi kwa saa 24. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiachana na hayo, Mheshimiwa Mbunge ni shahidi kwa kuwa ana macho; tuna mradi tunautekeleza Matosa, Hondogo, King’azi A na Mbezi Makabe. Mheshimiwa Mnyika nini au tukupe donda ufukuze nzi? Tunatambua kabisa Mheshimiwa Mnyika maji yamekuwa na uhitaji mkubwa sana lakini sisi kama viongozi wa Wizara tunaendelea kuwaagiza DAWASA kutenga asilimia 35 kwa mapato ya ndani kuhakikisha tunayafikia maeneo ambayo hayajafikiwa na maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwanza kwa kunipa nafasi hii adhimu na mimi nichangie hotuba ya Waziri Mkuu iliyopo mbele yetu. Pia naomba niipongeze Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi kubwa inayoifanya. Lakini pia nimpongeze Dkt. John Pombe Magufuli ni jembe, tena ni jembe la palizi ambalo limekuja kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania. Pia nimpongeze pia Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya, najua zipo changamoto nyingi lakini nasema bahari kubwa ndiyo ivukwayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia katika suala zima la uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Pamoja na mafanikio ya kukuza uchumi katika Taifa letu, pia kuna changamoto kubwa ya umaskini wa watu wetu, ninaiomba Serikali ihakikishe kwamba inatengeneza mazingira ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kuhakikisha kwamba inawasaidia katika kuepukana na umaskini uliokithiri katika jamii yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu imeahidi katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi kutenga shilingi milioni 50 katika kila kijiji, hii itakuwa ni solution ya kuwasaidia Watanzania kwa sababu wapo mama lishe, wapo wajasiriamali wadogo wadogo wakiwemo bodaboda, kilio chao kikubwa ni mitaji, leo ukitaka mtaji unawaambiwa upeleke hati ya nyumba, kiwanja huna hiyo hati utaitoa wapi! Naamini kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya shilingi milioni 50 katika kila kijiji itasaidia sana Watanzania na wananchi wa Pangani.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ningependa nilizungumzie ni suala zima la kilimo. Watanzania wanategemea sekta ya kilimo, lakini kilimo kilichopo sasa, ukuaji wake ni wa kusuasua na kutegemea kudra za Mwenyezi Mungu. Ninaiomba Wizara ya Kilimo ihakikishe kwamba inajikita katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji kwa sababu nchi yetu Mwenyezi Mungu ameijaalia, kuna mito na maziwa mengi tukijikita katika kilimo cha umwagiliaji nadhani suala la chakula kwetu litaisha kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mji wetu wa Pangani tumejaaliwa kuwa na Mto wa Pangani ambao unamwaga maji baharini, ninamwomba kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba ahakikishe kwamba anatutengenezea scheme ya umwagiliaji ili kuhakikisha kwamba jamii yetu ya Pangani tunajikita katika kilimo cha umwagiliaji ambacho kitakuwa katika mazao ya mbogamboga ambayo itaweza kulisha Wilaya ya Pangani na Mkoa wa Tanga pia tunachangia Pato la Taifa katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ninapenda kulizungumzia ni suala zima la miundombinu ya barabara. Ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara ni kichocheo cha maendeleo katika jamii yoyote. Lakini katika Wilaya yetu ya Pangani, barabara yetu imekuwa ni ahadi ya muda mrefu lakini mpaka sasa barabara hii imeweza kuzorotesha maendeleo katika jamii yetu ya Pangani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Serikali ya Awamu ya Tano iangalie kwa jicho la huruma kuhakikisha kwamba inajenga barabara hii ya Pangani, Tanga - Pangani - Sadani ili kuweza kuinua uchumi wa Pangani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Wilaya ya Pangani ilivyo ni kama kisiwa, ili uende Pangani lazima uende kwa makusudio maalum, unaenda kuzika au umesikia kuna kitchen party ndiyo watu waweze kwenda, madhara ya barabara hii ni makubwa, ingawa tumekuwa na fursa nyingi ya kiutalii, tuna uvuvi bahari kuanzia mwanzo wa mji mpaka mwisho wa mji. Ninaiomba Serikali itengeneze barabara hii ya Pangani ili kuhakikisha kwamba uchumi wa Pangani unapaa, badala ya kuwa pangoni, sasa tupae angani. Ninaamini Serikali hii kwa kazi inayofanya barabara hii itatengenezewa kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka nilizungumzie ni sekta ya uvuvi. Jamii yetu ya Pangani tunategemea sekta ya uvuvi, Lakini uvuvi tunaoufanya ni wa kutumia zana duni na ukitaka kwenda kuvua lazima utegemee ndoano na chambo; hivi samaki akishiba huyo samaki utamvua wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara ya Uvuvi iangalie sasa suala la uvuvi ili kuhakikisha kwamba inawasaidia wavuvi wa Pangani kwa kuwapatia pembejeo na zana na kuhakikisha tunatengenezewa bandari ya uvuvi kwa ukanda wa Pangani na Tanga ili kuhakikisha kwamba wavuvi wa Pangani wanafaidika ni rasilimali bahari tuliyonayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda nizungumzie ni suala la afya. Huduma ya afya bora ni njia nzuri ya kuinua uchumi katika jamii yoyote, lakini katika sera ya Serikali inasema kwamba itajenga zahanati katika kila kijiji na kituo cha afya katika kila Kata, lakini Pangani tuna kituo kimoja tu cha afya na asilimia kubwa ya wananchi wanakaa ng’ambo ya Mto Pangani ambapo hutegemea huduma katika hospitali yetu ya Wilaya ya Pangani. Hospitali ya Wilaya ya Pangani bado haijajitosheleza, ukitazama x-ray hakuna, bado dawa ni shida, leo ukitaka x-ray mpaka uende Tanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Serikali ya Awamu hii ya Tano katika bajeti yake ihakikishe kwamba inashirikiana na sisi kuhakikisha tunatengeneza vituo vya afya vya ziada ili kuisaidia jamii yetu ya Pangani katika suala zima la afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kusema kwamba wapo watu ambao wanajigeuza bundi kukitakia Chama cha Mapinduzi mabaya kife, lakini nasema watakufa wao na ofisi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi iliyofanya Chama cha Mapinduzi ni kubwa, ukiangalia katika Wilaya yetu ya Pangani mpaka mwaka 2005 tulikuwa na shule mbili tu za Serikali, lakini sasa hivi tuna shule saba hata mimi mtoto wa mama ntilie nimefika Chuo Kikuu, dogo hilo? Mungu atupe nini, hata Mwenyezi Mungu anasema katika vitabu vya dini waamma biniimati rabbika fahadith (zielezeeni neema za Mwenyezi Mungu kwa kushukuru). Sasa leo usiposhukuru kidogo unataka ukashukuru wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya kubwa lakini ninachokiomba iendelee kutengeneza miundombinu ya elimu, vilevile kuboresha maslahi ya elimu kwa watumishi ili kuhakikisha wanafaidika na kazi wanazozifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo sina maneno mengi ya kusema, naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwanza kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia hotuba iliyokuwepo mbele yetu. Lakini pia niungane na Mbunge wa Muheza kuhusu malalamiko yetu na masikitiko yetu kwa Wizara hii kwa namna mkoa wetu ulivyosahaulika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapata uchungu leo kuona baadhi ya maeneo ya wenzetu yanatekelezewa miradi mbalimbali lakini sisi Mkoa wetu wa Tanga tunasahaulika. Leo tunaona wenzetu wanashangilia wanakaa safu za mbele lakini sisi mkoa wetu wa Tanga tunawekwa katika jiko kazi yetu kusugua masufuria na sisi Mkoa wetu lazima atutizame kwa jicho la huruma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wa Tanga tumekuwa watu wa kupembuliwa tu. Ukiangalia bandari tunapembuliwa, ukiangalia sijui nini tunapembuliwa hivi sisi ni lini tutatekelezewa miradi yetu ya maendeleo? Kwani tumemkosea nini Mwenyezi Mungu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza haya kwa masikitiko makubwa kwa kuwa kila kukicha sisi tumekuwa watu wa kupewa ahadi tu. Wali ni mtamu sana kwa maini lakini ukikaa sana unakuwa kiporo na kiporo kikaa sana kinachacha na kikichacha kinaumiza tumbo, leo wananchi wa Tanga tunaumizwa kutokana na kutotelekelezwa miradi mbalimbali, inakuwa kazi ya kusuasua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine nataka nizungumzie kwa masikitiko makubwa barabara yetu ya Pangani – Tanga – Saadani. Barabara hii mimi tangu sijazaliwa, nimezaliwa, nimesoma msingi, sekondari mpaka Chuo Kikuu leo nimefika na mimi nimekuwa Mbunge lakini barabara yetu tumekuwa watu wa ahadi tu. Amekuja Mheshimiwa Rished miaka 15 tunaambiwa itajengwa, Mheshimiwa Pamba akaambiwa ipo kwenye upembuzi, mimi leo naambiwa pia barabara yetu African Development Bank wameonyesha nia sasa hii nia inaisha lini ili barabara hii sasa itengenezwe? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Pangani tupo pangoni, tuna fursa nyingi katika Wilaya yetu ya Pangani, leo tuna Mbuga Saadani ambayo ni kichocheo kikubwa cha kiutalii, ni mbuga pekee katika Afrika ambayo imeungana na bahari. Barabara hii ya Tanga - Pangani ndiyo inaunganisha na Mkoa wa Tanga na nchi jirani ya Kenya, tukijenga barabara Tanga - Pangani - Saadani tutaweza kuinua sekta ya utalii katika Wilaya ya Pangani na Mkoa wa Tanga. Lakini kwa kuwa tuna mahusiano vizuri na Zanzibar na Mombasa, Kenya ina maana tutainua sekta ya utalii katika Wilaya ya Pangani, lakini pia tutaweza kunyanyua sekta mbalimbali za kiutalii, uvuvi na kilimo kutokana na barabara hii ya Tanga - Pangani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sina maneno mengi sana ya kusema, ila nilikuwa namwomba Waziri katika majumuisho yake atuambie amejipanga vipi kuhakikisha kwamba atatutekelezea barabara hii ya Tanga - Pangani, Bandari ya Tanga pamoja na reli ya kutoka Tanga - Arusha na Musoma ili tuchangie katika pato la Tanzania.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru, ila nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Profesa Sospeter Muhongo pamoja na timu yake kwa kazi nzuri na uwajibikaji uliotukuka katika kuwatumikia wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nijielekeze kuchangia katika Usambazaji wa Umeme Vijijini (REA) katika hotuba iliyokuwepo mbele yetu. Nchi yetu ina malengo ya kuwa nchi ya viwanda na kufikia katika azma ya uchumi wa kati. Pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali, lakini ukweli ni kwamba, tuna changamoto kubwa ya vikwazo vya uchumi kimojawapo ni kukosekana kwa nishati ya uhakika ya umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia kubwa ya wananchi wetu wanaoishi vijijini wanakosa huduma hii muhimu ya nishati ya umeme ambao ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya watu wetu. Niiombe Serikali iongeze kasi ya usambazaji na kuiongezea fedha za kutosha Wizara ya Nishati kuhakikisha inasambaza umeme kwenye vijiji vingi na kwa wakati muafaka pia, kukamilisha miradi ya umeme ambayo haijakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukisambaza umeme vijijini tutawezesha wakulima kuongeza thamani ya mazao kwa kufungua viwanda vidogo vidogo, tukisambaza umeme vijijini wavuvi watahifadhi samaki; pia, itawawezesha wafugaji kuhifadhi nyama kwa muda mrefu, sambamba na kuongeza ajira kwa vijana kwa kuanzisha shughuli mbalimbali za kijasiriamali; mfano saluni za kike na za kiume, uuzaji wa vinywaji baridi, viwanda vya kuchomea vyuma na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nitumie nafasi hii kumwomba Mheshimiwa Waziri katika bajeti hii ahakikishe vijiji vifuatavyo katika Jimbo la Pangani vinapatiwa umeme huu wa REA; Kigurusimba Misufini, Mivumoni, Matakani, Kidutani, Jaira, Kikokwe, Langoni, Mtango, Mtonga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia, tunaomba Wizara iwe na mkakati maalum wa kuunganisha umeme katika shule za sekondari za kata, zahanati na vituo vya afya, ili kuimarisha huduma za jamii za wananchi wetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha leo kuchangia hotuba iliyoko mbele yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nitumie nafasi hii kumpongeza Waziri Profesa Maghembe kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya katika Wizara hii, kwa kweli anaitendea haki. Waswahili wanasema mzigo mzito mpe Mnyamwezi, naamini Wizara hii Mnyamwezi ni Mheshimiwa Profesa Maghembe na kazi anaifanya. Pamoja na changamoto kubwa anazokabiliana nazo, namwambia songa mbele bahari kubwa ndiyo ivukwayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina maneno mengi sana ila kubwa nataka nijikite katika suala zima la mambo kale. Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye hazina kubwa ya mali kale. Baadhi ya mali kale zilizopo ni pamoja na majengo ya zamani ambayo yalijengwa na matumbawe katika Miji ya Pwani ikiwemo Pangani, Bagamoyo, Kilwa na Kilindi lakini Serikali haijawekeza katika utalii wa mali kale hizi. Serikali inapoteza mapato mengi kwa kutowekeza kwenye utalii huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe katika bajeti hii itenge fedha za kutosha kuhakikisha kwamba inakarabati majengo yale ili yawe katika hadhi na kuongeza utalii katika mali kale na kuongeza pato la Taifa. Hii iende sambamba na kuajiri watumishi wanaohusiana na mambo ya kale ili kuhakikisha kwamba tunaongeza pato la Taifa katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii ya maliasili na utalii ni muhimu na mhimili wa maendeleo katika Taifa letu, lakini mchango wake siyo mkubwa pamoja na fursa zilizopo. Nchi yetu imejaaliwa kuwa na vivutio mbalimbali kama vya wanyamapori na hifadhi mbalimbali, lakini mchango wake umekuwa ni mdogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali itenge fedha na kuhakikisha kwamba inakuwa na mpango mkakati wa kuvitangaza vivutio hivi ili viende kuchangia pato la Taifa. Biashara ya utalii inategemea matangazo. Tunapovitangaza vivutio hivi kwa kasi kubwa, ndiyo tunapoongeza watalii kuja kuvitembelea na kuchangia pato la Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya yangu ya Pangani nataka nizungumzie mbuga ya Saadani. Mbuga ya Saadani ni miongoni mwa mbuga pekee Afrika ambayo imepakana na bahari. Mbuga hii inapata changamoto kubwa ya miundombinu mibovu ya barabara. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, ni muda muafaka sasa akae na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha kwamba wanaiangalia barabara hii ya Tanga - Pangani - Saadani na kuhakikisha inajengwa kwa kiwango cha lami ili kuweza kuwavutia watalii kutoka Kanda ya Kaskazini, Zanzibar pamoja na nchi jirani ya Kenya kuja katika Wilaya ya Pangani na kuinua sekta hii ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mengi sana ya kusema ila kikubwa tu nimwombe Mheshimiwa Waziri aendelee kufanya kazi na kuweza kuwatumikia Watanzania na sisi kama viongozi vijana tunaendelea kumuunga mkono kuhakikisha kwamba anafikia azma iliyowekwa katika Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie hotuba hii muhimu ambayo ni sekta yenye mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa letu. Pili, nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na watumishi wote wa Wizara hii. Binafsi nimevutiwa na utendaji wao wa kazi kama kauli ya Mheshimiwa Rais wetu ya Hapa Kazi tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Rais kwa ahadi zake kwenye Jimbo la Pangani na kuzitekeleza kwa wakati kwa kutupatia kivuko kipya cha MV Tanga na kutupatia fedha za ujenzi wa geti, umetugawia na tumekabidhiwa mradi huu muhimu wa geti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara; ujenzi wa barabara ni kichocheo cha shughuli za kiuchumi na hata kuongeza ajira. Maeneo ambayo yamebadilika kwa kiasi kikubwa katika uchumi hata huduma za kijamii yana barabara nzuri. Niombe Wizara hii iangalie kwa umuhimu wake Ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani – Saadani – Bagamoyo, ambayo ni ahadi ya muda mrefu. Hivyo ni wakati wa kujenga barabara hii ili iifanye Wilaya ya Pangani ipate maendeleo kutokana na fursa nyigine 21 zilizopo Pangani, ikiwemo Mbuga ya Wanyama ya Saadani. Pia ujenzi wa barabara hii uende sambamba na ulipaji wa hatua kwa hatua kwa wananchi wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Gati ya Pangani. Tunashukuru kwa kutujengea gati hili. Pia naomba Serikali ili gati hili liwe na tija na kuweza kupata mapato kuanzishwe usafiri wa majini, kwa maana ya kutupatia fast boat ya kutoka Pangani kwenda Mkokotoni. Mwekezaji ameshapatikana, cha muhimu ni kumpa ushirikiano wa dhati katika kufanikisha upatikanaji wa boat hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mawasiliano; jamii ili ipige hatua ya maendeleo lazima iwe na mawasiliano ya uhakika, hii itachangia urahisishaji katika shughuli za kijamii na kiuchumi. Hivyo, Serikali itusaidie mawasiliano kwa maeneo ya Mkalamo, Mrozo na Bushori.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu iliyopo mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema ili nami niweze kushiriki Bunge. Tulikuwa na wenzetu ambao walipenda kushiriki nasi lakini wamepoteza roho zao. Namwomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za Marehemu mahali pema
peponi. Amina.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimpongeze Rais wangu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa na nzuri anazozifanya katika nchi yetu. Kazi zinaonekana, yapo baadhi ya maneno, lakini nasema, unaweza kuwa na macho lakini usione, unaweza kuwa na masikio usisikie; na unaweza kuwa na pua pia ukashindwa kunusa. Ila kubwa naomba Mwenyezi Mungu aendelee kumpa nguvu kuhakikisha kwamba analeta maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Baraza lake la Mawaziri kwa kazi kubwa wanayoifanya. Naomba wasonge mbele pamoja na changamoto kubwa, lakini naamini bahari kubwa ndiyo ivukwayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa napenda nichangie baadhi ya maeneo hususan katika suala zima la barabara. Ujenzi wa barabara umeweza kuchochea shughuli mbalimbali za kiuchumi na kuwezesha hata kuongeza ajira katika baadhi ya maeneo. Pia natambua
shughuli kubwa inayofanywa na Wizara ya Ujenzi katika kuhakikisha kwamba inaimarisha miundombinu ya ujenzi katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nioneshe masikitiko yangu kuhusu kusahaulika ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani – Saadani - Bagamoyo. Ahadi ya ujenzi wa barabara ya Tanga – Pangani - Saadani ni ahadi ambayo tangu sijazaliwa mpaka sasa, leo hii nimeingia Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, alikuja hapa Mheshimiwa Rished miaka 15, ameizungumzia barabara ya Tanga – Pangani – Saadani, lakini Serikali
imemwahidi itajenga; amekuja Mheshimiwa Pamba akaambiwa barabara ipo kwenye upembuzi. Leo nimeweza kuibana Serikali, lakini bado inaniambia kwamba Serikali imeonesha nia, itaweza kutengeneza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, itambulike kabisa, hata ukitaka kufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ni lazima uoneshe nia; lakini ikifika saa 12.00 si unafuturu! Hivi kuna kizungumkuti gani katika kuijenga barabara ya Tanga – Pangani - Saadani?
Mheshimiwa Naibu Spika, binadamu wameumbwa na wivu, binadamu wameumbwa na matamanio; leo tunaona baadhi ya maeneo mbalimbali yanatengenezewa barabara za lami, hivi sisi Pangani tumemkosea nini Mwenyezi Mungu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya yetu ya Pangani uchumi wetu tulikuwa tukitegemea zao la mnazi. Mnazi umekufa, lakini leo ili mtu aje Pangani lazima aje kwa makusudi maalum. Tuna Mbuga ya Saadani, lakini wawekezaji au watalii wanashindwa kuja kwa sababu ya miundombinu mibovu ya barabara. Leo tunaona mvua zinazonyesha, shughuli mbalimbali zimekwama. Naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu katika hitimisho lake, kuna barabara ambazo zimeshafanyiwa upembuzi na usanifu, ni nini mkakati wa Serikai kuhakikisha kwamba inajenga barabara hizi ili sasa turudishe imani kwa wananchi? Wakati mwingine wananchi wanasema tumekuja Bungeni kusinzia na kunywa juice.
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Naomba katika bajeti hii Serikali ihakikishe kwamba inatujengea barabara ya Tanga – Pangani – Saadani. Kama tulikuwa pangoni, sasa na sisi tupae angani ili tuweze kupata maendeleo ya dhati kabisa katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nilikuwa nataka nilizungumzie ni kuhusu suala zima la maji. Tumekuwa na chanzo kikubwa cha maji katika Wilaya yetu ya Pangani. Tuna mto Pangani ambao unatiririsha maji baharini ambao umekata katikati ya mji, lakini tumekuwa na tatizo kubwa la maji. Leo tunaona wananchi wetu wakati mwingine wamepauka; siyo kwamba hawapaki lotion wala mafuta, ni kwa sababu tu ya tatizo la maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuhakikishe katika Wizara hii, Mheshimiwa atupe majibu, ana mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wanatumia vyanzo hivi vya maji ili kuhakikisha kwamba wanawatua ndoo mama zetu katika suala zima la maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nilikuwa nataka nilizungumzie ni kuhusu suala zima la upanuzi wa Shule za Sekondari na Vyuo. Kumesababisha mahitaji makubwa ya ajira hususan kwa vijana wenzetu na tunatambua kabisa sasa hivi kumekuwa na ongezeko kubwa la vijana, lakini wamekuwa na changamoto kubwa ya kukosa ajira. Vijana wenye degree wanashinda maskani, hawana shughuli kubwa ya kufanya, lakini natambua shughuli kubwa anazozifanya mama yangu, Mheshimiwa Jenista Mhagama pamoja na kaka yangu Mheshimiwa Anthony Mavunde kuhakikisha kabisa vijana wetu wanapata mafunzo, lakini Serikali ione kabisa nia yake ya dhati namna gani tunaenda
kutatua tatizo la ajira katika Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuwe na mkakati maalum ambao kutatolewa tamko maalum kwa Halmashauri zilizokuwepo katika Wilaya zetu kuhakikisha kwamba inatengeneza ajira kila mwaka na kutoa taarifa Bungeni ili vijana wetu wenye elimu na wasio na elimu wawe wanapata fursa mbalimbali za ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, naomba Wizara ya ajira iangalie baadhi ya mashamba kuhusu wawekezaji hususan katika mashamba ya Mkonge. Katika Jimbo langu la Pangani tuna mashamba makubwa mawili kwa maana ya shamba la Mwera Estate na Sakura Estate lakini
Watanzania wale maskini ambao wanafanya katika uzalishaji mkubwa wa mikonge, wamekuwa wanapata tabu, wananyanyasika; mikataba yao imekuwa ya ujanja ujanja; hali duni; mazingira mabaya! Kwa hiyo, naiomba Wizara hii, hususan Mheshimiwa Jenista Mhagama apate nafasi ya kupita kule ili kuwapa faraja na waone kwamba na wao ni sehemu ya Tanzania, kwa sababu wamekuwa kama wapo katika ukoloni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali kwa dhati kabisa iende katika maeneo yale ili wawekezaji wale wahakikishe kwamba wanawaboreshea maslahi na kutengeneza ajira ili waweze kunufaika. Wakati mwingine wanaweza kukwambia mkonge haulipi; sasa kama haulipi, kwa nini wasilime mihogo ambayo inaweza ikalipa? Kwa hiyo, unakuta ni ujanja tu wa wawekezaji lakini kubwa tunajua kabisa mkonge unalipa, lakini mkonge uendane na maslahi ya wale wafanyakazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niipongeze Serikali kuhusu suala zima la elimu bure, lakini pia itambue kuna baadhi ya maeneo katika nchi yetu ilichelewa kuwekeza katika suala zima la elimu. Katika Jimbo langu la Pangani, sisi mpaka mwaka 2005, tulikuwa na shule mbili tu za Serikali, lakini kwa jitihada ya Serikali kuhakikisha kwamba inatengeneza Shule za Kata, leo hata mimi mtoto wa Mama Ntilie nimefika katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, naipongeza kwa dhati kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa ni kwamba, tuna changamoto mbalimbali hususan ukosefu wa Walimu wa Sayansi. Naiomba Serikali, ili kuhakikisha katika bajeti hii na sisi tunapatiwa Walimu, sisi miaka ya nyuma katika Wilaya yetu ya Pangani tulikuwa tukiitwa KKY kwa maana ya
Kufuma, Kushona, Kupika na Kuzaa ndiyo kazi za watu wa Pangani na kukaa barazani. Kupitia Serikali hii, leo imeweza kuwezesha vijana mbalimbali katika nchi yetu, wameweza kushiriki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hilo ni jambo jema na tutaendelea kuliunga mkono, lakini kubwa tunaiomba Serikali iendelee kuhakikisha kwamba inaboresha miundombinu mizuri na kuhakikisha kwamba inatupatia Walimu wa Sayansi ili siku moja Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Magufuli atokee katika Jimbo la Pangani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sina maneno mengi sana ya kusema, itoshe kusema kwamba naunga mkono hoja na naomba kuwasilisha. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia hotuba muhimu katika maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Rais wangu, Mhshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kwa wananchi wa Tanzania. Imani huzaa imani, kwa namna anavyofanya kazi tutaendelea kumuunga mkono; na hata kama uchaguzi ungekuwa mwaka 2020, mimi kura yangu ningempigia tena Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli aendelee kuwa Rais wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine napenda niwapongeze Mawaziri pamoja na Naibu wake na Watendaji wote wa Wizara hii kwa namna wanavyofanya kazi. Nawaona ni namna gani wanavyoweza kushiriki na wakulima, wafugaji na wavuvi katika matatizo yao. Kikubwa nawaombea Mwenyezi Mungu awabariki waendelee kufanya kazi, lakini kubwa lililonifurahisha ni namna gani walivyoweza kuondoa tozo ambazo zilizua kero, ambazo zilikuwa zinadumaza maendeleo ya wavuvi, wakulima na wafugaji. Hongereni sana, Mwenyezi Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa, nilikuwa nataka nizungumzie kuhusu suala zima la zao la nazi. Pamoja na kwamba kilimo ni uti wa mgongo, lakini kila kilimo kinategemeana na mazingira yake. Ukienda Shinyanga wanategemea suala la pamba, Tabora wanategemea tumbaku na sisi wananchi wa Pangani tunategemea zao la nazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapozungumzia nazi, ninazungumzia uchumi na maisha ya wananchi wangu wa Jimbo la Pangani. Wananchi wa Pangani wamekuwa maskini kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi. Minazi ile imekufa, imekauka, hali ya maisha imekuwa duni sana. Naiomba Wizara hii ifanye tafiti ya dhati kabisa ili kulifufua zao hili la mnazi. Kwa sababu tunapozungumzia suala la zao la mnazi, ni moja ya kitega uchumi. Sisi binafsi tulikuwa tukichangia pato kubwa la Taifa kipindi cha nyuma; tulikuwa tukizalisha nazi kiasi cha 500,000 kwa mwezi lakini sasa hivi imeshuka tunazalisha chini ya 100,000. Kwa hiyo, tafiti zifanyike kwa haraka ili tuweze kujua ni namna gani tunaenda kulifufua zao hili la mnazi ili na sisi Wilaya yetu ya Pangani tuweze kuchangia pato la Taifa katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia juzi nilihudhuria kongamano la kuhusu suala zima la zao la korosho. Kwanza nampongeza Mkurugenzi wa Bodi hii ya Korosho kwa mkutano mzuri unaonipa matumaini. Na sisi katika Wilaya yetu ya Pangani tuna mazingira mazuri kabisa ya kufufua zao hili la korosho. Naiomba Wizara hii ituhakikishie kwamba inatupatia mbegu kwa haraka na bora ili kuhakikisha kwamba tunaenda sambamba, badala ya mnazi tunaenda sasa na zao hili la korosho kwa sababu tunaona kabisa Korosho ni zao la kijani. Kwa hiyo, tunapopanda korosho na tafiti zinafanyika kwa ajili ya kuinua zao la mnazi, nina imani uchumi wa Pangani utakuwa kwa kasi na maendeleo yatakuwa kwa kasi nasi tutaweza kuchangia pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka nizungumzie, tunaona kabisa nchi yetu inaelekea katika suala zima la viwanda. Kama tunahitaji suala zima la viwanda, lazima tuwekeze kwa dhati kabisa katika suala zima la kilimo. Ukiangalia kilimo tunacholima sasa, tunategemea kudra za Mwenyezi Mungu. Leo mvua ikinyesha kwa wingi, kilimo kinakuwa na athari kubwa, mvua isiponyesha, pia kuna athari kubwa. Ili tuweze kuingia katika uchumi wa viwanda na tupate maendeleo makubwa ya viwanda ni lazima tuwekeze katika kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu imejaaliwa kuwa na mito mingi mbalimbali. Sisi katika Jimbo letu la Pangani tumekuwa na Mto Pangani, lakini tunashindwa kunufaika nao, leo mto unamwaga maji baharini kwa kukosa miundombinu mizuri ya maji. Namuomba Mheshimiwa Waziri akae na Waziri wa Maji ili watuhakikishie kwamba wanatutengenezea miundombinu ya maji ili sisi wananchi wa Pangani tuwekeze katika kilimo cha umwagiliaji. Tukiwekeza katika kilimo cha umwagiliaji, leo tunaweza tukaulisha Mkoa wa Tanga, lakini tunaweza tukailisha Zanzibar na kanda ya Kaskazini kupitia mto huu wa Pangani.

Kwa hiyo, naomba tusiishie Pangani, lakini hii iwe ajenda ya nchi ili kuhakikisha kwamba tunawekeza katika kilimo cha umwagiliaji ili tuweze kupata manufaa makubwa na malighafi ambayo itatumika katika suala zima la viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka nilizungumzie hapa ni kuhusu suala zima la wavuvi. Wilaya yetu ya Pangani ina bahari ya Hindi, lakini wavuvi wale wanashindwa kunufaika kwa sababu ya kukosa uwezeshwaji wa nyenzo. Leo mvuvi wa Pangani anatumia ndoano na chambo. Hivi leo ikitokea samaki ameshamla samaki mwenzake kashiba, hivi kweli anaweza akamvua huyo samaki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Wizara sasa tuangalie namna gani tunaweza tukawawezesha wavuvi hawa wadogo ili kuhakikisha kwamba wanapata nyenzo za kisasa ambazo zitaweza kuwasaidia ili waweze kunufaika na rasilimali bahari iliyokuwepo katika Jimbo langu la Pangani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Mheshimiwa Waziri ambalo nataka nilizungumze ni kwamba, pamoja na kuwekeza katika bahari lakini pia tuna wafugaji katika Wilaya yetu ya Pangani. Ni sekta muhimu na ambayo inachangia mapato ya Halmashauri lakini ukiangalia wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi sana; hawana majosho wala hawana malambo.

Naiomba Wizara hii na Mheshimiwa Waziri aangalie namna anavyoweza kutusaidia. Wanasema unapozuru wengine, naomba na sisi utukumbuke, usitupite kwa kuhakikisha kwamba unatupatia majosho na malambo ili wale wafugaji wa Pangani waweze kunufaika na Wizara hii.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina maneno mengi sana, ila kubwa naomba niwapongeze sana Mawaziri hawa kwa namna wanavyofanya kazi. Naiomba Serikali itoe fedha kwa dhati na kwa haraka ili iweze kutekelezeka bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsanteni sana, Mwenyezi Mungu awabariki sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia bajeti iliyokuwa mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza naomba nimpongeze Dkt. Mpango kwa namna ya mpango wa bajeti alivyoipanga imepangika kweli kweli, bajeti ipo bomba. Nataka nimwambie Mheshimiwa Mpango wali wa kushiba siku zote unaonekana kwenye sahani. Na naunga mkono kama mimi Mbunge kijana kwa sababu bajeti hii imeenda kujibu matatizo ya wakulima, imeenda kujibu matatizo ya wafugaji, lakini pia imeenda kujibu matatizo ya wavuvi. Ni watu wenye sifa tu ya miembe ndio wanaweza wakapinga bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupinga si dhambi na ni jambo jema, lakini si kupinga kila kitu. Na ukisoma aya za Qurani Mwenyezi Mungu anasema; “waama bi neemati Rabbikka fahadith” (zielezeeni neema za Mwenyezi Mungu kwa kushukuru). Watanzania tulikuwa tunamuomba Rais ambaye ataweza kuleta maendeleo katika taifa letu. Unaweza pia usijue kusoma, lakini pia picha ukashindwa kuiona? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu Wabunge tutapata laana kubwa kwa Mwenyezi Mungu kama tutampinga Mheshimwia Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni jembe tena limekuja wakati mwafaka. Tulitumie ili tuhakikishe kwamba tunaenda kulima na kupanda kwa uhakika katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi katika Jimbo langu la Pangani tulikuwa na mabadiliko ya tabianchi bahari inakula Mji wa Pangani, lakini kwa muda mfupi leo tunatengenezewa ukuta wa bahari. Kulikuwa na maeneo ambayo hayajawahi kuona umeme leo wanapata umeme. Mungu atupe nini atupe gunia la chawa tujikune? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema awali, bajeti ni nzuri lakini naomba nishauri katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa barabara ni kichocheo kikubwa cha maendeleo katika Taifa. Lakini pia inaweza kuchochea ajira katika maeneo katika jamii yetu na hata katika kuboresha huduma za kijamii. Tunaona maeneo mbalimbali ambayo yalikuwa hayana barabara leo yamepatiwa barabara maendeleo yake ni makubwa. Niombe fedha zilizotengwa katika bajeti hii ili kuhakikisha kwamba zinafika kwa haraka ili miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali ya Taifa letu iboreshwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano katika Jimbo langu la Pangani tulikuwa na changamoto ya barabara, lakini katika bajeti hii tumetengewa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi. Naiomba Serikali fedha zile ziende ili kuhakikisha kwamba barabara ya Tanga - Pangani - Saadani inajengwa ili wananchi wangu wa Pangani waweze kupata maendeleo kwa kasi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la pili, ni suala zima la upatikanaji wa maji. Nchi yetu ina vyanzo vingi vya maji lakini maeneo mengi bado kumekuwa na tatizo la maji. Naomba niseme anayelala na mgonjwa ndiye anayejua mihemo ya mgonjwa. Sisi katika Jimbo la Pangani bado tunakuwa na changamoto kubwa ya maji. Tuna Mto Pangani ambao unapita katikati ya mji lakini bado wananchi wangu wanatatizo la maji. Niombe bajeti hii iende ikatatue tatizo la maji kwa wananchi wa Pangani ili twende kuwatua ndoo wananchi wale wa Pangani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina maneno mengi sana ya kusema, lakini kubwa kwa kumalizia nataka nizungumze tunapozungumzia uchumi wa viwanda lazima tuangalie afya za watu wetu. Hauwezi ukalima, hauwezi ukazalisha pasipokuwa na afya. Tunaona maeneo mbalimbali bado kumekuwa na changamoto ya vituo vya afya, na hata Zahanati. Niombe Serikali katika bajeti hii kuhakikisha kwamba inatenga fedha hizo zifike kwa haraka ili kuhakikisha kwamba vituo vya afya na zahanati vinajengwa na vifaa tiba vinapatikana ili wananchi wetu waweze kupata maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ahsante sana na Mwenyezi Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira wa Mwaka 2018
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda nimshukuru sana Mwenyezi Mungu, lakini nimshukuru Rais wangu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuendelea kuniamini. Pia kwa namna ya kipekee nimshukuru Waziri wangu, Katibu Mkuu na Wataalam wote wa Wizara ya Maji kwa ushirikiano mkubwa wanaotupa katika kuhakikisha tunatimiza majukumu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nitumie nafasi kwa namna ya kipekee nikushukuru wewe mwenyewe binafsi pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenye maslahi mapana katika kuhakikisha tunaenda kutatua matatizo ya maji kwa wananchi wetu. Pia kwa namna ya kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati yetu pamoja na Waheshimiwa Wajumbe wote wa Kamati kwa namna walivyoweza kuushughulikia Muswada huu mpaka leo tupo hapa katika Bunge lako Tukufu, Waheshimiwa Wenyekiti ahsanteni sana, Mwenyezi Mungu awabariki sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii, nitoe ufafanuzi katika hoja mbalimbali zilitolewa na Waheshimiwa Wabunge, moja, kwamba Wizara ya Maji ina Wakala wa maji, kwa maana ya uchimbaji visima, sasa je kuanzishwa kwa Wakala huu wa Maji Vijijini hatuoni kwamba tunaongeza taasisi zingine, nataka nilihakikishie Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Maji, kwa maana ya Wakala wa Uchimbaji Visima Vijijini (DDCA) itakuwa Idara tu ndani ya Wakala wa Maji Vijijini, kwa hiyo, suala la gharama ama kuongezeka kwa taasisi halitokuwemo. Kuhusu suala lingine limeongelewa suala zima la nafasi ya Local Government ina nafasi gani katika Wakala wa Maji Vijijini, suala la Local Government tumezingatia na Local Government itachangia fedha katika miradi ya maji katika own source lakini pia itatunga sheria ndogo katika suala zima la maji na sisi kama Wizara kwa maana ya utekelezaji kwa maana ya RUWASA itakuwa ikitoa taarifa mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya maji katika halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine kilichozungumziwa hapa ni kuhusu fidia kwa wananchi, hili jambo lipoje? Tumeona kumekuwa na utekelezaji wa miradi ya maji sehemu mbalimbali na inapitia katika maeneo ya wananchi ambayo yanamilikiwa, je, vipi kuhusu fidia? Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge sehemu ambapo itatekelezwa miradi ya maji na itapita maeneo ya wananchi, sisi kama Viongozi wa Wizara, tutaendelea kulipa fidia kama maeneo mbalimbali tulivyokuwa tukilipa fidia. Ukienda Arusha, tuna mradi mkubwa sana wa maji kabla ya utekelezaji wa mradi wa maji wananchi wale wameendelea kulipwa fidia. Kwa hiyo kila mwananchi ambaye anayestahili kulipwa fidia tutamlipa fidia yake na yule asiyestahili hatolipwa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu suala zima la tozo hapa limezungumzwa, sisi kama Wizara na kwa maana ya uanzishaji wa Wakala huu wa Maji tumelizingatia na katika jedwali hili la Mabadiliko ya Sheria lipo na limezingatiwa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa tuwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, ukiangalia Serikali inatekeleza miradi mingi kwa fedha nyingi sana lakini baadhi ya wananchi wamekuwa wakihujumu miradi ya maji. Ukienda Longido Serikali imetekeleza mradi wa maji kwa zaidi ya shilingi bilioni 15 lakini juzi tu wananchi wa kawaida wameenda kuharibu miundombinu ya maji ina maana asilimia kubwa ya wananchi waende kuteseka. Suala la maji tunasema maji ni uhai lakini maendeleo ya sekta ya maji yanaanza na mimi, wewe na sisi. Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge twende kutoa elimu kwa wananchi wetu katika kuhakikisha tunalinda miundombinu ya maji ambayo imewekezwa na Serikali kwa fedha nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo imekuja hoja sasa kuhusu suala zima la mabadiliko ya sheria kuhusu suala la rasilimali za maji. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge baada ya kupitishwa Wakala huu wa Maji Vijijini sisi kama Wizara tutaanza kupitia sasa Sheria ya Rasilimali za Maji ili tuainishe sehemu gani zenye mabadiliko ili tuweze kuleta Bungeni Muswada ule ili na ninyi muweze kupitia katika kuhakikisha tunakuwa na sheria ambayo itakuwa na tija na yenye maslahi mapana kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
The Water Resources Management (Amendment) Act, 2022
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nikushukuru wewe binafsi kwa mwongozo wako katika Bunge letu hili Tukufu. Pia nitumie nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote. Tumepata hapa michango zaidi ya Wabunge 11; Mheshimiwa Kiswaga, Mheshimiwa Anna Lupembe, Mheshimiwa Profesa Shukrani, Mheshimiwa Kimei, Mheshimiwa Festo Sanga, Mheshimiwa Khadija Aboud na Waheshimiwa wengine kama dada yangu Mheshimiwa Salome, Mheshimiwa Nusrat na Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia. Niseme tu maoni yao tumeyapokea na tunayafanyia kazi na mengine tutayajibu kwa maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango, ushauri na maoni yao waliyoyatoa, yamelenga siyo kuboresha Muswada pekee, bali pia yanaonesha umuhimu mkubwa unaochukuliwa katika suala la usimamizi wa rasilimali za maji nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishukuru tena Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji, ambapo kupitia mjadala huu wa leo inaonesha Serikali na Kamati ya Bunge ilivyopata muda wa kutosha kupitia na kuchambua kwa kina Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji ya Mwaka 2022 (The Water Resources Management Amendment Act, 2022).

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imepokea michango, ushauri na maoni yote yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge na yatazingatiwa katika utekelezaji wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiufupi naomba niseme kwamba nakubaliana na michango ya Waheshimiwa Wabunge lakini kuna jambo kubwa ambalo nimejifunza kama Waziri wa Maji. Unapokuwa kiongozi kwa maana ya Waziri wa Maji, faraja yako na hata Waheshimiwa Wabunge ni kuona unazindua mradi wa maji. Unatamani uone tu vituo vya kuchotea maji, unatamani uone matenki ya maji, lakini lazima tukubali ndugu zangu Watanzania na Waheshimiwa Wabunge, kwani tuna maji kiasi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu kutoa historia fupi. Rasilimali za maji tulizokuwanazo juu ya ardhi na maji yaliyokuwa chini ya ardhi ni mita za ujazo bilioni 126. Bilioni 105 ni maji yaliyokuwa juu ya ardhi na bilioni 21 ni maji yaliyokuwa chini ya ardhi. Lazima tukubali kujiuliza, mwaka 1961 tulikuwa na Watanzania takribani milioni 10. Je, leo hii tuna Watanzania wangapi? Tuna Watanzania takribani zaidi ya milioni 60 na sensa bado haijatoa majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiufupi mwaka 1961 Watanzania wale milioni 10 rasilimali tulizokuwanazo, kwa maana ya maji yaliyokuwa juu ya ardhi, mito, maziwa na maji ambayo yalikuwa chini ya ardhi ukimgawia Mtanzania aliyekuwepo kipindi kile ambao ni milioni 10 alikuwa akipata 12,600 mita za ujazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunakadiria Watanzania zaidi ya milioni 60 bado sensa haijatoa takwimu, maana yake watu wameongezeka, tukiwagawia maji rasilimali ile ile tuliyokuwanayo, sasa hivi Mtanzania anapata 2,250. Nini maana yake? Tumetoka kumgawia maji 12,600, leo ni 2,200 na kitu. Tunatambua maji yakienda zaidi ya 1,500 na kitu, nchi yetu inaingia katika water crisis. Nini maana yake? Ambacho ninakisema na ninachokubali, rasilimali hii ya maji imeumbwa na Mwenyezi Mungu, lakini jukumu la kulinda, kutunza na kuendeleza ni letu sote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pale Mara imeandika: “Ukinipamba nitapendeza.” Hata mke usipompamba, hata kama ni mzuri namna gani, atakongoroka tu. Kwa hiyo, tunatambua kabisa rasilimali zimeumbwa na Mungu lakini tusiache wajibu wa kulinda na kutunza rasilimali zetu za maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mifano dhahiri kabisa. Leo Dar es Salaam tumeona kabisa tulivyoingia katika crisis ya maji. Mto Ruvu umekauka, umepotea, watu wanateseka, lawama imebaki kwa Serikali. Sisi kama viongozi tuna wajibu: Je, tuendelee kuumia katika maeneo kama haya? Kwa hiyo, lazima tuchukue hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, naomba tuelewane. Tunaweka sheria hizi siyo kwa ajili ya kuwaumiza watu. Tunaweka sheria hizi ili ku-control tu. Nataka niwaambie Wakurugenzi ambao wanasimamia mabonde ya maji, pamoja na sheria hizi ambazo tumezitunga, lakini tusiende kupeleka taharuki kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya yote tunayoyafanya, yapo mambo ambayo tumejifunza. Kabla ya haya, nilifanya ziara katika maeneo yote ya mabonde. Katika Wizara yetu tuna mabonde tisa, lakini katika kuyazungukia na kujifunza, nimejifunza mengi tu. Moja ni changamoto katika Wizara yetu na hata baadhi ya watendaji. Unaweza ukasema bonde la maji; nini maana ya bonde la maji? Bonde la maji jukumu lake ni kulinda na kutunza vyanzo vya maji. Je, mwananchi anajua hilo bonde? Mwingine anajua hilo bonde labda ni kilima kidogodogo. Kwa hiyo, kuna wajibu wa kutoa elimu kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kubwa ambalo nakubaliana nanyi Waheshimiwa Wabunge, jamii ipo tu siku zote. Ukiishirikisha utafanikiwa, usipoishirikisha utakwama. Nikiwa mwenye dhamana katika Wizara hii ya Maji, tutashirikisha jamii na tutawashirikisha Waheshimiwa Wabunge kama tulivyoishirikisha Kamati yetu na tumekubaliana na maoni yao ambayo tumeona yana maslahi kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge pamoja na Mheshimiwa Festo Sanga pamoja na sheria hii. Hatutakuwa kikwazo kwa Wana-Makete kuhakikisha kwamba wanafanya shughuli zao za kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa, lazima tukubali kwamba maji ni rasilimali ya Taifa. Lazima tukubali Waheshimiwa Wabunge kwamba maji ni usalama wa Taifa. Ukiwa na maji toshelevu, una uhakika wa nishati ya umeme; ukiwa na maji toshelevu una uhakika na kilimo cha umwagiliaji; unapokuwa na maji toshelevu una uhakika wa afya ya Watanzania; unapokuwa na maji toshelevu una uhakika katika shughuli za kiuchumi na hata ukiwa na maji toshelevu una uhakika wa kulinda ndoa za mama zetu. Kwa hiyo, hatuwezi kama Wizara ya Maji kupoteza ndoa za mama zetu katika kuhakikisha wanapata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa ambacho tumepata, tutaenda kukizingatia pamoja na hii sheria, na nioneshe commitment katika Bunge letu Tukufu ni suala la elimu. Hili tutalipa kipaumbele sana na kuwashirikisha wananchi. Tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo tumeliona ni kweli unaweza ukawa na mifugo na unawaambia kwamba wasinywe kwenye rasilimali za maji, ataipeleka wapi mifugo? Tumekubaliana kufanya kazi pamoja na Wizara ya Mifugo kwa maana ya uchimbaji wa mabwawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, ninyi nyote ni mashahidi. Wizara yetu ya Maji tumepata fedha nyingi na tumenunua mitambo kwa ajili ya uchimbaji wa mabwawa na tumeshaanza kupokea. Kwa hiyo, maeneo ambayo tunaona haya ni ya ufugaji tutachimba mabwawa, siyo kwa ajili tu ya maji ya kunywa, ni kwa ajili ya mifugo na kilimo. Kwa hiyo, hakuna sababu ya mfugaji leo kupeleka ng’ombe wake katika vyanzo vyetu vya maji. Kwa hiyo, kwa mwenendo huu tutaweza kuwasaidia wafugaji wetu na tutakuwa pia na kilimo cha uhakika katika kuhakikisha kwamba nchi yetu inaenda katika uchumi ambao tunautaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo tulilitolea ufafanuzi ni juu ya sifa za Wakurugenzi ambao wanateuliwa wanatakiwa wawekwe katika sheria kama dada yangu Mheshimiwa Nusrat anavyolizungumza. Sifa za msingi kwa mtu kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Bonde la Maji ni muhimu zikaainishwa kwenye sheria ili kuhakikisha kuwa sifa hizo zinaakisi malengo ya sheria na majukumu kama yalivyoainishwa kwenye sheria hiyo. Hivyo kifungu cha 24 kibaki kama kilivyo kwenye Muswada ili sifa zilizoainishwa kupewa uzito unaostahili katika utekelezaji wake kuliko kuweka katika kanuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyokuwa nimeeleza awali michango ya Wabunge tumeipokea na mingine tutawajibu kwa maandishi naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.