Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Masoud Abdalla Salim (19 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue fursa hii, kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhuhana Wataallah aliyenijalia uzima na afya njema hadi nikichangia mapendekezo ya mpango mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti nami nisiwe mwizi wa fadhila, niwapongeze kwa dhati kabisa wananchi wa Jimbo la Mtambile kwa kunichagua kwa kura nyingi kwa kipindi cha Nne mfululizo, toka mwaka wa 2000. Miongoni mwa Wabunge senior mimi ni senior, nikimuona Mheshimiwa Bahati Ali Abeid pale na Mheshimiwa Faida Bakar kwa upande wa Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze moja kwa moja kwenye ukurasa wa 34 kwenye Mpango huu ambao unashughulikia zaidi kuhusu utawala bora na naomba ninukuu kwenye (vi), inasema, kuimarisha mfumo kujitathmini kiutawala bora (APRM) yaani African Peer Review Mechanism. Utawala bora ni jambo pana, jambo kubwa. Hakuna utawala bora kama Katiba inavunjwa katika nchi hii, hakuna utawala bora kama sheria hazifuatwi katika nchi hii, hakuna utawala bora kama haki za binadamu hazilindwi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yanayotokea Zanzibar ni kitu gani, ni utawala bora au bora utawala! Inasikitisha! Inaumiza! Inasononesha sana. Leo hii tunaimba kila wakati tukisema kwamba tunataka amani na utulivu, lakini amani na utulivu wa midomoni. Inakuwaje leo kuna watu wanatembea kwa magari wakiwa na silaha za moto, tena wakiwa wamebeba misumeno, wanapita wanapiga watu, wanavunja vibanda, na Polisi wapo. Hee! jamani. (Makofi)
Mwaka jana tulipitisha Sheria hapa ya The Firearms and Ammunition, nani wamiliki wa silaha. Leo niulize jamani, inakuaje watu wanaachwa, wanapita wamevaa ma-socks maninja, kama Janjaweed, wakiwa na silaha za moto, wanakatakata vibanda vya watu, wanapiga watu, na Jamhuri ya Muungano ipo! Tabia hii mbaya lini mtaacha Serikali, hawa si watu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Ulinzi na Usalama kwa kipindi kirefu, kwa muda wa miaka 10 sasa mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama. Naombeni sana Polisi mnisikilize kwa makini na naombeni sana Idara ya Usalama wa Taifa mnisikilize kwa makini sana. Usalama wa nchi hii ni wetu sote! Haiwezekani, haiingii akilini kwamba upande mmoja wa Muungano mmeuacha watu wanafanya watakavyo. Hii ni aibu, ni tabia mbaya. Ni aibu kwa Taifa hili, ndani ya nchi na nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili halikubaliki! Hili halikubaliki! Ni aibu. Nadhani kama tatizo ni uchaguzi, uchaguzi halali wa huru na haki ulioangaliwa na Mataifa mbalimbali, uliokubalika na Mataifa mbalimbali, ulikuwa tarehe 25, Oktoba. Umeshapita, Rais halali wa Zanzibar ambaye kwamba hatua zote za uchaguzi kuanzia kupiga kura, kuhesabu kura, matokeo yalibandikwa katika mabanda yote na Mawakala wakapewa matokeo na mshindi alikuwa ni Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye alipata kura 207,847 sawa na asilimia 52.84. (Makofi)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Taarifa !....
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuendelea. Kwamba matokeo yote katika hatua zote za uchaguzi kuanzia kupiga kura, kuhesabu kura na baadaye majumuisho katika maeneo mbalimbali, Majimbo yote yalibandikwa kwenye kuta. Matokeo ya Rais wa Zanzibar yote yamewekwa kwenye kuta, Mawakala wote walipewa ushahidi kamili, wapo. Wawakilishi wote walipewa vyeti vyao 27. (Makofi)
MWENYEKITI: Naomba urudi kwenye hoja iliyo mezani.
MHE. MASOUD ABDALLAH. SALIM: Utawala bora, Wawakilishi wa CUF 27.
MWENYEKITI: Suala la Zanzibar naomba lisizungumzwe kwenye ajenda hiyo kwa sababu halihusiani na Bunge la Jamhuri ya Muungano. Naomba tuheshimiane na tuheshimu Kiti, Mheshimiwa kama una hoja ya kuchangia katika maeneo mengine suala hili limo ndani ya mikono ya Serikali, tunaomba uheshimu vinginevyo kama hujasikia itabidi nichukue hatua ya kukutoa nje tafadhalli sana.
(Hapa Wabunge fulani walipiga kelele)
MWENYEKITI: Endelea na hoja nyinginem, kama ni hiyo naomba ukae.
MHE. MASOUD ABDALLAH. SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee niko katika APRM (Africa Peer Review Mechanism) Mpango wa kujitathmini wenyewe kwenye utawala bora suala la Katiba, suala la Sheria lazima hapa lizungumzwe. Kwa hiyo ,Wawakilishi ishirini na sita walipewa vyeti vyao kama ilivyo kawaida. Naomba niendelee. (Makofi)
MWENYEKITI: Naomba nimruhusu Mwanasheria Mkuu...
MWENYEKITI: Haya endelea
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Muda wangu ulindwe, niko makini, naendelea kusimamia hoja yangu kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachowaonesha Watanzania, ninachowaeleza tena kwenye Bunge hili ni jinsi gani ya uonevu ukandamizaji wa demokrasia, tusiwe na malumbano tusiwe na jazba, naomba niseme kwamba, wakati huo Mwenyekiti wa Wilaya ya Chakechake ambaye ni Mbunge wa Chonga, Mohamed Juma Khatibu Mwachawa, masaa mawili kabla ya kufutwa kwa shughuli ile pale waliitwa Makao Makuu ya Polisi na wakaambiwa hivi, naomba mtulie, wafuasi wenu muwatulize kwa lolote litakalotokea! Sasa hoja kwa nini tusiseme kwamba kuna mkono ambao ulilazimisha! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee nije kwenye mambo ya usafiri wa baharini.
MWENYEKITI: Endelea naomba utulivu tafadhali Bungeni.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeeleza mambo mengi katika hali ya kuwanusuru wananchi, sioni Mpango wa aina yeyote! Sioni mpango wa aina yeyote wa kununua meli kutoka Tanga kuja Pemba. Sasa Mheshimiwa Dkt. Mpango, Mpango huu uko wapi? Mpango wa kunusuru maisha ya watu, sioni Mpango wowote katika kitabu chako wa kununua meli kutoka Dara es salaam kuelekea Mtwara, meli za uhakika! Sioni mpango wowote ambao utanunua boti za kisasa katika Bahari ya Hindi na kwenye maziwa, pale inapotokea ajali, watu kila siku wanakufa! Mpango uko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo ambalo halikubaliki. Ni jambo ambalo linapaswa kuzingatiwa na lazima lifanyiwe kazi, lakini kubwa kuliko yote Rais aliyepita alisema wizi, ubadhirifu na ufisadi hautavumiliwa. Marehemu Dokta Abdallah Omari Kigoda, Mungu amlaze mahali pema peponi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Kigoda alisema kwamba, umaskini uliopo katika Mikoa ya Kusini kwa mujibu wa Viwanda vile vya Korosho, viwanda ambavyo vimebinafsishwa basi vitafanyiwa kazi, alituahidi kwamba, wale wote waliopewa viwanda na hawakuviendeleza atawaita, lakini sasa hadi leo hakuna aliyeitwa na kubwa zaidi tulikuwa tunauliza viwanda vile mmiliki wake ni nani?
(Hapa Kengele Ililia)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni kengele ya kwanza tulia! Viwanda vile wamiliki wake ni nani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbe viwanda vile imebainika na imedhihirika kwamba viwanda vile vimebinafsishwa Tanzania ilikopa dola milioni ishirini kwenye miaka ya 1970 na 1980 kutoka Japani vikajengwa viwanda vya korosho kule Lindi na Mtwara badaye wamekwenda kupeana vigogo wa Serikali kama njugu, wakapeana tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Dkt. Mpango na Msaidizi wako mniambie viwanda ambavyo hasa nataka kuvitaja ni nani waliomilikishwa? Kwanza naomba uniambie Mtwara Mjini, ambacho kinaitwa Taasisi ya Fursa kwa Wote nani mmiliki wake? Mheshimiwa Naibu, Newala One nani mmiliki wake, mtuambie hapa? Likombe nani mmiliki wake? Masasi nani mmiliki wake? Lindi Mjini nani mmiliki wake? Nachingwea nani mmiliki wake? Mtama nani mmiliki wake? Aibu tupu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema tunakopa mabilioni ya fedha, wananchi wanaendelea kuwa masikini! Watu wanauza korosho ghafi badala ya kuuza korosho safi, tatizo nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huu mimi naona sasa kwamba ni vyema Serikali ikae makini kwamba kama iliahidi kwamba kuna wakati ambapo watu wale ambao wamepewa viwanda vile kwa bei ya kutupa viwanda vile haviendelezwi vimekuwa ni maghala virejeshwe. Huo ndiyo msingi, ili wananchi wale wapate faida iliyokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya hayo, naomba nimalizie kwa kusema kwamba, tunaendelea na demokrasia ya kweli, nakipongeza Chama changu cha Wananchi CUF, nampongeza Rais halali Maalim Seif Sharrif Hamad wa Zanzibar na Baraza Kuu la Uongozi wa Taifa CUF kwa kutoingia katika uchaguzi,. Tunasema kwamba tuko makini, UKAWA tuko makini na Chama cha Wananchi CUF kiko makini. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wajibu wetu wa Kikatiba, Ibara ya 63(2) ni kuishauri na kuisimamia Serikali na Serikali inapaswa isiwe na hofu wakati tunaisimamia na kuishauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ili kuepuka wizi, ubadhirifu na ufisadi, mikataba yote yenye utata naomba iletwe Bungeni. Kitendo cha Serikali kusema kwamba mikataba ni siri, ni ushahidi tosha kwamba Serikali inataka kuongeza nguvu katika wizi, ubadhirifu na ufisadi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mikataba yote yenye utata ambayo inaashiria wizi, ubadhirifu na ufisadi ni lazima iletwe hapa Bungeni tujue mbivu na mbichi, tuweze kupambanua, tuishauri Serikali tuisimamie Serikali. Mikataba kuwa siri ni tatizo na ndiyo maana tunaunda Kamati siku hadi siku. Hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tatizo kubwa ambalo linaonekana ni namna gani ya udhalilishaji na matatizo ambayo yanawakumba wafuasi hasa wa upinzani kule Zanzibar. Tumekuwa tukisema muda mrefu sana kwamba kunakuwa na hila na njama za kuwadhalilisha Wapinzani Bara na Zanzibar, lakini kule Zanzibar tumeripoti Polisi kuhusu kuchomwa kwa Ofisi ya CUF, Dimani. Sasa ni mwaka mzima hakuna hata taarifa yoyote ya Polisi imesema. Tumeripoti Polisi, Baraza ya Dimani ya Chama cha Wananchi CUF kwamba ilichomwa moto, lakini nasikitika sana Polisi hadi leo hakuna walilojibu. Tumeripoti Polisi Baraza la Kilimahewa, Ofisi ya CUF ya Mjini Magharibi, lakini hadi leo hakuna kitu ambacho kimeonekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wetu wa CUF, Chwaka, walikamatwa, wakapigwa na mtoto wa kike akafanyiwa vitendo viovu, tuliripoti Polisi hakuna kilichotokea! Walivamiwa Mpendae kwenye Ofisi yetu ya CUF, wakapigwa, tukaripoti Polisi. Wote wanaopigwa hao ni CUF, tatizo ni nini jamani? Mmeruhusu mfumo wa Vyama vingi ninyi wenyewe! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haitoshi, kuna wengine wanabambikiziwa kesi. Tuambiwe akina Eddy Riyami, Mansour Yussuf Himid, Naibu Katibu Mkuu Mazuruwi, Hamad Masoud wote hao, lakini tunaambiwa wengine wana kauli za uchochezi, tuseme wanaosema kwamba nchi hii hata ninyi CUF mkishinda, haikupatikana kwa vikaratasi; huo si uchochezi! Tunaambiwa ninyi CUF kama mnataka Serikali Zanzibar, mpindue, hiyo si kauli ya kichochezi! Wanasema kama mnataka Serikali Zanzibar nyie CUF pindueni, huo si uchochezi! Mbona hawa hawakamatwi! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo haya hayakubaliki! Hayakubaliki kwa sababu Polisi inaonekana imeegemea upande mmoja. Tumbatu zimechomwa nyumba nane, Shambuli hana mahali pa kukaa, nyumba 61 zimevunjwa, tumeripoti Polisi, hakuna lolote ambalo limetokea; tatizo nini? Kuwa mpinzani ndiyo tatizo! Huo si uchochezi! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabango ya Kisonge yote yanaandika siku zote, lakini hii ndiyo hali halisi ilivyo. Tunaomba Polisi, mtuambie sasa, Serikali hii ni ya Chama cha Mapinduzi peke yake au ni ya Watanzania wote na vyama vingine? Hili halikubaliki! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa sana vitendo viovu ambavyo vinafanywa na watu, wanafanyiwa wafuasi wa Chama cha Wananchi CUF na Vyama vya Upinzani, lakini Polisi wananyamaza; hili ni tatizo kubwa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Baraza la Sarayevo, Dimani tuliripoti vizuri na Polisi walituambia tutafanya uchunguzi wa kutosha, upelelezi haujakamilika. Upelelezi mpaka lini? Hawa akina Mansour, Eddy Riyami na wengine wote, tatizo nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, nimshauri sana Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Ndugu yangu Masauni uwe makini. Hata sisi hapa unapotujibu, unatujibu majibu ya ovyo ovyo ya ufedhuli, ya kiburi na kejeli, ndiyo maana tulikuwa tunakushauri kwamba ni vyema uvae viatu vya Pereira vizuri. Vaa viatu vizuri ili twende vizuri. Vinginevyo sisi tutakuwa hatuendi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ulikuwa ni utangulizi, dakika zenyewe ni tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, NIDA, fedha ambazo zimetengwa hazitoshi, wanazalisha vitambulisho 3,000 kwa siku. Watanzania ambao wanatakiwa wapate vitambulisho hawapungui milioni 25; ina maana kwa hesabu, kila mwaka mmoja…
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. awali ya yote nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu-wa-ta‟ala amenijalia uzima na afya njema, nikapata nafasi au fursa ya kuchangia machache kwenye hotuba hizi mbili; hotuba ya Mheshimiwa George Boniface Simbachawene na Mheshimiwa Angellah Kairuki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nataka nimkumbushe ndugu yangu Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, wakati akitoa maelezo kwamba Bunge lililopita tulipitisha sheria kwamba Bunge hili lisioneshwe live, watu waliokwambia walikudanganya. Siyo kweli, ulikuwa ni uongo wa mchana kweupe bila giza. Hakuna mahali iliyopita hata mara moja kwamba ilifika wakati sisi kuna taarifa hiyo ilipita, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nashukuru sana kwa mujibu wa kitabu cha Mheshimiwa George Boniface Simbachawene ukurasa wa 74, ameelezea mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, ufuatiliwaji wa taarifa za fedha juu ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali; pili, Utawala Bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti...
KUHUSU UTARATIBU....
MWENYEKITI: Sawa. Mheshimiwa Masoud tuendelee, utatoa baadaye uthibitisho huo.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kutokana na tabia hiyo nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende moja kwa moja kwenye ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambapo kwenye kitabu cha Mheshimiwa George, Waziri huyu ameelezea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kuna tatizo kubwa ukiangalia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali; Serikali Kuu ukurasa wa 304 imeelezea kilio, deni ambalo Tanzania tunatakiwa tulipe la shilingi bilioni 90 juu ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kulipa kampuni ta China ya Wallys.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jipu la kwenye kichogo au kisogo, kwa maana nyingine jipu hili halionekani. ATCL iliingia mkataba na kampuni ya Sonangol kutoka China katika miaka iliyopita kwamba ingeleta ndege saba, tano zikiwa aina ya airbus na ndege mbili ndogo. Baadaye kampuni hii ya Kichina ya Sonangol ilimtaarifu kampuni mwenzake ya Wallys kwamba iweze kuleta ndege hapa Tanzania, lakini nini ambacho kilitokea? Ndege iliyofika ilikuwa moja tu aina ya airbus na ndani ya hapo ndege hiyo ilipofika hapa Tanzania ilikaa kwa muda wa miezi sita kwa sababu ndege hiyo ilikuwa ni mbovu. Baadaye hiyo ndege ikachukuliwa mkaipeleka Ufaransa; kufika Ufaransa ndege hiyo mpaka leo haijarudi. Ndege hiyo iko wapi Serikali? Mtuambie ndege hiyo mpaka leo iko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi kufika Ufaransa ndege hiyo ilipakwa rangi nyingine kwa nchi ya Guinea na rangi tunaambiwa iliyopakwa hatuelewi kama ilikuwa ni ya kijani au manjano, hatuelewi. Baadaye mtatuambia; lakini ndege hiyo ilipakwa rangi nyingine na ndege hiyo mpaka leo haikurudi, lakini cha kujiuliza ni kitu gani? Ni kwa nini kulikuwa na uharaka mkubwa kupita kiasi katika mikataba hii? Ina maana tunadaiwa shilingi bilioni 90 hivi sasa. Hilo ni jipu kubwa, kwa nini mnalifumbia macho?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunaposema sisi upande huu wa pili tunaambiwa kwamba ninyi mnapinga hiyo ndiyo ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha ulioisha Juni 30, 2015 kwenye Serikali kuu ukurasa wa 304. Hilo ni jipu, tumbueni au ni upele hamwezi kuukuna. Wahusika wapo, Mheshimiwa Waziri Simbachawene kwa nini hadi leo walioko Hazina, walioko ATCL hakuna hata mmoja aliyeulizwa? Kwa nini? Tunaambiwa tulipe sisi shilingi bilioni 90.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hilo halitoshi, nenda kwenye ukurasa wa 282 ambapo inaelezea juu ya wizi, ubadhirifu na ufisadi mkubwa kabisa. Ripoti inaeleza kwenye Sekretarieti ya Mkoa wa Dodoma ambapo mwenyewe Mheshimiwa Waziri ndipo anapotoka, kuna ufisadi, wizi na ubadhirifu wa shilingi bilioni 912 kwa mambo yafuatayo; hilo ni jipu au ni upele au ni uvimbe? Mtasema wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, sikiliza kwa makini sana; kuna salio ya shilingi 571,498,633 la vifaa vya dawa, mafuta na vifaa vingine vinavyotumika mara kwa mara havikuingizwa kwenye taarifa za fedha; ufisadi wa kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wa pili, kuna mali zenye thamani ya shilingi 209,809,780 zilizidishwa kwa taarifa za fedha na hakuna marekebisho yaliyofanywa; ubadhirifu wa pili Mkoa wa Dodoma kwenye Makao Makuu ya Chama cha Mapinduzi, hapa hapa mchana kweupe.
La tatu, kuna matumizi yaliyolipwa zaidi kwa shilingi 131,049,085 kama madai ya mwaka 2014/2015 yameingizwa kwa malipo mengineyo; ufisadi mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaosema sisi tunapiga kelele, tunapinga kila kitu, hatupingi kila kitu, tuna ushahidi wa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, inaonesha kuna wizi, kuna ubadhirifu, ufisadi wa kutisha na hii ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Sisi tukasemee wapi wakati Serikali ndiyo ninyi? Tutasema hapa hapa kweupe wala hatuvumilii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine haya yamekuwa ni mazoea. Mimi nikiwa Mbunge wa Bunge la Nane kuanzia mwaka 2001 hadi mwaka 2005 jumla ya fedha ambazo zilisababishwa na wizi, ubadhirifu na ufisadi ilikuwa shilingi bilioni 4,403; watu waliopelekwa mahakamani ilikuwa ni 321; lakini cha kustaajabisha walipofika mahakamani waliambiwa kwamba wahusika hawa hawana kesi, wametoroka. Aliwatorosha nani? Walitoroka kwenye vyombo vya dola. Sasa hili ni tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2006 shilingi bilioni 2.3; mwaka 2007 shilingi bilioni 3.5; mwaka 2008 shilingi bilioni 3.1; mwaka 2009 shilingi bilioni 11.1; mwaka 2010 shilingi bilioni 12.9; wote huu ni ufisadi wa kutisha unaofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Sisi tukayaseme wapi haya? Leo tunapoelezea mambo kama haya watu hawako serious, umakini wa Serikali uko wapi? Lazima tuyaseme haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora uko wapi? Tumekuwa tukisema mambo mengi ya msingi; leo hii ukiangalia manyanyaso ambayo yanatokea kwa watu wetu kule Tumbatu; na naomba nisome kwenye Ibara ya 13; “Watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki bila ubaguzi wowote kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.” Wananchi wa Tumbatu makosa yao ni nini? Unguja wamekuwa nyumba zao zikitiwa moto, hawana pa kushitaki. Lolote wanalolifanya wao kwao ni baya. Tatizo la Tumbatu ni kitu gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawa ni lazima nao walindwe. Inakuwaje leo watu wetu hawa wa Tumbatu kila siku wananyanyaswa na baadhi ya watu ambao wanajulikana lakini hakuna hatua. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, fanya ziara yako uende Tumbatu. Hali hairidhishi. Hili ni jambo kubwa sana na nadhani Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani utalichukua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tuje kwenye mafao. Ni mara kadhaa ambapo inaonekana kwamba mafao ya wastaafu wakati wa kupata haki zao wanapunjwa na hili ni tatizo kubwa. Sasa inakuwaje leo mnasema kwamba kwa mujibu wa ripoti iliyomaliza juzi mwaka 2015 kati ya majalada 1,683 wastaafu 200 wamepunjwa shilingi 385,304; je, hamjui kukokotoa? Angalieni ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ukurasa wa 99, kwa nini mwapunje na kwa nini msiwazidishie?
Mheshimiwa Kairuki, kwa nini msiwazidishie? Sasa huu ni ufisadi au siyo ufisadi? Mnawapunja, lakini watakapokufa wastaafu wale wengine ambao wana heshima zao mnakwenda pale na risala ya kutoa machozi ya uongo mtupu kweupe mchana, Marehemu alikuwa hodari, shupavu, jasiri mwaminifu na mtiifu; yeye atakumbukwa, atathaminiwa, mbona walipokuwa hai hamkuwathamini mliwapunja ninyi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ufisadi wa kutisha ni wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi, kama hata wastaafu hamwathamini pia mnawapunja...
MWENYEKITI: Mheshimiwa Masoud muda wako umeisha, naomba ukae.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwanza nataka Watanzania ambao wanatusikiliza waelewe kwamba sisi kama Kambi ya Upinzani tutaendelea kushikilia misimamo yetu dhidi ya ukandamizaji wa demokrasia na sisi tuko makini kweli kweli, hiyo ya kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wakati alipokuwa akitoa hotuba yake alisema miongoni mwa taasisi ambazo anaziongoza tatu ni APRM (African Peer Review Mechanism) mpango ni wa kujitathmini wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa huu mpango Tanzania inajitathmini yenyewe ningependa nimuulize Mheshimiwa Waziri atueleze, kwa sababu huu ni mpango wa utawala bora, huu mpango wa Bunge kutooneshwa live mmejitathmini kiasi gani? Mpango huu wa Bunge kutooneshwa live ni kiasi gani mmejitathmini ninyi wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, viongozi wetu kukatwa katwa mapanga na kupigwa na kuumizwa na wengine kuuawa kama kwa kamanda Alphonce Mawazo ambaye yeye ni Mwenyekiti wa Mkoa wa CHADEMA, kiasi gani mmejitathmini na nani waliohusika katika mpango huu wa utawala bora? Pia sambamba na hilo ningependa kuelewa kupigwa na kukatwa katwa na kuuawa kwa Diwani wetu kule Muleba, Faustine Mlinga, Kata ya Kimwani, kiasi gani mmejitathmini na kujua nini cha kufanya? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuelewa kuvamiwa kwa viongozi mbalimbali wa dini kule Mwanza juzi na kupigwa. Je, katika mfumo huu wa utawala bora ni kiasi gani mmejitathmini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuuawa kwa vikongwe, walemavu, wale albinism, kiasi gani mpango huu wa kujitathmini wenyewe mmeweza kukaa kitako na mkaona njia gani mbadala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya ili tuelewe sasa kiasi gani APRM, kwa sababu haina vote yake yenyewe hampewi fedha, kwa hivyo sasa ionekane kiasi gani katika kujitathmini ninyi wenyewe kama uwezo wenu ni mdogo, hamna fedha, mimi naishauri Serikali, APRM (African Pear Review Mechanism) ipewe vote yake yenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuna masikitiko makubwa, Watanzania ambao wanataka kwenda Uingereza viza zao zamani walikuwa wanazipata Kenya, sasa mpaka Afrika ya Kusini. Mheshimiwa Waziri, tuambie tatizo gani la figisu figisu baina ya Tanzania kutoaminiwa na Uingereza mpaka viza hizi kutoka sasa kwenda kutoa Kenya sasa unazipata Afrika ya Kusini, tatizo ni nini? Mna tatizo gani la kidiplomasia na hawa wenzetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni diplomasia ya kiuchumi. Nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri ingawa anaongea ongea pale, katika kuongeza kasi hii ya diplomasia ya kiuchumi baadhi ya nchi zimeweza ku-present credentials, kupeleka hati za utambulisho hapa kwetu, na sisi inaonekana bado kuna nchi mbalimbali hatujaweza kuwasilisha hati za utambulisho. Tanzania hapa Balozi wa Namibia na Botswana wako Tanzania lakini sisi Balozi wetu kule Botswana na Namibia naona kama sisi hatuna Balozi.
Lakini tarehe 05 Januari, 2016 kuna nchi tatu ambazo waliweza ku-present credentials hapa. Jamhuri ya Korea, Jumuiya ya Ulaya na Taifa la Palestina. Je, sisi tumejipanga vipi? Wakati wao tarehe tano walileta hiyo hati ya utambulisho kwa Rais John Pombe Magufuli, sisi je, kwa nchi ambazo nimezitaja. Jamhuri ya Watu wa Korea, Jumuiya ya Ulaya na Taifa la Palestina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba Mheshimiwa Waziri ukija unieleze, ni kwa nini sisi tunachelewa kuwasilisha hati za utambulisho? Mfano Balozi wetu pale Berlin, Ujerumani, nchi ambazo anaziwakilisha ni Ujerumani, Uswiss, Jamhuri ya Czechoslovakia, Poland, Hungary, Bulgaria, Romania, Australia na Vatican, lakini hati ambazo zimewasilishwa na Ujerumani, Uswiss, Austria na Vatican, nyingine zote mpaka leo hatujawasilisha hati za utambulisho, tatizo ni nini na hii ni diplomasia ya kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo Cairo, pale Misri Balozi wetu nchi ambazo anaziwakilisha ni Misri, Israel, Lebanon, Palestina, Libya, Iraq, Syria na Jordan. Lakini hati ambazo zimewasilishwa ni Misri peke yake, nyingine zote bado hatujawasilisha hati za utambulisho na hapa uchumi wetu utakuwa ukiendelea kudorora siku hadi siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba Mheshimiwa Waziri, utakapokuja uniambie…
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Masoud, dakika tano zako zimekwisha.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, Subhana Wataala kwa kunijalia uzima na afya na kuniwezesha kuchangia taarifa hizi mbili muhimu, ile ya LAAC ambayo imetolewa na Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale Mwiru, mtoto wa Kingunge, hongera sana kwa kazi nzuri na Mheshimiwa Kaboyoka, taarifa zao ni za kina kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa za CAG ndizo ambazo wenzetu hawa wanazifanyia kazi. Taarifa zote hizi mbili ni nzuri, lakini tatizo la kutopatikana kwa fedha kwa viongozi wa Kamati hizi mbili kwenda katika maeneo mbalimbali kujionea uhalisia wa miradi ya maendeleo, kuangalia value for money, jinsi gani fedha zilivyotumika, limekuwa ni kubwa kweli. Kazi ambayo wameifanya Wenyeviti hawa wawili ni kubwa lakini kama hawapewi fedha za kwenda katika maeneo mbalimbali kuangilia uhalisia na kile kitu kinachoitwa value for money ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi nimpongeze Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, naye vilevile nimwonee huruma kidogo baada ya kumpongeza, kama alihitaji shilingi bilioni 62, Serikali imekwenda kumpa shilingi bilioni 18 atafanya kazi vipi? Huu ni upungufu mkubwa sana! Kila mtu aliyepewa dhamana na Serikali atengewe fedha ya kutosha ili atakapotoa mapendekezo yake basi yawe ni kweli. Kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anaomba shilingi bilioni 62 anaenda kupewa shilingi bilioni 18 kuna jambo, tatizo kubwa. Kwa mara nyingine naishauri Serikali iandae mpango madhubuti, mpango makakati, ulio mzuri na mahsusi wa kuweza kutoa fedha hizi kwa wahusika hawa. Hiyo ili kuwa ni chombeza ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, wachangiaji wenzetu waliopita walisema kwamba moja ya tatizo kubwa hapa ni Hazina kuchelewesha kutoa fedha za maendeleo katika Halmashauri au kutopeleka kabisa. Utekelezaji wa miradi ambayo tumepanga sisi Waheshimiwa Wabunge na ikumbukwe kwamba asilimia 70 ya fedha za maendeleo zinakwenda kwenye Halmashauri, kama Serikali haitaki kutoa fedha kwa wakati, inachelewesha au haitoi kabisa ina maana sisi Wabunge ni kama danganya toto tu. Tatizo ni nini kwa Serikali? Ni lazima Serikali ikumbuke kwamba sisi Wabunge tunapopiga kelele na kuandaa mazingira mazuri basi hizi fedha waweze kuzitoa kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya upungufu mkubwa unaonekana ni suala zima la Wakurugenzi wengi katika Halmashuri kutokuwa na sifa na ndiyo maana miradi mingi ya maendeleo huwa inakwama. Wenyeviti wetu na Kamati kwa ujumla waliwaita baadhi ya Wakurugenzi kuja kutoa taarifa, unaona jinsi wanavyojikanyaga kanyaga, hawana sifa. Wakurugenzi hawa wanachukuliwa kwenye NGOs, ni vyema Wakurugenzi hawa watoke katika utumishi na wajulikane wana sifa fulani lakini wapi, tatizo nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya mikakati ya kuziboresha hizi Halmashauri zetu ni kwamba yale makusanyo ya ardhi ambapo fedha hizi zinakwenda moja kwa moja Serikalini inatakiwa asilimia 30 zirudi kwenye Halmashauri lakini hawapewi. Kwa hiyo, Halmashuri zinadhulumiwa, zinanyanyaswa, zimekuwa maskini na Serikali imekaa tu, tutafika kweli? Sijui. Niiombe sana Serikali iandae mpango mkakati na mzuri kabisa ili Halmashauri iweze kupata hizi asilimia 30 kutoka Serikali Kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende sasa katika lile la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambaye katika taarifa hizi ni jicho la kuona. Nitaanza na taarifa moja moja na naomba niende kwenye ukurasa wa 141 ambapo kuna ubadhirifu wa fedha ambao umefanywa. Kwa mujibu wa ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha unaoishia 30 Juni, 2005 kuna suala zima la Kivuko cha Kigamboni ambacho kinatoka Kigamboni kwenda Dar es Salaam. Kivuko hicho kilifanyiwa majaribio ni kibovu na kwa mujibu wa ripoti kilinunuliwa kwa dola za Kimarekani 4,980,000 karibu shilingi bilioni 10 lakini hakikufanya kazi, ni tatizo kweli, ina maana hapa Serikali imeingia hasara wakati tuliambiwa kivuko hiki ni kizuri, ni bora lakini hapa pametokea matumizi mabaya ya fedha za umma.
Niishauri Serikali kwa kuwa aliyekuwa Waziri katika Wizara hii sasa ni Mtukufu mwenyewe wa heshima, kiongozi wetu, ni vema ashauriwe kwamba watu wote waliompelekea Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingia katika mkataba huu mbovu wa shilingi karibu bilioni 10 kununua kivuko kibovu ambacho ni cha kutoka Bagamoyo kuja Dar es Salaam na hakifanyi kazi, watu hawa Mheshimiwa Rais awatumbue. Yeye mwenyewe anawajua, yeye mwenyewe Mheshimiwa Rais awatumbue watu hawa ambao walituingiza katika mkataba mbovu na Ujerumani kwa dola za Kimarekani 4,980,000 karibu shilingi bilioni 10 na kivuko hiki kikawa hakina sifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ikasema kwamba hati ya makabidhiano haikutolewa. Kivuko kilikabidhiwa bila hati ya makabidhiano jambo ambalo ni baya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa kuliko yote sifa ya kiwango cha kutembea ni tatizo. Ukiangalia kivuko cha Bakhresa kinatoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar ambacho kimenunuliwa shilingi bilioni nne, kinatumia saa moja na nusu lakini kutoka Bagamoyo kuja Dar es Salaam saa tatu. Ni vema kwa kuwa kiongozi mkuu yeye mwenyewe alikuwa ndiyo wakati huo ana dhamana mumshauri wale wote waliotuingiza katika mkataba huu awatumbue alfajiri mapema ili wananchi wapate imani nao, hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala zima la wastaafu. Mara nyingi kumekuwa na malalamiko, ripoti nyingi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zimekuwa zikizungumzia jinsi gani wastaafu wanavyoonewa, wanavyopunjwa na wanavyodhulumiwa. Ukiangalia ripoti zote za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, nianze na inayoishia mwaka 2015, kati ya majalada 4,683 ya wastaafu yaliyokaguliwa majalada 200 yalipunjwa jumla ya shilingi milioni tatu themanini na tano laki tatu na mia nne themani na moja. Utetezi wa Serikali na kinachoonekana tatizo ni kukokotoa, mnakokotoa jambo gani jamani? Majalada 200 wastaafu wamepunjwa, wamedhulumiwa na ndiyo maana wakawa maskini. Wastaafu hawa wakishakufa risala nzuri na mnatoa machozi, machozi ya nini wakati mliwaonea alfajiri mapema? Roho mbaya kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, inakuwaje leo ripoti inayoishia 2014, majalada 4,764 ya wastaafu yaliyokaguliwa majalada 283 yamepunjwa shilingi 481,456,311, jamani! Kila siku wakati wa kustaafu hawataki kuwatendea haki wastaafu. Wastaafu hawa na wao walikuwa ni wafanyakazi wetu, wameshastaafu jambo gani kubwa la msingi mnashindwa kukokotoa mkawapa haki zao. Kila siku ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anaonya kwamba wakati wa kukokotoa basi Serikali iwe makini au hakuna wataalam? Jamani, aibu si aibu, ni shida kweli. Kila mmoja ni mstaafu mtarajiwa kuna Wabunge wastaafu na watu wengine mbalimbali, lakini wastaafu hawa ni vema kwa vyovyote iwavyo waangaliwe kwa jicho la huruma ni jinsi gani wanavyodhulimiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye jambo lingine, nikuombe habari zifike kunakohusika, kwa sababu Serikali hapa ipo, inakuwaje sisi kila siku tunaingia kwenye mikataba mibovu? Tumeingia mkataba na Shirika la Ndege kipindi kile la South Africa na Shirika letu la Ndege la Tanzania (ATCL) tukakodi ndege (Airbus 320) na baadaye ndege hiyo ilikuwa ni mbovu, ikapelekwa Ufaransa kwa matengenezo, ikasuasua, ikaondolewa ikapelekwa Guinea, ikapakwa rangi, tumepata hasara ya shilingi bilioni 91 nani katumbuliwa? Mnatumbua maskini za Mungu waliokuwa hawana kitu, tumbueni hawa, hawa ndiyo wa kutumbuliwa. Wameiingizia hasara Serikali ya shilingi bilioni 91 mbona hawa hawatumbuliwi? Muwatumbue na hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali anapotoa maelezo yake kwamba kuna wizi, ubadhirifu na ufisadi mkubwa kama huu, Serikali lazima mtilie maanani, muone kwamba hili jambo ni la msingi sana vinginevyo ni shida kweli! Hata ukichangia kiasi gani, Serikali inasema ni sikivu, inasikia kilio chetu lakini usikivu uko wapi? Sisi wengine tunapata shida kweli Serikali ukiishauri haikubali. Kazi ya Bunge ni kuishauri na kuisimamia Serikali lakini Serikali haikubali kusimamiwa ni shida na inavyoonekana Serikali haitaki kusimamiwa, wanataka watusimamie sisi tutakubali wapi, hatukubali. Tutachombeza hivi hivi kidogo kidogo kuna siku mambo yatawaingia vizuri muweze kutufanyia yale ya haki na hasa kwa wananchi. Haiwezekani shilingi bilioni 91 ziende, ndege mbovu, muiondoshe Ufaransa muipeleke Guinea muipake rangi, lakini hakuna aliyekamatwa, ni shida kweli, tutafika sisi kweli? Sijui, kwa sababu ameingia Trump inawezekana akatusaidia pengine anasikia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo machache, mimi sitaki nichombeze chombeze sana, naomba jicho hili la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mumpatie fedha aende katika maeneo mbalimbali. Haiwezekani anaomba shilingi bilioni 62 anapewa shilingi bilioni 18. Mheshimiwa Kaboyoka na Mheshimiwa Ngombale nao hawakupewa fedha za kutembelea maeneo mbalimbali kujionea wenyewe, value for money iko wapi, hamna kitu! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumbe wao ripoti walitumiwa moja kwa moja kwenda site hakuna. Bunge ndiyo…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni sana nashukuru na naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nami kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyo mbele yetu. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu Subhanah- Wataallah aliyetujalia uzima na afya njema katika miezi hii mitukufu tunayoendanayo; na wale wanaofunga inshallah Mwenyezi Mungu awabariki na funga zao azikubali.
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuwapongeza wananchi wangu wa Jimbo la Mtambile kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya, lakini hasa pale ambapo Katibu Mkuu, kipenzi chetu, Maalim Seif Shariff Hamad ambaye alikuwa akipita katika ziara zake za kuongoza chama chetu. Hongera wananchi wa Jimbo la Mtambile, hongera Katibu Mkuu Mstahiki Maalim Seif Shariff Hamad, wewe ni kiboko ya viboko, tuendelee na kazi, hakuna Katibu Mkuu mwingine mpya. Ni wewe tuliyekuchagua katika Mkutano Mkuu mwaka 2014, hakuna Mkutano mwingine Mkuu uliofanyika. Chapa kazi Katibu Mkuu Maalim Seif Shariff Hamad, songa mbele, aluta kontinua.
Mheshimiwa Spika, la pili. Naomba niendelee. Kwenye ukurasa wa 10 wa Kitabu cha Mheshimiwa Waziri Mkuu alikipongeza Chama cha Mapinduzi kwa kupata viti 19 vya Udiwani katika chaguzi zilizopita.
Mheshimiwa Spika, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba Chama cha Mapinduzi kilipata pigo, kilishindwa vibaya katika uchaguzi wa marudio wa Lindi Mjini; mitaa yote saba Chama cha Wananchi – CUF kilishinda. Naomba, hawa ni jirani zako, CCM ilipata kipigo
kitakatifu; CCM ilishindwa vibaya na wananchi walisema hiyo rasha rasha tu, 2020 ndiyo muziki hasa. Hawa jirani zako lazima ilikuwa uwakumbuke kwamba CCM ilipigwa vibaya Lindi Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niwapongeze mitaa ambayo ilishinda katika Mitaa ya Mnubi, Migombani, Ndolo Juu, Mnazi Mmoja, Nachingwea, Tulieni na Runyu. Mitaa yote saba hii ilichukuliwa na Chama cha Wananachi – CUF kama taasisi. Hongera sana wananchi wa Lindi Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika mambo ambayo tunakwenda nayo naomba niseme kwamba, Serikali kwa wakati huu haioneshi wazi kwamba ina dhamira ya kuleta maendeleo. Kwa sababu, hata pale ambapo bajeti imepangwa itekelezwe, basi imekuwa ni kizungumkuti.
Mheshimiwa Spika, ni aibu na fedheha iliyotosha kwamba hadi hivi sasa bajeti ya maendeleo ambayo imeletwa ni 34% tu, hii ni aibu. Tena na bajeti hiyo, kinachosikitisha ni kwamba ilikuwa ni bajeti ya shilingi trilioni 29, mara hii Serikali imeleta bajeti ya trilioni 31, miezi iliyobakia ni mitatu wanasema kwamba fedha zilizobakia eti wataweza kuzileta. Hiyo miujiza itatoka wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ikiwa miezi tisa Serikali haikuweza kukamilisha fedha za 100%, eti miezi hii iliyobakia mitatu watakamilisha bajeti ya 66%. Ni aibu na fedheha kwa Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba, katika hili, jambo ambalo linatushangaza hata bajeti yako ya Bunge, bajeti ya maendeleo 2016/2017 ilikuwa ni bilioni saba, hadi leo ninavyojua, labda wameweka fedha jana au mchana huu, wametoa shilingi milioni 200 tu. Aibu na fedheha iliyotosha.
Mheshimiwa Spika, ni aibu kubwa kwamba Serikali haina dhamira iliyo wazi; ukiangalia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali bajeti iliyopita alitengewa fedha za maendeleo shilingi bilioni 10, lakini amepata shilingi bilioni 2.4 tu. Tena asilimia 90 ya fedha hizi, ni fedha za wafadhili. Ni aibu kwa Serikali inayosema hapa kazi na mwendokasi. Kasi iko wapi? Kutakuwa na kasi kweli mwaka huu hapa! Hii ni fedheha na aibu kubwa kwa Serikali.
Mheshimiwa Spika, ni imani yangu kwamba wakati sisi Wabunge tunapitisha bajeti za maendeleo Serikali iwe makini kuangalia ni jinsi gani ambavyo fedha za maendeleo zitatolewa kwa wakati, vinginevyo ni aibu na fedheha kwamba tunapitisha bajeti za maendeleo, lakini Serikali
inaendelea kutumia fedha za maendeleo kwa mambo ambayo Wabunge hatukupitisha. Ni jambo baya sana.
Mheshimiwa Spika, nini athari yake kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali? Ni kwamba hapewi fursa iliyo nzuri kuangalia miradi mbalimbali ili kuanika uozo na uovu ambao unaonekana kwenye Serikali. Huu ni mkakati maalum wa Serikali kwamba mnamdhibiti asifanye kazi zake vizuri kwa sababu mnajua kuwa kwenye Serikali kuna maovu yaliyo mengi. Hii ni aibu na fedheha kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaiomba Serikali ikubali ushauri kwamba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali apewe fedha inayostahiki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, aibu nyingine na aibu iliyoje, katika miaka kadhaa iliyopita sisi vyama vya siasa tumekuwa tukilelewa na mtu anayejulikana kama Msajili wa Vyama vya Siasa. Leo Msajili wa Vyama Vya Siasa amethubutu na kutoa ruzuku shilingi milioni 369 kwa akaunti isiyostahiki. Mbaya zaidi imekwenda mbali zaidi, huu ni ufisadi wa hali ya juu, fedha hizi kwenda katika benki isiyostahiki, NMB, baadaye fedha hizi kuhamishwa kupelekwa kwa mtu binafsi, fedha hizi zikatumika isivyo. Hii ni kama Escrow! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii ni aibu kubwa na fedheha. Kama taasisi naiomba Serikali iangalie sasa fedha za Msajili wa Vyama vya Siasa zinatumikaje? Hii ni aibu na fedheha kwamba fedha unazipeleka katika akaunti isiyostahili, baadaye fedha zinachukuliwa zinapelekwa kwenye akaunti ya mtu binafsi; zinachukuliwa zinatumika visivyo na bado Serikali ipo inachekacheka tu! Tatizo nini kwa Serikali? Aibu kwa Serikali inayosema Hapa Kazi na Mwendokasi. Kama kasi ndiyo hii, aibu kubwa! (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, aibu nyingine ambayo inakuja, Serikali inasema tuko katika mkakati wa uchumi wa viwanda, lakini siyo muda mrefu Kiongozi wetu Mheshimiwa Freeman Mbowe amesema hapa jinsi gani ambavyo fedha za viwanda zilivyotolewa asilimia ngapi ya fedha za Wizara ya Viwanda. Kama kweli tuna nia nzuri, inakuwaje hadi leo unaendelea kutoa 8% ya fedha za viwanda? Serikali ambayo inasema
tunaelekea katika uchumi wa viwanda! Hiyo ni aibu nyingine.
(Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niendelee kwa kusema kwamba ndani ya uchumi wa viwanda tuna sababu gani ya msingi, baadhi ya viwanda vilivyopo, baadhi ya wafanyabiashara bado wanaagiza baadhi ya bidhaa kama ngano kutoka nje? Leo viwanda hapa vipo. Kuna kiwanda
cha ngano cha Bakhresa, lakini 90% Bakhresa anaagiza kutoka nje.
Mheshimiwa Spika, hapa Serikali kazi yake ni kuchukua mikasi kukata utepe, ati mnazindua viwanda. Kazi gani! Njombe ngano inastawi, Iringa ngano inastawi, maeneo mengine ngano inastawi, lakini 90% ya ngano ya Bakhresa inatoka nje. Sisi kazi yetu ni kutembea na mikasi tu,
tunazindua viwanda. Si aibu hiyo! Aibu kubwa.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo naliona, tunazungumza habari ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA); tumeshuhudia kwamba wakati wa ukame Serikali ina mpango wa kudhibiti na kuweka chakula kwenye ghala la chakula – NFRA.
Mheshimiwa Spika, ni kwa nini tunaona mifugo yetu inakufa kwa kukosa majani au nyasi wakati tungeweza kuweka mkakati wa udhibiti katika maeneo mbalimbali ili hawa ng’ombe wetu wapate nyasi za kutosha? Hivi jamani hata hilo linahitaji mshauri mwelekezi kutoka nje?
Mheshimiwa Spika, ukienda katika mapori mbalimbali wakati wa ukame, unaona jinsi gani ambavyo ng’ombe wamekufa, lakini kumbe tuna nyasi za kutosha katika mikoa mbalimbali. Hili ni jambo ambalo Serikali ni lazima mliangalie. Sasa huo mkakati wa kupunguza umaskini uko wapi kama wafugaji wameachwa ng’ombe wao wanakufa, lakini nyasi kumbe zipo?
Mheshimiwa Spika, nchi nyingine duniani wanafanya hivyo, wanavuna nyasi, wanavuna yale majani wanayaweka kwa wakati maalum na wakati ukifika ule wa ukame ng’ombe wanapatiwa majani na wanakula, hawafi. Binadamu Tanzania wana njaa, ng’ombe wana njaa; shida
kweli! Hapa kazi kweli mwaka huu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nije kwa Walimu. Walimu mara nyingi wamekuwa na malalamiko yao na mara nyingi Walimu wamekuwa wakipuuzwa.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba Walimu madeni yao yanayostahili hawalipwi kwa wakati, ndio maana Walimu wanakuwa ni maskini. Walimu wana malalamiko mengi, lakini kwa sababu inaonekana labda watu hawaelewi maana ya Ualimu; Mheshimiwa Simbachawene herufi ‘U’ maana yake ni uvumilivu. Kwanza ni usumbufu; “A” maana yake ni adha wanayopata walimu; ‘L” ni lawama wanazopata walimu. Inda, mahangaiko, mwisho ni uvumilivu na umaskini… (Hapa kengele ilila kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, naomba walimu wapewe stahiki zao zinazostahili. Nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nimepokea taarifa kwa Mheshimiwa Fakharia Shomar akisema kwamba uchaguzi wa Zanzibar ulitawaliwa na Jeshi la Wananchi la Tanzania, hongera sana Mheshimiwa Fakharia tumepokea taarifa na sisi upande wa pili tujiandae zaidi kwa kushinda kura si kwa njia nyingine yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rweikiza nikwambie tu kwamba Jeshi la Marekani wakati wa amani linafanya shughuli za uchumi, watu waliotembea sana shughuli hizo wanajua na majeshi mengi duniani wakati amani yanafanya shughuli za uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukarasa saba Mheshimiwa Waziri anasema dhima kubwa ni kuwa na jeshi dogo na mahiri la ulinzi wa nchi lenye weledi. Hatuwezi kuwa na jeshi dogo, mahiri na lenye weledi ikiwa bajeti ya maendeleo yenye shilingi bilioni kumi unatoa shilingi bilioni moja, hakuna kitu. Hatuwezi kuwa na jeshi lenye weledi na mahiri ikiwa bajeti ya maendeleo ya JKT shilingi bilioni nane unatoa shilingi bilioni moja, hakuna kitu, hapo hakuna weledi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatutaki kuona sisi umeme unakatwa kwenye Kambi za Jeshi la Wananchi wa Tanzania, hatutaki. Hatutaki kuona kabisa wanajeshi wanafanya kazi pamoja na mkataba wao kula kiapo ndani ya masaa 24 lakini kwamba baada ya saa tisa na nusu ration allowance yao nayo inaondoka, hatutaki. Tunataka kuona ration allowance ya wanajeshi wetu inapandishwa si kwamba ration allowance inaondolewa kiaina aina hatutaki. Hiyo ilikuwa ni chombeza ya kwanza mambo hasa yanakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna malalamiko ya muda mrefu sana juu ya fidia kwa wananchi ambao maeneo yao yamechukuliwa na Serikali kwa ajili ya Jeshi la Wananchi. Maeneo haya ambayo wanajeshi wana shughuli zao jumla yake ni maeneo 262, kati ya maeneo haya ambayo yamepimwa ni maeneo 17 tu. Kwa kweli hii ni njia ya dhuluma, wananchi wamenyanganywa, wananchi wamedhulumiwa na mpaka leo Jeshi la Wananchi katika maeneo 262 maeneo 17 waliyoyapima na kuthamini hakuna fidia na mengine hayajapimwa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwaka 1966, 1970 mpaka leo miaka 50, wananchi wengine wameshakufa wameacha watoto wao wanadai, wala hawajui waende wapi, mmechukua maeneo yao mbalimbali, mbona mambo mnayotaka kufanya mnayafanya? Mbona hawa hamuwapi fedha zao? Hamtoi fidia zao? Kuna mambo mengine ambayo mnayafanya na fedha zinapatikana, kwa nini hamtoi fidia kwa hawa na tatizo ni nini? Nakuomba Mheshimiwa Waziri utuambie utakapokuja hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Fungu 57 - Wizara, katika mwaka 2016/2017 ulikuwa na shilingi bilioni 27.7 ni kasma 2004, zilitengwa hizi fedha hakuna shilingi iliyotoka! Wananchi wasemee wapi sasa? Wananchi wanadhulumiwa na wananyonywa hawana mdomo wa kusema, mdomo wao ni sisi, lakini Serikali inasema inatafuta fedha, fedha ikipatikana, mbona fedha za kuhamia Dodoma mlizipata, zilikuwa kwenye bajeti? Fedha za kuhamia Dodoma mlizipata wapi na hazikuwa kwenye bajeti? Kwa nini hawa fedha zao hamuwapi? Kuna wazee wamekufa wameacha watoto wao nao wamekufa, shida kweli Tanzania jamani! Twende wapi sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ndiyo mambo ya msingi ya kuwasemea wananchi wetu na kuwaonea huruma, kwamba Serikali inasema inawapenda wananchi wake, inawathamini wananchi wake lakini wapi! Miaka 50 fedha zao hamuwapi mnawatesa kwa njaa, tutafika kweli? Hatufiki, shida kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee, ni miaka kadhaa tumesema, tunajifunzaje baada ya mlipuko wa mabomu kule Mbagala na Gongo la Mboto? Baada ya hapo wakasema wanajenga maghala fedha mimi ni mmoja wa walioidhinisha, maghala yamekuwa magofu hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabilioni ya fedha yamepotea, maghala hayaendelezwi yako vilevile. Mungu asijaalie kutokea, likitokea la kutokea nani ataulaumiwa? Maghala mengi ambayo tumetoa fedha yakianzwa hayamalizwi. Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi utakapokuja naomba hili uliseme ni kwa nini mpaka sasa maghala haya bado hayajamalizwa na fedha hizo zimetumika zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Sera ya Ulinzi wa Taifa, umesema sana kwenye kitabu chako hiki. Mambo ya Sera bado hujakaa vizuri. Tangu mwaka 1966 mpaka leo sera ni ya zamani. Unataka jeshi la weledi lakini sera ndiyo itakayopelekea sheria, Sheria ya Ulinzi ni ya zamani. Kwa hiyo hili nalo ni tatizo kubwa. Mheshimiwa Waziri sasa utuambie hii sera lini itaweza kukamilika? Tatizo wewe unalijua zaidi, tena sana, tu kwamba utuambie hii sera ya ulinzi wa Taifa ni lini itakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pengine ningesema jambo linguine, wanajeshi wanakwenda kulinda amani Darfur, DRC na Lebanon wengine wameshaletwa tumeshawazika. Sawa ni kazi zao na wajibu wao lakini mbona familia zao hamzitunzi? Mnawapa fedha za muda wa miezi minne wale vizuka mpaka leo lakini watoto wao hawasomi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inakuwa ni tatizo kubwa, kwamba tumeshaletewa hapa sisi wale maiti tumeshazika lakini watoto hawasomi, familia zimekuwa masikini imekuwa kama wale wanajeshi wastaafu au wengine ambao walikwenda kwenye vita. Tunawapeleka Lebanon, Darfur na kwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri utuambie mpango mkakati wa ziada kuona kwamba watu hawa hasa wajane wanapatiwa fedha zinazostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hayo basi ningeomba kusema kwamba sambamba na hilo Mheshimiwa Waziri utakapokuja utuambie wastaafu walio kuanzia ngazi ya private hadi Brigadier General kwa nini hamrekebishi maslahi yao, tatizo ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ngazi nyingine wanalipwa vizuri wengine hawa mnawadhulumu na wewe ulisha ahidi mwaka wa jana kwamba kuanzia Private hadi Brigadier General, wastaafu hawa wa Jeshi hasa wale wa zamani basi mafao yako katika machakato na mkasema kwamba yako katika hatua ya mwisho ni hatua ipi, mbona mnachelewa sana na hakuna kitu? Naomba Mheshimiwa Waziri na hili uliseme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo machache, nashukuru lakini muda wangu naona kama mmenibia.
Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Malawi pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Amani na Usalama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nitaongea dakika nane na Mheshimiwa Bobali ataongea dakika saba.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nami nitajielekeza kwenye Azimio moja tu ambalo ni Azimio la Kuridhia Itifaki ya Amani na Usalama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (East African Community Protocol on Peace and Security). Katika muktadha wa shughuli nzima za ulinzi na usalama na jinsi ambavyo articles zilivyokuja, naomba nianze na Article 12 ambayo inasema combating trans-national and cross border crimes. Katika mambo ambayo yameelezwa, sitaki nisome sentensi zote lakini nataka niende kwenye ile
(e) illegal migration (uhamiaji haramu).

Mheshimiwa Naibu Spika, katika dhana nzima hii ya uhamiaji haramu, imeonekana kwamba wakati tukiweza kupitia Azimio hili kuridhia Azimio hili, naunga mkono Azimio hili lakini tuangalie ni kwa jinsi gani kwa muda mrefu, pamoja na vipengele vilivyomo katika Azimio hili, vya kuweza kuchukua taratibu, sheria na kanuni, lakini tuangalie ni kwa nini baadhi ya wahamiaji haramu wanaotoka Eritrea, Ethiopia, Somalia wanafika kwetu Tanzania ilhali wanapita katika nchi ya Kenya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo hapa ya kujifunza, tunataka kwenda katika utaratibu ambao tunataka kwenda vizuri na wenzetu kuona kwamba kuna hatua ambazo zitachukuliwa, kuna mikakati ambayo itafanywa, lakini wasiwasi ambao unakuja hapa sasa ni mahusiano, maelewano ya ziada katika shughuli nzima ya kutoka wahamiaji haramu kutoka Eritrea, Ethiopia, Somalia wanaopita Kenya kuja kwetu. Naomba hilo liwe angalizo kubwa katika mkataba wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nenda katika Article 13; preventing and combating cattle rustling, ule wizi wa mifugo. Katika shughuli nzima hii ya wizi wa mifugo kumekuwa na operesheni nyingi sisi wenyewe kwanza hapa. Tulikuwa na Operesheni Tokomeza ambayo ukiangalia Ukanda ule wa Kigoma kulikuwa na mambo mengi, lakini katika maeneo mengine ambayo viongozi hasa wa mipakani walio katika maeneo yale ya wafugaji, wamekuwa wakipata matatizo sana na malalamiko sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kutekeleza itifaki hii na kuiridhia inaonekana viongozi walioko mipakani, Watendaji wa Vijiji, Viongozi wa Chama, sisemi ni chama gani lakini inaonekana wale walio wengi zaidi kwa sababu ndio waliopata ushindi katika maeneo haya wengi wanapata, chama hicho, sitaki kutaja kwa sababu nikitaja itakuwa ni ukakasi, wataanza mambo ya hapa na pale lakini hili ni tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Viongozi hawa wanapokea rushwa, viongozi hawa ndio wanaoingiza mifugo, tumesema mara nyingi lakini bado Serikali imekuwa ikisema kwamba itachukua hatua hii, utaratibu unakwenda, tuna mipango kabambe, mikakati hapa na pale, lakini hakuna kitu. Hilo ni tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakwenda kuridhia mkataba huu, mimi sina pingamizi nimesema naunga mkono kabisa, lakini tuangalie jambo lingine, tunakwenda kuridhia itifaki hii, lakini tuna tatizo kubwa la urejeshaji wa alama za mipaka (beacons). Hili suala ni la ulinzi na usalama, amani na utulivu. Mheshimiwa Shamsi anajua, Mheshimiwa Hussein Mwinyi anajua na wengine wanajua. Tuna tatizo kubwa la urejeshaji wa mipaka katika maeneo mbalimbali, ripoti kadhaa zimesema kwamba baina ya Tanzania pale Tarime na Migori Kenya beacons zimeondolewa kwa muda mrefu, Serikali inasema tuna mkakati, suala hili ni mtambuka, itachukuliwa hatua hapa na pale, hakuna kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumetaja maeneo, kuna Vijiji vya Panyakoo, Ronche, Ikoma, leo kila wakati unasikia kwamba beacons zimeng’olewa, zimeondolewa, lakini utaratibu maalum haupo. Sasa tunakwenda kwenye Itifaki hii lakini kuna mambo sisi wenyewe kwanza kwa kuwa mambo haya ni mtambuka, Wizara ya Ulinzi, Wizara ya Mambo ya Ndani, TAMISEMI, Mambo ya Nje, zote tukae kwa pamoja katika nchi hizo husika wakati tunakwenda kuridhia itifaki hii kuweka utaratibu wetu, hili jambo likae vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, maana inaonekana kama tunasukumwa tu, kwanza tumechelewa. Tangu tarehe 12, Machi iliposainiwa tumekaa miaka minne, tumebakia sisi na Burundi tu, sisi Watanzania ni watu wa mwisho tu, kuna mambo kidogo ya kujifunza hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mambo haya ambayo tunakwenda nayo, basi napenda kusema kwamba Msemaji wa Kambi ya Upinzani alisema kwamba ni vema nchi zetu za Kiafrika ziendelee kujifunza katika kudumisha amani na utulivu katika mambo ya demokrasia pale ambapo mmoja kashindwa akubali matokeo. Unafuta uchaguzi, kwa nini ufute uchaguzi? Kwa mantiki ipi, kwa dhana ipi? Kwa manufaa ya nani? Umeshindwa kaa pembeni kwa sababu hakuna mwenye hatimiliki ya kuongoza, nchi ni yetu sote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo amesema Msemaji wa Kambi ya Upinzani, namshukuru sana Msemaji, Mheshimiwa Cecilia Paresso, amesema jambo kubwa kweli, jambo zuri, jambo jema, amewaambia kwamba katika kudumisha amani na utulivu katika demokrasia hizi za mfumo wa Vyama vingi pale ambapo mmoja atashindwa basi akae pembeni, ni jambo jema sana, na hili tupate kujifunza katika maeneo mbalimbali.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo machache, bila kupigiwa kengele ile ya mwisho, nashukuru sana na naunga mkono Azimio hili la Amani na Usalama, lakini amani iwe ya kweli, isiwe ile amani ya kuigiza igiza.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Sasa ni sauti kutoka Pemba ya kiyakhe inataka kuanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu Subhanah-wataalah kutujalia uzima na afya njema. Leo ni siku ya nane kwenye Kumi la Maghufira. Baada ya hapo, naunga mkono maoni ya Kambi ya Upinzani yaliyokuwa mazuri sana. Nawapongeza Viongozi wetu Wakuu wa UKAWA, Mheshimiwa Freeman Mbowe, Mheshimiwa Riziki pamoja na Mheshimiwa Mbatia. Tunaenda kwenye bajeti hii ambayo ni kiini macho, kizungumkuti na bajeti ya kusadikika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ni bajeti ambayo haitarajii kuondoa maumivu waliyonayo Watanzania kwa sababu zifuatazo: la kwanza, ikiwa tumefikia wakati tuna deni la Taifa shilingi trilioni 50.8 na tumejipangia sisi wenyewe kwenda kulipa kwa mwaka shilingi trilioni 9.6, ina maana kwamba tunaenda kulipa shilingi bilioni 788 kwa kila mwezi. Sambamba na hilo, kuna mishahara shilingi bilioni 600. Kwa hiyo, jumla itakuwa kwa kila mwezi tunatakiwa tulipe shilingi trilioni 1.3 na ushee, lakini makusanyo unaambiwa ni shilingi trilioni 1.4. Ina maana ni bajeti ya kusadikika, bajeti ya kufikirika, ni bajeti ya kwenda kulipa madeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nashangaa na hilo. Watu wanapiga makofi, kumbe tunaenda kulipa madeni tu sisi. Ninachohisi ni kwamba wakati huu mzunguko wa fedha haupo, umaskini unaongezeka, mfumuko wa bei uko juu na juzi tarehe 8 saa 4.10 niliuliza swali hapa Bungeni kwamba katika hiyo APRM Serikali mnajitathmini kiasi gani katika hali hii ya uchumi?

Mheshimiwa Spika, majibu ya Serikali ninayo hapa. Walisema kwamba; changamoto waliyonayo ni ukuaji wa uchumi usiowiana na kupungua kwa umaskini. Uchumi unakua, umaskini haupungui. Leo Mheshimiwa Waziri wa Mipango anakuja anasema aah, umaskini unapungua. Siku hiyo hiyo moja, Serikali hiyo hiyo moja! Tofauti ni dakika tu. Tutakwenda kweli? Nashangaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unapokwenda kuongeza shilingi 40/= za mafuta huko vijijini, wakati wanaotumia, wanaokoboa na kusaga mashine zao, wanaangalia kinachoongezeka kwa siku vijijini. Wanatumia generator, wananunua mafuta ya dizeli; ina maana umewaongezea mzigo wale watumiaji maskini ambao ni wakulima. Halafu unasema unapambana na umaskini. Kuna kitu hapo? Hakuna! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, shilingi 40/= iliyoongezwa huko vijijini ni taabu kweli. Wakoboaji na wanaosaga mashine zile pale huko basi ni shida. Sasa Mheshimiwa unaposema kwamba unataka kuwakomboa maskini, ni kweli! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashangaa. Wala wananchi wa Tanzania hawahitaji maneno yenu ya kitaalam, sijui urari wa kibiashara, deni himilivu eeh, mnasema kwamba maoteo hayajakamilika, amana za benki hazijaiva bado mbichi, madeni chechefu. Hawahitaji hayo madeni chechefu! Maoteo ya fedha yameota mbawa; amana za benki hazijaiva. Zikiwa mbichi? Ndiyo nikasema kama Bunge hili lingekuwa live tukawaambia wananchi haya madeni chechefu, maoteo hajakamilika, amana za benki bado mbichi, hazijaiva vizuri, wananchi wakatusikia, twende kwenye uchaguzi mtazame kama hamtatumia nguvu ya dola nyie. Tuseme sisi na nyie mseme yenu mtazame. Hamtaki kuweka Bunge Live kuwaambia ukweli wananchi. Ni hilo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, naomba niendelee. Kinachonisikitisha, alipotuachia Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, mwishoni tulikuwa tuna deni la Taifa shilingi trilioni 39.1. Ndani ya mwaka mmoja na nusu tumeongeza shilingi trilioni 11. Tuliondoka na shilingi trilioni 39 point, leo tuna shilingi trilioni 50.8. Mwendo kasi. Hapa kazi kweli mwaka huu za kulipa madeni. Nashangaa. Hii haihitaji kufikiri sana na utaalam, madeni chechefu kweli mwaka huu, tutafika kweli? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, shilingi milioni 50 vijijini ni ndoto. Hamna uwezo wa kutekeleza, imekuwa ni hadithi za hapa na pale, paukwa pakawa. Mimi natoka, shauri yenu, mtajua wenyewe.

Mheshimiwa Spika, deni chechefu ni deni baya lililokuwa huna; maana huwezi kulilipa kwa ufupi, ndiyo deni chechefu. Madeni yao chechefu, maana huna hakika ya kuyalipa. Madeni chechefu eeh, maoteo ya fedha, amana za benki hazijaiva bado mbichi, urari wa biashara. Wananchi wanataka nini bwana? Wapeni fedha wananchi sogezeni huko! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hakuna bajeti ya kupandisha mishahara ya wafanyakazi, hakuna. Ndogo sana! Pension ya wazee, watu ambao wametulea, hakuna pension ya wazee wasiojiweza. Hawana bajeti hawa. Wanasema aah, tunapunguza umaskini, deni chechefu. Haya. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, tumeambiwa ukanda ambao unataka uzalishe uvuvi katika Bahari Kuu, amesema Mheshimiwa Mbunge wa kule juu, mrefu mrefu kama mimi kidogo hivi; amesema kwamba uvuvi katika Bahari Kuu bado haujapewa nafasi yake. Ina maana ukiambiwa je, Serikali ina bajeti ya kununua meli za kisasa za uvuvi ambazo tutaweza kuvuna mazao yetu kwenye Bahari Kuu? Serikali hamna bajeti, hakuna kitu. Hawana! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi siku zote tule samaki kutoka China. Nunueni meli ya kisasa, meli kubwa za uvuvi ziende katika Bahari Kuu tuvue samaki. Samaki wanakufa tu huko! Eeh, hawana kitu! Hee, shida mwaka huu. Nashangaa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ukija kwenye afya, Watanzania ambao afya zao wanataka ziende vizuri, bajeti ya Afya kwa Azimio la Abuja 15% ya shilingi trilioni 32 waulize, wameweka? Hakuna. La kwanza hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo hilo tu, ukiangalia katika magonjwa makubwa sasa ambayo yanasumbua Tanzania, ni suala la TB. TB hivi sasa kwa mujibu wa wataalam ambao wametupa semina juzi, wagonjwa wa TB kwa kila siku wanakufa 150. Ni mabasi maana yake yanapotea, lakini ukiwaambia je, ni kiasi gani mmeweka fedha za kupambana na TB, hakuna.

Mheshimiwa Spika, kuna mkakati gani kwenye mikutano ya hadhara, mna mkakati gani katika maeneo mengine ya migodi kukomesha mambo haya na kupunguza mambo ya TB? Hakuna. Aah, urari wa biashara huo! (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, wastaafu. Aah, mwaka huu! Ukiwaambia wastaafu, wanakwambia aah, sisi tumetoka tangu mwaka 2016, kipindi gani, tumeweka wastaafu wa chini wale Sh.100,000/=. Hivi ni kweli inatosha? Itapunguza kweli umaskini!

Mheshimiwa Spika, hii Serikali, nikasema kwamba kwa nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, Ripoti ya CAG, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alisema hapa kwamba kuna wizi wa fedha karibu shilingi bilioni 92. Hii ni mkataba baina ya Shirika la Ndege la ATCL ilipoingia mkataba na South African Airways wakati wamekodi ndege kutoka China, Air Bus. Ndege hizi kwa bahati mbaya sana zimetusababishia hasara ambayo ni kubwa.

Mheshimiwa Spika, hapa imekuja wakati ndege hizi zililetwa hapa zikafanya kazi kwa muda wa miezi sita tena kwa kubahatisha. Ndege zikaondolewa zikapelekwa Ufaransa, mkazipaka rangi. Baada ya kupaka rangi, mkaziondoa mkazipeleka Guinea, mkazipaka rangi, baadaye hakuna aliyekamatwa. Deni chechefu hilo. Bado tu umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wapo, majibu ya Serikali yanasema kwamba TAKUKURU bado ipo kwenye mkakati wa kuchunguza, mnachunguza nini? Kumbe mnalindana? Wengine wakamatwe watumbuliwe, wengine wabinywe, wengine wapekuliwe. Hilo hamlijui Serikali au bado tu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashangaa! Sauti ya chombezo toka Pemba hiyo! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilifikiria kwamba Serikali hii itakuwa makini kuangalia namna gani ya kuwakomboa Watanzania katika hali ya umaskini? Ni namna gani ambapo mtapambana na umaskini? Namna gani mtadhibiti mfumuko wa bei? Namna gani ambavyo mtaangalia kwamba umaskini uliopo hivi sasa unachangiwa na mambo gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanasema katika ripoti yao Ukanda wa Pwani wana viwanda vidogo vidogo, sekta binafsi 82 ambavyo watajenga, lakini Serikali inasema itatoa vibali, watatoa leseni, sijui watatoa na ardhi. Ukiuliza huko Mkoa wa Pwani kwenyewe ni vichekesho.

Mheshimiwa Spika, sasa ninachoona ni kwamba, kwa hali tunayokwenda nayo hivi sasa ni kwamba, kuna tatizo kubwa sana, Serikali haijajipanga vizuri. Ukija kwenye mambo ya haya makinikia yanaitwa, haya sawa, kwani muda wote upungufu huu wa mabilioni ya fedha, matrilioni, Serikali iliyokuwepo; Serikali gani? Ya chama gani? Si Chama cha Mapinduzi! Serikali ipi? Mawaziri si ndio hao hao! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huo upotevu wa madini hayo yanayosemwa, kama kuna watu wamefanya ubadhirifu mkubwa, sawa nakubali, lakini tulipokuwa tukisema hapa Bungeni leteni mikataba, mlikuwa hamtaki kuleta mikataba. Ndiyo urari wa biashara huo. Haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siungi mkono hoja. Bajeti ni mbaya, inaenda kuumiza Watanzania. Nashukuru sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala kunijalia uzima na afya njema kuweza kuchangia mapendekezo ya Mpango huu wa mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze wananchi wangu wa Jimbo la Mtambile kwa kuendelea kuniamini na kunipa baraka zote, halikadhalika nikipongeze Chama Wananchi CUF kwa kuendelea kuwa imara katika harakati mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo nataka nianze kumwambia ndugu yangu Dkt. Philip Mpango wa Waziri wa Mpango, yeye mwenyewe kwanza alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mipango kwa muda wa miaka kumi, sasa kama si hivyo naomba basi niendelee kwa kusema kwamba mpango huu ambao umetuletea ningependa kujua kwanza tathimini ya mpango uliopita umefikia hatua gani na wakati huu mpango huu mpya, hilo lilikuwa la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kile kinachoitwa mkakati wa Tanzania ya viwanda kuelekea uchumi wa kati, ni kwamba Serikali mara kadhaa imekuja hapa Bungeni ikituambia kwamba ina mkakati wa kufufua viwanda vilivyobinafsishwa. Serikali mara kadhaa imekuwa ikituambia viwanda vyote vile ambavyo vilibinafsishwa lakini baadaye wakapewa wawekezaji ambao hawaviendelezi watatajwa majina yao na kitajulikana nini cha kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujielekeza katika viwanda vilivyobinafsishwa katika Mikoa ya Lindi na Mtwara, vile viwanda vya korosho, Mheshimiwa Waziri utuambie leo hii viwanda vya korosho vilivyobinafsishwa ambavyo asili yake/mwanzo wake kulikwepo na mkopo kutoka Italy na Japan kwenye miaka ya 1980 dola milioni 20, zikachukuliwa kujengwa viwanda vile ili kuondokana na tatizo la kuuza korosho ghafi nje ya nchi.

Leo viwanda vimebinafsishwa, vimechukuliwa, mmewapa mliowapa, mmepeana sadaka kwa watu mnaojuana. Mheshimiwa Waziri naomba unipe ujasiri na utuambie hapa viwanda vile mmewapa akina nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchunguzi unaonekana mmepeana wenyewe kwa wenyewe kwa bei chee, vigogo wa Serikalini, utuambie ni akina nani na kwa nini haviendelezwi? Leo bei ya korosho ghafi Mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Morogoro imefika shilingi 3,800; lakini mnasema kwamba watu wale mtawaita, mpaka leo hawapo. Mtuambie mmewapa akina nani? Mtuambie Kiwanda cha Lindi Mjini nani anayemiliki? Newala One nani anayemiliki? Newala Two nani anayemiliki?, TANITA yote One na Two ni nani anayemiliki? Kwa nini hamtuambii? Kwa nini hamko wazi kutuambia viwanda hivyo? Na mnasema kwenye Katiba ukurasa wa 20 kwenye haki na wajibu kuna haki ya usawa, kwamba watu wote ni sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuulize Mheshimiwa Waziri haki sawa iende kwa nani? Na wale wasiotenda haki? Nashangaa kwamba leo mmesema mtatuletea majina ya watu wote waliochukua viwanda hawaviendelezi, mkasema mko wazi, lakini leo hakuna kitu, wengine mnawataja, wengine hamuwataji, shida! Hilo ni tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kuna kiwanda mtuambie cha kusindika samaki (TAFICO) Dar es Salaam hatua yake imefikia wapi? Anayemiliki ni nani? Mtuletee Bungeni mtueleweshe, wananchi wanalalamika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala zima la wafanyabiashara wadogo wadogo. Kuna malalamiko makubwa ya jinsi gani ya hali ya maisha wakati huu ilivyokuwa ni ngumu. Mzunguko wa pesa umekuwa ni mdogo, wafanyabiashara mbalimbali katika masoko ya vyakula na mboga mboga wamekuwa wakilalamika, Kariakoo maduka yamefungwa wateja wamepungua, Mheshimiwa Waziri Mpango anasema uchumi umeimarika, uchumi kuimarika kuna takwimu zenu mnazosema umeimarika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mimi niseme, si muda mrefu hapa Mheshimiwa Mbunge wa Mtwara au Lindi kule Kusini amezungumzia tatizo la wakulima wa mbaazi. Leo mbaazi kilo shilingi 150, shilingi 200, shilingi 300. Mheshimiwa wewe mwenyewe unajua kwamba kuna Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015 kifungu cha 43(1) kinaeleza kwamba ikiwa fedha zilizoidhinishwa na Bunge hazikutosha kutokana na majukumu yake Serikali inaweza kuwasilisha Bungeni bajeti ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli mnawapenda wananchi wa Lindi na Mtwara Serikali mnashindwa nini kuleta hapa Bungeni kuongeza bajeti ya kununua mbaazi za Lindi na Mtwara na maeneo mengine kama ya huko Babati?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi mnazungumzia MKUKUTA kumbe MKUKUTA wa maneno. Serikali leteni hapa bajeti ya nyongeza ili sisi Wabunge tuweze kuidhinisha ili wakulima wale ambao wamegharamika kwa gharama kubwa ya kulima mbaazi, mbaazi zao zisiharibike, lakini leo wapi maskini! Tuseme nini? Huu ndio wakati maalum wa kuweza kuboresha maisha ya wakulima, lakini nashangaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Jenista umekaa miaka mingi, washauri wenzako hawa kwamba wakulima wanapata shida sana. Serikali ilete Bungeni tuidhinishe bajeti ya nyongeza ili mbaazi zinunuliwe ili angalau wakulima wapate manufaa wasiingie kwenye hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mambo kama haya yananitia uchungu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la wavuvi. Serikali mara nyingi imekuwa ikijisifia hapa Bungeni namna ya kuchoma nyavu tu za wavuvi. Mheshimiwa Mpango utuambie una mpango gani wa kuwaboresha wavuvi wadogo wadogo kwa kuwapa mikopo, kuwasaidia wavuvi katika bahari na katika maziwa? Mpango uko wapi? Nimeangalia mpango wako huu na nilikwambia mwanzo, tathmini yako ya mpango uliopita uko wapi kuhusu maeneo mbalimbali? Wavuvi wameachwa, wametupwa, hakuna jambo lolote la kuwasaidia, hakuna mikopo kwa wavuvi wa baharini na wale wa kwenye maziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikuombe Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango Waziri wa Mpango utuambie una mkakati gani, una mpango gani hasa wa kuboresha maisha haya ya wavuvi wadogo wadogo? Kuna kurasa kidogo tu umeandika hapa kuhusu wavuvi, lakini tatizo ni kubwa. Mvuvi ambaye ana mtungi wake wa gesi akienda katika maeneo mbalimbali anaambiwa anafanya uvuvi haramu, anakamatwa na anachomewa nyavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Mpango atuambie dagaa mchele wale ambao bila shaka nawe umeshawahi kula, wanavuliwa na nyavu ya aina gani? Utuambie. Umekula dagaa mchele wewe, mara nyingi, nasikia unapenda kweli. Tuambie nyavu zile mnazochoma, dagaa mchele winavuliwa na nyavu za aina gani? Mumekuwa mabingwa wa kuchomna nyavu kila wakati mnajisifia, utuambie mikakati yao. Wavuvi mikopo hamuwapi, nyavu zao mnachoma, mikakati ya kuboresha hakuna, Serikali haina mpango wa kununua meli za kisasa na kubwa za kuvua bahari kuu, Serikali haina mpango wowote. Mnakuja na mipango, mna mpango au mna mipangilio? Shida. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyeiti, suala la maji hapa ni kizungumkuti cha muda wa miaka na miaka. Leo wananchi wa Tabora hawa rafiki zangu Wanyamwezi na Wakisukuma ukifika wakati wa uchaguzi kampeni yao kubwa ni maji, wanakwenda kwenye majukwaa; “nalilomba kura zing’we mnine pye bhose wadugu wanu” hawa. (Makofi/Kicheko)

Leo waambie Tabora, Bwawa la Igombe limekauka, yaani Tabora maji hakuna kabisa. Kuna Mradi wa Ziwa Victoria ni wa muda mrefu, wa muda mfupi uko wapi? Ukienda zako Njombe Mjini, Makambako, Wanging’ombe, Maswa, Buchosa huko kwa Mheshimiwa Waziri kote maji ni shida, ni malalamiko matupu, kwenye tv tunaona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kule Magu tarafa ya Ndagalu maji hakuna, nako waende wakaseme sasa; “nalilomba kura zing’we mnine pye bhose wadugu wanu” kauli ndio shida, ndio taabu kama wataipata hawa, hawapati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la maji limekuwa la muda mrefu, tangu enzi na enzi. Sasa mkakati wa muda mrefu ni Ziwa Victoria, mkakati wa muda mfupi wa pale Tabora ni upi? Wale wenye visima vyao ni wachache sana, leo kuna shida kubwa lakini Serikali tukisema sisi eehh jamani! Serikali ichangamke, ihangaike kutafuta maeneo mengine au njia mbadala ya kuweza kupatikana kwa maji. Tatizo hakuna chochote kinachokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka nizungumzie suala la mafao ya wastaafu. Hamgusii mpango endelevu wa mafao ya wastaafu, hakuna, pension iliyobakia ni ile ile. Leo walimu uliwaahidi miaka kadhaa kwamba mtawapa teaching allowance, posho ya kufundishia lakini hakuna kitu, posho ya kufundishia hakuna kwa walimu na ile ndiyo motisha. Mliahidi tangu mwaka 2012, tena ni ninyi wenyewe Serikali kwamba mtatoa teaching allowance kwa walimu; hakuna kitu, mpango uko wapi? Mna mpango wa kweli wa kuboresha maslahi ya walimu? Maana mnasema elimu inashuka, tatizo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nadhani Serikali sasa inagalie mapungufu yake mbalimbali lakini mhakikishe kwamba wastaafu na…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pia niwapongeze wawasilishaji wote wawili. Nianze na dawa tu tunazotumia binadamu ambapo ni matumaini kwamba kiwango cha ubora wa dawa za binadamu zinafanyiwa utafiti wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina masikitiko, baada ya dawa kutumia muda wa miaka mitano au miaka kumi tunaambiwa dawa hizo hasa hazifai zina madhara, hivi hamkufanya utafiti wa kutosha? Leo kuna baadhi ya dawa unaambiwa kabisa dawa hizi chroloquine usitumie tena, metakelfin zina madhara, hivi sisi ndio majaribio ya hizo dawa? Tumeshapata matatizo mengi, watu wameshaathirika na matatizo mbalimbali wanaambiwa sasa ninyi hizo dawa msitumie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, wafanye majaribio ya kutosha kwa viumbe vingine sio binadamu, sio Watanzania. Nafikiri Mheshimiwa Waziri atuambie sasa kwa nini tunatumia dawa hizi, tunapata madhara ndio wanasema baadhi ya dawa hizi hazifai. Kwa nini wasifanye majaribio kwenye viumbe vingine ambavyo sio binadamu, tatizo ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ubora wa dawa zenyewe, unapokwenda maduka ya dawa (pharmacy) unaambiwa unataka ya India, Ujerumani, Kenya au ya Tanzania, dawa hiyo hiyo ya aina moja, imesemwa kwenye semina, tatizo ni nini. Sasa kumbe ni kiwango cha ubora wa dawa zenyewe, nchi zinakotoka kuna ubora tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi tunataka tujue Mheshimiwa Waziri atuambie sasa baadhi ya madhara wanayoyapata Watanzania baada ya kutumia dawa katika nchi fulani, nchi ambazo inaonekana dawa zake ni hafifu hazina standard inayotakiwa. Hilo pia Mheshimiwa Waziri atuambie ana mkakati gani wa ziada kuelimisha jamii juu ya jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo vya kulelea watoto yatima wanaoishi na VVU/UKIMWI na mazingira magumu. Mbona vitu hivi hamvipi umuhimu unaostahili? Ukienda katika maeneo mbalimbali unaona huruma, watoto hawa hawana lishe, masomo ni shida, nguo ni shida, ni tabu, lakini ukija hapa Serikali ukiwaambia wana mkakati gani wa ziada juu ya watoto hawa kujua maisha, masomo na lishe zao wanasema tuna mkakati wa ziada. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yote nikwambie, Serikali haitaki kukubali lile Azimio la Abuja la kutenga fedha inayostahili halafu wamewaachia wafadhili zaidi, umeona wapi wewe wa mwenye shamba unasema msaidizi mwenye shamba ndio atamaliza hiyo kazi. Hili ni jambo moja kubwa ambalo linatia wasiwasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti hasa wa takwimu za hali ya maambukizi ya VVU na UKIMWI. Ukiangalia TACAIDS, TACOSOA na mashirika mengine unaambiwa kwamba Dodoma ni 2.9, ukienda TACAIDS 2.9 na TACOSOA 2.9 na wewe ni mjumbe lakini ukikaa Dodoma yenyewe ukisoma mazingira ya Dodoma yenyewe, ukikaa na wataalam mbalimbali na ukifanya uchunguzi vizuri hospitali mbona mnadanganya watu Dodoma ni zaidi ya 2.9, tusidanganyane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu ambazo mnazitoa sio halisia, ni kwa nini ukienda TACAIDS 2.9, TACOSOA 2.9 Mheshimiwa Waziri mnapofanya sherehe mbalimbali hapa Dodoma waambieni hali halisi ya ukweli ulivyo. Ukiangalia hali halisi hapa na pale mikusanyiko mikubwa ya watu, vyuo vya hapa zaidi ya wanafunzi 15,000. Ukiangalia hapa madereva wanaosafiri masafa marefu wanakaa hapa na mambo mengine mbalimbali yapo hapa. Sasa waambieni ukweli wananchi wa Dodoma kwamba hali sio shwari sana, lakini mnawapa moyo aah! Dodoma ipo vizuri sana ni 2.9 jamani mnataka muwamalize hata Dodoma, shauri yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka nizungumzie ni suala zima la swali langu la asubuhi, suala la posho ya kufundishia kwa Walimu (teaching allowance). Huu ni mwaka wa sita tangu Serikali ikubali kwamba Walimu watapatiwa posho ya kufundishia, tangu Oktoba mwaka 2012 mpaka leo Walimu hawajapatiwa teaching allowance, wamepewa Wakuu wa Shule na Waratibu, wamepewa peke yao hao tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifika hapa, Serikali wanasema aaa tupo katika mkakati, Serikali ni sikivu, imepanga mikakati madhubuti, si muda mrefu Walimu watapata hizo fedha. Tunataka Mheshimiwa Waziri wa Elimu atuambie, simwoni sijui yuko wapo, yupo kule pembeni, atuambie sasa ni lini Walimu watapata teaching allowance. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Namshukuru Mwenyezi Mungu, Subhanah Wataalah kwa kupata fursa kuchangia juu ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na ulinzi wa amani. Sisi kama Tanzania kama wanachama wa Umoja wa Mataifa, tunaendelea na taratibu zetu hizo, lakini katika ukurasa wa 26 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri kuhusu ulinzi wa amani huko DRC Kongo, kuna wanajeshi 19 ambao wamepoteza maisha na 66 ambao wamejeruhiwa. Katika maelezo, Mheshimiwa Waziri alisema ni shambulio la kushtukiza na pia Maafisa Askari wetu walichelewa kupata msaada stahiki kwa wakati kutoka kwa MONUSCO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Mheshimiwa Waziri, suala la kupata msaada unaostahili kwa wakati, naomba mara hii iwe ni mwisho, kwamba vifo vimetosha; wanajeshi wetu wako vizuri. Ni kwamba hapa inaonekana bado kuna peace keeping, siyo enforcement keeping. Katika mtandao wa UN wa Peacekeeping wameleta jina la Private Mohamed Haji Ally ambaye tangu tarehe 7 Desemba, 2017 haonekani kule DRC, mbali na hawa 19.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari imesambaa kwenye mitandao ya kijamii. Wazazi wake wametupa maelezo haya tumuulize Mheshimiwa Waziri, Private Mohamed Haji Ally, je, yuko hai au ni miongoni mwa waliokufa? Maana hapa Pemba na Unguja hayupo. Maiti yake haijaletwa. Tunaomba maelezo wakati wa kuhitimisha hili jambo. Hilo lilikuwa la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, baada ya vifo kutokea, wale wajane wanaopaswa kupata stahiki, wanapata kutoka kwenye UN na baadhi ya fedha nyingine kwenda kwenye Serikali. Kama Askari huyu angekuwa hai, angekwenda kupatiwa mafao yake, wakati wa kustaafu anapata pensheni. Wajane hawa inaonekana hawapati pensheni kwa kipindi ambacho mume wake kama angekuwa hai au angestaafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, wakati anafanya majumuisho, atupe utaratibu stahiki, kuna malalamiko mengi. Je, baada ya vifo hivi 19 kutokea, wale wajane wataendelea kupata fedha wanayostahiki na pensheni mpaka umri wa kustaafu wa waume zao waliokufa? Hilo jambo lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba, mara nyingi Serikali imekuwa ikisema inawahurumiwa wananchi. Katika jambo linalowakera wananchi ni tathmini ya fidia ya malipo kwa wananchi wa maeneo yaliyochukuliwa na Jeshi. Tangu mwaka 2016, Serikali imekuwa ikiahidi hapa Bungeni itatoa fidia kwa maeneo waliyoyachukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mara kadhaa wamekuwa wakitenga shilingi bilioni 27, fedha hazitolewi. Safari hii nashukuru zimetengwa shilingi bilioni 20.9, lakini kwenye hotuba, nashukuru Mungu wamesema kwamba Rasi Mshindo, Mji Mdogo wa Kilwa Masoko, Vitongoji vile vya Chomolo na Kisangi vipewe kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nasisitiza, katika maeneo haya ya Rasi Mshindo, Mji Mdogo wa Kilwa Masoko, vitongoji vya Chomolo na Kisangi, fedha zitolewe haraka. Wananchi wengine wameshakufa, wamepoteza maisha, fedha hizi hazitolewi, Jeshi limechukua maeneo mengi kwa wananchi na fedha za maendeleo hazitolewi. Mheshimiwa Waziri, jambo hili limekuwa ni kubwa sana. Wananchi wamekata tamaa, wanasema wameshanyang’anywa, wamedhulumiwa na Jeshi. Ikiwa miaka na miaka, tangu miaka takriban 18 au 20, fedha hazitolewi, wananchi tayari wamepoteza imani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha hizi shilingi bilioni 20.9 zitolewe. Mbona mambo mengine Serikali wanafanya, mtashindwa na hili, kwa nini? Nashangaa!

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye JKT, wametenga shilingi milioni 225, wanataka kulipa fidia kwa maeneo ambayo yamechukuliwa na Jeshi. Ni jambo jema, lakini hizi fedha nazo zitolewe. Nashukuru sana, namwomba Mheshimiwa Waziri, fedha hizi nazo shilingi milioni 225 ambazo zimetengwa, zitolewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala zima la Sheria ya Ulinzi. Imezungumzwa kidogo hapa, tangu mwaka 1966 hadi leo miaka 52, Sheria hii haijabadilika, haijafanyiwa maboresho. Tunaambiwa ipo katika mchakato, sijui rasimu tayari, lakini kama Jeshi ambalo linaendana na taratibu za kisasa, ikifika miaka 52 halina maboresho, ni tatizo. Hii inasababisha mpaka athari ya mafao kwa wastaafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wale walio katika cheo cha private mpaka Brigadier General ni tatizo kubwa. Mafao yao wanapostaafu yanakuwa ni madogo sana. Tatizo ni kwamba sera haipo, sheria haijabadilishwa, Wanajeshi wanapata taabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri akija hapa leo kufanya majumuisho, atuambie kuhusu michakato hii, kwa sababu inaathiri mafao hasa wanapostaafu. Leo Askari private mpaka Brigadier General fedha anazopata wakati anastaafu ni aibu. Sasa watuambie, sisi tuko hapa kwa ajili ya wananchi. Kila mara michakato, mipango iko mbioni, nashangaa! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amezungumza alama za mipaka (beacons) akaeleza taratibu nzuri za kule Uganda. Mbona hatuambii urejeshaji wa alama za mipaka (beacons) kati ya Tanzania na Kenya, yaani Migori na Tarime? Kuna vijiji vimetajwa miaka kadhaa, kuna viashiria ambavyo siyo vizuri; Vijiji vya Panyakoo, Ronche na Ikoma, vimetajwa lakini hawarejeshi. Mheshimiwa Waziri hajatuambia kwenye hotuba yake.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala aliyetujalia uzima na afya njema katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani, tuwatakie sote tunaofunga Mwenyezi Mungu a-taqabbal funga zetu, atulipe ujira mwema, na Insha Allah bi-idhinillah malipo ya kheri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mhehimiwa Waziri muhusika, tatizo la mahujaji waliosota, waliokaa muda mrefu wakati wanakwenda Hija mwaka uliopita tatizo hili lisirejee tena. Ilikuwa ni aibu kubwa, tatizo kubwa, lilileta taswira mbaya miongoni mwa watu mbalimbali. Wizara husika ni Wizara hii hii. Kwa watu wote wanaoshughulika na kwenda nje kwa vyovyote iwavyo bado Wizara ya Mambo ya Nje inahusika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu wazi wazi; tumekuwa tukipiga kelele kwamba wameiandikia BAKWATA tena kuwapa Mamlaka na madaraka ya kuwapeleka watu Mahujaji hawa kwenda kuhijji, tafadhali sana BAKWATA kama Taasisi nyingine kwa hiyo msiwape mamlaka, yakitokea mambo mengine hasa tutasema kwamba BAKWATA ni sehemu ya Serikali na ndivyo inavyonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunachosema ni kwamba waacheni taasisi nyingine za kidini ziandae utaratibu wake wa kupeleka mahujaji Makka, ndiyo nikasema sasa ni vyema tujitathmini na hili. Upungufu huu wa kupeleka Mahujaji Makka dosari hii isitokee tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, APRM (African Pear Review Mechanism), mpango wa kujitathmini wenyewe kiutawala bora, kisiasa, kiuchumi na mambo mengine. Nashukuru kwamba wameongeza fedha. Hata hivyo, nataka Mheshimiwa Waziri aniambie kisiasa wamejitathmini kiasi gani kwa wakati huu pale ambapo mwendelezo au wanakaa mahabusu muda mrefu Mahakamani, unaambiwa upelelezi haujakamilika. Masheikh wa Uamsho wamekaa muda mrefu, juzi tu Mheshimiwa Waziri alisema kwamba ushahidi umepatikana, wanasubiri e-mail kutoka nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi watu wanakaa mahabusu miaka minne, miaka mitano hili hawalioni, wanataka tafsiri nyingine zije tafsiri za aina gani? Masheikh wa Uamisho wamekaa muda mrefu sana. Kwa hiyo wanajitathmini kiasi gani? Amesema Mheshimiwa Bwege mpaka akatoka machozi. Watu wamepigwa risasi Msikitini kule Chumo, damu imemwagwa msikitini Chumo. Tafadhali sana, hakuna kitu kibaya katika mambo haya ya hisia za dini. Waliopigwa risasi kule Chumo msikitini liwe jambo la mwisho tafadhalini sana. Mheshimiwa Mahiga anifahamu na walionifahamu wanifahamu, wale Taasisi za Serikali za kiulinzi wanifahamu, risasi msikitini isilie tena maisha, tafadhalini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina suala lingine ambalo ni juu ya mahusiano yetu ya mambo ya nje na Mataifa mbalimbali uko vizuri. Nafahamu uhusiano mzuri tulionao sisi na Msumbiji, nafahamu jinsi Tanzania ilivyoshiriki katika ukombozi ule wa Msumbiji, nafahamu mambo mengi mazuri yetu sisi na Msumbiji na mimi naunga mkono. Kuna Watanzania ambao wako gerezani kule Msumbiji katika Gereza la Beyo kule eneo la Pemba ambao wako gerezani hasa kwa muda wa miezi sita. Hawa ni wapiga kura na kwa mahusiano mazuri sisi na Msumbiji na nadhani nampongeza sana Balozi wetu Monica hapa leo yupo hongera, sana nampongeza sana Balozi Monica. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu hawa naomba sana niwataje kwa majina wapo Beyo hapo Msumbiji kwenye Gereza hilo. Kwanza kutoka Jimbo la Kiwani na Mtambile Jimboni kwangu na hawa wamefanya makosa madogo madogo tu, hawana yale makosa makubwa ukasema makosa yale labda ya madawa ya kulevya; nao ni Shahali Makame Omary wa Chole-Kiwani; Fadhili Khamisi Makame, Chole-Kiwani; Khamisi Fadhili Khamisi, Chole-Kiwani; Mussa Rare Mussa, Chole-Kiwani; Ally Zidini Ngali, Chole-Kiwani; Zahoro Ngwali Ally, Chole-Kiwani; Zaharani Fadhili Khamisi, Chole-Kiwani; Silima Yakoub Ally, Chole-Kiwani; Ally Shahali Makame, Chole-Kiwani; Mbarouk Hijja Silima, Chole-Kiwani; na Juma Tabu Mussa, Chole-Kiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Jimbo la Ziwani kuna Abdallah Khalfani, wa Wesha; na Hamza Fikira Sharif, wa Wesha. Kuna Jimbo la Mkoani nako kuna Makame Burhani Kombo, wa Chokocho; na Faki Shahali, wa Chokocho. Donge-Unguja yuko Mselem Khalfani Mohamed na Chumu Mshenga, hawa wako kwenye gereza la Beyo huko Pemba-Msumbiji. Tafadhali sana, kwa ujirani tulionao na ubora wa Balozi wetu Monica ninavyomwona yuko vizuri sana, hongera sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hili jambo walichukue, utaratibu wa nchi nyingine wanakuwa wanafahamiana, utaratibu wa kuwarudisha mahabusu au wafungwa kutoka nchi hizo sembuse hapo jirani tu. Naombeni sana hawa watu waandae mazingira mazuri waweze kuwarejesha. Nina imani kwa ujumbe huo Mheshimiwa ataweza kufanya jambo lolote la msingi la kuweza kufanya shughuli zinazohitajika.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye jambo lingine la tatu ambalo ni miradi ya maendeleo. Mara nyingi tunasema kwamba baadhi ya miradi ya maendeleo inataka itekelezwe kwa wakati wake. Kuna miradi inayopaswa kutekelezwa katika Visiwa vya Unguja na Pemba yaani Zanzibar. Mpiga duru yupo katika mikakati, naomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie suala la mpiga duru.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni miaka kadhaa wamekuwa wakisema kwamba wana mpango mkakati wa kuboresha uwanja wa ndege Pemba, lakini kila mara wanataja, wanataja katika mipango yao hii ya kiujumla katika bajeti hii ya Afrika mashariki. Ni kwa nini na ni sababu zipi za msingi zilizopelekea uwanja wa Ndege, Pemba haupewi kipaumbele ukapewa nafasi yake ili ile dhana ya uchumi unaohitajika ukaendelea, tatizo ni nini? Pemba ipo Tanzania nataka wafahamu haiko sehemu nyingine yoyote.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bandari ya Mkoani walisema muda mrefu kwamba nayo wataiboresha, watakwenda vizuri lakini hadi leo inaonekana bado ni danganya toto. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa aniambie habari ya mpiga duru, aniambie habari ya uwanja wa Ndege wa Pemba, anipe habari rasmi ya Bandari ya Mkoani na Bandari ya Wete. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, atumishi ambao wako katika Balozi inafika wakati Maafisa huwa hawapeleki kwa wakati na ile dhana ya diplomasia ya kiuchumi inakuwa inasuasua. Naomba waniambie sasa kwamba kwa nini wanakuwa na kigugumizi cha kupeleka Maafisa kwenye Balozi kwa haraka haraka pale ambapo wengine wameshamaliza muda wao. Anipe habari, nataka kujua kule Ankara, Uturuki, anipe habari ya Korea, Doha-Qatar, Brussels ambapo kuna vikao vingi ya European Union nako sasa hawapo au ni kidogo sana. Addis Ababa napo ni tatizo, New York nako vilevile.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hili tatizo ni lini wataweza kulisawazisha kwamba tunasema tuna economic diplomacy (diplomasia ya kiuchumi) lakini Maafisa wale wa Ubalozi ambao wanahitajika kwenda kule hawako, sasa hili nalo ni tatizo. Sasa Mheshimiwa Waziri aniambie jambo hili ni lini litakaa vizuri.

Mheshimiwa naibu Spika, la mwisho, tuepukane na aibu kubwa ambayo tunaipata kwenye vile viwanja ambavyo haviendelezwi. Majengo ambayo wanataka kuyakarabati hapa yapo, lakini kila wakati tunaweka bajeti tu lakini fedha zile hazipelekwi. Kwa hiyo atuambie sasa mkakati wa kuepukana na aibu ni upi. Leo tunaambiwa kwamba Tanzaia itashtakiwa katika nchi husika kwamba majengo yale ni machakavu, mabovu na viwanja haviendelezwi. Nimwambie Mheshimiwa Waziri, hii ni aibu kwa Taifa kama letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema sasa tujifunze, tuepukane na aibu kwa nchi za nje, tunajitia aibu sisi wenyewe kwa sababu hatupeleki zile fedha. Kama ingekuwa tunaona kwamba kuepuka aibu Mataifa ya wenzetu wasiweze kututafsiri vinginevyo, basi majengo hayo tungeyakarabati, tungepeleka fedha na vile viwanja ambavyo vilitaka kuchukuliwa ambavyo vimekuwa ni pori na tunataka kushtakiwa ile aibu sisi tungekuwa hatunayo. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, kwa sababu Serikali ni moja waandae mazingira kuona kwamba majengo yetu yanakarabatiwa, fedha zinapelekwa na vile viwanja ambavyo vinatia aibu, aibu hiyo inaondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie la mwisho, ni hati za utambulisho (Present Credential), wamepanga mara kadhaa Mheshimiwa Naibu Waziri, hizi hati za utambulisho katika maeneo ambayo tumepanga basi tufanye kweli.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru, kama Serikali inataka kuambiwa ukweli ili ijirekebishe bajeti ya 2018/2019 ni bajeti ya kuwadanganya Watanzania, ya kufikirika, ya kusadikika na isiyo tekelezeka. Ni bajeti ambayo kwa kweli imewahadaa Watanzania na hasa wakulima. Ikiwa leo wakulima wametengewa asilimia 0.4 ya fedha za maendeleo ndani ya fedha za bajeti ya maendeleo ya shilingi trilioni 12 ukiachia shilingi trilioni 2.1 fedha za nje, hivi Tanzania ya viwanda kuelekea uchumi wa kati ni kweli inawezekana? Mnawadharau wakulima tangu bajeti iliyopita mwaka 2017/2018 walitengewa shilingi bilioni 150.2 mkapeleka shilingi bilioni 16.5 hadi mwezi Machi sawa na asilimia 11, Tanzania ya viwanda iko wapi? Mmewatelekeza wavuvi, leo wavuvi bajeti ya maendeleo kwa mwaka huu mmetenga 0.06 ndani ya shilingi trilioni hizo ambazo nimezitaja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli Serikali kama inataka kuambiwa ukweli ni kwamba wavuvi wametelekezwa, wakulima wametelekezwa na mifugo imetelekezwa. Sasa nauliza mkakati wenu wa Serikali wa kuboresha uvuvi uko wapi, hauonekani. Wananchi wa Mtwara, Lindi, Dar es Salaam mpaka Tanga mkakati wa kuboresha maisha yao uko wapi? Kwenye maziwa nako vilevile, Mikoa ambayo iko katika Ziwa Viktoria, Ziwa Tanganyika na maziwa mengine, yote hakuna mkakati, bajeti yao ni 0.06 ya fedha za maendeleo, ina maana Serikali haina mkakati. Mkakati mkubwa unaojulikana ni kuchoma nyavu moto na kupeleka wapimaji wa samaki kantini, tutafika kweli? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nashangaa kweli kweli, ukiangalia Vote 99, Ministry of Livestock Development and Fisheries Livestock, Subvote 1001, item 22010 Travel-In-Country, hii ndiyo Waziri mwenyewe, wametoka kwenye Sh.108,960,000 hadi shilingi milioni 300 safari za ndani kumbe ni za kuchoma nyavu moto na kupima kantini samaki wa Bunge. Hili halikubaliki lazima tubadilike tuendane na wakati ulivyo kwamba wavuvi mmewaacha kuendelea kuwa maskini, nchi nyingine duniani wanaandaa mazingira mazuri kuwawezesha wavuvi wadogo wadogo kutafuta vyombo mbalimbali baadaye wanakwenda kuvua bahari kuu na Serikali inapata mapato, lakini nyie mkiambiwa mnasema sisi siyo wazalendo, hatuwezi kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nigusie jambo lingine, nimesema bajeti hii ni kiini macho, ni kizungumkuti kwa sababu kwenye ukurasa 78 hakuna uhalisia wa ukweli wa matumizi ya lazima yanayoendana na mapato. Deni la Taifa ni shilingi trilioni 10 kwa hivyo kwa kila mwezi zinatakiwa zipatikane shilingi bilioni 833, ukienda kwenye mishahara shilingi trilioni 7.4 kwa kila mwezi lazima zipatakine shiling bilioni 617, matumizi mengineyo ni shilingi bilioni 3, kila mwezi ipatikane shilingi bilioni 254, shilingi trilioni 1.7 mtaipata wapi na hamna makusanyo? Tukisema vyanzo chukueni vyanzo hamtaki, hamueleweki. Amesema Mheshimiwa mmoja pale Mheshimiwa Mgimwa, kwamba Waziri usiwe mgumu ukubali ushauri wa Waheshimiwa Wabunge. Ikiwa makusanyo ya mwisho ni shilingi trilioni 1.2 mpaka 3, leo mnataka ipatikane shilingi trilioni 1.7 ya lazima, hamna kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tena basi angalia ukurasa wa 74 wa kitabu chao kuna shilingi trilioni 12 hizi ni fedha za maendeleo ukiachia shilingi trilioni 2.1 ya fedha za nje. Bado haijakuja hapo, nazo zikusanywe shughuli iende. Ukiangalia kitabu cha Mheshimiwa Mpango na mwenzake Naibu Waziri picha ya juu hapa wanasema, uzinduzi wa mfumo wa ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielekitroniki, uzinduzi lakini hawawezi kumuonesha Rais, tena Rais yupo hapa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, muonesheni Rais vyanzo vipya vya mapato mbona hamumuoneshi? Kuna picha hapa, nawashangaa kweli kweli, andaeni mazingira, njia mpya ya mapato iko wapi, uzinduzi wa vyanzo vipya vya mapato iko wapi? Ni vilevile vya siku zote hivyo ni kuwaumiza wananchi, hamsomeki hamueleweke shauri yenu. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo linanikera Serikali hii hakuna ongezeko la mshahara, bajeti hii haijagusa kabisa wafanyakazi, hakuna nyongeza yao. Hata lile takwa la kisheria la nyongeza ya kila mwezi nalo haliko, annual increment hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo baya zaidi ni kwamba ukiangalia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali mbali na kwamba mishahara haikupandishwa, hakuna ile annual increment ile ya mfanyakazi ambayo ni ya kisheria haipo lakini hata pale wanapostaafu hawa wafanyakazi wanapunjwa, wanadhulumiwa na kunyonywa nakupa ushahidi. Ripoti ya Mdhibiti ninayo hapa, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha unaoishia 30 Juni, 2017, ukurasa wa 71 sikiliza uovu na ubaya walionao hawa jamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 71, majalada yanayokaguliwa wastaafu 406 asilimia 11 ya majalada, majalada hayo 176 yamepunjwa yakiwa pungufu kwa Sh.516,078,816. Hiyo ndiyo ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, mishahara haipandishi, hakuna ongezeko la mwaka la kisheria na wale wanaostaafu nao wanapunjwa mnataka nini kwa Mungu, mkaseme nini? Nawashangaa jamani mwogopeni Mwenyezi Mungu, nyie tumewapa kazi ya kusimamia kwamba hata wastaafu nao kumbe maslahi yao wanayopata mafao yao siyo, mwaka mbaya kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie Waheshimiwa wenzangu hapa kwamba jukumu mlilopewa ni kubwa sana na kama jukumu mlilopewa ni kubwa sana muandae mazingira kwamba mtende haki. Siyo hiyo tu, huu wizi na ubadhirifu katika nidhamu ya matumizi ya fedha umekuwa mkubwa sana na inaelekea kwamba Mawaziri wameshindwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kitabu hiki hapa kuna wizi na ubadhirifu unaonekana. La kwanza, naomba nianze na kwenye ukurasa wa 291 wa ripoti na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Katika ukurasa huu inaonekana kwamba hata Hazina yenyewe chombo ambacho wanakisimamia, Idara ya Hazina Fungu 21 kuna ubadhirifu mkubwa wa fedha umeonekana na wao ndiyo wasimamizi. Ukurasa wa 291 Naibu Waziri fungua uangalie lakini ukusara wa 290 pia mmepata hati isiyo na shaka, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kumbe ukiona kilemba kimeloa uchafu sijui shuka inakuwaje? Mtihani, tumewapa dhamana lakini hakuna kitu. Maisha yamekuwa magumu, mzunguko wa pesa hakuna. Mwaka 2017 baya zaidi, hii hapa hotuba ya Mheshimiwa Dkt. Mpango alituambia kwamba lengo lake ni kuwatoa wale wanaokula mlo mmoja kutoka asilimia 9.7 mpaka asilimia 5, nendeni Majimbo Wabunge wote hapa tuandae vikundi twende Mikoa yote Tanzania Bara tukachunguze wanaokula mlo mmoja wameongezeka au wamepungua?

Hali mbaya kupita kiasi. Sasa yale maelezo ambayo mnatupa siye tunayasoma na tunayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri akubali kwamba bado hali ya maisha ya Tanzania ni mbaya sana na Watanzania wana matumaini makubwa sana lakini hakuna kinachoeleweka, mpaka sasa hakuna kinachokwenda. Ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri, akae na wataalam wa kweli ambao wataweza kusadia hii Wizara angalau maisha ya Watanzania yabadilike lakini kwa hali tunayokwenda nayo Watanzania tumepigika. Bajeti hii ni mbaya, mbovu, ya kusadikika, funika kombe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu wataala aliyetujalia uzima na afya njema katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani katika kumi hili la Maghfira ikiwa ndio siku ya 19 na nikimwona rafiki yangu Mheshimiwa Ally Keissy ametulia kweli kweli leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Watanzania tulitegemea makubwa kutoka Wizara ya Fedha. Tulitegemea fedha ambazo Waheshimiwa Wabunge tunazipitisha sisi katika maeneo mbalimbali fedha hizi za maendeleo zitakuwa zikitolewa, lakini imekuwa ni kizungumkuti; haifahamiki, hali ni mbaya, tatizo limekuwa ni kubwa.

Mheshimiwa Spika, fedha za maendeleo katika Wizara mbalimbali hazitolewi kwa wakati hata zikitolewa basi inakuwa ni pungufu sana na inaonekana hadi sasa ni chini ya asilimia 40 ya fedha za maendeleo katika maeneo mbalimbali ya Wizara ambazo tumezipitisha. Hili ni janga kubwa, ni tatizo kubwa, tatizo ambalo wananchi mategemeo yao waliyokuwa na huyo yameondoka. Mheshimiwa Waziri wa Fedha atuambie tatizo hasa ni nini kwake Wizara ya fedha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwenye volume II Treasury mambo ambayo waliyojipangia katika maeneo mbalimbali, ukienda kwenye book four, nimwambie Waziri wa Fedha, kama kuna tatizo la vyanzo vya fedha, hana fedha ripoti ya Spika ambayo imewekwa juzi Jumamosi pale Mezani kuna fedha ambazo zilipatikana kwenye uvuvi wa bahari kuu, hivyo ni vyanzo, kuna mambo tayari yapo kwenye ripoti ya Tume ya Spika aliyoiunda, vyanzo vya kutoka bahari kuu kuna matrilioni ya fedha, hebu aingie atafute fedha tatizo nini, mbona haeleweki, hasomeki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kuhusu wastaafu, hali ya wastaafu ni mbaya sana, wastaafu wetu kwa kipindi kilichopita walikuwa kwenye kima cha chini kutoka Sh.50,000 hadi Sh.100,000 baadhi yao walio wengi, lakini ahadi yetu kwa wastaafu kwa hivi sasa inaonekana kama Serikali haina dhamira ya dhati kuboresha hawa wastaafu wetu ambao wastaafu walikuwa ni watumishi wetu, walifanya kazi kwa uadilifu kwa muda wa kipindi kirefu lakini hali zao za maisha ni mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba hii ukiangalia Waziri hana jambo ambalo la kushika zaidi akasema kwamba labda wastaafu hawa wataweza kupata maslahi yaliyo mazuri ukurasa 104 kaeleza mengi, lakini kasema tu kuna moja, mbili, tatu.

Mheshimiwa Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, wastaafu wetu katika kada mbalimbali hali zao ni mbaya sana. Nitoe mfano mmoja, wakati wastaafu kwenye Jeshi la Wananchi kuanzia cheo cha private hadi Brigadier General Jeshini mafao yao yanakuwa ni madogo sana mbali ya hao wengine, hawa walifanya kazi, walikwenda kwenye vita, vita va Kagera, walikwenda Msumbiji na kwingineko, leo wanayafungua mageti kwa watu binafsi inaumiza kweli kweli hasa kuanzia cheo cha private, Brigadier General hata hawa walinzi wetu hatuwathamini hawa walinzi wetu walipigana vita na Kagera, waliokwenda kuokoa Msumbiji hata hilo? Mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hili nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, mwenzake Waziri aliyepita Mheshimiwa Saada Mkuya aliweza kufanikisha kupandisha hizi pension za wastaafu kwa kila mwezi, hebu naye ajiandae, aandae mazingira mazuri apandishe hizi pension za wastaafu za kila mwezi kwa sababu hali imekuwa ni mbaya sana.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri aangalie vilevile katika suala la wastaafu pale wanapostaafu, kwanza mafao yao wanacheleweshewa sana, lakini yeye amesema kwamba wataandaaa mazingira, mazingira hayapo kwa sababu gani kumekuwa na kudhulumiwa, kumekuwa na kunyonywa kwa wastaafu kwa muda mrefu hata ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mbalimbali zimekuwa zikisema kwamba mafao ya wastaafu wanapunjwa.

Mheshimiwa Spika, watu wamefanya kazi kwa uadilifu, wamechoka hata mafao yao, ripoti za CAG zipo kibao, nyingi sana ripoti mbalimbali kwamba mafao ya wastaafu wanapunjwa tangu mwaka 2013, angalieni ripoti za CAG, jinsi wastaafu wanavyonyonywa na kupunjwa. Kumbe wazee wetu maskini kwa sababu ya Serikali wanawadhulumu na kuwapunja tatizo nini? Mwaka huu.

Mheshimiwa Spika, naomba niseme pale ambapo mstaafu anafariki. Anapofariki mstaafu wanafamilia wanafungua mirathi, lakini niseme tu kwamba inakuwa na milolongo mikubwa sana kuzipata zile haki. Familia inapofungua ile mirathi wakifika pale mahakamani ndani ya muda mfupi sana Hazina wanaambiwa kwamba hicho kitu faili lake halionekani. Baada ya mwezi mmoja kufa faili lake halionekani na hayo yapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mzee Bobali, baba yake mdogo Mheshimiwa Bobali hapa, muda mrefu tangu amestaafu huu ni mwaka wa kumi na hajapata mafao yake, ni tatizo kweli wanaofariki na wao mafaili yao wanaambiwa hayapo. Kwa kweli wastaafu wametupwa, wanaonewa hili ni jambo kubwa sana na jambo ambalo kwamba halikubaliki.

Mheshimiwa Spika, nadhani kwamba hakuna kitu kinachoumiza kwamba watu hao walitumika katika hali nzuri sana wakati wakiwa na nguvu lakini wameachwa Mheshimiwa Waziri atuambie tatizo ni nini alilonalo na ahadi ya Serikali kwa wastaafu, kuna kipi kikubwa zaidi ambacho wanawapelekea mpaka leo wanakuwa maskini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niache hilo, pale Hazina kuna bwana anaitwa nadhani Kasekwa, yule huyu ni mtu mmoja ambaye namwamini sana, kwa hiyo yale mafao ambayo yakitengenezwa na bila shaka hapa atakuwa yupo. Huyu aungane na wale na wenzake, ashauriane na wenzake ili hayo mambo yaende vizuri, ni mtu mmoja mzuri sana nadhani anakuwa ni Katibu Mtendaji si ndio ana cheo fulani pale, nina imani kubwa kwamba hili jambo wataweze kulifanya vile ambavyo inavyohitajika.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo linawaumiza sana ni suala zima la shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Volume four ukurasa wa 24, Poverty Eradication Department, subvote 81,000, item 6508 hapa wameweka. Wanaweka nini humu na hawatekelezi, huku ni kudanganyana bure. Najua ikifika wakati wanakuja kifungu hicho kimeafikiwa na ni cha mwisho kifungu hicho kimeafikiwa ohh, waoo, hamna kitu, hawatoi fedha wanadanganya, wananchi wanasubiri kwa muda mrefu na hawajatoa hizi fedha, wanaandika kwenye vitabu, lakini hakuna kitu, tatizo nini, bora muwaambie tu kwamba, ni kweli hizi fedha hazipatikani sababu ni moja, mbili, tatu.

Mheshimiwa Spika, ni ahadi kweli ya Mheshimiwa Rais, akishasema jambo, jambo hilo ni lazima litekelezwe, Mheshimiwa Waziri tatizo lake nini, kama hana vyanzo hata juzi Kamati ya Gesi imesema kuna mabilioni mengine hayo chukua fanyieni kazi, mbali ukiachia leo uvuvi wa bahari Kuu, nawashangaa.

Mheshimiwa Spika, nawauliza Serikali kuna nini huko mwaka huu, hayo ndiyo maisha, mbaya mzunguko wa fedha hakuna, kila tunaposema tuna vyanzo fulani wachukue vyanzo fulani wavifanyie kazi hawataki, sasa wanataka ushauri kutoka wapi na sisi ndio Wabunge wao, tena Wabunge, Wabunge kweli, shauri yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, randama hii hapa, wameeleza katika hii randama, ukurasa wa 119 mpaka 120, wameweka hii maelezo yao waliweka hapa, naombeni sana sisi ni Wabunge waelewa sana, wasitufanye hivi, Wabunge wote ni waelewa sana humu, waandae mazingira basi hizi fedha milioni 50 kwa kila kijiji wametenga bilioni 60, hizi kila mwaka wanatenga, lakini fedha hizi wananchi wanalalamika Wabunge wanasema labda jambo hili limewashinda Waheshimiwa Wabunge, tunawaambia lakini Serikali sio wasikivu, Serikali haitaki kusikia.

Mheshimiwa Spika, naomba kwa hili tena leo Ramadhani kumi la maghfira hili, anajua Mheshimiwa Ashatu nazungumza hivi taratibu sana, kama ingekuwa miezi mingine ningesema maneno mengine, wajitahidi sana waandae mazingira hizi fedha zitolewe, hali ni ngumu sana .

Mheshimiwa Spika, nimalizie jambo moja dogo, kwani kuna tatizo gani katika hali ya maisha wanayoiona Watanzania na mzunguko wa pesa na maelezo ya Mheshimiwa Waziri kuwa deni bado himilivu, tuendelee kukopa, sawa na utaalam wake mimi siko huko, lakini kwa nini kwenye hotuba yake ya mwaka jana alituambia hapa kwamba nia yake ni kuandaa mazingira, wale wanaokula mlo mmoja kutoka asilimia 9.7 sasa waende mpaka asilimia 5.5, hotuba yake ya mwaka jana hiyo, ni maelezo yake, lakini mbona wanaokula mlo mmoja wameongezeka, umaskini umeongezeka.

Mheshimiwa Spika, sasa alichokisema mwaka jana hajakisimamia Mheshimiwa Waziri, sisemi kama yeye ni mwongo lakini hakusema kweli, simwambii kwamba mwongo hapana, siwezi na Ramadhani hii, lakini hakusema kweli kwa sababu haya ni maandishi yake kwamba tutahakikisha katika bajeti zinazofuata wanaokula mlo mmoja wataondoka katika asilimia 9.7 mpaka asilimia tano, leo maskini wameongezeka, hiyo asilimia aliyosema haipo, wanaokula mlo mmoja wengi, wengine hakuna mlo, maisha magumu, hali mbaya kupita kiasi, tukisema kuna vyanzo chukueni… (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa wananchi, nenda Kongwa, nenda Mpwapwa, nenda Dar es Salaam , nenda Mbeya, nenda Iringa kusanya watu upate hiyo, tunaangalia takwimu yake ambayo ametupa awamu iliyopita, sisemi kwamba ni muongo lakini jambo limemshinda fedha ziko wapi, tatizo nini? Hamueleweki! Nawashangaa mwaka huu! Kama kweli Serikali sikivu andaeni mazingira basi msikie.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya fedha ni tegemeo kubwa sana kupita kiasi, Watanzania wote wako na sikio kuangalia Wizara ya Fedha itafanya nini kuboresha maisha ya Watanzania. Leo maisha ya Watanzania yamekuwa ni ombaomba walio wengi, kila siku umaskini unaongezeka, uchumi unakua umaskini unaongezeka nchi gani duniani hakuna uwiano baada ya uchumi kuongezeka…

Umaskini umeongezeka na uchumi unaongezeka…

Mwaka huu, haya tutawaona!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru ningependa kumuomba Mheshimiwa Waziri, matokeo ya mitihani ya kidato cha nne form four na form six kwa Visiwani hasa Unguja na Pemba kuendelea kila wakati kuwa siyo mazuri kulingana na takwimu ambazo zinatokea, hivi wewe halikukeri hili? Pia una mkakati gani hasa wa zaida kuona kwamba matokeo kutoka Visiwani, Unguja na Pemba kwenye mikoa yote sasa yanabadilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vifaa vya sayansi shule za sekondari (O’level) kuna upungufu mkubwa sasa wewe na mwenzako Wizara ya Elimu Zanzibar mna mkakati gani wa ziada? Leo yaani mitaala inabadilika inachukua muda mrefu kufika kule Zanzibar, sasa kuna tatizo gani la ziada ambalo linaonekana hili kuna upungufu kama huu na bado naona tu na matokeo ya Zanzibar kila siku yanaendelea kuwa mabaya hili jambo mkae mlione.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo la kusikitisha sana, kuna kwenye NECTA Baraza la Mitihani wewe ndio ulikuwepo Mheshimiwa mwenyewe huko, lakini uwiano wetu washiriki waliotoka Zanzibar ni wa aina gani kiasi ambacho kwamba Zanzibari kule wapo na washiriki wao na jinsi gani ya kushirikishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mlisema matokeo mabaya Kusini Pemba, Kaskazini Pemba, Kusini Unguja, Kaskazini Unguja, Mjini Magharibi, lakini wewe ulikuwepo jikoni. NECTA je, Zanzibar iko kiasi gani mtuambie na sisi tunapata uchungu kweli kuona Zanzibar bado hatupati matokeo mazuri kumbe kuna mambo ambayo yanahitaji yatelekezwe. Ningeomba sana Mheshimiwa Waziri utupe mpango makakati baina yako na mdau mwenzako wa Zanzibar kuona kwamba matokeo hasa ya form four na form six kwa upande wa Visiwani Unguja na Pemba yaani Zanzibar yanakuwa mazuri, hilo lilikuwa la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili suala la fedha za maendeleo kuhusu wahisani. Tumesema muda mrefu sana kwamba hatuwezi kupata maendeleo ya kweli kama tunategemea wahisani hawa wafadhili. Ukingalia katika maeneo mbalimbali kuna kuimarisha ubora wa elimu ya sekondari 4590 item kwenye Sub Vote 2001, bilioni 30.8 zote za wahisani. Kwenye Idara ya Udhibiti bora vilevile, nako kuna bilioni 16 Education Program for Result, fedha za wahisani. Kwenye elimu, Idara ya Elimu ya ualimu nako vilevile, Teachers Education Support Program billion 15.4, zote ni wahisani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa bajeti yote ya maendeleo imeenda kwenye wahisani, wahisani, wahisani hawa ambao hawaleti fedha, nawashangaa na ndiyo maana tukasema leo tutumie vitabu hivi na wale wenzangu waliosema kwamba hata kwenye fedha za maendeleo ambazo za mikopo zimeenda kule. Kwa hiyo kuna Volume II, kuna Volume IV, kuna Randama hapa, juzi tulipokuwa tunatumia vitabu hapa wengine wanasema tutavua nguo, tutavua nguo, alisema Waziri mmoja hapa na kama leo angekuwepo Waziri Kangi leo ningemwambia vua nguo kwa sababu sisi tunatumia vitabu, vua kweupe mchana kweupe hapa. Haiwezekani tunataka maendeleo ya kweli ikawa tunatenga asilimia zaidi ya 60 kwa wahisani, haiwezekani hata kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye higher education, elimu ya juu Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu na uko makini kweli leo. Nenda kwenye 2228 nako ni vilevile, kuna Support on Research and Development. Tunakwenda kufanya utafiti kutuwezesha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Ardhi, MUHAS kufanya utafiti kwa maendeleo ya elimu. Bilioni 10.4 kitabu cha Volume IV, mmedharau Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mmedharau MUHAS, mmedharau Chuo Kikuu cha Ardhi mmedharau, fedha hizi za wahisani yaani kila kitu wahisani, wahisani, hawa tunawaita mabeberu nawashangaa kweli kweli. Hakuna kitu ambacho kinakera kwamba fedha … (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante, mengine utaandika.

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Atakayevua nguo na avue! (Kicheko/Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala aliyetujalia uzima na afya njema ya kuweza kuchangia mapendekezo ya mpango huu tulionao leo mbele yetu. Nianze na mwenendo wa viashiria vya umaskini kama ambavyo wenyewe waliotuletea Madaktari wetu mabingwa kama hivi vifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, walituambia kwamba, mapato na matumizi ya Kaya binafsi yamepungua na umaskini umepungua kutoka asilimia 9.7 hadi asilimia 8.0 kutoka mwaka 2011 – 2017. Kwa hivyo umaskini unaelekea umepungua kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, najiuliza umaskini huu uliopungua ni kwa kiasi gani wameangalia Watanzania hawa wanakula milo mingapi, mwaka 2011 walikuwa wanakula milo mingapi, 2012, 2013, 2014, 2015, 2016 na 2017 kama wanatembea kweli vijijini na kama wataalam hawawadanganyi umaskini hata kipindi hicho haujapungua na haujapungua kwa sababu bei za bidhaa zimekuwa zikipanda. Mwaka 2011 debe la mahindi lilikuwa Sh.5,000 mpaka 6,000; debe la mahindi mwaka 2017 lilikuwa Sh.12,000, sasa debe la mahindi limefika Sh.18,000 na kuendelea, wanasema umaskini umepungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye unga wa sembe wenyewe, mwaka 2011 bei yake ilikuwa ni ndogo kwenye Sh.700, 800 hadi 1,000 leo 2019 bei ya unga wa sembe ni aibu imefika hivi sasa hadi Sh.1,500, umasikini umepungua! Jamani wataalam wetu madaktari hebu tuambieni ukweli, waliowaambia maneno haya, utaalam huu ni akina nani hata mtuambie hivi maana sisi wengine si Madaktari kama nyie, ni watu wa kawaida tu, ni Walimu tu wa shule za sekondari, lakini tunataka watuambie kupungua kwa umaskini huu na kupanda kwa bei; sukari, 2011 kama kweli kutoka asilimia 9.7 hadi asilimia 8.0 bei ya sukari mwaka 2011, 2012, 2013 na sasa waangalie 2017 sikuambii hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, wanasema kwamba mfumuko wa bei kwanza kutoka Januari 2019 hadi Septemba 2019 umetoka kwenye asilimia 2.3 hadi asilimia 3.2, wao wenyewe wamekiri kama kuna mfumuko wa bei, sijui madaktari wetu wanatuambia nini ningeomba niwashauri; kwamba bado hali ya umaskini nchini kwetu unaongezeka, wanaokula milo mitatu sasa wamepungua, kunakuwa na pasi ndefu, sasa wanasema ni pasi ndefu, wanakunywa tu chai mchana wakitoka hapo usiku kidogo, basi wanalala. Hiyo ndiyo hali halisi ilivyo, tembeeni vijijini muone hiyo ndiyo hali ya umaskini ulivyo msidanganywe na wataalam wanaoleta kwenye makaratasi, twende kwenye uhalisia mtembee vijijini muone shughuli, ni kizaa zaa, mwaka huu!

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumza kwenye umaskini ule mwingine wa kipato, kwamba nao umaskini wa kipato umepungua hapa ni sawa na utaalam wao, lakini hasa waangalie hasa na hali ya umaskini inavyoongezeka kwenye Jiji la biashara tuje Dar es Salaam ambapo ndiyo linaitwa Jiji la biashara, ukienda pale Kariakoo maduka yamefungwa, mpango huu hauna jibu, hauna jibu, hautoi tija yoyote kuonesha mkakati gani ambapo wataboresha maisha ya wafanyabiashara katika Jiji la biashara la Dar es Salam, maduka pale Kariakoo yamefungwa, mpango huu hauoneshi jambo lolote, hakuna mpango hakuna mpangilio. Watuambie wana mpango gani au wana mpangilio gani wa kufufua Jiji la kibiashara la Dar es Salam. Shughuli ipo kweli! Watuambie madaktari wetu sisi ni wadogo sana kwao, wao wamesoma zaidi sisi ndiyo hivyo tena, watuambie madaktari hawasomeki, hawaeleweki waliowandikia sijui ni akina nani, shauri yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, kwenye ukurasa huu wa 43 wamezungumza habari ya utawala bora. Hasa utawala bora umo kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuna Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Ibara ya 29 na 30 yaani majukumu yake. Sasa wamezungumzia moja kwenye utawala bora, mkakati wa Serikali kuhamia Dodoma, kwani utawala bora ni hilo tu? Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema ukienda kwenye Ibara ya 3(1) inazungumzia Tanzania ni nchi ya kidemokrasia yenye kufuata mfumo wa vyama vingi na ni nchi ya kijamaa. Ibara ya 5(1) inazungumzia haki ya kupiga kura yaani kuchagua na kuchaguliwa hawajagusa kitu hawa Madaktari, kule kwetu wanasema tawileni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali ya kawaida, katika hili la kupiga kura kuchagua na kuchaguliwa, tunaelekea kwenye chaguzi za Serikali za Mitaa demokrasia imeminywa, demokrasia imepuuzwa, leo ni malalamiko kila kona, vyombo vya habari kila kona ndani na nje ya nchi kwamba hali ya demokrasia Tanzania imeminywa, wagombea wote wa Upinzani wameondolewa, matatizo yamekuwa ni makubwa na kwangu mimi kama mdau wa ulinzi na usalama ambaye napenda amani na utulivu wa kweli naona hicho ni kiashiria kibaya cha ulinzi na usalama lazima niseme kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani watu kufanya madudu yao waliyoyafanya ukaondoa wagombea wa Upinzani kwenye demokrasia ya mfumo wa vyama vingi, iko ndani ya Katiba, leo ukasema na sisi tunataka amani na utulivu. Jamani, Madaktari Serikali nzima inisikie, Mheshimiwa Jafo kasema kwamba watu waendelee kupeleka pingamizi hapa na pale, imeelezwa na Mheshimiwa Mbunge mmoja hapa, kwamba hao wanaopelekewa wamekimbia hawapo.

Huu ni mfumo wa vyama vingi, kama hamtaki mfumo wa vyama vingi, futeni vyama vingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu najiuliza mambo ambayo kila siku ninyi mko kwenye redio masaa 24, mmefanya hiki, mmefanya hiki, anakuja Polepole anasema, mko peke yenu siku saba tu ambazo ni kampeni, waacheni watu wachague na kuchaguliwa, raha ya kushinda ni kushindana, msiende peke yenu muone mambo mengi mliyokwishafanya mnatutangazia wananchi watapima, lakini tunakwenda kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, ni aibu na fedheha kubwa ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali Mheshimiwa Jafo katoa tamko lake lakini pamoja na hayo hebu jamani angalieni hili, warudisheni hawa wagombea nchi hii twende kwenye amani na utulivu wa kweli lakini kilio kila kona hawa ni binadamu. Kumbe viashiria hivi vinavyofanywa najiuliza je, Serikali ya kijiji ndio inataka amani itoweke? Ni Serikali za kwenye kata au za kwenye wilaya au kuna baraza gani najiuliza mimi mwenyewe binafsi kwa sababu unapowanyima fursa watu kuchagua na kuchaguliwa hili ni tatizo ni kiashiria kibaya kwenye amani na utulivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri wanaohusika na vyombo vya ulinzi na usalama waliomo ndani na nje ya humu ndani niwaombe sana suala hili si la kulifumbia macho ni lazima wahakikishe kwamba watoe tamko la wagombea hawa wa upinzani kurejesha kugombea, nchi hii twenda vizuri tuko katika mfumo wa vyama vingi. Ama kama sikio la kufa halisikii dawa shauri yenu mimi nishasema na kwa sababu lugha yangu hii naizungumza mnaifahamu vizuri ni Kiswahili cha kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema haya nirudie tena kwa sababu mimi binafsi ni mdau mkubwa wa ulinzi na usalama, ukataka usitake huwezi kuzungumza masuala ya ulinzi na usalama humu ndani Bungeni usimtaje Masoud. Kwa hiyo, lazima niseme kwamba dawa mfumo wa vyama vingi tuangalie viashiria ambavyo vinaweza kuleta tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie mzungumzaji huku niko peke yangu dakika zangu mlizonipa hizo nimeongea na wenzangu kwamba niendelee na shughuli, nashukuru haya sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie mpango huu pia hautojibu hamna chochote mtazungumzia habari ya jibu la milioni 50 kila kijiji umaskini utapungua wapi. Serikali iliahidi kwamba mtatoa bilioni 50 kwa kila kijiji hamna kitu, mpango hauna jibu lolote kama kweli mnataka kukuza uchumi na kupunguza umaskini mpango hauna jibu lolote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mnaposema milioni 50 kwa kila kijiji mwaka wanne huu si mngetuacha tu tukaenda kwenye vijiji tukawaambia wananchi hiyo ndio hali kumbe mnaogopa kweli mfumo wa vyama vingi, shughuli ipo mwaka huu, hakuna jibu milioni 50 kila kijiji imekufa hivi hivi waziwazi. Madaktari mngekuja mtuambie milioni 50 kila kijiji uko wapi mpango bado mnao? Mpango huu hauonyeshi mkakati wa kuboresha maendeleo ya wafanyakazi, mishahara ya wafanyakazi annual increment nyongeza hata ya kila mwaka nayo ni tatizo shaghalabagala mwaka! Mtuambie madaktari nini mmekusudia mnataka kuipeleka wapi Tanzania? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzuri bahari kuu humu hakuna mpangilio maalum deep sea fishing ambao duniani kote tuna bahari ya kutosha, deep sea fishing humu mtueleze ukubwa wake mna maelezo kidogo tu. Uvuvi wa bahari kuu uko wapi watu wanakuja hapa na meli zao wanachukua samaki wanakwenda kuuza, sisi katika hali kama hiyo tuangalie mkakati wa kuboresha uvuvi wa bahari kuu, lakini Mheshimiwa Mpango huu haoneshi madaktari mtuambie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na suala zima la kilimo mmegusia sehemu ndogo ya uhitaji wa masoko lakini katika mwaka uliopita wakulima wa mbaazi waliathirika sana hadi leo wakulima wa mbaazi wana wasiwasi kupata soko la uhakika kwa sababu walikuwa wanalalamika wakauza kilo ya mbaazi shilingi 200 mpaka 300 mtuambie mkakati wa Serikali wa kuboresha soko la uhakika la wakulima wa mbaazi uko wapi, mpango unaonesha mtuambie na hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri anaangalia kwelikweli kumekucha kweli katika mkakati huu mimi nafikiri mtupe majibu mazuri. Kwa sisi wengine mwezi huu unaitwa mwezi wa mfungo sita mwezi ambao Mtume Muhammad Sallallahu alayhi wa sallam tupo wataratibu wapole tukimaliza hii tena uko mbele lakini tunataka Serikali itoe majibu sahihi ituambie mkakati madhubuti na endelevu wa kuboresha masoko ya uhakika ya mazao ya kulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo machache kwa sababu nilibamizwa na mambo mengine hapa niseme hayo yanatosha lakini nisisitize suala zima la utawala bora lifanyiwe kazi isiwe bora utawala. Kama tunataka utawala bora twende kwenye utawala bora kama unataka bora utawala endeleeni kwa sababu mna nguvu. Narudia tena kusema kama kuna utawala bora kama mlivyoandika ukurasa 43 twendeni kwenye utawala bora tuwe na chaguzi ya mfumo wa vyama vingi watu wachague wachaguliwe, kama mnataka bora utawala endeleeni kwa sababu mna nguvu. Lakini hii ina athari kubwa utawala bora nyie mnataka bora utawala, tatizo ni nini kuna hofu ya nini nyie ni watu wazima humu ndani katika Bunge hili upande huu wa upinzani huu mimi ndio mtu mzima wao na ukiona mtu mzima analia kuna jambo. Kama mnataka kusikia sikieni kama hamsikii shauri yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, asanteni sana nashukuru. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, nichukue fursa ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, Subhanah Wataalah anijalie uzima na afya njema, kuchangia bajeti ya mwaka 2019/2020 na nianze na Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake katika ukurasa wa 95 akisema kuelekea uchaguzi za Serikali za Mitaa, mwaka huu Oktoba, 2019. Akataja sifa 10 na kuna baadhi ya sifa ambayo moja ilikuwa kidogo na ukakasi na Spika akarekebisha, labda niseme kuna baadhi ya sifa ambazo uliziacha, naomba nikukumbushe.

Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa sifa ambazo tunataka kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuwachagua viongozi wanaofaa, awe anathamini utu wa binadamu, miongoni mwa atakayechaguliwa, lakini pia awe anatoka katika chama ambacho hakina tabia ya watendaji wake kuzikimbia fomu za wagombea wengine wanapopata fursa, akaingia mitini, hiyo ni sifa nyingine ambayo ya kuchaguliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sifa nyingine ambayo itakuwa ni nzuri kuliko yote, awe anatoka katika chama ambacho kinakubali kushinda, chama ambacho anakubali kushindwa pale ambapo anaposhindwa, asiwe na tabia ya kung’ang’ania na kuandaa mazingira ya amani kutoweka, akishindwa akubali kushindwa, hizo ni sifa ambazo Mheshimiwa Mpango uliziacha. Tunaomba ukija hapa uziingize sifa hizo, kwamba tunataka uchaguzi Serikali za Mitaa, sifa hizo kuzitaja uliziacha, naomba uzikubali na ninafikiri kwa unavyocheka, sifa hizi umezikubali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naanza na bajeti sasa; bajeti hii ya mwaka huu haina uhalisia, bajeti hii ya mwaka huu inaonekana mnakwenda kutumia fedha nyingi zaidi kutokana na mchanganuo ambao umeleta, mapato/ makusanyo ya muda wa miaka miwili, tunakwenda kutumia ndani ya mwaka mmoja, yaani ukusanye fedha za miaka miwili, ambayo makusanyo yetu kwa mwaka ni trilioni 1.2, makusanyo yetu ni trilioni 1.2 kwa mwezi, lakini kwa jinsi ambavyo umetuletea matumizi yako, tunakwenda kutumia trioni 2.5 kwa mwezi, kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Deni lako la Taifa unasemani trilioni 9.7; ukiangalia mchananuo kama utagawa kwa mwezi, utakuta kwamba ni lazima upate bilioni 810. Ukienda kwenye mishahara trilioni 7.558; ukiangalia je, kwa mwezi utakuta kwamba unapata bilioni 629. Ukienda kwenye matumizi mengineyo (OC) trilioni 3.576; ukienda kwa mwezi utakuta kwamba kuna bilioni 298; ukienda kwenye fedha za maendeleo, ukiachia fedha za wahisani zile, trilioni mbili pointi; trilioni 9.73, nazo lazima ukusanye upate bilioni 811, hizo ni trilioni 2.5! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unashangaa leo Waziri unakuja na bajeti ya matumizi ya trilioni 2.5 zipatikane, lakini unasema na makusanyo yetu sisi ni trilioni 1.2, kwa mwezi! Hiyo ni bajeti ya kiini macho, kizungu mkuti, haifahamiki, funika kombe! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, tunataka bajeti ya uhalisia, siyo bajeti hii, hii bajeti haitekelezeki, tunakwenda kuumiza watanzania. Mimi halafu nashangaa, namshangaa Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wake kwamba hii bajeti, kweli haitoi jibu! Haitoi jibu kwa sababu gani, inaelekea moja kwa moja, utaratibu unaonekana, hata wafanyabishara wenyewe, kilio kila kona, maduka Kariakoo yamefungwa, uvuvi bahari kuu hauna jibu, hamkujipanga, ni kivutio kikubwa, lakini kila tukitoa ushauri kwetu sisi, mama ntilie nako ni kilio. Sasa hii ni bajeti ya aina gani mwaka huu! Bajeti hii ni kiini macho, kizungumkuti, haifahamiki. Naomba huwezi kuchukua trilioni 2.5 ambayo lazima uzipate, lakini makusanyo yako ni trilioni 1.2. nimshauri Mheshimiwa Waziri, bajeti hii ifumiliwe upya, haifai kabisaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, suala la wakulima; wakulima wamekuwa na malalamiko makubwa kila wakati. Suala la korosho limekuwa ni kubwa, mmeweza, mmechukua muda mrefu, wakulima wa korosho wanalalamika, mara hii mmekwenda kuweza kuwakopa wakulima wa korosho, hamjawalipa, mmewalipa baadhi ya wakulima, baadhi ya wakulima wengine hamjawalipa na nini athari yake hii, athari yake wanashindwa kuandaa mashamba. Kama Serikali ni ya wanyonge, walipeni wanyonge wa korosho! Hata hawa wafanyakazi wa ngazi ya kati, walipeni fedha zao! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni jambo kubwa sana, lakini kama mkiendelea kutowalipa fedha zao za korosho, basi kinachoonekana, morali inashuka, morali kwa wakulima wa korosho inashuka kila siku! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hasa mimi nawashangaa, mnasema Serikali hii ni ya wanyonge, wakulima, lakini nashangaa kwa nini hamsikii kilio tunacholia, Halmashauri zinakosa mapato!

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri andaa mazingira, andaa mazingira kwamba ni jinsi gani mtaweza kulipa wakulima wa korosho na taarifa ambazo zipo, ambazo bado hazijathibitishwa, mna mpango wa kwenda kuwalipa wakulima wa korosho kwenye mwezi wa nane na wa tisa, kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa iwe kama ni kampeni. Ndiyo taarifa zilizopo zinazozagaa, ni kawaida yenu hamuwalipi, mpaka karibu karibu ama kuna uchaguzi fulani ndiyo mnafanya ujanja ujanja, mnakwenda kuwalipa na amesema Mheshimiwa Bwege, mkiwalipa mtapigwa, hamkuwalipa mtapigwa. Kwa sababu wao wana macho wanajua wapi wanachagua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, labda niseme kwenye miradi ya maendeleo; kwenye miradi ya maendeleo, taarifa ya miradi ya maendeleo, kwa upande za Zanzibar. Kitabu kile hakionyeshio kabisa jinsi gani ambavyo mnakwenda kutekeleza miradi ya maendeleo kwa upande wa Zanzibar, ni eneo dogo sana ambapo mmetaja. Ni sehemu moja tu ya ulinzi, kidogo tu, lakini kuna Mradi wa Mpigaduru kabisa hamkuutaja, kuna miradi kadhaa mlikwishaahidi zamani, kuna Bandari ya Wete, Bandari ya Mkoani, mliahidi. Sasa nimshauri Mheshimiwa Waziri, katika miradi yote 552, lakini ukiachia miradi ile ambayo iko katika mambo ya Muungano, hata miradi ambayo ipo katika Ofisi ya Makamu wa Rais, mabadiliko ya tabianchi, mnakwenda kujenga kuta katika fukwe, hamkutaja hata mradi mmoja kutoka Zanzibar, kwa upande wa Unguja na Pemba, hili ni jambo ambalo linatuumiza kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, hasa, na Mheshimiwa Waziri January Makamba, wewe unafahamu jinsi tatizo la fukwe, wewe umefika Kisiwa Panza na maeneo mengine, kwa nini katika kitabu kile hamkuonesha utaratibu wa kwenda kujenga kuta katika fukwe katika mabadiliko ya tabianchi, mmewatenga Wazanzibari, hili lazima tuliseme, tatizo nini? Niwashauri mara nyingine mtakapoandaa taarifa, basi Zanzibar muweze kuihusisha vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jambo lingine ni hali ya uchumi unavyoendelea; katika hali ya uchumi unavyoendelea, kumekuwa na aina fulani ambayo inaonekana wazi wazi kwamba ni kwanini baadhi ya benki zinafungwa! Serikali imekaa tu, kuna benki ambazo zimefungwa, unaifuata benki, imefungwa, kuna Kagera Farmer Cooperative Bank,imefungwa, Benki ya Wakulima imefungwa, lakini hata Benki ya Wanawake, nayo imefungwa! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni sababu zipi za msingi ambazo zinaonekana kwamba kuna kuwa na mdororo huu wa uchumi! Moja ya sababu inaonekana Benki ya Wanawake kufungwa, taarifa ambazo tunazo ni kwamba Serikali iliahidi kuboresha Benki hii ya Wanawake, lakini fedha hamkupeleka! Sasa kwa nini msipeleke fedha na mnasema kwamba wanawake kwanza, tunawajali mama zetu, hawa ni wazee wetu, kwa nini basi mlipelekea mpaka Benki hizi, Benki hii ya Wanawake kufungwa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhana Wataala aliyetulia uzima na afya nje ilikuwa bado siku 25 kufika mwezi mtukufu wa Ramadhan tumwombe Mwenyezi Mungu atufikishe salama wasalumini, tumwombe Mwenyezi Mungu atuepushe na janga la Corona ambalo linatukabili na sisi ni rai kwa watu wote duniani na watanzania rai yangu tuachaneni na dhambi ambazo zinamchukiza Mwenyezi Mungu tupunguzeni madhambi. Rai yangu kwa watanzania wote kwa imani na dini zote tuacheni dhambi dunia imebadilika, dunia imesimama.

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo, machache sasa nianze kuchangia. Niendelee na mwenzangu alipomalizia kuhusu Corona. Ni vyema mkakati ukaongezwa zaidi kupambana na Corona na inaonekana vitakasa mikono (sanitizers), bei zake sasa zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku. Ile ambayo ilikuwa inauzwa 1,500 kabla ya Corona sasa inauzwa 3,000 hadi 2,500 na ile ya 2,500 sasa ni 4,500 hadi 5,000. Ni ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba jambo hili ni jambo kubwa, Serikali haziko vijijini, elimu hakuna vijijini, viziba midomo navyo bei zimepanda. Niombe Serikali iingilie kati suala hili tuone kwamba tunafanyaje.

Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, bajeti yake mimi sina pingamizi nayo sana. Katika bilioni zake ambazo zimetajwa tumpitishie ila kwa sababu yeye ana Mafungu tisa, sina pingamizi na Fungu 15 lakini pingamizi yangu iko na Fungu 27; Registrar of Political Parties (Msajili wa Vyama vya Siasa). Shida yangu iko kwenye Fungu 61 - Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Fungu 41, Fungu 42 sina wasiwasi nalo, Mafungu 91, 92, 65, Mafungu yote tisa ambayo Waziri Mkuu anasimamia sina mapingamizi nayo, lakini Fungu 27 - Registrar of Political Parties; na Fungu 61 - Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ni shida. Nasema hayo kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Spika, Msajili wa Vyama vya Siasa yeye ni mlezi. Ningependa kuona kwamba Msajili huyu anakwenda vizuri na kuona kwamba vyama vyote ni sawasawa na sote ni Watanzania, lakini akitokea kiongozi yeyote akianza kutoa matamshi ya uchochezi akisema kwamba tutashika dola mwaka huu kwa kutumia dola, tafsiri si nzuri. Hata vyovyote ambavyo yeye amekusudia lakini haijengi taswira nzuri ya ulinzi na usalama, si jambo jema sana.

Mheshimiwa Spika, si muda mrefu umesema hapana, mambo haya si mazuri, hotuba hii si nzuri, hii si nzuri, lakini mtu anasema tutashika dola kwa kutumia dola na nchi ambayo haikutumia dola kama vile KANU ikaondoka, hatufanyi kosa hilo; why? Mambo gani hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kiongozi mkuu yeye haipaswi, mimi ningetarajia Msajili amuite amtake atoe maelezo kwa sababu vyama vingine vya Upinzani viongozi wakisema maneno mengine wanaitwa wanahojiwa wamekusudia nini, lakini sisi wapinzani tunaonekana kama vile sijui watu gani tumetoka nchi gani. Ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, ushauri wangu viongozi kama hawa muanze kuwafanyia utafiti; ni kweli? Stori ni za kweli? Maana yake wana uchungu kweli na nchi hii? Ni shida.

Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi; Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati anatoa hotuba yake ambayo ni nzuri sana na alisema kwamba tunakwenda kwenye Uchaguzi Mkuu na utakuwa huru na haki, lakini jambo la kwanza kabisa uchaguzi huru na wa haki ni Tume huru ya Uchaguzi. Tume huru ya Uchaguzi ni muhimu sana, kuanzia uandikishaji, tunakwenda kwenye kampeni, kwenye kupiga kura, kwenye kutangaza matokeo, lazima Tume ya Taifa ya Uchaguzi ifanye kazi yake kwa uadilifu mkubwa sana, vinginevyo kama hatutakuwa na Tume huru ya Uchaguzi uchaguzi hauwezi kuwa huru na wa haki tunaweza tukapelekana tena mahali ambapo sio pazuri sana.

Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu awe makini sana na uchaguzi wa mwaka 2020. Kenya wana kitu kinaitwa IEBC (Independent Electoral and Boundaries Commission), uchaguzi wa Kenya huo. Kuna hofu gani kuwekwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi? Tuige nchi jirani tu Kenya mipaka hii hapa.

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa uzoefu. Mimi nilikuwa mmoja wa Wasimamizi wa Uchaguzi wa Kenya, mimi nilikuwa Busia na Bungoma katika kaunti hizo, majimbo 16. Sasa kuna jambo gani? Nasema kwamba tubadilike tuone kwamba tunakwenda vizuri tuone kwamba kwa vyovyote iwavyo tunapata utambuzi zaidi.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini kwenye suala la Corona kuna jambo moja; mgonjwa kuthibitika kama ana Corona uthibitisho wake uko eneo moja tu la Hospitali ya Muhimbili peke yake. Mikoa yote hakuna kipimo hicho mpaka sampuli ipelekwe Muhimbili iende ikachunguzwe baada ya hapo ndipo inakuwa imethibitika kama mgonjwa huyo tayari ana maradhi ya Corona. Ushauri wangu; tuandae mazingira sasa angalau kila mkoa; tuna mikoa 32, sampuli ichukuliwe Kagera ipelekwe Dar es Salaam, kwa Wapemba wenzangu huko Dar es Salaam. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, hili liangaliwe. Ni jambo kubwa kwelikweli, kujua afya zetu wakati huu ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee, jambo lingine ambalo napenda niendelee ni suala zima la msongamano wa wafungwa. Amesema Mheshimiwa Mbunge mmoja hapa; suala la msongamano wa wafungwa linachangiwa na mambo mengi lakini mpaka sasa Bunge letu limeshindwa kuweka ukomo wa upelezi. Msongamano wa wafungwa na mahabusu, mahabusu hadi sasa wanafika 17,000, wafungwa 15,000 jumla 32,000. Mahitaji ya magereza ni nusu tu lakini mpaka sasa sheria bado haijaweka wazi ukomo wa upelelezi. Kuna watu wako magerezani miaka mitatu, wako miaka mine, wako miaka mitano, wako miaka sita, wako miaka saba. Ukomo wa upelelezi uko wapi? Na huyo akithibitishwa kwamba hana kosa tayari alikuwa ameshafungwa.

Mheshimiwa Spika, Bunge hili sasa, naishauri Serikali, Mheshimiwa Waziri Mkuu sina pingamizi naye sana mimi maeneo yangu ni mawili makubwa, lakini lazima Bunge hili tutoke na jambo moja kubwa; kuwepo na ukomo wa upelelezi, watu magerezani wanateseka na ni kesi za kubambikiza, kesi zingine ni za kubambikiza, watu wanateseka, watu wanaumia, watu wamepoteza imani na Serikali kwa sababu gani, muda umekuwa ni mkubwa kesi zinaendelea unaambiwa upelelezi bado haujakamilika; kwa nini?

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais mwenyewe alipita magerezani huko akasema hawa fyekelea mbali. Sisi Bunge tunashindwaje kuandaa mazingira ya kuweka ukomo wa upelelezi? Tutaendelea kuweka msongamano mkubwa, wanaendelea kula, wakati huu wa Corona sisi tuna sanitizers, wao ambao wanalala kama pipi hivi? Sisi huku tunaambiwa tukae mbalimbali Wabunge, wewe kaa kule, wewe kaa kule, wewe kaa kule; wale kule magerezani mmekwenda mkaona? Corona hii, mmekwenda mkaona? Niishauri Serikali, lazima kuwepo na ukomo wa upelelezi kwenye shughuli hizi.

Mheshimiwa Spika, baada ya maneno hayo, nashukuru sana.