Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Lolesia Jeremia Maselle Bukwimba (37 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. LOLESIA J. M. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa hotuba nzuri. Vile vile pongezi kwa Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na Naibu Makatibu Wakuu na watumishi wote wa Wizara kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni juu ya utekelezaji wa ahadi za Mheshimiwa Rais katika Jimbo la Busanda. Mheshimiwa Rais aliahidi kujenga barabara ya lami yenye urefu wa kilometa tano katika mamlaka ya Mji Mdogo Katoro na kilometa tano Buseresere wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2015. Mpaka sasa ni miaka mitatu hakuna kinachoendelea. Ningependa kujua ni lini ujenzi wa barabara hizi utaanza rasmi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ujenzi wa barabara katika Jimbo la Busanda kuna kero kubwa sana ya upatikanaji wa maji safi na salama. Kwa kuwa mamlaka ya Mji Mdogo Katoro kuna idadi kubwa sana ya watu na suala la maji ni kero kubwa ambapo tumezungukwa na Ziwa Victoria. Naomba Serikali iwe na mkakati maalum wa kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria ili kupata suluhu juu ya changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama. Kwa maneno machache naomba kuwasilisha ili Serikali iweze kutafutia ufumbuzi changamoto hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Ahsante.
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia hotuba hii. Kwa kuwa ni mara ya kwanza kabisa kuweza kuchangia katika Bunge hili la Kumi na Moja, nachukua nafasi hii kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Busanda kwa kuendelea kuniamini tena wakanipa ridhaa katika awamu hii. Napenda kuwahakikishia kwamba nitaendelea kufanya kazi kwa nguvu zote ili kuweza kuwatumikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kupongeza huu Mpango wa mwaka 2016/2017. Ninachopenda zaidi ni kusisitiza suala la reli ya kati. Nazungumzia suala la reli kwa sababu ni injini ya uchumi. Bila ya kuwa na reli, uchumi wetu hauwezi kukua kwa sababu hatuwezi kusafirisha mizigo kutoka Dar es Salaam kwa njia ya barabara, kiasi kwamba mizigo mingi inasababisha barabara zetu ambazo tumezitengeneza kwa fedha nyingi kuharibika kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kabisa kwamba hii reli ya kutoka Dar es Salaam kwenda Tabora, Mwanza, kutoka Tabora kuelekea Kigoma; kutoka Isaka kuelekea Keza na nyingine zote, naomba Serikali ituletee Mpango Mkakati, namna itakavyoweza kufanya ili kuweza, kutengeneza reli hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la maji. Naomba katika Mpango huu, Serikali iwekeze Mpango Mkakati wa uhakika, kwa suala la maji, kwa sababu maji ni tatizo kubwa sana hasa vijijini kwa wananchi wa Tanzania. Katika Jimbo la Busanda, pengine ni asilimia kumi tu ya wananchi wanaopata maji safi na salama. Kwa hiyo, nachukua fursa hii kuomba Serikali inapoleta mpango mkakati, ihakikishe suala la maji, linakuwa ni la kipaumbele kikubwa sana kwa sababu maji ni uhai. Hatuwezi kuwa na mapinduzi ya viwanda bila kuwa na maji ya uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa zaidi katika Mkoa wetu wa Geita tumebahatika kuzungukwa na maji ya Ziwa Victoria. Hebu Serikali basi ifikie hatua, iangalie uwezekano tuweze kupata maji ya uhakika kutoka Ziwa Victoria. Tayari katika Mji wa Geita, tumevuta maji kutoka Ziwa Victoria, kwa hiyo, basi Serikali iangalie uwezekano hata sisi vijijini tuweze kupata maji ya uhakika hasa maeneo ya Busanda na Sehemu nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile upande wa afya, napenda kuishauri Serikali iangalie katika Mpango wake wa mwaka 2016/2017, katika Mikoa mipya hatuna Hospitali za Rufaa. Katika Mkoa wa Geita, hatuna Hospitali ya Rufaa. Katika takwimu inaonesha kwamba vifo vya akina mama wajawazito, takwimu bado iko juu sana. Sasa ili tuweze kupunguza vifo vya akina mama wajawazito, ni vizuri Serikali iweke mkakati mkubwa wa kuwekeza katika upande wa afya hasa kwa kujenga Hospitali za Rufaa katika Mikoa ambayo hatuna Hospitali za Rufaa kama Mkoa wa Geita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo pia tuangalie katika Kata zetu, tuwe na hospitali, Vituo vya Afya, lakini pia katika Wilaya tuwe na Hospitali ya Wilaya. Kwa hiyo, naomba Serikali kweli iwekeze katika upande wa Afya, kwa sababu haiwezekani tukafikia uchumi wa kati bila kuwa na afya kwa wananchi wetu. Kwa hiyo, naomba sasa katika Mpango Mkakati, nahitaji kuona kabisa kwa dhahiri kwamba Hospitali ya Rufaa ya Geita ipo kwenye Mpango, lakini vile vile Mpango wa Vituo vya Afya katika Kata zetu na Zahanati katika Vijiji vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kwa upande wa elimu, nami naendelea kushukuru sana kwa huu mpango wa elimu bure. Baada ya kutangaza kwamba elimu ni bure, imeonekana hata watoto ambao wanapelekwa shule kuandikishwa Darasa la Kwanza, wameongezeka kwa kiasi kikubwa. Hili linaonesha jinsi ambavyo kumbe wazazi wengi walikuwa hawapeleki watoto wao shule kwa sababu wanaona kwamba ni gharama kuandikisha, ni gharama kulipa ile ada. Kwa hiyo, tunaipongeza sana Serikali kwa hatua hiyo na juhudi ambazo imezifanya.
Naomba tu sasa Serikali iendelee kuongeza zaidi namna ya kuwezesha hii elimu bure, ili iweze kwenda kwa utaratibu sahihi ili watoto wetu waweze kunufaika zaidi katika elimu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili sasa, ili tuweze kufikia katika uchumi wa kati, Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni amesisitiza sana suala la viwanda kwamba Tanzania yetu itakuwa ni Tanzania ya viwanda, nami hili suala nalipongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iwe na viwanda vya kimkakati kila Kanda. Kwa mfano, Kanda ya Ziwa, tuna mazao yetu, tuna dhahabu, tuna mifugo, tuna uvuvi; kwa hiyo, Serikali iangalie viwanda gani ambavyo itaweza kuwekeza ili wananchi wetu kulingana na mazao tuliyonayo tuweze kunufaika zaidi na vijana waliyo wengi waweze kupata ajira katika viwanda hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuangalie viwanda vya kimkakati katika Kanda ya Ziwa Viwanda vya Samaki; tunahitaji tuwekeze katika Viwanda vya Samaki, Viwanda vya Nyama na vile vile Viwanda vya Dhahabu, yaani kuongeza thamani ya dhahabu. Mkoa wa Geita tumebahatika dhahabu kwa wingi. Naomba pia Serikali katika mwaka huu wa fedha, tuangalie uwezekano wa kutoa maeneo ya kutosha kwa ajili ya wachimbaji wadogo, kwa sababu ndiko ambako vijana wengi wamejiajiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, kwa sababu hii imekuwa ni ahadi ya muda mrefu sana ya Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, lakini vile vile Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, naomba kweli mwaka huu Serikali iangalie uwezekano wa kutoa maeneo ya kutosha kwa ajili ya kuwapatia wachimbaji wadogo ili vijana wengi waweze kupata ajira katika shughuli za uchimbaji wa madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naiomba sana Serikali kwamba tunaupokea huu Mpango lakini iweke mkakati mzuri na itakapouleta vizuri tuone katika Mpango huu iguse hayo maeneo ambayo pengine hayajaweza kujionesha kwa dhahiri ndani ya Mpango ili basi tunapopitisha tuweze kuona kabisa kwamba Tanzania tunapiga hatua katika uchumi, kutoka uchumi wa chini kwenda uchumi wa kati kama ambavyo mategemeo na matarajio yetu yalivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa upande wa elimu…
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja, Serikali iendelee kutekeleza hayo.
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano.
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa jinsi ambavyo wametuletea Mpango huu wa Miaka Mitano ambao umezungumzia mambo ya msingi na muhimu kabisa kwa ajili ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la muhimu kabisa ambalo napenda kuisisitiza Serikali ni kwamba iwekeze zaidi katika suala la nishati. Tumeona jinsi ambavyo Serikali katika miaka mitano iliyopita imeweza kuwekeza kwenye nishati na tumeona jinsi ambavyo kuwepo kwa nishati hii kwa asilimia 30, wananchi wengi wameweza kunufaika kwa kutumia umeme ambao upo mpaka vijijini. Kwa hiyo, napenda kusisitiza sasa kwamba Serikali iongeze uwekezaji katika suala zima la umeme hasa vijijini ili tutakapokuwa na umeme wa uhakika vijijini, itawezesha wananchi wetu kuweza kujiajiri katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile tunaona jinsi ambavyo Awamu ya Tano tumekusudia kujenga viwanda, kwa hiyo kwa kuwa na umeme maeneo yote ya vijijini na mijini tutaweza kuongeza uwekezaji kwa suala zima la viwanda na vijijini wawekezaji wataweza kuwekeza katika viwanda. Kwa hiyo, niombe tu Serikali katika suala zima la umeme iongeze fedha nyingi katika Mpango huu wa miaka mitano ili tuweze kuona wananchi wengi hasa wa vijijini ambao kwa kipindi kirefu walikuwa hawana umeme waweze kunufaika zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika suala la madini, Serikali imesema kwamba itawezesha sekta muhimu za kiuchumi ikiwepo sekta ya kilimo na madini. Napenda kuomba Serikali iwekeze katika suala zima la madini hasa kwa wachimbaji wadogo kwa kuongeza mitaji ili kuwawezesha vijana wengi waweze kujiajiri. Wapo vijana wengi sana ambao wanatumia nguvu zao katika shughuli mbalimbali za kiuchumi hasa katika uchimbaji wa madini, lakini wanakosa vifaa muhimu kwa ajili ya uchimbaji wa madini.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imeona iangalie sekta hizi za kiuchumi kuweza kuziboresha zaidi, napenda kutoa msisitizo kwamba Serikali iongeze fedha hasa kuwawezesha wachimbaji wadogo kuwapa zana bora za kuweza kufanyia shughuli za kiuchumi ili vijana wengi waweze kujiajiri katika sekta hiyo ya kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina mapendekezo pia katika suala zima la maji. Ni muhimu sana Serikali iangalie uwezekano wa suala la maji hasa vijijini. Kwa miaka iliyopita tumeona jinsi ambavyo wananchi wengi hasa vijijini hawana maji safi na salama. Kwa hiyo, ili wananchi tuweze kufanya shughuli zetu vizuri na yaweze kupatikana maendeleo endelevu, tunapenda pia katika Mpango huu tuongeze fedha nyingi sana katika suala zima la upatikanaji wa maji safi na salama hasa vijijini ili akinamama ambao wamekuwa wakitumia muda mrefu kwenda kutafuta maji umbali mrefu zaidi ya kilomita tano wapate nafuu. Wakiweza kupatiwa maji safi na salama na kuwa karibu zaidi nina uhakika nguvu zao nyingi wataweza kuwekeza katika shughuli za kiuchumi zaidi na wengi wataweza kuongeza pato la Taifa hili la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vile vile katika maeneo ambapo tumezungukwa na maziwa kwa mfano katika Kanda ya Ziwa tumezungukwa na Ziwa Viktoria. Napenda kutoa msisitizo kwamba Serikali iweke mpango mkakati wa kutosha ili tuweze kuvuta maji kutoka Ziwa Viktoria na maziwa mengine kwa maeneo ambayo yamezungukwa na maziwa. Hii itawezesha wananchi walio wengi kuweza kupata maji safi na salama.
Mheshimiwa Spika, inasikitisha sana kuona kwamba nchi hii ya Tanzania tumezungukwa na mito, maziwa kama nilivyosema Ziwa Viktoria limetuzunguka lakini wananchi hawana maji safi na salama. Kwa hiyo, niombe sasa katika Mpango huu wa Miaka Mitano, Serikali hebu iwekeze vizuri, iweke mkakati mkubwa wa uhakika wa kuhakikisha kwamba inavuta maji kutoka Ziwa Viktoria na maziwa mengine ili wananchi waweze kufikiwa na maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika miaka iliyopita tumeona jinsi ambavyo Serikali wameweza kuvuta maji kutoka Ziwa Viktoria mpaka Kahama sasa yanaelekea Shinyanga yanaenda mpaka Tabora lakini Mikoa ambayo tumezungukwa na ziwa kama Geita wananchi hawana maji safi na salama. Kwa hiyo, nichukue tu fursa hii kusisitiza kwamba kwa kuwa imeweka kwenye Mpango wake hebu sasa iangalie uwezekano wa kupata fedha za kutosha iwekeze katika suala zima la upatikanaji wa maji ili maji haya yawezeshe shughuli mbalimbali kwa sababu huwezi ukawa na viwanda bila ya kuwa na maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba Serikali iangalie suala la maji kwa uhakika kwa sababu maji ni changamoto kubwa. Tumeona jinsi ambavyo kila mmoja hapa anasimama anasema naye ana changamoto hiyo ya maji. Kwa hiyo, suala la maji liwe kipaumbele katika mpango mkakati wa miaka mitano hii ili wananchi wetu waweze kunufaika na kuweza kufanya shughuli zao vizuri kwa sababu wana maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunajua pia suala la maji ni uhai, tukiwa na maji safi na salama hata afya za wananchi zitakwenda vizuri. Ndiyo maana napenda kusisitiza sana Serikali ijikite katika kuhakikisha kwamba maji safi na salama yanapatikana kwa wananchi wa Tanzania wakiwemo wa Mkoa wa Geita ambapo tuna changamoto sana ya maji. Tumezungukwa na ziwa lakini hatuna maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine la msingi kabisa katika Mpango huu ambalo limenigusa, nimeona jinsi ambavyo Serikali imejipanga kuwekeza katika suala zima la reli ya kati. Ili tuweze kuwa na uchumi imara, ni vyema Serikali ikawekeza zaidi katika reli. Nami naunga mkono kabisa iweke mpango mzuri kuwekeza katika reli ya kati kwa standard gauge ili kuwezesha usafirishaji wa bidhaa muhimu kutoka bandari ya Dar es Salaam kwenda katika mikoa ya pembezoni ambayo iko mbali na bahari ya Dar es Salaam ambako ndiko kwenye bandari kuu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile tunajua nchi yetu ya Tanzania imezungukwa na nchi mbalimbali ambazo hazina bahari. Nina uhakika kwamba tukijenga hii reli kwa sababu kupitia hii reli ya kati ambayo inakwenda Mikoa ya Kigoma na mikoa mingine mpaka nchi za jirani Burundi, Rwanda na sehemu mbalimbali uchumi utaimarika. Kwa hiyo, katika miaka mitano hii Serikali ikiwekeza katika mpango mzima wa reli ya kati na kuiwezesha vizuri kabisa nina hakika uchumi wetu wa Tanzania utaweza kuimarika vizuri zaidi na tutaongeza mapato ya Taifa kwa sababu wenzetu wa nchi za jirani wataweza kutumia bandari yetu ya Dar es Salaam na kuweza kuongeza pato letu la Taifa katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo vilevile na sisi ambao tunatokea mikoa ya pembezoni tutaweza kupata bidhaa katika bei nafuu zaidi. Kwa sasa hivi unakuta bei ya simenti Dar es Salaam inauzwa kwa bei ndogo mfuko Sh.15,000/= lakini ukifika Geita mfuko huo huo unauzwa Sh.22,000/= mpaka 25,000/=. Kwa hiyo, tunaona jinsi ambavyo maisha ya wananchi yanakuwa ni ya gharama kubwa sana, lakini Serikali ikiwekeza katika reli nina uhakika hata usafirishaji wa bidhaa muhimu kama simenti na vitu vingine itawezesha bei ya bidhaa kuwa bei ambayo inamwezesha Mtanzania hata wa hali ya kawaida kuweza kufanya shughuli zake za kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vile vile katika suala la reli, napendekeza kama kuna uwezekano tuweze kujenga hata bomba la mafuta kwenye njia hiyo hiyo ya reli kutoka Dar es Salaam kwenda mpaka Mikoa ya Kanda ya Ziwa hiyo ya Tabora kuelekea Kigoma hata katika nchi za jirani. Hii itasaidia kupunguza bei ya mafuta kwani kwa sasa hivi Dar es Salaam lita moja inauzwa Sh.1,400/= lakini ukifika Mikoa ya Geita, Mwanza bei inakuwa imepanda zaidi inakuwa zaidi ya Sh.2,000/=.
Mheshimiwa Spika, haya yote yatawezekana ili kuboresha uchumi wetu pale ambapo tutafikiria kuwa na bomba la mafuta kutokea Dar es Salaam kwenda katika mikoa ya pembezoni, Mikoa ya Kanda ya Ziwa na mikoa mingine ambapo itatuwezesha kuinua uchumi halisi wa wananchi katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vile vile katika suala zima la miundombinu, ni vizuri sasa Serikali iangalie katika mkakati wake ambao umekuwa nao na Sera ya Taifa ya kuunganisha kati ya mkoa kwa mkoa, wilaya na wilaya kwa barabara za lami. Napenda kuunga mkono kwamba Serikali iendelee kuwekeza fedha ili tuweze kuunganisha kwa barabara za lami mikoa kwa mikoa, wilaya kwa mikoa na wilaya kwa wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile tuangalie hata ile mipango mikakati iliyopita pamoja na Ilani ya Chama cha Mapinduzi iliyopita. Kwa mfano, katika Mkoa wangu wa Geita katika Ilani tulikuwa tumekusudia kujenga barabara ya lami kutoka Geita kuelekea Kahama kupitia Bukoli lakini vile vile kujenga barabara ya lami kutoka Geita kwenda Bukombe ambayo ni wilaya mpya katika Mkoa wa Geita. Kwa hiyo, niombe Serikali pia iangalie yale mambo yaliyokuwepo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi iliyopita ihakikishe inayafanyiwa kazi ili wananchi tuweze kunufaika zaidi. Kwa sababu tukiwa na barabara za lami Mkoa kwa mkoa, wilaya kwa wilaya, wilaya kwa mkoa, nina uhakika wananchi wengi wataweza kunufaika kwa sababu wataweza kusafirisha mazao yao vizuri na watafanya biashara zao vizuri na kwa uhakika na mwisho wa siku pato la Taifa litaweza kuwa la uhakika na litainuka na tutakuwa na uchumi ulio bora katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho, kwa kuwa Serikali hii imekusudia kuwekeza katika suala zima la viwanda na mimi kila nikisimama nimekuwa nikizungumzia suala la viwanda na mikoa mingine kama ya Geita ambayo ni mipya haina viwanda. Niiombe Serikali kwa kuwa imeamua kuwekeza katika masuala ya viwanda, tuiangalie mikoa hii kwa kuanzisha viwanda kutokana na rasilimali zinazopatikana kwenye maeneo yale.
Mheshimiwa Spika, naomba ikiwezekana tujengewe hata kiwanda cha simenti. Katika Kanda ya Ziwa hatuna kiwanda cha simenti hata kimoja. Wananchi wanahangaika sana kupata simenti, bei ni ghali sana ndiyo maana watu wanashindwa kujenga nyumba bora kwa sababu bei ya simenti ipo juu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ni ya viwanda, niombe awamu hii tuhakikishe Kanda ya Ziwa tunakuwa na kiwanda cha simenti ili wananchi waweze kunufaika kutokana na rasilimali ambazo tuko nazo katika maeneo yetu. Sambamba na hilo, tuangalie pia kwa kikanda kwamba kanda hii inazalisha mazao fulani tuwekeze viwanda vya aina hiyo kulingana na mazao yanayopatikana katika maeneo yale.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, napenda kutoa msisitizo kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kuwekeza zaidi katika masuala ambayo nimeyazungumzia, suala la umeme na viwanda katika maeneo yote ili wananchi wetu waweze kushiriki katika kuhakikisha kwamba uchumi wao unaweza kuinuka kwa sababu bila ya ushiriki wa wananchi wa kawaida haiwezekani uchumi kuinuka zaidi. Niombe tu Serikali itilie mkazo katika kuona kwamba yale ambayo imezungumzia katika Mpango ya Miaka Mitano yafanyiwe utekelezaji maana wakati mwingine tunapanga mipango lakini utekelezaji wake unakuwa ni asilimia ndogo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe yale ambayo tumeyapanga kwa miaka mitano hii tuhakikishe basi tunayafanyia kazi kama ni fedha tutafute fedha ili tuweze kuyatekeleza na kuhakikisha kwamba uchumi wetu unainuka kwa sababu ya uwepo wa mambo ambayo tumeyapanga katika miaka hii mitano na kwamba yametekelezwa hatua kwa hatua.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja nikiomba Serikali ihakikishe inayafanyia kazi mambo yote niliyoyazungumza. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi au hotuba nzuri. Pia nimpongeze Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni juu ya ujenzi wa Vyuo vya Ufundi. Katika hotuba ukurasa wa 59 umezungumzia juu ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Mkoa wa Geita. Hili nalipongeza na ninashauri ujenzi uanze mara moja kutokana na mahitaji tuliyonayo katika Mkoa wetu. Mkoa una Wilaya tano na hatuna chuo hata kimoja katika Wilaya za pamoja na mpango wa ujenzi wa Chuo cha VETA Mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe msisitizo pia kwamba Serikali ione umuhimu wa kujenga vyuo hivi katika Wilaya zetu. Sera ya Taifa ni kuwa na VETA kila Wilaya. Kwenye bajeti nimeona ujenzi wa VETA Wilaya ya Chato, tunapongeza, lakini Serikali ione uwezekanao wa kujenga VETA Wilaya ya Geita kulingana na wingi wa watu katika Wilaya yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaomaliza Shule za Msingi na Shule za Sekondari ni wengi ambao hawaendelei na elimu ya juu na hao wanahitaji ujuzi na ufundi stadi ili kuwawezesha kumudu maisha yao kiuchumi na mwisho wa siku wachangie katika pato la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya pili ni madeni ya Walimu. Hii ni changamoto sana maana Walimu bado wana madai yao makubwa sana. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita na Mkoa wa Geita madai ni makubwa na tayari madeni yamehakikiwa. Ili tuboreshe morale na ufanisi katika utendaji kazi kwa Walimu ni vema Serikali ikatilia mkazo katika kulipa madeni haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya tatu ni juu ya malalamiko ya wanafunzi wa UDOM kitengo cha Diploma ya Ualimu. Ni wiki ya nne sasa hawafundishwi kutokana na mgomo wa Walimu wao. Malalamiko haya yamewasilishwa na viongozi wa wanafunzi katika Kitengo cha Ualimu UDOM jana, ambapo walikuja hapa Bungeni kutoa shinikizo kwa Waziri juu ya hatma ya suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri kwa Mheshimiwa Waziri wakati wa majumuisho hebu utoe kauli kuhusiana na jambo hili. Naomba ulifuatilie na ulitafutie ufumbuzi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika bajeti hii muhimu. Napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya katika nchi yetu ya Tanzania. Hakika wananchi walio wengi wanamuunga mkono katika juhudi anazozifanya na wengi wanasema Wabunge tuweze kumuunga mkono katika shughuli zake anazozifanya hasa katika nchi hii ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika Taifa hili, aliweza kupata fursa ya kutembelea Mkoa wetu wa Geita, kwa kweli mambo aliyofanya ni mambo makubwa tunaimani kubwa kwamba katika utawala huu tutaweza kuona mabadiliko makubwa sana katika nchi yetu, hasa katika maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri, Ofisi ya Rais – TAMISEMI pamoja na Utumishi na Utawala Bora kwa jinsi ambavyo wanafanya kazi zao vizuri. TAMISEMI tunaona jinsi ambavyo wanaangalia changamoto mbalimbali ambazo zinakabili hasa katika Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Wote tunafahamu kwamba Majimbo mengi tunategemea sana TAMISEMI kwa ajili ya maendeleo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza katika sekta ya elimu, nilivyokuwa nikiangalia ile hotuba inaonesha jinsi ambavyo changamoto bado ni kubwa hasa katika upande wa elimu. Tumeona mwaka huu watoto wengi wamejiandikisha hasa darasa la kwanza, lakini miondombinu ni changamoto kubwa. Niiombe Serikali sasa iangalie uwezekano wa kuwekeza zaidi kwenye miundombinu ya madarasa, kwenye nyumba za walimu, yaani katika kila hatua, ili tuweze kuona kwamba watumishi ambao ni walimu na watumishi wengine wanafanya kazi zao kwa amani na utulivu kwa sababu wana sehemu nzuri ambapo wanaishi wanaenda kufundisha kwa amani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika upande wa elimu ninafahamu kwamba kweli Wizara imejipanga vizuri, nimeona jinsi ambavyo mmekusudia kujenga nyumba 183 katika Halmashauri 103. Ninapenda kujua je, Halmashauri yangu ya Geita imo katika mpango huo? Kama haimo naomba sasa Wizara iangalie namna ya kuweka pia Halmashauri yangu kwa sababu changamoto ni kubwa sana katika Halmashauri. Watumishi wa Halmashauri ambao ni walimu na watumishi mbalimbali kwa kweli wana changamoto kubwa sana na ndiyo maana naomba katika huu mpango wa nyumba 183 ambazo zinakaa watumishi sita kila nyumba, basi iwe pia katika Mkoa wangu na katika Wilaya yangu, Halmashauri ya Wilaya ya Geita ninaomba mpango huu pia uwe kipaumbele ili tuweze kuwawezesha watumishi waweze kufanya kazi zao vizuri kwa ajili ya ufanisi wa kazi zetu katika Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika upande wa elimu, watumishi wengi bado wanaidai Serikali, wanadai mishahara, wengine wamepandishwa madaraja lakini hawajalipwa mishahara wengine, wana changamoto aina mbalimbali. Napenda kusisitiza Serikali iangalie namna ya kuweza kuwalipa hawa watumishi ambao wana madai mbalimbali. Walipoona kwamba, tumekuja kwenye Mkutano huu wa Bajeti wengi wamenipigia simu, hasa katika Halmashauri yangu ya Geita na Jimbo la Busanda, wanasema sasa tunaomba kwa kweli jambo hili ulisemee. Naomba kama ni uhakiki wao tayari umeshafanyika, kilichobaki ni kulipwa tu madai yao. Ninaomba Serikali awamu hii ihakikishe watumishi wanalipwa madai yao vizuri kwa uhakika ili waweze kufanya kazi zao wakiwa na morali kubwa kwa sababu hawaidai Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, watumishi wengi ambao wanastaafu wana changamoto kubwa, wengi hawapati mafao yao. Nichukue fursa hii kuitaka Serikali iangalie namna ya kuweza kulipa madai haya hasa ya watu ambao wamestaafu, wengi wanafuatilia wanaenda pale wanakuta hawajawekewa fedha zao kwenye akaunti, hivyo niiombe Serikali, iweze kulifanyia kazi suala hili, watumishi waweze kulipwa stahili zao, hasa ambao wamestaafu waweze kupata haki zao kwa amani ili waweze kuendelea na maisha yao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nizungumzie kuhusu TASAF. Nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa jinsi ambavyo imeanzisha utaratibu wa TASAF wa kuweza kuwajali wanyonge katika shida zao na kuwapa fedha. Jambo hili ni jema na litailetea baraka Serikali kwa sababu tumeweza kuwajali wanyonge. Nilichokuwa ninaomba sasa ni vile vijiji ambavyo hawajapata mpango huu nao wanahitaji waweze kuwepo katika mpango huu wa TASAF ili tuweze kuwasaidia hasa watu wanyonge ambao wanahitaji huduma hii ambayo ni ya muhimu sana.
Kwa hiyo, niiombe Serikali kwamba TASAF III ambayo imekusudia kuweza kusaidia wanyonge iongeze wigo, iangalie kata na vijiji mbalimbali, kwa sasa haifanyiki katika kila kijiji kwa hiyo, Serikali iangalie uwezekano kila kijiji watu wenye mahitaji maalum, watu ambao wana shida mbalimbali tuweze kuwaweka kwenye utaratibu wa TASAF. Hii itawezesha wananchi kuishi maisha bora na kuweza kufanya kazi zao, pia ambao hawana uwezo wataweza kusaidia watoto wao kwenda shule, lakini vilevile wataweza kuchangia katika shughuli mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika utaratibu mpya ambao Serikali imesema italeta shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Kama ni jambo ambalo Serikali imefanya jambo kubwa ni hili la kupeleka shilingi milioni 50 kwenye kila kijiji. Hizi shilingi milioni 50 watu wengi wanazisubiri, hasa vijijini, niiombe Serikali iweke utaratibu mzuri, mnafahamu hizi shilingi milioni 50 itakuwa ni ukombozi kwa wananchi wanyonge ambao wako vijijini. Wote ni mashahidi kulikuwa na mabilioni ya JK ambayo wengi waliweza kufaidika na bilioni hizo.
Kwa hiyo, hata katika hizi shilingi milioni 50 nilikuwa naiomba Serikali ijipange vizuri namna ya kuweza kuzipeleka kule la sivyo, hizi hazitaweza kunufaisha wananchi wenyewe wa hali ya kawaida, kwa sababu hizi shilingi milioni 50 kwanza watu ni wengi, sasa namna ya kwamba nani achukue hizi afanyie nini huo ni mtihani. Kwa hiyo, niiombe Serikali iweke utaratibu mzuri, lakini kikubwa iwekeze kwenye elimu, bila ya elimu haiwezekani kuweza kuzifanyia kazi hizi shilingi milioni 50 na wakaweza kuleta mnaendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe Serikali iwekeze kwenye elimu, ikiwezekana kupitia SIDO ambao wanatoa mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali. Hizi shilingi milioni 50 ni jambo ambalo wananchi wamelifurahia na wengi wanasubiri jambo la msingi wekezeni sasa katika elimu, ili wananchi waweze kuelewa namna ya kuzitumia vizuri fedha hizi kwa ajili ya manufaa na familia zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika suala la kiutawala, maeneo ya utawala, napenda kuomba sasa kwamba katika Jimbo langu pale Katoro ni mji mkubwa, kwa sasa hivi ni Mamlaka ya Mji Mdogo, naomba Serikali ipandishe hadhi Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro iwe Mamlaka ya Mji kutokana na hali halisi, kuna watu wengi, yani tunahitaji kwa kweli, kufanya mipango miji mahali pale. Kwa hiyo, naomba sana wakati unapo-wind up nipate kusikia namna ambavyo mtaweza kupandisha hadhi Mji wa Katoro kuwa Mamlaka ya Mji, ni Mamlaka ya Mji Mdogo kwa sasa. Kwa hiyo, niiombe Serikali iliangalie, ilitilie maanani suala hili kwa sababu tumekusudia kupeleka maendeleo kwa wananchi wenyewe tunapoongeza Wilaya au Halmashauri, nina uhakika kwamba, tunaweza kupeleka maendeleo kwa wananchi wenyewe ili waweze kupanga shughuli zao kwa maendeleo ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa miundombinu, barabara za Halmashauri nyingi hazipitiki, nichukue fursa hii kuiomba Serikali mwaka huu iwekeze fedha nyingi za kutosha kwa ajili ya kutengeneza barabara za vijijini. Nasema hivyo kwa sababu wananchi wanazalisha lakini usafirishaji unakuwa ni mgumu sana. Unakuta kati ya kata na kata hazipitiki vizuri. Naiomba Serikali ijitahidi kwa awamu hii, zile bajeti ambazo zimewekwa kwenye bajeti zake tuhakikishe fedha hizi zinafika kule kwenye Halmashauri, ili barabara ziweze kutengenezwa, suala la maji na katika huduma zote ni muhimu liweze kufanyiwa kazi inavyostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa ni kuhusu suala la afya. Nimeangalia katika bajeti ya Serikali, inaonesha jinsi ambavyo Serikali imejipanga kujenga vituo vya afya kwenye kila kata, kujenga zahanati kwenye kila kijiji; nalipongeza suala hilo vizuri kabisa, naiomba Serikali sasa katika yale iliyozungumza iweze kuyafanyia kazi. Nikiangalia katika jimbo langu, jimbo ambalo lina kata 22, kuna vituo vya afya vinne tu. Bado kazi ni kubwa sana ambapo Serikali inahitajika ifanye kazi ya ziada ilete fedha, ihamasishe na wananchi tuko tayari kufanya kazi pamoja na Serikali iliyoko madarakani kuhakikisha kwamba, tunapata maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, nikiamini kwamba mtaenda kuyafanyia kazi yale yote niliyoyazungumza.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti,asante sana kwa kunipa nafasi, ili na mimi niweze kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Nishati na Madini. Nichukue nafasi hii kwanza kabisa kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Busanda kwa kuniamini na kuendelea kunipa ridhaa na niwahakikishie kwamba nitaendelea kuwatumikia kwa uaminifu wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Wizara kwa ujumla kwa kazi kubwa wanayoifanya. Kikubwa zaidi nimepitia kitabu cha bajeti ambacho kimejieleza vizuri sana katika ila hatua, kwa hiyo, napenda kuipongeza sana Wizara kwamba wameweka mipango mizuri, cha msingi ninachoomba ni utekelezaji wa mipango hii ambayo wameiweka katika kitabu cha bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa umeme nimeona jinsi ambavyo ndani ya bajeti mmeelezea vizuri sana katika aya zote 45 mpaka 49 nimesoma, nimeona jinsi ambavyo Wizara imejipanga kupeleka umeme kabambe katika maeneo ya vijijini. Kupeleka umeme kwa kuhakikisha kwamba wanaangalia taasisi muhimu katika maeneo hasa ya vijijini, kwa hiyo, hilo nalipongeza sana naipongeza Wizara, niombe tu muhakikishe basi muweze kutekeleza kulingana na mipango yenu mliyoiweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini cha pili, katika bajeti hii nimeona pia kuna ongezeko kubwa sana la fedha za bajeti za umeme vijijini kutoka shilingi bilioni 357 mpaka shilingi bilioni 534, ongezeko la asilimia 50. Kwa hiyo, ninaona jinsi ambavyo Wizara kusema ukweli imejipanga kufanya kazi kubwa na nina uhakika kwamba kupitia bajeti hii ya mwaka 2016/2017 wananchi wengi wataweza kunufaika zaidi.
Niombe sasa kulingana na mipango ambayo tumeipeleka, kwa sababu mimi nimeenda katika Mkoa wangu kupitia Ofisi ya TANESCO tumeweza kubaini vijiji ambavyo havijafikiwa na umeme. Niombe sasa Serikali iweze kutekeleza kulingana na jinsi ambavyo wamepanga ili tuweze kuona wananchi wanaweza kunufaika zaidi na upatikanaji wa umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika jambo la sekta ya madini ni kwamba katika upande wa madini, nimeona pia jinsi ambavyo Serikali imejipanga katika kuhakikisha kwamba inasaidia wachimbaji wadogo wa madini. Imesema kwamba mtapeleka mitaji kwa ajili ya kuwawezesha wachimbaji wadogo, niiombe Serikali iweze kulifanyia kazi hili, ni kilio cha kila siku. Kwa hiyo ninaomba Serikali iweze kuendelea kuwekeza, imetenga kweli shilingi bilioni 6.6 ni fedha nyingi, niombe Serikali ihakikishe inalifanyia kazi suala hili kusaidia wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niko sehemu ambapo wachimbaji wadogo wako wengi sana na mara nyingi hili bado ni lalamiko kubwa kwa wachimbaji wanyonge wadogo wadogo. Kwa hiyo, niombe Serikali pia inapotekeleza majukumu yake, itushirikishe na sisi Wabunge ili tuone kwa sababu malalamiko Wabunge ndio tunaoletewa kila siku kwamba mbona sisi hatujapata mitaji, lakini kwenye utekelezaji tunaona jinsi ambavyo Serikali inafanya kazi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kule kwa wananchi hatuoni hayo mambo, kwa hiyo niombe Serikali safari hii hizo shilingi bilioni sita ilizotenga, ikumbuke pia na wachimbaji wadogo wadogo wa Mkoa wa Geita hasa kule busanda ambako nina wachimbaji wadogo wengi ambao wanajikimu kwa kupitia shughuli za uchimbaji wa madini.
Vilevile katika suala la madini nichukue nafasi hii kwa kweli kuishukuru Serikali, kumshukuru Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri wamefika Geita mara kadhaa. Kulikuwa na changamoto kubwa sana pale Nyarugusu STAMICO kwa mara ya kwanza katika bajeti ya mwaka huu, nimeona Serikali imezungumzia namna ambavyo inakwenda kutatua mgogoro huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na imesema kwamba katika mwaka 2016/2017 Serikali inaenda kumaliza hasa huu mgogoro na wananchi wataweza kupewa eneo la STAMICO. Jambo hili naipongeza Serikali na niombe utekelezaji sasa uweze kufanyika katika mwaka huu wa 2016/2017 na wananchi wana furaha kubwa sana kutokana na jambo hili kwa sababu imekuwa ni kilio cha muda mrefu. Miaka mitano iliyopita kila bajeti nilikuwa nikizungumzia suala hili. Kwa hiyo, mwaka huu mkitekeleza jambo hili, mimi nina uhakika wananchi wote wa eneo hilo la Busanda wataweza kunufaika, na sio tu wa Busanda kwa sababu masuala ya uchimbaji wanakuja watu kutoka sehemu mbalimbali na wanakuwa katika maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe Serikali katika hiyo aya ya 139 imezungumzia habari ya kuwapatia eneo la STAMICO watu wa Nyarugusu, ninaipongeza na naomba Serikali iweze kulifanyia utekelezaji suala hili ili wananchi waweze kufanya kazi zao sasa, waweze kufanya kazi na kunufaika zaidi katika kuwekeza katika shughuli za uchimbaji wa madini katika eneo hilo. Lakini vile vile Serikali iliahidi kwamba ingeweza kujenga kituo kikubwa sana cha wachimbaji wadogo eneo la Lwamugasa, jambo hili limekuwa ni la siku nyingi lakini katika bajeti nimeangalia Serikali inajenga vituo saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika maelezo nimeangalia Mkoa wangu haupo, niombe Serikali sasa iniambie wakati wa majumuisho, kwamba kituo cha Lwamugasa kimemezwa na nini hakipo tena na wala hakisikiki. Niombe muweze kuangalia bajeti zenu za nyuma na muhakikishe wananchi wa maeneo haya waweze kujengewa hicho kituo cha kuweza kuwasaidia wachimbaji wadogo wadogo. Hasa katika maeneo hayo ili waweze kunufaika na ruzuku, kwa ajili ya kununua zana mbalimbali za kufanyia kazi katika shughuli zao za uchimbaji wa madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba suala hilo liweze kufanyiwa kazi kwa kiwango kikubwa kwa sababu ni ahadi ya Serikali ya muda mrefu na ninyi wenyewe mliahidi, hatukuwa tumeomba lakini ninyi wenyewe mliweka kwenye utaratibu. Lakini vilevile kuna kituo mlianzisha pale Lwamugasa tulifanya uzinduzi wa Benki ya Dunia kwamba ingeweza kusaidia wachimbaji wadogo, tumezindua tu lakini sasa hakuna kunachoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba Serikali pia inipe majibu kwamba inasemaje kwa habari ya hicho kituo cha Lwamugasa, ambacho Benki ya Dunia ilikuwa imekubali kuweza kutoa fedha kwa ajili ya kusaidia wananchi wachimbaji wadogo katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niiombe Serikali iweze kuyazingatia hasa eneo la STAMICO Nyarugusu ambalo limekuwa ni kilio cha muda mrefu. Waheshimiwa Marais waliopita wamlizungumzia na kuahidi sana na Mheshimiwa Rais Magufuli alivyokuwa anafanya kampeini zake alisema suala hili limekwisha. Kwa hiyo naomba suala hili liishe lifike mwisho, ili wananchi waweze kufanya kazi zao sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nilikuwa naomba kuzungumzia suala la afya katika sehemu za migodi. Ni kwamba nilikwenda workshop moja wiki iliyopita ya SADC, kuna suala la afya ambalo ni la msingi sana nilikuwa naomba Wizara iweze kulifanyia utafiti, inaonesha kwamba watu wanaoishi katika maeneo ya shuguli za uchimbaji wa dhahabu kuna vumbi la madini ya silica ambalo mara nyingi linasababisha ugonjwa unaitwa silicosis lakini vilevile inasababisha TB.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi niliogopa sana na kushtuka, kwa hiyo, niombe Serikali iweze kufanyia kazi ili wananchi wetu wasije wakaathirika na jambo hili. Kwa hiyo kupitia Wizara ya Nishati na Madini na Wizara ya Afya mjaribu kufanya utafiti wa kutosha ili kuweza kubaini kama kweli hiyo silica ina-affect vipi wananchi wetu katika maeneo ambayo yako karibu na uchimbaji wa dhahabu. Ninaomba suala hili Serikali ilifanyie kazi kwa karibu ili tusije tukajikuta wananchi wetu wanathirika kwa kiwango kikubwa kutokana na uwepo wa silica, ambao pengine wanakuwa wanaathirika na TB bila kujua na hatimaye baadae tukakosa nguvu ya Taifa, kwa sababu watu wataweza kuangamia kutokana na ugonjwa huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkifanya hiyo tathimini na kuweza kuitolea ufafanuzi pengine itatuwezesha sisi pamoja na wananchi kwa ujumla kuweza kujua tatizo na kuweza kutafuta namna ya kujikinga ili kuweza kuondokana na kuweza kupata madhara hasa ya ugonjwa wa TB na magonjwa mengine ambayo yataweza kupunguza nguvu kazi ya Taifa kwa sababu wakiugua hawawezi kufanya kazi zote na pengine uchumi wa Taifa utaweza kutumika pia kwa ajili ya kupeleka fedha katika matibabu ya TB na vitu vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Serikali ilifanyie kazi hilo kwa sababu katika machimbo ya sehemu za Afrika Kusini inaonesha jambo hili limeweza ku-affect watu wengi na sasa hivi ni kilio kikubwa na linazungumziwa sana katika nchi za Afrika ya Kusini. Sisi nchi ya Tanzania kama ni mojawapo ni vizuri Serikali iweze kuangalia suala hili kwa umakini, kikubwa zaidi kuweza ku-protect watu wetu ambao wataweza kuathirika na jambo hili kiafya.
Lakini vilevile na wale wanaofanya kazi migodini, mimi najua hawa wanaofanya kazi migodini wengi mwisho wa siku baada ya muda wanaathirika. Kwa hiyo Serikali ifanyie utafiti kwa watu wanaofanya migodini, ili wasije wakafika mahali sasa hata maisha yao yakaathirika na wakashindwa kufanya kazi zingine baadae baada ya kufanya kazi kwa muda fulani mgodini, baadae wanaathirika kiafya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema mambo hayo, niombe tu Serikali iendelee kuwekeza zaidi na napenda kushukuru naunga mkono hoja, nikiamini kwamba Serikali inaenda kufanyia kazi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. LOLESIA J. M. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kupongeza kwa hotuba nzuri iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri. Pia napongeza kwa kazi inayofanyika ndani ya Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto yangu ipo katika mipaka kati ya vijiji vinavyozunguka misitu ya hifadhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Jimbo la Busanda katika kijiji cha Saragulwa; kuna mgogoro wa mara kwa mara baina ya hifadhi ya msitu wa Geita na kijiji cha Saragulwa. Mgogoro huu unasababisha kero kubwa sana kwa wananchi waishio katika kijiji kutokana na adha za kutaka kuchomewa nyumba na kufyeka mazao ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali kupitia Wizara ione umuhimu wa kuangalia upya mipaka yake na kutoa elimu kwa wananchi juu ya mipaka hiyo na kuwaeleza bayana adhabu zinazotokana na kukiuka mipaka iliyowekwa.
Kijiji cha Saragulwa kimekuwepo tangu Azimio la Vijiji vya Ujamaa na kinatambulika TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni juu ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kutokuwa na Bodi. Hii ni changamoto kubwa katika utendaji wa shirika na tunakosa mapato kwa kutokuwa na Bodi. Nashauri Serikali ifanye utaratibu wa kupata Bodi mpya haraka iwezekanavyo ili kunusuru hasara tunayoipata kwa kukosa mapato kwa wakati (concession fees).
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, naipongeza TANAPA kwa kutoa madawati kwa Wilaya mbalimbali hapa nchini. Hata hivyo, naomba TANAPA ituangalie Wilaya zenye changamoto kubwa ya watoto kukaa chini. Natumia fursa hii kuiomba TANAPA mchango wa madawati katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita. Tuna changamoto kubwa sana, tunaomba support.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, mwisho liko tatizo la mamba katika vijiji vinavyozunguka Ziwa Victoria hasa katika vijiji vya Kasangalwa, Kageye, Bukando na Chankorongo. Mara kwa mara kunatokea matukio ya wananchi kuliwa na mamba. Naiomba Serikali ilifanyie utatuzi kwa haraka kwa sababu tunapoteza nguvu kazi ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuwa Wizara itayafanyia kazi matatizo yote niliyoyawasilisha. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri ambayo ameiwasilisha mbele zetu siku hii ya leo. Wote tunafahamu kwamba maji ni tatizo kubwa sana hasa katika vijiji vyetu. Nikiangalia katika Jimbo la Busanda, kero kubwa iliyopo kule ni maji. Nikiangalia kwenye Vijiji na Miji ambayo inachipukia naona jinsi ambavyo wananchi wanahangaika sana kwa suala la maji. Vile vile kwenye vituo vya afya, zahanati, shuleni za msingi, changamoto ni kubwa sana ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kuona changamoto hii kubwa ya maji, ni kweli kwamba kuna miradi mbalimbali ambayo ipo hasa hasa katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, kuna Mradi wa Maji wa Benki ya Dunia ambapo ni vijiji kumi na kati ya vijiji kumi, vijiji kama saba viko katika Jimbo la Busanda. Nasikitika kwamba mradi huu umekuwa ni wa muda mrefu sana, yaani haukamiliki, unaendelea tu kila mwaka, lakini hatuoni kukamilika kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitumie fursa hii sasa kuiomba Wizara, Mheshimiwa Waziri wa Maji, hebu sasa mradi huu wa Benki ya Dunia katika vijji saba ambapo katika Jimbo langu mradi uko katika Kata ya Nyakagomba na vijiji vyake ambavyo vimezunguka kata hiyo; vile vile Katoro na Kata ya Nyamigota. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, kwamba sasa ifike mahali mradi huu ukamilike ili wananchi waweze kunufaika na mradi huu wa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokuwa nikiangalia katika kitabu cha bajeti, nimeuangalia huu mradi kwa kweli sijaona. Sasa sijui fedha hizo zimejificha wapi? Naombe sasa nihakikishiwe na Mheshimiwa Waziri kwamba mradi huu wa Benki ya Dunia unakamilika ili wananchi waweze kunufaika na huduma ya maji katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kumekuwa na ahadi ambayo ni ya muda mrefu ya mradi mkubwa wa maji kutoka Chankorongo, kutoka Ziwa Victoria. Mradi huu unakusudia kupeleka maji katika maeneo mbalimbali hasa katika Tarafa ya Butundwe ambapo ina miji mingi kama Mji wa Katoro na Buselesele pale ambapo kuna population kubwa, watu ni wengi; wanafika watu zaidi ya 100,000. Kwa kweli mahitaji ya maji ni makubwa sana. Tukiamua kukamilisha mradi huu wa Chankorongo, nina uhakika tatizo la maji kwenye Jimbo la Busanda litakuwa ni mwisho.
Mheshimiwa Mweyekiti, kwa hiyo, naishauri Serikali sasa kupitia Wizara ya Maji, ihakikishe mradi huu wa Chankorongo unafanyiwa kazi. Nimeangalia kwenye kitabu cha bajeti sijaona mradi huu, lakini nitumie fursa hii kuomba sasa Wizara iweke msisitizo wa kuuwezesha huu mradi wa Chankorongo uweze kufanyiwa kazi kwa ajili ya manufaa ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nilipokuwa nikisoma kitabu cha bajeti, nimeona kuna miradi ya quick wins ambapo pale Katoro na Buselesele wametenga shilingi milioni 500. Ni kweli shilingi milioni 500 tunashukuru kwamba zimetengwa, lakini sina uhakika kama hizi fedha mmepanga kufanyia nini pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusisitiza kwamba hizo shilingi milioni 500 na pengine zingeongezwa fedha zaidi, ufanyike ule mradi wa Chankorongo ili kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria, tutaweza kumaliza kabisa tatizo hili; lakini kwamba shilingi milioni 500 tunachimba visima, kweli visima vinachimbwa, lakini havitoshelezi kutokana na wingi wa watu katika eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali sasa iangalie mradi wa Chankorongo wa kuvuta maji Ziwa Victoria. Nasema hivyo kwa sababu Jimbo la Busanda na Geita kwa ujumla tumezungukwa na Ziwa Victoria. Ni aibu pia kuona kwamba hatuna maji na wananchi wanahangaika, akina mama wanahangaika, hakuna maji. Ifike mahali sasa Serikali iwekeze kama ilivyopeleka maji kule Shinyanga na maeneo mengine ya Tabora kutoka Ziwa Victoria, sisi tumezungukwa na Ziwa, moja kwa moja. Yaani tunagusa Ziwa Victoria lakini hatuna maji. Kwa hiyo, naomba Serikali basi iangalie uwezekano wa kuvuta maji Ziwa Victoria ili wananchi waweze kunufaika na rasilimali maji ambayo imetuzunguka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kama nilivyosema kwamba changamoto ya maji ni kubwa, lakini napenda kuishauri Serikali kwamba tuanzishe hata Wakala wa Maji Vijijini kama ambavyo kuna REA kwenye umeme. Tukianzisha pia Wakala wa Maji Vijijini kama vile ilivyo REA nina uhakika kwamba changamoto ya maji itaweza kutatuliwa. Tunaona jinsi ambavyo REA inafanya kazi zake vizuri na tunaona kabisa na impact na vijiji vinapata umeme wa uhakika. Kwa hiyo, tukianzisha Wakala wa Maji Vijijini, nina uhakika pia tutaweza kutatua changamoto hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuongezea hapo, naomba sasa kwa sababu kumekuwa na tozo kwenye REA, sh. 50/= kwenye mafuta, kwa hiyo, naomba ile tozo iongezeke ifike sh. 100/= kama ambavyo wenzangu wamesema ili tuone kabisa umuhimu wa tatizo la maji, maana ni tatizo sugu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia hapo wachangiaji walioomba tu kwenye maji humu Bungeni; yaani kila mtu ni kilio kikubwa, kila mtu anataka achangie hii hoja ya maji, kwa sababu ya umuhimu wake. Kwa hiyo, naiomba Serikali hebu ilifanyie kazi suala hili, ikiwezekana tuongeze tozo iwe sh. 100 kwenye mafuta ili kuona kwamba suala la maji tunalipa kipaumbele kwa uhakika ili wananchi waweze kunufaika, kwa sababu tunajua maji ni uhai, hatuwezi kuwa na viwanda bila kuwa na maji na katika hospitali zetu tunahitaji maji, nasi wenyewe wananchi tunahitaji maji safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kama alivyotembelea Mji wa Geita tukazindua maji pale tarehe 5 Januari, namwomba Mheshimiwa Waziri hebu apange basi aje ziara na Jimbo la Busanda aone jinsi ambavyo watu wanahangaika na suala la maji. Mheshimiwa Waziri najua akifika pale na kuona changamoto hiyo, nina uhakika kwamba tutaweza kupata sulution ya changamoto hizi ambazo ziko katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu katika Jimbo langu kuna centers nyingi ambazo zina watu wengi kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini. Watu wanashughulika na mambo ya madini, kwa hiyo, watu ni wengi, population ni kubwa sana. Mara nyingi kutokana na shughuli za madini, wakati mwingine kuna uchafuzi pia wa vyanzo vya maji na kwa sababu hiyo tunaomba Serikali sasa iangalie uwezekano wa kuongeza bidii kuwezesha ili tuweze kupata maji ya uhakika. Waweke visima na ikiwezekana kuvuta maji Ziwa Victoria; nina uhakika tutaweza ku-solve tatizo la maji katika Jimbo la Busanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naiomba Serikali iweze kuanzisha Wakala wa Maji. Hili litaweza kutusaidia tuongeze tozo ili kuhakikisha kwamba tatizo la maji linakwisha kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, nikizingatia kwamba Waziri aweze kutekeleza kulingana na bajeti ambayo amepewa. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika bajeti hii. Nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Naibu Waziri wa Fedha kwa hotuba nzuri ambayo waliwasilisha hapa Bungeni kuhusiana na suala zima la uchumi na masuala ya fedha kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kwa suala la umaskini. Katika hotuba hii nimeona jinsi ambavyo amezungumzia habari ya hali ya umaskini hasa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ambapo umezungumzia kuna Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Kigoma na Singida. Kwa hiyo ni changamoto ambayo mimi binafsi ninaikubali kwa sababu kutokana na hali halisi ya uchumi na hali halisi ya maisha wananchi walio katika eneo hilo. Kwa hiyo, niombe sasa, nilivyokuwa nikiangalia bajeti kwa ujumla sijaweza kuona jinsi ambavyo Serikali imejipanga kuweza kufanya mabadiliko ya kiuchumi katika maeneo haya ambapo yameonekana kwamba yako nyuma sana kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda kuishauri Serikali kwamba kwa sababu tafiti hizi zimefanyika tangu mwaka 2012; kwa hiyo, taarifa hii inajulikana kabisa kwamba mikoa hiyo iko katika hali mbaya ya kiuchumi yaani wana umaskini uliokithiri.
Kwa hiyo, naiomba Serikali sasa iwekeze nguvu katika mikoa hii ili kuweza kunusuru maisha ya wananchi, hasa kiuchumi. Ninasema hivyo kwa sababu tukiangalia wananchi katika maeneo haya wanategemea shughuli mbalimbali za kiuchumi, wanategemea kilimo, wanategemea uvuvi na kuna shughuli nyingi sana za kiuchumi. Kwa hiyo, Serikali iangalie namna sasa ya kuwekeza katika shughuli hizi za kiuchumi ili kuwasaidia wananchi waweze kuondokana na hali ya umasikini iliyokithiri katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiangalia katika Mkoa wangu wa Geita, shughuli za kiuchumi ambazo zinafanyika kwenye mkoa huu ni kilimo, uvuvi, lakini sasa katika uvuvi hakuna jitihada za dhati katika Serikali za kuweza kuwasaidia wavuvi. Wanafanya shughuli hizi za kiuvuvi bila kupata msaada wowote wa kuwawezesha wavuvi ili waweze kujikwamua katika hali ya umasikini waliyonayo. Kwa hiyo, niombe Serikali iweze kutoka na Mpango Mkakati kwa ajili ya kuwasaidia wananchi ili waweze kuondokana na hali ya umasikini wa kipato cha sasa hivi na waweze kujikwamua. Kwa sababu tunakoelekea Serikali tumesema kwamba tunahitaji Tanzania ipige hatua ili tuwe na uchumi wa kati, sasa hatuwezi kufikia kwenye uchumi wa kati bila kuweza kuwasaidia wananchi katika shughuli mbalimbali za kiuchumi walizonazo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikizungumzia katika masuala ya uchimbaji wa madini, naomba pia Serikali iwekeze nguvu katika eneo hilo kwa sababu eneo hilo pia watu wanajishughulisha na shughuli hizo za uchimbaji wa madini. Kweli mmetenga shilingi milioni 900 lakini niombe Serikali ikiwezekana iongeze zaidi ya hapo, vilevile iweze kuwawezesha hata kielimu wananchi ili waweze kufanya shughuli hizi kwa ufanisi wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika upande wa afya, inaonyesha kabisa kwamba kweli katika upande wa afya bado changamoto ni kubwa sana hasa katika maeneo ya vijijini. Sera ya Taifa imezungumzia kwamba katika Mkoa tuwe na hospitali ya rufaa, katika Wilaya tuwe na Hospitali ya Wilaya, katika kata tuwe na kituo cha afya, vijijini tuwe na zahanati. Lakini hali halisi iliyoko kwa sasa inaonyesha jinsi ambavyo changamoto bado ni kubwa sana, unakuta vijiji vingi havina zahanati na ndiyo maana sasa katika harakati ya kuweza kupunguza vifo, hasa kwa watoto pamoja na akina mama wajawazito bado takwimu zinaonyesha kuwa ni juu sana.
Kwa hiyo, niiombe Serikali iangalie uwezekano mkubwa wa kuelekeza nguvu zaidi katika sekta hii ya afya ili kupunguza uwezekano wa vifo vya watoto pamoja na akina mama wajawazito. Kwa sababu haiwezekani unakuta wanawake, wanasafiri kwenda umbali mrefu sana kwenda kufuata huduma za afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hivyo katika zahanati hatuna wataalam wa kutosha, katika vituo vya afya wataalam wa afya ni wachache. Kwa hiyo, niiombe Serikali iangalie kwa kina katika mpango huu kuweza kuona kwamba basi iweze kuangalia uwezekano wa kuwasaidia kuongeza zaidi kasi na fedha nyingi kwa ajili ya kuwezesha kuweza kujenga zahanati za kutosha lakini vilevile kupeleka vifaa tiba katika vituo vya afya, zahanati, Hospitali za Wilaya na Mikoa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika mikoa mipya, natoka katika mkoa mpya, tunaomba Serikali iangalie mikoa hii. Kwa sababu ni mikoa mipya hatuna hospitali za rufaa, hata zile zilizopo ambazo zimetengwa kwa sasa bado zina changamoto kubwa sana, kwa hiyo niombe Serikali katika bajeti hizi iangalie uwezekano wa kuangalia mikoa hii kwa kina iweze kuhakikisha zinapata huduma, zinajenga hospitali hizi ili kuwawezesha wananchi katika mikoa hii kuweza kupata huduma iliyo bora. Lakini vilevile kuongeza vifaa tiba pamoja na wataalam ambao ni madaktari na watu muhimu ambao wanaweza wakasaidia wananchi. Tuna upungufu mkubwa sana wa wahudumu wa afya katika zahanati na katika hospitali hizi, mara nyingi watu wanakwenda kupata huduma, lakini wanachukua muda mrefu kuweza kupewa huduma kwa sababu tuna upungufu wa wataalamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niiombe Wizara inayohusika pia pamoja na Serikali kwa ujumla, hebu tuangalie namna ya kutatua changamoto hasa katika sekta ya afya ili wananchi waweze kupata huduma safi; mtu akiwa na afya atakuwa na uwezo wa kufanya kazi zake vizuri, usipokuwa na afya hata kazi huwezi ukafanya vizuri. Kwa hiyo, niiombe Serikali katika mpango wake huu iangalie namna ya kuboresha huduma za afya ili kuwawezesha wananchi kuweza kupata huduma bora, safi na hatimaye basi tuweze kuwa na afya njema hasa kwa wananchi wetu walioko vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika upande wa elimu, naona kweli kabisa Serikali imetenga fedha nyingi kwa upande wa elimu. Naomba hasa katika mikopo kwa wanafunzi, kuna wanafunzi wengi sana wanaotokea vijijini ambao hawapati mikopo hii. Namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Elimu kwa hatua anazozifanya kwa sasa kuweza kuiangalia sekta hii kwa undani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Naunga mkono hoja, naomba Serikali iweze kuifanyia kazi.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana kwa kunipa fursa ili niweze kuchangia katika hotuba iliyoko mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa kabisa ambacho nilitaka kuongelea ni kuhusiana na watu kukaimu kwenye Halmashauri zilizo nyingi ikiwemo Halmashauri yetu ya Wilaya ya Geita na mfano kwa sababu niko kwenye Halmashauri tangu miaka mitano iliyopita kwa hiyo ninaelewa hali halisi katika Halmashauri pengine na Halmashauri nyingine pia tatizo lipo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo sasa niombe tu Serikali suala hili iweze kuwachukulia kwa uzito sana, unakuta kwamba vijiji vingi kwa mfano katika jimbo langu kule wengi yani watendaji wa kata wanakaimu, sasa mtu anapokaimu atawezaje kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi? (Makofi)
Kwa hiyo nitumie fursa hii kuiomba Serikali ihakikishe iangalie namna kwenye vijiji ambako ndiko ambako tunapeleka shughuli za utekelezaji wa majukumu ya Halmashauri kwa sababu miradi yote inatekelezwa kwenye vijiji au kwenye kata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Serikali iangalie utaratibu mzuri kuona kwamba watu wanaokaimu basi waajiri moja kwa moja ili watu waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa. Wakifanya hivyo pengine itapunguzwa hata matumizi mabaya ya fedha ya Serikali, maana sasa kama mtu anakaimu anakuwa hana pia hata na uchungu maana hana uhakika na ile ajira yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ninaiunga mkono kabisa Kamati ambayo imelizungumzia kwamba watu wengi wanaokaimu katika ngazi ya Halmashauri, lakini vilevile kwenye kata na vijiji hili suala liangaliwe kwa umakini ili Serikali ione kwamba ni jambo la msingi kabisa kwamba watu wanapata, wanapewa fursa kama ni kukaimu basi iwe ni kwa muda mfupi baada ya hapo wapewe ajira za kudumu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ni ile asilimia kumi ya mfuko kwa ajili ya wanawake pamoja na vijana. Katika Halmashauri zilizo nyingi jambo hili halitekelezeki, unakuta kwamba Halmashauri hizi zinafanya shughuli mbalimbali za maendeleo lakini wanapopata mapato yao hawawezi kutenga hizi fedha asilimia kumi kwa ajili ya akina mama pamoja na vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe kwamba basi suala hili pia litiliwe mkazo kuwepo na usimamizi muhimu ili kuona kwamba sera na taratibu na sheria za nchi zinafanyiwa kazi na zinatekelezwa kulingana na inavyotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuhusu udhibiti katika usimamizi wa mambo ya udhibiti wa ndani. Ina maana kwamba kama hatutaimarisha usimamizi wa ndani ina maana kwamba katika Halmashauri miradi mingi itakuwa inatekelezwa pengine chini ya viwango, lakini tukiimarisha udhibiti wa ndani hasa kwenye Halmashauri zetu mimi nina uhakika kwamba hata zile changamoto ndogo ndogo za fedha za miradi pengine kutekelezwa chini ya kiwango tutaweza kupunguza changamoto hii. (Makofi)
Mheshimiwa naibu Spika, kwa hiyo nitumie fursa hii kuiomba Serikali iweze kuimarisha kabisa vizuri tuweke wasimamizi ambao watakuwa na maslahi kwa ajili ya wananchi kuweza kuona kwamba kweli wanasimamia na kukagua, lakini pia kuishauri Serikali kupitia Halmashauri kuona kwamba kuna umuhimu mkubwa wa kuweza kufanya shughuli za maendeleo kulingana na fedha ambazo zinatengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna suala lingine la ruzuku kutokupelekwa. Ni kweli kwamba kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kulikuwa na changamoto kubwa sana kwamba fedha tulikuwa tunatenga ndani ya Bunge, lakini mwaka unapita zilizokuwa zimepelekwa ni kiasi kidogo pengine chini ya asilimia 100 kwa hiyo zinakuwa chini pengine asilimia 60 au asilimia 50 jambo ambalo lilikuwa linapunguza pia utekelezaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nitumie fursa hii kuiomba Serikali iangalie sasa katika mwaka huu, hii ni awamu mpya na nimeona jinsi ambavyo tayari wamekwisha kuanza kufanya utekelezaji katika miradi mbalimbali kwa mfano kupeleka elimu bure kule wanapeleka zile fedha kila mwezi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe basi hata katika bajeti ya mwaka huu tumetenga asilimia 40 ya bajeti iende kwenye shughuli za maendeleo. Serikali ihakikishe inatekeleza suala hili, hata mwisho wa mwaka tutaweza kuona jinsi ambavyo miradi mbalimbali ya maendeleo imetekelezeka kule vijijini kwa sababu Serikali imeweza kutekeleza wajibu wake hasa Wizara ya Fedha ambayo inahitajika kuweza kufanya utaratibu huu vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona jinsi ambavyo kuna mifano ya baadhi ya nchi ambao bajeti ya maendeleo ni zaidi ya asilimia 50, kwa mfano tu hata wenzetu hapa Kenya bajeti ya maendeleo inakuwa ni zaidi ya asilimia 50 na bajeti kubwa wanategemea mapato ya ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuishauri Serikali pia iangalie namna bora kwamba tuimarishe ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuwezesha angalau asilimia 50 ya fedha za ndani ziwe zinapelekwa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi. Tunashuhudia kabisa kwamba fedha nyingi za makusanyo zinatumika kwa ajili ya kulipa mishahara tu na gharama aina mbalimbali. Lakini kumbe Serikali iangalie utaratibu mzuri angalau yale makusanyo tukiweza yani angalau zaidi ya asilimia 50 zikaenda kwenye maendeleo, wananchi wetu wataweza kunufaika zaidi hasa walioko vijijini ambao wanazo changamoto nyingi sana katika huduma za jamii kwa mfano afya, elimu na masuala mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na changamoto hizi niungane tu pamoja na Kamati ambazo zimewasilisha hoja hii kuona kwamba Serikali lazima katika masuala haya yote iangalie namna ya kuyatafutia ufumbuzi ili wananchi waweze kunufaika na rasilimali ambazo Mungu ametujalia katika Taifa letu la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wote ni mashahidi nchi ya Tanzania tumejaliwa kuwa na rasilimali mbalimbali, madini pamoja na mazingira mazuri ambapo yanaruhusu watalii kuja katika nchi hii. Kusema ukweli tukijipanga katika ukusanyaji wa kodi tayari imekwisha kuanza taunaona impact tayari tunaona jinsi ambavyo Serikali inakusanya kodi vizuri kabisa naunga mkono kabisa ukusanyaji wa kodi na niendelee kusisitiza kabisa kwamba tujipange zaidi kwa sababu badi kuna watu pia ambao wanaendelea kukwepa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nichukue fursa hii kuiomba Serikali iendelee kuongeza ili makusanyo yawe makubwa zaidi kwa sababu kulingana na rasilimali ambazo Mungu ametujalia katika nchi yetu ya Tanzania. Kupitia mapato hayo nina uhakika nchi yetu sasa tutaweza kupata manufaa makubwa hasa katika wananchi wetu ambao tunahitaji kupeleka huduma kwa wananchi ili wananchi waweze kunufaika na huduma hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi walio wengi vijijini wana changamoto kubwa ya maisha yao. Vilevile tunashukuru kwa ajili ya TASAF ambayo imeanza kupeleka huduma kwa wananchi. Lakini niombe sasa pia kupitia TASAF tuangalie wale wahitaji kabisa, kwa mfano, wanawake walio wengi vijijini ambao wanalea watoto yatima lakini vilevile wana maisha magumu, kwa hiyo, tuangalie pia hizi fedha zinapokwenda za TASAF tuangalie kweli wale wenye uhitaji hasa walioko katika mazingira magumu zaidi vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nitumie sasa fursa hii kushukuru sana na kuomba Serikali iweze kuyazingatia yale ambayo Kamati imeweza kuyasemea ili kwamba basi wakishayafanyia kazi ninauhakika kwamba suala la maendeleo katika Taifa letu yataweza kuonekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili
na mimi niweze kuchangia katika hotuba ya Kamati ya Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuunga mkono hoja ya Kamati inayozungumzia
habari ya wananchi kupewa maeneo ya uchimbaji, hasa katika eneo la STAMICO. STAMICO
kulingana na maelezo, Serikali imeliteua Shirika la STAMICO kwa ajili ya kusimamia shughuli za
madini kwa ujumla wake pamoja na kuwawezesha wachimbaji wadogo wadogo nchini kwa
ujumla. Lakini kwa hali iliyopo sasa tunaona jinsi ambavyo STAMICO imeshindwa kufanya kazi
yake vizuri. Kwa hiyo, mimi naishauri Serikali iweze kuangalia namna bora ya kuweza kuiwezesha
hii STAMICO ili iweze kutekeleza majukumu yake vizuri kwa ajili ya manufaa ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiangalia eneo moja la STAMICO ambapo imechukua
baadhi ya migodi; katika Mkoa wa Geita kuna mgodi ambao unaitwa Bacliff. Ni muda, tangu
mwaka 2011 mgodi huu umechukuliwa, wameingia ubia na kampuni nyingine ya kutoka nje
inaitwa royalty lakini tangu wamechukua 2011 mpaka sasa hatuoni ufanisi wowote, hatuoni kazi
yoyote inayoendelea ingawaje kwa hali ya kawaida kabisa tunaona wananchi wa kawaida
wanaona shughuli mbalimbali zinaendelea, uchimbaji ukiendelea. Kwa hiyo hatuelewi kitu
chochote hatuoni faida yoyote ambayo kwa mkataba huu imeweza kulinufaisha taifa na
wananchi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na kwasababu hiyo basi nilikuwa naomba Serikali kupitia
STAMICO, iangalie namna ya kuiboresha hii taasisi ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi kwani
kwa sasa hivi tunaona inafanya kazi zake tofauti yaani hatuoni tija katika shirika hili ambalo
Serikali imewekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi nyingine ya STAMICO ni kuangalia namna ya
kuwawezesha wachimbaji wadogo wadogo ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi. Lakini
katika suala hili ninaona jinsi ambavyo STAMICO bado inahitaji kujipanga zaidi kwani wapo
wachimbaji wadogo wadogo wengi sana ambao hawafanyi kazi kwa ufanisi zaidi kutokana na kwamba STAMICO bado haijaingia zaidi katika kuwawezesha. Kwa sababu hiyo sasa naiunga
mkono hoja ya Kamati kwa kuona kwamba STAMICO inabidi ijipange vizuri ili ione namna bora
ya kuweza kuwasaidia wachimbaji wadogo ili waweze kuchangia katika Pato la Taifa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. LOLESIA J. M. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kutoa pongezi kwa Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla kwa kazi kubwa inayofanyika katika Taifa letu. Wananchi wa Tanzania wanayo imani na matumaini
makubwa sana kwa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba hii napenda kuchangia kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwezeshaji wananchi kiuchumi katika eneo hili napenda kuishauri na kutoa msisitizo mkubwa juu ya ahadi ya Rais ya kupeleka milioni hamsini kwa kila kijiji. Serikali katika bajeti ya mwaka 2017/2018 ihakikishe inatenga fedha hizo ili utekelezaji wa ahadi hii uanze kwani wananchi wanategemea fedha hizi katika kuinua uchumi wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sekta ya Madini kazi inayofanyika ni njema hasa utoaji wa ruzuku kwa ajili ya kuimarisha shughuli za ugani. Kwenye hotuba maeneo
yaliyotengwa Mkoani Geita ni Msasa na Matabe tu. Maeneo haya hayatoshi ukilinganisha na mahitaji makubwa yaliyopo hasa kwa wachimbaji wadogo. Kilio kikubwa ni maeneo ya uchimbaji hasa eneo la STAMICO ambalo ni kero ya muda
mrefu. Uwekezaji unaofanyika STAMICO hauna tija kwa Taifa, hivyo, naomba Serikali itazame upya mikataba hii.
Ikiwezekana wananchi (wachimbaji wadogo) wapewe eneo hili la STAMICO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa ahadi ya Rais ya kujenga kilomita 10 za lami katika Mji Mdogo wa Katoro; naomba ahadi hizi za Rais ziangaliwe na zifanyiwe mkakati wa utekelezaji ikiwemo barabara ya Kahama – Bukoli – Geita ahadi ya Rais Awamu ya Nne Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete. Hivyo ili wananchi waiamini Serikali yao naomba ahadi hizi zifanyiwe kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. LOLESIA J.M. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Serikali na Wizara ya ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kazi nzuri inayofanyika katika Taifa letu hasa katika ujenzi wa barabara na reli. Katika hotuba nimeona jinsi ambavyo Serikali imepanga kuanza rasmi ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Geita – Bukoli
– Kahama. Napongeza kwa mpango huo mzuri kwani utaongeza na kuimarisha uchumi kwa Mikoa ya Geita na Shinyanga. Vile vile nashukuru kwa kilomita moja ya lami kwa barabara ya Geita – Bukombe. Pamoja na shukrani hizo ningependa kupata ufafanuzi, ni lini ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kilomita 10 za lami katika mamlaka ya Mji mdogo wa Katoro/Buserere itaanza kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni upandishwaji hadhi wa barabara ya Katoro – Kamena – Mwingiro. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kipindi kirefu sasa tumeomba barabara ya Katoro – Kamena – Mwingiro, ipandishwe hadhi kuwa barabara ya Mkoa. Mapendekezo hayo yamepitishwa katika ngazi zote kuanzia kwenye Baraza la Madiwani pamoja na DCC. Nilipoangalia kwenye bajeti ya 2017/2018 sijaona hatua yoyote ya Wizara katika utekelezaji wa ombi. Hivyo, napenda kujua ni lini sasa barabara ya Katoro – Kamena – Mwingiro itapandishwa hadhi kuwa barabara ya Mkoa? Barabara hii ni kiunganishi muhimu sana kati ya Wilaya ya Geita na Wilaya ya Nyang’hwale na kwa msingi huo ikiboreshwa (ikipandishwa hadhi) itasaidia sana kuimarisha uchumi ndani ya Mkoa wa Geita. Kwa sababu hiyo, nashauri Serikali kupitia Wizara ilichukue ombi letu na kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naunga mkono hoja.

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia Wizara muhimu kabisa Wizara ya Afya.

Kwanza nianze kwa kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya ndani ya Taifa letu hasa katika suala la maendeleo kwa ujumla. Wote tunaona kazi inayofanyika ndani ya nchi yetu kwa kipindi kifupi cha mwaka mmoja na tunaona mambo makubwa yanafanyika kwa namna ya kipekee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu kwa kutupatia gari la wagonjwa katika Kituo cha Afya Katoro. Napenda kutoa salamu hizi kutoka kwa wananchi wa Jimbo la Busanda hasa Katoro, salamu hizi kwa kweli wamekushukuru na wamekupongeza wamefurahia sana na wanasema hakika vifo vya akinamama vitakwisha sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri Kigwangalla, kupitia wataalam wa taasisi ya AMREF walikuja kuzindua mradi mkubwa sana wa kuweza kuboresha huduma za afya katika Kituo cha Afya Chikobe, Zahanati ya Nyamalimbe, Zahanati ya Rwamgwasa pamoja na Kituo cha Afya cha Kashishi. Kwa hiyo, kipekee nitumie fursa hii kushukuru sana AMREF kwa kazi kubwa kuweza kuungana pamoja na Serikali katika kuboresha huduma hizi kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nichukue nafasi hii kuwashukuru GGM kwa kuweza kujenga mochwari pale katika Kituo cha Afya Katoro. Hakika ushirikiano huu pamoja na Serikali yetu inaonesha jinsi ambayo tutaweza kutatua changamoto mbalimbali za afya katika sehemu mbalimbali katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo, napenda kuzungumzia suala la watumishi. Katika sekta ya afya kweli kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi, nikiangalia katika Halmashauri yangu ya Wilaya ya Geita kuna upungufu mkubwa sana, mahitaji ni watumishi 824, waliopo ni watumishi 345, kwa hiyo upungufu ni mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kwa kuwa Serikali inakusudia kutoa ajira iangalie upungufu huu katika Halmashauri ya Wilaya yangu ya Geita, ndiyo maana kunatokea hata hivi vifo, vilevile kunatokea changamoto mbalimbali kwa sababu kuna upungufu mkubwa sana wa wataalam wa afya hasa katika sehemu za vijijini ambapo kunakuwa na upungufu mkubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimesoma hii bajeti ambayo Mheshimiwa Waziri ameiwasilisha, kipekee sijaweza kuona ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita. Ninaomba katika majumuisho Mheshimiwa Waziri uweze kutueleza wananchi wa Geita kwamba kuna mpango gani sasa wa kuanzisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa katika Mkoa wa Geita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hivyo kwa sababu hospitali ambayo sasa hivi imepewa hadhi kuwa ya rufaa ni Hospitali ya Wilaya ya Geita na sababu hiyo hatuna kabisa hospitali ya Wilaya kwa sasa. Tunaomba Serikali ione umuhimu sasa wa kuanzisha hospitali ya Mkoa ili kurahisisha huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Geita. Kumbuka Mkoa wa Geita tuna watu wengi sana zaidi ya milioni moja, kwa sababu hiyo tunahitaji huduma. Nichukue fursa hii kumuomba Mheshimiwa Waziri muangalie uwezekano wa kipaumbele katika kuhakikisha kwamba tunapata Hospitali ya Mkoa wa Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika suala la mama na mtoto, nilikuwa nikiangalia bajeti, ninapenda kuunga mkono hoja ya Kamati ya Bunge ambayo imezungumzia katika ukurasa wa 33, kutokana na kwamba bajeti imepunguzwa hasa katika kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi kwa asilimia 33.8. Mimi naungana na Kamati, kuona kwamba Serikali iangalie umuhimu wa kuweza kuongeza bajeti hii kwani akina mama wengi wanakufa kutokana na suala la kujifungua. Kwa vile tunapunguza bajeti maana yake ni kwamba tatizo hili litashindwa kutatulika kwa sababu bajeti imepunguzwa.

Kwa hiyo, niiombe Serikali iangalie uwezekano mkubwa wa kuendelea kuongeza bajeti hasa katika suala hili, ili kuwezesha kupunguza vifo vya kina mama hasa wakati wa kujifungua na katika uzazi baada ya kujifungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la afya ni suala muhimu sana. Serikali kupitia Sera ya Taifa inasema kwamba kila kijiji tuwe na zahanati, kila kata tuwe na kituo cha afya. Suala hili ukiangalia kiuhalisia hasa katika sehemu mbalimbali Tanzania na hasa nikiangalia kwenye Jimbo langu tuna upungufu mkubwa kabisa. Mimi ninazo kata 22, lakini katika kata hizo ninavyo vituo vya afya vinne tu, hivyo bado tatizo ni kubwa. Naiomba Serikali iwekeze zaidi katika kuhakikisha kwamba iweze kutekeleza sera yake ambayo ni kuwa na kituo cha afya kwenye kila kata na kila kijiji tuwe na zahanati ili kuweza kuboresha huduma hasa kwa akina mama wajawazito pamoja na watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuzungumzia suala la watoto wetu wa kike waliopo hasa katika sekondari. Wakati wa hedhi, tunaomba Serikali iwaangalie watoto hawa tuweze kutoa hivi vifaa vya kujihifadhi, kutokana na kwamba wengine wanashindwa hata kuendelea na masomo kwa sababu hiyo.

Kwa hiyo, niombe katika bajeti hii iangalie uwezekano kwenye shule zetu za sekondari watoto wapewe huduma hii, wapewe vifaa vya kujihifadhi, wengine wanashindwa kuendelea na masomo hasa kipindi hicho wanashindwa ku- concentrate katika masomo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuiomba Serikali kama bajeti haijapangwa basi waangalie namna ya kuipanga ili kuweza kunusuru watoto wetu ili waweze kuendelea mbele zaidi hasa watoto wa kike ambao wapo shuleni. Sambamba na hilo nilikuwa naomba pia Serikali ipunguze kodi, iondoe kodi kabisa zile pad ziwe zinaingia free zisiwe na kodi zozote. Hii itawezesha pia akina mama pamoja na wasichana kuweza kupata vifaa hivi kwa bei nafuu ili waweze kujihifadhi. Kwa sababu hali ya hedhi ni hali ya kawaida tu ambayo Mwenyezi Mungu ameiweka kwa wanawake, ni nature, kwa hiyo Serikali inatakiwa ituangalie wanawake, iangalie namna yakutusaidia na kutu-support. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la maendeleo ya jamii, ninapenda kuungana na wenzangu, kusema kwamba Halmashauri nyingi kwa kweli hazitilii mkazo suala la maendeleo ya jamii. Haiwezekani kama tutaweza kushindwa kusimamia sekta ya maendeleo ya jamii, hatutaweza kufikia maendeleo ambayo tumekusudia katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema nchi yetu tunaelekea kwenye viwanda, tutafikaje kwenye viwanda bila kuimarisha sekta ya maendeleo ya jamii? Hivyo nitumie fursa hii kuiomba Wizara iweke mkazo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia hii Wizara ya Viwanda na Biashara. Kipekee kabisa, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya ndani ya Wizara hii. Pamoja na pongezi hizo, ninayo maswali hasa katika Mkoa wangu wa Geita.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipokuwa nikiangalia bajeti hii ya leo ya 2017/2018, kweli imezungumzia kwa habari ya kuwezesha kuwekeza kwenye miundombinu. Katika ukurasa wa 122 wa kitabu, umezungumzia kwamba Wizara imejipanga kujenga miundombinu hasa ya viwanda katika Mikoa mbalimbali ikiwemo na Geita, Dodoma pamoja na Katavi. Vilevile imejipanga kujenga mabanda ya viwanda kumi katika Mikoa hiyo hiyo ya Dodoma, Geita, Katavi, Manyara na Simiyu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kujenga hiyo miundombinu, lakini katika bajeti hii Mheshimiwa Waziri hajaweza kuzungumzia kabisa habari ya kufufua viwanda. Katika Mkoa wa Geita tunavyo viwanda ambavyo vimekufa.

Kwa mfano, kuna kiwanda cha kuchambua pamba pale Kasamwa. Vilevile katika Wilaya ya Chato tunaona jinsi ambavyo hakuna ambacho amekiandika katika hotuba hii. Kwa hiyo, wakati Mheshimiwa Waziri atakapokuwa ana-wind up naomba kufahamu kwamba Serikali inajipangaje kufufua hivi viwanda ambavyo kwa muda mrefu havifanyi kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda hivi vilipokuwa vinafanya kazi viliweza kuajiri vijana wengi katika Mkoa wa Geita na wengi walinufaika na kufaidika, lakini hapa sijaona. Kwa sababu azma ya Awamu ya Tano ni awamu ya viwanda; na nchi ya Tanzania kuelekea kwenye viwanda, kwa hiyo, ni vyema tuangalie uwezekano wa kuweza kufufua viwanda ambavyo kwa muda mrefu havifanyi kazi ili wananchi katika maeneo waweze kufanya shughuli katika viwanda hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika Halmashauri ya Wilaya yangu ya Geita, kuna watu walitoka Wizara ya Viwanda na Biashara, walisema wanataka kuanzisha Kiwanda cha Sukari katika Tarafa ya Butundwe pale Salagurwa, lakini nimejaribu kuangalia kwenye kitabu cha bajeti sijaona mpango wowote katika suala hili. Napenda kupata maelezo kuhusiana na uanzishwaji wa kiwanda hicho katika Tarafa ya Butundwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu Mkoa wa Geita hatuna viwanda kwa kweli. Wananchi wameitikia sana huu wito wa kuwa na viwanda katika Taifa la Tanzania na wanasubiri viwanda hivyo. Leo hii tunaona jinsi ambavyo muda unakwenda, lakini hatuoni viwanda. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri anieleze kabisa anapo-wind up hasa katika Mkoa wangu wa Geita juu ya suala la viwanda, tunajipangaje? Tunawekaje mkakati ili wananchi waweze kunufaika na viwanda hivi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa najaribu kuangalia katika suala la miundombinu; nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali hasa kupitia Wizara ya Ujenzi kwa kuweka mpango wa kujenga barabara ya lami kutoka Kahama kwenda Geita kupitia Bukoli. Barabara hii itawezesha kusafirisha bidhaa mbalimbali pamoja na kuwezesha suala zima la viwanda katika eneo la Mkoa wa Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba katika upande wa barabara Serikali inajitahidi, napenda pia kuulizia upande wa umeme. Vijiji vingi havina umeme. Kama kweli tuna nia ya dhati ya kufanikisha suala la viwanda, ni vizuri Serikali iweze kuhakikisha sasa inafanya utekelezaji wa mpango wa kuleta umeme hasa vijijini, kwa sababu ni kweli kwamba Serikali ina mpango wa REA awamu ya tatu kuleta umeme katika vijiji mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningependa pia kusikia kutoka Wizara ya Nishati na Madini, waniambie kwamba ni lini sasa watahakikisha umeme unawaka katika vijiji na hasa katika Vijiji vya Halmashauri ya Wilaya ya Geita ili kuhakikisha kwamba ile azma ya viwanda inaweza kufanikiwa kwa sababu kuna umeme?

Mheshimiwa Naibu Spika, wawekezaji wanapokuja mahali, wanaangalia kama kuna miundombinu muhimu inayohitajika; kama hakuna umeme, wawekezaji hawawezi kuja; kama hakuna barabara, hawawezi kuja na kama hakuna maji, haiwezekani wawekezaji wakaja katika eneo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa maji, tuna Ziwa Victoria, liko pale. Serikali iwezeshe upatikanaji wa maji ya uhakika ili wawekezaji wanapokuja waweze kukuta miundombinu ikiwa safi kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Mheshimiwa Waziri alizungumzia kiwanda cha kutengeneza matrekta kule TAMCO, Kibaha, lakini sasa hajaelezea kiundani kwamba ni namna gani basi wananchi wataweza kupata matrekta kwa ajili ya kuwezesha kilimo? Naomba pia Mheshimiwa Waziri anapo-wind up aweze kuwaeleza wananchi namna tutakavyoweza kupata matrekta ili tuweze kuimarisha kilimo na kufanikisha suala la viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la elimu; nikiangalia Mkoa wa Geita tuna wilaya tano, hatuna hata Chuo cha VETA hata kidogo. Haiwezekani tukafikia uchumi wa viwanda bila kuwa na elimu; bila kuwa na VETA. Kwa hiyo, naiomba Serikali kupitia Wizara ya Viwanda, ishirikiane na Wizara ya Elimu kuhakikisha kwamba kila wilaya, sawasawa na Sera ya Taifa ya Elimu na Ufundi Stadi, kwamba kila wilaya inatakiwa iwe na Chuo cha VETA. Kwa sasa katika mkoa wetu hatuna Chuo cha VETA hata kimoja. Wilaya zote tano hatuna Chuo cha VETA. Hata katika mkoa hatuna Chuo cha VETA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, natumia fursa hii kumwomba Mheshimiwa Waziri kushirikiana na Mawaziri wengine wa Wizara ya Elimu pamoja na TAMISEMI tuhakikishe kwamba tunakuwa na Chuo cha VETA katika kila Wilaya katika Mkoa wa Geita ili wananchi, hasa vijana wetu wanaomaliza elimu ya sekondari ambao hawaendelei na masomo mengine, waweze kupata elimu ya ufundi stadi, hatimaye waweze kufanikisha azma ya kuweza kufikia maendeleo ya viwanda. Bila ujuzi, haiwezekani kabisa kufikia maendeleo ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, katika suala zima la maji; napenda kuiomba Serikali kwamba iwekeze zaidi hasa katika miundombinu ya maji. Kwa sababu ukilinganisha na maeneo mengine hakuna maji, lakini sisi katika Kanda ya Ziwa tuna Ziwa Victoria ambapo tukilitumia vizuri tuna uhakika wa kuweza kupata malighafi. Tunalo zao la pamba na mazao mengine ambayo yanakubali. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri anapo-wind-up aweze kuelezea. Watu wa Mkoa wa Geita wana shauku ya kuwa na viwanda… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/2018
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi, ili na mimi niweze kuchangia Wizara ya Nishati na Madini. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa uwasilishaji mzuri wa bajeti ya Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi ambavyo amechukua hatua za makusudi kuweza kutetea na kuangalia changamoto mbalimbali zinazogusa wachimbaji wadogo wa madini Tanzania. Mwanzoni kulikuwa na unyanyasaji mkubwa sana wa wachimbaji wa madini, lakini tumemwona Mheshimiwa Rais akiwa Ikulu akiona wachimbaji wakinyanyaswa anatoa maagizo na maelekezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitumie fursa hii kwa niaba ya Wachimbaji wadogo wa Tanzania kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuhusiana na suala la ile Tume iliyochunguza mchanga unaosafirishwa nje ya nchi. Mimi binafsi natoka sehemu ambako madini yako kwa wingi ya dhahabu. Kweli, nitumie fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais na kumpongeza kwa hatua aliyochukua, kwa kweli, imetupa moyo sisi pamoja na wananchi kwani ilikuwa ni kero kubwa sana, hasa kwa sisi ambao tunatokea maeneo haya ya wawekezaji wakubwa wa dhahabu. Wananchi walikuwa kila wakati wakiuliza, inakuwaje mchanga unasafirishwa, walisema sisi hatuoni hata faida yoyote ya kuwa karibu na wawekezaji hawa wakubwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa hatua ambayo Mheshimiwa Rais ameichukua mimi binafsi nimefarijika na wananchi wamefurahi sana; na tunamwambia Mheshimiwa Rais aendelee na kasi hii na mikataba iangaliwe upya ili kuona jinsi ambavyo wananchi tunaweza kunufaika zaidi kutokana na madini ambayo Mwenyezi Mungu ametupatia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizo, binafsi napenda kuzungumzia kwenye madini. Jimbo la Busanda ni jimbo ambalo limebarikiwa na Mwenyezi Mungu, siku zote huwa nasimama hapa nasema tunayo madini ya kutosha. Nilipokuwa nikiangalia bajeti ya Mheshimiwa Waziri sijaona chochote kuhusiana na Jimbo la Busanda kwa kweli, japokuwa ndiko ambako madini mengi yanatokea, hasa wachimbaji wadogo wako wengi sana kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda Mheshimiwa Waziri atakapo-wind up aniambie maeneo ya Nyarugusu, hajazungumzia maeneo ya Rwamgasa, pamoja na Mgusu na sehemu mbalimbali za wachimbaji. Naomba azungumzie atakapo-wind up kwa sababu kwenye bajeti sijaona chochote kuhusiana na maeneo hayo niliyoyataja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kuna eneo la STAMICO ambalo limekuwa ni kilio cha muda mrefu sana kwa wananchi wa Nyarugusu na Mheshimiwa Waziri mwaka uliopita alisema kwenye bajeti kwamba analishughulikia na ataweza kulitafutia ufumbuzi suala hili, lakini mpaka sasa hata kwenye bajeti sijona akizungumzia hata kidogo. Kwa hiyo, naomba atakapo-wind up aniambie na wananchi waweze kusikia kwa sababu wanasikiliza na hata hivyo wako kwenye TV wanaangalia ili kuona kwamba, je, suala hili limeweza kushughulikiwa? Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri aliangalie suala hili na aweze kulifuatilia.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo pale Rwamgasa mwaka 2015, paliteuliwa kuwa sehemu maalum kwa ajili ya uanzishwaji wa eneo la uchenjuaji wa dhahabu wa mfano. Hata hivyo nimesikitika kwamba kwenye Kitabu cha Bajeti, ukurasa wa 103, kati ya vituo saba vya mfano vya kuchenjua dhahabu Rwamgasa haijatajwa tena; sasa napenda kuuliza, je, imeondolewa kwenye huo utaratibu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2015, Benki ya Dunia ilikuja kuzindua rasmi mradi huo pale Rwamgasa na hata leo hakuna chochote kinachoendelea na wananchi wanaendelea kuulizia juu ya suala hili. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atueleze, wawaeleze wananchi wa Rwamgasa kuhusiana na suala hili, kwa sababu Serikali ni kwa muda mrefu imeteua Rwamgasa kuwa Kituo Maalum kwa ajili ya uchenjuaji wa dhahabu lakini leo hii Rwamgasa haipo kwenye bajeti kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile maeneo ya Buckreef ni maeneo ambapo Serikali pamoja na TANZAM wamefanya uwekezaji, lakini sisi wananchi hatuoni faida yoyote kutokana na huo mgodi. Kwa nini Serikali isiangalie upya mkataba huo ili ikiwezekana wapewe wananchi maeneo hayo waweze kuchimba na kunufaika na rasilimali za Taifa zilizopo katika nchi ya Tanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile TANZAM wamechukua eneo Rwamgasa, wakulima wamenyang’anywa maeneo na mpaka sasa hawajapewa fidia yoyote. Naomba Mheshimiwa Waziri aniambie, kwa sababu maeneo hayo wananchi hawaruhusiwi kulima wala kufanya kazi yoyote pale, lakini hawajapewa fidia yoyote. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri wazungumzie suala hili, ili wananchi waweze kujua hatma yao kuhusiana na suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi binafsi napenda kuishauri Serikali kwamba Mkataba huu wa Buckreef na TANZAM uangaliwe upya na ikiwezekana eneo hili wapewe wananchi ili waendelee kuchimba dhahabu na kuweka mchango wao kwenye pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kwa upande wa umeme; nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali japokuwa tunaona Serikali inaendelea kupeleka umeme hasa katika Miji mbalimbali. Kwa mfano Katoro mpaka sasa hivi wanasambaza kwa kasi umeme, lakini bado jitihada zinahitajika zaidi kwa sababu wananchi wanahitaji umeme. Kati ya Kata zangu 22 ni kata 10 tu ndizo zilizofikiwa. Kwa hiyo, niombe Serikali iwekeze nguvu zaidi, ikiwezekana REA iongezewe fedha zaidi ili wananchi hasa walio wengi walioko vijijini waendelee kupata umeme wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo niangalie kwa habari ya mafuta. Kuna vinasaba ambavyo vimekuwa vikilipiwa dola 14 kwa lita 1,000. Hivi vinasaba kwa nchi ya Tanzania kwa kweli, vinaongeza gharama ya mafuta. Naiomba Serikali iondoe hii gharama, ifute kabisa vinasaba hivi kwa sababu sasa hivi bei ya mafuta ya dizeli na bei ya mafuta ya petroli na mafuta ya taa karibu zinalingana, kwa hiyo uchakachuaji haupo tena umepungua kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kwa kuwa, katika nchi nyingine za Afrika Mashariki kama Kenya vinasaba hivi gharama yake ni dola tatu mpaka nne, lakini sisi ni dola 14, kwa nini inakuwa hivyo sisi katika nchi ya Tanzania? Ndio maana sasa mafuta yanakuwa na bei ya juu zaidi kuliko nchi nyingine wakati sisi tuna bandari hapa hapa Tanzania. Kwa nini bei ya mafuta iwe juu ukilinganisha na nchi nyingine wakati sisi tumebarikiwa pia kuwa na bandari katika nchi ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo sasa nichukue nafasi hii kuiomba sasa Serikali iangalie kiundani habari ya wachimbaji wadogo wadogo ambao nimewazungumzia kwa miaka mingi, iangalie namna ya kutatua changamoto zao sasa, kwa sababu imekuwa ni kipindi kirefu wananchi wanahangaika, wanalia, wanahitaji kupewa maeneo ya uchimbaji. Hatuwezi kufikia uchumi wa kati bila ya kuwawezesha hawa wachimbaji wadogo wa madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo wakati ule ambapo Mheshimiwa Profesa Muhongo alikuwa Waziri alikuja Geita akatoa maelekezo kwamba ziangaliwe zile leseni ambazo hazifanyi kazi waweze kupewa wananchi. Mkoa wa Geita tu tuna zaidi ya leseni 1,700 ambazo ni za utafiti pamoja na wachimbaji wadogo wadogo na wa kati. Hata hivyo, kati ya leseni hizo zinazofanya kazi ni leseni 30 tu, kwa hiyo leseni nyingi hazifanyi kazi. Nitumie fursa hii kuiomba Wizara iangalie namna ya kuwapatia wananchi leseni hizi ambazo hazifanyi kazi, hasa vikundi vya wachimbaji wadogo ambao wanafanya shughuli mbalimbali za uchimbaji. Kwa hiyo...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika Mpango wa Taifa mwaka 2018/2019. Kabla ya hapo kwanza nianze kwa habari ya uwanja wa ndege wa Chato. Mimi binafsi napenda kusema kwamba Chato iko Geita na Geita kuna watu lakini na kanda yote ile kuna watu, kwa hiyo tunahitaji huduma ya kiwanja cha ndege. Kwa hiyo, Serikali haijafanya makosa kujenga kiwanja Chato kutokana na shughuli za kiuchumi zilizopo kule. Sisi Wabunge na wananchi kwa ujumla tunahitaji kuwa na kiwanja tena kikubwa zaidi ya hicho. Kwa hiyo, niombe Serikali iendelee kuwekeza fedha zaidi ili kuwezesha ujenzi wa hicho kiwanja cha Chato kwa sababu kitawezesha wananchi wote wa Geita, Kahama pamoja na sehemu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku za nyuma tulikuwa tunatumia uwanja wa Mwanza. Uwanja wa Mwanza ni mbali na wakati mwingine kuvuka feri pale unaweza ukakuta feri haipo kwa hiyo unaweza ukachelewa hata ndege. Sasa hivi kwa kuwa na kiwanja Chato kinaturahisishia maisha. Na sisi ni Watanzania vilevile kama Watanzania wengine ambao wana viwanja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la ujenzi wa jengo la TRA kule Chato. Mimi nadhani tunatakiwa kujenga vitu vya viwango. Kwa hiyo, mimi niipongeze TRA kwa kujenga jengo zuri katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niende sasa katika Mpango. Nampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake kwa kutuletea Mpango mzuri. Kwa upande wa barabara nilikuwa naangalia jinsi ambavyo wamejikita kuangalia miundominu muhimu kwa ajili ya kuwezesha uchumi wa kati, kulingana na Sera ya Taifa, kwamba tumejipanga kuwa na uchumi wa kati mpaka kufikia mwaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo nilikuwa napenda kupongeza kwa upande wa barabara. Niombe sasa kwamba kwa upande wa barabara ile Sera ya Taifa ya kusema kwamba tutaunganisha kwa barabara za lami mikoa kwa mikoa, lakini vilevile wilaya kwa mkoa. Kwa hiyo, mimi nilikuwa nashauri tuwekeze fedha nyingi kwenye upande huo ili kuweza kuwezesha kuiunganisha mikoa. Kwa mfano kuna hii barabara ya kutoka Geita ambayo inaunganisha Mkoa wa Shinyanga pamoja na Mkoa wa Geita. Barabara kutoka Geita kupitia Bukoli kwenda mpaka Kahama ni barabara muhimu sana kiuchumi. Kwanza ndio barabara inayotumika na magari mengi yanayobeba mizigo mbalimbali kwa ajili ya kupeleka shughuli bidhaa kwenye shughuli za madini katika mgodi wa GGM pamoja na wachimbaji wadogo wadogo. Kwa hiyo, ninaomba barabara hii isisahaulike kwenye mpango ujao ili ianze kujengwa kwa sababu ni barabara ya muda mrefu imekuwa siku nyingi inazungumziwa lakini hatuoni utekelezaji wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ili tuweze kufikia uchumi wa kati lazima Serikali iwekeze kwenye kilimo. Kwa mfano sehemu ambazo kuna maziwa pamoja na mito tuangalie kilimo cha umwagiliaji. Nikiangalia Getia tumezungukwa na Ziwa Victoria, tuanzishe miradi ya umwagiliaji ili kuwawezesha wananchi kuweza kuwa na vyakula pia kuwa na uwezo wa kupata bidhaa ili ziweze kutumika katika viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upande wa elimu. Ili tuweze kuwa na Tanzania ya viwanda lazima tuwekeze kwenye elimu. Kikubwa zaidi, kuwianisha na Sera ya Taifa ya kuwa na VETA kila wilaya mkoa. Niombe suala hili Serikali iwekeze kwenye mpango, kwamba kila mkoa tuwe na chuo cha VETA. Kuna wilaya na mikoa mingi ambako hatuna VETA. Kwa kuwa vijana wengi wanahitaji elimu ya VETA kwa hiyo niombe sasa kwenye mipango yetu na bajeti zijazo tuhakikishe fedha zinatengwa kwa ajili ya kujenga VETA katika wilaya na mikoa yote ili kuwawezesha vijana wetu kupata ujuzi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi tunatarajia kupeleka umeme kwenye kila kijiji…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia hoja iliyoko mbele yetu. Nianze kwa kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati ya Bajeti, PIC pamoja na Kamati ya Viwanda na Biashara kwa jinsi ambavyo wameweza kutoa hoja zao lakini pia wameweza kulishauri Bunge na Serikali kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya PIC ambayo inazungumzia masuala ya uwekezaji wa mitaji ya umma. Katika Taifa la Tanzania ni kwamba Serikali iliweza kuanzisha mashirika zaidi ya 269 kwa lengo kubwa kwamba mashirika haya yaweze kufanya kazi zake vizuri na hatimaye yaweze kuweka mchango mkubwa kwa ajili ya pato la Taifa katika Taifa hili la Tanzania. Hata hivyo kwa uhalisia, baada ya kuwa tumepitia mashirika haya tumeona changamoto zipo; na ndiyo maana mashirika mengi na taasisi za umma zimeshindwa kufikia yale malengo ambayo yamekusudiwa wakati yalipoundwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Kamati ya PIC ambayo imezungumzia kwamba Taasisi nyingi zimeshindwa kujiendesha kutokana na kuwepo na madeni makubwa ambapo Serikali inapata huduma kutoka katika Taasisi hizi, lakini Serikali inachelewa kulipa madeni hayo na hatimaye taasisi inashindwa kujiendesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo katika suala hilo tulivyokuwa tukichambua tuliona kabisa kwamba kuna baadhi ya mashirika mengi tu ikiwemo taasisi ya MSD ambayo inafanya shughuli kwa ajili ya kupeleka dawa sehemu mbalimbali katika nchi ya Tanzania. MSD inaidai Serikali zaidi ya bilioni mia moja kumi na nne; kwa hiyo kutokana na deni hilo kubwa taasisi hii inashindwa kujiendesha kwa ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo naishauri Serikali sasa iweke mkakati madhubuti, iangalie taasisi zote ambazo inadaiwa ihakikishe kwamba inalipa madeni yote ambayo inadaiwa na taasisi hizi muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile katika madeni haya tumeona kwamba si taasisi tu ambazo zinadaiwa, tumeona pia hata halmashauri nyingi kuna wakandarasi ambao wametoa huduma mbalimbali na hatimaye Serikali imeshindwa kuwalipa kwa wakati, matokeo yake taasisi nyingi au mashirika mbalimbali yameshindwa kufanya shughuli zao kwa ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo sasa naendelea tu kuiomba Serikali, kama ambavyo Mheshimiwa Rais anasisitiza kwamba unapopata huduma ni vizuri ukalipia kwa wakati. Kwa mfano katika suala la umeme yeye mwenyewe amesema kama mtu umetumia umeme ukishindwa kulipa basi watu wa TANESCO wakate umeme. Kwa hiyo, nasisitiza sasa kwamba Serikali iangalie uwezekano mzuri wa kuangalia madeni yote na kuweka mkakati maalum wa kuweza kuyalipa madeni hayo ili taasisi hizi ziweze kuendelea vizuri kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile katika sheria za manunuzi tuliona pia kuna changamoto kubwa kwamba taasisi nyingi zinashindwa kufanya kazi vizuri na kwa ufanisi kutokana na kwamba Sheria ya Manunuzi inakwamisha baadhi ya juhudi na shughuli mbalimbali katika kujiendeleza na kuweza kufikia ufanisi ambao taasisi inakuwa imekusudiwa. Kwa hiyo niombe Serikali sasa iangalie sheria hizi, hasa hii Sheria ya Manunuzi katika vipengele ambavyo vinakwamisha ifanye marekebisho ili taasisi hizi ziweze kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo katika taasisi nyingi tuliona kwamba hazimtambui Msajili wa Hazina, wakati Msajili wa Hazina ndiye ambaye anasimamia taasisi hizi. Kwa hiyo tuombe Serikali iboreshe zaidi ili taasisi hizi ziweze kumtambua Msajili wa Hazina, kwa sababu ndiye anayesimamia uwekezaji wa kila siku katika taasisi hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Msajili wa Hazina aimarishwe zaidi kama alivyo CAG, tunaona CAG anafanya kazi kubwa kwa sababu ana wafanyakazi wengi na ana bajeti kubwa. Kwa hiyo niombe Serikali ili tuweze kuona mashirika haya zaidi ya 269 yanafanya kazi kwa ufanisi, ni vizuri Serikali ikaangalia uwezekano wa kumwezesha sasa hivi Msajili wa Hazina ili aweze kufanya kazi zake vizuri kwa kuzisimamia taasisi vizuri na hatimaye ziwe na mchango mkubwa kwenye pato la Taifa la Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika masuala mazima ya uwekezaji. Tumeona pia kwamba Serikali inapeleka mtaji kidogo sana kwa baadhi ya taasisi ambazo ni muhimu kama benki. Kwa mfano kuna Benki ya TIB; ambapo benki hii ni muhimu sana kwa ajili ya kuwezesha masuala ya kilimo; na tunakoelekea kwenye suala la viwanda hatuwezi kufikia kama benki hii haitawezwa inavyostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sasa Serikali iangalie namna ya kuwezesha taasisi hii, hasa Benki ya TIB kwa kuwa ni benki ambayo inashughulika na kutoa mikopo pia kwa ajili ya wakulima; na tunajua zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanategemea kilimo na hasa waishio vijijini. Serikali ikitoa mtaji huu itaiwezesha TIB kuweza kujitanua zaidi hata kwenye mikoa kwa sababu sasa hivi ilivyo iko kikanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia kwa mfano kanda yetu ya ziwa Benki hii ya TIB iko Mwanza Mjini. Sasa mkulima atoke Geita huko vijijini aende asafiri mpaka Mwanza mjini kwenda kutafuta huduma za fedha ili kujiimarisha naona kama ni changamoto kubwa. Kwa sababu hiyo sasa, ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi mzuri taasisi hii TIB, tunaomba kwa kweli Serikali ingalie uwezekano mzuri wa kuweza kuiwezesha zaidi ili iweze kufanya kazi zake vizuri kwa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika masuala ya uwekezaji wa mitaji ya umma tumegundua kwamba taasisi nyingi za Serikali zinafanya kazi lakini zinafanya kazi vizuri hatimaye yale mapato ambayo inapata yanatumika yote au unakuta kwamba zaidi ya asilimia iliyowekwa kwamba kila taasisi inatakiwa itumie isizidi asilimia 60 lakini unakuta mashirika mengi yanatumia zaidi ya asilimia 60 mengine hata mpaka
90. Kwa hiyo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya ndani ya Taifa letu hasa katika sekta ya madini, ameanza kuonyesha mfano. Kwa kipindi kirefu sana kumekuwepo na malalamiko mengi kwa wananchi na watu mbalimbali na NGOs kuhusiana na suala la madini. Kwa kweli Mheshimiwa Rais amefanya kitu kikubwa cha ujasiri kuweza kuchukua hatua thabiti na kuweza kuona namna ya kukwamua mambo ya rasilimali katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ambao tunatoka maeneo ya madini tunaona jinsi ambavyo tunaachiwa mashimo. Ukienda kwa mfano GGM watu wanachimba madini kwa kiwango kikubwa lakini wananchi waliopo jirani na maeneo hayo hatuoni faida zaidi katika madini hayo. Kwa hiyo, kwa hatua ambazo Mheshimiwa Rais amechukua mimi binafsi pamoja na wananchi tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mwimbaji mmoja alisema kwamba niseme nini Bwana. Kwa kweli hata mimi nasimama hapa leo kuimba kusema niseme nini Bwana kwa kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Rais ameifanya katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niendelee sasa kuomba kwamba mikataba iendelee kuletwa hapa Bungeni ili tuweze kuipitia kuona namna ya kuwezesha zaidi rasilimali za Taifa hili ili tuweze kufaidika sisi wananchi wa Taifa la Tanzania. Sambamba na mikataba lakini pia ziangaliwe sheria ambazo zipo pamoja na sera, kama hazitupeleki mahali ambapo tunastahili, tuweze kuzifanyia kazi na kuzirekebisha ili wananchi tuendelee kufaidika zaidi na rasilimali ambazo Mungu ametupatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kutoa msisitizo pia kwenye usimamizi wa maliasili zetu. Mheshimiwa Rais ametuonesha mfano na viongozi wengine tuendelee kuonyesha mfano, tuwe wazalendo kwa Taifa letu. Kwa hiyo, niombe tu kwa ujumla sisi sote kwa pamoja wananchi na Wabunge tusimame imara tukiendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais lakini pia hata sisi wenyewe tuweze kusimamia kwa dhati rasilimali za Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri wa bajeti ya mwaka huu 2017/2018. Kama ambavyo wenzangu wametangulia kusema ni bajeti ya mfano. Ni bajeti ambayo kwa kweli ukiisoma inafurahisha na wananchi wengi tumeifurahia bajeti hii. Mimi nasimama kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Busanda kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa bajeti nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu gani? Wananchi walio wengi hasa vijijini walikuwa wanateseka sana na vikodi vidogo vidogo lakini bajeti hii imeweza kuondoa hizi kero. Mwananchi alikuwa anaenda kuuza gunia lake la mahindi analipa kodi, lakini kwa jinsi ambavyo bajeti hii imeweza kuondoa kodi ndogo ndogo, kwa kweli nichukue nafasi hii kwa niaba ya wananchi kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Wizara kwa ujumla kwa mambo makubwa ambayo ameyafanya kwa wananchi wetu na kwa Taifa zima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika bajeti tunaona jinsi ambavyo imejikita katika kuangalia miundombinu muhimu kwa ajili ya kujenga uchumi kuelekea kwenye viwanda. Tanzania ya viwanda inahitajika tuwe na reli na tayari kwenye bajeti imo, tunaenda kujenga reli ya standard gauge. Kwa hiyo, nipongeze kwa kweli kwa jinsi ambavyo ameangalia mifumo ya kiuchumi ikiwepo reli, maji na umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe tu msisitizo zaidi katika suala la maji. Katika bajeti mmeonyesha jinsi ambavyo mtaangalia vyanzo vya maji kwa mfano kwenye maziwa makubwa kama Ziwa Viktoria, Tanganyika na maziwa mengine. Kwa hiyo, niombe sasa katika utekelezaji wa bajeti tuhakikishe wananchi walio kandokando ya maziwa, kwa mfano, mimi Jimbo langu la Busanda lipo kandokando ya Ziwa Viktoria lakini hatuna maji. Kwa hiyo, nitumie fursa hii kuomba sasa utekelezaji, wananchi waweze kupewa maji ya kutosha na ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iweke utaratibu mzuri wa kuweza kutenga hizi fedha ikiwezekana tuwe na Mfuko Maalum wa Maji, kama jinsi ambavyo REA iko katika suala la umeme, inapeleka umeme vijijini, hata katika suala la maji tuangalie kuwa na Mfuko Maalum kwa ajili ya kusaidia upelekaji wa maji vijijini. Vijijini ndiyo kuna changamoto kubwa sana ya suala la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia kumtua ndoo mwanamke ni hasa wanawake waliopo vijijini. Kwa hiyo, niiombe Serikali sasa ituwezeshe kuwa na Mfuko Maalum kwa ajili ya maji ili utuwezeshe kutekeleza miradi ya maji katika vijiji vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa umeme, mimi napenda kuishukuru Serikali kwa mipango thabiti na ndiyo maana nasema nitaiunga mkono bajeti hii ya Serikali. Hii ni kwa sababu katika upande wa umeme Serikali imejipanga vizuri kupeleka umeme vijijini na tayari tumeshapata wale wakandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba sasa umeme huu tunapofikisha kwenye vijiji vyetu, tuhakikishe unafika kwenye taasisi muhimu za umma zikiwepo shule za sekondari, shule za msingi, vituo vya afya na zahanati ili kuwezesha wananchi kupata huduma vizuri kwa sababu kuna huduma muhimu ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika suala la umeme, naomba Serikali iangalie uwezekano miradi hii ianze mara moja, kwa sababu wananchi wamesubiri umeme kwa muda mrefu na wanahitaji umeme ili waweze kuwa na viwanda vidogo vidogo. Vilevile wachimbaji wa madini na wafanyabiashara wanahitaji umeme. Kwa hiyo, naomba sana utekelezaji mara tutakapopitisha hii bajeti uanze mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika bajeti tumezungumzia suala la elimu kwamba tutatoa mikopo kwa watoto wetu kwa masomo ya elimu ya juu. Napenda kuipongeza sana Serikali, tunaomba utekelezaji huo ufanyike ili watoto waweze kupata mikopo na waweze kuendelea na masomo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, ni vizuri kuwa na Vyuo vya VETA. Kwa mfano, kwenye Mkoa wa Geita hatuna Chuo hata kimoja cha VETA. Nitumie fursa hii kuiomba Serikali kupitia Wizara ya Elimu, hebu hakikisheni basi tunakuwa na Chuo cha VETA katika Mkoa wa Geita. Wilaya zote tano hatuna VETA hata sehemu moja na pia katika mkoa hatuna hata VETA moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sasa Serikali iangalie kutoa kipaumbele kwa mikoa na sehemu ambazo hawana kabisa huduma ya VETA. Hapo tutawazesha vijana wetu ambao ni wengi wanamaliza sekondari kupata ujuzi na hatimaye kuweza kuanzisha biashara zao na kujimudu katika maisha yao ya kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la zahanati pamoja na vituo vya afya, ni Sera ya Taifa inasema kwamba kila kijiji kiwe na zahanati na kila kata iwe na kituo cha afya. Ninachoomba sasa Serikali iangalie uwezekano wa kuendelea kutimiza, kweli imetenga fedha, lakini tuhakikishe zinafika kwa wananchi kwa wakati hasa katika Halmashauri zetu ili kazi iweze kufanyika, wananchi tuweze kujenga zahanati kwenye kila kijiji kama ambavyo Sera ya Taifa inasema, lakini vilevile kuwa na kituo cha afya kwenye kila kata na hospitali kwenye kila wilaya. Vilevile kuboresha huduma zote ambazo ni za muhimu ili wananchi wetu waweze kuwa na huduma bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kodi kwa wachimbaji wadogo wa madini. Napenda tu kuomba Wizara ya Fedha hebu tuiangalie hii kodi, haiwezekani hawa wachimbaji wetu wadogo tuanze kuwatoza kodi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia bajeti ya siku ya leo ambayo iliwasilishwa siku ya jana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kipekee kabisa kutoa pongezi, hasa kwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora kwa kazi kubwa ambazo wanazifanya, kwa kweli wanastahili kupongezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niwapongeze hata watumishi wa Serikali ambao ni Katibu Mkuu pamoja na wenzake wote na wafanyakazi wote kwa ujumla. Nikiangalia kwa kipindi cha miaka miwili na nusu sasa katika Serikali ya Awamu ya Tano nimeona jinsi ambavyo Ofisi ya Rais, TAMISEMI imefanya kazi kubwa sana, hasa Mheshimiwa Waziri kuweza kupitia sehemu mbalimbali kwenye Majimbo yetu, kwenye Halmashauri mbalimbali kwa ajili ya kuangalia changamoto mbalimbali ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu na hatimaye kuweza kuzifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo, nikianza na suala ambalo limezungumzwa na Wabunge walio wengi, nami lazima nilisemee suala la kuwarudisha Watendaji wa Vijiji na Kata ambao walikuwa ni darasa la saba ilikuwa ni kilio kikubwa sana ambacho kimekuwepo na binafsi pia katika Halmashauri yetu takribani Watendaji 83 walikuwa wameondolewa kazini. Jambo hili wiki iliyopita nilimuona Mheshimiwa Waziri, Kepteni Mkuchika, nikamuelezea changamoto hii na akanihakikishia kwamba Serikali inaangalia namna ya kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kipekee kabisa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla kwa jinsi ambavyo suala hili wameweza kulitendea haki. Niwaombe tu hao Watendaji wafanye kazi kwa bidii ili kuweza kuleta maendeleo katika Halmashauri pamoja na wananchi wote kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika sekta ya afya katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kipekee kabisa niishukuru Serikali kwa jinsi ambavyo imeweza kufanya jitihada kubwa katika sekta ya afya. Kulikuwa na changamoto kubwa siku za nyuma, kwa sasa tumeona jinsi ambavyo Serikali inafanya kazi. Iliweza kuleta shilingi milioni 500 katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita ambazo zilikwenda kwenye kuboresha Kituo cha Afya Nzela.

Nitumie tu fursa hii kuomba sasa, katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita ina majimbo mawili, Jimbo la Busanda kwa kweli hatujapata hiyo fedha, niombe kwa ajili ya kituo cha afya Katoro ni kituo ambacho kina watu wengi sana, kina msongamano mkubwa, hata wewe mwenyewe Mheshimiwa Waziri naomba utume watu waende pale wakajionee hali halisi. Ukienda kuangalia Hospitali ya Rufaa ya Geita watu wengi wanatoka Katoro, pale ambapo wodi ya wazazi inajaa inabidi wazazi hawa wapelekwe kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nichukue fursa hii kuomba sasa TAMISEMI kupitia Mheshimiwa Waziri, ikiwezekana tuma wataalam wako wakaangalie hali halisi, lakini kikubwa zaidi tunaomba fedha zaidi ili kuweza kukiboresha Kituo cha Afya Katoro ambacho kina msongamano mkubwa sana wa watu, hatimaye basi waweze kupata huduma bora kama maeneo mengine. Vilevile ninashukuru kwa ajili ya gari la wagonjwa ambalo nilipatiwa kwa ajili ya Kituo cha Afya Katoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizi, niombe tena kwamba katika Jimbo la Busanda kuna tarafa mbili, kuna Tarafa ya Busanda ambayo haina gari la wagonjwa hata moja. Kwa hiyo, nitumie fursa hii kuiomba Serikali katika Kituo cha Afya Bukoli pamoja na Gengekumi, niiombe Serikali basi iangalie, Kituo kinaitwa Kashishi na Igengekumi Serikali ione uwezekano wa kupeleka gari ya wagonjwa angalau hata gari moja kwa sasa kwa ajili ya Tarafa ya Busanda ili tuweze kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kanda ya Ziwa inaonesha inaongoza kwa vifo hivi vya akina mama wajawazito wakati wa kujifungua. Ili tuweze kupunguza vifo hivi ninaomba sasa Serikali iweze kutuletea gari ya wagonjwa ili kupeleka huduma hizi kwa akina mama. Tunajua kwamba vijijini watu hawana uwezo, pale ambapo mama anashindwa kujifungua kwenye kituo cha afya au zahanati anakuwa hana uwezo wa kukodisha gari kwenda kwenye Hospitali ya Rufaa, lakini mkiongeza magari ya wagonjwa yatawezesha kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa sababu kutakuwa na uwezekano wa kusafirishwa kwenda katika Hospitali ya Rufaa ili waweze kupata huduma iliyo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya afya tuna upungufu mkubwa sana wa watumishi. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita tu tuna upungufu wa watumishi zaidi ya 200. Niliuliza swali tarehe 30 Januari, ikaonesha kabisa kwamba upungufu uliyopo ni watumishi zaidi ya 240.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitumie fursa hii katika bajeti ya mwaka huu Halmashauri yetu ikileta maombi kwa ajili ya kibali cha ajira kwa watumishi, imeomba watumishi 121 niiombe Serikali basi iweze kutupatia hivyo vibali ili watu waajiriwe tuweze kupunguza adha na matatizo na changamoto mbalimbali, hasa katika sekta hii ya afya ambayo ni ya muhimu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua juhudi za Serikali jinsi ambavyo wameongeza bajeti katika sekta hii ya afya, nina imani kubwa kwamba hizi changamoto Serikali itaendelea kuzifanyia kazi ili hatimae wananchi wetu waweze kunufaika na kuwa na afya bora. Haiwezekani kuwa na maendeleo kama afya haipo katika hali nzuri. Kwa hiyo, naiomba Serikali hasa watumishi katika sekta ya afya tuna upungufu mkubwa, iweze kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii pia kuishukuru Serikali, hasa Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa jinsi ambavyo imeweza kupanga mpango wa kuweza kujenga hospitali ya wilaya katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, jambo hili nalipongeza sana. Ilikuwa ni hitaji kubwa kutokana na kwamba, iliyokuwa hospitali ya wilaya ilibadilishwa matumizi ikawa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Kwa hiyo, niombe sasa hizo shilingi bilioni 1.5, fedha hizi zije mara moja ili ziweze kuanza kazi kuweza kujenga Hospitali ya Rufaa katika Wilaya ya Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika sekta ya afya tunatambua kwamba katika Wilaya yetu, kwanza nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mkuu wetu wa Mkoa pamoja na Mkuu wa Wilaya kwa mkakati mkubwa ambao wamejipanga kuweza kutekeleza Sera ya Taifa ya Afya, kwamba kila kijiji kiwe na zahanati, kila Kata iwe na kituo cha afya, na tayari mpango huu umekwishaanza. Kwa sababu hii niiombe Ofisi ya Rais, TAMISEMI tujipange basi kuweza kuona kwamba utekelezaji huu unaungwa mkono kwa dhati, hasa kwa kuleta vifaa muhimu, lakini vilevile na watumishi pale ambapo zahanati zitakamilika pamoja na vituo vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nizungumzie sekta ya barabara. Tunatambua kwamba tumetunga sheria ya TARURA, TARURA kweli tunaona ipo tumeiazisha lakini bado haijaanza kufanyakazi yake vizuri, nitumie fursa hii hasa kuiomba Serikali iweze kuiongezea uwezo TARURA ili iweze kufanya kazi zake vizuri. Tunaona jinsi ambavyo barabara nyingi za vijijini asilimia kubwa zaidi ya 70 ni watu wanaishi vijijini, barabara za vijijini hazipitiki. Ninaiomba Serikali iwekeze hasa kwenye barabara za vijijini, haiwezekani tunaweza kufikia uchumi wa kati bila ya kuweza kufanikisha barabara vijijini.

Kwa hiyo, niombe Serikali kuhusu TARURA iongeze kasi zaidi na fedha ili tuone kwamba barabara za vijijini zinapitika wakati wote, hapo tunaweza kuwawezesha wananchi kuaanzisha viwanda wataweza kuuza mazao yao sehemu tofauti kwa sababu barabara zinapitika. Kwa hiyo, TAMISEMI iangalie sana TARURA ili hatimaye tuweze kuona mafanikio makubwa kutokana na kuwepo kwa barabara hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema hivi kwa sababu Jimbo langu la Busanda lipo vijijini ninaona changamoto iliyopo kubwa, barabara nyingi hazipiti. Kwa hiyo, niiombe TAMISEMI iwekeze kwenye barabara kwani ndiyo msingi wa maendeleo yetu hasa vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. LOLESIA M. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watumishi wote wa Wizara kwa kazi kubwa ambayo wamefanya katika Wizara hii ninasema hivyo kwa sababu kuna ongezeko katika pato la Taifa kwa asilimia 0.6 ambalo limechangiwa na sekta ya viwanda. Kwa hii inaonesha jinsi ambavyo Wizara hii inafanya kazi kubwa zaidi katika kuhakikisha kwamba uchumi wetu unaimarika siku hadi siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nikiangalia malengo yenyewe ya Wizara yenyewe ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwanza kabisa inahakikisha viwanda vilivyopo vinafanya kazi zake vizuri, kwa uhakika na kuweza kuongeza zaidi mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kuhakikisha kwamba viwanda vyote ambavyo vimebinafsishwa ambavyo havifanyi kazi vinafanya kazi vizuri. Vilevile kuhamasisha wananchi ili waweze kushiriki katika kuwekeza na kuanzisha viwanda vipya. Hayo ni malengo matatu ambapo Wizara imejiwekeza.

Mimi nitazungumzia zaidi kwenye kuanzisha viwanda vipya. Lazima Wizara sasa pamoja na Serikali kwa ujumla iweke mikakati ya dhati na kuhakikisha kwamba kupitia mikakati hii itawezesha uwanzishwaji viwanda hivi. Kwa mfano lazima kuwepo na mazingira wezeshi ya uwanzishwaji wa viwanda; kwanza ni kuhusu umeme. Haiwezekani kuanzisha viwanda tusipokuwa na umeme wa uhakikka. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kusimamia msimamo wake wa Stiegler’s Gorge, ule mradi mkubwa wa umeme; kwa sababu anakusudia tuweze kupata umeme wa uhakika. Vile vile mpango wa Serikali wa REA wa kuhakikisha kwamba watanzania mpaka vijiji wanapata umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Wizara inayohusika ya Nishati kuhakikisha kwamba suala la umeme linakuwa ni kipaumbele cha umuhimu kabisa kwa sababu wananchi vijijini hawawezi kuanzisha viwanda bila ya kuwa na umeme wa uhakiksha. Katika mpango wa Serikali wa kwamba kufikia mwaka 2020 na 2021 vijiji vyote vya Tanzania vitakuwa vimepata umeme, niombe Serikali hasa kwa REA iweze kuwekeza zaidi fedha nyingi kwenye REA ili kuhakikisha umeme wa uhakika unafika vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo wananchi wameitikia sana na hii Tanzania ya viwanda wengi hasa walioko vijijini wameitikia sana kuanzisha viwanda. Hata mimi katika Mkoa wangu watu wengi wanafuata wanataka kuanzisha viwanda, lakini changamoto kubwa ni upatikanaji wa uhakika wa umeme hasa vijijini ambako wanataka kuanzisha viwanda. Kwa hiyo niiombe Serikali sasa kwamba mwaka huu 2018 itenge bajeti kubwa, hasa kwenye Wizara ya Nishati, kwenye REA ili wananchi hasa wa vijijini waweze kupata umeme wa uhakika.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia jambo la pili la kimkakati ni suala la elimu. Haiwezekani kuanzisha viwanda ikiwa vijana wetu hawana uwezo, hawana ujuzi wa kutosha wa kuweza kufanya kazi viwandani. Kwa hiyo niombe katika sekta ya elimu pia tuangalie hili suala la kuwa na VETA kwenye kila Wilaya kama sera ya taifa inavyosema katika upande wa elimu. Kuna Mikoa mingi ambapo mpaka sasa hatujafikia hatuna vyuo vya VETA na Wilaya nyingine hakuna vyuo vya VETA .

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niiombe Serikali ijielekeze katika kuhakisha kwamba ile Mikoa na Wilaya ambayo mpaka sasa hawajapata vyuo vya VETA wahakikishe vyuo hivi zinajengwa kwa haraka ili kuwezesha wanachi hasa vijana kuweza kupata elimu ya ujuzi katika ufundi ili hatimaye waweze kushiriki vizuri katika viwanda kwa sababu Tanzania ya viwanda haitawezekana bila kuwa na ujuzi wa uhakika.

Vilevile niiombe Serikali iweke pia fedha kwa ajili ya kusomesha vijana wetu nje ya nchi. Kwa sababu kuna ujuzi mwingine tunaupata kutokana kupata kwa wenzetu, nilikuwa nikianagalia katika Awamu ya Kwanza ya Mheshimiwa Rais Marehemu Nyerere watu wengi sana walikuwa wanapelekwa nje kwa ajili ya kujifunza teknolojia na ndiyo maana pia hii sekta ya viwanda ilikuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe katika awamu hii Serikali itenge fedha ipeleke vijana hata kama ikiwezekana vijana wapelekwe nje ya nchi ili waweze kujifunza mbinu na ujuzi mbalimbali ili kuweza kufanya kazi na kuweza kuleta teknolojia mpya katika nchi yetu ili kuwawezesha vijana hao kuweza kufanya kazi zao vizuri, la sivyo viwanda hivi ambavyo vinaanzishwa hasa na wageni kama vijana wetu hawatakuwa na teknolijia wanayoijua na ujuzi itakuwa si rahisi kuweza kupata ajira za hali ya juu, watakuwa wanafanyakazi za kada ya chini kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali katika sekta ya elimu iendeleze zaidi Vyuo vya VETA ikiwezekana tufanye kila hata Jimbo, sasa hivi sera ni kila Wilaya lakini niiombe Serikali yaani iwezeshe kila Wilaya sasa ambazo hazijapata VETA ziweze kupata Vyuo vya VETA. Lakini hapo baadae pia ikiwezekana tuangalie hata kila Jimbo liweze kupata Chuo cha VETA kwa sababu vijana wengi sana wanamaliza sekondari, hawana ujuzi yaani hawana uwezo wowote, hawana ujuzi wowote lakini wanapokuwa na stadi za maisha hasa katika Vyuo vya VETA mimi nina uhakika vijana hawa wataweza kushiriki vizuri hasa katika Tanzania ya viwanda katika ujuzi waliokuwa nao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ni muhimu Serikali iwekeze hasa katika kuwezesha mazao ya kiuchumi. Kuna mazao mengi sana na wakulima asilimia 70 ya Watanzania wanaishi vijijini na ndiyo ambao wanashughulika na suala la kilimo. Tunaiomba sasa Serikali iangalie sana suala la kilimo kwa sababu haiwezekani kuweza kupata malighafi tusipowekeza katika suala zima la kilimo. Kwa hiyo, niiombe Serikali iangalie kabisa hata katika maeneo ambapo tumezungukwa na maziwa kwa mfano, Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika na maziwa mengine tuweke hata kilimo cha umwagiliaji ili kuwezesha upataikanaji wa mazao ya malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kikubwa zaidi wananchi wengi wa Tanzania wamehamasika sana katika hii sera ya Tanzania ya viwanda, watu wengi wamehamasika, wanataka kuanzisha viwanda, changamoto tu ni hizo, mambo muhimu kabisa hilo suala la elimu naomba Serikali izingatie na suala la umeme iwe ni kipaumbele cha uhakika ili kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanashiriki kikamilifu katika suala zima la viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la biashara, katika biashara ni kweli wafanyabiashara wengi wanazo changamoto nyingi sana. Nilikuwa ninaomba Wizara kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara tuwe na muda wa kwenda kukaa na wafanyabiashara hata katika maeneo yao vijijini. Tumezoea tu mikutano mingi inafanyika mijini, tuombe na vijijini pia wako wafanya biashara ambao wanahitaji pia tukae nao, tuangalie changamotyo zao hatimaye tuweze kutatua kero zao walizonazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwasababu nimekuwa na experience katika Jimbo langu kuna sehemu kubwa kuna centre ya biashara kunaitwa Katoro kulikuwa na changamoto kubwa watu wengi wanafanya biashara nyingi lakini sasa kumekuwa na changamoto za hapa na pale, TRA inasumbua, sijui zimamoto yaani wanakuwa na changamoto nyingi sana lakini Serikali kupitia Wizara husika ikipata fursa kwenda kukaa na hao wafanyabiashara itaweza

kusikiliza kero zao na hatimaye watakuwa na mazingira mazuri kabisa ya kuweza kufanya biashara na hatimaye sasa tutaweza kufikia lengo la taifa la kufikia uchumi wa kati kama ambavyo tumejipangia.

Kwa hiyo, niombe, nituie fursa hii kuomba Wizara tutoke nje kama wezangu walivyosema, tusijifungie tu ofisini, twende field, twende vijijini, twende mijini, tukae na wafanyabiashara tusikilize kero zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia changamoto nyingine katika biashara nimeona kwa sasa hivi watu wengi wamejikita kuchukua bidhaa kutoka Uganda. Sasa nilikuwa najiuliza kwamba kwanini hapa Kariakoo sasa watu hawaendei kuchukua bidhaa? Siku za nyuma tulikuwa tumezoea watu walikuwa wanatoka Zambia na sehemu mbalimbali wanakuja Kariakoo wananunua bidhaa wanakwenda kuuza kwao lakini sasa hivi imekuwa tofauti. Watu wengi wanakwenda kununua bidhaa Uganda kwa hiyo, ninaomba Wizara pia iangalie hili ni kwanini sasa watu wanakwenda Uganda kuliko kwamba watu wa Zambia na watu wa Uganda waje Tanzania kununua bidhaa ili waende wakauze huko kwao.

Kwa hiyo, niombe jambo hili Serikali ilifanyie kazi, ilifanyie utafiti wa kutosha kwamba ni kwanini bidhaa nyingi watu wanakwenda Uganda isiwe Tanzania ambapo Tanzania tuna bandari, tuna kila kitu, tunajenga standard gauge yaani tunafanya vitu vingi. Sasa ni kwa nini badala ya watu kuja Tanzania kununua bidhaa sasa wanakwenda Uganda kununua bidhaa kwa ajili ya kuuza katika nchi yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu maana yake tunapoteza pato la Taifa, tunapoteza uchumi, tusipolifanyia kazi jambo hili pengine tunaweza tukapoteza watu wengi, tunaweza tukapoteza biashara…

T A A R I F A . . .

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani kama yeye sababu yake ndiyo hiyo lakini ninatoa ushauri kwa Serikali waende walifanyie kazi jambo hili kwa sababu tunaona changamoto ipo na watafute namna sasa kujua, kufanya utafiti wa kutosha ili hatimaye wajiridhishe kwamba ni sababu gani na hatimaye hiyo sababu waweze kuifanyia kazi mwisho wa siku Tanzania basi tuwe hub, tuwe soko ambapo watu wengi watatoka sehemu mbalimbali nje ya nchi kuja kununua bidhaa katika nchi yetu ya Tanzania kama ilivyokuwa zamani. Kariakoo ilikuwa inajulikana ni sehemu ambapo watu walikuwa wanatoka Congo, wanatoka Zambia, wanatoka sehemu mbalimbali kuja kariakoo kwa ajili ya kununua bidhaa mbalimbali.

Kwa hiyo, niiombe Serikali jambo hili ilifanyiekazi na Mheshimiwa Waziri pengine uunde task force ya kuweza kulifanyiakazi jambo hili ili kuhakikisha kwamba uchumi wa Tanzania uendelee kwenda juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia bajeti ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri kwa kazi kubwa ambayo wameifanya hasa katika kuandaa bajeti hii muhimu ya Kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nichukue nafasi hii kupongeza kwa dhati kwa kuondoa kodi kwenye taulo za kike ambayo ilikuwa ni kero ya muda mrefu. Tuna imani kubwa huu ni mwanzo mzuri na kwamba wananchi sasa hasa akina mama na watoto wa kike wataweza kunufaika kwa kuondolewa kodi katika taulo za kike kwa ajili ya kujihifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nichukue nafasi hii kupongeza sana kwa jinsi ambavyo wameweka kipaumbele cha kwanza kabisa kwenye suala la kilimo ikifuatiwa na suala la viwanda, hatimaye kwenye huduma za jamii na mwisho kabisa kwenye miundombinu muhimu wezeshi kwa ajili ya uchumi kukua. Nikianza kwenye sekta ya kilimo, ni muhimu sana kwa sababu asilimia kubwa ya Watanzania wanajishughulisha na kilimo. Kwa sababu hiyo Serikali ikiangalia suala la kilimo hasa ambavyo imezungumza kwamba itawezesha kuanzisha skimu za umwagiliaji, nipongeze sana kwa ajili ya jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa tunalo Ziwa Viktoria na mikoa mingine kwa mfano Ziwa Tanganyika na maziwa mengine, tukianzisha skimu za umwagiliaji nina uhakika kwamba wananchi wataweza kunufaika, tutapata mazao ya uhakika mwaka mzima. Kwa hiyo, nipongeze tu na niombe sasa utekelezaji uwe ni wa kweli katika jambo hili, lisije tu kuonekana kwenye karatasi lakini kwenye vitendo halisi lisionekane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika suala la kilimo ni muhimu sana Serikali iangalie namna sasa ile Benki yetu ya Kilimo (TADB) ambayo tumeianzisha inavyoweza kufanya kazi. Hii benki kweli ipo lakini inapatikana mjini tu. Kwa mfano, kwenye Kanda yetu ya Ziwa Benki ya TADB inapatikana Mkoani Mwanza. Sasa mkulima wa kawaida siyo jambo rahisi kutoka Geita avuke kote kule mpaka Mwanza kwenda kuchukua mkopo kwenye Benki ya TADB. Kwa hiyo, Serikali iangalie sasa kujenga mazingira mazuri kuwezesha benki HII iweze kuwafikia wananchi hasa wakulima vijijini ili waweze kunufaika katika suala zima la kupata mikopo nafuu ili kujikimu na kujiendeleza katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo pia, suala la wataalam katika sekta ya kilimo ni muhimu. Nasema hivyo kwa sababu mara nyingi katika vijiji vyetu siku hizi hakuna wataalam kabisa wa kilimo. Unakuta mtaalam mmoja anapatikana kwenye makao makuu tu ya kata ambapo wakulima wanapatikana vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sasa Serikali imeweka kipaumbele kuboresha suala la kilimo, tuangalie uwezekano wa kuwa na wataalam wa kutosha kwenye vijiji na kata. Kikubwa zaidi wataalam hawa wafanye kazi zao vizuri kuwaelimisha wakulima badala ya kilimo tulichokizoea ambacho hakina tija, tuweze kubadilika kuwa na kilimo chenye tija na hatimaye tuweze kukuza uchumi wa Taifa letu.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika viwanda, nipongeze sana kwamba Serikali imejikita kujenga mazingira wezeshi ili wawekezaji wengi waweze kuingia ndani ya Tanzania na kuwekeza, pia hata wawekezaji wa ndani. Naomba sasa katika suala la uwekezaji na viwanda muwaangalie wafanyabiashara ambao kwa muda mrefu wafanyabiashara wengi wamekuwa na changamoto nyingi sana. Mimi natokea kwenye eneo ambapo kuna sehemu kuna biashara kubwa kwa mfano katika center moja ya Katoro, wafanyabiashara wana changamoto nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe Serikali kwa ujumla iangalie namna ya kutatua kero na changamoto mbalimbali za wafanyabiashara ili waweze kuendelea kuwekeza zaidi kwenye viwanda kwa sababu bila kuwalea hawa wafanyabiashara wadogo ambao wapo sasa haiwezekani wakaweza kuwa wafanyabiashara wakubwa. Naomba katika fedha hizi ikiwezekana kuwepo na fedha kwa ajili ya kuwaelimisha zaidi wafanyabiashara wadogowadogo, kikubwa zaidi mazingira yao ya utendaji wa kazi yaweze kuwa mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kutokana na kwamba mara nyingi unakuta TRA wana-harass sana wafanyabiashara vijijini, wanakwenda pale mtu anarundikiwa kodi hapa na pale, kunakuwa na mazungumzo ambayo siyo mazuri. Nashukuru kwenye bajeti hii Waziri ametoa kauli kwamba kuwepo na urafiki kati ya TRA na wafanyabiashara. Napongeza sana statement hiyo, niombe sasa walioko kule kwenye wilaya na mikoa wahakikishe wanafanyia kazi jambo hili ili kuwezesha wafanyabiashara wadogo waweze kufanya biashara zao vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la huduma za kijamii ikiwemo sekta ya afya, naishukuru sana Serikali kwa sababu imewekeza sana kwenye afya. Nilikuwa najaribu kusoma katika mpango huu, sijaona mpango wa Serikali kuajiri watumishi wa sekta ya afya. Natoa msisitizo kwamba katika bajeti ya mwaka huu tuangalie namna ya kuajiri watumishi katika sekta ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano tu kwenye Halmashauri yangu ya Geita tuna upungufu wa wataalam wa afya 200. Ndiyo maana kunatokea changamoto za vifo vya akina mama na watoto wakati wa kujifungua kwa sababu hakuna mtoa huduma katika zahanati au kituo cha afya. Kwa hiyo, napongeza kwa kazi kubwa kwamba tunajenga vituo vya afya na zahanati lakini tuongeze wataalam katika maeneo haya ili waweze kufanya kazi zao kusaidia wananchi, hasa ambao wanapata matatizo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu unakuta kituo cha afya au zahanati kina mtaalam mmoja au wawili, ni changamoto kubwa sana. Kwa hiyo, niombe Serikali kwa kuwa kwenye bajeti huku sijaona hilo, nimejaribu kuangalia lakini sikuweza kuona, nitoe tu msisitizo kwamba mwaka huu wa fedha tuajiri wataalam wa kutosha katika sekta ya afya ili kuwezesha akina mama na watoto waweze kuwa na afya pia waweze kufanya kazi zao vizuri. Unakuta hao hao wachache wanapata shida sana maana watu wanaosubiri huduma ni wengi. Kwa hiyo, wakati mwingine mtu anaweza akawa na majibu hata ambayo hayaeleweki kwa sababu amechoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile sekta ya maji ni muhimu sana hasa vijijini. Niombe tuweze kutekeleza kama ambavyo tumepanga, kwa sababu tulivyopanga hapa mipango ni mizuri sana. Nachoomba utekelezaji uweze kufanyika ili tuweze kuwafikia wananchi wetu katika kuwapa huduma kadri ambavyo Serikali imekusudia, otherwise bajeti iko vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa makusanyo, kuna changamoto kubwa sana. Kwenye matumizi ya vile vifaa vya kielektroniki kwa kweli kuna changamoto kubwa sana na ndiyo maana Serikali haipati mapato ya kutosha kwa sababu vifaa hivi havipatikani. Hata vilivyopo pale havifanyi kazi vizuri, unakuta unakwenda labda kituo cha mafuta lakini hupewi risiti, unaifuatilia risiti unaweza ukatumia nusu saa nzima kuipata. Kwa hiyo, watu wengi wanakata tamaa wanaziacha na mwisho wa siku Serikali haipati mapato yake sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango waangalie jambo hili kwamba namna gani tuweze kuboresha ili utoaji wa risiti na upatikanaji wa mashine hizi uwe mzuri. Kuna nchi nyingi za nje, nimebahatika kusafiri nje pia, kila ukipewa huduma yoyote mahali popote pale lazima utapewa risiti saa hiyo hiyo tena kwa haraka. Katika nchi yetu unapewa huduma labda ya mafuta lakini inakuchukua nusu saa kupata risiti, wakati mwingine unakata tamaa unasema labda niondoke. Niiombe Serikali hapo muendelee kuweka nguvu zaidi katika suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa zaidi tutoe elimu kwa wananchi kuomba risiti. Kwa sasa hivi elimu ipo lakini wanachi hawaombi zile risiti. Nnasema hivyo kwa sababu juzi tu kituo cha mafuta kina risiti nyingi watu hawachukui risiti zao. Kwa hiyo, Serikali iwekeze kwenye elimu ya mlipa kodi, kwa sababu bila ya kodi hatuwezi kupata maendeleo katika nchi yetu. Wananchi wana uelewa mkubwa wakielimishwa wanaelewa vizuri. Kwa hiyo niendelee kuomba Serikali kupitia Wizara husika tuendelee kutoa elimu hii na Wabunge tushirikiane kwa pamoja kuwaambia wananchi na wananchi wana uelewa mkubwa, tusisitize suala la kuomba risiti ni kitu muhimu sana ili kuweza kuchangia katika pato la Taifa.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa miundombinu, naipongeze sana Serikali kwamba imekusudia kujenga mradi mkubwa sana wa umeme Stiegler’s Gorge. Nina uhakika kwamba kupitia mradi huu wananchi tunaweza kupata umeme wa uhakika. Kikubwa zaidi niombe
sasa Serikali iendelee kusambaza umeme kwa kasi hasa vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, napongeza sana Serikali na naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara ya Madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais, kipekee kabisa kwa kuona umuhimu wa Wizara hii ya Madini, ndiyo maana akaanzisha Wizara kamili inayohusika na suala la madini. Kwa kweli nizidi kumtia moyo tu kwamba aendelee kuchapa kazi kwa sababu Watanzania tuko nyuma yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri, pamoja na Naibu Mawaziri wake kwa kazi kubwa wanayoifanya kwenye Wizara hii. Ni Wizara mpya lakini kazi wanazozifanya kwa kweli zinatutia moyo wananchi ambao tulikuwa na changamoto nyingi hapo siku za nyuma. Sasa hivi changamoto zinapungua siku hadi siku, hongera sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Mawaziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri baada tu ya kuteuliwa aliweza kufunga safari akafika mpaka Geita, akaangalia changamoto za wachimbaji wa madini, wakubwa, wa kati na wadogo. Kwa kweli nampongeza sana Waziri na Mheshimiwa Stanslaus Nyongo, ahsanteni sana kwa kusikiliza kero, wananchi wana imani na nanyi kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mheshimiwa Nyongo, Naibu Waziri alikuja Nyarugusu akasilikiza kero tukiwa pamoja na watu wakauliza maswali mbalimbali. Nina hakika wanaendelea kuangalia hizi changamoto ili kuzifanyia kazi, nasema ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishukuru Wizara ya Madini, kwa jinsi ambavyo wametupa heshima kwenye Kijiji cha Rwamgasa kwa kutengeneza kituo cha mfano kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Busanda na Geita kwa ujumla tunashukuru kwa ajili ya kituo cha mfano cha Rwamgasa. Kwenye bajeti hii wamesema kwamba kimefikia asilimia 70 ya utekelezaji, naomba mwaka huu kiweze kukamilika ili wananchi waweze kunufaika na kujifunza mambo mazuri hasa wale wachimbaji wadogo ambao wamekuwa na changamoto kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kwamba nchi hii ya Tanzania inao wachimbaji wadogo wengi sana. Katika takwimu baada ya utafiti wa UNEP mwaka 2012 ni kwamba wachimbaji wadogo 500,000 mpaka 1,500,000 wameweza kuwa na ajira kupitia shughuli za uchimbaji. Kwa sasa hivi hali halisi inaonesha kama watu 2,000,000 ni wachimbaji wadogo ambao wanajishughulisha na shughuli za uchimbaji madini. Niombe Mheshimiwa Waziri pamoja na Wizara waangalie namna ya kuwasaidia hawa wachimbaji wadogo. Ni kweli wana mchango mkubwa sana kwenye Taifa hili, wakiwezeshwa kwa kupewa mitaji, pengine hata kwa kukopeshwa kwa riba nafuu, wataweza kufanya kazi zao kwa umakini na mwisho wa siku watakuwa na uwezo wa kuchangia kwenye pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, japokuwa kwenye bajeti sikuweza kuona mahali ambapo mmezungumzia habari ya kuwawezesha kwa kuwapa mitaji, naomba Wizara iangalie uwezekano wa kufanikisha suala hili. Siku za nyuma kulikuwa na programu hiyo ya kuwapa ruzuku wachimbaji wadogo, hebu basi tuangalie namna ya kuwawezesha kwa ruzuku au kwa mikopo yenye riba nafuu ili waweze kujiinua kiuchumi kupitia shughuli hizi za uchimbaji. Uchimbaji ni shughuli ambazo zinahitaji mtaji wa kutosha ili kuweza kuzifanya kwa umahiri. Kwa hiyo, niombe Wizara iangalie namna ya kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa sababu wanahitaji kusaidiwa ili waweze kuchangia katika pato la Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna ule Mgodi wa Buckreef ambao uliingia ubia kati ya TANZAM pamoja na STAMICO. Ni miaka mingi sasa tangu mwaka 2011 lakini hatuoni kitu chochote kinachoendelea kwa ajili ya mchango wa wananchi. Wachimbaji wadogo waliondolewa akapewa TANZAM kwa ubia na STAMICO lakini hatuajaona faida ya mgodi huu. Nimefurahi kuona kwamba kwenye bajeti wamesema kwamba Serikali inaianyia utafiti kuona kama TANZAM na STAMICO waendelee au vipi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe suala hili lifanyiwe kazi kwa haraka zaidi kwa sababu tangu walivyoanza mwaka 2011 kuna baadhi ya wananchi walifanyiwa tathmini, wanatakiwa kulipwa fidia, mpaka leo hawajalipwa fidia yoyote na wanauliza ni lini sasa wataweza kulipwa fidia zao. Mashamba yao hawalimi, hawafanyi kitu chochote na hawayaendelezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, huu ubia kati ya TANZAM na STAMICO kwa kweli ni kero kubwa sana katika maeneo yetu ya Rwamgasa na sehemu mbalimbali. Niombe Mheshimiwa Waziri mlifanyie kazi jambo hili ili hatimaye liweze kuleta tija. Kwa sababu lengo kubwa ya uwekezaji ni kuleta tija kwa wananchi wanaozunguka maeneo husika lakini pia kwa wananchi wetu kwa ujumla. Mpaka sasa hatuoni tija yoyote kupitia huyu mwekezaji TANZAM na STAMICO, ni ubia kwa asilimia 45 kwa 55 lakini hatuoni faida yoyote ya kuhusiana na uwekezaji huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto hiyo, tunaiomba Serikali sasa iangalie na kuchukua hatua mapema ili hatimaye wananchi waweze kunufaika na uwekezaji au madini yaliyopo katikati yetu. Tunamshukuru Mungu kwamba nchi ya Tanzania tunayo madini ya kutosha, tuna mambo mengi makubwa lakini sasa vitu vingi vimekuwa havitunufaishi vizuri kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa ajili ya kubadilisha hizi sheria, mwaka jana tumeweza kubadilisha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 tumepata sheria mpya ya mwaka 2017. Kwa hiyo, najua kabisa kwamba kupitia mabadiliko haya, ndiyo tunaona tija na mabadiliko mazuri ambayo ni kwa manufaa ya wananchi wetu na kwa ujumla kama Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazidi kuiomba Serikali iangalie katika migodi mbalimbali midogo na mikubwa, kwa mfano, katika Mkoa wetu wa Geita tuna rasilimali dhahabu lakini bado wananchi wa pale hatunufaiki ipasavyo. Kwa mfano, mitambo ya uchenjuaji wa dhahabu mingi iko Mwanza wananchi wa Geita hawanufaiki. Kwa hiyo, tunaomba Serikali itusaidie, hata hizi carbon zinazosafirishwa kila wakati kutoka Geita kwenda kuchenjuliwa Mwanza siyo mzuri, wananchi wa Geita wanakosa mapato ambapo pengine watoto wetu wangepata ajira pale kupitia uchenjuaji huu. Kwa hiyo, ikiwezekana tunaomba Serikali itusaidie wawekezaji wajenge mitambo yao ya uchenjuaji hapo hapo Geita ili hatimaye process zote za uchenjuaji wa dhahabu zifanyike Geita ili wananchi wa Geita waweze kunufaika na madini ambayo Mwenyezi Mungu amewapatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkitusaidia hilo hakika wananchi wa Geita hawatawasahau, watajua kabisa kwamba Mheshimiwa Waziri amewasaidia na Mungu ataendelea kumuinua Waziri na kumbariki kwa sababu atakuwa amewasaidia sana. Kwa hiyo, niombe tu Serikali kupitia Wizara hebu wafanye utafiti kidogo juu ya jambo hili. Tunachotaka kupitia dhahabu wananchi wetu waweze kupata ajira. Tunajua kabisa Geita na maeneo mengi ambayo yanashughulika na kuchimba madini miji inakua kutokana na madini yaliyopo nasi tunahitaji kupitia dhahabu tuweze kunufaika zaidi. Kwa hiyo, uchenjuaji na viwanda vile vya kuongeza thamani ya madini, tunaomba pia vijengwe kwenye Mkoa wetu wa Geita ili wananchi waweze kunufaika zaidi. Ni kama korosho kule Mtwara, huwezi ukazungumzia korosho ukiwa Geita yaani kila kitu kinafanyika kule. Kwa hiyo, nasi tunaomba Geita sasa kila kitu kuhusiana na dhahabu kifanyike pale na kuwe na kituo kikubwa ili wananchi wetu pia waone umuhimu wa hiyo rasilimali ambayo Mungu ametupatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naiomba Serikali iangalie wachimbaji wadogo kwa kuwawezesha mitaji ili tuweze kuona umuhimu wa kuweza kuchangia katika Pato la Taifa kupitia kuwawezesha wachimbaji hao. Kikubwa zaidi Wizara itusaidie kuendelea kuboresha zaidi sekta hii ya madini hasa katika suala zima la usafirishaji wa carbon na kuhakikisha kwamba tunajenga mitambo pale Mkoani Geita ili tuweze kunufaika zaidi vizazi vyetu pamoja na wananchi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana, naunga mkono hoja kwa sababu mambo mengi yamekwisha kufanyika.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia taarifa ya Kamati ya Nishati na Madini kwa mwaka huu uliopita. Kipekee kabisa nimpongeze Mwenyekiti wa Kamati pamoja na Wajumbe kwa jinsi ambavyo wameweza kuandika ripoti nzuri nimeisoma, kwa kweli na ushauri ambao wameutoa ni ushauri muhimu sana katika sekta hii kwa ajili ya kuipeleka mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na Sekta ya Madini, nianze kipekee kabisa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya kwa miaka mitatu, lakini kikubwa zaidi tarehe 22 Januari, 2019 ambapo aliweza kukaa na wadau wa madini Mkoani Dar es Salaam, kwa kweli inaonyesha nia ya dhati kabisa kuweza kuondoa changamoto na kero mbalimbali zilizopo kwa wananchi hasa wachimbaji wa madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa niunge mkono kabisa Kamati ambayo imependekeza kwamba yale mapendekezo ya wachimbaji wadogo walivyokutana kule Dar es Salaam, Serikali iweze kuyachukua na kuweza kuyafanyia kazi. Kwa kunukuu yanapatikana katika ukurasa wa 32, 33 na 34. Kwa msisitizo zaidi nikianza na pendekezo la pili ambalo ni kuondoa baadhi ya kodi tumegundua kwamba wachimbaji wadogo na wachimbaji wanazo kodi nyingi ambazo wakati mwingine zinawarudisha nyuma kabisa katika shughuli zao za uchimbaji wa madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kutokana na ushauri ambapo wachimbaji wadogo wenyewe wadau wa wachimbaji walivyokutana, nilikuwa naishauri Serikali kipekee kabisa iweze kuangalia na kupunguza hizi kodi ambazo zinakuwa ni kodi zinazokandamiza wachimbaji wadogo wa madini na wachimbaji wakubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna ushauri ambao aliutoa kwamba wanahitaji kuanzisha benki ya madini, niunge mkono kabisa kwamba Serikali iangalie namna ya ku-support kuweza kuanzisha benki ya madini ili wachimbaji hasa wale wadogo ambao hawana uwezo wapate fursa ya kuweza kukopeshwa yaani kwa riba nafuu ili waweze kumudu shughuli zao za uchimbaji wa madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna eneo ambalo pia walizungumzia kwamba katika maeneo mengi ambayo yamepewa leseni za utafiti wa madini unakuta maeneo mengi sana yanachukuliwa kwa ajili ya utafiti wa madini. Lakini maeneo hayo wachimbaji wanakuwa hawaruhusiwi kufanya shughuli zao zozote zile. Kwa hiyo, niunge mkono mapendekezo hayo kwamba Serikali iangalie maeneo haya ambayo mengi yalikuwa yamepewa kwa ajili ya shughuli za utafiti wepewe wachimbaji hasa wadogo waweze kufanya shughuli za kiuchumi hatimaye waweze kuchangia pato la Taifa. Kwa sababu wachimbaji hawa watakapoweza kufanya shughuli zao za uchimbaji wataweza kupata fedha na mwisho wa siku wataweza kuchangia kwenye pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna suala la ruzuku kwa wachimbaji wadogo, niombe Serikali suala hili ni muhimu sana. Siku za nyuma Serikali ilikuwa inatoa ruzuku, lakini hivi karibuni hatuoni tana wachimbaji wadogo kupewa ruzuku. Niiombe sasa Serikali iangalie siri kwa macho mawili, ile benki kama vile wakulima wanavyopewa ruzuku hata wachimbaji wadogo tuangalie namna ya kuwapa ruzuku ili hatimaye waweze kuwekeza zaidi katika shughuli zao za uchimbaji wa madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna suala muhimu kabisa ambalo wamelizungumzia, ni suala la tozo na ada mbalimbali kwa wachimbaji wadogo wa madini ambazo wamekuwa wakilipa kwa dola. Kwa hiyo, niombe pia hata mimi nashauri kwamba Serikali iangalie tozo hizi zilipo kwa shilingi ya Tanzania, kama ambavyo tunasisitiza hata watu wengine wageni wakiingia ndani ya nchi walipwe kwa shilingi hata katika wachimbaji wa madini pia tuangalie namna ya tozo hizi kulipwa kwa shilingi za Kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda pia kusisitiza kuna baadhi ya maeneo ambayo yalichukuliwa kwa ajili ya uanzishaji wa shughuli mbalimbali za madini likiwemo lile eneo la Lwamgasa ambapo wamechukua kwa ajili ya kuanzisha shughuli mbalimbali za uchimbaji lakini kwa ubia na watu wengine. Watu hawa kwa muda mrefu sana eneo hili limechukuliwa lakini hawajapewa fidia. Kwa hiyo niiombe Serikali pia iangalie namna watu hawa wapewe fidia, miezi sita imepita hakuna chochote, ni mwaka sasa hakuna chochote kinachoendelea na sheria tunavyoijua ni kwamba kwa muda wa miezi sita kama wameshafanyiwa tathmini hawajalipwa Serikali inatakiwa kufanya tathmini upya tena ili waweze kulipwa haki zao za msingi. Kwa hiyo, niombe Serikali iangalie sasa namna ya kuweza kuhakikisha hawa ambao wanahitaji kulipwa fidia wanalipwa kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi hawa hawarusiwi kufanya shughuli zozote za kiuchumi katika maeneo yale. Sasa kwa sababu mtu hatumruhusu kufanya shughuli yoyote anapataje uchumi wake kama humruhusu kulima, haruhusiwi kufanya kitu chochote katika eneo lake. Kwa hiyo, naomba sana katika Sekta ya Madini Serikali iangalie namna zaidi ya kuangalia mapendekezo ambayo wachimbaji wa madini na wadau mbalimbali wa madini wameweza kuyapendekeza na kuweza kuiomba Serikali iweze kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika Sekta ya Umeme, Sekta ya Nishati nianze kipekee kabisa kupongeza Serikali hasa Wizara ya Nishati kupitia Mheshimiwa Waziri wa Nishati pamoja na Naibu wake kwa kazi kubwa hakika wanafanya kazi kubwa sana kwenye hii Wizara, kila wakati Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wanapita sehemu mbalimbali kukagua miradi mbalimbali ya umeme hata kwenye Jimbo langu wamefika, niwapongeze sana kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa ajili ya kupeleka umeme kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii REA III, katika awamu ya kwanza yake, ni kweli wamefanya kazi kubwa kuhakikisha kwamba wananchi wanapata umeme. Niombe sasa zile nguzo ambazo pengine tunapopeleka umeme labda kwenye kijiji fulani, unakuta nguzo zinakuwa chache sana wanaoweza kupata huo umeme ni wachache ukilinganisha na mahitaji. Watanzania sasa hivi wanahitaji kupata umeme kwa sababu umeme ndio maendeleo kupitia umeme watakuwa na uwezo wa kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi, wengine watatumia kwa ajili ya viwanda. Kwa hiyo, nitumie fursa hii kuiomba Wizara kupitia Mheshimiwa Waziri hebu tuangalie kuongezea nguzo za umeme hasa kwenye maeneo ambako wanapeleka umeme huu wa REA, watu wanahitaji umeme sana . (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitatolea mfano tu kwenye Jimbo langu, pale Nyakagomba wamepeleka kweli umeme wa REA III, katika awamu ya kwanza, lakini kila siku hata hivi leo natumiwa meseji sasa Mbunge mbona nguzo hazitoshi, watu wengi tunahitaji umeme? Kwa hiyo, nitumie fursa hii kuomba kabisa kwamba hebu tuangalie kuongeza nguzo kwa sababu wananchi wanapenda umeme kwa ajili ya maendeleo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niishukuru Serikali kwa mradi mkubwa sana wa Rufiji ule wa Stiegler’s Gorge, ni mradi wa kimkakati, naipongeza sana Serikali kwa kufanya maamuzi hayo. Tuna uhakika kwamba baada ya muda mfupi Tanzania itaondokana na tatizo la upungufu wa umeme. Kwa hiyo, niombe tu Serikali iendeleze huo mradi kwa sababu ni mradi mkubwa wa kimkakati ili tuweze kufikia azma ya Serikali ya viwanda. Hakika umeme wa Stieglers Gorge utatusaidia kuweza kufikia hiyo azma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna miradi mingine ya umeme, kwa mfano katika Mkoa wetu wa Geita kuna ule mradi wa 220 KV. Ni kweli Mheshimiwa Waziri amezindua huu umeme lakini hatujaona kinachoendelea. Tuombe hii miradi Serikali iendelee kuwekeza nguvu ili iweze kufanya kazi kwa wakati. Wananchi kama ambavyo nimetangulia kusema wanahitaji umeme… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele ya pili imeshagonga. (Makofi)

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia bajeti muhimu kabisa ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, kwa usimamizi mzuri ambao anaufanya kila wakati. Ameweza kusimamia, kwa kweli tunaona matokeo makubwa kwa kipindi kifupi tunaona mambo yanaendelea vizuri. Ni Serikali inaendelea kusimamia vizuri na kutekeleza sera kwa vitendo ambazo zipo katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na Mheshimiwa Waziri wa Utawala Bora na Naibu Mawaziri wote, watumishi wote wa Wizara kwa kazi kubwa wanazozifanya. Wote tunafahamu TAMISEMI imebeba wananchi wa nchi hii ya Tanzania. Inashughulika na changamoto nyingi katika Taifa hili. Masuala ya elimu, afya, barabara na kwa kweli TAMISEMI ni kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa nikianza katika Sekta ya Afya, nitumie nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa ya ujenzi wa vituo zaidi ya 352 Tanzania nzima. Kwa kweli ni kazi kubwa iliyotukuka. Napongeza kazi hii kubwa ambayo imeifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia pia katika mkoa wangu, hasa katika Halmashauri ya Wilaya yangu, nitumie fursa hii kuishukuru Serikali kutupatia shilingi bilioni 1.5 ambazo zimejenga Hospitali ya Halmashauri katika eneo la Nzela. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kutupatia shilingi milioni 400 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya Nyarugusu. Natoa shukrani hizi kwa sababu kusema ukweli kikikamilika kituo hiki kitapunguza changamoto kubwa ambayo wananchi wa Nyarugusu walikuwa wakiipata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kunatokea mambo ya vifo pamoja na changamoto mbalimbali, lakini kwa kupewa hizi shilingi milioni 400, kwa kweli kwa niaba ya wananchi, wanashukuru sana kwa kazi kubwa na fedha nyingi ambazo mmetupatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, katika Sekta ya Afya najua bado changamoto zipo. Kwa mfano hii hospitali ambayo tumepewa, inajengwa Nzela, lakini jiografia yetu katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita kwa kweli changamoto ni kubwa sana. Haiwezekani mtu akatoka Jimbo la Busanda kwenda kutibiwa Nzela, ni mbali. Afadhali hata akatibiwe Geita Mjini. Kwa hiyo, tunaona jiografia yake ni ngumu, itawezesha wananchi watapata changamoto kubwa kabisa kwa ajili ya usafiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja mwaka 2018 akatuahidi kujenga hospitali Katoro. Nimeangalia kwenye bajeti sijaweza kuona. Kwa hiyo, nitumie fursa hii kumwomba Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo, tuangalie, maadam Waziri Mkuu ametuahidi, alikuja Geita akatuahidi pale pale Katoro na wananchi wakafurahi wakiamini kwamba hospitali itajengwa Katoro. Kwa hiyo, nitumie fursa hii kumwomba Mheshimiwa Waziri kwamba hebu atutafutie fedha popote ili hospitali hii iweze kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunafahamu Katoro ni Mamlaka ya Mji Mdogo, lakini ukiangalia uhalisia ni zaidi ya Mamlaka ya Mji kamili. Kwa hali halisi ya kibiashara kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini, pamoja na shughuli za uvuvi na shughuli za biashara, watu wengi sana wako mahali pale. Kwa kweli ni Mji wa kibiashara, tunahitaji hospitali. Watu ni wengi, tunahitaji huduma. Ukienda kwenye kile Kituo cha Afya cha Katoro kimezidiwa. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri kwa kweli mtutazame kwa macho mawili. Ninajua kwamba wewe umeshafika Katoro, kwa hiyo, nakuomba kabisa, ikiwezekana tuma timu maalum ije iangalie changamoto ilivyo kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake wanahangaika sana. Mara kwa mara hata ukienda katika hosptali ya rufaa ya mkoa zaidi utakuta watu wengi wanatoka Katoro, kila dakika gari la Katoro linapeleka wagonjwa kwenye Hospitali ya Rufaa. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri atuangalie; na Mheshimiwa Waziri Mkuu ameshatuahidi kwa hiyo tunaomba sasa utekelezaji uweze kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo pia, katika Sekta hii ya Afya tuna upungufu mkubwa sana wa watumishi. Kwenye Wilaya ya Geita tu tuna upungufu wa takribani watumishi zaidi ya 150, ni wengi sana. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali katika bajeti hii tuangalie namna ya kuwekeza zaidi kuajiri watumishi katika Sekta ya Afya ili hatimaye tuweze kufikia ile azma ya kuweza kupunguza vifo kwa ajili ya akina mama pamoja na watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini kabisa kwamba kwa juhudi ambazo zinaendelea kufanyika na Serikali ile changamoto iliyokuwepo katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa ya vifo vya akina mama tuna imani kabisa kwamba itakwenda kupungua sasa. Cha msingi, naiomba Serikali iendelee kutuongezea kipaumbele, yaani mtupe kipaumbele zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sekta hiyo hiyo ya Afya, kuna Kituo changu cha Afya cha Bukoli ambacho kwa muda mrefu sana kimekuwa na changamoto kubwa sana. Hatuna gari la wagonjwa katika eneo hilo, tarafa nzima haina gari la wagonjwa. Bahati nzuri Mheshimiwa Waziri aliniahidi. Kwa hiyo naomba sana, mara magari yakipatikana, tunaomba sana ukumbuke Kituo hiki cha Afya cha Bukoli kiweza kupatiwa gari la wagonjwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile naomba Wizara ya TAMISEMI pamoja na Wizara nyingine kama Wizara ya Nishati. Wizara ya Nishati kuna changamoto kubwa sana, unakuta eneo umeme umefika, lakini unakuta kwenye huduma za afya, labda kwenye elimu; shule za sekondari hakuna umeme. Hii ipo, kwa mfano, Kituo cha Afya Bukoli, pamoja na kwamba umeme umefika Bukoli mwaka 2014 lakini mpaka leo kituo cha afya hakina umeme. Kwa hiyo, upasuaji hauwezi kufanyika bila ya kuwa na umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi wamefuatilia lakini wanaambiwa ili kuweka tu umeme pale watoe shilingi milioni 10. Yaani kituo cha afya kupatiwa umeme lazima shilingi milioni 10 zitolewe zilipwe TANESCO. Kwa hiyo, ninaiona hii ni changamoto kubwa sana. Kwa hiyo, naiomba Wizara ya TAMISEMI pamoja na Wizara nyingine; Wizara ya Nishati, hebu tuangalie namna bora ya kuweza kufanya kazi kwa ushirikiano. Hapa tutaweza kuokoa maisha ya wananchi wetu na wataweza kupata huduma zao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kipekee kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Utawala Bora. Nimeangalia katika kitabu chake ukurasa wa 83 ameweza kuzungumzia jinsi ambavyo ameandaa Mpango wa MKURABITA wa kurasimisha maeneo maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini katika Mkoa wa Geita. Kwa hiyo, nitumie fursa hii kumpongeza sana kwa mpango huu. Naomba utekelezaji uweze kufanyika kama ambavyo ameweza kupanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunafahamu mkoa wetu, tunategemea shughuli za uchimbaji wa madini. Kwa miaka mingi wachimbaji hawa walikuwa wadogo wadogo, walikuwa hawawezi kutambulika. Kwa mpango huu sasa wa kurasimisha wachimbaji wadogo, tuna imani kubwa kwamba tutaweza kupata mchango mkubwa sana katika pato la Taifa kwa ujumla pamoja na mkoa wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Lolesia Bukwimba.

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi ninaunga mkono hoja. Ahsante sana kwa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara hii muhimu kabisa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Manaibu Waziri pamoja na watumishi wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanayoifanya tunashuhudia jinsi ambavyo kazi kubwa inafanyika katika Taifa hili, barabara zinajengwa, flyover zinajengwa lakini barabara mbalimbali za mikoa zinajengwa. Nichukue nafasi hii kipekee kupongeza kwa kazi nzuri inayofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze na barabara muhimu kabisa katika Mkoa wetu wa Geita barabara ya kutoka Kahama kwenda Bukoli mpaka Geita, ni barabara muhimu sana kiuchumi, kumbuka katika Mkoa wa Geita na Mkoa wa Shinyanga ni mikoa ambayo imebobea katika masuala mazima ya madini, na kwa sababu hiyo tunahitaji barabara hii iwe ya lami ili iwezeshe shughuli za uchiumbaji wa madini ziende vizuri zaidi usafirishaji wa mizigo mbalimbali. Kwa hiyo niseme tu kwamba barabara hii ni muhimu sana na kila bajeti barabara hii huwa inakuwepo kwenye bajeti lakini kwenye utekelezaji sijawahi kuiona. Kwa hiyo nitumie fursa hii kuiomba Serikali iwekeze fedha sasa nimeona kwenye bajeti imeweka fedha kiasi fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninaomba barabara hii ianze kujengwa sasa kwa kiwango cha lami, barabara hii ni barabara ya kiuchumi, barabara hii imekuwepo kwenye bajeti kuanzia wakati wa Awamu ya Nne ya Mheshimiwa Rais Kikwete katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi barabara hii imekuwepo kila Ilani inakuwepo barabara hii kuwekewa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa Serikali awamu hii barabara hii ianze kujengwa kwa kiwango cha lami kwa kuanzia Geita kwenda Bukoli mpaka Kahama. Kwa kuwa tunafahamu kuna mradi mkubwa mgodi mkubwa wa Geita lakini pia kuna mradi mkubwa mgodi wa Bulyang’huru, ambao wote hawa wanafanya shughuli za uchumbaji wa madini katika mikoa yetu, kwa hiyo, tukiimarisha barabara hizi nina uhakika shughuli hizi za uchimbaji zitaweza kunufaisha Taifa letu kwa kiwango kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna barabara muhimu kabisa ya kutokea Katoro - Bukombe ambapo barabara hii pia ni muhimu sana kiuchumi katika Mkoa wetu wa Geita niombe Serikali pia iangalie uwezekano wa kuiwekea barabara hii lami ili kuwezesha uchumi ndani ya Mkoa kuwa mchumi mzuri. Ninafahamu sera yetu ya Taifa inasema kwamba mikoa yote itaunganishwa kwa kiwango cha lami, jambo ambalo ni la msingi sana na ndio maana ninatolea msisitizo kwamba tuunganishe Mkoa wa Geita na Mkoa wa Shinyanga ili hatimaye uchumi wetu uweze kwenda vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile katika upande wa barabara ziko barabara ambazo zimekuwa ni muhimu sana kuchumi kwa mfano, kuna barabara ya kutokea Katoro kwenda Nyang’wale kupitia Kamena - Nyalwanzaja- Busanda ni barabara ambayo kwa muda mrefu tumeiomba iwe barabara ya mkoa imekuwa ni barabara ya halmashauri lakini sasa hivi naiombea iwe barabara ya mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kwa bahati nzuri mwaka jana kuna watu walitoka Wizara ya Ujenzi walikuja kuikagua barabara hii lakini kwenye bajeti sijaweza kuiona haijapandishwa hadhi mpaka sasa. Niombe barabara hii pia kwa umuhimu wake niombe ipandishwe hadhi iwe barabara ya Mkoa ili hatimaye iweze kuwahudumia wananchi waliowengi kwa sababu tunatambua kabisa vijijini wananchi tunahitaji barabara nzuri ambazo ziwezeshe katika kuimarisha uchumi wa wananchi katika maeneo yote kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo mbalimbali, mazao, kupeleka katika viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaomba sana Serikali iangalie barabara hii ni muhimu kuweza kuipandisha kutoka halmashauri kwenda kwenye kuwa barabara ya Mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna barabara zingine ambazo tunaishukuru Serikali kwamba imeweza kupandisha hadhi barabara ya kutokea Mbogwe kupitia Bukoli kwenda mpaka Bujula kuwa barabara ya Mkoa ninaishukuru sana Serikali na naipongeza kwa hatua hiyo niombe sasa mwaka huu barabara hii ianze kutengenezwa vizuri ili wananchi waweze kunufaika zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kuhusiana na suala la mawasiliano. Mawasiliano ni jambo la msingi na ni suala muhimu sana kwa ajili ya wananchi hasa waishio vijijini. Nitumie fursa hii kuiomba Wizara iangalie sana maeneo ya vijijini. Natambua kwamba Mheshimiwa Waziri alituambia tupeleke majina ya kata zote ambazo hazina mawasiliano ya simu. Na mimi nilipeleka majina ya kata mbalimbali ikiwemo Kata ya Nyamalimbe, ikiwemo Kata ya Bujura ambazo zina matatizo makubwa sana ya mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitumie fursa hii kuiomba Serikali iangalie maeneo haya. Najua kibiashara pengine hayalipi sana, lakini kwa kuwa kuna Mfuko ule wa UCAF naiomba Serikali iwekeze zaidi vijijini kupeleka mawasiliano ili hatimaye kuimarisha zaidi wananchi waweze kufanya kazi zao kwa mawasiliano. Tunatambua mawasiliano ni kitu muhimu. Kupitia mawasiliano tunarahisisha biashara mbalimbali na zinaweza kufanyika bila shida yoyote. Kwa hiyo, naiomba Serikali iangalie sana katika suala hili la mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ziko kata mbalimbali ambazo zinahitaji mawasiliano kama ambavyo nimezitaja kwenye Jimbo la Busanda, lakini pia na maeneo mengine ya vijijini, kwani maeneo ya vijijini mengi yanahitaji mawasiliano ya simu ili kuweza kuimarisha na kuwezesha kustawisha zaidi hali ya uchumi katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, natumia fursa hii kuiomba Serikali iwekeze zaidi katika Mfuko wa UCSAF ili hatimaye kuweza kuyafikia maeneo mengi ya vijijini ambayo yamekuwa na changamoto kubwa sana ya mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile katika upande huo wa mwasiliano napenda kuomba Serikali iangalie minara. Minara mingi ambayo imesimikwa katika maeneo mengi wanakuwa hawalipi kwenye vijiji wanapochukua yale maeneo kwa ajili ya kusimika minara. Kuna changamoto kubwa, watu wengi wanafuatilia sana, lakini hawapati haki zao. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie pia suala hili hasa wananchi ambao ni wanyonge ambao wame… (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Lolesia Bukwimba. Mheshimiwa…

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. Nashukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na niweze kuchangia Mpango wa Taifa wa mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa lile agizo lake la kwamba Halmashauri ziweze kuhamia kwenye maeneo yao ya utawala. Mimi kidogo kwenye Jimbo langu tumepata changamoto, baada ya kuwa tumehamia Nzela kwa kweli jiografia imekuwa ngumu sana. Wananchi wa Busanda walikuwa wanafuata huduma kwenye ofisi za zamani yaani ni karibu kilomita 40/50 hivi lakini sasa hivi inabidi waende zaidi ya kilomita 100 kwa ajili ya kufuata huduma. Naomba Serikali pengine itupatie Halmashauri nyingine ili wananchi waweze kupata huduma vizuri na kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nilipo nimekuwa nikipata simu nyingi kutoka kwa Watendaji wa Serikali, Walimu Wakuu wa Shule lakini vilevile Watendaji wa Vijiji na Kata wanapata shida sana. Jambo ambalo siku za nyuma angetumia siku moja sasa hivi inabidi atumie siku mbili aende Nzela kwenda kusainisha cheki arudi, alale mjini ili kesho yake aweze kupata huduma, ni shida sana. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iangalie suala hili. Hata ikiwezekana kwa kuwa mwanzo ofisi zilikuwa Mji wa Geita basi turudishwe hata kama ni Mji kama hatutapatiwa Halmashauri sasa hivi ili angalau wananchi waweze kupata huduma kwa ukaribu zaidi kama ambavyo Serikali inakusudia kusogeza huduma kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la wakulima wa pamba. Kumekuwa na changamoto kubwa sana kwamba wananchi wameuza pamba yao lakini mpaka sasa kuna baadhi ya wananchi hawajaweza kulipwa haki zao, ni kilio kikubwa sana. Kwa hiyo, pia hilo naomba Serikali iweze kulifanyia kazi wananchi waweze kulipwa fedha zao kwa sababu wameuza pamba kwa mkopo sasa umeingia msimu mpya wanatakiwa angalau wanunue tena mbegu lakini wanashindwa kwa sababu hawajaweza kupewa fedha zao kutokana na mauzo ya pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo sasa nilikuwa naomba kwenye Mpango huu wa Serikali katika suala la kilimo hasa mazao ya biashara Serikali iangalie uwezekano wa kuwekeza zaidi fedha nyingi kwenye viwanda vya kuongeza thamani ya mazao. Kwa mfano, katika zao la pamba, Serikali iweke fedha nyingi kuhakikisha kwamba viwanda vya kuchakata pamba vinakuwepo ili hatimaye masoko ya pamba yawepo kwa sababu haiwezekani wananchi wanalima pamba ya kutosha lakini masoko hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa na viwanda vingi vya kuchakata mazao, nina uhakika kwamba wananchi wataweza kupata fedha zao kwa wakati na hatimaye watu wengi watahamasika zaidi kuongeza ulimaji wa pamba kwa wingi. Kwa hiyo, katika bajeti ijayo kwenye kilimo, Serikali iwekeze zaidi kwenye viwanda vya kuchakata mazao ya biashara ili hatimaye kuweza kuongeza thamani ya mazao hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kweli inafanya kazi kubwa sana kwa sababu Mpango huu wa Miaka Mitano naufuatilia mwaka hadi mwaka na kweli mipango yake na utekelezaji vinaonekana. Kwa mfano, katika sekta ya afya tumeona jinsia Serikali ambavyo imeweza kutekeleza mambo makubwa sana yanayoonekana katika taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya afya, Serikali imetujengea zahanati na vituo vya afya pamoja na Hospitali za Wilaya lakini vilevile tuna upungufu mkubwa sana wa watumishi katika sekta hii. Nitumie nafasi hii sasa kuomba katika bajeti tuangalie umuhimu wa kuweza kuweka bajeti kubwa kwa ajili ya kuajiri watumishi katika sekta ya afya kwa sababu upo upungufu mkubwa sana pamoja na kwamba tunajenga vituo lakini kama hakuna mtaalam wa kutoa huduma bado tutakuwa hatujatenda haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la umeme wa REA. Naipongeza sana Serikali kuona umuhimu wa kuwa na umeme vijijini. Wananchi wanaoishi vijijini wamehamasika sana kuhusiana na suala la umeme. Niombe Serikali iendelee kuwekeza fedha nyingi hasa kwenye upande wa kupeleka umeme vijini kwa sababu vijijini ndipo ambako wanaishi wananchi wengi, asilimia kubwa ya Watanzania wapo vijijini. Tukiwekeza kwenye suala la umeme wa REA vijijini kwa wingi kabisa, vijiji vikapata umeme, mimi najua kwamba tutaweza kufikia ile azma ya Serikali ya Tanzania ya viwanda lakini pia tutaweza kufikia ule uchumi wa kati mpaka mwaka 2020 - 2025. Kwa hiyo, niombe sekta ya umeme ipewe kipaumbele kikubwa zaidi ili wananchi waishio vijijini waweze kupata umeme huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu kila napokwenda Jimboni wananachi wanaulizia kuhusu umeme, kila mtu anataka umeme, kila kijiji kinahitaji kupewa umeme. Sina uhakika sehemu zingine lakini ni karibu kila sehemu katika nchi ya Tanzania sisi ambao tunatoka Majimbo ya vijijini tunahitaji umeme. Tunaomba sana wanapopanga bajeti tuhakikishe suala la umeme lipewe kipaumbele cha kutosha ili wananchi walio wengi waishio vijijini wapatiwe umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la msingi kabisa ni suala la barabara za vijijini. Mimi nazungumzia vijijini kwa sababu Jimbo langu ni vijijini. Bajeti ya TARURA haitoshi, tuongeze bajeti zaidi kwenye TARURA kwa sababu tukiwa na barabara nzuri vijijini tutawawezesha wananchi wetu kuweza kufanya shughuli zao na kuuza mazao yao vizuri na kwa wakati. Kwa hiyo, niombe tuongeze bajeti zaidi TARURA ambako ni barabara za mjini na vijijini lakini zaidi kwenye vijiji ambako ndipo kuna changamoto kubwa sana ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye suala la UKIMWI, tunafahamu kabisa kuna takwimu zinaonesha kwamba vijana kati ya miaka 15 mpaka 24 wanapata maambukizi makubwa sana ya UKIMWI lakini zaidi ya hapo asilimia 60 ya hao vijana ni watoto wa kike, jambo hili kwa kweli ni la kusikitisha. Kwa hiyo, naomba kwenye Mpango wa Taifa na bajeti tuone umuhimu wa kuwekeza mpango zaidi kuweza kunusuru suala hili hasa kupunguza maambukizi ya UKIMWI kwa vijana wetu ambao ndiyo Taifa tunalitegemea kesho na nguvu kazi ya Taifa. Kwa hiyo, niombe Serikali iangalie umuhimu, ikiwezekana tuendelee kuhamasisha zaidi masuala haya ya UKIMWI ili wananchi waendelee kujiepusha na na masuala haya ya UKIMWI. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu UKIMWI huu tunapoteza Taifa hasa vijana wetu, kwa hiyo, tuwekeze bajeti zaidi kuendelea na kampeni kuhusiana na suala hili la UKIMWI. Nasema hivyo kwa sababu miaka ya nyuma mara kwa mara kulikuwa na uhamasishaji sana kuhusu kuepuka suala la UKIMWI lakini leo hii tumepunguza kidogo hiyo kasi na ndiyo maana pengine maambukizi yameanza upya, yameongezeka zaidi kwa kipindi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, naipongeza Serikali hasa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa makusanyo ya fedha hasahasa kwa kielektroniki. Naomba tuendelee kuwa na msisitizo zaidi kwamba kila mtu ukinunua kitu uchukue risiti kwa sababu kuna wafanyabiashara wengine hawatoi risiti kwa hiyari hivyo tuendelee kuweka msukumo. Sasa hivi tumepunguza kidogo msukumo lakini tuendelee kama ambavyo Rais ameendelea kusisitiza, tuendelee zaidi kuhamasisha, kusisitiza kwa sababu wananchi wakilipa na kupata risiti, mapato haya yanaenda moja kwa moja kwenye Pato la Taifa yanaingia TRA kwa ajili ya mapato ya Taifa letu. Kwa hiyo, naomba sana Serikali kupitia Wizara hii iangalie namna ya kuendelea kusisitiza suala la kudai risiti na kulitolea msukumo mkubwa ili tuendelee kupata mapato zaidi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, napenda kuendelea kusema kwamba Serikali aingalie…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Lolesia Bukwimba kwa mchango wako mzuri.

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika taarifa hizi za Kamati. Kwanza nianze kipekee kabisa kuwapongeza Wenyeviti wote pamoja na Wajumbe wa Kamati hizi kwa kazi kubwa ambayo imefanyika. Kusema ukweli mmechambua vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujikita zaidi katika Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu shughuli zake za utekelezaji katika mwaka uliopita. Kabla sijaanza, nitoe kabisa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais kwa sababu tulikuwa na changamoto kubwa sana katika upande wa Sekta ya Afya lakini Serikali kupitia Mheshimiwa Rais ameweza kutupatia hospitali ambayo itajengwa katika eneo la Mji Mdogo Katoro, pia ni hospitali ambayo ni ya Umoja pamoja na Uselesele. Hii yote ni kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo katika Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba kwa kweli Serikali inafanya mambo makubwa sana hasa katika Serikali za Mitaa. Wote tumeshuhudia jinsi ambavyo mambo mengi yamefanyika. Siku za nyuma ilikuwa ni changamoto kubwa sana katika Sekta ya Afya, lakini kwa kweli kwa sasa hivi tunaona jinsi ambavyo Serikali inafanya mambo makubwa sana kupitia TAMISEMI. Tumeona katika Sekta ya Afya lakini pia katika Aekta ya Elimu Serikali imeendelea kutekeleza mambo mengi kwa kushirikiana na wananchi. Yote haya nina kila sababu ya kuweza kushukuru na kuipongeza Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo nilitaka kulizungumza hapa ni suala kubwa kuhusu barabara ambazo ziko chini ya TARURA. Kamati imezungumzia vizuri sana katika ukurasa wa tisa wa taarifa hasa ya Kamati ya Utawala wa Serikali za Mitaa kuhusu utekelezaji wa ujenzi wa barabara kupitia TARURA. Ni kweli kwamba barabara za TARURA zina changamoto kubwa sana na nilikuwa ninaomba kama ambavyo Kamati imeshauri, kwamba kutokana na ufinyu wa bajeti kwa bajeti zilizopita na mwaka huu tumeshuhudia kwamba kuna mvua nyingi sana ambazo zinaendelea Tanzania nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba Serikali katika bajeti ijayo kama ambavyo Kamati imesema kwamba waangalie uwezekano mkubwa wa kuweza kuongeza bajeti hasa katika TARURA ili kuweza kushughulikia barabara ambazo imekuwa ni changamoto kubwa sana. Tukiangalia kila sehemu katika nchi yetu ya Tanzania mvua zinanyesha kwa wingi lakini pia barabara hazipitiki kwa kiasi kikubwa, madaraja yamebomeka. Kwa hiyo, nilikuwa naomba Serikali sasa pengine iangalie sana suala hili la TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia, nami pia nikiangalia kwenye Jimbo langu ninaona kabisa kwamba bajeti za TARURA zinakuwa ni kidogo barabara za TARURA ni nyingi, lakini bajeti inayotengwa ni kidogo. Kwa hiyo, kama Mbunge nilikuwa naishauri Serikali iangalie suala hili kwa sababu barabara ndiyo kiungo kikubwa katika maendeleo ya jamii katika maeneo yetu ya vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona jinsi ambavyo mwananchi hawezi kusafiri kutoka point moja kwenda point nyingine. Kama barabara haipo kwa kweli changamoto inakuwa ni kubwa. Kwa hiyo, naomba sana kama ambavyo Kamati imesema, tuombe TARURA iongeze bajeti ya kutosha ili kuweza kuboresha barabara za mijini na vijijini ili hatimaye tuweze kuona utekelezaji na uboreshaji wa huduma mbalimbali za kijamii katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika upande wa TAMISEMI tumeshuhudia jinsi ambavyo Serikali inajenga Hospitali na Vituo vya Afya vilivyoboreshwa; tunaipongeza sana. Nilikuwa naomba sasa katika bajeti ijayo pengine Serikali iangalie umuhimu wa kuongeza watumishi katika sekta hasa ya Afya ambapo tuna upungufu mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia katika sehemu mbalimbali Waheshimiwa Wabunge wengi hapa wanalalamikia kwamba kuna upungufu mkubwa wa watumishi, ikiwemo pia kwenye halmashauri yangu kwakweli kuna upungufu mkubwa sana ambapo wanahitajika zaidi ya watumishi 200 katika Seta ya Afya.

Kwa hiyo nilikuwa ninaomba pengine Serikali kwa kuwa imeboresha zaidi katika miundombinu hasa kwa kujenga vituo vya afya na hospitali, nilikuwa naomba katika bajeti zijazo iangalie uwezekano wa kuangalia suala zima la kuhakikisha watumishi wanapatikana wa kutosha ili sasa tuweze kuhakikisha kwamba huduma sasa inaboreshwa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi hiki wananchi wanahudhuria kliniki au kwenye vituo vya afya, lakini kwa sababu ya wingi wa watu unakuta watumishi wanakuwa wachache, na hatimaye kunakuwa na changamoto kubwa sana katika utoaji wa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Serikali imeboresha kwa kiasi kikubwa, imeongeza dawa za kutosha; na ukiuliza hata sasahivi vijijini watu wanafurahia sana huduma kwa kiasi kikubwa. Juzi nilikuwa napigiwa simu naambiwa hata ukienda katika hospitali ya Rufaa ya Wilaya na hata ile ya Mkoa tumeshuhudia kwamba wazee wametengewa sehemu maalum kwa ajili ya kupewa huduma. Kwa kweli huduma zimeboreshwa vizuri, lakini tu ni mpungufu madogo hasa katika upungufu wa watumishi katika maeneo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile pamoja na sekta ya afya, napenda tu kuomba mimi binafsi kwenye jimbo langu tumeshuhuda Mheshimiwa Rais ametoa maelekezo kwamba kila halmashauri ihamie kwenye maeneo yao ya utawala. Sisi katika halmashauri yetu, ofisi yetu ya halmashauri imehamia Nzela, ambako kidogo ni mbali kiasi kwamba baadhi ya wananchi ndani ya halmashauri wanapata shida kubwa sana katika kuzifikia huduma hizi katika halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nitumie fursa hii kuiomba Serikali pia iangalie changamoto hizi. Najua inazifanyia kazi, lakini naomba sasa iharakishe jambo hili, ipitie hizi halmashauri ambazo zimefanya maamuzi ya kuhamia kwenye maeneo yao ya utawala kuangalia kama kuna changamoto ili hatimaye kuweza kuzirekebisha.

Nilipokuwa jimboni kwakweli maeneo mengi hasa vijijini watu wamekuwa wakiniulizia sana kuhusu suala hili, hasa la kuhamishiwa Halmashauri Nzela; ambako sasahivi zaidi ya kilometa 100 wananchi wanahangaika kwenda kufuata huduma. Hili pengine pia limechangia hata mapato kushuka, kwa sababu wengine wanajiuliza niende kweli, nikaandikiwe kibali Nzela kule halafu nije nilipe mapato. Kwa hiyo kumekuwepo pia changamoto kubwa sana katika suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu nimepata nafasi nilikuwa naomba tu Serikali iweze kuliangalia suala hili hasa kwangu kwa sababu watu wengi sana wanapata changamoto, kama ilivyofanya katika Halmashauri ya Lindi, Mkoa wa Lindi pamoja na Mkoa wa Morogoro, iweze kufanya marekebisho basi na kwenye mikoa baadhi kama halmashauri yangu ya Geita basi Serikali iangalie itusaidie, itupatie halmashauri mpya. Kama hakuna uwezekano huo basi Serikali iangalie namna utaratibu mzuri ili wananchi waweze kupata huduma kwa karibu kwa sababu lengo la Serikali ni kuona kwamba wananchi wanapata huduma kwa karibu zaidi kuliko kwenda kufuata huduma mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninaunga mkono hoja kwa ajili ya Kamati hizi. Najua mambo mengi mazuri yamezungumzwa, nikiamini kwamba Serikali inasikiliza na kuweza kuyafanyia kazi yaliyobakia. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara ya Nishati, Wizara ambayo ni muhimu sana kwa uchumi wetu wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Dkt. Kalemani, kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye Wizara hii; Naibu Waziri wetu ambaye ni Mheshimiwa Subira Mgalu; Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa REA, kwa kweli kazi wanayoifanya ni kazi ya uhakika nichukue nafasi hii kipekee kabisa kuwapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza kwa sababu gani, kwa kweli kwa kipindi kirefu, kumekuwa na tatizo kubwa la umeme, vijiji vingi katika nchi ya Tanzania vilikuwa havina umeme, lakini leo hii kutokana na taarifa ni vijiji vingi sasa vya Tanzania vimeweza kupatiwa umeme, vijiji zaidi ya 5,000 ni jambo ambalo la kipekee sana, tunapenda kupongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nipongeze kwa ajili ya mipango iliyopo, kwa sababu mpaka mwaka 2020 wanakusudia kufikia vijiji zaidi ya 10,278. Kwa hiyo mimi binafsi nina imani kubwa kwamba hata kwenye Jimbo langu la Busanda, vijiji vyote vitaweza kupatiwa umeme kwa mpango huu ambao wameuweka.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kanda ya Ziwa kuna Mradi mkubwa wa umeme wa kilovoti 220, kutoka Bulyanghulu kwenda Geita na mradi huu unapitia katika maeneo katika Jimbo langu la Busanda. Naomba sana, kwamba kupitia mradi huu viko vijiji 10 ambavyo vinatakiwa kupata umeme huu wa gridi ya Taifa, hivyo basi wakati ambapo utekekelezaji unavyoendelea naomba vijiji hivi viweze kupatiwa umeme mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo pia, jana nilikuwa napiga simu kule jimboni nimeambiwa tayari Wakandarasi wako wanafanya kazi maeneo ya Bujura. Kwa kweli, ni kiasi cha kupongeza kwa kazi kubwa ambayo Wizara inafanya kwa kweli wanafanya kazi njema sana kwa ajili ya Watanzania wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua kwamba suala la umeme, ni suala muhimu sana, ili tuweze kufikia uchumi wa kati katika Taifa la Tanzania, lazima vijiji vyetu viweze kupata umeme wa uhakika na ndiyo kazi ambayo Serikali inafanya kwa sasa hivi. Kwa hiyo niombe Serikali iweze kuongeza bajeti kwenye Miradi ya REA, kwa sababu REA ndiyo ambayo tunaitegemea kuweza kusambaza umeme vijijini. Kwa hiyo niombe sana bajeti ya REA, iweze kuongezeka zaidi ili hatimaye basi vijiji vya Tanzania viweze kupatiwa umeme kupitia REA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda pia kuiomba Serikali kwamba wanapofanya utekelezaji wa miradi hii umeme vijijini wahakikishe kwamba zile sekta muhimu za umma kwa mfano, katika shule, Vituo vya Afya, pamoja na sekondari, kwenye huduma za kijamii, tuhakikishe kwamba umeme huu unapelekwa kipaumbele katika sekta hizo. Nasema hivyo kwa sababu, katika maeneo mengi ya vijijini ambako wamepata umeme, unakuta shule hazina umeme, Vituo vya Afya havina umeme, mfano tu Bukoli pale umeme wamepata umeme tangu mwaka 2014 lakini hivi sasa naongea Kituo cha Afya Bukoli hakijaweza kupatiwa umeme mpaka sasa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa Bukwimba, ahsante sana.

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ili waweze kutekeleza miradi hiyo katika vijiji hivyo. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuipongeza Wizara katika usimamizi wa elimu. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri aliyofanya. Vilevile nimpongeze Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu umejikita zaidi katika elimu na mafunzo ya ufundi stadi (VETA). Katika kitabu cha bajeti cha mwaka 2017/2018 Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imepanga kutimiza malengo yafuatayo; itaendelea kufuatilia ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi vya mikoa mipya ya Njombe, Geita, Simiyu na Rukwa. Maelezo yanapatikana katika kitabu cha hotuba ukurasa wa 96.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sera ya Taifa inasema kila Mkoa na kila Wilaya kuwepo na Chuo cha VETA, nikiangalia katika Mkoa wa Geita wenye Wilaya tano hakuna kabisa Chuo cha VETA katika Wilaya zote na katika Mkoa. Wananchi wa Mkoa wa Geita tunayo mahitaji makubwa sana ya elimu ya ufundi stadi. Watoto wengi sana wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari ambao hawaendelei na masomo ya ngazi za juu hawana ujuzi wa kuwawezesha kujiendeleza katika maisha yao ya kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo tukiwa na vyuo vya VETA katika kila Wilaya itasaidia kuwawezesha vijana hawa kuwa na ujuzi. Vilevile Serikali ya Awamu ya Tano imekusudia kuwa na Tanzania ya viwanda. Hivyo tunahitaji vijana wawe na ujuzi ili tuweze kufikia azma ya Tanzania ya viwanda. Kwa melezo haya ningependa kujua na kupata maelezo ya kina ni lini ujenzi wa Chuo cha VETA Mkoa wa Geita utaanza rasmi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewiwa kuuliza kutokana na maelezo kwenye bajeti kwamba Serikali itandelea kufuatilia ujenzi, lakini haielezi bayana juu ya kuanza kwa ujenzi wa chuo hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya machache, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. LOLESIA J. M. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuchukua fursa hii kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa kuwasilisha hotuba vizuri juu ya maendeleo na utekelezaji kwa ujumla wa Wizara. Vilevile niwapongeze kwa dhati watumishi wote wa Wizara kwa kazi nzuri ya ulinzi wa Taifa letu. Hii imewezesha kuwepo kwa hali ya utulivu na amani ya nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishukuru Wizara kwa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa vijana wetu kwani wanapata maarifa na ujuzi hasa katika stadi za kazi zinazowawezesha kujiajiri na kujitegemea. Hivyo, ninaomba na kuishauri Serikali kuongeza idadi ya vijana wa kujiunga na JKT kutoka 20,000 hadi 25,000 kwa mwaka 2017/2018, hii itasaidia vijana wengi zaidi kujishughulisha kutokana na ujuzi wanaoupata kutokana na mafunzo ya JKT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo muhimu ninalopenda kuwasilisha ni juu ya wapiganaji vita vya Kagera. Wapo wanajeshi wengi nchini Tanzania wanadai mafao yao. Mwaka jana niliuliza juu ya suala hili na katika maelezo ya wanajeshi hawa ni kwamba Serikali Awamu ya Nne ya Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete waliahidiwa kulipwa mafao yao, mpaka sasa hakuna chochote. Nimeangalia kwenye bajeti iliyowasilishwa ya mwaka 2017/2018 sijaona kabisa kuzungumziwa suala hili. Ninaomba Mheshimiwa Waziri, nipate maelezo ya kina juu ya suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimelileta suala hili kutokana na wanajeshi walioko Jimboni kwangu Busanda wamekuwa wakifuatilia sana juu ya suala hili, ninaomba nipate maelezo ya kina na ufafanuzi juu ya suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo haya, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze maelezo yangu kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake aliyowasilisha Bungeni. Nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara. Sera ya Taifa inasema kuwa umbali wa kupata maji safi na salama usizidi mita 400 kutoka kwenye makazi. Hali halisi kwa sasa bado ni changamoto kwani wananchi wanasafiri umbali mrefu sana kilomita moja na zaidi kwa baadhi ya maeneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Ilani ya CCM ya mwaka 2015 – 2020 inasema hadi kufikia mwaka 2020 zaidi ya asilimia 70 ya wananchi vijijini watakuwa wanapata maji safi na salama. Leo ni mwaka 2017 ni miaka mitatu tu kufikia 2020 lakini utekelezaji hauonekani kabisa. Nimeangalia bajeti, fedha zilizotengwa katika mkoa wangu zimeelekeza tu katika kuboresha miji. Majimbo yaliyopo vijijini, sijaona mpango wowote. Je, tutawezaje sasa kufikia malengo ya asilimia 70 wakati kila bajeti hakuna mpango wowote?

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa majumuisho ningependa kufahamu mpango wa kupeleka maji katika Jimbo la Busanda. Kwanza tumezungukwa na Ziwa Victoria, naomba nipate mpango wa Serikali wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Jimbo la Busanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, naishauri Serikali iunde Wakala wa Maji Vijijini. Hii itasaidia utekelezaji wa miradi ya maji vijijini kama ilivyo REA. Miradi mingi ya maji vijijini tunaona inasuasua sana hasa ni kutokana na kutokuwa na usimamizi mzuri. Ni imani yangu kwa usimamizi kupitia Wakala wa Maji Vijijini utawezesha ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maji vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ni juu ya ongezeko la fedha kufikia shilingi mia kutokana na manunuzi ya petrol/diesel. Fedha hii ipelekwe kwenye Mfuko wa Maji. Vile vile tunaomba asilimia 70 ya fedha hii ilenge kuboresha miradi ya maji vijijini. Hii ni kutokana na ukweli kwamba katika bajeti iliyopita fedha hizi za Mfuko zilipelekwa kuboresha maji mijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wanaishi vijijini. Tukiboresha maji vijijini tutapunguza changamoto mbalimbali za magonjwa yatokanayo na maji machafu (water borne diseases). Vile vile tutainua uchumi unaopotea kwa kufuata maji umbali mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo yangu naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kazi nzuri. Vilevile pongezi ziwaendee Naibu Mawaziri pamoja na Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Wizara kwa utendaji mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri nimefurahi sana kwa maelezo yaliyopo katika ukurasa wa 11, aya ya 23, kipengele cha (iii) kwamba barabara ya Geita – Bulyanhulu Junction - Kahama (Lot 1 anda Lot 2) kuwa usanifu wa kina wa sehemu ya Geita – Bulyanhulu Junction (kilometa 58.3) na Bulyanhulu Junction – Kahama maandalizi ya ujenzi yanaendelea. Kwa kuwa barabara hii ni kiunganishi kikubwa sana na muhimu kiuchumi kati ya Mkoa wa Geita na Mkoa wa Shinyanga, naomba Serikali ianze ujenzi wa barabara hii maana ni ahadi ya muda mrefu sana kwa ajili ya kuimarisha uchumi katika mikoa husika. Vilevile ndiyo barabara muhimu inayotumika kusafirisha bidhaa na malighafi muhimu zinazotumika katika shughuli za uchimbaji wa madini. Ikikamilika barabara hii itasaidia kuinua uchumi utokanao na uchimbaji wa madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande na barabara za mkoa, kwanza nimpongeze sana Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Geita kwa kazi nzuri sana inayofanyika ndani ya Mkoa wetu wa Geita. Kwenye bajeti ipo barabara ya Geita – Bukombe ambapo Serikali imepanga kujenga kilometa moja ya lami, mimi nashukuru sana kwa mpango huu. Niombe kwamba baada ya kupitisha bajeti hii utekelezaji wa ujenzi wa barabara hii uanze mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo zipo ahadi za kilometa tano za lami katika Mamlaka ya Mji Mdogo Katoro ambazo ziliahidiwa na Mheshimiwa Rais kwenye mkutano wa kampeni mwaka 2015. Naomba pia ahadi hizi ziangaliwe na utekelezaji ufanyike. Tangu mwaka 2015 hadi leo ni miaka mitatu sasa sijaona utekelezaji wa ahadi hii. Naomba Wizara mlichukulie suala hili na mlifanyie kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru pia kwa mpango wa Serikali uliopo ukurasa wa 162 juu ya upanuzi wa vivuko mbalimbali ikiwemo ujenzi wa maegesho ya Bwina, Bukondo na Zumacheli katika kivuko cha Charo – Nkome. Kwa ujenzi wa maegesho ya Bukondo itarahisisha kwa kiasi kikubwa usafiri kwa wananchi wa Mkoa wa Geita kwani ilikuwa ni kilio kikubwa sana kwa wananchi wa maeneo ya Geita na Chato. Niombe sana ujenzi wa maegesho katika maeneo haya uanze mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa naomba barabara ya Katoro – Busanda – Nyakanga - Nyabulolo – Kamena – Nyamalimbe – Mwingiro ipandishwe hadhi kuwa barabara ya mkoa ili kurahishisha mawasiliano kati ya Wilaya ya Geita na Wilaya ya Nyang’hwale.

Mheshimiwa Naibu Spika, sina la ziada, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze mchango wangu kwa kutoa pongezi kwa hotuba nzuri inayogusa maisha ya Watanzania hasa walioko kwenye sekta ya madini. Hongera sana Mheshimiwa Angellah Kairuki, Waziri wa Madini bila kuwasahau Waheshimiwa Naibu Mawaziri wote wawili na watendaji wote wa Serikali. Hotuba imewatendea haki wananchi wa Jimbo la Busanda hasa wachimbaji wadogo wa madini wa maeneo yote ya Nyarugusu, Nyamyeye, Lwamgasa, Kaseme na Magenge.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa 49 na 50 hotuba imeongea bayana juu ya ujenzi wa mgodi wa mfano katika eneo la Lwamgasa. Tunashukuru sana kwa hatua iliyofikia ujenzi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napongeza kwa mpango wa Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia upya mkataba wa ubia kati ya STAMICO na Kampuni ya TANZAM 2000. Naunga mkono sababu za Wizara kuchukua hatua maana ni kweli kabisa kampuni hii imeanza kufanya kazi kwa muda mrefu, miaka nane sasa lakini hakuna uzalishaji wowote. Jambo hili limekuwa kero kubwa kwa wananchi wa maeneo husika maana maeneo mengi ya wananchi yamechukuliwa na mpaka sasa hawajalipwa fidia. Naomba Wizara ifuatilie suala hili kwani ni kinyume na taratibu na sheria za nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. LOLESIA J. M. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kushukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia kwenye hotuba hii. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kazi nzuri. Nimpongeze Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watumishi wote wa Wizara. Hotuba ya Mheshimiwa Waziri imeelezea kwa undani utekelezaji wa miradi mbalimbali kitaifa iliyofanyika katika mwaka wa fedha 2018/2019. Nimpongeze sana kwa utekelezaji mzuri uliofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Wizara ni juu ya uimarishaji wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi. Serikali ianzishe vyuo vya ufundi vyenye ubora ili watoto wakihitimu wawe na uwezo wa kujiajiri moja kwa moja. Kwa kuwa Sera ya Taifa inazungumzia juu ya kuwa na Chuo cha VETA kila Wilaya, nashauri sana sera hii itekelezeke kwa vitendo nikimaanisha kila wilaya ipate Chuo cha VETA chenye ubora. Hii itasaidia sana wahitimu wa darasa la saba na wahitimu wa kidato cha nne wapate ujuzi ili hatimaye wajiajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali irudishe mfumo wa zamani ambapo katika shule za msingi na shule za sekondari kulikuwa na elimu ya kujitegemea na shule zilikuwa na michepuo mbalimbali mfano kulikuwa na shule za sekondari zenye mchepuo wa biashara, zingine mchepuo wa kilimo, elimu hii ilikuwa inawajengea uwezo mkubwa wanafunzi kujitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naipongeza Serikali kwa ujenzi wa Chuo cha VETA katika Mkoa wa Geita. Kwa kuwa uhitaji wa elimu ya ufundi ni mkubwa sana, Serikali ione umuhimu wa kukamilisha mapema iwezekanavyo kwani katika Mkoa wa Geita na Wilaya zake hatuna Chuo cha VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukamilika mapema kwa VETA Mkoa itasaidia kupunguza changamoto katika mkoa wetu. Ujuzi wa ufundi stadi unahitajika sana katika kufikia azma ya Serikali ya Viwanda vilevile katika kuongeza kipato na kupunguza umaskini kwa wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Muswada huu muhimu kabisa kwa ajili ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuthubutu kuweza kuleta mabadiliko haya ya sheria. Vilevile nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kufanyia kazi kwa haraka zaidi na kuuleta Muswada huu hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Ibara ya 23, naipongeza sana Serikali kwa kuweza kubadilisha mrahaba kutoka asilimia tano kwenda asilimia sita katika madini ya vito. Vilevile katika madini ya metali kama mfano wa madini ya dhahabu kutoka asilimia nne mpaka asilimia sita, naipongeza sana Serikali kwa kuleta madadiliko haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishauri Serikali sasa kati ya hizi asilimia ambazo zimeongeka asilimia moja iende kuimarisha mikoa ambapo madini haya yanatokea. Nasema hivyo kwa sababu migodi hii inapoanzishwa kunatokea athari mbalimbali, watu wanakuwa wengi na huduma mbalimbali katika maeneo yale zinahitajika. Kwa hiyo, hiyo asilimia moja ikienda kwenye maeneo hayo nina uhakika kwamba maeneo hayo pia yataweza kunufaika. Kumekuwepo na malalamiko mengi ya muda mrefu wananchi wakilalamika hii migodi haitusaidii kitu chochote na mambo mbalimbali, lakini asilimia moja ikipelekwa tuna uhakika sasa itawezesha wananchi kuweza kunufaika katika huduma mbalimbali za kijamii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, migodi hii inaongeza idadi ya watu katika maeneo, kwa mfano Geita watu ni wengi sana kutokana na uwepo wa migodi hii, lakini huduma ziko vilevile hospitali ni ile ile moja yaani huduma mbalimbali
zinakuwa kidogo. Kwa hiyo, niiombe Serikali wanapo-wind up tunaomba hii asilimia moja tuhakikishe inaenda kwenye maeneo ambako madini haya yanapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni kuhusiana na suala la usimamizi wa migodi. Nimefurahishwa sana na jambo hili kwamba Serikali sasa itakuwa inasimamia migodi hii kuanzia katika hatua za uchenjuaji na uchimbaji wa madini. Kwa hiyo, niungane kabisa na Kamati iliposema kwamba usimamizi uanzie kwenye utafutaji. Ni mara nyingi katika maeneo mengi kumekuwa na udanganyifu mkubwa, watu wanatafiti wanatafiti kwa miaka mingi, miaka 20, 30 mtu anatafiti madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano tu mimi kwa vile niko kule Nyarugusu unaona kuna makampuni mengi ya utafiti na yametafiti kwa miaka mingi, miaka 10, 20 hakuna hata mgodi ambao unaanzishwa mahali pale. Kwa hiyo, naiomba sasa Serikali kwamba usimamizi uanzie hata kwenye utafiti ili mtu wetu wa Serikali awepo pale aweze kubaini kinachoendelea. Kwa sababu wengine wanatumia jina la utafiti lakini kiukweli wanachimba madini na kuweza kuchukua rasilimali za Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimefurahishwa sana na uwepo wa usimamizi hasa kwenye uchimbaji kwa maana kwamba migodi mingi imekuwa ikijifanyia shughuli zake bila kufahamu hata kinachoendelea na kujua thamani halisi ya dhahabu au rasilimali ambazo zinachimbwa na wenzetu na kupelekwa nje ya nchi. Kwa hiyo, usimamizi wa Serikali unapokuwepo tuna uhakika kabisa tutaweza kutambua hali halisi ya madini na thamani kamili ya madini yanayochimbwa pale lakini vilevile na wananchi wetu kuweza kufaidika kwa kodi ambazo zitapatikana kutokana na uhalisia wa madini haya ambayo ni rasilimali za Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kuishukuru Serikali kwa kuanzisha kamisheni kwa ajili ya usimamizi wa madini. Pengine kwa sababu kulikuwa hakuna chombo maalum cha usimamizi wa shughuli za rasilimali za Taifa ndiyo maana kumekuwepo na changamoto hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba …

(Hapa kengelee ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali (Na. 2) wa Mwaka 2019 (Toleo la Kiingereza).
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye Muswada huu wa Sheria ambao umeletwa mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, kipekee kabisa nianze kwa kuipongeza Serikali hasa Mheshimiwa Rais pamoja na Baraza la Mawaziri kwa kazi kubwa mnayoifanya. Kikubwa zaidi kwa hii hatua ambayo kwa muda mfupi tu wachimbaji wadogo na wachimbaji mbalimbali wametoa maelezo fulani kwa ajili ya kuomba Serikali kufanyiwa marekebisho leo hii tumeletewa Muswada kwa ajili ya marekebisho. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali na Mheshimiwa Rais, kwa kweli amewajali wachimbaji wadogo wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya wananchi na wachimbaji wadogo wa Geita na Tanzania nzima, nichukue nafasi hii kipekee kabisa kumpongeza na kumshukuru sana, hasa kwa ajili ya Muswada huu ambao umeletwa kwa ajili ya kupendekeza kuondoa kodi (withholding tax) kwa wachimbaji wadogo. Kwa hiyo, nashukuru sana kwa jambo hili, ni kubwa sana kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini katika nchi ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Sehemu ya Sita ya Muswada ambayo imekusudia kufanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura ya 148 ambapo sasa hivi ni asilimia zero, kwa maana kwamba wachimbaji wadogo hawatoi kodi yoyote ya Ongezeko la Thamani. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kupongeza sana Serikali pamoja na Wizara kwa ujumla kwa jambo hili kubwa ambalo limeweza kufanyika kwa wachimbaji wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo sasa, naomba tukishapitisha Muswada huu kuwa sheria Mheshimiwa Rais aweze kusaini ili hatimaye iweze kuwa sheria iweze kutumika kwa haraka. Pia niombe Wizara inayohusika iweze kuandaa zile taratibu na kanuni mapema zaidi ili hatimaye sheria hii iweze kutumika mapema kabisa na wananchi tuweze kunufaika na sheria hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kuleta Muswada huu hasa kwa ajili ya zabibu. Ni kwa muda mrefu tumekuwa tukisikiliza jinsi ambavyo watu wa Dodoma walikuwa wakilalamikia suala hili kwa sababu ya kodi mbalimbali ambazo zimekuwepo. Napongeza sana hatua hii, nina imani kabisa hata Wagogo sasa wataweza kunufaika zaidi na kwa sababu ndiyo Makao Makuu ya Nchi ya Tanzania itaneemeka vizuri sana kwa sababu masuala yao ya zabibu yameweza kuchukuliwa hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, sikuwa na mengi sana kikubwa zaidi ni kushukuru na kupongeza Muswada huu ambao umeletwa kwa haraka hapa Bungeni. Nilikuwa nashangaa yule anayehoji kwamba kwa nini umeletwa kwa haraka, mimi nashukuru sana kwa sababu Serikali inachukua hatua haraka kwa ajili ya kuondoa matatizo ya wananchi ili wananchi waweze kunufaika zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono Muswada huu kwa haraka zaidi. (Makofi)