Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mary Pius Chatanda (26 total)

Azimio la Bunge la Kumpongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Job Yustino Ndugai kwa Uamuzi wake wa Kulifanya Bunge Kutekeleza kwa Vitendo Dhana na Bunge Mtandao (e-Parliament)
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru Wabunge, wale waliochangia na Wabunge wote kwa ujumla kwa kuona umuhimu wa hoja hii ambayo tumeileta hapa Mezani.

Wabunge wanne wamechangia kwa niaba ya Wabunge wengine wameelezea yale ambayo tumeyazungumza ndani ya Azimio hili la Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuokoa muda, nami naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Spika kwa namna ambavyo ametuwezesha sisi Wabunge kuwa wa kisasa. Cha msingi niombe tu Wabunge waweze kuzitunza ili zisipotee maana zikipotea Bunge tena halitaingia gharama ya kuwanunulia itabidi wanunue wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipatia nafasi nami niweze kuchangia hotuba ambayo aliitoa Mheshimiwa Rais alipokuwa anafungua Bunge hili.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu na kuwashukuru wananchi wa Wilaya ya Korogwe Mjini kwa kunipa nafasi ya kuwawakilisha katika Bunge hili Tukufu. Mwenyezi Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii vilevile kumpongeza Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo kwa nafasi aliyoitumia jana usiku kupitia vyombo vya habari alipotoa ufafanuzi juu ya jambo ambalo wenzetu wameamua kufanya upotoshaji wa makusudi kabisa. Ni ukweli usiopingika kwamba Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo ameeleza wazi nia na madhumuni ya Shirika letu la TBC kusitisha matangazo kwa maana ya kutaka MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipatia nafasi nami niweze kuchangia hotuba ambayo aliitoa Mheshimiwa Rais alipokuwa anafungua Bunge hili.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu na kuwashukuru wananchi wa Wilaya ya Korogwe Mjini kwa kunipa nafasi ya kuwawakilisha katika Bunge hili Tukufu. Mwenyezi Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii vilevile kumpongeza Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo kwa nafasi aliyoitumia jana usiku kupitia vyombo vya habari alipotoa ufafanuzi juu ya jambo ambalo wenzetu wameamua kufanya upotoshaji wa makusudi kabisa. Ni ukweli usiopingika kwamba Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo ameeleza wazi nia na madhumuni ya Shirika letu la TBC kusitisha matangazo kwa maana ya kutaka wao. Kila mwananchi hivi sasa ikishafika kipindi cha taarifa ya habari saa moja, saa mbili, hata kama mtu hana TV anakimbia kwa jirani yake kwenda kusikiliza leo kunafanyika kitu gani, leo Rais atasema nini, leo Mawaziri watasema nini, jinsi walivyokuwa na hamu na utekelezaji wa hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niendelee kupongeza sana jitihada za Mheshimiwa Rais ambazo ameshaanza kuzichukua. Nawapongeza pia Mawaziri kwa kazi nzuri ambayo na wenyewe wameanza kufanya kazi, msirudi nyuma kazeni buti. Achene kuwasikiliza watu wachache wanaosema inawezekana huu ni moto wa kifuu, huu siyo moto wa kifuu utaendelea kuwaka na hautazimika ili kuweza kuwaletea maendeleo wananchi wetu wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nieleze juu ya kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba Tanzania yenye viwanda inawezekana. Mimi nafikiri kauli hii ya Mheshimiwa Rais ya Tanzania na viwanda inawezekana, itawezekana endapo tutaondokana na urasimu ambao unazaa rushwa. Wapo wawekezaji wengi ambao wanapenda kuwekeza katika nchi yetu, lakini wanapofika kwenye ofisi zetu za Serikali wanakutana na urasimu mkubwa. Urasimu ule unaashiria rushwa. Rais wetu amesikitishwa sana na suala la rushwa lililoko serikalini. Kwa hiyo, niwaombe ndugu zangu suala la urasimu tukiliacha Tanzania ya viwanda inawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono vilevile kauli ya Mheshimiwa Rais ya kukemea suala la rushwa. Shughuli zetu hata kwenye Halmashauri zetu zimeingiliwa sana na suala la rushwa hasa kwenye kitengo hiki cha ugavi, cha ukusanyaji wa mapato, watu wanafanya vile ambavyo wanataka wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe basi Waziri anayehusika kwenye hizi Serikali zetu za Mitaa, hebu tuingie kwenye vitengo hivi vya ugavi na ukusanyaji wa mapato, watu hawa wanatusababishia Serikali kukosa mapato katika Halmashauri zetu. Wanatumia vitabu vya aina mbalimbali katika ukusanyaji wa mapato, wanakubaliana na wafanyabiashara hawawatozi ushuru ambao unatakiwa. Kwa hiyo, niombe sana kama tunatumbua majipu hebu sasa tufike mpaka huku chini kwenye hizi Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la elimu. Suala la elimu bila malipo ni mpango mzuri ambapo wananchi wameufurahia sana. Nitoe ushauri kwenye Serikali mpango huu uende sambamba na kuwajengea mazingira bora walimu. Bila kuwajengea mazingira bora walimu mpango huu unaweza ukasuasua. Walimu wana matatizo mengi, wanatakiwa waandaliwe mazingira kama vile vitendea kazi, nyumba za kuishi, kuwalipa stahiki zao zile ambazo wanadai ikiwa ni pamoja na malimbikizo ya likizo.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais wa Jahmuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Waziri Mkuu na Mawaziri kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wameshuhudia juhudi zao katika kutekeleza dhamira ya uwajibikaji na maadili kwa viongozi, watendaji na watumishi wasiyo waadilifu kwa kuwatumbua majipu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikishafika sasa hivi saa moja kwenye taarifa ya habari, ikifika saa mbili kwenye taarifa ya habari wananchi wanakimbia kwenda kusikiliza leo kunatokea kitu gani. Wananchi walikuwa wameshachoka na tabia ya baadhi ya watendaji wa Serikali ambayo walikuwa wakiifanya, kwa hiyo, sasa wanafurahia juhudi ya Serikali ambayo inafanya ya kuhakikisha kwamba hakuna matabaka kati ya walio nacho na wasiyo nacho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nianze kwa kunukuu maneno aliyosema Kitilya Mkumbo kwenye mtandao wa twitter amesema; “Tunahitaji upinzani utakaojikita katika sera mbadala. Upinzani unaotegemea makosa ya Serikali ya CCM pekee unaweza kupwaya sana katika kipindi hiki.” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona ninukuu hili la Mkumbo kutokana na kitendo cha Kiongozi wa Kambi ya Upinzani kutowasilisha hotuba ya bajeti ya Kambi ya Upinzani na hasa ukiangalia bajeti yetu sisi ya Waziri Mkuu ina karatasi kama 100 kitu hivi lakini ya mwenzetu huyu amekuja na karatasi tatu. Matokeo yake kwa sababu kashindwa kuiandika bajeti anashawishi wenzake watoke nje. Hoja ya Kitilya Mkumbo iko sahihi kabisa hawa watu wamefilisika na wamepwaya kisiasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa kupata mradi mkubwa wa bomba la mafuta kutoka Uganda kuja Tanzania hususani Mkoa wa Tanga. Ni matarajio yangu kwamba fursa hii ambayo tumeipata tutaisimamia vizuri na kuweza kuanza kufanya maandalizi ya maeneo ambayo mradi huu utapita kwa kutoa elimu kwa wananchi wa maeneo yale na hatimaye kuanza kufanya maandalizi ya fidia kwa maeneo yale yatakayokuwa yamepitiwa na mradi kama kwenye mashamba na nyumba ili kuondoa usumbufu katika utekelezaji wa mradi huu. Ni matarajio yangu kwamba watatoa elimu kwa wananchi ili waweze kutambua faida ya mradi huu ambao umepatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikubaliane kabisa na kaulimbiu kwamba Tanzania kuwa ya viwanda inawezekana. Ili kufanikisha jambo hili ni vizuri tukaimarisha suala la kilimo. Tukiimarisha kilimo vizuri tukakipa kipaumbele kitaweza kuzalisha malighafi ambazo ndizo zitakazoweza kulisha hivyo viwanda.
Tusiposimamia vizuri kuhakikisha kwamba kilimo tunakipa kipaumbele tunaweza tukajenga viwanda na hatimaye tukakosa malighafi, viwanda vikawa vipo na havifanyi kazi na ile kauli mbiu ya kwamba Tanzania iwe ya viwanda ikawa ni kazi bure. Hivyo, naishauri Serikali tusimamie na tuhakikishe kwamba kilimo kinapewa kipaumbele, kiende sambamba na upatikanaji wa maji. Kama maji hayapo kiwanda hakiwezi kufanya kazi, kama hakuna umeme wa uhakika kiwanda hakiwezi kufanya kazi, kama miundombinu hakuna, kiwanda kinaweza kikafanya kazi lakini usafirishaji wa hayo mazao itakuwa ni shida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu ni pamoja na reli. Tunapozungumzia reli kama ambavyo wezangu wengine wametangulia kuzungumza reli ni kitu muhimu sana. Reli inapunguza uharibifu wa barabara, magari makubwa yanapita yanaharibu barabara kila siku inafanyiwa matengenezo. Reli ikitengenezwa nadhani mizigo yote itapita kwenye reli na viwanda vyetu vitakapokuwa vimezalisha mazao yatapitishwa kwenye reli, hivyo angalau shughuli za uzalishaji na mali kupeleka kwenye mikoa kupitia reli. Napozungumzia reli basi naomba ifahamike kwamba ni pamoja na reli ile ya kutoka Tanga - Kilimanjaro - Arusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizungumzie suala zima la Mfuko wa PSPF. Huu Mfuko wa PSPF unachelewesha mno mafao ya watumishi waliostaafu. Niiombe Serikali, watumishi hawa ambao wanakuwa wamestaafu hizi fedha zao ndizo zinazowasaidia kuweka maisha yao vizuri. Inapokuwa wanacheleweshewa kupata mafao yao inakuwa ni shida. Kwanza, inawapa ugumu wa maisha kwa sababu ameshajipanga kwamba amestaafu kuna hizo fedha anategemea kufanya shughuli ambazo zitamwezesha kupata kipato, lakini anacheleweshewa kupata fedha hizi. Niombe Serikali, hawa wastaafu wanapostaafu basi iwe ni muhimu sana kuwaandalia mafao yao mapema ili waweze kutoka wakiwa na fedha zao na hatimaye waweze kuishi muda mrefu kuliko ilivyo hivi sasa. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, suala la walimu. Lipo tatizo kwa walimu kuhusiana na upandishwaji wa madaraja. Walimu wamekuwa wanachukua muda mrefu kwenye kupandishwa madaraja na hata wakipandishwa mishahara yao kwa maana ya stahiki zao zile zinachelewa sana kufanyiwa marekebisho, inachukua hata miezi sita mtu hajarekebishiwa. Niombe wanapopandishwa madaraja basi na zile stahiki zao ziwe zimeandaliwa. Kule Korogwe wapo baadhi ya walimu wanadai malimbikizo toka 2010 hadi hivi sasa hawajalipwa na wamepandishwa madaraja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iangalie upya suala la posho ya kufundishia (teaching allowance) kwa walimu. Tuseme tusemavyo walimu wana jukumu kubwa sana, wanafanya kazi kuliko mfanyakazi mwingine yeyote.
Tukirudisha teaching allowance kwa walimu haki ya Mungu hii elimu itakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Serikali hebu tulitazame jambo hili. Walimu hawa wamekuwa wakitoka shuleni wakifika nyumbani ni kazi ya kuanza kufanya maandalizi, kusahihisha mitihani, kusahihisha madaftari na kuandaa maandalio ya kesho. Kwa bahati mbaya sasa itokee mama ndiyo mwalimu, baba labda ni mhasibu, yule mama anakaa kufanya kazi ya ualimu pale nyumbani mpaka saa nane ya usiku hebu niambie, baba amelala yupo kitandani. Unatarajia hiyo nyumba ya mwalimu na huyo mumewe inakuwaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali hata kama atafanya kazi kwa o kwa muda huo…
MWENYEKITI: Mheshimiwa umemaliza muda wako naomba ukae!
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya mwanzo ili niweze kuchangia. Kwanza kabisa naomba niuunge mkono hoja juu ya bajeti aliyowasilisha Waziri wa Elimu kwamba, amewasilisha kiufundi kabisa, nampongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi ya kumpa pole Naibu Waziri wa Elimu kwa msiba ambao umempata. Basi, namwombea kwa Mwenyezi Mungu amtie nguvu na Marehemu Roho yake iweze kuwekwa mahali pema peponi. Amina.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Waziri na Naibu Waziri, Wakuu wa Wizara kwa kazi ambayo wamekuwa wakiifanya pamoja na changamoto nyingi ambazo wanakabiliana nazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kusema kwamba, elimu ndiyo ufunguo wa maisha. Bila elimu hakuna viwanda, bila elimu hakuna kilimo chenye tija, bila elimu hakuna afya bora na kadhalika. Hivyo, ningeomba sana, Wizara ya Elimu ifanye kazi ya kuboresha suala zima la elimu. Suala zima la elimu likiboreshwa, tunaweza tukawapata wasomi wazuri, watakaoweza kuendesha nchi hii na kuweza kuingia kwenye soko la ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Wizara ya Elimu, kwa kuanza kutazama upya ufaulu wa darasa la saba. Ufaulu wa darasa la saba uanze sasa kwak kuzingatia vigezo vya kuingia kwenye elimu ya sekondari. Utaratibu wa mitihani wa kuchagua alama za a, b, c, d, tunawapata wanafunzi ambao wanakwenda sekondari wasiojua kusoma na kuandika. Hawa wanafunzi ambao wengine wana vipaji vile vya kubahatisha, wanabahatisha halafu wanaingia kwenye elimu ya sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakiingia kwenye elimu ya sekondari wanawapa tabu Walimu wa sekondari namna ya kuwafundisha, kwa sababu inabidi sasa waanze kuwafundisha kwa uelewa zaidi, masomo yale ambayo yalikuwa ni ya darasa la saba wanaanza kuwafundisha huku sekondari. Kwa hiyo, naomba sana utaratibu ule wa awali, uliokuwepo mara ya kwanza uweze kurejewa ili kuondoa usumbufu kwa Walimu wa shule za sekondari kuanza kuwafundisha wale wanafunzi ambao hawakufaulu vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara irejeshe utaratibu wa zamani wa kufanya masomo kwa kufikiri badala ya kufanya masomo kwa kuchagua. Wakifanya hivyo tutawapata watoto wanaojitambua, itawarahisishia Walimu kuwa na watoto wenye uelewa na ufaulu wenye tija kuliko ilivyo sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sasa uboreshaji wa elimu uende sambamba na uboreshaji wa maslahi ya Walimu na stahiki zao. Baadhi ya stahiki za Walimu wala hazihitaji kuwa na shida kiasi kwamba Walimu wanapata matatizo, wanapata shida za kuhangaika kufuata stahili zao. Walimu inajulikana siku zao za likizo, mwezi wa Sita ni mapumziko na mwezi wa 12 ni mapumziko, hivyo niiombe Wizara, kinapofika kipindi hicho, wanapojua kwamba Walimu wanataka kwenda likizo mwezi wa Sita, wale Walimu wanaotakiwa kwenda wawe wameandaliwa tayari nauli zao miezi miwili kabla, fedha zao zipelekwe kwenye Halmashauri ili Walimu hawa wanapokuwa wanakwenda likizo, wapewe nauli zao badala ya kuwakopa kwamba waende halafu watakuja kurudi ndipo wapate nauli zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la teaching allowance. Walimu hawa, ndugu zangu, wanafanya kazi kubwa, wanafanya kazi kiasi kwamba hawana nafasi ya kupumzika, hawana nafasi ya kufanya shughuli nyingine za kuwaongezea kipato. Kwa hiyo, naiomba Serikali iangalie utaratibu wa kurejesha teaching allowance ili Walimu hawa wapate moyo wa kufanya kazi, kwa sababu hawana njia nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi wengine wanapata muda wa kwenda kufanya kazi kujiongezea kipato, lakini Walimu hawana nafasi ya kufanya hivyo kwa sababu wanakuwa na shughuli nyingi ambazo zinawafanya waendelee kufanya maandalizi kwa ajili ya wanafunzi kwa kesho yake. Kwa hiyo, ni matarajio yangu kwamba Serikali, ombi hili ni la muda mrefu, ni vizuri basi wakaliangalia ili Walimu hawa walipwe hiyo teaching allowance ili iweze kuwasaidia katika kujikimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima la madarasa haya ya awali. Madarasa ya awali, Serikali kwa kweli imefanya kazi kubwa kuona kwamba watoto wote waende shule. Hata hivyo, niombe basi kwa kuwa Walimu hakuna wa madarasa la awali, sana sana wanawachukua wale Walimu ambao ni watu wazima ndiyo wamewapangia kufundisha madarasa ya awali. Niombe sasa waandaliwe Walimu maalum watakaokuwa wanafundisha madarasa haya ya awali, badala ya kuwatumia wale Walimu ambao wanaona ni watu wazima waliopo kwenye madarasa mengine na kuwaleta kwenye madarasa haya ya awali. Vile vile iende sambamba na suala zima la kuwapa vile vitendeakazi vya kufundishia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali, kwa sababu ruzuku inapelekwa kwa wanafunzi wale wa shule za msingi, basi ruzuku vile vile ya watoto wa shule ya awali, iunganishwe kwa kupelekwa kwenye shule za msingi ili angalau na wenyewe waingie kwenye hesabu, kwa sababu safari hii walipokuwa wamepeleka zile ruzuku, hawakuingiza kwenye orodha ya watoto ambao wako shuleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena nizungumzie suala la upandishwaji wa madaraja. Naomba upandishwaji wa madaraja uende sambamba na mabadiliko ya mishahara ya Walimu…
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia hotuba iliyowasilishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Mambo ya Ndani kwa kazi kubwa anayoifanya akishirikiana na viongozi wakuu kwa maana watendaji wakuu wa Wizara hizo pamoja na changamoto mbalimbali ambazo wanakabiliana nazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeanza na suala zima la magereza. Tumesema kwamba Serikali yetu tunataka nchi hii safari hii iwe nchi ya viwanda; ukiangalia kwenye taarifa ya Kamati imetoa ushauri kwa kuishauri Serikali kwamba tuiwezeshe magereza ili iweze kufanya kazi yake vizuri. Ninavyokumbuka, nilipokuwa nikikua, magereza wamekuwa wakilima mashamba kwa mfano yale magereza ya kilimo walikuwa wakilima mashamba na kuweza kutosheleza mazao ya chakula na ziada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kinachotakiwa hapa ni kurejesha ule utaratibu wa zamani ili magereza waweze kupatiwa zana za kufanyia kazi, waweze kupatiwa mtaji, kwa ajili ya uzalishaji. Magereza wakizalisha mazao ya kutosha inaweza ikapatikana malighafi ya kupeleka kwenye viwanda ambavyo tunasema tunataka tuwe na viwanda ili kusudi viweze kulishwa na malighafi itakayokuwa imezalishwa na magereza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii inawezekana kwa magereza kwa sababu wenzetu tayari wana rasilimali watu, tukiwawezesha magereza tukawapa mtaji wa kutosha hakuna kitakachoshindikana. Magereza zamani walikuwa wanafuga mifugo kwa maana ya ng’ombe wa maziwa. Nakumbuka nilipokuwa pale Mafinga yalikuwa yanatoka maziwa kwenye gereza la Isupilo, yanaletwa huku ukiuliza yametoka wapi, wanasema maziwa yanatoka Gereza la Isupilo. Kwa hiyo, kama tutataka kuanzisha viwanda vya maziwa, magereza hawa tukiwawezesha watafuga vizuri na viwanda hivyo vitaweza kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali yangu ili tuweze kuufufua huu uchumi tunaouzungumza wa kutaka tuwe na viwanda tuweze kuwawezesha magereza kwa kuwapa mtaji na hatimaye kuwawezesha kwa zana za kufanyia kazi ili kusudi wao wenyewe waweze kuzalisha kwa maana ya kulisha magereza yao, kuachana na kuendelea kuitegemea Serikali. Wakati huo huo ziada itapatikana kwa ajili ya kuuza na hatimaye kuweza kupata fedha ambazo zitapatikana kama sehemu ya maduhuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Kamishna Mkuu wa Magereza kule kwangu Korogwe kwenye gereza moja la Kwa Mngumi ameanza kufufua mabwawa 30 ya ufugaji wa samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabwawa yale ni makubwa na ameshaanza kupanda samaki mle ndani, lakini anachohitaji hapo kuna changamoto, nimwombe Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi aweze kutembelea lile gereza ili aende akaone yale mabwawa ambayo ameyaanzisha huyu Kamishna Mkuu wa magereza ili aweze kuona ni namna gani ambavyo anaweza kuwasaidia ili kusudi waweze kufanikisha kukamilisha ule mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kama walivyosema wenzangu suala la maslahi ya askari. Lipo tatizo pamoja na kwamba tunasema bajeti inakuwa ndogo, lakini inakuwa ndogo kwa hawa askari wa ngazi ya chini tu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, askari wa ngazi ya chini wanapata shida, wanakwenda likizo bila malipo ya likizo yao, hata wakirudi kutoka likizo wakiomba fedha hizo kulipwa hawalipwi. Niiombe Serikali katika bajeti ile ambayo inatengwa kwa ajili ya Wizara hii ni vizuri tukawapa fedha zote ili kusudi waweze kulipa madeni wanayodaiwa na askari wa ngazi za chini walipwe madai yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo lingine ambalo askari wa ngazi ya chini wanapata shida, suala la upandishwaji wa vyeo, wana utaratibu wa kila baada ya miaka mitatu askari wa ngazi ya chini anatakiwa kupandishwa cheo, lakini hawapandishi kwa wakati na hata wakipandishwa hawalipwi mshahara kulingana na cheo alichopandishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana tusiwafishe moyo vijana hawa askari wa ngazi ya chini hawa mishahara yao ni midogo, wanapandishwa vyeo halafu hawalipwi kulingana na vyeo walivyopewa, wapewe kulingana na vyeo vyao walivyopewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la kufiwa, askari wa ngazi ya chini akifiwa nitaomba Waziri anipe majibu anapo-wind up hivi ni kweli kwamba akiwa na baba yake mzazi, mama yake mzazi anakaa naye pale nyumbani na tuseme bahati nzuri huyu askari yeye kwao labda ni Musoma amefiwa na baba yake alikuwa akimlea hapo nyumbani alikuwa anaugua, askari yule hawezi kusafirisha na mzazi wake yule kupelekwa nyumbani, askari yule anahangaika anatafufa fedha za kusafirisha mwili ule hivi ni kweli?
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu askari si mtumishi wa Serikali inakuaje watumishi wa Serikali wengine wazazi wao wakifariki wanasafirishwa iweje askari polisi anafanyiwa kitu cha namna hiyo? Nitaomba majibu kama ni kweli, utaratibu ni huo naomba utaratibu huo ubadilishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba za Polisi, wenzangu wamezungumza sana, nimefanya ziara yangu nilitembelea taasisi ikiwemo Polisi, Magereza kama walivyosema wenzangu inasikitisha. Askari wa Korogwe Mjini wana nyumba chumba kimoja na sebule, ana watoto watano, wa kike wawili, wa kiume watatu, wote wana umri mkubwa hebu niambieni sasa maadili yako wapi hapo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, nimeona hapa mnazungumzia suala zima la Serikali kupitia mkopo wa China, sasa nimwombe Waziri atakapokuja ku-wind up aniambie huu ni mkopo ambao umeshapatikana au wanakusudia kupewa hizi fedha, naomba waje waniambie. Kama mkopo huu umepatikana, niwaombe askari wa Korogwe wawemo katika mpango wa nyumba hizi 4,136. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nichukue nafasi tena kumpongeza Waziri kwa kuwasilisha taarifa yake vizuri na haya mengine ni mapito, yeye apige mwendo, mti wenye matunda mazuri siku zote huwa unapigwa mawe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Naikumbusha Serikali suala la ujenzi wa bandari kavu ya Korogwe Mjini, eneo la Old Korogwe. Mheshimiwa Rais alipokuwa akiomba kura Korogwe, alikutana na hoja hii kutoka kwa wananchi na kuwaahidi atalifanyia kazi jambo hili, lakini kwenye vitabu vya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi hakuna mahali palipozungumzia suala hili la bandari kavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Mheshimiwa Rais alitoa ahadi ya lami Korogwe Mjini, kilometa tano, lakini ndani ya makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti hii, Korogwe haijaguswa. Niiombe Wizara hii kuona ni namna gani itatekeleza ahadi hii ili wananchi waendelee kuwa na imani na Serikali yao. Naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hotuba iliyowasilishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, napenda kumpongeza Waziri wa Ardhi na Naibu wake, pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa majukumu makubwa waliyonayo na utendaji wao mzuri ambao wameanza katika kipindi hiki cha uteuzi wa Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Mafuguli. Nawapongezeni sana kwa kazi nzuri pamoja na changamoto kubwa ambazo mnakabiliana nazo za migogoro ya ardhi iliyopo hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo Kamati yetu imesema, Serikali imekuwa haitoi fedha zilizoombwa katika bajeti ambayo ilikuwa imetengwa ya Wizara ya Ardhi. Kutotoa fedha kwa wakati na kutotoa fedha zote, kumechangia Wizara hii kutotekeleza majukumu yake vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itambue kwamba Wizara hii ina majukumu makubwa, imebeba mambo makubwa yanayohusiana na wananchi juu ya migogoro ya ardhi. Kwa hiyo, kutowapa fedha, kutopeleka fedha kwa wakati na kutopeleka fedha zote kunachangia kutotekeleza majukumu yao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali ihakikishe kwamba katika bajeti itakayokuwa imetengwa safari hii, wapewe fedha zao zote na kwa wakati ili waweze kutimiza majukumu yao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kuonyesha masikitiko yangu ambayo yamefanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuchelewesha mchakato wa maamuzi ya usimikaji wa Mfumo wa Utunzaji wa Kumbukumbu. Ucheleweshaji huu umekuwa ni wa miaka miwili na nusu. Tulipokuwa kwenye Kamati, tuliwaita Ofisi ya Waziri Mkuu tukataka watuambie, ni kwa nini wamechelewesha tender kwa ajili ya usimikaji wa mfumo huu wa kumbukumbu za ardhi? Majibu yaliyotolewa pale, yalikuwa ni ya ubabaishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sasa Ofisi ya Waziri Mkuu ifanye haraka suala la mchakato, ikamilishe mchakato huu haraka ili kusudi suala hili la usimikaji uweze kufanya kazi mapema ili kusudi matatizo yaliyopo ya ardhi yaweze kutatuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala zima la uendelezaji wa mji mpya wa Kigamboni. Naungana na maoni ya Kamati yetu kwamba wenzetu waliopo pale katika ofisi ile ya uendelezaji wa mji wa Kigamboni hawana kazi ya kufanya. Hata ukiangalia kwenye bajeti safari hii hawana fedha za maendeleo. Hata kipindi kilichopita, hawakuwa na fedha za maendeleo. Watu hawa wanapewa bajeti ya mishahara tu. Kwa hiyo, wanalipwa mishahara pasipo kazi. Hakuna haja ya kuendelea kuwepo na ofisi kule Kigamboni ya uendelezaji wa eneo lile wakati watu hawafanyi kazi. Ni vizuri watu hawa wakarejeshwa basi kwenye maeneo mengine wakaendelea kufanya kazi zao. Walipwe mshahara wakifanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamepanga jengo kubwa lenye gharama kubwa, wanakwenda wanasaini, wanatoka zao. Hata Biblia imesema asiyefanya kazi na asile. Iweje hawa wenzetu wanakuwepo katika kipindi cha miaka nane hakuna kazi inayofanyika pale na wala hakuna fungu la maendeleo! Tulipokuwa tunauliza, bahati nzuri Mheshimiwa Waziri alikuwa anawatetea kidogo, anasema waacheni tu, tutaangalia, tutatafuta fedha; utatafuta wapi wakati humu ndani ya bajeti hii ya maendeleo haipo? Fedha za kutafuta kuokoteza, zinatafutwa wapi? Ni vizuri watu hawa wakasambazwa kwenye maeneo mengine kwa sababu Wizara hii ina upungufu wa watumishi katika maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara iweke utaratibu sasa wa kuweka mabaraza ya ardhi kwa kila Wilaya. Ipo shida, pale kwangu Korogwe kuna Baraza la Ardhi, ni kero kubwa. Kesi za mabaraza ya ardhi haziishi, zimesongamana, ni nyingi. Baraza la Korogwe pale, linachukua Handeni, Kilindi, Lushoto na Korogwe yenyewe. Kuweka mlundikano wa kesi nyingi katika baraza lile, kunasababisha rushwa kubwa. Wananchi wanalalamika. Naiomba sana Wizara, ihakikishe kwamba kunafunguliwa mabaraza mengine, ikiwezekana kule Kilindi na Handeni wawe na baraza lao, Korogwe wawe na baraza lao na Lushoto wawe na baraza lao ili kuondoa usumbufu ambao wanaupata wananchi kuja kutoka Handeni kuja Korogwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kuhusu mashamba makubwa ya wawekezaji. Naomba hawa wawekezaji ambao wanapewa maeneo kwenye vijiji, basi waone umuhimu wa kuchangia masuala ya maendeleo kwa wananchi wa vijiji vile ambavyo wanaishi. Hiyo itajenga mahusiano mazuri na wanavijiji. Kutowasaidia kufanya hivyo, ndiyo unasikia migogoro mingine kwenye maeneo hayo, wawekezaji mara wanafukuzwa na wanavijiji, mara wanaingiliwa kuchomewa mali zao. Ni vizuri wakajenga mahusiano mzuri na wana vijiji ili kusudi wakiwasaidia kwa mfano miradi ya maji, ujenzi wa shule na mambo mengine mengi, hakutakuwa na matatizo na kero ambazo zinatokea sasa hivi kwa wawekezaji na wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Wizara ianze kuangalia namna ya kuwapa wawekezaji maeneo. Tuangalie maeneo ambayo yako wazi, tusiende kuwapa wawekezaji maeneo ambayo ni mashamba wa wananchi na makazi ya wananchi ili kuondokana na migogoro ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningependa kuishauri Serikali yangu sasa waanze kuona umuhimu wa kuanza kuwapatia wawekezaji maeneo ambayo sio makazi ya wananchi na siyo mashamba ya wananchi ili kuondoa migogoro ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja lakini naishauri Serikali bajeti inayotengwa itolewe yote na kwa wakati hasa ikizingatiwa Wizara hii inakabiliana na changamoto nyingi zinazohusiana na migogoro ya ardhi na maendeleo yanayohusiana na upimaji na uboreshaji wa mipango Miji na Majiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Waziri Mkuu ikamilishe haraka mchakato wa ununuzi wa vifaa vitakavyotumika kwenye mfumo wa utunzaji wa kumbukumbu za ardhi yaani Intergrated Land Information Management System, kutofanya haraka kunazorotesha ufanisi katika utawala wa ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya kuna mlundikano wa kesi nyingi kutokana na kushindwa kuhimili, kushughulikia zaidi ya Wilaya nne. Kwa mfano, Baraza la Ardhi la Korogwe linashughulikia Wilaya za Kilindi, Handeni, Lushoto, Korogwe Vijijini na Korogwe Mjini. Kwa kushika zaidi ya Majimbo na Wilaya tano kunasababisha uwepo wa rushwa jambo ambalo linazuia haki za wananchi.
Naishauri Serikali kuanzisha Mabaraza mengine kwa Wilaya ya Kilindi, Handeni, Korogwe Vijijini iwe na Korogwe Mjini na Lushoto iwe peke yake kulingana na ukubwa wa Wilaya hiyo yenye Majimbo makubwa matatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa uendelezaji Mji wa Kigamboni haujatekelezwa muda mrefu na hata haina bajeti ya maendeleo zaidi ya kuwa na bajeti ya mishahara na ulipaji wa pango la ofisi bila ya uwepo wa majukumu ya kufanya. Naishauri Serikali kuifunga ofisi hiyo na watumishi wapelekwe maeneo mengine yenye upungufu wa watumishi wa ardhi kwenye Miji na Majiji hadi Kata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuanza kuona umuhimu wa kutoa maeneo ya wawekezaji nje ya maeneo ya mashamba ya wananchi au makazi ya wananchi ili kuepuka ulipaji wa fidia. Wawekezaji wanaofaidika kupata maeneo kwenye Vijiji au Halmashauri wawe na mahusiano mazuri na wananchi katika maeneo yao kwa kuvisaidia vijiji huduma za jamii kwa maendeleo ya vijiji hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwepo wa master plan za vijiji, miji na majiji ni vema elimu ikatolewa kwa wananchi kabla ya ujenzi holela ambao unapoteza maana ya miji kwa kutokuwa na miundombinu ya barabara mifereji ya maji taka, maji ya mvua mabomba ya maji, viwanja vya michezo na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze juhudi za NHC kwa kazi nzuri wanayoifanya ya ujenzi wa nyumba bora na kauli mbiu yao ya maisha ni nyumba. Naishauri Serikali shirika hili lianze kuona umuhimu wa kujenga nyumba zenye bei nafuu ili kuwawezesha hata wale wenye kipato cha chini waweze kununua nyumba hizo. Aidha, Serikali ione namna itakavyoweza kuondoa VAT kwenye vifaa vya ujenzi wa nyumba hizi za NHC kwa lengo la kuwawezesha kufanikisha ujenzi wa nyumba zenye bei nafuu.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MARY P.CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze kwa kuunga mkono hotuba ya Waziri wa Fedha. Nipongeze jitihada za Serikali katika ukusanyaji wa mapato, lakini bado tuna safari ndefu ya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wetu juu ya kudai risiti pale wanapokuwa wamenunua bidhaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile niendelee kuishauri Serikali kwamba ni wakati muafaka sasa katika jambo hili la ukusanyaji wa mapato au kutoa elimu, tuanze kutoa kwa shule zetu za msingi na sekondari ili watoto wetu waweze kufahamu mapema juu ya suala la ulipaji wa kodi na kudai risiti pale wanaponunua bidhaa kwenye maduka.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbali ya hiyo Serikali imefanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato, lakini bado kuna ukwepaji wa kodi kwa baadhi ya vituo vya mafuta. Viko vituo vya mafuta ambavyo vyenyewe vinatumia ile mashine, ukienda kununua mafuta unapomdai risiti anakwambia mashine nimeipelekea kwenye chaji, unamwambia sasa inakuwaje umeshaniwekea mafuta, anakwambia sasa nifanyaje nimeipeleka kwenye chaji.
Kwa hiyo, pale hupati risiti kwa sababu ameshakwambia amepeleka kwenye chaji. Sasa niombe Serikali tuendelee kuwasimamia hawa wafanyabiashara wazifunge zile mashine kwenye zile mashine zinazotoa mafuta ili anapotoa mafuta na risiti inajitoa badala ya hizi mashine ambazo wanasema zinakwenda kuchajiwa huko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoteza mapato kwenye vituo vya mafuta kwa ujanjaujanja huo, kwamba wanapeleka kuchaji zile mashine.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala la TRA kukusanya mapato. Nakubaliana na jambo hilo lakini sasa tunaliwekaje kwa sababu Halmashauri zetu katika bajeti zao hususani Halmashauri yangu ya Korogwe ni sehemu ya own source ya mapato yao ya ndani kwa ajili ya shughuli za maendeleo katika Halmashauri. Sasa endapo TRA itakusanya mtatuwekea utaratibu gani wa kurejesha zile pesa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, bado nina uzoefu wa huko nyuma, viko vyanzo ambavyo Serikali ilivizuia kwamba Halmashauri isikusanye kwamba Serikali kuu itafidia, lakini bado kumekuwa na usumbufu na ucheleweshaji wa fedha hizo kurejeshwa kwenye Halmashauri baada ya kuwakataza kwamba wasikusanye yale mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Waziri aniambie baada ya kuwa TRA imekusanya fedha hizi na hasa ikizingatiwa kwamba ndiyo chanzo cha mapato katika Halmashauri zetu, watakuwa wanarejesha kwa wakati ili hizi fedha zikafanye kazi za maendeleo katika Halmashauri zetu? Nitamwomba Waziri aniambie atakapokuwa anafanya majumuisho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yako maeneo mengi ambayo yanapoteza mapato, tukikusanya vizuri hata upande huu wa madini tukiangalia vizuri hii mikataba ndugu zangu inaweza ikatusaidia kupata mapato ya kutosha tukaachana na hili suala hata la kutaka kukata kodi kwenye kiinua mgongo cha Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kukata kodi kwenye viinua mgongo hatukatwi Wabunge tu, nimeona kumbe wanakatwa mpaka Watumishi wa Serikali. Watumishi hawa wa Serikali na sisi Wabunge tunakatwa tayari kwenye mishahara yetu, sasa inakuwaje tena tunaendelea kukatwa kwenye kiinua mgongo? Niiombe Serikali iliangalie jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye Mfuko wa Maji na naungana na Kamati ya Bunge ambayo ilitoa taarifa yake kwamba iongezwe tena angalau Sh. 50/= kusudi iwe Sh. 100/=, ikiwa Sh. 100/= maana yake itatusaidia kwenye Mfuko wa Maji, lakini wakati huo huo zikajengwe zahanati na vituo vya afya. Wanawake wajawazito na watoto wanapata shida, endapo hatutajenga zahanati, endapo hatutakamilisha zahanati zilizokuwa zimejengwa na vituo vya afya, wanawake wataendelea kupata shida kwenda mwendo mrefu kwa ajili ya kwenda kujifungua na kwa ajili ya kuwapelekea watoto kupata matibabu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe Serikali yangu ikubaliane na suala la kuongeza Sh. 50/= ili iwe sh. 100/= na hatimaye fedha zile zigawanye ziende kujenga vituo vya afya pamoja na zahanati. Ukiangalia pale kwangu Korogwe Mjini sina hospitali ya Wilaya, nina zahanati pale ya Majengo, nakusudia sasa ile zahanati iwe ndiyo kituo cha afya ambacho kitakuwa kama sehemu ya Hospitali. Sasa kama hakijatengewa fedha hawa wananchi wangu wa Korogwe wanatibiwa wapi? Niombe Serikali tukubaliane kwa hili ambalo limependekezwa na Kamati ili kusudi fedha hizi ziweze kusaidia kujenga zahanati pamoja na vituo vya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha standard gauge, nakubaliana na naunga mkono kwa asilimia mia, lakini hebu tuitazame na reli ya Tanga, kwa sababu sasa hivi tunasema litajengwa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanga. Hebu tuiangalie na reli ya Tanga kuweza kuipa fedha ili kusudi iweze kujengwa kwa kiwango cha standard gauge.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumaini yangu kwamba Waziri naye ataliangalia hili kwa sababu tumekubaliana bomba hili linaanza kujengwa hivi karibuni, ni kwa nini sasa Tanga haijatengewa fedha kwa ajili ya kujenga reli kwa kiwango cha standard gauge? Wamesema hili bomba kwa taarifa nilizonazo litakuwa linapita kando kando mwa reli mle, niombe sana Serikali yangu iliangalie hilo kuona kwamba ni namna gani ambavyo inaweza ikajenga reli ya Tanga kwa kiwango cha standard gauge.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba niunge mkono hoja na kushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Naishauri Serikali, Sheria za Ardhi na Sheria za Uhifadhi, kwa maana ya mipaka inayohusiana na maeneo ya maliasili itazamwe upya kwa lengo la kuondoa migogoro na migongano kati ya wananchi na maliasili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha wataalam wa ardhi, maliasili, kilimo na maji wakutane ili kuisaidia Serikali kumaliza migongano na migogoro ya ardhi kwa kuifanyia uchambuzi wa kina na hatimaye watoe mapendekezo kwa Serikali ili yaweze kupitiwa na kufanyiwa kazi, bila hivyo migogoro hii haitaondoka au haitakwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mifugo kuingizwa kwenye hifadhi na hifadhi kufanywa malisho halikubaliki. Kuachia jambo hili liendelee litasababisha uharibifu mkubwa wa ardhi, mazingira, kuondoa uoto wa asili kutokana na ng‟ombe kukanyaga hovyo. Misitu itakwisha kwani wafugaji ndio wanaokata miti na kuchoma moto kwa lengo la kutaka nyasi ziote upya kwa ajili ya malisho yao, maliasili itatoweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la majangili, askari wa wanyamapori waendelee kupatiwa mafunzo na mbinu zitakazowawezesha kukabiliana na majangili. Aidha, vitendea kazi ni lazima vipatikane kwa askari hawa, bila kufanya hivyo kuhimili vishindo vya majangili itakuwa ngumu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kuboresha miundombinu itakayowezesha watalii kutembelea hifadhi kwa urahisi zaidi na kuingizia mapato ya Serikali kwa wingi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu. Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza Waziri Mkuu, Mawaziri pamoja na Manaibu Waziri kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kutekeleza majukumu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimwambie kaka yangu Mheshimiwa Khatib, kwamba ugomvi wa mke na mume mara nyingi huwa wanamalizia chumbani. Mnapogombana huko chumbani, mkitoka nayo nje, hayo mambo yanakuwa yako hadharani, kila mmoja anayaingilia.
Sasa msilichukulie kwamba Serikali ya CCM ndiyo inayowafitinisha ninyi. Ugomvi huu ninyi mmeutoa chumbani, mmeuleta hadharani. Sasa naomba sana, msiizungumzie Serikali kwamba ndiyo inayowahujumu ninyi. Hebu mkakae mmalize matatizo yenu, msiingize Serikali kwenye matatizo yenu. Sasa nimekujibu basi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nianze na bajeti ya Mfuko wa Bunge. Niungane na maoni ya Kamati ya Bajeti kwamba Mfuko wa Bunge unakabiliwa na changamoto nyingi za kutokupata fedha kwa wakati; na hata zinapopata hizo fedha, hazipati fedha yote. Naiomba Serikali iangalie huu Mfuko wa Bunge, kwani huu mhimili wa Bunge ndiyo unaopitisha bajeti zote hizi za Serikali ambazo zinakwenda kufanya shughuli za maendeleo. Ni mhimili huu wa Bunge. Sasa Mhimili huu, ndio huu huu tena ambao haupewi fedha za kutosha kuhakikisha kwamba zinatimiza majukumu yake ya kibunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali izingatie maoni na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Bajeti ili iweze kuhakikisha kwamba inatoa fedha za kuhakikisha zinaendesha shughuli za Bunge bila kusuasua.
Mheshimiwa Naibu Spika, safari hii Bunge limefika mahali Waheshimiwa Wabunge wamesafiri kwenda kwenye Kamati bila malipo kutokana na kutokuwa na fedha katika Mfuko wa Bunge. Sasa naiomba Serikali, pamoja na kwamba mihimili yote ina umuhimu wake, lakini mhimili huu una umuhimu zaidi kwa sababu ndiyo unaokaa kupitisha mambo yote haya ambayo hata wewe Mheshimiwa Waziri Mkuu huwezi kwenda kukagua shughuli za maendeleo kama fedha hazijapitishwa na mhimili huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana, katika mapendekezo yaliyotolewa kwenye kitabu cha bajeti ukurasa wa 14, tusipoangalia hili Bunge linaweza lisifike mwezi wa Sita. Wameomba mapendekezo pale wanasema, Kamati inaishauri Serikali kuridhia maombi ya bajeti ya shilingi bilioni 21 ili Bunge liweze kutekeleza majukumu yake mpaka kufikia mwezi Juni. Kwa hiyo, naiomba Serikali basi iweze kutekeleza hili angalau Bunge liweze kufanya shughuli zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la maji. Naishukuru Serikali, kule kwangu Korogwe nilikuwa na tatizo sugu la maji ambalo bado lipo halijakamilika, lakini angalau sasa limeanza kutekelezwa. Alikuja Naibu Waziri akatembelea akaona. Tuna Mto Pangani unapita katikati ya Mji wa Korogwe, alikuja akazungumza na akaenda kutekeleza, akatuletea fedha angalau shilingi milioni 500, tumeanza kuchukua maji kutoka kwenye Mto Ruvu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuwaomba Wizara ya Maji kwamba ni vizuri zile fedha ambazo walituahidi, shilingi bilioni mbili kwamba watatupa katika bajeti hii, basi waweze kuzitoa fedha hizo itakapokuwa tumepitisha kwenye bajeti ili ziweze kufanya kazi ya kutengeneza miundombinu pamoja na matenki ili kusudi wananchi wa Korogwe waweze kuondokana na tatizo la maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la afya. Pale Korogwe kuna Chuo cha Uuguzi na chuo kile kiko chini ya Wizara ya Afya. Chuo kile hakijawahi kutengewa fedha miaka 10, lakini kina jengo ambalo limejengwa limesimama, ni la muda mrefu, miaka 10 halijawahi kutengewa bajeti. Fedha ambayo imeteketea pale ni fedha ya walipa kodi wa nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, jengo lile badala ya kuwa limesimama vile, matokeo yake litaanza kupata crack, Serikali itaanza kutenga bajeti nyingine kwa ajili ya kukarabati jengo lile. Naiomba sana Serikali iangalie ni namna gani itakavyomalizia lile jengo la Chuo cha Uuguzi pale Korogwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri alitembelea eneo lile siku ambayo nimemwalika kwenye Jimbo langu kwa ajili ya kuja kuona shughuli za maendeleo, hususan ujenzi wa Kituo cha Afya ambacho ni cha ghorofa tatu. Namshukuru Mheshimiwa Waziri alikuja akaona
tunafanya kazi nzuri na nategemea Mheshimiwa Waziri kwamba Mwenyezi Mungu akikujalia basi mnaweza mkatupiga jeki katika kile Kituo cha Afya, hasa ikizingatiwa kwamba Halmashauri ya Mji wa Korogwe haina Hospitali. Sasa kwa kuwa haina Hospitali, basi kile Kituo cha Afya ndiyo kitatufanya sisi tuwe na hospitali.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa, kwa kuwa, Mheshimiwa Waziri alienda akaona kile chuo na akaliona lile jengo lilivyo, basi atusaidie zipatikane fedha kwa ajili ya kukamilisha jengo lile ili ile fedha ya wananchi iliyokuwa imetumika wakati ule isiweze kupotea.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nirudie tena suala la maji. Kuna miradi ile ya World Bank, ilikuwa itekelezwe pale Msambiazi, Lwengera Relini na Lwengera Darajani. Katika Bunge lililopita kulitengwa fedha, shilingi milioni 560 kwa ajili ya mradi wa Msambiazi na Lwengera Relini na Darajani, lakini fedha zile zinavyoletwa kule, maelekezo yanayofika kule, badala ya kujenga ule mradi wanasema zile fedha zilipe madeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara ya Maji na Umwagiliaji, mradi ule, wananchi wa Msambiazi wanachojua wao, wametengewa fedha. Sasa fedha inapokuja inaenda kulipa madeni ya miradi mingine iliyopita. Tunawaeleza nini wananchi wa Msambiazi na Lwengera Relini na Lwengera Darajani?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali itenge fedha za madeni, ilipe madeni na zile zinazotengwa kwa ajili ya miradi, zipelekwe kwenye miradi husika. Ni matumaini yangu kwamba, Waziri wa Maji amenisikia. Ni vizuri hizo fedha zikatoka zikaenda kujenga ule mradi wa Msambiazi kama ambavyo ilikuwa imepangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la barabara. Naiomba Serikali, hizi Halmashauri ambazo zinaitwa Halmashauri za Miji, naishauri Serikali kama inawezekana; kwa kuwa tayari inaitwa miji, Halmashauri za Miji au Manispaa, tuanze kutenga bajeti angalau ya kilometa mbili mbili au moja kwa ajili ya lami ili iendane na hadhi hiyo inayozungumzwa kwamba Halmashauri za Miji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pale Korogwe Mji, pale ni sebuleni; ukitoka Dar es Salaam, unakuja Korogwe, ndiyo hiyo inayokwenda moja kwa moja Kilimanjaro, Arusha, inaenda Nairobi, Kenya. Sasa pale sebuleni mkitusaidia kila mwaka tukawekewa angalau kilometa moja au mbili za lami, tutaishukuru sana Serikali angalau mji ule uweze kuwa na barabara za lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, naisema hiyo, inaweza ikasaidia sana kuondokana na zile barabara za changarawe ambazo zinatengewa fedha kila mwaka. Tukijenga hizi za lami zinakuwa na mifereji ambayo imejengewa, lakini hizi za changarawe hazijengewi na mawe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Serikali, kwenye miji hii ili tuifanye iwe miji mizuri, tujitahidi basi angalau kila mwaka tukiwatengea hiyo kilometa moja au mbili ili kusudi miji hiyo iweze kuwa mizuri kwa maana ya kuwa na lami katika mji wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba nishukuru tena, yangu machache yalikuwa ni hayo.
Nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kuhusu Mfuko wa Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Kamati ya Bajeti kutambua Mfuko wa Bunge kukabiliwa na changamoto za kutopata fedha za Bajeti kwa wakati na mara nyingine hutolewa zikiwa pungufu jambo ambalo linasababisha shughuli za Bunge kuendeshwa kwa kusuasua ama kubahatisha. Niishauri Serikali iangalie upya utoaji wa fedha za Mfuko wa Bunge kwa wakati na kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 (kifungu na 48). Hata hivyo ni vyema hata kama watatoa kwa kila mwezi basi fedha hiyo itolewe yote ili Ofisi ya Bunge iweze kutekeleza majukumu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, afya; yapo majengo yaliyotelekezwa miaka 10 mfululizo hayajatengewa fedha hususani jengo la Chuo cha Uuguzi Korogwe. Niiombe Serikali (Wizara ya Afya) iangalie upya namna itakavyokamilisha jengo hilo hata kwa kutengewa fedha kidogo kidogo
hadi kumalizika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza juhudi zinazofanywa na hii Wizara ya Ujenzi lakini niishauri Serikali fedha zinazotolewa kwa ajili ya barabara za changarawe hususani maeneo ya mjini kama vile Halmashauri ya Mji wa Korogwe Wizara ianze kuona uwezekano wa kutenga Bajeti kila mwaka angalau kilometa 1 - 2 kupitia bajeti ya Road Fund. Aidha, kama haiwezekani basi fedha za barabara za changarawe mijini zitengwe na za kutengeneza mifereji kwa kiwango cha mawe ili kuweka uimara wa barabara hizi.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kazi nzuri inayofanywa na Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ya Afya ndiyo Wizara Mama kwa maisha ya Watanzania. Hivyo, ipo haja bajeti inayotengwa kutolewa yote ili kuiwezesha na kuipa wepesi Wizara hii kutekeleza majukumu yake. Bila afya nzuri hakuna viwanda wala shughuli zingine zinazoweza kuinua uchumi wa nchi yetu. Hivyo basi, nashauri bajeti inayotengwa itolewe yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mji wa Korogwe haina hospitali. Asilimia 60 ya wananchi wanapata matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Korogwe Vijijini lakini jitihada za makusudi zinafanyika kujenga kituo cha afya chenye majengo ya ghorofa matatu. Nimshukuru kwa ziara aliyoifanya Korogwe, alishiriki shughuli za maendeleo (Msalagambo) na kuahidi kuchangia shilingi milioni 300 katika ujenzi unaoendelea. Aidha, nimshukuru ametuahidi kutupatia ambulance. Mwenyezi Mungu ampe wepesi kukamilisha ahadi ambazo wananchi wa Korogwe wamejenga matumaini makubwa kwake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jengo la Chuo cha Wauguzi Magunga lililopo Korogwe Mjini la ghorofa ambalo lilianza 2010 kwa ajili ya madarasa na Ofisi za utawala limetelekezwa kwa kutotengewa fedha kwa ajili ya ukamilishaji. Mwaka wa fedha 2016/2017 lilitengewa shilingi milioni 400 lakini hazikupelekwa hadi sasa. Niiombe Serikali kulitengea fedha jengo hili kwani linachakaa na litasababisha hasara kwa Serikali kutenga fedha zingine kwa ajili ya ukarabati, huko kutakuwa ni kufuja fedha za wananchi walipa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba Serikali iangalie upya kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuwanusuru akinamama wajawazito. Kutofanya hivyo kutaendelea kusababisha vifo vya wanawake hawa na kupunguza nguvu kazi ya Taifa ambayo kwa namna moja au nyingine wanawake ndiyo watenda kazi wazuri katika Taifa hili.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi nami niweze kuchangia Hotuba aliyoiwasilisha Waziri Mkuu. Aliiwasilisha kwa umahiri mkubwa, hatuna budi kuiunga mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi ya kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi kubwa anazozifanya akishirikiana na Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri na Naibu Mawaziri na Watendaji Wakuu wa Serikali. Kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu sisi wote tunaiona. Tunaiona kwa macho, tunaiona kwa vitendo na ushahidi wake upo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo kauli mbiu imezaa matunda kwa kuleta Bomba la Mafuta kutoka Hoima kwenda Tanga ambako ni kwetu, lazima nitaje Korogwe kwa sababu ni kwetu. Tumeona hizo juhudi za reli ya standard gauge, tunaona hizo juhudi za ununuzi wa ndege tatu ambazo wengine wanabeza, wanabeza halafu baadaye wanapanda. Tumeona juhudi za upelekaji wa umeme wa REA vijijini, tumeona juhudi za ujenzi wa viwanda, tunaona juhudi vile vile za ujenzi wa ukuta wa Mererani ambao Mheshimiwa Rais leo ameenda kuufungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juhudi zote hizi zinafanywa na viongozi wetu ambao tumewachagua kutoka 2015 hadi 2020, tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa ule wa 10 ameeleza ni namna gani Serikali inavyosimamia uhuru wa wananchi kujiunga katika vyama wanavyovitaka. Sasa nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kusimamia hayo hadi Chama cha Mapinduzi kimeweza kushinda Kata 58, kimeshinda Majimbo matano, haki ya Mungu hiki chama dume, hapana chezea CCM, kabisa hao wengine wajikaze. Pamoja na hayo naomba niendelee kuipongeza Serikali yangu na nitaipongeza sana, mtalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Serikali pale kwangu Korogwe kwenye Halmashauri yangu ya Mji wa Korogwe imeniwezesha kunijengea Stendi ya kisasa kwa gharama ya bilioni nne. Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokuja kuifungua ile stendi anasema haipo stendi kama ile ya Korogwe, naishukuru sana Serikali. Hata hivyo, tunajengewa Soko la Kimataifa kwa gharama ya bilioni moja point mbili, hivi kwa nini nisiipongeze Serikali? Hilo nalo ni dogo? Lazima niipongeze Serikali kwa kazi ambayo inaifanya. Piga makofi kabisa ndugu yangu wa CHADEMA huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Maji. Tuna mradi wa maji ambao umeanza, unafanya kazi, kwa maana ya Msambiazi; tulitengewa milioni mia sita na saba, mkandarasi yuko kazini, mradi ule umekamilika asilimia 96. Tuna mradi wa Lwengela Relini na Darajani tulitengewa milioni mia tano na nane, mradi ule mkandarasi yuko kazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na tatizo kubwa la maji pale Korogwe Mjini Waziri wa Maji alitembelea Wilaya ya Korogwe akaamua kwamba tuachane na kuchimba visima tutumie ule Mto Ruvu, walituletea milioni mia tano ambapo sasa hizo milioni mia tano zimeweza kujenga chanzo cha maji ambacho kitatupatia maji katika Mji wetu wa Korogwe. Ninachokiomba kwa Wizara ya Maji sasa, naomba sasa nipatiwe fedha kwa ajili ya miundombinu ambayo itafikisha maji kwenye maeneo hayo yote ambayo tumetengewa fedha kwenye mradi ule wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, nilipoonana naye aliniambia watatutengea bilioni mbili ili ziweze kutusaidia kuweza kupata miundombinu ili kusudi ile miundombinu iweze kusambaza maji katika ule Mji wa Korogwe. Kwa hiyo, hayo ni maendeleo mazuri yanayofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la viwanda. Niendelee kuipongeza Serikali yangu kwa kazi kubwa ambayo inaendelea kuifanya ya kuhimiza suala la viwanda. Pale Korogwe tulikuwa na kiwanda cha matunda, katika suala la ubinafsishaji kiwanda kile kilibinafsishwa. Yule bwana aliyepewa kiwanda kile aliamua kuondoa mashine zote akahamia nazo Dar es Salaam, jengo lile limebaki gofu. Kitendo cha kuondoa zile mashine kimesababisha akinamama na vijana hasa ikizingatiwa Korogwe, ikizingatiwa Muheza tunalima sana matunda, yanaoza hakuna kwa kupeleka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe Serikali yangu, kwa sababu jengo lile sasa limebaki ni gofu tuombe tupewe sisi Halmashauri ya Korogwe ili tuweze kulitumia kwa kuwawezesha akinamama na vijana waweze kutengeneza matunda kwa kutumia kile kiwanda, watengeneze juice kupitia kile kiwanda, viwanda vidogo vidogo ili kusudi waweze kujiwezesha kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la umeme wa REA. Naishukuru Serikali kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea nayo. Nami kama mmoja wa watu ambao nina uhitaji na umeme wa REA niliomba nipatiwe umeme wa REA kwa kata zangu kama tano, sita hivi; Kata ya Kwamgumi, Kwamndolwa, Old Korogwe, Mtonga, Mgombezi na Bagamoyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Naibu Waziri niliongea nao wamenipokea vizuri sana na waliahidi kwamba watanisaidia ili niweze kufanikisha hili. Hata hivyo, kwa bahati mbaya sana yule Mkandarasi anasema vile vijiji havipo kwenye orodha yao. Kwa hiyo walikuwa wanaomba ikiwezekana wapelekewe hiyo orodha ili kusudi waweze kuanza kuifanya kazi ya kuweka umeme katika wilaya yetu au katika kata zile ambazo nimezitaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara; naipongeza TARURA, natofautiana kidogo na ndugu yangu maana yake mwenzangu yuko vijijini mimi niko mjini. TARURA kwangu kwa maana ya barabara inafanya kazi vizuri. Inafanya vizuri isipokuwa kwa sababu ni wilaya ya mjini, naomba barabara za mjini; nilimsikia Mheshimiwa Waziri juzi nilipokuwa nimeuliza swali la nyongeza alisema halmashauri za miji zimewekwa kama halmashauri 25 ambazo zitaanza kujengewa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wakati tunaendelea kusubiri mpango huo wanatengeneza kwa kiwango cha changarawe. Sasa niombe hawa wanaotengeneza kwa kiwango hiki cha changarawe, TARURA, watengewe mafungu kwa ajili ya kujenga hii mitaro, mifereji kwa mawe ili kusudi barabara hizi ziweze kudumu kwa muda mrefu wakati tunaendelea kusubiria habari ya lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la elimu. Naishukuru Wizara ya Elimu ilinisaidia kunipatia fedha kwa ajili ya kujenga Maktaba ya Chuo cha Ualimu pale Korogwe, walinipatia milioni mia mbili na arobaini na tano. Naomba niwataarifu tu kwamba kazi inaendelea vizuri imefikia asilimia 85.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu ile maktaba ikikamilika itatusaidia kwa watoto wetu, wanachuo pamoja na shule zetu za sekondari; ni maktaba kubwa ambayo nadhani hata nchini hapa atakayekuja kuifungua ataiona kwamba ni kubwa kuliko za maeneo mengine yote ambayo wamejenga zile maktaba…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia katika hotuba aliyoitoa Mheshimiwa Waziri wa Afya, ndugu yangu, mdogo wangu Ummy Mwalimu. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hotuba hii ni nzuri, vilevile niunge mkono mapendekezo yaliyotolewa na Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi ya kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ambavyo wenzangu wamezungumza kwamba anafanya kazi kubwa ya kuhakikisha Watanzania wanakuwa na afya bora. Nimpongeze Waziri, nimpongeze Naibu Waziri, nimpongeze Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Ndugu yangu mpendwa Dkt. Chaula na Watendaji wote wa Wizara hii ya Afya kwa kazi kubwa na nzuri ambayo inaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii Mheshimiwa Ummy nimpe salamu za wanawake wa Mkoa wa Tanga wanasema kwamba wanashukuru kwelikweli kwamba Rais alimteua kuwa kwenye nafasi hii ameitendea haki, amewatoa aibu wanawake wa Mkoa wa Tanga. Kwa
hiyo, wanaendelea kumwombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kutimiza majukumu yake hayo vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitashukuru kwa sababu sikuchangia katika ile Wizara ya TAMISEMI. Wizara ya TAMISEMI wamenipatia hospitali ya Wilaya ya Korogwe ambayo ilikuwa ni Korogwe Vijijini, nawashukuru sana. Wananchi wa Korogwe Mjini wanawashukuru kweli, lakini vile vile nitakuwa sijamtendea haki kaka yangu Profesa Maji Marefu kwa sababu sisi ni mapacha, kwa kumtengea fedha bilioni 1.5 ili aweze kujenga hospitali katika Halmashauri yake ya Korogwe Vijijini, tunaishukuru sana Serikali kwa moyo huo wa upendo mliotuonesha katika Wilaya yetu hiyo ya Korogwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba nimepewa hiyo hospitali naomba hospitali ile ni kuu kuu, nitaomba sasa nisaidiwe kupewa fedha kwa ajili ya ukarabati wa hospitali ile. Lile jengo la mbele Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu analijua linavuja. Kwa hiyo, naomba wanisaidie fedha kwa ajili ya ukarabati pale watakapokuwa wametukabidhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matamshi ya humu ndani hayatoshi, niiombe TAMISEMI sasa ituandikie rasmi kutukabidhi ile hospitali ili kuanzia tarehe moja mwezi wa Saba tuweze kuanza kuisimamia Korogwe Mjini. Nitashukuru sana utekelezaji huo utakapokuwa umekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze Serikali kwa kuweza kuipatia fedha hospitali ya Muhimbili ambapo sasa imeweza kuanza kufanya kazi ya kutoa huduma ya upandikizaji wa figo. Hii imesaidia sana kupunguza gharama za kwenda kutibiwa nje hasa ikizingatiwa hata kwenye taarifa ya CAG imeonesha kwamba tumepeleka wagonjwa wengi India kwenda kwenye matibabu na gharama imekuwa kubwa, lakini kwa utaratibu huu ambao sasa hospitali ya Muhimbili imeanza ya kupandikiza figo, itatupunguzia sana kupeleka wagonjwa nje na gharama zitapungua. (Makofi)

Mheshimishiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Dkt. Janabi kwa kazi kubwa anayoifanya na wenzake katika hospitali ile, kile kitengo cha Moyo cha Jakaya Kikwete. Niiombe Serikali, naungana na Kamati kwamba zile bilioni mbili walizokuwa wametengewa tunaomba wawape fedha hizo ili waweze kununua hivyo vifaa tiba, tusipofanya hivyo maana yake tunataka hawa watu sasa wasiendelee kufanya kazi nzuri ambayo tayari imeanza kufanyika. Shida iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali ile inatusaidia kupunguza gharama za kwenda nje. Sasa kama waliomba bilioni mbili inashindikana kuwapa ni kwa nini? Naomba Serikali hebu iwatazameni katika hili, wapewe hizo bilioni mbili ili waweze kununua hivyo vifaa tiba waweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizungumzie suala la Chuo cha Uuguzi pale Korogwe. Jambo hili limechukua muda mrefu sana. Chuo cha Uuguzi Korogwe jengo hili limejengwa lina miaka sasa 15 halijawahi kutengewa fedha za kumalizia jengo lile. Mheshimiwa Waziri naomba mniambie leo, kulikoni jengo lile limejengwa mpaka kufikia ile hatua ya kutaka kuanza kupauliwa halitengewi fedha. Fedha na kodi za wananchi zimepotea pale maana yake lile jengo lisipomaliziwa, likianza kuchakaa tutaingia gharama nyingine ya kuanza kutenga fedha kwa ajili ya jengo lile pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe mdogo wangu Mheshimiwa Ummy alifika aliliona lile jengo, kile chuo kiko pale, watoto wako pale wanasoma, lakini kwa bahati mbaya sana majengo ya utawala hayapo, wamechukua madarasa ya wanafunzi wameweka partition zimekuwa ndio ofisi za Walimu, halafu watoto wanaenda kusomea kwenye bwalo la chakula, haiwezekani. Napata mashaka kwa nini fedha haitengwi, inawezekana kwa kipindi hicho ulikuwa ni uchochoro wa kupitisha fedha zile kwenda kuliwa, kama siyo kwa nini fedha hazitengwi kwa ajili ya jengo lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaomba majibu ya kunitosheleza hapa kwa sababu nimeona kwenye kitabu hapa wamezungumzia mipango yao, wamesema wataboresha vyuo vya afya ili kuendeleza uzalishaji wa wataalam, wakavitaja hapo. Sijaona kuzungumzia Chuo cha Uuguzi Korogwe, kuna nini? Mheshimiwa Ummy mdogo wangu nampenda kweli kweli na mimi ndiye mpiganaji wake kwa kura za maoni Mkoa wa Tanga. Katika hili hatutaelewana. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Nichukue nafasi hii kuunga mkono hotuba ya Waziri, aliiwasilisha vizuri na nimpongeze na nimtake asife moyo kwani Roma haikujengwa kwa siku moja. Hizi changamoto na mambo mengine yote yanayozungumzwa kwa maana ya kuchangia na kushauri ayachukue kama ni sehemu ya changamoto kuweza kuyafanyia kazi. Kama ambavyo nimesema Roma haikujengwa kwa siku moja basi mtaendelea kuyafanyiakazi kadri siku zinavyokwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze yeye Waziri pamoja na Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii ya Elimu kwa kazi nzuri ambayo wameendelea kuifanya. Wizara hii ni ngumu na ni nzito, lakini kwa sababu imekabidhiwa kwa Profesa na ndiyo maana hata Mheshimiwa Rais inawezekana aliona kwamba amkabidhi Profesa Mama Ndalichako kwa sababu amebobea katika masuala hayo ya elimu anaweza akasaidia kuendelea kuiboresha elimu katika nchi yetu hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi ya kumshukuru sana na kuishukuru hii Wizara. Shule ya Korogwe Girls ilipata tatizo la kuunguliwa na bweni, lakini walipopata taarifa waliweza kuja kutushika mkono, wakatusaidia na kuhakikisha kwamba lile bweni linarejea ili kuusudi watoto waweze kukaa na kuendelea na masomo, tunawashukuru sana kwa huduma ile mliyotupatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niendelee kushukuru vilevile kwamba shule ile ni kati ya shule ambazo ni shule kongwe ambazo zimepewa fedha za ukarabati. Nalo hilo naendelea kushukuru, tunashukuru sana, isipokuwa labda niombe tu kwamba shule ile ya Korogwe Girls ipo katikati ya Mji wa Korogwe na ni shule ya wasichana. Sisi wenyewe tumeanza kwa jitihada zetu kujenga uzio ili iweze kuwa ndani humo hasa ilizingatiwa kwamba ni watoto wa kike wale lakini humo ndani kuna wenye ulemavu Waziri mwenyewe unafahamu. Nilikuwa naomba sana Mwenyezi Mungu akupe wepesi katika haya nitakayokuomba ikiwezekana mtusaidie angalau tuweze kumaliza uzio wa shule ile ili watoto wale wa kike waweze kukaa mle ndani. Eneo lile ni kubwa sana kwa maana ile kazi tuliyoianza sisi wenyewe tutashindwa kuimaliza, kwa hiyo ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri ulione hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa hotuba yake ya jana pamoja na kwamba inawezekana wengine haikuwapendeza lakini kwa maelezo yake mazuri jinsi nilivyokuwa nimemsikiliza mimi, nimeamini kabisa kwamba ana nia nje na Serikali hii, ana nia njema na
wananchi wake wa Tanzania kwahiyo nampongeza kwa hotuba ile aliyoitoa hasa pale alipozungumza kwamba wako wafanyakazi ambao wamepandisha madaraja lakini walikuwa hawajalipwa zile stahiki zao sasa watalipwa. Ziko stahiki za wafanyakazi ambazo zilikuwa hazilipwi sasa zitalipwa, hiyo ni hatua nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaiomba Serikali kwamba sasa madeni yote yanayohusiana na wafanyakazi maadam Mheshimiwa Rais ana nia njema itakapofika wakati madeni hayo yote na stahiki zao zote waweze kulipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la Shule ya Sekondari Semkiwa ambayo Mheshimiwa Waziri ulikuja ukaiona pale, tuliaku lika ukaja kuweka jiwe la msingi, kwa maana ujenzi wa bweni ambalo sisi tulitumia nguvu zetu na tukalijenga lile bweni kwa ajili ya watoto wetu wa kike. Wazazi wanakushukuru sana Semkiwa. Baada ya kuona ile jitihada ukatusaidia kutupa fedha kwa ajili ya ujenzi wa bweni lingine shilingi milioni 75.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda vizuri Mwenyezi Mungu anatusaidia na tuna uhakika kwamba tutalimaliza na ikiwezekana sasa uje ufungue rasmi yale mabweni yote mawili kwa jitihada zako zile ambazo umeweza kututembelea pale na kuweza kutuongezea. Ila nikikumbushe tu Mheshimiwa Waziri kwamba ulituahidi pale vitanda na magodoro pale lile bweni ilikuwa ni vitanda 48 na magodoro 48, kwa lile bweni ambalo tulikuwa tumeshalijenga. Ni matumaini yangu kwamba utatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikuombe tena Mheshimiwa Waziri kwamba nina Shule ya Sekondari Mgombezi iko nje ya Mji wa Korogwe, ina vijiji sita. Nina shule ya Chifu Kimweri iko nje ya Mji wa Korogwe, ina vijiji vitano. Watoto wa kike wanatembea kilometa nne mpaka tano kwenda shule tena kwenye makatani, mnajua kule kuna mkonge, kwenye mkonge mule kwenda shule na kurudi, nilikua naomba sana. Kwa mfano Mgombezi, kule Mgombezi tayari tumejenga bweni moja, sasa kama utatusaidia kutuongeza bweni lingine ili watoto wa kike hawa waweze kukaa na kusoma wakiwa pale shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hii ya Chifu Kimweri tumeshaanza kujenga bweni. Nimuombe Mheshimiwa Waziri kwa shule hizi mbili ambazo zina umbali mrefu wa watoto wa kike kutembea, niwaombe sana, mimi najua Mwenyezi Mungu atakupa wepesi tu katika haya ninayoyasema ili angalau uweze kunisaidia hizi shule mbili ambazo ziko mbali sana nje ya Mji watoto wa kike waweze kusoma vizuri.

Mheshimiwa Nwenyekiti, suala la upuandishwaji wa madaraja; mimi nashukuru zoezi hili sasa linamuelekeo sasa kuendelezwa. Sasa niombe basi mna ile tabia ya kuwapandisha madaraja halafu hamuwapi zile fedha kulingana na madaraja yao. Niombe liende sambamba, mtu akipandishwa daraja basi liende sambamba na haki yake ile anayostahili kulipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakusudia kuanza kujenga Chuo cha VETA pale Korogwe, tuna eneo kubwa sana kule Mgombezi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba mbili; TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora. Nianze kwa kuunga mkono hotuba hizi lakini naomba uniruhusu ninukuu kutoka kitabu cha Mithali 15:2 inasema kwamba: “Ulimi wa mwenye hekima hutamka maarifa vizuri; bali vinywa vya wapumbavu humwaga upumbavu”. Mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mwenyezi Mungu anisaidie nitumie ulimi wa mwenye hekima katika kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya ndani ya nchi hii. Nampongeza Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Wasaidizi wao kwa kazi kubwa ambayo wameendelea kuifanya katika nchi hii.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwambie akae chini.

MWENYEKITI: Kuhusu utaratibu na msiingie na uchochoro wa utaratibu.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nasimama kwa mujibu wa Kanuni ya 64(1)(e). Tunapenda kuitumia Kanuni hii lakini labda ama waliyoitunga hawakuitunga vizuri au hatuielewi. Kanuni inasema: “Bila ya kuathiri masharti ya Ibara ya 100 ya Katiba inayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano katika Bunge, Mbunge, (e) hatazungumzia mwenendo wa Rais…”

MWENYEKITI: Hebu, rudia Kanuni ya 64 ngapi?

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya 64(1)(e).

MWENYEKITI: Endelea.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, inasema kwamba: “Mbunge, hatazungumzia mwenendo wa Rais, Spika, Mbunge na kuendelea.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, humu ndani tumekuwa tukizungumzia mwenendo wa Rais. Tofauti yetu sisi upande na huu na upande ule, huku tumekuwa tukizungumzia mwenendo wa Rais ambao tunaona una upungufu na wale wanazungumzia mwenendo wa Rais wanaoona hauna upungufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukabaliane na Kanuni ya 64(1)(e) kwamba ama wote tusizungumzie mwenendo wa Rais au kila mtu azungumzie mwenendo wa Rais kwa kadri anavyoona. Kwa mtazamo wangu naona Kanuni hii inakiukwa. Ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Soma Kanuni ya 68(10).

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya 68(10) inasema: “Uamuzi wa Spika kuhusu suala lolote la utaratibu utakuwa ni wa mwisho.”

WABUNGE FULANI: Aaa, sasa mmeamua nini?

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo?

MWENYEKITI: Ndiyo, uamuzi wa Spika ni wa mwisho.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Sikilizeni jamani, hizi Kanuni hazisomwi kama unasoma gazeti, zinasomwa kwa mtiririko.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Kaa chini, endelea Mheshimiwa.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naona mwanangu alikuwa ananipotezea muda tu lakini naendelea kuwaambia kwamba wananchi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaridhika na utendaji wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Kwa kuthibitisha hayo, wananchi wa Korogwe wanaridhika na mwenendo mzima wa utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi unaofanywa na Serikali hii kwa sababu tumeletewa fedha kwa ajili ujenzi wa vyumba vya madarasa, mabweni, za matengenezo ya barabara kwa kiwango cha changarawe na kiwango cha lami na za kumalizia maktaba katika chuo cha ualimu, kwa nini wasiwe na imani na Serikali ya Chama cha Mapinduzi? Naendelea kuwaombea viongozi wetu hawa Mwenyezi Mungu aendelee kuwapa afya njema ili waendelee kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ujenzi wa vituo vya afya, Korogwe Mjini tulipata Kituo cha Afya kimoja cha Majengo. Tunashukuru tulipata shilingi milioni 500 lakini niombe na Mwenyezi Mungu ikiwezekana aendelee kuwapa afya njema mkipata fedha muweze kunisaidia niweze kupata Kituo cha Afya Mgombezi, tuweze kupandisha Zahanati ya Mgombezi iwe Kituo cha Afya. Kule Mgombezi ni nje ya Mji wa Korogwe na kuna mashamba ya mkonge, wananchi wengi wako kule, ni vijiji sita viko pale Mgombezi. Kwa hiyo, tukiwapa kituo cha afya kitawasaidia wao katika matibabu kwa sababu akina mama wajawazito na watoto wanapopata shida usiku ni shida sana kwenda Mjini. Kwa hiyo, wakipewa Kituo cha Afya kule Mgombezi itawasaidia kupata huduma kwa urahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika, nina Kata ya Kwamsisi, iko nje ya mji, ni mbali na Kituo cha Afya cha Majengo na Hospitali ya Magunga. Nao napenda Mwenyezi Mungu akijalia basi niombe angalau waweze kupata fedha kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya kule Kwamsisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Waziri wa TAMISEMI, bajeti iliyopita walinipa shilingi bilioni 1.5 nijenge hospitali. Kwa bahati nzuri au mbaya hospitali ambayo ilikuwa ya Korogwe Vijijini iko kwenye Jimbo langu, mkasema hiyo hospitali ibaki mjini wakapewa zile fedha ambazo nilikuwa nimetengewa mimi kwenye Halmashauri yangu ya Mji wa Korogwe. Wenzangu wanajenga hospitali, hospitali ile ambayo imebaki sasa ni ya mwaka 1947, naomba sana muweze kuikumba hospitali hii angalau kupewa fedha kwa ajili ya ukarabati wa majengo hayo makuukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba mmetupa fedha tumefanya ukarabati wa shule kongwe ya Korogwe Girls, majengo yanapendeza lakini kwa bahati mbaya sana jengo moja la bweni limeshindikana kabisa kukarabatiwa kwa sababu lina nyufa kubwa ambapo Mhandisi amesema halitawezekana kabisa kufanyiwa ukarabati lijengwe moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa watoto waliokuwa wanakaa kwenye bweni lile ni 120 wamehamishiwa kwenye mabweni mengine, wamesambazwa huko, niombe basi ikiwezekana na Naibu Waziri wa Fedha alifika akaona lile jengo, tupewe fedha ili tuweze kujenga jengo jipya la bweni pale Korogwe Girls ili kusudi wale watoto waweze kurudi kwenye lile bweni lao kama walivyokuwa wanakaa mle. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie masuala ya watumishi, lipo tatizo la watumishi kupandishwa madaraja halafu hawalipwi zile fedha zao baada ya kuwa wamepandishwa yale madaraja. Niombe wanapopandishwa madaraja watumishi hawa basi fedha zao walipwe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika hotuba hii ambayo ameiwasilisha Waziri ma Maji.

Kwanza niunge mkono hoja na kwamba nawapongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara pamoja na watendaji wote wa Serikali kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea nayo pamoja na kwamba kuna changamoto za hapa na pale hizo tunatarajia kwamba kutokana na haya ambayo yanayozungumzwa na waheshimiwa Wabunge yatashughulikiwa ili kusudi kazi ya kuwapelekea maji wananchi wetu kwenye majimbo yetu na kwenye halmashauri zetu yanafanikiwa.

Mheshimiwa Spika, nishukuru Serikali kwamba Korogwe mji nimeona wanasema kwamba nimo kwenye orodha ya miji ambayo itapewa maji kutoka fedha za mkopo wa India. Nikiangalia kwenye kitabu ukurasa wa 148 kwenye ile orodha waliyoiweka pale hiyo Korogwe Mji yenyewe haijawekwa imewekwa HTM lakini miji iko 29 ni namba saba na HTM nachofahamu ni mradi ambao unapelekea maji Handeni.

Mheshimiwa Spika, sasa nisije nikawa vile napewa kama hisani niombe tu waniambie watakapokuwa wanasema hapa ili wananchi wangu nitakapokuwa naenda kuongea nao ninapowaonyesha kitabu hiki kwamba tupo kwenye mradi ule wa India lakini kwenye kitabu humu hatumo imeandikwa HTM na kule wanajua HTM ni Handeni basi ni vizuri atakapokuwa ana-wind up hapo atamke kwamba huu mradi na Korogwe Mji ambako ndio kwenye chanzo cha maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi huu wa HTM unatoka Tabora kwenye chanzo cha maji ni Tabora kwenye kata yangu ya Korogwe. Sasa kama sionekani humu naonekana tu kwamba nipo kwa kuelezwa tu maneno na kuambiwa humo humu sijui nawaambia nini wananchi wangu wa Korogwe. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri utakapokuwa una-wind up hapo ni vizuri basi ukawaeleza wananchi wa Korogwe wajue kwamba hicho chanzo cha maji cha Tabora ambacho kitapeleka maji kule Handeni basi na Korogwe mtapatiwa maji kutoka kwenye hichi chanzo cha maji, nashukuru sana endapo waziri atalisemea hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri nikupongeze na nikushukuru sana sana ulikuwa umepita umeenda ulifanya ziara kule Lushoto nilikupigia simu nikakuomba nikakwambia ndugu yangu naomba unipitie hapa kwenye ratiba yako haikuwemo uliweza kupita. Nikawa nimekueleza suala la mradi wa maji wa ule vijiji 10 nikushukuru sana sana kwa hatua ambazo umezichukua kwamba mradi ule wa vijiji kumi vile viwili tayari kwa maana ya kwamba Msambiazi tayari wanapata maji lakini sasa hivi wanaendelea yule mkandarasi anaendelea na ujenzi wa ule mradi wa Luengela relini na darajani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na bahati nzuri sana nakushukuru vilevile baada ya ku-raise ile certificate umeweza kumlipa yule mkandarasi hili nakushukuru sana Mwenyezi Mungu akubariki na kwamba kazi inaendelea vizuri kwenye ule mradi na bahati nzuri tena wameshatuma ile certificate nyingine ili kusudi muweze kuwalipa. Nimeona ni vizuri nikakushukuru kwa sababu nisipokushukuru kwa hili nalo nitakuwa sijakutendea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nimuombe Mheshimiwa Waziri nina mradi wa maji ambao tulipewa milioni 500 uko pale pale mjini, shida ya Korogwe Mji tuna mto unapita pale, Mto Pangani. Lakini tuna tatizo la maji pale mjini kana kwamba hatuna chanzo cha maji, Mheshimiwa Waziri aliyekuwepo wakati ule ndugu yangu Mheshimiwa Kamwele alitembelea Korogwe akazunguka akakuta kwamba tuna mto unapita pale akaamua kwamba tuutumie ule mto ndipo akatuletea fedha milioni 500 imeshajengwa intake imekwisha imejengwa tayari chujio limemalizika. Kilichobaki sasa ni miundombinu ya kuwapelekea wananchi maji.

Mheshimiwa Spika, hivi navyokwambia Korogwe kila siku kuna kipindupindu kuanzia mwezi wa tatu wananchi wangu ni kipindupindu, mwezi wa nne, mwezi huu hivi navyozungumza watu wako vitandani ni kipindupindu wanakwenda kuchota maji kwenye mto, lakini mkitumalizia mradi huu tutapunguza hili tatizo la kipindupindu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namuomba sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri alitembelea mradi huu aliuona na Mheshimiwa Rais alipokuwa amekuja kufungua ile stand yetu mpya alituahidi kutupa fedha za kumalizia hiyo miundombinu bilioni 2 ili kusudi mradi ule ukamilike. Sasa wananchi wa Korogwe kila siku wanasubiri na kuniuliza Mheshimiwa Mbunge kwamba Rais alituahidi mbona huu mradi haukamiliki.

Mheshimiwa Spika, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara naomba basi muutembelee ule mradi Naibu Waziri aliuona upo mradi ule pamoja na kwamba mnasema mmeniweka kwenye huu mradi wa fedha za India lakini zile milioni 500 ambazo zimeshajenga intake zimemaliza na intake nzuri zimejenga chujio imekamilika, tutaufanya nini huu mradi? Hivi tuendelee kusubiri mtoto anasema nataka nguo, unasema subiri na mwenzako mama yako ana mimba subiri kwamba atakapojifungua ndio niwanunulie wote nguo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri nakuomba sana, nakuomba utembelee mradi ule Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji nakuomba utembelee mradi ule uone jinsi ulivyojengwa na hatimaye wananchi wa Korogwe Mjini waweze kupatiwa maji yaliyo safi na salama waondokane na tatizo la kipindupindu, ni aibu kusikia kila siku tuna kipindupindu Korogwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Maji wanafanya kazi nzuri sana lakini kuna tatizo, tatizo liko kwa wasaidizi wao. Fedha zinazopelekwa kwenye miradi huko zinaweza zikapelekwa fedha zinaende kutengeneza mradi fulani unakuta ule mradi unaweza ukawa umekamilika lakini maji hayatoki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika niko kwenye Kamati ya LAAC tumepita kukagua miradi tumekuta matatizo ya aina hiyo, unaweza ukawa umejengwa mradi haujakamilika lakini amemaliziwa fedha zote amelipwa mkandarasi lakini mradi haujakamilika. Matatizo haya yanatokana na wasaidizi walionao huko chini wanaonekana ma-engineer wanakula pamoja na hawa wakandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani mkandarasi akalipwa fedha zote lakini mradi haujakamilika kwa nini alipwe fedha zote na hali mradi haujakamilika? Ushahidi ni pamoja na ninyi wenyewe tumewaona kabisa mnavyozunguka mnavyofanya ziara kwenye kukagua miradi ya maji mmeenda kuyakuta matatizo haya. Kwa hiyo, tukuombe sana tunakutakia kila heri Mheshimiwa Waziri tuajua unapambana unapata shida.

Mheshimiwa Spika, wapo ma-engineer wako sugu huku chini huko nyuma inaonekana walishazoea kuona kwamba miradi ya maji ni shamba la bibi, ndugu yangu jikaze funga mkanda, Katibu mkuu jikaze mfunge mkanda haya majitu yaliyokaa huku yaliyokuwa yamezoea huko nyuma yashughulikieni ili kusudi muweze kufanikiwa, msipofanya hivyo tutasema fedha hazitoshi tutatafuta fedha zitakwenda lakini zitakwenda kuliwa hivyo hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikuombe sana Mhehimiwa Waziri na tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu atakusaidia tu utafanikiwa, mkifanikiwa kuwashughulikia hawa huko chini basi nadhania hata hizi fedha tunazosema ziongezeke zitaweza kwenda kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa napenda kuunga mkono suala la kutumia force account. Fedha za maji kama tutatumia force account inawezekana kabisa tukafanikisha kama tulivyofanikisha kwenye miradi ya afya, kwenye miradi ya shule. Kuna ubaya gani? Ma-engineer hawa si wapo na tukitumia hii force account kwa sababu tuna watu ambao tayari kule kwenye wilaya zetu wastaafu waliostaafu kwenye masuala ya maji watafanya hizi kazi kwa kutumia hii force account. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutashuhudia tunafanya kazi ya miradi ya maji kwa gharama nafuu kuliko sasa, sasa hivi haya mambo ya wakandarasi mradi mdogo tu kwa mfano kisima cha maji mtu anakwambia kisima cha maji ni milioni 350 kitu ambacho mradi huo unaweza ukakamilika kwa milioni 20 tu wananchi wakapata maji kwa sababu mkipeleka kwa force account hata wananchi watashirikishwa na kwa sababu wanashida watafanya kazi zile ambazo wananchi wanahitajika kusaidia kuhakikisha Serikali inawapatia maji pale.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa naunga mkono suala la kutumia force account. Lakini naunga mkono vilevile suala la kuongezea ile shilingi 50,000 hebu tuzingatie kusimamia maazimio tuliyoyapitisha humu ndani. Tuliyapitisha wenyewe haya maazimio tukisaidia kuongeza hii shilingi 50,000 utatuna huu mfuko na hatimaye angalau hata tunayoshauri haya yanaweza yakatekelezeka vizuri.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nafikiri ni vizuri basi katika hili wenzetu watusikie na wasikilize ili kuona kwamba tunaweza tukafanikisha katika kuwapatia maji wananchi wetu huko kwenye miji yetu na kwenye halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasialiano. Kwanza, naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Wizara hii. Vile vile nampongeza Meneja wangu wa TANROAD wa Mkoa wa Tanga kwa kazi nzuri ambayo ameendelea kuifanya ndani ya Mkoa wetu wa Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye kitabu nimetengewa fedha kwa ajili ya kujenga madaraja; daraja la silabu moja ambalo linakwenda Old Korogwe kwenda Bombo Mtoni ile barabara ya kwenda Bombo mtoni na silabu mbili ambalo ni Maguzoni kwenda Old Korogwe. Naomba nichukue nafasi hii kushukuru kwani nisiposhukuru katika hili, nitakuwa sijamtendea haki Meneja wangu wa Mkoa kwa sababu eneo hili ni sugu na sasa hivi mvua zinanyesha pale Korogwe, huwa mara nyingi kunatokea mafuriko makubwa pale Old Korogwe. Kwa hiyo, kwa kitendo cha kutengewa hizi fedha, niombe sana basi fedha hizi zikitoka iende ikafanye kazi ili kusudi wananchi wa Old Korogwe waondokane na yale mafuriko ambayo wanayapata kila mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie barabara inayotoka Old Korogwe - Kwamote kwenda Kwashemshi – Dindira – Bumbuli - Soni, nimeona imeandikwa humu. Marehemu Profesa Maji Marefu alikuwa anaizungumzia sana barabara hii, iliwekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi lakini naona wameweka hapa kwa ajili ya upembuzi yakinifu. Niwaombe sana fedha hizi zikipatikana, huu upembuzi yakinifu uende ukafanye kazi kwa sababu ni miaka 15 sasa tunasikia tu upembuzi yakinifu; hata watu wa milimani wanahitaji barabara za lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimwombe Waziri pamoja na kututengea fedha hizi, fedha hii itoke ili kusudi ikafanye hiyo kazi ya upembuzi yakinifu, isiwe kila baada ya miaka mitano inaandikwa tu kwamba upembuzi yakinifu. Niombe sana barabara hii ni muhimu kwa uchumi na utalii. Barabara hii inazalisha kwa maana ya Kata zilizopo kule milimani kwa Korogwe Vijijini wanazalisha hiliki, maharage na chakula chungu nzima, kuna soko kubwa pale chini. Niombe sana safari hii naomba ifanyike hii kazi ili kusudi na watu wa milimani waweze kuonja barabara za lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba barabara ya Old Korogwe – Kwa Mndolwa – Bombo Mtoni – Maramba – Mabokweni, nayo iingizwe angalau kwenye upembuzi yakinifu. Hii barabara nayo ni ya kiuchumi, mkitusaidia barabara hii itasaidia masuala ya kiutalii na kiuchumi. Pia ni barabara muhimu sana kiusalama, endapo kunakuwa na jambo lolote kwa hizi barabara zilizopo huku mjini barabara hii itatumika. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri barabara hii muitazame kwa jicho la huruma angalau na yenyewe iingie kwenye upembuzi yakinifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe barabara ya Old Korogwe – Rwengela Darajani – Maguzoni nayo ianze kutazamwa. Barabara hii ikitokea pale Maguzoni, maana akitoka Tanga akija Maguzoni, anakuja Rwengela Darajani anatokea moja kwa moja Korogwe kwenda Arusha. Barabara hii kwanza inafupisha mwendo wa mabasi kuzunguka kutoka Tanga kupitia Segera lakini vilevile ni barabara ya kiuchumi. Engineer wangu Ndumbaro anaijua barabara hii, naomba sana ikiwezekana na yenyewe iwekwe kwenye mpango angalau wa upembuzi yakinifu ili iweze kuwekwa lami, hayo ndiyo maendeleo yenyewe tunayapeleka vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la TBA. TBA wanakabidhiwa miradi mingi ya ujenzi lakini inaonekana kabisa kwamba kazi wanazopewa ni nyingi kuliko uwezo wao. Mimi niko kwenye Kamati ya LAAC, tumekwenda kutembelea miradi pale Kahama, tumekuta kuna mradi ambao wamepewa kuujenga hawajaukamilisha na wameutelekeza hapo na fedha wamepewa wanakwenda kujengea miradi mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenykiti, kwa bahati mbaya sana TBA wanaonekana hawana fedha, wanasubiri wapewe fedha ndipo waende wakajenge miradi. Kwa kufanya hivyo tunachelewesha miradi, TBA ni lazima iwe na fedha za kwenda kufanyia hiyo miradi siyo wanapewa kazi halafu ndiyo itafutwe fedha waende wakatengeneze ile miradi. Kwa hiyo, naomba sana TBA ikiwezekana wapunguziwe miradi waliyopewa kwa sababu uwezo wa kuikamilisha hawana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nisaidiwe; kutoka pale Kwa Meta kwenda Kwa Mndolwa kumewekwa alama za X kwenye nyumba za wananchi. Nataka nielezwe; hawa wananchi wamewekewa alama za X toka 2016 na mwaka huu tena kuna nyumba zingine zimeenda kuwekewa alama za X, sijajua labda ndiyo hili ombi ninaloomba kwamba mnataka kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya kuweka lami, kama sivyo basi mniambie mmeweka alama za X kwa ajili ipi na kama hawa wananchi wangu waliowekewa alama za X watalipwa au hawatalipwa? Kwa sababu mmesitisha wasiendelee kujenga kwenye yale maeneo ambayo wamewekewa alama za X, kwa hiyo, wameacha kufanya maendeleo katika nyumba zao. Sasa niombe mniambie kwamba kwa kuwekewa alama zile za X watalipwa ili waweze kuendelea na shughuli zingine? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kushukuru, nimeona tumetengewa fedha kwa ajili ya kufunga mitambo ya ulinzi na usalama katika viwanja vya ndege pale Tanga. Pamoja na hilo, tunaomba basi tutengewe fedha ili uwanja ule uweze kukarabatiwa kama vinavyokarabatiwa viwanja vingine. Na sisi tunahitaji bombadier itue pale Tanga, tunaihitaji sana. Kwa hiyo, pamoja na kuweka hivyo vifaa vya ulinzi lakini iwe ni pamoja na kufanya ukarabati wa kutosha ili bombadier iweze kutua pale Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishukuru Serikali kwa kazi kubwa ambayo wameifanya ya ukarabati wa reli ile ya kutoka Tanga – Korogwe – Mombo na kuendelea huko mbele. Tumeona kabisa kazi nzuri ambayo inafanyika, naipongeza sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa sijatenda haki endapo sitampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya lakini kwa maamuzi ambayo ameyafanya ya uthubutu wa kutekeleza miradi mbalimbali kama vile ya ujenzi wa Reli ya Standard Gauge, ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia Mheshimiwa Chatanda.

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika taarifa iliyowasilishwa ya LAAC pamoja na PAC kwanza naziunga mkono. Nampongeza Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kwa namna alivyofanya kazi ya kuboresha na kuzisambaza PoS za kukusanyia mapato ambayo PoS hizi zinaweza kuzisaidia sana Halmashauri zetu kudhibiti wizi wa mapato katika halmashauri zetu, amefanya kazi kubwa tunamshukuru sana na tunakusudia sasa kuona kwamba kwenye halmashauri zetu mapato yataongezeka kutokana na vitendea kazi ambavyo vimepatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo mengi ambayo tumeyazungumza na wenzangu wameshayazungumza katika Kamati yetu ni pamoja na suala zima la ajira za watumishi. Tumejenga vituo vya afya, tunajenga zahanati, lakini kumekuwa na upungufu mkubwa wa watumishi katika vituo hivyo vya afya na zahanati. Jambo ni jema sana na tunaishukuru sana Serikali kwa kazi kubwa ambayo imeifanya kwa ajili ya kujenga hizo hospitali tunazojenga, tunajenga hivi vituo vya afya, tunajenga hizi zahanati lakini sasa tuna uhitaji mkubwa watumishi katika maeneo hayo. Kwa hiyo tuiombe sana Serikali angalau basi waweze sasa kutoa ajira ili kusudi hospitali hizi na zahanati hizi ziweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo mengi ambayo yamezungumzwa ni pamoja na suala zima la kutumia hii force account, ni jambo jema sana na linaisaidia sana Serikali katika kubana matumizi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, vituo vya afya na hospitali zetu na mambo mengi ya maendeleo. Hata hivyo, kama walivyosema wenzangu kwamba tunahitaji sasa Wahandisi katika halmashauri zetu maana Wahandisi waliokuwepo wakati huo wote wamechukuliwa, wako asilimia kubwa wamekwenda sasa TANROADS, wamekwenda TARURA. Sasa mara nyingine wanaenda kuwachukua TARURA au kuwaomba waje kuwasaidia kazi, inakuwa ni kazi kubwa sana katika kusimamia hii miradi ambayo tunatumia force account. Mradi wenyewe wa force account ni mzuri lakini tunahitaji watendaji angalau wale watakaokuwa wapo muda wote kuhakikisha kwamba wanasimamia hii miradi katika halmashauri zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka nilizungumzie ni suala la watumishi. Tumegundua kwamba watumishi wanapandishwa madaraja lakini wanapopandishwa madaraja hawaendi sambamba na maslahi yao. Wakishapandishwa tu basi mtu anaweza akakaa mwaka mzima, miaka miwili haongezewi yale maslahi ambayo yanahusiana na kule kupandishwa kwake daraja. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali, ili kuwapa motisha wafanyakazi hawa anapopandishwa basi aende sasa na maslahi yake kwa nafasi ile ambayo amepandishwa nayo daraja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu mengi yamezungumzwa nilikuwa nafikiri ni vizuri nikasema haya machache kwa sababu wenzangu wengi waliotangulia ambao tuko kwenye Kamati hii ya LAAC wamekwishayasema, hivyo nishukuru na niendelee kuipongeza sana Serikali kwa juhudi kubwa ambazo wameendelea kuzifanya katika kuyaletea maendeleo nchi yetu. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naunga mkono hoja. Nampongeza Waziri, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuikumbusha Serikali kwamba uwanja wa ndege Tanga unatakiwa kuboreshwa kama viwanja vingine kwa sababu uwanja huo utatumika sana baada ya bomba la mafuta toka Hoima hadi Tanga. Kwa hiyo, kutakuwa na wageni wengi watakaokuja Tanga kupitia usafiri wa ndege vikiwemo viwanda vingi vilivyopo na vinavyokusudiwa kujengwa pamoja na utalii uliopo Mkoani Tanga. Hivyo naiomba Serikali kuangalia uwanja huu kwa kutengea bajeti ya marorosho.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu barabara za lami Korogwe Mjini, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliahidi kilometa tano za lami ndani ya Mji huo. Niombe Serikali ahadi hii kama inawezekana ni kutoa kilometa 2.5 kila mwaka itakuwa imekamilika ahadi hiyo ndani ya miaka miwili tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, TARURA wanafanya kazi nzuri lakini bajeti waliyopewa ni ndogo. Ni kwa nini wasigawane nusu kwa nusu na TANROADS ili kuwawezesha TARURA kuwa na uwezo wa kutekeleza miradi ya barabara kwa uhakika. Vinginevyo ile shilingi 50 ya lita ya mafuta (disease/petrol) itolewe kwa TARURA ili kuwapa nguvu zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara za Mji wa Korogwe zinaharibika sana kwa mvua kutokana na Mji huu kuwa bondeni, ushauri wangu ni kwamba barabara zinazojengwa kwa kiwango cha changarawe zijengewe mitaro au mifereji ili kusaidia kupunguza uharibifu. Kwa msingi huo tunaomba kupewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mitaro/ mifereji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba ya bajeti ya Wizara hii ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara kwa kazi kubwa na nzuri ya kuboresha elimu kwa watoto wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono mapendekezo ya Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, ushauri na mapendekezo yazingatiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maombi ya kusaidiwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni shule ya sekondari Mgombezi ambayo ipo nje ya Mji wa Korogwe Mjini, ina vijiji sita na vitongoji kumi. Watoto wa kike wanatembea kilometa tano kwenda na kurudi, kwenye mashamba ya mkonge, usalama wa watoto hawa ni mdogo na mwendo ni mkubwa kiasi kwamba wanachoka kwa kutembea kabla ya kuanza masomo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule ya sekondari Chifu Kimweri iko nje ya mji, ina vijiji vinne, vitongoji saba watoto wanatembea umbali mrefu kiasi kwamba wanachoka kabla ya masomo. Naomba iangaliwe kupewa fedha za ujenzi wa mabweni ili watoto wa kike wabaki shuleni kwa ajili ya kuwanusuru na majanga yanayowasibu barabarani na nyumbani kukosa muda wa kujisomea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Korogwe Mjini tumetenga eneo la kujenga chuo cha ufundi Mgombezi, tunaiomba Serikali isaidie kuwaunga mkono wananchi ambao wameanza kwa nguvu zao wenyewe kama inavyosaidia kwenye vyumba vya madarasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kutoondoa masomo ya uraia na historia shule za msingi na sekondari na vyuo vya ualimu. Aidha, wakuu wa vyuo, walimu wa shule za msingi na sekondari wanaokaimu nao wapewe mafunzo ya uongozi (ADEM - Bagamoyo) kama zamani na kukaguliwa mara kwa mara kuinua elimu vyuoni na sekondari pia hasa Chuo cha Ualimu Korogwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ya bajeti ya Wizara hii. Aidha, nimpongeze Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mingi ya maji, baadhi ya watendaji walioko kwenye Halmashauri hawasimamii ipasavyo. Kumekuwepo na ubadhirifu ambao umepelekea kujengwa miradi iliyo chini ya viwango. Ninao mfano wa Halmashauri ya Igunga, mradi ulikamilika lakini wananchi hawapati maji na tenki kubwa likijazwa maji linavuja. Kamati ya LAAC imeagiza CAG akague mradi huo. Aidha, miradi mingi iliyotekelezwa ya World Bank haipo sawa, ni vema Mkaguzi Mkuu (CAG) akaikagua miradi hii ili tuweze kujua zaidi hali halisi kwani fedha hiyo ni ya jasho la wananchi ambao watarejesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru Korogwe Mjini tumeanzishiwa mradi wa maji kwa kupewa shilingi milioni 500. Mradi huu tenki limekamilika tatizo ni miundombinu ya kusambaza maji kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mradi ulitengewa fedha wa vijiji kumi vya Lwengera Darajani, Relini na Msambiazi. Nashukuru Msambiazi mradi upo karibu kukamilika asilimia 80 mpaka 85, tenki limejengwa na virura vimeshajengwa, mkandarasi hajalipwa na ndiye aliyepewa mradi wa Lwengera Darajani/Relini. Naomba Wizara imlipe mkandarasi huyu kwani madai yake (certificate) zilishawasilishwa ili aweze kuendelea na kazi ya Lwengera Darajani, vinginevyo Wizara inafanya kazi vizuri anahitaji kupewa fedha ili kukamilisha miradi iliyopo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba ya bajeti ya Waziri wa Kilimo na maoni ya Kamati. Kilimo ni uti wa mgongo, kauli hii haiendani na utekelezaji kutokana na changamoto zifuatazo;

Kwanza, kutopewa kipaumbele kwenye bajeti kwa kutengewa fedha kidogo zisizoweza kukidhi uhitaji wa utekelezaji wa yale yanayopaswa kutekelezwa.

Pili, kutopewa fedha yote iliyotengwa pamoja na uchache wake kunachangia kukwamisha Wizara hii kutekeleza majukumu yake na tatu, kutokuwa na Maafisa Ugani wa kutosha huko vijijini ambao wangeweza kuwasaidia wakulima kulima/kupanda mbegu bora/kupalilia na kuvuna mazao kwa lengo la kujiinua kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, vyuo vya utafiti kutopewa fedha za kutosha kufanya utafiti wa mbegu ili wakulima waweze kupanda mbegu bora na yenye kuwawezesha kuvuna mazao ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, uwepo wa migogoro ya ardhi kunachangia kwa asilimia 50 kati ya wakulima na wafugaji kukwamisha juhudi za wakulima kujipatia mazao ya kutosha kutokana na wafugaji kulisha mifugo kwenye mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuishauri Serikali kama ifuatavyo:-

Kwanza, Serikali ina mpango mzuri wa nchi yetu kuwa ya viwanda na kilimo ndicho kitakachotoa malighafi zitakazolisha viwanda hivyo. Ni vema bajeti ya kilimo iangaliwe upya na kupewa kipaumbele cha juu ili Wizara iweze kutekeleza majukumu yake vizuri na Tanzania ya viwanda itawezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, bajeti wanayotengewa wapewe yote kulingana na umuhimu wa majukumu yao yatakayowezesha na kuandaa Tanzania ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Serikali itoe ajira za wagani maeneo /vijiji ambavyo hawana watumishi wa fani hii waweze kupelekwa na kuwawezesha vitendea kazi, ili waweze kutenda majukumu yao kikamilifu. Vyuo vya utafiti viwe na bajeti ya kutosha ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakamilishe kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji ili wananchi hawa kila mmoja waweze kuishi kwa amani na shughuli za uzalishaji ziweze kufanyika kwa uhakika zaidi. Naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Korogwe Mjini; mpango mkakati wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe ulikuwa kujenga hospitali ya wilaya na kwa taarifa tulitengewa bilioni 1.5 lakini zimeondolewa na kupewa Korogwe Vijijini. Nimeridhika na maelezo ya Waziri kwamba imefanyika kwa nia njema baada ya kuona ipo Hospitali ya Wilaya Korogwe Vijijini kwenye Kata ya Magunga iliyopo mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, niombe unapohitimisha utamke wazi ndani ya Bunge kauli ya kukabidhi hospitali hiyo ili wananchi wa Korogwe Mjini wapate kusikia mabadiliko haya na kuzipeleka fedha, bilioni 1.5, Korogwe Vijijini ili kuondoa mkanganyiko uliopo. Hata hivyo, niiombe Wizara kunipoza kwa kunisaidia kunipatia fedha kwa ajili ya ujenzi na vituo vya afya; kata zilizo mbali na mji zina shida kubwa ya huduma ya afya nazo ni Kata ya Kwamsisi yenye vijiji sita na Kata ya Mgombezi vijiji vitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitashukuru Mheshimiwa Waziri akinisaidia ili wananchi hawa wa vijiji hivyo waweze kupata huduma nzuri.
Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini wa Mwaka 2016
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi angalau kwa dakika tano hizo, lakini naanza kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusimamia utawala wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania sasa hivi wanazijua mbivu na mbichi, wala watu wengine wasipoteze nguvu bure kwa ndoto za alinacha, wala wasijenge ukuta usiokuwa na matofali. Wamwache Mheshimiwa Rais atekeleze majukumu yake kwa mujibu wa Katiba ya nchi na jinsi ambavyo waliweza kumpa kura wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma kwenye hiki kitabu chao, ni kumzungumza yeye tu kwenye ukurasa wa kwanza, wa pili na wa tatu. Sasa naomba wajue kwamba Rais wetu anasema Hapa Kazi Tu, wala hahitaji ukuta ambao hauna matofali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na watendaji wake kwa kuleta Muswada huu ambao unahusu Mthamini Mkuu, Uthamini pamoja na …haya sasa! (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kwa kuletwa Muswada wa Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini wa mwaka 2016. Naungana na mawazo ya Kamati ambayo tumezungumzia na kukubaliana na mapendekezo yaliyoletwa na Serikali. Kwa mfano, katika kifungu cha 5 ambacho kinazungumzia suala la Mthamini Mkuu, kwenye sheria inasema Mthamini Mkuu atateuliwa na Rais, lakini ni miongoni mwa Watumishi wa Umma. Sisi kama Kamati tumekubaliana na wenzetu upande wa Serikali kwamba tupanue wigo zaidi kwa maana ya kuacha nafasi hii iweze kuwa na wigo mpana ili kusudi aweze kupatikana Mthamini Mkuu ambaye ana sifa na vigezo vya kuweza kuteuliwa. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kifungu cha 6 kinachohusu mamlaka ya majukumu ya Mthamini Mkuu, tumeangalia tukaona kwamba ni vizuri kikaongezwa kifungu cha (3) kitakachompa Mthamini Mkuu Mamlaka ya kutekeleza majukumu yake chini ya sheria hii kwa uwazi bila kuingiliwa na kutokuwa na upendeleo wowote. Vilevile tulifikiri ni vizuri basi kifungu hiki kikaendana na kifungu cha 6(1)(h) mbacho kinasema; “Kuandaa na kusababisha kuandaliwa, kusimamia na kuidhinisha taarifa zote za uthamini.” Kwa hiyo, kikiungana na hiki ndiyo kitaleta maana nzuri katika muswada huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia tena kwenye kile kifungu cha 6(1)(e) kinachohusu kuwasilisha report ya uthamini kwa Waziri; nakubaliana na Kamati kwamba report ni vizuri iwasilishwe mara mbili kwa mwaka badala ya miezi mitatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia sehemu ile ya tatu inayohusu Bodiya Usajili wa Wadhamini, Kifungu kile cha 13(1)(d) kinachohusu muundo wa Bodi; muundo wa Bodi umefanyiwa marekebisho makubwa. Tumeangalia na tumeona kwamba kuna taasisi ambazo zilikuwa zimeachwa, sasa sisi tumefikiri ni vizuri tukaingiza Wawakilishi toka Bodiya Taifa ya Uhasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) na Wawakilishi toka Chama cha Mabenki Tanzania kwani hawa ni wadau wakubwa namba moja wa uthamini wakati wa kutoa mikopo na wanao uwezo wa kushauri na kutoa mawazo zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi ya kushukuru tena kwa kunipa nafasi, niseme kwamba naungana na mawazo ya Kamati na vilevile naungana na mawazo ya Serikali. Ahsante sana.