Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Yussuf Haji Khamis (10 total)

MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kumuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa idadi ya watu ambao wanapoteza maisha kutokana na ajali za bodaboda basi hata tungekuwa vitani tungekuwa tunapigwa! Kwa hivyo, namuuliza Mheshimiwa Waziri, tuna mikakati gani ya ziada ya kutoa elimu juu ya waendesha pikipiki ili tuzipunguze ajali hizi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; barabara wanayokatisha Wabunge kuingia ndani na kutoka nje ya Bunge sio salama. Tarehe 5 juzi kagongwa Mbunge mwenzetu na kapata majeraha makubwa sana. Je, Serikali inawahakikishiaje Wabunge usalama wa eneo hilo? Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kupata concern hiyo. Ni kweli watu karibu 7,000 ni wengi na ajali zaidi ya 31,000 ni nyingi sana. Tunalolifanya, kwanza
tumesemea iwepo elimu kwa kila mkoa na kila wilaya ambazo zinafanywa na department yetu inayoshughulika na masuala ya usafiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili nitoe rai hata kwa Wabunge tunapokuwa na vijana wetu, watambue kwamba vyombo hivyo pamoja na kuwa na matairi mawili lakini ni vyombo vya moto. Wazingatie masharti ya uendeshaji wake kwa sababu kwa kiwango kikubwa kwenye upande wa magari huwa kuna sababu zingine ambazo
zinasababisha ikiwepo na uchakavu wa vyombo, lakini kwa bodaboda ajali nyingi zinasababishwa na kutokuzingatia utaratibu wa uendeshaji ikiwepo kwenda mwendokasi na kuendesha vyombo hivyo kabla ya kuwa wamejifunza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hili hapa alilosemea la pili kuhusu kuzingatia masuala ya usalama, tumeshaongea kuweza kuweka utaratibu mahsusi ambao utakuwa unadhibiti. Siku ile walikuwa wamesimamisha magari lakini
yule wa bodaboda akaja akapita moja kwa moja kama ambavyo nimesema wamekuwa na utaratibu huo wa kwenda kasi lakini tumeendelea kutoa elimu na tumesema ianzie hata ngazi za familia waweze kutambua kwamba kwenda kasi kwa vyombo hivyo vya moto pamoja na kuwa
na matairi mawili lakini vinasababisha ajali.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na mlolongo mrefu wa majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mataifa mbalimbali duniani wanapozikamata meli kama hizi wanazitaifisha kwa ajili ya kujenga uchumi wa ndani ya nchi yao. Ajabu sisi meli ile tumeiacha imezama mahali (bandarini) ambapo hapana upepo, hapana wimbi wala hapana dhoruba yoyote na kupoteza thamani kubwa ya meli ile. Je, Serikali inatamka tamko gani kuhusu suala hili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa washtakiwa wameingizwa hatiani: Je, utaratibu gani uliotumika kuwaachia huru mpaka muda huu wakawa wako nje? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA (K.n.y. WAZIRI WA SHERIA NA KATIBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ametolea mifano au ameelezea uzoefu wa nchi nyingine wanapokamata vyombo vya baharini au meli kama hizi. Kwanza, napenda tu kusema kwamba kwa Tanzania kufanya uamuzi ule waliouchukua imesaidia sana kukemea au ku-deter uvuvi haramu katika bahari zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia matukio ya aina hii kuanzia mwaka 2009 tangu uamuzi huu ulipochukuliwa, kwa kweli hata Wizara ya Uvuvi itakuwa ni shahidi na vyombo vyetu vinavyofanya doria katika bahari zetu, matukio ya aina hii yamepungua sana. Kwa hiyo, kwa kweli na sisi Tanzania kama nchi tumeweka mfano, tumeweka precedent ili nchi nyingine na watu wengine wenye masuala kama haya wasitumie bahari zetu kwa makosa na kuchezea rasilimali zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, kwamba ni utaratibu gani uliotumika katika kuwaachia huru watuhumiwa; kama nilivyoeleza, mwaka 2014 Mkurugenzi wa Mashtaka ali-enter nolle kupitia Kifungu cha 98 ambacho anayo mamlaka kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na masuala mengine yaliyofuata hapo ilikuwa ni masuala ya diplomasia na waliweza kuachiwa huru.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu marefu ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshiwa Naibu Spika, katika majibu yake Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba mashamba haya yamekuwa ya muda mrefu na uzalishaji wake umekuwa mdogo sana. Pia mashamba haya yanatumia hekari nyingi sana, kwa hiyo, yamechukua sehemu kubwa ya ardhi ya Tanzania. Pamoja na kukiri kwamba hakuna uhusiano baina ya Kiwanda ya General Tyre na mashamba haya. Namuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, je, Serikali iko tayari kuleta matumizi mbadala ya mashamba haya kwa sababu hayalisaidii Taifa?(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Kiwanda cha General Tyre si kiwanda kipya ni kiwanda cha zamani sana na kilikuwa kinazalisha. Hata hivyo, marekebisho yake naambiwa yafanyiwa utafiti, ukiuliza utafiti, ukiuliza utafiti, hakimaliziki kiwanda kufanyiwa utafiti ili kuzalisha. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri haoni kwamba hatujawa tayari kuingia katika Tanzania ya viwanda kwa mwendo huu?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusu mipira au zao la mpira kuchukua ardhi kubwa na hiyo ardhi kutoweza kutumika kwa tija zaidi, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa mashamba ya mpira tuliyonayo hayajachukua ardhi kubwa sana. Tunachofikiria sasa kama Wizara na Serikali ni kujaribu kutafuta ardhi nyingine ili tuongeze uzalishaji wa mpira. Kwa sasa tunafikiri mpira soko lake limeimarika tena hata jirani nchini Kenya kuna soko, lakini vilevile China kuna soko kubwa. Kwa hiyo, sasa tunajaribu kuangalia namna ya kuwekeza tena kwenye mpira ili liwe tena ni zao ambao wakulima wetu wanaweza kunufaika nalo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa sasa hatufikirii ile ardhi iende kwenye matumizi mengine lakini tunachofanya ni kuendelea kuimarisha mashamba yaliyopo lakini vilevile kujaribu kuongeza ardhi nyingine ili kilimo cha mpira kiweze kupanuka. Vilevile kujaribu kuimarisha teknolojia ambayo tunatumia kwa sasa ili iweze kuendana na mahitaji ya sasa ya soko la mpira duniani.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuhusiana na General Tyre. Kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, Serikali inaendelea kufanya tathmini kuhusu namna bora ya kurejesha tena Kiwanda cha General Tyre kiingie katika uzalishaji. Kimsingi tulichosema ni kwamba taarifa ya awali inaonyesha kwamba tunahitaji kuboresha teknolojia iliyopo, lakini vilevile mfumo wa uendeshaji uwe ni kwa utaratibu wa kushirikiana na sekta binafsi kwa maana ya PPP ili Serikali iweze kubakia na hisa chache tu na hasa zile zinazolingana na mali au uwekezaji ambao Serikali tayari umeshaufanya, lakini huku Serikali ikijaribu kuvutia wawekezaji ili iendeshwe kwa ubia na sekta binafsi. Kwa hiyo, siyo kwamba Kiwanda cha General Tyre kimetupwa lakini ni kwamba sasa jitihada zinaendelea ili kukifufua ili kiweze kufanya kazi tena.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru vyanzo vya maji vinaendelea kuathirika, na kupotea siku hadi siku nchini.
Je, Serikali imeanzisha vitalu vya miti inayotunza maji ili kuipanda na kuitunza kwenye vyanzo vya maji ili vyanzo vyetu vizidi kukua na kutoathirika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na Halmashauri pamoja na taasisi zingine kukosekana kwa wataalam wanaotuelekeza aina ya miti ya kupanda na wapi. Ndiyo tukasema TFS lazima iwepo kila sehemu, kwa sasa hivi huyu wakala wa misitu ndiye anayetoa ushauri wa miti aina gani inafaa kupandwa eneo gani, eneo la vyanzo vya maji linafaa kupandwa miti ya aina gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge huduma hizi zote mtazipata sasa kila Wilaya kwa kila Ofisi ya Wakala ya Misitu ambaye anatoa maelekezo haya.
Lakini Wakala hawa watai-guide vizuri sana halmashauri kuhakikisha kwamba inavipitia vile vyanzo vyote vya maji na kuenda kupanda miti inayofaa katika kulinda vyanzo vya maji.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri tuliyoyazoea, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, takriban tangu kuungua kwa kitu hiki ni miaka tisa na kipindi hicho chote askari wanafanya kazi katika mazingira magumu sana kiasi wanahatarisha afya zao. Kwa kuwa Serikali imeshindwa kukamilisha kituo hiki katia muda mwafaka, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kukifunga kituo hiki mpaka ujenzi wake ukamilike kwa usalama wa skari wetu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya kupunguza madeni ya wakandarasi. Kituo cha Mkokotoni kimetengewa shilingi milioni 200 kwa ajili ya mkandarasi aliyejenga kituo kile, nataka kujua, je, mkandarasi huyo ameshalipwa pesa zake? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi hatuna mpango wa kukifunga hiki kituo kwa sababu mipangilio ya kukiendeleza, kukikamilisha iko mbioni na ndiyo maana naomba nichukue fursa hii kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tumeshafanya uhakiki na kuwasilisha Hazina ili mkandarasi aweze kulipwa na ujenzi uweze kukamilika. Kitakapo kamilika kituo hiki kitatumika. (Makofi)
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kumwuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko la Majimbo yaliyoongezwa na Baraza la Wawakilishi Zanzibar mwingiliano wake unaleta usumbufu na kupunguza kasi ya maendeleo. Nataka kujua: Je, Tume ya Taifa iko tayari kuongeza Majimbo manne ili yaende sambasamba ili tufanye kazi vizuri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili ZEC ni Wakala wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi; NEC kwa Zanzibar kwa Uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Wabunge, lakini wanatumia daftari moja, kura inapigwa siku moja katika chumba kimoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uchaguzi wa 2015 ZEC walifuta matokeo ya Uchaguzi wakati ambapo Wawakilishi na Madiwani walishatangazwa katika Majimbo yao na wamepewa hati zao za ushindi, katika mazingira kama hayo, nataka kujua: Je, NEC wametumia sheria gani ya kukubali uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Wabunge kutoka Zanzibar?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, nikianza na swali la kwanza kuhusu Majimbo manne ya Uwakilishi, kama katika majibu yangu ya msingi yalivyosema, suala hili la ugawaji wa Majimbo yanafanyika kwa mujibu Ibara ya 75(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na katika maneno yaliyotumika ni baada ya kufanyika uchunguzi na kugawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa mujibu wa Katiba hii, ni kwamba pindi pale matakwa ya Katiba hii na hasa katika Ibara ya 98(1)(b) ambayo inasomwa pamoja na Orodha ya Pili ya Nyongeza item Na. 8 ya kwenye Katiba ambayo inahitaji ongezeko la Wabunge wa Zanzibar, lazima pia ipitishwe na theluthi mbili ya Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na wenzetu kutoka Zanzibar. Kwa hiyo, kwa mujibu wa Katiba, jambo hilo linawezekana baada ya taratibu hizo kufuatwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusiana na matokeo ya uchaguzi; kwa mujibu wa Katiba yetu inazungumza vyema kabisa kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi ina jukumu la kusimamia Uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wabunge kwa upande wa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, chaguzi nyingine zote zinakuwa chini ya ZEC ambao pia kwa mujibu wa Katiba nao wana majukumu ya kusimamia uchaguzi katika ngazi hiyo. Kwa hiyo, jambo ambalo limetokea ambalo Mheshimiwa Mbunge amelisema, maana yake ni kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitumia mandates yake ya Katiba ambayo inampa mamlaka ya kusimamia uchaguzi huo.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Waziri anakiri katika masuala yake kwamba elimu ilitolewa baada ya vita vya Kagera, lakini waathirika wakubwa katika kadhia hii ya mabomu ni watoto wadogo hasa wanafunzi wa shule za msingi. Inaonekana kabisa kwamba elimu hawajapatiwa ya kutosha au hata kama inapelekwa haiwafikii. Sasa swali langu lipo hapa; je, Serikali iko tayari kuingiza kipindi maalum katika masomo yao wanafunzi wa shule za msingi ili wapatiwe elimu ya kujikinga na mabomu na athari zake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, umiliki na udhibiti wa silaha za mabomu pamoja na silaha nyingine ni jukumu la vyombo vya ulinzi na usalama. Kwa hiyo, kutapakaa hovyo kwa mabomu kumepelekea wanafunzi wa Shule ya Kihanga, Ngara, Kagera kupoteza maisha na wengine wengi wao kujeruhiwa. Je, Serikali iko tayari kuwalipa fidia wale waliopata janga hili? Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kwanza kwamba Serikali iwe tayari kuingiza somo maalum katika mitaala ya shule za misingi, hili ni wazo zuri na linazungumzika na sisi tutaendelea kuzungumza na wenzetu wa Wizara zinazohusika na elimu ili kuweza kuona uwezekano wake. Wakati hayo yanaendelea, elimu imekuwa ikitolewa katika maeneo hususan yale maeneo ambayo yanaonekana yana matatizo na lengo ni kuwapa elimu wahusika na wao waweze kupeleka katika shule zinazopatikana katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la kwamba inapotokea kwamba mtu amepata tatizo linalohusiana na mabomu au silaha nyingine mbalimbali basi walipwe fidia, niseme tu kwamba kwa kiwango kikubwa ili kuweza kuondoa tatizo hili, ni muhimu kuhakikisha kwamba elimu inatolewa. Kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba wahandisi wetu wa medani mara zote wamekuwa tayari kwenda katika maeneo yenye mashaka, yenye matatizo ili kuweza kuondoa mabomu haya ili kuepuka athari badala ya kujikita katika suala la kusubiri watu wapate matatizo halafu fidia zitolewe. Hata hivyo, ikithibitika kwamba aliyepata madhara haya yametokana na mabomu ya kutupwa kwa mkono ambayo hayakuweza kuondolewa kwa wakati, basi kwa kawaida fidia huwa zinatolewa.
MHE. YUSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika mvua za masika za mwaka jana Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alisema kwamba tayari Serikali imepata mfadhili na watajenga mto Msimbazi badala ya kuwa adhabu itakuwa ni starehe kubwa kwa sababu utakuwa ni kivutio kikubwa cha utalii kwa mkoa wa Dar es Salaam. Leo Mheshimiwa Waziri anasema bado kuna mchakato. Je, Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam ilikuwa ina mradi wake na Serikali Kuu ina mradi wake au ni huo huo mmoja hamjakubaliana?(Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yangu yote kuanzia jibu la msingi na haya ya nyongeza, nimesema Serikali iko tayari na ina mpango wa kutekeleza mradi huu na ndiyo maana tumesema mradi huu utakuwa kivutio kikubwa utakayoipamba Dar es Salaam na kuwa Dar es Salaam nzuri sana kwa sababu ni mradi ambao ukisharekebisha Bonde la Mto Msimbazi kwa ukubwa wake, na kuweka parking za magari conference centers lakini pia maua na vitu kama hivyo basi maana yake ni mradi ambao utakuwa umeipamba Dar es Salaam na hivyo kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwamba Dar es Salaam itakuwa nzuri na Msimbazi itakuwa nzuri, bado inabaki pale pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachozungumzia hapa ni kumalizia mchakato wa kutafuta fedha, offers zipo lakini kama Serikali lazima tufanye utaratibu kwa kuzingatia sheria ya misaada na mikopo ili tuweze kupata mikopo au msaada ambao una tija, hapa ndipo tunaposema gharama hizi zilizoandikwa bado ni mapendekezo, lakini kama Serikali tunamalizia mchakato wa kuhakikisha kwamba tunatekeleza mradi huu. Kwa hiyo, mradi upo na utatekelezwa lakini Serikali lazima ijiridhishe na offers tunazozipewa. (Makofi)
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba ruhusa yako kabla sijauliza maswali mawili ya nyongeza, niwapongeze Simba Sports Club kwa kuchukua ubingwa wa Tanzania mara mbili mfululizo. (Makofi)

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mnajuana eeh! (Makofi)

MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza, mimi nina wasiwasi kwamba agizo analolitoa Mheshimiwa Waziri kwamba linafanyiwa kazi na vilabu na hili tatizo ni kubwa linajitokeza mara kwa mara: Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kuleta sheria hapa Bungeni kuvibana vilabu angalau vile vya daraja la kwanza na vile vinavyocheza Club Bingwa ya Tanzania kupima kwa lazima? Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali langu ya pili, hili suala la upimaji wa afya, basi Bunge tungekuwa mfano mzuri sana, kwa sababu tuna vilabu mbalimbali vya michezo hapa Bungeni, mfano Club ya Mpira wa Miguu Ndugai Boys na michezo hii inashirikisha Viongozi Mashuhuri. Mfano mzuri Waziri Mkuu amekuwa mchezaji, pia amekuwa Kocha ambaye ameleta ufanisi mkubwa katika timu ya Bunge hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nataka kujua, ni lini wamewahi kupima afya zao wakicheza michezo ya ndani? Au ile wanayotushirikisha katika Mabunge ya East Africa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri. Nikianza na swali lake la kwanza ambalo amezungumzia kwamba agizo hili huwa halifanyiwi kazi.

Mheshimiwa Spika, napenda nitumie nafasi hii kusema kwamba suala la kupima afya kwa wachezaji ni agizo ambalo sisi kama Wizara tunalisimamia. Ukiacha kwamba ni suala la kisera, ukiangalia kwenye kanuni za FIFA, vilevile kwenye kanuni za TFF imeelekeza wazi kwamba vilabu vyote na mashiriko yote ya mpira wa miguu yahakikishe kwamba yanapima afya ya wachezaji wao, siyo tu kipindi ambacho vilabu vinajiandaa kuingia kwenye mashindano, vilevile kabla ya usajili wowote kuweza kufanyika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hilo ni agizo, nasi kama Wizara tunalisimamia, lakini kwa ushauri ambao Mheshimiwa Mbunge ameutoa, kwamba sisi kama Wizara tulete sheria hapa Bungeni, niseme kwamba ushauri huo tumeupokea kwa sababu sisi Wabunge ndiyo ambao tunatunga sheria; na kama Mbunge ameona kwamba kuna haja ya kuwa na hiyo sheria, basi sisi kama Wizara tutakaa na kuangalia namna gani ambavyo tutaleta hiyo sheria ndani ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la pili amezungumzia kuhusiana na timu ya Wabunge. Ni kweli kwamba tunayo timu ya Wabunge na timu yetu imekuwa ikifanya vizuri sana katika mashindano mbalimbali ya East Africa. Kwa hiyo, kama ambavyo nimezungumza, suala la kupima afya kwa wachezaji siyo tu kwa timu ambazo zinashiriki ligi kuu, ni jukumu la timu zote ambazo zinashiriki mashindano mbalimbali, iwe ni timu ambazo zinashiriki ligi daraja la kwanza, daraja la pili, vilevile hata kwenye michezo ya UMISETA na UMITASHUMTA wanatakiwa kupima afya kwa wachezaji wao kabla ya kuanza kwa mashindano.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hata kwa sisi Wabunge, ni jukumu letu la kuhakikisha kwamba wanapima afya zao kabla ya kuweza kushiriki mashindano yoyote au kabla ya kwenda kushiriki kwenye mashindano ambayo huwa yanafanyika nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Suala la Sea Erosion lipo katika nchi yote ya Tanzania ambayo imezungukwa na ukanda wa bahari na linamega kwa kiasi kikubwa ardhi ya Tanzania hali ambayo inahatarisha usalama wa watu wetu, pia kupungua kwa ardhi yetu. Kwa mfano, Msimbati Mkoani Mtwara ardhi ilichukuliwa kwa zaidi ya mita kumi kwa wakati mmoja:-

Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuhamasisha na wao wenyewe Serikali kushiriki katika kupanda miti ya mikoko maeneo yale ili kuzuia athari hizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimeeleza kwenye majibu ya msingi kwamba tayari tunao mpango wa kuhimili mabadiliko ya tabia nchi wa mwaka 2007. Pia tuna mkakati wa mabadiliko ya tabia nchi wa mwaka 2012. Kwa hiyo, mkakati huu ulikwishaanza kwenye maeneo yote yaliyoathirika na nikuhakikishie tu kwamba mkakati unaendelea na pale utakapopata fedha kwa ajili ya kuokoa maeneo haya, maana yake tutafika kwa ajili ya kuhakikisha maeneo haya tunayaweka salama.