Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. CAN.RTD Ali Khamis Masoud (10 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. KAN. MST. MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nakushukuru nafasi hii na mimi ya kuchangia mambo machache tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kutoa maombi tu kwa Wizara hii ya Mambo ya Nje. Kwa kipindi kifupi ambacho tunaambiwa tunataka kujiunga na mtengamano wa Afrika ya Mashariki wasi wasi wangu mkubwa bado elimu hii haijafika kwa wananchi wa Tanzania. Na kama tukienda hivi itakuwa ni kama wale abiria tunaodandia gari lilishaondoka. Tumeona uzoefu, hasa kwetu hapa Tanzania na Zanzibar zaidi, sehemu nyingi za ajira wafanyakazi wengi wanatoka Kenya. Na tatizo si kwamba nafasi hizi Watanzania hawaombi, Watanzania wanaomba nafasi, sifa za kuajiriwa hawana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokwenda kwenye mtangamano huu wa Afrika ya Mashariki wasiwasi wangu tutakuja kukuta hapa sasa Wizara zote, sehemu zote za biashara na mambo mengine yamechukuliwa na wenzetu kwa sababu tayari walishajipanga. Ninaiomba sana Wizara hii ijitahidi, kwanza ifikishe elimu, tena tujipange sasa sisi wenyewe tunaingiaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huko tunakokwenda ni kugumu kwa mawazo yangu nadhani tutakwenda kuanguka huko. Hatujajipanga, kama tuliodandia gari vile. Kwa hiyo, ninaomba sana Wizara ijitahidi kufanya uwezo wanaouweza wao walionao kuhakikisha vijana wetu nao wanakuwa na sifa; kwanza kwa kuajiriwa lakini pili tupunguze na sisi kununua bidhaa kutoka nchi za wenzetu, tujitahidi na sisi kuzalisha kupeleka kwa wenzetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la kupeleka bidhaa nje ya nchi Serikali yetu ijitahidi kuondoa vikwazo, bado corruption ipo Tanzania. Wafanyabiashara wetu wanapata vikwazo vingi, wanapotaka kupeleka bidhaaa zao nje ya nchi wanapata vikwazo tofauti na wenzetu. Bidhaa zinazokuja tunapokea vizuri tu, lakini zetu sisi tukitaka kuzipeleka humo njiani mtu anakwama mpaka anaamua kuziuza njiani. Ninaomba sana Serikali hii ijitahidi na Wizara hii isimamie biashara na sisi tuwe tunanufaika na wenzetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninataka kuzungumza kidogo. Tunapokuja hapa Bungeni kuna watu wanazungumza mambo mengi, wengine hatujasafiri, tumesafiri kidogo nje ya nchi. Sasa tunalinganisha wenzetu na sisi, lakini ninasema tulinganishe wenzetu na sisi katika baadhi ya mambo. Baadhi ya mambo Tanzania tuko mbele sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo mengine, kweli, wala tusikatae, ziko nchi kubwa zimetushinda lakini yako mambo sisi tuko mbele. Yule anayesema amekwenda Washington DC mimi pia nimeshafika huko, na si mara moja. Lakini ukisema maendeleo wanaangalia watu wanavyotembea mitaani, maendeleo wanayaona mitaani kwa zile sura za mitaa. Mimi nilishawahi kufika Washington DC nanikakuta barabara ina shimo, katikati ya barabara. Barabara yetu ya Kimara ni nzuri. Kwa hiyo, bado tuseme tu, yako mambo tumezidiwa, lakini yako mambo wenzetu bado wametushinda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kaka yangu, ndugu yangu mmoja hapa, Mheshimiwa Msigwa, sijui kama ni mchungaji maana hajawahi kuniambia na ni rafiki yangu sana lakini hajawahi kuniambia. Amesema, sitaki kulijibu lakini sijafanya kazi sana foreign, nilikuwa nayaona mambo mengine ambayo yanafuatwa, hasa suala la Mabalozi. Anapozungumza Mabalozi wanakatazwa, sijafahamu, labda atakuja kunifahamisha nikikutana naye nje. Nina vyofahamu mimi Balozi kama Balozi, hakatazwi kukutana na mtu, isipokuwa kuna taratibu lazima Balozi azifuate.
Mheshmiwa Mwenyekiti Balozi atakapo kwenda kwenye Taasisi au kuonana na mtu yoyote, lazima Ofisi ya Mambo ya Nchi za Nje ielewe. Lazima atoe taarifa na taarifa zifikishwe kule anakokwenda, sio kukutana naye tu halafu useme. Mimi sidhani kama Balozi anakatazwa kukutana na mtu, tunakutana na watu binafisi hiki kitakuwa chama?
Mheshimwa Mwenyekiti, utaratibu, tunachozungumza utaratibu ukifuatwa, sidhani kama Balozi anakatazwa kukutana na mtu. Naomba tu wanapotaka kukutana na watu kama hao, si wafuate utaratibu tu! Wasiogope kwa sababu utaratibu upo, umepangwa na wautekeleze, hakuna haja ya kuleta mambo mengine hapa ambayo kwa kweli ni kupotosha, si kweli! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema tunapokuja Bungeni, hasa Bunge letu la Tanzania hili, tukitaka liwe na heshima, sisi wote kwanza tuheshimiane. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS - MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA VIWANDA, BIASHARA NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuhitimisha taarifa yetu ya Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira kama tulivyoiwasilisha asubuhi ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa yetu imechangiwa na watu takribani 15, pia na Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na Naibu Waziri. Nawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge kwa kutoa maoni yao na ushauri. Tunayathamini sana maoni yao na ushauri huo na ninaiomba Serikali, maoni na mapendekezo yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge, yachukuliwe na kufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana Mawaziri waliochangia, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ofisi Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira. Wizara ya hii ya Viwanda na BIashara ndio imebeba mwelekezo wa nchi kwa sasa, katika kuipeleka azima ya uchumi wa kati kupitia viwanda. Hivyo ni vyema na tuendelee kuiomba Serikali kuiwekea umuhimu na mkazo wa hali juu katika kuwapatia fedha za maendeleo ili waweze kuifikia azima hiyo tuliyoikusudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza azima hii na kufikia mahali tulipokusudia yapo mambo ya msingi ya muhimu yanatakiwa yafanywe na kuwajibishwa na wananchi wote wa Tanzania. Moja ambao lazima niwepo katika nchi nchi lazima kuwe na ulinzi au amani na utulivu ndani ya Taifa letu. Wapo Waheshimiwa Wabunge ambao walichangia hapa na kusema kwamba hata utawala bora haupo. Siamini, lakini nasema utawala bora kama ungekuwa haupo tusingeona wimbi kubwa la wawekezaji wanaoingia nchi hivi sasa kwa ajili ya kuja kuwekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza azima hiyo, yapo mambo ambayo sisi kama Kamati tuliyazungumza na kuyatolea ushauri kwa Serikali. Yapo mambo tuliyafanyia kazi katika Kamati hasa katika suala la ujenzi wa jengo la TBS. Ujenzi wa jengo la TBS katika kutembelea Kamati ilishuhudia na kuingia wasiwasi na thamani kubwa ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa jengo lile. Hivyo ilishauri Wizara kuhakikisha wanafanya tathmini au kuweka Kamati Maalum itakayofuatilia na kuhakikisha waone uhalali au wafanye uhakiki wa uhakika wa kuhakikisha kwamba jengo lile lina thamani ya kiasi gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe nizungumze suala la Liganga na Mchuchuma, limezungumzwa na Wabunge wengi. Sisi kama Kamati tumeliona, tumelijadili, tumelizungumza na tumelishauri sana Serikali kuhusu suala hili. Kweli suala hili ni la muda mrefu, lakini kwa sasa lazima tukubali kwamba Serikali baada ya kuona utata mkubwa katika mikataba ya jambo hili, waliona ni vyema sasa waanze kupitia tena mikataba na kufanya tathmini ya kuhakikisha tunakwenda kwenye mkataba ukao tusaidia kama Taifa. Kwa hiyo tunaiomba Serikali sasa ihakikishe mapitio haya yanafanyika haraka ili mradi huu uweze kufanya kazi na ulete tija kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la matrekta ya URSUS, Kamati ililiona hili na ilitoa mawazo yake na ushauri kwa Serikali kwamba kwa sasa inaonekana kampuni hiyo ya Poland imeshindwa kutekeleza wajibu wake na kutekeleza mkataba kama tulivyokubaliana. Hivyo tunaomba sasa Serikali ilichukulie uzito wake na kwa sababu Serikali imeshatoa fedha nyingi katika mradi huu, ni vizuri sasa Serikali ikalifualia kwa karibu na kwa haraka ili fedha yetu hiyo iweze kuleta tija na kutuletea maendeleo mengine hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la bandari la kuchelewesha mizigo nalo lilitufikia katika Kamati yetu kwa wadau. Wadau wengi walipokuja katika Kamati walilalamikia suala la uchelewashaji wa mzigo. Ni kweli suala hili limezungumza katika Kamati ya Miundombinu, lakini sisi kama Kamati ya Viwanda na Biashara, biashara yoyote nayo inahusisha bandari. Huwezi kufanya biashara kwa ufanisi kama huna bandari yenye uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi katika ripoti tuliyotoa leo tuliweza kuishauri Serikali kuhakikisha kwamba wale wadau wanaofanya kazi bandarini hatuna uhakika ni nani anayechelewesha mizigo inaweza ikawa TASAC Inawezekana wengine, lakini ushauri wa Kamati unasema TASAC, TRA,TPA na wengine wadau wote wanaoshughulika na mizigo bandarini wakae pamoja watafakari na kuona kwa nini mzigo inachelewesha hapa bandari na wafikie muafaka wa kutatua tatizo hilo kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kero za wafanyabiasha ni nyingi na nyingine tumetoa hapa vizuri na tumezielezea. Suala la VAT refund, suala la 15% ya sukari ya viwandani. Hili kwa kweli ni tatizo kubwa, sisi tunachokiomba sasa Serikali ilichukulie kwa uzito wake na kuhakikisha wanawapa faraja wafanyabiasha wetu waweze kutumia fedha zao zile kwa ajili ya maendeleo zaidi. Viwanda vingi vinapata shida ya kuendesha biashara zao kwa sababu fedha nyingi zipo Serikalini. Tunaomba sana Serikali ilichukulie hili na kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wetu wanapata faraja katika jambao hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza majukumu yetu kama Wizara tunashukuru wenzetu wa Tan Trade kwa kweli kuna mabadiliko makubwa ya sasa hivi yanaonekana yanayaanza kutekelezwa. Sisi tunasema tunawapongeza sana Tan Trade kwa kuunda Kitengo cha Intelejensia ya kutafuta biashara na mazao mbalimbali na kuhakikisha tunatangaza biashara zetu ili kusudi tupate masoko katika kutekeleza azima hiyo tunayokusudia ya viwanda katika uchumi wakati. Naomba sana tunapojenga viwanda katika nchi vitu hivi viwili lazima viende sambamba. Viwanda viende na masoko pia tukijenga viwanda bila kupata masoko havitaleta tija wala havitatusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaomba sana wakati wowote Tan Trade wahakikishe bidhaa zote zinazozalishwa ndani ya nchi zinapata masoko na zinauzwa ndani na nje ya nchi. Viko viwanda sasa hivi vimetia malalamiko makubwa sana ya bidhaa nyingi sana zinazozalisha ambazo zipo ndani ya magodauni na hazina wateja. Hivyo kiwanda kama hicho si vizuri kuwa nacho kwa sababu hakitatupa faida kubwa. Naomba sana wenzetu wa Tan Trade katika hili wahakikishe wanafanya kazi ya ziada ya kuhakikisha masoko ya bidhaa zetu zote zinapatikana ili waweze kuuza huko nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo lilizungumzwa hapa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia tu Mheshimiwa.

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS - MAKAMU MWENYEKITI WA KUDUMU WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA VIWANDA, BIASHARA NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, naomba Waheshimiwa Wabunge wakubali taarifa ya Kamati na ushauri, iwe kama azimio la Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. HASNA S.K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Napenda kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia na kunipa pumzi ya kusimama hapa pia niwashukuru wapigakura wa Jimbo langu la Mfenesini kwa kunipa nafasi hii adhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ulinzi kama lilivyo jina lake, ina majukumu ya kuhakikisha usalama wa Taifa letu kwa mipaka yake yote ya angani na ardhini. Wizara hii kwa kipindi kirefu sana, kwa uzoefu nilionao imekuwa na matatizo mengi mno na mengi yanasababishwa na ukosefu wa fedha ya kutosha ya kuendesha vifaa pamoja na huduma za wanajeshi.
Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia ulinzi kama ulinzi, lazima vitu viwili vyote vihusihwe kwa pamoja, ukihudumia askari/wapiganaji, basi lazima pia uhakikishe unahudumia vifaa vyao pia wanavyovitumia kufanyia kazi za ulinzi. Usiweke vipaumbele kwa watu halafu vifaa ukavidharau, uzoefu mkubwa nilionao katika vifaa vyetu vya kijeshi vya Tanzania, tuna vifaa vizuri vingi tu, vya kisasa kabisa, lakini bado hatujavipa uzito wa kuvihudumia ipasavyo.
Mheshimiwa Spika, vifaa vya nchi za wenzetu, nchi nyingi duniani, vifaa vyao vya kijeshi vinachakaa, vinaharibika kwa sababu ya kutumika sana kwa mazoezi na mambo kadhaa, lakini vifaa vyetu Tanzania vingi vinaharibika kwa kukaa bila kufanya kazi. Vifaa hivi ni kama binadamu, binadamu ukiwa unalala tu na kuamka, kula na kulala, siku utakayotoka pale baada ya miezi mitatu ukiambiwa ukimbie kilometa moja tu huwezi kuondoka na vifaa vyote vya kijeshi ndiyo vinatakiwa viwe katika mfumo huo, lazima viwe vinatumika, vinafanya kazi, magari wanaya-run, ndege zinarushwa kwa mazoezi na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukitaka kurusha ndege utaambiwa mafuta hakuna, ukitaka kufanya hiki utaambiwa mafuta hakuna. Baada ya muda fulani, usije ukategemea vimetokea vita una vifaa vya kutosha, unavyo vifaa vya kutosha lakini havina uwezo mkubwa wa kufanya kazi unayoitegemea. Niiombe sana Serikali iwe inatoa kipaumbele cha hali ya juu katika kuhakikisha kwamba vifaa vyetu vya kijeshi vinatunzwa ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine nizungumzie suala lililozungumzwa sana na baadhi ya Waheshimiwa hapa Bungeni, hasa la Jeshi la Akiba. Ni kweli wanajeshi wastaafu nao ni moja ya wanajeshi wanaotegemewa endapo ikitokea dharura ya janga la vita ndani ya nchi. Wengi walishaomba kuongezewa pensheni, lakini ninaomba pia Serikali iangalie utaratibu mpya wa kuhakikisha wananjeshi hawa sasa wanawalipa kila mwezi badala ya miezi mitatu mitatu, siyo rahisi, wengi tunaishi kwa kubahatisha kule mitaani, kukopa na kadhalika, siyo rahisi mtu leo akaenda kukopa halafu akamlipe mfanyabiashara baada ya miezi mitatu! Ninaomba sana Serikali iliangalie suala hili na ilipe kipaumbele chake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watu wengi wamekuwa wakisimama hapa, wanapenda sana, hawafurahi bila kuizungumza Zanzibar. Mimi niseme tu, wanajeshi kama wanajeshi, anaposimama Mheshimiwa Mbunge hapa Bungeni halafu akasema vifaru vinatembea, hivi anakijua kifaru. Vifaru vinatembea mjini, wanajeshi wanafanya mazoezi, wanajeshi wakafanye mazoezi mitaani! Mtu anapokuja hapa azungumze kitu halisi, azungumze kitu anachokifahamu. Najua huyu Mheshimiwa hakijui kifaru haijui APC, hajui chochote, ndiyo maana anazungumza kifaru kinatembea mtaani, siyo kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapozungumza hapa tusipotoshe wananchi, tusiwapotoshe wananchi tukawaambia kwamba majeshi sasa yameanza kuingia mitaani. Mimi ninachofahamu, nilikuwa mwanajeshi pia, ninachokifahamu Jeshi linaweza kuingia mtaani kwa kitu kimoja tu, kumetokea labda kuna kitu kimeonekana kimeingizwa kwenye mtaa na Jeshi likafanya quadrant search, basi! Lakini Jeshi kama Jeshi, mazoezi yote ya Jeshi yanafanywa porini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, unapotuambia vifaru vimeingia mitaani, binafsi sikuelewi na najua na wewe pia hujui kitu ndiyo maana ukasema hivyo. Lazima tukubali Jeshi letu bado linafanya kazi kwa nidhamu na kwa kulingana na sheria na Katiba ya nchi. Tunachotakiwa kufanya hapa tuhakikishe Jeshi letu linahudumiwa, linapatiwa uwezo wa kutosha wa kununua vifaa vyao kwa wakati wowote wawe tayari endapo tumevamiwa ama limetokea janga lolote wawe tayari na uwezo wa kufanya lile jukumu walilopewa na Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sana na napenda kusema wapo Waheshimiwa wanasimama hapa Bungeni, mishipa kabisa inawatoka, anakwambia kule Zanzibar uchaguzi haukuwa, mtu kazungumza lugha zote hapa leo, nimeshangaa anapozungumza mapinduzi, huyu katoka wapi, katoka shimoni leo, mapinduzi hayajui? Huyu naomba akatafsiri nini maana ya mapinduzi halafu aje atuambie, siyo vizuri watu wazima wenye heshima, Wabunge, kuja ndani ya Bunge hapa mkatoa lugha za ajabu, tabia hii siipendi, naomba irekebishwe kabisa. Watu tuje hapa tufanye kilichotuleta kulisaidia Taifa letu kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mbunge mmoja alisimama hapa akasema ile kesi kule Zanzibar haijaisha bwana, wasifikiri imekwisha. Mimi namwambia hivi, kesi ya Zanzibar tuliimaliza Januari 12, 1964. Kama kuna mtu hapa au taasisi yoyote leo inayoweza kumuondoa Dkt. Shein, basi ifanye lakini nakwambia Dkt. Shein atakuwa Rais wa Zanzibar kwa miaka mitano na hakuna mtu wa kumuondoa.
Mheshimiwa Spika, mtu anayesema yeye Mzanzibari mimi ninamwambia nimezaliwa. Sisi Wazanzibar tunasema hivi, Dkt. Shein hakuna atakayemuondoa na huyo anayesema kuna kesi na alete na sisi tupo tayari kufa na nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, najua watu wengine yanawaudhi kwa sababu hawana uchungu na Zanzibar. Mtu yeyote mwenye uchungu na Zanzibar na anayeijua Zanzibar, maneno mengine yanayosemwa hapa yanauma sana. Nataka niseme, wakati tukiwa nje hatujawa Wabunge wengine hapa, tulipokuwa tunaona vikao vya Bunge vinavyopita, mambo yanayofanyika humu ndani, watu wengi kule nje yanawakera sana, yapo mambo yanawakera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilipofika ndani ya Bunge tukajikuta tupo watu wengi wapya humu ndani ya Bunge nikafikiri labda safari hii tutakuwa salama, lakini kumbe bado tunarudi kulekule. Niseme tu na niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, yaliyopita tumeshamaliza, anayesema kwamba ule siyo uchaguzi…
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila mpangilio)
SPIKA: Utulivu Bungeni! Mheshimiwa nakulinda endelea!
MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Spika, anayesema ule uchaguzi si halali sisi tunasema ni halali, anayesema Rais wa Zanzibar siyo halali namwambia atakaa pale kwa miaka mitano na hakuna wa kumwondoa. Kilichotuleta hapa tukifanye kwa ajili ya Taifa lakini malumbano mengine yasiyokuwa na maana tusiyalete hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, najua watu wanachukia sana…
SPIKA: Jamani, Kanali anaongea halafu raia mnapigapiga kelele! Huyu ni Kanali wa Jeshi. Endelea Mheshimiwa Kanali! (Kicheko)
MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Spika, ninayoyasema kuna watu yanawakera, lakini tukubali tu kwamba sote tunaipenda nchi yetu, tuna wajibu wa kuhakikisha usalama wa nchi yetu unadumishwa. Niwaombe wenzangu Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania bado muendelee kudumisha nidhamu iliyokuwepo Jeshini, tutekeleze majukumu yetu kwa ufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na mimi naunga mkono hoja.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. KANALI (MST.) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi ya kuchangia machache katika Kamati yetu hii. Mimi mwenyewe ni Mjumbe wa Kamati hii ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Mapendekezo mengi tumeyatoa, lakini yapo mambo yanatukwamisha sisi wenyewe kwa kutokuwa watekelezaji wazuri wa majukumu yetu. Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ambalo tumeliona katika magereza yetu, mimi mwenyewe nilipata nafasi ya kutembelea magereza mengi hapa nchini lakini ninayoyakuta huko nashangaa kwa nini tunashindwa kuyasimamia. Wabunge wengi wanasimama hapa wanasema magereza wana maeneo makubwa ya kilimo na magereza wanaweza wakajiwezesha. Wanayo maeneo ya kilimo, tunawasaidiaje kuweza kuyalima hayo maeneo? Hilo ndiyo tatizo. Mheshimiwa Mwenyekiti, Gereza la Songwe mfano, wanasema wao wanaomba matrekta kwa ajili ya kufanyia kazi na mimi kwa mara ya kwanza toka nimezaliwa sijawahi kumuona mfungwa anaomba pembejeo, mfungwa analalamika hatuletewi pembejeo, hatuletewi matrekta, kumbe watu wanataka kufanyakazi lakini sisi wenyewe tunashindwa kuwawezesha. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, wanakwambia wanadai pesa nyingi ambazo hata hayo matrekta wangeweza kujinunulia, wanajilisha wenyewe, wanajitosheleza kwa chakula na wanalisha na magereza nyingine lakini bado tunashindwa kuwawezesha kuwapa vifaa vya kuongeza kilimo. Mimi nilikuwa naomba sana tuliangalie hili na ikiwezekana tuwapatie uwezo wa kukopeshwa hayo matrekta kama upo uwezo ili wafanyekazi watuzalishie na inawezekana wakaweza kulisha magereza mengi zaidi hapa nchini. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine nilikuta pia gereza moja hapa Morogoro; ni gereza linazalisha maziwa kwa wingi tu, lakini wanakwambia gari la kupelekea maziwa sokoni hawana. Sasa tufanyeje tuwaache wenyewe wanywe maziwa au tufanye nini? Lakini cha msingi kama kweli wanazalisha, wana uwezo mkubwa kwa nini tusiwapatie hata gari la kupeleka maziwa sokoni? Halafu ukiwauliza wanakwambia kwenye akaunti yao wanazo milioni 40; kwa nini hamnunui wanasema aah, utaratibu hauturuhusu. (Makofi/Kicheko) Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi sielewi mtu anakuzalishia, anakupatia pesa, lakini wewe kumuwezesha ili azidishe kuzalisha huwezi, mambo mengine haya hayataki kusoma shule wala wapi. Tukae kitako tu tuamue ili wenzetu hawa wapate kuzalisha na waweze kusaidia magereza mengine. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka niliongezee hapa kuna hawa wafungwa waliohukumiwa kunyongwa; wameshahukumiwa wale wanasema, mimi nimeshawatembelea nimezungumza nao na ni hatari kuzungumza na watu wale, lakini tumezungumza nao maana wamekaa mia mbili, mia tatu kama hivi wakikutizama unaweza ukachanganyikiwa. Wanasema haki yetu tuliyoipata mahakamani ni kunyongwa, sasa kwa nini hatunyongwi? Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunaona maana kuna viongozi wengine hapa tunatunga sheria, tunatakiwa tuzitekeleze lakini tunaogopa dhambi. Sasa kama lengo ni kuogopa dhambi kwamba hatuwezi kunyonga basi sheria ibadilishwe, lakini kama sheria imewekwa inatakiwa itekelezwe basi kila mtu atekeleze. Tunahimiza kila siku kila mtu atekeleze wajibu wake, kama hukumu ya kunyongwa imetolewa na hatuwezi kunyonga tubadili sheria au kama tunaweza kunyonga basi tunyonge maana wale wanadai haki yao na haki yao ni kunyongwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nilitaka kulizungumza hapa lililonisikitisha sana zaidi kule Mbeya; tumekwenda tunaambiwa kule hakuna gari la Zimamoto lakini tunaambiwa ikitokea tatizo la moto gari lazima litokee uwanja wa ndege. Sasa hebu tujiulizeni Waheshimiwa Wabunge hapa gari ya uwanja wa ndege; ndege bado dakika kumi ndege itatua na moto unawaka, tunafanya nini? Lakini la kushangaza zaidi tunaambiwa gari moja ya zimamoto limetolewa Mbeya kupelekwa Dar es Salaam kwa matengenezo. Mimi huwa najiuliza gari hili hivi fundi hawezi kupelekwa Mbeya? (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata kama lina mambo ya kiufundi, huyo fundi hawezi kwenda Mbeya akalicheki gari na baadae akarudi Dar es Salaam akachukua spea; gharama zake hapa zinakuwaje? Gharama za kupeleka gari Dar es Salaam na gharama ya kumpeleka fundi ipi ndogo? Lazima tukae wakati mwingine tuangalie haya mambo na pia tuyachukulie hatua zinazofaa. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumza haraka ni huu msongamano unaozungumzwa wa magereza. Msongamano huu unasababishwa na mambo mengi likiwemo pia baadhi ya Wilaya zetu hapa nchini kukosa magereza kabisa. Niombe sasa tujitahidi hasa kule Chunya tupate magereza ili wafungwa sasa waweze kuwekwa kule na kupunguza msongamano kule Mbeya. Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba pia wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Ndani katika kuyafanyia kazi mambo yenu haya muwape uwezo pia ndugu zetu wa polisi wa kule Chunya. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante ninaunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. KAN. MST. MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia kwa dakika hizi chache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Makatibu na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya. Muendelee kushika uzi huo huo wa utekelezaji wa majukumu yenu kama mlivyopangiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni dakika tano, naomba nichangie kitu kimoja, Wizara hii ni nyeti sana, ni Wizara ambayo inaonesha uso wetu nje ya nchi. Ikiwa leo Bunge linaamua kuiwekea siku moja ya kuchangia ni dhahiri kwamba Wabunge wengi hawataweza kutoa mchango wao wa kutosha wa kuweza kuboresha ofisi zetu kwa Watendaji walioko nje ya nchi. (Makofi)

Hivyo, naiomba ofisi hii iendelee kufikiria zaidi jinsi ya kuipatia nafasi Wizara hii ipate michango mingi ili iweze kuboresha zaidi na kuonesha sura nzuri nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mambo muhimu yanayotakiwa kufanywa nje ya nchi kwa sasa ni pamoja na kuboresha majengo yetu. Majengo mengi ya Wizara hii nje ya nchi hayapo katika hali nzuri. Kweli tuna uhaba wa fedha, lakini bado utumike utaratibu mwingine wowote utakaowezekana kuhakikisha tunaonesha sura nzuri nje ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale ambao hawajafika, sisi wengine tumeona, nchi mfano ya Msumbiji, hali ya Msumbiji siyo nzuri. Ukiangalia na sisi tabia hii tuliyoipata sijui tumerithi wapi? Tabia ya kwamba mtu nyumba yako ikichakaa unahama, ni tabia gani? Nyumba ikichakaa hurekebishwa na baadaye uendelee kuishi ndani ya nyumba hiyo. Balozi amehama kwa kuwa nyumba imechakaa, amepangishiwa nje. Tunapoteza fedha nyingi sana kwa kupangisha nyumba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi naishukuru Wizara hii kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kutumia fedha katika kipindi hiki kifupi kwa ajili ya pango la Balozi kutengeneza ile nyumba ya Balozi kule Msumbiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado naiomba Serikali na Wizara hii waendelee kuweka kipaumbele kuhakikisha jengo la ghorofa tisa nchini Msumbiji linamalizika haraka kwa kuwa hii ni njia moja itakayotukomboa na kuhakikisha kwamba tunafanya kazi nzuri, tunaboresha nyumba zetu na wafanyakazi wetu wanaishi katika mazingira mazuri. Ni kweli, nchi nyingi tulizo na Ubalozi hatuna majengo mazuri, lakini kama Wizara na Serikali itatoa kipaumbele kutoa fedha za kutosha, nina uhakika Watendaji katika Wizara hii wanaweza kufanya kazi nzuri sana na ya kupigiwa mfano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Naomba niachie nafasi wengine.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018
MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi kwa dakika hizi chache niweze kuchangia machache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapokuwa na safari ya maendeleo au yako binafsi na ukajiwekea malengo, ukichelewa kufika kwenye malengo uliyokusudia hutakiwi kwa mtu mwenye busara kutoa lawama, kutoa ukali au kukaripia watu. Mtu mwenye busara atakaa kitako kufikiria kitu gani kilimkwamisha asifikie yale malengo aliyojipangia na baadaye kutatua ili safari yake atakapoianza tena aweze kufika alikokusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano, imejikita kabisa katika kuleta maendeleo ya viwanda ili kwenda sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa, lakini safari hii kila taasisi imekabidhiwa jukumu lake. Kidogo nitaizungumzia SIDO ambayo kwa hakika nimeiona kwa macho yangu na kuwasikia watendaji wa sehemu hii wakizungumza mashaka na matatizo yanayowakumba. SIDO imepewa majukumu ya kukuza wajasiriamali, kutoa elimu, kutoa ushauri na mambo mengine kadhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majukumu yote waliyopewa, jukumu kubwa ni elimu inayotakiwa iwafikie wajasiriamali ili waweze kuzalisha kwa tija. Uwezo walionao SIDO hivi sasa hauwezi kabisa ukafanikisha malengo haya waliyopewa, hivyo niiombe sana Serikali katika jambo hili wawaangalie wenzetu wa SIDO kuwawezesha kwanza wapate nyenzo zitakazowasaidia lakini pia fedha ya kutosha itakayowafikisha walipokusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la viwanda vilivyobinafsishwa, limezungumzwa sana hapa na sisi katika kamati tumelizungumza sana hili. Nafikiri bado hatujawa serious katika hili, wapo watu wamepewa viwanda na hiki ni kipindi kirefu karibu miaka ishirini na, wamepewa mikataba hawajaitekeleza bado tunawaangalia tu, niiombe Serikali muda umefika sasa waliopewa viwanda wakavichukulia mikopo, waliopewa viwanda wakauza mashine sasa ni wakati wao wa kuanza kushughulikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo tumelijadili kidogo katika Kamati ni mkakati wa Serikali wa kuhakikisha sasa mafuta ya kula yanazalishwa nchini. Mikakati hi tumeiona kwa maandishi na ina lengo zuri, lakini mote nilimosoma, labda sikusoma vizuri, lakini mote nilimosoma sikuuona mkakati wowote ule ambao unazungumzia wazalishaji wa alizeti hapa nchini. Mkakati unazungumzia viwanda lakini haujalenga malengo gani yatafanywa, kipi kitafanywa, watasaidiwa nini wazalishaji ili zao hili lilimwe kwa wingi na viwanda vyetu vipate malighafi ya kutosha itakayowawezesha sasa kufikia lengo tulilolikusudia la Taifa la kuchakata mafuta hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nimekusudia kulizungumza kidogo, ni wafanyabiashara wa viwanda wanaosafirisha bidhaa zao hapa nchini kutoka Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Nichukue nafasi hii kwanza kuwashukuru wenzetu wa TFDA kwa mashirikiano mazuri wanayoyafanya kati yao na wenzao wa ZFDA. Bado nataka kuzungumzia tatizo linalojitokeza hasa kwa kiwanda chetu kimoja kule Zanzibar ambacho kinafungasha kahawa, chai, sukari kwa ajili ya Mashirika ya Ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaposafirisha mizigo kuja nayo Tanzania Bara wanapofika bandarini, custom wanasema hiyo ZFDA hawaifahamu, lakini mashirikiano kati ya ZFDA na TFDA, ni mazuri. Wanachofanyiwa hawa sasa wanatakiwa baada ya kufika na bidhaa bandarini waende TFDA wakachukue barua ya kuwatambua, wakishachukua barua wapeleke bandarini, baada ya kutoka bandarini ndio wanakwenda kufanya shughuli nyingine za kuhakikisha mzigo ule unafikishwa unakokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa la kushangaza zaidi watu hao hao kiwanda hicho hicho bidhaa hiyo hiyo, watakapopeleka tena mara ya pili wanatakiwa tena waende TFDA wakachukue barua ya uhakiki wa kuhakikisha kwamba hii ZFDA inatambuliwa. Niiombe sana Serikali katika jambo hili tuondoshe vikwazo hivi ili wenzetu wanaosafirisha bidhaa kutoka Tanzania Visiwani wanapozileta Tanzania Bara kusiwe na vikwazo vya kuwasumbua. (Makofi)
TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE KUHUSU SHAURI LA KUDHARAU NA KUDHALILISHA BUNGE LINALOMKABILI MHE. HALIMA JAMES MDEE (MB)
MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuongea na leo nitaongea kwa masikitiko makubwa sana. Masikitiko yangu ni kwamba katika Bunge hili wengine tulioingia kwa mara ya kwanza tulitegemea tujifunze sana tabia za wenzetu tuliowakuta lakini bahati mbaya tumekuta wengine ambao idhamu zao mimi mwenyewe sizifahamu.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wananong’ona hapa kwamba umepita Jeshini, ni kweli. Nami nasema unapoishi katika dunia hii mambo yako yote ukiyafanya kwa nidhamu utafanikiwa lakini kama ukijihisi wewe ni mwamba katika dunia na kuwa unaamua jambo unalolitaka, siku zote utapata matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huyu tunayemzungumzia leo mimi mwenyewe nashuhudia hapa siyo mara ya kwanza hii, amekuwa na tabia hizo hizo na hataki kujirekebisha. Mimi naendelea kupata wasiwasi mmoja, mwenzetu kwa jinsia nayomfahamu hii, mwanamke, ndani ya Bunge kama hili la heshima yupo hivi, huko nje sijui yukoje? (Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote haya…

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba kuongea, haiwezekani.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naomba mkae.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MBUNGE FULANI: Ametumia lugha ya kudhalilisha.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naomba mkae.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naomba mkae.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Lema, Mheshimiwa Mbatia, Mheshimiwa Joseph Mbilinyi naomba mkae. Naomba ukae Mheshimiwa Lema nimeshakutaja mara mbili, naomba ukae. Mheshimiwa Masoud, endelea.

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, nashangaa sana watu wakichukia kwa kauli hii kwa sababu mimi nilivyolelewa na navyofahamu mama ni mlezi, ni mtu anayetakiwa kulea na awe na nidhamu, ili watoto anaowalea wawe na nidhamu lazima yeye kwanza awe na nidhamu. Leo nashangaa watu wanasikitika, mimi nasema usipokuwa na nidhamu huwezi kuheshimiwa na wewe kama utaishi hivyo unavyojiona katika dunia hii, maisha yote utapata matatizo na matatizo yanatokea kwa sababu mtu hajielewi.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. ESTHER A. BULAYA: Mama Sitta yuko wapi?

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwakagenda, nimekataza taarifa na nadhani wewe ni shahidi, Mheshimiwa Masoud endelea.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nasema hili Bunge lina heshima yake iliyopewa na Taifa na sisi wenyewe tunatakiwa tujiheshimu, liwe na heshima na sisi lazima tujiheshimu.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Kuhusu utaratibu.

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Tusipojiheshimu hatuwezi kuheshimiwa. Kama tunaambiwa dhaifu mtu mwingine anasimama anasema…

KUHUSU UTARATIBU

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwakagenda, Kanuni iliyovunjwa?

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, Kanuni ya 68(7) imevunjwa.

NAIBU SPIKA: Kanuni ya 68(7) inazungumzia mwongozo, umeomba kuhusu utaratibu, Mheshimiwa Masoud, endelea. (Makofi)

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu.

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, bado…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbatia, Kanuni iliyovunjwa.

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, natumia Kanuni ya 64(1)(f) na (g), naomba kuinukuu, inasema: “Bila ya kuathiri masharti ya Ibara ya 100 ya Katiba yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo na majadiliano katika Bunge, Mbunge:-

(f) hatamsema vibaya au kutoa lugha ya matusi kwa Mbunge au mtu mwingine yeyote;

(g) hatatumia lugha ya kuudhi au inayodhalilisha watu wengine”. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimwombe tu Mbunge anayechangia aondoe yale maneno ambayo yalimdhalilisha wakati anachangia wanawake kwamba yanakuwaje, mambo ya ki-gender hapa hayapo. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Mbatia amesimama kwa mujibu wa Kanuni ya 64(2) akizungumza kuhusu utaratibu. Anasema Kanuni ya 64 imevunjwa kwa sababu Mheshimiwa Kanali Masoud ametoa maneno ambayo yanaudhi ama kudhalilisha mtu mwingine.

Waheshimiwa Wabunge, kwa mujibu wa Kanuni zetu hizi, maneno ambayo mimi nimeyasikia ambayo yameonyesha kuudhi baadhi ya watu nadhani ni maneno ya kuashiria tabia huko nje iko vipi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Kanali Masoud maneno hayo uyafute ili yasiingie kwenye Taarifa Rasmi za Bunge. (Makofi)

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Na mimi nafuta maneno hayo lakini message sent. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Hata hayo ya message sent hayaingii kwenye Taarifa Rasmi za Bunge. (Makofi)

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeyafuta na hayo.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, tunamjua vizuri yule.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Heche umeruhusiwa na nani kuzungumza kwa kuwasha microphone? Mheshimiwa Masoud malizia mchango wako.

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru lakini narudia tu kusema kwamba kama mtu anafikiria kwamba kweli sisi tupo dhaifu basi ni yeye mwenyewe yupo dhaifu lakini siyo Bunge. Nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia kidogo Wizara hii ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa azma yake nzuri ya kutaka kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati lakini pia Tanzania ya viwanda. Kila mtu ana mtazamo wake katika jambo hili. Mimi naona tatizo tulilonalo hapa Tanzania bado Waziri hajawa na usimamizi mzuri, yeye ni baba, kama ni baba anatakiwa alee wafanyabiashara na wenye viwanda wote. Anapopelekewa matatizo ni wajibu wake kuhakikisha anayashughulikia haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siamini na wala siwezi kukubali kama kuna mtu anataka kuwekeza nchini aje awekeze bila kufanya utafiti kwanza. Kwa hiyo, cha kwanza anachokuja kufanya ni kuhakikisha yale mazingira wezeshi yaliyowekwa na Serikali kama ni mazuri lakini ataangalia wale walioanzisha viwanda wana changamoto gani ndipo hapo atakapoamua sasa na yeye aje awekeze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi hapa Tanzania tuna changamoto nyingi za viwanda na inaweza ikachukua miaka, Kamati itapita leo itaikuta, itapita mwakani itaikuta, itapita mwaka miwngine itaikuta bado haijatatuliwa. Mimi nashauri sana Serikali mara nyingi wawe karibu na wafanyabiashara na wenye viwanda kuwasikiliza. Kuwasikiliza tu haitoshi, wawatatulie na matatizo yao pale yanapotokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumeshuhudia mengi katika viwanda lakini mimi nataka niseme jambo moja ambalo linanisikitisha tuna viwanda vingi hapa nchini tayari vina uwezo wa kuzalisha mali inayotosheleza mahitaji ya nchi lakini bado bidhaa zile zinaagizwa kutoka nje. Mimi nafikiri kama tunataka kweli tuwe na viwanda basi tuamue kuwalinda wale ambao tayari wana uwezo wa kuzalisha mali ya kutosheleza nchi hii. Mfano mkubwa ni viwanda vya plastiki, nondo na viwanda vingine. Kuna mwekezaji amewekeza kiwanda hapa cha nondo ametumia dola milioni 30, kiwanda kina uwezo wa kuzalisha metric tone 200,000 lakini leo anazalisha metric tone 15,000 tunategemea nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapotaka kukuza uchumi cha kwanza tuwalinde wenye viwanda ili kuongeza ajira kwa watu wetu. Tunaponunua bidhaa kutoka nje maana yake tunaongeza ajira kwa wenzetu wenye viwanda vya kule nje. Kwa hiyo, kama tunataka kukuza biashara kwanza tukuze viwanda, hiyo itatusaidia kuongeza wafanyakazi na ajira kwa vijana wetu. Imefika mahali sasa lazima tuamue, tusiogope. Yapo mambo tunaogopa kutatua lakini yapo mambo tunaweza tukayaamua tu na kuaona kama yataleta tija ama la. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetoa mfano huo mmoja wa kiwanda cha nondo lakini bado tuna viwanda vingine vinazalisha mali pia, saruji, mabati na vinginevyo, bado hatujaweka mkakati wa kuhakikisha tunapunguza uingizaji wa bidhaa hizo hapa nchini. Naiomba sana Wizara wahakikishe kama bidhaa zinazoagizwa zipo hapa nchini wapunguze uingizaji wa bidhaa hizo kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wengi wamezungumza lakini na mimi nataka niseme moja, TIRDO, SIDO, CAMARTEC na wengine tunawategemea ndio wazalishaji watakaowawezesha wajasiriamali wadogowadogo kule vijijini. Tunasema wao kazi yao ni kukuza teknolojia ili watu kule vijijini waweze kujitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumeshuhudia kabisa wenzetu hawa mashine wanazofanyia ni za toka mimi sijamaliza shule, tukienda na mfumo huo hatutafika. Tunachokiomba Serikali iweke mkazo wa kuongeza bajeti katika Wizara hii hasa katika bajeti ya maendeleo, kuhakikisha wanapewa teknolojia mpya, mashine mpya na wale wakufunzi wanapata mafunzo ya kisasa ili watu waweze kujiletea maendeleo kwa haraka zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata bidhaa zetu kwa mfano, tumekuta trekta pale Arusha, lakini naamini trekta lile pengine limetengenezwa siyo chini ya miezi nane au zaidi, moja tu. Sasa lile si kwamba watu hawana uwezo wa kutengeneza uwezo wanao lakini teknolojia za mashine zetu bado ni mno. Kwa hiyo, tujaribu, yako mambo tunaweza kuyafanya wenyewe na mengine tunaweza tukawatumia wataalam kutoka nje. Naomba sana Serikali ijitahidi katika hili lakini ifike mahali tuamue tufikie mahali pazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninataka kulizungumza ni hii ETS, kila mtu ameizungumzia. Ukiona Mheshimiwa Waziri tunaizungumzia sana maana yake inatuumiza. Inatuumiza kwa sababu mimi siamini, sasa hivi Kiwanda cha Bia TBL kwa hesabu zao za haraka kwa mwaka mmoja watalipa ETS shilingi bilioni saba. Wenyewe wanasema 10% wanayolipa ambayo ni shilingi bilioni 78 lakini mimi naona wala hapajaharibika kitu, Serikali ikae kitako tu, ikae na hawa wenzetu wazungumze wakubaliane na kama itashindikana kama walivyosema wenzangu au ilivyosema hii taarifa yetu, bora tutafute njia mbadala ya kuweza kusaidia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa hii inayolipwa kwanza haiendi Serikalini, sisi tungefurahi tungesikia ile pesa ya ETS inakwenda Serikalini tungeanza kuzungumza lugha nyingine, lakini pesa hii yote inakwenda kwa mtu. Mtu tu ambaye ameweka kifaa chake pale anakusanya pesa, kwa kweli, hii inatia uchungu sana. Mimi naomba sana Mheshimiwa Waziri suala hili liangalie na ulifanyie kazi kwa sababu wenye viwanda wanalalamika sana kuhusu jambo hili na jambo hili litakwenda kuleta athari kubwa siku zijazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli sasa hivi hawajapandisha baadhi ya bei ya bidhaa zao, lakini wakianza kupandisha bei Serikali ijue kwamba itapunguza mapato kwa sababu hata hiyo juice inayoitwa kijoti inayokwenda kuongeza Sh.9 watu watakuwa hawanunui, watakwenda kununua matunda sokoni wakoroge basi. Kwa hiyo, tuone kwamba hapa tutakuja kupoteza siku zijazo. Naiomba sana Serikali iendelee kuangalia hili na ikiwezekana ilifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna malalmiko makubwa kule kwa wenzetu wa TRA hasa katika mizigo inayoingia bandarini. Mimi nafikiri inawezekana lipo inawezekana halipo lakini sisi tunatoa tahadhari tu kwa Serikali kama kweli hili lipo linazungumzwa basi ni vizuri wakaanza kufanya mchakato wa kufuatilia na kuona kama ni tatizo gani liko bandarini kwa wenzetu wa TRA. Wanavyolalamika wenzetu hawa kwamba bidhaa zinaingia lakini wakati wa kuzifanyia tathmini inafanywa ndogo, kwa hiyo, zinaingia sokoni zinakuwa na bei rahisi na wengine wanasema wanaghushi risiti, vifaa vinaingia vingi vinalipiwa kidogo. Mambo kama haya ni madogomadogo sana, naomba sana Serikali iyasimamie na hatimaye tuone mafanikio gani tutayapata hapo mbele ili wote tuende kwenye huo uchumi wa viwanda tunaoukusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. KANALI MASOUD ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kwa kuendelea kuliamini sana Jeshi letu katika kuwapa kazi mbalimbali licha ya ulinzi walionao, lakini bado wanaendelea kutekeleza majukumu mengi ya Taifa letu na kupunguzia gharama kubwa ya matumizi ya fedha za hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi tunaochangia tunazungumzia habari ya ulinzi, lakini nafikiri wengine hatuna taaluma ya ulinzi sana ndio maana tuazungumza mazungumzo ambayo hayalingani. Dhima ya Jeshi la Ulinzi wa Wananchi la Tanzania ni kuhakikisha usalama wa Taifa letu na wao wana jukumu la kuhakikisha adui kama yuko ndani, kama yuko nje ni jukumu lao kuhakikisha ulinzi wa Taifa hili. Sasa leo tunapokuja kuwaambia kwamba wao waende tu kule mpakani wakakae huku ndani si kazi yao, hii si sahihi. Lazima ifahamike kwamba ili wao wahakikishe wanalinda Taifa hili lazima wahakikishe adui wa ndani, adui wan je wote ni jukumu lao kwa Taifa. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. KANALI MASOUD ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilifikiri tukisimama hapa tutaendelea kulipongeza Jeshi la Wananchi kwa kazi kubwa wanayoifanya na hili ndio nalofikiria. Lakini leo tunapokuja hapa tukawaambia wamekwenda kuchukua korosho, wameoka shilingi ngapi we chukulia wameokoa shilingi ngapi nchi hii katika kazi hiyo waliyoifanya, lazima tuwaeleze ukweli wenzetu wanafanya kazi ya kujituma na ya kuhakikisha Taifa liko salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uimara wa Jeshi lolote duniani likiwepo la Tanzania kwanza lazima liimarishwe katika baadhi ya nyenzo zake. Kwanza kuimarisha wapiganaji wenyewe kwa maana ya afya, nidhamu na mafunzo na kadhalika. Pia liimarishwe kwa zana za kisasa za kijeshi ambazo nazo ni gharama pia zinatakiwa zifanyiwe service, maintenance na vitu vingine kwa gharama kubwa. Kwa hivyo vyote hivyo viimarishwe lakini pia kuimarishwa kwa maslahi yao wenyewe askari, pia ni jambo muhimu, vitu vitatu hivi vikichanganywa Jeshi lolote duniani litakuwa imara na litafanya kazi kwa ueledi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumza hapa katika muundo wa majeshi ya duniani katika nchi nyingi duniani ikiwepo Tanzania askari wastaafu wa jeshi pia linakuwa ni Jeshi la Akiba.

Kwa hiyo nilikuwa nataka niiombe Serikali iendelee kuangalia jinsi gani ya kuwawezesha wastaafu, kuwaongezea pensheni yao ili wawe imara ili wakati wowote tukitaka kuja kuwatumia wawe bado wana nguvu zinatosha za kuweza kuwatumia na mifano hai ipo katika vita vya Uganda, wanajeshi waliokuwa wamestaafu walichukuliwa wale ambao walionekana hali zao bado ni nzuri walitusaidia katika vita vile. Naomba Serikali sana iliangalie hili na kuwafikiria wanajeshi wastaafu kuwaongezea pensheni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilitaka kulizungumza ni mipaka ya kambi yetu ya majeshi bado kumekuwa na malalamiko makubwa sana, uingiliano kati ya raia na wanajeshi na mara nyingi tunapouliza ndani ya Bunge hili tunaelezwa hali halisi kwamba fedha za kulipa fidia na mambo mengine na upimaji wa maeneo bado hazitoshi. Naiomba sana Serikali iendelee kuhakikisha inawasaidia wenzetu Wizara ya Ulinzi kuwapatia fedha za kutosha kuhakikisha wanapima makambi yote na kulipa fidia katika yale maeneo ambayo tayari yamekwishapimwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilitaka kulizungumza ni kuhusu Shirika la Nyumbu na Shirika la Mzinga, tunaamini kama Jeshi ni watu wanaolinda Taifa tu, lakini mimi naamini Jeshi bado linaweza likatoa ajira, pia linaweza likachagia fedha kupitia mashirika haya. Tumeyashududia tumeona wenyewe kabisa mfano Shirika la Mzinga wana uwezo wa kuzalisha bidhaa ambazo zinahitajika nchi za nje, lakini bado mashine zao, vifaa vyao walivyonavyo ni vya teknolojia ya zamani na vingine ni vimechoka naomba pia Serikali iendelee kuangalia sehemu hizi mbili ili kuwasaidia sasa waweze kuzalisha lakini pia kukidhi mahitaji yao ya ndani ili waweze kufanikisha malengo yao waliyoyakusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. KAN. MST. MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, umefika wakati sasa kuweka kipaumbele kutekeleza miradi ya ujenzi wa ofisi za balozi zetu nchi za nje ili kupunguza gharama za kukodisha nyumba kwa watendaji wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sana kuibana Wizara ya Fedha ili ikamilishe fedha za ujenzi wa ofisi ikiwa pamoja na ukarabati wa jengo la Msumbiji ambalo endapo litamalizika basi litakuwa na tija na ukombozi mkubwa kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna utata wa fedha zilizopelekwa Msumbuji na fedha iliyotolewa na Wizara ya Fedha. Je, shilingi milioni 900 ndiyo iliyotolewa au bado ipo fedha iliyobaki Wizarani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba utaratibu uliotumika Msumbiji wa kukarabati jengo la Balozi kwa kutumia fedha za pango ambazo zilikuwa zipangishiwe nyumba ya Balozi kufanyiwa ukarabati ni jambo jema sana, sehemu nyingine ifanyiwe ukarabati.