Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Hassanali Mohamedali Ibrahim (6 total)

MHE. KANALI (MST.) MASOUD ALI KHAMIS (K.n.y MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI) aliuliza:-
Serikali imeanzisha mabasi yaendayo kwa kasi katika Jiji la Dar es Salaam lakini madereva wengi wamekuwa wakiendesha magari hayo kwa kasi kubwa; kiasi cha kuhatirisha maisha ya watu waendao kwa miguu.
(a) Je, ni lini Serikali itawachukulia hatua madereva ambao hawafuati Sheria za Barabarani?
(b) Je, ni muda gani magari hayo ya DART yamepangiwa kuanza kazi na kuda wa kumaliza kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Muheshimiwa Ibrahim Hassanali Mohammedali Mbunge wa Kiembesamaki, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, (a), madereva wa DART wanapaswa kuzingatia Sheria ya Usalama Barabarani kama ilivyo kwa dereva yeyote. Tangu mabasi yaanze kutoa huduma madereva 20 wamepewa onyo kwa makosa ya usalama barabarani na wawili wamefukuzwa kazi. Aidha, madereva 40 wamekatwa mishahara kwa makosa mnalimbali kwa kukiuka sheria za barabarani.
Mheshimiwa Spika, ili kudhibiti mwenendo wa mabasi, mabasi yamefungwa vifaa maalumu katika magari ili kutoa ishara kwa dereva anapozidisha mwendo ambao ni kilomita 50 kwa saa. Aidha, Serikali imeweka utaratibu wa kuwajengea uwezo madereva kupitia semina zinazoendeshwa na wataalam kutoka NIT na VETA na Askari wa Usalama Barabarani ili kuwakumbusha taratibu na maadili ya kazi ya udereva.
Mheshimiwa Spika, (b), kwa kuzingatia mazingira ya Jiji la Dar es Salaam kuhusu huduma za usafiri, mkataba baina ya DART na mtoa huduma ambaye ni UDART umeainisha kwamba huduma ya mabasi yaendayo haraka itaanza saa 11.00 alfajiri hadi saa 06.00 usiku.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB (K.n.y. MHE. IBRAHIMU HASSANALI MOHAMMEDALI) aliuliza:-
Wenye maduka waliopewa kibali cha kuegesha magari yao kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi na moja jioni wameonekana wakihodhi nafasi hiyo kwa saa 24:-
(a) Je, ni lini watu wenye tabia hiyo watachukuliwa hatua za kisheria?
(b) Katika Jiji la Dar es Salaam wakati wa usiku inakuwa kama mji huo hauna sheria kwa sababu wenye magari huegesha magari hovyo na kusababisha adha kwa watu wengine. Je, ni lini Serikali itawachukulia hatua watu wa aina hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ibrahim Hassanali Mohammedali, Mbunge wa Kiembe Samaki, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria Ndogo ya Maegesho ya Magari GN. Na. 60 ya mwaka 1998 kifungu cha 6(1) kinaipa mamlaka ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Saalam kudhibiti na kusimamia maeneo ya maegesho ya magari yaliyoruhusiwa kwa mujibu wa sheria ili kuondoa kero, usumbufu na msongamano katika mitaa na barabara za umma. Kwa mujibu wa sheria hiyo, maegesho yote ya magari ya kulipia na maegesho yaliyohifadhiwa yanatumika kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 12.00 jioni. Baada ya muda huo maeneo hayo huwa huru kwa matumizi ya umma. Pale inapobainika mtu kuhodhi maeneo hayo baada ya saa 12.00 jioni, Halmashauri ya Jiji huchukua hatua kwa mujibu wa sheria.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya ukaguzi na udhibiti wa maeneo ya maegesho imetolewa kwa Mawakala katika Jiji la Dar es Salaam. Napenda kutoa wito kwa wamiliki wote wa magari kuacha kuegesha magari bila utaratibu hasa wakati wa usiku na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wengine. Serikali haitasita kuchukua hatua kwa wote watakaobainika kukiuka taratibu za maegesho ya magari katika Jiji la Dar es Salaam kwa sababu kufanya hivyo ni kusababisha msongamano na kero kubwa kwa wengine.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR (K.n.y. MHE. IBRAHIM MOHAMEDALI RAZA) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itachukua hatua kwa kuwasaidia vijana walioathirika na matumizi ya dawa za kulevya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ibrahim Mohamedali Raza, Mbunge wa Kiembe Samaki kama ifutavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua tatizo la matumizi ya madawa ya kulevya na athari yake kubwa kwa nguvu kazi ya Taifa letu ambayo asilimia kubwa ni vijana. Katika kukabiliana na tatizo hili, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imechukua hatua kadhaa kuwasaidia
vijana na makundi mengine walioathirika na matumizi ya dawa za kulevya. Hatua hizo ni pamoja na zifuatazo:-
(i) Kutoa tiba kwa waathirika ambapo hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2017 jumla ya vituo vitno vya tiba (methadone) kwa waathirika wa dawa za kulevya vilikuwa vimeanzishwa nchini katika Hospitali za Muhimbili, Temeke, Mwananyamala, Zanzibar na Mbeya. Kupitia vituo hivyo, jumla ya waraibu 5,830 walipatiwa tiba na wengine wanaendelea kupatiwa matibabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mwaka huu wa 2018, Serikali inatarajia kufungua vituo vipya vya tiba katika Mikoa ya Mwanza na Dodoma. Kutokana na utafiti uliofanywa mwaka 2014, Serikali imepanga kufungua vituo vya tiba katika Mikoa ya Pwani, Morogoro, Arusha, Kilimanjaro na Tanga kwa kulingana na upatikanaji wa fedha.
(ii) Kuanzisha kituo kikubwa cha kuwapatia waathirika tiba kwa njia ya kazi (occupational therapy) ambapo mafunzo ya stadi za kazi mbalimbali yatatolewa. Kituo hiki kinajengwa katika eneo la Itega, Mkoani Dodoma.
(iii) Serikali kwa kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, imetengeneza miongozo mbalimbali kwa ajili ya kusimamia utoaji wa huduma kwa waathirika wa dawa za kulevya kuanzia katika vituo vya afya hadi kwenye huduma za kijamii zinazotolewa na asasi mbalimbali za kiraia.
(iv) Kutoa elimu kwa njia ya redio na luninga ambapo viongozi wa ngazi tofauti wa mamlaka wamekuwa wakitoa elimu katika vipindi mbalimbali. Vilevile elimu imekuwa ikitolewa katika shughuli za Kitaifa kama vile Mwenge, Nane Nane, maadhimisho na matamasha mbalimbali.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ (K.n.y. MHE. IBRAHIM HASSANALI RAZA) aliuliza:-
Kituo cha Polisi Mazizini kilichopo Kiembe Samaki kipo katika hali mbaya na hakina vitendea kazi, jengo ni chakavu, hakina gari na mazingira yake hayaridhishi:-
Je, ni lini Serikali itaboresha kituo hicho kwa kutatua changamoto zilizopo?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ibrahim Hassanali Raza, Mbunge wa Kiembe Samaki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli hali na mazingira ya Kituo cha Polisi Mazizini hairidhishi kutokana na uchakavu wa jengo pamoja na uhaba wa vitendea kazi kama ilivyo kwa baadhi ya vituo katika maeneo mbalimbali. Kituo cha Polisi Mazizini kina majengo mawili. Katika mwaka 2015 Serikali ilifanya ukarabati wa jengo moja la kituo hiki ambapo ukarabati ulikamilika na tayari jengo hilo linatumika kwa kutoa huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mwaka wa Fedha 2018/2019, Jeshi la Polisi limependekeza kwa ajili ya maendeleo ya vituo kiasi cha shilingi bilioni 3.7 kwa ajili ya ukarabati na kuboresha miundombinu mbalimbali ya Jeshi la Polisi kote nchini ikiwemo ukarabati wa jengo la pili la Kituo cha Polisi Mazizini Jimboni Kiembe Samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kufanya ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya Jeshi la Polisi na kuongeza vitendea kazi kama vile magari awamu kwa awamu ili kutatua changamoto zinazokabili Jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali.
MHE. KANALI MST. MASOUD ALI KHAMIS (K.n.y. MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI) aliuliza:-
Jiji la Dar es Salaam linakabiliwa na tatizo la ombaomba wengi na katika baadhi ya maeneo wamejenga miundombinu ya kulala.
Je, ni lini Serikali itachukua hatua ya kuwaondoa
ombaomba katika Jiji la Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ibrahim Mohamedali Raza, Mbunge wa Kiembesamaki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wapo ombaomba katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar-es-Salaam kwa sababu vipo vivutio vingi ikiwemo watu wenye imani mbalimbali ambao huwapatia fedha na vitu vingine kama sehemu ya ibada. Kuzagaa kwa ombaomba kimekuwa chanzo kimojawapo cha uchafuzi wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto za ombaomba mara kadhaa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam imetekeleza hatua mbalimbali za kuwaondoa, ikiwemo kuwakamata na kuwasafirisha makwao, lakini wamekuwa wakirudi. Mfano mwezi Septemba, 2013 ombaomba 253 na watoto 135 walirejeshwa kwao ambapo watoto 33 walirejeshwa shuleni. Hii inathibitisha kuwa wapo watu wazima wanaotumia watoto kuombaomba. Watanzania wanatakiwa kuzitumia fursa za kupambana na umaskini zilizoandaliwa na Serikali, ikiwemo elimu msingi bila malipo, huduma za afya vijijini na uwepo wa Sheria ya Fedha 2018 inayotoa fursa kwa makundi mbalimbali ya uzalishaji mali kupata mikopo, wakiwemo walemavu. Vilevile watumie uwepo wa ardhi ya kutosha yenye rutuba kama fursa ya kuweza kujitegemea na hivyo, kujikomboa dhidi ya kuombaomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ombaomba wamekuwa wakisababisha watoto wengi kutopata fursa ya kusoma shule au kuwa watoro, nawaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri chini ya usimamizi wa Wakuu wa Mikoa kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama kuwakamata wototo wote ambao badala ya kwenda shuleni huzagaa mitaani wakiombaomba, wakamatwe pamoja na wazazi wao na washtakiwe Mahakamani chini ya Sheria ya Elimu ya mwaka 78 inayokataza utoro na Sheria ya Kanuni ya Adhabu Kifungu cha 166, 167 na 169A vinavyohusu wajibu wa wazazi na walezi kwa watoto. Aidha, Mabaraza ya Madiwani nayo yanaweza kutunga Sheria Ndogo za kuzuia utoro pamoja na kudhibiti mienendo ya baadhi ya watu kuombaomba.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH (K.n.y MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI) aliuliza:-
Wananchi au taasisi zilizopewa vibali vya kupaki magari hadi saa 12 jioni katika Jiji la Dar es Salaam sasa wanatumia vibali hivyo kupaki kwa saa 24. Hali hiyo imeibua usumbufu kwa wananchi wanaotaka kupaki magari yao kuanzia saa 12 jioni:-
Je, ni lini Serikali itakomesha suala hilo ili kuwaondolea wananchi usumbufu wanaoupata?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassanali Mohamedali Ibrahimu, Mbunge wa Kiembe Samaki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria Ndogo ya Maegesho ya Magari katika Tangazo la Serikali (GN) Na. 60 la mwaka 1998 na marekebisho yake (GN) Na. 41 ya mwaka 2017, maegesho ya kulipia pamoja na maegesho yaliyohifadhiwa (Reserved Parking) yanapaswa kutumika kuanzia saa 2.00 asubuhi mpaka saa 12.00 jioni, baada ya muda huo maegesho yote yanatakiwa kuwa wazi kwa ajili ya matumizi ya umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini ikiwemo Jiji la Dar es Salaam kusimamia vyema utekelezaji wa sheria hii na kuhakikisha chanzo hiki cha mapato kinasimamiwa ipasavyo ili halmashauri zinufaike na chanzo hiki.