Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Abdallah Haji Ali (13 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ABDALLAH HAJI ALI: Sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, muweza wa mambo yote. Pili shukrani zije kwako Mheshimiwa Naibu Spika kwa umahiri wa kazi yako.
Nikianza kwa kuchangia Wizara hii, naanza na suala zima la kilimo. Kilimo kama usemi ulivyozoeleka kuwa ni uti wa mgongo, maana yake ni kwamba kilimo ndiyo kila kitu, ni shughuli inayotoa ajira kubwa nchini kuliko sekta nyingine yoyote, yaani kilimo kimeajiri zaidi ya asilimia sabini . Changamoto iliyo ndani ya sekta ya kilimo ni kutokana na kutegemea mvua za msimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, dunia haisimami, ni lazima na sisi twende na wakati, naishauri Serikali tuondokane na kilimo cha kutegemea mvua za msimu peke yake, umekuwa ni wimbo wa siku nyingi juu ya suala la kilimo cha umwagiliaji lakini sijui tunakwama wapi? Naishauri Serikali kufanya utafiti wa hali ya juu kuona kwamba tunakwamuka na suala la umwagiliaji linachukuliwa nafasi na kuondokana na utegemezi wa mvua za msimu pekee.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la umwagiliaji, naishauri Serikali tujikite zaidi kwenye uvunaji wa maji ya mvua. Tazama tunasifika kuwa wamwagiliaji wazuri wa bahari, maana yake maji yote ya mvua tunayaruhusu kutiririka na kuingia baharini bila faida yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kwa kutumia miundombinu mbalimbali kuweza kujenga mabwawa takribani nchi nzima ili kuweza kuhifadhi kiasi kikubwa cha maji ya mvua ili kufanikisha kilimo cha umwagiliaji kwa ufanisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mabwawa tukiweza kuyaimarisha yanaweza kutuimarishia ajira nyingi hasa kwenye kilimo cha mbogamboga kwa maeneo kama yenye uhaba wa mvua. Aidha, yatatupunguzia migogoro kwa kiasi kikubwa kati ya wafugaji na wakulima kwa upatikanaji wa maji, pia wafugaji watanufaika sana katika kukidhi mahitaji ya wanyama wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, faida yenyewe ya uwepo wa mabwawa, watu watapewa kujitengenezea ajira kwa ufugaji wa samaki ambao samaki hao ni hitaji kubwa kwa chakula cha binadamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, maji ya mvua ni neema kubwa kwetu kutoka kwa Mungu iwapo tutaweza kuyavuna kitaalam na kuyatumia vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mifugo inasemekana Tanzania ni nchi ya pili kwa mifugo mingi katika Afrika. Ukweli huu unatudhihirishia kwamba tusingekuwa na shida ya aina yoyote itokanayo na mahitaji ya mifugo kama vile maziwa, siagi, samli, viatu na mazao mengine yatokanayo na mifugo, lakini bidhaa zote hizi nyingi au asilimia kubwa tunaagiza kutoka nje na hata nchi jirani, mfano Kenya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali hii, naishauri Serikali itimize kwa ufanisi ile azma yake ya kutaka kuifanya Tanzania iwe nchi ya viwanda. Kusudio hili likitimia naishauri sana Serikali kuzingatia ujenzi wa viwanda vya biashara za mifugo ikiwezekana kila mkoa wenye mahitaji haya ili kupunguza mahitaji na malalamiko ya wafugaji na hasa ikizingatiwa sekta hii imeajiri watu wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uvuvi; Tanzania tumejaaliwa na neema kubwa ya bahari, maziwa na mito ambayo ni mashamba yaliyosheheni mazao na ambayo mashamba hayo yaani bahari na mito hayahitaji mbolea wala pembejeo yoyote, bali yanataka kuvunwa tu. Ushauri wangu kwa Serikali, suala la uvuvi limekuwa likiongelewa kwa siku nyingi, sasa wakati umefika wa Serikali kuliangalia suala hili kwa kina kuona kwamba rasilimali hii inafanyiwa kazi ili inufaishe jamii na Serikali kwa ujumla. Serikali imezungumza sana juu ya kuishughulikia Sekta ya Uvuvi, naomba azma hii itekelezwe na tija ionekane kwa manufaa na ustawi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ABDALLAH HAJI ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa mambo yote duniani. Pili, nampongeza Mheshimiwa Spika kwa kusimamia majukumu yake vyema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia angalau machache kati ya mengi kwa Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Kwa nia njema kabisa Serikali katika kutafuta changamoto ya usafiri ilileta meli ya kisasa ili kupunguza tatizo la usafiri kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo. Lengo kuu la ujio wa meli ile ni kupunguza tatizo la usafiri kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo, lakini cha kushangaza meli ile haionekani ikifanya huduma iliyokusudiwa na tatizo lile la usafiri bado lipo vilevile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kwamba malengo na nia njema iliyokusudiwa haikufikiwa, lakini kubwa ni kwamba meli ile Wizara husika na Serikali kwa ujumla wanafahamu ilipo na matumizi yake. Hivyo ni vyema wananchi wakapata maelezo sahihi ili wafahamu meli ile iko wapi na inatumika vipi? Naomba Mheshimiwa Waziri atoe maelezo japo kidogo juu ya kutokufikiwa kwa dhamira nzuri iliyokusudiwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala zima la viwanja vya ndege. Kumekuwa na malalamiko makubwa kwamba viwanja vingi havina taa hivyo ndege zetu zinashindwa kutua usiku. Katika ulimwengu huu wa sasa wa sayansi na teknojia safari ni wakati wowote iwe usiku au mchana ili kwenda na wakati na kurahisisha mambo yawe sawa. Naishauri Serikali kuliona suala hili na kuwapatia huduma walipa kodi wa nchi hii ili waweze kwenda na wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuweka taa katika viwanja vyetu vya ndege ni miongoni mwa kuboresha miundombinu ili iwe mizuri na kuwaweka watu wetu katika hali ya kisasa zaidi.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. ABDALLAH HAJI ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa mambo yote. Pili, nakupongeza wewe binafsi kwa usimamizi mzuri wa shughuli za Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na mchango wangu katika hoja hii ya Wizara ya Afya ni kwamba kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu dhidi ya Wizara hii kutoka kwa wananchi. Wizara ya Afya ndiyo Wizara mama inayoratibu ustawi wa afya za watu nchi nzima, na la kukumbuka ni kwamba afya ndiyo mambo yote, pasipo afya miongoni mwa wananchi hapana Taifa endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, malalamiko yapo zaidi juu ya upatikanaji wa dawa, vifaa tiba kama mashine za x–ray, vitanda na mambo mengine. Kutokana na upungufu wa mambo haya jamii inawaangalia zaidi Waziri na watendaji wake kwamba ndio wanaohusika kukidhi mambo haya ikiwemo upatikanaji wa madaktari, wauguzi na hata magari ya wagonjwa. Mheshimiwa Waziri na watendaji wake wana nia nzuri juu ya ufanisi wa mambo haya ila wamekuwa wakikwamishwa na ukomo wa bajeti na kutokupatikana kwa kile pia ambacho kimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali ili kuliweka Taifa katika hali nzuri kiafya, Serikali isilifumbie macho suala la upatikanaji wa dawa na vifaa tiba. Serikali izishughulikie changamoto hizi kwa kuipa upendeleo Wizara ya Afya kwa kuitengea fungu la kutosha litakalokidhi upatikanaji wa vifaa, dawa na madaktari ili kukidhi huduma za afya za Watanzania.

Naishauri sana Serikali kutumia vyema kodi za wananchi kwa kuziondoa changamoto za huduma za afya katika ngazi zote ili kuondoa malalamiko ya wananchi ambao ndio msingi wa Taifa. Ni imani yangu kwamba Serikali baada ya maombi mengi ya Waheshimiwa Wabunge mbalimbali itatenga pesa za kutosha na kuzipeleka zinakohusika kwa wakati na kufanya ufuatiliaji ili kuhakikisha kwamba haya yanatimizwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie suala la haki za watoto. Watoto wana haki zao za msingi kutoka kwa wazazi, ndugu, jamaa na Serikali kwa ujumla. Usimamizi huu ni jukumu la Serikali na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Jukumu hili limekuwa ni kikwazo hususan kwa wazazi kukosa elimu au uelewa juu ya haki za mtoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na idadi kubwa ya watoto wanaokoseshwa haki zao za msingi kwa kukoseshwa elimu na badala yake kufanyishwa kazi zisizowahusu, watu wanafikiri kwamba ajira ya watoto ni sehemu ya maisha yao. Kuna idadi kubwa ya watoto chini ya umri wa miaka 18 wanaofanyishwa kazi za ndani wakikoseshwa elimu ambayo ndiyo wajibu wao kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali izidi kukemea masuala ya ajira za watoto hasa za kuajiriwa majumbani kwa kazi za mapishi, usafi na uangalizi wa watoto. Pia Serikali iweze kufanya sensa nchi nzima kuwatambua watoto wote wanaotumikishwa kinyume cha sheria na haki za mtoto na kuweza kudhibitiwa kwa wale wote wenye tabia ya kuwatumikisha watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha Tanzania ina waathirika wa HIV 1,538,382. Watanzania tuko zaidi ya milioni 50, haya ni makisio ya hivi karibuni, je, ni utaratibu gani utumikao kuwapima watu na kupata takwimu za uhakika? Ni dhahiri kwamba idadi kubwa haijafikiwa ili kupata takwimu inayowiana na idadi ya Watanzania, hivyo naishauri Serikali kuzidi kutoa elimu juu ya watu kuweza kupima kwa hiari ili kupata takwimu halisi za watu wanaoishi na HIV.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ABDALLA HAJI ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa mambo yote kutujalia kama hivi alivyotujalia. Pia nakushukuru wewe Mwenyekiti kwa kunipa nafasi hii ndogo na mimi nichangie angalau machache katika mengi ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa langu ni moja tu, napenda kuzungumzia kidogo suala la utafiti kwamba Taifa lolote duniani haliwezi kuendelea ikiwa halitatilia maanani suala zima la utafiti wa sayansi na teknolojia. Suala zima la utafiti wa sayansi na teknolojia ni lazima lipewe kipaumbele ndiyo maendeleo yapatikane katika nchi. Tanzania si kisiwa ni nchi kubwa, Tanzania ni nchi hai na ipo hatuwezi kuwa kinyume na teknolojia hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa Tanzania chombo kikubwa kinachodhibiti masuala ya utafiti ni Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH). Hiki ni chombo kinachodhibiti masuala ya utafiti na ndiyo chombo mama wa mambo yote ya utafiti yanayofanyika hapa Tanzania. Chombo hiki kazi yake kubwa kisheria ni kufanya utafiti katika nyanja za sayansi na teknolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mataifa yaliyoendelea tunaona kwamba wamekuwa wakitenga asilimia kubwa ya bajeti yao katika kuendeleza masuala ya utafiti. Hapa kwetu Tanzania tunaona kwamba Serikali inakuwa inaitengea sana Tume hii katika kufanya utafiti lakini tukiri kwamba pesa zinazotengwa katika kufanya utafiti hazitoshi, ni kidogo. Hapa Waziri mwenye dhamana wewe ndiyo mwenye kilio, ulie na sisi wa kando tukuone tulie pamoja Serikali ikuongezee mapato juu ya suala zima la utafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia takwimu za hizi karibuni za miaka iliyopita utaona viwango vilivyokuwa vikitolewa kwa ajili ya Tume hii. Mwaka 2010/2011 kilichotengwa ni shilingi bilioni 30, lakini kilichotolewa hakikuzidi shilingi bilioni 19. Aidha, mwaka 2011/2012 zilitengwa shilingi bilioni 25.7 lakini kilichotolewa kwa ajili ya masuala ya utafiti hakikuzidi shilingi bilioni 7.3.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2012/2013 zilitengwa shilingi bilioni 21.4 zilizotolewa ni shilingi bilioni 12.8. Mwaka 2013/2014 zilitengwa shilingi bilioni 16 na hapa kwa bahati mbaya hakuna chochote kilichotolewa. Mwaka 2014/ 2015 zilitengwa shilingi bilioni 16.5 na zikatoka shilingi bilioni
3.8 na mwaka 2015/2016 zilitengwa shilingi bilioni 4.3 na hakujulikana kitu gani kilichotokezea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa naishauri Serikali, Taifa lolote linalotaka kuendelea...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. ABDALLA HAJI ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ABDALLAH HAJI ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma anaye rehemu, muumba mbingu na ardhi na vilivyomo. Aidha, nakushukuru wewe Mheshimiwa Mwenyekiti kwa uongozi wako madhubuti hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ina majina mengi iliyopewa kwa sababu ya utukufu na ubora wake na kwamba aliye nayo huambiwa kaelimika. Elimu ni ufunguo wa maisha, elimu ni maisha na majina mengi mengineyo kuhusu elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la msingi, elimu hasa ni ile inayomkomboa mtu katika kusimamia majukumu yake na ya Kitaifa. Taifa lolote duniani haliwezi kuendelea bila ya mfumo mzuri wa elimu na mfumo bora wa elimu duniani ni ule unaozingatia mambo muhimu kama yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu imsaidie mlengwa mwenyewe na Taifa lake kwa ujumla wake. Pia elimu imuwezeshe msomi huyu kuweza kujitegemea na aondokane na kuwa tegemezi. Pia imsadie kuijua dunia yake anayoishi hususan katika dunia hii ya utandawazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hapa kwetu Tanzania mfumo wetu wa elimu ni tofauti kidogo na matakwa ya mfumo bora wa elimu. Katiba yetu inataja kwamba kupata elimu ni haki ya kila Mtanzania ya msingi kabisa, lakini elimu inayotolewa hapa haikidhi haja na matakwa ya mfumo bora wa elimu. Mfumo na mitaala yetu haijengi katika kutoa elimu bora (quality education) yaani ya muhitimu kuweza kujitegemea kutokana na elimu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uboreshaji wa mfumo mzuri wa elimu ni pamoja na kuongezea bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kukidhi haja zote za elimu. India ni nchi inayoendelea kama Tanzania lakini bajeti yao katika elimu ni zaidi ya asilimia kumi, jambo ambalo limeifanya India kufanikiwa na kuwa miongoni mwa nchi bora duniani kwa kuzalisha na kuuza wataalamu mabingwa nchi zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii yote ni kutokana na uwekezaji mzuri juu ya elimu nchini India. Takwimu zinaonesha katika kampuni kubwa mashuhuri sana duniani iliyoko Marekani ya Microsoft ya tajiri mkubwa duniani, Bill Gates ina wafanyakazi zaidi ya asilimia kumi kutoka India, madaktari bingwa wengi walioko Marekani ni Wahindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuiga jambo zuri si dhambi, wenzetu wamefanikiwa baada ya kuona umuhimu wa kuiongezea na kuikuza Wizara ya Elimu, hivyo naishauri Serikali itenge na kutoa pesa za kutosha kwa elimu ya ngazi zote, vyuo vya ufundi, kilimo na nyanja zote na sisi tuzalishe na kuuza wataalamu nchi za nje badala ya kuuza watumishi wa ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu yetu inayotolewa zaidi inapelekea kuongeza idadi ya wahitimu katika kila ngazi. Kwa mfano, idadi ya wahitimu wanaomaliza shule za msingi, sekondari, vyuo vikuu inaongezeka kila mwaka. Lakini idadi yote hii inayoongezeka kila mwaka ni tegemezi, hawana uwezo wa kujiajiri wenyewe, idadi kubwa ni lazima wapewe ajira Serikalini vinginevyo wahitimu hawa ndio hubakia wakizagaa tu mitaani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maombi kwa Serikali, hatujachelewa bado, Serikali itilie maanani suala la mfumo bora wa elimu ili elimu itolewayo iwe ya manufaa zaidi ili utegemezi juu ya ajira kutoka Serikalini ipungue sana. Ikiwa Serikali itaboresha Vyuo vya Ufundi (VETA) na huduma kamilifu, ni imani yangu kwamba wahitimu wetu wataweza kujiajiri wenyewe na kuondoa mrundikano wa wahitimu wanaosubiri kupata ajira.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. ABDALLAH HAJI ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu muumba wa mambo yote. Pili, nakushukuru wewe binafsi kwa ujasiri wako wa kuliongoza Bunge kwa umahiri mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia katika Wizara hii angalau kwa uchache kati ya mengi ya Wizara hii ya Biashara na Viwanda. Viwanda ni kichocheo cha maendeleo katika kila Taifa duniani, viwanda ni mkombozi wa wananchi kupitia ajira na kuimarisha biashara na ustawi wa hali za wananchi kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo na uimarishaji wa viwanda katika nchi na duniani kote unapitia hali au hatua mbalimbali, uamuzi wa nchi yetu kuja na mkakati wa kujenga viwanda ni wa busara sana ila kabla ya kufikia huko kwanza kuna hizi hali mbalimbali mpaka kufikia uchumi wa viwanda, lazima zitekelezwe ili manufaa tunayoyafikiria yaweze kupatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vinahitaji wataalam na injinia mbalimbali ili waweze kuviendesha kwa uzalishaji, hivyo naishauri Serikali kujipanga na wataalam wazawa na wazalendo kwa kuwasomesha vijana wa kutosha ili viwanda tuviendeleze viwe na wafanyakazi wazawa na wataalam wazawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo naishauri Serikali ikubali kutenga fedha kiasi cha kutosha ili kutoa nguvu kubwa juu ya kupata elimu kwa wataalam watarajiwa, ambao watafanya kazi katika viwanda hivyo. Lakini jambo la kusikitisha ni bajeti ndogo itengewayo Wizara ya Elimu ili kusimamia mafunzo na elimu ya kuzalisha wataalam, hivyo tumekuwa hatufikii lengo kutokana na bajeti ndogo itolewayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa uchumi tunaouendea ni wazi kwamba tunahitaji mafundi mchundo wa kutosha ili kukidhi haja ya viwanda vyetu vinginevyo kama Serikali haikutilia mkazo jambo la elimu tutakuwa siku zote wa kuajiri wataalam toka nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, India ni nchi inayoendelea kama Tanzania lakini sitaki kusema kwamba tuko sawa na India lakini India imelipa uzito mkubwa suala la elimu kiasi kwamba India wanatenga zaidi ya asilimia 10 ya bajeti ya nchi yao kwa upande wa elimu, sisi Tanzania bado tuko
nyuma si zaidi ya asilimia 4.5, hivyo India imefanikiwa kuzalisha wasomi na wataalam wengi sana wametosha India na wanauza wataalam duniani kote. Mfano, katika kampuni kubwa kama Microsoft ya Bill Gates takwimu zinaonesha zaidi ya wafanyakazi mabingwa asilimia 10 ni kutoka India. Pia Madaktari Bingwa wengi walioko Marekani na duniani kote ni Wahindi.

Mheshimiwa Naibu Spika, siri ya mafanikio hayo ni mkakati wa makusudi wa kuwekeza katika elimu. Kwa hali hii ni lazima na sisi tusiwe nyuma kwa kuiweka elimu kuwa ni kitu cha chini, huwezi kuendelea katika nyanja yoyote duniani bila elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri tena Serikali itilie maanani juu ya elimu katika nyanja zote hasa katika suala zima la utafiti, jambo ambalo halionekani kupewa nafasi kubwa wakati inafahamika wazi kwamba bila utafiti huwezi kuleta ufanisi wowote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali itakuwa tayari kuiwezesha elimu na sisi tutazalisha wataalam wengi kwa ajili ya viwanda vyetu na ziada tunaweza kuuza nje, vinginevyo kama hatukuwa makini kwa uwekezaji juu ya elimu baada ya kuzalisha wataalam tutakuwa tukizalisha watumishi tu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. ABDALLAH HAJI ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa mambo yote. Pili, nakushukuru wewe binafsi kwa umahiri wa kazi yako ya hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza mchango wangu juu ya suala zima la uvuvi. Uvuvi hapa Tanzania ni sekta ambayo ikiwekezwa vizuri inaweza ikatoa mchango mkubwa sana katika Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu imebarikiwa kwa kuwa na eneo kubwa la bahari, mito, maziwa na eneo kubwa la mabwawa ambayo maeneo hayo yamesheheni rasilimali kubwa ya samaki na mazao mengine ya baharini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahari ni kama shamba lililosheheni samaki wengi wa kutosha, shamba ambalo halihitaji mbolea, madawa wala halihitaji pembejeo ya aina yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahari yetu ni shamba linalotaka kuvunwa tu na mazao yake ni muhimu na ni bidhaa unayoweza kuuza duniani popote. Kwa fursa hii tuliyoipata kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwa na bahari kubwa yenye samaki wengi hatukuwa na sababu yoyote kuwa soko la kununua samaki kutoka nchi nyingine. Hata hivyo, ni ukweli usiopingika kwamba Tanzania kweli ni soko la nchi nyingine kama Afrika ya Kusini, China na nchi nyingine kwa kununua samaki na kutumika hapa kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa samaki baharini ni pamoja na kuwepo dhamira ya makusudi ya Serikali ya kuweka miundombinu ya kisasa na ya uhakika. Nipende kusema kwamba katika eneo hili Serikali haijaonesha utayari kwa kuifanya sekta ya uvuvi kuwa mchangiaji mkubwa kwenye pato la Taifa. Hii ni kwa sababu hatuoni juhudi kubwa ya Serikali kutayarisha miundombinu sahihi ya kumudu uvuvi kama vile zana za kisasa zenye uwezo mkubwa wa kuvua bahari kuu, lakini pia ujenzi wa bahari ya uvuvi, vyuo vya uvuvi vitakavyotoa wahitimu wenye uwezo mkubwa lakini pia uwepo wa viwanda ili samaki wakivuliwa waweze kushughulikiwa ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la sekta ya uvuvi kama Serikali itachukulia umuhimu wa kipekee ndio mwarobaini utakaolisaidia Taifa kuongeza mapato na kutoka katika hatua hii na kulisogeza Taifa mbele katika nyanja mbalimbali. Sekta hii ikipewa fursa pia itaweza kutoa fursa nyingi za ajira kwa Watanzania na kutoa unafuu wa maisha kwa kupunguza umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iitendee haki neema ya uvuvi na kuitendea haki neema hii ya bahari tuliyonayo tunaweza kuondokana na umaskini wa kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kiujumla wake. Namwomba Mheshimiwa Waziri japo kwa uchache atupe maelezo ya kina kuhusu uvuvi, Serikali imejipangaje?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ABDALLAH HAJI ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na muweza wa mambo yote.

Aidha, napenda kukushukuru wewe binafsi kwa kusimamia majukumu yako kwa juhudi kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza kuchangia katika Wizara ya Maji na Umwagiliaji ni kwamba mara kadhaa nimekuwa nikishauri juu ya mfumo mzima wa kudhibiti maji ya mvua. Nchi yetu haina uhakika wa kupata mvua za kutosha kwa kipindi cha mwaka. Aidha, baadhi ya maeneo katika nchi yetu hayapati mvua kabisa, yaani ni kame, lakini pia mvua zinazonyesha nchini kwetu bado hatujazitendea haki.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaambiwa kwamba Tanzania ni mabingwa wa kumwagilia bahari kwa maana kwamba mvua zinazonyesha hapa nchini na kutuletea maji mengi, tunashindwa kuyadhibiti angalau kwa kiwango kidogo na badala yake yote yanakwenda zake baharini na kupotea. Kwa kipindi kifupi maji hupotea mara moja na ukame ukarudia palepale.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba Serikali ifanye juhudi ya makusudi ya kuliangalia suala la udhibiti wa maji ya mvua kwa kutafuta uwezo kwa njia tofauti ili kuweza kujenga mabwawa ya kisasa ili kuongeza na haya yaliyopo tuweze kuhifadhi maji ya mvua ili yaweze kutumika katika shughuli mbalimbali za kijamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, dhana ya uhifadhi wa maji ya mvua ni pana sana na ina gharama sana, lakini pindi Serikali ikilikubali na kulifanikisha, litatatua changamoto nyingi za kijamii na kiuchumi. Serikali ikiwa italitilia maanani suala la uchimbaji wa mabwawa na uhifadhi wa maji ya mvua, kuna faida nyingi za kijamii na kuiuchumi ambazo zinaweza kutatua na kuondoa lawama, lakini pia na kuimarisha ustawi wa hali za wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na uwepo wa mabwawa nchini, watu watapata matumizi mbalimbali ya maji majumbani kama kupikia, kufulia na matumizi mengine. Aidha, yataimarisha uchumi kwa watu kufanya shughuli za ufugaji wa samaki na kuongezea vipato vya wananchi; lakini pia kuwapatia ajira vijana. Hivyo uwepo wa mabwawa ya kutosha nchini ni ukombozi wa maisha ya watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna changamoto kubwa ya malisho na unyweshaji maji kwa mifugo. Uwepo wa mabwawa utatupunguzia kero kubwa juu ya mifugo yetu kwa upande wa unyweshaji. Pia uwepo wa mabwawa unawasaidia wakulima katika suala zima la umwagiliaji, shughuli ambayo inawapatia faida kubwa wakulima wetu nchi nzima kwa kilimo cha mbogamboga na nyanya. Hii pia ni ukombozi mkubwa kwa wananchi juu ya upatikanaji wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwarobaini wa kuondoa ukame na shida ya maji nchini, suala la udhibiti wa maji ya mvua kwa kujenga mabwawa ni la msingi sana. Hata hapa Dodoma mvua iliyonyesha mwaka huu; kama maji yale yangedhibitiwa, Dodoma ingekuwa ni Mkoa wa neema mwaka mzima. Ila la kusikitisha, mvua imepita na maji yamepita, nchi inarudia hali ya ukame.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kuondokana na mazoea, tugharimike, tuhifadhi maji ili yatufaidishe kwa maendeleo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ABDALLAH HAJI ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa yote. Aidha, nakupongeza wewe binafsi kwa kuongoza Bunge vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tena kwa mara nyingine napenda kuzungumzia mwenendo mzima wa safari za ndege nchini hususan ndege ndogo ndogo. Namuomba Mheshimiwa Waziri ikimpendeza atoe maelezo kuhusu jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, takribani ndege ndogo ndogo za karibu mashirika yote yanayotoa huduma kwa safari za ndani zinaendeshwa na rubani mmoja. Nakusudia kwamba nyingi ya ndege hizi zinaendeshwa na rubani mmoja tu bila ya rubani wa akiba. Ndege hizi pamoja na udogo wake zimewekewa viti vya rubani wa akiba lakini cha kushangaza hakuna siku utakuta kuna rubani wa akiba katika kiti kile.

Mheshimiwa Naibu Spika, viti hivi huwa vinatumika kupewa abiria jambo ambalo sio sahihi. Rubani ni binadamu kama binadamu mwingine anaweza kupata matatizo wakati wowote na mahali popote na mifano imeshatokea. Hivi karibuni tulisikia kwenye vyombo vya habari nadhani ilikuwa Marekani bwana mmoja alikuwa akitokea kiwanja kimoja kwenda kingine kwa safari za kawaida yeye na mkewe tu. Katika safari yao walipokuwa angani yule bwana ulimpata ubinadamu kulekule angani akaumwa na kufariki kulekule angani. Kilichomsaidia yule mama kwa bahati na yeye alipitia mafunzo ya urubani na aliweza kuiongoza ndege na kutua salama na kutoa mwili/maiti kwenda kuzikwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ni kwamba naishauri Serikali itilie maanani juu ya kuwepo marubani wa akiba katika ndege za mashirika yote yanayomiliki ndege ndogo ndogo zinazotoa huduma ndani ya nchi na wasiachiwe vile viti vya rubani wa akiba kuviuza kwa abiria. Sina uhakika juu ya sheria zetu za anga hapa Tanzania juu ya marubani wa akiba, namuomba Waziri atufahamishe tupate uelewa mpana pengine ninavyodhani ni kinyume.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ABDALLAH HAJI ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa mambo yote. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Spika kwa uongozi wake hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Mikopo inafanya jambo zuri kwa kutenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi wa nchi hii wa elimu ya juu kuweza kulipia masomo yao ya vyuo vikuu. Pamoja na hayo, kuna changamoto nyingi juu ya upatikanaji wa mikopo ya elimu ya juu. Kwanza idadi ya wanafunzi wapatao mkopo wa elimu ya juu ni kidogo sana, idadi kubwa ya wanafunzi wanaohitaji mkopo wa kuendelea na elimu ya juu wanakosa fursa hiyo. Naishauri Serikali kuongeza bajeti ya Wizara ili na Bodi ya Mikopo ipate fungu kubwa la kuweza kuwakopesha wanafunzi wengi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha hayo, hao ambao wanapata mkopo kuna changamoto ya vigezo. Ili upatiwe mkopo wa elimu ya juu unahitajika kukidhi vigezo mbalimbali jambo ambalo ukiacha vigezo hivyo baadhi ya wanafunzi huwa wanapatiwa mikopo hiyo bila ya vigezo. Hivyo, naishauri Wizara husika kuzingatia vigezo na kutoa mikopo kwa wale wanaostahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ya Bodi ya Mikopo ni ukusanyaji wa mikopo hiyo. Mategemeo ni kurejeshwa kwa mikopo hii ili na wengine waweze kukopeshwa na wao wajiendeleze ila hili linategemea kupata ajira kwa wahitimu waliokopa ili Serikali iweze kuwabana na kukatwa kwenye mishahara yao kwa kiasi kilichokubaliwa na kurejeshwa Wizarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha ni pale wahitimu wengi wanapokosa ajira na kubaki mitaani bila kazi na hatua za kuwafanya walipe wakati hawana ajira ni ngumu. Hivyo, naishauri Serikali mara tu wahitimu wetu wa elimu ya juu wanapohitimu Serikali isiwe na kigugumizi cha kuwaajiri kwani ajira zao ndiyo njia ya kurejesha mikopo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu inahitaji kuwekewa miundombinu mikubwa. Wakati umefika wa kwenda na wakati na moja ya miundombinu ni lugha ya kufundishia. Kwa sasa naiomba Serikali kutilia maanani na mkazo juu ya lugha ya kiingereza. Sisemi kwamba lugha ya kiswahili iachwe lakini mkazo mkubwa uwekwe kwenye lugha ya kiingereza kwani ndiyo lugha inayotumika katika mambo yote ya kimaendeleo ya duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu inaingia katika uchumi wa viwanda, viwanda vinategemea wafanyakazi wenye taaluma na wataalam wetu tunategemea kuwapata katika vyuo vyetu vya ufundi. Nashauri Serikali kwa makusudi ilibebe suala hili na iziwezeshe shule na vyuo vya amali viweze kutoa mafundi wazuri ambao tutawatumia katika kukuza uchumi wetu wa viwanda. Walimu wa vyuo hivyo wapewe motisha na wawezeshwe ili na wao wawawezeshe wanafunzi wao kitaaluma kwa mafanikio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu motisha kwa walimu. Naiomba Serikali isiwasahau walimu kwani ndiyo mambo yote. Ikiwa walimu wanabaki na malalamiko kila kukicha basi na ufanisi kwa wanafunzi wetu utakuwa mgumu. Naishauri Serikali kukisikiliza kilio cha walimu kwa kuboresha maslahi yao. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ABDALLAH HAJI ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa mambo yote. Aidha, nakupongeza wewe binafsi kwa uongozi wako mzuri Bungeni na unaotumia busara.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni maisha ya kila kilicho hai duniani. Kutokana na umuhimu wa maji, takribani Wabunge wote wametoa malalamiko yao kuhusu matatizo ya maji katika majimbo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, cha kushangaza ni kwamba miradi mingi ya maji inalalamikiwa kwamba wakandarasi hawafanyi vizuri kwenye miradi hii ambayo huwa inaigharimu sana Serikali. Miradi mingi kwa mujibu wa maelezo ya Wabunge hukabidhiwa kwa wananchi kwamba imekamilika lakini kwa masikitiko ni kwamba miradi hiyo haitoi maji. Hii ni hasara kubwa kwa Taifa hakuna Mbunge yeyote ambaye alipopata nafasi ya kuchangia asitoe malalamiko ya shida ya maji kwa wapiga kura wake hususani majimbo ya vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hapa ndipo Serikali inapaswa kujitathmini yenyewe kwamba fedha inatoka kwa utekelezaji wa miradi ya maji, lakini upatikanaji wa maji hayo ni wa kusuasua na thamani ya fedha itumikayo ya walipa kodi na zile za wahisani ukweli haionekani. Hivyo wananchi wanolipa kodi wana haki ya kuilalamikia Serikali yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa maelezo ya Wabunge walio wengi kwamba sababu kubwa ya ukosefu wa maji ni wakandarasi wasio waaminifu au wasio na weledi wa masuala ya upatikanaji wa maji. Naishauri Serikali kwamba suala la maji ni mtambuka na ndio kipaumbele cha maisha ya kila kiumbe kilicho hai, sasa ikiwa Serikali imekusudia kumtua mama ndoo kichwani yenyewe ijiongeze na iweze kusimamia utekelezaji wa wakandarasi na ihakikishe unatoa tija ili kuondokana na shida hii. Aidha, kufanya upembuzi yakinifu kwa wakandarasi wenye uwezo wa weledi wa miradi ya maji ili kuepuka kupewa dhamana kwa wasio na uwezo. Hili likiwezekana angalau kwa asilimia 50 litaepusha malalamiko ya wananchi na kutoa thamani ya fedha ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo hii sio mara ya kwanza kulizungumzia ni upotevu wa maji ya mvua ambayo ni neema kubwa kutoka kwa Mungu. Kwa eneo hili bado naishauri Serikali kutenga bajeti maalum ya kutengeneza mabwawa maalum ya kuvuna maji ya mvua ambayo yakifanyika hayo tunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa shida ya maji. Mabwawa yataweza kusaidia kilimo cha umwagiliaji, kunyweshea mifugo, kufugia samaki na matumizi ya nyumbani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania tumekuwa wamwagaji wakubwa wa maji baharini kwa maana kwamba maji ya mvua yote kwa muda mfupi yanakimbilia baharini na kuiacha nchi ikiwa kame. Jambo la uvunaji na uhifadhi wa maji ya mvua pamoja na kwamba una hasara yake lakini una faida kubwa. Mfano hapa Dodoma mvua yote iliyonyesha lakini ni muda mfupi tu sasa maji yote hayaonekani. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ABDALLAH HAJI ALI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa mambo yote. Aidha, napenda kumpongeza Spika kwa uongozi wake mahiri Bungeni.

Mheshimiwa Spika, nichangie kuhusu uvuvi wa Bahari Kuu Tanzania. Bahari ni fursa kubwa kwa waliojaliwa kuwa nayo kama sisi hapa Tanzania. Mwenyezi Mungu katujalia mwambao mkubwa wa bahari kuu.

Mheshimiwa Spika, eneo hili kama Serikali ingeweza kulitumia vyema, nchi yetu ingeweza kujiongeza na kutoka katika hatua tulionayo sasa.

Mheshimiwa Spika, bahari ni shamba lililosheheni mazao mengi, yaani samaki na vitu vingine kama gesi na mafuta. Bahari ni shamba ambalo halihitaji madawa, mbolea na wala halihitaji pembejeo ya aina yoyote. Lipo tayari kwa ajili ya kuvunwa tu.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali iondokane na usingizi mzito ilionao ili iweze kuitumia rasilimali ya bahari ambayo imesheheni neema kubwa na ya maana kabisa.

Mheshimiwa Spika, nchi zote zenye bahari kama yetu wananufaika na neema hii kwa kuweka mikakati madhubuti ya kutumia teknolojia ya kisasa na vyombo vya uvuvi vya kisasa.

Mheshimiwa Spika, nchi za wenzetu wenye mikakati thabiti ya uvuvi katika bahari kuu wanakuja kuvua katika maeneo yetu na wanatuvulia samaki wetu kwa wingi na kupeleka neema hii katika nchi zao. Siyo vyema kwamba neema ipo kwetu na kuwaachia wengine kuwavua samaki wetu na kuwahamishia kwao na baadae kuwasafirisha kuja nchini kwetu tukawa ni wateja wao kwa rasilimali itokayo ndani ya bahari yetu.

Mheshimiwa Spika, imefika wakati sasa kwa Serikali kuifanya bahari kuwa ni chanzo kingine cha mapato ya nchi kwa kuwavua samaki waliomo ili wainufaishe nchi kimapato. Sasa Serikali ije na mpango mkakati wa uwekezaji kama unavyofanywa katika sekta nyingine, kwa mfano, sekta ya madini na utalii.

Mheshimiwa Spika, samaki ni chakula maarufu sana duniani kote. Nchi zote zinahitaji samaki. Ni biashara yenye tija na inayoweza kuipeleka mbele nchi yetu kimaendeleo.

Mheshimiwa Spika, Wabunge wameongelea mambo mengi kuhusu uvuvi kiujumla wake. Pamoja na mambo hayo, ni imani yetu kwamba Serikali imesikia ushauri huu na sasa Serikali itaichukulia sekta ya uvuvi kuwa ni chanzo kingine cha mapato, pia ni sekta inayotoa ajira nyingi kwa wavuvi, wachuuzi na wananchi wengine. Tuitumie bahari ipasavyo ili ituletee maendeleo. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. ABADALLAH HAJI ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na nchi na muweza wa mambo yote. Aidha, nakupongeza wewe binafsi kwa kuliongoza Bunge vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi ni chombo muhimu sana katika kila nchi duniani kote. Ni chombo cha ustawi wa jamii kinachostawisha amani na usalama, kwa mujibu wa sheria za nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa polisi ni chombo kinachotegemewa katika hali zote, ni matumaini ya wananchi wote kupata huduma na utumishi uliotukuka wa Jeshi la Polisi na Vitengo vyake vyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna malalamiko mengi ya Jeshi la Polisi kutumika vibaya au kisiasa zaidi. Naishauri Serikali chombo hiki kitumike vizuri kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Nchi. Ikiwa Polisi watafanya kazi zao kwa weledi na kutumia taaluma zao, jambo hili likifanyika vyema amani na utulivu wetu wa nchi utatengamaa. Waepukane na dhana ya kuwa Polisi wanaweka taaluma zao nyuma na kufanya kazi zao kwa kufuata maagizo kutoka upande mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira za polisi, kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu kuhusu nafasi za kuajiriwa vijana katika Wizara hii ya Mambo ya Ndani hususan Zanzibar yaani Unguja na Pemba. Sote tunafahamu sana kwamba kuna kasma maalum ya nafasi za ajira za Polisi na Jeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila Mkoa kuna idadi yake maalum inayotengewa lakini kuna malalamiko kwamba inapofika wakati wa mahojiano ili kupata nafasi hizo kuna mambo mengi yanayofanyika ambayo sio mazuri ili kuziparanganya nafasi hizo na kukoseshwa nafasi hizo wale wanaostahiki. Yasemekana kwamba watoto wa wakubwa ndio huchukua nafasi nyingi hata kama si wakazi wa mikoa husika. Mambo haya hasa huwa yanatokea Mikoa ya Zanzibar yaani Unguja na Pemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haya yanatendeka naiomba Serikali na Wizara husika kulishughulikia jambo hili ili kuzifanya nafasi hizi ziende kwa walengwa na kuondoa malalamiko ya siku nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matukio ya kihalifu na utekwaji wa raia. Jambo hili ni tatizo kubwa na sasa limekuwa likilalamikiwa sana na raia. Ni ukweli usiopingika jambo hili linaleta usumbufu kwani tuhuma zinakwenda kwa askari wetu na Serikali inalijua lakini jawabu la Serikali ni kwamba matendo hayo huwa yanafanyika au yanafanywa na watu wasiojulikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kwa kutumia weledi wa askari wetu kuwabaini watu hawa wanaofanya matendo haya ya uharamia na kuwabaini watu wasiojulikana na kujua ni akina nani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili la matendo maovu yanayotendwa na watu wasiojulikana tunaiomba Serikali ije na majawabu maridhawa na watu wasiojulikana iwe sasa ni watu wanaojulikana ili ufundi na weledi wa polisi wetu uwe wa manufaa zaidi.