Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Khalifa Mohammed Issa (23 total)

MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majawabu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
(a) Hoja ilikuwa ni kwa namna gani vyombo vya Kiserikali vinaweza kusaidia au kushirikiana na hawa watumiaji wa uraibu huu ili kuweza kuzifikia zile channel za waagizaji, wasambazaji na watumiaji. Je, kuna mlinganisho gani wa wale waliokamatwa pamoja na watumiaji wenyewe ambao wako mitaani? Serikali inaweza kutupa ulinganisho kwa sababu mitaani wako wengi lakini ambao wanakamatwa ni wachache?
(b) Ni kweli kuna baadhi ya watumiaji wako katika maeneo ambayo wanapatiwa huduma za kupata nafuu. Vijana hawa na watu wengine kwa jumla wanatumia dawa hizi na wakati mwingine kwa vishawishi lakini na wakati mwingine kwa kukata tamaa tu za maisha. Sasa mara baada ya kwisha kuwapa dawa hizi au nafuu hii wakitoka mitaani tumewaandalia mambo gani ambayo yanaweza kuwasaidia katika kujenga maisha yao huko mitaani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU - MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI): Mheshimiwa Naibu Spika, narudia tena.
(a) Serikali inatumia vyombo vyake na wakati mwingine nalazimika kupata taarifa kutoka kwa waraibu wa dawa hizi ili kuwakamata wafanyabiashara wakubwa na wadogo wa dawa hizi. Ndiyo maana tumefanikiwa sasa kukamata baadhi ya watu wenye majina makubwa katika biashara hii na ninavyozungumza wako vizuizini na kesi zinaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, limeulizwa swali kuhusu mlishanganisho; kuna mlinganisho gani kati ya wale wanaokamatwa na wale wanaotumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima niseme kweli, hakuna statistics lakini lazima tuweke wazi kwamba biashara hii tofauti na biashara ya nyanya au vitunguu ni biashara inayofanyika kwa kificho sana. Kwa hiyo, kusema kwamba utapata proper statistics itakuwa ni kudanganya watu. Wapo watu maofisini na katika maeneo mbalimbali wanatumia dawa hizo na huwezi ukajua moja kwa moja.
(b) Huduma za kupata nafuu. Kwanza naomba nirekebishe kitu kimoja ambacho kinaweza kikaonekana kama over generalization. Siyo kila mtumia dawa za kulevya anafanya hivyo kutokana na kukata tamaa ya maisha. Mifano ipo ndani na nje ya nchi. Akina Michael Jackson na wengine siyo kama walikuwa wamekata tamaa ya maisha. Vishawishi is fine!
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba juhudi za Serikali zinazochukuliwa za kukuza uchumi na kadhalika zina lengo la kuondoa ugumu wa maisha unaowaingiza vijana katika kutumia dawa za kulevya, kwa sababu sote tunafahamu kwamba vijana ndio nguvu kazi ya Taifa hili na nchi yeyote yenye nia thabiti ya kuendelea, ni lazima ichukue hatua madhubuti ya kuwalinda raia wake kutokana na kutumia dawa za kulevya.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo, niongezee tu kwamba juhudi za kuondoa watu kwenye vishawishi vya kutumia dawa za kulevya, siyo za Serikali peke yake, hili ni tatizo la kila mtu. Kwa hiyo, kila mtu awe ni kiongozi wa kisiasa, kiongozi wa familia na raia wote, wana jukumu la kuhakikisha kwamba wananchi wanaondokana na vishawishi vya kutumia dawa za kulevya mara baada ya kumaliza tiba inayohusika.
MHE KHALIFA MOHAMMED ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na jawabu refu sana la Mheshimiwa Naibu Waziri, bado nina maswali mafupi mawili ya nyongeza. Swali la msingi lilikuwa ni risk, kuweka rehani roho za abiria. Hii haijalishi ukubwa wa ndege, ubebaji wa abiria wachache au wengi. Jawabu ilikuwa rubani kabla ya kurusha ndege, au vipindi kwa vipindi wanafanyiwa check-up.
Mheshimiwa Naibu Waziri, haoni binadamu katika maumbile yake unaweza kumfanyia check up sasa hivi lakini akifika pale hali yake ikawa na mgogoro. Je, haoni kwamba bado suala ni kuweka rehani roho za abiria?
Swali la pili, pamoja na treaties nyingi za Kimataifa na kuridhiwa na Bunge, je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kulisimamia hili na kukawa na ulazima maalum wa ndege yoyote ya abiria kuweza kuongozwa na rubani zaidi ya mmoja?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, risk inapimwa. Katika eneo hili sheria tulizo nazo za kimataifa ambazo nchi yetu imeziingiza katika sheria zetu na Bunge hili limeidhinisha, hiyo risk imepimwa kwa uzito wake na ndiyo maana ni aina fulani tu za ndege zinazobeba abiria kiwango fulani zinazoruhusiwa kuendeshwa na rubani mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kuna marubani maalum wanaoruhusiwa kuendesha ndege usiku na wakati ambapo huwezi ukaona uwanja ulivyo, ni aina fulani tu ya marubani ambao wamepitia kozi maalum zinazozingatia leseni za IFR (Instruments Flights Rules). Ndege zile ambazo zinatumia CFR ambazo ni kwa marubani ambao hawaja-qualify sana hazihitaji masharti hayo na kwa kawaida hawaruhusiwi kuendesha usiku au kwenye kipindi ambacho mawingu ni mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa suala la afya, ambalo ndilo swali lake la msingi Mheshimiwa Mbunge, nadhani ukiweka hata marubani watatu, wanne, Mwenyezi Mungu kama afya hiyo hakubali nadhani siyo solution na ndiyo maana upimaji wa kila mwaka na kwa wale ambao wanarusha ndege za kimataifa za kibiashara upimaji wa kila baada ya miezi sita ni wa lazima. Ndugu zangu niwaambie, na niwaombe Wabunge wote tupime afya zatu. Tukiwa tunapima afya zetu kila wakati risk ya kupata labda pressure au nini ni ndogo sana. Wataalam wetu wanaotupima tuwaamini.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, kwanza mimi na-declare my interest kwamba ni Mjumbe wa Kamati yako ya Kudumu ya Utawala na TAMISEMI. Kwa hivyo,
katika ziara zetu mbalimbali tumepata ushuhuda wa wanufaika wa kaya maskini na kiwango fulani wamenufaika kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na kunufaika kwao bado haijaondoa umuhimu wa kuweza kuongezewa hii ruzuku kwa sababu kama nilivyosema katika swali langu la msingi kila siku maisha yanapanda, shilingi yetu inaporomoka
na bei ya bidhaa inaongezeka. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri anaonaje basi wakaweza kupewa viwango hivi wanavyopewa kwa mkupuo walau wa miezi sita ili ile tija ya kuweza kuendesha biashara zao, kujenga makazi yao ikapatikana?
Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili dogo, mimi
nashukuru katika Jimbo langu pia mradi huu katika baadhi ya shehia unaendelea lakini kuna usumbufu wale walengwa kutoka katika vijiji vingi wanakusanyika katika center moja.
Waziri anaonaje akaongeza vituo vya kulipia ili wale watu ambao wamekusudiwa kupewa ruzuku hii wasipate matatizo hasa ukizingatia wengine ni wanyonge sana, wengine ni watu wazima mno…
Mheshimiwa Spika, ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, nimeeleza katika majibu ya swali langu la msingi. Kwanza kabisa, ukiangalia mradi huu, kabla hatujaanza uhawilishaji mwaka 2013 tulianza mpango wa majaribio mwaka 2008 kwa miaka mitano katika Halmashauri tatu za Chamwino, Bagamoyo pamoja na Kibaha. Katika mpango huo wa majaribio, kaya 26,000 zilishiriki katika mpango huu.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia mwanzoni wakati
programu inaanza, wakati huo wa majaribio, kiwango cha juu kabisa kilikuwa ni Sh.17,500/=. Hata hivyo, tulipoanza mpango tulipandisha mpaka Sh.34,000/= na ilikuwa haiangalii watoto walioko katika kaya, haingalii watoto wanaopata huduma za kiafya na zinginezo. Nipende tu kumwambia Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeongeza, kwa sasa hivi kiwango cha juu kabisa ni Sh.76,000/= vilevile wanapata fursa pia ya kupata ujira, kwa siku 60 kila mwaka wanapata takribani Sh.138,000 kwa Sh.2,300 kwa siku.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda kusema
kwamba katika majaribio ilionekana ukiwapa kiwango kikubwa sana inawezekana wakabweteka na wasiweze kufanya shughuli zingine za ujasiriamali na wakajitegemea tu kupitia ruzuku hii. Kwa hiyo, ilionekana kwa kweli kiwango hiki kinafaa na tumefanya majaribio na wako wengi ambao wameweza kunufaika na kupata maendeleo katika maishayao.

Mheshimiwa Spika, katika swali lingine kwamba
wapewe sasa kwa mkupuo wa miezi sita, hoja yake Mheshimiwa tunaiona, napenda tu kusema kwamba tunaendelea kuifanyia kazi ili kuona kama inawezekana miezi sita au miezi mitatu na nini kinaweza kikafanyika. Kwa sasa nisiseme kama tumekubali, lakini niseme tunaona hoja ni ya msingi tuichukue twende tukaifanyie kazi.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja ya kuongeza vituo vya kulipia fedha na yenyewe pia niseme tunaichukua ili kuona ni kwa namna gani tunaweza tukawarahisishia na kuwasogezea huduma karibu zaidi walengwa wetu.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ushirikiano mzuri wa ndugu zetu hawa wa Cuba katika mambo ya tiba Tanzania, kwa kule Zanzibar ndugu zetu hawa walikuwa na programu maalum ya kuwafunza vijana wetu Udaktari na kwa kweli tayari sasa hivi intake mbili zimeshatoka, moja madaktari wanaendelea na kazi zao na wengine wako katika internship sasa hivi. Kwa kweli inaonekana kwamba wana mafanikio makubwa.
Je, kwa hapa Tanzania Bara programu hii imeanzishwa au imeshafikiriwa kuanzishwa kwa kuwatumia hawa ndugu zetu wa Cuba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza Cuba ni marafiki wa kihistoria wa Tanzania. Comradeship iliyotengenezwa na Fidel Castro na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ni ya muda mrefu na imezaa matunda mengi katika nchi zote mbili, zaidi sisi tukiwa wafaidika kuliko wenzetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ushirikiano huo, Watanzania wengi, hususan kwenye fani hii ya afya wamepelekwa Cuba kwa ajili ya masomo na wamesoma masomo ya ubingwa lakini pia katika nyakati mbalimbali hata wanajeshi wetu ambao wanahusika na mambo ya tiba na uokoaji pia wamepelekwa Cuba kwa ajili ya kusoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1986 ikaonekana kwamba isitoshe tu kuwa na exchange ya Watanzania kwenda kufundishwa kule Cuba mambo ya afya, ikaonekana kwamba tusaini mkataba mwingine ili waje hapa hapa watujengee uwezo. Kwa hivyo, harakati za kujenga uwezo zimekuwa zikifanyika kila mahali ambako madaktari wa Cuba wamekuwepo, pia wamekuwa wakifundisha katika vyuo vyetu hapa nchini, hivyo hata kwa Tanzania Bara tunao.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyozungumza hapa, tuna Madaktari Bingwa kumi na moja wanaotokea Cuba ambao wapo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma. (Makofi)
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini msingi wa swali langu katika introduction nilikuwa nazungumzia wajasiriamali kuwa hawapati fursa hii ya kukopeshwa au kuweza kujua fursa kwa sababu hawana utaalamu na uzoefu wa kuandika andiko la miradi.
Sasa nataka kufahamu ni lini hasa Serikali itatoa maelekezo na utaalamu wa kuweza kuwafanya wale wenye nia na hamu ya kupata fursa hii kuweza kuitumia vilivyo na kwa kupata taaluma?
Pili, ni kweli kwamba kuna vikundi vingi tu ambavyo vinasaidia ama kwa kujichanganya katika SACCOS hizi au VICOBA, lakini kuna wajasiriamali mmoja mmoja ambao wangependa kutumia fursa hii ya kupata michanganuo na kuweza kupata fursa ya kukopa, lakini pia hawajawezeshwa, wala ile fursa ambayo ipo kiuchumi hawajaweza kuitumia vizuri, kwa sababu ile taaluma bado haijawafikia. Kwa hiyo, ni lini Serikali italeta taaluma hii ili watu wenye hamu na ari ya kuweza kutaka kujikwamua kiuchumi katika maisha yao, waweze kuipata fursa hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la kwanza kwamba Serikali itatoa lini maelekezo ili wajasiriamali wengi waweze kupata elimu hii na wafahamu fursa zilizopo. Kwa taarifa tu ambayo napenda kumpatia Mheshimiwa Mbunge hapa ni kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu ndani yake lipo Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambao kazi yao kubwa kabisa ni kutoa elimu lakini vile vile kuwaandaa Watanzania kushiriki katika uchumi wa nchi yao kwa kuwatangazia fursa mbalimbali zilizopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanzia, tayari tuna ma-desk katika kila Halmashauri kwa nchi nzima ambapo kuna Kamati ya Uwezeshaji ambapo wao sasa wanasaidia katika kuwapa wananchi elimu, lakini vilevile wananchi wanapata fursa ya kufahamu fursa zilizopo za kiuchumi. Kwa hiyo, kupitia hiyo, ni rahisi wananchi wengi zaidi kuweza kupata elimu na kunufaika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuongezea tu, bado tumeendelea kufanya semina, makongamano na warsha mbalimbali za kuwafanya wananchi wetu wa Tanzania waelewe fursa zilizopo na watumie rasilimali zilizopo kwa ajili ya uchumi wa nchi yetu na tumefanya katika mikoa mingi na tumepata mafanikio makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili la nyongeza, ameuliza kuhusu namna ambavyo Serikali inaweza ikawawezesha mjasiriamali mmoja mmoja naye akapata fursa ya kushiriki katika uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda nitoe taarifa katika Bunge lako Tukufu na ninyi Waheshimiwa Wabunge mnisikilize ili mwende mkawasaidie wananchi wenu, katika nchi yetu ya Tanzania tunayo mifuko 19 ya uwezeshaji ambayo inatoa ruzuku na mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mifuko hii ina ukwasi wa kiasi cha shilingi trilioni 1.3 ambayo ni fursa ya kipekee kwa sisi Waheshimiwa Wabunge kwenda kuwaelimisha wananchi wetu kuzitumia fursa hizi badala ya kutegemea Mifuko ya Maendeleo ya Vijana au Mifuko ya Maendeleo ya Akina Mama na mifuko mingine, lakini bado ziko fursa nyingi sana. Kuna watu wanaitwa TFF (Tanzania Forest Fund) ambao wenyewe wanatoa ruzuku kuanzia shilingi milioni tano mpaka shilingi milioni 50 katika vikundi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge wengine wote, naomba tuichukue hii kama fursa ya kwenda kuwaelimisha wananchi wetu watumie fursa hii kujinufaisha. (Makofi)
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru lakini pia nishukuru kwa majibu ya kitaalam ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Hata hivyo pamoja na majibu hayo nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na sababu za kimaumbile pamoja na mabo mengine kama alivyotaja katika jawabu lake la msingi Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba bado kuna mila potofu za ukeketaji wa wasichana kwa kutumia zana za kienyeji, zana moja kwa watu wengi. Lakini pia kuna mila potofu ya kurithi wajane, kuna mila ambazo mjane anarithiwa baada ya mume kufa bila ya kupima au kujulikana amekufa kwa sababu zipi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, bado Virusi vya UKIMWI au UKIMWI katika nchi yetu ni tatizo na maambuzi kila siku yanazidi kuliko kupungua, na ziko njia nyingi ambazo zinasababisha maambukizi kama vile ngono na Serikali inajua kuna vishawishi vingi na kuna biashara ya ngono hasa katika maeneo ya mjini.
Je, Serikali ina mpango gani hasa hasa maalum ambao watautumia katika kuzuia biashara hizi za madangulo, biashara hizi zinafanyika na hatuwezi kuwalaumu…
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana naye kwamba kumekuwa na mila potofu za ukeketaji na kurithi wajane ambazo kwa njia moja au nyingine nazo zinachangia kwa kiasi katika maambukizi dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI. Serikali tunaendelea kuchukua jitihada za kuelimisha jamii kuhusiana na madhara haya ya masuala ya ukeketaji na ya kurithi wajane. Moja ya shughuli ambayo na mimi nitaifanya baada ya Bunge hili kukamilika ni kwenda katika Wilaya ya Kilindi katika Mkoa wa Tanga kwenda kushiriki pamoja na jamii wale wakeketaji ambao walikuwa wanafanya shughuli hizi za kuiacha shughuli hiyo na sasa kuanza sasa kuhakikisha kwamba taratibu za kawaida zinaweza kutumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Serikali inaendelea kuchukua juhudi ya kutoa elimu lakini vilevile kuamasisha jamii kuachana na mila potofu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili lilikuwa ni kuhusiana na suala la biashara ya ngono. Serikali inaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kwamba tunatoa elimu kwenye jamii kuhusiana na biashara hii ya ngono na kuchukua taratibu za kisheria pale tunapobaini kwamba kuna madangulo katika maeneo husika.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake. Lakini, hata hivyo ningependa kujua kuna mfano gani kwa waganga hao wa ramli chonganishi na manabii wa uongo hatua ambazo wamechukuliwa baada ya kupatikana na kadhia hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, je, Serikali haioni sasa wakati umefika wa wale manabii ambao wanadai wanao uwezo wa kuwafufua waliokufa ili kukaa nao kwa karibu ili kuweza kuwafufua wapendwa wetu. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza je ni mfano gani wowote ambao uliowahi kuchukuliwa hatua wa hawa waganga matapeli na Manabii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mheshimiwa Khalifa atarejea kwenye jibu langu la msingi ni kwamba mpaka kufika kipindi cha mwaka 2020 jumla ya kesi 57 za waganga chonganishi na wengine tayari zimesharipotiwa kwasababu ili kesi iwe kesi kwanza iwe reported. Kwa hiyo, kikubwa nimwambie kwamba zipo kesi ambazo zimeshafika kwenye ofisi yetu au zimeshafika Mahakamani, tayari zimo katika mchakato wa kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine nimwambie kwamba hili jambo ni jambo amablo linahitaji utulivu wa kukaa tukafanya utafiti na takwimu za kutosha ili tukilileta hapa tuliseme kwa mujibu wa uhalisia lilivyo. Kikubwa ni kwamba zipo kesi ambazo zimeshakuwa reported. Kuna kesi ilijitokeza Mkoa wa Njombe, yupo kijana aliambiwa na babu yake ili uwe Tajiri na huo utajiri tupate mimi na wewe basi lazima uwe unawaua watoto mpaka wafike idadi fulani. Mwisho wa siku ile kesi ikaripotiwa na tukamshtaki huyo mtu kwa kosa la mauaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kesi imejitokeza Misungwi huko ya mtu mmoja aliambiwa na mganga hivyo hivyo tapeli ili mimi na wewe tuwe matajiri hakikisha unawaua wanawake halafu unatembea nao. Lengo na madhumuni tuwe matajiri. Hii kesi imeletwa na tumeichukulia hatua kwa hivyo. Kikubwa niseme kwamba hizi kesi zipo kwa zile ambazo zimeripotiwa na hatua za kisheria kwa mujibu wa taratibu zinachukuliwa na majibu yatapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali jingine lilikuwa linauliza je, hakuna haja ya kukaa sasa na hawa wafufuaji ili tuweze kuwafufua wapendwa wetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, imani ya kibinadamu inaamini na ndivyo ilivyo kwamba mwenye uwezo wa kuondosha na kurejesha, yaani kufanya mtu akaondoka, akafa ni Mwenyezi Mungu peke yake. Ndiyo maana ilifika wakati tukawa tunasema kwamba kama kutakuwa kuna watu wa namna hii kama alivyoshauri Mheshimiwa Mbunge, tuko tayari kukaa nao tuwaeleweshe, tuwafahamishe ili wafike wakati wasije wakazua migogoro katika jamii. Kwasababu anaweza akatokezea mtu akasema mimi nina uwezo wa kufufua, akachukua pesa za watu. Mwisho mtu akazikwa akafa akasahauliwa. Mwisho wa siku migogoro katika jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa nimwambie tuko tayari kukaa na hao watu ili tujue namna ya kuwaelimisha kuwaeleza kwamba mwenye uwezo wa kufufua na kuondosha mtu kwa maana ya kufa ni Mwenyezi Mungu Subhana Wataalah. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuondoa tozo ile lakini pia mpango ambao Wizara ya Elimu inaupanga kuondoa tozo ya asilimia 10 kwa wanufaika baada ya grace period. Hata hivyo nina maswali mawili madogo ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali inakata asilimia 15 ya gross salary ya mnufaika baada ya kuajiriwa, je, haioni asilimia 15 ni kubwa haiwezi kuipunguza mpaka kufikia angalau single digit; asilimia 5, 6 mpaka 9? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa kuwa mfuko huu unanufaisha wale degree holders haioni sasa wakati umefika kushuka chini katika vyuo vya kati kama vile VETA, FDCs na kadhalika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba sasa kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Khalifa, Mbunge wa Mtambwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli wanufaika hawa huwa wanakatwa asilimia 15 kutoka kwenye mshahara wao ghafi kwa ajili ya kurejesha mikopo hii. Lengo la kukata asilimia 15 ni ili kuweza kurejesha fedha zile kwa haraka na kwa muda mfupi. Hata hivyo, tupokee mapendekezo ya Mheshimiwa Mbunge ya kuangalia namna gani tunaweza kupunguza eneo hilo. Kwa vile tarehe 4 na 5 ya mwezi huu tuliwasilisha bajeti yetu hapa na miongoni mwa mijadala iliyotokea ni kuhusiana na hii Bodi ya Mikopo na kwa vile tutakuwa na mjadala mpana wa kitaifa, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge tunakwenda kulijadili na hili tuweze kuangalia namna gani tunaweza tukalizingatia.

Mheshimiwa Spika, swali la pili anauliza mikopo hii imewalenga sana wale wanaochukua elimu ya juu kwa maana ya degree, ni namna gani tunaweza tukafikia zile kada za vyuo vya kati. Kwa vile tutakuwa na mjadala mpana wa kitaifa juu ya mwelekeo ya elimu katika Taifa letu basi na hili nalo tutakwenda kulijadili kwa kina na ninyi Waheshimiwa Wabunge mtakuwa ni sehemu ya mjadala huo, tunaamini tutapata mawazo endelevu kuona ni namna gani tunaweza nalo hili tukaliingiza kwenye mpango.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana; kama ilivyo vituo vingi vya polisi vilivyochakaa, Kituo cha Matangatuwani kilichoko katika Jimbo la Konde Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba kimechakaa na kwa kweli ni kibovu, ikinyesha mvua ni bora ukae chini ya mwembe utapata stara kuliko Kituo cha Matangatuwani.

Je, ni lini Serikali itakifanyia ukarabati mkubwa kituo hiki cha Matangotuwani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Khalifa Mohamed kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii nimpongeze sana Mheshimiwa Khalifa amekuwa ni mdau wetu muhimu wa kutusaidia kwanza kutuonesha maeneo ambayo tunatakiwa sisi kama Serikali tuyafanyie marekebisho, lakini pia amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba anatoa hata kilicho mfukoni kwake au katika Mfuko wa Jimbo kuhakikisha kwamba anawasaidia wananchi katika kupata huduma za ulinzi na usalama, hili nimpongeze sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kikubwa nimwambie kwamba nirejee tena kwamba bado tunatambua kwamba kuna baadhi ya changamoto ambayo sisi ni sehemu ya wajibu wetu kuhakikisha kwamba tunazitatua ili kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata huduma nzuri za kiulinzi na usalama. Kituo ambacho anakizungumza ni kweli kipo na mimi binafsi nimefika na hali nimeiona, lakini kikubwa nimwambie hata kama akinifaa kwenye bajeti ambayo tumeiwasilisha tumeisoma hivi karibuni tumezungumzia namna ambavyo tunaenda kurekebisha vituo vya polisi na nyumba na baadhi ya huduma nyingine ili sasa wananchi waweze kupata huduma bora za kiulinzi na usalama. Nimwambie tu kwamba na yeye ni miongoni mwa vituo ambavyo tutajitahidi turekebishe ili tuone namna ambavyo na wao wanapata huduma nzuri. Nakushukuru.
MHE. KHLAIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza namshukuru Waziri kwa majibu yake ya kina, lakini hata hivyo nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali langu lilihusu hasa usalama wa raia wanaporushwa katika ndege. Usalama wao huu siyo kwa sababu ya uchache na udogo wa ndege. Ndege nyingi takribani ndogo ndogo hizi ambazo tunaruka nazo ni chini ya kilogramu 4,000, lakini bado ni abiria: Je, Serikali itabadilisha sheria hata kuwa ndege ni ya watu watatu, kilogram 3,000 kuleta marubani wawili?

Mheshimiwa Spika, la pili, kuhusu marubani kufanyiwa uhakiki wa afya zao miezi sita au 12; mgogoro wa afya unaweza kutokea wakati wowote akiwa ndani ya anga. Sasa unaonaje, unanusuru vipi abiria wale ambao rubani wao amepata changamoto ya afya akiwa angani peke yake? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA
M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Khalifa, Mbunge wa Mtambwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza Mheshimiwa Mbunge anataka kujua, ni kwa nini ndege ambazo zinabeba watu chini ya kilo 3,000 haziwezi kutumia marubani wawili?

Kwanza, ndege inapokuwa inatengenezwa, yule mtengenezaji anatoa maelekezo marubani wangapi wanapaswa kuitumia hiyo ndege.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, ni kweli kwamba kutumia marubani wawili kwenye ndege moja ndogo pia ni gharama, maana yake huyo rubani inabidi alipwe. Ila sisi kisheria tumeruhusu kwamba unaweza ukatumia marubani wawili, lakini waendeshaji wadogo kwenye ndege zao hawazuiliwi kisheria kutumia marubani wawili.

Mheshimiwa Spika, la tatu, wanaangalia pia ile ndege aina ya mitambo na vipuri vinavyotumika. Ndege hizi ndogo zinabeba chini ya abiria 19 na haziendi umbali mrefu zaidi na hazitembei kwa saa nyingi na haziendi juu ya anga kwa maana ya kupata mikikimikiki ile ya mawimbi makubwa. Hata hivyo ikitokea kuna viashiria vya hali ambayo siyo nzuri kwa afya, kwa kuchukua tahadhani wanaweza kuongeza rubani wa pili katika ndege hiyo.

Mheshimiwa Spika, la pili ni uhakiki wa afya za marubani kwamba wale ambao wana miaka chini ya 40 ni mizei sita, lakini wale zaidi ya miaka 40 ni miezi 12. Hii ni ukweli kwamba kisayansi kwa mazoea ni kwamba hawa wenye chini ya miaka 40 ni vijana, tunaamini kwamba wana afya na nguvu ya kuweza kufanya kazi zaidi. Ila ikitokea kwamba kuna viashiria vya hali ya usalama kiafya wanaweza kufanyiwa utaratibu wa kupimwa afya zao hata chini ya miezi mitatu. Ni jambo ambalo linawezekana.

Mheshimiwa Spika, tunafanya mambo yote haya kwa kuzingatia Sheria ya Anga ya Kimataifa.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri ambaye anahusika na Mazingira katika Kikao cha Bunge kilichopita alitoa ahadi ya kuja kutembelea Kisiwa cha Pemba ili kuona athari ya mabadiliko ya tabianchi hasa katika Kisiwa cha Mtambwe Mkuu, Kojani na Kisiwa Panza.

Je, ni lini hasa atakuja kuona athari hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Khalifa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya Bunge hili tukijaaliwa tutajitahidi tupange ziara kwa ajili ya kwenda Kojani na maeneo mengine ya Mtambwe Mkuu kwenda kukagua maeneo hayo. (Makofi)
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami nimwulize swali moja dogo la nyongeza Mheshimiwa Naibu Waziri. Kituo cha Wete ndiyo Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba. Kituo kimechakaa, hakina hadhi: Ni lini Serikali itakikarabati kituo kile? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mbunge wa Wete, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nafahamu na Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba vituo vingi vilivyojengwa siku nyingi vimechakaa sana. Kama atafuatilia, tumeanza kukarabati vituo vya Polisi vikianzia Makao Makuu pale Zanzibar na makazi yao. Tutaendelea kufanya hivyo maeneo ya Pemba kutegemea upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, tumeshakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba awamu ijayo nitatembelea Pemba na eneo la Wete ni eneo nitakalolipa kipaumbele katika ziara yangu. Nashukuru.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza naomba kabla sijauliza maswali yangu mawili ya nyongeza, niruhusu nitoe shukrani zangu za dhati sana kwa ofisi ya Rais kupitia TASAF kwa mradi mkubwa ambao wamenipelekea katika shule yangu ya Peak, kukarabati na ujenzi wa uzio shule ambayo Baba wa Mheshimiwa wetu Mzee Suluhu Hassan alifundisha, hivyo wamepeleka fedha nyingi pale nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza niliuliza Wabunge wanashirikishwaje? Nashukuru kwa majibu. Je, Serikali haioni sasa ni wakati baada ya miradi ile ambayo imeibuliwa na wananchi Wabunge nao wakapata taarifa ili kuwa karibu na ile miradi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa mradi mkubwa huu uliopelekwa katika skuli ya Peak Jimbo langu la Mtambwe kukarabati madarasa na uzio kuna baadhi ya maeneo bado hayajakamilika. Je, Serikali haioni ni wakati mzuri sasa hivi wa kuweza kupeleka fedha pale ili kukamilisha baadhi ya maeneo ambayo hayajakamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Khalifa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu Je, sasa Serikali haioni umuhimu wa kuwapa taarifa Waheshimiwa Wabunge, naomba nitumie nafasi hii mbele ya Bunge lako hili kuelekeza ma-TMO wote ambao ni wasimamizi wa miradi hii ya TASAF katika Wilaya husika kuwa wanawapa taarifa Waheshimiwa Wabunge kwa miradi yote ambayo wananchi wameibua kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa tunafahamu Wabunge ndio wawakilishi wa wale wananchi wa yale maeneo husika hivyo ni muhimu sana kuweza kuwapa taarifa, nimtoe mashaka Mheshimiwa Mbunge, kwamba miradi mingine itakayoanza kuibuliwa ndani ya Majimbo husika basi Wabunge wataanza kupewa taarifa ile.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, kuhusu mradi wa Peak, bahati nzuri nimefika mpaka pale, hatua ya kwanza iliyoanza kwenye shule ile ilikuwa ni kujenga madarasa ambayo yalikuwa yamechakaa sana. Baada ya kumaliza ujenzi ule wa madarasa yale, wananchi wale wa eneo lile pia waliibua mradi mwingine ambao ni hitaji lao lilikuwa ni uzio katika shule ile. Kwa sababu ilikuwa ni njia ya wakazi wa pale kukatiza katikati ya skuli ile katika eneo la Peak. Baada ya kutambua hilo fedha ikatolewa na mradi wa TASAF baada ya kuibuliwa mradi na baada ya hapo ni uzio ule umejengwa.

Mheshimiwa Spika, kama kuna hitaji jingine wananchi wanaweza wakaibua na TASAF watafanyia kazi. (Makofi)
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba nimuulize swali la nyongeza Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, Zanzibar kuna polisi jamii, na polisi jamii hawa wanapelekwa kila Shehia katika Shehia za Zanzibar na shida yao kubwa ni mafuta.

Je, Serikali inatuambiaje kuwapatia walau mafuta, japo hawakupatiwa pikipiki lakini au maufta yakuwafikisha katika vituo vyao vya kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Khalifa Mohamed Issa, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli sio Zanzibar tu maeneo mbalimbali nchini Tanzania tunao utaratibu wa kuwa na polisi jamii kwa ajili ya kusaidia ulinzi shirikishi pale ambapo polisi wetu wanakuwa mbali na kwa sababu kama inavyoitwa polisi jamii uendeshaji wake kwa muda imekuwa ukichangiwa na wan jamii wenyewe. Sasa suala hili la kuzingatia kwenye upande wa mafuta ni suala kibajeti, tutalitafakari pale hali ya fedha na bajeti itakavyoruhusu tutaanza kuona uwezekano wa kuwafikiria mafuta na vyombo vya usafiri kama alivyotaja pikipiki. Nashukuru.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kwa niaba ya Mheshimiwa Mohamed Said Issa.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; je, utekelezaji wa makubaliano hayo umefikiwa kwa kiasi gani?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; je, Serikali ipo tayari leo kutoa tamko kuwa bidhaa zilizotambuliwa na moja katika mashirika mawili hayo hutumika nchi nzima bila ya utambuzi wa Shirika lingine lolote nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Khalifa Issa Mohamed, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa makubaliano haya umeshaanza na unaendelea kama nilivyosema kwenye maeneo yale yote matano kwa maana viwango vile tunavyokubaliana vinatekelezwa, lakini pia na bidhaa zote zinatambuliwa katika pande zote mbili.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali la pili, ndio hii moja ya vitu ambavyo tumesisitiza katika sehemu ya tano, kwamba lazima bidhaa zote ambazo zimethibitishwa na ZBS au na TBS kwa upande wa Bara zinatambuliwa katika pande zote mbili.

Mheshimiwa Spika, hii si kwa Tanzania tu ni kwa Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki kwamba hata ukienda kwenye bidhaa ambazo zimetoka kwenye nchi hizi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo taasisi zao za udhibiti wa viwango zimethibitishwa, zikija huku kwetu zinatambuliwa. Kwa hiyo, si kwetu tu kwa maana ya Zanzibar na Tanzania Bara, lakini pia hata Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nakushukuru sana.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jawabu zuri la Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; Magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza kwa kweli yanaongezeka kila uchao. Kwa mfano, kuanzia mwaka 2016 kulikuwa na wagonjwa takribani milioni nne na kumi na nane elfu, lakini kufika mwaka 2020 kumekuwa na wagonjwa wasiopungua milioni nne na laki nane. Magonjwa haya yanagharimu Serikali kupitia Wizara ya Afya takribani asilimia 20 ya bajeti yake na vifo takribani asilimia 33 ya vifo vyote. Je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba, wakati sasa umefika magonjwa haya kuyaundia Tume Maalum ambayo itayashughulikia kama vile TACAIDS?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; miongoni mwa magonjwa haya yasiyoambukiza ni saratani ambayo nayo inaua watu wengi sana na pia inagharimu pesa nyingi sana kwa kuagiza dawa kutoka nje. Je, Waziri haoni wakati sasa umefika wa kuwa na kiwanda ambacho kitazalisha mionzi tiba?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumjibu swali lake la kwanza Mheshimiwa Mbunge anashauri kwamba tuanzishe tume kama ya TACAIDS kwa sababu magonjwa haya yanaonesha kila mwaka yanaongezeka na yanakuwa ni tatizo kubwa kwenye nchi yetu. Tutalifanyia upembuzi yakinifu wazo lake, lakini kikubwa ni kwamba ni sisi kuongeza nguvu zaidi kwenye kuelimishana hasa haya magonjwa yasiyoambukiza, namna life style na mambo mengine ili kupunguza idadi ya watu ambao wanapata matatizo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuongeza bajeti na kubwa zaidi kwenye eneo hili ili elimu iwafikie watu wengi lakini watu wengi zaidi wapate huduma bila bughudha yoyote. Maana yake ukianzisha taasisi wakati mwingine tunarudi kule kule, fedha nyingi zinaishia kwenye masuala ya utawala badala ya kumfikia mgonjwa husika. Kwa hiyo nafikiri ni kuongeza nguvu katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ambalo kimsingi linaonyesha ni namna gani Serikali ilivyo serious kwenye eneo hili, ni suala alilosema kwamba kiwanda cha kutengeneza mionzi dawa. Kiwanda cha kutengeneza mionzi dawa kama tulivyosema hapa kwa Afrika ni nchi nne tu zilikuwa na uwezo na kiwanda hicho na sasa Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan ndani ya mwaka mmoja amewezesha na tayari hicho kiwanda kipo na mwezi wa sita kinaenda kuanza kazi rasmi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi na ukiangalia maana yake ni nini? Sisi kwa Afrika sasa Rais wetu ametufikisha mahali, katika nchi tano ambazo zina kiwanda cha kuzalisha mionzi dawa na sisi tuko. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge nafikiri eneo hilo linaenda vizuri na hatuna haja ya kutengeneza taasisi. Unajua watu wetu kwenye masuala ya utawala fedha nyingi badala ya kwenda kwa mgonjwa zinaweza zikaishia kwenye masuala ya utawala.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na mikakati ya Serikali ambayo imeianisha lakini bado kuna changamoto ya ufaulu hasa katika masomo ya sayansi na hisabati. Ni nini mkakati wa Serikali kupandisha ufaulu huo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, najua kuna mchakato unaendelea wa kuiangalia mitaala. Je, ni lini hiyo mitaala mipya itatumika katika sehemu zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Khalifa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza, anataka kufahamu juu ya mkakati wa Serikali hasa hasa katika masomo ya hisabati na sayansi. Nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, Serikali tumejipanga vizuri kwa kufanya mambo yafuatayo: -

(i) Kuweka kipaumbele hasa hasa kwenye ajira za walimu wa masomo haya ya sayansi pamoja na hisabati;

(ii) Kuhakikisha kwamba tunakwenda kujenga maabara katika shule zetu ambazo zinazotoa masomo haya ya sayansi;

(iii) Kuhakikisha kwamba tunapeleka vifaa vya kujifunzia na kufundishia kwa ajili ya ufundishaji wa masomo haya; na

(iv) Kuendelea kuhakikisha walimu wale wa masomo ya sayansi basi tunawapeleka kwenye mafunzo ili kuhakikisha kuwajengea uwezo wa kuweza kufundisha masomo haya kwa umahiri, kwa umahiri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili anataka kufahamu utaratibu wa mitaala. Ni kweli tumezungumza hapa kwamba tunaendelea na uratibu pamoja na maboresho ya mtaala wa mwaka 2014.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako Tukufu, mitaala yetu pamoja na sera tayari tuna rasimu ya nyaraka hizo na hivi sasa taratibu zinazoendelea ni kuendelea kupata maoni ya wadau ikiwemo na ninyi Waheshimiwa Wabunge. Tutaleta rasimu hiyo katika Bunge lako Tukufu ili kuweza kupata ridhaa na baadaye kwenda kwenda kwenye mamlaka zinazohusika na ithibati au kupitisha mitaala hii pamoja na sera ili iweze kuanza kutumika. Kwa hiyo, mara baada ya mchakato huu kukamilika, mitaala hii itaanza kutumika rasmi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kuna msemo wa kisheria unasema, kwa tafsri yangu mimi, haki inayocheleweshwa ni haki inayonyimwa. Kwa kuwa mfuko wa pamoja wa fedha ni takwa la kisheria na ni muda mrefu sasa jambo hili linapigiwa makelele haujaundwa;

a) Je, ni nini commitment ya Serikali juu ya kuundwa kwa mfuko huu?

b) Je, ni lini Zanzibar itapata mgao wake wa hisa wa iliyokuwa East African Currency Board na faida katika Benki Kuu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO
NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu masuala mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Khalifa Mohamed Issa Mbunge wa Jimbo la Mtambwe. Kwanza nataka nichukue fursa hii nimpongeze sana Mheshimiwa Khalifa amekuwa ni mfatiliaji mzuri wa masuala haya ya Muungano ambayo yanagusa mustakabali wa nchi zetu zote mbili. Mheshimiwa Khalifa hongera sana kwa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba moja miongoni mwa mambo ambayo hayajapatiwa ufumbuzi kama sehemu ya changamoto ni hili jambo la uundwaji wa hii kamati au Tume hii ya Pamoja ya Fedha. Tume hii ilikuwepo bahati nzuri imekwisha muda wake. Hata hivyo, sisi tayari tumeshapeleka mapendekezo kwa ajili ya kuteuliwa kwa tume hii. Nimwombe tu Mheshimiwa Khalifa awe na subra ili sasa tuzipe mamlaka zinazohusika zifanye uteuzi wa tume hii ili lengo na madhumuni sasa mambo haya ya muungano yaweze kwenda vizuri kama ambavo yanatakiwa kwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu swali la msingi kwa upande wa swali la pili; ni kwamba changamoto hizi zilikuwa ziko nyingi, lakini kupitia Serikali hii ya Mama Samia Suluhu Hassan tumefanya juhudi kubwa kupitia kamati zilizoundwa za pande zote mbili. Kwa hiyo nimwambie tu kwamba huu mgawanyo ambao ameuzungumza unakwenda kupatiwa ufumbuzi na tutahakikisha kwamba tunafanya moja miongoni mwa jambo muhimu la utatuzi wa hii changamoto kwenye changamoto ama miongoni mwa haya mambo ya muungano.
MHE. KHALIFA MOHAMMED ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa changamoto ambazo bado hazijatatuliwa ni upelekaji wa sukari ya Zanzibar katika soko la Tanzania Bara. Ni lini kero hii ambayo ni ya muda mrefu itatatuliwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba moja ya miongoni mwa mambo ambayo Kamati zimo mbioni kuhakikisha kwamba tunaliweka sawa ili kuondosha hii kama ni sehemu ya changamoto ya Muungano ni hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili ni jambo ambalo kama tulivyosema hapo awali kwamba jambo hili la utatuzi wa changamoto za Muungano limetengenezewa kamati maalumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe waheshimiwa Wabunge, ikiwa tumeweza kutoka tangu changamoto ya kwanza leo tumezipata changamoto 22 maana yake na hili kupitia Kamati zinazohusika kwa mujibu wa taratibu zote linakwenda kutatuliwa ili kupunguza changamoto kubwa ambayo inakabili Muungano wetu.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kuna wanajeshi wengi wastaafu waliopigana tokea baada ya uhuru, wamestaafu na mpaka leo wako hai, lakini pensheni zao za mwezi ni ndogo sana: Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwarekebishia ili waweze kukidhi maisha yao? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni kweli wapo watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na wanajeshi wastaafu ambao wamekuwa wakilalamikia pensheni zao kuwa ndogo. Hili ni suala ambalo linafanyiwa kazi kwa pamoja na sekta nyingine zinazohusika na masuala ya pensheni. Kwa hiyo, tutaendelea kuliangalia na kuona ni jinsi gani linaweza kufanyiwa kazi kwa kuzingatia umuhimu wa kazi ambayo wanajeshi hao walifanya na pia kwa kuzingatia uhalisia wa bajeti ya Serikali yetu, ahsante.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwani ni zao ambalo likisanifiwa linaweza likatoa bidhaa nyingi ambazo zinatoa faida kwa wakulima: Je, ni lini Serikali itawapelekea viwanda vidogo vidogo katika yale maeneo ambayo yanazalisha mwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Moja ya mpango wa Serikali ni pamoja na kuwawezesha wakulima wa mwani na ndiyo maana ukifuatilia katika Hotuba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambayo aliitoa hapa Bungeni, moja ya mikakati tuliyonayo ni pamoja na kuwanunulia vifaa vya kisasa na kuongeza tija katika zao la mwani ikiwemo kuwapatia viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya kuzalisha kama sabuni, mafuta yanayotokana na mwani. Kwa hiyo, hayo ni sehemu ya mpango ambao Wizara ya Mifugo na Uvuvi tunayo. Ahsante sana. (Makofi)

MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kisiwa cha Mtambwe Mkuu kilichopo katika Jimbo la Mtambwe, Pemba ni kisiwa ambacho kimeathirika sana na tabianchi, maji ya bahari yanaathiri sana makazi ya wananchi wasiopungua 500. Je, ni lini mradi huu wa climate change utawafikia watu wa Mtambwe Mkuu ili kunusuru kaya zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mohamed Issa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumeona hizo athari za kimazingira ambazo zimetokezea katika Kisiwa hicho cha Mtambwe Mkuu, lakini nimwambie kwamba aendelee kuwa na Subira, tupo kwenye michakato kuhakikisha kwamba maeneo yote ya visiwa ambayo yameathirika kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu, tunaendelea kutengeneza mazingira ili angalau visiwa hivyo viweze kuwa salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nataka nitoe wito, visiwa hivi vinakuwa vinapata athari za kimazingira kutokana na shughuli za kibinadamu, watu wanakata miti hasa mikoko, watu wanafanya shughuli za ujenzi lakini na mambo mengine. Kwa hiyo pamoja na kwamba Serikali tunaenda kufanya juhudi ya kukiokoa na kukinusuru kisiwa hiki lakini kwa ushirikiano wa Wabunge na viongozi wengine wa Serikali, tuendelee kuwaelimisha wananchi wetu ili sasa waone namna na umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwenye maeneo haya hasa maeneo ya visiwa.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naomba niulize swali moja. Mtambwe Mkuu ni kisiwa cha historia ambacho kwa kiwango kikubwa kimevamiwa na maji ya chumvi kiasi ambacho wananchi wanahama. Je, na hichi hakijapata kipaumbele cha kuonekana ipo haja ya kushughulikiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, moja miongoni mwa kazi kubwa ambayo tumeamua sasa tuanze kuifanya ni kuhakikisha kwamba tunarejesha mazingira yaliyoharibika kutokana na maji ya chumvi kwenye maeneo ya visiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya miongoni mwa maeneo ambayo tumeshataka kuyapa kipaumbele ni eneo la hichi Kisiwa cha Mtambwe Mkuu. Kubwa tu nataka nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba na yeye aendelee kutusaidia kusema na wananchi. Shughuli hizo zinazoendelea za kibinadamu zisiendelee kuliathiri visiwa vyetu, shughuli za utalii, shughuli za uvuvi, shughuli nyingine za ulimaji wa mwani zione namna ambavyo zinatunzwa na kuhifadhi mazingira haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kisiwa cha Mtambwe Mkuu tunakwenda kurekebisha ili kuondosha athari kubwa ya mabadiliko ya tabianchi, nashukuru.