Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dunstan Luka Kitandula (23 total)

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa na mimi niuliza swali la nyongeza. Mji wa Maramba una tatizo kubwa sana la kukatika kwa umeme kama ilivyo Mji wa Korogwe. Je, Waziri atatuhakikishia kwamba katika mipango hiyo anayoizungumza ina-consider vile vile Mji wa Maramba?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la kukatikakatika umeme, sababu mojawapo ni miundombinu kuwa inasafirisha umeme mdogo ambao haulingani na matumizi. Kwa hiyo, project kubwa kabisa ambayo tuna nyingine tunaizindua mwezi wa tisa ni kutoka kwenye miundombinu inayosafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 220 kwenda 400.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ndugu zangu wa Tanga, hii inatoka Dar es Salaam inapita Tanga ikielekea Arusha halafu kuna nyingine inatoka Iringa, Dodoma kuelekea Shinyanga. Ni lazima tuwe na umeme mwingi ndiyo tutakomesha ukatikaji wa umeme mara kwa mara na hilo tatizo linatatuliwa. Ahsante.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa hali ya kukamilika kwa vigezo vya kupandisha hadhi miji yetu kule Namanyere iko sawa sawa na kule Maramba ambapo tumetimiza vigezo vya kupata mji mdogo tangu kabla Mkinga haijawa Wilaya. Je, ni lini Mji wa Maramba utapewa hadhi ya kuwa Mji Mdogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli hawa wenzetu walikuwa na maombi yanayogusa sehemu mbili; walikuwa wanaomba hii Maramba iwe mji mdogo, lakini walikuwa wanaomba eneo hili la Mkinga. Naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge, nadhani maombi haya yamepita muda mrefu sana. Sasa nimwombe na nimwagize Mkurugenzi na timu yake kule Halmashauri wakishirikiana naye kwa sababu kulikuwa na maombi haya na muda mrefu sana umepita, waanze huu mchakato vizuri ilimradi itufikie Ofisi ya Rais, TAMISEMI, mwisho wa siku vile vigezo vikiwa vimefikiwa hatutosita kuhakikisha eneo hili linapandishwa hadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimwagize Mheshimiwa Mbunge na wengine wote, maana yeye ni rafiki yangu tupo humu ndani. Namwambia Mkurugenzi na timu yake yote waanze huu mchakato sasa vizuri ilimradi hili jambo lifike Ofisi ya Rais, TAMISEMI na wataalam wetu waende kuhakiki kwa ajili ya vigezo hivyo
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Umuhimu wa kimkakati wa daraja la Wami kwa maana ya usalama wa nchi yetu na uchumi wa Taifa letu unafanana sana na umuhimu wa kimkakati wa barabara ya Mabokweni - Maramba - Bombo Mtoni - Mlalo -Same kwa maana ni barabara inayopita kwenye maeneo ambayo ni mpakani, kwa hiyo, ina umuhimu wa kiusalama. Vilevile ni barabara ambayo inaunganisha mbuga za wanyama na inaunganisha Mkoa wa Tanga na Mkoa wa Kilimanjaro. Je, Serikali kwa umuhimu ule ule wa kimkakati, ipo tayari sasa kuijenga kwa kiwango cha lami barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni bahati mbaya kwamba Mheshimiwa Mbunge alipofika ofisini kuleta tatizo la barabara hii au tuseme umuhimu, changamoto ya barabara hii, tuliongea lakini hatukumalizia kwa sababu kulikuwa na mambo mengine yalituvuruga. Mimi naomba sana tukae tena tumalizie ile kazi ya kuijadili hii barabara kwa undani tukiwashirikisha wataalamu wetu ili hatimaye tuwatendee haki wanaotumia hii barabara.
MHE. DUSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri ningependa kujua tumeshuhudia vituo hivi vikijengwa lakini baada ya muda mfupi matumizi yake yanakuwa yamepitwa na wakati kwa sababu inahitajika kujenga eneo kubwa zaidi. Sasa swali kwa nini Serikali isiwe inafanya tathmini ya kina kujua mahitaji halisi ili kukwepa gharama ya kurudia ujenzi mara kwa mara?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, katika barabara hizi bado wananchi wamekuwa wana malalamiko kwamba fidia wanayopewa inachukua muda mrefu sana kukamilika kama ilivyo kwa barabara ya Tanga - Horohoro, ambayo mpaka leo bado kuna watu wanadai. Je, ni lini Serikali itahakikisha watu hawa wanalipwa stahili zao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kubadilika matumizi ya eneo la Mizani na kwamba ujenzi tunapoanza tunajenga eneo dogo na baadaye tunalazimika kubadilisha naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ombi lake tumelipokea na nitawataka watu wa TANROADs mikoa yote kuhakikisha kwamba wanapopanga matumizi ya vituo hivi wasiangalie muda mfupi waangalie muda mrefu ni afadhali kutumia gharama nyingi mara moja kuliko gharama kidogo, halafu tunaendelea kurekebisha kila mwaka. Kwa hiyo, tunamshukuru nimepokea ombi lake tutalifanyia kazi.
Kuhusu suala la stahili kwa watu ambao wanatakiwa kufidiwa katika maeneo haya, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ni nia ya Serikali kuwalipa fidia watu wote wanaostahili katika maeneo yote. Lakini lazima tukiri kwamba ili tuweze kulipa fidia lazima tuwe na uwezo sasa kwa mfano unaweza ukalipa fidia, lakini ukachelewa kuanza kujenga, unaweza ukaanza kujenga watu wanaanza kutumia barabara na baadaye ukalipa fidia kadiri uwezo unapopata.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiria hii njia ambayo Serikali inaitumia, ni njia sahihi, kwanza tuwape huduma watu, baada ya hapo tuendelee kutafuta fedha za kuwalipa fidia na mara fedha zitakapopatikana nakuhakikishia watu hawa watalipwa fidia.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Hali ya migogoro iliyoko Serengeti na vijiji vya Ngorongoro inafanana na hali iliyopo katika Wilaya yangu ya Mkinga eneo la Kimuni katika mpaka wetu na Kenya na Pori Tengefu la Umba na Mbuga ya Mkomazi. Wananchi kwa muda mrefu wameomba mgogoro huu ili utatuliwe eneo lile litangazwe kuwa WMA lakini kwa muda mrefu hatujapata majibu, nini suluhisho la jambo hili na Waziri anatuambia nini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote ambao wanaishi kwenye maeneo yanayopakana na hifadhi kila mmoja kwa wakati wake tuweze kupata nafasi ya kuwasiliana ili tuweze kuangalia maeneo yake ambayo anaona yana mgogoro ni kweli yameorodheshwa kwenye orodha ninayoizungumzia ambayo imetayarishwa na Serikali. Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kujibu swali mahsusi la Mheshimiwa Dunstan Kitandula kuhusu eneo la Kimuni, Umba, Mkomazi na hasa kuhusiana na suala la maombi ambayo wameyaleta Serikalini kwa ajili ya kuundwa kwa WMA. Ni kweli WMA inaundwa kwa makubaliano baina ya wananchi wa eneo linalohusika na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii. Sasa nimpe tu comfort Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa suala hili ni mahsusi itakuwa ni vigumu kukumbuka maombi haya kama yameshatufikia tayari na yako kwenye status gani kwa sasa, nimuombe baada ya kikao hiki mchana tuweze kuwasiliana kwa sababu wakati huo mimi nitakuwa nimewasiliana na ngazi zinazohusika ili kuweza kupata uhakika zaidi ya majibu ya status au hatua gani imefikiwa kuhusiana na maombi ya WMA kwenye maeneo anayoyazungumzia.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana
kwa kunipa fursa hii ili niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa Serikali iliwahi
kutoa orodha ya Wilaya za kipaumbele za ujenzi wa vyuo vya VETA na katika
orodha ile Wilaya ya Mkinga ilikuwa ni miongoni mwa Wilaya hizo. Je, ni lini sasa
Serikali itatekeleza ahadi yake ya kujenga chuo kile kule Mkinga?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu
Spika, ni kweli Serikali inatambua hilo na hata tunapojibu maswali ya VETA
tunajua tutapambana nna swali la Mkinga. Nimfahamishe tu kwamba katika
vipaumbele vya Serikali bado Mkinga iko pale pale. Tukipata fedha tunaamini
kwamba tutatekeleza.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Zaidi ya nusu ya Vyama vya Ushirika nchini havijafanyiwa ukaguzi kazi ambayo ilipaswa kufanywa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika. Kutokana na uwezo mdogo wa Tume yetu wa kifedha na watendaji tumeshindwa kufanya hivyo. Serikali ina mkakati gani wa kuiwezesha Tume ya Ushirika iweze kufanya kazi yake kikamilfu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba kumekuwepo na changamoto ya kufanya ukaguzi kwenye Vyama vyote vya Ushirika. Kwa sasa Wizara na Tume ya Ushirika imejipanga kuhakikisha kwamba katika mwaka unaokuja wa fedha Vyama vyote vya Ushirika vinakaguliwa, lakini zaidi kuweka mfumo ambapo utaratibu wa ukaguzi utakuwa unafanyika mara kwa mara bila kukosa.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya Skimu ya Umwagiliaji ya Ulumi inafanana sana na Skimu ya Umwagiliaji ya Mwakijembe. Mwaka 2010 Serikali ilitumia shilingi bilioni 1.2 kujenga Skimu ya Umwagiliaji ya Mwakijembe, lakini bahati mbaya sana skimu ile mifereji haikujengewa wala hakuna bwawa lililojengwa kuvuna maji. Matokeo yake, leo hii tunapozungumza its hardly 10 percent ya mradi ndiyo imetumika. Nini kauli ya Serikali kuhakikisha skimu ile inafanya kazi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa, ndiyo maana Serikali kwa kupitia msaada wa Serikali ya Japani sasa hivi mhandisi mshauri anapita nchi nzima ili kubaini matatizo ya miradi ya umwagiliaji ambayo imefanya efficiency ya miradi ya umwagiliaji isiwe nzuri. Ni kweli kabisa kwamba miradi mingi imejengwa lakini imekuwa na matatizo kwamba inalimwa mara moja tu, kipindi cha masika, baada ya hapo kilimo hakuna, kunakuwa hakuna maana. Ndiyo maana mpango huu unaoendelea wa mwaka 2002 kupitia miradi yote ya umwagiliaji kubaini shida ni nini ndipo tutagundua kwamba kumbe skimu zilijengwa lakini hazina maji kwa hiyo tuna mpango wa kujenga mabwawa. Lakini tusubiri ripoti ya wahandisi washauri, watakapokuwa wameikamilisha ndipo tutaendelea sasa kurekebisha mapungufu yote ili miradi hii iweze kufanya kwa uwezo mkubwa ule unaotarajiwa.
MHE. DUNSTAN. L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Serikali ilihaidi kwamba Kata ya Mwakijembe ambayo iko mpakani na Kenya vijiji vyake vilisahaulika lakini kuna umuhimu wa kiulinzi vijiji vile kupata umeme. Serikali ilihaidi kwamba kabla mkandarasi hajaondoka kufanya survey wataagizwa ili jambo hilo lifanyike. Je, ni lini jambo hili litakamilika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kata anayoitaja Mheshimiwa Mbunge ya Mwakijembe ni kata ambayo iko mpakani, laikini kama alivyosema aliliwasilisha ombi lake hilo. Kwa kutambua umuhimu wa maeneo ambayo yako mpakani suala lake linashughulikiwa na mkandarasi wa Mkoa wa Tanga katika maeneo ambao Wilaya ya Mkinga na Wilaya zinginezo ni Delimiki Electric Company Limited yupo site anaendelea na hiyo kazi. Kwa hiyo nimtoe wasi wasi Mheshimiwa Mbunge, kwamba Serikali inashughulikia. Na kwa kuwa nia yetu ni kusambaza umeme katika maeneo yetu hilo jambo litafanikiwa, ahsante.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa miaka kumi mfululizo ulimwenguni sekta inayokua kwa kasi katika sekta ya kilimo ni sekta ya samaki. Serikali ipo tayari sasa kuwasaidia wavuvi walioko Ukanda wa Pwani kuondokana na umaskini kwa sababu sekta hii imeonekana ni sekta inayokua kwa kasi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iko tayari kuwasaidia wavuvi kusonga mbele.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Barabara ya Tanga – Mabukweni – Malamba – Bombo Mtoni – Mlalo mpaka Same ni barabara inayounganisha Mkoa wa Tanga na Mkoa wa Kilimanjaro; na kwa mara kadhaa barabara hii imeahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami. Ni lini sasa barabara hii itajengwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Dunstan Kitandula tukutane ofisini na wataalam ili tuweze kujadili kwa kina suala hili ili huu usumbufu usiendelee, tuwe na lugha moja kati yetu sisi wataalam katika kuhakikisha kwamba wananchi na hasa wa Jimbo la Mkinga wanaotumia barabara hii waondokane na adha ambazo wanazipata kwa sasa. Nikuombe tukutane na wataalam, Katibu Mkuu pamoja na watu wa TANROADS tulijadili kwa kina na hatimaye tupate majibu sahihi na majibu ambayo wote tutakuwa tunaelewa kwa pamoja na hatimaye tuchukue hatua.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Tatizo la maji la Songea linashabihiana na kwa kiasi kikubwa na tatizo la maji katika Wilaya ya Mkinga. Hivi karibuni tumewasilisha taarifa ya Maafa kwa kuharibika mabwawa takribani saba katika Wilaya ya Mkinga na kwamba watu wanashida kubwa ya maji. Je, ni nini kauli ya Serikali kwa tatizo hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uharibifu mkubwa ulioharibu miundombinu ya maji Mkoa wa Tanga kutokana na mvua, Mheshimiwa Mbunge nimuahidi kwamba, ni kweli taarifa niliipokea ambayo imeandikwa kwenda upande wa maafa na mimi ninayo, lakini kabla hatujachukua hatua, basi baada ya Bunge tu naomba mimi na yeye mguu kwa mguu, twende nikajionee kule na nitakuwa na wataalam ili tuweze kuona sasa tutafanya nini. (Makofi)
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza:
Mheshimiwa Naibu Spika, Taifa letu linakabiliwa na tatizo kubwa ambalo kimsingi ni janga la utapiamlo na lishe iliyopitiliza, hii lishe iliyopitiliza ndiyo chimbuko sasa la magonjwa kama kisukari na magonjwa ya moyo.
Je, Serikali ipo tayari kwa maksudi kabisa kuandaa semina kwa Bunge zima ili Wabunge hawa wakielimika iwe chachu ya kutoa elimu kwa jamii nchini?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Kitandula ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wabunge, Masuala ya Lishe, kwa kusimamia vizuri masuala ya lishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumekuwa na changamoto kubwa sana ya utapiamlo pamoja na suala la lishe iliyopitiliza ambayo kwa lugha ya kitaalam tunaita viribatumbo (obesity) na sisi kama Serikali tumeweka mkakati ambao ni jumuishi na ambao ulizinduliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu mwaka jana, ambao unashirikisha sekta zote kuhakikisha kwamba tunajenga Tanzania yenye lishe. Wizara tupo tayari kutoa semina kwa Wabunge ili kuwajengea uwezo na uelewa na wao kwenda kusemea masuala ya lishe na viribatumbo katika jamii wanazotoka.(Makofi)
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Hali ya ahadi kwa barabara za Dar es Salaam inafanana sana na ahadi ya barabara ya Tanga - Mabokweni - Maramba - Bombo Mtoni - Kitivo hadi Same ambapo barabara hii ilikuwa kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami kupitia fedha za MCC II, lakini mradi ule ukashindikana. Sasa ni lini Serikali itaanza usanifu wa barabara hii ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, najua suala la barabara hii ya Tanga - Maramba Mawili- Bombo Mtoni kupanda mpaka kwenda upande mwingine tunakwenda Same na upande mwingine tunapita Lushoto, barabara hii nimeipita nimeiona.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile ilikuwa kwenye mpango hauku-mature nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge na mara nyingi nampa feedback kwamba tunaitazama sasa ili tuone namna bora ya kuweza kuitengeneza barabara hii muhimu. Wananchi wa Maramba kwa kweli barabara hii nilipita niliiona wana shauku kubwa sana ya barabara hii. Mheshimiwa Mbunge naomba avute subira na nitaendelea kumpa mrejesho namna tunavyoweza kujipanga kuitengeneza barabara hii.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu haya hayaridhishi hasa ukizingatia kwamba ahadi hii ya Serikali ni ya muda mrefu takriban miaka saba sasa. Pale Mkinga tunategemea uwekezaji mkubwa sana wa kiwanda kikubwa cha cement, uwekezaji wa takriban dola bilioni tatu. Uwekezaji ambao utavutia takriban viwanda 11. Sasa kwa muktadha huo, nini mkakati wa Serikali wa kuleta Chuo cha Ufundi pale Mkinga ili vijana waweze kupata stadi zitakazowawezesha kuingia kwenye uchumi huu wa viwanda? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wenzetu wa Singapore kwa kutambua changamoto ya ajira katika nchi yao, wametumia mfumo ambao umewawezesha kuondoka kwenye tatizo, mfumo wa ku-link mafunzo ya VETA na maeneo ya kimkakati ya uzalishaji (industrial park) je, Serikali iko tayari kujifunza kutoka kwa wenzetu ili tuondokane na tatizo tulilonalo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naelewa sana Mheshimiwa Kitandula anaposema jibu langu la msingi halijamridhisha kwa sababu kwa kweli kwa miaka mitatu sasa amekuwa kila wakati yupo Wizarani akifuatilia ujenzi wa VETA ya Wilayani kwake Mkinga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kupitia Bunge lako Tukufu nimhakikishie Mheshimiwa Kitandula kwamba tayari mchakato wa kujenga Chuo cha VETA Mkinga umefikia katika hatua za mwisho. Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya Dubai inayoitwa Planet Core iko katika hatua za mwisho za kuingia mkataba wa PPP ili waweze kujenga vyuo kumi nchini kikiwepo Chuo cha VETA cha Mkinga. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba awe na subira kidogo tu kwa sababu kile ambacho amekuwa akitafuta kwa muda mrefu sasa kiko mbioni kutekelezwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Skimu ya Mwakijembe ambayo imetumia fedha nyingi kujengwa, zaidi ya shilingi bilioni moja, mpaka leo hii haijakamilika kwa kukosa mifereji ya umwagiliaji lakini vilevile kukosa bwawa na sasa tunashuhudia maeneo ya wananchi yakichukuliwa na Jeshi bila fidia yoyote. Je, Waziri yuko tayari kuja kufanya ziara mahsusi Jimboni Mkinga ajionee hali hii ili kuweza kutatua tatizo linaloikabili skimu ile?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie kaka yangu, Mheshimiwa Dunstan Kitandula, mimi kama Naibu Waziri wa Maji nipo tayari.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka huu tumetenga fedha kwa ajili ya kufanya usanifu wa Mradi wa Kupeleka Maji Makao Makuu ya Wilaya ya Mkinga kutoka Mto Zigi kuelekea Horohoro lakini mpaka sasa hakuna dalili yoyote ya jambo hili kufanyika. Ni lini usanifu huu utaanza?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba usanifu huo utaanza mara moja, tunajipanga kuhakikisha kwamba tunatafuta wataalam ili wakafanye kazi hiyo.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ilivyo Chemba inafanana vilevile na kule Mkinga. Tunaishukuru Serikali katika kipindi hiki imetuwezesha kuanzisha sekondari za kidato cha tano na sita kwa Shule ya Mkinga Leo na Maramba Sekondari. Shule hizi zinakabiliwa na tatizo kubwa sana la maji na kukamilika kwa vyumba vya madarasa na mabweni. Je, nini kauli ya Serikali kuwezesha kukamilika kwa nia njema hii ya kuwa na sekondari za A-Level ili ziweze kutoa elimu stahiki kama walivyokusudia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda sana nimpongeze Mheshimiwa Jumaa Aweso kwa majibu yake mazuri. Pengine hakumalizia tu kwamba Wizara ya Maji na Umwagiliaji inakamilisha mchakato wa mwisho kabisa wa kupata dola milioni 350 ambazo ndani yake kuna programu nzuri sana ya kupeleka huduma za maji katika shule za sekondari na za msingi zote nchini ambazo hazina huduma ya maji, pamoja na hizo alizotaja Mheshimiwa Kitandula, Shule za Maramba ambayo ni shule ya zamani sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimhakikishie kwamba tumeshatoa agizo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri wote akiwemo Mkurugenzi wake, kuhakikisha kwamba shule ambazo wamezipangia kwamba zitaombewa kibali ziwe kidato cha tano na sita wanaweka kipaumbele cha haraka ili kusudi miundombinu yake iweze kukamilika, maombi yake yaweze kufikishwa Wizara ya Elimu ili zipate kibali ili angalau mwakani ziweze kuanza kuchukua vijana wa kidato cha tano na sita.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali moja la nyongeza. Wilaya ya Mkinga, Muheza, Korogwe na Lushoto ni maeneo ambayo yanalima kwa wingi mazao ya spices, lakini kwa muda mrefu maeneo haya yamekabiliwa na changamoto ya ukosefu wa huduma za Ugani, masoko duni ya bidhaa hizi na vilevile mazao haya kuuzwa kwa bei ya chini sana. Je, Waziri yuko tayari na wataalam wake kuja kwenye maeneo haya kujionea hali halisi ili kuweza kuondoa changamoto zinazowakabili wakulima wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Dunstan Kitandula kwa namna anavyofuatilia masuala ya spices kwa niaba ya wakulima hapa nchini ikiwemo Jimboni kwake. Nimeshamhakikishia kwamba Serikali kwa kutambua kwamba spices hizi zina potential kubwa ya kutuingia fedha za kigeni, niko tayari kwenda Mkoa wa Tanga na kufika maeneo ambayo ameyataja kuhakikisha wakulima hawa tunawasaidia kwenye upande wa kuzalisha kwa tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo tunawasaidia kwenye mambo ya branding na mikakati ya kimasoko ili kilimo chao kiweze kuwasaidia kuwakwamua kutoka kwenye umaskini, lakini uzalishaji wao usaidie kuchangia kwenye fedha za kigeni za nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kueleza masikitiko yangu kwa jinsi ambavyo wataalam wetu wanawapotosha Mawaziri wetu. Eneo tunalolizungumzia ni sehemu ya skimu ya umwagiliaji inayogusa vijiji vitatu katika Kata ya Mwakijembe yenye ukubwa wa takribani hekta 450 na tayari Serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 1.2 kuendeleza skimu hii. Kwa hiyo, siyo kweli kwamba sehemu tunayoizungumzia ilikuwa ni shamba darasa isipokuwa ni sehemu ya skimu ya umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, eneo lililochukuliwa siyo hekari moja kama inavyozungumziwa bali ni takribani hekari 50, watu takribani 28 wamekumbwa na kadhia hii. Kwa sababu Waziri amepotoshwa, je, yupo tayari kuja kujionea yeye mwenyewe kule Mkinga ili wananchi hao watendewe haki?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa jambo hili nimekuwa nikilizungumza mara kwa mara hasa kwenye michango yangu ya maandishi nimekuwa nikitoa na takwimu ya uonevu huu na mara ya mwisho nilisema ni watu 14 na hii ilikuwa mwaka jana sasa imeongezeka wamekuwa watu 28 na sasa ni hekari karibu 50 zimechukuliwa. Je, Waziri yuko tayari kutoa tamko hapa la zuio kwamba kikosi kile kilichopo kule kiache tabia hii ya kuchukua ardhi ya wananchi bila ridhaa ya kijiji?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa takwimu zilizopo katika Wizara yangu na zile anazotoa Mheshimiwa Mbunge zinapishana, nadhani ni busara tukafanya kile alichoomba kifanyike nacho ni mimi kufanya ziara katika eneo hilo ili kukagua kwa pamoja kati ya upande wetu sisi kama Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa tukifuatana na wataalam wa Jeshi pamoja na watu wa Wilaya na Kijiji husika ili tuthibitishe ukubwa wa eneo lililochukuliwa na nani anayewajibika kulipa fidia. Endapo itathibitika kwamba Serikali kwa upande wetu Wizara ya Ulinzi inalazimika kulipa fidia basi tutafanya hivyo.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti ninakushukuru, ninaomba niulize swali dogo moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ipo kwenye hatari kubwa la kupoteza fedha takribani shilingi bilioni moja na milioni 600 kutokana na mkandarasi wa Mradi wa Mbuta kuvunja mkataba, lakini vilevile mkandarasi wa Mwakijembe kuamua kusimama kufanya kazi kwa sababu ya uchelewashaji wa fedha.

Ni lini Serikali itachukua hatua za haraka kuhakikisha inaokoa fedha hizi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kaka yangu Dastan Kitandula kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika jimbo lake pale Mkinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti sisi kama Wizara ya Maji tulishasema kwamba hatukuwa na kisingizio chochote, kwamba sasa hivi mmetupa rungu kwa maana uazishwaji wa RUWASA kwa maana Wakala wa Maji Vijijini na tumejipanga vizuri kwa maana agizo la Mheshimiwa Waziri kwa maana baadhi ya miradi ya tutaifanya kwa kutumia wataalamu wetu wa ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kumhakikishi katika Mkandarasi yule aliyeondoka site hatuna nafasi tena ya kubembelezana ile kazi tutaifanya kupitia wakala wetu wa maji kwa maana ya Uchimbaji wa Maji Visima (DDCA) nawaagiza waende kuifanya kazi ile mara moja ili wananchi waweze kupata maji. Lakini kuhusu mkandarasi ambaye ametekeleza mradi hajalipwa certificate, nataka nimhakikishie ndani ya mwezi huu wa tisa tutamuweka katika orodha ili kuhakikisha kwamba tunamlipa ili wananchi waendelee kutekelezewa mradi wa maji, ahsante sana.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, na kama ulivyosema, ni kweli kwamba swali hili ni la muda mrefu. Kwa kuwa wananchi wa Mkinga wanazo taarifa kwamba mtaalam huyu amekwishapatikana tangu mwezi Novemba, na ilikuwa waingie mikataba lakini yakawa yanafanyika majadiliano yaliyokuwa na lengo la kupunguza scope ya kazi kwa vijiji vile 37, jambo ambalo limeleta taharuki. Je, Waziri yuko tayari kutuhakikishia kwamba hayo majadiliano hayatapunguza wigo ambao utawahakikishia wananchi wa Mkinga vijiji vile 37 vyote vipate maji? (Makofi)

Swali la pili, kwa kuwa mradi wa Horohoro umepigiwa kelele sana kwa muda mrefu na sasa unakwenda kutimia, kutekelezwa, na mwezi wa sita sio mbali. Je, Waziri yupo tayari mwezi wa sita utakapofika atoe ahadi kwamba ataandamana na mimi kwenda kuweka msingi wa kuanza ujenzi wa mradi ule kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kiukweli nitumia nafasi hii, dhati ya moyo wangu kwanza kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, amekuwa mfuatiliaji mkubwa sana si kuchangia tu Bungeni lakini hata ofisini amekuwa akija mara kwa mara kuhusu suala zima la mradi huo.

Mheshimiwa Spika, sisi kama viongozi wa Wizara tulikwishasema kwamba hatutakuwa kikwazo kwenye utekelezaji wa miradi ya maji. Wakati mwingine tunatumia muda mrefu sana kwa kuwatumia wakandarasi wetu, sisi kama viongozi tumejadiliana tumeona haja sasa kazi zile zifanywe na wataalam wetu wa ndani ili kuhakikisha kwamba hii kazi inafanyika kwa haraka na wananchi wake waweze kupata maji safi na salama katika kuhakikisha kwamba tunamtua mama ndoo kichwani.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Wizara ambayo yanatupa matumaini, nina maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa survey iliyofanyika Hemsambia ilifanyika kwa vitongoji viwili na kuacha vitongoji vingine vitano. Je, Waziri anatuthibitishia kwamba, kwa azma ile ya kuhakikisha kwamba, kila kijiji kinapofikiwa lazima kijiji chote kipate umeme; Je, vitongoji hivi vitajumuishwa kwenye kupatiwa umeme?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, wakati tunapeleka umeme kwenye Kata ya Bosha maeneo ya Vitongoji vya Miyongwe, Kwemsakazi, Kwashemwaondwa na Kibago B yalirukwa, lini maeneo haya yatapatiwa umeme?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi la Mheshimiwa Kitandula, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga na pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, katika maswali yake mawili ya nyongeza kwanza ni kweli, kwenye Kijiji cha Hemsambia tulifanya survey vitongoji viwili na tukabakiza vitongoji vitano ambavyo tayari wakandarasi tumeshaviingiza kwenye
marekebisho na yanafanyiwa kazi. Na hivi sasa Mheshimiwa Mbunge, pamoja na kupongeza, tulipokuwa katika jimbo lako wiki iliyopita tulitoa maelekezo na wakandarasi wameshaanza kuyafanyia kazi. Kwa hiyo, niwape taarifa tu Wananchi wa vitongoji vitano vya Kijiji cha Msambia kwamba, vitongoji vyote katika kijiji hicho vitafanyiwa kazi na vitakamilika mwezi Septemba mwaka huu.

Mheshimiwa Spika, katika swali la msingi la pili la Mheshimiwa Mbunge, ni kweli tunazo kata tano muhimu sana kwa Mheshimiwa Mbunge, lakini Kata ya Bosha yenye vijiji vinne vikiwemo Kijiji cha Kwashemhonda, pamoja na Kwesekazi, pamoja na Kibango vimeshaanza kufanyiwa kazi na Shirika la Umeme – TANESCO kwa sababu, sasa hivi bei ni ileile 27,000/=. Na jana tumewasiliana na Mheshimiwa Mbunge alikuwa kufuatilia na TANESCO pamoja na wataalamu wameshaingia site kuanzia leo. Kwa hiyo, ni matumaini yetu Mheshimiwa Mbunge na Wananchi wa Mkinga muwe na matumaini kwamba, Kata na Vijiji vyote vya Bosha vinakwenda kupatiwa umeme mwisho wa mwezi Disemba mwaka huu.