Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mattar Ali Salum (17 total)

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Ulinzi. Vilevile nampongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi yake nzuri anayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile nachukua nafasi hii kuwapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kumaliza uchaguzi wao kwa salama na amani na kuhakikisha CCM imeshinda kwa kishindo kikubwa Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Waziri wa Ulinzi kwa hotuba yake nzuri na bajeti yake nzuri inayoashiria mafanikio makubwa sana, ahsante sana kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwinyi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia na nitagusia kuhusu majengo ya makazi ya askari. Makazi ya askari imekuwa bado ni changamoto kubwa. Namwomba sana kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwinyi aweze kujitahidi kufanya kazi yake kuhakikisha kwamba askari wetu wanapata makazi bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya kikosi hicho wamo mafundi wazuri sana wenye uwezo wa kufanya kazi zao kwa uhakika, wenye ujuzi mzuri katika Jeshi letu la Tanzania. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri aweze kutumia vijana hawa ili kuleta maendeleo ya nchi yetu hata yale majengo yanayojengwa na Jeshi letu la Kujenga Taifa, basi waweze kujenga mafundi hawa kutoka ndani ya Jeshi hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nigusie sasa suala la majengo. Nimefurahi sana kusoma katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri kuwa kuna majengo takribani 5,000 ambayo anaendelea kuyajenga. Basi naomba sana kila ukiendelea kuyajenga majengo hayo, basi aweze kuwatumia wanajeshi hao kuhakikisha kwamba tunapunguza matumizi makubwa kuliko kuwapa wakandarasi wa nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika kusimamisha majengo hayo kwa upande wa Unguja, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aangalie kwa upande wa Unguja, wanajeshi wetu kule Unguja wanahitaji majengo haya na mpaka sasa wanakaa katika majengo ambayo siyo mazuri. Kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri ufanye jitihada zako binafsi kuhakikisha kwamba na upande wa Unguja unapata majengo mazuri. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, atakapokuja hapa ndugu yangu, Mheshimiwa Mwinyi, alieleze Bunge lako hili, kwa upande wa Unguja ni lini wanajeshi wetu wataanza kujengewa nyumba mpya? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea na kuchangia mchango wangu huu, niongelee kuhusu uchukuaji wa vijana na kupeleka JKT. Mheshimiwa Waziri, naamini kama Serikali ina nia nzuri ya vijana wetu kuwaajiri na kuwapa ajira. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri anapotaka kuchukua vijana hawa kuwapeleka ndani ya JKT, kwanza aangalie uwezo wake wa kuchukua vijana hawa. Vilevile achukue vijana wenye uwezo wa kuajiriwa na sifa za kuajiriwa. Mheshimiwa Waziri vijana hawa kuwachukua na kuwapeleka ndani ya JKT, watakuwa wamepata mafunzo. Vijana hawa wanakosa ajira na baadaye wanarudi mitaani. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, nakuomba sana kaka yangu, wanaporudi mitaani vijana hawa, basi inakuwa ni tatizo. Tunajijengea uadui sisi wenyewe. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kaka yangu, unapotaka kuchukua vijana, jipime na uwezo wako wa kuweza kuajiri pasipo na kuwabakisha kurudi mitaani tena. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Zanzibar tuna kikosi chetu cha JKU. Hiki kikosi ni imara, kizuri, kina mafunzo mazuri. Mheshimiwa Waziri nikuomba sana, hiki kikosi kinafanana na kikosi cha JKT. Nakuomba sana kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwinyi, kaka yangu mpendwa, uweze kuendeleza ushauri pamoja na Wizara husika ya Mapinduzi Zanzibar kuhakikisha vijana hawa unawachukua na kuwaweka pale ndani ya kikosi cha JKU, baadaye vijana hawa ndiyo uwachukue katika ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri vijana hawa ukiwaweka pale, basi nafikiri unaweza ukapata mafanikio mazuri na naamini utapata vijana wazuri wa kuwaajiri. Siyo kuwapeleka JKT na baadaye ukawarejesha tena Zanzibar. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, naamini Waziri wewe ni Waziri msikivu, mchapakazi, maoni yangu utayachukua kwa kina. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, utoaji wa ajira kwa upande wa Zanzibar. Bado hali siyo nzuri kwa utoaji wa ajira, vijana wetu ambao wanachukuliwa mpaka sasa ni vijana 300 tu. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, nakuomba sana kaka yangu, ajira ambayo imetoka takriban watu 5000. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba sana Mheshimiwa Waziri kwa upande wa Zanzibar nakuomba sana at least tupate vijana 500 angalau ifike asilimia 10 ya vijana ambao wanachukuliwa kutoka Zanzibar kwenda kuajiriwa ndani ya vikosi hivi vya Muungano. Mheshimiwa Waziri, bado hali siyo nzuri katika kuajiri hawa vijana, bado idadi yetu ni ndogo. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri ulione ili kuhakikisha vijana hawa wanapata ajira nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la Jeshi la Tanzania kutumika Zanzibar. Zanzibar ni kati ya sehemu moja ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nilishangaa sana, kuna Wabunge wanasema wanashtushwa na Kikosi cha Jeshi kutumika upande wa Zanzibar. Hili ni Jeshi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; likifanya kazi Zanzibar, Tanzania Bara, likifanya kazi Dodoma, linafanya kazi kwenye Katiba. Hili linaruhusiwa kufanya kazi popote kwa sababu hili ni Jeshi la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lina uhalali wa kufanya kazi mahali popote bila kupingwa na yeyote, ni kutokana na Katiba inayowaruhusu kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sana Wabunge wenzangu tuliachie Jeshi letu pendwa, Jeshi letu makini, Jeshi letu zuri liendele kufanya kazi zake kama ipasavyo. Tuliachie Jeshi, tusiliingilie katika kufanya kazi katika matakwa yake ya kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uchaguzi wa Zanzibar umeshamalizika tarehe 20 Machi, 2016 hautarudiwa tena, kilichobaki ndani ya Bunge hili tuje kuchangia mambo mengine; tuchangie bajeti ya ulinzi kuliboresha Jeshi letu kuendelea kufanya kazi, siyo ku-discuss masuala ya Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja mia kwa mia.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikupongeze wewe binafsi, kwa Waislamu tuna kauli tunasema Wallah umependeza kwenye Kiti hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri ambayo ameitoa mbele ya Bunge hili. Nimpongeze sana kwa hatua hii aliyochukua, bajeti hii imekaa vizuri na wananchi wengi wa Tanzania wamejenga imani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nigusie kuhusu bidhaa zinazotengenezwa Tanzania Bara na kuuzwa Zanzibar kutozwa kodi Zanzibar na bidhaa zinazotengenezwa Zanzibar na kupelekwa Tanzania Bara kutozwa kodi Tanzania Bara. Hatua hii ni nzuri sana, inatia faraja sana kwa wafanyabiashara wetu. Hatua hii ambayo imechukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kigezo chote cha kuondosha migogoro ya wafanyabiashara wetu, kupunguza kelele na mizozo isiyokuwa na maana kwa wafanyabisahara wetu. Niwaombe sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iweze kukusanya kodi hii kwa nguvu zake zote bila ya kuwa na kitatanishi chochote kwa sababu kodi hii kipindi kirefu ilikuwa hailipwi na inaleta usumbufu mkubwa kwa wafanyabishara wetu na kupelekea kuwa na mzozo usiokuwa na maana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hatua hii iliyochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Wizara husika kutoza kodi hii upande wa Zanzibar imesaidia kwa kiasi kikubwa ukusanyaji wa kodi kwa upande wa Zanzibar kukua, hata maisha ya upande wa Zanzibar basi yatakua ya hali ya juu kabisa. Kwa sababu kuna wafanyabiashara wachache walikuwa wakitumia mwanya huu vibaya kwa kuhakikisha hawalipi kodi hii kwa kuwa bidhaa hii inatengenezwa upande mmoja wa Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri afanye mazungumzo na Wizara ya Fedha ya Zanzibar ili na wao waweze kutumia mashine za EFD kwa ajili ya kukusanya vizuri kodi zake kwa sababu Zanzibar ukusanyaji wa kodi bado uko chini. Naamini Mheshimiwa Waziri anakaa na Wizara hii basi nimuombe sana kuhakikisha kwamba anawashauri wakusanyaji wa kodi wa Zanzibar, anaishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wafanyabiashara wetu wa kule Zanzibar waweze kutumia mashine hizi za EFD ili kuweza kukusanya kodi vizuri. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ambayo ameifanya kwa kugundua tatizo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nigusie vilevile maduka ya vyombo vya ulinzi kuondolewa msamaha wa kodi, hii ni hatua nzuri sana. Haya maduka kipindi cha nyuma watu wachache walikuwa wanatumia mwanya huu kujifaidisha kwa maslahi yao binafsi. Kwa hatua hii sasa itabana haya maslahi ya wachache. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri afanye jitihada binafsi kuhakikisha askari wetu wanapatiwa maslahi haya moja kwa moja wao wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nigusie mikopo ya elimu ya juu. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa kuwa imeongeza idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo hii. Serikali inachukua wanafunzi hawa inawapeleka katika vyuo vya watu binafsi, inawapa mikopo wanafunzi hawa lakini hivi vyuo binafsi gharama yake iko juu tofauti na vyuo vingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, naomba Serikali inapotoa mikopo kuwapelekea wanafunzi wa vyuo vya watu binafsi ifanye research mapema kabla ya kuwapeleka wanafunzi hawa katika vyuo hivyo kwani gharama zake ziko juu tofauti na vyuo vingine. Kwa hiyo, namuomba sana Mheshimiwa Waziri suala hili aliangalie kwa kina. Kiukweli wanafunzi wetu wanaosoma katika vyuo vya watu binafsi wanapata tabu, ada zake ziko juu mno. Inafikia mahali wanafunzi hawa hawafaidiki na mikopo hii ambayo imeandikwa humu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano ni Chuo cha Kampala International University (KIU). Chuo hiki kina wanafunzi wetu kutoka Tanzania ambao wanasoma hapa lakini jambo linalosikitisha zaidi ada ya Serikali wanayopelekewa wanafunzi hawa ni takribani Sh.3,100,000 lakini chuo hiki gharama zake ni takribani Sh.6,000,000. Namuomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie kwa kina tatizo hili. Wanafunzi hawa wanaendelea kupata taabu ndani ya vyuo hivi, wanashindwa hata kufanya mitihani yao, hata kuona yale matokeo yao wanashindwa kwa sababu ya kiwango kidogo cha fedha ambacho wanapelekewa katika vyuo hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba sana Mheshimiwa Waziri afanye kazi hii na nataka akija hapa aweze kueleza ni hatua gani Serikali itachukua kuwasaidia wanafunzi hawa kwa sasa ambao wanaendelea kupata shida. Wanafunzi hawa ni wa masomo ya sayansi wanasomea Udaktari na Serikali ina mategemeo makubwa na wanafunzi hawa. Kubwa zaidi wanafunzi hawa wanapewa mikopo ambayo watailipa, sasa ni kwa nini Serikali isiweze kuwapa mikopo ikakidhi mahitaji ya wanafunzi hawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kuhusu kuondoshwa kwa msamaha wa kiinua mgongo cha Mbunge. Kiukweli hili ni tatizo gumu sana. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, Ubunge wetu wa Majimboni ni tatizo sugu sana, ni tatizo kubwa. Mbunge Jimboni ni kila kitu, ni harusi, mchango wa mwenge lazima atoe. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, suala la kiinua mgongo cha Mbunge arudi tena kwenda kuliangalia pamoja na wataalam wake ili alipatie ufumbuzi mzuri. Suala hili kiukweli ndani ya Bunge lako hili Tukufu Wabunge wote akili zao hazifanyi kazi wanafikiria suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi. Pia nimpongeze Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kuwa Waziri Mkuu. Nimpongeze Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi sana na kuwa Rais wa Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Shaurimoyo kwa kunichagua mimi Mattar Ali Salum kuwa Mbunge wao, nawaahidi sitowaangusha.
Kuhusu kukabiliana na uamuzi wa kusababisha migogoro baina ya hifadhi zetu na watu wanaotumia kwa kulima au kufuga ndani ya hifadhi hizo, naiomba Wizara kukata mipaka na kugawa maeneo haya ili wakulima na wafugaji wapewe maeneo yao na kuweza kufanya shughuli bila ya kuingiliana na maeneo ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie upungufu wa watumishi na vitendea kazi ni mojawapo ya tatizo kubwa linalosababisha kuzorotesha kwa maendeleo ya utalii. Naomba Wizara ifanye kila linalowezekana kuongeza wafanyakazi na kuwaongezea uwezo watendaji wa Wizara kwa kuwapa vifaa vya kazi ili kuweza kukabiliana na ongezeko la utalii. Pia kupata wafanyakazi ambao wanajua utalii kwa kuwa utalii ni moyo wa uchumi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kupangua kwa watumishi na vifaa vya kutendea kazi husababisha kushuka kwa idadi ya watalii nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uvunaji wa mkaa unaathiri sana ubora wa misitu. Naomba Serikali kupambana na wavunaji mkaa ili kuondoa na kupunguza matumizi ya mkaa. Naomba Wizara kuendelea kushirikiana na Wizara nyingine juu ya uuzaji na ukataji wa mkaa na kuongeza juhudi kuhakikisha wananchi wetu wanaacha kuchoma mkaa na kupunguza kwa sana matumizi ya kuni, mkaa na kuanza kutumia matumizi mbadala kama gesi na umeme. Pia Wizara iwashauri wananchi wetu wote kuanza matumizi haya. Naiomba Serikali iwashauri au kuwapa ushauri wananchi wetu kuacha matumizi ya mkaa ili kulinda misitu yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali ipunguze gharama za gesi ili wananchi waweze kumiliki matumizi hayo wenyewe. Bei iliyopo hivi sasa ni kubwa sana kiasi kwamba hupelekea wananchi wetu kushindwa kutumia gesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara itoe mafunzo makubwa kwa wananchi wa vijijini ili waache ukataji wa miti ya kuchoma mkaa. Pia waache kupika kwa kutumia kuni na mkaa na waweze kutumia gesi. Nashauri Serikali kuongeza idadi ya pesa kwa kuongeza matangazo kwa kuwa sasa matangazo hayatoshi. Utengenezaji wa matangazo ndiyo sababu kubwa ya kukua kwa utalii wa nchi yetu na itazidisha mapato ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutolewa kwa mafunzo maalum kwa watumishi wa sekta ya utalii kutasababisha kupanda hali ya uchumi na pia kutengeneza ubunifu wa maeneo mengine ili kuweza kutumika na sio kubakia na yaliyopo tu. Nashauri Serikali kuongeza maeneo mengine, hii ni mojawapo ya kukuza utalii nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Zanzibar, namshukuru sana Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Jumanne Maghembe, pia naishukuru Wizara ya Utalii Zanzibar kwa kazi nzuri wanazozifanya, na sasa utalii umekua sana, watalii wanaongezeka kuja Zanzibar, na ni watalii wengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana, kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia siku ya leo. Lakini vilevile nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa kazi nzuri ambayo anaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niwapongeze watendaji wake wote wa Wizara hii ya Mambo ya Nje na vilevile, nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri, ambayo anaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niwapongeze Mabalozi wetu kwa kazi nzuri, ambayo wanaifanya wakiwa katika kazi zao huko nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana, Mabalozi wetu walioko nje, hawa Mabalozi wetu wa Tanzania, wafanye kazi nzuri, tuwatumie katika kazi ya kutangaza utalii wetu tukiwatumia Mabalozi hawa katika kazi ya kutangaza utalii na kazi ya kutafuta Wawekezaji katika nchi yetu, basi naamini hata sekta ya utalii katika nchi yetu hii itakua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunaamini katika sekta ya utalii ikikua, basi ni chanzo cha uchumi wetu kukua, kwa kuwa, tunaamini uchumi wetu, hii sekta ya utalii inachangia asilimia kubwa katika suala kuongezeka uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namuomba sana Mheshimiwa Waziri tufanye kazi ya ziada tuhamasishe Mabalozi wetu na tuwaambie Mabalozi wetu wahakikishe kwamba wanatangaza utalii wetu wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatembelea Balozi za wenzetu, basi ni kazi kubwa wanayoifanya, unapofika Mheshimiwa Waziri jambo la kwanza wanakuonyesha utalii wa nchi za zao. Kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri tuweze kufanya kazi hizi na Balozi zetu ziweze kufanya kazi hizi kwa maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kufanya Mabalozi wetu tunawapenda sana. Vilevile wahamasishe katika kuwatafuta wawekezaji ili kuhakikisha kwamba, nchi yetu inatumia njia hii ya Mabalozi. Sio Mabalozi hawa kuwepo kule, ikawa ndiyo imemaliza kazi tu. Tunawatumia Mabalozi wetu kuhakikisha kama wanahangaika na kazi ya kuwatafuta wawekezaji ili nchi yetu ipate maendeleo kwa kuwatumia Mabalozi hawa, tusiwe na Mabalozi tumewaweka tu wakati kazi haifanyiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana Mabalozi hawa wafanye kazi ya ziada ili wafahamu kwamba nchi yetu tukiwapeleka kule na sisi tunawategemea kwa hali na mali, tunawategemea wafanye kazi kwa huruma zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, jambo kubwa linasikitisha sana hili. Jambo la makazi, jambo la majengo ya ofisi za Balozi zetu, hizi hali zimekuwa mbaya, haziridhishi kabisa haya majengo. Mabalozi wetu na watendaji wetu, wanafanya kazi katika wakati mgumu, na wanakaa pahala pabaya, zinafika hatua hata nyumba nyingine, zinafika hatua ya kuvuja na tukitegemea majengo haya yatafika hatua ya kuporomoka tutapata hasara kubwa katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie suala la watendaji wetu. Watendaji wetu katika sekta hii, jambo kubwa sana wanatakiwa wapewe mafunzo ya kutosha. Inaonekana wafanyakazi wetu, watendaji wetu bado mafunzo yetu katika ufanyaji wao wakazi, umekuwa uko duni sana. Naiomba Wizara yako, naamini Waziri wewe ni msikivu utafanya hii kazi, hawa wafanyakazi wetu waweze kupata mafunzo bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wafanyakazi wanapopata mafunzo ya uhakika, basi hata utendaji wao wa kazi, utakuwa wa kuboresha sana katika kazi hii ya kutangaza utalii wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyakazi wetu tukiwapeleka wanakuwa kama si wafanyakazi tofauti na Balozi wa nchi za wenzetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii lakini hujaniambia nitachangia dakika ngapi? MWENYEKITI: Dakika tano tu. MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Kamati hii ya Mambo ya Ulinzi na Usalama. Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nijikite sana katika masuala ya kuchukua vijana wa JKT hasa kwa upande wa Zanzibar. Kuchukua vijana wa JKT kwa upande wa Zanzibar ni suala zuri sana, lakini kutokana na utaratibu ambao unachukuliwa hawa vijana siyo utaratibu ambao unaridhisha. Kupitishia vijana kwa Wakuu wetu wa Mikoa kwa upande wa Zanzibar ni tatizo sugu sana. Kule Zanzibar tuna Kikosi cha JKU ambacho kikosi hiki kinafanana na Kikosi cha JKT kina mahusiano mazuri na Kikosi hiki cha JKT. Namuomba Mheshimiwa Waziri Ndugu yangu Dkt. Hussein Mwinyi akubaliane na masuala haya tuhakikishe vijana wanaochukuliwa kwa upande wa Zanzibar kuja katika Kikosi cha JKT wapitie katika kikosi hiki cha JKU, ninaamini tutapata vijana wazuri ambao ni wasikivu na imara ambao tunawataka. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana hata bajeti nilichangia suala hili tuwaongeze vijana katika upande wa Zanzibar; vijana wanaotakiwa kuchukuliwa kwa upande wa Zanzibar angalau tufikishe asilimia kumi. Katika vijana 5,000 ambao wanatakiwa kuchukuliwa katika Jeshi la JKT angalau vijana 500 watoke upande wa Zanzibar, tupunguze msongamano wa ajira kwa upande wa Zanzibar. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri kwa kuwa katika bajeti yako ambayo umezungumza fedha zako hazitoshi, lakini uwezo wa kuchukua vijana hawa unao. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe sana Serikali itusaidie sana kwa upande wa wizara hii iwaongezee bajeti ya fedha ili waweze kuchukua vijana wengi kupunguza msongamano wa vijana katika jamii zetu. Nikuombe sana na tuiombe Serikali itusaidie juu ya hili kwa kuwa Mheshimiwa Waziri anasema nafasi anayo kubwa ya kuchukua vijana na anao uwezo mkubwa lakini tatizo ni fedha kidogo. Tumuombe Waziri wa Fedha akija na bajeti aweze kutusaidia atuongezee bajeti ili tuweze kumpa nafasi Mheshimiwa Waziri aweze kuchukua vijana wengi kwenda katika Jeshi la JKT. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie na suala la Wizara ya Mambo ya Ndani. Wizara ya Mambo ya Ndani inafanya kazi zake vizuri lakini vilevile tatizo ni fedha. Hawa askari wetu wanaishi maisha duni ambayo hata hayahesabiki, wanakaa katika makazi mabovu suala hili Mheshimiwa Waziri tunalizungumza kila siku ndani ya Bunge hili halijapatiwa ufumbuzi. Hebu leo nataka ukija utueleze hapo mbele, hivi nyumba za hawa askari ni lini utaanza kuzijenga? Isiwe kila siku maneno tu hapa katika Bunge lako hili. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia suala la fedha kwa Wakuu wa Vituo vyetu hawa wanahudumia mahabusu wao wenyewe, kuwalisha wao wenyewe na hata umeme ndani ya vituo vyetu hivi vya polisi wanatoa wenyewe Wakuu wa Vituo. Ukiangalia kiukweli hii kadhaa kubwa katika nchi yetu. Ni aibu Mkuu wa Kituo mshahara wake tunaujua basi anaendelea kuwalisha mahabusu kwa nguvu zake yeye mwenyewe. Tunakwenda wapi katika Wizara hii? Tukigusa makazi mabovu, uendeshaji mbovu na ndani ya vituo vyetu magari hatuna na nyumba za askari mbovu. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kama pale Ziwani wakati mmoja nilienda kutembelea pale Ziwani tumekuta nyumba za askari zinashangaza sana nyumba hizi na ni hatari kubwa. Mtu anaingia kwa kuinama, kama hakuna uwezo wa kuzitengeneza nyumba hizi basi hata marekebisho ya kuzifanyia repair hizi nyumba upatikane….
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe sana, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MATTAR ALI SALUM: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Spika kwa kunipa nafasi hii kwa ajili ya kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, jina langu naitwa Mattar Ali Salum, kwa hiyo naomba kidogo tuliweke sawa ili tuweze kufahamika vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi yake nzuri ambayo anaifanya katika kushughulikia tatizo la maji katika nchi yetu, maji ni uhai.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nigusie sana katika suala la Mfuko wa Maji. Ni suala ambalo ni sensitive sana ambalo Serikali lina haki sana ya kutusikiliza kwa macho mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Maji ndio mkombozi wa nchi hii. Kwenye ziara yote ambayo tumeifanya, ukaguzi tulioufanya Kamati katika maendeleo yaliyofanywa katika miradi ya maji yote asilimia kubwa imetoka katika mfuko wa maji. Kwa hiyo niiombe sana Serikali iangalie huu mfuko wa maji ili uweze kuendelea kuweza kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali na maombi yangu haya naamini yatakuwa ni ya Waheshimiwa Wabunge wengi ambao walichangia Bunge lililopita na hata Bunge hili. Tunaiomba sana Serikali iongeze sh. 50 ili ifike sh. 100 ili Mfuko wa Maji uwe mkubwa ili uweze kutekeleza majukumu yake kwa ufasaha zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba sana Serikali suala hili la kuongeza hii sh. 50 itimie sh. 100 kwenye kila lita ya petrol na diesel hili liwe important sana. Serikali tunaiomba sana iweze kusikia tatizo hili, iweze kusikia maoni ya Waheshimiwa Wabunge na hivyo kuhakikisha maji yanapatikana kwa ufasaha.

Mheshimiwa Naibu Spika tumeiona bajeti ya Serikali ilivyo ndogo, lakini tukipata pesa katika mfuko huu, ukikaa vizuri basi tunaweza tukafika katika hatua kubwa katika kutatua tatizo la maji katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la maji bado ni sugu sana ambalo kutatulika kwake ni kazi ngumu sana, inahitaji kazi ya ziada ili tuweze kutatua tatizo hilo la maji. Tumefanya ziara katika vijiji vingi, katika Wilaya nyingi tumekuta tatizo la maji linaendelea kusumbua sana. Niiombe sana Serikali iweze kusikia kilio hiki cha kuongeza hizi sh. 50 ili iwe sh. 100 kwa lita ya petrol ili iweze kufikia hatua ya kutatua tatizo hili la maji hasa katika vijiji vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, katika uongezaji wa sh. 50 hii ikawa sh. 100, nashauri shilingi 70 iende vijijini shilingi 30 ije mijini kwa kuwa vijijini ndiko kuna kero kubwa ya maji kuliko mjini. Kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri pesa hii iweze kugawia vizuri na niiombe Serikali iweze kutukubalia suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuendelea nigusie tatizo la pesa za Benki ya India zinazokwenda Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ni zito sana. Bajeti iliyopita fedha hizi zililetwa ndani ya vitabu tukaambiwa fedha hizi za Benki ya India zinazokwenda Zanzibar zimeshakuwa tayari; lakini kitu kikubwa mpaka sasa fedha hizi hatujui zipo wapi, hatujui zimefikia vipi. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri juu ya hili suala la pesa hizi za Benki ya India zinazokwenda Zanzibar ambazo ni mkombozi wa matatizo ya maji kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar; wananchi wa Zanzibar wana matatizo makubwa sana ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, fedha hizi za Benki ya India aje atuambie zimefikia hatua gani na ni lini fedha hizi zinaweza kwenda Zanzibar ili ziweze kutatua kero Zanzibar?

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee na umwagiliaji wa maji. Hali ya hewa ya nchi yetu sio shwari, kwa hiyo tunaomba suala la umwagiliaji wa maji ni suala nyeti sana, lazima tuongeze suala la umwagiliaji kwa nguvu zetu zote angalau tufikie hekta milioni moja, tunaweza ku-save matatizo ya maji tuliyo nayo. Mheshimiwa Waziri nimwombe sana, hali ya hewa iliyokuwepo nchini kwetu si shwari na tukitengemea kilimo cha mvua hatuwezi kufika mahali ambapo tunapatarajia. Nchi yetu inaendelea na ukame na matatizo ni mengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, tuliangaliengalie kwa macho mapana suala la umwagiliaji ili tuweze kufikia hatua ya kuhakikisha wananchi wetu wanaweza kupata kilimo cha umwagiliaji kwa asilimia kubwa. Hii itawezesha nchi yetu kuwa na kilimo cha mafanikio. Kilimo cha kutegemea mvua hakiwezi kuondoa hali ya njaa katika nchi yetu; lazima tugeukie upande wa kuangalia kilimo cha umwagiliaji kwa nguvu zote na tuhakikishe kwamba wananchi wetu wameelekea katika kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nigusie na miradi ya vijijini. Hii miradi ya vjijini bado ni tatizo sugu; wananchi wetu wa vijijini wanapata miradi hii kwa gharama sana na kwamba inawasumbua sana kupatikana kwake. Tunaomba sana Mheshimiwa Waziri, katika hii miradi ya vijijini tuache kutumia majereta twende katika system ya solar ili tuweze kupata maji kwa urahisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanya ziara, tumeona faida ya matumizi ya solar katika miradi ya vijijni, kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri juu ya hili suala la kutumia solar katika miradi yetu hasa ya vijijini. Tuache matumizi wa majenereta kwa sababu wananchi wetu wanapata maji kwa gharama zaidi, lakini tukitumia solar watapata maji kwa urahisi, watapata maji kwa bei rahisi, watapata maji kwa uhakika. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri akisikilize kilio hiki kwa makini ili aweze kufanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nirejee tena kukazia suala la fedha...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja (Makofi).
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika Wizara ya Ulinzi. Kwanza nimpongeze Waziri wa Ulinzi, kaka yangu Mheshimiwa Hussein Mwinyi kwa kazi nzuri ambayo anaifanya katika kuliendesha Jeshi hili, nikupongeze sana kaka yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nigusie katika uchukuaji wa vijana kwenda JKT. Kwa upande wa Zanzibar uchukuaji wa vijana kwenda JKT tulikuwa tukilipigia kelele sana, nafikiri hata Bunge lililopita nimelizungumzia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wetu wa Zanzibar bado uchukuaji wa vijana hawa ni kidogo sana.

Kwa hiyo nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, aweze kutusaidia kwa hili, aliangalie kwa macho mapana ili kuhakikisha vijana wetu kutoka Zanzibar wanaongezeka katika kuchukuliwa, na hasa kuangalia kwa sasa kama kauli yake juzi alivyoisema kwa makini kuwa vikosi vyote vya ulinzi, hata Jeshi la Polisi, basi watakuwa wanachukua vijana hawa kutoka ndani ya JKT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri aweze kutuongezea kwa upande wa Zanzibar kuchukua vijana hawa wa kwenda JKT angalau tufike vijana 600 kutoka vijana 300 ambao wapo sasa hivi. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri kwa hili aliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mheshimiwa Waziri nikuombe sana, nilikuwa nikilizungumza sana Zanzibar tuna Kikosi chetu cha JKU ambacho kinafanana sana na Kikosi hiki cha JKT, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri katika mipango yako na mazungumzo yako vijana hawa wa JKT ukitaka kuwachukua kwa kutoka upande wa Zanzibar ni bora sana kuchukua eneo hili la JKU kwa sababu unapata vijana ambao wanakuwa wameshapata mafunzo mazuri, vijana ambao wana mwelekeo mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri uweze kulifikiria hili. Mheshimiwa Waziri hili hata bajeti iliyopita mimi nililizungumzia sana kuhakikisha kama vijana unapotaka kuchukua basi uelekee katika kikosi hiki cha JKU kwa sababu, hiki kikosi tayari kuna vijana wameshaandaliwa kwa muda mrefu, vijana wazuri ambao wana haki ya kupelekwa katika JKT na kupata ajira ya jeshi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nigusie upandishaji wa vyeo vyeo vya juu kwa askari kutoka Zanzibar. Ni jambo la kushangaza sana kwamba hata hawa askari wetu kutoka Zanzibar bado upandishaji wao wa vyeo vya juu umekuwa hafifu sana katika jeshi hili. Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri aweze kuliangalia hili kwa makini, hata akija akatoa maelezo yake hapo atueleze kuna askari wa vyeo vya juu wangapi kutika Zanzibar, kwa sababu tuangalie katika uwiano mzuri, ili tuweze kufika pazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu nigusie ile pension ya askari wastaafu wa zamani. Hili ni jambo kubwa sana Mheshimiwa Waziri, hawa wazee wanapostaafu huko wanalalamika sana. Kuna Sajenti aliyestaafu, sasa hivi pensheni yake analipwa takriban zaidi ya shilingi 600,000, lakini jambo la kushangaza sana yule yule Sajenti wa zamani ambaye ameondoka katika hili Jeshi hata nusu yake hafiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana hawa ni wazee wetu ambao wamefanyakazi kwa nguvu zao katika Jeshi hili lakini hatimaye basi malipo yao ni madogo sana.Wanapata taabu na wanaadhirika sana. Nimuombe Mheshimiwa Waziri aweze kuliangalia kwa makini suala hili ili kuhakikisha kwamba hawa wazee wetu wanapandishwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nianze na suala la maji. Naiomba sana Serikali, Wizara ya Maji, Mamlaka za Maji, zinazidai taasisi za Serikali pesa nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazungumza hivi, lazima Mheshimiwa Waziri wa Fedha atufahamu. Taasisi za Serikali zinadaiwa fedha nyingi sana kiasi kwamba Mamlaka zetu za Maji zinafika wakati zinashindwa kujiendesha. Naomba sana Serikali iweze kulipa madeni yale. Ikilipa madeni yale kuna hizi Mamlaka za Maji zitaweza kujiendesha zenyewe bila kutegemea ruzuku kutoka Serikalini. Kwa hili namuomba sana Mheshimiwa Waziri na Serikali iweze kusimamia tatizo hili kuhakikisha taasisi zetu za Serikali zinalipa madeni ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliahidi kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi tutamtua mama ndoo ya maji, sasa leo twende katika hali ile. Mheshimiwa Waziri…

T A A R I F A . . .

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipokea Taarifa kwa mikono miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, sisi kama Wabunge, ndio wananchi. Hawawezi kuja wananchi wote ndani ya Bunge hili kuja kuchangia ndani ya Bunge hili, halitoshi. Tumeishauri Serikali mara nyingi iongeze shilingi 50 ifike shilingi 100 kwenye petroli na dizeli ili tukaokoe matatizo ya maji vijijini na mijini. Nashangaa sana Serikali hii haitaki kutusikiliza sisi Wabunge. Sisi ndio tunaokaa na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba sana, naiomba Wizara iweze kutusikiliza sisi Wabunge. Sisi ndio wananchi wenyewe tunaokuja hapa, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, wewe sio peke yako. Naomba sana kwa hili Serikali iweze kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni la uvuvi. Suala la uvuvi namwomba sana Mheshimiwa Waziri, uvuvi tunao mkubwa sana katika bahari. Namwomba Mheshimiwa Waziri tena, uweze kuelekeza macho yako katika bahari. Tunaweza kukuza uchumi mkubwa katika nchi yetu. Mheshimiwa Waziri, kuna nchi nyingi sana zinategemea uvuvi wa bahari kuendeleza katika kipato cha nchi yao, lakini Mheshimiwa Waziri tunashangaa Serikali yetu, tatizo tumeshazungumza mara nyingi la kupatikana bandari ya uvuvi, hakuna; kupatikana meli za uvuvi hakuna… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu lakini la pili nimpongeze sana Rais Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri ambayo anafanya. Vilevile nichukue nafasi hii kumshukuru Waziri Mkuu kwa kazi ambazo anazifanya, ni haki yake kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze katika mchango, kwa kuwa dakika zangu ni kidogo nigusie katika watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI. Niiombe Serikali yangu tukufu, watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI wanapata taabu sana katika kupata matibabu yao. Niombe sana kila Halmashauri iweze kutenga fedha kiasi cha asilimia mbili au asilimia tatu wapewe watu wanaoishi na maradhi ya UKIMWI ili waweze kuunda vikundi ili waweze kujiendesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalisema hili kwa kuwa kuna mifano ambayo imetoka, baadhi ya Halmashauri wamepewa nafasi hizi na wamepewa fedha hizi wameweza kujiendeleza kwa makini na wameweza kujiwekeza kupata mpaka kadi za matibabu wao wenyewe na mitaji yao imekuwa mikubwa. Nimuombe Mheshimiwa Waziri kama hawa watu watapewa fedha kutokana na Halmashauri zetu na kuwe kuna sheria maalum ambazo Halmashauri hizi zilazimike kuwapa pesa watu hawa ili waweze kufikia hatua tunayotaka. Tukiwapa fedha tutaondoa utegemezi mkubwa kwa watu wenye kuishi na maradhi ya UKIMWI kwa sababu wanaweza kujitegemea, lakini Serikali inahitaji lazima iweze kuwainua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niligusie sana hili suala la watu hawa wanaoishi na maradhi ya UKIMWI na wanaoishi na VVU, hata ukitoa fedha kwenye mfuko wa Waziri Mkuu wakipewa hawa watu basi wanaweza kujiendesha kwa hali kubwa sana na wana uwezo mkubwa sana. Nimuombe Dada yangu Jenista aliangalie kwa makini ili aweze kuzi… Halmashauri zote ziweze kutoa fedha kwa watu wenye kuishi naVVU.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika jambo la pili, suala la miradi ya maji. Miradi ya maji ndani ya nchi yetu inakwenda vizuri na uendaji wake vizuri ni kutokana na fedha za Mfuko wa Maji ambayo si fedha za bajeti. Fedha za bajeti zinazokwenda bado ni kidogo sana na niiombe Serikali iweze kuewekeza pesa za maendeleo za bajeti katika Mfuko wa Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna fedha zetu za Mfuko wa Maji ambazo ndizo tegemeo kubwa katika miradi yetu ya maji. Sasa tuiombe Serikali iweze kukubaliana na Waheshimiwa Wabunge ili kuongeza shilingi 50 iwe shilingi 100 ili wananchi wetu waweze kupata huduma ya maji kwa makini. Mimi nashangaa sijui ni kwanini Serikali inapata kigugumizi kuongeza hii shilingi 50 ili itimie shilingi 100 ili Wananchi wetu waweze kupata maji ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ilielekeza kabisa maji ni muhimu, sasa tunashangaa kama Serikali haiwezi kukubaliana na sisi Wabunge ambao tumetumwa na wananchi tuje kwenu ili tuweze kuiambia Serikali kwa yale ambayo tunayoyataka, tunashangaa Serikali inapata kigugumizi wakati hao wananchi wenyewe ndiyo wanataka hii fedha iongezwe ili wananchi wapate maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee na suala lingine la kilimo; sera ya nchi yetu imejielekeza katika uchumi wa viwanda. Ni kweli ni sera nzuri ambayo inaleta matumaini makubwa, lakini ili uchumi wa viwanda uende vizuri lazima kuwe na kilimo bora. Sisi mpaka sasa nchi yetu tuna ardhi nzuri ya kilimo, lakini hatujakaa vizuri katika suala la kilimo. Kwa hiyo, tukikubaliana kuimarisha kilimo cha uhakika basi ninaamini hivi viwanda ambavyo tunavyovitaka vitakuwa vinafanyakazi kwa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia suala la mradi wa kilimo hasa upatikanaji wa pembejeo, Mheshimiwa Waziri na Bunge lako tukufu lilipitisha uhakika wa unuaji wa mbolea wa pamoja lakini mpaka hivi sasa ule uendeshaji, upatikanaji wa zile mbolea bado ni tabu haujakuwa sahihi na kwa sababu moja, kwa kuwa leo Mheshimiwa Waziri wa Kilimo yupo ananisikia nimshauri nia halisi ya kufanya ili aweze kufika hatua hawa wakulima wetu wasiweze kupata taabu. Mheshimiwa Waziri nikushauri jambo dogo tu, huu ununuaji wa mbolea ni mzuri, lakini uweze kununua mbolea kwa wakati wote usingoje msimu wa kilimo ndipo uanze kuagiza mbolea. Hii mbolea inatakiwa iwepo kila wakati humu madukani Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia leo. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa mzima wa afya na kuweza kusimama katika hili Bunge kuweza kuchangia siku ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya ya kutoa passport mpya. Vilevile nichukue nafasi hii kumshukuru Rais kwa kuhakikisha Watanzania waliotimia umri wanapata vitambulisho vya Utanzania ili viweze kuwasaidia katika mahitaji yao ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Kamishna wa Jeshi la Polisi wa Zanzibar kwa kuteuliwa kuwa Kamishna wa Jeshi la Polisi wa Zanzibar. Nimpongeze sana na nimtakie kazi njema kwa upande wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niipongeze Wizara inafanya kazi nzuri ya kuhakikisha wanasimamia utoaji wa passport mpya. Vilevile niwapongeze sana Wizara kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuhakikisha Watanzania waliotimia miaka ya kupata vitambulisho vya Utanzania wanapata vitambulisho vya Mtanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar tuna vitambulisho vya Mzanzibar Mkaazi. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilifanya kazi kubwa sana kwa kutumia kodi za Wazanzibari kuhakikisha wanapata vitambulisho hivi ili viweze kuwasaidia katika majukumu yao ya kukuza uchumi. Kazi ya kwanza ambayo ni muhimu sana Serikali ya Zanzibar ilifanya ni kutoa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi ili kuhakikisha Wazanzibari wanapata passport ya Mtanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kushangaza sana vitambulisho vya Mzanzibari kwa sasa huwezi kupatia passport ya Mtanzania. Ili upate passport ya Mtanzania unatakiwa lazima uwe na kitambulisho cha Mtanzania. Kinyume na miezi mitatu iliyopita kitambulisho hiki cha Mzanzibari unaweza kupata passport ya Mtanzania. Hii leo huwezi kupata passport ya Mtanzania kwa kutumia kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia system ya Uhamiaji, kitambulisho cha Mtanzania na kitambulisho cha Mzanzibari kimoja hapo ukikitumia unaweza kupata passport ya Mtanzania. Jambo la kushangaza sana Mheshimiwa Waziri na nimwombe sana hivi sasa anapokwenda na kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi kinaambiwa hakifahamiki na huwezi ku-issue passport.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo ni la kushangaza sana, hiki kitambulisho cha Mzanzibari ikiwa Serikali ya Zanzibar imetumia gharama na kodi za Wazanzibari kuhakikisha wanapata kitambulisho hiki ili kujikwamua na maisha yao, leo unawaambia haiwezekani kupata passport mpaka mtu awe na kitambulisho cha Mtanzania. Niombe sana Wizara kama kitambulisho hiki cha Mzanzibari Mkaazi kina tatizo, basi waweze kutuambia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Wizara kama Serikali kama kitambulisho hiki kama kina tatizo wana uwezo wa kulitatua tatizo basi litatuliwe ili waliokuwa nacho kitambulisho hiki waweze kupata passport kwa kutumia kitambulisho hiki cha Mzanzibari. Wazanzibari wengi wamehamasika na wamechukua vitambulisho hivi vya Mzanzibari kwa nia nzuri ili waweze kupata passport ya Mtanzania na waweze kufanya kazi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa sana kwa nini kitambulisho hiki kwa sasa huwezi kupata passport na ni kipindi kifupi ndiyo limeanza hili suala kwamba kwa kitambulisho hiki huwezi kupata passport. Vilevile ukitaka kitambulisho cha Mtanzania kwa upande wa Zanzibar zaidi ya siku 30 ndiyo unapata kitambulisho hiki cha Mtanzania. Kama hakuna uwezekano wa kuhakikisha kitambulisho chetu cha Mzanzibari unaweza kupata passport wapunguze muda ili Wazanzibari waweze kupata kitambulisho hiki cha Mtanzania kwa haraka zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie jambo la pili kuhusu vituo vya polisi. Wakuu wetu wa vituo vya polisi wanapata shida sana. Mkuu wa Kituo cha Polisi anapewa mahabusu zaidi ya 40 ambao wanahitaji kula, lazima mkuu wa kituo kufanya maarifa wale mahabusu au watuhumiwa waweze kula kwa kutumia pesa zake mfukoni. Mkuu huyu wa kituo cha polisi atakuwa na uwezo gani wa kuwalisha mahabusu kila siku? Pesa za kula ndani ya vituo vyetu vya polisi haziendi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine unakwenda kituoni kushtaki, unaambiwa gari lipo lakini mafuta hakuna. Inabidi Mkuu wa Kituo atoe pesa za mafuta au Mkuu wa Kituo yule aweze kupata gari na aweze kwenda au Mkuu wa Kituo hana wewe uliyekwenda kushtaki kesi unatakiwa utoe pesa zako mfukoni kutia gari mafuta ili kesi yako iweze kushughulikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la umeme. Hata na mimi mwenyewe nimeshawahi kuchangia umeme ndani ya kituo cha polisi, hawana pesa za umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu ya Maji. La kwanza, niipongeze sana Wizara pamoja na watendaji wao wote kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ni muhimu, maji ni uhai wa binadamu mpaka wanyama. Mimi nitachangia kwa kuanza na Mamlaka za Maji na madeni ya taasisi za Serikali. Taasisi za Serikali zinadaiwa fedha nyingi na Mamlaka zetu za Maji, inafika wakati hizi mamlaka zetu zinashindwa kujiendesha. Niiombe sana Serikali, la kwanza iweze kulipa pesa hizi za Mamlaka za Maji ili ziweze kujiendesha kwa ufanisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi zetu za Serikali zinadaiwa fedha nyingi na Mamlaka za Maji inafika wakati mamlaka hizi haziwezi kujiendesha kabisa. Ni jambo la ajabu sana, mamlaka zinalalamika zinasema zikilipwa fedha na taasisi hizi zinaweza kujiendesha wao wenyewe. Ni jambo la ajabu sana ni kwa nini Serikali isiweze kulipa pesa hizi kwa Mamlaka za Maji ili hizi mamlaka ziweze kujiendesha kwa ufanisi zaidi na wakiweza kujiendesha maana yake ni kupunguza mzigo kwa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, leo nina mambo machache, ni suala la shilingi 50 kuongezwa katika petroli na dizeli. Suala hili tunaiomba sana Serikali, lazima ifanye jitihada zake zozote zihakikishe inaongeza shilingi 50 kwenye Mfuko wa Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna muarobaini wa tatizo la maji kwenye nchi hii isipokuwa kuongeza shilingi 50. Nashangaa kwa nini Serikali haiwezi kukubaliana na maoni ya Wabunge wake. Sisi Wabunge tukisimama hapa kuchangia, siyo kama tumesimama Wabunge ni wananchi wa Tanzania ndiyo wamesimama hapa wanaishauri Serikali. Wametuleta hapa kazi yetu ni kuisimamia na kuishauri Serikali. Mimi nashangaa sana, Serikali yetu hii kama Wabunge tunachangia, tunaishauri lakini haitaki kusikiliza mawazo yetu sisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali, suala la kuongeza shilingi 50 kwenye mafuta ya petroli na dizeli lipewe kipaumbele ili tuweze kufika hatua ambayo tunaitaka. Ukiangalia bajeti iliyopita, asilimia 80 ya miradi ya maendeleo imefanywa na Mfuko wa Maji, siyo pesa za Serikali ni Mfuko wa Maji. Tukiongeza shilingi 50, tukiwa tuna shilingi 100, tutafika mahali pazuri. Niiombe sana Serikali yangu, mimi naamini Serikali hii sikivu, Waziri wa Fedha yupo nimwombe aweze kulichukua hili jambo liweze kufanikiwa ili wananchi wetu waondokane na kadhia ya maji waliyo nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuligusia ni suala la DAWASCO kuunganishwa na DAWASA. Ni jambo zuri sana limefanywa, Serikali imewaza jambo zuri lakini je, wamefanya tathmini ya kina jinsi ya kuendesha maana ziko mamlaka mbili kwenda mamlaka moja? Je, Serikali imefanya tathmini ya kina kuhusu gharama za uendeshaji hasa katika suala la mishahara, lazima tuliangalie kwanza. Kama sisi Kamati hatukuletewa lolote na tumewaomba Wizara waweze kutuletea ili tujue, je, kuondoka kuwa mamlaka mbili na kuwa mamlaka moja kuna-benefit yoyote? Isijekuwa tunaondoa baadae tukawa tunapata hasara katika Serikali yetu tukaja tukataka turejeshe. Niiombe Wizara ikae chini iweze kufanya tathmini ili tujue tunakwenda kwenye faida au hasara? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee pesa za India. Hizi pesa hata na mimi kule Zanzibar kwa kuwa niko Mkoa wa Mjini nitafaidika nazo sana. Niiombe sana Serikali, sijui pana tatizo gani, hebu Serikali ituambie, hizi fedha zina tatizo gani? Huu mwaka wa tatu tunazichangia hizi fedha ndani ya Bunge hili. Fedha hizi hazipatikani, tunashindwa kusaini, sijui kuna tatizo gani? Kuna tatizo gani hapa ili hizi fedha ziweze kupatikana kwani zikipatikana tunaweza kutatua tatizo kubwa sana la maji kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni la Tume ya Umwagiliaji. Tume ya Umwagiliaji bado ni tatizo lakini ili kuondoa matatizo ya Tume naiomba Serikali leo hii iweze kunisikiliza kwa makini. Naishauri Tume hii iondoke kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji ipelekwe kwenye Wizara ya Kilimo. Hili ni jambo jema sana, tukiiondoa Tume hii kutoka katika Wizara ya Maji tukaenda nayo katika Wizara ya Kilimo ndiyo hasa yale mahitaji ya wananchi wetu yatafika mahali tunapotaka. Tume hii ikibakia kwenye Wizara ya Maji na Tume hii shida yetu ni wakulima na maendeleo kwa wakulima bado itakuwa ni shida. Tunaomba sana Serikali iiondoe Tume hii kutoka kwenye Wizara ya Maji ielekee kwenye Wizara ya Kilimo hapo ndipo tunaweza tukapata mafanikio katika nchi yetu kutokana na Tume hii ya Kilimo kwa sababu itafika pale ambapo wanataka iwaguse wananchi. Tukiibakiza katika Wizara hii tutakuwa tuna wakati wa kufanya zero na pasipo na Tume ya Umwagiliaji, ikafanya kazi vizuri kwenye nchi hii hapana kilimo wala hakuna maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii leo. Vilevile nimshukuru Mwenyezi Mungu kuniwezesha kuwepo hapa leo nikiwa mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri pamoja na timu yake, naamini Kaka yangu, Mheshimiwa Dkt. Mwinyi anafanya kazi vizuri na Mungu azidi kumpa uwezo wa kuliongoza Jeshi hili ili tuweze kufika mahali pazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nigusie kidogo suala ambalo amezungumza Mbunge mwenzangu hapa kuhusu Sera ya Ulinzi kwa upande wa Zanzibar. Sera hii kwa sasa imeshafanyiwa kazi kwa hatua kubwa kwa upande wa Zanzibar, naona katika suala la Wizara limeshafika hatua yake ya mwisho na hivi sasa wanaelekea kwenye kikao cha Makatibu Wakuu. Nafikiri baada ya muda mfupi kitakwenda katika Baraza la Mapinduzi ili kupewa baraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niliona niliseme hili ili Waheshimiwa Wabunge kidogo wasiwe na pressure na hii sera kuhusu Zanzibar kuwa hali iko hivyo na sasa tunakwenda vizuri na ninafikiri tunaweza tukafika vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la sera siyo suala jepesi. Ukitaka kuitafsiri sera na ukitaka kuiandaa ili upate mafanikio, sera ndiyo inayojenga sheria, kwa hiyo ukiipata sera bora maana yake unapata sheria bora isiyokuwa na vikwazo. Kama hukuipata sera iliyokamilika, utakuwa bado hujapata sheria nzuri, baadaye tutakwenda kwenye matatizo. Kwa hiyo, niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge, kwamba hali ya Zanzibar na hii sera iko vizuri na tunakwenda vizuri na ninafikiri tutafika mahali pazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, ni uchukuaji wa vijana wa JKT kutoka Zanzibar. Hili suala nalizungumzia, kwa Mheshimiwa Waziri kila muda, bado mdogo. Angalau vijana 500 waweze kutoka Zanzibar kwenda JKT, tunachukua vijana kidogo sana. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aweze kupaangalia hapo ili awe na uwezo mkubwa wa kuchukua vijana kutoka Zanzibar ili waweze kwenda JKT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taratibu za kuchukua vijana kutoka Zanzibar bado haziko vizuri. Nasema kila siku kumwambia Mheshimiwa Waziri, suala la uchukuaji kwa kule upande wa Zanzibar kupita kwenye Wilaya zetu, bado pana tatizo, hatupati vijana ambao Mheshimiwa Waziri au Jeshi wanakusudiwa kwenda. Kwa nini asibadilishe mfumo ili tukapata mfumo mzuri kwa upande wa Zanzibar ili kupata vijana wa kuweza kuja kufanya kazi vizuri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar tuna kikosi cha JKU ambacho kinafanana katika utendaji wake na Kikosi cha JKT. Kwa nini Mheshimiwa Waziri asikitumie hiki kikosi kwa awamu ya kwanza ili kuhakikisha vijana wa JKU wanakwenda JKT kutoka katika kikosi hiki? Kama haiwezekani vijana anaochukua kwenda kupata ajira basi watoke ndani ya kikosi hiki. Kama kina upungufu Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaweza kukiendesha kile kikosi ili kiweze kujipanga vizuri ili vijana wapate ajira kutokea JKU. Tukikitumia kikosi kile basi tunaweza kupata vijana wazuri ambao waweza kufanya kazi vizuri ndani ya Jeshi letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, ni vijana waliojenga ukuta. Vijana hawa wamepewa matumaini makubwa na wanasubiri. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri akija apate kutoa jibu la uhakika kuhusu vijana hawa waliojenga ukuta, wameahidiwa ajira, sasa wanasubiri ajira na Mheshimiwa Waziri ndiyo mdhamini wa vijana hawa, wako ndani ya JKT wanasubiri maamuzi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili Bunge wanakaa wanalisikiliza kwa kina watapewa maamuzi gani kutoka kwa Mheshimiwa Waziri. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri vijana hawa tuweze kuwajibu vizuri ili kama kuna ajira ya kuwapeleka kabla muda wao haujakwisha basi Serikali iweze kuwachukua kwa sababu wengine muda wao unakaribia kwisha na kazi ile wameifanya, wahakikishe na wao wameshapewa matumaini wajue wanakaa vipi. Nimwombe sana Kaka yangu, Mheshimiwa Dkt. Mwinyi, hili aweze kulijibu kwa uhakika zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la makazi. Tulimelizungumzia sana na sasa nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, hebu afanye utaratibu hawa Askari wetu waweze kupata makazi mazuri. Nyumba zao zimeshakuwa za muda mrefu, Wabunge wengi wanalizungumza hili suala, lina matatizo. Mheshimiwa Waziri afanye jitihada zake ili aweze kutatua kero hii ya makazi kwa Askari wetu, bado wanalitumikia Jeshi letu vizuri na hawana matatizo na Jeshi letu. Kwa hiyo, namwomba sana aweze kufanya hii kazi kwa uhakika zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu migogoro. Bado Wabunge tunasema baina ya Wakaazi na Wanajeshi kuna migogoro ya kimipaka, tatizo hili linaendelea kuwa kubwa. Wananchi wanasubiri malipo yao, hawajui watalipwa lini, wanasubiri angalau kauli ya Mheshimiwa Waziri tujue tunafanya nini, bado wananchi wetu wana matatizo makubwa na Jeshi lao kutokana na migogoro. Majeshi yamevamia au wananchi wamevamia, kwanza Mheshimiwa Waziri, haya madeni ambayo wanadai hawa wananchi basi tufanye maarifa ili waweze kulipwa kwa wakati ili hii sintofahamu baina ya Jeshi lao pamoja na wananchi wetu, tatizo hili linatatuliwa kwa kina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na kikosi chake na kazi ambayo anafanya iko vizuri, Jeshi letu liko vizuri, nchi yetu iko salama kwa sababu ya Majeshi haya. Lazima tuwaunge mkono na kitu kikubwa bajeti yao lazima iende kwa wakati, ifanye kazi vizuri. Tunalala na tunapata usingizi Tanzania kwa sababu Jeshi hili liko imara na tunaliombea dua liweze kufanya kazi zaidi ya hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, tunaweza kulitumia Jeshi katika uzalishaji, tusitumie Jeshi katika ulinzi tu bali na uzalishaji pia Jeshi letu tunaweza tukalitumia kwa hatua kubwa. Suala la kiuchumi, wenzetu wanalitumia Jeshi katika ulinzi lakini vilevile katika kuimarisha uchumi wa nchi. Jeshi lina uwezo mkubwa, mambo mengi wanaweza wakafanya katika nchi yao kuhakikisha wanakuza uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono bajeti hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Niendeleze hapa alipoacha kaka yangu Mheshimiwa Mgimwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tutakuwa na mikakati thabiti ndani ya Wizara hii na kama tutaishauri Serikali vizuri, itasikia tunavyosema Waheshimiwa Wabunge. Jambo la kwanza kwenye tasnia ya maziwa, lazima Wizara zetu yaweze kutumika maziwa ambayo tunazalisha nchini kwetu. Tunaweza tukai-promote sekta hii ikawa inafanya kazi vizuri kuliko kitu chochote, lakini sisi wenyewe ndani yetu tunaanza kutumia maziwa ya kuagiza nje. Hivi sekta hii itakua lini? Naomba sana Serikali tubadilishe utumiaji wa maziwa, twende katika utumiaji wa maziwa tunayozalisha ndani sisi wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ukiangalia bajeti ambayo ilikuwa imepangwa kutolewa katika Wizara hii, jambo la kusikitisha sana, bajeti hii haijaenda, haina hata kitu kimoja. Hawa Mawaziri wanachapa kazi vizuri, naamini wana jitihada sana ya kufanya kazi. Nawashukuru sana hawa Mawaziri, lakini kutokana na bajeti ambayo iko hapa, waliyopewa hawa, basi haiwezi kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ni uvuvi wa Bahari Kuu ambao nauzungumzia kwa kina. Nchi yetu tukitaka tuendelee, tufike mahali halisi tunapopataka pasipo kuangalia madini, basi tuangalie kwenye uvuvi wa Bahari Kuu. Tukisimamia uvuvi wa Bahari Kuu tunaweza kufika mahali pazuri kuliko kuangalia madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, baada ya macho kuangalia katika madini, basi tuangalie hapa kwenye uvuvi wa Bahari Kuu. Tukifanya kazi, tukipaimarisha vizuri katika uvuvi wa Bahari Kuu, haya matatizo ya uvuvi haramu na matatizo sijui ya maziwa, yote yataondoka. Nami kaka yangu Mheshimiwa Ulega namshauri kila siku, hebu twendeni kwenye uvuvi wa Bahari Kuu, tuangalieni, kuna nini? Sijui tumelogwa na nani?

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, tumesema katika Kamati tukilalamika kuhusu ununuaji wa meli na ujengaji wa gati. Ndani ya hotuba zetu hizi hatujaona mahali palipo na mkakati rasmi kwamba sasa tunaenda kuwekeza kwenye Bahari Kuu. Uchumi wa Bahari Kuu, wenzetu waliokuja kuwekeza ndani ya nchi yetu hii wanapata mafanikio makubwa, sisi tunabakia katika tozo ya leseni tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Wizara hii na Serikali iweze kusimamia uvuvi wa Bahari Kuu, kuhakikisha tunakwenda mahali pazuri. Naamini tukisimamia kidhati kwenye Bahari Kuu, basi tutakwenda tunapopataka.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, nigusie suala la ufugaji, bado hatujatoa elimu na bado hatujaamua kusimamia katika suala la ufugaji. Tukiangalia hata mifugo yetu, bado hatuna ng’ombe wanaoridhisha. Angalau ng’ombe unayemkamua maziwa umpe malisho bora. Kikitokea kiangazi kidogo tunashuhudia ng’ombe wanaokufa ni wengi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka tumekwenda ziara kuangalia ng’ombe, wanapukutika njiani kama majani. Tujipange katika suala la ufugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Ahsante. Tuwawezeshe wafugaji wetu, tuwape mikopo ya ng’ombe wa kisasa, tuwaelimishe ufugaji wa kisasa ili tupate maziwa mengi.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Pia nimshukuru sana Waziri wa Fedha kwa kazi nzuri ambazo anazifanya pamoja na Naibu Waziri wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Tanzania ni nchi ambayo inakwenda katika uchumi wa viwanda; na ili tujenge viwanda, viendelee na viweze kufanya kazi kama nchi nyingine ambazo zimeshaendelea lazima tuimarishe uchumi wa nchi yetu na ni lazima tusimamie kilimo. Viwanda vyetu ili viweze kufanya kazi kwa hali nzuri lazima Serikali yetu iweze kuangalia sekta ya kilimo. Bila kuangalia sekta ya kilimo tutakuwa tunaimba viwanda lakini hatujafika mahali ambapo tunapataka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia sekta ya kilimo bado Serikali yetu haijaweka mkakati rasmi wa kushughulikia tatizo la kilimo. Ukiangalia bajeti ya kilimo bado ni ndogo na vile vile na upelekeaji wa pesa katika sekta ya kilimo bado ni mdogo sana na sisi tunahitaji kwenda katika uchumi wa viwanda kwa nguvu zote. Tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, jitahidi sana fanya kazi kuhakikisha sekta ya kilimo ndiyo sekta mama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanategemea kilimo, ikiwa hatujaitizama kwa makini sekta ya kilimo basi hata hili suala la ajira kwa vijana wetu wa Tanzania bado haitofikia mahali pazuri. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha aiangalie sekta ya kilimo, ndiyo sekta mama katika nchi yetu, ndiyo sekta ambayo itatutoa hapa tulipo na kwenda kwenye uchumi wa viwanda. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aweze kusikiliza hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juzi tulikuwa Njombe, tulipata tabu sana; kuna kelele sana za wakulima wanakosa mikopo. Sasa nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha aliangalie; wakulima wetu bado wanakosa mikopo katika benki. Sasa wataweza kufanya kazi vipi na mahali pa kupata pesa ili waweze kuimarisha kilimo pasipo na Serikali ni lazima waweze kupata mikopo ndani ya benki zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, benki zimekuwa sugu katika kutoa mikopo kwa wakulima wetu, tumepata kelele nyingi. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha aweze kusimamia kwa makini utoaji wa mikopo kwa wakulima wetu. Wakulima wetu ukiwapa mikopo na ukisimamia vizuri ukiwapelekea watalaam vizuri tutatoka hapa tulipo na tutakwenda mahali pengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la maji. Hili bado ni tatizo; bajeti ya maji 2017/2018 ilipangwa kuwa takriban bilioni mia sita, zilizotoka ni bilioni mia mbili tu. Tulijadiliana na sisi kama Wabunge tumesema iongezwe Sh.50 kusaidia bajeti hii kuhakikisha wananchi wetu wanapata maji ya kutosha. Kama hatutaongeza Sh.50 tutakuwa hatufiki mahali pale ambapo tuliahidi Watanzania wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi ni Wabunge ambao tumekuja hapa kwa sababu ya kuwasemea wananchi wetu, tukiishauri Serikali tumwombe sana Mheshimiwa Waziri aweze kupokea mawazo yetu katika kuongeza Sh.50. Ukiangalia idadi ya bajeti hii, tukienda katika system ili tuweze kupata maji safi wananchi wetu wapate maji, tutachelewa kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aweze kulipokea, kuongeza Sh.50 katika lita ya dizeli na petroli ili tuweze kupata maji safi kwa sababu ukiongeza hakuna tatizo, mimi sijaona tatizo la kukosa kuongeza hili. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aweze kulichukua suala la ongezeko hili la Sh.50 kwenye lita ya petoli na dizeli ili tuweze kufika mahali tunapopataka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la uvuvi wa bahari kuu bado ni tatizo, bado Serikali haijakaa katika kulisimamia, kuweka mikakati rasmi ili kuhakikisha uvuvi wa bahari kuu unakwenda kwa kasi sana. Mahali hapa penye uvuvi wa bahari kuu tukipasimamia kikweli kweli kama Serikali, tukiamua kwenda kuwekeza katika uvuvi wa bahari kuu, nchi yetu itaweza kwenda mbele. Uvuvi wa bahari kuu unaweza kuchangia mapato mengi sana na sasa tunakosa mapato makubwa sana kupitia uvuvi wa bahari kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kila tukiangalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha hatujaona kipengele ambacho watasema sasa tutajenga bandari, kununua meli za uvuvi na kufanya tathmini ya samaki ndani ya bahari yetu ambayo tunayo; tuna uwezo gani na tuna samaki kiasi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, tukikaa tukisimamia suala la uvuvi, tukiweza kuwezesha hii sekta ya uvuvi kwa makini, tunaweza kufika mahali ambapo nchi yetu inapataka. Huu uvuvi tukiweza kusimamia kwa makini basi unaweza kuingiza Pato la Taifa kuliko hata hii sekta ya madini. Niiombe Serikali iweze kusimamia kwa makini kuhakikisha suala la uvuvi wa bahari kuu linatazamwa kwa jicho la huruma sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunao Waheshimiwa Mawaziri wetu wa Wizara ya Uvuvi wako vizuri, wanafanya kazi vizuri na wanashaurika vizuri, basi niombe sana Serikali iweze kuita•izama kuhakikisha kwamba uvuvi huu unakwenda mbio kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanafanya kazi. Uvuvi wa bahari kuu una uwezo wa kutengeneza ajira kubwa sana kutoka kwa wananchi wetu, ni kwa nini tusiweze kusimamia uvuvi wa bahari kuu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ndiyo hili la sekta ya uvuvi ambayo tuliiangalia kwa makini, tukiweza kujua tuna kiasi gani cha samaki katika bahari kuu, tukiweza kujua tuna uwezo gani na tukiweza kununua meli yale mapato ambayo tunakosa kutoka katika bahari kuu, tukiweza kuyapata tunaweza kufika mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la kupatikana kwa ajira kwa vijana, bado ajira kwa vijana upatikanaji wake upo duni sana. Niombe sana, Wizara ya Elimu ipo, tuanze kuwafundisha vijana wetu jinsi ya kujiajiri kutoka shule za msingi ili wakitoka pale wakimaliza chuo kikuu watakuwa wameweza kujiajiri wao wenyewe kuliko kukaa tu kuitegemea Serikali ili iweze kuwaajiri. Suala hili haliwezekani, hakuna Serikali ambayo inaweza kuajiri watu wake wote. Ni lazima kama Serikali tujipange tuhakikishe kwamba vijana wetu tunaanza kuwafundisha mafunzo ambayo hata wakimaliza basi wanaweza kujiajiri wao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri na timu yake yote pamoja na Naibu Waziri, Mheshimiwa Alhaj Masauni kwa kazi nzuri wanazozifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache ambayo nataka niyazungumze, nataka Mheshimiwa Masauni anisikilize vizuri.

MWENYEKITI: Unasemaje Mheshimiwa?

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka Mheshimiwa Waziri anisikilize vizuri sana.

MWENYEKITI: Eeeh, ndiyo Waziri mwenye hoja.

MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar kuna Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi ambapo leo ndani ya Bunge hili ni mara ya pili kuvizungumzia kwamba havitumiki katika kupata passport na leo vilevile havitumiki kupata hata laini ya simu. Sioni sababu kwa nini Vitambulisho hivi vya Mzanzibari Mkaazi haviwezi kutumika kwa sababu ya kupata passport ya Mtanzania wakati vitambulisho hivi ni halali ambavyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa pesa za walipa kodi kuhakikisha vitambulisho hivi wanavitumia Watanzania. Tunaomba Waziri wakati wa kuhitimisha atupe majibu mazuri kuhusu Vitambulisho hivi vya Mzanzibari Mkaazi ili Wazanzibari wapate fursa ya kuvitumia kusajili laini pamoja na kupata passport. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kushangaza leo tuna NIDA hapa ni kwa nini Vitambulisho hivi vya Mzanzibari Mkaazi haviunganishwi kwenye system kwa wakati ili vikapata hadhi yake? Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, Serikali yetu imefanya kazi kubwa na tuipongeze sana Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuhakikisha Wazanzibar wote wanapata vitambulisho hivi. Leo tunashangaa kitambulisho hiki kina kasoro gani mpaka hakiwezi kutumika katika matumizi hata ya kusajili line? Mheshimiwa Waziri naomba tuhakikishe kitambulisho hiki kinaweza kufanya kazi kwa maslahi ya Wazanzibari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni miradi ya Wizara hii, bado ni changamoto kubwa. Wizara hii ya Mambo ya Ndani wanapoanzisha miradi hasa ya Jeshi la Polisi mfano majengo hayamalizwi kwa wakati. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha alichukue suala hili ili Wizara hii aipatie fedha za kutosha ili ikamilishe miradi yake kwa wakati. Tukifanya nusu na fedha zikipelekwa nusu inasababisha miradi hii kutokamilika na hizi fedha zinaweza kupotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha atoe fedha kwa wakati kuhakikisha miradi hii inamalizika kwa wakati. Kama haikuwezekana kutoa fedha kwa wakati, nimwombe sana Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Kangi Lugola badala ya kutekeleza miradi yote basi achague miradi muhimu ili iishe kwa wakati tusibakishe majengo tu yasiyoisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tuna majengo ya kufanyia kazi hayakaliki, hayawezi kufanyia kazi. Siku moja nilikuwa sehemu moja katika Mkoa wa Kusini Unguja, nimekwenda katika Ofisi ya RPC haifai kufanyia kazi. Jengo lile ni la zamani na plan ya kujenga jengo lingine haijawa tayari. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aweze kulichukua suala hili, alitembelee jengo hili na kama kuna uwezekano wa kujenga jengo lingine wafanye haraka kujenga lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, wapo askari wanastaafu wakiwa na vyeo vya Sergeant lakini mafao yao wanalipwa na vyeo vya Corporal hawapati haki zao husika. Sasa Mheshimiwa Waziri ikiwa askari hawa wamefanya kazi na mmewapandisha vyeo wamefika wakati wa kustaafu kwa nini hawapati mafao yao ya cheo husika cha kustaafia?

Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri ulichukue hili na ulifanyie kazi na askari hawa waliostaafu ambao hawajapata haki zao kwa ukamilifu utoe haki kwa ukamilifu ili askari wetu waweze kulitumikia Taifa letu kwa makini zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ahsante kwa kunipa nafasi lakini la pili nikushukuru sana. La tatu niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Maji pamoja na Naibu wake, Mheshimiwa Aweso kwa kazi nzuri wanazozifanya ambazo zinaleta matumaini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache ya kuzungumza na la kwanza ni kuhusu miradi ya maji vijijini. Baadhi ya miradi ya maji wanatumia majenereta ambapo ni kuwapa mzigo mkubwa wapiga kura wetu. Niombe sana Serikali iweze kufikiria kutumia solar system kwa sababu upatikanaji wa maji unaweza kuwa rahisi zaidi kuliko kutumia majenereta. Kwa hiyo, nikuombe sana Waziri uweze kwenda mbali zaidi kwenye solar system ili kuwapunguzia mzigo wa gharama wananchi wetu. Unapotumia solar system hata Serikali inaweza ikawa imepunguza mzigo mkubwa katika matumizi ya maji na hili ndilo tunalolitaka kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, fedha za kwenda kwenye miradi ya maji bado ni tatizo kubwa na halijapatiwa ufumbuzi. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri ujue ni miradi gani ni muhimu uikamilishe kuliko kukusanya miradi mingi ambayo haimaliziki. Tunaziumiza fedha za Serikali kisha baadaye ile miradi haifanyi kazi, ina maana hakuna faida ambayo ninyi mnaipata na wananchi hawapati faida kutoka kwa Serikali yao. Kwa hiyo, nikuombe sana, Mheshimiwa Waziri unafanya kazi vizuri lakini kuwe na miradi maalum ambapo kwa fedha ambazo tunaweza tukapata basi tunaweza kuitekeleza na kuisha. Tukifanya jambo hili tunaweza tukafanya kazi nzuri na wananchi wetu wakapata mafanikio mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni shilingi 50 kuongezwa kwenye Mfuko wa Maji. Ninyi Serikali mnaweza mkatafuta chanzo chochote lakini shilingi 50 hii kwenda kwenye Mfuko wa Maji ni jambo la lazima kwa sasa ili tuwasaidie wananchi wetu. Ili tuweze kupata kile ambacho tulichokusudia ni lazima tuongeze shilingi 50, ikiwa ni kwenye mafuta, simu au mahali pengine popote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa tumwambie sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha hili suala la shilingi 50 ndiyo mwarobaini wa matatizo ya maji. Ukiangalia mtiririko wote wa fedha basi fedha inayotoka na inayokwenda kwenye miradi ya maji na inayotoka kwenye Mfuko wa Maji tu peke yake, ukiangalia fedha ya Serikali iliyokwenda ni ndogo sana. Ni kwa nini Mheshimiwa Waziri msiweze kuwakubalia Wabunge hawa, ndiyo wananchi, hiki kishilingi 50 kikienda kwenye Mfuko wa Maji tukatatua matatizo ya maji, nia yetu sisi ni safi, tunakushaurini vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui ni kwa nini Mheshimiwa Waziri wa Fedha huwezi kupokea huu ushauri wa Wabunge? Sisi tunakushangaa sana na tunaona mambo ya ajabu sana. Kubaliana na ushauri wa Wabunge, ukikubaliana na ushauri wa Wabunge maana yake umekubaliana na ushauri wa wananachi wote, sisi ndiyo wenye wananchi. Nikueleze tu Mheshimiwa Waziri na Serikali suala la shilingi 50 safari hii halina mbadala. Tunawaomba sana muweze kufanya kazi vizuri. Mkipewa shilingi 50, naamini tatizo la maji tutakuwa tumeliondoa kwa asilimia kubwa kwenye nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho nilizungumzie sana, Mamlaka za Maji zinadai sana, Serikali yetu inadaiwa. Ukiangalia tathmini za Mamlaka zote za Maji zinaidai Serikali yetu. Tuombe sana Serikali ikubaliane na kulipa madeni haya ili iwaachie hizi Mamlaka ziweze kujiendesha wao wenyewe, zina uwezo kujiendesha lakini bado madeni makubwa yako Serikalini. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri uweze kulipokea hili na uweze kutoa fedha kuzilipa hizi Mamlaka za Maji ziweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa muda huu niweze kuchangia hotuba hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wawili wamezungumza kwa makini kabisa na leo niliseme ili Mheshimiwa Waziri aweze kulifahamu. Tukiondoa mrabaha wa 0.4 hivi leo, kesho tu asubuhi kuna meli zaidi ya 50 zinataka kuja kuchukua leseni ndani ya Tanzania. Tukiweza kuondoa mrabaha huu ambao ndiyo kikwazo katika uvuvi wa nchi yetu, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aweze kuondoa mrabaha huu ili wavuvi na wawekezaji waweze kuja ndani kuvua katika Bahari Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweza kuondoa mrabaha huu na siwezi kufahamu tatizo ni nini linalomkwamisha Mheshimiwa Waziri, kuondoa mrabaha huu ambao ni usumbufu mkubwa. Huu mrabaha naamini hata Mheshimiwa Waziri akija anaweza akaja na majibu mazuri kuhusu kuondoa huu mrabaha ambao ni kero kubwa katika kuwekeza katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu bila ya uvuvi hatuwezi kusogea mbele, tukiwekeza kwenye uvuvi tunaweza tukapata mafanikio makubwa kuliko ambayo anayakusudia. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, nilizungumza nyuma ununuzi wa meli kubwa za uvuvi umeshindikana hapa haupo kabisa, mimi mwenyewe nashangaa. Sasa leo wawekezaji wanataka kuja, anawawekea kodi kubwa ambayo itawasumbua hawawezi kuvua katika bahari kuu. Sasa hawa samaki nia yake Mheshimiwa Waziri kuwafanya nini kwa sababu samaki huwa anatembea, samaki siyo mawe, akiwazuia yeye hapa basi huko wenzake wanawavua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, naamini akija hapa, anaweza kuondoa kwa mara moja huu mrabaha ili wawekezaji wetu waweze kuja kuvua ndani ya bahari yetu hii. Tuna shida ya wawekezaji, wawekezaji wapo, tunawazuia kwa vijisheria vidogo vidogo; hili suala Mheshimiwa Waziri siyo kweli na naamini anaweza akafanya hii kazi kwa mara moja ili hizi meli ziweze kufanya kazi. Tunasubiri tuwekeze meli zetu, meli hazipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, ukiangalia hii kodi hata na sisi upande wa Zanzibar tunafaidika asilimia kubwa tunategemea katika bajeti yetu ya Serikali, sasa leo akisema hizi fedha haziendi, leseni hakuna, sasa kule Zanzibar Mheshimiwa Waziri tufanye nini na sisi katika mategemeo yetu hili suala la uvuvi pia tunategemea kwa sababu Kisiwa cha Zanzibar kimezungukwa na habari kila mahali sasa maendeleo yetu yote yanategemea uvuvi wa bahari kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo akiendelea kuzuia uvuvi huu, hatutafika mahali pazuri. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri akija kesho kutoa majibu, jibu la msamaha wa huu mrabaha, basi namwomba sana aweze kuondoa na siyo kwa muda, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Saada kazungumza aondoe kwa muda; huu unatakiwa kuondolewa kabisa, usiwepo tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)