Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Yussuf Haji Khamis (12 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa ruhusa yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara ya kwanza nazungumza katika Bunge hili, basi nawapongeza na kuwashukuru Wapiga kura wa Jimbo la Nungwi kwa ujasiri wao wa kulirejesha Jimbo la Nungwi katika mikono ya Chama cha Wananchi CUF na wameielezea dunia kwamba Jimbo haliazimwi, kinachoazimwa ni kiberiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo, naanza na ukamataji wa Jeshi la Polisi unaoendelea siku hizi, unakuwa hautofautishi baina ya majambazi na Polisi, namna wanavyowakamata raia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku ya tarehe 19 mwezi wa Tatu, 2016 ndani ya Jimbo langu katika Shehia ya Kidoti, alikamatwa Mwalimu wa Chuoni, anaitwa Mwalimu Haji Mtumbwi. Mwalimu huyo alifuatwa Chuoni na mtu ambaye kavaa vizuri, hamjuwi kama ni Askari, isipokuwa ni mtu mzuri tu, akamwambia nina shida na wewe tuzungumze. Alipofika kwenye gari ambayo ilikuwa ni ya abiria, ndani anakuta watu wana bunduki na wanamwambia uko chini ya ulinzi na wakamwingiza kwenye gari kwa nguvu pasipo kujulishwa familia yake, pasipo kujulishwa Shehia, pasipo kujulishwa Kituo cha Polisi chochote kilicho karibu. Alipoingizwa ndani ya gari, akafungwa kitambaa cheusi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Polisi wana dhamana ya kulinda usalama na raia wake lakini wanakamata kama hawako katika sheria, wanamchukua mtu kama jambazi, siku tatu hajulikani aliko. Hii ni dhuluma. Jeshi letu la Polisi lisiendelee na mtindo huo. Kama kunatakiwa ushahidi, niko tayari twende na Waziri muda huu huu na mhusika yupo. Hii siyo njia nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nakuja Tumbatu. Tumbatu kumekuwa na mgogoro siku nyingi sana. Tangu uanze Mfumo wa Vyama Vingi 1993 na 1995 uchaguzi wa kwanza, basi kumekuwa na migogoro ambayo inasababishwa na Jeshi la Polisi wenyewe. Kwa sababu 1995 alichukuliwa Ngugu Abbas Ali, wakaingia watu wa CCM wakamkamata wakamchinja kama samaki akapoteza network; kwa hiyo, akachukuliwa akapelekwa hospitali, alipopata fahamu yake akasema kwamba fulani na fulani ndio walionifanya hivi. Mpaka leo hakuna kesi wala hakuna aliyekamatwa. Nani atakuwa anasababisha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 24, mwezi wa Kumi, 2015, siku moja kabla ya Uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba, vikosi vya SMZ vilivamia katika Mji wa Jongowe, matokeo yake wakawakamata vijana wanne, wakawakamata wakaenda wakawatesa mpaka wakapoteza fahamu, walipookotwa, kuliko Ulimboka, namna walivyo. Nyang’anyang’a! Ripoti ikapelekwa Polisi Mkokotoni, hakuna hatua iliyochukuliwa. Jeshi la Polisi linashiriki kikamilifu katika kufanya hujuma za kuwaonea wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 29, mwezi wa Kumi, 2015, siku aliyotangazwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dkt. John Pombe Magufuli, sherehe ziliwazidi wana-CCM. Sherehe ziliwazidi wasijifahamu, wakavamia Kijiji cha Kichangani, Tumbatu wakapigapiga watu kwa silaha za kijadi, wakachoma nyumba saba, wakavuruga hali ya amani na utulivu. Matokeo yake, walipokwenda kuweka ripoti hawa waliofanyiwa hivi, wamekamatwa wao na wana kesi wao, kesi namba 116/2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana hawa kumi ambao wamekamatwa na naomba nitaje majina yao Mheshimiwa Waziri uyachukue. Wa kwanza ni Baraka Haji Gora, Faki haji Makame, Haji Abdallah Juma, Haji Sheha Makame, Kombo Makame Kombo, Makame Juma Makame, Musa Haji Omar, Omar Haji Omar, Machano Omar, Faridi Hamis; wamefunguliwa mashtaka wao. Hili ni tatizo kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hujuma hizo kuna mama mmoja amechomewa nyumba yake, yumo ndani moto umeshika hadi juu ya paa.
Anapata tabu hajui pa kukimbilia. Alikimbilia uani. Alipokimbilia uani, akamshuhudia mtu ambaye anachoma, yule fulani.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Aaaah… (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii adhimu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema ya uhai na hewa safi ya oxygen ambayo haikati kodi (TRA) wala (ZRB). Pia nikushuku wewe kwa kuniruhusu nichangie Ofisi hii ya Waziri Mkuu. Nataka nianze na suala moja dogo akisimama Waziri Mkuu kujibu hoja za Wabunge anipatie jibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha aliyotoa Msajili ni fedha ya walipa kodi ambayo hukaguliwa na (CAG) Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali. Fedha hii iliyotolewa na Serikali ikaingizwa katika akaunti ya mtu binafsi zitakaguliwaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka kujua NMB Bank nani kawapa ruhusa fedha ya Serikali itolewe kiholelea pasipo kufuata miamala ya kibenki na sheria zake.
Inawezekanaje milioni mia tatu na sitini na tisa (369,000,000) zitolewe kwa siku mbili fedha nyingi kama hizi kutoka akaunti ya chama kwenda akaunti ya mtu binafsi au huyu mtu binafsi ana chama chake mwenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano inapigana vita ya ufisadi na rushwa, suala hili limepigiwa kelele takribani miezi minne sasa, lakini hakuna chombo chochote cha Serikali mfano, Polisi, Usalama wa Taifa na TAKUKURU na hizi ni fedha za wananchi; je, kuna nini au ugumu gani katika jambo hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, malalamiko ya watu wa usafirishaji wa majahazi katika bandari ya Dar es Salaam; wanalalamikia kodi kubwa wanayokatwa kiasi ambacho
wao hawapati kitu na wanashindwa kutoa huduma hiyo.
Wanakatwa kodi kwa kipimo cha (CDM) na CDM moja wanalipa Sh. 7,500/=. Gari moja la fuso linapakia CDM 80 ni sawa na Sh. 600,000/= ambapo wao wakipakia CDM 80 yaani fuso moja mfano wa mbao wanalipwa Sh. 1,000,000/= milioni
moja tu. Kama ni kweli na sahihi katika fuso moja Serikali inachukua 600,000 /= wenye Jahazi wanapata 400,000/= tu.
Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie tatizo hili. Nilimwomba zaidi ya mara tatu Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi akutane na watu wa Majahazi ili awasikilize na awasaidie katika hili lakini bahati mbaya shughuli za hapa kazi zilimzidi
hakuwahi. Naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu anisaidie juu ya hili. Mheshimiwa Mwenyekiti, nizunguzie (MIVARF); mradi huu wa MIVARF Mkoa wa Kaskazini Unguja Wilaya ya Kaskazini ‘A’ tumebahatika kupata mradi wa Soko la Kinyasuni, barabara ya Chaani Donge na barabara ya Lunga Lunga Polisi hadi binti Saidi. Barabara hizi zimesaidia sana wakulima wa maeneo hayo kwa kupata wepesi wa usafiri wa mazao yao. Ushauri wangu barabara hizi zingefanywa endelevu kwa sababu zinajengwa maeneo ya maji hivyo ni rahisi wakati wa mvua kifusi kuondolewa na matatizo kubakia palepale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu soko la Kinyasini, naomba Serikali isimamie kwa karibu sana ili limalizike kwa wakati kuondoa adha wanayopata wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja. Pia kuna watu waliobomolewa kupisha soko hilo na wanalalamika kutolipwa. Nataka kujua nani anawajibika kuwalipa? Naomba nipatiwe majibu; je, wamelipwa, watalipwa au hawalipwi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye kurehemu waja wake wote pasipo ubaguzi. Nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii muhimu na mimi nichangie mada iliyopo Mezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze mchango wangu kwa kuperuzi ukurasa wa 49 wa kitabu cha Waziri kuhusu fedha za Mfuko wa Maendeleo wa Jimbo. Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo upo kisheria, Sheria Na. 16 ya mwaka 2009, pamoja na nia njema ya Serikali ya Muungano wa Tanzania kuchochea maendeleo ya Jimbo, Mfuko huu bado zipo changamoto ambazo zinahitaji ufumbuzi wa kina kustawisha utekelezaji wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utoaji wa fedha umekuwa adha kwa majimbo ya Zanzibar – mara nyingi kama sio zote, majimbo ya Zanzibar huchelewa kupata fedha hii wakati majimbo ya bara wanapata mapema sana. Kwa mfumo huu na ucheleweshaji huu unasababisha kudumaza maendeleo yanayokusudiwa; Zanzibar tunapata fedha hizi ambapo vitu vimepanda, thamani ya fedha yetu imeshuka. Kwa muktadha huo, naomba nipate sababu ya kucheleweshwa kwa fedha hii kwa Zanzibar. Pia nipendekeze kwa kuwa Jamhuri ya Muungano ni moja na Bunge moja, fedha hii itolewe kwa muda muafaka kwa Wabunge wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuhusu Mfuko huu, hauongezeki tangu ulipoanzishwa wakati mahitaji yanakua, kila siku watu wanaongezeka. Naomba Serikali ipitie upya Mfuko huu ili ione mahitaji kwa sasa na kuongeza Mfuko huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwiano wa ajira za Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar. Pamoja na makubaliano yaliyopo Zanzibar 21% na Bara 79%, lakini bado utekelezaji wake hauko wazi na umebakia kwenye makaratasi tu. Naomba uwekwe wazi kwa vitendo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii adhimu na muhimu kumshukuru Allah Subhanahu Wataala, kwa neema kubwa ya uhai na uzima. Pia nikushukuru kwa kuniruhusu nichangie mada iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno haya niliyazungumza katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu lakini kwa umuhimu wa jambo lenyewe na Mheshimiwa Waziri ndiye mhusika mkubwa, naomba nirejee ili nipate jawabu muafaka. Mimi binafsi nimekufuata Mheshimiwa Waziri zadi ya mara tatu kukuelezea malalamiko ya wasafirishaji wa majahazi katika Bandari ya Dar es Salaam. Kwa bahati mbaya sana hukuwahi kukutana na wadau wa majahazi hata mara moja, jambo ambalo sikulaumu sana kwa sababu mchakato wa hapa kazi ni mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa majahazi wanalalamika kipimo cha (CDM) ambacho CDM moja (1) wanalipa 7,500/=, ambapo (fuso) gari moja linajaa kwa CDM 80. Kwa fuso moja CDM 80 wanalipa sh. 600,000 ambapo mzigo huu walilipia Sh. 600,000/= wao wanabeba kwa thamani ya milioni moja 1,000,000/=. Kwa maana hiyo kama jahazi lina uwezo wa kubeba CDM 160 ama mafuso mawili Serikali inachukua 1,200,000/= na wenye jahazi wanabakiwa na laki 800,000/=, kwa hiyo wanalalamika hawapati kitu na biashara hii inawashinda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda Mheshimiwa Waziri akutane nao wenyewe ili ajue kiini cha tatizo hili. Hata hivyo, naomba aiangalie suala hili na atoe tamko kuhusu malalamiko yao haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nizungumzie usafiri wa bahari kati ya Tanga – Pemba – Nungwi. Usafiri wa sehemu hizi wa bahari umekuwa na matatizo makubwa na husababisha ajali nyingi kwa kutumia vyombo duni na hafifu sana. Wananchi wamelalamikia Serikali yao kuhusu kuwapatia usafiri wa hakika mwishowe mfanyabiashara mkubwa Said Bakhresa ameleta meli kubwa ambayo itatoa huduma katika maeneo hayo. Nichukue fursa hii kupongeza Kampuni ya Bakhresa kwa ufumbuzi wa tatizo hili. Angalizo, Bakhresa ni mfanyabiashara. Kwa hiyo, anahitaji faida katika biashara yake. Abiria wa Tanga na Pemba kuna wakati wanakuwa wengi na wakati mwingine wanapungua. Wasiwasi wangu kama upungufu wa abiria na mizigo utakuwa mkubwa unaweza kukatisha usafirishaji na wananchi kukosa usafiri wa hakika. Je, Serikali ina mpango gani kwa wananchi hawa kama hali itakuwa kama hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri akisimama anitoe wasiwasi wangu huu.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii muhimu na adhimu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema ya uhai na uzima. Nikushukuru wewe Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuniruhusu na mimi nichangie ingawa kwa ufupi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapambano ya UKIMWI pamoja na kuendelea ndani ya nchi yetu lakini inaonekana bado UKIMWI unaongezeka pamoja na maambukizi mapya. Kama juhudi za makusudi hazitochukuliwa basi Taifa letu litafika pabaya sana. Kwa hivi sasa UKIMWI umekuwa uko sirini sana kiasi ambacho watu wengi wamekuwa na matumaini makubwa kwamba UKIMWI umepungua kwa style za watu zilivyo. Watu ambao wanaishi na virusi vya UKIMWI si rahisi kuwatambua kama hajajieleza mwenyewe. Hii inatokana na kuitikia wito wa kujiunga na vituo vya dawa za ARV, kwa hiyo watu wengi kwa kupungua athari za kuonekana moja kwa moja wanadhani kuwa UKIMWI umepungua.

Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba mkakati na juhudi ziendelee kuelimisha Watanzania kwamba UKIMWI upo na bado unaua. Wataalam wa UKIMWI wametoa taarifa kwamba Mkoa wa Njombe unaongoza kwa UKIMWI ambao una asilimia 14.8, hii ni asilimia kubwa na ya kutisha. Naomba Serikali ifanye utafiti ni jambo gani linalosababisha maambukizi makubwa kiasi hiki katika mkoa huu. Tatizo lijulikane na itolewe elimu ya uhakika ili kuondoa tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nazungumzia suala la wazee. Tunafahamu fika kwamba wazee wa sasa ndio vijana wa juzi na wa jana ambao walijituma kwa utumishi uliotukuka na mafanikio ya utumishi wao mwema ndio uliolifikisha Taifa letu hapa lilipo. Hivyo nashauri Serikali kutowasahau na kuwadharau wazee ambao ndio waliokuwa dira ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha ni kwamba wazee hawapati huduma inavyopaswa na badala yake wazee wanaonekana kama hawakuwa na mchango wowote katika Taifa hili. Kwa mfano katika huduma za matibabu wazee wamekuwa wakisumbuka kana kwamba hawastahili kupatiwa huduma hii, wamekuwa wakitozwa malipo makubwa ambayo hawamudu lakini ni haki ambayo imeidhinishwa na Serikali kupatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuliwekea kipaumbele suala la kuwajali wazee kwa kufuatilia huduma zinazostahiki kwao Serikali ina nia na dhamira thabiti juu ya wazee inaonekana changamoto hii inayowakumba ni utendaji mbovu usiojali mchango wa wazee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia hoja yangu napenda kugusia angalau kidogo suala la mazoezi ya viungo kwa jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazoezi ni jambo muhimu sana kwa afya ya mwanadamu na michezo ni sehemu ya mazoezi. Kwa hiyo, michezo ni muhimu sana kwa maendeleo ya jamii na kiuchumi na hasa katika kuimarisha miili yetu kiafya na kuwa wakakamavu. Sasa hivi nchi yetu imekumbwa na magonjwa mengi sana ambayo kama tungekuwa makini tusingeathiriwa sana na magonjwa haya, mfano wa magonjwa hayo ni kama vile kisukari, moyo na kadhalika. Magonjwa haya kwa ujumla wake yanaitwa magonjwa sugu na yanayogharimu fedha nyingi za wananchi na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali na Wizara ya Afya kuhamasisha jamii na suala zima la kufanya mazoezi na kutoa misaada pale inapobidi ili kuendeleza mazoezi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema ya uhai na uzima. Pia nakushukuru wewe kwa nafasi hii ya kuchangia katika Wizara hii ingawa kwa ufupi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze mchango wangu kwa kupongeza chombo hiki muhimu kwa ulinzi uliotukuka wa mipaka ya nchi yetu na kutoa nafasi kwa wananchi kushiriki kazi za ujenzi wa Taifa kwa amani na utulivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze Kambi ya Jeshi Mtoni-Zanzibar. Kambi ya Jeshi Mtoni ipo ndani ya Mji wa Unguja. Kambi hii kwa mtazamo wangu mazingira yake siyo mazuri kiusalama kwani uzio uliozunguka kambi hivi sasa umeanza kuvamiwa baadhi ya sehemu zake. Upande wa Kusini wa uzio tayari umevamiwa na watu kwa shughuli za kibinadamu kama maduka, baa, car wash na kadhalika. Huduma hizi zinafanywa na watu mbalimbali usiku na mchana. Naomba Waziri anieleze shughuli zile ni za Jeshi au za nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanajeshi wetu waliovamiwa Congo na kupoteza askari 14 na wengi kujeruhiwa vibaya kwa kiasi wameathirika kisaikolojia, nataka kujua lini watarejeshwa nchini ili warudi katika hali zao?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema kubwa ya uhai na uzima. Ninakushukuru wewe kwa kunipatia nafasi na mimi nichangie ingawa kwa muhtasari. Nianze kwa kupongeza utamaduni mzuri wa vijana wetu wanaomaliza vyuo na wale wengine kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa, kwa mujibu wa sheria na wale wa kujitolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni jema sana kwani vijana wetu hupata mafunzo mbalimbali yakiwemo ya ulinzi na usalama na yale ya ujasiriamali, vijana wanaopatiwa mafunzo ya ujasiriamali katika shughuli za kilimo, ufugaji, fundi uashi, fundi uchongaji, na mengine mengi hufanikiwa vizuri wakiwa kambini, wakishaondoka kambini elimu yote waliyopata hupotea kwa sababu vijana hawawezeshwi wanabakia vijiweni tu hawajui la kufanya na elimu waliyopata inapotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu vijana hawa wakusanywe vikundi mbalimbali, wasajiliwe kisheria, Serikali iwalee na kuwawezesha ili wajiajiri na kuendeleza elimu waliyopata kambini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa vijana wanapata mafunzo ya kijeshi na wana uwezo wa kutumia silaha mbalimbali, Serikali haiwezi kuwaajiri vijana wote, wengi wao hurudi nyumbani wakiwa hawajui la kufanya, vijana wanakuwa rahisi kujiunga na makundi ya uhalifu, hivyo ni hatari kwa Taifa na usalama kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu vijana hawa wawekwe katika orodha maalum sekta za ulinzi zinapohitaji kuajiri wafanyakazi, kwa mfano, Polisi, Magereza, Zimamoto, Usalama wa Taifa hata kampuni za ulinzi wa binafsi basi wapewe kipaumbele vijana wetu ambao wamepitia Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wabakie kama Jeshi la Akiba hivyo wapangiwe utaratibu kila baada ya muda fulani wanakusanywa kwa kukumbushwa majukumu yao juu ya wajibu wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie muingiliano wa kambi za Jeshi na makazi ya raia. Hili ni tatizo ambalo linahitaji kuangaliwa kwa makini sana. Shughuli za kijeshi ni maalum kwa Jeshi mambo mengi ya hatari ambayo yanawahusu wenyewe, mfano maghala ya milipuko mbalimbali ambapo ikitokea bahati ambayo inasababisha maafa makubwa kwa wote. Mfano, mkubwa na hai ni ule wa Gongo la Mboto na Mbagala taharuki kubwa kwa nchi na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ifanye juhudi za makusudi, kuepusha kambi zote za Jeshi zenye ghala za milipuko zitengwe na makazi ya raia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie ajira katika Jeshi na vyeti fake. Tatizo hili ni la Taifa zima na katika taasisi mbalimbali, lakini taasisi hii muhimu ina athari kubwa na ni hatari kuwaajiri askari na ukawapa mafunzo yote na siri zote za Jeshi wanazifahamu wamefanya kazi zaidi ya miaka 10 au 15 ndiyo unakuja kugundua vyeti vyao ni fake na kumfukuza kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii siyo vizuri kwa sababu hili ni kundi kubwa sana tunalolikufukuza na tunalifukuza wakiwa na taaluma. Naomba Serikali iangalie kwa umakini suala hili mwanzo wa kuajiri wabaini kasoro zote ambazo hazifai ikiwemo vyeti fake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niombe usawa wa ajira kati ya pande mbili za Muungano kwa kuwa Muungano wetu ndiyo unaunda taasisi hii muhimu ya ulinzi naomba ajira zake zifanywe kwa uwazi mkubwa tena kwa uwiano mzuri. Hii itajenga heshima na uimara katika Jeshi letu na kupata ushirikiano kwa pande zote na kwa watu wote.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS:Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Allah Subhanahu Wataala kwa neema ya uhai na afya njema. Nikushukuru wewe pia kwa nafasi hii muhimu sana kwangu ili nitoe mchango wangu ingawa kwa ufupi katika Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na bidhaa bandia. Pamoja na kwamba Serikali kupitia (TBS) imeweka program ya kudhibiti bidhaa bandia kutoka nje ya nchi lakini kinyume chake bidhaa bandia zinazagaa kila sehemu ya nchi yetu, wakati mamlaka ya udhibiti (TBS) wapo na jambo hili wanalijua na hakuna hatua madhubuti zinazochukuliwa. Jambo hili la bidhaa bandia linaweza kuleta madhara makubwa katika nchi na kwa wananchi wenyewe kwa ujumla. Pamoja na kuzorotesha bidhaa za ndani ya nchi lakini pia wananchi hawana elimu ya kutosha juu ya jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu juu ya jambo hili ni kwamba, kwa sababu (TBS) wanashughulikia bidhaa bandia, na kwa kuwa (TBS) hawana uwezo wa kushughulikia bidhaa bandia na kwa kuwa (TBS) hawana uwezo wa kushughulikia na bidhaa fake na kwa sababu (TFDA) pamoja na mambo mengine inajishughulisha na dawa zilizokuwa chini ya kiwango na kwa sababu (FCC) inashughulika na bidhaa fake, kwa mantiki hiyo ni bora taasisi hizi kufanya kazi kwa pamoja ili kuleta ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la ngozi. Tanzania tuna ng’ombe million 21.3; mbuzi millioni 1.5; na tunao kondoo millioni 6.4. Pamoja na kuwa na mifugo mingi kiasi hiki jambo la ajabu Tanzania tunasafirisha ngozi ghafi katika kiwango ambacho hakiendani na rasilimali tuliyonayo ukilinganisha na Kenya ambayo inasafirisha ngozi ghafi nyingi kuliko Tanzania. Pia Sekta ya ngozi haitengenezi ajira wala haiongezi pato la Taifa kwa hiyo inachangia pato kidogo sana la Taifa. Pamoja na juhudi za Serikali za mara kwa mara za kuongeza kodi mpaka kufikia asilimia 90 ili kuzuia usafirishaji wa ngozi ghafi nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, mpango huu haujasaidia kwa sababu bado ngozi zinasafirishwa kwa magendo hivyo kukosesha mapato ya Serikali kutokana na kodi iliyowekwa. Pia hata ngozi ingebaki ndani ya nchi zingeoza kwa sababu hakuna viwanda vya ku-process ngozi wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali iweke mkakati wa makusudi wa kuokoa sekta hii ya ngozi. Kama si hivyo basi wingi wa mifugo tulionao hautasaidia vema uchumi wa nchi yetu. Tutabaki na changamoto zile zile za siku zote kati ya wakulima na wafugaji kugombania malisho. Naomba tuwe makini kuhusu hili.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu muumba mbingu na ardhi na vilivyomo. Nikushukuru wewe kwa nafasi hii uliyonipatia ili na mimi nichangie, ingawa kwa muhtasari, katika Wizara hii muhimu sana kwangu kwa sababu imenilea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizobarikiwa na rasilimali muhimu za bahari, maziwa na mito. Tanzania Bara tunao mwambao wa bahari wenye kilometa 750 ambapo Unguja na Pemba wanazo kilometa 675. Maeneo haya ni muhimu kwa Taifa letu kwa sababu yana samaki wengi wa kila aina pamoja na vivutio vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa masikitiko makubwa na ni bahati mbaya sana Serikali imeshindwa kudhibiti eneo hili na chanzo hiki cha utajiri. Eneo hili muhimu linakumbwa na changamoto mbalimbali ambazo zinarejesha nyuma na kuvunja moyo wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya changamoto zinazokabili eneo hili la utajiri wetu ni pamoja na wavuvi haramu; (wavuvi wanaotumia mabomu, wavuvi wanaotumia nyavu zenye matundu madogo na wengine wanatumia gesi). Changamoto zote nilizotaja hapo juu ni baadhi tu lakini zote ni hatari sana. Kwa mfano, uvuvi wa kutumia mabomu unaharibu mazingira vibaya sana, unaharibu mazalia ya samaki (matumbawe), mapengo ya mikoko pamoja na kuharibu maji ya bahari; wanaua samaki wengi wadogo wadogo pamoja na kuharibu mazalia mpaka mayai ya samaki, hakuna kinachobaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya nyavu zenye matundu madogo vile vile ni hatari kwa sababu hazibakishi zinavua mpaka samaki ambao hawafai hata kwa kula, hivyo inakaribiana na bomu, gesi pamoja na wanaotumia kemikali; athari zake zinafanana ingawa uvuvi wa kutumia kemikali na gesi ni hatari zaidi kwa sababu ni sumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niangazie kidogo katika wizi wa kimataifa katika Bahari Kuu kwa meli za kigeni. Pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali lakini bado tatizo hili lipo na ni hasara kwa Taifa. Meli za kigeni bado zinafanya magendo katika bahari yetu na kuangamiza uchumi wa nchi yetu. Wataalam wanasema uvuvi haramu unalikosesha Taifa letu kila mwaka asilimia 80 ya mapato ambayo yanapatikana katika sekta ya uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia uvuvi huu haramu unawakosesha mapato wavuvi wadogo wadogo wapatao 40,000 ambao wanashindwa kupata samaki wa kutosha. Udhibiti wa Bahari Kuu bado ni dhaifu na ndiyo maana wahalifu wanaendelea na uhalifu kila siku ambao unatukosesha zaidi ya dola milioni 220 kila mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu tulipokamata Meli ya MFV TAWARIQ 2009 kuna meli gani nyingine ambayo imekamatwa? Takribani miaka saba (7) mpaka nane (8) hivi sasa. Je, Mheshimiwa Waziri hivi ndiyo tuseme hakuna meli zinazovua katika bahari yetu? Nishauri, ni lazima sasa Serikali iwekeze katika Bahari Kuu kwa maslahi ya Taifa na watu wake.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua fursa muhimu kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema mwenye kurehemu waja wake wote. Nakushukuru wewe kwa nafasi hii muhimu sana kwangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni uhai. Kila kitu duniani kama hakuna maji basi hakuna viumbe hai. Kwa hiyo, maji ni muhimu kwa maisha na maendeleo ya binadamu kwa jumla. Takriban karibu Waheshimiwa Wabunge wote wamelalamikia maji katika majimbo yao. Wananchi wanapata tabu sana, wanakunywa maji machafu ambayo siyo salama. Akinamama wanaenda umbali mrefu sana, kwa hiyo, wanakumbana na matatizo makubwa na mengi sana. Mfano, ndoa zao ziko hatarini kuvunjika, wanabakwa pia wanadumaa katika kazi za maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali ione kilio cha Waheshimiwa Wabunge kwa umoja wao, Serikali iongeze bajeti ya maji kwa kupunguza matatizo haya katika Majimbo yetu. Naomba nizungumzie uhifadhi wa maji ya mvua. Pamoja na matatizo makubwa tuliyonayo ya maji, lakini bado Serikali yetu haiko makini juu ya ukusanyaji wa maji ya mvua ambayo hupotea kwa wingi sana. Mvua takriban hunyesha kwa vipindi lakini mvua zinakuwa kubwa ambazo husababisha mafuriko. Wananchi hupoteza makazi yao, mashamba yao na hata kupoteza maisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali ingetafuta wataalam wafanye utafiti kujenga miundombinu na mabwawa ya ukusanyaji maji katika sehemu mbalimbali katika Mikoa ya Tanzania. Maji tutakayokusanya yatakuwa akiba ambayo yatasaidia jamii katika shughuli mbalimbali za kila siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie mafuriko. Mafuriko yamesababisha adha na uharibifu mkubwa sana hasa kwa wakulima. Wakulima wamepata hasara kubwa sana, mazao yao ya vyakula yamesombwa na maji, mashamba yao yamekuwa kama bahari na kwa msimu huu hawavuni chochote. Kwa hiyo, hawana makazi, hawana chakula. Naomba Serikali ifanye mitaro ya kupitisha maji kwa usalama pasipo kuleta usumbufu kwa wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nizungumzie uharibifu wa bomba za maji. Bomba nyingi za maji hupasuka ama kutoboka, lakini huchukua muda mrefu sana pasipo matengenezo. Hivyo, hupelekea maji mengi sana kupotea na haya yanasababishwa na wataalam wa maji kubaki maofisini tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kuwa makini katika jambo hili. Wafanyakazi wa Maji wafanye kazi kwa ufanisi kuondoa tatizo la upotevu wa maji ovyo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai na afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze mchango wangu kwa kuzungumzia mateso wanayoyapata Askari wa Kituo cha Mkokotoni Kaskazini A Unguja. Kituo cha Polisi cha Mkokotoni kiliteketea kwa moto usiku wa tarehe 27 Desemba, 2017 saa 7.30. Ujenzi wa kituo ulianza mara moja kwa lengo jema kujenga kitu bora daraja (A) na kuwaondolea usumbufu askari wetu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu kituo kiungue huu ni karibu mwaka wa tisa (9) ujenzi haujakamilika. Mazingira wanayofanyia kazi ni magumu sana kiasi cha kuhatarisha afya zao. Mfano mdogo mapokezi (reception) ni banda la mabati juu, chini, pembeni yaani limeezekwa kwa mabati, kuta zake mabati. Wakati wa joto kali askari wanapata shida kwa joto kali kiasi cha kusababisha uharibifu wa ngozi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka tisa ni kipindi kirefu kufanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi kwa afya za askari. Wabunge tumekuwa tukiuliza sana kuhusu kituo hiki lakini majibu ni yale yale, mwaka wa fedha 2016/2017 ukimalizika unaambiwa 2017/2018 lakini hakuna linalofanyika. Naomba sana na kwa heshima kubwa tuone huruma askari ni binadamu wanahitaji kupewa moyo. Nataka kujua ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa kituo hiki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi niliuliza kuhusu deni la mkandarasi wa ujenzi wa Kituo cha Mkokotoni, Naibu Waziri akajibu bado hajalipwa. Inawezekana kutolipwa kwa mkandarasi huyu ni sababu ya kutokamilika kwa jengo hili. Hata hivyo, huyu ni mfanyabiashara, kumcheleweshea kumlipa ni kumuua kibiashara. Mkandarasi huyu anaumwa, afya yake si nzuri, anataka matibabu hali yake ngumu, je, ni lini Serikali itamlipa deni lake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 25 Septemba, 2017, Mzee Ali Juma Suleiman alivamiwa nyumbani kwake Mtoni Kidatu Unguja saa 5.30 usiku na kundi kubwa la watu ambao wengine wana mapanga, marungu na silaha za moto. Kama kawaida ya mtu yeyote mwenye kuvamiwa aliomba msaada kwa kupiga kelele nyingi pamoja na watoto wake. Ili kuzuia jamii isisogee kutoa msaada zilipigwa risasi za juu, wakamchukua na kwenda kumtesa, akaokotwa kupelekwa Mnazi Mmoja siku ya tatu alifariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kushangaza Zanzibar kisheria umiliki wa silaha za moto ni vyombo vya usalama pekee. Inapotokea tukio kama hili risasi kama tatu mpaka nne zinapigwa halafu vyombo vyote vya ulinzi vinakaa kimya bila wasiwasi wowote, hili linatia wasiwasi mkubwa kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mzee Ali Juma Suleman alihojiwa akiwa hospitali na vyombo vya habari alisema na kutilia wasiwasi Jeshi la Polisi kuhusika kwao katika uvamizi uliomkuta. Jambo la kusikitisha na kwa mshangao mkubwa mpaka muda huu Jeshi la Polisi halijakamata mtu yeyote kuhusiana na tukio hili. Serikali inatuambia nini kuhusu dhuluma hii mbaya kabisa?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema ya uhai na afya njema. Nakushukuru wewe na mimi kwa kupata fursa nichangie ingawa kwa uchache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ina migogoro mikubwa ya ardhi katika sehemu mbalimbali, kwa kiasi kikubwa migogoro hii inarudisha nyuma maendeleo ya nchi yetu. Tanzania ya viwanda itakuwa ni ndoto kama hatutaweza kupima ardhi na tukatenga maeneo kwa shughuli mbalimbali za kilimo, ufugaji, viwanda na makazi ya binadamu na tukiweza kufikia katika hatua hiyo, kwa kiasi kikubwa tutapunguza migogoro isiyo ya lazima na kufikia malengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Ardhi ni muhimu sana katika kufikia malengo makubwa ya kimaendeleo Kitaifa. Napendekeza Wizara hii ipewe kipaumbele kwa kutengewa bajeti ya kutosha kukidhi mahitaji ya mipango ya Wizara. Naomba Wizara iendelee kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutekeleza mipango yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusu umiliki wa ardhi. Sheria za Ardhi zinatambua haki sawa, umiliki wa ardhi kati ya mwanamke na mwanaume. Hata hivyo uhalisia ni tofauti, kwani mila na desturi zilizopo nchini, nyingi hazitambui usawa huu hasa katika haki ya kurithi ardhi. Pamoja na wanawake kuwa zaidi ya asilimia 50 ya idadi ya watu wote nchini, pia wanawake wanazalisha kati ya asilimia 60 hadi asilimia 80 ya chakula tunachokula ukanda wa Jangwa la Sahara. Tafiti nyingi zinaonesha wanawake asilimia 20 ndio wamiliki ardhi Kusini mwa Jangwa la Sahara. Hali hii kwa kiasi kikubwa inachangia wanawake kuwa maskini, kunyanyaswa na kudhalilishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, usawa wa umiliki ardhi na urithi wa ardhi upo kisheria kati ya wanawake na wanaume, naomba Wizara isimamie usawa huu kwa ukamilifu hasa vijijini. Wizara ipige vita mila na desturi zenye kukandamiza wanawake katika urithi wa ardhi na umiliki.