Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Othman Omar Haji (10 total)

MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, iwapo itatokea kiongozi wa Umma atazungumzia masuala ya kisiasa ndani ya nyumba ya ibada; je, ni kifungu gani cha katiba au sheria kinachoweza kumtia hatiani kiongozi huyu? (Makofi)
Swali la pili, iwapo katika matamshi yake aliyoyazungumza katika nyumba hiyo inakwaza jamii moja katika Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania.
Je, ni adhabu gani amestahiki Kiongozi kama huyu? (Makofi/Kicheko)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilishaeleza katika jibu langu la swali la msingi kwamba mtu yeyote ambaye atafanya kinyume na ambacho Katiba inaelekeza na vilevile sheria, atakuwa amefanya makosa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisisitize tu hapa kwamba, Katiba ya nchi ndiyo inayozaa sheria. Kwa hiyo, siyo siyo tu mtu, hata chama cha siasa ambacho kinaendekeza masuala ya kidini nacho kinakuwa kimekosea, lakini siyo suala la mtu mmoja kuamua kuwa umekosea, kuna utaratibu wa kuweza kulifikisha hilo suala mbele ya Msajili wa Vyama vya Siasa na hatua za kisheria kuweza kuchukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hivyo kwa viongozi wa Kiserikali, anaingia kwenye Kanisa au Msikitini, siyo Serikali iweze yenyewe kuwa kila sehemu, lakini ijengwe hoja na wananchi ambao wamefika pale na huko ndiko kulinda utawala wa sheria katika nchi yetu. (Makofi)
MHE. OTHMAN OMAR HAJI:Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza madogo tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya tarehe 20 Machi, 2016 ambapo vyombo vya dola vilikamilisha kusimamia zoezi la uchaguzi wa Zanzibar, ambao uliiweka madarakani Serikali
haramu inaongozwa na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein jambo ambalo wakati huo palitokea tuhuma dhidi ya wafuasi wa CUF kwamba wanapita wakiharibu mali za wafuasi wa CCM, shutuma ambazo ziliwapelekea wafuasi wa CUF kukamatwa, kupigwa, kuwekwa mahabusu……
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na matokeo hayo ambayo yalitokea katika Kisiwa cha Pemba, katika Kisiwa cha Unguja maeneo ya Tumbatu kulitokea nyumba za wafuasi……
Mheshimiwa Naibu Spika, najenga hoja.
Nyumba za wafuasi wa CUF kuchomwa moto na wafuasi wa CCM, kwa kuthibitisha majibu ya Mheshimiwa Waziri Je, kwa nini wafuasi hawa walioshutumia na CUF katika Kisiwa cha Tumbatu, kwa nini mpaka leo hawajakamatwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, inapotokea Wapinzani wanataka kufanya mikutano, Jeshi la Polisi wanasema wana taarifa za kiintelijensia kwamba hakuna usalama. CCM wanapofanya mikutano yao, Jeshi la Polisi linakusanyika pote ili kulinda mikutano hiyo. Je, kwa nini Jeshi la Polisi linailinda mikutano ya CCM lakini pale ambapo Upinzani wanafanya mikutano hawataki kuilinda?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nataka nimthibitishie pamoja na Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein ni halali ambayo imechaguliwa na wananchi kupitia Uchaguzi Mkuu halali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kauli kama hizi katika Bunge lako Tukufu ambazo zinapotosha umma siyo tu kupotosha na kudhalilisha Serikali halali na maamuzi sahihi ya wananchi ziendelee kupingwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili anauliza swali kwamba baada ya uchaguzi kuna wafuasi wa CUF ambao walishutumiwa kwa tuhuma mbalimbali ambao walikamatwa na akatolea mfano wa Kisiwa cha Tumbatu kuna wafuasi ambao hawakuchukuliwa hatua nadhani alikusudia wa vyama vingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Uchaguzi Mkuu baadhi ya Vyama vya Upinzani ikiwemo chama chake, viongozi walijitokeza kuhamasisha wananchi kufanya mambo ambayo yanakiuka sheria za nchi yetu. Kuna matukio mbalimbali ambayo yamejitokeza ikiwemo kuchomwa moto kwa nyumba, kuchomwa mashamba, kurusha mabomu ikiwemo nyumba ya Kamishna Mkuu wa Polisi wa Zanzibar ambayo kwa uchunguzi uliofanyika mpaka sasa hivi tunavyozungumza watu ambao wamekamatwa kuhusika na urushaji bomu katika nyumba ya Kamishna ni Viongozi Waandamizi wa Chama cha CUF. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Polisi imeshakamilisha uchunguzi wake na suala lipo kwa DPP na linahitajika kupelekwa Mahakamani ili hatua za kisheria zichukuliwe. Kwa hiyo, nataka kusema kwamba, watu hawa ambao wamefanya matukio ya ukiukwaji wa sheria wapo wengi, mpaka sasa hivi zaidi ya watu 24 wameshapelekwa katika vyombo vya sheria na wengine wapo katika hatua mbalimbali za uchunguzi. Kwa hiyo, siyo sahihi kwamba Jeshi la Polisi linafumbia macho uvunjifu wa sheria. Iwe Tumbaktu, Pemba, Unguja ama sehemu yoyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yeyote ambaye anakiuka sheria za nchi atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni kuhusiana na hoja ya kwamba mikutano ya CCM inaruhusiwa na Polisi lakini mikutano ya CUF hairuhusiwi. Naomba nikuthibitishie pamoja na Wabunge na wananchi wote kwa ujumla, kwamba hakuna ubaguzi kama nilivyojibu katika swali langu la msingi katika kuhakikisha kwamba Jeshi la Polisi linafanya kazi yake kwa mujibu wa sheria, halibagui chama cha siasa. Tunapozungumza sasa hivi mikutano ya hadhara imezuiliwa kwa vyama vyote ikiwemo Chama cha Mapinduzi. Hakuna sehemu yoyote ambayo Chama cha Mapinduzi kinaruhusu mikutano ya hadhara zaidi ya Waheshimiwa Wabunge waliochaguliwa katika Majimbo yao. Mikutano ya ndani inaruhusiwa kwa vyama vyote na haijawahi kuzuiliwa kwa chama chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge kama ana uthibitisho wa mikutano halali ya chama chake ambayo imezuiliwa basi atuletee taarifa ili tufuatilie tuweze kuchukua hatua stahiki.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa mujibu wa Msajili wa Hazina, Benki ya Kilimo inawajibika kutoa huduma zake Tanzania nzima. Napenda kumuuliza Naibu Waziri, ni kwa nini benki hii haijafikisha huduma zake kule Visiwani Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la Msingi, katika utekelezaji wa mpango wa biashara wa Benki hii ya Maendeleo ya Kilimo, imepanga kufungua ofisi sita za kikanda na Zanzibar ikiwemo. Ni imani yangu baada ya kufungua Ofisi ya Kikanda Dodoma, Ofisi ya Kikanda ya pili itakayofunguliwa ni Ofisi yetu ya Visiwani Zanzibar.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswala mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, pamoja na kuhamasishwa Halmashauri mbalimbali kununua dawa hizi zinazotengenezwa na kiwanda hiki, Wizara ya Afya ni mteja mkuu ambaye alitegemewa kununua dawa hii inayozalishwa na kiwanda hicho, lakini wameshindwa kutokana na kukosa pesa, jambo ambalo limepelekea kiwanda kutafuta wateja kutoka nchi za nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba Naibu Waziri atueleze hapa imekuwaje Wizara kutokutenga pesa kwa ajili ya kuwanusuru Watanzania ambao wanasumbuliwa na ugonjwa huu wa malaria hapa nchini?
Swali la pili,kwa sababu teknolojia hii ya kuzalisha viuadudu vya kuulia viluilui vya mbu ni mpya hapa Tanzania na Bara zima la Afrika, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kutueleza ni maeneo gani katika Jamhuri yetu ya Tanzania wamewahi kuchukua angalau sampuli ya kiwanda kile na kuweza kuifanyia majaribio ili kuweza kujua ubora wa dawa hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba arudie swali la pili walikuwa wanapiga makofi, sikumsikia vizuri.

MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimemuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba kwa sababu teknolojia hii ya kuzalisha viuadudu vya kuulia viluilui vya mbu wanaoeneza malaria ni mpya hapa Tanzania na Bara zima la la Afrika.
Je, Wizara imewahi angalau kwenda kuchukua sampuli kule kiwandani na kuweza kuifanyia majaribio na kuweza kujua ubora wa hii dawa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nitaanza na swali la pili kwamba je, Wizara imewahi kwenda kuchukua sample kwenye kiwanda kile na kuzifanyia utafiti?
Kwanza naomba nimhakikishie kwamba teknolojia
ya biolarvicides kuingia hapa nchini na kukubalika kutumika kuna mchakato mrefu wa kisayansi ambao umefuatwa.
Kwa hivyo, katika hatua hii ambapo inazalishwa kwa wingi wala hakuna haja ya kufanya utafiti wa majaribio, kwa sababu pale mwanzoni wakati ugunduzi wa teknolojia unafanyika zilifanyika tafiti ambazo kisayansi zinajulikana kama clinical tries za kubaini efficacy ya biolarvicide ambayo inatumika lakini pia kubaini kama kuna any emergency ya resistance yaani usugu dhidi ya biolarvicide yenyewe ambayo inatumika na hatimaye ikafikiwa kuthibitishwa kwamba ni teknolojia ambayo ni effective.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano walipoanza kufanya tafiti hizi miaka hiyo ya zamani walitumia bacteria ambaye anajulikana kama bacillus sphaericus katika hatua za awali mpaka wakafikia mwisho wakakamilisha uchunguzi na ikaonekana kwamba bacillus sphaericus ana-develop resistance kiurahisi sana, wakahama wakaweka bacillus thuringiensis vara israelensis ambayo ni second generation.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kumuweka huyu bacillus wa aina ya pili yaani kwa kifupi BTI ikaonekana kwamba yeye ni effective zaidi kuliko yule wa kwanza. Kwa hivyo, ikaonekana kwamba sasa tutumie generaly BTI kwa ajili ya biolarvicide. Kwa hivyo ni teknolojia ambayo imethibitishwa na haina shaka, na sisi Tanzania tunapaswa kujivuna kwa kuwa tuna kiwanda hicho hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza kiwanda kile kitazalisha full capacity yake biolarvicides lita milioni sita. Malengo hasa ya kuanzisha kiwanda kile sio kwa ajili ya Tanzania peke yake, ni kwa ajili ya Tanzania na nchi nyingine za Afrika na dunia ambazo zitakuja kununua biolarvicide hapa nchini. Kwa mfano mpaka sasa tayari tuna nchi za Serbia, tuna nchi ya Cuba, yenyewe tuna nchi za Sweden, tuna nchi ya Niger ambazo zimenunua biolarvicide kutoka Tanzania, kwa sababu kuanzia hiyo mwezi Desemba, 2016 mpaka sasa tumezalisha lita milioni mbili na tumeuza kwenye hizo nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hapa Tanzania Halmashauri takribani tano zimeonesha nia ya kununua, Halmashauri mbili zimekwisha nunua japokua kwa kiasi kidogo na zimekwishatumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niwapongeze Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe na Halmashauri ya Wilaya ya Geita ambao wao walikuwa ni wa kwanza kwa Halmashauri za hapa nchini kununua biolarvicide. Kwa hiyo swali lake la msingi linasema kwamba Wizara ya Afya tungepaswa tununue si sahihi kwa sababu malengo ni sisi kuwezesha kiwanda kile kuwepo na baada ya hapo Halmashauri ziweke kwenye bajeti zao wao wenyewe waweze kununua pale kadri ambavyo wanahitaji. Ndiyo maana tunaendelea na uhamasishaji wa Halmashauri zote nchini kununua biolarvicide kwa ajili ya control ya malaria.
MHE. OTHMAN OMAR. HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu aliyoyatoa. Nina maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Zanzibar ni mshirika wa AICC na ina haki ya kupata gawio, lakini kauli za Mawaziri zinazohusu gawio la AICC zinakinzana. Mfano, wakati Mheshimiwa Naibu Waziri anasema kwamba AICC inapeleka gawio Serikali Kuu, lakini Mheshimiwa Waziri wa Fedha wakati akijibu swali la Na. 110 katika Kikao cha Sita, Mkutano wa Kumi alisema kwamba AICC bado haijawahi kupata gawio na kwamba Joint Finance Commission wakishirikiana na Msajili wa Hazina wameunda kikosi kazi ili kuiwezesha AICC kutengeneza faida na kuleta gawio Serikali Kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, Mheshimiwa Waziri kauli ya Waziri wa Fedha inakinzana na kauli ya Waziri mwenye dhamana. Kwa maana hiyo, gawio linalotoka AICC haliendi Serikali Kuu. Je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba Zanzibar sasa hivi inakosa gawio kutoka AICC toka ilipoanzishwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, AICC imekuwa ikifanya uwekezaji mkubwa sana kule Arusha kama alivyozungumza Mheshimiwa Waziri, lakini imeshindwa kuwekeza katika mazingira ya Zanzibar pamoja na kuwa mazingira yake yanaruhusu.
Mheshimiwa Naibu Waziri, anaweza kutueleza kwa sababu gani AICC imeshindwa kufanya uwekezaji katika Visiwa vya Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI):
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kwanza kwamba Mheshimiwa Waziri wa Fedha alidanganya, naomba niseme siyo sahihi. Mheshimiwa Waziri wa Fedha hakudanganya, alisema Msajili wa Hazina wameunda mkakati kwa kushirikiana na kituo husika ili kuona kituo kinatoa gawio.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama amesikiliza vizuri katika jibu langu la msingi, nimesema kituo kimeanza kutoa gawio mwaka 2016/2017 na katika gawio hili Serikali ya Zanzibar inapata mgao wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili kwamba kituo hakiwekezi Zanzibar. Napenda kuliharifu Bunge lako tukufu kwamba kituo kinatekeleza mpango mkakati wa miaka mitano ambao umeanza kutekelezwa mwaka 2017/2018 hadi 2021/2022 na ambao katika mambo yanayotakiwa kutekelezwa ndani ya mpango mkakati huo ni kujenga vituo vingine kwa uwekezaji na katika maeneo ambayo vituo vitajengwa mojawapo ni Zanzibar na kituo kwa sasa kinaanza kujenga Dodoma na baada ya Dodoma kinakwenda kujenga Zanzibar. Kwa hiyo, uwekezaji huu unakwenda katika pande zote mbili za Muungano.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba katika majibu yake wajipange sana katika mikakati yao kwa sababu Shirika la Anga la Kenya bado wanatufilisi kwa kuchukua mapato ya nchi. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ripoti ya CAG ya mwaka 2015/2016 TCAA iliingia mkataba na Kampuni ya COMSOFT GMBH ya Ujerumani. Kwa kuweka mitambo ya kisasa ya kuongozea ndege na kufuatilia safari za ndege yenye thamani ya shilingi bilioni 3.4. Kwa sababu mkandarasi huyu hakuweka dhamana katika kazi, yake mnamo mwaka 2014/2015 mzabuni alitangaza kufilisika.
Kwa kuwa shirika liko kimya kuhusu suala hili Mheshimiwa Waziri naomba kukuuliza, ni kwa kiwango gani shirika limeweza kuokoa fedha hii ya walipa kodi zilizopotea? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali namba mbili, Mheshimiwa Waziri, Mamlaka ilipokutana na Kamati ya PIC ilikuwa na kilio kwamba wana ukosefu wa wataalam wenye sifa katika usafiri wa anga. Katika hotuba yako uliyoiwakilisha muda mchache tu mwaka huu ulisema kwamba Chuo cha Usafiri wa Anga Dar es Salaam kinatoa wataalam wa mafunzo tofauti na wenye viwango vya kimataifa wa ndani na nje ya Tanzania. Je, Mheshimiwa Waziri wataalam hawa…
...wataalam hawa wanaomaliza chuo unawapeleka wapi?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, kwanza nimuhakikishie tu kwamba kwa ufungaji wa rada nne hizo ambazo Mheshimiwa Rais amezindua tarehe 2 Aprili, tuna hakika anga letu lote tutalimiliki sisi kwa maana ya kuhakikisha usalama wake. Kwa hiyo, asiwe na wasiwasi kwamba nchi jirani zitafanya hicho kitu badala yetu. Lakini nikijibu swali lake la kwanza nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha iliyolipwa na Serikali haijapotea bado ipo na sasa hivi kuna taratibu zinafanyika kuhakikisha kwamba pesa yetu inarudishwa kwa wananchi walipa kodi wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu ukosefu wa wataalam nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna wataalam 40 ambao wamepelekwa kusoma ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wanaiendesha mitambo yetu hii ya rada ambayo inafungwa kwa ufanisi wa kutosha.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini pamoja na hayo, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Sera ya Tanzania kuhusu Ukombozi wa nchi za Bara la Afrika na nje ya Afrika iliipatia heshima kubwa nchi yetu ya Tanzania. Nataka kujua Sera hii ya Ukombozi mpaka sasa inaendelea hasa kwa zile nchi ambazo bado hazijapata uhuru kama vile Sahara na Palestina?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, hivi karibu tulisikia kuzorota kwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Jumuiya ya Nchi za Ulaya na Tanzania mpaka ikapelekea mwakilishi wao kurudi nyumbani. Nini mustakabali wa kisera kwa pande hizi mbili ambazo zina mzozo huo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Othman Omar Haji, Mbunge wa Gando kwa maswali yake mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ni wazi kwamba Tanzania imejijengea heshima kubwa sana katika Sera yake ya Ukombozi wa nchi mbalimbali Barani Afrika. Heshima hiyo bado ipo kwa Tanzania kwa sababu bado Sera ya Tanzania ya kupinga unyanyasaji, ukoloni na kutweza utu wa nchi yoyote ile inaendelea. Hivyo, msimamo wa Tanzania katika suala la Sahara pamoja na Palestina bado upo kama ambavyo ulikuwepo mara tu baada ya uhuru.

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba Tanzania ni nchi ya kwanza duniani kuwa na Ubalozi Palestina. Bado tuna heshima hiyo na bado tuna mahusiano hayo mazuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kuhusu mahusiano kati ya Tanzania na Jumuiya ya Ulaya. Mahusiano ya kidemokrasia na diplomasia kati ya Tanzania na nchi zote duniani yanaratibiwa na Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961 na 1963.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa mkataba huo kila nchi inawajibu wa kuheshimu vipengele vya mkataba huo na endapo pande mmoja haitaheshimu vipengele vya mkataba huo, nchi nyingine ambayo imekosewa inawezaikachukua hatua stahiki. Na pale nchi inapochukua hatua stahiki haimaanishi kuwa mahusiano ya kidiplomasia yamevunjika hapana ni sehemu ya utekelezaji wa mkataba wa Vienna.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwakilisha.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, hadi natuma swali hili Mei 8, 2017, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ilikuwa inadaiwa na TANAPA zaidi ya shilingi bilioni 3 za Tanzania. Je, deni hili limeshalipwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Wizara kupitia Shirika lake la AICC inamiliki majengo ya kutosha pale Mjini Arusha ambapo ingetumia majengo yale ingewezesha mahakama hii kufanya shughuli zake kwa ufanisi mkubwa sana. Je, Mheshimiwa Waziri haoni upo umuhimu kuhamisha mahakama hii huko inakokodi na kuipeleka katika majengo haya ya AICC ili kuokoa matumizi yasiyokuwa ya lazima?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Othman Haji, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba TANAPA inadai fedha ya pango kwa ajili ya ofisi za Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu lakini taratibu zinaendelea ili ziweze kulipwa. Hata hivyo, naomba nimueleweshe Mheshimiwa Mbunge kwamba siyo mahakama ndiyo inadai Serikali bali ni Serikali na Serikali. Kwa hiyo, ni suala la kawaida, pesa hiyo italipwa muda ukifika na kama nilivyosema mchakato unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la pili kwamba kwa nini majengo ya AICC yasitumike kama ofisi za mahakama hiyo. Naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali imetafuta hekari 20 Arusha kwa ajili ya kujenga ofisi za mahakama hiyo na taratibu za ujenzi zimefika mbali sana. Kwa hiyo, tunategemea baada ya muda mfupi ofisi hizo zitajengwa na hakutakuwa na haja ya kwenda kubanana kwenye Ofisi ya AICC. Hata kama mahakama hiyo ingeenda kwenye majengo ya AICC labda suala lile lile la kudaiwa na TANAPA lingeweza kujirudia. Kwa hiyo, tunachotaka kufanya ni kujenga ofisi ambazo zitatosha na changamoto hii haitatokea tena.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa mujibu wa maelezo ya Serikali ni kwamba APRM Tanzania inafanya shughuli zake chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Kwa sababu hiyo basi, itawezaje kuisimamia Serikali na kutoa majibu yaliyo sahihi kwa wananchi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, moja kati ya masharti ya APRM kwa wanachama wake ni kwamba mwanachama anatakiwa akubali kufanyiwa tathmini na wanachama wenza. Je, ni mara ngapi Serikali ya Tanzania imewahi kufanyiwa tathmini hii na wanachama wenzake?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda kumpongeza Mheshimiwa Othman Omar Haji, Mbunge wa Gando kwa maswali yake mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ukisoma mkataba ambao umeanzisha APRM, inaongozwa na Baraza la Usimamizi la Taifa ambalo ni huru, linachaguliwa kutoka kwa watu mbalimbali, asasi za Kiserikali, vyama vya kisiasa na watumishi wa upande wa Serikali. Baraza hilo ni huru katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa kifungu cha 16 cha mkataba huo na kwamba iko chini ya Wizara lakini muundo na utendaji wake unawahakikishia kwamba baraza hilo liko huru na wala haliwezi kuingiliwa na mtu yeyote.

Mheshimiwa Spika, swali la pili la kuweza kuhakikiwa au kufanyiwa tathmini na wanachama wenza. Naomba tu nimkumbushe Mheshimiwa Othman Omar Haji kwamba APRM ilianzishwa na nchi za Kiafrika ili kuweka viwango vya kujitathmini ambavyo vinakubalika na Afrka na nchi za Kiafrika. Kwa hiyo, Tanzania imeruhusu nchi nyingi za Afrika, SADC na Afrika Mashariki kuweza kushiriki kwenye tathmini na kuweza kuzitathmini kwa mara nyingi zaidi. Ahsante.