Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Livingstone Joseph Lusinde (9 total)

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Livingstone Joseph Lusinde, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza Miradi ya Maji ya Vijiji Kumi kwa kila Halmashauri, Halmashauri ya Chamwino inatekeleza miradi kwenye vijiji saba ambapo miradi katika Vijiji vitano vya Mvumi Makulu, Itiso, Mvumi Mission, Chamuhumba na Membe imekamilika na wananchi wapatao 49,000 wanapata huduma ya maji. Mradi wa Wilunze unaendelea kutekelezwa na upo asilimia 60.
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi wa maji katika Kijiji cha Manzase umefikia asilimia 40. Kazi zilizofanyika hadi sasa ni ujenzi wa vituo 11 vya kuchotea maji, ujenzi wa nyumba ya mashine na ujenzi wa tanki lenye ujazo wa lita 80,000. Gharama ya ujenzi wa mradi ni shilingi milioni 355, ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi milioni 71 kimeshapelekwa kwenye Halmashauri hiyo kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu. Serikali itaendelea kupeleka fedha ili kukamilisha mradi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji katika Kijiji cha Chinoje ni kati ya miradi iliyokosa chanzo cha maji wakati wa utekelezaji wa awamu ya kwanza ya Program ya Maendeleo ya Maji. Utafiti wa chanzo kingine cha maji unafanyika na ujenzi wa mradi utafanyika katika mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa wananchi wa Manzase wanakabiliwa na kero kubwa ya maji na Mkandarasi hayupo kwenye eneo la Site, je, Naibu Waziri yuko tayari kuongozana na mimi kufika Manzase kwenda kuonana na wananchi na kuwahakikishia mwenyewe kwamba kweli mradi ule utakamilika?
Swali la pili, kwa kuwa Mradi wa World Bank, maeneo mengi maji yalipochimbwa vijijini hayakupatikana na wananchi wanaendelea kukabiliwa na shida kubwa ya maji. Serikali ina mpango gani wa kukamilisha miradi ya maji au Je, wananchi waendelee kusuburi tena, hawana mpango wowote Serikali mpaka Benki ya Dunia itusaidie tena? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji cha Manzase, kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi ni kweli Mkandarasi alikimbia na tayari tumeshafanya ufuatiliaji ni kwa nini alikimbia, tumemwagiza katika muda wa siku kumi arudi eneo la mradi, kama hatarudi basi tumeshapanga kuchukua hatua nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi huo utakamilika kabla ya nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha tunaouanza mwezi Julai. Pia sina tatizo kwa ruhusa ya Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa sababu hapa ni Dodoma sina tatizo Mheshimiwa Mbunge, tunaweza kwenda huko tukawaambia wananchi ni lini huo mradi utakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili Mheshimiwa ameuliza kwamba kuna miradi mingi ya World Bank ambayo ilifanyiwa kazi, lakini kuna maeneo ambayo maji hayakupatikana. Je ni lini sasa miradi hii itakamilishwa au tusubiri tena World bank?
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na Program ya kwanza ya Maendeleo ya Maji ambayo ilikwisha mwezi Desemba mwaka 2015, sasa tunaingia katika program ya pili. Maeneo yote yale tulikuwa tumeyapanga kwamba tunachimba maji, lakini katika kuchimba maji hayakupatikana, maeneo hayo mengi tumeshayafanyia utafiti, tumepata vyanzo vingine vya maji, kwa hiyo kuanzia bajeti ya mwaka wa fedha unaokuja 2016/2017, tutahakikisha kwamba maeneo hayo tunatekeleza hiyo miradi ili wananchi waweze kupata maji.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa wananchi wamezoea kabla ya barabara ya lami kujengwa huanza na upembuzi yakinifu: Mpaka sasa hivi hakuna hata dalili hizo: Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anatuhakikishiaje wananchi wa Jimbo la Mtera kwamba upembuzi yakinifu utakaopelekea ujenzi wa lami ya barabara ile utaanza kufanyika?
Swali la pili, Naibu Waziri amejibu kwamba Serikali itaendelea kuitengeneza barabara ile kwa kiwango cha changarawe; barabara ile haijawahi kutengenezwa kwa kiwango hicho kwa muda mrefu. Je, kwa majibu hayo, Naibu Waziri anataka kutuhakikishia kwamba kwa maneno yake tu ya leo barabara ile imepandishwa hadhi na kuwa barabara ya Mkoa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikiri kwamba Mheshimiwa Livingstone Joseph Lusinde, ni mfuatiliaji mahiri. Nami namhakikishia kwamba kutokana na juhudi zake anazozifanya, hatimaye hilo analolitaka litatekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili, naomba nimthibitishie kama nilivyosema kwenye swali langu la msingi kwamba hii barabara iko chini ya TAMISEMI na itaendelea kuhudumiwa chini ya TAMISEMI kwa maana ya Halmashauri. Haijapandishwa hadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza kuhusu upembuzi yakinifu, kwa kuwa kuna ahadi ambayo viongozi wetu waliitoa, kazi hiyo ya upembuzi yakinifu itaanza ili kuweza kuitekeleza ahadi hiyo na hatutaanza mwaka ujao wa fedha kwa sababu bajeti imepeleka vipaumbele katika maeneo yale ambayo Serikali tayari ilikuwa na commitment, na tunataka kwanza tumalize hizi commitment, baada ya kumaliza tutarudi kuhakikisha ahadi zote za Viongozi wetu zinatekelezwa, ikiwa ni pamoja na ahadi hii ya kupeleka lami kwenye barabara inayokwenda katika Hospitali ya Mvumi Misheni.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu, hata hivyo naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mkoa mzima wa Dodoma hakuna sehemu ambayo tuna mto unaotiririsha maji mwaka mzima, na kwa kuwa mradi ule haukuzingatia uchimbaji wa bwawa kwa maana ya kuyahifadhi maji ili baadaye wananchi waweze kuyatumia kwa kumwagilia.
Je, Mheshimiwa Waziri anatuambia nini juu ya uchimbwaji wa bwawa ili tuweze kuvuna maji na baadae tuweze kuyatumia na ili ule mradi uweze kuleta ufanisi?
Swali la pili, kwa kuwa kwenye majibu ya Serikali kuna baadhi ya vitu vingi vimeachwa, Naibu Waziri yuko tayari kuongozana na mimi kwenda kujionea kwa macho hali ilivyo kwenye mradi huo? Ahsante (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni kweli Mkoa wa Dodoma hauna mito ambayo inatiririsha maji mwaka mzima na ndiyo maana Mheshimiwa Lusinde wewe ni shahidi, kupitia Bunge la Bajeti ambalo limeisha juzi juzi hapa la mwaka huu wa fedha tuliagiza kwamba kila Halmashauri ifanye usanifu wa bwawa moja kila mwaka kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua na pia kukinga maji ya mifereji au mito ili tuwe na maji toshelezi kwa ajili ya matumizi ya binadamu mifugo na kilimo cha umwagiliaji.
Pamoja na hilo Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Maji tumeeamua kwamba miradi yote mikubwa ya maji kuanzia sasa tutakuwa tunaweka mabomba mawili, bomba la maji safi ya kunywa pamoja na bomba kwa ajili ya umwagiliaji na kwa kuanza, mradi ambao unakuja ambao utahusisha ujenzi wa Bwawa la Farkwa kwa ajili ya maji ya Dodoma tumesanifu na tumeweka mabomba mawili, moja kwa ajili ya maji masafi ya binadamu na maji ya umwagiliaji.
Mheshimiwa Spika, swali la pili umeuliza kama niko tayari kuongozana na wewe kwenda kwenye eneo lako kwa sababu sasa hivi ni kipindi cha Bunge, Mheshimiwa Spika kwa ruksa yako niko tayari, lakini baada ya Bunge basi itabidi nipewe ruhusa na Waziri wangu wa Maji na Umwagiliaji.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake. Hata hivyo napenda niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, punde wakati akijibu maswali leo asubuhi, amesema barabara ili ijengwe kwa kiwango cha lami inapitia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina; na kwa muda aliouonyesha ni kama vile kila kitendo kinachukua zaidi ya miaka miwili.
Je, kwa miaka iliyobaki kabla hata ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina haujaanza kufanyika, Waziri anawahakikishiaje wananchi wa Jimbo la Mtera kwamba barabara hiyo itakamilika mwaka 2020?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema barabara hiyo itaendelea kujengwa kwa kiwango cha changarawe na sasa hivi barabara hiyo bahati nzuri inajengwa. Je, Naibu Waziri yuko tayari kuongozana na mimi ili akaone hicho kiwango cha changarawe anachokisema kwamba kinajengwa badala ya kiwango cha changarawe naona wanajenga kwa kiwango cha tope, yuko tayari twende tukaone site? Ahsante
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Lusinde kwa kazi kubwa anayofanya ya kuwatetea wananchi wa Mtera.
Mimi nimhakikishie, Serikali hii iko pamoja naye na hicho anachokidhania kwamba inachukua zaidi ya miaka minne kufanya hizi kazi mbili, kwanza hii barabara siyo ndefu sana kwa hiyo, haitaweza kuchukua miaka minne. Ni barabara fupi na tunaweza tukaingia kwenye hatua ya design and build, kwa maana ya unafanya yote kwa wakati mmoja. Nikuhakikishie tu ahadi yetu kwenye hilo tutaitekeleza kwanza hii barabara ni ndogo sana. Siamini kama wewe unafahamu ni barabara fupi inayohitaji gharama siyo kubwa sana kwa hiyo, tutaikamilisha kwa wakati kabla ya kipindi hiki cha miaka mitano hakijaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, kwa kweli naomba kwa heshima kabisa ikiwezekana hata leo jioni hebu twende tukalione hili ili tuweze kulishughulikia kwa haraka. Kama ni kweli ni tope siyo sahihi kabisa.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kupata fursa hii. Kama alivyouliza Mheshimiwa Mgumba, majimbo ya vijijini yana matatizo makubwa sana ya umeme hasa katika center za Kata ya Mpwayungu, Kata ya N’ninyi, Manzase na Makao Makuu ya Kata ya Muungano ambako hakuna umeme kabisa. Sasa je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika maeneo haya hususan katika Kata ya Muungano? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa katika Jimbo la Mtera tunapeleka umeme katika vijiji (a) Katika maeneo aliyoyataja kimsingi nimhakikishie Mheshimiwa Lusinde kwamba katika maeneo ya Manzese, Muungano, Mpwayungu pamoja na eneo ambalo hujalitaja linaitwa N’ninyi wanaanza Ijumaa inayokuja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nichukue nafasi hii kumueleza Mheshimiwa Mbunge. Nichukue nafasi hii kwa sababu Waheshimiwa wengi wamesimama, kuwaeleza rasmi Waheshimiwa Wabunge kwamba kuanzia tarehe 20 mwezi huu wakandarasi wote katika mikoa 21 tuliyosaini mikataba wanaanza kazi rasmi ya ujenzi wa mradi wa REA Awamu ya Tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mikoa miwili ya Katavi pamoja na Kigoma, taratibu tunazikalimisha wiki ijayo na mwanzoni mwa mwezi Desemba wanaanza ujenzi katika mikoa hiyo miwili. (Makofi)
MHE. LIVINGSONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Naibu Waziri kwa majibu, hata hivyo napenda kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; urefu wa barabara alizotaja na milioni 350 kweli hapo kuna matengenezo ya barabara kwa kiwango cha changarawe au ni kwa kiwango cha tope?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa mvua za mwaka huu Mungu ametupa neema zimekuwa nyingi na zimetusaidia sana kwa upande wa kilimo, vilevile zimeleta uharibifu mkubwa sana wa barabara na madaraja, Mheshimiwa Waziri anatuambiaje juu ya matengenezo mazuri na yenye maana kwa ajili ya wananchi kuweza kupitisha mazao yao ambayo wanategemea kuyavuna ili waweze kujiletea maendeleo? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, anaulizia juu ya idadi ya kilometa ambazo nimezitaja na kiasi cha fedha ambacho kimetumika je, tumetengeneza kwa ubora uliotarajiwa au tumeyatengeneza kwa kutumia tope.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza hatujatumia tope kwa sababu yeye mwenyewe ni shuhuda kwamba tumehama kutoka katika matengenezo yaliyokuwa yanafanywa na Halmashauri pale ambapo kila Mheshimiwa Diwani alikuwa akiomba angalau apate hata kilometa moja au kalivati moja katika aeneo lake, mwisho wake inakuja inafikia kwamba hata ile thamani ya pesa ambayo imetumika haikuweza kuonekana na hivyo tukawa tunarudia kila mwaka katika matengenezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Lusinde na bahati nzuri na yeye ni shuhuda amekuwa akifanya kazi nzuri ya kupita kwenye Jimbo lake hebu akalinganishe kazi ambayo imefanywa na chombo hiki cha TARURA linganishe na jinsi ambavyo kazi zilikuwa zinafanyika hapo awali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili ameongelea neema ya mvua ambayo tumepata na sisi sote tukiwa ndani ya Mkoa wa Dodoma ni mashuhuda, tumepata mvua ya kutosha, mvua ni neema, lakini kila neema nayo inakuja na dhahama yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, naomba nimhakikishie chini ya TARURA na ndiyo maana kuna maeneo ambayo kumekuwa na mataengenezo na maombi maalum ili kuhakikisha kwamba barabara hizi zinapitika vipindi vyote na kiasi cha pesa ambacho chombo hiki kimeombewa kama Bunge lako Tukufu itaidhinisha chini ya usimamizi madhubuti hakika barabara zitatengenezwa kwa kiwango kizuri na kitakachoweza kupita katika vipindi vyote.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia kuuwawa kwa Ndugu Emmanuel Ernest wa Ilolo na Stefano Ndalu wa Nhinyi na Amani Joseph Sita wa Mvumi Mission kujeruhiwa vibaya na kupata malipo kidogo sana, je, ni lini sasa Serikali itaruhusu vijiji viweze kumiliki silaha kwa ajili ya kujilinda na wanyama hao wakali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, pesa aliyoitaja Mheshimiwa Naibu Waziri kuwa imelipwa kwa watu 27 ukiigawanya ni sawasawa na shilingi 278,518. Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kuwatangazia Watanzania kwamba katika nchi yetu tembo wana thamani kubwa kuliko uhai wa watu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu maswali hayo, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Livingstone Lusinde kwa kazi nzuri ambayo amekuwa akiifanya katika kufuatilia na kuwatetea wananchi wake. Kutokana na kazi yake ndiyo maana anajulikana kama kibajaji yaani kwa mambo makubwa anayoyafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie nafasi hii kuwapa pole wale wananchi wote ambao wameathirika ama wameuwawa na wanyama wakali, nawapa pole sana. Niseme tu kwamba hili suala alilolileta na kupendekeza kwamba tutoe silaha kwa wananchi na hasa katika vijiji kuweza kumiliki silaha, basi pale tutakapokuwa tunapitia sheria, pamoja na kanuni hizi tutaliangalia kama hilo litawezekana ili kusudi tuone kama linaweza kusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili alilouliza ni kwamba kwa mujibu wa Kanuni za Kifuta Jasho na Kifuta Machozi za mwaka 2011 ndiyo vinatoa viwango vile vinavyostahili. Nataka niseme kwamba tunachotoa siyo fidia, ni kifuta machozi na kifuta jasho. Ndiyo maana imeandikwa kabisa kwamba kifuta jasho kama binadamu ameuwawa ni shilingi1,000,000, kama amejeruhiwa ni shilingi 500,000, kama ni mazao yana viwango vyake kufuatana na kilometa. Kwa hiyo, hivi viwango vipo kwa mujibu wa sheria, lakini pale tutakapokuwa tunapitia tutavihuisha na kuona kama kuna haja ya kuvirekebisha ili kusudi vikidhi mahitaji ya wakati uliopo.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza nawapongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na Waziri wake kwa namna ambavyo wanafanya kazi kwenye Wizara hii. Hongereni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa eneo lile na Tarafa nzima ya Mkwayungu limegundulika kuwa na madini mengi sana ya gypsum na dhahabu kwa upande


wa Mafulungu na ninyi Serikali mlikuwa mmeona kabisa watu wanachimba na wanapata fedha na nyie mnapata kodi lakini baadaye mlisimamisha uchimbaji wa madini ya gypsum. Je, ni lini Serikali itawafungulia wale wachimbaji wengine ili waendelee kuchimba na nyie muendelee kupata mapato na wananchi waendelee kufanya kazi zao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuongozana nami ili twende tukajionee hali halisi ya watu wanaochimba dhahabu Mafulungu na wale wanaopata tabu ya kuchimba madini ya gypsum pale Manda ili tukaone na tukatatue matatizo yao kwa macho huku akishuhudia? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Livingstone Lusinde, Mbunge wa Mtera, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajibu nimpongeza Mheshimiwa Livingstone Lusinde kwa kuweza kufuatilia mambo ya wapiga kura wake na hasa wachimbaji wa maeneo ya pale Manda. Kwa kweli Mheshimiwa Mbunge anafanya kazi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba wachimbaji wa gypsum eneo la Manda na Mafulungu ni kweli walikuwa wamesimamishwa kwa sababu hawakufuata taratibu ambazo zilikuwa zimewekwa na Tume ya Madini katika uchimbaji huo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakwenda na watafunguliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niwataarifu wachimbaji wote wa gypsum na wachimbaji wengine wote Tanzania, madini ya gypsum tuliyazuia kwa maana ya madini ghafi kuyapeleka nje ya nchi, naomba wapitie GN Na.60 ambayo tumeitoa siku ya tarehe 25 Januari, waangalie ile GN ambayo imetoa mwongozo wa madini yote,
wanachenjua katika kiwango gani na kiwango kipi ambacho kinaruhusiwa kutoa nje ya nchi. Wakishapitia mwongozo huo wachimbaji watakuwa hawapati shida tena katika kufanya biashara hii ya madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Mbunge ameomba niongozane naye kwenda katika eneo la Manda kuangalia changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo. Nimhakikishie baada ya Bunge hili niko tayari kuongozana naye twende tukaangalie changamoto zinazowakabili wachimbaji wa Manda tuangalie namna ya kutatua changamoto hizo vilevile tuwawezeshe wachimbaji hawa waweze kuchimba wapate faida na waweze kufanya biashara hiyo ya madini. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Swali la kwanza Mheshimiwa Naibu Waziri katika jibu lake amesema ujenzi umeshaanza. Je, yuko tayari kuongozana na mimi kesho ili akaone ujenzi kama umeanza au watu wake wamemdanganya?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kutokana na kunyesha kwa mvua barabara nyingi siyo tu zimeharibika bali zimeoza na hii imepelekea wazazi kupata shida kufika hospitali hasa kwa barabara ya Huzi kuja Manda ambapo ukitoka Manda kuja Huzi kuja kwenye Kituo cha Afya cha Mpwayungu, lakini Mvumi Mission hakuingiliki pande zote, madaraja yamezingirwa na maji na yamevunjika.

Mheshimiwa Naibu Waziri anatuambiaje kuhusu kutengeneza kwa haraka ili kunusuru maisha ya akinamama na watoto na wagonjwa akinababa ili waweze kufika hospitali? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Lusinde, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, jibu langu la msingi nimesema kwamba maandalizi ya ujenzi wa barabara umeshaanza si kwamba barabara umeanza, maandalizi yamekwishaanza. Kama tumeshaanza niko tayari nipo tayari kuongozana naye kwenda kuangalia hatua ambayo imekwishafikiwa.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ambalo kimsingi ni swali ambalo linahusu Wabunge wote humu ndani kwamba baada ya mvua ambazo kimsingi zimeanza na zinaendelea sana barabara nyingi zimeharibika, Mheshimiwa Waziri wa Nchi ameshaagiza Meneja wa TARURA wa Tanzania na Mameneja wa Mikoa na Wilaya wafanye tathmini na walete bajeti ili tufanye utengenezaji wa haraka katika maeneo mbalimbali ili huduma muhimu ziweze kufanyika.

Kwa hiyo, naomba nitumie nafasi hii kuwaelekeza pia, Meneja wa TARURA wa Mikoa na Wilaya kwamba kazi ambayo wamepewa na Mheshimiwa Waziri wa Nchi waifanye haraka sana na kuchukukua hatua ya dharura ili kuhakikisha kwamba huduma za afya zinaendelea, vijana wanaenda shule na watumishi wa Serikali na watumishi wengine wanafanya shughuli zao za maendeleo. Ahsante.