Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Hamadi Salim Maalim (8 total)

MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Naibu Spika nafurahi sana kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri. Pamoja na majibu yake mazuri, nafurahi kwa kukubali kwamba kuna mradi unaotoa mafunzo na mitaji kwa wavuvi, lakini naomba niseme kwamba, mradi huu kuna bado katika Jimbo langu ambako kuna wavuvi wengi haujafika. Sasa naomba maelezo yake ni lini mafunzo na mitaji hii katika Jimbo langu la Kojani ili kuwafaidisha wavuvi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika mipango ambayo imepita, Jimbo la Mheshimiwa halikuwepo katika mpango, lakini katika bajeti inayokuja nitakuhakikishia kwamba wananchi wa Jimbo lako vilevile watapata mradi huo.
MHE. HAMADI SALIM MAALIM: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri lakini pia naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Wizara imekubali kwamba kumekuwa na ucheleweshaji wa mishahara kwa askari hawa wanaopandishwa vyeo, ni kwa nini basi askari hawa wacheleweshwe mishahara yao wakati kila bajeti inapopitishwa tayari nyongeza ya mishahara inakuwa tayari imeshaingizwa katika bajeti ile? swali namba moja.
Pamoja na kwamba Wizara pia imekubali kucheleweshwa kwa mishahara kwa askari hawa, kwa nini basi wanaporekebishiwa mishahara yao washindwe kulipa zile arreas za ile miezi ya nyuma au miaka ya nyuma ambayo imepita kabla ya kurekebishiwa mishahara yao?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mbunge kwa kufuatilia na kuwasemea vizuri vijana wazalendo hawa wanaojitolea kwa ajili ya Taifa letu. Mwenyewe nimezunguka katika mikoa mbalimbali na nimepata fursa ya kuwasikiliza. Matatizo ya aina hiyo si hilo tu, lakini kama Wizara tunaandaa utaratibu wa kila mkoa kuwa na watu wanaofuatilia masuala ya askari ili askari yeye kazi yake iwe ni kulitumikia Taifa na kuondokana na ucheleweshwaji wa marekebisho haya ambayo kimsingi yanatokana na taarifa kamili zinazokusanywa zinazohusu mabadiliko hayo kuchelewa kupatikana na kufikia Utumishi ambao wanahusika kwa ujumla wake kutambua nani anatakiwa alipwe kiasi gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunapanga si hilo tu la mishahara pamoja na stahili zingine zingine ambazo wanazipata zikiwemo wanapokwenda kufanya kazi nje ya kituo chake, anapokwenda kwenye operation maalum, anapopata haki yake anayo stahili, kuwa na malalamiko mengine hata ya posho anayostahili ambayo inatakiwa kimsingi iendane kwa asilimia ya mshahara wake, mshahara unapopanda posho ile inabaki constant licha ya kwamba ilitakiwa iwe kwenye uwiano wa asilimia.
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya…
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa askari wengi hufanya kazi mbali na walikozaliwa na hulazimika kuwa pamoja na familia zao, je, askari hawa wanapohamishwa na wanachotegemea ni mshahara tu, pamoja na familia zao na mizigo yao, watahamaje kufika maeneo waliyohamishiwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa kila mwaka Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani hupitishwa ikiwa na stahiki zote za askari polisi na sasa hivi askari wengi wamehamishwa, zaidi ya miaka mitatu hawajapata stahiki zao, ni lini Jeshi la Polisi litawalipa askari hao wanaodai stahiki zao za uhamisho?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kuwa na concern na maisha ya askari wetu. Hata hivyo, niseme tu kwamba askari anapohama kuna taratibu za Kijeshi pale alipokuwa anakaa ama pale ilipokuwa familia ipo huruhusiwa kukaa mpaka pale atakapokuwa amepewa fedha za kuhama na kuweza kuhamisha vifaa vyake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uwepo wa madai; katika mwaka wa fedha huu uliokwisha tumetumia zaidi ya bilioni tano kulipa madeni yaliyokuwa ya askari polisi wetu na tumetumia zaidi ya bilioni saba kulipa zilizokuwa stahili za askari wetu wa Magereza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotokea na kwa nini anaendelea kuona bado wapo wanaodai, ni kwa sababu uhitaji wa kuhama wa askari ni mkubwa kufuatana na mazingira na maeneo ambako anaweza akahitajika tofauti na watumishi wengine wa umma.
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo hayaridhishi pia nina maswali mawili ya nyongeza.
Katika jibu la msingi Mheshimiwa Waziri amesema kwamba busara na utu wa mwanadamu huwa unazingatiwa, lakini naomba niseme kwamba siyo kweli kwamba busara na utu wa mwanadamu unazingatiwa.
Mimi binafsi nimefanyiwa tendo hili na nilipodai kwamba kwa nini hamkuja na askari wa kike wakalazimisha kutumia nguvu. Sasa naomba niulize Jeshi la Polisi, je, tabia hii mbaya itamalizika lini?
Swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuniletea orodha ya malalamiko ya matendo haya yaliyotendeka? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la kwanza kwamba inawezekana kuna tukio ambalo Mheshimiwa Mbunge anathibitisha lilimtokea binafsi la kufanyika upekuzi bila kuhusisha askari wa kike, naomba hili tulichukue ili tuelewe ni sababu gani iliyosababisha hilo litokee, halafu tuone sasa mimi na yeye Mheshimiwa Mbunge labda baadae tukae tuweze kulijua suala hili lilikuwaje ili tuone hatua gani ya kuchukua. Orodha tutampatia lakini siwezi kumpatia hapa kama Mheshimiwa Naibu Spika alivyosema.
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, pamoja na kuwa Zanzibar ni mshirika katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini kuna mambo ambayo si ya Muungano kwa mfano kilimo, utalii, elimu ya msingi na sekondari, mifugo na mengineyo.
Je, kwa nini basi Zanzibar kama Zanzibar isiachiwe kujiwakilisha yenyewe katika masuala kama haya katika Jumuiya ya Afrika Mashariki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika ulimwengu huu kuna nchi ambazo zimeungana lakini zinaridhia baadhi yao kutoa mamlaka kushiriki katika mambo mbalimbali katika Jumuiya za Kikanda na Kitaifa. Kwa mfano, Switzerland kupitia tamko la Khartoum inaridhia baadhi ya nchi kushiriki katika masuala mbalimbali. Pia New Zealand kuna kisiwa cha Niue Island kinashiriki katika baadhi ya mambo. Pamoja na hayo kuna Umoja wa Visiwa vya Bahari ya Hindi ambayo Tanzania si mwanachama, kwa nini basi Zanzibar isiachiwe kujiunga na Jumuiya kama hii ikashiriki katika kufanikisha masuala yake? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ni kweli Serikali ya Zanzibar ina mamlaka katika sekta fulani za maendeleo kama vile kilimo, uchukuzi na kadhalika. Kutokana na makubaliano hayo chini ya Muungano mazao yatokanayo na uzalishaji ndani ya Zanzibar yanapata nafasi ya kuuzwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa kuuza ndani ya Afrika Mashariki Zanzibar inahakikishiwa soko la nafuu. Kwa hiyo, kile kinachozalishwa kule Zanzibar kinapata nafasi kwenye Jumuiya ambayo Zanzibar ni sehemu ya Serikali ya Muungano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kama ilivyo katika Muungano wetu kuna mambo ambayo yanaainishwa ambayo ni ya Muungano na kuna mambo ambayo yameainishwa na kukubalika ambayo yako chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Katika nchi ambazo umetoa mifano nao wanakuwa na taratibu za mgao wa madaraka katika sekta mbalimbali. Sisi katika Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania tumeainisha na kukubaliana kwamba masuala ambayo yatakuwa chini ya Muungano ni kama kwa mfano Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Ulinzi, Wizara ya Mambo ya Ndani na Mawasiliano ya Kimataifa. Haya inategemea na jinsi nchi ambazo zimeungana zinavyokubaliana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna maeneo ambayo Tanzania inatakiwa kushiriki na labda bado hatujashiriki hilo ni suala ambalo linaweza kuzungumzwa na kuainishwa ndani ya Bunge hili. Kwa sasa hivi hapo tulipo Muungano wetu unakidhi kabisa katika nafasi yake ndani ya Jumuiya ya Kimataifa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu ya Wizara bado nina maswala mawili ya nyongeza.
Pamoja na kuwa uvuvi si suala la Muungano, lakini uvuvi wa bahari kuu ni suala la Muungano, na kwa kuwa wavuvi wengi wa Visiwa vyetu vya Unguja na Pemba wanatumia uvuvi wa bahari kuu.
Je, ni lini Wizara ikishirikiana na Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu itatoa mafunzo kwa wavuvi wa Visiwa vya Unguja na Pemba ili waweze kuvua kwa ufanisi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili inaonesha kwamba uvuvi wa bahari kuu unakuwa unawasumbua sana wavuvi wetu wa Visiwa vya Unguja na Pemba ni juzi tu wavuvi zaidi ya 100 wamekamatwa nchini Kenya na sasa hivi wako ndani.
Je, ni lini Wizara ikishirikiana na mamlaka hiyo uvuvi wa bahari kuu itatoa vibali vya kudumu kwa wavuvi wetu wa Visiwa vya Unguja ili kuwaondolea usumbufu huo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza anataka kujua mafunzo na nataka nimhakikishie tu kwamba Taasisi yetu ya Usimamizi wa Bahari Kuu pamoja na Taasisi yetu ya Mafunzo ya Uvuvi (FETA) pale Mbegani Bagamoyo. Wanayo mafunzo wanayoyafanya kila mwaka, na hata mwaka jana kwa maana 2016/2017 wameweza kufundisha wavuvi takribani 150, kati ya hao 75 kutoka Visiwani na 75 kutoka Tanzania Bara. Kwa hiyo, hayo mafunzo huwa yanaendelea na hata mwaka huu 2018 yataendelea na mwakani 2019 yataendelea pia vilevile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni juu ya kadhia wanayoipata wavuvi wetu wa kutoka visiwani wanapokwenda kuvua maeneo ya jirani katika nchi ya jirani ya Kenya. Ukanda wetu sisi wa Tanzania ni mrefu sana tuna takribani kilometa 1424. Naomba niwasisitize sana wavuvi wetu wa Visiwa vya Unguja na Pemba watumie zaidi eneo letu ambalo Mungu ametujalia na lina samaki wengi zaidi. Lakini wanapotaka kwenda katika maeneo ya nchi nyingine sisi kama Wizara tuko tayari kushirikiana nao katika mamlaka zinazohusika ili kuhakikisha pia vilevile waweze kwenda kutumia fursa zinazopatikana katika maeneo mengine yanayotuzunguka.
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Wizara, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Wizara imekiri kwamba si mitaala na mihtasari yote iliyoko kwenye mtandao. Je, lini Wizara itahakikisha kwamba mitaala na mihtasari yote hii inapatikana kwenye mtandao?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mabadiliko ya mitaala na mihtasari yanayofanywa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia huwa inachuka muda mrefu sana kutufikia kule Zanzibar na hiyo kupelekea wanafunzi wetu kuathirika sana wakati wanatumia mitaala na mihtasari ile mikongwe. Je, ni lini Wizara itahakikisha kwamba mitaala hii na mihtasari hii inafikia Zanzibar kwa wakati ili waweze kujitayarisha katika masomo yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, kuhusu ni lini tutaweka mitaala na mihtasari yote kwenye tovuti, naomba nimhakikishie Mbunge kwamba kama nilivyosema, kwenye jibu la msingi kwamba tumeshaanza na tayari baadhi ya mitaala na mihtasari inapatikana. Sasa kuhusu ile ambayo bado, nimhakikishie kwamba Serikali, itachukua hatua kuhakikisha kwamba tunaweka kwenye tovuti haraka na mapema iwezekanavyo.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na changamoto iliyoko Zanzibar naomba nimhakikishie kwamba nimeipokea, tunaenda kuifanyia kazi ili kuhakikisha kwamba nako mihtasati na mitaala iwe inapatikana kwa wakati.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Labda tu nihakikishe kwamba utaratibu ambao uko kwa sasa hata mitaala inapofanyiwa mapitio kunakuwa na ushirikiano kati ya upande wa Tanzania Bara na upande wa Zanzibar na hata katika Bodi ya Taasisi ya Elimu pia kunakuwa na wawakilishi ambao wanatoka upande wa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, hivyo, inawezekana pengine changamoto ipo katika usambazaji inapokuwa imefika kwenye Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, lakini kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri tumelipokea, tutahakikisha kwamba, kama kuna mahali popote kuna mkwamo, basi iweze kufika, lakini ushirikiano ni mkubwa katika hatua zote tangu maandalizi.
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, bado nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa Serikali imekubali kuwasaidia wavuvi wadogo wadogo kujikwamua na umasikini na kuleta maendeleo ya Taifa: Je, ni kwa nini basi Serikali hii hii imeamua kuwachomea wavuvi nyavu zao ambazo nyingine hata hazistahiki kuchomwa kama ina lengo hilo?

Swali la pili; kwa kuwa uvuvi si suala la Muungano, lakini uvuvi wa Bahari Kuu ni suala la Muungano, kwa nini basi wavuvi wetu wengi wanaotoka Unguja na Pemba wanaokwenda kuvua katika mpaka wa Tanzania na Kenya wanapokamatwa Serikali yetu inashindwa kuwatetea?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, zoezi la uchomaji nyavu ni zoezi lililokwenda kwa mujibu wa sheria za nchi yetu. Katika kutekeleza zoezi hili la uchomaji nyavu haramu, tumetekeleza kwa kufuata Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya mwaka 2003 lakini na sheria zingine za nchi ikiwemo Sheria ya Mazingira.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wavuvi wote nchini kwamba Serikali iko pamoja nao katika kuhakikisha inawasaidia. Ndiyo maana yapo mambo ambayo tuliyaona kuwa yanafaa kuboreshwa, mathalan katika hili la nyavu, wavuvi wa upande wa bahari ambapo Mheshimiwa Mbunge wa Kojani anatokea, wameleta maombi yao ya kuona kuwa nyavu za milimita 10 siyo nyavu ambazo zinaweza kukamata samaki. Hivyo wametuletea maoni ya kuhakikisha kuwa tunawapelekea nyavu za milimita nane. Sisi kama Serikali tumechukua rai yao na tumeifanyia kazi.

Maboresho ya kanuni hiyo yako tayari, hivi sasa wakati wowote kuanzia sasa matumizi ya nyavu za milimita nane yatatangazwa rasmi ili wavuvi kote nchini hasa wale wa upande wa bahari waweze kunufaika na rasilimali za nchi yetu. Hivyo basi, ningewaomba waendelee kufuata sheria tulizonazo kwa muktadha mzuri wa kulinda rasilimali za Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ameuliza kuhusiana na Serikali kutokuwasaidia wavuvi wanaokamatwa upande wa kule Mkinga, mpakani na Kenya. Nataka nikuhakikishie na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote na miongoni mwa Wabunge nimashahidi, akiwemo Mheshimiwa Mbunge wa kutoka hukohuko Kojani, Mheshimiwa Kai, tumekuwa tukifanya jitihada nyingi sana, kila mara, wavuvi wetu wanapokamatwa na Serikali yetu kupitia Wizara ya Mambo ya Nje, imekuwa ikifanya mawasiliano na Serikali Kenya, wakati wote, kwa ajili ya kuhakikisha kuwa, wavuvi wale wanaruhusiwa na kupewa dhamana ya kurejea nyumbani kuendelea na shughuli zao. Wakati wote sisi tumekuwa tukiwaomba wavuvi wetu wajielekeze zaidi kuvua katika maeneo ya nchi yetu kwa sababu tunazo rasilimali zakutosha na hatuna sababu ya kwenda kuvua katika maeneo ya nchi nyingine.