Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Bhagwanji Maganlal Meisuria (13 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MAGANLAL M. BHAGWANJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi hii kuchangia leo. Kwanza, naomba kuipongeza Serikali kwa kupitia kwa Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Baraza la Mawaziri, kwa kufanya kazi nzuri na kurudisha imani kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Serikali iangalie zaidi kuboresha Utawala Bora, pamoja na jitihada hizo zilizofanywa ni vizuri kuwe na suala la huduma kwa mteja. Itolewe elimu katika ngazi zote, Tume au Sekretarieti ya Utumishi wa Umma iboreshwe ili waweze kufanya kazi ngazi zote Taifa, Mkoa na Wilaya ila zile kazi za kada ya chini zipewe Halmashauri jukumu la kuajiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, muhimu pia tuwe na Maafisa Mipango zaidi katika ngazi zote, Halmashauri, Kata na Vijiji ili miradi iweze kuibuliwa, pia wakiwemo, katika miradi ya TASAF wananchi wapate fursa ya kuibua miradi yenye manufaa kwao. Pia TAKUKURU isaidie kuondoa kabisa rushwa, kero ndogondogo mfano wa traffic barabarani, vibali vya dhamana, kupata leseni, ni mifano michache. Vile vile kwenye elimu, Serikali iangalie namna ya kuboresha na kukomesha shule na vyuo feki ambavyo havitoi elimu kwa viwango na zisizofuata Kanuni na Utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. BHAGWANJI M. MEISURIA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kushukuru Kiti chako kwa nafasi hii ya kuchangia kwa maandishi katika Wizara hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya ya kujenga Taifa hili kwa falsafa ya “Hapa Kazi Tu” na kwa kweli tunaona kazi inafanyika kweli kweli na wananchi walio wengi wana imani na Serikali ya CCM.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipompongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Tanzania kwa kumsaidia Rais wa Tanzania kutekeleza majukumu ya Serikali na sasa tunaanza kuona matunda yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nampongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa ushindi mkubwa alioupata hivi karibuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie hotuba ya Wizara hii ya Kilimo kwa kuzungumzia mambo machache. Napenda kuishauri Serikali kuweza kuwakusanya vijana wasio na ajira na kuwatengea maeneo maalum ya mashamba na kupewa taaluma ya mifugo, uvuvi na Kilimo na baadaye wapewe mikopo kutoka Benki ili waweze kujiajiri wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naiomba Serikali kujipanga vizuri katika kukabiliana na changamoto zifuatazo:-
(a) Uharibifu mkubwa wa mazingira ya Bahari, Mito na Maziwa; na
(b) Kukabiliana na migogoro mikubwa ya wafugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Rais na Makamu wake kwa kuchaguliwa kwao na kazi nzuri wanazozifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ninampongeza Naibu Spika, kwa ujasiri wake wa kuongoza vikao vyetu ndani ya Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa hotuba yake nzuri yenye mipango yake ya utekelezaji kwa kipindi hiki cha mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee chombo chetu cha habari TBC. Hatuna namna yoyote ya kutosaidia kukihudumia chombo hiki kama Serikali, ni chombo cha Serikali kinachotoa habari za ukweli na uhakika. Isingekuwa vizuri kuona chombo hiki kinashindwa kufanya kazi zake kama ilivyokusudia kwa kukosa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, chombo hiki kinasaidia sana kuitangaza nchi yetu kisiasa, kiutamaduni, kimichezo na mambo mbalimbali ya nchi yetu. Ninaomba Serikali kukisaidia kwa kukipa fedha tena kwa wakati ili katika mambo yanayoendelea katika nchi yetu wananchi wetu wapate kujua taarifa za ukweli na uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona ubadhirifu na uvunjwaji wa amani unatokea kwa sababu wananchi wamepata taarifa zisizo sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sina budi kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya ya kutumbua majipu, kwa hilo hongera sana. Pia naomba kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Spika kwa kazi nzuri anayoifanya na kuliongoza Bunge vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niishauri Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwamba zile za nyumba za National Housing Corporation zilizopo Dar es Salaam ambazo zinakodishwa kwa shilingi 370,000 kwa mwezi kwa kweli bei hiyo ni kubwa mno ukilinganisha na kipato cha wananchi kilivyo. Walio wengi hawamiliki fedha hizo na wakati mwingine nyumba hiyo ikiharibika unaambiwa fedha hakuna, inakubidi utekeleze mwenyewe kazi ya matengenezo au upakaji wa rangi. Kwa hiyo, naiomba Wizara hii ipunguze kiwango hicho ili wananchi walio wengi wafaidike asimilia mia.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru nimepata nafasi hii mara ya kwanza. Namshukuru Mwenyezi Mungu, tumejaliwa sote tuko pamoja na Insha Allah Mungu ataleta neema yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Spika wa Bunge pamoja nawe Naibu Spika kwa kazi yako nzuri. Katika Bunge hili mimi ni Baniani peke yangu. Kama nimekosea, mtanisamehe, lakini nitajitahidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napongeza Kamati yangu ya Miundombinu, imefanya kazi nzuri kabisa, pamoja nami, nimetembelea bandari, uwanja wa ndege, reli na barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Rais wangu wa Muungano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, yeye amefanya kazi nzuri kabisa katika Tanzania yetu na nchi yetu.
Ameboresha miundombinu, barabara na mambo mengine ya reli na bandari. Nasi Wabunge tunamsaidia kufanya kazi apate sifa, kazi tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nampongeza Mheshimiwa Rais wangu wa Zanzibar, amefanya kazi nzuri na kuiboresha Zanzibar kwa miundombinu ya barabara, taa za solar Michenzani, Amani na sehemu nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza vile vile Waziri Mkuu. Waziri Mkuu anafanya kazi nzuri pamoja nasi na anakwenda kila mahali anafanya kazi yake nzuri, nasi tuko pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunakuja katika mada yetu ya Kamati yetu ya Miundombinu.
Kamati yetu tumetembelea barabara zote na hivi juzi tumekwenda kuanzia Dar es Salaam, tumetoka Dodoma kwenda Arusha, tumeona barabara inajengwa na madaraja. Naipongeza Tanzania yetu na Mheshimiwa Rais amefanya kazi nzuri na kuweka uchumi bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nataka kuzungumza kuhusu Uwanja wa Ndege.
Nimetembea viwanja vya ndege mbalimbali. Tumetoka kwenda Arusha, tumeona mambo mazuri, lakini yanatakiwa kuboreshwa. Mnara wa uwanja wa ndege ni mdogo sana, unatakiwa ufanywe mkubwa upate kuonekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kamati yetu na mimi nimefaidika kumsaidia Mheshimiwa Rais, uwanja wa ndege wa Kilimanjaro wa International ni mzuri kabisa; lakini uwanja wa ndege wa Moshi, tunatakiwa tutie mkazo katika Serikali. Yaani uwanja wa ndege wa Moshi ile ndege inatua katika barabara mbovu kabisa. Tokea enzi ya British ipo pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali pamoja na Mheshimiwa Waziri, tuboreshe uwanja wetu ule, kwa sababu katika uwanja wa ndege wanakuja watalii. Watu wanakuja kwa utalii wanashuka Arusha wanateremka Kilimanjaro, lakini pale uwanja wa ndege wa Moshi upo
karibu na mlima wetu wa Kilimanjaro na Mount Meru. Uwanja wa ndege wa Arusha ndege nyingi zinatua pamoja na ATC, kwa hiyo, kwa nini usiboreshwe pale Moshi? Kwa sababu pale Moshi ni centre, wanakuja watalii wapate kwenda moja kwa moja katika mambo ya kutazama
wanyama pamoja na Mlima wetu wa Kilimanjaro.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumetembelea bandari nyingi sana. Bandari hii inahitaji kuboreshwa hasa. Tumekwenda Tanga, Mwanza, tumeona Bandari ya Mwanza ni nzuri, lakini inatakiwa kutiwa nguvu kabisa kuboreshwa ili kukuza uchumi, kusafirisha mizigo nchi za jirani.
Bandari ya Tanga ipo jirani na Zanzibar na Mombasa. Tumeona kuna uzito na ipo haja kubwa sana ya kuboresha, kupanua na kuleta meli kubwa za makontena makubwa kuliko Dar es Salaam ambapo tunateremsha kontena zetu. Ni bora kufika Tanga kwenda kwa nchi za jirani.
Vilevile tuboreshe bandari yetu ya Bagamoyo. Tumetembezwa, tumeridhika na tumesema Tanzania yetu naomba Mheshimiwa Rais aboreshe ile Bandari ya Bagamoyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kwenye sekta ya reli. Standard gauge ya reli sisi Kamati tulikwenda kutembea, nampongeza Mwenyekiti na Kamati yangu. Mara ya kwanza nimekwenda Tanzania nimeona reli. Standard gauge imekwama sehemu fulani, haikuweza kuboreshwa, lakini nashukuru Mheshimiwa Rais wetu amepata ufadhili mpya, tutaboresha tufanye kazi; reli yetu kwa upande wa Congo tupate kupeleka mali yetu Burundi na Rwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutakuwa tunaongeza uchumi wa nchi na hiyo ndiyo sekta muhimu. Wenzetu wa Kenya kutoka Mombasa wamefika Nairobi, wataunganisha na jirani pale Congo na wapi, sisi tutakosa soko. Naiomba Serikali tufanye kazi na namshukuru Mwenyezi
Mungu na naishukuru Serikali ya Awamu ya Tano, Mungu ampe uzima na afya Mheshimiwa Rais wetu afanye kazi ya ziada…
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa muda
wangu umekwisha, naunga mkono Kamati hii na Bunge letu. Ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme jambo moja, kama nimekosea, ulimi hauna mfupa. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante umenipa nafasi Mungu akuweke, nakupongeza sana. Naipongeza Kamati yangu ya Miundombinu, Mheshimiwa Mwenyekiti pamoja na Wajumbe wote wa Kamati yangu, kwa sababu tumetembea katika maeneo mbalimbali na nimefaidika, na sisi tumeona eneo lingine jipya. Vilevile Rais wangu Mheshimiwa John Pombe Magufuli amefanya kazi nzuri sana katika Tanzania yetu, Mungu amuweke maana yake ana mbinu ya Rais wetu Mheshimiwa Narendra Modi wa India, yaani Narendra Modi anafanya mambo yake na yeye anachukua mbinu hiyo hiyo, Mungu amsaidie. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Waziri wangu wa Miundombinu, Naibu Waziri, pamoja na watendaji wake wanafanya kazi nzuri pamoja ofisi yake wanafanya kazi nzuri wanamsaidia sana, Mungu amuweke.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunakuja katika mada yetu inayohusu Mkongo wa Taifa (Data Centre) yaani mitandao ya simu. Kamati yetu tumekwenda juzi kutembelea, nimeona mambo mazuri kabisa, yaani hiyo mitandao chini kwa chini (underground) imekuja kutoka India, South Africa na Zambia mpaka hapa Dar es Salaam, tumeona mitandao hiyo, nampongeza Mheshimiwa Rais wetu Magufuli, amefanya mambo hayo, yaani nchi nyingine hakuna lakini hapa Tanzania ipo. Mitandao hiyo imegusa Dar es Salaam, Zanzibar lakini wale watu ambao ni washirika wa mtandao huo, Zantel, Airtel Tigo pamoja TTCL wamefanya mambo mazuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, imetengeneza database ili hawa watu wa mitandao, wale wa Zantel na wengine wanunue hiyo data waje kutia katika mitandao yetu katika database. Kampuni hizo waje watie katika biashara yetu katika database, yaani wao wasitumie yao watumie ya Tanzania, ili sisi tupate pesa. Mheshimiwa Magufuli amefanya mengi pamoja na Rais wetu wa zamani Mheshimiwa Jakaya Kikwete safi yaani wamefanya vitu vya kuleta baraka na Tanzania yetu tushinde. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunakuja katika barabara, tumetembelea barabara nyingi sana na juzi tumetembelea barabara ambayo Mheshimiwa Rais amefanya kuwa barabara kubwa, ina watu wengi, amekatisha sasa, ameipeleka barabara hiyo mpaka Kiwanda cha Saruji cha Wazo pale. Halafu kutoka pale inakwenda moja moja mpaka bandari, inakwena uwanja wa ndege, amegawa sehemu mbalimbali, mjini pamoja na huko sehemu za Dar es Salaam. Barabara hiyo ina watu na magari mengi, kwa hivyo nampongeza Mheshimiwa Rais wangu Magufuli. Mimi naomba Rais wangu Mheshimiwa Magufuli asaidie kidogo barabara za Zanzibar. Uwezo wetu ni mdogo, lakini mimi naomba Mheshimiwa Rais wetu wa Muungano aisaidie Zanzibar ili na sisi barabara zetu ziboreshwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunakuja uwanja wa ndege. Kweli mimi nampongeza Mheshimiwa Rais amefanya maboresho mengi sana, ameleta ndege kubwa. Tunaona uwanja wa ndege wa Dar es Salaam umeboreshwa vizuri kabisa. Sisi tulikwenda kutembelea Terminal B, tumeona mambo mazuri, yaani watalii watakuja wengi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile naomba Serikali iboreshe uwanja wa ndege wa Zanzibar, sisi wote ni wa Muungano, ndugu mmoja hatuna ubaguzi, uwanja wetu wa Zanzibar na sisi tuuboreshe kwa sababu terminal ipo na wanakuja watalii pesa zote zinaingia Tanzania tutaondosha umaskini wetu. Vilevile viwanja vya ndege vidogo vidogo Tabora, Mwanza, Moshi, Kilimanjaro jamani hivi viwanja vya ndege kama sisi wananchi tuvitumie tunaongeza mapato, tunaongeza vitu mbalimbali, tutaondosha umaskini, tunatafuta mapato tunaleta maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, umenipa nafasi nakushukuru sana Mungu akuweke. Tunakuja katika bandari na bandari yetu imeboreshwa na tumekwenda kutembea bandari ya Dar es Salaam, tunataka kupanua bandari, na kupanua kwake kwa sababu zitapita meli mbili pamoja. Mimi nampongeza Mwenyekiti wangu wa Kamati, yaani mimi pia nimefaidika kwa kuingia ndani ya Bunge nafahamu nini maana ya Muungano na nini ni Serikali. Kumbe Serikali iko imara, na Marais wa awamu zote wamefanya kazi ya kuleta maendeleo katika nchi yetu kwa kuondoa umaskini wetu. Nampongeza na Mwenyezi Mungu aipe nchi yetu ya Tanzania ipate baraka na kila kheri. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bandari yetu ya Dar es Salaam tunapanua, lakini mimi ninaomba Serikali yetu vilevile, bandari ya Zanzibar tuko katika enzi yetu ya zamani, tunataka na sisi bandari yetu ya Zanzibar pia tuboreshe ili tupate kuweka makontena nyingi kuliko zile, ili pia watu mbalimbali waje. Vilevile mimi ninaiomba Serikali yangu, Waziri wangu, Rais wangu bandari ya Mwanza, Tabora,
Bagamoyo, Tanga umenifahamu pale…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naunga mkono hoja, ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, Mungu akuweke. Nimepata nafasi hii kuzungumzia bajeti yetu ya Serikali. Nataka niseme sisi Wabunge wote hakuna ubaguzi wa rangi wala Kabila tunaunga mkono bajeti ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake. Hicho kitabu alichoandika cha bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango, namuunga mkono, Mungu amweke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana sana Mheshimiwa Rais wetu Dokta John Pombe Magufuli, amefanya kazi nzuri, kwa sababu tulikuwa tunadhulumiwa madini yetu yanakwenda nje. Mungu ameweka neema yake awamu yake akafanya vizuri na anasaidia kuondoa umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wetu Magufuli amefanya mambo mengi, ujenzi wa barabara, uwanja wa ndege na ameleta ndege mbili na analeta ndege nyingine nne. Hayo yote yatasaidia kuondoa umaskini kwa sababu itaongeza mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, akinamama wa Zanzibar pamoja na Watanzania wote wamechoka kubeba mizigo ya maji, pesa hizo zitasaidia wananchi wetu wa Tanzania tutoke kwenye umaskini twende katika hali nzuri. Inshallah, Mwenyezi Mungu atampa nguvu Rais wetu Mheshimiwa Magufuli na ataondoa shida zetu zote na maji yatapatikana kwa kila mmoja wetu, Zanzibar pamoja na Bara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia Halmashauri, Halmashauri zetu wanakusanya pesa, tuwasimamie vizuri lakini naomba Serikali zile pesa milioni 50 tuzipeleke kwenye Halmashauri. Wananchi wanangoja kwa hamu pesa zile kwani zitasaidia kuondosha umaskini na tutasaidia wale watu waliokuwa na shida kwenye ushirika, asilimia nne au tano walikuwa wanapata na kukopeshwa basi Serikali isaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pamoja na Rais wetu amefanya kazi nzuri kwa kuanzisha mabasi ya mwendokasi, Watanzania wamekuwa wakifaidika. Pia tunaingiza pesa chungu nzima na pesa hizo tutaziweka katika kilimo, maji pamoja na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni viwanda, kweli nasema Serikali inajitahidi kusimamia viwanda. Kwa kuwa na viwanda itasaidia sana wananchi na vijana wetu kupata ajira na ajira ni muhimu kwa Tanzania yetu. Kwa kuanzisha viwanda mbalimbali mapato ya Taifa yataongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TRA yetu lazima isimamie ukusanyaji wa mapato. Mapato yapo kwenye viwanda, sekta ya utalii na bandari, haya yote tuyasimamie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine naomba Serikali yangu ya Muungano tuwasaidie watu wa Zanzibar. Mwenzangu Mheshimiwa Rehani amesema lakini mimi nazidi kusema sisi wote ni ndugu moja, hakuna upinzani wala ubaguzi. Wale watu wanyonge kutoka Zanzibar wanaleta biashara ndogo ndogo, wanatoa ushuru kule lakini ikifika hapa wanahangaishwa, basi tuwatazame na tuwaachie.

Wazanzibar tuwaache wafaidike kwa sababu kule Zanzibar unalipa ushuru namna mbili, ZRB pamoja na TRA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri tuboreshe biashara za viwanda. Kama tutasimamia kweli Tanzania yetu tutapata mapato mengi sana, asidharau. Vilevile tunataka tufufue viwanda vyetu, wale watu wanakuja kutoka nchi za nje wanataka kuanzisha viwanda tuwapokee. Hii ni kwa sababu vijana wetu watapata ajira na kuondokana na umaskini. Vijana wakifanya kazi na nyumbani akipeleka chochote itasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema kitu kimoja, sisi Zanzibar pamoja na Tanzania yetu tuna mambo mengi sana ya kusaidia kuingiza pesa. Tanzania tunazalisha mazao kama kunde, choroko na dengu, tunao watu kutoka nchi za nje kama India wanakuja kununua tuwakaribishe. Sisi tunataka maendeleo na mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri ameondoa kodi katika mazao ya kilimo kwa tani moja. Vilevile ameondoa kodi kwenye magari, tunamshukuru sana Mungu amweke. Serikali yetu inataka kufanya mambo, tumuunge mkono Rais wetu Mheshimiwa Dokta John Pombe Magufuli kwa sababu Mheshimiwa Waziri… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana nimepata nafasi hii, Mungu akuweke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa sisi Wabunge sita tuliopata ajali Morogoro, lakini sote tuko salama na amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nawashukuru watu wa Hospitali ya Morogoro, wananchi wake na madaktari wametuhudumia mara moja. Vilevile nawashukuru Hospitali ya Muhimbili na hospitali tuliyohamishiwa MOI Hospital.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawashukuru watu wa NHIF (watu wa Bima ya Afya), wameleta ndege mbili, ambulance nne, tumepata nafasi nzuri ya kupelekwa hospitali na tumepata huduma nzuri. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu na tunamshukuru Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunamshukuru Waziri wetu, Mheshimiwa Ummy, pamoja na Naibu wake, wamekuja hospitali kutuona, ametupa pole.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote wa Bunge letu hili, nawashukuru pamoja na watu wangu wa Jimbo, wamekuja kuniona katika hospitali. Kwa hiyo, nasema kwa wote, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018
MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru nimepata nafasi hii ili kuzungumzia mambo yetu ya bajeti. Nampongeza Rais wangu Dkt. Magufuli kwa Ilani yake ya CCM anaboresha Tanzania yetu na kutuondoa katika umaskini wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nawapongeza Mawaziri na Mwenyekiti wa Kamati yetu ya Miundombinu na wajumbe wote. Sisi tunafanya kazi kuendana na wito wa Rais wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia mambo machache mazito. La kwanza ni bandari. Bandari yetu Mheshimiwa Rais pamoja na Waziri wanasimamia vizuri kuanzia Dar es Salaam, Mtwara, Tanga na Zanzibar. Kwa upande wa Tanga tumepata mambo ya mafuta basi tutapata mapato zaidi na vilevile kwa Zanzibar tuboreshe bandari yetu, Muungano wetu inahusu kuboresha bandari yetu tuweze kuongeza makontena zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu Reli ya Standard Gauge. Nampongeza Mheshimiwa Rais pamoja na Waziri, sisi Kamati tumetembelea kuanzia Dar es Salaam, Morogoro kushuhudia ujenzi wa Standard Gauge. Reli hii italeta mapato kwa sababu tutaenda mpaka Mwanza na nchi za jirani kupakia mizigo na kupata fedha za kutatua matatizo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais na Kamati yaani Mheshimiwa Magufuli amesimamia kuleta ndege sita (6). Nia na madhumuni yake ni kuondoa umaskini katika Tanzania yetu, tunasimamia nchi yetu na wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameleta ndege sita (6) na zinafanya kazi moja kwa moja. Hata hivyo, naomba kuboresha iende ndege China na India kuleta watalii Tanzania mpaka Zanzibar. Mungu amsaidie Mheshimiwa Rais Magufuli, Inshallah, Mungu amzidishie alete meli pia na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naenda kuzungumzia barabara. Barabara yetu inafanya kazi nzuri kuanzia Dar es Salaam, Morogoro, Arusha, Mwanza. Barabara hii tukiiboresha basi italeta mapato zaidi na tutafikia uchumi wa kati. Kwa sababu unapotoka Zanzibar au nchi nyingine ile mzigo inafika mpaka nchi nyingine hivyo tutaongeza mapato na kuondoa umaskini wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu kuboresha Shirika la Posta na TTCL. Watu wa Posta najua wanafanya kazi kwa juhudi sana, amezungumza mwenzangu hapa, kwa hiyo tuongeze mishahara yao. Vilevile TTLC kuhusu mambo ya mtandao, wananchi wanapenda mitandao ya kuzungumza baina yao, basi tuwaongezee nguvu TTCL waweze kuongeza huduma hii kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa, naipongeza Serikali yangu, nampongeza Rais wangu Mheshimiwa Dkt. Magufuli, nampongeza Rais wa Zanzibar, tuwe pamoja na tuongeze mambo mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu na Tanzania. Kwa hayo machache, naipongeza nchi yetu na Tanzania yetu. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kupata nafasi hii. Kwanza naipongeza Kamati yangu, tumekwenda ziara. Vile vile nampongeza Mheshimiwa Rais, nampongeza pia Mheshimiwa Waziri kwa kufanya kazi nzuri katika Kamati hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze kuhusu bandari iliyojengwa Tanga, Mtwara na Dar es Salaam. Hiyo yote imeboresha zaidi. Vilevile nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kufanya juhudi sana kuhusu barabara. Tulitembea Mbeya na Kamati, tumeona kazi ya barabara imefanyika na watu wananchi wameridhika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Kamati yangu katika ziara yake tumeona Standard Gauge inakaribia kukamilika kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro. Hata hivyo wamejenga bandari kavu. Kwa hiyo, tunapongeza, ila kwa kuwa container zote zinakaa Dar es Salaam, basi zitakuwa zinakaa katika bandari ile kavu ya kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amechukua hatua nzuri sana katika mambo mbalimbali ya mawasiliano ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umenipa nafasi haraka haraka, lakini nilikuwa sijajiaandaa, nilikuwa nimejiandaa kwa jioni, lakini kidogo umenipa nafasi siyo mahala pake, mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze kuhusu bandari iliyojengwa Mtwara. Tulipokwenda Mtwara, tuliona bandari ya zamani ilikuwa ndogo lakini sasa imepanuliwa zaidi. Nimeona hata Bandari ya Dar es Salaam, Kamati tumeambiwa kwamba kunafanyika uboreshaji wa njia ya meli, badala ya kupita meli moja, zitapita meli mbili pamoja. Kwa hiyo, nashukuru kwamba hayo yote yatafanyiwa kazi. Namshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati amefanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Mheshimiwa Rais ameboresha uwanja wa ndege wa Dar es Salam tumeona, amenunua ndege nyingi na wanaleta utalii. Pia ndege itakwenda katika nchi nyingine kama India, China na sehemu nyingine na Iringa hivyo hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, namshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, anajitahidi kwa kukusanya pesa na kazi kwa Watanzania wanyonge na wengine wote. Kupitia mabasi ya mwendokasi, watu wamefaidika kwa bei ndogo na tunaingiza mapato chungu nzima, ila tu sasa hivi siku za mvua nashauri yajengwe madaraja kwa sababu tunapata taabu sana kwa kujaa maji barabarani. Hata hivyo...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Haya, ahsante Mheshimiwa.

MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia hoja hii ya Serikali inayohusu Mpango. Nampongeza Mheshimiwa Waziri na Kamati yake, lakini sana Mheshimiwa Rais wa Muungano pamoja na Rais wa Zanzibar, wamejitahidi kwa kuleta maendeleo katika Taifa letu. Mungu awasaidie na sisi Waheshimiwa Wabunge, Mawaziri pamoja na wananchi kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekitik, katika Mpango huu nitazungumzia mambo yetu ya uwanja wa ndege. Terminal three imejengwa kwa awamu ya Mheshimiwa Rais, ni mpya kabisa. Mungu akipenda, kesho kutwa naondoka kwa ndege yetu ya Tanzania. Naomba Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Dkt. Mpango ziongezwe ndege nyingi katika nchi yetu, kwa sababu sisi hatushindwi, tunakwenda mbele na hiyo mbele, ndiyo kazi yetu. Hapa ni Kazi Tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ndege inatoka Dar es Salaam moja kwa moja inakwenda India. Sasa wafanyabiashara, wagonjwa na wengine wanataka kitu kama hicho, nami nimekata tiketi, basi ndege zote ziko full kwenda na kurudi. Tutapata utalii na mambo mbalimbali. Naomba Serikali yetu ya Muungano ndege ndogo ndogo ziongezwe kwa sababu mpaka Zanzibar tunahitaji ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Zanzibar tuboreshe katika uwanja wetu wandege kwa sababu watalii wengi wanakuja kama Bara. Tutafaidika na mambo mbalimbali tutafaidika. Tukiondoka hapa bandari yetu; Mheshimiwa Rais katika awamu yake, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Miundombinu. Kuhusu bandari tumekubaliana ndani ya Kamati na inafanyiwa kazi. Tunakwenda mbele. Bandari yetu sasa hivi tunapanua, ili hata zikija meli kubwa ziweze kwenza mbili kwa pamoja. Tunatakiwa katika bandari yetu tuongeze mapato kutokana na makontena na mambo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri Mheshimiwa Rais, kwa uwezo wa Mungu, sisi wote ni ndugu moja, ni Muungano; kwa hiyo hata Bandari ya Zanzibar, kule Mpigaduri tuwasaidie. Kwa sababu tulikuwa nyuma, sasa hivi tuko mbele. Zamani haikuwa namna hiyo, sasa hivi imekuwa. Kontena nyingi zinaletwa na biashara nyingi zinaletwa mpaka Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wa Zanzibar anajitahidi katika mambo mbalimbali ya barabara, bandari, maji na umeme. Vile vile nampongeza Rais wa Muungano kwamba bandari yetu itaboreshwa. Siyo bandari hiyo tu, bandari ya Tanga na Mtwara. Nilikwenda katika Bandari ya Mtwara kutembelea, nimeona maendeleo yake. Bandari ya Mtwara siyo kama zamani, sasa hivi bandari ni kubwa, imepanuka na yataletwa mambo mbalimbali, kontena zote zitafika kule na kusafirisha korosho na mambo mengine.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maendeleo yetu vilevile, katika mipango ya reli pamoja na barabara (Standard Gauge), katika Kamati yangu nimeona, nimetembelea na karibu tutafika Dodoma. Standard Gauge hii, siyo Dodoma tu, tufike katika mipaka ya wenzetu; Mwanza na kwingine mpaka iende Zambia mpaka iende Burundi. Kwa hiyo, Standard Gauge inatakiwa iende katika mipaka ya nchi za nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuboreshe barabara vilevile, kwa sababu tunaongeza mapato vilevile. Standard Gauge zitapakia hizi kontena pamoja na barabara kwa biashara mbalimbali za kilimo, watasafirisha nchi za nje nasi tutafaidika. Naomba Mheshimiwa Rais aendelee mbele na anaendelea mbele kwa kiwango kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kilimo. Sasa hivi haturudi nyuma, tunakwenda mbele; tunazalisha pamba, alizeti, tumbaku pamoja na korosho na mambo mengine. Zanzibar tunazalisha karafuu. Kwa hiyo, tunataka hizi pamba na mazao mengine tunao uwezo wa kusafirisha India, China pamoja na hizi mazao mengine na kupata mapato katika nchi yetu na kuondosha umasikini wetu. Namwomba Mheshimiwa Dkt. Mpango, Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri, tumsaidie na tumpongeze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaondoka hapo, tunakuja katika viwanda. Viwanda ni lazima visaidiwe. Mheshimiwa Rais wetu tumpe nguvu; viwanda vya Serikali na viwanda vya watu binafsi, kwa mfano, kiwanda chetu cha sukari, alizeti pamoja na korosho, tufanye hapa tuboreshe. Maana yake, viwanda hivi ni uhai wa uchumi wa nchi yetu na uhai wa uchumi wa Taifa letu. Kiwanda cha Sukari vilevile sisi tunao uwezo. Tukisimamia, nashukuru Mawaziri wanasimamia viwanda. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mpango viwanda vyetu ni lazima tusimamie kwa nguvu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende katika elimu na hospitali. Elimu yetu inatakiwa kuboreshwa zaidi. Watoto wa leo wakisoma, kesho wanakuwa Mawaziri, Rais na elimu yetu inasongea mbele. Kwa sababu elimu inatoa faida nyingi sana kwa watoto. Kama umewakosa kusomesha watoto, namshukuru Mheshimiwa Rais, elimu yetu katika Skuli zote za Sekondari pamoja na Skuli ndogo zote wanafanya vizuri sana, wanaboresha halafu hata katika mitihani anasimamia Mheshimiwa Waziri na Serikali, watafaulu na watakwenda mpaka nchi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hospitali, nashukuru Mheshimiwa Waziri na Serikali ilikuwa zamani hakuna kitu. Leo sasa hivi katika zetu, Zanzibar na Bara kila kitu Kituo cha Afya, yaani kote na madawa yanapatikana. Kituo cha Wilaya vilevile na Mkoa, namshukuru Mheshimiwa Rais, tuko mbele. Hakuna mtu hapa katika Tanzania yetu… (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, jina lake nani?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Bhagwanji. Nilikuwa nimekuongezea muda kwa sababu unatelemka leo vizuri sana. (Makofi)

MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais anaitwa John Joseph Magufuli…

MWENYEKITI: Malizia Mheshimiwa Bhagwanji.

MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, okay naunga mkono hoja hii. (Makofi/Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nakupongeza kwa kunipa nafasi hii ya kuzungumza. Kamati yangu ni ya Miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Spika na Mheshimiwa Naibu Spika, wanafanya kazi nzuri sana katika Bunge hili na Mheshimiwa Spika yeye ni mlezi wangu na amekuja mpaka Jimboni kwangu amekagua miradi mbalimbali. Kwa hiyo, namshukuru sana, anafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwa Waziri pamoja na Naibu Waziri wa Mundombinu, wanasimamia kazi kubwa ya Sekta ya Bandari, Uwanja wa Ndege, barabara n.k kwa hivyo nimetazama na nimeona Waziri na Naibu wake wanastahili kupongezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze kitu cha maana kabisa. Mheshimiwa Rais, Dkt. John Joseph Magufuli amesimamia Tanzania na kufanya kazi nzuri kabisa katika awamu yake, Mungu amuweka na uchaguzi huu yeye atarudi. Mimi namuombea kwa Mwenyezi arudi yeye pamoja na mimi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mwenyekiti wangu wa CCM Taifa, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Magufuli hapa Bungeni Bhagwanji Maganlal Mesuria, Baniani peke yake arudi tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naangalia na nakupongeza kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rais wangu wa Zanzibar Ally Mohamed Shein, ametekeleza wajibu wake katika awamu yake mpaka leo. Wananchi wa Zanzibar wameridhika, barabara, maji, umeme, shule pamoja na hospitali n.k aliyoyafanya sana na amekuwa kifua mbele. Mungu amuweke Mheshimiwa Ally Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar, amefanya kazi nzuri sana na atazidi kufanya na mimi niko pamoja na yeye na yeye namuomba jina langu anirudishe tena. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Kamati yangu ya Miundombinu, Mwenyekiti pamoja na sisi Wajumbe tunasimamia Sekta ya Miundombinu kwa hivyo Sekta hii inakuwa ina matatizo mengi, Sekta hii tumepongezwa na Sekta hii ya miundombinu tumesimamia barabara, uwanja wa ndege, standard gauge na tumesimamia bandari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi katika Kamati yetu zikija taarifa kama hizi basi sisi tunakaa na Waziri, Katibu Mkuu wa miundombinu pamoja na wananchi na tunashirikiana kufanikisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia Bandari, Bandari ya Dar es Salaam inafanya kazi nzuri sana lakini pana kasoro moja tu inahitajika irekebishwe, ishikwe mkono kwa sababu hizi container zinatoka nchi za nje na meli inakaa sana na container hazitoki sana katika bandari kwenda nchi zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo hata wafanyabiashara wanalalamika kwa sababu wanafanya kazi sana TRA, bandari na wale watu wa Shirika la Bandari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali, Bandari ya Dar es Salaam isimamiwe na kwamba likija kontena, basi ianze kutoka nje haraka sana. Kwa sababu wafanyabiashara wengine wameamua kutoa mizigo yao kupeleka Mombasa kwenda nchi ya Burundi, Zambia na sehemu nyingine nasi tutakosa mapato. Kwa hiyo, naiomba Serikali isimamie bandari yetu ili kontena zote zipate kutoka kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile namwomba Mheshimiwa Rais wetu kuhusu Bandari ya Zanzibar ambayo ina kontena nyingi pamoja na mambo mengine, ni bandari ndogo kabisa. Tunataka tushiriki Muungano wetu kupitia Bandari yetu ya Zanzibar 2020 na kuendelea mbele. Ipanuliwe na tusaidiane kwa sababu sisi ni ndugu moja na tunataka kuboresha Zanzibar na Tanzania. Kwa sasa Bandari ya Zanzibar kontena zinakuja nyingi sana na hakuna pa kuweka. Kwa hiyo, naomba Serikali ya Tanzania tufanye kazi pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia uwanja wa ndege. Terminal III imekamilika, nashukuru sana. Bunge lililopita niliwaambia nitasafiri, kwa hiyo kweli nampongeza Mheshimiwa Rais, nilikuwa naenda India na nchi nyingine. Nilikwenda India nikafuatana na mama mtoto wangu pamoja na familia, nimeshuhudia ndege ile inafanya kazi, inajaa sana. Ndege hiyo wakati wa kurudi vile vile inajaa kwa sababu moja; ndege hii Serikali imeamua kwenda direct. Kwa hiyo, wananchi, watalii wa India na nchi mbalimbali wamekubali kupanda ndege yetu ya Tanzania kuja hapa. Hii itatusaidia na kutuongezea kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba jambo moja lingine kuhusu uwanja wetu wa ndege wa Zanzibar. Kwa kuwa sisi ni Muungano, lazima tuboreshe kwa sababu wanakuja watalii wengi na tunapata mapato mengi. Sasa kwa sababu ni Muungano, Zanzibar na Dar es Salaam, Tanzania basi tutaongezea; na tulikwama uwanja wetu wa ndege Terminal II, basi tumalize haraka na tuongeze ndege nyingi kutoka Zanzibar kuja Dar es Salaam zinaunganisha kwenda India na sehemu nyingine. Naomba Serikali isaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, mitandao ya simu pamoja na minara yetu katika mipaka inakuwa na matatizo, wananchi wanakosa mawasiliano. Naiomba Serikali na Mheshimiwa Waziri asimamie Tanzania yetu katika sekta mbalimbali na sehemu mbalimbali hususan kwenye mitandao ya simu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zetu tunajitahidi kufanya vizuri na tutazidi kutengeneza. Namshukuru Mheshimiwa Rais, bajeti yetu kwa upande wa miundombinu amesaidia na amesimamia na tumepata pongezi. Kamati ya Miundombinu pamoja na Mheshimiwa Waziri na Kamati yake, vile vile na Katibu Mkuu wanafanya kazi nzuri, nawapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Makamu wa Rais, wamefanya kazi nzuri sana kwa Tanzania kwa kutembelea kila mahali mpaka Zanzibar. Kwa hivyo, tunampongeza na Mungu amuweke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naunga mkono Kamati hii pamoja na Bunge. Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu ya CCM pamoja na Rais wangu, CCM oyee! Nami nataka nirudi tena. CCM oyee! (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kupata nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Fedha na Mipango nakupongeza sana kwa bajeti yako pamoja na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango pamoja na Watendaji wote, kwa sababu ya hiki kitabu walichoandika basi naunga mkono moja kwa moja kwa sababu kitabu hiki kimeandika uhakika na Serikali itasimamia, Wabunge na Watanzania sote tunaunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, nampa hongera Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dkt. John Joseph Magufuli kwa kusimamia Ilani ya CCM, amesimamia wanyonge wote Tanzania kwa kufanikisha kupunguza mambo mbalimbali kama ushuru pamoja na matatizo mengine, sekta zote amesimamia. Vilevile Rais wangu wa Zanzibar pamoja na Makamu wake wamefanyakazi nzuri Zanzibar kwa kusimamia Zanzibar nzima, maji, umeme pamoja na nyumba, barabara, nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu barabara; barabara za Tanzania zinatakiwa kuboreshwa kwa sababu wanapakia container kutoka Dar es Salaam mpaka kwenda mipakani, pamoja na mizigo midogo midogo, Serikali tunapata ushuru kutokana na mizigo, hawa watu wanapakia mizigo wanafika mpaka sehemu za Burundi, Kenya pamoja na Malawi, nashukuru sana Serikali kusimamia kutengeneza barabara iboreshwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri Mkuu pamoja na Makamu wa Rais wamesimamia Serikali yetu, Mheshimiwa Waziri Mkuu anasimamia Mawaziri wote, Mheshimiwa Waziri Mkuu anasimamia Wabunge wote kwa kushikamana na kufanyakazi nasi tunaunga mkono.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuzungumzia kuhusu bandari ya Zanzibar na bandari ya Dar es Salaam. Mheshimiwa Rais amekwenda kutembea nchi mbalimbali na bahati nzuri tumepata Rais wa Congo amekuja kutembelea Bandari yetu ya Dar es Salaam pamoja na reli ya standard gauge. Bandari ya Dar es Salaam inatakiwa kupanuliwa kwa sababu meli moja inapita, inatakiwa kupanuliwa ili zipite meli mbili kwa pamoja, kwa hivyo nampongeza Rais na Rais wetu wa Congo wakae pamoja tupate kuiendeleza bandari yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, bandari ya Zanzibar Mpigaduri, naomba Rais wangu wa Muungano amsaidie Rais wa Zanzibar ili bandari ya Mpigaduri itengenezwe kwa sababu container nyingi zinakuja na container zetu za Zanzibar zinakwamba Mombasa na mahali mbalimbali, hivyo ninaomba Serikali yetu ya Tanzania, naomba Muungano wetu Zanzibar tupate msukumo kutokana na Tanzania, Rais wetu wa Muungano Mheshimiwa Dkt. Magufuli aisaidie Zanzibar kutengeneza bandari yetu na kuboresha kwa sababu container kutoka Dar es Salaam inakwenda mpaka Burundi, inakwenda Kenya mipaka yote basi Serikali tunaongeza kipato.

Mheshimiwa Naibu Spika, reli ya standard gauge namshukuru Rais amefikiri Mheshimiwa Magufuli kufanya kitu cha muhimu sana kwa Tanzania itapakia mali mbalimbali, biashara ndogo, biashara kubwa, container na wananchi watafaidika kwa hivyo, peleka salama kwa Mheshimiwa Rais hongera sana kwa kutengeneza reli ya standard gauge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu viwanda, ninaomba Mheshimiwa Rais asimamie viwanda vyote. Viwanda vinatakiwa kuboreshwa kwa sababu viwanda vipo vya aina nyingi, kuna viwanda vya sukari, viwanda vya pamba, tumbaku, alizeti, pamoja na korosho na vingine. Viwanda hivyo lazima tusimamie vifanyekazi, vikifanyakazi viwanda basi tunaongeza mapato na TRA wanapata mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakuja…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bhagwanji muda wako umekwisha, ahsante sana. Ahsante sana Mheshimiwa Bhagwanji. (Kicheko/Makofi)

Waheshimiwa Wabunge tunaendelea na Mheshimiwa Sophia Mwakagenda atafuatiwa na Mheshimiwa Dkt. Godwin Mollel, Mheshimiwa Injinia Lwenge ajiandae.

MHE. BHAGWANJI MAGANLAL MEISURIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima yako, naunga mkono Serikali na bajeti. (Makofi)