Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Hassanali Mohamedali Ibrahim (12 total)

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya nzuri kusimama hapa mbele ya jengo hili na niweze kusema kwamba ni mara yangu ya kwanza kuchangia katika Bunge hili. Nawashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Kiembe Samaki kwa imani yao kwa kunileta katika jengo hili, nawaambia ahsanteni sana wananchi wa Jimbo la Kiembe Samaki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, kwa kweli ameonyesha kwamba anataka kuibadilisha Tanzania katika sekta zote za uchumi na hususan Tanzania yenye viwanda. (Makofi)
Katika kipindi kifupi Mheshimiwa Rais, ameweza kweli kuleta mabadiliko na matumaini kwa Watanzania wanyonge ambayo sisi Wabunge lazima tumuunge mkono kwa asilimia mia.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza vilevile ndugu yangu Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara kwa hotuba yake nzuri. Kwa kweli naweza kusema Mheshimiwa Waziri ambaye kapata hii Wizara ni kweli Mheshimiwa Rais hakufanya makosa kumchagua ndugu yangu. Nina imani ni mtu ambaye amebobea, ni mtu ambaye anajua, nasi tumuunge mkono katika kufanikisha yale ambayo yeye amejipanga, na sisi tuwe nyuma yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara. Kwanza nilikuwa namuomba Mheshimiwa Waziri kwamba hawa TIC wawe serious kidogo katika hao wawekezaji ambao wanakuja Tanzania kutaka kuwekeza. Kwa sababu Serikali inategemea TIC na kama TIC hawatakuwa serious katika suala hili kwa kweli tutawavunja moyo wafanyabiashara ambao kwa nia moja nzuri kabisa wanataka kuja kuwekeza Tanzania, kwa sababu Tanzania ni kisiwa cha amani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri katika jengo la TIC pawepo na One Stop Centre ambayo mambo yote yanaishia kwenye jengo lile. Mfanyabiashara, tena mwekezaji asihangaike kwenda katika masuala mengine ya kutafuta vibali ambayo mwisho tunamvunja nguvu mwekezaji na huondoka hapa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nilikuwa nataka Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara aweke vivutio maalum kwa wale wawekezaji ambao wanataka kwenda kuwekeza Mikoani, kwa sababu sasa hivi wawekezaji wengi sana wanawekeza katika Mkoa wa Dar es Salaam. Kwa hiyo, pawepo na vivutio maalum kwa wale ambao wanataka kwenda kuwekeza Tanga, Mtwara au mikoa mingine ya Kigoma. Kuwe na vivutio vizuri vya kuwawezesha waje hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwa ruksa yako ni kuhusu soko. Kwa kweli sisi Tanzania tuna nafasi nzuri sana ya kuzalisha mambo mengi sana. Mungu ametupa ardhi yenye rutuba nzuri sana, lakini hatuitumii ile ardhi, hatukitumii kile ambacho Mwenyezi Mungu aliyetupa. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara awaangalie katika kutafuta masoko. Tanzania leo hii tuna mananasi mpaka yanaoza yanatupwa. Leo Tanzania hii tuna embe mpaka yanaoza yanatupwa na matunda mengine, kwa kweli soko lipo nje, lakini hao ambao wanazalisha mashambani upeo wao mdogo kwenda kutafuta soko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naweza kusema kwamba embe hapa Tanzania ukiuziwa shilingi 500 au shilingi 700 unaona nyingi sana, lakini embe hii hii ikipelekwa nchi za Arabuni, basi tunanunua kwa dola moja au dola moja na nusu. Kwa hiyo, naweza kusema kwamba soko lipo lakini hawa wakulima bado hawajasaidiwa katika kutafuta masoko ya nchi za nje.
Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri, kwa kweli Tanzania tumejaliwa kuwa na ardhi na matunda tunayo ya kutosha, kwa hiyo, tuwasaidie wakulima wetu katika kuwatafutia masoko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine tuje katika hawa ndugu zetu Watanzania waliowekeza katika Kiwanda cha Saruji. Kwa kweli wanajitahidi kuzalisha saruji katika kiwango kizuri ambapo sasa hivi tunafurahi tofauti na siku za nyuma tulikuwa tunanunua saruji kutoka nchi nyingine lakini ilikuwa haina quality. Leo wenzetu ambao wamewekeza Tanzania katika viwanda vya saruji wanatupa saruji nzuri na tuwapongeze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilio chao hawa viwanda vya saruji wanakuwa wanalipa ten percent ya clinker. Kwa hiyo, naomba Wizara ya Viwanda na Biashara iwaangalie katika hiyo kulipa ten percent kama kuna uwezekano wa kutolipa au wa wapunguziwe hiyo ten percent ili saruji tupate kwa bei nzuri ambayo sisi Watanzania wengi ambao sasa hivi tuko katika kujenga majumba, hata tukitembea mikoani huko vijijini, watu sasa hivi hawajengi tena kwa udongo, wanatumia saruji, Tanzania hii inabadilika!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri aliangalie na suala hili. Vile vile nami niko tayari kumsaidia Mheshimiwa Waziri kama atataka nimtafutie masoko, kwa sababu mimi ni mfanyabiashara, ninakwenda nchi mbalimbali. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri niko tayari kufanya kazi na Wizara yako, niko tayari kukutumikia na Inshallah tutafika mahali ambapo Mwenyezi Mungu atatusaidia, Tanzania hii itakuwa ya viwanda na biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, namshukuru tena Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii adhimu katika jengo hili Tukufu na ninamwombea dua Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Mungu ampe nguvu, kutekeleza yale ambayo yeye mwenyewe, sisi tunayajua na tunayaona na nataka kumthibitishia Mheshimiwa Rais kwamba tutamuunga mkono kwa asilimia mia moja, wapinzani wetu wataisoma namba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache, kwa heshima zote, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii adhimu na naunga mkono hoja hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi hii kuchangia Wizara ya Utawala Bora na TAMISEMI. Sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha hapa nikiwa mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na utawala bora, kwanza nachukua nafasi hii kumpongeza kwa dhati kabisa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya na sisi wote tukiwa ni mashahidi, kwa muda mfupi kwa kweli ameweza kutuletea maendeleo ambayo sisi wote tumestaajabu katika kipindi kifupi sana Mheshimiwa Rais Magufuli ameweza kufanya mambo ambayo yametupa imani na wananchi wamekuwa na imani kubwa sana juu ya Mheshimiwa Rais. Nikitolea mfano, kwa mambo makubwa ambayo Mheshimiwa Rais ameweza kuyafanya katika muda mfupi, kwanza ni katika kupiga vita rushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nchi hii ya Tanzania ilikuwa inanuka kwa rushwa, hakuna mtu ambaye alikuwa haelewi, lakini leo ukienda Wizara yoyote au taasisi yoyote ya Serikali, unahudumiwa bila kuambiwa kutoa chochote, hii kwa kweli imetujengea heshima kubwa sana. Zamani ukienda kwenye nafasi yoyote nyeti, kama mfuko wako mdogo, huwezi kufanikiwa kupata haki yako. Kwa hiyo, namshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kurejesha nidhamu katika taasisi za Serikali na katika Wizara za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuwaondoa watumishi hewa. Kwa kweli pesa zetu mabilioni ya pesa yalikuwa yanaliwa na watu wajanja sana. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais amefanya kazi nzuri kupitia Wizara yake ya Utawala Bora ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Kairuki, ni dada mmoja ambaye kwa kweli amepewa Wizara na ameweza kuimudu vizuri sana. Nampongeza sana dada yangu Mheshimiwa Kairuki. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kuwaambia, anachofanya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, anafanya kwa ajili yetu sisi, kwa sababu mambo anayofanya sasa hivi katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu, fikiria baada ya miaka mitano Tanzania itabadilika, na sisi tunataka kwenda mbele, hatutaki kurudi nyuma. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais amesisitiza kwamba maendeleo kwanza, Tanzania kwanza. Kwa hiyo, sisi Waheshimiwa Wabunge, bila kujali itikadi zetu za kisiasa, lazima tumuunge mkono Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekitil, mimi nina imani kubwa sana na Mheshimiwa Rais katika kipindi cha miaka mitano yatakuja mambo kubadilika Tanzania hii na tulishaanza kuona mabadiliko. Ameanza mambo ya reli kiwango cha standard gauge, ameshaanza kuleta ndege mbili, kuna ndege mbili nyingine zinakuja mwakani, mambo ya flyover bridge haya; Mheshimiwa Rais ameweza kufanya mambo chungu nzima! Sasa mnasema kwamba utawala, utawala gani mnaotaka nyie? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kwamba tuwe wastahimilivu katika kipindi hiki ambacho Mheshimiwa Rais anataka kuijenga Tanzania mpya. Mimi nazidi kumwombea Mungu ampe umri, ampe afya ili tupate maendeleo ambayo itakuwa siyo maendeleo yetu sisi bali ya vijukuu vyetu ambao ni Taifa letu la kesho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija katika Wizara ya TAMISEMI, kwanza nampongeza sana ndugu yangu Mheshimiwa Simbachawene pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kwa kweli masuala ya elimu, leo Watanzania watoto wao wanakwenda kusoma shule bure. Mtoto wakati wa miaka ya nyuma alikuwa hawezi kwenda kusoma kwa sababu alikuwa hana ada. Leo Mheshimiwa Rais amesema kwamba watoto wote wasome bure na Mheshimiwa Rais kwa kupitia Wizara yake TAMISEMI, wamejitahidi sana kwamba leo asilimia 75 ya shule zetu zina madawati. Seventy five percent, hayo mengine twenty five percent, basi ma-desk yatakuja tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda cha kuwaomba TAMISEMI, ni kwamba watupatie na walimu wazuri ili watoto wetu wawe na education bora. Hapa walipofika TAMISEMI kwanza niwapongeze sana na Inshallah Mwenyezi Mungu atawapa nguvu Mheshimiwa Simbachawene na Naibu wake ili kuona kwamba elimu na kwa sababu elimu ndio ufunguo wa maisha, sasa watoto wetu watakapopata elimu nzuri basi naamini na Taifa hili tutakuwa na watoto wenye vipaji.

Mheshimiwa Mwneyekiti, nikija kwenye masuala ya Jiji letu la Dar es Salaam, nataka kumwambia Mheshimiwa Simbachawene kwamba sasa Dar es Salaam unapokwenda mtaa wowote pale mjini kama mitaa ya Libya, Bibi Titi Mohamed, Samora ukienda wapi pamukuwa na ombaomba ambao sasa wameweka magodoro yao na usiku wanaweka vyandarua, wana lala kabisa, asubuhi wanaoga pale pale, kwa kweli mandhari ya Jiji la Dar es Salaam inapotea kabisa na kama huamini mimi nipo tayari kufuatana na wewe usiku nikakuonesha hali ilivyo Dar es Salaam. Wakati wa asubuhi inanuka kwa sababu pale pale wanamaliza haja zao. Mimi mwenyewe binafsi nimeshuhudia mtu asubuhi anafanya haja yake, anamwaga maji.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Simbachawene kupitia Jiji lako la Dar es Salaam naomba sana, itafika wakati Dar es Salaam patakuwa tena ni kama Bombay ya pili. Hali ni mbaya sana, mimi ninashangaa Jiji la Dar es Salaam, Manispaa ya Dar es Salaam wamekaa kimya, sijui hawaoni! Ni kitu cha ajabu sana. (Makofi)

Vilevile wenzetu ambao wanafanya biashara ya nyama choma, kuku choma na chips, usiku wanakuja wanavunjiwa meza, wanavunjiwa viti na wanachukuliwa na wanadaiwa rushwa. Hivi juzi wamechukuliwa wafanyabiashara wote, wamepelekwa pale Manispaa, wamedaiwa rushwa na wametoa na ushahidi upo.

Mheshimiwa Rais Magufuli anajitahidi kupiga vita rushwa lakini bado watu katika kudai rushwa. Kwa hiyo, nilikuwa nakuomba Mheshimiwa Simbachawebe hawa watu ambao wanawekeza usiku wapo tayari kulipa kama kuweka viti, meza wapo tayari kulipa na mimi nitakupa mfano mmoja wa Bangkok, na hivi karibuni nilikuwa huko. Kuna mitaa fulani ikifika saa 12.00 wanaruhusiwa kuchoma nyama, kuku, chipis na kuweka nguo mpaka usiku saa 6.00 usiku, lakini hawapigwi wala hawatozwi rushwa. Hawa wenzetu wa Dar es Salaam, baada ya saa 12.00 jioni wapo tayari kulipa hata shilingi 500,000 au 1,000,000 kwa mwezi, lakini kila unapoenda kudai kibali, hawapewi wanazungushwa na matokeo yake wanakuja kudaiwa rushwa. Mheshimiwa Simbachawene, hili vilevile wanaipaka Serikali yetu matope.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu inafanya kazi nzuri lakini kuna baadhi ya watu wanaiharibu sifa ya Serikali yetu kwa tamaa yao tu na ubinafsi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwa Wizara ya TAMISEMI ni kuhusu hao wenzetu wanaopewa parking za magari, ni ruksa. Wanapewa kuanzia saa 2.00 asubuhi mpaka
12.00 jioni lakini utakuta mtu anamiliki parking saa 24, lakini ukimwambia muda hapa saa 12.00 jioni ondoa parking yako muda umekwisha, anakwambia hapana, mimi nimelipia. Hujalipia kwa saa 24. Mheshimiwa Simbachawene imekuwa ni matatizo ya parking Dar es Salaam ni sugu sana. Watu ikifika saa 12.00 jioni tunaomba uwaambie Manispaa waondoe kile kibao chake, kichukuliwe... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja Wizara zote mbili, Wizara ya Utawala Bora na TAMISEMI. Nakusuhuru sana kaka yangu Chenge.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. IBRAHIM HASSANALI RAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha hapa leo Bungeni nikiwa mzima wa afya. Vilevile nichukue nafasi hii kutoa mkono wangu wa pole wa rambirambi kwa wazee ambao walifiwa na watoto wao juzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuelezea changamoto yangu katika Wizara hii Mambo ya Ndani ya Nchi, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya kuweka nchi hii katika hali ya utulivu na amani. Tukienda kwenye changamoto katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi nitazungumzia upande wa Zanzibar. Kwa kweli Vituo vingi vya Polisi Zanzibar vipo katika hali mbaya sana vimekuwa kama magofu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza kwenda Kituo cha Polisi ukastaajabu kwa sababu vitendea kazi kwanza hamna, Polisi wanafanya kazi katika mazingira magumu sana, jengo limechaa, mapolisi wengi Zanzibar hawana radio call za kuwasiliana na viongozi wao na hawana magari. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri aiangalie Zanzibar kwa jicho la huruma kwa sababu mapolisi wanafanya kazi katika mazingira magumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwa upande wa trafiki, kwanza nichukue fursa hii nimpongeze kaka yangu Kamanda Mohamed Mpinga na timu yake nzuri kwa kazi wanayofanya kwa kweli wametusaidia sana katika Jiji letu la Dar es Salaam, sasa hivi madereva wanafuata sheria na nidhamu imekuwepo lakini bado kuna matatizo mengi sana hasa katika suala la kupaki magari sehemu ambapo hairuhusiwi. Kwa hiyo, namwomba kaka yangu Mohamed Mpinga suala hili alitilie mkazo zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna suala hili la mapolisi wanapotaka kwenda likizo wanaambiwa waende halafu wakirudi ndiyo watapewa haki zao kwa maana ya posho zao. Mimi namuuliza Mheshimiwa Waziri wakati polisi anapokwenda likizo unamwambiaje aende likizo halafu akirudi ndiyo apewe marupurupu yake, inakuwa si haki. Polisi anapopangiwa kwenda nyumbani basi apewe haki zake zote aende akastarehe na mama watoto na watoto wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili kwa kweli linawavunja nguvu Jeshi la Polisi kwa sababu wanafanya kazi katika mazingira magumu sana. Naomba Wizara hii walitupie macho Jeshi la Polisi kwa sababu wanafanya kazi katika mazingira magumu sana na wanastahiki posho muda ukifika na kama kuna uwezekano posho zao ziongezwe kwa sababu wao ndio wanatulinda sisi na mali zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti,tukiwavunja nguvu Jeshi la Polisi hakuna litakaloendelea katika nchi yetu hii. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie Jeshi la Polisi kwa macho ya huruma kwa sababu wanafanya kazi ngumu na ya hatari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hawa maafande wetu wanapokwenda kwenye kazi maalum (task force) nashauri wapewe vifaa ambavyo vitawasaidia hususan mapolisi. Dar es Salaam kuna mapolisi ambao tunawaita Polisi Tigo kwa kweli zile uniform wanazovaa akitokea mtu yeyote mwenye nia mbaya na kuwapiga risasi basi inapenya tu kwa sababu hazistahili kutokana na kazi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda katika upande wa Uhamiaji, niwapongeze kwa kazi nzuri wanayofanya, lakini naomba wazingatie suala la wakimbizi. Kuna hawa wakimbizi wanaotoka nchi jirani wanakuja nchini kwetu na kutuharibia amani yetu, kwa sababu wakija nchini kwetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. IBRAHIM HASSANALI RAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii adhimu. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha hapa salama nikiwa mzima wa afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia hii bajeti ambayo iko mbele yetu, nimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya. Katika kipindi kifupi sana ameweza kusimamia mambo ya barabara, mambo ya umeme, mambo ya reli, makusanyo mazuri vilevile katika ununuzi wa ndege. Kwa kweli, Mheshimiwa Rais anapaswa kupongezwa kwa kazi kubwa anayofanya na sisi tunamuombea aendelee na speed hiyo, sisi Wabunge tuko nyuma yake kwa nguvu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye bajeti hii Wizara ya Fedha kwanza nimpongeze ndugu yangu Mheshimiwa Waziri Mpango na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji. Kwa kweli, bajeti ya safari hii ni nzuri, ni bajeti ya matumaini na mimi ni imani yangu kwamba bajeti hii kwa mwaka huu itaipa nafasi kubwa katika nchi yetu na kwa mwananchi wa kawaida, vilevile itampunguzia mzigo mkubwa sana. Nikupongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa bajeti nzuri pamoja na msaidizi wako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze hawa TRA kwa ukusanyaji wa mapato. TRA kwa kweli safari hii wamekuwa watu wastaarabu sana katika kuzungumza na wafanyabiashara tofauti na miaka ya nyuma, nina matumaini makubwa ikiwa TRA watakwenda hivi kukaa na wafanyabiashara tukafika mahali ikawa ni win-win situation basi, mapato ya nchi yataongezeka sana. Wasichukuliwe wafanyabiashara kama ni maadui katika nchi, lakini wafanyabisahara kwa kweli wana nafasi kubwa sana kuliingizia Taifa mapato. Kwa hiyo, niwapongeze sana wenzangu wa TRA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naunga mkono ongezeko la shilingi 40 kwenye mafuta. Hii itatusaidia sana katika kutatua matatizo yetu ya maji na umeme, lakini si vibaya Mheshimiwa Waziri ikiwa tutaongeza airport tax japo kwa dola tano kwa sababu, hizi dola tano hizi wasafiri wamekuwa wengi na itatuingizia Taifa pesa nyingi sana. airport tax ambayo haimuumizi mwananchi wa chini kwa sababu, wanaosafiri wote Alhamdulillah ni watu wanaojiweza ndio maana wanaruka. Kwa hiyo, mimi hilo nilikuwa nataka kuliongezea kwamba, kama kutaongezwa na aiport tax dola tano sio vibaya, kwa sababu nchi itapata pesa nyingi na tutapata kufanya mambo yetu mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu umenipa dakika tano ninakushukuru. Mimi naunga hoja ya bajeti hii asilimia mia moja. Inshallah... (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. HASSANALI MOHAMEDALI IBRAHIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha hapa Bungeni salama nikiwa na afya nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri aliyowasilisha leo asubuhi hapa Bungeni. Kabla sijakwenda huko, kwanza nitakuwa mwizi wa fadhila kama sijachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli. Haya tunayozungumza hapa Bungeni kujadili bajeti mbalimbali za Wizara zote, huu ni mkakati ya Mheshimiwa Rais kwa kukusanya kodi. Ndiyo maana leo tuko hapa kifua mbele kuzungumzia bajeti zetu za Wizara mbalimbali ikiwepo bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kumwambia Mheshimiwa Rais kwamba sisi Wabunge wa CCM tuko nyuma yake na tutakuwa nyuma yake mpaka atakapomaliza kipindi chake 2025. Nasema hivi kwa sababu gani? Sisi wote hapa ni mashahidi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli anapofanya kazi kwa bidii, upendo na uzalendo katika kuwasaidia Watanzania waliokuwa wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda kwa sababu siwezi kuyataja mambo yote, nitaje mambo mawili matatu ambayo Mheshimiwa Rais katika kipindi kifupi alichokuwa madarakani ameweza kununua ndege ATC, ameanza vilevile kutujengea reli ya SGR (Standard Gauge Railway); ukusanyaji wa pesa wa mapato ambayo ni historia katika nchi hii katika awamu zote zilizopita, Awamu hii ya Tano, kwa kweli pesa zinazokusanywa na TRA kwa sababu mwenyewe Mheshimiwa Rais anafuatilia hilo suala, limekuwa historia ya TRA wanakusanya pesa kwa wingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika ujenzi wa bomba la mafuta, tumeona Mheshimiwa Rais alivyojitahidi na vilevile ufuaji wa umeme ambapo hata juzi hapa Mheshimiwa Rais amekwenda kuzindua Kinyerezi ambayo tutapata megawati 2,500. Hayo ni baadhi ya mambo tu, siwezi kuyataja yote lakini nampongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mambo haya anayofanya naweza kuwaambia Wapinzani 2020 Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli hana upinzani nchi hii. Kwa utabiri wangu huu Waheshimiwa Wabunge wa CCM watakuja kuniambia, Mheshimiwa Raza kweli asilimia ambayo Mheshimiwa Rais atapata ni zaidi ya 90. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, mambo anayofanya Mheshimiwa Rais, vilevile nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kumteua ndugu yangu Mheshimiwa Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa Awamu hii ya Tano. Niseme kwa sababu gani nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kumteua Mheshimiwa Waziri Mkuu; kwanza Waziri Mkuu wetu masha Allah ni handsome. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua Mheshimiwa Waziri Mkuu ana hadhi ya kipekee ninapokwenda popote, basi huna haja ya kumwambia mtu huyu ndio Waziri Mkuu wa Tanzania, anajulikana tu. Sifa nyingine ambayo Waziri Mkuu anayo, kwanza ni mtu makini sana, mwenye busara, mwenye upendo, mchapa kazi, kwa ufupi tunaita kwa kizungu all- rounder. Mheshimiwa Waziri Mkuu hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze vilevile dada yangu Mama Mary kwa kukupata mtu kama wewe, hii pia ni sifa kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuje katika bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nimefuatilia bajeti hii, nimeona ni bajeti ambayo ni ya matumaini na hususan Mheshimiwa Waziri Mkuu nakupongeza kwa kusimamia masuala ya mbolea na mbegu bora. Kama tunavyojua, nchi yetu ya Tanzania asilimia kubwa sana ni wakulima na wafugaji. Kwa hiyo, naomba vilevile haya masuala ya upatikanaji wa mbolea yawe ni endelevu kwa sababu tukiwa na mbolea nzuri na mbegu nzuri, tutapata matunda mazuri na wakulima watapata nguvu na watakuwa na imani na Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nataka nipongeze kwa kuongezwa bajeti kwenye Wizara ya Afya kwa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu. Hapa nimesoma na nimeona kwamba imeongezwa mpaka kufikia shilingi bilioni 269. Hii inaonesha Serikali ilivyokuwa makini katika kuwasaidia Watanzania ambao ni wanyonge na maskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upatikanaji wa umeme, napongeza vilevile kwa sababu umeme ni kitu muhimu sana katika nchi hii. Bila umeme hakuna viwanda, hakuna chochote. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais anapokwenda na speed hii na naamini Mheshimiwa Waziri Mkuu yuko nyuma yake kumsaidia ili kuona kwamba baadhi ya vijiji ambavyo havijapata umeme, natumaini mpaka mwaka 2020 hivyo vijiji vitafikiwa na umeme ili wananchi wetu nao wapate kumwona Mheshimiwa Rais angalau katika kuangalia TV zao na kusikiliza redio zao. Hiyo ni moja katika maendeleo ya nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jiji la Dar es Salaam, naweza kusema ni kioo cha Tanzania, kwa sababu watalii wote, wafanyabiashara wakubwa wote wanakuja katika Jiji la Dar es Salaam. Leo Mheshimiwa Waziri Mkuu kuna baadhi ya sehemu Dar es Salaam huwezi ukapita usiku kama hujaziba pua. Kwa sababu kuna watu wanalala, kuna watu wanaoga, kuna watu wanafanya choo hapo hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninao ushahidi kwenye simu yangu kwamba watu katika mitaa fulani Dar es Salaam wanachafua mazingira kabisa, yaani mazingira yanakuwa machafu sana. Sehemu hiyo siyo kwamba wanalala watu wawili au watatu, wanalala watu 50 na kuendelea. Ushahidi huo ninao kwenye simu yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Jiji letu la Dar es Salaam liangaliwe kuhusiana na mazingira yetu kwani haya mambo yamepita kiasi. Watu wanaoga kabisa, wanachukua maji wanachota wanaoga hapo hapo, wanafanya haja zao; haileti picha nzuri sana. Naona iko haja kwa Mkurugenzi wetu wa Jiji Dar es Salaam kuliona hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais kama atanipa nafasi kuwa Mkurugenzi wa Jiji wa Dar es Salaam kwa muda wa wiki mbili au tatu, nitafanya kazi hiyo kwa wiki tatu na mtaiona Dar es Salaam itakavyokuwa safi. Naamini huyu Mkurugenzi aliyekuwepo sasa hivi, baada ya kusikia maneno haya, atajirekebisha na atafanya yale ambayo yanastahiki katika jiji letu la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi ya kuzungumza…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. HASSANALI MOHAMEDALI IBRAHIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Namshukuru Mwenyezi Mungu vilevile kwa kunipa uzima wa afya nikiwa nimesimama hapa kwa nguvu zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kaka yangu Waziri wa Biashara na Viwanda, Mheshimiwa Mwijage. Kwa kweli, hiki kitabu nimekipitia leo mchana vizuri kabisa, nakiona kipo vizuri sana. Nimpongeze yeye na timu yake nzima kwa jinsi walivyoandaa bajeti hii na ripoti ya Wizara ya Biashara na Viwanda, Mheshimiwa Mwijage na timu yako hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nichukue nafasi hii nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa mambo aliyoyaweka jana vizuri sana. Amewatoa wananchi wasiwasi, maneno yalikuwa mengi kwamba katika Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan kutakuwa hakuna mafuta na sukari. Tunamshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Mwijage kwa kutuhakikishia kwamba, hakutakuwa na suala hilo wala matatizo hayo ya mafuta wala sukari. Nawashukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Mwijage. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mwizi wa fadhila kama sijampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa jinsi anavyohangaika kufufua viwanda ambavyo vilikuwa vimekufa. Naweze kusema kwamba jitihada ya Mheshimiwa Rais imetuletea faraja kubwa sana na naamini kwa Waziri aliyekuwa naye ni Waziri jembe kabisa, Mheshimiwa Mwijage. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwijage nimefanya naye kazi wakati nilipokuwa kwenye Kamati ya Biashara na Viwanda miaka miwili iliyopita. Namjua kazi yake, ni mtu ambaye yuko straight kabisa na makini kabisa, hongera sana Mheshimiwa Waziri kwa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilikuwa na ushauri kwa Wizara ya Biashara na Viwanda. Mheshimiwa Mwijage nataka utusaidie au uwasaidie wafanyabiashara ambao wanapakia mizigo yao Dubai kuja Dar-es-Salaam wanalipia SGS kule Dubai na kila item wanatozwa kwa Dola 20 mpaka Dola 30. Baada ya ku-register SGS Dubai wanatakiwa baada ya mali kufika hapa TBS inawa-charge tena katika kuchunguza vile vitu walivyoleta. Kwa hiyo, wanakuwa wanalipa SGS kule Dubai wakija huku wanachajiwa tena na TBS. Sasa utakuta mfanyabiashara analipa mara mbili ya kile kitu ambacho amekinunua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa SGS kule Dubai wamekuwa very slow yaani ukiwapelekea sampuli, huchukua more than four or five weeks, sasa utakuta mfanyabiashara anaumia na kule ameweka mzigo kwenye godown za watu analipa zile gharama kwa sababu Dubai hakuna mtu ambaye atakuwezesha kukuwekea mali kwa mwezi mmoja, mwezi mmoja na nusu. Kwa hiyo, nashauri Mheshimiwa Waziri labda ukae na hawa wenzetu wa SGS Dubai na TBS, kwa nini wanakuwa wana-charge mara mbili mzigo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwa sababu, tukiwasaidia wafanyabiashara naamini watapata nguvu ya kutuletea mali kwa wingi na Wizara ya Fedha itapata kodi. Kwa hiyo, hapa tunampa motisha mfanyabiashara at the same time Wizara ya Fedha na TRA wanapata pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna tatizo moja kubwa la wenzetu hawa wa TFDA. Naweza kusema kwamba TFDA sio wote, sitaki kuwakaanga wote, baadhi yao hupelekewa sampuli ikiwa ya maziwa, juice au kitu chochote wanakwambia kwamba utapata ripoti after 60 or 70 days. Mheshimiwa Mwijage wenzetu hawa TFDA hivi kweli wanatutakia mema Tanzania hii? Wakati wewe unapigania wafanyabiashara walete mali wauze nchi ipate pesa tupate kodi, wanaambiwa warudi after 70 days?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi navyozungumza haya huwa nina ushahidi, sizungumzi tu kwa kuwaelemea TFDA. Kwa hiyo, naomba TFDA kama kuna upungufu wa watu basi waajiriwe watu wengine lakini huwezi kumuweka mtu 60 or 70 days ndiyo unampa report, inarejesha nyuma maendeleo yetu na sisi tunataka kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu hata hizo ada ambazo wana-charge TFDA ni kubwa sana Mheshimiwa Waziri. Ningeomba kidogo hizo ada ziteremshwe ili watu wawe na hamu ya kuleta mali nchini. Kiwango kinachotozwa sasa hivi ni kubwa sana. Hata hivyo vitu ambavyo SGS wana- charge kule Dubai kwa kila item ni Dola 30 nyingi Mheshimiwa Mwijage. Wewe ni msikivu naamini utachukua hatua. Haya ndio yalikuwa ni kero na nilikuwa natoa ushauri kupitia Wizara yako ifuatilie kwa karibu sana hili suala ili tufike hapo tunapotaka kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa sana watu wanapoiponda Serikali hii, mimi siwafahamu. Kwa sababu, hiki kitabu kimeeleza kuna wawekezaji 99 wamesajili kuanzisha viwanda Tanzania hii. Ina maana hao wawekezaji ambao wanakuja kuwekeza hapa si wendawazimu, wameshajua Tanzania ni nchi ya amani, Tanzania kuna kuna moja, mbili, tatu. Sasa wanapoponda kwamba hakuna viwanda au hakuna chochote wasome hiki kitabu ambacho kimeandikwa kwenye ukurasa wa 186, miradi mipya ya viwanda vilivyosajiliwa na TIC mwaka 2017/2018. Hii ni ushahidi tosha kwamba watu wana imani na Serikali ya Mheshimiwa Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna wengine wanakuwa na choyo na binadamu sisi tunakuwa na choyo. Mheshimiwa Mwijage ukivaa suti nzuri kama mtu hakupendi atakwambia unaringa lakini kwa sababu umevaa suti nzuri. Kwa hiyo, nasema tupunguze uchoyo, tumpe haki yake Mheshimiwa Rais Magufuli anavyofanya hii kazi kwa sababu, kuileta Tanzania katika amani ni kitu kikubwa sana ndio maana hawa wawekezaji 99 wamekuja kuwekeza Tanzania billions of Dollars, it is billions of Dollars. Leo kwa nini tunakaa tunaiponda hii Serikali? Why? Badala ya kuipa nguvu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini katika miaka michache ijayo tutakwenda kwenye uchumi wa kati, hapa tulipo tutasonga mbele. Ni juhudi zetu sisi Watanzania, Wabunge waliokuwa humu ndani tumpe nguvu na ushirikiano Mheshimiwa Rais pamoja na Mawaziri wake wote walikuwa humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanaposema kwamba labda kiwanda kiwe na ekari tano, ekari sita, kule China unaweza kukuta kichumba kidogo sana wanazalisha mambo ambayo huwezi kuyaamini Mheshimiwa Mwijage. Wana vyerehani 10, 15 lakini the production ambayo wana- make ni kubwa sana. Kwa hiyo, kiwanda si lazima kiwe na ekari 10 ndiyo ukaita kiwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana na naipongeza sana Wizara hii na naiunga mkono asilimia 100 Wizara ya Biashara na Viwanda. Inshallah Mwenyezi Mungu atatusaidia na tumuombee Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, ahsanteni sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI RAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uwezo na pumzi yake kusimama hapa kuchangia bajeti hii muhimu sana katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji, pamoja na timu yake nzima kwa jinsi walivyoandaa hii bajeti ya fedha ambayo itatusukuma mpaka 2019. Hongereni sana Mheshimiwa Waziri na timu nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niwashukuru wenzetu wa TRA. Unajua tunapozungumzia masuala ya bajeti ya Serikali lazima tuwashukuru na wenzetu wa TRA namna wanavyohangaika kutafuta mapato ambayo yanatusaidia wananchi. Bila TRA kukusanya mapato leo hapa tusingeweza kuzungumzia bajeti hii. Kwa hiyo, nimshukuru sana Kamishna Charles Kichere na timu yake nzima ya TRA kwa jinsi wanavyofanya kazi nzuri ya kukusanya mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naweza kusema sasa hivi kwa kiasi fulani TRA wamekuwa marafiki sana kwa wafanyabiashara na wameweza angalau kukaa kwenye meza kumaliza yale matatizo ambayo wafanyabiashara wamekuwa wanahangaika nayo. Kwa hiyo, lazima tuwape sifa TRA tofauti na miaka ya nyuma hawakujenga mahusiano mazuri na wafanyabiashara lakini sasa hivi wamekuwa wasikivu na wenye nidhamu ila baadhi yao bado siyo waaminifu lakini kwa asilimia kubwa wanafanya kazi nzuri. Nawapongeza sana TRA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa sababu bila nguvu zake tusingefika hapa tulipo. Watu ambao wanataka tusimsifu Rais, hivi jamani kwenye Bunge hili tumsifu Uhuru Kenyata au tumsifu Museveni? Sisi tuko hapa kumsifu Rais John Pombe Magufuli, hatuko hapa kuwasifia Marais wa nchi nyingine, huo ndiyo ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kiongozi yeyote anapofanya mazuri usitegemee wapinzani kukusifu sana hiyo ni kawaida. Nchi zote duniani hakuna chama kinachoongoza wananchi halafu wapinzani wakakisifu, si India, Ulaya hata huko Marekani. Kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Rais asivunjike nguvu, aendelee na katika miaka yake miwili na nusu tumeona mambo makubwa aliyofanya Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kushirikiana na Waziri Mkuu na Mawaziri. Mawaziri wa Awamu hii ya Tano wamekuwa ni Mawaziri ambao wanafanya kazi usiku na mchana, kwa hiyo, niipongeze Serikali nzima ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nizungumzie bajeti hii. Kwanza niipongeze Wizara kwa kuondoa VAT katika masuala haya ya taulo kwa sababu kweli yatawasaidia akina mama na wanafunzi kwa kiasi kikubwa sana, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia kuongezea ushuru baadhi ya bidhaa kwa nia ya kuvilinda viwanda vya ndani. Kwa kweli, tulikuwa tunawafanyia biashara kubwa wenzetu wa nchi jirani, wao wanatuletea hapa sisi tunafanya manunuzi tu, tunawachumia wao, ajira zinakwenda nchi za jirani, nchini kwetu viwanda vinaumia na wafanyakazi wakati mwingine wanapunguzwa. Katika kuongeza Ushuru wa Bidhaa katika bidhaa mbalimbali hatua hiyo itavilinda viwanda vyetu vya ndani. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri na timu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija katika masuala ya nguo zetu za mitumba, naomba Wizara hii iangalie kwa jicho la huruma hizi nguo za mitumba kwa sababu huwa zinatumiwa na wananchi wa hali ya chini kabisa Tanzania hii. Nguo za mitumba zinauzwa rahisi, kila mmoja wetu anajua zinakwenda mpaka vijijini na mikoani. Sasa hivi container moja la mitumba linatozwa shilingi milioni 40. Naomba tu Wizara, kama kuna uwezekano wa kupunguza angalau kidogo tukawapa nguvu hawa wananchi wa chini ambao hawawezi wakanunua shati la Sh.40,000 au Sh.50,000 wajipatie mashati hayo kwa bei rahisi na hii itatusaidia kujenga uhusiano mzuri na watu wa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niombe Waziri aangalie sana sekta ya kilimo kwa sababu ni sekta moja muhimu sana katika nchi yetu ya Tanzania na asilimia 70 ya Watanzania wanategemea kilimo. Kwa hiyo, namwomba sana wakulima wawezeshwe, wapatiwe mikopo, wapewe
initiative ambayo itawasaidia kuwekeza katika kilimo. Kilimo kikiwa kizuri Tanzania tutapata foreign exchange. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchini India wanategemea sana agriculture, wana-export kwa hali ya juu. Serikali ya India inapata pesa nyingi sana katika kwa ku-export bidhaa za agriculture. Hata wenzetu wa Thailand kwa kiasi kikubwa cha fedha wanategemea export ya agriculture. Kwa hiyo, siyo vibaya nasi tukaipa umuhimu sana sekta hii ya kilimo ambayo kwa kiasi fulani itatusaidia kupata foreign exchange kwa sababu, njia kubwa ya kupata foreign exchange ni kuuza mazao yetu nje. Sisi Tanzania Mungu ametupa ardhi kubwa sana ambayo mimi naweza kusema asilimia kama 40 hazijatumika, bado tunayo ardhi ya kuwekeza katika kilimo. Tukikipa umuhimu kilimo basi Serikali yetu itapata foreign exchange. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kasoro kidogo imejitokeza, wafanyabiashara wengi Dar-es-Salaam hawana mashine za EFD, wanatumia receipt book. Serikali inakosa mapato, TRA inakosa mapato na naona hawawatendei haki wafanyabiashara wengine wanaotumia mashine za EFD. Kwa hiyo, naomba TRA kupitia Wizara yako ihakikishe katika kipindi cha miezi miwili kila mfanyabiashara anatumia mashine ya EFD.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono asilimia 110. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hi kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambayo ameisoma Bungeni leo hii asubuhi.

Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa pumzi zake mimi kusimama hapa nikiwa mzima. Nichukue nafasi hii adhimu kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu katika hotuba yake iliyojaa busara na matumaini ya Watanzania. Kwa kweli naweza kusema katika timu aliyokuwa nayo Rais Mheshimiwa John Pombe Magufuli basi siyo vibaya tukampa Mheshimiwa Waziri Mkuu jina la mchezaji mashuhuri duniani kama Messi kwa sababu Messi kama anavyojulikana basi na Waziri Mkuu naye anafanyakazi nzuri sana kwa kumsaidia Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii nimpongeze vilevile Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa sababu hayo maendeleo ambayo tunayaona katika nchi hii ni moja katika jitihada zake kubwa anazochukua kuwasaidia Watanzania wanyonge na ni mashahidi wetu Watanzania pamoja na sisi Wabunge kwamba kazi anayoifanya Mheshimiwa John Pombe Magufuli ni kazi kubwa sana na kwa kweli anastahili pongezi katika miaka yake mitatu hii amefanyakazi, extra job au extra miles amekwenda Mheshimiwa Rais, kwa kweli tuzidi kumuombea Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nije katika changamoto sasa katika Wizara hii au katika mambo ambayo yataweza kusaidia kutupeleka mpaka 2019/2020. Changamoto iliyokuwepo mwanzo kwamba ni ajira (permit work). Permit work imeleta vilio kwa wale wawekezaji. Wanapokuja watu wao kutaka kufanyakazi katika nchi hii basi kupata permit work imekuwa kazi ngumu sana na hii inarudisha maendeleo ya Mheshimiwa Rais. Kuna watu wanapanga hujuma ya kurejesha maendeleo ya Mheshimiwa Rais na sisi hatutakubali kuona hayo yanafanyika katika nchi hii.

Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu nina ushahidi ya kwamba mtu ana kitega uchumi ambacho ame- invest billions of shillings halafu anaomba kupeleka permit yake ya engineer wake anakataliwa wakati katika kile kitega uchumi ana wafanyakazi 150 ambao wanategemea kupata riziki zao. Sasa kwa ajili ya mtu mmoja hiyo nafasi inakuwa inafungwa, wale wafanyakazi 150 ambao ni Watanzania wanakuwa hawana kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka Wizara hii ambayo inahusika na work permit kidogo walegeze kamba, tusiwavunje nguvu watega uchumi wetu wanaokuja kuleta maendeleo katika nchi yetu ili vilevile Mheshimiwa Kairuki ambaye sasa ameteuliwa karibuni kuwa Waziri wa investors protocol ningemuomba na Mheshimiwa Kairuki atusaidie katika masuala haya kwa sababu ni moja katika kuleta maendeleo katika nchi yetu na kuwavutia wawekezaji na ninamuamini sana huyu Dada Kairuki atatusaidia katika suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine tukija katika masuala ya mawasiliano, mimi nashukuru kwamba terminal III imemalizika kwa 95 percent, niishukuru sana Serikali, lakini kuna changamoto mbili, tatu katika uwanja wa ndege ambao sasa hivi tunatumia terminal II. Utakuta wale ma-porters ambao wanasaidia abiria ambao wanakuja nchini, hakuna hata porter mmoja ambao yupo uwanja wa ndege wote wameondolewa. Sasa nauliza kwamba watu wazima ambao ni walemavu au watu wazima watawezaje kuchukua mabegi yao kuchukua kwenye ile belt kutia kwenye trolley na kupeleka nje? Hii kidogo inaleta picha mbaya sana katika Uwanja wetu wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere ambao sisi tunatumia terminal II lakini tusijetukafanya makosa haya ambapo tunakwenda katika terminal III ambayo tunataka kuiboresha zaidi ili kuvutia watalii ambao watakuja nchini kutumia uwanja wa ndege wetu huu mpya ambao umekamilika kwa asilimia 95. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine nilikuwa nataka wenzetu hawa wa ATC wajipange vizuri kwa sababu ushindani umekuwa mkubwa na wasipojipanga vizuri watakuja kuwa katika hali ngumu kutokana na haya mambo ya ndege inatakiwa mkakati maalum wa kupanga programs kwamba ndege ziende sehemu gani ili mapato ya nchi yaongezeke na kuinua Shirika la Ndege ya ATC.

Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa lingine lipo katika Halmashauri zetu hapa nchini, Halmashauri nyingi sana katika mikoa mingi sana hazikufanya vizuri katika asilimia 10 ya vijana, akinamama na walemavu. Kuna Halmashauri nyingine katika hizo asilimia 10 ya hizi pesa wanazipangia kuzitumia kwa kazi nyingine ambapo hizi asilimia 10 tumepitisha katika Bunge hili tukufu kwamba zinakwenda kwa vijana, akinamama na walemavu, sasa Halmashauri nyingi sana hazikufanya vizuri, lakini tunaomba Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi watusaidie kuhusu masuala haya ya asilimia 10 ili hii itakuwa ni changamoto kwa vijana, akinamama na walemavu katika nchi hii.

Mheshimiwa Spika, nikija katika masuala ya madini, mimi nimshukuru Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli katika kukutana na wadau wa madini ambao kwa kweli ameyatatua matatizo mengi sana. Lakini pamoja na kwamba Serikali imeweka mkakati maalum wa kuuza hizi dhahabu kwa kutumia utaratibu utakaotambulika, lakini bado madini yanasafirishwa nje kwa njia za panya. Bado dhahabu zetu, Tanzanite zetu zinasafirishwa nchi za nje kwa kutumia njia za panya.

Nilikuwa naomba sana wahusika ambao wapo katika boarders zetu wawe wanalifanyiakazi hili na mimi nitakaa na Mheshimiwa Waziri wa Madini ili nimpe changamoto ambapo mimi nafahamu vipi haya madini yanasafirishwa, kwa sababu tukiachia madini yasafirishwe, Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakosa mapato mengi sana na sisi tuna kazi kubwa sana ya kuwapelekea maendeleo wananchi wetu ambao wengi ni wanyonge na wanategemea hizi pesa za maendeleo zifike katika shughuli za maendeleo katika nchi yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, mwisho katika kumalizia kwangu, katika kuwasaidia wafanyabiashara ambao wanataka kufanya biashara ambapo hiyo inaongeza changamoto, inaongeza mapato katika Halmashauri zetu, wenzetu wa TFDA na TBS kwa kweli wamekuwa na urasimu mkubwa sana, inavunja moyo. Mtu anataka kuanzisha biashara ya kuleta maziwa au kuleta dawa ya mbu, miezi mitano hajapata report kwamba anafaa kuruhisiwa kuleta au haruhusiwi. Sasa kwa kipindi cha miezi mitano inakuwa Serikali kwanza inakosa mapato ya ndani, Halmashauri inakosa mapato. Kwa hiyo, wenzetu wengine wanataka kama kumuhujmu huyu Mheshimiwa Rais ambaye kwa kweli mimi siwezi kueleza mfano wake kwa kazi anayoifanya, anaifanya kazi kwa imani kubwa sana Mheshimiwa Rais na anataka nchi hii iendelee, isonge mbele lakini kuna watu makusudi wanamkwamisha.

Mheshimiwa Spika, kuna watu wanakuwa wanamkwwmisha Mheshimiwa Rais lakini watajibu kwa Mwenyezi Mungu wanajua wao. Lakini mimi naomba TFDA na TBS msiwakwaze wafanyabiashara ambao wana nia ya kuleta mali kuuza Tanzania. Hakuna urasimu wa miezi mitano, miezi sita sijawahi hata kuona katika nchi nyingine ambazo nimetembelea mimi sijapata kuona urasimu huo naona hapa tu Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa haya machache, nichukue fursa nyingine ya kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri sana iliyojaa matumaini ya Watanzania na sisi In Shaa Allah Wabunge tutafanyanae kazi Mheshimiwa Wazitoi Mkuu kumsaidia kuona kwamba hii bajeti yake inapita na tunakwenda mbele mwaka 2020 na vilevile kumsaidia Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli ili kazi ya mwaka 2020 kushika hatamu Tanzania iwe kazi rahisi kwetu sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa haya machache, nichukue fursa hii vilevile niwapongeze Mawaziri wote ambao wako chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, niwapongeze kwa jitihada zao wanazofanya na Mungu atawasaidia, lakini haya niliyoyazungumza nimeona bora nitoe changamoto hii ili tupate kusogea mbele siyo katika kumlaumu mtu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa haya machache nakushukuru sana, ahsante sana, naunga mkono hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE.IBRAHIM HASSANALI RAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nimshukuru kaka yangu kwa imani yake aliyonipa hizo dakika tano nichangie, kwa hiyo zitakuwa ni kumi, Mwenyezi Mungu amzidishie. Pia nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hotuba za Mheshimiwa Waziri kaka yangu Mheshimiwa Jafo na Mheshimiwa George Mkuchika katika hotuba zao. Kabla sijaendelea huko mbele nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa pumzi zake mie kusimama hapa na kuweza kuzungumza mambo mawili matatu ambayo yatasaidia kueleza changamoto zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na Wizara ya TAMISEMI, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Jafo kwa kazi kubwa anayoifanya. Kwa kweli naweza kusema ni Waziri mwenye kiwango, nikisema Waziri mwenye kiwango kwamba ni Waziri ambaye kwa kweli ameleta matumaini mapya kwa wananchi na kwa Serikali yetu hii ya CCM. Nampongezasana Mheshimiwa Jafo pamoja na wenzake, Manaibu wake kwa kazi kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka vilevile nizungumzie changamoto ambazo zinatokana na hii Wizara. Kwanza kabla sijakwenda huko niwapongeze Wakuu wa Mikoa, kwa sababu Wakuu wa Mikoa kwakweli kwa awamu hii wanafanya kazi nzuri na wanasimamia mapato ya halmashauri, lakini baadhi ya halmashauri hawajafanya vizuri katika ku-collect zile ten percent ya vijana akinamama na watu wenye ulemavu. Kwahiyo, naomba sana Wakuu wa Mikoa wawe kidogo wakakamavu na wawafuatilie Wakurugenzi wao kwasababu tunayo taarifa kwamba halmashauri nyingi zimekuwa hazifanyi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ambazo nataka kuzungumzia hapa kwanza hii ya ten percent ambao kwa kweli baadhi ya Wakurugenzi wanakuwa hawazikusanyi hizi pesa zinavyotakiwa na vilevile wanazitumia kwa matumizi mengine ambapo hii ten percent ya vijana, akinamama na walemavu, tumepitisha hapa Bungeni ikawa ni sheria mama kwamba zitumike katika mambo tuliyokusudia. Kwahiyo, ningeomba sanaWakurugenzi hili suala la ten percent, huu ndiyo uhai wa wananchi wetu maskini ambao wanategemea hii asilimia kumi kufanya miradi yao ambayo inayaendeleza mbele maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Mheshimiwa Waziri nikija kwenye suala la usafiri waDART, hili limekuwa janga katika Jiji la Dar es Salaam. Nasema janga kwa sababu nimeshuhudia na nimepata malalamiko mengi sana kwa wananchi wetu kwamba mabasi hayatoshi, mabasi mengi yameharibika na vilevile pale Kimara pamekuwa watoto na akinamama wanavyobanwa hata kuvuta pumzi wanashindwa wengine wanarudi nyumbani hawaendi makazini. Sasa hili suala la DARTnamwomba sanaMheshimiwa Waziri alivalienjuga, kwa kweli nikimpelekea picha ambazo ninazo kwenye simu zangu atawaonea huruma akinamama na watoto wanavyobanwa, yaani wamebanwa na wengine wanakanyangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya matatizo ya DARThao Wapinzani wanaidakia sana hii, kuikemea Serikali na kuitukana Serikali yetu ya CCM, hiyo ndiyo imekuwa ajenda yao wapinzani, lakini hawajui kwamba matatizo haya yanawahusu na wao vile vile siyo watu wa CCM tu. Kwahiyo, namwomba Mheshimiwa Jafo suala la DARTna kama huyu mwekezaji amefeli hawezi basi aniambietu Mheshimiwa Raza hebu tutafutie mwekezaji mwingine, nitamtafutia mwekezaji mzuri sana ambaye ataondoa matatizo haya ya usafiri wa mabasi Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwa mzee wangu KapteniGeorge Mkuchika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, ni kaka yangu, ni mzee wangu, nimpongeze kwa hotuba yake nzuri ambayo haina mashaka. Sisi nimashahidi wa Tanzania, utawala huu wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli hauna doa hata zeropointone percent. Nataka niwaambie Wapinzani kwamba huu utawala bora uliokuwa Tanzania, tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa Mungu alivyompa imani Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa mambo anayoyatenda, lakini kuna nchi huwezi ukasema jambo lolote la ubaya wa yule mfalme ambaye anaongoza katika nchi ile, utapotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa leo Tanzania hii, watu wana fursa ya kuzungumza, wanafursa ya kusema, wanafursa ya kutembea, leo mwisho tunakuwa hatuthamini utawala bora ambao unaongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli. Kwa kweli naweza kusema kwamba, Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amekuwa ni mfano katika Afrika na sasa hivi katika Afrika sisi tupo post ya juu kabisa katika nchi ambayo ipo amani katika nchi hii yaani tujipongeze sisi Wabunge wote kwamba Tanzania ipo juu katika amani. Isitoshe katika Afrika tu hata katika nchi za Afrika Mashariki na kati we are top number one katika amani. Kwahiyo, hii peke yake inasadikisha kwamba kweli utawala bora uliokuwepo na amani ipo, ungekuwa utawala bora si mzuri, basi na amani isingekuwepo, ingetoweka. Kwahiyo,Mheshimiwa Waziri, MheshimiwaKapteni George Mkuchika, namwambia aendelee hapo hapo na kama kuna msumeno aendelee, lakini tuweke nchi katika hali ya nidhamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile niwapongeze ndugu zangu wa TAKUKURU, wameweza kufanya kazi kubwa sana ya kuwapeleka mahakamani mafisadi wakubwa ambao walikuwa wanajulikana mapapa wa nchi hii. Nataka nimwambie Mkurugenzi wa TAKUKURU, Diwani Athman kwa sababu namwamini na pale alipowekwa na Mheshimiwa Rais kwa sababu naye kamwamini, kwahiyo Ndugu Diwani Athuman apige kazi, asiogope sura ya mtu, bado kuna mafisadi wamefichika ndani ya pazia, wamefilisi nchi hii, kwahiyo Mheshimiwa Waziri nataka ashirikiane na huyu Mkurugenzi wetu wa TAKUKURU ili aweze vile vile kuwafichua wengine ambao wamefilisi nchi hii na kutufikisha hapa tulipofika.

Mheshimiwa Mwenyekiti,kwahiyo nampongeza sana. Kwa kweli rushwa imeondoka Tanzania sivyo kamatulivyokuwa miaka ya nyuma, sasa hivi nidhamu imerejea katika kazi. Rushwa ndogo ndogo ipo bado, lakini na hakika chini ya Wizara yaMheshimiwa George Mkuchika na hizo rushwa ndogo ndogo nazo zitaondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, nafikiri nimetumia muda wangu dakika kumi kama ipasavyo, nikushukuru kwa kunipa nafasi na naiunga mkono Wizara hii hundred percent. Pia Wizara ya Mheshimiwa Jafo naiunga mkono hundred percent.Mwenyezi Mungu ampe afya na umri Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Amini.(Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi kwa mara nyingine kuchangia hii Wizara ya Viwanda na Biashara. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa pumzi zake mimi kusimama hapa nikiwa na afya, mzima, Alhamdulillah. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nachukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Kakunda na timu yake, kwa kweli bajeti aliyowasilisha leo ni bajeti ambayo inalenga kuwasaidia wafanyabiashara na wenye viwanda na matumaini yangu mimi ni kwamba Mheshimiwa Kakunda, katika nchi hii ya Tanzania tunawategemea sana wafanyabiashara na wenye viwanda. Wao ndiyo wanatuletea revenue kubwa sana katika nchi hii. Kama Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kila anaposimama kwenye kiriri akiwahimiza wafanyabiashara wa nje waje Tanzania kuwekeza, hii ni kwa sababu anawatakia mema Watanzania ili Tanzania iwe nchi ya viwanda tukifika 2025 na vilevile Watanzania watakuwa wanapata ajira kuongezeka katika viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nimsaidie ndugu yangu Mheshimiwa Waziri Kakunda. Kwa kweli tatizo lililokuwepo kubwa sana kwanza kwa wenzetu wa TFDA. TFDA huwa wanachukua muda mrefu kutoa ripoti ya kile kitu ambacho kimewasilishwa kwao, wanachukua miezi mitatu. Mheshimiwa Waziri mimi ninao ushahidi. Wenzetu nchi za nje kama South Africa hapa, within 10 days wanakupa ripoti kwamba kitu hiki kinafaa au hakifai. Sasa wenzetu wa TFDA nataka wabadilike sana kwa sababu kumweka mtu miezi mitatu hujampa ripoti, kwanza unamvunja moyo kwamba asilete bidhaa na pili, vilevile unawarejesha nyuma wale ambao wanataka kuleta bidhaa katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine kubwa kwanza hii ada ya dola 200 kwa kila sampuli moja Mheshimiwa Kakunda kwa kweli ni nyingi sana. Naomba Wizara yako iliangalie hili suala kwa sababu mtu kwenye kontena ameleta item 20 na kila item dola 200, fanya hesabu hapa, huyo analipa kiasi gani? Kwa hiyo, badala ya kuwa-support wafanyabishara tunawa-discourage wasilete vitu nchini na wakileta vitu nchini, Tanzania inapata revenue, TRA wanakusanya pesa. Kwa hiyo, naomba TFDA wabadilike sana katika masuala haya ya haya mambo tunayokwenda nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka wenzetu wa TBS na ZBS washirikiane, waaminiane katika kazi hii kwa sababu mzigo unaotoka Zanzibar kuja huku kwa kweli inakuwa ni shughuli kubwa sana. Kwa sababu wafanyabishara wa Zanzibar wanapoleta vitu Zanzibar wanakuwa wameshapewa kibali kule na ZBS, sasa unapokuja huku TBS nao wanaweka mguu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri hili pia ni changamoto kubwa sana katika Wizara yako. Naomba TBS na ZBS washirikiane ili wafanyabiashara wawe wanafanya biashara kwa amani, wanatuingizia pesa, lakini hizi changamoto inatuletea vilevile sintofahamu katika Muungano wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka nikupe taarifa kwa sababu sisi ni watu ambao tupo mjini tukaa na wafanyabiashara. Hawa TBS wakikupa cheti cha kwamba wewe hiki kitu unaweza ukakiuza mfano, lakini wanakuja watu wa FTC wanaipinga TBS. Sasa hapo Mheshimiwa Waziri watu wanakuwa wanaonyesha mimi ni mkubwa kuliko wewe. TBS anasema sawa lakini anakuja FTC anakanusha anasema hapana, mimi sijaridhika. Sasa nani tumsikilize? Tumsikilize FTC au TBS? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema nizungumzie zaidi biashara kwa sababu nakaa na wafanyabiashara wakubwa na wadogo. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mpina, juzi alikagua kiwanda cha maziwa Arusha na alihakikisha kwamba hakuna kitu kutoka nje kitakuja Tanzania ili kukilinda kile kiwanda. Wewe Mheshimiwa Waziri na hilo pia ulichukue kwamba viwanda vyetu vya ndani lazima uvilinde kwa sababu ukivilinda viwanda vya ndani ndipo ajira ya Watanzania itakapopatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Waziri, tatizo lingine kubwa lililokuwepo ni OSHA. Nasema tena OSHA. Hawa wanakuja maofisini wanasema kwamba huu umeme haujakaa sawa, hii meza haijakaa sawa; hii feni haijakaa sawa; hivi ni kazi ya OSHA, tunauliza? Kama ni kosa la umeme au nini, ni la mwenye nyumba mwenyewe aliyejenga siyo yule aliyekodi; na ushahidi ninao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni kuna wafanyabiashara Dar es Salaam wametozwa shilingi 850,000/=, wengine shilingi 650,000/=, wengine wametozwa shilingi 420,000/=. Ninao ushahidi OSHA wamekwenda kwa sababu eti huu umeme haufai, hii meza uliyokuwa umeweka hapa siyo mahali pake, jamani hawa OSHA wanataka kutupeleka wapi? Hivi OSHA wamepewa kazi ya kwenda maofisini na kuchaji pesa nyingi kiasi hicho? Mheshimiwa Waziri, ushahidi pia ninao ukitaka, nazungumza haya kwa ushahidi.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri Kakunda kwa sababu upo na Mheshimiwa Kairuki kwa sababu ni Waziri wa Uwekezaji, atakusaidia sana Mheshimiwa Kairuki kukuletea wawekezaji, lakini suala la wawekezaji kupata kibali cha kufanya kazi nchini, naomba hili ulibebe kwa sababu kuna malalamiko mengi sana. Kuna watu wanaenda ku-apply labor hawapati, wanahangaishwa, nenda rudi, nenda rudi. Kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Waziri Kakunda, hili suala uliangalie kwa sababu kuna watu wamekuja wanawekeza hapa, Watanzania wanapata ajira lakini mwisho wa siku hawapati kibali cha kufanyia kazi. Kwa hiyo, nani anapata hasara? Ni wale Watanzania wanakuwa wanakosa ajira kwa yule mtu mmoja ambaye amekosa labor.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hili Mheshimiwa Waziri ulibebe sana. Nami ukitaka ushahidi wa mambo yote nitakuletea ofisini kwako. Tupo hapa kuwajenga Watanzania ili nao wapate kazi. Masuala haya ya nenda rudi haituletei sifa Tanzania. Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli anahangaika nchi nzima, anasema wawekezaji njoo, jengeni, fanyeni lakini kuna watu makusudi wanamkwamisha Mheshimiwa Rais. Hatukubali! Tunasema tena, hatukubali sisi! Mheshimiwa Rais anakufa na nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Kakunda mimi hayo nilitaka niyaweke wazi na vilevile naomba Manispaa zetu watenge nafasi ili mashine/viwanda vidogo vidogo wajasiliamali wetu wapate kuwekeza kama nchi zetu za China na India, kuna Manispaa wamewekeza nafasi maalum kwa viwanda vidogo vidogo kwa vijana wetu ili nao wachangie hii fursa ya biashara ya Tanzania ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na nimshukuru tena Mheshimiwa Waziri Kakunda kwa kuwasilisha hotuba yake hii nzuri. Naunga mkono hii hoja mia fil-mia na Inshallah Mungu atatusaidia. Naitakia kila la heri nchi yetu ya Tanzania, nchi ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie hotuba ya bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Spika,nichukue nafasi hii adhimu nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa jinsi jana alivyotueleza namna ofisi yake ilivyokuja na mkakati wa bajeti hii ya mwaka 2020/2021. Mimi nipongeze Wizara zote zilizopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi kubwa wanayofanya kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi na kwa kweli kwa miaka minne hii, tunakwenda mwaka wa tano (5) Wizara zote zilizo chini ya Mheshimiwa Waziri Mkuu zimefanya kazi kubwa sana akiwemo yeye mwenyewe Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekuwa na kiungo mzuri sana katika kumshauri na kumsaidia Rais wetu Mheshimiwa John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mwizi wa fadhila kama sijakushukuru wewe, Kiti chako pamoja na Naibu wako kwa kuweza kutuongoza sisi Wabunge kwa kipindi cha miaka mitano. Kwa kweli kazi mliyoifanya ni kubwa, sisi Wabunge tunakushukuru sana tunakuombea maisha marefu wewe na Naibu wako, Mungu akupeni afya na umri na Inshallah Mungu awarejeshe tena katika jengo hili mwaka huu wa 2020. Amen. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nipongeze Wizara zote ambazo zimetekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi, lakini nizipongeze sana Wizara ya Madini na Wizara ya Nishati. Kwa kweli katika kipindi hiki kidogo Wizara ya Madini imefanya kazi kubwa sana katika kubadilisha sheria zetu za ukusanyaji wa mapato. Kwa muda mfupi sana Wizara hii ya Madini imeweza kutuingizia mabilioni ya fedha katika uuzaji wa dhahabu, tanzanite na almasi. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wake kwa kusimamia hilo na vilevile nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri ambaye anasimamia Nishati, kwa kweli leo Watanzania kwa asilimia kubwa sana wanapata umeme mpaka vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile niipongeze Wizara ya Mambo ya Ndani kwa habari njema waliyotulea kwamba wamenunua mashine ya kuweza kutengeneza kadi za NIDA ambayo ime-cost8.5 billion na itaweza kutengeneza kadi za NIDA 9,000 kwa muda wa saa moja. Kwa kweli niipongeze sana Serikali ya CCM ikiongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nije sasa katika suala hili la Corona. Corona ni janga la kimataifa na kila ukisikiliza taarifa za habari ni Corona tu sasa hivi. Nipongeze Serikali zote mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jinsi walivyochukua jitihada ya kuweza kusimamia masuala haya ya Corona na kuwaelimisha wananchi kwa ujumla na wale ambao wanaingia nchini.

Mheshimiwa Spika, nataka kumshauri Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye ndiye anatuongoza na ndiye mshauri wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Kipindi hiki Watanzania wengi wanatumia maji, kila nyumba, mtaa na kila unapokwenda wanatumia maji. Maji yale pengine hata huyo mtu ambaye hana lakini anasaidiwa na mtu mwingine anaambiwa chukua ndoo ya maji hii nawia mikono.

Mheshimiwa Spika,mimi natoa ushauri lakini Serikali ndiye mwenye maamuzi ya mwisho. Ushauri wangu ni kwamba Serikali isamehe kodi ya miezi mitatu katika sekta ya maji kwa sababu sasa hivi kila mahali maji yanatumika. Kwa hiyo, ushauri wangu hii miezi mitatu Serikali isamehe kodi kwa wale wote ambao wanatumia maji akiwepo mtu wa chini mpaka mtu wa juu. Hii itatusaidia, watu watapata kidogo matumaini ya kuweza kuwasaidia wengine maji zaidi ya ndoo moja kwa sababu sasa hivi nyumba ambayo ilikuwa inatumia ndoo mbili ya maji au tatu kwa siku, sasa pengine inatumia ndoo zaidi ya kumi au kumi na tano.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu mwingine kwa Serikali yetu ya CCM, naomba sana kwamba labda hali ikizidi kuwa mbaya basi Serikali ichukue hatua ya kuweza kutuambia kwamba saa mbili za usiku ukiingia ndani mpaka alfajiri saa 12 ndiyo uweze kutoka kwenda kufanya shughuli zako za kiuchumi. Ikiwa hali itazidi kuwa mbaya, huu ni ushauri pia mzuri, wenzetu nchi nyingi duniani wameshaanza kwenda kwenye lock down. Hata juzi Dubai, Mascat na nchi nyingine za Ulaya ambazo tunazijua za Italy, Spain, London na nchi nyingine zimekwenda katika lockdown kabisa twenty four hours. Mimi ushauri wangu iwe ni kuanzia saa mbili za usiku mpaka asubuhi saa 12, hii itasaidia kupunguza haya matatizo ya Corona. Huu ni ushauri.

Mheshimiwa Spika, ushauri mwingine ni naomba Jeshi la Polisi na Uhamiaji wawe makini sana katika hizi njia za panya. Watu watakuwa wanatoka nchi za jirani kuja huku Tanzania wakisema Tanzania Corona bado haijafika asilimia kubwa, watakuja kutuambukiza sisi. Watu wanapita njia za panya, kwa hiyo, Jeshi la Polis na Uhamiaji wawe makini sana katika hizo njia za panya wasije wakatuumiza huku kwa sababu sasa hivi huko nchi za jirani wameshaanza kuchanganyikiwa na masuala ya Corona.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli huu ndiyo ushauri wangu na kabla sijamalizia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya. Kwa kweli kila Mtanzania ni shahidi wa anayoyafanya Mheshimiwa Rais kupitia Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi. Mimi nataka niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge humu ndani tusiwe na wasiwasi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017.
MHE. IBRAHIM H. MOHAMMEDALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuchangia huu Muswada ambao umeletwa na Waziri, Mheshimiwa Profesa Kabudi. Kwa kweli kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha siku hii nikiwa mzima wa afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimshukuru Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayofanya kuhusu mambo haya ya madini ambapo itatuletea faida kubwa sisi Watanzania kwa sababu kila mmoja anajua kwamba katika madini ndipo kwenye pesa. Mheshimiwa Rais anapofanya kazi hii, anafanya kwa maslahi ya Watanzania. Kwa kweli sisi Watanzania miaka yote tulikuwa tunaibiwa tu basi, tulikuwa kama tumekaa kwenye ICU. Watanzania tulikuwa tumekaa kwenye ICU, tunamshukuru Mheshimiwa Rais amekuja kutukomboa na kututoa ICU. Kwa hiyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja asilimia 200 sio 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikija katika Muswada huu wa Sheria za Madini, kwanza nimpongeze kaka yangu Mheshimiwa Profesa Kabudi. Kwa kweli Mheshimiwa Profesa Kabudi wewe ni jembe, nimekuamini, kwa sababu huu Muswada uliouleta kila kitu kimeelezwa humu ndani. Vilevile nimpongeze AG kwa ushauri wake mzuri anautoa kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu nimepewa dakika tano siwezi kuzungumza mambo yote, lakini naweza kusema kwamba nayaunga mkono haya yote ambayo Mheshimiwa Profesa Kabudi ameyaleta mbele yetu na hii ni kwa ajili ya maslahi yetu. Hata hivyo, naomba hii asilimia 16 ya hisa ambayo tumesema tupate angalau iwe hisa asilimia 20 ambayo itatupa faida kubwa na itatuletea pesa ili mambo yetu katika nchi yetu ya Tanzania yaende vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naunga mkono Muswada huu kwa kusema kwamba kutakuwepo na utaratibu wa Serikali kufanya ukaguzi wa udhibiti na uzalishaji wa madini. Ni safi sana hiyo, naunga mkono asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naipongeza kwa kusema kwamba Serikali ina uwezo wa kudhibiti na kutambua viwango vya madini vyote ambayo yanatolewa kwenye maeneo ya migodi. Hii itatusaidia sisi kutoibiwa tena. Nasema kwamba tulikuwa tunaibiwa kwa sababu kulikuwa hakuna sheria nzuri ya kutulinda sisi na watu walikuwa wanasafirisha hizi dhahabu kwa kutumia njia za panya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naweza kusema kwamba Muswada huu ni kwa ajili ya Watanzania wote na sisi tunapaswa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kweli amekuwa mstari wa mbele kuona kwamba maslahi ya Watanzania yanapatikana. Kwa kweli tumuombee Mwenyezi Mungu ampe umri na afya Mheshimiwa Rais ili aendelee kutusaidia na sisi Wabunge wa Chama cha Mapinduzi na Watanzania kwa ujumla tupo nyuma yake na tutakuwa siku zote nyuma yake kwa nguvu zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi kwa kweli naunga mkono hoja hii na naweza kusema kwamba baadhi ya mambo yaliyofanyiwa marekebisho ni marekebisho mazuri. Vilevile nimpongeze tena Mheshimiwa Profesa Kabudi na kwa jambo lolote atakapoona kwamba ipo haja kwa maslahi yetu asisite kutuletea sisi tuko hapa kwa maslahi ya Watanzania si kwa maslahi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla hujanipigia kengele, nakushukuru sana na nashukuru timu nzima ya Wizara ya Madini na Wizara ya Sheria na ahsante sana Mheshimiwa Profesa Kabudi wewe ni jembe kweli kweli, nimekuamini safari hii.