Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mattar Ali Salum (15 total)

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kunipa nafasi hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa tunafahamu majengo haya yanazidi kuwa magofu na baadaye gharama, fedha za Serikali zinapotea kwa wingi kwa sababu haya baadaye yanabomoka tu, vilevile watu wanafugia ng‟ombe. Je, Mheshimiwa Waziri, ni lini Wizara itampatia Mkandarasi huyu amalize kituo hiki? Je, Wizara itachukua jitihada gani kuhakikisha kituo hiki kinamalizwa mapema? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kituo hiki ambacho kimeanza kujengwa mwaka 2011 kimechukua muda mrefu kukamilika. Hata hivyo, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Mkokotoni, Mheshimiwa Juma Hija ambaye naye amekuwa akifuatilia kwa karibu ujenzi wa kituo hiki. Nilichomwambia ambacho naendelea kukizungumza hapa mbele ya Bunge lako Tukufu ni kwamba, ni kweli tumempatia tayari Mkandarasi karibu shilingi milioni 50 ili kuweza kukamilisha hiki kituo, lakini bado kuna deni ambalo anahitajika alipwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefikiria kwamba, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, tuweze kushughulikia madeni ya Wakandarasi mbalimbali ambao wamekuwa wakifanya kazi za vituo katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu ikiwemo Mkandarasi ambaye anajenga Kituo hiki cha Mkokotoni.
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafsi hii, kwanza nishukuru sana kwa kuwepo kwangu hapa leo.

Mheshimiwa Waziri hizi ajira kwa upande wa kule kwetu Zanzibar zimekuwa hali ngumu kweli upatikanaji wake na ili uipate basi ufanye kazi ya ziada kubwa sana. Je, ni kwa nini Wizara yako isikae na Wizara husika ya Zanzibar ajira hiyo ipitie sehemu ya JKU peke yake?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kwanza nataka nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara yangu imeshakaa na Wizara inayoshughulikia vikosi vya SMZ na katika mazungumzo yetu tumewaeleza kwamba sisi tutatoa nafasi za kujiunga na JKT kupitia Wizara hiyo. Na ni hiari yao wao Wizara hiyo inayoshughulika na vikosi kuamua endapo watawachukua vijana walioko JKU ili waje kujiunga na JKT au watazigawa kama wanavyozigawa sasa kupitia Wilaya na Mikoa.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, ninachosema ni kwamba kukaa tumeshakaa, uamuzi bado unabaki kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Nataka nifahamishe Bunge lako Tukufu kwamba, kuna idadi maalum isiyopungua vijana 300 kila mwaka, zinapelekwa kama nafasi za kujiunga na JKT kutoka Zanzibar.

Kwa hiyo, vijana hao huwa wanapatikana kwa njia tofauti Wilayani na Mikoani na hatimaye wakishajiunga na JKT wakati wa usaili wa vyombo vya ulinzi na Usalama vyote, Jeshi la Wananchi lakini pia Magereza, Uhamiaji, Polisi na kadhalika wanachukua vijana kutoka JKT na wale ambao wana sifa zinazotakiwa wanapata ajira katika vyombo hivyo.

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kero hii inalalamikiwa sana na wafanyabiashara wetu na hufikia hatua kupoteza wafanyabiashara hawa kuendelea na biashara. Je, ni lini Wizara hii itaanza utatuaji wa kero hii kwa wafanyabiashara wote?
Swali la pili, Wizara itamaliza lini kero hii ya kutatua suala hili la kodi ya wafanyabiashara wanaotoka Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, utofauti huu unatokana na tatizo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutokutumia mfumo nilioutaja kwenye jibu langu la swali la msingi. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuishawishi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kujiunga na mifumo inayotumika ndani ya Idara ya Forodha ili kuondoa changamoto hii inayowakumba wafanyabiashara wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba, progress ni nzuri na kwa kuanzia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika bajeti yake ya mwaka 2016/2017 imeridhia kutumia mfumo wa Import Export Commodity Database kwa bidhaa ya magari yatakayoingia Zanzibar ili kuweza kuondoa changamoto hii. Kwa hiyo, naona huu ni mwanzo mzuri. Tunaendelea kuishawishi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iweze kujiunga moja kwa moja kwa bidhaa zote zinazoingizwa Zanzibar na hatimaye kuletwa Tanzania Bara.
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mweyekiti, ahsante sana kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nisawazishe jina langu, mimi naitwa Mattar Ali Salum, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri akilijibu alijibu vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake ambayo ameyatoa.
Mheshimiwa Waziri, wapo wanafunzi wanaendelea kupata mikopo ya Serikali kwa kima kidogo hadi sasa, husababisha kukosa kukidhi mahitaji ya vyuo husika ambavyo wamepangiwa. Je, Serikali ni kwa nini isiwaongezee fedha wanafunzi hawa ili waweze kukidhi mahitaji ya vyuo husika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wako wanafunzi walikuwa wakipata mikopo kwa kipindi kirefu, ghafla Serikali imewafutia mikopo yao, sijui ni kwa nini. Je, Mheshimiwa Waziri, Serikali ina mpango gani wa kuwarejeshea mikopo hawa wanafunzi ili waweze kukidhi na kuendelea na masomo yao vizuri? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama alivyorekebisha jina lake, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba kiuhalisiatulingependa kutoa mikopo kwa wanafunzi wengi zaidi, lakini vilevile ingewezekana hata kila mwanafunzi akapata mkopo kwa kadiri ya mahitaji ya chuo anachosoma; lakini kwa sababu fedha hazitoshi inakuwa ni vigumu kufanya hivyo na tunaangalia zaidi ni uhitaji wa kiasi gani upo.
Kwa hiyo, kwa misingi hiyo niseme tu kwamba, Serikali itaendelea kutenga fedha ya kuona kwamba, inawasaidia wanafunzi wengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuhusu kufuta mikopo. Ni kweli kuna baadhi ya wanafunzi walifutiwa mikopo kutokana na kutokuwa na vigezo vinavyostahili. Hata hivyo Serikali imeendelea kulifanyia kazi suala hilo ili kuona kwamba, anayefutiwa mkopo iwe kweli ni mtu ambaye hana uhitaji. Kwa yule mwenye uhitaji na kwamba vigezo vyote vimetimia basi, baadhi yao tumeweza pia kuwarejeshea.
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, lakini nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo ameyatoa. Nina maswali mawili madogo ya kuuliza.
Mheshimiwa Spika, zipo nyumba za zamani kabisa ambazo wanajeshi wetu wanazitumia hadi sasa na hali yake siyo nzuri kabisa.
Je, Wizara ina mikakati gani ya kuzifanyia marekebisho angalau zikaendana na hali ya sasa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Katika majibu ya msingi ya Mheshimiwa Waziri, amesema hana uhakika kama atajenga nyumba Unguja kwa awamu hii.
Je, ni lini anaweza kutueleza anaweza akatuanzia nyumba za Unguja wakati Unguja bado pana matatizo makubwa ya nyumba za kijeshi? Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Spika, kuhusu nyumba za zamani kufanyiwa ukarabati, hilo liko katika bajeti zetu. Nataka niwaeleze tu kwamba kwa kawaida bajeti inakuwa na miradi mipya na fedha za ukarabati.
Mheshimiwa Spika, sasa kwa mwaka huu wa fedha tuliweka fedha za ukarabati katika Bajeti ya Ngome na ni mategemeo yetu kwamba fedha zikipatikana tutakuwa tukirekebisha nyumba hizo awamu kwa awamu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, ni lini za Unguja zitajengwa? Kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi ni kwamba mchakato wa mazungumzo ya kupata fedha ajili ya kumalizia awamu ya pili unaendelea na utakapokamilika tu, basi bila shaka tutaanza awamu hiyo. Nataka nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba awamu hiyo itahusiaha kambi zilizokuweko upande wa Unguja.
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa jibu lake zuri. Vilevile lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Masauni kwa ziara aliyoifanya ndani ya Jimbo langu na kupunguza uhalifu, nimpe hongera sana. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Je, ni lini nyumba hizi zitaanza kujengwa kwa upande wa Unguja?
Swali la pili, kuna vituo vya polisi ambavyo hali yake ni mbaya sana kwa sasa hasa ukiangalia kama kituo cha Ng’ambu pamoja na Mfenesini na vipo vingi ambavyo hali yake ni mbaya sana, je, Serikali ina mkakati gani wa kuvifanyia marekebisho vituo hivyo angalau vilingane na hadhi ya Jeshi la Polisi kwa sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru sana kwa pongezi zake. Ni kweli Jimboni kwake kuna eneo ambalo lilikuwa ni hatarishi sana kwa usalama wa wananchi na tulifanya ziara pamoja na yeye na tukaweza kuchukua hatua. Napongeza sana Jeshi la Polisi kwa kuweza kudhibiti ile hali. Sasa hivi nimeambiwa kwamba hali ni shwari na wananchi wanafanya shughuli zao vizuri. Kuhusiana na hizi nyumba kwamba ni lini zitajengwa, ni pale ambapo taratibu za kifedha zitakapokamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lingine anazungumzia kuhusu vituo vya polisi kwamba vina hali mbaya. Ni kweli tuna matatizo ya vituo vya polisi, siyo tu vina hali mbaya, lakini ni pungufu. Tuna upungufu wa takribani vituo 65 hasa katika Wilaya za Kipolisi nchini. Kwa hiyo, hili vilevile linakwenda sambamba na hali ya kibajeti. Pale ambapo hali ya kibajeti itaruhusu tutajenga vituo vipya katika maeneo ambayo hakuna, lakini vilevile kukarabati vile ambavyo viko katika hali mbaya.
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake ambayo yanaridhisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wako wafanyabiashara wanaendelea kuingiza na kufanyabiashara ya vipodozi hivi ndani ya nchi na vipodozi hivi vinawapatia madhara wananchi wetu kwa kiwango kikubwa sana, wanapata maradhi makubwa kutokana na vipodozi hivyo. Je, Serikali yako inatoa kauli gani iliyokuwa kali kuhakikisha hawa wafanyabiashara hawatoingiza wala hawafanyi tena biashara ya vipodozi hivi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali ina mkakati gani wa kuwasidia wale watumiaji ambao wametumia vipodozi hivi bila kuvitambua kurudi katika hali yao ya kawaida? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mattar Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo. Niendelee tu kusisitiza kwamba Serikali inaendelea kuimarisha ukaguzi katika vituo vyake kama nilivyoainisha hapo awali, tunaendelea kuboresha maabara zetu, lakini vilevile sasa hivi nimezungumzia kifungu cha adhabu tunafikiria kukiboresha zaidi ili kutoa adhabu kali kwa wale ambao wanaingiza vipodozi haramu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili lilikuwa linauliza je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wahanga wa vipodozi vilivyo chini ya viwango. Kwa sasa hivi Serikali hatuna mkakati wowote wa kuwasidia wale wahanga, lakini tunachokifanya ni kutoa elimu ya kutotumia vipodozi ambavyo havijasajiliwa nchini. Vilevile tunashirikiana na mamlaka mbalimbali ikiwa ni pamoja na TFDA, Polisi na Halmashauri kubaini vipodozi ambavyo vimeingia nchini kinyume cha taratibu na kuvikamata na kuchukua hatua stahiki kwa wale ambao wanahusika.
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri Mheshimiwa Masauni, nina maswali mawili ya nyongeza.
Je, ni lini Serikali au Wizara yake itaanza kufanya ukarabati wa nyumba hizo?
Swali la pili, nafahamu Wizara ina mpango mzuri wa kulinda raia na mali zake, kuna kituo cha Shaurimoyo, kuna kituo kidogo cha Mwembeladu lakini vituo hivi vimefungwa kwa muda mrefu sasa.
Je, ni lini Wizara yake itavifungua vituo hivi na kuendelea na kazi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, anauliza ni lini ukarabati huo utaanza. Kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi kwamba pale tu ambapo tutaweza kupata fedha tuaanza huo ukarabati. Kwa hiyo, siwezi kusema exactly ni siku gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia swali lake la pili alikuwa alitaka kujua kwa ni nini kituo cha Shaurimoyo pamoja na kituo cha Mwembeladu havitumiki. Kituo cha Shaurimoyo hakitumiki kwa sababu kwanza, takwimu zinaonyesha kwamba eneo hilo la Shaurimoyo halina uhalifu.
Lakini pili kuna vituo vingi sana ambavyo vipo karibu na kituo cha Shaurimoyo ikiwemo kituo cha Ng‟ambo, kituo cha Mwembemakumbi na Makadara ambapo imezidi maili moja kutokea kituo kilichopo kituo cha Shaurimoyo. Kwa hiyo, kwa kutilia maanani kwamba hali ya kituo hicho siyo nzuri kituo kimechakaa sana tumeamua kituo hicho kwa sasa hivi kitumike kwa ajili ya matumizi ya Polisi Jamii na wananchi wanaendelea kutumia vituo vilivyo karibu na kituo cha Shaurimoyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusiana na kituo cha Mwembeladu ambapo kipo mpakani mwa Jimbo langu vilevile, kituo hiki kilijengwa kwa ajili ya matumizi ya traffic, lakini kutokana na mkakati wa kipolisi wa matumizi ya shughuli za ki-traffic Wilaya, uratibu huo unafanyika katika kituo cha Malindi ambacho nacho hakipo mbali sana na eneo hilo. Pia miundombinu ya kituo cha Mwembeladu haikidhi haja ya kufanya shughuli za traffic kwani hata ukikamata magari siyo zaidi ya gari moja linaweza kukaa katika eneo hilo. Kwa hiyo, kwa kutilia maanani hoja hizo kwa sasa hivi tunaangalia uwezekano wa kubadilisha matumizi ya eneo ili tuweze kupata maeneo mengine ya kuweze kuimarisha shughuli za traffic badala ya kutumia kituo cha Mwembeladu.
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwa kunipa nafasi hii kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa baadhi ya majibu yake yamekuwa mazuri, lakini katika majibu yake anasema kutokana na usafiri huu hautoshelezi, bado wananchi wetu wanapata taabu sana kupatikana usafiri huu wa kwenda Pemba. Wananchi wetu wanafika kulala bandarini kusubiri meli ya kwenda Pemba. Sasa ni kwa nini Serikali isitenge bajeti mahususi kwa ajili ya kununua meli ili iweze kufanya kazi hizi kuwahudumia wasafiri wetu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, bado usafiri huu ni ghali sana kwenda Zanzibar na kwingineko, sasa ni kwa nini Serikali isiingize mkono wake kuzisaidia kampuni hizi kwa wakati huu ili bei ya tiketi zishuke zisiwe hapa zilipo? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama nilivyokiri katika swali la msingi kwamba usafiri wa majini kuelekea visiwa vya Pemba na Unguja hautoshelezi. Na ndiyo maana nikatoa wito kwa wawekezaji wengine wanaoweza kutoa huduma hizo wajitokeze kwa wingi washirikiane na Serikali katika kutoa huduma hiyo. Naamini watakapofanya hivyo matatizo yatapungua kwa kuwa ni kweli kabisa tunakiri kwamba bado kuna changamoto ya usafiri wa majini kwa ajili ya kutoka Dar es Salaam au Tanga kwenda visiwa vya Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu gharama; kwanza kabisa, Serikali inazo meli mbili; kuna MV Maendeleo halafu MV Mapinduzi, zote zilinunuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, lakini bahati mbaya sasa hivi zipo kwenye matengenezo na marekebisho mbalimbali. Ninaamini zitakapokuwa katika hali yake ya kawaida zitasaidia katika kutoa huduma kwa wananchi wa visiwa vya Pemba na Unguja na bei itapungua. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri anafanya kazi vizuri, lakini nimfahamishe Mheshimiwa Waziri eneo hili la uvuvi na ununuaji wa meli za uvuvi na ujengaji wa Bandari ya uvuvi ni suala very important lazima tulifanyie kazi kwa kina. Sasa swali la kwanza, Shirika la TAFICO ni lini litakamilika ili hizi meli ziweze kununuliwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kila siku tunasema tuna wataalam ambao wanafanya upembuzi yakinifu, lakini nimwambie Mheshimiwa Waziri hebu atueleze ni lini hawa wataalam watakamilisha huu upembuzi wao yakinifu ili hii bandari ya uvuvi iweze kujengwa kwa maslahi ya Watanzania. Ahsante.
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kama ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza hapa kwamba tumeshampata mshauri elekezi na tayari ataingia mkataba mwezi huu huu na kulipwa malipo ya awali na atafanya kazi ndani ya miezi nane. Baada ya miezi nane tayari tutakuwa tumeingia hatua sasa ya ujenzi wenyewe. Kwa hiyo, atuvumile katika hiyo hatua, Mshauri Elekezi ameshapatikana na tayari zoezi litaanza. (Makofi)
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Alhaji Masauni.
Mheshimiwa Spika, wapo askari wanaowaweka ndani watuhumiwa zaidi ya saa 24 wakati hawana makosa ya kuwekwa ndani zaidi ya saa 24. Serikali inawachukulia hatua gani askari hawa wakibainika wanakiuka Sheria za Jeshi la Polisi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Watanzania wengi hawana elimu ya Sheria ya Jeshi la Polisi. Serikali ina mkakati gani wa kutoa elimu ili Watanzania wakafahamu haki yao ya kimsingi ili waweze kujua taratibu za kuwekwa ndani zaidi ya saa 24 na sheria ambazo haziwahusu kuwekwa ndani zaidi ya saa 24? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, nataka nimjibu Mheshimiwa Mattar kwamba sheria niliyoizungumza inahusisha watu wenye makosa ya aina ambayo nimeyataja.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama kutakuwa kuna Askari Polisi ambaye amemweka mtu ndani na hakufanya makosa ambayo nimeyataja, naye Mheshimiwa Mattar anamfahamu, basi ni wajibu wake kuweza kuwasilisha taarifa hiyo ili tuweze kuchukua hatua kama ambavyo tumefanya kwa askari wengine wenye makosa mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, katika kipindi cha miezi sita ya mwaka huu, takriban askari 15 ambao walifanya makosa ya kukiuka maadili ya utendaji wao wa kazi ambao tumeweza kupokea taarifa zao na kati ya hao mpaka sasa hivi tayari askari wawili wameshachukuliwa hatua. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mattar kama ana taarifa hizo aziwasilishe katika mamlaka husika ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, suala la elimu linaendelea kutolewa na ni wajibu wa kila mtu akiwemo yeye Mheshimiwa Mbunge kuweza kutusaidia kutoa elimu kwa wananchi wake, ingawa kutokufahamu sheria hakuhalalishi juu ya uvunjifu wa sheria.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi kwamba tutaendelea kujitahidi kadri itakavyowezekana watusaidie Waheshimiwa Wabunge akiwemo Mheshimiwa Mattar kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na ufahamu wa sheria mbalimbali katika nchi yetu. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba niongezee majibu ya nyongeza kwenye majibu mazuri ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ameyasema.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kulikuwa na malalamiko kwa wananchi kwa kuwekwa ndani na baadhi ya askari ambao sio waaminifu, siyo waadilifu kwenye makosa ambayo hayastahili, lakini pia wamekuwa wakiwaweka ndani baadhi ya wananchi kwenye makosa ambayo pia hayahitajiki hata kuwekwa ndani, hata nusu dakika au sekunde.
Mheshimiwa Spika, tayari nimeshatoa maelekezo kwamba Makamanda wote wa Polisi wa Mikoa na Wakuu wa Polisi wa Wilaya, kituo chochote ambacho kitaonekana na malalamiko ya kukiuka utaratibu huu wa kuweka wananchi ndani, viongozi hao watawajibika. Hivi karibuni nitaanza ziara kwenye mikoa yote ya Tanzania pale ambapo nitakuta vituo, askari bado wanalalamikiwa, askari hao hawatakuwa na nafasi ya kuendelea kulichafua Jeshi zuri la Polisi ya nchi yetu.(Makofi)
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali la kwanza, kuna askari ambao wanawaweka ndani wananchi wetu bila ya kuwa na makosa ya kuwekwa ndani. Vilevile, wengine wanawaweka ndani zaidi ya saa 24 wakiwa hawana makosa ya kuwekwa ndani saa 24. Je, Wizara yako inatoa kauli gani juu ya Maaskari hawa kuhakikisha wanaepuka kuwaweka ndani wananchi wetu zaidi ya saa 24?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Watanzania wengi hawana elimu ya sheria hii ya Jeshi la Polisi. Je, Serikali ina mikakati gani ya kutoa elimu kwa wananchi wetu ili waweze kujua haki zao za msingi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mattar, Mbunge wa Shaurimoyo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu la msingi nilieleza kwamba ukiachilia mbali Kifungu 148(5) ambacho kimeainisha makosa ambayo hayana dhamana, lakini kuna Kifungu cha 65 pamoja na 66 vya sheria hiyo hiyo ambayo vinaeleza ni kwa jinsi gani hayo makosa ambayo yana dhamana itatolewa kwa utaratibu upi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Kifungu cha 65 kinaeleza umuhimu wa kufahamu historia na familia ya mhusika lakini kifungu cha 66 kinaeleza kwamba mtuhumiwa huyu ambaye anaomba dhamana anatakiwa aweze kuandika kwa mkono wake kwamba atarudi siku ya kesi yake itakapokuwa imeitwa. Kwa hiyo, pamoja na mambo mengine, dhamira kubwa ni kuona jinsi gani mtu huyu anapoachiwa kwenda nje hawezi kuwa hatari kwa usalama wake mwenyewe ama kwa jamii ambayo inamzunguka. Kwa hiyo, inawezekana labda wananchi wanashindwa kufahamu kwamba Polisi wanapomweka mtu zaidi ya saa 24 wakati makosa yana dhamana kwamba kuna mambo ambayo masharti yake hayajatimizwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitutoe wito kwa wananchi kuweza kutumia fursa ya Jeshi letu la Polisi pamoja na Serikali kwa ujumla tunapoweza kuzungumza mara kwa mara kuwaelimisha ili wafahamu sheria za nchi yetu na wafahamu haki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni jukumu la Wabunge kuweza kuwaelimisha wananchi wetu ikiwemo Mheshimiwa Mattar kupitia mikutano yake mbalimbali katika jimbo lake…

MWENYEKITI: Ahsante.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: …atumie fursa hiyo kuweza kuwawezesha wananchi kufahamu sheria za nchi hii ili waweze kuepuka madhara…

MWENYEKITI: Haya, ahsante sana Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Selasini.
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, ameeleza suala la sheria tofauti. Nimfahamishe Kenya na Tanzania tuna sheria tofauti, Uganda na Tanzania kuna sheria tofauti lakini bado magari ya Kenya yanapewa kibali kwa urahisi kuweza kutembea Tanzania Bara lakini magari yanayotoka Zanzibar mpaka uweke deposit (pesa nyingi) ambapo ndiyo unaweza kupewa kibali cha kutembelea Tanzania Bara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimuulize Mheshimiwa Waziri wana utaratibu gani utakaokuwa rahisi kuweza kusaidia watu wa Zanzibar kuweza kutembelea gari ndani ya Tanzania Bara? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali moja la Mheshimiwa Mattar, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu rahisi uliopo ni huo uliopo sasa mpaka pale sheria nilizozieleza kwenye jibu langu la msingi zitakaporekebishwa kwa pamoja.
MHE. MATTAR ALI SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Bandari ya Zanzibar kiukweli kwa sasa imekuwa ndogo sana na haiwezi kufanya kazi lakini Serikali zetu zimefanya mazungumzo na Benki ya Exim ya China, mpaka leo ni kimya hakuna kinachoendelea mpaka sasa. Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha hii bandari ya Mpigaduri inajengwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mattar kwa sababu mara nyingi nimemsikia akizungumzia sana juu ya Bandari ya Mpigaduri. Mheshimiwa Matar nikuhakikishie kwamba kweli Serikali imefanya kazi kubwa, kumekuwa na hatua mbalimbali, jitihada nyingi zimefanyika kupanua bandari na wewe unafahamu kwamba juhudi za kupanua bandari zimeanza muda mrefu tangu mwaka 2011 lakini hatua ambayo imefikia sasa hivi baada ya hiyo Benki ya Exim kuchukua hatua za kufanya funding kwa ajili ya upanuzi wa bandari hii sasa hivi draft financial agreement ilishasainiwa kwa hiyo wanafanya mapitio ya mwisho ili sasa kwenda kwenye hatua ya kwenda kwenye financing na kuanza kufanya maboresho Bandari hii ya Mpigaduri au Maruhubi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana. Watanzania wengi wanapata hasara kubwa sana katika hili suala abiria akichelewa boti tu tiketi yake imekufa kabisa hawezi kutumia kwa wakati mwingine wowote inasababisha kadhia kubwa kwa Watanzania wetu.

Hakuna Shirika lolote la Ndege duniani ambalo ukichelewa tiketi yake inakuwa imekufa, unalipa kiwango cha fedha kama ni dola 50 tiketi yako inaweza kuendelea kufanya kazi, hata Shirika letu hili la Tanzania pia hata ukichelewa unaweza kupanda ndege kwa wakati mwingine lakini Kampuni hii ya Azam Marine ukichelewa tiketi imekufa kabisa wala huwezi kutumia tena ni jambo la ajabu sana. Sasa ni lini Serikali itaondosha kadhia hii ili hawa abiria wetu wapate maslahi makubwa kutumia vyombo hivi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, kwanza siyo kweli kwamba mashirika yote ya ndege huwa tiketi yake ukichelewa yanarudishwa kuna zile Easy Jets ambazo kwa mfano Fastjet ukichelewa tiketi huwa haurudishiwi wala haupangiwi safari siku nyingine kwahiyo siyo kwamba ni mashirika yote ya ndege.

Mheshimiwa Spika, pia najaribu kuwashauri hata Watanzania wenzetu unapokuwa umepanga safari basi ujue kwamba kuna muda wa kuondoka na muda wa kufika. Haiwezekani tuwe tuna panga safari halafu unafanya mambo mengine tofauti na safari yako.

Katika majibu yangu ya msingi nimeeleza tu kwamba Shirika la Azam Marine huwa lina utaratibu ukitoa taarifa mapema tena waliandika kwenye tiketi yao nyuma ukitoa taarifa mapema kabla ya safari kwamba hutasafiri wana utaratibu wa kuiuza hiyo tiketi kwa watu wengine ili wewe wakupangie wakati mwingine, lakini sasa muuliza swali Mheshimiwa Mbunge yeye nafikiri anafikiri kwamba akishachelewa bila kutoa taarifa anaweza akapewa, sasa yeye Azam Marine atakuwa ameingia hasara kitu ambacho siyo kweli.

Mheshimiwa Spika, nawashauri Watanzania tupange safari zetu tuwe na uhakika wa kusafiri siku husika, tujiandae, halafu tuweze kuwahi ili tusipate matatizo kama hayo. (Makofi)