Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Rashid Ali Abdallah (11 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha leo hii kusimama hapa, lakini pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Spika, Wabunge wengi ambao wamechangia katika Wizara hii walionesha umuhimu wa Wizara hii ya Afya na umuhimu wenyewe ni kuhakikisha kwamba Wizara hii ndiyo yenye jukumu la kuokoa maisha ya Watanzania. Sielewi kwamba Wizara hii inaona umuhimu hasa wa kuokoa maisha ya Watanzania na nasema hivi kutokana na kuangalia kwa mfano Hospitali yetu ya Taifa ya Muhimbili jinsi gani inavyopangiwa bajeti zake.
Mheshimiwa Spika, nitataja miaka mitatu ya nyuma; kuanzia mwaka 2013/2014 hospitali hii ya Taifa ya Muhimbili iliomba shilingi 84,991,000,000 na Bunge likapitisha shilingi 5,074,000,000, lakini Serikali ilitoa shilingi 2,184,000,000. Mwaka ulioendelea 2014/2015, wenyewe Muhimbili waliomba shilingi 113,025,000,000 Bunge likapitisha shilingi bilioni 3.8 na Serikali ikapitisha shilingi bilioni 1.29. Mwaka 215/2016, Muhimbili iliomba shilingi bilioni 118,993,000,000, Bunge lilipitisha shilingi 1,694,000,000 na hatimaye Serikali ikatoa nusu bilioni yaani shilingi milioni 553.
Mheshimiwa Spika, katika hali hii hospitali ambayo ni tegemeo kubwa la Taifa kila mwaka kushuka kwa bajeti yenyewe inadhoofisha huduma za matibabu kwa Wizara hii. Ukiangalia hospitali hii inakusanya maduhuli yake, mapato yake ya ndani, lakini mapato haya ya ndani wanayatumia kwa kuwatibu wale wananchi ambao wana msamaha, kwa mfano wazee, watoto ambao wapo chini ya miaka mitano na walemavu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuthibitisha hii ni kwamba, mnamo mwaka 2015 Hospitali ya Muhimbili imetumia bilioni 7.2 kwa wagonjwa 89,644 jambo ambalo limedhoofisha hospitali hii kuweza kufanya shughuli zao za muhimu ambazo walijipangia, wakati huo Serikali imechangia kiasi kidogo sana. Hii itaifanya Hospitali ya Muhimbili kushindwa tena kutoa huduma kwa watu wa aina hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende katika jengo la wagonjwa wa akili. Mheshimiwa jengo hili ni hatari sana, limefanywa kama vile gereza, kama vile halina maana. Jengo hili toka mwaka 1965 halijawahi kukarabatiwa, ni jengo ambalo halifai kukaa binadamu. Watu hawa ni wagonjwa, wametupwa kabisa na Wizara wamewasahau. Nataka Mheshimiwa Waziri ahakikishe jengo hili analifanyia ukarabati ili hawa wagonjwa ambao wapo katika jengo hili na wale watumishi wawe kama binadamu na wafanye kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukija katika Taasisi ya Upasuaji wa Moyo. Taasisi hii ni muhimu sana inaokoa fedha za kigeni. Ina vyumba viwili tu ambavyo vimejaa kabisa wapasuaji. Mheshimiwa katika hotuba yake, ukurasa wa 43, amesema kwamba: “Wizara itajengea uwezo Taasisi kwa kuweka vifaa ili chumba cha tatu kianze kufanya kazi.”
Mheshimiwa Spika, chumba hiki kinahitaji dola milioni mbili ambayo ni sawasawa na bilioni 4.28. Wizara hii imepangiwa bajeti kiasi ambacho kinasikitisha, ni kiasi gani Waziri atatuhakikishia kwamba chumba hiki cha tatu kinafanya kazi ili kuweza kuokoa fedha za kigeni na kuingiza fedha za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nije katika hospitali ya Ocean Road. Hospitali hii ni hatari sana, ni hospitali ambayo imepewa fedha shilingi milioni 399 kuweza kutoa huduma kwa wagonjwa, lakini wastani wa matibabu kwa mgonjwa mmoja kwa chemotherapy ni shilingi milioni moja hadi milioni mbili. Wagonjwa ambao wanaweza kutibiwa kwa fedha hizi ambazo zimetolewa ni wagonjwa takribani 200 mpaka 400, lakini angalia wagonjwa waliopokelewa kipindi hiki ni wagonjwa 3,512, hapa kuna ongezeko la wagonjwa 3100…
MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Kuna ongezeko la wagonjwa 3,100, hawana dawa, wagonjwa wa saratani, gonjwa la hatari, hawana dawa, waende wapi au wakatibiwe na nani? Serikali iangalie suala hili vizuri otherwise inasababisha kifo, pale kila saa moja anapita maiti. Nataka mtu aende pale, achukue muda wake, kila saa moja maiti inapita. Hospitali ya Ocean Road lazima iangaliwe vizuri.
Mheshimiwa Spika, pale kuna mkataba wa kujenga lile jengo la Shirika la Atomiki Duniani, lipo pale, wameshamaliza, bado kukamilisha matengenezo, Serikali imeshindwa kabisa kutoa fedha asilimia 74. Mashine moja ambayo inahitajika pale ni shilingi bilioni nane, wanataka shilingi bilioni 48 ili ziweze kuondolewa zile mashine mbovu na kuwekwa mashine nyingine mpya, Serikali imeshindwa na hawa watu wamevunjika moyo kabisa. Hii inaleta picha gani kwa Serikali?
Mheshimiwa Spika, naomba Waziri anijibu, jengo lile na mashine zile zitapatikana lini kwa sababu hawa tayari wameshavunja mkataba na fedha inayohitajika ni shilingi bilioni 48 kuweza kununua mashine hizi. Ni lini mtaweza kununua mashine hizi ili kuondosha vifo pale vinavyotokea bila sababu yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nije kwenye vifo. Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza vifo, vinasikitisha sana, tunapoteza nguvu kazi nyingi, akinamama na watoto, sitaki nielezee idadi, nataka nijue mwaka 2010 Serikali ya Tanzania iliingia katika mkataba katika nchi 260 za kuweza kutoa huduma bora kuanzia asilimia 28 mpaka asilimia 60 ifikapo mwaka 2015. Katika huduma hizo ni kuhakikisha vituo vyote vya afya vinapata mashine ya upasuaji na kupata damu bora ambayo ni salama. Pia kuhakikisha kwamba inaokoa akinamama milioni 16 ifikapo mwaka 2015, kama hiyo haitoshi ni kuokoa watoto ambao wanakufa milioni 120, ifikapo mwaka 2015.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2015 umepita, tunataka tupate maelezo, wamewaokoa akinamama wangapi kwa mujibu wa mkataba ule uliowekwa mwaka 2010, ni watoto wangapi wamewaokoa na ni vituo vingapi wamesambaza mashine za upasuaji pamoja na damu salama ili kuokoa maisha haya?
Mheshimiwa Spika, nirudi kwenye kero za madaktari wetu. Madaktari walifanya mgomo mkubwa na wakawa na changamoto nyingi, wanatakiwa stahili zao na mishahara yao, lakini hadi sasa tunaona kimya. Hawa hawajakaa kimya, wanaangalia utendaji wa Serikali, nadhani kuna siku watafumuka. Nataka Serikali kupitia Waziri itueleze stahili gani za madaktari wetu ambazo mpaka sasa wamezitekeleza katika maombi yao yaliyopita. Inasemekana kwamba madaktari wanaondoka wanakwenda nchi kama sikosei Berlin na kule wanapata mshahara kuanzia shilingi milioni tatu hadi milioni tisa za Tanzania…
SPIKA: Ya pili hiyo, Mheshimiwa Rashid.
MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Ahsante sana Mheshimiwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha leo hii kusimama hapa. Pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii. Leo nitakuwa na mada mbili tu kuhusu Wizara ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na nitaongelea masuala ya ajira pamoja na utawala bora.
Tatizo kubwa la watumishi wetu ni maslahi yao na siyo maslahi yao tu lakini pia ni kujengewa uwezo wa kazi zao. Wafanyakazi wanalipwa mshahara ambao haulingani na maisha ya sasa. Pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri alisema mwaka 2010 uliongezwa mshahara kwa asilimia 13.2 tatizo siyo kuongeza tu mshahara, je, mshahara unakidhi mahitaji ya lazima ya mfanyakazi, hilo ndilo swali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mshahara wanaolipwa, kiwango cha chini ni kuanzia shilingi 300,000 au 400,000 kwa wafanyakazi mbalimbali haufiki hata wiki moja. Wafanyakazi ambao wanautumia muda wao kuanzia saa moja mpaka saa tisa na anafika nyumbani saa kumi na moja afanye nini, hizi wiki tatu atafute wapi fedha za kuweza kuendesha maisha ya lazima, mfanyakazi huyo atatafuta njia ya kuweza kujisaidia. Nasema kwamba mtatumbua majipu mpaka mtatumbuana wenyewe kwa wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia watumishi ambao wanaondoka nchini na kwenda nchi za nje, Mheshimiwa Waziri hakuligusia suala hili katika hotuba yake. Tuna wataalam ambao tunawasomesha kwa fedha za umma ambao wanahitajika katika nchi, lakini baada ya kufundishwa na kupewa utaalam wa kutosha wanaondoka kwenda kujenga Taifa lingine. Ni vizuri Mheshimiwa Waziri uangalie upya suala hili ili uhakikishe watumishi hawa ambao ni wataalam wanajengewa vivutio ili kuwawezesha kuishi na kufanya kazi katika Taifa lao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni upungufu wa wafanyakazi. Kuna malalamiko kwamba zaidi ya wafanyakazi 16,443 na wale wa wakala 2,552 bado wanahitajika. Huwezi kutoa service kama hakuna wafanyakazi. Uchumi unajengwa kwa watu kufanya kazi. Leo nguvu kazi, rasilimali watu zaidi ya 16,000 ukiongeza na 2,500 almost 18,000 na zaidi wanahitajika, leo Waziri anasema anakwenda kufanya mchakato. Hapa hakuna haja ya kufanya mchakato, nenda kafanye mchakato katika Wizara yako utuambie ni lini utaajiri watu hawa waweze kufanya kazi katika Wizara na sehemu nyingine mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja katika utawala bora. Ninavyofahamu mimi utawala bora ni msingi mkubwa wa kuendesha Taifa. Utawala bora kama utausimamia vizuri hakuna haja ya kuhangaika kutumia nguvu, utawala bora unagusa kila maeneo ya nchi, kila mwananchi, kila kiongozi na kila mfanyakazi. Utawala bora ni kuheshimu Katiba na sheria ya nchi na ni kuheshimu demokrasia. Utawala bora ni kuheshimu utawala wa sheria na utawala bora ni kusimamia misingi mikuu ya uchumi na kuleta maendeleo ya Taifa. Utawala bora ni kusimamia haki na usawa na uwajibikaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sioni kwa nini tunapata kazi kubwa ya kupambana na watu kwa nini tusitumie nyenzo kuu ya utawala bora kujenga misingi mizuri ya kuendesha Taifa hili? Kwa vyovyote vile kama hatutadumisha utawala bora tutazorotesha uchumi na maendeleo ya jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba ni vizuri tuige kwa wale viongozi waliopita ili tujifunze walifanya nini. Kwa mfano, ukiangalia Waraka wa Programu ya Pamoja (Joint Program Documents), Rais wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa William Benjamin Mkapa alichukua suala la utawala bora kama mhimili mkuu wa utawala wake katika Urais wake. Mnamo mwaka 1999 alijenga mazingira ya nidhamu ili kuweza kurekebisha masuala ya uchumi na kuweza kuleta maendeleo ya Taifa. Sera na mabadiliko yalikuwa ndiyo nguzo kuu ya mwelekeo pamoja na kuhakikisha kwamba utawala bora ndiyo dira ya Taifa. Kwa kufanya hivyo, aliweza kubadili mfumo wa dola ya Afrika katika nchi zile za Jangwa la Sahara. Matokeo yake aliweza kualikwa na World Bank kuweza kutoa hotuba ni kwa vipi ameweza kubadili masuala ya uchumi na utawala bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunataka kutenda haki na kuleta uchumi wa nchi hii hakuna haja ya kutumbuana majipu kwa nguvu. Silaha yetu tuliyonayo ni utawala bora, kila mtu atawajibika kwa nafasi yake. Rais atawajibika kwa nafasi yake, Waziri atawajibika kwa nafasi yake na Wizara mbalimbali zitawajibika kwa nafasi zao. Tanzania leo kwa kukosa haya niliyosema ni nchi ya 51 ambayo inakosa sifa za utawala bora katika nchi 72 na itaendelea kuwa chini kwa sababu misingi ya utawala bora imekiukwa, wanawekwa Mashehe ndani bila kosa. Watu wa aina hii hawataweza kuleta maslahi yoyote nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho kimenishangaza tena sana na nitaendelea kushangaa ni Waziri anayehusika na Utawala Bora anasimama mbele ya Bunge kupongeza utawala haramu uliovunja Katiba ya nchi hii, hili ni tatizo kubwa. Zanzibar wamenyang’anywa haki yao, Waziri anakuja hapa mbele ya Bunge kusifu uvunjaji wa Katiba ya nchi, kunyang’anya demokrasia ya Wazanzibari, hili halikubaliki. Nasema Zanzibar itendewe haki yake na kamwe haki haikai chini, itakaa juu na mapambano yanaendelea hatuko kimya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili limetoa sura mbaya kwa Taifa na sura mbaya kwa Mataifa. Kukandamiza demokrasia ya wananchi ambao wamemchagua Rais wao waliomtaka na kuvunja Katiba na hatimaye kusaidiwa kupelekwa majeshi na zana nzito katika Visiwa vya Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanzazibar wameumia sana, lakini dhuluma haidumu, yana mwisho, kila kitu kitaonekana. Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu haki itaonekana ilikiukwa wapi. Asilimia 51.8 hawaitambui Serikali ya Shein, Serikali haramu, Serikali batili kabisa, tunasema waziwazi na tuna ushahidi wa kutosha kabisa.
MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasihi Waheshimiwa Wabunge wasome Katiba, hili ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nenda Sura ya Nne ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utaona kwa nini Zanzibar inazungumzwa. Hakuna hata mmoja aliyekuwa hajui, akiwa mtoto, mtu mzima na wanyama wanajua ukweli uko wapi na ukweli utaendelea kujulikana uko wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia niseme kwamba msaidieni Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba aspect 22 za utawala bora anazifuata vizuri. (Makofi)
Narudia, msaidieni Mheshimiwa Rais aangalie aspect 22 za utawala bora anazitekeleza. Hakuna haja ya kutumbua majipu, hakuna haja ya fujo, uongozi si mabavu, mabavu yamepitwa na wakati. Mabavu ya Rais ni kufuata Kanuni na utaratibu wa utawala bora, basi! Utawala bora umejengeka katika Wizara zote hata vijijini, nadhani tukifanya hivyo haki itatendeka. Hakuna amani bila ya haki. Kama mtu unamnyang’anya haki yake na ananyamaza kimya hana imani huyo na imani haipo. Ni kama ilivyo Zanzibar, Zanzibar hakuna amani. Amani siyo kupigana kwa mtutu wa bunduki, amani ni ndani ya roho yako. Ukiwa huna amani ndani ya roho yako ndiyo unaanza kufanya mashambulizi. Kwa hiyo, nasema Zanzibar hakuna amani, tunasema waziwazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uwezo leo hii kusimama hapa. Pia nakushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na kupongeza hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa jinsi ilivyoelekeza Serikali kwa mwelekeo wa mwaka 2017/2018. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nitazunguka katika maeneo machache kabisa kuhusu ulinzi na usalama wa taifa, utawala bora na uchumi wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yoyote duniani inaongozwa kwa kutegemea Katiba na Sheria. Ni hatari kubwa sana kuona Katiba na Sheria za nchi zinavunjwa wakati watawala wanasaidia na kufurahia. Narejea, Katiba na Sheria zinavunjwa katika nchi hii, watawala wanasaidia lakini pia wanafurahia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri zaidi ni uchaguzi haramu wa Zanzibar wa Machi, 2015. Uchaguzi huu ulivunja Katiba ya nchi, viongozi walifurahia na wamesaidia, lakini tunasema mapambano yanaendelea, haki ya Zanzibar tutaidai na tunaendelea kuidai na itapatikana kwa hali yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vitendo vya uvunjaji wa sheria kwa Msajili wa Vyama Siasa, Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ni Kamati ya Bunge, inapofanya kazi Kamati ya Bunge ina maana Bunge zima linafanya kazi. Taarifa za Kamati ya Katiba na Sheria inaweka wazi kwamba Msajili
wa Vyama vya Siasa amevunja Sheria za Vyama vya Siasa na kuingilia uhuru wa vyama vya siasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni taarifa ya Bunge na taarifa ya Bunge inakemea kitendo hiki cha Msajili wa Vyama vya Siasa. Kauli hii ni ya Bunge, siyo Kamati ya Katiba na Sheria.
Waheshimiwa Wabunge wote lazima mwone hili lipo na limekemewa na Kamati ya Katiba na Sheria. Kwenda kinyume kwa Msajili kwa vitendo hivi, atakwenda kinyume na taarifa za Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hiyo siikubali na Kamati ya Sheria ilimwita Msajili, ikamhoji (ukurasa wa 30 naendelea kusoma) na ikamwonya Msajili huyo. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba masikitiko yangu na nitaendelea kusikitika sana kuona Jeshi la Polisi linashiriki kisiasa wazi wazi na kuleta hujuma na kuvunja sheria wakati Jeshi la Polisi linalinda uvunjaji wa sheria. Nalaani sana vitendo hivi. Watu wote mnafahamu, mnajua na mnaona, halihitaji ushahidi, Serikali imenyamaza kimya. Hii nasema ni mkakati wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi limepoteza mwelekeo kwa wananchi na litaendelea kupoteza mwelekeo kwa wananchi kwa sura hii, tutakuwa hatuna imani kabisa na Jeshi la Polisi. Na mimi nilishasema, sitaki kuchangia Jeshi la Polisi, sina imani kabisa na Jeshi la Polisi.
Baadhi ya Jeshi la Polisi wanavunja sheria, Serikali ipo inayamaza kimya, wanashiriki uvunjaji wa majengo ya chama, Jeshi linalinda na linaangalia tu bila kuchukua hatua yoyote. Kitendo hiki ni kibaya sana kwa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Msajili pamoja na washirika wake mlivunja Katiba ya Vyama vya Siasa na mlivunja Sheria za Usajili. Kwa kufanya hivyo, amevunja msingi mkubwa wa utawala bora na kwa misingi hiyo, amevunja demokrasia nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba Msajili ajue, matokeo yake ni nini? Matokeo yake ataliingiza Taifa hili katika mgogoro mkubwa kwa Muungano wetu, lakini atahatarisha amani ya Taifa hili, la tatu, ataingiza Taifa hili katika mgogoro wa kiuchumi. Mnalifurahia lakini matokeo
yake mtayaona mbele tunakokwenda. Kwa kufanya haya, uchumi wetu utadorora, ndani na nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende haraka haraka kuhusiana na masuala ya uchumi. Sekta za uzalishaji mara nyingi zinakuwa ni sekta za kiuchumi na kwa maana hiyo kuna nchi nyingi ambazo zimejikita katika maeneo mahsusi ya kiuchumi, kwa mfano, nchi ya Afrika Kusini imejikita katika biashara, madini na utalii; Algeria mafuta na uzalishaji; Nigeria mafuta na mawasiliano, Morocco utalii, viwanda vya nguo pamoja na kilimo. Tanzania kuna msururu kabisa, series!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania kuna series za mambo ya kiuchumi, kuna kilimo, viwanda, maliasili, madini, gesi, usafirishaji and so on and so forth. Kilimo kinawakilishwa kwa asilimia 75 na Watanzania, kilimo kinabeba Watanzania wengi sana, lakini awamu hii inaelekea kana kwamba kilimo siyo kipaumbele chake hasa, kina viashiria hivyo. Nasema hivyo kwa sababu mwaka 2015/2016 Serikali iliyopita ilitoa pembejeo za kiasi cha shilingi bilioni 78, lakini Serikali hii hadi kufika hapa imetoa pembejeo za shilingi bilioni 10. Kutoka shilingi bilioni 78 mpaka shilingi bilioni 10, hivi kweli Serikali hii inawaambia nini wakulima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kusema kwamba kilimo kinaanza kushuka na kwa sababu hakuna mbolea ya kutosha ambayo imetolewa na Serikali, tutegemee upungufu mkubwa wa mazao katika kipindi kinachofuata. Hili litakuwa ni tatizo kubwa kweli kwa wananchi walio wengi wa
Tanzania.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha leo hii kusimama hapa. Mchango wangu wa leo si mkubwa nitazungumza mada fupi kwa sababu tayari nilishachangia kwa maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo langu kubwa ambalo naliona katika kilimo ni wakulima wadogo wadogo, Wabunge wote wanawaona wanavyohangaika katika kilimo; mvua, jua, usiku na mchana na mazao yao tunayaona barabarani yanavyooza. Huu ni mtindo wa kila mwaka. Wakulima wanalima wanatumia nguvu zao jasho lao ni maskini kabisa, lakini hatimaye mazao yao yanapotea ovyo. Serikali wanaona, Mheshimiwa Magufuli Rais, alikuwa ni Mbunge alikuwa anapita barabarani anaona mazao yanavyooza lakini amechukua hatua gani? Soko liko wapi la wakulima?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri kama anataka kutumikia Taifa hili kwa kilimo tafadhali awajali wakulima wadogo wadogo. Wakulima wadogo wadogo ndio wanaoleta maendeleo ya Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika Uvuvi wa Bahari Kuu. Uvuvi wa Bahari Kuu kwa taarifa za Waziri kwamba wanatoa leseni kwa dola elfu 50 kwa mwaka. Meli zinakwenda kuvua huko kwa samaki wanaotaka wenyewe na wale wa ziada wanawapoteza, kuna meli za uvuvi mia moja na tano kwa taarifa ya Waziri. Wanavua bahari kuu wanachukua samaki wanaowataka wa ziada wanawapoteza. Serikali ina utaratibu upi wa kuweza kulinda mazao haya ambayo yanaingiza fedha za kigeni kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imetulia kimya Waziri mwenyewe anasema, anawaagiza, samaki wa ziada mlete juu kama vile ni kampuni yake. Kuna sheria ipi ya kuhakikisha samaki wale wa ziada wanaletwa huku katika nchi yenyewe. Kwa hiyo, wanakwenda katika vyombo vya habari anazungumza na Waandishi wa Habari, anawaambia samaki wa ziada leteni nchini huku. Hasa watu watoe meli zao huko deep sea walete huku nchini wapoteze mafuta yao bure, kuna utaratibu upi ulioweka Mheshimiwa Waziri kuweza ku–save mapato haya ya Serikali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, kuna masuala haya ya migogoro ya wakulima, migogoro hii inazidi kukua kwa Wakulima na Wafugaji. Tuna hekta milioni 88. Kati ya hekta milioni 88 kuna hekta milioni 60 ambazo zinafaa kwa wafugaji. Hata hivyo, unit tulizonazo za ufugaji ni unit bilioni 20 lakini mahitaji yetu ni unit 17.1 tuna tatizo gani la kuweza kuondoa mzozo huu wa wakulima na wafugaji. Kwa hiyo Serikali imetulia kimya tu. Mmechukua hatua gani watu wanauwana, mifugo inakufa, mizozo yao hii haishi. Uwezo wa kuweza kuyatatua tunao, kitakwimu tunafanya kazi.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ana dhima kubwa ya kuhakikisha kwamba mizozo hiyo ya wakulima na wafugaji wakishirikiana na Wizara nyingine inatatuliwa ili ku– ave maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala ya mbolea, Serikali hii imekuja na dhana ile ya viwanda na kila ninavyoona ninavyopima tafsiri ya kilimo kwanza imeondoka. Kwa hiyo dhana iliyopo ni ya viwanda, sasa matokeo yake ni nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2015/2016, Awamu iliyopita ilitoa mbole na pembejeoyenye dhamani ya bilioni 78, lakini mwaka 2016/2017, Awamu ya Mheshimiwa Rais Magufuli wametoa bilioni 10 hii inaonekana kama ni dharau hivi! Bilioni 78 ambapo wakulima wenyewe wamelalamika kwamba hazikutosha, leo Serikali hii imeweka bilioni 10, is nothing. Hii ni dharau kwa wakulima, kama hukutia mbolea basi mazao yatapungua. Mvua tumepata za kutosha lakini mvua pekee hazitoshi, lazima tuzi-support na mbolea na nina imani kwamba mazao kipindi yatapungua kwa sababu mbolea kipindi kilichopita haikutosha, wala haikufika kwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi ya chakula; wakulima wamelima kipindi kilichopita na kwa bahati nzuri wakapata mazao mengi, wakazuiliwa kabisa kusafirisha mazao yao nje. NFRA wakanunua mazao tani milioni 13 something ambazo zina thamani ya bilioni sita. Zimekuwa declared kwamba zimeharibika kwa mvua kwenye maghala. Waziri mwenyewe anasema katika maelezo yake kwamba zile tani hazikuharibika, ni watu wamefanya michakato yao tu. Waziri anajua, amechukua hatua gani kwa watu hawa?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ya Serikali imepotea bilioni sita (6) na zaidi, mazao ya wakulima yamenunuliwa na yalizuiliwa kupelekwa nje, wakulima wamepewa fursa zote halafu wahuni wanasema yamenyeshewa na mvua lakini hadi sasa hakuna hatua iliyochukuliwa. Mheshimiwa Waziri nataka kujua fedha ya umma iliyoharibika kwa uzembe wa stoo hizi za NFRA na kupoteza bilioni sita, watu hawa wamechukuliwa hatua gani?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba, kama tutakwenda hivi katika kila Wizara kama haipo serious na nguvu za wakulima haipo serious na kuwasaidia wakulima, haioni huruma, nataka Waziri hebu tumpe hekta moja tu au robo heka tu aende akalime, amwagilie maji avune mazao yake, halafu mazao yale yaharibike arudi tena mwaka wa pili alime tena na hakuna support yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la wafugaji, mara hii tumeona kwamba ng’ombe wengi wamekufa, lakini Mheshimiwa Rais Magufuli anawaambia nendeni mkauze ng’ombe akauze wapi ng’ombe? kwani ng’ombe wanauzwa vipi. Ng’ombe wanakufa kila maeneo hakuna malisho, lakini sasa hizi mvua zinavyonyesha utakuta majani yamezagaa tele, hakuna utaratibu wa ku-process majani yale. Kuna mashine nyingi unavuna majani unaweka katika stoo wakati wa kiangazi Serikali inapata mapato wanauzia wakulima ambao hawana majani, majani mashambani yanapotea bure.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashine ya kuyasindika majani yale ziko tele na ni rahisi. Serikali imekaa tu, fedha ile pale na ng’ombe wanakufa, mifugo inakufa, watu wametulia hapa, wanakwenda huko na kurudi, tujenge raslimali yetu kwanza, tutunze rasilimali yetu, tutunze kilimo, tutunze mifugo, zile initiative tulizonazo tuzitumie hizo kwanza usianzishe viwanda vikubwa lakini viwanda vidogo vya wakulima huku wanakufa, wewe unaanzisha viwanda vikubwa tu, what for ? Maana yake nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira ya kilimo ni asilimia 65.5 kwa mujibu wa taarifa zako, wengine wanasema asilimia 75 sijui who is wrong kama Waziri yuko sahihi au tuzungumze hapa, lakini vyovyote itakavyokuwa ni kwamba sekta ya kilimo inabeba Taifa. Kwa sababu inabeba Taifa Sekta hii ya kilimo nguvu za Awamu hii ya Tano ziko wapi, hatujaziona, tunasikia zimeagizwa matrekta lakini, hebu kwanza tuimarishe kilimo. Kilimo ndiyo uti wa mgongo wanasema, kilimo ndiyo maisha.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wako mwingi wa Bunge hili umetumika zaidi kwa kujadili makinikia, na zaidi ya hilo umekwenda mbali zaidi kwa kuwataja Mawaziri ambao walifuatia, kuwataja wanasheria ambao walipita. Kufanya kitendo hiki cha kuwataja Mawaziri au wanasheria waliopita kisheria hasa sio sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameteua Kamati yake, na ameelekeza nini cha kufanya muache Rais afanye shughuli zake, sisi tujadili hotuba ya Bunge ambayo ni bajeti. Cha msingi ni kuhakikisha kwamba sheria zote za madini, maliasili na sehemu nyingine zote zinafumuliwa upya na kufanywa vizuri na kupitiwa mikataba mbalimbali ili tujue tunaanza wapi katika kuleta uchumi huu wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo niseme kwamba bajeti ni mpango maalum wa kupanga mfumo ule wa mapato na hatimaye kuweka matumizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha msingi baada ya kukusanya ni matumizi, Mheshimiwa Waziri nitamnukuu katika ukurasa wake wa 14 anasema ifuatavyo; “Nidhamu ya hali ya juu katika matumizi lazima isimamiwe kwa nguvu zote ili kuhakikisha tathmini ya fedha inapatikana” lakini pia aliendelea; “kutokufanya matumizi pasipokuwa na kasma iliyoidhinishwa kwenye bajeti husika katika fungu husika.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri hapa amesisitiza nidhamu ya matumizi, mwaka jana tulikusanya 70.1% lakini Wizara zote zinalalamika hazina fedha za maendeleo, sasa fedha hii imetumika wapi, je, Waziri amekuja kutuambia kuna tatizo wapi, kwa nini Wizara zisipate hela za kutosha, kwa mfano, Wizara ya Kilimo 3.8%; Chuo Kikuu Dar es Salaam 0%; Wizara ya Maji 8%. Katika mwendo huu ni dhahiri kwamba kulikuwa hakuna nidhamu ya matumizi ya fedha za Serikali. Na nasema kwamba nidhamu lazima ianze juu ije chini, nidhamu ikianza chini isiende juu haina maana yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sidhani kwamba matumizi yaliyofanywa kwa mji kuhamia Dodoma ilikuwa budgeted, sifikirii kama hii ilipita katika bajeti. Na hii ndio iliyotikisa bajeti hii kufikia Wizara zote hazina fedha, kwa hiyo, nidhamu ni lazima ijengwe kutoka juu kwanza, halafu chini ifuate. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika suala la utekelezaji wa bajeti. Kuna kasoro kubwa, bajeti mara hii ya maendeleo ilitekelezwa kwa 35% mpaka 40% na nchi haihesabiwi kama ina maendeleo mpaka itekeleze miradi ya maendeleo. Lakini OC 80% na maendeleo 35% mpaka 40%, Wizara haijatuambia ni kwa nini bajeti hii hata masuala ya maendeleo hayakupita vizuri, hawajatueleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika vipaumbele. Mheshimiwa Rais ailipohutubia hapa alisema atahakikisha anafuata maelekezo yote ambayo viongozi wengine walipita, ni vizuri ninukuu anasema katika hotuba ya uzinduzi wa Bunge la Kumi na Moja mwaka 2015 Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alieleza Watanzania kwamba; “vipaumbele vya Serikali kuhusu uchumi ni kuendeleza na kuimairsha misingi imara ya uchumi wa nchi iliyojengwa katika awamu ya uongozi uliotangulia.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi bado nina wasiwasi Serikali hii ya Awamu ya Tano imetoa kipaumbele zaidi na msukumu mkubwa zaidi kwenye viwanda lakini msukumo mdogo kuja kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kinaongeza pato hasa mifugo 4.4% na nasema kwa mfano FAO ilifanya utafiti na ikesama kwamba kama Mtanzania atakula nyama kilo 11 kwa mwaka ambapo kwa mwezi ni kilo moja au atakunywa maziwa lita 45 kwa mwaka ambapo kwa mwezi ni lita nne, au atakula mayai 72 kwa mwaka ambapo kwa mwezi ni mayai sita basi tutakusanya shilingi trilioni 20. Hii ni sehemu ndogo tu, lakini pia Misri na Zambia ilitaka kununua nyama Tanzania tani 50,000. Lakini Tanzania ilikuwa inazalisha tani 23,000, nchi ziko tayari kununua tani 50,000 sisi tuna tani 23,000, ng’ombe wanakufa, mifugo wanapigana na watu huko, nini soko la wakulima? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania inapoteza fedha hizi. Sasa ninasema wakulima elimu yao ni kilimo, maskini matibabu yao ni kilimo, maskini afya zao ni kilimo, leo Wizara haijapewa kipaumbele na Wizara hii ya kilimo. Tumepewa kipaumbele viwanda, viwanda hatujajua changamoto zipi, kilimo tumezoea changamoto zake, mwaka 2015/2016 awamu iliyopita Rais Kikwete alitoa pembejeo zenye thamani ya shilingi bilioni 78, lakini Mheshimiwa Magufuli kipindi cha mwaka 2016/2017 alitoa pembejeo shilingi bilioni 10, kutoka shilingi bilioni 78 mpaka shilingi bilioni 10 hii maana yake nini? Maana yake nyingine kwamba hana habari na kilimo, 65% ni kilimo, hii sekta kubwa ambayo inaajiri Watanzania, ni sekta ambayo sasa tunaipa mgongo tunakwenda kwenye viwanda hatujui changamoto zake zikoje. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri ni lazima ukitaka tusitake kilimo ndio asili yetu, wewe hukuwa na profesa umekwenda kwenye kilimo, watu wote waliosoma hapa wamesomeshwa na kilimo, leo kilimo unatoa shilingi bilioni 10. Kwa hiyo hii kilimo sio mvua tu, kilimo mvua na pembejeo, pamoja na dawa za kilimo ili kuimaisha kilimo kiwe viruzi zaidi na kilimo cha biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii haiwezekani kabisa kuvumilika ni lazima tubadilishe mwelekeo turudi kwenye kilimo kwanza.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
MHE. RASHID A. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia leo hii kusimama hapa nikiwa na afya. Pia, nakushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TAMISEMI ndiyo roho ya nchi hii na Watanzania wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wote wamo kwenye TAMISEMI. Nachukua fursa hii, katika uhai wangu wa miaka nane sasa ya Bunge, kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na Naibu Mawaziri wake kwa kazi ambazo wanazifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, natoa ushauri kwamba wale Wakurugenzi wa Halmashauri wapewe nafasi ya kupewa zawadi maalum kwa wale wanaofanya vizuri na kama inawezekana kwa kila bajeti waweze kutangazwa Wakurugenzi ambao wamefanya vizuri katika Halmashauri zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ni pongezi tu. Leo nitahamia kwenye utawala bora zaidi. Duniani kote tunahitaji utulivu, amani na demokrasia ya kuendekeleza uchumi wa Taifa. Kama hatutaweza kudumisha utawala bora, hatutaweza kabisa kuendesha Taifa hili. Utawala bora kwa tafsiri yake, umeenea kila pembe ya Taifa hili. Kwa umuhimu wa utawala bora, nimeamua leo nijikite kwa makusudi kujadili kwa undani zaidi kuhusu shughuli za Serikali yetu juu ya utawala bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa umuhimu wa utawala bora ndiyo maana katika Dua yetu tunayoliombea Bunge na Taifa huwa tunasema “Mjalie Rais wetu pamoja na wanaomshauri wadumishe utawala bora.” Hii imeingizwa katika Dua ili wanaomshauri wawe karibu kumwambia Rais ajitahidi kusimamia na kutekeleza utawala bora katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, niseme utawala bora ni kusimamia Katiba na Sheria ya nchi. Utawala bora ni kusimamia utawala Sheria; ni kusimamia demokrasia ya kweli; ni kusimamia misingi mikuu ya uchumi ili kuendeleza Taifa hili; na kusimamia haki, usawa na uwajibikaji. Tukifika hapo sote, basi tutakwenda vizuri, wala hakutakuwa na mivutano katika Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba yetu sasa kuna dalili zote za kuchezewa chezewa. Demokrasia hasa ya vyama vingi inapigwa vita na kushambuliwa kabisa. Yote haya yanaleta athari kwa Taifa letu. Kwa maana hiyo ile kasi ya maendeleo ya haraka inakwama sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu kwa heshima yako nisome maelezo ya aliyekuwa Mheshimiwa Waziri wa Utawala Bora wa 2014 na 2015 Mwenyekiti wangu Mheshimiwa Mkuchika. Alisema hivi, migogoro ya ardhi, mauaji ya albino na vikongwe, wananchi kujichukulia sheria mikononi, rushwa pamoja na ujangili, vimesaidia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa Tanzania katika kiwango cha utawala bora duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aliendelea kusema kwamba Tanzania ilikuwa ikishika nafasi ya 10 katika miaka miwili iliyopita na kuongeza kwamba kuporomoka huko kumekithiri kwa ukiukwaji wa haki za binadamu. Aliendelea kusema kwamba duniani tuko katika nafasi ya 102 kati ya nafasi 176. Hii ni nukuu ya Mheshimiwa Mkuchika alipokuwa Moshi alipokuwa akitoa maelezo yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimenukuu haya nikiwa najielekeza katika kitabu cha Mheshimiwa Mkuchika, kuona ni kiasi gani ameeleza katika kitabu chake hiki kuhusiana na matokeo mbalimbali yaliyotokea nchini mwetu. Jambo la kusikitisha kabisa katika ukurasa wa 112, alieleza mistari miwili tu tena katika majumuisho. Kwa hiyo, sidhani kama ile Dua tunayosoma, sijui kama inatakabaliwa au kuna wachawi humu ndani au vipi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na makundi yanayofanya utekaji. Makundi haya toka yateke watu sijaona hata siku moja mtu mmoja kufikishwa Mahakamani. Nchi ambayo ina usalama wa uhakika na wa kuaminika kabisa, ni juzi tu vijana wetu kule Mtambwe sita walitekwa wakaenda maeneo yasiyojulika, wamerudi watatu wako taabani, wamepigwa na kuteswa na watatu hadi leo hawajaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utesaji na uuaji. Vitendo hivi vingi vinatokea sana katika nchi ambazo zina dalili ya kukosa utawala wa sheria. Vitendo hivi vya kivamizi ni ukiukwaji mkubwa wa sheria, ni uvunjaji wa amani na ni kinyume na haki za binadamu na utawala bora. Watu mbalimbali wanaotekwa hutekwa kwa sababu ya maoni yao au kujieleza kwao; na haki hii imelindwa chini ya Katiba ya Ibara ya 18; lakini haki hii pia imelindwa chini Mikataba ya Kimataifa Ibara ya 19 inayoshughulikia haki za kiraia na haki za kisiasa za mwaka 1986. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia haki hii imelindwa katika Ibara ya (9) ya Mikataba ya Kimataifa kuhusu Haki za Binadamu ya mwaka 1986. Kwa hiyo, sioni sababu yoyote kama kuna watekaji wanaowateka Watanzania, kuna wauaji wanaowaua Watanzania, hakuna hata mmoja aliyehojiwa na kupelekwa Mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza hapa, hatuzungumzi kwa vyama, tunazungumza kama Wabunge na tunapozungumza hapa, tunaiambia Serikali, wanakoelekea ni kubaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhuru una mipaka yake, lakini pale anapoonekana mtu amekwenda kinyume na sheria yoyote nyingine, sheria ichukue mkondo wake. (Makofi)

Hivi sasa kuna watawala, kuna wanasiasa hasa Wapinzani, kuna Wanahabari, kuna vikundi vya dini, kuna wafanyakazi...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Kumi na Moja wa Bunge
MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, jina langu lilikuwa ni Rashid Ali Abdallah.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Pia, nishukuru kwa wasilisho lililotolewa na Mwenyekiti wangu na kufahamika vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge ndicho chombo pekee cha kutunga sheria na mara baada ya kutunga sheria, sheria hii lazima iende ikatekelezwe, na utekelezaji wa sheria hii kunahitajika kuandaliwa kwa kanuni chini ya Ibara ya 97(5) ya Katiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesikia jinsi uchambuzi ulivyotolewa na hiyo ndiyo hali halisi ya baadhi tu ya sheria, kanuni ambazo zimeletwa katika Bunge hili. Kwa utaratibu sheria zinatungwa huko zinakotungwa, aidha, Waziri au Wizara yake, lakini zinapitia kwa Mwanasheria Mkuu halafu baaday ndipo zinatangazwa katika Gazeti Rasmi la Serikali na kupewa GN. number. Sheria hizi baada ya hapo zinaendelea kutumika kabla ya kupita kwenye Kamati hii ya Sheria Ndogo. Kwa hiyo, tutaona hapa sheria chache tu ambazo zimewasilishwa kwenye Bunge zina makosa ambayo yamekwenda kinyume na Katiba ya nchi, zimekwenda kinyume na sheria na hata zimekwenda kinyume na haki za binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utaona trend ilivyo, kwamba sheria ngapi zimepita hapa na sheria ngapi ziko nje zinatumika kimakosa na kwa maana hiyo, tunasema kwamba, sheria hizi nyingi ambazo zinatungwa watungaji hawana uangalifu wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kama ni Halmashauri basi tunao Wanasheria wa Halmashauri, zikitoka kwenye Halmashauri zinakwenda kwa Waziri, zikitoka kwa Waziri zinakwenda kwa Mwanasheria Mkuu, lakini bado makosa yanakuwa makubwa, yanakuwa kinyume na Katiba. Kwa hiyo, tunaona ni jinsi gani kazi inavyofanyika na jinsi gani wananchi wanaumia huko vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba kama tunabadilisha sheria, Kamati imependekeza sheria ibadilishwe, lakini bado sheria inatumika huko, kwa hiyo huu ni mzunguko. Kwanza uende ukabadilishe sheria, sheria inaendelea kutumika, kwa hiyo haileti maana halisi. Mimi nadhani huu ni mfumo wa Serikali kuweza kutumika sheria kabla ya kupita kwenye Kamati, lakini kuna haja sasa ya mfumo huu kutazama upya kwa sababu, sheria inaumiza wananchi, lakini inatumika na baadaye ndipo sheria inakuja kwenye Bunge na hiyo sio sheria zote ni baadhi tu ya sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, angalia hizo sheria ambazo ziko huko ni kiasi gani zinakandamiza wananchi hawa? Kuna mazao, ulipaji wa kodi ya mazao, kuna masuala ya uendeshaji wa shughuli mbalimbali za biashara zao, kuna kanuni hizo zinaendelea kutumika, basi wanyonge huko ndio wanaoumia zaidi. Sheria hizi ni za nchi nzima, kila unapokwenda ziko sheria hizi ndogo zinaendelea kutumika na zinaendelea kwa sababu kuna sheria mama inatekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina wazo kwamba kwa mujibu wa Katiba Bunge limekasimu madaraka kutunga hizi kanuni, lakini hao ambao wanatunga hawako serious, na makosa haya yataendelea kuwepo.

Mimi nilisema kuna haja ya kubadilisha mfumo huu, sheria zile ambazo ni very serious au ni emergency majesty, ni haraka sana, zinaweza zikaenda, lakini zile sheria ambazo hazina umuhimu sana kabisa, basi ni lazima zipitie kwenye Kamati ya Sheria Ndogo, ili kuhakikisha kwamba, ziko sahihi; lakini tukiendelea na mfumo huu bado Wananchi wataendelea kukandamizwa na hakuna mtu wa kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano hata Serikali nayo inapata matatizo, kuna uendeshaji wa shughuli za petroli. Kama unaendesha shughuli za petroli lazima uwe na kibali, na sheria inasema kama huna kibali basi ni faini isiyopungua shilingi milioni 20. Hata hivyo kanuni inasema kama utaendesha shughuli hizi za petroli bila kibali ni faini ya shilingi milioni tano. Kwa hivyo, hapo tunaona Serikali imepeta hasara kiasi cha shilingi milioni 15 zimeondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kanuni inasema milioni tano; na hiyo, sijui kama imeletwa wakati gani kwenye Bunge. Kwa hiyo, ni kusema kwamba Serikali pia inakosa mapato, lakini pia wananchi nao pia wanakandamizwa na sheria hizi kwa sababu zinakuwa ni kinyume na Katiba na hata pengine wakaenda Mahakamani sheria hizi hazina support yoyote, zinafutwa na kwa maana hiyo ni kupoteza nguvu ya Serikali, kupoteza nguvu ya Wananchi wenyewe walioshitakiwa na haileti tija yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi pendekezo langu ni kwamba, sheria hizi zinagusa Wabunge wote katika majimbo yao na Halmashauri zao. Kuna haja ya kubadili mfumo ili kuhakikisha sheria kwanza zinathitishwa ziko sahihi, lakini pia, ninachokisema mimi na kinachonisikitisha kabisa ni kwamba, kwa nini sheria inapita kwa Mwanasheria Mkuu? Kwa nini sheria inapita kwa Mheshimiwa Waziri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri anakuja kwenye Kamati basi haelewi ni sheria ipi anakuja kui-defend. Sasa sijui hizi sheria zinakwendaje, hawaeleweki; Waziri unamwambia funua ni sheria gani, anamuuliza Katibu Mkuu, haelewi. Kwa hiyo Mawaziri hawako serious na masuala haya, Mwanasheria Mkuu pia katika ofisi yake hawako serious na katika Halmashauri, Wanasheria wa Halmashauri hawako serious. Kwa hiyo, hii mamlaka waliyopewa hawaietendei haki ni vizuri turudie katika mfumo ambao ni sahihi. Nakushukuru sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiisikiliza kwa makini taarifa ya Kamati ya Bajeti na ukawasikiliza kwa makini wachangiaji mbalimbali utaona kwamba wanatilia mashaka bajeti yetu hii. Mimi nasema kwamba nina mashaka makubwa sana kuhusiana na bajeti yetu hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia bajeti hii vipaumbele vyake havitoshelezi. Nasema hivi kwa sababu Mheshimiwa Waziri wakati akiwasilisha hotuba yake alisema uchumi umepanda kwa asilimia 7, jambo ambalo ni mashaka makubwa sana. Kama uchumi umepanda, tukija kwenye kilimo, kilimo kimekua kwa asilimia 3.7, ambapo ili uweze kupunguza umaskini kwa wakulima ni lazima kilimo kipande angalau kwa asilimia 8 hadi asilimia 10. Sasa tuna asilimia 3.7 kwa miaka kumi, Mheshimiwa Waziri anasema uchumi umepanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna barabara kilometa 86,472 lakini barabara za lami ni asilimia 9.7 tu, lakini tunaambiwa bado uchumi wetu umepanda. Tunahitaji megawati 3,000 lakini tangu nchi hii ipate uhuru tuna megawati 1,424.6, bado tunahitaji megawati 1,575.4 ili tufikie mahitaji yetu. Sijui ni miaka mingapi tunahitaji ili tufikie lengo hili kwa sababu hizi megawati 1,400 tumechukua miaka 57, sasa megawati 1,500 tutachukua miaka mingapi? Sidhani kwamba katika Bunge hili tutakuwepo na sidhani kwamba CCM itakuwepo katika madaraka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali Kuu ilitakiwa ikusanye shilingi trilioni 19 lakini imekusanya shilingi trilioni 14, huu uchumi umepanda vipi? Halmashauri zetu zinatakiwa zikusanye Sh.687,304,000,000, zimekusanya Sh.437,607,000,000 ambapo tofauti ni shilingi bilioni 249.699, ni nusu yake. Sidhani hawa wataalam ambao wanafanya tathmini za makusanyo wako sawasawa na wanazijua halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu chochote kinaathiriwa na idadi ya watu. Kila mwaka idadi ya watu inaongezeka asilimia 3.1, katika miaka mitano kuna watu milioni 7.6 kwa hivyo kwa muda wa miaka 10 tutakusanya watu milioni 15.2. Hawa watu wanataka matibabu, madawa, shule na wana mahitaji mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ambacho nakieleza, kila mwaka deni linapanda, kwa hiyo, kwa mwaka huu deni limepanda mara mbili ya mwaka uliopita. Kila mwaka wahitimu wetu wanaomaliza shule ni 800,000 lakini Serikali ina uwezo wa kuajiri 40,000, kwa hivyo, kuna watu 760,000 kwa kila mwaka wanakosa ajira. Kwa hivyo, tukifanya miaka mitano tuna watu milioni 3,800,000 wako bench wanasubiri ajira, leo tunaambiwa uchumi umepanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma ukurasa wa 79 wa kitabu cha Mheshimiwa Dkt. Mpango katika hitimisho lake anasema:-

“Naomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla tuunganishe nguvu zetu, vipaji vya wananchi wetu na biashara zetu ili kufikia malengo tunayoyakusudia. Hivyo, tunahitaji uzalendo na nidhamu ya kazi ya hali ya juu tukikusudia kuondoa umasikini”.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri hapa amesema Wabunge na wananchi wote kwa jumla, hii ni kusema kwamba uchumi wa Taifa unategemea wananchi wote. Hata hivyo kwa sasa wapinzani katika Taifa hili wanaonekana ni maadui wakubwa na nusu ya wananchi ni
wapinzani na uchumi unahitaji mshikamano wa umoja katika Taifa kwa mwendo huo uchumi huu utakua kwa kaisi gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima kuwe na uhusiano wa kimataifa kwani umeporomoka, haupo. Ni lazima tuwe na demokrasia, demokrasia haipo. Ni lazima tuwe na utawala wa sheria, utawala wa sheria haupo. Ni lazima tuwe na utawala bora, utawala bora unanuka kabisa katika nchi hii. Katika hali hii, vipi tutaweza kujenga uchumi wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, nitoe ushauri kwamba turejee nyuma tuweze kuimarisha kilimo. Sijaona msukumo wa Serikali katika kilimo.

T A A R I F A . . .

MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa naibu Spika, taarifa hiyo siipokei, tuna ushahidi wa kutosha, mauaji yanayotokea katika nchi hii, watu wanafungwa hovyo katika nchi hii, maonevu yanayotokea katika nchi hii na ushahidi upo. Hawezi Mheshimiwa Waziri akafananisha Tanzania na nchi ile ya Rwanda na Burundi, zile ni nchi ndogo sana (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema malengo makuu katika Taifa hili ni lazima tuwekeze kwenye kilimo. Adui mkubwa wa nchi hii ni yule ambaye anashindwa kuwekeza katika kilimo, anashindwa kutoa misaada katika kilimo kwa sababu asilimia kubwa ya wananchi wake wako kwenye kilimo. Serikali bado haijaamua kuwekeza kwenye kilimo. Nchi moja ya Rwanda imewekeza kwenye kilimo takribani shilingi trilioni 7 lakini leo Tanzania wametoa pesa za maendeleo asilimia 11.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachangia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kuangalia mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakulima Wadogo; Tanzania ni nchi ya wakulima na wafanyakazi lakini sekta hii ya kilimo inachukua asilimia 65.5 ya wakulima kama alivyosema Mheshimiwa Waziri katika ukurasa wa nne wa hotuba yake. Kwa maana hiyo, ajira hii kwa Taifa ni kubwa sana na kuna haja ya Serikali kupitia Wizara yake kufikiria hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wadogo wadogo wana juhudi kubwa za kilimo na kwa kiasi fulani wanazalisha sana. Tatizo mazao ya wakulima yanaharibika na kuoza kwa kukosa soko. Mazao kama mahindi, maembe, nyanya, mananasi; matunda haya yanapotea kila mwaka na hivyo wakulima hawa wanapata hasara kubwa na kupoteza nguvu zao. Kwa sababu hiyo ni lazima kuwepo na soko la wakulima wadogo wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Matumizi ya Ardhi; wakulima wengi sana wanatumia ardhi kinyume na mahitaji ya mazao yanayotakiwa. Ardhi ambayo inafaa kuotesha kunde wanaotesha mananasi na vinginevyo. Hivyo, ushauri wangu ni kwamba kuwe na utafiti kuhusu zao gani lioteshwe katika ardhi gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Utunzaji Mbaya wa Chakula; ni jambo la kusikitisha sana kuona wakulima wakizuiliwa kuuza mahindi yao nje na matokeo yake yakanunuliwa na Serikali na kuhifadhiwa NFRA, tani 13.583 yenye thamani ya Sh.6,793,310,000/=. Mahindi haya yaliharibika na yamesababisha hasara kubwa kwa Serikali. Hata hivyo, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi akizungumza na waandishi wa habari alisema anatarajia kuwa mahindi hayo hayakuharibika. Je, ni hatua gani Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi alichukua dhidi ya uzembe huu uliosababisha hasara kubwa kwa Serikali? (kwa kupoteza Sh.6.793,310,000/=)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Migogoro ya Wakulima na Wafugaji; kwa taarifa tunazo hekari milioni 88.6 za nchi kavu. Hekari milioni 60 ni mbuga zinazomfaa mfugaji. Mbuga hizi zina uwezo wa kulisha mifugo milioni 20 (livestock unit), zilizopo ni 17.1 milioni. Unit tulizonazo ni 20, kwa maana hiyo Serikali ina uwezo mkubwa wa kuondoa mzozo/mgogoro huu. Kwa hiyo zitumiwe hizo units milioni 17.1 kutoka units milioni 20 kutatua mgogoro huu wa wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uvuvi wa Bahari Kuu; meli za uvuvi wa Bahari Kuu zinatolewa leseni dollar 50,000 na kuruhusiwa kuvua samaki idadi yoyote na wale wa ziada wanatupwa. Mheshimiwa Waziri analijua hili, lakini agizo lake la samaki wa ziada waletwe nchini ni kwa sheria gani? Huu ni upotevu wa makusudi wa mazao ya bahari kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima kuwe na sheria maalum kwa idadi ya uvuvi wa samaki wa Bahari Kuu na kuwe na sheria inayowataka wavuvi kuwapeleka samaki wa ziada nchini kinyume na angazo la Waziri pekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu sekta ya kilimo inabebea asilimia 65.5 ya Watanzania ni lazima Wizara itoe kipaumbele ili kutoa au kupunguza umaskini kwa wakulima na kuongeza pato kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuaji wa kilimo hauridhishi hata kidogo, inasikitisha tangu tupate uhuru mwaka 1961 huu ni mwaka wa 57 bado kilimo kinasuasua. Ili kupunguza umaskini ilikuwa ni lazima kilimo kikue kuanzia asilimia 8 hadi 10 hadi sasa. Huu ni mwaka wa 57 kilimo kinakua kwa asilimia 2.7 hadi 3.0. Ni lini tutapunguza umaskini wakulima wetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, uelekezaji katika kilimo, Serikali bado haijaamua na kuonesha nia ya kupunguza umaskini kwa wakulima; bajeti inapungua kila uchao. Inasikitisha kuona nchi kama Rwanda imewekeza jumla ya dola bilioni 32 na Tanzania kushindwa kufanya uwekezaji wa kuwapunguzia wahusika umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuwe na tahadhari na umakini mkubwa katika kilimo. Jambo la kwanza ni lazima kuwa na watafiti wa kutosha kuwa na vyombo vya kilimo kama tractor na power tillers, kutumia ardhi kitaalam; kwa mfano tunazo hekta 1,955,270 zinazohitajika kulimwa. Hata hivyo jambo la kusikitisha ni hekta 13,915 zimelimwa na tractors na power tillers.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko hekta 3,404,494, hizi zinalimwa na wanyama na hekta 8,560,517 zinalimwa kwa jembe la mkono. Kwa takwimu hizi ni wazi kwamba Wizara ya Kilimo haijajiandaa kwa ajili ya kupunguza umaskini kwa wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhuru wa wakulima, wakulima lazima wapewe uhuru wa kuuza mazao yao yote. Kama Serikali wanahitaji basi iweke mazingira ya soko la ndani ili wakulima waweze kuuza mazao yao na kupata faida.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, kwanza sina budi kumshukuru Mungu kwa kuweza kuchangia Wizara hii muhimu ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Spika, Tanzania ni nchi ya tatu inayoongoza kwa idadi kubwa ya mifugo Barani Afrika. Bahati nzuri Wizara hii inachangia 4.4% ya pato la Taifa. Pamoja na kuwa na mifugo mingi bado haijitoshelezi mahitaji ya ndani na nje ya nchi mfano:-NA. FAO TANZANIA
1. Nyama 50kg yr 11kg/yr – 0.03
2. Mazi wa 200 ltr/yr 45 ltr /yr– 0.013
3. Mayai – 300/yr 72/yr – 0.2.

Mheshimiwa Spika, FAO inataka kila Mtanzania atumie kilogramu 50 ya nyama kwa mwaka, lakini anatumia kilogramu 11 ya nyama kwa mwaka. Pia kila Mtanzania anatakiwa kunywa maziwa lita 200 kwa mwaka lakini anakunywa lita 45 tu kwa mwaka. Hata hivyo, kila Mtanzania anatakiwa ale mayai 300 kwa mwaka lakini anakula mayai 72 kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, viwango halisi vinavyotakiwa kuzalishwa ni kama ifuatavyo:-


NA. FAO TANZANIA - UZALISHAJI
Nyama 50x50,000,000 (peoples) = 2,500,000,000 kg/yr 550,000,000 kg/yr
Maziwa 200x50,000,000 ltrs = 10,000,000,000 ltrs 2,250,000,000 ltrs
Mayai 300x50,000,000 = 15,000,000 /yr 3,600,000,000

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa FAO, Watanzania 50,000,000 kila mmoja anatakiwa kula 50 kg ya nyama, kwa hivyo Tanzania inatakiwa kuzalisha 2,500,000,000 kg/yr. Hata hivyo kwa mujibu wa FAO kila Mtanzania anatakiwa kunywa maziwa lita 10,000,000,000 yr kwa mwaka. Pia kuhusu mayai, FAO wanataka Watanzaia 50,000,000,000 watumie mayai 15,000,000,000 kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, hivyo Tanzania inazalisha mayai 3,600,000,000 kwa mwaka kwa mfano hai ni dhahiri kabisa kwamba mahitaji ya uzalishaji ni mdogo mno kulingana na mahitaji mengine. Kwa hiyo basi mambo yafuatayo ni lazima yazingatiwe:-

1. Kuzingatia ufugaji wa kitaalamu.
2. Kuwawezesha wafugaji kutunza mifugo yao kibiashara.
3. Kuimarisha malisho ya uhakika hasa wakati wa kiangazi.
4. Kuimarisha matibabu kwa mifugo yote nchini.
5. Kutenga maeneo maalum ya wafugaji.

Mheshimiwa Spika, hii itawezesha kuongeza kipato na pia kuongeza uzalishaji ili kutosheleza mahitaji ya watanzania lakini pia kuongeza pato la Taifa.