Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Omari Mohamed Kigua (16 total)

MHE. OMAR M. KIGUA aliuliza:-
Ulipaji kodi ni chanzo kikuu cha mapato ya nchi kwa ajili ya maendeleo na Serikali inao wajibu mkubwa wa kuhakikisha kwamba wafanyabiashara, wakulima na wafanyakazi wanalipa kodi kwa mujibu wa sheria na ili Serikali iweze kukusanya kodi kwa ufanisi mkubwa ni lazima kuwe na Ofisi za TRA katika maeneo mbalimbali nchini:-
(a)Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwa na Ofisi ya TRA katika Wilaya ya Kilindi?
(b)Kwa kutokuwa na Ofisi za TRA Serikali haioni kama inadhoofisha maendeleo ya Wilaya hususani katika suala la mapato?
(c)Kwa kuweka Ofisi za TRA Wilaya ya Handeni na kuacha Wilaya ya Kilindi, Serikali haioni kama inawajengea wananchi tabia ya kukwepa kulipa kodi kutokana na umbali uliopo kati ya Wilaya hizo mbili?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a)Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kufungua Ofisi ya Mamlaka ya Mapato Wilayani Kilindi kama ilivyo katika Wilaya zingine. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ina mpango wa kufungua ofisi za Mamlaka ya Mapato katika Wilaya mbalimbali nchini ikiwemo Kilindi baada ya kukamilisha zoezi la utafiti na uchambuzi wa kina kuhusu fursa za mapato ya kodi zilizopo katika Wilaya zote ambazo hazina ofisi za TRA.
(b)Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzisha ofisi za Mamlaka ya Mapato katika Wilaya ni fursa mojawapo ya kuleta maendeleo katika eneo husika. Aidha, uamuzi wa kufungua ofisi ya Mamlaka ya Mapato unazingatia zaidi gharama za usimamizi na ukusanyaji wa mapato. Kwa msingi huo, Serikali haidhoofishi maendeleo ya Wilaya ya Kilindi isipokuwa ni lazima tufanye utafiti kwanza kubaini gharama za usimamizi na ukusanyaji wa mapato kabla ya kufungua ofisi.
(c)Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Kigua kuwa uwepo wa ofisi za Mamlaka ya Mapato katika maeneo yetu unaongeza ari ya wananchi kulipa kodi kwa hiari. Napenda kutoa rai yangu kwa wananchi wa Wilaya ya Kilindi na Watanzania wote kwa ujumla kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kwa mujibu wa sheria. Aidha, wananchi wasiache kulipa kodi kwa kutumia kisingizio cha maeneo yao kukosa ofisi za Mamlaka ya Mapato kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wamevunja sheria na kuikosesha Serikali yao mapato ambayo yangetumika kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza:-
Ili kuleta ufanisi wa kimaendeleo na kusogeza karibu huduma za kijamii kwa wananchi, Serikali hugawa Wilaya na Majimbo kwa kuangalia ukubwa wa eneo, idadi ya watu kwenye eneo husika, pamoja na shughuli za kiuchumi na Wilaya ya Kilindi ni miongoni mwa Wilaya chache zinazozalisha mazao ya kilimo na biashara kwa eneo kubwa:-
Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuligawa Jimbo hilo lenye ukubwa wa mita za mraba 6,125?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tukijibu hoja za Waheshimiwa Wabunge hapa Bungeni wakati wa Hotuba ya Bajeti ya Waziri Mkuu kwa Mwaka 2016/2017 tuliainisha vigezo vilivyotajwa na Mheshimiwa Mbunge kama sehemu ya vigezo vinavyotumiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika kugawa Majimbo ya Uchaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vigezo vingine ni pamoja na hali ya jiografia, upatikanaji wa mawasiliano, mgawanyo wa watu, mgawanyo wa wastani wa idadi ya watu na idadi ya Kikatiba ya Wabunge wa Viti Maalum pamoja na uwezo wa Ukumbi wa Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutumia fursa hii kumshauri Mheshimiwa Kigua, kupitia Mamlaka ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi kuwasilisha maombi yake kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kupitia vikao husika ili wakati muafaka ulikifika yaweze kufanyiwa kazi kwa kadiri itakavyoonekana inafaa.
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza:-
Moja ya Changamoto alizokutana nazo Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni katika Wilaya ya Kilindi ni tatizo la maji hususan maeneo ya Makao Makuu ya Wilaya, Kata za Saunyi, Mabaranga na kadhalika na Serikali ina Mradi wa Maji wa HTM ambao unatarajia kuwapatia jirani zetu wa Wilaya ya Handeni huduma ya maji ambapo utekelezaji huo utafanyika mwaka huu:-
Je, Serikali haioni umuhimu wa kufanya extension katika Wilaya ya Kilindi ili nayo ifaidike na mradi huu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Jimbo la Kilindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa HTM umepangwa kutekelezwa katika awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza itahusisha upanuzi wa chanzo cha maji kilichopo, kuongeza uwezo wa mtambo wa kusafisha maji, kukarabati mfumo wa kusukuma maji, kusafirisha maji pamoja na matenki ya kuhifadhi maji. Awamu ya pili itahusisha kuunganisha vijiji vyote vilivyopo umbali wa kilometa 12 kila upande kutoka bomba kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Songe, Wilaya ya kilindi uko mbali, wastani wa kilometa 120 kutoka Handeni linapoishia bomba kuu la Mradi wa Maji wa HTM; hivyo gharama ya kufanya upanuzi wa mradi ni kubwa na ikizingatiwa linapoishia bomba kuu hakutakuwa na maji ya kutosheleza kufikisha katika Mji wa Songe pamoja na vijiji vilivyo jirani. Hata hivyo, Kata ya Saunyi kuna mradi wa maji unaoendelea ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 25, na Kata ya Mabaranga mradi wake wa maji utekelezaji katika awamu ya pili ya programu ya utekelezaji wa miradi ya maji vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, samahani nitarudia hapo. Hata hivyo Kata ya Saunyi kuna mradi wa maji unaoendelea ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 25. Kata ya Mabaranga mradi wake wa maji utatekelezwa katika awamu ya pili ya programu ya utekelezaji wa miradi ya maji vijijini (Water Sector Development Program II)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Uchimbaji wa Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) imeanza kazi ya uchimbaji wa visima katika Mji wa Songe ambapo hadi sasa visima viwili vimeshachimbwa. Kazi ya usanifu na ujenzi wa miundombinu ya maji itafanyika baada ya kazi hiyo kukamilika.
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza:-
Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini kwa kutambua umuhimu wa wachimbaji wadogo wadogo imekuwa ikitoa ruzuku ili kuwawezesha wachimbaji kunufaika na madini yapatikanayo maeneo mbalimbali nchini:-
(a) Je, mpango huo umenufaisha wachimbaji wangapi nchini?
(b) Je, ni Mikoa na Wilaya zipi zinazonufaika na mpango huo?
(c) Je, Serikali ipo tayari kuweka utaratibu wa kuwakopesha wachimbaji wadogo wadogo ili kuwawezesha kuchimba madini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omar Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mpango wa utoaji wa ruzuku uanze Serikalini mwaka 2013/2014, jumla ya Wachimbaji Wadogo wa madini 118 wamenufaika na mpango huu. Hadi mwaka 2015/2016 jumla ya shilingi bilioni 8.1 zimetumika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ruzuku hutolewa kwa Wachimbaji wadogo wa madini kwa njia ya ushindani na kwa kuzingatia vigezo husika kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010. Wanufaika 118 wa ruzuku walitoka katika mikoa yote 22 na katika wilaya 53 yenye shughuli za madini hapa nchini. Wanufaika sita walitoka katika Mkoa wa Tanga na katika Wilaya za Handeni pamoja na Tanga yenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2013/2014 Serikali ilianzisha Mfuko wa kusaidia Wachimbaji Wadogo na kutenga jumla ya shilingi bilioni 2.3 ambazo zilitengwa na kuwekwa katika Benki ya Rasilimali Nchini (TIB) kwa ajili ya mikopo hiyo. Wachimbaji wadogo wengi walishindwa kukidhi vigezo vya mikopo na hapo sasa Serikali iliamua kutoa ruzuku. Kazi inayoendelea sasa ni kuwapa elimu ya namna sasa ya kunufaika na Mifuko hiyo ili kusudi wananchi waweze kupata fedha hizo kwa kupitia mabenki na taasisi za kifedha hapa nchini.
MHE. OMARI M. KIGUA Aliuliza:-
Serikali imekuwa ikisisitiza na kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kulinda na kutunza vyanzo vya maji kwa kutokata miti ovyo na kutojenga karibu na vyanzo hivyo, lakini wako baadhi ya wananchi wenye tabia ya kushirikiana na baadhi ya watumishi wachache wa Serikali kukata miti ovyo na kujenga karibu na vyanzo vya maji.
(a) Je, ni lini Serikali itasimamia kikamilifu sheria za kulinda mito na miti nchini?
(b) Je, Serikali haioni umefika wakati sasa kutunga sheria kali zaidi ili kujihami na global warming?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua changamoto za uharibifu wa vyanzo vya maji na misitu nchini, Serikali imechukua hatua za kisera, sheria na kimkakati kukabiliana nazo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Namba 20 ya mwaka 2004, kifungu cha 57(1) kinazuia shughuli yoyote ya kibinadamu yenye athari kwa mazingira kufanyika ndani ya mita 60 kutoka kwenye kingo za bahari, mito, maziwa na mabwawa ili kulinda vyanzovya maji.
Aidha, kifungu 55 cha sheria hiyo kimetoa mamlaka kwa Halmashauri kuweka miongozo ya kulinda vyanzo vya maji na kuchukua hatua kali kwa yeyote anayekiuka sheria. Vilevile Halmashauri zote nchini zimelekezwa kutunga na kusimamia utekelezaji wa sheria ndogo kwa ajili ya kulinda vyanzo vya maji na misitu katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Sheria ya Misitu ya mwaka 2002 imeweka utaratibu wa kusimamia na kuhifadhi ya misitu ikiwemo kutoa adhabu kwa uharibifu wa misitu na ukiukwaji wa miongozo ya uvunaji endelevu wa rasilimali za misitu. Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji na kuchukua hatua kali kwa wote wanaokiuka Sheria hizi kwa lengo la kulinda vyanzo vya maji na misitu nchini.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, kifungu cha 75 (a) mpaka (e) inaelekeza hatua za kuchukua ili kulinda na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na kuongezeka kwa joto la duniani yaani global warming, katika sekta mbalimbali nchini. Aidha, Serikali itaendelea kuhamasisha utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2012 kupitia sekta, halmashauri, taasisi za umma na binafsi katika kutekeleza miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika maeneo yaliyoathirika.
MHE. OMARI M. KIGUA alijibu:-
Moja ya changamoto kubwa inayokabili maeneo mbalimbali nchini ni huduma ya maji safi na salama. Serikali kwa kushirikiana na mashirika ya kitaifa kama Benki ya Dunia wamekuwa wakitoa ahadi za kuwezesha miradi mikubwa ya maji nchini lakini mara nyingi wamekuwa hawatekelezi ahadi zao.
Je, Serikali haioni sasa imefika wakati wa kuweka mikakati ya dhati ya kutenga bajeti kwa kutumia mapato ya ndani ili kutoathiri miradi ya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NAUMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa kama Benki ya Dunia wameendelea kutoa ahadi na kutekeleza miradi mbalimbali ya maji safi na salama hapa nchini. Kuanzia bajeti ya mwaka wa fedha ya 2006/2007 hadi Julai 2017 Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ilianzisha Mpango wa Utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ambapo jumla ya miradi 1,810 iliibuliwa na tayari miradi 1,333 imekamilika na miradi 477 ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha fedha za ndani zinazotengwa na zinatekeleza miradi ya maji nchini kote, Serikali imeanzisha Mfuko wa Maji ambao umeimarisha upatikanaji wa fedha za kutekeleza miradi ya maji kwa wakati na fedha na hizo za mfuko zimetoa kipaumbele kwa miradi ya maji vijijini. Serikali itaendelea kubuni vyanzo vingine vya fedha za ndani ili miradi mingi ya maji itekelezwe kwa wakati na wananchi wengi zaidi wanufaike na huduma hiyo.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutumia mapato ya ndani pamoja na uanzishaji wa mfuko wa maji inaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya miradi ya maji mfano mwaka wa fedha 2016/2017 kiasi cha shilingi bilioni 690 ambayo ni sawa na asilimia 75 ni fedha za ndani na mwaka wa fedha 2017/ 2018 shilingi bilioni 408.6 sawa na asilimia 66 ya bajeti yote ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza:-
Mwaka 2014 Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Makao Makuu ya Wilaya ya Kilindi hadi Wilaya ya Gairo.
Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Barabara ya Kilindi kuanzia Songe kuelekea Gairo ina urefu wa kilometa 111.29. Sehemu ya barabara hii kutoka Songe hadi Kwekivu Junction na mpaka Iyogwe yenye urefu wa kilometa 69.5 inahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania Mkoa wa Tanga na sehemu ya barabara ya Iyogwe hadi Chakwale mpaka Ngilori yenye urefu wa kilometa 41.79 inahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa Mkoa wa Morogoro.
Mheshimiwa Spika, barabara hii imekuwa ikitengewa fedha kila mwaka na kufanyiwa matengenezo ya kawaida, matengenezo ya muda maalum, matengenezo ya sehemu korofi, ujenzi wa madaraja na matengenezo makubwa ya madaraja. Matengenezo haya yameifanya barabara hii iweze kupitika majira yote ya mwaka. Aidha, mwaka 2014 Mheshimiwa Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alitoa ahadi ya kujengwa kwa kiwango cha lami kwa barabara hii.
Mheshimiwa Spika, nia ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa barabara hii ya kutoka Makao Makuu ya Wilaya ya Kilindi inayoanzia Mji wa Songe hadi Kwekivu Junction - Iyogwe - Chakwale hadi Ngilori, Wilaya ya Gairo yenye urefu wa kilometa 111.29 inaingizwa kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami. Kwa kutambua umuhimu wa barabara hii kiuchumi na kijamii, Serikali itaendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali ili iweze kupitika majira yote ya mwaka. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza:-
Je, Serikali ipo tayari kutuma timu ya tathmini ya kukagua Miradi ya Maji ya Kwediboma, Kwekivu, Sange, Chamtui na Mafuleta ili kuona kama vigezo na viwango vya ujenzi wa miradi hii mikubwa vimezingatia thamani ya fedha (value for money audit)?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Jimbo la Kilindi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maji nchini ikiwemo maeneo ya vijijini ili kuweza kuwapatia wananchi huduma ya maji safi, salama kwa asilimia 85 ifikapo mwaka 2020. Ili miradi ya maji iweze kutekelezwa kwa ufanisi, Serikali hufanya ufuatiliaji na tathmini ili kupima matokeo ya mradi uliokamilika na unaoendelea kulingana na vigezo vitano (kufaa, kutekelezeka, ufanisi, athari na uendelevu) katika mpangilio unaoeleweka ili kusaidia kuboresha miradi mingine inayoendelea.
Mheshimiwa Spika, kufuatia ombi la Mheshimiwa Mbunge, naomba nimshukuru kwanza kwa kuona umuhimu wa kufuatilia miradi ya maji iliyoko jimboni kwake. Hivyo namhakikishia kuwa nitatuma timu ya wataalam kwa ajili ya kwenda kufanya ukaguzi wa ujenzi wa miradi hiyo ili kuona kama vigezo na viwango vya ujenzi wa miradi hiyo mikubwa vimezingatiwa.
MHE. OMARI A. KIGODA - (K.n.y. MHE. OMARI M. KIGUA) aliuliza:-
Wilaya ya Kilindi ni miongoni mwa Wilaya chache zinazopata mvua nyingi nyakati za mvua lakini maji hayo yamekuwa yakipotea:-
• Je, Serikali ipo tayari kuweka utaratibu wa kuvuna maji hayo kwa kujenga mabwawa makubwa ya kuhifadhia maji hayo kwa matumizi ya binadamu?
• Je, Serikali imejipangaje kujenga mabwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na ufugaji wa samaki?
NAIBU WAZIRI MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Jimbo la Kilindi, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Wilaya ya Kilindi ni miongoni mwa wilaya zinazopata mvua nyingi hasa mvua za vuli. Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi inaendelea kujenga mabwawa ya kuhifadhi maji ambapo hadi sasa mabwawa matatu (3) katika vijiji vya Saunyi, Jungu na Kwinji/Muungano yamekamilika na hatua inayofuata ni kujenga miundombinu ya maji. Bwawa moja la Mafuleta miundombinu yake imekamilika na linatoa huduma ya maji. Aidha, Serikali itaendelea na ujenzi wa mabwawa na miundombinu yake katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuvuna maji ya mvua.
• Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, inaendelea kukamilisha mapitio ya Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji wa Mwaka 2002 ambapo masuala ya ujenzi wa mabwawa yamepewa kipaumbele. Mapitio haya yatabainisha maeneo mbalimbali yanayofaa kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa ya umwagiliaji kwa lengo la kukifanya kilimo cha umwagiliaji kuwa endelevu. Serikali katika mwaka wa fedha 2018/2019, itaendelea kutenga na kutoa fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa maeneo yanayofaa kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa ya kuhifadhi maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo kilimo cha umwagiliaji.
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Tano inatoa elimu bure hali iliyosababisha wananchi wengi kupeleka watoto wao shule, huku ufaulu wa wanafunzi kuingia kidato cha tano ukiongezeka:-
Je, Serikali haioni umuhimu wa kila wilaya kuwa na Shule za Kidato cha Tano na Sita kuwa ni wa lazima hasa ikizingatiwa kuwa kuna baadhi ya wilaya hazina shule hizo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuongeza Shule za Kidato cha Tano na Sita na kuhakikisha zinakuwa kwa kila wilaya hasa wakati huu ambapo wahitimu wa Kidato cha Nne wameongezeka kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge. Hii ndiyo sababu ya Serikali kuelekeza kuwa na Shule za Sekondari za Kidato cha Tano na Sita kwa kila tarafa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa utaratibu huu, Wilaya/ Halmashauri inaweza kuwa na Shule za Kidato cha Tano na Sita zaidi ya moja kutegemea idadi ya tarafa zilizopo. Hivyo, inashauriwa wadau wa Wilaya/Halmashauri ambazo hazina Shule zenye Kidato cha Tano na Sita kushirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri husika kujenga shule au kuongeza miundombinu katika shule zilizopo na kufuata taratibu husika kusajili shule mpya iliyojengwa au kupata kibali cha kuanzisha kidato cha tano na sita katika shule zilizopo. Utekelezaji huo utasaidia kuondoa changamoto ya baadhi ya wanafunzi wenye sifa za kuendelea na masomo ya kidato cha tano kukosa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukumbusha kwamba Shule za Sekondari za Kidato cha Tano na Sita ni za kitaifa, ambapo hudahili wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali za nchi kulingana na tahasusi (combinations) za masomo zilizopo. Hivyo kwa sasa wahitimu wenye sifa kutoka wilaya zote nchini hupangwa katika shule hizo.
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza:-

Serikali imekuwa na utaratibu wa kukarabati shule zake za sekondari na za msingi nchini:-

Je, ni lini Serikali itafanyia ukarabati Shule za Sekondari Masagulu, Lwande, Mkuyu na Shule za Msingi Songe na Masagulu zilizopo Wilayani Kilindi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA C. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi ina jumla ya Shule za Msingi za Serikali 111 na Sekondari 22. Kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2017/2018 kupitia Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R), Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi imepatiwa kiasi cha Sh.122,823,097 kwa ajili ya ujenzi na umaliziaji wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari ambapo shule tatu za sekondari na 14 za msingi zimenufaika.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza programu mbalimbali za kuboresha miundombinu mashuleni ikiwemo ukarabati wa shule kongwe 89 nchini. Serikali kwa kushirikisha nguvu za wananchi na wadau wengine wa maendeleo itaendelea kuweka kipaumbele cha ukarabati wa miundombinu ya shule ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunza. Aidha, natumia fursa hii kuzielekeza Halmashauri zote kutenga bajeti kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule.
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza:-

Kwa muda mrefu sasa Wilaya ya Kilindi haina Hospitali ya Wilaya lakini wanayo Hospitali ya Rufaa inayomilikiwa na Kanisa la KKKT, lakini watumishi wote na huduma zote za Hospitali hiyo zinagharamiwa na Halmashauri ya Wilaya (DED) na wao KKKT ni wamiliki wa majengo:-

Je, Serikali haioni imefika wakati wa kufanya makubaliano ya kununua Hospitali hiyo ili kupunguza gharama kwa Serikali ya kujenga Hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omary Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2010 Serikali kupitia Halmashauri ya Kilindi iliingia mkataba na Kanisa la Kilutheri Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kwa lengo la kutumia majengo yanayomilikiwa na kanisa hilo kwa ajili ya utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wa Kilindi. Hospitali hiyo Teule ya Wilaya (DDH) ya Kilindi inahudumia wananchi wapatao 264,000. Serikali inatumia utaratibu huo ikiwa ni ushirikiano na Taasisi binafsi yakiwemo Mashirika ya Dini pale ambapo hakuna Hospitali ya Wilaya ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hospitali hiyo, Serikali inalipa mishahara ya baadhi ya watumishi walioajiriwa na Serikali na kupeleka fedha kwa ajili ya uendeshaji wa hospitali ambazo zinatumika kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, hospitali hiyo iliidhinishiwa shilingi 153,646,500/= kutoka Mfuko wa Pamoja wa Afya ambapo ni asilimia 25 ya fedha zote za Mfuko wa Afya kwa Hospitali ya Wilaya. Vilevile, katika mwaka wa fedha 2019/2020, hospitali hiyo imetengewa jumla ya shiligni 153,646,500/= kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haina mpango wa kununua Hospitali ya Wilaya ya Kilindi inayomilikiwa na KKKT. Mpango wa Serikali ni kuhakikisha kila Halmashauri inakuwa na Hospitali ya Halmashauri ya Serikali. Pale ambapo bado Serikali haijajenga, itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kama inavyofanyika sasa.
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza:-

Serikali imekuwa na utaratibu wa kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa Mahakama za Mwanzo:-

Je, ni lini Serikali itafanya ukarabati wa Mahakama za Kata za Kimbe, Kwekivu na Kata ya Mswaki ambazo zimechakaa sana?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa changamoto zinazoikabili Mahakama ya Tanzania ni uhaba na uchakavu wa miundombinu. Kwa sasa, kuna jumla ya Mahakama za mwanzo 960 katika mikoa yote nchini. Idadi kubwa ya majengo ya Mahakama hizi ni chakavu na ni finyu kuweza kutoa huduma kwa mahitaji ya sasa hususan kukidhi ongezeko la mashauri. Hivyo, majengo mengi yanayohitaji kujengwa upya, ngazi ya Mahakama ya Mwanzo ni muhimu sana kwa kuwa inabeba takriban asilimia 70 ya mashauri yote yanayopelekwa Mahakamani.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hii, Mahakama imejiwekea mpango wake wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya Mahakama kwa awamu.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Kilindi ina Mahakama za Mwanzo tatu zinazofanya kazi ambazo ni Songe, Mswaki na Kwediboma. Majengo ya Mahakama zote hizi ni ya zamani kiasi cha kuhitajika kujengwa upya, siyo kukarabatiwa. Aidha, Mahakama tatu za Kimbe, Kwekivu na Mswaki alizouliza Mheshimiwa Mbunge, majengo yake hayafanyi kazi kabisa, yamefungwa kutokana na uchakavu.

Mheshimiwa Spika, wananchi waliokuwa wanapata huduma katika Mahakama za Mwanzo za Kwekivu na Kimbe wanalazimika kufuata huduma Mahakama ya Mwanzo Songe ambako ni mbali. Mahakama ya Mwanzo Mswaki inatumia jengo la Kijiji kwa shughuli za Mahakama. Kutokana na hali hiyo, Mpango wa Serikali ni kujenga upya kabisa Mahakama hizi na siyo kufanya ukarabati.

Mheshimiwa Spika, pamoja na ukweli kwamba Mahakama zote zilizotajwa na Mheshimiwa Mbunge ni chakavu sana, lakini bado mahitaji ya Mahakama kwa nchi nzima ni makubwa na hivyo, tutaendelea na kazi ya ujenzi na ukarabati wa Mahakama za Mwanzo na Mahakama za ngazi nyingine kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, kupitia Mpango huo, napenda kumthibitishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Mahakama ya Mwanzo Kwekivu na Kimbe zitajengwa katika mwaka wa fedha 2020/2021.

Mheshimiwa Spika, mwisho, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kuendelea kushirikiana na Serikali na Mahakama na kuona umuhimu wa kuidhinisha fedha zinazohitajika kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa Mahakama zetu nchini. Ninaomba tuendelee kuona umuhimu wa mhimili huu katika utoaji wa haki nchini. Ahsante. (Makofi)
MHE. OMARI M. KIGUA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza ahadi ya muda mrefu ya ujenzi wa barabara kutoka Kilindi kwenda Gairo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nitoe shukrani kwa Mwenyezi Mungu na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kuniamini ili niweze kumsaidia katika nafasi ya Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kilindi – Yogwe – Gairo yenye jumla ya kilometa 115.7 ni barabara ya Mkoa inayounganisha mikoa ya Tanga na Morogoro kupitia Wilaya ya Kilindi na Gairo na inahudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) katika mikoa ya Tanga na Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ufinyu wa bajeti, kwa sasa Serikali haijapata fedha ya kuanza ujenzi wa barabara ya Kilindi – Iyogwe – Ngirori hadi Gairo kwa kiwango cha lami. Aidha, Serikali itaendelea kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara hii ili kuhakikisha kuwa inaendelea kupitika vizuri katika majira yote ya mwaka. Ahsante.
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza:-

Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali itaanza mkakati wa kusambaza maji kutoka Mto Dibuluma kata ya Kibati Wilaya ya Mvomero na kuyasambaza katika kata ya Tunguli, Kwekivu, Masagalu na Songe Wilayani Kilindi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa niaba wa Waziri wa Maji naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango wa muda mrefu wa kutekeleza mradi wa maji kwa kutumia chanzo cha mto Diburuma kwa lengo la kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi. Hatua iliyofikiwa ni kufanyika kwa utafiti wa ubora na uwingi wa maji katika chanzo hicho ili kujiridhisha na kiwango cha maji kwa ajili ya kunufaisha vijiji vilivyopo kwenye kata nne (4) za Tunguli, Kwekivu, Masagalu na Songe. Utafiti huo utakamilika kabla ya mwezi Juni, 2021 na takwimu zitakazopatikana zitatumika kufanya usanifu wa kina kwa mradi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kata za Tunguli, Kwekivu, Masagalu na Songe zinapata huduma ya maji safi na salama kupitia visima virefu vitano (5) na visima vifupi kumi na tano kwa lengo la kuendelea kuboresha huduma ya maji katika kata hizo na Halmashauri ya Kilindi kwa ujumla, na mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 2.14 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji.
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga daraja linalounganisha Wilaya ya Kilindi na Kiteto kupitia Kijiji cha Sambu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA ZIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mnadani – Sambu - Pagwi ni barabara ya mkusanyo (Collector Road) yenye urefu wa kilomita 38. Barabara hii inaanzia barabara ya TANROADS ya Kwaluguru-Songe-Kibirashi inapita katika maeneo ya Changanyikeni, Kigunga, Sambu, Makelele, Lumotio, Pagwi na kuishia katika eneo la Lugira katika Wilaya ya Kiteto ambako inaungana na barabara ya Kijungu – Sunya – Dongo katika Mkoa wa Manyara.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango na bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 barabara hii imetengewa kiasi cha shilingi milioni 182.52 kupitia fedha za Mfuko wa Barabara (Road Fund) kwa ajili ya kufanya matengenezo ya barabara yenye urefu wa kilomita 10.5, ujenzi wa kalvati tisa na vivuko mfuto (drift)vinne.

Mheshimiwa Spika, barabara hii itaendelea kutengewa fedha kulingana na upatikanaji wa fedha kila mwaka ili kutatua changamoto iliyopo ya kutopitika kwa barabara hii.