Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. CAN.RTD Ali Khamis Masoud (4 total)

MHE. KANALI (MST.) MASOUD ALI KHAMIS : Mheshimwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nilikuwa naomba kuuliza swali la nyongeza.
Je, mabasi haya yana idadi maalum ya kupakia abiria na kama hayana idadi ni kwa nini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza tuna mabasi ya aina mbili, yale mabasi marefu zaidi na mabasi mafupi, na mabasi haya kila basi lina idadi yake.
Kwa hiyo, nimuondoe shaka Mheshimiwa Mbunge, mabasi haya yana idadi maalumu isipokuwa wakati mwingine katika vituo mabasi yakifika watu huwa wanakimbizana kuingia ndani ya mabasi.
Mheshimiwa Spika, utaratibu umewekwa kuhakikisha kuwa watu wanapanda mabasi hayo kwa kuzingatia idadi yake ili kulinda usalama wa raia katika suala zima la usafiri.
MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kuna magari 13 yanatoa huduma za doria katika maeneo hayo. Nataka nimfahamishe tu Mheshimiwa Naibu Waziri, mimi naishi karibu na kituo hiki, hata kilomita moja haitimii. Yameshatokea matukio kadhaa na Askari wanawajibika kuondoka kituoni kwenda kwenye matukio yale wanashindwa kufanya hivyo na wakati mwingine tumekuwa tukitoa msaada wa magari yetu binafsi kuwasaidia. Je, kati ya magari haya 13, kwa nini sasa gari moja lisipelekwe Kituo cha Polisi Mfenesini.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa ufahamu wangu mkataba wowote wa kuagiza vifaa vyovyote vile vya kijeshi ama vya kiraia unakuwa na makubaliano na supplier vitu vile vitawasili lini. Magari haya tunaambiwa yanakuja kwa awamu na swali lilikuwa yatawasili lini hata kama kwa awamu, je, magari yatawasili lini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimejibu katika majibu ya msingi, kwamba tutapeleka gari katika kituo cha Wilaya cha Mfenesini kwa kutambua kwamba magari haya 13 ya Mkoa na gari ambalo anatumia OCD hayakidhi haja. Nimhakikishie tu kwamba hivi sasa tuna mpango wa kupata magari 50, bahati mbaya hatuna hakika kama yapo magari ya kutosha yenye sifa za kukidhi kuwa magari ya kituo, kwa sababu mengi ya magari ambayo tunatarajia yaje sasa hivi ambayo tayari yameshafika tupo katika mkakati wa kuyatoa mengi ni malori.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ikionekana kwamba magari hayo yanakidhi vigezo vya kuweza kuhudumia Kituo cha Mfenesini, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kituo chake cha Mfenesini ni moja katika maeneo ambayo yatapata gari hizo.
MHE. KANALI MST. MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, tatizo la ombaomba lina muda mrefu na limekuwa likishughulikiwa na Serikali na likiulizwa mara kwa mara lakini bado ombaomba wanaonekana wakirudi mitaani. Je, ni hatua gani madhuhuti sasa Serikali imeziweka ili hao ombaomba wasirudi tena?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni kweli kama alivyosema Naibu Waziri, wakamatwe na washtakiwe, lakini je, hawa hawafanyi kwa makusudi, wanafanya kutokana na hali ngumu ya maisha. Je, wanapotoka huko gerezani baada ya kuwafunga na vitu vingine, hatua gani za Serikali zinachukuliwa kuwasaidia kimaisha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, hatua ambazo Serikali inazichukua ni kutoa fursa kwa wananchi wote ili waweze kuzitumia kwa ajili ya kujikomboa kiuchumi na kupambana na umaskini. Hatua hizo nimezitaja kwenye jibu la msingi kama vile kutoa fursa mbalimbali za mikopo, kuwepo kwa ardhi ya kutosha yenye rutuba na vilevile kuwa na programu nyingi za kuboresha huduma mbalimbali katika maeneo ya vijijini ili watu wasitoke vijijini wakaja mijini kufuata huduma hizo. Kwa hiyo, hiyo ni mojawapo ya hatua madhubuti lakini hii hatua ya kuwakamata na kuwarudisha makwao imeonekana ni kama vile haisaidii sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la pili, hali ya maisha ni ngumu ni kweli na ndiyo maana nimesema kwamba tutumie hizo fursa. Kwa kusema ukweli fursa ya Elimu Msingi Bila Malipo ni muhimu sana tuifuatilie vizuri ili watoto wetu wote ambao wanastahili kuwa shuleni wawe shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombaomba wengi wamekuwa wanatumia watoto ambao wanatakiwa kuwa shuleni na wanazagaa hovyo mitaani, ndiyo maana nikatoa wito kwamba Sheria ile ya Elimu na Kanuni ya Adhabu itumike kikamilifu katika kuhakikisha kwanza watoto wote warudishwe shuleni na vilevile wazazi ambao hawatekelezi wajibu wao nao vilevile wachukuliwe hatua za kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hali ngumu ya maisha, fursa ziko nyingi, naomba sana zitumike ili kujikomboa na hali ngumu ya maisha.
MHE. KANALI (MSTAAFU) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ambayo yamefafanua na itawasaidia wale ambao walikuwa na utata kuhusu jambo hili, lakini pia nina swali moja la nyongeza;

Mheshimiwa Spika, nyumba nyingi za Jeshi wanazoishi Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania kupata athari na kuharibika wakati mwingine hufika wakati hawa wakashindwa hata kuishi Askari. Je, Serikali haioni sasa umefika muda wa kuwapa uwezo wanaoishi katika nyumba hizi kuzifanyia matengenezo kwa kupitia kitengo cha ujenzi ndani ya Jeshi, kuzifanyia tadhimini na baadaye kumruhusu anayeishi kufanya matengenezo na kumrudishia hela zake.(Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, wazo hilo ni nzuri, kwamba kitengo cha ujenzi cha Jeshi kifanye tathmini na kuwaruhusu wanaoishi wazitengeneze na kisha kulipwa lakini utekelezaji wake una shida kidogo kwa sababu ya uwezo wa kulipa fedha hizo, ndiyo maana sasa hivi kupitia bajeti ya maintenance ya Ngome tunafanya ukarabati mdogo mdogo kwa maofisi na makazi ya Wanajeshi katika kambi mbalimbli lakini kasi yake ni ndogo kutokana na uwezo uliopo. Kwa hiyo, wazo hili linapokelewa na pale uwezo utakapo ruhusu basi litafanyiwa kazi. (Makofi)