Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Abdallah Haji Ali (2 total)

MHE. ABDALLA HAJI ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa masikitiko tu kidogo kwamba hili suala tunasema ni la Muungano lakini katika majibu ya Naibu Waziri naona hakutaja upande wa pili hata neno moja, sijui kama tumo au hatumo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Sheria ya Mafuta na Gesi ni ya Muungano na hivyo kila nchi inastahiki kupata gawio stahiki kutokana na mauzo ya gesi. Je, ni kiasi gani cha gawio kilichopelekwa kwa Hazina ya Zanzibar tangu mauzo haya ya gesi yafanyike?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kitaalam tunaambiwa kwamba gesi inayozalishwa Tanzania ni gesi safi kabisa, yaani haihitaji gharama kubwa kufanyiwa mchakato kwa matumizi. Sasa tulitegema kwamba umeme unaotokana na uzalishaji kutokana na gesi hii ungekuwa rahisi kwa watumiaji lakini kila siku umeme unapanda bei. Ni kwa sababu gani? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA NISHATI NA MADINI): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyosema kwamba suala la gesi asilia ni suala la Muungano kwa mujibu wa Ibara ya 4 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 na Nyongeza ya kwanza ya Katiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu gawio la Zanzibar kutokana na mapato ya gesi ni suala la takwimu, ningeomba niweze kulifanyia kazi halafu niweze kumpatia Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili kwamba katika hali ya kawaida gesi inatakiwa iweze kuzalisha umeme ambao ni bei rahisi, naomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba huo ndiyo ukweli na toka tuanze kuzalisha umeme kwa kutumia gesi tumeweza kuokoa fedha nyingi sana. Kwa mwaka inakadiriwa tunaokoa dola za Kimarekani bilioni 1.6 ambapo kama tungetumia umeme wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimweleze tu kwamba pamoja na bei ya umeme kuendelea kubadilika badilika lakini bado itabakia kwamba tokea tumeanza kutumia umeme wa gesi tumeweza kupunguza gharama kubwa sana za fedha tunazotumia katika kuzalisha umeme.
MHE. ABDALLAH HAJI ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Niseme tu kwamba urasimu huu kwa kweli umekuwa ukitupa usumbufu mkubwa sana sana kwa majimbo ya Zanzibar. Nilikuwa naomba ikiwa hili suala halipo kisheria bora lifutwe ili na sisi hizi pesa tuzipate kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nina maswali ya nyongeza mawili madogo kabisa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Mfuko huu wa Maendeleo ya Jimbo umeanzishwa mwaka 2009, takribani sasa ni miaka 10. Majimbo yamekua, watu wameongezeka na mahitaji yameongezeka vilevile lakini kiwango kinachotolewa hadi sasa ni kilekile. Je, Serikali ina mpango gani wa kuuongezea Mfuko huu fedha ili upate uweze wa kuendana na mahitaji ya majimbo yetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kumekuwa na malalamiko kwa utendaji wa baadhi ya Wakurugenzi katika Halmashauri; wanakuwa hawatendi vizuri. Je, Waziri yuko tayari kuzitembelea Halmashauri hususani Halmashauri zetu za Zanzibar kukaa na Wabunge na Wakurugenzi wa Halmashauri ili kulizungumzia au kupeana uzoefu juu ya suala hili ili twende sambamba?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hi kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abdallah Haji, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikiri kabisa kweli kuna ongezeko la watu, mahitaji na vitu vingine lakini nimuahidi tu kwamba kuna haja ya kufanya tathmini ili kubaini hayo ambayo tunayasema sasa. Baada ya tathmini hiyo tutajua nini kifanyike kuhusiana na ongezeko la kiwango kinachotolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwa kweli nimshukuru na mimi wakati wowote nitakuwa tayari kwenda Zanzibar na nimuahidi tu kwa sababu nakwenda Zanzibar mara nyingi, nitakuja tukae nanyi pamoja na Wakurugenzi wote kama ambavyo ameshauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.