Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mwantakaje Haji Juma (9 total)

MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Waziri nina swali moja la nyongeza.
Je, nyumba hizo zilizojengwa ziko wapi na Mkoa gani unaendelea kujengwa hizo nyumba? Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, nyumba hizi ziko katika Mikoa mingi ya nchi yetu, kwa upande wa Zanzibar, nyumba wameanza kujenga upande wa Pemba, bado Unguja wataingia katika awamu ya pili. Kwa hiyo, orodha ya Mikoa ni mingi siwezi kuorodhesha yote hapa, lakini nitakuwa tayari kumpatia Mheshimiwa Mbunge kwa maandishi endapo atahitaji.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa migogoro ya ardhi hapa nchini ni mingi na kwa kuwa migogoro ya ardhi inafanana, je, Serikali ina mapango gani wa kumaliza tatizo la Tabora Manispaa katika Kata ya Malolo ambalo mpaka Mheshimiwa Waziri wa Ardhi alifika akaona hali halisi na akatoa maelekezo lakini mpaka sasa halijatekelezwa? Je, kwa leo Serikali inatoa tamko gani kwa tatizo la Malolo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwanne Mchemba ambaye anataka kujua ni lini Serikali itamaliza mgogoro katika Manispaa ya Tabora kama alivyolielezea. Naomba niseme kwamba, Waheshimiwa Wabunge wote ni mashahidi kwamba migogoro ya ardhi imekuwa ni mingi sana kama hivyo amekiri wazi kwamba Mheshimiwa Waziri alikwenda na akatoa maelekezo lakini bado mgogoro ule haujamalizika na hata wakati amekwenda bado kulikuwa na migogoro mingine katika maeneo hayo. Kwa hiyo, tumejikuta kama Wizara pengine unakwenda ku-solve mgogoro mmoja ukirudi unakuta mwingine uko pale pale katika lile eneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilichukue hili suala la Mheshimiwa Mchemba kwa sababu tayari maelekezo yapo. Nitakachofanya ni kufuatilia kuweza kujua kwa nini yale maelekezo ya Mheshimiwa Waziri hayakutekelezwa mpaka leo halafu tuweze kuchukua hatua kwa wale ambao walipewa maelekezo hayo. Kwa sababu kwa sehemu kubwa wale Makamishina Wasaidizi katika Kanda ambao wapo wanatakiwa pia maagizo yakishatolewa na Mheshimiwa Waziri waweze kusimamia utekelezaji wake mpaka mwisho. Kama hili halijatekelezwa, ni wazi hata Kamishna Msaidizi wa Kanda ile hajatekeleza wajibu wake kama jinsi anavyopaswa kufanya. Kwa hiyo, tutalifuatilia kuweza kujua ili hatua ziweze kuchukuliwa.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri nina maswali madogo tu ya nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri. Kwanza, je, wanatumia vigezo gani vya usajili wa hivyo VICOBA?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wakiwa wanakopesha wanaanzia na kiwango gani cha hiyo mikopo, ili wananchi nao waweze kukopa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza vigezo vinavyotumika ni kuangalia kikundi husika kinajishughulisha na nini na kama kina wadau muhimu katika kikundi hicho, pamoja na aina ya shughuli kinachotaka kujishughulisha kikundi hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na swali lake la pili, ameuliza ni shilingi ngapi wanakopeshwa, hapa kinaangaliwa tu kikundi husika kina mtaji kiasi gani na kimeomba kiasi gani na hivyo, kuangalia kama wanaweza kukopesheka, kuangalia viashiria hatarishi ndani ya kikundi kile kama waliwahi kukopa na uwezo wao wa ku-manage biashara walianza lini. Kwa hiyo, tunaangalia mtaji wao endelevu na sustainability yao katika biashara wanayofanya.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, je, ni vikundi ngapi zilizochukuliwa hatua mpaka sasa?
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, je, ni vikundi ngapi zilizochukuliwa hatua mpaka sasa?
Mheshimiwa Naibu Spika, samahani ni shule ngapi zilizochukuliwa hatua mpaka sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu ameonesha concern kubwa ya suala zima la janga la moto katika maeneo yetu. Hili nimelisema katika jibu langu la msingi takribani shule 29.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la chanzo nani alisababisha imeonekana maeneo mbalimbali ni hitilafu ya umeme, lakini bado hatujabaini hasa watu mahsusi ambao wameshughulika katika suala la kuhujumu miundombinu hii na ndiyo maana tumeunda Kamati hizi shirikishi katika jamii zetu hasa katika ngazi za shule, lengo ni kuzuia baadae watu watakapobainika basi tuweze kuwachukulia hatua katika maeneo hayo.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu wa Waziri, nina swali dogo la nyongeza. Je, ni nini kipaumbele cha Serikali kiuchumi kwa watu wenye ulemavu kwa sasa na baadaye?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi ya kwamba Serikali tulitunga sheria hii pamoja na sera lengo kubwa ni kusaidia katika kutoa huduma mbalimbali kwa watu wenye ulemavu vilevile kuwajengea uwezo katika masuala ya kiujuzi ili waweze kujitegemea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika mipango mbalimbali ya Serikali tumehakikisha kwamba kundi hili la watu wenye ulemavu wanapewa fursa mbalimbali na kipaumbele; hasa ukizingatia katika Ofisi ya Waziri Mkuu ipo program ya ukuzaji ujuzi kwa ajili ya maendeleo ya vijana nchini ambapo tumetumia fursa hii pia kuwawezesha watu wenye ulemavu kupata ujuzi na wengi wao wameonesha uwezo mkubwa hasa baada ya kuhitimu mafunzo haya na kwenda kujiajiri na kuajiri vijana wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kama Serikali tunawapa kipaumbele sana watu wenye ulemavu na vilevile tutahakikisha kwamba tunaendelea kutoa fursa zaidi ili watu hawa waweze kujitegemea pia.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa fungu la mafuta katika magari hayo linakuwa ni kidogo, je, ni lini Serikali itaongeza mafuta hayo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili katika Mkoa wangu wa Magharibi ‘A’ mafuta wanapokea kwa siku lita saba au hawapokei kabisa, je, ni lini Serikali itawaongeza mafuta hayo? Ahsante (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia kwa ukaribu sana mazingira ya kazi ya askari wetu na kwa kweli watu wa Bububu hawakukosea na mimi mwenyewe nilishafika Bububu nikaona hali ya uhitaji wa usalama unavyohitajika.
Mheshimiwa Spika, niseme tu katika muhula kwanza, katika mwaka wa fedha uliopita nusu mwaka ya kwanza ukilinganisha na nusu mwaka ya pili utaona kwamba bajeti ya mafuta iliongezeka. Katika bajeti tuliyoipitisha fedha ambazo tulitenga kwa ajili ya mafuta ziliongezeka. Nashukuru wenzetu wa Wizara ya Fedha wamekuwa wakizitoa fedha hizo ambazo zinaenda kwa ajili ya mafuta ili kuweze kuwezesha vijana wetu waweze kufanya doria kikamilifu. Kwa hiyo jambo hilo litafanyiwa kazi tunavyomaliza bajeti ili waweze kupata fedha hizo waweze kufanya doria kikamilifu. (Makofi)
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini kidogo hayaniridhishi, kwa sababu yeye mwenyewe Naibu Waziri amekwenda kujionea kituo hicho cha Bububu, alikitembelea.
Je, kituo kile kwa sababu hakina computer, hakina photocopy machine na mpaka hivi sasa hivi wanaenda kutoa photocopy nje ya kituo. Ni lini Serikali itachukua hatua ya kukipatia computer na photocopy machine?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa sababu huko nyuma niliulizwa suala la gari ya polisi, kwa sababu kituo changu kipo barabarani na kina uhalifu mwingi katika Jimbo langu la Bububu.
Je, ni lini Serikali itatupatia gari hilo la Polisi ili kupunguzia wananchi usumbufu? Kwa sababu sasa hivi wakiomba gari binafsi wanachukua ili kwenda kusaidia kufanya doria?
Naiomba Serikali ijitahidi ili kituo changu kipate gari ya doria ili kupunguza usumbufu kwa wananchi. Ahsante.
NAIBU WAZIRI MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mwantakaje kwa jitihada zake za kuhakikisha kwamba mazingira ya askari wetu hasa katika Kituo cha Polisi Bububu katika Jimbo lake yanakuwa mazuri.
Mheshimiwa Spika, ni kweli tulifanya ziara ya pamoja kwenye kituo hiki na kuna mambo mengi tuliyarekebisha, lakini nimhakikishie, kama tumeweza kurekebisha mambo makubwa ambayo mwenyewe anafahamu, sidhani kama hili la photocopy na computer litatushinda. Nimwombe tu avute subira, tutalifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, upande wa suala la pili kuhusiana na gari, kwa sasa bado hatuna magari, lakini tunatarajia kupata magari. Kwa hiyo, tutaangalia ukubwa wa changamoto zilizopo nchi nzima, kwa sababu upungufu haupo Bububu peke yake, yako maeneo mbalimbali nchini. Kwa hiyo, kadri ya idadi ya magari itakapopatikana, tutaangalia uwezekano vilevile wa kukipatia Kituo cha Polisi cha Bububu. (Makofi)
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na maswali mawili ya nyongeza.
Je, Serikali inatumia vigezo gani kwa wananchi kupata hiyo mikopo?
Swali la pili, atakubaliana na mimi Mheshimiwa Naibu Waziri akiongozana na watalaam wake waende Jimboni kwangu kwenda kutoa elimu na kwa sababu wananchi wanataka kukopa fedha hizi ili wananchi na wao waondokane na umaskini. Je, Serikali lini watakwenda Jimboni kwangu Bububu ili kwenda kutoa mikopo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lako la kwanza kuhusu vigezo, kigezo kikubwa ambacho benki yetu ya kilimo inaangalia ili iweze kumkopesha mkulima ni kuangalia kama mradi ule unaotekelezwa na mkulima unaweza kukopesheka yaani valuable agricultural activity ambayo inaweza akawekeza na akapata faida yake na akaweza kurejesha mkopo huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakatika hili ndio maana Benki Kuu imetoa maelekezo kwa mabenki yetu yote kuhakikisha kwamba wakopeshwaji ambao wanaomba mikopo wanakuwa ni wale ambao taarifa zao zinaonesha wameweza kukopa na wakarejesha mikopo ili kuondokana na tatizo la mikopo chechefu ambayo mabenki yetu mengi yanapambana nayo. Serikali yetu ya Awamu ya Tano imepanga kuhakikisha wakulima wetu wanafikiwa na mikopo hii ya benki ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, namuahidi Mheshimiwa Mwantakaje baada ya Bunge hili mimi na watalaam wangu wa Benki yetu ya Kilimo tutakuja Jimboni kwako Bububu kuja kuwatembelea wakulima wa Bububu. (Makofi)
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini niiombe Serikali. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuondoa kabisa vitendo hivi vya udhalilishaji hasa vya kijinsia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kumekuwa na changamoto kubwa na ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia nasi kama Serikali tumeliona hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017 tuliandaa mpango mkakati wa kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto ambao unatambulika kama MTAKUWA na katika mpango mkakati huu Serikali imetoa maelekezo ya kuanzishwa Kamati za Ulinzi wanawake na watoto katika ngazi zote kuanzia ngazi ya Taifa mpaka ngazi ya Kitongoji na Vijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumeendelea kutoa elimu katika jamii kuhusiana na masuala haya lakini tumeendelea kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Idara ya Mahakama na Jeshi la Polisi kuhakikisha kwamba tumeanzisha madawati ya jinsia takribani 417 katika Jeshi la Polisi, vilevile tumeendelea kufanya kazi kwa karibu sana na Idara ya Mahakama pamoja na wenzetu wa Katiba na Sheria kuhakikisha kwamba mashauri haya yanapotokea basi hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya wale watuhumiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu kwa jamii, nitumie fursa hii kusema matukio mengi ya ukatili wa kijinsia yanafanywa na watu ambao wako karibu na ndani ya familia, niiombe sana familia wasimalizane ndani ya familia na badala yake watoe ushirikiano kwenye vyombo vya dola ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa. (Makofi)