Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mboni Mohamed Mhita (5 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MBONI M. MHITA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata fursa ya kuweza kuchangia katika suala zima la maji. Awali ya yote, naomba nitumie fursa hii kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Handeni Vijijini kwa kunichagua kwa kura nyingi na za kishindo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nijikite moja kwa moja kwenye adha ya maji katika Jimbo Handeni Vijijini. Maji ni tatizo sugu katika Jimbo la Handeni Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiwa ni mtoto wa kike, nateseka sana kushuhudia akinamama wakitembea umbali mrefu kuhangaika kwenda kuyafuata maji. Naamini kwamba, moja ya sababu kuu ya akinamama kujitokeza sana kwenye uchaguzi huu kunipigia kura ni matumaini makubwa kwamba mtoto wa kike basi nitakuwa mstari wa mbele kwenye kuhangaika kuhakikisha kwamba adha ya maji inaisha ama kupungua katika Jimbo la Handeni Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite moja kwa moja katika mradi wa HTM (Handeni Trunk Main). Mradi wa HTM ndiyo mradi ama ndiyo chanzo kikuu cha maji katika Jimbo la Handeni Vijijini. Nina hakika mradi huu ukitiliwa nguvu zaidi shida ya maji kwa wananchi wa Handeni Vijijini itakwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu ulitengenezwa mwaka 1974 ukiwa na tegemeo la kuwa na life span ya miaka 20. Hivyo basi, tangu mwaka 1994 miundombinu ya mradi huu ni chakavu na hakika wananchi wa Handeni Vijijini wanateseka sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu ulianzishwa ukiwa na lengo la kuweza kuhudumia vijiji 60 na sasa hivi Jimbo la Handeni Vijijini lina vijiji 122. Hivyo basi, ni dhahiri kwamba kuna ongezeko kubwa sana la wananchi. Mahitaji ya kuweza kufufua huu mradi ni USD milioni 84.4. Nimeona hapa kwamba Wizara inategemea Euro milioni 60 kutoka BAM International ya nchini Uholanzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetenga shilingi bilioni mbili kwa ajili ya mradi huu kwa mwaka 2016/2017. Hivyo basi, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, nguvu ya ziada iongezwe ili hizi Euro milioni 60 ambazo zinategemewa kutoka BAM International ziweze kupatikana; kwa sababu hakika mradi huu ukiweza kufanyiwa kazi, basi hakika Jimbo la Handeni Vijijini na Handeni nzima kwa ujumla adha ya maji itakwisha kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Jimbo la Handeni Vijijini tulibahatika kupata mabwawa matatu chini ya mradi wa World Bank.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bwawa la kwanza lipo Manga, lingine Mkata na la tatu liko Kwandugwa; mabwawa ambayo tulitarajia ndani ya miezi sita yaweze kuwa yamemalizika, lakini mpaka nasimama hapa, huu ni mwezi wa 30 na bado yale mabwawa hayajamalizika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, basi tumwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Maji, fedha ziweze kuelekezwa kwenye miradi hiyo ili wananchi wa Manga, Mkata na Kwandugwa waweze kuondokewa na shida na adha hii ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niishie na ahadi kwa wananchi wa Handeni ambayo ilitolewa na Rais wa Awamu ya Nne ya mradi wa Wami Chalinze, mradi ambao kwa namna moja ama nyingine ungepunguza adha ya maji kwa wananchi wa Jimbo la Handeni Vijijini, tukiwa tuna maana kwamba mradi huu wa Wami, Chalinze ambao uko kwenye Jimbo la jirani, kaka yangu Ridhiwani Kikwete ametoka kulizungumzia sasa hivi, angeweza kutuvutia maji mpaka Manga na maji yakifika Manga, basi hakika yamefika Mkata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, basi naomba pia Mheshimiwa Waziri aweze kutukumbushia kwa sababu Handeni Vijijini bado tunaingoja ahadi hii; tunangoja utekelezaji wa hii ahadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
MHE. MBONI M. MHITA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba kutumia fursa hii kwanza kuwapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri pamoja na Naibu Mawaziri kwa kazi nzuri ambayo wameendelea kuifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nitumie fursa hii kumshukuru sana kaka yangu Mheshimiwa Jafo kwa kiasi cha shilingi milioni 400 ambacho wametuletea Handeni Vijijini kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya kwenye Kata ya Kabuku. Pia ninashukuru sana maana nimeona tumetengewa bilioni moja na milioni mia tano kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Mkata katika Jimbo la Handeni Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri tuna changamoro kubwa sana, naomba nikupe taarifa kwamba Wilaya ya Handeni kwa sasa ina Halmashauri mbili, Halmashauri ya Mji na Halmashauri ya Handeni Vijijini, kwa maelekezo ambayo tulikuwa tumepata ni kwamba Halmashauri ya Handeni Vijijini iondoke kwenda kuanza Ofisi mpya na zile Ofisi ambazo tulikuwa tukichangia na wenzetu wa Halmashauri ya Mji tuwaachie wenzetu wa Halmashauri ya Mji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa zaidi ni kwamba tulikuwa tunategemea pesa kutoka kwenye Serikali ili Handeni Vijijini tuweze kuhama na kuanzisha ofisi mpya. Kwa mshangao mkubwa zimeingia fedha kiasi cha bilioni 3.3 kwa maelekezo kwamba zile fedha ziende kwenye Halmashauri ya Mji ambao wao tayari wana ofisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na hili nilishaongea na kaka yangu Mheshimiwa Jafo na nikamweleza mshangao mkubwa ambao nimeupata, kwa sababu nilitegemea hizi fedha zioweze kuja kwenye Halmashauri ya Handeni Vijijini ili ambao hatuna ofisi tuweze kuhama, lakini kwa mshangao mkubwa ni kwamba hizi fedha sasa zimekwenda kwenye Halmashauri ya Mji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa zaidi ni kwamba hizi fedha za miradi ambazo zimekuwa zikija katika maeneo yetu ni fedha nyingi ambazo kwa namna moja ama nyingine zinahitaji uangalizi wa hali ya juu na ndiyo hapa sasa nitaingia upande wa baba yangu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na nitajikita zaidi kwa Prevention and Combating of Corruption Bureau (TAKUKURU).

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiofichika kwamba rushwa inachangia umaskini kwa kasi ya juu sana. Ni dhahiri kwamba unapodhibiti upotevu wa fedha kwenye maeneo mbalimbali basi ni hakika kwamba unapunguza umaskini. Nayasema haya kwa sababu mimi ni mwanamke na nimeona ni jinsi gani ambavyo wanawake na akinamama wa Jimbo la Handeni Vijijini wamekuwa wakitembea umbali mrefu, wakihangaika kwenda kutafuta maji na siyo kosa lao na wala siyo kosa la Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetuletea pesa kwa ajili ya miradi ya maji, lakini nasikitika kusema kwamba miradi yote ya maji ambayo ililetewa fedha katika Jimbo la Handeni Vijijini hakuna hata mradi mmoja ambao tumeona matokeo yake, kwa nini? Kwa sababu kumekuwa na ubadhirifu mkubwa sana wa fedha na kuna harufu ya rushwa katika miradi yote. Kuna mradi mmoja wa mabwawa ambao uliingiziwa bilioni nne na zile fedha mpaka leo zimeingia kwenye huo mradi, lakini mradi ule mpaka leo hakuna ambacho tumekiona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa na mradi wa visima ambao mpaka leo wananchi wa Jimbo la Handeni Vijijini hakuna ambacho wamenufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini sasa kifanyike? Naomba Serikali iweze kwa namna moja ama nyingine kuwawezesha wenzetu wa PCCB ama TAKUKURU kwa namna zifuatazo:-

Kuna maeneo mengine ambayo tumejionea kabisa kwamba Ofisi za TAKUKURU haziko katika kiwango ambacho kinatakiwa ama zile basic needs za ofisi, pia wawezeshwe kwa vitendea kazi kama magari. Nasema haya kwa sababu wangekuwa na vitendea kazi ambavyo viko imara hakika wanaweza kufanya kazi zao kwa umahiri na kufika kwenye maeneo hayo na kuepusha upotevu mkubwa sana wa fedha ambazo kuna baadhi ya Watumishi wamekuwa siyo waaminifu sana, wamekuwa wakitumia zile fedha kwa manufaa yao wenyewe na matokeo yake wananchi wetu wameendelea kuteseka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu yangu, naomba nitoe reference kwa wenzetu wa Luxemburg, wenzetu wa Sweden ambao wao wana National Anti-Corruption Unit, wenzetu wa Finland ndiyo Mashirika makubwa ama taasisi kubwa za uzuiaji wa rushwa duniani zinazoongoza. Kigezo kikubwa ambacho kimefanya hizi taasisi katikan hizi za Sweden na Finland kuongoza ni kwa sababu ya transparency na access to information ama uwazi na upatikanaji wa taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali ofisi zetu ziwe na ushirikiano na wenzetu hawa wa TAKUKURU ili taarifa ziweze kupatikana, kwa sababu kama tunavyoona hawa ni prevention and combating, lakini tumezoea kuona kwamba wao wanafanya combating zaidi siyo prevention. Kwa hiyo, naamini kwamba wakiwa na access ya kupata taarifa basi wataweza kuepusha matumizi mabaya ya fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niokoe muda wako, naomba nihitimishe kwa kusema tu:-

Moja; naomba sana Serikali itusaidie kuweza kuona nini ambacho kimetokea katika Wilaya ya Handeni hasa kwenye hizi bilioni tatu na milioni mia tatu. Mbili; Uwezeshwaji wa wenzetu wa TAKUKURU. Tatu; Waweze kupata ushirikiano hasa kwenye access to information na transparency ambayo ni uwazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii kukushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuongea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MBONI M. MHITA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naomba awali ya yote nitumie fursa hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu pamoja na watendaji wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba niendelee kutoa kilio cha wananchi wa Wilaya ya Handeni, niendelee kutoa kilio cha wananchi akina mama wa Handeni Vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya maji Handeni imegeuka kuwa janga la kiwilaya. Nasema janga kwa sababu ukosefu wa maji katika Wilaya ya Handeni pamoja na Jimbo la Handeni Vijijini umezuka sasa na kusababisha changamoto mbalimbali ambazo sasa zimeanza kuingia katika sekta mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukosefu wa maji Handeni umechangia kwa kiasi kikubwa kusababisha milipuko ya magonjwa. Historia ya kupatikana Ugonjwa wa Kipindipindu Handeni ni kwa sababu ya ukosefu wa maji katika Wilaya ya Handeni ambayo sasa hiyo imeingia kwenye Sekta ya Afya. Lakini wakati huohuo, ndoa za akina mama Wilaya ya Handeni zinalegalega, akina mama wanaamka alfajiri saa kumi kwenda kutafuta maji, na haina guarantee kwamba wakirudi wanarudi na maji. Wakati mwingine wanatoka saa kumi wakirejea ni saa saba au saa nane za mchana na wakati huo hawajarudi na maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe mwenyewe utajionea, uaminifu kwenye zile ndoa unapungua, ndoa nyingine zinalegalega, na akina mama wengine wamekosa ndoa zao kwa sababu ya changamoto ya maji. Hilo ni tatizo la kijamii sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtagundua kwamba watoto wa kike Mkoa wa Tanga tumekuwa tukishika mkia kwenye ufaulu, sasa hapo tumeingia kwenye elimu. Kwa sababu mabinti hao badala ya kutumia muda huo kwenda kujisomea wanautumia kwenda kusaka maji. Wakati wenzao wa wilaya na mikoa mingine wakitumia muda huo kujisomea, sisi mabinti wa Handeni Vijijini tunatumia muda huo kwenda kusaka maji, hali kadhalika mtajionea kwamba comparison ya ufaulu utatofautiana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati huohuo, muda ambao akina mama wanaamka kwenda kusaka maji ndiyo muda ambao na wanyama wakali pia wanatoka kwenda kusaka maji. Sasa hebu tuangalie mwanamama in a very vulnerable situation anakutana na mnyama mkali, wengine wamedhurika na wengine wamepoteza maisha kabisa, hilo ni tatizo la kiusalama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tatizo kubwa kabisa ni kurudi nyuma kiuchumi. Wakati ambao wenzetu wa wilaya na mikoa mingine wanajijenga kuanzisha miradi ya akina mama na kutumia mikopo mbalimbali sisi akina mama wa Wilaya ya Handeni na Jimbo la Handeni Vijijini tunatumia kwenda kusaka maji. Ni ukweli usiofichika kwamba hata ukituangalia hatuwezi kulinga na akina mama wa mikoa mingine, hatuwezi kulingana na akina mama wa wilaya nyingine kiuchumi kwa sababu muda ambao wenzetu wanatumia fursa za Serikali za kutengeneza vikundi, za kuanzisha miradi, sisi tumejitwika ndoo tunasaka maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nini kifanyike? Naomba nitoe maoni yangu; kwanza niishukuru sana Serikali ilitupatia bilioni mbili ili kuweza kukarabati Mradi wa HTM ambao kwa kirefu ni Handeni Trunk Main. Lakini mradi huu ulianza mwaka 1974 ukiwa na lifespan au uhai wa miundombinu wa miaka 20, nikiwa na maana kwamba mwaka 1994 ile miundombinu itakuwa imechoka. Sasa wenyewe tufanye hesabu kuanzia mwaka 1994 mpaka 2004 mpaka 2014 mpaka 2019, miaka mingi imekwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashukuru Mungu Serikali imetuweka kwenye mpango lakini naomba sasa pendekezo langu liwe Serikali iharakishe ukarabati wa miundombinu ya HTM ili akina mama wa Handeni ambao wamekuwa sasa wamezoea kuisikia hii ahadi, imekuwa kama ni ahadi sugu, angalau waone utekelezaji wa kuonekana. Naamini kwamba Serikali ina mipango mizuri lakini bado iko kwenye paperwork Wizarani, hatujaanza kuona implementation katika Wilaya yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo langu la pili, naomba Serikali iridhie sasa Mji wa Mkata ambao ndiyo Makao Makuu ya Halmashauri ya Handeni Vijijini, itegemee vyanzo tofauti vya maji. Pale kunategemewa HTM, kunategemewa visima, lakini tunategemea CHALIWASA ambao ni mradi wa Chalinze, ambao tunashukuru Mungu mpaka sasa hivi ile miundombinu imefika Manga, na Manga ni kijiji ambacho kiko ndani ya Kata ya Mkata. Kwa lugha nyingine ni kwamba Serikali ikiridhia basi miundombinu ile inaweza ikasogea mpaka Mkata Mjini na kata ile ikawa ina sources mbalimbali za kuweza kujipatia maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa lakini si kwa umuhimu ni Serikali ifuatilie ubadhirifu mkubwa ambao umefanyika kwenye mabwawa ya Manga, Mkata na Kwandugwa, pamepotea zaidi ya bilioni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru Mungu kwamba Waziri alifika, Naibu Waziri amefika na amejionea. Tulifanya ziara na Mheshimiwa Waziri, na tukafanya ziara na Mheshimiwa Naibu Waziri, kaka yangu, Mheshimiwa Aweso alifika mpaka eneo na alijionea na siku hiyo baadhi ya wakandarasi pale walishikiliwa. Lakini kushikiliwa kwa wale bado hakujaokoa hali ya changamoto ya pale Handeni, Handeni Vijijini na Kata nzima ya Mkata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisitumie muda naona kengele ya pili imelia, kwa hiyo naomba Serikali ichukue hatua kali. Baba yangu, Mheshimiwa Keissy alisema fedha zile zitapikwe, bilioni moja ni nyingi sana kupotea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba niunge mkono hoja. Nashukuru sana, ahsante sana kwa kunisikiliza.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. MBONI M. MHITA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nilitamani sana niweze kumwelewesha ndugu yangu Mheshimiwa Salome. Sasa asiweze kunitoa kwenye reli na maelezo mazuri ambayo yamezungumzwa na mama yetu Mheshimiwa Jenista, naomba niendelee.

Mheshimiwa Spika, naomba kwa namna ya kipekee, kwanza kabisa nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Katika jarida la The Diplomat toleo la Januari, 2020 limetamka au limemwita
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni A Game Changer kwenye mining industry.

Sasa wenyewe tunaweza tukajipima na tukaona kama jarida kubwa kama hilo la The Diplomat limeweza kutambua wazi na kumwita An African Mining Game Changers, siyo Tanzania Game Changer kwenye mining sector, lakini African Game Changer kwenye Sekta nzima ya madini. Sisi tunajua na wao wanaanza kutambua hilo.

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuipongeza sana Wizara ya Mambo ya Nje kwa namna ya kipekee katika kipindi hiki cha miaka minne ya utekelezaji wa Ilani, kimefanikiwa au Wizara imefanikiwa kuongeza Balozi saba.

Mheshimiwa Spika, naomba nizitaje, ya kwanza ni Algeria, ya pili Israel, Sudan, South Korea, Quba, Namibia pamoja na Qatar. Hii inaonesha ni jinsi gani ambavyo Wizara inaendelea kujipambanua kwenye kukuza uhusiano wa kimataifa na diplomasia ya uchumi. Pia, ni jinsi gani ambavyo kupitia hizi Balozi zetu mpya itashughulika na watanzania ambao wako kwenye nchi hizo, nikiwa na maana ya diasporas lakini pia kupitia uchumi (economic diplomacy) itaendelea basi kushughulika na wawekezaji ambao wana interest ya kuja kuwekeza Tanzania. Vilevile kikubwa zaidi pia kuweza kuvutia utalii.

Mheshimiwa Spika, hapa niwe muwazi kabisa, kuna Balozi ambazo zimekuwa ni mfano wa kuigwa kwenye suala zima la watalii. Ubalozi wa kwanza ni China, Ubalozi wa pili ni Israel, Ubalozi wa tatu ni Urusi. Mabalozi hawa wamekuwa; natafuta neno sahihi la kuwaita; lakini wazalendo kupindukia kwa sababu wamejitoa kwa namna ya kipekee kwa kujiongeza kufanya marketing kwenye sekta nzima ya utalii, na tumeshuhudia watalii ambao wamekuja nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna changamoto moja hapa; hawa mabalozi hawana fungu lolote la marketing, marketing funds ziko kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii. Hivyo basi, naomba nitumie fursa hii kuwashauri wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Nje ione ni jinsi gani itakuja na utaratibu wa kuweza kupata fedha kidogo za kuweza kuwasaidia Mabalozi wetu kwenye nchi hizo ili waendelee basi kujipambanua zaidi na kuja na njia latest au more ways za kuona ni jinsi ambavyo wanaweza kukuza utalii.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kuipongeza sana Wizara kwa namna ya kipekee. Katika kipindi hiki kifupi tumeshuhudia SADC ikipitisha Kiswahili kuwa ni an official and working language; na tunakumbuka wazi kwamba SADC ina nchi 16 lakini wakati huo huo na nchi za Maziwa Makuu (Great Lakes) ambayo imekusanya nchi 13 nao pia wamepitisha kuwa Kiswahili kuwa ni official language na official working language. Wizara haikuishia hapo, imeenda mbali zaidi kwa kushirikiana na Baraza la Kiswahili imeanza kuandaa mitaala ambayo itatumika sasa katika nchi hizo. Hapa tumeona kwamba Wizara imeamua kujipambanua na imeamua ku- champion hili suala zima la Lugha ya Kiswahili.

Mheshimiwa Spika, Wizara yetu ya Mambo ya Nje inamiliki nyumba 106 lakini wakati huohuo ina viwanja takribani 12. Naomba nitumie fursa hii kuishauri basi Wizara ione ni namna gani sahihi hivi viwanja 12 vitajengwa ili kuweza kupunguza gharama ambazo kwa sasa Serikali inapata lakini pia adha ambayo Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje wanayopata kupitia kutokuwepo kwa nyumba za kudumu katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, nimalizie sasa, na ninaomba nimalizie kwa kuzungumzia Chuo cha Diplomasia ambacho ni chuo sasa hivi, au kilianzishwa kupitia uhusiano kati ya Tanzania na Mozambique, Tanzania wakiwa na asilimia 50 na Mozambique wakiwa na asilimia 50. Kwa muda mrefu sana wenzetu wa Mozambique wamekuwa hawatoi mgao wao au hawachangii katika makubaliano yale; na kwa namna moja ama nyingine hiyo imekuwa inaturudisha nyuma. Nilikuwa naomba niishauri Wizara basi, kwa namna ya kipekee iangalie mfumo gani mzuri na wa kidiplomasia wa kuweza kuachana na wenzetu waweze kuendelea kwa sababu ni dhahiri kwamba hawana nia ya kuendelea na muungano huu na sisi tujiongeze. Tuna majengo ya kutosha Dar es Salaam sasa hivi Serikali imehamia Dodoma, tuna mitaala mipya katika sekta nzima ya diplomasia ya uchumi ambayo sasa; na ninaamini kupitia Wizara hii makini ikifanya hivyo kwa kutumia majengo yetu ambayo yako pale Dar es Salaam chuo kitaendelea kukua na kitasaidia vijana wengi ambao wanataka kujiongeza katika sekta nzima ya diplomasia.

Mheshimiwa Spika, niishie kabisa sasa kwa kuipongeza Wizara ya Mambo ya Nje kwa kuendelea kuimarisha uhusiano wa kimataifa na nchi mbalimbali, nchi zetu ambazo tunapakana nazo nchi za Afrika Mashariki, nchi za African Union, nchi za ACP, European Countries, American Countries. Tumeshuhudia juzi wenzetu wa EU tuko nao wamekuja kutusaidia hiyo Euro milioni sitini lakini pia tumeshuhudia wenzetu wa Marekani jana tu wametoa vifaa vya kijeshi kwa Wizara ya Mambo ya Ndani. Naomba kutumia nafasi hii Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje na kuwatakia kila la kheri.

Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii sasa kuishia hapa, nashukuru sana kwa kunipa fursa. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii
MHE. MBONI M. MHITA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa nami niweze kuchangia katika Wizara hizi nyeti. Naomba nitumie fursa hii kwanza nikiwa Mbunge mwanamke, kumshukuru sana Mheshimiwa Rais na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa namna ya kipekee na jinsi ambavyo amejitoa kuweza kuimarisha na kudumisha sekta ya afya nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kumpongeza sana dada yangu Mheshimiwa Ummy na kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile kwa namna ya kipekee kwa jinsi ambavyo wanatumikia Wizara hii kwa weledi wa hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amechukua initiatives za kipekee kabisa katika kuhakikisha kwamba, anamaliza changamoto kwenye Sekta ya Afya. Ushahidi wa kwanza ambao wengi ulituonyesha dhahiri kwamba Mheshimiwa ameamua kujitoa ili kuweza kumaliza changamoto hizi, ni pale alipoelekeza gawio la fedha zinazopatikana kutoka kwenye Kampuni ya Simu ya Airtel kuja na kujenga hospitali katika Makao Makuu ya Nchi hapa Dodoma. Ni Rais wa kizalendo sana anayeweza kufanya maamuzi hayo ya kishujaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tumeshuhudia katika kipindi hiki cha miaka minne ya utekelezaji Vituo vya Afya 352 vimejengwa Tanzania. Nasi wananchi wa Handeni Vijijini tulibahatika kupata shilingi milioni 800 ambazo tukazigawa kwenye Kituo cha Afya cha Kabuku pamoja na Kituo cha Afya cha Mkata. Hakuishia hapo, tumeshuhudia Hospitali za Wilaya 67 zikijengwa katika kipindi cha miaka minne tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu kwa haraka haraka mtu anaweza akaona ni chache, lakini tujikumbushe huko nyuma; toka tumepata uhuru tulikuwa na Hospitali za Wilaya 77 tu. Sasa sisi wenyewe tufanye hesabu hiyo, yaani toka tumepata uhuru tuna hospitali 77 dhidi ya miaka minne tu ambayo zimeongezeka hospitali za ziada 67. Kwa hesabu za haraka haraka hapo mtu unaweza ukajiongeza na ukaona. Hospitali 77 kwa miaka yote tangu uhuru versus miaka minne na upatikanaji wa Hospitali za Wilaya 67. Hiyo ni takriban amepiga jiwe kwa asilimia 70 ndani ya miaka minne. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, naendelea hapo. Katika kipindi hiki cha miaka minne tumeshuhudia ujenzi wa hospitali tano za mikoa; Njombe, Songwe, Katavi, Simiyu, Geita na Hospitali ya Kikanda Mtwara. Nadhani habari hii itamfurahisha sana mama yetu Mheshimiwa Riziki Lulida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie fursa hii pia kugusia kidogo kwenye mpango wa kidunia wa 90, 90, 90, ambapo mpango huu unasema asilimia 90 ya wale ambao ni suspects wa maambukizi ya UKIMWI wafikike na wapimwe. Asilimia 90 ya wale waliopimwa waweze kuanza kupata huduma ya dawa, lakini 90 ya mwisho ni wale ambao wameanza dawa, zile dawa ziweze ku-suppress yale maambukizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kuwapongeza sana Wizara ya Afya. Dada yangu Mheshimiwa Ummy na kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Faustine, Tanzania tuko mbali. Katika 90 ya mwanzo tuko kwenye 85% tunakwenda juu; 90 ya pili tuko kwenye asilimia 90; na tisini ya tatu tuko kwenye asilimia 90. Pongezi nyingi sana kwa Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna sehemu ambako kunakosekana changamoto. Changamoto ambayo tunaipata na ninaamini kwamba Wizara iko katika hatua za mwisho kabisa kutatua changamoto hii ni changamoto ya watumishi. Naomba nigusie Jimbo la Handeni Vijijini. Handeni Vijijini tuna changamoto kubwa ya watumishi kwenye Sekta ya Afya. Katika hitaji la watumishi asilimia 100, sisi tuna access ya watumishi asilimia 25 tu. Kwa lugha nyingine ni kwamba, tuna uhaba wa asilimia 75, yaani katika hitaji la watumishi 896 sisi tuna watumishi 226.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutumia fursa hii kushauri Wizara, naelewa wazi kwamba Wizara iko kwenye hatua za mwisho kabisa kuweza kutatua changamoto hii ya kuajiri. Ushauri wangu na wito wangu, namwomba sana dada yangu na kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Faustine basi mpango huu waweze kuufanya kwa uharaka, ili kuweza kumaliza changamoto hii ya uhaba wa watumishi kwenye Sekta ya Afya katika maeneo mbalimbali, hususan Jimbo la Handeni Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana.