Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Twahir Awesu Mohammed (3 total)

MHE. TWAHIR AWESU MOHAMMED aliuliza:-
Kumekuwa na malalamiko ya baadhi ya watuhumiwa wa makosa mbalimbali kunyanyaswa na kupigwa na vyombo vya ulinzi na usalama hasa Jeshi la Polisi na kusababisha matatizo makubwa ya kiafya kwa watuhumiwa:-
Je, Serikali inasema nini juu ya Polisi wanaofanya vitendo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Twahir Awesu Mohammed, Mbunge wa Mkoani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa kunawezekana kukawa na malalamiko katika vituo vyetu vya Polisi kwa mujibu wa PGO Na.103 (1) inaelekeza kuwa japokuwa lalamiko ni dogo kiasi gani lazima Kamanda wa eneo afungue jalada na kuchunguza ukweli wa malalamiko hayo na ikibainika Askari aliyefanya kitendo hicho atachukuliwa hatua za kinidhamu dhidi yake kama vile kukatwa mshahara ama kufukuzwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeweka mfumo madhubuti wa kushughulikia malalamiko hayo kwa Mikoa yote ya Polisi, Makao Makuu ya Polisi na kama haitoshi Wizarani kwangu kuna dawati la kushughulikia malalamiko.
Kwa nafasi hii, nitoe rai kwa wale wote ambao hawatendewi haki wafuate utaratibu huo na hatua zitachukuliwa kikamilifu. Pia, Jeshi la Polisi limeendelea kutoa elimu kupitia mfumo wa mafunzo kazini, vilevile mafunzo ya vitendo ili kuhakikisha kuwa Askari wote wanafanya kazi zao kwa weledi na usasa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN (K.n.y. MHE. TWAHIR AWESU MOHAMMED) aliuliza:-
Tanzania ni nchi yenye amani kubwa katika nchi za Maziwa Makuu.
• Je, Serikali imejipanga vipi kuimarisha amani katika nchi yetu?
• Je, mipaka yetu na nchi zenye mizozo na wakimbizi imeimarishwa kiasi gani kiulinzi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA aliuliza:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Twahir Awesu Mohammed, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, kimsingi suala la kuimarisha usalama na amani ya nchi yetu ni jukumu la kila Mtanzania. Hata hivyo, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ambalo ndilo lenye jukumu la kulinda mipaka yetu ya Kimataifa na kuimarisha amani nchini limekuwa likishirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama pamoja na wadau wengine kuhakikisha kuwa hakuna adui wa ndani au wa nje anayeweza kuhatarisha au kuvuruga amani ya nchi yetu.
(b) Mheshimiwa Spika, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limejipanga kikamilifu katika kuhakikisha kuwa mipaka ya nchi yetu inalindwa muda wote dhidi ya adui yeyote atakayejitokeza kuivamia.
Aidha, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama limeimarisha ulinzi katika maeneo ya mipaka yenye wakimbizi kwa kuweka viteule na vifaa vya kutosha. Hatua hii imesaidia kuzuia na kukabiliana na vitendo vyote vya kihalifu vinavyoweza kusababishwa na wakimbizi katika mipaka na katika makambi waliyopangiwa.
MHE. TWAHIR AWESU MOHAMED aliuliza:-
Jeshi la Polisi lina dhamana kubwa ya kulinda usalama wa raia na mali zao na ni msimamizi mkuu katika haki za binadamu:-
(a) Je, ni lini Jeshi hilo litafanya kazi zake kisayansi zaidi na kuondokana na kutumia nguvu zisizo za lazima wakati wa kutekeleza majukumu yake?
(b) Je, suala la weledi kwa watendaji wa polisi linasimamiwa vipi ili polisi waweze kupambana na uhalifu unaokua kitalaam kila siku?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Twahir Awesu Mohamed, Mbunge wa Mkoani lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi ni chombo kilichoanzishwa kwa mujibu wa Katiba kusimamia usalama wa raia na mali zao na katika utendaji wake linaongozwa na sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali. Aidha, Jeshi la Polisi limejiwekea kanuni za kudumu (PGO) ambazo zimetafsiri na kutoa mwongozo wa utekelezaji wa sheria zote zinazoongoza utendaji wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji wa kazi zake askari anaruhusiwa kutumia nguvu inayoendana na mazingira ya tukio. Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kifungu namba 11(2) kinamruhusu askari kutumia nguvu katika ukamataji iwapo mkamatwaji atakaidi. Pia PGO 274 inaeleza mazingira ya matumizi ya nguvu na aina ya nguvu inayopaswa kutumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiwajengea uwezo wa kiutendaji askari kwa kutoa mafunzo mbalimbali sehemu za kazi yenye lengo la kuwakumbusha taratibu za kazi, pia limekuwa likitoa mafunzo ya weledi ya ndani na nje ya nchi ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha linafanya kazi zake kwa weledi Jeshi la Polisi limekuwa likiajiri wasomi wenye taaluma mbalimbali kama vile TEHAMA, maabara, uchunguzi wa nyaraka na taaluma zingine zinazohusiana na makosa yanayosababishwa na ukuaji wa teknolojia.