Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Masoud Abdalla Salim (64 total)

MHE. MASOUD ABDALLA SALIM: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Spika, la kwanza, ni aibu na fedheha kwa Serikali kwa jinsi ilivyowatelekeza wastaafu wake. Ukiangalia nchi ya Kenya na Rwanda, wastaafu wana hali nzuri. Serikali mmepandisha pensheni kutoka shilingi 50,000/= mpaka shilingi 100,000/=, wastani wa shilingi 3,300/= kwa siku, fedha ambayo hata chai haitoshi! Serikali inasemaje sasa? Kuna mkakati wa ziada angalau kuwaongezea pensheni wastaafu kwa shilingi 250,000/= kwa mwezi? Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, la pili, kwa mujibu wa Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, miaka kadhaa, miaka mbalimbali, imekuwa ikiripoti kupunjwa, kudhulumiwa kwa mafao ya wastaafu na Serikali imekuwa ikisema kwamba wataalamu wake ndio wanaokosea. Tunataka tuelewe, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuweza kutoa mafao stahiki kwa wastaafu wetu?
Pale ambapo wastaafu wanafariki, Serikali imekuwa ikitoa risala za kutoa machozi na kulia, uwongo mtupu! Tabia hii mbaya lini mtaacha? (Kicheko/Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba niseme, siyo sahihi kwamba imekuwa ni fedheha kwa Serikali. Kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya swali la msingi ni kwamba tumekuwa tukiongeza kiwango hiki cha pensheni kwa wastaafu kulingana na uchumi unavyoimarika na tumekuwa tukiliangalia kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mkakati wa wazi wa kuongeza shilingi 250,000/= kwa mwezi kama pensheni; kama nilivyosema mwanzo, tunaangalia kiwango cha uchumi wetu, uchumi utakakaa vizuri kuturuhusu kulipa shilingi 250,000/= tutalipa hiyo shilingi 250,000/=.
Mheshimiwa Spika, kuhusu mkakati wa kutoa mafao sahihi kwa wastaafu kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge katika swali lake la pili; naendelea kusisitiza kwamba uchumi utakapokuwa umeimarika vizuri; na kama mlivyoona kwa speed ya Serikali ya Awamu ya Tano, tunakusanya mapato kwa kiasi kikubwa na tunatarajia kuongeza tax base ya kukusanya kodi ambayo tunazingatia. Moja ya watu wa kuwaangalia ni Wastaafu wetu, wamelitumikia Taifa na tuna uhakika tutaweza kuwahudumia. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLA SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Katika azma ya kuboresha maslahi ya walimu, katika sherehe ya siku za walimu duniani katika awamu iliyopita, Rais mstaafu aliwaahidi walimu kuwapatia posho ya kufundishia yaani teaching allowance, lakini hadi leo posho ya kufundishia (teaching allowance) hawajapatiwa. Je, Serikali ina mkakati gani wa ziada kuhakikisha kwamba ahadi ambayo aliitoa Rais inatekelezwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kumekuwa na tabia ya kutolipa madeni ya walimu kwa wakati unaostahili na mara nyingi madeni ya walimu hulipwa hasa wakati wa kukaribia uchaguzi, hii ni tabia mbaya. Ni lini na Serikali ina mkakati gani wa ziada kuhakikisha kwamba walimu wanalipwa madeni yao kwa wakati unaostahili? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na posho ya kufundishia niseme tu kwamba ni kweli kwamba Rais mstaafu Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, wakati huo alipokwenda katika sherehe za walimu alielezea kwamba suala hili litafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme tu kwamba sisi kupitia Baraza Kuu la majadiliano katika utumishi wa umma tutaliangalia na kila mwaka tunakaa mara moja. Kwa hiyo, tusubiri tutakapokaa na vyama hivyo vya wafanyakazi katika Baraza hili Kuu la Majadiliano tuone tutasemaje. Tunaweza tukapanga viwango lakini tukajikuta vinakuwa ni viwango ambavyo Baraza Kuu kupitia Vyama vya Wafanyakazi wakawa hawajaviridhia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa madeni ya walimu, kwa upande wa Serikali inaweka mkazo mkubwa sana kuhakikisha kwamba walimu wanapata stahiki zao, lakini si kwa walimu tu na kwa watumishi wote mbalimbali wa umma. Ukiangalia katika mwaka huu peke yake, tumeshalipa takribani bilioni 3.7, lakini vilevile kwa mwaka jana tu peke yake tulilipa takribani shilingi bilioni 27.9.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokifanya hivi sasa tunahakikisha tunakamilisha kulipa na kuhakiki, maana huwezi ukalipa tu. Wapo wengine vilevile wanafanya madai ambayo si ya kweli. Kwa hiyo, niseme tu kwamba sisi kama Serikali tupate nafasi tuendelee na uhakiki lakini wakati huo huo tukiendelea kulipa kwa kadri inavyowezekana. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLA SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru nina maswali mawili ya nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na malalamiko mengi ya muda mrefu kwa wafanyakazi viwandani kupewa mishahara midogo lakini zaidi maneno ya kuudhi kwa wamiliki wa viwanda jambo ambalo halikubaliki.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuulize Mheshimiwa Waziri, je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuunda Tume Teule ya kufuatilia malalamiko ya wafanyakazi hawa?
Swali la pili, katika jibu la Mheshimiwa Waziri amesema kwamba wale wote watakaobainika kukiuka makubaliano yaliyomo katika mikataba ya awali hatua stahiki zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuvitwaa na kutafuta wawekezaji mahiri wa kuviendeleza hivyo viwanda.
Kwa kuwa viwanda vya korosho vilivyobinafsishwa miaka 1970 na 1980 ambapo Serikali ilikopa kutoka Italia na Japan dola milioni 20 na viwanda hivyo hadi leo haviendelezwi wamiliki wake wanajulikana. Sasa tatizo nini kwa Serikali mnaelewa kila kitu tumekuwa tukisema muda mrefu.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Je, nini mkakati wa ziada wa kuhakikisha kwamba viwanda vya korosho vimebinafsishwa kule Mtwara na Serikali mkatoa kwa vigogo wengine mnaowajua kwa bei chee! Je, viwanda hivyo ni lini vitarudi kwa wananchi?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika viwanda kuna malalamiko na kama mnavyojua tunao ndugu zetu wanafanya kazi viwandani, sioni haja ya kuunda Tume, Wizara yetu ikishirikiana na Wizara ya Ajira tumeanza kazi ya kufuatilia masuala haya na Kamishna wa Kazi yuko ana kazi maalum ambapo tutahakikisha kwamba wafanyakazi wetu wanatendewa haki.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaeleze wawekezaji, sisi tunatengeneza viwanda kutengeneza ajira, kuzalisha bidhaa na kuwafanya mlipe kodi hatutengenezi viwanda kusudi waje kuteseka watu katika nchi yao, huo ndiyo msimamo wa Serikali na tunawahakikishia tushirikiane Waheshimiwa Wabunge, ninyi ndiyo macho yetu mtushauri na mtuelekeze. Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kutoa viwanda, viwanda vile viliuzwa kisheria, nimeshasema mara tatu bei waliyolipa ni pamoja na masharti ya kuzalisha bidhaa kwa tija, kutoa ajira na kulipa kodi.
Kwa hiyo, kama ulimuuzia kisheria utamnyang’anya kisheria na niwahakikishie watu wanaotoka kwenye ukanda wa kulima korosho hakuna tatizo viwanda vitafanya kazi. Pamoja na hivyo wako wawekezaji wako tayari kuwekeza kwenye kutengeneza korosho, yaani korosho inatoka pale kiwandani inaingia mikononi mwa mteja tuna-add value, na tutatoka hapa tunakwenda kuuza Ulaya siyo tunatoka hapa tunauza India, India ipeleke Ulaya. Tunakwenda moja kwa moja sokoni na kazi hiyo naiweza tushirikiane. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLA SALIM: Mheshimiwa Spika, na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri katika jibu la muuliza swali la msingi (b) alieleza kwamba yuko tayari kukarabati kituo cha polisi husika ambacho kimetajwa, lakini kituo cha polisi cha Kengeja ni kibovu, chakavu, kinavuja na kuta zake zimeanza kudondoka na ni athari sana kwa polisi na kituo hicho mmerithi kutoka kwa wakoloni.
Je, hamuoni kwamba ni aibu na fedheha kwamba hamuwezi kukikarabati na inawezekana kikapelekea askari hawa kupoteza maisha? Hamuwezi kukarabati hata lile ambalo mmerithi kwa wakoloni!?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nakiri kabisa kwamba kituo cha Kengeja hali yake siyo nzuri, hata mimi niliwahi kufanya ziara pale, lakini siyo Kengeja tu, ni maeneo mengi ndani ya nchi yetu vituo vya polisi haviko vizuri sana. Kwa mfano, Mkoani ni zaidi! Nadhani Kituo cha Mkoani kina hali mbaya zaidi kuliko Kengeja.
Mheshimiwa Spika, kama alivyozungumza mwanzo Mheshimiwa Mbunge, ni kwamba tuna mkakati wa kuvifanyia ukarabati vituo hivi na utaratibu huo utakuwa unaenda hatua kwa hatua kulingana na hali ya fedha itakavyoruhusu. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Masoud uvute subira.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, nina maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, uvunjwaji huu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora inaathiri sana usalama wa raia na mali zao. Katika majibu ya Mheshimiwa Waziri amekiri na amesema kwamba mambo yaliyochunguzwa ni matumizi mabaya ya madaraka ya watendaji na matumizi ya nguvu ya vyombo vya dola.
Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri kile kinachoitwa Uchaguzi wa Marejeo kule Zanzibar na kubadilika kuwa Uchafuzi wa Makusudio, ni kwa kiasi gani Serikali ilifanya uchunguzi ikagundua udhalilishaji huu wa watu kupigwa bila hatia na kule Tumbatu nyumba zao kuchomwa moto? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika majibu ya Mheshimiwa Waziri amesema kwamba wametembelea magereza na kufanya uchunguzi wa kina. Naomba Mheshimiwa Waziri aniambie katika kutembelea magereza, wamefanya uchunguzi kiasi gani, wakafuatilia kiasi gani na wakagundua jambo gani pale ambapo Mashehe waliotoka Zanzibar waliopelekwa Tanzania Bara, waliofanyiwa vitendo vibaya, viovu, vichafu, vya kikatili na vya kishenzi walipolawitiwa. Tarehe 28 mimi nilikwenda kwenye Gereza la Segerea na wakasema kwamba hali yao ni mbaya na kinyesi chao hakizuiwi wanavuja mavi. (Makofi)
Je, tuambie Serikali hii, katika misingi ya uvunjaji wa haki za binadamu…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Masoud hilo ni swali la tatu sasa.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Hilo ni la pili.
NAIBU SPIKA: La pili umeshauliza…
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Sijauliza swali la pili.
NAIBU SPIKA: Kwa namna gani, kwa namna gani mara tatu, sasa hayo ni maswali mengi already. Kama unafuta hilo la pili basi uliza sasa hili lile la katikati ulifute. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Waziri wakati unajibu umesema kwamba mlikwenda kwenye magereza na kufanya uchunguzi, ni kiasi gani mmegundua malalamiko yaliyoko kwenye magereza na hasa pale ambapo kuna malalamiko ya muda mrefu ya Mashehe waliotoka Zanzibar ambapo walilawitiwa, vitendo vichafu, viovu…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Masoud, tafadhali uliza swali, umeanza na je, malizia. Uliza swali tafadhali, hayo maelezo tumeshayasikia.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Waziri, ni kwa kiasi gani malalamiko haya ya vitendo hivi viovu, vichafu, vibaya, vya kishenzi na vya kinyama walivyofanyiwa Mashehe wetu mtavifuatilia kwa kina?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kazi yake kubwa ni kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi. Mheshimiwa Mbunge anaposema kumetokea udhalilishaji wa haki za binadamu za kupindukia, napenda kujua kama hayo masuala malalamiko yalipelekwa kwenye Tume kwa sababu nachozungumzia hapa ni Tume ya Haki za Binadamu na jinsi ninavyojibu ni malalamiko ambayo yametolewa na wananchi. Kama nilivyosema kati ya mwaka 2010 mpaka mwezi huu ninapoongea Tume imepokea na kushughulikia zaidi ya 13,709. Sasa kama hiyo ni mojawapo taarifa ya Tume nitaletewa na nitakuja kuiweka hapa Mezani kama Katiba inavyonitaka chini ya Ibara ya 131(3).
MHE. MASOUD ABDALLA SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Pamoja na maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, kuna mkakati wa kupeleka Polisi
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
18
kwenye Kisiwa cha Tumbatu siku hadi siku kukabiliana na matatizo ya usalama, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri bado hujatueleza ni mkakati gani wa ziada wa kuweza kuwabaini na kuwakamata wale ambao walifanya uhalifu wa kuchoma moto nyumba za watu kule Tumbatu, ambapo hadi sasa watu wengine wamekosa makazi. Je, kuna mkakati gani wa Waziri na Serikali kuhakikisha kwamba, matatizo yale hasa yanaepukwa na hayatokei tena na yanakoma na wahusika wanakamatwa? Naomba maelezo!
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, siku zote Jeshi la Polisi limekuwa likichukua hatua kadri ya matukio ya uhalifu yanapotokea ikiwemo tukio la uhalifu ambalo limetokea Tumbatu. Kuna mambo mawili makubwa ambayo tumefanya tayari, la kwanza, ni kuhakikisha kwamba, tunachukua hatua kwa wale ambao tumewakamata, watuhumiwa kwa ufupi kwa kuwapeleka katika vyombo vya sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya pili, ni kudhibiti hali ile isijitokeze tena, ndiyo maana katika jibu langu la msingi nilizungumza kwamba kumeongezeka doria na sasa hivi nadhani kwa kipindi kirefu kidogo, matukio yale ya uhalifu ya kuchomeana moto nyumba yamepungua ama yamesita Tumbatu.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nina swali moja dogo tu la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vilivyobinafsishwa ni kikwazo cha maenedeleo katika maeneo mengi. Katika hotuba ya Mheshimiwa alisema kuna viwanda 34 ambavyo vilibinafsishwa na Serikali ina mkakati wa kuweza kuvifufua. Pia kwenye majibu yako Mheshimiwa Naibu Waziri umesema kwamba mnapitia upya mikataba. Je, katika mikataba hiyo, mna mkakati gani wa ziada kuhakikisha kwamba mikataba ya Viwanda vya Korosho vya Lindi na Mtwara ambavyo vilibinafsishwa na hadi leo kuna tatizo kubwa la kupatikana kwa maendeleo katika mikoa hiyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati ya ziada ambayo Serikali inaifanya, cha kwanza kabisa, viwanda vingi vilikufa kwenye miaka ya 1990 na 1998. Jambo la pili, viwanda vingi vilikufa kwa sababu ya kukosekana kwa malighafi au kuwepo kwa malighafi lakini kupungua kwa soko.
Mheshimiwa Naibu Spika, cha tatu ni Sera ya Ubinafsishaji. Sasa mikakati ya kikatiba, kisheria na kimkataba, kwanza ni kutazama sasa hali halisi ya soko la dunia lakini hali halisi ya viwanda vingine na ku-review mikataba hiyo ya kiuwekezaji. Hatua ya pili, ni kutazama sera yetu sasa ya uchumi ambapo tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda na kutazama sasa mikataba yetu iwe namna gani ili kuvifufua viwanda hivyo.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza mimi nasikitika kwa sababu Serikali inaonekana haina nia njema juu ya jambo hili. Mimi nikiwa Mbunge mwaka 2004 Serikali ilitoa majibu haya haya, mwaka 2008 Serikali ikatoa majibu haya haya, mwaka 2012 Serikali ikatoa majibu haya haya. Mimi ni Mbunge kwa kipindi cha nne sasa, nasikitika sana juu ya majibu yenu ambayo … (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa swali kwa ufupi naomba tafadhali.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni moja tu, uzee na kuzeeka nani ataukwepa, hakuna na kila mmoja ni mzee mtarajiwa. Serikali ituambie sasa ina mkakati gani wa ziada na kama mlivyosema kuwa hatua chache zimebakia, hizo hatua chache ni zipi? Je, ndani ya miezi mitatu mnaweza kumaliza suala hili ili wazee wapate pensheni zao hasa ukizingatia na wale baadhi waliopigana Vita vya Kagera?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE WALEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masoud, lakini nikiendelea kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina nia ya dhati ya jambo hili na ndiyo maana katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 jambo hili limewekwa na kutafsiriwa vizuri sana. Kipindi cha nyuma jambo hili halikuwa limechukua picha ya kutosha kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Hiyo tu kwanza ni nia ya dhati ya Serikali kuhakikisha jambo hili linatekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri hapa ameeleza vizuri sana na naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba suala hili sio la kulala na kuamka ndani ya miezi mitatu halafu ukasema unaanza tu kulipa pensheni, hapana.
Narudia kusema Serikali imeshaanza kutengeneza miundombinu ya kulifanya jambo hili liweze kutekelezeka.
Sheria inayompa mamlaka Mdhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, kifungu cha 5(1)(e), kimemuagiza na kumwelekeza Mdhibiti kuhakikisha anasimamia suala zima la kuona namna gani Watanzania wengi wanafikiwa na sekta ya hifadhi ya jamii ikiwemo wazee.
Kwa hiyo, naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu Serikali inalifanyia kazi suala hili na mara litakapokamilika litaanza kuchukua nafasi yake na wazee watapata pensheni.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, taarifa ya utekelezaji wa ahadi za Serikali mwaka 2006 (miaka kumi iliyopita), Serikali iliahidi kuyapima, kutathmini na kutoa fidia maeneo kadhaa na ndani ya maelezo hayo maeneo yote mliyaeleza mkaainisha katika kitabu ambacho mlitupatia.
Swali linakuja, inakuwaje leo ndani ya muda wa miaka kumi Serikali haijaona umuhimu, ahadi zenu ambazo mlituambia maeneo hayo mtayapima, kutathmini na kutoa fidia na baadhi ya wameshakufa katika maeneo hayo; je, Serikali ina nia njema kulipa fidia wananchi hao? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali na kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, ni kweli kwamba tumeorodhesha maeneo yote yenye migogoro na tumeyaorodhesha maelezo ya nini kinachohitaji kufanyika. Yapo maeneo ambayo yanahitaji kwanza kufanyiwa tathmini ya fidia, yapo yanayohitaji kupimwa, yapo yanayohitaji kutolewa fidia lakini yako vilevile kama nilivyosema awali yale ambayo wananchi walivamia na hawastahili kuwa hapo. Na ukweli wa mambo ni kwamba fedha zinazohitajika ni nyingi, kila mwaka tumekuwa tukitenga katika bajeti yetu, fedha kiasi fulani ili kupunguza awamu kwa awamu mpaka tumalize. Kwa bahati mbaya sana kama mnavyofahamu Waheshimiwa Wabunge ni kwamba fidia ni gharama kubwa. Mheshimiwa Spika, maeneo mengi wananchi wamejenga na kila nyumba ina thamani yake, kwa hiyo kuweza kulimaliza hili tatizo haraka ni vigumu kwasababu ya uwezo wenyewe wa kifedha. Tunachoweza kuendelea kusema ni kwamba kila mwaka, mwaka huu wa fedha tumetenga shilingi bilioni 12, zikipatikana tutaanza sehemu moja baada ya nyingine ili kuweza kuondoa hili tatizo la muda mrefu. Mara nyingi nimekuwa nikisimama hapa nikijibu suala la migogoro ya ardhi kati ya Jeshi na Wananchi lakini ningependa kutoa wito vilevile kwa Waheshimiwa Wabunge kwamba tusaidiane.
Mheshimiwa Spika, zamani Jeshi lilikuwa lina maeneo makubwa sana. Kwa sababu ya uhaba wa ardhi, wananchi sasa hivi wamekuwa wakivamia maeneo hayo. Kwa hiyo, yale maeneo yote ya Jeshi yaliyovamiwa ambayo wananchi hawastahili kuwa hapo ni vema wakatoka katika maeneo hayo na sisi kama Serikali, wale ambao wanastahili ya kulipwa fidia tutaendelea kuwalipa kadri uwezo utakavyokuwa unaruhusu.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwanza nina masikitiko kwamba majibu ambayo ametoa Mheshimiwa Waziri, ama wataalam wake hawaijui sekta ya uvuvi na wanaelekea zaidi kwenye shughuli za mifugo au itakuwa kuna danadana za hapa na pale. Nina maswali mawili ya nyongeza yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufikia mkakati wa Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati, Serikali imekuja na majibu wanasema wanataka kuanzisha viwanda vitatu vya kutengeneza boti aina ya fibre glass. Tanzania ya viwanda
kuelekea uchumi wa kati wanataka kutengeneza boti sasa ndogo (fibre glass), Serikali ituambie ina mkakati gani wa kuweza kununua meli za uvuvi za kisasa kwenda kwenye bahari kuu ambapo watavua samaki ambao wanavuliwa na nchi nyingine? Hiyo, tunataka mkakati wa ziada, sio mnasema mnataka kununua fibre glass? Fibre glass kwenye uchumi wa kati, Tanzania ya viwanda? Maajabu makubwa haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, wanasema Serikali kwamba sekta ya uvuvi hii wanataka kuboresha maisha ya wavuvi, wametenga wana shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuboresha ruzuku za uvuvi na mambo mengine. Shilingi milioni 400 Mheshimiwa! Wavuvi ni maskini, shilingi milioni 400 ndio kitu gani? Kwenye bahari na kwenye maziwa? Serikali ituambie mna mkakati gani wa ziada kuboresha maisha ya wavuvi hasa wadogo wadogo sio shilingi milioni 400. Ndio Tanzania ya viwanda kuelekea uchumi wa kati hiyo? Tupe majibu ya uhakika, Serikali inasemaje juu ya kuboresha maisha ya wavuvi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Masoud kama ifuatavyo:-
Kuhusu uwekezaji wa ununuzi wa meli kwa ajili ya uvuvi katika bahari kuu nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali yenyewe haina nia ya kununua meli, lakini kinachofanywa ni kuweka mazingira wezeshi na kuhamasisha sekta binafsi iweze kuwekeza katika ununuzi wa meli pamoja na uvuvi katika bahari kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Shilingi milioni 400, nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba hiyo ni sehemu ndogo tu shilingi milioni 400 zilizotolewa kwa ajili ya kuwawezesha wavuvi ni sehemu ndogo tu ya jitihada mbalimbali zinachokuliwa na Serikali kwa ajili ya kuendeleza sekta ya uvuvi.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nina swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, madai ya walimu yasiyo ya mshahara ni pamoja na deni la walimu kwa Serikali juu ya posho na kufundishia yaani teaching allowance ambayo ni ahadi ya Serikali tangu mwaka 2012 ambayo ilitolewa kule Mtwara siku ya Walimu Duniani.
Je, Serikali ina mkakati gani wa ziada kuweza kuwalipa na kuwapatia fedha zao walimu hawa deni wanalolidai, posho la kufundishia yaani teaching allowance kwa haraka inavyowezekana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA YA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, kwa hali ya sasa tunachokifanya ni kuhakikisha kwa kadri iwezekano kusaidia sekta ya elimu. Ndio maana kabla sijajibu hili swali sasa hivi ukiangalia Serikali yetu kwa kazi kubwa waliyoifanya sasa hivi, mwanzo ukiangalia Walimu Wakuu, hata Waratibu wa Elimu mwanzo walikuwa hawalipwi hizi allowances.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Serikali hivi sasa toka mwaka jana kuanzia Waratibu wa Elimu, Wakuu wa Shule za Msingi na Wakuu wa Shule za Sekondari hivi sasa wote wanalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kama kuna madeni mengine yoyote Serikali iko katika michakato mbalimbali kuyalipa madeni haya yote. Naomba niwahakikishie ndugu zangu Wabunge kwamba Serikali yetu jukumu letu kubwa ambalo tunalilenga sasa hivi, kwa sababu tunataka kuhakikisha ubora wa elimu lazima madeni haya yote yatalipwa na kama nilivyosema madeni yote ambayo yamehakikiwa kupitia Hazina yatalipwa madeni hayo. Tunataka walimu wetu wawe na morali ya kufanya kazi katika mazingira yao ya kazi.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Nami naishukuru Kampuni ya Azam Marine kwa kurahisisha usafiri kutoka Tanga kwenda Pemba. Swali langu ni moja dogo lifuatalo:-
Kwa kuwa kuna malalamiko ya muda mrefu ya kutokupatikana kwa usafiri wa uhakika kutoka Dar es Salaam kuelekea Bandari ya Mtwara; na Serikali imekuwa ikiahidi mara kadhaa kwamba wako katika mkakati kabambe wa kuhakikisha kwamba usafiri kwa njia ya baharini kutoka Dar es Salaam kwenda Mtwara utapatikana kwa haraka; Serikali ituambie, ahadi hii ya muda wa miaka saba iliyopita, ni lini Serikali itaandaa mikakati ya kurahisisha usafiri huu? Naomba majibu.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, ni hivi karibuni tu humu Bungeni nilisema kwamba Serikali inaangalia uwezekano wa kutatua tatizo la usafiri kwenye Bahari ya Hindi, kwa sababu maamuzi yetu ya nyuma yalilenga kutoa fursa hii kwa wawekezaji binafsi. Ndiyo maana tulipotoa hizo fursa, wawekezaji kama Azam Marine walijitokeza na wengineo kuwekeza. Ni kwenye Maziwa Makuu tu ndiyo Serikali tuliendelea kutoa huduma.
Mheshimiwa Spika, tutaendelea kuhamasisha wawekezaji binafsi lakini pale itakapoonekana kwamba wawekezaji binafsi, hawawezi kabisa kutoa huduma hiyo, Serikali itaangalia uwezekano wa kurudisha TACOSHILI ya zamani ili iweze kutoa huduma katika Bahari ya Hindi. Nimhakikishie tu kwa sasa hivi watu wa Mtwara wanasafiri kwa raha sana kwa njia ya barabara.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jengo la Polisi la kituo cha Kingeja ni bovu, chakavu, linavuja na jengo hili Serikali walinyang’anya kutoka kwa hao wanaitwa Wakoloni. Kwa bahati mbaya sana wamenyang’anya kutoka kwa hawa wanaitwa wakoloni wakawa wameshindwa kueliendeleza na linahatarisha maisha ya polisi na Naibu Waziri amefika kituo cha Polisi cha Kingeja huku akiwa na ahadi lukuki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka utuambie leo Mheshimiwa Waziri, una mikakati gani ya ziada kuhakikisha kwamba kituo cha polisi cha Kingeja ambacho mlinyang’anya kwa wakoloni, jengo lile sasa hivi linapatiwa ukarabati wa hali ya juu ili polisi wale wasipate madhara yoyote? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, anachokizungumza Mheshimiwa Masoud ni sahihi, binafsi nilifanya ziara katika Jimbo hilo la Mtambile na nilikitembelea hiki kituo, kwa kweli hiki kituo kiko katika hali mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba hatujakaa kimya wala hatujadharau. Tunatambua changamoto kubwa ya ubovu wa kile kituo kama ambavyo vituo vingine vingi katika nchi yetu na kama ambavyo nimezungumza mwanzo kwamba pale ambapo tutapata fedha za ujenzi na ukarabati wa vituo hivyo tutafanya hivyo haraka sana.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika nakushukuru, nina maswali madogo mawili ya nyongeza
kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, la kwanza; kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ameliambia Bunge na kuwaambia Watanzania kwamba kuna kero 11 ambazo zimeshapatiwa ufumbuzi, naomba Mheshimiwa Waziri ututajie kero zote 11
ambazo tayari zimeshapatiwa ufumbuzi.
Mheshimiwa Spika, la pili; Mheshimiwa Waziri, Benki Kuu ni chombo cha Muungano na kilianzishwa mwaka 1966
baada ya kuvunjika kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki yaani East African Currency Board. Tangu kipindi hicho gawio la upande wa pili yaani ya Zanzibar imeonekana kwamba gawiwo (shares) hilo la upande wa pili hazitolewi kama ambavyo tulivyoweka shares zetu.
Mheshimiwa Spika, ni tatizo gani la msingi lililopelekea shares zetu za upande wa Zanzibar, kulingana na fedha ambazo tuliziweka, kwamba fedha hizi hazitolewi kama tulivyopangiwa au inavyotakikana kupatiwa sisi kutoka Zanzibar? Kama ni hivyo, sababu hizo ni kwa nini basi isionekane kwamba kuna haja ya haraka kuweza kupatiwa
ufumbuzi na fedha hizo kutolewa upande wa Zanzibar, naomba majibu ya haraka.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali ambalo limeulizwa na Mheshimiwa Mbunge la kwanza kama ulivyonielekeza ambapo ameomba kujua hizo
kero 11 ni zipi ambazo zimeshapatiwa ufumbuzi naomba kuzisema kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kero za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi ni:-
(1) Utekelezaji wa sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
(2) utekelezaji wa Merchant Shipping Act katika Jamhuri ya Muungano na uwezo wa Zanzibar kujiunga yaani
International Maritime Organization (IMO).
(3) Uvuvi kwenye ukanda wa uchumi wa bahari kuu.
(4) Ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki
(5) Uwezo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukopa ndani na nje ya nchi.
(6) Wafanyabiashara wa Zanzibar kulalamika kutozwa kodi mara mbili.
(7) Mfuko wa maendeleo ya Jimbo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
(8) Ongezeko la gharama za umeme kutoka TANESCO kwenda ZECO.
(9) Ushiriki wa Zanzibar na Taasisi za Kimataifa
(10) Ajira ya Watumishi wa Zanzibar katika Taasisi za Muungano.
(11) Utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia. Ahsante.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imekiri kuwepo kwa mahitaji mbadala ya usafirishaji wa mizigo kutoka Mtwara - Dar es Salaam, Dar es Salaam - Mtwara; na kwa kuwa Kampuni ya Dangote peke yake ina magari 600 ambayo Mheshimiwa Rais aliyazindua na GSM ina magari 300 jumla yote ni magari 900 ambayo yanasafirisha saruji kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam; na kwa kuwa barabara hii inaenda kuharibika; Serikali ituambie ina mkakati gani wa dharura na wa makusudi inaopanga kuchukua ili kuinusuru barabara hii isiharibike? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa inavyooneka mtazamo wa Serikali ni kwamba haitaki kufahamu ukubwa wa tatizo hili. Ikitokea Mheshimiwa Naibu Waziri kwa muda mrefu hamjampata mwekezaji kama mlivyosema na barabara hii inaenda kuharibika, je, Serikali haioni kwamba mtakuwa mmeanza kutafuta mkandarasi mwingine ambaye atatumia fedha nyingi kujenga barabara hii ya Dar es Salaam - Mtwara, jambo ambalo ni matumizi mabaya ya fedha za umma? Je, uko tayari kuwajibika kwa hili?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni muhimu kuwa na usafiri wa baharini hasa ukiangalia kwamba barabara zetu zinaharibika sana. Ukichukua kwa upande wa Bandari ya Mtwara, sasa hivi ipo meli ambayo inasafirisha saruji ya Dangote kutoka Mtwara kwenda Zanzibar. Takribani kila mwezi meli hiyo inasafirisha tani 6,000 sawa na magari 200. Sasa hivi Serikali ikishirikiana na Dangote na watu wengine tunaendelea kuhakikisha kwamba mzigo mkubwa wa saruji kutoka kwa Dangote unasafirishwa kwa meli ili kuhakikisha kwamba barabara yetu ile inadumu kwa muda mrefu.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika swali la msingi muuliza swali Mheshimiwa Joram Hongoli alisema kwamba wamekuwa wakipoteza maisha kule Njombe kutokana na kutembea umbali mrefu bila kupata matibabu.
Pia kule Njombe na maeneo mengine ya karibu kuna tatizo au tabia ya kurithiana wajane na wagane pale ambapo mmoja amefariki bila kupimwa vizuri afya zao. Wengine wamekwenda mbali zaidi, kumekuwa na tabia ya kwenda katika mapango jambo ambalo linaongeza matatizo ya VVU na UKIMWI na viongozi ndani ya Halmashauri wamekuwa wakilifahamu suala hili.
Je, Serikali ina mkakati gani wa ziada ili kuhakikisha kwamba tabia ya kurithiana wajane na wagane na matambiko katika mapango unakomeshwa katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala analozungumzia Mheshimiwa Masoud ni kweli ni jambo halisia na lipo. Miongoni mwa sababu kubwa zinazosababisha hili janga la UKIMWI liweze kuongezeka ni ile tabia ya kwamba mtu amefariki halafu mtu mwingine anamrithi, lakini kuna visababishi mbalimbali. Jukumu letu kubwa hapa sisi kama Serikali ni kutoa elimu kwa wananchi ni vitu gani ambavyo vinasababisha ongezeko la UKIMWI katika maisha yetu. Katika suala hili zima la kurithiana, Serikali imekuwa ikitoa elimu mara kwa mara kwamba utaratibu ule wa zamani wa kimila kwamba mtu amefariki bila kujua afya zao zikoje basi shemeji au mtu mwingine anamrithi si utaratibu mwema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaelekeza maeneo mbalimbali hasa katika Halmashauri zetu kwa sababu Serikali za Mitaa ziko kwenye maeneo yote kuendelea kutoa elimu hii. Ni vyema wananchi wote sasa wajue kwamba programu ya upimaji wa afya zetu ni jambo la msingi kwa sababu sio wagane peke yake hata katika hali ya kawaida katika suala zima la ndoa ajenda ya kupima afya zetu ni jambo la msingi ili kuzilinda familia zetu na watoto watakaozaliwa.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ningependa nimuulize Mheshimiwa Waziri swali lifuatalo:-
Kwa kuwa fedha za Mfuko wa Jimbo pale ambapo zinaingizwa kwenye akaunti kwa upande wa Tanzania Bara, kwa upande wa Zanzibar zinachukua karibu miezi minne mpaka mitano kutokana na mlolongo mrefu ambapo fedha hizi zinaingizwa katika akaunti zetu za Majimbo ndani ya Wabunge wa Visiwa vya Unguja na Pemba.
Ningependa kumuuliza Mheshimiwa Waziri, je, ni sababu zipi za msingi zinazopelekea fedha zinapoingia katika akaunti za Majimbo ya Tanznaia Bara zinachukua miezi sita kwa upande wa Tanzania Zanzibar. Je, nini kifanyike ili fedha hizi ziweze kufika kwa wakati kama ambavyo zinavyoingia upande huu? Nashukuru sana.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima kubwa naomba kujibu swali ambalo nadhani litakuwa swali maarufu la mwaka na limeulizwa kwa staili ambayo haijawahi kufanyika, ninakupongeza Mwenyekiti kwa utaalamu wa kujua Kanuni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali hili linahusu Mfuko wa Jimbo na Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Ester Mmasi, Mheshimiwa Munde Abdallah na wengine wengi Wabunge wa Viti Maalum wanataka na wao wapate mgao wa fedha za Mfuko wa Jimbo. Swali hili siyo kwamba linaulizwa kwa mara ya mwanzo leo, limekuwa likiulizwa na mara nyingi tumekuwa tukitoa majawabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu maarufu ambayo tumeyatoa kwamba tutakwenda kushughulikia tuone utaratibu wake, lakini kila tunaposhughulikia tunapata ugumu kwa sababu mfuko huu umezaliwa kwa mujibu wa sheria, sheria yenyewe inaitekeleza Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mfuko wenyewe unaitwa Mfuko wa Jimbo na kwa hiyo, kuupa jina linguine lolote lile ni kazi ngumu kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, humu ndani kuna Wabunge
wa Majimbo, kuna Wabunge wa Viti Maalum, kuna Wabunge wa Mikoa, kuna Wabunge wanaoteuliwa na Mheshimiwa Rais. Bunge hili likitambua kwamba Wabunge wa aina hizi zote wapo, lilitunga Sheria ya Mfuko wa Jimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kwenye instrument yangu kwa mujibu wa sheria nilizopewa kuzisimamia nina sheria inayosema nitasimamia Mfuko wa Jimbo, haisemi vinginevyo. Ndiyo maana kwenye jibu letu la msingi nimesema kama Bunge litaona vinginevyo suala hilo linakuja kwa utaratibu mwingine, lakini kwa sasa mimi ninasimamia Mfuko wa Jimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata wale Wabunge waliokuwa wanadai sana mfuko huu, waliokuwa wa Viti Maalum, walipopata majimbo na wenyewe msimamo wao umebadilika, ni kwa sababu ya majukumu anayoyapata Mbunge wa Jimbo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali mengine yameulizwa na Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim ambaye ameuliza suala la fedha kuchelewa Zanzibar, hili tumelichukua, tunawasiliana na Ofisi ya Makamu wa Rais tuone utaratibu bora zaidi wa kuweza kufanya fedha hizo ziwafikie Wabunge wa Zanzibar, hasa tunatambua yapo mapendekezo ya kwamba bora zikapita katika Ofisi ya Bunge Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine dogo limeulizwa na Mheshimiwa Paresso kwamba Wabunge wa Viti Maalum hawaingii kwenye Kamati za Fedha. Kamati za Fedha zinatambua uwepo wa Madiwani na Mbunge unapoingia kwenye Halmashauri huwi Mbunge unakuwa Diwani, kule kwenye Kamati ya Fedha wanaoteuliwa kuingia kwenye Kamati ya Fedha huwa ni Madiwani. Sasa nadhani ni utaratibu wa Halmashauri zenu, kama wewe Mbunge kuteuliwa kuna baadhi ya Wabunge ambao wanaingia kwenye Kamati ya Fedha, lakini kule wameingia kwa tiketi ya Udiwani wao kwenye Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napata shida hapa
kwa sababu la kwanza, kwamba kwa Majimbo ambayo yana Wabunge wengi wa Viti Maalum, na mfahamu kikao kile kina utaratibu wa gharama zake na mambo mengine. Ingawa gharama siyo hoja kubwa, lakini kwa Jimbo ambalo lina Wabunge wa Viti Maalum nane, 10, sijui hali itakuwaje kwa sababu gharama za uendeshaji wa Halmashauri zitakuwa kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ingelikuwa Wabunge labda ni mmoja au wawili pengine unaweza kuichukulia hili jambo likawezekana, lakini kwa hali ilivyo kuna tatizo kubwa sana na ninadhani ni vema hili jambo likabaki kama ilivyo na ndio utaratibu ulivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa tiketi ya Udiwani, Mbunge anaweza akateuliwa na Mwenyekiti kwa utaratibu ule akawa Mjumbe wa Kamati ya Fedha.(Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya haki za wafungwa zinazovunjwa ni pamoja na makazi duni sambamba na kukosekana kabisa kwa rufaa za hukumu jambo ambalo linafanywa kwa makusudi na baadhi ya maafisa husika na Case Flow Management Committees haziendi kwa wakati. Swali, Serikali ina mkakati gani wa ziada kukamilisha taratibu hizi ili wafungwa wapate haki zao inavyostahili? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Masoud kwa swali hilo. Niseme tu kama nilivyotaja baadhi ya haki, zile nilizotaja ni baadhi tu, lakini kwa upana wake kuna vitu vingine vingi zaidi na kama Serikali tumejipanga na hivi vinahusisha zaidi ya Wizara moja. Utaona Mheshimiwa Rais anapoweka nguvu upande wa mahakama anamaanisha kesi zisikae sana kwa sababu haki ikicheleweshwa inakuwa haki iliyokataliwa, unaona jambo hilo linavyofanyika. Anavyoiwezesha magereza kupata magari ya kubebea mahabusu waweze kupelekwa kusikilizwa kesi zao anawezesha connection kati ya mahakama, magereza pamoja na polisi waweze kufanya kazi hizo ambazo zote hizo zikipunguza mahabusu waliokuwa magerezani automatically inakuwa zimepunguza msongamano kwenye magereza hayo na kuwafanya wapate haki hiyo mojawapo aliyoitaja.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme tu maswali yenu yote mliyouliza yale ambayo yana mlengo wa kiushauri kama Serikali tumepokea na tutaenda kuyafanyia kazi ili kuweza kuleta ustawi katika maeneo haya mliyoyataja.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
La kwanza, Serikali imesema kwamba wanaendelea kuwahamasisha wakulima kutafuta masoko ya uhakika, lakini hata pale ambapo wakulima wanavuna mazao yao ya ziada hawaruhusiwi kuuza mazao hayo nje ili kujipatia kipato cha ziada. Baya zaidi ni kwamba Wakala wa Hifadhi ya Chakula wa Taifa, (National Food Reserve Agency - NFRA) hawapatiwi fedha za kutosha kununua mazao ya wakulima pale ambapo yanakuwa ni mengi, jambo ambalo linasababisha wakulima hawa kupata hasara kubwa. Je, Serikali ina mkakati gani wa ziada kuhakikisha kwamba, NFRA wanapewa fedha za kutosha ili kununua mazao ya wakulima pale ambapo yanakuwa ni mengi? La kwanza.
La pili, ni kwamba wanaonunua mazao ya wakulima, wafanyabiashara ndogo ndogo katika masoko ya Temeke, Tandika, Buguruni, Mbeya na maeneo mengine mbalimbali, Mabibo, Mwananyamala, kote huko wana malalamiko makubwa kwamba mzunguko wa pesa kwa ujumla wake, basi umekuwa ni mdogo, wafanyabiashara hawa wamepigika; umaskini unakua, hawana uhakika wa mambo ambayo wanayafanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali sasa ituambie mkakati wa ziada kuhakikisha kwamba wafanyabiashara ndogo ndogo wanaofanya biashara za mazao ya wakulima katika masoko mbalimbali nchini mnawahamasisha kiasi gani ili kuweza kupata mikakati yao ya ziada ya kujiongezea kipato cha uhakika? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwanza kwamba ni lazima tufahamu kwamba, lengo la Serikali la kuzuia kuuza chakula nje ni kwa ajili ya maslahi ya Taifa. Ni lazima tuangalie hali yetu ya chakula ikoje, tukifananisha na majirani zetu wanaotuzunguka.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyozungumza, nchi za Ukanda wetu wa Afrika Mashariki watu zaidi ya milioni 20 mwaka huu wanategemewa kuwa na njaa ambayo haijatokea hivi karibuni. Ethiopia pekee watu milioni nane wana njaa; Sudani ya Kusini watu 4,600,000 wana njaa, Somalia watu 6,100,000 wana njaa; Rwanda kuna shida; nchi za pekee ambazo zina ziada ya chakula katika ukanda wetu ni Zambia, Malawi na Uganda. Katika mazingira kama haya, kama Taifa ni lazima tutangulize maslahi ya Taifa mbele na ni lazima tuhakikishe kwamba tumejitosheleza huku ndani kuliko kukimbilia kuuza chakula nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nataka nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba na hili ni lazima tuseme kwa uwazi, biashara inayofanyika ya kupeleka chakula nje siyo biashara, ni utoroshaji wa chakula. Mwaka 2016 mnafahamu huku ndani karibu mtutoe macho Waheshimiwa Wabunge kwa kusema kwamba kulikuwa na upungufu wa chakula. Mwaka huu tusipoangalia hali itakuwa ni mbaya zaidi. Kwa hiyo, ni lazima tuendelee kuhakikisha kwamba tunakuwa na usalama wa chakula ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile soko la chakula lipo ndani. Hatutaki tuwakimbize wakulima wetu waanze kuuza wakati wanalanguliwa. Bei wanayopata sasa hivi siyo nzuri. Mkulima ambaye anasubiri, anaweza akauza kwa urahisi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo mafupi, niseme sasa kwamba NFRA mkakati ambao tumejipanga, kwa sasa tunaanza kwanza na kuimarisha au kujenga uwezo wetu wa kuhifadhi. Kwa sasa tuna uwezo wa kuhifadhi chakula tani 251,000 tu. Tumepata shilingi bilioni 100; tunajenga maghala ili tuweze kuongeza uwezo huo kufikia tani 500,000. Ni kitu cha kwanza kwa sababu hata tukisema tununue, hatuna mahali pa kuhifadhi. Kwa hiyo, tunaongeza uwezo wa kuhifadhi. Baada ya hapo, NFRA itaongezewa uwezo wa kununua mahindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwa sababu NFRA haijaanzishwa kwa ajili ya kufanya biashara ya chakula, imeanzishwa kwa ajili ya hifadhi ya usalama wa chakula. Bodi ya Mazao Mchanganyiko tunavyozungumza Serikali imeshaagiza vinu vitatu vikubwa kwa ajili ya kuongeza uwezo wa kusindika katika vinu vya Dodoma, Mwanza na Iringa.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo ni kwamba, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko iweze kununua chakula kingi na kusindika na kuuza nje. Huko ndiyo tunakoelekea. Kwa hiyo, naomba tuvute subira, hayo yatafanyiwa kazi, lakini hatuwezi tukakimbilia kuanza kuruhusu chakula kiondoke nchini kiholela.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu masoko, Mheshimiwa Mbunge amezungumza kuhusu changamoto iliyoko Temeke na masoko mengine ya mjini kama alivyosema. Mkakati ambao Serikali inafanya, tunawashauri na kuwasaidia wafanyabiashara wadogo wadogo waweze kujiunga kwenye SACCOS, waweze kujiunga kwenye Vyama vya Ushirika ili iwe ni rahisi wao kupata mitaji kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo, lakini vilevile Benki za Biashara kwa sababu mara nyingi sana suala la mitaji linaweza likatatuliwa kwa kuwezesha kupata mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali kwa sababu tunaposema kwamba uwezo wa mzunguko wa fedha umekuwa ni mdogo, mikakati yote ambayo tunaijenga kama Serikali ni kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wananchi wanakuwa na uchumi imara ambao utawasaidia kuendelea kufanikiwa zaidi. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nina swali moja tu dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, ni muda mrefu hapa Bungeni Serikali imekuwa ikiahidi kukitengeneza Kituo cha Polisi cha Kengeja ambacho ni kibovu, chakavu na cha zamani ambacho mnasema mlirithi kutoka kwa wakoloni lakini mara nyingi hamkitengenezi na kimekuwa kikihatarisha maisha ya askari na baadhi ya wale wanaowekwa pale kwa muda.
Je, ni lini Serikali hasa itaandaa mazingira ya ziada kuhakikisha mnakikarabati kituo hiki ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nishukuru kwa swali la nyongeza kutoka kwa Mheshimiwa Mjumbe makini wa Kamati inayosimamia Wizara ya Mambo ya Ndani, naye nimhakikishie tu kwamba kikosi chetu kinachosimamia masuala ya ukarabati kitafanyia tathmini pamoja na kituo anachokiongelea.
Mheshimiwa Spika, ni kipaumbele cha Wizara kufanya ukarabati na kukamilisha majengo ya vituo ambavyo vimeshafikia hatua za kuweza kutumika ili vianze kutumika na cha kwake tutaweka umuhimu huo kama alivyohitaji kwenye swali.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kupata nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, imekuwa ni mazoea ripoti kadhaa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika miaka mbalimbali zimekuwa zikionyesha kwamba mafao ya wastaafu yanakuwa yakipunjwa kwa makusudi na Serikali imekuwa ikieleza kwamba ni wakati wa kukokotoa ndiyo matatizo hayo yanatokea.
Je, ni kwa nini basi mmekuwa mkiwapunja na kuwanyanyasa kwa makusudi na hali zao za maisha zimekuwa ni mbaya na tatizo hili limekuwa la muda mrefu, CAG analalamika lakini Serikali imekuwa haifuatilii kwa makini, tabia hii mbaya ya Serikali ya kuwapunja/kuwadhulumu wastaafu mtaacha lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ni kwamba shilingi 50,000 ambayo ilikuwa miaka iliyopita mkapandisha mpaka shilingi 100,000 ambayo ni wastani wa shilingi 3,300 kwa siku. Katika majibu yako ukasema kwamba sasa mnajielekeza kwenye miundombinu ya usafiri, usafirishaji, nishati na umeme, hivi watu hawa ambao mliwatuma wakiwa wazima wakafanya kazi hii kwa uadilifu na uaminifu mkubwa mnawapatia shilingi 3,300, mtuambie waziwazi mkakati wa Serikali wa ziada wa kuboresha maisha ya wastaafu kwa kuongeza pensheni hii utafanyika lini siyo kubakia na majibu haya tu kwamba mnajielekeza kwenye usafirishaji na usafiri hawa mnawatuma wakiwa na nguvu sasa mmewaacha mnawatelekeza, tabia hiyo mbaya Serikali mtaacha lini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la kwanza, kusema kwamba Serikali ina tabia mbaya ya kuendelea kuwapunja wastaafu wetu, hii siyo sahihi hata kidogo. Nasema siyo sahihi hata kidogo kwa sababu nimemueleza mafao ya wastaafu hukokotolewa kwa kanuni ambayo imekubalika ndani ya Serikali na wastaafu, kwa hiyo, hakuna sehemu yoyote ambako mstaafu anapunjwa na Serikali yetu, hilo halipo hata kidogo. Kwa hiyo, kanuni iko wazi na inatumika na kila mstaafu anapojiunga na mfuko wowote huiona kanuni hii kabla ya kujiunga na mifuko hii.
Kwa hiyo, napenda wananchi wetu waelewe, Serikali yetu ina nia njema na dhamira ya dhati ya kuhakikisha wastaafu wanalipwa katika msingi ambao ni mzuri kabisa na ndicho ambacho Serikali tumekuwa tukifanya. Ndio maana 2015 tumeongeza kiwango hiki kutoka shilingi 50,000 mpaka shilingi 100,000 kima cha chini. Wapo wanaolipwa vizuri zaidi kwa sababu nimesema formula hii inategemea na muda wake wa utumishi pamoja na mshahara wake wa mwisho aliostaafu nao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili kwamba Serikali ina mkakati gani, nimemueleza vizuri kabisa kwamba Serikali yetu na sote sisi ni mashahidi tunapambana kuhakikisha tunaongeza mapato ya Taifa letu, tunaweza kukusanya kodi yetu na sote tunaona.
Pia nimesema wazi, ukiongeza pensheni kwa ajili ya wastaafu tu wakati hakuna dawa, maji na huduma nyingine muhimu za jamii haitoleta maana yoyote kwa Taifa letu. Tunawathamini wastaafu wetu, tunaendelea kufanya nao kazi vizuri na tutaendelea kuwalipa jinsi ambavyo mapato ya Taifa letu yanavyoimarika.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri, kumekuwepo na ongezeko kubwa la jamii ya Warundi katika Kambi ya Ulyankulu kule Tabora, hali ambayo inatishia usalama wa raia na mali zao, lakini zaidi wazawa maeneo ya Ulyankulu. Je, unafahamu ongezeko hili na una mikakati gani ya ziada kuweza kukabiliana na tatizo hili ili ongezeko hili lisiendelee tena?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na jitihada mbalimbali ambazo zinafanyika kuweza kuhakikisha kwamba tunapunguza idadi ya wakimbizi katika makambi yetu, na ni shahidi hivi karibuni mmeona kuna zoezi la kurudisha wakimbizi ambao wanarudi Burundi kwa hiari yao ambalo linaendelea. Hii yote ni kwa sababu ya kazi kubwa ambayo Serikali yetu pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki imefanya katika kuhakikisha kwamba amani inarudi Burundi na wananchi wanaendelea kufanya shughuli zao za kawaida.
Mheshimiwa Spika, kwahiyo, kitu ambacho nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ni kwamba kambi zetu zote za wakimbizi hivi tunavyozungumza, kuna pungufu la wakimbizi ambao wanaingia, lakini pia harakati za kurudisha wakimbizi Burundi zinaendelea kwa kasi kubwa sana. Niendelee kumtoa wasiwasi, lakini vilevile niendelee kuwaomba kuwa nasihi wananchi ambao wanaishi mipakani kuendelea kutoa ushirikiano wao kwa baadhi ya wale wakimbizi ambao bado wanahisi kwamba sio wakati muafaka wa kurejea Burundi kwa sasa hivi, kuendelea kuwa- host kama ambavyo tumekuwa tukifanya miaka yote mpaka pale ambapo wataamua kuondoka wote kwa pamoja.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Pamoja na tatizo la malimbikizo ya mishahara ya walimu na kupandishwa madaraja bila kurekebishiwa mishahara yao kuna tatizo kubwa la walimu la muda mrefu ambalo ni ahadi ya Serikali karibu miaka sita sasa kwamba walimu wangepewa posho ya kufundishia yaani teaching allowance. Ni mara kadhaa Serikali imekua na kigugumizi hapa Bungeni na imekuwa haina jibu. Madaraja hayo au teaching allowance hiyo wamekuwa wakipewa Wakuu wa Shule na Waratibu wa Elimu tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuiuliza, je, Serikali ina mkakati gani wa ziada kuhakikisha kwamba ahadi waliyoiweka mwaka 2012 kwamba watawapatia walimu posho ya kufundishia (teaching allowance) sasa itakuwa imepatiwa ufumbuzi wa kudumu.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inajipanga kwa mambo mengi na ahadi zetu ni nyingi ambazo bado tunaendelea kuzitekeleza na hii ahadi ambayo anaisema Mheshimiwa Mbunge, nayo tutaitekeleza mara tutakapokuwa vizuri kifedha.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kituo cha Polisi cha Kingeja, Jimbo la Mtambire ni kibovu, chakavu na kimekaliwa tangu enzi ya ukoloni. Kumekuwa na ahadi ya Serikali karibu miaka 13 kwamba watakijenga kituo kile, lakini dalili hazioneshi kwamba kuna nia njema ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali ituambie ina mkakati gani wa ziada kuhakikisha kwamba, Kituo cha Polisi cha Kingeja kinajengwa sambamba na Kituo cha Polisi cha Mkoani hasa ukizingatia kuna vifaa vya Polisi ambavyo tayari vimewekwa katika eneo la Wilaya ya Mkoani ambavyo vinatakiwa viweze kusambazwa. Je, Kituo cha Polisi cha Kingeja…
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nia ya Serikali ni njema na utaona kwamba, wiki moja iliyopita Mheshimiwa Makamu wa Rais alikuwa ziarani kule pamoja na Naibu Waziri. Pia utaona kwamba, wamefanya shughuli kubwa ambayo inahusu ujenzi wa vituo na kazi inaendelea. Kwa hiyo kazi ile inayoendelea itafika pia mpaka Jimboni kwako pamoja na kituo kile ulichokitaja na vituo vingine ambavyo vinahitaji huduma kama hiyo.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru taarifa ya Serikali inaeleza kwamba kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo kuna bandari bubu 32. Serikali muda wote imekuwa ikisema kwamba iko katika mikakati ya kuhakikisha kwamba bandari bubu hizi zinaweza kudhibitiwa, lakini tatizo linaloendelea la kuingia kwenye nyaya za umeme, matairi ya magari fake pamoja na maziwa ya watoto fake yanaendelea kuadhiri afya za binadamu na matukio mengine ya hapa na pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anaweza akawaambia nini Watanzania juu ya mkakati wa ziada kuhakikisha kwamba matairi ya magari fake, nyaya za umeme, maziwa ya watoto fake yanadhibitiwa katika bandari bubu kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo? Naomba majibu ya haraka. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZINA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli katika bandari bubu zilizoko katika mwambao wa Pwani kuanzia Tanga hadi Bagamoyo na Kunduchi tuna kazi kubwa sana tunaifanya pale ya intelijensia pamoja na kazi ya kuhakikisha kwamba chochote kinachotoka pale hakingii katika soko kabla hakijakamatwa na Serikali. Nadhani unakumbuka ni mara nyingi tu tumeshika bidhaa mbalimbali zinazotoka upande wa pili kuingia upande huu mwingine wa nchi kwa maana inatoka Zanzibar kuingia huku kupitia hizi bandari bubu tumefanyakazi kubwa sana ya kuhakikisha kwamba zinasimamiwa haziathiri soko la nchi yetu na pili, hawaleti bidhaa ambazo ni fake kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafanya kazi hiyo na kwa kweli nichukue nafasi hii kuwapongeza sana vyombo vya ulinzi na usalama vya maeneo hayo kwa kazi kubwa wanayofanya.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Kulelea Watoto Wenye Ulemavu Shule ya Mgeza Mseto, Bukoba Mjini na Kituo cha Kulelea Wazee cha Ibosa cha Bukoba Vijijini hawajapata matibabu bure kama Sera ya Serikali inavyosema. Je, Serikali inasema nini kurekebisha dosari hii? Hilo ni la kwanza.
La pili, katika mapambano ya VVU na UKIMWI, sisi Waheshimiwa Wabunge tulipitisha hapa sheria ya mapambano haya na tukatoa adhabu ambayo kwa wale wanaoeneza VVU na UKIMWI kutakuwa na adhabu maalum. Katika hili Serikali hadi sasa haijaweza kufuatilia kwa makini kuwagundua wale wanaoeneza VVU na UKIMWI kwa makusudi na mpaka sasa Serikali haijaweza kudhibiti hali hii kwa kutoa adhabu kali kwa wanaohusika. Je, Serikali kwa sasa inasema nini juu ya kudhibiti tatizo hili ambalo bado kuna watu wanaeneza UKIMWI kwa makusudi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Kituo cha Watoto pamoja na kile cha Wazee cha Bukoba Vijijini kwamba kuna dosari ya matibabu kwamba wazee hawapati, naomba niwafahamishe Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwa ujumla wanaonisikia kwamba huduma kwa wazee wasio na uwezo kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007 ni bure and this comes automatic. Hii ni automatic, wala haina mjadala.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, kama ni mzee na hajiwezi, sera imempa msamaha automatically. Kwa hiyo, ni yeye sasa mzee kwenda kuidai huduma hiyo kwenye Kituo cha Afya ambacho anakwenda na ninakuhakikishia hawezi kudaiwa gharama za matibabu na kama ikitokea amegharamia pengine bila kujua ama pengine kwa kukosea ama yeye mwenyewe hakutaja umri wake vizuri, basi anaweza akalalamika kwenye mamlaka mbalimbali na mamlaka ya haraka kabisa ya kufikisha malalamiko hayo, ni kwa Afisa Ustawi wa Jamii ambaye anakuwepo kwenye hospitali hiyo. Kwa mfano, kama ni kwenye Wilaya, kila Hospitali ya Wilaya nchini ina Afisa Ustawi wa Jamii (Social Welfare Officer), lakini pia kila Halmashauri ina Ofisi ya Maafisa Ustawi wa Jamii na Maafisa Maendeleo ya Jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama mtu anataka kuidai haki yake kwenye sekta ya afya, anaweza akawaona hao Maofisa na watamsaidia na hata kama amedaiwa naye anajua kwamba sera inampa msamaha, anaweza akaenda kwenye ile ofisi ya pale Wilayani akaomba apewe barua ya msamaha. Atapewa barua yake ya msamaha, atakwenda kwenye kituo chochote kile hapa nchini na atapata huduma hizo bure. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kuna watu wanaambukiza virusi vya UKIMWI kwa makusudi kwamba Serikali haijafuatilia; hapana. Bunge hapa tukishatunga sheria tukaiweka kwamba imekuwa ni sheria sasa katika nchi hii, ku-enforce kuna pande mbili zinazohusika na kuna ya tatu ambayo inaaangalia pande hizo mbili, pande ya mlalamikaji, pande ya mlalamikiwa lakini pia kuna wanaosikiliza mashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama kuna mtu anahisi kwamba ameshuhudia mtu ambaye ameambukiza virusi vya UKIMWI kwa makusudi na anamfahamu, ni vyema mtu huyo akaenda ku-report kwenye mamlaka zinazohusika na usimamizi na ufuatiliaji wa utekelezaji wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya ku-report, sasa Serikali itachukua hatua, lakini kusema sisi tuanze kufuatilia, kuwatafuta watu wanaoambukiza virusi vya UKIMWI watu wengine kwa makusudi, itakuwa ni suala gumu sana. (Makofi)

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini nataka kusisitiza jambo moja, Mheshimiwa Naibu Waziri alisema kwamba ni wajibu wa Halmashauri kuwapa wazee barua za matibabu bure, nilishaelekeza. Siyo kila siku mzee anapoumwa apewe barua. Halmashauri zinatakiwa kuwapa wazee wote wasio na uwezo vitambulisho vya matibabu bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilishasema kwamba itakapofika tarehe 30 Desemba, wazee wote wasio na uwezo wapewe vitambulisho vya matibabu bure. Otherwise hatuwatendei haki wazee, kila siku akiumwa anakwenda kwa Mtendaji wa Kata apewe barua. Kwa hiyo, tunataka vitambulisho vya matibabu bure na Halmashauri kama za Kasulu, Mbarali na Shinyanga Vijijini zinafanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimeona nitumie Bunge lako kusisitiza Halmashauri zote, Wakurugenzi wote kuwapa wazee wasio na uwezo vitambulisho vya matibabu bure ili wanapokwenda kwenye Vituo vya Afya waweze kupata matibabu bila usumbufu wowote. (Makofi). Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Hoja ya msingi ambayo inaonekana ni usalama wa raia wakati wakivuka. Mbunge wa Mafia alisema kutoka Nyamisati na Kilindoni, maboti yaliyoko pale ni maboti ya mbao, Serikali ina mikakati ya mrefu ufumbuzi haupatikani.
Swali la msingi sasa, Serikali ina mkakati gani wa ziada sasa kuhakikisha maboti haya yanayochukua abiria yamepewa uwezekano wa kuwa makoti ya kuokolea maisha (life jacket) ili kunusu maisha ya abiria?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tukianzia na lile swali la Mheshimiwa Dau, Serikali ina mpango wa kupeleka kivuko eneo lile, kwanza kazi inayofuata ni kufanya feasibility study, baada ya kufanya feasibility study na kujua bei ya hicho kivuko then tutapanga pesa kwa ajili kununua kivuko hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la Mheshimiwa Masoud ni kweli kwamba kuna tatizo hilo na tutahakikisha kwamba sasa hivi tunapeleka vyombo vyote kuhakikisha kwamba vinakuwa na life jacket ili ikitokea matatizo wananchi wale waweze kujisaidia. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, msingi mkubwa wa Serikali iliyopo madarakani unatokana na ridhaa ya wananchi, lakini hali ya maisha ya wananchi wetu ni duni, mzunguko wa fedha ni mdogo sana, wananchi wanalalamika sana kwamba fedha imepotea/haipo mtaani na kasi ya ongezeko la maisha magumu imekuwa kubwa kupita kiasi. Kwa muda mrefu sana Serikali hii imekuwa ikijisifia wanakusanya zaidi lakini hali ya uchumi wa wananchi wetu imekuwa mbaya sana. Nimuombe Mheshimiwa Waziri atuambie leo fedha ambazo zilikuwa zinaonekana kwa muda mrefu katika mzunguko mtaani sasa ziko wapi na wana mkakati gani wa kuboresha hali ya maisha ya Watanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, anasema kwamba mwaka huu 2017 mnataka kujitathmini wenyewe, katika kujitathmini wenyewe mtaandika kweli? Kwanza mambo yafuatayo, haki ya kupata habari kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba yetu, Bunge haliko live, mikutano ya hadhara imepigwa marufuku…

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, swali sasa linakuja, kwa kuwa Bunge haliko live, mikutano ya hadhara imepigwa marufuku, katika kujitathmini wenyewe mtaandika kweli haya au kuna haja ya kutafuta chombo kingine huru APRM Number Two ili iandike uhalisia kwa sababu mambo kama haya kweli mtaandika wenyewe? Nashukuru. (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, kwanza nalitaka nimuombe Mheshimiwa Masoud avute subira kidogo. Leo nitapata fursa ya kueleza kwa kirefu hali ya uchumi ambayo ni pamoja na masuala ya maisha magumu, mzunguko wa fedha, fedha imekwenda wapi, kwa hiyo, namuomba avute subira tu kidogo, asubuhi hii na mchana leo.
Mheshimiwa Spika, la pili, kuhusu kujitathmini, kila robo mwaka Serikali inajitathmini katika vigezo mbalimbali, kila robo mwaka, kila nusu mwaka na kila baada ya mwaka mzima. Taarifa zipo, ukienda kwenye tovuti ya Wizara ya Fedha taarifa zipo, tovuti ya Wizara ya Fedha na Mipango taarifa zipo na sasa hivi mmeanza kugawiwa vitabu ambavyo vinatoa tathmini.
Mheshimiwa Spika, siyo hivyo tu, katika ngazi ya Afrika Mashariki tunajitathmini ili kuweza kujua kama kweli tunaelekea kwenye vigezo ambavyo tulikubaliana tunapokwenda kwenye Umoja wa Shirika la Fedha. Kwa hiyo, tuna convergence criteria ambazo tunazitathmini nchi baada ya nchi na tunakwenda vizuri. Tanzania ni moja kati ya nchi ambazo kwenye macro-economic convergence criteria tuko vizuri. Nikuhakikishie tu kwamba hizi taarifa ziko wazi na hakuna mahali popote zitaminywa. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna la ziada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa Wakuu wa Wilaya wanatumia madaraka vibaya ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini ambapo amemsimamisha kazi Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) wa Mtaa wa Mlimwa Kusini, kwa hila na ujanja na mpango wa kutengeneza. Jambo ambalo inapelekea kunakuwa na malalamiko makubwa miongoni mwa wananchi wa Mtaa wa Mlimwa Kusini ambapo ni Kiongozi wao wamemchagua na wanampenda. Je, tabia hii mbaya ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, ni lini ataacha kusimamisha watu kiholela? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, scenario anayoizungumzia is a very specific scenario na pengine tungeweza kuisikiliza chanzo chake, imekuwaje, ilitokeaje. Si rahisi kwa muda huu kuweza kufanya hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wote humu Wabunge tunafahamu, namna ambavyo Wenyeviti wetu wa Vijiji na Mitaa wanavyouza maeneo, wanavyoharibu mali za umma, wanavyochezea mali za umma. Kwa hiyo, kuna mambo mengi yanayotokea huko; na sisi kama nchi tumewapa madaraka hawa watu wawakilishe mamlaka ili kuhakikisha kwamba maslahi ya umma inalindwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kutekeleza majukumu haya, mazingira hayawezi yakafanana, yanatofautiana kutoka sehemu moja na sehemu nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara tunayosimamia, Utawala katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, tupo tayari kupokea jambo lolote mahsusi na kulishughulikia namna ilivyo. Lakini si kweli kwamba Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya hawa wanafanya mambo ya ovyo. Wanafanya mambo ambayo yanasababisha tunakuwa na amani katika nchi hii na tunawapongeza wanafanya mambo haya katika mazingira ambayo ni tata, kwa sababu pia kuna siasa ndani, kuna mambo mengi; tuwasaidie lakini pia tulete mambo ambayo yamekwenda sio sawa ili tuweze kuyashughulikia kulingana na yalivyo. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza majengo ambayo yatajengwa katika nchi mbalimbali na ukarabati ambao utafanyika katika nchi mbalimbali katika Balozi hizo. Hata hivyo, Mheshimiwa Naibu Waziri atakumbuka kwamba katika jambo kubwa ambalo linatupa aibu nje ya nchi ni viwanja ambavyo tumepewa na wenzetu walioko nje na hasa nchini Uingereza ambapo imetishia usalama wetu na inaonekana kwamba sisi kama Watanzania hatukuwa na fadhila nzuri ya kupewa vile viwanja na tunatishiwa hata kupelekwa Mahakamani au kunyang’anywa viwanja vile ambavyo viko Uingereza na Sweden.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anawaambia nini Watanzania kuepukana na aibu hii ya viwanja tulivyopewa kule Uingereza ambavyo vimekuwa ni pori/kichaka na tunatishiwa kunyang’anywa sambambana majengo ya kule Sweden ambayo hayaendelezwi? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza hapa suala zima la mikakati ya kibiashara, lakini moja ya mkakati mkubwa katika suala zima la biashara ni diplomasia ya kiuchumi (economic diplomacy). Hata hivyo, inaonekana Serikali haina mkakati na dhamira iliyo nzuri kuelekea kwenye economic diplomacy. Nini mkakati husika wa nchi ambazo amezitaja wa kuelekea kwenye diplomasia ya kiuchumi ili nchi yetu ipate manufaa zaidi? Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, kuhusu viwanja vyetu 11 vilivyoko nje ya nchi nimesema kwamba tumeweka mkakati na mkakati huu Mheshimiwa Masoud kama Mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama anaufahamu. Mkakati huu ulianza mwaka 2002/2003 na ukaisha 2017. Katika jibu langu la msingi nimesema kwamba katika mkakati huo tumeainisha viwanja vyetu vyote na kuvitengenezea utaratibu wa kuhakikisha kwamba tunavijenga ili kuweza kuweka vitega uchumi. Hilo ndiyo jibu langu kwa swali lako la kwanza.
Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili kwamba Serikali ina mkakati gani wa kutekeleza diplomasia ya uchumi, nataka tu nimweleze kwamba moja ya majukumu makuu ya Mabalozi wetu tunapowateua kwenda nje ya nchi pamoja na watumishi ambao tunawapeleka katika Balozi zetu ni kuhakikisha kwamba wanatekeleza diplomasia ya uchumi kwa kuhakikisha kwanza wanajenga mahusiano mazuri baina yetu na nchi hizo zilizoko nje ya nchini lakini pili waweze kutangaza na kutafuta fursa mbalimbali za kijamii, kiuchumi na za uwekezaji na wanapimwa kwa mambo hayo ili kuhakikisha kwamba sisi tunafaidika na uwepo wao nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Abuja kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba iko katika mpango na tayari mazungumzo yanaendelea na Mheshimiwa Masoud anajua.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza.
Katika majibu yake Mheshimiwa Waziri, amesema kwamba wamekuwa na teknolojia mpya ya upimaji na ugunduzi wa vimelea vya TB kwamba sasa ndani ya masaa mawili badala ya siku tatu.
Napenda kujua nini hasa mkakati wa Serikali wenye kutoa kampeni maalum ya elimu ambayo itaweza kuenea kwa kasi zaidi katika maeneo ya migodi, viwanja vya michezo, mikusanyiko ya wavuvi pamoja na mikusanyiko ya wasafiri?

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, inaonekana kwamba mkakati wa kukabiliana na tatizo hili ni kwamba ndani ya taratibu hizi za kibajeti, fedha hizi wameachiwa wahisani ambao ni Wazungu. Matatizo ni ya Watanzania, ugonjwa ni wa Watanzania, lakini matibabu ni kwa wahisani wafadhili, Wazungu.
Napenda kujua, kwa nini Serikali imetenga shilingi bilioni 33.3 na ni fedha za nje, hakuna hata senti tano ambayo ni fedha za ndani ambapo fedha hizi za nje huwa hazitolewi kwa wakati na wakati mwingine hazitolewi kabisa. Kwa nini Serikali isipange mkakati wake wa kuweka fedha za ndani badala ya kutegemea fedha za wahisani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Masoud kwa kuwa amekuwa ni mfuatiliaji mzuri sana wa masuala ya afya, TB pamoja na masuala ya UKIMWI. Nakupongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa na nzuri ambayo umeendelea kuifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijielekeza katika maswali yake ya msingi, ni kwamba sasa hivi Serikali baada ya kuona kwamba tumekuwa na changamoto kubwa sana katika utambuzi wa makundi maalum ambayo wengi wamekuwa wanaathirika kama nilivyoyataja katika majibu yangu ya msingi, tumeelekeza juhudi mahususi katika masuala ya makundi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama utakumbuka, mara nyingi ugonjwa huu wa UKIMWI umekuwa ni ugonjwa pacha vilevile wa ugonjwa wa UKIMWI. Sasa hivi mikakati ambayo tunayo, kwanza tumejielekeza kutoa elimu kwa njia mbalimbali kwa vyombo vya habari pamoja na mitandao ya jamii. Vilevile sasa hvi tuna mkakati mahususi wa kuwatafuta wagonjwa wa TB katika migodi. Sambasamba na hilo, katika mikakati yetu tumetengeneza mikakati jumuishi kati ya ugonjwa wa UKIMWI na ugonjwa wa TB.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumeanza kijielekeza mahali pengi ambapo tunaweza tukapata wengi kwa pamoja na hususan wanaume. Tumeelekeza nguvu kwenye migodi, tumeelekeza nguvu kwenye kambi za uvuvi na sasa hivi tunataka twende mbali sana katika upande huu wa UKIMWI, hata kule ambapo wanaume wanakuwa katika bar, msishangae na sisi tukiwa tunapita kule tunawaomba kufanya upimaji wa masuala ya UKIMWI pamoja na masuala ya TB.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali lake la pili alilielekeza katika suala la fedha akihoji kwa nini Serikali na katika kitabu pale inaonesha kwamba kuna fedha za nje na kwa nini sisi kama Serikali hatujaweka fedha za ndani. Naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015/2016 kufikia shilingi bilioni 269 katika mwaka wa fedha 2017/2018 na katika bajeti ambayo Waheshimiwa Wabunge mmetupitishia hapa juzi, bajeti ya dawa imeongezeka mpaka shilingi bilioni 270. Katika hiyo bajeti, ni kwa ajili ya dawa, vitendanishi na vifaatiba na ndani ya hiyo tumetenga shilingi bilioni tano kwa ajili ya ugonjwa wa TB. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru lakini nasikitika na majibu haya kwani ni majibu yale yale ya muda mrefu ambayo yamekuwa yakitolewa hapa Bungeni na imekuwa kidogo hayaleti taswira nzuri kwa pande mbili za Muungano. Nina maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, katika majibu yake anasema kwamba Tume ya Pamoja haijaanza kufanya kazi kwa kuwa majadiliano kati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu mapendekezo ya Tume hayajakamilika. Miaka yote hiyo mapendekezo wanajadiliana kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sasa mpewe muda gani? Mtuambie wananchi wanataka kusikia leo, mupewe muda gani mtaweza kukamilisha hayo mapendekezo? Ni miaka 33 ya Tume lakini tangu mapendekezo mwaka 2003 ni miaka kadhaa sasa, lakini hakuna kitu na wakati huo mnaendelea kutumia bilioni 31 point; mtuambie mnataka muda gani hasa, nusu karne au karne moja?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, majibu ya Serikali yanasema kwa makini sana, Tume ya Pamoja ya Fedha imeandaa rasimu ya Mwongozo wa uendeshaji wa Akaunti ya Fedha ya Pamoja ambao unatarajiwa kutekelezwa mara baada ya majadiliano ya pande mbili za Muungano yatakapokamilika. Wameandaa rasimu sasa, miaka yote hiyo.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri atuambie maeneo machache ya rasimu hiyo, maana hakuna anayeamini tunaona ni kiini macho, kizungumkuti, tuambie hayo maeneo machache.
Mheshimiwa Spika, maeneo machache ya rasimu yaliyotayarishwa ni yapi? Kwa sababu tayari wameshaandaa rasimu lakini hakuna anayeamini, tunaona haya ni majibu tu ya kizungumkuti, kiini macho, kusadikika, tuambie hilo.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, napenda kuongezea majibu ambayo yamejibiwa na Mheshimiwa Naibu Waziri. Majibu ambayo sisi kama Serikali tunaamini yalikuwa ni majibu mazuri, majibu yanayojitosheleza, lakini kwa kiu ya Mheshimiwa Masoud anasema bado Serikali haina dhamira ya kuhakikisha kwamba hiyo Akaunti ya Fedha ya Pamoja inaanza kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti yetu ambayo ilipitishwa na Bunge hili, Serikali kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, aliliarifu Bunge lako Tukufu kwamba mwezi wa Aprili, tarehe 22, Kamati ya Pamoja ambayo inahusu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na ya Muungano watakaa kwa ajili ya kuchambua mapendekezo ambayo yametoka kwenye Tume ya Fedha.
Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya Mheshimiwa Rais wa nchi yetu ilikuwa ahudhurie Mkutano wa Commonwealth kule London, Uingereza, lakini akawa amemtuma Mheshimiwa Makamu wa Rais ambaye ndiye Mwenyekiti wa hicho kikao cha Kamati ya Pamoja, kwa hiyo, matokeo yake kikao kile hakikufanyika. Aliporudi wakati kikao kile kilikuwa kimeandaliwa tena, akatumwa na Mheshimiwa Rais kwenda kwenye Mkutano wa SADC.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba yale yote aliyoyasema tuko katika hatua nzuri. Mapendekezo yalishawasilishwa kwenye ile Kamati, ni uchambuzi tu ambao ukishafanyika yale maeneo ambayo alikuwa anasema ni maeneo gani yataweza kufanyiwa kazi na Mheshimiwa Mbunge atayafahamu. Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Itakumbukwa kwamba kuna vituo vya polisi ambavyo walijenga wakoloni, mkarithi lakini mmeshindwa kuviendeleza. Hivi karibuni kuna vifaa ambavyo mmepeleka Kisiwani Pemba viko Wilaya ya Mkoani.
Swali, je, vifaa hivyo ndiyo vinaenda kujenga Kituo cha Kengeja ambapo ni muda wa miaka 16 unaahidi lakini hutekelezi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masoud, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, vifaa ambavyo tumepeleka si kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi cha Kengeja bali ni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Askari Polisi katika Mkoa wa Kusini na Kaskazini Pemba.
MHE. MASOUD ABDALLA SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nina swali moja dogo la nyongeza. Kuna malalamiko kadhaa kwa vijana wale ambao walioajiriwa kwenye Shirika la Uzalishaji Mali la SUMA JKT, kiwango chao cha fedha ni kidogo sana na vijana hawa wanalinda katika maeneo kadhaa na maeneo muhimu kama vile benki. Ni mara kadhaa wamekuwa wakisema kwamba mtapandisha kiwango cha posho cha vijana hawa wa SUMA JKT Guard, ni kwa nini basi Serikali imekuwa ikisuasua kwa muda mrefu hawapandishi pesa hizi na ni vijana hwa wanafanya kazi kubwa?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masoud kuhusu vijana wanaofanya kazi kwenye Shirika la SUMA Guard. Ni kweli malalamiko hayo na sisi tumeyapata, tumezungumza na Uongozi wa SUMA Guard ili waweze kuongeza viwango ambavyo wanawapatia vijana hawa. Hivi sasa tunavyozungumza ukiacha mshahara ile basic salary, kuna posho wanazopata za usafiri, za chakula na kadhalika; lakini bado tunakiri kwamba viwango wanavyopewa havikidhi haja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea kujitahidi kufanya kila linalowezekana ili maslahi kwa ujumla ya vijana hawa yaweze kuboreka. Kwa ujumla ni kwamba viwango vinavyofuatwa vinaendana na mashirika mengine ya ulinzi. Kwa hivyo ni vyema sisi kama Serikali tuone umuhimu wa kuboresha haya. Jambo hilo limechukuliwa na Uongozi wa SUMA JKT na ni mategemeo yetu kwamba wataweza kuwaboreshea viwango hivyo.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru; nina swali moja la dogo la nyongeza.
Serikali au JKT inatoa stadi za kazi ikiwemo suala zima la ushonaji; na Serikali kwa mara kadhaa kwa miaka mingi imesema ina mkakati kabambe wa kuongeza viwanda vya ushonaji nguo na hasa sare zile za jeshi, lakini imeonekana kwamba…
: ...inaonekana
kwamba kunakuwepo na kusua sua kwenye shughuli hizi, swali, je, Serikali ina mkakati gani wa ziada kuona kwamba ahadi yake ya muda mrefu ya kuongeza viwanda vya ushonaji nguo sambamba na Tangamsino mbali ya Kamesuma?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tunao mkakati wa kuongeza idadi ya viwanda vya kuzalisha nguo katika jeshi letu na tunavozungumza tuna viwanda viwili tayari, kimoja kiko pale katika Kambi ya Mgulani na kingine kipo katika Kambi ya Ruvu. Vinafanya kazi na lengo ni kuviboresha kwanza hivi kabla hatujaanzisha vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo ukifika pale kwenye kambi ya Mgulani utaona kwa macho yako kwamba kwa kweli juhudi kubwa zimefanyika. Sasa hivi nguo za kombati kwa mfano hatuagizi kutoka nje zina vitambaa vinanunuliwa hapa na zinashonwa hapa. Kwa hiyo, tumeanza na juhudi hiyo na hatua kubwa imepigwa na tutaendelea kuendeleza juhudi hizo. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nina swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kuna vikundi vya waasi ambavyo vinapelekea kufanya hujuma kwa Vikosi vyetu vya Kulinda Amani DRC - Kongo na maeneo mengine na pale inapotokea maafa kwa hawa askari wetu kupoteza maisha huwa kuna malipo maalum kutoka Umoja wa Mataifa lakini hata Serikali yetu nayo huwa kuna kiwango cha fedha ambacho wanatoa. Je, Serikali hasa ina mkakati gani wa ziada kuleta Muswada hapa Bungeni kuongeza muda wa kulipa wajane au wagane pale ambapo wanajeshi wanapoteza maisha katika kulinda amani DRC Kongo na Sudan Kusini na maeneo mengine? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Masoud, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Umoja wa Mataifa na Serikali ya Tanzania imekuwa ikilipa mafao yanayohusiana na ushiriki wa askari wetu katika Ulinzi wa Amani sehemu mbalimbali. Vinapotokea vifo basi kuna fedha maalum na kuna viwango maalum vilivyopangwa ambavyo hutolewa na Umoja wa Mataifa na Tanzania sisi tunatoa kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi na Kanuni za Majeshi zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuongeza fedha kwa wajane, ni suala ambalo tunalitafakari kwa madhumuni ya kuweza kuboresha maslahi yote kwa ujumla siyo moja moja. Kwa sababu kuna maslahi mengi ambayo wanajeshi hawa wanatakiwa wayapate. Sasa hivi Sheria ya Ulinzi wa Taifa inapitiwa pamoja na Kanuni zake ili kuangalia ni viwango gani vya maslahi gani ambavyo vimepitwa na wakati ili viweze kuboreshwa kwa pamoja.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri anasema kwamba anaiagiza Tume ya Taifa ya Walimu kutatua changamoto za walimu, lakini Serikali iliwaahidi walimu kuwapatia posho ya kufundishia (teaching allowance)ili iwe motisha kwao lakini hadi sasa Serikali imekuwa na kigugumizi, fedha hizo (teaching allowance) bado hawatoi kwa walimu.
Je, sasa Serikali inataka ituambie mliwadanganya walimu au mna nia ya kutoa teaching allowance iwe kama ni motisha?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niwapongeze Naibu Mawaziri wote kwa majibu mazuri sana ya awali na ufafanuzi na ningependa kujibu swali la kaka yangu Mheshimiwa Masoud kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mjuavyo kwamba Serikali kwa kubaini kwamba kuna changamoto nyingi, si kwa walimu pekee isipokuwa kwa watumishi wa kada mbalimbali; kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma iliunda bodi maalum kwa ajili ya kupitia swala zima la kazi mbalimbali za mazingira magumu. Sehemu nyingine posho nyingine huwa zinaingizwa katika mishahara kwa kadiri itakavyoonekana inafaa.
Kwa hiyo, Serikali imeangali kwa ujumla wake ndiyo maana kwa upande wa walimu, kwanza ilianza baadhi ya kada mbalimbali hasa katika Walimu Wakuu wa Sekondari na Msingi na hali kadhalika kwa Maafisa wale wetu wa Kata wa Elimu (Waratibu wa Elimu) kwa ajili ya kuwapatia responsibility allowance. Kwa hiyo, ni jukumu la Serikali kuangalia nini cha kufanya kwa ajili ya kuboresha si maslahi ya walimu peke yake isipokuwa kwa watumishi wote wa umma kwa kadiri itakavyoona inafaa kwa ajili ya kuboresha maisha yao.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muda sasa Serikali imekuwa na mkakati wa kuchoma nyavu za wavuvi kwenye maziwa na kwenye bahari kuu wakisema nyavu hizo hazina viwango na kuwaongezea wavuvi wetu walio wengi umaskini. Tatizo hili ambalo Mheshimiwa Waziri mwenyewe alikuwa akijifahari kwamba tutaendelea kuchoma nyavu moto. Nini mbadala wa wavuvi hao kuwaondoa kwenye umasikini baada ya nyavu hizo kuzichoma moto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masoud kwamba nini mbadala wa kuchoma moto nyavu zile?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nyavu zile zimechomwa kwa mujibu wa Sheria Namba 22 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2009. Hatukufanya kwa ajili ya kumwonea mtu, ni kwa ajili ya ulinzi wa rasilimali zetu leo na hata vizazi vyetu vijavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mpango wa kuwasaidia; tunao mpango mzuri ambao unaitwa SWIOFish. Huu mpango utakwenda kujibu namna ya kuwasaidia wavuvi wetu wa ukanda wa Pwani kuweza kupata namna nzuri zaidi ya kuweza kutumia vyombo na zana bora zaidi za kuweza kufanya shughuli zao za uvuvi.
Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Masoud ya kwamba Serikali imejipanga. Hivi sasa mradi unafanyika na wao vilevile kule katika visiwa vya Unguja na Pemba utawafikia.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na baada ya maelezo ya Mheshimiwa Waziri, nina swali moja dogo la nyongeza.
Kwa kuwa Tanzania ni nchi ya Mfumo wa Vyama Vingi na kwa kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ndio Msimamizi wa Uchaguzi.
Je, Serikali sasa iko tayari kuleta mabadiliko ya Sheria ya Mkurugenzi wa Halmashauri asiwe msimamizi wa uchaguzi hasa kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria zilizopo sasa, zilizotungwa na Bunge hili zinasema Mkurugenzi wa Halmashauri, Mkurugenzi wa Jiji, Manispaa unapofika wakati wa uchaguzi ndiyo msimamizi wa uchaguzi. Pale inapotokea kwamba Bunge hili litaona haja ya kubadili, hoja iletwe, tutaijadili. Ikibadilishwa, mimi mtumishi wa Bwana nitatenda kama Bwana anavyotaka. (Makofi)
MHE. MASOUD A. SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza nionyeshe masikitiko yangu na mkanganyiko wa majibu ya taarifa zao mbalimbali za hali ya uchumi pamoja na utaalam wao wakitoa shule hapa Bungeni.
Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza, Deni la Taifa linaongezeka na mnaendelea kukopa madeni ya masharti ya kibiashara ambayo yanapelekea sisi Watanzania kupata matatizo makubwa wakati mkiandaa mazingira ya kutaka kulipa deni hilo nje au kama inavyotakiwa. Ukiangalia taarifa nyingine zinaeleza kwamba bado mna mpango wa kukopa Sh.4,840,000,000 kwa ajili ya kulipa Deni hilo la Taifa. Je, kwa hali hii ya uchumi ilivyo na mkakati huo wa kulipa Deni la Taifa mtahimili kweli au mnataka mnataka nchi iendelee kufilisika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kwamba Deni la Taifa halijafanyiwa uhakiki (credit rating) ili nchi yetu iweze kujiridhisha kwamba Serikali inakopesheka au haikopesheki. Naomba atuambie ni lini mkakati huo ufanyika haraka ili nchi yetu ifanyiwe credit rating hali iwe nzuri kama ambavyo inavyoendelea katika nchi nyingine?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya Mheshimiwa Masoud Abdallah, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza kuhusu mkakati wa kulipa na kama deni letu ni stahimilivu, naomba nimwambie, kwanza Serikali yetu haijawahi ku-default hata mwezi mmoja katika kulipa madeni ambayo yameiva kwenye taasisi zote ambazo tumekopa. Ndiyo maana bado Taifa letu limeendelea kuaminiwa na taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa na tunaendelea kukopa kwa uangalifu wa hali ya juu. Tunapokopa tunahakikisha mikopo yote tunayoikopa tunapeleka katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi, ambapo tutaendelea kunyanyua uchumi wa Taifa letu na hasa tunapotelekeza azimio hili la Mheshimiwa Rais wetu la Tanzania ya Viwanda ambapo mpaka mwaka 2025 kwa uchumi wetu unavyokuwa tuna uhakika Taifa letu litakuwa ni Taifa la pato la uchumi wa kati. Napenda kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba, kwa viashiria vyote kuhusu ukopaji na kulipa bado Taifa letu deni lake ni himilivu.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu credit rating, kama nilivyosema wakati tuna-conclude bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwamba mkataba ule upo ndani ya Ofisi ya AG na anaendelea kuufanyia rating ya mwisho. Tuna uhakika ndani ya mwaka ujao wa fedha Taifa letu litafanyiwa credit rating ili kujua sawasawa na mataifa yote duniani yaweze kufahamu kwamba Tanzania ni Taifa makini linaloaminiwa kiuchumi ndani na nje ya Taifa letu.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa uzazi salama haujafanikiwa ipasavyo kwani kunakuwepo na upungufu mkubwa wa Madaktari, wauguzi na wakunga katika vituo vingi vya afya hasa huko vijijini.
Serikali ituambie ina mpango gani mkakati wa ziada kuhakikisha kwamba mnapeleka madaktari, wakunga na wauguzi katika vituo vya afya na zahanati katika maeneo ya vijijini zaidi ili kuokoa maisha ya akina mama?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli suala la uzazi salama linategemea kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa rasilimali watu wenye sifa na ujuzi, lakini asilimia 64 kwa mujibu wa utafiti wetu sasa hivi ya wanawake wanajifungua katika vituo vya afya na wanahudumiwa na wataalam wenye ujuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nakiri kwamba zipo changamoto, Mheshimiwa Jafo ameeleza pale Serikali itaajiri watumishi wa afya 6,000 kupitia TAMISEMI na watumishi wa afya 2,000 kupitia Wizara ya afya, lakini tumeenda mbali zaidi, tumepata fedha bilioni moja, tunasomesha watumishi wa afya 200 katika kutoa huduma za dawa za usingizi na tutawapeleka katika vituo vya afya ambavyo vinaboreshwa ili sasa pale ambapo wanawake watafanyiwa upasuaji kwa ajili ya huduma za dharura watapata huduma ambazo ni salama lakini pia zinazofikika kwa wanawake wengi zaidi.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali moja la nyongeza. Bajeti inayomalizika hivi sasa ya 2017/2018, kulikuwa na tathmini ya fidia juu ya maeneo ambayo ya jeshi yalichukuliwa kwa wananchi, bilioni 27 na eneo mahususi Jimbo la kilwa masoko la Mheshimiwa Bwege na linaloitwa Rasi Mshindo, Mtaa wa Mpala ni eneo muhimu nyeti ambalo Jeshi wanataka kufanyia kazi kwa ajili ya shughuli zao. Je, nini mkakati wa Serikali kuweza kulipa kwa dharura eneo la Rasi Mshindo, Mtaa wa Mpala, Kilwa Masoko? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI (K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Masoud ni mjumbe Veterani kwenye Kamati inayosimamia Wizara hizi. Mapendekezo yaliyoletwa na Mheshimiwa Waziri yalikubaliwa na Bunge hili bila hata shilingi moja kushikwa. Niseme tu kwa sababu ndio tunamaliza bajeti tumpe tu Mheshimiwa Waziri muda wa kwenda kuyatekeleza hayo na haya yote ambayo ya kipaumbele kama ambavyo Mjumbe wa Kamati amesema yatapewa uzito unaostahili.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la wavuvi kupata matatizo katika nchi za nje, inaendana na tatizo hili ambalo liko ndani ya Jimbo langu la Mtambile katika Kijiji cha Likoni na Chole upande wa Shehia ya Mwambe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muda wa miezi saba sasa wavuvi hao wako uko Pemba wamewekwa Gerezani, walifuata sheria na taratibu zote, lakini hadi leo wale ambao wanashughulikia wenzao ambao wako Gerezani wamefanya bidii kubwa ya kwenda katika Ubalozi wetu huko Msumbiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inasema nini na ina mkakati gani wa ziada kuhahakisha kwamba wale wavuvi wa Chole pamoja na Likoni wanaotendewa ndivyo sivyo wanapatiwa taratibu zilizo sahihi? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimhakikishie Mheshimniwa Mbunge kwamba tutakapokuwa tumetoka hapa, tukutane ili niweze kushughulikia hilo kwa karibu zaidi.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kupata nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hali ya maambukizi katika Jiji la Dodoma inaongezeka kwa kasi sana; na kwa kuwa katika baadhi ya nchi nyingine duniani wanatumia njia mbadala mbali na damu, wanatumia mate kuweza kutambua wale waathirika wa VVU. Naomba Serikali ituambie ina mkakati gani wa ziada wa kuwatambua wale waliopata athari hii ya VVU kwa njia ya kutumia mate na hasa tukianzia na Mkoa huu wa Dodoma?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masoud, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mkoa wa Dodoma maambukizi yamepanda kutoka asilimia 2.4 hadi asilimia 5, sawa na Mikoa ya Tanga na Mwanza. Kwa hiyo, tunafanya utafiti maalum wa kuangalia kwa nini katika baadhi ya mikoa maambukizi ya UKIMWI yamepanda mwaka 2012 mpaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la njia mbalimbali za kupima, ni kweli tumekuwa na changamoto ya kuwapata watu kupima hasa wanaume na tumeona njia ambayo itaweza kusaidia wanaume kupima UKIMWI ni njia ya mtu kujipima mwenyewe. Jana tulikuwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu na moja ya kifaa ambacho tutakitumia; lakini sheria kidogo zinatukwaza, inasema kipimo cha kujipima mwenyewe haiwezekani. Kwa hiyo, tumemuandikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili aweze sasa kuleta mabadiliko madogo ya sheria iweze sasa kuruhusiwa kwa mtu kujipima ikiwemo kwa kutumia kipimo cha mate ambapo ndani ya dakika 15 utaweza kujua kama una maambukizi ya UKIMWI au hapana. Tunaamini mtu akishajipima mwenyewe na kujiona kwamba ana maambukizi itakuwa ni kichocheo cha kwenda katika kituo cha afya ili aweze kuthibitika na hivyo tumuingize katika mpango wa dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai, kama alivyosema Naibu Waziri, dawa za HIV zipo kwa asilimia 100, changamoto yetu watu wapime. UKIMWI si tena sentensi ya kifo, ukiwa na UKIMWI ukipima tunakuingiza mara moja kwenye mpango wa dawa unaishi maisha safi na salama bila changamoto zozote. Ahsante sana.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, wananchi wa Kenyambi na Bugosi huko Tarime wameanza kukata tamaa baada ya huo uthamini uliofanyika tangu mwaka 2013, ni miaka mitano sasa. Bajeti iliyotengwa ya mwaka 2017/2018 ni shilingi bilioni 20, je, katika mwaka huu unaoisha fedha hizi kama zikipatikana wananchi wa Kenyambi na Bugosi huko Tarime watalipwa fidia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa muda mrefu Serikali imekuwa na kawaida wanapochukua maeneo ya wananchi kwa matumizi ya jeshi hawalipi fidia, wanafanya hivyo kwa sababu wananchi hawana cha kufanya. Serikali ituambie, ni kwa nini tangu mwaka 2006 imekuwa ikitoa taarifa ya utekelezaji wa kupima maeneo, kuthamini na kutoa fidia lakini haifanyi hivyo? Ni kwa nini Serikali isifanye utaratibu wa kufanya matembezi ya hisani ili wananchi wapate fidia zao kwa sababu Serikali inaonekana imeshindwa? Nashukuru sana.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi kwamba fedha zikipatikana ndiyo kipaumbele kitatolewa kwa wananchi wa eneo hili tunalolizungumzia kwa sababu tumewapa ahadi muda mrefu, tangu mwaka 2013 uthamini umefanyika. Mheshimiwa Mbunge anayehusika, mwenye jimbo lake, mara nyingi amekuwa akiniuliza na mimi huwa nampa majibu kwamba fedha tukizipata basi kipaumbele kitatolewa kwa eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pilli, kwamba Serikali huwa hailipi fidia, kwa kweli lengo la kulipa fidia lipo, lakini kama mnavyotambua kuna changamoto za kibajeti. Ni mategemeo yetu kwamba fedha hizi zikipatikana kwa kweli tutapunguza maeneo mengi sana ambayo yanatudai, kwa sababu hizi shilingi bilioni 20 zikipatikana siyo kwamba tutaweza kufikia maeneo mengi. Ni mategemeo yetu kwamba fedha hizi zitapatikana kama ambavyo Wizara ya Fedha ilishatoa ahadi hapa. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba hakuna sababu ya kufanya matembezi ya hisani katika hili, tutakachofanya ni kuendelea kuhimiza wenzetu wa Wizara ya Fedha wakiweza kupata fungu hili basi watupatie ili na sisi tuweze kutimiza ahadi zetu.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru nina maswali mawili ya nyongeza.

Katika majibu ya msingi Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba wanaandaa kampeni mbalimbali kwa ajili ya kuamasisha wananchi kujitokeza kupima VVU na Serikali inasema inautaratibu wa wananchi kujipima wenyewe kwa kutumia mate yaani HIV self-testing. Napenda kujuwa mkakati huu wa Serikali wa kuwaruhusu wananchi kujipima wenyewe kwa kutumia mate umefikia hatua gani hadi sasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, waathirika wakubwa wa VVU ni vijana wa rika balehe kuanzia 15 hadi 24 ambayo baadhi yao wapo katika shule za sekondari na kwenye vyuo, ningependa kujua mkakati wa ziada wa kuwafikia vijana hawa hasa walio shule ya sekondari na kwenye vyuo ili kujuwa hali zao katika mkakati wa kufikia 90, 90, 90?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Masoud kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imeingia imeridhia malengo ya kidunia ya 90, 90, 90 na moja ya mkakati ni kuakikisha kwamba sasa tunapanua wigo wa upimaji na hususani kulenga yale makundi ya wanaume ambayo imekuwa ni changamoto kidogo. Kwa hiyo, Serikali inataka kuja na mkakati wa self-testing kama mtu kujipima mwenyewe kwa kutumia sampuli ya kina na hatua ambayo tumefikia sasa hivi mchakato ndani ya Serikali tumeshaazisha na sasa hivi ipo kwenye hatua za mwisho za maamuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, Mheshimiwa Masoud aliongelea kwamba rika balee umri kati ya miaka 15 mpaka 24. Ni kweli kwa mujibu wa takwimu za hali na viashiria vya UKIMWI vya Mwaka 2017 imeonyesha wazi kwamba maambukizi katika kundi la vijana kati ya miaka 15 mpaka 24 yanazidi kuongezeka ndani ya nchi na hususani kwa mabinti wa kike. Baada ya sisi kulibaini hilo tumekuja na afua mbalimbali moja ni kuweka msisitizo katika suala la elimu, lakini la pili tunataka tufanye mabadiliko ya sheria kwa sababu ni wazi na dhahiri kabisa kwamba takwimu zinaonyesha mabinti wetu wanaanza kujamiana wakiwa na umri mdogo sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunataka tufanye mabadiliko ya sheria kushusha umri wa kuweza kutoa ridhaa ya kupima kwa sababu kwa sasa kwa mujibu wa sheria ya sasa, Sheria inasema mtu atapimwa ni mtu mzima mwenye miaka 18 na atapima kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na mtoa huduma katika sehemu za afya. Kwa hiyo, katika mabadiliko haya ya sheria tunataka sasa kushusha age of consent ili sasa hao mabinti ambao wameanza kujiamiana katika umri mkubwa na maambukizi yamekuwa ni makubwa waweze kupata ridhaa ya kuweza kupima.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nina swali moja dogo sana kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la msingi lilikuwa kuhusu ucheleweshaji wa fedha za Mfuko huu upande Zanzibar. Nimefuatilia majibu kwa makini sana, Mheshimiwa Naibu Waziri amejaribu kujibu kwa kiasi alichoweza. Kwa kuwa fedha hizi zinatoka kwenye Serikali ya Muungano na inachukua zaidi ya miezi sita, saba au nane, ametoa mlolongo wa taratibu jinsi fedha hizi zinavyokwenda Zanzibar, naomba atuambie mkakati gani wa ziada walio nao kurekebisha utaratibu huu ili kasoro hii iweze kuondoka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumjibu Mheshimiwa Masoud swali lake la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeeleza utaratibu wa kisheria ambao tuna kila sababu ya kuufuata. Kwenye majibu yangu ya msingi nimesema pia kama ziko changamoto zingine za ucheleweshwaji tutafanya kila jitihada tunavyoweza ili fedha hizi zisichelewe. Niwahakikishie tu ndugu zangu na nichukue fursa hii kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hususani Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais kwa namna inavyoratibu zoezi hili la kuhakikisha fedha hizi za Mfuko wa Jimbo zinafika kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu yake kwa swali la msingi la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, nataka niwahakikishie tu kwamba bado kuna ongezeko kubwa la watoto hawa katika Barabara ya Sita, Barabara ya Tisa hapa Dodoma na katika Soko la Dodoma la Matunda na Mboga Mboga.

Mheshimiwa Spika, nataka nikuhakikishie kwamba hali hii Jiji la Dodoma wanaifahamu. Sasa utuambia mwarobaini au mkakati madhubuti ama mkakati mahususi wa kuweza kuwasaidia watoto hawa, kwa sababu kila siku ongezeko hili kidogo linatisha.

Mheshimiwa Spika, swali la pili Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba baadhi ya watoto hawa wazazi wao tayari wamefariki kwa maradhi mbalimbali, lakini kuna baadhi ya watoto hawa wazazi wao wako hai na wako katika maeneo ya karibu katika maeneo mbalimbali. Sasa wanasema kwamba watatoa elimu, atuambie mkakati wa ziada kuhakikisha kwamba wale watoto ambao wazazi wao wapo hai wanachukua hatua gani ya dharura kuhakikisha wazazi hawa wanapatikana na suala hili kulikomesha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kwanza suala kwamba kuna ongezeko, hiyo inakuwa kidogo ni relative term, kwa sababu ongezeko hilo unalipima kuanzia lini? Kama nilivyojibu katika swali langu la msingi, kwa mujibu wa sheria ni wajibu kuhakikisha kwamba mtoto analelewa katika mazingira mazuri. Jitihada zimefanywa na Serikali kwanza kuwatambua hawa watoto.

Kwa mfano, kwa Mkoa wa Dodoma na hasa Jiji la Dodoma, jitihada za makusudi zimefanyika kwanza kuhakikisha kwamba wale watoto ambao wana wazazi wao wanarudishwa na kuunganishwa na familia kwa sababu wajibu wa kwanza wa kumlea mtoto ni wa familia.

Mheshimiwa Spika, kuna cases kama ambazo watoto wanalazimika kuondoka katika mazingira na kwenda katika mazingira hayo kwa sababu aidha, wameondokewa na wazazi wao kwa magonjwa masuala kama hayo, ndiyo maana katika jibu langu la msingi nimesisitiza kwamba ni wajibu wetu sisi kama jamii kwa ujumla kuhakikisha kwamba watoto ambao wanatakiwa kwenda shule waende shule na kuna mpango wengine wanaweza kupelekwa VETA. Ni jitihada za Serikali kuhakikisha kwamba watoto hawaishi katika mazingira magumu.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nina swali moja dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mikakati ya Serikali ya kuweza kutoa adhabu kali na sheria ya kifungo cha miaka 30 kwa wale ambao wanawapa mimba wanafunzi lakini inaonekana bado wanafunzi wanapata mimba na idadi inaongezeka. Je, Serikali ina mkakati gani wa ziada kwa baadhi ya madereva wa bodaboda wanaowachukua wanafunzi wetu ambapo wamekuwa wakilalamika kwamba wanatendewa vitendo visivyo za kutoa elimu ya kutosha kwa madereva hao wanaowachukua wanafunzi kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masoud, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu langu nilitoa katika majibu yangu ya swali la msingi kwamba Serikali inachukua hatua kadha wa kadha. Moja ni kuzuia na tunazuia kwa njia mbili na kubwa kupitia kitu tunachoita deterrence; kwa kuwaadhibu wale wanaofanya makosa ili wengine wasije wakafanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu changamoto ambayo watoto wanapata wakiwa wanaelekea shuleni, Serikali imeendelea kujenga shule karibu na wananchi lakini vilevile kwenye maeneo ambayo shule ziko mbali tumejenga mabweni. Vilevile tunatoa elimu kwa umma na wanafunzi kwa kupitia huduma za unasihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nachotaka tu kusema ni kwamba Serikali inajua hili ni tatizo kubwa lakini hatujakaa kimya tumeendelea kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba hayatokei. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kutokana na takwimu tulizonazo tatizo haliongezeki limepungua.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mapitio ya Sera ya Elimu na kuweka mikakati ya ubora wa elimu, ni mara kadhaa hapa Bungeni Serikali imekuwa ikiahidi kuboresha maslahi ya walimu ikiwemo posho ya kufundishia (teaching allowance). Vilevile kwenye sherehe mbalimbali za walimu katika maeneo kadhaa Serikali wamekuwa wakiahidi kuboresha posho ya kufundishia (teaching allowance) lakini hadi sasa waliopata fedha hizo ni Wakuu wa Shule na Waratibu wa Elimu. Naomba kujua kama Serikali iliwadanganya walimu na lini fedha hizo zitatolewa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali na Mheshimiwa Masoud, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika azma ya kuboresha elimu maslahi ya walimu na wafanyakazi wengine katika sekta ya elimu ni kitu muhimu. Ndiyo maana kwa sasa Serikali inajaribu kupitia upya utaratibu mzima wa maslahi ya watumishi wa umma kwa jumla wakiwemo na walimu ili baada ya hapo tuweze kuwa na maslahi ya walimu ambayo yataenda na wakati wa sasa lakini vilevile ili waweze kufanya kazi yao vizuri katika sekta ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu swali la madeni, naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ilijikita kwanza katika zoezi la kufanya uhakiki ili kubaini madeni ya kweli. Baada ya hapo tayari baadhi ya malipo yalishafinyika na mengine yataendelea kulipwa.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nami kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Pamoja na mabadiliko ya Muswada wa Sheria ya Usalama Barabarani ambayo inatarajiwa kuletwa hapa Bungeni, kuna malalamiko kwa madereva mbalimbali kwamba kosa lolote linapotokea, basi hakuna onyo, hakuna karipio. Karipio kubwa ni shilingi 30,000/= kwa haraka sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, inaonekana kwamba Polisi kwa wakati huu wanakusanya zaidi fedha kwa njia ya mapato zaidi kuliko kutoa karipio au kutoa onyo. PGO inaelekeza nini pale ambapo dereva amefanya kosa dogo la kwanza juu ya tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza ni imani yetu na imani ya Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote waliomo humu ndani kwamba mtu yeyote ambaye amechukua chombo cha usafiri na kuingia barabarani, maana yake kwanza amepata mafunzo ya kutosha na ana leseni.

Mheshimiwa Spika, hiyo ni moja, lakini la pili nina hakika Mheshimiwa Masoud anatambua kwamba tumekuwa tukifanya kazi kubwa sana ya kutoa elimu kuhusiana na usalama barabarani kwa kutumia njia mbalimbali ili kuwakumbusha wale madereva ambao wamekuwa wakighafirika katika kufuata Sheria za Usalama Barabara.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa kuzingatia hayo mawili ni imani yetu kwamba mtu yoyote ambaye yuko barabarani anaendesha gari, anatambua wajibu wake na hivyo basi, sidhani kama ni jukumu la Jeshi la Polisi kuanza sasa kutoa elimu barabarani wakati mtu anahatarisha uhai wa raia wengine. Kwa hiyo, niendelee kusisitiza kwamba, ni vizuri kila mmoja ambaye anaendesha gari barabarani ajue kwamba kuna sheria na afuate sheria hizo.

Mheshimiwa Spika, jukumu la Jeshi la Polisi ni kuhakikisha kwamba wale ambao hawafuati sheria basi wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria ikiwemo kutozwa faini. Hata hivyo, kuna baadhi ya changamoto ambazo tumekuwa tukizizungumza kila siku zinahitaji busara katika kuzikabili na niendelee kutoa wito kwa Askari Polisi kuzingatia busara wakati mwingine pale ambapo kuna matatizo ambayo yanaweza kuepukwa. Kwa mfano, kama ambavyo hata Mheshimiwa Waziri amekuwa akizungumza mara zote, unakamatwa mtu kwa kosa moja linazalisha makosa mengi, mtu anashtakiwa kwa makosa zaidi ya matano au sita. Kwa hiyo, mambo kama haya na mambo mengine ambayo yamekuwa kero kwa wananchi, hayo tumekuwa tukitoa maelekezo kwa Jeshi la Polisi litumie busara katika kuyakabili. Hata hivyo, tunataka kusisitiza umuhimu wa kutii sheria bila shuruti ili kuepusha ajali na kuokoa maisha ya Watanzania ambao wamekuwa wakipoteza maisha yao na kupoteza vyombo vyao kila siku.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika miaka ya 70 na 80 Serikali ilikopa kutoka Japan na Italia dola milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya korosho katika Mikoa ya Lindi na Mtwara. Wakati wa ubinafsishaji viwanda hivyo vilibinafsishwa lakini hadi leo viwanda hivyo havifanyi kazi. Mara nyingi Serikali imesema hapa Bungeni itakaa na wawekezaji kuona kwamba…

MWENYEKITI: Hebu uliza swali Mheshimiwa.

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali linakuja, ni kwa nini Serikali imelidanganya Bunge mara kadhaa kwamba itakaa na wawekezaji ili waweze kusaidia viwanda hivi na wananchi wapate manufaa yanayohitajika?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masoud, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi katika viwanda hivyo vipo ambavyo vinafanya kazi vizuri na vimeajiri zaidi ya watu 750 kwa kimoja. Kwa mfano, kiwanda cha Tunduru, cha Korosho Afrika lakini pia Kiwanda cha Newala Micronics, hivyo vimeajiri watu 750 kila kimoja lakini pia Micronics pale Mtwara kimeajiri kama watu 350. Vilevile kuna Kiwanda cha Mtwara kinachohusika na korosho pia ambacho sasa hivi ndicho kinachosaidia kufungasha hizo korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri kuna baadhi ya viwanda havikufanya vizuri, kwa mfano, Kiwanda cha Mtama na Kiwanda cha Nachingwea, hivyo tumeshavinyang’anya. Pia kuna Kiwanda cha Lindi Buko, nacho tumeshakinyang’anya na tumeshaanza kukifufua. Hiyo ndiyo hali halisi.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kasi ya uzalishaji wa kilimo cha viungo kama vile hiliki, mdalasini, pilipili manga, binzari nyembamba kwa nyumbani Zanzibar tunaita uzile, imekuwa bado ni ndogo sana na kuna maeneo mengi ambayo yanaweza yakastawi mazao haya.

Mheshimiwa Spika, Serikali ituambie katika kuhakikisha kwamba kwa hali ya hewa na udongo, mahitaji ya mazao haya bila mbolea, ina mkakati gani wa ziada kuona kwamba mazao haya yanalimwa na wakulima wakapata faida na Serikali inapata tija kubwa?

Mheshimiwa Spika, la pili, kuna malalamiko makubwa kwa baadhi ya wakulima kwamba Maafisa Ugani hawatoi elimu inayostahili katika maeneo ambayo wakulima wangeweza kulima kilimo cha aina yoyote bila kutumia mbolea: Serikali ituambie ina mkakati gani katika kuwawezesha Maafisa Ugani ili waweze kuwafikia wakulima walio wengi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru. Swali la kwanza la Mheshimiwa Masoud anataka kujua mkakati wa Serikali ambao tunaweza kuwawesha wakulima ili waweze kuongeza uzalishaji na tija.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, yaani kilimo tulichokuwa tunalima, kilikuwa cha kubahatisha; mkakati mkubwa wa Serikali uliopo sasa kwanza ni kufanya utafiti wa afya ya udongo ili kubaini asili na kuangalia aina ya udongo iliyoko pale ili kuwashauri wakulima ni zao gani ambalo linakubali kwa udogo wa ikolojia eneo walipo? Kwa hiyo, huo mkakati ambao utakamalizika muda mfupi ili kwamba tutoe elimu sahihi na kuwashauri wakulima aina gani ya zao walime? Mbolea gani watumie? Namna gani ambayo wanaweza kufaidika kwa kuongeza uzalishaji na tija?

Mheshimiwa Spika, katika swali la pili, anazungumzia kuhusu Maafisa Ugani kwamba wapo lakini hawawafikii wakulima kutoa elimu sahihi. Kwanza, nichukue nafasi hii kueleza kwamba Maafisa Ugani ni kweli anachosema Mheshimiwa Mbunge kwamba wako wachache. Mahitaji Maafisa Ugani ni zaidi ya 20,000 nchini hii, tuliokuwa nao ni 8,600. Kwa hiyo, tuna upungufu zaidi ya 11,400.

Mheshimiwa Spika, kama Serikali, kwa kujua hilo kwa sasa hivi ni kwamba Serikali imeshaanza kutoa vibali kwa ajili ya kuajiri watumishi na mkazo mmoja utaelekezwa huko ili tupate Maafisa Ugani kwa ajili ya kwenda kutoa elimu.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kama Serikali tuna mkakati ambao ulikuwepo tangu katika ASDP I wa kujenga vituo vya elimu kwa wakulima kila Kata, mkakati huo utaendelea, lengo ni kuwakusanya wakulima kutoka katika vijiji mbalimbali kukutana pale kunapokuwepo na mashamba darasa ya mazao yanayokubali katika maeneo yao ili wapate elimu ya pamoja kwa ajili ya kuwasaidia katika kuongeza tija na uzalishaji.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kukosekana kwa nyongeza ya mwaka kwa Walimu na wafanyakazi wengine (annual increment) kunapelekea wakati wakistaafu wanakosa haki yao ya msingi ya mafao ya kijumla, sambamba na pension yao wakati watakapostaafu.

Je, Serikali inawaambia nini Walimu ambao tayari wamestaafu mwaka jana na mwaka juzi ndani ya awamu hii ambao sasa wamekosa hiyo increment ambapo inaenda kuathiri mafao yao ya kustaafu na pension yao ya kila mwezi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masoud kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe maelezo kwa ufupi sana. Jambo la kwanza kuna tofauti kati ya madai na nyongeza ya mishahara. Tumesema kwenye nyongeza ya mshahara Serikali inapanga bajeti kulinga na mwaka husika wa bajeti. Kama hujaongezewa hilo sio deni la hupaswi kudai na nimejibu kwenye jibu la msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, madeni, haya ndio haki ya watumishi kudai na utaratibu wake ni kama nilivyoeleza namna ya kuweza kuyafidia. Walimu hata juzi Waziri wa Nchi ametoa tamko hapa, hata kupandisha madaraja imeelekezwa vizuri kwenye Waraka wa Waziri kwamba ni muhimu izingatiwe kama kuna watu wanakaribia kustaafu na hawajapandishwa daraja na wamekidhi vigezo, tuanze na hao.

Kwa hiyo hilo jambo la kuwa karibu na kustaafu limezingatiwa na hakuna mtu atakayenyimwa haki yake, deni ni deni hata kama mtu atakuwa amestaafu, atapewa na tutakapoanza kulipa madeni kimsingi tunaangalia wale wenye shida, wale waliostaafu ndiyo tunaanza kuwalipa na wengine wanaendelea. Ahsante.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nina swali moja dogo la nyongeza. Annual increment ipo kisheria, kutowapatia wafanyakazi annual increment kunasababisha wakati atakapostaafu kupungua, kupunjwa kwa mafao yao sambamba na kupungua kwa pension zao za uzeeni na wanasema kwamba, hii awamu ya kuwasaidia wanyonge na maskini.

Je, hawaoni sasa kuendelea kutowapatia annual increment wafanyakazi hawa wanaendelea kuwapunja, kuwadhulumu wanyonge hawa na lini Serikali wataacha tabia hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Masoud, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudie tena kujibu kile nilichojibu kwamba, suala la annual increment mwaka 2017/2018, Serikali imeshalipa annual increment kwa watumishi wote wa umma bila kujali kada zozote. Pia nimesema imelipa zaidi ya bilioni 72, lakini sio kwamba, Serikali inawapunja ni sehemu ya mtumishi wa umma kupata motisha; tena nilitegemea kaka yangu hata angeshukuru kwamba, Serikali inawajali watumishi na ndio maana imeweza kuongeza hiyo mishahara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme jibu langu nilishalijibu, Serikali inawajali watumishi na ndio maana mwaka 2017/2018 imelipa zaidi ya bilioni 72. Ahsante.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, fedha ambayo Mheshimiwa Waziri ameitaja ya malipo ya shilingi bilioni 3 ni ile ambayo inaenda kulipwa kule Kilwa Masoko, Rasi Mshindo na Navy Command. Kuna maeneo yaliyotwaliwa na Jeshi baadhi ya wananchi wameshafariki dunia na Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa kwa fedha za ndani ikionyesha kwamba wananchi hawa tayari wamedhulumiwa na hawana chao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali utuambie ni kwa nini basi mmechukua muda mrefu hamtaki kuwalipa wananchi hawa ili hali mnaenda kutekeleza miradi mikubwa ndani ya nchi kwa fedha za ndani? Lini fedha za wananchi hawa zitapatikana?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, taarifa ya utekelezaji wa ahadi za Serikali mwaka 2006 ilieleza wazi kuna maeneo kadhaa ya Jeshi yaliyoorodheshwa ambapo wananchi wanadai fidia na Serikali ikaahidi kwamba itaendelea kulipa. Ukiangalia bajeti iliyopita shilingi bilioni 27 fedha hazikutolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atuambie bajeti yake ya kesho anawaambia nini wananchi hawa wanaolalamika kwa muda mrefu, wamekata tama na wengine wameshafariki na lakini hawana mategemeo ya kulipwa fedha zao? Naomba Waziri atuambie waziwazi wananchi hawa ambao wamekata tamaa, wanyonge hawa na ninyi ndiyo watetezi wa wanyonge watapata lini? Naomba majibu ya kweli.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Masoud Abdalah Salim, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba shilingi bilioni 3 zilizotolewa ni kwa ajili ya Rasi Mshindo kule Kilwa. Nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba kati ya fedha tulizoidhinishiwa bajeti iliyopita shilingi bilioni 20.9 ukiacha shilingi bilioni tatu ambazo zimeshalipwa shilingi bilioni 16 zimeshatengwa na kazi inayofanyika sasa hivi ni uhakiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ukichukua zile shilingi bilioni tatu na shilingi bilioni 16 utaona shilingi bilioni 19 zitatolewa katika bajeti hii ambayo tunamalizia. Kwa hiyo, hatuna shaka kwamba baada ya uhakiki maeneo mengi haya yatalipwa.

Kuhusu bajeti ijayo, namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira. Ukweli ni kwamba kama tutafanikisha kulipa shilingi bilioni 19 kati ya shilingi bilioni 20 zilizotengwa katika bajeti tunayomalizia basi bila shaka kwa sehemu kubwa tutakuwa tumetimiza ahadi zetu.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Katika majibu ya msingi ya Mheshimiwa Naibu Waziri alituambia kwamba yuko katika mkakati na mchakato wa kuendeleza Kiswahili nje ya nchi lakini inaonekana kwamba Kiswahili kinachofundishwa nje ya nchi siyo standard Swahili, siyo lugha sanifu ndani ya Tanzania ni Kiswahili cha nchi jirani. Je, wana mkakati gani wa ziada kuhakikisha Kiswahili chetu cha Tanzania ambacho ni Kiswahili sanifu (standard Swahili) ndicho ambacho kinatumika nje ya nchi na siyo Kiswahili cha nchi ya jirani?

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Masoud, Kiswahili si ni lugha, sijaelewa unamaanisha lafudhi au lugha, hebu uliza swali lako vizuri.

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, standard Swahili (Kiswahili sanifu) ndicho ambacho kinaongelewa au kinaandikwa hapa Tanzania lakini katika nchi nyingine, unapokwenda huko duniani katika nchi za Ulaya Kiswahili ambacho kinafundishwa ni cha nchi jirani siyo cha Tanzania.

MBUNGE FULANI: Kweli.

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ni kweli na ndiyo uhalisia. Mheshimiwa Naibu Waziri atuambie …

NAIBU SPIKA: Sawa, umeeleweka Mheshimiwa.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa ya kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba katika matumizi ya lugha yoyote duniani kuna kitu kinaitwa standardization, kila mtu lazima atumie lugha ambayo ni sanifu. Ndiyo maana Jumuiya ya Afrika Mashariki imeunda Kamisheni ya Kiswahili ambayo Makao Makuu yake yako Zanzibar na moja ya kazi yake kubwa ni kufanya lugha ya Kiswahili iwe na urari wa aina moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, tuna kazi pia kubwa ya kufanya kati ya sisi upande wa Tanzania Bara na upande wa Zanzibar kuoanisha baadhi ya misemo na maneno ili tusiwe na lugha mbili. Kwa mfano, jana nimeona Kamusi kutoka Zanzibar inaitwa ‘Kamusi Sanifu la Kiswahili’ wakati sisi huku Bara Kamusi haiwezi kuwa ‘likamusi’ ni ‘Kamusi ya Kiswahili’. Sasa sisi wenyewe tuna matatizo ndiyo maana inabidi tukae, Baraza la Kiswahili la Zanzibar na Baraza la Kiswahili la Tanzania wakae pamoja kwanza tuwe na lugha ya aina moja ili tuweze kuwashawishi wenzetu wa Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Baada ya majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kwamba Serikali imezuia mikesha ikiwemo ngoma na mambo mengine ili kuondokana na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI, hiyo ni dhahiri kabisa. Pili, kazi ambazo zinafanywa na Mbio za Mwenge zinaweza kufanywa na baadhi ya Watendaji wa Serikali katika ngazi mbalimbali na tumeshuhudia uzinduzi wa miradi ya aina mbalimbali ukifanywa na watendaji hao. Je, kwa kuwa condom zimekuwa zikigaiwa maboksi na maboksi katika mikesha ya Mwenge, hamwoni sasa kuna haja Mwenge wa Uhuru ukawekwa makumbusho badala ya kutembezwa katika maeneo mbalimbali? (Makofi/ Kicheko)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (WATU WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimeweza kujibu wakati najibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mwengenge wa Uhuru una mambo mengi, mwenge wa uhuru ni tochi ambayo inaangaza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo mengi ambayo yanafanwa na mwenge wa uhuru kama ambavyo nimesema. Hii itaendelea kuwa alama yetu. Mbio hizi zitaendelea kukimbizwa kila mahali kwa sababu mwenge huu wa uhuru tukisema kwamba tunauhifadhi, je, hii miradi, kwanza nikielezea faida moja, mwenge wa uhuru unakagua miradi mbalimbali, miradi ambayo kama mwenge wa uhuru usingepita; sasa hivi tunaona kwamba Wakandarasi wengi wamekuwa wanahofu, wanajitahidi kuhakikisha kwamba mwenge unapofika mahali pale, ukute ule mradi wake uko vizuri. Sasa kama tukisema kwamba tuuhifhadhi huu mwenge wa uhuru, Mheshimiwa Mbunge nadhani tutakuwa hatujafanya kitu. Faida ambazo zinapatikana na mwenge wa uhuru ni kubwa kuliko vile ambavyo tunafikiria. Ahsante. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri, amefanya kazi nzuri sana na ametoa majibu fasaha kabisa. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, napenda tu niwakumbushe na niwarudishe kwenye dhana yenyewe ya mwenge wa uhuru. Tunapokwenda kwenye dhana ya mwenge wa uhuru tujue falsafa yake na chanzo chake ndani ya Taifa letu. Sasa tukifika mahali hapo, nadhani sisi wote tutakuwa na uelewa wa pamoja. Tukumbuke kwamba, chombo hiki mwenge wa ukuru ni ukumbusho wa uhuru wa Taifa letu la Tanzania ambao uliasisiwa na Baba wa Taifa hili la Tanzania, ukiwa na falsafa ya kujenga umoja, mshikamano, ukombozi ndani ya Taifa letu na Bara zima la Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenge huu umekimbizwa miaka hii yote na faida ya kuendelea kuenzi falsafa ya Baba wa Taifa imekuwa ni mfano mzuri hata kwenye Mataifa mengine kwenye Bara la Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mmeona, ziko nchi katika Bara la Afrika kwa sasa nao wameanza kuwa na mienge yao katika matukio ya Kitaifa ambayo yanaashiria mambo yao ya msingi na ya muhimu kabisa katika Taifa lao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, hakuna jambo linalofanywa wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru ambalo halijaratibiwa kwa faida ya Watanzania tu ni kwa faida ya Taifa letu na nchi nzima kwa ujumla, hata Mataifa ambayo yako nje ya mipaka ya nje ya mipaka ya nchi ya Tanzania. Tuungane pamoja, tuenzi falsafa ya mwenge wa uhuru, tumuenzi Marehemu Baba wa Taifa na chombo hiki ni muhimu katika historia ya ukombozi wa Taifa letu. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nina maswali mawili madogo kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri ametuambia kwamba kila upande wa Muungano una sheria, kanuni na miongozo yake ya shughuli za uvuvi lakini wakati huohuo wavuvi wetu wanaotoka Zanzibar kuja kuvua huu upande wa pili wa Tanzania Bara maeneo ya Bagamoyo, Tanga na maeneo mengine baadhi ya maeneo wanatozwa tozo ya Sh.10,000 hasa pale Tanga askari wa Marine Park wanalazimisha kutoa tozo hiyo kwa mwezi kwa kila mvuvi. Je, hiyo ni sheria, kanuni ama miongozo kuwatoza tozo ndugu zenu wa damu wa Zanzibar ya Shilingi 10,000? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Masoud, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, wavuvi wanaotoka upande wa Tanzania Visiwani kuja Tanzania Bara katika mwambao na wanatozwa tozo mbalimbali. Ameuliza maswali hapo akitaka kujua hizi tozo zipo kwa mujibu, moja, wa sheria; mbili, wa kanuni; tatu, miongozo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa jambo hili laweza kuwa ni geni, naomba tu nichukue hoja hii ya Mheshimiwa Mbunge. Nataka nimhakikishie kwa sababu ameitaja Marine Park and Reserve Unit ambayo iko ndani ya Wizara yangu, nitalifuatilia kutaka kujua uhalali na inatozwa kama alivyouliza katika maswali yake hayo matatu kwa mujibu wa ama sheria, kanuni au mwongozo gani. Ahsante sana.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu ya Mheshimiwa Waziri anasema kutakuwepo na uchaguzi wa huru na haki. Nataka nimwambie tu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 3(1) inasema, “Tanzania ni nchi ya kidemokrasia yenye kufuata mfumo wa vyama vingi.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na malalamiko kila kona juu ya tabia mbaya iliyoonekana, kuhusu kuondolewa kwa Wagombea wa Upinzani hasa katika uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa unaofanyika tarehe 24 kwa vyama vya ACT Wazalendo, CUF, CHADEMA, NCCR-Mageuzi. Imeonekana huu ni mkakati maalum wa Serikali katika kudhoofisha upinzani hapa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri utuambie, mna makakati gani wa ziada kuhakikisha kwamba tabia hii mbaya, chafu iliyofanywa makusudi na Serikali kwamba wagombea hawa wa upinzani wanarejeshwa na wanashiriki uchaguzi tarehe 24 mwaka huu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili,…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Masoud, hilo siyo swali.

MBUNGE FULANI: Ni swali.

MWENYEKITI: Endelea swali lingine.

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Waziri mhusika, Mheshimiwa Jafo alisema, wasimamizi wa uchaguzi na wote waliohusika kuwaondoa Wagombea wa Upinzani, wasilikilize malalamiko hayo na baadaye kutoa haki ambayo italeta tija katika uchaguzi huu ndani ya mfumo wa vyama vingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uniambie, pamoja na kauli ya Waziri ambapo hadi sasa baadhi ya watendaji hawa, wasimamizi wanakimbia katika ofisi: Je, mna mkakati gani wa kuhakikisha kwamba maandalizi haya yataweza kufanikisha uchaguzi huu na ukawa wa haki na huru?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Hili swali ni muhimu kwa ajili ya uelewa. Nalitumia jukwaa lako ili uniruhusu nitoe elimu pia kwa wale wote ambao hawajaelewa utaratibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni kwamba Waheshimiwa Wabunge wamelalamika sana kwenye Bunge hili, naomba niwaarifu kwamba Wabunge hawana haki ya kuweka pingamizi wala kulalamikia uchaguzi kama wametendewa haki ama lah! Wenye haki ya kulalamika ni wale watu wote ambao walijaza fomu na kusema wameondolewa. Utaratibu umeainishwa vizuri kwenye Kanuni yetu na Waheshimiwa Wabunge na Vyama vya Siasa wamepewa Kanuni hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, muda wa vipingamizi haujaisha. Kanuni imeeleza, baada ya uteuzi, kuanzia tarehe 5 mpaka tarehe 6 ambayo ilikuwa ni jana, wale wote ambao wamekuwa hawajaridhika na uteuzi au kuondolewa ama kuteuliwa kugombea walipaswa wapeleke pingamizi kwenye Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi. Kama hawajaridhika na maamuzi hayo, pia wanayo fursa mpaka tarehe 9 kwenda kupeleka pingamizi kwenye Kamati ya Rufaa.

Pia kama hawataridhika na maamuzi ya Kamati ya Rufaa ambayo inapatikana kwenye ngazi ya Wilaya, wanayofursa ndani ya siku 30 kwenda kwenye Mahakama yoyote kuanzia na wilaya kwenda kuweka pingamizi kuweza kupata haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hayupo hapa Bungeni leo, lakini jana alikuwa Singida. Yanayozungumzwa Bungeni na kule site hali ni tofauti sana. Ameenda Manyara na sasa hivi ninavyozungumza yuko Iringa, ataenda Njombe. Tumetuma watu kule Liwale na Moshi. Mazungumzo mengi ya Waheshimiwa Wabunge humu ndani yanatofautiana sana na hali halisi kule site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, yaliyozungumzwa hapa kuna Wabunge wamechukua clip wameweka kwenye mtandao. Nimeuliza kwa mfano Tarime Mjini, Mheshimiwa Mbunge alitoa taarifa hapa kwenye clip akisema wagombea wote wameondolewa, siyo kweli. Taarifa za leo asubuhi!

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge, maelekezo ya Mheshimiwa Waziri wa nchi ni kwamba, Kanuni inaelekeza, yule ambaye hajaridhika na uteuzi wake apeleke pingamizi kwenye vyombo vile na asiporidhika ndiyo aseme. (Makofi/ Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwatie moyo Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Watanzania, utaratibu unaeleweka, lazima ufuatwe…

MBUNGE FULANI: Wamefunga Ofisi.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SRIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): …na uchaguzi huu utakuwa ni huru na haki kwa wale ambao watazingatia taratibu na sheria za uchaguzi.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Katika maelezo ya Mheshimiwa Waziri, yaani majibu yake, anasema kwamba ajali zimepungua lakini vifo vimeongezeka.

Mheshimiwa Spika, kwa idadi ya vifo ambavyo wamevitaja kuanzia mwaka 2017, 2018, 2019 hadi Juni inaelekea kwamba jumla ya vifo vilivyotokea ni 1,270. Hawa ni Watanzania, idadi ni kubwa. Mheshimiwa Naibu Waziri tuambie hasa mkakati wa ziada wa mwarobaini ili kukomesha vifo hivi visiendelee tena. Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, niliposoma takwimu tokea mwaka 2016 mpaka 2019 kwa ujumla ajali, vifo na majeruhi vyote vinaonekana kushuka, lakini takwimu ambazo nilisema kwamba vifo vinaongezeka ni za kipindi cha Januari mpaka Juni 2019. Kwa hiyo, ni kipengele kimoja na cha kipindi kimoja ambacho tumeona kwamba upande wa vifo umeongezeka, lakini kwa ujumla ajali zimepungua.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimeeleza, haya ni mafanikio ya usimamizi wa Sheria ya Usalama Barabarani ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupunguza ajali za barabarani ambao tumeuandaa kupitia Baraza la Usalama la Taifa kwa maana mkakati huu umegusa katika maeneo mengi. Moja, ndiyo hili eneo ambalo nimezungumza katika jibu langu la msingi kwamba ni kuhakikisha kwamba Askari wetu wanasimamia Sheria ya Usalama Barabarani kwa nguvu zote na kwa mujibu wa sheria.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inapotokea athari ya vifo au majeruhi kwa wananchi waliopata milipuko ya mabomu au kuokota mabomu, Serikali mara nyingi huwa wanatoa fidia kama kule Mbagala na Gongo la Mboto. Mheshimiwa Waziri utakumbuka kwamba kule Tunguu kuna watoto waliokota mabomu na walifariki wawili na wananchi wengine walipata majeruhi. Narudia hili kwa Mheshimiwa kwamba wale watu wataweza kupewa fidia. Ni kwa nini basi hadi leo wale watoto wawili au na majeruhi kule Tunguu ambao walipata athari hii hawajapata fidia? Na ni lini watapata fidia yao?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea tatizo hili lililotokea Tunguu, nitamuomba Mheshimiwa Mbunge anipe uhakika wa suala lenyewe kwa maandishi ili liweze kufanyiwa kazi. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Waziri ni mara kadhaa Serikali imekuwa ikichukua ahadi ikisema kwamba itaweza kujenga Bandari ya Wete, hayo ni masuala ya mdomoni lakini ukija kwenye vitabu halisi, kwenye Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kimataifa kwenye Vote 34 fedha hizo haziko, mmekuwa mkidanganya mara nyingi watu wa Pemba. Mmekuwa mkisema uongo mchana kweupe bila giza. Kwenye Vote 34 ndiyo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, fedha hizo huwa haziko, hamtengi lakini mmekuwa mkisema mdomoni tu. Mtuambie hasa mna mkakati gani wa ziada muone kama fedha hizi mara hii mtazipeleka na bandari hii ya Wete mtaenda kujenga. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimualike tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tuonane uone ile document ya retreat nzima. Ninapozungumza juu ya miradi 17 ambayo kwa Afrika Mashariki ambayo inasimamiwa na wakuu wa nchi, kuna commitment ya jumla ya dola 61,000,212, ni fedha nyingi sana na ukiangalia kwa undani utaona miradi ilivyochambuliwa na hatua zinazokuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ukiiangalia hii document na hii commitment ambazo tunzisema hapa ni commitment ambazo zinachukua muda mrefu na kuna action plan. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge, nikuombe tu tuonane ili kwa pamoja tuzungumze ili upate picha, na uweze pia kuisema kazi nzuri Serikali inayofanya kuhusu maendelezo ya bandari hii muhimu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, nina maswali mawili ya nyongeza kama yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza; kumekuwepo na hofu na malalamiko makubwa juu ya mbinu chafu ambazo zimeweza kujitokeza hivi karibuni wakati wa urejeshaji wa fomu kwa vyama vya upinzani kuambiwa kwamba viongozi hao/wagombea hao wa upinzani hawana sifa jambo ambalo limekuwa likileta hisia mbaya kwamba Chama cha Mapinduzi kinataka ibaki peke yake katika uchaguzi.

Je, huoni Mheshimiwa Waziri mbinu hii chafu ya kusema wagombea wa upinzani hawana sifa kwa hila na ujanja kutaweza kupelekea uchaguzi huu usiwe wa haki na huru na kweli atakayeshinda mtatangaza? La kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; kumekuwa na taratibu ambazo zimekuwa zikiendelea hivi sasa katika baadhi ya maeneo kuanza kufanya kampeni kwa njia ya ujanja ujanja. Mfano, pale Morogoro kumekuwa na uzinduzi wa Morogoro ya Kijani huku wakieleza kwamba tunaelekea chaguzi za Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji wakati uchaguzi uko Oktoba.

Je, ni kwa nini basi matangazo haya, mabango haya na utaratibu huu unaofanywa kwa upande mmoja tu wa Chama Tawala usidhibitiwe mapema ili kutuondoa na matatizo ambayo yanaweza kujitokeza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kwanza hakuna mbinu chafu. Utaratibu wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa utatangazwa tarehe na mwenye mamlaka, uwekwe utaratibu wa kujiandikisha kwa muda utakaotajwa, yatabandikwa majina kwenye mbao za matangazo kila watu watahakiki wakazi katika mtaa husika na kijiji au kitongoji, wataenda kwenye kampeni sawa kwenye vyama vyote na uchaguzi utafika watachaguliwa ila kwa sababu Mheshimiwa Masoud anajua kwamba watakaochaguliwa wengi wagombea wa Chama cha Mapinduzi hiyo ndiyo hofu uliyonayo kwa sababu kazi nzuri ya Chama cha Mapinduzi ambayo imefanywa chini ya Dkt. John Pombe Magufuli, miradi mikubwa ya kimkakati, Rais ambae ni wa mfano katika Afrika na dunia anayekutana na makundi mbalimbali, uchaguzi ukitangazwa uwezekano mkubwa wa kupata asilimia 98 wagombea wa Chama cha Mapinduzi ndiyo huo ambao unakutisha, lakini tutakwenda kwenye uchaguzi, watu wako wajiandae vizuri, kanuni zipo, kuna Kamati za Rufaa, kama hujaridhia unaweza ukaenda Mahakamani ukapata haki yako Mheshimiwa Mbunge usiwe na hofu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge anauliza kuanza kufanya kampeni na CCM ya Kijani. Hapa ni mipango ya Chama cha Mapinduzi. Chama hiki ni Chama Tawala, kinakagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na kujipanga na uchaguzi ujao. Chama makini, chama kikongwe lazima kiwe na mbinu nyingi kila wakati na ndizo zonachanganya watu akiwepo Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachofanyika na CCM wanaita wanachama wao, wanakagua kadi za uanachama, wanapata taarifa ya uchaguzi, usiwe na hofu na hata hivyo ukiangalia CHADEMA wale CHADEMA ni msingi walikuwa Katavi, wameenda Rukwa, wapo kila mahali tuna taarifa hizo na wanafanyakazi.

Sasa ndugu yangu Mheshimiwa kama wewe hujajipanga usiwaonee nongwa wenzako. CCM ipo kazini, CCM ya Kijani itaendelea kila mahali hata mimi Bunge likiaihirishwa nifanya Ukonga na nakushauri uende kwenye chama chako andaa mkakati. Watanzania wake mkao tayari, Serikali ya Chama cha Mapinduzi iko makini imejiandaa, sheria zitafuatwa, kanuni zitafuatwa na sheria zipo. Kama hujaridhika mahali popote uko aggrieved unakeenda Mahakamani lakini uchaguzi huu utakuwa uchaguzi mzuri sana, hofu yako nikutoe, wananchi ndiyo watakaochangua, wana macho wanaona, wana masikio wanasikia, CCM ndiyo habari ya mjini. Ahsante sana. (Makofi)