Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Khalifa Mohammed Issa (9 total)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE.KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza mimi nimshukuru Mwenyezi Mungu pia kwa kunijalia kupata fursa hii ili kuchangia hoja tatu hizi zilizoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mjumbe wa Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa. Kwa sababu ya muda nitaomba nijikite katika taarifa hii/katika hoja hii ya Kamati yangu na nitakwenda kidogo tu kuchangia habari ya Mfuko Maalum huu wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfuko huu wa TASAF hapana ubishi kwamba umewakomboa wanyonge wengi kwa Serikali ya Muungano pamoja na Serikali ya Zanzibar. Mfuko huu umesababisha kuwapatia wale watu wa Kaya ya masikini walau milo yao mitatu kwa siku, lakini pia imewezesha watoto kwenda shule, lakini pia kwenda clinic. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata katika ripoti yetu katika kamati yetu imekuwa ikieleza mara kwa mara kwamba Zanzibar mfuko huu umekuwa ukifanya vizuri kuliko hata Tanzania Bara. Na kama Wajumbe sisi tulipata fursa mara nyingi tu kutembelea sehemu mbalimbali na mashuhuda wakawa wametoa ushahidi kuonekana kwamba mfuko huu umewasaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kidogo ambalo ni dosari na nilitaka Mheshimiwa Waziri wetu aweze kulijua, kwamba Zanzibar mfuko huu upo, lakini ni kama vile makao makuu unapeleka pesa kule lakini hawafuatilii utelekezaji wake mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tulipata fursa ya kutembelea Shehia moja ya Kilindi iliyoko Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba. Pale wananchi wenyewe waliibua mradi wa kuzuia maji ya bahari yasiingie katika mashamba yao na mradi ule ukakubaliwa na ukatengewa pesa za kutosha. Hata hivyo jambo la kusikitisha na haitakiwi maana si lazima uwe mchunguzi wa kada ya CAG ndipo uweze kuweza kujua value for money pale. Tuta lile lilikuwa na urefu wa mita 125; lakini tuliambiwa limejengwa kwa shilingi milioni 47. Kwa hesabu za haraka haraka unaweza kuona kila mita moja, basi imejengwa kwa zaidi ya shilingi 350,000. Sasa hapo unaweza kuona tu kama value for money haiwezi kupatikana hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiondoka hapo, sisi kama Wabunge, mimi kwa bahati nzuri pia katika shehia yangu ambayo imo katika jimbo langu na ndiyo shehia mimi mwenyewe naishi hapo kuna mradi kama huo wa tuta la kuzuia maji ya bahari yasiingie katika makonde/mashamba ya watu, lakini mimi kama Mbunge sijawahi kushirikishwa wala kuambiwa kama kuna mradi kama huo. Kwa hiyo, tungeomba walau na sisi tukapata fursa ya kushirikishwa tukajua miradi ambayo ipo katika shehia zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ambalo limenikwaza sana, kama nilivyosema mwanzo miradi hii ikifika Zanzibar labda haina uangalizi mzuri. Tulikwenda tukatembelea ujenzi wa shule ya sekondari Muyuni mwaka jana. Shule ile ilijengwa hafla sana na takribani kwa zaidi shilingi 120, lakini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuzungumzia changamoto za kiutendaji Polisi - Kaskazini Pemba kuhusu mafuta, vipuri na umeme. Polisi wetu wanapatiwa lita 900 badala ya mahitaji ya lita 3,000. Vilainishi (lubricants) na spare wanapewa shilingi milioni 1.5 badala ya shilingi milioni 4.5 ya mahitaji. Umeme wanapatiwa Sh.400,000 kwa mwezi wakati mahitaji ni shilingi milioni 2.4 kwa mwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jengo la Maofisa wa Polisi Wilaya ya Wete linavuja, jengo la utawala la Polisi Kaskazini Pemba ni chakavu, jengo la Askari Polisi - Konde ni chakavu, Bweni la Askari wetu ni bovu, nyumba za Askari FFU ni chakavu zinahitaji ukarabati wa miundombinu ya majitaka na makaro na kuezekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni Maafisa na Askari kutolipwa mishahara kulingana na vyeo vyao kwa muda mrefu, wastaafu kuchelewa kulipwa mafao yao bila ya sababu ya msingi, kutolipwa posho mbalimbali kama za nyumba, upelelezi, nguo na malipo ya uhamisho huchelewa sana. Vile vile kuna uchache wa Askari ambapo Askari wengi wanahamishwa na kustaafu bila ya kupatiwa mbadala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Ofisi ya Teknohama Mkoa ipatiwe vifaa vya kisasa pamoja na computer.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri asimamie upatikanaji wa stahiki za Idara ya Uhamiaji Makao Makuu kama vile vinywaji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kunijalia asubuhi hii afya na uzima nikaweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyojua Wizara ya Mambo ya Ndani ni miongoni mwa Wizara za Muungano. Kwa hiyo, taasisi zake zote zilizomo katika Wizara hii zinapaswa zifanye kazi katika maeneo yote ya Tanzania Bara pamoja na Tanzania Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukizungumzia kuhusu Jeshi la Polisi ambalo kwa mujibu wa utaratibu ndiyo ambao wanalinda mali na raia wa nchi hii kwa ujumla. Pia tamko hilo liko supported na Ibara ya 15(2)(a) na (b) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Nasema hivyo kwa sababu nataka kuelewa hili jukumu la kulinda raia na mali zake lipo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar au kuna mpaka baina ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu inaonekana dhahiri chombo hiki kikija katika maeneo ya Zanzibar labda kuna vyombo vingine ambavyo vimepewa majukumu haya ya kufanya kinyume na ule utaratibu wa kuweza kulinda raia na mali zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninao mfano hai wa siku ya Alhamisi, tarehe 5 Aprili, katika Kijiji cha Mitambuuni, Jimbo langu la Mtambwe, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, kama alivyosema Mheshimiwa Khatib jana vijana sita wadogo kabisa, innocent, wapo mbali kabisa na hata maendeleo ya teknolojia maana hakuna umeme, hawana television wala hawana habari yoyote, ambao wana umri kati ya miaka 16 na mkubwa wao ana miaka 30 wamekamatwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamekwenda watu sijui tuite ambao hawajulikani wakiwa na magari manne yenye namba za private, namba ambazo baadhi ya majirani walizichukua, wakawagongea, wakawachukua vijana hawa, nyumba tofauti wakawafunga vitambaa vya uso, wakawasweka katika magari wakaenda nao mahali pasipojulikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana hao wakapelekwa katika nyumba, kwa sababu wamefungwa hawakujua wamekwenda wapi. Kulipokucha asubuhi wazee wao na jamaa zao wakaenda katika Kituo cha Polisi cha Wete ambapo ni Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba kuuliza, kwa sababu tumezoea mambo haya lakini mara nyingi tunazoea Polisi wanawachukua watu wanakwenda nao vituoni, lakini walipofika pale wakaambiwa hapa hawapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakaenda Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Chakechake napo wakaambiwa watu hao hawapo. Vijana hawa baada ya siku nne vijana watatu katika sita, majina ninayo hapa, alfajiri wakatupwa mahali mbali kabisa na makazi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walipokuja vijijini wakaeleza wakasema kwa kweli sisi tunashukuru hatukufanyiwa mateso lakini wenzetu ambao tumebagulia wapo katika vyumba tofauti wana mateso ya ajabu. Sasa just imagine hali ya wazee na jamaa itakuwaje watoto wao wameambiwa wapo katika mateso makubwa kama hayo. Wale vijana watatu wakakaa ndani kwa siku 11 kuanzia tarehe 5 mpaka Jumapili ya tarehe 15 na wao wakaenda wakatupwa mahali wakiwa wamefungwa mikono na vitambaa vya uso. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni msiba mkubwa nchi kama Tanzania ambayo tunajivunia ni kisiwa cha amani, miaka 54 ya Muungano leo wanakwenda maharamia kwenda kuwachukua vijana wadogo. Waliporudi tulipokwenda kuwaona kwa kweli hali zao haziridhishi, wakikueleza mateso waliyoyapata basi huwezi kustahamili, unaweza kutoa machozi. Kwa kweli hali ni mbaya, wamepigwa kila eneo la mwili wao. Kwa hiyo, unaweza kujiuliza nyuma ya Jeshi la Polisi kuna nani ambaye ni super power ana-organize uharamia huu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni uharamia ambao kwa kweli unasikitisha mno. Kamishna wa Zanzibar yupo hapa ampelekee shukrani zetu RPC wa Kaskazini, katupa ushirikiano siku zote tulipokuwa tunakwenda lakini yeye muda wote alikuwa na yeye anasikitika, mimi hawa watu sinao jamani nendeni mkakague katika maeneo yangu yote, lakini unamhisi kuna jambo ambalo limefichika nyuma yake, anajua baadhi ya mambo. Yeye anasema hanao lakini anatupa moyo baada ya siku mbili au baada ya siku ngapi mtawapata watu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha zaidi tumepeleka hata namba za gari, hapo ndiyo mwanzo, kama ni upelelezi unaanzia hapo. Tungetarajia kwa kupitia namba za gari zile watu hawa wangekuwa traced na wakajulikana na tunasikia wamehojiwa lakini mpaka leo wanadunda, hakuna ambaye amepatikana na ameshtakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ndiyo maana tukauliza, je, wajibu na jukumu la Jeshi la Polisi hasa kule Zanzibar kuna watu mme-delegate powers kwao, wao ndiyo washughulikie usalama lakini wakati huo huo washughulikie mateso ya watu? Hapa ndipo ambapo tunapata shaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunamuuliza Waziri Inshallah akija hapa kutoa majumuisho, ni lini hawa watu ambao hawajulikani wataanza kujulikana na mateso haya yatakoma lini. Au kama hiyo haiwezekani basi atamke hapa leo akija Mheshimiwa Waziri kwamba sasa jukumu la kujilinda liwe lenu wenyewe wananchi. Tukishapata kauli hiyo tutajua namna gani ya kuweza kukaa kulinda wananchi, kujilinda wenyewe na mali zao, vinginevyo kwa kweli itakuwa hatuwafahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tungeomba kabisa nchi hii ni yetu sote, kama kuna mtu yeyote na kwa kawaida kila raia ni mtuhumiwa mtarajiwa. Mimi naweza kutuhumiwa leo lakini kuna utaratibu, niitwe polisi au popote pale nikahojiwe ikionekana labda kuna makosa nipelekwe katika vyombo vya haki (mahakama).

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani kwenda kumgongea mtu usiku ukamfunga kitambaa ukaenda ukamtesa bure. Mtakuja kuwaona wananchi ni wabaya kumbe wabaya wakati mwingine ni Jeshi la Polisi. Hii ni kwa sababu wao wameshindwa kuwalinda wananchi pamoja na mali zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sasa niseme kwamba pamoja na yote hayo, tunaona kwamba polisi wana matatizo mengi katika maeneo yao ya kazi. Hata bajeti yao ya mafuta ni ndogo mno. Kwa mfano, hata tulipowaita wao kwenda katika site watu wale walipokuwa dumped kikwazo kilikuwa ni mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwingi wa Rehema mwenye kurehemu, ambaye ametujalia kuwepo katika nyumba hii Tukufu. Pia nikushukuru wewe kunipa nafasi hii ya kuchangia huu Mpango ambao uko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka nijikite sana katika Mpango huu hususan niende katika Wizara yetu mama ambayo iko katika Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo ni ya Muungano pamoja na Mazingira. Kama tunavyojua Tanzania ni pamoja na Zanzibar, bila Zanzibar hakuna Tanzania. Sote sisi ni waumini wa Muungano na mimi ni muumini wa Muungano wa haki na wa usawa. Kwa hivyo, napenda Muungano huu udumu katika mfumo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi jambo ambalo tuna shida kule katika visiwa ni kuhusu mabadiliko ya tabianchi. Mabadiliko ya tabianchi yametukumba sana katika Visiwa vyetu vya Unguja na Pemba na visiwa vidogovidogo ambavyo vimeizunguka Zanzibar. Wizara inayohusika nahisi kwa upande wangu haijafanya vya kutosha, leo ukiangalia visiwa vinavamiwa na maji ya bahari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoa mfano kuna visiwa vidogovidogo kama Kisiwa Panza, Pemba kuna Kisiwa kinaitwa Kisiwa Panza. Kisiwa kile kimevamiwa mpaka sehemu ya kuzikia makaburi yamezolewa na maji, wakati mwingine unaweza ukaenda ukakutana na mafuvu ya vichwa ya maiti. Kadhalika kuna Kisiwa cha Mtambwe Mkuu, Mtambwe Mkuu ni katika jimbo langu ambacho ni kisiwa cha historia kilichokaliwa na Wareno katika karne ya 18 ambacho kinatishia amani, wananchi wake wanakaribia kuhama kwa sababu maji ya bahari yamevamia kisiwa kile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viko visiwa vingine vingi kwa mfano Misali ni kisiwa vilevile cha utalii, lakini nacho kimevamiwa na maji, lakini bado Serikali kupitia ofisi yetu hii haina jitihada yoyote ya makusudi ambayo inaifanya na mpango endelevu kuweza kushughulika na mambo haya ili kukinga maji yale yasiweze kuvamia makazi ya watu. Kwa hivyo, hofu yangu baada ya karne si nyingi zinazokuja tunaweza tukavipoteza visiwa hivi, kwa hivyo, yale matamanio na utashi tuliokuwanao wa kuwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikaondoka kwa sababu visiwa vile vimeondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huo ni mfano ambao uko hai kabisa. Sisi wazee wetu ambao wameishi katika miaka sitini, sabini siku za nyuma wanatueleza tunapita katika bahari ya kina sasa hivi lakini miaka sitini iliyopita ilikuwa watu ni mashamba wakilima mipunga katika maeneo yale, lakini kwa sababu hakuna jitihada maalum kwa hivyo, bahari inapanda juu kila uchao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Ofisi, Wizara kattika Ofisi ya Makamu wa Rais kwa makusudi kabisa ifanye bidii tuje tuvitembelee visiwa. Awamu iliyopita ya Bunge tulifanya jitihada kubwa kuonana na Mawaziri lakini haikuwezekana, hawakupata nafasi ya kuja kuvikagua na kuweza kupata ufumbuzi. Kwa hivyo, huo ni msisitizo wangu mkubwa ambao napenda kuutoa kwenye Mpango huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, athari hii kwa kweli inaanza kuonekana. Hata hizi mvua ambazo hazina misimu, unakuta mvua zinanyesha wakati mwingine, mafuriko yanatokea wakati wa kiangazi, lakini wakati wa msimu wa mvua yenyewe mvua haipatikani. Ndio maana wakati mwingine tunapata hii collusion katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nilitaka niliseme kwa ufupi ni kuhusu huu Mfuko wa Kunusuru Kaya Masikini ambao unajulikana kwa TASAF. Mfuko huo kwa kiasi kikubwa nikiri umeleta manufaa makubwa katika kaya zile ambazo ni masikini. Familia zile za kaya masikini zimemudu kuwapeleka watoto wao shule, kupata uniform, kupata chakula, kupata ada za shule na wakati mwingine kupata pesa za matibabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, ni jambo zuri, lakini tatizo linakuja, uteuzi wa hawa wanufaika unakuwaje? Wakati mwingine unaweza kuona watu ambao wanastahiki hasa kuingizwa katika mpango huu wameachwa, lakini wale ambao wana uwezo kidogo ndiyo ambao wamechukuliwa. Hii inatokea wakati mwingine utashi wa viongozi wa Shehia, kama mnaendana pamoja na kiongozi wa Shehia, Sheha, basi anaweza kukuingiza katika listi.

T A A R I F A

MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusema kwamba…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Khalifa kuna Taarifa.

MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe Taarifa mzungumzaji…

MWENYEKITI: Jitambulishe tafadhali.

MHE. OMAR ISSA KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, jina naitwa Omar Issa Kombo, Mbunge wa Jimbo la Wingwi, Pemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe Taarifa mzungumzaji kuhusu utaratibu unaotumika kuwapata wanufaika wa kaya maskini kule Pemba. Kunafanyika kikao cha jamii ambapo wanajamii hawa wanachagua watu wa kuratibu na kuorodhesha wanufaika wa kaya masikini ambao wanaitwa CMC si Sheha.

WABUNGE FULANI: Aaaaa.

MHE. OMAR ISSA KOMBO: Sheha hashiki daftari kuandika wanufaika wa kaya masikini, ni wananchi wenyewe ndiyo wanaoandika kupitia wajumbe wanaowachagua wao wenyewe ambao wanaitwa CMC, asipotoshe umma. Ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Khalifa, unaipokea Taarifa hiyo?

MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri tuendelee, asiyejua maana haambiwi maana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusema kuwa upande wa pili miradi hii, hasa ule mradi wa kutoa ajira ya muda, tatizo lililopo pia ni ule uteuzi wa ile miradi. Wakati mwingine miradi inateuliwa au inawekwa lakini haiangaliwi sustainability yake, nini uendelevu wake na nini tija yake mwisho? Kwa hivyo, unaweza kuanzisha mradi lakini baadaye ukawa haukufika mwisho, tija yake inakosekana. Pia wakati mwingi mradi ule unakosa ile value for money. Utakuta mradi umefanywa lakini value for money haipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mimi kuna mradi wa tuta la kuzuia maji ya bahari ambao umefanywa katika kipindi fulani, ukiangalia umechukua muda mrefu, lakini tija yake haikuonekana kwa sababu leo tuta lile limevurugika, maji yanaendelea kuingia katika mashamba ya watu kwa hivyo, ile sustainability inakosekana. Hata ukiangalia tuta lile labda lingejengwa na watu kwa kulipwa shilingi milioni mbili, milioni tatu, lakini limegharimu zaidi ya shilingi milioni 10, lakini tija yake haikupatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa zaidi tunasikitika Wabunge katika maeneo ya miradi hatushirikishwi. Mimi kipindi kile nilikuwepo, mradi huo uko karibu tu, umo katika kata au shehia yangu, lakini mimi sikushirikishwa vyovyote ili kuweza kutoa ushauri wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, yangu ni hayo niliyosema kwa ufupi, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote nimshukuru Allah Subhanallahu Wataallah kwa kutujaalia uzima na afya na kuukabili huu Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa salama. Inshaallah Mwenyezi Mungu atujaalie tuukamilishe kwa salama.

Mheshimiwa Spika, nataka nijikite katika jambo hili la mazingira kwa maana ni jambo muhimu sana katika uhai wa binadamu. Mazingira yanayotuzunguka yanaakisi uhai wa binadamu na viumbe hai ambao wapo ndani ya ardhi yetu hii tunayoishi. Kuharibika kwa mazingira au kuharibiwa; ni kuharibika kwa maisha ya binadamu na viumbe hai vilivyomo. Mazingira uharibiwa ama kwa makusudi au bila kujua na binadamu wenyewe katika maisha yao ya kila siku ya kutafuta riziki zao. Sasa ni juu ya Serikali kusimamia na kuona kwamba mazingira haya kwa namna yoyote hayawezi kuharibiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikija katika Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na inajumuisha Visiwa vya Unguja na Pemba na visiwa vidogo vidogo ambavyo vimezunguka visiwa hivyo. Kwa hivyo, uwepo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unategemea pia uwepo wa Visiwa vya Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, tumeona mabadiliko ya tabia nchi yameathiri sana na kama nilivyosema mwanzo hata matendo ya binadamu wenyewe ya siku kwa siku yameathiri mazingira yetu hivyo bahari imechukua sehemu kubwa sana. Tumeambiwa katika tafiti nyingi kwamba katika miaka 50 zaidi ya sentimeta 19 – 20 zimekuwa maji ya bahari kwa maana ya kwamba kina cha bahari kimekuja juu. Kwa hiyo, imeathiri visiwa vingi sana vya Zanzibar kwa maana ya Unguja na Pemba kutaka kutoweka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niruhusu nitoe mifano michache kwa Zanzibar ambapo ni ushuhuda wa wazi wa kuondoka kwa visiwa. Kwanza, kuna Kisiwa cha Mtambwemkuu ambacho kimo katika Jimbo langu; Kisiwa kile kinavamiwa kwa kasi sana na maji ya bahari kiasi kutishia watu kutaka kuhama katika maeneo yao. Mfano wa pili; katika Jimbo langu pia kuna sehemu inaitwa Tosawana. Sehemu hii ina mashamba ya mpunga; watu wanajitafutia riziki zao kwa kulima katika maeneo yale, lakini kwa kweli kila baada ya muda maji ya bahari yanavamia mashamba yale ikabidi watu kuhama. Kwa kweli TASAF katika kipindi cha miaka miwili iliyopita walijitahidi kujenga tuta pale lakini kwa sababu lile tuta halikujengwa kitaalam, wala halikusimamiwa baada ya muda mfupi limeyeyuka kwa hivyo bado maji yanaingia kwenye mashamba ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mfano mwingine katika eneo la Jimbo langu hilo hilo, kuna sehemu tunaambiwa miaka 50 iliyopita au zaidi kidogo ilikuwa ni mashamba watu wanalima mpunga, maji baridi lakini leo huwezi kupita kwa mguu lazima upite kwa kidau. Hii ni kutokana na maji ya bahari kupanda kila kukicha. Kuna mfano kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, Kisiwa cha Misali; Kisiwa cha Utalii; baada ya muda mfupi kinaweza kupotea kwa sababu ya kuvamiwa na maji. Kuna Kisiwa cha Mnemba pia Kisiwa cha Utaliii, nacho kiko hatarini kukikosa. Jimbo la Mheshimiwa hapa Bandani kuna Shehia ya Mjananza kuna sehemu inaitwa Uvuni kuna wakulima zaidi ya 100; leo wamehama kwa sababu maji ya bahari kuvamia mashamba yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile katika Kisiwa Panza bahari inakaribia shule, kwa hiyo makazi ya watu yako hatarini kuondoka. Mwambeshidi mashamba yamevamiwa na maji, Ukunda Kengeja, Mwambe Shamiani, Nanguji, kote watu wamejitahidi kupanda miti kwa jitihada zao lakini bado kasi ya maji ni kubwa kwa hiyo athari inaweza kutokea wowote.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa ushauri tu kwa Serikali, kipindi kilichopita tuliomba sana lakini haikuwezekana, naomba tena Waziri na wataalam wake watembelee maeneo haya ili wakague na kuona zile athari ili wajue hatua za kuchukua.

Mheshimiwa Spika, mwisho niseme…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Khalifa.

MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atueleze Tanzania ina Mabalozi wangapi na watumishi wangapi katika Bilozi zetu nchi za nje, lakini napenda utufamahishe ni Mabalozi wangapi kutoka Zanzibar na wangapi kutoka Tanzania Bara na hivyo hivyo kwa watumishi wa Balozi zetu zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kama kuna kasoro katika hili ulete utaratibu utakaotumia kuondoa kasoro ili isiwe kero ya Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia ulieleze Taifa ni kwa nini taasisi nyingi za Tanzania Bara ambazo sio za Muungano zinatumia jina la Tanzania hadi kufikia Zanzibar taasisi kama hizo kukosa uwakilishi wa kimataifa kwa kuambiwa tayari Tanzania ni mwanachama au vinginevyo, lakini Zanzibar inakuwa haina tena nafasi kwa mfano Tanzania Football Federation (TFF) ni mwanachama wa FIFA lakini Zanzibar imekataliwa sababu ya TFF.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kutujalia jioni hii ya leo uzima na afya kuweza kuzungumza machache kuhusu Wizara yetu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mama Samia, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchagua safu makini katika Wizara hii ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kwa kweli Mheshimiwa Balozi Mulamula na Mheshimiwa Balozi Mbarouk, hawa ni watu wabobezi ambao wanajua diplomasia ya kidunia. Kwa hiyo, ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hayo, mimi mchango wangu utakuwa mfupi tu ambao sanasana utakumbusha ziara ambayo imewahi kuandaliwa kama sikosei, mwaka 2019. Ubalozi wetu ulioko kule Abu Dhabi ukishirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje uliandaa ziara ambayo aliyekuwa Rais wa Zanzibar wa Awamu ya Saba, Dkt. Ali Mohamed Shein, alifanya ziara katika nchi zile za Falme za Kiarabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, na miongoni mwa matunda ambayo yamepatikana katika ziara ile ni kupatikana kwa ahadi ya msaada kwa Zanzibar, msaada wa dola za Kimarekani zisizopungua milioni kumi ambazo zingesaidia wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo wadogo wa Zanzibar kwa ujumla. Dola Kimarekani milioni kumi si pesa ndogo kwa nchi kama ya Zanzibar, ni pesa ambazo zingeweza kuzunguka na zikasaidia pato la nchi na uchumi wa nchi kwa ujumla; kwa hiyo hili lilikuwa moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi, katika Mfuko wa Abu Dhabi (Abu Dhabi Fund) nao uliahidi kutoa dola milioni kumi hivyo hivyo kwa ajili ya Hospitali ya Wete iliyoko katika Mkoa wa Kaskazini Pemba. Yaani kuifanyia ukarabati mkubwa hospitali ile, lakini pia kuifanyia mambo makubwa, pamoja na kuleta vifaa tiba pamoja na dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo ninachokumbusha ni kwamba msaada ule kila kitu mwaka 2019 walishakuweka saini ule mkataba, kilichobakia ilikuwa maafisa wale wajumbe wa mifuko ile wa Khalifa Fund pamoja na Abu Dhabi, waje Tanzania Zanzibar ili kukagua miundombinu na namna gani zile pesa watakazozileta zitatumika vipi, lakini kwa sababu ya mlipuko wa Covid duniani, basi mpaka leo hawakuweza kuja katika nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachokumbusha ni kwamba Ubalozi wetu wa Abu Dhabi ukitiwa hima na Wizara yetu hii basi waweze kuhimiza, kukumbusha na kuwaambia Tanzania sasa iko salama kwa Covid-19. Kwa hiyo, waje wakague ili baadaye watupatie pesa hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba katika Bunge lililopita tulikuwa na mvutano kidogo hapa wa nani anahusika kuweka saini katika msaada fulani wa kujenga barabara iliyoko Pemba vilevile; kutoka Wete – Piki – Melitano – Chakechake. Tuliambiwa watu wa ADB pamoja na Saudi Fund walikuwa tayari watoe msaada wa kujenga barabara ile ambayo ni muhimu sana katika maendeleo ya uchumi wa Pemba kwa mazao ya biashara pamoja na mazao ya chakula. Lakini mpaka leo tunasikia danadana, hatujui msaada ule umekwama wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninamuomba Mheshimiwa Waziri akija hapa aki-summarize basi atueleze nini position ya msaada ule wa kuijenga barabara hii ya Wete, wanaita barabara ya Njia Kongwe kufika Melitano mpaka Chakechake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kadhalika pia tumeona katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri akizungumza kwamba China wako tayari kusaidia ujenzi wa barabara kuu za Zanzibar, kilometa 148. Lakini hakukuwa na ufafanuzi. Kwa hiyo, tunamuomba Waziri pia akija hapa atueleze ni barabara zipi hizo ambazo China watatusaidia na lini tunategemea kuanza kazi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, mimi nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia kwa kuwateua majembe mawili makubwa haya. Tunasema kama Wizara hii ni upele basi upele umepata mkunaji. Kwa hiyo tunawatia moyo, waendelee kuchapa kazi ili maendeleo ya nchi hii kupitia Wizara hii yapatikane. Ahsante sana (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote namshukuru Mwenye Mungu Mtukufu kwa kutujalia uzima na afya katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan na kuweza kutekeleza nguzo hii muhimu katika dini ya Uislam. Pia nakushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia mchana huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba hii haiwezi kupita bure kama sikumshukuru sana Mama yetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mheshimiwa Samia kwa kweli amekijaa kiti chake na amekuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kujali siasa, itikadi za vyama, wapinzani na chama Tawala. Kwa hiyo, Mheshimiwa anakusudia, na ni dhamira ambayo tunaiona wazi kabisa ya kuliunganisha Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli sasa nimekuwa mshabiki wake mkubwa wa kusikiliza hotuba zake. Ninafuatilia ratiba zake, nafuatilia hotuba zake. Hotuba zake zote zinaonesha anataka kuiunganisha nchi, na anazungumzia utengamano wa wananchi wote bila kujali itikadi zao. Hivyo basi, mfano mkubwa katika kipindi kifupi cha mwaka mmoja hiki, Mheshimiwa Rais ameshakutana na viongozi wa vyama vya upinzani. Pia karibuni hivi, alikuwa katika Mkutano wa TSD; karibuni pia alikuwa akipokea taarifa ya kikosi kazi ambacho amekiunda na ameyakaribisha mapendekezo yote kwa mikono miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba wasaidizi wake wasimwangushe. Nia njema hii ambayo Mheshimiwa Rais ameionesha ya kuliunganisha Taifa, basi taifa hili ni letu sote, tuna tofauti ya mawazo yaheshimiwe, naye ndiyo mwelekeo anakwenda nao. Kwa hiyo, ningetoa tena wito kwa wasaidizi wake Mawaziri, wamsaidie kutufikisha pale ambapo tunataka. Tuna mambo mengi kwa sababu mapendekezo yanakusanywa, anapelekewa. Sina haja ya kwenda huko, najua kuna muda mfupi wa kutekeleza mambo, kuna muda wa kati na kuna muda mrefu. Kwa hiyo, tuwaachie mambo haya yachakatwe yapelekwe ili yatolewe maamuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuondoka hapo, nami nipate fursa ya kuzungumzia hali ya maisha ya wananchi kwa ujumla. Kwa kweli hili halitaki tochi, halitaki taa ya mwangaza mkali wa kuona hali halisi ya maisha ya wananchi wetu. Kwa kweli purchasing power ya wananchi imepungua sana kwa sababu mifumuko hii ya bei ya vitu mbalimbali na upandaji wa mafuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimefanya utafiti mdogo katika masoko yetu haya hapa Dodoma ambapo mahitaji yetu mengi tunakwenda kuchukua. Utavikuta vitu vipo kwa wingi sana katika masoko; ukitaka vyakula vya maganda hivi, mboga mboga, matunda na bidhaa nyingine, lakini ukimwuliza muuzaji, atakwambia unaweza ukakaa kutwa nzima ukauza shilingi 2,000/= au shlingi 3,000/=. Watu wanavitaka vitu, lakini bei ni kubwa na mifukoni kunakuwa hamna kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili jambo ni la kuzingatiwa mno. Biongozi wetu na wataalam wetu wakae waone kwa namna gani watamnusuru huyu mwananchi hasa wa kipato cha chini kuweza kumudu maisha yake na kipato chake na chakula chake walau cha siku nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo nizungumzie hali ya UKIMWI katika nchi, kwa sababu mimi ni Mjumbe wa Kamati yako ya Mambo ya UKIMWI, Dawa za Kulevya, Magonjwa yasiyoambukiza pamoja na TB. Kwa kweli hali ya UKIMWI katika nchi yetu, bado UKIMWI upo katika nchi na wananchi waelewe UKIMWI bado ndio ule ule unaua. Kwa hiyo, ipo haja ya Serikali, wananchi na jamii kwa jumla kuweza kupiga vita hivi ili tuweze kuvishinda walau tumudu kutokupata maambukizi mapya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu inakisiwa tu, na mpaka takwimu za Desemba, 2020 tuna watu ambao wanaishi na virusi vya UKIMWI karibia 1,700,000, ingawa ukiangalia trend ile toka miaka ya 2004 huko mpaka sasa, ile graph linakuwa declined, linapungua pungua yale maambukizi mapya.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kuna rika muhimu kweli kweli ambalo linapata maambukizi mapya. Hili ni group la vijana wetu ambao wana umri kuanzia miaka 15 mpaka 24. Vijana hawa wanachangia asilimia 40 ya watu wote ambao wana maambukizi. Katika vijana ambao wana umri huo, vijana wa kike kwa asilimia 80 katika maambukizi hayo, wao wanaongoza vijana wasichana; na hao wasichana katika group hili ndio ambao wapo katika vyuo vikuu, wapo katika Shule za Sekondari nakadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, wasichana hawa ndio target kubwa ya wanaume wakwera, Mheshimiwa Mwenyekiti wangu wa Kamati ya UKIMWI ana neno lake analitumia kwa hawa wanaume ambao wanawanyemelea vijana hawa. Ukiangalia, ni dhahiri kwamba hata hapa Dodoma ukifuata nyendo fulani fulani hivi unaweza kuona vijana hawa wadogo ndio ambao wameingia katika ushawishi huu mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, wajumbe wenzangu wa kamati hii ya mambo ya UKIMWI tulipokuwa katika ziara ya kukagua maendeleo, tulikuwa katika mkoa mmoja huko sitaki niutaje, lakini walipokwenda kufanya utafiti katika maeneo yao, walikaribishwa pale. Ajabu ni kwamba, unapewa option; walipofika wakapewa option, kama unataka kula ndizi na ganda lake au unataka ule ndizi ganda ukiwa umelitoa? Kwa hiyo, kuna viwango; ukitaka ule na ganda lake, basi ni shilingi 10,000/=, lakini ukitaka ulitoe lile ganda, basi kuna shilingi 15,000/=. Kwa hiyo, hii ni hatari ambayo Serikali pamoja na jamii na wazee, lazima tushirikiane tuwalinde vijana hawa. Hawa vijana ni wetu na kwa kweli tusi… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Hiyo ya pili, malizia sekunde moja.

MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa ufupi mimi niseme tu kwamba kuna magonjwa haya yasiyo ya kuambukiza pia, ni janga, kwa hiyo…

NAIBU SPIKA: Ahsante.
Azimio la Bunge kuhusu Mapendekezo ya Kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2012
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kutoa mchango wangu katika mjadala uliopo hapa ama Azimio lililoletwa na Serikali. Pia napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kunijalia afya nikaweza kusimama kwenye Bunge letu hili kuchangia Azimio hili ambalo limeletwa kwetu leo ili kuweza kuleta mustakabali wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Azimio lililopo leo ni Protocol of Trade in Service. Protocol hii ni kwa ajili ya nchi za Kusini mwa Afrika kuweza kushirikiana katika biashara ya huduma katika nchi hizi ambazo ni wanachama. Itifaki hii inalenga kuondoa vikwazo na masharti ya taratibu za huduma ya biashara katika nchi wanachama. Kwanza ningependa kuipongeza Serikali kwa kuleta Azimio hili kwa sababu linakuja kuleta maendeleo chanya kwa wananchi wetu ambao wanatoka katika Jumuiya hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mategemeo yetu Azimio hili litakuja kuisaidia nchi yetu baada ya kuridhiwa. Kwa nini nasema hivyo? Watanzania tumekuwa tukifanya biashara hizi kabla ya kuridhiwa Azimio hili, lakini tumekuwa tukifanya biashara kwa mashaka na vikwazo vingi bila kuweza kupata njia ya kutatua vile vikwazo, sasa muarobaini wa matatizo ya wafanyabiashara ya huduma unakuja kupatikana. Biashara hizi za huduma kama vile elimu, transport na mambo mengine, nchi yetu imekuwa ikipata changamoto nyingi, kwa hiyo sasa tukiridhia Azimio hili, changamoto hizi zitakuja kuondoka. Napenda kushauri mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukipata changamoto tukitumia zile certificates za Jumuiya hii bila ya kupata huduma stahiki kwa sababu tulikuwa hatujaridhia Azimio hili. Azimio hili wenzetu nchi wanachama walianza kuridhia mwaka 2022 ingawa lilisainiwa mwaka 2012. Kiukweli hatujachelewa kuridhia Azimio hili, ni kwamba tupo katika wakati mzuri na si vizuri katika jambo ukawa mtu wa kwanza ni bora kuchunguza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza Serikali kwa kuchelewa kulileta Azimio hili kwa sababu ni lazima tuangalie kwamba wale wenzetu walioingia wamekutana na changamoto gani ili na sisi tuweze kujifunza kupitia kwao. Kwa hili, naipongeza Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye hoja ambazo nahisi zinahitaji kurekebishwa. Nchi yetu ya Tanzania imeingia mikataba mingine na nchi ambazo si wanachama wa Jumuiya hizi. Napenda Wizara yetu au Serikali yetu ikaliangalia hili tusije tukaathiri ile mikataba ambayo tumeingia na nchi nyingine tukashindwa kufanya nao biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, napendekeza nchi yetu ijikite kwenye kutoa hizi National ID na siyo nchi yetu tu, nchi wanachama zote ili kusiwe na mgongano kwa raia ambao hawahusiki ndani ya nchi hizi wanachama ama wakaenda kutoa huduma wakasema kwamba wanatoka katika nchi wanachama. Kama vile watu wanaoongea Kiswahili sana katika nchi ambazo siyo wanachama, wakaenda nchi nyingine wakasema wanatokea Tanzania. Kwa hivyo, suala la National ID ni muhimu sana ili liweze ku-facilitate mambo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kama lilivyosemwa na Kamati yetu hapa, kuhusu Sera na Sheria zilizopitwa na wakati. Ni muhimu sana hili tuweze kulipitia, tukazitengeneza ili wananchi wetu wasiwe wana vikwazo kuingia kwenye soko hili la Jumuiya hii ya Nchi za Kusini mwa Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo jema. Tufanye haraka turekebishe sheria ambazo zimepitwa na wakati ili wananchi wetu waweze kuingia kwenye soko hili vizuri. Nchi yetu itoe elimu kwa wananchi wote kulifahamu Azimio hili ili waweze kuchangamkia fursa ambazo zipo katika katika hili Azimio. Hilo ni jambo kubwa sana kwa sababu wananchi wakati mwingine kama hawana uelewa, basi inaweza ikawa fursa hizi zikatumiwa na watu wengine kuja hapa kuwekeza wakati sisi tuna uwezo wa kwenda kuwekeza katika nchi ambazo tumeridhia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nilalopenda kuchangia ni suala la leseni za biashara. Leseni za biashara ziweze kutolewa katika masharti ambayo ni nafuu na kwa haraka na ikiwezekana kusiwe na mlolongo wa leseni. Leseni ya biashara iwe moja ili kuweza ku-facilitate kwa haraka ufanyaji wa biashara wa wananchi wetu katika nchi nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto nyingi ambazo wananchi wetu wanakuwa wanazipata. Mfano, madereva wanavyokwenda nchi nyingine, wanakwama mipakani kwa sababu ya logistics nyingi ambazo zinafanyika pale, ukitoka Tanzania kuingia border nyingine. Napendekeza suala hili lifanywe kwa haraka, ianzishwe one stop center kwa nchi hizi za Jumuiya ili watu wanapokwenda au wafanyabiashara hawa wa ma-truck au wasafiri, wasikutane na changamoto hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakaribia mwisho wa mchango wangu, kuhusu suala la usimamizi wa sheria. Usimamizi wa sheria zetu inakuwa ni changamoto, kwa hiyo, hili napendekeza kwamba Serikali iwe makini katika usimamizi wa sheria ili kuona kwamba hii fursa haitumiwi na watu ambao siyo wanachama. Azimio hili linakuja lakini pia nchi mwananchama itazingatia sheria zake ilizojiwekea. Siyo kwamba watu wataingia tu kiholela kwa vile tupo kwenye Azimio, napendekeza nchi yetu, watendaji wasimamie sheria tulizoziweka ili kuepuka kupoteza haki zetu kwa sababu katika nchi yetu, nataka nitoe mfano. Mfano ni upande wa Zanzibar, mtu mgeni haruhusiwi kumiliki ardhi lakini sasa hivi ukienda Zanzibar, ukifanya utafiti, basi utakuta asilimia 25 – 30 ni wageni wanamiliki ardhi bila kufuata sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili ndilo nchi tunakwama kwa hiyo tunatakiwa tusimamie zile sheria zetu tunazojiwekea na kama hazifai basi tuziondoe, kama tunavyoshauri kwamba sheria zilizopitwa na wakati. Kwa sheria ambayo tunaona ina maslahi, isimamiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nataka kuchangia suala la lugha ya Kiswahili. Lugha ya Kiswahili original ni Tanzania. Lugha hii kwa nini isiwe ni moja ya tunu yetu? na kwa nini tusiisimamie dunia ikajua kwamba original ya lugha ya Kiswahili ni Tanzania. Hili, kwa sababu tumeridhia vitu kama hivi, kuna soko la Afrika pia linakuja, kwa nini tusijidadavue kuona kwamba lugha ya Kiswahili original yake ni hapa ili kuweza kutengeneza icon ya nchi yetu kwamba lugha ya Kiswahili inatoka hapa na tukaweza kupata mambo mengi ya ndani ya Azimio letu hili na dunia kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Bunge liridhie Azimio hili. Ahsante, nakushukuru. (Makofi)