Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Margaret Simwanza Sitta (36 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nichangie katika hoja iliyoko mezani. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai. Nawashukuru wapiga kura wa Urambo ambao wameniwezesha kuwa hapa na nawahakikishia sitawaangusha.
Vile vile nachukua nafasi hii kuishukuru familia yangu inayoongozwa na Mheshimiwa Mzee Sitta, kwa kuniwezesha kufanya kazi ninayoifanya sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu muda ni mfupi na mengi ninayo ya kuongea, pengine naweza kushindwa kumalizia; kwanza kabisa, naomba nianze na kutoa maombi na shukurani. Kwanza shukurani kwa Mheshimiwa Dkt. Magufuli, amefanya kazi kubwa sana kuteua Baraza zuri, linafanya kazi sana. Nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo mmeonesha tayari kwamba mnaiweza. Hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye maombi kwanza halafu ndiyo nieleze ninayoyataka. Mimi najikita katika zao la tumbaku tu, sina jambo lingine. Ndugu zangu, kwa Mkoa wa Tabora tumbaku ndiyo maisha, tumbaku ndio siasa. Kama sitataja tumbaku, sitawatendea haki wanyonge; wakulima walioko Urambo na Mkoa mzima wa Tabora. Mheshimiwa Waziri Mwigulu Nchemba, nakuheshimu sana na najua unaiweza hiyo kazi, ombi langu kwako, huu ni wakati muafaka ambapo masoko ya tumbaku huanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kawaida huwa masoko ya tumbaku yanaanza mwezi wa Nne. Nakuomba Mheshimiwa Waziri, katika kipindi hiki cha Bunge ukipata mwanya, uje Tabora ukutane na wakulima wa Urambo, Sikonge, Uyui, Nzega na Ulyankulu, ukutane na wakulima wote, uongee nao ujionee mwenyewe mateso wanayoyapata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia 60 ya tumbaku inatoka Mkoa wa Tabora na kwa msingi huo, ni vizuri Mheshimiwa Waziri ukafika Tabora kwanza ukutane na wakulima wenyewe watakutafutia uwakilishi wao; pili, ukutane na Vyama vya Msingi; na tatu, utakutana na wanunuzi wenyewe. Uwasikie kila watu na vilio vyao ambavyo vinasababisha hali ya mkulima isipande hata siku moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuna haja ya kumbembeleza mkulima alime, yeye mwenyewe anahitaji fedha; ukimwezesha masoko ukamwezesha na pembejeo, inatosha, huna haja ya kumbembeleza. Wewe mwezeshe tu, kwa sababu masoko ndiyo kishawishi kikubwa cha mtu alime. Halafu pili, pembejeo zinazofika kwa wakati na bei nafuu. Kwa hiyo, naishauri Serikali yetu kwa kupitia Wizara ya Kilimo ishughulikie masoko kwanza, ndiyo kilio kikubwa cha walima tumbaku. Hilo ombi la kwanza, ufike wewe mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitashukuru pia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa heshima kabisa, nakuomba kama ulivyokwenda Mtwara na Lindi ukaona korosho, tunakuomba na wewe Mheshimiwa Waziri Mkuu, uje Tabora uone makato wanayokatwa wakulima. Naamini kabisa, yako mengine utatoka umeagiza huko huko yapunguzwe ili kumpunguzia mkulima makato ambayo yanamfanya aendelee kuwa maskini, katika pembejeo na pia katika bei ya tumbaku yenyewe. Karibuni sana na nitashukuru Mheshimiwa Waziri atakapokuwa ana-wind up atueleze anakuja lini, angalau akituambia yuko tayari na sisi tujiandae kumpokea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, namwomba Waziri katika ku-wind up, hebu atusaidie, mpaka sasa hivi, Serikali imejitahidi imetafuta wanunuzi kutoka Japan na kadhalika. Bado hawatoshi. Tuna wanunuzi wakubwa watatu kule wamejikita, wamekuwa kitu kimoja. Wewe uliona biashara gani ambayo haina ushindani? Wote wanatoka na lugha moja; si hasara tu kwa mkulima hiyo? Wameshaelewana! (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, utakapokuwa una-wind up tunaomba utueleze, mpaka sasa hivi Serikali imefikia hatua gani ya kutafuta wanunuzi wengine wa tumbaku ili zao liwe na ushindani na mkulima naye apate anachostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ambalo naomba ujibu wakati unapo-wind up, ni jinsi gani ambavyo Serikali inalifikiria suala la kuwa na Kiwanda cha Tumbaku Tabora? Mkoa wa Tabora unaotoa asilimia 60 ya tumbaku, halafu cha ajabu, inabebwa na magari yanaharibu barabara yanapeleka Morogoro. Sisi tunataka kiwanda kijengwe pale pale. Siyo hivyo tu, ubaya wake ni kwamba, wanunuzi wajanja sana, wanaipima tumbaku ikiwa Urambo au Tabora kwa ujumla; ikifika Morogoro wanapima tena. Kwa hiyo, ile bei anayopewa mkulima ni ile ambayo wamepima Morogoro. Ni haki hii? Gari ikiharibika njiani, ikikaa wiki nzima! Kwa hiyo, Serikali inasemaje kuhusu kujenga Kiwanda cha Tumbaku Mkoa wa Tabora? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia cha ajabu jamani ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, mliona zao gani lina grade 72? Tumbaku eti ina grade 72! Miaka ya nyuma ilikuwa grade saba; sasa hivi wamenyumbuisha mpaka zimekuwa sasa eti grade 72. Wewe uliona wapi? Shina la tumbaku ni majani 12 mpaka 16; eti majani 12 - 16 yana grade 72, si uonevu tu huo! Kwa hiyo, Mheshimiwa utuambie mtapunguzaje grade za tumbaku utakapokuwa una-wind up. Huu ni uonevu wa hali ya juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hivi sasa ninavyoongea, Urambo na naamini Wabunge wenzangu, kwenu masoko ya tumbaku hayajaanza. Kwa kawaida Masoko ya tumbaku yanaanza mwezi wa Nne na kuitendea haki mara nyingi, iishe mwezi wa Nane na ikizidi kabisa mwezi wa Tisa mwisho. Mwaka 2015 wameendelea mpaka mwezi wa Kumi na Moja. Unajua tatizo lake ni nini? Inavyozidi kukawia na thamani inazidi kushuka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nashangaa! Naomba Mheshimiwa Waziri utakapokuwa una-wind up utuambie, kwa nini bodi mpaka sasa hivi hawajaenda kuhimiza uanzaji wa masoko ya tumbaku na kwamba mtaiwezeshaje Bodi ya Tumbaku ili ifanye kazi kikamilifu ili kweli masoko ya tumbaku yaanze kwa wakati na yaende kwa haraka? Sasa hivi masoko ya tumbaku yanaweza kufanyika hata mara moja tu kwa mwezi, ambapo miaka ambayo ilikuwa inafanya vizuri, ilikuwa na masoko hata mara tatu au mara nne kwa mwezi, jambo ambalo lilikuwa linawasaidia sana wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hayo ndiyo ambayo naomba mtakapokuwa mna-wind up mtuelezee mikakati yenu kama Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nadhani nimezungumzia kuhusu makato mbalimbali ambayo mtatueleza kwamba makato haya, mtayapunguza kwa kiasi gani. Nilikuwa naangalia makato ya mkulima, jamani ndugu zangu, kama kuna mtu anayeyonywa hapa duniani, ni mkulima wa tumbaku. Eti kuna Kodi ya Kupakua, Kodi ya Usafirishaji, Kodi ya Damage, yaani kuharibika; eti Kodi ya Insurance! Ninyi mliona wapi mkulima na mambo ya insurance. Halafu sasa akishauza, anakatwa; Halmashauri inachukua, Union inachukua, Vyama vya Msingi vinachukua; yeye mkulima abaki na nini? Kwa hiyo, nafikiria haya ndiyo makato ambayo tunategemea mtatusaidia kuona ni jinsi gani ambavyo mnayapunguza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu kama nilivyosema, tukija kwa upande wa kilimo cha tumbaku, nimeomba kwamba wakati wa ku-wind up Mheshimiwa Waziri azungumzie jinsi gani atakavyoiwezesha Bodi ya Tumbaku.
Bodi ya Tumbaku ndugu zangu ndiyo ambayo inaajiri classifiers, wale wanaopanga madaraja (grade) za tumbaku. Sasa utakuja kukuta kwamba wengi wamestaafu, Serikali haijaajiri mpaka sasa hivi. Kwa Wilaya zetu za Mkoa wa Tabora, Wilaya moja haipaswi kuwa na chini ya classifiers watano. Eti sasa hivi katika Wilaya zetu zote zilizoko Mkoa wa Tabora, zile zinazolima tumbaku wako classifiers watatu. Mmoja aende Kaliua, mwingine aende Ulyankulu na mwingine Sikonge. Wataweza wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unakuta classifier mmoja anapanga mabelo 1,500 kwa siku, saa 3.00 mpaka saa 11.00, si wizi tu huo! Yeye ana akili gani ya kupanga belo 1,500 kwa siku? Kwa hiyo, badala yake bei wanabambikiziwa tu. Halafu walivyofanya ni kwamba, mpaka uipate hiyo hela; tumbaku inatakiwa kama ikiwa nzuri ilipwe Dola tatu angalau kwa kilo, lakini walivyozipanga sasa.
MHE. MARGARET S. SITTA: Sijui hiyo kengele ndiyo ya kwanza au ya mwisho!
NAIBU SPIKA: Ya mwisho Mheshimiwa!
MHE. MARGARET S. SITTA: Ooh! karibuni sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, mjionee wenyewe tunavyonyanyaswa huko.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampa hongera sana kwa kazi nzuri Mheshimiwa Waziri na Wizara kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 60 ya tumbaku Tanzania inalimwa Urambo Mkoa wa Tabora. Je, Serikali hii haioni kuna umuhimu wa kiwanda cha Tumbaku? Kwa sasa tumbaku inasafirishwa kwa magari kwenda Morogoro jambo ambalo limepunguza kiwango au daraja la tumbaku, wakati huo huo barabara zinaharibika. Aidha, kuwakosesha ajira vijana wa Urambo na Tabora kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haoini umuhimu wa kuokoa matunda ya Tanzania kwa kushawishi wawekezaji?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa dakika tano niseme niliyokuwa nimepanga kusema. La kwanza, namuunga mkono Mwalimu Bilago kwamba hili suala la watoto wa kike wanaopata mimba wanaachwa bila kushughulikiwa amelichokoza leo kwa Waziri anayehusika na usawa wa jinsia, namwomba na nawaomba Waheshimiwa Wabunge tulirudishe wakati Wizara ya Elimu itakapokuja kuleta bajeti yake hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawaunga mkono Waheshimiwa Wabunge wote waliosema kwamba vifaa vinavyowasaidia akina mama na wasichana kujihifadhi vipunguziwe kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwa upande wa Urambo. Kama walivyosema vifo vya akinamama tunaweza kuvipunguza pale ambapo tu kutakuwa na mkakati maalum, nami naamini Waheshimiwa Mawaziri waliochaguliwa wana uwezo, mwakani watakuja na mikakati mizuri zaidi, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue mfano kwa upande wa watumishi, tazama Urambo ilivyo, tuna zahanati 20, ni zahanati tano tu ambazo zina Matabibu. Sasa unategemea nini anapopelekwa mwanamke mwenye mimba ambaye ameshindwa kujifungua kwenye zahanati 15 ambazo hazina Matabibu? Pia kama walivyosema wenzangu, kuna mradi wa ADB, umetuacha sisi Urambo na Zahanati ya Wilaya; nusu imejengwa, pia theatre kwenye upande wa Kituo cha Afya, Usoke imeachwa nusu kwa upande wa Usoke na Isongwa; kliniki zilizokuwa zinajengwa, zimeachwa nusu halafu Serikali inatuambia sisi wenyewe tumalize, haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sisi wote Wabunge ambao tumeguswa na huu mradi wa ADB tufanye mpango wa kuona Serikali itajibu nini kuhusu kutuachia jukumu la kumaliza majengo ambayo yapo nusu. Pia chukua kwa mfano, wenzangu wamezungumzia juu ya OC zilivyopunguzwa, mwaka 2015 Urambo ilipewa shilingi milioni 185, mwaka huu imepewa OC milioni 60. Jamani itafanya kitu gani? Kulisha wagonjwa na kila kitu! Kwa hiyo, tunaiomba Serikali iangalie jinsi ambavyo inakata mambo mengine ambayo yataathiri sana afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia On call Allowance kwa mfano Urambo tangu Januari mpaka leo hawajapata On call Allowance, mnategemea wafanyakazi watafanya kazi kwa moyo kweli! Kwa hiyo, tunaomba On call Allowance zipelekwe ili wenzetu waweze kufanya kazi kwa moyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wafanyakazi wapya wanaopelekwa kwenye wilaya hizi hawapelekewi fedha za kujikimu kabla hawajafika. Kwa hiyo, hilo nalo tunaomba litendeke. Pia Wilaya ya Urambo haina gari la chanjo. Tunaomba gari la chanjo, Mheshimiwa Waziri atakapojibu atuambie lini angalau watu wa Urambo tutapata gari la chanjo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naunga mkono wenzangu waliosema mfumo wa watumishi katika Wizara ya Afya uangaliwe upya. Kwa mfano, sisi tumepata kibali cha kuajiri, lakini tuliomba kibali wakasema mtaajiri, lakini eti tunaambiwa tusubiri mpaka Wizara itangaze. Itatangaza lini? Tunaomba Serikali ituambie ni lini Serikali itatangaza ajira? Kwa sababu kama nilivyowaambia ni kwamba, tuna Matabibu watano tu katika zahanati 20, lakini wametuacha tusubiri mpaka Wizara itakapotangaza. Kwa hiyo, naunga mkono wenzangu waliosema kwamba mfumo wa kuhudumia watumishi ndani ya Wizara au Sekta hii ya Afya uangaliwe upya, inawezekana pengine tukahitaji mfumo mzima ubadilishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu sasa kutokana na maingiliano ya majukumu inakuwa ni vigumu sana kuajiri kwa wakati, mambo ambayo yangeweza kufanyika ndani ya TAMISEMI, unaambiwa yasubiri huko juu. Kwa hiyo, nami naunga mkono kwamba mfumo mzima uangaliwe wa jinsi ya kuhudumia watumishi ndani ya Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia hivi vifo vya akinamama, ndugu zangu, ni vita! Kila siku wanawake 42 wanakufa! Kungekuwa labda na uwezekano wa hawa akinamama 42 kila siku wakazikwa pamoja, nadhani lingekuwa shamba la ajabu kabisa kwa sababu kama kila siku ni 42 kwa mwezi ni elfu moja mia tano na ngapi huko! Kwa hiyo, ingekuwa hata pengine tunakwenda kuzuru sisi, kuwasalimu wenzetu ambao wamefariki wakifanya wajibu wao waliopewa na Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Afya aje na mkakati mzuri zaidi…
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hotuba ya Bajeti iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naipongeza Serikali yote kwa jinsi ambavyo imeleta mpango na bajeti ya kuthubutu, tusiogope kuthubutu, changamoto zitakazojitokeza huko mbele ya safari tutazitatua, lakini naipongeza sana Serikali pamoja na Waziri kwa uwasilisho mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naishukuru sana Serikali kwa kuamua kujenga reli kwa standard gauge, kwetu sisi tunaotoka Tabora, Kigoma na Mwanza ni ukombozi mkubwa. Natunaomba mpango uanze mara moja mwaka huu wa fedha ili tusaidie kupunguza bei kutokana na usafiri wa reli utakaopunguza bei ya bidhaa zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napongeza Serikali kwa kuja na mpango wa maji, ombi langu mimi ni kwamba ili akina mama watokane na ubebaji wa maji kwenye vichwa, badala ya shilingi 50 kama walivyopendekeza Kamati ya Bajeti tuongeze zifike shilingi 100 ili akina mama vijijini wapate maji wajikomboe na wafanye kazi zingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika mimi ningeanza na upandewa mtu ni afya. Bila afya hakuna chochote kinachowezekana. Ningejikita zaidi kwa upande wa mama na mtoto. Ndugu zangu tuwapongeze wakinamama na nafasi ingeniruhusu ningewaomba akina mama na akina baba wote tusimame tuwape heshima akina mama wanaofariki kwa njia ya uzazi, wanafanya kazi kubwa na wanafariki katika kutimiza wajibu wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona zimetengwa asilimia tisa ya bajeti nzima kwa ajili ya afya. Naiomba Serikali ifikishe asilimia 15 kama walivyokubaliana katika Azimio la Abuja. Lakini pia mimi ningependa katika kujumuisha tupate majibu mpango wa MMAM uliishia wapi? Kwa sababu mpango wa MMAM ulikuwa na lengo la kuongeza zahanati ili wakinamama wafike haraka kwenye zahanati ili wasipoteze maisha yao. Tunataka tathmini ya mpango wa MMAM. Zahanati nyingi hazijajengwa, lakini pia zina upungufu mkubwa wa watumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwapeni mfano wa Urambo tuna zahanati 20 ni zahanati tano tu zenye Maafisa Tatibu. Ni haki mama mjamzito mwenye complication kweli akapewe prescription ya dawa na muuguzi?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali katika mwaka huu wa fedha iangalie; na ndiyo maana nasema iongezewe bajeti ili kuwe na wafanyakazi wengi wa kutosha wa hospitali na zahanati. Urambo ina uhaba wa wafanyakazi 150, na nimeshatoa mfano kwamba zahanati tano tu ndizo zina Maafisa Tabibu ambao siyo haki hata kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kulikuwa na mradi huu wa ADB. Mimi naiomba Serikali iangalie jinsi gani ya kukamilisha zile theaters zilizokuwepo, najua hii bajeti katikati huko italeta tu mabadiliko ya kuomba nyongeza ya fedha, kwa sababu Serikali hii inathubutu. Tuna theater Urambo na sisi tulikuwa tunafikiri kwamba njia mojawapo ya kupunguza vifo vya kina mama na watoto ni kuwa na theater katika vituo vya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha ajabu ni kwamba Urambo nzima yenye kata 18 tuna kituo cha afya kimoja tu halafu hakina theater ni haki hii? Halafu theater iliyokuwa inajengwa imeishia kwenye linter kwa mpango wa ADB.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Urambo jamani tunahudumia mpaka Uvinza na ile miji ya karibu ya Mkoa wa Kigoma kutokana na umbali, lakini cha ajabu theater iliyokuwa inajengwa Urambo imeishia kwenye linter. Ndugu zangu nipeni pole mimi Mbunge wa huko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwa kuthamini afya ya mama na mtoto mpango wa ADB ulikuwa unajenga clinic ya mama na mtoto, jamani imeachwa imechimbwa msingi mpaka leo. Lakini pia kulikuwa na kliniki ya mama na mtoto katika sehemu ya Isongwa imeachwa katika hatua ya msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, na ninasikitika, nina barua hapa kutoka Wizarani inayotutaka sisi wenyewe tumalize, Halmashauri inaweza kupata shilingi milioni 500 za kumaliza theatres? Na hayo ni majengo tu hayahusiani na vifaa. Nina barua hapa ya kusikitisha sana ya kutuambia sisi kama Halmashauri tumalize miradi ya ADB, kwa nini walileta mradi ya ADB kama walikuwa wanajua sisi tuna uwezo? Mimi ningeomba suala hili la theatres zilizoachwa bila kumalizwa zote pamoja na majengo ya kliniki yamaliziwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia sisi Kanda ya Magharibi hatuna Hospitali ya Rufaa, je, Serikali inafikiriaje kuhusu Kanda ya Magharibi nayo kupata Hospitali ya Rufaa?
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye kilimo. Mimi naipongeza hii Serikali kwa kushughulikia sana suala la viwanda ili kuinua hali ya wananchi. Tunaomba badala ya tumbaku kutoka Tabora kupelekwa Morogoro tuwe na kiwanda, na sisi tuna hitaji viwanda kwa sababu vitatupa pia ajira kwa watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ukurasa wa 45 nimesoma, Serikali imeandika hapa kwamba inafahamu vizuri sana changamoto za wakulima. Nimeona hapa nikafarijika nikasema ahaa kumbe Serikali inajua. Ukurasa wa 35 inasema kwamba hata hivyo bado sekta hii ya kilimo inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo za kodi na tozo za mazao zisizo na tija. Tumbaku ina kodi zaidi ya 12, halafu wanasema tena uhaba wa pembejeo ambazo pia zina kodi nyingi, vifaa duni, masoko na uhaba wa Maafisa Ugani, kumbe Serikali inajua? Je, Serikali inachukua hatua gani katika kutimiza haya kutatua changamoto hizo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la zao la tumbaku, tumbaku ni jani, mwezi wa pili tu jani linaiva, jani likishaiva masoko yanatakiwa yaanze mara moja mwezi wa tatu, lakini utaona cha ajabu masoko yanasuasua hadi leo hii. Bodi ya Tumbaku haina fedha nimeongea nao hawana fedha, wakulima watafanyaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, tumbaku ndugu zangu inavyokaa inapoteza ubora na inapoteza uzito. Inapofika Morogoro imepoteza uzito, je, ni haki hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nawashukuru, Naibu Waziri wa Kilimo amesema na mimi naomba nirudie sijui kama itakuwa ni vibaya, kwamba anakuja Tabora, pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu waone shida zinazowakabili wakulima wa tumbaku waongee nao, vyama vya msingi vinakufa watafanyaje? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, makato kwenye pembejeo ni mengi, makato kwenye zao lenyewe mengi, kuna uhaba wa wanunuzi. Naomba mtuambie; kwa kuwa mnatambua; kwenye ukurasa wa 35; Serikali inachukua hatua gani ya kupata masoko zaidi ili kuwe na ushindani wa masoko? Haya makampuni matatu hayatoshi, yana ukiritimba, tunataka masoko mengine kutoka nje, nchi za Japan pamoja na China, Serikali inasema nini kuhusu hili?
Lakini pia wenzetu, kwa mfano wa Uganda wajanja wale wame-market kahawa yao wameiuza ndiyo maana unaona watu wa Kagera wanapeleka kahawa kuuzia Uganda. Kwa nini na sisi tusishirikishe Wizara ya Mambo ya Nje ili tumbaku yetu iuzwe? Kwa sababu ladha na harufu iliyo kwenye tumbaku tunayolima sisi watu wa Tabora ndiyo inayofunika duniani kote waulizeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa nini na sisi tusiitangaze kwa kutumia pia Wizara ya Mambo ya Nje, Mabalozi, nchi majirani ili tumbaku yetu na sisi ivutie tupate wanunuzi wengi zaidi. Mimi ninachoshukuru ni kwamba Mheshimiwa atakuja ajionee mwenyewe. Lakini naomba sana Bodi ya Tumbaku iwezeshwe ili iweze kufanya kazi, na pia nimesema kiwanda cha tumbaku kijengwe Mjini Tabora.
Mheshimiwa Naibu Spika, itakuwa kwa kweli siyo haki kama nikimaliza bila kusemea mtoto wa kike. Nimeona mipango mingi ya Wizara ya Elimu, mimi naomba kujua elimu bure inayotolewa itamsaidiaje mtoto wa kike hapa katikati pasiwe na tatizo lolote la kumfanya atoke nje ya darasa ili amalize kuanzia kidato cha kwanza hadi mwisho? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba Wizara itakapokuja kumalizia ituambie kutokana na wingi wa taasisi za elimu zilizo nchini ni lini Mamlaka ya Ukaguzi itaundwa ili ukaguzi kweli ufanyike kikamilifu?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni mengi ambayo ningeongea lakini bado nawakumbuka walimu wangu, tunaomba chombo kile kinachoundwa kwa ajili ya walimu kifanye kazi ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hiyo.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. MARGARETH S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira; pongezi sana kwa kazi nzuri inayofanyika. Ombi, naomba kwa heshima Mto Ugalla ulioko Usoke, Urambo usaidiwe kuondoa magugu yanayokausha maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi lakini vile vile namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kusimama humu Bungeni siku ya leo na wakati huo nawashukuru wapiga kura wa Urambo ambao wanaendelea kunipa ushirikiano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kwanza kupongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya na hasa kwa hii elimu bure. Kwa kweli hata kwenye Wilaya yangu Urambo imesaidia sana kuongeza wanafunzi madarasani, namwombea kwa Mungu aendelee kufanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo nachukua nafasi kumpongeza Profesa Ndalichako, Naibu Waziri wake, Makatibu Wakuu na wasaidizi wake na watendaji wote wa Wizara ya Elimu kwa kazi nzuri wanayofanya. Jamani Wizara ya Elimu si mchezo mimi nimekaa pale kwa miaka miwili na nusu ni kazi kubwa, hongera Profesa Ndalichako, kazi ni kubwa na unaiweza, Mungu akusaidie usikilize tu yale tunayopendekeza ya kusaidia kuboresha yale unayoyafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naunga mkono Waheshimiwa Wabunge wote walioongea hapo awali waliopendekeza kuwe na Independent Education Regulatory Board. Kwa jinsi hali ya elimu inavyokwenda lazima tuwe na chombo ambacho kitaangalia na kuchambua Sera ya Elimu ikoje, itaangaia elimu ya msingi maana yake nini, kwa sababu mpaka sasa hivi watu wengi hawajui maana ya elimu ya msingi inatoka wapi inakwenda wapi. Kwa hiyo, Regulatory Board itatusaidia kuelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia itazungumzia suala la lugha za kufundishia, tuendeje wakati huu wa karne hii ya 21 wakati huo huo itaangalia mitihani inayotungwa iendelee kama ilivyo au iangalie aina ya shule, mazingira ya shule na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi naunga mkono kwamba kuwe na Independent Education Regulatory Board. Kwenye Sheria ya Elimu ilivyo sasa hivi kuna chombo kinaitwa Education Advisory Board hakifanyi kazi, kwa hiyo, mimi naomba kabisa Serikali itusikie wengi ambao tumeongea kwamba kuwe nan Independent Education Regulatory Board.

Mheshimiwa Mwenyekiti, humu ndani huwa tunaongea sana, tunapiga sana vita ndoa za utotoni, lakini niambie kwenye Jimbo langu kama Urambo, mtoto amemaliza darasa la saba hakuchaguliwa, wazazi wake hawana uwezo kumpeleka private, anafanya nini? Mimi huwa najiuliza sana, ili huyu mtoto afikie umri wa kuolewa anafanya nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi napendekeza kwa Serikali itilie mkazo sana vyuo vya maendeleo ya wananchi, FDCs, lakini pia VETA. VETA zikitoa mafunzo ya aina mbalimbali ambayo wasichana hata na wavulana pia watakwenda yatawasaidia kukua kidogo, lakini niambie mahali ambako hakuna VETA kama Wilaya ya Urambo, FDC haina hela, huyu mtoto wa kike ili nimtunze mimi mpaka afikie umri wa kuolewa anafanya nini pale nyumbani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi natoa wito kwa Serikali itusaidie kuwa na Vocational Training Centres nyingi ili angalao ziwafanye wototo wapate ujuzi ambao utawasaidia kwenye hii sera ya viwanda, lakini pia na wenyewe kujiajiri, ili angalao kuwafanya wakue kidogo kuliko kuwaacha kama ilivyo.

Kwa hiyo, wakati huu naomba nitoe ombi kwa Mheshimiwa Waziri Urambo haina VETA, karibuni nitaleta barua ili watoto wangu wa kike wakuekue kidogo, wajifunze sayansi kimu, wajifunze ushonaji na mambo mengine, mapishi wawe ma-caterers na kadhalika, kwa hiyo, nitaleta ombo maalum Mheshimiwa Waziri kwenye ofisi yako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia hili jambo ambalo naliongelea sasa hivi ni suala la TSC. Nimeshasema jambo hili mpaka wakati mwingine natamani sijui nilie hivi au nifanyeje? Maana ya TSC ni nini na functions zake ni nini? Mimi nakuomba Mheshimiwa Waziri, najua iko TAMISEMI, ilishtukia tu ikahamia TAMISEMI, lakini mimi kwa maoni yangu ungeniuliza ingekuwa kwako Mheshimiwa, kwa sababu wewe ndiye unayetaka Sera ya Elimu ifanye kazi, hawa watu wanavyohudumiwa ni sawa? Wanatekeleza sera yako kama ilivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi ningeomba msaidiane na Mheshimiwa Jafo, Waziri wa TAMISEMI, mupime hiki chombo TSC kinafanya kazi iliyokusudiwa au ni li jitu tu limekaa au unaweza kuita a white elephant? TSC inafanya nini? Imerahisisha vipi kutoa huduma kwa walimu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi ninaamini kabisa ukimtaka mwalimu afanye kazi vizuri, wanasema wajibu na haki. Je, hii TSC inafanya kazi iliyokusudiwa? Ukiangalia majukumu yake mengi tu kuajiri, kuhamisha, sijui kufanya nini, inafanya kazi hiyo? Ili kurahisisha kweli wanaotekeleza Sera ya Elimu wafanye kazi vizuri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ningeomba kuishauri Serikali kuhusu mtoto wa kike. Kuna wakati mimi nilifanya kazi Wizara ya Elimu kwenye miaka ya themanini na kitu palikuwa na kitengo kilichokuwa kinaangalia elimu ya mtoto wa kike. Mimi ningeshauri kwa hali ilivyo ya watoto wa kike na mambo tunayoyaona, napendekeza kwa Serikali kwamba iwe na kitengo kinachoangalia mtoto wa kike na elimu. Kwa sababu ukichukua pale wanapoanza elimu ya msingi wote wako karibu idadi sawa tu, inaweza kuwa 50/50, lakini ukiangalia inaenda kwa msonge mpaka unafika chuo kikuu wote wameshaisha hapa njiani. Sasa kulikuwa na haja ya kuwa na chombo ambacho kitamshughulikia mtoto wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba niwaambie Serikali kwamba, haijafikia hatua ambayo tukaridhika, kwamba watoto wa kike na wa kiume wanaenda sawa kwa upande wa elimu. Kwa hiyo, natoa wito kwa Serikali kuwa na kakitengo kadogo ambako zamani kalikuwepo, sijui Serikali iliridhika ikakaondoa. Mimi nilikuwa naomba bado kitengo cha kumuangalia mtoto wa kike na elimu kirudishwe, ili watoto wa kikenao wafike kama wenzao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ni in-service training. Naishauri Serikali in-service training, yaani mafunzo kazini yanavyotolewa mpaka sasa kwangu mimi naona bado. Nimesoma kitabu nimeona idadi ya walimu waliopata mafunzo ni wachache sana. Naomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi bado ibebe jukumu la mafunzo kazini kwa ajili ya walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu wanapotoka chuoni wengine wameshafundisha miaka 30 wanahitaji kupigwa msasa ili waende na wakati. Kwa hiyo, mimi naomba kabisa kwamba, in-service training bado inahitaji kufanyiwa kazi na kusimamiwa na Wizara ya Elimu yenyewe, lakini ukiwapa TAMISEMI kwa jinsi ambavyo Wilaya zilivyo, Wilaya nyingine zitakwenda juu nyingine zitabaki chini. Kwa hiyo, mimi nilikuwa nafikiria kwa upande wa mafunzo kazini Mheshimiwa Waziri tusaidie ili in service training iendelee kutolewa na Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, nilitaka niipongeze Serikali kwa hii performance based (P4R). Mimi nimeipenda sana kwa sababu, utaratibu ulioko sasa hivi unakwenda kwenye shule, shule yenyewe inaangalia utaratibu gani wa kutafuta fedha, kwa hiyo, inapunguza gharama kuliko ile ambayo fedha inachukuliwa anapewa mtu contractor na nini. Kwa hiyo, mimi nilikuwa nafikiri hii P4R ni nzuri, naomba tu iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nadhani la mwisho ambalo ningependa kulizungumzia ni suala la ukaguzi. Bado mimi kwa mtazamo wangu na understanding yangu, tunahitaji chombo cha ukaguzi kinachojitegemea. Wakaguzi walivyo bado wako chini ya idara, hawapewi fedha za kutosha, lakini kule Wilayani kwenye Halmashauri wanapokosa mafuta kwenda kukagua wanamuomba Mkurugenzi. Huyu uliyekwenda kumpigia magoti asubuhi, ukamuomba mafuta ya dizeli au petroli, huyo huyo akakusimanga ukaenda ukamkagulia shule zake halafu jioni unamletea taarifa, ataisoma?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama kukiwa na independent kabisa chombo ambacho kinaangalia quality assurance na jinsi idadi ya taasisi zinazotoa elimu zilivyoongezeka kwa kweli, nakusihi kabisa Mheshimiwa Waziri anayehusika muangalie umuhimu wa kuwa na chombo cha ukaguzi kinachojitegemea ili kikague shule za Serikali na shule za binafsi bila kujali kwamba haya mafuta yametolewa. Kwa sababu, watakuwa wanajitegemea wanapata mafuta yao wao wenyewe kuliko kwa hali ilivyo bado ni idara tu ndani ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo mimi naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Ndalichako na wote wanaofanya kazi katika Wizara ya Elimu nikiamini kwamba wametusikiliza mengi na hasa hili la Independent Education Regulatory Board. Kwa kweli, Mungu awasaidie abariki kazi yenu ni ngumu, lakini mnajitahidi kadiri muwezavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, pongezi kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote. Nawatakia kila la heri katika kazi zenu muhimu na ngumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kuomba kwa niaba ya wananchi wa Urambo mradi wa Lake Victoria ufike Urambo. Naomba DDCA ianze kazi, Urambo tuna shida kubwa ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 272 wa kitabu cha Wizara, Kituo cha VETA cha Ulyankulu ambacho kipo Wilaya ya Kaliua imeandikwa kipo Urambo, naomba pasahihishwe. Kila la heri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Urambo na Kaliua ni Wilaya zinazoongoza hapa nchini kwa kilimo cha tumbaku. Pamoja na Wilaya hizi kuongoza kwa kilimo hiki, Mkoani Tabora bado hakuna kiwanda cha kusindika tumbaku pamoja na uwepo wa miundombinu ya reli na hata barabara inayojengwa. Je, ni lini Serikali itajenga kiwanda cha kusindika tumbaku Wilayani Urambo?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. La kwanza kabisa, kwa niaba ya familia yetu ya marehemu mzee Sitta, nachukua nafasi hii kuishukuru Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Serikali nzima,
uongozi wa Bunge unaoongozwa na Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, viongozi wa vyama kisiasa, viongozi wa dini, wananchi wote Tanzania kwa jinsi ambavyo walitufariji sana sisi familia ya marehemu Mzee Samuel Sitta; tunawashukuru sana, tunaomba ushirikiano mliotupa sisi uendelee. (Makofi). Mungu ibariki Tanzania, lakini pia tunamwomba Mungu aiweke roho ya marehemu Samuel Sitta mahali pema peponi, Amina.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukue nafasi hii kumpa pole Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge kwa kifo cha mwenzetu, Mheshimiwa Dkt. Macha, tumwombe Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu Dkt. Elly Macha mahali pema peponi, Amina.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia katika sekta tatu. Kwanza kabisa naomba nianze na Sekta ya Kilimo. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Urambo, nasema wazi kwamba huwezi kuzungumzia hali ya kiuchumi na maendeleo ya kiuchumi ya wananchi wa Urambo bila kuzungumzia suala la tumbaku. Nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote mnapoongea mkizungumzia suala hili kwa sababu ni muhimu
sana katika maendeleo ya wananchi wa Urambo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa niaba ya wananchi wa Urambo kwa jinsi alivyochukua hatua mbalimbali katika kunusuru zao la tumbaku, nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. Pamoja na hatua mbalimbali ambazo Mheshimiwa Waziri
Mkuu amezichukua bado kuna maswali ambayo ningeiomba Serikali ichukue hatua za haraka kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kwa kuwa Bodi ya Tumbaku imevunjwa, je ni lini Serikali itaunda bodi mpya kwa sababu sasa hivi mwezi wa Nne ndiyo masoko ya tumbaku yanatakiwa yaanze? Pia, pamoja na kuunda bodi mpya, Serikali imejipanga vipi kuiimarisha Bodi mpya ya
Tumbaku ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi hususan upatikanaji wa classifiers, wale ambao wanapanga tumbaku katika grades zinazotakiwa wakati wa kuuza tumbaku na msimu ndiyo huu mwezi wa Nne?
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile ningependa Serikali itueleze, wakulima wana tozo nyingi, sasa hizi tozo Serikali imejipangaje kuziondoa ili mkulima naye anufaike na zao lake analolihangaikia mwaka mzima?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wakati huo huo amri ilitolewa na Serikali ya kuvunja uongozi wa AMCOS mbili za Utenge na Nsenda, lakini msimu wa tumbaku umefika, lini Serikali itaondoa amri hiyo ili kuwe na uongozi katika AMCOS hizo waweze kushughulikia uuzaji wa tumbaku haraka iwezekanavyo kwa sababu kama nilivyosema mwezi wa Nne ndiyo wanaanza?
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tumbaku, tunaiomba sana Serikali itilie mkazo hasa upatikanaji wa mbolea. Tunapoanza na mbolea kuchelewa kutakuwa na matatizo makubwa. Je, wakati huu ambapo Bodi ya Tumbaku imevunjwa nani atakayeshughulikia suala la upatikanaji wa mbolea haraka iwezekanavyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kwenye upande wa changamoto nyingine tuliyonayo, upande wa suala la maji. Sasa hivi sisi Urambo hatuna maji na kuna mpango ambao Serikali imeuandaa wa kupata maji kutoka Malagarasi, lakini utachukua muda mrefu, je, Serikali imejipangaje kipindi hiki ambacho mradi wa Malagarasi unaendelea, hawawezi kutuchimbia visima, hawawezi kutuchimbia mabwawa ili tutumie wakati tukisubiri mradi huu wa maji wa muda mrefu kutoka Mto Malagarasi? Kwa hiyo, tunaiomba Serikali ifanye hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ni suala la afya. Ningeiomba Wizara ya Afya kwanza kwa kuanzia hebu ibane halmashauri kwa kushirikiana na viongozi wa halmashauri (TAMISEMI); kwamba ni jinsi gani halmashauri zimepanga fedha hususan kwa ajili ya kuokoa maisha ya mama na
mtoto? Kila siku wakati wa kujifungua hapa Tanzania tunapoteza akinamama 30. Je, Serikali kwa kupitia Wizara ya Afya imejipangaje ili kuhakikisha kwamba fedha mahususi zinapangwa kwa ajili ya kuokoa vifo vya akinamama na watoto?
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huohuo nichukue nafasi hii kuishukuru sana Serikali kwa kuchagua Jimbo la Urambo au Wilaya ya Urambo kuwa miongoni mwa wilaya ambazo zitapata fedha moja kwa moja kupelekwa kwenye vituo vya afya, zahanati na hospitali.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, nauliza moja tu; je, Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba zahanati zetu zinakuwa na watumishi waliotosha? Kwa mfano, sisi tuna zahanati 21, hamuwezi kuamini katika zahanati 21, 15 hazina maafisa tabibu, sasa wagonjwa wanaandikiwa matibabu na nani? Wakati huo huo upungufu ni asilimia 77, yaani ufanisi wa utumishi ni aslimia 33 tu. Sasa fedha zikipelekwa moja kwa moja kwenye zahanati na vituo vya afya nani anashughulikia fedha hizi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, natoa ushauri kwamba haraka iwezekanavyo tusaidiwe sisi wa Jimbo la Urambo kupewa wafanyakazi wa kutosha haraka sana ili waweze kutekeleza hili zoezi la kupeleka fedha moja kwa moja kwenye zahanati. Wewe fikiria mahali ambapo kuna
watumishi wawili nani anamwangalia mwenzake? Nani anatimiza wajibu wa kuhudumia wagonjwa? Nani anatunza fedha? Kwa hiyo la kwanza ni upatikanaji wa watumishi haraka iwezekanavyo lakini pili, tunaiomba Serikali iajiri wahasibu ili hizi fedha zitakazokuwa zinapelekwa kwenye
zahanati ziweze kutunzwa kadri iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, kutokana na uhaba mkubwa watumishi kwa asilimia 77 katika Jimbo langu, naamini na wenzangu wako kwenye matatizo ya hivyo hivyo. Mimi kama Mbunge wa Jimbo la Urambo naomba Wizara husika ituanzishie Chuo pale pale
kama ilivyo Nzega na kadhalika ambacho kitafundisha Watumishi wa kada ya kati ili na sisi tupate watumishi haraka iwezekanavyo kutokana na uhaba tuliokuwa nao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Kanda ya Magharibi, ukichulia hasa Mkoa wa Kigoma na Tabora, hatuna Hospitali ya Kanda. Tunachukua nafasi hii kuiomba Serikali na sisi Mkoa wa Kigoma na Tabora tujengewe Hospitali ya Kanda kwa sababu inatubidi kuja Dar es Salaam au kwenda Mwanza wakati wenzetu wanazo karibu kadri iwezekanavyo. Kwa hiyo, tunaomba Serikali ifanye hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nilikuwa nafikiria kwamba hili suala la upatikanaji wa Watumishi wa Afya, Serikali ilitilie maanani ndugu zangu. Kwa hali ilivyo, kama Serikali haitachukua mkakati maalum, tutapata shida sana kuhusu watumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri suala la upungufu wa Watumishi wa Afya liangaliwe ipasavyo na nitashukuru sana. Kama viongozi wetu, Mawaziri mtakuja kwetu kule kama alivyofanya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuja Tabora kuangalia suala la Tumbaku na Mawaziri husika naomba mje mwangalie uhaba wa watumishi tulionao kwenye Mkoa wetu wa Tabora kwa ujumla lakini pia Wizara Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nashukuru kwa kupata nafasi, lakini naomba sana, katika kujumuisha hapa, tupate majibu, lini tumbaku itapata uongozi wa haraka iwezekanavyo? Ile Bodi ya Tumbaku ipate uwezo wa kuajiri wafanyakazi wa kutosha ili masoko sasa yanayoanza mwezi huu yaende kama yalivyopangwa. Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami nichangie katika hoja iliyopo mezani. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na nawashukuru pia wananchi wa Urambo kwa kunipa ushirikiano. Aidha, naipongeza Serikali ya Mheshimiwa Rais Magufuli kwa kazi kubwa wanayofanya akisaidiana na Mawaziri wake, hongereni Mawaziri kwa kazi kubwa. Vilevile pia nawapongeza wanawake wenzangu walioshinda uchaguzi jana, hongereni akinamama mnaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kwenye maji. Naomba nianze mchango wangu kwa kuuliza maswali manne. Kila ninapozungumzia suala la uhaba wa maji Urambo naambiwa subiri mradi wa maji kutoka Malagarasi kilomita 200 kutoka Urambo. Swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri anayehusika aniambie ni hatua gani za dharura zitachukuliwa ili wananchi wa Urambo wapate maji wakati wakisubiri mradi kutoka kilomita 200? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kama kweli mradi wa Malagarasi umetiliwa maanani, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa ana-wind up aniambie ametenga shilingi ngapi za kuanza mradi huu katika mwaka huu wa fedha 2017/2018. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la tatu, je, Serikali haioni kwamba ni rahisi kuchukua maji kutoka Lake Victoria kuyapeleka Tabora na kuyafikisha Urambo kilometa 92 badala ya kusubiri maji kutoka kilometa 200? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la nne, kama kweli Wizara imejipanga kutatua tatizo la maji, naomba waniambie kwa nini hadi leo shilingi milioni 647 zilizotengwa kwa ajili ya kutafuta vyanzo vingine vya maji na mradi maalum wa Kijiji cha Izimbili mpaka leo hazijapatikana? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeuliza maswali hayo kwa makusudi kwa lengo zuri tu la kuonesha kwamba tukisubiri utaratibu wa fedha uliozoeleka kila siku hatuwezi kupata maji. Ndiyo maana ukiangalia bajeti ya mwaka jana shilingi bilioni 900 zilitengwa hatimaye tukapata shilingi bilioni 181 tu na kati ya hizo shilingi milioni zipatazo 90 zilitokana na Mfuko wa Maji. Ndiyo maana unaona Wabunge wengine wote waliochangia wanasema hivi, tutunishe Mfuko wa Maji kwa kuongeza Sh.50 ziwe Sh.100 kwa sababu kwa bajeti ya kawaida imeshindikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, natoa ombi kwa Serikali, kwanza ianzishe Mfuko wa Maji Vijijini kama ilivyo umeme. Tunaamini kukiwa na Mfuko wa Maji Vijijini itakuwa rahisi kusambaza maji. Kwa msingi huo, Serikali ikikubali kupata shilingi 50 zaidi kutoka kwenye petroli au dizeli, sawa, cha maana hapa tupate tu shilingi 100 kuchangia Mfuko wa Maji. Hata hivyo, iwapo Serikali itaona kutoa shilingi 50 kwenye petroli na dizeliinaweza kuathiri sehemu nyingine basi ile shilingi 50 itokane na Mfuko wa REA tuchukue kidogo na Mfuko wa Barabara ili tupate Mfuko wa Maji Vijijini wenye fedha ambazo zimechangiwa kwa shilingi 100. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna asiyefahamu umuhimu wa maji, kila mtu anafahamu umuhimu wa maji. Kwa msingi huo, naomba Waziri atakapokuwa ana-wind- up hebu atoe kauli ya kuwapa moyo wananchi wa Urambo kwamba mwaka huu ni nini kitafanyika ili wapate maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la tatizo la maji la kudumu katika shule za msingi. Shule za msingi na sekondari nyingi ukipita, mimi juzi nimezungukia kwenye shule hawana maji. Sasa napendekeza, hii nipamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia waone umuhimu wa kutokusajili shule hadi pale shule imeshawekewa miundombinu ya kuvuna maji ya mvua pamoja na taasisi nyingine. Kwa sababu kwa utaratibu ulivyo hata kama maji yatatoka Lake Victoria, Malagarasi mpaka maji yafike kwenye shule na nyingine ziko mbali sana, kwa kweli ufumbuzi wa kudumu ni kwamba shule au taasisi za aina hiyo zisipate usajili mpaka zioneshe miundombinu ya kutega maji ya mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia napenda kusema kwamba Serikali ikikubali ombi la kuongeza Sh.50 ili kutunisha Mfuko wa Maji. Pia ianzishe Mfuko wa Maji Vijijini ili kumtua mwanamke ndoo. Bila hivyo kwa bajeti ya kawaida imeonekana haiwezekani. Naamini Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Magufuli ni sikivu kwa upande wa maji mtakubali hilo kuwe na Mfuko wa Maji Vijijini. Hii itasaidia wanawake kuondokana na kubeba maji kutoka mbali jambo ambalo linawasababisha washindwe kufanya kazi nyingine za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu na wafanyakazi wote kwa kazi kubwa wanazofanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya watumishi wa Urambo,nashukuru sana kwa vituo viwili vya afya. Ahsante sana, ni msaada mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Wilaya ya Urambo ina kata 18 na kwa sasa tumepata vituo viwili vya afya, kwa heshima tunaomba vituo viwili vya afya kwenye kata zenye wakazi wengi na ziko kwenye barabara kubwa katika eneo la Songambele na Vumilia. Pia, tunaomba walimu na wafanyakazi wa afya ili wakafanye kazi kwenye vituo hivi, tunatanguliza shukrani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Urambo ni moja ya Wilaya inayonufaika na Mfuko wa Rais wa Kujitegemea. Wananchi wa Urambo wameufurahia sana huduma ya mikopo. Je, Serikali inawaambia nini waliokuwa wanaendelea kupata huduma za Mfuko huu ambapo ghafla wameambiwa umesitishwa?Wafanyaje kuhusu marejesho? Je, isingekuwa vizuri Serikali kuwapa nafasi wanufaika na wanafakazi kukamilisha mikopo kwa mfano isingeweza kutoa noticena kusema kuanzia mwaka wa fedha 2020/2021 hakutakuwa na Mfuko wa Rais? Je, Serikali haioni kuwa Mfuko imesitishwa ghafla sana? Tunaomba Mfuko huu upewe muda wa kutosha ilivyo sasa ambapo taarifa imetolewa ghafla sana na masuala ya fedha hajakaa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Urambo wanashukuru sana huduma ya MKURABITA. Tunaomba MKURABITA iendeleze huduma zake za biashara na kurasimisha ardhi ili wananchi wanufaike kwa kupata hati. Aidha, tunaomba fedha ziongezewe ili MKURABITA ifanye kazi kwa ufanisi zaidi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie, pia namshukuru Mwenyezi Mungu na ninaendelea kuwapa pole wenzetu wa Lucky Vincent, shule ambayo ilipoteza wanafunzi, Mwenyezi Mungu azilaze mahali pema roho za marehemu. Amen.

Naendelea kuwashukuru wananchi wa Urambo kwa ushirikiano wa wanaonipa. Nichukue nafasi hii kuwapongeza Mheshimiwa Profesa Ndalichako na Mheshimiwa Injinia Stella Manyanya kwa kazi kubwa wanayoifanya. Wizara ya Elimu ni kazi kubwa na tumewaona jinsi ambavyo wanachakarika, ninawapa pongezi sana. Naomba tu yale tunayowapa myapokee ili yale mnayoyafanya yaendelee kuwa mazuri zaidi. Hongera, akina mama wanaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Kamati ya Huduma za Jamii inayoongozwa na Mheshimiwa Peter Serukamba kwa kweli kwa taarifa yao ambayo inatusaidia wote tunaounga mkono suala la watoto wa shule wanaopata mimba warudi shuleni. Katika taarifa yao kwa ruhusa yako, ukurasa wa 29 unasema hivi; “Kamati inashauri Serikali kutoa tamko rasmi kwamba mwongozo huo unaoruhusu wanafunzi wa kike wanaopata mimba kurudi shuleni utangazwe, uanze kutumika ili wanafunzi wa kike ambao wamekuwa wakifukuzwa shule kutokana na kupata ujauzito kurudishwa shuleni ili kuendelea na masomo yao. Hii itasaidia Taifa liweze kunufaika na usomaji wa watoto wa kike.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, tuunge mkono kauli hii ya Kamati. Ninavyofahamu Kamati husika huwa inakaa pamoja na Wizara, kwa hiyo, naamini kabisa kumeshakuwa na mashauriano kati ya Wizara na Kamati kwa hiyo kilichobaki, tuiunge mkono Kamati ambayo inafanya kazi kwa niaba yetu. Tunategemea Waheshimiwa Mawaziri wakati wa kuhitimisha mtoe tamko kama mlivyoombwa na mlivyoshauriwa na Kamati husika, watoto wetu wa kike warudi shuleni baada ya kujifungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikwenda Kenya, tunapokwenda kwenye nchi nyingine tunajifunza. Unayachukua yale ambayo unaona kwako yatakufaa. Tulipozungumzia wenzetu mnafanyaje kuhusu watoto wa kike wanaopata mimba, walitushangaa, wakasema jamani kwao ni historia, walishaamua zamani, Watanzania na sisi tufanye hivyo kwa sababu ni jambo zuri ambalo na litatusaidia ikikumbukwa kwamba watoto wa wasomi kama sisi tuliopo hapa na viongozi, mtoto akipata mimba tu anarudishwa shule. Wanaopata shida ni watoto wa wakulima na wasiokuwa na uwezo, tuwasaidie. Ndugu zangu, hilo halina ubishi tuunge mkono tu Azimio la Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine labda niongezee kidogo tu kuongelea mazingira wanayopatia mimba hawa watoto sisi tunayajua, ni wenzetu wajanja, wenye hela basi, halafu hao hao wanakataa, watoto lazima warudi shuleni. Kwa msingi huo tuombe, tumesikia changamoto zinazowapata watoto wa kike pamoja na umbali wa shule, tunaomba katika maazimio mengine ambayo tupitishe hapa kwamba kama Serikali ilivyochukua hatua ya kujenga maabara ichukue nguvu ile ile kuhakikisha kwamba shule ziwe na mabweni ya watoto wa kike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitaka hili suala pia liende vizuri, ndugu zangu tuulize Wizara ya Elimu imejipanga vipi kuimarisha elimu ya kujitambua katika shule. Wazazi wengine wanaogopa kuongea na watoto wao ili wajitambue kwamba ukifikia umri huu utaona haya na haya. Nawapongeza wazazi wanaofanya hivyo, kwa wale ambao hawafanyi hivyo naomba Serikali ijikite katika kuimarisha elimu ya kujitambua katika shule ili waweze kujua. Of course elimu hii ikitolewa itazingatia pia umri wa watoto, Serikali imejiandaa vipi kuhusu elimu ya kujitambua katika shule? Je, kuna walimu ambao wameandaliwa? Mimi naelewa, kuna walimu wengine ukiwaambia wafundishe somo hilo hawawezi, yeye mwenyewe anaona aibu. Je, kuna walimu ambao wameandaliwa kwa somo hilo ili litolewe vizuri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda upande wa walimu; mimi pia ni mwalimu, ndugu zangu ualimu sio mchezo, inahitaji moyo mkubwa sana, changamoto nyingi walizonazo walimu wa nchi hii ninaamini zinaweza zikatatuliwa kama chombo kilichoundwa mwaka 2015, TSC, chombo cha kuhudumia walimu kitafanya kazi kama ipasavyo. Najua kipo chini ya Ofisi ya Rais, Waheshimiwa Mawaziri ninyi mnaelewa, ndiyo mnaosimamia mafanikio ya elimu, kwa hiyo mshauriane na TAMISEMI jinsi gani mtaimarisha TSC ambayo itasaidia lakini kama TSC itakuwa kama ilivyo sasa hivi ndugu zangu TSC haijaanza kufanya kazi vizuri. Kesi nyingi za walimu hazifanyiki kwa sababu hazipati fedha za kutosha, ofisi hakuna na wakati mwingine mahali ambapo Halmashauri nyingine zinafanya chini ya Ofisi ya DC, tunaomba Halmashauri zote zipewe uwezo na TSC ziweze kuimarika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mshirikiane na TAMISEMI ili TSC ifanyekazi, lakini tukiichukulia kama ilivyo definition au maana ya mwajiri, mwajiri wa walimu ni nani? Mpaka sasa hivi ninavyojua waajiri ni 139 kutokana na idadi ya Halmashauri, TSC haijawa mwajiri. Sasa tunapokuwa na waajiri 139 hatuwezi kuwasaidia walimu, huwezi kujua changamoto zao kwa pamoja. Hata hii ya walimu fake, wangeweza kutambuliwa sana kama kungekuwa na TSC ambayo inampima mwalimu kabla haijampa mkataba, naomba TSC iimarishwe.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana tulimaliza Wizara ya Maji, nawaomba Wizara ya Elimu nayo kabla haijasajili shule kwanza iitake shule iwe na miundombinu ya kukusanya maji. Watoto wa shule wanapata taabu sana, unakutana nao barabarani wanabeba vidumu kwenda kutafuta maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu shule binafsi nami na-declare interest, shule binafsi zinasaidiana na Serikali kuimarisha watoto wetu, kodi zimezidi. Kodi ni muhimu lakini zimezidi, tunaomba kodi wanazotozwa shule binafsi ziangaliwe ili na wao watoe mchango wao kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba labda nisimalize kuzungumza kabla sijasema suala la VETA. VETA ni muhimu sana kwa wanafunzi wowote wale wa kidato chochote kile. Urambo ilikuwa na VETA, Wilaya ilipogawanywa VETA imejikuta ipo Kaliua, kama Urambo tulikobaki hatuna VETA. Nawasihi wapenzi wangu, Waheshimiwa Mawaziri mtufikirie Urambo nasi tuwe na VETA kwa sababu naamini kwamba watoto wanaomaliza kidato cha nne, wanaomaliza darasa la saba ambao hawakupata nafasi ya kuendelea kwingine, mafunzo ya ufundi yatawasaidia sana kujiajiri na kuajiriwa na hasa kipindi hiki ambacho tunataka uchumi wa viwanda, Mafundi Mchundo na wengineo wote watapatikana kupitia VETA. Nawasihi VETA ziimarishwe zaidi ya yote mtusaidie na Urambo tupate VETA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaamini sana Waheshimiwa Mawaziri, najua kabisa mengi mnayafanya mazuri, lakini naomba mpokee yale yote yanayochangiwa na Waheshimiwa Wabunge kwa lengo la kuimarisha yale ambayo mnayafanya. Nawatakia kila la heri, akina Mama wanaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunisikiliza.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi nichangie hoja iliyopo mezani. Nichukue nafasi hii pia kuwashukuru wapiga kura wa Urambo na wakati huo nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Kilimo hii ni ngumu, kwa kweli nichukue nafasi hii kuwapa pole Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu wawili pamoja na watendaji wote kwa kazi ngumu wanayoifaya, lakini wasikate tamaa, waendelee kufuatilia ili hatimaye wafanye kazi nzuri kwa manufaa ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kipekee kwa kazi nzuri aliyoifanya Mkoani Tabora alipokwenda kushughulikia changamoto za tumbaku, ahsante sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mambo aliyafanya Mheshimiwa Waziri Mkuu pia ni kuteua Bodi mpya ya Tumbaku ambayo imeanza vizuri, nawatakia kila la kheri na hasa kwa vile wameongeza ndani yake wajumbe wenye uwezo na uzoefu wa zao hili la tumbaku, nawatakia kila la kheri. Pia nichukue nafasi hii kuiomba Serikali ikamilishe uteuzi wa Mwenyekiti ili bodi iweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nachukua nafasi hii kumuuliza Mheshimiwa Waziri na Wizara nzima kwa ujumla, hivi kweli ina kalenda ya kilimo kwa mikoa yote ya Tanzania? Kama ina kalenda ya lini mvua zinaanza mkoa gani, wakati gani pembejeo zinatakiwa; iweje wakulima waanze kulima baadae washtukie hawana mbolea, inakuwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kitu ambacho kinawasaidia wakulima wapate mazao mazuri ni kuwa na pembejeo hususan mbolea kwa wakati, lakini inasikitisha pale ambapo wakulima wamelima lakini hakuna mbolea unaambiwa zitakuja wiki ijayo na mazao yanaharibika pale ambapo hayapati pembejeo kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atuambie hivi kweli wanafanya kazi kwa kufuatana na kalenda ya misimu mbalimbali ya mvua katika mikoa kwa sababu mikoa inatofautiana ili tuache usumbufu wa wakulima kulima bila kuwa na matumaini ya kuwa na pembejeo yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kukumbusha Wizara kwamba katika mazao ambayo yamekuwa na matatizo hapa Tanzania moja wapo ni tumbaku; wakisahau kwamba tumbaku inaiingizia nchi hii fedha za kigeni zaidi ya asilimia 40. Sasa kama zao linaingiza zaidi ya asilimia 40 ya fedha za kigeni, iweje lisipewe kipaumbele ili nchi yetu iendelee kupata fedha za kigeni?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu ukiangalia sana changamoto hizi si kwamba tunazizungumzia leo kwa mara ya kwanza, tumezungumzia kila wakata hasa hata mimi mwenye kama Mbunge wa Jimbo la Urambo nimekuwa nikilizungumzia suala la tumbaku na pembejeo kila ninapopata nafasi ya kuongea humu Bungeni. Sasa iweje zile changamoto bado ziendelee pamoja na jitihada kubwa ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano tumbaku tofauti na mazao mengine, tumbaku inatakiwa mbolea iwe imefika kabla ya mwezi wa saba. Je, Serikali inatuhakikishia kwamba mbolea inayotumika na tumbaku hasa NPK itakuwa imefika nchini hapa na kupatikana kwa wingi kabla ya mwezi wa saba? Kwa sababu ndipo ambapo wanaanza kuandaa mabedi (seed beds) kwa ajili ya kupanda mbegu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi ningeomba hili suala Mheshimiwa Waziri husika alizungumzie pia anapo- wind-up, kweli wakulima wa tumbaku wanahakikishiwa kwamba kuna mbolea ya NPK tayari nchini mwezi wa saba karibu unafika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumekuwa na tatizo kubwa sana la pembejeo hasa NPK ambayo inategemewa sana na wakulima wa tumbaku. Kwa sasa hivi bei ya tumbaku inatofautiana kwa sababu ya utaratibu wa uingizaji wa mbolea nchini. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kutuhakikishia kwamba kama wamefanya utaratibu wa bulk procurement kwa ajili ya mbolea za mahindi, hawawezi kufanya utaratibu huo huo pia kwa ajili ya zao la tumbaku ili wakulima wapate tumbaku nyingi kwa wakati mmoja lakini pia iondoe tofauti ya mbolea inayojitokeza kutokana na manunuzi ya mbolea kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala ambalo tumekuwa tukiliongelea sana Mheshimiwa Waziri anajua, msimu uliopita sasa hivi wa zao la tumbaku tumepata shida sana wakulima wa tumbaku kutokana na tumbaku nyingi kushindwa kuuzwa, na hii imetokana na uhaba wa masoko. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kutuhakikishia sisi wakulima wa tumbaku kwamba ameweka utaratibu mpaka sasa wa kupata wanunuzi wangapi ili waingie nchini wasaidie kuinua bei ya tumbaku? Kwa sababu panapokuwa na wanunuzi wengi kunakuwa na ushindani.

Je, Mheshimiwa Waziri utakuja utuambie hatua ambazo tayari Serikali imeshachukua, hata kwa kutumia Waheshimiwa Mabalozi waliopo nchi za mbali ili kupata wanunuzi ili kuwe na ushindani katika kuuza tumbaku yetu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la masoko ni la muhimu sana ukiangalia adhabu waliyopata wakulima wa tumbaku mwaka huu. Kwa vyovyote mkulima anapolima kitu cha kwanza anachoangalia ni soko, sasa anapokuwa na uhakika wa soko ndipo analima vizuri ili aweze kujiendeleza yeye mwenyewe kibinafsi lakini pia kusaidia nchi yetu kuingiza fedha za kigeni kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala muhimu sana la Bodi ya Tumbaku, kweli Bodi ya Tumbaku ipo lakini nasikitika kusema kwamba bado haijawezeshwa kufanya kazi vizuri, maana yake ni kwamba kupata fedha za kutosha… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami nichangie hoja iliyoko mezani. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na wakati huo huo nawashukuru wapiga kura wa Urambo wanaoendelea kunipa ushirikiano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali na hasa Wizara inayohusika, Mawaziri wote na watendaji wote kwa kazi nzuri waliyoifanya na hasa kwa bajeti hii ambayo inalenga kujenga uchumi wa viwanda utakaochochea ajira na ustawi endelevu wa jamii.

Mheshimiwa Spika, nimeangalia ukurasa wa 40 ambako kumetolewa maelezo wazi kabisa kwamba bajeti hii itaangalia suala la upatikanaji wa maji vijijini kama walivyopendekeza pia Kamati inayohusika, pia itazingatia suala ala afya. Hapa naomba niikumbushe Serikali kwa upande wa afya, pamoja na jitihada nzuri zinazofanywa na Serikali, bado tuna tatizo kubwa sana la uhaba wa wafanyakazi. Tunaomba suala la wafanyakazi lipewe kipaumbele; na pia uendelezaji wa ujenzi wa Vituo vya Afya ambavyo bado vinahitajika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa elimu pia imeelezewa, lakini nielezee tu kwamba, kuna kifungu hiki kimoja katika ukurasa wa 40 ambacho nimekipenda sana, ila naomba Mheshimiwa Waziri wakati wa kuhitimisha afafanue. Kinasema: “Aidha, mahitaji ya makundi maalum katika jamii yetu; wanawake, vijana, watoto, watu wenye ulemavu na wazee wataendelea kuangaliwa kipekee.’ (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha, atueleze ‘kipekee’ maana yake ni nini? Je, wenzetu wenye ulemavu wa ngozi wategemee mafuta wanayotumia pengine yatapunguzwa bei? Je, wenzetu wasioona watapata pengine fimbo za kutembelea? Tunaomba aneo hili liwekwe wazi ili watu waendelea kuishi kwa matumaini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Wabunge Wanawake na Wabunge Wanaume wanaotuunga mkono katika kutetea haki za wanawake na watoto wa kike, naipongeza sana Serikali kwa ukurasa wake wa 46 ambapo wametamka wazi kabisa kwamba wanaondoa kodi katika taulo za kike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wewe ni shahidi, hii ajenda ni ya wanawake wote chini ya Chama chetu au Umoja wetu unaoitwa TWPG. Tumekuwa tukilizungumzia suala hili kwa muda mrefu na nachukua nafasi hii pia kuishukuru Serikali, imekuwa ikikubali kuwaleta Wawakilishi wao katika vikao mbalimbali ambavyo tumekaa pamoja ili kuhakikisha kwamba hili leo walilolitamka linafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kwa niaba ya wanawake wa Bungeni wote kuishukuru sana Serikali kwa ukurasa wake wa 46 ambao umekubali kupunguza kodi ya ongezeko la thamani. Nimefanya hesabu hapa, nimeona kwamba VAT asilimia 18 kwa taulo za kike zinazouzwa Sh.2,000/= zitakuwa zimepungua kwa Sh.360/= na kwa taulo za kike ambazo zitauzwa kwa Sh.3,500/= gharama itapungua kwa Sh.630/=.

Mheshimiwa Spika, tumechukua hili kwa uzito wake kwamba angalau Serikali imefikiria. Ndugu zangu akinamama na akinababa mnaotuunga mkono, tuipongeze Serikali kwa hatua hii. Kwa sababu kwa watoto wa kike wanaoshindwa kwenda shuleni kila mwezi kutokana na kukosekana kwa taulo za kike, wanapoteza siyo chini ya siku nne au tano. Kwa hiyo, kwa nusu muhula wanapunguza karibu wiki tatu wanashindwa kwenda shuleni na ukichukulia kwa muhula mzima wanashindwa kwenda shuleni kwa wiki sita na kwa miaka minne kuanzia form one mpaka form four, wanapoteza wiki 24 za kutokwenda shule.

Mheshimiwa Spika, tumezungumzia sana habari za utoro kwa watoto wa kike na kwa taarifa au utafiti uliofanywa na UNESCO umeonesha wazi kwamba katika watoro wa kike 10, mmoja anashindwa kwenda shule kutokana na ukosefu wa taulo za kike. Kwa hiyo, hii hatua ya Serikali tunaipongeza sana nikiamini kwamba pengine itachukua hatua zifuatazo ili huu msamaha huu wa kodi uwe na manufaa zaidi:-

Mheshimiwa Spika, kwanza, tunaiomba Serikali iwashawishi wawekezaji wa viwanda wengi zaidi wawekeze katika eneo hili. Viwanda vikijengwa vingi, hizi taulo zitapatikana kwa wingi zitasaidia pia hata kushusha bei zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, tunaiomba Serikali sasa, katika malighafi zitakazotumika kutengeneza taulo za kike, VAT pia iondolewe, yaani wapate msamaha wa kodi ili malighafi zipatikane kwa bei nafuu ili wengi zaidi watengeneze taulo hizo. Tunaiomba Serikali, siyo iwaombe tu wafanyabiashara kupunguza bei, hapana; tunaomba hata ikiwezekana itoe bei elekezi ili angalau hizi taulo za kike zipatikane. Naamini, ndugu zangu kwamba hizi taulo za kike kupunguziwa kodi ni hatua ya kwanza. Tunaiomba kwa heshima Serikali tukitegemea kwamba iko siku itafikiria kutoa hizi taulo za kike bure kwa kadri ya uwezo wa bajeti utakavyowezesha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali kwa kuja na uamuzi wa kuondoa riba katika mikopo inayotolewa kwa akinamama na vijana. Tunaomba hili suala liendelee, sheria itakapowekwa vizuri, basi kusiwe na riba yoyote katika mikopo.

Mheshimiwa Spika, itakuwa sikutenda haki kama sikukutaja wewe siku ya leo kwamba umekuwa mstari wa mbele kutuunga mkono akinamama tunapoangalia vipingamizi vya watoto wa kike kuhudhuria shule. Moja ilikuwa ni hili la taulo za kike ambalo Serikali imelifikiria, lakini la pili ni uhaba wa vyoo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vyoo vingi karibu asilimia 52 vinavyotumiwa na watoto wa kike havina milango. Kwa hiyo, tunakupongeza wewe kwa kutuunga mkono kwa fund raising tunayoitegemea tarehe 22 Juni, 2018, ili tuchangie upatikanaji wa vyoo vya kike, tutoe vyoo vya mfano ili vyoo vitakapojengwa sasa viweze kumsitiri mtoto wa kike na wa kiume pamoja na walemavu. Tunakushukuru sana kwa kutuunga mkono kwa suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine nililotaka kuzungumzia ni suala la kodi za mazao. Tumbaku ifikiriwe pia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nakupongeza wewe kwa kutuunga mkono.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili nami nichangie. Kwanza, namshukuru Mungu kwa kunipa nafasi lakini pia nawashukuru wapiga kura wangu wa Wilaya ya Urambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuwapongeza Mawaziri Mheshimiwa Jafo na Mheshimiwa Mkuchika na Naibu wao; Mheshimiwa Kakunda na Mheshimiwa Kandege na Makatibu Wakuu; Mhandisi Iyombe na Dkt. Ndumbaro na Naibu wao; Dkt. Chaula na Ndugu Nzunda pamoja na watendaji wote wa taasisi za TASAF, MKURABITA na Mfuko wa Rais, kwa kweli wanafanya kazi nzuri. Mungu awasaidie na naomba Serikali iwaongezee fedha waweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona ni muhimu kwangu kwa niaba ya wananchi wa Urambo kuishukuru Serikali kwa kutupa ambulance, ahsante sana itatusaidia kukimbiza wagonjwa pale inapobidi. Pia nashukuru kwa kupewa wafanyakazi kumi na nne na kutembelewa na Waheshimiwa Mawaziri, ahsanteni sana kwa kufika kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Serikali kwa kupewa milioni 400 ambayo inasaidia kumalizia Kituo cha Afya cha Usoke ambacho kilikuwa ni kiporo cha mradi wa ADB. Wakati huo huo, niiombe Serikali yetu sikivu itusaidie kumalizia theatre ambayo pia ni kiporo cha mradi wa ADB, iliyoko katika Wilaya ya Urambo kwani itakuwa na manufaa sana kwa sababu bado tunasaidia wenzetu wa Kaliua na maeneo mengine kutoka Wilaya ya Uyui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani za kupewa milioni 400 ya kusaidia kituo cha afya bado tuna uhaba mkubwa sana wa vituo vya afya. Tunaiomba Serikali yetu itusaidie kupata Kituo kingine cha Afya cha Vumilia ambacho kipo katika barabara ya kwenda Sikonge ili ajali zinapotokea kisaidie. Pia kituo hiki kitasaidia ajali zinazotokea kati ya Kigoma na Urambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo kingine cha Afya cha Usoke nacho tunaomba kisaidiwe. Kwa hiyo, tunaomba msaada wa kupata vituo vya afya cha Vumilia na Kata ya Usoke kwa sababu mpaka sasa tuna kituo kimoja tu cha afya kati ya kata 18. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kuiomba Serikali iangalie sana suala la wafanyakazi wa afya. Sisi Urambo peke yetu tuna uhaba wa wafanyakazi zaidi ya 300, lakini ili angalau kupooza makali tunaomba wafanyakazi 75. Tutashukuru sana tukipata haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali iajiri na hasa hasa Wakunga. Tunapozungumzia kupunguza vifo vya mama na mtoto tunaangalia sana uwepo wa Wakunga. Kwetu sisi kuna zahanati ambazo zina mfanyakazi mmoja tu, sasa anapougua au anapokwenda kwenye semina mama mjamzito anapokuja pale inakuwa ni vigumu sana kupata huduma. Tunaomba Serikali iajiri wafanyakazi na kwa kuanzia waanzie Wakunga ambao tunaamini kabisa watatusaidia kupunguza vifo vya akinamama na watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna uhaba mkubwa sana pia kwa upande wa elimu. Orodha ya mahitaji yetu sisi kama Urambo tulishapeleka TAMISEMI. Kwa hiyo, tunaomba Walimu wa shule za sekondari na shule za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kuunda TSC ilikuwa ni kuangalia jinsi gani tunaweza kuwapunguzia Walimu adha katika kupata haki zao. Ombi langu kwa Serikali ifanye tathmini, kweli TSC iliyopo inakidhi mahitaji iliyoundiwa? Kwa sababu mpaka sasa hivi matatizo bado ni mengi tu, Mwalimu anapodai haki zake au anapotaka kuhama na kadhalika. Tunaiomba Serikali ifanye tathmini, je, TSC kweli inafanya kazi zake ilizokusudiwa? Naamini Serikali inaweza kuchukua hatua za kurekebisha ili Walimu waweze kupata huduma kwa wakati hasa hasa mahitaji ya kupanda daraja na wakati huo huo kurekebishiwa mishahara yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwa upande wa elimu lakini hasa kwa kugusa mtoto wa kike. Naomba niseme wazi kabisa mimi nimo katika Kamati ya Utawala na TAMISEMI na naiunga mkono kabisa taarifa ya Kamati yangu kwenye ukurasa wa 37 ambapo inasema, naomba kwa ruhusa yako nisome, kutokana na kushindwa kumudu gharama za taulo za kike, wanafunzi wa kike wamekuwa wakikumbwa na athari za kushindwa kuhudhuria masomo kwa siku kati ya tatu mpaka tano kwa mwezi na hivyo kuathiri mahudhurio yao na wakati mwingine kuacha shule kabisa hasa wanaotoka katika familia duni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili ni muhimu sana. Naiomba kwa heshima na taadhima Serikali kuliangalia suala hili kwa undani na kuona jinsi gani ambavyo itaweza kumsaidia mtoto wa kike. Suala hili kama nilivyosema tunaiomba Serikali iliangalie kwa makini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tuna tatizo moja sugu kwenye Kamati yetu tulilitilia sana mkazo na tulimwambia Mheshimiwa Waziri husika wa TAMISEMI kuangalia suala la vyoo. Suala la vyoo pia limekuwa likisababisha wakati mwingine watoto wa kike kushindwa kuvitumia kutokana na kukosa milango na vilevile na Walimu kuchangia vyoo na watoto yaani wanafunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali kwa heshima kabisa kuangalia jinsi gani wanaweza kuweka mkakati ambao utaondoa kabisa tatizo la vyoo na wakati huo kuiomba Wizara ya Elimu kwa kupitia taarifa hii hii, shule zisisajiliwe kabla ya kujenga vyoo. Vyoo vianze halafu ndiyo majengo mengine yakaguliwe. Nadhani jambo hili linahitaji mkakati wa karibu kabisa ili iweze kusaidia kuondoa tatizo la vyoo visitajwe kabisa tena kwa sababu ni jambo la kusikitisha kwamba tunazungumzia choo katika karne ya 21 kwa sababu tunaamini kabisa mtu ni afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeweza nikaongea mengi zaidi ya hayo lakini hasa hasa ni kuomba kwa heshima kabisa vituo vya afya kama nilivyosema Vumilia na Usoke;
kuomba theatre yetu Urambo ambayo ni kiporo cha ADB imaliziwe, lakini wakati huo huo kuiomba kabisa Serikali yetu kwa heshima na taadhima kabisa kuangalia upatikanaji wa wafanyakazi wa Idara ya Afya na hususan Wakunga ambao watasaidia kuondoa vifo vya akinamama au kupunguza kwani hali ilivyo sio nzuri tunahitaji huduma haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, nikiamini Serikali yetu nzuri itasikia haya niliyoyasema. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hoja iliyoko mezani, lakini pia namshukuru Mungu kwa kunipa nafasi hii na wakati huo huo nawashukuru wapiga kura wa Urambo ambao wamekuwa wakinipa ushirikiano kila siku, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inanibidi nimshukuru Mheshimiwa Waziri Kamwelwe pamoja na Naibu Waziri Aweso pamoja na Katibu Mkuu Profesa Kitila Mkumbo, Wakurugenzi wote wa Wizara hii kwa jinsi ambavyo wanajitahidi kutatua tatizo hili kubwa tulilonalo nchini mwetu. Mheshimiwa Waziri ulikuja Urambo na ninakushukuru ulikuja kwa kituo, tukazunguka tukaona shida ya maji tuliyonayo Urambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwetu sisi Urambo changamoto ya kwanza ni maji na wewe mwenyewe ulishuhudia. Tulikwenda Usoke Mheshimiwa Waziri, ukaona jinsi ambavyo wanaume na wanawake wamezunguka kisima kimoja, wote wanasubiri maji yajae kwenye kisima na kisha wanatumia neno ambalo wewe mpaka leo Mheshimiwa Waziri unalijua, wakisema amsha popo, wote kwa pamoja wanashusha ndoo ndani ya kisima, Mheshimiwa Waziri uliona. Ni jambo lilikuhuzunisha wewe mwenyewe binafsi na mimi mwenyewe, hatukuaga kwa jinsi ya uchungu tulioupata. Tukaanza kuhangaika na wewe Mheshimiwa Waziri je, tupate maji kwenye Mto Ugala ikashindikana.

Mheshimiwa Spika, niko mbele yenu ninyi viongozi wa Wizara hii kwa uchungu uliouona Mheshimiwa Waziri nakusihi, nakuomba kwa niaba ya wapiga kura wa Urambo mtupatie maji ya kutoka Lake Victoria. Wewe mwenyewe umeona hakuna mbadala, visima tunavyochimba vitoe maji kama walivyoongea wenzangu kutoka Mkoa wa Tabora maji yako chini sana. Kwa hiyo, tunapokuomba visima ni ufumbuzi wa muda tu, lakini kwa ufumbuzi wa kudumu Mheshimiwa Waziri nakusihi kwa niaba ya wananchi wa Urambo tupate maji kutoka Lake Victoria. Naomba Mwenyezi Mungu akuongoze Mheshimiwa Waziri utakapokuwa unahitimisha angalau utamke neno la kuwapa matumaini watu wa Urambo, shida ya maji ni kubwa mno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika jitihada ya kupata suluhisho la muda tuliomba kuchimbiwa visima, tukapata Mkandarasi akatuchezea akili, tukarudi kwako wewe Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara yako wakatusaidia kutuunganisha na Wakala wa Uchimbaji Maji inayoitwa DDCA. Tunaomba Mheshimiwa Waziri utusaidie, kwa kupitia wizara yako ili huu wakala unaochimba maji uje uchimbe maji angalau kwenye vijiji 17 ambavyo vina shida sana ya maji.

Mheshimiwa Spika, naamini Mheshimiwa Waziri utaisukuma hii DDCA ili angalau ilete vyombo vyake tuone tuanze kupata matumaini, kwa sababu mpaka sasa hivi hawajafika na sisi tuna shida sana ya maji na hatuombi kwamba ishindikane fedha zirudi, zishindwe kutumika katika mwaka huu wa fedha. Tunakusihi sana Mheshimiwa Waziri utuangalie Urambo kwa jicho la huruma kutokana na shida ya maji tuliyonayo.

Mheshimiwa Spika, la pili Mheshimiwa Waziri tunaona kwamba katika kupata suluhisho la muda tukisubiri mradi huo mkubwa ambao naamini Mwenyezi Mungu atakusaidia tupate kutoka Lake Victoria, tunaomba tuchimbiwe bwawa. Kuna eneo zuri sana wataalam wetu walishaleta udongo Wizara ya Maji ili upimwe udongo ule kuona aina ya udongo ambayo unaweza kufaa kwa ku-retain maji yaani kwa kutunza maji. Eneo hilo zuri sana, bonde zuri sana ukija tena tutakupeleka Mheshimiwa ukaone, lakini tutafurahi kama wakija wataalam waone eneo ambao linaweza kuchimbwa bwawa zuri sana eneo la Kalemela.

Mheshimiwa Spika, nimeona, mimi nina wivu wa maendeleo, nimeangalia kwa wenzangu wanachimbiwa mabwawa, naamini kwa jicho lako la huruma pia na sisi Urambo tutachimbiwa bwawa la maji katika eneo la Kalemela ili na sisi tuwe na chanzo kimojawapo cha kupata maji ya kutusaidia wakati tukisubiri maji kutoka kwenye mradi mkubwa ambao naamini kwa jicho la huruma utatuingiza na sisi katika huo mradi ambao unahusisha milioni kama 500 hivi za fedha za kigeni kutoka India.

Mheshimiwa Spika, mimi nachukua nafasi hii kuwaunga mkono Wabunge wenzangu wote waliotangulia kuzungumzia umuhimu wa kuwa na Mfuko wa Maji Vijijini. Tumeona jinsi ambavyo REA inafanya kazi vizuri, tunaamini tukianzisha Mfuko Maalum wa Maji Vijijini, hili suala la maji linaweza kupata ufumbuzi. Kwa hiyo, naunga mkono wenzangu waliotangulia walioongea kusema tupate angalau ushuru au jina lolote mtakalotumia wa shilingi 50 kutoka kwenye dizeli na petroli ili isaidie kuunda mfuko huo ambao tunaamini utasaidia upatikanaji wa maji vijijini.

Mheshimiwa Spika, la mwisho kwa siku ya leo ni tatizo hili ambalo nadhani linahitaji si wizara moja tu, nadhani linahitaji Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakati huo huo TAMISEMI na Wizara yako mkae pamoja muone jinsi gani ambavyo mtahakikisha kwamba tunathamini kuvuna maji ya mvua. Kwa kweli ukiangalia maji ya mvua yanavyopotea na shuleni watoto wa kike, wa kiume wote wanashindwa kupata hata maji ya kunawa mikono baada ya kwenda sehemu zile wanazokwenda. Kwa hiyo, mimi ningeomba kuwe na sheria fulani ya uvunaji wa maji ya mvua ili tuondokane na shida ya maji hasa katika maeneo ya taasisi zetu za shule na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, pengine Wizara ya Elimu inaweza ikaamua kwamba shule isifunguliwe mpaka kuwe na utaratibu wa kuvuna maji ya mvua. Kwa sababu ni jambo la kusikitisha mvua inavyonyesha hasa kwa mfano kama sasa hivi mvua inanyesha Dar es Salaam na wapi, lakini maji yanapotea, na wakati huo huo unakuta watoto hawana maji mashuleni na kwenye taasisi kama hizo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nilikuwa nafikiri kuwe na kautaratibu fulani ka kulazimisha, wenzetu kwa mfano, kwa taarifa niliyonayo na nimeshuhudia nilikwenda Bamuda. Kwenye Kisiwa cha Bamuda wameweka utaratibu kwamba hujengi nyumba yako wewe ya kuishi kabla hujaonesha jinsi utakavyovuna maji ya mvua. Sasa na mimi nilikuwa nafikiri na sisi tungekuwa na utaratibu huo hasa hizi taasisi zetu isifunguliwe mpaka utaratibu wa kuvuna maji uwekwe. Wakati huo huo nichomekee na hapa hapo, maji na choo yaani kuwe na maji uvunaji wa maji na choo ndio taasisi iandikishwe. Nimechomekea hilo kwa sababu naona vinaenda karibu pamoja tu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi naomba kumalizia kwa kurudia tena kilio chetu sisi watu wa Urambo. Pamoja na shukrani zetu kwako wewe Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri ambaye pia alikuja akitokea Kigoma nawasihi mtuweke. Hata kama hamkututaja kwenye kitabu hiki muone jinsi ya kutuingiza sisi kama Urambo kwenye mradi wa kupata maji kutoka Lake Victoria kama ukombozi wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru nawapongeza kwa kazi ngumu mnayoifanya lakini niko mbele yenu kuwaomba mtukumbuke Urambo, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hoja iliyoko mezani, lakini pia namshukuru Mungu kwa kunipa nafasi hii na wakati huo huo nawashukuru wapiga kura wa Urambo ambao wamekuwa wakinipa ushirikiano kila siku, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, inanibidi nimshukuru Mheshimiwa Waziri Kamwelwe pamoja na Naibu Waziri Aweso pamoja na Katibu Mkuu Profesa Kitila Mkumbo, Wakurugenzi wote wa Wizara hii kwa jinsi ambavyo wanajitahidi kutatua tatizo hili kubwa tulilonalo nchini mwetu. Mheshimiwa Waziri ulikuja Urambo na ninakushukuru ulikuja kwa kituo, tukazunguka tukaona shida ya maji tuliyonayo Urambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwetu sisi Urambo changamoto ya kwanza ni maji na wewe mwenyewe ulishuhudia. Tulikwenda Usoke Mheshimiwa Waziri, ukaona jinsi ambavyo wanaume na wanawake wamezunguka kisima kimoja, wote wanasubiri maji yajae kwenye kisima na kisha wanatumia neno ambalo wewe mpaka leo Mheshimiwa Waziri unalijua, wakisema amsha popo, wote kwa pamoja wanashusha ndoo ndani ya kisima, Mheshimiwa Waziri uliona. Ni jambo lilikuhuzunisha wewe mwenyewe binafsi na mimi mwenyewe, hatukuaga kwa jinsi ya uchungu tulioupata. Tukaanza kuhangaika na wewe Mheshimiwa Waziri je, tupate maji kwenye Mto Ugala ikashindikana.

Mheshimiwa Spika, niko mbele yenu ninyi viongozi wa Wizara hii kwa uchungu uliouona Mheshimiwa Waziri nakusihi, nakuomba kwa niaba ya wapiga kura wa Urambo mtupatie maji ya kutoka Lake Victoria. Wewe mwenyewe umeona hakuna mbadala, visima tunavyochimba vitoe maji kama walivyoongea wenzangu kutoka Mkoa wa Tabora maji yako chini sana. Kwa hiyo, tunapokuomba visima ni ufumbuzi wa muda tu, lakini kwa ufumbuzi wa kudumu Mheshimiwa Waziri nakusihi kwa niaba ya wananchi wa Urambo tupate maji kutoka Lake Victoria. Naomba Mwenyezi Mungu akuongoze Mheshimiwa Waziri utakapokuwa unahitimisha angalau utamke neno la kuwapa matumaini watu wa Urambo, shida ya maji ni kubwa mno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika jitihada ya kupata suluhisho la muda tuliomba kuchimbiwa visima, tukapata Mkandarasi akatuchezea akili, tukarudi kwako wewe Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara yako wakatusaidia kutuunganisha na Wakala wa Uchimbaji Maji inayoitwa DDCA. Tunaomba Mheshimiwa Waziri utusaidie, kwa kupitia wizara yako ili huu wakala unaochimba maji uje uchimbe maji angalau kwenye vijiji 17 ambavyo vina shida sana ya maji.

Mheshimiwa Spika, naamini Mheshimiwa Waziri utaisukuma hii DDCA ili angalau ilete vyombo vyake tuone tuanze kupata matumaini, kwa sababu mpaka sasa hivi hawajafika na sisi tuna shida sana ya maji na hatuombi kwamba ishindikane fedha zirudi, zishindwe kutumika katika mwaka huu wa fedha. Tunakusihi sana Mheshimiwa Waziri utuangalie Urambo kwa jicho la huruma kutokana na shida ya maji tuliyonayo.

Mheshimiwa Spika, la pili Mheshimiwa Waziri tunaona kwamba katika kupata suluhisho la muda tukisubiri mradi huo mkubwa ambao naamini Mwenyezi Mungu atakusaidia tupate kutoka Lake Victoria, tunaomba tuchimbiwe bwawa. Kuna eneo zuri sana wataalam wetu walishaleta udongo Wizara ya Maji ili upimwe udongo ule kuona aina ya udongo ambayo unaweza kufaa kwa ku-retain maji yaani kwa kutunza maji. Eneo hilo zuri sana, bonde zuri sana ukija tena tutakupeleka Mheshimiwa ukaone, lakini tutafurahi kama wakija wataalam waone eneo ambao linaweza kuchimbwa bwawa zuri sana eneo la Kalemela.

Mheshimiwa Spika, nimeona, mimi nina wivu wa maendeleo, nimeangalia kwa wenzangu wanachimbiwa mabwawa, naamini kwa jicho lako la huruma pia na sisi Urambo tutachimbiwa bwawa la maji katika eneo la Kalemela ili na sisi tuwe na chanzo kimojawapo cha kupata maji ya kutusaidia wakati tukisubiri maji kutoka kwenye mradi mkubwa ambao naamini kwa jicho la huruma utatuingiza na sisi katika huo mradi ambao unahusisha milioni kama 500 hivi za fedha za kigeni kutoka India.

Mheshimiwa Spika, mimi nachukua nafasi hii kuwaunga mkono Wabunge wenzangu wote waliotangulia kuzungumzia umuhimu wa kuwa na Mfuko wa Maji Vijijini. Tumeona jinsi ambavyo REA inafanya kazi vizuri, tunaamini tukianzisha Mfuko Maalum wa Maji Vijijini, hili suala la maji linaweza kupata ufumbuzi. Kwa hiyo, naunga mkono wenzangu waliotangulia walioongea kusema tupate angalau ushuru au jina lolote mtakalotumia wa shilingi 50 kutoka kwenye dizeli na petroli ili isaidie kuunda mfuko huo ambao tunaamini utasaidia upatikanaji wa maji vijijini.

Mheshimiwa Spika, la mwisho kwa siku ya leo ni tatizo hili ambalo nadhani linahitaji si wizara moja tu, nadhani linahitaji Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakati huo huo TAMISEMI na Wizara yako mkae pamoja muone jinsi gani ambavyo mtahakikisha kwamba tunathamini kuvuna maji ya mvua. Kwa kweli ukiangalia maji ya mvua yanavyopotea na shuleni watoto wa kike, wa kiume wote wanashindwa kupata hata maji ya kunawa mikono baada ya kwenda sehemu zile wanazokwenda. Kwa hiyo, mimi ningeomba kuwe na sheria fulani ya uvunaji wa maji ya mvua ili tuondokane na shida ya maji hasa katika maeneo ya taasisi zetu za shule na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, pengine Wizara ya Elimu inaweza ikaamua kwamba shule isifunguliwe mpaka kuwe na utaratibu wa kuvuna maji ya mvua. Kwa sababu ni jambo la kusikitisha mvua inavyonyesha hasa kwa mfano kama sasa hivi mvua inanyesha Dar es Salaam na wapi, lakini maji yanapotea, na wakati huo huo unakuta watoto hawana maji mashuleni na kwenye taasisi kama hizo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nilikuwa nafikiri kuwe na kautaratibu fulani ka kulazimisha, wenzetu kwa mfano, kwa taarifa niliyonayo na nimeshuhudia nilikwenda Bamuda. Kwenye Kisiwa cha Bamuda wameweka utaratibu kwamba hujengi nyumba yako wewe ya kuishi kabla hujaonesha jinsi utakavyovuna maji ya mvua. Sasa na mimi nilikuwa nafikiri na sisi tungekuwa na utaratibu huo hasa hizi taasisi zetu isifunguliwe mpaka utaratibu wa kuvuna maji uwekwe. Wakati huo huo nichomekee na hapa hapo, maji na choo yaani kuwe na maji uvunaji wa maji na choo ndio taasisi iandikishwe. Nimechomekea hilo kwa sababu naona vinaenda karibu pamoja tu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi naomba kumalizia kwa kurudia tena kilio chetu sisi watu wa Urambo. Pamoja na shukrani zetu kwako wewe Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri ambaye pia alikuja akitokea Kigoma nawasihi mtuweke. Hata kama hamkututaja kwenye kitabu hiki muone jinsi ya kutuingiza sisi kama Urambo kwenye mradi wa kupata maji kutoka Lake Victoria kama ukombozi wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru nawapongeza kwa kazi ngumu mnayoifanya lakini niko mbele yenu kuwaomba mtukumbuke Urambo, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami nichangie hoja iliyoko mezani. La kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai, lakini la pili nawashukuru sana wananchi wa Urambo kwa kunipa ushirikiano wakati wote, Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kipekee kuishukuru Wizara ya Maji ikiongozwa na Profesa Mbarawa, Mheshimiwa Aweso, Katibu Mkuu Profesa Mkumbo, Naibu wake na watendaji wote kwa kweli kazi wanachapa, nawatakia kila la heri waendelee kuchapa kazi, kazi wanaiweza, kitu kikubwa ni kuwezeshwa kifedha tu. Ni uhakika usiopingika kwamba chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kazi inafanyika katika Wizara ya Maji, hongera sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa niaba ya wananchi wa Urambo nichukue nafasi hii kushukuru sana Wizara kwa kutuwezesha sisi watu wa Urambo kuingizwa katika Mradi wa Maji kutoka Lake Victoria. Nawashukuru sana sana kwa sababu tulikwenda sisi kwenye Mto Malagarasi tukaona umbali ulioko kutoka Malagarasi mpaka Urambo halafu pia na mwinuko wa nchi, kwa kweli tunashukuru kwamba tunapata maji kutoka Lake Victoria kwa sababu ni kilomita 90 tu kutoka Tabora, tunashukuru sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali moja tu ambalo ningeomba wanijibu kwa niaba ya wananchi wa Urambo wakati wa kuhitimisha ni kwamba, sasa huu mradi wa maji kutoka Lake Victoria ni wa mwaka gani wa fedha ili na sisi tuishi kwa matumaini. Kwa hiyo tutashukuru sana kujua ni lini tunapata maji kutoka Lake Victoria, mwaka gani wa fedha. Kwa kuwa Urambo kuna shida kubwa sana ya maji kwa kweli nikiulizwa wakati wowote kipaumbele au shida kubwa inayowakabili wananchi wa Urambo; la kwanza nitasema maji kwa sababu sisi water table imeshuka, yaani maji yameshuka chini sana kwa hiyo ni vigumu kupata maji na hakuna njia nyingine ambayo inaweza kutuwezesha kupata maji kipindi hiki ambako tunasubiri Mradi wa kutoka Lake Victoria isipokuwa visima. Kwa hiyo naomba sana Wizara ya Fedha izingatie hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka wa fedha 2018/ 2019 tulitengewa fedha kama shilingi milioni 620 kwa ajili ya kujenga visima 30 katika vijiji, tunaomba Wizara mtuwezeshe hilo kwa sababu naanza kutetemeka kidogo kwa kuwa sasa hivi tayari tuko mwezi Mei na bado fedha hazijatoka. Uzuri wetu sisi watu wa Urambo, tuliipa Wakala wa Serikali (DDCA) kazi hii ya kuchimba visima. Kwa hiyo, tutashukuru tukipata hiyo shilingi milioni 620 ili DCCA iweze kuchimba visima 30 kwenye vijiji wananchi waweze kupata maji wakati tunasubiri mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo mjini Urambo kuna shida ya maji sana na mtandao mzima wa maji una changamoto. Katika mwaka huu wa fedha 2018/2019, tuliomba na tukaahidiwa kupata shilingi milioni 429 ili tuchimbe visima Mjini Urambo lakini pia tuweze kurekebisha miundombinu. Tutashukuru sana Mheshimiwa Waziri na Wizara kwa ujumla mkitupa fedha hizo ili tuweze kupata maji kwa njia ya visima wakati tukisubiri mradi mkubwa kutoka Ziwa Viktoria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mmojawapo kati ya watu waliopata bahati kwenda Bermuda ambacho ni Kisiwa America Kusini. Jambo ambalo nilijifunza, naomba niliseme hapa, wao wamegundua kwamba nchi yao hawawezi kupata maji mazuri, wakajiwekea wenyewe katika sheria yao kwamba yeyote anayeomba kibali cha kujenga, kwanza wanakagua kama ameweka miundombinu wa kuvuna maji. Mimi niliona ni jambo zuri sana lakini kwetu sisi kwa sababu bado halijawekwa katika sheria na utaratibu wa ujenzi kwamba lazima mtu anapojenga nyumba aweke miundombinu ya kuvuna maji, mimi ningeomba ianzie na shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule zetu nyingi sehemu wanazojengwa maji huwa ni haba, kwa hiyo, utakuta watoto barabarani wanatembea na chupa na vidumu vya maji. Niiombe Serikali kwa sababu ni moja wakashirikiana Wizara ya Elimu pamoja na TAMISEMI kuona waweke sharti gani kwa watu wanaojenga shule ili miundombinu ya kukusanya maji iwepo. Mimi nasema inawezekana, kwa sababu bila maji ni changamoto kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Waheshimiwa Wabunge kwa kushirikiana na Mheshimiwa Spika tumeendesha zoezi zuri sana la uchangiaji wa vyoo ili watoto wa kike wapate vyoo vya kuwahifadhi. Pia katika ramani ile ambayo tulipendekeza, inaonesha lazima kuwe na maji na njia pekee ambayo inaweza kutuhakikishia upatikanaji wa maji ni kuweka miundombinu ya ukusanyaji wa maji ya mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naunga mkono Kamati ya Kilimo, Uvuvi na Maji ambayo kwenye kitabu chake ukurasa 20, wamependekeza kwamba Serikali itilie mkazo suala la uvunaji wa maji ya mvua. Kwa hiyo, ni suala tu la kuongea na sekta husika ili tuone kama wanaweza kuweka kiwe ni kipengele kimojawapo kwamba kabla shule haijafunguliwa au haijajengwa lazima kuwe na ramani ya utaratibu wa ukusanyaji wa maji shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo, naomba nichomekee hapo hapo, kama wataweka sharti mojawapo la ujenzi wa shule kwamba kuwe na miundombinu ya kuvuna maji, pia naomba nipendekeze kwamba kuwe na utaratibu kwamba kabla shule haijakaguliwa au inapokaguliwa la kwanza kuangaliwa ni suala la vyoo ambapo Waheshimiwa Wabunge wamependekeza ramani nzuri ambayo inawahifadhi watoto wa kike, watoto wenye ulemavu na watoto wote kwa ujumla. Kwa kweli vyoo na maji iwe kama ni sharti mojawapo la kwanza la kuzingatiwa kabla shule haijajegwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji halina ubishi, sisi wanawake ndiyo tunahitaji sana maji kwa sababu baba anapokuja nyumbani anategemea akute maji. Kwa hiyo, nashukuru sana kwamba Wabunge wote tumeungana kuiomba Serikali ione utaratibu ambao unaweza kuiwezesha kupata fedha kutuwezesha sisi Wabunge na wananchi kwa ujumla kupata maji katika maeneo yetu jambo ambalo litakuwa ni ukombozi. Sisi wote tunasema mtu ni afya lakini huwezi kuwa na afya bila kuwa na maji kwa sababu maji hayana mbadala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishie hapo kwa kuishukuru tena Serikali kwa kutuwezesha sisi watu wa Urambo kuingizwa katika Mradi wa Maji kutoka Lake Victoria kama inavyooneshwa kwenye ukurasa wa 88 wa kitabu hiki halafu pia imerudiwa kwenye ukurasa wa 148 kwamba tutapata maji kutoka Lake Victoria. Tunawashukuru sana kwa niaba ya wananchi wa Urambo na tunaomba tu Mheshimiwa Waziri mtakapokuja kujibu hapa basi mtupe matumaini lini tunapata maji kutoka Lake Victoria kama ukombozi wa kudumu au suluhisho la kudumu la upatikanaji wa maji katika Wilaya yetu ya Urambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi name nichangie hoja iliyoko mezani. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai, lakini bado naendelea kuwashukuru wananchi wa Urambo kwa kunipa ushirikiano. Nami niungane na wenzangu kuipa pole familia iliyoondokewa na Mzee wetu, Marehemu Reginald Mengi, naomba Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema Peponi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawajibika kuishukuru sana Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na kadhalika kwa jinsi ambavyo wanachapa kazi katika Awamu hii ya Tano. Namwomba Mwenyezi Mungu awabariki sana Mheshimiwa Ummy mwenyewe ambaye anathibisha wanawake wanaweza. Pia nampongeza Mheshimiwa Dkt. Ndungulile kwa namna anavyochapa kazi na Mwenzie. Nampongeza pia Katibu Mkuu, Dkt. Chaula, kwa kweli hawa watu wanafanya kazi wakisaidiwa na wafanyakazi. Mwenyezi Mungu awapeni nguvu, endeleeni kuchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni shukrani kwa niaba ya wananchi wa Urambo kwa kumaliziwa Kituo cha Afya cha Usoke. Naishukuru sana Serikali kwa kutupa shilingi milioni 400 kwa kumalizia Kituo cha Afya cha Usoke na sasa hivi wametuongezea kimoja ambacho kinaendelea kujengwa katika Kata ya Uyumbu Usoke Mlimani.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya shukurani hiyo, naomba niielezee Serikali kwamba sisi kama Urambo tuna kata 18. Maana yake ni kwamba kituo hiki cha pili kikimalizika tutakuwa na vituo viwili vya afya. Ni ombi kwa niaba ya wananchi wa Urambo kwamba tuongezewe kituo cha afya angalau katika Kata ya Songambele; na ikiwezekena hata viwili katika kata pia ya Vumilia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni jambo la uwazi kwamba sisi kama Urambo bado tunahudumia Wilaya ya Kaliua ambao bado; ukienda kwenye wodi ukitembelea wagonjwa waliolazwa utashangaa, wengi wanatoka Kaliua, wengine wanatoka kwa jirani zangu Uyui hasa maeneo ya Ndono na mpaka Uvinza sisi tunapata. Kwa hiyo, tunapoomba huduma ya afya kuongezewa ni kwa sababu pia tunahudumia wananchi wanaotoka katika maeneo ya jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe shukrani za pekee kwa Mheshimiwa Waziri Ummy. Alikuja kufanya ziara na ziara yake ilizaa matunda. Tulipoenda Usoke alifurahishwa sana na kazi iliyofanywa pale Usoke ya kumalizia kituo cha afya ambapo ulikuwa ni mradi uliokuwa wa ADB tangu 2010. Mheshimiwa Ummy alifurahi kwa jinsi ambavyo kituo kilimalizwa vizuri na akaahidi kwamba majengo mengine ambayo yapo yanaharibu sura ya kituo kile kwamba atatoa shilingi milioni 50. Mheshimiwa Waziri tunashukuru sana kwa ahadi yako, naamini itatimizwa tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Kituo cha Afya cha Usoke kilikuwa ni mabaki ya mradi wa ADB, ADB iliacha mradi mwingine ambao bado haujakamika. Inasikitisha kwamba tangu mwaka 2010 theater ambayo ipo karibu na wodi ya akina mama ilianza kujengwa pale, sasa hivi iko kwenye ngazi ya lenta, kwa kujua kwamba wakitoka pale theater wanaingizwa kwenye wodi ya akina mama. Mpaka leo haijaisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali imalize ilie theater nasi tunaamini kwamba tukipewa shilingi milioni 200 itamaliza hiyo theater ili akina mama ambao wapo karibu, ambao walikuwa walengwa, wakitoka theater pale wanaingia wodini na vice versa, wakitoka wodini wanapelekwa theater. Tunaomba theater ikamilishwe ambayo iko kwenye ngazi ya lenta. Inasikitisha, jengo zuri lakini tangu 2010 halijaisha ambayo itausaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi theater kwa kuwa tunahudumia na watu kutoka maeneo mengine, wengine inabidi wasubiri lakini theater ikiisha wagonjwa, wakiwepo akina mama na watoto watanufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika tuna mradi mwingine ambao uliachwa, ni mradi wa LGDB ambapo ni ICU. Huwezi kuamini Urambo hatuna ICU na ni Hospitali ya Wilaya. Tunaomba kwa heshima na taadhima kabisa Awamu ya Tano itusaidie tuwe na ICU na sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika na X-Ray, nimeshukuru Wabunge wengine wamesimama hapa wanafurahi kwamba tuna X-Ray ya kisasa ya kidijitali, sisi bado tupo kwenye analogy.

Mheshimiwa Naibu Spika, nisaidie nawe kuiomba Serikali itusaidie X-Ray ya kisasa. Kwa sababu hata haya majibu tunayopata sasa hivi tuna wasiwasi nayo, kwa sababu bado tupo kwenye enzi ya Ujima, tunatumia X-Ray ya analogy. Tunaomba tusaidiwe hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika, suala la wafanyakazi ni la muhimu sana. Bado tuna uhaba wa wafanyakazi kwa asilimia 48. Tunaomba nasi mtakapokuwa mkipanga wafanyakazi mtukumbuke nasi Urambo tuongezewe wafanyakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilifurahi sana ziara ya Mheshimiwa Waziri Ummy. Namwomba Mwenyenzi Mungu ampe afya ili arudi tena aone mabadiliko gani tumeyafanya tangu alipotoka. Kuna maneno mazuri uliyaacha Urambo bado watu wanakukumbuka nayo na hasa pale ulipokumbuka kile Kituo cha Afya cha Uyogo kinachojengwa kwa kushirikiana na Waingereza. Nawe ulitaka kuonyesha kuunga mkono nguvu ya wananchi na marafiki zao kutoka Uingireza ukaahidi shilingi milioni 20. Tushukuru sana kama utawapa shilingi milioni 20 Uyogo ili wamalizie kituo chao.

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya yote, bado wanamkumbuka Mheshimiwa Waziri alipotamka neno la maana sana kwamba atawapa ambulance. Kwa sababu wao wapo mbali na Hospitali ya Wilaya, akiwapa ambulance itawasaidia sana kuwawahisha akina mama hasa wanaokwenda kujifungua usiku, maana yake saa za kujifungua huwa hazijulikani; usiku na kadhalika, ambulance itasaidia sana. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika Mheshimiwa Waziri alipokwenda zahanati ya Itebulanda, aliahidi nako shillingi milioni 20. Mheshimiwa Waziri tuna imani kabisa utatimiza kwa sababu uliipenda sana ile zahanati, inafanya kazi vizuri na imeanzisha wodi ya akina mama na kwamba utawaunga mkono kwa shilingi milioni 20.

NAIBU SPIKA: Muda wako umeisha Mheshimiwa. Ahsante sana.

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri, nashukuru Wizara nzima na ninaunga mkono hoja. Endeleeni kuchapa kazi. Ahsanteni sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili nichangie hoja iliyopo mezani. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na wakati huo nawashukuru sana wananchi wa Urambo kwa kunipa ushirikiano wa hali ya juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Kigangwalla, Naibu Waziri Mheshimiwa Kanyasu, Wakuu wa Idara wote wa Misitu, Wanyamapori na kadhalika. Watendaji wote kwa kweli Wizara hii wanastahili sifa hongereni sana. Wameanza vizuri, tunawatakia kila la heri, waendelee na kazi kubwa wanayoifanya hadi wakati huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukue nafasi hii kushukuru ushirikiano ambao nimeshakuwa naupata na Wizara hiyo. Kwa mfano, alipokuwepo Naibu Waziri wakati huu Mheshimiwa Hasunga nilimwelezea kuhusu mgogoro wa mpaka nilionayo na tukaenda naye mpaka Urambo namshukuru sana. Aliiona, akajaribu kusuluhisha lakini baadaye akaondolewa kwenye Wizara hiyo. Kwa hiyo naamini waliopo watafuatilia huo mgogoro ambao nazungumzia kati ya wananchi na mipaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, sijui kama wenzangu Waheshimiwa Wabunge kama wanajua Urambo nasi tuna game reserve, wanaongelea Ngorongoro lakini wasisahu na sisi Urambo tuna game reserve, kuna wanyamapori hawa wanaowaona huko nasi tunao, lakini pia tuna Hifadhi ya Msitu wa Ugalla.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kumekuwa na mgogoro wa mipaka kwa muda mrefu hasa katika Kata za Nsenda, Ukondamoyo, Ugalla na Uyumbu na hasa katika maeneo ya Lunyeta ambapo tulikwenda na Mheshimiwa Hasunga, Holongo, Utenge, Mwagimagi, Izengabatogwile, Magangi, Tebela na sehemu nyingi tu, chanzo chake ni nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaambie Wizara kwamba katika miaka 2007 Serikali ilirasimisha mipaka ya vijiji na wakaweka mawe ambayo yapo mpaka sasa. Baada ya kurasimisha mipaka Wizara ya Maliasili na Utalii nao wakaja na mipaka yao ambayo ikawarudisha nyuma kama kilometa 54 hivi na bahati mbaya wakachomewa nyumba na mali zao. Tukalileta hapa hapa wakati huo akiwa Mheshimiwa Pinda, Waziri Mkuu kwa sababu tume iliundwa na matokeo yake yakaonekana kweli wale wale wananchi walionewa. Wamechomewa mali zao, lakini walikuwa katika mipaka ambayo ni halali ambayo ipo mpaka sasa kwa kurudishwa nyuma. Tukawabembeleza wananchi wale tukasema suala hili litaendelea kushughulikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mipaka ile sasa ipo miwili, mpaka wa Serikali wa kwanza ambao ni wa halali kabisa na Mheshimiwa Hasunga aliiona. Wananchi wa kule wameendelea wanakuonesha mipaka kwa kufukua kwa mikono tu. Kwa hiyo kuna mipaka kwa kufufua kwa mikono tu kwa hiyo kuna mipaka ile ya zamani ipo na ni mipaka ya sasa hivi ambayo imewarudisha nyuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni nini? Ni kwamba, sasa Serikali iende ikakae na wananchi ione, nami ningetoa wito kwa Serikali yenyewe kuwa ni Maliasili lakini waende na Ardhi kwa sababu wao ndio waliweka ile mipaka ya kwanza kabla Maliasili haijaja na mipaka ya pili. Kwa hiyo wananchi wanaomba waende wakaone na nitafurahi sana kama watafuatana na uongozi wa Wizara ya Ardhi ili wakaone kosa la wananchi nini, walikaa pale kihalali lakini wakawachomea mali zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Maliasili ilipokuja na mipaka ya pili ndio ikasababisha wale wananchi hawapo pale kihalali. Sasa wananchi wanauliza, je, mpo tayari kuwarudisha pale walipokuwa? Kwa sababu kwa kuwapunguzia kilomita nne sasa hivi hawana mahali pa kutosha pa kulima na walizoea mashamba yao na wafugaji pia hawana mahali pa kufugia. Kwa hiyo tunaomba sana Serikali iende kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kuna tatizo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na wafanyakazi wote kwa kazi wanazozifanya, hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Urambo ina Mto Ugalla. Mto huu ni muhimu sana kwa uhai wa wananchi lakini pia uhai wa Mto Malagalasi ambao unapata maji kutoka Mto Ugalla. Serikali ina mpango gani wa kuondoa magugu yaliyovamia Mto Ugalla?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Urambo, naomba Serikali yetu isome tena barua rasmi iliyotumwa Wizarani kuhusu magugu yaliyovamia Mto Ugalla na kuchukua hatua za kuokoa mto huo haraka iwezekanavyo. Aidha, tunaomba semina za kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira na kuacha kukata miti hovyo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Kamishna wakuu wa Idara na wafanyakazi wote kwa kazi nzuri na ngumu mnayofanya. Kwa niaba ya wananchi wa Urambo pokeeni shukrani za dhati kwa kukubali kuanzisha Chuo cha VETA Urambo asante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ombi tunaomba sana Chuo hicho kiwe na miundombinu hususan Karakana ili wapate ufundi wa aina mbalimbali pamoja na mafunzo yote mafunzo ya udereva (Driving) isikosekane kwa kuwa hakuna Urambo inabidi waende Tabora. Hakika ndoto yetu ya kuwa na VETA imetimia. Watoto wa kike watapata mahali pa kukua baada ya kumaliza masomo wakiwa na umri mdogo, Mwenyezi Mungu awabariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba pia mabweni hasa kwa high schools za Vyumbu na Urambo. Tutashukuru sana mkituruhusu tuongeze shule mbili za high school za Ukondamoyo na Usoji. Tutaleta maombi karibuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali, je, Serikali haioni umuhimu wa kuagiza kwamba shule mpya inapojengwa ianze na vyoo kwa kuwa madarasa yanapojengwa wa fedha huisha na kushindwa kujenga vyoo bora na vya kutosha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri. Pamoja na kwamba mabweni si utatuzi pekee wa suala la mimba shuleni lakini linachangia kwa kiasi kikubwa. Ni vyema kukawa na mkakati wa kujenga mabweni kama ilivyo kuwa maabara na madawati. Nawatakia kila la heri kazini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami nichangie katika hoja hii iliyopo mezani. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai, lakini pia nawashukuru sana wapiga kura wa Urambo ambao wananipa ushirikiano wa hali ya juu. Nawashukuru, nawaomba waendelee kuniunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii pia kumshukuru sana Rais na Jemedari wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya. Hii siyo mara ya kwanza, nimeshasema mara nyingi na ninaomba nirudie hapa, katika mambo ambayo nimejifunza kwa Rais huyu, kwanza nikuthubutu. Anathubutu; pili, anaamua, anafanya maamuzi na tatu, anatekeleza. Nampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza pia na Mheshimiwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu ambao wote kwa pamoja kwa kweli wametusaidia katika awamu hii kuleta maendeleo makubwa sana wakisaidiana na Waheshimiwa Mawaziri na wananchi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nitumie nafasi hii pia kuwashukuru sana viongozi wote waliopo TAMISEMI. TAMISEMI kazi mnaifanya, hongereni sana. Mheshimiwa Jafo unafanya kazi kubwa sana ukisaidiwa na Mheshimiwa Kandege, Mheshimiwa Waitara, Mtendaji Mkuu, Nyamhanga; wote akina Dkt. Gwajima; Dkt. Bakari na Engineer Seif, wote tunawajua wanafanya kazi, hongereni sana. Mheshimiwa Jafo endelea kuchapa kazi na kundi lako lote unalofanya nalo kazi. Kazi wanaiweza; ukiiangalia TARURA, Afya, wote wanafanya kazi kubwa sana upande wa Afya na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasi Urambo tumenufaika, tunashukuru. Tumepata Vituo vya Afya viwili, lakini naomba na hapo hapo mtuongezee tupate na cha tatu tupate kwa sababu tuna Kata 18. Kwa kweli mmefanya kazi kubwa sana. Barabara tumeziona, maji tunategemea kutoka Lake Victoria; mambo mengi tumeyaona lakini tunategemea kutakuwa na mengi yanayokuja. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nilete maombi yafuatayo: la kwanza kabisa naomba mwaangalie wafanyakazi. Ndugu zangu wafanyakazi wana tatizo moja kubwa ambalo naiomba Serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi, wafanyakazi kupanda madaraja sasa hivi ni kazi. Wakipanda madaraja, kuwarekebishia mishahara ni tatizo kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba waangaliwe sana wafanyakazi ambao wako karibu na kustaafu. Hakuna ambacho Serikali yetu haiwezi kukifanya. Naomba Utumishi na waajiri ambao ni Wakurugenzi na mfuko ule unaohudumia walimu pamoja na wafanyakazi wa afya, ule unaoitwa PSSSF wakae pamoja waone jinsi gani ya ku-coordinate ili wafanyakazi wanapopandishwa mishahara, basi na mishahara yao irekebishwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, mimi nina walimu 30 ambao wamestaafu, lakini mishahara yao haikurekebishwa baada ya kupanda madaraja, wamepata matatizo. Jambo hili linaweza kufanyiwa kazi kwa kuhusisha hayo maeneo matatu kama nilivyosema; Waajiri, Mfuko na Utumishi mkaweka utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika kama walivyoongea wenzangu, kuna uhamisho mwingine kwa kweli ni wa lazima. Naomba suala la uhamisho kwa wafanyakazi liangaliwe. Kwa mfano, mtu mume wake amestaafu, amekwenda Tanga. Unamwambia wewe mwalimu tafuta mtu wa Tanga anayekuja Urambo, ambayo ni kazi kubwa sana. Kwa hiyo, kuna uhamisho mwingine kwa kweli kuna haja ya Serikali kuangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali iangalie; Utumishi na Wakurugenzi jambo gani ambalo mnaweza kufanya likawasaidia walimu wanaotaka kuhama kwa genuine issues? Kuna wengine ambao kwa kweli ni genuine, kwa mfano, anafuata familia yake na mambo ya namna hiyo au maradhi. Naomba masuala haya mawili yaangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, naomba tuangalie suala la upungufu wa wafanyakazi. Sisi kwa mfano Urambo tuna upungufu wa Walimu wa Sayansi 230, walimu wa Msingi 458 na wafanyakazi katika sekta ya afya 124. Naomba masuala haya pia yaangaliwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia itakumbukwa kwamba Serikali yetu ilikuwa na nia nzuri, ilipeleka fedha za maboma katika Halmashauri zote. Kwa bahati mbaya sana, sijui computer ili-skip Urambo! Tunaomba Mheshimiwa Waziri ukaangalie Urambo peke yake sijui ilifanyaje yenyewe ikarukwa hatukupata fedha za maboma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huo huo, tuna shule nzuri na kubwa sana inaitwa Uyumbu High School, ni ya sayansi, inachukua wanafunzi kutoka nchi nzima, lakini kwa bahati mbaya sana hali yake siyo nzuri, ina upungufu wa mabweni na madarasa. Naomba Uyumbu iangaliwe kwa jicho la huruma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huo huo nirudi kwa Waheshimiwa Wabunge. Waheshimiwa Wabunge tulicheza ngoma kwa ajili ya vyoo. Vyoo ambavyo ni vya mfano wa chumba kuwahifadhi watoto wa kike, lakini pia chumba cha kuhifadhi watoto wenye ulemavu. Kazi tuliifanya, lakini kwa ubunifu uliotokea baadaye tukaamua kwamba basi tuje na Shule ya Sekondari. Mmeona kwenye magazeti. Karibuni mkaone shule ambayo tunategemea itaitwa Bunge Girls High School, mkipata nafasi mkaione. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wanawake tupige makofi kazi tulifanya kubwa tukaungwa mkono na wanaume. Naomba sana siku tukipanga mkaangalie Bunge High School ambayo natumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Spika na ofisi yake na Mheshimiwa Naibu Spika, ambao wanaisimamia ile shule. Sasa hivi imefikia hatua ya kuwekwa mabati. Basi tumuunge mkono Mheshimiwa Spika, tukipata nafasi tukaone kule kazi kubwa inayofanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, msifikiri tulipoteza muda, hatukupoteza muda. Kwa taarifa iliyoletwa na Mheshimiwa Jafo kwenye Kamati yetu imesema kwamba sasa hivi TAMISEMI wamechukua zile ramani na tayari wameshajenga majengo 1,233 kwa kufuata yale maelekezo ambayo tuliwaomba wayafuate. Kwa hiyo, tunamwomba Mheshimiwa Jafo na uongozi mzima wa TAMISEMI, mmefikia 1,233; tunajua mnaweza kufanya zaidi ili watoto wetu wa kike na wenye ulemavu wapate hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kama mnakumbuka TWPG, yaani Wabunge Wanawake kwa kusaidiana na ofcourse Wabunge wanaume wakiwemo akina Mheshimiwa Mwalongo na wengine, tulizungumzia sana umuhimu wa taulo za kike. Kama alivyoongea Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Rweikiza kwenye taarifa yake, amepongeza Mkoa wa Mara.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu wa fedha unaoisha 2019/2020 tayari wameshatoa taulo za kike 33,000 na mwaka huu 2020/2021 wameweka lengo la kutoa taulo za kike 43,000 kwa kutumia fedha zao za ndani. Ni jambo la kupongeza sana TAMISEMI. Mheshimiwa Jafo umehimiza Wakuu wa Mikoa wamelihimiza hili, naomba tu uendelee kwa kweli kwa sababu watoto wa kike kwa taarifa ya UNICEF ya mwaka 2008 ni kwamba tunapoteza watoto wa kike asilimia 10 kwa kutokwenda shule kwa kuogopa kutokupata hifadhi wanapokuwa shuleni. (Makofi)

Kwa hiyo, mimi nakupongeza Mheshimiwa Jafo, mnachapa kazi, endeleeni kuchapa kazi na niseme tu, kwa kweli lipo hili jambo ambalo wenzangu wameongea sana, TARURA inafanya kazi kubwa. Mwaka huu ndiyo mvua imetuadhiri, nakwambia barabara huko kwetu zinahitaja makalavati. Wananchi wanaweza kujitolea kwa kusaidiana na TARURA, lakini wanahitaji makalavati. Kwa hiyo, tunaomba kwa kweli TARURA iangaliwe kwa jicho la huruma, iongezewe fedha. Tunajua TANROAD wanafanya kazi nzuri sana lakini pia na TARURA waongezewe fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, narudia tena kuwapongeza sana TAMISEMI kwa kazi kubwa wanayoifanya na tunaomba mwendelee kufanya kazi kubwa sana chini ya Jemedari wetu Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli ambaye kama nilivyosema ni mtu anayetufundisha sisi tuige viongozi kuthubutu, ubunifu na kutekeleza. Naogopa kuishia kusema CCM oyee! (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

La kwanza kabisa ni shukrani kwa Mungu ambaye amenipa uhai, lakini la pili shukrani ziende kwa Chama changu cha Mapinduzi ambacho kimenipa nafasi ya kuchaguliwa kuwa Mbunge. Wakati huo huo nawashukuru sana wananchi wa Urambo wamenipa kura nyingi sana najivunia kura zao nawaahidi nitajitahidi kadri ya uwezo wangu nisiwaangushe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia naikumbuka familia yangu imenisaidia sana, nawaombea kwa Mungu nao waendelee vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, umenipa nafasi hii wakati muafaka, nashukuru sana kwa sababu leo umetangaza kwamba kutakuwa na uchaguzi wa TWPG na nimeona ni vizuri nichukue nafasi hii kwa niaba ya wenzangu wote tuliofanya kazi ndani ya TWPG kumshukuru sana Mungu alitupa nafasi tukafanya kazi nyingi sana, ahsanteni sana Wabunge Wanawake mliokuwepo, ahsante sana Wabunge wanaume mliokuwepo wote tulifanya kazi kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee tukushukuru wewe, akinamama wenzangu Wabunge naomba na kinababa wote waliotuunga mkono tumpigie sana makofi mengi sana Mheshimiwa Spika kwa jinsi alivyotusaidia. Ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema mbele ya Mwenyezi Mungu ametusaidia sana ndugu zangu tulikuwa na shughuli kubwa wa mradi ule unaoendelea wa Bunge Girls High School, bila wewe tusingefanikiwa jamani, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii pia kwa niaba ya wenzangu kushukuru ofisi yako bila kumsahau Naibu Spika, Katibu wa Bunge, ofisi yake yote wafanyakazi wa Bunge walisimama mstari wa mbele chini ya uongozi wako tukafanikiwa sasa Waheshimiwa Wabunge tuna Bunge Girls High School, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilifika ofisi kwako kukushukuru na pia nakuaga kwamba tumefanya kazi kwa karibu sana na wewe na ofisi yako na wote nakushukuru sana. Tuwatakie wenzetu mema ambao watakuwa kwenye uongozi unaokuja, lakini muwe na uhakika Spika tunaye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kushukuru kwa upande wa TWPG, nirudi sasa kwa hotuba ya Mheshimiwa Rais. Hotuba ya Mheshimiwa Rais inahitaji sana kupongezwa kwa hali ya juu, mambo mengi yamefanywa, wenzangu Wabunge mliotangulia mmeongelea mambo ya afya ambayo pia imetugusa Urambo, mambo ya maji, umeme, mengi kwa kweli yaliyofanyika pia na sisi yametugusa Wilaya ya Urambo, cha maana tumuombee Rais wetu maisha mema na kuitakia la heri Serikali kwa kuwa kweli Mawaziri, Naibu Waziri na Makatibu Wakuu wanafanya kazi kubwa tuwaombee na kuwatakia kila la heri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ningeomba kama ifuatavyo, kwa kweli kwa sasa hivi wenzangu wameshaongea sehemu za vijijini barabara ni mbaya, tuombe Serikali yetu iongezee fedha TARURA kwa sababu barabara zetu zinahitaji kutengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kwa upande wa kilimo, nafahamu kabisa Mawaziri walioko na Serikali kwa ujumla wanajitahidi, lakini bado tuwaombe pembejeo zifike kwa wakati lakini pia mazao yetu yapate bei ya kutosha kwa kupata wanunuzi wengi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nishukuru Serikali yetu, tuna VETA zipo na Urambo ninayo lakini kama walivyotangulia kuongea wenzetu ziongezewe aina mbalimbali za ufundi. Nishukuru sana kuona kwenye kipindi kimoja VETA moja tayari inatengeneza simu hayo ndiyo mambo tunayotaka. Kwa hiyo, tunaomba kwamba VETA iongezewe aina mbalimbali za ujuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa upande wa wafanyakazi nitakuwa sikutenda haki bila kutajia suala la wafanyakazi, kuna ukurasa hapa ambao unasema Serikali itaendelea kuwajali wafanyakazi. Naomba kwa siku ya leo wafanyakazi kwa kweli wanapopandishwa madaraja warekebishiwe mishahara kwa haraka ili isilete matatizo wanapostaafu. Nina orodha ya walimu wengi ambao wanaendelea kuomba wamestaafu, lakini mishahara yao haikurekebishiwa kwa hiyo, kutengenezewa mafao yao inakuwa shida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo limejitokeza nashukuru kwamba Serikali yetu imeanzisha mtindo wa e-Government yaani mambo ya kutumia mtandao, wasaidiwe kwa upande wa uhamisho, inawapa tabu sana wafanyakazi.
Baada ya kusema hayo nampongeza Mheshimiwa Rais…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. MARGARET S. SITTA: Lakini bado nakupongeza Mheshimiwa Spika kwa kutusaidia TWPG, Mwenyezi Mungu isaidie TWPG. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Wakurugenzi na wafanyakazi wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya. Hakika mnaitendea haki Wizara hii, nawatakia kila la kheri.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru sana kutembelewa na Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu kwa nyakati tofauti. Ziara zote zimezaa matunda ya msaada wa kifedha na vifaa, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Wilaya ya Urambo ina vijiji 59, zahanati 22, tunaomba tusaidiwe kumalizia maboma 8 ambayo yamejengwa ili tuongeze huduma kwa wananchi. Tuna kata 18, vituo vya afya vipo viwili, kimoja kimekamilika tunashukuru na kimoja kinaendelea kujengwa. Tunaomba tuongezewe vituo viwili katika Kata za Songambele na Vumilia ambapo wananchi wameanza msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Kituo cha Afya Uyogo ambacho wananchi wanajenga kwa kushirikiana na marafiki kutoka Uingereza. Tunaomba ahadi za Waziri zitimizwe za ambulance kwa kuwa ni mbali na Hospitali ya Wilaya na tupewe shilingi milioni 20 alizoahidi ili kukamilisha kituo kinachojengwa. Vilevile, tunaomba tupewe shilingi milioni 50 alizoahidi Waziri alipotembelea Kituo cha Afya cha Usoke kwa lengo la kukamilisha miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kupitia mradi wa ADB ulianza kujenga jengo la theater ambalo liko tangu mwaka 2010. Tunaomba Serikali itusaidie kumalizia jengo hilo ambalo linahitaji fedha zipatazo shilingi milioni 200.

Mheshimiwa Naibu Spika, Urambo haina chumba cha wagonjwa mahututi (ICU). Kuna jengo lililoanza kujengwa kwa mpango wa LGDG linaloweza kukamilika kwa gharama ya shilingi milioni 20. Tunaomba Waziri akumbuke ahadi hii na aitekeleze.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Waziri aliahidi kutoa shilingi milioni 20 kwa ajili ya kukamilisha wodi ya akina mama. Tunaomba tusaidiwe fedha hizo kwa ajili ya Zahanati ya Itebulanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Urambo ina X- ray ya kizamani ya analogue. Tunaomba X-ray ya kisasa ya digital.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tunaomba tuongezewe wafanyakazi kwa kuwa tuna upungufu wa asilimia 48.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nichangie hoja iliyopo mezani. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai, lakini pia nawashukuru sana wananchi wa Urambo na familia yangu kwa jinsi ambavyo tunashirikiana nao. Nawaomba tuendelee kushirikiana kwa lengo la kuendeleza Wilaya yetu.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuipongeza Serikali inayoongozwa na Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo wanachapa kazi kwa kuzingatia yaliyopo ndani ya Ilani ya Uchaguzi. Hongera sana kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii pikumpongeza Mheshimiwa Waziri, Profesa Mkenda pamoja na Naibu Waziri, Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Wizara hii na naamini wanasikiliza yote ambayo Waheshimiwa Wabunge wameongea ili kesho tupate mrejesho mzuri. Ninapoongea kwa niaba ya wananchi wa Urambo siwezi kuacha kutaja tumbaku, tumbaku hoyee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumbaku ndio uhai wetu sisi kwa sababu ndio zao ambalo linatuingizia fedha na miaka ya nyuma wakati wa mauzo kama huu uliopo sasa hivi, mitaani kote watu wangekuwa wanafurahia kwa sababu tumbaku ilikuwa inauzwa tani kwa tani kadri ambavyo mkulima alivyokuwa akilima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuwapongeza wenzangu wote waliotangulia kwa kusema kwamba changamoto kubwa ya Wizara ya Kilimo ni masoko, masoko ndio ambayo yanaamua mkulima alime kiasi gani na kumpa ari pia. Tumbaku bado ina changamoto kubwa sana. Kwa sasa hivi bei ambayo ingeweza kutolewa kama tungekuwa na wanunuzi wengi ingekuwa dola 1.63 lakini mpaka sasa hivi ni JTI tu ambao wamefikisha angalau dola moja 1.54, wakifuatiwa na wenzao ambao ni akina Alliance na wengineo ambao wananunua kwa dola 1.45.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo suala la soko ni la muhimu sana, tunaomba wanunuzi zaidi, tunaomba soko liwe la uhakika Zaidi. Sasa hivi tumbaku inauzwa lakini bado haijafikia peak ambayo tutasema kweli mkulima anapata haki yake na jasho lake alilotoa. Namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja mezani kuja ku-wind up yaani anapokuwa anahitimisha atuambie kama changamoto kubwa ni soko iweje TLTC waondoke ambao ndio walikuwa wananunua tumbaku nyingi Mkoa wa Tabora. Kwa hiyo tunaomba atakapokuja kueleza hapa atuambie TLTC wapo, wameondoka na kama wameondoka kweli imeshindikana kukubaliana nao ili waendelee kununua ili tupate wanunuzi wengi zaidi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia itakuwa ni vizuri kama Waziri atatuambia kwamba TLTC ndio waliokuwa wamenunua Kiwanda cha Tumbaku, TLTC ndio walikuwa wamechukua ma-godown yote, kama wanaondoka nini hatma ya ma- godown na kiwanda walichokuwa wanamiliki? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, ni suala la makisio, kutokana na kutokuwa na wanunuzi wengi, sasa hivi pamoja na kwamba mnasema Maafisa Ugani watembee, inasaidia nini Maafisa Ugani wakitembea, halafu baadaye unaambiwa wanunuzi wote wanataka kilo labda1,000,000 tu, lakini tungekuwa na wanunuzi wengi wangenunua nyingi.

Mheshimiwa Spika, fikiria, sasa hivi mkulima anaambiwa wewe lima mwisho labda kilogram 100 au 200 tu, why? Sasa kuna haja gani ya kuhimiza watu walime, halafu baada ya pale wanakosa soko au wanapewa makisio madogo. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri atusaidie tunafanyaje ili wakulima walime tani yao kadri wanavyopenda kutokana na jinsi wanafundishwa kilimo cha kisasa.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo ni la muhimu sana ni suala la mbolea. Wenzangu waliotangulia wameongea kwamba ni vizuri mbolea ikafika kwa wakati, Wizara wanajitahidi lakini bado wajitahidi zaidi ili mkulima anapoanza kuandaa shamba, sio anaanza kuuliza kwanza mbolea inakuja lini? Inabidi mbolea iwe tayari ipo nchini. Wizara imekuwa na utaratibu mzuri wanaleta katika bulky yaani nyingui, sawa, lakini kufika kwa wakati ili mkulima anapoandaa shamba lake mbolea iwe tayari imeshafika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo naona ni matatizo makubwa, Bodi ya Tumbaku inatusaidia kuwasiliana kuhusu bei, lakini haina vitendea kazi. Kwa hiyo tunaomba Bodi ya Tumbaku wawe na vitendea kazi. Kwa mfano, kama kwangu hata gari hawana, wakitaka kuzunguka mpaka waombe gari ya Mkurugenzi ni aibu. Kwa hiyo nadhani Bodi ya Tumbaku ipewe vitendea kazi na vingine vyote ambavyo wanajua wao hawana ili waendelee kutekeleza majukumu yao.

Mheshimiwa Spika, lingine, wametaja mikoa mitatu ambayo itafanyiwa utafiti wa mazao ya alizeti na kadhalika, wametaja Dodoma, Singida na Simiyu lakini wamesahau Mkoa wa Tabora, Mkoa wa Tabora ni jirani ya Singida, tupo sawasawa na wao na cha ajabu kuhusu pamba, Igunga ndio ina shamba la mbegu. Sasa mkoa ambao una shamba la mbegu wameuacha katika haya majaribio ya mikoa mitatu! Kwa hiyo naiomba sana Serikali itusaidie kuirudisha au kuiingiza Tabora katika mikoa ile mitatu ili iwe mikoa minne; kwanza kwa sababu ardhi ni sawasawa, na sisi alizeti inakubali na kama nilivyosema shamba la mbegu yaani utafiti kuhusu mbegu upo Igunga ambao ni Mkoa wa Tabora. Kwa hiyo tunaomba kwa heshima na taadhima Mkoa wa Tabora uwekwe katika mikoa ile ya majaribio.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hivyo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Margaret Sitta.

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nami nakupongeza kwa kupewa nafasi kubwa kama hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai siku ya leo. Pia nawashukuru wananchi wa Urambo wakiwemo ndugu zangu kwa ushirikiano wanaonipa. Nachukua nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Urambo kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na viongozi wote ndani ya Wizara yao. Hongereni kwa kazi kubwa mnayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii pia kwa niaba ya wananchi wa Urambo kuishukuru sana Serikali kwa kutupa Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugala. Mwaka 2019 lilipitishwa azimio, kwa hiyo, sasa tuna Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugala. Hata hivyo, Serikali inapokuja na mambo mazuri kama haya ya Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugala, kuna umuhimu wa kuwapa elimu wananchi wanaohusika. Sasa tunajua wananchi wangapi wanajua faida ya kuwa na Hifadhi ya Msitu? Watanufaika vipi? Wataishije? Kwa hiyo, kuna umuhimu wa Serikali inapochukua hatua kubwa kama hizi, kuwaelimisha wananchi wajue wataishije? Watanufaika nini? Kwa sababu, lengo kubwa ni kujenga mahusiano kati ya Serikali na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka pia niwaambie kwamba Kata nne za Nsenda, Ukondamoyo, Ugala na Kasisi, maeneo yao yalipunguzwa na mwaka 2014 kulitokea mgogoro. Wao wanaamini kwamba jiwe lao halali ni Namba 23 ambalo lilikuwepo kabla maliasili na utalii haijaweka mipaka yake. Kwa hiyo, wakawa wamerudishwa nyuma kilomita zipatazo 10. Kwa hiyo, likawapunguzia nafasi ya kulima, kufuga mifugo yao yaani ng’ombe na kadhalika na pia kuweka mizinga yao ya asali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa eneo kama hili ambalo lilisababisha askari kuchoma nyumba zao na lililetwa mpaka humu Bungeni, kwa kupitia Mheshimiwa Waziri Mkuu, wakati huo alikuwa Mheshimiwa Pinda na wakatoa pole kwa wananchi. Kwa hiyo, tayari kulikuwa na msuguano ambapo Serikali ingetafuta nafasi ya kuweka mahusiano mapya ili kuwe na ujirani mwema. Badala yake sasa hivi imekuja na hifadhi kabla haijaweka mahusiano mazuri na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pamoja na shukurani kwa Serikali kutupa hifadhi, bado kuna haja ya kwenda kuwapa wananchi elimu, wataishije baada ya kuwa na Hifadhi ya Taifa? Maeneo yao yaliyopungua sasa, kwa sababu wamerudishwa nyuma kilomita 10, watapata wapi eneo lingine? Kwa hiyo, naomba niwasilishe maombi yao wananchi wa Urambo hasa katika Kata hizo nne ambazo zimeathirika kwa njia mojawapo ingawa wamepata faida ya kupata hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, tulikuwa tunaomba wapewe elimu ya faida ya TANAPA na kadhalika na wataishije? La pili, naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge waliomo humu, walioiomba Serikali kufikiria upya kwa kuwaongezea maeneo ya kulima, kufuga na kuweka mizinga yao ya nyuki. Kwa hiyo, tunaomba kwa heshima na taadhima tupatiwe angalau kilomita tano kwa sababu, walirudishwa nyuma kilomita 10. Angalau tupate kilomita tano wananchi waweze kulima, kufuga na kuweka mizinga yao ya asali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, tunaomba baada ya kuongezewa eneo, tupate mashine za kuchuja asali, nasi tupeleke Urambo asali, kwa sababu ndiyo maendeleo yenyewe hayo. Watu walikuja pale wanaita Follow The Honey kutoka America, lakini sasa tena ndio mmetufukuza, haturuhusiwi kuweka mizinga ndani ya eneo. Kwa hiyo, tunaomba kabisa kwamba tupewe mashine za kuchuja asali lakini wakati huo huo tuweze kuruhusiwa kuweka mizinga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali imetupa ruhusa tarehe 6 mwezi huu wa Juni mpaka tarehe 6 mwezi wa Julai kuvuna asali, lakini baada ya hapo mizinga tunaweka wapi? Kwa hiyo, tunaomba tuongezewe eneo kama nilivyosema tulime, tufuge na tuweke mizinga yetu ya asali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala siyo la leo. Mheshimiwa Naibu Waziri na aliyekuwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Hasunga namwona pale. Alikuja, wazee wakamwonyesha mawe yao ya asili, alikuja Mheshimiwa Ramo akiwa Naibu Waziri, alikuja Mheshimiwa Naibu Waziri Angelina Mabula na yeye akawaweka wataalam, anajua. Kwa hiyo, suala hili siyo jipya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia alikuja Mheshimiwa Kigwangala lakini bahati mbaya siku alikuja, mvua ikanyesha akashindwa kuingia. Maana yake nini? Nataka kusema hili tatizo au mgogoro huu wa mipaka siyo wa leo, ni wa siku nyingi na tulileta hapa Bungeni kwa barua hii hapa, kwamba Serikali katika ile Tume iliyokuwa inapitia migogoro, nasi tulileta. Kwa hiyo, nashukuru Mheshimiwa Waziri wa Ardhi naye anasikiliza, naamini kabisa katika hili atatusaidia kwa kushirikiana na Waziri mhusika wa sasa ili tupate maeneo yale kama yalivyokuwa yamekusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa heshima na taadhima kabisa, pamoja na kuipongeza Serikali kutupa hifadhi, bado tunahitaji waje wajenge mahusiano, watuongezee maeneo kama tulivyoomba, Serikali yetu ni Sikivu, inawapenda wananchi wake, tuongezewe eneo la kulima na kufuga na kuweka mizinga yetu. Tuna asali nyingi sana, karibuni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtajie Mheshimiwa Waziri maeneo ambayo atayakuta kule ambayo kweli yana changamoto katika hizo Kata nne. Atakuta Izengabatogilwe, Lunyeta, Mwagimagi, Msumbiji, Utewe, Mkola, Utenge, Mwengemoto na Holongo; katika hizo Kata nne ambazo nimezitaja hapo awali. Kwa hiyo, kwa heshima na taadhima, pamoja na kuunga mkono, nawapenda hawa Mawaziri kwa sababu ni wasikivu. Mheshimiwa Waziri mhusika, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, wote ni wahusika. Hayo matatu naomba nirudie kwa mara ya mwisho kabla kengele haijalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kujenga mahusiano kwa kutupa elimu; pili, kuomba eneo, tuongezewe angalau kilomita tano, Serikali yetu ni nzuri; na tatu, tunaomba mashine ili mizinga tutakayoweka, tuweze kuchuja asali yetu, Urambo tupeleke asali duniani. Waamerika wanasema nzuri sana kwa ajili ya chocolate, kwa sababu ya kwetu ni nyeusi safii. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na wafanyakazi wote wa Wizara kwa kazi kubwa na ngumu wanayoifanya. Hongereni sana.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya wananchi wa Urambo, tunashukuru sana barabara iliyokamilika katikati ya Mji wa Urambo. Ahsanteni sana kwa kuongeza uzuri wa mji. Barabara hii nzuri ni muhimu sana ikaunganishwa vizuri pale inapoungana/kuchepuka kutoka barabara inayoendelea Kigoma.

Mheshimiwa Spika, tunaomba round about kwanza kwa usalama wa magari na waenda kwa miguu na pili kwa mwonekano mzuri wa barabara inayoingia mjini.

Mheshimiwa Spika, tunaomba minara ya simu katika maeneo ambayo hayana mtandao wa simu; na orodha ya kata na vijiji imeletwa Wizarani.

Mheshimiwa Spika, tunaomba maombi mawili ya round about na minara yafikiriwe kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. MARGRET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, nawapongeza sana kwa kazi kubwa Mheshimiwa Waziri, Waheshimiwa Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu na wafanyakazi wote wa Wizara na Taasisi zake, hongera kwa kazi nzito wanazofanya.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu, kwa niaba ya wananchi wa Urambo, naomba wafanyie kazi kwanza upatikanaji wa pembejeo kwa wakati, hususan mbolea. Kwa mfano, sisi tunaolima tumbaku inabidi tupate mbolea kabla ya mwezi Agosti na kwanza, bei ipunguzwe. Pili, ili wakulima walime zaidi masoko ya mazao yawe ya uhakika na tatu, wanunuzi wawe wengi ili ushindani wa bei uwepo kwa manufaa ya wakulima wetu na wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, nina maswali yafuatayo:-

Kwanza, kwa kuwa kampuni ya TLTC ilikuwa mnunuzi mkubwa wa tumbaku kwa tani zipatazo milioni 14 kwa msimu; je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kuwa iwapo kampuni hii itajitoa wakulima wasikose makisio msimu ujao na wakiondoka pengo lao litazibwa na nani?

Pili, je, kuna makubaliano yoyote kati ya BAT (British American Tobacco) katika kuwa wanunuzi wa tumbaku?

Tatu, je, Serikali ina mpango gani kuhusu bima kwa wakulima na mazao yao?

Mheshimiwa Spika, mwisho, kwa niaba ya wananchi wa Urambo tunaomba mtaalam wa zao la alizeti aje atuambie mbegu ipi ni nzuri kwa ardhi yetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, hongera sana kwa kazi kubwa mnayofanya, tunaona mabadiliko makubwa katika kusimamia maliasili za nchi yetu, kazi mnaifanya, hongereni.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi, wananchi wa Kata za Nsenda, Uyumbu, Ugaila na Ukondamoyo zilizo Urambo zina malalamiko mengi kuhusu kupunguzwa kwa maeneo yao ambayo kabla ya mpaka mpya maeneo yalikuwa yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, tafadhari sana Serikali itatue migogoro ya mipaka na ikiwezekana warudi kwenye uhalali wa kuishi kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri, matangazo vivutio vyetu yaongezwe hasa nje ya nchi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Spika, pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri wa Nishati, Katibu Mkuu na Wakuu wa Idara zote kwa kazi kubwa wanazofanya za kusambaza umeme nchini, Urambo ikiwemo, tunashukuru sana. Naomba jitihada za kujenga kituo cha kupoza umeme Urambo ziendelee, nawatakia kila la heri.

Mheshimiwa Spika, naomba maeneo yafuatayo yapate umeme. Orodha ya awali imeletwa Wizarani. Kata Kapilula eneo la Ulasa B, Kata ya Urambo, eneo la Ubalani, Mabatini, Boma Village, Kata ya Kiyungi eneo la Tulieni na Kata ya Imalamakoye eneo la Imalamakoye D. Taasisi- Magereza Urambo - pump ya maji, Shule ya St. Lucia - Kata ya Ukondamoyo na Shule ya Magole - Kata ya Vumilia. Tunaomba umeme wa REA ufike vijiji vyote vilivyobaki.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Serikali kwa jitihada kubwa ya kuendeleza nchi yetu. Hongereni Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kuwa wanunuzi wa tumbaku wanaendelea kununua kwa kujadiliana jinsi ya kutatua suala la VAT? Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kuwa mbolea inafika nchini kabla ya mwezi Agosti?
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hoja iliyopo mezani. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na wakati huo huo nawashukuru sana wananchi wa Urambo wakiwamo Ndugu zangu kwa ushirikiano wanaonipa mimi katika kutafuta maendeleo ya eneo letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali yetu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, akiwemo Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Mawaziri wote kwa jitihada zao kubwa ambazo zimetuletea hii bajeti ambayo tunaijadili siku ya leo. Hongera sana Serikali kwa bajeti nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Urambo tumenufaika pia na bajeti hii tumehakikishiwa maji yatakuja, barabara zitatengenezwa, umeme utafika kwenye vijiji vyote. Ombi letu kwa siku ya leo ni kwamba lini mafundi watafika Urambo kuhakikisha kwamba ule mradi wa maji unaotoka Lake Victoria unaanza kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kilimo ni muhimu sana katika Wilaya yetu kwa sababu tunategemea sana zao la tumbaku ili lituwezeshe kumudu maisha kwa upande wa biashara. Nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa sababu imetambua kwamba kuna umuhimu wa kufanya vikao na wanunuzi wa tumbaku. Kwa sababu kilio chetu kikubwa ni kuongeza makisio, wakulima wanapenda walime kadri wanavyoweza kwa hiyo tunapopata makisio makubwa yanatupa nguvu na sisi ya kulima zaidi. Kwa hiyo naipongeza Serikali kwa kitendo chake cha kukutana na wanunuzi mwaka jana mwezi Februari, 2020. Serikali kwa kupitia wizara ya fedha na wakati huo alikuwa Mheshimiwa Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ambaye alikutana na wanunuzi wa tumbaku.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba utaratibu wa kukutana na wanunuzi uendelee kwa sababu kikao cha mwaka jana mwezi Februari, 2020 kilizaa matunda tukaongezewa makisio kutoka tani elfu 36 hadi kufikia tani 67 elfu. Kwa hiyo vikao tunaomba viendelee vya kukutana na wanunuzi, kwanza vinawapa nguvu wale wanunuzi waliopo lakini pia kinatoa fursa ya kujadili tozo mbalimbali, changamoto wanazokutana nazo ili weendelee kununua tumbaku. Kwa hiyo, tunaomba Serikali iendelee na utaratibu wa kukutana na wanunuzi, tunategemea kwamba wanunuzi watakapokuwa wengi kwanza watatoa makisio zaidi lakini pia kutakuwa na changamoto ya kuongeza bei, kutakuwa ushindani wa bei, kwa hiyo tutanufanika zaidi. Hivyo, utatatibu wa Serikali kukutana na wanunuzi tunaomba uendelee.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii tumeiona ina bilioni 294 zikiwepo bilioni 30 za umwagiliaji. Lakini Serikali inajua, kwamba kuna Azimio la Maputo ambalo walikuwa wamekubaliana kwamba kutenga asilimia 10 ya bajeti nzima iende kwenye kilimo. Tunajua kwa mwaka huu haiwezekani kwa sababu tayari wameshatenga bilioni 294. Ombi sasa kwa Serikali kweli kwamba zile bilioni 294 basi zipatikane ziende kwa kilimo, fedha zote zilizotengwa ziende kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kuipongeza Serikali kwa kuondoa VAT kwa upande wa cold rooms vyumba vya kuhifadhi baridi ili watu wanaosafirisha mazao nje, maua na mazao mengine yanayotokana na horticulture wapeleke. Tunaipongeza Serikali kwa suala hilo lakini tunaomba basi Serikali ituambie kwamba ina vituo vingapi vya kuhifadhi baridi yaani cold rooms. Na je, ina mpango wa kuongeza, kama ina mpango wa kuongeza inaongeza vyumba vingapi ili wenzetu wanaosafirisha bidhaa nje kwa kutegemea hivyo vyumba basi na wenyewe wanufaike.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niiombe Serikali imeweka asilimia mbili ya Kodi ya Zuio. Tunaomba hii kodi asilimia mbili iondolewe kwa upande wa mazao ya wakulima ili waweze kupelekea mazao yao vizuri zaidi. Naiomba Serikali kwa kuwa ina mpango wa kuongeza zao la alizeti, sisi kama Mkoa wa Tabora nasi pia tunalima alizeti, tunaomba tuongezwe kwenye mpango wa kuongeza zao la alizeti ili na sisi tuliwe kwa sababu tunajua kwa sasa hivi zao la alizeti ni muhimu katika upande wa kuongeza mafuta kama tunavyoona sasa hivi mafuta yamepanda bei sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Serikali kwa ujumla mimi mwalimu, ningependa sana nizungumzie suala la elimu naona sintatenda haki bila kuzungumza suala la elimu. Nampongeza Mheshimiwa Prof. Ndalichako nimemuona kwenye vikao vingi sasa hivi anatafuta maoni na jinsi gani ya kuboresha elimu nchini. Ni jambo zuri sana, nakupongeza kwa sababu sisi wote tumeomba Serikali ifanyie kazi suala la elimu ili liende na wakati lijibu hoja na mahitaji ya kipindi hiki. Lakini mimi nilikuwa namuomba Mheshimiwa Prof. Ndalichako na Wizara ya Elimu kwa ujumla iangalie uboreshaji wa elimu lakini iwaanglie na Walimu. Kwa sababu huwezi kuboresha suala la elimu bila ya kuangalia Watendaji, sasa hivi tumeona walimu wana changamoto nyingi sana, wengi hawapandi madaraja kwa wakati na wengine wanapanda madaraja lakini mishahara yao hairekebishwi kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi ningeomba Serikali iwachukue wale wote ambao wana mhudumia Mwalimu kwa sababu Mwalimu hahudumiwi na mtu mmoja anahudumiwa na vyombo vingi sana. Kwa hiyo mimi ningeomba kuwe na kikao cha kuangalia wote wanaomuhudmia mwalimu wanafanyaje yaani kuwe na co-ordination ili walimu waweze kupata haki zao kwa wakati na waweze kufanya kazi kwa bidi zaidi hata baada ya kuletewa maboresho hayo. Kwa mfano nilikuwa naangalia suala la TSC ilipoundwa ilikuwa na malengo gani? Mimi nilikuwa nategemea kwamba TSC itasaidia kuleta co-ordination yaani itaunganisha vyombo kwa pamoja ili mambo ya upandaji wa madaraja, kama ni kuchukuliwa hatua za nidhamu na vitu vya namna hiyo, lakini je, najiuliza TSC ilipoundwa na ikapewa majukumu yale kweli ndiyo tunachotegemeWa. Matokeo ya utendaji kazi wa TSC ndiyo yale tuliyoyategemea baada ya kuomba iundwe? Kwa hiyo naomba TSC ifanyiwe tathmini kama kweli inafanya kazi iliyokusudiwa ya kurahisisha huduma kwa Walimu ambao ni walengwa. Wakati huo huo, pamoja tukija na maboresho ya elimu lakini pia tuangalie suala la ukaguzi. Je, ukaguzi inafanya kazi inavyopaswa kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naomba nimalizie kwa kuzungumzia suala la posho kwa Watendaji wa Kata. Naipongeza Serikali kwa kwa Watendaji wa Kata wamefanya vizuri sana lakini niiombe pia na Watendaji wa Vijiji na Mitaa waangaliwe. Kwa sababu wao nao pia wanasaidia kuhamasisha suala la uchaguzi, sensa inakuja watatumika, masuala ya usalama, kwa hiyo naomba pia Watendaji wa VIjiji nao waangaliwe wapate posho kama walivyopata wenzao wa upande wa Kata. Itasaidia kuwapa motisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia data, nikaangalia kuna vijiji 12,319, mitaa 4,263 wakichanga na wale Watendaji wa Kata 3,956 naamini Serikali inaweza, penye nia pana njia. Naipongeza sana kwa bajeti hii lakini naomba narudia tena kuomba watusaidie sana suala la kilimo kwa sababu kilimo ndiYo Uti wa Mgongo. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Reli wa Mwaka 2017
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hoja iliyoko mezani inayohusu uanzishaji wa shirika jipya la reli.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naipongeza sana Serikali, mimi natoka Mkoa wa Tabora Wilaya ya Urambo, kwa miaka yote tumetegemea usafiri wa reli, kwa hiyo, katika mambo ambayo naipongeza Serikali ya awamu hii hasa ni uamuzi wa kujenga reli hii kwa standard gauge.

Hongera sana Serikali, endeleeni kuimarisha reli inayotarajiwa kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yafuatayo ni maombi na ushauri wakati huo huo; sisi kama wananchi wa Urambo tunategemea sana station ya Urambo, natoa ombi maalum kwa Serikali kwamba station ya Urambo iimarishwe kwa sababu huwa inakuwa na wasafiri wengi sana wanaoshuka pale. Lakini wakati huohuo sio kuimarishwa station tu lakini pia iwekewe ulinzi kwa sababu mara nyingi kama ratiba itabadilika, ikiwa treni inapita usiku ni jambo la hatari sana. Kwa hiyo, naomba ulinzi uimarishwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili katika Wilaya ya Urambo tuna check line mahali ambao wananchi wanavuka reli. Tunaomba zile check line ziendelee kuwepo na ziimarishwe, zikiwemo za Usoke, Sipungu, Ulasa, Urambo nakuomba pia Kata ya Vumilia haina check line, tunaomba iwekewe pale kwa sababu kuna kijiji watu wanaishi upande wa kaskazini ambayo inawapa shida sana kuvuka reli. Tunaomba check line iwepo katika Kata ya Vumilia.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naishauri Serikali, magenge yaliyokuwepo yarudishwe, yaimarishwe, yalikuwa yanasaidia kuimarisha ulinzi wa reli. Wakati huo huo, zamani kulikuwa na wakaguzi wa reli, tunaomba wakaguzi wa reli waendelee kuwepo kwa sababu walikuwa wanasaidia kukagua reli kila siku badala ya kusubiri ajali itokee. Walikuwa wanatambua sehemu zenye matatizo kabla reli haijafika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kumekuwa na matukio mabaya sana ya uhalifu ndani ya mabehewa. Naomba pia ndani ya mabehewa kuwe na ulinzi hasa wanaposhuka usiku au wanapopanda usiku tunaomba ulinzi uwepo ndani ya mabehewa wanayosafiria wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunatoa wito kwa Serikali kuwalipa wafanyakazi waliokuwa katika shirika ambalo sasa linaisha muda wake ambalo limeunganisha kwenda kwenye hili shirika jipya la reli TRC. Tunaomba wafanyakzi wote kabla hawajahamia huko wawe wamelipwa fedha zao kuondoa usumbufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuiambia Serikali kwamba suala hili ni la biashara, litatusaidia wananchi kwa usafiri wetu wenyewe na mizigo ikiwemo tumbaku ambayo mizigo hii ilikuwa inaharibu sana barabara zetu ambazo zimejengwa kwa gharama kubwa. Kwa hiyo mizigo hii mikubwa itasaidia kuokoa barabara zetu. Pia tutapata fedha nyingi kutokana na mizigo inayotoka Congo, Uganda, Rwanda na nchi nyingine za jirani, kwa hiyo itasaidia pia kuimarisha uchumi wa nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimaliziae kwa kusema kwamba wananchi wa Urambo na Tabora kwa ujumla tunakaribisha sana Serikali ijenge hii reli haraka iwezekanavyo ili itusaidie, ulikuwa ni utaratibu wetu kutegemea zaidi reli kuliko barabara. Baada ya kusema hayo naendelea kuipongeza Serikali, tunaomba reli ijengwe haraka iwezekanavyo ili tuondokane wa njia zingine za usafiri ambazo pia zimekuwa ghali kwa wananchi wenye uwezo mdogo kifedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Kulitangaza Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi wa Mwaka 2018
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nichangie katika huu Muswada wa Sheria ya Kutangaza Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi yetu ya Tanzania. Awali ya yote naomba nitoe pole kwa wazazi walioondokewa na watoto wao yaani wanafunzi waliopigwa na hata kufariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya TWPG natoa pole nyingi lakini wakati huo huo tunatoa wito kwa Walimu kuwa waangalifu wanapotoa adhabu kwa wanafunzi hawa kwa kuzingatia kwamba wao pia ni wazazi, walezi lakini wakati huo huo kazi ya ualimu ni wito basi watumie taratibu nzuri za kuwaadhibu kutokana na taratibu zilizopo, tunaomba Mwenyezi Mungu aweke roho za Marehemu mahali pema peponi. Amina. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Muswada uliopo mezani la kwanza kabisa naomba niipongeze Serikali kwa uamuzi wake wa kuleta Muswada huu hapa Bungeni.

Kipekee naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake alioufikia hadi kufikia hatua hii ya kutengeneza Muswada ili Dodoma kuwe Makao Makuu ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mfano na nasema kwa dhati mimi mwenyewe, huu ni mfano mzuri wa kiongozi kuwa na maamuzi. Naamini ukienda kwenye ofisi nyingi utakuta mafaili karibu yawafunike na Maafisa wenyewe, sio kwamba wana kazi nyingi, wanashindwa kuamua. Huu uwe ni mfano wa sisi viongozi kufanya maamuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, marehemu Samweli Sitta mume wangu, Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi, yeye pamoja na marehemu Sir George Kahama walikuwa ndio viongozi wa kwanza Watendaji Wakuu wa Mamlaka ya Ushawishaji Makao Makuu mpaka wamefariki bado hakuna kitu chochote kilichotokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukiangalia kwamba kama tangu mwaka 1973, Mheshimiwa Nyerere marehemu Mungu naye ailaze mahali pema peponi roho yake, mwaka 1973 alitamka mpaka leo hii bado tunajadili jambo hili. Hii inanipa fundisho gani? Inanipa fundisho kwamba sisi viongozi ambao tunachukua nafasi ya wale waliotutangulia ni vizuri tukaangalia mambo gani mazuri waliyoyafanya, lakini mambo gani hawakumaliza tuyamalizie sisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Magufuli, Rais wetu kwa kuangalia viongozi waliomtangulia walifanya nini, kitu gani hawakukamilisha yeye anakamilisha, ndio unaona uamuzi wa Makao Makuu ya Dodoma, unaona Stiegler’s Gorge safi kabisa. Nimejifunza kwamba kama viongozi lazima nifanye maamuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejifunza pia mambo mengine, sisi Watanzania sio wote, wako baadhi ya watendaji ambao kiongozi akitoa tamko juu ya uamuzi fulani hawamtengenezei mazingira ili ule uamuzi utekelezeke. Nina mfano hata nikiulizwa naweza kuelezea, iko mifano mingi ya matamko mazuri tu ambayo Marais wetu wametamka lakini watendaji baadhi yao wamehakikisha kwamba ule uamuzi ufanyike hivyo. Labda ni hapa kwetu tu, lakini nadhani kitu kizuri ni pale ambapo baada ya kiongozi kutamka jambo, watendaji wao ni kumtengenezea mazingira ili lile tamko lake liweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiri, kwa hiyo, nachukua nafasi hii kuwashukuru sana wote watendaji Wizara nzima zilizohusika zote mbili TAMISEMI, Katiba na Sheria na wote waliohusika kuhakikisha kwamba wanamsaidia Rais wetu ili tamko lake lianze kufanya kazi, nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe labda kitu kimoja tu, kwa kuwa Dodoma ni katikati na hilo halina ubishi na uamuzi ulishafanyika, niiombe Serikali sasa ihakikishe kwamba njia zote kutoka mikoa yote pamoja na jitihada nzuri iliyofanyika na Serikali yetu kuweka nyingi lakini bado iangalie ni maeneo gani ya mikoa gani ambayo si rahisi wao kufika Dodoma ambapo wataweza kupata huduma wanayoitaka ya ngazi ya kitaifa. Kwa hiyo, ombi langu ni hilo, lakini kwa kifupi tumejifunza na nitaendelea kujifunza kwamba ukiwa kiongozi fanya maamuzi, usiogope kama kuna changamoto utazirekebisha kadri mambo yanavyokwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kwa kusema naunga mkono taarifa yote ya Kamati yangu ya Utawala na TAMISEMI pamoja na Muswada mzima, hoja nzima iliyowekwa mezani naiunga mkono. Ahsante.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira wa Mwaka 2018
MHE. MARGRET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie hoja iliyoko mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nachukua nafasi hii kwa niaba ya wapiga kura na wananchi wote wa Urambo kuishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kukubali Urambo iwe moja ya Miji Midogo itakayopitiwa na mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria, tunaishukuru sana sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nichukue nafasi hii pia kuishukuru Serikali kwa kuja na muswada huu mzuri ambao unalenga hasa kusaidia upatikanaji wa maji hususan katika maeneo ya vijijini, naishukuru sana Serikali jambo zuri imefanyika siku ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama mama najua jinsi wanawake wanavyopata shida. Ni kweli akina baba wanajua, lakini kwa sehemu kubwa ndugu akina mama ndio tunaopata tabu ya maji. Kwa hiyo, kwa niaba ya akina mama waliomo humu Bungeni na walioko nje tunaipongeza Serikali kwa kuja na muswada ambao utasaidia upatikanaji wa maji, jambo ambalo ni muhimu sana hasa kwa sisi wanawake ambao huwa tunaamka alfajiri kwenda kutafuta maji, naishukuru sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo ambalo limenifanya hasa niulize ni uwakilishi wa wanawake katika bodi mbalimbali za RUWA (Mamlaka ya Maji Vijijini). Ukiangalia kwenye ukurasa wa 50, Bodi ya Mkoa, katika jedwali la kwanza kifungu cha 1(f)(v) Waziri ataunda Bodi ya watu kumi watakaoingia katika Bodi ya Mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipengele cha tano kinaonesha ni mwanamke mmoja tu katika watu kumi. Mmoja tu ndiye atakayeingia kwenye Bodi hiyo atakayewawakilisha wenzao. Je, ni kwa nini mmoja na labda inawezekana pia ni bahati mbaya, katika watu kumi mwanamke mmoja ndiye atakayewakilisha wanawake, ambapo wanawake ndio wangesaidia sana kuelezea changamoto wanazozipata kule vijijini, lakini kati ya watu kumi, mmoja ndiye mwanamke. Naomba suala hili liangaliwe ili uwakilishi katika ngazi ya mkoa uwe mkubwa zaidi kuliko ilivyo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika ukiangalia kwenye Bodi ya Wilaya kwenye ukurasa wa 51, kati ya wajumbe saba wanaoteuliwa na Waziri hakuna mwanamke hata mmoja katika ngazi ya Wilaya. Je, imesahaulika kwa bahati mbaya? Naomba suala hili liangaliwe; katika Bodi za Wilaya hali ni mbaya uwakilishi wa wanawake. Hali kadhalika mahali ambapo mamlaka itahudumia zaidi ya Wilaya moja, kati ya wajumbe wanane watakaoteuliwa ni mwanamke mmoja tu, ukurasa ule wa 51.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba suala la uwakilishi wa wanawake katika bodi uangaliwe vizuri zaidi ili haki itendeke, kwa sababu wao ndio wanajua na watawapa taarifa nzuri zaidi. Kwa hiyo naomba uwakilishi uzingatiwe katika ngazi zote ambazo nimezizungumzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la muhimu ambalo nimetaka kuzungumzia ni suala la upatikanaji wa fedha za kuendeshea huo mfuko wa RUWA utakaoanzishwa, chanzo chake ni nini? Tunaomba kiwe wazi kwa sababu kwa muda mrefu Waheshimiwa Wabunge walikuwa wakizungumza labda asilimia 50 au senti 50 zichangie katika mfuko utakaoanzishwa vijijini, lakini sasa hivi hatujapata uhakika juu fedha zitakazoendeshea huu mfuko wa vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hata kama vile Urambo tutapata maji kutoka Lake Victoria haisaidii vijijini sana kwa sababu labda itakuja kilometa 12 kutoka kwenye bomba kubwa milimita 12 pande zote mbili. Kwa hiyo bado kuna haja ya kuwa na mfuko imara utakaohudumia vijijini. Kwa hiyo suala langu mimi ni kwamba tuwe na uhakika wa chanzo cha fedha cha kuendeshea RUWA utakaowezesha RUWA kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, hoja yangu kubwa ilikuwa ni uwakilishi wa wanawake, kushukuru Serikali kwa kuanzisha RUWA na kushukuru pia Urambo kuingizwa katika kupata maji kutoka Lake Victoria. Hata hivyo jambo la leo Waheshimiwa Wabunge wote upatikanaji wa maji vijijini ni muhimu, kwa hiyo RUWA iangaliwe kwa makini fedha ziwe za kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, na ninaunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)