Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Omari Mohamed Kigua (65 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. OMAR M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nikushukuru kwa kunipa fursa jioni ya leo niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Sheria. Kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri husika wa Wizara hii kwa bajeti nzuri sana ambayo ameiwasilisha kwa siku ya leo. Bajeti hii imechukua mambo mengi sana ambayo yalikuwa ni kilio cha wananchi, nikiamini kabisa kwamba imeweza kujibu kilio cha wananchi wa maeneo mbalimbali, hususan wa Jimbo la Kilindi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakililia Mahakama ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa hatua zake anazochukua za kutumbua majipu.
Vilevile nimpe moyo kwa changamoto anazozichukua kwa wale watendaji ambao kwa muda mrefu wamekuwa ni matatizo ya nchi hii, ninaamini kabisa Waheshimiwa Wabunge na hata wale wa upande mwingine wanajua Mheshimiwa Rais anachukua msimamo ulio sahihi kabisa. Mambo haya ni ya msingi tukiweza kuyazungumzia kwa mustakabali wa nchi yetu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze moja kwa moja kuchangia hususan kwenye Mahakama zetu. Tanzania hii ina Mahakama za Mikoa, Mahakama za Rufaa na Mahakama za Mwanzo, lakini ninaamini kabisa changamoto za Mahakama hasa hizi za Mwanzo na Wilaya zimekuwa ni kubwa sana, kwa maana kwamba mahakama nyingi zimekuwa chakavu na hazijafanyiwa ukarabati wa muda mrefu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna maeneo ambayo yana Wilaya lakini hayana Mahakama za Wilaya. Mfano katika Jimbo langu la Wilaya ya Kilindi ni takribani miaka 13 toka tumepata Wilaya lakini hatuna Mahakama za Wilaya. Jambo hili limekuwa ni kero kubwa sana kwa sababu wakazi wa Jimbo la Kilindi wamekuwa wakifuata huduma hii ya Mahakama kwa takribani kilometa 200 au 190 kutoka Wilaya moja hadi Wilaya nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kilindi kwa ujumla ina changamoto nyingi sana za migogoro hasa ya wakulima na wafugaji. Kwa hiyo, unakuta kwamba, jambo hili limekuwa ni kero ya muda mrefu na hata Mbunge aliyepita alikuwa akilipigia kelele suala hili, lakini ninamshukuru Mheshimiwa Waziri husika kwenye bajeti yake ameweza kuliona hili na miongoni mwa Wilaya 12 ambazo zimetengewa hela kwa ajili ya kujengewa Mahakama ya Wilaya basi na Wilaya ya Kilindi imepata fursa hiyo. Naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine ni suala la Mahakama hizi za Wilaya kutokuwa na Mawakili wa Serikali. Mawakili wa Serikali wamekuwa ni msaada mkubwa sana kwa wananchi ambao hawana uelewa wa elimu ya sheria. Nashauri hususan kaka yangu Waziri, Mheshimiwa Mwakyembe kwamba muda umefika sasa hivi wa kuwa na Mawakili katika kila Mahakama ya Wilaya, kwa sababu watu hawa wanawasaidia wananchi wasiokuwa na uwezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda niseme jambo moja, Mawakili katika kitabu chako umeeleza hapa kwamba mna mpango wa kupunguza idadi ya mrundikano ya kesi, kwa maana ya kwamba zero case backload! Mheshimiwa Waziri hebu nikuulize swali moja pengine utanipa maelezo wakati unajibu hoja hizi kwamba unatarajia Mahakama ya Wilaya at least iweze kujibu kesi 250 kwa mwaka, sasa Hakimu wa Wilaya ambaye anabeba Wilaya mbili kwa maana ya Wilaya ya Kilindi na Wilaya ya Handeni anawezaje kutatua kesi hizi kwa kipindi cha mwaka mmoja? Haya ni mambo ya msingi kabisa na unaweza tu ukaenda ukauliza pale Mahakama ya Wilaya ya Handeni kwamba, Hakimu ana idadi kiasi gani ya kesi za kutoka Wilaya hizi mbili?
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba wakati tunasubiria kujenga Mahakama ya Wilaya, sisi tunayo majengo katika Jimbo la Kilindi tunaweza tukapewa Hakimu wakati tunasubiri jengo likijengwa. Mimi nadhani fursa hii ni nzuri, ili tuweze kuwapa haki wananchi wa Wilaya ya Kilindi. Ninadhani changamoto hii haipo katika Jimbo langu tu, ipo katika Wilaya mbalimbali ambazo hazina Mahakama za Wilaya, nikiamini kwamba wananchi wanayo haki ya kuwa na huduma hizi za kimsingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kuchangia siku ya leo ni suala la Serikali kupoteza kesi. Serikali inapokuwa inawashtaki watu mbalimbali mara nyingi huwa inapoteza kesi! Sasa tunatakiwa tujiulize sababu za msingi ni kwa nini Serikali inapoteza kesi? Haya ni mambo ya msingi kwa sababu wakati mwingine Serikali inashtaki mambo ambayo watu wamehujumu nchi! Tuchukulie mfano wa kesi ya samaki wale, Serikali imepoteza na inatakiwa kulipa fidia. Sasa ni nini kilichosababisha Serikali ikapoteza kesi hiyo wakati Serikali inao wataalam, inao Waendesha Mashitaka wa kutosha na wenye elimu yakutosha! Nadhani imefika muda sasa tuangalie utaratibu mzuri wa namna gani tunaweza kupata watu ambao wamebobea wanaoweza kuishauri Serikali katika mambo ya kesi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kulichangia ni juu ya bajeti ya Wizara hii. Mheshimiwa Waziri husika wa bajeti hii amezungumza sana kwamba ana changamoto ya bajeti, nadhani kwa sababu Wizara hii inahusika na mambo ya sheria na mambo ya mahakama ifike wakati kwamba, Wizara hii yenyewe tuiongezee hela ili tuweze kuondokana na changamoto mbalimbali kwa ajili ya kutatua kesi za wananchi na kutoa haki kwa wananchi wa Tanzania kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ningependa kuchangia katika upande wa Mahakama za Mwanzo. Nichukulie mfano katika Jimbo langu la Kilindi, Mahakama za Mwanzo ziko chache sana! Jimbo lenye Kata 21 na vijiji visivyopungua 102, Mahakama za Wilaya nadhani ziko kama tatu kama siyo nne! Maana yake ni kwamba wananchi wanakosa haki zao za kimsingi. Kwa hiyo, imefika wakati Mheshimiwa Waziri husika ahakikishe kwamba ule mpango wa kuwa na Mahakama za Mwanzo katika kila Kata, basi mpango huo Serikali kwa dhati ya moyo wake ihakikishe kwamba mahakama hizo zinaanzishwa na zinakuwa na Mahakimu wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kushauri ni juu ya idadi ya Mahakimu katika Mahakama zetu. Sehemu nyingi sana utakuta utakuta kwamba, hatuna Mahakimu, lakini tunacho Chuo cha Mahakama Lushoto! Kwa nini Serikali isingetia nguvu pale tukahakikisha kwamba wataalam wengi wanapatikana, Mahakimu wanapatikana, ili Mahakama zetu ziweze kuwa na Mahakimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango huu kuna uanzishwaji wa Mahakama ya Mafisadi ambayo inatarajiwa kuanza mwaka wa fedha huu. Jambo hili nataka niipongeze sana Serikali hususan Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wa dhati wa kuanzisha Mahakama hii. Mimi naamini kabisa kwamba muda umefika sasa hivi wa kuwa na Mahakimu wa kutosha katika kila Wilaya, kila Kata, ili wananchi wetu waweze kupata haki za msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ningependa kuchangia juu ya ukusanyaji wa maduhuli katika mahakama zetu. Nadhani utaratibu uliopo sasa hivi ni mzuri lakini inabidi uboreshwe sana. Uboreshwe kwa sababu mahakama hizi zina mahitaji mengi sana, wakitegemea OC ya Serikali maana yake uendeshaji wa mahakama hizi hautakwenda vizuri. Mimi ni imani yangu kwamba Serikali imesikia haya na imesikia michango ya Waheshimiwa Wabunge mbalimbali tukiamini kwamba muda umefika wa kuweza kutoa haki kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo machache, naomba kuunga mkono hoja ya bajeti hii. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa fursa hii. Awali ya yote naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Ujenzi lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Waziri husika wa Wizara hii kwa mara ya kwanza ameweza kuona umuhimu wa Jimbo la Kilindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka nianze kwa kuchangia hususani katika upande wa barabara kwenye dhana ya kuunganisha mikoa kwa mikoa kwa maana ya barabara kiwango cha lami. Nikienda ukurasa wa 41, hapa nataka nizungumzie barabara inayoanzia Handeni kwenda Kibirashi, Kijungu, Kibaya, Njoro, Chemba, Kwa Mtoro hadi Singida, ina urefu wa kilometa 460. Dhana hii ya kuunganisha mikoa ni dhana pana na ina maana kubwa sana kwa sababu inalenga katika uchumi wa mwananchi mmoja mmoja, Wilaya, Mkoa hadi Taifa. Unapofungua barabara maana yake unaruhusu mazao yauzwe kwa wepesi, unaruhusu movement za watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii katika mwaka wa fedha unaoanza 2016/2017 wametufikia katika stage ya visibility study na detailed design. Mimi nataka niamini kabisa kwamba barabara hii ni muhimu sana kwa sababu inaunganisha mikoa minne, Mkoa wa Tanga, Mkoa wa Manyara, Singida pamoja na Dodoma. Muda umefika wa kuweza kuitengeneza barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ambalo limezungumzwa na Wabunge wa Mkoa wa Tanga na mimi lazima nizungumze, hususani suala la reli ya Tanga kwenda Moshi hadi Musoma, na pia nataka nizungumzie habari ya bandari. Mambo yote haya ni ya msingi kwa sababu yanalenga kuinua uchumi wa Tanga. Waziri wa Viwanda alizungumza hapa kwamba kuna wawekezaji ambao wanataka kufungua viwanda katika Mkoa wa Tanga. Sasa kama unataka kufungua Mkoa wa Tanga maana yake nini, ni lazima uwe na bandari na reli iliyo imara ili uweze kusafirisha cement ile katika mikoa ya pembezoni mwa nchi. Mimi naomba Mheshimiwa Waziri hili ulitie mkazo mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kuchangia kwa sababu muda hautoshi ni juu ya wakandarasi wetu ambao wanatengeneza barabara. Barabara nyingi hususani katika Halmashauri zinatengenezwa chini ya kiwango na wakati mwingine mkandarasi anatengeneza barabara haweki matoleo. Hili linasababisha barabara hizi kuharibika hasa wakati wa mvua. Mfano katika Jimbo langu la Kilindi lenye squire meter 6,125, Mheshimiwa Waziri nikuambie barabara hizi sasa hivi hazipitiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamenituma kwamba tuangalie ni namna gani mfuko huu wa TANROADS unaweza kusaidia kuikarabati barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ni ushauri tu katika Wizara hii kwamba pawepo na performance audit katika miradi yetu mikubwa ya barabara. Miradi hii wakandarasi wanapewa hela nyingi sana, lakini baada ya mwaka mmoja, miezi sita barabara hazipitiki. Hii haiwezekani, Serikali lazima iwe very serious na hili, ili fedha za Watanzania ziwe na maana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine ambalo ningependa kuchangia ni suala la mawasiliano…
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuipongeza Serikali na Waziri husika kwa hotuba nzuri inayohusu makadirio na matumizi kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi zimekuwa mahali muhimu kwa ajili ya kutoa haki katika nchi yetu. Hata hivyo, nimesikitika sana kuona kuwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 Wizara ilitaja Wilaya 17 zitakazojengwa Mahakama ya Wilaya na moja ya Wilaya hizo ni Kilindi. Naomba kupata majibu ya kuridhisha kwa nini Wilaya ya Kilindi si miongoni mwa Wilaya zilizopo katika ujenzi kwa mwaka huu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni takribani miaka 30 sasa wakazi wa Wilaya ya Kilindi wamekuwa wakipata huduma za Mahakama za Wilaya katika Wilaya jirani ya Handeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upo umbali mrefu sana kutoka Kilindi na Handeni hususani kwa Kata za Pagwi, Kikunde, Tunguli kata hizo zipo karibu kabisa na Wilaya ya Gairo. Utaona kwa kiasi wananchi wa kilindi wanahitaji Mahakama hii kwani kupata Mahakama ni sehemu ya haki za msingi kwa wananchi wa Kilindi. Halmashauri inalo eneo kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama. Niombe sasa Wizara ione umuhimu wa kuwapatia wananchi Mahakama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Uhaba wa Mahakama za Mwanzo; Mahakama za Mwanzo pia zimekuwa ni chombo muhimu sana katika kutoa haki kwa wananchi wetu, lakini maeneo mengi hayana Mahakama za Mwanzo na hata kama zipo basi zimechakaa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano katika Jimbo langu la Kilindi yote tarafa nne, kata 21 na vijiji 102 tunazo Mahakama za Mwanzo zisizozidi tano, hali hii ni mbaya sana. Ningeomba kauli ya Wizara na Waziri mwenye dhamana ya Mahakama hizi ni lini watu wa Kilindi watapata Mahakama za Mwanzo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na Mahakama za Mwanzo Kata za Kimbe, Mgora, Kwekiku, lakini Mahakama hizi zote majengo yake yote yamekuwa magofu na hakuna Mahakimu, je, lini Mahakama hizi zitajengwa upya? Niombe Waziri alichukue jambo hili kwa uzito mkubwa unaostahiki
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. OMAR M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuwa mchangiaji wa pili kwenye taarifa ya Kamati hizi mbili. Awali ya yote nichukue fursa hii kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukutana na wachimbaji wadogo wadogo. Mimi niupongeze uamuzi huu nikiamini ulikuwa ni uamuzi wa busara na nikiamini kabisa moja ya maeneo ambayo yanaweza kutusaidia kuongeza pato la Taifa ni kwenye sekta ya madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika sekta hii ya madini, wachimbaji wadogo wadogo hawa wamekuwa hawapewi kipaumbele. sasa kutokana na Mheshimiwa Rais kukutana na wachimbaji wadogo wadogo maana yake tunaona kabisa dhamira ya Serikali kuwatambua wachimbaji wadogo wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili zipo changamoto mbalimbali na moja ya changamoto hizo Mheshimiwa Rais ameweza kuzizungumzia na majuzi nimemsikia Waziri mwenye dhamana akizungumzia kwamba wapo watu wenye maeneo ambayo wameyashikilia kwa muda mrefu na hawajayafanyia kazi. Ushauri wangu, Waziri mwenye dhamana na eneo hili afanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mmoja tu, katika eneo langu la Wilaya ya Kilindi, kwenye Kijiji cha Kwafumbili, Kata ya Negelo, kuna mwekezaji mmoja ana maeneo mengi sana, ameyashikilia maeneo haya hajayafanyia kazi, lakini wachimbaji wadogo wadogo ambao wangeweza kupewa eneo hili wangeweza kuhakikisha kwamba wanafanya shughuli hizi na Serikali ingeweza kupata mapato ya kutosha. Naamini kabisa Mheshimiwa Waziri atalifanyia kazi hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo mafupi katika eneo hili sasa naomba nichangie katika eneo la sekta ya gesi. Kwa kweli kwanza nimpongeze sana Waziri mwenye dhamana ya nishati hususan katika eneo la REA, amefanya kazi kubwa sana. Ameweza kupita katika maeneo mbalimbali na ameweza kutusikiliza shida zetu. Naamini kabisa umeme huu utakaposambaa katika Vijiji vyetu vyote maana yake wananchi wetu wataweza kupata maendeleo. Ukizingatia dhamira ya Serikali ya nchi ya viwanda, hatuwezi kuendesha viwanda bila kuwa na umeme wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri eneo hili lipewe umuhimu wa hali ya juu lakini pia wakandarasi hawa ambao wamepewa kusambaza umeme vijijini, wamepewa maeneo makubwa sana. Tuangalie namna ambavyo wanaweza kupunguziwa mzigo huu ili dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kwamba kila kijiji kinapata umeme, iweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye eneo la sekta ndogo ya gesi na nikizungumzia eneo la SONGAS. Eneo hili nimzungumzie mtu anayeitwa Pan African Energy. Huyu mtu Pan African Energy alikuja kwa jina la Ocelot; hii ni kampuni ambayo ilikuwa inatokea Canada. Watu hawa walikuja kama wawekezaji kwa ajili ya kusaidia suala la umeme, ikaanzishwa kampuni ya SONGAS ambayo tunasema ni special purpose vehicles.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiiangalia kampuni hii na muundo wake unasikitisha sana. Unasikitisha kwa sababu SONGAS yenyewe ambayo ni special purpose vehicles ukiangalia umiliki wake watu wa TANESCO wana asilimia 9.0, TPDC asilimia 28 na huyu Globeleq ana asilimia 54. Sasa unajiuliza huyu Globeleq huu mtaji aliouwekeza mpaka akapata asilimia 54 ameupata wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kushangaza sana ni kwamba hakuna kampuni iliyosimamia kufanya tathmini, yaani kwamba TANESCO ana asilimia tisa, TPDC asilimia 28 ni nani alisimamia tathmini hizi? Ukiangalia na maelezo ya kutoka kwa watu wa Globeleq wanakwambia kwamba eneo lile la SONGAS ambapo lilikuwa ni eneo la TANESCO thamani yake ilikuwa ni dola milioni moja. Sasa ni nani alisimamia uthamini ambao umehakikisha kwamba Serikali inapata asilimia tisa peke yake? Maana yake unaona kwamba kuna matatizo makubwa sana hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda mbali zaidi unaangalia eneo la TPDC. TPDC wana visima vinne na visima hivi vinne ndivyo ambavyo vinatoa gesi; lakini vinatoa gesi thamani yake imethaminishwa kwa asilimia 28 tu, huu ni wizi mkubwa sana. Naishauri Serikali iangalie namna gani inaweza ikalisimamia suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hilo kuna mambo ambayo yana upungufu mwingi sana na moja ya upungufu ambao upo katika mkataba huu ni eneo ambalo Globeleq katika taarifa zake za pesa anaonesha mkopo wake mwanzoni ulikuwa unaonyesha kama ni preferential, lakini sasa hivi inaonesha kama ni debit note. Debit note maana yake ni kwamba anapotaka kulipa madeni atapunguza gharama zake zote mwishoni ndio atalipa deni. Mkataba huu una upungufu mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nalisema eneo hili kwa sababu naamini kabisa Serikali inapoteza mapato mengi sana; na hii ni kinyume kabisa na mikataba ya madini ya nishati/petroli ya mwaka 2015. Naomba Serikali ilipitie eneo hili vizuri sana na nina uhakika Mheshimiwa Naibu Waziri mwenye dhamana na eneo hili ananisikiliza na atalifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna upungufu mbalimbali ambao nimeuona na ambao Mwenyekiti wa Kamati ameuzungumzia na naamini Serikali itaufanyia kazi. Moja ya upungufu huo ambao nadhani ni mikataba hasi ni suala la TANESCO na Pan African Energy. PAET –Pan African Energy (PAET) wao wanatoa vipaumbele vya kwenye kuwauzia gesi kwanza wanawauzia SONGAS pili viwanda 32 na wa mwisho anakuwa ni TANESCO. Jambo hili halijakaa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu mwingine ambao upo katika mikataba hii ni suala la tozo ambalo TANESCO wanatozwa. Katika Mkataba huu kuna kipengele kinachosema kwamba TANESCO asipoweza kununua kiwango cha juu na cha chini anatozwa faini; eneo hili limekaa vibaya na kwa taarifa yako ni kwamba hadi kufikia Januari, 2018 TANESCO wanadaiwa bilioni arobaini na milioni mia tatu. Mkataba huu haujakaa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo lina upungufu na ambalo ningependa kulizungumzia ni eneo linahusu Production Sharing Agreement. Huu ni mkataba ambao Serikali iliingia na watu wa Pan African Energy. Moja ya upungufu mkubwa ni kwamba watu wa Pan African Energy wao wana-operate kwenye mikondo yote mitatu kwa maana upstream, midstream na downstream, kitu ambacho sio sahihi hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Petroli, inaruhusu Pan African Energy ku-operate kwenye upstream. Tafsiri yake ni kwamba gharama za midstream na downstream zote wanazipeleka juu, maana yake wanaiibia Serikali; Serikali lazima iangalie katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, baya zaidi ni kwamba Pan African Energy katika Production Sharing Agreement wameiwekea sharti TPDC kwamba ili aweze kushiriki katika shughuli za uzalishaji ni kwamba lazima aweze kuweka dhamana na dhamana hiyo lazima ipitiwe na Pan African Energy. Hili jambo ni mkataba hasi na ni lazima Serikali iweze kupitia eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ufupi utaona kwamba suala la Pan African Energy kuna upungufu makubwa sana, niiombe Serikali…

MHE. YOSEPHER F. KOMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kigua kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Yosepha Komba.

T A A R I F A

MHE. OMAR M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea lakini ina upungufu kimsingi, hoja ninazozizungumzia ni kubwa zaidi kuliko hiyo anayoizungumza yeye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia kwamba TPDC wao hawaruhusiwi kushiriki kwenye shughuli za uzalishaji mpaka waweke dhamana, lakini dhamana hiyo haiwezi kuwa na thamani yoyote ile mpaka iwe imekubaliwa na Pan African Energy. Kimsingi utaona kwamba kuna matatizo makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ufupi niseme Mkataba wa Pan African Energy au Production Sharing Agreement una matatizo makubwa sana. Ushauri wangu kwa Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, naomba wakae chini waone namna gani ambavyo wanaweza kuhakikisha kwamba tunakaa chini kwa sababu Serikali inapoteza mapato mengi. Pamoja na hayo mkataba huu umekwenda vibaya zaidi, unaisha 2024, sasa kwa nini tusubiri mpaka 2024? Nashauri kwa kupitia njia zile tulizoptia kwenye madini basi tuweze kutumia njia hiyo hiyo kwenye sekta ya gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo machache, naunga mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019
MHE. OMARY M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia taarifa ya Kamati ya PAC.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kama Mjumbe wa Kamati ya PAC ambayo kwa takribani kwa miaka minne nimekuwa kwenye Kamati hii. ni lazima niseme wazi kabisa kwamba mabadiliko makubwa yapo katika uandaaji wa hesabu na hoja nyingi zimepungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, na yasema hayo kwa sababu ukipitia hesabu za Serikali Kuu, Mashirika ya umma. Pale mwanzoni kulikuwa na hoja za ukaguzi nyingi sana. Sasa ukiangalia kwa taarifa hii tunayopitia hapa tunazungumzia taarifa ya Mwaka 2017/2018 na msingi wa taarifa hii ni taarifa ambayo inaandaliwa na Kamati ikishirikisha wataalam.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilikuwa namsikia mzungumzaji mmoja hapa anaanza kuhoji kwamba jambo fulani halipo, jambo fulani halipo. Msingi wa Kamati ni kwamba ni maoni ya washiriki wote na ukitaka kuona hilo limefanyika ni kwamba hata Mwenyekiti ambaye anatoka upande mwingine ndiye ambaye ameongoza vikao hivyo. Kwa hiyo, nataka kutoa wasiwasi kwamba haya ambayo yameingia kwenye taarifa hii ya Kamati ya PAC ni maoni ya Kamati ya PAC na wala siyo maoni ya mtu mmoja kwa sababu msingi wa hoja za Kamati ni hoja za CAG na kama CAG ameleta hoja anaitwa accounting officer au Katibu Mkuu, anapoleta majibu lazima yapelekwe kwa CAG ayaptie apate majibu sasa inawezekana haya unayoyauliza sasa hivi ni miongoni mwa mambo ambayo yanafanyiwa kazi na CAG ili yarudi tena katika Kamati. Hilo nilitaka kuliweka sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ambalo lingependa kulzingumzia ni juu ya mambo mbalimbali ambayo Kamati yetu imeiona na ambayo kwa kiasi kikubwa Kamati ya PAC imetoa maoni yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nijikite eneo ambalo ni eneo muhimu sana kwenye Ofisi za Mamlaka ya Mapato (TRA); tumegundua changamoto nyingi sana, Kamati imegundua changamoto nyingi sana sasa hizi kwa kiasi fulani zinaonekana ni changamoto ambazo inaonekana kwamba Serikali haijakusanya mapato kwa kiasi kikubwa sana lakini ukitazama hoja za CAG utaona kwamba kile kinachoonekana katika hesabu za Mamlaka ya Mapato (TRA) ni mambo ambayo yemafanyika kitaalam ambayo pengine yamefanyika kwa makusudi au yemefanywa na watu ambao hawana utaalam.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mmoja, ni juu ya kodi la zuio (withholding tax); utaona kwamba maeneo mengi inaonekana mapato hayajakusanywa kwenye eneo hilo. Lakini pia yapo maeneo mbalimbali ambayo mamlaka ya mapato yanaonekana hayajafanya vizuri. Mfano, kuna kesi takribani 417 ambazo zilipaswa ziwe tayari zimetolewa maamuzi hazijafanyika mpaka sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nini ushauri wangu? Najua Ofisi ya Mamlaka ya Mapato (TRA) wanafanyakazi nzuri sana kupitia kwa Kamishina wa TRA na watu lakini naona sasa umefika umuhimu sasa wa kuhakikisha kwamba hoja hizi ambazo zinaonekana Serikali haijakusanya mapato wakati hakuna uhalisia wa mapato basi ziweze kutafutiwa majibu na namna gani wanaweza wakafika hapo ni kuhakikisha kwamba wanakuwa na wataalam wa kutosha ambao wanafanya assessment ya kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii unaweza ukamkadiria mtu kwamba kwa mwaka anaweza kukusanya milioni 800 kumbe pato lake ni milioni 200. Hesabu zile zitaingia kwenye Ofisi ya Mamlaka ya Mapato CAG akipitia ataona kwamba TRA hawajakusanya mapato kumbe ni makadirio mabaya ambayo yamefanyika. Mimi nimuombe Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha yuko hapa alione hilo wakae na watu wa TRA waone namna ambavyo ukadiriaji ufanywe na watu sahihi kwa wakati sahihi na watu ambao wana taaluma ya kutosha vinginevyo itaoneonekana siku zote kwamba hesabu hizi haziko sawa, Serikali haijakusanya mapato kumbe siyo mapato sahihi hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ningepanda kulitolea maelezo au kulichangia ni hija ambayo imeonekana kwamba watu wa mfuko wa Bima walitoa pesa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Benjamin. Sasa ukiangalia hapa utaona kwamba hapa hakuna hoja ya matumizi mabaya ila no hoja ya kuweka hesabu vizuri kwa maana kwamba hesabu za watu wa National health Insurance hazionyeshi kwamba wamewekeza kiasi hicho kwa ajili ya ujenzi wa hospitali.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni jukumu la Serikali sasa hivi kuangalia watu wa National Health Insurance wakae na watu wa Wizara ya Elimu kupitia Benjamin pale kuona kwamba hesabu hizi, uwekezaji huu wa National health Insurance utaweza kuwekwa kwenyte vitabu kiasi gani. hilo ndilo ambalo linesemekana ndiyo maana hoja ya CAG imeonyesha kwamba uwekezaji ule hauonekani kwenye vitabu vya wenzetu wa National Insurance kwa sababu wanaonekana mfuko wa Bima ya afya wao mfuko ule hauendi vizuri lakini kama hesabu hizi, kama uwekezaji huu wa ujenzi wa hospitali ya Benjamin ungeweza kuonekana katika hesabu zao pengine wangeonekana wanafanya vizuri sana. Naomba wahusika walisikie hili na waweze kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ambalo ningependa kuchangia ni juu ya Shirika letu ya Nyumba; sisi Wajumbe wa Kamati ya PAC tulifanya ziara kutembelea miradi mbalimbali. Tulipata fursa ya kwenda pale Morocco kuangalia ujenzi wa majengo makubwa lakini tulienda Kawe. Sasa kinachoonekana pale ni kwamba watu wa National Housing miradi ile imesimama. Mkandarasi yupo pale site na kila siku analipwa takribani milioni 20, uwekezaji ule umesimama lakini unajiuliza kwanini umesimama? Ndiyo tunaamini na Kamati inaamini kabisa kwamba uwekezaji ule haukuwa mzuri, sasa nii kifanyike?

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauari wangu kama Mbunge; kwa sababu ukiangalia kama Serikali itasitisha miradi ile maana yake yule Mkandarasi tutamlipa bilioni 99.99 ni takribani bilioni 100 lakini tayari watu wa Shirika na Nyumba wameshapokea kodi ya bilioni 2.6 sasa nini kifanyike hapa? Waziri wa Ardhi yupo hapa ambae Shirika la Nyumba liko chini yake; hebu wakae chini waangalie namna gani wanaweza kutoka kwa sababu kuendelea kutokuendeleza ile miradi maana yake ni kuipelekea Serikali kupata hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri sana tuangalie waliofanya makosa hawapo sasa hivi, menejimenti iliyopo ni mpya sasa tuangalie kwamba Serikali isiendelee kupata hasara. Miradi ile iko pazuri ukichukulia mfano mradi wa Kawe uko karibia na bahari pale kwa maana tukimalizia majengo pale Serikali inaweza ikapata kiasi kikubwa sana cha pesa na ukianglia unapofanya investment lazima return yake ile ionekane. Sasa pesa ile tumeiweka chini tunatarajia nini maana Mkandarasi yule hawezi kuondoka, ukiondoka maana yake utalipa bilioni 100. Hebu tuangalie namba ya kutafuta pesa miradi ile tuyikwamue itoke hapo ilipo iende mbele zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni juu ya Bodi hizi za kusuluhisha kwa sbabau mwaka jana hapa tulipitisha Sheria kwamba tunaanzisha kitengo pale Wizara ya Fedha kwamba kama umekadiriwa vibaya basi unahakikisha unapeleka malalamiko yako Wizara ya Fedha pale. Ninaushauri mmoja; kuna Bodi hizi ambazo ndizo zinazotatua kesi, naona Bodi hizi hazifanyikazi sawasawa na ndiyo maana bado kuna kesi nyingi sana zinazohusu ukadiriwaji wa mapato. Namuomba Waziri wa Fedha aliangalie hili pengine kama hawana wataalam wa kutosha ili kesi ziendelee na hoja hizi ambazo zimekwama ziweze kuondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningependa kuchangia ni juu ya Kamati ya LAAC; yupo Mheshimiwa mmoja amezungumza hapa kwamba mfumo wa Force account ni mfumo ambao una tija. Ni kweli una tija kwa sababu kwa kiasi kikubwa umeweza kuokoa fedha lakini kitu ambacho nimekiona na ambacho hata halmashauri yangu ya Wilaya ya Kilindi inacho ni kwamba hatuna wataalam, hatuna Mainjinia wa Civil engineering ambao ndiyo wasimamizi wakuu wa miradi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni kwamba kama hatuna wataalam, imefika wakati Waziri wa TAMISEMI yupo hapa naomba anisikilize; hakikisha unapeleka wataalam, fundisha wataalam, wapeleke katika halmashauri. Miradi hii lazima iwe na wataalam wa kusimamia vinginevyo thamani ya pesa haitapatikana hata kidogo. Tutasimama hapa, tutasema Force account ni nzuri lakini bila wasimamizi wenye taaluma ya kutosha hatuwezi kufika mbele na wala hatuwezi kufanikiwa. Naomba Serikali ione kwamba ni eneo lenye changamoto kubwa sana ambalo lazima lifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ningependa kulizungumzia, Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia juu ya TBA, mimi ushauri wangu kama Mbunge, naamini kabisa TBA wamefanya kazi nzuri lakini walikuwa wameelemewa na mzigo, nadhani kama Serikali inaweza ikachukua njia iliyo sahihi, wachukue miradi hii ya ujenzi wawapelekee watu wa National Housing waweze kufanya kazi hizo kwa sababu wao wameonekana baadhi ya miradi wanafanya kazi vizuri sana, vinginevyo tutapelekea kuwalaumu, tutawalaumu lakini kumbe wamezidiwa. TBA wamezidiwa kwa sababu walipewa kazi nyingi sana na hili linaonesha wazi kwamba wakiendelea kutopewa kazi hizi basi watafeli hawataweza kufanikiwa kwa sababu Kamati yetu sisi imepitia miradi mingi ikaona kwamba TBA wameshindwa kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naomba kurudia kusema tena kwamba tulipoanza na tulipo ndio ni vitu viwili tofauti, Serikali inakusanya mapato ya kutosha, TRA wanafanya kazi vizuri, lakini waangalie mapengo, waangalie namna ya kuimarisha utendaji wa TRA hususani kwa wataalam wanaofanya makadirio kwa sababu malalamiko ni mengi sana ili tuweze kutengeneza hesabu ambazo ni hesabu sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. OMAR M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote kabla sijaanza kuchangia juu ya Mpango huu wa Serikali, napenda kwanza nikushukuru wewe na niwashukuru Wanakilindi walionipa fursa hii ya kuweza kuwa Mbunge wao wa Jimbo la Kilindi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimepitia Mpango huu, una mambo mengi mazuri, nami naamini kabisa nia ya Serikali hii ni kuleta maendeleo ya dhati kwa wananchi wa nchi hii ya Tanzania. Mpango huu umeangalia mambo muhimu sana ambayo kwa muda mrefu yalikuwa hayaendi sawasawa, sasa basi ni mambo gani ambayo nayadhamiria kwa leo kuyazungumzia? Nitaanza moja kwa moja kwenye Sekta ya Mawasiliano tunapozungumzia barabara.
Mheshimiwa Spika, suala la miundombinu ni suala muhimu sana, nikiamini kwamba miundombinu ikiwa ni mizuri, basi maendeleo ya maeneo mbalimbali na ya nchi kwa ujumla yataweza kufanikiwa. Katika eneo la barabara, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuliwekea uzito unaostahili kwa sababu maeneo mengi yalikuwa hayapitiki hususan barabara katika kiwango cha lami. Hili limeweza kufanikiwa, nami naomba niipongeze Serikali katika suala hili.
Mheshimiwa Spika, katika eneo langu ambalo nimetoka katika Jimbo la Kilindi, kuna mpango wa kuijenga barabara ile kwa kiwango cha lami ambapo barabara ile itaanzia Handeni kwenda Kibirashi hadi Kiteto kupitia Namrijo Juu pamoja na Jimbo la Mkoa wa Singida.
Mheshimiwa Spika, nataka nilizungumzie suala hili kwa sababu kama nilivyozungumza awali kwamba mawasiliano ni kitu muhimu sana, katika eneo langu ninalotoka kuna mazao yanalimwa hususan mahindi na utakuta hata nchi jirani mazao mengi yanakuja kuchukuliwa Jimbo la Kilindi, lakini kwa sababu miundombinu siyo mizuri, unakuta mazao mengi yanaishia kuozea katika mashamba.
Mheshimiwa Spika, namshauri kaka yangu, Mheshimiwa Profesa Mbarawa pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri waliangalie hili, japokuwa najua kwa mwaka huu wa fedha unaoanza Julai hautakuwepo Mpango huu, lakini barabara hii ipewe kipaumbele cha hali ya juu kwa sababu italeta maendeleo ya dhati kwa wananchi wa Kilindi na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine ambayo ningependa kuchangia ni Sekta ya Madini. Nimeona imezungumziwa hapa; na tunapozungumzia madini, tunazungumzia Sekta ya Nishati. Ni kweli kwamba umeme ndiyo kila kitu na Mheshimiwa Waziri hususan Waziri wa Nishati na Madini, ameweza kuweka mipango mizuri sana juu ya nishati, lakini nishati hii haijafika maeneo mengi hususan katika vijiji.
Mheshimiwa Spika, nitolee mfano tu katika Jimbo langu la Kilindi. Tunavyo vijiji kama 102, lakini vijiji vichache sana ambavyo vimenufaika na huduma hii ya umeme kwa maana ya REA, ushauri wangu ni kwamba, yale maeneo ambayo kwa asilimia kubwa wameshapata huduma hii, basi waangalie maeneo mengine ambayo hayajanufaika na huduma hii, kwa sababu wananchi hususan wa vijijini wanahitaji umeme kwa ajili ya maendeleo, wanahitaji umeme kwa ajili ya shughuli mbalimbali. Ni imani yangu kwamba Serikali italiangalia hili kwa umuhimu wa juu sana.
Mheshimiwa Spika, lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni suala la maji. Maji imekuwa ni kilio, kila Mbunge anayesimama hapa anazungumzia suala la maji. Labda tu nizungumzie kwa eneo ninalotoka mimi. Ni kwamba eneo lile lina maji mengi sana lakini hatuna visima na miundombinu kwa kweli ni ya muda mrefu kiasi kwamba maji imekuwa ni tatizo kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri wa Maji ni kwamba, maji yanapotea sana. Kuna Mpango kule wa bwawa katika Kata ya Kibirashi; utaratibu ule wa kuhifadhi maji kwa njia ya mabwawa ni utaratibu mzuri sana. Badala ya kuchimba visima tuwe na njia ya kuweza kuhifadhi maji kwa njia ya mabwawa. Nadhani utaratibu huu ni mzuri sana. Ni utaratibu ambao unaweza ukaisaidia Serikali kupunguza kero ya maji kwa muda mrefu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, utakuta sasa hivi mvua zinanyesha kule lakini maji mengi yanapotea kwa sababu hatuna utaratibu mzuri wa kuhifadhi maji. Nadhani muda umefika sasa, tuone namna ya kuwashirikisha wananchi pamoja na Serikali juu ya kuweka visima au kuweka mabwawa ambayo yanaweza kuhifadhi maji kwa muda mrefu. Kwa sababu ukiangalia katika eneo langu, siyo rahisi kusema labda maji yatoke Ruvu yafike Kilindi; lakini njia mbadala ambayo inaweza kusaidia kutatua tatizo hili la maji ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na mabwawa.
Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali yangu kwamba imeweza kuliona hili, tuna bwawa la mfano kabisa ambalo halijakamilika, liko Kata ya Kibirashi. Bwawa hili litawanufaisha wafugaji pamoja na wakulima, naishukuru sana Serikali yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ningependa kugusia ni suala la viwanda. Nimeona Serikali yetu ina mpango mzuri sana wa viwanda hususan kufufua viwanda vya zamani pamoja na viwanda vipya. Naomba niipongeze Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi katika hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa kinachonishangaza hapa, ukiangalia upande wa Tanga ambapo tulikuwa na viwanda vingi sana; tulikuwa na viwanda vya matunda, lakini viwanda vile vimekufa. Nashauri kwamba muda umefika wa kuvifufua viwanda vile pamoja na kuanzisha viwanda vingine.
Mheshimiwa Spika, eneo ninalotoka kuna wafugaji wengi sana, lakini nikiangalia Mpango huu, sioni namna ambavyo wananchi hususan wafugaji wa Wilaya ya Kilindi wanaweza kunufaika na Mpango huu wa viwanda vidogo vidogo. Sasa najiuliza, mifugo hii ambayo Wanakilindi wanayo, watanufaika na nini katika hili? Namshauri kaka yangu Mheshimiwa Waziri wa Viwanda pale aangalie namna ambavyo tunaweza na sisi wananchi wa Kilindi tukaweza kupata kiwanda kidogo cha kuweza hata kutumia maziwa haya mengi ya mifugo ya Wilaya ya Kilindi ili wananchi waweze kunufaika na fursa hii ambayo wanapata wananchi wa sehemu nyingine.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ningependa kuchangia ni suala la utalii kwa ujumla. Ni kwamba eneo la utalii ni eneo muhimu sana ambalo naamini Serikali yetu lazima itie msisitizo wa hali ya juu sana. Wengi wamezungumza hapa kwamba watalii wanafika Kenya, halafu wana-cross wanakuja Tanzania. Hili limeelezwa kwamba mpango mzuri wa Serikali ni kununua ndege kusaidia kufanya watalii waweze kufika nchini kwetu kwa urahisi zaidi.
Mheshimiwa Spika, napongeza mpango huu, ni mzuri na wale ambao wana-discourage suala hili, naona hawako pamoja na sisi. Naomba Serikali yangu iendelee mbele na utaratibu huu. Pia kuna maeneo ambayo Mheshimiwa Waziri wa Utalii naona hawajafika maeneo mengi, labda nitoe mfano mmoja, katika eneo ninalotoka, kuna Mbuga ya Wanyama ya Saunyi. Mbuga ya Saunyi ina wanyama wa aina mbalimbali, lakini nina wasiwasi kama Serikali inajua kama kule kuna mbuga za wanyama.
Mheshimiwa Spika, fursa ile inawezekana hata wanyama ambao wanachukuliwa kwenda nje ya nchi, wanachukuliwa kutoka kule kwa sababu sijawahi kusikia hata siku moja watu wanaizungumzia Mbuga ya Saunyi.
Mheshimiwa Spika, nashauri kwamba ili tuweze kuimarisha utalii, ni kwamba Serikali iwe na utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba kila fursa ya utalii iliyopo, inatumika vizuri. Haya ni mambo ya msingi ambayo wenzetu wa nchi jirani wameweza kuzitumia na kwa hakika uchumi wao umeweza kwenda juu sana kwa kutumia utalii vizuri. Nina imani kwamba tunavyo vivutio vingi sana lakini Serikali haijatumia vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia napenda kuchukua fursa hii kuzungumzia changamoto ambazo tunazipata katika madini. Ni kwamba nchi yetu ina madini mengi sana, maeneo mengi yana madini na Wilaya ninayotoka mimi, Jimbo langu la Kilindi lina maeneo mengi sana yenye madini, lakini wachimbaji wadogo hawajaweza kunufaika na Mpango huu. Hawajanufaika pengine kwa sababu ya sheria zilizopo.
Mheshimiwa Spika, nitoe mfano mmoja tu kwamba hawa wachimbaji wadogo wadogo ndiyo watu wa kwanza ambao huwa wanagundua wapi pana madini. Mchimbaji huyu mdogo akishapatiwa license, inapokuwa muda wake umepita, hapewi fursa mchimbaji huyu kwa sababu hana uwezo. Unakuta license hizi wanaopewa watu wengine wenye uwezo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo hili limeleta malalamiko makubwa sana na namwomba kaka yangu Waziri wa Nishati na Madini aliangalie tena na atakapoleta Muswada wake hapa tuangalie upya sheria hizi zinazohusu wachimbaji wadogo wadogo kwa sababu naamini Serikali ina nia nzuri ya kuwawezesha wananchi wadogo ili waweze kusimama vizuri kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, haya mambo ni ya msingi sana kwa sababu sisi kama Wawakilishi wao tunapata malalamiko mengi sana hususan katika maeneo ambayo yana wachimbaji wadogo wadogo. Ni imani yangu kwamba itakapofika muda wa kuchangia Bajeti ya Nishati na Madini, hili tutalichangia kwa nafasi nzuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni elimu. Elimu ni kila kitu. Elimu imezungumzwa hapa na nashukuru kwamba Serikali imeliangalia kwa kulipa kipaumbele. Kama alivyozungumza Mheshimiwa mwingine aliyepita hapa, amezungumzia juu ya kuvipa kipaumbele hivi Vyuo vya VETA. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Vyuo vya VETA vimeweza kuinufaisha nchi hii kwa muda mrefu sana hususan wanafunzi ambao hawajapata fursa kwenda Sekondari. Nashauri kila Wilaya, kila Mkoa, ikiwezekana tuwe na VETA ili iweze kuwasaidia vijana wetu, kwa sababu tumezungumzia kwamba tunataka tuwe na viwanda. Viwanda hivi watendaji au wafanyakazi hawatakuwa ni ma-graduate peke yake, ni lazima tutahitaji kada za katikati ambazo zitazalishwa kutokana na VETA.
Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu nilikuwa nafuatilia kabla sijawa Mbunge, ni kwamba kulikuwa na ahadi ya kujenga Chuo cha VETA katika Jimbo la Kilindi Kata ya Kibirashi. Bahati mbaya ahadi hiyo imekuwa ni hewa, lakini naamini kabisa Serikali yangu ni sikivu, watanisikiliza na wataweza kutimiza wajibu wao katika hili, kwa sababu wananchi wanahitaji VETA kwas ababu watoto wengi hawapati fursa ya kupata mafunzo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimezungumzia hili kwa uchungu mkubwa sana kwa sababu maeneo tunayotoka sisi, wananchi vipato vyao ni vya chini sana na sio wote ambao wana uwezo wa kupeleka watoto wao sekondari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, labda nikwambie tu, Wilaya yangu ya Kilindi kwa mwaka huu imekuwa ni Wilaya inayoongoza kimkoa katika matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2015. Naomba kwa niaba ya Halmashauri ya Kilindi, nimshukuru pia Waziri wa Elimu kwamba amefanya jitihada kubwa sana kuhakikisha kwamba pamoja na changamoto nyingi tulizonazo tumeweza kusonga mbele.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya. Kwa mwelekeo wa bajeti hii inayoonesha wazi Serikali imedhamiria kuboresha elimu kuanzia ngazi ya shule ya msingi hadi elimu ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze uamuzi wa Serikali kuhamishia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) kuhamishwa Wizara ya Elimu kwa dhana ya dhamira ya kuvifanya vyuo hivi kutoa elimu ya ufundi, jambo hili litasaidia sana kuwezesha vijana wetu wengi ambao hawajapata fursa ya elimu ya sekondari wapate elimu ya ufundi ambayo wataweza kujiajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo hivi kwa muda mrefu vimekuwa vikiendeshwa katika mazingira magumu sana, vimekuwa havipati fedha za kutosha, dhamira ya kutoa elimu imefikiwa kwa kiasi kidogo.
Sasa Serikali iongeze bajeti kwenye vyuo hivi viweze kutoa elimu bora na wanafunzi bora, yale maeneo ambayo hayana vyuo hivi vya FDC‟s basi Serikali ijenge vyuo vya VETA. Mfano ni Jimbo langu la Kilindi halina FDC‟s wala VETA japo kwa mwaka wa fedha unaoanza Julai 2016 Serikali imedhamiria nasi tupate chuo cha VETA. Naomba nipate uthibitisho wa dhamira ya Serikali katika hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie juu ya upungufu wa walimu katika shule zetu za msingi na Serikali, japo Serikali kwa sasa inaonesha kutatua tatizo hili hususani katika masomo ya sayansi, hisabati, fizikia na kadhalika. Mfano, katika Jimbo langu la Kilindi shule za sekondari Mafisa, Kibirashi, Kikude hazina walimu wa kutosha, nitaleta ofisini kwa Mheshimiwa Waziri upungufu wa walimu ili Serikali ione namna ya kutatua tatizo hili vinginevyo kiwango cha elimu katika Wilaya ya Kilindi kitashuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nieleze juu ya suala la Maafisa Elimu na Walimu kukaa katika eneo moja la kazi. Jambo hili kwa kweli halileti ufanisi katika utendaji. Mtumishi kukaa eneo moja kwa muda mrefu kunamfanya mtumishi kutojifunza changamoto na morali ya kazi kwa mfano, katika Jimbo langu la Kilindi, Afisa Elimu Sekondari na Elimu ya Msingi wamekaa muda mrefu, Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI, tupate watumishi wapya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba suala la Wilaya kupata High School lipo chini ya Serikali za Mitaa lakini bado Wizara hii inalo jukumu la kusimamia Wilaya ambazo hazina kabisa shule za kidato cha tano na cha sita zinapewa fursa hizo. Mfano katika Wilaya yetu ya Kilindi hatuna hata shule moja, hii inanyima fursa kwa vijana ambao wazazi wao hawana uwezo kujiunga na shule ambazo zipo mbali na Wilaya ya Kilindi. Wazazi, uongozi wa maeneo hawana nguvu za kiuchumi. Wanafunzi wanachaguliwa mbali na Wilaya ya Kilindi mara nyingi hawaendi. Wizara ituone nasi, itusogezee shule ya wavulana na wasichana katika ngazi za kidato cha tano na cha sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa dhamira yake ya kutoa elimu bure kwa wananchi. Wananchi wa Tanzania na wa Kilindi wamenufaika sana na fursa hii. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hotuba hii kwanza kwa kumpongeza Waziri na Naibu Waziri wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya kumsaidia Rais, Mheshimiwa John Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo nitachangia kwenye maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, usikivu wa redio Tanzania ni mdogo sana kwenye maeneo mengi ya nchi yetu ya Tanzania. Redio hii kwa jina TBC ndiyo wananchi wengi wanaitegemea kwa ajili ya taarifa za uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano katika Jimbo langu la Kilindi kwa kweli, wananchi wa eneo hili kwa muda mrefu wamekuwa wakililia kupata haki yao ya kupata taarifa, hususan za TBC, japo zipo baadhi ya redio zinasikika. Naishauri Wizara hii na Wizara ya Mawasiliano wahakikishe mawasiliano ya uhakika ya redio yanapatikana katika Jimbo langu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kuchangia suala la michezo hususan mpira wa miguu. Mchezo huu muhimu ni sehemu ya ajira kwa vijana wetu. Utaratibu wa Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF) katika kuandaa soka letu Tanzania siyo mzuri. Hatuna utaratibu wa kupata timu ya Taifa, hususan timu ya vijana, Serikali haina budi kuwekeza zaidi kwenye soka la vijana kuanzia soka la vijana chini ya miaka 14, miaka 17 na chini ya miaka 20 huko ndiko tunakoweza kuwekeza soka la uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira (TFF) ni lazima tuwekeze kwenye mpira kwa kushirikiana na makampuni mbalimbali ambayo yatatoa udhamini mkubwa ili Taifa liweze kusonga mbele. Nchi za wenzetu za Afrika kama Nigeria, Algeria, Ivory Coast na kadhalika wamefika mbali kwa nchi zao kuweza kuwekeza katika soka la vijana. Vilevile Wizara ya Elimu ihakikishe kuwa michezo shuleni inarudishwa kwa kasi kubwa kwani huko ndiko waliko vijana wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ningependa kujielekeza kwenye upatikanaji wa vifaa vya michezo kwa bei nafuu. Vifaa vingi vya michezo vipo bei ya juu sana, Serikali ilione suala hili kwa kusimamia bei za vifaa vya michezo ili wananchi wengi hususan vijana waweze kupata vifaa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ni muhimu katika michezo nchini ni suala la uchaguaji wa timu ya Taifa. Timu ya Taifa imekuwa na utaratibu mbovu sana, timu hii ya Taifa imekuwa haiangalii wachezaji kutoka Wilayani na Mikoani kama ambavyo miaka ya nyuma ambapo timu ya Taifa ilitazama uwezo wa mtu na siyo timu kubwa tatu za Dar es Salaam, Simba, Yanga na Azam. Wakati umefika sasa pawepo na Kamati ya wachezaji wa zamani waliocheza timu ya Taifa kuhusishwa na utafutaji wa vipaji mikoani kuanzia ngazi ya vijiji, wilayani na mkoani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hotuba.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa jioni ya leo niweze kusema machache, hususani katika Wizara hii iliyopo mbele yetu. Naomba nichukue fursa hii kwanza, kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuiletea maendeleo nchi yetu. Watanzania ni mashahidi kwamba, Profesa Muhongo na Naibu wake wanafanya kazi iliyotukuka na sote hatuna budi kumpa pongezi na kum-support afanye kazi ya ziada. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, itakuwa sio busara pia, kutokumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuhakikisha kwamba, Tanzania inapata bomba lile ambalo linatoka Uganda hadi Tanga. Bomba hili litatoa fursa ya ajira kwa vijana wetu, ndugu zetu, kabla na baada. Naomba niseme kwa niaba ya wachangiaji au Wabunge wa Mkoa wa Tanga, nikupe shukrani za dhati sana katika hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo sasa naomba nichangie kuhusu REA, Umeme Vijijini; Waziri na Naibu Waziri ni mashahidi, mara nyingi nimekuwa nikizungumza nao na kupeleka ushahidi kwamba, Jimbo la Kilindi lina vijiji visivyopungua 102, lakini katika vijiji hivyo ni vijiji 20 tu, tena vilivyopo usoni mwa Makao Makuu ya Kata. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anaangalia suala la umeme wa REA vijijini, basi ajue Wilaya ya Kilindi wana changamoto kubwa sana. Naomba vijiji vilivyobaki, kama siyo vyote, tuweze kupata hata nusu ya vijiji hivyo kwa sababu, wananchi wa Jimbo la Kilindi wanahitaji umeme kwa ajili ya maendeleo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia sambamba na mambo ya umeme hapo hapo, ni kwamba umeme uliopo Kilindi uliletwa kwa ajili ya wakazi wachache sana. Jimbo lile sasa hivi lina wakazi takribani laki tatu, umeme ule unakatika mara kwa mara, wakati mwingine hata wiki umeme unakuwa haupatikani! Nashauri basi, kwamba Wizara iangalie namna gani inaweza ikaboresha ili wananchi wa Wilaya ya Kilindi waweze kupata umeme wa uhakika. Najua hilo kwamba, kuna utaratibu wa kuleta umeme kwa kiwango kikubwa, basi na Wilaya ya Kilindi kwa ujumla iweze kunufaika na mpango huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, napenda kuzungumzia suala la madini. Wilaya ya Kilindi imebahatika kuwa na madini ya dhahabu na ruby yanapatikana kwa kiwango kikubwa sana pale, lakini nimepitia kitabu hiki cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri, sijaona ni wapi! Sasa Serikali inatia msisitizo kuweka nguvu ili wananchi wa Kilindi waliobahatika kwa nguvu ya Mwenyezi Mungu kupata madini yale waweze kunufaika na madini yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwamba kuna utaratibu wa kupima, Mheshimiwa Waziri, Ukanda wa Ziwa unajulikana kwamba ni Ukanda wa Green Belt. Mzungumzaji aliyepita hapa amezungumza kwamba, migodi mingi kule inafungwa, Kilindi ina dhababu nyingi sana, kwa nini sasa tusiharakishe upimaji katika Jimbo la Kilindi ili wawekezaji wanaokuja kwa ajili ya dhahabu na ruby wakimbilie katika Wilaya ya Kilindi, hivyo wananchi wa Kilindi wanufaike na Taifa kwa ujumla. Naomba, Mheshimiwa Waziri aliangalie hili kwa jicho la tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ningependa kuzungumzia juu ya Sheria za Madini, Wilaya ya Kilindi kuna migogoro mingi; Mheshimiwa Waziri kwa sababu, utaratibu wa kutoa license mtu anaweza kupata license yupo Mwanza, yupo popote pale, lakini naamini na anafahamu hilo kwamba, wagunduzi wa madini mara nyingi ni wananchi au wakulima wa maeneo yale. Sasa inapokuwa mtu huyu kaja na license, amemkuta mwenyeji pale ambaye vizazi vyote kazaliwa pale, kazeekea pale, halafu anamwambia azungumze naye namna ya kumpisha ili aweze kuchukua madini pale ardhini! Mtu alikuwa analima mahindi, leo kaambiwa kwamba, pana dhahabu, hivi ni rahisi kuondoka eneo hilo? Siyo rahisi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri sheria hii iangaliwe kwa jicho lingine tena kwa sababu, wananchi wa maeneo haya wanadhani ndio wanapaswa kupata fursa ya kunufaika na madini yale. Hatukatai kwamba, wawekezaji wasije Tanzania, lakini utaratibu uwape fursa wananchi wa maeneo yale kwa sababu, migogoro ya mara kwa mara imetokea na Mheshimiwa Waziri ni shahidi. Nimeshakwenda ofisini kwake nikamwambia kwamba, tunahitaji Ofisi ya Madini katika Wilaya ya Kilindi ili iweze kusimamia taratibu za madini Wilaya ya Kilindi. Ni kwamba, ofisi ya madini ipo Handeni, lakini umbali kutoka Wilaya ya Handeni mpaka Wilaya ya Kilindi ni umbali mkubwa unahitaji gharama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri tu hakuna ulazima wa kujenga ofisi pale, tusogezee maafisa watakaoweza kuwahudumia wananchi kwa sababu, wananchi wa Kilindi na wenyewe wanayo fursa ya kupata huduma ya madini pale. Hii pia itapunguza migogoro ya ardhi ya mara kwa mara. Mheshimiwa Waziri naomba wakati ana-wind up aweze kunipa majibu katika hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kuchangia ni suala la REA. Inavyoonekana hapa wale wakandarasi, makampuni yale yanayosambaza umeme vijijini, inaonekana wamepewa maeneo mengi sana. Nilipokuwa nazungumza na Meneja wa Wilaya ya Kilindi aliniambia, mtu anayesambaza umeme vijijini amepewa Mkoa wa Morogoro na Mkoa wetu wa Tanga na Mkoa mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani wakati umefika wa kuwapunguzia wale work load ili waweze kufanya kazi hizi kwa ufanisi wa hali ya juu sana. Wakati mwingine tutakuwa tunawalaumu hawa watu, lakini hawafanyi kazi kwa ufanisi kwa sababu, kazi hizi wanazopewa vijiji vinakuwa vingi sana. Nashauri na naamini kabisa kwamba, kwa phase ya tatu, basi kazi zitakwenda kwa haraka ili wananchi waweze kufaidika na umeme huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia suala la kumsaidia Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla kwamba, tunatakiwa tuongeze wigo wa mapato. Wigo wa mapato upo katika maeneo haya ambayo nayazungumzia, hususani ya madini. Siku moja Mheshimiwa Waziri nimeshawahi kumwambia kwamba, watu wanagawana milioni 200, mia 300 Kituo cha Polisi, maana yake Serikali inapoteza mapato! Hebu, Wizara ya Madini ione namna ya kuweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba, mapato haya yanayopotea ya Serikali, basi yanadhibitiwa. Haiwezekani mtu anayechimba pale, mwekezaji mdogo apate milioni 300 wakagawane Kituo cha Polisi, usalama hapo uko wapi? Wizara ya Madini iko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani wakati umefika, Mheshimiwa Waziri aone na kunisikiliza kwa sababu maneno haya ninayozungumza siyo yakwangu mimi, ni ya Wapigakura wa Wilaya ya Kilindi. Naamini wananisikiliza na wanajua Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi itawasikiliza na itawaletea Ofisi Wilaya ya Kilindi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni juu ya hawa wachimbaji wadogo wadogo na wakubwa wa madini, wamekuwa wakifanya shughuli hizo wakati mwingine wakiathiri mazingira. Kwa mfano, katika Kata ya Tunguli, kuna mwekezaji pale ambaye anafanya shughuli za madini, lakini kwa taarifa nilizonazo ni kwamba, maji yanayomwagika…
MWENYEKITI: Ahsante, muda wetu ndio huo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia hotuba iliyopo mbele yangu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wake kwa kazi kubwa na umahiri wa hali ya juu katika Wizara hii nyeti kwa jinsi wanavayojitoa kulitumikia Taifa hasa katika kusimamia huduma ya umeme kwenye maeneo yote ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, naomba kuchangia katika huduma ya umeme vijijini (REA). Huduma hii ni nyeti na imelenga kusambaza umeme kote nchini, lakini zipo changamoto kwa baadhi ya maeneo nchini. Mfano, katika Jimbo langu la Kilindi lenye ukubwa wa sm2 za mraba 6,125 vijiji 102 na kata 21 ni vijiji 24 tu ambavyo vimepata umeme, tena ni maeneo ya Bura. Je, Waziri na Wizara kwa ujumla, ni lini vijiji vilivyobaki vitapata umeme?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa yapo maeneo yenye huduma za kijamii hatuna umeme, mfano zahanati, shule za sekondari na shule za msingi. Ni imani yangu Serikali italitazama suala hili katika awamu ya tatu ili maeneo nyeti yaliyobaki yapate umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika Wilaya ya Kilindi kuna tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara, hali hii imetokana na umeme mdogo, miundombinu chakavu na ukosefu wa transformer. Umeme uliopo ulilenga kutoa huduma kwa wananchi wachache na wakazi 300,000. Nishauri hatua za haraka za dhati zichukuliwe ili wananchi wapate huduma hii kwa uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia juu ya sheria ya utoaji wa leseni kwa wachimbaji wa madini. Sheria hii imesababisha migogoro ya mara kwa mara kwa kuwa Sheria hii ya Madini na Sheria ya Ardhi zinafofautiana. Mwenye leseni anapotaka kuchimba madini ni lazima akubaliane na mwananchi aliye katika eneo husika kwa ajili ya fidia. Sasa, inakuwa vigumu mwananchi kuondoka eneo hilo pale anapojua dhahabu au aina nyingine ya madini yamegundulika eneo hilo, hususani pale inapotokea fidia inayotolewa ni ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna changamoto kwa Ofisi ya Madini ya Handeni inayohudumia Wilaya ya Kilindi kutoa leseni kwa watu waliopo nje ya Kilindi na kuwaacha wazawa wa wilaya husika. Hali hii imechangia migogoro ya mara kwa mara. Naishauri wizara isogeze huduma ya ofisi wilayani Kilindi, naomba jibu kwa Wizara husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia kitabu chote cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri sijaona sehemu ya hotuba yake inayoonesha dhamira ya Serikali katika kuwasaidia wachimbaji wadogo wadogo katika Jimbo la Kilindi. Naomba majibu ya kuridhisha kutoka kwa Mheshimiwa Waziri. Aidha, kama Serikali ikitoa ruzuku basi fedha hizo hazifiki kwa walengwa. Nashauri kila Mbunge anayetoka kwenye eneo lenye madini ahusishwe katika kusimamia zoezi hili ili walengwa wanufaike na nia nzuri ya Serikali katika kuwasaidia wananchi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuchangia hotuba hii juu ya kutokuwa na ofisi yenye hadhi ya wilaya, kwa maana ofisi ya TANESCO. Watumishi wa TANESCO kiukweli ni wachache, hawana vitendea kazi vya kutosha kuweza kuwafikia wananchi wenye jiografia ngumu. Naomba Waziri ashirikiane na Shirika la Umeme tupate ofisi bora na watumishi wa kutosha wa kuwahudumia wananchi wa wilaya hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa jitihada kubwa alizofanya za kufanikisha upatikanaji wa mkataba wa kujenga bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanga litakalosaidia kukuza uchumi wa Mkoa wa Tanga na Taifa kwa ujumla; ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa ajira wakati wa ujenzi na baada ya ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Jeshi letu kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba hii naomba nichangie kwa kumuomba Mheshimiwa Waziri maana anajua na kama amesahau nimkumbushe, ni ukweli usiofichika Wilaya ya Kilindi katika Mkoa wa Tanga ni eneo ambalo linanyemelewa na watu wabaya wenye kuhatarisha usalama wa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo wananchi takribani 50 au pungufu wamekamatwa kwa kujihusisha na vikundi vya ugaidi na kwa kuzingatia jiografia ya Wilaya ile yenye misitu, milima mingi, hivyo kuwa ni sehemu ya kujificha. Nimuombe Mheshimiwa Waziri kwa kushirikiana na viongozi wetu wa Jeshi la Ulinzi kama taratibu zitaruhusu basi tupatiwe Kituo cha Jeshi ambacho kitasaidia kulinda amani ya eneo hili pamoja na Taifa kwa ujumla, tusisubiri mpaka hali mbaya ikatokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeyasema haya nikifahamu kabisa katika Mkoa wa Tanga tuna Kambi ya JKT iliyopo Wilaya ya Handeni lakini pana umbali baina ya Wilaya hizi mbili. Mimi naamini kabisa kuna gharama ya kuanzisha vituo hivi lakini usalama wa eneo hili ndiyo wa muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watumishi wote wa Wizara hii kwa jitihada kubwa wanazochukua katika kusimamia ardhi ya nchi hii pamoja na dhamira ya dhati katika kutatua migogoro mbalimbali ya ardhi nchini kwetu. Nimepitia hotuba hii na kuona dhamira ya Wizara hii na ilivyojipanga kuona namna gani ambavyo Serikali yetu inasimamia ardhi yetu kwa kuithaminisha kwa taratibu na sheria zilizopo, hili ni jambo jema sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia juu ya migogoro ya ardhi. Suala hili limekuwa likichukua muda mwingi wa wananchi wa kufanya shughuli za kiuchumi badala yake wanakuwa wakitumia kutatua migogoro ya ardhi. Mfano mzuri ni mgororo wa ardhi wa mpaka baina ya Wilaya ya Kilindi na Kiteto, mgogoro huu umechukua muda mrefu sana. Naomba kauli ya Mheshimiwa Waziri hivi ni lini mgogoro huu utakwisha. Naamini mgogoro huu umeasisiwa na watumishi wa Halmashauri wasio waaminifu walioshirikiana na baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Kiteto. Ili wananchi waone Serikali yao inawajali muda umefika sasa kupata suluhu ya kudumu ya mgogoro huu. Nashauri Serikali iwachukulie hatua watumishi wote waliobadili ramani ya mipaka ya Wilaya hizi mbili kwani awali mgogoro huu haukuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha kuna migogoro ya wafugaji na wakulima, hii pia imekuwa ni migogoro ya muda mrefu. Wafugaji wamekuwa wakigombana na wakulima mara kwa mara kwa wafugaji kulisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima na wakulima kulima maeneo ya wafugaji. Nashauri maeneo haya yapimwe na wafugaji wawe na maeneo yao na wakulima wawe na maeneo yao ili kupunguza migogoro hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, uwepo utaratibu wa kuwa na maeneo ya kufuga na kunyweshea ili wafugaji wapate malisho ya uhakika kwani imeonekana hili ndilo tatizo kubwa kwa sababu wafugaji wamekuwa wakihamahama kutoka sehemu moja kwenda nyingine kutafuta malisho ya mifugo yao. Vilevile wafugaji wasihame na mifugo yao kutoka Wilaya moja kwenda nyingine bila kuwa na kibali maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala la watumishi hasa wale wanaopima maeneo ya ardhi. Nashauri watumishi hawa wasikae kwenye vituo vyao vya kazi kwa muda mrefu. Mfano katika Kata ya Newiro watumishi wa Halmashauri wameuza kwa wafanyabiashara maeneo mengi ya kata hii, leo hii hakuna hata eneo la wazi, maeneo yote yameuzwa. Wasiwasi wangu vizazi vijavyo vitakosa mashamba ya kulima. Mashamba haya yamepimwa na Wizara kutoa hati. Nitaleta hati hizo zenye maeneo makubwa ambayo hayakufuata utaratibu unaotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, naomba Wizara hii ifute hati ya shamba la Tanzania Leaf Tobacco Company Ltd., lenye ukubwa wa hekari 2,133 lililopo Kata ya Kwadibona. Shamba hili limetelekezwa kwa muda mrefu sana, takribani miaka 20 bila kuendelezwa. Nashauri hati hii ifutwe ili eneo hili litengwe kwa ajili ya wawekezaji. Barua ya kufuta hati hii imekwishafika Wizarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kujibu kilio cha muda mrefu sana cha Baraza la Ardhi. Kwa niaba ya wananchi wa Kilindi tunashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa jitihada kubwa anazofanya kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali wa Wizara yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia hotuba hii nikiamini kabisa nchi yoyote duniani ambayo ina viwanda imara vinavyozalisha, uchumi wa nchi yake utakuwa imara. Nchi yetu ina fursa pengine kuliko nchi zilizo jirani nasi je, tutapataje fedha za kigeni bila kuuza nje? Tuna maeneo mengi ambayo yana fursa ya mali lakini tatizo ni usimamizi ambao siyo mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maeneo ya nchi yetu miaka ya nyuma yalikuwa na viwanda, mfano Mkoa wa Tanga lakini viwanda vimekufa, japo nimeona jitihada za kuvirejesha hali hiyo kwa kuona ujenzi wa viwanda vya sementi katika mkoa wetu. Tanga tuna reli inayoanzia Tanga kupitia Moshi, Arusha baadaye Musoma, tukijenga viwanda vingi Tanga na uwepo wa reli ya Tanga tutarejea mafanikio makubwa kwenye fikra ya nchi ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, nia ya nchi yetu kuelekea kuwa nchi ya viwanda, bado kuna tatizo la wawekezaji wetu kukosa mazingira au ushirikiano kutoka baadhi ya taasisi zilizo chini ya Wizara, hili litazamwe sana. Mfano yupo mwekezaji ambaye anataka kujenga kiwanda cha mabati, Wilaya ya Mkuranga ameshindwa kuanza uzalishaji kutokana na Baraza la Mazingira (NEMC) kutompa kibali, hili lifuatiliwe kwa karibu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lingine juu ya ugawaji wa fursa hizi katika maeneo ya nchi yetu, baadhi ya mikoa ya nchi yetu ina viwanda vingi kuliko mikoa mingine na si kwa sababu tu maeneo haya yana fursa zaidi kuliko mikoa mingine bali kuna tatizo la kutotoa fursa sawa. Nashauri sana tena sana tutoe fursa sawa kwa kila eneo muhimu, fursa ipatikane eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, Wilaya ya Kilindi ni eneo lenye shughuli kubwa za kilimo, pamoja na shughuli za mifugo. Naomba sana nasi tupewe fursa katika maeneo hayo. Mfano tunaweza kupewa kiwanda cha uchakataji wa siagi kwa sababu tuna mifugo mingi, aidha tunaweza kupatiwa kiwanda cha ngozi kwa sababu tunayo mifugo ya kutosha. Naomba Mheshimiwa Waziri achukue ushauri huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu wake pamoja na uongozi mzima wa Wizara hii kwa jitihada na kazi kubwa wanayofanya katika kusimamia majukumu makubwa ya Wizara hii. Wizara hii inasimamia majukumu ya rasilimali muhimu ya nchi yetu kwa maana mbuga zetu za wanyama, misitu yetu ya asili pamoja na vivutio vya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii inachangia kwa kiasi kikubwa Pato letu la Taifa kutokana na ujio wa utalii, mazao mbalimbali ya asili mfano magogo ya mbao, lakini bado jitihada za dhati zinahitajika ili kusimamia maeneo haya pamoja na kuongeza usimamizi wa uvunaji wa misitu yetu, Serikali inapoteza fedha nyingi kutokana na watu wengi wasio waaminifu wanaoshirikiana na Watanzania wasio wazalendo kuhujumu misitu yetu. Lazima Wizara ihakikishe udhibiti mkubwa unafanyika. Mfano katika Jimbo langu la Kilindi, Kata ya Msanja, Kitongoji cha Twile kuna uharamia mkubwa wa ukataji wa miti na magogo hivi hawa Wakala wa Misitu (TFS) wanafanya kazi gani? Mimi nadhani kama hawashirikiani na wahalifu hawa basi hawajui makujumu yao, mara nyingi wanapokamata magogo haya yanapelekwa Handeni badala ya kusafirishwa Kilindi, huu ni utaratibu gani? Nashauri Wakala hawa pia ofisi zao zihamishwe au zianzishwe ama kufunguliwa Wilayani Kilindi, eneo hili la uharibifu wa misitu halina usimamizi wa dhati. Nashauri Wizara husika iangalie namna ya kuwa na njia sahihi ya kuwasimamia watumishi wasio waaminifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia kuchangia namna ambavyo Wizara inaweze kupanua maeneo ya utalii kwa kuongeza maeneo ya utalii. Mfano, katika Jimbo langu la Kilindi yapo maeneo mengi ya utalii ambayo tanaweza kuchangia pato la Wizara hii, mfano pori tengefu la Handeni milima ya asili ya Kimbe, milima ya Kilindi asilia, milima ya Lulago yenye miti na uoto wa asilia haya yote ni maeneo muhimu sana ambayo wataalam wake tuijenge nchi. Nashauri ijenge utaratibu wa kufuatilia haya tunapowaambia kwani yana lengo la kuchangia pato la nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kuchangia ni upungufu wa wafanyakazi katika Wizara hii ambao wangekuwa na jukumu la kusimamia na kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa misitu na rasilimali ya nchi yetu, mfano katika Jimbo na Wilaya yangu ya Kilindi hatuna Afisa wa Wilaya anasimamia misitu, aliyepo ni Afisa katika ngazi ya Kata, Wizara ituletee mtumishi haraka kwani maeneo mengi katika Wilaya yanaharibiwa kwa kukosa usimamizi wa dhati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni juu ya maeneo ya hifadhi za misitu yaliyopo karibu kabisa na mijini, hifadhi hizi pamoja na faida tunayopata ya kuhifadhi mazingira na kupata mvua lakini maeneo haya yamekuwa ni maficho ya wahalifu hasa majambazi. Mfano msitu wa pale Kipala mpakani Wilaya ya Mkuranga hifadhi hii majambazi yametumia kama mafichio na hata askari zaidi ya sita wameuwawa pale kwenye check point. Nashauri Wizara sasa isafishe kwa kukata miti kwa mita 50 ili kuleta ulinzi na usalama kwa wakazi wa eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kuwapongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kujitahidi kwa dhati kabisa katika kuhakikisha kuwa suala la maji linatimia kwa nguvu zote, ukizingatia kwamba maji ni uhai.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na changamoto zilizopo napenda kuishukuru Wizara kwa kututengea fedha kwenye mradi wa HTM ambao kwa muda mrefu ulitakiwa uwe umeshakamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri alitembelea Jimboni kwetu na kuahidi kwamba tukiwa tunasubiri mradi mkubwa kutoka kwenye ufadhili wa India, basi Serikali itatoa shilingi bilioni mbili ili kukarabati mradi wa HTM uliopo sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru Engineers wamekuja na wameshafanya kazi zote za michoro ya ukarabati wa HTM na wameshakabidhi Wizarani. Basi naomba utekelezaji ufanyike kama ahadi ya Mheshimiwa Naibu Waziri alivyowaahidi wakazi wa Handeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri kwenye majumuisho yake atufafanulie ni lini mradi huu mdogo unaanza, wakati tukiwa tunasubiri ule mkubwa? Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. OMARI A. KIGODA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kuwapongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kujitahidi kwa dhati kabisa katika kuhakikisha kuwa suala la maji linatimia kwa nguvu zote, ukizingatia kwamba maji ni uhai.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na changamoto zilizopo napenda kuishukuru Wizara kwa kututengea fedha kwenye mradi wa HTM ambao kwa muda mrefu ulitakiwa uwe umeshakamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri alitembelea Jimboni kwetu na kuahidi kwamba tukiwa tunasubiri mradi mkubwa kutoka kwenye ufadhili wa India, basi Serikali itatoa shilingi bilioni mbili ili kukarabati mradi wa HTM uliopo sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru Engineers wamekuja na wameshafanya kazi zote za michoro ya ukarabati wa HTM na wameshakabidhi Wizarani. Basi naomba utekelezaji ufanyike kama ahadi ya Mheshimiwa Naibu Waziri alivyowaahidi wakazi wa Handeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri kwenye majumuisho yake atufafanulie ni lini mradi huu mdogo unaanza, wakati tukiwa tunasubiri ule mkubwa? Ahsante.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kabla sijachangia mpango huu wa Serikali naunga mkono hoja. Nimpongeze Waziri wa Fedha na Naibu wake pamoja na watumishi wote wa Wizara ya fedha walioshiriki katika kuandaa mpango huu ambao unalenga katika kuinua uchumi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia mpango huu mambo mengi yaliyomo ndani mpango huu yana nia ya kuinua uchumi wa nchi yote kwa leo. Nitajikita kwenye maeneo machache ambayo yanahitaji usimamizi na mkakati wa hali ya juu. Maeneo hayo ni Sekta ya Kilimo cha Umwagiliaji, Sekta ya Utalii pamoja na kutazama upya aina ya kodi mbalimbali zinazotozwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) hususan kwa wafanyabiashara wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Kilimo ni muhimu sana ikisimamiwa kwa karibu na kwa njia za kisasa ni eneo ambalo kwa kiasi kikubwa itachangia pato la Taifa letu. Eneo ninalosisitiza hapa ni kilimo cha umwagiliaji, nchi yetu imebahatika kuwa na ardhi nzuri yenye rutuba, pia na mabonde mengi. Je, Serikali haioni umefika muda badala ya kutegemea kilimo tulichozoea cha kutegemea mvua, tutumie fursa za mabonde yetu kuzalisha mazao mbalimbali ya chakula na biashara. Aidha, kupitia mpango huu tunaweza kuchimba mabwawa makubwa pamoja na visima virefu ili kilimo chetu kisitegemee mvua tu. Ni muhimu sana kwani ni Mataifa mengi yameweza kupiga hatua, aidha tatizo la vifaa la kila wakati litatuliwa
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ningependa Waziri wa Fedha alitazame katika kuinua pato la nchi yetu ni Sekta ya Utalii. Nchi yetu ina maeneo mengi ya utalii kwa maana mbuga mbalimbali za utalii, lakini bado sekta hii inachangia kiasi kidogo si kwa kiwango ambacho kama Wizara husika ingekuwa na mkakati na mpango thabiti, Taifa lingefaidika sana. Bado naamini hatujaweza kutangaza sekta hii ipasavyo, aidha, gharama au tozo tulizoweka katika utalii zimepunguza ujio wa watalii ni vema tukubaliane wenzetu wa nchi jirani nao wana fursa kama yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mbuga zetu zina wanyama wengi, hivyo tuweke mkazo katika eneo hili, niipongeze Serikali kwa kununua ndege mpya nikiamini zitasaidia ujio wa watalii ambao awali walikuwa wakifikia nchi jirani. Niiombe Serikali yetu pia iboreshe huduma katika mahoteli ambapo watalii wanafikia, pia kodi kwa watalii ipunguzwe kwani imepunguza idadi ya watalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ningependa kutoa mchango juu ya kodi mbalimbali zinatozwa na Mamlaka ya Mapato (TRA), nchi yoyote duniani haiwezi kusonga mbele bila ya kodi; mipango yote ya maendeleo inategemea kodi hata nchi yetu bila ya kodi haiwezi kusonga mbele. Naunga mkono suala la kodi ila nina mawazo tofauti juu ya utitiri wa kodi na juu ya ukadiriaji wa kodi, eneo hili lina matatizo kwani ukadiriaji huu hauna uhalisia, aidha watumishi wote wa TRA wanakosa njia iliyo sahihi ya ukadiriaji kwani wananchi wengi wamekuwa wakilalamika sana kukadiriwa kiwango kikubwa ambacho hakilingani na uhalisia wa biashara zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali ione njia nzuri ya kupitia TRA ili ipunguze malalamiko haya. Wananchi wengi wana nia ya kulipa kodi, tusiwakatishe tamaa wananchi wote nikiamini kabisa bila kodi hakuna uhai. Ni imani yangu Mheshimiwa Waziri na Serikali watayapokea maoni haya.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa kumpongeza Waziri wa Fedha, Naibu Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu, Manaibu Makatibu Wakuu, pamoja na Uongozi mzima wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa hotuba yao nzuri ya mwaka wa fedha 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kwa leo nichangie eneo la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Hili ni eneo muhimu sana na ni sawa na mishipa ya binadamu inavyopitisha damu. Mapato yanayotokana na kodi mbalimbali ndiyo ambayo yanaweza kupeleka maendeleo ya dhati ya nchi yetu. Naishauri Wizara kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania bado haijaweza kuinua wigo wa kukusanya mapato kwa sababu bado kuna maeneo mengi ambayo wenzetu wa TRA hawajaweka utaratibu wa kukusanya mapato, nako ni sekta isiyo rasmi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko kuna mapato mengi sana, lakini TRA hawakusanyi kodi, mfano ni watoa huduma za ushauri (consultants), wafanyabiashara ndogo ndogo; jamii yote hii inatumia miundombinu kama barabara, hospitali na kadhalika ambazo zinajengwa kutokana na sekta rasmi. Nadhani umefika wakati sasa Wizara kupitia TRA waandae mazingira rafiki ya sekta isiyo rasmi iwe sehemu ya kuongeza chanzo cha mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ni muhimu katika kukusanya mapato na ambalo halijawekewa mkazo mkubwa ni kutumia EFDs machine. Mfano wa kutumia mashine za kielektroniki katika kukusanya mapato ya Serikali ni vyanzo muhimu sana. Bado Wizara kupitia TRA haijasimamia utaratibu wa kutumia mashine hizi kwa mantiki kwamba siyo taasisi zote pamoja na watu binafsi wenye kuendesha biashara kubwa na ndogo, wanaotumia mashine hizi. Hili linaisababishia Serikali upotevu wa mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri ahakikishe mashine hizi zinapatikana kwa wingi na kwa bei za chini ili kila mtu aweze kununua na kutumia. Mfano ni mahoteli mengi hata hapa Dodoma hawatumii stakabadhi za EFDs na sijaona kama wenzetu Mamlaka ya Mapato wakichukua jitihada za dhati za ukaguzi. Tulichukulie suala hili kwa umakini mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia nichangie juu ya bajeti za Wizara na taasisi zetu kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Utaona kwamba kiasi kilichopelekwa kwa ajili ya matumizi mengineyo na fedha za maendeleo, takriban utaona ni asilimia 50 au pungufu ndizo zilizopelekwa. Hii inatoa tafsiri kwamba bajeti yetu haitoi uhalisia wa makisio yetu. Nashauri sasa tuweke bajeti ambayo itaakisi uhalisia japokuwa asilimia 80 hii itasaidia kufikia malengo ya Serikali yetu, kuliko kuweko makisio makubwa ambayo ni nadra kuyafikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayofanya katika kusimamia shughuli za kila siku za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba hii mambo mengi yaliyomo ndani ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu mengi ni mazuri, lakini ningependa kuchangia baadhi ya maeneo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa walimu wa shule za msingi na sekondari, baadhi ya maeneo mengi hasa katika Halmashauri zetu hayana walimu wa kutosha; uwiano wa mwalimu mmoja kufundisha idadi ya watoto inatofautiana. Mfano Mkoa wa Tabora mwalimu mmoja
anafundisha watoto 40 uwiano huo unaonyesha dhahiri kuna ugawaji mbaya wa watumishi hususani katika kada ya walimu naomba suala hili litazamwe kwa umakini na kurekebishwa kwa sababu inarudisha juhudi za Serikali za kutoa huduma sawa kwa wananchi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile suala la usimamizi wa miradi ya maji katika miji yote na Halmashauri zetu kunakuwa na mapungufu mengi. Serikali haina utaratibu ulio imara wa kukagua mradi mingi ya maji ambayo imegharimu Serikali fedha nyingi hali inayopelekea miradi
mingi kutoa huduma chini ya kiwango au kuharibika kwa muda mfupi naishauri kuanzia sasa Wizara ya Maji na TAMISEMI waweke utaratibu wa shughuli zao kila siku ziwe zinafuatilia miradi hii yote ilete matokeo yanayotarajiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali imuongezee CAG uwezo wa kifedha ili afanye kazi ya ukaguzi kwa ufanisi (performance auditing) kwa sababu ukaguzi huu umeonyesha kwa kiasi kikubwa namna gani Serikali inaweza kuufanyia kazi ushauri unaotolewa na CAG. Ukaguzi huu ni muhimu sana kwa sababu unalenga katika kuonyesha je, miradi imetekelezwa kwa ufanisi au la. Je, wakandarasi wa miradi mbalimbali wanatimiza wajibu wao? Na Wizara au Halmashauri nazo zinatimiza utaratibu wao? Kupitia ukaguzi kwa ufanisi Ofisi ya CAG imefanya kazi kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naishauri Wizara ya Elimu iimarishe ukaguzi katika shule zote, kitengo hiki hakifanyi kazi sawasawa ndio maana hata baadhi ya shule zote zinafanya vibaya katika matokeo ya mitihani yao, zamani kiwango cha ukaguzi wa shule zetu zilikuwa zikitoa
taarifa za shule leo hii wakaguzi hawana vyombo vya usafiri ambavyo vinaweza kuwasaidia kutembelea shule zote. Wakaguzi hawa wapewe magari, ofisi pamoja na kuwezeshwa posho za mazingira magumu kuwapa moyo na kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuchangia eneo la migogoro ya ardhi baina ya wafugaji na wakulima.
Serikali wakati inafikiria kuleta sheria na mabadiliko juu ya ufugaji wa kisasa idadi ya wafugaji imeongezeka, wananchi wanaongezeka lakini ardhi haiongezeki.
Nashauri sasa ukifuga mifugo michache kwa njia bora kabisa ya kisasa hii itapunguza migogoro. Lakini vilevile ione kuwa ufugaji bora wa mifugo utasaidia Serikali kuongeza pato lake la Taifa ikijikita katika kutoa elimu ya ufugaji bora. Vilevile elimu itolewe kwa wananchi wafugaji
lakini Serikali iandae miundombinu bora ya zero grazing hii italeta mapinduzi makubwa lakini itapunguza migogoro ya mara kwa mara ya wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utunzaji wa vyanzo vya maji ni eneo lenye matatizo makubwa wananchi wamekuwa wakilima katika vyanzo vya maji lakini pia wananchi wengi kulima katika maeneo ya milima, ulimaji huu unaleta athari kubwa katika kuharibu mazingira. Lakini mbaya zaidi ukosefu wa mvua maeneo mengi umesababishwa na shughuli zisizo rasmi katika maeneo ya mabonde na milima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu kulima mita 60 kutoka vyanzo vya maji usimamiwe kwa dhati ikiwezekana iwe ni sheria kamili kulinda maeneo yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Uongozi mzima wa Wizara. Ni jambo lisilo na shaka hata kidogo Wizara hii ni miongoni mwa Wizara chache sana zinazochapa kazi hasa chini ya uongozi wa Mheshimiwa William Lukuvi, pamoja na Naibu Waziri, hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie hotuba hii katika maeneo yafuatayo:-

Migogoro ya Ardhi, kila kona ya nchi utasikia migogoro hii. Nipongeze tena jitihada zinazofanywa na Wizara katika kutatua migogoro mfano ni upimaji wa maeneo ya wafugaji na wakulima katika Mkoa wa Morogoro. Bila shaka mfano huu utakwenda maeneo yote nchini mfano katika Jimbo langu la Kilindi lenye nusu wakulima na nusu wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mfumo huu pia uelekezwe huku kwa sababu migogoro inaongezeka kila siku. Suluhu ni kupima tu. Wizara imeelekeza Halmashauri zitenge fedha kwa ajili ya kupima, lakini ni ukweli usiofichika bado Halmashauri zetu hazina uwezo wa kupima kwani baadhi ya Wilaya zina maeneo makubwa sana mfano wilaya yangu ina vijiji 102, vitongoji 650, hivi itachukua miaka mingapi kupima?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Migogoro ya Ardhi, (mpaka kati ya Kilindi na Kiteto). Mimi binafsi nichukue fursa hii nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu; Waziri wa Ardhi; na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ambao walifika mpakani na kujionea mgogoro uliodumu zaidi ya miaka 30 ambapo Mheshimiwa Waziri Mkuu aliagiza Wizara kupitia wapimaji kupitia GN 65 ya mwaka 1961 inayotenganisha Mkoa wa Tanga na Arusha kwa sasa Manyara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa jitihada zake wapimaji walifika na kufanya kazi kubwa ya kubainisha mpaka huu, gharama za fedha za umma zimetumika kwa watumishi hawa lakini cha kusikitisha ni kuona zoezi hili limesimama alama (Beacons) hazijawekwa, wananchi wanataka wapate majibu ya Wizara hii, tatizo liko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wamekwishatambua wapi mpaka wao upo kwa mujibu wa taarifa ya wapimaji ambapo, mimi, Mkuu wa Wilaya na Mkoa wa Tanga tunazo, nadhani zoezi hili ni vema lingekamilishwa ili wananchi wa wilaya hizi mbili, (Kiteto na Kilindi) ambao wanaishi kwa hali ya wasiwasi na kutofanya shughuli za kilimo na mifugo wanachoomba kupata suluhu ya kudumu ambayo ni kuweka alama za kudumu (Beacons).

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kauli ya Wizara juu ya jambo hili ambalo linabeba mustakabali wa maisha ya wananchi wa Kilindi na Kiteto, kutowaona wapimaji kumalizia zoezi hili kunatoa picha isiyoleta matumaini. Wananchi wana imani kubwa na Mheshimiwa Waziri kwani utendaji wake bila shaka umemletea sifa kila kona ya nchi hii, ni imani yangu hatapata kigugumizi katika hili ili kuleta haki kwa wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa hotuba nzuri yenye kuonesha mwelekeo wa kujali maslahi ya nchi. Katika hotuba hii nitachangia katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Mazingira, hali ya uharibifu wa mazingira kwa sasa nchini mwetu imekuwa mbaya sana. Jamii kwa ujumla suala la mazingira imelipa mgongo, maeneo ya vyanzo vya maji shughuli za kilimo ndiyo mahali pake. Ushauri wangu shughuli za mifugo na kilimo zisiendeshwe katika maeneo hayo ili kulinda vyanzo vya maji. Pia hata shughuli za makazi kwa maana ya ujenzi wa nyumba pia upigwe marufuku, Sera na Sheria zilizopo ni nzuri, tatizo ni usimamizi wa wenye dhamana ya kusimamia sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia maeneo ambayo yameathirika kwa kiasi kikubwa na uhifadhi wa mazingira kukosa rasilimali fedha kwa ajili ya kupanda miti. Napongeza uanzishwaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Mazingira, ni imani yangu maeneo ambayo yatakuwa yameathirika na mazingira yatapatiwa fedha kutoka Mfuko huo. Tusipokuwa makini vyanzo vyote vya maji vitakauka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuenea kwa hali ya jangwa, maeneo mengi nchini yameshuhudia ukataji wa miti kwa matumizi ya mkaa, mbao pamoja na kuanzisha mashamba kwa shughuli za kilimo. Kasi ya ukataji wa miti imesababisha maeneo mengi kukosa mvua nchini, hali hii nchini isipodhibitiwa nchi yetu itakuwa jangwa. Mfano mzuri katika Jimbo langu la Kilindi katika Kata za Negero, Msanja, Kilindi Asilia na Kimbe, zimeshuhudia kasi ya ukataji wa miti wa hovyo huku wahusika ambao ni Watumishi katika ngazi zote wakiacha hali hii kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Taarifa ya Wanazuoni wawili wa Chuo Kikuu cha SUA Morogoro, Profesa Dhahabu na Maliado, Wilaya ya Kilindi ni eneo ambalo limeathirika sana na ukataji hovyo wa miti. Taarifa yao ni ya mwaka 2003 hadi 2012 ilionyesha eneo la Kilindi lisipochukuliwa tahadhari Wilaya yake itakuwa jangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na sheria zilizopo na Watendaji katika maeneo ya Vijiji hadi Wilaya bado tatizo hili linaendelea. Nimwombe Waziri mwenye dhamana ahakikishe Timu Maalum inakwenda hasa kwenye maeneo ya Kata za Negero, Msanja, Kimbe na Kilindi Asilia na vijiji vyote kwenye maeneo ya kujionea uharibifu mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuchukua jitihada kubwa na kutenga fedha za kutosha kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi tutegemee athari kubwa zaidi. Bila msisitizo wa kusimamia sheria husika na kuwa na wataalam wa kutosha tatizo halitaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni Baraza la Mazingira (NEMC), Baraza hili sehemu kubwa ya shughuli zake zinafanyika mijini. Niliombe sasa Baraza litanue shughuli zake vijijini kwa kuhakikisha wanakuwa na watumishi wa kutosha. Naamini kwa dhati, shughuli nyingi za ukataji miti na shughuli za kibinadamu pamoja na ufugaji zinafanyika vijijini. Baraza lipewe uwezo mkubwa wa kisheria katika kusimamia na kuratibu misitu na kuhakikisha maeneo yetu yanalindwa. Aidha, Baraza liongezwe bajeti yao waweze kutekeleza majukumu yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Hoja ya Dharura (Changamoto ya Kupanda kwa bei za Mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Ni ukweli usiopingika kwamba Watanzania na dunia nzima wanajua kwamba kuna changamoto ya kupanda kwa haraka sana kwa mafuta ya petrol, diesel pamoja na mafuta ya taa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukipandisha bei ya mafuta ya taa, petrol na diesel umepandisha kila kitu.

MBUNGE FULANI: Amen!

MHE. OMARI M. KIGUA: Jambo hili Tanzania nzima sasa hivi kelele ni suala la mafuta. Sasa sisi kama Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunao wajibu mkubwa sana wa kuisimamia na kuishauri Serikali katika jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli isingekuwa busara kama wananchi ambao wametupa dhamana kubwa ya kuweza kuwasemea hapa Bungeni tusiposema jambo hili na Serikali isiposimama hapa kusema jambo lolote lile maana yake tunakuwa hatuwatendei haki wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wenzetu wa EWURA juzi wametoa bei elekezi ambazo zimeanza jana tarehe 4 Mei. Nilikuwa natazama hapa petrol Kagera ni shilingi 3,385/=. Jambo hili ni lazima sasa tusimame kama Wabunge, tuzungumze na tuishauri Serikali. Nina uhakika Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi chini ya uongozi wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ina uwezo wa kufanya jambo kama ambavyo Serikali nyingine katika dunia wanafanya, kwa sababu wananchi hawawezi kuzungumza, wananchi hawawezi kulalamika, halafu Serikali haisemi jambo lolote.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba ridhaa yako kutoa hoja kwamba Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tuzungumzie hoja hii ili tusikilize Serikali inasema nini juu ya ongezeko la mafuta?

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye amenijalia kusimama katika Bunge hili Tukufu ili niweze kutoa mchango wangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kuchangia ningependa nitoe shukrani zangu za dhati hasa kwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake ya Awamu ya Tano kwa jitihada kubwa sana ambazo wamechukua hususan katika ujenzi wa flyover, ujenzi wa barabara na standard gauge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kabisa kwamba nchi hii sasa inakwenda kwenye maendeleo ambayo Watanzania wote tulikuwa tunayatarajia ndiyo maendeleo tunayoyataka. Nina imani kwamba siku atakapomaliza muda wake Watanzania watamkumbuka, kama siyo sisi watoto wetu basi watakuwa wanakumbuka historia ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo ya utangulizi ningeomba sasa nianze kuzungumzia suala la barabara, barabara nitakayozungumzia ipo katika kitabu hiki cha hotuba yako Mheshimiwa Waziri, ukurasa 42 unazungumzia barabara hii ambayo inaanzia Handeni, inapita Kibirashi, Kijungu, inaenda Kondoa, Nchemba hadi Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii inaunganisha Mikoa Minne, inaunganisha Mkoa wa Tanga, Mkoa wa Manyara, Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Singida. Mwaka jana nimezungumzia sana barabara hii. Barabara hii ina urefu wa kilometa 460 na ipo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Mheshimiwa Waziri, nimeshakuja ofisini kwako kuizungumzia barabara hii, nimeona mwaka huu katika kitabu chako katika hotuba hii umesema mnatafuta fedha, lakini katika kupitiapitia nikaona mmetenga shilingi milioni 500. Sasa sijajua shilingi milioni 500 ni kwa ajili ya kufanyia kitu gani. Ningependa wakati una-wind up niweze kupata maelezo ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema kwa nini tunahitaji barabara ya kiwango cha lami. Wilaya ya Kilindi ndiyo Wilaya peke yake ambayo haina barabara ya kiwango cha lami, lakini Wilaya ya Kilindi ina shughuli nyingi za kiuchumi, kuna ufugaji, kilimo, madini na barabara hii ni shortcut sana Mheshimiwa Waziri kwa mtu anayetokea Handeni akipita Kilindi anakuja kutokea Gairo hapa kwa Mheshimiwa Shabiby. Sijaelewa ni kwa nini mliamua kutengeneza barabara ya kupitia Turiani na kuiacha hii inayotokea hapa Gairo. Anyway siwezi kulaumu kwa sababu zote hizo ni barabara za Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachokiomba Mheshimiwa Waziri, tafadhali sana iangalieni barabara hii, wananchi wa Kilindi wanahitaji mawasiliano kwa sababu kujenga katika kiwango cha lami maana yake mtakuwa mmeinua maisha ya wananchi wa Kilindi, Mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla. Utaruhusu upitaji kwa rahisi kwa watu wanaotoka Manyara, kwa watu wanaotoka Tanga kufika Dodoma ambako ni makao makuu ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakuomba Mheshimiwa Waziri ufanye ziara uje uangalie ni nini kinachoendelea kule. Sasa hivi tuna kiwanda cha tiles kinachojengwa Mkuranga. Material yote yanatoka Wilaya ya Kilindi, yanapita magari mazito sana takribani tani 40 kwa siku zaidi ya malori 100. Barabara ile iko katika kiwango cha vumbi, barabara inaharibika na kipindi hiki ni kipindi cha mvua. Nikuombe Mheshimiwa Waziri najua wewe ni msikuvu, muadilifu, utaiona barabara hii, tutafutie wafadhili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hiyo naomba nizungumzie kilomita tano Makao Makuu ya Wilaya, narudia kusema tena, wananchi wa Kilindi wana kilio, mwaka jana nilikuomba tunaomba tujengewe kilometa tano ukatutengea hela ndogo sana shilingi milioni 150 ambazo hazitoshi hata kuwa na nusu kilometa, mwaka huu nimepitia kitabu hiki nimeona umetenga shilingi milioni 120. Ninakuomba Mheshimiwa Waziri, ukizungumza na wataalam wanasema kiasi hicho hakitoshi. Najua mahitaji ni mengi Watanzania wanataka barabara lakini nasi wananchi wa Kilindi tunahitaji, ungeanza hata kilometa mbili tu, kwa sababu inabadilisha hata sura ya mji. Ninaomba Mheshimiwa Waziri uje makao makuu ya Wilaya uangalie hali halisi au mtume Naibu Waziri baada ya bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ningependa kuzunzungumzia barabara ambayo inaanzia makao makuu ya Wilaya inapita Kikunde inaenda mpaka Gairo. Barabara hii Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne aliahidi kujenga katika kiwango cha lami, wakati huo Mheshimiwa Rais sasa hivi John Pombe Magufuli alikuwa ni Waziri wa Ujenzi aliahidi kujenga. Ninakuomba hebu iangalie katika taratibu zako baadaye ni namna gani mnaweza kujenga barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kuzungumzia ni suala la minara ya simu. Leo asubuhi nilipata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, kuna matatizo ya mawasiliano Wilaya ya Kilindi, mawasiliano ni tatizo sana. Tunayo kata moja inayopakana na Simanjiro inaitwa kata ya Saunye kule kuna mbuga ya wanyama, kuna wafugaji wengi sana hawapati mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naamini Mheshimiwa Waziri mawasiliano ni biashara, hakuna sababu Wabunge tusimame hapa kulalamika. Ni juu ya makampuni kutafuta wateja ili waweze kupata mapato, mapato yasaidie Serikali. Nakuomba Mheshimiwa Waziri uchukue Kata zifuatazo kwa ajili ya kuweka minara ambazo ni kata ya Tunguli, Saunyi, Misufuni na Kilindi Asilia.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa Mheshimiwa Waziri kulichukua hapa ni suala la wakandarasi. Wizara inachelewa sana kuwalipa wakandarasi. Unapochelewa kumlipa mkandarasi maana yake una-entertain gharama kubwa zaidi kwa mfano mradi ulikuwa na shilingi bilioni kumi, ukichelewesha mradi ule kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja maana yake unaruhusu gharama ya mradi iwe kubwa zaidi. Mimi naomba sasa muwe mnafanya tathmini ya muda, mnayo miradi mingi sana, lakini msianzishe miradi mingine mipya bila kuangalia ile ya zamani, nadhani hapo mtakuwa mmepunguza gharama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia sisi Kamati yetu tulienda katika barabara inayopita Turiani kupita kwa Mheshimiwa Murrad, mkandarasi pale muda umepita sana na gharama anazodai ni mara mbili ya gharama ya mradi ule. Kwa hiyo, nikashauri Mheshimiwa Waziri muwe mnafanya tathmini sana kuangalia gharama za hii miradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni suala la reli ya Tanga. Waheshimiwa wengi wamezungumzia reli ya Tanga, wapo wazungumzaji waliosema kwamba ni ya muda mrefu sana na sisi watu wa Mkoa wa Tanga tunahitaji standard gauge. Reli ile inayotoka Tanga inaenda Moshi, inapita Kilimanjaro hadi kwenda Musoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa Tanga tuna Kiwanda cha Saruji, saruji ile inayotoka Tanga ukiipeleka kwa njia ya standard gauge maana yake utaruhusu iuzwe kwa bei ya kiwango cha chini sana. Mimi nina uhakika kwamba mkishamaliza utaratibu wa kufika mpaka Mwanza na Kigoma basi mtarudi na Mkoa wa Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo machache naomba nikushukuru, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa ujumla kwa jitahada kubwa wanazochukua kwa kuleta maendeleo ya dhati hususan katika kujikita katika suala la usafiri wa anga kwa ununuzi wa ndege mpya pamoja na ujenzi wa reli iendayo kwa umeme (standard gauge). Aidha, dhamira ya dhati ya kujenga na kukarabati viwanja vya ndege, ujenzi wa bandari za ndani, Mtwara na mwisho ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie hotuba hii katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Handeni – Kibrashi – Kijungu – Njiro – Mrijo Chini – Dalai – Bicha – Chambalo – Chemba – Kwamtoro – Singida (kilomita 460). Barabara hii ni muhimu sana kwa sababu ipo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kwa sababu inapita katika mikoa minne. Nishukuru kwa mwaka huu wa fedha Wizara imetenga kiasi cha sh. 500,000,000/=. Je, kiasi hiki ni kwa ajili ya fidia au jibu gani? Maana ni kiasi kidogo sana kwa ujenzi wa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii kipindi cha mvua inapitika kwa shida sana, barabara hii ina shughuli nyingi za kiuchumi. Wananchi katika maeneo yote yaliyotajwa ni wazalishaji wakubwa wa mazao mbalimbali hususan mahindi. Wananchi hawa hawapati faida ya mazao yao kwa sababu wanalazimika kuuza chini ya bei ambapo kama barabara ingekuwa ya kiwango cha lami, wigo na fursa ya kuuza kwenye masoko watakayokuza ingekuwa kubwa sana. Niiombe Wizara yangu watafute wadhamini wa kutujengea barabara hii au Serikali itoe fedha za kutosha kutujengea barabara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine katika ujenzi wa barabara ni ujenzi wa barabara kwa kilometa tatu kwenye Makao Makuu ya Wilaya. Mwaka wa jana tulitengewa fedha kiasi cha sh. 150,000,000. Kiwango hiki ni kidogo sana.

Nimeshangazwa sana kwa mwaka huu wa fedha hakuna fedha zilizotengwa, hivi Kilindi kuna tatizo gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Tanga, Wilaya ya Kilindi ndiyo wilaya pekee ambayo haina kilometa tatu au tano za barabra katika Makao Makuu ya Wilaya ambayo haina lami. Naomba majibu kutoka kwa Waziri mwenye dhamana, ni kwa nini hatujapewa fedha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Songe – Kwekivu – Iyogwe – Gairo. Barabara hii kwanza ni shortcut kwenda Dodoma, ni mto unaotoka Arusha, Tanga kuja Dodoma. Barabara hii ina shughuli za kiuchumi na pia ina wigo wa magari. Naomba Mheshimiwa Waziri barabara hii nayo ingeingia katika utaratibu wa kujengwa katika kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upandishwaji wa madaraja wa barabara kutoka ngazi ya kijiji kwenda wilaya na wilaya kwenda mkoa. Tunazo barabara nyingi ambazo kwa muda mrefu hazijapandishwa hadhi. Mfano katika Jimbo langu la Kilindi tunaomba barabara zipandishwe hadhi kwa sababu zinakidhi sifa na tayari Meneja wa TANROADs alikwisha fikisha maombi Wizarani. Barabara hizi za vijijini ndizo zilizo na shughuli nyingi za kiuchumi, zikijengwa vema na kuhudumiwa ni dhahiri uchumi wa wananchi wetu utakua. Ni vyema Serikali ilipe uzito mkubwa jibu hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hoja ya Dharura (Changamoto ya Kupanda kwa bei za Mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, binafsi nikupongeze sana wewe, nikupongeze kwa hekima kubwa uliyoonesha ya kuruhusu jambo hili ambalo linawagusa Watanzania liweze kuzungumzwa na Waheshimiwa Wabunge huku tukiamini kabisa Waheshimiwa Wabunge ndiyo wawakilishi wa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la pili niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote takribani 17 ambao wamesimama, wamechangia vizuri sana haitakuwa busara ya kurejea tena yale ambayo yamezungumzwa.

Sasa ukiangalia hoja za Waheshimiwa Wabunge hapa maeneo mawili ndiyo yaliyoguswa, wamegusia role ya Serikali kuweka ruzuku, lakini la pili wamezungumzia suala la tozo kwenye bei ya mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hatukupaswa kufika hapa tulipofika kwa sababu tunazo Kamati; unayo Kamati yako ya Bajeti, una Kamati ya Nishati ambayo wangeweza kukaa na Serikali haya mawazo ambayo wamezungumza Waheshimiwa Wabunge wangeweza kuzungumza katika Kamati hizo. Lakini nadhani hatujachelewa, naomba nirejee maelezo ya Mheshimiwa Simbachawene aliyosema kwamba jambo la dharura linatatuliwa kwa dharura. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naiomba sana Serikali jambo hili linawagusa Watanzania takribani milioni 60 maisha haya ya Watanzania yanazidi kwenda juu kwa sababu ya gharama ya mafuta na hatujui vita ya Ukraine na Urusi itaisha lini.

Mheshimiwa Spika, wamezungumza watu hapa kwamba ipo sheria ya kuwalinda consumers, lakini nataka niseme hatuna sheria moja ambayo inamlinda consumer. Sasa Mheshimiwa Waziri Makamba amesema hapa kwamba ataleta regulation, lakini mimi nadhani way forward ya jambo hili tuwe na policy ambayo itaenda kutengeneza sheria ya kuwa na mfuko ambao ni imara kabisa, inapotokea dharura kama hii Serikali iweze kuchukua fedha pale na kuweka ruzuku katika maeneo kama haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo mimi nimefarijika sana nikiamini kabisa suala hili limezungumzwa kwa mapana na niiombe Serikali, naamini kabisa chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ninyi Mawaziri mliopo hapa mnaenda kuleta majibu ya haraka ili watanzania waone kwamba Serikali yao inawajali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii jioni ya leo ili na mimi niweze kusema machache juu ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri pale. Pengine nianze tu kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi kubwa wanayoifanya katika Wizara yetu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa pongezi hizo, sitakuwa na maneno mengi sana, nitajikita kwenye maeneo matatu. Kwanza nitaanza na Shirika letu la Utangazaji (TBC). Inasikitisha sana kuona kwamba TBC haifanyi vizuri hata Kamati yetu imesema kwamba TBC waongezewe pesa, TBC haifiki maeneo mengi nchini hivi, tatizo liko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri, TBC ndiyo wanatusaidia sisi hapa wakati wa kampeni TBC, ndiyo inasikika kila eneo. Kuna baadhi ya TV hazifanyi coverage kabisa hasa kwa upande wetu wa Chama cha Mapinduzi, hebu tuone sasa wakati umefika tuwekeze TBC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa kwenye kitabu hiki kwamba Azam TV wametumia dola milioni 40 takribani shilingi bilioni 90 tunashindwa nini kuwekeza kwenye TBC? Biashara ni ushindani kwa sababu hata ukipita mtaani unaona watu hawangalii TBC wanaangalia tv nyingine wakati hili ni Shirika kubwa la Taifa, tatizo liko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe wakati Mheshimiwa Waziri ana-wind tupeleke kwenye Kamati yetu ya Bajeti suala hili ili tuwawekee pesa TBC. Hili haliwezekani kwa sababu TBC ni shirika la wananchi, linatakiwa lifike kila kona ya Tanzania hii. Mimi nasikitika sana kwa sababu kama michango yetu haitazingatiwa maana yake TBC itakufa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sasa naomba nijikite kwenye TFF (Shirikisho la Mpira Tanzania). Sote tunakumbuka enzi ya Ndolanga wadau wa mpira ilikuwa kila siku ni mahakamani mpaka ikafika FIFA. Alipokuja Tenga nchi hii ilitulia na mpira ukaanza kwenda. Leo hii tunashuhudia Rais wa TFF kila siku ni migogoro. Tumeshuhudia migogoro imeanzia kwenye chaguzi za mikoa, kila siku unasikia huyu hana sifa, huyu hana personality, TFF imejaa Usimba na Uyanga. Tunashuhudia Kamati za TFF unakuta mtu ni Mwenyekiti/Rais wa Simba au Yanga huyo huyo unamkuta ni mshiriki wa TFF, tutafika wapi? Tunazungumzia mpira kwa sababu mpira ni biashara na ni ajira sasa tutafikaje kama tuna migogoro kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mzungumzaji wa mwanzo leo Mheshimiwa Juma Nkamia alisema kwamba FIFA wanaruhusu Serikali ku-interfere, mimi najua hairuhusiwi. Mimi naomba mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi tuhakikishe kwamba tunachagua viongozi ambao watasimamia maendeleo ya mpira ya nchi hii. Tuache habari ya Simba na Yanga. Hebu Rais wa TFF nenda kajifunze kwa wenzetu wa West Africa wanafanya nini, kwa nini wanafika mbele? Inasikitisha leo Tanzania yenye zaidi ya watu milioni 50 tuna mchezaji mmoja ambaye anacheza Europe, Mbwana Samatta, hivi imefikia hapa? Hebu tujiulize tumekosea wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine hatuna viwanja vya kutosha. Uwanja mzuri upo Dar es Salaam mikoani kote hakuna viwanja, sisi Chama cha Mapinduzi tuna viwanja vingi tu. Tunaomba Wizara husika ianze kukarabati viwanja vile tusitegemee tu ufadhili. Tuangalie namna gani ambavyo tunaweza kukarabati viwanja vile ili mpira uweze kuchezwa pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba nimeona kwamba Wizara itaanza kushirikiana na TAMISEMI kwa ajili ya kujenga vituo vya michezo mikoani. Ni jambo la kupongeza sana Mheshimiwa Waziri na mkashauri Waheshimiwa Wabunge pia waanzishe vituo katika majimbo yao, nadhani litakuwa ni jambo la busara sana. Nashauri Wahemishiwa Wabunge wachukue ushauri uliotolewa kwenye hotuba hii kwani una tija na manufaa kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 20 amezungumzia kwamba takribani asilimia 90 ya watumishi ambao wanafanya kazi katika vyombo vyetu vya habari hawana weledi au ujuzi wa mambo ya habari, hili jambo ni la kusikitisha sana. Hivi inawezekanaje mwandishi wa habari awe hana weledi wa kufanya kazi hii? Ndiyo maana yanazungumzwa mambo mengi kwamba hata utangazaji hauendi sawa, maneno yanayotamkwa siyo sahihi kwa sababu hawazingatii weledi. Nimwombe Mheshimiwa Waziri kupitia TCRA hebu angalieni weledi wa wafanyakazi hawa katika vyombo vyetu vya habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo maneno machache, naomba nikushukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Mawaziri wote wawili kwa hotuba nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa. Niipongeze Wizara kwa jitihada kubwa za usimamizi wa sekta hii ambayo imeongeza mapato ya Serikali hii, ni jambo la kupongeza sana. Hata hivyo, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ukurasa wa 25 katika marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017, Majukumu ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na baadhi ya majukumu ya Kamishna yamehamishiwa Tume ya Madini, hili ni jambo jema pia. Ofisi zilizokuwa za Kanda na Maafisa Madini wakazi zipo chini ya Madini. Aidha, kila Mkoa utakuwa na Afisa Madini Mkazi na kila mgodi mkubwa na wa kati utakuwa na Afisa Mgodi Mkazi. Swali hapa ni kuwa, kwa wachimbaji wadogo wadogo, mfano Jimbo langu la Kilindi je, Serikali haijaona umuhimu wa kuwa na Afisa wa kusimamia? Mheshimiwa Waziri naomba kupata majibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wachimbaji wadogo wadogo wana mchango mkubwa sana katika kuongeza pato la Taifa. Nashauri Kamisheni hii ya Madini ihakikishe kuwa katika maeneo yote ya wachimbaji wadogo wadogo pawepo na utaratibu wa Afisa Madini kwani watasaidia kutoa elimu na kutatua migogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuimarisha usimamizi wa mapato ya Serikali, kwa mfano katika hotuba hii ukurasa wa 72 inaonesha makusanyo katika Wilaya ya Handeni hadi Machi 2018 ambao wanasimamia na Kilindi waliweza kukusanya Sh.191,177,340 tu. Hiki ni kiasi kidogo sana na hii imesababishwa na usimamizi mdogo na pengine baadhi ya watumishi kukosa uaminifu kwa kushirikiana na wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Wizara kuwa, kwa kushirikiana na Kamisheni ya Madini waone umuhimu wa kuleta Maafisa Madini katika maeneo ambayo yana wachimbaji wadogo wadogo. Hivi leo Afisa Madini yupo Tanga ambako kiukweli hakuna shughuli za uchimbaji, Serikali itakuwa na dhamira ya kusimamia mapato kweli?

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuinua Sekta ya Sanaa, Michezo pamoja na kusimamia mambo yote yanayohusu Wizara hii. Naomba kuchangia katika hotuba hii maeneo yafuatayo:-

Kuimarisha huduma na mitambo ya TBC; niungane na hotuba ya Kamati husika juu ya ushauri wao wa kuwekeza kiasi cha kutosha kwa Shirika letu la TBC kama ambavyo Kituo cha AZAM walivyofanya, naamini pamoja na majukumu mengi ya Serikali, lakini kuimarisha TBC ni muhimu sana.

Mheshimiwa Spika, TBC ndio ambayo imetapakaa nchi nzima na Shirika la Taifa haiwezekani tuliache shirika letu litoe huduma dhaifu. Watu wengi sasa hawaangalii vipindi vingi vya TBC kutokana na ubora hafifu unaotolewa na TBC na hatimaye watazamaji kupendelea huduma za vituo vingine kama vile AZAM, ITV na kadhalika. Nashauri Serikali ichukue maoni ya Kamati na sisi Wabunge na yafanyiwe kazi.

Mheshimiwa Spika, Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF); Shirikisho letu la Mpira Tanzania (TFF) kwa kiasi kikubwa wanajitahidi kutekeleza wajibu wao wa kila siku mfano ni jinsi walivyosimamia timu yetu ya mpira iliyopo Gabon kwenye mashindano ya vijana chini ya miaka 17 .

Mheshimiwa Spika, kuna mambo ningependa nishauri juu ya Shirikisho letu la Mpira Tanzania (TFF), hivi kwa nini inajitokeza mara kwa mara Shirikisho letu limeingia katika mgogoro na vilabu vyote vya mpira? Mfano ni suala la klabu ya Kagera kunyang’anywa pointi tatu walipocheza na Simba, suala hili linalichafua sana Shirikisho letu la mpira. Hivi

TFF haina wataalam wa kutosha ambao wangeweza kushauri hili kumalizika kwa haraka na kutoa haki.

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana atoe majibu yenye kuridhisha kwa sababu TFF wapo chini ya Wizara yake.

Mheshimiwa Spika, Viwanja vya Mpira; viwanja vya mpira ni chachu ya maendeleo ya mpira nchini, tunavyo viwanja vichache vyenye hadhi, nishauri Serikali isimamie viwanja vilivyopo mikoani vifanyiwe ukarabati hususani maeneo ya kuchezea mpira. Inasikitisha kuona kwa takribani miaka 50 sasa tuna viwanja visivyozidi 10 vyenye hadhi ya Kimataifa. Nishauri Wizara hii kwa kushirikiana na TAMISEMI ihakikishe kila Wilaya inakuwa na kiwanja cha mpira ili kuleta maendeleo ya mpira nchini.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri asilimia 90 ya watangazaji na waandishi kukosa sifa stahiki ya taaluma ya uandishi wa habari na utangazaji. Jambo hili linasikitisha sana niombe sasa TCRA wahakikishe kuwa vituo vyote vya utangazaji vinazingatia sifa na vigezo ili huduma zitolewe na watu wenye sifa. Hivi inakuwaje vituo kuajiri watu wasiokuwa na sifa? Je ni hatua zipi zimechukuliwa kwa vituo vya utangazaji vilivyo na waandishi na watangazaji wasio na sifa?


Mheshimiwa Spika, nipongeze sana Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI kwa utaratibu wa kuandaa vijana na TFF kuandaa vituo vya Ufundi kila mkoa kwa madhumuni ya kulea vijana. Jambo hili ni zuri sana na kama litasimamiwa vema litaleta maendeleo ya dhati na ya kweli ya mpira nchini.

Mheshimiwa Spika, jambo hili linahitaji kuwa na rasilimali fedha, sijaona wapi Wizara imetenga fedha katika kutekeleza mpango huu. Vile vile napongeza ushauri wa sisi Waheshimiwa Wabunge kuanzisha vituo vya mfano huu katika maeneo yote ya Majimbo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri wake wawili Mheshimiwa Jenista Mhagama na Mheshimiwa Kairuki pamoja na Naibu Mawaziri wawili katika ofisi hii kwa hotuba nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaomba kuchangia eneo la sekta ya uwekezaji ambalo ni sehemu muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu. Kitengo cha Uwekezaji ni muda mrefu kimekuwa kikilalamikiwa sana kwa kuchelewesha uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani na nje na kubwa zaidi ni urasimu kwa watendaji kutochukua maamuzi kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa ambalo napenda kumsahuri Waziri mwenye dhamana kwenye Ofisi hii kwanza ni kwa watendaji kubadilika kifikra, wasifanye kazi kwa mazoea. Hili litawezekana kwa kutambua umuhimu wa ofisi kwamba ni nyeti na ikitekeleza majukumu yake ipasavyo nchini hii itasongo mbele katika kuvutia wawekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna umuhimu wa kutazama na kupitia kuona kama sheria za uwekezaji zilizopo kama zinachangia katika kurudisha nyuma uwekezaji. Kama hivyo ndivyo ni vema zikaletwa hapa Bungeni tuzifanyie mabadiliko lakini hili litawezekana kama tathmini itafanywa na Ofisi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia Waheshimiwa Wabunge wakichangia humu kwamba wawekezaji wengi wanakimbilia nchi jirani wakati fursa nyingi zipo hapa nchini. Naomba Waziri mwenye dhamana aliambie Bunge sababu hasa ni nini? Nashauri kiwepo kitengo katika Ofisi ya Waziri Mkuu cha kufanya tathmini na stadi ya mara kwa mara labda kila baada ya miezi sita ambayo itakuwa inatoa tathmini ya mafanikio, changamoto na wapi uwekezaji umekua. Hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuleta ufanisi wa kitengo hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kutoa mawazo yangu ni ajira hususani kwa vijana. Idadi ya vijana wasiokuwa na ajira inazidi kuongezeka. Kwa sasa tuna vyuo vingi na vinazalisha vijana wengi wa kada mbalimbali lakini pia wapo ambao hawajabahatika kuendelea na masuala ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri elimu ya ufundi hususani ya VETA ipewe kipaumbele, kila wilaya lazima iwe na chuo cha VETA. Hii itatoa fursa kwa vijana wetu kujifunza stadi mbalimbali na itapunguza changamoto ya ajira. Pia ni vema ofisi hii ikawa na utaratibu wa kuhakikisha vijana wanapata elimu ya ujasiriamali na iratibu na upatikanaji wa mikopo midogo midogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 4 ambayo inatozwa na Halmashauri zetu kutokana na mapato ya ndani kamwe haiwezi kusaidia vijana kujiwezesha kuwa na miradi kwa sababu Halmashauri nyingi uwezo wa mapato umepungua na hata zile zenye uwezo huo watendaji wengi hawatimizi takwa hili la kisheria. Tusipokuwa makini kulitazama kundi hili muhimu la vijana kwa jicho la tatu hakika siku za usoni Serikali itakuwa katika wakati mgumu wa kutatua changamoto za vijana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu wake na timu nzima ya Wizara kwa hotuba yao ambayo imeonesha matumaini ya dhati kabisa ya kuinua sekta ya utalii, wanyamapori pamoja na misitu. Nichukue fursa hii kuchangia maeneo machache katika hotuba hii, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 59 unazungumzia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania. Kwa mujibu wa Sheria ya Misitu ambayo ilianzisha Wakala wa Misitu, lengo kubwa la uanzishaji wa TFS lilikuwa ni kusimamia na kuhifadhi rasilimali za misitu na ufugaji wa nyuki. Wakala wanatekeleza wajibu wao vema, ila yapo baadhi ya meneo nchini utendaji wa wakala unagubikwa na baadhi ya watumishi wachache kuwa sehemu ya uharibifu wa misitu na kutosimamia uharibifu wa misitu, hili ni tatizo kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano katika Wilaya ya Kilindi ambako ndiko liliko jimbo langu kuna uharibifu mkubwa wa uvunaji wa misitu ambao haufuati utaratibu. Katika Kata za Kilwa, Kilindi Asilia, Kata za Msanja na Kata za Mswaki, maeneo haya kuna uvunaji wa mbao ambao si rasmi. Wakala yupo Wilaya ya Handeni, lakini cha kushangaza mbao zinasafirishwa usiku. Hivi Wizara na Mkurugenzi wa Wakala taarifa hizi mnazo? Nimuombe Mheshimiwa Waziri na timu yake wafuatilie suala hili kwa karibu sana na ningependa kupata maelezo ya kutosha kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni Mbuga Tengefu ya Wanyama ya Saunyi. Serikali ina dhamira ya kuongeza Pato la Taifa kupitia utalii wa wanyama na kadhalika, lakini bado kuna maeneo ambayo Wizara haijayapa kipaumbele, mfano katika eneo la kitalii la Mbuga Tengefu ya Saunyi iliyopo Kata ya Saunyi, Wilaya ya Kilindi, eneo hili kuna wanyama mbalimbali, lakini sijaona jitihada za Wizara. Hivi Wizara haijui kama eneo hili lingesaidia kuinua Pato la Taifa? Wapo wawindaji wengi wanawinda isivyo rasmi, naomba Wizara itupie jicho eneo hili kwani Wizara isipofanya haya ni kuvunja moyo wananchi wa Saunyi ambao kwa muda mrefu ni wafugaji na ambao wamekuwa sehemu ya kulinda hifadhi ya mbuga hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie eneo lingine katika ukurasa wa 79 kuhusu Wakala wa Mbegu. Wakala huyu ni muhimu sana katika kuhakikisha mbegu zinapatikana za kutosha. Mbegu hizi ndizo ambazo zinatumika katika kuhakikisha maeneo ambako kuna ukataji wa miti kwa wingi ambayo husababisha kuleta jangwa. Mbegu hizi zinasaidia kupunguza athari, lakini naona jitihada za Wakala katika eneo hili ni ndogo sana. Niombe sana jitihada ziongezwe kuhakikisha mbegu zinapatikana kwa wingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la mara kwa mara la wafugaji kuvamia misitu. Hivi kweli dhamira ya Wizara na Serikali kulinda misitu itafanikiwa kweli?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano katika Kata ya Msanja, Kijiji cha Mswaki, kuna msitu wa Bondo. Msitu huu ni wa Serikali, lakini viongozi wa Serikali katika kata hii wameruhusu wafugaji kufanya shughuli za ufugaji katika eneo hili, hivi hili ni sahihi kweli? Naomba Wizara ichukue hatua haraka ili kuhakikisha kuwa misitu hii inalindwa kwa gharama kubwa. Aidha, Wizara iweke utaratibu wa kuwa na timu katika Wizara ya kufuatilia watendaji wao ambao wana dhamana ya kusimamia misitu ya nchi yetu. Vilevile kwa wale wanaovamia misitu watozwe faini kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uvunaji wa Asali na Ufugaji wa Nyuki. Tanzania ina misitu mingi na maeneo ambayo kama ufugaji wa nyuki utasimamiwa kwa dhati tunaweza kuzalisha kiasi kikubwa cha asali. Miongoni mwa mikoa ambayo ni wafugaji wa nyuki na kurina asali ni Mkoa wa Tanga na sisi wa Wilaya ya Kilindi. Tunafuga nyuki na kurina asali pia, ila kuna tatizo moja ambalo ningependa Wizara ilifanyie kazi, nalo ni kutuletea Wataalam wa kutosha ambao watatoa elimu ya utengenezaji wa mizinga pamoja na njia za kisasa za kufuga nyuki kwa sababu, Kilindi kuna nyuki na misitu mingi sana ambayo kama jitihada za kuwekeza zitafanywa basi, tutawapa wananchi wetu fursa ya kupata mapato katika eneo la ufugaji wa nyuki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira), Mheshimiwa Naibu Waziri, viongozi wote katika ofisi kwa hotuba yao nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeze Mheshimiwa Waziri kwa uamuzi wake wa kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya nylon ifikapo tarehe 1/6/2019. Kimsingi jambo hili limekuwa ni kubwa kuliko faida ya mapato ya kodi ambayo Serikali imekuwa ikipata kutoka kwa wazalishaji na wafanyabiashara wa mifuko hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uamuzi huu mkubwa wenye manufaa mapana kwa Taifa, binafsi naona kama taarifa ya sitisho la matumizi ya mifuko hii halijatangazwa sana. Nimemsikia Mheshimiwa Waziri akisema kwamba wamekaa na wadau wa mifuko hii kwa muda mrefu, lakini naamini kutokana na uamuzi huu mzuri wa Serikali, nina ushauri kwamba ofisi yako kupitia vyombo mbalimbali vya habari, kupitia Watendaji mbalimbali Serikalini hususan katika Halmashauri zetu, nao wawe sehemu ya kusambaza katazo hili kwa sababu siyo wananchi wote wanatazama TVs, wanasikiliza Redio na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani itakuwa ni busara sana kuhakikisha wafanyabiashara wa kada zote pamoja na watumiaji wanapata taarifa hii kwani ni takribani miezi miwili tu imebaki kufikia mwisho wa matumizi ya mifuko ya plasitiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha katazo hili muhimu, Mheshimiwa Waziri amesema katika hotuba yake kwamba, baadhi ya bidhaa zitaendelea kutumia mifuko ya nylon, kama vifungashio vya dawa na kadhalika. Nadhani kwa umuhimu siku za usoni kuhakikisha matumizi yote ya plasitiki au nylon yanapigwa kabisa marufuku kwa kuzingatia athari za mazingira na hata uzalishaji wa mazao umepungua kwa sababu ya ardhi imeathirika kwa matumizi ya mifuko hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naipongeza Serikali kwa jitihada kubwa za ofisi yako kwa namna inavyokabiliana na uharibifu wa mazingira hususan ukataji wa miti ovyo. Naiomba ofisi yako pia itoe katazo la wananchi wote kulima kwenye milima. Kama ambavyo katazo la kufanya shughuli za kilimo kwenye vyanzo vya maji, pia kulima kwenye milima kumekuwa na athari za kuleta mabadilikoo ya tabia nchi hususan kwa mvua kupungua, pia tumeshuhudia kuona vyanzo vyote vya maji vinachafuliwa na maji ya mvua yanayochanganyika na udongo kutoka milimani. Naiomba sana Serikali itazame katika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa suala la mazingira ni suala mtambuka, napongeza maelezo ya Mheshimiwa Waziri kusema Halmashauri zetu zina wajibu mkubwa wa kusimamia suala la mazingira. Swali hapa ni je, Halmashauri zetu zina watumishi wa kutosha kusimamia mazingira? Je, Serikali inajipangaje kuhakikisha Halmashauri zinapeleka watumishi wenye elimu na weledi wa kutosha juu ya mazingira? Ni vyema tukajipanga katika eneo hili.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi mchana wa leo ili niweze kusema maneno machache juu ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu. Nimpongeze sana mama yangu pale Mheshimiwa Profesa Ndalichako na Naibu Waziri Injinia Stella kwa kazi kubwa sana mliyoifanya pamoja na uongozi mzima wa Wizara ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina maeneo mengi ya kuchangia lakini nitaanza hasa na pongezi hususan ya ujenzi wa hosteli ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hili ni jambo jema sana kwa sababu Mheshimiwa Rais pengine na ushauri wako ameona awaondolee usumbufu watoto wetu. Wizara iliamua kujenga hosteli za Mabibo lakini Mabibo na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pana umbali kidogo lakini hili lengo la Mheshimiwa Rais kujenga hosteli pale ameondoa usumbufu mkubwa sana kwa sababu hosteli hizi zimelenga hasa watoto wa maskini. Wapo wenye uwezo ambao wana magari ya kwenda na kurudi vyuoni mfano Waheshimiwa Wabunge hapa wana watoto wanaosoma pale wana uwezo/magari ya kwenda na kurudi vyuoni lakini hosteli zile zitasaidia sana watoto wetu na kuondoa usumbufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri kwa sababu Mheshimiwa Rais ametoa fedha kwa ajili ya ujenzi hosteli za chuo kikuu aangalie sasa namna ambavyo anaweza kusaidia kujenga hosteli katika shule zetu za kata. Waheshimiwa Wabunge wanazungumzia hapa watoto wetu kupata mimba lakini sisi tunaotoka katika majimbo ambayo ni ya vijijini kule tunaona watoto wetu wanatoka mbali sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu nimwombe sasa Mheshimiwa Waziri, najua Wizara ya Elimu na TAMISEMI wanashirikiana lakini leo hii lawama zinakuja kwa Waziri wa Elimu. Nimwombe, tuone umuhimu wa kujenga hosteli hususan kwa watoto wetu wa kike katika shule za vijijini hususan katika shule zetu za kata. Hii itaongeza uwezo wa ku-perform watoto wetu ufaulu utaendelea kwa sababu watapata utulivu wa kusoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nizungumzie juu ya suala la udhibiti na ukaguzi wa elimu. Wabunge wengi wamelizungumzia hapa na pengine kitendo hiki cha kukosa udhibiti wa elimu katika shule zetu hizi za sekondari na shule ya msingi ndiyo imepelekea vyeti feki. Leo hii ni takriban wafanyakazi 11,000 au 12,000 wana vyeti fake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri hili jambo lisipite hivi hivi, tuone umuhimu wa kufanya tathmini na kufanya research ndogo tatizo lipo wapi, ni NACTE au ni nani kakosea? Kwa sababu haya tunayozungumzia hapa tunazungumzia Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kati, tunazungumzia ajira, leo hii inaonekana Watanzania wengi wana vyeti fake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri aone namna ambavyo itanyika research ndogo na taarifa ije Bungeni hapa tuone tumekosea wapi aidha ni NACTE au ni nani ametufikisha hapa tulipo. Pia naomba wale wote ambao wameshiriki katika kutufikisha hapa sheria ichukue nafasi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kuchangia ni juu ya ujenzi wa vyuo vya VETA. Tunakwenda kwenye nchi ya viwanda. Sio wote ambao watapata fursa ya kwenda sekondari au kwenda katika vyuo. Vyuo vya VETA vitasaidia watoto wetu ambao hawajapata fursa waweze kusoma. Ukiangalia hapa maeneo mengi katika wilaya zetu hayana vyuo vya VETA mfano katika Jimbo langu la Kilindi toka 2010 tunazungumzia kujenga chuo cha VETA katika Wilaya ya Kilindi. Mwaka wa fedha mwaka jana walisema kwamba Wilaya ya Kilindi itakuwa ni miongoni mwa wilaya chache ambayo itajengewa chuo cha VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha aniambie nini hatma ya Chuo cha VETA katika Wilaya ya Kilindi. Kwa sababu Halmashauri ya Wilaya Kilindi ilishatenga eneo kubwa sana takriban heka 20 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA. Tunahitaji Chuo cha VETA kwa sababu kitasaidia vijana wetu wa Wilaya ya Kilindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo suala la kidato cha tano ni muhimu sana. Sisi tunatoka maeneo ambayo miundombinu ni mibaya sana wapo vijana ambao wamefaulu lakini wameshindwa kwenda kidato cha tano katika maeneo mengine kwa sababu wazazi hawana uwezo lakini Wilaya ya Kilindi haina shule ya kidato cha tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna shule nyingi sana takriban tano ambazo zina sifa ya kuwa na kidato cha tano. Mfano shule ya Kikunde, Mafisa, Kilindi Asilia, hizi shule zina sifa, zina Walimu wazuri na miundombinu mizuri. Hivi tatizo liko wapi Mheshimiwa Waziri, kwa nini hatuna shule ya kidato cha tano? Nimwombe sana aone namna ambavyo na sisi tunaweza tukapata shule ya kidato cha tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni motisha kwa Walimu wetu. Nimepitia katika hotuba hii hapa ni kwamba wanatoa motisha kwa Walimu Wakuu lakini hawa Walimu wengine vipi? Kwa sababu motisha siyo pesa tu unaweza ukampeleka semina, ukawapeleka Walimu kusoma, hizo ni motisha. Tusitengeneze gap ya Walimu, tuwape motisha Walimu wote na hii itasaidia pia kuinua kiwango cha elimu Tanzania hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka pengine Mheshimiwa Waziri aliangalie ni suala la uwiano wa upangaji wa Walimu, hapa pana tatizo kubwa sana. Kwa mujibu wa taarifa ya CAG ya performance auditor aliyoifanya ni kwamba kuna mikoa Tanzania hii Mwalimu mmoja anafundisha darasa la watoto 26 lakini maeneo mengine mwalimu mmoja anafundisha watoto 46 maana yake ni nini? Maana yake maeneo yale ambayo Mwalimu mmoja anafundisha watoto 46 elimu haitakuwa nzuri na Walimu wengi sana wako mijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri kwa kushirikiana na TAMISEMI pitieni tena kuona uwiano na upangaji wa Walimu ulivyokaa kwa sababu Walimu wengi wako mijini, vijiji kule hakuna Walimu. Kuna baadhi ya shule Walimu wanagawana topic ya somo moja labda la historia au sayansi, hili haliwezekani. Hebu tuone namna ya ku-balance uwiano wa Walimu Tanzania nzima ili maendeleo ya nchi hii yawe kila kona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo machache, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na watumishi wote wa Wizara kwa hotuba ya Wizara yao ambayo inaonesha mwelekeo wa kutatua changamoto za wakulima wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii bila kilimo cha kisasa, chenye kutumia mbolea na zana za kisasa, bado ndoto ya kuzalisha mazao mengi haitafanikiwa. Niipongeze Wizara, katika hotuba hii inaonesha mwelekeo wa kuleta ukombozi kwa mkulima, kwa mfano uagizaji wa mbolea kwa pamoja (bulk). Eneo hili lilisababisha wananchi wengi kushindwa kuzalisha mazao yenye tija kwa sababu mbolea ilikuwa juu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri awe makini sana katika mpango huu, kwamba wale watakaopewa majukumu haya wawe watu makini na wazalendo wa dhati kwa sababu bado baadhi yao wanaweza kutumia nafasi hiyo vibaya. Kwa kuwa mpango huu ni mpya changamoto nyingi zitajitokeza, naomba tu uwekwe utaratibu wa kufuatilia utekelezaji wa mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kuchangia na ambalo naona Wizara haijalipa uzito ni kilimo cha umwagiliaji kwani yapo maeneo mengi nchini yanapata mvua za kutosha na yana mabonde mengi ambapo yangetumika vizuri nchi hii isingepata tatizo la njaa. Mvua zinanyesha maeneo mengi na maji yote yanaishia baharini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano katika Jimbo la Kilindi, Kata za Kilwa, Kilindi Asilia, Masagulu, Kibirashi pamoja na Mgera. Maeneo yote haya yana mabonde ambapo hata kwa shughuli za kilimo cha mbogamboga kingefaa pia. Tatizo Wizara haina mpango mkakati ili kuwasaidia wananchi kwa kutoa elimu, zana na hata mikopo ambayo ingeweza kusaidia katika kuboresha maisha yao kwa shughuli za kilimo.

Niombe Wizara hii, pamoja na mipango yake mizuri, wakati umefika Benki ya Kilimo isaidie sasa wananchi wakulima wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kuchangia ni eneo la Mkoa wa Tanga na maeneo mengine ambayo yana fursa za kulima mazao ya matunda. Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa michache nchini ambayo inazalisha matunda lakini uzalishaji wake umekuwa hauna faida kwa sababu wanachopata, kwa maana ya bei, ni ndogo kwa sababu tu Wizara haina utaratibu mzuri wa kuwatafutia soko la uhakika wananchi hawa. Nishukuru, pengine kwa mpango wa Serikali wa kujenga tena viwanda, unaweza kurudisha tena imani na uchumi wa wananchi wetu. Niombe Serikali kupitia Wizara hii iwaangalie wananchi kutoka kwenye maeneo yenye fursa za kilimo kama ilivyo Mkoa wa Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia migogoro ya wakulima na wafugaji; je, zoezi la Wizara tatu au nne la kutaka kutatua migogoro ya wananchi wetu limefikia wapi? Nchi hii inawahitaji wakulima na wafugaji, hivi kwa nini jamii hizi mbili hazipatani? Tatizo ni upimaji wa maeneo; hivyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri ashirikiane na TAMISEMI na Wizara ya Ardhi kuhakikisha maeneo ya kilimo yanatengwa na ya wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inajitokeza mara kwa mara wafugaji wanaingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima lakini tatizo lingine la wakulima kupanua maeneo ya kulima kwenye maeneo ya wafugaji, tatizo hili halitakwisha kama Serikali haitapima maeneo ya ufugaji na kilimo, huu ndio mwarobaini pekee. Kwa mfano maeneo ya Wilaya ya Kilindi, Rufiji na Mkoa wa Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri lakini niwapongeze Katibu Mkuu na viongozi wote wa Wizara hii.

Mheshiimiwa Mwenyekiti, nipongeze Serikali kwa jitihada kubwa za uamuzi wa kujengaMahakama Kuu na Mahakama za Wilaya maeneo ambayo hayakuwa na Mahakama. Napenda kujua ni lini Mahakama ya Wilaya ya Kilindi itakamilika maana toka msingi ukamilike, mkandarasi ameondoka site.Napata maswali mengi kwa wananchi wa Kilindi kwamba ni lini Mahakama hiyo itakamilika? Wameisubiri Mahakama hii kwa muda mrefu sana. Natumai Mheshimiwa Waziri nitapata majibu ya swali hili ili nikawajibu wananchi wa Kilindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni ushauri kwa Wizara hii, tumeshuhudia baadhi ya miradi imesimama mfano Shirika la NHC, wakandarasi wapo site na gharama zinaendelea kuongezeka. Ili Serikali isije kuingia kwenye migogoro na kulipa gharama za kumweka mkandarasi site kwanini Wizara isifuatilie miradi yote ambayo siku za usoni inaweza kuileta Serikali hasara zisizokuwa za lazima kwa kuangilia mikataba yote ambayo haijakaa sawa?Tumeshudia haya kwenye maeneo ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. OMARY M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii jioni ya leo niweze kusema machache juu ya Hotuba ya Wizara ya Ardhi. Nami nitakuwa ni mnyimi wa fadhila kama sitamshukuru Waziri wa Ardhi, Naibu Waziri pamoja na timu nzima ya Wizara ya Ardhi kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba hii nitakuwa na maneno machache sana lakini yatalenga kwenye ushauri zaidi. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Ardhi ikiwezekana alete sheria hapa ambayo itakayozuia maeneo ya kilimo yasitumike kwa ajili ya makazi. Jambo hili tumeliona, kila anayesimama hapa analalamika juu ya migogoro ya ardhi, hakuna kilimo bila mipango bora, kwa sababu tumeruhusu ardhi yenye rutuba tunaanza kujenga. Naona hili haliwezi kufanyiwa kazi bila kuleta sheria hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Ardhi kwamba Bunge litunge sheria ya namna ya kuzuia wananchi wetu wasiuze ardhi; isiwe mtu ana heka, kumi ishirini au zaidi anaamua kuuza tu kwa sababu ya shida yake. Ni kwa nini nasema haya? Hii ni kwa sababu migogoro mingi tunayoiona ya wakulima na wafugaji imesababishwa na wananchi kuuza maeneo yao. Nadhani Mheshimiwa Waziri analo jukumu hilo kuangalia, kupitia kuona ni namna gani tunaweza kupunguza migogoro kwa namna hii ya kuzuia wananchi kutouza ardhi ovyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeliona hili kwa sababu mimi natoka Jimbo la Kilindi ambako kuna migogoro mingi sana. Mtu mwenye pesa yake anatoka Arusha au Manyara huko anauza heka moja anakuja kununua heka 500 kule Kilindi. Sasa hawa wananchi ambao hawana uwezo, mafukara wanauza ardhi wanabakia kuwa vibarua katika ardhi hiyo. Kwa hiyo ili kulizuia hili naomba Mheshimiwa Waziri wa Ardhi alichukue hili aweze kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kuchangia ni juu ya migogoro ya wafugaji na wakulima. Kila aliyesimama hapa anazungumzia migogoro ya wafugaji na wakulima. Katika Jimbo langu la Kilindi nina wafugaji na wakulima wengi sana lakini najiuliza tatizo ni nini? Suluhisho
la kudumu, Mheshimiwa Waziri, ni kupima ardhi. Tupime ardhi hii ili wafugaji wajue maeneo yao ni yapi, wakulima maeneo yao ni yapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini najiuliza zaidi, hivi mimi Wilaya ya Kilindi ambayo ina vijiji 102 tutaweza kuvipima leo kwa muda mfupi hivi? Sasa kama mlianza Morogoro, nadhani muanze na maeneo ambayo yana migogoro ya ardhi Mheshimiwa Waziri anajua, Kilindi ni miongoni mwa maeneo ambayo yana migogoro mikubwa sana ya wafugaji na wakulima, nimwombe baada ya Morogoro aje Kilindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Ardhi juu ya mgogoro wa Wilaya za Kilindi na Kiteto ambao umedumu kwa takribani miaka 30. Mheshimiwa Waziri wa Ardhi alikuja mpakani pale, yeye na Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Waziri wa TAMISEMI. Nimshukuru kwa sababu aliweza kutupatanisha mikoa miwili ya Manyara na Tanga pamoja na wilaya hizi mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza, alifanya jitihada kubwa sana na akatenga shilingi milioni mia moja kwa ajili ya kupima. Kwa sababu kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa katika mkutano ule Mheshimiwa Waziri Mkuu aliagiza kwamba ili kutatua mgogoro ule ni lazima tutumie GN ya mwaka 1961, GN namba 65. Mheshimiwa Waziri wa Ardhi alituma wapimaji, wamefanya kazi nzuri sana na wameweza kuandika ripoti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tatizo hapa ni kwamba Mheshimiwa Waziri alielekeza ziwekwe beacons, leo takribani miezi miwili mitatu imeshapita wapimaji hawapo pale. Wananchi wa Jimbo la Kilindi wamenituma, wanajua kwamba yeye ni kiongozi mwadilifu, ameweza kutatua migogoro mingi, hivi tatizo liko wapi? Kwa nini wapimaji wale hawajaweza kuweka beacons kwenye mpaka huu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa kwenda mbele zaidi, lakini niamini kabisa, Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, wananchi wa Wilaya za Kiteto na Kilindi wana imani kubwa sana na Wizara yake, wana imani kubwa na utendaji wake Mheshimiwa Lukuvi. Mimi nimwombe, pale ambapo pamebaki sasa hivi ahakikishe kwamba wapimaji wanaweka mipaka ile ili shughuli za kilimo na ufugaji ziweze kwenda mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nmkwambie, toka wamepita pale, toka Mheshimiwa Waziri Mkuu amekuja pale wananchi wamekaa kimya wananiuliza Mbunge wao, Mheshimiwa Mbunge tatizo liko wapi, mbona hawa wapimaji wameondoka? Nimwombe Mheshimiwa Waziri, suluhu ya kudumu ni kuweka alama za beacons na kufuata maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya kwamba GN namba 65 ya mwaka 1961 inayogawa Mikoa ya Tanga na Arusha ndiyo alama sahihi, ndiyo GN sahihi na mimi nina imani kwamba na wewe utayasimamia hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo machache, nakushukuru na naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nikushukuru jioni ya leo kwa kunipa nafasi niweze kuzungumzia juu ya Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2018/ 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumzwa mengi. Waliozungumza wamezungumza lakini nataka tu niwaambie Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba ukipitia kitabu hiki mengi ya msingi Mheshimiwa Waziri ameyazungumza ukianzia ukurasa wa 42 mpaka 53 yote ambayo yanayohusu maendeleo ya Tanzania yamezungumzwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitajikita kwenye vitu vitatu au vinne tu, ni Public Private Partnership. Mheshimiwa Waziri mimi naomba ujikite hapa, tutapunguza matatizo kwa sababu nchi hii ni kubwa, ina changamoto mbalimbali hatuwezi ku-invest kwa kutumia our own funds, lazima tujikite kwenye Public Private Partnership. Mfano mzuri tu ni Daraja la Kigamboni. Tumeona jinsi ambavyo return kubwa inapatikana pale. Kuna usafiri DART, yote hiyo ni mifano mizuri. Mimi naomba usipate kigugumizi Mheshimiwa Waziri, hebu tuone namna gani tunaweza kujikita huko zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni suala la VETA, naomba mfumo wa VETA ubadilike. Elimu inayotolewa kwenye VETA ni nzuri sana na tunakwenda kwenye nchi ya viwanda, lakini elimu inayotolewa si ya kisasa. Tuone namna ya kuwaandaa vijana wetu tuweze kutoa elimu ambayo itasaidia kupata vijana tuweze kuwaajiri katika viwanda vyetu hivi. Ukizingatia viwanda ni vya kisasa, kwa hiyo vitahitaji vijana ambao wanasoma au wanapata elimu yenye IT base.

Meshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la viwanda, tunazungumza kufufua viwanda, mimi naamini vile viwanda vya enzi ya Mwalimu Nyerere havifai tena. Viwanda sasa hivi ni teknolojia ya kisasa ni eneo dogo kwa hiyo tujikite kuwa na viwanda vichache lakini ambavyo vitakuwa na tija na nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni suala la bomba la mafuta ambalo linatokea Uganda hadi Tanga. Nimeona katika Mpango huu mmezungumzia namna ya kuweka miundombinu na moja wapo ya eneo ambalo mmeligusia ni eneo la barabara ambalo linatokea Handeni hadi Singida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kabisa kwamba mpango huu ni lazima utekelezeke kwa sababu njia hii ukiacha bomba la mafuta linapita, lakini pia litasaidia kuinua uchumi wa mikoa minne ya Tanga, Singida, Dodoma. Nimeona niyazungumzie hapa nikiamini kabisa ni maeneo muhimu ambayo yatasaidia kuinua uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kwenda haraka haraka ni eneo la research and development. Watu tunazungumza hapa, yamezungumzwa mengi sana lakini naomba sasa Mheshimiwa Waziri wa Fedha hebu tuwekeze kiasi kikubwa sana kwenye research. Research na development ndiyo ambayo inaweza kututoa hapa kuona kwamba tubebe yapi tuache yapi na tuwe pia na mpango wa muda mfupi na mpango wa muda mrefu. Kwa sabbu mipango ni mingi na yote inatakiwa kutekelezeka lakini tukitumia research and development maana yake tunaweza tukajua kwamba tuwe na priority ipi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano mmoja tu; hata nchi za China na Malaysia, wenzetu viongozi waliotoka huko mbali walitumia wataalam. Hebu nikuombe Dkt. Mpango na Naibu Waziri hebu kaa na timu, kaa na panel ya wachumi uje na mpango mdogo ambao unaweza kututoa hapa Tanzania tulipo na kwenda mbele zaidi. Haya wanayolamimika Waheshimiwa Wabunge ni maeneo ya msingi kabisa na ninaamini mawazo ambayo yanatoka katika maeneo yetu ya uwakilishi yana maana kubwa.

Mimi sipendi kukulaumu lakini naamini kabisa haya ambayo waheshimiwa Wabunge wameyasema yana tija na yana faida kubwa na mimi naomba kupitia wataalam wako, hebu yachukue yafanyie kazi. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba nimechangia, lakini naomba tena kuchangia kwa maandishi hoja yangu ya mwisho ambayo sikutaka sana kuisemea kwa upana nilitaka kuandikia hapa na naomba Mheshimiwa Waziri anipatie majibu.

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ni kwamba, Mzee Ally Mwegango mkazi wa Kibirashi, Wilaya ya Kilindi ambaye alinunua gari kwa bwana Karl Muller kwa Sh.23,000,000 tarehe 7/7/2015 kwa akaunti namba 9120000187753 Benki ya Stanbic na gari hii kukabidhiwa kwa Mzee Ally Mwegango . Tarehe 12/12/2017 gari hili lilikamatwa na Kampuni ya COPS Auction Mart & Court Brokers kwa maelekezo ya Benki ya Redstone Financial Services. Kimsingi muuzaji Mzee Karl Muller aliuza gari hili huku akijua amechukua mkopo kwenye Financial Services, kimsingi ni tapeli au mwizi. Jeshi la Polisi limeshindwa kuchukua hatua kwa mtu huyu na kumnyima haki Mzee Ally.

Mheshimiwa Spika, Mzee Ally huu ni mwaka wa pili sasa anafuatilia gari lake na lipo barabarani linafanya kazi. Nina imani kubwa sana na jeshi hili na pia naamini Mheshimiwa Waziri na wote waliopo chini yake wanalijua vema suala hili, hivi kama mimi Mbunge na mlalamikaji sote hatusikilizwi, hivi wanataka tuamini kwamba mhalifu huyo ana nguvu au yupo juu ya sheria?

Mheshimiwa Spika, ili kutenda haki kwa mlalamikaji Mzee Ally ambaye aliamini kabisa gari alilonunua lingemsaidia kujipatia riziki yake na familia, leo hii gari hili lipo kwenye mikono ya mtu mwingine, nina imani kubwa na nina uhakika suala hili linaweza kumalizika kwa kumkamata huyu tapeli au mwizi ambaye anafahamika wazi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa jioni ya leo niweze kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita zaidi kwenye ripoti hii ya PAC kwa sababu mimi ni Mjumbe kwenye Kamati hiyo. Yamezungumzwa mengi na kuna dosari nyingi sana lakini yote yameainishwa katika ripoti nisingependa kuyarejea. Kikubwa ambacho nataka nikizungumze ni juu ya ushauri kuhakikisha kwamba yale maoni ambayo yametolewa na Kamati yetu ya PAC yanafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumzwa mengi juu ya dosari katika Mkataba wa Mlimani City, Mkataba wa Dege Kigamboni. Nadhani Serikali imefanya jambo kubwa na imeshaanza kuchukua maamuzi, niipongeze sana Serikali kwa sababu baadhi ya viongozi walishasimamishwa na hii ni kuonesha kwa dhati kabisa kwamba tayari Serikali ilishaona upungufu na imechukua uamuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo nina ushauri mdogo, katika ripoti ya CAG imezungumza juu ya upungufu wa Benki ya Kilimo. Benki hii bado haijapewa nguvu, pesa au mtaji ambao Benki yetu ya Kilimo imepewa ni ndogo sana. Nashauri Wizara ya Fedha pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo wakae chini waone namna ambavyo wanaweza wakaiongezea mtaji kwa sababu sehemu kubwa ya maisha ya Watanzania yanategemea kilimo na nina imani kwamba uanzishaji wa benki hii ulikuwa na lengo la kuwasaidia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo liko sambamba na hilo ni juu ya suala la Mkaguzi wa Mahesabu (CAG), yote haya tunayoyaona kwenye Kamati za PAC na LAAC yametokana na ripoti ya CAG ambayo ndiyo jicho la Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lazima tukubali kwamba CAG anafanya kazi kubwa sana, lakini anakwama kwa sababu hawezeshwi pesa nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano tu kwamba, katika kazi yake ya auditing (ukaguzi) performance auditing ndiyo kazi ambayo inaonesha mapungufu mengi sana, lakini ukikaa na CAG anakwambia pesa anayopewa ni ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu unaojionesha katika miradi mingi ya maji, miradi ya barabara ambayo inatokea katika Halmashauri zetu inaonekana kutokana na ripoti ya CAG. Nadhani muda umefika sasa wa kuhakikisha kwamba tunamsaidia CAG ili aweze kuwa na nguvu na ili aweze kutoa ripoti nzuri.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miradi ya maji, nimepitia taarifa hapa ya LAAC imeonekana miradi mingi ya maji haiko vizuri. Lakini nina ushauri mmoja kwa Serikali kwamba Wizara ya Maji na wenzetu wa TAMISEMI waweke utaratibu na kuunda kikosi kazi cha kuhakikisha na kuangalia kwamba miradi hii inafuatiwa na kukaguliwa ili kuangalia ile value for money inapatikana, vinginevyo malengo tunayokusudia malengo ambayo Serikali wanayokusudia hayatafikiwa kwa sababu maeneo mengi miradi hii iko chini ya kiwango. Mimi nashauri tuangalie namna ambavyo suala la ufuatiliaji wa miradi linakuwa ni suala muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nina ushauri juu ya makusanyo ya mapato katika Halmashauri zetu. Tumeona Serikali imeweka utaratibu wa kukusanya mapato kwa kutumia njia ya kielektroniki kwa maana TAMISEMI wanaona moja kwa moja Halmashauri fulani inakusanya kiasi gani, lakini bado utaratibu huu haujakaa vizuri, zipo baadhi ya Halmashauri ambazo bado mapato hayakusanywi sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri Waziri wa TAMISEMI aangalie namna ambavyo anaweza akaongeza udhibiti, au kwa kuongeza mafunzo kwa watumishi wetu wa TAMISEMI ili nia thabiti ya Serikali ya kukusanya mapato katika Halmashauri zetu ifikiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo napenda kulizungumzia ni juu ya suala la Mlimani City. Mlimani City imezungumzwa sana juu ya mkataba ule. Ushauri ninaoutoa ni kwamba upungufu huu Serikali ichukue hatua haraka sana kwa sababu tunapoteza mapato mengi, hata taarifa hii nina uhakika haijamaliza mambo mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nataka kushauri kwamba taasisi ambayo ilikuwa inasimamia mkataba huu ni taasisi nyeti. Nina imani kwamba Serikali itachukua hatua za haraka sana kuhakikisha kwamba dosari zote ambazo zimejitokeza kwenye mikataba hii zinafanyiwa kazi haraka sana ili wananchi wa Tanzania wawe na imani kubwa na Serikali yetu na nina imani kabisa kwamba maoni yetu na ushauri wetu utafanyiwa kazi haraka sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Manaibu Katibu Wakuu pamoja na watumishi wote wa wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuipongeza Wizara kwa maboresho ya utendaji wa kazi hususani katika maeneo yote yanayohusu elimu, hii ni pamoja na Taasisi zote za Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya maneo muhimu yanayochangia ufaulu ni pamoja na kuwa na Maktaba za kisasa zenye vitabu. Nalisema hili kwa kutolea mfano wa maktaba ya kisasa iliyojengwa kwa ufadhili wa nchi hisani ya China katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hakika naipongeza Nchi ya China na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyakiti, nashauri sana kuwa na maktaba kama ile katika vyuo vyote. Najua ni gharama lakini katika elimu huwezi kuepuka suala la gharama. Tuanze kidogo kidogo katika vyuo vyote hii itasaidia sana kuzalisha wataalam wazuri na kuimarisha elimu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niishukuru Serikali kwa kutupatia Gari kwa ajili ya udhibiti wa elimu katika jimbo langu kwani Jimbo la Kilindi ni miongoni mwa maeneo yenye changamoto sana kwa sababu ya ukubwa wake lakini miundombinu isiyoridhisha. Pamoja na kutupatia Gari tunayo changamoto kubwa nayo ni kukosa Dereva lakini hatuna kasma ya matengenezo ya Magari na mafuta pia kwa maana kifungu cha mafuta hakipo. Niishauri sana Serikali, ili tija ipatikane ya uwepo wa chombo hiki pamoja na stahiki za watumishi na eneo hili. Aidha, hatuna jengo kwa ajili ya watumishi, tunalo eneo naiomba sana Serikali itujengee Ofisi za Watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nipongeze juhudi za Serikali katika kuhakikisha ujenzi wa vyuo vya VETA katika ngazi za Mikoa na pia katika ngazi za wilaya. Vituo hivi vitatoa tija kwa vijana wetu katika kutatua changamoto ya ajira kutoa ufundi mbalimbali lakini dhima ya viwanda vya kati haitofanyiwa bila kujenga VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 43 wa hotuba yako kipengele (vii) nimeona jitihada za Serikali za maandalizi ya michoro na zabuni kwa ajili ya ujenzi wa vyuo viwili vua ufundi stadi vya Wilaya ya Kilindi na Karagwe. Hili jambo kubwa sana Kilindi wanasubiri ujenzi wa VETA kwa hamu kubwa sana kwani ni miongoni mwa maeneo ambayo yana vijana wengi ambao hawabahatiki kuendelea na masomo lakini ni miongoni mwa maeneo yenye fursa za madini, jamii ya wafugaji pia hivyo kupata chuo cha VETA kitasaidia sana vijana wetu. Niiombe sana Serikali iongeze jitihada za ujenzi kama inavyoahidi hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Waziri na Naibu Waziri, kwa jitihada kubwa wanazochukua katika kuinua elimu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia hotuba ya Wizara hii katika maneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, shule ya kidato cha tano. Naipongeza sana Serikali kwa kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne. Hatua hii ni ya kupongezwa sana kwa sababu imetoa fursa kwa Watanzania wengi sasa kupata elimu bila kujali idadi, uwezo au rangi. Hata hivyo, kuna tatizo katika baadhi ya maeneo mbalimbali nchini kutokuwa na shule za kidato cha tano mfano ni Wilaya ya Kilindi. Naomba hoja yangu ipate majibu, hivi ni kweli hatuna hata shule moja katika hizi zilizopo Kilindi ambazo tunaweza kuzipandisha ziwe za kidato cha tano? Naomba majibu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni kuhusu VETA. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Wilaya ya Kilindi ilikuwa ni miongoni mwa Wilaya chache ambazo zilitengewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA. Wilaya tayari ilikwishatenga eneo kwa ajili ya ujenzi na ikumbukwe toka mwaka 2014 Wizara ilitamka itajenga chuo. Hivi ni hatua zipi zimefikiwa au kuna tatizo gani hasa?

Vyuo vya VETA vinatoa fursa kwa wananchi hususan vijana wetu ambao hawajabahatika kuendelea na kidato cha kwanza kupata fursa ya kupata ujuzi mbalimbali. Kilindi hatuna FDC, Chuo cha VETA ni hitaji muhimu kwa Wana- Kilindi, vijana wetu wa Kilindi wanahitaji la chuo hiki. Naomba Wizara iliangalie suala hili kwa jicho la ziada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, uhaba wa walimu hasa wa sayansi. Tatizo la walimu ni changamoto kubwa sana, shule nyingi zina walimu wachache kuanzia shule za msingi hadi sekondari. Katika Jimbo langu la Kilindi tuna tatizo la walimu wa masomo ya sayansi. Niipongeze Wizara kwa kutupatia walimu sita wa shule za Serikali, lakini bado uhitaji ni mkubwa sana. Naiomba Wizara itupatie walimu wa kutosha. Ili dhana ya Serikali yetu kwenda kwenye nchi ya viwanda ifanikiwe ni lazima Serikali isomeshe walimu wa kutosha wa masomo ya sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri ili tuondokane na tatizo la uhaba wa walimu wa sayansi, Wizara ione namna ya kupunguza gharama za masomo katika vyuo vyetu ili kuwapa wazazi motisha. Vilevile ajira za walimu wa sayansi zipewe kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne ni kuhusu uwiano wa ugawaji wa walimu. Bado kuna tatizo la uwiano wa ugawaji na upangaji wa walimu katika nchi yetu. Kwa mujibu wa Ukaguzi wa Ufanisi (Performance Auditing) iliyofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti wa Serikali (CAG) kuna tatizo kubwa katika eneo hili. Kuna baadhi ya mikoa mwalimu mmoja anafundisha watoto 26 wakati Mikoa mingine mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 46, hili ni tatizo kubwa, hali hii inadumaza maendeleo ya elimu. Niiombe Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na TAMISEMI, ipitie upya mgawanyo huu ili kuleta usawa wa maendeleo nchini kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuamua kujenga hosteli pamoja na maktaba, yote haya yamefanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ujenzi wa mabweni utapunguza usumbufu na kuleta utulivu kwa vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kwanza kuunga mkono hoja iliyopo mezani. Pili, kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na uongozi mzima wa Wizara kwa kazi na jitihada ambazo wamefanya hususani katika kuwapelekea Watanzania umeme.

Mheshimiwa Spika, binafsi nitakuwa mnyimi wa fadhila kama sitomshukuru Waziri na Naibu wake kwa ziara zao walizofanya Jimboni kwangu, hakika zimezaa matunda.

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo, naomba sasa nijielekeze juu ya vijiji vyangu ambavyo havijapata umeme. Kilindi ina vijiji 102 na vitongoji 615, lakini ni vijiji 50 ambavyo mpaka sasa vitakuwa au vinatarajia kuwa na umeme, vijiji 52 havina umeme kabisa. Niombe sana tena vijiji 52 vilivyobaki vipatiwe umeme na naamini kabisa vijiji hivi navyo vitapata katika awamu ya tatu ya REA III.

Mheshimiwa Spika, kwa hali ya jiografia ya wilaya yangu ilivyo ina changamoto nyingi sana, hii ni pamoja na kukatika kwa umeme mara kwa mara na hii inasababishwa na idadi ya watumiaji imeongezeka na chanzo pekee cha umeme ni kutoka Mkata, Wilaya ya Handeni. Kwa kiasi kikubwa umeme umekuwa ukikatika mara kwa mara ni kuwa kero kubwa kwa watumiaji, lakini pia hii imekuwa sehemu ya Ofisi ya TANESCO Kilindi kuendesha ofisi kwa gharama kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, natambua jitihada za Wizara za kufanya interconnection network ya kutoka Mbigili, Wilaya ya Kiteto hadi Kufungu kilomita 55; mradi huu ni muhimu sana kwani utakuwa ni suluhu ya kupata umeme wa uhakika. Pia ningeomba kama tungepata network interconnection kutoka Kikunde hadi Kukivu kilomita 41 ambayo itasaidia Vijiji vya Ludeva, Mafalila, Tunguli, Mtoro na Kitingi vitafaidika na umeme.

Mheshimiwa Spika, vijiji tajwa hapo juu vipo mbali na Makao Makuu ya Wilaya, mfano Kijiji cha Kikunde, Kata ya Kikunde umeme umetokea Wilaya ya Mvomero, Morogoro. Niiombe sana Serikali iitazame Kilindi kwa Kijiji cha Tatu.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watumishi wote wa Wizara hii. Nichangie hoja hii katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Bajeti ya Wizara. Nioneshe masikitiko makubwa sana kuona kuwa bajeti ya Wizara hii muhimu na inayomgusa kila Mtanzania badala ya kuongezeka, imepungua. Ni ukweli usiofichika kila Mheshimiwa Mbunge hapa ana shida ya maji katika jimbo lake. Kwa mfano mdogo tu bajeti ya Halmashauri yangu ya Kilindi ya mwaka wa fedha 2016/2017 ilikuwa shilingi bilioni 3.7 lakini mwaka huu imeshuka hadi shilingi bilioni 1.6. Hivi Wilaya hii yenye ukame mkubwa na yenye vijiji 102, kata 21 na vitongoji 650 bajeti hii itatosha kweli?

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inao Mfuko wa Maji, nasikitika kiasi kilichokusanywa ni kidogo sana. Ushauri wangu; badala ya kutoza sh.50/= katika lita ya mafuta ya dizeli na petrol tozo hii ipande iwe sh.100/=. Hii itasaidia kupunguza kero ya maji. Vile vile naamini tusipopunguza kero hii wananchi watakata tamaa na Serikali yao. Ikumbukwe wanaopata shida sana ni mama zetu na hasa waishio vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ukaguzi wa Miradi. Katika maeneo ambayo Serikali imetoa fedha nyingi hakuna utaratibu ulio rasmi kati ya Wilaya hii na TAMISEMI na hii imepelekea miradi mingi kutekekelezwa chini ya kiwango. Nishauri sasa miradi yote ya maji ifanyiwe “Perfomance Auditing” kupitia ofisi ya CAG.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili litaimarisha uwajibikaji na miradi mingi iwe na tija. Mfano mzuri ni mradi wa maji kutoka Wami kwenda Vijiji vya Chalinze, mkaguzi alibainisha namna ambavyo wakandarasi wanavyoisababishia Serikali hasara. Ni imani yangu Serikali itaona umuhimu wa kufanya ukaguzi wa ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Visima vya Maji Makao Makuu ya Wilaya. Niipongeze Wizara kwa kunichimbia visima vinne katika halmashauri yangu kwa msaada mkubwa kupitia Katibu Mkuu wa Wizara ambaye kwa sasa ni mstaafu. Visima hivyo vimeainishwa katika jedwali Na. 13.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Vijiji vya Sanje, Vilindwa, Nkama na Mafisa vimechimbwa lakini bado miundombinu ya kukamilisha miradi hii iweze kufanya kazi bado. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, maeneo haya yote yana shida kubwa sana ya maji. Miradi hii ikikamilika itasaidia mamlaka ya maji ya Songe iweze kufanya kazi kwa kujitegemea na ni takribani miezi sita sasa imepita toka wakala wa visima alipochimba.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ushiriki wa Sekta binafsi katika Sekta ya Maji na Umwagiliaji. Nipongeze juu ya wazo hili, ni wazo sahihi na pengine limechelewa. Naamini kabisa kwa changamoto hii ya tatizo la maji bila kushirikisha sekta binafsi kwa mpango wa PPP hatutaweza kufika mbali. Niishauri Serikali ifanye hima kwa kushirikiana na Mshauri Mwelekezi jambo hili lianze haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii ni kubwa na yenye wananchi wengi. Kwa kushirikisha sekta binafsi ni wazi kutakuwa na gharama katika kuleta huduma hii ya maji, lakini vyema wananchi wetu wachangie katika kupata huduma ya maji kuliko kusubiri huduma ya bure kutoka Serikalini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Uchimbaji wa Mabwawa. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri nimeona ametaja bwawa moja tu la Kwamaligwa, wakati katika Jimbo langu tunalo bwawa lingine la Jungu ambalo lipo katika hatua za umaliziaji, lakini sijaona mahali popote tulipotengewa fedha. Nitaomba sana majibu ya Mheshimiwa Waziri, kwa nini bwawa hili halijatengewa fedha, lakini pia Wilaya yote? Njia bora ya kuwapatia wananchi hawa huduma ya maji ni kuchimba mabwawa mengi ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunalo bwawa moja tu la Kwamaligwa. Niombe Mheshimiwa Waziri tupatiwe mabwawa ya kutosha katika Jimbo langu lenye jamii ya wafugaji na wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kilindi kuomba Mradi wa Maji. Wilaya ya Kilindi hatuna mto hata mmoja wala ziwa, nashangaa Wizara imeweza kutenga fedha katika maeneo yenye changamoto kama zetu wamepewa au kutengewa fedha nyingi za miradi ya maji lakini maskini Wilaya yangu haipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri amtume Mheshimiwa Naibu Waziri au watumishi waliopo chini yake waje Jimboni kwangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupata mradi mkubwa kama vile HTM ambao umefika Handeni kwa kutoa maji Mto Ruvu. Kwa nini Wizara imeshindwa kufikisha mradi huu Kilindi?

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri afike na kutazama Wilaya ya Kilindi kwamba nao ni miongoni mwa maeneo yenye ukame na wanahitaji sana kupatiwa mradi wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. OMARY M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba nimechangia hotuba kwa kuzungumza naomba tena kusisitiza juu ya hoja yangu ya kuongoza Tax base ambayo inaweza kuongezeka kwa kuzingatia vifungu vipya kwenye jedwali Na.2 ukurasa 42 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2014 idadi ya Watanzania ni 55,890,744 kwa tofauti ya umri kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2014 Idadi ya Watanzania ni 55, 890,747 kwa tofauti ya umri:-

(1) Umri kati ya mika 0 – 5 watu 9,628,845;

(2) Umri kati ya 6 – 19 watu 20,836,171;

(3) Umri kati ya 20 – 64 watu 23, 691, 680;

(4) Umri kati ya 65 na kuendelea watu 1,734,051

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita kwenye kundi namba (3), umri wa mika 20-64 ambapo ndipo kwenye idadi kubwa. Hapa ukichukua Idadi ya watu 3,000,000 tu, tukizingatia kuwa hawa si miongoni mwa wale wadogo kwenye kundi la sekta isiyo rasmi, na ni kundi jipya. Wakifanikiwa kutoa shilingi laki moja (100,000) Serikali itaweza kukusanya bilioni mia tatu. Makundi mengine yaliyobaki yanaweza kusaidia Serikali kupata takribani billion mia saba; hii itakuwa imesaidia Serikali kupata takribani trillion moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania ambao hawajalipa wako wengi. Serikali inakusanya kodi kwa watu wale wale na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hawajafanya jitihada za kutosha kuongeza wigo wa idadi ya watu kulipa kodi. Nashauri; umefika wakati wa kupunguza mzigo wa Watanzania wanaolipa kodi kuwa ni wale wale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kila siku kila Mtanzania anatumia barabara, zahanati viwanja vya ndege, shule na vyuo vikuu bila kulipa kodi; ni lazima sasa kila Mtanzania alipe kodi kwa hiyari, na hili linawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ningependa kutoa ushauri ni eneo la wataalamu wa TRA wanaofanya makadirio (tax Assessors).Eneo hili ndilo ambalo limelalamikiwa sana na Watanzania hususani wafanyabiashara. Hapa lazima wawepo watumishi wenye weledi mkubwa wa tasnia au elimu ya kodi; watu ambao watakuwa na uadilifu wa hali ya juu pamoja na uzoefu katika sekta ya kodi kiwe ni kigezo kikubwa. Si busara kijana awe amemaliza Chuo Kikuu na ana muda mfupi kazini halafu anapewa jukumu la ukadiriaji wa kodi

Mheshimiwa Naibu Spika, Naunga mkolo hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa fedha 2018/2019 katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, eneo hili ni muhimu ambalo Serikali ililipa umuhimu mkubwa sana. Ili Serikali ijipunguzie mzigo wa kubeba miradi mingi mikubwa ambayo yote ina dhamira ya kuliletea Taifa maendeleo, mimi sioni sababu kwa nini Serikali isichukulie mradi wa Daraja la Kigamboni na Mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi Dar es Salaam kama kielelezo cha mfano. Tatizo lipo wapi? Inaonekana wazi kuna hofu katika eneo hili ambayo haina msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo mifano duniani ambako nchi nyingi zimepiga hatua kupitia utaratibu huu. Naomba Serikali iwekeze katika sekta ya barabara, hospitali, kilimo, usafiri wa anga, reli pamoja na usafiri wa maji kupitia public private partnership (PPP) hii njia pekee itafanya nchi isonge mbele, kwani nchi yote ni kubwa na kila mkoa, wilaya na jimbo ina changamoto tofauti, tusipochukua hatua itachukua miaka kama si karne kutimiza matarajio ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi, wanyamapori na misitu, hili pia ni eneo ambalo Serikali anabidi kuweka msisistizo ili kufanya nchi iongeze Pato la Taifa. Yapo maeneo mengi ambayo yana fursa, kama yangetumika vema basi uchumi ungeongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi ya nchi yetu hasa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini yanalima sana mahindi. Hivi ni lini Serikali itatoa utaratibu wa kuhakikisha kuwa eneo hili linakuwa eneo maalum kwa ajili ya uzalishaji wa mazao ya mahindi ili nchi izalishe kwa ajili ya ndani, pia ili tuweze kuuza nje ya nchi? Hili linawezekana tukiweka utaratibu wa kulima kwa njia ya kisasa. Wananchi wa maeneo haya kupata pembejeo za kisasa, mikopo ya riba nafuu na kupatiwa ruzuku kama nchi nyingine duniani wanavyofanya. Hii pia itafanikiwa katika sekta nyingine za mifugo, uvuvi, wanyamapori na mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bomba la mafuta kutoka Hoima (Uganda)- Chongoleani (Tanga), niipongeze Serikali kwa mradi huu mkubwa ambao utatoa fursa kubwa ya kiuchumi katika nchi na hasa katika mkoa wetu wa Tanga ambapo bomba la mafuta litapita katika Wilaya nyingi ikiwemo Wilaya ya Kilidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona Serikali itatengeneza barabara ya kiwango cha lami kutoka Handeni hadi Singida ambapo barabara hii itapita. Jambo hili ni zuri sana na niipongeze Serikali. Ni dhahiri kwa ukubwa wa mradi huu na thamani si busara eneo la bomba linapopata kuwa na barabara mbovu. Niiombe Serikali itenge fedha kwa mwaka wa fedha 2018/2019 ili ijenge barabara hii kama ilivyokusudia. Aidha, barabara hii ni kiungo muhimu cha mikoa minne ya Tanga, Manyara, Dodoma na Singida na zipo shughuli nyingi tu za kiuchumi kwa barabara hii. Wakati muafaka umefika kujenga barabara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA), uanzishaji wa Wakala wa Barabara ya Vijijini utasaidia kufungua mawasiliano ya barabara za vijiji vyote; hii itasaidia sana kutimiza uchumi wa wananchi wote. Ni wazi maeneo mengi ya nchi yetu hususan barabara za vijiji vyote bado yana changamoto za kutopitika. Niishauri Serikali iimarishe Wakala wa TARURA kwa kupatiwa wataalam wa kutosha na iongeze ujuzi wa kutosha hasa katika barabara hizi, hii itasaidia sana kuunganisha barabara za vijiji na barabara kuu. Aidha, wakala huyu wapatiwe vitendea kazi vya kutosha vinginevyo utendaji utazorota.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Muswada wa Sheria ya Bodi ya Kitaalam ya Walimu Tanzania wa Mwaka 2018
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Waziri mwenye dhamana ya Elimu nchini, Naibu Waziri na Uongozi mzima wa Wizara kwa Muswada mzuri ambao kwangu mimi naona umekuja wakati muafaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi hii uanzishwaji wake utakuwa ni sababu kubwa sana katika kuimarisha kiwango cha elimu, kitu ambacho kimelalamikiwa kwa muda mrefu na Watanzania wengi. Tumeshuhudia vijana wengi wakimaliza darasa la saba, kidato cha nne, sita na hata vyuo lakini uelewa wa vijana hawa ukiwa ni mdogo au wastani. Hii imepunguza ufanisi katika maeneo mengi ya kazi sababu ya kutokuwa na Walimu wenye viwango vinavyokubalika. Kazi ya ualimu kwa muda marefu haikuzingatia tena weledi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Muswada huu wa Uanzishwaji wa Bodi ya Walimu haijaelezwa wazi kama ili Mwalimu aweze kusajiliwa atafanya mitihani ya kitaaluma kama ilivyo katika Bodi zingine mfano Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi (NBAA), Bodi ya Wahandisi, Bodi ya Manunuzi na kadhalika. Naomba kupata majibu juu ya suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli kwamba, Walimu hawa watakuwa wamemaliza vyuo mbalimbali vya ndani na nje ya nchi, pia watakuwa wamepata vyeti kwa kuzingatia taratibu za vyuo husika lakini ili uwe mwanachama na mwenye sifa katika bodi za kitaaluma duniani kote ni lazima ufanye mitihani ya bodi husika ili uweze kutambulika, kwa sababu utakuwa umekidhi sifa zinazotakiwa, nataka kujua, je, bodi hii ni tofauti na bodi nyingine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu mwingine, naomba kipengele cha kumtaka Mwalimu asajiliwe baada ya mwaka kisiwepo, kwa sababu tutawanyima fursa Walimu wengi ambao watakuwa wamemaliza vyuo na wana sifa za kusajiliwa, hili litazamwe upya. Ikumbukwe kwamba, tunavyo vyuo vingi vya ualimu nchini, vya Serikali na binafsi ambavyo kila siku wanahitimu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sheria hii haijasema kama chombo kipi ambacho kitaisimamia bodi hii ikizingatiwa kuwa bodi hii itakuwa na dhamana kubwa ya kubeba kundi kubwa la Walimu. Jambo hili ni muhimu kwa sababu kukosekana kwa chombo cha kutazama shughuli za utendaji wa Bodi hii ya Walimu kunaweza pia kupunguza ufanisi wa utendaji, nashauri chombo hicho kiwe ndani ya Wizara ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Serikali kwa ujumla kwa hotuba nzuri iliyosheheni mambo mazuri yenye masilahi mapana kwa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri Mkuu, mambo mengi ya msingi yamezungumzwa juu ya Sekta za Mawasiliano, Kilimo, Madini, Elimu, Miundombinu na kadhalika. Kwa leo napenda kuchangia maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi; changamoto ya ardhi imeathiri maendeleo ya wananchi wetu hususan katika Sekta ya Kilimo na katika maeneo mengi ya nchi yetu. Migogoro hii ni baina ya Vijiji na Vijiji, Kata na Kata na Wilaya na Wilaya. Kwa sehemu kubwa Watendaji wetu wa Vijiji, Kata na kushirikiana na baadhi ya Wenyeviti wa Vijiji wanakuwa ni chanzo cha changamoto hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la mgogoro wa mpaka baina ya Wilaya ya Kilindi na Kiteto, suala hili limechukua muda mrefu sasa. Binafsi nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye mwaka 2017 alifika katika eneo hili kwa kuambatana na Waziri wa Ardhi na TAMISEMI na kutoa maagizo kwa Wataalam kupitia upya mpaka huo kwa kutumia Government Notice No. 61. Taarifa hiyo toka mwezi Machi, 2017 ilitoka ikibainisha wazi wapi mpaka wa Wilaya hizi upo. Jambo la kushangaza, mpaka leo hakuna utekelezaji wa kuweka alama za mpaka wakati Serikali ilitenga kiasi cha shilingi milioni mia moja kwa ajili ya utekelezaji wa agizo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa maeneo ya mpakani wa Wilaya hizi bado wanaendelea kusubiri hatima ya jambo hili. Vile vile shughuli za kilimo na mifugo kwa kiasi kikubwa zimesimama kusubiri hatima ya suluhisho la mgogoro huu na mara kadhaa wananchi wa maeneo haya wameendelea kugombana kwa sababu ya wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima. Ni matumaini yangu Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kupitia Wizara hizi mbili (TAMISEMI na Ardhi) watakwenda na kuweka alama za kudumu ili kutoa suluhisho la kudumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kutoa mchango wangu ni suala la maji vijijini. Changamoto ya maji vijijini bado ni kubwa, pamoja na jitihada kubwa za Serikali za kutatua changamoto hii. Naipongeza Serikali kwa dhati kwa jinsi inavyohakikisha na kudhamiria kutatua changamoto hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingi ya maji katika Vijiji na Miji yetu mingi inakosa ubora unaotakiwa. Hii inatokana na baadhi ya Watumishi wetu kwa kushirikiana na Wakandarasi kukosa uadilifu. Naishauri Serikali iweke utaratibu kwa Wizara zenye dhamana na Sekta ya Maji na TAMISEMI wahakikishe kuwa wanaunda Kitengo Maalum cha ufuatiliaji wa miradi hii ya maji, inajengwa kwa kiwango na kuzingatia thamani ya fedha (value for money) badala ya kusubiri hadi Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali kupitia hesabu za maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke fedha zikitengwa kutekeleza mradi fulani huchukua miaka mingi eneo husika kupata tena fedha kwa mradi wa maji. Ni vema kwa sasa Serikali ikawa na mpango thabiti wa kusimamia miradi hii na kuwadhibiti wachache ambao hawana uchungu na rasimali za nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa dhati kwa kuanzisha Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini. Uamuzi huu una dhamira ya kuhakikisha barabara zetu zinapitika katika kipindi chote cha mwaka. Dhamira hii nzuri ya Serikali inatakiwa iende sambamba kwa kuwa na chombo cha ufuatiliaji wa kazi za TARURA kwa kuangalia ubora wa kazi za TARURA. Je, ni nani msimamizi wa kazi za TARURA? Uwepo wa chombo hiki utasaidia dhamira nzuri ya Serikali juu ya uanzishaji wa chombo hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu na Serikali sasa ione umuhimu wa uanzishaji wa chombo kinachofanana na TARURA kwa kuanzisha Mamlaka ya Maji Vijijini. Hii itasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa kero ya maji vijijini. Chombo hiki kitakuwa na usimamizi wa huduma ya maji vijijini tukikumbuka sehemu kubwa ya Watanzania wanaoishi vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi jioni ya leo niweze kuchangia hotuba hizi mbili za Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Utumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia nitakuwa mnyimi wa fadhila kama sitamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya. Kabla sijawa Mbunge katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nilikuwa nafuatilia sana midahalo humu ndani, moja ya changamoto kubwa ilikuwa ni malalamiko kwamba Tanzania hii hatuna ndege, Tanzania hii hatuna rail way za kisasa, lakini Mheshimiwa Rais amethubuti kuhakikisha kwamba tunakuwa na rail way ya kisasa, amethubutu kuonesha kwamba tumenunua ndege kwa kweli lazima tumpongeze. Itakuwa ni jambo la kusikitisha sana kama hatasisima Mbunge katika Bunge hili bila kumsifia Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo machache sasa nianze mchango wangu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita zaidi kwa kuanza na TARURA (Mfuko wa Barabara Vijijini). Mimi nipongeze maamuzi ya Serikali kuwa na TARURA, ni kweli kabisa kwamba TARURA imesaidia utengenezaji wa barabara zetu vijijini, lakini zipo changamoto mbalimbali ambazo mimi kama Mbunge sina budi kuzungumzia, wamezungumza wenzangu hapa kwamba TARURA inachangamoto ya fedha na mimi niseme kwamba tuone namna ambavyo tunaweza tukakaribisha mfumo wa TARURA, tuweke chombo ambacho kinaweza kuwa kinasimamia utekelezaji wa majukumu ya TARURA ili kile chombo kinaweza kufanya tathmini ya majukumu ya TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi tuone namna ambavyo TARURA wanaweza kuongezewa watumishi, natoa mfano katika Jimbo la Kilindi ambalo lina kilometa za mraba takribani 845.2, eneo hili ni kubwa sana, lakini tunalo gari moja, tu utaona kwa kiasi gani kwamba dhamira ya kuwa na TARURA inaweza isifanikiwe katika Jimbo langu la Kilindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto hii naiona ipo katika maeneo mbalimbali. Kwa hiyo tuangalie namna ambavyo tunaweza kuwaongezea TARURA vitendea kazi tuwaongezee staff.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitofautiane kidogo na wazungumzaji wengine kwamba tuone chombo hiki kiende kwa Waheshimiwa Madiwani hili sikubaliani nalo, kwa sababu TARURA iko katika maeneo yetu ya Majimbo. Mheshimiwa Diwani anaweza kumwona Meneja wa TARURA akamweleza barabara yake, hata Mheshimiwa Mbunge anaweza akazungumza jambo hili. Kwa hiyo, sioni umuhimu wa kuipeleka chombo hichi katika chombo cha Madiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni zahanati. Ninamshukuru Ndugu yangu Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo kwamba tumepata shilingi milioni 500 kwa ajili ya kituo chetu cha afya Songe, niseme wazi kabisa nilikuwa miongoni mwa watu ambao niliomba kuwa na Hospitali ya Wilaya, lakini kwa sababu nimepata shilingi milioni 500 na zimeweza kwa kiasi kikubwa tumejenga majengo naomba tuongezewe shilingi milioni 500 nyingine ili ikiwezekana tuweze kupandisha hadhi Kituo cha Songe iwe ni Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linakwenda sambamba na suala la watumishi. Watumishi imekuwa changamoto sana, tumeona juzi tu watumishi wengi wameondolewa. Ushauri wangu kwa Waziri wa TAMISEMI na Ofisi ya Rais, Utumishi tuone namna ambavyo tunaweza tukawaajiri watumishi wa kada ya chini, huko ndiko kwenye watendaji wengi sana tuone namna gani zoezi hili ambalo limepita na lile la nyuma tuweze kuhakikisha kwamba mapengo haya ambayo yapo maeneo mengi yanafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, katika Jimbo langu la Wilaya ya Kilindi tunaupungu wa walimu 589, sekondari walimu 135, kada ya afya 320. Kwa hiyo, utaona uhitaji huu uko kila sehemu. Ninakuomba Mzee wangu Waziri wa Ofisi ya Rais, Utumishi waangalie namna gani wanaweza kupitia mahitaji haya katika Halmashauri zetu ili tuone kwamba huduma zile za wananchi zinakwenda vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo mchango wangu mwingine utaenda kwenye suala la utawala bora. Imejitokeza changamoto katika maeneo mbalimbali watumishi wengi wanakaimu, hili limekuwa ni tatizo kubwa sana. Mimi nina uzoefu kwa sababu nimefanya kazi Serikalini, zamani ilikuwa kwamba Katibu Mkuu akistaafu unajua kabisa ni nani anayefuata kuwa Katibu Mkuu, Mkurugenzi akistaafu unajua ni nani anafuata kuwa Mkurugenzi. Hii succession plan sasa hivi katika Serikali haipo na hii ndiyo inasababisha kwamba unamteua mtu anakaimu unamfanyia upekuzi kwa muda mrefu kwa sababu humfahamu. (Makofi)

Ninakuomba Katibu Mkuu Dkt. Ndumbaro wakae chini walitafakari hili, utaratibu wa succession plan urudi ili tuwe na uhakika kwamba Katibu Mkuu leo akistaafu tunajua nani anayefuata, badala ya kwenda kuchukua hapa na hapa ma-gap haya yanakuwa ni ya muda mrefu sana. Haya kwa kiasi fulani yana zorotesha utendaji wa Serikali kuanzia Serikali Kuu mpaka Halmashauri. Jambo hili ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo nirudi kwenye suala la huduma hizi za afya. Katika Jimbo langu la Wilaya ya Kilindi pamoja kwamba nimemsifia Mheshimiwa Waziri hapa kwamba amenipa shilingi milioni 500 kwa ajili ya Kituo cha Afya Songe, lakini vipo vituo mbalimbali katika Jimbo langu la Kilindi ambalo jiografia yake ni ngumu sana, nimuombe Mheshimiwa Selemani Jafo ikiwezekana zikipatikana fedha unitengee fedha kwenye vituo vifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya cha Jaila ambacho kina takribani watu 20,000, Kituo cha Afya Kwediboma kina takribani watu 50,000 na Kituo cha Afya cha Negero, wananchi wangu pamoja na Mbunge wao tumeshaweka majengo yameshakuwa ni makubwa sana, tunahitaji fedha za kumalizia, nitashukuru sana Mheshimiwa Waziri kama utapata fursa ya kuja kwenye Jimbo langu na kutembelea maeneo haya kwa sababu wananchi wa Wilaya ya Kilindi bado wana changamoto ya afya. Najua dhamira ya Serikali ni nzuri ya kuwasogezea huduma ya afya lakini katika eneo langu la Wilaya ya Kilindi tulikuwa tunaomba sana sasa maeneo niliyoyataja yaweze kujengewa vituo vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nipongeze japo kuwa halijaja suala hili dhamira ya Serikali ya kuwa na mamlaka kama chombo kama cha TARURA cha maji vijijini, hii itasaidia kwa kiasi kikubwa sana. Ni juzi tu nimeuliza swali juu ya miradi ya maji katika Jimbo langu la Wilaya ya Kilindi, kuna mapungufu hapa ya usimamizi wa miradi ya maji. Naomba watu wa TAMISEMI na Wizara ya Maji wawe na Tume maalum wale na Kamati maalum ya kufuatilia miradi hii wasisubiri mpaka Wabunge tuje tuzungumze Bungeni hapa au CAG aandike ripoti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa inapopelekwa katika maeneo yetu tuhakikishe kwamba inafuatiliwa, kwa sababu unapokuwa umeleta mradi halafu mradi ule haujakidhi viwango, mradi ule haojatoa matokeo yanayotarajiwa maana yake wanaoathirika ni wananchi wa maeneo husika na Serikali hairudishi tena pesa inachukua muda mrefu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kabisa Waziri wa TAMISEMI na Naibu Mawaziri wake wote wanafanya kazi kubwa sana, kwa sababu wanafanya ziara za mara kwa mara, jambo hili ni jema sana kwa sababu linasaidia Waheshimiwa Mawaziri kujua changamoto katika maeneo yetu na hii linafanywa na Mawaziri wengine pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kusema kwamba naonga mkono hoja na ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kunipa nafasi jioni ya leo niweze kusema machache juu ya hotuba ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Waziri, Mheshimiwa Profesa Mbarawa, Naibu Waziri wote wawili; ndugu yangu Mheshimiwa Nditiye pale na Mheshimiwa Kwandikwa wanafanya kazi kubwa sana. Namini kabisa Mheshimiwa Rais amechagua watu sahihi kwa ajili ya kumsaidia kazi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze Serikali hususan Wizara hii nimeona wametukumbuka juu ya barabara ya kutoka Handeni – Kibirashi – Kijungu - Nchemba

- Singida, ina kilometa 460. Barabara hii mara nyingi nimekuwa nikiizungumzia sana kwamba ina umuhimu mkubwa sana. Bahati nzuri kwamba barabara hii ndipo ambapo bomba la mafuta linalotoka Uganda hadi Tanga linapita. Nimeona wametutengea shilingi bilioni moja hapa, lakini niombe Waziri mwenye dhamana na uongozi mzima wa Wizara hii watutafutie pesa kwa sababu wanasema wanatafuta pesa lakini nasema watutafutie pesa wajenge barabara hii kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ukiacha suala la mafuta ina shughuli nyingi sana za kiuchumi kwa sababu inaunganisha mikoa minne kwa maana ya Mkoa wa Tanga, Manyara, Dodoma na Singida. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, afanye atakachoweza ahakikishe kwamba anatupatia pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ni kwamba barabara hii itakuwa na umuhimu kwa sababu upanuzi wa Bandari ya Tanga unakwenda sambamba na hilo. Kwa hiyo, mizigo ambayo itakwenda bandarini pale itatumia barabara hiyo, kwa hiyo, barabara hii ina umuhimu mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, naomba nizungumzie sana suala la reli ya kutoka Tanga – Moshi - Arusha - Musoma. Reli hii ni muhimu sana kwa sababu pia inalenga kuinua kipato cha nchi hii. Naamini kabisa hata mafuta yale yatakayokuwa yanakuja Bandari ya Tanga yataweza kutumia reli hii. Nimwombe Waziri mwenye dhamana ahakikishe kwamba wanaitengea kiasi cha pesa cha kutosha reli hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri kwa ndugu yangu Waziri mwenye dhamana. Nimeona Wabunge wengi wakisimama hapa kila mmoja anazungumzia kuhusu barabara, lakini naamini kabisa nchi hii ni kubwa sana kwa maana kwamba siyo rahisi kwa Serikali kutenga pesa kwa kila barabara. Najiuliza kwa nini tusitumie sekta binafsi kwa maana ya PPP (Public Private Partnership)?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali iweke mpango maalum ikiwezekana i-train watu wetu waje na taarifa hapa Bungeni namna gani hii PPP inaweza ikafanya kazi na siyo katika barabara peke yake, tunaweza kwenda pia katika maeneo mengine. Tumeona nchi nyingi duniani wametumia PPP katika kufanikisha maendeleo hususan katika sekta ya barabara. Naomba Waziri mwenye dhamana alichukue hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la pongezi. Nimeona barabara zangu nyingi sana za Wilaya ya Kilindi zimetengewa pesa. Kwa niaba ya Wanakilindi nawapongeza sana Waziri na Naibu Waziri kwa sababu naamini kabisa mazingira ya Jimbo langu la Kilindi kwa kweli yana changamoto nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nina ushauri, wale wakandarasi ambao huwa wanapewa tenda za kutengeneza barabara, kwa mfano barabara hii ambayo nimeizungumzia kipindi cha wiki nzima iliyopita magari hayakupita kwa sababu wakandarasi hawa wanapotengeneza barabara hawatengenezi mitaro, magari yanakwama. Kwa hiyo, naomba Wizara iwasimamie wakandarasi hawa wanapowapa tenda hizi wahakikishe kwamba wanatengeneza katika viwango vinavyokubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni mawasiliano. Mara nyingi nimewasiliana sana na ndugu yangu Mheshimiwa Nditiye pale kwamba Wilaya ya Kilindi hususan katika Kata za Sauji, Kilwa, Lwande, hazina mawasiliano kabisa. Nimeona kuna taarifa imepita hapa kwamba kupitia Mfuko wa Mawasiliano wataweza kutujengea minara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri jambo hili walichukue kwa sababu kuna maeneo ambayo kabisa wananchi hawana mawasiliano. Jambo hili ni muhimu na ni haki ya Watanzania Wanakilindi kuhakikisha kwamba wanapata mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni Mfuko huu wa Barabara. Mfuko wa Barabara ni muhimu sana, najua nilizungumzia kwenye TARURA lakini bado napenda nizungumzie kwamba Waziri mwenye dhamana lazima ahakikishe barabara hizi zinapitiwa mara kwa mara kwa sababu utengenezaji huu haukidhi viwango. Hili tumeona hata katika maeneo ya Mkoa huu wa Dodoma hapa, barabara nyingi haziko katika viwango vinavyotakiwa. Serikali inatenga pesa, ni lazima pesa hizo ziwe na thamani…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. OMARY M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uwezo wa kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu ili niweze kusema machache katika bajeti hii ya WIzara ya Mambo ya Ndani. Awali ya yote nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu wake pamoja na uongozi mzima wa Mambo ya Ndani kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba Jeshi la Polisi linafanya kazi kubwa sana. Sote Wabunge hapa katika Bunge hili tunakuja humu ndani na kutembea lakini amani na usalama wetu unategemea Jeshi la Polisi. Kwa hiyo, mtu mwenye akili timamu na busara ni lazima asifie Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kesi chache chache tu ambazo kwa kweli kama Wabunge ni lazima tuziseme na ni jukumu letu kama Wabunge tushauri pale ambapo pana changamoto hizo. Kwa hiyo, ni ukweli usiopingika kwamba Jeshi la Polisi linafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kuzungumza ni kulipongeza Jeshi la Polisi hususan Kitengo cha Magereza. Magereza wanafanya kazi nzuri sana hasa katika utekelezaji wa Sera ya Uchumi wa Viwanda.

Tumeona namna gani ambavyo wamefanya shughuli mbalimbali, mfano ni Karanga. Karanga wao wanatengeneza viatu, lakini tumeona katika hotuba hapa kwamba watu wa Jeshi la Magereza wanataka kuingia ubia na Mifuko ya Jamii kwenye Gereza la Mbigiri Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kuonesha kwamba Jeshi letu hususan Magereza na wao wako sambamba na Serikali yao kuonesha kwamba Sera ya Uchumi na Viwanda inakwenda vizuri zaidi. Hilo napongeza vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika hotuba hapa nimesoma, nimeona kwamba mfungwa kwa siku gharama yake ni Sh.1,300/=, kum-retain mfungwa mmoja Gerezani kwa maana gharama ya chakula. Nasema, hivi kweli Magereza hawawezi kujilisha wao wenyewe? Tunao wataalam Magerezani mle; wanaweza kujenga majumba. Kuna kitengo hapa cha ujenzi. Hivi kwa nini hao wasi-compete tender na wengine kwa ajili ya kujenga shule, hospitali na kadhalika? Hili linawezekana. Magereza wana nafasi kubwa sana ya kuchangia uchumi wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Kamanda wa Magereza, hebu tuifanye Magereza iwe ni Magereza ya kisasa, iwe na wataalam, wawe ni sehemu ya kuchangia maendeleo ya nchi hii; wasitegemee sana ruzuku ili na wao waweze kusogeza gurudumu la maendeleo mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha kuona hata baadhi ya Magereza, kwa mfano Ofisi za Magereza mikoani ziko katika hali mbaya sana. Nilipata fursa ya kwenda kwenye Ofisi ya Magereza Mkoa wa Tanga, nikawa najiuliza, hivi kweli hata kupiga rangi inahitaji ruzuku? Hii inachekesha sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri Mheshimiwa Waziri kwamba tujiwekee utaratibu kutumia Magereza, wafungwa wetu waweze kufanya ukarabati wa Magereza yetu na taasisi mbalimbali. Tunawapa watu binafsi lakini nadhani Magereza wana nafasi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuzungumzia juu ya changamoto ya ukosefu wa Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Kilindi. Mheshimiwa Waziri, nilizungumza hapa siku moja kwamba Wilaya ya Kilindi ina takriban miaka 13 toka imekuwa Wilaya. Wilaya yetu haina Kituo cha Polisi, tunatumia kama post tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri na IGP yuko hapa, afanye ziara kuja Kilindi, aangalie ambavyo hata OCD hana nyumba ya kukaa; OCCID watumishi hawana. Hivi inawezekanaje, Polisi huyu aweze kuhudumia watu katika mazingira magumu kama haya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, leo hii mahabusu pale hatuna. Leo mtu kama ana kesi pale inabidi apelekwe Handeni. Kutoka Kilindi hadi Handeni ni takriban kilometa 130. Maana yake tumewanyima haki wananchi hawa wa Kilindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, kwenye bajeti ijayo ahakikishe kwamba Wilaya ya Kilindi inatengewa kujengewa Kituo cha Polisi kwa sababu ni haki yao wananchi hawa kuwa na Kituo cha Polisi. Vile vile ni kwamba Wilaya ya Kilindi, tuna eneo takriban heka 100 ambazo tumetenga kwa ajili ya kujenga Gereza kwa sababu hatuna Gereza Wilaya ya Kilindi. Sasa eneo lile linaweza kutumika kwa ajili ya uzalishaji, pia litatupunguzia usumbufu wa kupeleka wananchi kutoka Kilindi kwenda Handeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo nimelizungumza mwaka 2017, nimeandika lakini namwomba Mheshimiwa Waziri, najua changamoto ziko nyingi, lakini nimeona hapa zimetengwa shilingi milioni 400 ambazo Mheshimiwa Rais aliahidi. Namwomba sasa kwamba nasi mwakani kama siyo mwaka huu tuweze kutengewa kujengewa Gereza na Mahakama katika Wilaya ya Kilindi. Hilo linawezekana kwa sababu tunao mafundi, tunao wafungwa ambao wamefungwa katika Magereza yetu haya, ni mafundi wazuri tu maana yake tunaweza kutumia pesa hizo hizo kuhakikisha kwamba tunapunguza gharama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumza ni suala la kulinda mipaka yetu. Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamezungumza hapa, lakini ni ukweli usiopingika kwamba haiwezekani watu wa Home Affairs wasifuatilie wageni wanaoingia katika mipaka yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ni kubwa, ni pana kwa hiyo lazima watu wa immigration wahakikishe kwamba wanatekeleza wajibu wao kwa kuhakikisha kwamba kama wageni wanaingia lazima wafuatilie. Ni kitu cha kushangaza sana kama mtu anaweza kuhojiwa juu ya uraia wake, unasema kwamba watu wanafuatiliwa. Hilo jambo haliwezekani. Ni wajibu wa Jeshi la Polisi kuhakikisha kwamba mipaka yetu inakuwa salama na watu hawaingii ovyo nchini kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo machache, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma katika Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2017
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuzungumza jioni ya leo. Kwa kweli ni jambo la kusikitisha sana kama kila mmoja wetu miongoni mwa sisi Wabunge anaweza kusimama tu na kutoa taarifa ambayo inaweza ikawa ina- distort nchi hii. Nchi hii ina wafadhili, nchi hii ina walipa kodi; unaposema 1.5 trillion imepotea, imetumika vibaya, maana yake unawafanya walipa kodi wasiweze kulipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli usiopingika ni kwamba Kamati za PAC na LAAC msingi wa kazi zao ni kupitia ripoti ya CAG. CAG ndio jicho la Kamati hizi mbili. Niwakumbushe wazungumzaji waliopita hapa kwamba Ripoti ya CAG inapopita, inapokuja kwenye Kamati zetu, tunapitia lakini pia tunawashirikisha Makatibu Wakuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la audit query ni suala la kawaida kabisa. Huwezi ukasema kwamba hoja hazitakuwepo. Tukumbuke kwamba suala la mifumo hii ni ya kawaida kabisa. Wamezungumza hapa ndugu zangu, baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya PAC, wanasema kwamba Hazina wanatumia excel. Haiingii akilini hata kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi ukajumuisha hesabu za Serikali za Mitaa, Serikali Kuu na mashirika kwa kutumia excel. Hii haiingii akilini hata kidogo. Narudia kusema tena kwamba ripoti ya CAG siyo conclusive. Maana yake ni kwamba bado kuna room ya kukaa na kuweka sawa. Ndiyo maana kwenye taarifa hii kuna sehemu kuna neno “reconciliation” na “adjustment.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tafsiri yake ni nini? Maana yake hoja ya CAG walikaa na watu wa Hazina. Sasa wapo Wajumbe hapa ambao hawakupata fursa ya kumsikiliza Accountant General kazungumza nini. Sasa kuna watu hapa wamefundishwa taarifa, ambao nawalaumu sana. Nadhani hili siyo jambo zuri. Mtu kuwa na weledi mkubwa wa mambo ya hesabu, usikubali kuchukua taarifa za mitaani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, limezungumziwa suala la shilingi bilioni 290, sheria inasema kwamba BoT wanaweza wakatoa 1.2 expenditure kwa Serikali kwa hiyo bado Serikali iliweza kutumia kiasi kidogo sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Zanzibar, mapato yale yanakusanywa na TRA Zanzibar, lakini ni lazima yaingie kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali lakini yanarudi Zanzibar. Ubaya uko wapi hapo? Sasa tukubaliane jambo moja; hebu tuweke utaratibu wa kutoruhusu kila mtu kuzungumza jinsi mtu anavyoona.

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe unazungumza taarifa ya CAG ambayo haijawa-verified, sisi tumemwona CAG hapa, amesema mwenyewe kwamba hakuna matumizi mabaya wala hakuna wizi. Suala la CAG yeye hagundui theft na fraud, anatoa opinion. Hawa wenzetu suala la wizi wamelitoa wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Mjumbe hapa kasema kwamba siyo 1.5 trillion, imekwenda mpaka trilioni mbili, atuambie ana ripoti nyingine ya CAG nyingine? Hilo naomba athibitishe, kwa sababu sisi tume-rely on Taarifa ya CAG, yeye taarifa ya shilingi trilioni mbili kaipata wapi? Huwezi uka-distort profession yako kwa sababu ya mambo ya kisiasa. Umeapa, lazima uwe mkweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani Wajumbe badala ya kuipitia taarifa vizuri na kuangalia maoni ya Kamati yetu, tumezungumza mambo mazuri sana. Serikali hii mambo yote ambayo hayako sawa yamezungumzwa kwenye taarifa hii, kwa nini wanang’ang’ania eneo ambalo tayari CAG ameshali-clear? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, labda nitoe ushauri mmoja, kama kuna Mjumbe ambaye bado ana wasiwasi, anaweza bado akamwomba CAG na utaratibu unaruhusu, lakini suala la 1.5 trillion tayari limeshafungwa page na halipo tena. Naomba msiwaaminishe Watanzania kuwa kuna wizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashangaa sana, wakati tunaandika ripoti hii tulikuwa pamoja na wenzetu. Walikuwa na nafasi ya kumwuliza CAG. Vile vile PST kwa maana ya Paymaster General, alikuja, kwa nini hawakumwuliza maswali hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikuthibitishie jambo moja; watumishi waliopo Wizara ya Fedha pale ni watu ambao ni very professional. Mhasibu Mkuu wa Serikali, Mhasibu Mkuu Msaidizi wa Serikali, wote ni CPA holders. Hiyo ni sambamba na watu wa CAG. (Makofi)

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusu Utaratibu.

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuanza kuhoji competence yao, nadhani siyo sahihi. Tukubaliane kabisa kwamba suala la kurekebisha mifumo ni sawasawa…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kigua subiri. Mheshimiwa Salome, kanuni inayovunjwa.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pengine labda niendelee kwa kusema maneno yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mahusiano kati ya Ofisi ya Bunge na CAG ni mazuri sana na Kamati za LAAC na PAC zimeweza kufanya kazi nzuri sana kwa kupitia Ofisi ya CAG. Tukubaliane kwamba hata katika utaratibu wetu wa Kamati hizi, pia watumishi wa CAG wakija pale huwa tunawapa challenge, umekagua hili; hili siyo sawa na hili siyo sawa. Huo ndiyo utaratibu wetu wa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapozungumzia suala la kutumia excel, nazungumza professionally kwamba haiwezekani kutumia excel kuweza ku-consolidate hesabu za Serikali nzima, haiwezekani. Pia na-refer majibu ya Accountant General kwamba hilo halijafanyika. Sasa haya ni mambo tu ya kawaida. Hizi zinaitwa hoja za ukaguzi na hoja za ukaguzi zipo kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kueleza eneo hilo, sasa nirudi kwenye suala la mikataba hasi ya NDC. Hapa tulijikita zaidi, tuliona ni eneo ambalo haliko vizuri, nadhani katika taarifa yetu ya Kamati hapa tumeelezea vizuri sana. Ushauri wangu kwa Serikali, kupitia kwa Attorney General pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, wapitie waangalie mikataba ya TANCOAL, haijakaa vizuri hata kidogo. Kwa sababu tunaiona dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kuhakikisha kwamba tunapata mapato, sasa inawezekana vipi kama una mikataba hasi? Maana yake gawio lile haliwezi kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nashauri sana, maeneo yote ambayo tumeainisha yahakikishwe kwamba yanafanyiwa kazi. Naamini kabisa kwamba taarifa hii, kwa sababu tumewashirikisha wenzetu wa upande wa pili, italeta mafanikio makubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, nashukuru sana. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mngu kwa kuweza kusimama leo tena leo jioni hii katika Bunge lako Tukufu niweze kuchangia kwenye hotuba mbili za Waheshimiwa Mawaziri waliopo. Nichukue fursa hii kwanza kuwapongeza Mawaziri wote wawili, nimpongeze Waziriwa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kaka yangu Jafo, lakini nimpongezee Mheshimiwa Mzee Mkuchika na Manaibu Waziri wote kwa kazi ambayo mnaifanya. (Makofi/)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa kwanza nianze eneo la TARURA, watu wamezungumza sana kuhusu TARURA. Natambua umuhimu waTARURA na katika Bunge hilihili ndipo tulipopitisha TARURA, lakini wapo ambao wanasimama hapa kusema kwamba TARURA sasa irudi tena kwa Madiwani. Naomba niseme kwamba TARURA ibaki kama ilivyo; pamoja na changamoto nyingi sana kuhusu TARURA, lakini ni ukweli usiopingika kwamba TARURA ikirudi kwa Waheshimiwa Madiwani kutakuwa kuna vurugu nyingi sana. Ushauri wangu ni nini kuhusu TARURA, ni kwamba wanakosa usimamizi wa kutosha, Meneja wa TARURA anasimamia barabara za halmashauri.(Makofi/)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nani anasimamia ubora wa kazi ya TARURA, hatuna chombo ambacho kinasimamia kazi za TARURA, namshauri Mheshimiwa Waziri na timu yake waangalie namna ambavyo TARURA wanaweza kusimamiwa. Nalisema hili kuna changamoto nyingi sana pamoja na upungufu wa bajeti, mathalani nizungumzie katika Jimbo langu la Kilindi, ambalo lina idadi ya barabara 139, kilometa 844, pesa ambayo tumetengewa ni shilingi bilioni moja na milioni mia moja sitini na tisa. Kiasi hiki hakitoshi, hebu fikiria barabara 139 unaweza kuzigawa vipi kwa kiasi hiki cha pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wazungumzaji wa mwanzo wamezungumzia kwamba tuongeze bajeti nami niungane nao kwamba tuchukue ile asilimia kumi kwenye TANROADS tuiongeze kwenye asilimia 30 iwe asilimia 40. Hii itasaidia kupunguza changamoto za TARURA. Nalisema hili kwa sababu Wabunge wanasimama hapa wanalalamika na niseme ukweli tu, kiasi hiki ambacho kimetengwa kwa ajili ya Jimbo la Kilindi hakitoshi. Tunamlaumu sana Meneja wa TARURA; lakini ukiangalia uhalisia wa pesa zilizotengwa ni ndogo sana. Hali halisi ya Jimbo langu la Kilindi ni mabonde na milima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenye kusema wamesema kwamba,ni heri uone mara moja kuliko kusikia mara 20. Mheshimiwa Naibu Waziri dada yangu Dkt. Mary Mwanjelwa amefika pale Kilindi, hata Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMIamefika ameiona Kilindi ilivyo, nyakati za mvua, magari hayapiti kule, mvua ni nyingi, lakini na barabara pia hazipitiki. Sasa tuone dhamira hii ya Serikali ya kuanzisha TARURA, basi iendane sambamba na maeneo husika, huwezi ukampa mtu mwenye barabara 139 na barabara zenye urefu wa kilometa 844 na mtu mwenye kilometa chache unakuwa hutendi haki.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,niiombe Serikali sana kwenye eneo hili watazame, wanao wataalam, wasikae maofisini, tunasimama hapa Waheshimiwa Wabunge kuyazungumza haya,wawe wanawatuma Maafisa wao waje kutembelea na kuona hali halisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo pengine nataka kulizungumzia pia ni eneo la huduma ya afya. Nimpongeze Waziri wa TAMISEMIna timu yakewamefanya kazi kubwa sana. Nitoe mfano mmoja tu kwenye Jimbo langu la Kilindi, Mheshimiwa Waziri ameweza kutoa pesa ya vituo vitatu vya afya; hili ni jambo kubwa sana sana. Eneo la Kilindi ni eneo pana, tuna vijiji 102, kata 21 bado vituo vya afya hivi ambavyo tumepata havitoshelezi; lakini wanasema asiyeshukuru kwa kidogo hata kikubwa hawezi kushukuru. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri katika hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nizungumzie suala la utawala bora, mzee wangu Mheshimiwa Mzee Mkuchika, nimpongeze sana baaada ya kuchaguliwa katika eneo hilo. Kulikuwa kuna kelele sana sana juu ya ugomvi wa Wenyeviti, Wabunge na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, lakini naona hali imetulia. Sasa naomba nijielekeze kwa mtazamo wangu mimi nini maana ya utawala bora, Serikali hii imejikita kuwaletea maendeleo wananchi, imeamua kujenga vituo vya afya 352, huo ni utawala bora. Unapoamua kujenga mradi kama wa Stiegler’s Gorge maana yake huo ni utawala bora, SGR ni utawala bora kwa sababu ungeweza kuchukua pesa hizo ukapeleka maeneo mengine, lakini Mheshimiwa Rais kwa sababu ana dhamira nzuri ya kuwapenda Watanzania ameamua kuwekeza kwenye miradi na hii lazima tukubaliane nao tu huu ni utawala bora, ni lazima tumsifie na tumpongeze Mheshimiwa Rais katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mmoja ana mtazamo wake katika hili; lakini naamini kabisa dhamira ya Serikali hii ya kuwekeza katika miradi mikubwa, dhamira ya Serikali hii ya kupeleka umeme vijijini ni utawala bora, kwa hiyo ni lazima tuipongeze Serikali katika hili na naamini ipo siku Watanzania watakumbuka dhamira ya Mheshimiwa kwamba atakuwa ni Rais anayesimamia utawala bora na sisi kama Wabunge wa Chama cha Mapinduzi tuko pamoja na yeye.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia kwenye utawala bora ni suala la eneo la utawala. Mzee wetu Mkuchika ameshawahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mkoa wa Tanga ni mkoa pekee ambao una halmashauri 11, Mkoa wa Tanga una shule za msingi 1028, lakini ipo baadhi ya mikoa ina halmashauri chache sana. Nimemsikia Mheshimiwa Rais juzi akisema kwamba hawezi kuongeza maeneo ya utawala, lakini sasa lazima tutazame,kama hatuongezi eneo la utawala, tufanye nini ili kwenda sambamba na maeneo makubwa kama haya? Lazima tuhakikishe kwamba resources zile ambazo ni chache tupeleke kwenye maeneo haya ambayo ni makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu leo tuchukulie mfano, Afisa Elimu wa Mkoa wa Tanga ambaye shule za msingi tu ni 1,022, lakini baadhi ya Mkoa wana shule za msingi 177, unawezaje kufanya tathmini kwa watu hawa wawili, hapo hakuna usawa hata kidogo. Nashauri tuangalie namna ambavyo maeneo ambayo ni mapana kwa utawala tuhakikishe kwamba resourceszinakuwa za kutosha.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kusema nikuhusu watumishi kukaimu. Hili kwa kweli halijakaa vizuri sana. Mimi kama Mjumbe wa Kamati ya PAC mara nyingi tumekutana na Wakurugenzi, wanakaimu mwaka mzima, miezi sita, hivi unawezaje kufanya upekuzi kwa miezi sita, nchi hii hii, Tanzania hii hii. Namwomba Mheshimiwa Waziri, najua watu hawa wako chini ya Ofisi yake Mheshimiwa Mzee Mkuchika, hebu tuangalie kamahawana weledi katika hili, tuangalie namna ya kuwapa mafunzo ili suala la kukaimu lisichukue muda mrefu sana. Kuna umuhimu wa mtu kukaimu kwa muda mfupi, unapomkaimisha mtu kwa muda mrefu, kwanza unampotezea confidence, uwezo wa kufanya kazi unakuwa haupo kwa sababu hana uhakika na nafasi aliyopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,nishauri katika dhana ya utawala bora ni pamoja na mtu kutokaimu muda mrefu. Hii nadhani nilikwishazungumza awali kwamba zamani tulikuwa na utaratibu wa succession plan, yaani leo Mkurugenzi anastaafu tayari tunajua nani atachukua nafasi yake. Sasa haiwezekani unastaafu leo, miezi sita ijayo ndiyo unaanza kumtafuta mbadala wake. Ningependa kusema kwamba hebu tuliangalie hili kwa sura nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo, naomba kusema kwamba naunga mkono hoja zote za Waheshimiwa Mawaziri wawili. Ahsante sana.(Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kupata fursa ya kusimama leo kuweza kuchangia katika Hotuba ya Wizara ya Mambo ya Ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Maafisa wote wa Wizara ya Mambo ya Ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba Wizara hii ina changamoto nyingi sana lakini lazima tukiri kwamba kuna kazi kubwa inafanyika na lazima tuwapongeze. Nayasema haya kwa sababu Watanzania ni mashahidi wameona kwa kiasi kikubwa kwamba ajali na uhalifu umepungua kwa kiasi kikubwa sana. Zamani tulikuwa tunashuhudia uhalifu unafanyika katikati ya Dar es Salaam pale Kariakoo lakini sasa hivi hali hiyo imepungua. Ni lazima tulipongeze Jeshi la Polisi katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimponeze Waziri, Naibu Waziri na Wizara kwa ujumla kwa jitihada kubwa ambazo wanachukua kuhakikisha kwamba wanajenga vituo vya polisi pamoja na magereza. Changamoto ni kubwa kila maeneo, hususan wa wilaya mpya. Binafsi nikushukuru Mheshimiwa Waziri, tumepata shilingi milioni 150 kwa ajili ya kujenga nyumba za Polisi Wilaya ya Kilindi. Bado tuna changamoto ya kituo cha kisasa, wilaya ile ni ya muda mrefu, toka 2002 hatuna kituo cha kisasa. Naibu Waziri ni shahidi alifika Kilindi, nikuombe Mheshimiwa Waziri muiangalie Wilaya ya Kilindi tuwe na Kituo cha kisasa cha Polisi, vituo vya kata vilivyobaki tutajenga sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Katika ukurasa wa 57 umezungumzia Vitambulisho vya Taifa. Hapa pana shida kwa sababu zoezi hili linakwenda taratibu sana. Juzi tumepata taarifa kwamba kuanzia tarehe 1 Mei kila aliye na Kitambulisho cha Taifa ndiye atakayesajiliwa laini, sasa hili ni tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Wizara ya Mambo ya Ndani iliingia mkataba na Kampuni inaitwa Iris Corporation Berhad ya Malaysia, ilisainiwa Septemba, 2014 na ulikuwa unakwenda hadi 2016 lakini wakaongezewa tena mkataba hadi Septemba, 2018. Jambo hili ni lazima tuseme kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani lazima mlifanyie kazi. Vitambulisho vya Taifa ni haki ya msingi na ni lazima muongeze speed mhakikishe kwamba vitambulisho vinapatikana katika ngazi ya vijiji hadi mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili kwa sababu tunapata malalamiko kutoka vijijini huko kwamba vitambulisho hivi bado. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri lisimamie hili ili Watanzania waweze kupata vitambulisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie juu ya ujenzi wa vituo vya polisi. Nimezungumzia Kituo cha Polisi Kilindi hapa lakini kulikuwa na utaratibu au mkataba na Kampuni ya STAKA ambao walitakiwa kujenga vituo vya Polisi Tanzania nzima. Sasa hapa pametokea changamoto japokuwa naipongeza Serikali iliweza kuchukua hatua kwa wale ambao hawakuweza kutekeleza majukumu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, moja ya mapungufu makubwa katika mkataba huu ni kwamba ujenzi wa vituo hivi ulikuwa chini ya kiwango lakini pia waliweza kubadili mipango ya ujenzi. Mahali pengine ni kwamba hapakuwa na mikataba ya ujenzi. Nitoe mfano mmoja tu, ujenzi wa Kituo cha Polisi katika Wilaya ya Lushoto kwa Mheshimiwa Shangazi ambao uligharimu takribani milioni 500 haukwenda sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nakuamini sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na uongozi mzima pamoja na Katibu Mkuu, nina imani pamoja na mapungufu yote haya yaliyofanyika basi wale ambao hawakutekeleza wajibu wao ipasavyo lazima wachukuliwe hatua. Fedha za umma lazima zifanyiwe kazi, haiwezekani pesa zitolewe labda na wadau halafu watu wafanye ndivyo sivyo. Mimi naamini kabisa Mheshimiwa Waziri ulishakuwa Polisi, majukumu haya unayajua vizuri na Katibu Mkuu na viongozi wote wataweza kusimamia vizuri eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kulizungumzia ni suala la kisera zaidi kwa sababu naiona Wizara hii ni kubwa sana. Afisa Masuuli ambaye ndiyo mwenye wajibu wa kusimamia fedha za umma ana maeneo makubwa sana ya kusimamia. Hili siyo la kwako Waziri, ni suala la Serikali kuliangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuchukue mfano mdogo tu, tuichukulie NIDA yenyewe ambayo inasimamia Vitambulisho vya Taifa, Jeshi la Magereza, Uhamiaji, Zimamoto na Polisi, Katibu Mkuu ni mmoja tu, anaweza vipi ku-manage? Hebu naomba Waheshimiwa Wabunge na Serikali kwa ujumla tuangalie namna ya kufanya restructuring ya Wizara hii. Kwa sababu ukiangalia NIDA yenyewe na hizi taasisi ni takribani Wizara tano. Mimi nadhani wakati umefika tukupunguzie lawama na malalamiko ili Serikali iweze kufanya vizuri katika maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, pengine niseme tu kwamba kuna mambo ambayo kwa kweli si Polisi wote ambao siyo waadilifu. Kuna tukio moja limetokea Wilaya ya Kilindi, nina Mzee wangu mmoja ambaye yeye amenunua gari kupitia mnada na Mheshimiwa Waziri unalifahamu vizuri sana hili. Cha kushangaza ni kwamba baada ya kununua kwenye mnada yule Mzee amenyang’anywa gari. Mzee yule miaka karibia 40 ametafuta pesa kanunua gari lakini amenyang’anywa. Suala hili liko kwenye Wizara yako, nisingependa kutoa maelezo marefu, naomba wale ambao wanashughulikia suala hili walishughulikie kwa dhati kabisa wampe huyu Mzee haki yake kwa sababu kama mtu ni mhalifu lazima afikishwe kwenye vyombo vya sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo machache, nakushukuru sana, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru na mimi kunipa nafasi niweze kuchangia Wizara ya Maji leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Waziri wa Maji Prof. Mbarawa, Naibu Waziri mdogo wangu Mheshimiwa Aweso na viongozi wote wa Wizara ya Maji kwa jinsi wanavyopambana kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisikiliza mdahalo huu toka tumeanza majuzi utaona kwamba kilio kikubwa cha Wabunge ni juu ya changamoto ya miradi ya Maji ambayo haikamiliki. Mimi binafsi najiuliza, tatizo liko wapi kwa sababu ingekuwa hakuna tatizo Wabunge wasingekuwa wanalalamika juu ya miradi yetu,

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa sababu katika hotuba yake amekuwa mkweli sana kwa kuainisha changamoto za Wizara hii. Ziko changamoto kama nne hivi, mojawapo ni upatikanaji wa fedha. Mimi hii siwezi kumlaumu Mheshimiwa Waziri, hata kidogo, kwa sababu mambo mengine ni ya kiserikali zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie zaidi changamoto namba mbili ambayo inasema uwezo mdogo katika usimamizi wa miradi. Hapa ndipo kwenye tatizo na lazima nikubali na tukubaliane kwamba hapa pana syndicate, kuanzia Halmashauri mpaka Mikoani. Wahandisi hawa tunaowapa miradi, mimi Mheshimiwa Waziri nikuombe sana, nimeona pana mabadiliko katika Wizara pale lakini hili zoezi lazima liende mbali zaidi ikiwezekana unda timu ndogo ianzie kwenye malalamiko ya Waheshimiwa Wabunge hapa kwamba kwa nini miradi inalalamikiwa, kwa nini kuna ufisadi kwenye miradi, utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuweza kujua sababu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano mmoja tu na nitamwomba Mheshimiwa Waziri na timu yake watafute ripoti moja tu ya CAG ambayo inahusu performance audit kwenye miradi ya maji. Ukiipitia taarifa moja utapata picha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kuanzisha RUWASA kwamba ma-engineer wale wa Halamashauri moja kwa moja watawajibika Wizarani lakini inawezekana ikawa ni mvinyo wa zamani kwenye chupa mpya. Watu ni walewale na utaratibu ni uleule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana hapa aliyekuwa Waziri wa Maji alianzisha utaratibu wa kufuatilia miradi ya maji kwa kutembelea Tanzania nzima kuangalia status ya miradi ya maji. Kuonyesha pana syndicate kubwa, siku moja wakati Wizara imeitwa kwenye Kamati ya PAC nilimwambia Katibu Mkuu Profesa kwamba vijana wako hawakufika Kilindi na maafisa pale Kilindi wakasema hawa tumekutana nao Handeni tu, hawakufika. Kwa hiyo, taarifa kuhusu miradi ya maji Kilindi ni ya uongo. Hii ndiyo kuonyesha kwamba pana syndicate kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amefanya ziara Jimboni Kilindi alijionea hali halisi ya changamoto ya maji na nikakuomba kwamba Kilindi haitofautiani na Handeni Vijijini na Handeni Mjini, wao wamefaidika na mradi wa HTM sasa huwa mbapa leo najiuliza hao wataalamu ambao walisema kwamba mradi wa maji ufike Handeni ambayo ina changamoto sawa kabisa na Wilaya ya Kilindi, hivi hawakuiona Kilindi? Hayo tuyaache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimwambia Mheshimiwa Waziri tunahitaji mradi mkubwa unaofanana na HTM kwa sababu Wilaya ya Kilindi tuna vijiji 102 na vitongoji 615 ni vijiji 30 tu kati ya 102 vyenye maji. Ili tuweze kupata suluhu ya kudumu ya maji lazima tupate mradi mkubwa kuanzia Mto Pangani ambao uko Korogwe sawa na ambavyo watu wa Handeni wanapata. Hii itakuwa ni suluhu ya kudumu Wilaya ya Kilindi kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri uliangalie hili, najua kwa bajeti ya mwaka huu haiwezekani lakini kwa mwakani ututazame kwa jicho la tatu kwa sababu wananchi wa Wilaya ya Kilindi wana changamoto kubwa sana ya maji. Nadhani nilikuambia jambo hili, naomba nikukumbushe kupitia hotuba hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nilikumbusha kwamba Serikali ilitoa fedha kwa ajili ya mradi mkubwa wa vijiji vitatu, Vijiji vya Mtakuja na Nyamaleli lakini mpaka leo Mheshimiwa Waziri havitoi maji na uliahidi utafanya ziara kwenda kuangalia inakuwaje Serikali itoe fedha za kutosha lakini hakuna hata tone la maji ambalo linatoka pale. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri uweze kulifanyia kazi suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, Mheshimiwa Waziri, naomba nizungumzie namna ambavyo hizi mamlaka ndogondogo ambazo huwa hazina uwezo wa kusimamaia miradi, mathalani Kilindi na Miji mingine midogo unakuta Tanga UWASA wao wanasimamia mradi wa Kilindi, Muheza, Handeni, hii ina changamoto kubwa sana Mheshimiwa, changamoto yake ni kwamba unakuta kwamba miradi hii inakuwa ni mingi watu wa Tanga UWASA hawawezi kusimamia miradi yote kwa pamoja wakati mwingine unakuta kwamba Mhandisi au Mkandarasi analalamika kwamba watu wa Tanga UWASA hawajafika kwenye site, ni jambo zuri kabisa Mheshimiwa Waziri kwa sababu mamlaka yetu haina uwezo au mamlaka hizi za wilaya nyingine hazina uwezo, lakini lazima tutazame na namna nyingine ya kusimamia ili miradi hii iweze kwenda kwa speed nzuri sana, nilikuwa naomba Mheshimiwa utazame hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine linakuja pale pale kuhusu miradi hii kuna mradi huu Mheshimiwa Waziri wa Maji wa Jiji la Arusha ambao Serikali imepata mkopo kutoka ADB African Development Bank, ni mkopo wa dola bilioni 233.9, ukizi-covert hizi ni takribani milioni 530. Lakini nikuambie mradi ule haujakaa sawa unakwenda taratibu sana, nakuomba Mheshimiwa Waziri tupia jicho pale tusisubiri ripoti ya CAG ije iseme kwamba mradi ule una ufisadi. Na mimi Mheshimiwa Waziri nakuomba sana hebu katika Wizara yako anzisha kitengo cha ufuatiliaji cha tathimini na ufuatiliaji Monitory and evaluation itakusaidia sana Mheshimiwa Waziri kujua status ya miradi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wabunge huku tunapata mengi sana Mheshimiwa na sisi tunapozungumza hapa yapo mengi tunayasikia mradi huu wa Jiji la Arusha uangalie sana haupo katika taswira nzuri, Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla wameona kwamba Jiji lile ni Jiji la utalii lazima maji ya uhakika lakini mambo hayaendi vizuri, mimi nakuomba sana litazame hili utapata uhalisia wa kitu hichi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho Mheshimiwa waziri nikuombe tena ulituhaidi kutuchimbia bwawa la kisasa kwenye Kata ya Mafisa ni eneo ambalo takribani miaka 50 wananchi wale hawajawahi kupata maji, nikushukuru sana ulitupatia visima vitano, lakini kwa hali halisi ya eneo lile ni kwamba maji hayapatikani suluhu ya kudumu ya kupata maji pale ni kuchimba bwawa la kisasa kabisa katika Kata ya Mafisa ambayo ina takribani wakazi 18.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri ulitazame hilo. Pia nikuombe tunayo Kata ya Tunguli ambayo ina wakazi takribani 10,000 sasa kuna mradi wa Kata ya Kibati ambao upo katika Wilaya ya Mvomero, ni karibia ni kilometa kumi tu. Nikuombe utume wataalamu wako waweze kuangalia namna waweze kutupatia maji sisi kutokea Wilaya ya Kilombero itaweza kutusaidia kwa sababu tuna vijiji vingi sana ukiangalia kwa asilimia maana yake vijiji 30 kati ya vijiji 102 ina maana ni asilimia 20 au 30 tu ya wakazi wa Wilaya ya Kilindi ndiyo wanaopata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Waziri, nipongeze Taasisi hizi ambazo sizo za Kiserikali kwa kuna watu wa World Vision, AMREF, wao wamekuwa ni wadau wazuri sana, wametusaidia sana kuchimba visima kwa kweli tuwapongeze katika hili. Baada ya kusema hayo mimi naomba nikupongeze Mheshimiwa Waziri nikupe moyo sana, nasema naunga mkono asilimia, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya jioni ya leo nami niweze kusema machache juu ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Manaibu Waziri wote wawili kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kuchangia nataka nitoe somo dogo tu, dhana ya uwekezaji katika miradi mikubwa. Serikali imedhamiria kujenga SGR. Huu ni mradi mkubwa sana. Sasa wapo waliozungumza kwamba wanatarajia mafanikio ya muda mfupi. Huu ni mradi mkubwa sana ambao return yake itapatikana baada ya miaka 50 ijayo. Ku-recoup costs zake au payback period ni zaidi ya miaka 20. Kwa hiyo, usitarajie kwamba faida utaipata kwa muda mfupi, lakini lazima tuangalie multiplier effect ya mradi huu. Huwezi ukajenga SGR kwa sababu ya kubeba abiria peke yake, hapana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Tanzania tunapakana na nchi ambazo hazina bahari; Uganda, Burundi na Rwanda. Tunatarajia SGR ndiyo ambayo itakayoweza kupeleka mizigo huko. Kwa hiyo, lazima tutarajie mafaniko makubwa sana kutokana na mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna mtu amesema hapa kwamba suala la mradi huu halina kitu kinaitwa local context, siyo kweli hata kidogo. Naomba nithibitishe kwamba SGR ina mafanikio makubwa sana. Nitataja machache tu eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, SGR itakapokamilika, tunatarajia viwanda vyetu vya cement vya ndani vitaweza kuzalisha takribani mifuko milioni 110.2. Vilevile tunatarajia viwanda vyetu vya ndani, vitaweza kuzalisha nondo tani 115,000. Kama hiyo haitoshi, viwanda vya kokoto vitatoa mita milioni 2.7. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni suala la ajira. Ajira mpaka sasa hivi, kutokana na SGR ni takribani watu 9,639 wamepata ajira. Hii ni dhana ya local context kwenye SGR. Kwa hiyo, mtu asipotoshe kusema kwamba SGR katika suala la local context haijazingatiwa. Siyo kweli hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utangulizi huo, sasa naomba nizungumzie suala lingine la ATCL. Umuhimu ni mkubwa sana sana. Narudia kusema kwamba faida ya ATCL au katika mambo ya ndege huwezi ukaiona moja kwa moja na wala usitegemee kwamba ATCL irekodi profit katika muda mfupi. Hata Mashirika yale kwa mfano, Rwanda Airlines, Ethiopian Airlines, hawajawahi kurekodi profit hata siku moja, lakini kuna suala la multiplier effect, hili lazima lizingatiwe na umuhimu wa jambo hili ni mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo sasa naomba nirudi kwenye barabara ambayo inaunganisha Mikoa minne. Barabara hii ni muhimu sana, nayo ni barabara ambayo ipo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Barabara hii ina kilometa 460 ya kuanzia Handeni, Kibirashi, Kibaya na Singida. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei kwa sababu hili ni suala la kitaalamu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unapofanya investment…

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, unapofanya investment maana yake, return yake hutarajii kupata kwa muda mfupi na maana yake SGR hii faida yake itakuwa kwetu sisi na vizazi vijavyo.

T A A R I F A

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei kwa sababu hajataja source ya taarifa ni wapi.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

WABUNGE FULANI: Endelea.

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee.

MHE. ALLY SALEH ALLY: Reuters, Reuters Financial. (Kicheko)

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie barabara hii ambayo nimesema ni barabara ya Handeni – Kiberashi - Kibaya na Singida. Barabara hii ni muhimu sana. Kama katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri alivyosema kwamba barabara hii ndiyo ambapo bomba la mafuta litapita, nami nataka niseme kwamba pamoja na kwamba bomba la mafuta kutoka Uganda kwenda Tanga litapita katika eneo hili, pia barabara hii ina umuhimu mwingine ambapo watu wa mikoa hii minne niliyoitaja wanahitaji barabara hii sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri ametenga kiasi cha shilingi 1,450,000,000/=, namshukuru sana na ninampongeza katika hilo. Namwomba Mheshimiwa Waziri, barabara hii ni muhimu sana, sana, sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba Serikali ya Tanzania imetenga kiasi hicho nilichokitaja, lakini naomba tuangalie namna ambavyo inaweza kujengwa kwa kiwango cha lami, kwa sababu eneo hili ambalo barabara hii inapita, ina uzalishaji mkubwa sana, sana, sana; na ukizingatia kwamba kuna matarajio ya kutengeneza Bandari ya Tanga, kwa hiyo, ni matumaini yangu kwamba barabara hii ikitengenezwa kwa kiwango cha lami, basi mizigo yote ambayo inatoka Tanga kwenda Magharibi huko itapita katika barabara hii. Nina imani kwamba Mheshimiwa Waziri atazingatia katika hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine naomba nizungumzie huku minara. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwamba Wilaya ya Kilindi ni miongoni mwa maeneo ambayo yamepata minara mingi sana, lakini lipo eneo moja ambalo linapakana na Wilaya ya Simanjiro, Kata ya Saunye, haijapata minara. Naomba sana Mheshimiwa Waziri kupitia Mfuko huu wa Mawasiliano wahakikishe kwamba Kata hiyo inapata mawasiliano kwa sababu ni eneo muhimu sana, ni eneo ambalo lina mbuga ya utalii, lakini maeneo haya hayasikiki kabisa. Ni matumaini yangu kwamba Serikali itasikia tuweze kupata mawasiliano katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo machache, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema, ambaye ameniwezesha kusimama leo kuweza kuchangia bajeti iliyoko mbele yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, maendeleo siyo upepo. Upepo huwa hauonekani, lakini yakifanyika mambo ambayo yana maslahi mapana na wananchi wa Tanzania na watu wanaona, hatuna budi kupongeza. Naomba tuipongeze Serikali katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo vibaya kupongeza kwa mambo ambayo yanaonekana. Nitoe mfano mdogo tu, hapa katika Mkoa wa Dodoma ambao sisi Waheshimiwa Wabunge tupo. Leo hii Dodoma imebadilika sana; ukipita mitaani, barabarani huko unaona mabadiliko. Ila katika maeneo yetu tunakotoka tunaona namna ambavyo vituo vya afya, barabara, majengo ya shule yanavyokwenda. Sasa siyo vibaya hata kidogo Mheshimiwa Mbunge anaposimama na kuanza kusifia. Nadhani ni wajibu wetu Wabunge kuweza kusema yale mazuri ambayo yamefanywa na Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri, imesheheneza mambo mengi sana. Imegusa kila eneo na hususan mambo ambayo yanagusa wananchi. Tukianzia kwenye Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya, yote yameonyeshwa hapa. Mimi nina ushauri ambao naomba Mheshimiwa Waziri auchukue.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni Mjumbe wa Kamati ya PAC na nilipata bahati ya kutembelea baadhi ya Hospitali za Wilaya ambayo Serikali ilitoa shilingi 1,500,000,000/=. Moja ya changamoto ambayo niliishuhudia na ni jirani tu hapa kwenye Hospitali ya Mtera; tuliona hospitali ile imejengwa kwa force account, jambo ambalo ni zuri kabisa, gharama ilikuwa ni ndogo, lakini kuna baandi ya mambo ambayo hayakuzingatiwa na pengine kama yangezingatiwa leo hii Hospitali hizo za Wilaya zingekuwa zimemaliza kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mmoja ni kwamba katika majengo yale hatukuzingatia nyumba za Madaktari, nyumba za kuweka maiti (Mortuary). Naomba sasa, maeneo yale ambayo yana Hospitali za Wilaya angalieni maeneo haya, hatuwezi kuwa na Hospitali ya Wilaya bila kuwa na Hospitali ya Mganga. Hili ni jambo la kuzingatia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia na nyumba za wahudumu ni jambo ambalo tulitakiwa tulizingatie. Kama Serikali Kuu hatuwezi kutoa fedha, basi tuangalie namna ambavyo Halmashauri zetu zinaweza zikatoa fedha ili Hospitali ya Wilaya ikikamilika, basi na nyumba za wahudumu ziweze kupatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo napenda kulizungumzia ni suala la TARURA. Mwaka huu maeneo mengi Tanzania yamepata mvua za kutosha. Nichukulie mfano katika Wilaya yangu ya Kilindi mvua zilianza mwezi wa Kumi hadi leo hii, mvua zinaendelea kunyesha. Mvua ni baraka kwa Watanzania na mvua ni baraka kwa wakulima, lakini pia zimeharibu sana miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Waziri mwenye dhamana kupitia TARURA, hebu angalieni maeneo ambayo mvua zimekuwa nyingi sana. Timu zipite kwenda kuangalia kwa sababu wakulima hawa watapata mazao ya kutosha, lakini mazao haya yatapita wapi kama barabara zitakuwa hazipitiki? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano mmoja. Ni kwamba nina barabara kubwa ambazo takribani miezi mitano sasa hivi hazipitiki. Kuna barabara ya Kwinji - Muungano hadi Kilindi Asilia. Ni eneo ambalo lina uzalishaji mkubwa sana, lakini ni eneo ambalo hata pikipiki haipitiki. Mheshimiwa Waziri aliniahidi akaniambia kwamba timu yako itapita Wilaya ya Kilindi kufanya tathmini kuona maeneo ambayo yameharibika. Hadi leo nazungumza hapa ni kwamba watu wake hawajafika. Namwomba Mheshimiwa Waziri kwa heshima kubwa sana, najua Mheshimiwa Waziri ni msikivu, najua Serikali inasikia, maeneo hayo ambayo nimeyataja yaweze kupitiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo eneo lingine ambalo pia ni muhimu sana, ni barabara ambayo inaunganisha Wilaya ya Kilindi na Simanjiro kwenye Kata Saunyi. Pia ni miezi sita haipitiki. Barabara hii ni muhimu sana kwa sababu ina pori tengefu la Handeni, ni pori ambalo lina wanyama sana na eneo la utalii. Namwomba Mheshimiwa Waziri tuangalie namna ambavyo barabara hizi ni za kutengenezwa ili ziweze kupitika.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni kwamba nilibahatika mwezi wa Tatu mwaka 2020, Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya ziara kwenye Jimbo langu la Kilindi. Katika maeneo ambayo alipita ilikuwa ni kwenye Kata ya Kwediboma ambayo Mheshimiwa Waziri alitupatia shilingi milioni 300. Ni kweli kabisa kwamba fedha zile zimefanya kazi nzuri lakini kituo kile hakijakamilika. Bahati mbaya zaidi, Wilaya ya Kilindi ina Vijiji 102, Vitongoji 611, Tarafa nne tuna Kituo cha Afya kimoja tu ambacho kinafanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, hebu tuongezewe shilingi milioni 200 ili Kituo cha Afya cha kwenye boma kiweze kufanya kazi. Kama hiyo haitoshi, tuna Tarafa na Kata ya Tungule ambayo ina umbali takribani kilometa 200 wananchi hawa ili waweze kufika Kituo cha Afya cha Songwe ambayo ni Makao Makuu ya Wilaya, ni umbali wa kilometa 240.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani kuna umuhimu wa hali ya juu sana kwamba Kata ya Tungule ambayo iko karibu kabisa na Wilaya ya Gairo tuweze kupatikwa Kituo cha Afya. Kwa mawazo yangu ukiniuliza, nitakwambia Vituo vya Afya ni bora zaidi kwa sababu vikijengwa katika ubora unaotakiwa kama ambavyo tunaona vilivyojengwa sasa hivi, tuna uhakika kabisa wa kuwasogezea wananchi huduma hii badala ya kujenga Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, japokuwa sipingi kwamba Hospitali ya Wilaya ina umuhimu, lakini kwangu mimi ukiniuliza Mbunge wa Wilaya ya Kilindi, nahitaji zaidi Vituo vya Afya kwa sababu ndivyo ambavyo vinaweza vikahudumia wananchi wangu na kuweza kufika kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni ushauri juu ya watumishi katika Halmashauri zetu. Imejengeka kwamba watumishi wanatakiwa waweze kuhama baada ya kufikisha miaka mitano au sita, lakini kuna baadhi ya watumishi katika baadhi ya Halmashauri zetu wanakaa miaka hadi 20. Jambo hili halina afya hata kidogo. Halina afya kwa sababu wakati mwingine halimfanyi mtumishi aweze kufanya kazi wala kujifunza mambo mapya. Namwomba Mheshimiwa Waziri; angalia, pitia Halmashauri zako zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa mfano katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, tuna watumishi wamekaa miaka 18 mpaka 20 wilaya hiyo hiyo. Watumishi hawa hawajifunzi jambo lolote lile, hawapati changamoto mpya hususan katika sekta ya elimu. Wakati mwingine unaona kwamba elimu katika baadhi ya maeneo yetu, ufaulu wa wanafunzi hauendi sawa, kwa sababu mwalimu amekaa shule moja miaka 15 mpaka 20 hajajifunza jambo, anaona mazingira ni yale yale. Nashauri sana, namwomba sana hebu aliangalie katika mtazamo ambao unaweza kutusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine namwomba Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI aangalie namna ambavyo force account inatumika. Force account ni nzuri lakini nadhani elimu haijaenda sawa sawa hususan kwa Wakurugenzi. Na sisi kama Wabunge tunao wajibu wa kueleza nini dhana ya force account, kwa sababu force account inatakiwa isaidie kupunguza gharama, lakini wananchi wanakuwa hawaielewi force account.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hili pengine utengenezwe waraka maalum uende kwa Wakurugenzi waweze kuelezwa nini dhana ya force account kwa sababu wananchi hawaelewi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele ya pili imeshagonga.

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana, shukrani. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa mwanzo kabisa kwenye suala la Waheshimiwa au mashahidi kwenye jambo ambalo liko mbele yetu hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mjumbe wa Kamati hii kwa muda mrefu kidogo. Kwa uhakika naweza kusema kwa uzoefu mdogo ambao nilikuwa nao katika Kamati hii nimeshuhudia vituko vya ajabu kabisa kabisa.

Mheshimiwa Spika, Kamati yako inafanya kazi kwa mujibu wa taratibu na kanuni ambazo tumezitunga sisi wenyewe Wabunge na tunategemea kabisa wewe kama Mbunge umeaminiwa na wananchi na siyo Mbunge tu wa Jimbo ni Mbunge wa Tanzania nzima. Mwenendo wako, kauli zako, tabia zako lazima zifanane na nafasi uliyopewa. Kwa hiyo, siku zote unapozungumza lazima utafakari wewe ni nani? Unazungumza na akina nani? Hayo ndiyo yatakayokusaidia kuepuka haya ambayo leo tunayazungumza mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikianza na shahidi namba moja, ndugu yetu Mheshimiwa Josephat Gwajima, mimi namuita ni shahidi kwa mujibu wa taratibu tulizojiwekea. Hakika hakuitendea haki hata mara moja Kamati hii, hakuwa na nidhamu, hakuwa na heshima hata mara moja, hata ujio wake mbele ya Kamati ilikuwa inaonyesha dhahiri kabisa kwamba alikuja kwa kejeli na dharau iliyopitiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitoe mfano mmoja tu, tulipomuuliza ni wapi unapotenganisha shughuli za Kanisa na shughuli za Ubunge hakuweza kutoa jibu la moja kwa moja, hakuwa na jibu. Aliiambia Kamati kwamba anazungumza na waumini wake kwenye Makanisa zaidi ya 140 duniani. Tulipomuuliza ni wapi unaweza ukabana taarifa zako kwamba hizi ziwafikie waumini wako na wananchi duniani kwa ujumla hakuweza kutoa majibu hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la kusema kwamba wapo watumishi wamepewa pesa, alipoulizwa hakutoa majibu. Pia tulijiuliza heshima ya chombo hiki na heshima ya mihimili mingine inalindwa na wewe, tulipomuuliza hilo hakujibu hata mara moja.

Mheshimiwa Spika, lakini tupime athari ya kauli zake toka ameanza, mimi niungane na ushauri wa Kamati hii kwamba ukiacha Maazimio leo ambayo mimi naunga mkono vyombo vingine viende vikatazame athari ya kauli zake ni nini. Nani asiyejua hapa kwamba wananchi wa Tanzania wanakufa kwa Corona na ni kiongozi gani wa Serikali amesema kwamba kuchanja ni lazima lakini yeye kauli zake zinathibitisha na zinaonyesha kwamba viongozi wetu wa Serikali wamelazimisha wananchi wachanjwe. Hili jambo kwa kweli halina afya kwa maendeleo ya nchi yetu na lazima tusimame imara tulinde chombo hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la ndugu yetu Mheshimiwa Jerry Silaa mimi na Waheshimiwa wenzangu wajumbe wa Kamati hii tulijiuliza huyu ni Mbunge mgeni kweli, lakini huyu ameshika nafasi kadhaa katika nchi yetu katika nafasi ya kuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam. Pia ulimpa nafasi aombe au arekebishe maneno yake hakufanya hivyo, hii ni dharau kwa Bunge na ni dharau kubwa kwako wewe Spika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini alipofika mbele ya Kamati kwa kuonyesha kwamba alidhamiria alichodhamiria na alisimamia kwa kile alichokuwa amekizungumza alikuja na ushahidi wa vitabu zaidi ya kumi, hakuwa na dhamira ya kuomba radhi.

Mheshimiwa Spika, wewe ni shahidi zimekwishaletwa kesi nyingi tu na kwa sababu Kamati hii ni ya kwako ulisamehe watu wengi hata Kamati imesamehe watu wengi lakini kwa jinsi alivyokuja mbele ya Kamati alikuja na msimamo kwamba alichokizungumza ni sahihi. Jambo hili siyo sahihi hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nikumbushe hakutii wito wa Kamati kwa sababu hata katika taratibu za kawaida unapokuwa una kesi ukipewa summons ya kwanza hupewi summons nyingine hakufika mbele ya Kamati. Kibaya zaidi alipoona kuna wito wa kukamatwa na Polisi aliamua kufika saa 12 asubuhi ndani ya ukumbi wa Kamati kinyume cha utaratibu wa kuendesha shughuli zetu pale. Pia huo ni uvunjifu na ukosefu wa adabu wa Mheshimiwa Silaa. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, tunapochaguliwa tuna taratibu tunapewa mafunzo na watumishi wetu, hata kwenye iPad kuna mada zipo hapa za kuonyesha stahili zetu, Kamati ilimuuliza Shahidi Mheshimiwa Jerry Silaa, je, unajua kwamba allowance hizi hazikatwi kodi? Anasema hajui. Aliposomewa akakiri kwamba leo ndiyo amefahamu kwamba allowance hazikatwi kodi. Sasa leo unawezaje kumuamini na kumpa nafasi hiyo kuwa Mjumbe wa PAP mtu ambaye hajui hata sheria kwamba allowance za kibunge hazikatwi kodi. Kwa hiyo, kwa utaratibu ule ule anakosa sifa za kuwa mjumbe wa PAP. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ili kuweka utaratibu ulio imara na sifa kwa Bunge lako Tukufu wakati mwingine tunapowapa Wabunge nafasi za uwakilishi tuwapime katika viwango tofauti tofauti. Sisi imetuwia vigumu sana kuwazungumza Wabunge wenzetu ambao ni wajumbe wa Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, basi baada ya kusema hayo, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kusema neno kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu juu ya bajeti yake.

Pia nampongeza Waziri Mkuu, Mheshimiwa Jenista Mhagama na Manaibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa sababu wamekuwa wakifanya kazi nzuri sana kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina mambo machache. Katika maendeleo duniani kote, tafiti na maendeleo ni kitu muhimu sana, kwa maana ya research and development. Waheshimiwa Wabunge wengi wamesimama hapa wakizungumzia kwamba, nchi yetu inaelekea kwenye maendeleo na sehemu ambayo Watanzania walio wengi wapo kwenye kilimo. Kwa hiyo, nilikuwa namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kupitia Wizara ya Kilimo tuwekeze fedha nyingi sana kwenye Sekta ya Kilimo kwa sababu ndio Watanzania wengi wanaitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la amani na migogoro katika nchi yetu limetapaa kila sehemu. Nami nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, amekuwa akisimamia maeneo haya kwa weledi wa hali ya juu sana. Mwaka 2017 Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya ziara kwenye mpaka wa Jimbo letu la Kilindi na Wilaya ya Kiteto. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu alitumia saa nane kwa ajili ya kutatua mgogoro baina ya wilaya hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mgogoro huu umechukua miaka takribani 30 na wananchi wamekuwa hawafanyi shughuli za maendeleo kwa sababu ya migogoro ambayo kwa kweli haiishi. Nakumbuka Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa maelekezo, watalaam wakaja wakapitia mpaka ule, kilichobaki ni kuweka alama.

Mheshimiwa Waziri Mkuu wananchi wa maeneo haya, mpaka huu ambao unajumuisha Kata nane wananchi hawafanyi shughuli za kilimo, hawafanyi shughuli za maendeleo; na wapo Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa, wanashindwa kusimamia kwamba agizo lako la kuweka alama bado halijatekelezwa.

Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati ana-wind-up asiseme neno lolote na atoe maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa; Mkoa wa Tanga na Manyara; na Wakuu wa Wilaya wa Kilindi na Kiteto wahakikishe kwamba wananchi wanafanya shughuli zao kwa usalama na amani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mgogoro huu umechukua miaka takriban 30 na wananchi wamekuwa hawafanyi shughuli za maendeleo kwa sababu ya migogoro ambayo haiishi. Nakumbuka Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa maelekezo wataalam wakaja, wakapitia mpaka ule kilichobaki ni kuweka alama. Wananchi wa maeneo haya katika mpaka huu ambao unajumuisha kata nane, wananchi hawafanyi shughuli za kilimo wala shughuli za maendeleo na wapo Wakuu Wilaya, Wakuu wa Mikoa wanashindwa kusimamia na kwamba agizo lako la kuweka alama bado halijatekelezwa. Namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati ana wind-up aseme neno lolote na atoe maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa, Mkoa wa Tanga na Manyara na Wakuu wa Wilaya ya Kilindi na Kiteto wahakikishe kwamba wananchi wanafanya shughuli zao kwa salama na amani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, naomba nizungumzie suala la barabara ya kuanzia Handeni - Kibirashi - Kiteto hadi Singida ambapo ndipo bomba la mafuta litokalo Hoima Uganda litakwenda hadi Tanga. Sasa nafahamu fika na ndio ukweli kwamba barabara hii itakuwa na shughuli nyingi kutokana na ujenzi wa bomba la mafuta, lakini barabara hii haijajengwa kwa kiwango cha lami. Naomba sana eneo au kipande kilichobaki ni cha kilometa 460 tu kuanzia Singida - Manyara hadi Handeni, kuna umuhimu barabara hii ikajengwa kwa haraka sana ili wakati wa ujenzi wa bomba la mafuta wenzetu ambao wameamua ku-invest fedha nyingi sana, wasipate usumbufu wakati wa ujenzi huo.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kunipa nafasi niweze kuchangia hoja ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi iliyopo mbele yetu. Mimi nitajikita kwenye eneo moja tu nalo ni barabara ambayo inaunganisha mikoa minne ya Tanga, Manyara, Dodoma na Singida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni shahidi upo toka Bunge la Kumi na Moja, kila nikisimama hapa hoja yangu ilikuwa ni moja tu kuizungumzia barabara hii. Cha kushangaza Mheshimiwa Waziri kwa makusudi kabisa ameamua kutenga shilingi bilioni 3 mwaka huu ambayo haiwezi kutosha hata kujenga kilometa tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii mwaka wa Bunge lililopita au mwaka huu wa fedha tulio nao zilikuwa zimetengwa shilingi bilioni 6 za kitanzania, lakini leo hii nimesimama mbele ya Bunge lako Tukufu barabara hii haijatangazwa kwa maana bado mwezi mmoja, kwa hiyo, matarajio ya barabara hii kujengwa kwa kiwango cha lami yanazidi kupotea. Mimi naomba Mheshimiwa Waziri aniambie barabara hii inatangazwa lini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini naizungumzia barabara hii? Ni kwa sababu ni barabara ambayo Wabunge takribani sita wameizungumzia; Mbunge wa Singida Kaskazini, Mashariki, Chemba (Dodoma), Kiteto, halikadhalika Mbunge wa Handeni na mimi wa Kilindi tumeizungumzia barabara hii. Kwa nini Mheshimiwa Waziri haoni umuhimu wa barabara hii? Haoni kwamba Watanzania wa kwenye maeneo haya wanahitaji na wao kuwa na afya ya maendeleo ya barabara ya kiwango cha lami? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ndipo bomba la mafuta ambalo nchi ya Tanzania na Uganda linaenda kupita ambapo Mheshimiwa Rais anakwenda kusaini mkataba keshokutwa. Wenzetu wa Uganda tayari miundombinu iko vizuri, sisi wa eneo hili la Tanzania ambapo sehemu kubwa barabara hii inapita haijajengwa kwa kiwango cha lami. Tunataka kuwaambia nini wenzetu ambao wameamua kupitisha bomba hili la mafuta kwenye nchi ya Tanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba sana Mheshimiwa Waziri, ni mgeni kwenye Wizara hii lakini naamini watendaji wake wanafahamu umuhimu wa barabara hii. Hata Mpango wa Maendeleo ulioishia mwaka jana umeitaja barabara hii kwamba ina umuhimu sana kwa ajili ya uchumi wa nchi hii, kwa nini Mheshimiwa Waziri ametuwekea hela ndogo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi huwa sipendi kuzungumza kwa hali ya kukasirika lakini kwenye hili Mheshimiwa Waziri amenikwaza. Ni lazima niseme Wanakilindi, Dodoma, Singida wanahitaji barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami. Tunazungumzia kudumaa kwa uchumi, leo unapokuwa huna barabara ya kiwango cha lami; barabara ambayo haipitiki maana yake uchumi wa wananchi wa maeneo hayo unadumaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili ndilo ambalo linasafirisha kwa kiwango kikubwa mazao kwenda Kenya, Kilimanjaro, Arusha, yote yanapita kwenye njia hii. Sasa iweje Mheshimiwa Waziri usitenge fedha ili barabara hii ijengwe kwa kiwango cha lami? Sitegemei kushika shilingi lakini naomba unipe maelezo ya kutosha ni lini ataitangaza barabara hii kujengwa kwa kiwango cha lami? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine ambayo napenda kuizungumzia ni ya kanzia Songe - Gairo ambayo Mheshimiwa Mbunge mwenzangu wa Gairo ameizungumzia jana. Waheshimiwa Wabunge mtakumbuka kwamba mwaka juzi ilitokea Daraja la Kiyegeya lilikatika wiki nzima magari yanayoenda Rwanda, Burundi yalikuwa hayapiti. Njia iliyo rahisi ambayo inaweza kuwa ni suluhu wakati barabara hii ikiwa imepata tatizo ni njia hii ya kutoka hapa Dodoma - Kilindi - Tanga ni takribani kilometa mia tatu na zaidi. Barabara hii itasadia kwa sababu tunatarajia kujenga Bandari ya Tanga, ili bandari hiyo iweze kuwa na faida ni lazima tujenge barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia kusimama mbele ya Bunge lako tukufu siku ya leo ya Ijumaa ili niweze kuchangia bajeti ya Ofisi ya Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nitangulize shukrani za dhati sana kwako wewe. Pili, naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kwa Watanzania ya kuwaletea maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, dada yetu Mhagama, kwa kazi kubwa na Naibu Waziri, hali kadhalika Katibu Mkuu na watumishi wote wa Ofisi hii, kwa sababu ofisi hii ndiyo jicho na tegemeo la watumishi wote wa Tanzania, wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, ningependa kujielekeza kwenye maeneo ambayo ni kama ushauri. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri katika maeneo mbalimbali alijitokeza na katika hotuba yake amezungumzia kwamba kuna umuhimu wa kufanya ukaguzi au auditing ya watumishi. Ni ukweli usiopingika kwamba hitaji la watumishi katika maeneo mbalimbali nchini ni kubwa sana, lakini ni ukweli pia usiopingika kwamba watumishi hawa kwa hakika bado hawajawekwa vizuri, kwa sababu kuna maeneo ambayo wapo watumishi wengi ukilinganisha na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajenga vituo vya afya, tunajenga shule za sekondari, tunajenga shule shikizi na zote hizi zinahitaji watumishi. Bila kufanya auditing ya kutosha, itafikia wakati haya majengo yote yatakuwa kama ni white elephant. Kwa hiyo, jambo la kwanza kabla hatujafikiria kwenda kwenye kuongeza watumishi kwa sababu lazima tukubali Wabunge wote kwamba bajeti yetu haiwezi kutosheleza kuweza kuwaajiri watanzania wote. Kwa hiyo, hatua ya kwanza ni kufanya auditing ya kutosha. Hebu leo tuchukulie mfano kuna Maafisa Ugani Kinondoni au Ilala wanafanya kazi gani? Wakati katika majimbo ya vijijini hakuna Afisa Ugani. Kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri jambo hili lina umuhimu mkubwa sana sana kufanya auditing na auditing ndiyo itakayosaidia kuhakikisha kwamba watumishi hawa wanaenda kutatua changamoto ya ajira kwenye maeneo yetu huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, naomba nizungumzie suala la kukaimu. Suala la kukaimu imekuwa ni changamoto kubwa sana. Kwenye vikao vyetu unakuta Kaimu Mkurugenzi, Kaimu Mtendaji, kwa nini iwe hivyo? Kuna kitu kinaitwa Tange katika utumishi wa Serikali. Tange ndiyo inayoonyesha seniority ya watumishi ameanza kazi lini, ana elimu gani, tange hii haifanyi kazi? Hii ndiyo ambayo inaenda kutatua changamoto ya promotion. Unapomweka mtumishi kwenye nafasi ya kukaimu miezi sita, mwaka mmoja humtendei haki hata mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii sisi ambao tuliofanya kazi Serikalini miaka ya nyuma huko, kulikuwa na utaratibu nadhani utaratibu huu bado unaendelea kufanya kazi, kitu kinaitwa succession plan. Leo Katibu Mkuu anapokaribia kustaafu anajua yupo Naibu Katibu Mkuu, anajua yupo Mkurugenzi watu hawa wanaijua taasisi vizuri, kwa nini uende ukamkaimishe mtu kutoka eneo lingine wakati institution memory ya taasisi hiyo wapo watu wanayoielewa. Kwa kiasi kikubwa hii inadhoofisha utendaji wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba turudi kwenye historia, turudi kwenye utaratibu, kwa sababu mtu kafanya kazi miaka 20 au 25 unaenda kumtoa mtu eneo lingine hata kuandika dokezo hawezi, hili jambo halina afya hata kidogo katika utendaji wa Serikali. Nakuomba Mheshimiwa Waziri, twende turudi kwenye utaratibu huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, wapo watu mnapokuwa mnawateua kwenye baadhi ya mashirika wanawaondoa watumishi, wanaondoa watumishi takribani 30 mpaka 40 halafu analeta tena kibali cha kuomba kuajiri watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, hawa watu wanaoteuliwa na Mheshimiwa Rais wanapokuwa wanaondoa watumishi kuwapeleka maeneo mbalimbali, asitoe kibali cha kuajiri tena kwa sababu watumishi wale wengine ni very senior, hili jambo halina afya hata kidogo na hili jambo Mheshimiwa Waziri kwa kweli….

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge nimeona umesimama.

T A A R I F A

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti,…

MWENYEKITI: Ni kanuni gani Mheshimiwa.

MHE. AMANDUS J. CHINGUILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, 77(1) nataka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba wapo wanaokaimu zaidi ya miaka miwili, mitatu mpaka minne na kinachotokea ni kwamba anakuja kuletwa mtu mwingine kuthibitishwa kuwa Mkuu wa ile Idara. Kwa hiyo wanawaacha hawa watu wakiwa na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo sonona, pressure na magonjwa mengine. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kigua unapokea taarifa ya Mheshimiwa Amandus.

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru na nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge anachozungumza ni sahihi na jambo hili halitoi motivation kwa watumishi wetu…

MWENYEKITI: Unapokea taarifa.

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa.

MWENYEKITI: Ahsante, endelea.

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kusema kwamba, dhana hii kwa kweli si dhana nzuri, tuendelee kuwaamini watumishi wetu, watumishi ambao wanafanya kazi kwa weledi mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine katika eneo langu la Jimbo la Kilindi, wapo watendaji ambao ni darasa la saba ambao wamefanya takribani miaka 20 sasa hivi, lakini watumishi hawa wapo baadhi yao ambao wamestaafu lakini hawajapata pension kwa sababu wamekosa sifa. Sasa fikiria Mtanzania huyu ambaye ulimwambia afanye kazi za utendaji wa kijiji na hivi ninavyozungumza ni kwamba watumishi hawa tayari Mkurugenzi wa Halmashauri wa Jimbo la Kilindi alikwishaleta barua Ofisi ya Rais, Utumishi miezi sita hawajatoa majibu, wengine wanakaribia kustaafu hawapati pension, tunatoa ujumbe gani kwa Watanzania? Naomba sana Mheshimiwa Waziri jambo hili liweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, tuangalie namna ya kuwapa motivation watumishi wetu, motivation siyo cheo tu au motivation siyo fedha tu, hata wakati mwingine mtumishi anapofanya vizuri unamwandikia barua ya reward ya kumshukuru kwamba kafanya kazi vizuri hiyo ni njia moja ya kum-reward. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja hii. Nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watumishi wote wa Wizara kwa hotuba yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia maeneo yafuatayo nikianza na kuongezeka kwa madai na kutokuwepo kwa ukusanyaji wa madeni kwa Hospitali yetu ya Muhimbili kwa mujibu wa taarifa ya CAG ya tarehe 30 Juni, 2016 yalifika shilingi bilioni 30.8 ilikilinganishwa na mwaka uliopita ya shilingi bilioni 17 sawa na ongezeko la asilimia 45. Hali hii si nzuri hata kidogo na hii inaashiria kwamba uongozi wa Hospitali ya Muhimbili hausimamii vyema eneo hili, je, tatizo ni Kitengo cha Fedha? Wizara lazima ihakikishe madeni yote yanakusanywa kwa sababu fedha ndio ikakayosaidia kuimarisha huduma za afya ukizingatia hii ni hospitali inayotegemewa na Watanzania wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo lipo tatizo la madai ya bima za afya yaliyokataliwa ya shilingi bilioni 1.86; kiasi hiki kimekataliwa kulipwa na makampuni ya bima eti kwa sababu ukaguzi ulibaini, mfano NHIF ilikataa madai ya shilingi milioni 241.97 ya Hospitali ya Muhimbili ikidai ni madai ya madawa ambayo NHIF ilibaini hayakutolewa kwa waganga. Udanganyifu huu ulifanywa na watumishi je, hatua zipi zimechukuliwa na Serikali kwa watumishi hawa? Mheshimiwa Waziri naomba majibu ya kina juu ya mapungufu ambayo kwa hakika hayapaswi kufungiwa macho hata kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ukarabati wa vyuo vya CDIIS na fedha za maendeleo; changamoto ya kukarabati vyuo vya maendeleo (CDIIS) ni suala linalopaswa kutupiwa macho sana, nipongeze juhudi ambazo Wizara mmeonesha kufanya ukarabati kwa baadhi ya vyuo hivi, vyuo hivi ni muhimu sana, vimesaidia vijana wetu kuzalisha wataalam katika sekta ya ujenzi na ufundi, kuna umuhimu mkubwa kwa Wizara kuhakikisha inaweka msisitizo wa kufuatilia fedha za maendeleo kukarabati vyuo hivi kwani itasaidia kupunguza tatizo la ajira nchini. Waasisi wa nchi hawakufanya makosa kuvianzisha vyuo hivi, nikuombe Mheshimiwa Waziri na uongozi mzima wa Wizara jitahidi pia mtoe mafunzo ya kutosha kwa walimu (lectures) ili watu kuongeza ujuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi la kupandisha Kituo cha Afya Songe kuwa Hospitali ya Wilaya; niipongeze Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kutupatia kiasi cha shilingi milioni 500 kukarabati kituo chetu cha afya Songe. Wizara ya Afya ndio wenye dhamana ya Hospitali za Wilaya, kituo hiki kina sifa zote za kupandishwa kuwa Hospitali ya Wilaya baada ya ukarabati huu kwa sababu tumepatiwa pia shilingi milioni 220 kwa ajili ya vifaatiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, jitihada hizi zinatoa fursa kwa kituo chetu kuwa na sifa zote za kuwa Hospitali ya Wilaya, nimuombe Mheshimiwa Waziri atume timu kwenda Wilayani Kilindi kufanya tathimini ya kitaalamu na wakiridhika kituo hiki kipandishwe hadhi, Wanakilindi wanauhitaji mkubwa wa Hospitali ya Wilaya tunayo Hospitali ya Rufaa ya KKKT lakini yapo malalamiko makubwa kwa gharama kubwa na huduma dhaifu inayotolewa na hospitali hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri wote wawili wa Wizara na uongozi mzima wa Wizara hii kwa hotuba yao nzuri ambayo imejikita zaidi katika kuhakikisha kuwa sekta ya ujenzi (barabara), mawasiliano na usafiri wa maji unasimama vema. Niipongeze sana Serikali kwa kuweka kipaumbele barabara ya Handeni - Kibereshi - Kijungu - Kibaya - Mjaro - Olbolotiri - Singida kilometa 460. Kujenga kwa kiwango cha lami barabara hii ukiacha kwamba bomba la mafuta kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga bado barabara hii ni muhimu kwa shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa mikoa hii minne (Tanga, Manyara, Dodoma na Singida).

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wananchi wa mikoa hii mimi naamini kabisa barabara hii itasaidia kufungua fursa nyingi za kiuchumi, niombe sasa Serikali ifanye jitihada kubwa kupata fedha za kutosha ili barabara yote iongezwe kilometa 460. Barabara hii ina faida kubwa hata kwa wafanyabiashara wa nchi jirani, mfano Burundi, Rwanda na Uganda. Bandari zikishakarabatiwa wafanyabiashara watanufaika kwa punguzo la gharama za usafiri kwa sababu barabara hii kwa kiasi kikubwa itakuwa fupi.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ningependa kuchangia ni ubora wa kazi za ukarabati, ujenzi wa barabara zetu kwamba baadhi ya wakandarasi wanapopewa zabuni za barabara matengenezo ya barabara yapo chini ya kiwango. Naomba sana tena TANROADS wasimamie kwani Serikali inapoteza fedha nyingi kwa kazi zinafanyika chini ya kiwango. Kwa mfano ukarabati wa barabara ya Handeni – Kibarashi – Sange baadhi ya maeneo vifusi vilivyomwagwa vilikuwa ni vumbi badala ya kuweka vifusi vyenye mawe hasa katika maeneo ya Korosi. Hii imesababisha barabara hii kutopitika kwa takribani siku tano; mimi najiuliza kwa nini viwango vya kazi hivi kusimamia? Jambo hili litazamwe kwa jicho la karibu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu pia naomba uende kwenye Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (USCAF) mfuko huu ni muhimu sana hususani kwenye maeneo yenye changamoto za mawasiliano kama katika jimbo langu la Kilindi. Nipongeze jitahada zilizofanywa na mfuko kwa kupitia maeneo yote yenye uhaba wa mawasiliano ya simu, nimeona orodha ya vijiji na kata ikiwemo eneo langu la Kilindi niombe maeneo yote yapatiwe mawasiliano ukizingatia mawasiliano ni ajira pia maeneo hayo ni Kata ya Sanyi, Kata ya Kilwa - Kijiji cha Kilwa, Kata ya Twande - Kijiji cha lwande, Kata ya Tunguli, Kata ya Kwekivu, Kata ya Kilindi asilia Kijiji cha Misufini Kata ya Masagalu na vijiji vyake vyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho lakini si kwa umuhimu ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga barabara ya lami ya kwa kilometa tano kwa kiwango cha lami, napongeza, jitihada za ujenzi zimeanza lakini kiasi kilichotengwa ni kidogo sana, ni motor zoo tu ndio zimeanza kujengwa. Niombe Wizara itenge fedha za kutosha kuhakikisha ahadi hii ya Rais wetu inatekelezwa naamini kabisa umuhimu wa kujengwa kilometa tano hizi zitasaidia kupandisha hadhi ya mji wetu wa makao ya Wilaya (Songe) na kubadilisha mwelekeo pia na mwisho barabara zote zinazosimamiwa na TANROADS, wakandarasi wahakikishe mitaro yote inayopitisha maji pembeni mwa barabara zetu inakarabatiwa na kusafishwa mara kwa mara ili kulinda barabara zetu. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watumishi wote wa Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba hii nitajikita katika maeneo yafuatayo; moja, ni ukweli usiopingika kuwa Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) ni muhimu kwa sasa ukizingatia kuwa nchi hii inaelekea kuwa ni nchi yenye mwelekeo kuwa ni nchi ya viwanda vidogo, vya kati na vikubwa, hivyo, tunahitaji wataalam wa ufundi katika kuendesha mashine katika viwanda hivi na suluhisho la wataalam hawa litapatikana kwenye vyuo hivi. Niipongeze Serikali kwa jitihada inazozichukua kujenga vyuo hivi. Nishauri vyuo hivi vijengewe katika Wilaya na Mikoa yote nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa vyuo hivi pia utasaidia katika kupunguza changamoto ya ajira kwani vyuo hivi vitasaidia katika kufanya vijana wote wajiajiri katika maeneo mbalimbali ya ufundi. Niuombe uongozi wa Wizara uharakishe zile asilimia tano za Skill Development Levy zinazokusanywa na Wizara ya Fedha zinafuatiliwa na kupelekwa katika VETA na FDC’s. Umuhimu wa vyuo hivi nimeuona katika Mkoa wa Shinyanga jinsi VETA inavyofanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni ukaguzi wa shule. Eneo hili nalo lina changamoto katika kuimarisha ubora wa elimu, utendaji wa kazi wa walimu na tathmini ya elimu yetu yote. Haya hayawezi kufanyika bila kuimarisha Idara ya Ubora na Ukaguzi wa Elimu. Maeneo mengi katika Wilaya au Majimbo yote Idara hii haipo vizuri kwa kukosa vitendea kazi kama magari mfano ni Jimboni kwangu Kilindi. Jiografia ya Wilaya imekaa vibaya, lakini hakuna gari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiimarisha eneo hili hakika malalamiko ya kudidimia kwa elimu katika shule za msingi na sekondari yatapungua. Vilevile kuna umuhimu kwa Serikali kuboresha maslahi ya watumishi wote wanaosimamia eneo hili la elimu, hayo yamezungumzwa sana. Zamani kitengo hiki kilikuwa imara na matokeo yake yalikuwa yanaonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, ni kuhusu Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi. Napongeza mamlaka hii kwa kazi kubwa inayofanya ikiwa ni pamoja na kusimamia ukarabati wa shule zetu za sekondari nchini. Hili ni jambo jema sana kwa sababu shule hizi zilikuwa zimechakaa sana. Maamuzi haya hakika yanafanya hata watoto wetu wanaosoma katika shule hizi ufaulu wao kuongezeka kwa sababu watasoma katika mazingira mazuri, hiki ni kigezo cha kuinua ufaulu pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, zipo changamoto ambazo naomba zifanyiwe kazi. Mamlaka lazima iwe na utaratibu mzuri unaoeleweka katika shule zote, mfano kama mtatumia force account basi itumike katika shule zote. Mfano ukarabati wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Bwiru wametumia mfumo wa force account na kazi imefanyika vizuri, lakini katika Shule ya Sekondari Nganza Girls zote hizi zipo Mwanza wametumia mkandarasi. Wote hawa walitengewa kiasi cha shilingi milioni 900.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea ni kwamba mkandarasi wa Nganza sekondari ametumia jumla ya shilingi 1,300,000,000 ongezeko limekuwa ni kubwa. Hivi TEA walifikiria au walitumia vigezo gani katika utaratibu wa kazi yenye madhumuni yanayofanana? Nashauri Serikali isimamie eneo hili kwa sababu dhamira ya Serikali ni kukarabati shule zote za sekondari Tanzania, tusipokuwa makini ni shule chache zitakarabatiwa. Wizara isimamie vinginevyo majukumu ya ukarabati yatolewe katika Mamlaka hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, ombi kwa Shule ya Sekondari ya Kilindi Girls kupatiwa fedha za uzio. Katika Jimbo la Kilindi tunayo shule ya sekondari moja ya wasichana ambayo inapokea wasichana kutoka maeneo mbalimbali ukiacha Kilindi, Handeni, Korogwe na Wilaya jirani wote wanakuja kusoma hapo ila tatizo kubwa hatuna uzio unaozunguka shule na hii ni hatari kwani shule hii inazungukwa na makazi ya watu. Ili kulinda usalama wa watoto wetu na pia katika kuleta ufaulu katika masomo. Niombe Wizara itusaidie kutujengea uzio (fence).

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2018
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nakushukuru kwa kunipa fursa hii nami niwe mchangiaji wa pili kwenye jambo muhimu sana katika historia ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza Serikali hususan Waziri wa Fedha kwa kuleta jambo hili la PPP ambalo mimi kama Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nilipata fursa kulizungumzia hapa kwa sababu nilikuwa najua umuhimu wa Muswada huu au nini maana ya PPP kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Muswada huu au marekebisho haya ya PPP ni kwamba Serikali itafaidika na mambo mengi sana hususan katika huduma za kijamii, kwa maana ya hospitali, barabara na kadhalika. Serikali ina majukumu mengi; inataka ujenzi wa barabara na hospitali, lakini yote haya Serikali isingeweza kuyabeba, imeona ni muafaka sasa hivi kuweza kuruhusu sekta binafsi iweze kushiriki katika mambo haya. Hili ni jambo la kupongeza sana kwa sababu tutaruhusu Halmashauri zetu, miradi mingi ambayo ilikuwa imekwama, watu wenye uwezo wao sasa waweze kuisaidia Serikali na mambo yaweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia maelezo ya Mheshimiwa Waziri na Kamati hapa, nina mambo machache ya kushauri ambayo pengine wakiona yana maana au yana umuhimu, basi waweze kuyachukua. Nimeona kwamba baada ya kupitia kwenye center ya PPP kwenye uidhinishaji wa fedha, ataidhinisha Waziri mwenye dhamana. Nadhani hili jambo tulitazame sana kwa sababu baadhi ya miradi itakuwa ina fedha nyingi. Nashauri tuone namna ambavyo ikiwezekana Mheshimiwa Waziri apitishe kwenye Baraza la Mawaziri kabla ya kuidhinisha Waziri mwenye dhamana ya fedha peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu hili linakwenda sambamba na kipengele kile ambacho kinaonesha kwamba kuna miradi ambayo ikiletwa sekta binafsi inaweza kupitishwa bila kupitia kwenye competition. Sasa hii inaweza ikatoa mwanya kwa Waziri asiyekuwa mwaminifu akaweza kupitisha vitu ambavyo baadaye vinaweza kuwa na sura ambayo siyo nzuri. Naomba ikiwezekana kwenye Muswada huu tuone namna ambavyo Waziri wa Fedha peke yake asipitishe, lazima ipite kwenye Cabinet. Nadhani huo ushauri ni muhimu zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, nimepitia kwenye Taarifa ya Kamati ya Bajeti, wao wamependekeza kwamba kifungu cha 4(5) hizi Halmashauri au Wizara kabla hawajapeleka kwenye center ya PPP ni kwamba lazima taarifa ile apelekewe Waziri wa Fedha. Nadhani hilo halina umuhimu kwa sababu huku tuna wataalam watakuwa wameshapitia na Waziri sehemu yake itamfikia. Kwa hiyo, hakuna sababu hiyo taarifa imfikie Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nimeona kwamba hii PPP center itakuwa na role kubwa sana ya kupitia hii miradi. Ushauri wangu naona hapa wawepo wataalam wabobezi sana, wenye negotiation skills za hali ya juu sana ili isije ikatokea baadaye tukaonekana tulipitisha miradi ambayo haina tija kwa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kama inawezekana, kwa nini hii PPP center isiwe sehemu ya TIC kama department pale? Kwa sababu naona tunaanzisha idara kama vile kuongeza majukumu na ajira pasipokuwa na sababu. Nadhani dhamira ya Muswada huu ina lengo la kutaka kuipunguzia Serikali majukumu mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo napenda kutoa ushauri wangu ni suala la elimu. Elimu katika Halmashauri zetu ni muhimu kwa sababu jambo hili ni geni sana, linahitaji uelewa wa hali ya juu sana. Leo hii hata mtu ukimwambia Public Private Partnership, mwingine anaona ni jambo geni sana. Nashauri Wizara yenye dhamana ya jambo hili, basi ianze kuandaa mafunzo ya msingi kabisa kwa ajili ya watu wetu katika Halmashauri na Idara ili wananchi au watumishi hao wawe wana uelewa mpana wa kushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kipengele cha kufungua akaunti kwenye Benki Kuu ya Tanzania. Naliona jambo hili kidogo halijakaa sawa, kwa sababu mwekezaji anayetaka kuja kuwekeza mradi hapa Tanzania usimwekee condition ya kufungua akaunti Benki Kuu. Nadhani ushauri mzuri zaidi ni kufungua investment banks, yaani hizi benki kwa ajili ya miradi ziwe nyingi kwa sababu tunayo moja tu TIB ambayo ukiangalia kwa uhakika haifanyi kazi vizuri sana. Sasa kwa sababu dhamira ya Serikali imeamua kukaribisha sekta binafsi, nashauri kwamba Serikali iangalie namna ya kufungua benki nyingi ambazo zitakuwa zinawezesha watu kwa ajili ya uwekezaji katika sekta hii ya PPP.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo napenda kushauri ni kuangalia watu watakaoshiriki katika hii PPP center wamekuwa vetted kiasi gani na wana uadilifu kiasi gani? Kwa sababu miradi hii itakuwa ni miradi ya fedha za umma. Ukiiangalia dhana ya PPP ni kwamba mtu ana pesa yake, anatoka nje ya nchi anakuja hapa, anataka kujenga barabara au hospitali, lakini miradi ile baada ya miaka 10 maana yake itakuwa ni mali ya Serikali. Sasa ikiwa ni miradi ambayo ina taswira kidogo ya kutokuwa na uaminifu, maana yake gharama ile itakuwa ni gharama ambayo Serikali imeingia. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba watu watakaokuwa wanapitia miradi hii wawe ni watu ambao wana uadilifu wa hali ya juu sana na ni watu ambao wana uzalendo, wenye kuangalia maendeleo mapana ya nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja hii. Ahsante sana.
Sheria ya Fedha ya Mwaka 2019
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kusema machache juu ya hoja iliyopo mezani. Ni ukweli usiopingika kwamba kodi ndiyo kila kitu, bila kodi nchi haiwezi kwenda mbele, lakini moja ya sifa ya kodi lazima kuna mambo mawili kwanza iweze kulipika kwa urahisi, lakini wale walipa kodi pia wawe willing wao wenyewe kuilipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa haya yatafanyika vipi? Haya yanaweza kufanyika kwanza kwa kutoa elimu kwa walipakodi, lakini kuweka utaratibu ulio mzuri kwa walipakodi wenyewe. Wazungumzaji wengi waliozungumza hapa wamezungumzia namna ya ku-wide tax base, unapozungumzia namna ya ku-wide tax base maana yake utoe fursa kwa wananchi walio wengi waweze kulipa kodi na wasilipe wananchi wachache.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nina taarifa juu ya wananchi wa Tanzania kwamba population kwa mwaka 2019 tupo takriban 55,890,747; umri wa kuanzia mwaka sifuri hadi miaka mitano, ni 9,628,845; umri wa miaka sita hadi 19 ni 20,836,171; na umri kuanzia miaka 20 hadi miaka 64 tuko takriban 23,691,000. Hapa ndipo ambapo nataka nizungumzie kwamba, hapa ndipo tunataka tukusanye kodi.

Ukichukua wafanyakazi wa Tanzania hawazidi 500,000. Katika kundi hili hili wakulima ni takriban asilimia 65, sasa unaona kuna Watanzania takriban 13,000,000 ambao hawapo katika mfumo rasmi wa kulipa kodi. Sasa hapa ndipo ambapo Mheshimiwa Waziri namwomba sana kupitia Kamishna wa TRA hebu wakae chini waangalie ni Watanzania wangapi ambao wanalipa kodi na wapi ambao hawalipi kodi, kwa sababu kodi hizi zisilipwe na watu wachache kwa manufaa ya watu wengi, kila Mtanzania anao wajibu wa kulipa kodi ili tuweze kujenga barabara, tujenge zahanati, pamoja na mashule yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka kulizungumzia tu hapa nipongeze kwenye hasa kwenye mabadiliko yenye Cap 233 ambayo mabadiliko yamefanyika hapa. Niipongeze sana Serikali wamelenga hapo hapo kwenye kuongeza tax base kwamba wameona waongeze na wamepunguza kodi kutoka 150,000, wamepeleka mpaka 100,000 na hapa wamelenga kukusanya mapato ya kutosha, lakini pia wamewapa relief hawa wafanyabiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nimeliona na ambalo pengine watu wengi hawajaliona ni hili la kwamba hawa walipakodi walipaswa kupeleka mahesabu yao kwa watu ambao ni wataalam wenye CPA. Hata hivyo, wamesema sasa kuanzia 20,000,000 hadi 100,000,000 ndiyo watakaopeleka pale, kwaiyo kundi hili kubwa maana yake kwanza litakuwa limepunguza gharama ya hawa wataalam wa mahesabu. Hili ni jambo zuri sana ni jambo la kupongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la Blue Print. Blue Print hii haipo Wizara ya Fedha, lakini ipo kwenye Wizara nyingine, lakini blue print hii ndiyo ambayo inaleta conducive environment kwa ajili ya wafanyabiashara, kwa ajili ya investors wa nje, lakini na Watanzania kwa ujumla. Naomba jambo hili Serikali ilione kwamba ni jambo la kufanyia haraka sana na wameanza kwa kuondoa kodi hizi 54. Hili kwa kweli nipongeze sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni sehemu ndogo sana ya mabadiliko haya. Ili tuweze kupunguza kero hizi kwa kweli lazima blue print ifanye kazi sana, lakini suala la blue print lisiwe kwa Waheshimiwa Wabunge tu, liende mpaka kwa wataalam kule, liende kwa wananchi wetu waone kwamba dhamira ya Serikali hii sasa hivi ina lengo la kuhakikisha kwamba inatengeneza mazingira mazuri sana kwa wafanyabiashara na hii kwa kweli nadhani itatusaidia sana, tumeanza lakini nadhani sasa Wizara ya Fedha ambayo ndiyo wenye dhamana ya kukusanya kodi, nashauri sana sana wawe serious na jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni uanzishwaji wa Ofisi hii ya Malalamiko, kwa kweli ni jambo la kupongeza sana. Nimeona wametaja sifa za huyo atakayeongoza ofisi hii, hii ni ofisi muhimu sana, ni ofisi ambayo itahitaji mtu ambaye ni mbobezi mkubwa sana wa mambo ya kodi, lakini pia mbobezi wa mambo ya fedha, lakini mtu huyu au ofisi hii pia tuiruhusu iweke utaratibu wa kwenda kwa wananchi kupata maoni yao, kwa sababu wakikaa tu ofisini hii inaweza isisaidie sana. Pia napongeza kwamba haitakuwa ni ofisi ya mwisho ya malalamiko, wanaweza kwenda kwenye Tax Tribunal, hili ni jambo pia la kupongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningependa kulizungumza naomba niende kwenye maoni ya Kamati ya Bajeti. Kwenye ukurasa wa 19 wameomba Serikali, Wizara ya Fedha wafanye mabadiliko katika Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura 2009 ambayo ni The Local Government Finance Act. Hapa nimekuwa very interested kuzungumzia kwa sababu inahusu Mkoa wa Tanga. Eneo la Mkoa wa Tanga kuna mashamba ya katani na maeneo yale kuna halmashauri kama tatu hivi tukizungumzia Korogwe Vijijini, Wilaya ya Mziha na sehemu ya Handeni halmashauri hizi zilikuwa zikikusanya kodi kupitia zao hili la katani, lakini halmashauri hizi zimekuwa zikikosa mapato hayo kwa muda mrefu kutokana na sheria hii ambayo inanyima halmashauri kukusanya kodi kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niwapongeze sana watu wa bajeti kwa kuliona hili kwa sababu kupitia sheria hii halmashauri au Mkoa wa Tanga wameweza kukusanya shilingi milioni 932 tu kiasi ambacho ni kidogo, lakini mabadiliko yakifanyika Mkoa wa Tanga kupitia hizi halmashauri tatu watakusanya Sh.9,324,511,377.90. Sasa unaona kwamba sheria hii ilikuwa inanyima mapato hizi halmashauri, kwa kweli namwomba sana Waziri wa Fedha aone umuhimu wa kuchukua maoni ya Kamati ya Bajeti kwa sababu ni eneo ambalo litasaidia kuwapa mapato halmashauri zetu na mapato mengi ya halmashauri sasa hivi yamepungua. Nina uhakika suala hili likifanyiwa kazi, basi halmashauri hizi ambazo zinategemea mapato makubwa kutokana na tozo hii ya asilimia tatu ambayo itatokana na zao la mkonge itaweza kuongeza mapato ya halmashauri zetu

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo pengine ningependa kuchangia, kwa siku ya leo ni eneo ambalo linahusu kodi tena. Nimeona kwamba kuna maeneo mengi ambayo wamefanya mabadiliko, lakini bado nishauri, namwombe Kamishna wa TRA analo jukumu kubwa sana sana na timu yake kuweza kupitia sheria mbalimbali, tumepitisha sheria hizi, lakini bado wao wana nafasi kupitia mkutano ule na Mheshimiwa Rais wao kuweza kujifungia kuona kwamba ni maeneo gani mengine ambayo wananchi wamekuwa wakiyalalamikia na hususan eneo la Kariakoo. Eneo la Kariakoo watu wengi wamelizungumzia ni kitovu cha mapato pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo ambalo wengi wamelizungumzia, suala la property tax, hawa wenye majumba Kariakoo, property tax hizi wakizipeleka kwa wafanyabiashara hawa wadogo wadogo ambao ni wapangaji pale, jambo ambalo kimsingi siyo sahihi hata kidogo. Namwomba Mheshimiwa Waziri na watu wake wa TRA waangalie namna ya kulipitia hili ili wale wafanyabiashara ambao wana dhamira ya kulipa kodi ambayo siyo wakwepaji wa kodi waweze kulipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Finance Bill ambayo iko mbele ya meza yako. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye amenijalia leo kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu, bila ya yeye pengine tusingesimama au tusingekuwepo hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, naomba nimpongeze kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu Samia Suluhu Hassan. Niseme kwa maneno machache kabisa ameanza na mguu mzuri. Haya yote ambayo tunayapongeza, tunayaona hapa, ni fikra pana na hekima kubwa ya Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Naibu Waziri wa Fedha. Niseme ushirikiano ambao wameutoa kwenye Kamati yetu ya Bajeti ni ushirikiano wa hali ya juu sana. Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Naibu wake wanatosha kwenye nafasi hiyo. Wameonyesha kwamba wana uwezo mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme, Mheshimiwa Waziri jana wakati anahitimisha ametumia lugha nyepesi sana, hakutaka kutumia lugha ya kiuchumi, na nina uhakika Watanzania wamekuelewa; kwamba maendeleo ya nchi hii yataletwa na Watanzania wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna mjomba, hatuna baba, tuchangie hata kwa senti moja kwa ajili ya kutatua changamoto ya maji, barabara na afya katika nchi yetu. Mimi nikupongeze sana katika hilo. Na ninaahidi, Wajumbe wa Kamati ya Bajeti na Watanzania wamekusikia, wataku-support kwa ajili ya kuiletea maendeleo nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwashukuru wenzetu wa Wizara ya Fedha; Katibu mkuu na staff wote. Kwa sababu katika kipindi cha miezi mitatu yote kila tulipowahitaji walikuja bila kusita na hakika wamekuwa ni msaada mkubwa sana kwenye Kamati yetu ya Bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika, nimshukuru Mheshimiwa Spika, Naibu Spika, Wenyeviti wa Kamati na watumishi wote wa Bunge ambao wameipa ushirikiano mkubwa sana Kamati ya Bajeti katika kuhakikisha kwamba taarifa yetu leo imeweza kusomwa hapa na imeweza kusikilizwa na Wajumbe wote wa Kamati hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yetu ya Kamati ya Bajeti nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, nenda kayafanyie kazi, haya yote ambayo yamesemwa hapa. Kikubwa twende tukasimamie fiscal policy. Tukasimamie utekelezaji. Mifumo hiyo tuliyoizungumza bila kuisimamia haya matarajio ya mabilioni na mabilioni hayawezi kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwenye maeneo machache ambayo ninapenda kutoa ushauri wangu mahususi. Nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kukubali ushauri wetu, hususan wa kukupa ridhaa wewe Waziri wa Fedha kwa kuruhusu kutoa msamaha kwenye GN.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa palikuwa pana changamoto kubwa sana. miradi mingi katika halmashauri, katika majiji, ilikuwa inachelewa kwa sababu fedha au misamaha hii ilikuwa inasubiri mlolongo mpaka Baraza la Mawaziri. Leo hii tumempa dhamana Mheshimiwa Waziri, na nina uhakika ataitumia vizuri; miradi yetu katika vijiji na halmashauri itakwenda vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze Serikali na nipongeze Kamati yangu hususan kwa kurekebisha, Serikali kwa kuona kwamba eneo la bandari fedha zile zinakwenda kuwekwa kwenye akaunti maalum; fedha za TCRA, fedha za TASAC. Bandari ni kiungo kikubwa sana, ndipo ambapo Serikali ikisimamia kwa dhati kabisa hii miradi mingi ya kimkakati na miradi mingine ya maendeleo inaweza kukamilishwa kwa kuisimamia bandari yetu ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ninayoiona, bandari wana changamoto ya vifaa chakavu vya kupakua mizigo pale, lakini wana tatizo la mifumo ya kukusanya mapato. Kwa mfano, kuna mfumo wa TEHAMA unaitwa Electronic Data Interchange ambao unamfanya mwenye meli ajue ni lini mzigo wake umefika na meli itaondoka lini pale. Mfumo ule pale haupo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Waziri mwenye dhamana, hakikisha kwamba tunanunua vifaa vya kutosha, lakini hakikisha kwamba mfumo huu unawekwa ili uweze kusaidia utendaji wa kazi katika bandari yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mifumo kwa ujumla; katika halmashauri zetu fedha nyingi za mapato zinapotea. Twende tukaimarishe mifumo yetu ya mapato isomane. Maeneo ya halmashauri mapato bado yanapotea sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, kwa kushirikiana na Mheshimiwa Ummy, Waziri wa TAMISEMI, tuhakikishe tunaimarisha mifumo ya mapato katika halmashauri zetu ili fedha zile ambazo zinakusanywa na halmashauri zetu ziweze kusaidia kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)