Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Jamal Kassim Ali (10 total)

MHE. JAMAL KASSIM ALI aliuliza:-
Je, ni utaratibu gani unaotumika kukokotoa kodi katika forodha zetu zinazopokea bidhaa na vitu mbalimbali vinavyotokea Zanzibar, wakati vitu vilevile vinavyozalishwa Zanzibar ni vilevile vinavyotoka nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jamal Kassim Ali, Mbunge wa Magomeni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tathmini na ukokotoaji wa ushuru au kodi ya bidhaa mbalimbali kutoka nje, ikiwa ni pamoja na bidhaa zinazopitia Zanzibar kuja Bara, unafanywa kwa kutumia mfumo ujulikanao kama Import Export Commodity Database. Mfumo huu unatunza kumbukumbu ya bei ya bidhaa mbalimbali zilizoingizwa nchini kutoka nje na kutumiwa na Mamlaka ya Mapato kama kielelezo na rejea wakati wa kufanya tathmini na ukokotoaji wa kodi au ushuru wa forodha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyaraka za bidhaa zinapowasilishwa Central Data Processing Office, ikiwa ni pamoja na bidhaa zinazotoka nje ya nchi kupitia Zanzibar, bei au thamani ya bidhaa husika huingizwa kwenye mfumo wa Import Export Commodity Database, ili kuhakiki uhalali wa bidhaa na bei husika na kukokota kiwango cha kodi anachotakiwa kulipa mteja. Endapo bei au thamani ya bidhaa iliyopo kwenye nyaraka itakuwa chini ya ile iliyopo kwenye mfumo wa wetu, mfumo utachukua bei iliyopo kwenye database na kukokotoa kiwango halali cha kodi. Hata hivyo, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba bidhaa zinazozalishwa Zanzibar na kusafirishwa kuja Tanzania Bara hazilipiwi kodi.
MHE. RASHID A. SHANGAZI (K.n.y. MHE. JAMAL KASSIM ALI) aliuliza:-
Serikali katika kipindi hiki imejipanga kufufua viwanda vyetu:-
Je, katika mipango hiyo mizuri, Serikali imejipanga vipi kusaidia wananchi kuweza kuanzisha viwanda hivyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jamal Kassim Ali, Mbunge wa Magomeni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kufufua viwanda vilivyobinafsishwa ambavyo havifanyi kazi ili kuongeza ajira kwa vijana na pato la Taifa. Kupitia Wizara yangu na kwa kushirikiana na Msajili wa Hazina tunafuatilia mikataba ya viwanda vilivyobinafsishwa ili kuona utekelezaji wa mikataba ya mauzo kama kufanya uperembaji wa kina ili kujiridhisha kabla ya kuvirejesha kwa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu inaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa wazawa na tunahimiza Halmashauri za Wilaya zote nchini pamoja na Mamlaka za Mikoa kutenga maeneo katika wilaya, vijiji, kata ili yaweze kutumika kwa ajili ya uwekezaji. Serikali imejipanga kuwezesha upatikanaji wa maeneo ya kujenga viwanda, kuhamasisha uwekezaji katika viwanda, kushauri kuhusu upatikanaji wa mitaji na teknolojia ya kisasa, kuwaibua wanaviwanda, kuwalea na kuwaendeleza kupitia viatamizi (incubators) lakini kadhalika kutoa ushauri wa kitalaam na kujenga miundombinu wezeshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wawekezaji wazawa wanashauriwa kutafuta wabia wenye mitaji au kuungana nao na kuomba mikopo katika benki mbalimbali hususan TIB. Pia, Taasisi za Serikali za TBS, TIC, TIRDO na Benki ya Wakulima, zinaelekezwa kutoa maelekezo na huduma inayotakiwa ili kufanikisha wazalendo kuwekeza katika viwanda.
MHE. JAMAL K. ALI aliuliza:-
Kwa miaka mingi nyuma TANESCO ilikuwa ndicho chombo kilichohusika katika kuuza na kupanga bei za umeme kwa wateja wake katika makundi tofauti ya wateja wake katika nchi yetu mpaka pale EWURA ilipoanzishwa na kuanza kufanya kazi:-
(a) Je, ni vigezo gani ambavyo EWURA inavitumia katika kupanga bei hizo?
(b) Je, kuna unafuu gani wanaopata kwa wateja wanaochukua umeme katika mikondo mikubwa ya KV 11, KV 33 na KV 132?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jamal Kassim Ali, Mbunge wa Magomeni, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, EWURA hupanga bei ya umeme kwa kuzingatia gharama halisi za uendeshaji wa biashara kama ilivyobainishwa kwenye Sheria ya Umeme ya mwaka 2008. Bei hiyo ya umeme hupangwa kulingana na makundi ya watumiaji ili kila kundi libebe gharama zake.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, TANESCO ina wateja mbalimbali ikiwa ni pamoja na wateja wa majumbani ambao ni D1 na T1. Wateja wa viwanda vidogo vidogo ambao pia wanatumia msongo wa volti 400 na matumizi kwa mwezi ni zaidi ya uniti 7,500 ambao ni T2, lakini wateja wakubwa waliounganishwa katika msongo wa kati wa medium voltage yaani T3 na MV na wateja wakubwa waliounganishwa katika msongo mkubwa (high voltage: T3-HV).
Mheshimiwa Naibu Spika, unafuu wanaopata wateja wanaounganishwa katika msongo mkubwa wa umeme ni kuwa na bei ya chini (energy charge) ukilinganishwa na wateja wadogo, hasa majumbani ambao ni T1. Unafuu huo unatokana na ghrama za usambazaji na upotevu wa umeme kuishia kwenye mfumo wa HV na medium V, yaani kilovoti 220, Kilovoto 132, KV 66, KV 33 pamoja na KV 11.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana bei za umeme zilizopo hivi sasa, mteja wa T1 analipa shilingi 292/= kwa unit moja; mteja wa viwanda vidogo vidogo (T2) wanalipa shilingi 195/= kwa unit moja na mteja wa T3-MV analipa shilingi 157/= kwa uniti moja; na mteja wa T3 yaani high voltage ikiwemo migodi mikubwa ya madini kama GGM na mingine, pamoja na ZECO wanalipa shilingi 152/= kwa unit moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, h•Hata hivyo, wateja wadogo wadogo, hasa wa majumbani ambao ni D1 wanaotumia chini ya unit 75 kwa mwezi wanalipa shilingi 100/= kwa unit moja.
MHE. JAMAL KASSIM ALI aliuliza:-
Serikali imeanzisha mfumo ambao wafanyabiashara wanapouza au kutoa huduma wanatoa risiti kupitia mashine za EFD na mfumo huu umeelekezwa na Sheria na Kanuni za kodi.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka utaratibu ambao utawezesha TRA kupata rekodi za moja kwa moja ambayo inapata kupitia mfumo wa EFDs kwa mauzo ya huduma ambayo yanafanyika kwa njia ya Electronic Commerce.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jamal Kassim Ali, Mbunge wa Magomeni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilitunga Sheria na Kanuni za matumizi ya mashine za EFDs ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa takwimu sahihi za miamala ya mauzo ya kila siku kutoka kwa wafanyabiashara. Lengo ni kurahisisha ukokotoaji na ukadiriaji wa viwango vya kodi ikiwa ni hatua ya kuhakikisha kuwa Serikali inapata kodi stahiki na mlipa kodi analipa kodi stahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu wa matumizi ya EFDs unaiwezesha Mamlaka ya Mapato kupata taarifa zote za mauzo yanayofanyika ndani ya nchi, hata kama mauzo ya bidhaa au huduma yatakuwa yamefanyika kwa njia ya mitando (E- Commerce). Ili kufanikisha azma ya Serikali ya kupata takwimu sahihi za mauzo, Mamlaka ya Mapato Tanzania inaendelea na jitihada ya kuhakikisha wafanyabishara wote wenye sifa za kutumia mashine za EFDs wanafanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto za kiteknolojia, hususan teknolojia ya kufanya manunuzi kupitia mitandao. Hatua tunazochukua ni pamoja na kuongezea wafanyakazi wa mamlaka uwezo wa kukusanya kodi kwenye biashara zinazofanyika kwa njia ya mitandao. Aidha, mamlaka inaendelea kuingia kwenye makubaliano ya kubadilishana taarifa mbalimbali na taasisi na mashirika mbalimbali (Third Party Information) ili kuweza kupata taarifa za miamala ya mauzo, hususan zile zinazofanyika nje ya upeo wa kawaida tunaoweza kuona kupitia mitandao.
MHE. JAMAL KASSIM ALI aliuliza:- Je, Dar es Salaam Stock Exchange Market (DSE) na Capital Markets and Securities Authority (CMSA) mpaka sasa zimetoa mchango gani kwa wafanyabiashara wazalendo?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jamal Kassim Ali, Mbunge wa Magomeni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi yetu Soko la Mitaji (Capital Market) linahudumiwa na taasisi mbili ambazo ni: Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ambaye ni msimamizi wa soko (regulator) na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ambaye ni mwendeshaji (operator) kwa kuuza hisa na dhamana kwa taasisi na watu binafsi kwa niaba ya makampuni ambayo yanayohitaji kuongeza mitaji baada ya kupata kibali kutoka CMSA. Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya kampuni zilizoorodhesha hisa zao katika Soko la Hisa, baada ya kubinafsishwa ni pamoja na TBL, TOLGases, TCC, Swissport, Tanga Cement, Twiga Cement na NMB Bank. Makampuni haya yamekuwa yakitoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi ikiwemo ajira, gawio kwa Serikali na wanahisa, lakini pia ni miongoni mwa walipa kodi wakubwa. Kwa mfano mwaka 2015 NMB iliweza kutoa gawio la shilingi bilioni 16.5 na TCC gawio la shilingi bilioni 1.4 kwa hisa zinazimilikiwa na Serikali. Mheshimiwa Mwenyekiti, wanahisa wengineyo walipata gawio la shilingi bilioni 35. 4 kutoka NMB na shilingi bilioni 58.6 kutoka TCC. Mapato yanayotokana na kodi pamoja na gawio, vinatumiwa katika kutoa huduma mbalimbali ambazo jamii ikijumuisha wafanyabiashara wadogo ambao wananufaika nazo. Vilevile Serikali imekuwa ikitumia masoko ya mitaji kama chanzo cha upatikanaji wa fedha za bajeti kwa miradi ya maendeleo, kwa kutoa hatifungani za Serikali (treasury bonds). Miradi inayotekelezwa na fedha hizi pamoja na mambo mengine imekuwa ikitoa ajira na fursa za kibiashara kwa wafanyabiashara wazalendo wadogo na wa kati. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua mchango mkubwa wa makampuni madogo katika kukuza uchumi wa nchi, mwaka 2013 Soko la Hisa Dar es Salaam lilianzisha dirisha la makampuni madogo na ya kati (enterprises growth market) kwa lengo la kutoa nafasi kwa makampuni za wazawa zilizokidhi vigezo vya dirisha kuu la soko (main investment market) kuweza kutumia soko la hisa katika kupata mitaji na kuorodheshwa kupitia soko la hisa. Dirisha hili linatoa fursa kwa makampuni madogo na yanayoanza kulitumia soko kikamilifu kupata mitaji kutoka kwa umma wa Watanzania. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa njia hii Watanzania wengi wananufaika na uwepo wa soko la hisa na kushiriki moja kwa moja katika umiliki wa uchumi wa nchi. Baadhi ya wanufaika na dirisha hili dogo ni pamoja na Mwalimu Commercial Bank, Swala Oil and GasTanzania, Maendeleo Bank PLC, Yetu Microfinance na Mkombozi Commercial Bank. Makampuni haya mpaka sasa yana jumla ya mitaji isiyopungua bilioni 120. Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge kuwahamasisha wananchi na hasa wafanyabiashara wazawa kutumia fursa hii ya dirisha dogo kwa ajili ya kujiongezea mtaji.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB (K.n.y. JAMAL KASSIM ALI) Aliuliza:-
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mwaka 2013 zilikubaliana kuwa kodi ya PAYE kwa wafanyakazi wa Serikali na Taasisi zote za SMT ambao wanafanyakazi Zanzibar kodi yao ya PAYE ikusanywe na TRA Zanzibar na kuiwasilisha kwa SMZ.
Je, Serikali haioni ipo haja sasa kufanya hivyo kwa kampuni zote binafsi ambazo zina matawi/ofisi Zanzibar kulipia Corporate Tax ambayo kutokana na faida inayotokana na shughuli zao za biashara ndani ya Zanzibar ili kodi hiyo iende kusaidia masuala ya maendeleo kwa
wananchi wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jamal Kassim Ali, Mbunge wa Magomeni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato Sura ya 66, kifungu cha 4 sehemu ya (a) na (b); Kodi ya Kampuni (Corporation Tax) ni kodi ya Muungano na inakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Kikatiba kodi zote za Muungano zinakusanywa na TRA. Hata hivyo, kampuni ambayo imesajiliwa Tanzania Bara na ikawa na matawi Zanzibar inatakiwa kulipa kodi ya kampuni TRA Bara. Iwapo kampuni imesajiliwa Zanzibar na ikawa na matawi Tanzania Bara inatakiwa kulipa Kodi ya Kampuni Zanzibar. Kwa msingi huo, Kodi ya Kampuni inatozwa sehemu ambapo kampuni imesajiliwa, yaani Tanzania Bara au Zanzibar.
MHE. JAMAL KASSIM ALI aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani katika kuwasaidia wafanyabiashara wa Kitanzania kuwekeza kwenye viwanda nchini?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jamal Kassim Ali, Mbunge wa Magomeni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa viwanda nchini unategemea zaidi mazingira ya uwekezaji yaliyopo ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa ardhi yenye miundombinu wezeshi, sera mbalimbali, mifumo ya kodi na mifumo ya upatikanaji wa vibali vinavyotakiwa kisheria ambayo ni majukumu ya Serikali. Baada ya kuwepo mazingira wezeshi, Serikali inabaki na majukumu ya kuhamasisha wawekezaji wakiwemo wa Kitanzania kuweza kuwekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu ina mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara wa Kitanzania ili kuwekeza kwenye viwanda hapa nchini. Miongoni mwa mikakati hiyo ni mafunzo yanayotolewa kwa Watanzania wenye nia ya kuwekeza katika viwanda juu ya kuibua mawazo ya kibiashara, kuanzisha, kuendesha na kusimamia biashara kupitia SIDO, kutoa ushauri wa kitaalamu wa jinsi ya kuchagua teknolojia sahihi inayoendana na wazo la ujenzi wa kiwanda alilonalo Mtanzania kupitia TIRDO, TEMDO na CAMARTEC na namna ya kupata ama kukuza mtaji wa ujenzi wa viwanda kupitia NEDF, SIDO na TIB.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuboresha utendaji, Wizara imeanzisha Dawati la Wepesi wa Kufanya Biashara (Easy of Doing Business) ambalo lina jukumu la kuondoa ugumu wa kuanzisha na kuendesha biashara hapa nchini. Vilevile, imeandaa mwongozo kwa Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji kutenga maeneo, kusimamia sheria, kanuni, taratibu na kutoa maelekezo kwa wawekezaji. Aidha, Watanzania wanaotaka ama walio na mitaji mikubwa wanaweza kuwekeza kupitia maeneo ya EPZA ambayo yametengwa mahsusi kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa zinazouzwa nje ya nchi. Vilevile, wanaweza kuwasiliana na TIC kupata vivutio mbalimbali vilivyowekwa na Serikali kwa ajili ya uwekezaji.
MHE. HALIMA A. BULEMBO (K.n.y. MHE. JAMAL KASSIM ALI) aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kulifanyia Shirika la Umeme (TANESCO) lijiendeshe kwa faida?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jamal Kassim Ali, Mbunge wa Magomeni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) linakabiliwa na gharama kubwa za uendeshaji ambapo zaidi ya asilimia 80 ya gharama zinatokana na uzalishaji wa umeme, ukarabati wa mitambo na miundombinu mingine muhimu ya umeme. Mapato ya Shirika yamekuwa hayakidhi vya kutosha gharama za uendeshaji hususan katika maeneo ya uzalishaji wa umeme kwa kutumia mafuta mazito ambayo ni ghali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika pia linakabiliwa na tatizo la malimbizo ya madeni ya wateja wakubwa, wa kawaida na wadogo kushindwa kulipa ankara za umeme kwa wakati zikiwemo Taasisi na Mashirika ya Umma pamoja na wateja wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mikakati madhubuti ya kuliwezesha Shirika la TANESCO kujiendesha kibiashara na kuondokana na hasara. Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kufanya uwekezaji katika mitambo ya kufua umeme kwa kutumia gesi asilia na maji ili kuepukana na mitambo inayotumia mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari mipango inaendelea kuanza utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 2100 wa Rufiji Stigler’s Gorge utakaozalisha umeme kwa gharama nafuu na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za kuzalisha umeme na kulifanya Shirika lijiendeshe kibiashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingine ni megawati 300 zitokanazo na gesi asilia eneo la Mtwara pamoja na megawati 330 katika eneo la Somangafungu Mkoani Lindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha karibuni, maeneo ya Kibiti, Ikwiriri na Ngara yameunganishwa katika gridi ya Taifa, hivyo kupelekea kupunguza gharama za uendeshaji iliyokuwa ikitokana na matumizi ya mafuta mazito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango mingine ya Serikali ni kuunganisha baadhi ya maeneo katika Gridi ya Taifa kwa utekelezaji wa miradi ya njia kusafirisha umeme kwa Mikoa ya Ruvuma, Rukwa na Kigoma na hivyo kuachana na mitambo inayozalisha umeme kwa mafuta ambayo ni ghali. Ahsante sana.
MHE. JAMAL KASSIM ALI aliuliza:-
Idadi kubwa ya Watanzania wanajishughulisha na kilimo ili kujipatia mapato na moja kati ya changamoto kubwa wanayokabiliwa nayo ni ukosefu wa mitaji ya kuwezesha shughuli zao kuwa na ufanisi na tija zaidi:-
Je, Serikali ina mikakati gani kupitia Benki ya Kilimo kuwasaidia wananchi hao kupata mitaji ya kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jamal Kassim Ali, Mbunge wa Jimbo la Magomeni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto za upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya shughuli za kilimo kutokana na taasisi nyingi za fedha kuweka masharti magumu hususan kwa waombaji kutoka sekta ya kilimo. Kutokana na umuhimu wa mitaji kwa ajili ya shughuli za kilimo, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali, kama kuhamasisha uanzishwaji wa Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOs), VICOBA na Mfuko wa Taifa wa Pembejeo. Mikakati mingine ni pamoja na kufungua Dirisha la Kilimo katika Benki ya Rasilimali (TIB) na kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo.
Mheshimiwa Spika, Benki ya Maendeleo ya Kilimo iliandaa Mpango wa Biashara ambao umeainisha mikakati na hatua za kuchukua. Benki pia inatoa mikopo kwa muda mfupi, muda wa kati na mrefu kwa riba nafuu kupitia vikundi vya wakulima wadogo. Benki imejikita katika utafuta vyanzo vipya vya mtaji ili kuimarisha uwezo wa benki. Aidha, Serikali imeshaipatia benki hiyo mkopo wa gharama nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika wa shilingi bilioni 103.
Mheshimiwa Spika, mikakati mingine ambayo imeshaanza ni pamoja na kuratibu utoaji wa dhamana kwa mikopo itakayotolewa na mabenki na taasisi nyingine za fedha kupitia Mfuko wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo (Smallholder Farmers Credit Guarantee Scheme) ambapo kiasi cha fedha USD milioni 20 kimetengwa; kufadhili miradi ya ubunifu vijijini kupitia Mfuko wa Ubunifu Vijijini (Rural Innovation Fund) ambapo kiasi cha fedha USD milioni 5 kimetengwa.
Mheshimiwa Spika, mikakati mingine ni kuanzisha Progaramu za Uwezeshaji wa Vijana wa Wanawake na kupanua huduma za kibenki kwa kuanzisha Ofisi za Kanda sita (6). Hadi sasa Benki imefungua Ofisi ya Kanda ya Kati Jijini Dodoma na Ofisi ya Kanda ya Ziwa Jijini Mwanza. Katika mwaka wa fedha 2018/2019 itafungua Ofisi ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Jijini Mbeya na Ofisi Ndogo ya Kanda ya Magharibi Mjini Kigoma. Aidha, Kanda tatu zilizobaki ambazo ni za Kusini, Kaskazini na Zanzibar zitafunguliwa baadaye.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Julai, 2018, Benki imeshatoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 48.67 ambayo imewanufaisha wakulima 527,291 katika Mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Morogoro, Tanga, Manyara, Kagera, Arusha, Zanzibar na Mikoa ya Kanda ya Ziwa. Aidha, Serikali itaendelea kuongeza mtaji wa Benki ya Kilimo na kuhamasisha uanzishwaji na usimamizi wa vyama vya ushirika ili kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa wakulima.
MHE. RICHARD P. MBOGO (K.n.y JAMAL KASSIM ALI) aliuliza:

Mwaka 2017, Umoja wa Afrika (AU) ulipitisha Azimio kwa nchi za Afrika la kuhakikisha kuwa nchi hizi zinavuna faida itokanayo na Demografia iliyopo kwa kuwekeza kwa vijana:-

(a) Je, Serikali ya Tanzania imechukua hatua gani katika utekelezaji wa Azimio hilo?

(b) Je, ni mafanikio gani yamepatikana kama nchi baada ya utekelezaji huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI,VIJANA NA AJIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jamal Kassim Ali, Mbunge wa Magomeni kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Spika, katika Kikao cha 29 cha Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika kilicofanyika Mjini Addis Ababa kiliweka Azimio Na. 601 lililotangaza mwaka 2017 kuwa ni mwaka wa “Kuvuna Faida itokanayo na Demografia kupitia Uwekezaji kwa Vijana” (Harnessing the Demographic Dividend Through Investments in Youth).

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azimio hilo Serikali imechukua hatua zifuatazo:-

(i) Kutoa mikopo ya kuwawezesha vijana kuanzisha na kuendelea miradi yao ya uzalishaji mali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, ambapo katika kipindi cha mwaka 2014/2015 hadi 2019 Serikali imewezesha vikundi vya vijana 755 ambavyo vimepatiwa mikopo ya shilingi bilioni 4.2 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi.

(ii) Kurekebisha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 ya Mwaka 2017 inayozitaka Halmashauri zote nchini kutenga fedha asilimia 10 kutokana na mapato yao ya ndani kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kwa ajili ya mikopo.

(iii) Kuibua bunifu 31 za vijana katika Sekta ya Sayansi na Teknolojia. Kati ya hizo, bunifu 11 zimefanyiwa tathmini ya kisayansi na kwa sasa ziko katika hatua mbalimbali ikiwemo kuwekwa kwenye kiota atamizi (incubator) kabla ya hatua ya majaribio ya uzalishaji.

(iv) Kutoa mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana 5,875 kupitia taasisi ya Don Bosco Net Tanzania, kurasimisha ujuzi wa vijana 10,000 walioupata nje ya mfumo rasmi ya mafunzo kupitia VETA na Serikali kwa kushirikiana na waajiri imeibua fursa 1,800 za mafunzo ya vitendo mahali pa kazi, ambapo wahitimu 292 wameshapelekwa kuanza mafunzo.

(v) Kutoa mafunzo maalum ya vitalu nyumba kwa Halmashauri zote nchini ili kufikia vijana wasiopungua 18,000, tayari Mikoa 12 imeanza programu hii kwa awamu ya kwanza.

Mheshimiwa Spika, kutokana na utekelezaji wa Azimio hilo mafanikio makubwa yaliyopatikana ni pamoja na:-

(i) Ongezeko la ajira kwa vijana katika sekta binafsi;

(ii) Ongezeko la vijana wanaojitegemea kutokana na kujiajiri wao wenyewe;

(iii) Ongezeko la vijana wenye ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa; na

(iv) Upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana.