Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ali Hassan Omar (3 total)

MHE. ALI HASSAN OMARY KING aliuliza:-
Tatizo la Mazingira ni tatizo mtambuka na tumeona jinsi Serikali ilivyojipanga kutatua tatizo hili kwenye maeneo tafauti:-
Je, Serikali imejipanga vipi kutatua tatizo la mazingira linalojitokeza la kudidimia kwa ardhi kwenye makazi ya watu?
NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA (MHE. LUHAGA J. MPINA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ali Hassan King, Mbunge wa Jang’ombe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa kumejitokeza tatizo la kudidimia kwa ardhi na nyumba za makazi ya watu kwa vipindi na maeneo tofauti katika maeneo ya Zanzibar hususani 1998 na 2015. Kufuatia matukio haya, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) iliunda timu ya wataalam kutoka sekta mbalimbali ili kufanya utafiti wa kina na kubaini chanzo cha tatizo hili chini ya utaratibu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, kupitia Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti huo ulibaini sababu kubwa ya kudidimia kwa ardhi ni udhaifu wa ardhi hususani katika eneo la Jang’ombe ambalo liliwahi kuchimbwa udongo na mchanga kwa ajili ya kujengea nyumba za Mji Mkongwe katika kipindi cha zaidi ya karne tatu zilizopita. Uchimbaji huo uliacha mashimo makubwa yaliyofunikwa na udongo kidogo kidogo kwa miaka mingi na hatimaye maeneo hayo kujengwa nyumba za makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hiyo pia ilichangiwa na kujaa maji katika maeneo hayo kutokana na kiwango kikubwa cha mvua zilizonyesha katika miaka ya matukio yaani 1998 na 2015. Aidha, sababu nyingine zinazoweza kusababisha kudidimia kwa ardhi ni pamoja na udhaifu wa miamba ya chini ya ardhi kuhimili uzito wa majengo, maeneo husika kuwa na asili ya unyevu mkubwa (wetlands) pamoja na sababu zitokanazo na athari za mabadilliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuzuia madhara yanayotokana na kudidimia kwa ardhi, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuchukua hatua zifuatazo:-
(i) Kuyafanyia uchunguzi wa kina maeneo yote yenye matatizo ya kudidimia kwa ardhi na kuorodhesha nyumba zilizomo katika maeneo hayo na wahusika watapatiwa maeneo mengine kwa ajili ya kujenga nyumba za makazi ya kudumu. Hivi sasa upimaji wa viwanja 500 katika eneo la Tunguu unafanyika ili wananchi watakaohamishwa katika maeneo yanayodidimia wapatiwe viwanja. (Makofi)
(ii) Kuandaa utaratibu wa kudhibiti ujenzi holela katika maeneo ya miji na vijiji na kuboresha barabara na njia za maji ya mvua ili kuzuia madhara ya mafuriko na kudidimia kwa ardhi; na
(iii) Kuelimisha wananchi kupitia vyombo vya habari na matangazo kuhusu madhara ya mvua kubwa ikiwemo kudidimia kwa ardhi na mafuriko ili kuchukua tahadhari na kuepusha maafa.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING aliuliza:-
Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo la makazi kwa askari wa Jeshi la Polisi na Mheshimiwa Rais aligusia azma hiyo alipokuwa akilihutubia Bunge hili la Kumi na Moja kwenye kikao cha ufunguzi.
Je, Serikali imepanga kujenga mikoa mingapi majengo hayo ikiwemo Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ali Hassan King, Mbunge wa Jang‟ombe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza kuchukua hatua za makusudi kukabiliana na uhaba wa nyumba za Jeshi la Polisi. Kwa kutumia mifuko ya Hifadhi ya Jamii, chini ya mpango wa mikopo wenye riba nafuu Serikali imeshajenga nyumba 360 katika Mikoa ya Dar es Salaam, Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia inakusudia kujenga nyumba nyingine 4,136 katika mikoa 17 ya Tanzania Bara na Zanzibar. Aidha, Serikali itaendelea kutatua changamoto za uhaba wa nyumba za askari kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo mikopo yenye riba nafuu, Miradi Shirikishi (PPP) na kwa kutumia fedha za bajeti ya Serikali kadri hali ya uchumi itakavyokuwa ikiimarika.
Mheshimiwa Spika, mkakati huu utakwenda sambamba na Mipango ya Maendeleo ya Serikali ukilenga kufikia idadi ya nyumba za makazi kwa askari wote waliopo sasa na watakaotarajiriwa kuajiriwa baadaye.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING aliuliza:-

Je, kwa nini uvuvi wa kuzamia kwa kutumia chupa umezuiliwa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ali Hassan King, Mbunge wa Jang’ombe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, shughuli za uvuvi nchini zinasimamiwa kwa mujibu wa Sheria Na.22 ya Mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2009 na Miongozo mbalimbali ambayo hutolewa kwa ajili ya kusimamia na kuhakikisha kuna matumizi endelevu ya rasilimali za uvuvi. Kwa mujibu wa Kanuni ya Uvuvi ya Mwaka 2009, kifungu cha 66(I – Q), vifaa vya kupumulia chini ya maji au scuba au mitungi ya gesi haviruhusiwi kutumika kwa ajili ya kuvua samaki au viumbe wengine wa baharini. Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 66(2), vifaa vya kupumulia chini ya maji au mitungi ya gesi vinaweza kutumika tu kwa ajili ya uvuvi wa burudani (sport fishing), uvuvi wa samaki wa mapambo, mafunzo na utafiti na ni kwa kibali maalum.

Mheshimiwa Spika, wavuvi haramu wanaotumia milipuko hutumia mitungi ya gesi kuzamia kwa ajili ya kukusanyia samaki waliowaua kutokana na milipuko hiyo. Athari za milipuko ni pamoja na kuharibu matumbawe, (coral reefs) na mazingira ya baharini kwenye maji ambayo ni mazalia na makulia ya samaki pamoja na viumbe wengine na hivyo kuharibu mfumo wa ikolojia ambao unatishia kutoweka kwa kizazi cha samaki. Kuua samaki bila ya kuchagua wakiwemo samaki wachanga na mayai yake na hivyo kuhatarisha uendelevu wa rasilimali za uvuvi nchini.

Pia milipuko husababisha wavuvi kupata ulemavu na hata kifo, hivyo kutokana na sababu hizi Serikali iliamua kupiga marufuku uvuvi wa kutumia chupa au mitungi ya gesi.