Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Livingstone Joseph Lusinde (23 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mungu kwa kupata muda, lakini mimi siyo wa kuzungumza dakika chache ila nitajitahidi maana mara nyingi huwa napiga hapa nusu saa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Dkt. Mpango kwa kuleta taarifa nzuri. Nianze na suala la viwanda mimi nizungumzie kilimo cha biashara. Ni vema Serikali ikajikita kwenye kuanzisha viwanda vidogo ili wakulima hasa wa matunda, badala ya makampuni yanayotuuzia juice kununua juice nje ya nchi, yanunue matunda yetu ya ndani. Tukifanya hivyo tutakuza na tutakuwa na kilimo cha biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme watu wamekuwa wakizungumza sana humu ndani ya Bunge, wanazungumza kuhusu Polisi kuingia humu ndani. Nataka leo nisimame kuwatetea Polisi kwa sababu wao hawawezi kuja humu. Polisi ukimwona mahali popote kaenda kama Field Force, ujue ameitwa na watu wa eneo hilo. Wabunge, tuache tabia ya kuwaita Polisi, ukifanya fujo unawaita Polisi, na Polisi wameshaingia Kanisani wakati wa mgogoro ule wa Dayosisi ya Pare, Polisi wameshaingia Msikitini wakati wa fujo, Polisi wameshaingia Bungeni baada ya Wabunge wa Upinzani kuanzisha fujo. (Makofi)
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ukimwona Polisi kaingia mahali ujue kaitwa, na kama ninyi ni wageni hamuelewi utaratibu wa humu ukianzisha fujo umeita Polisi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua kuna watu wamekuja hapa bado hawajapigwa semina, kwa hiyo ngoja leo niwaelimishe. Mmesema vizuri na mfano uliotolewa na Mheshimiwa Heche hapa mdogo wangu ambaye mimi nimemfundisha siasa, kwamba eti anataka kulinganisha Chama hiki na kina Hitler, lakini leo nawaambia Chama chochote cha Upinzani duniani kikishindwa kushinda uchaguzi katika vipindi vitatu, kinageuka kuwa chama cha kigaidi, ndiko wanakoelekea hawa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ndipo wanapoekelea, maana kinakuwa chama sugu, kinakuwa Chama cha Upinzani sugu, tulikubaliana wakati ule, kwamba ili kuthamini haki za binadamu walau kila chama kitakachoshinda basi kilete mtu mmoja walau mwenye ulemavu wa ngozi. Yupo wapi albino wao hawa? Wabaguzi hawa na inawezekana hata wakati ule wa mauaji wako inawezekana walikuwa wanahusika hawa, yuko wapi? CUF waliwahi kuleta hapa alikuwepo Mheshimiwa Barwany, CCM yule pale wa kwao yupo wapi hawa? (Makofi).
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze hapa, kwamba usiwaone wanazungumza hivi na nataka nichukue fursa hii kumpongeza sana, nimpongeze sana Mzee Lowassa, Lowassa aligundua hawa wamemchafua sana akaamua kwenda kwao wamsafishe. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mzee Lowasa aligundua walimwita fisadi, walimwita fisadi papa, Edward Lowasa ana akili sana. Mchawi mpe mtoto amlee, akajua nakwenda kwao wanisafishe. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna Mtanzania mwenye akili atakayewasikiliza tena hawa, hivi wewe unakaa na jirani yako mwanaume anakuja anakwambia mke wako malaya, mke wako mhuni unamuacha, asubuhi anamuoa utamwamini tena? Hawa hawaaminiki, hakuna kitu watakachokieleza wakaaminiwa duniani. Kwa sababu wana ndimi mbili kama za nyoka hawa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanachokisema leo kesho watakibadilisha hawa, ndimi mbili za nyoka…
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana mnawaona leo wanasema hiki, leo wanageuka hivi, nataka nichukue fursa hii kumpongeza Jecha, kwa utaratibu huu wa kila Mzanzibar kuwa Tume ya uchaguzi, Jecha alikuwa sahihi kufuta yale matokeo. (Makofi)
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mtu anajifanya Tume, wenyewe unaowaona hapa wameletwa baada ya Tume ya Uchaguzi kuwatangaza ila Mheshimiwa Seif wanamtangaza wao, hawa ni wanafiki wakubwa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Lusinde, nakushukuru. Muda wako umekwisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kawaida yangu, nataka nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia zawadi ya uhai, kunipa afya bora ili niweze tena kusimama kwenye Bunge lako na niweze kutoa mchango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niweke sawa kumbukumbu, katika Bunge hili kuna Wizara tatu zinachangiwa kwa mfumo wa aina yoyote mchangiaji anayotaka. Wizara ya kwanza ni Ofisi ya Waziri Mkuu, unachangia kwa hoja zozote unazojisikia Mbunge. Wizara ya pili ni TAMISEMI, unapiga kokote Mbunge unakotaka kupiga; na ya tatu ni Finance Bill, kwa hiyo, kama mtu huelewi, Mbunge ukisimama Wizara hizo, usiache kitu! Kula moto, tema madini, watu watakusikiliza. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Waziri Mkuu, amefanya kazi kubwa tangu ameteuliwa kuwa Waziri Mkuu. Tuna uhakika kwamba Rais hajakosea kukupa kiti hicho Mheshimiwa Majaliwa na wala sisi Wabunge hatujakosea kukuidhinisha. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, katika Majimbo ya Waheshimiwa Wabunge wengi hapa Tanzania likiwepo la Mtera, kuna baadhi ya miradi imekuwa ya muda mrefu, imekuwa miradi sugu. Tufanye utaratibu wa kila Mbunge akuandikie ni mradi gani umechukua muda mrefu haujatekelezwa, tukuletee ili kuwe na bajeti maalum ya kuondoa viporo vya miradi iliyopita. Tukifanya hivyo, tutakufanya uanze sasa kutekeleza miradi mipya wakati umekamilisha ile miradi ya zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nilisema kwenye Bunge hili kwamba, ndugu zangu hawa wamechanganya mayai yote kwenye kapu moja, tupige. Nilizungumza nikiwa mahali hapa! Leo tumepiga, si mnaona biashara imekwisha?
Kwa hiyo, niwaambie tunampongeza sana Mheshimiwa Rais, kuna wengine wanasema anatafuta umaarufu; hivi ukimshinda mtu anayesema mafuriko hayazuiwi kwa mikono, wewe ukayazuia, unataka umaarufu gani tena? Mheshimiwa Dkt. Magufuli anatafuta umaarufu upi kama amekuwa binadamu wa kwanza duniani kuzuia mafuriko kwa mikono? Anatafuta umaarufu upi? Tuliwaeleza hawa na leo nataka niwathibitishie, nataka niseme na nchi, nataka niwaambie Watanzania kwamba hawa jamaa mliowapigia kelele, leo hii wameonesha wamefeli, hawana uwezo wowote hata ndani ya Bunge hawa! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Rais. Leo wanasimama hapa, watu wa Dar es Salaam mnisikilize. Anasimama hapa Kiongozi wa Upinzani anasema, Rais anafanya makosa kuamrisha pesa zilizokuwa ziende kwenye sherehe zijenge barabara ya Morocco. Wapinzani wanasema ni makosa. Hivi watu wa Dar es Salaam mnawapendea nini hawa? Hawa watu hawataki maendeleo! Wanataka domo! Mnawaona, wanataka waonekane kwenye TV wanasema bajeti ile na hela za kutengenezea barabara ya Mwanza, wanataka tukupe Mheshimiwa Nape halafu urushe live TBC ili waonekane hawa. Kutengeneza barabara na kuonekana kwenye TV lipi bora jamani?
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme hapa na nazungumzia hapa kwenye ukurasa wa 11, 17 kipengele kinachohusu demokrasia. Someni hapo! Mheshimiwa Waziri Mkuu huwezi kukuza demokrasia kama una Wapinzani wa jinsi hii. Haiwezekani! Utakuzaje demokrasia katika nchi kama Wapinzani ulionao ni wa aina hii?
TAARIFA
MBUNGE FULANI: Taarifa Mwenyekiti! Mwenyekiti taarifa!
MWENYEKITI: Mheshimiwa Lusinde kaa!..
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka kumwonya mzungumzaji anayezungumza. Mimi ni Mbunge senior na mwenye jina kubwa kuliko wewe. Unaposema kwenye Bunge hili, unamtolea mtu taarifa; wewe kama unaweza kusema umeambiwa, sema; kama hujafukuzwa Chama! Simama useme humu! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia kukua kwa demokrasia. Mimi hapa nataka leo nitoboe ndiyo maana nimesema leo najitoa muhanga. Katika maisha yangu nimewahi kuwa Kiongozi; Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la CHADEMA. Kule ndani kulikuwa na siri kubwa! Tulikuwa tumepanga siri wakati huo, niliyoikataa mimi, mpaka nikahama Chama hiki ya kuua Vyama vingine. CHADEMA wamefanikiwa kuua Vyama vyote hapa Tanzania.
Kwa hiyo, tunapozungumzia kukuza demokrasia tujue kwamba NCCR-Mageuzi ilikuwa na Wabunge watano na sasa ina Mbunge mmoja tu. Sijui ni maendeleo gani hayo? Wanaviua Vyama! Hawa wako kwa ajili ya kuua Vyama vingine! CUF walikuwa na Wabunge chungu nzima, sasa hivi Zanzibar sifuri. Hawa! Hawa wanaua Vyama vingine. Wanataka kubaki peke yao.
Kwa hiyo, nakuomba Msajili wa Vyama vya Siasa, endelea kusajili Vyama, ukifanya mchezo nchi hii demokrasia itakufa kwasababu kuna Chama kinataka kuhodhi Vyama vingine vyote viwe ndani yake. Hawa wanataka kufanya hivyo! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, CCM huko nyuma tulikuwa na zidumu fikra za Mwenyekiti. Tumetoka, hawa wameingia huko. Hawa sasa hivi zidumu fikra za Mwenyekiti, ndiyo maana unaona kila wakiambiwa kitu, wanafanya. Jambo la aibu sana! Unasimama kwenye Bunge hili, unasema Serikali imevunja Katiba, haiko Kikatiba, Serikali hii imekosea, kwa hiyo, hatutasema, lakini posho wanachukua, hawa! Yaani kama ni Waislamu; kama una Muislamu anasema hali nguruwe, anakula maini tu, ndiyo hawa! Wanasema Serikali hii imekosea, haiko Kikatiba, lakini mishahara na posho wanachukua hawa. Hawako tayari kusema! (Kicheko/Makofi)
Kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, sasa nimegundua siyo tu tuna wafanyakazi hewa, tuna Wabunge hewa; hawa! Bunge hili lina Wabunge hewa! Nataka nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Nape. Wizara yako Mheshimiwa Nape ilikuwa haijawahi kuchangia maendeleo yoyote vijijini zaidi ya habari, tunasikia michezo lakini kwa mara ya kwanza, pesa ulizozizuia ambazo mmeshauri, sasa zinaelekea kuchimba visima vya maji. Tunakupongeza sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanataka maji, hawataki kumwona Mbunge kwenye TV. Tunafahamu wamepata political mileage sana kwa sababu ya kusema mambo ya hovyo, watu wanayasikia, lakini kwa sasa watatakiwa kwenda kufanya kazi na kutoka jasho ili wananchi wawakubali. Ofisi ya Waziri Mkuu inashughulika na TASAF. Kwenye TASAF kuna malipo hewa. Wako watu wamekufa, lakini wanaendelea kupokea zile hela kama ambavyo tuna Wabunge wamekufa, hawazungumzi Bungeni, lakini wanapokea hela. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyakazi hewa wako wengi sana kwenye nchi hii, tuwashughulikie. Kuna watu hapo wanazungumza habari ya kumponda Rais kwamba anakurupuka kuchukua maamuzi. Rais, watu wote anaowafukuza na wanaosimamishwa ni kweli majipu. Kwa mfano, mchukulie ndugu yangu Kabwe. Mbunge wa Upinzani alisimama hapa, Mheshimiwa Wenje akasema Kabwe ni jipu hafai atolewe na hawa wakampigia makofi. Leo kasimamishwa, hawa wanasema anaonewa. Huwezi kuwaelewa hawa! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu wana-CCM pamoja na Waheshimiwa Mawaziri, kwa Baraza hili aliloliunda Mheshimiwa Rais, kule Mheshimiwa Majaliwa, pembeni Mheshimiwa Nape, kule kuna Mzee Handsome boy, hapa Mheshimiwa Mavunde, Mheshimiwa Jenista Mhagama; hawa hawachomoki, ndiyo maana mnaona wanapiga kelele! Mnawaona wanapiga kelele hawa, anazungumza habari ya shule wakati CHADEMA ilimsimamisha Rajabu Jumbe kugombea Umakamu wa Rais akiwa darasa la saba, wewe umesahau? Sasa kama ninyi mlitaka kuleta Makamu wa Rais darasa la saba, itakuwa Mbunge! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza sana Serikali. Nataka niwaambieni, katika siasa duniani, mimi ni Mwanafalsafa, nikija kufa ndiyo mtaelewa kwamba yule mtu alikuwa wa namna gani. Katika watu ambao wanajua siasa na wamefanya, nawaambieni Tanzania hatuwezi kusonga mbele. Wana-CCM tujigawe; wawepo Wabunge wa Upinzani kutoka CCM, tuisaidie Serikali. Hawa tuachane nao! Hakuna kitu wanachokifanya hawa! Tukiendelea kuwaamini hawa, tutapoteza point nyingi sana. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, duniani kote, Chama cha Upinzani kinakuwa na hoja moja tu. ANC wameshinda uchaguzi pale, hoja yao ilikuwa Ubaguzi; lakini hawa umeme, barabara, maji nini, hawa Wapinzani wa wapi? Hakuna Wapinzani wa namna hiyo! Mpinzani anakuwa na hoja moja tu. Anaijenga na anaaminika kwa watu. Hawa hawaaminiki, wanazungumza kila kitu! (Kicheko/Makofi)
Nakuomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, maendeleo katika nchi yetu kuna mikoa imechelewa kupata maendeleo kwa sababu resources zetu kuwa ndogo, igeukieni hiyo, acheni mikoa ambayo wananchi wameshiba, wanachagua Mbunge kuja kunyamaza tu Bungeni, achaneni nayo! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, wakati wa kutekeleza hoja hii, fanyeni kazi kwa Waheshimiwa Wabunge waliochangia shida zao; hawa walionyamaza achaneni nao, hawana shida hawa. Mbunge anatoka nyumbani anakuja kukaa hivi, hasemi shida yoyote halafu baadaye wanakuja kwenye viti vya Mawaziri kunong’ona; Waziri mtu mzuri. Unafiki wa namna hiyo haukubaliki! Tunataka waseme wazi. Wakisimama hapa, wanakashifu Mawaziri, wanawatukaneni, halafu wanakuja kwenye kiti, naomba umeme. Tunataka maombi wanayoyaleta mezani kwenu, wayaseme wazi. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri wa Fedha, tunakufahamu, wewe ni mtaalam; umekuwa Bwana Mpango, umeongoza maeneo mengi. Tunataka safari hii, Serikali ya Awamu ya Tano, mipango yenu yote mliyoipanga na mkatupa asilimia 41 ya pesa, zishuke kwa wananchi ili maendeleo yapatikane, tuwakate mdomo hawa. Sasa hivi tutafanya!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie, tutatengeneza umoja wa kutembea Jimbo kwa Jimbo kuwaambia hawa wasichaguliwe tena 2020. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuzungumzie barabara. Ukitoka hapa kwenda Iringa, kuna kipande cha barabara ambacho Mheshimiwa Rais ameshakiahidi kutoka barabara ya lami inayokwenda Iringa ipite barabara ya lami mpaka Hospitlai Teule ya Mvumi. Naomba kipande hicho mkikamilishe ili mimi niwe Mbunge wa maisha wa Jimbo lile. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie, katika wanasiasa wanaoniuma; nazungumzia demokrasia, lazima niwe mkweli; ananiuma sana kaka yangu Mheshimiwa James Mbatia. Mheshimiwa Mbatia ni mwanasiasa wa siku nyingi kuliko Mheshimiwa Mbowe. Sijui kalishwa nini, siku hizi anaambiwa na Mheshimiwa Mbowe, nyamaza! Naye ananyamaza kweli! Ananyamaza! Yaani sielewi kilichotokea!
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mbatia ni Mwanasiasa wa siku nyingi, Chama chake kilikuwa na Wabunge watano. Akanambia yeye amesoma, mimi sijasoma, sasa anakwenda mbele. Kutoka watano kuja mmoja! (Kicheko)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Lusinde inatosha kwa leo, muda wako umemalizika!
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Kweli hata mimi ambaye sijasoma siwezi kufanya ujinga kama huo! Hata mimi ambaye sijaenda shule, siwezi kufanya kitu cha namna hiyo. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Hawa tunawamudu, hamna kitu na tutahakikisha tunawafagia. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni ya leo na mimi niweze kusema mambo machache ya muhimu kuhusu hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kaka yangu Mheshimiwa George Boniface Simbachawene. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nachukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais ameonesha namna gani anataka kuirudisha Tanzania kwenye msimamo hasa wa nidhamu, uwajibikaji na uadilifu. Kwa sisi Wagogo tuna usemi unasema; mdabula nhili mwana na kalanga ganyina mmeso. Ukitaka kuonja uji wa mtoto, mtazame kwanza mama yake usoni. Ukimwona namna alivyokaa, unaweza ukaamua aidha, uonje au usionje. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Magufuli ameonesha yuko makini na mkali sana kwenye matumizi ya hovyo hovyo. Nataka niseme haya mnayoyaona wengine kushindwa kumwelewa ni kwa sababu Rais Magufuli amewashangaza wengi katika utendaji wake wa kazi. Ndiyo maana mtasikia mengi! Mtasikia Katiba imevunjwa, mtasikia nini! Kwa sababu wengine hawana namna ya kusema, inabidi waseme hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Waziri, tunakufahamu kwa msimamo wako Mheshimiwa Simbachawene. Tuna hakika utaitendea haki kama ambavyo umeonesha tangu mwanzo Wizara hiyo, ni Wizara kubwa, tuna hakika mkijipanga vizuri na Jafo kama mlivyokaa, mna uwezo wa kuhakikisha nchi yetu inasonga mbele. Tunawapa big up, tunawaomba mwendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme maneno machache hapa. Tunapozungumzia pengine kuna mtu hapa ameshindwa kuelewa anasema Mwanasheria Mkuu wa Serikali anatafsiri mambo ki-CCM. Ndugu zangu, nchi hii Ilani inayotekelezwa ni ya CCM. Nchi hii hakuna Sera ya Serikali peke yake tu inayojiendesha! Mlikataa wakati wa Bunge la Katiba. Tulipowaambia tuwe na Sera ya Serikali tuachane na Sera za Vyama, mkakataa! Leo tumeenda kuuza sera kwa wananchi; CHADEMA walikwenda nayo, CUF walikwenda nayo na CCM walikwenda nayo. Wananchi wamechagua ya CCM. Sasa mtu anaposema unaongea ki-CCM hata wewe Mbunge unatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM. Tuelewane hapo! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wala tusitake kuzungumza hapa vitu kama vile tunaimbiana mapambio. Upinzani watakuwa wanafanya kazi kama vile ambavyo tunaweza tukasema, wanafanya kazi waki-support kazi ya shetani, kwamba unapinga lakini wenzako wanaotawala wanafanya kazi ya Mungu. Wakati unaeleza upungufu, kwanza unashukuru kwa vichache vilivyotolewa. Hawa kazi yao ni kuponda, halafu baadaye wanaomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kazi yetu ni kusifu baadaye tunaomba. Wote kazi yetu ni moja, lakini utajiuliza mwenyewe, je, wa kuponda anafurahisha? Maana kwanza anaponda, halafu baadaye anapiga mzinga. Sisi tunasifu baadaye tunapiga mzinga. Kwa hiyo, tunafanya kazi ya Kimungu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa namwomba Mungu sana, anipe uwezo watu wanielewe. Sitaki kuingia kule kwenye siasa ambazo watu wamepanga; anasema tu kwa sababu Lusinde tumemwona, yeye anataka kuhamisha vita kutoka kwa Mawaziri kuja kwake; tutampakazia! Wewe useme kwamba Lusinde amepigiwa simu ya Mheshimiwa Rais, kaambiwa asiwatetee. Mimi Wakili? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siyo Wakili, sifanyi kazi ya Mahakama na wala simtetei mtu yeyote katika Mahakama yoyote ya nchi hii. Kwa hiyo, unaweza ukaona; na mimi nataka niwaambieni mkitaka kuleta siasa za uzushi mimi ndiyo natisha kwenye upande huo. (Makofi)
Nirudie tena kuwaonya, mimi mtu kunitaja namruhusu kwasababu hili jina kubwa na nimelitengeneza kwa gharama kubwa. Kwa hiyo, kuna watu watajitahidi kutaka kulifikia jina hili, lakini ni kazi ngumu sana. Waitara nimemfundisha siasa akiwa CCM, leo tena yuko CHADEMA nitaendelea kumsaidia taratibu lakini asifikie huko; Rais ni matawi mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, humu ndani tunafanya kazi mbili tofauti. Wako Wabunge ambao kazi yao tangu anasimama mwanzo, ataponda halafu mwishoni anakuja kwenye kiti, nisaidie maji. Yupo Mbunge atasimama, atasifu halafu baadaye atatoa shida zake. Ndiyo tofauti! Ninyi Mawaziri mtapima, yupi anayezungumza vitu vya msingi? Mtapima maana mimi siamini, hata kutafuta mchumba umkute msichana wa watu, umwambie dada una sura mbaya, lakini naomba nikuoe. Akikubali, ujue huyo hana akili. Hana akili huyo! Lazima umsifu kwanza! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewaeleza juzi kwa uchungu sana, nikasema nchi yetu tunajenga demokrasia, tuangalie kwa umakini sana. Hii nchi inapita kwenye mawimbi makubwa ya kujengwa demokrasia. Tunapojenga demokrasia, ni lazima hivi vyama tuvipe uhuru mkubwa wa kufanya mambo yao kama ambavyo tunafanya. Ndiyo maana nikawashtua wenzangu, Chama cha CUF, nikawashtua NCCR Mageuzi; siamini kwamba katika ndoa waliyonayo wanajenga demokrasia. Naamini wanakwenda kuuawa! (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaweza kumwona Mheshimiwa Zitto hana akili, yuko peke yake, lakini nawaambia katika miaka ijayo, pengine chama chake ndiyo kitakuwa maarufu kuliko vyama vingine hivyo. Maana kinapata muda wa kufanya siasa. Leo kuna watu wanazuiwa na Mwenyekiti, usiseme; wanakaa kimya. Sema, wanasema! Watu wa namna hii ni watu wanaoendeshwa kwa remote, hawawezi kuwa wanasiasa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaambia Tanzania ina Chama cha Upinzani pengine kimoja tu, ACT, vingine vyote ni vyama shindikizo. Ni Vyama vinavyokwenda na hoja. Meli ikizama, wanahamia kwenye meli; ikitokea kashfa, wanahamia kwenye kashfa. Serikali hii inaziba kila kitu. Wamehamia kwenye tv live. Hebu ngoja nizungumze kidogo hapa! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninyi wasomi mnasema nchi ina Executive, Parliament na Judiciary, hebu tujiulize; mbona Executive mambo yao hayaoneshwi live kila siku? Nayo ndiyo Executive inayoongoza nchi! Mbona hatuoni live kila siku mambo ya Ikulu? Mbona hatuoni Mahakimu wakiendesha kesi live kila siku na wao ni mhimili? Mbona hatuoni Majaji Mahakamani wakiamua mashauri wakiwa live na wao ni mhimili? Iweje watu wang’ang’anie mhimili mmoja? Huku ni kufilisika! Watu wamefilisika, hawana nafasi, wanataka kwenda kujitangaza kwa njia hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikasema leo nitoe somo. Katika nchi yenye mfumo wa vyama vingi tuangalie hivi vyama, tuangalie hata aina ya Wabunge. Mimi nawaambia tutakwenda mahali tutajikuta tunatumia resource kubwa, kupoteza muda hapa, hatuisaidii Serikali. Kwa hiyo, naomba niwaambie Waheshimiwa Mawaziri, tunapokuja kuwaambia shida zetu na juzi nilisema, hapa mnatukanwa, mnadharauliwa, halafu wakija wanasema naomba maji. Leo nchi ielewe hakuna Jimbo lolote la mpinzani linalopelekwa maendeleo. Maendeleo katika Majimbo yao tunapeleka sisi CCM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ndio tunakubali bajeti itekelezwe. Leo tunamwomba Waziri wa maji apeleke maji Moshi, Arusha; Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa huo wanakataa. Mwisho wa siku wanasema tumeleta maendeleo. Unaleta maendeleo kwa kusema hapana? Haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ifahamu maendeleo yanaletwa na Wabunge wa Chama cha Mapinduzi.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Aah, niendelee! Niliona Mheshimiwa Mch. Msigwa amesimama nami namheshimu kwa sababu nimeoa kwao. Unajua mimi nimeoa Iringa. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, watu waelewe hata barabara zilizojengwa Iringa Mjini aliposimama Mheshimiwa Msigwa, mimi nilitetea humu ndani ya Bunge. Maana mke wangu anatoka pale.
KUHUSU UTARATIBU.......
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru na nimshukuru hata Mheshimiwa Mch. Msigwa. Mheshimiwa Msigwa na mimi hatujawahi kupingana, sijui leo kimemkuta nini? Mimi juzi nimemwacha ameongea propaganda zake hapa, lakini leo yeye kashindwa kuvumilia. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa George Simbachawene, Mheshimiwa Waziri kupitia Bunge hili, aitazame Halmashauri mpya. Tumezungumza kuhusu mgawanyo wa nchi yetu. Tumeomba Halmashauri mpya ya Mtera, lakini atazame hata jina la Jimbo la Mtera. Kata ya Mtera iko kwako, Kijiji cha Mtera kiko kwako, mimi naitwaje Jimbo la Mtera? Haiwezekani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nikasema Mheshimiwa George hakuna sababu ya Jimbo langu kuitwa Jimbo la Mtera. Unanipa jina la utumwani. Mimi ningependa Jimbo langu liitwe Jimbo la Mvumi ambako anatoka Chifu Mazengo. Kwa hiyo, naomba Halmashauri yetu uitazame, Jimbo letu libadilishwe jina, lisiitwe jina la kijiji kilichoko kwako, kwa sababu sisi hatuwezi kuitika kwako. Watu wengi wanafikiri sisi tuko Mtera; Mtera ni ya George Simbachawene. Sielewi mzee alipoiita, aliita kwa sababu gani.
Mheshimiwa Mweyekiti, naomba kwenye Bunge hili uturudishie majina ya kwetu ya asili. Sisi pale tuna Mvumi karibu ziko 20. Kwa hiyo, ungetuita Jimbo la Mvumi ungekuwa umetutendea haki zaidi kuliko kutuita Jimbo la Mtera ambalo liko kwako wewe Mheshimiwa Simbachawene.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tunaloliomba, kuna barabara za TANROADS na kuna barabara za Halmashauri. Halmashauri nyingi hazina uwezo wa kujenga barabara ndefu.
Kwa hiyo, naomba kwa niaba ya Wabunge wenzangu, angalia kila Jimbo lenye barabara ndefu, badala ya kuiachia Halmashauri ambayo haina uwezo, zipandishwe hadhi ziende TANROADS ili ziweze kutengenezwa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza hivi kwasababu tuna uzoefu; kuna barabara nyingine Halmashauri hazina mapato ya kuweza kutengeneza urefu wa hizo barabara, lakini mkiwapa TANROADS wana uwezo. Kwa mfano, chukulia barabara inayotoka Dodoma Mjini. Kuna barabara inatoka Dodoma Mjini, inapita moja kwa moja kwenye Jimbo la Bahi kwa Mheshimiwa Badwel, inaenda moja kwa moja tena kwenye Jimbo langu la Mtera, halafu ndiyo inaenda kupakana ng’ambo kule kwa Mheshimiwa Waziri wa Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba ile barabara tuipandishe hadhi iwe barabara ya Mkoa kwasababu inapita kwenye Manispaa na kwenye Halmashauri mbili. Ukipata hela Chamwino ukitengeneza kipande, wenzako Bahi wanakosa, panabaki mashimo; kunakuwa hakuna mtengenezaji. Kwa hiyo, naomba kupitia Wizara yako, barabara tulizoziombea zipandishwe hadhi, mzipandishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuangalie, kuna Halmashauri nyingine, kata nne Halmashauri; kata tatu Halmashauri; hebu tuangalie, sisi tuna Jimbo lina kata 22. Tumeomba tugawanywe Wilaya, mkasema hapana tutawapa Halmashauri. Tupeni Halmashauri ili tuweze kusukuma maendeleo mbele. Tunataka kuendelea kufanya kazi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tulisema…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
Aaah, naendelea, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. Naona jamaa wanasema umemaliza. Ahsanteni, nimemaliza.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii kubwa, kunipa zawadi ya uhai ili nami nisimame leo kuchangia katika Bajeti ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamekupongeza kwa umahiri wako wa ufanyaji kazi, lakini nataka nifafanue kidogo. Kuna kipindi watu wanachanganya sana hizi mada. Wapinzani walipotaka kuelezea kutoridhishwa kwao na Naibu Spika, kwanza walianza kuzungumzia habari ya uteuzi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo Mbunge wa kwanza kuteuliwa na Rais wa nchi yetu. Katika Bunge lililopita Mheshimiwa James Mbatia alikuwa Mbunge wa kuteuliwa na Rais na hapo ndipo alipopatia na mtaji wa kugombea Ubunge; lakini siku zote tulikuwa tunamwita Mheshimiwa Mbunge na Wapinzani walikuwa wanamwita Mheshimiwa Mbunge Mbatia. Hakuna mtu aliyemwita ndugu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo wamekuja na hoja nyingine tena; imekuwaje umetoka kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ghafla, umeingia na kuchaguliwa kuwa Naibu Spika? Nikawaambia tu, ndugu zangu, mbona Mheshimiwa Tulia alishaoneshwa njia na Mzee Lowassa? Mheshimiwa Lowassa Jumatano katoka CCM, kahama; Alhamisi ni Mgombea Urais CHADEMA. Mheshimiwa Tulia naye alitumia ile ile! Amechomoka kwenye Unaibu Mwanasheria Mkuu, amezama Bungeni – Naibu Spika wa Bunge.
Tena kwa kupigiwa kura, wala siyo kwa kuteuliwa. Wewe tumekuchagua sisi. Mheshimiwa Rais alikuteua kuwa Mbunge, lakini nafasi hiyo tumekupa sisi Wabunge. Siyo kwamba Rais amesema Mheshimiwa Dkt. Tulia awe Naibu Spika, aah, tumesema sisi kwa kukuamini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme jambo lingine ambalo watu wengi wamelisahau. Tanzania imezalisha viongozi wanawake wengi mahiri. Akina mama Mongella tunakumbuka, walikuwepo akina Bibi Titi Mohamed, wapo sasa hivi akina Samia Suluhu Hassan, akina mama Magreth Sitta; wamefanya kazi kubwa kwenye nchi hii. Leo nataka niwaambie msifikiri Wapinzani wanakimbia tu, kushindana na kiongozi shupavu mwanamke siyo kazi rahisi. Ni kazi ngumu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliwaambia wakajifanya mahiri wa kujenga hoja za kisheria, sijui wana uwezo mkubwa; huyu ni Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, yaani amebobea kwenye nafasi hiyo. Kwa hiyo, walipoona yameshindikana, ndiyo unaona wanachomoka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, duniani wanaume ndio tumeshika nafasi kubwa ya kuwa viongozi mahali pengi, lakini ikitokea mwanamke akapata nafasi, ogopa! Angalia akina Magraret Thatcher, amekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza pale. Mwangalie Indira Gandhi, amekuwa Waziri Mkuu wa India pale; mwangalie Golda Meir, amekuwa Waziri Mkuu wa Israel. Hawa ni akinamama wachache waliofanya mambo makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka nikuhakikishie kwamba unakoelekea ni kuzuri. Komaa, endelea kufanya kazi nasi tunakuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie Bajeti ya Serikali. Waheshimiwa Wabunge wamesema kwa uchungu sana, tunakuomba Mheshimiwa Waziri; tumefikia kipindi ambacho makusanyo sasa ni makubwa. Impact ya makusanyo yenu yatakuwa na maana sana kama yatashuka kwa wananchi wa chini maskini. Vinginevyo, hata mkijisifu kukusanya itakuwa haina maana. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais anabana matumizi, Serikali nzima inabana matumizi, lakini mategemeo yetu ni kuona bajeti hiyo ni kwa namna gani itashuka kumaliza matatizo ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wamesema habari ya kujichanganya kwenu hapa. Amesimama Mheshimiwa Waziri hapa anasema amefuta ushuru. Hao vijana mnaotaka tuwainue kiuchumi, mwaka huu ndio wamelima ufuta na alizeti. Leo bado kuna mageti ya vijana kuchangishwa kutoka kwenye kilimo chao duni walicholima, siyo sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ufuta umeshuka bei, alizeti haina bei, halafu mageti ya kuwachangisha ushuru mkubwa. Hili mlitazame, linatupaka madoa Waheshimiwa Wabunge tuliotoka kwenye Majimbo ya vijana wakulima. Watu wanataka kuinuka kiuchumi. Kwa hiyo, naomba Serikali wakati wa kutoa majibu ilisemee hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumezungumzia habari za Zahanati hasa za Vijijini, zinahitaji pesa. Akinamama wengi wanaojifungua wanapoteza maisha yao kwa kukosa vyumba vya kufanyia upasuaji kwenye hospitali zetu za Kata. Tumesema tuwe na Vituo vya Afya kwenye kila Kata. Vituo vile havina theatre maalum ya kuwafanyia upasuaji akinamama wajawazito.
Mheshimiwa Naibu Soika, kwa hiyo, inatupa shida na Kata nyingine zina kilometa ndefu sana kutoka Kata moja kwenda Kata nyingine. Kwa hiyo, tunamwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, asukume fedha kwenye Wizara muhimu; Wizara ya Afya na Wizara ya Maji ili kuweza kuwapunguzia usumbufu wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mchezo wa kuigiza unaofanyika kwenye nchi yetu ni wa ajabu sana. Mwaka 2015 tulikuwa na mashindano ya kisiasa ya nchi nzima. Kila mwanasiasa maneno aliyokuwa nayo aliyasema. Wananchi wamepiga kura, siasa zimehamia Bungeni. Haiwezekani tena ukakimbia Bungeni ukaenda kuwaambia wananchi yanayoendelea Bungeni, wamekutuma kazi hiyo? Hili lazima niweke sawa! Serikali haiwezi kuleta maendeleo kama nchi haina utulivu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nchi lazima iwe na utulivu, iwe na amani yake ili hayo makusanyo ya Serikali yanayotafutwa yaweze kuwafikia wananchi. Kwa hiyo, hiki kiini macho kinachotumiwa na Wapinzani kwamba tunaenda kuwaambia wananchi yanayotokea Bungeni, tuko Wabunge wa Majimbo, hiyo tutaenda kuwaambia wananchi wetu waliotutuma! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka kila Mbunge akafanye kazi kwenye Jimbo lake. Hivi, Mbowe anavyosema anaenda Kahama, Kahama kuna Mbunge wa CHADEMA? Kwa nini asiende kuwaambia wananchi wa Hai? Aende akawaambie wananchi wa Jimbo lake; lakini kwenda Kahama ambako hakuna Mbunge wa CHADEMA, ni uchokozi na ni kuwapotezea muda wananchi wa Kahama wasifanye kazi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme kuhusu udikteta. Hili sitaki kuficha, moja ya viongozi madikteta kwenye nchi hii ni pamoja na Mheshimiwa Mbowe. Anawatoa Wabunge kwa nguvu. Waheshimiwa Wabunge wako hapo kwenye chai, wamenituma nije niwasemee humu ndani. Wameniomba, wamesema, Lusinde, kuna mambo sisi hatuwezi kumwambia Mbowe, nenda kamwambie.
Mheshimiwa Naibu Spika, natumia fursa hii kumwambia Mheshimiwa Mbowe warudishe Wabunge ndani ya Bunge! Usiwanyanyase! Anawapigia simu wakae kwenye chai badala ya kuingia Bungeni. Tabia gani hiyo? Hiyo ni kutumia Uenyekiti vibaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya siyo maamuzi ya Chama ndugu zangu, tusiwalaumu. Hawa wamepigiwa simu, wamekatazwa; atakayeingia atapewa adhabu. Kwa hiyo, wako kwenye chai, wameniomba; nenda katusemee Bungeni, sisi hatuwezi kusema. Najua huko waliko wananipigia makofi kwa sababu natekeleza agizo walilonituma. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiendeleza siasa uchwara za kufanya fujo wakati Serikali imeshapatikana, tutamnyima fursa Mheshimiwa Dkt. Magufuli ya kuwahudumia Watanzania. Tumpe nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu, wengi hapa mnajua mpira; mpira una sheria zake. Hivi mchezaji wa Simba au wa Yanga anapewa kadi nyekundu kwenye mchezo wa mpira, Wanayanga wanaweza kuandamana nchi nzima kupinga? Haiwezekani! Mbunge akipewa kadi nyekundu ndani ya Bunge, ni kwa kufuata kanuni za ndani ya Bunge, siyo nje ya Bunge. Haiwahusu wananchi hiyo. Hiyo inatuhusu wenyewe; tumewekeana sheria, tumewekeana kanuni; Mbunge akifanya kosa hili, red card, anatoka nje. Hiyo huwezi ukaandamana nchi nzima kwenda kuwaambia ooh, demokrasia inaminywa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna demokrasia isiyo na mipaka. Demokrasia isiyo na mipaka ni fujo. Tunaitaka Serikali isimamie amani, Serikali idumishe utulivu ili pesa zinazokusanywa ziende ziwahudumie wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia habari ya usambazaji wa umeme. Mkisambaza umeme kwenye vijiji, mnainua uchumi na mnapunguza msongamano mijini. Leo kama kila kijiji kitakuwa na umeme; kila kijiji wananchi watakuwa wamejiwekea pale miundombinu ya kujiletea maendeleo, wana sababu gani ya kwenda Dar es Salaam? Hawana sababu. Kwa hiyo, hata ile foleni ya Dar es Salaam itapungua na hayo yote yatafanyika kama nchi ina utulivu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni mjumbe wa Kamati ya PAC, hapa nataka ku-declare interest. Naiomba Serikali badala ya kupeleka bajeti ya shilingi bilioni 72 kwa TAKUKURU, waitazame Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali. Leo unawapa shilingi bilioni 34 na point ngapi sijui, siyo sawa. Huyu ndio Mkaguzi. Huyu ndiye anayekwenda kuwaonesha TAKUKURU hapa kuna wezi. Huyu ndiye anayekwenda kuonesha ubadhirifu, ndio jicho la Bunge. Kwa hiyo, naomba, sisi Wabunge kwa kulithamini jicho letu, tunaomba jicho lisafishwe, liwekewe dawa, liwekewe miwani ili likawaone wabadhirifu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Serikali iwe makini kwenye ushauri wa Waheshimiwa Wabunge. Waheshimiwa Wabunge tunapoomba, Serikali itusikilize; Ofisi ya CAG ni Ofisi kubwa. Ndiyo Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali; akikosa pesa hawezi kufanya kazi hiyo.
Kwa hiyo, tunawaomba waongezewe pesa ili wakafanye ukaguzi ili hata hiyo Mahakama ya Mafisadi iende na ushahidi. Hawa wasipofanya kazi yao vizuri, wote mtakaowashtaki watashinda kesi kwa sababu kutakuwa hakuna ushahidi wa kuaminika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme, kwenye Bunge, tunapokutana Waheshimiwa Wabunge, yanakutana Majimbo yote kuzungumzia maendeleo ya nchi nzima. Wabunge wa CCM tunao wajibu; sisi ndio tumepewa dhamana na wananchi wa Tanzania kuongoza nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata Wabunge wao wanapokosa hoja za msingi, tusimame kutetea Majimbo yale kwa sababu yana wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tutakapofika, wananchi watagundua, wananchi sio wajinga, watagundua kwamba amekuja Mheshimiwa Rais, anafanya mabadiliko ya vitendo; Mheshimiwa Rais anapozungumza, unamwona mpaka macho yanalenga lenga machozi kwa uchungu alionao. Watu wanamwona, wamemwamini, leo hawa wamekosa hoja wanapokimbia nje kutekeleza kauli ya Mheshimiwa Mbowe, inawauma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi Waheshimiwa Wabunge wa CCM tuzibe lile pengo kuhakikisha kwamba tunayasemea Majimbo yao, wananchi watusikilize kwamba Iringa ipelekewe maji, kwamba Kigoma ipelekewe maji na miundombinu ijengwe na Moshi Mjini pale patekelezewe miradi yao. Hiyo ndiyo kazi tuliyonyo Wabunge wa CCM maana sisi ndio mama, sisi ndio baba, sisi ndiyo tumeaminiwa na wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kweye miradi ya maendeleo. Kwa mara ya kwanza, Serikali imetenga asilimia 40 kwenye bajeti ya maendeleo. Miaka yote Wapinzani wamekuwa wakilalamika, bajeti ya maendeleo ndogo, hakuna pesa zilizotengwa; lakini mwaka huu Mheshimiwa Dkt. Magufuli na Serikali yake amekuja na asilimia 40 ya maendeleo…
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na namshukuru sana Mheshimiwa Kanyasu kwa kuniongezea dakika zake tano kwa niaba ya nchi hii, nami naendelea sasa kupiga dawa taratibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tujifunze. Kama nchi inataka kufanya siasa za ustaarabu, tufanye siasa za ustaarabu. Tusiige kila kinachofanywa na watu wengine na sisi tukakileta hapa Tanzania, haiwezekani. Hata mashindano ya ma-miss tu, yakiisha, hakuna ugomvi tena. Hakuna mtu anapita kujitangaza kwamba yeye mzuri kuliko aliyechaguliwa, hakuna! Wanakuwa wamemaliza. Siasa za Tanzania ni siasa gani ambazo hazina muda? Lazima tuwe na muda wa kampeni, ukiisha tumwachie Rais atekeleze kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nalisema hili kwa sababu tukiendeleza tabia hii, nataka niwaambie, itakuwa ndiyo Taifa peke yake ambalo watu hawafanyi kazi, wanafanya siasa muda wote. Haiwezekani! Lazima tuwe tunajitenga. Tukimaliza kampeni, viongozi wamechaguliwa, tunawapa fursa ya kutekeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais aliyeko wa Awamu ya Tano, slogan yake na msimamo wake ni Hapa Kazi Tu! Anachotaka ni watu wafanye kazi. Watu tufanye kazi, siyo turudi kwenye majukwaa tena sijui ooh, Dkt. Tulia kafanyaje! Haiwezekani. Mheshimiwa Dkt. Tulia hawezi kuwa msingi wa Wapinzani kutoka; wamekimbia kwa sababu hoja haipo. Mheshimiwa Mbowe ametumia nafasi hiyo vibaya kuwaambia sasa tokeni, kaeni kwenye chai mpaka mtakaponisikiliza. Huo ndiyo uongozi bora? Siyo uongozi bora! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia uongozi bora, tunazungumza kwa wote sisi, ndiyo kodi yetu inatumika kulipa Upinzani, kulipa Chama kinachotawala na kuleta maendeleo ya nchi. Kwa hiyo, mchango unapokosekana, lazima CCM tuzibe lile pengo, kama ambavyo imetokea Kambi Mbadala. Huo ndiyo wajibu wetu na tuwaambie wananchi kwamba kinachofanywa na Wapinzani siyo kweli, siyo sahihi. Hata viongozi wa dini wanajua, akishachaguliwa Mufti, hakuna uchaguzi mwingine tena. Anaachiwa Mufti aongoze. Akichaguliwa Askofu, hakuna uchaguzi mwingine wa Askofu. Anaachiwa aliyechaguliwa afanye kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kinachotaka kufanyika kupitia upinzani, ile ni fujo; kuiweka nchi katika fujo za maandamano yasiyo na msingi. Haiwezekani! Serikali isimamie amani, isimamie haki, isimamie maendeleo kwa nchi nzima. Mbunge anayejisikia kwenda kuwaambia wananchi wake kaonewa Bungeni, akafanye kwenye Jimbo lake, siyo kwenye Jimbo la Mbunge mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge yeyote akitoka hapa Bungeni naye ataenda kueleza nini tumepata, nini Serikali itafanya katika miaka mitano. Hatuhitaji msaada toka kwa Mheshimiwa Mbowe wala kwa mtu mwingine yeyote. Pale Kahama yuko Kishimba wamemchagua, atakwenda kuwaeleza yanayotokea hapa. Hatuhitaji msaada wa mtu mwingine. Hatuwezi kufanya siasa muda wote, haiwezekani. Tunafanya siasa, tukishamaliza, siasa zinahamia Bungeni, wananchi wanachapa kazi kuleta maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumza kidogo kuhusu kiinua mgongo. Waheshimiwa Wabunge, naomba mnisikilize. Naamua nijitoe muhanga kwenye jambo hili. Kujitoa kwangu muhanga ni hivi, hili jambo Serikali imesema kama yatakuwepo hayo makato, yatakatwa 2020. Sisi tunahoji kwamba kwa nini hoja hiyo muilete saa hizi? Sisi hatuitaki saa hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka niwaambie Waheshimiwa Wabunge, jambo hili tukae wote. Serikali hii ni ya kwetu na sisi ni Wabunge tunaoongoza nchi hii. Wananchi wasije wakatuelewa vibaya wakafikiri sisi hatutaki kuchangia maendeleo, hapana. Moyo wa kuchangia maendeleo na sisi tunao. Tunachosema, jambo hili linahitaji mazungumzo, twende tukae, tukubaliane, utaratibu gani utumike ili kuweza kusonga mbele, wala siyo la kubishania hapa. Wala hatuwezi kusema hatutaki, haiwezekani. Huu ni ushauri wa Serikali na sisi hatuwezi tukailazaimisha Serikali kwa nguvu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunawashaurini kwamba jambo hili linahitaji mjadala wa pande zote mbili. Waheshimiwa Wabunge, tunalipa kodi, tunakatwa kwenye mishahara yetu. Kama mnataka kuendelea mbele kukata tena gratuity, tuzungumze, tuone impact yake, maendeleo yatakavyosukumwa, wala siyo jambo la kubishania hapa. Jambo hili ni zuri. Isije ikachukuliwa kwamba Waheshimiwa Wabunge wote wanapinga kukatwa hela zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaambie, kuna waandishi wanasema, Waheshimiwa Wabunge wa CCM, imewauma kusikia wanakatwa hela. Mimi haijaniuma, niko tayari hela yangu ikatwe, lakini kwa mazungumzo. Tuone hiyo hela inakatwa kuelekea wapi na utaratibu gani utatumika ku-balance jambo hili ili liweze kuleta afya badala ya malumbano hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii ni yetu wote. Siyo kazi yetu kuwashtaki wengine kwamba viongozi wote wa kisiasa lazima wakatwe. Hiyo siyo kazi yetu. Kazi yetu sisi ni kuangalia kitakachopatikana. Kama hakitoshi, ndiyo tutashauri Serikali sasa iangalie na viongozi wengine ili kuongeza mfuko, maendeleo yaweze kupatikana. Tusikae tunabishania hapa, tunabishania kitu gani? Kwa sababu juzi hapa tumeondoa matangazo live ili pesa itakayopatikana iende kuwahudumia wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na hoja za msingi hapa, tukasema anayetaka kurusha live, hata harusi siku hizi watu wanarusha live; kalipie mwenyewe. Nenda lipia pale TBC, mtakapopewa dakika 15, rusheni live wananchi wako wakuone. Mbona tulipitisha na tukakubaliana? Hili lisilete ugomvi. Hili ni jambo dogo sana. Tunahitaji muda wa kuzungumza na Serikali kukubaliana juu ya jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna Mbunge anayepinga Bungeni, sijui kumekucha, sijui Waheshimiwa Wabunge wameamua kumkatalia Mheshimiwa Dkt. Magufuli. Mheshimiwa Dkt. Magufuli tumemchagua sisi, ni Rais wetu, tutamuunga mkono kwa hoja yoyote atakayoileta humu ndani, tukiwa na imani kwamba Rais hakosei. Rais hawezi kukosea. Nia yake ni njema katika kuitumikia nchi hii. Anataka Waheshimiwa Wabunge pamoja na wananchi wote turudi katika mstari sawa. Kama Mheshimiwa Mbunge ulikuwa unakunywa bia kumi, kunywa moja ili tuweze kusonga mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kuna mwezi Mtukufu huu, Waislamu wamefunga, wanaweza kuombea nchi hii watu wakaachana kabisa na ulevi. Nawahakikishieni kabisa, tutapata maendeleo makubwa ya kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka kuwatia moyo sana Waheshimiwa Mawaziri, Dkt. Mpango na dada yangu pale, fanyeni kazi. Tuna imani na nyie. Mheshimiwa Rais anawaamini na sisi Waheshimiwa Wabunge tunawaamini. Tutafanya kazi kwa mshikamano kuhakikisha nchi hii inasonga mbele bila mikwaruzano, bila nini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza kabisa nimshukuru Mungu kwa kunipa nafasi na kunijalia zawadi ya uhai ili niweze kusimama kwenye Bunge lako Tukufu niweze kutoa mchango wangu kwa Wizara hii ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kikanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza hii ni kwa ajili kuweka rekodi vizuri tu, nataka nichukue nafasi hii kuwapongeza sana wananchi wa Iringa na hasa makanda wa Chama cha Mapinduzi wa pale Iringa Mjini. Kumbe walifanya kazi nzuri sana ya kumkaba mpinzani wao mpaka leo anaonesha kwenye Bunge hili kwamba ushindi wake ni ajabu sana hakuutegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma taarifa hii ya Kambi Rasmi ya Upindani, unaona kuna vitu vimeandikwa kijinga kabisa. Moja ya kitu kulichoandikwa kijinga neno Mungu anaandikwa kwa herufi ndogo mimi sijawahi kuona mahali popote pale, ukitaka kutaja Mungu lazima uandike kwa herufi kubwa. Kwa hiyo, uchungaji wa Msigwa unanitia mashaka makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuzungumzia Chuo cha Diplomasia. Chuo cha Diplomasia ni chuo kinachofanya kazi kubwa sana ya kuwaelimisha, kuwafundisha, watu, wananchi wanaoteuliwa kuwa mabalozi, wake wa viongozi, Wakuu wa Nchi, ili kuweza kujua diplomasia inafanyaje kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali itenge fedha ya kutosha kwa chuo hiki ili kiweze kufanyakazi yake kwa ufanisi na nimuombe Waziri atakaposimama hapa kutoa majibu atueleze ni fedha kiasi gani zimetengwa kwa ajili ya chuo hiki ili kiweze kufanya kazi yake kwa ufanisi.
Tunasemwa maneno mabaya lakini tunavumilia mpaka wasemaji wamalize, lakini sisi tukitaka kujibu kidogo unasikia kelele za kuwashwa washwa upande wa pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme moja ya diplomasia kubwa iliyojengwa katika nchi yetu ni kuwa na upinzani japo kwamba upinzani wenyewe ni dhaifu. Tunao upinzani lakini ni dhaifu hata kwenye kujenga hoja. Mtu anasimama hapa kuzungumzia habari ya Mabalozi hawafanyi kazi, anasimama hapa kuzungumzia habari ya Rais haendi nje. Tulikuwa na Rais Kikwete, anasafiri kila siku. Hawa walisimama Bungeni hapa kusema kwamba Rais anasafiri sana, Rais anatumia fedha nyingi, leo tumempata Dkt. Magufuli, Rais anabana matumizi, fedha zinaelekezwa kwenye maendeleo, hawa wanasimama kupinga, watu gani hawa. (Makofi/Vigelele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanataka tufanye nini, leo nataka niwaambie ndugu zangu kweli kazi kubwa ya upinzani ni kupinga lakini sio huu, huu ni upinzani hewa kwa sababu hakuna wanachopinga, wao wenyewe wanaingia wanasaini wanaondoka bila kufanya kazi, leo hii wanataka kusema kwamba nchi hii haina demokrasia wangekuwepo hawa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo upinzani wa Tanzania naufananisha kama mtoto mchanga tumboni. Mtoto mchanga tumboni haelewi ukubwa wa dunia. Kwa hiyo, anafikiria eneo la tumbo la mama yake ni eneo kubwa linalostahili hata kucheza. Hajui kwamba akitoka duniani kuna eneo kubwa mno, kuna eneo la kukimbia atachoka, kuna eneo la kucheza atachoka, kuna eneo la kulima atachoka, kuna eneo la kutembea atachoka. Hawa wanafikiria kama mtoto mchanga tumboni anayefikiria eneo la tumbo ni eneo kubwa sana. Leo unamkosoa Balozi eti kwamba tunao Mabalozi wenye hadhi ya nyumba kumi, haya ni matusi wa Mabalozi wetu. Mabalozi wetu ni Mabalozi waliochunjwa, wameiva, ukiwepo Balozi Mahiga, nani asiyejua kwamba Mahiga ni moja ya watu waliobobea katika masuala ya kidiplomasia ya kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii wanasimama hapa kutuambia as if kwamba sisi ni watoto wadogo. Hivi ingekuwa Watanzania wote au viongozi wote wa nchi hii wanatakiwa kusafiri nje ya nchi kwenda kuwasilisha masuala ya nchi hii wao wangekuwa Wabunge hapa. Si kila mwananchi wa Jimbo lao angekuja hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani wananchi wote kuja kwenye jengo hili ndio maana tumekuchagua Msigwa, ndio maana tumekuchagua Januari, ndio maana umechaguliwa Lusinde, kwa sababu wana nchi wa Jimbo zima hawawezi kuhudhuria katika kikao hiki. Sasa leo wanataka nchi nzima kila mtu akajiwakilishe kule, katika kimataifa aende akazungumzie matatizo ya nchi, haiwezekani ndio maana kuna Mabalozi wameteuliwa. Jifunzeni ninyi! Kwa hiyo, nataka niwaambie, anazungumza pale mwisho, anasema nchi ya kifisadi kama hii wakati fisadi mkuu mnaye nyie. (Makofi/Vigelele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao upinzani ambao unachosema haukielewi, wanachopinga hawakielewi, walichosema mwaka jana mwaka huu wanakuja wanajijibu. Walichokataa mwaka juzi, mwaka huu wanakuja wanakikubali. Nataka nimpongeze Rais Magufuli, amewafanya wapinzani wa nchi hii hawana hoja, ndio maana mnawaona wakisimama humu hakuna lolote la msingi wanalolisema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Magufuli, amewafanya wapinzani wa nchi hii hawana hoja ya msingi, sasa imekuwa moto ukiwaka wanatoka nje ya Bunge, daladala ikiungua wanatoka nje ya Bunge kwa sababu hoja ya msingi hawana maana Rais anafanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuhakikishe Rais akienda kwa speed hii kufika mwaka 2020 hawa watakuwa hawapo ndani ya Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaitumia diplomasia ya nje kuhakikisha kwamba nchi hiii inapata uchumi mkubwa utakaowafanya wananchi wanufaike, na utakaowafanya wapinzani wa nchi hii waondolewe na wananchi kwenye Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuhakikishie, nina uzoefu wa kuongeza na hawa, nina uzoefu nao, unapowaona wanapiga kelele jua sindano zinaingia ndio maana unaona wanapiga kelele. Huwezi ukasimama kwenye Bunge hili ukiita Tanzania ni nchi ya kifisadi wakati fisadi mkuu mmemchukua, na itafika mahali nataka nikuambie, hata Mheshimiwa Mahiga hawa wakubeze vipi, siku ukijiunga kwao utakuwa mgombea Urais wa chama hicho, za kwao hawa ni kuokoteza tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namtia moyo Mheshimiwa Waziri na Naibu wako, Katibu Mkuu na Mabalozi wote wakilisheni nchi kama Rais alivyowaamini, watanzania tunawaamini, na ndio maana tuko nyuma yenu tunawaunga mkono.Chapeni kazi na hiyo kazi italeta manufaa hata kwenye Majimbo ya hawa wanaopiga kelele leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuhakikishie, nina uzoefu wa kuongeza na hawa, nina uzoefu nao, unapowaona wanapiga kelele jua sindano zinaingia ndio maana unaona wanapiga kelele. Huwezi ukasimama kwenye Bunge hili ukiita Tanzania ni nchi ya kifisadi wakati fisadi mkuu mmemchukua, na itafika mahali nataka nikuambie, hata Mheshimiwa Mahiga hawa wakubeze vipi, siku ukijiunga kwao utakuwa mgombea Urais wa chama hicho, za kwao hawa ni kuokoteza tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namtia moyo Mheshimiwa Waziri na Naibu wako, Katibu Mkuu na Mabalozi wote wakilisheni nchi kama Rais alivyowaamini, watanzania tunawaamini, na ndio maana tuko nyuma yenu tunawaunga mkono.Chapeni kazi na hiyo kazi italeta manufaa hata kwenye Majimbo ya hawa wanaopiga kelele leo.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kutuzawadia uhai na kwa huruma yake tuko salama na tuko ndani ya Bunge hili kwa sababu ya kujadili Mpango wa Maendeleo wa Serikali 2016/2017 na 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, nataka nichukue fursa hii ndugu zangu kwa unyenyekevu mkubwa sana kutoa pole kwa wananchi wenzangu watatu watafiti kutoka Chuo cha Seliani waliouawa katika Kijiji cha Iringa-Mvumi, katika Wilaya ya Chamwino, nawapa pole sana familia. Vilevile nitoe pole sana kwa wananchi kadhaa wa Kijiji cha Mvumi Mission pamoja na Kata ya Manda na Kijiji chenyewe cha Iringa-Mvumi kwa familia ya Tatu ambaye naye pia aliuawa wiki moja kabla ya wale watafiti kukumbwa na kadhia hiyo. Naomba Mungu azipumzishe roho za marehemu wote mahali pema peponi, lakini niitake Serikali kuchukua hatua madhubuti kuwatafuta watu waliokimbia ambao kwa kweli kwa kiasi kikubwa wanatajwa kuhusika na mambo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, nina mambo machache ya kuzungumza. Jambo la kwanza, naomba niipongeze sana Serikali kwa kazi nzuri. Ndugu zangu nataka nirudie tena maneno ambayo nimekuwa nikiyasema mara nyingi kwamba katika kazi rahisi duniani, hakuna kazi rahisi kuliko kupinga, kupinga jambo lolote ni kufanya kazi rahisi sana. Maana mtu anajenga nyumba kwa gharama kubwa wewe unatumia dakika mbili tu kumwambia nyumba yako mbovu. Kwa hiyo, unaweza kuona namna ambavyo kupinga ni kazi rahisi sana na inayoweza kufanywa na mtu yeyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango, maneno mengi mazuri ameyaandika katika kitabu chake, mojawapo ni kukua kwa uchumi ambapo sasa hivi umekua kwa 5.7% na unategemewa kukua kwa 5.9%. Tatizo tulilo nalo Dkt. Mpango ni namna gani tunahusianisha kati ya ukuaji wa uchumi kwenye vitabu na hali halisi kwa wananchi wenyewe. Hapa ndiyo inatakiwa sasa mtusaidie ku-link kwa sababu tunavyoelewa ni kwamba uchumi unapokua ni lazima uguse baadhi ya wananchi au pengine wananchi wengi zaidi hasa wanaoishi maeneo ya vijijini. Huko bado tuna matatizo makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia viwanda vidogo vidogo, nashauri Serikali tujikite zaidi kwenye viwanda ambavyo vitainua kilimo. Tujikite kwenye viwanda vya mazao yanayolimwa na wananchi. Kwa mfano, kwa Mkoa wa Dodoma ukianzisha kiwanda kwa ajili ya kuinua zao la zabibu utakuwa umetusaidia zaidi kuliko tukiwa tunazungumza ukuaji wa uchumi wa point za kwenye karatasi ambao hauakisi wananchi wenyewe wanainukaje kimaendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niyaseme haya maana imeonekana kwamba Wabunge wa CCM tuna uoga wa kumshauri Rais, lakini leo nataka nitamke kwenye Bunge hili, Rais anafanya kazi nzuri sana na aendelee kuifanya. Bahati nzuri tumekuwa na Rais kama Mbunge mwenzetu kwa miaka 20, anatujua Wabunge, anaijua nchi, anajua namna ambavyo tuna tabia za kuzusha, hawezi kubabaishwa na maneno yanayotoka humu. Katika nchi yetu kwa miaka mingi sana tumekuwa na malalamiko kwamba Serikali yetu inalindana, mtu anaharibu hapa anahamishiwa hapa, mtu anaharibu hapa anapelekwa hapa, tunataka mabadiliko, amekuja Rais wa mabadiliko, ukiharibu unakwenda kupumzika nyumbani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndugu zangu nataka niwaambie wala hakuna mtu anayetisha wala hakuna mtu anayeshindwa kumshauri. Ila nataka niwapongeze sana, mimi mara chache sana huwa nawapongeza Wabunge wa Upinzani lakini safari hii nataka niwapongeze, nawapongeza kwa sababu wamejitoa mhanga. Wanaposimama kusema Serikali imefilisika msifikiri wanaisema Serikali, hapana, wana sehemu wanayolenga kwa sababu ili ujue kwamba huyu mtu amefilisika kuna vielelezo. Cha kwanza, lazima ashindwe kulipa madeni, mtu akishindwa kulipa madeni ujue amefilisika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Wabunge wa Upinzani acheni uoga, badala ya kusema Serikali imefilisika, Serikali inayolipa mishahara, Serikali inayowalipa nyie, Serikali inayosomesha watoto bure, tamkeni wazi kwamba Mbowe umefilisika maana umeshindwa kulipa madeni. Tamkeni wazi, hakuna sababu ya kuzungukazunguka unapiga kona ooh mimi nitakamatwa, sasa unatuambia sisi tuje tukuwekee dhamana, ukikamatwa ni kwa makosa yako. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais ameteua Wakuu wa Mikoa wengi wazuri, lakini wachache nitawataja hapa, wa kwanza Mrisho Gambo, nampongeza sana. Wa pili Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rugimbana Jordan nampongeza sana. Wa tatu, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, nampongeza sana Mongella anafanya kazi nzuri. Rais anawajua watu wake, anapowapanga anajua kabisa nani anaweza kufanya kazi wapi. Big up sana Dkt. Magufuli, endelea kufanya kazi ukiamini kwamba nyuma yako wako watu wanaokuombea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie msamiati mgumu sana. Ni bora mtu ufe mawazo yako yabaki hai kuliko mtu uwe hai halafu mawazo yako yawe yamekufa, ujue wewe umepotea kabisa. Hatuwezi kuogopa kuchukua hatua. Leo hii tunasimama ndani ya Bunge hili tunasema utumishi ni uti wa mgongo, kwenye utumishi haitakiwi kuingiza siasa inakuwaje mtu aliyefikia level ya kuwa mtu mkubwa mpaka Katibu Mkuu leo Mbunge wa CHADEMA, alianza lini? Lazima alianza akiwa huko huko katika Utumishi, ndiyo maana lazima tufukue kila sehemu kuangalia tunao watumishi au tunao watu wanaopiga porojo za siasa badala ya kufanya kazi, lazima tusimamie nidhamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna mtu anafikiria kwamba eti tutakuwa na Taifa ambalo halina mabadiliko, haiwezekani! Tumeyaomba sana mabadiliko, tumelala tunasisitiza kwamba tunataka mtu atakayekuja kubadilisha. Kama kuna mfanyakazi anaenda kazini akiwa hana hakika kwamba ajira yake ipo, sawasawa, yeye akachape kazi. Kazi peke yake ndiyo itasababisha ajira yako iendelee kuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tusidanganyane hapa. Tunasimama hapa na kuanza kusema ooh kwenye kikao cha chama cha Wabunge wa CCM wamepewa hela, aaah, wamepewa hela na nani? Mbona ninyi mnachangishwa kila siku hapa? Wabunge wanachangishwa kila siku milioni moja moja, wengine wanakuja wanalia wanasema Lusinde angalia meseji hii tunatakiwa tutoe milioni moja moja kwa ajili ya kesi, mbona sisi hatuyasemi yenu? Sisi tupewe pesa na nani? Wabunge wote tulipewa fursa ya kwenda kukopa, kila Mbunge kakopa, wengine wamekopa 200, wengine 300, leo hii uje upewe milioni 10 ili iweje, ni kutudhalilisha tu.
Msichukue fursa hiyo kutudhalilisha, Wabunge wa nchi hii wote wa Upinzani, wa CCM tulipewa fursa, tumekopa hela nyingi, hakuna Mbunge wa kuhongwa milioni 10 wala wa kupewa milioni moja. Ndiyo maana nyie mnachukua hela zenu kukichangia chama chenu, hakuna mtu anayewazungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri sana wakati huu ambapo tunazungumzia mpango, baada ya kuwa nimeshawapa dawa kidogo, ni vyema tukajikita kwenye sekta binafsi. Serikali imeambiwa uti wa mgongo ni sekta binafsi. Rais amekwenda kufungua kiwanda kuna watu wanapiga kelele tena, mnaenda kwa Bakhresa, katika sekta binafsi kuna mtu mjasiriamali jamani katika nchi hii anayemfikia Bakhresa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bakhresa akimuita au akimuomba Rais kwenda kufungua kiwanda chake, uharamu wake uko wapi? Au Bakhresa kuacha kuwachangia wapinzani ndiyo imekuwa nongwa? Maana nashangaa unaanza kumlaumu eti kwa nini Rais kaenda kufungua kiwanda cha Bakhresa kampa na ardhi, kuna vivutio vya kuwafanya wawekezaji wa ndani nao waweze kuwekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri Mpango kelele anazozisikia uchumi wa ndani una booster yake. Booster yake ni kuwalipa wadeni wa ndani, ukiweza kuwalipa wadeni wa ndani hela itaonekana mtaani na hizo kelele zitapungua. Mnapokumbuka madeni ya nje ni sawa, lakini kumbukeni na madeni ya ndani. Kuna wazabuni mbalimbali waliofanya kazi kwenye Serikali, hawa wakipata pesa mzunguko wa pesa ndani ya nchi nao utaonekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunawashauri Serikali muangalie pande zote. Mnaposomesha bure tunaona, mnaponunua ndege tunaona, tunajua yatasemwa mengi lakini endeleeni kufanya kazi kwa sababu hata Mungu angeleta majadiliano na wananchi hicho kikao kisingekwisha. Ndiyo maana ukaona akakaa mbali akaamrisha kama ni mvua, mvua, kama jua, jua. Mwambie Rais tunamuunga mkono, kazi anayofanya ni njema, tumepata Rais wa kunyooka, akinyooka na jambo linaenda kama alivyopanga na ndicho tunachokitaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanalalamika hapa ooh Rais anafanya kazi yeye mwenyewe. Halafu mimi nashangaa hawa jamaa wanasema halafu wanajijibu wenyewe. Wananikumbusha Sauli kwenye Biblia alipokutana na kibano cha Mungu Sauli alisema, ni nani wewe Bwana? Yaani aliuliza swali halafu akajibu kwamba huyu ni Bwana, ndiyo hawa! Huku unasema Rais anafanya kazi zote, huku tena unabadilika unasema Rais anawatisha watumishi. Mtu anayewafanyia kazi zote atawatishaje sasa wakati kazi zote anafanya yeye mwenyewe. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka Rais ananyooshe hii nchi na tuna uhakika Magufuli nchi hii atainyoosha kutoka pale ilipokuwa imeishia kwenda mbele zaidi. Nawaambia moja ya vitu ambavyo nataka Watanzania watusaidie 2020 nchi zetu za ulimwengu wa tatu hizi kuwahi kila kitu nalo ni tatizo, hata kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi tuliwahi ndiyo maana mnaona hoja zenyewe…..
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Nimalize? Sasa unaingiaje Bungeni kujadili kaptura ya Mfalme wa Morocco hiyo ina uhusiano gani na matatizo ya wananchi? (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru sana Mungu kwa kutupa nafasi nzuri kabisa ya kujadili juu ya huu Mkataba wa EPA. Vilevile sina budi nichukue fursa hii katika Bunge hili kumpongeza sana Profesa Kabudi kwa namna alivyotufumbua macho. Profesa Kabudi ni moja ya Watanzania wenye uwezo wa walichonacho kuwasaidia na wengine waweze kuelewa. Hilo ni jambo zuri sana na kwa kweli tunajivunia sana kwamba elimu yako inawafaa wengi na inaifaa nchi. Hongera sana Profesa Kabudi.
Mheshimiwa Spika, ni ngumu sana kusimama hapa kuutetea huu mkataba na ndiyo maana unaweza kuona kuna baadhi wanaojaribu wanapata shida sana. Hauna namna yoyote ya kuuzungumzia uzuri wa Mkataba huu, hata kama umeandaliwa au umejiandaa; ni jambo gumu sana. Ndiyo maana umeona hata waliojaribu kufanya hivyo, wamejikuta wao wenyewe wakipata shida sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, nataka nimpongeze sana Mheshimiwa Khatib, ameonyesha kwamba isiyo kongwe haivushi, kwamba ukongwe wa CCM ni jambo zuri na inaendelea kuvusha nchi hii. Amesema chama hiki ni kikongwe. Ukishasema kikongwe, maana yake hicho ndicho chenye uwezo wa kuvusha baadhi ya mambo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama umewasikiliza wazungumzaji wachache waliotangulia, nataka niungane nao kwamba hata kuchukua muda mwingi kuujadili mkataba huu ni kutumia tu fedha za Watanzania vibaya, huu mkataba haukustahili hata kufika huku. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huu ni moja ya mikataba mibovu kabisa ambao pengine nimsaidie hata mzungumzaji aliyepita, kwa nini Kenya wamesaini? Wamesaini bila kuutafakari kwa makini. Wangetafakari kwa makini; na nikubaliane na Mhesimiwa Zitto kwamba wamesaini kwa ajili ya kufanya biashara ya maua, siyo kwa ajili ya usalama wa mkataba wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kifungu cha 140, hakiruhusu nchi moja kujitoa baada ya kuingia. Mimi nataka niseme, Jumuiya yetu ya East Africa, kama kuna jambo mmetuangusha ni katika jambo hili. Kwa nini msingekaa wenyewe kwanza mkaupitia huu mkataba? Secretariat ya Jumuiya ya East Africa mkakaa mkausoma kwa pamoja kabla ya kuruhusu nchi moja moja kwenda kujisainia yenyewe? Kwa hiyo, hapa tunaanza kona kuna problem kwenye Jumuiya yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lazima Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki iwe inakaa pamoja kwenye mambo ya muhimu na mazito kama haya, leo tusingeona aibu ya Kenya kutangulia kusaini kama mngekaa pamoja mkashauriana, kwamba jamani hivi unaingiaje kwenye mkataba ambao unakuchagulia rafiki? Unaingiaje kwenye mkataba ambao unakulazimisha kushirikiana na adui? Huu mkataba kadri unavyousoma, kuna sehemu unakuchagulia rafiki wa kufanya naye biashara na kuna sehemu unakulazimisha kukaribiana na mtu ambaye wakati huo humhitaji.
Mheshimiwa Spika, ukitazama kwa makini mkataba huu wa EPA, ni sawa sawa na mzee wangu pale kijijini kwenda kupelekewa zawadi ya kuku halafu akachukuliwa ng‟ombe wake kumi; kitu ambacho hakiwezi kukubalika!
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni moja ya mikataba mibovu kabisa. Nasi tunapoukataa mkataba huu na kuitaka Serikali, isiusaini, tunaukataa ili kuwaonesha Jumuiya ya Ulaya kwamba Afrika sasa inao wataalam, wanajitambua na wanaweza kufanya biashara huria na mtu yeyote. Sisi sio watu wa kupangiwa na kuletewa mikataba ya namna hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka niishauri Serikali; kwa mkutadha huu, huu mkataba haufai kusainiwa hata kidogo kwa sababu una vipengele vingi vinavyodhalilisha Afrika.
TAARIFA...
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, namshukuru na namheshimu sana Mheshimiwa Millya, lakini ni mmoja wa watu wachache ambao wamerubuniwa na wazungu. Hawa wazungu waliokuja wamemwona Millya. Maana hapa hatutakiwi kutafuna maneno; kuna baadhi ya Wabunge wamewaona, inawezekana na Mheshimiwa Millya akawa ni mmojawapo kati ya waliowaona. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama hukatazwi, unawezaje kutoa notice halafu mwaka mzima ukaendelea kubaki mle? Unabaki humo kwa sababu zipi? Khah, maana wewe mwenyewe unasoma, halafu unajijibu. Bahati nzuri wewe mwanasheria na pengine unaelewa zaidi, lakini umepata majibu kwamba ukishatoa notice, mwaka mzima unaendelea kubaki mle. Ukifanya nini kama unao uhuru wa kutoka moja kwa moja? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nirudie, hili ni jambo letu wote kama Bunge, tusianze kushindana humu. Tukubaliane kwamba mkataba huu haufai, maana ndani una vi-package vya ushoga, una vitu vya ovyo ovyo vimefichwa humo, Watanzania watatushangaa sana.
Mheshimiwa Spika, sisi hatuwezi kuburuzwa na nchi yoyote, sisi ni Taifa huru! Iwe wamasaini nchi nyingine ambazo pengine wao wanavutiwa na ushoga, sisi hatuvutiwi nao. Kwa hiyo, hatuko tayari kukubaliana na jambo hili.
TAARIFA...
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, hiyo itakuwa imetusaidia wote, lakini zaidi sana, Mheshimiwa Millya ameelewa kwamba ni ile block ndiyo inatakiwa kuomba kutoka lakini siyo nchi moja ambayo imezuiwa na mkataba huu.
Mheshimiwa Spika, tuseme tu kwa kifupi, mkataba huu haufai. East Africa wawe makini na mikataba ya namna hii, waipitie wao wenyewe kama Sekretatieti na wao na uchungu na nchi zao kabla ya kuangalia manufaa watakayopata. Kwa sababu wakati mwingine kuna hadithi moja; watu waliwahi kushangilia kwenda kufanya kazi kwa Mfalme, wakati huo huo kulikuwa kuna agizo kwamba ili ukafanye kazi kwa Mfalme, ni lazima uhasiwe kwanza ndiyo uruhusiwe kufanya kazi kwa Mfalme. Kuna watu wakashangilia, walipofika pale kukuta masharti, yakawa magumu kwao. Kwa hiyo, kila mikataba ya kimataifa inapokuja, tuwe na Sekretarieti zinazotazama kwa makini, siyo kukurupuka! Tutakuja tuingie kwenye matatizo makubwa na tuziingize kwenye shida kubwa. Tutakuja kupata adhabu ambazo hazina msingi. Maana kadri unavyousoma unakutana na sehemu inasema EU inaweza kuchukulia hatua.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, unaweza kuona ambayo tunaweza tukaingia kwenye matatizo makubwa ya kuchukuliwa hatua na uhuru wa nchi zetu ukawa unatekwa bila sisi wenyewe kuelewa.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono mkataba usisainiwe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na kwa namna ya pekee nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge aliyeketi kwa kutoa mchango mzuri ambao hauna unafiki wala ubabaishaji.
Ameeleza vizuri kuhusu utawala bora na Wabunge wa namna hii ndiyo wanaotakiwa ili kuijenga Tanzania kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri iliyofafanua mambo mengi ya msingi kuhusu kilimo, afya, maji na maendeleo mbalimbali ya nchi yetu. Hata hivyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa upande wa afya mmefanya kazi kubwa lakini bado zipo changamoto nyingi sana. Changamoto kwenye majimbo ya vijijini ni kubwa mno. Tukija mijini huku tunawakuta madaktari bingwa wa akinamama na magonjwa mbalimbali lakini vijijini tunakuwa na daktari mmoja halafu huyo ndiyo bingwa wa magonjwa yote. Kwa
hiyo, nataka nichukue fursa hii kuwapongeza sana madaktari wanao-save katika vijiji vyetu, wanafanya kazi kubwa sana kwa sababu magonjwa ya akinamama ni yao, ya watoto ni yao na ya akinababa ni yao. Hawa ndiyo ambao nataka kuwatambua leo kwenye Bunge kwamba ni madaktari bingwa kwelikweli kwa sababu wanashughulika na matatizo makubwa sana ya wananchi vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa uamuzi sahihi wa kuamua kujenga baadhi ya vituo vya afya kwenye maeneo yaliyotengwa sana na maeneo makubwa ya kupata huduma nzuri za afya. Kwa mfano, ukitazama Tarafa yangu ya Mpwayungu, pale usiponipa kituo kikubwa cha afya ni hatari sana kwa akinamama wajawazito, kwa sababu kutoka Mpwayungu mpaka kuja Hospitali Teule ya Wilaya pana kilometa kama 85 niambie barabara ya vumbi, mama mjamzito anafikaje hapo kuja kuwahi operesheni. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa uamuzi wenu sahihi na nina hakika hili mtaliangalia kwa jicho la huruma kwenye majimbo mengi ya vijijini hasa yaliyokosa huduma za msingi za kiwango hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia habari ya Wizara ya ujenzi, itazame vilevile barabara za vijijini.
Tunazungumza sana ujenzi wa barabara za mijini lakini za vijijini tunaacha. Barabara za vijijini zikipitika kwa kiwango kizuri zitarahisisha sana huduma za maendeleo kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumie kwa haraka haraka Wizara ya Maji. Maji ni Wizara mtambuka. Tukipata maji safi na salama tutapunguza kwa kiasi kikubwa sana matumizi kwenye Wizara ya afya kwa sababu magonjwa mbalimbali ambayo yanaweza kutibika kwa
kupata maji safi na salama yatakuwa yameji-solve yenyewe na kuruhusu wananchi wafanye shughuli zingine za maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, pamoja na pongezi zangu kwa Wizara zote ambazo Mheshimiwa Waziri Mkuu ameziwasilisha katika hotuba yake hii, nataka nizungumzie vile vile suala la ulinzi na usalama. Suala la ulinzi na usalama limezungumzwa hapa kwa mapana na marefu lakini nataka nizungumze kwenye kipengele kimoja. Nichukue fursa hii kusema watu wanaotuhumiwa, unajua Wabunge tunachanganya kuna wengine wanasema kuna kikundi kidogo ndani ya Usalama wa Taifa wengine wanasema Usalama wa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwapongeze sana watu wanaofanya kazi kwenye idara hiyo. Idara ya Usalama wa Taifa inafanya kazi kubwa sana, inafanya kazi nyeti sana na kuna baadhi ya watu nitawataja hapa bila kuwepo ulinzi na usalama kwenye maeneo yao wasingekuwepo hapa.
Mnakumbuka wakati wa msiba wa Chacha Zakayo Wangwe, ni watu wa Usalama wa Taifa ndiyo walimuokoa Mbowe pale Tarime nani hajui? Kwa hiyo, wakati mwingine tusiwe tunawalaumu tu pale wanapofanya vizuri tuwasifie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme habari ya kupotea watu mimi mwenyewe ni mhanga, wako ndugu zangu walishapotea siku nyingi wengine walipotea mwaka 1980 na hwakuwa wanasiasa. Tanzania hii hata ukitaka kila Mbunge aorodheshe watu waliowahi kupotea wapo.
Hawapotei kwa sababu kuna kikundi kinapoteza watu, hapana! Kupotea kwa wananchi ni jambo la kawaida ila tunaitaka Serikali
iendelee kutafuta wananchi waliopotea hata wale ambao hawana majina. Kwa sababu nchi hii tusiseme tu akipotea mtu fulani maarufu ndiyo tunaanza kuzungumza. Upotevu wa wananchi ni jambo la siku nyingi. Kwa hiyo, tuitake Serikali, Idara ya Upelelezi ifanyie kazi mambo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnazungumza mnasema eti ooh kuna Mkuu wa Mkoa alisema mtu fulani aliyepotea ataonekana kesho mbona Kubenea alisema kwamba huyu Saanane anafahamika na kila siku anaonekana, mbona hamumhoji Kubenea? Kubenea si huyu hapa mhojini? Mbona alisema kwamba Saanane yupo anatafuta kiki tu? Kwa nini msianze na Kubenea mnaanza kuisakama Serikali? Anzeni na Kubenea atuoneshe Saanane yuko wapi, Kubenea anajua.
Taarifa...
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Wabunge wengi
hawana ofisi. Tunaitaka Ofisi ya Waziri Mkuu kukamilisha ujenzi
wa ofisi za Wabunge ili Wabunge waweze kufanya kazi zao
kwa ufanisi. Tunaitaka Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia TAMISEMI
isimamie ujenzi wa Ofisi za Wabunge ili Wabunge waweze
kupata Ofisi zao na waweze kufanya kazi zao kwa uhakika,
waweze kuheshimika kwenye majimbo yao tofauti na sasa
ambapo Wabunge wengi wanafanyia kazi zao nyumbani,
hili haliwezekani. Ofisi zimejengwa hazijakamilika, kuna
maeneo fulani mpaka frame zinaanza kung’olewa, kuna
maeneo fulani majumba yanaoza kabla hayajamalizika,
tunaitaka Serikali ikamilishe ujenzi wa Ofisi za Wabunge ili
Wabunge wafanye kazi zao kama sheria inavyotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpongeze sana
Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kipindi cha mwaka mmoja
mmefanya kazi kubwa sana. Mheshimiwa Rais amesimamia
maadili, nidhamu na uwajibikaji. Leo tunapozungumza hapa
Rais anazindua ujenzi wa reli ya standard gauge ambayo
itatumia saa moja kufika Morogoro na baadaye
watakamilisha Dodoma na kuelekea Mikoa ya Kanda ya
Ziwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano imefanya kazi kubwa sana kwa vitendo na tunamwomba Rais aendelee kusimamia nidhamu ya uwajibikaji, nidhamu ya mapato na matumizi, aendelee kusimamaia amani ya nchi yetu ili watu tuweze kuishi kwa amani na tufanye kazi kwa bidii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili na mimi nichangie kuhusu hizi Wizara mbili. Wabunge wengi wamepongeza na mimi nawaunga mkono kwa pongezi walizotoa kwa Waheshimiwa Mawaziri kwa uchapakazi na hata zile tahadhari zilizotolewa kuhusu namna gani wanatakiwa kukaza buti kwa ajili ya kuhakikisha Taifa linasonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hizi ni Wizara nyeti sana na zimepewa watu barabara kabisa ambao wanafanya kazi kwa ufanisi na weledi mkubwa. Kazi yetu siis kama Wabunge ni kujaribu kuonesha ni maeneo gani Serikali iyatilie mkazo na ni maeneo gani yanahitaji uangalifu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mbunge kutoka jimbo la Mtera na ni jimbo la vijijini, naiomba Serikali itazame kwa jicho la huruma sana majimbo ya vijijini. Hata hili ongezeko la watu mijini tunalolisema linatokana na vijijini kukosa huduma nyingi za msingi, huduma nyingi za msingi zikipatikana vijijini, nataka niwahakikishie mlundikano wa watu mijini utapungua kwa kiwango kikubwa. Tukizungumzia maji safi tunazungumzia mjini, tukizungumzia umeme wa uhakika, tunazungumzia mjini na tukizungumzia matibabu ya uhakika tunazungumzia mjini. Vijijini watu hawatakaa, watakimbilia mijini ili waje wapate huduma hizo muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namuomba sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, suala la kuhakikisha kila kata, hata ikiwezekana kila tarafa ipate kituo cha afya cha uhakika, gari la kubeba wagonjwa la uhakika, hii itasababisha watu wabaki vijijini na wasukume mbele gurudumu la maendeleo. Tukiweka bajeti kubwa za maji mijini, tukaweka bajeti kubwa za afya mijini, watu wa vijijini hakuna namna yoyote ya kuwaacha wao wakae vijijini wasije huko mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie barabara. Barabara za vijijini Halmashauri nyingi hazina uwezo wa kuzitengeneza. Uharibifu wa barabara ni mkubwa! Kuna majimbo ni makubwa mno. Kwa mfano, Jimbo langu mimi, ukitoka hapa ilipodondoka treni wakati ule, ukatoka Igandu mpaka mwisho Ilanga kuna kilometa zaidi ya 220; haiwezekani ambulance ziwe mbili au moja, inachakaa haraka kabla ya muda, kwa sababu inapita kwenye barabara mbovu halafu hazitoshi ambulance zenyewe. Kwa hiyo, naiomba Wizara ya TAMISEMI ihakikishe inatoa msukumo mkubwa kwenye bajeti za kutengeneza barabara za ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumza na Waheshimiwa Wabunge hapa, wamesema sana kuhusu Halmashauri zetu, kwa Waheshimiwa Madiwani. Tunawapozungumzia Waheshimiwa Madiwani kuna baadhi ya Halmashauri Madiwani wana hali mbaya, hata posho zao zile stahili zao hawapati, sembuse hiyo ya kuongeza! Hawapati hata zile za ndani za kwao. Wanakopwa kuendesha vikao, kwa sababu ya ugumu wa Halmashauri; katika vyanzo vya mapato wengine wanategemea kilimo; ukame umekuja, hawawezi kukusanya mapato ya ndani. Kwa hiyo, hata hiyo asilimia 10 tunazosema wapewe akina mama na vijana haziwezi kupatikana kwa sababu Halmashauri hazina makusanyo ya kutosha. Zile kodi za kero zilizofutwa, hakikisheni Serikali mnazifidia kuzilipa Halmashauri ili zipate uwezo wa kujiendesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumza sana kuhusu mapato ya Madiwani, tukiyaboresha Diwani ndio anayezika, anauguza, anasomesha. Akibaki na mapato yake madogo Diwani anakimbilia kwa Mbunge, anamkuta vilevile naye yupo taabani, inakuwa shida kubwa sana kuendesha majimbo. Kwa hiyo, naomba sana Waheshimiwa Madiwani wapewe uangalizi mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia maji. Miradi ya maji inasuasua sana. Ukienda unakuta hela ipo. Nauzungumzia mradi wa Kata ya Manzase, umechukua muda mrefu sana. Tumempeleka Katibu Mkuu wa CCM, tumempeleka Waziri Mkuu, Mzee Pinda na ndio alikuwa aufungue, imeshindikana. Leo ukienda anakwambia BOQ imefanyaje; ukienda wanakwambia mkandarasi sijui amefanyaje, wananchi hawataki kusikia maneno, wanataka kuona wanapata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imefika wakati mpaka wananchi wanakata tama. Mheshimiwa Jafo kaenda pale kasukuma akaweka na tarehe, lakini bado. Wanakwambia sijui tutangaze tenda upya, tubadili kutoka mfumo wa diesel kwenda solar, maneno hayatusaidii, tunataka maji katika katika Kata ya Manzase, hatutaki maneno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze kwa utulivu sana kwenye suala la ulinzi na usalama; nadhani juzi sikupata muda wa kutosha. Nashauri Serikali iunde dawati kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani au Wizara yoyote, ambalo wananchi watakwenda kuripoti pale juu ya ndugu zao waliopotea. Tusizungumze pale anapopotea mtu maarufu tu, Watanzania wengi sana wamepotea katika mazingira ambayo watu wengi hawajui wako wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tengenezeni dawati halafu mruhusu wananchi waje watoe taarifa za upotevu wa ndugu zao, mtashangaa idadi ya watu waliopotea bila taarifa.

Kwa hiyo, nashauri Serikali badala ya kulaumiana sisi wenyewe sijui kuna kikundi kinafanya nini, nilisema juzi mimi mwenyewe ni muhanga, nina mjomba wangu anaitwa Nikanoli, aliondoka mwaka 1980 mpaka leo hatujui yuko wapi. Wala siyo maarufu, wala hakuwa Balozi wa Nyumba Kumi useme ametekwa; aliondoka akapotea. Yupo mwingine alikuwa anaitwa Yoel, ameondoka tangu miaka ya 1970, hata kumjua watu hawamjui. Kwa hiyo, ukienda kwa kila Mbunge inawezekana ukakutana na taarifa za upotevu wa watu kwenye majimbo mengi sana, kama siyo yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali, badala ya kuanza kushutumiana sijui nani anafanya nini, tutengeneze dawati watu wapeleke habari za upotevu wa ndugu zao, za upotevu wa jamaa zao ili waweze kutafutwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge hapa tunazungumzia juu ya heshima na Daktari tena kazungumza vizuri sana. Daktari akasema tubadilishe fikra na huu ni mchango wake karibu wa pili anatushauri tubadilishe fikra kwamba tuwe na mtazamo mpya. Sina hakika kama yeye anao, lakini anasema katika huo mtazamo mpya, tuache kushughulika na watu wadogo wanaomtukana Mheshimiwa Rais. Ila Daktari huyo huyo anayetaka tubadilishe fikra, anasema Kiongozi wa Upinzani aheshimiwe ni mtu mkubwa. Mheshimiwa Rais atukanwe, Mheshimiwa Mbowe aheshimiwe, hatuwezi kwenda hivyo! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunataka heshima, turudi kwenye Katiba inayosema kila mtu anastahili heshima, bila kuangalia cheo chake. Watanzania wanastahili heshima, Mheshimiwa Rais anastahili heshima, Kiongozi wa Upinzani anastahili heshima, Mbunge anastahili heshima, Diwani anastahili heshima. Tutaheshimiana na tutaona kuendesha nchi ni kazi rahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukibadili fikra zetu tukaacha eti watu wadogo wadogo wanamtukana Mheshimiwa Rais kwenye simu, hao tusishuhulike nao, ila tushughulike na viongozi waliotengeneza, aaah, sidhani kama ni sawa sawa!

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nalishauri Bunge hili, kama tunataka kutoka hapa tulipo, kwanza kuna baadhi ya mazoea tuyaache. Pale tunaposema tunahitaji mabadiliko kwenye nyanja fulani, nina hakika kabisa Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri kabisa ya kubadilisha mfumo wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi yetu kubwa badala ya kumrudisha nyuma tumpe moyo, tumtie nguvu, Mawaziri tuwape moyo, tuwatie nguvu wasukume gurudumu mbele. Nani asiyejua maeneo mengi yaliyokuwa yamesimama? Wizara kama ya Ardhi ilikuwa na matatizo chungu nzima! Tulikuwa na kesi chungu nzima, lakini sasa hivi zinatatuliwa kwa speed kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe sana, tunapozungumzia heshima tuzungumze pande zote mbili. Nataka niseme kwamba, jana ilitolewa hoja hapa, watu wameidharau na wengine wakaona kama inachomekwa. Nasikia ninyi mna vyombo hapa mnaweza kutuambia, kuna Mbunge amekamatwa na konyagi anaingia nayo Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi juzi hapa Serikali imemwajibisha Kitwanga kwa kudhaniwa tu amelewa, akawajibishwa. Leo Mbunge anaingia na konyagi ndani ya Ukumbi wa Bunge, huko amekamatwa. Tunataka tuone na ninyi meno yenu yako wapi katika kumwajibisha huyo Mbunge, kama mtaweza! Maana kazi yenu ni kusema tu, siyo kutenda. Bahati nzuri Mbunge mwenyewe anatoka upande huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tuone mtakuwa wakali kwa kiwango gani kwa Mbunge anayeingia amelewa, halafu ana chupa ya konyagi ndani ya eneo la uzio wa Bunge! Sisi tumeshaonyesha njia, Mheshimiwa Waziri amekuja anatikisika, hana chupa, hana nini, mkasema ooh, amelewa sijui nini na Uwaziri kaupoteza. Ninyi sasa tuone sasa mtachukua hatua gani ili...(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kuchukua fursa hii kumshukuru Mungu kwa kupata nafasi hii, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ya kusimamia na kuliongoza Taifa hili kwa speed inayotakiwa. Nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uteuzi wa Profesa Kitila Mkumbo, ninahakika akiungana na wenzake pale wanaweza kufanya kazi kubwa sana ya kusukuma nchi hii mbele pamoja na vijana wadogo wakina Luhemeja ambao sasa hivi wamepata nafasi ya kushughulikia matatizo ya maji katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ambayo wanaifanya Wizara ni kazi nzuri sana, lakini kuna baadhi ya mambo wanakutana hapa na upinzani mkubwa hasa wa takwimu zao, mimi nadhani wanatakiwa vilevile kufanya vile vile kazi ya RITA ya kusajili vizazi na vifo. Wanatakiwa wasajili visima vilivyokufa na vilivyo hai. Pengine kwenye orodha, wana orodha ya visima lakini vimeshapigwa radi siku nyingi vingine vimepigwa tetemeko wao kwenye vitabu wameandika kwamba visima vinatoa maji. Watajikuta wanapata matatizo makubwa bila sababu za msingi, sajilini takwimu za visima ambavyo havifanyi kazi na vinavyofanya kazi, mtapata kwa uhakika kwamba maji yapo kwa kiasi gani si kuleta tu kwamba kuna visima kadhaa na maeneo kadhaa yanapata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata visima vya zamani ambavyo vimekufa Halmashauri hazina uwezo wa kuvifufua. Kuna baadhi ya maeneo walikuwa na maji sasa hivi hawana maji. Kwa mfano ukija kutazama kwenye Jimbo la Mtera kuna Kata kadhaa zinahangaika kupata maji. Kata ya Handali, ukienda kutembelea Idifu, ukienda kutembelea Mlowa Bwawani wote hawana maji lakini ukija hapa unakuta takwimu vijijini ni 72. Kwa hiyo, nina uhakika wakisajili visima vilivyo hai na vilivyokufa wanaweza wakaja na mahesabu ya uhakika. Lakini nchi hii tuigawe kwenye vipande, kuna baadhi ya maeneo yanasubiri muda mrefu sana kupata huduma hii, tujue tu kwamba tutapata lini, nayo tukijua hiyo inaweza kutusaidia. Tumeona kuna ongezeko kubwa sana la huduma za maji mijini tumekubali na sisi tunayaona lakini kuna baadhi ya maeneo hata wananchi waelewe tu kwamba mwaka gani basi hii huduma muhimu ya maji itawafikia vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Maji ni Wizara mtambuka sana, na nashangaa tunapoijadili Wizara hii halafu Wizara ya Fedha haina Waziri wala Naibu Waziri humu ndani ya Bunge, hii si sawa. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais aliwaweka wawili mmoja akiwa hayupo mwingine yupo, hii ni dharau kubwa sana kwa Bunge lako Tukufu. Kwa hiyo, tungependa, tunapojadili Wizara muhimu kama hizi Mawaziri wa fedha wawepo, Bunge maana yake karibu ni Wizara tatu tu; ni kiti cha Spika, Waziri Mkuu na Waziri wa Fedha maana humu tunazungumzia hela sasa tukiwa tunazungumzia pesa wahusika wa fedha hawamo kidogo inatupa matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vitu hapa vinazungumzwa, jana kulikuwa na Mbunge mmoja alikuwa anaicheka Serikali na kuibeza kwanini Rais ameanza na ndege asianze na maji. Jamani, nataka leo nitoe somo kidogo hapa. Ndege ni sawa sawa na mkulima mwenye kilo moja ya mahindi ndani hana chakula na mvua zimeanza kunyesha, anatakiwa achague akaange ile kilo moja afe au apande apate mahindi mengi ili aweze kuishi? Mheshimiwa Rais alipoleta ndege ameleta biashara ili izalishe tupate hela za kutengeneza maji mengi zaidi, kwa hiyo, badala ya kumbeza tumuunge mkono,Waheshimiwa Wabunge tumuunge mkono Mheshimiwa Rais, nchi haiendeshwi kwa hapana.

Nataka niwambie, kwamba duniani kuna aina tatu za upinzani; uko uoinzani shinikizo wanashinikiza hoja, upo upinzani kioo na uko upinzani serious, huu wa Tanzania ni upinzani kioo. Kama hujachana wanakwambia hujachana kesi inaisha unaendelea na shughuli zako. Kwa hiyo, Serikali msiwe na wasiwasi tuendelee kujipanga kufanya kazi za maendeleo ya nchi hii, tusishughulike na upinzani kioo ambao kaa hawajachana wanakwambia umechana kasoro Zitto tu ndiyo anajitahidi na kwa sababu yuko peke yake. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi umeona walivyomuabisha Makamu Mwenyekiti wa Chama, amekuja Profesa Safari kugombea hapa amepewa kura 30 na hawa, hawamtaki Makamu Mwenyekiti wa Chama chao awe kiongozi, hawa ndiyo wanaweza kupewa Serikali, haiwezekani watu ambao hawaheshimiani, haiwezekani. Kwa hiyo, nakushukuru sana, mimi naunga mkono hoja, lakini nawaambia Serikali msihofu upinzani tufanye kazi. Ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mungu kupata nafasi hii ya kuchangia hoja za Wenyeviti wa Kamati walizoziwasilisha mbele yetu. Nami nitoe pole kwa familia ya Ndugu Kingunge Ngombale-Mwiru, Mwanasiasa Mkongwe wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati mwingine Bunge zinapokuja hoja za msingi kama hizi tatu kwa pamoja zinaletwa na Kamati halafu sisi wenyewe Wabunge tunajinyima tena nafasi ya kuzichangia, kidogo hapo Bunge tunakuwa ni kama vile hatujitendei haki. Ukiangalia hoja hizi ni za Kamati zetu na wachangiaji ni sisi Wabunge, kuna sababu gani ya kujipa dakika saba wakati uamuzi ni wa Bunge lenyewe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno hayo, nataka kwa haraka haraka nichambue baadhi ya mambo machache, nikijikita zaidi kwenye hoja ya Kamati ya Viwanda na Biashara. Kuna tofauti kubwa kati ya kujenga uchumi wa viwanda na kujenga viwanda vyenyewe. Unapotaka kujenga uchumi wa viwanda hasa kwa sisi Wabunge wa Vijijini ni vyema viwanda hivyo vikawa na chain. Kama vinahusu kilimo vikajipanga katika mpango ambao utawafanya wakulima wanufaike moja kwa moja na uwepo wa viwanda hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, unapokuwa na viwanda vya mazao ya mifugo, halafu kukawa na viwanda vya mbolea ambavyo vinagusa moja kwa moja wakulima, kutaifanya nchi yetu ipate kodi ya kutosha kwa wakulima na wakulima wenyewe wakajiletea maendeleo makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo kubwa sana la mwingiliano wa Taasisi za Serikali. Kwa mfano, ukiangalia kazi zinazofanywa na TFDA na TBS unaona ni kazi ileile moja, mfanyabiashara anaweza kupata certificate ya TFDA lakini TBS wakamkatalia. Kwa hiyo, unaweza kuona jinsi vyombo Serikali vinavyokuwa kikwazo cha kuhakikisha wanapata kodi ya kutosha na kupata maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati Kamati ya Viwanda na Biashara iliwahi kutembelewa na watu wa konyagi, wakaleta aina 32 za viroba na zikaonekana ni hatari Serikali ikazipiga marufuku, lakini leo viroba vinarudi tena kwa mlango wa uani, watu wanavipaki kwenye chupa, havina
stika za ubora za TBS, hazina stika za TRA wanakwepa kodi lakini vinauzwa. Wale wafanyabiashara ambao wanafuata utaratibu wanatozwa kodi kubwa wanajikuta wenzao wanauza kwa bei ya chini wao wanauza kwa bei ya juu, hawapati wateja, matokeo yake Serikali inashindwa kukusanya fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi mtu anayeuza kinywaji kikali kwenye chupa ya plastiki, haina nembo zozote za Serikali, nani atajua ubora wa kinywaji hicho? Matokeo yake bado tunaendelea kuwaangamiza vijana wetu kutokana na uwepo wa viroba kwa njia ya uani. Tunaomba leo Mheshimiwa Mwenyekiti utakapokuwa ukipitia tupate majibu ya kutosha kwenye jambo hili.

Mheshimiwa mwenyekiti, unajua Mungu akikupa kilema anakupa na mwendo wa kukitembelea, hawezi akakupa kilema akakunyima mwendo. Nataka niweke usahihi kidogo tu, ukitazama makusanyo ya kodi, walipokuwa wakikusanya Halmashauri, 2014/2015 walikusanya shilingi bilioni 18.9. Baada ya Serikali Kuu kuchukua na kuanza kukusanya wenyewe kupitia TRA kwa mara ya kwanza mwaka 2015/2016 walikusanya shilingi bilioni 28.2. Mwaka uliofuata, 2016/2017, Serikali walikusanya shilingi bilioni 34.9 maana yake kuna ongezeko hapo. Mwaka wa 2017/2018, kwa robo mwaka wamekusanya shilingi bilioni 16.6.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo langu mimi siyo kukusanya ila ni namna gani zinarudi kwenye Halmashauri ili ziweze kujitegemea. Ni kweli mmekusanya sana kuliko walipokuwa wanakusanya Halmashauri wenyewe lakini ni namna gani zinarudi ili ziweze kuleta maendeleo kwenye Halmashauri zenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine kubwa linaloleta mgongano kati ya Kamati ya Bajeti na Wizara ya Fedha. Kwenye Halmashauri kunakuwa na bajeti ndogo za Halmashauri, wanapitisha vyanzo vyao vya ndani, wanapitisha namna ya kukusanya, inapokuja kwenye bajeti

kuu, vile vyanzo vinafutwa halafu hakuna namna ya kuvifidia. Kwa hiyo, tunajikuta tunakuwa na bajeti za Halmashauri ambazo zimefelishwa na kutokuwepo na vikao vya mwanzoni kati ya Kamati ya Bajeti na Wizara ya Fedha. Mkiweza kukutana mapema mkaondoa mkanganyiko huu, maana yake Halmashauri haziwezi kupanga bajeti ambazo huko mbele ya safari zitakuja kukataliwa na Serikali Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kuwe kuna vikao vya kutazama bajeti vya mapema, tunashindwa nini? Kwa sababu leo hata zile tozo za kero ambazo tulizifuta, bado hazirudishwi kwenye Halmashauri. Kwa hiyo, Halmashauri zinashindwa kujiendesha, zinakosa mapato ya kutosha kuweza kuwaletea maendeleo wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia kuwaomba sana, Wizara ya Viwanda na Biashara hebu tuleteeni orodha kati ya vile viwanda 130 na kitu vilivyobinafsishwa vingapi vinafanya kazi na vinafanya kazi kwa ufanisi gani? Leteni hapa orodha ili Waheshimiwa Wabunge tujue kumbe tangu tumeanza kuongelea viwanda kuna viwanda kadhaa vimeanza kufanya kazi na viwanda kadhaa bado vipo kwenye maandalizi ya kuhakikisha vinaendelea kufanya kazi. Vinginevyo tutakuwa tunapiga kelele hapa ya viwanda, viwanda kumbe hakuna kiwanda hata kimoja ambacho kinafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie habari ya namna gani tunaweza kuzisaidia Halmashauri zetu. Halmashauri zinaweza kujiendesha zenyewe lakini pale ambapo vyanzo vyake vya makusanyo ya ndani vinaheshimiwa na Serikali Kuu. Tusiwe tunakuja tunafuta halafu baadaye tunazitaka zijiendeshe, hawataweza! Waheshimiwa Madiwani wamepitisha vizuri makusanyo yao ya ndani, wameyatungia sheria ndogo tunapokuja sisi kukataza huku juu maana yake tunawaweka katika mazingira magumu sana ya kuhakikisha wanapata mapato ya kuendelea kujiendesha wao wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, niombe sana Serikali na Wenyeviti wa Kamati watakapokuwa wanayapitia haya wayatilie maanani sana ili tuweze kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dokta John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua anazochukua kukabiliana na Upotevu wa Mapato ya Serikali katika Sekta ya Madini
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa dakika tatu za kuunga mkono Azimio la Bunge kwa ajili ya kumpongeza Rais kwa hatua madhubuti alizochukua kuhakikisha kwamba nchi yetu inanufaika kikamilifu na uchimbaji wa madini hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli viongozi wote waliotangulia, naomba unyamaze usiniite, nitakutakana halafu nitaonekana sina maana. Eeh kwa sababu wewe unaniita jina la nini mimi mume wako niache nichangie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli viongozi wote waliotangulia waliunda Tume na ni kweli wakati ule sheria zetu zilikuwa zina wa-favour sana wawekezaji kwa wakati ule wa 1977, 1979, tulihitaji wawekezaji waje wawekeze kwenye sekta ya madini ambapo hawakuwepo wawekezaji wakubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume zile zilizoundwa zilifanya kazi zake lakini Tume ya Mheshimiwa Magufuli kwa nini tunaipongeza, imefanya kazi na yeye mwenyewe ameenda mbele zaidi. Ameweka wazi ripoti za hizi Tume tena hadharani na kila mtu amezisikia tofauti na Tume zilizoundwa hapo kabla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa hatua hii kubwa kwa sababu haiwezekani Taifa lisimpongeze kiongozi wake anapochukua hatua zinazoonekana kwa macho. Hapa nilisema na leo tumegawana, ukishindwa kupongeza, utapongeza wale wanaotuibia na imekuja hiyo wazi kabisa kwenye Bunge hili, umeona ripoti za Maprofesa, wataalam zinaitwa za upuuzi kwa sababu kuna watu wanaunga mkono upande mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi ambao tuko kwenye Bunge hili ambao tunaona kazi nzuri iliyofanywa na Rais, nataka niwaambie tu, siyo msemaji wake lakini nimeona kuna clip Mzee Lowassa naye kampongeza Rais. Sasa sijui hawa ambao wanakataa kumpongeza Rais wanaitoa wapi, kwa sababu hata Sumaye amempongeza Rais na ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA. Kwa hiyo, ndiyo maana tunasema Bunge zima lina wajibu wa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa hatua kubwa alizozichukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kurekebisha sheria, hivi kwenye Bunge la Bajeti hili, umeletwa Muswada wa kurekebisha sheria ya madini? Labda uelewa wangu mdogo, kwa sababu haiwezekani ulete Muswada sasa hivi turekebishe hizo sheria wakati tuko kwenye Bunge la Bajeti. Hapa tunachukua hatua ya kumpongeza Mheshimiwa Rais halafu tuitake Serikali ilete haraka Miswada ya kurekebisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, na mimi naungana na Waheshimiwa Wabunge wote, ambao wamemshukuru Mungu kwa ajili ya afya yako tunaendelea kukuombea. Inawezekana hata sisi wenyewe tuna matatizo lakini bado hatujapimwa sawasawa. Kwa hiyo, kwa kweli tunakuombea Mheshimiwa Spika uendelee kuimarika ili uweze kuwatumikia wananchi wako wa Jimbo la Kongwa lakini na sisi Wabunge wenzako.

Mheshimiwa Spika, pongezi zangu za pili zinakwenda kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri wanaomsaidia kazi. Hotuba ni nzuri, wameiwasilisha vizuri lakini imegusa maeneo mengi muhimu. Isipokuwa kuna baadhi ya maeneo Waheshimiwa Wabunge tutawakumbusha ili nanyi muweze kuongeza nguvu kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, tunamshukuru Mungu sana kwa sisi wakazi wa Mkoa wa Dodoma kutupatia mvua za kutosha mwaka huu ingawa baadhi wa maeneo zimeleta majanga makubwa sana, kama uharibifu wa barabara inayotoka Dodoma Mjini kwenda Ilangali. Pale daraja limesombwa kwa hiyo, tuna uhakika kwamba Serikali watafuatilia kulitengeneza haraka ili kuweza kuwanusuru wananchi wa ukanda ule wa Tarafa ile ya Mpwayungu ili mazao yao ya biashara yaweze kufika kwa wakati hapa Dodoma ambapo kwa kweli ndiko kwenye soko kubwa tunalolitegemea.

Mheshimiwa Spika, yamezungumzwa mengi nami naomba nitoe mchango wangu kidogo katika baadhi ya masuala ambayo yamezunguzwa mahali hapa.

Mheshimiwa Spika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa, kuna mambo ambayo yamefanyika kwa miaka miwili na nusu unaweza kusema ni miujiza. Kwa sababu matukio makubwa na ya kutisha tumeyaona yakifunguliwa na haya yote yakikamilika, reli ikakamilika, umeme wa maji ukakamilika, barabara zetu zimekamilika nina hakika kabisa kwamba yatachagiza maendeleo kwa kiwango kikubwa. Kwa hiyo tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na tunamwomba Mungu aendelee kumlinda.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ununuzi wa ndege; nataka niwakumbeshe baadhi ya watu wanaweza kuwa aidha wadogo au wamesahau. Uamuzi wa kulifufua shirika la ndege sio mara ya kwanza, baada ya iliyokuwa Jumuiya ya East Africa kufa na ndege nyingi kubakishwa nchini Kenya na sisi tukapata moja. Mwalimu Nyerere mwaka 1977 alifufua shirika lile kwa kununua ndege zinazokadiriwa kufikia kama nne au tano kwa wale watu wazima kama mimi mnaweza kukumbuka.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Rais anachokifanya sasa anafufua shirika la ndege, ni kama vile una debe moja la mbegu unajiuliza ukaange ule au uende ukapande zizae ili waweze kutumia wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa wengine wamezungumza kwa dharau sana. Mtu anasema eti watu wanaenda kupiga picha kwenye ndege, watu wanashangilia ndege. Hapa wako Wabunge hapa wako humu ndani kwa sababu wameletwa na ndege. Wengine helicopter zilipokuwa zikikusanya watu ndiyo wakachaguliwa kuingia humu ndani ya Bunge wamesahau.

Mheshimiwa Spika, kuna chama hapa hakina ofisi ya mkoa, hakina ofisi ya wilaya, kimepata ruzuku zaidi ya mabilioni ya pesa, lakini huwa wanakodia ndege wakati wa uchaguzi ili Wabunge wao waweze kushinda. Wamesahau wanaingia humu ndani kutukana ndege maskini wa Mungu. Hivi kama kweli isingekuwa helicopter zinawasaidia, si tungeona mmejenga hata ofisi ya Mkoa?

Mheshimiwa Spika, tumeona NCCR Mageuzi mahali pengine wana ofisi, tuwameona CUF wana ofisi ya kueleweka lakini kuna chama kina kaofisi squatter pale Kinondoni wanapiga kelele kila siku hapa.

Mheshimiwa Spika, unashindwa kuwaelewa kabisa kwa nini msioneshe hayo maendeleo kwenye chama chenu kwa ruzuku mlizopewa? Mbona mnakodia helicopter hizo hizo? Kwa hiyo, kununua ndege Mheshimiwa Rais mimi naona ni jambo jema kwa sababu tutapanda sisi, watapanda Watanzania na lile shirika litaleta maendeleo makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, dharau kwenye viwanda vidogo si njema. Tunadharau mafundi cherehani, hivi hapa Waheshimiwa Wabunge bila mafundi cherehani si tungekuwa uchi tu hapa. Wengi tunashona tunashona nguo huko. Leo nataka niwaambie kiko kiwanda ambacho kinatusaidia sana juzi tu ndiyo nimekiona. Kiwanda cha Saloon jamani kumbe Wabunge tunalindwa sana na saloon. Kuna Mbunge mmoja amekosa kwenda Saloon siku tatu, sura yake imebadilika kabisa, wala siyo yeye.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunataka tuwashukuru sana hata watu wa saloon; akinadada wa saloon, akinababa wa saloon kumbe mnatuweka vizuri mpaka tunaonekana watu wa maana mbele za watu. Kwa hiyo hivi ni viwanda vidogo ambavyo Watanzania vinatuletea maendeleo lakini na sisi vinatuletea heshima fulani. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nataka nikubaliane, Waheshimiwa Wabunge wameongea vizuri sana hapa kuhusu gharama za uchaguzi, hili nataka niwaunge mkono. Kuna gharama kubwa sana kurudia chaguzi ndogo, lakini ambao wanaweza kutusaidia kwa kweli wanaweza kutusaidia Wapinzani, kwa sababu Serikali imeshaundwa Wabunge wengi wa CCM una uhakika Mbunge wa Upinzani hata akishinda haendi kubadili Serikali. Kwa nini mnaweka wagombea msiweke ili kunusuru mapesa hayo yaende kwenye maendeleo. Hakuna sababu maana hata ukishinda kiti kimoja, kilo moja ya sukari haiwezi kwenda kukolea kwenye pipa la maji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hakuna sababu ya vyama vya upinzani kuweka wagombea kwenye uchaguzi mdogo, maana tayari umeshafahamika aliyeshinda kafahamika kuna sababu gani za kuweka mgombea kwenda kupoteza hela za nchi. Kwa hiyo ni vema wakatuunga mkono, kuanzia sasa hivi kukitokea uchaguzi mdogo hakuna sababu ya wao kuweka mgombea na sisi tutapita bila kupingwa, hakutakuwa na gharama pesa zote zitaenda kwenye maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna Waheshimiwa Wabunge wamezungumza sana leo hapa, wamezungumza kwa uchungu mkubwa sana. Mbunge mmoja wa CHADEMA amezungumza sana kuhusu Rais kutoka Kanda ya Ziwa na kwamba ni aibu sana Kanda ya Ziwa kukosa maji. Akasimama ndugu yangu Nape akasema Waziri Mkuu anatoka Kusini ni aibu kukosa maendeleo. Sasa najiuliza tuna Waziri Mkuu wa Kusini, tuna Rais wa Kanda ya Ziwa? Tuna Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jamani. Hatuna Rais wa Kanda, tuna Waziri Mkuu wa Jamhuri Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, tusiwafanye viongozi wetu wakawa viongozi wa Kanda haiwezekani na mtakuwa hamtutendei haki. Hivi na sisi ambao Spika unatoka Dodoma mbona unawaruhusu wao kusema, kwa nini usituruhusu sisi wa Dodoma tuseme sana ili shida zetu zisikilizwe. Haitawezekana!

Mheshimiwa Spika, hili jambo lazima tujue Viongozi wakishakuwa wa Kitaifa, wanaongoza Taifa la Tanzania na sio sehemu walikotoka. Kwa hiyo kama Rais anahakikisha kwamba kwao hakuna maji lakini wengine wamepata huyo ndio Rais bora analitazama Taifa, hatazami upande wake. Kama Mheshimiwa Waziri Mkuu anaelekea sehemu zingine za Tanzania anazunguka kuhakikisha maendeleo yanapatikana huyo ndio Waziri Mkuu bora.

Mheshimiwa Spika, sikutegemea kwamba tuanze kuwagawa viongozi wetu kwa namna ya wanakotoka haiwezekani. Tusimame katikati tuishauri Serikali mambo ya msingi yafanyike ili nchi nzima ipate maendeleo. Nchi hii ni kubwa ndugu zangu, nchi hii changanya Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi ndipo unaweza ukaikaribia ukubwa wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, huwezi ukapeleka maendeleo kwa haraka na maeneo yote yakaridhika ndugu zangu, twendeni taratibu. Twendeni taratibu, twendeni awamu kwa awamu. Sehemu zingine ukipeleka sehemu zingine wanasubiria, sehemu zingine ukipeleka sehemu zingine wanasubiria, tutafika tu mahali na nchi nzima itapata maendeleo. Kwa hiyo nawaombeni sana Waheshimiwa Wabunge tuvute subira, viongozi wanahitaji kuungwa mkono.

Mheshimiwa Spika, watu wanazungumzia habari ya usalama…

T A A R I F A . . .

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa yako Mheshimiwa Musukuma. Bahati mbaya tu mwenyewe hayupo maana na mimi nilitaka asikie lakini atakusikia. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaomba sana sisi kama Taifa kama nchi, viongozi wetu wagawanye rasilimali za nchi kwa usawa maeneo yote. Hata yale ambayo haya vivutio vikubwa vinavyokusanya hela nayo wayatazame. Kwa mfano tunaelewa sisi Dodoma hapa tuna zao la zabibu. Zao la zabibu hili likifunguliwa viwanda vya kutosha tutanufaika, watu wetu watapata pesa, watalima, watauza.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mifugo, sisi tumepata kiwanda kizuri kabisa cha kuandaa ngozi pale katika Kijiji cha Idipu, namwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu umeme upelekwe kwenye kile kiwanda. Kile kiwanda hakiishi kwa wakati kwa sababu umeme wenye nguvu kubwa haujafika pale kiwandani.

Mheshimiwa Spika, umeme ukiweza kufika na sisi ni wafugaji, tuna ng’ombe wengi wanachinjwa kwenye minada, ngozi nyingi zinapelekwa pale, wananchi wa jimbo la Mtera nao watapata maendeleo makubwa. Tutanufaika na hii hoja ya uanzishwaji wa viwanda maana kiwanda tayari kinajengwa.

Mheshimiwa Spika, naomba tuitazame Tanzania katika yale maeneo ambayo yamesahaulika kwa muda mrefu tuyatupie macho. Maana kuna mwingine ana maji ana barabara nzuri akija hapa kupiga porojo ni sawa, lakini kuna wengine vitu vyote vitatu hawana, tuangalie kimoja wapate. Watu ambao wanaishi kijijini; tunapoteza akinamama wengi sana wakati wa kujifungua, kwa sababu unaweza kukuta wakati wa kujifungua njia imefunga, maji yamekata barabara, gari haliwezi kufika.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kupata ambulance, lakini kuna mahali ambulance hazipiti kwa sababu barabara ni mbovu. Tumeondoa barabara kutoka Halmashauri tumezipeleka TARURA, lakini ukitazama uwezo wa TARURA na bajeti yao bado ndogo bado hai-reflect maendeleo ya barabara za vijiji. Kwa hiyo, tunaomba waongezewe pesa, ziwe nyingi ili waweze kutengeneza zile barabara kwa kiwango kinachotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuwatazame sana! Watu tumejenga sekondari za Kata, tumejenga mashule vijijini, lakini bado namna ya kuwachagiza wananchi wa vijijini ni umeme ufike kwa wakati. Kuna baadhi ya maeneo hayana umeme Tarafa nzima ya Mkwayungu haina umeme. Tukiwapelekea umeme watu wa Mkwayungu baadhi ya mambo yao mengi watafanyia kule, watakamua alizeti zao kule, hawana haja ya kuzileta Dodoma Mjini. Dodoma Mjini wataleta mafuta. Kwa hiyo viwanda vidogo vitaanzishwa Mkwayungu.

Mheshimiwa Spika, nakuomba sana tunaposimama hapa na sisi lengo letu ni kuwaunga mkono na kuwatia moyo Waheshimiwa Mawaziri. Ukilitazama Baraza hili ni dogo kuliko lililopita, lakini Mawaziri wake wanafika kila kona ya Tanzania, lazima tuwapongeze na kuwatia moyo. Hawa ni binadamu usiku kucha wanasafiri wanafika kwenye majimbo yetu wanaongea na wananchi, lazima na sisi tuwaunge mkono.

Kwamba Waheshimiwa Mawaziri tunatambua kazi kubwa mnayoifanya sisi kama Wabunge wenzenu tunawaungeni mkono, endeleeni kuchapa kazi ili Taifa hili liweze kusogea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wamezungumza hapa kuhusu amani. Amani na utulivu ipo lakini ipo kwa sababu na wahalifu nao wapo. Tuwaombe Serikali waendelee kuwasaka wahalifu kwenye kila nyanja ya uhalifu unavyotokea. Tusiichafue Serikali kwa sababu ya kosa moja.

Mheshimiwa Spika, ikitokea kiongozi mmoja wa dini amekengeuka pengine amezini Mungu aepushe mbali hatuwezi kulaumu dini nzima, haiwezekani. Tunamlaumu huyo huyo kwa kufanya hilo kosa. Kwa hiyo lazima tukubaliane, kwamba uhalifu upo lakini tuitake Serikali kupambana na uhalifu kama inavyofanya siku zote.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa uongozi wako na Mungu aendelee kukujalia kwa namna unavyotenda haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana hapa kuna Waheshimiwa Wabunge walikuwa wanataka kubomoka lakini leo nataka kusema ukweli sasa, maana yake Tanzania ukweli watu hawaupendi, nami nataka leo niseme ukweli halafu nitatumia kauli ya mdogo wangu Mwenyekiti wa Vijana wa CCM Ndugu Kheri James kuwaomba wanipigie makofi kwa kusema ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI pamoja na Waziri mzoefu Kaka yangu Kapt. George Mkuchika. Nawapongeza sana Waheshimiwa Naibu Mawaziri wa TAMISEMI, Katibu Mkuu, Mhandisi Iyombe pamoja na timu yako mnafanya kazi nzuri. Wakati nikiwapongeza niwashukuru kwa kunipatia milioni 700 kwa ajili ya kujenga kituo cha afya pale Mpwayungu, milioni 400 kwa ajili ya ujenzi na 300 kwa ajili ya vifaa. Hii itasaidia sana wakazi wa Tarafa ya Mpwayungu kupata huduma za afya kwa urahisi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe tu watu wa TARURA watengeneze daraja lile la Manda limevunjika kwa mvua, hii inatupa shida sana ambulance kupita pale kuleta wagonjwa kwenye kituo cha afya cha Mpwayungu. Kama ambavyo Wabunge wengi wameeleza tunaomba bajeti ya TARURA na utendaji wao wa kazi uwe wazi ili Wabunge waweze kuasaidiana nao kuhakikisha kwamba maendeleo yanakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nilitolee ufafanuzi kabla sijaingia kwenye utawala bora, nizungumzie kuna baadhi ya Wabunge walikuwa na mashaka juu ya kugawana mali za Chama. Wengine wanafikiri kwamba mali ambazo walizijenga kabla hawajahama CCM wana haki nazo. Ndugu zangu hata Maaskofu hilo mkiwauliza watawasaidieni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiwa Muislam ukachangia matofali siku utakayokuwa Mkristo yale matofali ya Msikiti hayatakuhusu tena, wala huwezi kuyadai tena, ukiwa Mkristo ukachangia matofali ya kujenga Kanisa siku utakayohama kwenda kuwa Muislam matofali yale ukidai ni ugomvi. Kwa hiyo, ndugu zangu muelewe tu kwamba ile michango mliyoitoa wakati wa Chama kimoja kuijenga CCM mkitaka kufaidi rudini CCM ili muweze kufaidi vizuri. Hata kwenye harusi tu, michango ya harusi inaishia mlangoni huingii chumbani kwa maharusi kwa sababu ya mchango uliotoa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo sasa ninukuu tu kwenye Biblia huo mstari siukumbuki. Kuna mstari unasema toa kwanza boriti jichoni mwako ndipo uone vema kibanzi kilicho kwenye jicho la mwenzako. Wapinzani wa nchi hii, tuoeni kwanza boriti iliyomo kwenye macho yenu kabla hamjaona boriti iliyopo kwenye Serikali ya CCM. Nasema hivi kwa sababu nataka niingie sasa kwenye ukweli mtupu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kwenye ripoti ya CAG ukurasa 266 nanukuu “mkopo ambao haukuthibitishwa mapokezi ndani ya Chama cha CHADEMA, mnamo tarehe 11 Aprili, Menejimenti ya CHADEMA (Mkopaji) iliingia makubaliano na mwanachama wake (Mkopeshaji) kuhusu kukopeshwa kiasi cha bilioni mbili.” Mnisikilize hapo, wanakopa hewa yaani deni hewa hilo. Mkopo waliingia makubaliano na mwanachama wake mkopeshaji kuhusu kukopeshwa shilingi bilioni mbili kwa shughuli za Chama. Hakuna nyaraka zinazoonesha kuwa kiasi cha mkopo walichokubaliana kilitolewa na kupokelewa na Chama husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, CAG anaendelea tarehe 26 Agosti, kiasi cha shilingi milioni 866 kililipwa kwa mwanachama kwa niaba ya Chama kwa ajili ya mabango ya matangazo yaliyotolewa na kampuni ya MS Milestone International Company Limited nje ya deni hilo. Kiasi cha shilingi milioni 715 kililipwa kwa mwanachama kama marejesho ya fedha iliyokopwa kulipia ununuzi wa mabango bila ya kuambatanisha makubaliano ya kisheria. Wajinga ndio waliwao, mmeng’ang’ania maandamano mnaacha wenzenu wanapiga hela. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukaguzi wangu wa taarifa ya makusanyo ya Chama umebaini kiasi cha Sh. 2,302,305,500 kilikusanywa bila kuingizwa kwenye akaunti ya Wadhamini.” Angalia mambo hayo! Hazikupelekwa benki na matumizi yake hayakutolewa kwa ajili ya ukaguzi. Kutokupeleka makusanyo benki kunaonesha Chama kutokuwa na mfumo mzuri wa udhibiti wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, manunuzi yaliyofanyika, nimebaini kuwa CHADEMA kimefanya manunuzi ya bidhaa na huduma zenye thamani ya Sh.24,216,625,309 bila kufuata utaratibu.” Wajinga ndio waliwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wajinga ndio waliwao kuna Kwaya imeimba. Badala ya kushughulikia matatizo makubwa ya ufisadi ndani ya Chama chao wameng’ang’ana kila siku kukosoa Serikali, kukosoa Chama chenye Serikali. Ndugu zangu ndani ya Chama chenu kuna wizi na ubadhirifu mkubwa wa pesa, watu wanakula hela na ninyi mpo hapo! Madeni hewa yanatengenezwa, helcopter hewa zinakodiwa ninyi mmekaa hapa mnang’ang’ania CCM, toeni kwanza boriti kwenye macho yenu ndiyo muone vibanzi vilivyopo kwenye Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Watanzania waelewe kwamba ufisadi mkubwa upo kwenye Chama kinacholalamikia ufisadi kumbe wao ndani hawajikagui. Kwa mara ya kwanza ipo humu na ndiyo maana nasema hakuna mtu atapinga kwa sababu haya ni mawe ya uhakika. Nipigieni makofi kwa ukweli ninaowapa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni ukweli mtupu, ndugu zangu mkienda mkajisimamia mkawa wakweli kwenye mambo yanayowagusa ninyi mtakuwa na haki ya kutukosoa, lakini kama ninyi wenyewe mnakumbatia ufisadi na wizi wa mabilioni ya pesa yanakusanywa kwa wanachama yanaingia kwenye Chama chenu, watu wanagawana wanakula, michango ya Wabunge inaliwa, mmekaa hapo mmenyamaza kazi yenu kukosoa hii! Nawaambia hamtakaa mfike popote. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nimewaambia huu ni ukweli mchungu, nimesema natumia maneno ya Kheri Denice James kwamba ifike mahali kama tunataka kutengeneza Upinzani tutengeneze Upinzani wenye kusema kweli. Ukianza kumulika nyoka anzia kwenye miguu yako ndipo uanze kumulika kule. Niliwaambia hata juzi mna Chama kilichopokea ruzuku zaidi ya bilioni 10 hakina Ofisi hata moja wilayani, hakina ofisi hata moja mikoani, mnataka kufanana na Chama cha Zitto! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mnazungumzia utawala bora nataka niwaambie, Mheshimiwa Zitto yupo peke yake anahangaika. Wapo Wapinzani Wazalendo, mimi nataka niseme kwenye Bunge hili mtakuja kunikumbuka, Mheshimiwa Zitto wewe ni hazina lakini badili Chama, njoo CCM uje ufanye kazi ya wananchi, kubaki huko unapoteza muda bure, tutakukosa mtu mzuri kwa sababu ya muda na huko unakopoteza muda. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwambie hivi tangu CHADEMA imesajiliwa, nazungumzia utawala bora, tangu CHADEMA imesajiliwa imezaa vyama viwili. SAU imevunjika kutoka CHADEMA, ACT imevunjika kutoka CHADEMA, sasa Chama hiki kingekuwa na Serikali si kingekuwa kimeleta vita kubwa sana ndani ya nchi? Kingeleta vita kubwa ndani ya nchi. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, tunapozungumzia utawala bora tuanze kujitazama sisi wanasiasa, tutazame miongozo na mienendo ya Viongozi wetu. Kuna Vyama hapa vina Mwenyekiti wa kudumu, kila unapokuja uchaguzi Mwenyekiti wa kudumu, Chama cha namna hiyo hakiwezi kujenga demokrasia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie Bunge lako Tukufu kuwaomba Waheshimiwa Wabunge, tukikosoa tuanze kujikosoa wenyewe ndipo tuende tuwakosoe watu wengine tunaotaka kuwakosoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hotuba hizi zote mbili na naunga mkono kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mungu kupata nafasi asubuhi hii ili nami niweze kuchangia Wizara hii ya Maji ambayo nyeti na muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mtera niweze kueleza machache kwa ajili ya Wizara hii ya Maji.

Mheshimiwa Spika, ni maneno mazuri sana yanazungumzwa na Waheshimiwa Wabunge tangu jana mpaka asubuhi hii na wengine wanashauri sasa Serikali hii itolewe ingiizwe Serikali ambayo hamna kitu wala ofisi haina, halafu ilete maji. Vitu vya ajabu sana! Hata aliyeanzisha benki alihakikisha jengo zuri, imara, wahudumu wazuri ili kuweka imani ya watu kuweka hela zao. Lakini hiyo benki nyingine mtu aende akaweke huko, benki ya makuti, ofisi hakuna, matete, haiwezekani. Nadhani alikuwa anajifurahisha, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hilo, kama alivyotoa utangulizi aliyezungumza, na mimi naingia kwenye Wizara ya Maji. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, wanafanya kazi nzuri. Hata katika umri alionao Engineer tunamwona namna anavyohangaika kwenye Majimbo na mpaka Mheshimiwa Aweso anazidi kutoka kipara kwa kujitwisha ndoo za maji, pamoja na Katibu Mkuu Profesa Kitila Mkumbo, tunawashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, Wizara na Maji ni Wizara muhimu sana na kama ikifanikiwa, kwa kiasi kikubwa itapunguza bajeti za Wizara nyingine, maana Wizara hii ni mtambuka, inaweza kusaidia Wizara ya Afya, inaweza kusaidia hata ongezeko la watu mijini. Hivi kwa sisi Wabunge wa vijijini, kwenye vijiji kule hakuna maji, hakuna barabara, hakuna afya, watu wataachaje kuja mjini kuzifuata huduma hizo?

Kwa hiyo, Wizara hii ikiweza kufanya kazi zake sawa sawa, watu wakapata maji safi na salama, baadhi ya magonjwa kama ya matumbo yanafutika kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nataka niishauri Serikali, wakati mwingine ijifunze kupitia vitu vidogo. Nataka nichukue nafasi hii kuwashukuru sana watu wa WFP chini ya uongozi wa dada Neema Sitta kwa kazi nzuri waliyoifanya kwenye Jimbo la Mtera.

Mheshimiwa Spika, hapa Mheshimiwa Waziri akinisikiliza vizuri, anaweza kuona namna ambavyo Serikali wakati mwingine inashindwa kusimamia matumizi mazuri tu. Ikisimamia matumizi mazuri, value for money ikazingatiwa, tutapata maji mengi na kwa uhakika.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano watu wa WFP wametupa shilingi milioni 799 kwenye Jimbo la Mtera. Katika milioni hizo hizo 799 tumepata matenki makubwa matatu ya lita 800,000, tumepata visima 18, tumepata mashamba heka 300 kwa ajili ya umwagiliaji, tumepata visima12 vilivyofungwa solar power kwa ajili ya wananchi kupata maji.

Mheshimiwa Spika, hebu angalia matumizi haya ya shilingi milioni 800 tu hizi kasoro moja yameweza kuleta vitu hivyo vikubwa ambavyo wananchi leo hii wananufaika. Ukija kwenye Serikali, hamna kitu. Inatolewa shilingi bilioni moja pale Mkwayungu kwa ajili ya kujenga bwawa la umwagiliaji, bwawa halijakamilika, hakuna miundombinu na shilingi bilioni moja imeliwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, unaweza ukaona matumizi mabaya kwenye miradi ya maji kwa upande wa Serikali yanatuletea matatizo makubwa. Hawa wameweza kutoa shilingi milioni 800 zimetengeneza mambo ambayo ni maajabu kabisa. Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu na Naibu Waziri piteni mwone kwa macho namna ambavyo pesa ikisimamiwa hata ikiwa kidogo inaweza kufanya vitu vikubwa.

Mheshimiwa Spika, watu wamepata maji ya kunywa, wamepata irrigation wanamwagilia na maisha yao yako safi. Ukienda kwenye Kata ya Fufu katika Vijiji vya Suri, Chibori na Fufu yenyewe, WFP wametufanyia mambo makubwa kwa pesa kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda mahali pengi kwenye miradi ya Serikali, hela nyingi zimetumika, zaidi ya shilingi bilioni moja imeliwa pale Mkwayungu na maji hakuna. Kwa hiyo, nakuomba sana, hebu twende tuangalie wenzetu hawa wamewezaje? Wamefanikiwaje? Wamefunga solar system katika visima vyote. Hakuna mwananchi anayehangaika kutafuta bill ya umeme, kutafuta nini na pampu za kisasa, zinazomwagilia mashamba kwa uhakika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali, tumepata Makao Makuu ya Nchi, haitakuwa na maana kama Mkoa wa Dodoma hautakuwa scheme za umwagiliaji. Vijana wakiweza kumwagilia huko kwenye Majimbo ya vijijini waleta bidhaa zao hapa mjini, zitakuja kuwanufaisha na wao na watoto wao. (Makofi)

Msheshimiwa Spika, Wizara ya Maji ikijitahidi kusimamia resource kidogo iliyopo, nina uhakika inaweza kutosha kutusukuma mbele. Kwa mfano, nimekuja hapa kuomba maji kwa ajili ya vijiji vyangu; Kijiji cha Loji hakina maji, Kijiji cha Ng’aheleze hakina maji, kijiji cha Handali hakina maji. Hivi ni vijiji vikubwa mnoo! Kijiji cha Ng’ng’i leo hii kina wakazi karibu 8,000 lakini hakina maji ya uhakika. Halafu Halmashauri baadhi ya visima vya zamani vikiharibika vinashindwa kuvitengeneza. Kwa hiyo, utakuta kuna matatizo ya visima vya zamani na kuna matatizo ya visima vipya, havipatikani.

Mheshimiwa Spika, naomba sana, Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa kujibu, atupatie maji katika Jimbo la Mtera na atupatie maji katika Kijiji cha Muheme.

T A A R I F A . . .

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, taarifa yake wala siwezi kuikataa, naipokea. Naipokea kwa maana ya kwamba akasimamie na pesa alizosema CAG zimeliwa kwenye chama chake, kama anao uwezo huo akasimamie ili ziweze kuleta maendeleo. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilijua tu, ukisikia kelele ujue tayari tiba. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Mkoa wa Dodoma ambao hamna mito inayotiririka maji kwa msimu mzima, uangaliwe kwa makini hususan katika uchimbaji wa mabwawa. Sisi maji yetu yanapita tu, mvua ikinyesha, yanapita yanaondoka moja kwa moja. Hatuna mito inayotiririsha maji msimu mzima. Kwa hiyo, tunaiomba Wizara ilitazame hilo kama eneo mahususi tukipata mabwawa ya kutosha, tuna uwezo mkubwa sana wa kuzalisha, tuna uwezo mkubwa sana kwa kulima kilimo cha kisasa, tuna uwezo mkubwa sana wa kujisimamia. Tunachotaka Serikali mtuangalie muwe mnafanya research basi, kuna Mkoa huu tofauti yake na Mkoa huu.

Mheshimiwa Spika, WFP wameleta hela kidogo lakini zimefanya mambo makubwa, zimejenga mpaka matanki ya maji ya shule za msingi, hela kidogo hii! Ndiyo maana namwomba Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu na Naibu Waziri watembelee wakaone, siyo vibaya kuona kwa macho na kuja kusimamia pesa zenu mlizonazo ili ziweze kutusogeza mbele. Hata mabwawa ya zamani yaliyochimbwa enzi za Mwalimu Nyerere, leo hii yapo; mengine yameshajifukia. Liko bwawa la Mkulabi hapa Dodoma Mjini, lipo Bwawa Mlowa Bwawani pale. Mwalimu alichimba mabwawa makubwa lakini leo hii hayana maana yoyote.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba sana atakaposimama Mheshimiwa Waziri atusaidie sana kupata maji katika vijiji nilivyovitaja vya Jimbo la Mtera na kuhakikisha kwamba tunapata kilimo cha umwagiliaji. Mbona nimewaomba sana kwenda Mkwayungu kuona ule mradi ambao Serikali imetumbukiza shilingi bilioni moja, lakini hamna kitu chochote? Mbona hamuendi? Twendeni mkaone kwa macho ili mfananishe yale yaliyofanyika pale Mkwayungu na ambayo wenzenu wanaweza kufanya.

Mheshimiwa Spika, tukifanya namna hiyo tutakuwa tunazuia ulaji, tutakuwa tunazuia wizi na umangimeza na nina uhakika Serikali ya Awamu ya Tano itazuia mambo hayo na ndiyo maana nawasihi mfike mwone ufisadi uliofanyika, mchukue hatua ili wananchi wa Kijiji cha Mkwayungu waweze kupata maendeleo kwa kilimo cha umwagiliaji ambacho kilikusudiwa kufanyika eneo lile.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema maneno hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naipongeza sana Serikali kwa kazi nzuri mnayoifanya. Wizara hii lazima iwe na kelele kwa sababu maji ni muhimu sana. Tunataka kuwatua ndoo kichwani akina mama. Tusiwatue wa mijini tu, hebu tazameni na Majimbo ya vijijini jamani. Vijijini nako kuna akina mama wengi wanaoteseka, wanatoa maji mbali, wanachelewa kufanya kazi zao za kujiletea maendeleo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri anafanya ziara mwenyewe anakutana na hiyo hali, tusaidieni na sisi Wabunge wa vijijini. Hawa wa mjini ambao wana lami, wana hospitali nzuri na nini, nao kwa maji wangesubiri kidogo, geukieni upande mwingine.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, ahsante na ninaunga mokono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na namshukuru Mungu kupata nafasi hii ya kuzungumzia taarifa mbili za Kamati. Nitaanza kuzungumzia taarifa inayohusiana na kilimo.

Mheshimiwa Spika, mimi ni Mbunge ninayetokana na wazazi maskini kabisa kwenye Taifa hili. Ukitaja watu maskini wa nchi hii unataja wakulima. Kama kweli tumedhamiria kuwainua wakulima basi ni lazima Serikali ijielekeze walau tuwe na kiwanda hata kimoja cha zana za kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni jambo la aibu sana panga tunaagiza kutoka nje, shoka tunaagiza kutoka nje, jembe tunaagiza kutoka nje, hivi huyu mkulima ambaye tunataka kumuinua tutamsaidiaje kwa karibu kama hatuna uzalishaji wa zana hizo ndani ya nchi? Kwa hiyo, ningeshauri kwamba walau tufufue kile kiwanda cha zana za kilimo Mbeya au tujenge kingine kipya ili mradi uzalishaji wa hizi zana za kilimo upatikane ndani ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nimekuwa nikisema mara nyingi sana kuhusu zao la zabibu. Bahati mbaya sana kila majibu yanapotolewa wanasema zabibu iko katika Bodi ya Mazao Mchanganyiko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zabibu ni zao la kipekee kwa hapa Tanzania linalimwa katika Mkoa wa Dodoma na halilimwi Dodoma yote. Unajua kuna watu hawaelewi wanafikiri Dodoma nzima ukipanda zabibu zinakubali, hapana, zabibu zinalimwa eneo kidogo la Kongwa, baadhi ya maeneo ya Dodoma Mjini, baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Chamwino na Wilaya ya Bahi. Kwa hiyo, unaweza kuona ni muhimu sana hata kutambuliwa tu yale maeneo ambayo zao hilo linastawi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tumekuwa Makao Makuu ya Nchi unaweza kukuta ardhi ileile inayostawi zabibu watu wakaenda kulima na wakaweka vitu vingine tukajikuta hata maeneo tunayotegemea kuzalisha zabibu yakakosekana. Kwa hiyo, kutambua tu peke yake kwamba eneo hili linaweza kustawi zao hili na eneo hili linaweza kustawi zao hili ni jambo zuri na litasababisha wakulima wetu waweze kuinuka na kuendelea kupata uchumi mzuri. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Juma Selemani Nkamia, mdogo wangu kwa siku mbili kwa kuzaliwa. Nikimtangulia mimi kwa siku mbili zinazofuata yeye, taarifa nimeipokea.

Mheshimiwa Spika, haya ndiyo mambo ambayo tunayaelekeza. Mwanzoni kila ukanda ulikuwa una zao lake la biashara, huku wanalima pamba, huku wanalima korosho, huku wanalima kahawa, ule utaratibu ulikuwa mzuri sana kwa sababu wananchi walikuwa wanaangalia ardhi na mazao yanayostawi kwenye ardhi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima tukubaliane dunia nzima ina vitu vikubwa viwili, kuna nuru na kuna giza. Kama unataka kufanya vizuri lazima uvitambue sio kwa sababu humu ndani tuna upande wa Chama Tawala na upande wa Upinzani ndiyo upinge kila kitu. Hivi Mheshimiwa Rais analetewa na Wizara juu ya mchakato wa kufuta shamba fulani ambalo limemilikiwa kwa miaka mingi, watu maskini wa eneo hilo wamekosa maeneo ya kulima, Rais anafuta, leo Mbunge unasimama kutetea kwamba Rais asifute. Mimi sielewi hapa tunatoa wapi hoja hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wabunge wanaokataa maskini wa nchi hii wasipewe ardhi hebu wajitambulishe kwa majina yao na majimbo yao ili wananchi wapate kuwafahamu. Tunaposema Rais anatetea wanyonge tunamaanisha na Mheshimiwa Rais hizi Wizara zote zilizotajwa katika hizi taarifa ni Wizara ambazo zinaweza kumsaidia sana katika vita hii ya uchumi. Maana tunapozungumzia vita hatuzungumzii ya kuuwana moja kwa moja kuna vita ya uchumi sasa, kilimo kikifanya vizuri, viwanda vikafanya vizuri, utalii ukafanya vizuri, maisha ya Watanzania hayatategemea tena wafadhili, tutakuwa huru hata kujitungia sheria zetu wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juzijuzi mmeona umaskini mbaya sana, tunalazimishwa tukubaliane na sheria ambazo zinakiuka hata mila na desturi yetu kwa sababu tu tunasaidiwa. Mambo mengine hata ukiyatazama kwao hao walioendelea kidemokrasia hayapo.

Mheshimiwa Spika, juzi nilikuwa na-Google kama Mheshimiwa Musukuma rafiki yangu kuangalia tangu Uchaguzi Mkuu wa Marekani umepita Hillary Clinton hajafanya mkutano hata mmoja wa kushukuru wananchi lakini ndiyo haohao wa kwanza kusema sisi hatuna demokrasia. Mbona Marekani walioshindwa hawazunguki kufanya mikutano ili kuwashukuru wananchi? Haya mambo unayona kwetu tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kingine, Trump, Rais wa Marekani, hataki ushoga, hakuna mtu anamuuliza, hakuna mtu anampinga, watu wamenyamaza kimya, lakini sisi kwa sababu ya umaskini wetu kila kitu kibaya wanataka kutuletea. Kwa hiyo, Serikali ikijikita kuinua wakulima, kukuza sekta ya utalii tunaweza kupata pesa nyingi ambazo zitasababisha tupange maendeleo yetu wenyewe bila kufuatwafuatwa na mtu mwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi leo hii Wabunge tunazungumzia umeme wa Stiegler’s Gorge wakati tayari saini zimeshawekwa, huu ni utovu wa nidhamu wa hali ya juu sana. Saini zimeshawekwa, mikataba imeingiwa, halafu sisi tunataka kuonesha kwamba eti kuna tatizo, tatizo liko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeelimishwa…

SPIKA: Tena Mheshimiwa Lusinde na Spika nilialikwa nikashuhudia kwa niaba yenu wote. (Makofi)

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Kwa niaba ya Bunge hili. Maana popote anapoalikwa Spika anaalikwa kwa niaba ya Bunge. Kwa hiyo, Bunge lilishuhudia utiaji saini na ujenzi unaanza, tunaanza kuzungumzia eti inawezekana kuna matatizo, jamani tumetumwa au ni akili yetu sisi wenyewe? Mbona tunazungumza kama Bunge la Ujerumani hivi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana Wizara ya Maliasili na Utalii mmeboresha mazingira. Jimboni kwangu kule tembo wameongezeka mpaka juzijuzi walikunywa pombe za wananchi. Kulikuwa na mnada pale tembo wawili wakakuta wananchi wangu wanakunywa, wananchi wakakimbia tembo wakanywa pombe, ilikuwa shughuli. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa sijawahi kushuhudia tembo akilewa balaa lake ni kubwa. Kwa hiyo, tunachokiomba walau Serikali sasa kupitia KDU itengeneze ulinzi wa kuzuia wanyama waharibifu ili wasiwafikie wananchi na kuchukua pombe yao. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru sana Mungu kwa kunipa nafasi ya kuchangia leo katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kunipa afya na kutuwezesha sisi Wabunge kuweza kukutana mahali hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi wamempongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na watendaji wote wanaofanya kazi kwenye ofisi yake na mimi nichukue fursa hii kukubaliana nao. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anazozifanya za kiutendaji lakini tumeona yeye na watendaji wake wakuu wote wakitembea na kuzunguka taifa zima ili kuchagiza maendeleo kwenye nchi yetu, tunasema hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani za pekee zimuendee Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kuiongoza Serikali hii ya Awamu ya Tano ambayo imejielekeza kabisa kwenye kuondoa changamoto zilizokuwa zikiwakabili wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi punde kuna Mbunge ametoka kuchangia hapa akiisifu Serikali ya Awamu ya Nne kwa kazi kubwa ilizofanya. Nina hakika Wabunge wengine watakuja kuisifu Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri inazofanya kwa sababu siyo wote tutaona mara moja, wengine wataona baadaye. Kwa hiyo, nina uhakika hata haya yanayofanyika sasa hivi baadaye watakuja kuyaona na kuyapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nisimame kama shuhuda kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mtera kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano imefanya kazi kubwa kutuletea pesa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Mpwayungu. Wametuletea Sh.1,500,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya pale Mlowa Barabarani njia ya kwenda Iringa. Vilevile upande wa maji wamefanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona Prof. Kitilya Mkumbo akitembea hata yeye kuangalia miradi kadhaa ya maji na kuikamilisha pamoja na Waziri na Naibu Waziri wamefanya kazi kubwa sana kuhakikisha Watanzania wanaondokana na dhiki ya maji. Kwa hiyo, mimi kama Mbunge ninayeongoza wananchi ambao wamechanganyika maskini wengi kuliko pengine matajiri, nachukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayofanya kuhakikisha kwamba nchi yetu inapata maendeleo makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuendelee kuomba mjielekeze zaidi kwenye kumaliza miradi ya maji ambayo haijakamilika. Vilevile kuanzisha visima vipya na kuna maeneo mengine visima vya zamani vimekauka tuweze kuvifufua ili akina mama wasipate adha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo niliamua wakati napewa nafasi hii kwamba nataka kusema na Waheshimiwa Wabunge wote kwa ujumla. Tumekuwa tukipokea misaada mingi sana, mingine kutoka nje lakini sisi wenyewe pengine Bunge hili lilishawahi lenyewe kujinyima fursa halafu likachukua pesa zake za Bunge tukaenda kununua madawati. Napongeza sana Bunge kwa uamuzi ule ambao tulijinyima tukasema tuchukue hizi pesa twende tukanunue madawati ya watoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema maneno haya? Nasema maneno haya kwa sababu tumepata misaada mingi sana ya kusaidia jamii yetu lakini sasa naomba Taifa hili hebu na sisi tujinyime jambo moja ili tuweze kutoa msaada mkubwa sana kwa nchi yetu. Jambo lenyewe ni hili, ukisoma kwenye ukurasa wa 7 utaona kuna mafanikio lakini ukienda kwenye hotuba ya Waziri Mkuu ukurasa wa 17 kuna habari za Tume ya Taifa ya Uchaguzi inategemea kuongeza vituo 858, hivi vituo vinavyoongezeka bado tunaongeza gharama kubwa kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini nachotaka kushauri? Tumeona uchaguzi mwingine tunaoufanya na wenzetu wamelalamika sana kwamba wakati mwingine tunaingia gharama kubwa bila sababu, naomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote hivi kwa nini mwakani tusifanye uchaguzi wa Diwani na Mbunge tu Rais tukaacha apite bila kupingwa? Kwa nini tusifanye hivyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tutakuwa tumeokoa fedha nyingi wakati Rais anaapishwa tumkabidhi cheque ambayo Taifa hili limeokoa ili Rais aende akatumie hizo fedha kuondoa matatizo ya maji na barabara vijijini. Kuna faida gani kwenda kupoteza pesa chungu zima kwa uchaguzi wa Rais, Rais ambaye hana mpinzani? Hii ni kwa sababu tumeona hata mshindi wa pili aliyepata kura 6,000 ameunganishwa na 8,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndugu zangu nataka niwashauri, naomba mitandao yote na wanazuoni wote hoja hii naiweka mezani tuangalie faida ambayo tunaipata na hasara zake tupime. Jamani sisi ni Wabunge tuliotokana na familia maskini, tusijisahau tunaongoza watu maskini; watu maskini wakati mwingine huwa wanajadili katika milo mitatu ambayo ni haki yake anaamua kukata milo miwili anakula mlo mmoja, sisi kwa nini tusile mlo mmoja? Tule mlo wa Udiwani na Ubunge, kwenye Urais tumuache Mzee Magufuli apite bila kupingwa. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi aliyoifanya Rais ni kubwa, Taifa hili sasa na lenyewe lijinyime kwenye upande huo badala ya kupoteza pesa bila faida tumkabidhi Mheshimiwa Rais pesa ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya uchaguzi wake tumwambie Rais kamata cheque hii ondoa shida ya maji kwa Watanzania. Mshindi namba mbili Ulipo Tupo tayari tayari yupo kule kule na Walipo Tupo wamemfuata huko huko, hivi kweli kuna chama nchi hii kinaweza kutengeneza mgombea Urais kwa miezi tisa (9) akamshinda Magufuli jamani? Ukweli tuuseme, haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, badala ya kupoteza muda mimi nawakaribisha tuje tushindane kwenye Ubunge na Udiwani, kwenye nafasi ya Urais tumpe heshima huyu mtu amefanya kazi kubwa. Ameonyesha kwamba yupo tayari kuondoa changamoto za Watanzania, kusimamia pesa za Watanzania na kuhakikisha mambo yanakwenda.

WABUNGE FULANI: Katiba.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Hiyo Katiba ni ya kwetu sasa tuangalie faida ya Katiba na umaskini wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua kuna Wabunge wengine humu wanapiga kelele Katiba, kwa sababu Majimbo wanayoongoza hayana watu maskini lakini sisi ambao tunaongoza watu maskini ukiwauliza, ndiyo maana nimesema tujadiliane, naomba tujadiliane hasara na faida ya kufanya huo uchaguzi kwa sababu kwa vyovyote vile hakuna mtu atakayeweza kusimama 2020. Mimi naweka wosia kwenye Bunge hili siyo tu akamshinda, akamtikisa Mzee Magufuli, hayupo! (Makofi)

(Hapa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge waliongea bila utaratibu)

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa sababu hiyo hatuna sababu ya kutumia mabilioni ya pesa kwenda kupoteza muda na kitu ambacho tuna uhakika. Katiba ni yetu, matatizo na changamoto ni zetu, tupime kama Watanzania. Ndiyo maana nimesema naruhusu mjadala huu na naomba Wabunge mtulie nasema makubwa sana hapa, mnaweza mkapata matatizo wengine hapa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza na nchi, tuangalie kwa namna nchi yetu ilivyo, ufadhili tunaopokea, na sisi tutoe ufadhili kwa nchi yetu. Tutakumbukwa kwa kitendo hicho kuliko kwenda kupoteza pesa bila sababu yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri Mkuu lakini nilikuwa nataka kuweka hoja hii mezani Watanzania waijadili waone faida na hasara zake halafu waamue kuniunga mkono au wasiunge mkono. Naunga mkono hoja hii asilimia mia. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutuzawadia tena pumzi yake leo bure ili tuweze kukaa kwenye Bunge lako Tukufu na tuweze kuchangia hoja za Wizara mbili; ile ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na ile ya Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wamesema juu ya Waheshimiwa Watendaji Wakuu wa Wizara hizi; nami nachukua fursa hii kuwapongea sana ndugu yangu Mheshimiwa Selemani Jafo, Waziri; pamoja na Mheshimiwa George Huruma Mkuchika, Waziri; pamoja na Waheshimiwa Manaibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa; pamoja na ndugu yangu Mheshimiwa Waitara na Naibu Waziri mwenzake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mawaziri hawa wanafanya kazi kubwa sana. Tunaona namna wanavyopambana na shida za watu wetu, siyo vizuri sana kuwavunja moyo, wakati mwingine tuwapongeze kwa kazi nzuri wanazozifanya. Mheshimiwa Jafo pamoja na timu yake ya Watendaji wametusaidia sana sisi wa Jimbo la Mtera kutuletea pesa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Mpwayungu. Wametupa shilingi milioni 700 pale, wakatupa shilingi bilioni 1,500,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya; vilevile wametusaidia miradi ya maji yenye thamani karibu ya shilingi bilioni mbili hivi na ushee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunawashukuru sana ingawa nina ombi maalum kwa ajili ya ambulance ya Tarafa ya Mpwayungu, ilipata ajali na ikachakaa kabisa, lakini tunamshukuru Mungu haikuua. Tunaomba tusaidiwe kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Tarafa ya Mvumi, kile Kituo cha Handali ili kwa kushirikiana na Kituo cha Mpwayungu, hospitali ya wilaya iweze kupumua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile timu ya ukaguzi wa zahanati, naomba Mheshimiwa Jafo hii aitilie maanani sana. Huko vijijini kuna zahanati nyingine hazina sifa hata za kung’oa meno, lakini wanang’oa meno. Hatujui vile vifaa kama viko katika hali ya ubora. Kuna magonjwa mengi sana ya kuambukiza ambayo ni hatari sana kama zahanati zile hazikugaliwa sawasawa hasa kwenye upande wa tiba ya kinywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno mengi yemezungumzwa, nami bahati nzuri nimepewa kazi ya kupiga penalty ya mwisho. Unapopiga penalty ya mwisho lazima uwe umetulia. Ndugu zangu tunapozungumzia habari ya utawala bora kwanza tukubaliane mambo ya msingi. Utawala Bora, vyama vya siasa vinashindana kwa sera. Kila chama kinapeleke sera kwa wananchi kwenda kuomba kichaguliwe. Uchaguzi Mkuu umepita, chama kilichochaguliwa ni CCM, ndiyo kimechaguliwa kwa wingi. Chama hiki hakichaguliwi kwa rangi zake tu, kinachaguliwa pamoja na ubora wa sera zake. CCM ndiyo inapewa nafasi Serikali itafsiri ilani yake kwa miaka mitano bila kujali kwamba Jimbo hili la CHADEMA wala Jimbo hili la NSSR, wala Jimbo hili la chama gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilani inayotekelezwa pale ni ilani ya mshindi wa ujumla. Wapinzani wanapewa kazi ya ku- oppose, kuleta sera mbadala kama wanazo, lakini wetu hawa kwa sababu hawana, ndiyo maana mnasikia madudu haya. Kama wangekuwa na sera mbadala, wangekuwa wanaeleza kwa hoja. Unasikia hoja, hivi ni Serikali gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi namwombea sana Mheshimiwa Rais, Mungu ambariki aendelee kutumia hekima. Nyie Mawaziri, mwendelee kutumia hekima. Hivi ni Waziri gani anatukanwa, anasemwa vibaya halafu tena anatakiwa apeleke maendeleo kwenye Jimbo la huyo anayemtukana? Hii iko Tanzania tu. Ndiyo maana mnaona tunapata tatizo kwa sababu uchaguzi ukiisha, wale walio shinda ndio wanakuwa na kazi ya kutafsiri ilani yao ya uchaguzi kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo upinzani wa Tanzania mnaona wanapiga kelele, wanataka kufaidi kwenye kushindwa. Mimi sijawahi kuona. Ninyi mmeshindwa, mnataka kufaidi nini? Mmeshindwa, lazima m-face problem, lazima m-face utulivu, lazima mkae muwaache walioshinda watekeleze ilani ya uchaguzi. Sasa leo eti timu imefungwa bao tatu bila, hiyo hiyo inataka ishangilie. Nyie mbona mnachekesha! Mimi sijawahi kuiona hii. Hii naiona Tanzania tu. Mtu anasimama anasema, ohoo, tunanyimwa hiki, tunanyimwa hiki. Si mmeshindwa, mtulie. Lazima... (Makofi)

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Bwege kaa chini, Mheshimiwa Lusinde endelea.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ndiyo maana unaona kunaundwa Kambi ya Serikali na Kambi Rasmi ya Upinzani na wanaundwa Mawaziri wa Serikali na Mawaziri Kivuli. Leo wanaona aibu hata kutaja Wizara zao, kwamba huyu ni Waziri Kivuli. Hawasemi, kwa sababu wanajua kivuIi hakiaminiki. Nani ataamini kivuli? Wanajua kivuli saa sita kiko sawa na mtu, saa saba kinaanza kuwa kirefu, saa 12 kivuli ni kirefu kuliko mtu, wanajua. Wewe uliwahi kuona wapi Mbunge unasimama unampangia Mheshimiwa Rais kitu cha kufanya? (Kicheko/Makofi)

Jamani hii nchi mbona hatuna heshima, unampangia Rais kwamba akija kwangu afanye moja, mbili, tatu, hivi nyumbani kwako hata baba yako mzazi unaweza kumpangia wewe kwamba, leo baba tule hiki, inawezekana? Haiwezekani, kwanza hamjasoma vizuri Katiba ya nchi, Rais wa nchi ni mkuu wa nchi, Rais wa nchi ana madaraka makubwa ambayo hata kikatiba hajayatumia, mnapiga kelele; Rais hayo madaraka yake akiyatumia hamponi ninyi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana mimi sasa nawaomba Watanzania hebu mwakani tukubaliane, unajua wakati mwingine kuwahi sana nalo ni tatizo, kuwahi sana nayo ni shida.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaambiwa kwamba, kuwahi sana ni tatizo. Tunaambiwa hata mtoto wa kike wakati mwingine asubiri akomae via vyake vya uzazi ndio abebe ujauzito, kinyume cha hapo ataugua. Upinzani wa Tanzania uliwahi sana, kwa hiyo, nahisi umepata matatizo, uliwahi sana. Kwa hiyo, sishangai kuwaona Kambi nzima ya Upinzani badala ya kujenga hoja za kisiasa zenye muelekeo wa kusisimua Serikali mnaleta hoja za udumavu; angalia upinzani ulivyodumaa kwa sababu ya kuwahi, wamewahi sana kabla ya wakati wao wamejikuta wamedumaa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natangaza kwenye Bunge hili, tatizo tulilonalo tuna upinzani mdumavu. Wamedumaa kisiasa, wamefika mahali hawawezi kujenga hoja mbadala, kazi yao ni kulalamika na kupiga kelele kama unavyowasikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri nchi yetu Mheshimiwa George Mkuchika kwenye utawala bora ashikilie hapohapo. Hakuna nchi yenye utawala bora usio na mipaka, haipo duniani. Wameng’ang’ana wanataka kufanya maandamano ya nini? Mbona mazoezi asubuhi hawaendi sembuse maandamano? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna Serikali ya namna hiyo duniani, uruhusu watu wafanye fujo tu. Eti mtu anasema ooh, mimi nataka niende nikahutubie mkutano, wewe jimbo lile umeshindwa ukahutubie kitu gani? Utaeleza nini? Huna sera, huna ilani, huna kazi unayoifanya pale unataka ukahutubie ueleze nini? Kama sio kufanya kampeni kabla ya wakati? Ninyi mnataka mpate ruhusa ya kwenda kufanya kampeni kabla ya wakati, sisi ndio washindi jamani tunashindwa hata na Miss Tanzania? Kachaguliwa mrembo mmoja, wengine wote wamekaa kimya, wamekaa kimya, lakini hawa wanashindwa; sisi ndio washindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakasikia kadada kamoja kanasema Lusinde nakupenda, tulia dawa iingie. Mimi nina mke na watoto watano, tukikutana nao kwenye chai wanaongea maneno ya unafiki kabisa, ooh tunaunga mkono, mnachapa kazi vizuri, tunaunga mkono. Tukija humu ndani wanajifanya ooh, Mwenyekiti patachimbika, pachimbike kwa hawa? Hakuna kitu cha kuchimbika hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali ishikilie hapohapo. Angalia kuna watoto wanawaona wanavyozomea, wanawaona ni watu wamechanganyikiwa kabisa. Humu ndani ya Bunge kuna watu wanakuja kujifunza uendeshaji bora wa Bunge, wao wameongea sisi tumenyamaza…

MBUNGE FULANI: Umechanganyikiwa wewe.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: …sisi tunawapa dawa, ooh, ooh. Watoto wadogo hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakusihi, tunaomba Serikali kwenye kusimamia sheria isiangalie huyu mpinzani, isiangalie huyu CCM, wote kula kichwa, wakivuruga amani weka ndani, hizo siku 120 walizosema ni kidogo. Kwa hiyo, nataka nikwambie dawa yake ukitaka nchi inyoke, sheria zifanye kazi asiwepo mtu wa kubembelezwa. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hiyo dawa kuingia naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya asubuhi ya leo ili na mimi niweze kuchangia hili Fungu 28 la Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Spika, Wabunge wengi wamempongeza sana Mheshimiwa Waziri Kangi Lugola pamoja na Naibu wake Masauni pamoja na Katibu Mkuu na watendaji wote wa vyombo vya ulinzi na usalama walioko chini ya Wizara hiyo wanafanya kazi nzuri sana. Mimi niwe shuhuda tu kuthibitisha kwamba Jeshi la Polisi, Magereza na Uhamiaji ni miongoni mwa vyombo muhimu sana kwa ajili ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, wakati tunajadili leo, kuna tofauti kubwa sana kati ya mjadala wa leo na mjadala wa jana Waheshimiwa Wabunge mtakubaliana nami. Jana tulifikia mahali hata kuambiwa kwa nini mnawapa pole Polisi ya kung’atwa na mbu wakati ni kazi yao. Sasa mimi nikawa napata taabu sana, hii ni kazi ya kizalendo, si tu kazi yao kazi wanayoifanya ni ya kizalendo ambayo ina mazingira magumu yanayohitaji kupongezwa.

Mheshimiwa Spika, aliyesema maneno hayo akasema ninyi wengine hamjawahi kulala hata ndani ninyi, wewe si umelala ndani kwa kujitakia mwenyewe? Kwani ukiwa hutaki kulala ndani utalala ndani jamani! Siyo rahisi, maana Polisi wanashughulika na watu waovunja sheria. Polisi hawashughuliki na kila mtu barabarani hapa, ingekuwa kila mtu basi kakamatwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nature ya chombo chenyewe tunachokijadili, kwanza ni chombo chenye mafunzo, lakini chombo kina watu wanahenya, kuna watu wanasoma na kuhenya juu.

Mheshimiwa Spika, unajua hapa Wabunge, Bunge lililopita muliamua wewe na Mheshimiwa Spika Anna Makinda, tukaenda JKT, tulikwenda na mdogo wangu Mheshimiwa Neema hapa, nadhani tulijifunza kidogo utofauti wa hivi vyombo, kwa hiyo, nataka nikupongeze Mheshimiwa Neema kwa ajili ya ukakamavu, kumaliza. Jamani counter ya jeshi la polisi haiwezi kufananishwa na counter ya hoteli, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, counter ya polisi lazima umkute mtu ana sura ya jiwe, ametulia, anakusikiliza umasema nini, ya hoteli utamkuta mtu anatabasabu, karibu, chumba kipo, hiyo ni ya hoteli, siyo polisi! (Makofi/Vicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, polisi lazima wawe wakakamavu, siyo kitu cha mchezo.

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Tena ndiye ninayemtaka huyo.

SPIKA: Wewe unampa taarifa Lusinde, haya toa taarifa. (Kicheko)

T A A R I F A

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, mzungumzaji anayezungumza, ni vizuri tukaweka rekodi sawa hapa, anayesema hajanitaja lakini najua ananisema kwa hiyo, lazima niweke rekodi sawasawa. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, na ni rafiki yangu, hoja niliyozungumza jana kwamba polisi wanatimiza majukumu yao, Serikali huwa inatoa nafasi za kazi, mtu yeyote anapokwenda kuomba kazi yoyote huwa wanajua consequences zake, anajua polisi wana kazi gani, Askari wana kazi gani.

Mheshimiwa Spika, hata wewe hapo unafanya kazi ya kizalendo, tunategemeana kama Taifa. Tulichokizungumza jana, na nilivyosema jana wengine hamjalala polisi, na nimetoa ushahidi kwamba nimesingiziwa nimelala kwa makosa. Kwa hiyo, ninachotaka kusema, kufanya kazi ngumu kisiwe kisingizio cha kuvunja sheria, hiyo ndiyo hoja tunayoizungumza, lakini siyo kwamba tunadhalilisha kazi ya polisi.

MWENYEKITI: Mbona unahutubia sasa si taarifa iwe fupi!

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, ndiyo hiyo.

SPIKA: Mchungaji ahsante sana, Mheshimiwa Lusinde unapokea taarifa!

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, ukipenda kachumbali upende na pilipili. Watu wote, wanaofanya upinzani kwenye maeneo yao, wote wanaingia kwenye matatizo! Mheshimiwa Zitto alijaribu kufanya upinzani ndani ya CHADEMA, kumpinga Mheshimiwa Mbowe, yupo CHADEMA? Amemalizwa, ameondoka, alijaribu Kafulila, yupo salama CHADEMA! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, muelewe kazi mnayoifanya ina hatari yake, ndiyo ninachotaka kukwambia ukweli hapa, yaani huwezi ukajiita upinzani, yuko wapi, Mheshimiwa Komu alijaribu juzi kumteta Mwenyekiti na mwenzake, wako wapi! Kwa hiyo, ninachotaka kusema, hamuwezi kuwa wapinzani, halafu mkawa salama tu, haiwezekani! (Makofi/Vicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka niwasaidie, kwamba kazi wanayoifanya ni kazi inayoweza kuwapa matatizo wakati wowote! (Makofi/Vicheko)

MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, nitulie kaka yangu kasimama amua.

SPIKA: Mheshimiwa Komu, nini tena rafiki yangu! (Kicheko)

T A A R I F A

MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Haya, dakika moja bwana maana yake tunakaribia mwisho.

MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa taarifa Mheshimiwa Lusinde, ambaye tuna historia nzuri sana na yeye kwa sababu tumemkuza sisi na anajua. Sasa nipo, na sijazurika, sijateteleka, nipo, maana yake yeye amesema yuko wapi, nipo hapa. (Makofi)

SPIKA: Ila jambo moja tu, hajakanusha kama alimteta Mwenyekiti wake. (Makofi/Vicheko)

Mheshimiwa Lusinde, endelea!

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, nilichotaka kusema, kwanza namheshimu sana kaka Komu na ni mmoja wa watu waaminifu sana na alichokuwa anakisema Komu kwa kweli, naweza nikakiamini kwa upande wangu, kwamba kweli kuna matumizi mabaya ya ruzuku mle ndani. Na yeye ndiye aliyekuwa mhasibu wa chama, kwa hiyo, hata, alichofanyiwa alisema ameonewa. Nilitaka kumuonyesha Mheshimiwa Msigwa, kwamba wanaoonewa hawako huku tu, hata ndani ya chama chenu mnaonea watu, mmojawapo mmemuonea Mheshimiwa Komu! Mheshimiwa Komu amesema, kuna matumizi mabaya ya ruzuku, amevuliwa nafasi zake zote, ameonywa, yuko kwenye uangalizi hapo alipo. Sasa hii siyo sawa na Mheshimiwa Kubenea, (Makofi/Vicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jeshi la polisi linafanya kazi nzuri sana. Niombe Waziri wa Mambo ya Ndani, nichukue fursa hii kumpongeza sana Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Mroto. (Makofi/Vigelegele)

Mroto anafanya kazi nzuri, jeshi la polisi ni beat, huwezi kucheka na waharifu, kwamba hapa kuna Bunge, Wabunge wanavaa cheni za dhahabu kama unavyowaona wengine humu, halafu Mroto acheze na maandamano maandamano hapa, Wabunge mtaporwa hizo cheni. (Kicheko)

Kwa hiyo, Mroto anaposema hataki mchezo watu watachakaa, yuko sahihi kwa ajili ya kuwalinda ninyi. (Makofi/ Vigelele)

Mheshimiwa Spika, jeshi la polisi kazi zake nyingi, kazi za operation, kwa hiyo, tunaomba Makao Makuu yamehamia hapa Dodoma na jeshi la polisi liimarishwe hapa Dodoma! Wapeni magari ya kufanyia kazi, njia nzima ya kutoka Dodoma kwenda Iringa, kuna vituo viwili tu vya polisi navyo vyote havina gari na wanapita Wabunge wengi, wanapata matatizo huko, kwa hiyo, wapeni, wapeni magari waweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Mtera tuna Tarafa tatu, tumeomba pikipiki tatu tu Mheshimiwa Kangi, mpaka leo! Tusaidieni, ili wale polisi waweze ku-move kwenda sehemu moja hadi nyingine. Majuzi hapa kuna mtu alijinyonga, ilichukua karibu siku nzima, mtu kuweza kufika pale, polisi hana pikipiki, hana nini mpaka Mbunge nimetoa gari kwa ajili ya kwenda ku-rescue hiyo situation. Kwa hiyo, sisi tunaomba jeshi la polisi liimarishwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine ambalo limezungumzwa hapa, mikutano ya hadhara, kuna mikutano ya hadhara kama mtakumbuka Waheshimiwa Wabunge, kila mkutano ulikuwa unasababisha mauaji! Iringa alikufa mtu, Morogoro alikufa mtu, Singida alikufa mtu, ni mikutano gani hiyo, Arusha, mikutano hiyo imetuletea matatizo. Kwa hiyo, jeshi la polisi wakati mwingine linapima, hivi kama Bungeni tu tunaongea kwa mihemko hivi, Mbunge anaongea mpaka anasema rubbish, jana hapa. Sasa unajiuliza huyo Mbunge akiwa kwenye mkutano wa hadhara wa kwake binafsi ataongea maneno gani huyu! Lazima jeshi la polisi lipige marufuku, jamani uchaguzi ukishakwisha siasa zinahamia humu, nje tuache watu wachape kazi, tutakutana 2020! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimewaambia siku zote nazidi, unajua wakati mwingine huwa natema madini sijui kama huwa mnasikiliza, uchaguzi ukiisha, mnaachia washindi wafanye kazi waliochaguliwa, na washindi ni Chama cha Mapinduzi. Wapeni nafasi watekeleze Ilani, maswali mtatuuliza mwakani kama yapo, na nina uhakika yatakuwa hayapo, vituo vya afya vinajengwa, maji yanapatikana, sasa kutakuwa na maswali gani tena, hakuna! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nasema, baadhi ya Askari wachache ambao wametajwa, kwamba siyo waaminifu, hao waendelee kuchukuliwa hatua, kama sheria inavyosema, lakini tusiliharibu jeshi la polisi lote kwa sababu ya mtu mmoja kakosea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jamani ikitokea bahati mbaya Padre, au Shekhe kakamatwa ugoni, siyo dini mbaya, haiwezekani, ni huyo huyo aliyeshikwa, dini inaendelea kuaminika, dhehebu linaendelea kuaminika ila yeye aliyevunja masharti ya imani yake huyo ndiye anayechukuliwa hatua. Tusiwatukane Askari wote kwamba wote hawafai, wote wanakosea, hapana, lakini kuna mambo yamezungumzwa.

Mheshimiwa Spika, jana kilizungumzwa kitu hapa na nataka nikiseme, kwenye taarifa ya CAG iliguswa hapa jana kwamba, Mbunge wa CHADEMA alikopeshwa fedha za kununua gari. Nasema, jambo lile lina harufu ya ukwepaji wa kodi, kwa nini nasema hivyo, Wabunge tuna exemption, leo CCM wakinitumia kununua gari la chama, maana yake CCM wanataka kukwepa kodi, kwa sababu wanajua mimi nitasamehewa kodi fulani, lakini ukiniambia kwamba eti alikopeshwa na chama, halafu ameshindwa kulipa chama kimemnyang’anya, si kweli, hapo CHADEMA msikwepe mlitaka kuwepa kodi! (Makofi)

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu.

SPIKA: Nini tena Chief Whip!

KUHUSU UTARATIBU

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, jambo analolizungumza rafiki yangu anayeongea sasa hivi, Mheshimiwa Chenge akiwa kwenye Kiti chako, alishatolea uamuzi na hiyo hoja anayoisema haiko kwenye taarifa ya CAG! (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Selasini ni hoja gani.

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, ni suala la Mbunge wa CHADEMA kukwepa kodi. Sasa CAG hakuliweka hivyo, hoja ni kwamba kuna gari lilinunuliwa kwa mkopo kutoka CHADEMA na ile gari iko kwa jina la mwanachama, haliko kwenye jina la Baraza la Wadhamini la chama. Kwa hiyo, agizo ni kwamba lile jina liondoke kutoka kwenye jina la mwanachama liende kwenye jina la Baraza la Wadhamini na siyo kukwepa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na Mheshimiwa Chenge akiwa kwenye kiti chako alitoa hiyo ruling.

SPIKA: Hivi huyo mwanachana ni nani!...

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, huyu mwanachama hatajwi, huyu mwanachama ni Mbunge, Mbunge, siyo mwanachama wa kawaida, na CHADEMA ituambie kabla ya mwaka huu, au mwaka gani iliwahi kumkopesha mtu fedha ya kununua gari, wakati Wabunge wote tunakopeshwa hapa! Jamani kuna harufu ya kukwepa kodi, ndicho ninachosema na niko wazi, niiteni popote hata kwenye maadili niiteni nithibitisha, nyie mnataka kukwepa kodi kwa kumtumia Mbunge mwenye exemption! Ninyi siyo watu wasafiki kiasi hicho! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumze kuhusu mauaji, jeshi la polisi…

SPIKA: Mheshimiwa malizia.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, jeshi la polisi tunaliomba sana. Kuna watu wengi tu, siyo wale wanaotajwa maarufu, kwamba wameuawa taarifa zao hazipo, wako wengi, nina mjomba wangu anaitwa Nikanoli, amepotea tangu mwaka 1979 mpaka leo. (Kicheko)

Tunaomba jeshi la polisi lipewe vifaa vya kisasa vyenye weledi ili viwasaidie katika uchunguzi hasa wa mauaji, hasa wa mauaji. Watanzania wengi, siyo hawa tu wanaotajwa, wako wengi ambao wamepotea wengine wameuliwa, bila sisi kujua wala bila familia zao kuelewa.

Mheshimiwa Spika, lakini la mwisho kabisa, niombe suala la uraia limezungumzwa sana, hili suala halijawahi kujadiliwa humu Bungeni, lakini kwa kuwa limeanza kusemwa humu, tuombe mamlaka za Serikali zilifanyie kazi. Watu wamezungumza sana kuhusu wafanyabiashara maarufu, kuna siku hapa ametajwa Vedagri wa Mwanza ni mfanyabiashara mkubwa amewekeza sijui Mafya, wapi, Mwanza, hawa watu wote ambao wengine siyo maarufu wakulima ambao wanataka kuhamia nchi hii wapewe huo uraia, kama ni haki yao na kama kuna matatizo vyombo vichunguze, viangalie ubaya wao, viwakatalie kama ambavyo wengine wamewahi kukataliwa bila kusemwa Bungeni na wengine wamewahi kupewa bila kusemwa Bungeni, Serikali iendelee kuchapa kazi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mungu sana kwa kupata fursa hii ya kuchangia Wizara ya Nishati, lakini zaidi sana nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa mchango.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kukupongeza sana, unapokaa kwenye kiti chako Bunge linaendeshwa kisayansi na linaendeshwa kwa utulivu mkubwa sana. Wabunge tunaheshimiana na kuthamini kila mchango wa Mbunge anayesimama na hivi ndivyo inavyotakiwa iwe hata kwa wenzako wengine wote unaowaachia nafasi ya kiti wanatakiwa kwa kweli kulinda heshima ya Bunge na hasa pale Mbunge anaposimama na kutoa mawazo yake ambayo pengine wewe unaona kwako hayakufurahishi lakini ni lazima umpe nafasi ya kumsikiliza na zogo la Bunge la juzi halikuwa jambo zuri sana.

Mheshimiwa Spika, nitoe pongezi sana kwa Mheshimiwa Waziri Dkt. Mendrard Chanancha Matogolo Kalemani pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Subira Mgalu pamoja na Katibu Mkuu na timu nzima ya Wizara. Watu hawa wanafanya kazi kubwa ya kuzunguka nchi nzima, lakini kubwa zaidi kwao hawa wawili ni mahusiano mazuri na Waheshimiwa Wabunge. Hili ni jambo zuri sana, lazima kujenga PR ya pamoja maana hii kazi ni ngumu, kazi inahitaji ushirikishwaji na ushirikiano wa karibu.

Mheshimiwa Spika, vilevile spidi ya Mheshimiwa Waziri na Naibu wake naiona ni kubwa kuliko spidi ya makandarasi, yaani Waziri anagawa umeme kwa spidi sana kuliko wajenzi, kama ni forward wakati mwingine unasema inaweza ikaingia kwenye nyavu yenyewe ikaacha mpira nje, sasa kidogo hapo inatupa mazingira magumu sana.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie Jimbo la Mtera katika tarafa zangu tatu, Tarafa ya Mvumi Mission, Tarafa ya Makangwa na Tarafa ya Mpwayungu. Tunavyo vijiji ambavyo bado havijafikiwa umeme, lakini kama unavyojua ukijua kulaumu ujue na kushukuru. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kufikisha umeme kwa mara ya kwanza katika Tarafa ya Mpwayungu katika Kijiji cha Nagulo na Kijiji cha Mpwayungu chenyewe.

Nimwombe sana vile vitongoji anavyovitaja, vijiji anavyovitaja kwamba umeme hautamruka mtu, wale watu wanaorukwa wote kimbilio lao ni kwa Mbunge. Kwa hiyo unajikuta Mbunge anafanya kazi kubwa sana baada ya Waziri kuondoka, wakisema mbona Waziri alisema tusirukwe, sasa kwa nini tunarukwa. Kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake na timu nzima washughulike kwa namna ya pekee kuhakikisha kwamba yale maeneo waliyoagiza maagizo yao yanatekelezwa.

Mheshimiwa Spika, ukisoma ilani za hivi vyama ambavyo vina Wabunge humu unaweza ukacheka sana. Nimepitia ilani ya CHADEMA hapa sioni mahali wameahidi megawati 18,000 alizokuwa anazisema mzungumzaji wa CHADEMA, kwa hiyo unaweza ukaona wakati mwingine maneno haya yanayozungumzwa ni maneno ya kufurahisha tu Bunge. Unajua faida kwenye uongozi wa nchi wakati mwingine haionekani moja kwa moja…

T A A R I F A

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Esther.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa Mheshimiwa Lusinde taarifa kwamba wakati Mheshimiwa Silinde anachangia alisema trilioni sita ambazo zinatarajiwa kujenga Stiegler’s Gorge zikilinganishwa na extension one ya Kinyerezi ambayo inajengwa kwa bilioni ambazo ni megawati 185 equivalent yake ni ya kujenga megawati 18,500, hakusema inatokana na Ilani ya CHADEMA.

SPIKA: Mzungumzaji pia hajasema hivyo kama inatokana ameuliza tu kwenye ilani yenu hakuona. Endelea Mheshimiwa Lusinde.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, shemeji yangu Matiko nataka nimsaidie tu kwamba unajua wakati mwingine faida kwenye shughuli za Serikali haifananishwi na faida ya genge la nyanya au pengine mgahawa. Huwezi ukaiona moja kwa moja wakati mwingine unaona MSD wananunua dawa nyingi mpaka zile za ugonjwa wa Ebola, sio mpaka wasubiri ugonjwa uwepo ndio wanunue.

Kwa hiyo, wakati mwingine tunasema kwa nini dawa zina-expire zina-expire kwa sababu zilikuwepo na ugonjwa haukutokea, sasa huwezi ukangoja mpaka utokee ndio uanze kununua. Kwa hiyo kuongoza Serikali tunawafundisha tu, ni mambo makubwa sana, huwezi kufananisha na biashara ya genge au mama ntilie, kwa hiyo kuna faida unaweza ukazitafuta kwa macho usizione.

Mheshimiwa Spika, nimezungumzia sana kuhusu kuwabana wakandarasi ili waendelee kusambaza umeme katika vijiji vyote. Tumeona namna ambavyo…

T A A R I F A

SPIKA: Mheshimiwa Lusinde unapewa taarifa na Mheshimiwa Getere.

MHE.BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji anayeongea kwamba CHADEMA katika miaka ijayo itakapokuwa kwenye madaraka tutahakikisha tunafanya utafiti wa kina kuhusu vyanzo mbalimbali vya nishati hatimaye kutunga sera ya kupata nishati hizo. Kwa taarifa kamili ni kwamba mpaka leo CHADEMA haina chanzo cha nishati, kwa hiyo anachosema Silinde ni sawa tu.

SPIKA: Mheshimiwa Lusinde, tafadhali.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, nimesema kuongoza nchi faida zake ni wananchi kunufaika. Sisi Rais wetu na Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kujitoa muhanga kujenga kinu cha kufua umeme katika maporomoko ya Rufiji. Haya ni maamuzi makubwa ambayo impact yake itaonekana wakati Watanzania watakapoanza kunufaika na ndio maana hakuna Mbunge humu ndani anayesimama na kusema umeme huo nisipewe humwoni. Kwa hiyo ni kweli kwamba Serikali imepatia na iendelee kujenga huo umeme ambao utatunufaisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu sasa kwenye vijiji ambavyo vilikuwa vimesahaulika kabisa, tumeona mawaziri wetu wakiwasha umeme mpaka kwenye nyumba za nyasi, nyumba za tembe, kule waliko Watanzania, hili ni jambo jema. Tumeona umeme unawashwa mpaka Loliondo, kwa babu wa kikombe, hili ni jambo jema. Kwa hiyo nataka nimsihi sana Mheshimiwa Waziri aendelee.

Mheshimiwa Spika, nimeachiwa hapa taarifa na jirani yangu na mimi ni mtu muungwana Mheshimiwa Mwamoto amesema nizungumzie habari ya Kata ya Image. Kwa bahati nzuri naomba ku-declare interest, Kata ya Image ndiko nilikoolea mimi, Waziri apeleke umeme kwa wakwe zangu pale Image katika Jimbo la Kilolo na wakwe zangu nao kule wafurahie waseme na mzee alitaja ili mtoto wao aendelee kubaki mikono ni mwangu. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwenye suala la kuongoza nchi ni suala ambalo hata wenzetu wameonyesha kwamba kuna kipindi unahesabu faida, ukiona faida ni kubwa unachukua huo huo uamuzi. Tumeona CHADEMA ni chama cha kidemokrasia na maendeleo lakini tumeona demokrasia hawaitendi, wana Mwenyekiti ana miaka 20 kwa sababu gani, pengine wanaona kuna faida kubwa kuendelea na huyo Mwenyekiti. Kwa hiyo wakati mwingine huwezi kuona faida ya moja kwa moja mpaka watu wakuelimishe kwamba hapa sasa unatoka kwenye reli. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika,Jambo lingine ambalo naliona hapa naona hapa tunazungumzia madeni ya TANESCO. Mheshimiwa Waziri hapa nataka anisikilize kwa makini sana. TANESCO imekuwa na madeni makubwa sana…

SPIKA: Mbona hakuna anayesimama upande huu huo msumari. (Kicheko)

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, TANESCO ina madeni makubwa sana na madeni haya yanatokana na capacity charge za makampuni, makampuni haya matatu yanaipa mzigo mkubwa sana TANESCO. Kuna IPTL, kuna Aggreko, kuna Symbion, haya makapuni kila kampuni moja kwa mwaka linaitia deni TANESCO karibu bilioni 635, sasa hii si sawa. Serikali iondoe haya makampuni, iondoe mitambo yao, wanaipa TANESCO madeni makubwa sana, wanaagiza mafuta, wanaagiza vitu gani, matokeo yake ni kwamba tunapoteza fedha nyingi na tunaipa TANESCO mzigo mkubwa sana wa madeni.

Mheshimiwa Spika, vilevile ukiangalia kwa hesabu tu za shule ya msingi ukiondoa mitambo ya haya makampuni matatu utaokoa karibu trilioni mbili, maana ni trilioni moja na bilioni 930 na kitu, kwa hiyo utakuwa umeokoa karibu trilioni mbili. Hii itasaidia sana kuboresha uendeshaji wa TANESCO na wao watafika mahali watafanya kazi zao vizuri.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nimeona linatupa tabu, umeme ukikatika kutokana na mvua inawachukua muda mrefu TANESCO kwenda kushughulikia kwa sababu tuna umeme sehemu nyingi vitendea kazi vichache, magari machache ya TANESCO, mafundi wachache sasa wanachukua muda mrefu na kupoteza muda mrefu na kupoteza fedha nyingi, maana hivyo vijiji vina wateja tayari.

Mheshimiwa Spika, nimeona kuna kipindi Ndebo walikosa umeme, Mvumi Mission walikosa umeme inachukua mpaka wiki moja na nusu sasa hii si sawa, tuwarahisishie, aidha kwenye maeneo ambayo wanaona udongo wake haustamili sana wakati wa mvua wapitishe umeme chini au wanaweza kutumia umeme wa nguzo za zege, ukitumia umeme wa nguzo za zege ukazipitisha umeme juu maana yake eneo hilo hata kama mvua ikinyesha zege lile linazidi kujiimarisha.

Mheshimiwa Spika, tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano, haya maamuzi wanayoyafanya ni maamuzi ya utekelezaji wa Ilani ya Chama chetu. Hatuwezi kurudi nyuma kwa sababu tuliwaahidi Watanzania na wenzetu hawa ambao wanatupinga nao ni maamuzi ya chama chao, lakini hakuna mmoja hapa anayesema hataki umeme, sisi tuendelee kuwahudumia na wao kwenye majimbo yao tuwahudumie. Tunapopitisha hii bajeti tunapitisha pamoja na kusaidia majimbo ya Upinzani wa nchi hii kwa sababu kule kuna Watanzania, tunawahudumia Watanzania.

Mheshimiwa Spika, tuwahudumie wananchi wote kwa sababu mwakani nataka nikuhakikishieni kutakuwa na mabadiliko makubwa sana kupitia hii Wizara ya Nishati, Watanzania wamewashiwa umeme mpaka vijijini kitu ambacho kilikuwa ni ndoto, mwakani wanakwenda kuitunza Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa kuipigia kura ambazo hazijawahi kupigwa kwenye Bunge hili, ambazo hazijawahi kupigwa kwenye nchi hii kwa sababu kazi iliyofanyika. Umeme uzuri wake ni kitu kinachoonekana kwa macho, kwa hiyo kila wanapokwenda akina Mheshimiwa Subira tunawaona na wananchi wanavyowapokea tunawaona, hawawezi kuwashangilia vile halafu kesho wakatunyima kura, haiwezekani! Kwa hiyo wanatufanyia kazi njema sana, wanatupa hoja za kwenda kuyasemea hata majimbo yao kwa sababu wanawasikia wanavyokataa bajeti wanawasikia, wanavyokataa umeme wanawasikia, lakini sisi wana CCM kwa sababu tumebeba dhima ya kuongoza Taifa hili tunapeleka umeme nchi nzima bila kujali Mbunge wa Jimbo hilo kasema nini humu ndani ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe sana kazi ya kusambaza umeme iongezeke nguvu, vinginevyo kama Waziri atatuhakikishia kwamba anayo awamu nyingine ya nne, lakini kama ni awamu zile zile tatu maana yake hii ndio finally. Sasa kwenye finally kusiwe tena na kulegalega maana wametuambia kuna REA awamu ya kwanza, awamu ya pili na ya tatu, hatuna REA awamu ya nne. Kwa hiyo speed yao lazima iwe kubwa kuhakikisha kuwa mambo yanafanyika na yanafanikiwa ili kutupa hoja za kwenda kuwaambia wananchi umeme upo au haupo, wanasema upo, piga kura kwa Magufuli, shughuli imekwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesema gharama za kuendesha nchi ni kubwa, umeme wa maji utatuletea punguzo kubwa sana la gharama na hivyo kuifanya nchi yetu iweze kusonga mbele. Kwa hiyo naomba sana Mheshimiwa Waziri atakaposimama hapa vijiji vyangu avikumbuke; nimeomba umeme Kijiji cha Huzi, Kijiji cha Manda, Kijiji cha Ciifukulo, Kijiji cha Muheme, Kijiji cha Mpwayungu umalizike pale na Mvumi Mission tuhakikishe maeneo yote Chihembe yanapata umeme na kule nilikozaliwa mimi ili wananchi wenzangu waweze kupata maendeleo.

Mheshimiwa Spika, leo tumeona saluni zinafunguliwa vijijini, tumeona watu wanachomelea madirisha vijijini, tunaona vijana wanajiajiri kwa kupitia sekta hii ya umeme. Kwa hiyo niombe sana Mheshimiwa Waziri atakaposimama atuhakikishie kumalizika kwa REA III itakuwa ni lini ili vijiji vyote viweze kupata umeme na mambo yaweze kwenda.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia hoja hiyo hapo juu hasa nijikite katika masuala ya miundombinu ya barabara zote za Jimbo la Mtera zilizopo TARURA. Mwaka huu 2018 mvua zimeharibu sana barabara zote, naomba Mheshimiwa Waziri atusaidie kupata fungu la matengenezo ya uhakika wa barabara hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atupatie majibu ya uhakika kuhusu ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka barabara kuu ya kwenda Iringa pale Mlowo barabarani mpaka Mvumi Mission Hospital kama ambavyo Mheshimiwa Waziri aliwaahidi wananchi wa Jimbo la Mtera mwaka 2015. Naomba kujua ni lini barabara hiyo itajengwa? Ahsante.
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda nimshukuru Mungu kwa kunijalia zawadi ya uhai na afya njema ili na mimi niweze kusema machache juu ya mchango wangu kuhusu Muswada wa Upatikanaji wa Taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichukue fursa hii kuipongeza sana Serikali kwa kuuleta Muswada huu. Kabla ya Muswada huu, suala la kutoa taarifa halikuwa la lazima. Mtu angetaka kutoa anatoa; hataki, anakaa hivyo hivyo; lakini leo kwenye Muswada huu Afisa analazimishwa kutoa taarifa kama sheria tutakavyoipitisha. Kwa hiyo, tunaipongeza sana Serikali kwa uamuzi wake wa kuleta Muswada huu Bungeni ili watu wasitafute habari kwa kuomba, wasitafute habari kwa hisani, bali wazitafute habari kisheria. Hili ni jambo zuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi yanazungumzwa humu ndani kwamba Katiba inatoa haki, ndugu zangu, Waheshimiwa Wabunge, Katiba haifanyi kazi ya utendaji wanaotenda ni watu sio Katiba yenyewe ndiyo inayotekeleza. Leo Katiba inasema kila Mtanzania ana haki ya kuishi popote, lakini Rais au Waziri mwenye dhamana ya makazi ana uwezo wa kusema watu watoke hapa kuna mafuriko wakati Katiba haisemi hivyo. Kwa hiyo, tusiishi kama tumejifungia; maana yake kila mtu hapa anasema Katiba, Katiba. Katiba haitekelezi, Katiba ni sheria mama ya nchi. Zinatungwa sheria kutafsiri Katiba na ndiyo kazi ambayo tunataka kufanya hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasikitika sana ninapoona watu wanakimbilia kujificha kwenye Katiba. Katiba haitekelezi, wanatekeleza watu na hao watu wanaweza kutekeleza kitu ambacho kiko kwenye Katiba. Leo hii hapa tuna jengo la Bunge, lakini pakipita mafuriko litahama, hata kama imeandikwa hivyo kwenye sheria kwamba jengo la Bunge liwe hapa. Kwa hiyo, watu waelewe tu kwamba hapa tunatunga Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa na hakuna sehemu tunapokwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hakuna sehemu tunapokwenda kinyume.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona Waheshimiwa Wabunge wanajaribu kuwatisha baadhi ya Mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hivi kumbe ninyi mngeshinda nchi mngetunga sheria ambazo zingewa-favour akina Lowassa? Sheria ni msumeno, inatakiwa ikate kote kote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kama kuna mtu alikuwa Waziri akaivunja sheria amefungwa ni sawasawa. Hatutungi sheria kwa ajili ya wananchi tu; tunatunga sheria kwa ajili ya Watanzania wote na sisi wenyewe. Sasa naona kuna mtu anasimama anasema, shauri yenu, akina Mramba walikuwa hapo, leo wamefungwa. Hata ninyi mtafungwa, hata sisi Wabunge tutafungwa, hata mimi nitafungwa. Sheria inataka kila mtu aitekeleze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbe wenzetu wangepata Serikali hawa, wangetunga sheria za kukandamiza wananchi, wao zisingewahusu. Ndiyo maana mnaona kila wakisimama hapa, wanajaribu kukutisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wanajaribu kukwambia eti leo hii Lowassa anapigwa mabomu, angepigwa mabomu angekuepo? Amepigwa gesi za kutolea machozi, siyo bomu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusidanganyane hapa! Watu wanaowazungumza, hata kukimbia hatua tano hawawezi, apigwe bomu ataweza kuvumilia yule? Acheni mambo ya kudanganya kwenye Bunge hapa. Tusidanganyane! Watanzania lazima tuelewe, tunapotunga sheria na Wabunge tuelewe, hatuwatungii watu, tunajitungia na sisi wenyewe, hili ndiyo nataka lieleweke.
Kwa hiyo, isije ikafikiriwa kwamba kuna kundi tu tunalolilenga, hapana. Kumbe wenzetu wametupongeza kwamba Serikali ya CCM inatenda haki, inatunga sheria zinazowalamba mpaka Mawaziri, wametupongeza. Hizi tuzichukulie kama pongezi kabisa, kwa sababu leo hii kila kitu wanataka kiandikwe kwenye Katiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kuna Chama kimoja, Mwenyekiti wao anadaiwa, walikutana kikao kujadili deni, kwenye Katiba yao imeandiwa wapi? Imeandikwa wapi? Wapi kwenye Katiba yao imeandikwa Mwenyekiti akidaiwa mtaacha shughuli zote mkutane kwenye kikao kujadili deni? Kwa hiyo, kuna mambo mengine ya utekelezaji yanafanyika nje ya hizo Katiba kwa sababu ya hali halisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa namna unavyoliendesha Bunge kisayansi na linavyokwenda. Nataka niseme leo, tajiri hanuniwi! Ukimnunia tajiri, inakula kwako. Kwa hiyo, hizi siku mbili mnazowaona watu wana uhuru fulani wanazungumza humu ndani, ndiyo uhuru umepatikana hivyo. Kwa hiyo, tuendelee kuwavumilia, tutakwenda nao vizuri tu hawa wa kwetu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya adhabu; hakuna sheria inayoweza kutekelezwa kama haitoi adhabu. Haiwezekani. Sheria yoyote ili itekelezwe, ni lazima iwe na adhabu. Kwa hiyo, kama kwenye sheria hii kuna mtu ataikosea sheria, atakwenda jela miaka mitano, iko sawa. Kumbe tutatungaje sheria bila kuweka adhabu? Hiyo sheria itatekelezwaje sasa? Sheria ili itekelezwe ni lazima iwe na upande wa kuadhibu ili watu tuogope; ili watu waogope. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kusimama hapa na kusema upatikanaji wa habari ni haki ya Kikatiba. Kweli ni haki ya Kikatiba, lakini kwa mfano, kama mtu nyumbani kwake hajanunua redio, hana betri, anapataje habari? Hawa watu wa ajabu sana! Ni haki kweli, lakini kuna haki ambazo ni lazima uzigharamie. Leo upatikanaji wa habari, huna TV, huna umeme unapataje hiyo habari? Wenzetu wanalazimisha, ooh, ni haki ya Kikatiba, haki ya Kikatiba, sasa Serikali igawe TV nchi nzima, Serikali igawe redio nchi nzima, igawe betri nchi nzima? Kwa hiyo, kuna vipande kwa vipande. Kuna haki na kuna wajibu. Uko wajibu! Ukitaka habari, ni lazima uwe na wajibu. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tusitake kutumia fursa hii kudanganya. Zipo haki zimetajwa kwenye Katiba, lakini uko wajibu. Kila Mtanzania ana haki ya kuishi, lakini ana wajibu wa kulima ili apate chakula kitakachomfanya aishi. Sasa kama hafanyi kazi, hapiki chakula, anaishije? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tusidanganye watu kwa kutumia kisingizio cha Katiba, inatoa haki, Katiba inaminywa. Katiba inatoa haki na Katiba hiyo hiyo inatoa fursa. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, watu wakikusonga sana, jua uko sahihi. Kwa hiyo, wewe endelea kufanya kazi zako, ndiyo maana unaona wanasimama wanakushutumu. Mawaziri endeleeni kupiga kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kila mtu akisimama hapa, mnataka kupotosha watu kwamba Mheshimiwa Rais amekataza kufanya mikutano!
Hakuna mahali Mheshimiwa Rais amekataza kufanya mikutano. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila Mbunge anatakwa kufanya Mkutano kwenye Jimbo lake. Kilichokatazwa ni kuendelea na kampeni kwa tabia ambayo tulikuwa tumezoea. Uchaguzi unaisha, watu wanaendelea na kampeni miaka mitano, hiyo ndiyo haikubaliki. Mbunge gani, wa Jimbo gani, kaenda kufanya mkutano kwenye Jimbo lake akakatazwa? Nani? Hakuna mahali. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa walikuwa wameshazoea. Watanzania kwa sasa hivi hawana nafasi ya kupokea tena maneno, wanataka kupokea maendeleo, siyo maneno. Maneno mengi yameshazungumzwa, maneno mengi yameshasemwa, nyimbo nyingi zimeimbwa mpaka nyingine zimezuiwa kuimbwa, sasa hivi ni wakati wa kufanya kazi, siyo wakati wa maneno kama walivyokuwa wamezoea hawa.
Kwa hiyo, mkisikia wanalaumu, ooh, Mheshimiwa Rais ametukataza kufanya mkutano; wewe Jimbo lako la Tarime, nani kakukataza kufanya mkutano? Nenda kahutubie wananchi wako waliokuchagua, isipokuwa kutoka Tarime unafunga safari kwenda Mpwapwa; Mpwapwa wana kiongozi wao waliomchagua, acheni afanye kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho leo nataka nikiseme, kauli ya Mheshimiwa Rais imewaumiza baadhi ya watu. Walikuwa wanatumia ruzuku vibaya, wakati huo wanajifanya kuna operesheni sijui nini; sijui operesheni ndorobo; sijui operesheni nini, kumbe wanakula hela za wananchi kwa kutumia mgongo wa operesheni. Sasa hiyo hakuna. Hakuna nafasi hiyo, kila Mbunge afanye mikutano kwenye Jimbo lake, ahamasishe maendeleo, shughuli za maendeleo zifanikiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuja kumsingizia Mheshimiwa Rais kwamba kazuia mikutano, siyo sahihi, lazima tuliweke vizuri jambo hili. Ulaji wa ruzuku kupitia vyama vya siasa umezuiwa, ndiyo maana mnaona kelele. Maana ilikuwa saa hizi unaona maspika yamefungwa, bendera zimefungwa; wapi? Mtera, kufanya nini? Mtera kuna Mbunge wake, mnakwenda kufanya nini? Miezi mitatu imepita tumefanya uchaguzi, leo hii tuendelee tena kuwajaza watu maneno? (Makofi)
Ukisikia kelele, ujue tayari!
MWENYEKITI: Ahsante. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru sana Mungu kupata nafasi hii, ya kutoa mchango kwa ajili ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa. Nikushukuru kwa sababu nilikuwa miongoni mwa wajumbe wa hiyo Kamati ambayo walichakatachakata kidogo na ndio maana unaona hata namna yangu ya kuzungumza sasa ni ya Kisheria zaidi kuliko ambavyo siku zote huwa nazungumza kwa verse za kisiasa zaidi. Kwa hiyo, leo nitajikita kwenye kuongea kwa Kisheria na kushawishi Wajumbe, Waheshimiwa Wabunge, waiunge mkono hoja hii kwa ufasaha wake. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwanza nishukuru sana Serikali kwa kuleta Muswada huu kwa wakati huu muafaka kabisa, Muswada umelenga kuviimarisha zaidi Vyama vya Siasa, kutoka kwenye vingine kuwa Vyama shinikisho kuwa Vyama vinavyotetea hoja ndogondogo na kwenda kuwa Vyama vya Kisiasa kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu, tunaishukuru sana Serikali kwa kuleta Muswada huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ujio wa Muswada huu, na namna ambavyo tulisaidiana sana na Wanasheria kama Kaka yangu Mheshimiwa Ally Saleh alikuwepo hapo, walikuja wakina Mheshimiwa Zitto Kabwe na wote tulitoka mle tukiwa tumekubaliana kwamba Muswada huu sasa uende kama ulivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini nasema hivi, kuna vipengele hapa ukiondoa kimoja unaharibu maudhui yote ya Muswada mzima, kwa hiyo, ndio maana tunasema Muswada huu upite kama ulivyo kwa sababu vipengele vinabebana na kuleta maana kulingana na umuhimu wa Muswada. Na hii maana yake nini? Wanasiasa Watanzania sasa tukomae, tufahamu kwamba nchi hii ina Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wazee wetu wametetea uhuru wa nchi hii na Sheria peke yake zinatungwa ndani ya Bunge, sio kwenye korido za Mabalozi tusiende kuwapotezea muda Waheshimiwa Mabalozi tukafikiri labda kwenye korido zao ndio zinatungwa Sheria, hapana, Sheria ya nchi hii inatungwa ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitaka niwakumbushe tu, maana kuna wengine mpaka viatu vilishaisha soli kila siku Ubalozi huu, Ubalozi huu kuzungumzia Muswada huu. Huu Muswada sasa unataka Vyama Misaada yote ambavyo Vyama vitapata, Serikali ijue Misaada hii ina lenga kuimarisha nini kwenye Chama hiki. Maana yake nini? maana yake Muswada huu sasa unakiimarisha Chama, unajua anayetunza mara nyingi kwenye ngoma ndio anachagua wimbo, sasa ukiacha Vyama vipewe pesa, bila Serikali kujua maana yake wale wanaotoa pesa ndio watachagua nyimbo za kuimbwa na hivyo Vyama, Muswada huu unakataa hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Muswada huu unavitaka Vyama kutambua nembo za Kitaifa, hivi kuna ubaya gani? Waheshimiwa, utambue Mwenge wa Uhuru, utambue Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huu Muswada watu wanauzungumzia juu juu hawajaingia ndani, huu Muswada unakwenda kuviimarisha Vyama vya Siasa Tanzania, kuzungumzia mambo ya msingi ya Kitaifa. Ndio maana nimesema vipengele vyake vyote vilivyomo humu vipitishwe kama vilivyo, Muswada huu unakwenda kumpa nguvu Msajili sasa, Msajii alikuwa akihudhuria Mikutano Mikuu ya Vyama vya Siasa kama mwalikwa tu, lakini Sheria haimtambui. Sasa anahudhuria na kusimamia demokrasia kuona inafanyika ndani ya Vyama hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajabu sana, Watu wanasema oooohh! Muswada huu unampa Mamlaka makubwa Msajili ya kumbana Mwanachama mmoja mmoja, jamani, kama Shirikisho la Mpira tu Duniani linaweza, mpira una adhabu zake, una kadi ya njano, una kadi nyekundu lakini mpira huo huo, unakufungiwa maisha, kwa hiyo shabiki ambaye atakuwa anakiuka mambo yaliyowekwa kwa ajili ya kuhakikisha mchezo wa mpira wa mguu unafanyika salama, sasa itakuwa sembuse kwenye Chama cha Siasa! Chama cha Siasa lazima kiwe na Sheria ambayo inawatazama Wanachama, na sasa Watu wajue uhuni tena kwenye kufanya mambo ya siasa haupo, sasa tufanye kwa ukomavu huku tukijua kwamba kuna Sheria inayo tu-guide kuhakikisha kwamba tunatekeleza mambo haya kwa kufuata utaratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nishukuru sana, kwa namna ambavyo Muswada umeletwa na namna ambavyo vipengele muhimu vimewekwa kama ulinzi na usalama, Watu wanapotosha wanafikiri Muswada huu unakataza Mtu kulindwa, hapana mlinzi wa kwako binafsi wa kumuajiri kutoka group four ukamlipa Mshahara kitambulisho kikapelekwa kwenye Wizara ya Kazi kwamba nimemuajiri mlinzi Muswada haukatazi, haukatazi, hakuna mahali Muswada huu unakataza mlinzi binafsi, tusipotoshe, huu Muswada unakataza vikundi vya Kijeshi vya Ulinzi, ambavyo vilikuwa vinapewa mafunzo porini tunavijua kwa hiyo tunasema Muswada huu haujamkataza Mtanzania kulindwa. Naomba utulie, tulia, mama watoto tulia, tulia, mimi nakujua, huyu ni mama watoto wangu kwa hiyo achana naye. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, eehe! Jamani mambo ya mapenzi hayaingii kwenye Chama jamani.

Mheshimiwa Spika, ulinzi binafsi mtu akatazwi, anaruhusiwa kujilinda, yeye mwenyewe kwa kuajiri mlinzi lakini sio chama, kianzishe kundi la vijana kiliite Kundi la ulinzi hiyo Muswada huu umekataza, kwa hiyo mimi nimesimama hapa kusema mambo ya msingi kwanza Muswada huu umetambua nembo za Kitaifa, Mwenge wa Uhuru pamoja na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitaka Muswada huu uspite bila kusema, kwamba Sheria sasa zinatungwa, sisi ni nchi huru jamani na wote diplomasia waliokuwa kwenye nchi yetu watuheshimu kwamba hili ni Taifa huru linajifanyia mambo yake lenyewe na hatujawahi kuingilia nchi yoyote kwenye kutunga Sheria za nchi zao, nilitaka niseme kwa sababu
wenyewe wapo, wasikie kwamba Mbunge amesisitiza watuachie uhuru wetu na sisi tutaheshimu uhuru wa nchi zao, na Waheshimiwa Wabunge wajue Sheria zinatungwa ndani ya Bunge sio kwa Mabalozi, hayo nilitaka yaeleweke vizuri halafu mambo ya vifungu sasa nawaachia Wanasheria asante sana.

Mheshimiwa Spika, naunga Mkono hoja. (Makofi/ Kicheko)