Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Twahir Awesu Mohammed (3 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. TWAHIR AWESU MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyenzi Mungu kwa kunijalia uzima na kuniwezesha kuandika maelezo yangu haya na kuyawasilisha mbele ya Bunge lako hili. Nazungumzia kipengele cha siasa ukurasa wa kumi (10) cha kitabu cha hotuba ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kukamilika kwa uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 hata haiwezekani kuweka siasa pembeni kwa baadhi ya vyama vya siasa kuwa na uhuru wa kufanya shughuli za kisiasa na vyama vingine kumnyima fursa ya kufanya shughuli zake za kisiasa. Kauli ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuzuia vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara hadi mwaka 2020 jambo ambalo ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, demokrasia ina uwanja mpana sana ukiwemo uhuru wa kujieleza, uhuru wa kupata habari haki ya kukosoa na kukosolewa na mengineo. Leo hii Taifa linashuhudia jinsi wananchi wanavyokosa fursa ya kuhoji ama kuwakosoa viongozi wao. Pia vyombo vya habari vinavyoshindwa kufanya kazi zake kwa uhuru na uwazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siasa za amani na utulivu ni za muhimu sana kwa wakati huu katika Taifa letu ili maendeleo yaweze kupatikana. Siasa ya amani na utulivu haziwezi kustawi hapa nchini kwa taasisi zilizojengwa kuvilea vyama vya siasa kugeuka na kuanza kuvihujumu vyama vya
siasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini alipaswa abadilike na achane kabisa na dhamira aliyonayo ya kutaka kukisambaratisha Chama cha Wananchi CUF na aache kulazimisha kuwachagua viongozi wa kukiongoza kwani vyama vina Katiba na Kanuni zake Aviachie vyama vifanye maamuzi yake na asiviamulie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amani ya nchi ni muhimu sana kwa Muungano wetu una maslahi mapana kwa wananchi wa pande zote mbili za Jamhuri na ni jambo la hatari; huyu Msajili wa Vyama vya Siasa asiachiwe akaliendeleza jambo hili litaleta mtafaruku mkubwa. Kwa upande wa pili wa Muungano wetu, hautariridhia hali ambayo amani ya nchi yetu itarudi kule kule tunakotoka katika siasa za chuki na uhasama baina ya wana CUF na wana CCM kule Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu:-
(i) Ili kudumisha mfumo wa Vyama vingi nchini Msajili wa vyama vya siasa afanye kazi kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na aachane kabisa kuvipangia ama kuviamulia Vyama vya Siasa.
(ii) Asaidie kutatua migogoro na sio kupandikiza migogoro.
(iii) Awe karibu na vyama vya siasa ache kujenga uadui na baadhi ya vyama vya Siasa.
(iv) Yeye ni mlezi kama baba atoe haki sawa kwa vyama asionyeshe ubaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasilisha.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. TWAHIR AWESU MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na kunifanyia wepesi na fursa ya kupata nafasi ya kutoa mchango wangu huu kwa njia ya maandishi katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakiri na kuamini suala la Muungano wetu ni la msingi na la umuhimu sana kwa faida ya washirika wa nchi zote mbili za Muungano wetu. Nakubali wananchi wa nchi zote mbili hawalalamikii kuwepo kwa Muungano, lawama zinakuja ni namna gani ifanyike kuuboresha na kuondoa malalamiko yaliyopo ikiwa ni pamoja na zinazoonekana kama ni kero kubwa kwa Muungano wenyewe
Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa vikao viwe vimekaliwa na watu wa pande zote mbili kukubaliana tatizo siyo vikao kukaliwa, tatizo kubwa hapa siyo kukaliwa kwa vikao tatizo ni kupatiwa ufumbuzi kero zile zilizolalamikiwa kutatuliwa lakini pia tatizo hapa ni kukaliwa vikao lakini wakimaliza vikao wahusika kukaa kimya wananchi wanaolalamika hawapewi taarifa za yale yaliyoamuliwa na kukubaliana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF III) una manufaa na faida kwa wananchi wa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uendelezwe na uimarishwe. Nashauri ili makusudi yaliyoazimiwa yawafikie walengwa halisi na wale waliokusudiwa ni vyema mfuko ukabadilisha utaratibu wa kuifikia jamii inayohusika kwa kuwatumia viongozi wa kijamii wenyewe kuliko kuwatumia viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiwemo Masheikh. Nashauri kwa nia njema kabisa viongozi wa mfuko wawatumie viongozi wa NGO’s ili wananchi wayafaidi vyema matunda halisi ya mfuko huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. TWAHIR AWESU MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia na kuwezesha kupata fursa hii muhimu ya kutoa mchango wangu huu katika hoja hii iliyopo mbele yenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haki za binadamu, tumekuwa na tabia kwa Serikali yetu hii tukufu kuweka maneno kwenye makaratasi mazuri yenye kuonesha kwamba nchi inafuata taratibu nzuri za kisheria suala zima la utoaji na utekelezaji wa haki za binadamu wakati haki hiyo haipo na haipatikani badala yake Serikali na vyombo vyake vya dola vinatumia nguvu kupita uwezo kwa kuwakandamiza na kuwanyanyasa raia zake kuwekwa magerezani na kuwapa vifungo kwa makosa ya kuwabambikiza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na watuhumiwa wa makosa ya ugaidi zaidi ya miaka minne sasa Watanzania wenzetu wamo wanateseka na kufanyiwa vitendo vya kinyama na kiudhalilishaji wako mbali na familia zao. Kesi hadi leo inaelezwa ushahidi haujakamilika, naiomba Serikali kwanza itambue hapa duniani tunapita, iache kutesa raia zake, basi kama wanahatia ni vyema wakahukumiwa, wakapewa adhabu kulingana na ukubwa wa makosa yao na kama makosa hayakukidhi wakaachiwa huru wakarudi na kuishi na familia zao ambazo hivi sasa zinateseka sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la katiba mpya, suala hili sasa si suala rahisi tena kutekeleza ni dhahiri Serikali halimo kabisa katika mpango wake wa utekelezaji wake, pamoja na Watanzania kuhitaji sana suala hili. Ni vyema kwa Serikali kuzingatia na kusikiliza maoni na matakwa ya wananchi wake kuepusha nchi yetu kuingia katika kutoelewana kitu ambacho kinaweza kuleta mgawanyiko mkubwa, utakaopelekea Taifa kusambaratika na kugombana wenyewe kwa wenyewe. Naiomba Serikali ikae na ilifikirie jambo hili kwa umakini mkubwa ili thamani ya kazi na michango waliyotoa Watanzania ionekane umuhimu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.