Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Capt. Abbas Ali Mwinyi (6 total)

MHE. KAPT. ABBAS ALI MWINYI aliuliza:-
Ndege za Serikali aina ya Fokker 50 iliyoletwa nchini mwaka 1992 na Fokker 28 iliyoletwa nchini mwaka 1978 ni chakavu na teknolojia zake zimepitwa na wakati. Aidha, Kampuni iliyotengeneza aina hizo za ndege imeshafungwa hivyo upatikanaji wa vipuri vya ndege hizo kuwa mgumu na gharama kuwa kubwa.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuzibadilisha ndege hizo na kuleta mpya?
Je, ni lini Serikali itarekebisha hali ya hanger la kuegeshea ndege za Serikali?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimwa Kepteni Abbas Ali Mwinyi, Mbunge wa Fuoni lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli ndege aina ya Fokker 28 na Fokker 50 zina umri mkubwa. Hata hivyo kiutaalamu usalama wa ndege huwa haupimwi kwa miaka iliyonayo bali hupimwa kwa masaa iliyoruka. Hivyo, kwa hali ya kawaida muda wa masaa ya ndege kuwa chakavu (beyond economic benefit) ni masaa 90,000 na kati ya ndege hizi mbili hakuna hata ndege moja yenye masaa zaidi ya 15,000. Aidha, ndege hizo zimekuwa zikifanyiwa matengenezo kwa kuzingatia ratiba.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa ndege ya Fokker 50 ipo kwenye ubora wa kutumika na inaendelea kuhudumia viongozi wetu. Ndege ambayo haitumiki ni Fokker 28 kwa sababu ina matatizo ya breki na engine ya kulia. Serikali imewasiliana na mtengenezaji ili kuweza kutatua matatizo hayo. Ndege hizi mbili bado zina teknolojia ya kisasa na zimekuwa zikipelekwa kwenye matengenezo ya lazima kwa mujibu wa matakwa ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA). Kimsingi vipuli vya ndege hizo bado vinapatikana.
Mheshimiwa Spika, Kampuni ya kutengeneza ndege hizi haijafungwa bali wamesimamisha utengenezaji wa ndege mpya na wanaendelea kutoa huduma ya matengenezo (maintenance support) kwa zile ndege ambazo zimekwishawahi kutengenezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, Serikali inatambua changamoto za karakana ya kutengeneza ndege za (TGFA) kutokana na uchakavu. Tayari nimeshawaagiza Wakala wa ndege za Serikali TGFA kufanya tathimini ya gharama halisi zitazotumika kwa ajili ya kukarabati Karakana hiyo. Gharama halisi zitakapopatikana, Serikali itafanyia kazi marekebosho ya hanger hilo. Ahsante. (Makofi)
MHE. JUMA OTHMAN HIJA (K.n.y. MHE. CAPT. ABBAS ALI MWINYI) aliuliza:-
(a) Je, Mfuko wa Bima ya Afya una wanachama wangapi na ni asilimia ngapi ya Watanzania wamejiunga na bima hiyo?
(b) Je, kwa nini baadhi ya hospitali, hasa za binafsi, hazikubali malipo kwa kutumia kadi hizo za Bima ya Afya?
(c) Je, Mfuko wa Bima ya Afya umefikia malengo ya kuanzishwa kwake?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kepteni Abbas Ali Hassan Mwinyi, Mbunge wa Fuoni, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ulianzishwa mwaka 2001 kwa Sheria Sura ya 395. Hadi kufikia Juni, 2018 Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ulikuwa una wanachama wachangiaji 858,137 ambao wanaufanya mfuko kuhudumia jumla ya wanufaika 3,918,999 sawa na 7% ya Watanzania wote. Katika kipindi hicho hicho Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ulikuwa na jumla ya wanufaika 13,398,936 sawa na 25% ya Watanzania wote hivyo, kufanya wananchi wanaonufaika na Mpango wa Bima ya Afya nchini chini ya NHIF na CHF kufikia 17,317,935 sawa na 32% ya Watanzania wote, lengo la mfuko ni kufikia 50% ya Watanzania wote ifikapo mwaka 2020.
(b( Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya hospitali zinakataa kadi za NHIF kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo hospitali kutosajiliwa na mfuko, kufutiwa usajili na kufanya vitendo vya udanganyifu na kukataa bei za huduma za NHIF.
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unahudumia watumishi wote wa umma, kama ilivyokusudiwa wakati wa kuanzishwa kwakwe pamoja na kuchangia kwa kiasi kikubwa kwa rasilimali fedha katika sekta ya afya, mfano, zaidi ya 80% mpaka 90% ya mapato ya vituo vya kutolea huduma za afya zinategemea fedha za NHIF.
Hata hivyo, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unaendelea kutekeleza mkakati wake wa kuongeza wigo wa wanachama kwa kuandikisha makundi mbalimbali katika sekta rasmi na isiyo rasmi, ikiwemo wajasiriamali wadogo wadogo na watoto chini ya miaka 18 chini ya Mpango wa Toto Afya Card na makundi ya wakulima kupitia Mpango wa Ushirika Afya ambao mpango huu ulizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Waziri Mkuu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kahama, Shinyanga, hivi karibuni.
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD (K.n.y. MHE. ABBAS A. H. MWINYI) aliuliza:-

Changamoto za Muungano wetu bado zipo licha ya vikao vya Kamati za pamoja kati ya SMT na SMZ kukutana mara kwa mara:-

(a) Je, ni changamoto zipi zilizopata ufumbuzi tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani?

(b) Je, changamoto hizo ni ngapi?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abbas Ali Hassan Mwinyi, Mbunge wa Fuoni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2015 mpaka 2019 Serikali ya Awamu ya Tano iliyoingia madarakani, changamoto mbili zimepatiwa ufumbuzi. Hoja zilizopatiwa ufumbuzi katika kipindi cha Serikali Awamu ya Tano ni utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia na kutoa VAT kwa asilimia sifuri kwa umeme unaouzwa na TANESCO kwa ZECO ikiwa ni pamoja na kufuta deni la kodi ya VAT lililofikia shilingi bilioni 22.9 kwa umeme uliouzwa kwa ZECO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi hizo, Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuitisha vikao vya kisekta, kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizobakia na zinazoendelea kujitokeza. Sekta hizo ni Sekta ya Fedha, Uchukuzi, Biashara, Mifugo, Uvuvi na Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja zilizojadiliwa ni pamoja na Taarifa ya Mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha, hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na mgawanyo wa mapato yanayotokana na faida ya Benki Kuu, usajili wa vyombo vya moto, upatikanaji wa fursa za masoko Tanzania Bara, ushirikiano kati ya Taasisi ya Viwango na Zanzibar (ZBS) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) na Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Zanzibar (ZFDA), ZBS kupatiwa nakala ya usaili kiwango cha Afrika Mashariki ili kurahisisha usaili wa kiwango hicho kwa wakati; Leseni za viwanda, Zanzibar kuwa designated member country wa mashirika ya African Regional Intellectual Property Organization (ARIPO) na World na World Intellectual Property Organisation (WIPO) na upatikanaji wa fursa za miradi inayohusisha maendeleo ya viwango na ubora wa bidhaa kwa maendelo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo miradi inayohusu maendeleo ya wajasiriamali na kuzuiwa kwa bidhaa ya maji ya kunywa inayozalishwa Zanzibar kuingia Tanzania Bara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali zote mbili za SMZ na SMT zimeendelea kuhakikisha kuwa makubaliano yaliyofikiwa na pande mbili yanatekelezwa na kuhakikisha kuwa changamoto zinazojitokeza zinashughulikiwa ipasavyo.
MHE. CAPT. ABBAS ALI MWINYI Aliuliza:-

(a) Je, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ina Taasisi ngapi na zipi zina uwezo wa kujiendesha zenyewe?

(b) Je, ni zipi kati ya Taasisi hizo zinapeleka gawio Serikalini?

(c) Je, gawio ni takwa la kisheria?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu Swali la Mheshimiwa Captain Abbas Ali Hassan, Mbunge wa Fuoni lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inasimamia jumla ya Taasisi 25, kati ya hizo, Mamlaka za udhibiti zipo nne, Taasisi za Utendaji zipo 14, Bodi za Usajili wa Kitaalamu zipo tatu, Vyuo vya Mafunzo ya Kisekta viwili, na Mabaraza ya Walaji ni mawili. Aidha, kuna Vyuo vya Mafunzo ya Kisekta vinne vinavyosimamiwa moja kwa moja na taasisi za kiutendaji. Kati ya hizo, jumla ya taasisi saba zinajitegemea. Taasisi hizo ni TASAC, TCAA, LATRA, TPA, SINOTASHIP, KADCO na CRB.

(b) Mheshimiwa Spika, Serikali ni mmiliki katika Taasisi na Mashirika ya Umma kwa kuwa imewekeza kiasi kikubwa cha fedha. Umiliki wa hisa unatofautiana kulingana na kiasi cha mtaji kilichowekezwa. Kuna taasisi zinamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 na nyingine chini ya hapo.

Mheshimiwa Spika, mchango hutolewa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha, Sura Na. 348 ambayo inataka taasisi ambazo shughuli zake zinahusisha kukusanya maduhuli ya Serikali, kutoa asilimia 15 ya makusanyo ghafi kwa mwaka kama mchango wake katika Mfuko Mkuu wa Serikali. Aidha, Mashirika ambayo hufanya biashara na Serikali ni mwanahisa mwenza, yanapaswa kutoa gawio kwa serikali kama mbia katika biashara hiyo. Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi isipokuwa TAZARA na SINOTASHIP zinamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100. Taasisi hizi mbili ndizo zinapaswa kutoa gawio Serikalini na zilizobaki zinatakiwa kutoa mchango kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Hata hivyo, kutokana na utendaji usioridhisha, TAZARA imekuwa haitoi gawio la asilimia 50 inayopaswa kutolewa kwa Serikali ya Tanzania. SINOTASHIP ambayo Serikali inamiliki asilimia 50 imekuwa inatoa gawio Serikalini.

Aidha, Taasisi nyingine zilizobaki chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi zimekuwa zinatoa michango yao kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Taasisi ambazo zimekuwa zinakusanya maduhuli na kutoa asilimia 15 ya mapato yao ghafi kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali ni pamoja na LATRA, TASAC, TCAA, TPA, TAA na KADCO. Taasisi zilizobaki hazizalishi mapato na nyingine zimekuwa zinapata ruzuku kutoka Serikalini.

(c) Mheshimiwa Spika, suala la utaratibu wa matumizi na mgawanyo wa gawio na michango ni la kisheria. Suala la gawio limeainishwa kwenye Sheria ya Makampuni Sura Na. 212 ambapo faida inayopatikana baada ya kutoa matumizi yote, Serikali hupata gawio kulingana na kiwango cha hisa kilicho kwenye Kampuni au Taasisi husika. Ahsante.

Mheshimiwa Spika, ahsante.(Makofi)
MHE. CAPT. ABBAS ALI MWINYI aliuliza: -

Je, Serikali imewekeza kiasi gani cha fedha katika ununuzi wa ndege 11 za ATCL na ni lini uwekezaji huo utarudisha fedha zilizowekezwa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu, nikiwa kwenye nafasi hii ya Naibu Waziri kwenye Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, kwenye Sekta ya Uchukuzi, napenda nimshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kupitia mtumishi wake Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuniona na kuniteua kwamba nimsaidie kwenye Sekta hii ya Uchukuzi. Naahidi kwamba nitafanya kadri ya uwezo wa Mwenyezi Mungu lakini pia kwa nguvu, weledi na uadilifu mkubwa. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizi, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, napenda nijibu swali la Mheshimiwa Abbas Ali Mwinyi, Mbunge wa Fuoni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Ndege za Serikali kwa maana Tanzania Government Flight Agency-TGFA imewekeza kiasi cha Shilingi trilioni 1.44 katika ununuzi wa ndege 11 ambapo, kati hizo, ndege mbili ni za safari za masafa marefu aina ya Boeing 787-8 Dreamliner, Ndege nne ni za safari za masafa ya kati aina ya Airbus A220- 300 na ndege Tano za safari za masafa mafupi aina ya De Havilland Dash 8 Q400.

Mheshimiwa Spika, biashara ya usafiri wa anga faida yake haitokani na uendeshaji wa ndege zinazotumiwa na Kampuni katika kutoa huduma zake tu, bali hutokana pia na mchango wake katika ukuaji wa sekta nyingine za kiuchumi kama utalii, viwanda, madini, kilimo, mifugo, uvuvi, biashara, kuitangaza nchi kimataifa na kuwezesha usafirishaji wa abiria na mizigo ndani na nje ya nchi. Aidha, ATCL imeleta ushindani mkubwa na kuzuia upandaji wa nauli katika usafiri wa anga.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuchangia kwenye ukuaji wa Sekta nyingine, ATCL imeendelea kujiendesha kibiashara na kupunguza utegemezi kwa Serikali kwa kuanzisha vitengo vya kibiashara ambavyo vinasimamia huduma za matengenezo ya ndege, huduma za chakula cha abiria wa ndani ya ndege na huduma za abiria na mizigo kwa maana grounds handling services. Uwepo wa vitengo vinavyotoa huduma hizo umewezesha ATCL kupunguza gharama za uendeshaji. Mashirika mengine ya ndege yanayotumia utaratibu huu ni pamoja na Shirika la Ndege la Ethiopia. Ahsante. (Makofi)
MHE. ASYA MWADINI MOHAMED K.n.y. MHE. KAPT. ABBAS ALI MWINYI aliuliza:-

Je, ni kero gani za Muungano bado hazijapata ufumbuzi hadi sasa; na ni jitihada gani zinafanyika ili kero zilizosalia zipate ufumbuzi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Kapt. Abbas Ali Hassan, Mbunge wa Fuoni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kero za Muungano ambazo bado hazijapatiwa ufumbuzi mpaka sasa ni saba ikiwa ni pamoja na:

(i) Moja ni mgawanyo wa Mapato yatokanayo na Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na faida ya Benki Kuu;

(ii) Usajili wa Vyombo vya Moto;

(iii) Ongozeko la gharama za umeme kutoka TANESCO kwenda ZECO;

(iv) Malalamiko ya Wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili;

(v) Kodi ya Mapato (PAYE) na kodi ya Mapato inayozuiliwa (Withholding Tax);

(vi) Mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha;

(vii) Changamoto ya uingizaji wa sukari katika soko la Tanzania Bara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuimarisha uratibu wa utatuzi wa hoja zilizobaki kati ya sekta zenye hoja za pande zote mbili za SMT na SMZ na kuwasilisha maamuzi kwenye Sekretarieti ya Kamati ya Pamoja yenye jukumu la kufuatilia hatua za utekelezaji wa maagizo ya Kamati ya Pamoja na kutoa ushauri kwa sekta zenye hoja namna ya kuendelea kuzitatua hoja hizo. Aidha, Serikali za pande zote mbili zinashirikiana kwa karibu kuhakikisha vikao vya pamoja vilivyokubaliwa kwa ajili ya kupata ufumbuzi hoja zilizosalia vinaendelea kama utaratibu ulivyopangwa.