Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Hamadi Salim Maalim (9 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala kwa kutujalia asubuhi hii tukaamka tukiwa wazima. Pia nikishukuru chama changu kwa kunipa nafasi hii na kuniamini kwamba nitaweza kuwawakilisha vizuri katika Bunge hili al Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya shukrani hizo, naomba nianze mchango wangu moja kwa moja katika suala zima la elimu. Tunaelewa fika kwamba elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya mwanadamu na elimu ndiyo kioo cha maisha ya mwanadamu. Ndani ya Tanzania yetu niseme kwamba kuna sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni Zanzibar ambapo ni mdau mkubwa katika elimu ya juu Tanzania. Pia katika sekondari ya kati ambapo tunakuwa na kidato cha tatu na kidato cha nne Zanzibar pia ni mdau katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo kubwa ambalo linatukumba Zanzibar katika suala zima la sekondari ya kati ni kwamba mara nyingi inapotokea mabadiliko ya mitaala huwa yanatuathiri sana Tanzania Zanzibar kiasi kwamba wanafunzi wetu inafika kufanya mtihani wakati mwingine hatujapata yale mabadiliko yaliyotokea. Wakati mwingine mabadiliko yanatokea wenzetu wanaanza kuyafanyia kazi kutoka Januari sisi tunayapa kuanzia mwezi wa nane. Inaonekana kwamba hapa kuna daraja kubwa sana baina ya Tanzania Bara na Tanzania Visiwani katika suala hili la elimu katika sekondari ya kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naishauri Wizara husika kwamba katika kufanya mabadiliko haya ni vyema wadau wenzao wa Tanzania Zanzibar wawashirikishe vizuri ili kuondoa hili daraja lililopo baina ya pande mbili kwani kufanikiwa kwa vijana wetu katika suala zima la elimu ndio kufanikiwa kwa Taifa letu. Hatutegemei kwamba vijana wetu tuwaone wanafeli kila baada ya mitihani. Hii inatuathiri sana walimu ambao tunajitayarisha kwa kiasi kikubwa sana lakini ikafikia mahali tukakuta matokeo ya wanafunzi wetu yanakuwa ni mabaya kutokana na dosari ndogo ndogo kama hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naenda kipengele cha pili cha TASAF. Niipongeze Wizara husika ya Utumishi na Utawala Bora katika suala zima la Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF). Wamejitahidi sana katika suala la kusaidia kaya maskini. Tumeona katika maeneo mengi tuliyopita nadhani hata katika ziara yetu ya Kigoma. Hata hivyo, kuna dosari ambazo zimetokea kwamba mbali ya kusaidia kaya maskini tumekuta kuna vijana wadogo ambao wanamudu kufanya kazi ndiyo wameingizwa katika mfuko huu wa kusaidia kaya maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tulipofika pale Kigoma tulimkuta mama mmoja wa miaka karibu 120 hakuingizwa katika mfuko wa kaya maskini lakini kuna vijana wa miaka 25 wameingizwa. Imani ilitujia Wabunge kama watano tukamchangia yule mama shilingi 50,000/=. Kwa kweli naomba suala hili liangaliwe vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kupitia Mfuko huu wa Maendeleo wa TASAF mbali ya kuhudumia kaya masikini unatengeneza barabara. Naomba mfuko wa TASAF uangalie kwamba kule Pemba kuna barabara mbili ambazo zinazozalisha sana. Katika kipindi cha mvua kama hiki barabara zile huwa hazipitiki hata kidogo. Barabara hiyo ni ya Mgelema na barabara ya Mjini Kiuyu. Kwa hivyo kwa kuangalia imani yao Mfuko wa TASAF, naomba kwa kutumia njia hii ya kaya maskini basi barabara zile wazipatie msaada wa kuzitengeneza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipengele cha tatu ni suala zima la vyombo vya habari. Na mimi pia naomba nigusie suala la vyombo vya habari kwamba wenzetu wanaonyesha wanaongopa. Jamani Serikali ya CCM msiogope. Ukiwa na mtoto nyumbani ikiwa siku zote unampiga yule mtoto unamchonga ukali. Itafikia mahali itakuwa baba hakuogopi tena na mama hakuogopi. (Makofi)
Mheshimwia Naibu Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 18(d) inaeleza kwamba haki ya kupata taarifa ni haki ya kila mtu tena kila wakati siyo saa nne za usiku mpaka saa tano za usiku. Hivi jamani Bunge la Jamhuri ya Muugano wa Tanzania linaendesha mijadala kwa saa saba kila siku kuanzia saa nne mpaka saa saba na kuanzia saa kumi mpaka saa mbili za usiku. Tunachukua kipindi cha saa moja tunakionyesha kwenye vyombo vya habari, uhalali uko wapi? Hivi kweli watu wetu watapata zile taarifa ambazo wanazitegemea kuzipata kutoka kwetu? (Makofi)
Mheshimwia Naibu Spika, naomba CCM msiogope acheni vyombo vya habari binafsi kama ninyi mmenyima chombo chenu cha habari, viingie Bungeni, vichukue taarifa, vipeleke kwa jamii. Naomba mfanye tathmini ndani ya Dodoma muangalie je, hata hao wana-CCM wenzenu kwa ninyi kuzuia vyombo vya habari wanawaunga mkono kwa suala hili? Nina imani kwamba kama kuna watu 100 basi 60% watakuwa hawaungi mkono suala hili. Wana-CCM msiogope jamani viacheni vyombo vya habari vifanye kazi vizuri na watu wote waweze kupata taarifa kwa wakati unaostahiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya suala hilo, naomba niende kwenye suala zima la madaraka na mamlaka kwa Serikali za Mitaa. Dhana ya Serikali za Mitaa ni pana na hii inapatikana kutokana na ushiriki mkubwa wa wananchi yaani wananchi wenyewe kushirikishwa vizuri ndiyo inapatikana ile dhana ya Serikali za Mitaa. Leo tuone Meya, Naibu Meya, Wenyeviti wa Vijiji wanaonekana hawana hadhi ndani ya Serikali za Mitaa wenye hadhi ni Wakurugenzi, Makatibu Tawala na Wakuu wa Wilaya. Hivi kweli jamani ile dhana ya kwamba wananchi ndiyo wanaotoa mamlaka kwa Serikali iko wapi? (Makofi)
Mheshimwia Naibu Spika, naomba Waziri husika kama kuna kubadilisha sheria basi wabadilishe, Wakurugenzi, Makatibu Tawala na viongozi wengine wa Halmashauri wachaguliwe kwa kura kama ambavyo anachaguliwa Meya, Naibu Meya na Wenyeviti ili kutoa mamlaka zaidi kwa viongozi hawa. Tukifanya hivi, ule utata wa kwa nini Meya, Naibu Meya, na Wenyeviti hawana ile hadhi utaondoka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata jana kuna Mbunge mmoja wa CCM alisema hapa kwamba wao wanaonekana kwenye Serikali za Mitaa si chochote si lolote. Watu wanapitisha bajeti zao, wanajenga majengo, wao wanakuja kuambiwa tu kwamba kuna jengo limejengwa kwa shilingi milioni 90 pengine jengo lile ni shilingi milioni 45. Hii inaonyesha kudhalauriwa kwamba hata kudhalauriwa Wabunge wetu waliomo kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano hawana hadhi kwenye Serikali za Mitaa. Jamani naomba Serikali iwe wazi katika suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ni suala zima la mipango mibovu ya Wizara za Ofisi ya Rais. Nadhani katika ziara zetu tulizopita tulipitia taasisi mbalimbali zilizoko chini ya Ofisi ya Rais, Utawala Bora. Kitu cha kusikitisha tulikuta kuna taasisi moja imepangisha jengo kwa mwezi wanalipa shilingi 80,000,000, kuna taasisi nyingine mbili zinalipa shilingi 40,000,000, hivi tuangalie kwa mwezi mmoja taasisi hizi zinalipa shilingi 120,000,000 kwa mwaka wanalipa shilingi 144,000,000,000.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha
muda wa mzungumzaji)
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba nikae.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kutupa uwezo walau wa kukamata kalamu na kuandika haya machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianzie mchango wangu wa bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika ukurasa wa 10 wa kitabu chake kwenye mada ndogo ya siasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kifungu hiki tumeelekezwa kuwa hali ya siasa nchini ni shwari ambapo ukiangalia kwa umakini unaona kuwa kauli hiyo haina ukweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizuia Vyama vya Siasa kutofanya kazi zake kama ilivyoelekezwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Vyama vya Siasa vina viongozi wake waliochaguliwa kwa mujibu wa Katiba zao ukiachia mbali na Wabunge. Unapomruhusu Mbunge kufanya mikutano ya hadhara katika Jimbo lake lakini ukamzuia Mwenyekiti au Katibu Mkuu kutofanya mikutano katika maeneo yaliyomo ndani ya nchi ni kinyume na Katiba na kwa maana hiyo
hatuwezi kusema kuwa hali ya siasa ni shwari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la demokrasia ambalo limeelezewa ukurasa 11 wa kitabu cha bajeti ni kweli kwamba nchi yetu inajenga demokrasia lakini demokrasia kama tunavyojua ina uwanja mpana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, demokrasia ni pamoja na
uhuru wa watu wa kutoa maoni yao, uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kukosoa na kukosolewa kwa Serikali iliyo
madarakani na mengineyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nchi hii inashuhudia jinsi raia wanavyoishi kwa woga na hofu, kosa ni kuisema Serikali. Vyombo vya habari navyo vinashindwa kufanya kazi zake kwa ufanisi huku vikijua kwamba kukosoa mamlaka ya dola ni kujitafutia balaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vielelezo vyote hivyo ni uthibitisho tosha kwamba suala la demokrasia tunalihubiri tu, lakini kivitendo halipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ni kwamba tunaelewa fika kwamba yeye si muamuzi wa kuwachagulia vyama vya siasa viongozi wa kuwaongoza. Ofisi hii ipo kwa mujibu wa Katiba kwa lengo la kusajili vyama vya siasa na pia kuvishauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Msajili wa Vyama vya Siasa hana mamlaka ya kuwachagulia wala kuwapangia vyama vya siasa viongozi ambao kwa mujibu wa Katiba za vyama hivyo si viongozi tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vyama vya siasa vinaongozwa na Katiba zao, lakini mbali na Katiba zao, pia kuna Katiba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Msajili wa Vyama vya Siasa atuelekeze ni Katiba ipi kati ya hizo tatu inayotoa uhuru wa kiongozi kujiuzuru na baadaye akarejea kwenye nafasi yake hiyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hayo ambayo Lipumba alijiuzulu na baadaye Ofisi ya Msajili ikamtambua kama Mwenyekiti halali wa chama, tunamuomba Msajili wa Vyama kama vile ambavyo anaheshimu maamuzi ya vyama vingine kwani vyote ni sawa kwa matakwa ya Katiba zao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii adhimu ya kuchangia katika hotuba ya bajeti ya TAMISEMI na Utawala Bora.
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanah Wataallah kwa kunijalia uzima nikasimama hapa leo kwa ajili ya kuchangia hotuba hii.
Baada ya shukurani hizo, pia naomba nikipongeze chama changu kwa kukamilisha ziara ya Wilaya zote za Unguja na Pemba kwa kuimarisha chama, ziara hiyo iliyofanywa na Katibu Mkuu wa Chama Maalim Seif Sharif Hamad. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, naomba niende moja kwa moja katika suala zima la utawala bora. Hapa naomba nigusie kipengele kizima cha uhuru wa kuabudu.
Mheshimwa Spika, naelewa kwamba suala la uhuru wa kuabudu ni suala la kikatiba, lakini pia katika suala zima la utawala bora ni suala ambalo limejadiliwa kwamba suala la ibada ni suala ambalo linadumisha amani ndani ya nchi. Ni suala ambalo haliangalii itikadi za vyama, ni suala ambalo linawakutanisha watu wa vyama vyote.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba katika suala hili la ibada ndani ya Jimbo langu lilizua mtafaruku mkubwa sana kwamba katika kufanya ibada upande wa chama kimoja walilazimisha kwamba lazima atajwe Mheshimiwa Rais kwenye hotuba ya Ijumaa, suala ambalo
lilizua mtafaruku mkubwa sana, ikabidi kwamba Mkuu wa Wilaya aingilie kati, achukue Jeshi la Polisi livamie kijiji kile, masuala ambayo ni kinyume na taratibu na sheria na nchi.
Mheshimiwa Spika, suala la ibada tunajua kwamba ni suala ambalo ni huru, jamii inatakiwa iabudu yenyewe kwa kufuata dini yao ambavyo inawaelekeza. Sasa Mkuu wa Wilaya aliamrisha Jeshi la Polisi livamie kwenye msikiti ule na baada ya kuvamia ule msikiti kwa kweli ikawa ni tafrani kubwa sana ndani ya Jimbo lile.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba Jeshi la Polisi tunaomba lifuate masuala mazima ya utawala bora, lisiingilie masuala ambayo yako nje na mamlaka yao. Suala la ibada ni suala la uhuru wa kila mtu.
Mheshimiwa Spika, baada ya Jeshi la Polisi kuvamia, lilikamata watu wawili. Naomba niseme kwamba kuna mzee wa miaka 65 alikuwa anahuzunisha, lakini pia kuna kijana wa miaka 35. Huyu kijana kwa sababu wazee wake walikuwa ni CCM, Mkuu wa Wilaya alikwenda akamtoa ndani.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme kwamba Jeshi la Polisi lisivae magwanda ya kijani, litumie sheria, yule mzee maskini jamaa zake walifika kumwombea dhamana, lakini kwa sababu RPC alikataa katakata, siku iliyofuata alipelekwa mahakamani na akawekwa ndani kwa muda wa wiki mbili. Yule kijana alitolewa baada ya dhamana ya Mkuu wa Wilaya. Hivi kweli Mkuu wa Wilaya anatoa dhamana kwa mshitakiwa
aliyefika polisi au polisi ndiyo wanaotoa dhamana? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Wizara husika ya Utawala Bora, Mheshimiwa Waziri alisema hapa kwamba anatoa mafunzo kwa viongozi wa polisi. Wawaelimishe kwamba watende kazi zao bila kuangalia itikadi za vyama.
Mheshimiwa Spika, naomba niende kipengele kingine. Suala hili la utawala bora nilisema kwamba linaingia katika taasisi mbalimbali. Tuliona hapa kwamba suala la vyama vya siasa kuingiliwa na Msajili wa Vyama ni kukiuka suala zima la utawala bora. Tulieleza kwa kina hapa kwamba
Profesa Lipumba alijiuzulu kwa hiari yake na baada ya kujiuzulu, Msajili wa Vyama akaingilia kati kumrejesha kwenye chama.
Mheshimiwa Spika, naomba niseme jamani au naomba niulize Wizara ya Utawala Bora, Katiba ya Chama; kuna Katiba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, kuna Katiba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, naomba mtueleze ni Katiba ipi kati ya hizi tatu inayota uhuru wa mtu yeyote
ambaye ni kiongozi kujiuzulu halafu akarudi katika nafasi yake? Mtueleze kama kuna kifungu ambacho kinaeleza, basi mtuambie kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano kifungu namba fulani kinamruhusu mtu kujiuzulu halafu akarudi katika nafasi yake au Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaruhusu mtu kujiuzulu halafu akarudi katika nafasi yake?
Mheshimiwa Spika, iweje leo Msajili wa Vyama aingilie maamuzi ya chama yaliyofanywa kihalali? Yeye anasema kwamba kikao kilikuwa ni halali, kilifikia quorum lakini maamuzi yalikuwa ni batili. Hii ni sawa na kumchanganya nguruwe na kuku ukawapika mahali pamoja halafu ukasema kwamba kuku ni halali, nguruwe ni haramu. Hiyo naona itakuwa haileti tija jamani. Tuangalie suala zima la utawala bora.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli suala la utawala bora ni suala lenye uwanja mpana sana na ni suala ambalo linastahili kuangaliwa kwa macho yote kwa kweli. Wenzangu walizungumzia hapa kwamba hata ajira zinatolewa kwa kuangalia itikadi za vyama.
Mheshimiwa Spika, hivi kweli mnalipeleka wapi Taifa hili kama kweli mpaka leo hata ajira inaangalia mtu kwa chama jamani? Hivi tutalipeleka wapi Taifa leo? Ina maana kwamba watendaji ambao ni wa vyama vya upinzani hata kama ana sifa kiasi gani, asiajiriwe ndani ya nchi hii kwa
sababu yeye ni mpinzani? Nafikiri tutakuwa hatulitendei haki Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Wanaoajiriwa kwa dini; kwa sababu inayohusika na Utumishi na Utawala Bora ni Wizara ya Utumishi
na Utawala Bora. Ndiyo niliyosema kwamba naongelea suala zima la Wizara ya Utumishi na Utawala Bora. Nilipoanza utangulizi wangu nilisema hivyo.
Mheshimiwa Spika, samahani. Sikusema wanaajiriwa kidini, nilisema wanaajiriwa kufuatana na itikadi za vyama na hili nilisema hata kule kwetu Zanzibar linafanyika, kwa sababu binafsi nina mwanangu alifanya usaili wa benki, lakini wakawa wanafuatiliwa majumbani kwao. Wanaulizwa hasa, wewe baba yako ni nani, mama yako ni nani, yuko chama gani? Kwa kweli unafikia mahali…
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Spika, ulitaka ushahidi. Sasa nilikuwa nakupa hata ule ushahidi kwamba haya yameanza hapa mpaka Visiwani yameendelea. Ahsante, namalizia suala hilo la ajira.
Mheshimiwa Spika, sasa nije kwenye suala zima la TASAF. TASAF kwa kiasi fulani wameonesha mwelekeo mzuri kwenye suala zima la kunusuru kaya masikini, lakini pia katika ajira za muda. Kwa kweli katika kaya maskini, wamesaidia pakubwa sana, isipokuwa niseme kwamba kwa upande wetu kule Zanzibar kuna suala zima la usimamizi wa hizi kaya maskini. Usimamizi wa kaya maskini umelengwa zaidi kwa upande wa Masheha. Tunakuta kwamba baadhi ya Masheha wanazitumia vibaya nafasi zao kwamba wanaingiza watu ambao hawastahili kwa sababu ni jamaa zao. Kwa hiyo, TASAF walifuatilie suala hili
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza hoja yangu kwenye suala zima la viwanja vya ndege. Viwanja vya ndege si suala la Muungano lakini ndani ya viwanja vya ndege mna mambo ambayo ni ya Muungano. Suala la anga ni suala la Muungano na kwa maana hiyo utendaji wake wa kazi pia utakuwa uko chini ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuondosha sintofahamu ya utendaji kwa section hii kwa upande wa Zanzibar ningeomba Wizara husika ikaliangalia suala hili kwa kina na baadaye kupeleka mapendekezo yao kwa Serikali ya Muungano ili suala hili kwa upande wa Zanzibar libakie kama suala la Zanzibar na utendaji wake usimamiwe na SMZ.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya suala hilo sasa naomba niende moja kwa moja kwenye suala la bandari. Wafanyabiashara kwa mfano wanaoleta magari kutoka nje ya nchi na kuyateremsha kwenye Bandari ya Zanzibar hulazimika kuyalipia magari hayo kodi zote zinazostahilil. Hata hivyo, mfanyabiashara huyo huyo akiamua sasa kusafirisha gari hilo na kulipeleka Tanzania Bara pia hulazimika kulipia kodi mbalimbali Bandarini Dar es Salaam. Je, hatuoni kwamba kufanya hivyo ni kuwarudisha nyuma wafanyabiashara hao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hayo tu bali hata gari iliyonunuliwa Zanzibar na baadaye kusafirishwa kupelekwa Tanzania Bara basi ushuru wake ni mkubwa sana, kwa nini hali iwe hivyo na hii yote ni nchi moja? Nashauri hili liangaliwe ipasavyo ili kuwaondolea wafanyabiashara ugumu wa biashara.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala, kwa kunijalia uwezo huu wa kusimama hapa kuchangia hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Baada ya shukrani hiyo, pia nikushukuru wewe kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze moja kwa moja kwenye vyuo vikuu. Kwenye nchi yetu kuna vyuo vikuu mbalimbali na kwenye vyuo vikuu hivi kuna wanafunzi ambao wanalipiwa na Bodi ya Mikopo, lakini pia kuna wanafunzi ambao hawakupata mkopo kutoka Bodi ya Mikopo wanagharamiwa na familia zao, familia za kimaskini na kinyonge. Leo kuna baadhi ya vyuo vikuu baada ya kumalizika mwaka wanabadilisha malipo yaani malipo yanaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyoelewa kwa ambavyo nilisoma mimi katika vyuo vikuu, mkataba ule unapobadilika kwa yule ambaye anaendelea mwaka mwingine unakuwa haumuathiri lakini kilichotokezea kwa baadhi ya vyuo vikuu ni kwamba wanapobadilisha mkataba mwanafunzi aliyepo mwaka wa pili na wa tatu pia mkataba ule unamuathiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, juzi nilikutana na wanafunzi wa Zanzibar University, kuna wanafunzi wanafanya degree ya nursing na walikuwa wanalipia kwa mwaka shilingi 2,197,000 kwa wale walioanza mwaka jana lakini mabadiliko yalipotokea mwaka huu uliopita wamepandishiwa kutoka shilingi 2,197,000 mpaka shilingi 2,486,000. Tumuangalie mwanafunzi huyu ambaye analipiwa na familia ya kinyonge, ataelekea wapi mzazi keshajipangia kwamba hana uwezo wa kuongeza shilingi 400,000 kwa mwaka za kumsaidia mtoto wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanafunzi wa diploma ambaye alikuwa analipa shilingi 1,500,000 sasa anatakiwa alipe shilingi 1,900,000, athari hii ilitakiwa imuangalie yule ambaye anaanza sasa. Naomba Waziri atakapokuja kujumuisha atupe maelezo, vyuo kama hivi ambavyo vinapandisha tuition fee katika hali ambayo si ya kiutaratibu wanavichukulia hatua gani? Kwa sababu wanafunzi hawa tayari walishaanza na mkopo ambao unakubalika lakini wanapandishiwa mkopo ule katikati ya masomo, hilo ni la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni suala zima la upungufu wa walimu. Tunasema kwamba hakuna elimu bila ya walimu, kama hatuna walimu na elimu inakuwa haipo. Upungufu wa elimu uliopo katika nchi yetu ni mkubwa sana. Tukichukua data ya mwaka 2016/2017 na suala hili Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ililisema katika bajeti ya mwaka 2016 na ya 2017 na mara hii tunalizungumza tena kwamba upungufu wa walimu ni mkubwa sana. Kwa mfano, katika bajeti ya 2016/2017 kwa shule za msingi kulikuwa na upungufu kutoka walimu 191,772 mpaka kufikia walimu 179,291 ambapo hii ni sawa na asilimia 6.5. Ushukaji huu mkubwa wa idadi ya walimu umesababisha uwiano wa mwalimu mmoja kuweza kufundisha wanafunzi zaidi ya 50 mpaka kufikia 70. Tuangalie, hapa tutapata elimu bora au tutapata bora elimu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Waziri atakapokuja atueleze ni mkakati gani wameuandaa kwa sababu toka 2016 mpaka leo hakuna ajira ya walimu iliyofanywa. Hali kadhalika kuna walimu ambao wanastaafu katika kipindi chote hicho, kwa hiyo, ina maana kwamba bado idadi hii niliyoisema hapa inawezekana ikawa ni kubwa zaidi kufikia leo kwa sababu hii ni idadi ambayo ilikuwa imeoneshwa katika bajeti ya mwaka 2016/2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika shule za awali hali kadhalika upungufu nao ni mkubwa. Katika shule za awali alitakiwa ratio iwe ni 1:25 lakini ratio hiyo inakuwa ni 1:150. Hebu tuangalie, wanafunzi hawa wanaoanza sasa tunawasomeshaje wanafunzi 150 kwa mwalimu mmoja, matokeo yake yatakuwa ni yapi? Mtoto anatoka shule ya awali anarudi nyumbani, ukimuuliza umefundishwa nini anakwambia kwamba nimefundishwa kukata (kuvuka) barabara. Hivi kweli ufanisi utakuwepo jamani? Mkakati unahitajika, Waziri atueleze ni mkakati gani pia wameuandaa katika kutatua suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la maslahi ya walimu, madeni pamoja na kupandishwa madaraja. Jamani ni kitu cha aibu, tulisema kwamba tunafanya uhakiki ukikamilika tutapandisha walimu madaraja na tutalipa madeni. Kuna walimu tokea siku waliyopewa barua za kulipwa madeni yao ni mwaka mzima sasa hivi Halmashauri zimeshindwa kuwalipa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pia nashukuru kupata nafasi hii ya kuchangia bajeti hii ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019. Naomba nianze na Kitabu cha Mpango kama Mheshimiwa Waziri Mpango alivyoelezea, kwenye ukurasa wa tisa uchumi wa Taifa, Mheshimiwa Waziri ameeleza kwamba Pato la Taifa limepanda kutoka asilimia 7.0 hadi asilimia 7.1 ambapo pato hili lilikuwa ni trilioni 47.173 mpaka trilioni 50.5.

Mheshimiwa Spika, pato la Taifa najua ndilo linalo- determine kile kima cha kila mtu kwa nchi ile, sasa tukija kwenye kima cha kila Mtanzania kutokana na pato hili la Taifa Mheshimiwa Waziri amesema kwamba kima cha kila Mtanzania kitakuwa ni Sh.2,275,000 kutoka Sh.2,086,000.

Mheshimiwa Spika, tukichukua Pato la Taifa ambalo ni trilioni 50.5 sijui tugawe kwa idadi ya watu wangapi tulionao mpaka tupate milioni 2,275,000; kwa kweli naona kwamba bajeti imetudanganya katika kiwango hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hivyo kitabu cha CAG ukurasa wa 63 amesema kwamba Pato la Taifa ni trilioni 106.8 lakini kitabu cha Waziri Mpango kinasema ni trilioni 50.5, sasa sijui tushike ipi iliyo na ukweli ya CAG au ya Waziri Mpango? Inawezekana pengine na Kamati ya Bajeti na wao wana kima chao sijui ni ngapi. Kwa hiyo naomba Waziri atueleze je, wametumia takwimu ipi ya CAG ya kitabu cha Mpango katika kutuelezea pato la kila Mtanzania la 2,275,000 kwa kila mtu. Hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, naomba niende kwenye mapato ya Taifa na matumizi. Bajeti ya 2018/2019, imekisia kwamba itakusanya trilioni 32.48, sasa tukija katika matumizi yaliyopangwa, tumepanga kwamba tutalipa madeni ya Serikali ambayo ni trillioni 10, sasa trilioni 10 hizi tukizilipa kwa mwaka tunakuta kila mwezi tukichukua calculation ya kila mwezi tunatakiwa tulipe bilioni 833.33, lakini baadaye tunakuwa na mishahara ambayo tumepanga kwamba kwa mwaka tutatumia trilioni 7.409. Hii tukiigawa kwa mwezi tunapata kwamba kila mwezi tunatakiwa tutumie bilioni 617, ambazo tukujumuisha hizi za madeni tu na mishahara ni karibu trilioni 1.4 wakati makusanyo ya Taifa tunasema ni kati ya trilioni 1.2 mpaka 1.3, hatujaingiza matumizi mengine hatujaingiza miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, matumizi mengine Serikali imepanga kwamba itatumia trilioni 3.054 kwa mwaka ambapo kwa kila mwezi tunatakiwa tutumie bilioni 254. Miradi tumepanga kwamba tutatumia trilioni 12, hizi tumesema trilioni 2.13 ni mapato ya nje, tuyaweke mbali inamaana tuna trilioni 10 ambazo zinatokana na mapato ya ndani. Trilioni 10 hizi tukigawa kila mwezi tunapata bilioni 833.33. Sasa tukijumlisha yote tunakuta kwamba tukitoa zile bilioni mbili tuwe na makusanyo ya shilingi trilioni 2.529, hivi kweli Serikali tuna uwezo wa kukusanya mapato haya kwa kila mwezi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watueleze Serikali wana mikakati gani wakati trend ya 2016/2017, imeonesha tumekusanya trilioni 21, trend ya 2017/2018 tumekusanya pia trilioni 21.89 je, kuna mikakati gani waliyoiandaa mpaka kuweka makisio makubwa kiasi hichi. Hii bajeti ni ya udanganyifu na wala haitekelezeki. Kwa hali hii inaonesha kwamba mkakati huu uliopangwa wa mapato na matumizi wote ni hewa, bajeti haitekelezeki. Hilo ni jambo la pili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la tatu, naomba niende kwenye kueleza kwamba bajeti yetu ni hewa, tunapanga makubwa makusanyo yetu lakini uwezo wa kukusanya ni mdogo. Mwaka 2016/2017 tulipanga makusanyo ya trilioni 29.54 tukakusanya trilioni 20 ambayo ni sawa na asilimia 70, asilimia 30 hazipo, kwa hivyo inaonesha kwamba hizi asilimia 30 tulijikusanyia tu kumbe ni hewa hazipo, sawa tulijipangia kumbe ni hewa hazipo.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2017/2018 tukaongeza yaani ule mzigo mdogo tuliokuwa nao 2016/2017, tukauona kwamba ni mdogo tukaongeza mwingine tukajikusanyia huku mgongoni kutoka 29 tukaja 31, hii 29 haikutekelezeka jamani tunakuja 31. Nashauri bora tungerudi nyuma tukaangalia ule uwezo wetu, kwamba hatuna uwezo wa nakusanyo ya trilioni 29 tuangalie reference kwamba reference inaonesha kwamba uwezo wa makusanyo yetu ni mdogo sana, kwa hivyo tusisogee mbele wakati pale tulipokisia mwanzo hatukupafika, nashauri kwamba tungerudi nyuma tukaweka makisio ya makusanyo ambayo tunaweza kuyatekeleza. Kwa hali hii inaonesha kwamba mipango tunayoipanga yote inakuwa ni mipango hewa, Serikali tupangieni mipango inayotekelezeka msitupangie mipango ya kisiasa, sawa jamani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie na kifungu cha nne ambapo ni suala zima la asilimia 10 ya vijana na wanawake. Naomba nimalize kwamba kwenye asilimia 10 hii ya vijana na wanawake mimi ni Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI, inaonesha kwamba takribani halmashauri nyingi zinakuja na bajeti yao kwamba 10 percent ya wanawake na vijana ni kwa mfano makusanyo ni bilioni 50, inawekwa ten percent kwamba ni pengine 25 millions lakini ukiangalia kilichotumiwa ni milioni 5,000,000! Sasa ukiuliza hiki chingine kiko wapi?

Mheshimiwa Spika, Kila Mkuu wa Mkoa anayekuja ukimuuliza hichi chingine kimepelekwa wapi, hakuna majibu. Kwa hiyo, ningeshauri kwamba asilimia 10 hii ya vijana na wanawake itolewe katika hali inayostahiki kwa sababu katika kupitia kwetu kwenye Halmashauri tumekuta kwamba asilimia 10 hii inatumika vizuri sana kwa vijana na wanawake na inatuondolea lile tatizo la ajira. Nashauri kwamba Wizara husika waisimamie katika hali ya asilimia mia moja ili itekelezwe kama inavyopasa.

Mheshimiwa Spika, namalizia na ushauri mwingine kidogo.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, siungi mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi hii. Kwanza, naomba ni- declare interest kwamba ni Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze na asilimia kumi ya wanawake, vijana na walemavu. Kwa kweli Halmashauri au Mikoa yetu mingi sana kwenye asilimia kumi hii ya wanawake na vijana inaonesha kwamba hela hii inatiwa mifukoni. Naomba nitoe mfano hai wa kitabu hiki cha Mkoa wa Manyara kwa bajeti ya 2016/2017. Mkoa wa Manyara asilimia kumi ya bajeti ya 2016/2017 ilitenga Sh.1,552,261,255 lakini kati ya hizo zilizotolewa kwa vikundi ni shilingi milioni 511.3 sawa na asilimia 33.

Mheshimiwa Spika, nasema pesa hizi zinaingizwa mifuko kwa sababu ukipitia kitabu chote hiki hukuti popote hiyo Sh.1,040,000,000 ambazo hazikutumiwa zilipoelezwa kwamba zimetumiwa kwa shughuli fulani. Ukiwauliza wao wenyewe wanapokuja na randama zao hizi wanasema kwamba zilizobakia zimetumiwa lakini unapopitia kitabu chote hiki hakuna eneo lolote linaloeleza kwamba hii shilingi bilioni moja iliyobakia imetumiwa ama katika ujenzi wa madarasa au katika ununuzi wa meza na viti au vitu vingine. Inasemekana kwamba hela hii inaingia kwenye mifuko ya wahusika. Naomba Halmashauri/TAMISEMI ifuatilie kwa kina suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ajenda yangu nyingine ni Mfuko wa Rais wa Kujitegemea. Mfuko huu tunajua kwamba umeanzishwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anachaguliwa na pande mbili za Muungano (Zanzibar na Tanzania Bara) na safari iliyopita najua Zanzibar alipata kura zaidi ya laki tatu, inawezekana hivyo.

Mheshimiwa Spika, sasa Mfuko huu wa Kujitegemea hadi leo unatumika upande mmoja tu wa Muungano. Ushauri wangu, ama mfuko huu ubadilishwe jina uwe ni Mfuko wa Rais wa Tanzania Bara au kama ni Mfuko wa Rais wa Kujitegemea kwa sababu Rais ni wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mfuko huu pia ufike Zanzibar kwa kusaidia Wazanzibar walioko kule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipengele kingine ni suala zima la...

SPIKA: Mheshimiwa, hakuna Rais wa Tanzania Bara.

MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Spika, sawa hakuna Rais wa Tanzania, sasa kama ni hivyo mfuko utumike pande mbili ijulikane kwamba ni Rais wa Jamhuri ya Muungano usitumike upande mmoja, ndiyo tunachodai.

Mheshimiwa Spika, kipengele kingine ni upande wa TASAF kwenye kunusuru kaya maskini. Naomba niseme kwamba suala hili kwa kweli kwa Zanzibar limepiga hatua kubwa sana. Wenzetu wa upande wa Bara kwa kiasi fulani tunapotembelea miradi tuki-compare wa kule na huku kwa kweli wenzetu wamepiga hatu kubwa sana. Katika kipindi kifupi tu kilichopita kwenye malipo ya Oktoba na Desemba imeonyesha kuna tofauti ya malipo yale waliyokuwa wakilipwa mwezi Oktoba na mwezi wa Desemba. Kwa hivyo, nitawaomba wahusika…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana, dakika tano zimeisha.

MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Spika, naomba nimalize tu kidogo, naomba dakika moja.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kuna wahusika ambao Oktoba walilipwa Sh.60,000 lakini Desemba wakalipwa Sh.36,000; mwingine akalipwa Sh44,000 mwezi Desemba akalipwa Sh.32,000 bila kupewa taarifa kwamba makato haya yanatoka wapi. Naomba suala hili lifuatiliwe ili tupate ufumbuzi wa kujua watu wetu wanakatwa pesa hii kwa misingi gani?

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia uzima wa kuweza kusimama hapa katika Bunge hili na kupata nafasi ya kuchangia katika bajeti hii ya Serikali Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze mchango wangu kwa kunukuu maelezo yangu niliyoyatoa katika bajeti ya mwaka jana nilipoichambua bajeti na kusema kwamba bajeti iliyoletwa ni hewa. Bado narudia maelezo yangu yale yale kwamba na bajeti mara hii pia ni bajeti hewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya mwaka jana mpaka kufikia mwezi Aprili, 2019 imechangia shilingi trilioni 21.22 ukiachia miezi mwili iliyobakia kuna shilingi trilioni 11.24 ili ikamilishe bajeti yote. Siamini kwamba miezi miwili tunaweza tukakusanya shilingi trilioni 11 tukaweza kukidhi bajeti nzima ya Serikali. Bajeti ya mara hii imeongezwa kutoka shilingi trilioni 32.48 kufikia shilingi trilioni 33 kwahivyo bado naendelea kusema maelezo yangu kwamba bajeti iliyoletwa ni hesa na haitekelezeki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanini nakasema ni hewa? Bajeti hii imepanga kutumia shilingi trilioni 9.721 kwa Mfuko Mkuu wa Serikali ambapo ukizigawa hizi kwa miezi 12 tunalazimikiwa ni kila mwezi kupata shilingi bilioni 810.08; mishahara imapangwa kutumia shilingi trilioni 7.558 ambapo kwa kila mwezi tunatakiwa tutumie shilingi bilioni 629.83; OC ni shilingi trilioni 3.576 ambapo kwa kila mwezi tunatakiwa tutumie shilingi bilioni 298.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kwenye fedha za maendeleo, ukitoa fedha za nje, tuchukue yale makusanyo ya ndani tu tumepanga kutumia shilingi trilioni 9.737 ambapo kwa kila mwezi ni shilingi bilioni 811.416. Jumla ya makusanyo yote haya na matumizi yaliyopangwa ni shilingi trilioni 2.548 kwa kila mwezi. Hivi kweli tuna uwezo wa kukusanya shilingi trilioni 2.5?

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi siamini kwamba Serikali yetu ina uwezo wa kukusanya shilingi trilioni 2.5 labda iwe ni mara mbili zaidi tuichukue kama tutumie miaka miwili ndiyo tutaweza kukusanya hiyo, lakini kwa mwaka mmoja hatuna uwezo wa kukusanya shilingi trilioni 2.5 ukichukua uzoefu wa miaka yote mmine tuliyoingia katika Bunge hili na makusanyo yaliyokuja na bajeti ilivyotekelezwa inaonesha kwamba bado bajeti hii ni hewa na itapelekea ugumu sana kutekelezwa katika Wizara mbalimbali za Serikali. Hapo nimetoa malipo ya wafadhili yaani wahisani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukichukua na wahisani ina maana tunatakiwa tupate shilingi trilioni 2.757 kila mwezi ili tuweze kutekeleza bajeti yetu na iweze kwenda sawa, lakini kwa maana hiyo nasema kwamba bado bajeti ni hewa na italeta ugumu katika utekelezaji wake. Kambi Rasmi ya Upinzani ilipowasilisha mawazo yao ilijaroibu kuivuta bajeti kutoka shilingi trilioni 33 mpaka kufika shilingi trilioni 29 angalau na Serikali ingeona mapendekezo kama hayo kidogo tukawa na lile gap ambalo halitekelezeki likawa ni dogo, lakini leo tunafikia gap ambalo halitekelezeki karibu shilingi trilioni tisa/ trilioni nane. Bajeti ambayo haitekelezeki kwa kiasi chote hicho jamani? Hebu Waziri wa Fedha akija hapa atueleze kwanini wanatuletea bajeti ambayo inakuwa na gap kubwa sana ambalo halitekelezeki kiasi kwamba tunashindwa hata kutekeleza miradi ya maendeleo, kulipa madeni ambayo Taifa linadaiwa na nchi za nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kifungu hicho naomba sasa niende kwenye kifungu cha pili ambacho ni Zanzibar ndani ya Muungano. Mheshimiwa mwenzagu aliyetangulia hapa Mheshimiwa Ally Saleh alijaribu kuelezea mapato ya Muungano, mimi nitakwenda upande mwingine. Katika kitabu hiki cha bajeti ambacho Mheshimiwa Waziri aliwasilisha hapa ndani ya kitabu hiki ukianza ukurasa wa mwanzo mpaka mwisho, Zanzibar imetajwa mahali pawili tu alipotajwa Rais, Dkt. Salmin na pale ambapo Zanzibar iliondolewa VAT kwenye suala la umeme. Hivi Zanzibar haipo kwenye Muungano hata iguswe katika maeneo hayo tu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiachia mbali kitabu hiki cha bajeti, kitabu cha miradi ya maendeleo Zanzibar haikuguswa hata sehemu moja. Miradi yote ya maendeleo iliyoelezwa mle ipo Tanzania Bara tu, hivi kweli Zanzibar mnaitendea haki gani jamani kiasi kwamba nimenukuu humu kwamba ndani ya kitabu kile cha miradi ya maendeleo kuna Wizara ya Elimu ya Juu inatekeleza miradi chungu nzima kwenye vyuo vikuu, mbona Zanzibar hawakupewa kwenye Chuo Kikuu cha SUZA angalau japo kile kimoja? Kuna shule zenye form five na form six angalau wangetengenezewa maabara japo moja tukajua kwamba na Zanzibar ipo kwenye sehemu ya Muungano, lakini kwa kweli mnachofanya katika suala zima la bajeti hii Zanzibar hamkuifanyia fair na wala hamko sahihi kuitenga Zanzibar wakati Zanzibar ni sehemu ya Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilijaribu kuangalia kitabu hiki ukurasa wa 16 mpaka ukurasa wa 25; yameleezewa mafanikio ya Awamu ya Tano ya Serikali ya CCM. Kuanzia ukurasa huo mpaka hapo niliposema wa 16 mpaka 25 hivi Serikali ya CCM iko Tanzania Bara tu? Maana ikiwa Zanzibar hakuna Serikali ya CCM, mafanikio haya yaliyoelezwa humu kwa upande wa Tanzania Bara tu Zanzibar hakuna miaka yote hiyo jamani? Sijui kama Zanzibar mnaitendea haki kwa kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba jamani, tunaomba kama Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano itendewe haki. Kuna miradi ambayo ipo kwenye kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kwa mfano; kuna Bandari ya Wete, Bandari ya Mkoani, Bandari ya Mpigaduru, Uwanja wa Ndege wa Zanzibar, uwanja wa Ndege wa Pemba basi hata mmoja angalau mkasema kwamba tunaondoa mdudu mchuzini tunawapa angalau hii Bandari ya Mpigaduru angalau japo moja jamani, hivi kweli mnayotundea ni haki jamani? (Makofi)

MBUNGE FULANI: Sio haki.

MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kwenye kifungu cha madeni ya Taifa; kwenye madeni ya Taifa mwaka jana hapa tuliambiwa mpaka Aprili, 2018 deni la Taifa lilikuwa shilingi trilioni 49 na katika bajeti ile ya mwaka jana ikapangiwa kwamba deni la Taifa litalipwa kwa shilingi trilioni 10 na juzi wakati wa uwasilishaji wa bajeti ya Wizara ya Fedha hapa Waziri alipoulizwa suala la madeni ya Serikali akasema kwamba tumeanza kulipa ila tumeanza kulipa ya miaka ya 1980, hivi hiyo miaka ya 1980 haipo kwenye ile jumla ya deni lililowasilishwa mwaka jana? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maana ikiwa haimo mtuambie kwamba deni lile la trilioni 49 ni la mwaka jana tu 2018 na hivyo katika mwaka jana 2018 halikutekelezwa kwa sababu inaonyesha kwamba mara hii deni lile limeongezeka kufikia shilingi trilioni 51, zile shilingi trilioni 10 zilizotengwa mwaka jana kwa ajili ya kulipa deni zilipelekwa wapi hebu tuambieni mlizipeleka wapi shilingi trilioni 10 za mwaka jana? Waziri wa Fedha ukija hapa utueleze shilingi trilioni 10 zilizotengwa mwaka jana kwa kulipa madeni ya Taifa zilipelekwa wapi mpaka deni lile la shilingi trilioni 49 la mwaka jana likaja tena mwaka 2019 vilevile kama lilivyo likiongezwa tena linafikia shilingi trilioni 51. Itabidi ukija hapa mtupe maelezo kwa nini halikulipwa shilingi trilioni 10 za madeni ya nje zilizopangwa kulipwa zilipelekwa wapi mtuambie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo naomba niende kwenye kifungu cha tozo; nina imani kwamba ukienda dukani kununua vitu ukinunua kidogo bei itakuwa ni kubwa, lakini ukinunua vingi kwa vyovyote vile muuza duka atakupunguzia. Hali kadhalika ukienda kwenye kiwanda ni hivyo hivyo nashangaa kuona kwamba madereva wamepigwa changa la macho kwenye leseni, madereva walivyokuwa wanalipwa miaka mitatu leseni ilikuwa shilingi 40,000, juzi Mheshimiwa Waziri katika kuwasilisha bajeti yake akasema sasa tunahamisha kutoka miaka mitatu hadi miaka mitano kutoka shilingi 40,000 mpaka shilingi 70, 000 hivi jamani hamuoni kwamba mnawapiga changa la macho madereva?

Mheshimiwa Naibu Spika, ukinunua khanga pair tatu dukani utauzia kila khanga pair shilingi 7000 lakini ukinunua pair tano utauziwa bei ya jumla hivi miaka mitatu na miaka mitano mingi ni ipi tuambieni mimi nashangaa kuona kwamba Mheshimiwa Waziri wa Fedha anatupandishia bei kwenye miaka mingi, lakini miaka midogo bei inakuwa ni ndogo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. HAMAD SALIM MAALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze mchango wangu kwa kumshukuru Allah kwa kunijaalia afya njema na kuweza kutoa mchango wangu katika Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Nchi yetu ni nchi ya kilimo ambapo wakulima huzalisha matunda kama maembe, machungwa, mananasi na mengineyo. Kwa vile tumekusudia kujenga Tanzania ya Viwanda kwa nini basi mazao kama hayo ambayo nimeyataja hapo juu ambayo huzalishwa kwa msimu tunashindwa kuyatengenezea viwanda na kuyasindika kwa matumizi ya baadaye?

Mheshimiwa Naibu Spika, matunda hayo kama yangesarifiwa nina imani kwamba nchi yetu ingeweza kuuza nje ya nchi na kupata fedha za kigeni na hivyo kupelekea kuongeza uchumi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kweli tunataka Tanzania ya Viwanda ni vema tukaangalia kwa kina nini kilisababisha viwanda vyetu vingi vimekufa, tena vile ambavyo malighafi zake zinapatikana ndani ya nchi yetu. Kama tatizo ni wataalam basi kabla ya kuanzisha ufufuaji wa viwanda hivyo, basi vijana wapewe taaluma inayolingana na viwanda hivyo; lakini lakini tatizo ni uongozi mbovu basi ni vema kukawa na usimamizi wa hali ya juu au wa mara kwa mara ili kugundua hizo kasoro zinazopelekea viwanda kufa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania yetu ya leo tunazalisha mpira kwa wingi lakini General Tyre imekufa na tunaagiza mipira kutoka nje ya nchi. Pia tunazalisha ngozi kwa wingi lakini tunashindwa kuzalisha viatu, mabegi na hata mikanda, vitu vyote hivi tunaagiza kutoka nje ya nchi. Hivi kweli kwa msingi huo tuna lengo thabiti la kuwa na Tanzania ya Viwanda?

Mheshimiwa Naibu Spika, masikitiko yangu makubwa ni kushindwa hata kuanzisha viwanda vidogo vidogo ambavyo vingeweza kusaidia kutoa ajira ndogo ndogo kwa vijana wetu. Leo Tanzania ni nchi ya tatu katika Afrika kwa ufugaji lakini tunaagiza maziwa kutoka nje. Pia maembe yanazalishwa kwa wingi Zanzibar lakini yanasafirishwa katika nchi za kiarabu tena huuziwa hapa nchini kwa fedha zetu za Tanzania. Hili linalikosesha mapato mengi Taifa letu.