Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Bhagwanji Maganlal Meisuria (4 total)

MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA aliuliza:-
Inapotokea wazazi wametengana na mama akaondoka na mtoto na kwenda kuishi naye, lakini tangu wazazi hao watengane mama hatoi nafasi kwa baba kwenda kumtembelea mtoto:-
Je, baba ataipata wapi haki hiyo ya kumwona mtoto?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Bhagwanji Maganlal Meisuria, Mbunge wa Jimbo la Chwaka, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 imezingatia suala zima la utoaji wa malezi, matunzo na ulinzi wa mtoto kwa kutoa majukumu kwa wazazi, walezi pamoja na Serikali. Kifungu cha 7(1) cha sheria hii kimempa mtoto haki ya kuishi na wazazi wake au kuishi na mlezi. Aidha, kifungu cha 26(1) kimeeleza haki za mtoto endapo wazazi watakuwa wametengana. Haki hizo ni pamoja na kuendelea kupewa matunzo pamoja na elimu kama ilivyokuwa kabla ya wazazi kutengana, kuishi na mzazi mmojawapo baada ya mahakama kujiridhisha kuwa mzazi huyo anao uwezo wa kumlea mtoto. Pia mtoto kuwa na haki ya kumtembelea na kukaa na mzazi wake mwingine pale atakapotaka kufanya hivyo isipokuwa kama itabainika kuwa kumtembelea mzazi mwingine kutaathiri masomo na ustawi wa mtoto.
Mheshimiwa Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa zipo taratibu za kufuata endapo mzazi mmoja (baba au mama) atakosa haki ya kumwona mtoto wake ambaye anaishi na mzazi mwingine. Kwa mujibu wa taratibu, mlalamikaji atatakiwa kuripoti ofisi za Ustawi wa
Jamii za Halmashauri pale ambapo mzazi mwenza anaishi na mtoto ili waweze kukutanishwa na kufanyiwa unasihi ili hatimaye waweze kufikia makubaliano ya pamoja ya kumlea mtoto.
Mheshimiwa Spika, aidha, pale inaposhindikana, mashauri haya huelekezwa kwenye Baraza la Usuluhishi lililoko chini ya Kamishna wa Ustawi wa Jamii na pindi wasipofikia makubaliano kwenye Baraza la Usuluhishi, shauri hupelekwa Mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA aliuliza:-
Je, lini Serikali itapeleka gari, radio call pamoja na vitendea kazi vingine katika Kituo cha Polisi cha Chwaka na Jozani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bhagwanji Maganlal Meisuria, Mbunge wa Chwaka, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uhaba wa magari pamoja na vitendea kazi katika Vituo vya Polisi nchini kikiwemo Kituo cha Polisi Chwaka na Jozani. Hata hivyo, Jeshi la Polisi linaendelea na mchakato wa upatikanaji wa magari mapya yaliyonunuliwa na Serikali. Baada ya mchakato huu kukamilika, hatua za kuyagawa zitafuata kwa kuzingatia kiwango cha uhalifu katika maeneo husika, idadi ya watu na ukubwa wa eneo la doria.
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi Chwaka kinatumia mawasiliano ya radio ya mezani kwa sababu umbali wa ilikofungwa mitambo ya mawasiliano ya radio za mkononi. Aidha, radio za mezani kwa ajili ya Kituo cha Polisi Jozani imekwishapatikana na mafundi wa Radio za Polisi wanamalizia ufungaji wake ili kurejesha mawasiliano ya uhakika katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, ni azma ya Serikali kuhakikisha kuwa inaboresha mawasiliano katika vituo vyote vya Polisi nchini kwa kutafuta repeaters (mitambo wa radio za mkononi) ambazo zitafungwa katika vituo visivyokuwa na mawasiliano ya radio za mkononi ikiwemo Chwaka na Jozani.
MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA aliuliza:-

Kituo cha Polisi Chwaka na Kituo cha Polisi Jozani vina tatizo kubwa la gari la kufanyia doria na ulinzi:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia upatikanaji wa magari mawili kwa Vituo hivyo katika bajeti ya 2018/2019?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bhagwanji Maganlal Meisuria, Mbunge wa Chwaka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Polisi Chwaka na Kituo cha Polisi Jozani vipo katika Mkoa wa Kusini Unguja. Tayari Mkoa wa Kusini Unguja umeshapatiwa magari mawili aina ya Ashock Leyland – Trooper na Sauvana kwa ajili ya kusaidia utendaji kazi wa Polisi Mkoani humo ikiwemo doria.

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi bado linaendelea kupokea magari mapya kupitia mkataba wa magari 777 kutoka Kampuni ya Ashock Leyland Limited ya India. Hivyo kutokana na hitajio kubwa la rasilimali ya magari lililopo katika mikoa yote ikiwemo Mkoa wa Kusini Unguja na Jimbo la Chwaka, Jeshi la Polisi litaendelea kugawa magari katika mikoa kwa kadri magari yatakavyopatikana na kwa kuzingatia vipaumbele ambavyo ni kiwango cha uhalifu katika maeneo husika na ukubwa wa maeneo ya doria.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID (K.n.y. MHE. BAGWANJI MAGANLAL MEISURIA) aliuliza:-

Mara nyingi wakati wa chaguzi mbalimbali Zanzibar kunatokea hali ya fujo na ukosefu wa amani na kusababisha wananchi kukosa amani na wakati mwingine kutoshiriki katika chaguzi husika:-

Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Zanzibar juu ya suala hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maganlal Meisuria, Mbunge wa Chwaka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa nyakati za uchaguzi hukumbwa na vitendo vya uvunjifu wa amani hususani wakati wa kampeni na wakati wa kupiga kura. Hata hivyo, Serikali kupitia Jeshi la Polisi huchukua hatua mbalimbali kudhibiti vitendo hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, napenda kuwafahamisha wananchi kuwa ni jukumu la Serikali kuhakikisha amani na utulivu vinatamalaki nchini wakati wote bila kujali nyakati au majira mbalimbali katika mwaka. Jeshi la Polisi linaendelea kutoa mafunzo mbalimbali kwa Askari ya ukakamavu, upelelezi na kuongeza vitendea kazi ili kuwajengea uwezo na weledi wa kuzuia na kukabiliana na vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyojitokeza hususani wakati wa uchaguzi.