Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Masoud Abdalla Salim (17 total)

MHE. MASOUD ABDALLA SALIM aliuliza:-
Hali ya maisha ya wastaafu wetu ni mbaya sana na Serikali imeshindwa kuongeza pensheni zinazolingana na gharama halisi za maisha kwa sasa.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha pensheni za wastaafu hao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdalla Salim, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha viwango vya pensheni kwa ajili ya kuwapunguzia wastaafu makali ya ongezeko la gharama za maisha. Ili kukabiliana na changamoto za ugumu wa maisha kwa wastaafu, Serikali imekuwa ikiongeza pensheni kwa wastaafu pale ambapo hali ya uchumi inaruhusu.
Kwa mfano, mwaka 2004 pensheni ilikuwa shilingi 21,606.05 ambayo iliongezwa hadi shilingi 50,114.43 kwa mwezi wa Julai, 2009 sawa na ongezeko la 132%. Mwezi Julai, 2015 Serikali imeongeza pensheni hadi kufikia Sh. 100,125.85 sawa na ongezeko la 100%.
Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto za kiuchumi zilizopo kuanzia mwaka 2004 hadi 2015 kiwango cha pensheni kimeongezeka mara tano na Serikali itaendelea kuboresha pensheni za wastaafu kwa kadiri uchumi wa nchi utakavyokuwa unaimarika.
MHE. MASOUD ABDALLA SALIM aliuliza:-
Kumekuwepo na malalamiko mengi ya walimu kulipwa mishahara midogo ambayo hailingani na gharama halisi za maisha:-
Je, Serikali ina mikakati gani ya kuboresha maslahi ya walimu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdalla Salim, Mbunge wa Jimbo la Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mshahara wa Watumishi wa Umma wakiwemo walimu hailingani na gharama halisi za maisha. Hata hivyo, Serikali imekuwa ikitoa nyongeza ya mishahara kila mwaka kwa kadri hali ya uchumi inavyoruhusu. Aidha, wakati wa kutoa nyongeza hiyo ya mishahara walimu hupewa nyongeza kubwa kuliko watumishi wengine wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2007/2008 hadi mwaka 2015/2016, mshahara wa walimu wenye cheti au astashahada uliongezeka kutoka shilingi 163,490/= hadi kufikia shilingi 419,000/= kwa mwezi ambayo ni sawa na asilimia 156.28.
Kwa upande wa mwalimu mwenye stashahada, mshahara uliongezeka kutoka shilingi 203,690/= hadi shilingi 530,000/= ambayo ni sawa na asilimia 160.20.
Kwa upande wa mwalimu mwenye shahada mshahara uliongezeka kutoka shilingi 323,900/= hadi kufikia shilingi 716,000/= sawa na asilimia 121.05.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Serikali inafanya tathmini ya kazi au job evaluation katika utumishi wa umma ili kubaini uzito wa kazi kwa watumishi wa umma wakiwemo walimu ili kupanga upya mishahara kwa kulingana na uzito wa kazi. Kazi hii imeanza mwezi Oktoba, 2015 na inatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 15 ijayo.
MHE. MASOUD ABDALLA SALIM aliuliza:- Ajira iliyotarajiwa kuongezeka kutokana na ukuaji wa sekta ya viwanda haijafikiwa hasa baada ya viwanda vingi kubinafsishwa na kuachwa bila kuendelezwa:-
Je, Serikali inasema nini kuhusu hili?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdalla Salim, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nia njema kabisa Serikali ilibinafsisha viwanda na mashirika ya umma ikiwa na matumaini kuwa sekta binafsi ingeliweza kuendesha taasisi hizo kwa faida na kulipa kodi kwa Serikali, kuzalisha bidhaa au huduma na kutoa ajira kwa wananchi. Pamoja na malengo hayo Serikali ililenga kuachana na shughuli za biashara ikielekeza nguvu zake katika shughuli zake za msingi za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Masoud, makampuni mengi yaliyobinafsishwa hayakufanya vizuri, ikiacha mfano wa makampuni machache yakiwemo Tanzania Breweries, Morogoro Polister ambayo inaitwa Twenty First Century na Tanzania Cigarette Company.
Mheshimiwa Naibu Spika, tathimini inayoendeshwa na Wizara yangu kwa kushirikiana na Msajili wa Hazina juu ya viwanda, mashamba na mashirika ya Serikalil yaliyobinafsishwa kuanzia mwaka 1992 inadhihirisha ukweli tunaoujua kuwa wengi kati ya waliyopewa taasisi hizo hawakutekeleza mikataba ya mauziano kikamilifu. Hivyo tunawafuatilia kwa karibu wale wote waliopewa mashirika ya umma kwa utaratibu wa ubinafsishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo letu ni kuhakikisha makampuni yote haya yanazalisha kwa tija ili tupate bidhaa, kodi ya Serikali na ajira kwa wananchi wa Tanzania. Wale wote watakaobainika kukiuka makubaliano yaliyomo katika mikataba ya awali, hatua stahiki zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuvitwaa viwanda au mashirika hayo na kutafuta Wawekezaji mahiri wa kuviendeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutimiza adhma ya kutoa ajira kwa Watanzania, Wizara inafanya yafuatayo chini ya viwanda vidogo na vya kati unaoshirikisha SIDO na Halmashauri za Wilaya na Mikoa tunahamasisha shughuli za ujasiriamali ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani mazao na kilimo, uvuvi na ufugaji huku Mikoani.
Pia kupitia mamlaka zetu za EPZA, TIC na NDC tunakaribisha na kuwaongoza wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika shughuli za kutoa ajira zaidi. Serikali kupitia Wizara yetu inaboresha mazingira ya uwekezaji hali itakayowajenga imani wawekezaji na kupelekea kupanua shughuli zao zaidi za kibiashara kupitia njia hii ajira zaidi itaongezeka.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-
Moja ya majukumu ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa mujibu wa Ibara ya 130(c) ya Katiba ya nchi ni kufanya uchunguzi juu ya mambo yanayohusu uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora:-
Je, ni kwa kiasi gani Tume imefanikiwa kutekeleza jukumu hilo kwa kipindi cha mwaka 2010 - 2016?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora katika majukumu yake kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2010 - 2016 ilipokea na kuyachunguza jumla ya malalamiko 13,709. Kati ya malalamiko hayo, malalamiko 6,169 yalihitimishwa na malalamiko 7,540 yanaendelea kuchunguzwa. Mchanganuo wa malalamiko ni kama ifuatavyo:-
(i) Migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wawekezaji, wakulima na wafugaji, wananchi wa maeneo ya hifadhi;
(ii) Matumizi mabaya ya madaraka kwa watendaji;
(iii) Ukatili dhidi ya wanawake na watoto;
(iv) Ucheleweshwaji wa haki kwa mahabusu na wafungwa; na
(v) Matumizi ya nguvu kwa vyombo vya dola.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na taarifa hiyo, katika kipindi cha mwaka 2010 - 2016 Tume ilifanya tafiti kuhusu haki za watoto, ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi, kutoa elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora, kutembelea magereza na kufanya uchunguzi wa matukio ya uvunjwaji wa haki za binadamu.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA (K.n.y. MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM) aliuliza:-
Kumekuwepo na ajali nyingi zinazosababisha vifo na majeruhi barabarani, baharini na kwenye maziwa.
Je, ni ajali ngapi zimetokea barabarani, baharini na kwenye maziwa kuanzia Januari, 2015 hadi sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdalla Salim, Mbunge wa Mtambile, lililoulizwa kwa niaba yake na Mheshimiwa Kakunda Joseph, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipindi cha Januari, 2015 hadi Februari, 2016 jumla ya ajali zilizotokea ni 9,864 ambazo zimesababisha vifo 3,936 na majeruhi 9,868 katika Mikoa yote ya Tanzania Bara.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi kama hicho jumla ya ajali 15 za baharini na kwenye maziwa zilizotokea, ambapo tisa zilitokea baharini na sita zilitokea katika maziwa. Katika ajali hizo, jumla ya watu 24 walipoteza maisha na watano walijeruhiwa.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-
Uvuvi ni miongoni mwa sekta inayochangia Pato la Taifa, lakini Serikali imekuwa na kigugumizi cha kuboresha sekta hii wakati tukielekea katika Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati.
Je, Serikali ina mkakati gani madhubuti wa kuboresha sekta ya uvuvi nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeendelea kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kutengeneza zana za uvuvi. Hadi sasa jumla ya viwanda vitatu vya kutengeneza boti aina ya fibre glass na viwanda viwili vya kutengeneza nyavu vimeanzishwa. Aidha, viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi 48 vinavyojumuisha viwanda vikubwa 15 na vidogo 33 pamoja na maghala ya kuhifadhi mazao ya uvuvi 38 yameanzishwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Sambamba na hilo Serikali ikishirikiana na sekta binafsi inafanya juhudi ya kutafuta wawekezaji wa kujenga viwanda vya kuchakata samaki aina ya jodari katika huu Ukanda wa Pwani wa Bahari ya Hindi, hili likifanikiwa litawezesha wavuvi kuongeza thamani ya mazao ya samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imedhamiria kuongeza uzalishaji wa Samaki kupitia ufugaji wa samaki (aquaculture) kutoka metriki tani 10,000 mpaka metriki tani 50,000 ifikapo mwaka 2020. Aidha, Serikali ina dhamira ya kuanzisha vituo vipya vitatu na kuboresha vituo vingine 15 vya uzalishaji wa mbegu bora za samaki, kushirikisha sekta binafsi na taasisi za kitafiti katika kuboresha teknolojia na uzalishaji wa mbegu na chakula bora cha samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hatua zake za kuendeleza uvuvi wa bahari kuu, Serikali imekamilisha mazungumzo kati yake na Mamlaka ya Bandari ya Dar es Salaam ambapo gati namba sita litatumiwa na meli zinazovua katika ukanda wa uchumi wa bahari, ili kushusha samaki. Aidha, juhudi za ujenzi wa bandari ya uvuvi zinaendelea ambapo tayari mtaalam elekezi wa kufanya upembuzi yakinifu amepatikana.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-
Serikali imesema ina mkakati wa kujenga viwanda katika Mkoa wa Mtwara, lakini njia ya usafirishaji wa mizigo inayotumika ni barabara tu hali inayosababisha barabara hiyo kuwa na uwezekano wa kuharibika kwa haraka:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha meli ya mizigo itakayotoka Dar es Salaam kwenda Mtwara ili kuinusuru barabara hiyo isiharibike?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa uwepo wa huduma mbadala za meli za mizigo na abiria kati ya Dar es Salaam na Mtwara na maeneo mengine ya mwambao ni jambo muhimu kwa maendeleo na kuzifanya barabara zidumu kwa muda mrefu zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wa mahitaji ya huduma za usafiri wa majini katika mwambao wa bahari yetu ni fursa kwa sekta binafsi nchini. Serikali kwa upande wake inaendelea kujenga mazingira wezeshi na kuhamasisha sekta binafsi kutumia fursa hii kutoa huduma za usafiri wa majini katika mwambao kwa kutumia meli za kisasa. Hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa kwa lengo la kuchochea sekta binafsi nchini kufanya uwekezaji katika huduma hii. Moja ya hatua hizo ni kuzuia meli za kigeni kujiingiza katika usafirishaji wa shehena katika maeneo ya mwambao yaani cabbotage restriction ambapo lengo la zuio hili ni kuwalinda wawekezaji wa ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuendelea kutoa wito kwa wawekezaji kuwekeza katika vyombo vya kisasa vya usafiri wa majini ili kutoa huduma ya usafiri katika maeneo ya mwambao wa Tanzania ikiwemo Mtwara.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-
Wakulima wamezitumia vyema mvua kwa kulima mazao ya chakula na biashara lakini wanaendelea kupata hasara kubwa kwa kukosa masoko ya uhakika:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa ziada wa kuwapatia wakulima masoko ya uhakika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, Mbunge wa Jimbo la Mtambile kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inatambua changamoto ya upungufu wa masoko ya uhakika kwenye mazao ya chakula yanayozalishwa kwa ziada hapa nchini pamoja na hasara ambayo wanaweza kupata kwa kukosekana masoko hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati ya Wizara katika kupambana na hali hii ni kuanzisha Mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani ambao unawasaidia wakulima kutunza mazao yao sehemu salama huku wakisubiria bei itakayowapa faida. Vilevile kupitia mfumo huo, wakulima wanahamasishwa kujiunga na SACCOS zilizoko ndani ya AMCOS zinazowasaidia kupata mikopo yenye riba nafuu ili kukidhi mahitaji yao kwa wakati wanaposubiri kuuza mazao yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu pia unatia hamasa kwa wakulima kuwa na soko na sauti ya pamoja ambayo inapelekea kuuza mazao yao kwa bei nzuri na siyo kiholela kama ilivyozoeleka kwa wakulima wengi. Pia inawasaidia wafanyabiashara kutumia muda mfupi kununua bidhaa kutoka sehemu moja badala ya kununua kwa kuzunguka kutoka kwa mkulima mmoja mmoja. Hii yote inasaidia kuimarisha masoko ya mazao ya uhakika. Aidha, Wizara itaendelea kuwaelimisha na kuhamasisha wakulima kuuza mazao yaliyokwisha ongezwa thamani ambapo itasaidia kuongeza ubora na bei nzuri za bidhaa hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutafuta masoko nje ya nchi na kutoa vibali vya kusafirisha mazao na bidhaa za mazao ya chakula kwa wafanyabiashara na kuwahamasisha wafanyabiashara wa ndani kununua sehemu zenye ziada na kuuza sehemu zenye upungufu. Lakini pia Serikali inasisitiza juu ya kufufua viwanda ambavyo vitaongeza soko la uhakika la bidhaa zinazozalishwa na wakulima ili kuendana na mikakati ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali na wadau mbalimbali wa kilimo wanaendelea kuhamasisha wakulima kutafuta masoko ya uhakika kama vile kilimo cha mkataba na kuboresha miundombinu ya masoko na barabara ili kuwaunganisha wakulima na masoko. Hii itasaidia kurahisisha usafirishaji wa mazao kutoka mashambani kwenda sokoni, hivyo kupunguza gharama za usafirishaji, muda wa kusafirisha, kiwango cha uharibifu na upotevu wa mazao baada ya mavuno.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-
Kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa wastaafu ambao wakati wa utumishi wao walilitumikia Taifa hili kwa uaminifu na uadilifu mkubwa lakini kumekuwa na hali ya kucheleweshewa mafao yao ya uzeeni yasiyolingana na kupanda kwa gharama za maisha, hali inayosababisha kuwa na maisha magumu.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mafao ya uzeeni ili kuondoa malalamiko hayo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mafao ya kustaafu hukokotolewa kwa kutumia muda wa utumishi ambao mtumishi alikuwa katika utumishi na mshahara ambao mtumishi alikuwa analipwa kabla ya tarehe ya kustaafu. Ukokotoaji huo ndiyo unaotoa kiwango cha kiinua mgongo anachostahili kulipwa kwa mkupuo na kiwango cha pensheni atakachoendelea kulipwa kila mwezi. Kwa utaratibu huo, viwango vya pensheni hutofautiana kati ya mstaafu mmoja na mwingine kutegemea muda wake wa utumishi na mshahara kabla ya tarehe kustaafu. Iwapo katika ukokotoaji, itajitokeza pensheni ya mstaafu kuwa chini ya kima cha chini cha kiwango cha pensheni anacholipwa, mstaafu atalipwa kima cha chini cha pensheni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha viwango vya pensheni ili kukidhi mahitaji muhimu ya kila siku ya wastaafu. Kwa kutambua hivyo, Serikali iliboresha viwango vya pensheni mwezi Julai 2015 ambapo kima cha chini kiliongezwa kutoka shilingi 50,114 hadi shilingi 100,125 kwa mwezi. Hata hivyo, maboresho ya viwango vya pensheni kwa wastaafu yasiyoendana na maboresho ya miundombinu ya kiuchumi na huduma za kijamii hayawezi kuondoa malalamiko ya wastaafu wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunatambua kwamba mapato ya Serikali ni madogo ikilinganishwa na mahitaji muhimu ya kitaifa. Kwa kutambua kuwa ni miaka miwili tu tangu tuongeze kima cha chini cha pensheni, Serikali kwa sasa imejielekeza zaidi katika kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, nishati ya umeme, maji, huduma za afya na elimu. Maeneo haya yana uhitaji mkubwa sana wa rasilimali fedha. Aidha, matokeo mtawanyiko ya maboresho ya maeneo haya yanaleta unafuu mkubwa wa maisha ya wastaafu wetu na wananchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali inafanya juhudi za makusudi za kuboresha mifumo ya kukusanya mapato sambamba na kuboresha miundombinu ya kiuchumi na kijamii ili kujenga uwezo wa kuboresha maisha ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nyongeza ya pensheni kwa wastaafu, mishahara na maslahi mazuri kwa watumishi wa umma itawezekana tu kama tutafanikisha mikakati na azma ya Serikali ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wetu. Hivyo basi, tuendelee kuiunga mkono Serikali yetu katika juhudi zake za kujenga uchumi imara, uchumi wa viwanda ambao ndiyo msingi mkuu wa kuimarisha mapato ya Serikali.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-
Tanzania ni moja kati ya nchi wanachama wa Nchi za Kiafrika wa Kujitathmini Wenyewe kwa Vigezo vya Utawala Bora (APRM).
Je, Serikali imejitathmini kwa kiasi gani katika dhana nzima ya demokrasia na utawala bora, utawala wa kisiasa, usimamizi wa uchumi na maendeleo ya kijamii?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika (APRM) ulibuniwa na Wakuu wa Nchi za Kiafrika kwa lengo la kuimarisha utawala bora katika nchi zao. Nchi hujitathmini yenyewe kwanza na kutoa ripoti na mpango kazi na kisha nchi nyingine zilizojiunga katika mchakato huu huja kuitathmini nchi hiyo na kutoa ripoti ya nchi ya utawala bora. Tanzania ni nchi mojawapo kati ya nchi 35 zinazoshiriki katika mchakato huu ambapo ilijiunga mwaka 2004 na Bunge la Tanzania liliridhia makubaliano hayo mwaka 2005.
Mheshimiwa Spika, katika mchakato wa kujitathmini, Watanzania wa kada mbalimbali walieleza mambo bora yaliyofanywa na nchi yetu na kuonesha changamoto zilizopo. Tathmini hizi ziliangazia maeneo makuu manne ambayo ni utawala bora katika siasa na demokrasia, usimamizi wa uchumi, utendaji wa mashirika ya kibiashara na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, katika tathmini iliyofanyika na ripoti yake kutolewa mwaka 2012, baadhi ya maeneo ambayo Tanzania ilibainika kufanya vizuri ni pamoja na kuingia kwa amani katika Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa, kurithishana madaraka ya Urais kwa mujibu wa Katiba, matumizi ya lugha kuu ya Kiswahili, kuimarika kwa jitihada za kupambana na rushwa, kuboresha usawa wa jinsia, usuluhishi wa migogoro, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuwekwa wazi na mafanikio katika kupanuka kwa utoaji huduma za jamii na nyinginezo.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya changamoto za utawala bora zilizobainishwa ni pamoja na changamoto kama Tume ya Uchaguzi; ukuaji wa uchumi usiowiana na kupungua kwa umaskini; tatizo la fedha haramu na dawa za kulevya; changamoto katika utoaji wa huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na elimu iliyo bora na uhaba wa vifaa katika huduma za afya.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa uratibu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inaendelea kutekeleza hatua zenye lengo la kutatua changamoto za utawala bora zilizobainishwa kwenye Ripoti ya APRM. Inatarajiwa mwaka huu 2017, Serikali ya Tanzania itawasilisha Ripoti ya Utekelezaji wa Mpango Kazi wa APRM kwenye kikao cha Wakuu wa Nchi na Serikali wanaoshiriki mchakato wa mpango huu.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-
Imebainika kuwa ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) umeendelea kuathiri jamii ya Watanzania.
Je, Serikali ina mikakati gani ya kukabiliana na ongezeko la wagonjwa wa TB?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, TB au Kifua Kikuu ni ugonjwa wa kuambukizwa na huambukizwa kwa njia ya hewa. Ugonjwa wa TB hushambulia mapafu na viungo vingine ikiwa ni pamoja na mifupa, uti wa mgongo, ubongo, moyo, ngozi na sehemu nyingine za mwili. Kwa ujumla TB inaweza kushambulia kila kiungo katika mwili. Ugonjwa huu husababishwa na vimelea aina ya bacteria na mgonjwa akitibiwa kwa dawa tulizonazo anaweza kupona kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu yeyote anaweza kuambukizwa au kuugua TB lakini makundi yafuatayo yako katika hatari kubwa zaidi kuugua ugonjwa huu ni pamoja na watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI, watoto wadogo chini ya miaka mitano, wazee, watu wanaougua magonjwa ya muda mrefu ikiwemo saratani, kisukari, wenye utapiamlo, wafungwa, wachimbaji wadogo wadogo migodini na wale wanaotumia madawa ya kulevya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumgundua mgonjwa wa TB mapema na kumweka katika matibabu ndiyo njia kuu ya kupambana na kushinda tatizo la kifua kikuu. Hivyo basi, mikakati ya Serikali imejikita katika afua za kuongeza uwezo wetu wa kuwafikia watu wote wanaohitaji huduma za TB ili kuwagundua wagonjwa hawa mapema na kuwatibu kikamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati na hatua zinazochukuliwa na Serikali ni kama ifuatavyo:-
(a) Kufanya upimaji wa TB kwa watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI;
(b) Kuingiza teknolojia mpya nchini ya upimaji na ugunduzi wa uhakika na uharaka wa vimelea vya TB kwa kutumia Gene Xpert. Hadi hivi sasa mashine 97 zimeshafungwa katika Hospitali za Mikoa na baadhi za Halmashauri na mashine nyingine 90 zimeshanunuliwa na zinatarajiwa kufungwa kwenye Hospitali za Wilaya zilizobakia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, teknolojia hii inawezesha sasa hivi badala ya siku za nyuma ambapo mgonjwa alihitaji kupima makohozi mara tatu kwa siku tatu, sasa hivi ugunduzi unaweza ukanyika ndani ya masaa mawili badala ya siku tatu kama ilivyokuwa awali.
(c) Tumewezesha maduka muhimu na Waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala kufanya utambuzi wa dalili za TB na kutoa rufaa kwa wahisiwa wote kwenda katika mfumo wa tiba.
(d) Kufanya uchunguzi kwa wafanyakazi wote migodini na kwenye mahabusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara nyingine tena, Wizara yangu inatoa wito na kuwahimiza Waheshimiwa Wabunge kushiriki kikamilifu katika mapambano ya kutokomeza TB na kuhakikisha kwamba TB inakuwa ni ajenda yao ya kudumu katika vikao vyote vinavyoendelea na wanavyovihutubia.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-
Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizojiunga na Mpango wa Kujitathmini Wenyewe (African Peer Review Mechanism) kisiasa, kiuchumi na kadhalika.
Je, Serikali imejitathmini kwa kiasi gani hali ya uchumi wa Tanzania unaokwenda sanjari na kupungua kwa umaskini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, Mbunge wa Mtambile kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Tanzania ilifanya tathmini ya APRM na kutoa ripoti yake ambayo iliwasilishwa kwenye Kikao cha Wakuu wa Nchi mwaka 2013. Tathmini hiyo ilifanyika katika maeneo makuu manne, usimamizi wa uchumi, utendaji wa mashirika ya biashara, siasa na demokrasia na maendeleo ya jamii.
Mheshimiwa Spika, katika eneo la usimamizi wa uchumi, tathmini hiyo ilibainisha masuala mbalimbali yaliyofanywa na Serikali katika kuboresha hali ya kiuchumi ya wananchi wake ikiwa ni pamoja na ushirikishwaji wa wananchi katika kuibua miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao; kuimarisha mfumo wa kifedha ikiwa ni pamoja na kutunga Sheria ya Kuzuia Utakatishaji wa Fedha Haramu; ongezeko la taasisi za kifedha, hivyo kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa wananchi; na kuimarisha ushiriki wa nchi kwenye taasisi za kikanda kama Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Mheshimiwa Spika, pamoja na tathmini hiyo kubainisha masuala mazuri yaliyofanywa na Serikali, imebainisha pia changamoto mbalimbali za usimamizi wa uchumi. Baadhi ya changamoto zilizobainishwa na Watanzania ni ukuaji wa uchumi usio sanjari na kupungua kwa umaskini na kukosekana kwa mfumo maridhawa wa uwiano wa mapato yanayotokana na mikataba ya kiuchumi ya kimataifa.
Mheshimiwa Spika, tangu ripoti ya APRM Tanzania itolewe na kujadiliwa na Wakuu wa Nchi mwaka 2013, hatua mbalimbali zimechukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kukuza uchumi kwa lengo la kupunguza umaskini wa wananchi. Hatua hizo ni pamoja na kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya kujenga uchumi wa viwanda ambao unaendelea kutengeneza ajira na kupunguza umaskini; kuimarisha ukusanyaji, usimamizi na matumizi sahihi ya mapato ya Serikali; kudhibiti ukwepaji kodi; kusambaza umeme vijijini ili kuchochea shughuli za kiuchumi hususan viwanda vidogo vidogo; ujenzi na uboreshaji wa miundombinu; uwekezaji katika kutoa elimu bure na kuongeza bajeti ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi; na kupitia upya sera na sheria mbalimbali kwa lengo la kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji nchini na kuleta uwiano wa mapato yanayoendana na mikataba ya kiuchumi ya kimataifa.
Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kwamba inafikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Kwa juhudi hizi za Serikali, ni dhahiri kuwa umaskini utaendelea kupungua hatua kwa hatua ambapo hadi kufikia mwaka 2017 kiwango cha umaskini kimepungua na kufikia asilimia 26.3.
MHE. MASOUD A. SALIM aliuliza:-
Kwa mujibu wa Ibara ya 141(2) ya Katiba ya Nchi, Deni la Taifa maana yake ni deni lenyewe, faida inayolipwa juu ya deni hilo, fedha zilizowekwa akiba kwa ajili ya kulipa deni hilo polepole na gharama zote zinazoambatana na deni hilo:-
a) Je, Deni la Taifa hadi swali hili linajibiwa ni kiasi gani?
b) Je, mchanganuo wa fedha zilizowekwa akiba kwa ajili ya kulipa deni hilo ukoje?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kabla ya kuanza kujibu swali hili, naomba nikushukuru sana kwa safari yako muhimu uliyoifanya Jimboni kwangu Kondoa juzi tarehe 9 Juni, 2018. Mwenyezi Mungu akubariki na akupe afya njema sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, Mbunge wa Mtambile, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, hadi kufikia 30 Aprili, 2018, Deni la Taifa lilikuwa Dola za Kimarekani milioni 26,161.02 sawa na shilingi bilioni 59,480.74.
(b) Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Deni la Taifa linajumuisha deni la Serikali na deni la sekta binafsi, Serikali inawajibika kufanya malipo ya deni la Serikali na si Deni la Taifa kwa ujumla wake. Aidha, fedha kwa ajili ya malipo ya Deni la Serikali inatengwa kwa kuzingatia taratibu za kawaida za kibajeti kupitia Fungu 22. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi bilioni 1,262.42 kwa ajili ya malipo ya deni la ndani na shilingi bilioni
685.06 kwa ajili ya malipo ya deni la nje. Hivyo basi, hakuna fedha iliyowekwa akiba kwenye mfuko maalum kwa ajili ya kulipia deni la Taifa.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-

Tume ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) ina mikakati mbalimbali ya kupunguza maambukizi mapya ya UKIMWI (VVU).

Je, Serikali ina mkakati gani wa ziada kuhakikisha inafanikiwa na Kampeni ya Mpango wa asilimia 90, 90, 90 hasa ukizingatia jiji la Dodoma UKIMWI umeongezeka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA IKUPA ALEX) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah Hassan Mbunge wa Mtambile kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maafikiano ya malengo ya Tisini Tatu yaliyopitishwa na wadau wa Kanda zote za UNAIDS, Serikali ya Tanzania ilianza kuyatekeleza kwa kufanya yafuatayo ili kuhakikisha tunafikia malengo ya 90, 90, 90:-

(i) Kuanzia mwenzi Oktoba, 2016 ilitoa Waraka nchi nzima wa kuridhia utekelezaji wa Mkakati wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wa kupima VVU na kutibu bila ya kuzingatia kiwango cha kinga mwilini (CD4);(ii) Imeweka utaatibu wa kuhakikisha watu wote wanaogundulika kuwa na VVU wanaanzishwa dawa za kufubaza VVU (ARV) mara moja;

(iii) Kuandaa kampeni mbalimbali kwa ajili ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kupima VVU ili kujua hali zao na hasa mkazo mkubwa umeelekezwa kwa Wanaume ambao utafiti umeonyesha kuwa hawajitokezi sana kupima na kujua hali zao;

(iv) Kufanya mapitio ya Mkakati wa kudhibiti UKIMWI wa Mkoa wa Dodoma (2017) ili kuhuisha mahitaji ya afua za UKIMWI baada ya Serikali kuhamia Dodoma na kuongezeka kwa wawekezaji katika Jiji la Dodoma;

(v) Kurekebisha Mwongozo wa huduma za VVU na UKIMWI wa mwaka 2014 kwa makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kuambukiza au kuambukizwa ili kuboresha mikakati ya kuwapatia huduma za UKIMWI, ikiwemo upimaji wa VVU; na

(vi) Kuanza mchakato wa kufanya marekebisho ya Sheria ya Virusi vya UKIMWI na UKIMWI (Kuazuia na Kudhibiti) Sura ya 431 ili kushusha umri wa watoto kuruhusiwa kupima VVU kutoka miaka 18 hadi 15 na kuanzisha utaratibu wa wananchi kuruhusiwa kujipima wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa wito kwa wananchi wote kuendelea kupima afya zao ili watambue hali zao na kuchukua hatua stahiki.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-

Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu ya wananchi ambao maeneo yao yametwaliwa na Jeshi la Wananchi (JWTZ) pasipo kulipwa fidia:-

Je, Serikali ina mpango gani wa haraka kulipa fidia kwa wannachi hao?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdalah Salim, Mbunge wa Ntambile, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika ni kweli yapo maeneo mbalimbali yaliyotwaliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa jukumu la ulinzi wa nchi na mipaka yake. Baadhi ya maeneo hayo yamelipwa fidia na mengine mchakato wa kulipa fidia kwa wamiliki unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali uliopo ni kuendelea na utaratibu wa kulipa fidia stahiki kwa wananchi kadri hali ya fedha itakavyoruhusu na kwa mujibu wa Sheria ya Utwaaji Ardhi kwa ajili ya matumizi ya umma. Kwa mwaka wa fedha 2018/2019, Wizara ilitenga shilingi bilioni 20.9 kwa ajili ya kulipa fidia maeneo yaliyotwaliwa na jeshi. Baada ya uhakiki wa malipo ya fidia tayari kiasi cha shilingi bilioni 3 kimelipwa kama fidia. Aidha, uhakiki wa madai ya fidia unaendelea katika maeneo mengine na mara uhakiki utakapokamilika Serikali kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa italipa fidia hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba wananchi wawe na subira wakati Serikali inakamilisha uhakiki ili kuwalipa stahiki zao.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji unatarajiwa kufanyika mwezi Novemba, 2019:-

Je, Serikali inasema nini juu ya ushirikishwaji wa Vyama vya Siasa katika mkakati wa kutoa elimu ili kufikia lengo la uchaguzi huru na haki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa ngazi ya Vijiji, Vitongoji na Mitaa za mwaka 2019, chini ya Matangazo ya Serikali ya Na. 371, 372, 373 na 374 ya mwaka 2019, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeandaa Mwongozo wa Elimu ya Mpiga Kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mwaka 2019. Mwongozo huo umevitambua Vyama vya Siasa kama mdau muhimu katika suala la utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura.

Aidha, katika hatua za maandalizi ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019, wadau wote muhimu vikiwemo Vyama vya Siasa vyenye usajili wa kudumu vilishirikishwa katika hatua zote na kutoa maoni yao ili kuwezesha kuwa na Uchaguzi Huru na Haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yetu kuwa Vyama vyote vya Siasa vitashiriki katika kutoa elimu ya mpiga kura kwa wanachama wao kwa kuzingatia miongozo na Kanuni zilizotolewa.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-

Mwaka 2019 kutafanyika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mujibu wa sheria.

Je, Serikali ina mkakati gani unaoendelea katika maandalizi ya mchakato wa uchaguzi huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, Mbunge wa Jimbo la Mtambile kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 unafanyika kwa ufanisi, Serikali imekamilisha maandalizi ya Kanuni za uchaguzi zitakazotumika kuendesha uchaguzi huo. Kanuni hizo zimetangazwa katika Gazeti la Serikali la tarehe 26 Aprili, 2019 kwa kupewa namba kama ifuatavyo:-

(i) Tangazo la Serikali Namba 372 kuhusu Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mtaa na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa katika mamlaka za Miji.

(ii) Tangazo Namba 371 linalohusu Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji.

(iii) Tangazo Namba 373 linalohusu Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Wilaya na

(iv) Tangazo Namba 374 linalohusu Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Halmashauri za Miji.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imehakiki maeneo ya utawala na kufanya mafunzo na mikutano kwa wadau wa uchaguzi huo. Vilevile Serikali inaendelea na maandalizi ya ununuzi wa vifaa vya uchaguzi na imetenga kiasi cha shilingi 82,975,994,000.148 Kwa ajili ya kuendesha uchaguzi huo. Ahsante.