Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Jamal Kassim Ali (7 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa kupata nafasi hii ya kuchangia, nitumie nafasi hii kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Magomeni kwa kunichagua kuja kuwa mwakilishi wao katika Bunge letu hili Tukufu. Ni imani yangu ya kwamba tutashirikiana pamoja katika kuleta maendeleo ndani ya Jimbo letu na Taifa letu kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, niwapongeze Watanzania kwa kuendelea na kuwa na imani na Chama cha Mapinduzi na kukipa fursa kuongoza nchi yetu kwa kipindi kingine. Naamini hivyo hivyo kwa Wazanzibari wenzangu wataendelea kukipa fursa chama chetu kuiongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na wachangiaji waliotanguliwa kumpongeza Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania; Waziri Mkuu na timu yote ya Serikalini kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wameanza kuifanya kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu. Nimpongeze Dkt. Mpango na timu yake yote kwa kuwasilisha Mpango mzuri kabisa ambao umekwenda kujibu au kutafsiri ile dhana ya Rais wetu ya kusema anataka kuipeleka nchi yetu kuwa nchi ya viwanda. Niwapongeze sana Wizara kwa kuandaa mpango wetu huu mzuri na kuwasilisha vizuri katika Bunge lako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ambayo nitayagusia, eneo la kwanza, ni eneo la kodi. Nimpongeze Rais, Waziri Mkuu na Waziri mwenyewe kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuweka mikakati kuona namna gani tunaendelea kukuza makusanyo yetu ili tuweze kumudu mahitaji yetu ya maendeleo katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejionea ongezeko kubwa kabisa la ukusanyaji wa kodi ambalo taasisi yetu ya TRA kwa kipindi hiki cha miezi miwili ambayo imefikia. Niwapongeze sana na juhudi hizo waziendeleze ili kukuza makusanyo, kwa sababu tunaamini kabisa makusanyo hayo ndiyo yatafanya Mpango wetu utimie na yale maendeleo ambayo tunakusudia kuwapelekea wananchi yafikiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili la kodi, kwa kipindi kirefu kabisa, kumekuwa na masikitiko au malalamiko yanayohusu masuala ya bidhaa na vitu ambavyo vinatoka Tanzania Zanzibar kuja Tanzania Bara. Mfumo wetu wa kodi uliokuwepo hivi sasa kwa bidhaa hizi zinazotoka Tanzania Zanzibar kuja Tanzania Bara kunakuwa na tozo la kodi ambalo linaitwa difference.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati tunajiuliza, iweje tufikie hapo? Tuna Taasisi moja ya kodi ambayo ni TRA, Taasisi hii na Zanzibar ipo, inatumia sheria moja na mwongozo huo huo mmoja, wa Kamishna huyo huyo mmoja wa Forodha. Tumekwenda kutengeneza mfumo ambao umetengeneza urasimu, manung‟uniko na baadhi ya wakati hata ukokotoaji wa kodi hizi hauko wazi, wananchi wetu hawajui.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu ana television yake tu akifika pale Bandarini Dar es salaam anaambiwa alipie kodi hajui alipie kodi vipi na ile TV ameinunua Zanzibar. Kwa hiyo, mambo kama haya, are very peanut, lakini huko mtaani tunakwenda kutengeneza bomu ambalo wananchi wetu wanalinung‟unikia lakini Serikali yetu inachukua muda mrefu kabisa kulipatia majawabu mambo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi najiuliza, TV ili itozwe kodi ya forodha maana yake lazima mkadiria kodi aijue CIF yake, aliijuaje? Kwa hiyo, hizi kodi hazina base yoyote, tumekuwa tunatengeneza fursa ya maafisa wetu kujiamulia tu haya mambo na kwa asilimia kubwa yametengeneza urasimu na mifumo ya rushwa. Kwa hiyo, nimwombe kabisa Mheshimiwa Waziri, hili jambo linawezekana, halihitaji mshauri mwelekezi, yeye mwenyewe anatosha kulielekeza, kulifuta, hao wananchi basi wa-enjoy fursa ya Muungano wetu, Wabara waende Zanzibar na bidhaa zao bila tabu, Wazanzibari wakija bara, waje bila taabu yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nitalizungumzia, eneo la viwanda. Tumeona kabisa Mheshimiwa Rais, toka alivyokuwa katika kampeni zake na alivyozindua Baraza lake la Mawaziri alikuwa anazungumza sana kuhusu suala la viwanda. Lengo lake ni kuipeleka Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Nampongeza na namuunga mkono katika hilo na naamini kabisa, viwanda ambavyo tutavianzisha ndiyo vitakwenda kujibu matatizo ambayo nchi yetu inayakabili kwa sasa, viwanda hivi hivi ndiyo vitaenda matatizo ya ajira kwa vijana wetu, viwanda hivi hivi ndiyo vitaenda kujibu matatizo ya masoko kwa wakulima wetu, wafugaji na wavuvi. Viwanda hivi hivi ndiyo vitakwenda kujibu tatizo letu…
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha. Hiyo ni kengele ya pili nimeshauriwa hapa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami kuchangia jioni ya leo. Awali ya yote, napenda kuwashukuru Wabunge wa Chama cha Mapinduzi kwa kunichagua kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM. Nawaahidi kwamba nitaitumikia nafasi hii kwa maslahi yetu na maslahi ya chama chetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo nampongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa bajeti nzuri kabisa ambayo imetafsiri ile dhana ya Mheshimiwa Rais ya kwenda kwenye Tanzania ya viwanda, Mheshimiwa Waziri Profesa Muhongo nakupongeza sana. Hao wanaokubeza, naamini kabisa ndani ya nafsi zao wanajua kwamba katika viongozi wenye dira wewe ni miongoni mwao. Naweza kudiriki kusema kwamba wewe sio wa Kitaifa, bali wewe ni wa Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze moja kwa moja, kwenye upande wa umeme. Tumeona jitihada za Mheshimiwa Waziri na wataalam wake katika kuipeleka Tanzania kuondokana na changamoto mbalimbali za umeme ambazo ilikuwa inakabiliwa nazo huko nyuma. Tumeona coverage ya umeme ilivyoongezeka, upungufu wa bei, ongezeko la install generation capacity, kwa hiyo, nawapongeza sana. Naamini bado tuna changamoto kubwa katika sekta hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kumshauri Waziri na Wizara na sekta husika kwamba kuna maeneo inabidi tuzidi kuyafanyia kazi ili kuhakikisha kwamba ile dhamira ya kuwa na umeme wa uhakika na wenye kutosheleza inafikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye mpango wetu wa miaka kumi hadi mwaka 2025 tunatarajia kuwa na umeme usiopungua megawatts 10,000 na sasa tupo kwenye megawatts 1461. Kwa hiyo, tunatakiwa kwa hesabu za haraka haraka, kwa wastani kila mwaka tuongeze install generation capacity isiyopungua megawatt 948.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema ukweli Megawatts hizi ni nyingi sana na kwa kuiachia TANESCO peke yake hawataweza. Ninachokusudia kusema ni kwamba kuna haja ya kufanya reform katika sekta yetu ya umeme. Tunajua TANESCO imekabiliwa na changamoto nyingi katika muda mrefu. (Makofi)
Kwanza, shirika letu hili la umeme kwa kipindi cha takriban miaka minne sasa limeshindwa kuzalisha faida, linaendeshwa kihasara, kwa hiyo, halina mtaji wa kwenda kuwekeza kwenye uzalishaji wa umeme wote ule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, hata ukiangalia vitabu vyao vya mahesabu, pia wana-operate katika deficit working capital. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba kabisa wakati umefika kwenda kufanya reform ya sekta ya umeme nchini mwetu. Serikali ifungue milango, wawekezaji binafsi waingie katika uzalishaji na katika usambazaji wa huduma hii muhimu kwa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itatufanya kwanza kupata ongezeko kubwa la umeme kwa sababu tutafungua mwanya kwa wazalishaji wengi kuingia, lakini tutapata nafasi ya mashirika haya ambayo yanafanya usambazaji wa umeme ku-compete na kushusha bei ya umeme; na yenyewe yata-compete kwasababu yatakuwa katika business oriented. Naamini kabisa yataendeshwa kibiashara na yatazalisha faida tofauti na sasa ambavyo TANESCO inavyoenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa East Africa wote walikuwa na matatizo kama ya kwetu, wenzetu Wakenya walikuwa na kama ya kwetu au kuzidi ya kwetu; Waganda hali kadhalika, lakini walifanya reform kubwa kabisa katika sekta hii muhimu ya umeme, lakini hatimaye leo mashirika yao yanazalisha faida, hayaendi kwa ruzuku na pia wanapata wasaa wa kuchangia pato kwa Serikali kama sehemu ya gawio la Serikali. Kinyume na hapa kwetu ambapo Shirika letu la TANESCO mara zote limekuwa kila mwaka likiendeshwa kwa ruzuku ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naamini kabisa Mheshimiwa Profesa nia hii unayo, dhamira unayo na uwezo unao. Kwa hiyo, ni wakati sasa wa kufanya reform kubwa ya kuhakikisha tunaenda katika uzalishaji ambao ile dhamira ya kufikia kwenye Tanzania yenye viwanda tunafikia. Kwa sababu bila kuwa na umeme wa kutosha na uhakika, suala la viwanda litabakia kwenye vitabu vyetu na mipango yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huo, niende kwenye upande wa EWURA. Nimepitia kitabu cha bajeti, ukurasa wa 80 kuna jedwali lile la bei elekezi za EWURA za umeme. Katika jedwali lile kuna vitu nimebaini niweze kusema ni changamoto ambazo naomba Mheshimiwa Waziri uzifanyie kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia upande wa tariffs hizi za bei ya mahitaji ya juu (demand charges); mteja ambaye yuko katika T3HV (high voltage) wanachajiwa shilingi 16,550 kama tozo lao la bei ya mahitaji ya juu, wakati logic hapa hawa waliokuwa kwenye transmission line, cost ya kuupeleka umeme kwenye transmission line ni ndogo compared na cost ya kuupeleka umeme kwenye T3MV na T2, lakini wamebebeshwa mzigo mkubwa ambao hata najiuliza EWURA walipoweka hii bei walikusudia nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia wateja waliokuwepo hapa ni watatu tu waliokuwepo kwenye T3HV. Kuna Shirika la Umeme la Zanzibar, Bulyankhulu na Twiga Cement. Kwa mfano, kwa upande wa Shirika la Umeme la Zanzibar, ni bulk purchaser ambao waliingia mikataba na TANESCO ya Purchase Power Agreement ambayo sasa baada ya kuja EWURA ile mikataba imekuwa haina nguvu tena. Huyu ni bulk purchaser ambaye mwenyewe anatarajia huu umeme auze kwa wateja wake wa kati na wadogo. Sasa kama tunam-charge katika bei hii tunatarajia yeye auze kwa shilingi ngapi? Kusema ukweli katika kipindi kirefu kumekuwa na mlundikano wa madeni ambayo ZECO inadaiwa na TANESCO. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huenda moja ya sababu ya madeni haya naweza kusema ni appropriate tariff ambayo ZECO imekuwa ikitozwa kama ambavyo tunavyoona katika mwongozo huu wa bei ambao EWURA wameutoa mwezi Aprili. Kwa sababu wao wanachukua umeme katika transmission level ambapo gharama za depreciation, gharama za maintenance katika level hiyo ukilinganisha na wanaochukua T3MV na T2 ni ndogo lakini wamepewa…
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi asubuhi ya leo kuchangia katika bajeti hii ya Serikali. Kwanza, nikupongeze kwa umahiri ambao umeuonesha ndani ya Bunge hili na kwa Watanzania wote katika kuendesha vikao vya Bunge kwa uimara na ujasiri mkubwa kwa kufuata kanuni na taratibu ambazo tumejiwekea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kwenda, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mipango na timu yake kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya kuhakikisha kwamba Serikali inakusanya pesa za kutosha kwenda kugharamia gharama mbalimbali za maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwenye suala la VAT. Mheshimiwa Dkt. Mpango katika mawasilisho yake ya mapendekezo ya bajeti, katika marekebisho ya Sheria ya VAT amesema kwamba sasa VAT baina ya pande hizi mbili za Muungano yaani Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara zitatozwa at a point of destination.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie Mheshimiwa Waziri, biashara baina ya pande hizi mbili za Muungano zimekuwa zikikabiliwa na changamoto kubwa ya kodi mpaka sasa bado hatujaweza kuzitatua. Kuruhusu utaratibu huu ni sawasawa na kwenda na kijinga cha moto kwenye petrol, tunakwenda kuongeza matatizo ya kodi ambazo wafanyabiashara wetu wamekuwa wakizilalamikia, wale ambao wanafanya biashara zao baina ya pande mbili za Muungano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Afrika Mashariki tumeona wameingia makubaliano ya redemption, kodi zikusanywe at a point of entry, na kule mzigo unapofika basi atakuwa remitted ile kodi yake iliokusanywa. Na mfumo huu ndio uliokuwa unatumika hapo kabla ya mabadiliko ya Sheria mpya VAT ya mwaka 2015. Nimwambie Dkt. Mpango, katika utaratibu huu mpya, kwanza tunaenda kutengeneza mgogoro wa kikodi kwa wafanyabiashara wetu, lakini pia tunaenda kusababisha au kutengeneza loophole ya watu kukwepa kodi. Kwa mfano leo hii, mtu akinunua mabati yake hapa Dar es Salaam akasema anayapeleka Zanzibar hatotozwa VAT. Lakini yale mabati yanaweza yasifike Zanzibar yakaishia hapa hapa Dar es Salaam, kwa hiyo, tutakuwa tunapoteza kodi yetu. Kwa hiyo, nikuombe kabisa katika hili tunaomba utaratibu ule ambao ulikuwa unatumika hapo awali uzidi au uendelee kutumika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye mabadiliko ya Sheria ya Kodi ya Mapato, niungane na baadhi ya Wabunge wenzangu ambao hawakuunga mkono hoja ya kutozwa kodi Wabunge katika gratuity, niunge mkono hilo. Nilivyopitia Sheria Namba 11 ya mwaka 2004 ya Kodi ya Mapato katika jedwali la pili nilikuta kwamba watu na taasisi ambazo zinasamehewa kodi si Wabunge peke yake. Wapo watu wengine, zipo taasisi zingine ambazo zinasamehewa kodi. Kwa hiyo, Dkt. Mpango katika hiyo hoja yako ya kusema unataka ujenge mazingira ya usawa naona kwa hapo itakuwa haina mashiko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe kabisa, kama ambavyo umeona kuna hoja na haja ya wale wote wengine waendelee kusamahewa kodi za mapato kwa mujibu wa sheria yetu ile kama ilivyo katika jedwali lake la pili basi, hoja na haja hizo bado ipo kwa Wabunge; Wabunge waendelee kusamehewa kodi katika gratuity zao ambazo wanalipwa baada ya kumaliza kipindi chao cha Ubunge. Hoja na haja hiyo ipo, wenzangu wengi wamezungumza na mimi nikuombe kabisa, niombe Serikali yangu sikivu katika hili itufikirie sana. Kwa vile muda ni mdogo sitaki kuzungumza mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini eneo lingine kwanza nikupongeze na niwapongeze wafanyabiashara wa Tanzania kwa kuutikia wito wako wa kuanza kutumia mashine za kielekitroniki yaani hizi za EFDs katika kutoa risiti pale ambapo wanauza bidhaa zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ningependa kujua kwa sasa ukuaji wa sayansi na teknolojia umepelekea mabadiliko makubwa kabisa hata katika transaction zetu hizi za mauzo. Kumekuwa na ukuaji mkubwa katika e-commerce na naamini Wabunge wenzangu mnashuhudia hilo. Leo hii kuna miamala inayofanywa kupitia moja kwa moja baina ya benki zetu kwenda kwa wauzaji. Kuna miamala ambayo inafanywa kupitia simu zetu, mfano mdogo tu asilimia kubwa leo ambao wanatumia ving‟amuzi, hawalipi cash dirishani wanatumia simu zao kulipia gharama mbalimbali za ving‟amuzi hivyo vya televisheni. Katika eneo hili Mheshimiwa Dkt. Mpango tunaomba uje utuambie basi Serikali kupitia TRA imejipangaje, ku-track records zote za mauzo hayo kuhakikisha kwamba na wao basi, wanachangia au wanakuwa sehemu ya kuchangia katika kodi ya Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwa upande wa CAG. Ofisi yetu ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Serikali imefanya kazi kubwa na nzuri sana kwa Taifa letu. Imefanya kazi kubwa na nzuri kwa Taifa letu na sote mashahidi, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali imekuwa ikitoa mapendekezo ya maboresho mbalimbali ambayo yameisaidia Serikali yetu hii kutokuingia katika hasara au upotevu mbalimbali wa fedha za umma. Lakini ofisi hii hii imesaidia Serikali kurudisha pesa mbalimbali ambazo aidha, watu walikwepa kulipa au watu walifanya ubadhirifu na kuwa sababu ya watu kuchukuliwa hatua kisheria kwa makosa hayo. Nimuombe Mheshimiwa Waziri katika Bajeti ya mwaka jana, ofisi hii tuliitengea shilingi bilioni 74; katika bajeti ya mwaka huu tumeitengea shilingi bilioni 44.
Mheshimiwa Naibu Spika, nini maana yake? Maana yake tunaenda kumfunga miguu CAG asiende kukagua tunaenda ku-reduce ile scope yake ya ukaguzi na hii athari yake ni nini kwa Taifa letu? Kwanza kwa vile mwaka huu tumeona asilimia 40 ya pesa za bajeti ya Serikali zinaenda kwenye miradi ya maendeleo tutatengeneza mianya ya watu ambao hawana nia nzuri na Serikali yetu kwenda kuzitumia hizi pesa kutokidhi yale malengo ambayo yamewekewa kwa sababu ambayo watajihakikishia kwamba, hakutokuwa na ukaguzi wa kutosha ambao unaweza ukabaini huenda ubadhirifu au wizi katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika nimepitia ripoti ya CAG ya Taarifa za Ukaguzi kwa Mwaka wa Fedha 2015, ukisoma tu katika preamble ripoti ile inabainisha kwamba CAG amefanya kazi kubwa na nzuri. CAG katika ripoti yake ile ile ameweza kutubainishia kwamba Serikali imepoteza takribani shilingi bilioni 100 katika eneo la ukwepa wa kodi.
Baada ya kusema hayo, naamini Mheshimiwa Waziri atakuja na hoja ya haya niliyoyaibua. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango na Bajeti ya Serikali. Kwanza nianze kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ambayo ameifanya hususani katika suala la kusimamia rasilimali la taifa hili kuhakikisha rasilimali hizi zinanufaisha taifa hili na wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote ni mashahidi toka alivyoanza kazi, toka alivyoapishwa mambo aliyoyafanya ni makubwa ni mambo ambayo yanajieleza yenyewe kwamba ni miongoni mwa Marais ambao wameji-commit katika kutusaidia kuleta maendeleo katika Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri, Naibu Waziri na timu yao kwa bajeti nzuri, kusema la ukweli bajeti hii imeenda kujibu ile dhana ya kwamba tunaenda kwenye Tanzania ya viwanda, tumeona namna gani sera za fiscal yaani kodi zilivyowekwa ili kusaidia uanzishwaji wa viwanda vya kati na vikubwa. Kwa hiyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa na maeneo machache ya kuchangia kama sehemu ya ushauri, eneo la kwanza ambalo ningependa kuchangia ni suala la kodi ya mapato. Kodi ya mapato kwa mujibu wa Katiba yetu ni kodi ya Muungano na chombo ambacho kinasimamia kodi hii ni Mamlaka ya Mapato ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyojua nchi yetu ina sehemu mbili kuna sehemu ya Zanzibar ambayo Zanzibar ina Serikali yake ambayo kwa upande mmoja inategemea kodi ambazo zinatokana na mapato ambayo kwa upande wa Zanzibar TRA ndio inakusanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa sheria yetu ya kodi ya mapato taasisi zote ambazo zitafunguliwa kama sehemu ya tawi la makao makuu, basi ofisi hizo hazitatoza kodi ya mapato, yaani kodi ya mapato itatozwa at a corporate level.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni nini, kwa upande wa Zanzibar tumekuwa na makampuni mengi ambayo Makao Makuu yake yako Dar es Salaam yanaendesha shughuli zao za kibiashara Zanzibar. Kwa harakahara tuna taasisi za fedha kumi yaani mabenki kumi ambayo zinafanya biashara Zanzibar. Tuna kampuni za simu tano, tuna kampuni za bima na kampuni mbalimbali ambayo yanatoa huduma na yananafanya biashara Zanzibar lakini kwa mujibu wa sheria yetu ya kodi ya mapato hazilipi kodi Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi ambayo inayokuswanya na TRA Zanzibar ndiyo kodi ambayo inaenda Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya shughuli zake za uendeshaji na kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunajua Zanzibar, kiuchumi, uchumi wake ni mdogo, pia vyanzo vyake vya mapato ni hafifu. Naamini sasa busara itumike kwa makampuni haya ambayo yanafanya shughuli zake Zanzibar kama sehemu ya matawi basi na yenyewe yaanze kulipa kodi Zanzibar ili iweze kusaidia kuongeza mapato kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na hivyo basi iweze kufanya shughuli zake za maendeleo na kijamii kama ambavyo tumeahidi kwenye ilani yetu ya chama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo ningependa kuchangia kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani. Mwaka jana tulivyokuwa tunapitisha Finance Act kwenye Sheria ya VAT, tulipitisha kwamba bidhaa zote ambazo zitatengenezwa Tanzania Bara na kununuliwa Zanzibar na mnunuzi ambaye atakuwa amesajiliwa na VAT basi biashara hizi hazitatozwa kodi au bidhaa hizi hazitatozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kumekuwa na uzito katika utekelezaji wa suala hilo, kuna kesi nyingi sana, wafanyabiashara wetu ambao wananunua bidhaa hizi ambazo zinatengenezwa Tanzania Bara ikiwemo mabati, bidhaa za urembo wakitozwa kodi hiyo na wakienda Zanzibar wanatozwa tena. Kwa hiyo, kumekuwa na tozo mara mbili ambayo wafanyabiashara wetu wamekuwa wakitozwa na sheria iko wazi imeainishwa na tuliipitisha. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri utakapokuja ku-windup labda utupe msimamo wa Serikali juu ya hili pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mwaka jana tulipitisha Sheria ya Finance Act tulifanya mabadiliko katika Sheria ya The Electronic and Postal Communication Act kwa kuyataka makampuni yetu ya simu kwanza yawe listed katika Dar es Salaam Stock Exchange, lakini pia yatoe asilimia 25 ya hisa zake kwa wananchi au wakazi wa Tanzania. Lengo kuu ambalo Mheshimiwa Waziri alilolisema ilikuwa kwanza kuwapa fursa Watanzania nao kushiriki katika uchumi huu mkubwa ambao unakuwa wa sekta ya mawasiliano lakini pili kujenga uwazi wa kujua kwamba nini hasa biashara hii ya makampuni haya ya simu yanapata kutokana na muda mrefu kutokuchangia vile ipasavyo kwenye kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Watanzania kupitia Rais wetu tumeamka kwamba kwenye sekta ya madini tunaibiwa. Kila mtu aliyenyanyuka katika Bunge hili kuchangia, watu wote wamezungumza kwamba kwenye sekta ya madini tunaibiwa. Aidha, tunaibiwa kutokana na kutokuwa na uwazi wa kutosheleza kwenye biashara hii au sababu zinginezo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali kwa vile Rais amesema sheria hizi atazileta Bungeni tuzifanyie maboresho na mikataba hii.

Kwa hiyo, niishauri Serikali itakapoleta sheria hizi wakati umefika sasa wa sheria hizi pia, makampuni haya makubwa ya madini yawe listed kwenye Dar es Salaam Stock Exchange iwe sharti namba moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sharti la pili lazima kuwe na local content participation. Lazima nao wafaidike na rasilimali yao, japo hatuna pesa nyingi lakini kwa kidogo kidogo tulichokuwa nacho naamini kabisa tunaweza tukachangachanga hicho na tukapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sheria nimezungumzia suala la sheria, lazima iwe mandatory si suala la mtu kupenda, tuna makampuni mengi zaidi ya Acacia, yanachimba madini. Kwa hiyo, lazima tuweke sheria ambayo makampuni yote ya madini yawe listed.

Mheshimiwa Mwenyekiti, makampuni haya yote kuna umuhimu yakawa listed kwenye Dar es Salaam Stock Exchange.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumalizia kwa kuunga mkono hoja, kuipongeza bajeti hii, naamini ni bajeti ambayo inatupa mwanga wa dira yetu ambayo tumeiweka ya kwenda Kwenye Tanzania ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ya Kamati ya PAC. Nianze moja kwa moja nami kujielekeza katika masuala manne kama muda utatosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza ambalo nimekusudia kulichangia leo hii jioni ni suala la NSSF. Bahati nzuri Kamati yetu ya PAC tulibahatika kuonana na uongozi wa NSSF, tukabahatika kukagua hesabu zilizokaguliwa za NSSF. Kumekuwa na hoja potofu ambayo baadhi wa Wajumbe wamezungumza na imekuwa inazungumzwa. Nimewanukuu Mheshimiwa Mussa Mbarouk, nimemnukuu Mheshimiwa Catherine Ruge katika michango yao wamesema kwamba kwenye suala la mradi wa Dege, NSSF imenunua ardhi heka moja kwa thamani ya Sh.800,000,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwape challenge, nimepitia hesabu na wao tumepitia pamoja, ukipitia taarifa ya ukaguzi ya CAG, kile kitabu kina kurasa karibia 200 na kitu, hakuna hata sentensi moja iliyoandika kwamba NSSF wamenunua ardhi kwa shilingi milioni 800. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipitia taarifa za hesabu za NSSF, ukiangalia financial statements zake, hakuna sehemu yoyote ambayo NSSF wameripoti au kurekodi kwamba kuna pesa au miamala ambayo wamefanya ya ununuzi wa ardhi kwa hekari moja shilingi milioni 800. Kwa hiyo, nawaomba wasipotoshe, kama wana ushahidi waulete na nipo tayari hata kujiuzulu Ubunge wangu katika hili. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge waelewe nini hasa kinachoendelea katika mradi wa Dege. Mradi wa Dege ni miongoni mwa miradi ambayo inaendeshwa kwa mfumo wa land for equity na mradi huu sio umeingiwa mara ya kwanza na NSSF, miradi hii imefanywa na National Housing na taasisi mbalimbali za umma na za binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la Dege, mradi wa Dege ni mradi wa ubia baina ya NSSF na Kampuni ya Azimio Limited ambayo imesajiliwa Tanzania. Hawa wawili ndio wabia wa mradi huo. Katika modality ya miradi hii, katika soko yule ambaye anakuja na ardhi kawaida ana- carry an interest of 20 percent ya ule mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waheshimiwa Wabunge wajue, ukienda Arusha kuna Palace Hotel, ile property ardhi ni ya National Housing waliingia ubia na mwekezaji Palace Hotel Limited, National Housing ina asilimia 20 na Palace Hotel Limited ina asilimia 80. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, isitoshe ukienda Morogoro leo kuna stand kuu ya mabasi eneo lile ni la Manispaa ya Morogoro, NSSF wamewekeza pale, Manispaa ya Morogoro kwa vile ardhi ni yao wame-carry an interest ya ule mradi ya asilimia 23 na NSSF wamebakizwa asilimia 77. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wajue, hiyo hoja ni hoja potofu na sijui waliokuja nayo wana malengo gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile hili suala lilianza kwenye taarifa ya CAG ya mwaka 2014/2015 ambayo bahati nzuri mwaka jana tuliichambua na tukabahatika kutoa mapendekezo, niwapongeze Serikali kwa hatua mbalimbali ambazo wamezichukua, lakini kubwa niwaombe mradi ule NSSF imeingiza takribani bilioni 219, pesa hizi ni pesa za wanachama wananchi wa Tanzania ambao Serikali yetu hii ndiyo trustee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana mradi ule ukiendelea kukaa vile ulivyo, hauna tija kwa Taifa letu. Tumewekeza pesa nyingi, ipo haja sasa ya ule mradi kuhakikisha unatoka pale na unaenda kwenye level nyingine ambayo tumekusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naitaka Serikali ikae na mbia ambaye Azimio Housing Limited kuhakikisha yale makubaliano ambayo yameanza basi yanafikia tamati mapema na ule mradi unaendelea na kuleta tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulivyoenda NSSF Dege bahati nzuri wenzetu Management team ya NSSF walitueleza mipango mizuri kabisa juu ya huu mradi. Kwanza, walituambia zile nyumba kwa bei ya mwanzo kabisa zitauzwa kwa takribani dola 120,000 na wametoa fursa kwamba Watanzania na mwananchi yeyote anaweza kununua nyumba ile kwa muda wa miaka 15 bila kupitia benki. Kwa hiyo, hii ni fursa pekee ambayo makampuni yote yanayo-deal na property business hakuna hata moja inayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kidogo nichangie eneo lingine la pili eneo la Mlimani City. Kwa upande wa Mlimani City nami niungane na maelezo ya Kamati na mapendekezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo haja mkataba wa Mlimani City ukapitiwa upya.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mungano na Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kunipa nafasi, acha nijielekeze moja kwa moja kwenye kuchangia hotuba na mimi nitajiekeza kwenye suala la mikopo ya nje. Suala la mikopo ya nje linasimamiwa na Serikali ya Muungano, ni suala la Muungano. Kumekuwa na ucheleweshaji wa muda mrefu sana kupatia approval miradi ya kimkakati ambayo inafanyika kupitia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni shahidi, jengo la Terminal II katika Uwanja wa Amani Abeid Karume International Aiport limesimama toka mwaka 2014. SMZ imeomba extension ya mkopo kwa ajili ya kukamilisha mradi ule lakini mpaka leo hii bado. Sote tunajua uchumi wa Zanzibar unategemea utalii na bila kuwa na airport kubwa yenye uwezo hatuwezi kufikia lengo lile ambalo tumejiwekea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa Zanzibar kwa takribani 40% unachangiwa na sekta ya utalii. Matarajio ya Zanzibar ni kupokea mwakani wageni wapatao 500,000. Kwa infrastructure iliyokuwepo pale haitoshi. Tunaomba kabisa suala la approval ya mikopo hii lifanywe kwa wakati na kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini siyo hivyo tu, tuna mradi mwingine wa Bandari ya Mpigaduri. Kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015 tumeahidi katika kipindi cha miaka mitano hii tutajenga Bandari ya Mpigaduri kwa ajili ya mizigo, lakini mpaka leo bado approval za mikopo hii haijatoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu miradi hii mikubwa miwili ni toshelezi kabisa kwa kusaidia uchumi wa Zanzibar. Kukamilika kwa miradi hii kutaufanya uchumi wa Zanzibar kuimarika, lakini si kuimarika kwa uchumi wa Zanzibar tu, pia kuimarika kwa uchumi wa Tanzania kwa ujumla wake. Uchumi wa pande zote hizi zina-compliment each other, tunajua mizigo itakayoshushwa Bandari ya Mpigaduri mingine itaenda Rwanda, Burundi, Zaire, Congo lakini itaenda kupitia wapi, itapitia Bandari ya Dar es Salaam. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri aje atuelezee nini hasa tatizo katika approval ya mikopo hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini eneo lingine ni suala la biashara ya pamoja. Mimi naamini kabisa moja ya sababu kubwa na faida za Muungano wetu ni fursa za biashara kwa upande wa Zanzibar kuja Bara na upande wa Bara kwenda Zanzibar. Ukifanya trade analysis, hizi changamoto za leo miaka ya 1990 hazikuwepo. Ukichukua analysis za miaka ya 1990 Zanzibar ilikuwa inauza zaidi Bara kuliko Bara inavyouza Zanzibar. Nimeona jitihada ambazo Waziri anasema kuna ZBS na ZFDA, lakini kwa nini haya mambo yako upande mmoja tu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vitu vikija Bara ndiyo kunakuwa kuna TBS na TFDA lakini vitu vya Bara vinakuja Zanzibar bila ya haya matatizo. Hizi changamoto zimechukua muda mrefu kutatuliwa. Kwa hiyo, mimi pia nimuombe Mheshimiwa Waziri, hili suala alitizame kwa upana na uzito wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kuzungumza ni suala la kodi ya foroddha. Kodi ya Forodha iko kwa mujibu wa utaratibu. Leo hii ukienda kukaa Bandari ya Dar es Salaam pale, watu wanaotoka Zanzibar, mtu akinunua kitu chake kidogo tu akifika pale anatozwa kodi. Unajiuliza hizi base za kodi wanazotozwa ni zipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mfano hai, juzi kuna mwananchi wa Jimboni kwangu amesafiri na cherehani moja tu, amefika Bandari ya Dar es Salaam ametakiwa alipe shilingi 100,000. Cherehani ya shilingi 200,000 Dar es Salaam, alivyofika bandarini ametozwa shilingi 100,000. Kwa hiyo, haya tunayoyazungumza ni muhimu sana yatizamwe na haya mazungumzo yanazungumzwa nenda, rudi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Awali ya yote niungane na wenzangu kuipongeza Serikali na hususani Wizara yetu hii kwa jitihada kubwa ambayo wanaifanya katika kuhakikisha nchi yetu inapata umeme wa kutosheleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika hotuba leo nitachangia maeneo mawili. Eneo la kwanza nitaanza kuchangia suala la TAENESCO. Kusema ukweli kwa takribani kipindi cha miaka 10 sasa Shirika letu la Umeme la TANESCO halifanya vizuri kifedha. Ukiangalia hesabu zake za fedha kwa takribani miaka 10 shirika letu hili lilikuwa linajiendesha kwa hasara. Hii nini maana yake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kwamba tutoke kwenye kuwa Taifa la chini kwenda kuwa Taifa lenye uchumi wa kati na hatuwezi kuwa Taifa la uchumi wa kati kama hatuna viwanda na hatuwezi kuwa na viwanda kama hatuna umeme wenye kutosheleza na uhakika. Hatuwezi kuwa na umeme wa uhakika na wa kutosheleza kama hatuna Shirika la Umeme imara kifedha na kiufanisi. Ukiangalia hesabu zetu hizi za TANESCO inaonesha kabisa ipo haja ya kufanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji ndani ya shirika letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hili limeongelewa sana. Mwaka 2002, Mercado Energético Company ya Argentina ilifanya stadi ya Shirika la Umeme la TANESCO na mapendekezo yake yakawa ili shirika hili liwe la ufanisi lazima unbundling ifanyike, tuwe na kampuni ya generation, tuwe na kampuni ambayo itasimamia masuala ya transmission na tuwe na kampuni ambayo itasimamia masuala ya distribution. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, mwaka 2003 Consultancy Company ya Marekani nao walifanya utafiti wa Shirika la TANESCO wakaja na mapendekezo hayo hayo. Sio hayo tu, mwaka 2005 iliundwa Presidential Team on Privatization Review of Utility ikiongozwa na Profesa Chijoriga nao walipendekeza hayo hayo. Mwaka 2014, Price Waterhouse Coopers waliajiriwa wafanye study ya Shirika la TANESCO nao walipendekeza hayo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niishauri Serikali baada ya mapendekezo ya Price Waterhouse Coopers wakaja na mpango wa miaka 11 wa Electricity Supply Industry Reform Strategy Roadmap ambao ulikuwa ni mzuri kabisa ulitafsiri mapendekezo yote ambayo washauri elekezi na hizi timu ambazo ziliundwa kuyaingiza katika utekelezaji lakini mpaka leo hii kimya. Ukiangalia taarifa za CAG za hesabu za TANESCO kuanzia mwaka 2010 TANESCO ilipata hasara ya shilingi bilioni 47, mwaka 2011 ilipata hasara ya shilingi bilioni 43, mwaka 2012 ilipata hasara ya shilingi bilioni 178, mwaka 2013 ilipata hasara ya shilingi bilioni 467, mwaka 2014/2015 ilipata hasara ya shilingi bilioni 124.5, mwaka 2015/2016 imepata hasara ya shilingi bilioni 346. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi reform sio sisi wa kwanza wenzetu wa Kenya na Uganda walifanya. Mwaka 1996 Kenya walikabiliwa na changamoto kama zetu, Shirika la Umeme la Kenya lilikuwa moja tu mwaka 1996 wakali-unbundling wakawa na shirika ambalo linasimamia masuala ya uzalishaji, shirika linalosimamia transmission na shirika ambalo linasimamia masuala ya distribution. Nini hatima yake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu Kenya leo hii wana- realize matunda ya reform yao. Mwaka 2015 taarifa za ukaguzi wa Shirika la Umeme la Kenya (KPLC) zimeripoti faida ya Kenya shilingi 7.56 bilioni, mwaka 2016 faida ya 7.2 bilion Kenya shilingi, mwaka 2017 faida ya 7.27 bilioni Kenya shilingi na miaka yote wamekuwa wanagawa gawio kwa Serikali. Mwaka jana wameweza kugawa gawio la jumla ya shilingi milioni 493 Kenya shilingi kwa Serikali lakini leo hii Shirika letu la Umeme la TANESCO bado linategemea lipewe pesa na Serikali kijiendesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika na Uganda hivyo hivyo. Uganda mwaka 1999 walikuwa na hali mbaya zaidi kuliko ya kwetu lakini wakafanya reform. Leo hii ni aibu Uganda walitoka kwenye vita miundombinu yote ya umeme ilikufa lakini leo hii Shirika lao la Umeme linazalisha faida. Mwaka jana tu waliweza kuzalisha faida shilingi bilioni 100 za Uganda na kugawa gawio bilioni 57.5.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe Wizara iniambie kwa vile ina mpango, huu mpango upo na ni mpago wa Wizara kabisa ina kugugumizi gani kuufuata? Mwaka huu katika ule mpango ilikuwa Shirika letu la Umeme la TANESCO liwe unbundling tuanze hizo reform. Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up aje aeleze tatizo ni nini, kwa nini hatuendi kwenye mpango ambao tayari Serikali iliukubali na kuupitisha na kwa nini mpaka leo haujatekelezwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nataka kuchangia ni suala la mauziano ya umeme baina ya TANESCO na Zanzibar. Kusema ukweli kwa kipindi kirefu sasa hili suala limekuwa vuta nikuvute.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakubaliana nami kwamba kuna tatizo kubwa baina ya biashara hii ya umeme kati ya TANESCO na upande wa Zanzibar yaani ZECO, muda mrefu sana wamekuwa wakirumbana kuhusu bei stahiki ya kuuziwa umeme na muda mrefu sana hili suala halijapatiwa ufumbuzi. Nimshauri Mheshimiwa Waziri, theory zote za upangaji bei ya umeme zinaelekeza kwamba jambo la kwanza bei ya umeme itapangwa kwa kuzingatia gharama za kuufikisha umeme kwa ngazi ya mteja husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar inachukua umeme katika level ya transimision line 132Kv. Gharama za kuufikisha umeme katika 132Kv ni ndogo kuliko kufikisha umeme katika medium voltage na low voltage. Ukiangalia bei ya umeme ambayo Zanzibar imekuwa inauziwa haiwiani kabisa, kwanza Zanzibar ni bulk purchaser lazima preferential treatment ambayo ipo, ukienda South Africa kuna bulk purchaser ambao wao wanapewa preferential treatment na sehemu nyingine mbalimbali duniani ukiachilia mbali suala la kwamba gharama za kuufikisha umeme katika 132Kv ni ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia bei ambayo Zan- zibar inanunua umeme, naomba nisome, unity moja ya KVA Zanzibar inanunua kwa Sh.16,550, wakati wateja ambao wapo katika media voltage ambapo gharama ya kupeleka umeme katika media voltage ni kubwa wanauziwa na TANESCO hiyo hiyo unity moja kwa Sh.13,200. Hili si sawa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukua Kenya, nadhani nichukue na Kenya Mheshimiwa Waziri aone mteja wa high voltage anachajiwa Sh.4,900 za Kenya wakati mteja wa low voltage anachajiwa Sh.6,000, umeona? Kwa hiyo, hapa suala la umeme na bei inayouziwa Zanzibar si sawa na haya madeni hayatokaa yalipike kwa sababu hili tatizo la bei ni kubwa ambalo linaathiri Shirika la Umeme la Zanzibar kulipa madeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru kwa kunipa nafasi.