Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Rashid Ali Abdallah (5 total)

MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Baada ya majibu hayo, nitakuwa na swali moja tu la nyongeza

Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na malalamiko makubwa sana hasa kwa baadhi ya wanafunzi wenye familia masikini na wenye sifa za kupata mkopo huo, lakini wameshindwa kupata mikopo hiyo na kuendelea na masomo yao jambo ambalo linawadhoofisha wanafunzi wenyewe, lakini pia, linadhoofisha familia zao na Taifa kwa ujumla. Mheshimiwa Naibu Waziri anawaeleza nini wananchi kuhusiana na madai haya?
NAIBU WAZIRI ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ni kweli kabisa mikopo inayotolewa kwa sasa haiwezishi kuwapa wanafunzi wote wakiwemo watoto wa masikini. Hiyo ni kutokana na uhalisia kwamba nchi yetu inayo mahitaji mengi katika sekta mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, nachukue nafasi hii pia kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutambua tatizo hilo. Katika mwaka huu wa fedha tulikuwa na bajeti ya shilingi bilioni 306 tu, lakini baada ya kuingia kwake madarakani ameweza kuongeza shilingi 132, 299,067,500/= ambazo zimewezesha sasa kuwapa mikopo wanafunzi ambao walikuwa wanaendelea na wale ambao wanaanza mwaka wa kwanza. Mpaka sasa, jumla ya wanafunzi takribani 121,000 watafaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge kwa kutumia nafasi yetu hii ambayo sisi ndio tunaopitisha bajeti, nawaomba wakati wa bajeti ukifika tulipe kipaumbele eneo hili. Ahsante sana.
MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri, nitakuwa na maswali mawili kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, makundi ya Watanzania ambao wapo Ocean Road kusubiri matibabu ya ugonjwa hatari wa saratani, wagonjwa hao, ukifika pale Ocean Road utatokwa na machozi. Daktari hawezi kufanya matibabu kama hajafanya planning baada ya kuwekewa x-ray. Kuna mashine ya C-Arm ambayo ni mbovu haifanyi kazi. Hiyo ndiyo ambayo inamfanya daktari aweze kujua mgonjwa huyu ameathiriwa kiasi gani.
Je, ni lini Wizara itachukua hatua za dharura na za muhimu kabisa kuweza kuhakikisha mashine hii inafanya kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wapo watumishi katika Kitengo cha Saratani mmoja anaitwa Christopher; huyu amehamishwa Temeke; na mwingine ni Sefue ambaye amehamishwa Hospitali ya Amana. Hao walikuwa ni wataalam wazuri, wamesomeshwa katika Kitengo cha Mionzi. Watu hawa wamehamishwa, wamepelekwa katika Hospitali ambazo hawafanyi kazi wanayotakiwa kwa mujibu wa taaluma yao! Ni lini Waziri anayehusika atalifuatilia suala hili ili hatua zinazostahili zichukuliwe?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza hatua za dharura. Serikali tayari imekwishachukua hatua za dharura kufanya matengenezo ya mashine anayoizungumzia. Kwa maana hiyo, hapa ninapozungumza hakuna mashine hata moja ambayo haifanyi kazi pale Ocean Road. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, Serikali kupitia agizo alilotoa Mheshimiwa Waziri wa Afya, mara ya kwanza tu alipoenda kujitambulisha kwenye Hospitali hii, imetenga shilingi bilioni nne kwa ajili ya kukamilisha ununuzi wa mashine ya LINAC (Linear Accelerator) pamoja na CT Simulator ambayo inapanga utaratibu wa matibabu ya saratani kwa wagonjwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi hivi shilingi bilioni 2.5 zimeahidiwa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa ajili ya kuanza mchakato wa ununuzi wa mashine hizo. Hivyo, ile kero anayoizungumzia Mheshimiwa Rashid Ali Abdallah ya matibabu, tunaifahamu na Mheshimiwa Waziri alitoa machozi mara ya kwanza alipokuwa pale na ametoa maelekezo ambayo tunayatekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu hawa watumishi waliohamishwa. Ni kweli walihamishwa, lakini walihamishwa kwa taratibu za kiutumishi, suala hilo tunalifahamu na tayari tumechukua taratibu za kuunda Kamati Maalum ambayo inachunguza kama walihamishwa kwa fitina ama walihamishwa kwa taratibu za kiutumishi ambazo zilifuatwa. Kwa maana hiyo, kama itabainika kuna matatizo yalijitokeza tutachukua hatua za kuwarudisha.
Hata hivyo, kuondoka kwao pale hakujaleta upungufu wowote wa matibabu katika Hospitali ya Saratani ya Ocean Road.
MHE. RASHID ALI ABDDALLAH: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba kuuliza maswali mawili kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Chuo Kikuu cha Dodoma kilijengwa kwa mkopo wa shilingi bilioni 44.29 kutoka katika Mfuko NHIF bila ya kuwa na mkataba na bila ya uthinbitisho wa udhamini kutoka Serikalini.
Mheshimiwa Spika, swali langu, je, Serikali haioni kwamba imeshindwa kutekeleza jukumu lake kisheria?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kama Serikali imeshindwa kutekeleza jukumu lake jukumu lake kisheria haioni kwamba inasababisha upotevu mkubwa wa fedha za wanachama kama angetokea mkopaji yule si mwaminifu?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Spika, nikianza na swali la kwanza, kama nilivyoeleza pale awali katika majibu yangu ya msingi katika taratibu zote hizi za uwekezaji zinasimamiwa kwa miongozo ambayo ipo chini ya SSRA na BOT. Kwa sababu sekta ya hifadhi ya jamii inasimamiwa na SSRA, na upo utaratibu amabo SSRA umekuwa ukiufanya kuhakikisha kwamba yale madeni yote ambayo mifuko inaidai Serikali utaratibu umewekwa wa namna ya kuweza kuyalipa ili mifuko hii iendelee kuwa endelevu.
Mheshimiwa Spika, ndiyo maana katika majibu yangu ya awali nimesema kwamba actuarial evaluation ambayo inajumuisha pamoja na madeni yote, inaonesha kwamba mfuko huu bado unauwezo kuwa endelevu mpaka kufikia mwaka 2040.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la upotevu wa fedha za wanachama maelezo yangu ni yaleyale kama nilivyosema pale awali; kwamba katika utaratibu wa miongozo ambayo imetolewa na SSRA na BOT imetoa namna gani mifuko ifanye uwekezaji na baada ya tathimini kufanyika imeonesha kabisa kwamba mifuko hii bado endelevu. Nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hakuna upotevu wa fedha za wanachama, mfuko huu bado ni utakuwa endelevu sana.
Mheshimiwa Spika, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba kilichofanyika pale juu Dodoma ni uwekezaji mkubwa ambao una tija kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania. Kwa hiyo, hakuna upotevu wowote na Serikali katika hakuna jambo lolote kuonyesha upotevu. (Makofi)
MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali hili ni la muda mrefu sana kabla hata dhana ya kuunganisha Mifuko ilikuwa haijafikiwa, ndiyo linakuja leo. Pamoja na mambo hayo nitakuwa na swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, deni la trilioni 2.1 ndani yake kuna malimbikizo makubwa ya riba ambayo yamesababishwa na Serikali kwa kutokulipa kwa muda mrefu. Mifuko bado haijaunganishwa lakini riba haisubiri Mifuko kuunganishwa inaendelea. Ni hatua gani Serikali inachukua kuhakikisha kwamba Mifuko hii inaunganishwa haraka ili kunusuru riba hii isiongezeke? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba sheria tayari imeshasainiwa na Mheshimiwa Rais na kanuni zimeshakamilika. Ndani ya mwezi huu wa Tano Serikali inazipeleka kanuni kwa wadau ili tuweze kupata maoni yao na sisi kama Serikali tunatambua umuhimu wa kuiwezesha Mifuko kwa madeni yao haya, tuko tayari kulipa pale kanuni zitakapokuwa zimekamilika. Ahsante.
MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, niMshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake. Kama utafiti wa UNICEF - Tanzania ni sahihi kwamba akina mama 24 na watoto 144 wanafariki kwa siku na kwa mwezi kufanya idadi ya 5,040 na Serikali iliingia makubaliano mbalimbali ya Umoja wa Mataifa ili kuhakikisha kwamba wanaboresha huduma za afya kutoka asilimia 28 hadi asilimia 60 ili kuokoa watoto 102,000,000 na wanawake 16,000,000, je, ni kwa nini sasa Serikali imeshindwa kufikia makubaliano haya ya asilimia 60 ya huduma ya afya ili kuokoa maisha ya watoto na akina mama hawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali kwa sababu imeshindwa kufikia asilimia 60 ya huduma ya afya, ina mikakati gani ya makusudi kuweza kuimarisha ili kuondokana na vifo hivi vya watoto na akina mama?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Abdallah, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haijashindwa kufikia hayo makubaliano na haya niliyokuwa nayasema ni mlolongo wa utekelezaji wa maazimio hayo. Katika takwimu zangu nimeonyesha kwamba tunaendelea kupata mafanikio. Moja ni kwamba sasa hivi tumeongeza idadi ya akina mama ambao wanajifungulia kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma ya afya kutoka asilimia 50 – 73, haya ni mafanikio, akina mama wengi wanaenda kujifungulia katika vituo vyetu vyakutolea huduma ya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimesema kwamba akina mama wanaohudumiwa na wataalam wa afya wameongezeka kutoka asilimia 40 – 72. Sambamba na hilo, tumeendelea kuboresha mifumo mbalimbali ikiwa ni pamoja na vituo vya kutolea huduma za afya ili viweze kutoa huduma za dharura na uzazi na vituo zaidi ya 300 vimeboreshwa na kuwekewa vifaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tumezindua Mpango wa Tujiongeze Tuwavushe Salama ambapo Makamu wa Rais alizindua ukishirikisha Wakuu wa Mikoa na kila Mkuu wa Mkoa amepewa majukumu yake na kila Mkuu wa Mkoa ameenda kusimamia haya katika wilaya zake. Kama Wizara tumeanza kuchukua takwimu ambazo siyo rasmi lakini mwelekeo wetu unaonyesha kwamba vifo vya akina mama vimepungua sana ndani ya nchi.