Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dunstan Luka Kitandula (6 total)

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza:-
Serikali iliweka Wilaya ya Mkinga kuwa miongoni mwa Wilaya za kipaumbele kujengewa Chuo cha VETA.
Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi ya kujenga Chuo cha VETA Wilayani Mkinga?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali naomba kama itakupendeza, kupitia Bunge lako tukufu niwapongeze na kuwatakia kila la kheri vijana wetu 960,202 wanaofanya mitihani ya darasa la saba leo kwenye shule tofauti 16,845. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa ajili ya kuandaa rasilimaliwatu watakaotumika katika viwanda na shughuli nyingine za uzalishaji, hasa wakati huu ambapo Serikali imeazimia kufanya nchi yetu kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Vyuo hivi vitasaidia kuwaandaa vijana ili waweze kujipatia ajira kwa kujiajiri au kuajiriwa ikizingatiwa kuwa kundi kubwa la vijana wetu halipati fursa ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na mpango wake wa ujenzi waVyuo vya Ufundi Stadi vya Mikoa na Wilaya, ikiwemo Wilaya ya Mkinga, kutegemeana na upatikanaji wa fedha. Lengo ni kila Mkoa na Wilaya kuwa na Chuo cha Ufundi Stadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Stadi za Kazi (Education and Skills for Productive Jobs – ESPJ) ambapo kupitia Mradi huu Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC’s) vitakarabatiwa ili kuongeza fursa za mafunzo. Hivyo, katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea na jitihada hizi, nashauri wananchi wa mikoa na wilaya zote ambazo hazijawa na Vyuo vya VETA kutumia Vyuo vya Ufundi vilivyopo nchini, hususan kwenye mikoa na wilaya jirani ili vijana wetu waweze kupata ujuzi na stadi muhimu kwa maendeleo ya nchi kwa ujumla.
MHE. DUSTAN L. KITANDULA aliuliza:-

Katika kuimarisha ulinzi wa mipaka yetu na nchi jirani ya Kenya, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limechukua mashamba ya baadhi ya wananchi wa Kata ya Mwakijembe:-

Je, ni lini wananchi hao watapewa fidia kwa ajili ya ardhi/mashamba yao yaliyochukuliwa na Jeshi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limeanzisha Kituo cha Ulinzi katika eneo la Kata ya Mwakijembe, Wilaya ya Mkinga lenye hekari moja mwaka 2017. Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga iliona umuhimu wa kutenga eneo hilo kwa matumizi ya Jeshi ili kuimarisha ulinzi kwenye maeneo ya mpakani. Eneo hilo awali lilikuwa ni shamba darasa la mradi wa umwagiliaji uliokuwa unaendeshwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa eneo hili lilikuwa linasimamiwa na uongozi wa Wilaya kabla ya Jeshi kuingia hapo, ni busara suala la fidia kama lipo likawasilishwa kwenye uongozi wa Wilaya ya Mkinga.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA (K.n.y. MHE. DUNSTAN L. KITANDULA) aliuliza:-

Kata za Kigongoi, Mhinduro na Bosha Wilayani Mkinga zinalima kwa wingi viungo vya chakula kama vile hiliki, mdalasini, pilipili manga na karafuu:-

Je, Serikali ipo tayari kuwawezesha Wakulima hao kupata mbegu bora ili waweze kuongeza uzalishaji wa mazao yao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwekeza katika mazao mbalimbali ya kilimo yakiwemo mazao ya viungo ambayo mahitaji yake yanaendelea kuongezeka ndani na nje ya nchi. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imeanza kufanya utafiti wa kupata mbegu bora za mazao ya viungo na mazao mengine ya bustani aina ya horticulture ili kuongeza uzalishaji na tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inapitia Sera ya Kilimo ya Mwaka 2013 ambapo sekta ndogo ya mazao ya bustani ni miongoni mwa maeneo muhimu yanayozingatiwa. Vilevile, kutokana na umuhimu wa mazao hayo, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo itafanya kikao cha wadau wa mazao hayo tarehe 8 Novemba, 2019 ili kuandaa Mkakati wa Miaka Mitano wa Kuendeleza Mazao ya Bustani. Mkakati huo unalenga kuongeza uzalishaji, ubora wa mazao na kuimarisha mifumo ya masoko ya mazao hayo. Aidha, mkakati huo utakuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa unaolenga Taifa letu kufikia uchumi wa kati mwaka 2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hatua hizo, Serikali inaendelea kutoa elimu ya kilimo bora cha mazao ya viungo na mazao mengine; uhifadhi, usindikaji na masoko kwa kushirikiana na Sekta Binafsi kikiwemo Chama cha Wadau wa Mazao ya Viungo Tanzania (Tanzania Spices Association – TASPA), Sustainable Agriculture Tanzania (SAT) na vyama vingine vya wakulima.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza:-

Je, ni lini mradi wa maji kutoka chanzo cha Mto Zigi kwenda Mkinga na Horohoro utaanza?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Jimbo la Mkinga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeshaanza maandalizi ya mpango wa utekelezaji wa mradi wa kutoa maji Mto Zigi kwenye mji wa Kasera ambao ni Makao Makuu ya Wilaya ya Mkinga, pamoja na Mji wa mpakani wa Horohoro. Kwa sasa taratibu za kumpata Mtaalam Mshauri atakayefanya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na uandaaji wa makabrasa zabuni zinaendelea. Matarajio ni Mtaalam Mshauri atakayepatikana atakamilisha kazi hiyo mwezi Septemba, 2019. Ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuanza baada ya kukamilika kwa usanifu.

Mheshimiwa Spika, wakati tunasubiri usanifu wa mradi wa kutoa maji Mto Zigi kukamilika, Serikali imeandaa mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji kwa mpango wa muda mfupi katika Mji wa Horohoro kwa gharama ya kiasi cha shilingi milioni 595. Kazi zitakazotekelezwa ni ulazaji wa bomba, ujenzi wa mtambo mdogo wa kusafisha na kutibu maji, ukarabati wa tanki la maji na ujenzi wa vituo vitano vya kuchotea maji. Mradi huo unatarajiwa kuanza mwezi Juni, 2019 na kukamilika baada ya miezi sita.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka umeme wa REA III katika Kijiji cha Hemsambia na Vitongoji vyake vyote?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Vijiji vya Hemsambia na Kindundui ni miongoni mwa Vijiji vya Kata ya Kigongoi, Wilaya ya Mkinga vilivyofaidika na Awamu ya Tatu ya utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini, REA III, mzunguko wa kwanza. Mkandarasi Kampuni ya Ubia ya JV Radi Service Limited, Njarita Contractor Limited na Aguila Contractor Limited yuko site anaendelea na kazi ya kusambaza umeme katika maeneo husika.

Mheshimiwa Spika, kazi za kupeleka umeme katika Vijiji vya hemsambia na Kindundui imejumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 2.1, njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa mbili, ufungaji wa transfoma mbili za KVA 50 pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 62. Gharama ya mradi ni shilingi milioni 184.23.

Mheshimiwa Spika, vijiji vingine vya Kata ya Kigongoi vya Vuga, Kwekuyu, Kindundui, Mgambo Shashui na Bombo Mbuyuni vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA III Mzunguko wa Kwanza unaoendelea kutekelezwa Wilayani Mkinga na kukamilika mwezi Juni, 2020. Ahsante sana.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza:-

Kijiji cha Segoma Wilayani Mkinga ni miongoni mwa vijiji vitakavyopata umeme wa REA III.

Je, kwa nini Serikali isitumie fursa hiyo kuunganisha umeme katika Sekondari ya Lanzoni iliyopo karibu na Kitongoji cha Darajani?
WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Mkinga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) inatoa kipaumbele kupeleka umeme katika Taasisi za umma na za kijamii ikiwa ni pamoja na Shule za Awali, Msingi na Sekondari, Vyuo vya Ufundi Stadi, Vituo vya Afya, Zahanati, Visima vya Maji na Nyumba za Ibada.

Mheshimiwa Naibu Spika, Katika Mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali kupitia TANESCO inaendelea na kazi ya kusambaza umeme katika Vijiji vya Mgamboshashui, Kumbamtoni na Mpale. Kazi hiyo inahusisha kupeleka umeme katika Shule za Sekondari Duga na Lanzoni zilizopo katika Jimbo la Mkinga.

Mheshimiwa Naibu Spika, Gharama ya kazi ya kupeleka umeme katika vijiji hivyo vitatu pamoja na shule hizo za Sekondari ni Shilingi Milioni 91. Utekelezaji wa kazi hiyo ulianza mwezi Machi, 2020 na utakamilika mwezi Mei, 2020. Jumla ya wateja wa awali zaidi ya 175 wataunganishiwa umeme.