Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dunstan Luka Kitandula (27 total)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuhitimisha hoja yangu. Nianze kwa kuwashukuru Waheshimiwa Bunge ambao wamepata fursa ya kuichangia hoja hii na kutoa mchango wa mawazo. Hoja hii imechangiwa na jumla ya Waheshimiwa Wabunge 27, katika hao Wabunge 25 wamechangia kwa kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge wanne wamechangia kwa maandishi. Katika hao wanne waliochangia kwa maandishi lakini vilevile walizungumza, kwa hiyo, tunabaki na Waheshimiwa Wabunge wawili ambao walichangia kwa maandishi. Kwa hiyo jumla ni Waheshimiwa Wabunge 27.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuchangia hoja hizi karibu kila Mheshimiwa Mbunge ameunga mkono hoja ya Kamati yetu. Kwa hiyo, nitumie fursa hii kuwashukuru sana kwa kuunga mkono hoja za Kamati hii. Vilevile kwa niaba ya Kamati, nichukue fursa hii kuwashukuru kwa pongezi mlizotoa kwa kazi iliyofanywa na Kamati, tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri ambao wamefanya kazi kubwa ya kujibu sehemu kubwa ya hoja zilizokuwa zimetolewa. Zipo hoja ambazo zilikuwa ni nje ya hoja ya Kamati, kwa hiyo, sitarajii kuzijibu lakini tunazichukua kama rejea ya Kamati kwa ajili ya kuzifanyia kazi kwa siku zijazo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitajikata katika maeneo manne yaliyojitokeza kwa upana ambayo Waheshimiwa Wabunge kwa uwingi wao waliyagusia. Eneo ya kwanza ni eneo la REA. Waheshimiwa Wabunge wameonesha kwamba Mradi wa kupeleka Umeme Vijijini ni hitaji la kila Mtanzania na kwamba kama Taifa tuna kila sababu ya kuhakikisha tunafanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba tunakamilisha utekelezaji wa miradi hii kwa wakati. Kamati iliainisha changamoto kadhaa ambazo bahati nzuri na Waheshimiwa Wabunge wamezitolea maelezo. Niishukuru Serikali imekubali kufanyia kazi changamoto zote zilizojitokeza upande wa REA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni umeme wa Mto Rufiji. Namshukuru Mheshimiwa Waziri ametoa maelezo ya kina sana katika eneo hili. Mradi huu kama tunavyofahamu utachukua miezi 36 ya utekelezaji. Mradi huu ulitiwa saini Desemba, 2018 na baada ya kutiwa saini miezi sita itakuwa ni kipindi cha mkandarasi kuji-mobilize kabla ya kuanza kuutekeleza mradi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Kamati tunasema mradi huu ni wetu. Kwa hiyo, kama Taifa kwetu sisi mradi huu ni wa kufa na kupona. Tulipofika sasa siyo sehemu tena ya kuzodoana na kurudishana nyuma, tulikofika sasa ni kusema tunafanya vipi vizuri zaidi ili mradi huu, hiki chetu kiweze kufanikiwa vizuri. Ndiyo maana katika mapendekezo yetu kama Kamati tumeiomba Serikali ihakikishe kwamba tunasimamia vizuri utekelezaji wa mradi huu na kwamba fedha za utekelezaji mradi huu zitolewe kwa wakati ili usiweze kukwama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine linagusa mapendekezo ya wadau wa sekta ya madini. Waheshimiwa Wabunge wengi waliozungumza wameonesha ipo haja kubwa ya kuwawezesha wachimbaji wadogo. Wameonesha nia na matarajio kwamba tukiisimamia vizuri sekta hii basi mchango wake utakuwa mkubwa kwa uchumi wa Taifa letu. Hicho ndicho ambacho sisi katika Kamati tulikiona na ndiyo maana tumependekeza yale mapendekezo yote ya mkutano wa wadau yafanyiwe kazi. Nafurahi kwamba Mheshimiwa Waziri wa sekta husika ameonesha utayari wa kuyafanyia kazi maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo limezungumzwa kwa mapana na kwa hisia tofauti ni mradi wa Songas na mikataba yake. Mazungumzo yalivyoendelea hapa ndani yalijikita zaidi kwenye mradi Songas lakini sisi tuliiangalia sekta nzima ya gesi nchini tukifanya rejea ya Kamati ndogo iliyoundwa na Mheshimiwa Spika ya kuishauri Serikali jinsi Taifa linavyoweza kunufaika na mapato ya gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili tunampongeza sana Mheshimiwa Spika kwa ujasiri na umakini mkubwa alioufanya kwa kuunda Kamati ile. Namshukuru Mungu nilipata fursa ya kupata nafasi ya kuongoza Kamati ile. Ni Kamati iliyokuwa na watu wa makini, ushauri uliotolewa sina hofu na mashaka hata kidogo kwamba ukifanyiwa kazi utatutoa hapa tulipo ili Taifa liweze kunufaika na rasilimali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, rai yetu kama tulivyoonesha kwenye mapendekezo yetu ni kwamba jambo lile lifanyiwe kazi ili tuweze kurekebisha kasoro zilizojitokeza. Nafurahi kusikia kwamba Serikali inasema imeanza kufanyia kazi jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, lipo jambo lilijaribu kusemwa mwanzo hapa kwamba taarifa hii pengine siyo matokeo ya kazi ya Kamati. Napenda niwahakikishie taarifa hii ni matokeo ya mchango wa mawazo ya Kamati. Kamati ilikutana tarehe 24 kujadili rasimu ya kwanza ya taarifa ya Kamati, wakatoa mapendekezo. Kamati ilikutana tarehe 25 kujadili mapendekezo waliokuwa wameyatoa mwanzoni. Kumbukumbu za vikao hivyo ninazo hapa, ukihitaji tutaweza kuziweka Mezani. Ndiyo maana hata mapendekezo yaliyotolewa na wasemaji yalishabihiana moja kwa moja na kile ambacho Kamati ilikipendekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naomba sasa Bunge lako liridhie na kuidhinisha maoni na mapendekezo ya Kamati ili yawe ni maamuzi ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Kamati naomba niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia katika hoja yetu. Katika mjadala huu, Waheshimiwa Wabunge ambao waliochangia Taarifa yetu ni Wabunge 14. Sehemu nyingi ya michango hii ilikuwa ni ushauri, tunaichukua michango ile kama ushauri lakini yako mambo machache ambayo nilidhani ni vizuri tuyatolee ufafanuzi.

Mheshimiwa Spika, Kaka yangu Mwijage amesema hapa kwamba mimi nimepitia kwenye mikono yake, ni kweli. Kipindi kile naanza kufinyangwa katika Utumishi wa Umma nilianzia pale TPDC na miongoni mwa watu waliofanyakazi kubwa ya kutuonyesha sekta ya Nishati iko vipi ni Kaka yangu Mwijage, na siku zote manshukuru sana kwa kazi kubwa aliyoifanya.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mwijage ameibua mambo makubwa katika Taarifa yetu. Kwanza ameonesha hofu kwamba yapo mambo ya msingi hatukuyatendea haki katika taarifa yetu. Jambo kubwa alilolizungumzia ni uwekezaji unaofanywa na TPDC katika suala zima la kutafiti mafuta na gesi. Ukipitia taarifa yetu ni kweli hatulisema kwa undani jambo hili; na tulifanya hivi makusudi kwasababu mbili:-

Mheshimiwa Spika, jambo hili tumekuwa tukilisema mara kwa mara kwenye Taarifa zetu zilizopita; ni jambo ambalo Serikali inalifanyiakazi. Nataka nimtoe hofu; katika Bajeti tuliyopitisha hapa tulitenga fedha kwa ajili ya kazi ya utafiti; ipo kazi inaendelea kufanywa na TPDC. Hata hivyo kama Kamati tuliamua kufanya uamuzi wa makusudi wa kutoliibua sana jambo hili ndani ya nyumba yako hii kwasababu tuna mfano halisi, nchi inapojenga matumaini makubwa kwa wananchi msipoya-manage matumaini hayo mnaweza kuzalisha tatizo ndani ya Nchi.

Mheshimiwa Spika, kwahiyo kimsingi tuliamua ku-manage expectation kwa taifa letu; na kama kuna jambo ambalo huwa linajenga matumaini makubwa kwa wananchi ni wanaposikia suala la mafuta. Ukiwaambia tu kuna utafiti kesho yake asubuhi wanakwambia nchi yetu ina mafuta. Kwahiyo tulidhani tuwe makini katika kufanya jambo hili. Itoshe kusema, katika bajeti ya mwaka huu tulitenga shilingi bilioni 33.2 kwa ajili ya Kitalu cha Mnazi Bay kule Kaskazini. Ipo kazi inafanywa kule na TPDC, zipo kazi zimeshafanyika, anatafutwa mshauri mwelekezi ili aweze kushauri jinsi ambavyo tunaweza kufanyakazi ya kuchoronga visima kwa ajili ya utafiti wa mafuta.

Mheshimiwa Spika, vilevile kwenye kitalu cha Easi Wembere nako tulitenga bilioni 6.3, ipo kazi inafayika na kazi inakwenda vizuri. Pia lipo eneo la Kitalu Namba Nne kwenye maji ya bahari ya kina kirefu, tulitenga bilioni 22.62, ipo kazi inaendelea. Nataka niliambie Bunge hili kwamba utafiti uliofanya na TPDC ulitumia the best technology in the World katika kufanya utafiti wa kupata mambo haya. Kwahiyo, itoshe kusema kwamba ipo kazi kubwa inafanyika.

Mheshimiwa Spika, lipo jambo lingine kaka yangu Mwijage amelisema. Hili msingi wake ni kazi ambayo Kamati imekuwa ikiifanya kwa muda mrefu. Hoja ya kuwa na hifadhi ya pamoja (Strategic reserve) ya mafuta katika nchi hii ni hoja ambayo Kamati yangu imekuwa ikiishughulikia kwa muda mrefu. Hivi tunavyozungumza, TPDC ina mkakati wa kutumia matenki yaliyopo Kigamboni kufanya ukarabati ili matenki yale yaweze kuhifadhi mafuta. Kama haitoshi, TPDC imeshapata maeneo kule Tanga kwa ajili ya kujenga matenki ya kuhifadhi mafuta.

Mheshimiwa Spika, vilevile yamekuwepo mazungumzo kwamba tunaweza kutumia refinery yetu iliyoko kule Kigamboni ili kuwa na mfumo huu wa uingizaji wa mafuta kwa pamoja. Imekuwa na changamoto zake, wadau wamekuwa wakipishana, na jambo hili alikabidhiwa TR ili kuweza kuja na majibu ya jinsi gani tunatoka hapa. Kuna kazi inaendelea, kwasababu haijafika sehemu nzuri tulidhani tusillibue ndani ya Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hilo, wenzetu wa Mamlaka ya Bandari nao huenda wakaingia wkenye kujenga matenki haya ili yaweze kutumika katika uhifadhi wa mafuta. Ninachoweza kukubaliana nae ni kwamba ni kweli, jambo hili ni la msingi sa, pengine tumechelewa kulifanyiakazi, ni vizuri Serikali ikaongeza kasi katika kushughulikia jambo hili.

Mheshimiwa Spika, amezungumzia katika suala la upotevu wa mafuta, amezungumzia suala la flow meter na margin; haya ni mambo ambayo yanajenga ule msingi wa dhamira yetu ya kuwa na hifadhi ya pamoja ya mafuta. Kwahiyo, nimuondoe hofu, mambo haya Kamati inayashughulikia.

Mheshimiwa Maige kuna jamno amelibua la utozaji wa loyalty katika mawe lakini vilevile katika dhahabu. Hili tunalichukua, nikuahidi Kamati itali-persue tuone tunatokaje katika mkwamo huu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja, ahsante sana. (Makofi)

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DUSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili nichangie kwenye Mpango uliowasilishwa na Serikali. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye kwa rehema zake amenipa kibali niwe miongoni mwenu kuwatumikia Watanzania kupitia Bunge hili Tukufu. Vile vile, nitumie fursa hii kuwashukuru sana ndugu zangu wa Mkinga kwa kunipa heshima kwa mara ya pili, kuwa Mbunge wao niweze kuwawakilisha katika Bunge letu ninawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaahidi kuwatumikia kwa uwezo wangu wote kwa maarifa ya hali ya juu, na niimani yangu kwamba, kile tunachokikusudia tutakipata. Nitumie fursa hii vilevile kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo ameanza kushika hatamu za kuliongoza Taifa letu. Watanzania wana imani kubwa na uongozi wake, nimpe maneno ya kumu- encourage kwamba, tupo pamoja naye katika kuwatumikia Watanzania na Watanzania wanaamini kwamba, kasi ya mabadiliko waliokuja nayo itakuwa ni kasi ya ukweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie maneno, niazime maneno ya Rais wa 33 wa Marekani aliyekuwa akiitwa Harry Truman aliandika katika memo yake, Years of Trial and Hope katika ile volume ya pili anasema, „‟Being a President is like riding a tiger, a man has to keep on riding or be swallowed.”
Anaendelea kusema: “A President either is constantly on top of events or if he hesitate events will soon be on top of him.” Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumwambia Mheshimiwa Rais Watanzania wana imani naye, aendelee na mwendo huo aliouanza nao bila ku-hesitate, tunaiona Tanzania yenye mabadiliko na mafanikio makubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo sasa nichangie mpango huu ulioko mbele yetu. Nimejaribu kuusoma mpango huu, lakini vilevile nikapata fursa ya kusoma Household Survey Report, lakini vile vile nikasoma report ile Human Development Report nikajaribu ku-combine maudhui tunayoyapata kutokana na taarifa zile. Maudhui ya taarifa zile yanatuambia kwamba tuna namba nzuri sana za mafanikio ya ukuaji wa uchumi. Namba zile zinatofautiana, ukisoma household survey na ile report nyingine zinatofautiana takwimu kidogo lakini bottom line ninachosema ni kwamba, hatujafanya vizuri sana katika maendeleo ya binadamu, maendeleo ya watu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi ni viongozi lazima tuwe wakweli kwamba, tuna changamoto kubwa mbele yetu ya ku-translate ukuaji wa uchumi ili uweze kuleta maendeleo ya watu. Ndiyo maana hapa naipongeza Serikali kwa kutuletea Mpango huu wa Pili ambao una vionjo vinavyoonyesha kwamba, tunakwenda sasa kwenye kuunganisha ukuaji wa uchumi lakini vilevile ku-translate ukuaji huo kwenye maendeleo ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia kujenga uchumi wa viwanda ambavyo vitazalisha ajira, viwanda ambavyo vitapelekea kupunguza umasikini, tunaelekea huko. Lakini lazima tujiambie kama viongozi, tuwe wakweli tujiambie kwamba mMango huu tuliouleta ambao tunaenda kuufanyia marekebisho ili baadaye uje upitishwe ndani ya Bunge hili, utekelezaji wa Mpango huo tutakaokuwa tumeuleta, ukiwa chini ya asilimia 70 tutakuwa tumeshindwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima tuwe na mikakati madhubuti ya kuhakikisha hatushindwi. Takwimu zinatuambiaje, takwimu zinatuambia tulilenga kuwa na maeneo ya kilimo cha umwagiliaji hekta 1000 tumetoka kutoka kwenye hekta 345 tumekwenda kwenye hekta 461. Lakini hekta tulizonazo zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji katika nchi yetu tuna hekta milioni 29.1, tulichofanikiwa ni asilimia 0.39.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuje na mikakati ya kuhakikisha tunakwenda mbele. Nimeona hapo ujenzi wa viwanda, ujenzi wa bandari ya uvuvi ni jambo zuri, lakini ili tufanikiwe lazima tuunganishe jambo hili la ujenzi wa bandari ya uvuvi tuliunganishe na jambo la ufugaji wa samaki maana dunia ndiyo inapokwenda huko. Haiwezekani leo hii nusu ya samaki wanaoliwa duniani wanatokana na ufugaji wa samaki halafu sisi tusione umuhimu wa kufuga samaki, lazima tubadilike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari ile itakapojengwa lazima tujenge miundombinu ya ufugaji wa samaki, twende kisasa lazima tuwe na aquaculture industrial zone. Tuunganishe pale, bandari ya uvuvi, viwanda vya kuchakata samaki, viwanda vya kuchakata barafu na kadhalika na kadhalika na ufugaji wa samaki uwe pale pale. Katika maeneo yaliyotajwa katika kujenga bandari. Nilisema kipindi kilichopita iliainishwa bandari ya Dar es Salaam wote tunajua. Bandari ya Dar es Salaam hapafai kuna msongamano mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, Moa kule Mkinga namshukuru Rais maana kila alipokuwa akisimama kutoa hotuba yake anasema ukanda wote wa bahari kutoka Moa kule Tanga mpaka Mtwara hakuna kiwanda cha samaki. Njooni pale Moa wekeni bandari ya uvuvi maana katika maeneo yaliyotajwa matatu Moa ipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu lilitajwa Bagamoyo lakini Kamati iliyopita ilitushauri hapa ndani. Ikasema hivi tunaondoaje Chuo cha Mbegani, twende tukajenge bandari ya uvuvi, ni imani yangu Serikali imesikia njooni Moa tuweke mambo vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa viwanda lazima uzingatie vile vile kuweka mkazo kwenye kujenga.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Muda wako umekwisha.
MHE. DUSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili nami nipate wasaa wa kuchangia kwenye Bajeti iliyoko mbele yetu. Namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma kwa kunipa tunu ya uhai. Kwa namna ya kipekee niwashukuru wananchi wa Mkinga kwa heshima waliyonipa ya kuwa mtumishi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kugusia eneo la afya. Mwezi Februari, tulizindua taarifa ya tathmini ya utoaji wa huduma za afya nchini. Taarifa ile ukisoma inakupa matumaini kweli kweli. Ni taarifa inayosema kwenye vituo vya afya vya private sector, huduma za afya za mtoto zinatolewa kwa asilimia 80, lakini kwenye vituo vya Serikali huduma za kisasa za huduma ya mama na mtoto zinatolewa kwa asilimia 97. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali lakini napongeza yale yaliyomo kwenye taarifa ile. Nilipokuwa nikiisoma taarifa ile nikasema hapa barabara, kwenye suala la universal health tunakwenda vizuri; lakini nikapata mashaka makubwa nilipokuja kuiona hotuba. Nilipokwenda ukurasa wa 32, ukajaribu kunionyesha mambo tofauti. Ukurasa ule utuambia katika Halmashauri 181, Halmashauri 84 ndiyo zina hospitali za Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri 97 zinapata kudra ya Mwenyezi Mungu ya huduma kutoka kwa Taasisi za Mashirika ya Dini na kadhalika. Hili likanishtua kwa sababu Mkinga leo hii tunapozungumza, Wilaya iliyoanza mwaka 2005 na kupata hadhi ya kuwa Halmashauri mwaka 2007 mpaka leo hatuna Hospitali ya Wilaya. Tunapata huduma kutoka Tanga kwenye Hospitali ya Bombo, tunapata huduma kwenye Hospitali ya Wilaya ya Muheza. Tumekuwa tukitenga kwenye bajeti fedha kwa ajili ya ujenzi tangu mwaka 2011, fedha haziji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ndani utaambiwa kwamba nendeni mkatenge kwenye bajeti. Tunatenga, fedha haziji! Tusaidieni! Tusaidieni ili watu wetu waweze kupata huduma hizi, maana Serikali ina wajibu wa kulinda maisha ya watu wake. Wananchi wametuamini, tuwatendee haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma hotuba hii ukurasa wa 32 ule, unatuonyesha kwamba tunatakiwa kuwa na direction mpya ya kuhudumia mambo. Sweeping statement kwamba tunataka kila kijiji kiwe na zahanati, tunataka kila kata iwe na kituo cha afya, pekee haitoshi tunatakiwa tufanye zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zile ukiziangalia zinaogopesha! Vituo vya afya 484 katika kata 3,506. Maana yake, tumeweza kujenga vituo vya afya 12% tu katika maeneo yetu, hii haikubaliki hata kidogo! Tuna vijiji 12,500 na kitu, vijiji 8,043 havina zahanati. Maana yake nini? Maana yake tumeweza kupeleka huduma hii kwenye vijiji siyo zaidi ya asilimia 36. Lazima tubadilike! Mkakati wetu wa kutufikisha kwenye kutoa huduma hizi una walakini. Mawaziri mliopo kwenye Wizara hizi, tunawaamini, tunaamini mtatoa uongozi utakaotutoa hapa twende mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Nataka ni-declare interest, mimi nimetoka kwenye huduma hizi za fedha. Kumbukumbu zangu zinanionyesha, zimekuwepo jitihada mbalimbali za kupelekea huduma za kifedha kwa wananchi, kuwawezesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbukumbu zangu za haraka haraka zinaniambia tumekuwa na miradi takribani 17 yenye lengo la kutoa huduma za kifedha kwa wananchi. Utazungumzia SELF, utazungumzia PRIDE, utazungumzia mradi wa huduma za kifedha vijijini, utazungumzia miradi ya vijana; miradi karibu 16, yote hii inafanyika kwa lengo zuri la kuwawezesha wananchi, lakini changamoto tuliyonayo, mitaji hiyo haitoshi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuja na Shilingi milioni 50 hizi kwa kila kijiji; tusiende kichwa kichwa. Wapo wenzetu walikwenda hivi wakaumia. Uganda walianzisha mradi wa namna hii wakiuita Entandikwa. Mwaka 2000 nilikuwa Uganda nikaenda kuungalia, repayment 0%, hakuna hela ilirudi. Wenzetu wa Thailand walifanya kitu cha namna hii, lakini wao walikuwa makini kidogo, mambo yao yamekwenda vizuri. Tusiwe na haraka ya kutoa fedha hizi bila ya kuwa na utaratibu makini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mifumo yetu ya kifedha, Bunge lililopita tulikuwa tunalalamika hapa, tunasema tupewe mitaji ya kuwezesha kuanzisha community bank. Leo hii community bank ukitaka kuianzisha, unazungumzia shilingi bilioni mbili. Kama tungekuwa makini, tungeweza kujipanga. Mimi nina vijiji 85, ukiniambia unapeleka shilingi milioni 50 kwenye kila kijiji, ni shilingi bilioni nne na kitu. Ningeweza kukwambia peleka Shilingi bilioni mbili ifunguliwe community bank ambayo kila mwananchi katika Wilaya yangu atakuwa na hisa kwenye benki hiyo na hizi fedha nyingine tuweze kuzikopesha. Tungekuwa na uhakika kwamba fedha hizi zitawafikia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimeambiwa mtakuwa na pilot katika kugawa fedha hizi. Twendeni kwenye hiyo pilot, lakini tuangalie vile vile uwezekano wa kuanzisha community bank kupitia fedha hizi. Wale tutakaoweza kuwa na regional bank, tukikubaliana mimi na Mheshimiwa January na wenzangu wengine wa Tanga tuwe na regional bank katika Mkoa wa Tanga, tukikubali kwamba mafungu yatoke kwenye fedha hizo ambayo inafikia shilingi bilioni tano kwa kuwa na regional bank, mtukubalie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji. Makao Makuu ya Wilaya ya Mkinga hayana maji. Kuna mradi pale tumebuni chanzo cha Kinyatu, tumeambiwa tutapata ufadhili wa Benki ya Dunia. Tumepeleka maandiko yanayotakiwa tupate mshauri mwelekezi tangu mwaka 2011, hakuna kitu! Tusaidieni watu wa Mkinga tupate huduma ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia bajeti iliyoko mbele yetu. Nitamke bayana kabisa kwamba naunga mkono bajeti hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa karama hii ya uhai na kwamba leo napata fursa ya kuzungumza ndani ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nizungumzie eneo la REA, nitumie fursa hii kupongeza kazi kubwa iliyofanywa na wenzetu wa REA, imefanyika kazi kubwa sana, kazi ambayo ripoti inaonesha kwamba tumefikia kupeleka umeme vijijini sasa kwa asilimia 40, ni jambo zuri. Wakati tumefanya kazi hii vizuri ni ukweli vilevile kwamba zipo changamoto kubwa sana katika utekelezaji wa miradi hii ya REA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Nishati, kwa hiyo nilipata fursa ya kuzungukia miradi ya REA, vilevile nina hazina ya uzoefu kwa miradi ya REA kule kwenye Jimbo langu. Kubwa tuliloliona ni kwamba kuna changamoto kubwa sana ya kusimamia utekelezaji wa miradi hii. Maeneo mengine yamerukwa kwenye vitongoji, maeneo mengine vijiji vimerukwa bila sababu za msingi na maeneo haya ni maeneo ambayo awali yalikuwemo kwenye mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilayani kwangu vipo vitongoji vimerukwa na bahati mbaya sana vitongoji vilivyorukwa wananchi wamekatiwa mazao yao ili umeme uweze kufika, mimea imekatwa hakuna fidia, lakini mwisho wa siku wanakosa umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano na hili Naibu Waziri analijua kwa sababu nililisema tukiwa kweye Kamati, kijiji ninachotoka mimi zimepelekwa nguzo 15, hivi nguzo 15 zinapelekaje umeme kwenye kijiji? Sasa matokeo yake taasisi muhimu kama zahanati, sekondari, shule za msingi zimekosa huduma hii, ukiacha wananchi ambao wamekatiwa mazao yao. Nadhani hii siyo sahihi tujitahidi katika kusimamia ili tuondokane na kero hii ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeliweka tena eneo hili la Kata ya Kigongoi kwa matumaini kwamba linaingia kwenye REA Awamu ya Tatu. Hivyo, naomba miradi hii ya REA tuisimamie iende vizuri, mapungufu yote ambayo yameonekana sasa yasije yakaathiri utekelezaji wa REA Awamu ya Tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haingii akilini, kwamba umeme unapelekwa kwenye kijiji lakini wananchi wanaambiwa umeme ulioletwa hauwawezeshi ninyi kuendesha mashine za kusaga unga na mambo kama hayo, tufanye marekebisho, tufanye usimamizi wa karibu ili changamoto hizi ziweze kuondoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine linalokwenda sambamba na hilo ni kukatika umeme katika maeneo ya Mkoa wa Tanga, nilisema hapa eneo la Maramba, mwenzangu Majimarefu akazungumzia kule Korogwe, dada yangu Chatanda akazungumzia Korogwe Mjini na Waziri akatuambia kwamba upo mradi mkubwa wa kuboresha upatikanaji wa umeme, naomba jambo hili lisimamiwe kwa karibu ili tuondokane na tatizo hili.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kwenye eneo la uchimbaji wa madini ya graphite. Taarifa zilizopo sasa zinasema Tanzania itakuwa miongoni mwa Mataifa makubwa yanayozalisha graphite, tutakuwa ndani ya nchi kumi zinazozalisha graphite ulimwenguni. Wakati tukielekea huko nataka tujiulize, tumejipanga namna gani kusimamia eneo hili ili yasije yakatukumba kama yaliyotokea malumbano wakati tunaenda kwenye uchimbaji wa dhahabu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwnyekiti, taarifa zilizopo ni kwamba tayari wapo wajanja wachache ambao hawastahili kuajiriwa kwenye sekta hii, makampuni ya nje yamewaajiri watu ambao vibali vyao vinatia mashaka kuajiriwa kwenye sekta hii, taarifa zilizopo zinasema wapo watu wameajiriwa kwa fani ambazo Watanzania wanaweza kuzisimamia. Hivi inakuwaje leo tunaajiri mtu wa sekta ya ununuzi kutoka Australia, kwamba Watanzania hawapo wenye uwezo wa kusimamia mambo haya? Mheshimiwa Waziri naomba tufanye due diligence katika mambo haya ili tusije tukaingia kwenye matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo taarifa kwamba ipo kampuni imepewa leseni, kampuni hiyo tunaambiwa inatoa asilimia tano ya hisa kwa Tanzania, madini yetu tunapewa asilimia tano, mimi sitaki kulikubali hilo, lakini kama ni kweli Mheshimiwa Waziri hebu lifuatilie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni madini ya vito. Tumelizungumza kwenye Kamati tukajielekeza moja kwa moja kwenye Tanzanite, ripoti za kitafiti duniani zinaonesha kwamba madini ya vito asilimia 50 yanazalishwa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki. Lakini kwa bahati mbaya sana nchi hizi zimeshindwa kunufaika ipasavyo kwenye madini haya, hapa ndipo linapokuja suala la Tanzanite, tumezungumza kwenye Kamati nini cha kufanya, naiomba Serikali imuelekeze Mkaguzi na Mthibiti Mkuu Hesabu za Serikali aende akafanye ukaguzi maalum kule Tanzanite ili ripoti hiyo ituwezeshe Bunge kuishauri Serikali ipasavyo, hatujanufaika na Tanzanite. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu yangu Lema pale anasema, sasa jamaa wameondoka kutoka kununua Arusha, Tanzanite inafungashiwa Mombasa, nataka wakati tukiyasikia haya turudi kwenye tafiti, taarifa ya Umoja wa Mataifa inasema nini, taarifa ya Umoja wa Mataifa inasema madini haya gemstone ndiyo imekuwa kichaka cha magaidi, kujificha kwenye jambo hili. Sishangai kusikia kwamba badala ya watu wale kuwa Nairobi sasa Tanzanite inafungashiwa Mombasa, nikisema hivi nafikiri mnaelewa ninasema nini, tuyasimamie madini yetu vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni EWURA, tulifanya uamuzi wa kuanzisha EWURA na tulipoanzisha work load ya sekta ya nishati haikuwa kubwa sana, kwa hiyo ilikuwa ni sahihi pengine EWURA kusimamiwa na Wizara ya Maji. Sasa workload ya upande wa nishati imepanuka sana, nadhani siyo sahihi kuendelea kuiacha EWURA ikasimamiwa na Wizara ya Maji, nafikiri busara itumike, Mheshimiwa Rais ashauriwe ili ile instrument inayoelekeza EWURA kusimamiwa na Wizara ya Maji sasa ibadilishwe na hata ikibidi EWURA igawanywe, tuwe na kitengo kinachosimamia sekta ya nishati ibaki Wizara ya Nishati, na ile inayoshughulikia sekta ya maji ibaki Wizara ya Maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni matumizi ya gesi, tumekuwa tukijielekeza kwenye matumizi…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuisimamia Wizara hii, Wizara ambayo kwa muda imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi sana kiutendaji na kimfumo. Hongera sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utakubaliana na mimi kuwa rasilimali ardhi ina umuhimu wa kipekee kwa uhai na maendeloe ya binadamu. Aidha, kwa uchumi wa Taifa letu ambalo wanancni walio wengi wanategemea sana kilimo, sekta muhimu katika kukidhi mahitaji yao ya kila siku. Ni kutokana na ukweli huu rasilimali ardhi inabeba sifa ya kuwa haki ya kila Mtanzania na kwamba kumnyima Mtanzania yeyote haki ya kumiliki na kuitumia ni uvunjaji wa haki za binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wimbi la kuwepo kwa migogoro ya mipaka na uvamizi wa ardhi katika maeneo ya vijiji limekuwa tatizo kubwa katika nchi yetu. Tatizo hili ni kikwazo kwa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla. Migogoro hii imeendelea kusababisha upotevu wa mali, vifo na kuendeleza uhasama kati ya jamii na jamii na hivyo kuwafanya wananchi kubaki maskini na kuishi maisha duni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, uwepo wa mashamba makubwa yasiyoendelezwa ni chanzo kingine kikubwa cha migogoro ya ardhi nchini. Kwa muda mrefu, mfumo wetu wa kufuta miliki ya ardhi isiyotumika ipasavyo kwa mujibu wa makusudio ya umiliki wa ardhi husika umetumika kutoa mwanya wa watu wachache kuhodhi ardhi bila kuitumia na kuwaacha wananchi wengi kutaabika kwa kukosa ardhi. Naipongeza sana Serikali kwa jitihada kubwa zinazofanyika sasa kuhakikisha mashamba yaliyotelekezwa yanafutiwa hati za umiliki na hatimaye kugawanywa kwa wananchi. Hongera sana Mheshimiwa Waziri kwa kusimamia vyema jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mkinga ni miongoni mwa Wilaya zinazokabiliwa na migogoro ya umiliki wa ardhi na uwepo wa mashamba yaliyotelekezwa kwa muda mrefu. Kwa nyakati tofauti ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkinga na mimi binafsi tumewasilisha Wizara ya Ardhi, mapendekezo ya Wilaya kuhusu utatuzi wa migogoro hiyo. Wakati mapendekezo ya ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkinga yaliwasilishwa Wizara ya Ardhi mapema mwaka 2007, wakati huo Mkinga ikiwa bado ni sehemu ya Wilaya ya Muheza; Ofisi yangu iliwasilisha tena maombi hayo kupitia barua yenye Kumb.MB/MKN/Ardh01/2011 ya tarehe 17 Novemba, 2011.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi chote cha uhai wa Bunge la Kumi mara kwa mara nilikuwa nakumbushia jambo hili kwa michango kwenye hotuba za bajeti za Wizara, na barua. Pamoja na jitihadi hizi bado changamoto hizi hazijapatiwa ufumbuzi. Mheshimwia Waziri nilifarijika sana kupata barua yako iliyotaka Wabunge kuorodhesha migogoro ya ardhi katika Majimbo yetu. Hivyo basi, natumia fursa hii kuikumbushia Wizara juu ya maombi haya ambayo kimsingi yamechukua muda mrefu kupatiwa ufumbuzi:-
(i) Shamba la Kilulu - shamba hili ndipo sehemu ambayo Makao Makuu ya Wilaya ya Mkinga yamejengwa. Shamba hili kwa mara ya kwanza lilimilikishwa kwa Ndugu Van Brandis na Bibi Mary Van Brandis hadi 31/10/1959 ambapo umiliki ulihama kwenda kwa Ndugu Akberali Walli Jiwa. Mmliki huyu hakuendeleza shamba hili lenye ukubwa wa ekari 5,699.9 hadi umiliki wake ukafutwa mwaka 1972. Baada ya kufuta umiliki, Serikali ililipa fidia na shamba likawa chini ya Serikali.
Baadaye Wilaya ya Muheza ilipokea maombi ya kumilikishwa shamba hilo toka Kampuni ya M/S Arusha Farms Ltd. (CHAVDA). Taratibu zote zilifanyika na alimilikishwa ekari 2,699.9 na ekari 3000 walipewa wananchi wa vijiji jirani vya Vuo, Mwachala na Purungu Kasera waliokuwa na shida ya ardhi. M/S Arusha Farms Ltd walipewa barua ya toleo (leter of right of occupancy) ya tarehe 10/05/1991 ambayo ilisajiliwa na Msajili wa Hati tarehe 13/05/1990 kwa Land Office Number 125127.
Mmiliki huyu aliomba mkopo kutoka CRDB kwa kuweka rehani barua ya toleo. Aidha, alishindwa kurejesha mkopo huo na CRDB waliuza shamba kwa M/s Mbegu Technologies Ltd. tarehe 27/03/2004 ambao walilipa mkopo huo, lakini pia hakuweza kuliendeleza shamba hilo. Ndugu Akberali Jiwa licha ya kunyang‟anywa shamba hilo na kulipwa fidia aliwasilisha ombi lake la kurejeshewa umiliki wa shamba hilo. Ombi lake liliwasilishwa katika kikao cha Kamati ya kugawa ardhi tarehe 10/10/1996 na iliazimiwa liwasilishwe katika Kamati ya Ushauri ya Ardhi Mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati hiyo chini ya Uenyekiti wa Mkuu wa Mkoa iliridhia Ndugu Akberali Jiwa apewe shamba hili kwa vile M/s Arusha Farm Ltd. wameshindwa kuliendeleza. Halmashauri ya Muheza ilitoa barua ya toleo kwa miliki ya miaka 99 kuanzia tarehe 1/10/1998 kwa Akberali Jiwa kwa jina la Kampuni ya Kilulu (2000) Ltd. Baada ya tatizo hilo la double allocation kujitokeza, Halmashauri ya Muheza iliandika barua yenye Kumb Na. MUDF/3844/63 ya tarehe 2/4/2007 kwenda kwa Kamishna wa Ardhi kwa ajili ya kuomba kufuta miliki hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa taarifa ya Halmashauri hadi leo Halmashauri haijapata majibu yoyote licha ya ufuatiliaji uliofanywa wa mara kwa mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali halisi kwa sasa ni kwamba eneo hili lina michoro ya mipango miji minne, mitatu iliandaliwa na Katibu Tawala wa Mkoa kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Muheza kabla ya kuanzishwa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga na mchoro mwingine umeandaliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga. Aidha, eneo hili limepimwa jumla ya viwanja 400 kwa matumizi mbalimbali ikiwemo, taasisi, majengo ya Serikali, majengo ya umma, viwanja vya michezo, maeneno ya kuabudia, makazi biashara na maeneo ya wazi. Kwa mara nyingine tena naiomba Serikali ifute milki ya Kilulu Plantation kwa manufaa ya umma.
(ii) Moa Estate - shamba hili lina ukubwa wa ekari 15,739.60 na linamilikiwa na Mkomazi Plantations Ltd. ya S.L.P 2520 Dar es Salaam ambayo baadaye ilibadilisha jina kuwa Mao Plangation and Aquaculture ya S.L.P 364 Dar es Salaam, kwa hati Na. 2468, 9780 na 9781. Halmashauri ya Wilaya ilituma notisi ya kuwafutia hati miliki yao kwa kutelekeza shamba na kulipia kodi. Baada ya hapo Halmashauri ya Wilaya iliwasilisha barua ya mapendekezo kwa Kamishna wa Ardhi yenye Kumb. Na. MKG/LD/F/2/54 ya tarehe 28/07/2009. Taratibu za ufutaji hati miliki ziliendelea Wizarani lakini Halmashauri ilipokea barua ya mmiliki ikieleza kuwa jina la umiliki lilibadilika na kuwa Moa Plantation and Aquaculture wa S.L.P 364 Dar es Salaam na kwamba wanataka kuendeleza shamba hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ilikwishawasilisha Wizarani barua ya mapendekezo ya kufuta hatimiliki, ililazimika kumwandikia Kamishna wa Ardhi barua yenye Kumb. Na. MKG/LD/F/2/56 ya tarehe 09/06/2001 kumweleza kupokea barua hiyo na kwamba shamba hilo lina vijiji vinne ambavyo vimeanzishwa na kusajiliwa Moa, Ndumbani, Mayomboni na Mahandakini. Aidha, vijiji hivyo tayari vina huduma za jamii kama shule, zahanati, barabara na kadhalika. Katika maeneo hayo hivyo aendelee na taratibu za ufutaji hatimiliki au kama atasitisha ufutaji basi wamiliki wakubali kumega maeneo yanayokaliwa na vijiji na kuendelezwa na wananchi. Kamishna wa Ardhi kwa barua Na. LD/70503/76 ya tarehe 23/11/2011 alisitisha ufutaji huo kwa masharti kwamba walipe kodi ya ardhi kuanzia mwaka 1996 hadi 2011/12 na kumega maeneo ambayo yenye vijiji tajwa. Hata hivyo, hawakutimiza masharti hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia hali hiyo, Halmashauri iliandika barua kwa Kamishna wa Ardhi yenye Kumb. Na. HW/MKG/LD/F/2/62 ya tarehe 27/07/2012 ili aendelee na taratibu za ufutaji. Kamishna wa Ardhi kupitia barua yenye Kumb. Na. LD/70503/76 ya tarehe 23/11/2011 alisitisha ufutaji huo kwa masharti kwamba walipe kodi ya ardhi kuanzia mwaka 1996 hadi 2011/2012 na kumega maeneo ambayo yenye vijiji tajwa. Hata hivyo hawakutimiza masharti hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia hali hiyo, Halmashauri iliandika barua kwa Kamishna wa Ardhi yenye Kumb. Na. HW/MKG/LD/F/2/62 ya tarehe 27/07/2012 ili aendelee na taratibu za ufutaji. Kamishna wa Ardhi kupitia barua yake Kumb. Na. LD/70503 ya tarehe 15/01/2013 iliitaka Halmashauri kuwasilisha vielelezo jambo ambalo Halmashauri ilifanya. Aidha, barua ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi yenye Kumb. Na. LD/NZ/12931/18/DW ya tarehe 15/04/2013 kwenda kwa Kaimu Kamishna wa Ardhi nayo inahusika akishauri ufutaji wa hati hizo uendelee. Kwa sasa Halmashauri ya Wilaya inasubiri uamuzi wa Kamishna wa Ardhi.
(iii) Mwele Seed Farm - shamba hili lina ukubwa wa hekta 954, mmiliki ni Wizara ya Kilimo. Wakati ambapo shamba hili lilikusudiwa kuwa shamba la kuzalisha mbegu, hali halisi ni kwamba kwa kipindi cha takribani miaka 15 sasa shamba hili limeshindwa kutumika kama ilivyokusudiwa na sehemu kubwa kubaki kuwa pori. Wananchi wa vijiji vinavyozunguka shamba hili Mbabakofi, Maramba A, Maramba B na Lugongo ndiyo wamekuwa nguvu kazi ya kulifanyia usafi shamba hili pale wanaporuhusiwa kufungua mashamba mapya na kulima mazao ya muda mfupi kila msimu mpya wa kilimo unapowadia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 21/09/2007, Halmashauri ya Wilaya iliandika barua kwa Kamishna wa Ardhi yenye Kumb. Na. MUD/ASF/VOL.VI/35 ikipendekeza kumegwa kwa shamba hili na kugawiwa kwa wananchi wa vijiji jirani kutokana na uendelezaji wake kuwa mdogo sana na kodi kutolipwa. Hata hivyo, maombi haya hayakuwahi kupatiwa majibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shamba hili linapakana na kijiji cha Mbambakofi chenye takribani kaya 500 zenye jumla ya wananchi wapatao 3,173. Mbambakofi ni kijiji pekee katika Wilaya ya Mkinga ambacho kimekosa hata eneo la kujenga huduma muhimu za kijamii kama shule ya msingi na zahanati. Aidha, shamba hili linapakana na Mji Mdogo wa Maramba ambao unakua kwa kasi kubwa, ukiwa na takribani watu 30,000 na kuzungukwa na mashamba ya Maramba JKT hekta 2445, Lugongo Estate hekta 6040, Kauzeni Estate hekta 189.66, Mtapwa Estate hekta 476.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya kutelekezwa kwa shamba hili imezidi kuwa mbaya sana sasa kuliko ilivyokuwa mwaka 2007, wakati Halmashauri ya Wilaya ilipoomba mara ya kwanza kumegwa kwa shamba hili. Kwa sasa hali imekuwa mbaya kiasi kwamba hata majengo mengi yaliyokuwepo yameanguka na machache yaliyosalia yamekuwa magofu, mashine na mitambo yoyote ya kilimo iliyokuwepo shambani hapo imeharibika na michache iliyosalia imehamishiwa Morogoro. Kwa sasa shamba limebaki na wafanyakazi wasiozidi watano kutoka waliokuwepo miaka ya 1990.
(iv) Shamba la Maramba JKT - ukubwa wake ni hekta 2,445 na linamilikiwa na Jeshi. Eneo kubwa halitumiki na halilipiwi kodi. Barua iliyoandikwa kuhusu Mwele Seed Farm iliunganishwa pia mapendekezo ya kumega shamba hili ili wananchi wa Mji Mdogo wa Maramba waweze kupata eneo la kujenga makazi yao.
(v) Shamba la Segoma - msitu wa Segoma wenye ekari 2,311 upo ndani ya shamba la Sigi Segoma lenye ukubwa wa ekari 2829. Shamba hili lilimilikishwa kwa Shirika la Uchumi la Wilaya ya Muheza (SHUWIMU) kwa hati Na. 7675 ya tarehe 01/04/1990 ya miaka 33. Kutokana na kukosa mtaji na kuzorota kwa SHUWIMU, hati hii ilibadilishwa umiliki kuwa Muheza District Council kuanzia tarehe 16/02/2007.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1992 SHUWIMU kwa kukosa mtaji na utaalam iliingia ubia na M/s Sigi Agricultural Co. Ltd., na SHUWIMU ilipovunjwa shamba lilimilikiwa na Muheza District Council ambayo ilifuta ubia uliokuwepo na kuingia ubia na SWIFTCOM ya Tanga. Hii ilisababisha M/s Sigi Agricultural Co. Ltd. kufungua kesi namba 18 ya 1996 kupiga kupinga kufutwa kwa ubia wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2011 hukumu ya kesi hii ilitolewa na Halmashauri ya Muheza kupewa ushindi. Mwaka 2007 Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga ilianzishwa kwa kumegwa toka Muheza. Katika zoezi la kugawana mali, shamba hili liligawiwa kwa Halmashauri ya Mkinga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hukumu kutolewa, Halmashauri kwa ufadhili wa Tanzania Forest Conservation Group (TFCG) ilifanya ukaguzi wa uhalisia wa wakati huo na kutoa taarifa katika kikao kilichofanyika tarehe 08/10/2012 kikihusisha viongozi wa kijiji cha Songea, Kata, wataalam wa Halmashauri, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania - Kanda ya Kaskazini na wataalamu wa Mkoa. Aidha, kikao kilitoka na mapendekezo kwa kuwa na kijiji cha Segoma kina tatizo kubwa la uhaba wa ardhi, ekari 518 za shamba zigawanywe kwa wananchi kwa shughuli za kilimo na makazi na ekari 2,311 zitengwe kuwa eneo la hifadhi ya msitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 15/12/2012 kikao cha Baraza la Madiwani kama wamiliki halali wa rasilimali hii kiliridhia mapendekezo haya na kuagiza ekari 518 zigawiwe kwa wananchi wa kijiji cha Segoma kwa shughuli za makazi na kilimo na ekari 231 zimilikishwe kwa kijiji cha Segoma kuwa msitu wa kijiji. Ili kutekeleza agizo la Baraza la Madiwani, Menejimenti iliwasiliana na Meneja wa Kanda wa Wakala wa Huduma za Misitu kwa makabidhiano. Hata hivyo Meneja wa Kanda wa Wakala wa Huduma za Misitu aliomba kuonana na uongozi wa Halmashauri kwa majadiliano juu ya kijiji kumilikishwa misitu. Taarifa ya ombi hilo ilipofikishwa kwenye kikao cha Baraza cha tarehe 16-17/07/2014, Baraza liliagiza kuwa wataalam wa Ardhi na Misitu wa Wilaya watekeleze Azimio la Baraza la tarehe 05/12/2012.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Menejimenti kutekeleza agizo hilo, tarehe 28/11/2014 kwa mshangao mkubwa Halmashauri ilipokea barua kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ikiamuru kusitishwa kugawa ardhi kwa wananchi kwa ajili ya kilimo na makazi na hali kadhalika kukabidhi msitu kuwa wa kijiji cha Segoma. Jambo hili limeleta taharuki kubwa kwa wananchi kiasi kwamba walikuja Dodoma wakati wa vikao vya bajeti kuwasilisha malalamiko yao. Aidha, wakati wa kuhitimisha mjadala wa bajeti nililazimika kuomba ufafanuzi kuhusiana na jambo hili na Naibu Waziri alikiri kuwa wananchi wa Segoma wanayo haki ya kupatiwa ardhi tajwa na kwamba atatembelea Mkinga ili kulipatia ufumbuzi jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tukiendelea kusubiri utekelezwaji wa ahadi ya Naibu Waziri kutembelea Mkinga kuja kuupatia ufumbuzi mgogoro huu, Halmashauri ilipokea barua toka kwa Katibu Tawala wa Mkoa yenye Kumb. Na. BF 174/314/02/35 ya tarehe 02/12/2015 ikiagiza eneo la ekari 518 likabidhiwe rasmi kwa kijiji na eneo la msitu lenye ukubwa wa ekari 2311 kuwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Huduma za Misitu hadi hapo uamuzi mwingine utakapotolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi haya ya kuinyang‟anya Halmashauri ya Mkinga rasilimali yake siyo tu kwa nia ya uonevu mkubwa bali pia yanakinzana na Sheria ya Misitu ya mwaka 2002 ambayo inabainisha wazi kuwa jamii inaweza kulinda, kuhifadhi, kusimamia na kutumia kiuendelevu misitu katika ardhi ya kijiji ili kukidhi mahitaji yao ya kimaendeleo ya muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikimbukwe kuwa zaidi ya hekta milioni mbili za misitu hapa nchini zinasimamiwa na Serikali za vijiji zaidi ya 1000. Hivyo kijiji cha Segoma kukabidhiwa kusimamia msitu wao wa asili haitakuwa mara ya kwanza. Tungependa kuona busara iliyotumika mwaka 2015 kuruhusu Kata ya Enguserosambu katika Wilaya ya Ngorogoro kusimamia msitu wa Longido II ikitumika hata kwa msitu wa Segoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kutokana na ukweli kuwa wananchi hawa ndiyo wameutunza msitu wa Segoma na kuwajibika kuhakikisha msitu unabaki salama pasipo kuombwa wala kukukabidhiwa na Serikali. Inasikitisha kuona leo wananchi hawa wakiporwa rasilimali hii kwa mabavu, kejeli na udhalilishwaji kuwa wao ni wavamizi. Halmashauri ya Mkinga na wanakijiji wa Segoma wanataka kunufaika na umiliki wa rasilimali yao kupitia mapato yatokananyo na mavuno ya msitu huu ili kuboresha huduma za kijamii na kuleta maendeleo ya kijiji.
(vi) Kwamtili Estate - shamba hili lina ukubwa wa hekta 1,150 na lina milikiwa na Kwamtili Estate Ltd. yenye certificate of Incorporation No. 2649 iliyosajiliwa tarehe 09/01/1961 ikiwa na wanahisa wafuatao:

S/N JINA LA MWENYE HISA ANAPOISHI MAELEKEZO

1 Dennis Martin Fielder 4 Market Square Tenbury,Wells Worcestershine – UK Amerudi Uingereza
2 National Agriculture &
Food Corporation (NAFCO) Box 903 DSM Shirika limefutwa
3 Handrik Tjails Scheen C1/30 Algami nes Bank, Amsterdam, Netherland Amefariki
4 Louis Van Wagenburg Layscian Ag Vaghel, Holland Amefariki
5 Schoonmarkers Bart
Venderburg De Conqabsen, 163 Schlkher, Holland Amefariki
6 Tracey Elan Allison The Willos Terrigton, Herefordenshire, UK Amefariki
7 Juvent Magoggo 42 Block S. Mikanjuni Box 5855 Tanga Anaishi Tanga
8 W.J. Tame Ltd Box 118 Tanga Amefariki
9 Jacobus Cornelius Logtanburg Vaghel, Holland Amefariki
Josephus Moris


Mheshimiwa Mwenyekiti, shamba hili lililopo katika eneo la Kwamtili, Kata ya Bosha, Wilaya ya Mkinga lilitumika kwa kilimo cha kibiashara cha zao Kakau. Hata hivyo kwa muda wa miaka takribani 26 saa shughuli za kilimo cha zao la Kakau zimesimama baada ya aliyokuwa Menejiment ya Kampuni chini ya Ndugu Dennis Fielder kutelekeza shamba. Aidha, baada ya shamba kutelekezwa, mmoja wa wanahisa Ndugu Juvent Magoggo amekuwa akifanya shughuli ndogo ndogo ikiwemo kuvuna miti ndani ya shamba hili kwa lengo la kupata fedha za kufanyia uzalishaji mdogo mdogo; na hali kadhalika kuruhusu wananchi wanaozunguka shamba hilo kulima mazao ambayo siyo ya kudumu. Hata hivyo, kwa sasa ndugu Magoggo ameshindwa kuendelea kufanya shughuli hizo baada ya kunyimwa vibali vya kuvuna miti na kusafirisha magogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kuwepo kwa ombwe la umiliki wa shamba hili yamezuka makundi ya watu yanayodai kuwa na haki ya kumiliki shamba hili na hivyo kuwakodisha wananchi wanaozunguka shamba hili maeneo ya kulima kwa kuwalipisha sehemu ya mavuno yatokanayo na matumizi ya ardhi hiyo. Aidha, kumekuwa na wimbi la kujitokeza raia wa kigeni kwa kutumia kivuli cha aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shamba na kulitekeleza Ndugu Dennis Fielder kufanya uharibifu wa mali za kampuni, ikiwemo upasuaji wa mbao na kuanzisha michakato ya kujimilikisha ardhi hii. Katika hili, wananchi wanainyooshea kidole ofisi ya Wakala wa Hifadhi ya Misitu - Wilaya ya Mkinga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kwamtili na Kata ya Bosha kwa ujumla wamebaki katika umaskini wa kutupa baada ya shughuli za kilimo cha Kakau katika shamba la Kwamtili ambacho kilitoa ajira kwao kusitishwa. Nusura kwa wananchi hawa ni kupatiwa maeneo katika shamba hili ili kwa kutumia utaratibu wa wakulima wadogo waweze kufanya shughuli ya kilimo na hivyo kujikimu kimaisha. Naiomba Serikali ifanye uamuzi wa kufuta hati ya shamba la Kwamtili na kisha kuligawa kwa wananchi kwa ajili ya kilimo, na sehemu nyingine kutengwa kuwa hifadhi ya msitu wa kijiji.
(vii) Mjesani Sisal Estate - shamba hili lenye hati Na. 48108 na ukubwa wa ekari 22,725 lilitelekezwa kwa muda mrefu na hali iliyosababisha ardhi kumegwa na kuanzishwa vijiji vinne ndani ya shamba ambalo ni Kwangena, Mchangani, Bomba Mavengero na Mnyenzani. Aidha, Kampuni ya Mohamed Ltd. ya S.L.P 20600 Dar es Salaam imejitokeza na kuanza kuendeleza baadhi ya maeneo ya shamba hili. Hali hii imeleta changamoto kubwa hasa ikizingatiwa kuwa tayari vijiji vilivyomo ndani ya shamba hili vimepatiwa usajili na TAMISEMI. Mfano kijiji cha Kwangena chenye ukubwa wa hekta 300 kimepewa hati ya kuandikishwa kwa kijiji Na. TA/KIJ/603 ya tarehe 03/01/1997, aidha, upimaji wa vijiji ulifanyika na ramani za upimaji kupata vibali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia mkanganyiko huu wa umiliki wa ardhi katika vijiji tajwa, wananchi wa vijiji husika wamekuwa na kilio cha muda mrefu kuiomba Serikali iingilie kati ili kuondoa utata wa umilikishwaji wa maeneo ya vijiji vyao. Mfano, Mkutano Mkuu wa Kijiji cha Kwangena ulikaa na kuomba kupewa ardhi kwa mujibu wa ramani ya kijiji aliyoidhinishwa. Baraza la Madiwani iliyobariki ombi hilo na Halmashauri kupitia barua yenye Kumb. Na. HW/MKG/D.35/138/5 ya tarehe 17/072012 iliwasilisha ombi hilo kwa Kamishina wa Ardhi, mnamo mwaka 2015 Wizara ilituma wataalam wake kuja kufufua mipaka ya shamba na kwa mshangao mkubwa wananchi wa Kwangena wakamegewa ekari 216 tu. Aidha, ndani ya kipindi kifupi sana ramani ya upimaji ikisajiliwa kwa namba 82741, na wakaandaliwa hati nyingine yenye LONO. 560486 na hati ikasajiliwa tarehe 26/11/2015. Tunaomba Serikali iangalie upya suala hili ili wananchi wa vijiji vya Kwangena, Mchangani, Bamba, Mavengero na Mnyenzani waweze kupatiwa ardhi itakayowawezesha kuishi kwa fahari katika nchi yao huku wakiweza kukidhi mahitaji yao ya kimaisha.
(viii) Mgogoro wa Kijiji cha Mkota na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi - wananchi wa Kitongoji cha Kimuuni katika Kijiji cha Mkota Kata ya Mwakijembe wamekuwa wakiishi katika eneo hilo tangu kabla ya uhuru. Kitongoji hiki kina takribani kaya 170 na wakazi wapato 530. Wananchi hawa wa muda wote wamekuwa msaada mkubwa kwa ulinzi na rasilimali za nchi yetu hasa ikizingatiwa kuwa eneo hili linapakana na nchi jirani ya Kenya. Wananchi hawa wanalalamika kuwa eneo lao limechukuliwa na hifadhi ya Taifa ya Mkomazi na Pori Tengefu la Umba na kwamba sasa wanatakiwa kuondoka kwenye eneo hilo licha ya kufanya uwekezaji mkubwa kwa kutumia nguvu zao kuchimba mabwawa makubwa ya kunywesha mifugo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro huu nimeufikisha Serikalini na nimelizungumzia jambo hili mara nyingi sana katika Bunge la Kumi, lakini hadi sasa halijapatiwa ufumbuzi. Mheshimiwa Anna Tibaijuka wakati akiwa Waziri wa Ardhi akiongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, alifanya ziara katika Wilaya ya Mkinga na kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji hiki. Katika mkutano ule, Mheshimiwa Waziri aliwaahidi wananchi kuushughulikia mgogoro huu. Aidha, aliyekuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Mahmood Mgimwa akiandamana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa naye alifanya ziara katika eneo la mgogoro (Kimuni) na kufanya mkutano wa hadhara ambapo alipokea ombi la wananchi kwa eneo hili kupewa hadhi ya kuwa Wildlife Management Area (WMA) na kuahidi Wizara kuanzisha mchakato wa kulitanga eneo hili kuwa WMA. Tunaamini kuwa suluhisho la mgogoro huu ni Serikali kukamilisha mchakato huu ili wananchi waweze kuishi kwa amani.
(ix) Manza Bay Sisal Estate - ni mkusanyiko wa mashamba manne yenye ukubwa wa jumla ya ekari 2,217.6 shamba na. 273 hati na. 7047 LONO. 124814 ekari 461, shamba Na. 196 hati Na. 14275 LONO. 12621 ekari 498.6, shamba Na. 272 hati Na. 3576 LONO. 642 ekari 507 na shamba hati Na. 14322 ekari 764. Mmiliki wa mashamba haya ni Mbegu Technologies Inc. Ltd. wa S.L.P 173 Moshi. Mashamba haya yote yameingia katika eneo la Mji wa Kasea ambao ndio Makao Makuu ya Wilaya ya Mkinga. Kwa muktadha huu naiomba Serikali ione umuhimu wa kufuta hati hizi ili eneo hili liweze kufanyiwa matumizi ya kuendeleza mji wa Kasera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na migogoro hiyo hapo juu, ipo migogoro mingine iliyoibuka kutokana na zoezi la upimaji wa vijiji mwaka 2007 lililohusisha wataalam wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wataalam wa Halmashauri ya Mkinga. Kiini cha migogoro hii ni zoezi kufanyika bila kuhakikisha ushiriki wa viongozi wa pande zote za vijiji husika katika kubainisha mipaka, jambao ambalo limepelekea vijiji ambavyo havikuwa na uwakilishi kugomea kutambua mipaka iliyowekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti orodha ya vijiji vyenye migogoro hii ni kama ifuatavyo:-
(a) Kijiji cha Daluni Kibaoni na Kijiji cha Ng‟ombeni; (b) Kijiji cha Daluni Kibaoni, Kijiji cha Mgambo Shashui na Kijiji cha Movovo;
(c) Kijiji cha Mnyenzani na Kijiji cha Jirihini;
(d) Kijiji cha Magodi na Kijiji cha Mwanyumba;
(e) Kijiji cha Dima na Kijiji cha Mazola Kilifi;
(f) Kijiji cha Doda na Kijiji cha Magaoni;
(g) Kijiji cha Monga Vyeru na Kijiji cha Kichalikani;
(h) Kijiji cha Mwakijembe na Kijiji cha Mkota;
(i) Kijiji cha Msimbazi na Kijiji cha Dima; na
(j) Kijiji cha Bosha na Kijiji cha Churwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kuwa sasa changamoto za muda mrefu za uwepo wa migogoro ya mipaka ya vijiji umiliki wa ardhi na uwepo wa mashamba yaliyotelekezwa kwa muda mrefu katika Wilaya ya Mkinga yatapatiwa ufumbuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha hoja ya bajeti hii atueleze nini kauli ya Serikali kuhusiana na changamoto hizi, na tunamuomba atoe kipaumbele cha kuitembelea Mkinga ili kuja kutatua migogoro hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia kwenye mawasilisho ya bajeti iliyopo mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nianze kwa kuipongeza sana Kamati ya Bajeti, imefanya kazi kubwa, na naomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu tusome sana hotuba ya Kamati ya Bajeti, wamekuwa wazalendo kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niungane nao kuzungumzia masikitiko yangu kwamba kama kweli Bunge hili linataka kutumika kama rubber stamp Wabunge tukatae kwa nguvu zetu zote. Tulifanya kazi kubwa ya kuja na Budget Act, tukasema ni sheria inayokuja kututoa kwenye kufanya mambo kama business as usual. Ninyi leo mnataka kuturudisha kule?
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya Kamati inalalamika kwamba haikuzingatia maoni ya Kamati, Wabunge tusikubali asilani. Serikali hii ni sikivu, sikieni haya yanayosemwa na Kamati ya Bajeti, sikieni haya yanayosemwa na Wabunge. Nchi hii yetu sote, tukifika mahali kikundi fulani kikajiona chenyewe kinajua zaidi ya Wabunge tuna tatizo kama nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma mpango, Ripoti ya Hali ya Uchumi inatuambia sekta ya ujenzi imeongoza kwa kuchangia kwa asilimia 16.8, sekta ya habari na mawasiliano asilimia 12, sekta ya fedha na bima asilimia 11, sekta ya madini asilimia 9.1; lakini sekta zote hizi zinashughulisha watu wachache. Sekta inayoajiri asilimia 70 ukuaji umeshuka. Sekta ya kilimo ukuaji umeshuka kutoka asilimia 3.4 sasa ni asilimia 2.3 and yet we are happy, hii haikubaliki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nataka nijielekeze kwenye eneo moja, sekta ya uvuvi hivi tunataka tuambiweje ili tuelewe?
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma ripoti ya mwaka 2014 ya state of the fisheries ya Shirika la Chakula Duniani inasema kwamba uzalishaji wa samaki kupitia ufugaji (aquaculture) ulikuwa ni tani milioni 100 ulimwenguni; pasipo kuzungumzia uvuvi bali ufugaji wa samaki; zenye thamani ya bilioni 144.4. Hivi watanzania hatutaki kushiriki kwenye uchumi mkubwa kiasi hiki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika uzalishaji huo Asia imezalisha asilimia 88 ya hizi, Amerika asilimia 4.7, Europe asilimia 4.3, Afrika asilimia 2.2, kwa maana kwamba imezalisha tani milioni 1.4. Lakini angalia kichekesho chake katika tani milioni 1.4. Lakini angalia kichekesho chake, katika tani milioni 1.4 Misri peke yake imezalisha tani milioni 1, nchi nyingine za Afrika ndio tunanyanganyia 0.4. Lakini Misri hii ufugaji huu wa samaki inategemea maji kutoka Mto Nile, Tanzania ikiwa sehemu ya uchangiaji wa maji ya Mto Nile. Sisi tuna ziwa Victoria, Tanganyika, tuna bahari, tuna Ziwa Nyasa tumelala usingizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uchumi mkubwa kama China wanaona umuhimu wa kushiriki kwenye uchumi huu, wanazalisha nusu ya samaki wanaofugwa ulimwenguni. Sisi Watanzania tunaona sekta hii ya kipuuzi, tubadilike. Ni kwa kupuuza vitu kama hivi ndiyo maana leo hii mchango wa sekta ya uvuvi umeshuka, na umekuwa ukishuka tangu mwaka 2007. Mchango wa sekta hii ilikuwa asilimia 1.7, tumeporomoka mpaka asilimia 1.2 mwaka jana, lazima tubadilike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Kamati kwa kuzungumzia suala la mfuko wa maji, safari hii msitufanyie kiini macho. Mwaka wa jana tulisema fedha zile ziende vijijini mkazipeleka mijini safari hii pelekeni fedha zile vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya Bajeti imesema tuweke tozo kwenye mafuta mbona Wakenya wameweka bajeti yao ya juzi? Tuweke tozo kwenye mafuta, twende tukajenge zahanati. Hii ni aibu kwamba tangu mwaka 2000 tunaweka kwenye Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi kwamba tutapeleka zahanati kwenye kila kijiji tumekwenda kwa asilimia 20 tu. Tutenge bajeti twende tukajenge zahanati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuongeze fedha za maji, wananchi wetu wanataabika vijijini. Pale Mkinga kuna one stop border post, tumeambiwa kimekamilika; kituo kile hakina maji. Mheshimiwa Mpango watu wako watakuwa kwenye ofisi ile haina maji; yatakuwa yanachukuliwa kutoka Kenya. Tuna mradi wa bilioni sita tupeni fedha tukafanye mambo pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuunga mkono hoja ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuhusiana na Makadirio na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu imejaaliwa kwa wingi wa vivutio vya utalii ulimwenguni, vivutio ambavyo kwa bahati mbaya hatujavitumia ipasavyo kutuwezesha kuwa na fursa kubwa ya kiushindani katika sekta ya utalii. Wakati ambapo taarifa mbalimbali zimekuwa zikiisifu Tanzania kwa uwepo wa vivutio hivi, ikizidiwa tu na nchi kama Brazil, kama Taifa tumekuwa na changamoto kubwa ya udhaifu katika mikakati yetu ya kuvitangaza vivutio tulivyonavyo. Ni ukweli uliowazi kuwa endapo vivutio hivi vingetangazwa na kutumika vizuri, mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa nchi yetu ungekuwa mkubwa zaidi kuliko ilivyo sasa. Ni lazima tuwe na mkakati mahsusi wa kutangaza vivutio tulivyonavyo na mkakati huo lazima utengewe fedha za kutosha zitakazowezesha kutumika kwa mashirika makubwa ya utangazaji duniani kutangaza vivutio tulivyonavyo na fursa za uwekezaji katika sekta hii zilizopo hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kusuasua kwa ukuaji wa Dodoma kunasemakana kwa kiasi fulani kunachangiwa na mji huu kukosa bahari na maziwa ambayo husababisha utalii. Kwa kiasi cha maji tunachoona kinapotea kwa wingi kila msimu wa mvua unapofika hapa Dodoma, nani anasema hatuwezi kuanzisha state of the art artificial lake kama walivyofanya Malaysia kwenye mji wao mpya? Nani anasema hatuwezi kuwa na zoo ya kisasa kwenye viunga vya Dodoma? Nani anasema hatuwezi kuanzisha utalii wa zao la zabibiu hasa ikizingatiwa kwama Dodoma inasifika kuwa sehemu pekee ulimwenguni ambapo uzalishaji wa zabibu unafanyika kwa misimu miwili katika mwaka? Au nani anasema hatuwezi kunufaika kwa kuanzisha utalii wa tamaduni za Wagogo na nyumba zao za tembe? Hii ni mifano michache tu ya fursa za uwekezaji na vyanzo vipya vya sekta yetu ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Waziri inaonesha kuwa idadi ya watalii waliotembelea nchini imeshuka kidogo ikilinganishwa na mwaka uliopita. Hali hii inashabihiana na taarifa zilizomo kwenye ripoti ya World Tourism Organisation inayoonesha kumekuwa na kushuka kwa idadi ya watalii waliotembelea Bara la Afrika wakati hali kwa Mabara mengine kama Amerika, Asia na Ulaya ni tofauti kwani Mabara hayo yameshuhudia ongezeko la idadi ya watalii katika maeneo yao. Funzo tunalopata hapa ni kuwa lazima tuwekeze katika ubora wa vivutio tulivyonavyo na huduma tunazotoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kama Taifa lazima tuhakikishe kiwango tulichofikia cha idadi ya watalii wanaotembelea nchi kinalindwa kisishuke na wakati huo huo kuja na mikakati mipya ya kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini. Ripoti ya World Tourism Oraganisation inaonyesha kuwa kwa mwaka 2015 safari za kiutalii zinazofanywa na Wachina zimeongezeka kufikia safari milioni 120, ukuaji ambao umeizidi Marekani na mataifa mengine ya Ulaya. Ukuaji huu wa safari za kiutalii zinazofanywa na Wachina unamaanisha kuwa kwa kila safari kumi za kiutalii zilizofanyika ulimwenguni, safari moja ilihusisha raia wa China. Ukuaji huu wa safari za kiutalii zinazofanywa na Wachina ni fursa muhimu sana kwetu katika kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania. Nashauri Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje kuchukua hatua za haraka kuweka mikakati ya pamoja itakayotuwezesha kulikamata soko hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu sasa wadau muhimu katika sekta ya utalii nchini wamelalamikia mfumo mbovu wa utoaji leseni kwa kampuni za wazawa na masharti magumu ya uanzishaji kampuni za kusafirisha watalii ikilinganishwa na zile za kigeni. Lazima tuondokane na urasimu usio wa lazima ili kuwezesha Watanzania wengi zaidi kuwekeza katika sekta ya utalii. Ieleweke kuwa urasimu katika utoaji wa leseni na masharti magumu kuhusiana na viwango vikubwa vya mitaji si tu unazuia uanzishwaji wa makampuni ya utalii bali pia unadumaza ukuaji wa huduma zinazotolewa na sekta nyingine za uchumi kama uzalishaji wa chakula, usafiri, hoteli, wapagazi na watu wengine wanaotegemewa kutoa huduma kwa watalii wawe wa ndani au nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa mbalimbali zinaifananisha Tanzania na nchi kama Australia kwa kuwa na mfumo mbovu wa utoaji leseni, mfumo ambao hautoi mwanya kwa ukuaji wa sekta ya utalii. Aidha, utafiti wa IFC unabainisha kuwepo kwa urasimu mkubwa katika udhibiti wa leseni za utalii na upatikanaji wa mtaji hali ambayo inasababisha ugumu kwa wanaotaka kuingia katika sekta ya utalii hususani wazawa. Kwa kuwa kama Taifa tunakubaliana kimsingi kuwa sekta binafsi ni injini ya kukuza uchumi wa nchi yetu, lazima tuhakikishe tunatoa fursa pana kwa wazawa hususan wale wenye mitaji midogo ili nao waweze kushiriki katika kuwekeza. Lazima tuwaondolee vikwazo vinavyowanyima haki ya kujituma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya utalii ina nafasi kubwa ya kuendelea kuwa mhimili muhimu wa kukuza uchumi wa nchi yetu. Hata hivyo, kufanikiwa kwa hili kunategemea sana kufanyika mambo kadhaa muhimu kama vile kuongeza jitihada katika kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika kila kona ya nchi yetu, kuboresha miundombinu muhimu, kuboresha taaluma ya utalii ili kuwa na watu wenye elimu na taaluma stahiki na hali kadhalika kuondoa urasimu katika maeneo mbalimbali yahusuyo sekta ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na jitihada hizo ni muhimu vilevile kuelekeza nguvu zetu katika kukuza utalii wa ndani. Kuna umuhimu sasa wa kuja na mkakati mahsusi wa kukuza utalii wa ndani. Lazima mkakati huo uweke bayana jinsi ambavyo tutaweza kutumia makundi yenye ushawishi hapa nchini kama Wabunge, wasanii na hata timu zetu za mpira wa miguu kwenye ligi kuu kushiriki kwenye kuanzisha utamaduni wa utalii wa ndani hapa nchini. Jambo hili ni muhimu kutokana na ukweli kuwa utalii wa ndani ni uti wa mgongo katika ukuzaji wa sekta ya utalii katika nchi yoyote ile. Ni kutokana na ukweli huu hatuna budi kama Taifa kuelekeza nguvu zetu katika kujenga utamaduni wa wananchi kutembelea vivutio vilivyopo nchini na kuwa na mikakati ya kuhamasisha wanafunzi na vijana kwa ujumla kutembelea mbuga zetu na maeneo ya vivutio katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuwe na mkakati kabambe wa kuongeza jitihada zetu katika kutangaza vivutio tulivyonavyo ikibidi suala la utalii wa ndani liwe sehemu ya mitaala yetu ya kufundishia katika shule zetu, tufanye hivyo. Aidha, wakati umefika wa kuanzisha wiki maalum ya uzinduzi wa utalii wa ndani kila msimu wa utalii unapoanza nchini. Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa jitihada zetu za kukuza na kutangaza utalii zinalenga makundi mbalimali ya watu nchini kwa kuzingatia umri, jinsia na uwezo wa kipato ili kumuwezesha kila Mtanzania kushiriki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ninalotaka kulizungumzia ni eneo la migogoro ya ardhi iliyopo katika Wilaya yangu ya Mkinga, migogoro ambayo kimsingi inaigusa Wizara hii. Migogoro hii imechukua muda mrefu kupatiwa ufumbuzi licha ya jitihada kubwa zilizofanyika kuishauri Serikali kuipatia ufumbuzi. Jambo hili limekuwa chanzo cha manung‟uniko makubwa na wananchi kupoteza imani kwa Serikali yao. Migogoro hii ni kama ifuatavyo hapa chini:-
(i) Mgogoro wa wananchi wa Segoma na TFS. Msitu wa Segoma wenye ekari 2,311 upo ndani ya shamba la Sigi Segoma lenye ukubwa wa ekari 2,829. Shamba hili lilimilikishwa kwa Shirika la Uchumi la Wilaya ya Muheza (SHUWIMU) kwa hati Na. 7675 ya tarehe 01 Aprili, 1990 ya miaka 33. Kutokana na kukosa mtaji na kuzorota kwa SHUWIMU, hati hii ilibadilishwa umiliki kuwa Muheza District Council kuanzia tarehe 16 Februari, 2007.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1992 SHUWIMU kwa kukosa mtaji na utaalam iliingia ubia na M/S Sigi Agricultural Co. Ltd. na SHUWIMU ilipovunjwa shamba lilimilikiwa na Muheza District Council ambayo ilifuta ubia uliokuwepo na kuingia ubia na SWIFTCOM ya Tanga. Hii ilisababisha M/S Sigi Agricultural Co. Ltd. kufungua kesi Na. 18 ya 1996 kupinga kufutwa kwa ubia wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2011 hukumu ya kesi hii ilitolewa na Halmashauri ya Muheza kupewa ushindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2007 Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga ilianzishwa kwa kumegwa toka Muheza. Katika zoezi la kugawana mali, shamba hili lilikuwa sehemu ya mali zilizogawiwa kwa Halmashauri ya Mkinga. Hivyo basi, kufuatia kutolewa kwa hukumu iliyohusisha shamba hili, Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga kwa ufadhili wa Tanzania Forest Conservation Group (TFCG) ilifanya ukaguzi wa uhalisia wa shamba kwa wakati huo na kutoa taarifa katika kikao kilichofanyika tarehe 08 Oktoba, 2012 kikihusisha viongozi wa kijiji cha Segoma, Kata, wataalam wa Halmashauri, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – Kanda ya Kaskazini na wataalam wa Mkoa. Kikao kilitoka na mapendekezo kuwa kwa kuwa kijiji cha Segoma kina tatizo kubwa la uhaba wa ardhi, ekari 518 za shamba zigawanywe kwa wananchi kwa shughuli za kilimo na makazi na ekari 2,311 zitengwe kuwa eneo la hifadhi ya msitu. Mnamo tarehe 05 Disemba, 2012 kikao cha Baraza la Madiwani kama wamiliki halali wa rasilimali hii kiliridhia mapendekezo haya na kuagiza ekari 518 zigawiwe kwa wananchi wa kijiji cha Segoma kwa shughuli za makazi na kilimo na ekari 2,311 zimilikishwe kwa kijiji cha Segoma kuwa msitu wa kijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Meneja wa Kanda wa Wakala wa Huduma za Misitu aliomba kuonana na uongozi wa Halmashauri kwa majadiliano juu ya kijiji kumilikishwa msitu. Taarifa ya ombi hilo ilipofikishwa kwenye kikao cha Baraza cha tarehe 16 – 17 Julai, 2014, Baraza liliagiza kuwa wataalam wa ardhi na misitu wa Wilaya watekeleze Azimio la Baraza la tarehe 05 Disemba, 2012 bila mabadiliko yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Menejimenti kutekeleza agizo hilo, tarehe 28 Novemba, 2014 kwa mshangao mkubwa Halmashauri ilipokea barua kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ikiamuru kusitishwa kugawa ardhi kwa wananchi kwa ajili ya kilimo na makazi na halikadhalika kukabidhi msitu kuwa wa kijiji cha Segoma. Jambo hili limeleta taharuki kubwa kwa wananchi kiasi kwamba walikuja Dodoma wakati wa vikao vya bajeti kuwasilisha malalamiko yao. Aidha, wakati wa kuhitimisha mjadala wa bajeti nililazimika kuomba ufafanuzi kuhusiana na jambo hili na Naibu Waziri alikiri kuwa wananchi wa Segoma wanayo haki ya kupatiwa ardhi tajwa na kwamba atatembelea Mkinga ili kulipatia ufumbuzi jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tukiendelea kusubiri utekelezwaji wa ahadi ya Naibu Waziri kutembelea Mkinga kuja kuupatia ufumbuzi mgogoro huu, Halmashauri ilipokea barua toka kwa Katibu Tawala wa Mkoa yenye Kumb. Na. BF 174/314/02/35 ya tarehe 02 Disemba, 2015 ikiagiza eneo la ekari 518 likabidhiwe rasmi kwa kijiji na eneo la msitu lenye ukubwa wa ekari 2,311 kuwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Huduma za Misitu hadi hapo uamuzi mwingine utakapotolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi haya ya kuinyang‟anya Halmashauri ya Mkinga rasilimali yake siyo tu kuwa ni ya uonevu mkubwa bali pia yanakinzana na Sheria ya Misitu ya mwaka 2002 ambayo inabainisha wazi kuwa jamii inaweza kulinda, kuhifadhi, kusimamia na kutumia kiendelevu misitu katika ardhi ya kijiji ili kukidhi mahitaji yao ya kimaendeleo ya muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kuwa zaidi ya hekta milioni 21.7 sawa na asilimia 45.7 za misitu hapa nchini zinasimamiwa na Serikali za Vijiji zaidi ya 1,000. Aidha, hekta milioni 3.5 sawa na asilimia 7.3 za msitu nchini zinasimamiwa na watu binafsi au vikundi. Hivyo, Kijiji cha Segoma kukabidhiwa kusimamia msitu wao wa asili haitakuwa kioja wala mara ya kwanza kwa kijiji kumiliki msitu. Ni kwa msingi huu tungependa kuona busara iliyotumika kuruhusu vijiji zaidi ya 1,000 hapa nchini kusimamia misitu yao ikitumika hata kwa msitu wa Segoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kutokana na ukweli kuwa wananchi hawa ndiyo wameutunza msitu wa Segoma na kuwajibika kuhakikisha msitu unabaki salama pasipo kuombwa wala kukabidhiwa na Serikali. Inasikitisha kuona leo wananchi hawa wakiporwa rasilimali hii kwa mabavu, kejeli na udhalilishwaji kuwa wao ni wavamizi.
Halmashauri ya Mkinga na wanakijiji wa Segoma wanataka kunufaika na umiliki wa rasilimali yao kupitia mapato yatokanayo na mavuno ya msitu huu ili kuboresha huduma za kijamii na kuleta maendeleo ya kijiji.
(ii) Kwamtili Estate - shamba hili lina ukubwa wa hekta 1,150 na linamilikiwa na Kwamtili Estate Ltd.yenye Certificate of Incorporation Na. 2649 iliyosajiliwa tarehe 09 Januari, 1961 ikiwa na wanahisa wafuatao:

S/N JINA LA MWENYE HISA ANAPOISHI MAELEZO
1. Dennis Martin Fielder 4 Market Square Tenbury, Wells Worcestershire - UK Amerudi Uingereza
2. National Agriculture & Food Corporation (NAFCO) Box 903 DSM Shirika limefutwa
3. Handrik Tjails Scheen C1/30 Algamines Bank, Amsterdam, Netherland Amefariki
4. Louis Van Wagenburg Laycisan Ag Vaghel, Holland Amefariki
5. Schoonmarkers Bart Vanderburg De Congabsen, 163 Schlkher, Holland Amefariki
6. Tracey Elan Allison The Willos Terrigton, Herefordenshire, UK Amefariki
7. Juvent Magoggo 42 Block S. Mikanjuni Box 5855 Tanga Anaishi Tanga
8. W. J. Tame Ltd Box 118 Tanga Amefariki
9. Jacobus Cornelius Josephus Moris Logtanburg Vaghel, Holland Amefariki

Mheshimiwa Mwenyekiti, shamba hili lililopo katika eneo la Kwamtili, Kata ya Bosha, Wilaya ya Mkinga lilitumika kwa kilimo cha kibiashara cha zao la kakau. Hata hivyo, kwa muda wa miaka takribani 26 sasa shughuli za kilimo cha zao la kakau zimesimama baada ya iliyokuwa Menejimenti ya Kampuni chini ya Ndugu Dennis Fielder kutelekeza shamba hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, baada ya shamba kutelekezwa, mmoja wa wanahisa Ndugu Juvent Magoggo amekuwa akifanya shughuli ndogo ndogo ikiwemo kuvuna miti ndani ya shamba hili kwa lengo la kupata fedha za kufanyia uzalishaji mdogo mdogo na hali kadhalika kuruhusu wananchi wanaozunguka shamba hilo kulima mazao ambayo si ya kudumu. Hata hivyo, kwa sasa Ndugu Magoggo ameshindwa kuendelea kufanya shughuli hizo baada ya kunyimwa vibali vya kuvuna miti na kusafirisha magogo.
Kutokana na kuwepo kwa ombi la umiliki wa shamba hili, yamezuka makundi ya watu yanayodai kuwa na haki ya kumiliki shamba hili na hivyo kuwakodisha wananchi wanaozunguka shamba hili maeneo ya kulima kwa kuwalipisha sehemu ya mavuno yatokanayo na matumizi ya ardhi hiyo. Aidha, kumekuwa na wimbi la kujitokeza raia wa kigeni kwa kutumia kivuli cha aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shamba na kulitelekeza Ndugu Dennis Fielder kufanya uharibifu wa mali za kampuni, ikiwemo upasuaji wa mbao na kuanzisha michakato ya kujimilikisha ardhi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili, wananchi wanainyooshea kidole Ofisi ya Wakala wa Hifadhi ya Misitu Wilaya ya Mkinga kutaka kujiingiza katika kufanya udalali wa ardhi hii. Wananchi bado wana kumbukumbu nzuri ya jinsi watumishi hawa wa TFS Wilayani Mkinga walivyotumika kuwezesha mwekezaji wa Kiitaliano aliyejaribu kupatiwa ardhi ya Mkinga takribani hekta 25,000 kinyume na taratibu ili kulima jatropher.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Serikali haijaweza kulipatia ufumbuzi tatizo lingine ambalo kimsingi limeanzishwa na TFS kutaka kupora ardhi ya wananchi katika shamba la Segoma, TFS hiyo hiyo inataka kuzalisha mgogoro mwingine wa kupora ardhi nyingine katika Wilaya ya Mkinga. Hatupo tayari kuona hili likitokea hasa ikizingatiwa kuwa Kwamtili inakabiliwa na tatizo kubwa la ardhi. Tunaiomba Serikali kutumia busara kuacha jambo hili na kuirejesha ardhi hii kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kwamtili na Kata ya Bosha kwa ujumla wamebaki katika umaskini wa kutupwa baada ya shughuli za kilimo cha kakau katika shamba la Kwamtili ambacho ndicho kilitoa ajira kwao kusitishwa. Nusura pekee kwa wananchi hawa ni kupatiwa maeneo katika shamba hili ili kwa kutumia utaratibu wa wakulima wadogo waweze kufanya shughuli ya kilimo na hivyo kujikimu kimaisha. Naiomba Serikali ifanye uamuzi wa kufuta hati ya shamba la Kwamtili na kisha kuligawa kwa wananchi kwa ajili ya kilimo na sehemu nyingine kutengwa kuwa hifadhi ya msitu wa kijiji.
(iii) Mgogoro wa Kijiji cha Mkota na Hifadhi ya Taifa Mkomazi; wananchi wa Kitongoji cha Kimuuni katika Kijiji cha Mkota, Kata ya Mwakijembe wamekuwa wakiishi katika eneo hilo kabla ya uhuru. Kitongoji hiki kina takribani kaya 170 na wakazi wapato 530. Wananchi hawa kwa muda wote wamekuwa msaada mkubwa kwa ulinzi na rasilimali za nchi yetu hasa ikizingatiwa kuwa eneo hili linapakana na nchi jirani ya Kenya. Wananchi hawa wanalalamika kuwa eneo lao ambalo ni sehemu ya kijiji cha Mkota kwa mujibu wa ramani ya kijiji iliyosajiliwa, eneo lao limechukuliwa na Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi na pori tengefu la Umba na kwamba sasa wanatakiwa kuondoka kwenye eneo hilo licha ya kufanya uwekezaji mkubwa kwa kutumia nguvu zao kuchimba mabwawa makubwa ya kunywesha mifugo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro huu nimeufikisha Serikalini na nimelizungumzia jambo hili mara nyingi sana katika Bunge la Kumi lakini hadi sasa halijapatiwa ufumbuzi. Mheshimiwa Profesa Anna Tibaijuka wakati akiwa Waziri wa Ardhi akiongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa alifanya ziara katika Wilaya ya Mkinga na kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji hiki. Katika mkutano ule, Mheshimiwa Waziri aliwaahidi wananchi kuushughulikia mgogoro huu. Aidha, aliyekuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utaliii Mheshimiwa Mahmoud Mgimwa akiandamana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa naye alifanya ziara katika eneo la mgogoro (Kimuuni) na kufanya mkutano wa hadhara ambapo alipokea ombi la wananchi kwa eneo hili kupewa hadhi ya kuwa Wildlife Management Area (WMA) na kuahidi Wizara kuanzisha mchakato wa kulitangaza eneo ili kuwa WMA. Tunaamini kuwa suluhisho la mgogoro huu ni Serikali kukamilisha mchakato huu ili wananchi waweze kuishi kwa amani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kuwa sasa changamoto za muda mrefu za uwepo wa migogoro ya mipaka ya vijiji, umiliki wa ardhi na uwepo wa mashamba yaliyotelekezwa kwa muda mrefu katika Wilaya ya Mkinga yatapatiwa ufumbuzi. Namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha hoja ya bajeti hii atueleze nini kauli ya Serikali kuhusiana na changamoto hizi na tunamuomba atoe kipaumbele cha kuitembelea Mkinga ili kuja kutatua migogoro hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja nikiamini kuwa Wizara itachukua hatua stahiki katika kutatua changamoto nilizoelezea na kuzielekeza taasisi zilizo chini yake kuacha kuwa chanzo cha migogoro na kuwanyima haki wananchi wetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, nipongeze jitihada zinazofanyika katika kuanzisha Vituo vya Pamoja vya Utoaji Huduma Mipakani (OSBP). Kituo cha Horohoro/Lungalunga ni miongoni mwa vituo vilivyokamilika. Hata hivyo, kituo hiki kinakabiliwa na tatizo kubwa la maji. Kituo hiki kimejengwa upande wa Tanzania eneo ambalo kuna tatizo kubwa la maji kiasi kwamba wananchi wanalazimika kufuata huduma ya maji umbali mrefu upande wa Kenya. Halmashauri ya Mkinga imejitahidi kuibua miradi itakayokuwa suluhisho la tatizo la maji katika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari ripoti ya detailed design imepatikana ikionesha kuwa mradi huu unahitaji kiasi cha takribani shilingi bilioni sita na nusu. Halmashauri ya Mkinga haina uwezo wa kifedha wa kujenga mradi huu. Nashauri Wizara ya Mambo ya Nje ichukue mradi huu kwa kutafuta fedha toka vyanzo vya Jumuiya ya Afrika Mashariki au ufadhili mwingine wowote utakaowezesha kutekelezwa kwa mradi huu. Itakuwa jambo la aibu endapo kituo hiki kitafunguliwa bila ya kuwepo jawabu la utatuzi wa tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni European Union kushinikiza nchi za kiafrika kutia saini mkataba ujulikanao kama Economic Partnership Agreement. Mkataba huu ni mbovu na una madhara makubwa kiuchumi kwa nchi za kiafrika Tanzania ikiwemo. Taifa linapaswa kuwa na tahadhari kubwa na mkataba huu hususan sasa ambapo kama Taifa tumedhamiria nchi yetu kuwa nchi ya uchumi wa kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iweke wazi ndani ya Bunge hili msimamo wetu kama nchi kuhusiana na jambo hili. Waziri atakapokuwa anafanya
majumuisho alieleze Bunge lako ni kwa vipi nchi yetu itaachana na mkataba huu wa kinyonyaji. Wizara ilishirikishe mapema Bunge katika kufahamu kwa undani suala hili la EPA ili Wabunge wawe na uelewa mpana utakaowawezesha kufanya maamuzi sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache, naunga mkono hoja.
Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa hii. Nimshukuru Mungu sana kwa siku ya leo kufika, kwa sababu ni siku ambayo niliitarajia na niliitegemea sana. Nasema haya kwa sababu nimepata bahati ya kushiriki makongamano ya kitaalam ya jambo hili, mwaka 2013 kule Rwanda na mwaka 2014 kule Brussels, Ubelgiji.
Mheshimiwa Spika, kiufupi mkataba huu ni hovyo! kiufupi wenzetu hawana nia njema kupitia mkataba huu. Mkataba huu umejadiliwa kwa miaka 12, miaka 12 nchi zetu zimekuwa kwenye majadiliano ya mkataba huu and yet tuna mkataba mbovu kiasi hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huu ni mkataba ambao nchi yetu imeamua kuchukua njia ya kidiplomasia kusema kwamba inajitoa kwa sababu Uingereza inajitoa kwenye European Union, kauli ya kidiplomasia, lakini nchi ya Tanzania tumeheshimika duniani kwa kusimamia tunachoamini, tusijifiche kwenye diplomasia hii, tuwaambie ukweli hawa wenzetu ambao hawana nia njema na sisi. Tuwaambie ukweli kwamba tunathamini Utanzania wetu, tuwaambie ukweli kwamba tunajiheshimu na hatuko tayari kupuuzwa kupitia mkataba huu.
Mheshimiwa Spika, mambo mengi yamesemwa, loss of revenue, kulinda viwanda vya kati na vidogo, yamesemwa kuhusu rendezvous clause, mimi nataka niya-sum up kwa mambo haya machache nitakayouliza.
Mheshimiwa Spika, wakati nikisoma mkataba huu najaribu kujiuliza hivi mkataba huu unakusudia kutuongezea uzalishaji katika nchi zetu? Jibu ni hapana. Hivi mkataba huu unatuhakikishia usalama wa chakula? Jibu ni hapana. Hivi mkataba huu unatuongezea fursa za ajira zenye staha katika nchi zetu? Jibu ni hapana. Hivi mkataba huu unatuwezesha kutoka katika uchumi wa kutegemea natural resources exportation na kwenda kwenye production of sophisticated products? Jibu ni hapana. Lakini kilichowazi ni mkataba wa kutweza utu wetu, tufike mahali tuwaambie mchana kweupe macho makavu, kwamba hatutakubali kudhalilishwa.
Mheshimiwa Spika, tuupinge mkataba huu. Nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuunga mkono hoja kuhusiana na Bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji katika Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwepo wa miundombinu ya uhakika ya barabara katika maeneo ya vijijini una umuhimu mkubwa katika kufungua fursa za kiuchumi na hivyo kuharakisha maendeleo kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapojiwekea lengo la ujenzi wa barabara za lami kuunganisha Mkoa kwa Mkoa, tuna wajibu vile vile wa kutoa msukumo kwa barabara za aina hiyo zenye umuhimu wa kimkakati katika usalama na kukuza fursa ya kuongeza/kuunganisha vivutio vya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabokweni – Gombero – Maramba – Bombo Mtoni – Kitivo – Mlalo hadi Same ni barabara mbadala ya kuunganisha Mkoa wa Tanga na Mkoa wa Kilimanjaro. Barabara hii inapita kwenye maeneo makuu ya uzalishaji mazao ya chakula na biashara. Ni barabara inayounganisha maeneo haya ya Bandari ya Tanga na nchi jirani ya Kenya. Aidha, kwa upande wa usalama wa nchi, barabara hii ni barabara ambayo ina umuhimu wa kiusalama kwa nchi yetu kutokana na ukweli kuwa inaambaa katika mpaka wetu na nchi ya Kenya. Hivyo, kufanya zoezi la kukagua na kulinda mpaka wetu kuwa na uhakika zaidi kinyume na ilivyo sasa ambavyo tunalazimika maeneo mengi kupitia Kenya ili kuweza kukagua mpaka wetu na Kenya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mabokweni – Maramba – Bomba Mtoni – Mlalo hadi Same ni barabara muhimu kwa kukuza utalii, kwa kuunganisha Mbuga ya Saadani na Mkomazi ambayo inagusa Wilaya ya Mkinga eneo la Mwakijembe ambako yapo maeneo ya asili ya mazalia ya faru. Kwenye Umba Game Reserve, Wilaya ya Lushoto eneo la Mlalo hadi Wilaya ya Same kwenye Mkoa wa Kilimanjaro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami kutaimarisha na kuunganisha Sekta ya Utalii siyo tu kwa Mbuga ya Sadaani na Mkomazi, bali kutaunganisha utalii kwa watalii kutoka Zanzibar kuweza kutembelea vivutio kutoka Saadani, Amani, Nature Reserves, Mapango ya Amboni hadi maeneo ya utalii ya Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro na kadhalika. Aidha, barabara hii itavutia watalii toka Mombasa, Kenya; kuvutika kwa urahisi zaidi kuja Tanzania kupitia Horohoro, Mbuga ya Mkomanzi kuanzia Mkinga hadi Kilimanjaro. Naiomba Serikali kuipa kipaumbele barabara hii kwa kuanza kufanya upembuzi yakinifu ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kuanza ujenzi wa reli kwa standard gauge. Naishauri Serikali kwamba, umefika wakati sasa tuanze kuweka mfumo wa infrastructure bond katika ujenzi wa reli na barabara zetu. Nashauri tujifunze kwa wenzetu wa Nigeria, India na Israel katika kutumia infrastructure bonds katika kujenga miundombinu muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kutenga shilingi milioni 865 kwa ajili ya fidia kwa wananchi katika barabara ya Tanga - Horohoro. Hata hivyo, naisihi Serikali ihakikishe fedha hizi zinapatikana kwa sababu hii imekuwa kero ya muda mrefu kwa wananchi. Aidha, ni vyema kukawa na ushirikishaji wa karibu kwa uongozi wa eneo husika pindi malipo yatakapokuwa yanafanyika ili kuhakikisha kila anayestahili kuliwa anapata haki yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa kutenga fedha, shilingi milioni 120 ku-upgrade Mkinga Township Road kilometa nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, nikikumbusha kuwa bado barabara ya TANROADs kuunganisha Maramba na Makao Makuu ya Wilaya katika Mji wa Kasero haijakamilika. Aidha, eneo la Magoli bado ambalo barabara itapita pembeni ya Kijiji halijakamilika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili na mimi niweze kuchangia kwenye hotuba iliyoko mbele yatu. Nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa kibali cha kusimama mbele ya Bunge letu Tukufu na kuweza kuwasilisha mawazo ya watu wa Mkinga.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie firsa hii vilevile kuwapa pole ndugu zangu wa Mkinga kwa maafa makubwa waliyoyapata kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika Jimbo letu la Mkinga na kwa Mkoa wa Tanga kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa za Kituo cha Utafiti cha Mlingano zinasema mvua zinazoendelea kunyesha sasa zimefikia milimita 316 katika span ya siku tatu. Kiwango hiki ni kikubwa sana, mvua hizi hazijawahi kuoneka kunyesha kwa miaka 40 iliyopita. Kwa hiyo, tunapozungumzia madhara yaliyotokana na mvua hii tunaiomba Seriakli ilichukulie jambo hili kwa umakini mkubwa. Hivi ninavyozungumza mabwawa yangu saba katika Wilaya ya Mkinga ambayo yanatusaidia kupata maji yamepasuka. Miradi ya maji ambayo mabwawa yamepasuka ni Bwagamacho, Horohoro border, Doda, pamoja na Machimboni na mradi wa maji Maramba mabomba yamesombwa na maji, kwa hiyo, mpaka kwenye hospitali yetu ambayo sasa tunaitumia kama Hospitali ya Wilaya imekosa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, bwawa la maji Mwanyumba ambapo sambamba na hilo kuna daraja kubwa limepsuka na daraja limekatika, kwa hiyo, mawasiliano kati ya Tarafa ya Maramba na Makao Makuu ya Wilaya ya Mkinga yamekatika. Scheme yetu ya umwagiliaji Mwakijembe imesombwa na maji, mitaro imejaa mchanga, hekta karibu 98 za mazao zimesombwa. Athari yake; takribani watu zaidi ya 10,000 hawana maji.

Naiomba Serikali ilichukulie jambo hili kwa uzito mkubwa na kwa uharaka ili huduma ya maji iweze kurejeshwa. Ninawaomba ndugu zangu wa Mkinga waendelee kuwa wavumilivu Serikali ninaamini italifanyia kazi jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo ya utangulizi naomba nianze mchango wangu kwa kunukuu taarifa ya wataalam katika jarida la World Water and Sanitation. Katika mchango wao pale wanasema na ninanukuu:-

“The world does not stand a chance without water, it spread disease, compromise safety, makes education elusive and economic opportunity further out of reach. The lack of access to safe and clean water is deadly, dangerous and major obstacle to people of developing world becoming economically empowered and it is what it is standing between billions of people and their health, safety, opportunity to unlock their potential.” Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali yangu isikubali ukosefu wa maji ukazuia fursa za maendeleo kwa watu wetu. Naiomba sana Serikali yangu isikubali ukosefu wa maji ukawa chanzo cha vifo vya watu wetu.

Wale tuliokuwemo kwenye Bunge lililopita wanakumbuka, tulijadili mambo kwa kina hapa katika Bunge hili wakati tunazungumzia kuweka tozo kwenye mafuta ya taa ili kupata fedha za kupeleka umeme vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia watakumbuka sentiments zilizokuwepo, hofu ya kuleta mfumuko wa bei na kadhalika, lakini tuliishauri Serikali na hatimae ikakubali, tukaweka tozo kwenye mafuta ya taa na leo kila mtu anashangilia upatikanaji wa umeme vijijini. Wananchi walikubali maumivu yale na leo wanashangilia umeme vijijini. Tusiwe wazito kukubali ushauri wa Bunge hili kuongeza tozo ya mafuta ili tupate fedha za kupeleka maji vijijini, let us unlock the potential of our people, tuwape maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Makao Makuu ya Mkinga hayana maji. Nimelisema hili kwa muda mrefu, nafurahi leo katika hotuba hii nimeona Wizara imetenga fedha kwa ajili ya kutengeneza mradi wa maji pale, lakini fedha zile nimeona zinagusa maeneo mengi, nimeona shilingi bilioni mbili pale; lakini fedha zile zinaigusa Handeni na maeneo kadhaa. Hofu yangu ni kwamba inawezekana fedha zile zisiweze kutosha kukamilisha jambo lile. Shida ya maji kwenye mji wa Kasera ni kubwa mno, naomba twendeni tukatekeleze mradi ule wa kutoa maji Kinyatu ambao utagusa kata za Mkinga, Parungu- Kasera, Boma pamoja na Manza. Tusaidieni tupate maji kwenye Makao yetu makuu ili tuweze kuujenga mji wetu, tuweze kuwahakikishia watu wetu afya bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine nilisema hapa kwenye bajeti iliyopita kwamba mji wa mpakani wa Horohoro ambako tumejenga Kituo cha Biashara ya Pamoja (One Stop Border Post) hauna maji. Tunapata aibu, watu wanakwenda kuchota maji Kenya. Tulikuwa na bwawa dogo pale ambalo lilikuwa linasaidia watu, leo hii ni miongoni mwa maeneo niliyosema hata bwawa hilo limepasuka.

Mhesimiwa Naibu Spika, tunao mradi, tumeshafanya usanifu unaotoa maji Mwakikonge, mradi ule unahitaji shilingi bilioni sita, tutakuwa tumemaliza tatizo lote la maji kwenye eneo lile. Naomba Serikali tusaidieni watu wale wapate maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni yamekuwepo malalamiko ya maji ya mji wa Tanga kuchafuka. Chanzo cha maji yale yanatoka Bosha na Mhinduro…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wale hawana maji, tunaomba muwapatie maji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii nami nichangie kwenye hotuba hii ya Wizara ya Viwanda. Namshukuru sana Mungu kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuzungumza katika Bunge lako Tukufu. Nianze kwa kusema naiunga mkono hoja iliyoko mbele yetu, nikiwa na reservation kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpongeze ndugu yangu Mheshimiwa Mwijage kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuleta hamasa kwa Watanzania kuona umuhimu wa kumiliki viwanda. Amefanya kazi kubwa ya kuwahamasisha Watanzania kubadili mitazamo ya uwekezaji ili wajielekeze kwenye kumiliki viwanda; viwe viwanda vidogo, viwanda vya kati, lakini vile vile viwanda vikubwa. Hongera sana, ameitendea haki taalum yake ya Masoko. Naomba sasa hili lisiwe jukumu lake peke yake, Wizara ilichukue hili kwa ujumla wake. Ongezeni nguvu katika kuhamasisha Watanzania wabadilishe mitazamo katika umiliki wa viwanda katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, nataka nieleze masikitiko yangu; pamoja na nia nzuri ya kuanzisha viwanda, lakini yapo mambo yanakwamisha sana ukuzaji wa viwanda katika nchi yetu. Ukifuatilia mijadala na sisi tunaopitia pitia tafiti zinazofanyika katika nchi hii, moja kubwa ni lack of coordination. Kuna maeneo tunakwenda hatua moja mbele, tunarudi hatua mbili nyuma; na nitatoa mfano.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nataka nizungumzie Sekta ya Maziwa. Utafiti wa wenzetu wa ESRF unaonesha kwamba mwaka 2010 tulikuwa tunaingiza maziwa kutoka nje takriban lita milioni 40 zenye thamani ya dola milioni 20. Ilipofika mwaka 2014 uingizaji wa maziwa ukaongezeka kutoka lita milioni 40 ukapanda mpaka lita milioni 70 zenye thamani ya dola milioni 40. Unaweza kuona ni jinsi gani tunapoteza fedha kwa kuingiza maziwa kutoka nje. Wakati tukiingiza maziwa kwa kiasi hicho, sisi tunazalisha takriban lita bilioni mbili, lakini zinazosindikwa hazifiki lita 150,000. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia 62 ya maziwa tunayoingiza yanatoka Kenya, asilimia 32 yanatoka South Africa, asilimia nne Uganda. Hata haya yanayopitia South Africa, kuna walakini mkubwa. Tunaambiwa ni uchochoro wa kukwepa kodi. Nitayasema baadaye haya. Masikitiko yangu ni yapi? Kiwanda cha Tanga Fresh ambacho ndiyo kinazalisha kwa wingi sasa, kinazalisha lita 50,000 kwa siku. Ni kiwanda ambacho tulitakiwa kukilinda kwa nguvu zetu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda hiki miaka minne iliyopita, walitaka kuongeza uzalishaji kutoka lita 50,000 kwenda lita 120,000 na tulikuwa tumepata grant ya kuweza kufanya jukumu hilo. Wenzetu wa Bodi ya Ushindani wakawapiga faini ya shilingi bilioni nne wakisema walinunua assets kinyume na utaratibu. Assets zilizonunuliwa zilikuwa za kiwanda kilichokufa, kwa hiyo, hoja ya kuua ushindani haipo. Tumeminyana, faini ile imepungua mpaka sasa hivi bado imeng’ang’aniwa shilingi milioni 400. Hiki ni kiwanda ambacho kingeongeza uzalishaji katika nchi yetu. Fedha ile imepotea! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanga Fresh wameamua kukopa sasa. Wanataka kutumia assets zao, majengo yao waende wakakope. TRA wanakuja wanazuia wanasema hawawezi kutumia majengo yale kukopa kwa sababu aliyewauzia hakulipa kodi stahiki. Vitu vya ajabu sana! Yaani aliyekwepa kodi yupo, anajulikana; anaendelea kufanya biashara kwenye nchi hii, TRA, hawaendi kumbana, wanaenda kumbana Tanga Fresh ambaye hahusiki. Mambo ya ovyo sana! Tunashindwa kukuza viwanda vyetu kwa mambo ya ovyo kiasi hiki! Leo hii ninapozungumza, vituo 28 vya kukusanya maziwa kule Morogoro vimefungwa, wananchi hawana sehemu ya kuuzia maziwa yao kwa sababu hayawezi kupokelewa Tanga Fresh. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanga Fresh wananunua maziwa Mkoa mzima wa Tanga; Tanga Fresh wananunua maziwa kutoka kwa wakulima Mkoa wa Pwani; Tanga Fresh wananunua maziwa kutoka Morogoro. Hivi ninavyozungumza, Tanga Fresh wameombwa na wakulima kutoka Mbeya wanunue maziwa yao, wanashindwa! Maziwa yanamwagwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaingiza maziwa ya mabilioni haya kutoka Kenya, halafu tunakuja hapa tunasema tunataka kuendeleza viwanda, hii haiwezi kuwa sawa. Napiga kelele kwa Mheshimiwa Waziri wa Viwanda kwa sababu sera ya ukuzaji wa viwanda iko kwake, lakini najua mchawi wetu hapa ni Wizara ya Fedha. Najua jitihada alizofanya ndugu yangu Mheshimiwa Mwijage ili jambo hili liishe, lakini barua ile aliyoandika mpaka leo imekaliwa pale Wizara ya Fedha hakuna kinachoendelea. Tutaendelea namna hii namna gani? Lazima tubadilike. Naiomba Serikali yangu jambo hili lishughulikieni, tuondoleeni aibu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kichekesho kingine, tulipitisha hapa Sheria ya VAT kwenye bidhaa za maziwa, tuliingizwa mkenge na wenzetu Kenya lakini Kenya wananchi walipopiga kelele, wenzetu wakafuta kodi ile, sisi tumeendelea nayo. Wabunge tukisimama tukisema hapa, tunaonekana vituko. Tuliyasema hapa kwenye Sekta ya Utalii hatukusikilizwa, Sekta ya Maziwa nayo imeingiliwa, hebu tuwe smart; tunapokubaliana na hawa wenzetu, tukiona wamekiuka makubaliano, mara moja na sisi tugeuke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu korosho; nilikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda, kipindi kilichopita, tuliahidiwa viwanda sita vya Korosho, leo hii havipo. Ndugu yangu Mheshimiwa Mwijage, taarifa za Bodi ya Korosho wanatuambia mwaka huu, tani zilizouzwa korosho ghafi, tani 260,000 tusiendelee kuangalia jambo hili, tutumie Mfuko ule wa Export Levy kujenga viwanda. Nendeni mkafanye utafiti tujue, kama tunataka korosho yetu ibanguliwe hapa, angalau nusu ya tani hizi, tunahitaji viwanda vingapi, tutengeneze Mfuko wa Mikopo kutokana na Export Processing Levy tuitangaze, watu waje wakope fedha zile tujenge viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa na mimi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa pumzi na uhai na kwamba naendelea kuwatumikia wananchi wa Mkinga, lakini vilevile kutoa mchango kwa Taifa langu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Kamati inayohusika na Wizara hii. Kamati imefanya kazi kubwa, Kamati imetufumbua macho juu ya hali mbaya iliyopo katika sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapoambiwa ukuaji wa sekta hii ni 1.7%, lakini unapoambiwa kwamba 65% ya Watanzania nguvu kazi hiyo inafanya kazi kwenye sekta hii halafu unapoambiwa kwamba mikopo inayokwenda kwenye sekta hii is only 2% na unapoambiwa kwamba fedha za maendeleo zilizotoka ni 3% tu, unachanganyikiwa. Kama nchi lazima tujitazame upya, lazima tujitafakari, tukishindwa kufanya hivyo tutaendelea kuwa soko la nchi nyingine.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii usindikaji wa maziwa yetu is only 3% ya tunachozalisha. Tunaagiza 62% ya maziwa kutoka Kenya, tunaagiza twenty something percent kutoka South Africa, tunaagiza 4% ya maziwa kutoka Uganda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa hapa ni mashahidi leo hii Tanzania imekuwa jalala la matunda kutoka South Africa. Tunaagiza apples, machungwa na kadhalika. Hatuwezi kwenda namna hii lazima tubadilike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri anapoambiwa kwamba usindikaji wa maziwa katika nchi yake ni 3% tu, hili lazima limuumize kichwa. Nawasihi sana tuongeze nguvu katika kurekebsha mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye korosho halikadhalika. Korosho yetu yote tunaipeleka ikiwa ghafi kwa kiasi kikubwa. Nilisema juzi hapa na wapo baadhi ya Wabunge wenzangu waliniunga mkono kwamba tutumie fedha zile za export levy, twendeni tukajipange tuseme walau tuanze kwa kuhakikisha 50% ya korosho yetu inabanguliwa hapa ndani, tutumie fedha zile kujenga viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Wizara wamekuja na initiative ile ya kugawa bure dawa zile za kunyunyiza. Vilevile mnaangalia uwezekano wa kutoa hata magunia, ni hatua nzuri. Hata hivyo, ili twende haraka zaidi hebu twende kule kwenye kujenga viwanda vya kubangua korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine, tuliwahi kuambiwa hapa ndani ya Bunge, wakati watu wa Tanga tunapiga kelele kuhusu viwanda vya matunda, tukaambiwa Tanga machungwa yenu hayafai kwa kutengeneza juice. Sasa Serikali mkishasema hivyo halafu mnaishia hapo, kwa nini hamji na utaratibu wa kuhakikisha mnabadilisha mbegu ile ili tuwe na mbegu zinazofaa kwa wakulima wetu? Kwa nini hatuipi nguvu Mlingano iweze kufanya utafiti au tukaingiza mbegu kutoka nje ili kubadilisha machungwa katika nchi yetu tuwe na machungwa hayo yanayofaa kwa kutengeneza juice? Nawasihi sana liangalieni hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Tanga tunalima mazao ya viungo, Muheza, Korogwe na Mkinga, lakini tuna tatizo kubwa la utafiti wa mbegu bora katika maeneo hayo. Mbegu inayotumika ni ya tangu Adam na Hawa. Tunaomba mfanye kazi katika eneo hilo. Najua huko mbele ya safari mtasema tumieni ASDP na kadhalika lakini toeni maelekezo ili kutumia ASDP II mambo haya yaweze kuonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine. Hivi Serikali mmeshindwa kutusaidia watu tunaolima zao la minazi kuweza kuondokana na tatizo lile kwa zaidi ya miaka 20 sasa? Kweli mmeshindwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu Philipines walipopata tatizo la janga lile la mafuriko na minazi yao ikaondolewa walikimbilia kwa watu wa FAO, walipata fedha dola milioni 35. Leo hii Philipines imerudi kwenye chart yake ya kuwa nchi ya pili kwa uzalishaji wa zao la nazi duniani. Tunaomba mtusaidie tuondokane na umasikini kwa watu wetu. Zao la minazi ndani yake unapata bidhaa karibu 11 lakini zao la minazi ukilienzi maana yake hata mazingira unayatunza. Hebu tujielekeze kwenye eneo hili tuondoe tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nisipolisema nitakuwa sijatenda haki ni kuhusu uvuvi. Nimekuwa nikisema hapa sekta ya ufugaji wa samaki ndiyo sekta inayokua katika ulimwengu kwa kasi kuliko sekta yoyote ndani ya sekta za kilimo. Hapa nimeona taarifa kwamba kwa mwaka jana mazao ya samaki kutokana na ufugaji wa samaki yameongezeka kutoka tani 3,000 mpaka tani 11,000. Nina uhakika hizi ni jitihada binafsi za watu kwa sababu jedwali hili linatuonesha kwamba hatukuwa na fedha za maendeleo kwa mwaka uliopita lakini hii ni sekta ambayo tukiwekeza tunaweza kuvuna zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu Kenya miaka sita iliyopita waliwekeza takribani bilioni 35. Mwaka huu wa fedha wametenga bilioni saba kwa sekta ya ufugaji wa samaki peke yake. Jirani zetu Zambia wameanzisha mradi mkubwa, wamewekeza bilioni 112 kwa ajili ya sekta ya ufugaji wa samaki peke yake, halikadhalika Uganda. Hii maana yake nini? Maana yake wenzetu wameiona hii opportunity wanawekeza, sisi hatuwekezi maana yake tutakuwa soko la samaki watakaowazalisha. Nawasihi sana twendeni tukawezeke kwenye eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni bandari ya uvuvi. Hivi tunapata kigugumizi gani kwenye jambo hili? Mimi niliwahi kusema hapa hebu tujiongeze…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Itifaki ya Nagoya ya Kusimamia Upatikanaji na Mgawanyo Sahihi wa Faida zitokanazo na Matumizi ya Rasilimali za Kijenetiki.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi nichangie kwenye itifaki hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema naiunga mkono itifaki hii kwa sababu inazungumzia maisha ya sisi watu wa Pwani na sisi watu wa Pwani bila bahari maisha hayapo. Vilevile niseme kwamba itifaki hii itakuwa na maana tu kama itatuhakikishia watu wa Pwani maisha yetu yataboreka. Kama itifaki hii haitatusaidia maisha yetu kuboreka haina maana, kama itifaki hii haitatuhakikishia kuboreka kwa maisha ya watu wa Pwani basi itifaki hii haina maana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya kwa sababu mwaka 1996 tulisaini mkataba ule uliokuwa unazungumzia udhibiti wa bahari ukanda wa Afrika Mashariki. Mwaka 2010 tukaiboresha itifaki ile tukasaini. Nataka tu nijiulize hivi tangu 1996 tuliposaini watu wa Pwani maisha yamekuwa bora? Nini kinatuhakikishia leo kwa kusaini itifaki hii kwamba maisha ya Pwani yataboreka? Utafiti umetuonyesha kwamba itifaki hii katika utekelezaji wake tangu mwaka 1996 umekuwa na changamoto kubwa ya kimfumo wa usimamizi wa taasisi za usimamizi, vilevile changamoto kubwa ya kifedha. Tafiti hazifanyiki na zikifanyika zinafanyika kwa ufinyu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka leo watu wa Pwani zana tunazotumia kwenye uvuvi ni zana duni, tumekuwa tukitamani tuyaone yanayofanyika kwenye sekta ya kilimo kupewa pembejeo na vitu vya namna hii, yafanywe kwenye sekta ya uvuvi hayafanyiki. Tumekuwa tukitamani tuyaone yanayofanyika kwenye sekta ya mifugo kwa watu wa sekta ya uvuvi hayafanyiki. Ndiyo maana mnashuhudia watu wale wanaendelea kutumia zana duni za tangu enzi ya Nabii Nuhu. Ndiyo maana mnashuhudia uvuvi wa kutumia mabomu unaendelea, ndiyo maana mnaona mazalia ya samaki yanaendelea kuharibika kwa sababu tumeitupa mkono sekta ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifurahi kwenye Ilani yetu tuliposema kwamba katika kipindi hiki tutaleta meli tano za uvuvi. Nataka tu niikumbushe Serikali yangu, mwaka wa pili huu sasa wa utekelezaji, tumebakia na miaka mitatu tujitahidi ahadi ile itimie. Lakini hata ahadi hiyo ikitimia bado asilimia kubwa ya wavuvi watakuwa hawana zana za kisasa kwenda kuvua, ndiyo maana leo unaona hata kwenye uuzaji wetu wa samaki tunategemea sana samaki wa kutoka Ziwa Victoria, uvuvi kwenye eneo la baharini uko duni. Twendeni tukawekeze kwenye blue economy, twendeni tukahakikishe ufugaji wa samaki unafanyika kwenye ukanda wa Pwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jarida la Sofia la FAO linatuambia hivi takribani watu milioni 57 wana… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia kwenye hotuba mbili hizi za Kamati; Kamati ya Miundombinu lakini vilevile Kamati ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya Kamati ya Miundombinu imesisitiza umuhimu wa kuimarisha barabara zetu. Katika ule ukurasa wa 37, anazungumzia umuhimu wa kuunganisha makao makuu ya mikoa kwa mikoa. Vilevile katika ukurasa wa 38, naomba kunukuu kipengele (d), anasema, kuendelea na ujenzi wa barabara za lami hasa maeneo yanayochochea uchumi wa Taifa letu kama vile maeneo yenye vivutio vya utalii, kilimo, viwanda na madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili, napenda niikumbushe Serikali, imekuwa ikitoa ahadi nyingi kwa barabara za namna hii hasa katika Mkoa wa Tanga na upande kwa Kilimanjaro. Ipo barabara inayounganisha Mkoa wa Tanga na Kilimanjaro lakini ni barabara ya kimkakati maana inapita kwenye maeneo muhimu ya ukuzaji wa uchumi, utalii na viwanda. Ni barabara kutoka Tanga – Mabokweni – Maramba - Mtoni Bombo - Mlalo - Same.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili kwanza linagusa usalama wa nchi yetu, maana ni eneo la mpakani lakini vilevile kiutalii ni eneo ambalo ukitokea ukanda wa Tanga mpaka kule Same unazungumzia kuunganisha utalii kutoka Mombasa, Saadani na Mbunga ya Mkomazi ambayo inaanzia upande wa Mkinga inakuja mpaka Mlalo, inakuja mpaka Same tunaelekea Kilimanjaro na maeneo ya namna hiyo.

Kwa hiyo, rai yangu, barabara hii imekuwa ikipewa ahadi kwa muda mrefu, ni wakati sasa upembuzi yakinifu ufanyike barabara hii iwekewe utaratibu wa kuwekewa lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka kwenye taarifa ya Kamati hiyo, sasa nizungumzie taarifa ya Kamati ya Nishati. Nataka niipongeze Serikali kwa kazi kubwa inayofanya kwa kupeleka umeme vijijini kupitia mradi wa REA. Tulipoanza na REA I tulifanya makosa lakini ilikuwa ni sawasawa tufanye makosa kwa sababu tulikuwa tunajifunza. Tumekwenda REA II hali kadhalika tumefanya makosa, yapo tuliyorekebisha lakini bado kuna makosa tumefanya katika usimamizi wa miradi ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tumeingia REA III, hatuna nafasi ya kufanya makosa kwa sababu tulishapata fursa ya kufanya majaribio na ku-test jinsi yakwenda. Tunakwenda kwenye REA III tumekubaliana kwamba kila kijiji kitakachoguswa tuhakikishe hakuna kitongoji kinaachwa. Naisihi sana Serikali tusije tukarudia makosa ya REA I na REA II ya kuacha baadhi ya vitongoji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu zipo changamoto tumeanza kuziona. Kule Jimboni kwangu kwenye maeneo ya Kidiboni, Kitongoji cha Chakachani kimesahaulika. Ninayo ahadi kwamba kitafanyiwa kazi naiomba Serikali ilikumbuke hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulipofanya REA I tuliacha baadhi ya sekondari, Sekondari za Reanzoni, Duga na Kigongoi. Tunapokwenda sasa kwenye REA III kwa sababu sekondari hizi zipo jirani na maeneo haya basi tuhakikishe tunaziingiza kwenye mpango ili ziweze kupatiwa umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine nataka kuzungumzia deni la TANESCO. Ukienda ukurasa wa 23, Kamati inasema, madeni ya TANESCO yanasababisha kuzorota kwa utendaji wa shirika. Aidha, madeni yameendelea kuongezeka na hakuna jitihada zozote za Serikali za kusaidia kumalizika madeni haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii siyo hali nzuri, TANESCO ina madeni makubwa. Ukienda kwenye ukurasa ule inaonesha kwamba deni la TANESCO limefikia bilioni 913 na katika hizo takribani bilioni 200 ni madeni yanayotokana na taasisi za Serikali. Naisihi sana Serikali ije na mkakati maalum wa kuhakikisha deni hili la TANESCO linalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Kamati tuliwahi kuletewa taarifa kwamba Serikali ina mpango wa kukopa fedha Benki ya Dunia ili tulipe madeni haya. Naisihi sana Serikali yangu isiende kukopa Benki ya Dunia ili tulipe madeni haya, tutafute njia nyingine za kulipa madeni haya. Wenzetu Afrika Kusini wana mzigo mkubwa sana kutokana na ESKOM inashindwa sasa kufanya kazi, inakuwa mzigo hata kwa nchi zinazopata umeme kutokana na Shirika la Umeme la South Africa. Tusije tukaingia kwenye mtego huo wa kusababisha tukapata umeme kutoka Afrika Kusini ambao bei yake ni ghali. Tuisaidie TANESCO iweze kutupatia umeme kwa bei ya chini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba tujifunze kwa wenzetu wa Ghana. Wenzetu Ghana waliamua kuanzisha energy bond na katika kufanya hivyo wameweza kukusanya dola milioni 750 ambazo zinaelekezwa katika sekta ya umeme. Kama tunataka kuisaidia TANESCO tuangalie option hii, tujifunze wenzetu walifanya nini, tuone kama tunaweza kuleta energy bond, wananchi wanunue bond hizo na tuweze kusaidia Shirika letu la TANESCO liondokane na mzigo wa madeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine nataka kuipongeza sana Serikali kwa uamuzi wake thabiti wa kuamua kuja na Mradi wa Umeme wa Mto Rufiji, ni hatua kubwa ya kimapinduzi, tumechelewa. Wenzetu Ethiopia wameamua kuwa energy hub saa hizi wanazungumzia kuzalisha megawatt 10,000 kutokana na chanzo cha Mto Nile. Sisi tutumie mto huu vizuri kuwekeza ili tuweze kupata umeme wa uhakika ili ndoto yetu ya kuwa na uchumi wa viwanda iweze kutimia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu tuko katika hatua za mwanzo ambazo utekelezaji utaanza hivi karibuni. Naipongeza Serikali kwa kuanza utekelezaji huu kwa kutumia bajeti za Wizara mbalimbali ili hatua za mwanzo ziweze kutekelezwa. Rai yangu, Bunge hili lishirikishwe ipasavyo, Wabunge wa Bunge hili wapate semina ya nguvu ili kujenga uelewa wa pamoja ili tutakapokuja kuleta bajeti ya mradi huu iweze kupita kwa urahisi tukiwa kitu kimoja, tukiwa tunaelewana kwamba jambo hili ni jambo la kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia kwenye mjadala uliopo mbele yetu. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa rehema na baraka zake ambazo siku zote zimetuwezesha kuwatumikia Watanzania vyema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napenda kuipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali inazochukua katika kuhakikisha maisha ya watu wetu yanaendelea kuboreka siku hadi siku. Tumekuwa na mjadala mrefu juu ya mambo ya makinikia lakini taarifa za hivi punde zinaonesha kwamba tunaelekea kwenye right direction, hongera sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 nilipochangia nilikuwa bitter, nilitumia lugha kali kwa Wizara hii na nilikuwa na sababu ya kufanya hivyo. Nilifanya hivyo kwa sababu Kamati ya Bajeti walikuja hapa wakalalamika kwamba Wizara hii imekuwa na shingo ngumu, ilikuwa haisikilizi ushauri inayopewa na Kamati. Nafurahi mwaka huu mambo yamebadilika. Wizara imekuwa sikivu, hongereni sana. Huo ni mwanzo mzuri, tuendelee kuwa wasikivu, maana wote tunajenga nchi hii kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa mapendekezo ambayo watu wengi humu tumekuwa tukipigia kelele ni kuongeza tozo ya mafuta ili twende kupata huduma za maji vijijini. Serikali imesikia hilo, imeongeza tozo kwenye mafuta. Wenzetu wa Kamati ya Bajeti wanashauri kwamba fedha yote itakayopatikana na ongezeko hili, asilimia 70 tuipeleke kwenye maji vijijini, asilimia 30 iende kwenye maji mijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunapiga kelele kuhusu maji vijijini? Kwa nini tunapiga kelele kuhusu huduma ya maji? Takwimu za Wizara ya Maji zinaonesha kwamba tumepeleka maji vijijini kwa asilimia 72 peke yake. Hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba takriban Watanzania zaidi ya milioni 10 vijijini hawana maji. Hatuwezi kuiacha hali iendelee kuwa hivi. Lazima tuongeze nguvu kuhakikisha tunapeleka maji vijijini. Ndiyo maana naipongeza Serikali kwa kuwa sikivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zimekuwepo hisia za hofu kwamba pengine uamuzi huu wa kuweka tozo umekuwa ni blanket, utagusa kila aina ya mafuta. Naiomba Serikali itakapokuja kuhitimisha hapa, itueleze tozo ile imewekwa kwa mafuta ya aina gani? Vilevile, Wizara itakapokuja kuhitimisha hoja ituambie ina mkakati gani wa kuhakikisha tunafuta Railway Development Levy kwa mafuta ya ndege? Kwa sababu jambo hili limetusababishia kukosa biashara ya kuuza mafuta ya ndege kwa sababu kampuni za ndege zinajaza mafuta Kenya kwa sababu wenzetu hawakuweka levy hii. Kwa hiyo, naomba wakija watupe ufafanuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipochangia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji nilisema mchawi wetu wa Tanga ni Wizara ya Fedha na Mipango. Nilisema hivyo specifically kwa sababu ya Kiwanda cha Tanga Fresh. Tunaingiza maziwa ya dola milioni 40; tuna uzalishaji wa maziwa hapa nchini lita bilioni mbili; lakini usindikaji tunasindika only 1.4 percent. Hii haiwezi kuwa sawa. Tanga Fresh kwa miaka miwili sasa wanahangaika kutaka kuongeza uwezo wa kiwanda chao wanazuiwa na TRA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanazuiwa na TRA kutumia majengo yao kama dhamana ya kukopea. Kwa sababu gani? Kwa sababu aliyewauzia majengo Tanga Fresh, alikwepa kodi. Mkwepaji kodi huyu anajulikana, anafanya biashara katika nchi hii. TRA wanaacha kwenda kumkamata mkwepa kodi, wanamuadhibu Tanga Fresh. Hii haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanga Fresh wamemwandikia barua Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji; Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji ameandika barua tangu mwanzoni mwa mwezi wa Tatu kuja Wizara ya Fedha na Mipango. Mpaka leo hatuna jibu. Nataka mtakapokuja kuhitimisha mtuambie, nini hatma ya Kiwanda cha Tanga Fresh? Kwa nini wanawaadhibu Tanga Fresh kwa kosa ambalo siyo la kwao? Kwa nini uzembe wa wafanyakazi wao usababishe Tanga Fresh wakose haki yao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, naipongeza Serikali kwa jitihada inazofanya za kuhakikisha suala la lishe linapewa kipaumbele. Tuna watoto milioni 2.7 waliodumaa; tuna watoto 600,000 wenye utapiamlo; hii ni hatari kwa Taifa letu. Naipongeze Serikali kwamba kwa mwaka huu wameonesha commitment ya kutenga shilingi bilioni 11.4 zipelekwe kwenye Halmashauri zetu. Rai yangu ni kwamba tuhakikishe fedha hizi zinakwenda kwa wakati. Ziende zikaondoe baa hili. Pili, mtakapopeleka fedha hizi, mpeleke maagizo maalum kwamba huko kwenye Halmashauri fedha hizi zisibadilishiwe matumizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie sula la huduma za kifedha. Tunayo Taasisi inaitwa SELF Microfinance. Mwaka 2016 walipanga kutoa mikopo ya shilingi bilioni 12, lakini wakatoa shilingi bilioni tisa; mwaka huu 2017, wamepanga kutoa shilingi bilioni 20. Naipongeza sana taasisi hii kwa kazi kubwa inayofanya. Wakati nikiipongeza Serikali, hebu fanyeni mambo pale. Mmeondoa Bodi, haipo in place, wanashindwa kutoa mikopo kwa sababu bodi haipo. Harakisheni mhakikishe bodi inakuwa in place ili SELF iweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni shilingi milioni 50 za kila kijiji. Fedha hizi hebu tuziwekee utaratibu maalum. Tumeshasema hapa kwamba njia nzuri ya fedha hizi kwenda kwa wananchi hebu tuhakikishe mfumo wa benki za jamii (Community Banks) unaimarishwa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii nami nichangie kwenye hoja iliyopo mbele yetu. Nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi wa baraka zake ambazo amezidi kutukirimia siku hadi siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumpongeza na kumshukuru sana Naibu Waziri, ndugu yangu Mheshimiwa Kwandikwa kwa ziara aliyoifanya kule Mkinga. Nashukuru sana kwa sababu ziara ile ilijenga matumaini kwa watu wa Maramba, Gombero, Mtonibombo, Daluni, wakijua kilio chao cha muda mrefu sasa kimepata jibu, lakini nimepitia vitabu hivi, bahati mbaya sana kilio chao hakijasikika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Mabokweni – Maramba – Bombomtoni – Umba – Kisiwani – Same - Mkomazi ni barabara ya kuunganisha Mkoa wa Tanga na Kilimanjaro, ni barabara ya kimkakati, kiuchumi na ni barabara ya ulinzi. Ni barabara ambayo wagombea wetu wote wa urais kila wakati wa kuomba kura wamekuwa wakiipitia barabara hiyo, ni barabara ambayo imepewa ahadi mara nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawa wamekuwa na subira sana kwa barabara hii lakini barabara hii ni kero na imekuwa mateso kwao. Nilikuwa nasoma kitabu hiki nikadhani angalau safari hii tutaona neno feasibility study inafanyika kwa barabara ile lakini hakuna. Ni barabara ambayo nimeisemea sasa kwa miaka saba mfululizo, lakini Serikali haisikii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii mzee wangu Mheshimiwa Kikwete alipopita aliposikia kelele hizi akasema tuiweke kwenye utaratibu wa Performance-Based Management and Maintenance ili angalau iwe inapitika, tukafanya hivyo. Baadaye tukasema iingizwe kwenye mpango maalum kupitia MCC, namshukuru sana dada yangu aliyekuwa Mkuu wa Mkoa, dada Chiku Galawa akapambana tukaleta maombi barabara hii itengenezwe kupitia MCC, lakini haikuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano alipokuja kwenye kuomba kura ndugu zetu wa Maramba wakaomba, akasema amesikia. Alipofika Daluni Kibaoni pale wananchi wakamlilia, akatoa ahadi. Tumeisemea barabara hii lakini kwa masikitiko makubwa kilio chetu hakijasikika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kweli barabara inayounganisha Mbuga ya Saadani na Mbuga ya Mkomazi hatuioni umuhimu wake? Hivi kweli barabara inayounganisha Mbuga ya Tsavo na Mbuga ya Mkomazi na Kilimanjaro hatuioni umuhimu wake? Hivi kweli tunashindwa kukamata kundi la watalii kutoka Mombasa ili waje kutembelea eneo la Mto Umba na Mbuga ya Saadani mpaka Kilimanjaro hatuoni umuhimu wake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi barabara inayotupa uhakika wa usalama wa nchi yetu kiulinzi hatuoni umuhimu wake? Hivi barabara inayopita kwenye maeneo ya uzalishaji wa kahawa, chai, mpunga, mkonge hatuoni umuhimu wake? Barabara hii haituweki vizuri kisiasa. Mheshimiwa Waziri alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama chetu, ninaposema barabara hii haituweki vizuri kisiasa, najua anaelewa. Naomba kilio hiki kisikike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni bandari. Pale Mkinga tuna wawekezaji wa Hengya Cement na kampuni ya Sinoma wameamua kuja kuwekeza pale watajenga viwanda kumi. Miongoni mwa viwanda hivyo kutakuwa na kiwanda kimoja cha cement chenye uwezo wa kuzalisha tani milioni saba kwa mwaka. Maana yake unazungumzia kiwanda ambacho production inayofanyika sasa nchini inakuja kufanywa na kiwanda kimoja. Tunazungumzia uwekezaji wa trilioni 7.5.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wameomba pamoja na uwekezaji huo, wapewe ruhusa wajenge gati itakayowawezesha kusafirisha mizigo yao wenyewe. Wanataka kujenga gati ile kwa utaratibu Build Operate and Transfer watumie fedha zao wenyewe. Sasa huko bandarini kuna mtu nasikia ameweka ngumu hataki kutoa kibali. Uwekezaji wa trilioni saba kuna mtu mmoja anakwamisha, hatuwezi kukubali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisipopata majibu ya kuridhisha nakusudia kushika shilingi. Waheshimiwa Wabunge, naomba kwenye hili mniunge mkono. Hatuwezi kuacha uwekezaji mkubwa wa trilioni saba uzuiwe na mtu mmoja. Hatuwezi kukubali ajira ya watu 4,000 izuiwe na mtu mmoja eti ana ndoto ya kutujengea bandari ya Tanga iwe na uwezo wa kuwa valid kwa miaka 200 ijayo, lakini wakati akisema hayo sisi tunazo taarifa watu wa Tanga kwamba tangu mwaka 77 kwenye business plan ya Mamlaka ya Bandari imekuwa ikisema itajenga Bandari ya Mwambani haijatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna mtu ana hela zake anataka ajenge gati ili uwekezaji mkubwa wa namna hii utokee sisi tunaweka ngumu, haiwezekani. Wakati tunaweka ngumu hii ya kuruhusu kujenga gati pale Pangani Mamlaka hiihii ya Bandari imejenga gati, kwa nini Pangani tujenge gati lakini Mkinga iwe nongwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaunga mkono hoja nikipata majibu ya uhakika. Nashukuru.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuchangia kwenye hoja zilizoko mbele yetu. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye kwa rehema zake ametuwezesha tumeendelea kuwa wazima na kuwa na afya njema ya kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuchangia kwenye eneo moja ambalo nisipolichangia nitakuwa sijajitendea haki. Hali yetu ya lishe nchini siyo nzuri. Katika bajeti ya mwaka jana, kwenye fedha tulizotenga ziende kwenye halmashauri zetu ilikuwa ni shilingi bilioni 11 lakini tulipeleka asilimia 8 tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nayasema haya kwa sababu nataka kama Taifa tulione jambo hili ni tatizo. Takwimu zinatuambia nini juu ya hali yetu? Takwimu zinatuambia kwamba asilimia 34 ya watoto wetu walioko chini ya miaka mitano wamedumaa. Takwimu zinatuambia asilimia 58 ya akina mama waliko kwenye kipindi cha kuweza kuzaa wana upungufu mkubwa wa damu. Hii ndiyo hali ya Taifa letu kwamba tuna changamoto hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande mwingine wakati tuna lishe duni lakini tuna tatizo lingine la lishe iliyopitiliza, viriba tumbo. Ttizo hili linatuletea sasa magonjwa yasiyoambukiza mfano BP, kisukari na kadhalika. Kwa hiyo, tuna matatizo ya aina mbili kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Rais wa Benki ya Afrika anatuambiaje? Anasema stunted children today means stunted economy tomorrow. Tukiwa na watoto ambao hali yao ni mbaya leo basi tusitegemee kuwa na uchumi mzuri siku zijazo. Ukiangalia hali ya uchumi takwimu zile zinaonyesha kwamba uchumi wetu unakua lakini kwa taarifa hizi maana yake tunakoelekea ni kubaya. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mpango mwaka huu hakikisha fedha hizi tulizotenga kwa ajili ya kupambana na tatizo la utapiamlo tunazipeleka zikafanye kazi. Maana wataalam wa economics wanatuambia stunted children today means stunted economy tomorrow. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye eneo lingine, naipongeza Serikali nimeanza kuona jitihada za kuzigeuza halmashauri zetu kuwa ni center za investment, ni jambo nzuri. Nasema ni jambo nzuri kwa sababu tumeanza kuona trend ya kuzinyang’anya vyanzo vyake vya mapato lakini sasa tunapoziwezesha kuwa na vyanzo vingine mbadala vya kupata mapato hili ni jambo nzuri. Maana tumeanza kushuhudia kupitia TAMISEMI tunashawishi halmashauri zianzishe miradi, vituo vya maegesho, standi za magari na mabasi, masoko na kadhalika. Yawezekana ni jambo nzuri lakini uwekezaji huu usipogusa maisha ya mtu wa chini, mtu wa kawaida yatakuwa hayana faida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ndipo napokuja kwenye lile jambo mahsusi la sisi watu wa Pwani. Tafiti zinaonyesha kwamba we have unattempted potential kwenye bahari na maziwa yetu. Mheshimiwa Dkt. Mpango Tanzania tuna Ukanda wa Pwani kilometa 1,424, tuna EEZ kilomita 220,000 lakini kwenye eneo la maziwa na mito tuna takribani kilomita 64,500 lakini tunatumiaje rasilimali hii. Uzalishaji wetu wa samaki ukoje? Takwimu zinaonyesha kwenye mpango kwamba kwa takribani miaka mingapi hii, tumekuwa tukivua kati ya tani 325,000 na 380,000. Katika hizo, asilimia 85 uvuvi huu umefanyika kwenye maziwa, asilimia 14 tu ndiyo umefanyika kwenye eneo la bahari. Mbaya zaidi, ufugaji wa samaki kwenye nchi hii, katika hizo tani 380,000 its only one percent, hii haikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta hii ambayo ina potential kubwa namna hii, inachangia ajira asilimia 0.7, haikubaliki. Ukisikiliza taarifa ya Kamati wanasema kwamba tuna tatizo kwenye ajira, tuna tatizo kwenye kuagiza zaidi bidhaa kutoka nje kuliko tunavyoweza kuuza nje, lazima tuwekeze.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuwaige wenzetu South Africa, wao kwenye kutatua jambo hili la ufugaji wa samaki, walichofanya wameanzisha Aquaculture Investment Zone. Wanachofanya wanaenda kuanzisha zone maalum kwenye maeneo fulani fulani, kule Eastern Cape, wanazo hizi karibu saba na maeneo haya yameweza kuzalisha ajira karibu 150,000. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uzalishaji kwenye eneo hili leo hii wanazungumzia mapato yanayotokana na sekta ya ufugaji wa samaki ya shilingi bilioni 115, sisi hatuzitaki hizi? Wenyewe wamejipanga ndani ya miaka miwili ijayo waweze kufikia mapato yanayotokana na ufugaji wa samaki yanayofikia shilingi bilioni mita tano, sisi hatuzitaki hizi? Mheshimiwa Dkt. Mpango tusaidieni watu wa Ukanda wa Pwani, hizi jitihada mnazotuambia tuanzishe standi za mabasi, masoko, tuwezesheni sisi kwenye ufugaji wa samaki kuanzisha Aquaculture Special Economic Zone, tuweze kupiga bao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine, Bunge hili liliridhia tuingie kwenye matumizi ya sarafu moja kwa Ukanda wote huu wa Afrika Masharika. Sijaona kwenye bajeti hii tumeelezwa vipi. Nafikiri ni vizuri kila tunavyokwenda tuwe tunapeana taarifa kwamba maandalizi ya kuelekea huko tumefikia wapi tukijipima na wenzetu. Vilevile tuelezane vihatarishi tunavyoviona, maana taarifa zilizopo wenzetu Kenya wameshafikia ukomo wa kukopa nje. Kila wanavyokopa wamekuwa wakiambiana kwamba deni linahimilika, hii iwe changamoto kwetu kwamba tukope vizuri tusifike huko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye eneo la umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili na mimi niweze kuchangia kwenye hoja zilizoko mbele yetu. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amezidi kutupa baraka zake na hatimaye tunaweza kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajielekeza kwenye mambo matatu. Nitajielekeza kwenye suala la elimu, afya na lishe. Nitumie fursa hii kuishukuru sana Serikali kwa kutupatia fedha za kujenga mabweni na madarasa kwa Sekondari zetu mbili za Maramba na Mkinga ambazo zimekuwa high school, nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani hizo bado sekondari hizi ambazo zimekuwa high school zina changamoto nyingi kwani kuna uhaba mkubwa wa nyumba za Walimu. Sekondari ya Mkingaleo hakuna nyumba za Walimu na high school ile inachukua wasichana, kwa hiyo, unaweza kuona hatari iliyopo. Nawasihi sana Serikali tuchukue hatua za haraka kusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Sekondari ya Maramba, sekondari ile tulipoianzisha tulichukua majengo ya yaliyokuwa mashamba ya mkonge. Kwa hiyo, nyumba wanazotumia Walimu ni nyumba zile za wafanyakazi wa mkonge, za chini kabisa. Kwa hiyo, unaweza kuona picha Walimu wetu tunawaweka katika mazingira gani. Nawasihi sana, tumezipandisha hadhi shule hizi, basi tuziboreshe na kuzipa hadhi inayostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile shule hizi zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa Walimu, taarifa tumekwishapeleka naomba waziangalie. Pia shule hizi zinakabiliwa na tatizo la maji, naomba waangalie. Wingi ule wa wanafunzi katika shule zile halafu shule hazina maji ni changamoto kubwa kwelikweli. Vilevile lipo lingine, shule hizi hazina usafiri, tumewaweka vijana wetu pale, lakini shule hizi hazina usafiri ni changamoto kubwa kwelikweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tunayo madai ya Walimu. Tuna Walimu takribani 271 wanadai madai mbalimbali, ukiacha mishahara, wanadai takribani shilingi milioni 312. Hata orodha ile ya malipo ilipotoka kwa Wilaya ya Mkinga walikuwa ni wafanyakazi wawili tu, naomba waliangalie vizuri jambo hili, halitupi hali nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ndugu yangu Mheshimiwa Waziri atakumbuka niliwahi kuja na timu ya Madiwani kutoka Mkinga, wanastahili posho zao baada ya kumaliza muhula uliopita wa Bunge. Mpaka leo madai yao bado hayajatimia, naomba tuwalipe fedha zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni kwenye afya. Hapa naomba vilevile niipongeze na niishukuru sana Serikali, imetupatia shilingi milioni 500 kwa ajili ya kujenga kituo cha afya. Kituo kile kimekamilika, tunaomba zile shilingi milioni 200 zilizobaki ili kufika shilingi milioni 700 kwa ajili ya vifaa tiba, naomba watupatie ili tuweze kukamilisha kituo kile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado ombi langu liko palepale la kuhakikisha Wilaya ya Mkinga tunapatiwa fedha za kujenga hospitali ya wilaya. Wilaya ile tuna kata 22, sasa hivi tuna vituo vya afya vitatu. Kwa hiyo, unaweza kupata picha kwa wilaya yenye kata 22, haina hospitali ya wilaya ina vituo vya afya vitatu, unaweza kujua ukubwa wa tatizo ni kiasi gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikilisema hili muda mrefu, naomba ifike mahali sasa Serikali isikie. Tunawashukuru World Vision kwa kutusaidia kujenga jengo la kisasa la upasuaji katika Kituo cha Afya cha Mkingaleo, tunaomba na wahisani wengine waige mfano huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna upungufu mkubwa kwenye sekta ya afya, tuna mahitaji ya watumishi 395 waliopo ni 183, tuna uhaba wa karibu asilimia 58 ya watumishi. Maombi haya tumekwishayapeleka muda mrefu, tunaomba wayafanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nihamie kwenye lishe. Hapa nataka ku-declare interest kwamba mimi ni Mwenyekiti wa Kikundi cha Ma-champion wa Lishe katika Bunge letu. Niishukuru Serikali juzi imetoa commitment ya kutoa semina kwa Wabunge wote juu ya tatizo tulilonalo la lishe katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai kwamba kwa ukubwa wa tatizo tulilonalo katika nchi yetu ingekuwa busara sana kama Wabunge wote mngeona umuhimu wa kujiunga na kikundi hiki cha lishe. Mwaka jana tulifanya jambo kubwa, tulipitisha hapa shilingi bilioni 11 ziende kwenye halmashauri kwa ajili ya kutatua tatizo la lishe. Lilikuwa ni jambo kubwa kweli kweli lakini cha kushangaza na imenisikitisha kidogo kwamba nimeisikia hotuba ya Waziri Mkuu sikusikia chochote kuhusu lishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeisikiliza hotuba ya ndugu yangu Mheshimiwa Jafo hakuna sehemu imetajwa lishe. Ndugu zangu tuna tatizo kubwa kwenye lishe, wala
tusimumunye maneno, tuna tatizo kubwa. Haiwezekani kwamba takribani asilimia 45 ya vifo vya watoto katika nchi hii vinahusishwa na utapiamlo, haiwezekani asilimia 57 ya watoto katika nchi hii wana upungufu wa damu, haiwezekani asilimia 34 ya watoto wetu wamekuwa stunt halafu hotuba zetuhazigusii jambo hili, si sahihi, si sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jafo yeye alikuwa miongoni mwa Wabunge tulioanzisha kikundi cha lishe, najua passion yake kwenye jambo hili, Waziri wa Fedha najua passion aliyonayo kwenye jambo hili, hebu tuchukue hatua. Taarifa zilizopo ni kwamba katika shilingi bilioni 11 tulizoidhinisha it’s only eight percent ya fedha hizo ndiyo zimekwenda. Taarifa hii ni ya mwezi wa Pili. Katika shilingi bilioni 11 tumepeleka shilingi milioni 888, hii haiwezi kuwa sawa. Nawasihi sana tuchukue hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua changamoto tuliyonayo ni kwa sababu fedha hizi tunazipitishia kwenye Health Basket Fund, fedha hizi tunataka zitoke kwenye own source, fedha hizi tunataka zitoke kwenye OC. Njia hii haitatufikisha, tuangalie uwezekano wa kutumia njia ya ku- ring-fence fedha hizi, kuzi-page kwenye GDP asilimia fulani ili tuhakikishe fedha hizi zinakwenda moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitumia bajeti za halmashauri kule tukategemea tutaenda kutatua tatizo kubwa kama hili tunajidanganya. Tumekubaliana kwenye vision 2020-2025 kwamba tutaweka kipaumbele kwenye kuboresha human capital na productivity haya hayawezi kupatikana kama hatutahakikisha tunaondokana na tatizo la lishe duni na lishe iliyopitiliza.

T A A R I F A . . .

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa lakini hali ni mbaya zaidi ya hapo. Tathmini inaonesha kwamba kama hali ikiendelea hivi ikifika mwaka 2025 Taifa litakuwa limepoteza nguvukazi ya shilingi trilioni 28.8, this is very serious. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri atakapokuwa anahitimisha taarifa yake atueleze, tulikubaliana kwamba tutaajiri Maafisa Lishe 600, nini kimetokea mpaka sasa hatujaweza kuajiri? Vilevile mpaka kufikia kipindi hiki ni fedha kiasi gani tunazipeleka kwenye lishe? Nawasihi sana tunapofanya mabadiliko ya miundo katika Wizara tujitahidi Kitengo cha Lishe kisije kikamezwa tukahatarisha jitihada hizi tulizozianza.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili na mimi nitoe mchango wangu kwenye hoja iliyopo mbele yetu. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye ametupa uhai na tunaweza kuwatumikia Watanzania. Namuomba anipe uwezo wa kuchangia vyema, nichangie nikiwa sober katika suala hili muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa ziara yake aliyoifanya Jimboni kwangu Mkinga, kuja kujionea mwenyewe changamoto kubwa ya maji katika Wilaya ya Mkinga. Ulijionea mwenyewe kwamba Makao Makuu ya Wilaya ya Mkinga hatuna maji, lakini uliona vilevile miradi inayoendelea na changamoto zake. Mheshimiwa Waziri nikukumbushe tu ziko hati tatu mezani kwako, Hati ya Mradi wa Doda shilingi milioni 166, hati ya Mradi wa Bwagamacho shilingi milioni 54, Hati ya Mradi wa Mbuta shilingi milioni 227. Tunaomba fedha hizi zilipwe ili kazi ya miradi ya vijijini iendelee. Mheshimiwa Waziri utakumbuka pale Parungu Kasero ulipokuja tulikumbana na changamoto ya kupeleka umeme mwezi wa 11 ulipokuja ukaahidi kutoa shilingi milioni 49 fedha zile hazijafika, tunaomba sana utusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mara kadhaa tumesikia kwamba maji ni uhai, tumekua tukisikia kauli hiyo kwamba maji ni uhai lakini kitabu hiki cha Mheshimiwa Waziri kinatuambia takribani asilimia 41 ya wananchi wakioko vijijini hawapati maji, maana yake hakuna uhai.

Mheshimiwa Spika, Umoja wa Mataifa mwaka 2010 kwa kutambua changamoto hii ikasema maji safi na salama ni haki ya msingi kwa maisha ya binadamu na kwamba ikifika mwaka 2015 tuwe tumetatua tatizo la maji vijijini kwa asilimia 50. Sasa ukiangalia Human Development Report ya recent na ukiangalia machapisho ya wenzentu wa ESRF wanatuambia nguvu yetu kwenda kutatua tatizo la maji inakwenda taratibu mno. Kutoka asilimia 45 mwaka 2004/2005 mpaka leo tunazungumzia asilimia 58 tunakwenda taratibu mno. Wakati hali ikiwa hivyo, leo hii tunazungumzia cases 5,800 za kipindupindu zinaripotiwa kila mwaka nchini. Wakati hali ikiwa hivyo tunapoteza vijana wetu wa chini ya miaka mitano vinapatikana vifo vya watoto 18,500 na katika hao asilimia 90 vinasababishwa na kukosekana kwa maji safi na salama. Kama Taifa tutaendelea kuiachia hali hii mpaka lini? Mpaka lini tutakubali kupoteza nguvu kazi hii.

Mheshimiwa Spika, takwimu hizi zinaonesha kwamba kila mwaka kwa kutopeleka maji safi na salama tunapoteza bilioni 301mpaka lini kama Taifa tutakubali udhaifu huu. Nimesoma ripoti ya Kamati wanasema tumepeleka kwa asilimia 22 tu za fedha zile. Kwenye umwagiliaji ndiyo usiseme, hapa tunasema kilimo kitukwamue kutoka kwenye umaskini wetu, kilimo cha kisasa cha umwagiliaji hatupeleki fedha, tunakusudia nini. Nawasihi sana tupeleke fedha hizi.

Mheshimiwa Spika, mwaka jana nilisema hapa kwamba tulipoamua kupeleka umeme vijijini tulipoamua kuweka tozo Serikali walikuwa wagumu kukubali tozo ile lakini leo hii tozo ile ndiyo inatusaidia kupeleka umeme vijijini. Nikashauri hapa mwaka jana kwamba hii tozo inayopigiwa kelele na Wabunge kwenye mfuko wa maji tuiongeze tufikie shilingi 100; hatukuongeza. Lakini leo kinachotuondoa aibu ni Mfuko wa Maji kupitia tozo ile. Nawaomba sana Serikali muwe wasikivu tunaposhauri mambo haya tuongeze tozo lile ili twende tukaondoe tatizo la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado narudia kusema Makao Makuu ya Mkinga hatuna maji nimeona kwenye vitabu mmetupangia shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuanza usanifu kwa Miji kama mitano hivi ya Mkoa wa Tanga. Nawashukuru kwa gesture hii, lakini nikumbushe tu mwaka jana mlifanya hivi na fedha hazikwenda. Tunaomba safari hii fedha hizi zitoke ili usanifu ule uweze kufanyika.

Mheshimiwa Spika, nimeona mmetupangia shilingi milioni 500 pale Horohoro lakini mkumbuke wakati mkitupa shilingi milioni 500 mradi ule wa kupeleka maji Horohoro lakini mkumbuke wakati mkitupa shilingi milioni 500 mradi ule wa kupeleka maji Horohoro unazungumzia bilioni sita ni mradi unaoenda ku-save kile kituo chetu pale cha one stop boarder center, tuondoleeni aibu ya watu wetu kwenda kuchota maji Kenya. Haipendezi sana kila siku tukisema maneno haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi ule wa kupeleka maji kutoka Mto Zigi ni muhimu sana. Ni mradi ambao utatusaidia kupeleka maji kwenye viwanda vile 10 ambavyo tunakusudia kuvijenga, uwekezaji wa trilioni 7.6 hautaweza kufanikiwa kama hatutapeleka maji kwenye eneo lile, tunawasihi sana muone umuhimu wa kupeleka maji kwenye eneo lile.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ametuwezesha kuiona siku hii ya leo. Pili, niwapongeze Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara zote zenye hoja hii na kwa bahati nzuri sana wote wamefika Mkinga, wanaifahamu Mkinga, wanajua changamoto za Mkinga, nawapongeza kwa jitihada mnazozifanya za kutusaidia watu wa Mkinga tuweze kupiga hatua, ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuishukuru sana Serikali kwa jitihada ambazo imefanya kuhakikisha kwamba sekta ya afya katika Wilaya yetu inapiga hatua. Mwaka jana tulipata fedha za vituo viwili vya afya takribani Sh.1,100,000,000. Vituo vile vimekamilika na nimepata taarifa tumepata vifaa vya takribani shilingi milioni 300, kwa hiyo, vituo vile vitaanza kufanyakazi haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia bajeti ya mwaka huu unaokuja nimeona kilio chetu kimesikilizwa. Moja ya kilio ambacho nimekuwa nakipigia kelele sana kila mwaka ilikuwa ni ujenzi wa hospitali ya wilaya. Waziri alipokuwa akiniahidi nilikuwa naona kama vile ananidanganya lakini leo nimeona tumetengewa milioni 500 tuanze ujenzi wa hospitali ya wilaya, nashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba mmeweka benchmark kwenye ujenzi wa hospitali za wilaya, tumezoea tukisikia Sh.1,500,000,000 sasa sisi mmetuanzia na Sh.500,000,000 tunajua hizo bilioni zinafuata. Kwa hiyo, tunaomba muemndele kuweka nguvu ili tuweze kupata fedha hizi. Jambo hili litawasaidia sana watu wa Mkinga lakini litatusaidia vilevile kwenye hospitali yetu ya Mkoa ya Bombo ambayo imekuwa na msongamano mkubwa wa kupata wagonjwa kutoka Mkinga, jambo hili sasa linakwenda kuondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokuwa nikipitia hotuba ya Waziri ukurasa wa 32 mpaka 34 nimefarijika kwa sababu mwaka jana kwenye eneo la lishe nilishangaa kwamba hakukuwa na neno lolote kuhusu lishe. Waziri akaniambia ilikuwa ni kupitiwa na kweli kwa sababu mwaka huu naona ameweka page maalum kwa ajili ya lishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze dada yangu Mheshimiwa Sakaya amezungumzia jambo hili la lishe. Mimi kama Mwenyekiti wa kikundi cha lishe napokuwa na Wajumbe makini namna hii wanaoweza kuzielezea issue tunazozijadili kwa umahiri nafarijika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tusikilizane kidogo, kama Taifa tuna tatizo kubwa la lishe. Utafiti wa Hali ya Afya Nchini wa mwaka 2015/2016 unatuambia kwamba watoto wetu chini ya miaka mitano asilimia 30 wana udumavu. Hii maana yake ni kwamba watoto milioni 2,700,000 wamedumaa katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake nini? Maana yake watoto hawa hawawezi kufundishika vizuri, makuzi yao ni tatizo na fursa huko mbele ya safari za kuijiondoa kwenye umasikini ni giza. Kwa kuwa na watoto hawa ambao wa udumavu maana yake watazalisha vilevile kizazi chenye udumavu, kwa hiyo, hili ni janga kwa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana Bunge hapa tulipitisha shilingi bilioni 15 kwa ajili ya lishe. Kinachonisikitisha ni kwamba mpaka Desemba, fedha zilizotoka kwa ajili ya jambo hili ni asilimia 40 tu. Takribani Halmashauri 31 zilikuwa hazijatenga fedha kwa ajili ya jambo hili, hii haikubaliki. Najua kazi kubwa mnayoifanya Wizara lakini hebu tuwabane hawa ambao hawaoni kwamba tuna changamoto na tuna janga kubwa kama hili kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Mikoa ambayo utapiamlo ni zaidi ya asilimia 40. Mikoa hiyo ni Dodoma, Ruvuma, Rukwa, Kigoma, Katavi na Geita. Cha kusikitisha katika Mikoa hiyo ni Dodoma peke yake ndiyo ilikuwa imetenga fedha zile na zimetumika, mikoa mingine utumikaji wa fedha zile ni kwa kiasi kidogo sana. Niwaombe Serikali muwabane watendaji katika maeneo haya ili waone umuhimu wa kutenga fedha hizi na kutumika ili tuweze kuondoa tatizo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie elimu. Tunashukuru Serikali kwa kutupatia fedha wka ajili ya ujenzi wa madarasa, mabweni na mabwalo katika shule zetu mbili za Maramba Sekondari na Mkingaleo Sekondari ambazo hivi sasa zinakwenda kuwa za kidato cha tano na cha sita. Mkingaleo tayari imeanza, imani yangu ni kwamba tukikamilisha kutoa fedha za haraka, Maramba Sekondari nayo mwaka huu inaweza kupokea vijana wa kidato cha tano na cha sita. Nawasihi sana tupeleke fedha hizi ili tumalizie ile kazi ndogo iliyobaki pale ili Maramba Sekondari na yenyewe iweze kupokea vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto ya maboma kwenye shule zetu. Tuna maboma karibu 40 ya shule za msingi lakini hatujapata fedha. Tuna upungufu wa walimu ambapo mahitaji yetu ni walimu 883 waliopo ni 481, karibu asilimia 50 upungufu, naomba tulitupie macho jambo hili. Hata kwenye sekondari walimu wa sayansi tuna upungufu karibu walimu 60, walimu 38 kwenye masomo ya baiolojia, fizikia na chemistry lakini walimu 22 kwenye somo la hisabati, tunaomba mtuangalie kwa jicho pekee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini maombi mahsusi, shule yetu ya Kigongoi wiki mbili zilizopita tumepata balaa, madarasa matatu yameezuliwa na upepo. Tunaomba jitihada za haraka zifanyike ili tuweze kupata fedha za kurejesha madarasa yale kwenye hali yake ya kawaida ili wanafunzi wasipate shida ambayo inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana nilizungumzia Shule yetu ya Lanzoni kwamba shule ile ya sekondari hatuna maji. Watoto wanalazimika kwenda kuchota maji mtoni, mto ule umejaa mamba. Hebu tuwaondolee balaa hili ili watoto wale wasije wakajeruhiwa au wakauawa na mamba. Tunahitaji fedha pale karibu shilingi milioni nane ili tuweze kupeleka maji kwenye shule ile, tusaidieni tuondokane na kadhia hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, Mheshimiwa Waziri unajua kwa muda mrefu nimekuwa nikizungumzia suala la upungufu wa fedha za kiinua mgongo cha Madiwani. Shilingi milioni 11 zisisababishe kilio hiki bila sababu. Mheshimiwa Waziri ukiamua najua ndani ya wiki mbili zijazo hili litakuwa limeondoka, tusaidie kelele zimezidi.

Mheshimiwa Mwenyeiiti, baada ya kusema hayo, nawashukuru sana, ahsanteni. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ili nami niweze kuchangia. Nianze kwa kuipongeza Wizara kwa kazi kubwa inayofanya, tunajuwa wanafanya kazi kubwa lakini vilevile wanafanya kazi hiyo katika mazingira magumu, tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nitazungumzia mambo mawili, kwanza nizungumzie hali ya uraia kule Mkinga. Wilaya ya Mkinga ni wilaya inayopakana na nchi jirani ya Kenya na kwa muda mrefu sasa tumekuwa na tatizo ambalo limekuwa ni kero kubwa kwa wananchi wangu, kero ya uraia. Bahati nzuri jambo hili unalifahamu lilifika Mezani kwako ukataka nikupe ufafanuzi tukafanya hivyo lakini jambo hili mpaka leo bado halijapatiwa ufumbuzi.

Mheshimiwa Spika, ipo changamoto kubwa sana kwa wananchi wangu wa makabila ya Wataita, Wakamba, Waduruma, ambayo haya ni makabila ambayo unayapata vilevile upande wa pili wa nchi jirani ya Kenya. Hili jambo la kuwa na makabila ambayo unayakuta kwenye nchi mbili tofauti si jambo geni. Kwenye maeneo yetu ya mipakani hili ni jambo la kawaida lakini wananchi wangu kule Mwakijembe wanapata usumbufu mkubwa sana kwa kuambiwa siyo raia kwa sababu tu wanaasili ya makabila ya Kenya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo hili siyo sawa kwa sababu wananchi hawa wamekuwepo kwenye maeneo yetu kabla ya Uhuru. Wamekuwa wakitambulika kama raia wa Tanzania lakini imeingia sasa kadhia tulipoanza kuandikisha raia wetu, wale wananchi wote wanaoonekana wanamajina ya makabila haya moja kwa moja wanaambiwa siyo raia, hii siyo sawa.

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri jambo hili nimeshawasiliana na Waziri tangu mwaka jana, nikamuomba ikiwezekana afanye ziara aje aone kadhia hii. Naamini muda bado upo na Waziri atajipanga ili tuje tutatue tatizo hili lakini kwa kweli ni jambo linalowaumiza sana wananchi wangu kwa sababu wananyimwa haki yao ya msingi ya kuchagua na kuchaguliwa kama viongozi lakini vilevile wananyimwa haki ya kushiriki kwenye shughuli nyingine za kimaendeleo kama wananchi halali wa Tanzania. Naiomba Serikali yangu ilifanyie jambo hili uharaka ili wananchi hawa wasione wananyanyasika katika nchi yao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni vitendea kazi. Wilaya yetu ya Mkinga baada ya kuanzishwa, pale Makao Makuu ya Wilaya hatuna kituo cha polisi. Kituo tunachokitumia kama kituo cha polisi kiko takriban kilomita 40 kutoka makao makuu ya wilaya, hili si jambo zuri. Naiomba Serikali ione umuhimu wa kujenga kituo cha polisi kama Makao Makuu yetu ya Polisi katika Wilaya ya Mkinga pale kwenye mji wetu mkuu wa wilaya pale Kasera.

Mheshimiwa Spika, vilevile kwa upande wa Tarafa ya Maramba ambayo hii inajumuisha kata 10 tuna jengo la kituo ambalo limechoka, jengo hili ni condemned lakini ndipo kilipo kituo chetu. Wananchi wamejitahidi kwa nguvu zao kujenga jengo la kisasa. Tunachohitaji ni msaada wa Serikali tuweze kumalizia jengo lile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali ifahamu kwamba tuna askari wale wanaohudumu katika kata 10 hawana makazi, hii haiwezi kuwa sana. Naiomba Serikali yangu iliangalie jambo hili na iangalie jambo hili ikijua kwamba maeneo haya ni ya mpakani. Sasa unapokuwa na kituo cha polisi kwenye kata kinachohudumia kata 10 lakini kiko kwenye jengo ambalo ni condemned, Mheshimiwa Waziri wewe unajua mambo ya kiusalama silaha na kadhalika, unajua nisiendelee kwa details hapa, lakini tuna changamoto kubwa tunaomba msaada huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vipo vitendea kazi vingine ni changamoto kubwa kwa askari wetu kule Mkinga ambao wanafanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama katika maeneo ya mpakani inakuwa shwari. Tunawaomba sana muwaangalie kwa jicho la pekee. Gari moja kwa eneo lile halitoshi, lile gari lililoko kwenye Kata ya Maramba ni bovu. Tunaomba msaada wetu tuweze kupata gari ambalo litasaidia kulinda usalama kwenye maeneo yetu ya mipakani.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nawashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ametujalia uzima na sisi wote leo tuko hapa tukiwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishukuru Wizara kwa kutupatia fedha za maji. Mwaka 2018 tulitengewa shilingi bilioni 1,400, tumepata shilingi milioni 960, tunazungumzia takribani asilimia 67. Nawashukuru sana. Wakati nikishukuru, nikumbushe tu kwamba kuna kiporo cha shilingi milioni 461, tunategemea fedha hizi zitapatikana ndani ya kipindi cha mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nikisema hayo vilevile natambua katika bajeti ya mwaka kesho tumepangiwa shilingi bilioni 1,139 kwa ajili ya miradi ya kule Mbuta, Mwakijembe, miradi miwili ile ambayo ili ikamilike tunahitaji shilingi bilioni 2,300. Hii maana yake nini? Maana yake tuna upungufu wa shilingi bilioni 1,160 ili miradi hiyo iweze kukamilika. Kwa hiyo, naiomba Serikali ifanye kazi kuhakikisha kwamba fedha hizi zinapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, nizungumzie tatizo la maji katika nchi yetu kwa ujumla. Nilikuwa nasoma taarifa ya World Bank, inaitwa Reaching for SDG The Untapped Potential of Tanzania Water Supply Sanitation and Hygine Sector ya mwaka 2018. Taarifa inatuambia kwamba takribani Watanzania milioni 20 hawapati maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposikia jambo hili, siyo jambo zuri hata kidogo. Kwa vigezo vyovyote vile, haiwezekani kama nchi tukaona Watanzania milioni 20 hawapati maji safi na salama halafu tukaona ni jambo la kawaida, lazima tuchukue hatua. Hapa ndipo linapokuja suala hili sasa kwamba lazima tutafute maarifa mapya ya kuhakikisha kwamba kama Taifa tunatoka hapa tulipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili liliazimia, moja ya maarifa iliyotumia Bunge ni kuongeza fedha za Mfuko wa Maji. Najua wenzetu wapo wanaosema kwamba tukiongeza kule tunaweza ku-trigger inflation, lakini statistics zinatuonesha kwamba kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita tumeweza ku- control inflation. Kwa mwaka huu ndiyo tumeweza kupata kiwango kikubwa sana cha inflation iliyochangiwa na Sekta ya Usafirishaji, maana yake mafuta yako humu. Wakati tumefikiwa kiwango hicho, bado inflation yetu ni asilimia 3.1. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake nini? Hii maana yake tusijifiche kwenye kichaka cha inflation, bado tuna room ambayo tunaweza kufanya tukatumia Sekta hii Mafuta kupata fedha za maji na hatimaye tukaondoa tatizo hili kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili la maji ni kubwa vilevile Mkinga; na hili nimekuwa nikilisema mara kwa mara. Mkinga imegawanyika katika maeneo mawili, kuna eneo la milima na ukanda wa Pwani. Maji yanayotumika katika Mji wa Tanga, chanzo chake ni Mkinga, katika Kata ya Bosha na katika Kata ya Mhinduru. Tangu kuumbwa kwa dunia watu wa Kata hizi mbili hawajawahi kuona maji ya bomba. Hii haiwezi kuwa sawa hata kidogo. Watu wale wamejitahidi kuhakikisha wanalinda vyanzo vya maji. Maji yale yananywewa Tanga Mjini, wao hawana huduma ya maji. Haiwezi kuwa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikileta maombi, Halmashauri tumekuwa tukileta maombi kwamba tujenge miradi ya maji kwenye maeneo yale, tumekuwa hatupati majibu. Mwaka huu tumeleta maombi, tunahitaji shilingi bilioni nane ili maeneo katika Kata ya Mhinduru, eneo la kwa Mtiri, Churwa, Muheza, Mhinduro, Bamba, Mazengero, Kichangani na Segoma na vile vile maeneo ya Bosha, Kuze, Kibago, Bosha, Kwamtindi na Buzi Kafishe yaweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wapeni maji watu hawa, ndiyo wanaotunza vyanzo vya maji vinapeleka maji Tanga, ndiyo wanaotunza vyanzo vya maji vinavyopeleka maji sasa Muheza wao hawana maji safi na salama, haiwezi kuwa sawa hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini eneo la pili ni ukanda wa Pwani. Ukanda wa Pwani hatuna Mito, tungetegemea tupate maji kwa kuchimba visima, lakini kila visima tunavyochimba, chumvi inakuwa ni nyingi mno, kwa hiyo, maji yale hayafai kwa matumizi ya binadamu. Sasa wakati ikiwa hivyo nataka mwelewe kwamba Watanzania wenzenu wanakunywa maji yasiyo safi na salama kwa sababu tu tumeshindwa kuwapelekea maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, alikuja Mheshimiwa Kamwelwe akawaahidi watu wale kwamba suluhisho la tatizo lile ni kutoa maji Mto Zigi kuyapeleka kule. Maji yale leo hayajapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi ule uliambiwa utengenezwe ili wananchi wa Mkinga wapate maji, nimeambiwa Wizara ilitoa tangazo la mradi ule, amepatikana Mhandisi mwelekezi, lakini mpaka leo hakuna kinachoendelea. Tangu mwezi wa Kumi nasikia Mhandisi amepatikana, lakini kuna majadiliano yasiyoisha juu ya mradi ule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana, nimeangalia vitabu hivi vya bajeti, mradi ule haupo. Hivi mnataka watu wa Mkinga tukapate wapi maji? Mheshimiwa Waziri alikuja mpaka Horohoro akaiona kadhia ile, watu wetu wanaenda kuchota maji Kenya. Tuondoleeni aibu ile. Aliwaahidi watu wale kwamba tutapata mradi wa maji wa quick-win. Aliagiza watu wa Tanga, UWASA walete mapendekezo; nimeambiwa mapendekezo yako Wizarani kwake, tunaomba fedha hizo ili tatizo lile liweze kuondolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anajua, amefika Mkinga, Makao Makuu ya Wilaya hayana maji. Hivi tunakuwaje na Wilaya ambayo haina maji? Tuna mradi pale wa ubabaishaji tu, tunatoa maji kutoka kwenye Kijiji jirani ndiyo ki-save Makao Makuu ya Wilaya. Hii haiwezi kuwa sawa. Tusaidieni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikisema jambo hili tangu Mzee Maghembe ni Waziri, ameondoka Mheshimiwa Prof. Maghembe wamekuja wengine, sasa uko wewe, imani ni yangu ni kwamba jambo hili litapatiwa ufumbuzi. Tusaidieni tuweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa ya Mheshimiwa Waziri, Wilaya ya Mkinga ndiyo eneo lenye Ukanda mkubwa wa bahari kuliko Wilaya nyingine zote katika Mkoa wa Tanga. Kwa hiyo, tuna potential ya ujenzi wa mahoteli katika ukanda ule, lakini tunashindwa kujenga mahoteli kwa sababu hatuna maji. Mahoteli yanajengwa upande wa pili wa nchi ya Kenya, upande wa Mombasa, sisi tunaangalia. Nawasihi sana, tusaidieni tupate maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakusudia kujenga kiwanda kikubwa kabisa cha uzalishaji wa cement katika nchi hii. Mapato yanayotegemewa pale ni shilingi bilioni 450 kwa mwezi. Kiwanda kile kitafanyaje kazi tusipokuwa na maji? Kiwanda kile kinategemewa kuvutia viwanda vingine 11 pale Mtimbwani, tunajengaje viwanda vile kama hatuna maji?

Mheshimiwa Waziri, tusaidieni, watu wa Mkinga wana shida ya maji, tupeni maji ili tuweze kupiga hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili na mimi niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mungu kwa kutupa uhai na uzima na kwamba tunaendelea kuwatumikia Watanzania. Niendelee kuwashukuru ndugu zangu wa Mkinga kwa jinsi ambavyo wanaendelea kuniunga mkono ninapotimiza majukumu yangu ya kuwatumikia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze vilevile kwa kuishukuru Serikali kwa jitihada inazofanya katika kuwezesha miundombinu ya nchi yetu, hususan Bandari ya Tanga tunaiona kazi inayofanyika ya kupanua na kuongeza kina cha bandari ile, tunawashukuru. Tunawashukuru vilevile kwa Barabara ya Tanga – Pangani – Bagamoyo ambayo tunaambiwa muda si mrefu itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami, tunaishukuru Serikali kwa jitihada hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikitoa pongezi hizo, nieleze masikitiko yangu katika maeneo mawili. Kwa muda mrefu sasa tumekuwa tukipigia kelele barabara ya kutoka Mabokweni – Maramba – Bombo Mtoni – Umba Junction – Mkomazi – Same. Barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa Mkoa wa Tanga na ni muhimu sana kwa watu wa Maramba, Mkinga, Korogwe, Lushoto na Same. Ni barabara inayounganisha Mkoa wa Tanga na Mkoa wa Kilimanjaro lakini vilevile na nchi jirani ya Kenya. Ni barabara ya kiusalama kwa sababu ipo kwenye ukanda wa mpakani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni barabara ya kiuchumi kwa sababu inaunganisha maeneo ya kiutalii. Unapozungumzia utalii unaofanyika Zanzibar fursa hiyo vilevile inakuja kwa upande wa Tanga, unaiunganisha na eneo lile la Bagamoyo lakini vilevile unaunganisha na Mbuga ya Mkomazi ambayo inaanzia upande huu wa Mkinga eneo la Mwakijembe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni barabara muhimu sana kwa uchumi wa kiutalii lakini uchumi wa kusafirisha mazao, kama walivyosema wenzangu, bidhaa za mazao ya matunda, mbogamboga, karafuu kutoka kule Kigongoi na mazao ya viungo kutoka Muheza na kule Bosha. Kwa hiyo, ni barabara ambayo tukiona kunakuwa na kigugumizi cha kuishughulikia tunapata shida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba Serikali ihakikishe barabara hii sasa inawekewa fedha ili iweze kufanyiwa usanifu. Barabara hii kwa upande wa Kilimanjaro tayari usanifu umekwishafanyika, tunashangaa kwa nini upande huu wa pili barabara hii haifayiwi usanifu? Tunaomba suala hili liweze kushughulikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kuna matengenezo yanayoendelea katika barabara hiyo lakini kuna maeneo korofi. Eneo la kwa Mukamba, pale tunahitaji kifereji na kuweka kifusi cha changarawe ili barabara ile iweze kupitika wakati wote. Eneo la Majumba Matatu na lenyewe ni korofi, najua kuna mifereji inaanza kujengwa pale lakini ikamilishwe kwa wakati na iongozewe eneo refu zaidi ili barabara ile iweze kupitika kwa wakati wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni bandari. Mwaka 2014 Kampuni ya Kichina inayojulikana kama Hengia ilionesha nia ya kuja kuwekeza katika nchi yetu kiwanda cha kuzalisha tani milioni 7 kwa mwaka, uwekezaji wa dola bilioni 3, lakini vilevile walisema wataanza na uwekezaji wa bilioni 1, hapa unazungumzia trilioni 2.3 hivi zingeweza kuwekezwa katika kujenga kiwanda kikubwa katika Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara. Hata hivyo, pamoja na jitihada zao za kuomba vivutio mbalimbali vya uwekezaji bado tangu mwaka 2014 mpaka leo kiwanda hiki kimekwama kupata vibali kianze kujengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu hawa walitaka sambamba na kujenga kiwanda cha kuzalisha simenti vilevile waweze kupata fursa ya kujenga jet. Tumekuwa na kigugumizi cha kuwapa ruksa ya kujenga jet kwa sababu za kiusalama. Ni jambo ambalo unaweza kulielewa ukielezwa lakini maswali tunayojiuliza hivi sisi tumeshindwa kuvi-engage vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vikasimamia jet ile hata kama wameijenga wao? Tukawaweka watu wetu wa TRA wakasimamia mapato yetu? Tukaweka vyombo vingine vya bandari vika-manage jet ile ili uwekezaji hu mkubwa tusiweze kuupoteza? Watu wa Mkinga tunahitaji kupata majibu ni lini kitendawili hiki kitateguliwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapata hofu kwamba tunaenda kupoteza uwekezaji mkubwa huu wa trilioni 6.5 ambazo zingeingia kwenye uchumi wetu. Tunaiomba Serikali ifanye maamuzi ili watu hawa waweze kuanza ujenzi na kuzalisha simenti. Kama tunadhani hatuwezi kuwaruhusu wao kujenga basi twendeni tukajenge sisi jet ile ili uwekezaji huu usiweze kupotea. Naiomba Serikali ifanye maamuzi ya haraka ili jambo hili liweze kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuunga mkono hoja ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kuhusiana na makadirio ya matumizi ya fedha ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia inashuhudia mabadiliko makubwa katika mifumo ya maisha na mazingira ya kiusalama yasiyotabirika. Katika mazingira haya, ulinzi wa mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na uhuru wa nchi yetu ni jambo la kufa na kupona linalopaswa kupewa umuhimu mkubwa na wa kipekee sasa kuliko wakati mwingine wowote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika zama hizi za mabadiliko makubwa ya teknolojia na changamoto za ushindani katika ukuzaji uchumi wa viwanda, kama nchi usalama wetu na uhuru wetu unategemea sana uwepo wa jeshi imara la kisasa lenye weledi, vifaa vya kisasa, uzalendo na nidhamu ya hali ya juu. Hivyo basi ni wajibu wetu kama Taifa kuhakikisha inakuwepo bajeti ya kutosha itakayoliwezesha jeshi letu kukabiliana kikamilifu na changamoto za sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mkinga inapakana na nchi jirani ya Kenya. Katika jitihada za kuimarisha ulinzi Halmashauri ya ilitenga fedha za kujenga daraja ili kuwezesha ulinzi na ukaguzi wa mpaka wetu. Hii ni kutokana na ukweli kuwa kabla ya uwepo wa daraja hilo, ukaguzi wa mpaka wetu ilibidi ufanyike kwa kupitia Kenya. Kazi ya kujenga daraja hilo ilikabidhiwa kwa JWTZ. Natoa pongezi kwa JWTZ kwa kukamilisha kazi ya kujenga daraja hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuiomba Serikali iongeze nguvu katika ulinzi wa mipaka yetu kwa kuweka miundombinu muhimu kama barabara na madaraja yanayokidhi viwango na mahitaji ya kijeshi katika maeneo yote ya Wilaya za mipakani.

Aidha, fedha na jukumu la kujenga miundombinu muhimu katika maeneo haya ya kimkakati, kiulinzi na kiusalama lisiachwe mikononi mwa Halmashauri bali liwe jukumu la moja kwa moja la JWTZ.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Mwakijembe ni miongoni mwa kata 22 za Wilaya ya Mkinga. Kata hii ipo katika mpaka wetu na nchi ya Kenya na kwa miongo kadhaa wananchi hawa wamefanya kazi kubwa ya kuwa walinzi wa mpaka wetu. Naipongeza sana Serikali kwa uamuzi wake wa kuimarisha ulinzi katika Kata ya Mwakijembe kwenye mpaka wetu na nchi ya Kenya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, wakati naipongeza Serikali kwa hatua hii, utekelezaji wake umekuwa na dosari na hivyo kuitia doa Serikali. Doa hili linatokana na JWTZ kutwaa mashamba ya wananchi bila kutoa fidia stahiki kwa wananchi. Inasikitisha kuwa Jeshi lilitumia mabavu kuwapora wananchi ardhi yao tena kwa kufyeka mazao yaliyokuwa mashambani. Hali hii imeleta manung’uniko na wananchi wanaona wamedhulumiwa na Serikali yao wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kihistoria eneo hili limekuwa mali ya wananchi kwa miongo na vizazi kadhaa. Hata pale Halmashauri ilipoamua kuanzisha skimu ya umwagiliaji, iliamua kuyajumuisha maeneo haya ya wananchi kwenye skimu lakini ikahakikisha umiliki wa maeneo hayo unaendelea kuwa mikononi mwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali ifanye tathmini ya haraka kwa ardhi ya wananchi iliyotwaliwa ili wananchi hawa waweze kulipwa fidia stahiki. Wananchi ambao mashamba yao yametwaliwa ili kuwekwa kambi/ makazi ya jeshi ni Ndugu Benard Kinyili (ekari moja); Ndugu Ngoma Joseph (ekari moja na nusu); Ndugu Hamisi Joseph (ekari moja na nusu); Ndugu Mlewa Malonza (ekari mbili) na Ndugu Mwanza Kiziku (ekari mbili).

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja nikiamini kuwa malalamiko ya wananchi wa Mkinga yatapatiwa ufumbuzi wa haraka.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa jitihada kubwa walizofanya kuleta mabadiliko makubwa ya kiutendaji katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rasilimali ardhi ina umuhimu wa kipekee kwa uhai wa maendeleo ya binadamu, wanyama, mimea na viumbe vyote. Kwa uchumi wa Taifa letu ambalo wananchi walio wengi wanategemea sana kilimo kama sekta muhimu katika kukidhi mahitaji yao ya kila siku; rasilimali ardhi inakuwa na umuhimu wa kipekee, kiasi kwamba ni haki ya kila mwananchi kupata, kuimiliki, kuitumia na kuitunza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wimbi la kuwepo kwa migogoro ya mipaka na uvamizi wa ardhi katika maeneo ya vijiji limeendelea kuwa tatizo kubwa katika nchi yetu. Tatizo hili ni kikwazo kwa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla. Tumeendelea kushuhudia migogoro hii ikisababisha upotevu wa mali za wananchi, vifo na kuendeleza uhasama kati ya jamii na jamii na hivyo kuwafanya wananchi kubaki maskini na kuishi maisha duni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kasi ndogo ya upimaji ardhi imeendelea kuwa donda ndugu, wataalam wa ardhi kutowashirikisha wananchi wakati wa uwekaji wa mipaka; na kutowaelimisha wananchi juu ya mipaka iliyowekwa, kama Taifa hatuwezi kuiacha hali hii iendelee. Wizara ichukue hatua za makusudi kuhakikisha kuwa wataalam wa ardhi wanawashirikisha na kuwaelimisha wananchi wakati wa uwekaji wa mipaka. Wizara iongeze kasi ya upimaji wakati wa uwekaji wa mipaka. Wizara iongeze kasi ya upimaji ardhi ili kuzuia wajanja wachache kuvamia maeneo pasipo viongozi wa vijiji kujua na hatua kali zichukuliwe kwa viongozi wa vijiji wanaogawa ardhi kinyume na taratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya wakulima na wafugaji imeendelea kuwa chanzo cha machafuko na umwagaji damu nchini. Lazima kasi yetu ya kutenga maeneo maalum ya wafugaji na wakulima iandamane na utunzaji wa sheria kali utakaozuia uvamizi wa maeneo unaofanywa na pande hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, bado mashamba makubwa yasiyoendelezwa yameendelea kuwa chanzo kikubwa cha migogoro ya ardhi nchini. Bado mfumo wetu wa kufuta miliki ya ardhi isiyotumika ipasavyo kwa mujibu wa makusudio ya umiliki wa ardhi husika umeendelea kutoa mwanya wa watu wachache kuhodhi ardhi bila kuitumia na kuwaacha wananchi wengi wakitaabika kwa kukosa ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kufanya mapitio ya Sheria ya Umiliki Ardhi na kanuni zake ili tupunguze urasimu katika mfumo wetu ili mashamba yaliyotelekezwa yaweze kufutiwa hati za umiliki mara tu yanapothibitika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara nyingine nilete kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Wilaya ya Mkinga, ambayo ni miongoni mwa wilaya zinazokabiliwa na migogoro ya umiliki wa ardhi na mashamba yaliyotelekezwa kwa muda mrefu. Licha ya jitihada kadhaa ambazo kwa nyakati tofauti Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkinga na mimi binafsi tumewasilisha Wizara ya Ardhi mapendekezo ya Wilaya kuhusu utatuzi wa migogoro hiyo; bado utatuzi wa migogoro hii umekwama kupata majawabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mapendekezo ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkinga yaliwasilishwa Wizara ya Ardhi tangu mapema mwaka 2007 wakati huo Mkinga ikiwa bado ni sehemu ya Wilaya ya Muheza; ofisi yangu iliwasilisha tena maombi hayo kupitia mchango wangu wa maandishi wakati wa Bunge la Bajeti mwaka jana na kufuatiwa na barua kwa Waziri wa Ardhi yenye Kumb. Na. MB/MKN/Ardh 01/2016 ya tarehe 30 Mei, 2016. Napenda kuikumbusha Wizara juu ya maombi haya ambayo kimsingi yamechukua muda mrefu kupatiwa ufumbuzi.

(i) Shamba la Kilulu; shamba hili ndipo palipojengwa Makao Makuu ya Wilaya ya Mkinga. Shamba hili kwa mara ya kwanza lilimilikishwa kwa Bwana Van Brandis na Bibi Mary Van Brandis hadi tarehe 31 Oktoba,1959 ambapo umiliki ulihamia kwenda ama Bwana Akberali Walli Jiwa. Mmiliki huyu hakuendeleza shamba hili lenye ukubwa wa ekari 5,699.9 hadi umiliki wake ukafutwa mwaka 1972. Baada ya kufuta umiliki, Serikali ililipa fidia na shamba likawa chini ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadaye Wilaya ya Muheza ilipokea maombi ya kumilikishwa shamba hilo toka Kampuni ya M/S Arusha Farms Limited (CHAVDA). Taratibu zote zilizofanyika na alimilikishwa ekari 2,699.9 na ekari 3,000 walipewa wananchi wa vijiji jirani vya Vuo, Mwachala na Parungu Kasera waliokuwa na shida ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, M/S Arusha Farms Limited walipewa barua ya toleo (Letter of Right of Occupancy) ya tarehe 10 Mei, 1991 ambayo ilisajiliwa na Msajili wa hati tarehe 10 Mei, 1991 ambayo ilisajiliwa na Msajili wa hati tarehe 13 Mei, 1990 kwa Land Office Number 125127.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmiliki huyu aliomba mkopo kutoka CRDB Bank kwa kuweka rehani barua ya toleo. Aidha, alishindwa kurejesha mkopo huo na CRDB waliuza shamba kwa M/S Mbegu Technologies Limited tarehe 27 Juni, 2004 ambao walilipa mkopo huo. Hata hivyo, pia hakuweza kuliendeleza shamba hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bwana Akberali Jiwa licha ya kunyang’anywa shamba hilo na kulipwa fidia aliwasilisha ombi lake la kurejeshewa umiliki wa shamba hilo. Ombi lake liliwasilishwa katika Kikao cha Kamati ya Kugawa Ardhi tarehe 10 Oktoba, 1996 na iliazimiwa liwasilishwe katika Kamati ya Ushauri wa Ardhi Mkoa. Kamati hiyo chini ya Uenyeviti wa Mkuu wa Mkoa iliridhia Bwana Akberali Jiwa apewe shamba hilo kwa vile M/S Arusha Farms Limited ameshindwa kuliendeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Muheza ilitoa barua ya toleo kwa miliki ya miaka 99 kuanzia tarehe 1 Oktoba, 1998 kwa Akberali Jiwa kwa jina la Kampuni ya Kilulu (2000) Limited. Baada ya tatizo hilo la double allocation kujitokeza, Halmashauri ya Muheza iliandika barua Kumb. Na. MUDF/3844/63 ya tarehe 2 Aprili, 2007 kwenda kwa Kamishna wa Ardhi kwa ajili ya kuomba kufuta miliki hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, licha ya ufuatiliaji uliofanywa wa mara kwa mara, kwa mujibu wa taarifa ya Halmashauri hadi leo Halmashauri haijapata hati yoyote inayoonesha kufutwa milki ya shamba tajwa. Kikao cha RCC kilichofanyika mwaka jana kiliridhia hati ya shamba tajwa ifutwe; hivyo kuagiza taratibu za kutoa notice zifanyike. Hata hivyo, tangu wakati huo kumekuwa na urasimu mkubwa wa utoaji notice tajwa. Naiomba Wizara ifuatilie jambo hili.

(ii) Shamba la Moa; shamba hili lina ukubwa wa ekari 15,739.60 na linamilikiwa na Mkomazi Plantations Limited wa S.L.P. 2520 Dar es Salaam kwa hati Na. 4268,9780 &9781. Halmashauri ya Wilaya ilituma notisi ya kuwafutia hati miliki yao kwa kutoendeleza na kutolipia kodi. Baada ya hapo Halmashauri ya Wilaya iliwasilisha barua ya Mapendekezo kwa Kamishna wa Ardhi yenye Kumb. Na MKG/LD/F/2/54 ya tarehe 28 Julai, 2009.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taratibu za ufutaji hati miliki ziliendelea Wizarani, lakini Halmashauri ilipokea barua ya mmiliki akieleza kuwa jina la umiliki lilibadilika na kuwa Moa Plantation & Aquaculture wa S.L.P. 364 Dar es Salaam na kwamba wanataka kuendeleza shamba hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ilishawasilisha Wizarani barua ya mapendekezo ya kufuta hati miliki, ililazimika kumwandikia Kamishna wa Ardhi barua yenye Kumb. Na. MKG/LD/F/2/56 ya tarehe 9 Juni, 2011 kumweleza kupokea barua hiyo na kwamba shamba hilo lina vijiji vinne ambavyo vimeanzishwa na kusajiliwa (Moa, Ndumbani, Mayomboni na Mhandakini).

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, vijiji hivyo tayari vina huduma za jamii kama shule, zahanati, barabara na kadhalika katika maeneo hayo; hivyo aendelee na taratibu za ufutaji hati miliki au kama atasitisha ufutaji basi wamiliki wakubali kumega maeneo yanayokaliwa na vijiji na kuendelezwa na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati hali ikiwa hivyo, mwaka 2013 mmiliki wa shamba atengeneze PP na kuomba kubadilisha matumizi ya sehemu ya shamba ili kupima viwanja 450 vya makazi. Hata hivyo, viwanja hivyo havikuwahi kupimwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatilia ucheleweshaji usioeleweka wa kufuta hati ya shamba hili, mnamo mwezi Oktoba, 2016 mmiliki wa shamba alitumia mwanya huo kutengeneza PP nyingine ya eneo lote la shamba ili kupima viwanja. Aidha, amekabidhi hati ya shamba tajwa ili ipelekwe kwa Afisa Ardhi Mteule-Moshi ili taratibu zinazokusudiwa ziweze kufanywa. Naiomba Wizara iingilie kati mchakato huu ili ardhi tajwa irejeshwe mikononi mwa Halmashauri ya Wilaya.

(iii) Mwele Seed Farm; shamba hili lina ikubwa wa hekta 954. Mmliki ni Wizara ya Kilimo. Wakati ambapo shamba hili lilikusudiwa kuwa shamba la kuzalisha mbegu, hali halisi ni kwamba kwa kipindi cha takribani miaka 15 sasa shamba hili limeshindwa kutumika kama ilivyokusudiwa na sehemu kubwa kubaki kuwa pori.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa vijiji vinavyozunguka shamba hili Mbambakofi, Maramba A, Maramba B na Lugongo ndio wamekuwa nguvukazi ya kulifanyia usafi shamba hili pale wanaporuhusiwa kufungua mashamba mapya na kulima mazao ya muda mfupi kila msimu mpya wa kilimo unapowadia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 21 Septemba, 2007, Halmashauri ya Wilaya iliandika barua kwa Kamishna wa Ardhi Kumb. Na. MUD/ASF/VOL.VI/35 ikipendekeza kumegwa kwa shamba hili na kugawiwa kwa wananchi wa vijiji jirani kutokana na uendelezaji wake kuwa mdogo sana na kodi kutolipwa. Hata hivyo, maombi haya hayakuwahi kupatiwa majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shamba hili lilipakana na Kijiji cha Mbambakofi chenye takriban kaya 500 zenye jumla ya wananchi wapatao 3173. Mbambakofi ni kijiji pekee katika Wilaya ya Mkinga ambacho kimekosa hata eneo la kujenga huduma muhimu za kijamii kama shule ya msingi na zahanati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, shamba hili limepakana na Mji Mdogo wa Maramba ambao unakua kwa kasi kubwa, ukiwa na takriban watu 30,000 na kuzungukwa na mashamba makubwa ya Maramba JKT, hekta 2,445; Lugongo Estate, hekta 6,040; Kauzeni Estate, hekta 189.66; na Mtapwa Estate, hekta 476.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya kutekelezwa kwa shamba hili imezidi kuwa mbaya sana sasa kuliko ilivyokuwa mwaka 2007, wakati Halmashauri ya Wilaya ilipoomba kwa mara ya kwanza kumegwa kwa shamba hili. Kwa sasa hali imekuwa mbaya kiasi kwamba hata majengo mengi yaliyokuwepo yameanguka na machache yaliyosalia yamekuwa magofu, mashine na mitambo yote ya kilimo iliyokuwepo shambani hapo imeharibika na michache iliyosalia imehamishiwa Morogoro. Kwa sasa shamba limebaki na wafanyakazi wasiozidi watatu kutoka ishirini na vibarua thelathini waliokuwepo miaka ya 1988 – 1995.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Halmashauri ya Wilaya kusubiri kwa muda mrefu jibu la Kamishna wa Ardhi bila mafanikio, kikao cha RCC kiliiagiza Halmashauri kuandaa maelezo kuhusiana na shamba hili ili Mkuu wa Mkoa aweze kuandikia Wizara husika kuomba rasmi Halmashauri kukabidhiwa eneo tajwa. Tayari Halmashauri imetekeleza maagizo haya. Naiomba Wizara ya Ardhi isaidie katika utatuzi wa kero hii ambayo inawasumbua sana wananchi.

(iv) Kwamtili Estate; shamba hili lina ukubwa wa hekta 1,150 na linamilikiwa na Kwamtili Estate Limited yenye Certificate of Incorporation Na. 2649 iliyosajiliwa tarehe 9 Januari, 1961 ikiwa na wanahisa wafuatao:-

S/N JINA LA MWENYE HISA ANAPOISHI MAELEZO
1 DENNIS Martin Fielder 4 Market Square Tenbery,Wells Worcestershinre –UK Amerudi Uingereza
2 National Aggriculture
& Food Corporation (NAFCO Box 903 Dar es Salaam Shirika limefutwa
3 Handrick Tjails Scheen CI/30 Algamines Bank, Amsterdam, Netherland Amefariki
4 Louis Van Wagenburg Laycsan Ag Vaghel, Holland Amefariki
5 Schoonmarkers Bart Vandrbug De Congqabsen,163 Schikher, Holland Amefariki
6 Tracey Elan Allison The Willos Terrigton, Herefordenshire, UK Amefariki
7 Juvent Magoggo 42 Block S. Mikanjuni Box 5855 Tanga Anaishi Tanga
8 W.J. Tame Ltd Box 118 Tanga Amefariki
9 Jacobus Cornelius Josephus Moris Logtamburg Vaghel Holland Amefariki

Mheshimiwa Mwenyekiti, shamba hili lililopo katika eneo la Kwamtili, Kata ya Bosha Wilaya ya Mkinga, lilitumika kwa kilimo cha kibiashara cha zao la kakau. Hata hivyo, kwa muda wa miaka takriban 26 sasa shughuli za kilimo cha zao la kakau zimesimama baada ya iliyokuwa Menejimenti ya Kampuni chini ya Ndugu Dennis Fielder kutelekeza shamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, baada ya shamba kutelekezwa, mmoja wa wanahisa Ndugu Juvent Magoggo amekuwa akifanya shughuli ndogo ndogo ikiwemo kuvuna miti ndani ya shamba hili kwa lengo la kupata fedha za kufanyia uzalishaji mdogo mdogo; na hali kadhalika kuruhusu wananchi wanaozunguka shamba hilo kulima mazao ambayo si ya kudumu. Hata hivyo, kwa sasa ndugu Magoggo ameshindwa kuendelea kufanya shughuli hizo baada ya kunyimwa vibali vya kuvuna miti kusafirisha magogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kuwepo kwa ombi la umiliki wa shamba hili, yamezuka makundi ya watu yanayodai kuwa na haki ya kumiliki shamba hili na hivyo kuwakodisha wananchi wanaozunguka shamba hili maeneo ya kulima kwa kuwalipisha sehemu ya mavuno yatokanayo na matumizi ya ardhi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kumekuwa na wimbi la kujitokeza raia wa kigeni kwa kutumia kivuli cha aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shamba na kulitekeleza Ndugu.Dennis Fielder kufanya uharibifu wa mali za kampuni, ikiwemo upasuaji wa mbao na kuanzishwa michakato ya kujimilikisha ardhi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili, wananchi wanainyooshea kidole Ofisi ya Wakala wa Hifadhi ya Misitu, Wilaya ya Mkinga kutaka kujiingiza katika kufanya udalali wa ardhi hii. Wananchi bado wanakumbukumbu nzuri ya jinsi watumishi hawa wa TFC Wilayani Mkinga walivyotumika kuwezesha mwekezaji wa Kiitaliano aliyejaribu kupatiwa ardhi ya Mkinga takriban hekta 25,000 kinyume na taratibu ili kulima Jatropher.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Serikali haijaweza kulipatia ufumbuzi tatizo lingine ambalo kimsingi limeanzishwa na TFC kutaka kupora ardhi ya wananchi katika shamba la Segoma, TFC hiyo hiyo inataka kuzalisha mgogoro mwingine wa kupora ardhi nyingine katika Wilaya ya Mkinga.

Hatupo tayari kuona hili likitokea hasa ikizingatiwa kuwa Kwamtili inakabiliwa na tatizo kubwa la ardhi. Tunaiomba Serikali kutumia busara kuacha jambo hili na kuirejesha ardhi hii kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kwamtili na Kata ya Bosha kwa ujumla wamebaki katika umaskini wa kutupa baada ya shughuli za kilimo cha kakau katika shamba la Kwamtili ambacho ndicho kilitoa ajira kwao kusitishwa. Nusura pekee kwa wananchi hawa ni kupatiwa maeneo katika shamba hili ili kwa kutumia utaratibu wa wakulima wadogo waweze kufanya shughuli ya kilimo na hivyo kujikimu kimaisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali ifanye uamuzi wa kufuta hati ya shamba la Kwamtili na kisha kuligawa kwa wananchi kwa ajili ya kilimo na sehemu nyingine kwa wananchi kuwa hifadhi ya msitu wa kijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua changamoto kubwa inayowakabili wananchi wa Kwamtili, RCC iliagiza mmiliki wa shamba hili kupewa notice ili taratibu za kufutiwa hati ziweze kufanyika. Kwa masikitiko makubwa kumekuwa na urasimu mkubwa wa taratibu wa kutolewa notice tajwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya Afisa Ardhi Mteule toka Ofisi ya Kanda-Moshi kuja Mkinga kufanya zoezi la uhakiki mwanzoni mwa mwezi Aprili hadi leo hakuna kinachoendelea licha ya kukumbushwa mara kadhaa kwa simu na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mkinga. Naiomba Wizara iingilie kati jambo hili ili ujanja ujanja usitumike kuvuruga mchakato wa kuwapatia haki wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo haya, naunga mkono hoja. Aidha, naomba Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na TAMISEMI itusaidie Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga tuweze kuajiri Afisa Ardhi Mteule ili atusaidie kuondoa migogoro.