Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mary Pius Chatanda (11 total)

MHE. MARY P. CHATANDA aliuliza:-
Umeme katika Mji wa Korogwe uliingia miaka 50 iliyopita ukitokea kwenye mitambo ya kuzalisha umeme iliyopo Mji wa Hale kilometa 30 toka Mji wa Korogwe. Umeme huo ulikusudiwa kupelekwa kwenye mashamba makubwa ya mkonge na chai na ili kuupata umeme huo kwa Mji huo ilibidi upite kwenye mashamba ya mkonge Magunda, Kwashemshi na kwenda kwenye mashamba ya chai ya Ambangulu na Dindira:-
Je, Serikali haioni ni wakati muafaka Mji wa Korogwe na viunga vyake kuunganishwa na Gridi ya Taifa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mary Chatanda, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba hadi sasa Mji wa Korogwe hupata umeme kutoka kituo cha kuzalisha umeme cha Hale kilichounganishwa katika Gridi ya Taifa. Viunga vya Mji wa Korogwe navyo vimeunganishwa kwenye Gridi ya Taifa na hivyo vitaendelea kupata umeme kutoka katika vyanzo vya maji vya Hale. Mji wa Korogwe una maeneo ambayo pia bado hayajapata huduma ya umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo haya ni pamoja na Vitongoji vya Bagamoyo, Habitat, Kilole Sobibo, Kitopeni, Kwandungwe, Makwei, Ruengera Relini, Ruengera Darajani na baadhi ya maeneo ya vitongoji vya Mtonga, Kwamkole pamoja na Kwasemangube. Maeneo haya yataingizwa katika mpango wa utekelezaji wa bajeti ya TANESCO kwa mwaka 2017/2018.
MHE. MARY P. CHATANDA aliuliza:-
Mfuko wa PSPF unachelewesha sana mafao ya wastaafu, watumishi wengi waliostaafu mwaka wa fedha 2015/2016 hawajalipwa mafao yao, hususan walimu wa Korogwe Mjini:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuondoa changamoto hii ambayo imekuwa kero kwa wastaafu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mary Pius Chatanda, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha changamoto ya kulipa wafanyakazi mafao inaondoka, Serikali katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Agosti, 2016 imefanikisha mkakati wa kuweza kulipa kiasi cha shilingi bilioni 511.8 ikiwa ni malimbikizo ya michango ya mwajiri. Pia katika kipindi hicho Serikali imelipa jumla ya shilingi bilioni 83 kama malipo ya deni la kabla ya mwaka 1999 (Pre 1999 Liability). Kwa hali hiyo, Serikali imeendelea kulipa malimbikizo ya madai ya wastaafu na mafao mengine yatolewayo na mfuko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha katika kipindi cha mwezi Januari hadi Julai, 2016 mfuko umelipa mafao ya pensheni ya mwezi kwa kiasi cha shilingi bilioni 117 na kwa sasa mfuko unaendelea na kulipa malimbikizo ya mafao ya mkupuo kwa wastaafu wapya na mafao mengineyo.
MHE. MARY P. CHATANDA aliuliza:-

Mwaka 2014 katika Chuo cha Ualimu Korogwe yalifanyika mabadiliko ya udahili, udhibiti ubora na tunu yaliyofanywa na Baraza la Elimu ya Ufundi la Taifa – NACTE lakini chuo kimekuwa kikipata wanachuo wachache kuliko miundombinu na rasilimali watu waliopo; na kwa kuwa chuo hiki kwa sasa kimepelekewa wanachuo wapatao 827 kutoka Chuo Kikuu UDOM kwa mafunzo ya Stashahada ya Kawaida ya Elimu:-
Je, Serikali itaendelea kuwapeleka wanachuo wa kutosha ili kuendana na miundombinu na rasilimali watu waliopo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mary Pius Chatanda, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Ualimu Korogwe kina uwezo wa kudahili wanachuo 1,200 kwa wakati mmoja na ndiyo sababu wanachuo wapatao 827 kutoka Chuo Kikuu UDOM walidahiliwa kwa mafunzo ya Stashahada ya Kawaida ya Elimu. Hata hivyo, chuo hicho kimekuwa kinadahili wanachuo wachache kuliko uwezo wake hususan mwaka 2015/2016 kilidahili wanachuo 234 kutokana na kuhuishwa sifa za kujiunga kuwa ufaulu wa daraja la I - III na kuwepo kwa ushindani wa wahitimu wa kidato cha IV kuwa na fursa nyingine za kujiunga na kidato cha V na wahitimu wa kidato cha VI kujiunga na vyuo vikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa dhamira ya kuwapokea wanachuo wa kutosha katika Chuo cha Ualimu Korogwe ili kuendana na miundombinu na rasilimali watu waliopo.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI (K.n.y. MHE. MARY P. CHATANDA) Aliuliza:-
Serikali imekuwa ikitoa majibu ya upandishwaji wa madaraja na fedha za likizo kwa walimu nchini na katika Chuo cha Ualimu Korogwe kuna walimu na watumishi ambao wanadai kupandishwa vyeo na fedha za likizo.
(a) Je, Serikali ina mpango gani kuwapandisha daraja wale wanaostahili?
(b) Je, ni lini Serikali italipa madai yao ya fedha za likizo ambazo hawajawahi kulipwa?

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mary Pius Chatanda, Mbunge wa Korogwe Mjini,
lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekuwa ikiwapandisha vyeo watumishi wake wenye sifa kila mwaka. Kwa mfano, katika mwaka wa 2015/2016, Wizara iliwapandisha vyeo watumishi 2,272 kati yao watumishi 71 ni wa Chuo cha Ualimu Korogwe.
(b) Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kulipa madeni mbalimbali ikiwa ni pamoja na fedha za likizo kwa walimu/watumishi katika sekta ya elimu, ambapo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016 hadi mwezi Juni, 2016 jumla ya shilingi 22,629,352,309.99 zililipwa kwa walimu 63,814. Aidha, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017 hadi kufikia Machi, 2017 jumla ya shilingi 10,505,160,275.80 zimelipwa kwa walimu 22,420 na hivyo kufanya jumla ya walimu waliolipwa katika kipindi hicho kufikia 86,234. Katika malipo haya, jumla ya shilingi 13,415,410 zimelipwa kwa ajili ya madeni ya fedha za likizo kwa watumishi sita wa Chuo cha Ualimu Korogwe. Uhakiki wa madeni ya miaka ya nyuma unaendelea kuratibiwa na mamlaka husika na taratibu za malipo zitakamilishwa kwa wale watakaostahili.
MHE. MARY P. CHATANDA aliuliza:-
Mwaka 2001, Chuo cha Ualimu Korogwe kwa kushirikiana na wananchi, walianza ujenzi wa maktaba ambayo bado haijakamilika; na kwa kuwa wanachuo na wananchi wa Korogwe wanahitaji sana maktaba hiyo:-
Je, Serikali itakuwa tayari kusaidia juhudi zilizokwishaanza ili kukamilisha jengo hilo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mary Pius Chatanda, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa maktaba hiyo kwa Wanajumuiya wa Chuo cha Ualimu Korogwe na wananchi kwa ujumla, Wizara yangu iko tayari kusaidia ujenzi wa maktaba hiyo na hivyo itatuma wataalam kwenda kufanya tathmini ya hatua iliyofikiwa na msaada unaohitajika ili ujenzi huo uweze kukamilika katika mwaka wa fedha wa 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kutokana na jinsi wananchi wa Korogwe wanavyoshirikiana vizuri na Mbunge wao, Mheshimiwa Mary Pius Chatanda, kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha elimu.
MHE. MARY P. CHATANDA aliuliza:-
Hospitali za Serikali zimeandaliwa kupata huduma za dawa MSD lakini wakati mwingine baadhi ya dawa zimekuwa hazipatikani MSD na hospitali haziruhusiwi kununua dawa nje ya MSD.
Je, Serikali imetoa maelekezo gani pale ambapo MSD wamekuwa hawana baadhi ya dawa hizo zinazohitajika kwa wagonjwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nakushukuru na kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mary Pius Chatanda, Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2011 na Kanuni zake za mwaka 2013 kifungu cha 140, inavitaka vituo vyote vya kutolea huduma za afya kuleta MSD (Medical Stores Department) maoteo ya mahitaji ya mwaka mwezi Januari ya kila mwaka ili kuiwezesha MSD kuyaingiza kwenye mpango wake wa manunuzi. Vituo vya kutolea huduma za afya vinatakiwa kununua mahitaji yake kutoka MSD na pale ambapo madawa hayo yatakosekana katika maghala ya MSD yaliyopo kwenye Kanda na Makao Makuu ya MSD, MSD anapaswa kumtaarifu mteja ndani ya siku moja ya kazi ili akanunue kwa watu binafsi.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI (K.n.y. MARY P. CHATANDA) aliuliza:-
Mahakimu na Watumishi wa Mahakama hawajapandishwa vyeo kwa muda mrefu na hata wanaobahatika kupandishwa hawabadilishiwi mishahara:-
(a) Je, ni lini Serikali italifanyia kazi tatizo hilo?
(b) Kwa kuwa Wanasheria wengine hupewa house allowance: Je, kwa nini hawa nao wasipewe kama sehemu ya motisha lakini pia wapewe extra duty allowance?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mary Pius Chatanda, Mbunge wa Korogwe Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuwapandisha vyeo Watumishi wenye sifa stahiki ni wajibu endelevu wa Serikali. Mahakama ya Tanzania imekuwa ikichukua hatua kuwapandisha Mahakimu na Watumishi wa ngazi mbalimbali vyeo kuzingatia vigezo vilivyowekwa kisheria ikiwa ni pamoja na muda wa utumishi kazini, utendaji wa kazi, weledi na maadili pamoja na upatikanaji wa vibali kutoka Idara Kuu ya Utumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013, jumla ya Mahakimu na Wasaidizi wa Sheria wa Majaji 52 walipandishwa vyeo. Mwaka 2013/2014, jumla ya Watumishi 200 walipandishwa vyeo, mwaka 2014/2015, jumla ya Mahakimu na Wasaidizi wa Sheria wa Majaji 22 na Watumishi 686 walipandishwa vyeo na mwaka 2015/2016, jumla ya Mahakimu na Wasaidizi wa Sheria 59 na Watumishi 447 walipandishwa vyeo.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kutoa posho kwa watumishi wake kama sehemu ya motisha. Mahakama imeendelea kutoa motisha ya posho mbalimbali na stahili za watumishi kwa mujibu wa sheria, kulingana na uwepo au hali ya bajeti.
MHE. MARY P. CHATANDA aliuliza:-
Mhimili wa Mahakama kama ilivyo mihimili mingine unahitaji kuwa na eneo la uhakika la kufanyia kazi na vitendea kazi vya uhakika:-
(a) Je, ni lini Wilaya ya Korogwe itajengewa Mahakama ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU - K.n.y WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mary Pius Chatanda, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa Mahakama kama Mihimili mingine, wanahitaji mazingira mazuri na muafaka kwa kufanyia kazi zao. Aidha, napenda kukiri kuwa moja ya changamoto kubwa inayozikabili Mahakama zetu ni pamoja na uhaba wa majengo na uchakavu wa miundombinu iliyopo.
Mheshimiwa Spika, Mpango wa maendeleo wa ujenzi wa Mahakama kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ni pamoja na ujenzi wa Mahakama za Mkoa ikiwemo ujenzi wa Mahakama sita za Hakimu Mkazi, ujenzi wa Mahakama 15 za Wilaya na Ujenzi wa Mahakama 10 za Mwanzo.
Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Mahakama imepanga kujenga Mahakama ya Wilaya ya Korogwe kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Aidha, katika Mkoa wa Tanga Wilaya zilizopewa kipaumbele katika ujenzi ni Kilindi, Korogwe na Mkinga. (Makofi)
MHE. MARY P. CHATANDA aliuliza:-

Ujenzi wa Jengo la Utawala na vyumba vya madarasa katika Chuo cha Uuguzi Korogwe bado haujakamilika:-

Je, ni lini ujenzi huo utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mary Pius Chatanda, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Jengo la Utawala na vyumba vya madarasa katika Chuo cha Uuguzi - Korogwe bado haujakamilika kutokana na changamoto za fedha za ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya vyuo vya afya hapa nchini. Kutokana na ufinyu wa bajeti ya Serikali katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali haikutenga fedha kwa ajili ya ujenzi katika vyuo vya afya nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuona changamoto hii, Serikali inaandaa zoezi la uhakiki wa miradi yote ya maendeleo iliyokuwa inatekelezwa katika vyuo mbalimbali vya hapa nchini ili kupata taarifa za hali ya sasa ya miradi hiyo. Lengo ni kupata taarifa zitakazosaidia katika kuandaa maandiko na mipango itakayotumika kutafuta fedha pamoja na mgawanyo wa fedha kulingana na vipaumbele na mahitaji ya kila chuo. Hivyo basi, mara pesa zitakapopatikana chuo hiki pamoja na vile ambavyo ujenzi umesimama vitapewa kipaumbele cha ukamilishaji.
MHE. MARY P. CHATANDA aliuliza:-

Umeme umekuwa ukikatika mara kwa mara Korogwe na kufanya uharibifu wa mali za Wananchi:-

Je, ni lini tatizo hilo litapatiwa ufumbuzi.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mary Pius Chatanda, Mbunge wa Korogwe Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kutokana na ukarabati wa miundombinu ya umeme unaoendelea kwa sasa Wilayani Korogwe, TANESCO hulazimika kukata umeme katika maeneo husika ya wilayani humo ikiwa ni pamoja na maeneo ya Mji wa Korogwe. Hali hiyo inasababishwa na kazi zinazoendelea za kukarabati wa miundombinu ikiwa ni pamoja na kubadilisha vikombe vibovu, nguzo mbovu, ukataji wa miti na matawi katika njia za umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kazi za kukarabati miundombinu ya kusambaza umeme zifanyike hulazimika kuzima umeme katika maeneo yanayofanyiwa ukarabati. Kukamilika kwa ukarabati unaoendelea kutawezesha kuimarika kwa umeme na kurudi katika hali yake ya kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara zote kabla ya kuzima umeme taarifa zimekuwa zikitolewa katika vyombo mbalimbali vya habari katika Wilaya ya Korogwe na Mkoa wa Tanga. Hali ya kukatika umeme kwa ajili ya kupisha matengenezo kumeimarisha sana upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo. Aidha, tunaomba wananchi waendelee kuwa wavumilivu katika kipindi cha matengenezo ya miundombinu hiyo.
MHE. MARY P. CHATANDA aliuliza:-

Serikali imefanya kazikubwa sana ya ukarabati wa Shule ya Sekondari Korogwe lakini haikuunganisha nyumba za Walimu zilizopo Shuleni hapo.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuzikarabati nyumba hizo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mheshimiwa Mary Pius Chatanda, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Shule ya Sekondari Korogwe ni miongoni mwa shule 45 zilizokarabatiwa katika awamu ya kwanza ya ukarabati wa shule kongwe nchini. Ukarabati wa shule kongwe awamu ya kwanza ulihusisha vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, mabweni, maabara, ofisi za walimu, majengo ya utawala, mabwalo ya chakula na majiko, mifumo ya maji safi na taka na mifumo ya umeme.

Mheshimiwa Spika, ukarabati wa shule kongwe awamu ya kwanza haukuhusisha nyumba za walimu kutokana na sababu za kibajeti. Awamu ya pili ya ukarabati unaoendelea inahusisha shule shule kongwe 19 ikiusisha halikadhalika nyumba za walimu kwenye shule zinazokarabatiwa. Serikali inatafuta fedha ili kukarabati nyumba za walimu ambazo hazikujumuishwa kwenye mpango wa ukarabati wa shule kongwe awamu ya kwanza.